Search This Blog

Friday, 20 May 2022

BARUA KUTOKA JELA - 2

 







    Simulizi : Barua Kutoka Jela

    Sehemu Ya Pili (2)



    Afande Kubuta alibisha hodi Ofisini kwa Bosi wake na kutoa heshima za kijeshi kama inavyotakiwa na kuketi kitini baada ya IGP kumuashiria kufanya hivyo.



    IGP akanyoosha mkono kuchukua vitu alivyoagiza kutoka kwa afande Kubuta na kitu cha kwanza kuanza kuangalia zilikuwa ni zile albam nne zilizokuwa mbele yake.



    Aliangalia moja baada ya nyingine huku akiangalia hadi zile picha zilizokuwa zimewekwa nyuma ya picha, mwisho akazimaliza zote albam nne bila kuona kitu alichokikusudia!



    Akainua uso na kumtazama usoni kijana wake afande Kubuta. Na kwa mara ya kwanza akanyanyua mdomo wake kusema.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kuna picha humu ambazo zimetolewa! Kwani zipo sehemu zilizokuwa tupu kuonyesha kwamba kulikuwa na picha! Kwani si kama picha zilizomo humu hazitoshi kuijaza albam kwani kuna picha nyingi hadi nyingine zimewekwa picha tatu katika sehemu moja! Je picha hizo umezitoa wewe? Na kwa sababu gani wakati nilikwambia ulete kama utakavyozichukua?”



    Akauliza IGP huku akiwa amechukia na amefula kwa hasira!



    “Hapana Mkuu, kama ulivyoagiza ndivyo nilivyotekeleza. Ila picha zilizopungua, nimeambiwa kwamba amekwenda afande Jamila amezichukua na kuahidi angezirudisha baada ya upelelezi kukamilika!”



    Sasa ikawa zamu ya IGP kufadhaika, aliinuka kwenye kiti chake na kusimama huku akiwa ametoa macho pima! Kitu ambacho hata afande Kubuta naye alishangaa. Kwani alidhani labda huyo afande Jamila, alitumwa na Bosi huyo kama yeye alivyotumwa kwenda kuchukua zile albam. Sasa kama naye anashangaa je kuna nini kinachoendelea. Na je hizo picha ni za nini? Hatimaye IGP akauliza.



    “Huyo afande Jamila nani kampa kesi hii?!” Sasa IGP alionekana kama ana hofu katika sura yake lakini pia jazba ilimtawala vile vile.



    Afande Kubuta akaisoma hali ya Bosi wake akawa makini sana.

    “Sielewi mkuu, lakini pia katika kituo chetu cha Magomeni hatuna jina la afande Jamila, achilia mbali kuwa mpelelezi. Pia nilidhani labda amri hii imetoka juu, katika kuweka askari mwingine bila mimi kujua! Ili naye afatilie mwenendo mzima wa kesi hii. Sasa kama mkuu hujui lolote kuhusu afande Jamila, nini kinaendelea katika kesi hii?”



    Afande Kubuta aliuliza huku akiwa amechanganyikiwa kwa mawazo. Pia baada ya maelezo yake “IGP” akagundua mchezo wote atakuwa anaufahamu huyo afande Jamila, lakini yeye kwa nini asifahamishwe alipohitaji kujua mpelelezi anayeendesha kesi ya marehemu Hamida?!



    Ila yeye alipewa jina la afande Kubuta, nambari ya faili na nambari ya simu ya afande Kubuta. Sasa huyo afande Jamila anafanya kazi kwa kutumwa na nani na kwa faida ipi hatimaye “IGP” aliwaza na kuinua mkono wa simu kisha kubonyeza nambari kadhaa na simu ikawa inaita upande wa pili.







    *******



    Madereva Taxi katika Kituo cha Taxi Magomeni Usalama, walikuwa katika harakati za kazi yao. Wapo waliokuwa wakifuta magari, wengine kuyaosha kabisa. Pia wapo waliokaa juu ya Boneti na wapo waliokaa juu ya Buti. Wapo waliokuwa ndani ya magari yao wakisinzia ili mradi kila mtu alikuwa na harakati zake.



    “Karibu dada, hii hapa pamba nyepesi full kiyoyozi na bei sina, ngoma full tank siyo mafuta ya kidebe.”



    Dereva wa taxi alijinasibu kwa kuipamba gari yake, na kumshawishi Yule abiria ili apande kwenye gari yake. Huku akifungua mlango wa nyuma wa gari yake, ili abiria aweze kuingia, kisha watapatania ndani bei ya sehemu atakayompeleka.



    Yule abiria aliekaribishwa bila kujishauri wala kusita, akazama ndani ya gari ile.



    Dereva badala ya kuingia ili waanze safari, akaanza kupiga honi mfululizo! Mara kijana mmoja mfupi mweupe alikuja mbio alitokea upande wa kushoto wa gari lile ambalo walikuwa wamekaa vijana wengine kadhaa wakicheza draft.



    “Mpeleke huyo Dada sijaongea naye kitu chochote mtaelewana.”



    Aliongea yule kijana aliyemkaribisha yule abiria.

    Alipopanda yule dereva na kuwasha gari, yule abiria akatambua kwamba, yule kijana wa mwanzo alikuwa ni shanta, huyu sasa ndiye Dereva.



    “Samahani Dada tunaelekea wapi?” Yule Dereva Taxi aliuliza huku akiondosha gari.



    “Nipeleke Kimara Suka, itakuwa shilingi ngapi?”

    “Ahaa Kimara Suka kubwa dada yangu, unakwenda pale pale kituoni, au kule shule, au kule Golan au kwa yule Mwandishi maarufu wa riwaya Hussein Tuwa?”



    “Nakwenda Kimara Suka Hotel utanichaji shilingi ngapi?”



    “Alaa kama pale ni shilingi elfu nane tu Dada yangu!” Alijibu yule dereva wa Taxi huku akigeuza Gari na kuanza safari.



    “Wewe una bei sana kwani nilikuwa nikimchukua yule kijana Mwaduga, alikuwa akinipeleka kwa shilingi Elfu sita tu! Sijui leo kapakia, kwani sijamuona yeye wala gari yake!”



    Yule abiria alimwambia Yule dereva wake kwa upole.



    “Usinikumbushe sister Bwana. Mshikaji wetu jumba bovu limemdondokea! Jamaa ana bahati mbaya sana Yule.”



    Dereva alimwambia abiria wake kwa masikitiko huku akionyesha huzuni usoni mwake!



    “Umesema jamaa kaangukiwa na jumba bovu siatakuwa ameumia sana?!”



    “Sio hivyo unavyofikiria, jamaa yetu kapatwa na matatizo. Kapewa msala wa mauaji hivi hivi, majambazi na wauaji wanaachwa wanatembea mitaani tu!”

    Alijibu Yule taxi dereva, katika lugha yao ya kijiweni, ambayo ilimpa wakati mgumu, abiria wake kumuelewa kwa urahisi, maana ya baadhi ya maneno!



    “Aaaaaa Bwana usiniambie!”

    Yule abiria aliuliza swali kwa mfadhaiko, na fadhaa kubwa.



    “Kweli sister wangu, jamaa ana miezi miwili na kitu, sasa yupo katika maisha mabovu mahabusu. Yaani kama alikupakia basi ni siku nyingi kidogo. Sasa bei zimebadilika mafuta yamepanda bei sana.”



    Alijibu yule dereva Taxi nakutoa ufafanuzi huku akibadilisha gia, sasa wakiwa maeneo ya Aljentina Manzese.



    “Kwani kilimpata nini jamani kaka wa watu duh kama namuona vile!?”



    Yule abiria aliuliza kwa masikitiko, na kuonyesha sura ya huruma na kuendelea kueleza.



    “Mimi nilikuwa Chuoni nimekuja pale kituoni kwenu kama miezi mitatu iliyopita, na Mwaduga ndiye alikuwa ananizungusha katika mizunguko yangu!”



    “Yaani sister we acha tu, kwani kesi ya mshikaji imekaa vibaya sana!”



    Dereva Taxi akaongeza msisitizo wa jambo lile.



    “Umesema kesi ya Mwaduga imekaa vibaya sana, kwa sababu gani, wakati umesema ni jumba bovu tu limemwangukia, yaani yeye hakufanya jambo lile?”



    “Dada, yule mshikaji keshapotea yule kwani amepewa soo nne. Mauaji, kukutwa na silaha, kula njama ya kutenda kosa na wizi wa kutumia silaha. Haya yote anaweza kuchomoa, lakini kosa lakukutwa na silaha, jamaa si washamuachia msala?! Huwezi kuamini sister lakini nakuambia yule Demu alieuliwa ni mali ya wakubwa, kwani Bosi wa polisi wa cheo cha juu kabisa, ndiyo alikuwa anaburuza ule mzigo”



    “Ha ha haa, sasa kaka unafika mbali sana, yaani wewe unajua pia kuwa huyo marehemu, anaeshitakiwa Mwaduga kuwa alimuua, kuwa ni kimada wa mkubwa wa jeshi la polisi!?”



    Yule abiria alionyesha kutaharuki kupita kiasi, lakini pia alijiona ni mwenye bahati kubwa kuichagua gari ile, kwani dereva wake ni mtu mropokaji! Kwani anatoa taarifa nyeti kwa gharama nafuu sana!



    “Siyo mzaha sister wangu, mimi nina mshikaji wangu anapaki Town yeye ndiyo ilikuwa kazi yake! Ameisha mpakia sana yule Demu kumpelekea Bosi wa polisi, karibu mara tatu! Na yule Bosi alikuwa anamlipa pesa nzuri sana! Yaani jamaa anaweza kumchukua yule Demu Mikocheni nyumbani kwake, na kumpeleka labda bwalo la polisi ostabey akalipwa shilingi elfu ishirini! Au siku nyingine humpeleka Bagamoyo na kumuacha kwenye hoteli za kitalii siku za mwisho wa wiki, akalipwa laki moja! Sasa aliposikia mshikaji wetu Mwaduga yuko ndani tena kwa kesi ya mauaji ya yule Demu, mshikaji aliniambia haya ninayokwambia, na akasema Bel white mshikaji wangu jamaa yenu keshapotea, kwani ile ni mali ya wazee Yaani tumsahau! Sasa wewe sister unadhani hiyo ni kesi ya kitoto hiyo?”



    Yule abiria alisogea katikati ya kiti cha dereva na abiria, huku akiwa na simu yake mkononi muda wote tangu amepanda gari ile, akasema kwa shauku kubwa.



    “Duh ebwana we! Hiyo kweli ni kasheshe, Yaani ndiyo ilivyokuwa hivyo? Na mbona kule mwanzo ulisema wauaji na majambazi wanaachiwa tu wanatembea na jamaa yenu anaozea jela, kwa nini msiisaidie polisi kuwakamata na jamaa yenu akaachiwa?”



    Yule abiria akazidi kuchimba. Na hadi walipofika Kimara Suka hotel akawa ameshapata hadi jina la yule Dereva Taxi wa mjini na namba yake ya simu, pamoja na namba yake Dereva Taxi huyu aliempeleka Kimara aliemtambua kwa jina la Bel white.



    ******

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilikuwa siku ya Ijumaa Dokta Zahala akiwa nyumbani kwake maeneo ya Keko bora, alikuwa anaonekana kuwa ni mtu wa mawazo mengi, kisha kama aliyekumbuka jambo akatoa simu yake kwenye “Hand Begi” na kubonyeza tarakimu kadhaa na simu ya upande wa pili ikatoa maelezo badala ya kuita!



    “IMU UNAYOPIGA IMEZIMWA AU IPO NJE YA ENEO, TAFADHALI JARIBU TENA BAADAE.”



    Dokta Zahala akakata na kubonyeza namba zingine na simu ya upande wa pili ikaanza kuita.



    “Shoga vipi mbona kimya au ndiyo nimekupa kazi kubwa kiasi hata simu yako ya kawaida umeizima?”



    Aliongea Dokta Zahala mara tu simu ya upande wa pili ilipopokelewa, na kuongeza kuwa.



    “Duh pole sana, sasa leo nipo mapumziko, kama unayo nafasi njoo nyumbani nitakuwepo. Kwani nina neno lililonifanya nikupigie simu!”



    Aliongeza Dokta Zahala na kisha akakata simu.



    Dakika Arubaini baadae kengele ya geti la mlango iliita, na mfanyakazi wa Dokta Zahala akakimbilia kwenda kufungua mlango. Dokta Zahala akamkaribisha shoga yake, na wakakumbatiana kama kawaida yao wanapokutana!



    Dokta Zahala na Inspekta Jamila walikuwa marafiki tokea chuoni pale Mlimani, walipomaliza masomo, Jamila akaenda kujiunga na Jeshi la Polisi na kutokana na Elimu yake haikumchukua muda mrefu kupata nafasi aliyonayo, baada ya kuongezeka utendaji kazi wake katika Jeshi la Polisi.



    Na Dokta Zahala alikuwa anachukua masomo ya udakitari, Baada ya mama yake mdogo aliekuwa nesi katika hospitali ya Kcmc Moshi, kumshawishi asomee mambo ya utabibu akimwambia unalipa sana, na kweli leo hii yupo katika nyumba yake mwenyewe pale Keko Bora!



    “Leo soda yako ya lemon unayoipenda sina kwenye jokofu langu, je ukatafutiwe huko nje madukani au utakunywa hizi zilizopo?”



    Dokta Zahala alimwambia shoga yake huku akiangua kicheko.



    “Akili yangu ilivyovurugwa, sina chaguo lolote lililo bora, wewe nipe kinywaji chochote mimi nitakunywa, ilimradi kisiwe na kilevi!”



    Alijibu Inspekta Jamila na akamalizia kwa kicheko. Baada ya wote kupata vinywaji cha juice, hatimae Dokta Zahala akavunja ukimya.



    “Haya shoga yangu ukamwona yule Dada siku ile na mwanae sijui umefikia wapi, kwani alinitia huruma sana yule Dada.”



    Inspekta Jamila akamuhadithia shoga yake kila kitu bila ya kumficha chochote huku akimwambia kuwa, ameamua kumueleza yote kwa ukamilifu! kwani kazi na maisha yake yapo hatiani toka yeye kujihusisha na kesi ile bila maelekezo kutoka kwa wakubwa zake, na ikija kubainika kwamba anajua hadi uhusiano uliokuwepo wa “IGP” na Marehemu Hamida, basi atakuwa katika mashaka mazito!



    “Lakini pia nataka wewe shoga yangu uwe unalifahamu kwa undani jambo hili, ili ikitokea lolote kuhusu maisha yangu uwe na pakuanzia!”



    Alisema kwa masikitiko Inspekta Jamila.

    “Duh pole na hongera shoga!” Alisema Dokta Zahala.



    “Sasa mimi nilikutafuta ili nijue kama ulimsaidia yule Dada, lakini pia kuna kitu kipya nataka kukueleza!”



    Alisema Dokta Zahala na kuinua glasi ya Juice nakupiga funda moja, huku akimuangalia shoga yake alivyokaa kwa umakini mkubwa.



    -



    “Dokta yale uliyonipa yananinyima Raha hadi sasa, Leo unataka kunipa mzigo mwingine?!” Alilalamika Inspekta Jamila.



    “Hili ni jambo nyeti sana ndio maana nikaona nikwambie wewe shoga yangu, lakini pia kama Raia Mwema nina haki kwa nchi yangu kuisaidia kwa kutoa mchango wangu!”



    Alikazia Dokta Zahala.

    “Mmmh” alishusha pumzi ndefu Inspekta Jamila na kukohoa kidogo kisha akasema.

    “Haya Raia Mwema lete taarifa!”



    Dokta Zahala akaangua kicheko, kisha akaanza kwa kusema.

    “Jana imeletwa maiti pale kazini ikielezwa ni ya Ajali, kiasi kila mtu anaamini hivyo! Ila baada ya saa kadhaa nilipokwenda kuifanyia uchunguzi, maiti ile ilinishangaza! Kwani “Rigor Mortis”, Yaani zile athali za kifo kwa maiti zilijitokeza mapema sana, ukizingatia maiti ile haikutokwa na damu nyingi,wala haikuwa na majeraha makubwa!”



    “Basi nikiwa ni Daktari, jambo lile lilinifanya nifanye uchunguzi wa kina. Nakweli niligundua mtu yule hakufa kutokana na ajali, bali alikufa kabla ya ajali!”



    Dokta Zahala alipeleka funda lingine la juice kinywani mwake, kisha akaendelea.



    “kwani vipimo vimenijulisha kwamba, mwili ule ulitokwa na uhai mapema sana asubuhi, na amekunywa au amenyweshwa sumu! kwani mabaki ya sumu ile imeonekana katika mwili wake! Sasa swali linakuja. Askari wa Doria wakati wanaelekea sehemu ya Bagamoyo kiasi cha saa moja nyuma hawakukuta ajali ile, wakati wanarudi ndiyo wakaiona gari iliyopata ajali. Marehemu alikutwa amebanwa kwenye usukani wa ile gari akiwa ameshafariki. Mnamo saa tano za asubuhi. Je aliendeshaje gari ikiwa mtu amekufa asubuhi mishale ya saa moja, kisha saa tano ndiyo apate ajali tena akiwa anaendesha gari?!”



    Dokta Zahala alisimama kidogo kisha akaendelea.

    “Ndipo nikaona nikwambie wewe, kwani askari walioandika maelezo hayo ninayokwabia, wanaamini yule Bwana waliemtambua kwa jina la Kiyarwenda Mwemezi Mkazi wa Mikocheni B, kutokana na kitambulisho cha kupigia kura alichokutwa nacho katika eneo la tukio, amefariki kwa ajali ya gari.”



    Inspekta Jamila alitoa macho pima baada ya kusikia habari ile hasa jina la marehemu Kiyarwenda Mwemezi. Kwani ni yule jirani yake Hamida kule Mikocheni, aliyekuwa akimuhoji kuhusu kifo cha marehemu Hamida. Hata naye aliposikia ajali ile, alikuwa anahisi kuna kitu kilichojificha katika ajali ile kumbe alikuwa sahihi na mawazo yake!



    “Sawa Dokta, sasa ugumu wa swala hilo nikumpata au kuwapata watu waliofanya hivyo, Yaani waliohusika katika mauaji yale. Na kwa nini walifanya mauaji yale. Kwani nahisi bado yapo katika mlolongo wa kesi hii niliyojipachika, na sasa naona mambo mengi sana kiasi yanazidi kuniweka katika wakati mgumu. Kwani kama kuuwawa kwake jirani yule kunatokana na kujua mambo mengi ya marehemu Hamida na mumewe, au imeshabainika kama niliongea nae, sasa wahusika wa kadhia hii wanajaribu kuharibu ushahidi!”



    Inspekta Jamila, alisema maneno hayo huku, akionekana kuwa ni mwenye chembechembe za woga, hasa akizingatia kuwa kesi ile, yeye hakukabidhiwa jalada lake.

    Watu gani hao wanaofatilia nyendo zake katika muda mfupi namna ile.



    Akaiweka wazi hisia yake kwa Dokta Zahala wote wakaingia katika lindi la mawazo mazito!



    “Kitu cha hatari nilichokifanya shoga ni kwamba, nilichukua vipimo vile kitaalam zaidi, kwani niliweka kile kifaa maalum cha kisasa kilicholetwa hivi karibuni kutoka China, ambacho kina uwezo wa kung’amua tukio la mwisho kabla mtu hajafa aliloliona!”



    Dokta Zahala huku akimkazia macho Inspekta Jamila, alichukua gilasi iliyokuwa na juisi akainywa yote, kisha akaendelea kusema.



    “Ukitaka kupata picha ya aliyoyaona mtu kabla hajafa, itakubidi ufumbue macho ya marehemu, kisha uweke kifaa kile kama miwani ,na kifaaa kile kita scan picha ya mtu au kitu cha mwisho macho yale kuona! Hivyo nimefanikiwa kupata picha za watu wawili ambao marehemu kabla ya kukata roho, alikuwa anatazamana nao ana kwa ana!”



    Dokta Zahala akakandamiza jambo lingine lililomfanya Inspekta Jamila kuinuka katika kiti alichokalia na kwenda kumkumbatia shoga yake yule huku akitamka maneno mfululizo.



    “mungu wangu, mungu wangu!”



    Sasa wakiwa bado wamekumbatiana, Dokta Zahala akaendelea kusema ile azma yake iliyomfanya amwite shoga yake nyumbani kwake muda ule.



    “Hivyo lililonifanya nikuite wewe, ni pamoja na kukupa habari hii kwa kina, na nikukabidhi picha zenyewe, ili uanze kazi yako!”



    “Sio nianze kazi yangu, niendeleze kazi yangu, kwani kazi nilishaianza tokea Jumapili, alipofika ofisini kwangu, yule Dada anayeitwa Eshe Muhidini, ambaye wewe ndiyo uliemuelekeza aje kwangu.”



    Alijibu Inspekta Jamila na kuendelea.



    “Sasa huyo maiti uliyemfanyia uchunguzi ndiyo yule jirani yake Hamida aliyenipa Mwanga katika upelelezi wangu, kwani ukimtoa yule mahabusu Mwaduga, mtu wa kwanza kumuhoji alikuwa ni Ndugu Kiyarwenda Mwemezi ambaye sasa ni marehemu! Yeye ndiyo aliyenifungua ya kwamba, kabla sijapeleleza kifo cha Hamida, napaswa kwanza kufahamu kifo au kilichopelekea kifo cha mume wake Hamida, Bwana Bartazal Halimu!”



    Alisema kwa msisitizo Inspekta Jamila huku akiwa amesimama wima na akiachiana na shoga yake kutoka katika kukumbatiana.



    Dokta Zahala akainuka nakuenda chumbani kwake, alipotoka alikuwa ameshika bahasha mkononi ikiwa imefungwa, na juu ya bahasha ile kuliandikwa maneno Dear Jamila! Akamkabidhi Inspekta Jamila bahasha ile na kumwambia.



    “Mambo yote yapo humo ndani ya bahasha hii!”



    Inspekta Jamila akaipokea ile bahasha na saa hiyo hiyo akaaga na kuondoka!



    *******



    Ilikuwa ni saa kumi na mbili za jioni, kikao kilikuwa kinafanyika katika ofisi ya “IGP” kilichokuwa na watu wasiozidi sita.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “IGP” mwenyewe na mlinzi wake, Afande Kubuta, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, Kamanda wa Kanda Maalum na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, watu wote hawa wakiwa wametoa kofia zao katika vichwa vyao, kasoro “IGP” walikuwa katika mjadala mzito wa namna matukio ya uhalifu Mkoa wa kipolisi wa Kinondoni yanavyoendelea, pia kushughulikiwa kwa kesi ya marehemu Hamida Baltazal.



    Baada ya “IGP” mwenyewe kutaka faili la kesi hiyo ili kutazama mwenendo mzima wa kesi hiyo, na baada ya kusoma kwa makini taarifa zilizoandikwa katika faili lile ndipo alipoitisha kikao hicho cha dharula.



    “Sasa nimewaita hapa, baada yakuona maelezo yaliyopo katika faili hili hayatoshelezi, na hayaridhishi katika kuiendesha kesi hii, lakini pia kuna jambo lisilo la kawaida limejitokeza!”

    “IGP” alisema maneno hayo huku akiwaangalia maafande wale walivyokuwa makini na utulivu wa hali ya juu, wakienda sanjari na ukakamavu!



    “Kesi hii amepewa kijana hapo!”



    Alisema “IGP”, huku akimnyooshea mkono ulioshika faili Afande Kubuta, kisha akaendelea.



    “Kuna mtu amejiingiza katikati, nae akifanya upelelezi wa kesi hii! Ambapo ni kinyume na utaratibu wa Jeshi la Polisi. Kwani askari asipotambulika na Mkuu wake kama anafanya nini kwa wakati gani kuna “Risk” nyingi sana zinazoweza kupatikana, kama vile Rushwa, askari kuuwawa au kuumia wakati akiwa hayupo kazini kisheria. Pia anaweza kuharibu upelelezi wa kesi, hivyo ni lazima atafutwe mara moja na aletwe kwangu ili anipe maelezo yatakayoniridhisha. Vinginevyo atapoteza kazi yake, ikiwa kweli ni askari halali wa jeshi la polisi, na atakaa selo.”



    “IGP” alisema maneno hayo huku akiwa amefura kwa hasira. Mwisho wa yote “IGP” akaagiza kesho saa mbili asubuhi wahakikishe huyo afande Jamila anakuwa ofisini kwake!



    Baada ya kikao kile, maafande wale wakaanza kazi ya kumtafuta afande Jamila, baada ya afande Kubuta kumpigia simu ndugu wa marehemu Hamida na kutaka kufahamishwa umbile la huyo Jamila, na baada ya kama dakika 40 tu hivi mara moja wakawa wanachambuliwa maaskari wenye majina ya Jamila walioko katika Mkoa wa Kinondoni, na wakakosa mwenye sifa au wasifu unaomfanana huyo afande Jamila, alieelezwa na Neema, ndugu wa marehemu Hamida ambae alimuona!



    Mara moja Kamanda wa Kanda Maalum akawasiliana na Makamanda wa Mikoa ya kipolisi ya Ilala na Temeke, ili wawasiliane na wakuu wa vituo katika sehemu zao za kazi, ili atambuliwe huyo Afande Jamila, ambaye wasifu wake umeelezwa kuwa ni mweusi wa chokoleti, mrefu wa wastani, mwenye umbo namba nane, ana hipsi kubwa na makalio yaliotokeza, miguu minene, meno meupe sana na lipsi nene katika midomo yake, na macho manene yanayoonekana muda wote kama yamerembuliwa mithili ya mwanamke aliyekula kungu manga! Na anapotabasamu hubonyea mashavuni!



    Lakini pia majibu yaliyotoka kutoka Temeke na Ilala ni kama yale ya Kinondoni.



    Hakuna afande mwenye jina la Jamila mwenye sifa hizo!



    Sasa maafande wale walichanganyikiwa vibaya sana, kiasi wakahisi labda kuna mtu aliyejifanya ni askari akaenda kwa marehemu Hamida ili akaharibu ushahidi wowote uliopo!



    “Sasa hii nini”, alijikuta akisema Kamanda wa Kanda Maalum!



    “Kuna sehemu moja bado hatujaiangali.”



    Alisema Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Nchini, na wale askari wengine wakawa wamemtumbulia macho.



    Yeye akaendelea. “Ni hapa Makao Makuu kwenyewe!”



    Wote wakatamka, “Yes” na kazi ikaanza tena na mara moja Inspekta Jamila akapatikana kuwa ndiye mwenye sifa zilizotajwa.



    Kamanda wa Kanda Maalum akawa anasoma namba ya simu ya Inspekta Jamila kutoka katika orodha ya majina iliyobandikwa ukutani pale makao makuu, Cheo chake na nambari yake ya kazi, alipoziweka kichwani akaenda hewani moja kwa moja akiwasiliana na Inspekta Jamila.



    “Kamanda wa polisi Kanda Maalum ya D’Salaam, popote ulipo kesho unahitajika ofisini kwangu saa moja na nusu asubuhi bila kukosa! Kumbuka hii ni amri, hivyo ufanye hivyo haraka iwezekanavyo”.



    Baada ya kusema hayo kamanda wa kanda maalum akakata simu bila ya kutaka kusikiliza upande wa pili utajibu nini.



    Bila shaka Inspekta Jamila alikuwa katika wakati mgumu sana. Hivyo akajikaza na kuahidi kwenda kusikiliza wito wa mkuu wake ili akajue mbichi na mbivu!



    ********

    -

    ********



    Saa moja na nusu juu ya alama, Inspekta Jamila alikuwa amekaa katika kochi akitazamana na Kamanda wa Kanda Maalum, huku akiwa katika ukakamavu mkubwa.



    “Binti nimekuita hapa kwa mahojiano na wewe”. Alinza kwa kusema Kamanda wa Kanda Maalum, kisha akaendelea.



    “Hivyo nataka kujua nani aliyekupa idhini yakufatilia kesi ya Marehemu Hamida inayomkabili yule Dereva wa Taxi Mwaduga Dingo?! Kwa nini umefanya upelelezi katika kesi mbayo uongozi wako umempa mtu aliyeonekana anafaa kufanya kazi hiyo! Na pia nataka kufahamu ulipofikia katika huo upelelezi wako!”



    Kamanda Kanda Maalum alihoji maswali hayo huku akiwa amechukia vibaya sana. Kabla Inspekta Jamila hajajibu chochote akiwa bado anasubiri mkuu wake amalize ili yeye aanze kujitetea, simu ikawa inaita ya Kamanda wa Kanda Maalum.



    “Nakusoma mkuu”, akaitikia Kamanda wa Kanda Maalum. “Ndiyo afande, sawa afande” Kamanda wa kanda maalum alikuwa anapokea maagizo kutoka kwa mkuu wake “IGP”.



    Baada ya kumaliza kuongea na simu,Kamanda wa kanda maalum alimuangalia Inspekta Jamila na kumwambia.



    “Okey sasa maelezo yako utakwenda kuyatoa mbele ya “IGP”, Ofisini kwake sasa hivi. Inuka twende ofisini kwake.”

    wote wakainuka wakaelekea katika ofisi za “IGP”, zilizopo palepale katika jengo la Wizara ya Mambo ya ndani.



    Kamanda wa Kanda Maalum aliingia ofisini kwa “IGP” akiwa na Inspekta Jamila.

    Baada ya kumtolea heshima ya kijeshi, “IGP” aliwaelekeza kukaa vitini. Walipokwisha kuketi, Kamanda wa Kanda Maalum akaanza kwa kusema;



    “Afande yule kijana ni huyu nilimwita ofisini kwangu asubuhi hii ili anipe maelezo ya kina kabla hujakutana naye, ili niweze kuyachekecha, lakini kwa ulivyoniamrisha uonane naye sasa hivi ndio nimemleta, huyu ndiye Inspekta Jamila”.



    “Sawa Afande kazi nzuri, sasa niachie nimuhoji mimi mwenyewe, wewe kaendelee na kazi yako”.



    Kamanda wa kanda maalum aliinuka na kupiga Saluti, kisha akatoka nje ya ofisi ile na kuelekea ofisini kwake.



    Tofauti na Kamanda wa Kanda Maalum alivyokuwa mbogo kwa Inspekta Jamila, “IGP” alikuwa anaongea katika hali ya utulivu kama anayeongea na wakuu wenzake!



    Hali ile ilimshangaza sana Inspekta Jamila kwani alitarajia kukutana na ukali, ukifatiwa na Amri nyingi kama sio kuwekwa lumande!



    Basi hali ile ilimfanya awe mpole na mwenye kujiamini. Pia akishukuru kuongea na “IGP” moja kwa moja, ingawa angeweza kuhojiwa na Askari wa chini yake.



    Lakini kitendo cha kumuhoji yeye mwenyewe, Inspekta Jamila alielewa ni ile picha ya “IGP” aliyokuwa nayo yeye wakati ule na si kitu kingine!



    “Afande nataka kufahamu upelelezi wako umefikia wapi, umegundua vitu gani vyenye maana na bila shaka utanambia au kutaka kujua juu ya picha yangu uliyoichukua kutoka katika albam ya Marehemu Hamida.”



    “IGP” aliongea kwa utulivu mkubwa huku akitambua anachokifanya!!!



    Inspekta Jamila alikuwa ametulia kama kawaida yake, kisha akajibu.



    “Afande kwanza sina budi kukushukuru kwa kuweza kunita na kukaa na wewe kama hivi, na tukawa tunazunguza, kwani ni nafasi adhimu sana! Lakini pia nilihitaji kupata nafasi kama hii kwa wakati huu ili nikupe taarifa ambazo yawezekana huna, au unazo juu juu si kwa undani”.



    Kisha akaanza kumhadithia toka alipopewa jambo lile na mke wa Mwaduga, na namna alivyolishughulikia hadi kufikia muda ule! Alimwambia kila kitu alichokutana nacho katika upelelezi wake, ikiwemo picha yake “IGP”. Dereva Taxi aliemkodi kwenda nae Kimara suka, na taarifa za mahusiano ya kimapenzi kati yake na marehemu Hamida, bila kusahau taarifa ya ajali ya jirani wa Marehemu Hamida, Bwana Kiyarwenda Mwemezi kwa kina, pamoja na picha za wahalifu waliohusika katika ajali ya kutengenezwa, iliyogharimu maisha ya Bwana Kiyarwenda Mwemezi!



    “IGP” alikuwa anamsikiliza Inspekta Jamila kwa makini na kushangaa ujasiri aliouonyesha kijana wake yule, lakini pia utendaji wake! Na kuona kuwa tayari ameshafahamu uhusiano wake na marehemu Hamida!



    Waliweza kuongea kwa muda mrefu, hatimaye “IGP” aliamua kumkabidhi faili la kesi ya marehemu Hamida, na kumwambia.



    “Upelelezi wako umejua mambo mengi sana kwa muda mfupi wa wiki moja tu, kiasi aliyekuwa akiiendesha kesi hii toka awali hakufika hata robo ya ulipofika wewe, ingawa yeye ana zaidi ya siku sitini!”



    “Hivyo nitaongea na mwanasheria Mkuu ili kuliondosha suala la kijana Mwaduga Dingo Mahakamani ili awe huru, ili aweze kukusaidia kwa upelelezi wako kwa kuwatambua waalifu wale! Kwani akiwa nje atakuwa na imani na jeshi la polisi, pia atakuwa mkweli na muwazi kuliko akiwa mahabusu. Lakini pia kutokana na upelelezi wako, nami pia naungama ya kwamba yule kijana Mwaduga Dingo hana hatia!”



    Mkuu wa jeshi la polisi, alikuwa mtulivu sana, akitawaliwa na hekima na busara, akiwa ameiweka mbali sana jazba.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Hivyo hatuna muda wa kupoteza, picha hizo za sura za watu wawili alizokupa Dokta Zahala, utazipeleka kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai ili azifanyie kazi. Na suala hili kutoka sasa utakuwa ukiliripoti kwangu moja kwa moja!”



    Inspekta Jamila alifurahi kupita kiasi, kwani kuweza kufanikisha yule dereva wa Taxi kuachiwa huru, kwake ulikuwa ni ushindi mkubwa. Lakini pia kupewa kazi rasmi na “IGP” na kuiripoti kazi hiyo moja kwa moja kwake pia ulikuwa ni ushindi mwingine.



    Hivyo alimshukuru”IGP” na kumhakikishia kwamba ataifanya kazi hiyo kwa uaminifu na kwa utii.



    Kisha Inspekta Jamila alitoa picha ya “IGP” aliyopiga na marehemu Hamida akamkabidhi “IGP”.



    “IGP” akaipokea picha ile huku akitabasamu na kumwambia Inspekta Jamila.



    “Nakuaminia askari wangu!”

    Kisha wote wakatabasamu kwa pamoja. Na “IGP” akamalizia kwa kusema.

    “Nakutakia kazi njema yenye mafanikio tele.” Kisha wakaagana.



    Inspekta Jamila aliporudi ofisini kwake akiwa na furaha tele huku mkononi akiwa na faili la kesi ya Mwaduga, alimkuta Eshe Muhidini mke wa Mwaduga Dingo akiwa ameketi anamsubiri.



    “Karibu mgeni upo muda mrefu?”

    Inspekta Jamila alimkaribisha Eshe Muhidini na kumuuliza.



    “Hapana afande nina kama dakika tatu toka kufika hapa.”

    Eshe alijibu, kisha akaendelea, “leo ni Jumamosi nimekuja kukuona katika ile ahadi yetu ili nijue ulipofikia.”



    “Ohoo! sawa nakumbuka kwani nilikwambia uje leo ili kwanza niwe nimefatilia ili nione nawezaje kukusaidia.

    Na hapa nilipo nimepata namna ya kukusaidia, na haitachukua muda mrefu kutoka sasa mumeo utakuwa naye uraiani akiwa huru kabisa!”



    Alijibu Inspekta Jamila kwa kujiamini. Jibu hilo lilimfanya Eshe atoe machozi ya furaha na kutoamini alichokuwa anakisikia.



    “Afande umesema haitachukua muda mrefu mume wangu atatoka?!”

    Aliuliza Eshe kwa fadhaa kama kwamba hakumsikia pale awali alipojibiwa.



    Inspekta Jamila alipa jibu, kama lile la awali huku akiongeza neon.



    “Sasa hivi tutakwenda wote gerezani tukamuone Mwaduga ili pia nizungumze naye suala hili, na vitu fulanifulani.”



    Eshe alikuwa katika mshangao mkubwa sana, kwani aliona kama anaota ndoto za mchana. jambo kama lile ambalo hakutoa pesa hata senti tano ya hongo, kama baadhi ya watu wanavyodhani kwamba, huwezi kumaliza kesi bila kuwa na pesa! Sasa yeye hajatoa chochote kisha ndani ya wiki moja suala lile anaambiwa halina muda mrefu litakuwa limetatuliwa.



    Jambo alilohenyeka nalo kwa zaidi ya miezi miwili!.

    Eshe alimshukuru mwenyezi Mungu, Dokta Zahala na Inspekta Jamila kwa kuweza kumsaidia.



    Aliinuka katika kiti alichokuwa amekaa na kwenda kumkumbatia Inspekta Jamila huku akilia kwa kwikwi na machozi yakilowanisha mashavu yake.

    Inspekta Jamila alimtuliza na kumnyamazisha, kisha wakatoka wote wakitumia gari ya Inspekta Jamila wakaelekea Gereza la Keko.





    *******



    Siku ya Jumamosi jiji la Dar es Salaam huwa na foleni za magari sana, hivyo iliwachukua kama saa moja kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani hadi Gereza la Keko.



    Baada ya kufika pale na kufanya taratibu za kiofisi, Mwaduga aliitwa katika chumba maalum akaweza kumuona mkewe na Inspekta Jamila, yule afande aliyemuhoji wiki moja iliyopita. Askari magereza aliekuwa amewasimamia ili kusikiliza mazungumzo yale ikiwa ni taratibu za kawaida za jeshi la Magereza.

    Baada ya kumjulia hali, Inspekta Jamila akamwambia Mwaduga.



    “Nipo hapa ili kukufahamisha jambo moja kuwa, huna muda mrefu kutoka sasa utakuwa raia huru. Jeshi la polisi limefanya uchunguzi wa kina na kuridhika kuwa huusiki kwa namna yoyote katika kesi zinazokukabili, hivyo jeshi nalo linataka ulisaidie katika mambo fulani fulani!”



    Alisema Inspekta Jamila huku akimuona Mwaduga macho yamemtoka pima na kuacha kinywa wazi kwa mshangao, huku machozi yakimlengalenga machoni mwake.



    Afande Jamila hakumpa nafasi Mwaduga ya kusema neno akaendelea.



    “Kwa kuanzia, jeshi la polisi linataka ututajie wasifu wa wale jamaa watatu waliokodisha gari yako namna walivyo. Na je ikitokezea kuziona picha zao au wao wenyewe kwa mara nyingine tena utaweza kuwatambua?”



    Inspekta Jamila alimwambia Mwaduga taarifa ile muhimu zaidi ya sana, na Mwaduga Dingo sasa akiwa na nguvu mwilini, mwake na matumaini mapya katika moyo wake alijibu.



    “Afande nakushukuru sana, kwanza wewe binafsi kwa juhudi zako za kuweza kulifikisha hapa suala hili, na jeshi la polisi kwa ujumla. Pili kwa mke wangu Eshe kuweza kulifikisha kwako jambo hili! Yaani siamini naona kama nipo ndotoni, kwani kwa zaidi ya miezi miwili hivi sasa, mimi nimekuwa katika maisha mabovu. Hali ya kuwa sijawahi kukamatwa na kuwekwa kituo chochote cha polisi tangu nimezaliwa. wachilia mbali kuletwa gerezani kama mahabusu. Hivyo nimejifunza mambo mengi sana na sasa ninaamini kuwa si wote wanaofungwa jela kwamba wana hatia. Na ama hujafa hujaumbika! Kwani jambo hili haliwezi kusahaulika katika maisha yangu, hadi naingia kaburini.”



    Mwaduga Dingo badala ya kujibu maswali aliyoulizwa, yeye alianza kutoa risala, yenye wingi wa shukurani.



    “Nikiwa huku jela kama mahabusu nimeiweka nadhiri ya kwamba, ikiwa nitashinda kesi hii na kuachiwa huru, basi nitauandika mkasa huu uwe filamu. Ili wale wote waliodhani kuwa mimi ni jambazi na Jamii yote ya Tanzani kwa ujumla wapate somo kutokana na filamu hiyo. Lakini pia kuielimisha Jamii yetu ijue kwamba serikali ipo na inawajali raia zake.

    Na pia watambue wapo maaskari wanaojali haki za raia na kuthamini ubinaadamu, ambao hawafanyi kazi kwa nguvu ya rushwa, kama wewe Inspekta Jamila!”



    Alipofika hapa Mwaduga sasa akawa analia kwa sauti akiwa hawezi kuongea kwa vile donge la uchungu lilivyomkaa rohoni.

    -



    Inspekta Jamila na Eshe walimnyamazisha Mwaduga na Eshe akampa mkono wa pole mumewe huku akimpa moyo.

    “Hakuna lenye mwanzo lisilokuwa na mwisho, lakini pia likiwapo la kuchukiza lipo na la kupendeza. Hivyo usilie sana, kwani tambua ya kwamba, Mbwa hafi maji akiuona ufukwe!”



    Inspekta Jamila akafungua mkoba wake na kutoa picha nne alizokuwa nazo, akaziweka mbele ya macho ya Mwaduga Dingo na kumwambia!



    “Je kuna yeyote katika picha hizi unayemfahamu?”



    Zilikuwa ni zile picha ambazo mbili kati ya tatu alizozichukua nyumbani kwa Marehemu Hamida, na mbili ni zile picha alizopewa na Dokta Zahala.



    Zile picha mbili alizochukua kwa marehemu Hamida, moja alishaifahamu ni ya Dr. Masawe. Zile nyingine bado hajazitambua.



    Mwaduga akaziangalia picha zile, kwa umakini mkubwa kisha akasema.



    “Hapa nimeitambua picha moja tu”

    Mwaduga alisema maneno hayo huku akionyesha picha aliyoitambua.



    Ilikuwa ni ile picha aliyoipata kwa marehemu Hamida iliyomuonyesha marehemu Hamida akinyweshwa kinywaji na kijana mmoja aliyeonekana mtanashati.



    Mwaduga akasema “huyu jamaa anaitwa Bitozi ni muuzaji magari maarufu kule Kijitonyama. Hata gari nililokuwa ninaendesha, aliyekuwa tajiri yangu Bwana Shaame aliinunua kwenye Show Room yake.”



    Inspekta Jamila aliandika neno Bitozi nyuma ya ile picha iliyotambuliwa.



    Baada ya mahojiano ya hapa na pale kuhusu ofisi ya bwana Bitoz ilipo, Inspekta Jamila alipata taarifa za kutosha, na wakaagana na Mwaduga. Yeye na Eshe wakaondoka, wakimuacha yule askari Magereza na Mwaduga akiwa na matumaini tele.



    *****



    Siku ya Jumatatu Inspekta Jamila alikuwa amekaa ofisini kwake akifuatilia ripoti ya picha zile alizozipeleka kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, ili kuzifanyia kazi.



    Picha zile za watu wawili moja kati ya picha zile ilitambuliwa!

    Na ile picha nyingine haikuwepo kumbukubu yoyote ya sura ile katika ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai.

    Hivyo majibu ya picha zile yalikuwa kama ifuatavyo.



    Picha ya mwanaume aliyevaa fulana nyeupe anatambulika kwa jina la Geradi Mwaipopo, kabila Mnyakyusa, aliwahi kuwa askari wa Jeshi la Polisi aliyekuwa na cheo cha Staf Sajent ambaye alifukuzwa kazi katika Jeshi la Polisi, baada ya kugundulika kufanya vitendo vya uhalifu katika kivuli cha Jeshi la Polisi.



    Alipobainika aliachishwa kazi mara moja. Kiasi miaka miwili iliyopita! Wakati huo alikuwa anaishi Magomeni Mwembechai, Mtaa wa Mengo, Nyumba Namba 8. Hupendelea kutembelea Mikoa ya Mbeya, Songea, Tanga, Arusha,Pwani na Dar es Salaam. Kwa sasa haijulikani anaishi wapi wala anafanya nini. Ni mrefu wa futi 6 na inchi 3, rangi ya mwili wake ni nyeusi ya asili. ilimalizia ripoti ile. Na nyuma ya picha ile liliandikwa jina kamili la mwenye picha na kufuatiwa na maandishi “WANTED”.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Inspekta Jamila alitingisha kichwa kwa taarifa ile, kwani aliona askari anafukuzwa kazi hali ya kuwa ana ujuzi wa kutumia silaha, lakini pia mbinu mbali mbali za kijeshi halafu hajulikani anaishi wapi na anafanya nini, hii ni hatari kubwa kwa taifa letu.



    Inspekta Jamila baada ya kuipitia ripoti ile kwa kina, akaiendea gari yake aina ya Toyota RAV 4 maarufu kwa jina la “Kitchen Party” yenye milango mitatu, akafungua mlango wa gari na kuingia ndani ya gari. Kisha akatoa simu na kumpigia Dokta Zahala akitaka kujua kama yuko kazini muda ule.



    Alipopata jibu la ndiyo akamwambia.

    “Nipo njiani nakuja Muhimbili ofisini kwako”



    Inspekta Jamila akakata simu.

    Baada ya dakika kumi Inspekta Jamila alifunga breki katika Hospitali ya Muhimbili nje ya jengo la ofisi ya Dokta Zahala.



    Akatia lock milango ya gari yake, akahakikisha vioo vimefunga vyote, na kuelekea ofisini kwa Dokta Zahala.



    “Dokta nashukuru kwa msaada wote ulionipa tangu unipe kazi hii! Ila sasa siifanyi kwa siri tena kwani sasa nimekabidhiwa faili rasmi kwa ajili ya kufuatilia kesi hii.”



    Alisema Inspekta Jamila akimshukuru shoga yake wakiwa wawili katika ofisi ile na kuendelea.



    “Hivyo basi sikuja hapa kwa ajili ya kukushukuru peke yake laa! Ila bado ninahitaji msaada wako mwingine.”



    Inspekta Jamila alisema huku akimwangalia shoga yake ambaye alikuwa kimya muda wote akiwa anamtazama.



    “Wee! Hongera shoga kwa kupewa rasmi kazi hiyo, sasa msaada upi huo unaouhitaji kutoka kwangu?”

    Aliuliza Dokta Zahala.



    “Nataka unifahamishe kwa Dokta Masawe ofisini kwake na hata nyumbani kwake ikibidi.”



    Alijibu Inspekta Jamila.

    “Ahaa sawa shoga, Dokta Masawe ni Daktari Bingwa, hapa huwa kazini siku za Jumanne na Alhamisi. Siku kama ya leo anapatikana katika Hospitali yake iliyopo maeneo ya Sinza Madukani. Karibu na Guest ya Namnani. Nyumbani kwake ni Kinondoni Mtaa wa Kasaba nyumba ya mwisho kwenye kona, kabla hujafika baa maarufu sana inayoitwa Patchoto.”



    Inspekta Jamila aliposikia jina la Sinza, Karibu na Namnani moyo wake ukamlipuka na akaazimia kwenda muda ule ule kwa Dokta Masawe.



    Akamshukuru shoga yake na akaagana naye,kisha akatoka nje ya ofisi ile akaielekea gari yake tayari kwa safari ya Sinza kwa Dokta Masawe.



    Akiwa hatua kama tatu hivi, kutoka eneo alipoegesha gari yake, Inspekta Jamila aliona kitu kisicho cha kawaida katika gari yake!



    Kwani alipoondoka pale katika eneo la maegesho ya magari, vioo vya gari yake vyote vilikuwa vimefungwa kama kawaida yake, ila wakati huu pale aliposimama, aliweza kuona kioo cha upande mmoja kipo nusu mlingoti!



    Yaani kimefunguliwa nusu. Moyo wake ukaenda mbio akihisi kuwa ameshaibiwa na vibaka!



    Akiwa mwenye hasira aliiendea gari yake, nakuanza kuikagua kwa nje kabla hajapanda. Lakini gari yake yote kule nje ilikuwa salama usalimini!

    Akatazama Lock za milango, akaziona kama alivyozifunga ndivyo zilivyo kaa!

    Alipofungua mlango ili aingie ndani ya gari, alipatwa na mshangao asioutegemea!



    Bahasha ya khaki ilikuwa imewekwa ndani ya gari yake, katika kiti cha dereva.



    Inspector Jamila aligeuka kushoto na kulia, ili kuangalia kama kuna mtu anaeshughulika nae, akaona kila mtu aliekuwa katika eneo lile, alikuwa yupo katika hamsini zake!



    Akaingia ndani ya gari yake huku akiwa na tahadhari zote katika kichwa chake.



    Aliichukua ile bahasha na kuiweka katika kiti cha pembeni na kuwasha gari, huku akikipandisha kile kioo na kutumia vioo vya pembeni vya gari yake, akawa anatazama kama kuna mtu yeyote anaeshughulika nae, kwa mara nyingine kukawa kupo shwari!



    Aliiondosha gari kwa mwendo wa pole, akielekea Sinza kupitia Barabara ya Morogoro.



    Alipofika Magomeni Mapipa, akaegesha gari yake katika kituo cha basi, kisha akaiangalia kwa mara nyingine ile bahasha, akaichukua na kuifungua.



    Ndani ya bahasha ile kulikuwa na karatasi iliyoandikwa maneno yafuatayo; HABARI INSPEKTA JAMILA. NAKUSHAURI KWAMBA, WACHA KUJIINGIZA KATIKA MATATIZO YASIYOKUWA YA LAZIMA! KWANI HUU NI MTEGO WA PANYA. BORA KWAKO KUACHANA NA KESI HII. NA KAMA UTAKAIDI UTAKIONA CHA MTEMA KUNI!



    Alimaliza kuusoma waraka ule Inspekta Jamila, huku akipigwa na mshangao wa mwaka!



    Kilichompa mshangao ni kwamba, huyo mtu au watu alieandika walaka huu ni nani, amejuaje kama yeye ndiyo anaefatilia kesi ile kwa sasa, kwani alipokabidhiwa kesi ile, alikuwa yeye na “IGP” tu, watatu wao ni mwenyezi mungu! Lakini pia mtu alieandika walaka ule, amejuaje kama yeye atakuwa pale kwa Dokta Zahala muda ule?!



    Isitoshe walaka ule haukuandikwa kwa mkono, bali umechapishwa kwa kutumia kompyuta, kisha ukaprintiwa!



    Kazi ile rasmi alipewa Jumamosi, na leo ni Jumatatu, iweje ndani ya siku mbili tu iwe imeshavuja kwamba yeye ndiye! Ukizingatia kwamba hata shoga yake Dokta Zahala, ndiyo amempa taarifa ile muda mfupi uliopita!



    Alipofikia hapo ubongo wake ukawa unazidiwa kwa maswali yasiyokuwa na majibu. Pia akikubali kimoyomoyo kama kweli ule ni MTEGO WA PANYA. Mara akaona vipele vya baridi vikizizima katika mwili wake.





    Akapeleka mkono mgongoni mwake usawa wa kiuno na kuigusa bastola yake ndogo ya kipolisi na faraja ikamrejea upya!

    Alisonya msonyo mkubwa kiasi gari yake ingekuwa imefunguliwa vioo basi hata watu wa nje wangesikia.

    Akaiweka ile karatasi ndani ya bahasha na kuitumbukiza katika mkoba wake.

    Akaiweka gari barabarani na safari ya Sinza kwa Dokta Masawe ikaendelea.



    Alipofika Sinza maeneo ya madukani akachepukia barabara inayoelekea katika Guest ya Namnani, na mbele kidogo akakiona kibao kinachoitambulisha Hospitali ya Dokta Masawe, kilichoandikwa “DOCTOR MASAWE DISPENSARY”, huku kikionyesha mshale kuelekeza ilipo Hospitali hiyo.



    Inspekta Jamila akazidi kusisimkwa na damu isivyo kawaida.

    Katika kona ya pili mbele ya barabara ile akaona maandishi mekundu na meupe pamoja na picha ya nyoka yanayosomeka “Doctor Masawe Dispensary.”



    Inspekta Jamila akatambua kwamba amefika eneo alilolikusudia.

    Katika eneo la maegesho ya magari la hospitali ile kulikuwa na magari kadhaa yaliyokuwa yameegeshwa katika sehemu hiyo.



    Naye akawa katika harakati za kutafuta eneo la kuegesha gari lake ndipo moyo wake ulipompiga ghafla!



    Gari nyekundu aina ya Toyota Caldina ilikuwa imeegeshwa mbele ya hospitali ile.

    Akagundua kwamba Dokta Masawe amemkuta. Akatafuta sehemu nzuri ya kuegesha gari lake na kuiegesha gari na kushuka, akajichoma ndani ya hospitali ile.

    -



    “Hapana mwanamke, siwezi kuondoka hapa bila kuonana na Dokta Masawe ambaye wewe unamuita Bosi. Lakini pia sikutishii kukukamata, bali nitakukamata kweli usipokuwa makini. Kwani kwa kauli hiyo ni kupuuza agizo halali la Jeshi la Polisi na huyo bosi wako hawezi kunifundisha kazi akafanya kwa utaratibu anaoutaka yeye! Sasa mwambie hivi Inspekta Jamila anasema hataondoka hapa hadi unaongea naye. Vinginevyo anaweza kutumia PLAN, B!”



    Inspekta Jamila aliongea bila kuifafanua hiyo “PLAN, B”.



    Kufikia hapa yule dada akataharuki kupita maelezo, akainua tena mkono wa simu na kubonyeza namba kadhaa, akasubiri kwa muda kisha simu ile ikampa maelezo SIMU YA MTEJA UNAYEMPIGIA HAIPOKELEWI!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akarudia tena na tena kuipiga simu ile, huku Inspekta Jamila akishuhudia lakini bado ulikuja ujumbe kama wa mara ya kwanza.



    Yaani ilikuwa inaonyesha kwamba simu aliyokuwa akiipiga yule dada, mkono wake wa simu haukuwekwa katika sehemu yake.



    Inspekta Jamila akamwambia yule dada, “Nipe namba ya simu yake ya mkononi.”



    Yule dada akamjibu “siyo utaratibu kutoa namba ya simu ya mtu ya mkononi bila ridhaa ya mwenyewe!”



    Hivyo Inspekta Jamila akawa haelewi kwa wakati ule nini amfanye dada yule kwa majibu yale.

    Inspekta Jamila akatoka nje ya hospitali ile hadi katika gari yake akatoa simu yake kwenye mkoba akabonyeza nambari kadhaa na simu yake ikawa inaita.

    “Dokta Zahala tafadhali naomba unipatie namba ya simu ya mkononi ya Dokta Masawe, kwani nipo kazini kwake na napata usumbufu kiasi kumuona”.



    “Sawa shoga nitakutumia katika meseji sasa hivi.”



    Alijibu Dokta Zahala na Inspekta Jamila akakata simu.

    Kiasi cha kama sekunde ishirini simu ya Inspekta Jamila ikaingia ujumbe na kwa wahka mkubwa Inspekta Jamila akaufungua ujumbe ule uliotoka kwa Dokta Zahala, na kukuta namba zenye

    tarakimu kumi, ilikuwa niyamtandao wa Voda Com.



    Naye bila Ajizi akaipiga namba ile akawa anasubiri. Jibu alilolisikia kutoka katika simu ile lilimkatisha tamaa.



    “Simu unayopiga kwa sasa haipatikani, tafadhali jaribu tena baadae.”



    Inspekta Jamila alilewa bila ya kunywa!. Mara akakata shauri kuwa siku hizi watu huwa wana namba moja kwa mitandao tofauti.



    Basi alichofanya ni kuipiga namba ile katika mitandao mingine. huku akiiseti simu yake katika mfumo wa “PRIVATE NUMBER” Alipoipiga namba ile katika mtandao wa Airtel ikawa inaita na Inspekta Jamila pumzi zikampaa.



    Moyo wake ukaanza kwenda mbio kama saa mbovu kwa mchecheto mkubwa uliomjaa. Huku akiombea isiwe simu ya mtu mwingine!



    “Dokta Masawe hapa nani mwenzangu?” ilisikika sauti baada ya kupokelewa ile simu.



    Inspekta Jamila aliguna kwa kihoro aliposikia sauti nzito ya mtu aliyehitaji kuonana naye, hatimaye amefanikiwa kuisikia sauti yake.



    “Ohoo! Dokta Shikamoo. Mimi ni Jenipha niko Mwenge nataka kukuona nina mgonjwa wangu. Je upo kazini kwako au upo nyumbani?”



    Inspekta Jamila aliongopa huku akitoa heshima ya shikamoo pia akisikiliza uongo wake kama utaleta jibu gani!



    “Wewe nani aliyekupa namba hii? Kwani hakuna mtu zaidi ya mke wangu na baadhi ya watu wangu muhimu ndiyo niliowapa namba hii.”



    Dokta Masawe alipatwa na mshituko kwani aliyepiga namba ile lazima jina lake litokee kwenye kioo cha simu yake, Kwa sababu wote aliowapa namba ile alihifadhi namba na majina yao katika simu ile. Lakini pia namba ile ilikuwa katika simu yake inayojitegemea, hakuiweka katika mfumo wa kuidivert ingawa ilikuwa inafanana na namba yake ya voda ambayo watu wengi aliwapa namba hiyo. Na alifanya hivi kwa sababu zake maalum!



    Inspekta Jamila akajibu.

    “Aliyenipa namba hiyo ni katika hao watu wako muhimu na wakaribu.” Kisha akaendelea.

    “Dokta sasa simu inakwisha pesa naomba unijibu basi kama leo inawezekana kukuona ili tuonane kwanza tuzungumze ili nijue gharama kabla sijamleta mgonjwa. Pia tutapoonana tutapata wasaa mzuri wa kunihoji chochote upendacho, kwani kutakuwa hakuna gharama yoyote itakayosababishwa na maongezi hayo kwangu”.



    Inspekta Jamila alijibu huku akiilegeza sauti yake kidogo.



    “Sawa, sasa muda huu nina kikao kidogo, wewe unaweza…”

    Dokta Masawe hakumalizia kauli yake akamuuliza swali.



    “Kwa nini simu yako umeiweka katika mpango wa Private Namba?”

    Dokta Masawe kama aliyegutuka, alitaka kufahamu.



    “Jamani Dokta simu yangu haina pesa ya kutosha bwana, inaweza kukatika muda wowote.”



    Inspekta Jamila aliongea kwa sauti ya mapozi iliyotokea puani.



    “Simu yangu ipo katika hali hii muda mrefu sana kiasi miezi mine, miezi miwili baadae ndiyo itakuwa katika hali ya kawaida. Kwani nimeongea na huduma kwa wateja wa kampuni yangu ya Vodacom na kuwataka waniwekee simu yangu katika hali hii, kwani mimi ni mfanyabiashara nina watu wengi niliowakopesha bidhaa zangu, nilipokuwa nawapigia katika kufuatilia madeni yangu, walipokuwa wanaona namba ya simu yangu, walikuwa hawapokei simu au uwapa watu wengine na wakanijibu majibu ya utumbo. Ndipo nilipoamua kutumia mtindo huu.”



    Inspekta Jamila alitumia uongo unaofanana na ukweli na Dokta Masawe akaingia katika mtego.



    “Okey sasa nimekuelewa kwani nilifikiri ni askari mmoja wa kike anayeitwa Jamila alikuwa analazimisha kuongea na mimi muda mfupi uliopita. Hivyo nilidhani labda ndiyo wewe unanichezea. Samahani sana kwa usumbufu uliojitokeza.”



    Dokta Masawe alijibu kisha akatoa majibu ambayo Inspekta Jamila hadi anaondoka katika eneo lile alikuwa katika tabasamu pana, akaiwasha gari yake na kuondoka eneo lile taratibu, huku moyoni akiwa na matumaini ya kushinda kesi ile kwa kishindo baada ya mtego wake kunasa muda mfupi ujao.



    Inspekta Jamila aliendesha gari yake hadi Magomeni Mwembechai, akaegesha gari yake na kushuka nje katika Mgahawa wa Mwembechai Plazza.



    Akaenda katika viti vya mgahawa ule na mara baada ya kukaa tu muhudumu akamfuata na kutaka kujua mteja wao anataka kula au kunywa nini.



    Inspekta Jamila akaagiza maziwa ya moto ya Ng’ombe na mayai mawili ya kuchemsha pamoja na juice ya parachichi.



    Alipoletewa vitu hivyo akawa anaburudika taratibu akiwa anavuta muda wa kwenda kuonana na Dokta Masawe kama walivyopanga. Hiyo ilikuwa ni saa tano ya asubuhi.



    Inspekta Jamila akawa anatafakari mambo aliyokutana nayo toka muda ule alipotoka nyumbani kwake asubuhi hadi kwenda ofisini kwake, na alipokwenda kwa Dokta Zahala namna alivyokuta waraka uliyopenyezwa ndani ya gari yake na yote yaliyotokea kwa Dokta Masawe. Alipokuja kutahamaki, Hamad! Maziwa yalikuwa yameishapoa.



    Inspekta Jamila akapiga tarumbeta maziwa yale na kisha akawa anakunywa juice na mayai kwa taratibu.



    Ilipotimu saa tano na dakika ishirini, Inspekta Jamila akalipa bili yake na kuiendea gari yake ili aende katika mtego wake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alifungua mlango wa gari na kuondoka eneo lile, akielekea kwenye mtego wake, kwani zilikuwa zimesalia kama dakika thelasini na tano, ili kuonana na Dokta Masawe ana kwa ana!



    Inspekta Jamila aliwasha gari yake na kuondoka eneo lile kwa mwendo wa taratibu, akielekea maeneo ya Manzese. Dakika tano baadae, Inspekta Jamila alikuwa ameegesha gari yake katika Hoteli ya Friends Corner pale Manzese Aljentina.



    Akajichoma ndani ya hoteli ile,huku wateja wachache waliokuwa pale kwa ajili ya mlo wa mchana, na wale wanywaji wa pombe wasiokuwa na muda maalumu wa kunywa, walikuwa wakimtumbulia macho Inspekta Jamila toka alipoingia hotelini pale hadi sehemu aliyokwenda kukaa!



    *******



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog