Simulizi : Farida
Sehemu Ya Nne (4)
"Sasa yatupasa kutoka usiku wa manane kuelekea huko nyumbani kwa nesi Rehema " Farida alishauri.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Ila si itabidi nimtaarifu kwa simu kama tutaenda nyumbani kwake?" Nilimuuliza Farida.
"Hapana, usitumie simu. Wanaweza kuyanasa mazungumzo yenu. Wakatuvizia na kutukamata. Tutam'surprize' tu" Alinijibu.
"Haiwezi kuwa mbaya hiyo?" Nilimuuliza tena Farida.
"Ni nzuri zaidi kwa wakati huu mgumu tuliokuwa nao"
*****
Ilipotimu saa sita ya usiku, tulitoka katika kipori kidogo ndani ya pwani ya Jimbiza.
Kwa mwendo wa tahadhari kubwa sana tulikuwa tunaelekea nyumbani kwa nesi Rehema.
Tulikuwa tumeongea mengi sana na Farida. Kuhusu huu mkasa, kuhusu mustakabari wa maisha yetu yatakavyokuwa baada ya kuisha mkasa wa hatari uliotukumbuka.
Nilimuelewa, alinielewa.
Saa sita na dakika arobaini na tatu ilitukuta tukiwa nje ya mlango wa nesi Rehema.
Niligonga mlango taratibu sana, lakini hakuna mtu aliyekuja kutufungulia.
Niligonga tena, safari hii kwa nguvu kidogo, tofauti na hapo awali.
Bado ilikuwa kimya.
Nikagonga tena, safari hii huku nikiita jina la nesi Rehema kwa sauti ndogo.
Bado ilikuwa kimya.
Ilitokea kama bahati mbaya nikalizungusha komeo la mlango.
Mara, mlango ulifunguka!
Moyo ulinipiga vibaya sana!
"Inamaana Nesi Rehema amesahau kufunga mlango leo?" Niliwaza kimoyomoyo.
Nilianza kuingia ndani huku nikiita kwa sauti ndogo. Farida nae alinifata kwa nyuma akiwa kimya.
Nilivyofika sebuleni, nilipatwa na mstuko mkubwa sana!
Sebuleni kulikuwa na mwili wa mtu umelala chali ndani ya dimbwi la damu.
Mwili ukiwa mtupu kama ulivyozaliwa. Sehemu ya tumbo ya mwili huo kulikuwa na jeraha kubwa na baya sana, kulikuwa na uwazi mpana katika sehemu ya tumbo, bila shaka yule mtu alikuwa ametobolewa tumbo na kutolewa utumbo!.
Hakuwa na matiti kifuani. Matiti yake yote mawili yalikuwa yamekwata na kusweka ndani ya lile shimo lililopo pale tumboni.
Hakuwa na macho. Alikuwa ametobolewa macho, na damu kutapakaa uso mzima wa yule dada.
Kwa chini alikuwa na mguu mmoja, huku mguu mwengine ukiwa umening'inizwa kwa kamba kutokea darini.
Sebule ilikuwa inanuka damu! Ilihitaji roho katili sana kuweza kuendelea kuiangalia ile maiti mara mbilimbili. Bila shaka yule mwanamke alikuwa amepitia mateso makali sana kabla ya kifo chake...
"Ni nani huyo Nass?" Sauti ya iliyojaa woga ya Farida ilinitoa mawazoni.
"Ni nesi Rehema" Nilijibu kwa sauti ndogo sana. Sauti ya kukata tamaa.
Niliuona mstuko wa wazi toka kwa Farida. Akasema "Itakuwa Vampire ameshapita hapa!"
Kusikia neno Vampire ule mstuko aliokuwa nao Farida ghafla ulihamia kwangu. Niliikumbuka taswira ya mwanamke yule mrembo sana jinsi nilimvyomkuta katika ofisi ya Dokta Martin akiwa, kashamtoa roho yake.
Pamoja na kuwa na uhakika Vampire alikuwa ni muuaji, lakini sikuwaza kama anaweza kuua kikatili namna ile.
"We umejuaji kama mauaji haya kayafanya Vampire?"
Farida alinyoosha mkono wake kuelekea ukutani.
Nami niliyaelekeza huko macho yangu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Niliona mchoro uliochorwa kwa alama nyekundu. Mchoro wa damu. Bila shaka damu ya nesi Rehema ilitumika kuchora pale ukutani. Mchoro ule ulikuwa ni herufi kubwa V.
Fikra zangu zilirudi nyuma harakaharaka. Nilikumbuka kuiona alama kama hiyo katika ofisi ya Dokta Martin.
"Yaani Vampire anaua na kuweka chata yake ukutani? Ama hakika yule ni mwanamke wa ajabu sana" Nilikuwa naongea kwa sauti ya taratibu, lakini nilikuwa na uhakika Farida alikuwa ananisikia.
" Sio mahali salama hapa Nass. Tuondoke, wanaweza kuja anytime kutumaliza" Farida alishauri.
"Kwanini sasa wamuue nesi Rehema?" Niliuliza katika hali ya kuchanganyikiwa.
"Hutumia akili wale. Itakuwa wana sababu zao za kufanya hivi. Nakuonea huruma sana Nass kwa kukuingiza katika mkasa huu" Farida alisema kwa majuto.
"Huna haja ya kunionea huruma. Nafurahi kuingizwa katika hatari na mwanamke ninayempenda zaidi duniani. Naamini tutatoka salama Laaziz" nilisema kiujasiri na kwa kujiamini sana.
Farida alinikumbatia kwa nguvu.
Alininong'oneza sikioni huku akiwa kanikumbatia " Nakupenda sana mwanaume wewe"
"Na Vampire anawapenda pia" Tulisikia sauti kutoka kusikojulikana.
Ilikuwa sauti ileile, iliyokuwa inaongea na mimi mchana. Sauti ya mwanamke mrembo sana, lakini katili sana.
Mwanamke ambaye sikuwa tayari kabisa kwa sasa kuisikia sauti yake.
"Na Vampire anawapenda pia" Maneno ya Vampire yalijirudia tena katika kichwa changu.
Tuliachana harakaharaka. Kila mmoja aliangaza huku na huko kutafuta mahali ilipotokea ile sauti ile.
Hatukuona. Na wala hatukuisikia tena.
Nilimwangalia Farida, alikuwa anatetemeka pasi na kifano. Alikuwa anaogopa. Sauti ya mwanamke anayekwenda kwa jina la Vampire ilimtetemesha Farida. Ilimuogopesha.
"Usiogope Farida, tutatoka salama" Niliongea kwa sauti ndogondogo.
Farida alinisogelea. Alinikumbatia kwa nguvu. Niliyasikia mapigo yake ya moyo yakivyopiga kwa nguvu, tena harakaharaka.
"Namuogopa sana Vampire, Nass". Alisema tena, kwa sauti ya hofu. Huku akilengwa na machozi.
" Usihofu Farida, hapa yatupasa kukimbia. Sio sehemu salama tena" Nilimwambia kwa sauti ndogo sana, sauti ambayo nilikuwa na uhakika alikuwa anaisikia Farida pekee, hata Vampire ama mtu yeyote aliyekuwepo mle ndani nilikuwa na uhakika hawezi kuisikia.
Kisha niliongea kwa sauti kubwa kidogo ambayo nilikuwa na uhakika Vampire na washirika wake kama walikuwepo walikuwa wanaisikia " Usihofu Farida tutatoka salama"
"Tutakimbiaje sasa" Farida alinielewa, nae aliongea kwa sauti ambayo nilikuwa naisikia mimi pekee, kisha aliongea kwa sauti kubwa kuijibu ile sauti yangu kubwa "Sawa Nass. Siogopi"
Nikajua Farida ameuelewa mchezo. Sasa tulikuwa tunamchezea Vampire kwa maneno popote pale alipokuwa. Tuliongea kwa sauti ndogondogo kwa manufaa yetu, kisha tuliongea kwa sauti kubwa kwa manufaa ya Vampire na washirika wake.
"Nahesabu hadi tatu kisha tunakimbia kupitia mlangoni" Niliongea kwa sauti ndogo. Kisha nikasema kwa sauti kubwa nilisema "Tukague chumba kimojakimoja. Tumtafute huyo Vampire!"
"Sawa Nass" Farida aliitikia kwa pamoja.
"Nahesabu hadi tatu kisha tuende" Nilirudia kusema kwa sauti kubwa.
"Moja" Nilianza kuhesabu.
"Mbili" Tuliacha kukumbatiana.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Tatuuu" Nilisema kwa nguvu.
Tulitoka nje ya chumba cha Nesi Rehema mkuku mkuku. Tulifika nje ya mlango na kuanza kukimbia bila uelekeo maalum. Zilikuwa mbio, mbio kweli. Mbio kama za marathon. Ijapokuwa ulikuwa usiku wa manane lakini bado umahiri wangu katika mbio ulionekana. Na Farida pia hakuwa lelemama. Tuligeuka nyuma mara kwa mara, lakini hatukumuona mtu. Labda Vampire alikuwa anasubiri ukaguzi wetu wa nyumba.
Sikujua hata tulipita njia gani. Lakini akili yangu ilipokaa sawa nilijikuta tupo karibu na shule ya msingi Mnazimmoja. Tuliongeza kasi kuelekea upande iliopo shule ya Sekondari Kilwa.
Tulipofika njia panda, niliona mwanga wa gari ikitokea upande wa kanisa kubwa la Roman Catholic. Tuliongeza kasi ya kukimbia. Kichwani mwangu lilinijia wazo moja tu.
"Range Rover nyeusi ilikuwa inatufuata"
Kila nilivyokuwa ninawaza kwamba gari lililopo nyuma yetu ni Range rover nyeusi, basi na kasi ya kukimbia iliongezeka maradufu.
Tulivyokaribia mtaa wa Dodoli. Niliushika imara mkono wa Farida. Farida alikuwa anaelekea kuchoka. Niliuona uzito wa mwili wake jinsi nilivyokuwa namvuta. Alikuwa anahema vibaya sana. Huku akilia kwa sauti ndogondogo, kilio cha kike, kilio cha kuchoka.
Niligeuka nyuma, taa za ile gari hazikuwepo.
Tulikata upande wa kulia kuelekea upande ilipo shule ya Sekondari Kilwa. Tulikimbia kidogo, kabla hatujafika mahali ulipokuwepo uwanja wa mpira wa miguu wa shule hiyo, tulikata kushoto. Tukawa tunapita katika shamba kubwa la mikorosho la shule, tulikuwa tunaipita mikorosho iliyoshonana vyema.
Ulikuwa usiku wa manane, usiku wa giza totoro, lakini sikuwa na hofu hata chembe moyoni mwangu. Nilijua pale ndio mahali salama pengine kuliko popote pale kwa wakati huo. Giza ndilo tukilolihitaji zaidi, kutuficha na mkono mbaya wa Vampire pamoja na kina Nassoro.
Tuliendelea kutembea kwa mwendo mdogo wa tahadhari porini. Tulizidi kuelekea mbele.
Hali ya porini ilikuwa kimya. Michakato ya miguu yetu tu ndio iliyokuwa inasikika. Hakuna aliyekuwa anaongea, ilikuwa inasikika mihemo na pumzi zetu tu. Niliangalia saa yangu mkononi. Ilikuwaa saa nane na dakika sita usiku.
"Nimechoka sana Nass, naomba tupumzike" Farida alisema kwa sauti ya kuchoka kweli. Alikuwa hatanii.
Nilimuelewa.
Tukapumzika, tulikaa chini ya mti wa mkorosho. Nilinyoosha miguu yangu huku nikiwa nimeliegemea shina la mkorosho. Farida alijilaza katika katikati ya mapaja yangu. Alidumu macho dakika zisizozidi nne. Kisha alipitiwa na usingizi.
Nilikaa nikiwa nimeegemea shina la mkorosho. Kwangu usingizi haukuja hata. Nilibaki macho nikitafakari mambo magumu niliyoyapitia siku ile.
Taswira ya maiti ya Dokta Martin ilinijia kichwani mwangu. Taswira ya maiti ya nesi Rehema aliyeuwawa kinyama ilinijia kichwani mwangu.
Nikiwa katikati ya mawazo ghafla nilisikia muungurumo wa mlio wa gari.
Nilitulia tuli.
Nilimwangalia Farida usoni. Alikuwa ametopea katika lindi la usingizi. Sura nzuri ya Farida ilikuwa inaonekana vizuri. Weupe wake wa asili uling'ara gizani. Nilimwangalia mwanamke yule nzuri. Mwanamke mwenye urembo usio na mfano. Mwanamke aliyeyashuhudia mengi katika umri wake mdogo. Mwanamke aliyepitia mengi sana katika maisha yake.
Na muungurumo wa gari ulikuwa unazidi.
Nilisikia Farida akitikisika. Alikuwa anaongea peke yake. " Wanakuja, wanakuja, nakwambia wanakuja Nass"
Farida alikuwa anaweweseka.
Na ilikuwa kweli wanakuja. Maana sasa nilisikia muungurumo wa magari matatu tofauti.
Nilimuamsha Farida taratibu. Alikurupuka kutoka usingizini.
"Wanakuja Nass!" Alisema kwa sauti kubwa akiwa amesimama wima.
"Tulia Farida. Tuko sehemu hatari, usipige kelele" Nilimwambia kwa sauti ndogo.
"Nassoro ni Rick Ross" Farida alipayuka bila kujielewa.
Nilinyanyuka haraka. Nikamfata Farida na kumziba mdomo, nilihisi Farida bado alikuwa usingizini.
Anaweweseka.
Macho yalimtoka pima. "Nass, Nass, Nass" Farida alikuwa anajitahidi kuita. Lakini sauti yake haikuweza kutoka kama akivyotaka.
"Tulia Farida, usipige kelele, unajua tuko katikati ya hatari" Nilimwambia kwa kumnong'oneza sikioni.
Sasa alinielewa.
Alitulia tuli.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sasa nilisikia muungurumo wa pikipiki.
"Watakuwa wapo wengi sana" Nilijisemea mwenyewe kimoyomoyo.
"Tutoke hapa Nass, sio sehemu salama" Farida alirudi katika akili zake za kawaida.
"Yeah ni kweli, lazima tutafute namna ya kutoka hapa. Itakuwa tumezungukwa na maadui wengi sana" Nilimwambia.
"Nimeota Nassoro anakuchinja Nass" Farida alisema kwa sauti ya kutetemeka.
"Ndomana ikaitwa ndoto. It can't be, never ever. Nitahakikisha Nassoro anafungwa!" Nilisema kwa kujiamini.
" Safi my gentlemen " Farida alisema huku akinipigapiga mgongoni.
Mara, tulisikia ukelele wa kukanyagwa majani makavu ya mikorosho karibu kabisa na pale tulipokuwa. Bila shaka kuna mtu au watu walikuwa wanapiga hatua kuja pale tulipokuwa
"Tukimbie Nass" Farida alisema kwa sauti iliyojaa wasiwasi.
Nilimshika mkono Farida na kuanza kuelekea mbele. Tulianza kutembea kidogokidogo, mwishowe tukaanza kukimbia.
Tulikimbia zaidi ya dakika kumi na tano. Ulikuwa usiku wa shida sana. Tulijigonga na miti mara kadhaa, tulikwaruzwa na miiba. Tuliingia katika mashimo, tukianguka na kuinuka. Lakini hatukukoma bado tulizidi kukimbia...
Baada ya kukimbia kwa muda wa kama nusu saa, tulianza kutembea tena, huku tukiwa makini kusikilizia kama kuna ukelele wa kufuatiliwa kwa nyuma.
Kulikuwa kimya.
Farida alisema kwa sauti ya kuchoka "Nass nimechoka, nimechoka sana Nass"
Nilisema huku ninahema " Najua umechoka mpenzi wangu lakini lazima tukimbie. Kutokukimbia ni kukisubiri kifo. Kifo kibaya sana bila shaka. Lazima tukiepuke kifo kwa kukimbia".
Farida alisema kwa sauti ya huruma sana "Daaah sawa Nass lakini..."
Nilimshika mkono imara. Haikuwa muda wa majadiliano. Tulitembea gizani harakaharaka. Ulikuwa usiku mbaya sana. Sikuwa nimezoea shurba hata chembe, lakini ilinipasa kujikaza kiume.
Tulitembea. Tulitembea. Tulitembea sana.
*****
Mkoa wa Lindi ni miongoni mwa mikoa iliyopo kusini mwa Tanzania. Mikoa mengine ya kusini ni Mtwara na Ruvuma. Ingawa nilizaliwa katika wilaya ya Kilwa lakini sikuwa nimewahi kufika katika mji wa Lindi, ambao ndio makao makuu ya mkoa.
Nilifika Lindi kipindi cha matatizo makuu. Nilifika Lindi kwa shida sana. Nilikuwa sina kitu chochote, sina pesa, sina nguo, sina ndugu, lakini nilikuwa na mwanamke akiyenitegemea kwa kila kitu.
Sikuwa na hela ya kula, lakini Farida alikuwa ananitegemea mimi ili ale. Sikuwa na pakulala lakini Farida alikuwa ananitegemea mimi juu ya sehemu ya kulala. Sikuwa na wakumtegemea, Farida alinitegemea.
Tulifika katika mji wa Lindi saa mbili usiku. Baada ya safari ndefu ya kuwakimbia wakina Nassoro. Usiku ule tulipita katika mapori mazito, vichaka vingi. Tulitembea maporini zaidi ya saa tatu. Tulipatwa na kila aina ya shida. Tulipokuja kuibuka katika kijiji tulijikuta tupo katika daraja la Mbwemkuru.
Baada ya kutembea kama robo saa kutokea daraja la Mbwemkuru tuliomba lifti katija lori. Lori lililotufikisha katika mji wa Lindi saa mbili usiku.
Tulijisikia huru kuwa mbali na wakina Vampire, lakini tulipofikiria maisha yetu yataenda vipi ndani ya Lindi ulitupata uwoga mkuu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Usiku huo tulilala katika stendi ya Lindi. Laiti ningejua madhila ya usiku huo haki ya Mungu nisingelala stendi ya mabasi..au pengine nisingeenda Lindi kabisa...
Tulikaa katika kibaraza cha duka moja katika stendi ya mkoa wa Lindi hadi saa tano usiku. Farida alidai amechoka sana. Alikuwa anahitaji kupumzika.
Nilitandika maboksi machache mbele ya kile kibaraza cha duka. Nilikaa chini nikiwa nimenyoosha miguu yangu yote miwili. Farida alilala katika miguu yangu. Hazikufika hata dakika sita, Farida alikuwa anakoroma.
Sikutaka kukaa mahali pale. Mimi ndiye nilikuwa mwanaume, nilikuwa tegemezi. Ilinipasa kutafuta namna sahihi ya kuona kesho yetu inakuwaje. Nilimuinua Farida taratibu akiwa usingizini, nikamuweka chini ya boksi.
Nilimwangalia.
Nikainama.
Nilikuwa naiangalia sura nzuri sana ya Farida. Ilikuwa imelala kitulivu sana. Sura nzuri. Sura nzuri ya mwanamke wa maisha yangu. Nilisogeza mdomo wangu karibu na mdomo wake. Nikambusu.
Nilisema kwa sauti ndogo sana
"Nakupenda sana Farida. Nakuacha hapa mpenzi lakini nitarudi. Naenda kutafuta baby, na nitarudi muda si mrefu. Nakuahidi mpenzi, nitakupenda siku zote za maisha yangu Farida. Nitakupenda milele. Nitakupenda kwa kuwa nimeamua kukupenda. Nimekupa moyo wangu Farida. Moyo wangu wote. Nipo tayari kuwa na wewe katika nyakati zote, nyakati za shida, nyakatu za raha. Amini upo na mtu sahihi, mtu atakayekupigania katika nyakati zote za maisha. Sitothubutu kukuacha peke yako Farida, Sitokutesa hata sekunde moja mpenzi. Siwezi kabisa kumtesa mwanamke ninayempenda sana duni.."
Sikumalizia kuongea. Niliona machozi yakitiririka katika mashavu ya Farida. Kumbe alikuwa ananisikia. Alifumbua macho. Tuliangaliana.
Alisema kwa sauti ya kwikwi " Unaenda wapi Nass usiku huu?"
Nilimjibu kwa upole " Naenda kutafuta Farida, kutafuta ili tuweze kuishi kesho, tuweze kuishi na kesho kutwa. Lazima tuendelee kuishi Farida ili kutimiza ndoto zetu, na ili tuishi lazima tule mpenzi. Hatuwezi kula bila kuwa na pesa. Naenda kutafuta pesa mpenzi, na.."
Farida alinikata kauli "Kutafuta pesa usiku huu Nass?" Farida aliniuliza huku akiinuka.
"Wapi utapata pesa usiku huu. Sahivi ni usiku, saa tano usiku. Utaenda kufanya nini ili upate pesa Nass. Tulale, kesho asubuhi tutajua nini cha kufanya"
Nilisema tena kwa sauti ya kusisitiza "Kesho maisha hayaanzi Farida, kesho maisha yataendelea. Lazima tuwe na fedha za kuweza kutuwezesha kuendelea na maisha. Lazima nikasake pesa na nina hakika nitazipata usiku huu. Nakuahidi nitarudi hapa kabla ya saa saba"
Niliongea huku nikinyanyuka. Farida nae alinyanyuka. Alinisogelea. Alinikumbatia kwa nguvu. Akanipiga busu katikati ya paji langu la uso. Akanipiga busu tena katika shavu langu la kulia. Akanipiga busu lengine katika shavu langu la kushoto. Akanibusu mdomoni.
Midomo yetu iligandana kwa muda. Alitoa ulimi wake. Nikaupokea vizuri kwa ulimi wangu. Nilinyonya ulimi wa Farida. Niliunyonya ulimi mtamu sana.
Tulitumia dakika kumi tukiwa katika hali hiyo. Tukipeana denda. Lilikuwa denda refu zaidi kuwahi kupiga hapa duniani. Tukaachiana.
Tuliangaliana usoni. Farida alikuwa analia. Mimi halikadhalika nilikuwa ninalia.
Alisema kwa sauti yake nyororo "Nakupenda sana Nass"
Nilimjibu "Nakupenda zaidi Farida"
Alisema tena Nakuahidi nitakupenda siku zote za maisha yangu. Wewe ni shujaa kwangu. Shujaa wangu. Shujaa wa kweli. Hakuna mwanaume kama wewe Nass. Wewe ni mwanaume bora sana katika zama hizi. Zama za wanaume wasaliti. Kwangu, wewe ni mwanaume wa pekee sana. Kama kuna mwanamke mwenye bahati basi ni mwanamke anayeishi na wewe Nass. Na Farida nimeipata hiyo bahati. Siko tayari kuipoteza hata kitokee nini."
Nilimziba mdomo Farida. Machozi yalikuwa yanambubujika. Nilimuonea huruma sana. Kumuona mwanamke niliyempenda zaidi akilia. Iliniuma sana.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Niliangalia saa yangu. Ilikuwa saa tano na nusu. Nusu saa kabla ya muda wa miadi yetu. Nilimuacha Farida, nikatokomea gizani. Nilisikia kilio cha kwikwi toka kwa Farida. Sikugeuka nyuma. Nilijua nikigeuka nyuma nisingeweza kuondoka. Nilikuwa naenda, naenda kutafuta pesa. Na ilinipasa niende kabla saa sita usiku haijafika...
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment