Search This Blog

Friday, 20 May 2022

MTIKISIKO WA HIRIZI - 5

 







    Simulizi : Mtikisiko Wa Hirizi

    Sehemu Ya Tano (5)





    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Huyo mtu kasemaje?” Panga Sakanyoka alimdaka.

    “Kwamba Mzee Songoro anaishi na mkewe na mwanae mmoja tu, ambaye amekuja majuzi kutoka Dar. Anadai kuwa yeye anaishi nyumba ya tatu kutoka kwa Mzee Songoro, na huwa anamwona Shaka kila asubuhi akinawa uso nje ya nyumba hiyo.”



    Banda na Panga Sakanyoka walitazamana kisha Banda akasema, “Naona twende. Matokeo yote tutayapata hukohuko. Kama yupo au hata hakulala hapo tutajulia hukohuko.”



    Maandalizi yakafanyika chapchap. Askari wengine kumi wenye silaha wakawekwa tayari. Muda mfupi baadaye Land Rover ilikuwa barabarani ikielekea Mtaa wa Mabatini.

    Walipoikaribia nyumba hiyo waliteremka na kuanza kupangiana majukumu.



    Hawakutaka kuivamia nyumba hiyo mapema kiasi hicho. Ilikuwa ndiyo kwanza inatimu saa 12.20. Bado kijigiza kilitawala anga. Hivyo Panga Sakanyoka aliwapanga wale askari, akawapa majukumu ya kuizingira ile nyumba na kuhakikisha kuwa hakuna mtu atakayetoka.



    “Lakini msifanye chochote,” Panga Sakanyoka aliwaambia askari hao. “Kuweni makini, mkihakikisha hatoki mtu humo ndani, na wala isije ikatokea kuwa jamaa yumo ndani na akagundua kuwa tumemzingira! Na kuweni makini kwa huenda ana silaha. Kama ana silaha, akigundua kuwa amezingirwa hataacha kuitumia. ”



    **********



    ILIKUWA ni kawaida kwa Mzee Songoro kuzinduka usingizini saa 11 alfajiri. Na alfajiri hii, kama alfajiri nyingine zilizopita pia alizinduka saa 11 lakini hakutoka kitandani. Alibaki amekodoa macho huku akihisi hirizi iliyokuwa kiunoni mwake ikicheza.



    Kucheza kwa hirizi hiyo, kwake ilikuwa ni ishara kuwa kuna tukio kubwa mbele yake. Na wazo lililomjia kichwani ni kumhusu mwanawe, Shaka. Tangu Shaka arejee kutoka Dar, amekuwa mtu wa kutoka mara kwa mara, na majuzi aligundua kuwa alikuwa na pesa nyingi.



    Mzee Songoro hakupenda kujidanganya kuwa Shaka anaweza kuwa amezipata pesa hizo kwa njia yoyote ya halali. Alijua kuwa kuna mtu au watu ‘waliolizwa.’ Kitendo cha hirizi hii kucheza kilimpa ishara kuwa Polisi walikuwa wameshamshuku Shaka kuwa ni mhusika wa matukio mawili makubwa ya majuzi; kuuawa kwa wale wakazi wawili wa Lumumba Road na Kibirizi Road.



    Hata hivyo, kwa kuwa alijiamini, hakuwa na wasiwasi. Alijua jinsi ya kutatua tatizo lolote litakalotokea. Akanyanyuka kitandani na kutwaa msokoto wa tumbaku uliokuwa umehifadhiwa vizuri kwenye kipande cha gazeti. Akauwasha na kuanza kuvuta taratibu. Akamtazama mkewe ambaye bado alikuwa ametopea usingizini. Akamwacha. Hakuwa na sababu ya kumzindua na kumshirikisha katika hisia zake za hirizi kutikisika kiunoni.



    Saa 12 alfajiri ilimkuta papohapo kitandani aking’aa macho. Mara akasikia kikohozi kizito kutoka chumba cha pili. Hakikuwa kikohozi kigeni masikioni mwake. Alishakizoea. Ni kikohozi kilichomtambulisha kuwa mwanaye, Shaka yumo chumbani mwake.



    Hirizi kiunoni mwake ilizidi kutikisika.



    Mara akasikia vishindo vya miguu nje ya nyumba, vishindo vizito vya watu waliokuwa wakitembea taratibu. Hirizi ikazidi kutikisika. Sasa akauzima msokoto wake wa tumbaku.

    Akajitoa kitandani na kwenda sebuleni huku kavaa msuli peke yake. Akasimama katikati ya sebule huku akiuangalia mlango wa chumba cha Shaka.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hirizi ikazidi kutikisika kiunoni! Na sasa ikawa kama inayomtekenya.



    Mara mlango ukagongwa. Mzee Songoro akashtuka na kuutupia macho. Ukagongwa tena, safari hii kwa nguvu zaidi. Mzee Songoro akahisi hatari. Haukuwa ugongaji wa heri. Hata hivyo akapiga moyo konde na kuufuata.



    Akaufungua.



    MACHO yake yakakutana na ugeni wa ajabu. Moyo ukapiga paa! Kupatwa na mshtuko mkubwa pindi aonapo au asikiapo chochote huwa ni ishara mbaya kwake. Na jambo lingine ambalo huashiria hali mbaya huwa ni pale hirizi aliyovaa kiunoni inapoanza kumbughudhi kwa kujitikisatikisa.

    Ni bibi yake ambaye alimpa tahadhari kuhusu ishara hizo kabla hajafariki. Na ni bibi yake huyohuyo aliyempika, akaiva na kutokota vilivyo katika nyanja ya ushirikina.



    Mara kwa mara alikuwa akienda kwenye makaburi ya Katubuka ambako marehemu bibi yake alizikwa zaidi ya miaka thelathini iliyopita. Alikuwa akienda huko kufanya tambiko maalumu kama ilivyo kawaida katika mila na desturi za kabila lao la Kibembe. Na kwa kufanya hivyo aliamini kuwa ndipo mambo yake yangeendelea kunyooka.



    Sasa akaamua kuwa makini. Mbele yake walisimama wanaume watatu waliovaa kinadhifu. Akawatazama kwa makini nyusoni na kugundua jambo moja. Sura zao zilitangaza kazi zao.



    “Askari!” alinong’ona kwa sauti ambayo haikuweza kuyafikia hata masikio yake mwenyewe. Hata hivyo alijiamini, na kwa sauti ya kujiamini vilevile alisema, “Karibuni…karibuni vijana.”



    Ni Inspekta Banda aliyetangulia kuingia akifuatiwa na Sajini Kessy kisha afande Panga Sakanyoka. Wakamsalimia kwa heshima huku wakionyesha nyuso za bashasha. Na Mzee Songoro akiwa na umakini wa hali ya juu, hakudanganyika kwa nyuso hizo za tabasamu bali naye aliwakaribisha kwa mfumo huohuo.



    “Mzee tumetoka kituo cha Polisi,” Inspekta Banda alianza kuzungumza, sasa sura yake ikiwa imeshabadilika, tabasamu likiwa limeshayeyuka. “Tunataka utupe taarifa kuhusu mwanao, Shaka.”



    “Shaka?” Mzee Songoro alijitia kushangazwa na swali hilo.



    “Ndiyo, Shaka,” Banda alisisitiza. “Yupo? Kama yupo mwambie atoke na ajisalimishe. Hatutaki kutumia nguvu. Tumekuja kistaarabu, tuondoke kistaarabu.”



    Mzee Songoro aliguna. “Vijana, mbona siwaelewi?” hatimaye aliwauliza.



    “Kitu gani ambacho hukielewi?” Panga Sakanyoka alimbana. “Umeambiwa kamtoe Shaka huko ndani, eti unadai kuwa hutuelewi. Una maana gani mzee?”



    Tabasamu la kujiamini lilizidi kuchanua usoni pa Mzee Songoro. Akawatazama kwa zamu askari hao. Kisha akasema, “Mnanishangaza kwa kauli yenu, vijana. Shaka ni mwanangu, ndiyo. Lakini nina mwaka sasa sijamtia machoni. Aliondoka hapa akaelekea Dar, na majuzi tu nimesikia taarifa kuwa amekamatwa na kuhukumiwa kifungo cha maisha hukohuko Dar!”



    “Umeisikia wapi taarifa hiyo?” Banda alimdaka kwa swali.



    “Nilikuwa nikiangalia taarifa ya habari kwenye televisheni, nd’o nikaipata taarifa hiyo.”



    “Una hakika kuwa Shaka aliyetangazwa kwenye televisheni ndiye huyo mwanao?”



    “Jina. Lilitajwa jina la Shaka Songoro.”



    “Yaani mwenye jina la Shaka hapa duniani ni mmoja tu, huyo mwanao, na mwenye jina la Songoro pia ni mmoja tu, wewe. Si nd’o maana’ake?” Panga Sakanyoka alimuuliza.



    “Hapana.”



    “Sasa kumbe?”



    “Pamoja na habari ile kutangazwa, hata picha yake ilionyeshwa.”



    “Taarifa hiyo ilisema kuwa amehukumiwa kifungo?” Kessy alimdaka.



    “Ndiyo.”



    “Kwa kosa gani?”



    Akilini mwa Mzee Songoro aliliona swali hilo kuwa la kimtego. Lakini ulikuwa ni mtego alioweza kuutegua. “Hata mimi sijui lilikuwa ni kosa gani,” hatimaye alijibu. Akaongeza, “Hata habari yenyewe niliisikia ikiwa ni muhtasari wa mwisho.”



    “Hata hivyo tunajua kuwa Shaka yuko hapa!” Panga Sakanyoka alisema kwa ukali. “Sema ukweli wako kabla hatujaamua kuchukua hatua nyingine. Yupo au hayupo?”



    “Hayupo!” Mzee Songoro alijibu kwa msisitizo.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mzee,” Inspekta Banda alimnyooshea kidole. “Usidhani kuwa tunakuogopa. Usijidanganye kwa hilo. Tukitaka, tunaweza kuondoka na wewe na kwenda kukusweka ndani sasa hivi! Hatuujali umri wako, utatupwa ndani, na kibano utakachokipata huko kitakufanya uutapike ukweli, kama kwa sasa umeshindwa kuusema. Umeelewa?”



    Mzee Songoro alicheka kidogo. “Vijana mna vituko! Yaani mnataka kuniweka ndani kwa kosa lisilo langu!”



    “Utatupwa ndani kwa kosa lako!” Panga Sakanyoka alijibu.



    “Kosa gani?”



    “Hilo sio swali.”



    *********





    SHAKA alikuwa kitandani kajilaza huku akisikiliza maongezi kati ya baba yake na wageni walioingia. Alijua kuwa wageni hao ni askari, na wamekuja kumkamata. Akavuta pumzi ndefu na kunyanyuka. Akasimama na kulifuata begi lake, akalifungua, akautoa msokoto wa bangi na kuuweka juu ya meza.



    Hakuishia hapo, aliichukua pakiti ya sigara na kuchomoa sigara moja. Akaichokonoa na kupunguza tumbaku iliyomo kisha akachomeka bangi. Ukawa ni mchanganyiko maalumu aliouhitaji.



    Kilichofuata, aliuwasha mchanganyiko huo wa sigara na ile bangi kisha akavuta mikupuo miwili ya nguvu. Akili ikachangamka! Papohapo akazivamia nguo zake na kuzivaa. Akaitwaa bastola na kuifungua haraka katika kuchunguza idadi ya risasi zilizomo.



    Akaridhika baada ya kukuta kuna risasi sita. Akaifunga huku akiachia tabasamu hafifu, tabasamu lililofuatiwa na kicheko cha chini sana lakini cha kujiamini. Kila anapokuwa anamiliki chombo cha aina hiyo, chenye gololi kadhaa ndani yake, basi hujiona kuwa yuko salama, hakuna chochote kitakachomletea taabu.



    Katika muda huo, alitambua kuwa alipaswa kufanya chochote kile ili anusurike. Aliamini kuwa hatima ya maongezi au mabishano kati ya baba yake na hao askari, ni askari kuvivamia vyumba vyote vya nyumba hiyo kwa upekuzi. Na alijua kuwa matokeo ya upekuzi huo ni yeye kujikuta katika wakati mgumu zaidi.



    Akaamua kuchukua uamuzi wa haraka, lakini ukiwa ni uamuzi alioamini kuwa ungemnufaisha kwa asilimia mia moja.

    Papo hapo akatupa macho dirishani na kujiwa na wazo la kupitia hapo ili atoke chumbani humo. Hiyo ikiwa ni nyumba ya kawaida, iliyojengwa kwa mianzi na kukandikwa udongo wa mfinyanzi, haikuwa na ukuta ulioweza kuhimili konde moja zito la kono la kulia la Shaka.



    Hivyo, hata hilo dirisha halikuwa katika hifadhi madhubuti kiasi cha kuweza kuwa kikwazo kwake. Kwa kutumia nguvu alizojaaliwa, alilishika dirisha hilo na kulitikisa mara mbili; nje, ndani, nje, ndani! Jibu likapatikana.



    Dirisha liling’oka!



    Mwanamume akachupa nje! Huko alitua kwa kishindo kikubwa puu! Wakati akichukua uamuzi huo hakuwa na wazo kuwa huenda ulinzi katika eneo hilo umeimarishwa hadi nje ya nyumba. Hivyo hakumwona askari aliyekuwa kando ya dirisha hilo, ambaye alikuwa tayari kwa utekelezaji baada ya kuusikia kukurukakara za kung’olewa kwa dirisha hilo.



    Wakati Shaka alipoanza kuigeuza shingo yake kutazama upande wa kulia, askari yule hakumpa nafasi. Alimwahi kwa konde zito la shavuni, konde ambalo kwa Shaka lilikuwa limemkuna tu na kumtambulisha kuwa amekumbana na adui.



    Akili yake ikafanya kazi maradufu. Alikuwa mwepesi na alikuwa na nguvu, hivyo alimtazama askari huyo kwa sekunde moja tu, sekunde ya pili alikuwa amemsukumia konde kwa kono la kushoto, konde lililotua sawia kidevuni mwa askari huyo na kumpeleka chini, taya likiwa halina kazi!



    Shaka akahema kwa nguvu huku akitupa macho huku na kule. Kwa jumla alijiona bado yuko katika kipindi kigumu zaidi. Alitarajia kuwa kuruka dirishani ingekuwa ni hatua ya kwanza katika kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutokumbwa na mshikemshike wa askari hao. Lakini kumbe hajafanya lolote! Amekumbana na askari huku nje, na askari huyo akiwa ana silaha. Hilo tu lilitosha kumfanya ajue kuwa kuna askari mwingine au wengine zaidi ya wale waliokuwa ndani wakimsumbua baba yake.



    Kwa hali hiyo aliamini kuwa bastola peke yake isingetosha kukabiliana na misukosuko iliyokuwa mbele yake. Ndipo alipoinama na kuitwaa bunduki iliyokuwa kando ya yule askari aliyekuwa hoi akikoroma. Akaikamata madhubuti mikononi na kuanza kuufuata uchochoro uliokuwa mbele yake huku akiwa makini katika kujilinda.



    Alikuwa hajavuta hata hatua kumi mara risasi zikamiminika katika uelekeo wake. Akashtuka! Sasa badala ya kutembea, akakimbia hadi kwenye kiambaza cha nyumba ya pili ambako alibana na kuikamata bunduki vizuri tayari kwa kukabiliana na lolote.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sekunde kadhaa zikapita kukiwa na utulivu, kisha akawaona askari takriban kumi wakiwa na bunduki mikononi.

    Askari hao walionyesha kuwa wanamtafuta. Ni hapo ndipo kumbukumbu ya kinga aliyofanyiwa na baba yake ilipomjia kichwani! Hirizi!



    Wahaka ukamtoka, ujasiri ukamjaa! Akainua bunduki na kufyatua risasi kadhaa mfululizo. Askari watano, mmoja baada ya mwingine walianguka chini, maiti! Hakutulia, aliendelea kuitumia bunduki hiyo kikamilifu. Kipindi kingine kifupi kilichofuatia askari wengine wanne walifuata nyayo za wenzao.

    Naam, ulikuwa ni kama muujiza! Askari waliendelea kupukutika huku Shaka akiwa hana hata jeraha!



    *********



    KULE ndani Inspekta Banda aliwatazama wenzake kwa mshangao, bastola ikiwa mkononi. Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi, Panga Sakanyoka alikuwa amechanganyikiwa wakati Sajini Kessy alionekana kama anayejaribu kukumbuka jambo fulani.



    Ukimya ukatawala kwa muda mfupi. Kisha, kama aliyezinduliwa usingizini Sajini Kessy alisimama, bastola ikiwa mkono wa kulia, akawatazama Banda na Panga Sakanyoka kwa zamu, na kwa sauti ya kujiamini akasema, “Nakwenda…! N’achieni n’ende.. n’takufa naye!”



    Hakusubiri ruhusa, alitoka kasi hadi nje ambako alimwona Shaka umbali wa hatua kama ishirini na huku maiti za askari zikiwa zimetapakaa huku na kule. Wakagonganisha macho, dalili za kuua zikiwa bayana ndani ya mboni za macho yao!

    Shaka alikuwa na bunduki na Kessy alikuwa na bastola! Kila mmoja alikuwa mwepesi wa kuuinua mkono na kumwelekezea mwingine silaha, hivyo kila mmoja kujikuta akitazamana na kifo!



    Hata hivyo, ni Shaka aliyekuwa mwepesi wa kufikiri na kutekeleza kwa haraka uamuzi wake. Alifyatua haraka risasi moja bila ya shabaha kamili. Risasi hiyo ikamkosa Kessy kidogo sana.



    Lilikuwa ni jambo lililomfanya Sajini Kessy ahisi kuwa kifo kilikuwa kikimnyemelea kwa kasi ya kutisha. Hivyo akaamua kuchukua hadhari kubwa zaidi. Akajirusha hadi ndani ya banda moja.



    Ujenzi wa banda hilo ulikuwa haujakamilika, hata hivyo urefu wa ukuta wake ulitosha kumhifadhi mtu yeyote aliyeinama au kuchuchumaa. Kessy aliporukia ndani alichuchumaa na kujiandaa kukabiliana na mashambulizi ya Shaka. Moyoni mwake alijua kuwa kazi iliyomkabili mbele yake ni kubwa kuliko alivyofikiria na kukadiria. Adui yake alikuwa na silaha nzito, iwezayo kumwaga risasi kama mvua. Yeye alikuwa na bastola yenye risasi tatu! Hivyo, timbwili-timbwili lililokuwa mbele yake aliamini kuwa halitakuwa la kawaida.



    Kazi nzito, alijisemea kimoyomoyo huku akikumbuka jinsi alivyowaaga wenzake, maafande wake kule ndani kuwa anajitoa mhanga kumvaa Shaka, na kwamba yuko tayari kwa lolote. Ni kauli ile aliyoitoa kule ndani na kutoka bila ya kusubiri ruhusa yao, ndiyo iliyomfanya ajipe ujasiri wa aina yake na kuamua kuitimiza nadhiri aliyokwishaiweka. Aliamua kufa au kupona!



    Anga ilikuwa ikizidi kutakata. Jua lilichomoza mashariki na kushusha miali yake ardhini, hali iliyomfanya Kessy ajawe na matumaini ya kufanikisha lolote lile alilodhamiria kulitekeleza. Katika kukamilisha azma yake ya kumpata Shaka akiwa hai au maiti, mwangaza wa jua ulikuwa ni muhimu sana kwake.

    Aliamini kuwa, mwangaza huo wa jua ndiyo utakaotoa ufumbuzi wa kizungumkuti hicho. Lakini pia aliamini kuwa alipaswa kuwa makini na kuchukua hadhari kubwa dhidi ya Shaka, mtu ambaye hakutofautiana na shetani.



    Dakika mbili, tatu zilikatika wanaume hao wakiwindana. Mara kadhaa walirushiana risasi ambazo hazikuzaa matunda kwa upande wowote.



    Hatimaye ikatimu dakika ambayo huenda Kessy aliihitaji kuliko dakika nyingine zote zilizotangulia! Shaka alikuwa ‘peupe’ akimulikwa vizuri na miali ya jua. Kessy aliikamata bastola yake vizuri na kuielekeza kwenye kivuli cha Shaka kisha akafyatua risasi moja iliyosalia katika bastola yake.



    Kilichotokea kilikuwa hakitofautiani na muujiza! Kessy alifyatua risasi akikilenga kivuli cha Shaka badala ya kumlenga mlengwa!



    Shaka alitoa yowe kubwa, akaruka juu kidogo kisha akaanguka chini, tii! Chali, bunduki ikiwa imemtoka mkononi na kuanguka hatua chache kulia kwake!



    Hakuvuta pumzi zaidi ya sekunde tano!



    **********



    LILIKUWA ni tukio lililozua patashika vichwani mwa Inspekta Banda na Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi, Panga Sakanyoka. Hawakuamini mara moja kuwa Sajini Kessy amefanikiwa kumuua jambazi hatari, Shaka Songoro kwa namna ya ajabu kiasi kile.



    Wangeamini vipi wakati tangu enzi na enzi kifo hutokea pale tu risasi inapozama mwilini moja kwa moja na wala siyo kwa kupitia katika kivuli cha mlengwa? Na kuna uhusiano gani kati ya kivuli na umbo halisi? Mbona hata hao wazungu waliozitengeneza silaha hizi hawajaivumbua teknolojia hiyo ya ajabu?CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Kulikuwa na giza nene mbele ya askari hao. Na

    hata wakati maiti ya Shaka ilipofikishwa katika Hospitali Kuu ya Mkoa, Maweni, wao waliharakisha kukutana ofisini ambako waliamua kumdadisi Sajini Kessy.



    “Hili ni jambo la kushangaza, Sajini,” Panga Sakanyoka alisema huku akimtazama Sajini Kessy kwa macho makali. “Naamini hata RPC akisikia habari hizi, japo atafurahi lakini pia atashangaa sana.



    “Mauaji aliyoyafanya yule mshenzi yalikaribia kumtia wazimu mzee wa watu, na siyo yeye peke yake. Hata sisi wengine tulikuwa tumebaki njiapanda, zaidi ni kama vile tulikuwa tukitapatapa. Nadhani RPC alikwishaamini kuwa Shaka ni shetani la aina ya kipekee, hivyo, kukamatwa au kuuawa ni jambo lisilowezekana. Ndiyo maana kabla hamjaitwa, hakuwa na imani na sisi -askari wa hapa.”



    “Lakini sasa ataamini,” Inspekta Banda alisema huku tabasamu la mbali likichanua usoni pake.



    “Ndiyo ataamini lakini atahoji sana ni mbinu gani tuliyotumia hadi kummaliza mshenzi huyo,” Panga Sakanyoka alisema.

    “Kuzijua mbinu tulizotumia kutamsaidia nini?” Kessy alihoji huku naye akitabasamu.



    Panga Sakanyoka alikohoa kidogo. Yeye, tofauti na wenzake, kwa muda wote huo uso wake haukuwa na tabasamu hata la bandia. Alionyesha wazi kusumbuliwa na jambo kichwani mwake.



    Akasema, “Yule nd’o bosi wa mkoa. Ni msemaji mkuu kwa masuala yote ya kipolisi hapa Kigoma. Kwa vyovyote lazima ataniuliza mimi, na mimi sijui chochote.” Papohapo akamkazia macho Sajini Kessy na kuongeza, “Wewe nd’o unaweza kutufumbulia kitendawili hiki.”



    Tabasamu la Sajini Kessy liliendelea kuchanua usoni, kisha kwa sauti ya kujiamini alisema, “ Ilikuwa ni kazi ndogo tu, afande. Nakumbuka jana asubuhi wakati wa kikao na RPC niliahidi kumtia mikononi Shaka. Kumkamata au kumuua! Sikuwa nabahatisha, wala sikuwa natoa hadithi ya kubuni. Nilikuwa na hakika ya n’nachokisema!”



    Alishusha pumzi ndefu, akameza funda la mate kisha akaendelea, “Afande, majambazi wengi wa huku Kigoma wana tabia ya kuushirikisha ushirikina katika kazi zao. Naifahamu vizuri Kigoma hii; nimezaliwa hapa, nimekulia hapa na nimesomea hapa. Kwa nini nisiyajue vizuri mazingira ya hapa?



    “Namfahamu vizuri Mzee Songoro,” aliendelea. “ Habari zake nimeanza kuzisikia tangu utotoni. Anasifika kwa mambo ya ushirikina. Ni mchawi wa kipekee! Na katika mizunguko yangu ya jana nimedokezwa kuwa yeye ndiye nguzo kuu ya Shaka.”



    “Yaani anamkinga kiuchawi?” Inspekta Banda aliuliza.



    “Nd’o maana’ake.”



    “Hilo ni jambo linalowezekana?” Panga Sakanyoka alihoji kwa namna ya kutomwamini Kessy.



    “Ni jambo linalowezekana, afande,” Sajini Kessy alijibu kwa mkazo. “Japo si vizuri kwa kofia zetu za dola kujenga imani za kishirikina, lakini huo nd’o ukweli wenyewe. Mzee huyo alimpa kinga mwanaye ili asidhurike. Ndiye kinara wa mpango wote wa Shaka tangu alipotoroka kule gerezani. Lakini…”



    Alisita kidogo na kumeza tena funda la mate, kisha akaendelea, “Hata hivyo namshukuru sana marehemu, baba’angu mzazi.”



    “Kwa nini?” Panga Sakanyoka alimuuliza huku akimtumbulia macho.



    “Ni yeye aliyenidokeza juu ya mbinu ya kummaliza mtu ambaye hafi kwa mkuki, mshale, kisu, panga au risasi.”



    “Ni hiyo tunayohitaji kuijua!” Panga Sakanyoka alionyesha shauku ya kuteguliwa kitendawili hicho.



    Sajini Kessy alimtazama Inspekta Banda kisha akayahamishia macho kwa Panga Sakanyoka, tabasamu lake likizidi kuchanua. Na akionekana kutokuwa na haraka, akasema, “Mzee Songoro anaweza kutufumbulia kitendawili hiki. Ni vyema tumtoe mahabusu aje kutupatia hadithi kamili.”



    Muda mfupi baadaye Mzee Songoro alikuwa ameketi sakafuni, mbele ya askari hao. Machoni mwake, hakuonekana kuwa na wasiwasi wowote. Aliwatazama askari hao kwa zamu, kisha akacheka kwa sauti yenye mkwaruzo, kitendo kilichowashangaza askari hao.



    “Unacheka nini we’ mzee?” Banda alimuuliza huku akimtazama kwa macho makali.



    “Unataka ninune?” badala ya kujibu, Mzee Songoro naye alimuuliza, sauti yake ikiwa ni ya kujiamini, akimtazama bila hata ya chembe ya woga.



    Akaendelea, “ Sina sababu ya kununa, nina sababu ya kusikitika. Na siyo lazima nisikitike kwa kuwaonyesha usoni kuwa nimesikitika. Japo mmemuua mwanangu kipenzi, hata hivyo sina budi kumpongeza sana kijana huyu,” akamnyooshea kidole Sajini Kessy.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Banda na Panga Sakanyoka wakayahamishia macho kwa Kessy. Wakamtazama kwa nukta chache tu na kumrudia Mzee Songoro.



    “Ni kijana hatari sana na shupavu vilevile!” Mzee Songoro aliendelea. “Sikudhani kuwa kuna yeyote ambaye angeweza kuigundua siri ya nguvu na uwezo wa kinga ya hirizi iliyo kiunoni mwa marehemu mwanangu. Kwa kweli kijana huyu amefanya jambo la ajabu sana…”



    “Siki’za mzee,” Panga Sakanyoka alimkata kauli. “Hatutaki mahubiri. Toa siri iliyofanya mwanao asipatwe na risasi! Hatutaki mlolongo wa maneno kama unatusimulia riwaya hapa!”



    “Huko ndiko tunakoelekea, bwa’mdogo,” Mzee Songoro alisema bila hata ya chembe ya woga. Akajipapasa katika boksa yake iliyokuwa ndani ya kanzu ndefu aliyovaa. Mara akautumbukiza mkono katika mfuko mmoja wa boksa hiyo na kuutoa ukiwa na kibiriti na msokoto wa tumbaku. Akauwasha msokoto ule na kuvuta mikupuo miwili, mitatu ya nguvu kisha akauzima.



    Moshi mzito, wenye harufu kali ukatapakaa ofisini humo. Moshi huo ulikuwa ni kero tupu kwa askari wengine, siyo Inspekta Banda ambaye alikuwa mvutaji wa sigara na zaidi, enzi za kukua kwake aliwahi hata kuvuta bangi na tumbaku za kusokota.



    Hata hivyo, kero hiyo haikuwa ya kudumu kwa askari hao. Walivumilia kwa dakika moja hivi na hali ikarudi kuwa ya kawaida.



    “Shaka alikuwa ni mwanangu wa pekee,” hatimaye aliendelea. “Nilimpenda sana. Kwa hivyo niliamua kumlinda; nikamfanyia zindiko la pekee, zindiko kubwa. Katika zindiko hilo, nilimpatia hirizi ambayo ilimfanya asidhurike; si kwa risasi tu bali hata kwa panga, kisu, mshale, mkuki hata nondo. Ili uweze kumdhuru ulipaswa kushughulika na kivuli chake tu!”



    “Kivuli?” Inspekta Banda na Panga Sakanyoka walibwata kwa pamoja.



    “Ndiyo, kivuli chake tu!” Mzee Songoro alisisitiza. “Na ndivyo alivyofanya huyu kijana wenu. Eti bwa’mdogo?” kufikia hapo alimgeukia Sajini Kessy.



    “Ndiyo,” Kessy alijibu huku akiachia tabasamu dhaifu.



    “Uliipata wapi mbinu hiyo?” Mzee Songoro alimuuliza.



    Kessy hakujibu. Badala yake alilizidisha tabasamu lake huku akiwatupia macho kwa zamu Banda, Panga Sakanyoka na Mzee Songoro.



    “Najua hutaki kuitoa siri hiyo,” Mzee Songoro alisema huku akikenua meno na kuupeleka tena ule msokoto wa tumbaku yake mdomoni. Akavuta mkupuo mmoja na kutulia. Muda mfupi baadaye moshi ukatoka kwa kupitia mdomoni na puani.



    Akakohoa kidogo na kuutupa msokoto ule sakafuni kisha akausaga na kandambili zake chakavu. Akamkodolea macho Inspekta Banda na kwa sauti ya unyonge akasema, “Mwanangu amekufa. Mmemuua mwanangu wa pekee. Sikutarajia kama ingetokea hivi! Wallahi sikutarajia! Mwanangu kafa kiajabuajabu!”



    Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi mkoani Kigoma, Panga Sakanyoka, alishusha pumzi ndefu, akamtazama Mzee Songoro kwa macho makali yasiyopepesa. Alipowageukia wenzake akamwona Inspekta Banda akimtazama Sajini Kessy kwa namna ya kumpongeza. Wote wakatabasamu.



    Hata wakati Mzee Songoro aliponyanyuka na kuondoka mbele yao, wao walikuwa wameduwaa, wakitazamana, huku wakitabasamu.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ni Inspekta Banda aliyewazindua akisema, “Hakuna cha kutukalisha hapa. Huyu mzee hakuna haja ya kuhangaika naye. Kilichobaki ni RPC kuwaita waandishi na kulitangazia taifa kuwa kikosikazi kimemaliza kazi!”



    MWISHO





0 comments:

Post a Comment

Blog