Search This Blog

Friday, 20 May 2022

MTIKISIKO WA HIRIZI - 2

 







    Simulizi : Mtikisiko Wa Hirizi

    Sehemu Ya Pili (2)

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Kwa hesabu ya muuzaji, hata kama angeuza mavazi hayo kwa shilingi 12,000 bado angekuwa na faida. Isitoshe, hakuwa ameuza hata nguo moja katika nguo hizo tangu alipozileta kiasi cha mwezi mmoja uliopita. Hivyo, hakuwa na sababu ya kukataa.



    “Leta pesa.”



    Muda mfupi baadaye Shaka alikuwa katika mwonekano tofauti. Alitumia chini ya dakika mbili kuvaa zile nguo za uraiani juu ya mavazi ya jela huku yule muuzaji akiwa amepigwa butwaa.



    Bado Shaka hakuwa amehitimisha kilichomleta humo. Akaendelea kuangaza huku na kule. Macho yakagota sehemu ambayo kulitundikwa visu vya aina mbalimbali na vya ukubwa uliotofautiana.



    “Kile kisu bei gani?”



    “Alfu mbili na mia tano.”



    “Nipe.”



    Kisu kikatua mfukoni mwake. Akatoka hapo kwa mwendo wake uleule, mwendo wa taratibu na wa kujiamini. Na sasa hakutaka kuchelewa katika eneo hilo, alikodi teksi iliyomfikisha Magomeni Kondoa ambako alipata chumba katika gesti moja isiyokuwa na hadhi.



    Mara tu alipokwishaingia chumbani na kujifungia, alizivua zile sare za jela na kuzifutika chini ya kitanda. Akabaki na zile nguo mpya pekee. Kisha akatoka na kwenda dukani ambako alinunua lita moja ya mafuta ya taa na kurejea pale gesti.



    “Nionyeshe sehemu ya kuweza kuchomea makabrasha nisiyoyahitaji,” alimwambia mhudumu wa gesti.



    Mhudumu huyo, akiwa hajui hili wala lile, alimwonesha sehemu kulikokuwa na shimo dogo lililotumika kwa kutupia taka. Shaka aliporudi chumbani alizitwaa zile nguo za jela, zilizokuwa ndani ya fuko la nailoni, akatokanazo hadi huko shimoni ambako alizimwagia mafuta na kuzitia moto.



    Alirudi chumbani mwake baada ya kuhakikisha kuwa zile nguo zote za jela zimeteketea.



    *******



    ASKARI jela aliyesimamia kundi la wafungwa waliopaswa kwenda Viwanja vya Maonesho, aliendelea kuduwaa huku akimtazama Shaka aliyekuwa akiyoyoma taratibu machoni pake. Huenda alipaswa kuchukua hatua pale tu Shaka alipokaidi amri ya kuingia garini, lakini hakufanya hivyo. Na alipokuja kuzinduka, Shaka alikuwa ameshatokomea machoni pake.



    Akakurupuka kupuliza filimbi. Eneo hilo lote likazingirwa na askari, na wengine wakamwagwa mitaani kumsaka mfungwa aliyetoroka katika mazingira ya kutatanisha.



    Pamoja na msaada wa raia wema waliowaonesha njia alizopita mtu aliyekuwa amevaa nguo zilizoshabihiana kwa kila kitu na sare za wafungwa wa jela, na pamoja na mwanamke muuza duka kuthibitisha kufikiwa na mteja aliyevaa sare za jela na kuongeza kuwa mteja huyo alinunua nguo mpya na kuzivalia humohumo dukani, juu ya mavazi ya jela, bado haukuwa msaada ulioweza kutoa matunda mema.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Shaka hakuonekana, japo msako mkali uliendelea takriban kitongoji chote cha Keko.



    Naam, kilikuwa ni kizungumkuti cha aina yake!



    ********



    AKITAMBUA fika kuwa lazima msako mkali dhidi yake ungefanyika, Shaka hakutoka nje ya gesti hiyo siku nzima. Njaa ilipomsakama alimtuma chipsi mhudumu wa gesti. Koo lilipomkauka aliagiza bia. Kwa jumla alihakikisha hafanyi kosa atakalolijutia baadaye. Japo aliamini kuwa kwa ‘nguvu’ za baba yake, Mzee Songoro, asingepatwa na baya lolote, hata hivyo aliamua kuwa makini.



    Usiku ulipoingia alihitaji faraja ya mwanamke. Ndiyo, usiku kucha awe na mwanamke mrembo, mwanamke anayeyajua majukumu yake pale anapokumbana na mwanamume mwenye njaa ya mwanamke.



    Bia tano zilizosambaa katika mishipa yake ya damu zilimpa mhemuko kiasi cha kuamua kuzungumza kiutu uzima na mhudumu mmoja wa kike wa gesti hiyo, mazungumzo yaliyoanzia kwa ‘gia’ ndogo tu, bia mbili, chipsi-kuku na shilingi 10,000.



    Usiku huo ukawa wao. Wakakesha wakizungumza kwa furaha, wakanywa kwa kujidai na wakaikanda miili yao kwa fahari, wakifanya kila walichopenda kukifanya, na wakafanya kwa namna ya kipekee kiasi cha kujikuta kukipambazuka huku kila mmoja bado akimhitaji mwenzie.



    Hata hivyo, Shaka hakuwa limbukeni wa mapenzi. Kwa siku hii, zikiwa ni saa zisizozidi ishirini na nne tangu alipotoroka gerezani, aliamua kuwa makini zaidi na kuzitumia fedha zake chache alizonazo kwa uangalifu ili awe na uhakika wa kuliacha jiji hilo na aweze kufika mwisho wa safari yake.



    Akiwa bado kitandani, mkono wake mmoja ukilipapasa paja la Rukia, alikuwa akiwaza hili na lile kuhusu ratiba yake ya siku hiyo huku pia akifikiria ni hatua gani ambayo askari watakuwa wameichukua baada ya kutoroka gerezani jana katika mazingira ya kutatanisha.



    Aliamini kuwa kwa vyovyote vile nguvu ya msako dhidi yake itakuwa kubwa na ikiambatana na hasira kali kutoka kwa hao askari. Kwa kiasi fulani itachukuliwa kuwa amelidhalilisha Jeshi la Magereza.



    Itakuwa ni habari kubwa kwa vyombo mbalimbali vya habari hususan vile vyenye sera ya kuishambulia serikali kwa dosari yoyote itakayojitokeza katika taasisi zake. Itakuwa ni kashfa kwa Jeshi la Magereza. Kwa hali hiyo alipaswa kuwa makini zaidi katika muda atakaokuwa jijini Dar es Salaam.

    Alipaswa kuchukua tahadhari kubwa!



    Ni Rukia aliyemwingilia katika fikra zake. “Vipi, mpenzi, na jioni tutakuwa wote?” alimuuliza.



    “Nd’o maana’ake,” Shaka alijibu huku akitambua fika kuwa alikuwa akiongopa. Kumchukua mwanamke huyo jana usiku siyo kwamba alikuwa na chembechembe za mapenzi kwake. Hapana. Kwa kipindi hicho hakuwa ni mtu wa kumpenda wala kumwamini mwanamke yeyote. Ni tamaa ya kimwili tu iliyomwangusha kwa Rukia.



    “Tutakuwa wote,” aliongeza huku akiendelea kulipapasa paja lake. “Umeonyesha kuwa ni mwanamke wa shoka. Kwa vyovyote vile bwana’ko anaringa na kujisikia fahari kuwa na wewe.”



    “Nani kakwambia kuwa nina bwana?” Rukia aliuliza huku akijitia kukasirika, akaukunja uso na kumtazama Shaka kwa macho makali.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mwanamke mzuri kiasi hiki, mwenye sura inayovutia na umbo linalotamanisha, mwanamke unayejua kumtoa jasho mwanamume mwenye uchu wa ngono, uwe huna bwana?” Shaka alitiririsha maneno bila ya kutishwa na macho yale.



    Rukia alicheka kidogo kisha akasema, “Amini usiamini, mie niko peke yangu. Sina mume wala sina hawara hapa Dar.”



    “Kwa nini?”



    “Basi tu, nimeamua. Ni wewe nd’o nimejikuta nakuvulia nguo tangu niachane na aliyekuwa bwana’ngu kiasi cha miaka mitano iliyopita.”



    Shaka hakuwa mtu wa kumwamini mwanamke mapema kiasi hicho. Hata hivyo hakutaka kuuendeleza mjadala huo. Badala yake akasema, “Ok, nimekuelewa mrembo. Sidhani kama utakuwa umenihadaa. Nakuamini. Ni kwa kuwa tu muda huu nina majukumu mengine lakini kama siyo hivyo, nilitaka tuendelee kujichimbia hadi jioni.”



    “Na njaa?”



    “Yap, na njaa yetu.”



    Rukia alicheka kidogo. Akaupeleka mkono wake mahala fulani mwilini mwa Shaka ambako ulifinya kidogo kiasi cha Shaka kujikuta akipumua kwa nguvu, mwili ukimsisimka.



    “Kwa hiyo itakuwaje?” Rukia aliuliza.



    “Saa mbili usiku tuonane,” Shaka alijibu. “Wewe si upo hapahapa?”



    “Hapana. Nina kwangu. Hapa ni kazini tu. Saa hizi nitatoka, nitarudi saa nane mchana.”



    “Poa. Kwa hiyo ni kama nilivyokwambia. Mi’ nitakuwa humu ndani kuanzia saa mbili usiku.”



    *****

    RUKIA alipoondoka, Shaka aliingia bafuni haraka, akaoga kisha akamfuata kijana mmoja wa kiume ambaye ndiye aliyekuwa mhudumu wa mapokezi asubuhi hiyo. Akampatia shilingi 7,000 huku akimwambia, “Niletee magazeti yote ya leo.”



    “Yote ya leo?” kijana yule alishangaa. “Mbona kila siku yanatoka magazeti mengi sana! Pesa hii itatosha?”



    “Magazeti ya kila siku!” Shaka alisisitiza. “ Siyo gazeti linalotoka leo na kutoka tena baada ya siku tatu au wiki. Nataka magazeti yanayotoka tangu Jumatatu hadi Jumapili. Umenielewa?”



    “Ya Kiingereza na Kiswahili?”



    “Ya Kiswahili tu!”



    “Nimekusoma mkuu.”



    Kijana huyo alitoka na kurejea baada ya dakika kumi, mkononi akiwa na magazeti saba ya Kiswahili. Mara tu alipokwishamkabidhi Shaka magazeti hayo, alitoka huku akimwangalia kwa namna ya kumshangaa.



    Shaka hakumjali, alijilaza kitandani na kuanza kuyapitia magazeti hayo. Magazeti yote yalikuwa na tangazo lililohusu kutoroka kwake gerezani, tangazo lililoambatana na picha yake kubwa katika ukurasa wa mbele!

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    TANGAZO hilo lilinakshiwa na ahadi ya zawadi nono ya shilingi milioni kumi kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwake.



    Alitarajia kuwa tangazo hilo lingetolewa kwenye vyombo mbalimbali vya habari yakiwamo magazeti, redio na televisheni na picha yake kutumika katika kuikoleza habari au tangazo hilo. Lakini hakutarajia kuwa magazeti yote yatokayo kila siku kwa lugha ya Kiswahili yangetoa tangazo hilo. Alidhani kuwa gazeti moja au mawili tu ndiyo yangetumika na tangazo hilo au habari hiyo ingekuwa katika kurasa za ndani, siyo mbele!



    Hali hii ilimtia shaka na akahisi kuwa kuendelea kujichimbia hapo gesti hata kwa nusu siku kusingemsaidia, zaidi kungempeleka katika matatizo.



    Akayatupa magazeti yote kitandani. Akasimama na kuzichomoa fedha zilizokuwa mfukoni mwake. Akaguna. Zilikuwa ni shilingi 50,000 tu. Hakushangaa, aliyakumbuka matumizi ya jana yake; nguo, kisu, teksi, chakula, bia, gharama ya chumba na zile 10,000/- alizompatia Rukia kwa makubaliano ya kumstarehesha usiku.



    Hizi fedha alizonazo si lolote si chochote kama atataka kwenda Kigoma. Zisingeweza kumfikisha popote. Ili aweze kufika huko kwa kutumia usafiri wa treni alipaswa kutumia si chini ya shilingi 50,000 kwa usafiri wa daraja la tatu, na hapo bado akiwa na upungufu wa fedha za matumizi njiani mathalani kula na kadhalika.



    Kama atataka kutumia usafiri wa basi, itabidi ajipinde upya kusaka nyongeza. Zingehitajika si chini ya shilingi 70,000! Kwa upande wa treni, aliona kuna kizungumkuti cha aina yake. Aliuona usafiri huo kama haustahili kuendelea kuwepo. Tangu Shirika la Reli libinafsishwe, utaratibu wa usafiri umekuwa haueleweki. Mara leo treni ipo, mara haipo, mara leo treni ya mizigo imepinduka na kuziba njia, matokeo yake zinapita siku sita hata wiki kwa ukarabati, usafiri hakuna!



    Hadi asubuhi hii hakuwa na taarifa yoyote kuhusu usafiri wa treni kwa siku hiyo. Na hakuwa na muda wa kufuatilia. Muhimu kwake ilikuwa ni kupata pesa zaidi na kuiacha Dar, basi! Kama ataondoka kwa treni, Ndege, lori au basi, hilo litajulikana mbele kwa mbele.



    Wazo moja likamjia akilini. Ubabe. Atumie ubabe ili aongeze kipato na kwa kutumia ubabe huohuo apate usafiri wa kumfikisha Morogoro au hata Dodoma ambako angetumia mbinu nyingine kupata usafiri wa kumfikisha Kigoma.



    Mara akatoka chumbani humo kwa hatua ndefu hadi mapokezi. Hapo akasita baada ya kutomkuta mhudumu. Hakujali, zaidi alifurahi kwa kutomkuta kwani hakuwa na muda zaidi wa kuzungumza naye, isitoshe alishakuwa na shaka kuwa huenda akawa amezitazama vizuri picha zilizotanda kwenye magazeti yale manne ya Kiswahili na hivyo kuamua kwenda kuripoti kituo cha Polisi.



    Hakuendelea kuduwaa eneo hilo. Alitoka na kuingia mitaani. Baada ya kuvuka mitaa miwili, mitatu mara akasimama kwenye duka moja. Hapo akanunua kofia pana na kutoka baada ya kukosa miwani. Akaendelea kukata mitaa.



    Hatimaye akakutana na kijana mmoja, maarufu kwa jina la ‘Machinga’ akiuza miwani. Akanunua moja na kuipachika usoni papohapo. Naam, sasa akajiona yu timamu, na tayari kwa safari!



    Ni eneo hilohilo la Magomeni, kando ya kituo cha daladala cha Usalama ndipo alipotarajia kupatumia kwa kuianzia safari yake. Kutoka hapo aliponunua miwani hadi kwenye kituo hicho kulikuwa ni umbali wa hatua kama mia moja au mia mbili hivi. Akavuta hatua ndefu akielekea mahali hapo.

    Mara akaamua kuvuka barabara hiyo na kushuka upande wa pili ambako kuna baa mbili ambazo kwa wakati huo kulikuwa na watu wachache walioketi chini ya miti baadhi wakinywa soda, baadhi wakinywa bia na baadhi wakiwa wamekaa tu labda kwa kufuata kivuli.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mbele kidogo kulikuwa na teksi zisizopungua kumi kituoni hapo, baadhi zikiwa na utambulisho rasmi kuwa ni teksi halali, na nyingine zikiwa ni zile ambazo huitwa ‘teksi bubu.’



    Yeye hakujali uhalali au uharamu wa teksi, alijali ubora.

    Mbele yake aliiona teksi moja maridadi, akaifuata. Alipoifikia na kuchungulia ndani akamwona dereva kaegemea kiti, usingizi umemteka. Akamgusa bega kidogo. Dereva akashtuka na kufikicha macho. Akajiweka vizuri kitini. Kisha: “Karibu anko, karibu sana.”



    Shaka hakujibu, alifungua mlango wa mbele, kushoto na kujipweteka kitini. “N’ambie, gari iko fiti?”



    “Iko fiti, mjomba,” dereva alijibu. “Hapa nd’o umekuta gari. Hiki ni chuma cha reli.”



    “Mafuta? Tukiondoka hapa, sio unasema eti unapitia petrol station.”



    “Hapana,” dereva alijibu haraka. “Mimi sio kama madereva teksi wengine. Nina mafuta ya kutosha.”



    “Kiasi gani?”



    Dereva alifikiri kidogo kisha akajibu, “Kama lita kumi, hivi.”



    “Ok, twende. Shika Morogoro Road. Tukifika Ubungo nitakuelekeza zaidi.”



    Teksi iliondoka taratibu katika eneo hilo. Walipofika Ubungo dereva akasema, “Tuko Ubungo, mzee. Inakuwaje?”



    “Twende!”



    Gari likazidi kusaga lami. Wakafika Kimara.



    Wakaivuka.



    “Tunakwenda mbali, mzee?” hatimaye tena dereva alihoji.



    Kwa kiasi fulani alianza kuingiwa na wasiwasi. Hakutarajia kuwa wangekuwa na safari ndefu kiasi hicho. Kama angejua, angewahi kutamka kiwango cha nauli iliyopaswa kulipwa.

    Sasa walikuwa wakiipita Mbezi.



    “Ni Kibamba. Kama tatizo lako ni pesa, nipe chaji yako.”



    “Kwenda na kurudi?”



    “Kwenda tu.”



    “Hamsini tu, mzee wangu.”



    “Nakupa arobaini.”



    “Poa.”



    **********



    TEMBA, kijana aliyetumwa na Shaka kununua magazeti, alijawa na dukuduku kila alipozitazama picha za kurasa za mbele za baadhi ya magazeti hayo. Akiwa ndiye aliyewapokea wageni wote wa gesti hiyo siku iliyopita, tayari alikwishaikariri vizuri sura ya Shaka.



    Alichokifanya mara tu baada ya kumkabidhi Shaka magazeti yake ni kwenda kununua gazeti lingine moja. Na hakurudi kule gesti moja kwa moja bali aliganda sehemu fulani na kulisoma kwa kina tangazo lile sanjari na kuitazama kwa makini zaidi picha husika iliyokuwa na maelezo chini yake:



    JINA: SHAKA SONGORO

    KABILA: MMANYEMA

    DINI: HAIJULIKANI

    UMRI: MIAKA 35-40



    MWENYE PICHA HIYO HAPO JUU NI JAMBAZI HATARI ALIYEKUWA AKITUMIKIA KIFUNGO KATIKA GEREZA LA KEKO JIJINI DAR ES SALAAM. KATIKA MAZINGIRA YA KUTATANISHA MTU HUYO AMETOROKA AKIWA CHINI YA ULINZI. ZAWADI NONO YA SHILINGI MILIONI KUMI (10,000,000/-) ITATOLEWA KWA YEYOTE ATAKAYEFANIKISHA UPATIKANAJI WAKE.



    Temba akashusha pumzi ndefu na kuanza tena kutembea akielekea gesti. Alipofika aliingia moja kwa moja kwenye chumba kilichotumiwa kwa kuhifadhi shuka na vifaa vingine vya gesti hiyo. Huko alimkuta Mado, mmoja wa wafanyakazi wenzake akiwa anafanya usafi.



    “Mado,” alimwita kwa sauti ya mnong’ono huku akiingia chumbani humo na kuurudishia mlango. Akampa gazeti lile huku akimwonyesha picha ile iliyoutawala ukurasa wa mbele.

    Mado aliitazama picha ile kwa makini kisha akasema, “Hii sura siyo ngeni sana machoni mwangu.”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unadhani umeshamwona wapi?”



    “Sikumbuki. Lakini kama sio jana basi juzi nimemtia machoni.”

    Temba akacheka kidogo kisha akasema, “Soma maelezo hayo hapo chini.”



    Mado alitulia na kuyasoma maelezo kwa makini. Hatimaye akahema kwa nguvu na kunong’ona, “Anaitwa Shaka Songoro.”



    “Na kuna bonge la mshiko kwa atakayemtosa kwa maafande,” Temba alidakia. “Milioni kumi ziko nje, nje mwanangu!”



    “Upuuzi,” Mado aliponda. “Dar ni kubwa sana. Isitoshe jamaa mwenyewe huyo sio bwege, mwanangu. Hawezi kuwa bado anabunya-bunya na kumbwela-mbwela kwenye mitaa hii ya Dar. Mtu anajua fika kuwa atasakwa, sa’ unafikiri atalemaa hivihivi? Atakuwa kishasepa mwana.”



    Ukimya wa kitambo kifupi ulitawala, Mado na Temba wakitazamana. Kisha Mado akasema, “Achana na dili hilo lisilokuwa na maana…”



    “Hapana, Mado,” Temba alimkata kauli. “Nina wasiwasi na mtu mmoja.”



    “Nani?”



    “Huyu jamaa aliyeingia jana.”



    “Yule bonge la mtu?”



    “Ndiyo. Hebu itazame vizuri picha hii.”



    Kwa mara nyingine Mado aliikazia macho picha ile kisha akaguna. Akaunyanyua uso na kumkazia macho Temba.



    “Kwani huyu jamaa anaitwa nani?”



    “Sijui anaitwa nani. Tatizo hapa tunafanya biashara kisirisiri.



    Hakuna cha leseni na wala hatulipii kodi ya mapato. Mteja akija ni kuongea naye tu na kupeana malipo, basi. Haandikishwi kwenye leja wala nini.”



    “Tabia yake umeionaje?”



    “Ni hiyo inayonishangaza,” Temba alijibu. “Aliingia jana kitu kama saa nne hivi, asubuhi. Na hakutoka tena. Msosi aliagiza, bia pia aliagiza. Usiku kucha akawa na Rukia.”



    “Anaweza kuwa ni yeye?!”



    “Kwa asilimia tisini na tano naamini ni yeye!” Temba alisema kwa msisitizo.



    “Na hadi muda huu yuko chumbani?”



    “Atakuwemo! Nimempelekea magazeti yake muda huuhuu, kama dakika kumi zilizopita.”



    “Basi kumbe shwari tu,” Mado alisema huku akiacha kila alichokuwa akikifanya. Akaongeza, “Kuna milioni kumi za bure! Zinaelea-elea tu kudadadadadadeeeeek! Hakuna kuziacha!”



    Wakati wakikurupuka kutoka chumbani humo, hawakuwa wakijua Shaka alikuwa akiwaza nini chumbani alikokuwa.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ********



    “PAKI pembeni, kuna dharura,” Shaka alimwamuru dereva teksi. Wakati huo walikuwa katika eneo lisilokuwa na watu wala nyumba yoyote.



    Dereva alitii amri hiyo.



    Mara Shaka akaangaza macho huku na kule; mbele, nyuma, kushoto na kulia kisha akakichomoa kisu chake taratibu bila ya dereva yule kugundua.



    Kwa wepesi wa aina yake, akitumia asilimia kubwa ya nguvu alizojaaliwa, alikitumbukiza kisu kile tumboni mwa dereva kisha akakichomoa na kukizamisha mara mbili kifuani! Damu nyingi ilimtoka dereva yule, na Shaka alikuwa makini kuhakikisha kuwa damu hiyo haimrukii. Akimwinamisha huku kamziba kinywa ili asipige kelele.



    Alimwacha katika hali hiyo hadi alipohakikisha kuwa amekata roho. Kilichofuata ni kumpekua mifukoni ambako alikuta fedha, shilingi 50,000. Akazichukua na kuzitia katika himaya yake.



    Hakuwa tayari kuendelea kuwa na maiti hiyo humo garini, hivyo alipogundua kuwa hakukuwa na mtu yeyote ambaye angemwona, na wala hakukuwa na gari lolote lililokuwa likija, alimtoa garini, akamburuta hadi kando ya barabara, nyasini na kumwacha katika eneo ambalo aliamini kuwa haitakuwa rahisi kuonwa kwa mbali na mpitanjia.



    Aliporudi garini alichukua muda mfupi kuifuta michirizi michache ya damu akitumia tambara bovu alilolikuta humohumo.



    Sura yake ikiwa imeshabadilika na kutangaza bayana kuwa yu tayari kwa lolote, liwe la shari au heri, aliketi nyuma ya usukani na kulitia gari moto.



    Hakuwa dereva mzuri wa gari, isitoshe, alikumbuka kuwa dereva yule alimwambia kuwa kulikuwa na lita kama kumi tu hivi za mafuta, hivyo hakutaka kujidanganya kuwa kulitumia gari hilo kutakuwa na maana yoyote. Ni dhahiri kukamatwa kulikuwa wazi.

    Hakufika hata Kibaha, alilitelekeza kwenye kijiji kimoja na kupata usafiri wa basi lililokuwa likielekea Dodoma. Saa 11 jioni akawa ndani ya Mji wa Dodoma, mji aliouzoea na kuupenda kutokana na hali yake ya hewa.



    Usiku huo akaumalizia mjini hapo. Asubuhi ya siku iliyofuata, alikwenda stesheni kusubiri treni. Hakutaka kupoteza muda kwa kufuata taratibu za upatikanaji wa tikiti, aliamua kusafiri ‘kimagumashi’ hadi Kigoma.



    Treni ilipowasili aliingia katika behewa la vinywaji na vyakula.



    *******



    MARA tu baada ya Temba na Mado kutoa taarifa katika kituo cha Polisi cha Magomeni, mkuu wa kituo hicho aliwasiliana haraka na Kituo Kikuu ambako aliongea na Inspekta Banda na kumpa taarifa hiyo.



    Ilikuwa ni taarifa iliyomshtua na kumshangaza sana Inspekta Banda, lakini pia ikimpa matumaini ya kulipatia ufumbuzi suala hilo. Papohapo akamhoji mkuu wa kituo cha Magomeni: “Vijana hao waliokupa taarifa bado uko nao hapo kituoni?”



    “Wapo,” Mkuu wa kituo cha Magomeni alijibu na kuongeza, “Nadhani vichwani mwao wanaziwazia milioni kumi.”



    Kicheko cha dhihaka kikamtoka Inspekta Banda. “Yaani wanataka kutajirika kupitia kwa Shaka?”



    “Labda.”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ok, utusubiri, baada ya muda mfupi tutakuwa hapo.”



    Dakika chache baadaye, Inspekta Banda na Sajini Kessy walikuwa ndani ya gari dogo lisilokuwa na nembo ya Jeshi la Polisi wakielekea Magomeni.



    “Shaka ametugeuza mabwege sisi wote; Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi,” Banda alisema kwa hasira wakati gari likiteleza kwa kasi katika Barabara ya Morogoro. Kisha akaongeza, “Safari hii nikimtia machoni nitamshindilia risasi kwa hasira. Hatuwezi kukosa la kusema kwa vyombo vya habari kuhusu kifo chake. Ni kwamba alijaribu kutoroka wakati akiwa chini ya ulinzi. Basi!”



    “Kwa kweli ni jitu la ajabu sana,” hatimaye Kessy alisema. “Kinachonishangaza ni jinsi alivyowatoka askari pale Keko. Hivi afande, inakuingia akilini kuwa Shaka alitoroka?”



    “Una maana gani?” Inspekta Banda alimtazama kessy kwa macho makali.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog