Simulizi : Mtikisiko Wa Hirizi
Sehemu Ya Nne (4)
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
HAUKUMCHUKUA muda mrefu kachero Kisu kupata picha halisi ya kile alichokifuata katika Baa ya Bigabiro. Aliwahoji wahudumu wawili tu wa kike na wakampa majibu ya kuridhisha.
“Jamaa yule anajisikia sana, na hana tabia za kistaarabu,” yalikuwa ni maneno ya mhudumu wa kwanza.
Mwingine alisema, “Yule bwana haeleweki-eleweki. Ni ka’ jambazi vile! Mambo yake!”
Maneno hayo pamoja na yale aliyoambiwa na yule kijana juzi, yalitosha kumfanya ayaamini macho yake na kuziamini hisia zake. Isitoshe, alikwishaiona picha iliyotumwa kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi. Sura ya mtu huyu haikutofautiana na ile picha. Hivyo hakutaka kupoteza muda. Alimfuata hukohuko msalani.
Vyoo vya baa hiyo vilikuwa katika sehemu ambayo wateja wengine wasingeweza kujua kinachoendelea endapo watu wangeamua kukutana huko na kuzungumza au kufanya chochote.
Alipofika huko alisimama mlangoni, akaichomoa bastola na kuishika katika mkono wa kulia.
********
MLANGO ulipofunguka Shaka alishtuka. Mbele yake alimwona Kisu akiwa amesimama kikakamavu huku akimwelekezea bastola! Hiyo tu ilitosha kumthibitishia kuwa askari mjini humo wameshatambua kuwa yupo. Kwa hali hiyo hakutaka kuchezea shilingi chooni.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alimrushia kachero Kisu teke la kushtukiza, teke zito lililoipeperusha bastola umbali wa hatua takriban kumi nyuma yake. Na hakumpa muda wa kujiandaa kuyakabili mashambulizi, kwa kasi ya ajabu alimvurumishia makonde matatu mfululizo yaliyoivuruga kabisa programu yake, yakamsomba mzima-mzima na kumbamiza ukutani kabla ya kuanguka sakafuni ti!
Sasa Shaka hakutaka kuchelewa katika eneo hilo. Aliiwahi ile bastola na kuichukua kisha akatoka. Wakati akiondoka hakujua kuwa askari wengine wawili walikuwa nje na walipomwona akitoka walimfuata kwa hadhari huku wakijiuliza ni vipi kachero Kisu awe ‘amemwachia huru mtu wao.’
Shaka alitembea taratibu, moyoni mwake akijisikia raha kwa kupata chombo kilichokuwa na umuhimu mkubwa kwake kwa kipindi hicho.
Bastola!
*********
NGUVU zilimrudia kachero Kisu muda mfupi tu baada ya kunyweshwa ‘mvua’ ya makonde na Shaka. Akajizoazoa pale sakafuni akidhamiria kuendelea kumwandama Shaka.
Sasa alichanganyikiwa kwa kiasi kikubwa. Kuzidiwa ubavu na Shaka na hata kufanikiwa kuchomoka huku pia akiwa ametwaa bastola, ilikuwa ni aibu kwake na kwa jeshi zima la Polisi.
Kupokonywa bastola!
Atamweleza nini mkuu wake wa kazi? Chochote atakachomweleza kitaeleweka na kukubalika kichwani mwa bosi wake? Kwamba hana cha kumweleza mkuu wake wa kazi, na wala chochote atakachosema hakitaeleweka wala kukubalika ni imani iliyojengeka kichwani mwake wakati huo.
Hata hivyo aliondoka, akielekea nje ya baa hiyo bila ya kujua matokeo ya operesheni aliyoendelea nayo. Hakuwajali wateja wachache waliomtazama kwa mshangao, alijali kuitekeleza kazi iliyompeleka hapo.
Huko nje aliwafuata askari wenzie na wakamwonyesha njia aliyopita Shaka. Wawili kati yao walikuwa na bastola. Kisu akatwaa bastola moja na kutangulia, akifuata njia aliyoelekezwa na hao wenzake. Nao wakamfuata.
Muda mfupi baadaye walifanikiwa kumwona Shaka akitembea kwa hatua ndefu katika mtaa wa Legeza Mwendo. Hakuwa mbali sana, ni kiasi cha kama hatua hamsini hivi mbele yao.
Papohapo Kisu akapaza sauti: “Shaka! Shaka! Simama! Jisalimishe!”
Shaka alishtuka, akageuka nyuma. Akahisi hatari ikizidi kumjia. Hakuwa tayari kuitii amri ya Kisu. Akaendelea kwenda mbele, safari hii akikaza mwendo zaidi.
Risasi ikafyatuka katika bastola ya Kisu.
Patupu!
Risasi ya pili!
Patupu!
Alifyatua risasi ya kwanza kwa kudhamiria kumtegua Shaka mguu. Risasi ya pili alitaka itue mgongoni, na zote zilimkosa!
Hata hivyo hakumwacha, alifyatua risasi ya tatu lakini nayo, kama zile mbili za awali iliishia kuchana anga. Akashangaa! Hakuwa na kumbukumbu ya kukosa shabaha tangu alipotoka mafunzoni kiasi cha miaka mitano iliyopita.
Hii ilikuwa ni mara ya kwanza!
Akasimama na kuwatazama wenzake huku jasho likimtoka usoni. Akahema kwa nguvu akionyesha dhahiri kukumbwa na mshangao kwa hali iliyojiri. Akataka kutamka neno lakini hakuipata sauti yake.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati akiwa katika hali hiyo, alikuwa akitumbua macho ilhali haoni. Ndiyo, ni kama pia hakumwona Shaka akisimama na kugeuka kisha akafyatua risasi moja tu kwa shabaha kali! Hakumwona, lakini alihisi kitu cha baridi kikipenya kifuani kwa namna ya kipekee na kisha ubaridi huo kutoweka ghafla na nafasi yake kutwaliwa na joto kali lililoambatana na maumivu makali!
Maumivu hayo yalizinyong’onyesha nguvu maungoni mwake kwa kasi ya kutisha. Punde kiza kikaanza kutanda machoni pake.
Hakuvuta pumzi zaidi ya nusu dakika!
*********
KAMA kuna taarifa iliyomshtua, ikamshangaza na kumuumiza moyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, Katembo Shabana kwa kiwango kisichokadirika, basi ni ile iliyomfikia wakati akijiandaa kulala. Taarifa ya kifo cha Kisu, askari shupavu, ambaye Jeshi la Polisi lilimtegemea kwa kiasi kikubwa.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi, Panga Sakanyoka iliufukuza usingizi wa Katembo kwa kasi ya kutisha. Robo saa baadaye wakakutana ofisini kwa kikao cha dharura.
“Nina wasiwasi kwamba wewe na kikosi chako hamtamkamata Shaka,” Katembo alimwambia huku akimtazama kwa macho makali.
“Afande, kwa nini unasema hivyo?” Panga Sakanyoka alimuuliza.
“Sioni dalili ya kumkamata. Sijui mnafanya nini mpaka sasa.”
Ukimya wa muda mfupi ukatawala. Kisha Katembo akaongeza, “Wewe binafsi unadhani mnaweza kumtia mbaroni?”
“Ndiyo, afande.”
“Una hakika na unachokisema?”
“Nina hakika, afande,” Panga Sakanyoka alijibu kwa kujiamini. “Kuna asilimia tisini na tisa za kumtia mbaroni.”
“Kwa utaratibu wenu huu usio na kichwa wala miguu?”
Panga Sakanyoka hakujibu. Alimtazama kidogo mkuu wake na kuziona hasira zake zikijitangaza bayana kupitia macho yake makali.
“Mtamkamata lini?” Katembo Shabana aliendelea kumwaga maswali.
“Ndani ya saa ishirini na nne zijazo.”
“Siamini,” Katembo Shabana alitikisa kichwa kutoafikiana na kauli ya Panga Sakanyoka. Akaongeza, “Tatizo lako ni kwamba, unachukulia kumkamata Shaka kama vile kuwakamata hawa vibaka wako wa mitaani. Nadhani kuna haja ya kupata msaada kutoka Makao Makuu. Vinginevyo tunaweza kupoteza maisha ya watu wengi.”
“Lakini afande, ni aibu kufikia hatua ya kuomba msaada kutoka Dar...”
“Bora iwe aibu!” Katembo Shabana alisema kwa msisitizo mkali. “Lakini usiku huuhuu lazima niwasiliane na makao makuu.”
Kabla ya mapambazuko taarifa za kuhitaji msaada wa askari wenye uzoefu wa kupambana na majambazi sugu zilifika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam.
Saa tatu asubuhi Inspekta Banda na Sajini Kessy walikuwa ndani ya helikopta wakielekea mjini Kigoma. Saa moja baadaye walikuwa mjini Kigoma katika kikao cha dharura na Panga Sakanyoka na Katembo Shabana.
Na, ni baada ya maelezo ya kina kutoka kwa Panga Sakanyoka ndipo Inspekta Banda akasema, “Kwa vyovyote huyo atakuwa ni Shaka tu! Ni mwenyewe, na akiachiwaachiwa ataweza kuleta madhara zaidi.”
“Ni kweli,” Katembo aliafiki. “Tatizo ni kwamba, kumkamata mtu ka’ Shaka siyo sawa na kumkamata kibaka anayevizia kupora walevi mitaani au kuwapokonya simu wapita njia. Kuamua kumvalia njuga Shaka ni sawa na kumkaabili chatu mwenye njaa, ana kwa ana.”
Inspekta Banda alitikisa kichwa akiashiria kukubali. Uso wake wa kiaskari ulizidi kuonyesha umakini na wakati huo alikuwa akilikumbuka tukio la miezi kadhaa iliyopita wakati jambazi hatari, Kamba Kiroboto alipolitoroka Jeshi la Polisi lenye kikosi madhubuti huku akiwa amewaua askari waliokuwa nguzo kuu na tegemeo kwa matukio makubwa, Inspekta Maliyatabu na mwenzake, Sajini Kitowela.
Tukio lile lililofanyika Manzese jijini Dar es Salaam lilikuwa ni la kulidhalilisha jeshi hilo kwa kiasi kikubwa! Kamba Kiroboto aliwapiga risasi askari wote hao kisha akadandia pikipiki na kutokomea!
Lilikuwa ni tukio ambalo kutokana na kauli hii ya Katembo, alihisi kukumbana na yale ambayo yaliwakuta Maliyatabu na Kitowela kwa Kamba. Hata hivyo, alijipa ujasiri na kusema, “Tunamjua vizuri Shaka,” Inspekta Banda alisema. “Lakini hilo haliwezi kuwa jambo la kututia shaka. Kwani ni kipi kinachokufanya umhofie kiasi hicho?”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Katembo Shabana alitabasamu kidogo kisha akajibu, “Maafa aliyokwishaleta. Kishatoa roho za watu watano kwa kipindi kifupi sana!”
“Watano!” Inspekta Banda alishangaa.
“Yeah, kaua raia wawili wafanyabiashara kwa kisu, na askari watatu kwa risasi!”
**********
BAADA ya kumuua kachero Kisu, Shaka alikumbana na askari wawili wa doria ambao walimtaka ajisalimishe. Hakuwa tayari kutii amri yao. Aliendelea kutembea kwa mwendo wake uleule wa kawaida na wa kujiamini.
Risasi kadhaa kutoka katika bunduki za wale askari hazikumpata na badala yake, yeye alipogeuka na kufyatua risasi mbili akapata majibu ya kuridhisha. Wakati wale askari wakikata roho taratibu, Sudi, askari mwingine wa doria alikuwa umbali mfupi tu kutoka alipokuwa Shaka.
Akitumia bunduki yake iliyokuwa imesheheni risasi, alifyatua risasi mbili akiwa amemlenga Shaka kwa shabaha kali!
Patupu!
Risasi ya tatu!
Patupu!
Sudi aliduwaa, akabaki akimtazama Shaka ambaye alizidi kutokomea machoni pake. Kisha, kama aliyezinduliwa usingizini alikurupuka na kukimbilia kituoni ambako alimsimulia kwa kina Katembo Shabana kuhusu muujiza huo aliokumbana nao.
Taarifa hiyo ya Sudi iliyokolezwa na muujiza wa Shaka kutopatwa na risasi ilimtia jakamoyo kamanda huyo wa Polisi.
Ilikuwa ni taarifa iliyomshangaza sana kiasi cha kumchukulia Shaka mithili ya shetani. Na ili askari hawa kutoka Makao Makuu jijini Dar wakubaliane naye, ilimlazimu kuwasimulia kwa kina na kwa tuo kuhusu muujiza huo wa Shaka.
Inspekta Banda na Sajini Kessy walitazamana kwa sekunde chache na kumgeukia tena Katembo Shabana. “Kwa hiyo kwa usiku wa jana tu kaua watu wangapi?” Banda alihoji.
“Watatu!” Katembo alijibu kwa msisitizo. “Kaua askari watatu jana tu! Kwa wiki ataua wangapi?”
“Na alitupiwa risasi ngapi zikamkosa kiasi cha kumchukulia kuwa ni jitu lenye miujiza?”
“Zaidi ya tano!” Katembo Shabana alijibu. “Taarifa ni’zopata ni kwamba, marehemu Kisu alimrushia risasi tatu. Na kwa jinsi ninavyomjua Kisu, akidhamiria kumtungua mtu atatumia risasi moja tu. Na kwa risasi hiyo, akikosea sana shabaha basi atakuwa katengua bega la mlengwa. Ana rekodi nzuri ya kutokosa shabaha. Cha ajabu, jana risasi zake tatu zote zilipita patupu! Nashindwa kuamini!”
“Una hakika kuwa alipopiga risasi alikuwa amedhamiria kumuua au kumjeruhi mtuhumiwa? Hakuwa anamtisha tu ili ajisalimishe?”
“Hapana,” Katembo alijibu. “Tulishazungumza mwanzoni kabisa wakati tukiingia katika operesheni hii. Tulikubaliana kuwa siyo lazima tumkamate akiwa hai. Yule sio mtu wa kumlinganisha na kibaka wa vichochoroni. Ukikutana naye, mtie risasi kwanza, maswali baadaye. Kwa hali hiyo Kisu aliujua wajibu wake.”
Ukimya ukatanda kwa sekunde chache kisha Katembo akaendelea, “Isitoshe, askari wengine wawili walimrushia risasi kabla hata ya Kisu, lakini nao waliambulia patupu. Badala yake ni wao waliouawa!”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa mara nyingine Inspekta Banda na Sajini Kessy walitazamana. Tabasamu la mbali likamtoka Sajini Kessy, tabasamu lililowashangaza wenzake kufuatia jukumu zito lililokuwa mbele yao.
“Afande,” hatimaye Kessy alisema huku akimkazia macho Inspekta Banda. “Unaikumbuka vizuri taarifa ya kutoroka kwa Shaka gerezani ilivyo ya kutatanisha?”
“Naikumbuka.”
Sajini Kessy alikuwa na sababu ya kuuliza swali hilo. Akiwa ni mzaliwa halisi wa Mkoa wa Kigoma, alikwishazisikia simulizi kuhusu majambazi wanaotumia kinga maalumu zinazowasaidia kutopatwa na risasi na pia hata kuweza kutoroka chini ya ulinzi. Kwa taarifa hizi kuhusu maajabu ya Shaka alijikuta akianza kuziamini simulizi zile kwa asilimia kubwa.
“Lilikuwa ni tukio la ajabu sana,” Kessy alisema. “Aliondoka mbele ya askari jela kama vile kakubaliana naye.”
“Utajuaje? Labda walikubaliana,” Inspekta Banda alisema.
“Huenda yule askari jela alivuta mshiko wa nguvu ili amwachie.”
“Inaweza kuwa hivyo, na pia isiwe hivyo, afande,” sauti ya Kessy ilitoka kwa utulivu. “Kwa upande wangu nina wazo tofauti.”
Inspekta Banda na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Katembo Shabana walimkazia macho wakionyesha kujawa na shauku ya kulisikia hilo wazo tofauti.
“Mambo kama ayafanyayo Shaka sikuanza kuyasikia leo,” Kessy alisema. “Mkoa huu una historia ya muda mrefu ya uchawi wa aina hiyo. Tangu zamani majambazi wengi wamekuwa wakitumia mbinu za kishirikina zilizowanyooshea sana mambo yao. Na ushirikina wa aina hiyo sio kwamba uko huku Kigoma tu. Hata Dar kuna waganga wa jadi wanaotumiwa na majambazi. ”
“Hiyo ni stori ya vijiweni,” Inspekta Banda aliponda.
“Serikali na imani za kishirikina havipikiki chungu kimoja,” Katembo Shabana aliongeza.
“Nilijua utapinga,” Kessy alisema akionyesha kuwa kauli hiyo ilimlenga Inspekta Banda. “Lakini afande, amini usiamni, jambo hili lipo. Ni kweli, serikali, kama serikali, haiamini mambo ya kishirikina. Lakini asilimia kubwa ya jamii ya Watanzania inaamini kuwa ushirikina upo na una nguvu kiasi chake katika utendaji. Mimi binafsi naamini kuwa kuna ushirikina duniani, na una nguvu.”
“Imani yako siyo yangu wala ya RPC hapa,” Banda alisema, akimalizia kwa kunyoosha kidole kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Katembo Shabana. Akaongeza, “Mimi najua kuwa kuna ushirikina lakini siamini kuwa unaweza kuwa na nguvu yoyote ya kutisha.”
“Unamwamini Yesu, eti?” Kessy alichomeka swali kwa namna ya mzaha.
“Yeah, namwamini Yesu.”
“Hata mimi ni Mkristo, na ninamwamini Yesu. Lakini ukae ukijua kuwa nguvu za giza zipo!”
Kwa mara ya kwanza Katembo Shabana alicheka. Akasema, “Sajini, hiyo hoja ni nzito na huenda ikatuchukulia muda mrefu. Tutafute kwanza ufumbuzi wa suala hili.”
Mara tu baada ya kusema hivyo alikunja uso na kuonyesha kuwa hahitaji mzaha kwa kipindi hicho.
Inspekta Banda akasema, “ Sikia Sajini, tuko ‘serious’ kwa suala hili. Ni suala lililoyagusa maisha ya watu hivyo jiepushe na mzaha wa aina yoyote kwa kipindi hiki.”
Kessy aliwaelewa lakini hakubabaika. Badala yake, kwa msisitizo mkali akasema, “Afande,” akamkazia macho Inspekta Banda, “unaweza kunichukulia kuwa ninafanya mzaha au mchezo wa kitoto. Lakini siwafichi, ni ushirikina wa kiwango cha juu ndiyo uliomsaidia Shaka akatoroka Keko na pia akafanikwa kutopatwa na risasi.”
Akatulia kidogo akiwakazia macho kwa zamu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Katembo Shabana na Inspekta Banda. Akapata ujasiri wa kuendelea kuzungumza. “Huo ndio ukweli, na kwa hilo naomba msinichukulie pia kuwa ninafanya masikhara. Hapana. Niko serious. Na ninawahakikishia kuwa dawa yake ninaijua, na nitamuua mwenyewe!”
“Una hakika na hayo uyasemayo?” Inspekta Banda alimuuliza huku akimtazama kwa namna ya kutomwamini.
“Muhimu nimtie machoni tu,” Kessy alijibu.
********
MCHANA kutwa kulikuwa na hekaheka mjini Kigoma. Mipaka yote ya mji ilidhibitiwa. Hata hivyo, hadi jua lilipotokomea hakukuwa na taarifa zilizoweza kutoa nuru ya kupatikana kwa Shaka.
Ndipo Sajini Kessy alipoomba kwa wakuu wake wa kazi, apewe uhuru wa kumsaka Shaka. Autumie uhuru huo akiwa peke yake, avichimbe vichochoro vyote vya mji huo kwa kina katika operesheni hiyo.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akiwa amezaliwa katika kitongoji maarufu cha Mwanga, akapata elimu ya msingi katika shule ya Muungano kitongojini hapohapo, na kisha ‘akainywa’ elimu ya sekondari katika shule ya Mlole, aliamini kuwa hakuna litakalomshinda katika operesheni hiyo.
Mizunguko yake ilianzia Bangwe-Kamala kisha akaenda Gungu, Ujiji, Katubuka kabla hajaingia Mwanga usiku akiwa hoi bin taaban licha ya kutumia usafiri katika mizunguko yote hiyo.
Tofauti na Mwanga, katika vitongoji vingine hakupata chochote cha kumsaidia.
Akiwa Mwanga usiku huo, saa mbili kasoro dakika chache, alikuwa katika harakati za kumfahamu mtu yeyote aliyejulikana kwa jina la Songoro. ‘Vijiwe’ viwili, vitatu vya kahawa alivyozungukia ndivyo vilivyompatia mwanga fulani alioamini kuwa ungemsaidia kwa kiwango kikubwa.
Aliambiwa kuwa kuna watu wengi wenye kutumia jina hilo, baadhi wakiwa ni wafanyabiashara wakubwa, baadhi wakiwa ni wavuvi na wengine wakiwa ni wakulima.
Pamoja na taarifa hiyo, hata hivyo alipewa taarifa moja iliyompa matumaini ya mafanikio. Kwenye kijiwe kimoja Barabara ya Lumumba, kijana mmoja alimwambia kuwa mtu mmoja mwenye jina hilo ni mzee wa makamo na ana umaarufu wa aina yake.
“Umaarufu gani?” Kessy alimbana.
Kijana yule alisita na kumtazama zaidi Kessy. Kisha akamuuliza, “ Kwani una shida gani nae? Ni jamaa yako au wewe ni mgeni wake?”
“Mgeni wake.”
“Anakufahamu?”
“Ananifahamu. Ni muda mrefu tulipoonana, zaidi ya miaka mitano, lakini sidhani kama atakuwa amenisahau.”
Kijana yule alizidi kumkazia macho. Akamuuliza, “We’ ni mgeni wa heri au shari? Useme kabisa, mwanangu. Maana’ake kama unamwendea kwa ubaya…” akaiacha sentensi hiyo ikielea.
Vicheko vikatawala kijiweni hapo. Wanywaji wengine wa kahawa wakamkodolea macho Kessy. Kisha kijana yule akaongeza, “Kwa kweli jamaa yangu, sikufichi, huyo mzee Songoro n’nayekwambia, s’o mtu mwepesi. Ni mzito, mzito kikwelikweli. Kama unamtafuta kwa ubaya, jihadhari sana.”
“Nijihadhari?”
“Ndiyo!”
“Kwa nini unasema hivyo?”
Kijana yule alicheka kidogo kisha akasema, “Sina kahawa. Unataka kunikausha koo bure kwa shida zako.”
Banda akiwa ni ‘mtaka cha uvunguni’ alitoa noti ya shilingi 1,000 na kumkabidhi muuza kahawa. Kitendo hicho kikazua zogo. Baadhi ya waliokuwepo wakamkaba muuza kahawa:
“Mie nipe ya mia…”
“Mie nakula kashata za mia…”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mie sinywi kahawa nipe pesa, shi’ng mia mbili…”
Naam, pesa ya Kessy ilizua kizaazaa. Kila mmoja akataka mgawo wake. Wa kunywa kahawa, alikunywa. Wa kula kashata, alikula. Na ambaye hakutaka vyote hivyo, alidai pesa taslimu, akapewa.
Muda mfupi baadaye amani ilirejea.
Ni wakati huo ndipo yule kijana alipomgeukia Kessy na kusema, “Mshikaji wangu hapo umecheza. Wahenga walisema, mkono mtupu haulambwi. Sasa mambo shwari.”
Akatulia na kuchomoa sigara mfukoni, akaiwasha na kuvuta mikupuo miwili ya nguvu. Mara tena akakipeleka kikombe cha kahawa kinywani na kugugumia mafunda kadhaa.
Kisha akayarejesha macho kwa Kessy. “Kwa hiyo unataka kupajua kwa Mzee Songoro, sio?” hatimaye alimuuliza.
“Ndiyo,” Kessy alijibu. Kisha akaongeza, “Lakini umenitisha kidogo. Unaweza kunieleza kwa kina kuhusu hadhari ninayopaswa kuichukua dhidi ya mzee huyo?”
“Wala us’konde, mshkaji,” kijana yule alijibu. “Kwa kweli Mzee Songoro ni mtaalamu. Nikisema ni mtaalamu uelewe kuwa ni mtaalamu kweli. S’o mtu wa kuchezea. Ni mtu ngangari kwa masuala ya ki-utu uzima. Hii teknolojia ya Kiafrika, pale nd’o imelala.”
Ukimya wa muda mfupi ukatawala kijiweni hapo. Kisha mmojawao akasema, “Na n’nasikia mzee huyo ana mtoto mmoja tu anayeishi Dar, na mtoto mwenyewe ni moto wa kuotea mbali! Hafai! Ni heri ukutane na jini lenye sura ya binadamu kuliko kukutana na huyo mtoto wa mzee Songoro!”
“Acha tu baba’ke,” yule kijana aliyekuwa akizungumza awali alidakia. “Shaka! Yule ni jambazi la kutupa, mwanangu. Usiombe kukutana nae. Ile nyumba ya Mzee Songoro imejengwa kwa pesa za ujambazi wa Shaka. Na majuzi si mlisikia kuwa Shaka kafungwa?”
“Ndiyo,” wawili, watatu walijibu.
“Na baada ya siku mbili, tatu ikatangazwa kwenye magazeti kuwa Shaka huyo katoroka kwa mazingira ya kutatanisha,” kijana yule aliongeza. “Mnadhani atakuwa ametorokaje, kama s’o kwa nguvu za uchawi wa baba’ake?”
Sajini Kessy hakuhitaji ufafanuzi zaidi wa maneno hayo. Papo hapo akauliza, “Anaishi wapi?”
“Nani, Shaka au Mzee Songoro?”
“Mzee Songoro.”
“Anaishi Mwanga hiihii.”
“Mtaa gani ?”
“Mabatini. We’ nenda tu huko Mabatini. Ukimuuliza mtu yeyote, hata mtoto mdogo wapi kwa Mzee Songoro, utaonywesha. Yule ni mtu maarufu. Kila mtu anamjua. Lakini mtaa wenyewe unaufahamu?”
“Napajua.”
“Basi ukimuuliza yeyote mtaani hapo atakuonyesha kwa mzee huyo. Lakini kama nilivyokuonya mwanzoni, kama unakwenda kwa ubaya, ni bora ugeuze njia mapemaaa! Yule s’o mtu wa kumjaribu, mwana!”
Kessy hakuwa mtu wa kutishwa, akatishika. Alitupa shilingi 500 mezani na kusema, “Poa, wash’kaji. Endelezeni kahawa.”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Shukrani, mjomba,” mmojawao alisema.
“Duh, ubarikiwe sana, mwanangu,” mwingine aliongeza.
“Tuchabhonana,” muuza kahawa alimwaga kwa lugha ya Kiha.
Dakika kumi baadaye Kessy alikuwa Mtaa wa Mabatini ambako kwa kutumia pesa kidogo, kijana mmoja alimpeleka hadi hatua chache kabla ya kuifikia nyumba ya Mzee Songoro.
*********
SAA 11 alfajiri ya siku iliyofuata Inspekta Banda, Sajini Kessy na Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi mkoani Kigoma, Panga Sakanyoka walikuwa ofisini kwa kikao maalumu.
Taarifa iliyotolewa na Sajini Kessy ilikuwa nzito na iliyohitaji utekelezaji wa haraka, utekelezaji ambao ungeweza kufanyika jana usiku baada ya Sajini Kessy kuitambua nyumba iliyoaminika kuwa ndiyo iliyomhifadhi Shaka.
Hata hivyo, uchovu mwilini kutokana na mizunguko ya kutwa nzima ya jana yake ilikuwa ni sababu mojawapo iliyomfanya Sajini Kessy avute subira kwa kuvipumzisha viungo ili kuviandaa na zoezi hili ambalo aliamini kuwa litakuwa na mambo makubwa.
Na kwa hali hiyo aliamua kutowapa taarifa yoyote wakuu wake kuhusu hatua aliyofikia kwa kuhofia kuwa wangetoa uamuzi wa kuifanya operesheni hiyo usiku huohuo baada ya kutaarifiwa.
Ingekuwa ni operesheni ambayo angelazimika kuwa bega kwa bega na wakuu wake, jambo ambalo aliamini kuwa lingeathiri utendaji kwa jumla kutokana na uchovu uliokiandama kila kiungo mwilini mwake.
Baada ya usiku wa jana kupelekwa na yule kijana hadi mbele ya nyumba ya Mzee Songoro, na kumkuta mzee huyo akipunga hewa kibarazani, Kessy hakufanya lolote hata kumjulia hali mzee huyo bali aliamua kurudi hotelini alikofikia, akala kisha akalala hadi saa kumi alfajiri alipoamua kumpigia simu Inspekta Banda, akipendekeza wakutane haraka ofisini pamoja na mkuu wa kitengo cha upelelezi mkoani.
Lilikuwa ni pendekezo ambalo halikupata pingamizi lolote kutoka kwa Banda.
Robo saa baadaye walikutana.
“Unasikia, afande,” Kessy alisema akiwatazama kwa zamu wakuu wake. “Tunapaswa kuizingira ile nyumba ya mzee Songoro kikamilifu. Inatupasa kutambua fika kuwa pamoja na miujiza aliyonayo Shaka, pia bila ya miujiza hiyo bado jamaa ni nooomaa kishenzi. Hafai! Ana bastola! Sasa yule sio mtu wa kufananishwa na shetani bali tunapaswa kumchukulia kuwa ni shetani kamili!”
“Lakini una hakika kuwa Shaka anaishi pale kwa baba yake? Na kama anaishi pale, tukienda tutamkuta?” Inspekta Banda alimuuliza Kessy. “Nauliza hivyo kwa kuwa nahofia kuwa kama machale yatamcheza, tunaweza kufika pale na kuambulia patupu!”
“Siyo rahisi kwa Shaka kuishi gesti au kufichwa na mtu baki wakati baba yake ambaye ni maarufu sana kwa ushirikina na anayesadikiwa kuwa ndiye aliyesababisha Shaka atoroke Keko, yuko hapa…”
“No! Tusijenge imani hiyo,” Panga Sakanyoka alipinga. “Jambazi ni jambazi tu! Akiwa na pesa anaweza kufanya lolote na kuishi popote ambako roho yake inataka. Shaka ana pesa, hivyo anaweza kwenda popote kuishi na kufanya chochote apendacho. Pesa zinamruhusu.”
Ukimya wa muda mfupi ukatawala, kisha Banda akauliza,“ Sajenti, ulichokuwa ukitaka ni kuivamia ile nyumba ya Mzee Songoro, si nd’o maana’ake?”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiyo, afande.”
“Kwa madhumuni ya kumtia nguvuni Shaka?”
“Ndiyo!”
“Una hakika ya asilimia ngapi kuwa Shaka atakuwepo?”
“Asilimia tisini na tano,” Kessy alijibu. “Kinachonifanya niamini hivyo ni taarifa nilizozipata mitaani jana na uthibitisho wa mtu aliyenipeleka jana hadi mita chache kutoka kwenye nyumba hiyo.”
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment