Search This Blog

Friday, 20 May 2022

PIGO LA MWISHO - 3

 







    Simulizi : Pigo La Mwisho

    Sehemu Ya Tatu (3)





    Kevin akaendelea, “Na sijui kama kuna usalama huko ndani! Juma kachomwa kisu, damu chepechepe! Sijui mabosi wake wako vipi? Sijui nd’o waliomuua?”



    “I’shakuwa soo mshkaji wangu,” Sele alisema. “Tutambae mwanangu…maana’ake hapa ku’shakuwa msalani mwanangu…duh!”



    Dakika iliyofuata walikuwa Mtaa wa Libya wakitokomea.



    MAMA Safi alikosa raha tangu mumewe alipomwambia kuwa lazima afanye jambo kwa wote waliohusika na kifungo chake. Alimjua vizuri mumewe jinsi alivyo na msimamo pale anapokuwa ameamua kutekeleza jambo lolote. Ni mtu ambaye hakuwa tayari kuutengua uamuzi wake hata kwa mtutu wa bunduki!



    Aliyakumbuka maneno ambayo Kamba alimwambia siku ile usiku: “Miaka saba jela kwa kosa la kusingiziwa! Haiwezekani! Nakwambia Mama Safi haiwezekani! Lazima wanitambue!” Yalikuwa ni maneno ambayo Kamba aliyatoa kwa hasira, akionesha bayana kutobadilika kimsimamo. Na kuna yale mengine: Inaniuma sana hivyo, usijali. Acha nifanye kile ninachotaka kufanya ili roho yangu isuuzike. Sawa?”



    Huyo ndiye Kamba. Kamba Kiroboto, ambaye sasa ameingia katika hatua kubwa ya kufanya kile alichodhamiria kukifanya. Mama Safi alikosa amani moyoni, akakosa utulivu akilini. Akashindwa kuvumilia. Akaamua kuchukua hatua. Akatoka na kwenda kwa shoga yake, Mama Sikudhani na kumweleza kuhusu hatua ambayo mumewe amedhamiria kuichukua. Hakuficha kitu!

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilikuwa ni taarifa iliyomshtua na kumsikitisha sana Mama Sikudhani. Kwa unyonge akasema, “Jitahidi kumsihi aache hasira. Najua hiyo yote ni hasira tu. Mbembeleze aache hasira!”



    “Habebembelezeki wala hasikii kitu, mwenzangu! Hivi unamfahamu Baba Safi au unamsikia-sikia tu?”



    “Kwa hiyo utafanya nini?” Mama Sikudhani alimuuliza huku akionekana kukosa ushauri mwingine.



    “Nina wazo la kutoroka, shoga.”



    “Kutoroka? Uende wapi?”



    “Kwetu!”



    Mama Sikudhani aliguna na kusema, “Wazo lako siyo baya, lakini kutorokea kwenu, mmh! Hapana hilo ni kosa, tena ni kosa kubwa sana!”



    “Kwa nini?”



    “Kama askari watakutaka, watakukamata kirahisi sana!” Mama Sikudhani alisema. “Kwani huna pengine pa kukimbilia?”



    “Pa kukimbilia kwingine siyo tatizo. Tatizo ni mwanangu, Safi.”



    “Safi? Safi kawaje?”



    “Hayupo.”



    “Yuko shuleni?”



    “Ndiyo!”



    “Anasoma wapi?”



    “Hapo Hananasif.”



    “Ok, hilo siyo tatizo. Mfuate uondoke naye. Kwani huna pesa kidogo hapo?”



    “Ka’ shi’ ngapi?”



    “Alfu kumi hivi isiyo na kazi muhimu.”



    “N’nayo.”



    “Basi kaongee na mwalimu wa darasa,” Mama Sikudhani alimwambia. “Mwimbishe. Mwambie kuna matatizo kwa wazazi wako hivyo unalazimika kusafiri na mwanao. Mtupie hako ka-msimbazi na kumwambia kuwa utachukua kama wiki moja au mbili tu utakuwa umerudi. Hapo utakuwa umemwachia mpira, na atajua mwenyewe jinsi ya kuucheza. Kila kitu atakiweka sawa. Siku hizi njaa kali mwenzangu, husikii walimu wanataka kugoma kila kukicha, kisa, mshahara mdogo na malimbikizo kibao hawajalipwa! Unadhani huyo mwalimu wako atakataa elfu kumi? Subutu yake!”



    “Umesema kweli shoga’angu,” Mama Safi alisema kwa unyonge lakini sasa sura yake ikionesha matumaini.



    “Halafu,” Mama Sikudhani aliendelea. “ Kumbuka, nimekwambia usikimbilie kwa wazazi wako, Kisarawe. Jichimbie hapahapa Dar! Kwani huna ndugu hapa Dar anayeweza kukuficha ukafichika?”



    “Yupo.”



    “Mbali kidogo na hapa Moscow?”



    “Siyo mbali tu na hapa Kinondoni Moscow bali ni nje ya Wilaya ya Kinondoni.”



    “Wapi?”



    Mama Safi alisita kuwa muwazi. Na kwa wakati huo hakutaka kuweka kila kitu bayana. Aliamini kuwa hadhari ni jambo lililopaswa kupewa kipaumbele. Akaishia kujibu, “Ni mbali tu.”



    “Baba Safi hapajui huko na wala hamjui huyo nduguyo?”



    “Hamjui wala hajui kuwa nina ndugu mwingine zaidi ya kwa wazazi wangu Kisarawe.”



    “Hapo mambo shwari. Kumbe yuko gizani! Basi fanya hivyo. Kumbuka, usithubutu kukimbilia kwenu kwani kama askari watakutaka, watakupata ka’ vile kumsukuma mlevi aliyechuchumaa!”



    Mama Safi alifuata maelekezo ya Mama Sikudhani na hakupata kipingamizi chochote wakati alipokwenda kumtiririshia uongo mwalimu, shuleni Hananasif. Mambo yakaenda vizuri. Baada ya saa moja hivi alikuwa akiondoka na mwanaye, Safi huku akiwa na begi lililosheheni nguo zake na za mwanaye. Alikokwenda ilikuwa ni siri yake. Hakumwambia Mama Sikudhani wala mtu mwingine yeyote!



    Mbagala kwa dada yake!



    **********

    SIRI ilishavuja. Baada ya Mama Safi kumdokeza Mama Sikudhani, muda mfupi baadaye Mama Sikujua wa nyumba ya tatu, Mama Tatu wa mtaa wa pili na Mama Semeni wa mtaa wa nne wote wakawa na habari hiyo.



    Mdomo wa Mama Sikudhani!



    Siri ilizidi kuvuja pale Mama Semeni alipomdokeza mumewe. Hapo sasa mambo yakazidi kuchukua sura mpya! Mume wa Mama Semeni hakuwa na subira. Alitumia gari lake kwenda Kituo cha Polisi cha Oysterbay ambako aliripoti taarifa hiyo.



    Ndiyo, siri ilishavuja!CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    **********

    TEKSI iliposimama mbele ya Hospitali ya Tumaini, Mtaa wa Magore eneo la Upanga, Kamba aliteremka na kumpa ujira dereva kisha akavuta hatua akiingia ndani ya hospitali hiyo. Hata hivyo, hakuwa na chochote kilichomwingiza huko ndani. Alipofika mapokezi akashangaa-shangaa akiwatazama wagonjwa walioketi vitini. Yote hiyo ilikuwa ni katika kusubiri dereva teksi yule aondoke.



    Kisha akatoka tena na kuifuata teksi nyingine iliyompeleka hadi kituo cha daladala cha Studio, Kinondoni na kuachana nayo. Sasa akaswaga kwato akipita mtaa huu na ule hadi alipozukia kwake ambako alipoingia ndani na kutomkuta mkewe, hakushtuka. Alihisi kuwa kaenda sokoni kuhemea. Hisia hizo zilimtawala kichwani wakati alipoingia sebuleni lakini alipoingia chumba cha malazi, zikayeyuka ghafla. Vitu vilikuwa shaghalabaghala. Nguo za Mama Safi na za Safi hazikuwapo. Lile begi kubwa lililokuwa juu ya kabati sasa halikuwapo! Viatu vya Mama Safi havikuwapo!



    Hakuhitaji kufikiri sana ni kipi kilichotokea. Usiku wa jana yake Mama Safi alionesha kutoafikiana naye kuhusu maazimio yake ya kuwasaka wote waliosababisha atumikie kifungo cha miaka saba jela. Na hata alipokuwa akiondoka asubuhi aliusoma uso wa Mama Safi na kubaini kuwa hakuwa katika hali nzuri.



    Hivyo, kwa kuzingatia hali aliyokuwa nayo Mama Safi na picha aliyoikuta humo chumbani, aliamini kuwa Mama Safi ametoroka. Na alihisi kuwa huenda kaenda kwa wazazi wake Kisarawe.



    Akashusha pumzi ndefu na kuamua kumwondoa mawazoni Mama Safi na mwanaye. Ndiyo, aliamua hivyo kwa kuwa tayari alishaanza kutekeleza majukumu aliyopanga. Alishaanza, na bado kulikuwa na mengine mbele ambayo hakutaka kujidanganya kuwa ni mepesi kama yaliyotangulia.



    Haraka akazivua nguo na kuzitupa kitandani. Kisha akaifungua kabati na kutoa suruali ya rangi ya kaki aina cadet na shati jeupe. Akazivaa nguo hizo. Vile viatu vyeusi alivyovivaa wakati akielekea katikati ya jiji, alivivua na badala yake akatinga raba nyeupe. Alijiona hajapendeza kama awali lakini hakuhitaji kupendeza, alihitaji mabadiliko. Na safari hii kofia haikutua tena kichwani, wala miwani haikuganda machoni. Hata hilo shati jeupe, pana na refu aliliacha limwagike bila ya kulichomekea. Akawa katika mwonekano wa mtu wa kawaida.



    Sasa hakupenda tena kuzubaa ndani ya nyumba hiyo. Aliipachika bastola mfukoni na kutoka, safari hii akidhamiria kuzuru Regent Estate, Mikocheni.



    *********



    HUENDA taarifa ya Baba Semeni ingewaacha njiapanda askari wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay. Ndiyo, aliwatajia bayana jina la Kamba Kiroboto, kwamba ni mtu aliyemaliza kifungo majuzi tu. Na aliwaambia kuwa mke wa Kamba ndiye aliyemweleza mkewe (baba Semeni) kuwa Kamba aliondoka asubuhi akielekea mjini kuwaua wote waliohusika kwa kiwango kikubwa kumfanya asote jela miaka saba.



    Hata hivyo, askari walioipokea taarifa yake, waliichukulia kama taarifa ngumu kwa utekelezaji. Kilichofanyika ni kutoa taarifa Kituo Kikuu. Baba Semeni ambaye aliandamana na askari wa Kituo cha Oysterbay hadi hapo Kituo Kikuu aliketishwa na Inspekta Maliyatabu aliyekuwa na jukumu la kufuatilia suala hilo.



    “Unasema taarifa hii umepewa na mkeo?” Maliyatabu alimuuliza.



    “ Ndiyo, afande.”



    “Na mkeo kaambiwa na nani?”



    “Kasikia kwa watu walio marafiki na mkewe Kamba!”

    Inspekta Maliyatabu alimkazia macho makali Baba Semeni na kuguna. Kisha akasema, “Hayawezi kuwa ni majungu na chuki binafsi?”



    Baba Semeni aliinua mabega na kuyashusha. “Siwezi kujua, afande,” hatimaye alisema. Kisha akaongeza, “Lakini nakumbuka wakati Kamba alipokuwa na kesi, mkewe alikuwa akilalamika sana kuwa mumewe kaonewa, na kwamba siku aliyotuhumiwa kuwa kavamia duka hakuwa ametoka nyumbani kwake.”



    “Yaani alituhumiwa kimakosa na kuhukumiwa kimakosa?!”



    “Nd’o maana’ake!”



    Inspekta Maliyatabu alikuna kidevu huku akitazama dirishani. Akaachia cheko dogo la dhihaka. Alikuwa akijaribu kuwakumbuka majambazi kadhaa aliowajua. Hakutaka kukisumbua sana kichwa chake. Akacheza na kompyuta iliyokuwa mbele yake. Muda mfupi baadaye akawa na kumbukumbu za baadhi ya wahalifu aliowahitaji. Kuna Shoka na Chopa ambao tayari walishauawa wakati walipokuwa wakipambana na askari. Shaka naye alishakufa. Kasha bado yuko kifungoni.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Huyu Kamba ni nani? alijiuliza swali hilo huku akikunja uso. Akaliandika kwa mara nyingine jina la Kamba Kiroboto na kuiamuru kompyuta kuziweka bayana taarifa zilizohusu jina hilo. Kompyuta ikapekua kumbukumbu zake kwa muda na hatimaye ikamjibu 'no items match your search.' Akasonya na kutwaa simu kisha akabonyeza tarakimu kadhaa na kuitega sikioni.



    Wakati huo pia alikuwa akiendelea kutafuta kumbukumbu za matajiri ambao waliwahi kuvamiwa na majambazi sugu ndani ya miaka kumi iliyopita na majambazi hao wakapatikana na kuhukumiwa vifungo. Kompyuta ikamtii kwa kumpa jina la Ladhu H. Ladhu. Kumbukumbu hizo zikamwonyesha kuwa Mtanzania huyo mwenye asili ya Kiasia alivamiwa na jambazi aliyeitwa Kamba Kiroboto miaka saba iliyopita. Akashusha pumzi ndefu na kuendelea kusoma taarifa kuhusu huyo Kamba Kiroboto huku simu sikioni ikiendelea kuita tu bila ya kupokewa huko alikopiga.



    Hatimaye akaachana na kumbukumbu alizokuwa akizisoma. Akapiga tena simu hiyo huku akishangaa iweje haipokewi? Hata hivyo, safari hii iliita kidogo tu na kupokewa. Dakika chache zilizofuata alikuwa akizungumza na James Ntilampa, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay aliyekuwa mwendesha mashtaka wakati Kamba akikabiliwa na kesi ya kumvamia Mwasia huyo.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Katika mazungumzo yao, James Ntilampa akathibitisha kuwa Kamba alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela na kuongeza kuwa kilichochangia zaidi kumtia hatiani ni ushahidi wa mwanaye Ladhu pamoja na Wahindi wengine kadhaa ambao hakukumbuka idadi yao. Pia alisema kuwa uzito mkubwa ulimwelemea Kamba kwa kuwa mzee Ladhu H. Ladhu aliichagua picha ya Kamba kati ya picha kadhaa alizoonyeshwa pale kituoni.



    Kwa maelezo hayo, Inspekta Maliyatabu hakuhangaika kuzungumza zaidi na James Ntilampa. Sasa akaamua kupanga hatua moja baada ya nyingine katika kulishughulikia suala hilo.



    Ndiyo, aliamua kupanga jinsi ya kuianza operesheni ya kudhibiti utekelezaji wa maazimio ya Kamba, maazimio ambayo ameambiwa na huyu Baba Semeni. Hata hivyo, hakupata hata dakika moja ya kufikiri, mara ikamjia taarifa nzito, taarifa ya kutisha na kusikitisha.



    Watu watatu wameuawa!



    **********



    DAMU ya Kamba ilikuwa ikichemka. Tayari alishaua, akaua na kuua tena ndani ya dakika tano tu! Na mauaji hayo kayafanya ndani ya jengo moja! Sasa alirejea katika ile hali aliyokuwa nayo miaka mingi iliyopita, hali ya kuchukulia kuwa kuua mtu ni moja ya kanuni zake za kulinda masilahi na maisha yake.



    Hivyo, pindi alipotoka nyumbani kwake, alikwenda katika kituo cha teksi cha Mkwajuni bila ya kutumia uchochoro wowote. Alijua jinsi ya kukabiliana na kashkash zozote kama zingezuka. Aliwajua wakazi wengi wa Dar kuwa ni watu wanaoyapenda maisha, waoga wa kufa! Ni kiasi tu cha kuiweka wazi bastola mkononi mwake, itatosha! Kila mtu atatafuta pa kujificha!



    Aidha, alitambua kuwa wakati mwingine huwa kuna askari ambao wanakuwa kwenye doria muda wote na mahali popote. Hata hapo Mkwajuni alijua kuwa huenda kukawa na askari wa doria. Hata hivyo, hilo halikumtia jakamoyo. Japo alitambua kuwa msako mkali utakuwa umeshaanza, kwa upande wake hakuwa na wasiwasi; aliamini kuwa hatasakwa na askari wasiozidi kumi. Askari kumi, kwake walikuwa ni sawa na askari wawili; angepambana nao.



    Na kwa kuamini hivyo, ndiyo maana alitembea kwa kujiamini hadi akafika kwenye kituo cha teksi cha Mkwajuni, ambako alikodi teksi kwa ajili ya kwenda Mtaa wa Ursino eneo la Mikocheni.



    Ilikuwa ni saa 4 asubuhi.



    **********



    “WAMEUAWA watu watatu?!” Inspekta Maliyatabu alihoji huku akimkodolea macho Konstebo Katapanga wa Kituo Kidogo cha Polisi cha Kisutu.



    “Ndiyo, afande.”



    “Mtaa gani?”



    “Mosque.”



    “Kwa ajali au?”



    “S’o kwa ajali, afande.”



    “Ila?”



    “Kwa risasi na kisu!”



    “Sababu ya mauaji? Uporaji?”



    “Hapana, afande,” Katapanga alijibu kwa utulivu. “Mazingira yanaonyesha kuwa muuaji alikuwa…”



    “Keti!” Inspekta alifoka. “Keti unieleze kwa tuo. Maana’ake sikuelewi-elewi!”



    Katapanga alitii amri na kumsimulia Inspekta Maliyatabu kwa tuo mkasa wote kulingana na hali halisi aliyoshuhudia pamoja na taarifa za waliokuwa jirani na eneo la tukio.



    “Una hakika aliyeuawa ni mzee Ladhu?” Maliyatabu alimuuliza Katapanga.



    “Ndiyo, afande.”



    Inspekta Maliyatabu aliachia tabasamu dhaifu, tabasamu ambalo halikutoa taswira yoyote ya mtu mwenye furaha. Baada ya kulikata tabasamu hilo, alitamka kwa sauti nzito, sauti iliyotoka kwa kukereketa na iliyosheheni hasira: “Ni Kamba Kiroboto!”



    *********



    TEKSI ilipoiacha Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na kuuvaa Mtaa wa Ursino, ndipo Kamba alipotambua kuwa hakuwa akiijua nyumba ya mtu aliyemfuata. Hivyo, aliamua kuachana na teksi hiyo. Akateremka na kutembea taratibu akimsogelea mvulana aliyekuwa akicheza kando ya barabara. Akamgusa bega na kuuliza, “Wapi kuna duka hapa jirani?”



    “Paleeee!” mvulana huyo alijibu huku akionesha kwa kidole. Kisha papohapo akaongeza, “Nikupeleke?”



    “Ndiyo, mtoto mzuri,” Kamba alijibu huku akimpigapiga begani. Aliifurahia nafasi hiyo na kuiona kuwa ni hatua moja kubwa katika mkakati wake. Njiani akamuuliza mtoto huyo kuhusu Hakimu John Mwakipesile.



    “Hakimu?! Unataka kupajua kwa hakimu?” mtoto huyo aliuliza huku akisita kutembea. Akamtazama Kamba kwa namna ya kumshangaa. Kisha akaongeza, “Unasema baba yake na Solomoni”Kamba akawaza haraka na kujibu, “Ndiyo, mtoto mzuri. Ukinionyesha tu kuna soda yako. Nd’o wapi?”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mtoto huyo akageuka nyuma na kunyoosha mkono. “Unaiona nyumba ile nyekundu?”



    “Ndiyo.”



    “Basi baada ya hiyo, ile inayofuata nd’o ya hakimu. Ile yenye geti jeusi.”



    Safari ya kwenda dukani ikafa. Mtoto akapata shilingi 1,000. Urafiki wao uliozaliwa dakika chache zilizopita, ukafa ghafla. Kila mmoja akashika hamsini zake.



    **********



    SI tu kwamba historia ya Kamba ilikuwa ni ya kutisha bali pia ilikuwa ni historia yenye kuweza kuutikisa moyo wa jasiri yeyote aliyejitolea kupambana naye. Ni hilo lililomfanya Inspekta Maliyatabu amwite Sajini Kitowela ili ampe nguvu kimawazo na hata kiutendaji. Alimwamini sana Kitowela na hivyo kwa kipindi kama hiki alimhitaji sana kwa ajili ya kutatua tatizo hili lililozuka.



    “Yule s’o binadamu wa kawaida!” Maliyatabu alisema huku akimtazama Sajini Kitowela kwa macho makali. “Ametoka jela juzi tu, na leo kishaua watu watatu! Tena kwa risasi na kisu!”



    “Yote hiyo ni kwa ajili ya kulipa kisasi tu?”



    “Ndivyo inavyoonesha.”



    “Lakini afande,” Kitowela alisema. “Kama kweli atakuwa amefanya hivyo kama hatua ya kulipa kisasi kwa kuhukumiwa jela kimakosa, basi nadhani atakuwa hajafika mwisho wa safari yake.”



    “Kwa nini?”



    “Siyo kwamba hao aliowaua nd’o pekee waliohusika katika kumsotesha jela. Kuna hakimu. Kwa vyovyote kama atamtia machoni hakimu aliyeiendesha kesi ile, hataacha kumtia risasi. Na hata akimwona yeyote aliyetoa ushahidi wa kumkandamiza, atammaliza!”



    Inspekta Maliyatabu alikunja uso na kusonya. Kisha akasema, “N’na wasiwasi kuwa hata maisha ya James Ntilampa yako hatarini.”



    “Kwa vipi?”



    “Alikuwa ni Mwendesha Mashtaka katika kesi ile.”



    Ukimya mfupi ukatawala. Askari hao wakabaki wakitazamana kama waliokosa utatuzi. Kisha, kama aliyezinduliwa usingizini, Kitowela akasema, “Itabidi tumpe taarifa ili achukue tahadhari. Tatizo ni kwamba hata huyo Kamba mwenyewe haijulikani yuko wapi saa hizi. Lakini siyo rahisi baada ya kuua eti akaenda nyumbani kwake kupumzika. Hawezi kuwa bwege kiasi hicho.”



    “Ni kweli,” Maliyatabu aliafiki. Kisha akaonekana kufikiri kidogo kabla hajasema, “Lakini tutambue pia kuwa yule mshenzi ana moyo wa chuma! Anaweza kufika pale kwake kimachale-machale, akatumia dakika mbili, tatu na kuyeyuka!”



    “Na anaishi wapi?” Kitowela aliuliza.



    “Nani anajua? Lakini wakati alipokamatwa alikuwa akiishi Kinondoni. Sasa sijui ni Kinondoni ipi.”



    “Na umelisachi jina lake kwenye kompyuta?”



    “Kilikuwa ni kitu cha kwanza, na ikaonyesha kuwa hakuna document yoyote ya Kamba!”



    Kwa mara nyingine ukimya ukatawala. Kila mmoja akaonekana kuzama mawazoni. Hatimaye Kitowela akashusha pumzi ndefu huku akikikuna kidevu. Akasema, “Nadhani jambo muhimu afande, kwa sasa, ni kumtaarifu James, ajiwekee ulinzi madhubuti huku pia tukihakikisha yule hakimu aliyeisimamia kesi ile naye anapewa ulinzi wa kutosha.”



    “Kuhusu James, sidhani kama atakuwa na tatizo lolote,” Inspekta Maliyatabu alisema. “Yuko fresh. Anaweza kujipa ulinzi yeye mwenyewe. Ni nusu komando yule. Ila kama ulivyosema, ni muhimu kumtahadharisha.”



    “Na hakimu aliyeishika kesi ile ni nani?” Kitowela aliuliza.



    “Mheshimiwa John Mwakipesile.”



    “Tangu wakati ule hadi leo yuko hapohapo Mahakama ya Kisutu?”



    “Hajahamishwa. Cha kufanya ni kumwekea ulinzi wa siri. Namjua vizuri yule mzee. Ana presha. Kama ataijua ishu hii mapema na kwa mapana yake, linaweza kuwa ni kosa kubwa! Tutampoteza!”





    SAJINI Kitowela alitikisa kichwa akionesha ishara ya kuafiki. Kisha: “Na ni vizuri ulinzi huo uanzie nyumbani kwake na kumfuata popote atakapokuwa.”



    “Yeah,” Inspekta alikubali. “Ni wazo zuri. Na kazi hiyo naamini inaweza kufanywa na Makela kwa ufanisi.”



    **********

    KAMBA alipoifikia nyumba ya Hakimu John Mwakipesile, aligonga geti mara mbili huku akiomba kimoyomoyo amkute mlengwa. Haukupita muda mrefu mara geti likafunguliwa. Mbele yake alisimama mwanamke mwenye tambo kubwa, ambaye kwa makadirio ya haraka alikuwa na umri wa kati ya miaka thelathini na mitano hadi arobaini.



    “Karibu,” Kamba alikaribishwa.



    Akaingia hadi sebuleni kama mgeni wa kawaida, mwenye shida ya kawaida na labda akitaka kuonana na mheshimiwa hakimu kwa maongezi ya kawaida. Baada ya kujitambulisha kama mtu mwenye kesi iliyoshikwa na hakimu huyo ndipo na mwanamke huyo naye alipojitambulisha kuwa ni mkewe hakimu.



    Dakika tano baadaye Kamba alinyanyuka kitini tayari kwa kuondoka. Na hiyo ni baada ya kuambiwa kuwa hakimu John Mwakipesile hakuwapo hapo nyumbani wakati huo bali alikuwa kwenye mizunguko yake ya kawaida. Akavuta hatua mbili akielekea mlangoni lakini akasita na kumgeukia tena huyo mama. “Unadhani anaweza kurejea saa ngapi?”



    “Kwa kweli siwezi kujua,” mkewe hakimu alijibu kwa lafudhi ya Kinyakyusa. “Lakini mara nyingi haizidi saa tano.”



    “Saa tano mchana huu?”



    “Hapana. Saa tano usiku,” mwanamke huyo alijibu huku sasa akimtazama Kamba kwa makini zaidi. Akaongeza, “Kwani una shida isiyoweza kusubiri kesho?”



    Huku Kamba akiachia tabasamu dhaifu, la kirafiki zaidi, alijibu, “Ni kama vile unajua yaliyo moyoni mwangu.”



    Mwanamke yule alicheka kidogo. “Ok, naweza kumpigia simu akaja kama wito huo utampa uhakika wa kumnyooshea njia ya kwenda kwenye kiti kirefu jioni. Nimpigie?”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hapana,” Kamba alimzuia. “Kwa sasa sijajiweka sawa. Lakini hilo ni tatizo dogo sana kwangu. Kwa kuwa ni mimi ndiye mwenye shida, najua nitafanya nini afurahi leo hii.”



    “Vipi una kesi?” mkewe hakimu alimuuliza.



    “Tena ni kesi kubwa, shemeji,” Kamba alijibu haraka huku akiirejesha kumbukumbu ya ile kesi iliyomkaabili, akituhumiwa kuvamia duka la Mwasia, Ladhu H. Ladhu na kupora mamilioni ya fedha.



    Akashangazwa na haya maneno ya huyu mkewe hakimu, maneno yaliyodhihirisha bayana kuwa hakimu huyo hakujali kufuata kanuni na sheria katika uwajibikaji wa majukumu yake bali pesa zilipewa kipaumbele. Mbele ya pesa alifanya lolote hata kama ni katika kupinda sheria.



    Ni hapo ndipo alipoamini kuwa hata uchaguzi wa Ladhu kwa zile picha ulikuwa wa kubahatisha. Alijichanganya pale alipokabidhiwa picha lukuki akitakiwa kumtambua mhusika wa tukio lile. Na kwa namna Jitu alivyosema, huenda ni kweli mzee huyo wa Kihindi alijikuta akichanganyikiwa zaidi pale aliopozishika picha za Jitu na yake. Huenda kichwa chake kilitunza kumbukumbu kwa mbali, kumbukumbu ya sura ya mtu aliyevamia dukani kwake hivyo kidole chake cha shahada kilipoangukia kwenye picha mojawapo, ulimi ukaropoka.



    Ndiyo, Ladhu alidai kuwa yeye, Kamba ndiye aliyevamia dukani, lakini mbona mahakama haikumtendea haki kwa kumruhusu ajitetee? Hata dhamana alinyimwa kwa kile kilichodaiwa na mwendesha mashtaka kuwa dhamana inaweza kuvuruga mwenendo wa kesi hiyo. Akasota rumande!



    Kesi ikawa ikiunguruma kila baada ya wiki kadhaa. Wakati wote huo ni yeye mwenyewe ndiye aliyekuwa akisimama kizimbani na kujitetea. Hakutumia wakili. Ndiyo, hakutumia wakili kwa kuwa aliamini kuwa hakuhusika na lile kosa. Ingawa sababu nyingine iliyomfanya ajitetee kizimbani peke yake ni kutokuwa na pesa za kutosha kumgharimia wakili, hata hivyo aliamini kuwa utetezi wake ambao ni kweli tupu utatosha kumaliza tatizo hilo na ataachiwa huru!

    Kilichokuja kutokea ni kile ambacho hakukitarajia!



    Hii haikuwa kumbukumbu nzuri hata kidogo. Sasa alijisikia kupandwa na hasira maradufu. Papohapo akaugeukia tena mlango na kukishika kitasa kisha akauvuta kidogo, lakini kabla hajatoka akamgeukia tena mkewe hakimu na kumuuliza, “Mheshimiwa huwa anapendelea kupatia wapi bia?”



    “Kinondoni ‘A,’” mkewe hakimu alijibu. “Kuna baa moja maarufu inaitwa Machopi. Ukimuuliza mtu yeyote wa Kinondoni anaijua, hata kama hanywi pombe. Karibu kila siku anakuwa pale jioni, sasa sijui kama ni kwa ajili ya bia tu au kuna mwenzangu…”



    Kamba alicheka kidogo na kusema, “Usiwe na mawazo hayo shemeji. Wanaume huwa tunapenda kuliwaza akili kwa kwenda sehemu kupata moja, mbili baada ya majukumu mazito ya kutwa nzima. Na kuna watu wengine huwa hawapendi kuhamahama, leo anakunywa hapa kesho pale.”



    “Ni kweli lakini sio wote wenye tabia hiyo unayosema.”



    “Ndiyo, sio wote, lakini wengi tuko ivo.”



    Mkewe hakimu akacheka.



    Kamba akaamua kuyakata mazungumzo. Alichokihitaji ameshakipata, hakuwa na sababu ya kuendelea kuzubaa hapo. Akamwambia,“Asante, shemeji, ngoja nikuache. Nitamtafuta.”



    “Haya karibu tena.”



    Kamba akaanza kutoka lakini akasita. Aligundua kuwa kungekuwa na ugumu wa kuonana na Mheshimiwa Hakimu John Mwakipesile. Hata kama atakwenda hapo Machopi Bar, bado hatakuwa na hakika ya asilimia mia moja kuwa hakimu huyo atafika. Kwani kwa kuwa amezoea kufika katika baa hiyo ndiyo ichukuliwe kuwa kawaida kwake imegeuka sheria? Kwamba, iwe, isiwe, awe anaumwa au haumwi, lazima atie mguu hapo?



    Hapana, hakukubaliana na hilo, na kwa namna nyingine ni kwamba pia hakukubaliana sana na mkewe hakimu. Kwa hali hiyo, aliamua kuomba namba ya simu ya hakimu. Alipopewa, akajiona kapiga hatua moja kubwa zaidi katika utekelezaji wa jukumu lililokuwa mbele yake.



    “Asante sana, shemeji,” alisema huku akimtazama mkewe hakimu kwa uso uliochangamka. Akaongeza, “Nadhani sasa kazi itakuwa nyepesi zaidi.”



    “Unaona, eeh?” mkewe hakimu alidakia huku akiachia tabasamu kubwa. “Basi poa, na umwambie aniletee na mimi bia walao mbili. S’o namuunganishia ishu lakini hanipi asilimia yangu.”



    “Ni kweli, lazima nimsisitize akuletee na wewe mgawo wako shemeji,” Kamba alisema huku moyoni akicheka kwa hasira na kujisemea laiti ungelijua…



    **********



    ASKARI waliopewa jukumu la kumpatia ulinzi madhubuti Hakimu John Mwakipesile walifika nyumbani kwa hakimu huyo nusu saa tu baada ya kuanza kazi hiyo. Hapo wakamkuta mkewe hakimu ambaye aliwaambia kuwa kila atokapo asubuhi basi rudi yake ni usiku.



    Kwa taarifa hiyo askari hao wakaiona kazi iliyo mbele yao ni kubwa na ngumu kuliko ilivyo.



    “Unaweza kutusaidia namba yake ya simu?” Makela alimwambia mkewe hakimu.



    “Hee sasa imekuwa kazi, kila anayekuja anaomba namba ya simu. Kwani nyie mmetoka wapi?”



    Makela alikausha uso na kupata jibu la papohapo japo halikuwa la kweli. “Tuna kesi mama.”



    “Mna kesi? Sasa kama mna kesi hapa ndo mahakamani?”



    “Hapana, siyo mahakamani. Lakini tuliwahi kuongea naye akatuambia tuje ili tumalizie maongezi yetu hapa.”



    Mkewe hakimu aliguna na kuwatazama askari hao kwa makini zaidi kisha akasema, “Leo imekuwa ni siku ya kipekee. Muda huuhuu katoka tena mtu hapa akitaka namba yake, naye anasema ana kesi ambayo mzee ameishika. Siku zote alipokuwa likizo haikuwahi kutokea hivi, sasa hata likizo haijaisha tayari mmeshaanza kumsumbua mume wangu, nyie bwana!”



    Makela akacheka kimzaha na kusema, “Usijali mama. Huenda kumwona kwetu na maongezi yetu yakazaa matunda mema au hutaki iwe hivyo?”



    “Aah, nani asiyetaka neema hapa duniani wanangu? Dunia ya leo si ya kulemaa…vipi mko vizuri nini?”



    “Tena kwa sana, mama,” Makela alijibu haraka huku akimtazama mwenzake.



    Mkewe hakimu hakuwa na hiyana, akawapatia namba ya simu ya Hakimu John Mwakipesile. Makela naye hakuchelewa, papohapo akampigia simu hakimu na kama alivyotarajia, hakupata majibu mabaya baada ya kujitambulisha kuwa yeye ana kesi ambayo hakimu huyo ameishika. “Kama unaweza njoo Kinondoni jioni, kuna baa moja maarufu, Machopi. Fanya saa kumi na mbili au saa moja.”



    Simu ilipokatwa, Makela alimgeukia mkewe hakimu na kumuuliza, Kuna mtu yeyote mwingine aliyefika hapa na kumuuliza mheshimiwa?”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndiyo. Tena ni kama robo saa tu imepita.”



    Askari hao wakashtuka japo walihakikisha kuwa mshtuko huo hauwi bayana machoni mwa mkewe hakimu. “Yukoje?” Makela aliuliza haraka.



    “Mrefu na yuko kibaunsa-baunsa. Mweusi.”



    Martin, yule askari mwenzake na Makela akatoa picha moja na kumpatia mkewe hakimu huku akimuuliza, “Anafanana na huyu?”



    Mkewe hakimu alitwaa picha ile na kuitazama kwa makini kisha akasema, “Anafanana vipi wakati nd’o huyuhuyu?”



    “Una hakika?” Makela alimbana.



    “Ndiyooo! Kwani vipi, ni mwenzenu?”



    Makela akawahi kujibu, “Hujakosea, mama. Ni mwenzetu. Huenda alitangulia akitarajia kutukuta hapa.”



    “Basi na yeye alisema ivoivo ka’nyie. Eti ana kesi, na nikampa namba ya simu ya mzee.”



    “Ni kweli,” Makela alijibu “Na kesi hiyo inatuhusu wote. Kwani hakumkuta mheshimiwa?”



    “Hata yeye hakumkuta, ila nilimpa namba ya simu.”



    “Akampigia?”



    Mkewe hakimu akapandisha mabega juu na kuyashusha akishiria kukataa. “Kachukua tu namba na kuondoka zake.”



    Askari hao walitazamana na kupeana ishara ya kutoka. Makela akamgeukia mama huyo na kumwambia, “Asante sana mama. Tunatoka.”



    *****



    Kuazimia kutenda jambo na kutafakari matokeo ya utendaji ni moja ya kanuni alizojiwekea Kamba kabla ya utekelezaji wa jambo lolote zito.



    Wakati alipotoka nyumbani kwa Mheshimiwa Hakimu John Mwakipesile alikuwa akitambua fika kuwa kazi aliyoifanya katika Mtaa wa Mosque ilishayafikia masikio ya Jeshi la Polisi na operesheni ya kumsaka itakuwa imeshaanza.



    Alitambua hivyo, lakini hakuwa na wasiwasi japo alikumbuka kuwa wakati akiliacha jengo la Ladhu H. Ladhu macho ya wengi yalimtazama kwa mshangao wenye mchanganyiko wa maswali yaliyoganda vichwani mwao.



    Ndiyo, hakuwa na wasiwasi. Wasiwasi wa nini wakati huyu hakuwa yule Kamba wa miaka kadhaa iliyopita, Kamba ambaye alishaamua kuiuza bastola yake kwa bei rahisi na kukitupa kisu chooni?



    Yule Kamba ‘mtakatifu’ siye huyu tena! Huyu ambaye kwa siku hii tu, tena hata hazijapita saa sita tayari kishazing’oa roho za watu watatu!



    Wakati huu akiuacha Mtaa wa Ursino na kushika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, alisita na kusimama akiwaza jambo lililomjia ghafla kichwani, jambo ambalo alilazimika kutafakari matokeo ya utekelezaji wake kabla ya kulitekeleza. Kama ndoto, ilimjia ile kumbukumbu ya kesi yake iliyoisha kwa kutupwa jela miaka saba.

    Tofauti na juzi alipokuwa akimtamkia bayana mkewe, mama Safi kuwa alidhamiria kuwawinda Ladhu, Hassanali na hakimu aliyeitolea hukumu kesi yake, adhuhuri hii kumbukumbu nyingine ilimjia.



    Alikumbuka kuwa siku alipozungumza na Jitu Kobelo alimtamkia bayana kuhusu dhamira yake ya kuonana na wale wote waliohusika na kesi yake iliyomtupa Keko miaka saba. Katika mazungumzo hayo alimtaja pia mtu ambaye juzi hakukumbuka kumtaja mbele ya mama Safi. Mtu huyo ni aliyekuwa Mwendesha Mashtaka, James Ntilampa.



    Ndiyo, juzi alimsahau lakini hata jana alipokuwa akizunguka mjini pia hakumkumbuka! Na hata asubuhi ya leo alipoianza operesheni yake jina la James Ntilampa halikuwa mawazoni mwake. Lakini akiwa hapo Barabara ya Ali Hassan Mwinyi ndipo alipomkumbuka James Ntilampa. Na akayakumbuka yale maneno ambayo Jitu alimwambia akimaanisha kuhusu hali ya James Ntilampa. Sasa hivi kaula. Ni Mkuu wa Kituo cha Oysterbay.



    Kutoka hapo alipokuwa hadi Kituo cha Polisi cha Oysterbay alijua kuwa angetumia chini ya dakika kumi na labda angemkuta James au asingemkuta. Kilichomsumbua akilini wakati huo ni juu ya hatua ambayo ingefuata kama angemkuta. Na ni hilo lililomfanya aduwae hapo barabarani akiifuata ile kanuni ya kutafakari matokeo ya jambo lolote zito kabla hajalitekeleza.



    Wakati wa ile kesi, James aliishauri mahakama kumnyima dhamana akidai kuwa dhamana ingechangia kwa kiwango kikubwa kuvuruga mwenendo wa kesi nzima. Kamba alilikumbuka hilo akiwa hapohapo barabarani.



    Aliponyimwa dhamana alijikuta akikumbwa na maradhi ya ngozi huko rumande, maradhi ambayo aliamini kuwa yalisababishwa na hatua ya kunyimwa dhamana na hivyo kuwa miongoni mwa mahabusu waliorundikana rumande katika mazingira yasiyoridhisha.



    James alishakuwa mbaya wake, lakini sasa huyu siye yule James mwendesha mashtaka, hapana. Huyu ni mkuu wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay. Kumwingia pale kituoni ulihitajika ujasiri, ilihitajika mbinu na kwa vyovyote vile ilihitajika silaha nzito ili aamue moja, kuua au kufa!



    Kumfuata mtu wa aina ile, mwenye wadhifa mkubwa kiasi kile, kwenye kituo kikubwa cha polisi kama kile, ilikuwa ni sawa na kujitoa mhanga. Na Kamba aliamua kujitoa mhanga! Hakujali kufa, alijali kufa kabla hajatimiza malengo yake.



    Taratibu akaanza kuvuta hatua akielekea katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay akiwa kama mtu asiye na jukumu maalumu linalompeleka huko. Dakika kama ishirini hivi baadaye alikuwa kituoni hapo. Akawakuta askari wawili wa kike nje wakizungumza. Akawafuata na kuwasalimia kisha akauliza kama amemkuta mkuu wa kituo.



    Askari wale wakatazamana kisha mmoja akamuuliza mwenzake, “Si nasikia afande kaenda kwake eti mwanae anaumwa?”



    Mwenzake akatikisa kichwa akionesha kukubali. Kisha akamwambia Kamba, “Kaka, afande James hayupo. Una shida ya kiofisi au binafsi?”



    “Yote pamoja. Anaishi mbali? Nadhani si vibaya hata nikienda huko kwake nikazungumza naye.”



    “Siyo mbali,” askari huyo alimjibu na kumwelekeza nyumbani kwa James Ntilampa.



    *****



    James Ntilampa alilazimika kuikimbia ofisi baada ya kupigiwa simu na mkewe kuwa mtoto wao mwenye umri wa mwaka mmoja alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kuhara. Alimkuta mkewe akihangaika kumhudumia mtoto ambaye kwa mwonekano wa haraka alionyesha kuishiwa nguvu.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Vipi?” James alimuuliza mkewe huku akionekana kuchanganyikiwa.



    “Kama unavyomwona,” mkewe alimjibu bila ya kumtazama.

    Mara James akakumbuka. Akamuuliza, “Umeshampa ile dawa yake ambayo tulipewa wakati tatizo kama hili lilipotokea mwezi jana?”



    Mkewe alionekana kuzinduka. “Aaaa…nilisahau. Iko kwenye droo! Nisaidie basi kuniletea.”



    James aliharakisha kuifuata dawa hiyo na kumletea mkewe.

    Sara alikuwa mtoto wa kwanza wa James tangu alipofunga ndoa na Martha kiasi cha miaka mitatu iliyopita. Kuchelewa kupata mtoto kulitokana na tatizo lililokuja kugundulika kwa madaktari bingwa baada ya kumpima mkewe James. Na ilipotokea Martha akapata ujauzito na hatimaye kujifungua salama mtoto huyo, madaktari walimwambia kuwa atalazimika kufungwa uzazi kwa usalama wake. Hivyo kwa namna moja au nyingine walimwona Sara kama dhahabu na kumtunza kama mboni ya jicho.



    Nusu saa baada ya kumpatia mtoto dawa hiyo, hali yake ikaanza kuridhisha. Hata macho yakaanza kupata nuru. James akayakumbuka maneno aliyoambiwa na madaktari waliyempa dawa hiyo: Hii dawa inafanya kazi vizuri sana kwa watoto wenye matatizo ya kuhara. Mpe mwanao kijiko kimoja kidogo na baada ya nusu saa atakuwa katika hali njema.



    Na ndivyo ilivyoonekana sasa. Utulivu ukiwa umerejea akilini mwa James, aliketi kitini na kushusha pumzi ndefu. Akawaza kama kuna umuhimu wa kuwahi kurudi ofisini lakini akakumbuka kuwa hakuwa na majukumu mengi ya kumfanya arudi ofisini muda huo. Akatwaa rimoti ya televisheni na kuanza kuseti stesheni hii na ile.



    *****



    Wakati Kamba alipokuwa akiisogelea nyumba ya James Ntilampa, kumbukumbu ya kesi yake iliyomtupa jela miaka saba ilimrudia kwa kasi kubwa. Kumbukumbu hiyo ikaiunda hasira na kujikuta akiifuta kichwani ile kanuni ya kutafakari matokeo kabla ya kutekeleza azimio lolote. Kilichofuata baada ya kufutika kwa kanuni hiyo, ikawa ni kuchukua uamuzi wa kutekeleza lile alilolidhamiria, tena bila ya kuchelewa.



    Alipoufikia mlango wa mbele alisita kidogo na kuangaza kama kuna sehemu ya kubonyeza king’ora kwa minajili ya kufunguliwa. Hapana. Ulikuwa ni mlango wa kawaida kama ilivyo milango mingine ya nyumba za kawaida. Akaamua kuugusa na kuusukuma kidogo badala ya kutumia ustaarabu wa kubisha hodi. Ukasukumika.



    Akaingia taratibu na kujikuta katika sebule pana na maridadi. Mbele yake, James Ntilampa alikuwa kaketi sofani na Kamba hakuhitaji kukisumbua kichwa chake kumkumbuka. Huyu hakuwa mtu ambaye Kamba angeweza kumsahau. Atamsahau vipi wakati ni huyuhuyu ambaye alitoa shinikizo mahakamani kuwa kitendo cha mahakama kumpa dhamana kingeweza kuharibu mwenendo mzima wa kesi?



    James alishangazwa na ugeni huu wa ghafla na mgeni mwenyewe anaingia bila kubisha hodi! Ni ustaarabu wa wapi huu? alijiuliza kwa hasira huku akimtazama mgeni huyo kwa mshangao, bila ya kumbukumbu kuwa ni wapi aliwahi kumwona.



    Kamba aliurudisha mlango taratibu huku akiendelea kumtazama James bila kuonesha wasiwasi wowote, zaidi, macho yake yalikuwa na kitu kingine ambacho uaskari wa James haukuchelewa kukibaini. Hasira!



    Ndiyo, Kamba alikuwa akimtazama James kwa namna ya mtu mwenye hasira. Hakuwa na kumbukumbu yoyote kuwa huyu mtu waliwahi kuonana au la na kama kuna jambo lolote lililomfanya amjie hapa nyumbani kwa mfumo huu wa ajabu.





    Huku bado akiwa akili yake haijatulia kutokana na maradhi ya mwanaye yaliyomtoa ofisini bila ya kutarajia, na kutokana na kukwazwa na jinsi mtu huyu alivyoingia bila ya kutumia ustaarabu uliozoeleka kwa wabantu hususan Watanzania labda hata kwa watu wa mataifa mengine, alijikuta akipandwa na hasira na kumbwatukia, “Unataka nini? Na wewe ni nani?”



    Kamba aliachia tabasamu dogo ambalo hata hivyo James aliligundua papohapo kuwa halikuwa na uhalisia wowote. Ni tabasamu lilionyesha hasira badala ya amani. “Unaweza kuwa umenisahau?” hatimaye alimuuliza.



    Lilikuwa ni swali ambalo James hakulitofautisha na tusi. Lilimuudhi, likamkera. Hata hivyo, papohapo akajiuliza huyu mtu kwa nini ana kiburi cha kiwango hiki? Kuna nini kilichojificha nyuma ya pazia? Maswali hayo yakamfanya aitulize kidogo jazba katika ulimi wake na kuwa makini akitaka kuijua sababu ya ujio wa mtu huyu.



    “Afande, umeshanisahau?” Kamba alilirudia swali hilo, safari hii akivuta hatua kuingia zaidi katika sebule hiyo pana. “Lakini siyo ajabu, siyo ajabu sana. Miaka saba ni mingi, mjomba.”



    James alishindwa kuvumilia. Akasimama na kuvuta hatua mbili, akawa amemfikia Kamba. Wakiwa na urefu ulioshabihiana, walijikuta wakitazama uso kwa uso mithili ya majogoo yaliyojiandaa kwa pambano. Mara James akamnyooshea kidole baada ya kumfikia. “Toka! Kama una shida na mimi nifuate ofisini! Toka! Nahesabu moja mpaka tatu, kama utakuwa haujapotea humu ndani…”



    “Tulia…tulia afande…jazba ya nini?” Kamba aliinua mkono wa kulia na kumnyooshea kiganja kwa namna ya kusihi, ilhali macho yake yakionesha kutojali vitisho vya James.



    Kimya kifupi kilipita huku wakitazamana. Kisha, James akihema kwa nguvu kama mbogo mwenye hasira, aligeuka na kuelekea ndani ya chumba kimojawapo, lakini kabla hajafika, aligeuka akidhamiria kumpa karipio na amri ya mwisho Kamba, kabla kutekeleza jambo lolote lingine alilopanga akilini mwake.



    Hata hivyo, hakuweza kufanya chochote kile pale tu alipokutanisha macho na Kamba! Bastola ilikuwa ikimtazama!



    “Usithubutu kusogeza hata hatua nyingine moja, wala usithubutu hata kugeuka nyani wee…na una bahati, nilitaka nikumalizie mgongoni wakati unakwenda huko msalani unakopaita chumbani mwako!” Kamba alifoka kwa sauti nzito na ya chini lakini ikiwa haitofautiani na radi masikioni mwa James.



    James alijiona kama yuko katika sayari nyingine! Akaduwaa na kumkodolea macho Kamba kama asiyeamini akionacho.



    Akitumia ishara kwa bastola hiyo, Kamba alikuwa akimwamuru kurudi kitini, amri ambayo James alilazimika kuitekeleza bila kuleta ubishi wa aina yoyote. Alifanya hivyo akihofia kuwa huenda mtu huyo akachukua uamuzi wowote ambao utaweza kumwondolea uhai, hivyo, aliamua kutii huku akifikiria njia ya kujiokoa na kumtia mbaroni.



    Mara mlango wa chumba cha kulala ukafunguliwa. Mkewe James akatokea huku kambeba mtoto wao, Sara. Akashtuka, akataka kupiga yowe na kurudi chumbani pale alipomwona Kamba kamwelekezea James bastola.



    “Tulia hapohapo…usirudi nyuma!” amri ilipenya masikioni mwake na kumvunja nguvu ya kufanya chochote.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Njoo uketi hapa chini!” amri nyingine!



    “Na wewe keti hapo,” James aliamriwa aketi chini lakini mbali na mkewe.



    Hakukuwa na aliyekuwa na uwezo wa kubishana na amri aliyopewa, na hapo ndipo Kamba alipoanza kuzunguka huku na kule kwa madaha, tabasamu la uchungu likizidi kujitokeza usoni pake.



    “Bwana James…James Ntilampa…! Mkuu wa kituo kikubwa saaaaaana cha Polisi cha Oysterbay! Hahahahaaaa…Unaikumbuka kesi ya kuvamiwa kwa duka la Mhindi, Ladhu Hassanali Ladhu kiasi cha miaka saba iliyopita?” hatimaye Kamba alimuuliza James huku akiwa ameukita mguu mmoja kwenye sofa na kuuegemeza mkono wa kushoto, akawa kama aliyewainamia James na mkewe japo walikuwa umbali wa hatua kama tano hivi. Alikuwa katika utulivu wa majidai.



    Sasa James aliiona dunia ikizunguka! Alikumbuka kuwa kiasi cha saa moja iliyopita alikuwa akizungumza na Inspekta Maliyatabu wa Kituo Kikuu kuhusu jambazi mkongwe aliyeitwa Kamba Kiroboto. Lakini Maliyatabu alipomuuliza hakumwambia kuwa mtu huyo yuko huru na kwamba kuna mpango wowote aliopanga kuhusu wale waliohusika na kesi yake.



    Alikumbuka kuwa Maliyatabu alimuuliza tu kuhusu ukweli kuhusu uvamizi wa Mwasia Ladhu Hassanali Ladhu na kwamba ni nani aliyetuhumiwa zaidi kuhusu uvamizi huo wa miaka saba iliyopita.



    Kwa jumla Maliyatabu hakuwa muwazi kuwa kuna tuhuma zinazomhusu Kamba kutokana na mauaji yaliyotokea asubuhi hiyo yakiwahusu Ladhu, mwanaye na mlinzi wao. Hivyo baada ya mazungumzo yao, James hakuchukulia kama ni suala lililokuwa likitokota mekoni. Alilisahau palepale!



    **********



    KAMA alivyofanya dakika chache kabla ya kuwazamishia risasi Ladhu na mwanaye, Hassanali sasa pia alilazimka kumtamkia James Ntilampa kile ambacho James alikifanya kikiwa ni mbali sana na ubinadamu japo alikuwa akitekeleza majukumu yake, akiwa ni Mwendesha Mashtaka, Inspekta Msaidizi pale Mahakama ya Kisutu.

    Na hakuacha kumthibitishia kuwa aliyehusika na uvamizi ule wa duka alikuwa ni Jitu Kobelo ambaye kwa huruma na utu aliojaaliwa tayari alishampoza kwa pesa lukuki. Ni wema ulioje?



    “Siyo mimi niliyefanya ushenzi ule, James!” alimaka huku akimtazama James kwa macho makali. “Aliyefanya vile mlimwacha atanue na mimi mkanitosa na kunibambikia makosa yasiyo yangu kama ilivyo kawaida yenu mkishakatiwa mkwanja na wenye pesa. Na wale Wahindi walikupa kiasi gani hadi ung’ang’anie kuwa nikipewa dhamana upelelezi au mwenendo wa kesi utavurugika?”



    Kimya!



    “Ulichukua pesa, James!” Kamba aliendelea kubwata. “Ulichukua pesa na leo utazitapika! Nd’o ni’shakwambia ivo!”



    Akili ya James ilisimama kufikiri chochote. Aliduwaa! Kilichokuwa kikitokea hakikutofautiana na ruya ipaayo hewani usiku! Hatimaye aliipata sauti yake. Kwa tabu akasema, “Yalikuwa ni majukumu ya kikazi tu, bwana Kamba. Sikuchukua pesa kwa yeyote kwa minajili ya kukukandamiza…hapa…hapana…!”



    “Yameshapita…uwe umechukua au hukuchukua tayari mimi nimeshaumia miaka saba jela, na nimeumia kwa kuwa wewe ulikataa nisipewe dhamana…huenda ningepewa dhamana ningepata hata wakili wa kunisaidia….lakini ukanifanya nisiwe na mawasiliano hata na dunia ya nje! Hapa unataka nikuelewe vipi? Eti majukumu ya kikazi! Sawa yalikuwa ni majukumu ya kikazi….na leo mimi pia niko kwenye majukumu ya kikazi kwa upande wangu. Sirudi nyuma!”

    Sasa uamuzi wa kutekeleza azimio ukamjia Kamba ghafla. Ndiyo, aliamua kuwa wakati huohuo afanye kile alichopanga kukifanya.



    Lakini pia, sasa alitaka abadili mfumo. Atimize azma yake bila ya kutumia risasi. Hii bastola yake haikuwa na kiwambo maalumu cha kuzuia mlio wa risasi. Kitendo cha kuitumia hapo kingeweza kumletea tatizo kwa kuwa masikio ya wengi yangeupokea mlio wa risasi.



    Atanusurika vipi kama kundi la watu litazuka? Labda atajaribu kulisambaratisha kundi hilo kwa kurusha risasi angani, lakini atatumia risasi ngapi? Bastola hiyo ilisaliwa na risasi tatu tu, na bado alikabiliwa na majukumu mengine mazito yaliyohusu matumizi ya chomb hicho.



    Akaamua kutoitumia bastola. Na wala hakuuhofia uamuzi huo kwa kuwa alijiamini kupita kiasi. Alishawahi kupambana na askari watatu na akawashinda. Atakuwa huyu mmoja, tena ambaye anaonyesha dhahiri kuwa hiki kitambi chake cha bia kimetokana na uvivu wa mazoezi ya viungo?



    Kufumba na kufumbua James alikuwa sakafuni akigaagaa. Ilitokea mithili ya kasi ya umeme; teke moja la mbavuni na lingine la sehemu za siri lilitosha kummaliza nguvu askari huyo. Na Kamba hakumpa muda hata wa kufikiri au kutafakari kilichomkuta, au kutaabishwa na maumivu ya vipigo hivyo. Alimfuata hapo sakafuni na kwa mikono yake iliyokakamaa, alimkamata kichwa, akakizungusha kwa namna ya ajabu, ukafuatia mlio mkali wa kitu kinachoalika.



    Shingo ilivunjika!



    **********

    MHESHIMIWA Hakimu John Mwakipesile alipotoka nyumbani kwake asubuhi, breki ya kwanza ilikuwa ni kwa rafiki yake wa siku nyingi, Wakili wa Kujitegemea, Atupele Antony. Na hakwenda ofisini kwa wakili huyo bila ya sababu maalum, hapana. Sababu alikuwa nayo.



    Kiasi cha miezi miwili iliyopita, mfanyabiashara maarufu alikamatwa na nyara za serikali. Kesi ikatinga mahakamani. Mheshimiwa John Mwakipesile akaishika kesi hiyo. Lakini wakili Atupele Antony ambaye mfanyabiashara huyo alimtumia, aliamini kuwa mchezo utachezwa na utachezeka.



    Hakimu Mwakipesile na wakili Atupele walikuwa marafiki wakubwa, hivyo Atupele alimwona hakimu, wakazungumza ya kuzungumzika. Pesa zikatembea kutoka kwa wakili hadi kwa hakimu.



    Kiporo kikabaki, milioni kumi!





    Katika likizo yake hii ndipo alipoamua kuvifukuzia viporo vyake. Ndipo asubuhi hii alipoamua kumfuata Atupele.

    Walipokutana, mazungumzo yao hayakuwa marefu. Wakili alimwahidi hakimu kuwa siku hiyohiyo atampatia pesa yake iliyosalia.



    Saa ngapi?



    Saa moja usiku.



    Wapi?



    Machopi Bar.



    Ilikuwa ni ahadi iliyoganda kichwani mwa Hakimu Mwakipesile kama luba. Milioni kumi za ahadi aliziona kama vile zimeshakaa katika himaya yake. Ndipo alipoamua kuvuta muda kwa kuzunguka huku na kule na gari lake huku akiburudika na muziki laini wa bendi za zamani.



    **********CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    MKEWE James Ntilampa hakuwa na hali wakati aliposhuhudia mumewe akipokea vipigo viwili vizito na kisha kuuawa kikatili kwa kuvunjwa shingo. Na hata hakuwa na hali pia wakati Kamba alipokuwa akiondoka ndani ya nyumba hiyo kwa madaha, akionekana dhahiri kutokuwa na wasiwasi wowote.



    Dakika takriban mbili hivi baadaye ndipo alipozinduka, akamtupa mtoto sofani na kuanza kupiga yowe kubwa: “Uwiiiii….jamani eeeeeh!.....mamamaaaa….mume wanguuuu! Baba Saraaaaa! Baba Saraaaaa!”



    Masikio ya majirani yaliyanasa mayowe hayo, wakakurupuka na kukimbilia hapo kwa James. Kila mmoja akajali kuwahi kwenye tukio. Hakukuwa na yeyote ambaye alijali kumtazama mtu, pandikizi mwenye upara kichwani, shati jeupe la cadet, suruali ya rangi ya kahawia aina ya jeans na raba nyeupe aliyekuwa akipishana nao huku akitembea kwa mwendo wa kawaida.



    Ndiyo, hakuna aliyemtazama, na labda hata yeyote angemtazama, asingekuwa na shaka naye na kumhusisha na yowe hilo lilitolewa na mke wa James. Kwanza, wakati yowe likipasua anga, yeye alikuwa mbali na nyumba hiyo. Pili, ile tembea yake ilionesha kuwa ni mtu anayejiamini na asiyekuwa na makuu. Hakutembea kwa namna yoyote inayoweza kutoa taswira kuwa kuna jambo lolote kubwa na baya alilolitenda huko nyuma.



    Giza hilo lililotanda mbele yao lilimwondolea Kamba kikwazo chochote ambacho kingeweza kumtokea. Baada ya dakika tano akawa mbali zaidi na eneo hilo, na sasa akawa ametokea eneo la Namanga ambako alikodi teksi na kumwamuru dereva ampeleke katikati ya jiji ilhali akiwa hana sababu yoyote ya kumpeleka huko, na hata hivyo alichokuwa akitaka ni kutoka tu katika eneo hilo na huko mbele ya safari ndipo angejua wapi alipaswa kwenda.



    Teksi ilishika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na wakati dereva akikoleza mwendo, Kamba alitwaa simu na kumpigia Mheshimiwa John Mwakipesile.



    “Haloo,” sauti nzito, sauti ya kimadaraka ilipenya masikioni mwa Kamba kwa usahihi, bila mikwaruzo.



    “Mheshimiwa hakimu, Mwakipesile?”



    “Yeah. Naongea na nani?”



    “Advocate Salum Suleyman.”



    “Salum Suleyman?” hakimu alihoji kwa mshangao uliokuwa dhahiri hata kwenye masikio ya upande wa pili.



    “Ndiyo.”



    Ukimya mfupi ukapita kisha hakimu akamuuliza, “Enhe, sema!”



    “Nahitaji kukuona, mheshimiwa,” Kamba aliunda upole wa kulazimisha. Akaongeza, “Ni issue ya kama nusu saa tu. Nadhani itakuwa nzuri kwetu wote. Jioni utakuwa na nafasi?”



    “Jioni?” hakimu alitamka kwa sauti ya chini, kisha akaikuza kidogo,

    “Ok, njoo Kinondoni. Sidhani kama ninakufahamu lakini tutafahamiana hukohuko.”



    “Sawa, mkuu,” Kamba alijibu kwa upole uleule. “ Kwa hiyo nije wapi, nyumbani?”



    “Unapafahamu nyumbani kwangu?” mshangao wa mbali ulijidhihirisha masikioni mwa Kamba wakati alipoulizwa swali hilo.



    Kamba aliguna kidogo kisha akajibu, “Hapana mkuu. Sipafahamu.”

    “Hata nikikuelekeza si rahisi kunikuta, labda uje saa sita usiku. Machopi Bar unaijua?”



    Kamba alisita tena kisha akajibu, “Ukinielekeza nitafika tu mheshimiwa. Kinondoni mi’ ni mwenyeji sana.”



    “Ukifika Kwa Manyanya, muulize taxi driver yeyote, atakuleta au kukuelekeza. Si una usafiri?”



    “Ndiyo.”



    “Basi hutapata shida. Iko Mtaa wa Kazima. Ni baa maarufu sana. Ukimuuliza mtu yeyote atakuonyesha.”



    Ukimya ukapita kisha Kamba akauliza tena, “Kwa hiyo mkuu nije jioni ya saa ngapi?”



    “Fanya kuanzia saa kumi na mbili.”



    “Ok, mheshimiwa.”



    Akitambua fika kuwa bado kulikuwa na muda mrefu kabla ya kukutana na Mheshimiwa Hakimu John Mwakipesile, Kamba aliamua kwenda sehemu atakayovutia muda hadi jioni ifike. Akamwamuru dereva ampeleke Zanzibar Hotel katikati ya jiji.



    Zanzibar Hotel ikiwa ni kongwe kuliko hoteli nyingine jijini Dar, huwa na wateja tangu alfajiri. Nyama choma, supu na michemsho ya aina mbalimbali huwa ni miongoni mwa vivutio kwa baadhi ya wateja.

    Wanywaji wa bia na vinywaji vingine nao huanza kutia mguu hapo tangu asubuhi huku pia kinadada wanaoinadi miili yao na wanaume-mashoga nao wakiwa wamejipweteka vitini, macho yao yakirandaranda kwa huyu na yule kibiashara zaidi.



    Kamba alipenda uchangamfu wa eneo hilo japo alikerwa na mandhari yake, hususan kwenye suala la usafi. Hapakuwa katika hali iliyostahili kutoa huduma ya vinywaji na vyakula kwa wateja. Kwa jumla haikustahili kupewa leseni halali ya biashara ya baa. Kero nyingine ilikuwa ni hao machangudoa na mashoga ambao kila alipowatazama alihisi kukumbwa na kichefuchefu.



    Hivyo, ili wasimsogelee, hakuonyesha uchangamfu hata kwa kiwango cha chini. Zaidi, alikuwa ni yeye na bia huku sigara ikivutwa mfululizo na macho kayatua kwenye televisheni iliyokuwa ukutani.



    Bia ya kwanza, ya pili hadi nne zikashuka tumboni akiwa hapohapo Zanzibar Hotel na sasa aliona kijua kilikuwa kikishuka mawinguni, hali iliyompa faraja kwa kiasi kikubwa. Hakunywa bia ya tano badala yake aliagiza supu ya mbuzi na kuishambulia kiasi cha kujikuta akipata nguvu mpya, stamina zaidi sanjari na hali ya kujiamini zaidi.

    Akashushia na maji baridi lita nzima. Kijasho chembamba kikamtoka. Akapumzika kwa dakika kumi ndipo akaamua kuliacha eneo hilo.



    **********

    “KINONDONI ‘A’ ,” Kamba alimwambia dereva teksi wakati akifungua mlango wa mbele na kujipweteka kitini.



    Dereva teksi alikuwa mwepesi katika kazi yake. Haraka akaliingiza gari barabarani japo kwa wakati huo, mtaa huo wa Zanaki kulikuwa na watu wengi na magari yaliyosababiosha foleni.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakiwa njiani, Kamba alifumba macho na kujitia kusinzia ilhali alikuwa akiwaza hatua aliyofikia na aliyopaswa kufikia katika utekelezaji wa majukumu yake. Kutokana na foleni kubwa jioni hiyo walijikuta wakiingia Kinondoni baada ya nusu saa.



    Akamwamuru dereva apaki gari mwanzo wa Mtaa wa Kazima. Hakutaka amfikishe mwisho wa safari yake kwa sababu alizozijua mwenyewe. Akatembea taratibu akiifuata Machopi Bar iliyokuwa katikati ya mtaa huo.



    Aliikuta imeshaanza kuchangamka. Baadhi ya wateja walikuwa wakishusha matumboni michemsho, wengine bia, wengine wakicheza pool na wengine wakiwa wamezama kwenye televisheni wakiangalia mpira.



    Wahudumu walikuwa wengi na wachangamfu, wakionekana kuwa wepesi wa kukaribisha wateja. Hata yeye kabla hajajua akae wapi tayari mhudumu wa kike alikuwa mbele yake.



    “Karibu anko,” alikaribishwa.



    Kamba alimtazama mhudumu huyo na kuvutiwa na mavazi yake nadhifu sanjari na tabasamu lake maridhawa lililochanua usoni. Kwa kiasi fulani aligundua kuwa baa hii iko juu maradufu ya Zanzibar Hotel. Usafi, ukaribisho mzuri wa wahudumu na mandhari kwa jumla vilikuwa ni vigezo vilivyotosha kuiweka katika daraja la juu.



    Aliongozwa kwenye meza ambayo kwa wakati huo hakukuwa na mtu mwingine, na ilikuwa sehemu yenye kijigiza cha wastani tofauti na meza nyingine zilizoshushiwa mwangaza mkali wa globu zilizoning’inia hapa na pale katika ukumbi huo. Akaipenda sehemu hiyo. Ndiyo, hakupenda kumulikwa na taa kali wakati huo ambao amekuja hapo kwa lengo maalum.



    Kwa siku hiyo alipaswa kuwa makini kwa kila jambo, na mojawapo ni kukaa sehemu ambayo anaweza kumwona kila mtu na siyo kila mtu amwone yeye.



    Wakati akiketi, alimwagiza bia mhudumu huyo, agizo lililotekelezwa haraka na hivyo kumfanya azidi kuvutiwa na baa hiyo japo hakujua kama atakuja tena mahali hapo kustarehe au ndiyo hiyo itakuwa mara yake ya kwanza na ya mwisho.



    Aliinywa bia hiyo taratibu, akijua kuwa hakupaswa kulewa kwani ulevi halikuwa lengo lake kwa siku hiyo. Akili yake ilikuwa ikiwaza na kuwazua, akijaribu kupanga kila hatua aliyotaka kufikia katika mkakati wake. Mirindimo ya muziki na kelele za wateja waliochangamka kwa vinywaji, huku wengine wakicheza muziki huo, vilisababisha Machopi Bar izidi kuchangamka.



    Ndiyo, watu walichangamka. Ni wengi waliochangamka, wengi sana, siyo wote. Kamba Kiroboto alikuwa tofauti na wale waliochangamka. Japo usoni alilazimisha kuonesha uchangamfu, hata hivyo moyoni alikuwa mtu mwingine kabisa. Hakuwa na amani hata chembe. Hata pale watu wawili walipoungana naye katika meza hiyo na kuzua mazungumzo ya kisiasa ambayo mara kwa mara alipenda kuyasikia na hata kuchangia hoja, bado kwa siku hii alishindwa kuungana na maongezi yao kikamilifu.



    Alipoitazama saa ya kwenye simu yake ya mkononi, akajikuta akiguna. Ilitimu saa 12. 30 jioni. Huenda hatakuja, alijisemea kimoyomoyo, macho yakiwa yameganda mlangoni ambako watu waliingia, watu walitoka.



    **********



    SAA 12:45 Mheshimiwa Hakimu John Mwakipesile alikuwa akiteremka kutoka kwenye gari lake la kifahari, Range Rover nje ya Machopi Bar. Alitambua kuwa aliwahi robo saa kabla ya muda aliokubaliana na wakili, Atupele Antony, lakini hakuona kuwa hilo ni tatizo. Kuwahi kabla ya muda si kosa, kosa ni kuchelewa. Aliamini hivyo.



    Ndani ya ukumbi wa baa hiyo alikaribishwa kwa mbwembwe za aina yake, kila mhudumu akionekana kutaka kuwa wa kwanza kumkaribisha. Mhudumu mmoja alimbusu kwenye paji la uso, mwingine alimkumbatia kwa nguvu asitake kumwachia hadi mwingine alipomng’atua kwa nguvu.



    Na kuna huyu ambaye hakuwa na woga wala aibu. Yeye alipoona sasa hakimu yu huru, akielekea kuketi kitini, alimwahi, akamkumbatia na kulazimisha busu la kinywani, busu ambalo hakimu naye hakujali kuwa yuko katika hadhara, anaonwa na kadamnasi, akalipokea kwa nguvu zote. Wakaganda kwa muda katika busu hilo, mhudumu huyo akitumia mkono mmoja kumpapasa mgongoni na mwingine ukiwa mahala fulani, chini ya tumbo la mheshimiwa huyo, ukipapasa, ukatomasa na kutofya kitaalamu kiasi cha kumfanya hakimu ajisikie yu katika sayari nyingine na kusahau yu wapi na anaonwa na nani.



    Ilikuwa bayana kuwa ile hadhi ya UHESHIMIWA ilikuwa na nguvu ndani ya uzio wa Mahakama ya Kisutu tu lakini nje ya hapo alikuwa ni mwananchi wa kawaida, John Mwakipesile, anayeweza kukaa popote, kuzungumza lolote na kufanya chochote bila ya kujali umri wake, wadhifa wake serikalini, heshima yake mitaani na katika parokia yake kanisani.



    Mapokezi haya yalikuwa ni ya kawaida kwa hakimu huyo kila alipotinga ndani ya baa hiyo ya Machopi. Wale waliokwishaizoea baa hiyo hawakushangazwa na vimbwanga hivyo vya wahudumu. Lakini wale ambao leo wapo, kesho hawapo walijikuta wakikodoa macho wakishangazwa na yale ambayo hayakupendeza machoni pa wasiostahili kushuhudia.



    Kamba alivishuhudia vituko hivyo huku akiwa kama ambaye hajali, kila baada ya sekunde chache akawa akizama kwenye televisheni ukutani na baada ya muda mfupi tena anairudia glasi yake ya kinywaji.



    Ndiyo, alikuwa kama mtu ambaye hajali, lakini alijali. Miaka saba ambayo alisota katika Gereza la Keko haikumpotezea kumbukumbu ya yeyote aliyehusika na kesi yake. Japo ukumbi huu ulikuwa na mwangaza wenye taa zenye rangi hafifu hata hivyo hakushindwa kuikumbuka sura ya Mheshimiwa Hakimu John Mwakipesile mara tu alipoingia.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kulikuwa na tofauti ndogo katika uso wa hakimu huyo. Tofauti na miaka ile saba iliyopita sasa alionekana kusogeza umri zaidi, lakini bado alionekana kuwa na nguvu na Kamba aliamini kuwa hali hiyo ilitokana na ukwasi uliomfanya awe katika daraja jingine. Pesa huweza kumfanya mtu aonekane ni kijana kila siku, alijiambia huku akiendelea kumtazama hakimu huyo.



    Kwa kipindi kifupi akashuhudia wahudumu watatu wa kike, wale waliokuwa mstari wa mbele katika kumkaribisha kiaina-aina wakiagiziwa bia mbili-mbili na nyamachoma. Kisha, kama vile haitoshi, akawakabidhi kila mmoja noti ya shilingi 10,000. Tukio hili la kuwapa fedha wahudumu hao ndilo lililomshangaza Kamba, na halikumshangaza peke yake bali hata wateja wengine walioshuhudia.

    Mmoja akamwambia mwenzie, “Na mimi nitasomea Sheria.”



    “Ukiwa hakimu au wakili, hauwezi kufulia hata siku moja,” mwenzake alichangia na kuongeza, “Kila siku wewe mkwanja unaingia tu kudadadeki!”



    Maneno hayo yalipenya kwa usahihi masikioni mwa Kamba. Yalizama moyoni kwa kasi ya risasi na kumuunguza mithili ya msumari wa moto kiasi cha kumtia jeraha lisilovumilika. Hasira zikampanda na kujikuta akitetemeka kwa mbali hata akashindwa kuitwaa glasi ya kinywaji akihofia kuiangusha. Akatulia na kuepuka kumtazama hakimu katika kile alichoamini kuwa kitamsaidia kumpunguzia hasira.



    Akayatupa macho tena kwenye televisheni na kujitia kuzama kwenye kipindi cha komedi kilichokuwa kikianza kurushwa. Lakini akili haikuwa yake, hakutaka kujidanganya kuwa anaweza kuangalia kipindi hicho japo kwa dakika mbili na kukielewa anachokitazama. Kwa hilo hakutaka kujidanganya asilani.



    Alichokifanya ni kunyanyuka na kutoka taratibu akielekea msalani. Huko, alijifungia na kisha akaitoa bastola na kuitazama huku akisonya. Hatimaye, kwa mnong’ono uliojaa uchungu mkubwa alisema, “Leo…” akaiacha sentensi hiyo ikielea.



    Akafungua mlango na kutoka.



    **********



    WAKATI Hakimu John Mwakipesile alipokuwa akiinyanyua glasi ya bia na kuipeleka kinywani, mawazo yalikuwa kwa Wakili Atupele Antony. Mafunda kadhaa yalipopenya kinywani, aliirejesha glasi mezani. Akaitazama saa ya mkononi kisha akaguna. Ilitimu saa 1: 25. Giza lilikwishaitawala anga!



    Alikubaliana na Atupele kuonana hapo saa 1:00 usiku. Dakika ishirini na tano zilishakatika, hakuna cha Atupele wala kivuli cha Atupele. Waswahili! Alijikuta akisonya na kunywa kwa nguvu bia yake kama aliyeshinikizwa. Kisha akaitwaa simu na kuanza kulisaka jina la Atupele ili ampigie na kumuuliza kulikoni?



    Alipolipata na kupiga akapata ujumbe, “Namba unayopiga inatumika kwa sasa. Tafadhali subiri au jaribu tena baadaye.”



    Kwa mara nyingine akasonya na kuiweka simu mezani. Punde alipotupa macho mbele, akamwona mtu akiisogelea meza hiyo kwa hatua za asteaste. Akamtazama kwa makini mtu huyo huku bado mawazo yakiwa kwa Atupele, shilingi milioni 10 zikirandaranda kwenye ubongo wake.



    Mtu huyo alipomfikia alivuta kiti na kuketi huku tabasamu la mbali likijitokeza usoni pake. “Ndiyo, mheshimiwa,” alisema kwa sauti ya chini, akimtazama hakimu kwa macho ya kujiamini lakini yaliyotangaza urafiki. “Samahani kwa kujikaribisha mezani kwako bila ya ruksa yako.”



    Hakimu aliguna kidogo na kusema, “Aaah, sina meza hapa. Mtu anaweza kuwa na meza yake ndani ya baa? Mi’ ni mteja kama wateja wengine.”



    “Ndiyo, ni mteja kama wateja wengine, lakini ukiwa unaheshimika na labda hata kutukuzwa tofauti na wateja wengine.”



    “Una maana gani?” hakimu alimuuliza huku mikunjo ikiwa imejitokeza katika paji la uso wake.



    “Mapokezi. Mapokezi uliyopata yanaonyesha ni kwa jinsi gani unavyoheshimika, unavyotetemekewa, unavyopendwa labda hata jinsi unavyoogopwa.”



    Hakimu John Mwakipesile hakuyafurahia maneno hayo, lakini katika kuilinda heshima yake hakutaka kuwa na papara kwa kumfokea kijana huyu mwenye macho baridi, yaliyowaka na kuzungumza mengi kuliko kinywa chake. Hakutamka chochote na wala hakumtazama tena.



    “Sikujua kuwa mtu ukiwa na ajira ya kuhukumu watu unachukuliwa kama Mungu-mtu,” aliendelea mtu huyo. “Ukiwa hakimu unaweza kuamua chochote katika kesi yoyote hata kama utajua fika kuwa hukufuata kanuni za sheria. Ukiwa hakimu hulali njaa, washtakiwa na walalamikaji wako kibao na lazima watakutafuta na hutawasikiliza mpaka wawe na chochote mifukoni.”



    Kufikia hapo akacheka kwa sauti ya chini iliyojaa dhihaka kisha akamalizia kwa: “Ukiwa hakimu hukosi mademu wa kukuliwaza kwa kukufanyia vitu adhimu ilhali una mke uliyemwacha nyumbani.”



    Sasa hakimu alishindwa kustahimili. Maneno haya aliyoambiwa yalikuwa hayatofautiani na kaa la moto moyoni mwake.



     Akamtazama mgeni huyo kwa macho makali kisha kwa sauti nzito, ya chini lakini iliyosheheni hasira kali, akambwatukia, “Bwa’mdogo, jaribu kujitunzia heshima. Umekuja hapa na utamaduni wako wa ajabu unaonifanya kwanza niamini kuwa niko na mtu asiye Mtanzania. Ni Mtanzania gani asiyejua hata kusalimia?”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog