IMEANDIKWA NA : INNOCENT A. NDAYANSE
*********************************************************************************
Simulizi : Pigo La Mwisho
Sehemu Ya Kwanza (1)
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
KAMBA Kiroboto alishusha pumzi ndefu mara tu alipokuwa nje ya Gereza la Keko jijini Dar es Salaam. Akaangaza macho huku na kule kama mgeni aliyeletwa hapo huku kafumbwa macho. Akageuka na kulitazama lango kuu la gereza, kisha akageuka tena na kuyatupa macho mbele ambako aliwaona watu wakipita na hamsini zao.
Kama aliyezinduliwa usingizini, alianza kuvuta hatua ndefu akiliacha eneo hilo. Akatembea kikakamavu, akijihisi kama ambaye bado hajawa huru na kwamba labda muda mfupi ujao atapigiwa filimbi ya kuashiria kuwa ametoroka. Baada ya hatua kama mia mbili hivi, akasikia honi nyuma yake.
Alipogeuka, akaliona gari dogo, jeupe likimsogelea. Akakunja uso na kulitazama kwa makini huku na yeye akipunguza mwendo. Lilipokuwa usawa wake, likasimama kisha vioo vikashushwa. Kamba naye akasimama na kuinama kidogo ili amwone huyo anayeliendesha gari hilo.
Nyuma ya usukani kulikuwa na mwanamume aliyevaa suti nyeusi, maridadi huku uso wake ukiwa umenawiri na akitabasamu. Macho yake ya kujiamini, macho yaliyowaka ukwasi sanjari na ndevu changa zilizochongwa kiufundi na kinyozi aijuaye kazi yake, ilikuwa ni taswira tosha iliyomweka mtu huyo katika kundi la wenyenazo.
“Twen’zetu mshkaji wangu,” mtu huyo alimwambia Kamba huku akimfungulia mlango.
Kamba alishangaa na kusita. Huyu mtu ni nani? alijiuliza. Hata hivyo, hakuwa na hisia za kujiwa na mtu huyu kwa dhamira mbaya. Hakuwa na kumbukumbu ya kufanya kosa lolote dhidi ya mtu mweusi au mweupe kiasi cha miaka saba iliyopita. Na kosa lililomfanya asote humu Keko hadi siku hii halikumhusu mtu mweusi, hivyo akaamua kuingia garini akiamini kuwa hiyo ni lifti ya msamaria mwema.
Gari likaondoka huku muziki laini ukisikika sanjari na kiyoyozi kilichoongeza starehe ndani ya gari hilo la kifahari.
“Pole sana msh’kaji wangu,” mtu yule aliuvunja ukimya. “Maisha ni mzunguko. Mtu hupita kwenye milima na mabonde hadi siku ya mwisho wa uhai wake hapa duniani. Yote ni maisha na mwanamume umezaliwa ili upite kwenye mfumo huo wa maisha. La kushukuru Mungu ni kuwa umetoka ukiwa salama salimini. Unaona, unatembea, unanusa, unasikia, mikono mizima, ilimradi uko fiti na tayari kupambana tena na maisha ya huku uraiani.”
“Ni kweli,” Kamba aliitika bila ya kuwa hapo kimawazo. Akili yake ilikuwa nyumbani kwake akimkumbuka mkewe na mwanaye, Safi.
Hata hivyo, mara kwa mara mawazo hayo yalikatishwa na sura mpya ya Jiji la Dar es Salaam lenye majengo makubwa yaliyooteshwa kando ya barabara na hivyo kumfanya ajikute akiyakodolea macho na kujiona kuwa yuko katika Tanzania nyingine na Dar es Salaam nyingine. Kwa maana nyingine alichukulia kuwa miaka aliyosota gerezani ni karne nzima.
Waliiacha Keko, wakaipita Kariakoo eneo la Karume, wakaikanyaga Kigogo, Magomeni hadi wakaja kuibukia Mkwajuni Kinondoni. Pale, mtu huyo akakanyaga breki na kumuuliza Kamba, “Njia gani?”
“Niko huko uswahilini, Moscow,” Kamba alijibu huku akifungua mlango.
“Naweza kukupeleka,” mtu huyo alisema, akionesha kumtaka Kamba asiteremke.
Kamba akatulia. Hata hivyo, akashangazwa na ujenzi wa barabara hiyo; hakukuwa na eneo la kuweza kuchepuka na kuingia eneo la Moscow. Mtu huyu alilazimika kuendesha gari hadi Kinondoni ‘A’ kisha akageuza na kuanza kurudi Mkwajuni.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nikatie hapa Studio au Mkwajuni,” alimuuliza wakati wakipita eneo la Studio.
“Hata hapa panafaa,” Kamba alijibu huku akiwa hafurahishwi na msaada huu unaozidi kutolewa. Hakuwa radhi kumfunulia kila kitu huyu mtu. Hivyo, baada ya kupita mitaa kadhaa akamwamuru asimame.
Ulikuwa ni mtaa wa pili kutoka ule alioishi Kamba. Hakutaka kumfikisha mlangoni. Utampelekaje mtu hadi mlangoni kwako ilhali humjui? Lifti tu ndiyo kiwe kigezo cha kumkaribisha hadi chumbani? Siwezi kuwa bwege kiasi hicho, alijisemea kimoyomoyo huku akijiandaa kuteremka.
“Kwangu hapafikiki kwa gari,” alimhadaa mtu huyo. “Kama unavyoiona Moscow imekaa shaghalabaghala, hapa kuna mtaa, hapa uchochoro. Kwangu ni ndani, ndani sana msh’kaji wangu.”
“Ok, hakuna tabu,” mtu huyo alisema huku akiingiza mkono ndani ya mfuko wa shati na kuchomoa noti ya shilingi 10,000 na kumpatia Kamba.
“Dah! Poa wangu, umeniwezesha, ” Kamba alishukuru huku akiachia tabasamu kubwa.
“Us’jali,” aliambiwa. “Eeh…” mtu huyo alisema na kusita.
Kamba akamgeukia. Wakatazamana, kimya kikitawala katika vinywa vyao kwa nukta chache. Kisha mtu huyo akafunguka, “Unaweza kuwa na chance kesho tuonane na kuongea kwa kirefu?”
Kamba akafikiri haraka na kusema, “Inawezekana au isiwezekane, kwa sababu hata home sijatia tim mwanangu. Naweza kuwa na jibu sahihi nitakapofika home.”
“Yeah, ni kweli. Ok, us’konde. Fika kwanza home na kama mambo yatakuwa shwari basi fanya juu, chini kesho tuonane.”
Kamba alikunja uso na kuuliza, “Kwani kuna ishu gani hasa?”
“Mojawapo ni kufahamiana,” mtu huyo alijibu. “Lakini pia kuna mengine ya kawaida ya kuzungumza kama wanaume.”
“Kwa hiyo tutawasiliana vipi?”
Mtu huyo alitwaa kijikaratasi na kalamu katika dashibodi, akaandika tarakimu kadhaa za mitandao mitatu ya simu kisha akampatia Kamba, akisema, “Hizo nd’o namba zangu. Nitafute kwenye mtandao wowote utanikuta hewani.”
“Poa,” Kamba aliitika huku akikipachika kijikaratasi hicho mfukoni.
*****
Saa tano asubuhi, mama Safi alikuwa bafuni akioga. Hiyo ilikuwa ni baada ya kumaliza kufanya usafi wa nyumba na kufua. Wakati akiendelea na hicho kilichompeleka bafuni humo, mara akasikia mlango ukigongwa.
Akashtuka na kutulia kidogo. Baada ya ukimya kurejea, akahisi labda masikio yake hayakuwa sahihi, akachota tena maji na kujimwagia. Lakini tena akasikia mlango ukigongwa. Sasa akayaamini masikio yake na akahisi huenda ni rafiki yake, mama Sikudhani wa nyumba ya tatu ndiye aliyegonga mlango.
Mlango ukagongwa kwa mara ya tatu.
“Nakuja, niko bafuni,” alisema kwa sauti ya juu, akidhamiria huyo mgongaji asikie, mgongaji ambaye bado akili yake ilimtuma aamini kuwa ni mama Sikudhani.
Ukimya ukarejea tena. mama Safi akaendelea kuoga lakini sasa akiongeza kasi ili amalize mapema. Hatimaye alimaliza. Akajifuta maji harakaharaka na kutoka. Moja kwa moja hadi mlango mkubwa.
Akiwa ndani ya vazi moja tu la kanga bila nguo nyingine huko ndani, na akiamini kuwa huyo mgongaji wa mlango ni mama Sikudhani, alikizungusha kitasa na kuuvuta mlango.
Hakuwa mama Sikudhani!
*****
Siku ya mwisho kwa Kamba na mkewe, mama Safi kuonana gerezani, Kamba hakumwambia bayana kuwa alibakiza siku chache kuachiwa huru. Wala hakumwambia kuwa lini atakuwa huru. Na alifanya hivyo ili amshtukize.
Akitambua fika kuwa ametumikia kifungo kwa muda mrefu, alijenga hisia kuwa mkewe hataweza kuvumilia kwa kipindi chote hicho. Akiwa ni binadamu, kama binadamu wengine wenye afya njema, wanaoweza kupatwa na hisia na msisimko wa mapenzi, kwa vyovyote vile naye angejikuta akiingia majaribuni na hatimaye kutafuta njia ya kuyatuliza mashetani yatakayokuwa yakimsumbua.
Atatongoza au atatongozwa. Hapo atampata mwanamume, na huenda hatimaye mwanamume huyo akapewa mamlaka ya kuitawala nyumba hiyo hadi kitandani. Hisia hizo zilimtawala Kamba, zikiambatana na kilo lukuki za wivu!
Wivu!
Ndiyo, alikumbwa na wivu kwa kuwa alijua jinsi mkewe, mama Safi anavyojua kulea, malezi ya hadharani na faraghani. Je, kwa hii miaka saba ambayo hawakuwa pamoja, huyo mwanamume atakayebahatika kupewa malezi ya faraghani hatachanganyikiwa kiasi cha kuhamia hapo moja kwa moja?
Ni fikra hizo zilizomfanya asite kumtamkia moja kwa moja mkewe kuwa ni lini ataachana rasmi na maisha ya gereza hilo la Keko. Zaidi, alimwambia, “Vumilia tu mama Safi. Nitatoka na nitarudi tuishi kama zamani na mwan’etu, Safi.”
Ni asubuhi hii ndiyo alikuwa amerudi. Alirudi bila ya kutoa taarifa yoyote kabla. Hapo mlangoni walitazamana kwa sekunde kadhaa. Kamba akaugundua mshtuko na mshangao uliompata mama Safi, mshangao na mshtuko uliompeleka Kamba mbali kimawazo kiasi cha kuibua ule wivu wa mapenzi.
Kwa nini ameshtuka? Kwa nini anashangaa? Kuna mwanamume ndani? Kuna…kuna... Maswali mengi yalimjia kichwani na akajisikia kunyong’onyea.
“Mbona hunikaribishi?” hatimaye alijikakamua kumuuliza. “Au sina nafasi tena ndani ya nyumba hii?”
Mama Safi alizinduka, na badala ya kutamka chochote alimrukia Kamba na kumkumbatia kwa nguvu. Kwa sekunde kadhaa walikumbatiana kisha Mama Safi akajing’atua taratibu na kunong’ona, “ Karibu…karibu mpenzi…karibu Baba Safi.”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*****ENDELEA KUTIRIRIKA*****
MUDA mfupi baadaye Kamba na Mama Safi walikuwa ndani, wameketi katika sofa ambalo Kamba alishuhudia jinsi lilivyochakaa. Hakushangazwa na uchakavu huo; miaka saba iliyopita aliyaacha masofa hayo yakiwa katika hali iliyovutia macho ya mtu yeyote. Hata hivyo, alitambua kuwa miaka saba siyo siku saba. Hivyo halikuwa jambo la ajabu kuyakuta masofa katika hali hiyo. Kwa kuwa yalitumika basi pia yalikuwa na haki ya kuchakaa.
Hata hivyo, hakutaka kuzungumza chochote kuhusu uchakavu wa samani hizo za ndani pamoja na dosari nyingine zilizodhihirika machoni pake. Alihitaji mapumziko. Ndiyo, apumzike kwanza kabla ya kuchukua hatua yoyote nyingine atakayoona inafaa.
Alitulia hapo sofani akimtazama mkewe alipokuwa akiiwasha televisheni na kuseti kituo fulani chenye muziki mfululizo. Kisha akamtazama kidogo na kusema, “Njoo chumbani ubadili nguo, mpenzi.”
Kamba alijinyanyua kitini taratibu na kumfuata mkewe chumbani. Huko akakabidhiwa taulo kisha akakumbatiwa na kuambiwa kwa sauti nyororo, “Kaoge, kaoge mpenzi utoe nuksi za jela, kisha uje nikupokee vizuri, nikukaribishe kwa jinsi inavyokustahili. Najua una njaa; nitakupa chakula chochote unachohitaji. Najua una kiu; nitakupatia kinywaji chochote utakachopenda.”
Yalikuwa ni maneno matamu masikioni mwa Kamba. Yalipenya na kutua moyoni kiasi cha kumletea msisimko wa kipekee pale alipovuta kumbukumbu ya utundu wa Mama Safi kitandani.
Ilimlazimu kutumia nguvu za ziada kuustahimili mhemko huo uliomjia. Hakumtazama Mama Safi usoni, katika kuyaepuka yale macho yake mazuri yanayoshawishi na kubembeleza. Badala yake alijing’atua kistaarabu mikononi mwake na kuelekea bafuni.
Alipokwishaoga alikuwa Kamba mwingine, Kamba aliyechangamka, Kamba aliyeoga akatakata kwa sabuni yenye manukato yaliyovutia. Chumbani akamkuta Mama Safi akiwa tofauti na alivyokuwa sebuleni. Ile kanga ambayo lilikuwa ni vazi pekee lililousitiri mwili wake awali, sasa hakuwa nayo. Na siyo kwamba badala ya ile kanga kulikuwa vazi lingine, la hasha. Mama Safi alikuwa mtupu! Mtupu kama alivyozaliwa! Alikuwa kasimama mbele ya kioo kirefu, kilicholibeba umbo lake lote, akijitazama.
Kama kuna kipindi ambacho Kamba alichanganyikiwa na kujikuta akikumbwa na sintofahamu akilini mwake basi ni hiki. Mbele yake alimwona Mama Safi mpya, Mama Safi ambaye ana mvuto wa kipekee, Mama Safi anayeshawishi kwa mwonekano wa umbo lake.
Miaka saba aliyosota gerezani haikutokea hata mara moja aliyostarehe kimwili na mwanamke. Na siyo kustarehe tu na mwanamke bali kustarehe na mtu wa jinsia yoyote. Kule gerezani alishuhudia mengi. Walikuwapo wanaume ambao walilazimika kuingiliwa kinyume na maumbile kwa minajili ya kupata chakula kizuri na kupata unafuu wa kutosulubishwa kwa kazi nzito.
Aligundua kuwa wale waliowatendea wenzao unyama huo walifanya hivyo kutokana na kuzidiwa na hamu ya kustarehe kingono. Waliwahitaji wanawake lakini hawakuwa na uwezo wa kuwapata kulingana na mazingira. Lakini pia alikuwa akiwaza kuwa si kila mwanamume anayefanya hivyo, hufanya kwa kukosa mwanamke. Hapana! Kuna wanaume ambao kuwaingilia wanaume wenzao ni maradhi yasiyotibika. Hawawataki wanawake, wanawataka wanaume wenzao!
Yeye, akiwa ni mwanamume rijali, mwenye mwili mkubwa na nguvu za kutosha kuua mtu, angeweza, kama angependa kujipatia mfungwa yeyote wa kumstarehesha kimwili iwe kwa maelewano au kwa mabavu.
Ndiyo, angeweza, kama angependa, lakini hakupenda. Na hakupenda kwa kuwa aliamini kuwa kitendo hicho huchangia kwa kiasi kikubwa maambukizo ya gonjwa hatari la UKIMWI. Hiyo ni kwa upande mmoja. Kwa upande wa pili, aliamini kuwa kwa ubavu aliokuwa nao, hakutakuwa na mfungwa yeyote atakayethubutu ‘kumgeuza mwanamke.’ Umbo lake la kikakamavu lilikuwa ni silaha thabiti ya kumlinda na ushenzi wa aina yoyote gerezani.
Hadi alipomaliza kifungo, hakuwa amepata msukosuko wowote wa kumdhalilisha na wala hakuwahi kupata kiumbe wa kike wa kumstarehesha kimwili. Hali hiyo ndiyo iliyomfanya ajikute katika wakati mgumu chumbani humu akimtazama Mama Safi katika hali hii.
Alishindwa kuvumilia. Akamvaa na kumkumbatia kwa nguvu, akihema kwa tabu huku mikono yake ikipita hapa na pale mwilini mwa Mama Safi. Halikuwa tendo ambalo Mama Safi angeweza kustahimili. Hapana. Na yeye akiwa na miaka saba tangu Kamba aondoke, ni wazi alihitaji huduma muhimu akiwa ni mwanadamu aliyekamilika kila kiungo. Ile tiba mbadala ya maji ya moto, tiba aliyokuwa akiitumia mwenyewe chumbani kila alipohisi kuzidiwa na matamanio haikuweza kuyatibu maradhi yake kwa asilimia mia moja. Alihitaji tiba halisi, tiba kutoka kwa mwanamume!
Hii mikono ya Kamba ilipokuwa ikipita hapa na pale, ikitomasa na kupapasa, ilimletea hali tofauti na kujikuta akikumbuka kila walichokuwa wakikifanya kabla Kamba hajakumbwa na tuhuma zilizompeleka jela. Na ndipo naye alipoamua kujibu. Zikapita dakika takriban tano wakichezeana kimahaba kama wanaoigiza sinema.
Kisha ikafuata hatua nyingine muhimu kwao.
**********
NUSU saa baadaye, nyuso za Mama Safi na Kamba zilikuwa zimekunjuka maradufu. Zilikuwa ni nyuso zilizotangaza matumaini. Kila mmoja alimtazama mwenzake kwa macho yaliyotamka neno moja tu: asante. Na ni wakati huo ndipo Kamba alipomkumbuka mwanaye, Safi ambaye alimwacha akiwa na umri wa mwaka mmoja.
“Mwanangu yuko wapi?” aliuliza.
“Nd’o umemkumbuka?” Mama Safi alimuuliza huku akimtazama kwa namna ya msuto wa kimasihara. “Umefikia kifuani kwa mwenzio bila hata ya kujua hali ya mwanao, nyooo!”
Kamba akacheka kidogo kisha akasema, “Si unajua tena baby, siku nyingi!”
“Na kweli siku nyingi, maana’ake…” Mama Safi alisema na kuiacha sentensi hiyo ikielea.
Wakacheka kwa pamoja.
“Kwa hiyo yuko wapi Safi wangu?” Kamba alilirudia swali lake.
“Bwana, yuko shule, na akitoka labda hatakuja huku moja kwa moja.”
“Hatakuja huku!” Kamba alishangaa. “Atakwenda wapi?”
Mama Safi akaguna. Kisha naye akarusha jibu kwa swali, “Kwani hukumbuki kuwa kuna siku nilikuja gerezani nikakwambia kuwa Safi anaishi na mama’ake mdogo?”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nakumbuka.”
“Basi nd’o ivo.”
“Nd’o ivo? Hapana, nataka kumwona mwanangu.”
“Utamwona tu. Maisha yenyewe haya tabu tupu aje kukaa huku ya nini?”
“Ivoivo!” Kamba aling’aka. “Mtoto aishi na wazazi wake! Tutakachokula sisi ndicho atakachokula yeye. Tukilala njaa, na yeye atalala njaa au ndipo tutakapotafuta njia ya kumnusuru yeye asilale njaa. Lakini ni muhimu aje, aishi na baba na mama yake!”
“Sawa, jioni nitamfuata,” Mama Safi alisema kwa unyonge.
Kwa mtazamo halisi, siku hiyo ilikuwa ni ya kipekee katika nyumba hiyo. Siku njema. Siku ya furaha. Kila mmoja alikuwa na furaha ya aina yake. Mtoto Safi alifurahi na kuchangamka, alipoonyeshwa na mama yake kuwa “huyu ndiye baba yako. Alikuacha ukiwa na mwaka mmoja…” Mara nyingi Safi alikuwa akiwasikia wenzake wakisema “baba kasema hivi…mama kanifokea… baba kaninunulia madaftari…” na kadhalika na kadhalika. Yeye alikuwa na uwezo wa kusema “mama kanipikia wali…mama kaninunulia… ” siyo “ baba kaninunulia…”
Hakuwa na chochote cha kuzungumzia kuhusu baba. Leo ndiyo anamwona! Kwa jumla alifurahi. Na sasa akajiona kuwa ni sawa na watoto wengine.
Mama Safi naye leo kwake ilikuwa ni siku mpya. Kwa muda wa miaka saba ameishi kwa upweke wa aina yake, akilala na mwanaye tu chumbani bila ya mwenzi wake kipenzi, Kamba Kiroboto. Amekosa huduma nyingi na muhimu tangu Kamba afungwe jela. Angeweza, kama angependa kuwa na urafiki na mwanamume yeyote mtaani, ambaye angemtulizia haja zake za kimwili. Lakini hakuwa mtu wa aina hiyo.
Alijiheshimu, na alimheshimu Kamba Kiroboto. Kwake, Kamba alikuwa ni zaidi ya mume. Alijiona atakuwa ametenda kosa la jinai kama atadiriki kumchojolea nguo mwanamume mwingine wa ‘kupita’ kwa ajili tu ya kukidhi matamanio ya mwili wake. Aliamini kuwa atakuwa ametenda dhambi isiyosameheka mbele ya Mungu.
Kumbeba mwanamume mwingine kifuani huku Baba Safi akiwa anateseka jela….hapana haiwezekani! Mara kwa mara alikuwa akijiapiza hivyo. Na alifanikiwa kujilinda hadi siku hii ambayo ghafla, bila ya kutarajia amemwona Kamba akiingia!
Ndiyo, Kamba amekuja na kuzikuta mali zake zikimsubiri. Akakabidhiwa kwa mifumo yote ya makabidhiano na kuzitumia kwa nguvu, utaalamu na pumzi zote alizojaaliwa. Kisaikolojia, sasa Mama Safi alijisikia mzima na mkamilifu tofauti na siku nyingi zilizopita.
Kwa Kamba, ilikuwa ni siku ya furaha isiyo kifani.
Kwanza, hiyo ilikuwa ni siku aliyoanza kuvuta hewa tamu, hewa ya uhuru baada ya kutoka gerezani, Keko alikokuwa akitumikia kifungo cha miaka saba.
Pili, hii ilikuwa ni siku ambayo hawezi kuifananisha na siku zote alizokuwa akiishi kule gerezani. Mapokezi. Ndiyo, mapokezi maalumu, mapokezi ya kitaalamu aliyopewa na mkewe, Mama Safi, mchana, yalikuwa ni dawa iliyomweka katika hali nzuri kisaikolojia. Alimpokea kwa heshima zote za mwanamke anavyompokea mumewe. Shahidi wa yote vikiwa ni chumba na kitanda kile kipana kilichowalaki.
Tatu, baada ya miaka saba, sasa aliweza kula chakula kilichoandaliwa vizuri. Siyo yale maharage yaliyooza na ugali mbichi uliojaa wadudu. Hapana, siku hii alipata mlo safi, ulioandaliwa na Mama Safi; ugali moto wa sembe na kuku aliyekaangwa vizuri sanjari na mchicha, embe dodo lililoiva vizuri bila ya kukosa glasi ya maziwa ya mtindi baridi.
Nne, baada ya kusota kwa miaka saba, hatimaye amejikuta akipata wasaa wa kukaa na mwanaye kwa muda apendao, akiongea naye kwa uhuru, maongezi ayapendayo na kwa sauti yoyote.
Sababu hizo, pamoja na nyingine nyingi ndizo zilizomfanya awe na furaha isiyo kifani hata usiku ukaingia na kukomaa bila ya kukumbuka kuwa kesho yake alikuwa na makubaliano ya kukutana na yule mtu, pandikizi aliyempa msaada wa usafiri kutoka Keko.
UTARATIBU wa kukurupushwa kila alfajiri wakati akiwa gerezani Keko, ulimfanya Kamba, hata akiwa nyumbani kwake ajikute aking’aa macho tangu saa 10 alfajiri ya siku ya pili, usingizi ukiwa umetengana naye kwa maelfu ya kilomita.
Ingawa jana mchana aliutumia muda fulani kuvipa mazoezi viungo kupitia mwili wa mkewe, mama Safi, hata hivyo alipata usingizi wa kutosha mchana huohuo. Usiku ulipoingia alikula vizuri kama mchana, akanywa bia mbili za afya na kisha akalala tena, huo ukiwa ni usiku mzuri wa kwanza baada ya miaka saba, usiku ambao alifarijika kwa mazoezi mengine yaliyovichangamsha viungo vyake kwa kiwango cha juu.
Usingizi ulimvaa saa sita, lakini saa kumi alfajiri alishazinduka! Na alizinduka kwa mshtuko, hisia kuwa bado yuko Keko zikikitawala kichwa chake. Hata hivyo, hali hiyo haikudumu sana. Harufu nzuri ya manukato iliyotapakaa chumbani humo ni taswira ya kwanza iliyomzindua kifikra. Na ulaini wa godoro alilolilalia lilikuwa ni jambo lingine lililomtambulisha kuwa yuko ‘paradiso.’
Isitoshe, alipodiriki kutupa mkono kulia kwake na kuugusa mwili mwororo, mwili wenye joto liburudishalo na ngozi isisimuayo, kumbukumbu ikajitengeneza kichwani mwake. Ndiyo, alikumbuka kila kitu kilichojiri tangu alipozinduka usingizini jana kule gerezani Keko, hadi utawala wa gereza ulipomtamkia bayana kuwa yu huru.
Kilichofuata hadi alfajiri hii pia alikikumbuka. Ilikuwa ni kumbukumbu iliyomrejeshea ile furaha aliyodumu nayo kabla usingizi haujamtwaa. Na furaha hiyo ikamfanya akose subira. Taratibu, mikono ikaanza kutalii maungoni mwa mama Safi.
Mama Safi hakuwa usingizini, hii mikono yenye sugu kilikuwa ni kichocheo halisi cha kuyapandisha mashetani yake yaliyopaswa kutulizwa na mumewe kipenzi, Kamba Kiroboto! Hivyo, bila ya hiana, alimpokea maungoni kwa namna ya kipekee, akionesha ukarimu na nidhamu yote ya kike sanjari na utaalamu wa mapokezi ya kimahaba.
Ilikuwa ni alfajiri njema.
*****
“…na ukikuta hakuna tatizo lolote, piga simu kwa kutumia namba hii ili tupange jinsi ya kukutana. Sawa?”
Maneno hayo ambayo Kamba aliambiwa na yule mfadhili aliyemleta hapo nyumbani kutoka gerezani, yalimrudia kichwani asubuhi hii. Na yakawa yakijirudia kila baada ya dakika chache.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipokwishaoga na kuinywa chai, akatupa macho ukutani kulikokuwa na saa. Akaguna. Ilikuwa ni saa moja na dakika arobaini. Akamtazama Mama Safi na kusema, “Nitatoka baada ya muda mfupi.”
“Kwani vipi tena?” mama Safi alimuuliza huku akimtazama kwa macho makali. Hakusubiri jibu, akaongeza, “Unakwenda wapi asubuhi yote hii?”
Kamba alimtazama kidogo tu mkewe na kuyaepusha macho yake. Alitambua fika kuwa mkewe hakupenda kumwona anaondoka mapema hivyo. Miaka saba ni mingi, alijisemea moyoni. Hata hivyo, hakuwa na jinsi. Bila ya kumtazama alisema, “Nitakaporudi ndipo nitakwambia nilikuwa wapi na ni kipi kilichonipeleka huko ninakokwenda.”
‘Baba Safi, mbona sikuelewi?”
“Us’jali, utanielewa vizuri nitakaporudi,” Kamba alijibu huku akinyoosha mkono na kuitwaa saa ya mkononi ya mama Safi iliyokuwa mezani. “Naazima saa yako kidogo inisaidie kucheki muda,” aliongeza.
*****
Tangu Tanzania ilipopata uhuru mwaka 1961, simu ilikuwa ni bidhaa ya kipekee na wakati mwingine ikichukuliwa kuwa ni kifaa kinachostahili kukaa kwenye ofisi za serikali, kwa viongozi wa ngazi za juu serikalini na kwenye mashirika makubwa ya umma au binafsi. Na kwa zile za mkononi, huwa ni kwa maofisa usalama, makamanda wa jeshi na askari wengine maalum wenye kazi maalum.
Hali hiyo ilidumu hadi mwanzoni mwa miaka ya tisini na ikaanza kutokomea taratibu kutokana na kushamiri kwa mfumo wa sayansi na teknolojia duniani na hivyo simu za mkononi kuanza kumiminika mikononi mwa watu.
Nchini Tanzania, kuna wakati kulikuwa na vibanda vilivyojihusisha na uuzaji wa vocha na kupigisha simu. Hatimaye biashara ya kupigisha simu ikaanza kupotea kwa kile kilichoaminika kuwa ni bei za simu kushuka kwa kiwango kikubwa. Watu wakawa wanahoji, ya nini kuendekeza kwenda kupiga simu kwenye vibanda badala ya kutoa pesa kidogo na kununua simu yako? Nunua simu yako kwa bei ndogo kisha utanunua vocha nazo kwa bei ya chini karibu na bure!
Hata hivyo, pamoja na hali hiyo kushamiri, Kamba hakuwa na simu. Alitoka gerezani na kukuta takriban kila aliyepishana naye ana simu, tangu watoto hadi watu wazima! Ni hao aliokutana nao, siyo mkewe. Mama Safi hakuwa hata na simu ya bei ya chini zaidi. Makali ya maisha yalimwathiri Mama Safi.
Hata hivyo, hali hiyo haikumwathiri Kamba wakati alipoondoka nyumbani asubuhi hiyo. Alitembea hatua chache tu na kufika kwa muuzavocha ambaye alimpatia noti ya shilingi 500 na kumwambia, “Tafadhali msh’kaji, kama una simu niazime nimshtue jamaa yangu.”
Muuzavocha hakuwa na hiana. Akasema, “Simu ipo. Na hii pesa?”
“Weka vocha. Sina maongezi mengi ni chini ya dakika moja.”
Kijana yule akaingiza vocha na kumtaka Kamba amtajie namba za huyo anayetaka kuzungumza naye. Kamba akachomoa kijikaratasi mfukoni mwa shati lake na kuzisoma namba husika. Kijana yule ‘akacheza’ na simu kwa muda mfupi kisha akaiweka sikioni. “Inaita,” hatimaye alisema huku akimpatia Kamba.
Kamba alipoiweka simu sikioni tu akasikia sauti kutoka upande wa pili:
“Haloo nani naongea naye?”
Ilikuwa ni sauti iliyoonesha majivuno na kujidai kwa kiasi fulani. Lakini masikioni mwa Kamba ilikuwa ni sauti ambayo asingeweza kuisahau. Alijizuia kucheka, badala yake akajibu, “Yule uliyempa namba zako jana.”
“Aaah, ok, ni mista Kamba?”
“Nd’o maana’ake.”
Ukimya ukatawala kwa sekunde kadhaa. Kisha upande wa pili ukasema, “Umeniangusha Kamba!”
“Nimekuangusha?!” Kamba alihoji kwa mshangao, sauti yake ikiwa ya juu kidogo tofauti na awali.
“Nilitarajia ungenipigia simu jana ileile!”
Kamba alicheka, lakini hakikuwa kicheko cha furaha bali kicheko cha hasira. Hakumwelewa huyu mtu kwa kumwambia kuwa amemwangusha. Walipoagana jana mtu huyo hakuwa amesisitiza kupigiwa simu jana hiyohiyo. Walikubaliana kuwa pale Kamba atakapokuta nyumbani kwake hali ni shwari, basi ampigie simu ili wapange siku na mahali pa kukutana kwa mazungumzo zaidi. Sasa kwa nini aseme kuwa amemwangusha? Eti alitarajia kupigiwa simu jana ileile!
Sasa hasira zikawa zikipanda kila sekunde ya dakika. Na akajikuta akibwata, “Kumbuka, haikuwa sheria kuwa nikupigie simu jana ile! Huu ndio muda wangu mwafaka. Umenielewa? Isitoshe, ni wewe ndiye uliyetaka tuonane, siyo mimi! Kama uliona kuwa jana ilikuwa ni muhimu zaidi ungesema!”
“Ok, usipaniki msh’kaji,” upande wa pili ulisihi. “Yaliyopita si ndwele. Nadhani umenipigia kwa ajili ya kupanga namna ya kukutana.”
“Nd’o maana’ake.”
“Poa. Unaonaje kama tutakutana Uhuru Peak?”
Uhuru Peak ni baa iliyo jirani na ukumbi mkongwe wa Vijana, Barabara ya Mwinjuma, Kinondoni. Inatazama na ukumbi mwingine maarufu wa Mango Garden. Kamba hakuwa anapajua hapo Uhuru Peak kwa kuwa wakati baa hiyo inafunguliwa yeye alikuwa bado kifungoni.
“Nd’o wapi?”
Ukimya ukapita kidogo kisha: “Inatazamana na Mango Garden. Unaweza kufika?”
“Siwezi kupotea. Niambie muda.”
“Tufanye baada ya nusu saa. Au?”
“Poa.”
“Ok, unaweza kutangulia na kuanza kupata bia mbili, tatu wakati unanisubiri. Au u’shaacha kunywa?”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kamba alicheka na kusema, “Kwa mtu mwingine kukaa miaka saba bila ya kupenyeza walao tone la bia kinywani ingekuwa ni tiketi tosha ya kumfanya asirudie tena kunywa maishani. Ni mtu mwingine, siyo Kamba Kiroboto. Hivi ulivyotaja bia tu, koo limenikauka ghafla!”
Kicheko kikali kikatoka upande wa pili. Kisha: “Ok, unywe kwa gharama yangu. Ukifika ulizia binti anayeitwa Jennifer. Ni binti mstaarabu na mcheshi. Nitampigia simu sasa hivi nimtaarifu kuwa kuna mgeni wangu. Atakutafutia sehemu poa ya kupozi ili nikifika tuzungumze bila ya kubughudhiwa na mtu. Sitachelewa zaidi ya nusu saa kutoka sasa. Kwani uko pande zipi mida hii?”
“Mkwajuni.”
“Ok, baadaye basi.”
“Poa.”
*****.
Kamba hakuhitaji kupanda daladala ili afike hapo Uhuru Peak. Alitembea taratibu hadi kituo cha Studio kisha akaifuata Barabara ya Mwinjuma hadi akajikuta Vijana Social Hall. Pale alikwenda kwenye kijiduka kidogo na kumuuliza muuzaji wapi ilipo hiyo Uhuru Peak.
“Vuka barabara halafu uende mbele kidogo utaiona,” aliambiwa.
Dakika mbili baadaye alijikuta mbele ya Uhuru Peak. Ni eneo ambalo lilikuwa na miti mingi kwa nje hivyo wateja waliweza kukaa chini ya miti hiyo na wengine walikaa ndani. Televisheni zilitapakaa ndani na nje na hivyo kuwa ni kivutio tosha kwa wapenzi wa vitu hivyo.
Kamba alipofika alikuta viti vichache chini ya miti na watu wasiozidi kumi. Mandhari hiyo ilimvutia, akachagua meza iliyokuwa mbali na hao wateja wengine, akavuta kiti na kuketi. Muda mfupi baadaye mhudumu wa kiume alikuwa mbele yake.
“KARIBU, mjomba.”
Asante. Naweza kumwona Jennifer?”
“Yupo.”
“Kaniitie.”
Mhudumu huyo aliondoka na baada ya dakika mbili, tatu mhudumu mwingine huyu akiwa ni wa kike alikuwa mbele yake. Alikuwa ni binti mwenye mvuto mkali. Sare yake ya heshima ilimkaa vyema maungoni huku tabasamu lililochanua usoni pake likimwongezea mvuto.
“Shikamoo,” alisalimiwa.
Hakuitika. Hakuiona ile shikamoo kama ilimstahili. Kwani ameanza kuzeeka? Au hii miaka saba iliyomsotesha Keko ndiyo iliyomzeesha? Hakukubali, na alipanga kuwa pindi atakaporejea nyumbani ajitazame vizuri kwenye kioo sanjari na kujilinganisha na picha alizopiga kabla hajahukumiwa kifungo. Hapo ndipo atakapotambua kama 'maharage ni mbegu au mboga.'
“Shikamoo,” mhudumu alirudia.
“Asante,” Kamba aliendelea kuikwepa ile ‘shikamoo.’ “Wewe nd’o Jennifer?”
“Ndiye mimi.”
“Ok, kuna mtu kaniambia nikuone na unihudumie vinywaji hadi atakapokuja mwenyewe. Una taarifa?”
Mhudumu yule alikunja uso kidogo kisha akamuuliza, “We’ nd’o Kamba?”
“Hujakosea.”
Mhudumu alimtazama toka juu hadi chini na kushusha pumzi ndefu. Kisha, kwa upole huku akiendelea kumtazama Kamba alisema, “Kanipigia simu muda si mrefu, kaniagiza kuwa nikuhudumie hadi atakapofika.”
Tabasamu la mbali likachanua usoni pa Kamba kisha akauliza, “Inawezekana?”
“Hakuna noma, kaka. Jitu ni wetu kabisa, usiwe na hofu.”
“Poa. Leta nondo, Safari baridi,” Kamba alimdaka.
Muda mfupi baadaye mafunda kadhaa ya bia aliyoagiza yalikuwa yamepenya kooni na kushuka tumboni mwake. Lakini hakuwa amekuja hapo kulewa, alikuja kwa miadi maalumu japo aliruhusiwa kunywa tani yake.
Alipoianza bia aliyoletewa, mara akaitupia macho saa ya mkononi aliyopewa na Mama Safi asubuhi. Na kila baada ya muda mfupi akawa akiitazama, akizingatia ile nusu saa aliyokubaliana na yule mtu ambaye alihitaji sana kumfahamu kwa undani.
Bia ya kwanza ikakatika. Akaletewa ya pili, ambayo kabla hata haijafika nusu, mara akamwona mtu, pandikizi, mweusi akimjia kwa mwendo wa kikakamavu japo si kama wa askari. Akili ya Kamba ilikuwa ikiona labda zaidi ya macho yalivyoona. Kumbukumbu kuhusu mtu huyu haikupotea. Ni yule aliyempa lifti jana kutoka gerezani, Keko.
Kwa yeyote apendaye kuchunguza ubora au thamani ya mavazi yaliyovaliwa na mtu mwingine, asingehitaji kuchukua hata sekunde tano kutambua kuwa huyu mtu kavaa vya kuvalika mbele ya watu.
Utakapodiriki kusema kuwa mtu huyu kavaa nguo zenye thamani ya shilingi 10,000 hata mwendawazimu atakucheka. Ukigusia kwenye 50,000 wajanja na walio makini watakudharau, washamba na wajinga-wajinga wengine wakiafikiana nawe, ilhali mwendawazimu hatakuwa mbali sana na fikra za wajinga-wajinga na washamba wa jijini.
Ni pale tu utakapothubutu kudai kuwa mavazi ya mtu huyu yanagota kwenye thamani ya shilingi 200,000 au zaidi ndipo hata tajiri mdogo atakapokiri kuwa una akili ya utambuzi sanjari na upeo mkubwa wa kupambanua mambo.
Kamba alimtazama kwa makini mtu huyu na kujiona kuwa hakustahili kuketi naye meza moja. Kwa haraka alipojilinganisha na mtu huyu alijiona yu duni. Yeye hakuwa na uso uliomeremeta, uso wa mtu aliyeridhika na maisha! Isitoshe, haya mavazi yaliyouhifadhi mwili wake hayakuwa ya kuvutia hata chembe. Ni vipi basi ajisikie huru kuketi na mtu huyu?
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alifadhaika, lakini hakuwa na la kufanya. Kilichomleta hapo ni kukutana na mtu huyu, hivyo kwa hali yoyote ile awe nadhifu au dhalili alipaswa kuketi naye, meza moja, wazungumze.
**********
“SIDHANI kama nimechelewa sana,” lilikuwa ni tamko la awali la mtu huyo wakati alipoifikia meza hiyo huku akinukia manukato ya bei ghali.
Kamba alikohoa kidogo na kujibu, “Aaa… hujachelewa.”
“Ni kawaida yangu,” mtu huyo alisema huku akivuta kiti na kuketi. Naye akaletewa bia.
Dakika chache baadaye, baada ya kunywa mafunda kadhaa ya nguvu, akaegemea kiti kivivuvivu na kushusha pumzi ndefu. Akamtazama Kamba kwa macho makali kisha: “Nimekuomba tuonane kwa kuwa nina suala moja muhimu. Kwanza, nakupa pole kwa mara ya pili japo jana tulionana.”
“Nashukuru,” Kamba alisema. “Gerezani na uraiani ni sayari mbili tofauti! Kwa kweli sasa najisikia ahueni kwa kiasi fulani.”
“La pili, naomba uniambie kama unanifahamu au una lolote unalojua kuhusu mimi.”
Kamba alimtazama mtu huyo na kukunja uso. Alimwona mwenyeji wake huyo akiwa na uso wa kujidai, akionyesha bayana kuwa yuko katika daraja la juu la maisha. Ilikuwa ni taswira iliyomkera Kamba lakini kwa wakati huo hakuwa na jinsi, aliamua kuwa makini aijue hatima ya kukutana kwao.
Hakutaka mtu huyu amshtukie kuwa labda kuna hali isiyompendeza katika kikao hicho. Kwa ujumla hakutaka mtu huyo amshuku kwa lolote. Kwa upole akasema, “Ukweli ni kwamba niko gizani. Sina chochote wala lolote ninalolijua kuhusu wewe.”
“Ok, poa,” mtu huyo alisema kwa sauti yake ya maringo. Akakuna kidevu huku akiwatazama watu wengine waliokuwa katika eneo hilo na kisha akayatazama magari yaliyopita kwa kasi katika Barabara ya Mwinjuma ambayo haikuwa mbali na eneo hilo.
Kisha akatoa pakiti ya sigara ndani ya mfuko wa shati, akachomoa sigara moja na kuiwasha. Akavuta mikupuo kadhaa kwa maringo huku akitazama juu kama anayeangalia kitu fulani kilichoiteka akili yake.
Alikuwa akiwaza kama angepaswa kutaja jina lake halisi, au asilitaje na badala yake alitafute haraka jina bandia la kujitambulisha kwa Kamba. Jina bandia? Hapana, nafsi ilimkatalia. Ndiyo, hakuiona mantiki ya kumdanganya Kamba kwa kumtajia jina bandia. Aliamini kuwa tangu astaafu shughuli za ‘roho mkononi’ zilizomwingizia mamilioni ya pesa, sasa ilishatimu miaka saba.
Miaka saba bila ya kutuhumiwa kwa kosa lolote, kwake ilikuwa ni rekodi ya mtu mwema. Aliamini kuwa sasa jamii nzima hata vyombo vya dola vinamchukulia kuwa ni raia mwema, asiye na mawaa. Ni rekodi hiyo iliyomfanya asisite kutaja jina lake halisi.
“Naitwa Jitu,” alijitambulisha kwa sauti ya chini na nzito akimtazama Kamba sawia.
“Jitu?” Kamba alionyesha kutomwamini.
“Ndiyo, Jitu.”
“Ni jina halisi au la kish’kaji?”
“Naamini ni jina halisi kwa kuwa tangu nikiwa mtoto nilikuwa nikiitwa hivyo na wazazi wangu na hadi wanafariki sikuwahi kuwauliza kama ni jina langu halisi au la utani.”
Ukimya wa sekunde kadhaa ulitawala huku wote wakipeleka vinywani vinywaji vyao. Glasi ziliporudishwa mezani ni Jitu aliyeuvunja ukimya huo.
“Nilihitaji kukutana na wewe ili tuzungumzie sababu na kiini cha wewe kuingia Keko.”
Kamba alishtuka, akamtazama Jitu kwa makini, moyoni akihisi kuna jambo muhimu na zito alilopaswa kulijua.
“Unaukumbuka vizuri mwanzo wa masaibu yaliyokupata?”
“Yeah, naukumbuka vizuri,” Kamba alijibu huku akimtazama Jitu kwa macho makali.
**********
ILIVYOTOKEA ni kwamba, usiku wa Jumamosi moja, Kamba akiwa ndani ya ukumbi wa baa ya African Stereo, Kinondoni, alikokuwa akihudhuria sherehe ya harusi ya rafiki yake, ghafla aliwaona watu wanne, wanaume, wawili wakiwa katika sare za Jeshi la Polisi na wawili wakiwa katika mavazi ya kawaida wakiingia ukumbini humo.
Mmoja wa watu hao alinong’ona na msimamizi wa sherehe hiyo kisha wenzake wakajitoma katikati ya watu waliohudhuria, wakimtazama huyu na yule kwa makini. Hatimaye waliifikia meza aliyokuwapo Kamba na mkewe, Mama Safi.
“Samahani, anko, tunakuhitaji kidogo,” mmoja wa watu hao alimwinamia Kamba na kumwambia kwa upole.
“Mimi?!” Kamba alimuuliza mtu huyo huku akiwatazama wote kwa zamu.
“Yeah, wewe. Tunakuhitaji kidogo hapo nje.”
“Sasa hivi?” Kamba aliuliza tena.
“Ndiyo, sasa hivi.”
“Kuna tatizo gani?” Kamba aliendelea kumuuliza, na safari hii kengele ya hatari ilianza kulia kichwani mwake.
KUPATA wageni wa ajabu kwa muda huu, wageni ambao baadhi yao wamevaa kiaskari na wote wakakujia na kukuzunguka huku ukiwa na familia yako, kwenye sherehe, ilikuwa ni dalili mbaya. Kuna tatizo gani?
Hata hivyo, rekodi ya maisha yake ilimsuta. Akajenga hisia kuwa kutakuwa na tuhuma mbaya inayomkabili. Ni tuhuma gani? Swali hilo nalo likakosa jibu. Akamtazama kwa makini askari huyu aliyemwinamia.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Macho yao yalipokutana, askari huyo akasema, “Nadhani haitakuwa busara kuzungumzia humu ukumbini. Tuwapishe kidogo wenzetu waendelee na ratiba, sisi twende nje tukazungumze. Ni suala dogo tu, halitatuchukua hata dakika kumi.”
Ujanja wa askari!
Kamba hakuwa mbumbumbu kwa kauli za askari, hususan askari wa Tanzania. Alikumbuka kuwa Mwingereza fulani aliwahi kuandika makala katika jarida moja na katika makala hayo kulikuwa na sehemu iliyosema, askari wa Tanzania ni wastaarabu sana. Ukiwa na tuhuma yenye uzito mkubwa au mdogo, askari atakufuata kistaarabu na kuzungumza na wewe kirafiki kiasi kwamba hata kama kuna watu wengi si rahisi kwa watu hao kujua ni kipi kinachoendelea. Kisha atakutaka muondoke, mwende kituo cha Polisi. Njiani, mtatembea kirafiki zaidi. Mnaweza kupita mgahawani mkanywa chai kwa gharama zake. Ukiwa na hamu ya kuvuta sigara, atakununulia. Ilimradi mtakwenda kirafiki na kuzungumza kirafiki, zaidi ya urafiki wa kawaida, kiasi cha kukupa matumaini kuwa dakika chache baada ya kukaa huko kituoni, utaruhusiwa kurudi nyumbani au ofisini au popote pale alipokutoa.
Ni hadi pale mtakapofika kituoni ndipo utakapoiona sura yake ikibadilika sanjari na sauti na kauli zake. Ndiyo, ni hapo ndipo utakapotambua kuwa umefika kituo cha Polisi. Atakuamuru kuvua viatu, mkanda na amri nyingine zikifuatia, akitumia sauti kali na amri kali vilevile.
Hata hivyo, pamoja na hayo, bado atabaki kuwa ni askari mstaarabu, aliyelinda hadhi yako mitaani, badala ya kukuchukua kimsobemsobe kiasi cha kila jicho kukumbwa na mshangao na kufuatilia ni kipi kilichokusibu.
Ni falsafa hiyo ambayo hata Kamba alitambua kuwa ndiyo itakayotumika muda huu. Hata hivyo, yeye atakuwa amefanya kosa au uhalifu gani katika miaka hii ya karibuni? Mbona alishastaafu kujihusisha na mambo ya kishenzi? Hata hivyo, akaamua kutii akitambua fika kuwa kitendo cha kukaidi amri hiyo ya kistaarabu kitazaa hatua nyingine na hapo ndipo askari hao watakapotoa makucha nje. Watageuka mbogo na kumwadhiri mbele ya kadamnasi iliyomzunguka.
Ndiyo, aliamua kutii, mengineyo baadaye.
Akashusha pumzi ndefu na kumtazama mkewe, kisha akayarejesha macho kwa yule askari. Safari hii akakutana na kitambulisho kikimtazama! Kamba akakitazama kidogo kitambulisho hicho kisha akanyanyuka taratibu. Akasogeza kiti nyuma taratibu vilevile na kutoka. Alipovuta hatua mbili, tatu hivi, akageuka na kumtazama tena mkewe kwa macho ambayo ni kama vile yalisema, nitarudi sasa hivi.
Hakurudi!
**********
SIKU hiyohiyo ya Jumamosi, saa 6.30 mchana, maduka mengi ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam yalikuwa wazi. Duka la Mwasia, Ladhu H. Ladhu lililoko Mtaa wa Mosque lilikuwa miongoni. Hilo lilikuwa ni kati ya maduka maarufu kwa mauzo ya bidhaa za jumla. Wafanyabiashara wenye maduka ya rejareja katika maeneo ya Kinondoni, Temeke, Buguruni, Ubungo, Manzese na kwingineko walimiminika kwa wingi dukani hapo kwa minajili ya kujipatia bidhaa mbalimbali.
Wakati pilikapilika zikiendelea dukani, Jitu aliegesha gari kando ya barabara, hatua chache kutoka dukani hapo. Akaangaza macho huku na kule kwa chati kisha akakodolea dukani na kutikisa kichwa, tabasamu la mbali likichanua usoni pake.
Uchache wa wateja dukani humo ilikuwa ni taswira njema sana kwake. Aliamini kuwa baada ya dakika chache wateja hao watakuwa wameondoka, na hapo ndipo atakapopata nafasi ya kutekeleza lolote lile alilolidhamiria. Alitulia garini akisubiri idadi ya wateja hao izidi kupungua na wakati huohuo, akautumia muda huo kujitazama yu katika mwonekano gani kwa mavazi aliyotinga mwilini.
Kwa yeyote ambaye angemwona wakati huo, asingekuwa na shaka naye hususan yule mtu mwenye macho ya kawaida na akili ya kawaida. Hakutofautiana na mbunge au waziri yeyote mwenye kupenda kufanya mazoezi ya viungo ilhali akijali utanashati katika kuilinda hadhi yake na hadhi ya mamlaka aliyonayo. Suti yake ya gharama ya kutisha, iliyomkaa vyema mwilini sanjari na viatu vilivyong’ara miguuni, zilikuwa ni taswira halisi kuwa yu mtu aliyekwishaufukuza umaskini.
Hili gari alilomiliki, gari maridadi la rangi ya nyeusi aina ya Toyota Carina, lenye nambari za usajili ambazo hakukuwa na mtu aliyebaini kuwa zilibadilishwa siku hadi siku, pia lilimfanya aheshimike na kutukuzwa katika jamii. Kwa jumla alionekana kuwa ni miongoni mwa wale ambao Tanzania inawanyenyekea, Afrika inawasujudia na dunia inawachekea.
Aliitupia jicho saa iliyokuwa kwenye gari hilo na kushtuka. Akaguna. Ilitimu saa 6:40. Alijua kuwa maduka mengi hususan yale yanayomilikiwa na Waasia, kwa siku ya Jumamosi hufungwa kati ya saa 6:30 na saa 7:00. Na ni kawaida kwa milango ya maduka kufungwa pindi zisaliapo dakika chache, ili kumalizia huduma kwa wateja watakaokuwa ndani.
Katika kuepuka kosa lolote ambalo huenda akalijutia baadaye, alitoka garini humo na kuelekea dukani huku mkono wa kulia ukiwa umezama ndani ya mfuko wa suruali, tayari kwa utekelezaji wa hatua nyingine endapo itamlazimu.
**********
HUENDA siri ya mafanikio ya wafanyabiashara wengi ni ule utaratibu wa kumjali, kumheshimu na kumthamini mteja. Na yawezekana kuwa utaratibu huo ndiyo uliozaa ule usemi wa mteja ni mfalme.
Mzee wa Kiasia, mwenye umri wa miaka sitini na mitano, Ladhu H. Ladhu aliufuata utaratibu na usemi huo pindi tu alipomwona mteja mtanashati akiingia dukani mwake. Huo ulikuwa ni muda ambao mzee huyo alitaka kumwamuru mfanyakazi wake afunge mlango ili awahudumie wateja waliosalia.
Mara tu mteja huyo alipoingia, Ladhu aliita kwa sauti: “Hamisiiiii, Hamisiii funga lango!”
Ilikuwa ni amri. Muda mfupi baadaye mlinzi aliyekuwa nje alifunga mlango na kuwaacha wateja wanne waliokuwa ndani wakihudumiwa.
Mzee Ladhu H. Ladhu aliharakisha kuwahudumia wateja wengine kisha akamgeukia huyu mteja mtanashati. Akakenua meno na kuachia tabasamu ambalo liliiharibu sura yake iliyosheheni mikunjo ya uzee. “Karibu…karibu ndugu yangu,” alisema kwa Kiswahili kilichonyooka huku lile tabasamu lake lililotisha likiendelea kuchanua usoni.
Walitazamana kidogo huku huyu mteja naye akionyesha sura iliyokunjuka na kutangaza urafiki, zaidi ya urafiki wa kawaida. Tabasamu maridhawa lilijitokeza katika uso wa huyu mteja na kuongeza ukaribu baina yao.
“Nikusaidie nini mheshimiwa?” Ladhu aliongeza.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kilichofuata hakikuwa matarajio ya Mzee Ladhu H. Ladhu! Fadhaa ikamkumba ghafla, lile tabasamu lake likayeyuka na sasa, sura iliyochukua nafasi ya lile tabasamu ilikuwa ni sura iliyotisha maradufu. Kama angepigwa picha dakika hiyohiyo, na picha hiyo ikayafikia macho ya mtoto mdogo, isingekuwa ajabu kusikia kuwa mtoto huyo aliweweseka usiku.
“Nipe pesa,…nataka pesa…!” sauti nzito, sauti ya chini ilimtoka yule mteja mtanashati huku bastola ikiwa mkono wa kulia tayari kwa matumizi. Bastola hiyo ilikuwa sentimeta chache kutoka kwenye paji la uso wa Ladhu ikimtazama.
Walitazamana, mzee Ladhu akayaona macho ya huyu mteja yakiwa tofauti na yale ya muda mfupi uliopita. Haya yalikuwa ni macho baridi, yaliyotangaza hatari zaidi ya hatari halisi. Mzee Ladhu angefanya nini? Mlango ulishafungwa na mlinzi alikuwa nje. Labda angepaswa kufumbua mdomo tu na kupiga yowe la kuomba msaada. Lakini je, kitendo hicho kingemsaidia au kumsalimisha?
Aliyajua matumizi ya chombo hiki cheusi, kilichokamatwa na kono hili la kikakamavu la huyu mteja mtanashati. Hakikuwa chombo cha kukifanyia masihara na hasa kwa wakati huu ambao kimeshikwa na mtu mwenye kila dalili za kuua! Isitoshe, hakukuwa na dalili ya masihara ndani ya mboni za macho ya huyu mteja.
Mzee Ladhu aligwaya! Kifo kilikuwa mbele yake! Afanye nini?
WAZO moja likamjia kichwani. Kwamba, pesa ni kitu kidogo cha kuja na kuondoka. Pesa zinatafutwa na zinapatikana, achilia mbali zimetafutwa wapi, kwa mfumo gani na wakati gani. Ni pesa ambazo zinatafutwa, siyo uhai wa mtu. Uhai wa mtu si kitu cha kawaida kinachoweza kutafutwa na kupatikana kwa njia ya kawaida. Uhai haununuliwi dukani! Uhai hauokotwi barabarani wala uhai hausakwi kwa kucheza bahati nasibu! Hivyo, katu thamani ya uhai haiwezi kulinganishwa na pesa. Pesa ni jambo moja na uhai ni jambo lingine!
Kwa kulitambua hilo, Ladhu aliamua kutii amri. “Nitakupa pesa… nitakupa pesa yote baba…” alisema kwa sauti yenye kitetemeshi kilichokuwa bayana.
“Kimya!” mteja alifoka kwa sauti ya chini huku akimtazama mzee Ladhu kwa macho makali zaidi. Kisha ikafuata amri nyingine: “Kusanya pesa zote haraka na uziweke ndani ya fuko hilo nyama wee!” alimwonesha fuko moja maarufu kwa jina la Rambo lililokuwa sakafuni kama uchafu. Akaongeza, “Hakikisha kuwa fuko hilo ni zima. Isidondoke hata noti moja!”
Amri hiyo nayo ikatekelezwa haraka!
Dakika chache baadaye mtu huyo alikuwa na fuko la Rambo lililofurika pesa. Hata hivyo hakuondoka, alitulia na kuangaza macho huku na kule dukani humo. Akaiona simu ya mkononi iliyokuwa mezani. Akaitwaa na kuitazama kidogo kisha akairusha sakafuni kwa nguvu!
Haikutamanika!
Macho yakaiona simu nyingine, hii ikiwa ni ya mezani. Nayo hakuiacha. Aliinyanyua na kuitupa sakafuni!
Ikasambaratika!
Bado hakuridhika! Alimfuata mzee huyo na kumpekua katika kuhakikisha kuwa hakuwa na silaha wala simu nyingine mfukoni inayoweza kumsaidia kwa kuomba msaada. Upekuzi wake ukamthibitishia kuwa mzee Ladhu hakuwa na chochote cha maana mifukoni mwake.
Hata hivyo, bado hakuridhika, huku akimwelekezea bastola, alimwonya akisema, “Unaiona hii? Piga kelele uone! Nitakisambaratisha hicho kichwa chako kibaki kama mtori wa moto! Ujue kuwa akili yangu haina akili! Ok, lala kifudifudi!”
Mzee Ladhu akafanya kama alivyoamriwa.
“Weka kichwa sakafuni na usithubutu kukinyanyua kenge wee!”
Ladhu akaendelea kutii.
Ni hapo ndipo mgeni huyo alipoondoka kwa kunyata. Akafungua mlango mkubwa na kutoka kwa kujiamini, akiwa ameshaubadili mwonekano wake usoni. Sasa uso wake wa upole ukawa na tabasamu lililomfanya aonekane kama mtu yeyote asiye na mawaa. Alipokutanisha macho na mlinzi, kama kawaida akaachia tabasamu changa kisha akampungia mkono wa kumuaga. Mlinzi naye akajibu kwa kumpungia mkono.
Hadi alipoingia ndani ya gari lake na kutokomea, hakuna yeyote pale nje aliyemshuku kwa lolote.
**********
HAIKUMWINGIA akilini Mzee Ladhu H. Ladhu kuwa tukio la muda mfupi uliopita lilikuwa ni moja ya michezo ya kuigiza.
Zilimchukua dakika mbili akiwa ameduwaa, kisha, ghafla alikurupuka hadi ndani ya chumba fulani ambako mwanaye mkubwa, Hassanali alikuwa akitazama televisheni.
Taarifa za wizi huo zilipoyafikia masikio ya Hassanali hatua za haraka zikachukuliwa. Hassanali akaitumia simu yake kuwataarifu Polisi. Robo saa baadaye askari polisi wanne walifika dukani hapo.
Mahojiano yakafanyika, mahojiano yaliyoambatana na uchunguzi wa hapa na pale kama kawaida ya askari pindi wafikapo eneo la tukio.
Hata hivyo, pamoja na maswali yao, pamoja na uchunguzi wao, bado hawakupata mwanga halisi wa ufumbuzi wa tatizo hilo. Wakaamua kuandamana na Mzee Ladhu na mwanaye, Hassanali hadi kituo cha Polisi kwa hatua zaidi.
Huko kituoni Mzee Ladhu H. Ladhu alionyeshwa picha kadhaa za waliosadikiwa kuwa na historia ya ujambazi sugu. Baadhi yao walikuwa rumande wakisubiri hukumu za kesi zao, baadhi walikuwa wakitumikia vifungo, baadhi ilisadikiwa kuwa walishakufa, na wengine, iliaminika kuwa walishamaliza vifungo, wako uraiani kama raia wengine.
Macho ya Ladhu H. Ladhu yalizipitia picha kumi na nane kwa makini akishirikiana na mwanaye ingawa huyo mwanaye hakuwa na msaada mkubwa kwa suala hilo kwa kuwa hakuwahi kumwona yule mteja.
Hatimaye alizitenga picha tatu pembeni. Kisha likaanza zoezi la kuzitazama hizo tatu kwa makini zaidi. Dakika kama moja hivi baadaye, picha moja kati ya hizo tatu ikatemwa. Zikabaki mbili.
Kutambua kwa usahihi kuwa picha hizo ni za watu wawili tofauti, ulihitajika utaalamu wa hali ya juu.
Picha moja ilikuwa ni ya mtu mrefu mwenye mwili mkakamavu na nywele fupi kichwani. Alikuwa na sharubu huku akitabasamu. Alivaa fulana iliyombana, suruali ya jeans na raba miguuni. Picha ya rangi.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Picha ya pili ilikuwa vigumu kuitofautisha na ile ya kwanza. Tofauti pekee ilikuwa ni mavazi. Huyu mtu wa pili alikuwa kavaa shati lililombana. Chini alitinga jeans na raba na isitoshe sharubu na nywele fupi vilikuwa ni vitu vilivyoshabihiana kwa asilimia mia moja na picha ile ya kwanza huku pia huyu mtu akitabasamu ingawa tabasamu lake lilionekana kwa mbali. Hii pia ilikuwa ya rangi.
Hali hiyo ilimfanya Ladhu H. Ladhu ajikute katika wakati mgumu wa kuwatambulisha hawa askari kuwa ni nani kati ya hao aliyehusika na uporaji kule dukani. Akahema kwa nguvu na kuitoa miwani usoni labda kwa kuhisi kuwa itakuwa inachangia katika kumpa utambuzi sahihi wa mbaya wake kulingana na picha hizo mbili.
Akatwaa kitambaa na kujifuta machoni kisha akazishika tena picha hizo. Akaguna! Bado aliona maluweluwe! Moyoni akajiuliza, mbona ni mtu mmoja? Lakini hapana, akajikana papohapo. Sasa akaigeuza picha moja nyuma na kukuta kuna jina: JITU KOBELO. Akaiweka pembeni na kutwaa picha nyingine. Hiyo alipoigeuza akakuta jina: KAMBA KIROBOTO.
Ni watu wawili!
Akilini mwa mzee huyu hiki kilikuwa ni kitendawili kigumu kuteguliwa. Akamtazama askari aliyesimamia zoezi hilo na kumwambia, “Kijana naomba nikavute sigara kidogo.”
Askari yule alitabasamu kidogo na kumuuliza, “Vipi mzee, kuna utata kidogo mpaka unaona ushtue akili?”
“Yeah,” mzee Ladhu alijibu kwa sauti nzito na ya unyonge zaidi. “Ni utata ambao si mdogo. Nadhani ninahitaji kupata akili.”
Askari walimruhusu kutoka nje ambako alifuatana na mwanaye, akawasha sigara na kuvuta mikupuo kadhaa kwa nguvu kisha akaitupa chini na kuisagasaga. Akamgeukia mwanaye na kusema,
“Zile picha zina utata mwanangu.”
“Kwa vipi baba?”
“Hazina tofauti. Mwenyewe si umeona? Ni kama vile ni za mtu mmoja na ni kama pia ni za watu wawili tofauti. Yaani zimenichanganya kwa kiasi kikubwa!”
“Nimeona. Lakini nadhani ukitulia unaweza kumtambua mbaya wetu.”
Mzee Ladhu alitabasamu kidogo na kumgusa bega mwanaye, kisha akasema, “Turudi nikitegue kitendawili hiki. Sasa akili imetulia.”
Waliporudi ndani mzee Ladhu alizishika tena picha hizo na kuzitazama kwa muda bila ya kupepesa. Askari watatu waliokuwa hapo nao walikuwa kimya wakiisubiri kauli yake. Hata mwanaye alitulia akisubiri kitendawili kiteguliwe. Wote walimkodolea macho wakimsubiri.
Uso wake uliosheheni mikunjo ya uzee ulizidi kutisha wakati akiwa katika zoezi hili ambalo kwa namna nyingine kwake ilikuwa ndiyo fainali.
Punde akaachia kinywa wazi, akitabasamu. Hili lilikuwa ni tabasamu lililotisha zaidi kwa kuwa lilifurika uchungu na hasira maradufu. Lilikuwa ni tabasamu lililofuatiwa na kauli fupi kutoka kinywani mwake: “Ni huyu!”
Kidole chake cha shahada, cha mkono wa kulia kilitua kwenye picha mojawapo. Macho na akili za wengine waliokuwa wakimsubiri zikahamia kwenye picha hiyo. Hata walipomuuliza maswali haya na yale wakimbana kwa hoja hii na ile, bado alisimamia kwenye uchaguzi wake.
“Ni huyuhuyu!” alisisitiza. “Nina hakika ni huyuhuyu! Mungu kanionyesha! Ni mwenyewe! Sina sababu ya kumsingizia!”
**********
PICHA iliyotajwa na mzee Ladhu H. Ladhu ilikuwa ni ya mmoja kati ya raia wenye historia ya ujambazi sugu. Lakini huyu alikuwa kishamaliza kifungo miaka mitano iliyopita. Na siku alipotengana na gereza aliweka nadhiri ya kutorejea katika mfumo huo wa maisha, mfumo uliomlazimu hata kuua mtu huku akiishi kwa kuwahofia na kuwachukia askari polisi.
MTU huyo ni Kamba Kiroboto. Ndiyo, katika kipindi ambacho aliishi kwa kupata pesa kwa mabavu, Kamba alijiwekea malengo ya maendeleo. Na katika kuhakikisha kuwa malengo hayo yanafanikiwa, hakuwa tayari kujihusisha na matukio ya kumwingizia pato hafifu. Matukio yake yalikuwa ni yale tu yaliyomwingizia mamilioni ya pesa. Alikuwa makini katika kufanya kazi zake. Na kwa malengo hayo, akafungua akaunti benki ambako alihifadhi pesa si haba.
Akiba hiyo iliyojilimbikiza benki hatimaye ilikuja kumfaidisha mara alipotoka. Akaunti yake ikasheheni mamilioni ya pesa aliyoyatumia kwa kununua nyumba na kufungua biashara ya maduka mawili Kinondoni Moscow. Kisha akajitwalia mwanadada aliyeitwa Febronia. Wakaishi kama mke na mume. Miaka miwili baadaye familia yao iliongezeka; Febronia alijifungua mtoto mzuri wa kike. Wakampatia jina la Safi.
Sasa alitulia, na aliamini kuwa anaweza kuishi kwa amani na utulivu hadi kufa kwake bila ya kutegemea kupata pesa kwa kumshikia mtu bastola.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ni mabadiliko hayo ya maisha ndiyo yaliyomfanya asisite kuiuza bastola yake kwa jambazi mwingine kwa bei ya kutupa; shilingi laki mbili tu!
Ndiyo, aliiuza, tena ni baada ya kufikiri kwa dakika mbili tu, kwamba hana hati halali ya kumiliki silaha hiyo iliyowahi kuisimamisha mioyo ya watu wasiopungua kumi na watano. Itakuwaje itakapobainika kwa wahusika serikalini kuwa anamiliki silaha hiyo kinyume cha sheria?
Ni kipi kitakachofuata kama siyo kutiwa mbaroni na kufunguliwa mashtaka? Na ili ajiokoe na janga hilo, atapaswa kutumia mbinu ipi kama siyo kujikamua mifuko kwa minajili ya kuwafunga vinywa, kuwaziba masikio na kuwafumba macho waendesha mashtaka na mahakimu?
Kwa kuwa alishaamua kuwa nusu mlokole, hakuiona sababu ya kuendelea kumiliki vitu hatari. Hivyo, hiyo bastola iliyomwingizia mamilioni ya pesa, aliiuza. Kile kisu kilichowahi kuzama vifuani na matumboni mwa watu wasiopungua watano, alikitumbukiza chooni.
Sasa hakuwa yule Kamba, jambazi hatari. Huyu alikuwa Kamba mwingine, Kamba ambaye aliheshimika mitaani kwa kuonekana kuwa yu mtu mpole, mstaarabu mwenye mke na mtoto. Baba wa familia.
Rekodi ilimlinda. Wakati alipokuwa akiwazungukia wale wenye pesa na kuzichukua kama zake baada au kabla ya kuzing’oa roho zao, hakuwa akiishi hapo Kinondoni Moscow. Makazi yake yalikuwa Mwananyamala B. Ni watu wa Mwananyamala, tena wachache sana waliojua kuwa ana mfumo gani wa maisha. Wengine hawakuijua siri ya maisha yake. Huku Kinondoni Moscow hakukuwa na mtu aliyemjua kwa kina. Hivyo alionekana kuwa ni mtu wa kawaida, anayeishi maisha ya kawaida, lakini akiwa katika daraja zuri, tofauti na wakazi wengi wa Kinondoni Moscow.
Alikuwa ameanza kuwa muumini mzuri wa kanisa. Kila Jumapili alikwenda kanisani kuhudhuria ibada yeye, mkewe, na mtoto wao. Kwa jumla, macho yake, ongea yake na tembea yake vilimweka katika kundi la watu wenye maadili mema.
Hata hivyo, hayo yote hayakuzibadili kumbukumbu za ndani ya majalada yaliyohifadhiwa ndani ya vituo vya Polisi, kumbukumbu zilizoonyesha kuwa Kamba Kiroboto ni jambazi sugu, ambaye miaka kadhaa iliyopita alituhumiwa kumpora mtalii, raia wa Uholanzi dola 10,000 za Marekani na pauni 20,000 za Uingereza katika mazingira ya kutatanisha. Tuhuma hizo za kumpora fedha hazikuweza kuthibitishwa na upande wa mashtaka lakini alipatwa na hatia ya kumwagia pombe kali usoni mtalii huyo katika klabu ya usiku.
Alikamatwa na kuhukumiwa jela miaka mitatu. Kwa mujibu wa kumbukumbu hizo za polisi, kifungo hicho kilishamalizika.
Hakukuwa na kumbukumbu zozote zilizoonyesha kuwa Kamba alituhumiwa kutenda uhalifu wowote mwingine tangu alipotoka jela, lakini hicho hakikuwa kigezo cha kuwajengea imani askari polisi kuwa baada ya kifungo Kamba alibadili mfumo wa maisha yake. Eti aliokoka!
Ilishajengeka imani miongoni mwa jamii za mataifa mbalimbali kuwa jambazi hastaafu wala hana likizo. Likizo yake ni pale tu anapokumbwa na kifungo. Jambazi hawezi kustaafu kazi labda akatwe mikono na miguu na ikibidi hata kung’olewa au kupofushwa macho.
Kwa imani hiyo, na kwa msisitizo wa kauli ya Mzee Ladhu H. Ladhu, askari polisi walichukua uamuzi wa kumsaka Kamba Kiroboto. Saa moja baada ya kuzungumza na Mzee Ladhu, askari wanne, wawili wakiwa wamevaa sare za Jeshi la Polisi na wawili wakiwa katika mavazi ya kiraia walifika nyumbani kwa Kamba.
Hawakumkuta, lakini hawakukata tamaa. Wakazunguka tena hapo nyumbani kwake saa mbili usiku na kupata taarifa kuwa Kamba na mkewe walikuwa African Stereo Bar kwenye sherehe ya harusi.
Ilikuwa ni taarifa iliyowarahisishia kazi askari hao. Wakapiga mguu hadi huko African Stereo Bar ambako walimkuta mlengwa.
**********
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
HISTORIA ilimponza Kamba Kiroboto. Rekodi chafu zilizomhusu, zilizofurika katika majalada ya vituo vya Polisi zilimfanya aumalizie usiku huo akiwa ndani ya chumba cha mahabusu. Siku mbili baadaye alisimama kizimbani akituhumiwa kuvamia duka la Mwasia Ladhu H. Ladhu Mtaa wa Mosque katikati ya Jiji la Dar es Salaam, na kwamba alipora fedha taslimu shilingi milioni 70 na kuharibu simu mbili, moja ya mkononi na nyingine ya mezani.
Ilikuwa ni kesi ngumu kwa upande wake. Japo alijitetea kwa kadri ya uwezo wake, bado uzito ulimwelemea. Hakuweza kupambana na ushahidi wa mlinzi wa duka la Ladhu H. Ladhu aliyeiambia mahakama kuwa Kamba aliingia dukani akiwa ni mtu wa mwisho na alipotoka alikuwa na mfuko uliokuwa umejaa pesa. Ushahidi wa uongo!
Hakuuhimili uzito wa Wahindi wawili waliobuni maneno kuwa walimwona akitoka dukani akikimbia huku akiwa na fuko kubwa la plastiki; uongo mwingine! Na kati ya mashahidi wote hakuna aliyedai kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa na gari. Hata mwanaye Ladhu H. Ladhu, Hassanali naye alidiriki kutoa ushahidi, akidai kuwa Kamba alimtishia bastola na kumtaka aondoke eneo la tukio.
Naam, uzito wa tani nyingi za tuhuma ulimwelemea Kamba. Angeweza kutumia wakili lakini gharama zilimshinda. Hakuwa na pesa ambazo wakili mmoja alimtajia. Hakuwa na uwezo wa kulipa hata nusu ya kiwango kilichotakiwa. Akaachana na fikra za kutumia wakili japo aliamini kuwa wakili angeweza kumsaidia sana katika sakata hilo.
Kwa muda wa miezi mitatu kesi hiyo ikaunguruma mara kadhaa katika Mahakama ya Kisutu. Na kwa kipindi chote hicho hakupewa dhamana kwa kile kilichodaiwa na mwendesha mashtaka, James Ntilampa kuwa dhamana inaweza kuvuruga mwenendo mzima wa kesi hiyo.
Madai hayo ya mwendesha mashtaka yalikubaliwa na Hakimu John Mwakipesile na kwa hali hiyo Kamba akajikuta akiwa katika kipindi kigumu zaidi, akilazimika kuishi katika maisha aliyokwishayaepuka na wakati huohuo akiona kuwa Mungu kamtupa. Kwa nini atuhumiwe na hata kukosa dhamana kwa kosa ambalo hakulifanya?
Moyo ulimuuma kwa kiasi kikubwa, lakini afanye nini? Hakuwa na budi kurudi rumande kusota. Na akiwa huko aliona kuwa picha ilizidi kuwa mbaya kwa upande wake. Kila alipopelekwa mahakamani kwa mfululizo wa kesi yake, aliona mambo yakizidi kumwendea kombo. Dalili ya kunusurika na kifungo ilikuwa ikiyoyoma.
Awali alishuhudia maji hayajafika magotini, lakini hatimaye yalifika. Hayakukomea hapo, yakavuka, yakatua kiunoni. Siku moja alipokuwa akirudishwa rumande aliyaona maji hayo yamegota kifuani! Ile siku ambayo Hakimu John Mwakipesile aliitaja tarehe ya hukumu, Kamba aliyashuhudia maji yakikichezeachezea kidevu chake!
Hatimaye hukumu ilitolewa, hukumu iliyomtupa Keko gerezani miaka saba!
**********
“HUKUSTAHILI kuhukumiwa!” Jitu alimzindua Kamba aliyekuwa katopea mawazoni. “Ulionewa, na ungetumia wakili ungeshinda!”
Kamba alivuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha. Akamtazama Jitu kwa makini kisha kwa sauti ya chini akasema, “Nadhani sijakuelewa vizuri.”
“Nasema msh'kaji hukustahili kuingia Keko!” Jitu alisema kwa kusisitiza lakini safari hii akiishusha zaidi sauti yake na akawa makini kuhakikisha kuwa maneno hayo hayayafikii masikio yasiyohusika. Akaendelea, “Ile ilikuwa ni mvua yangu. Yaani basi tu, msala ulikuangukia msh’kaji wangu.”
Kufikia hapo Jitu aliitwaa tena glasi na kunywa mafunda mazito ya bia. Alipohakikisha glasi imefilisika, alimwita mhudumu kwa ajili ya kuongeza bia nyingine. Wakati wakimsubiri akawasha sigara nyingine na kuvuta taratibu. Akamtazama Kamba huku akitabasamu. Akamwona Kamba akiwa yupo kama hayupo, akionesha dhahiri kutoamini akisikiacho.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“WEWE?” hatimaye Kamba alizinduka na kutupa swali hilo.
“Ndiyo, mimi.”
“Kwa nini?”
“Ni hadithi ndefu,” Jitu alisema huku tabasamu likizidi kuchanua usoni pake.
“Huwezi ukanisimulia hiyo hadithi yenyewe?”
“Barida. Nitaku-brief.”
**********
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment