Simulizi : Mtikisiko Wa Hirizi
Sehemu Ya Tatu (3)
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“N’na maana kuwa Shaka hakutoroka. Aliruhusiwa kuondoka!”
“Aliruhusiwa? Aliruhusiwa na nani?”
“Hilo ni jambo lingine. Lakini mimi binafsi hainiingii akilini kuwa Shaka alitoroka. Atatoroka vipi chini ya ulinzi, akiwa ni mtu mwenye rekodi mbaya sana anayepaswa kuchungwa kama mtu yeyote anavyoichunga mboni ya jicho lake?”
Inspekta Banda aliguna.
“Unasikia afande,” Kessy aliendelea. “Shaka alihukumiwa jela akiwa ni mtu hatari, jambazi sugu ambaye vyombo vyote vya dola vinamtambua. Pale Keko wanamjua vizuri Shaka. Walimpokea wakiwa wanamjua vizuri. Kwa vyovyote, walipaswa kumchunga vilivyo.”
“Lakini nadhani hujaisahau ripoti ya kutoweka kwake pale gerezani,” Banda alisema. “Shaka aliondoka katika mazingira ya kutatanisha…”
“Kutatanisha vipi afande wakati inasemekana kuwa yule askari aliyekuwa na kundi la wafungwa alibaki ameduwaa tu wakati Shaka akiondoka taratibu?” Kessy alikuwa king’ang’anizi.
“Kwa hiyo unataka kusema kwamba kulikuwa na njama za kumtorosha?”
“Ndivyo picha inavyojionyesha.”
“Ok, lakini hilo silo jambo linalotuhusu kwa sasa,” Banda alisema. “Twende kwanza Magomeni. Ni huko tutakapopata la kufanya.”
Walipofika Magomeni na kuwahoji Mado na Temba wakapata picha ya matumaini. Wakatoka.
“Anaweza kuwa yeye?” Kessy alimuuliza Banda wakati akiondoka hapo kituoni.
“Ndiye,” sauti ya Inspekta Banda ilikuwa kavu. “Niliepuka kusema hivyo mbele ya wale vijana ili kuepusha usumbufu ambao wangetupa. Kwa vyovyote wangetaka kujua watazipataje milioni zao kumi.”
Kicheko kikamtoka Kessy. Akauliza, “ Wana ndoto za milioni kumi kabla hata mtuhumiwa hajapatikana?”
Inspekta Banda hakujibu.
********
SHAKA alitambua fika kuwa alipaswa kuwa makini dhidi ya askari, hivyo alipoingia ndani ya treni, alikwenda moja kwa moja kwenye behewa la vinywaji na vyakula. Huko aliketi na kuagiza chupa ya maji lita moja. Akatulia kitini akinywa taratibu.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hadi treni ilipofika kituo cha Saranda hali ilikuwa shwari. Kituoni hapo akashuka na kuagiza kuku na viazi mbatata kisha akarudi behewani. Akiwa na miwani yake mieusi usoni, miwani ambayo hakuwa tayari kuitoa bila ya sababu muhimu, huku kofia ikiwa imeganda kichwani pake, Shaka alianza kukifakamia chakula hicho kwa pupa na baada ya dakika chache tu zoezi hilo likawa limehitimishwa.
Akaingiza mkono mfukoni na kutoa noti zilizokuwamo. Alipozihesabu, akafarijika. Zilikuwa ni pesa za kumtosha kiasi. Kwa kiwango hicho hakuiona sababu ya kumfanya ashindwe kunywa bia mbili, tatu katika kuiliwaza akili yake kama alivyoamini. Saa moja baadaye koo likawa limeshateremsha bia mbili. Akaongeza ya tatu.
Hadi treni ilipokuwa inaingia Tabora, bia tano zilikuwa zimeshatua tumboni mwake na kuichangamsha akili yake. Naam, kwa kiasi fulani alijihisi kuwa timamu kisaikolojia huku pia akijali kuwa makini katika maongezi na mtu yeyote.
Kwa jumla hakutaka kuzoeana na yeyote kwa kiwango kikubwa, na hilo alilifanya kwa kuwa hakumwamini yeyote kwa kipindi hicho.
Aliendelea kukaa humo katika behewa la vinywaji na maakuli hadi saa 7 usiku. Na wakati huduma ilipositishwa na wateja kutakiwa kuondoka, yeye alimwita mmoja wa wahudumu wa behewa hilo na kunong’ona naye pembeni. Muda mfupi baadaye kijana huyo alikuwa na shilingi 5,000 kibindoni.
“Us’konde mwanangu,” Shaka aliambiwa. “Pumzika humu hadi kunakucha. Na kama unataka bia unaweza kuendelea kuagiza.”
Alichohitaji Shaka siyo kuendelea kukaa humo ili anywe bia, hapana. Shida yake ilikuwa ni kupata nafasi ya kulaza mbavu hadi kunakucha. Kama angekuwa na pesa za kutakata asingesita kuonana na TT na kumpa nauli ya chumba cha daraja la kwanza. Baada ya hapo angemtafuta ‘mrembo’, kati ya ‘warembo’ wengi wanaozagaa-zagaa ndani ya mabehewa, na ‘mrembo’ huyo angeifanya safari kuwa fupi kuliko ilivyo.
ASUBUHI ya siku iliyofuata treni iliingia Kigoma mjini. Na kama alivyokuwa makini safarini, hata pale stesheni Shaka hakupachukulia kwa uzito wa kawaida. Alijua fika kuwa askari nchi nzima watakuwa na taarifa kuhusu yeye, hivyo watakuwa wakimsaka kama gaidi au haini.
Hadhari ikapewa kipaumbele. Akatulia behewani akiwaacha wenye haraka zao wateremke, yeye akawa miongoni mwa wachache wa mwisho. Na alipoteremka alikwenda moja kwa moja kukodi teksi moja kati ya nyingi zilizokuwa zimefurika mbele ya jengo la kituo hicho.
Teksi hiyo haikumpeleka mbali, alipofika mbele ya soko kuu aliteremka na kumtupia dereva shilingi 3,000. Kwa hatua ndefu akaingia katikati ya soko ambako alizunguka hapa na pale bila ya sababu maalumu kisha akatokea upande wa pili, jirani na Benki ya Taifa ya Biashara ambako alikodi teksi nyingine.
Muda alioutumia tangu kuachana na ile teksi ya kwanza, kuzunguka ndani ya soko hadi kukodi teksi ya pili, hazikuzidi dakika tatu, na alifanya hivyo katika kuchukua hadhari dhidi ya hatari yoyote ambayo ingemnyemelea.
Dakika kumi baadaye alikuwa akiteremka kwenye makutano ya Barabara za Lumumba na Mwembengoma, kitongoji cha Mwanga. Kutoka hapo alipita hapa na pale akielekea nyumbani, Mtaa wa Mabatini.
Alipofika nyumbani wazazi wake walishtuka lakini wakampokea kwa furaha.
“Kuna msukosuko wowote uliokupata?” Mzee Songoro alimuuliza wakati wameketi sebuleni.
“Hapana, sijapata msukosuko wowote, baba.”
“Nilijua,” Mzee Songoro alisema. “Nilijua tu kuwa hutapata matatizo yoyote. Sasa tulia. Najua Polisi wanahaha kukutafuta. Wanajua wewe ni mzaliwa wa hapa Kigoma. Kwa hiyo hata polisi wa hapa watakuwa wameshapewa taarifa ili wakusake. Lakini hilo lisikutishe. Dawa yao ninayo. Mimi ndo Songoro mzaliwa wa Tongwe. Hapa ni maji marefu.”
Asubuhi ya siku iliyofuata Mzee Songoro aliamka mapema, akaenda kituo cha Mwembetogwa ambako alipanda basi lililomfikisha katika ule msitu ambao alikwenda siku moja kabla hajafunga safari ya kwenda Dar es Salaam ‘kumkomboa’ Shaka.
Huko aliutafuta mti mwingine na alipoupata, aliuparua magamba, akayachuma majani na kuyafutika kwenye mkoba. Ni hilo tu lililompeleka huko. Kilichofuata ni kurudi kando ya barabara kuu ambako zilimchukua dakika chache tu kupata usafiri wa basi lililomrudisha mjini.
Akiwa nyumbani aliyachemsha majani na magamba hayo kwa moto mwingi hadi yakalainika kwa jinsi alivyotaka. Rangi ya maji yale nayo ilibadilika na kuwa nyekundu kupindukia.
Kazi hiyo ilipokamilika alimwita mwanaye, chumbani na kumwambia, “Mambo tayari. Vua nguo zote ulale hapo kwenye mkeka.”
Shaka alitii agizo hilo. Mzee Songoro alitwaa kitambaa, akachovya ndani ya yale maji yaliyochanganyika na majani pamoja na magamba kisha akaanza kumkanda mwilini. Maumivu makali yalipenya maungoni mwa Shaka kiasi cha kumfanya atoe miguno mizito.
“Jikaze! Vumilia mwanangu,” Mzee Songoro alimwambia. “Hili ndilo zoezi la mwisho katika kuiimarisha kinga yako. Vumilia, we’ ni mwanamume! Jikaze!”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kazi hiyo iliendelea.
Baada ya kumkanda mwili wote, mzee Songoro alitwaa wembe, akamtia chale mikononi, miguuni, kifuani, tumboni, shingoni na kwenye paji la uso. Kisha alimpaka unga mweusi katika chale hizo huku akinong’ona maneno fulani ambayo hayakufika masikioni mwa Shaka.
Likafuata agizo lingine: “Sasa vaa nguo zako, halafu kasimame pale juani.”
Wakati Shaka akiwa pale juani, Mzee Songoro alikifuata kivuli chake, akachota mchanga kidogo na kuuchanganya na unga mweusi uliokuwa kiganjani mwake. Kwa mara nyingine akanong’ona maneno machache huku akimwagia mchanganyiko huo wa mchanga na unga mweusi toka kichwani hadi nyayoni.
“Kazi imekamilika,” hatimaye alimwambia huku akimkabidhi hirizi. “Hii hirizi uivae kiunoni. Na hakuna kuoga hadi jua litakapozama. Dawa hii inatakiwa kupenya vizuri mwilini, hivyo usikiuke haya maagizo ninayokupa. Umenielewa?”
“Ndiyo, nimekuelewa, baba,” Shaka alijibu kwa unyenyekevu.
********
TAARIFA kuhusu maiti iliyokutwa mtaroni, kando ya Barabara ya Morogoro, kilometa chache kabla ya kufika Kibaha, ziliyafikia masikio ya Inspekta Banda na mwenzake, Sajini Kessy saa saba mchana wakati wakiwa ofisini katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam. Muda mfupi baadaye zikapatikana taarifa za kutambuliwa kwa maiti hiyo.
Baada ya taarifa ya kutoweka kwa mfungwa katika gereza la Keko siku iliyopita, mfungwa aliyekuwa na sifa ya kutenda uhalifu mkubwa hata kutoa roho za watu, akili ya Inspekta Banda ilizama kwa mtu mmoja tu; Shaka Songoro!
Hadi kufikia siku hiyo, hakuwa na tetesi zozote kuhusu ni wapi atakakokuwa Shaka, lakini alijenga imani kuwa lazima atakuwa kwenye mpango wa kulikimbia jiji. Hivyo, hata alipokuwa meza moja na Sajini Kessy, hakusita kuziweka bayana hisia zake. “Kwa vyovyote huyo atakuwa ni Shaka tu,” alisema.
“Kwa nini unadai hivyo, afande?” Kessy alimuuliza.
Banda alikohoa kidogo kisha akasema, “Inasemekana marehemu alikuwa ni dereva teksi. Na alitoka Magomeni akiwa na abiria mmoja aliyevaa kofia pana kichwani na miwani myeusi usoni.
“Madereva wa pale Magomeni wanadai kuwa marehemu aliondoka na abiria huyo kitu kama saa tatu hivi, asubuhi. Hakurudi tena hadi ilipokuja kupatikana maiti yake.”
“Lakini afande,” Kessy alisema na kusita. “Wale vijana wa gesti wanasema mpangaji wao anafanana sana na huyu mtu,” akamwonyesha picha ya gazetini. Kisha akaendelea, “Na hao madereva wanadai kuwa huyo abiria alivaa kofia na miwani myeusi. Huoni kuwa hao ni watu wawili tofauti?”
“Wanaweza kuwa watu wawili tofauti au ni mtu yuleyule,” Inspekta Banda alisema. “Kumbuka, yule ni jambazi sugu na mkongwe. Unadhani atakuwa mjinga kiasi gani, aiache sura yake hadharani huku akitambua fika kuwa anasakwa? Hawezi kuwa bwege kiasi hicho. Kwa vyovyote lazima atapitia dukani ambako atapata kofia na miwani kwa nia ya kuubadili mwonekano wake kwa watu. Au atafanya chochote kile katika kuhakikisha hatambuliki kwa urahisi kwa watu. ”
Kessy aliyatafakari maneno hayo ya Banda na kwa kiasi fulani akajiona yu mpumbavu kwa kutolitambua hilo mapema kabla hajatamka chochote.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hatashindwa!” Inspekta Banda alisisitiza. “Shaka siyo chizi. Ana akili timamu. Lazima afanye mambo yake kwa mpangilio, umakini na kwa tahadhari kubwa. Ni mhalifu mwenye uzoefu na kazi yake!”
“Kwa hiyo, afande, operesheni yetu ilenge kumsaka Shaka pekee?”
“Shaka nd’o apewe kipaumbele huku upelelezi zaidi ukiendelea.”
******
SHAKA aliupenda uhuru. Na alipenda kuutumia uhuru huo kwa starehe. Pesa zilipojikita mifukoni mwake, pesa zinazoweza kumtia kiburi, alipenda kuingia kwenye kumbi za dansi kuburudishwa na muziki na kujistarehesha kwa vinywaji.
Si hayo tu, bali pia ni pesa hizo zilizompa kiburi cha kuwadaka wanawake warembo ambao walijua ni kipi cha kumfanyia mwanamume mkware, apendaye kujistarehesha na wanawake watundu.
Ndiyo, aliuzoea mfumo huo wa maisha akiwa jijini Dar es Salaam, jiji aliloamini kuwa ni kitovu cha maraha Tanzania. Lakini alifanikiwa kuponda raha hizo pale tu pesa zilipofurika mifukoni mwake.
Siku tatu za mwanzo akiwa mjini Kigoma alijiona kama vile yu jehanamu. Zile starehe alizozipenda na alizozizoea hakuzipata. Na hakuzipata kutokana na ukosefu wa pesa. Akiba pekee aliyokuwa nayo haikuzidi shilingi 10,000. Kwake, hizo hazikuwa ni pesa za kumfanya ajisikie yu miongoni mwa wanaume duniani. Ataingia baa kufanya nini akiwa na vijisenti hivyo? Ataupata wapi ujasiri wa kuzungumza na mwanamke mzuri akiwa na kiwango hicho kidogo cha pesa?
Hivyo hakutaka kuendelea kutaabika, aliamua kutumia mbinu zake alizozizoea ili apate pesa zaidi. Ndipo alipoanza kuvinjari kwenye vibanda vya gongo ambako zaidi ya kuuza pombe hiyo pia zilipatikana bia za Tanzania hata za Burundi na Kongo.
Aliingia katika nyumba hizo akiwa ni mteja wa bia na watu wakampapatikia hususan wale wanywaji wa gongo ambao aliwanunulia chupa moja ya ‘fanta’ iliyotosha kuzichangamsha akili zao huku yeye akinywa bia taratibu.
Ni katika nyumba moja kati ya tatu alizoingia ndiyo aliyoiona inafaa kwa malengo yake. Japo ndani ya nyumba hiyo kuliuzwa gongo na bangi, hata hivyo isingekuwa rahisi kwa mtu wa kawaida kubaini hivyo. Wateja wake walikuwa ni ‘wastaarabu,’ wasiopenda kelele wala kulewa sana.
Isitoshe, mandhari ya sebule ambayo wateja waliitumia ilikuwa ni ya kuvutia. Pangaboi kubwa darini lilizunguka kwa nguvu muda wote na kuifanya hewa ya humo ndani kuwa nzuri. Pia kulikuwa na televisheni kubwa iliyowaburudisha wateja waliokuwa wameketi kwenye masofa ya kuvutia.
Kwa aliyehitaji kuvuta bangi aliwasiliana na muuzaji na alipopewa msokoto, alikwenda katika vyumba vya uani ambako ‘alipata stimu’ bila ya kuwakera wasiovuta.
Siku yake ya kwanza katika nyumba hiyo alipata marafiki wawili. Siku ya pili alikuwa na marafiki watatu. Kwa kuwatumia marafiki hao akafanikiwa kuwajua watu wawili wa mjini hapo, alioamini kuwa angeweza kupata pesa kwao iwe kwa hiari yao au kwa shinikizo lake!
Mmoja wa ‘matajiri uchwara’ hao aliishi Kibirizi Road na mwingine alikuwa Lumumba Road. Hazikupita siku tatu kabla ya watu hao hawajakutwa wamekufa kwa majeraha ya visu, mmoja kisu cha shingoni na mwingine cha kifuani.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa ni kazi yake!
Kwa Mji wa Kigoma, kutokea mauaji ya watu wawili kwa siku moja, tena yakiwa ni mauaji ya kikatili, na waliouawa wakiwa ni watu maarufu, ilikuwa ni habari kubwa na ya kushtua moyo wa kila mwenye akili timamu.
Yalikuwa ni matukio yaliyoitikisa Kigoma kwa kiasi kikubwa. Jeshi la Polisi likaingia kazini. Ikawa ni operesheni kubwa na ngumu. Kamanda wa Polisi mkoani humo, Katembo Shabana akamwamuru mkuu wa kitengo cha uchunguzi kulivalia njuga suala hilo sanjari na kuhakikisha kuwa ulinzi wa mipakani unaimarishwa.
“Sidhani kama mauaji haya yanaweza kuwa yamefanywa na majambazi wa Kitanzania,” Katembo alimwambia mkuu wa kitengo cha uchunguzi. “Sidhani. Hawa wanaweza kuwa Warundi au Wakongo. Itatubidi tuwe serious kwa suala hili.”
********
KUUA, hususan kuua mtu, halikuwa jambo la ajabu kwa Shaka. Alishaua zaidi ya watu saba katika historia ya maisha yake. Na alikuwa tayari kufanya hivyo wakati wowote na dhidi ya mtu yeyote kwa dhamira ya kupata pesa. Katika utekelezaji wa hayo majukumu yake ya kuua, silaha zake kuu zilikuwa ni visu na bastola.
Baada ya kuwaua wale watu wawili, alijua kuwa lazima Jeshi la Polisi litakuwa katika operesheni kubwa ya kumsaka mhusika wa matukio hayo. Na operesheni hiyo lazima imguse yeye kwa kuwa hata kitendo chake cha kutoroka kule gerezani, Keko, kitawafanya Polisi jijini Dar wamfuatilie hadi hapo Kigoma.
Matukio haya ya vifo vya watu wawili yatawafanya askari wamshuku yeye kwa asilimia mia moja. Hivyo alipaswa kuwa makini na kujiwekea ulinzi madhubuti japo baba yake alimwambia kuwa tayari ana kinga nzuri dhidi ya hatari yoyote.
Alihitaji kuwa na bastola, lakini ataipata wapi? Hakuwa na jibu. Na alipotafakari zaidi akaona uwezekano wa kupata bastola haupo. Hivyo akaamua kujichimbia ndani mchana kutwa na kutoka usiku tu, akienda katika baa zilizotulia ambako alijipatia bia mbili, tatu na kurejea nyumbani.
Hata hivyo, japo alishindwa kuutumia uhuru wake kwa kustarehe bila ya wasiwasi, bado hakuacha kuwachukua kina dada, mmoja baada ya mwingine kwa siku tofauti na kwenda nao nyumbani, chumbani mwake ambako aliupitisha usiku akiburudika.
Matukio yale ya mauaji ya watu wawili yalimwingizia shilingi 1,700,000 tu pesa ambazo hazikuwa za kumfanya yeyote mwenye kuhitaji pesa za kutanulia ajione kuwa sasa kapata.
Hata hivyo, pamoja na uchache huo wa pesa hizo, kwa kiasi fulani alijiona yu mwanamume kati ya wanaume; anaweza kuvuta sigara huku akili imetulia, anaweza kunywa bia kwa kujidai na anaweza kujipatia mwanamke mwenye mvuto mkali na ‘kumhukumu’ apendavyo.
Kwa siku tatu mfululizo alikuwa mtu wa kutoka nyumbani giza linapoingia, bila ya kujali kuwa kwa kufanya hivyo alikuwa akilipunguza pato lake taratibu huku akiwa hana uhakika wa kuliongeza kwa mbinu gani, kupitia kwa nani na wakati gani.
Siku ya nne alikwenda katika baa ileile aliyokwenda tangu majuzi. Ni Bigabiro Bar iliyokuwa Mtaa wa Kitambwe. Na siku hii hakutaka kuchelewa sana katika baa hiyo. Alipanga kuwasiliana na mhudumu mmoja aliyeitwa Mary, ili, kama ilivyokuwa siku iliyopita, usiku huo pia ndiye amstareheshe.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Saa 3.00 alikuwa akiingia ndani ya baa hiyo kwa madaha, shilingi laki moja na kitu zilizokuwa mfukoni zikimtia kiburi.
Bia ya kwanza ilipotua mezani aliinywa taratibu huku akimsubiri Mary, aje, wapange vya kupangika. Hazikupita hata dakika tano, mara Mary akamjia huku akitembea kwa madaha.
“Inakuwaje bwana we?” Mary alimuuliza huku akiutikisatikisa mguu wa kulia.
Mary huyu alikuwa tofauti na yule Mary wa jana. Alikuwa ndani ya vazi laini ambalo japo halikumbana mwilini hata hivyo lilimvutia hususan pale alipokuwa akitupa mguu mmoja baada ya mwingine, akitembea kwa madaha. Umbo lake lililojaajaa liliyavuta macho ya wanywaji wengi waliofika hapo baa. Na wengi wao hawakukosa kumsumbua kwa maneno ya kumtaka kimapenzi.
Hata hivyo, hakuwa na tabia ya kuwakubali kirahisi wateja wanaomtongoza baada ya kufakamia bia. Na zaidi, hakupenda kuwakubali watu ambao mwanzo wao wa utongozaji ni kutamba kuwa wana pesa nyingi na pia kumwahidi mambo mengi mazuri, ahadi ambazo alitambua fika kuwa ni uongo mtupu.
Pia, baadhi yao walikuwa na tabia ya kutamka matusi ya nguoni na kumtania kwa kiwango kikubwa, utani usiopendeza, wakionyesha kuwa mwanamke yeyote anayefanya kazi ya uhudumu wa baa ni malaya.
Alimkubali Shaka kwa kuwa kwanza, aligundua kuwa ni mgeni wa eneo hilo, na pili, alimwona kuwa ni mtu ambaye hakuwa na marafiki ambao huenda wakamshawishi aachane na wanawake wa baa.
“Kama jana,” Shaka alimjibu huku macho yakimkagua kutoka juu mpaka chini. Kisha akaongeza, “Au leo una miadi na mtu mwingine?”
“Nani huyo?” Mary alijitia kukunja uso kama aliyekerwa na swali la Shaka. Kisha akavuta kiti na kuketi jirani naye. Akamtazama usoni sawia, kisha huku akiibinua-binua midomo yake kwa madaha na kuichezesha pua yake kwa maringo, akamuuliza, “Hivi unanionaje? Unaniona mie malaya sana, sio? Yaani kufanya kazi ya baa nd’o umeniona kuwa mimi ni maharage ya Mbeya?”
Shaka alitabasamu kidogo na kumpigapiga begani Mary. “Basi, beibe. Nakutania tu. Acha kuhamaki. Yaani hutaniwi hata kidogo?”
“Bwana, utani mwingine s’o mzuri,” Mary alisema kwa deko huku akimpapasa Shaka kidevuni. Kisha mkono huo ukahama na kushuka kifuani ambako vifungo kadhaa vya shati la Shaka havikuwa vimefungwa. Akampapasa na kuzitomasa chuchu zake.
Shaka akaguna na kuutoa mkono huo kistaarabu. Lakini Mary hakutulia, papohapo akaushusha mkono hadi chini ya kitovu ambako ulifanya kile kilichomchanganya zaidi Shaka. Alitomasa kwa namna ya kipekee na kumshuhudia Shaka akihema kwa tabu.
Hata hivyo, Mary alijua kuwa hapo hapakuwa mahali palipostahili kwa michezo ya aina hiyo. Akautoa mkono na kuketi kistaarabu.
“Si utanisubiri?” hatimaye alimuuliza Shaka kwa sauti ya chini.
“Mpaka saa ngapi?”
“Leo tunafunga saa tano.”
“Poa tu. Mimi sina noma, muda unaniruhusu. Na leo hakuna kulala.”
“Wewe tu, mie niko ngangari kwa saa ishirini na nne. Pumzi yako tu.”
“Tutaona.”
“Sawa, tutaona,” Mary alisema huku akinyanyuka na kuondoka kwa madaha yaleyale, umbo lake likiendelea kuyavuta macho ya watu kwa mitikisiko yake.
Shaka akaagiza bia ya pili.
*********
KITENGO cha Upelelezi cha Jeshi la Polisi mkoani Kigoma, kilimtumia Kisu katika operesheni ya kumsaka Shaka baada ya kupatikana taarifa kutoka Dar es Salaam kuwa jambazi huyo ambaye ni mzaliwa wa mjini Kigoma alitoroka gereza la Keko katika mazingira ya kutatanisha.
Ni kwa kushuku kuwa huenda Shaka akawa amejichimbia hapo mjini Kigoma, ndipo walimhusisha na mauaji ya wale watu wawili, mauaji ambayo kwa mtazamo wao hayawezi kufanywa na mtu asiyekuwa mzoefu kwa vitendo vya kikatili.
Kisu akiwa ni kachero aliyeaminika sana kwa wakuu wake wa kazi, alihaha kwa siku mbili mfululizo bila ya mafanikio ya kupata walao fununu za kuweza kumsaidia. Ni siku ya tatu, saa tano asubuhi ndipo alipopata taarifa ambazo kwa kiasi fulani aliona kuwa zingeweza kumsaidia.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwamba, mtu mmoja alionekana katika baa moja akitamba kuwa hakuna wa kumsumbua iwe kwa ngumi au silaha ya moto.
“Mimi ni mtoto wa town, ukiniletea umbulula wako nakutoa roho ka’ vile sikujui daaadek…!”
Ni kauli hiyo, na nyingine nyingi zifananazo na hiyo ndizo zilizomfanya kijana mmoja amtilie shaka na hivyo kupata nguvu ya kukimbilia kwa kachero Kisu ambaye walifahamiana kwa muda mrefu.
Kisu, akiwa bado yu gizani katika operesheni ya kumsaka mtuhumiwa wa vifo vya watu wawili na wakati huohuo akiwa pia katika zoezi la kumsaka Shaka, ambaye kwa mujibu wa taarifa kutoka Dar huenda akawa kakimbilia hapo Kigoma kwa kuwa ndiko alipozaliwa, hakutaka kuipuuzia taarifa hii aliyopewa na huyu kijana.
Saa tatu usiku aliingia ndani ya baa hiyo na kukuta idadi ya watu ikiwa kubwa tofauti na alivyopazoea. Hakushangazwa na wingi huo wa wateja. Kulikuwa na sababu. Tarehe. Ndiyo, siku hiyo ilikuwa ni tarehe 31, ikiwa ni siku ya mwisho kabisa ya mwezi huo, hivyo aliamini kuwa watu wengi walioajiriwa walikuwa wamepata mishahara yao na kuamua kuja hapo na sehemu nyingine ‘kujipongeza.’
Yeye hakujali hilo, alijali kilichomwingiza humo. Akaangaza macho huku na kule akitafuta sehemu nzuri ya kukaa. Na alipoipata alivuta kiti na kuketi kisha akaagiza kinywaji.
Katika meza aliyokuwapo pia kulikuwa na mtu mmoja, mwanamume ambaye alionekana kukolewa vilivyo na kilevi. Hakumjali, akawa katika zoezi la kuangaza macho kwa takriban kila aliyekuwemo.
Dakika chache baada ya kulianza zoezi hilo, macho yaliganda kwa mtu mmoja, mwanamume pandikizi ambaye alikuwa ameketi katika kiti kirefu kilichokuwa kaunta, bia mbele yake.
Kilichomfanya Kisu amgande mtu huyo ni jinsi alivyokaa katika eneo hilo. Ulikuwa ni ukaaji wa ajabu, ambao kwa mtu yeyote mstaarabu usingekuwa wa kupendeza. Alikuwa amepandisha mguu mmoja juu ya kiti kilichokuwa jirani yake na hivyo kuwa kama aliyezuia mtu yeyote mwingine kuketi hapo.
Kwa dakika nne, tano hivi ambazo Kisu aliendelea kumchunguza mtu huyo, aligundua kuwa hata wamiliki na wahudumu wa baa hiyo hawakuthubutu kumwonya mteja wao.
********
SIGARA ikivutwa kila baada ya muda mfupi, kuketi huku guu moja likiwa juu ya kiti cha pili, na kumtomasatomasa Mary kila alipofika kumpa huduma ya kinywaji ni vitendo ambavyo Shaka alitarajia kuwa visingewafurahisha wateja wengi katika baa hiyo. Na alitarajia kuwa wengi wao wangemkodolea macho wakimstaajabia.
Ndiyo, alitarajia hivyo, lakini hakutarajia kuwa wateja hao wangetekwa na vitendo vyake kiasi cha kuahirisha mara kwa mara kuzipeleka vinywani glasi zao za vinywaji.
Mtu mmoja tu kati ya hao wateja alimtilia shaka. Kwa uzoefu wake katika kazi ya kupambana au kutafutwa na vyombo vya dola hakusita kumjumuisha mtu huyo na wale ‘askari kanzu.’
Macho ya mtu huyo yalitangaza bayana uaskari wake! Pia Shaka hakushindwa kung’amua kuwa mtu huyo yuko hapo kwa sababu maalum na wala siyo kustarehe.
Akilini mwake aliona kuwa ni mapema mno kwa askari kumfuatilia hadi kuwa hatua chache kabla ya kumtia mbaroni. Bado alikuwa hajayafaidi maisha, na bado alikuwa hajazifaidi pesa alizopora kwa wale matajiri wadogo.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hata hivyo alikwishaona kuwa dudubaya limeingia katika himaya yake. Sasa hakutaka kupoteza muda. Alikunywa bia yake haraka kisha akatoka. Kwa hatua ndefu na kwa hadhari alitembea akielekea msalani.
Hakuwa amebanwa na haja ndogo wala kubwa, aliamua tu kwenda huko ili apate wasaa wa kupanga nini afanye katika kukabiliana na hali tete iliyokuwa mbele yake. Tayari alishaamini kuwa ujio wa yule aliyeamini kuwa ni askari sio ujio wa heri, hivyo alipaswa kuwa makini na ikibidi, achukue hatua haraka iwezekanavyo katika kujihami.
Akajipapasa mifukoni na kukigusa kisu chake. Ujasiri ukamjaa. Akakikamata kitasa cha mlango akitaka kurudi ukumbini.
********
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment