Search This Blog

Friday, 20 May 2022

PIGO LA MWISHO - 4

 







    Simulizi : Pigo La Mwisho

    Sehemu Ya Nne (4)



    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Acha kuhamaki, mheshimiwa,” mtu huyo hakuonesha kubabaika. “Na usijali sana mambo ya kizamani ya kuendekeza ‘shikamoo’. Nilidhani kuwa kwa elimu yako na madaraka makubwa uliyokabidhiwa na serikali, kichwa chako kingekuwa na busara walao kidogo. Kumbe nilikosea sana kuamini hivyo! Duh!”



    “Bwa’ mdogo...” hakimu alipandwa na jazba. “ Zipo sehemu nyingi za kuketi! Sihitaji mashairi ya kipumbavu, yanayotolewa na hayawani! Tafadhali, tafuta sehemu nyingine ukaketi. Kama shida yako ni kinywaji kamwone mhudumu, akupe. Nitalipa.”



    Mtu huyo alitabasamu kidogo huku akimtazama hakimu kwa macho yaliyozungumza mengi yaliyokuwa mafichoni. Na akionekana kutotekeleza amri hiyo ya hakimu, alisema, “Mheshimiwa, nadhani unatambua fika kuwa hapa ni baa.”



    “Kwa hiyo?”



    “Mimi ni mteja.”



    “Na kama ni mteja?”



    “N’nayo haki ya kuketi popote penye nafasi.”



    “Lakini siyo hapa!” hakimu alipaza sauti kidogo. “Zipo sehemu nyingi ambazo ziko tupu. Kakae huko!”



    Mtu huyo alicheka, cheko la dhihaka na lenye mapozi ya dharau iliyokuwa dhahiri. Kisha akasema, “Mheshimiwa, unaweza kupinda sheria pale uvutapo mshiko wa nguvu kutoka kwa mtuhumiwa au mlalamikaji yeyote aliyekuletea kesi, lakini huna mamlaka ya kunichagulia siti humu baa. Tuko pamoja?”



    “Kijana… Kijana…Toka! Toka mbele yangu!”



    Mgeni yule hakutii amri hiyo, badala yake aliachia cheko la dhihaka. Kisha, katika kuonesha kuwa hana wasiwasi na wala hana mpango wa kutekeleza alichoambiwa, aliwasha sigara na kuvuta mkupuo mmoja wa nguvu kisha akapuliza moshi angani. “Huna haja ya kuhamaki, mheshimiwa,” hatimaye alisema, bado sauti yake ikiwa ya kawaida, isiyoonesha hasira hata chembe, japo macho yake yalikuwa na kitu kisichoelezeka wala kupendeza akilini mwa hakimu.



    “Jitahidi kutumia busara zako unisikilize.” Mtu huyo aliendelea. “Uwe mvumilivu kidogo mkuu. Najua hunikumbuki. Miaka saba ni mingi sana. Lakini naomba uniwie radhi kwa lolote nililokukosea kwa kipindi hiki kifupi nilichoketi hapa.”



    Kwa mara nyingine akaipeleka sigara mdomoni na kufanya kile alichokifanya awali, macho yakiufuatilia moshi angani. Kisha akayashusha macho usoni pa mheshimiwa hakimu. “Mheshimiwa, una umri wa miaka mingapi?” alimuuliza.



    Hakimu alitwaa glasi na kugugumia bia kisha akairejesha mezani. “Uliza swali lingine na liwe la mwisho!” alifoka kwa sauti ya chini.



    “Naomba jibu,” mtu huyo alikunja uso.



    “Sina jibu!”



    “Jibu unalo!”



    “Sikia bwa’mdogo,” hakimu alimnyooshea kidole mtu huyo huku sasa akimtazama kwa hasira zilizovuka kiwango. Akawa akihema juu-juu. “Mimi ni mtu mzima,” aliendelea. “Nina akili timamu, nina elimu, nina familia na nina nyumba. Siyo mwendawazimu kama wewe. Kwa hiyo utambue kuwa sishindwi kutumia dakika moja tu kufanya mawasiliano na wahusika walio nje ya eneo hili na ukajikuta ukijuta kuzaliwa au ukijuta kunifahamu. Sishindwi kufanya hivyo! Na sasa nakwambia kwa mara ya mwisho, toka! Toka mbele yangu! To…!”



    “Shhh! Kimya!”



    Ilikuwa ni amri iliyotaka kwa sauti ya chini zaidi, amri ambayo hakimu, John Mwakipesile hakuwa na budi kuifuata. Ndiyo, alilazimika kutii baada ya macho yake kukumbana na kitu asichokitarajia, kikiwa kimeshikwa na mtu huyu aliyekuwa akimsumbua kwa hili na lile.



    Ni bastola!



    **********



    “SIKUJA hapa kama kibaka, tapeli au ombaomba. Nina pesa, hivyo nikitaka kunywa bia nitakunywa tani yangu. Nimekuja kwa lengo maalum. Umenielewa?” Kamba alinguruma, macho yake baridi yakimtazama hakimu bila ya kupepesa!

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maneno haya yalipenya kwa usahihi mkubwa masikioni mwa hakimu, John Mwakipesile kiasi cha kumlazimisha atulie tuli, macho yakiwa yameganda kwenye bastola iliyomtazama. Mapigo ya moyo yalimwenda kasi, akawa si yule Mwakipesile aliyeingia dakika kadhaa zilizopita huku akiwa mchangamfu na kunywa bia zake kwa amani na utulivu.



    Ile bastola ilirudishwa taratibu ndani ya mfuko mpana wa suruali kisha mtu huyo, kwa sauti ya chini lakini ikiwa na msisitizo mkali akasema, “Nadhani ni vyema kwanza ningejitambulisha kisha nikakueleza madhumuni ya uvamizi wangu mezani kwako, kama kweli ni uvamizi.”



    Ukimya ukatawala kwa muda mfupi, mgeni huyo akivuta sigara na hakimu akiwa kakunja uso akionyesha dhahiri kukumbwa na taharuki.



    “Nakuomba usiwe na wasiwasi,” mtu huyo alisema. “Tulia tuzungumze kwa utulivu. Weka sura yako katika hali ya kawaida, vinginevyo nadhani hatutaelewana na utanifanya nikulazimishe kutabasamu bila kupenda. Kaa kama mtu wa kawaida, tuonekane ni marafiki. Hiki kifaa kisikutie woga. Ilikuwa ni sinema fupi tu, sinema ya kawaida na imekwishapita. Sawa mheshimiwa?”



    Hakimu John Mwakipesile aliitika kwa kutikisa kichwa lakini bado akiwa katika mwonekano usiokuwa na utulivu moyoni.



    “Naitwa Kamba. Kamba Kiroboto. Najua utakuwa hunikumbuki, lakini huwezi kujitia kunidanganya na nikadanganyika kuwa hata ile kesi ya Mhindi aliyevamiwa dukani na kuporwa mamilioni ya pesa nayo utakuwa umeisahau. Huwezi kunidanganya kwa hilo.”



    “Mhindi? Mhindi gani?” hakimu aliuliza kwa mshangao.



    “Ladhu Hassanali Ladhu!”



    “Yule wa Mosque Street?”



    “Yeah. Unakumbuka kuwa miaka saba iliyopita aliporwa fedha dukani kwake?”



    Hakimu alikunja uso na kutazama juu kidogo kisha akayarejesha macho kwa Kamba na kusema, “Nakumbuka niliwahi kushika kesi iliyohusu Mhindi huyo kuporwa pesa lakini sikumbuki ni mwaka gani.”



    Kwa mara nyingine Kamba alivuta mkupuo mkubwa wa sigara na kisha kipande kilichobaki akakikanyaga na kukisagasaga kwa kiatu. Akaupuliza moshi angani huku akiutazama kwa mikogo kama anayeusubiri umpe mwongozo nini alipaswa kukifanya. Kisha akamrudia hakimu na kumuuliza, “Yule Mhindi ulikuwa ukimfahamu kabla ya kushika hiyo kesi yake ya kuporwa?”



    “Sikuwa namfahamu hapo kabla.”



    “Na wala huna kumbukumbu yoyote kuhusu kesi nyingine yoyote ambayo ama huyo Mhindi alikuwa mlalamikaji au mshtakiwa?”



    “Sina kumbukumbu yoyote. Mambo mengi yamepita hapa kati.”



    “Na umesema hukuwa unamfahamu hapo kabla. Hapo una maana kuwa ulimfahamu katika kipindi ulipokuwa umeishika kesi yake, si nd’o maana’ke?”



    “Yeah.”



    “Na ulikuwa ukionana naye wakati wa kesi tu au hata nje ya hapo? Uwe mkweli, ukijaribu kunipa jibu la kubuni, utakuwa umejiponza mheshimiwa.”



    Hakimu alishusha pumzi ndefu, akili ikiitafakari hii kauli ya kitisho kutoka kwa Kamba, kauli ambayo hakupenda kujifariji kuwa ilikuwa hata na asilimia moja ya mzaha ndani yake. “Tulikuwa tukionana,” hatimaye alijibu.



    “Wapi?”



    “Nyumbani kwake.”

    “Unataka kun’ambia ile kesi ilizaa urafiki mkubwa kati yenu kiasi cha kufikia hatua ya kutembeleana?”



    “Siyo kutembeleana,” hakimu alikana.



    “Ila?”



    Hakimu hakujibu, badala yake akajipa ujasiri wa kutomtazama tena Kamba na akanyanyua glasi ya bia na kuipeleka kinywani. Akashusha mafunda mawili kooni na kutulia. “Sidhani kama mengine yanakuhusu,” hakimu alionyesha kukerwa na maswali ya Kamba.



    Kamba aliuma meno kwa hasira huku akimtazama hakimu kwa jicho kali. Mkono ukazama kwenye mfuko mpana wa suruali ambako uliigusa ile bastola. Hata hivyo alihisi kitu fulani kikimnong’oneza ‘tulia acha papara.’



    “Mheshimiwa, umechoka kuishi?” Kamba alifoka kwa sauti yake nzito na ya chini. “Sema, umechoka kuishi? Unajua kilichojiri ndani ya jiji hili kiasi cha saa tatu hivi zilizopita? Ok, chezea kichwa changu uone! Jambo ninalotaka ujue ni kwamba, ni kwa nini nimekuja kwako mida hii.”



    Alianzia mbali, akifuata hatua kwa hatua, bila ya kusaza chochote alichoona kuwa ni muhimu kukimwaga mbele ya Hakimu John Mwakipesile. Mwisho wa maelezo yake akamtupia swali hakimu, “Ulifuata kanuni za sheria katika uendeshaji wa ile kesi yangu?”



    “Nilitimiza wajibu wangu ipasavyo. Unanilaumu kwa kifungo chako?”



    “Hilo ni jibu siyo swali.”



    Kwa nini usiwalaumu polisi?”



    “Niwalaumu kwa?”



    “Ni wao waliokutuhumu na wakakuleta mahakamani!”



    Kamba alicheka kidogo, moja ya vile vicheko vyake visivyokuwa hata na chembe ya furaha. Kisha akasema, “Ndiyo, ni wao walionitia mbaroni, wakinituhumu kumvamia huyo rafikiyako gabachori. Lakini tuhuma siyo kigezo cha kumtia mtu hatiani. Hapana, hapo hatuwezi kukubaliana.



    “Waliponikamata, walinileta mahakamani. Nikatoa utetezi kwako uliyekuwa umeishika kesi ile. Nikasema bayana kuwa siku niliyotuhumiwa kutenda uhalifu kwa huyo swahiba wako, sikuwa nimetoka dukani kwangu tangu asubuhi hadi saa kumi na moja jioni.



    “Upande wa mashtaka ulidai kuwa tukio lile lilifanyika kati ya saa sita u nusu na saa saba mchana, muda ambao hata malaika wa Mungu anaweza kukuthibitishia kuwa nilikuwa dukani kwangu!



    “Wewe hukuniamini, hata mwendesha mashtaka naye hakuniamini! Labda kanuni zenu za sheria haziwaruhusu kumwamini mtu eti kwa kuwa kasema hili ilhali hakukuwa na mtu yeyote mwingine wa kuthibitisha. Kwa hilo siwalaumu, lakini mimi roho inauma!”



    Ukimya ukatawala kisha Kamba akaendelea, “Mheshimiwa, ninakuchukia zaidi wewe kwa kuwa ndiye uliyenihukumu kifungo. Ulinifunga bila ya kuwa na hatia, hayo ma-kanuni yenu ya sheria kwangu hayaniingii akilini asilani! Muhimu ni kwamba ulinifunga wakati siye mimi niliyemvamia yule rafiki yako wa Kihindi.



    “Kitendo cha kunichapa miaka saba jela kilikuwa ni pigo zito lisilofutika maishani mwangu. Umenitia majeraha yasiyopona! Ni pigo lililoyateteresha maisha yangu kwa kiwango kisichokadirika. Mheshimiwa, nilipoingia jela niliacha maduka matatu ya rejareja nyuma yangu. Umenisoma? Nilipotoka, nimekuja kukuta hakuna duka hata moja! Hayo ni matokeo ya pigo ulilonipa! Na kwa kweli siwezi kuvumilia…ni vigumu mheshimiwa!”



    Baada ya kusema hivyo alishusha pumzi ndefu na kuupeleka mkono ndani ya ule mfuko wa suruali.





    HII ilikuwa ni siku ambayo wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam walikuwa na jambo moja tu kubwa la kulizungumzia. Haikuwa siri, wengi walikaa makundi na kuzungumzia tukio la mauaji yaliyotokea katikati ya jiji, mauaji ya kikatili yaliyowahusu watu watatu kwa mpigo, tajiri Ladhu Hassanali Ladhu , mwanaye, Hassanali na mfanyakazi wao, Juma, ndani ya nyumba moja saa tatu asubuhi.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Lilikuwa ni tukio lililowashangaza sana watu na kuzua minong’ono mingi, baadhi wakidai kuwa ni tukio lililohusu ujambazi, wengine wakisema eti ni suala la visasi. Kila mmoja aliserma alivyohisi na alivyoamini. Redio moja iliyokuwa na utaratibu wa kutangaza taarifa za matukio ya papo kwa papo nayo ikazua mshangao na taharuki nyingine pale ilipofika saa tisa alasiri.



    Ndiyo, ilikuwa ni taarifa ya kushangaza na kushtua baada ya kutangazwa kuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay ameuawa!

    Ndani ya saa sita tayari watu wane wameuawa katika mazingira ya kutatanisha! Kwa Inspekta Maliyatabu taarifa hii ya kifo cha James Ntilampa ilikuwa ni kama taarifa ya uongo. Hakuweza kuiamini mara moja. Ni saa chache tu zilizopita alizungumza naye kuhusu jambazi sugu aliyeitwa Kamba Kiroboto, na sasa anapokea taarifa ya kifo chake! Haiwezekani!



    Kwa nini isiwezekane? Alihisi sauti ikimuuliza kwa namna ya kumsuta. Ilikuwa ni taarifa ya kumtisha kwa kuwa ilidai kuwa James kauawa na mtu! Nani kamuua? Na kwa nini kamuua? Inspekta Maliyatabu, alisikitika lakini masikitiko hayo hatimaye yalizaa uchungu na hasira kali dhidi ya huyo aliyehusika na mauaji hayo.

    Kiti hakikukalika. Akawa katika hekaheka kubwa, hatimaye akapata taarifa kuwa kwa mujibu wa maelezo ya mkewe James, muuaji alidiriki kulitaja jina lake kwa marehemu na pia kutaja dhamira ya ujio wake.



    Kamba Kiroboto!



    Inspekta Maliyatabu akalazimika kutafuta ufumbuzi wa haraka wa kumtia mbaroni Kamba. Kulingana na maelezo ya jirani wa Kamba, Baba Semeni, mauaji yaliyopangwa na Kamba yaliwahusu tu wale waliohusika na ile kesi yake iliyoishia kwa yeye kusota jela miaka saba.



    Vifo vya Mzee Ladhu H. Ladhu na mwanaye, Hassanali vilimfanya Inspekta Maliyatabu amtilie shaka na uzito wa juu Kamba. Haikuhitaji mtu mwenye shahada ya juu katika masuala ya kiusalama kuwaza kuwa ni nani atakuwa mshukiwa wa kwanza wa mauaji hayo. Hivyo Inspekta Maliyatabu aliamua jambo moja, kumsaka Kamba kabla hajaleta madhara zaidi.



    Hata hivyo aliuona ugumu wa utekelezaji wa azma hiyo kwa wakati mwafaka. Bado kulikuwa na kiza kinene mbele yake. Hakujua wakati huo Kamba yuko na wapi na anadhamiria kufanya nini kingine kitakacholeta habari nyingine isiyopendeza.



    Akaamua kutoka ofisini huku akisonya, akaenda nje na kujikuta akiduwaa kwa kuyatazama magari yaliyopita barabarani bila ya kujua afanye nini. Kila baada ya sekunde chache akawa akisonya. Kisha tena akarudi ofisini na kumwita msaidizi wake, Sajini Kitowela na kuanza kuzungumza kwa kina kuhusu janga hilo.



    Kilichovisumbua vichwa vyao ni jinsi ya kuhakikisha kuwa Kamba haui tena. Na hisia zao ziliegemea kuwa huenda na hakimu atakuwa kwenye mpango huo.



    “Kama amefanikiwa kuwaua mzee Ladhu na mwanae na pia akafanikiwa kumuua Ntilampa, basi kwa vyovyote msitari utakuwa unaendelea kwa Mheshimiwa Mwakipesile,” Sajini Kitowela alisema.

    “Inawezekana,” Maliyatabu aliafiki. “Kina Makela wameniambia kuwa walipofika kwa hakimu waliambiwa kuwa kuna mtu aliyefika pale muda mfupi kabla yao na mtu huyo alikuwa akimhitaji hakimu! Mke wa hakimu aliwaeleza jinsi mtu huyo alivyokuwa kimaumbile na kimavazi.



    “Kulingana na maelezo ya waliomwona mtu aliyeingia na aliyetoka kwa mzee Ladhu baada ya milipuko ya risasi, na ukilinganisha na maelezo ya mke wa hakimu, hapo utaona kuwa mtu anayezungumziwa ni yuleyule japo kimavazi ni tofauti. Anaweza kuwa alivaa nguo nyingine asubuhi na akabadili baada ya kufanya tukio la kwanza katika tu kujaribu kutuchanganya!”



    “Afande,” Kitowela alidakia. “Hatuna muda wa kupoteza. Taarifa kutoka nyumbani kwa hakimu ni kwamba mheshimuwa huyo ana tabia ya kurejea nyumbani usiku kila siku. Inasemekana kuwa kila jua lizamapo yeye huripoti Machopi Bar, Kinondoni.” Akameza funda la mate na kuendelea, “Inasemekana kuwa mke wa hakimu kamtaarifu hivyohivyo yule mgeni aliyemfikia kabla ya akina Makella.”



    “Yaani Kamba?”



    “Ndiyo!”



    “Basi ipo kazi!”



    “Siyo siri, kazi tunayo, afande,” Kitowela alisema. “Naamini Kamba atakwenda hapo kumvizia hakimu. Lakini pia kama ndiye aliyefanya mauaji yote hayo, kwa vyoyote hawezi kuwa bwege akaenda bila ya kuwa makini. Anajua tayari jiji lmetikiswa na mauaji aliyoyafanya. Hatakuwa bwege, afande!”



    “Hiyo baa iko maeneo gani kwa pale Kinondoni?” Inspekta aliuliza.



    “Peupe tu, Kazima Street,” Kitowela alijibu. “Ni jirani sana na lile jumba tulimowakuta wale wazungu wa unga mwaka jana. Ni baa maarufu sana kwa machangu wenye mvuto mkubwa. Wateja wengi wanaofika pale huwa na dhamira mbili; kunywa bia na kuchukua mademu.”



    “Kwa hiyo una maana na mheshimiwa hakimu naye huenda ni kati ya wateja wa daraja hilo?”



    “Sina hakika, lakini ni kwa nini apageuze hapo kama kijiwe cha kahawa ambacho ni kama sheria kwa wanywaji wake kuhudhuria?”



    “Hayo hayatuhusu,” Inspekta Maliyatabu alisema. “Hii ni saa saba na dakika ishirini na tano. Watu wanne wamekwishauawa. Hatujui kitakachofuata, huenda ni vifo zaidi.”



    Ukimya mfupi ukatawala, askari hao wakitazamana. Kisha Inspekta Maliyatabu akasema, “Tunapaswa kuingia kazini moja kwa moja. Hatuwezi kumwachia Makela na kundi lake peke yao. Kazi inaweza kuwa ngumu kwao. Na kwa hali ilivyo, hatulazimiki kumkamata Kamba akiwa hai lakini tunalazimika kuhakikisha hakimu hadhuriki.”



    **********

    MKAKATI mzito ulipangwa dhidi ya Kamba. Dakika thelathini baada ya kikao cha Inspekta Maliyatabu na Sajini Kitowela, tayari askari wanane wasiovaa sare walikuwaa ndani ya Machopi Bar. Baadhi ya askari hao walikuwa wakinywa soda na wengine wakinywa maji.



    Kati ya wateja wengi waliokuwa ukumbini humo hakuna hata mmoja ambaye alibaini kuwa wateja hawa wawili, wale pale wawili na wale kule wanne walikuwa ni kundi moja na kwamba walikuwa wameamua tu kujitenga katika kufuata utaratibu wa kazi iliyowapeleka hapo.



    Saa nane ikapita.



    Saa tisa!



    Saa kumi!



    Kumi na moja!



    Waliokuwa wakinywa soda matumbo yakawajaa. Waliokuwa wakinywa maji sasa yakawakinai. Hata hivyo, hawakuwa na budi kuendelea kuwemo humo kwa sababau maalum kulingana na jukumu walilopewa na Inspekta Maliyatabu.



    Mara mmoja akalitoroka eneo hilo na kwenda sehemu ambayo wenzake hawakumwona. Huko akamwita mhudumu kwa siri na kumwagiza bia ambayo ilipoletwa aliinywa kwa mfumo wa kuimwaga tumboni. Mwingine ambaye kichwa chake kilishakomaa kwa pombe kali, yeye alichoropoka bila ya kuwaaga wenzake na kwenda kwenye kaunta ya nje ambako aliagiza toti kadhaa na kuzinywa kama anayefukuzwa.



    Sita kati yao walifanya hivyo kila mmoja akinywa kile alichopenda, kwa njia alizojua na ilipotimu saa 12, kila mmojawao alikuwa kachangamka kwa namna yake kama wateja wengine.



    Wakati Kamba alipoingia katika eneo hilo saa 1:05 jioni baadhi ya askari hao walimwona. Na hao ni wale ambao hawakufika kule kwa Hakimu John Mwakipesile mchana wakiwa na picha kamili ya Kamba.

    Hivyo walimchukulia kama mteja yeyote afikaye hapo, ambaye amependa huduma na mandhari ya hapo. Isitoshe, hawakutarajia kuwa mlengwa wao atawahi kufika hapo mapema kiasi hicho.



    Aidha, haikuwaingia akilini kuwa mtu wao atakuwa ametinga mavazi ya kawaida, yatakayotazamwa kwa macho ya kawaida na mtu yeyote. Hawakumjali, wala hawakuwashtua wenzao, wale watatu ambao walikuwa na picha ya Kamba vichwani mwao na pia ambao walifika nyumbani kwa Hakimu Mwakipesile mchana wa siku hiyo. Na hawakufanya hivyo wakiwa wamekwishajenga hisia kuwa Kamba hatakuwa mtu wa kuvaa shati jeupe la cadet lisilochomekewa na hatakuwa mtu wa kuvaa suruali ya jeans iliyotapakaa mifuko.



    Matarajio yao na walichojali ni kuwaona Inspekta Maliyatabu na Sajini Kitowela wakiingia hapo na kuwapa majukumu. Makela, ambaye alikuwa ni kiongozi wa kikosi hiki, askari hao walimchukulia kama askari mwenzao, wa kawaida, asiye na uwezo wa kutoa amri ya kuitoa roho ya mtu yeyote kwa risasi ya serikali.



    **********

    GARI dogo jeupe aina ya Toyota Carina liliegeshwa hatua chache kutoka Machopi Bar saa 12 jioni. Ndani ya gari hilo kulikuwa na watu wawili tu, Inspekta Maliyatabu na Sajini Kitowela wote wakiwa katika mavazi ya kiraia. Kwa kuwatazama tu usingeweza kuwaweka kwenye kundi la wenye njaa. Ile suti nyeusi iliyotinga mwilini mwa Inspekta Maliyatabu haikuwa ya kawaida. Jaribu kuingia ndani ya yale maduka maarufu kwa suti maarufu, utaiona suti kama hiyo. Uliza bei yake!



    Kwa lile shati alilovaa Sajini Kitowela, ile suruali na vile viatu hutakosa kumweka kati ya wale ambao maisha yameshawakubali. Alivutia kwa kiasi kikubwa.



    Isitoshe, nyuso zao hazikuwa katika hali itakayomfanya yeyote awatilie shaka au watazamwe kama wageni wasiostahili kuingia hapo. Walionekana kuwa ni watu wema sana lakini wasiokuwa katika daraja la watu wa kawaida na ambao ukwasi kwao ni jambo lillilokwishakuwa la kawaida.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Walipoingia, macho yao makali yaliwaona wale askari wanane waliokuwa wameketi kwenye meza mbili tofauti wakiwa na vinywaji vyao. Kwa mbali Inspekta Maliyatabu alijiuliza, kulikuwa na ulazima wa kuja kundi la askari kubwa kiasi hicho kwa ajili ya kumfuatilia mtu mmoja tu? Je, hii siyo hali inayoweza kulishushia hadhi Jeshi la Polisi? Kamba ni kinyangarika kimoja tu kisichokuwa na pumzi ya kulisimbua Jeshi la Polisi. Ya nini kumchukulia kama gaidi namba moja duniani?



    Mtu mmoja tu, Mtanzania ambaye inaaminika kuwa hana mabomu ya kulipua majengo, watu au kujilipua, anafuatwa na kundi la watu kumi! Lakini papohapo akajipinga na kujiaminisha kuwa ni afadhali kuwa na kundi kubwa kwa sababu hawaujui uwezo kamili wa mlengwa wao. Na huenda wakawa wanajua wanamfuata mtu mmoja tu hapo kumbe huyo mtu mwenyewe ana wenzake. Al- Shaabab au Boko Haram! Hapo ndipo kazi itakapokuwa pevu!



    Kijigiza kilishaanza kuitawala anga. Maliyatabu na wenzake walisimama kando ya mlango huu ambao haukuwa ukitumiwa sana na wateja kwa kuwa ulikuwa ukitokea upande wa nyuma ya baa hiyo.



    “Vipi, tukajiunge nao?” Kitowela alimuuliza Maliyatabu.



    “Hakuna haja,” Inspekta Maliyatabu alipinga. “Ukifika wakati wa kujiunga nao tutafanya hivyo. Kwa sasa tutafute chemba yetu tutulie.”



    “Poa.”



    Labda kauli au pendekezo la Inspekta Maliyatabu lingedumu kama macho ya Sajini Kitowela yasingekuwa juu-juu, yakiwa ni mazoea yake tangu alipojiunga na jeshi hilo na hatimaye kujichimbia ndani ya Idara ya Upelelezi. Ni kwa kuangaza hayo macho ndipo aliposhtuka baada ya kutua kwenye meza moja na kujikuta akivutiwa kutazama zaidi katika eneo hilo.



    “Yule siye mheshimiwa hakimu?” hatimaye alimuuliza Maliyatabu kwa sauti ya chini.



    Macho ya Maliyatabu yakahamia kwenye meza hiyo. Kwa sekunde chache wakatulia wakimtazama mtu huyo.



    “Ndiye,” Maliyatabu alikiri. “Ni mwenyewe, na yuko na mtu wetu!”



    “Vipi, tukamvae?”



    “Taratibu,” Maliyatabu alimtuliza. “Tumvutie pumzi. Cheki, pale wanaongea lakini ukimcheki vizuri mtu wetu utagundua kitu. Hayuko fresh. Anaonekana amepaniki. Tuwe makini tukicheki kila kinachoendelea. Pupa yoyote inaweza kumponza mheshimiwa. Lakini uwe tayari. Ukimwona ana dalili ya kumdhuru mheshimiwa, usimwachie, ukifumue kichwa chake! Umenisoma?”



    Kitowela alitikisa kichwa, akiashiria kuyaafiki maneno ya Maliyatabu.



    **********



    KAMBA alipouingiza mkono mfukoni na kuikamata bastola, hakufanya haraka kuitoa. Aliangaza macho huku na kule katika ukumbi huo ulioanza kujaa watu ili tu kujihakikishia usalama kabla ya kuendeleza ratiba yake. Alikwishakuwa na uzoefu wa kuyatambua macho ya kibaka, macho ya askari polisi na hata macho ya fuska. Kwa kipindi hicho kifupi alichozungusha macho tayari akagundua jambo.



    Askari! alijisemea kimoyomoyo alipowaona Inspekta Maliyatabu na Sajini Kitowela kwenye mlango wa nyuma wakiwa wamesimama kama watu wa kawaida, wateja walioamua kutulia hapo mlangoni kwa sababu wanazozijua wenyewe.



    Yeye hakuwa mbumbumbu wa kutowashuku watu hao na kudanganyika kuwa ni wateja kama wateja wengine. Hapana. Simama yao, tazama yao kwa macho yanayozunguka kama ya nyoka ilikuwa ni taswira halisi iliyomfanya awacheke kimoyomoyo kwa kuwa alijua, hawajui kuwa anatambua uwepo wao hapo. Na kwamba pia anatambua fika kuwa wamejipanga kwa ajili ya kumtia mbaroni.



    Kwa hilo hakutaka kujidanganya eti atakuwa anawaza kimakosa. Alitambua fika kuwa pigo alilolitoa mchana kwa kuivunja shingo ya Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay, James Ntilampa litakuwa limeitikisa serikali nzima kuliko kuwaua wale Wahindi na mfanyakazi wao.



    Hivyo, msako mkali unaofanyika ndio uliowafikisha hapo na alitambua kuwa wamekuja kwake. Wanamsaka yeye! Ni kwa vipi wamejua kuwa yupo hapo, hilo hakutaka kujisumbua kulifikiria. Jambo moja aliloamini ni kwamba, mwibie, muue au mfanyie jambo lolote la kihalifu askari yeyote halafu utokomee; kitakachofuata ni msako dhidi yako, msako mkali…hawatakula, hawatalala!



    Macho yake baridi pia yalitua kwa watu wengine watano walioketi katika meza mbili tofauti, nao macho yao yakionekana kutazama zaidi ya utazamaji wa kawaida. Macho ya ki-kacher!

    Sasa akajiona kuwa yuko kwenye wakati mgumu tofauti na alivyotarajia. Bastola yake ilikuwa na risasi nne tu. Na hawa watu wenye sura zilizotangaza kazi zao walikuwa zaidi ya wanne. Atapambana nao vipi kama wako pale kwa nia ya kumtia yeye mbaroni?



    Aliamini kuwa kwa hasira walizonazo, kikwazo chochote atakachoweka dhidi yao pale watakapotaka kumweka chini ya ulinzi kitawafanya wachukue uamuzi wa juu zaidi na huenda ikawa ni kumzamishia risasi mwilini. Na baada ya hapo, kama kawaida taarifa itatolewa kuwa ameuawa baada ya kujaribu kutoroka chini ya ulinzi!

    Hata hivyo, hakuhofia kufa bali alihofia kufa kabla hajaitimiza azma yake. Ndipo alipoamua kuchukua uamuzi, akidhamiria kutoa pigo la mwisho na kuwa tayari kwa matokeo yoyote baada ya utekelezaji wa hilo alilolidhamiria.



    Kufumba na kufumbua akawa ameitoa bastola na kupiga risasi moja juu! Kishindo cha risasi hiyo kikautawala ukumbi huo na kuzua taharuki kwa watu wengi. Kukazuka pilikapilika, kila mmoja akihangaika kutaka kutoka ndani ya jengo hilo kwa minajili ya kuinusuru roho yake.



    Kamba alikuwa makini zaidi, akichukua hadhari ya kutomwamini mtu yeyote aliyekuwa mbele na nyuma yake. Isitoshe, alikuwa mwepesi wa kuhakikisha kuwa anawatoroka askari waliojazana humo.



    Akitumia nguvu alizojaaliwa, aliwapiga kumbo watu wawili, watatu na kuuegemea ukuta ambao haukuwa mbali na ile meza aliyokuwapo hakimu lakini kukiwa na kivuli kizito kilichotokana na mwanga wa taa kutolifikia eneo hilo. Kivuli hicho kilitengeneza kijigiza cha wastani kiasi cha kutoweza kuonwa na mtu wa mbali. Akabaini kuwa wengi wa watu waliompitia mbele yake hawakuwa wabaya wake kwani walikuwa wakijali kukimbilia nje, hawakujali uwepo wake.



    Hata hivyo, bado alijua kuwa kuna hatari kubwa mbele yake na huenda asitimize lengo lake kama hatakuwa mwepesi zaidi na makini, zaidi ya kiwango chake cha kawaida. Meza aliyokuwa kakaa hakimu ilikuwa hatua kama kumi tu kutoka hapo alipo Kamba, hivyo akaamini pia kuwa mtafaruku huu uliozuka unaweza kumsaidia kwa kiasi kikubwa kutekeleza chochote kile atakachopenda na alichopanga kukifanya.



    Akayatupa macho kwenye meza ile aliyoikimbia muda mfupi uliopita. Akamwona hakimu amesimama, kaduwaa, akionekana dhahiri kuchanganyikiwa. Alikuwa akiangaza macho huku na kule, taharuki ikiwa bayana katika macho hayo.



    Kono la kulia la Kamba, lililokuwa limeishika bastola madhubuti, liliinuka huku misuli yake ikikakamaa. Kidole cha shahada kikajikita kwenye kitufe cha kufyatulia risasi kwa uthabiti! Domo la bastola hiyo likamwelekea hakimu, John Mwakipesile. Risasi ya pili ikatoka, safari hii ikiwa ni kwa shabaha kali kwa dhamira ya kutimiza lengo lililokusudiwa!







    TUKIO la kufadhaisha ambalo hakimu John Mwakipesile hakuweza kulisahau ni siku alipokuwa na mkewe, wakitoka ndani ya duka maarufu la simu, Mtaa wa Samora katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Yeye na mkewe walikuwa wamenunua simu mbili kwa jumla ya shilingi milioni moja na nusu saa nne asubuhi. Ni miaka saba iliyopita.



    Wakiwa nje ya duka hilo, wakilifuata gari ili waondoke, ghafla hakimu alipigwa ngwara iliyoshiba, akabinuka mzima-mzima chali! Na kabla hajafika chini, simu aliyonunua, ambayo ilikuwa bado ndani ya kasha lake ilichukuliwa na mmoja wa vijana watatu waliomzunguka. Mkewe naye, kabla hajajua ni kipi kilichotokea, alishtukia mkoba wake ukikwapuliwa mkononi mwake kisha akazabwa kofi kali kwenye paji la uso, kofi lililomtia kiza machoni na kujikuta akiwa kama zuzu, akaanguka kama gunia la mashudu chali puu!

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Lilikuwa ni tukio lililochukua muda mfupi sana na kuwaacha baadhi ya watu wakistaajabu, baadhi wakigwaya. Fahamu zilimtoka hakimu kwa muda na alipokuja kuzinduka, ndipo ilipobainika kuwa simu imebebwa! Mifuko yote ya suruali yake ilikuwa nje, pesa zote zilizosalia, shilingi laki tatu zikiwa zimetoweka isipokuwa funguo za gari na nyaraka chache ambazo wahusika waliziacha hapo chini!

    Mkewe alikuwa amepatwa na presha! Alilala chini huku akihema kwa tabu. Watu walijaa katika eneo hilo kwa muda mfupi baada ya tukio.



    Hata hivyo, wasamaria wema waliibuka na kuwasaidia hakimu na mkewe kwa kuwapeleka kwenye gari lao. Kisha, kijana mmoja akashika usukani na kuendesha gari akiwarudisha nyumbani. Kwa siku tatu hakimu hakuwa timamu kisaikolojia, hata kazini hakuweza kwenda. Na hata alipopata ahueni na kuanza kwenda kazini, bado kwa takriban mwezi mzima alikuwa akiota ndoto mbaya zilizofanana na tukio hilo.



    Zilimchukua siku nyingi hadi kurudiwa na hali ya kawaida japo hakusahau. Hata hivyo, maisha yalisonga mbele. Ni tukio hili la leo la kuonyeshwa bastola na mtu huyu ndilo lililomrejesha kwenye tukio lile la miaka saba iliyopita. Likamtia jakamoyo na taharuki isiyo ya kawaida. Kwa muda akili ikawa imesimama kufikiri chochote.



    Wakati mtu huyo alipofyatua risasi juu, hakimu alijihisi yu katika sayari nyingine, mbele yake akimwona mtu anayemeremeta ndani ya mavazi meupe, akitabasamu huku akimwashiria kwa mkono amfuate.



    Wakati watu wengine wakikimbia huku na kule katika kuzinusuru roho zao, yeye alibaki kaduwaa na akajikuta yuko peke yake mezani asijue la kufanya. Kikawa ni kipindi kingine kigumu katika maisha yake, zaidi akiona kama matukio hayo ni miongoni mwa sinema za Hollywood.



    Ni wakati bado ameduwaa, ndipo ghafla akahisi kitu kisichoelezeka lakini chenye joto kali, kikipenya kifuani kwa namna isiyoelezeka vilevile. Punde joto likatoweka na kuzua ubaridi ambao pia ulipotea ghafla na kuibua maumivu makali. Kiza kikaanza kutanda machoni pake, miguu nayo ikaanza kupoteza uwezo wa kuubeba mwili. Kwa mbali akijisikia kushindwa kupumua vizuri. Kabla haijatimu dakika moja akaiangukia meza ya vinywaji kwa kishindo kikubwa, meza nayo ikashindwa kuuhimili uzito wa mwili wake mkubwa, ikapinduka na kuvunjika vipande kadhaa. Alianguka chini huku akiwa amekodoa macho ilhali haoni na kinywa kikiwa wazi!



    **********

    MACHO ya Sajini Kitowela na Inspekta Maliyatabu yalimshuhudia Hakimu John Mwakipesile akiiangukia meza na hawakuhitaji kufikiri zaidi kuwa ni kipi kilichotokea. Amepigwa risasi! Ni mlipuko wa risasi hiyo ya pili uliowapa taswira halisi ya kifo cha hakimu huyo.



    Hata hivyo, hawakuweza kujua mtu waliyemfuatilia yuko wapi. Wakiwa wameshazishika bastola zao mikononi, walihaha wakimsaka na tayari walishajenga imani kuwa amewatoroka. Kutorokwa, tena kutorokwa huku kukiwa na zaidi ya askari wanane ndani ya baa hiyo, lilikuwa ni tukio la aibu kwa Jeshi la Polisi.



    Haraka wakatoka nje ya ukumbi huo huku wakipamiana na wateja, bastola zao zikiwa juu-juu! Askari wengine nao wakawa wakihaha huku na kule. Makela akiwa miongoni mwao kwa jukumu la kumfuatilia Kamba, yeye alikuwa mwepesi zaidi. Alimwona Kamba akipenya mlangoni kwa kasi ya kufa-mtu, naye akamfuata bila ya kujali nani yuko mbele yake na nani yuko kando yake, akimsukuma huyu na kumpamia yule!



    Muda mfupi baadaye alikuwa nje ya baa hiyo na akafanikiwa kumwona Kamba akitokomea kwenye mtaa wa pili baada kukatisha kwenye uchochoro uliokuwa jirani na baa hiyo. Makela akaikamata bastola mkononi madhubuti na kumfuata mbio. Muda mfupi baadaye alikuwa mtaa wa pili na kumwona Kamba umbali wa hatua kama hamsini hivi.



    Makela akainua bastola na kulenga, kisha akafyatua risasi moja! Patupu! Risasi hiyo ikaishia kwenye ukuta wa nyumba ambayo Kamba alikuwa jirani. Tukio hilo likamzindua Kamba na kuamua kuingia kwenye uchochoro mwingine. Kisha akasimama ghafla kama sanamu, kwenye kona ya ukuta wa nyumba moja. Akajipanga kukabiliana na lolote litakalojiri.



    Masikio yake yakanasa vishindo vya miguu vikimjia upande huo kwa kasi. Mara mtu akatokea. Alikuwa ni Makela, ambaye hakumwona Kamba aliyekuwa amesimama bila ya kutukutika, akiwa hatofautiani na kiza! Ni hapo Kamba alipoamua kufanya kitu. Teke zito lilitua kifuani pa Makela na kufuatiwa na konde lililoshiba, konde ambalo nalo lilitumwa kwa shabaha kamili, likiwa ni la uzito wa juu na halikukosea njia, likatua usoni pa Makela na kung’oa meno mawili papohapo!



    Isitoshe, kwa kuwa teke na ngumi vilitoka vikifuatana kwa tofauti ya sekunde zisizozidi mbili, Makela alirushwa juu na kujigonga kwenye ukuta wa nyumba iliyokuwa nyuma yake tii! Mishipa ya fahamu ikakata mawasiliano papohapo!



    Alipokuja kutua chini, kifudifudi, tayari Kamba alikwishampokonya bastola na kuondoka kwa mwendo wa kawaida kama mtu ambaye hakuwa amefanya jambo lolote kubwa na la hatari. Akatembea kwa hatua za kawaida lakini ndefu kisha akachepuka kwenye uchochoro mwingine na kutokea kwenye kijibaa kingine ambako alikuta pikipiki mbili zikiwa zimeegeshwa.



    Alipoisogelea moja, mara akatokea kijana mmoja na kumwambia, “Karibu mzee.”



    Haraka Kamba akadandia nyuma huku akimwambia, “Fasta Kinondoni Moscow. Ingia main road kama dereva unayejua kazi, sitaki ubunyebunye!”



    Kijana huyo alikuwa akiijua kazi yake. Kwa namna alivyoiondoa pikipiki hapo, watu wote walibaki midomo wazi, na alipokuja kuingia Barabara ya Rashid Kawawa hata Kamba mwenyewe alijikuta akijisemea kimoyomoyo Mungu nisaidie tufike salama.



    Kwa maelekezo ya Kamba, kijana huyo alitumia dakika chache tu kukanyaga breki nje ya nyumba ya Kamba na kuambiwa, “Subiri dakika mbili tu.”



    **********

    INSPEKTA Maliyatabu na Sajini Kitowela walipofika nje, walikutana na wale askari wengine na kuwahimiza kumfuatilia Kamba. Wakati Makela alipokurupuka kumkimbilia Kamba, wale wasaidizi wake walimwona na mmojawao akamwambia Maliyatabu, “Afande, mhalifu kakimbilia upande huu. Afande Makela naye kamfuata!”



    “Twendeni!” Maliyatabu alibwata huku akifuata uelekeo alioutaja askari huyo. Kiza kilichokuwa kimetanda kiliwapa wakati mgumu askari sanjari na mchanganyiko wa wapitanjia waliokuwa wakienda huku na kule mtaani hapo.



    Ilibidi kundi la askari hao ligawanyike. Kila mmoja akawa akipita kila penye uchochoro huku bastola zikiwa zimewatangulia. Lakini hawakumwona Kamba wala hawakumwona Makela. Ni katika hekaheka hiyo na sakasaka hiyo ndipo walipozuka katika uchochoro ambao walimkuta Makela akigaagaa chini huku akiugulia kwa maumivu. Na hata walipomuuliza kilichojiri alizungumza kwa tabu, “Ameniumiza…ame…” akakata kauli huku akinyoosha mkono upande wa kulia ambako uchochoro huo uliendelea.



    Baadhi ya askari wakambeba Makela na kumpeleka kwenye gari. Inspekta Maliyatabu akiwa amepandwa na ghadhabu, akasema, “Mwahisheni hospitali! Hii ni fedheha! Nikimwona huyu mshenzi, sipotezi muda kumtia mbaroni, namlipua!”



    Ndipo alipotoa taarifa kwa vituo vyote vya Polisi kuhusu msako mkali wa mtu aitwaye Kamba Kiroboto, anayesadikiwa kuwa ndiye aliyelitikisa jiji kwa mauaji tangu asubuhi. Nusu saa baadaye akawa amepata taarifa ya kuimarishwa kwa doria kali kwenye barabara zote kuu zinazotoka nje ya jiji huku pia msako mkali ukiendelezwa katika mazingira ya Kinondoni.



    Akiwa amerudi ofisini, Inspekta Maliyatabu alijiona kama mtu aliyevuliwa nguo. Tangu asubuhi ya siku hiyo hadi kufikia usiku huo tayari watu watano wameshauawa! Na inasadikika kuwa wameuawa na mtu mmoja! Zaidi, alijisikia kufadhaika kwa kuuawa mmoja wa ‘majembe’ ambao Jeshi la Polisi liliwategemea; James Ntilampa.



    Kabla ya saa sita mchana alipata taarifa kuwa Mwasia Ladhu H. Ladhu, Hassanali na mfanyakazi wao, Juma wameuawa dukani kwao. Kabla ya saa tisa alasiri anapata taarifa nyingine kuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay ameuawa!



    Kwa matukio hayo ya mfululizo, akaamua kujipanga na timu yake kupambana na muuaji huyo ambaye tayari walishamshuku kuwa ni Kamba Kiroboto. Akakusanya kikosi cha askari wanane, yeye na mwenzake Sajini Kitowela wakiwa vinara wa zoezi hilo.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakaizingira Machopi Bar kama wamtafutaye gaidi namba moja duniani. Kilichotokea ni aibu! Hakimu John Mwakipesile kauawa wakiwapo hapo baa na muuaji kawazidi kete na kuwatoroka! Si hilo tu, muda mfupi baadaye, wakihaha kumfuatilia, wanajikuta wakiambulia kumkuta mwenzao, Makela akigaagaa kwenye uchochoro, bastola yake imechukuliwa na vipigo alivyozawadiwa vikimwacha katika hali tete kiasi cha kuwahishwa hospitali.



    Kwa nini asijione kuwa amevuliwa nguo hadharani? Taifa litamwelewa vipi hata akitoa sababu zozote za kitaalamu za kutoweza kumkamata Kamba? Taswira iliyomjia akilini ni kuwa, Inspekta Jenerali wa Polisi hataelewa chochote atakachoelezwa kuhusu mauaji hayo na kwamba eti mhusika hajakamatwa!



    Pia, alitambua kuwa wanasiasa, hususan wa vyama vya upinzani, wanasheria na wananchi waliokwishaichukia serikali moja kwa moja kwa sababu za msingi na hata zisizo za msingi nao watakuwa na la kusema, wakilishambulia Jeshi la Polisi na kulishutumu kwa uzembe wa asilimia mia moja.



    Kwa hali hiyo, alitamani afe kwa siku kadhaa kisha afufuke, labda atakuta mambo yamepoa. Na kwa namna nyingine alijiona kama akiitwa ofisini kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, akitakiwa kujieleza ni kwa nini asichukuliwe hatua kwa kuliaibisha Jeshi la Polisi kwa kutoweza kumkamata mtuhumiwa na badala yake watu wanazidi kufa!



    'Unajiona kuwa bado unastahili kuwa askari wa Jeshi la Polisi? Bado unajiona kuwa unastahili kuitwa Inspekta? Nadhani inafaa uanze kutafuta ajira kwenye kampuni za ulinzi. Huko ndiko panapokufaa. Andika barua ya kuacha kazi mwenyewe. Si vizuri nikuandikie barua ya kukufukuza; nitakuwa nimekudhalilisha. Lakini kwa kweli, Jeshi la Polisi ni maji mrefu kwako!'



    Aliona kama ataambiwa hivyo muda mfupi ujao. Na hapo ndipo utakuwa mwisho wake wa kuitwa Inspekta Maliyatabu. Ataitema ajira kwa namna isiyopendeza. Atarudi uraiani na kuanza kuzungukia kwenye vijiwe vya kahawa, akiilaani serikali kwa hili na lile bila hata sababu ya msingi.



    Akavuta pumzi kwa nguvu na kujiegemeza kitini. Hakutaka kumtaarifu chochote mkuu wake kwa wakati huo na ili asipate presha, aliizima simu yenye laini inayojulikana kwa wakuu wake, badala yake akaiacha wazi ile ambayo huitumia zaidi kwa kuwasiliana na familia yake na marafiki zake wasiokuwa askari wa jeshi hilo.



    SURA YA KUMI NA SITA



    KAMBA aliingia ndani mwake haraka na moja kwa moja akaenda kwenye kibegi chake ambako alikifungua na kutoa pesa. Hakuwa na muda wa kuzihesabu lakini alihisi kuwa hazipungui milioni tatu kwa kuwa matumizi yote aliyokwishayafanya aliyakumbuka, hususan yale yaliyogusa zaidi ya shilingi laki moja.



    Akaziangalia na kuzirudisha ndani ya begi hilo. Haraka akaifungua ile bastola aliyompora Makela. Akakuta ina risasi tano. “Yaap!” akabwata kwa majivuno huku akiipachika katika mfuko wa kulia na ile ya kwake akiipachika mfuko wa kushoto.



    Mara akakumbuka. Akajishika kidevu na kufikiri kuhusu hatima yake kuanzia siku hiyo. Aliamini kuwa huenda asirudi hapo leo, kesho, keshokutwa au hata mwaka huu. Aliyokwishayafanya ni makubwa, lakini aliipenda nyumba yake hii, hivyo, hakutaka kuipoteza kijinga. Haraka akalifuata kabati kubwa ambako alifungua saraka moja na kunyofoa nyaraka mbalimbali. Alichakura waraka huu na ule na kufanikiwa kupata kile alichokihitaji. Hati za nyumba.



    Ndiyo, alizihitaji hati hizo. Kwake, hazikuwa ni hati bali almasi! Akazifutika ndani ya begi. Akafikiri ni kipi kingine muhimu cha kuchukua. Akafikiri kidogo na kuamua kuchukua uamuzi wa kubadili tena mavazi. Haraka akazivua nguo hizi zilizokumbana na mshikemshike. Akavaa shati jekundu la mikono mirefu na suruali nyeusi. Koti jeusi likafuata juu.



    Pia aliamua kuweka shati moja na suruali nyingine ndani ya begi. Vikatosha. Hakutaka kuwa na zigo zito.



    Akalipachika begi begani kisha akaitwaa simu na kutaka kumpigia Jitu. Akasita akiamini kuwa askari wanaweza kumfuatilia haraka hapo kwake ikiwa ni katika kumsaka kwa hasira zote. Akairejesha simu mfukoni na kuamua kutoka kwanza na baadaye, akiwa mbali na hapo ndipo ampigie.



    Alifunga mlango wa chumba chake cha malazi kwa funguo na akafanya vivyohivyo kwa mlango mkubwa wa mbele. Haraka akamfuata dereva wa pikipiki na kumwamuru, “Twende Mwenge lakini tusipite Kinondoni A. Umenisoma?”



    “Poa.”



    “Na iwe fasta!” Kamba aliongeza huku akipanda kwenye pikipiki hiyo. “Katisha Mkwajuni eneo la msikiti kisha upite vichochoro vitakavyotutokeza Vijana Social Hall au hata Komakoma. Kanyaga mafuta, mwanangu!”



    Dereva hakusema kitu, haraka akatia moto, pikipiki ikaingia barabarani kwa mwendo wa ajabu! Baada ya dakika chache wakawa wameshakatisha Mkwajuni na dereva akaonyesha kuwa yeye ni mtoto wa mjini anayevijua vichochoro vyote vya Kinondoni. Walipoingia Barabara ya Mwinjuma eneo la Komakoma, pikipiki ni kama vile ilikuwa ikipaa!



    Machozi yakawa yakimtoka Kamba kutokana na mwendo mkali wa pikipiki. Baada ya dakika kama kumi wakawa Mwenge ambako Kamba aliteremka na kuachana na pikipiki hiyo. Jirani na kilipokuwa kituo cha daladala zamani kuna baa kadhaa zilizosongamana, zikiwa katika eneo ambalo ni kama vile linaweza kuitwa mafichoni.



    Kamba alikwenda katika baa mojawapo na kuchagua kiti ambacho kilikuwa peke yake, akaketi na kuagiza maji baridi. Hakuwa na amani japo alijisikia kutua mzigo mzito uliokuwa ukimwelemea.



    Mara akajiwa na wazo ambalo lilimuumiza kichwa. Alimkumbuka mkewe, mama Safi na mwanaye, Safi. Hakujua wakati huo watakuwa wapi, lakini alihisi kuwa watakuwa mbali na wamefanya hivyo baada ya mama Safi kujua kuwa kuna jambo zito litakalotokea.



    Hakumlaumu mama Safi kwa kuchukua uamuzi wa kukimbia. Angebaki nyumbani wangemkuta na hata huko aliko, kama ni kwa ndugu zake Mungu amsaidie wasije wakambamba.

    Uchungu ulimjia alipomkumbuka mwanaye, Safi ambaye hata hajakaa naye walao kwa wiki moja. Na sasa kishafanya matukio ambayo yatamlazimu achukue hatua ya kujilinda zaidi, ikibidi aliweke Jiji la Dar es Salaam mbali na macho yake.



    Hata hivyo, papohapo akaamua kupiga moyo konde na kuiondoa mawazoni hiyo familia yake. Mwanamumume unapaswa kuwa na moyo wa jiwe. Alihisi sauti ikimwambia. Nguvu fulani zikamjia kama muujiza akiwa hajui zilikotoka. Ni kama kapandwa na nguvu za jini. Ujasiri ukamjaa. Akashusha pumzi ndefu na kuitoa simu mfukoni. Akaanza kulipekua jina la rafiki yake, Jitu. Alipolipata akaamua kumpigia.





    Gari la kifahari la rangi ya kijivu, Honda Civic lilikuwa limeegeshwa kando ya Barabara ya Old Bagamoyo eneo la Mikocheni jirani na Hospitali ya TMJ huku vioo vyake vya giza vikiwa vimefungwa. Ndani ya gari hilo kulikuwa na watu wawili, Jitu na rafikiye wa kike, Salsha. Walikuwa na zaidi ya saa nzima tangu walipokutana hapo, Jitu akitokea nyumbani kwake Mwananyamala-Komakoma na Salsha naye akitokea kwake, Ada Estate, Kinondoni.



    Jitu akiwa ni mume wa mtu, baba wa watoto watatu, Salsha alikuwa ni mke wa mtu na akiwa ni mama wa watoto wawili. Uhusiano wao ulizaliwa kiajabu-ajabu tu.



    Ilikuwa ni siku ambayo foleni ya magari ilikuwa kubwa na mvua ilikuwa imenyesha sana tangu mchana na kukatika wakati giza likipiga hodi. Jitu aliamua kuiepuka kero ya kumaliza saa kadhaa kwenye foleni barabarani hivyo alichofanya akiwa maeneo ya Posta ni kwenda Break Point na kuamua kunywa bia taratibu ili tu avute muda foleni ipungue.



    Ni wakati yuko hapo, akiwa peke yake katika meza aliyoichagua, ndipo alipompata mwenza huyu, mwanadada aliyevaa blauzi nyeupe na suruali ya rangi ya samawati iliyomshika maungoni. Macho ya mwanadada huyo yalimvutia Jitu kiasi cha kumfanya aisahau kwa muda bia yake iliyokuwa mezani.



    Ile tembea yake ya madaha na hayo macho yake yaliyotazama zaidi ya utazamaji wa kawaida, yakishawishi na kubembeleza, yaliivuruga akili ya Jitu na kujikuta akimkumbuka Mwanahamisi, mwanamke ambaye japo ilishapita miaka mitatu tangu walipoachana, hata hivyo bado hakuweza kumsahau kwa kile alichoamini alikuwa ni mrembo sana hadharani, hodari sana jikoni na fundi mzuri kitandani.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Akahisi mwili ukimsisimka kadri alivyozidi kumtazama mrembo huyo huku akijiwa na kumbukumbu ya yale aliyokuwa akifanyiwa na Mwanahamisi faraghani enzi za uhusiano wao.



    Hata huyu ni kama Mwanahamisi…uwe ni mwanamume uliyekamilika…mwingie kwa kujiamini…mbona ulishawapata wengi wazuri zaidi yake? alihisi sauti ikimnong’oneza.



    Ujasiri ukamjia, uvumilivu ukatoweka. Japo hakuwa mpenzi wa kutoka nje ya ndoa kwa kuwa alimpenda na kumheshimu sana mkewe, hata hivyo hakuwa amepigwa pingu ya kutofikia hatua ya kumpenda mwanamke mwingine.



    Hivyo, alijikuta akimpenda huyu mrembo lakini zaidi, alimtamani. Wakati walipokutanisha macho, Jitu alimkonyeza huku akitabasamu kisha akamwashiria kwa mkono aende pale mezani.

    Tabasamu lake likajibiwa na tabasamu hafifu kutoka kwa mrembo huyo na wito wake ukakubaliwa. Dakika iliyofuata walikuwa pamoja, Jitu akiendelea kunywa bia huku mrembo huyo akipata mchemsho wa samaki aina ya sato. Dakika kadhaa baadaye, Jitu alikuwa ameshalijua jina la mrembo huyo kuwa ni Salsha, anaishi Ada Estate, mke wa mtu.



    Salsha naye akajua kuwa Jitu ni mume wa mtu na anaishi Mwananyamala, Komakoma. Wakawa marafiki wa kawaida, wakiwa na mazungumzo ya kawaida, mazungumzo ambayo baadaye yalianza kubadilika kutokana na mazoea kukomaa sanjari na Salsha kuanza kunywa bia.



    Hoja ya mapenzi ikatumbukizwa na Jitu. Salsha akajitia kusitasita kwa aibu za kike. Jitu akajua kuwa ni katika kufuata falsafa zao; Usiwe maharage ya Mbeya mwanamke…usikubali kirahisi-rahisi kama changudoa… maneno hayo yalikwishazoeleka katika vinywa vya wanawake pale wanapokutana na kuanza kuzungumzia mapenzi.



    Hata hivyo, Jitu aliamua kuchokoza, mkono ukapotea njia na kutua kwenye paja la Salsha. Salsha hakuutoa, akaishia kuguna. Bia zilizokwishapenya matumboni mwao ziliizibua mishipa ya aibu vichwani. Kila kitu kikawa sawa kwao kwa wakati huo, kikawa sawa kukisema na kukitenda.



    Sasa mkono wa Jitu ukateleza kwa mapozi ya aina yake, ukipanda juu zaidi huku ukitomasa kwa namna ya kipekee. Salsha akaguna na kuushika, akiuzuia usiendelee na ziara yake, likiwa ni zuio la kimagumashi. Jitu alipotii, Salsha naye akaanza uchokozi, mkono wake laini ukitua katikati ya miguu ya Jitu na kugusa eneo fulani kwa namna iliyomfanya Jitu ajihisi tofauti na awali. Msisimko wa ajabu ukampata.



    Mkono huo ukaendelea kufanya mchezo huo kwa chati bila ya watu waliokuwa katika meza nyingine kutambua na hata hivyo, kutokana na mwangaza hafifu wa glopu zilizokuwa ukumbini hapo, na kwa kuwa waliketi pembezoni, hiyo ilitosha kuwafanya wateja wengine wasibaini kilichokuwa kikiendelea.



    Kikafikia kipindi Jitu na Salsha walitamani umeme ukatike, kiza kitawale maradufu na waamue kufanya chochote kingine walichokihitaji. Hata hivyo, haikuwa kama walivyotaka, umeme haukukatika na idadi ya watu ikaongezeka, hali iliyowakosesha uhuru wa kuendelea kufanya yale waliyohitaji kuyafanya. Wakaamua kuondoka.



    Njiani Jitu alidadisi, “Mzee huwa hakufuatilii?”



    “Hayupo.”



    “Kasafiri?”



    Salsha akaitika kwa kutikisa kichwa.



    Lilikuwa ni jibu zuri kwa Jitu. Walipofika kituo cha daladala cha Mbuyuni, Salsha aliteremka na wakakubaliana kuonana baada ya siku mbili.



    Uhusiano wao ukawa umezaliwa siku hiyo. Ukakua na kukomaa japo kwa siri, wakikutana kwa siri katika hoteli zenye hadhi ambako walijichimbia kwa saa kadhaa, wakifanya kile walichopenda kukifanya.



    Jioni hii hawakutaka kwenda katika hoteli yoyote, walitaka kubadili mazingira ilimradi nafsi zao ziburudike na kuridhika. Ndipo walipokuja kukutana hapa kando ya barabara, eneo hili la Mikocheni na kujichimbia ndani ya gari hili la kifahari. Jitu alikuwa amebeba vinywaji vya bei ghali na mara tu alipoegesha gari hapo, kitu kama saa 12 jioni, alifungua chupa kubwa ya pombe kali, Ballantine’s iliyotengenezwa Scotland na kuanza kunywa taratibu huku akimsubiri Salsha.



    Japo joto kali lilikuwa likinyanyasa ndani ya jiji hilo, hata hivyo ndani ya gari hili la kifahari, Honda Civic joto lilikuwa ni kitu kisichojulikana kuwa ni nini na kina umbo gani.



    Akatwaa simu yake na kufungua kwenye mtandao wa facebook. Akashtuka baada ya kukuta kuna hoja kuhusu matukio ya kutisha yaliyotokea siku hiyo jijini Dar. Kwamba, watu wanne wameuawa kikatili na muuaji hajapatikana.



    Blogu mbalimbali nazo zikalizungumzia tukio hilo la vifo vya kushangaza huku habari hizo zikikosa tamko rasmi la Jeshi la Polisi kuwa nani mhusika au nani anashukiwa kuhusika. Kilichomshtua Jitu ni kusoma maandishi ya mtu mmoja aliyeandika kuwa watu watatu wameuawa katika jengo moja kwa risasi na kisu Mtaa wa Mosque na akawataja majina kuwa ni Ladhu H. Ladhu, Hassanali na Juma.



    Jina la Ladhu likamshtua Jitu. Na akazidi kushtuka pale aliposoma kuwa mtu wa nne aliyeuawa mchana ni Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay, James Ntilampa. Papohapo Jitu akamkumbuka Kamba. Akakumbuka kuwa siku walipokutana pale Uhuru Peak, Mwinjuma Road, Kinondoni, baada ya maongezi yao kufikia tamati Kamba alimuulizia Ladhu H. Ladhu, tajiri wa Kihindi aliyekuwa na duka kubwa Mtaa wa Mosque na alitamka bayana kuwa alitaka amfanyizie. Huenda ni yeye aliyemuua Ladhu!



    Hata hivyo, hakutaka kuliwazia sana tukio hilo japo aliamini kuwa kwa vyovyote vile, Kamba ndiye atakayekuwa amefanya mauaji hayo. Yeye alikuja hapo kuiburudisha nafsi yake. Alihitaji kuiliwaza akili na kustarehe na mwanamke mzuri, Salsha kisha awahi kurudi nyumbani.



    Akawa akiendelea kuchat na marafiki zake wengine wenyenazo huku akinywa taratibu whisky yake.



    Mara akaona gari likiegeshwa mbele kidogo kutoka pale alipoegesha yeye. Ilikuwa ni teksi. Dakika iliyofuata akamwona Salsha akiteremka na kumjia. Alipofika, alifungua mlango na kujitupa kitini.



    “Ooohh baby…” Jitu alimkaribisha kwa kumkumbatia. Vifua vyao vikagusana. Manukato makali aliyojipulizia Salsha yakamfikia Jitu sawia. Ndimi zao zikakutana na kuganda kwa muda katika busu hilo. Walipoitenganisha midomo, Salsha akahema na kumkumbatia Jitu kwa nguvu.





    “Vipi, nimechelewa sana?” hatimaye Salsha alijikakamua kuuliza.

    “Hujachelewa,” Jitu alijibu kwa sauti nzito ya majidaidai, sauti iliyotoa taswira ya kujiamini kimasilahi, sauti ya mtu aliyekwishautupa umaskini kilomita mia moja. Kisha akajikohoza kiukwasiukwasi na kuongeza: “Umekuja muda mwafaka. Unajua kutunza muda.”



    “Asante,” Salsha alisema huku akikiseti kiti, kikalala na yeye akajilaza kivivu.



    Ukimya mfupi ukapita kisha Salsha akasema, “Kijigiza kimeingia, utakunywa baadaye ukiwa na mkeo…mimi ni mwizi tu, hivyo nikipata nafasi inabidi niitumie kikamilifu ili nifaidi eti, baby?” wakati huo mkono mmoja ulikuwa ukifungua vifungo vya shati la Jitu na kifua kilipobaki wazi akaanza kuzinyonya chuchu zake.



    Jitu akahema kwa shida, msisimko ukampanda na kabla hajafikiria achukue hatua gani, akahisi mkono mwingine wa Salsha ukimpapasa tumboni na kisha ukashuka taratibu hadi chini ya kitovu ambako sasa ulishughulika na lisani ya suruali yake. Salsha alikuwa ni mtaalamu ajuaye jinsi ya kutumia ulimi na mikono kwa namna ya kipekee na kuivuruga akili ya mtendewa kwa kiasi kikubwa.



    Hizi ‘fujo’ zake zilimfanya Jitu ajione kama anayepaishwa hadi katika dunia nyingine, dunia yenye kila kitu kizuri na kitamu, dunia isiyojua kuwa kuna kuugua au kufa. Viganja laini vya mikono ya Salsha vilivyojua kutomasa kitaalamu sanjari na joto la kinywa ambacho sasa kilikuwa kimehama kutoka kwenye chuchu za Jitu na kutua mahala pengine, katika shughuli nyingine pevu, vikamfanya ashindwe hata kutamka chochote alichotaka kutamka. Jitu na ujanja wake akakamatika mwanamume!

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    KILICHOFUATA dakika kadhaa baadaye ni mtikisiko mdogo wa gari na mihemo ya hanjamu vilivyotawala na hata simu ya Jitu ilipoita hakujali. Alikuwa katika dunia nyingine aliyoamini kuwa ndiyo dunia ambayo binadamu wa leo anastahili kuishi. Salsha alikuwa akionyesha ni kwa kiwango gani anastahili kuwa kwenye daraja la mwanamke mrembo sana hadharani na mtundu sana faraghani.

    Nafsini mwa Jitu, Salsha alikuwa ni zaidi ya binadamu wa kawaida.



    Dakika kumi baadaye walitengana, nafsi zao zikiwa zimeridhika. Wakatazamana, kila mmoja akimwazia mwenzake. Salsha alikuwa akikumbuka jinsi Jitu alivyokuwa akijituma na kwa mara ya kwanza akajikuta akijisemea moyoni, ‘Hata Baba Wema hamfikii…’



    Jitu naye alijikuta akitenda dhambi, kama kweli ni dhambi kwa kumlinganisha mkewe, Mama Hadija na huyu Salsha na ndipo alijikuta akikiri, ‘pamoja na kuwa waifu ana mambo yake mazuri hasa anapokunywa bia, lakini mmh… Salsha anatisha…nampa asilimia zote…ana viwango kama wacheza sinema za ngono wa Uholanzi, Italia, Japan na Amerika Kusini.’



    Wakati wakiyawaza hayo, walikuwa wamejilaza kwenye kiti, burudani ya kiyoyozi ikiendelea kuwapata. Ukimya ulitawala na wala Jitu hakukumbuka kuwa muda fulani uliopita simu yake ilikuwa ikiita. Alikuwa akiyakumbuka aliyotoka kuyafanya dakika chache zilizopita.

    Alizinduka baada ya kuisikia kwa mara nyingine simu yake ikiita.



    Akanyanyuka na kuichukua. Sasa hakujilaza tena kitini, badala yake aliketi na kuangalia kwenye kioo cha mbele. Akaguna. Zilikuwa ni namba ambazo hakuzijua. Na hakuwa na kawaida ya kupokea simu zenye namba ambazo hajazihifadhi katika simu yake. Simu iliita hadi ikakatika. Akatulia. Punde ikaanza kuita tena.



    “Mbona hupokei?” Salsha alimuuliza.



    “Sina kawaida ya kupokea simu nisizozijua.”



    “Na huwezi kupigiwa simu kwa namba unazozijua tu maishani mwako,” Salsha alisema. “Simu nyingine ni mpya kwako na huna budi kupokea. Huwezi kujua, huenda anayekupigia kapewa namba na mtu anayekufahamu.”



    Ni nani huyu, alijiuliza kimoyomoyo, akiamini kuwa siyo kwamba mtu huyo atakuwa amekosea namba kwa sababu hii alikuwa akipiga kwa mara ya tatu! Akapiga moyo konde na kubonyeza kitufe cha kupokelea kisha akaitega sikioni bila ya kutamka chochote.



    “Haloo, Mr. Jitu,” aliisikia sauti kutoka upande wa pili, sauti ya kiume.



    “Yaap,” Jitu alijibu kwa sauti ya chini na nzito.



    “Kamba.”



    Moyo wa Jitu ukapiga pa! Hakujua ni kwa nini ameshtuka kwa kulisikia jina hilo. Tangu alipowasiliana na Kamba na kumkabidhi pesa za ‘pole’ kisha akampa bastola, hakukuwa na mawasiliano yoyote tena baina yao. Alikumbuka kuwa alimpa namba ya simu siku alipompokea uraiani nje ya gereza la Keko siku Kamba alipoachiwa huru. Walipokuja kukutana na kuzungumza, Jitu hakupewa namba yoyote ya simu na Kamba. Mawasiliano yao yalipotea zaidi baada ya bastola kutua katika himaya ya Kamba.



    Leo huyu aliyepiga anajitambulisha kuwa ni Kamba! Halikuwa jambo la kushangaza sana kwa Jitu kwani alihisi kuwa huenda Kamba aliihifadhi namba ile na baada ya kununua simu ndiyo kampigia.

    “Kamba? Kamba wa wapi?” aliuliza swali la mtego.



    “Kamba Kiroboto.”



    “Ehee…sema bro!”



    “Sikia Jitu,” Kamba alisema kwa utulivu, “Nimeshaharibu.

    Nimelikoroga.”



    “Unasema?”



    “Nimeshaharibu, mshkaji wangu. Kazi nimemaliza. Lakini nataka tuonane.”



    Jitu hakuwa mtu wa kuyatafakari sana maneno ya Kamba. Alimjua, na alipolinganisha na maneno aliyoyakuta kwenye mtandao wa facebook kuhusu mauaji yaliyotokea asubuhi na mchana, aliielewa haraka maana ya neno hilo, nimeshaharibu.



    Papohapo akamuuliza, “Uko wapi?”



    “Mwenge.”



    “Mwenge ipi?”



    “Hapa jirani na kituo cha daladala cha zamani lakini kwenye baa moja kwa ndani kidogo.”



    Ukimya ukapita, Jitu akiwaza. Tayari alishahisi kuwa Kamba anatafuta msaada wa hifadhi au mawazo ya kumnusuru na tatizo la msako kama litakuwa kubwa. Akamuuliza, “Unadhani hapo ulipo ni pazuri kwa kukutana?”



    “Kwa kiasi fulani. Siyo baa inayovuta watu wengi.”



    “Ok, toka hapo kwenye kibaa unachosema, nenda Maryland. Acha woga. Nenda hapo. Nitakukuta baada ya dakika zisizozidi ishirini. Sawa?”



    “Poa.”



    Jitu alikata simu na kumtazama Salsha aliyekuwa bado amejilaza kitini. Akamwambia, “Kuna dharura, baby.”



    “Na wewe!” sauti ya Salsha ilikuwa ikilalamika. “Sasa kuna maana gani ya kunileta huku?”



    “Ndiyo maana nimesema ni dharura. Sikutarajia kuwa hili lingetokea. Usijali. Twende nikakuache pale kwenye kituo cha daladala cha Morocco, uchukue teksi.”



    “Lakini mbona sikuelewi baby?” uso wa Salsha ulisomeka kutomwamini Jitu.



    “Unapaswa kuwa mwelewa Salsha,” Jitu alijibu. “ Aliyenipigia ni jamaa yangu ambaye yuko Mwenge Mlalakuwa. Mkewe ni mjamzito. Anahitaji msaada wangu fasta! Mbona hunielewi? Au huniamini?”



    “Basi yaishe. Kama ni kweli au uongo Mungu nd’o anajua. Nipeleke Morocco.”



    Jitu aliwasha gari na kuliondoa kwa makeke akielekea kituo cha daladala cha Morocco. Amani ilitoweka, Salsha alinuna lakini Jitu hakujali. Alikuwa na msimamo wa kutoyumbishwa na mtu yeyote pale anapochukua uamuzi wa kufanya chochote alichoamua.

    Hakuwa mtu wa kutengua uamuzi wake eti kwa kuwa anayempinga ni mkewe, hawara yake, shehe, askofu au askari polisi.



    Walipofika Morocco Jitu akamwita dereva teksi na kumwambia, “Mpeleke huyu sister Ada Estate.?”



    Kisha akachomoa noti mbili za shilingi elfu kumi, kumi na kumpatia Salsha. “Utamlipa,” alimwambia kasha akambusu kwenye papi za midomo na kumalizia, “Baadaye basi.”



    “Poa,” Salsha alijibu kwa unyonge huku akiteremka na kumfuata dereva wa teksi.



    Jitu alitulia mpaka alipoiona teksi hiyo ikiondoka ndipo na yeye akaing’oa Honda Civic akielekea Mwenge.



    *******



    KAMBA alifuata maagizo ya Jitu. Akaenda Baa ya Maryland na kukuta wateja wengi lakini nafasi ilikuwapo. Akaketi na kuagiza bia katika meza ambayo kulikuwa na mhudumu wa kike ambaye alikuwa akisubiri oda. Kisha akaiweka simu mezani na kuitazama mara kwa mara akitarajia kupigiwa muda wowote na Jitu pindi atakapofika. Dakika tano baadaye simu ikaita. Alikuwa ni Jitu.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nimefika.”



    “Niko ndani,” Kamba alisema.



    “Siingii. Nimepaki gari hapa nje. Honda Civic ya kijivu. Huko ndani hapaaminiki.”



    Kamba aliinywa bia kama anayefukuzwa, kisha akaitua chupa mezani na kunyanyuka. Alipotokeza nje akaliona gari hilo likiwa limefungwa vioo. Akalifuata na alipofika akaona mlango ukifunguka. Hakufikiri mara mbili, akajitoma ndani kwenye kiti cha mbele.



    “Enhe, n’ambie!” Jitu alimwahi.



    “Nd’o kama nilivyokwambia. Ni’shaharibu.”



    “Najua,” Jitu alisema kwa utulivu akionekana kutoshtushwa na kauli ya Kamba. “Nimekuta status za kumwaga kwenye facebook, kila mmoja akisema lake, mwanangu. Ina maana ni wewe uliyewamwaga wale Wahindi?”



    Kamba aliitika kwa kutikisa kichwa.



    “Na OCS wa Oysterbay?”



    “Mkono wangu.”



    “Duh! Vichwa vitatu kwa muda mfupi hivi!”



    “Ni afadhali vingekuwa vichwa vitatu. Ni vitano!”



    Jitu aliguna, akamtazama kwa macho makali. “ Mbona sikuelewi?” hatimaye alimuuliza.



    “Kijakazi mmoja wa wale Wahindi alijitia kutaka kuleta za kuleta, nikamweka kwenye listi, nikamwondoa! Na sasa hivi nimetoka kumzimisha yule dingi…hakimu dadadadek!”



    Jitu alikunja uso na kutazama mbele. Ukimya ukapita, akiiwazia taarifa hiyo. Kisha akasema, “Imeshatokea. Kwa hiyo umeniita ili?”



    “Nilitaka ujue kuwa nataka nisepe. Najua wajeda wananisaka kama gaidi kwa kutaka kwao sifa mabwege hao. Wakinipata msh’kaji wangu wanaweza kunigeuza mshkaki…hawana akili nzuri wale! Utanipigaje tafu?”



    “Nikupige vipi tafu tena Kamba?” Jitu alionekana kumshangaa. “Umekuwa na pupa sana kwa hasira zako! Sidhani kama ilibidi uwe na haraka kiasi hicho!”



    “Imeshatokea Jitu. Na sasa roho yangu imesuuzika. Ninachojua ni kwamba IGP, waziri wa mambo ya homu na rais wake, wote wana hasira na mimi! Hawali, hawalali mpaka wanipate!”



    “Unalo hilo,” Jitu alisema kama anayemdhihaki. “Kwa hiyo unataka kuniambia nikusaidieje?”



    “Please, niongeze pesa,” Kamba alisema kwa utulivu.



    “Pesa!” Jitu alimtolea macho Kamba. “Msh’kaji sikusomi ujue…!”

    “HUNISOMI vipi tena msh’kaji wangu? Usishtuke. We’ nifanyie mpango wa pesa niondoke hapa bongo. Unataka wajeda wanidake mtu wangu?”



    “Unataka kwenda wapi?”



    “Siyo Ulaya. Jirani tu. Nadhani Bujumbura patanifaa. Yeah, Bujumbura au Kigali. Kongo hapana, kule hapatofautiani na Ukanda wa Gaza, hapanifai.”



    Jitu alikodoa macho mbele kama anayetazama kitu chochote kwa umakini. Hata hivyo hakuwa akitazama chochote, alikuwa kazama mawazoni kuhusu ombi hili la rafikiye, Kamba. Ni majuzi tu kampa shilingi milioni tano za pole ya kusota gerezani. Na kwa kipindi hiki kifupi, tena kwa siku moja, kishaua watu watano!



    Hakumlaumu kwa mauaji aliyoyafanya, alijua kuwa mateso aliyoyapata kwa kipindi chote alichokuwa gerezani ndiyo yaliyomwathiri kisaikolojia na hivyo kuwa na hasira dhidi ya kila aliyehusika katika kumfanya asote miaka saba jela. Sasa anahitaji msaada mwingine, tena msaada wa fedha taslimu kwa ajili ya kuondoka Tanzania!



    Lilikuwa ni suala zito na lililomshangaza Jitu. Papohapo akaitwaa ile chupa ya kinywaji kikali, akafungua dashibodi na kutoa kijiglasi, akamimina kiasi kidogo cha pombe na kunywa kwa mkupuo. Akashusha pumzi ndefu na kukunja uso.



    “Sasa tuzungumze kama wanaume,” Jitu hatimaye kwa sauti yenye uthabiti. Akatulia kidogo akikodoa macho mbele. Kisha akachomoa pakiti ya sigara kwenye dashibodi, akaipigapiga kwa kidole cha shahada, sigara mbili zikachomoza ndani yake. Akatoa sigara moja na kuiwasha.



    Akazima kiyoyozi, akafungua dirisha na kuvuta huku akipuliza moshi nje. Akakohoa kidogo na kusema, “Hoja yako inahusu pesa. Ni suala ambalo siyo la kulichukulia kwa wepesi wa kawaida. Unataka kiasi gani na kwa misingi gani?”



    Kamba alishusha pumzi kwa nguvu. Akajiweka vizuri kitini kisha akasema, “Milioni kumi! Na siyo ki-hivihivi. Hapana, naacha dhamana ya kitu.”



    “Kitu gani kwa milioni kumi zote?”



    “Nyumba yangu.”



    Jitu alitikisa kichwa na kusema kwa dharau, “Nyumba isiyokuwa na hati ni nyumba hewa, Kamba. Viwanja vya Kinondoni Moscow vyote ni vya uvamizi.”



    “Siyo vyote,” Kamba alipinga. “Wengi tumeshahalalishwa na kupewa hati za umilikaji wa viwanja na hata kodi za majengo tunalipa.”



    “Usiniletee stori za kimagumashi mtu wangu,” Jitu alisema kwa madaha na sauti ya dhihaka.



    “Ya nini kupoteza muda, Jitu?” Kamba alihoji huku akifungua begi na kutoa hati za nyumba yake. “Hebu zicheki hizi.”



    Jitu alizipokea nyaraka alizopewa, akatumia simu yake kuzitazama kwa makini, kisha akahoji,“Kwa muda gani unataka nizishike hizi karatasi zako?”



    Lilikuwa ni swali ambalo lilimpa matumaini Kamba. Kwa mara nyingine akashusha pumzi ndefu na kumnyooshea dole gumba Jitu.



    “Miezi sita,” alijibu.



    “Ikizidi?”



    “Nyumba halali yako.”



    “Hata hivyo bado kuna jambo hapo,” Jitu alisema. “Hapa inatakiwa tuweke mkataba wa maandishi na ikibidi tuwe na mwanasheria. Kuaminiana kihivihivi tu katika dunia ya sasa siyo rahisi mshkaji wangu. Lakini muda huo haupo. Hapo ndipo ugumu unapokuja. Halafu kuna jambo lingine.”



    “Jambo gani tena?”



    “Timu ya IGP lazima itakusaka hadi kwako, na watakapogundua kuwa haupo, nyumba yako itatupiwa macho kwa saa ishirini na nne. Hapo ndipo inaponiwia vigumu kusema kuwa nitakuwa naimiliki nyumba hiyo au nitakuwa nazimiliki hizi karatasi zako. Kwa vyovyote vile wajeda wakijua kuwa ni mimi ndiye nimebaki nayo, napigwa pingu. Nakwenda kuozea jela. Kudadadadeek! No! Kwa kweli siko tayari kuingia choo cha kike msh’kaji wangu! Inabidi unielewe hivyo. Umenisoma?”



    Kamba alishusha pumzi ndefu za kukata tamaa. Kisha kwa unyonge akauliza, “Sasa utanipaishaje msh’kaji wangu?”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Umelikoroga…lakini cha kufanya sasa ni kutafuta pa kujichimbia kabla ya kuondoka,” Jitu alimwambia. “Usikurupuke kuondoka ovyo, watakudaka njiani ka’ kuku aliyelowa. Tafuta hoteli yoyote ujichimbie kwa siku mbili, tatu. Kuna hoteli nyingi zisizo maarufu lakini ziko fresh maeneo ya Kariakoo na Manzese. Tena ni za bei poa tu. Hizi hati zako kaa nazo. Mjengo wako una thamani ya zaidi ya milioni hamsini. Tulia, huenda mambo yakapoa, ukaja kuuza bila ya matatizo. Jaribu kupoa kwa kama wiki hivi ukisikilizia. Kama mambo yatakuwa bado moto na ukaona kweli wanakusarandia hapo nitakubusti kidogo ili usepe, mwana.”



    Saa tano usiku huo Kamba alikuwa Manzese, Tanganyika Hotel ambako aliamua kukaa kwa siku mbili kabla hajaamua cha kufanya.



    **********



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog