IMEANDIKWA NA : INNOCENT A. NDAYANSE
*********************************************************************************
Simulizi : Mtikisiko Wa Hirizi
Sehemu Ya Kwanza (1)
SIYO KWAMBA KILA MWANADAMU ANAAMINI KUWA ILI UTATUE TATIZO LOLOTE LINALOKUKABILI LAZIMA UWE NA ELIMU YA KIWANGO KIKUBWA, UWE MJANJA WA MJINI AU MCHA MUNGU UTEGEMEAYE MAOMBEZI KWA KUFANIKISHA MAMBO YAKO. WAPO AMBAO HAWAPO KATIKA MAKUNDI YOTE HAYO. WAO HUAMINI ZAIDI KATIKA KILE KINACHOITWA ‘NGUVU ZA GIZA.’ KATIKA RIWAYA HII UTASHUHUDIA MAMBO YANAYOFANYIKA CHINI YA JUA, YAKIWASTAAJABISHA WALE WENYE AKILI ZA KAWAIDA NA KUWASISIMUA WENYE MIOYO YA KIJASIRI. ANZA KUTIRIRIKA…
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MWAKA 2002
MVUA ya rasharasha iliyoanza kunyesha tangu asubuhi mjini Kigoma, iliendelea hata usiku ulipotinga. Na hakukuwa na dalili ya kukatika au kuongezeka. Hilo halikuwa jambo la ajabu kwa kipindi hicho cha masika mvua kunyesha kwa zaidi ya saa 10. Lilikuwa ni jambo la kawaida.
Usiku huo, Mzee Songoro alikuwa nyumbani kwake, itongoji cha Mwanga, Mtaa wa Mabatini akisubiri mlo wa usiku uliokuwa ukiandaliwa na mkewe. Alikuwa ameketi sebuleni akitazama televisheni huku pia akisubiri taarifa ya habari.
Ilipotimu saa 2.00 kituo fulani cha televisheni kikaanza kutangaza taarifa ya habari, muhtasari ukiwa utangulizi wa habari yenyewe. Kwanza Mzee Songoro alishtuka, kisha akashangaa. Hakuyaamini masikio wala macho yake. Akatega masikio kwa makini na kukikodolea macho makali kioo cha televisheni.
Kisha habari kamili ikaanza:
JAMBAZI SUGU, ALIYETUHUMIWA KWA MAKOSA MBALIMBALI YAKIWAMO YA UBAKAJI, WIZI WA KUTUMIA SILAHA NA MAUAJI, SHAKA SONGORO, LEO AMEHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA BAADA YA MAHAKAMA KURIDHIKA NA MAELEZO YA UPANDE WA MASHTAKA, MAELEZO YALIYOAMBATANA NA USHAHIDI MZITO ULIOMTIA HATIANI MSHTAKIWA…
Ilikuwa ni habari ndefu iliyoambatana na picha ya mtuhumiwa huyo. Na ikawa ni habari iliyomshtua na kumsononesha Mzee Songoro kwa kiasi kikubwa. Hakuendelea kuitazama televisheni hiyo wala kutega masikio kusikiliza habari nyingine.
Alinyanyuka na kuvuta hatua mbili akielekea jikoni, lakini mara akasita. Akarudi sofani na kujipweteka pwaa!
Akashusha pumzi ndefu. Kisha akaita kwa sauti kali: “Mama Shaka! Mama Shaka weee!”
Ilikuwa ni sauti iliyoyafikia masikio ya mkewe kwa usahihi, ikamshtua na kumshangaza. Akaacha kufanya alichokuwa akikifanya. Akaenda sebuleni huku akitweta.
“Vipi, baba Shaka?”
“Keti,” Mzee Songoro alimwamuru huku kakunja uso.
“Kuna nini baba Shaka, mbona unaniweka roho juu?” Mama Shaka alihoji huku akijipweteka sakafuni puu!
Mzee Songoro hakuwa na pupa ya kuzungumza. Alitulia na kushusha pumzi kwa nguvu. Kisha akaingiza mkono ndani ya mfuko wa koti lake jeusi na kutoa msokoto wa tumbaku.
Akauweka mezani na kuingiza tena mkono huo ndani ya mfuko wa suruali. Huko akatoa kibiriti. Akahema kwa nguvu na kumtupia jicho Mama Shaka. Akagundua kuwa amekumbwa na woga.
“Tulia,” alimwambia. “Tulia. Usihofu, Mama Shaka.” Akauwasha msokoto wa tumbaku yake na kuvuta mikupuo miwili, mitatu kwa nguvu. Muda mfupi baadaye akapuliza moshi angani. Sasa akayarejesha macho kwa mkewe, Mama Shaka.
“Shaka amefungwa!” alisema kwa sauti nzito na ya chini sana akionyesha dhahiri kukumbwa na fadhaa.
“Nini?!” mkewe alitokwa macho pima. “Unasemaje Baba Shaka?”
“Shaka amefungwa!” Mzee Songoro aliirudia kauli yake, safari hii kwa msisitizo mkali.
“Nani kakwambia?”
“Hiyo hapo,” Mzee Songoro alisema huku akimwonesha mkewe kwenye televisheni. “Wametangaza sasa hivi na nimeiona picha yake kwa macho yangu haya!” akakielekeza kidole cha shahada usoni pake.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mama Shaka alijikunja na kujikunjua pale sakafuni. Akahema kwa shida akiwa hayaamini masikio yake.
“Unaikumbuka ile kesi iliyokuwa ikimkabili?” Mzee Songoro alimuuliza.
“Ndiyo, naikumbuka.”
“Basi ni hiyo iliyomfunga.”
“Mungu wangu! Mwanangu Shaka!” Mama Shaka aliomboleza. “Mwanangu Shaka kafungwa! Kafungwa miaka mingapi?”
“Miaka mingapi?” Mzee Songoro alimtazama mkewe kwa namna ya kumshangaa. Kisha akaongeza, “ Siyo wa kutoka leo au kesho. Ni mpaka kiama!”
“Mungu wangu!” mkewe aliomboleza tena huku akitokwa machozi. Akajipigapiga kifuani kwa uchungu. Kisha akauliza, “Una maana kahukumiwa kifo?”
”Hakuna tofauti na kuhukumiwa kifo,” Mzee Songoro alijibu. “Hatutakaa naye tena hapa nyumbani tukizungumza. Kuonana kwetu ni mpaka twende gerezani, na huko mtu unapewa dakika mbili, tatu tu za kuzungumza naye, tena askari akiwa kando yenu.”
Ulipita ukimya mfupi, wote wakiwa wamezama mawazoni. Mara Mzee Songoro akaibuka tena, na kwa msisitizo mkali akasema, “Mama Shaka, siwezi kumwacha mwanangu wa pekee afie jela. Kwa hilo siko tayari!”
Mkewe aliunyanyua uso na kumtazama, kisha akauliza, “Sasa utafanya nini Baba Shaka?”
“Nitajua la kufanya, lakini ni lazima nimwokoe mwanangu!”
*******
KILIKUWA ni kiapo cha Mzee Songoro, kiapo alichokitoa kwa dhati, kutoka moyoni mwake. Alfajiri ya siku iliyofuata aliamka na kutwaa kijimfuko kidogo, cheusi kisha akaondoka. Akachapa mguu hadi Mwembetogwa ambako alipata usafiri wa basi lililokuwa likielekea Kasulu. Yeye hakuwa na safari ya Kasulu, gari lilipokipita Kijiji cha Simbo na kwenda kilometa chache mbele, aliteremka.
Hapo alipoteremkia hakukuwa hata na nyumba wala dalili ya uhai wa binadamu. Kulikuwa na pori zito. Abiria wenzake, dereva na kondakta walimshangaa, lakini hawakumdadisi kuhusu hilo.
Akapenya ndani ya pori hilo, akitembea taratibu huku akijitahidi kuiepuka miba na kujihadhari na nyoka waliosemekana kulitawala eneo hilo. Alikuwa makini wakati akilivaa pori hilo, akiangaza macho huku na kule na kwenye mti huu na ule hadi alipokomea chini ya mti aliouhitaji.
Akautazama mti huo huku kwa mbali akitetemeka. Hakuwa akitetemeka kwa hofu, bali alitetemeka kutokana na baridi kali iliyopenya maungoni mwake. Akafungua ule mfuko wake mweusi na kuchomoa kisu. Akausogelea mti huo na kuanza kuuparua magamba taratibu na kwa umakini wa hali ya juu.
Magamba hayo alikuwa akiyaweka ndani ya mfuko huo. Alipotosheka na idadi ya magamba aliyopata, alianza safari ya kurejea nyumbani, moyoni akiwa amesuuzika kwa mafanikio ya safari yake.
Alipofika nyumbani hakuwa na haraka ya kumtaarifu chochote mkewe. Alitulia hadi baada ya mlo wa usiku ndipo alipomwita na kumwambia, “ Kesho n’taondoka.”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sijakuelewa, baba Shaka,” mkewe alisema huku akiondoa vyombo vilivyotumika kwa maakuli.
“Kesho n’taondoka!” Mzee Songoro aliirudia kauli yake, safari hii kwa msisitizo. “Nakwenda Dar kumkomboa mwanangu.”
“We baba Shaka, utamkomboaje mwan’etu?” Mama Shaka aliuliza huku akiacha kufanya kila alichokuwa akikifanya. Akasimama wima na kumtazama mumewe kwa mshangao, mikono kaikita kiunoni.
“Hayo nitayajulia hukohuko,” Mzee Songoro alisema. “Lakini kwenda ni lazima. Nina hakika Shaka hataendelea kusota gerezani, labda mimi nisiwe Songoro niliyezaliwa Tongwe na kukulia Kasingirima Ujiji kabla ya kuja kujenga huku Mwanga.”
Naam, Mzee Songoro hakuwa na mzaha kuhusu suala hilo. Alidhamiria kumtoa mwanaye kifungoni, iwe, isiwe.
Asubuhi ya siku iliyofuata alikwenda Stesheni na kuonana na mtu mmoja, mfanyakazi wa Shirika la Reli ambaye alimpatia tikiti ya Daraja la Tatu ya kumtoa Kigoma hadi Dar es Salaam.
Kisha alirudi nyumbani na kuanza kujiandaa rasmi kwa safari hiyo ya dharura. Alikwenda kwenye duka la jirani ambako alinunua chupa ya maji yenye ujazo wa nusu nusu lita, akaweka akayanywa maji kidogo mbele ya muuza duka kisha akaondoka na mbele kidogo akayamwaga maji yaliyosalia.
Kwa kujidai akaenda nyumbani ambako alitwaa yale magamba aliyoyatoa porini jana yake na kuanza kuyaponda.
Zoezi la kuyaponda magamba hayo lilidumu kwa takriban nusu saa hadi yakalainika na kupatikana unga ambao ndio ulikuwa muhimu kwake. Akautwaa unga ule na kuumimina kidogo ndani ya chupa ile ya maji. Unga mwingine aliuweka ndani ya kijichupa kidogo. Kisha alitwaa mzizi, akauzungushia karatasi na kuuweka kando ya ile chupa ya maji.
Baada ya kufanya hiki na kile katika maandalizi hayo, hatimaye alijipweteka sofani na kupumua kwa nguvu. Akaisumbua akili yake kufikiri ni kipi cha muhimu ambacho huenda amekisahau. Dakika mbili, tatu alizotulia zilitosha kumfanya aamini kuwa hakukuwa na kitu chochote kingine kilicho muhimu katika safari hiyo ambacho amekisahau.
NDIPO akamwita mkewe na kumwonya, “Uwe mwangalifu na vijizi vinavyozurura usiku kucha kwenye majumba ya watu. Sitarajii kuchukua zaidi ya siku tatu kule Dar. Na kama sitarudi na Shaka, basi nitahahakisha kuwa namwacha katika mazingira mazuri ya kurudi uraiani ndani ya siku saba tu. Lazima kifanyike kitu.”
“We Baba Shaka!” mkewe alisema huku akijishika shavu kwa mshangao. Kisha akaongeza, “Una hakika na hayo unayon’ambia?”
“Naamini Mungu atanisaidia. Najua mwan’etu, Shaka anapata pesa kwa njia ambazo dini mbili kubwa duniani, Uislamu na Ukristo haziafikiani nazo. Ni mwizi! Tuseme ni jambazi! Ukweli ndio huo! Lakini sisi tunatakiwa kujali kuwa ni mwan’etu. Ni damu yetu. Ni mwanangu, ni mwanao! Umenielewa?”
“Nimekuelewa kidogo.”
“Siyo unielewe kidogo, unielewe sana!” Mzee Songoro alifoka. “Yule ni mtoto wetu! Tunapaswa kumwokoa. Pesa alizokuwa anatutumia ndizo zimefanikisha kupata hii nyumba. Yeye halijui hilo! Hivi unadhani koo na familia mbalimbali zinashamiri vipi mitaani na kuonekana kuwa wameendelea? Unadhanai watu wanaendelea kilahali tu? Na siku hizi nd’o mambo yamezidi hasa kwa hao wanaowaua wanadamu wenzetu; albino….dah…
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sijui dunia inakwenda wapi…lakini tuachane na hao washenzi was’ojali uhai wa wanadamu wenzao, mimi nazungumzia mapenzi yangu kwa mwanangu. Yeye hachuni ngozi, hamtafuti albino, hamtafuti mtu mwenye upara wa asili…mwanangu ni tofauti mama Shaka! Yeye anasaka pesa kivyake! Akikuotea, unaye!”
Mzee Songoro akasitisha kuzungumza, akahema kwa nguvu na kumtazama mkewe kwa jicho kali, jicho lililomtisha mama Shaka.
“Basi, baba Shaka,” Mama Shaka alimkatiza. “Nimekuelewa Baba Shaka. Nenda…nenda ukamwokoe mwan’etu. Nenda!”
********
TRENI ya abiria iliondoka mjini Kigoma saa 11.00 jioni. Siku ya pili Mzee Songoro alikunywa chai mjini Tabora saa 12.30 alfajiri. Mchana huo akasota ndani ya treni hiyo hadi jioni alipotinga ndani ya Mji wa Dodoma. Siku ya tatu, saa nne asubuhi aliingia jijini Dar es Salaam.
Hakuwa mgeni wa jiji hilo. Mara kadhaa kwa miaka kadha wa kadha iliyopita alikuwa akifika katika jiji hilo kwa shughuli zake binafsi au kwa kutembelea ndugu, jamaa na marafiki.
Kwa hali hiyo, hakupata shida kutafuta usafiri wa kumfikisha Magomeni Mapipa. Kwanza alitembea taratibu hadi eneo la Mnazi Mmoja katika kituo cha ‘Baridi’ na hapo alisubiri kwa dakika chache tu kabla hajapata usafiri wa daladala.
Alipofika Magomeni alikodi teksi iliyompeleka katika gesti moja ambako alichukua chumba na kuanza kupanga hatua moja baada ya nyingine katika kazi iliyomkaabili, kazi ngumu lakini aliyoamimi kuwa isingemshinda.
********
JUMAPILI asubuhi, hii ikiwa ni siku ya pili baada ya kuingia jijini Dar es Salaam, Mzee Songoro aliamka mapema, akaoga na kupata stafutahi katika mgahawa uliokuwa jirani na gesti hiyo.
Mazingira ya hali ya hewa ya jiji hilo yalimpa shida lakini alivumilia. Japo ndiyo kwanza ilikuwa ni saa 1.30 asubuhi, hata hivyo alihisi joto kali mwilini tofauti na hali ya hewa ya Kigoma. Alikunywa chai kwa kuwa tu ilimlazimu afanye hivyo kutokana na njaa kali iliyomsakama tumboni.
Alipomaliza alitoka huku akijifuta jasho kwa leso yake chakavu. Akaliacha eneo hilo kwa mwendo wa asteaste huku akiwa na chupa ya maji baridi mkononi na kijibegi chake begani.
Mfukoni alikuwa na shilingi 250,000 tu ambazo alizichukulia kuwa ni kiasi kidogo cha pesa kisichostahili kujivunia kutokana na majukumu mengi na muhimu yaliyokuwa mbele yake. Lakini pamoja na hayo, bado aliamini kuwa akiwa makini katika matumizi, fedha hizo zitatosha kwa jambo lolote alilodhamiria kulifanya.
Alipanga kuanza operesheni yake kwa kuzungukia magereza ya Keko, Ukonga na Segerea. Kama Shaka hatakuwa katika magereza hayo, angeitumia siku hiyo kufanya utafiti zaidi, ajue gereza lililomhifadhi na kumfuata hukohuko aliko hata kama ni mkoa mwingine.
Alianzia Segerea. Jibu alilolipata huko ni kwamba hakukuwa na mfungwa mwenye jina la Shaka, wala kwa wiki nzima iliyopita hawajawahi kumpokea mtu mwenye tuhuma nzito kama alizowaeleza.
Akaenda Ukonga.
Patupu!
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ni katika gereza la Keko ndipo alipopata jibu zuri. Askari mmoja alimwambia kuwa majuzi walimpokea jambazi sugu mwenye jina hilo. Likawa ni jibu lililomtia faraja mzee Songoro. Papohapo akatwaa mzizi ndani ya mfuko wa shati na kuutia mdomoni. Akaanza kuutafuna taratibu bila ya kuumeza. Na alikuwa na sababu ya kufanya hivyo.
Mzizi huo ulikuwa na nguvu za ajabu. Mtu yeyote akiutia mdomoni, na kuutafuna huku akizungumza na mtu mwingine, basi chochote atakachokisema huyo mtumiaji mzizi kitakubaliwa na msikilizaji.
Watumiaji wengi wa mzizi huo ni wale wanaokwenda mahali kutafuta ajira, wakware na wenye kesi mahakamani. Mzee Songoro alikuwa ni miongoni mwa watu hao. Na alipoutia mzizi huo kinywani, matumaini ya mafanikio yakazidi kumjaa.
Jumapili hiyo ilikuwa ni siku maalumu kwa ndugu, jamaa na marafiki kuruhusiwa kuonana na wafungwa. Na nje ya gereza hilo kulikuwa na umati mkubwa wa watu waliokuja kwa madhumuni hayo ya kuonana na ndugu zao ambao baadhi walikuwa wakitumikia vifungo na baadhi walikuwa rumande wakisubiri hukumu za kesi zilizowakaabili.
Mzee Songoro alikuwa miongoni mwa watu hao. Akilini mwake aliamini kuwa kitendo cha kuruhusiwa kuonana na Shaka kingetosha kuzaa matunda mema. Huo ungekuwa mwanzo mzuri.
Hatimaye nafasi hiyo ikapatikana. Mzee Songoro akafurahi kumwona mwanaye akiwa hai, mwenye afya njema japo alikuwa ndani ya mavazi ya jela. Hata hivyo hakuanza kuongea naye bali alimfuata askari jela na kumwomba kuzungumza na Shaka, faragha.
“Huo siyo utaratibu wetu, mzee,” askari alimjibu. “Jaribu kufuata utaratibu kama wengine. Kwani kuna tatizo gani hadi mkae pembeni?”
“Mwanangu,” Mzee Songoro alisema kwa sauti ya upole, mzizi ukiendelea kutalii kinywani mwake. “Naomba utambue kuwa Shaka ni mwanangu. Ni mwanangu wa kuzaa. Na mimi nimetoka mbali. Hebu fikiria, Kigoma hadi hapa ni safari fupi? Tena usafiri wenyewe wa hii treni yetu isiyokuwa na uhakika lini itasafiri na treni yenyewe iko hoi bin taaban!”
Akatulia kidogo kisha akaendelea, “Uwe na utu mwanangu. Nadhani na wewe una mtoto au watoto. Na kama huna, basi nadhani utakuwanao. Damu nzito, mwanangu. Shaka ni damu yangu, sikumnunua dukani.”
Ilitosha.
Sheria ya jela ikavunjwa! Mzee Songoro akaruhusiwa kuketi faragha na mwanawe, Shaka.
Hatua ya kwanza imefanikiwa!
Mzee Songoro alikumbuka kuwa dakika tano alizopewa na yule askari jela ni chache hivyo bila ya kupoteza muda alifungua mkoba wake na kutoa kichupa kidogo chenye maji yaliyochanganywa na dawa ya unga maalumu. Kisha akatoa kijikaratasi kidogo kilichokuwa na unga kidogo.
“Unaiona hii?” alimuuliza kwa mnong’ono huku akimpa ile chupa ya maji. “Ifiche vizuri. Kesho asubuhi, yaani ile alfajiri pwee, amka ujinyunyizie katika nguo zako. Matone mawili, matatu yatatosha. Baada ya hapo unaweza hata kuitupa chupa hii. Umenielewa vizuri?” alimkazia macho.
“Nakuelewa, baba.”
Sasa Mzee Songoro akatoa kile kijikaratasi chenye unga na kumkabidhi Shaka. “Hii ni muhimu sana,” alimwambia. “Elewa kuwa wewe nd’o mwan’etu wa pekee. Hatutaki kukupoteza! Wewe nd’o taa ya maisha yetu! Umenisikia mwanangu?”
Shaka aliitika kwa kutikisa kichwa huku akikitazama kile kijikaratasi chenye dawa ya unga.
“Ficha vizuri dawa hii,” Mzee Songoro aliendelea. “Kesho asubuhi ujipake usoni, mikononi na miguuni. Hakikisha unafanya hivyo bila ya mtu mwingine kugundua. Dawa itakayosalia, tia kinywani na kuimeza. Umenielewa?”
Kwa mara nyingine Shaka alitikisa kichwa akiashiria kukubali. Hakushangazwa na maneno hayo ya baba yake. Aliyajua makali aliyonayo katika nyanja ya ushirikina. Kwa kipindi hicho kifupi alijua kuwa atakuwa na saa zisizozidi kumi na nane kabla ya utawala mzima wa gereza hilo haujahaha kuhoji kuhusu yeye huku msako mkali dhidi yake ukiendeshwa ndani na nje ya gereza hilo.
MZEE Songoro alimtazama yule askari jela kwa chati. Akafurahi alipogundua kuwa alizamisha akili na macho yake kwenye kundi lingine la watu waliokuwa wakiongea na ndugu zao ambao baadhi yao kesi zao zilikuwa hazijaisha na baadhi wakiwa wamekwishaanza kutumikia vifungo.
Kwa jinsi askari huyo alivyoonekana, Mzee Songoro aliamini kuwa maongezi kati yake na Shaka hayakumfikia, hivyo kwa sauti ileile ya mnong’ono aliendelea, “Ukishabugia dawa hii, subiri muda wa kwenda kwenye kazi za nje.”
Akatulia na kuzidi kumkodolea macho Shaka. Kisha akaongeza, “Wakati mtakapotolewa nje ndipo ujue kuwa ni muda wako wa kuwaacha. Ukishajiona uko nje ya jengo hili tu, usizubae. Anza safari.”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Shaka aliguna. Akashusha pumzi kwa nguvu. Kisha kwa sauti ya chini zaidi, akauliza, “Baba, nitawezaje kufanya hivyo huku nikiwa na miguo hii ya jela?”
“Usihofu,” Mzee Songoro alimtuliza. “Hutapata matatizo yoyote! Utoke hivyohivyo ulivyo! Utakapokuwa mbali kidogo, ndipo utumie mbinu zako upate nguo za kubadili. Una akili na una nguvu; sidhani kama utashindwa kwa lolote.”
Wakatazamana huku wote wakiwa kimya. Kisha Mzee Songoro akaendelea, “Ukishakuwa uraiani tafuta usafiri wa kukuleta Kigoma. Jiji hili ni lako. Sidhani kama utashindwa kupata pa kujichimbia wakati ukitafuta usafiri wa kukuleta nyumbani. Na huna haja ya kutumia usafiri wa hii treni yetu isiyokuwa na uhakika wa kuondoka. Tumia usafiri wowote hadi ufike Kigoma ndani ya siku mbili, tatu hivi zijazo.”
“Sina pesa!”
“Hilo s’o tatizo,” Mzee Songoro alimtuliza. Papohapo akaingiza mkono mfukoni na kuchomoa noti kumi za shilingi elfu kumi-kumi. Akampatia Shaka kiuficho huku akinong’ona, “Laki hiyo.”
Shaka naye akazipokea kisirisiri na kuzifutika kwenye mfuko wa kaptula yake.
“Najua hizo pesa hazitoshi,” Mzee Songoro aliendelea. “Lakini najua hutakwama. Nasema tena, nguvu unazo, akili unayo. Hakikisha kesho hulali humu ndani. Utakapokuwa mitaani fanya unavyojua upate nyongeza ya pesa. Lakini usiendelee kukaa hapa Dar. Uje nyumbani nikupe kinga kamili ya maisha yako yote.”
Baada ya mzee Songoro kusema hayo, alimshika mkono Shaka kwa nguvu huku akimtazama kwa macho makali, tabasamu la mbali likijiunda katika uso wake uliosheheni mikunjo ya uzee. Kisha kwa mnong’ono mkali zaidi, akasema, “Kwaheri mwanangu. Kwaheri. Tutaonana nyumbani.”
Akatoka.
******
SAA 9 usiku, Shaka alizinduka usingizini. Akaangaza macho huku na kule. Akakunja pua kutokana na harufu kali ya mchanganyiko wa jasho kutoka kwa wafungwa wengine ambao walikuwa wakikoroma usingizini.
Akamtazama aliyekuwa jirani yake upande wa kushoto. Huyo alikuwa hoi usingizini, ni kama alikuwa ameyazoea maisha ya jela. Usingizi wake ulionekana kuwa ni wa kustarehe, kama aliyelalia godoro zuri ndani ya chumba kizuri. Hata afya yake ilikuwa ikitoa taswira kuwa ameridhishwa na mazingira aliyomo. Akamgeukia mfungwa wa upande wa kulia. Huyo alikuwa kadhoofu na alikohoa mfululizo.
Hakuwajali. Mawazo yake yalikuwa juu ya maagizo aliyopewa na baba yake.Taratibu akajitoa pale sakafuni na kwa mwendo wa kunyata akaenda kusimama kiambazani, mkononi akiwa na kile kijikaratasi chenye dawa ya unga na kijichupa kidogo chenye dawa ya maji.
Hatua iliyofuata ilikuwa kufanya kile alichoelekezwa na baba yake; kujinyunyizia matone matatu ya ile dawa ya majimaji nguoni kisha akajipaka ule unga usoni, mikononi na miguuni kabla ya kuutia kinywani na kuumeza.
Hakupaona mahali palipostahili kuitupa ile chupa, hivyo aliirejesha mfukoni na kurudi kwenye malazi yake kwa mwendo uleule wa kunyata.
Aliamini kuwa hakuna ambaye alimwona wakati akiyatekeleza maagizo yale ya baba yake, na hata hivyo, pia alijipa imani kuwa hata kama ameonwa na yeyote yule asiyehusika, bado hakutakuwa na litakaloharibika.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Saa 11:30 alfajiri hakuna mfungwa aliyekuwa amelala. Pilikapilika za hapa na pale zilitawala hadi anga ilipotakata. Muda wa kazi za nje ulipotimu, makundi kadhaa yalipangwa. Shaka alikuwa katika kundi la wafungwa kumi ambao walitakiwa kwenda kwenye ujenzi wa banda la maonyesho katika Viwanja wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa vya Julius Nyerere.
Kundi hilo liliamriwa kupanda ndani ya lori lililokuwa likiwasubiri. Askari jela alikuwa akifoka, akiwahimiza kufanya haraka. Wafungwa, mmoja baada ya mwingine walianza kupanda garini. Wakati huo, Shaka alikuwa nyuma akisitasita kuitii amri ya askari huyo. Mawazo yake yalikuwa juu ya maagizo aliyopewa na baba yake mzazi, jana yake.
Aliamini kuwa kama hatachukua uamuzi wa kuondoka hapo, wakati huohuo, basi huenda akawa ametibua kila kitu kuhusu maagizo aliyopewa na baba yake.
“Oyaa! We mtoa roho za watu, jambazi mkubwa unawaza nini? Hii nd’o Keko! Usidhani uko kwa hawara yako huko uswazi! Panda gari haraka!” Amri kutoka kwa askari jela iliyafikia masikio yake kwa usahihi.
Ni amri hiyo iliyomzindua, na akazinduka. Papohapo akaamua kuanza utekelezaji wa maagizo aliyopewa. Badala ya kuitii amri ile ya askari, aligeuka na kuondoka. Akavuta hatua kwa mwendo wa taratibu lakini kwa kujiamini, akiliacha eneo hilo.
Yule askari aliduwaa, akamtazama bila ya kuchukua hatua yoyote. Shaka aliendelea kutembea taratibu, bila ya kuonesha hofu yoyote. Alipotokeza barabarani akakutana na askari wengine wawili wenye sare, ambao walimwangalia kidogo tu, kwa mshangao, kisha wakaendelea na safari yao, yeye na safari yake.
Alipita hapa na pale, kwa mwendo uleule wa kujiamini huku akiwa amekwishaitupa ile chupa iliyokuwa na dawa ya unga kando ya barabara, mtaroni bila ya mtu yeyote mwingine kubaini.
Hatimaye akaingia ndani ya duka moja ambako alimkuta mwanamama akimhudumia mteja. Bado mwanamume Shaka hakuwa na wasiwasi. Alitulia akisubiri mteja huyo aondoke, na baada ya dakika mbili, tatu akajikuta akitazamana ana kwa ana na muuzaji yule.
“Karibu, kaka,” muuzaji yule alimkaribisha huku akimtazama kwa mshangao.
Shaka aliugundua mshangao wa muuzaji huyo, lakini hakujali. Alijua kuwa mavazi yake ambayo ni sare rasmi ya mfungwa ndiyo yaliyomshangaza muuzaji huyo.
Aliangaza macho pande zote za duka hilo. Lilikuwa ni duka lililofurika bidhaa mbalimbali; vipodozi, vyakula vilivyosindikwa na visivyosindikwa, soda hata bia na pombe kali. Pia, kulisheheni nguo za aina mbalimbali za kike na kiume.
Alivutiwa na mashati pamoja na suruali kadhaa zilizokuwa zimening’inizwa. Akalinyooshea kidole shati moja jeusi la mikono mifupi lenye ua jekundu mgongoni. Akauliza, “Lile shati, vipi?”
Muuzaji hakuchelewa, mara akalifuata na kulinyofoa, kisha akampatia Shaka huku akisema, “Liangalie vizuri kaka’angu. Na kwa mwili wako lazima litakupendeza.”
Shaka alilitwaa shati hilo, akalitazama kidogo na kuliweka mezani. “Na ile suruali?” akainyooshea kidole suruali nyeusi.
Kama alivyofanya kwa shati, muuzaji aliitoa suruali hiyo na kumwachia huru Shaka aichunguze-chunguze.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Dakika ya pili Shaka aliamua. “Nipe bei ya jumla,” alimwambia muuzaji huyo.
“Elfu ishirini.”
“Chukua kumi na tano.”
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment