Simulizi : Pigo La Mwisho
Sehemu Ya Pili (2)
ILIKUWA ni hadithi ya kusisimua masikioni na akilini mwa Kamba. Na ilikuwa ni simulizi iliyompeleka Kamba katika sayari nyingine. Hakujisikia kuwa yu binadamu kama binadamu wengine mara baada ya kuisikia simulizi hiyo, la. Sasa alijiona kuwa ni mtu-nusu na mnyama-nusu. Aliyachukia maisha na alijichukia mwenyewe.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa ni hadithi iliyounyofoa ule moyo wa binadamu uliomfanya aiuze bastola yake kwa bei ya kutupa na kukitumbukiza kisu chake cha kazi chooni. Nafasi ya moyo huo ikachukuliwa na kitu kingine kisichoelezeka kwa urahisi, zaidi ni moyo wa kiumbe mwenye ukatili usiokadirika.
Kwa sekunde kadhaa baada ya kusimuliwa hadithi hiyo, Kamba alikuwa akimtumbulia macho Jitu bila ya kutamka chochote. Hatimaye alishusha pumzi ndefu na kunong’ona, “Mungu mkubwa!” Kisha ghafla akaongeza sauti na kuuliza, “Ina maaana msh’kaji uliondoka na milioni sabini?”
“Zilikuwa ni milioni sabini na nane nilipozihesabu,” Jitu alimsahihisha. “Siku walipokusomea shtaka walitaja milioni sabini na uharibifu wa simu mbili. Lakini zilikuwa ni milioni sabini na nane na simu mbili. Walichosahau ni kuunganisha na ule mfuko wa rambo ambao nao ulitoka kwao. Mzee Ladhu ndiye aliyenipa nibebee pesa zangu.” Kufikia hapo akacheka kwa sauti ya dhihaka akiamini mkuwa ule mfuko wa Rambo usingeweza kujumuishwa katika vitu vyenye thamani vilivyoibwa.
Mara akasita kuongea baada ya kumwona mhudumu mbele yao akiwa na chupa nyingine za bia.
Walipobaki peke yao, Kamba alisema kwa mshangao lakini kwa sauti ya chini, “Milioni sabini na nane! Dah! Ulikuwa ni mkwanja wa nguvu dadeek!”
“Yeah, kwa wakati ule zilikuwa ni pesa nyingi kidogo,” Jitu alikiri kwa upole huku akiipeleka kinywani glasi ya bia.
“Siyo kwa wakati ule tu,” Kamba alisema. “Hata sasa. Hata leo, mwanangu! Kwani mipesa ya kibongo imeshuka sana? Wapi, basi tu ni ufisadi umetawala vichwani mwa viongozi wa serikali hii na wingi wa vikao vya mabunge mengii mara sijui Bunge la Bajeti, mara Bunge la Katiba, sijui Bunge la nini…Bunge la nanihinooo… basi tu wanapiga pesa, mwana.”
Ukimya wa sekunde chache ulitawala kisha, Kamba akasema, “ Kuna jambo moja linalonishangaza kufuatia maelezo yako.”
“Jambo gani?”
“Ubinadamu.”
“Ubinadamu?!”
“Ndiyo. Kwani hujanielewa?”
Jitu alikunja uso kidogo akionyesha kufikiri kisha kwa upole akasema, “Kwa kweli sijakuelewa.”
“Inawezekana kweli hujanielewa,” Kamba alisema huku akiachia tabasamu la mbali ambalo halikuwa hata na chembe ya furaha. Bado huyu alikuwa ni Kamba ambaye alikuwa hajairejesha ile sura yake ya uchangamfu, sura aliyokuwa nayo kabla hajakumbwa na mkasa uliomtupa gerezani.
Nyuma ya tabasamu hili kulifichika dhamira ya kufanya chochote kwa mtu yeyote na kwa wakati wowote bila ya kujali kama hicho atakachokifanya kinaweza kuigharimu roho yake. Lilikuwa ni tabasamu lililotisha badala ya kupendeza. Lakini ni watu wachache sana ambao wangeweza kuibaini hali hiyo, mmojawao akiwa ni huyu Jitu, ambaye ana uzoefu wa kuyasoma macho ya mtu kwa wakati wowote kuwa mtu huyu ana furaha, huzuni, hasira au vyovyote vile.
Jitu alitambua kuwa Kamba hakuwa na amani moyoni mwake lakini alilazimika kuwa makini akijaribu kwenda naye taratibu ili wafikie tamati ya mkutano wao.
Kamba aliinyanyua glasi na kuipeleka kinywani ambako aligugumia funda zito la bia kisha akairejesha mezani. Akasema, “Ninaposema kuhusu ubinadamu, nina maana kuwa, katika kipindi nilichokuwa nasota na kesi hukunijali…”
Jitu alitaka kumkata kauli lakini Kamba alikwishatambua hali hiyo na hivyo akamnyooshea mkono huku akisema, “Tulia. Usiwe na haraka. Taratibu. Subiri nimalize.”
Jitu akapoa.
“Ulicheza dili lako kwa umakini na ukafanikiwa,” Kamba aliendelea. “Mambo yako yakawa supa, mshkaji. Milioni sabini na nane kibindoni kwa siku moja na kwa dakika chache tu! S’o mchezo! Dili lako lilitiki. Lakini pamoja na hali yako nzuri, hukunisaidia kunikwamua kwenye lindi la matope! Uliniacha nisote na kesi peke yangu huku mamilioni ukiwa nayo wewe na kisha nikatupwa jela ukishuhudia! Unataka nikueleweje?”
Ukimya ukapita kwa muda mfupi. Kila mmojawao akaipeleka glasi ya kinywaji kinywani. Kisha Jitu akauliza, “Vipi, umemaliza?”
“Yeah, unaweza kuongea.”
Jitu alijiweka sawa kitini kisha, kwa sauti yenye kijimkwaruzo cha mbali, macho yake makali yakimtazama Kamba sawia, akasema, “Ilikuwapo sababu. Ilikuwa ni vigumu sana kuwasiliana na wewe ana kwa ana kwa kuwa ulinyimwa dhamana.”
Kamba aliachia kicheko hafifu. “Nilinyimwa dhamana,” akayasema maneno hayo kwa sauti ya chini zaidi huku akiitazama glasi ya bia yake mezani. Akatikisa kichwa na kuongeza, “Ni kweli nilinyimwa dhamana. Lakini haikuwekwa karantini ya kuja kuniona rumande, Jitu!”
Jitu alitikisa kichwa akiashiria kukubaliana na maneno ya Kamba. Kisha akasema, “Ni kweli hakukuwa na kizuizi chochote cha kukuona rumande. Lakini hapo inapaswa ujue jambo moja.”
Wakatulia kwa muda wakitazamana. Kamba akaonekana kuwa na shauku ya kukisikia hicho anachotaka kukisema Jitu. Haraka akadaka, “Endelea.”
“Ni kuhusu sura zetu,” Jitu alisema kwa kujiamini.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sura zetu! Sura zetu zikoje?!” Kamba alishangaa.
Uso wa Jitu ulikunjuka, tabasamu likachanua zaidi. Kisha akasema, “Kamba, mimi na wewe ni pacha. Ni vigumu sana kuzitofautisha sura zetu na maumbile yetu. Nilipoiona picha yako gazetini siku mbili baada ya wewe kukamatwa, nilijaribu kuilinganisha na picha zangu kadhaa nilizonazo kwenye albamu yangu. Na nilikuwa na maana ya kufanya vile.
“Ile siku niliyomfanyizia yule gabachori sikuwa na miwani yangu ya giza. Nilikuwa uso mkavu na nikatazamana jicho kwa jicho na babu yule wa Kihindi, mwanangu. Isitoshe, hata mlinzi wake aliniona vizuri wakati nilipoingia na nilipotoka. Kwa dakika takriban tano au kumi nilizokuwa mle dukani zilitosha kabisa kuwafanya wanishike sura vizuri. Mpaka hapo tuko pamoja?”
“Nakusoma. Endelea.”
“Ok, kwa kawaida tukio la aina ile liyafikiapo masikio ya ‘wazee’ haliwezi kuchukuliwa kama tukio lililofanywa na vibaka. Kwa hiyo walichokifanya wao ni kuchunguza rekodi na picha za watu wa kazi baba’ake!
“Nina hakika kuwa picha yangu iko Polisi. Hawawezi kukosa kuwa nayo kwa sababu mimi bado ni mbaya wao. Siaminiki! Sasa ni hapo ndipo ninapojiwa na shaka kuhusu hatua waliyochukua askari, ya kukukamata wewe. Ina maana askari walikuwa na uhakika kuwa ni wewe uliyecheza dili lile. Na ina maana hata picha yako wanayo. Inaniingia akilini kuwa huenda zoezi la utambulisho wa picha ndilo lililokuponza. Huenda walimtumia yule babu wa Kihindi na mimacho yake ya kizee, na akakutaja wewe. Watu wa kazi tuko wengi hapa Dar na hata huko mikoani. Unadhani ni kwa nini wakuchague wewe kama siyo kumrundikia yule babu wa Kihindi mipicha kibao iliyomchanganya?”
Akainyanyua chupa ya bia na kumimina kinywaji ndani ya glasi. Kwa mara nyingine akanywa mafunda mawili mazito na kutua glasi mezani. Kisha tena akawasha sigara na kuvuta mikupuo kadhaa huku akipuliza moshi hewani.
Kamba alimtazama bila ya kutamka chochote. Alihitaji kuijua hatima ya simulizi hii. Alichofanya ni kunywa tu bia yake taratibu, ilhali hakuonekana kuwa na hamu na kinywaji hicho.
Hatimaye Jitu aliendelea, “Ni kutokana na uchaguzi wa picha yako nd’o maana nilijaribu kuilinganisha picha yako na yangu. Picha yako ya gazetini ilikutoa mzima-mzima, mwanangu, toka utosini hadi nyayoni! Nilipoilinganisha na picha zangu mbili, tofauti ilikuwa ndogo sana, na tofauti hiyo ni mimi na wewe tu tunaoweza kuigundua. Zaidi yetu, labda awe ni askari mtaalamu sana wa mambo ya picha.
“Kwa hali hiyo, nilihofia kujitokeza sana kwako kwa kuhofia kuharibu mambo. Kungeweza kutokea mabadiliko ya ghafla, nikaswekwa ndani na labda hata wewe bado ukaendelea kusota ndani vilevile. Hapo tungekuwa tumejiingiza choo cha kike kichaa wangu. Milioni sabini na nane zingechina bila ya kutusaidia hata chembe.”
Kamba akaibuka: “Kwa hiyo ukaamua kuniacha mie nisotee mvua saba, wewe ukila bata, si nd’o maana’ake msh’kaji wangu?”
“HILO nd’o kosa ninalokiri kulifanya,” Jitu alisema huku akiachia tabasamu la mbali lililodumu kwa sekunde chache na kulikata. “Kwa hili nakuomba radhi, na ndiyo maana nilihitaji tuonane. Sikudhamiria kukutupa. Ni vijimambo tu. Muhimu ilikuwa ni kuliepuka janga ambalo lingetukuta.”
“Wewe ulifanikiwa kuliepuka janga, lakini hiyo haikunisaidia mimi kwa namna yoyote ile!” sauti ya Kamba ilionyesha jazba kwa mbali.
“Ndiyo, haikukusaidia kitu,” Jitu alisema kwa upole huku akiupeleka mkono kwenye mmoja wa mifuko iliyotapakaa katika suruali yake ya bei. Akaendelea, “Japo haikukusaidia, lakini nilishapanga kukupoza kwa sehemu ndogo tu ya pato lile. Nilipanga hivyo katika kuonyesha kuwa niliguswa na mkasa uliokukuta.”
Baada ya kusema hivyo, alichomoa fungu la noti kutoka katika mfuko wa suruali uliokuwa usawa wa magoti. Lilikuwa ni fungu lililofungwa kwa ile mipira maalumu na zilionekana ni noti mpya za shilingi elfu tano, tano za Tanzania. Akaziweka mezani na kusema, “Ziko milioni tano. Nategemea zitakusogezea siku kabla ya kuyazoea haya maisha ya uswazi kwetu.”
Kamba hakuamini! Milioni tano kimchezo-mchezo kiasi hiki! Aliduwaa akiziangalia pesa hizo bila ya kuzigusa, japo kuduwaa huko hakukuwa bayana machoni mwa Jitu. Kisha, kama aliyezinduliwa usingizini, Kamba alizivuta pesa hizo na kuziweka jirani yake.
Hakuzihesabu na aliona huo haukuwa muda mwafaka wa kuzichambua kutoka kwenye mipira ile na kuanza kuzihesabu.
Hatimaye kwa sauti ya upole alisema, “Sasa nimeamini kuwa umenijali. Sidhani kama kuna mtu wa kazi mwenye moyo wa kiutu kama wewe. Nakuona kama wewe ni ndugu yangu wa kuzaliwa, mshkaji wangu.”
Jitu aliachia tabasamu changa, la kifahari. Akaitwaa glasi na kuipeleka kinywani. Mafunda mawili ya bia yalipopenya kooni, aliirudisha glasi mezani. Akageuka kushoto na kulia, akawatazama wahudumu na wateja wengine waliokuwa wakizunguka hapa na pale. Akaridhika kwa hali iliyokuwa ikiendelea, ikionyesha kuwa watu wengine walikuwa na mambo yao. Hakukuwa na yeyote aliyewajali.
Akamrudia Kamba na kumwambia, “ Usijali, ni mambo madogo tu hayo.” Kisha kama aliyekuwa amesahau jambo akamuuliza, “Mara ya mwisho ulicheza dili gani?”
“Ilikuwa ishu ya kawaida tu, mwanangu,” Kamba alijibu kwa kujiamini.
“Nilifuma mkwanja wa nguvu baba’ake.”
“Lilikuwa dili gani?” Jitu alisisitiza swali lake.
“Nilimvaa mtasha mmoja nikachukua vijisenti vyake kidogo, ikawa noma. Wazee wakaniandama, wakanidaka. Wakanitupa ndani. Lakini baba’ake nikacheza na askari mmoja wa upande wa mashtaka, shtaka la kupora likauawa na badala yake likabaki la kumwogesha whisky mtasha huyo. Ubalozi wa Uholanzi ukalivalia njuga baba’ake na kutishia kuvunja uhusiano na Tanzania eti kwa sababu ya kudhalilishwa kwa raia wake na kuporwa pesa. Pakachimbika mwanangu! Ngoma ikawa nzito!”
“Ulichapwa mvua ngapi?”
“Mvua tatu, mwanangu! Na nilipotoka nikaamua kuachana na kazi hii. Nikafungua biashara ya maduka mawili ya bidhaa za kawaida. Ni haya maduka yetu ya kiuswazi-uswazi. Biashara ikakubali baba’ake. Nakwambia kama siyo hii skendo yako, leo ningekuwa mbali kichaa wangu.”
“Kwani ulipokuwa Keko biashara yako haikuwa na mwangalizi?”
“Waifu wangu alikuwepo. Lakini yeye hana ujuzi wala uzoefu wa biashara yoyote ile. Biashara ilikufa, maduka yalifilisika kishenzi! Kwa mtaji huu ulionipa nd’o natarajia kujaribu tena.”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jitu alikunja uso na kuuliza, “Mtu akikuletea kazi huwezi kufanya?”
“Hii kazi yetu?’
“Ndiyo!”
“Ningeweza kufanya au kushiriki,” Kamba alijibu kwa utulivu huku akiipeleka glasi yake kinywani na kunywa mafunda mawili mazito ya bia yake. Akaendelea, “ Yeah, ningeweza kufanya, lakini ningefanya kwa ajili ya kutafuta pesa ya kuanzishia tu maisha. Wewe umenipa milioni tano! Ya nini kurudi tena nyuma? Kwani wewe tangu ulipozikwaa zile milioni sabini u’shafanya tena matukio?”
Jitu alitikisa kichwa akionyesha ishara ya kukataa, kisha akasema, “Sijafanya chochote hadi leo. N’na daladala zangu tatu, teksi nne, saluni tatu za masaji na nyumba zangu tatu, moja ya kuishi na mbili za kupangisha, na hizo za kupangisha zimechukuliwa na kampuni kubwa ya Wazungu, mkataba wa miaka mitano na zimeshalipiwa kwa dola kudadadeki! Maisha yanakwenda! Ila tu, siwezi kudai kuwa nimestaafu. Hapana, kwa hilo nitakuwa najidanganya. Kama utaniambia kuwa mahala fulani kuna mzigo, kitu kama milioni mia tano au sita, saba hivi, siziachi. Naingia kazini. Chuma ninacho, siwezi kuacha asili, mwanangu.”
Kamba alicheka kwa chinichini na kuuliza, “Jambazi hastaafu?”
“Hastaafu na wala hana likizo.”
“Hapana, hapo umechemka.”
“Kwa vipi?”
“Jambazi ana likizo na anastaafu,” Kamba alisema kwa msisitizo. “Likizo yake ni pale anapobebeshwa miaka, jela, tena miaka michache ya kuweza kumfanya arejee kazini pindi atakapotoka. Kustaafu ni pale atakapokatwa mikono au kupofushwa macho. Umenisoma?”
“Barida.”
Ukimya mfupi ukapita huku wakinywa bia zao, na kuangaza macho kwa watu wengine waliopitapita mbele yao. Ni Kamba aliyeuvunja ukimya huo aliposema, “Jitu, pamoja na hii pole uliyonipa, bado najiona kama nina kitu f’lani moyoni.”
“Kitu gani?” Jitu alimkazia macho.
Kamba hakuwa mwepesi wa kujibu. Akavuta pumzi na kuzishusha. Kwa mara nyingine akayatupa macho kwa watu waliokuwa ukumbini humo kama vile anayechunguza jambo fulani. Alipoyarudisha kwa Jitu, kwa sauti ya chini zaidi alisema, “Unyama niliotendewa na yeyote aliyenifanya niingie jela, unanifanya nikose amani moyoni. Sijisikii kukaa tu nikifurahia au kuridhika kwa pole hii uliyonipa. Hapana. Nadhani napaswa kupiga hatua nyingine muhimu zaidi ili roho isuuzike.”
“Sijakuelewa,” Jitu alisema huku akionekana kuwa makini zaidi baada ya kuyasikia maneno hayo ya Kamba.
“Yeah, inawezekana hujanielewa, lakini us’jali. Ipo siku utanielewa. Cha muhimu kwa sasa ni kunisaidia jambo lingine moja tu!”
“Nini tena?!”
Kamba alikohoa kidogo na kusema, “ Siamini kuwa yule Mhindi alikuwa na uhakika kuwa ni mimi niliyemfanyizia. Najisikia kuamini kuwa moyoni mwake alitambua fika kuwa alikuwa akibahatisha.”
“Hata mimi naamini hivyo,” Jitu alisema.
“Kingine ni kuhusu yule hakimu.”
“Mwakipesile?”
Kamba aliitika kwa kutikisa kichwa.
“Na yeye amekuwaje?”
“Akili yangu inaniaminisha kuwa alitumia zaidi historia ya maisha yangu katika kunikandamiza,” Kamba alijibu kwa uchungu, akimtazama Jitu sawia. Akaendelea, “Na ingawa sina ushahidi, lakini naamini kulikuwa na mazingira ya rushwa katika mzunguko mzima wa kesi ile. Hakimu huyo, na labda hata mwendesha mashtaka, wanaweza kuwa walivuta mshiko wa nguvu kutoka kwa wale Wahindi.”
Yalikuwa ni maneno yaliyomshtua na kumchanganya Jitu. Akavuta pumzi na kuvuta sigara kwa nguvu kisha akapuliza moshi mwingi hewani bila ya kumtazama Kamba. Wakati huo Kamba yeye alikunywa bia iliyosalia kwenye glasi, kisha akamimina iliyobaki kwenye chupa na glasi ilipojaa, kwa mara nyingine akanywa, safari hii akibugia.
Hatimaye Jitu alimrudia Kamba. Akamtazama na kugundua kuwa hana amani moyoni na usoni. Alionyesha bayana kutokuwa timamu. Akamuuliza, “Unaongeza?”
“Tosha,” Kamba alijibu huku akisisitiza kwa kutikisa kichwa na kupunga mkono wa kulia. “Tumekuja kuzungumza, hatukuja kulewa. Ipo siku tutakayokaa kwa utulivu, tukinywa na kustarehe.”
“Ok, kwa hiyo unataka kuniambiaje?” Jitu alimtega.
“Kwanza nahitaji kuonana ana kwa ana na yule Mhindi. Yupo?”
“Yupo. Kabadilika ukimlinganisha na miaka ile. Kazeeka kiasi.”
“Kuzeeka si hoja. Muhimu ni kuwa bado yu hai.”
“Na kwa nini unataka kumwona?” Jitu alimbana.
“N’takwambia,” Kamba alijibu kwa upole. “Usiwe na haraka. Pia nahitaji kuonana na mwanae, Hassanali.”
“Hata yeye yupo, kajaa tele. Tena nasikia sasa hivi yeye nd’o kashika miradi yote ya baba’ake.”
Kamba hakuyajali maelezo mengine kuhusu Hassanali. Akaendelea, “Nahitaji kuonana na hakimu John Mwakipesile na yule mwendesha mashtaka. Una taarifa zozote zinazowahusu?”
JITU alikunja uso akifikiri kisha akasema, “Kuhusu hakimu, kwa kweli sina taarifa yake yoyote ya siku za karibuni. Yule mwendesha mashtaka sasa hivi, kaula, mwanangu. Ni Mkuu wa Kituo cha Oysterbay.”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kamba alitabasamu kidogo na kufuatiwa na kicheko kilichoonyesha kutokuwa na furaha hata chembe. Kisha akasema, “Poa, nitaonana naye hukohuko Polisi na safari hii anitupe tena ndani.”
Wakacheka kwa pamoja. Kisha ghafla Jitu akamdaka, “Hivi una ishu gani ya kutaka kuonana nao?”
“Stori.”
“Stori?!” Jitu hakumwamini. Akazidi kumbana. “Unataka kusema wewe Kamba wa leo uliyetoka jela jana unataka kuwa na stori gani na watu hao? Ni stori za kawaida au magumashi tu unaniletea?”
“Ni stori za kawaida,” Kamba alisema huku akiyaepuka macho ya Jitu yaliyokuwa yamemganda kwa namna ya kutokiamini akisemacho.
“Hapana,” Jitu alisema akishusha zaidi sauti. “Kamba, nadhani huu si wakati wa kuendelea kufichana jambo lolote. Uwe wazi, unataka kufanya nini?”
Kamba alifikiri kidogo kisha akasema, “Sina nia mbaya kwa kutaka kuonana nao. Naomba uelewe hivyo. Ninataka wanione kuwa niko hai na ni mzima wa afya. Nitakachofanya ni kuwaambia kuwa, Mungu ameona waliyonitendea. Please naomba unielewe, najua unadhani nataka kulipa kisasi! No! Siwezi kufanya hivyo, hayo ni mambo ya kizamani. Dunia itanilipia tu.”
Kisha, akageuza uso huku na kule, na kumrudia Jitu. Kwa sauti ya chini zaidi lakini yenye msisitizo akaongeza, “Na kuna msaada mwingine nauhitaji kutoka kwako.”
“Upi tena?” Jitu alimuuliza huku akimtazama kwa jicho kali.
“Sina uhakika na usalama wangu. Na ninahitaji kufanya kazi kidogo ili niwe na pesa zaidi, msh’kaji wangu. Nataka niwe na usafiri wangu wa maana, heshima irudi. Kwa hiyo, kama una kifaa cha ziada please niazime.”
“Sijakusoma.”
“Chuma, msh’kaji wangu,” sauti ya Kamba ilikuwa ya chini zaidi.
“Manati?!” Jitu alishangaa.
“Nd’o maana’ake. Nataka nifanye walao tukio moja tu nipate mkwanja wa maana halafu labda nimrudie Mungu.”
Jitu aliguna huku akivuta mkupuo mmoja wa nguvu wa sigara kisha akakitupa chini kipande kilichosalia na kukisaga kwa kiatu. Akatulia akiupuliza moshi angani huku macho kayatuliza kwenye miti iliyokiunda kivuli kizito. Kisha akamtazama tena Kamba na kumuuliza, “Kwa kuazima au jumla?”
“Kuazima, hata kama ni kwa kukodi!”
Malipo, Jitu aliwaza. Ndiyo, angeweza kumuuzia bastola yake kwa malipo ya shilingi milioni moja, si chini ya hapo. Lakini alijenga imani kuwa Kamba asingeweza kuinunua. Kama kweli amemwambia kuwa ametoka jela na kukuta nyumbani kwake biashara zake zote zimesimama, je, ataweza kutoa milioni nzima kati ya hizi milioni tano alizompa sasa hivi ilhali hana pesa nyingine za ziada? Na kama hatamuuzia, akimwazima atarudisha? Chombo kama bastola hii, G 231- Peacemaker ya Kirusi ni cha kumwazima binadamu mwenzako ambaye kuua ni sehemu ya maisha yake?
Hapo likaja suala la uaminifu. Jitu aliamini kuwa mtu wa aina ya Kamba si wa kumwamini asilani. Vipi umwamini mtu ambaye historia ya maisha yake inatisha zaidi ya kifo? Mtu wa aina ya Kamba ni wa kumwamini hata kwa asilimia moja? Alijiuliza maswali hayo na kukumbana na jibu moja; hapana. Kamba si wa kumwamini. Kamba ni jambazi! Ni kipi kitamzuia asimgeuke na kumuua kama atahitaji chochote kutoka kwake?
Aliwaza mengi, lakini hatimaye alipiga moyo konde na kulikubali ombi la Kamba. Na alichukua uamuzi huo baada ya kukumbuka kuwa mahali fulani, maeneo ya Upanga atainunua bastola nyingine kwa mtu mmoja aliyefanya biashara hiyo kwa siri kubwa.
“Unaihitaji lini?” hatimaye alimuuliza.
“Ikiwezekana, hata leo.”
“Utanipa shilingi ngapi?”
“Unauza au kuniazima?”
“Vyovyote vile.”
“Ok, sema wewe.”
Jitu alicheka kidogo, kicheko cha kifahari, kicheko chenye kumweka kwenye daraja la wale wenye ukwasi. Akakikuna kidevu chake chenye sharafa changa, kisha, kwa sauti ya majivuno akasema, “Huna pesa Kamba. Najua huna kitu. Nitakupa bure lakini usije kunigeuka na kujaribu kunifanyizia. Kwa hilo usijidanganye mtu wangu. Nakuhakikishia, nitajua wakati bado unafikiria kutekeleza azma yako. Na hapo ndipo kichwa chako kitakapokuwa halali yangu. Nakuapia ivo.”
“Yamekuwa hayo tena?” Kamba alishangaa. “Mimi na wewe! Acha hizo msh’kaji.”
“Ok, poa, us’jali,” Jitu aliendelea kusema kwa maringo ya kipesapesa. “Nitakupa ila unatakiwa ufanye kazi ya kuzisaka gololi zake. Nitakupa ikiwa tupu. Kama uko tayari, sema.”
“Hilo s’o tatizo, Jitu. Muhimu ni kitu chenyewe. We vipi?”
Wakacheka tena.
“Gololi siyo tatizo. Kwa Bongo hii sina wasi. Nitazipata kwa ulainiiii!”
“Kwa hiyo tutawasiliana vipi?” Jitu alimuuliza.
“Sijui, labda wewe nd’o upange taimu na wapi pa kuonana.”
“Nitakuja kwako saa moja usiku. Utakuwepo?”
“Nitakuwepo. Unapafahamu?”
Jitu alicheka. “Nilipafahamu tangu kipindi ulipokuwa na kesi.”
**********
SIKU ya pili baada ya Kamba kukabidhiwa bastola na Jitu, alikivaa kitongoji cha Kariakoo. Moja kwa moja hadi Mtaa wa Amani ambako alionana na Pengokubwa, mmoja wa watu walioshi jijini Dar es Salaam kwa mbinu hii na ile, huyu akiwa ameamua kujishughulisha na mipango mikali na ya hatari. Miongoni mwa kazi hizo ni kuuza risasi kwa siri kubwa. Dakika chache baadaye Kamba aliondoka kwa Pengokubwa huku akiwa na risasi sita kibindoni.
Kwa kiasi fulani sasa alifarijika kwa hatua aliyofikia. Akarudi nyumbani huku akiwa na amani tele moyoni. Hata hivyo, hakumwambia chochote mkewe, Mama Safi kuhusu safari yake hiyo ya Kariakoo wala jana yake pia hakumwambia kitu kuhusu kile kikao baina yake na Jitu. Hata ile bastola na zile risasi hakumwonyesha Mama Safi!
Ilikuwa ni siri yake. Kwamba kuna siku atamwambia mkewe kuhusu sababu ya kuimiliki bastola hiyo, hilo lilikuwa ni jambo linguine, ambalo hakutarajia kulifanyia utekelezaji wa haraka.
Asubuhi ya siku iliyofuata, aliamua kuanza utekelezaji wa kile alichokidhamiria. Pesa anazo, ni kipi kitamshinda? Baada ya kunywa chai alitoka taratibu hadi katika kituo cha teksi ambako alikodi teksi iliyompeleka Kariakoo. Huko alinunua nguo za kumfanya aonekane mtu mbele ya watu. Shilingi laki tatu zilitosha katika kushughulikia mavazi ya thamani ambayo alitaka yamweke katika daraja la juu. Aonekane mwanamume mbele ya wanaume. Siku ikaisha.
Siku ya tatu, akiwa na nguvu ya kiuchumi mfukoni na bastola ndani ya himaya yake, alikodi teksi tena, safari hii akielekea maeneo ya ‘Uhindini’ Mtaa wa Mosque. Safari yake ilikomea kwenye duka maarufu la mauzo ya jumla na rejareja lililomilikiwa na Mwasia, Ladhu H. Ladhu. Akamkuta.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Miaka saba iliyopita, wakati kesi yake ikiunguruma mahakamani, mara kadhaa alimwona mzee huyu wa Kihindi, Ladhu H. Ladhu akitoa maelezo kuhusu tukio la uvamizi lililotokea dukani mwake. Yule Ladhu wa wakati ule hakuwa huyu Ladhu wa leo. Huyu alikuwa mzee maradufu. Wakati yule Ladhu wa miaka ile aliweza kusimama dukani na kuwahudumia wateja kwa zaidi ya saa tatu, huyu alikuwa akionyesha dhahiri kutoweza kusimama hata kwa nusu saa.
Ndiyo, huyu alikuwa Ladhu asiyeweza kuzimudu kashkash za wateja wanaopishana hapo dukani mmoja baada ya mwingine. Alikuwa ameketi kwenye kiti cha kivivu, akitafuna tambuu huku akishuhudia pilikapilika zilizokuwa zikiendelea. Lakini alichohitaji Kamba ni kumwona Ladhu akiwa hai, waonane na kuzungumza. Kwamba bado ni kijana au ni mzee hiyo haikuwa hoja ya msingi.
Ndani ya duka hilo kulifurika wateja ambao walihudumiwa na kijana aliyekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya thelathini na mitano na arobaini na mitano. Kamba alimtazama kijana huyo kwa dakika moja tu na kuachia tabasamu la siri. Alimkumbuka kijana huyo.
Ni Hassanali!
Kwa nini asimkumbuke ilhali ni Hassanali huyu aliyediriki kutoa ushahidi wa uongo mahakamani eti yeye, Kamba alimshikia bastola na kumwamuru kutoka dukani ile siku waliyodai kuvamiwa na kuporwa fedha? Asingeweza kumsahau. Akajisikia kutua mzigo mzito. Huku akiachia tabasamu la siri na lisilokuwa hata na chembe ya furaha, alitoka dukani humo taratibu.
Robo saa baadaye alikuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, moja kwa moja hadi kwa makarani ambako alizungumza na karani wa kike, Mwanaisha.
“N’NA shida ya kuonana na mheshimiwa Mwakipesile,” ndivyo alivyomwingia.
“Yuko likizo,” Mwanaisha alijibu. “ Kaanza likizo kiasi cha wiki mbili au tatu hivi zilizopita.”
Kamba alihisi kuishiwa nguvu. Kwa unyonge akahoji, “Anaweza kuwa amesafiri?”
“Hapana, kama alisafiri labda ilikuwa ni mwanzoni mwa likizo yake. Lakini majuzi tu nimemwona hapa ofisini. Nadhani alikuja kwa shida zake binafsi.”
“Likizo yake itaisha lini?”
Mwanaisha aliigeukia kalenda ukutani na kuitazama kwa muda kisha akasema, “Ni kama bado siku nne hivi. Jumatatu ijayo anapaswa kuwa kazini.”
Kamba alitikisa kichwa kidogo, akiashiria kukubali kisha akauliza, “Siwezi kuonana naye kabla ya siku hiyo?”
“Unaweza. Nenda nyumbani kwake.”
“Sipajui.”
“Ursino,” Mwanaisha alijibu haraka kama mtu aliyeonesha kuchoshwa na maswali ya Kamba. “Ursino, Regent Estate Mikocheni.”
“Ok, nashukuru,” Kamba alisema na kutoka.
Bado muda ulimruhusu. Hakwenda nyumbani, alikwenda mitaa mingine ya katikati ambako alipita duka hili na lile akisaka simu ya kumfaa. Hatimaye alijinunulia simu iliyomvutia na ya bei nafuu. Sasa akaridhika. Akaamua kurudi nyumbani ambako alipofika tu kitu cha kwanza kufanya ilikuwa ni kuchaji simu hiyo akifuata maelekezo kuwa alipaswa kuchaji kwa muda wa saa sita kabla ya kuanza kuitumia.
Usiku ulipoingia aliichukua ile bastola ya Jitu na kuanza kuikagua. Wakati akiendelea na zoezi hilo Mama Safi akatokea na kushtuka. “Baba Safi!” aliita kwa sauti ya chini iliyojaa woga. Akarudia, “We Baba Safi! We Baba Safii ni nini hicho?”
Kamba hakujibu, badala yake aliachia kicheko cha dhihaka, kicheko ambacho hakikufika mbali.
“Baba Safi!”
“Sidhani kama wewe ni mgeni kwa kitu hiki,” hatimaye Kamba aliipata sauti yake na kujibu kwa kujiamini. “Yaani miaka hii michache tu niliyokuwa huko ughaibuni ndiyo imekufanya ukione kifaa hiki kama kitu kipya sana machoni mwako?”
Mama Safi alijitupa sofani na kushusha pumzi ndefu. Kisha, kwa sauti ya chini akasema, “Nakumbuka ulishaiuza ile bastola yako. Ninachotaka kujua ni kwamba hii ni ya nani na unayo kwa madhumuni gani.”
“Hilo tu?” Kamba aliuliza bila ya kuyabandua macho kwenye kazi yake ya ukaguzi wa silaha hiyo.
“Ndiyo.”
Kamba alifikiri kidogo kama ingemstahili kumweleza kila kitu Mama Safi kuhusu silaha hiyo. Lakini akakumbuka kuwa mwanafalsafa mmoja wa Italia aliwahi kunukuliwa akisema mume hapaswi kumweleza mkewe kila kitu kuhusu maisha yake au hata mipango yake ya maisha. Na kama akimweleza inampasa kuchuja kipi cha kuweka bayana na kipi kibakie kuwa siri yake.
Hata hivyo, hakutaka kuyachukulia maneno ya mwanafalsafa huyo kama kanuni. Hapana. Alikuwa huru kuchukua uamuzi atakaoona kuwa unamfaa, hata kama utakuwa ni uamuzi mgumu. Hivyo, akapiga moyo konde na kuamua kumweleza mkewe dhamira ya kuwa na silaha hiyo.
Akahema kwa nguvu na kuiweka pembeni bastola ile. Kisha akamkazia macho mkewe na kumuuliza, “Unaweza kukumbuka vizuri siku niliyokamatwa kwa kesi ile iliyonipeleka Keko?”
“Ndiyo, nakumbuka,” Mama Safi alijibu.
“Ok, kama unakumbuka ni vizuri,” Kamba alisema kwa utulivu. “Na, nadhani unajua vizuri kuwa sikuhusika hata chembe na ishu ile, sio?”
“Najua.”
Kamba alikohoa kidogo kisha kwa sauti nzito na ya chini, akasema, “Basi kaa ukijua kuwa siwezi kuwa bwege wa kuliacha suala hili lipite hivihivi.”
Mama Safi aliguna na kumtazama Kamba kwa macho makali. “Baba Safi!”
“Unashtuka na kushangaa nini?” Kamba alisema bila ya kuonesha kuujali mshangao wa Mama Safi.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unataka kufanya nini?”
“Lazima nifanye kitu,” Kamba alisisitiza. “Miaka saba jela kwa kosa la kusingiziwa! Haiwezekani! Nakwambia Mama Safi haiwezekani! Lazima wanitambue!”
“Mungu wangu!”
“Ndiyo, lazima wanitambue!” Kamba aliirudia kauli hiyo japo sauti yake ilikuwa ya chini zaidi. Macho yake makali yalimtazama Mama Safi kwa namna zote za kuua. Alitisha!
Akaongeza, “Na ninakwambia Mama Safi, hii iwe siri yako. Ikivuja, ujue na wewe utavuja! Kwa hilo sina mzaha! Sijui kwa nini unapaniki. Huna hata huruma na mimi mumeo!
“Nimesota miaka yote hiyo jela huku washenzi wakitanua mitaani. Isitoshe, aliyefanya tukio lile ametajirika mara kumi zaidi kudadadadeki! Halafu mimi leo unanishangaa kwa hatua ninayotaka kuchukua!
“Sikia Mama Safi,” sasa alikuwa mpole na alimtazama Mama Safi kwa namna ya kusihi. “Inaniuma sana, hivyo usijali. Acha nifanye kile ninachotaka kufanya ili roho yangu isuuzike. Sawa?”
Mama Safi hakujibu, aliinamisha kichwa na kuonyesha kutingwa na huzuni.
“Ndiyo, niache tu Mama Safi!” Kamba alisema akikazia. “Na ikitokea siri hii ikavuja najua ni wewe nd’o utakuwa umenichoma. Hivi kweli unaweza kunisaliti katika kipindi hiki ilhali tumevumiliana kwa miaka yote hiyo?”
Bado Mama Safi alibaki kimya.
“Sasa kesho naianza operesheni yangu,” Kamba alisema kwa utulivu. “Niombee kwa Mungu nifanikiwe. Maisha yetu yameharibika kwa kufungwa jela nikituhumiwa kutenda kosa ambalo sikulifanya…”
Walilala tofauti na siku nyingine, usiku huu ukiwa hauna tofauti na usiku wa kuamkia kuuawa. Kulipopambazuka Kamba alimuaga Mama Safi kuwa anakwenda Mkwajuni kuonana na jamaa yake. Hakuwa mtu wa kumwambia kila kitu mkewe. Huu ulikuwa ni uongo mwingine.
Mama Safi hakumjibu. Bado amani ilikuwa imetoweka kati yao. Hata hivyo, Kamba hakujali, alijali kutimiza nadhiri yake.
Akakodi teksi iliyokwenda kumwacha Posta Mpya ambako alichepuka na kuingia ndani ya jengo la Posta. Humo hakukuta watu wengi hivyo akalifuata dirisha moja na kumkuta dada aliyekuwa makini na kazi yake, macho akiwa ameyakodoa kwenye kioo cha kompyuta.
Kamba alitulia kwa muda, akikiheshimu kile alichokuwa akikifanya dada huyo. Yuko kazini hivyo isingekuwa busara kumvamia na kuanza kumwambia shida yake. Muda mfupi baadaye dada huyo aliinua uso na kumtazama Kamba. “Nikusaidie kaka?” alimuuliza.
“Ndiyo,” Kamba alijibu na kusita kidogo, akigeuka huku na kule kama vile hakutaka mtu mwingine awasikie.
“Nakusikiliza,” dada huyo alimshtua huku akimkazia macho.
Akili ya Kamba ikampeleka mbali. Aliwaza kuwa huenda hili analotaka kuhoji likakosa jibu zuri au sahihi. Ni miaka saba tangu alipoliacha jiji hili, na leo anakuja kumuulizia mtu ambaye hakuwa na mawasiliano naye ya aina yoyote kwa kipindi chote hicho! Je, akipewa majibu ya “kafariki siku nyingi zilizopita” au “kafungwa jela” atajisikiaje?
Hata hivyo, alijijua kuwa yeye ni mwanamume, na mwanamume hupaswa kukabiliana na hali yoyote iliyo mbele yake. Hivyo akamuuliza, “Rukia nimemkuta?”
Dada huyo alikunja uso na kumtazama Kamba kwa macho makali zaidi. Kisha akashusha pumzi ndefu na kuuliza, “Rukia yupi?”
“Rukia Edward.”
Dada huyo akatikisa kichwa kama anayekubali jambo fulani, kisha akasema, “Ahaa…Rukia…” sauti yake ikaonesha unyonge na akaendelea kumtazama Kamba kwa macho ya huruma. Akarusha swali, “Ni nani yako?”
“Ni dada yangu, kwani vipi?”
Dada huyo akaachia tabsamu dhaifu. “Nashangaa kuja kumuulizia mtu ambaye aliacha kazi siku yingi! Kwani huwa hamuwasiliani?”
“Kaacha kazi?” Kamba aliliepuka swali.
“Nd’o maana’ake. Huna namba yake ya simu?”
Kamba alikataa kwa kutikisa kichwa. “Ilipotea katika simu iliyoibwa,” aliongopa.
“I see. Basi nd’o ivo kaka’angu. Kaacha kazi kama miaka miwili hivi iliyopita.”
Kamba alitulia na kuonekana akiwaza. Kisha akamrudia dada huyu na kumuuliza, “Hapa si mna kile kitabu cha orodha ya namba za simu na sanduku la posta?”
“Ndiyo. Kwani nd’o unataka kuangalia namba ya Rukia?”
“Ndiyo.”
“Haisaidii,” dada huyo alimkata maini. “Rukia ana mobile. Namba yake ya sasa sina. Kabla hajaondoka alikuwa akitumia mtandao wa Voda na Zantel, lakini sasa nasikia alihamia Airtel. Hiyo mitandao mingine aliachana nayo. Hiyo namba yake ya sasa nd’o sina.”
Bado Kamba alikuwa king’ang’anizi. “Lakini sista naomba tu hicho kitabu nicheki pia namba za kampuni fulani.”
Yule mfanyakazi alimwelekeza dirisha la tatu ambako alipewa kitabu hicho. Akashusha pumzi ndefu na kwenda kuketi kitini. Akaanza kupekua ukurasa huu na ule. Dakika takriban kumi zikateketea katika zoezi hilo. Hatimaye akapata kile alichokihitaji. Akatoka huku roho yake ikiwa imesuuzika.
**********
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
HASSANALI, mtoto wa Ladhu H. Ladhu alikuwa dukani saa 5 asubuhi. Hakuwa akitoa huduma kwa wateja bali alikuwa mezani akifanya hesabu za mapato na matumizi ya jana yake. Baba yake ndiye aliyekuwa akiendelea kuwahudumia wateja akisaidiana na kijana mmoja.
Mara simu ya mezani alikokuwa Hassanali ikaita. Papohapo naye akakitwaa kiwiko na kukitega sikioni.“Haloo.”
“Nazungumza na Mr. Hassanali?” sauti kutoka upande wa pili ilipenya masikioni mwa Hassanali.
“Yeah, nikusaidie?”
“Mr. Masanja nazungumza.”
“Masanja wa wapi?”
“Natoka Shinyanga.”
“Ok, nakusikiliza.”
Kimya kifupi kikatawala kisha sauti ikapenya tena masikioni mwa Hassanali: “Kuna bidhaa ninazozihitaji kutoka hapo kwako.”
“Bidhaa gani?”
MARA simu ya mezani alikokuwa Hassanali ikaita. Papohapo naye akakitwaa kiwiko na kukitega sikioni.“Haloo.”
“Nazungumza na Mr. Hassanali?” sauti kutoka upande wa pili ilipenya masikioni mwa Hassanali.
“Yeah, nikusaidie?”
“Mr. Masanja nazungumza.”
“Masanja wa wapi?”
“Natoka Shinyanga.”
“Ok, nakusikiliza.”
Kimya kifupi kikatawala kisha sauti ikapenya tena masikioni mwa Hassanali: “Kuna bidhaa ninazozihitaji kutoka hapo kwako.”
“Bidhaa gani?”
Televisheni aina ya Samsung zipo?”
“Zipo. Ngapi?”
“Kumi na tano, lakini ziwe za ukweli!”
“Siuzi vitu feki mimi!” Hassanali alikuwa mkali kidogo. “Kila kitu changu ni original.”
“Ok, kuna simu hapo kwako?”
"Zipo. Aina gani?”
“BlackBerry.”
“Zipo.”
“Nokia?”
“Zipo.”
“Huawei?”
“Pia zipo. Ngapi?”
“Nahitaji nyingi lakini nikifika nitachagua idadi n’nayotaka. Hata za Kichina nachukua. Na ninahitaji katoni hamsini za sabuni aina ya Omo.”
“Zipo.”
Ukimya ukapita tena kisha mtu huyo akasema, “Ok, nakuja. Lakini mzee pia awepo maana kuna suala fulani niliwahi kuongea naye.”
“Suala gani tena?” Hassanali alirusha swali haraka.
“Ni la kibiashara kama hivi. Tulizungumza kiasi cha wiki mbili hivi zilizopita.”
Hassanali aliguna. Alishangaa kusikia eti baba yake, Mzee Ladhu amezungumza na mtu huyu maongezi ya kibiashara ilhali ana kumbukumbu sahihi kuwa kiasi cha wiki mbili zilizopita alikuwa akishinda chumbani amelala kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya kisukari na presha.
Hata hivyo hakupenda kudadisi zaidi kuhusu hilo wakati huo. Alichohitaji kujua ni uhakika wa ujio wa mtu huyo. Akamuuliza, “Utakuja lini?”
“Kesho asubuhi.”
“Una hakika?”
“Nadhani hunijui bwa’mdogo,” sauti hiyo ilikuwa thabiti. “Sikuja kuleta longolongo. We n’ambie tu unachukua cheki au mpaka keshi?”
Hassanali alisita kidogo kisha akajibu, “Ukija na keshi itakuwa poa zaidi kwa sababu bado mtandao baina yako na sisi haujakomaa.”
Ukimya mfupi ukapita kisha mtu huyo akasema kwa suti ya chini, “Ok, hilo s’o tatizo. Hebu nipe hesabu inayoeleweka kwa upande wa simu kwanza.”
“Kwa simu ngapi na aina gani? Zipo aina tofauti na bei tofauti.”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nokia Lumia-635 ziwe hamsini.”
“Zipo.”
“Huawei Ascend G-6205. Nataka ishirini.”
Hassanali aliguna kidogo kwa mshangao kisha akajibu, “Zipo. Nyingine?”
“BlackBerry Z-30. Ziwe hamsini.”
Kimya kifupi kikapita kisha Hassanali akauliza, “Na hizo tivii kumi na tano na katoni hamsini za Omo nisizihesabu kwanza?”
“Zijumuishe tu.”
“Ni pesa nyingi kidogo.”
“Kama kiasi gani?”
“Itabidi tukae tufanye hesabu inayoeleweka.”
“Ok, tufanye hivi, nakuja na milioni ishirini. Zikipungua au zikizidi tutajua hukohuko. Sawa?”
“Poa.”
Ok, kesho basi.”
**********
SIKU iliyofuata, asubuhi, Kamba alijiandaa harakaharaka na kutoka. Dakika chache baadaye alikuwa Mkwajuni ambako aliwaza kama akodi teksi au apande daladala. Akaamua kukodi teksi iliyokwenda kumwacha Kariakoo ambako alinunua briefcase nzuri aliyoamini kuwa ni ya hadhi kwa kulinganisha na suti kali aliyotinga mwilini.
Alipotoka hapo alikodi teksi nyingine ambayo nayo nayo aliitema alipofika Mtaa wa Jamhuri Sasa akaamua kutembea taratibu akiufuata Mtaa wa Mosque.
Saa 2:50 alikuwa nje ya duka la Ladhu H. Ladhu. Eneo hilo lilikuwa tupu kwa kuwa duka lilikuwa bado limefungwa. Zaidi ya mlinzi aliyekuwa kaegemea nguzo, hakukuwa na mtu mwingine.
Lakini katika jengo la pili kushoto na lile la kulia kulikuwa na vijana waliokuwa wakifanya biashara ndogondogo na wengine wakiwa wamekaa kwenye mabenchi wakivizia vijikazi vya papo kwa papo. Kamba alimsogelea yule mlinzi taratibu, mkono wa kushoto mfukoni, mkoba, mkono wa kulia.
Mlinzi naye akamtazama kwa makini huku akijiweka sawa. Kamba alipomfikia aliitoa miwani yake mieusi machoni na kumtazama huku akitabasamu.
“Karibu mheshimiwa,” mlinzi alimwambia huku naye akitabasamu, tabasamu la kutojiamini, akimtazama Kamba kiwogawoga.
“Asante,” Kamba alijibu kwa sauti nzito na ya kujiamini, sauti ya kipesapesa. Akauweka chini mkoba kisha akamuuliza mlinzi huyo, “Vipi, nimewahi sana?”
“Siyo sana. Duka litafunguliwa saa tatu na nusu. Bado kama nusu saa hivi.”
Kamba alikunja uso na kutikisa kichwa. “ Nusu saa ni muda mrefu,” hatimaye alisema kwa sauti ya chini. Kisha akaongeza, “Nimeongea na Hassanali jana, na ana taarifa ya ujio wangu. Naweza kuonana naye?”
“Sasa hivi?”
“Yeah. Suala langu ni nyeti sana.”
“Subiri,” mlinzi alisema huku akiitoa simu mfukoni na kubonyeza vitufe kadhaa kisha akaitega sikioni. Baada ya sekunde chache akasema, “Bosi kuna mgeni anasema ana apointimenti na wewe…yeah…anaitwa…” akasita na kumgeukia Kamba: “Eti unaitwa nani mkuu?”
“Masanja. Masanja kutoka Shinyanga,” Kamba alijibu haraka.
Mlinzi yule akairudia simu na kusema, “Ni Mista Masanja kutoka Shinyanga.”
Ukimya ukapita, mlinzi akionekana kusikiliza kwa makini. Kisha akakata simu na kumgeukia tena Kamba. “Ni wewe uliyetoa oda kubwa jana?”
Kamba alikubali kwa kutikisa kichwa juu, chini.
Mlinzi akaonekana kushangaa. “Mbona huna usafiri mheshimiwa?” hatimaye alimuuliza.
“Sina haraka. Kwanza nahitaji kuiona mizigo yenyewe.”
“Poa. Karibu ndani. Bosi anakusubiri.”
Kamba akafuata maelekezo, akipita mlango ambao haukuwa wa kuingilia dukani.
**********
MZEE Ladhu H. Ladhu na mwanaye, Hassanali walikuwa sebuleni wakinywa kahawa na kutafuna tambuu wakati simu ya Hassanali ilipoita. Baada ya kuzungumza na mlinzi, akamwambia baba yake,“ Kuna Mnyantuzu mmoja sijui kauza ng’ombe wake huko Unyantuzuni sasa kaja na oda kubwa!”
“Ya kiasi gani?”
“Si chini ya milioni ishirini.”
“Yuko wapi?”
“Anakuja. Nimemwambia Juma amruhusu.”
Mzee Ladhu alitaka kutamka neno akasita baada ya kumwona mtu mlangoni. Wote wakamtazama mtu huyo kisha na papohapo Hassanali akaingiwa na hisia kuwa huyo ndiye yule mgeni ambaye Juma alimwambia.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Karibu..Karibu Bwana Masanja,” Hassanali alimkaribisha huku akimtazama kwa bashasha kubwa.
“Asante sana,” Kamba alijibu huku akiitoa miwani usoni na kuipachika ndani ya mfuko wa shati taratibu na kwa maringo. Kisha akaanza kuvuta hatua taratibu na kwa madaha, hatua za mtu mwenye ukwasi.
“Karibu kiti,” Hassanali alimwambia huku akimwonyesha sofa kubwa lililokuwa kando ya mlango.
Kamba aliketi huku akiendelea kuwatazama wenyeji wake mmoja baada ya mwingine, macho yake baridi yakiwa hayatofautiani na nyoka mwenye hasira. Akauweka mkoba katikati ya miguu yake kisha akamtazama sawia Hassanali na kumwambia, “Nd’o nimekuja mheshimiwa. Inakuwaje?”
“Nadhani tuanze kwa kwenda stoo ukazicheki mali unazozitaka,” Hassanali alisema huku akichekacheka.
“Hakuna haja ya kufanya hivyo,” Kamba alipinga kwa upole. “Kuna vijana wangu watakuja kuziangalia. Ninakuamini. Sidhani kama unaweza kunifanyia uhuni kwa bidhaa za thamani ya shilingi milioni ishirini au hamsini hivi. Sidhani.”
Hassanali alishangaa. Akamtazama baba yake kama anayemuuliza, mbona simwelewi-elewi mtu huyu? Kisha akamrudia Kamba na kumuuliza, “Kwa hiyo inakuwaje?”
“Nataka niache advance.”
“Kama kiasi gani?”
“Twenty million.”
Hassanali alitikisa kichwa akiashiria kukubali. Kisha akasema, “Ok, s’o mbaya, inatosha. Najua mzigo ulioutaja haupungui fifty million.”
Kamba akautwaa mkoba na kuuweka mapajani mwake. Kisha kwa chati akaupeleka mkono ndani ya mfuko wa suruali na kuichomoa bastola kubwa ya Kirusi, G- 231- Peacemaker. Akawaelekeza mmoja baada ya mwingine kwa zamu Hassanali na baba yake.
Hassanali aligwaya, hali kadhalika baba yake. Wakabaki wakimtazama Kamba kwa macho yasiyoamini yakionacho.
Kamba aliachia tabasamu changa lisilotoa taswira yoyote ya furaha. Macho yake makali yaliwatazama Hassanali na Mzee Ladhu kwa ishara ya kuua!
“Msishangae wala msihofu,” hatimaye alisema kwa sauti nzito, yenye kijimkwaruzo cha hasira, macho yake baridi yakiendelea kuwazungukia Ladhu na mwanaye. Kisha akaendelea, “Najua hamnikumbuki…lakini mimi nawakumbuka, ndiyo maana leo nipo hapa tena.”
Kufikia hapo akasita na kuchanua zaidi tabasamu lake ambalo bado lilizidi kutisha badala ya kupendeza. Akaitoa miwani usoni na kuipachika katika mfuko wa shati.
“Kamba,” alisema kwa sauti ya chini zaidi. “Ni yule Kamba Kiroboto!”
“Haa!” Hassanali na baba yake walibwata kwa mshtuko, macho yao yakimkodolea Kamba kwa woga usiofichika.
KILICHOFUATA ni kipindi ambacho Kamba aliwasimulia kwa kina tukio la yeye kukamatwa na Polisi na kutuhumiwa kuhusika na uporaji ambao hakuufanya.
“Nilikuwa kwenye sherehe ya harusi, na tangu asubuhi nilikuwa katika pilikapilika zilizohusiana na harusi hiyo. Askari polisi waliponitia mbaroni, nikafikishwa mahakamani, wewe,” akamwelekezea kidole Hassanali, “ukawa shahidi mkubwa eti ni mimi ndiye niliyewavamia!
“Cha ajabu,” sasa alimgeukia Mzee Ladhu. “Hata wewe mzee ulikuwa mkali, ukidai kuwa una uhakika na unachokisema! Kwa taarifa yenu tu, mtu aliyehusika na tukio lile kajileta kwangu siku niliyotoka gerezani na akanipa pole. Kanipoza kwa mkwanja wa maana! Yule ni binadamu kati ya binadamu, sio nyie! Nawaaambia hivyo ikiwa ni taarifa ya mwisho kwenu kuisikia kutoka kwangu, mabaniani ms’okuwa na adabu!”
“Tafadhali Bwana Masanja…” Mzee Ladhu alisihi.
“Nani Masanja?” Kamba alibwata kisha akaachia kicheko kikali cha dhihaka. “ Hivi kwa vichwa vyenu vyenye ubongo uliooza mmekuwa mkiamini kuwa mimi naitwa Masanja?”
“Oooh…samahani…bwana…bwana…” Hassanali aliomboleza akiwa hajui aseme nini. Alibakia kubabaika.
“Kimya!” Kamba alifoka. “Mnataka kuniambia nini? Na mnafikiri mnaweza kuniambia nini ambacho nitakielewa?”
Sura ya Kamba ilishabadilika. Macho yake makali yalikuwa yakitua kwa Mzee Ladhu na mwanaye kwa zamu kila baada ya sekunde chache. Hasira ilizidi kumpanda. Akakumbuka siku moja wakati akiwa kizimbani, Mzee Ladhu alipozungumza kwa kujiamini:
“Alininyooshea bastola na kunishinikiza nimpa pesa…akachukua pesa yooote ya mauzo ya siku mbili…”
Maneno hayo yalijirudia akilini mwake mara mia moja kwa sekunde tano tu. Yakamtia uchungu maradufu. Akawatazama Ladhu na mwanaye mithili ya atazamaye chochote kile kitiacho kinyaa.
Akasimama na kuwaambia, “Nimekuja leo kwa kazi moja tu! Moja tu!”
Hakuongeza neno, badala yake aliikamata bastola kwa uthabiti katika kono lake la kulia, akaielekeza kwa Mzee Ladhu na kufyatua risasi moja tu, risasi iliyotekeleza wajibu wake kwa usahihi! Ndiyo, ilipenya kwenye jicho la kulia la Mzee Ladhu na kuacha tundu kubwa kisogoni!
Tukio hilo lilikuwa ni kama kiinimacho akilini na machoni mwa Hassanali. Kushuhudia baba yake mzazi akipigwa risasi iliyoyakatisha maisha yake papohapo, ilikuwa ni kama tamthiliya isiyostahili kuonwa na mstaarabu yeyote!
Hakuamini!
Kwa jazba, bila ya kutafakari kama hatua yoyote anayotaka kuchukua itazaa matunda mema au madhara yatakayoigharimu pumzi yake, alikurupuka na kumrukia Kamba kwa staili ya judo, tendo ambalo hakupata hata nafasi ya kulijutia!
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kamba alikuwa makini na mwepesi kuliko Hassanali alivyomchukulia. Wakati Hassanali akiwa hewani, risasi ya kichwa ilikutana naye hukohuko na kutengeneza taswira isiyotofautiana sana na ya baba yake.
Akapiga kelele kubwa, mikono kainyoosha juu na kuanguka sakafuni kwa kishindo puu!
**********
JUMA alikuwa ndiyo kwanza anamaliza kuwasha sigara aliyoinunua kutoka kwa kijana aliyepita nje ya duka la Ladhu H. Ladhu. Milio miwili ya risasi kutoka ndani ya jengo la mabosi wake ilimshtua na kumfadhaisha kwa kiwango kikubwa. Akaduwaa kwa sekunde chache. Kisha, kama aliyezinduliwa usingizini aliitupa sigara chini na kuikamata ala ambayo ndani yake kulikuwa na kisu kirefu na chenye makali ya kutisha.
Akakitoa kisu hicho na kukikamata imara katika mkono wa kulia akivuta hatua za kikakamavu akielekea ndani. Lakini hakufanikiwa kuingia sebuleni, mlangoni alikutana na Kamba ambaye bado alikuwa na bastola mkononi.
“Tupa chini!” aliamriwa, bastola ikimtazama usoni.
Juma hakuwa na kumbukumbu ya lini maishani aliwahi kutazamana na chombo hicho na huku kikiwa kimeshikwa na mtu kama huyu, mtu mwenye macho yaliyotamka neno moja tu: Nitakuua!
Wala hakutarajia kuwa ipo siku itatokea kama hivi, zaidi ya kuishia kuangalia kwenye sinema. Kwa hali hiyo, mshtuko alioupata ulimfanya ajikute akikiachia kisu hicho pasi na kujitambua.
Kamba akamsogelea na kumsukumia teke zito, teke la kukandamiza lililomtupa chini sawia, chali na kabla hajatanabahi, kisu chake hichohicho ambacho sasa kilikuwa mkononi mwa Kamba kilizama tumboni mwake akishuhudia!
Alitoa macho pima akishangaa, akimtazama Kamba bila ya kupepesa! Mara maumivu makali yakajitokeza! Akakunja uso na kugugumia kwa uchungu. Kisu kilipoibuliwa na kuzamishwa kwa mara ya pili, alianza kutapatapa huku bado akimtazama Kamba kwa macho yaliyofurika maswali yaliyokosa majibu.
Alikufa huku akiwa amekodoa macho angani na meno yakiwa
yamezikandamiza papi za mdomo.
Wakati damu ilipoanza kububujika kwa wingi, Kamba alikuwa hatua tano kando ya mwili huo na aliutazama kidogo tu kisha akajikagua kama alikuwa na doa lolote la damu.
Alipojiona kuwa yuko safi, aliirejesha miwani usoni na kuukamata mkoba wake vilevile kama alivyoingia kisha akaukita mkono ndani ya mfuko wa suruali ambako uliikamata bastola tayari kwa matumizi kama itabidi.
Akatoka taratibu kwa mapozi yake yaleyale na kukuta vikundi vya watu nje vikiukodolea macho mlango aliotokea na huku kila mmoja akinong’ona lake. Kila mmoja alimtazama kwa mshangao, macho yao yakionyesha kujawa na shauku ya kutaka kumhoji kuhusu kilichojiri huko alikotoka. Lakini nani angethubutu kumuuliza?
Kila aliyemtazama alimgwaya. Na yeye aliligundua hilo, akabaki akichekea moyoni. Akaendelea kutembea kwa hatua za kawaida, akionekana kutokuwa na wasiwasi wowote lakini akiwa makini, akiwa amechukua tahadhari kwa lolote ambalo lingeweza kumzukia.
Mbele kidogo baada ya kujiona amekata mtaa mmoja tu, akaingia ndani ya teksi na kumwamuru dereva ampeleke Upanga.
“Upanga ipi?”
“Tumaini Hospital. Unapajua?”
“Si pale jirani na Diamond Jubilee?”
“Kumbe unapajua.”
Dereva alicheka na kusema, “Ukiwa mtu wa teksi kwa jiji hili inabidi ulijue zaidi ya nusu, vinginevyo kazi itakuwa ngumu kwako.”
**********
UTULIVU ulikuwa umetoweka katika eneo la duka la Ladhu na majirani zake. Taharuki iliwatawala wengi waliosikia milio ile ya risasi. Baadhi ya maduka ya jirani yaliyokuwa yamefunguliwa, wamiliki wake waliyafunga haraka. Watu wakawa wakikimbia huku na kule katika kuzinusuru roho zao.
Hata hivyo, siyo wote waliokimbia moja kwa moja. Vijana wawili waliokuwa na kijiwe chao kwenye duka la Mhindi mwingine lililokuwa likitazamana na duka la Ladhu, walijificha kwenye uchochoro uliokuwa kando ya kijiwe.
Walikuwa hapo huku wakichunguza kule kwenye duka la Ladhu. Baada ya dakika mbili, tatu za ile milipuko ya risasi huku yule mlinzi wa Ladhu akiwa ndani ya jengo la Ladhu, mara wakamwona mtu, mwanamume akitoka ndani ya jengo hilo, mkoba mkononi.
Vijana hao wakaguna. Kila mmojawao alikuwa na kumbukumbu ya kumwona mtu huyo mtanashati akiongea na mlinzi wa Ladhu muda mfupi uliopita, kisha akaingia ndani. Sasa ni kipi kilichojiri huko ndani? Kwa nini risasi zirindime wakati mtu huyo alipoingia ndani? Na mbona ni yeye pekee aliyerudi huku nje? Je, mlinzi wa Ladhu yuko ndani? Na kuna usalama?
Maswali yalivisumbua vichwa vya vijana hao. Ndipo, mmojawao aliyeitwa Kevin alipowaashiria wenzake kuwa anakwenda ndani. Akanyanyuka na kuvuta hatua ndefu akilifuata jengo la Ladhu.
Huku nyuma aliwasikia wenzake wakimuunga mkono, “Kacheki msh’kaji,” Sele alisema. “Kwa vyovyote kutakuwa na noma huko ndani.”
Hata hivyo, dakika iliyofuata Kevin alikuwa akirudi mkuku, macho yamemtoka pima! Akakimbia bila ya umakini kiasi cha kukoswakoswa kugongwa na gari wakati akivuka barabara.
“Kafa! Wamekufa!” yalikuwa ni maneno ya kwanza mara tu alipowafikia wenzake.
“Nini?” Sele alimuuliza.
“Jamani Jumaaa!” Kevin aliendelea kuomboleza huku akiinua mikono juu na kuwa kama aliyepagawa.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Vipi Kevin?” Sele alimdaka.
Kevin aligeuka nyuma, kushoto na kulia kisha akamvuta Sele, wakaingia ndani zaidi ya uchochoro huo wa jengo hilo. Walipofika sehemu waliyoona ina usalama zaidi, Kevin alisimama na kusema, “Juma kauawa! Maiti yake iko kwenye mlango wa kuingilia sebule ya Mzee Ladhu!”
“Nani kamuua?”
“Sijui!”
“Mungu wangu!”
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment