Simulizi : Barua Kutoka Jela
Sehemu Ya Tatu (3)
Inspekta Jamila alikuwa amekaa katika eneo ambalo, alikuwa akimuona kila anaeingia na kutoka. Alipokuja muhudumu akamuagiza amletee kinywaji kisichokuwa na kilevi cha Malta Guness, na yule muhudumu akadai pesa yake kabisa, na Inspekta Jamila akamlipa kabisa muhudumu yule.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kiroja kilikuja yule muhudumu alipokuja, alileta chupa tatu badala ya ile moja aliyoagizwa!
Inspekta Jamila alifikiri labda ni “Order” ya watu wengine wameagiza. Lakini tofauti na mawazo yake, muhudumu yule aliweka mezani kwake zote zile chupa tatu! Na akasema.
“Dada uliagiza chupa moja ya Malta Guness, ila kuna Buzi moja pale limejipendekeza limekupa ofa hizi chupa mbili hivyo usilaze damu.”
Inspekta jamila alishangaa sana kwa kitendo kile, pia akichukia kufikiriwa labda ni Malaya aliekwenda pale kutafuta wanaume!
“Poh, mungu anipishie mbali”, alisema Inspekta Jamila huku akimalizia kwa msonyo hafifu.
Inspekta Jamila akiwa anapata kinywaji chake taratibu mara wakaingia watu wanne wanaume katika Hoteli ile na mara moja moyo wa Inspekta Jamila ukapiga chemba kifuani mwake!
Kwani aliweza kumuona Dokta Masawe akiwa na jamaa wengine watatu, moja kwa moja wakatafuta sehemu wakakaa.
Inspekta Jamila alipowaangalia wale jamaa kwa makini zaidi ndipo sasa alipopigwa na Butwaa zaidi!
Kwani katika wale jamaa watatu waliongozana na Dokta Masawe, kuna jamaa mmoja sura yake ilikuwa si ngeni machoni mwa Inspekta Jamila, alimtambua kuwa ni Geradi Mwaipopo! Yule mtu aliyepata kuwa askari katika Jeshi la Polisi kisha akafukuzwa kazi!
“Ndiyo yeye huyu,” alijikuta akiongea mwenyewe huku akiwaangalia wale watu kwa macho maalum!
“Hawa jamaa wana uhusiano na Dokta Masawe bila shaka Dokta Masawe atakuwa anahusika katika maswala yao,” alijikuta bado akiongea peke yake Inspekta Jamila!
“Sasa huyu Dokta Masawe nimfuate pale alipo au nimuache kusudi niwafatilie watakapoondoka ili nijue nyendo zao?!”
Alikuwa anapanga na kupangua Inspekta Jamila kwani aliona kuwa mambo sasa yameiva!
Na hata pale alipokuwa anaongea kimoyomoyo, aliangalia saa yake nakuona ni saa sita kasoro dakika kumi! Ikiwa ni tofauti ya dakika kumi tu iliyosalia ili kutimia ahadi ya kuonana na Dokta Masawe pale FRIENDS CORNER HOTEL kama alivyopendekeza Dokta Masawe!
Inspekta Jamila akajipongeza kwa kuweza kuificha namba yake ya simu alipompigia Dokta Masawe, kwani sasa hatoweza kumtambua kwa kuwa hawajawahi kukutana ana kwa ana kabla ya sehemu ile, ila yeye anamtambua Dokta Masawe kutokana na tukio moja la ajali iliyotokea pale Kibaha, na jopo la madaktari kutoka Muhimbili na hospitali zingine walipokwenda kutoa msaada ili kuokoa maisha ya watu, Dokta Masawe ndiyo alikuwa kiongozi wa msafala ule wa Madaktari!
Hivyo mara kwa mara alipokuwa anaongea kupitia vyombo vya habari, kuelezea maendeleo ya wagonjwa, Inspekta Jamila alikuwa anamuona kupitia kwenye Luninga!
Ndiyo maana hata alipoiona picha yake katika Albam ya marehemu Hamida, mara moja alimtambua!
Lakini kabla hajaongea na Dokta Masawe, kimaajabu na kiulaini anamuona pia Geradi Mwaipopo ambaye yeye alikuwa akimtafuta kwa Udi na Uvumba! Ambaye picha ya sura yake ilinaswa kwenye macho ya marehemu Kiyarwenda Mwemezi Baada ya kufanyika vipimo vya kitaalam.
Hakika Mungu ni Mkubwa kwani hakutegemea watu wale kama wangekuwa na uhusiano! Duh ama kweli usilolijua ni kama usiku wa kiza!
Inspekta Jamila akiwa pale alipo, alimuona yule Dada aliyemletea vinywaji, akiwahudumia Dokta Masawe na kundi lake, akaangalia saa yake na kuona ni saa sita kasoro dakika tano za mchana.
Dokta Masawe aliangalia saa yake kisha akawa anaongea jambo na wenzake, ambalo Inspekta Jamila kwa umbali aliokaa, hakuweza kuwasikia wanachoongea.
Mara bila ya kutarajia Inspekta Jamila alimuita yule Dada Muhudumu, na alipofika pale akamtuma akamwambie Dokta Masawe kuwa, yule mgeni wake wa saa sita ameishafika kitambo yupo pale anamuhitaji! Na yule dada kama umeme akawasilisha ujumbe ule kwenye meza ya Dokta Masawe walioijaza kwa nyama za kuchoma na pombe! Na wote waliokuwa wamekaa katika meza ile wakageuka kumtazama Inspekta Jamila.
ndipo Inspekta Jamila alipoiona sura ya Geradi Mwaipopo kwa ufasaha na uwazi kabisa, kwa haraka haraka aliwatupia macho na wale jamaa wawili lakini hakuambua kitu, kwani hakuweza kumtambua hata mmoja kati ya wale wawili!
Na nukta chache baadae Dokta Masawe alikuwa amehamia katika meza ya Inspekta Jamila wakawa wanatazamana uso kwa uso mdomo kwa mdomo!
“Ndiyo Bi Jenipha habari za tokea muda ule?” alianzisha mazungumzo Dokta Masawe, huku akilikariri lile jina la Jenifa!
Inspekta Jamila ilibakia kidogo tu aangue kicheko, kwani yeye alishasahahu lile jina alilomuongopea Dokta Masawe.
“Nzuri tu Dokta Masawe, pole na kikao. Je! wale waheshimiwa uliokuwa nao, ni miongoni mwa wajumbe katika kikao chako?”
Inspekta Jamila aliongea huku akijichekesha.
“Wewe umejuaje? Watu hawa ndiyo wanaoniweka mjini na muda huu nikawa napata kilaji hapa!”
Alijibu Dokta Masawe, na Inspekta Jamila akatambua kuwa mtu anayeongea nae , ni mualifu anaejiweka katika kivuli cha udaktari.
Ila ana kazi nyingine ya ziada tena ya haramu, inayompa pesa nyingi zinazomfanya awe jeuri na kulewa wakati wa kazi!
“Kumbe nimepatia, basi nipe zawadi yangu.”
Inspekta Jamila akazidi kujizoesha kwa Dokta Masawe ili awe naye Karibu, na hatimaye aendeleze kazi yake iliyomfanya awe pale wakati ule.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ehee Lete habari zako, kwani sina muda mrefu nataka kutoka, kuna sehemu nakwenda kumuhudumia mgonjwa.”
Dokta Masawe alianzisha Mazungumzo.
Inspekta Jamila, bila ya kupanga alijikuta akiongea hivi.
“Dokta Masawe Samahani sana tena sana, kwani nina mdogo wangu, amepatwa na matatizo amekuja yupo nyumbani kwangu, hivyo ninahitaji msaada wako umuhudumie!”
Inspekta Jamila aliongea kwa sauti ya upole, huku akiwa macho yake ameyalegeza, na kwa kuwa macho ya Inspekta Jamila tokea asili yake tayari yasharembuliwa! Basi alivyoyalegeza, loo Salale utadhani macho ya mtoto mchanga aliepatwa na ugonjwa wa Degedege!
Na hata kama ungekuwa mgumu kiasi gani, kwa macho yale uzalendo ungekushinda lazima!
Na ndivyo ilivyotokea kwa Dokta Masawe! Akaingia katika mtego wa Inspekta Jamila.
“Do pole sana bibie, je huyo ndugu yako amepatwa na matatizo gani?”
Aliuliza Dokta Masawe huku akionyesha huruma na moyo wakusaidia!
“Yeye amepigwa Risasi na Polisi na risasi imebaki mwilini kwake! Lakini pia imemvunja bega alikuwa katika harakati za kutafuta maisha unajua tena vijana Dokta, hivyo akiwa na wenzake, wameshafanikiwa kupora pesa, wakatokea askari wa doria na kuanza kutupiana risasi, na yeye ikampata risasi ya bega, lakini alifanikiwa kuwatoroka polisi na kuondoka!”
Inspekta Jamila, alisema maneno hayo huku akimtazama Dokta Masawe usoni mwake, na kuendelea.
“Hivyo tafadhali sana Dokta Masawe nakuomba nisaidie kama itawezekana, nitakupa kiasi chochote cha pesa ukiweza kufanikisha jambo hili tafadhali Dokta, tafadhali. Niokoe katika kadhia hii!”
Inspekta Jamila sasa aliuwa kabisa, kwani mtego huo ukinasa, moja kwa moja atakuwa analipigia mstari jibu lake tu kwamba, Dokta Masawe ana uhusiano na wahalifu, wakiwemo Geradi Mwaipopo na wenzake!
Hivyo inawezekana, majambazi kuwa wanamtumia Dokta Masawe katika maswala kama haya, kwani majambazi wanapopigwa risasi, hawaendi katika hospitali za Serikali kwa kuhofia kukamatwa na polisi, Lakini huwa wanatibiwa katika hospitali za watu binafsi au madaktari huenda na vifaa vyao katika nyumba za majambazi hao, na kuwatibia kisha kupewa pesa nyingi sana kwa kitendo hicho!
“Duh Dada unanitisha kidogo, kwani hatujazoeana kabisa, unawezaje kuniambia kitu kama hicho, na wewe nani kakwambia kama mimi nashughulika na vitu hivyo! Yaani unaniweka katika wakati mgumu na sina amani hata kidogo!”
Dokta Masawe alikuwa yupo njia panda, Pesa anaitaka, lakini pia anaogopa kwani hamtambui huyu Dada asije akawa ni askari akaingia katika matatizo, ukizingatia leo hiyo hiyo alitembelewa na askari tena wa kike!
Inspekta Jamila muda wote tokea afike Dokta Masawe alikuwa haishi kuchezeachezea simu yake mara kwa mara kama mtu aliekuwa limbukeni wa simu!
Dokta Masawe baada ya kujiumauma, mwisho wa yote akamwambia yule mwanamke mrembo aliyekuwa mbele ya macho yake, mwenye pua ya upanga iliyochongoka mithili ya pua ya kisomali, ambaye akimwita kwa jina la Jenipha akasema.
“Sawa nimekuelewa na kwa sababu yako nitaifanya kazi hiyo kwa moyo mmoja, na kijana atarejea katika hali yake ya kawaida! Je umeniandalia kiasi gani?”
“Kwa kweli Dokta Masawe kwanza nakushukuru sana kwa moyo wako wa huruma, kuhusu pesa inabidi utaje wewe Dokta, kwani wewe ndiyo mtendaji ila usinigonge sana kwani ndugu yangu atakuletea Tenda kutoka kwa jamaa zake ili nao uwe unawatibia wanapopatwa na matatizo kama yake!”
Inspekta Jamila alizidi kumtega yule Dokta dhalimu ambaye hadi kufikia pale, alikuwa anamchukia vibaya sana!
“Kwanini Dokta unafikiria kunitajia bei, inamaana hujawahi kuwatibu wagonjwa wa namna hiyo?! Kama umeshawahi wewe nipe bei kama hao ulizowapa siku za nyuma!”
Inspekta Jamila aliyasema hayo huku akiendelea kuchezea simu yake!
Dokta Masawe alikohoa kidogo kisha akasema.
“Nakuwa mzito kusema kiasi cha pesa kwa sababu sijamuona mgonjwa mwenyewe nikaweza kumkagua, ili kwanza nijue hiyo risasi imemchuna tu, au imeingia kwenye nyama, lakini pia nijue risasi ya bunduki gani iliyomuathili ndiyo ningeweza kukwambia bei kwa urahisi. Hao ambao tayari nimekwisha watibia Hospitalini kwangu na wengine majumbani mwao wote kwanza niliwaona kisha baada yakuwafanyia uchunguzi, nikawapa bei na kuwashughulikia!”
Dokta Masawe alikuwa anaeleza kitaalam namna anavyofanya kazi yake kwa ufasaha, na kuendelea.
“Labda kwako tuseme hivi, itabidi tukubaliane moja kwa moja hata kama mgonjwa sijamuona kwa kiasi cha shilingi Laki Tano!”
Inspekta Jamila alishusha pumzi nzito kwa jibu lile kwani Dokta Masawe alimthibitishia kuwa ndiyo zake, hivyo kwa kuwa yeye alikuwa yupo kazini, alikubali bila hata kulilia hali!
“Sawa Dokta nimekubali, kwani pesa kitu gani bwana, pesa zinatafutwa! Hasara Roho pesa makaratasi!”
“Thatha Bwana Mathawe ndiyo umehamia moja kwa moja kwa huyu bibie hadi jamaa dhako umetuthahau?!”
Ilikuwa ni kauli ya mmoja kati ya wale jamaa alioingia nao Dokta Masawe, na mara moja Inspekta Jamila mapigo ya moyo yakaanza kumwenda mbio!
Kwani aliikumbuka kauli ya Bwana Masudi, yule jirani yake Mwaduga, alipomwambia kuwa.
“Nilimsikia akiongea kwa kithethe, tunatho Elfu tatu tupeleke kwa macheni”
Leo akiwa na Dokta Masawe anamsikia jamaa akiongea kwa kithethe, na hata wasifu wake alioambiwa na Masudi, hakika unashabihiana nae.
Huyu bwana ni katika wale watu wawili, ambao Inspekta Jamila, hakuweza kuwatambua awali.
Inspekta Jamila Pia akafikiri kuwa, wale jamaa huenda ikawa ndiyo waliopanda Taxi ya Mwaduga pale katika barabara ya Namnani! Hapo mapigo ya moyo yakazidi kumuenda mbio, huku damu ikimchemka!.
Inspekta Jamila aliinua simu yake juu kuelekea kwa yule Jamaa wa Kithethe huku akiwa anacheka hadi jino la mwisho linaonekana,huku akiendelea kuchezea simu akamwambia yule bwana kithethe.
“Huo wivu sasa unaouleta, kama unaona Dokta anafaidi basi njoo na wewe ukae!”
Hatimae kwa jibu lile wote watatu wakaangua kicheko.
Dokta Masawe alimjibu yule bwana; “Nakuja sasa hivi kwani namalizia malizia maongezi ya mwishomwisho!”
Na yule jamaa akamwambia, “Mimi thikuonei wivu, ila ulithema kuna thehemu unatakiwa thaa nane, na hivi thatha ni thaa thaba na nuthu”
Baada ya kusema hayo mzee wa kithethe akarudi kwa wenzie kwenda kuendelea na makulaji!
Dokta Masawe na Inspekta Jamila wakakubaliana kesho jumanne baada yakutoka Muhimbili katika “Clinic” yake wakutane maeneo ya Ilala Amana, ili waongozane hadi nyumbani kwake Inspekta Jamila, ambaye Dokta Masawe alimtambua kwa jina la Jenipha, ili akatoe huduma kwa mgonjwa.
Baada ya kuafikiana, Dokta Masawe, aliondoka katika meza ile, na kurudi katika meza ya maswahiba zake.
Inspekta Jamila akifurahia kuwa mtego wake umenasa vizuri na hasa umekuwa ni MTEGO WA PANYA kwani huingia aliyekuwepo na asiyekuwepo! Au labda niseme ilikuwa jiwe moja kwa ndege watatu!
Inspekta Jamila akaendelea kunywa kinywaji chake cha ofa baada ya kile alichoagiza kwa pesa yake kukimaliza.
Huku macho yake yakiwaangalia wale jamaa waliokuja na Dokta Masawe, mara akamuona Dokta Masawe ameinuka na kuagana na jamaa zake kisha akatoka nje ya hoteli na kutokomea kusikojulikana.
Inspekta Jamila alingoja kama kiasi cha dakika tatu toka kuondoka kwa Dokta Masawe, aliinuka katika kiti alichokalia na kwenda chooni huku akipita Karibu kabisa na meza ya wale jamaa, kisha ule mkono uliokuwa umeshika simu yake, akawanyooshea mkono na kuwapungia akiwapa salamu, huku nao wote wakiwa wanamtazama na walimuitikia salamu yake huku wakiwa wamepigwa na ganzi kwa mshangao! Wakistaajabia urembo wake.
Geradi Mwaipopo alikuwa yupo tofauti na wenzake, kwani yeye aliitazama ile simu ya Inspekta Jamila, kisha akamkazia macho ya udadisi mkuu!
Inspekta jamila, yeye akapitiliza moja kwa moja hadi katika vyoo vya wanawake na kuingia chooni.
Ilimchukua kama dakika tatu hivi akiwa kule chooni, alipotoka nusura aanguke kwa mshangao, kwani sehemu waliokuwa wamekaa kina Jeradi Mwaipopo, sasa ilikuwa na viti vitupu!
wale jamaa walishatoka eneo lile.
Inspekta Jamila alimuona yule muhudumu wa kike akiondosha chupa zilizokuwa zimezagaa kwenye meza ile!
Inspekta Jamila kwa mwendo wa haraka alitoka nje ili awawahi watu wale, na hatimae awafatilie kusudi iwe rahisi kuwatia mkononi mwa Sheria.
Alipotoka nje akaiona gari moja aina ya Toyota Mark II nyeupe ikiingia barabarani kuelekea maeneo ya Kagera ikiwa inatoka katika sehemu ile ya hotel!
Kitendo bila kuchelewa, Inspekta Jamila aliwahi kwenye gari yake ili awafatilie wale wahalifu, lakini alipofika usawa wa gari yake, ilibidi akae chini kwa jinsi alivyochoshwa!
Tairi la mbele upande wa dereva wa gari yake lilikuwa limelala chini lina pancha!
“Nooo! Haiwezekani.”
Hatimaye Inspekta Jamila, alipata nguvu na kutoa kauli.
Inspekta Jamila, alikuwa hakubaliani na hali aliyoiona katika gari yake.
Tairi za gari yake, zilikuwa mpya kabisa, tena ni TUBE LESS hivyo hata kama angekuwa amekanyaga msumari tairi lisingelala mapema kiasi kile!
Akiwa pale chini kwenye kikuta akiwa amekaa, aliishuhudia ile gari ikipotea machoni mwake,huku naye akiwa amekata tamaa!
Mara walitokea jamaa wawili waliokuwa wanaosha magari katika eneo lile, wakamwambia Inspekta Jamila.
“Vipi sister unayo jeki na spana tuchakarike chap chap?”
Inspekta Jamila akawaangalia wale jamaa na kuridhika kwamba siyo watu wabaya, akapatana nao bei ili wambadilishie tairi wamuwekee tairi la akiba.
Inspekta Jamila akainuka pale alipokuwa na kuuendea mlango wa gari yake, ili afungue apate kutoa jeki na spana yakufungulia tairi, akasikia sauti kutoka kwa wale jamaa ikimwambia.
“Tulia hivyo hivyo Inspekta Jamila! Kwani kujaribu kubisha ni sawa kabisa na kusaini kifo!”
-
Mmoja kati ya wale jamaa wawili alimwambia Inspekta
Jamila huku mkononi akiwa ameshikilia Bastola aina ya
Chinise.
Inspekta Jamila alisikia maneno yale yakimuingia hadi kwenye damu,huku akiwa amemuelekezea mgongo yule jamaa anaemuamrisha maneno yale.
Inspekta Jamila alitaka kugeuka,lakini jamaa aliikoki ile bastola huku akimwambia.
“Stop!Mkononi kwangu nina silaha ya moto,na ndani yake
kuna risasi nane hivyo sitosita kuitumia kama tu utaleta ukaidi.sikiliza ujumbe wangu kwa makini,na nitakuacha huru uendelee kupumua!Kwani maisha yako nimeyashika
yapo mkononi mwangu!”
Wakati jamaa mmoja amemtuliza Inspekta Jamila,yule mwengine alitoka mbio akaingia katika gari iliyokuwa
imeegeshwa jirani kabisa na gari ya Inspekta Jamila
akaiwasha na kuiweka mkao wa kutoka!
“Elekea kwenye hiyo gari na upande,kisha nikupe ujumbe
wangu huku gari ikiwa inatembea,nikishamaliza kukupa ujumbe wangu na ukaukubali nitakuacha huru na hai,ila kama utaendelea kukaidi kama tulivyokuagiza katika waraka mfupi kule Muhimbili,nitayakatiza maisha yako Inspekta!”
Moyo wa Inspekta Jamila ukapiga Pah huku ukimuenda
mbio!
Alichofanya nikuelekea katika ile gari huku damu ikimchemka,na jamaa akimfatilia kwa Karibu nyuma yake.
Alipofika katika mlango wa ile gari,aliangalia mle ndani ya gari nakumuona mtu mmoja tu aliekaa nyuma ya usukani ambae ni yule jamaa aliejifanya muosha magari,gari waliyokuwa wanaiosha ndiyo iliyofunguliwa mlango ili aingie!
Hapo kulitokea kitu mbacho hakuna aliekitegemea katika
wale jamaa.Inspekta Jamila aliinama kama anaetaka
kupanda ile gari,na yule jamaa aliemshikia bastola nyuma yake, akasogea Karibu zaidi ili aingie pamoja nae.
Inspekta Jamila kwa wepesi wa ajabu alirusha teke aina ya OSHIRO na kuipangusa ile bastola mikononi mwa yule
jamaa,na ile bastola iliruka juu!{OSHIRO,ni teke la kisigino linalopigwa kwa kuzunguka ukiwa umempa adui mgongo.}CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Yule jamaa akiwa amefadhaishwa kwa kitendo kile,akaruka juu ili aidake ile bastola.
Na hilo lilikuwa ni kosa la mwaka kwake,Inspekta Jamila alirusha teke lingine,safari hii akipiga teke aina ya
MAIGERI na kumpata yuje jamaa katika kifua usawa wa
chembe,na yule jamaa akatupwa nyuma kama gunia
nakuanguka kwa kishindo akidondokea kisogo!
{MAIGERI,ni teke linalopigwa kwa unyayo wa chini ya
vidole vya mguu ukiwa unatazamana na adui}
Inspekta jamila kwa kasi ya ajabu, aliitoa bastola yake
mgongoni kwa mkono wake wa kushoto,na kuikoki wakati
huohuo akiidaka ile bastola ya yule baradhuli kwa mkono
wake wa kulia, akawa na bastola mbili mikononi mwake!
Inspekta Jamila aliichanua mikono yake ikawa kila mtu
katika wale jamaa wawili anatazamana na mdomo wa
bastola.
Moja akiielekeza magharibi, na nyingine upande wa
mashariki kwa namna walivyokaa wale watekaji wake!
Yule jamaa aliekuwa ndani ya gari, alipoona mambo
yamegeuka akakanyaga mafuta kwa nguvu, na gari ile aina ya Toyota Chesser Automatic yenye Silinda sita, iliondoka kasi huku ikichimba eneo lile ikiwacha vumbi la hali ya juu!
Inspekta Jamila sasa kwa mikono miwili ambayo
imekamata bastola mbili,alijitupa chini kama Mkizi akilala kifudifudi huku akizielekeza zile bastola kule kwenye ile gari na kufyatua risasi mfululizo zilizopiga kwenye tairi za gari ile, na akaishuhudia gari ile ikiruka juu na kupinduka juu chini! Huku ikiwa imeshaingia katika barabara ya morogoro ikawa Boneti la gari ile ikipanda kikuta kinachotenganisha barabara,na Buti lake likiwa barabarani
huku Magurudumu yake yakizunguka hali ya kuwa yapo juu!
Kilichofatia ni mtafaruku na fadhaa ya hali ya juu kwa
wakazi wa maeneo yale,kwani watu walikuwa wanakimbia hovyo huku wakipiga kelele,pia wapo waliokuwa wanakimbilia ili waone kilichotokea.
Inspekta Jamila akamgeukia yule jamaa pale chini,akapiga
goti na kumuelekezea zile bastola mbili zilizokuwa
mikononi mwake, akamuona yule jamaa anakohoa damu
tena mfululizo.
Inspekta Jamila akaingiza mkono katika mkoba wake
uliokuwa unaning’inia begani muda ule,akatoa simu yake
na kubonyeza tarakimu kadhaa kisha baada ya kupokelewa simu ile alisema.
“Specil order nipo manzese Aljentina hapa,Friends corner
hotel ongeza nguvu tafadhali,kuna wahalifu nimepambana
nao.”
Baada yakusema yale akakata simu na kumsogelea yule jamaa pale chini, huku watu wakiwa wamejaa eneo lile,akairudisha simu yake katika mkoba wake kisha akaitoa risasi iliyokuwa Chemba tayari kwa kufyatuka kutoka katika bastola ya yule jambazi pale chini pamoja na magazine yake,akaitumbukiza katika mkoba wake.
Akabakiwa na bastola moja tu sasa akamnyooshea yule
mtekaji wake na kumwambia.
“Safari yetu ya pamoja bado ipo! Ila itabidi tusubiri gari
nyingine,kwani yangu ina pancha na ile yenu imepinduka!”
Kiasi cha dakika tano baadae Gari aina ya Land Rover 110
Difender mbili za polisi,huku mitutu ikiwa mikononi
ziliwasili eneo lile,na tafrani ikaanza upya kwani watu
walikuwa wanakimbia hovyo eneo lote likajaa hekaheka
tupu.
Inspekta Jamila akatoa maelekezo kwa wale askari wa Doria Kenda,na mara moja yule jambazi alisombwa msobemsobe akarushwa ndani ya ile gari ya polisi huku afande mwingine akishughulikia kubadilisha tairi katika
gari ya Inspekta Jamila.
Kule katika Barabara ya Morogoro,askari wa usalama
barabarani walikuwa wanayaongoza magari kupita,huku simu za upepo zao zikiwa zinawasaidia kuwasiliana na watu wa ‘Break Down’ ili kuja kuiondosha ile gari iliyopata
ajali.
Yule jambazi alietaka kutoroka na gari,baada yakuona wamedhibitiwa, alikuwa anatolewa chini ya uangalizi wa askari polisi, kwani alikuwa amenaswa na usukani wa gari ile.
Inspekta Jamila akamuendea yule Jambazi aliepambana
nae pale alipolala ndani ya gari ya polisi na kumwambia.
“Kabla hatujaendelea na safari yetu, itabidi upelekwe
hospitali kwanza,ukishapata uzima safari yetu kama kazi
itakuwepo!”
Dakika tano baadae Inspekta Jamila aliondoka eneo lile
akielekea ofisini kwake, huku zile Gari mbili za askari polisi
moja ikiwa imebeba majeruhi wawili ikiwakimbiza katika
hospitali ya taifa ya muhimbili na nyingine ikimsindikiza Afande jamila!
Namna gari zile zilivyokuwa zikiondoka, na wale askari
walivyokuwa wananing’inia huku bunduki zao aina ya SMG walivyozidhibiti mikononi mwao,raia walijikuta wakishangilia kama wapo mpirani vile!
Huku nyuma magari matatu aina ya Land Rover 109
yalikuwa yanakuja kwa kasi eneo lile ili kuwahi Tenda ya
kuinua na kuivuta ile gari iliyopata ajali,zilikuwa ni ‘Break Down!’ Na hiyo ilikuwa ni saa nane na robo ya mchana mbuzi anakula majani.
*******
Saa kumi na moja ya jioni, Inspekta Jamila alikuwa ameketi
katika kiti ofisini kwa IGP akimpa maelezo ya kazi yake
kama alivyoelekezwa na bosi wake huyo.
“Afande kuna jambo linaniumiza kichwa,kwani leo ikiwa ni siku ya kwanza tu kuanza rasmi kufatilia kesi hii
nimegundua kwamba kuna watu ambao tayari wana taarifa ya mimi kuishika kesi hii! Na wanajaribu kunitisha
nisiendelee kuifanya kazi hii, kazi ambayo ina heshima
kubwa kwangu katika maisha yangu ya uaskari.”
Inspekta Jamila alikuwa anaongea kwa hisia ya hali ya juu sana,huku akionekana mzuka kumpanda.
“Hasa yule bwege aliepelekwa hospitali,yule anajua kila kitu kwani ameshanithibitishia mimi mwenyewe pale alipojaribu kuniteka!”
IGP alikuwa kimya akimsikiliza kijana wake,lakini bado akiendelea kumshangaa!
Kwani Inspekta Jamila alikuwa anajiamini na nimtendaji mzuri.
“Sasa Inspekta,hebu nipe taarifa kwanza namna
ilivyokuwa,kisha kujulikana kuwa wewe ndiyo mwenye
kesi hii tutajadili mwisho wa ripoti yako.”
IGP alimwambia Inspekta Jamila.
Nae Inspekta Jamila akamuhadithia kila kitu,toka asubuhi matukio ya kikazi aliyopambana nayo, hadi kufikia wakati ule walipokuwa wamekaa katika ofisi ile!
IGP alikuwa akimsikiliza kijana wake huku akisisimkwa na damu katika baadhi ya maelezo ya kijana wake.
Inspekta Jamila baada ya kumaliza kutoa ripoti yake,IGP alikuwa katika tafakari nzito,kisha akasema.
“Umesema ulikuwa ukiwarekodi kupitia simu yako yenye uwezo wakupiga picha za video,na wale wahalifu wote umepata sura zao, kazi nzuri sana kijana.”
IGP alimpongeza Inspekta Jamila kwa ujasiri na kuweza
kufanikisha kuwatambua wahalifu wale, lakini pia wale
aliowatia mbaroni!
“Sasa kuna kitu kimoja nataka uwelewe kutoka sasa kuwa,kwa vyovyote vile,wale wahalifu wameshakugundua kuwa wewe ni askari,tena hatari kwao!
Hivyo hata Dokta Masawe kwa kuwa ana mawasiliano na wale jamaa,kuna uwezekano mkubwa tukampoteza,hivyo
itabadi leo usiku atiwe mbaroni ili tuweze kuwakamata na wahalifu wenzake!”
IGP alikuwa anachangia mawazo yake baada yakupata ripoti kutoka kwa kijana wake.
“Sawa kabisa mkuu,pia naomba afande,yule kijana aliopo mahabusu Mwaduga Dingo,ufanyike mpango wa haraka aachiwe ili aje kuwatambua wale jamaa niliowapiga picha.”
Inspekta Jamila alitoa pendekezo kwa mkuu wake wa kazi.
“Kijana Mwaduga nilishaongea na mkurugenzi wa mashtaka kila kitu,na kesho kutwa siku ya jumatano,mkurugenzi amenambia,atamuondolea mashtaka yanayomkabili,hivyo ataachiwa huru.”
-
“IGP” alihitimisha suala la Mwaduga Dingo.
Inspekta Jamila na mkuu wake wa kazi walipanga mikakati ya namna ya kushinda kesi ile kwa ushahidi usio na chembe ya shaka, kisha wakaletewa chakula mlemle ofisini wakala, walipomaliza kula ilikuwa imeshatimu saa mbili za asiku!
“Sasa wewe nenda ukapumzike kazi nzuri sana uliyoifanya katika siku ya leo, na kama ulivyopendekeza katika ripoti yako, Afande Kubuta awe ndiyo askari utakaeshirikiana nae, hilo litakamilika na usiku huu yeye ndiye atakaekwenda kumkamata Dokta Masawe nyumbani kwake.”
“IGP” akaagana na Inspekta Jamila ambae alikuwa amechafuka na amechoka, huku yeye akiinua simu na kumtafuta Afande Kubuta na kumwita ofisini kwake usiku uleule!
Afande Kubuta alipofika alipewa mikakati yote ya kazi inayotakiwa kufanyika usiku ule, pia atafanya kazi ile akiwa chini ya Inspekta Jamila, na atatoa ripoti ya kazi yake kwa Inspekta Jamila, huku akisisitiziwa kwamba kwa kipindi hiki chote watakachokuwa wanashughulikia kesi ile, hatakiwi kujihusisha na kesi nyingine yoyote, na mkuu wake wa kituo atafahamishwa suala lile.
Inspekta Jamila alipofika nyumbani kwake alikwenda kuoga ili kupunguza uchovu, kisha akavaa kaptula na fulana nyepesi, akaisogelea Compyuta yake nakuchukua simu yake akachomeka waya kwenye simu, na upande mwingine akachomeka kwenye Compyuta.
Akawasha Compyuta na kufungua faili maalum, na baada ya muda picha za video zikawa zinaonekana.
Zilikuwa ni zile picha alizokuwa akiwarekodi Dokta Masawe na wenzake bila wao kutambua, kiasi alikuwa akionekana kama limbukeni wa simu!
Alihamisha picha zile za video kutoka kwenye simu, nakuingiza kweye Compyuta kisha hakuishia hapo, alizitoa zile picha kutoka kwenye Compyuta akazituma kwenye FLASH DISC kisha akazifuta kutoka kwenye simu yake ya mkononi.
Mara simu yake ikawa inaita alipoitazama namba ya simu ile, ilikuwa ni namba ya Dokta Zahala.
“Vipi shoga upo Nyumbani?”
Dokta Zahala aliuliza baada ya kupokelewa ile simu.
“Ndiyo Dokta vipi una habari nyingine, manaake shoga wishi habari kama Idara ya habari maelezo!”
Inspekta Jamila alianzisha utani kwa rafiki yake kipenzi.
“Nitakosa wapi habari wakati mie ni Salatul Habari? Washa sasa hivi TV stesheni ya ITV uone vitu!”
Inspekta Jamila akafanya kama alivyoambiwa na shoga yake, akaona taarifa ya habari ya saa nne usiku ikiendelea, ikionyesha lile gari lililoanguka baada ya Inspekta Jamila kulishambulia, katika lile tukio la pale Friends Corner Hotel.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Pia baadhi ya watu wakihojiwa tukio lilivyotokea, huku kila mtu akisema lake!
Jambo lile lilimchukiza sana Inspekta Jamila, kwani litaharibu upelelezi wa kesi hasa wale majambazi watakapoona taarifa ile au usikia.
*******
Dokta Masawe akiwa nyumbani kwake, aliangalia habari ile kwa makini, huku moyo ukimuenda mbio! Kwani hakuamini hata kidogo kama yule mwanamke aliekuwa akiongea nae ni Askari polisi.
“Mimi nilikuwa mle hotelini nakunywa, yule dada alipoingia pale nilimuagiza muhudumu ampe ofa ya chupa mbili, za kinywaji alichokuwa anakunywa! Alipotoka nilikuwa namfatilia kule nje, ndiyo nikakutana na kasheshe aisee! Yule dada anapiga Karate bwa shee usisikie!”
Alikuwa ni jamaa aliekuepo eneo la tukio akitoa ushuhuda kwa aliyoyaona. Na ndiye aliemfungua macho Dokta Masawe, lakini akimuudhi Inspekta Jamila!
Kwani alijua kuwa kwa vyovyote vile wale majambazi wanaweza kuona taarifa ile waka kimbia!
*******
Saa tisa kamili ya usiku, Afande Kubuta alikuwa na askari wengine saba, walikuwa katika Gari yao ya polisi aina ya Land Rover 110 Defender.
Walikuwa wameiegesha gari yao katika Baa ya Patchoto pale Kinondoni, wakiwa jirani kabisa na nyumba ya Dokta Masawe.
Wale askari wakiwa na silaha aina ya SMG walitelemka katika gari ile, na kwenda kuizingira nyumba ya Dokta Masawe!
Afande Kubuta yeye alikuwa anamuhoji mlinzi wa Baa ile, ili amtajie anapoishi, mjumbe wa Shina wa mtaa ule.
Yule mlinzi akamuelekeza katika nyumba moja ya kota iliyokarabatiwa vizuri, na Afande Kubuta bila ya kupoteza muda, alikwenda kubisha hodi katika nyumba ile.
“Ndugu Mjube mimi ni Mwana Usalama, naomba utoke nje ili tuzungumze.”
Afande Kubuta alijitambulisha, na baada ya muda yule mjumbe aliekuwa anatambulika kwa jina la Mohamedi Mwinyi Kheri alitoka huku akiwa na mashaka!
“Vipi mbona usiku jamani! Kumetokea nini katika Mtaa wangu?”
Mjumbe Bwana Mohamedi Mwinyi Kheri alimuuliza yule afande aliekuwa amevaa koti la kipolisi.
“Samahani Ndugu mjumbe kwa kukusumbua saa hizi ukiwa umepumzika, ila tunakuhitaji kwani katika mtaa huu, tunataka kuingia kwenye nyumba ya Dokta Masawe ili tumpekuwe katika nyumba yake, lakini pia twende nae kituoni kwa mahojiano zaidi, hivyo nataka uwe shahidi tutapokuwa tunafanya hivyo.”
Afande Kubuta alimwambia Mjumbe wa nyumba kumi Bwana Mohamed Mwinyi Kheri. Na dakika tatu baadaye wanaume wale walikuwa ndani ya nyumba ya Dokta Masawe.
Dokta Masawe hakuwemo mle ndani toka saa nne na nusu ya usiku!
“Alipokwisha kuangalia taarifa ya habari, walikuja wenzie wakamfuata!”
Yalikuwa ni majibu ya Mke wa Dokta Masawe ambayo yalimwacha hoi bin taabani Afande Kubuta na vijana alioongozana nao!
“Je alikuaga kuwa anakwenda wapi?” Afande Kubuta alimuuliza yule Mama wa kichaga mke wa Dokta Masawe.
“Hapana kwa kweli Babangu, hakusema anakwenda wa..wapi kweli. Yeye alisema anatoka mara moja hatochelewa kurudi ila sisi tufunge milango, atakaporudi atatugongea!”
Mke wa Dokta Masawe, alikuwa akiongea kwa lafudhi ya kichaga, alikuwa anajibu akiwa na uhakika na majibu yake.
Afande Kubuta alikuwa amehemewa! Kwani sasa mambo yote yalikuwa yameelekea kwenda kombo.
“Sasa?!”
“Hakuna cha sasa, hapa tutamsubiri hadi asubuhi, mjumbe wewe nenda kapumzike, huyu bwana atakaporudi tutakwita!”
Yalikuwa ni majibu ya Afande Kubuta alipokuwa anamjibu mke wa Dokta Masawe aliposema sasa, akiwa anataka kujua kinachoendelea!
“Humu ndani ya nyumba yangu hamtosubiri peke yenu, labda awepo na mjumbe, kwani pia mtu mliyemfata hamkumkuta, hata mlipoingia vyumbani kumtazama hamkumuona sasa mtabakiaje humu?!”
Mke wa Dokta Masawe alikuja juu akiwa amekasirika, asionyeshe woga hata kidogo!
“Samahani jamani sio kama naingilia kazi yenu, ila huyu mkewe ampigie simu mumewe amuulize alipo nasi tutajua chakufanya!”
Mjumbe alitoa rai na mke wa Dokta Masawe akajibu mara moja
“Simu yangu haina Dola mzee!”
Afande Kubuta akatoa simu yake akataka namba ya simu ya Dokta Masawe, Mke wa Dokta Masawe alichukua Business Card pale sebuleni walipokuwa wamekaa nakumpa Afande Kubuta.
Afande Kubuta aliipiga namba ile zaidi ya mara tano lakini ilikuwa haipatikani ilikuwa imefungwa!
“Lakini kwani mume wangu amefanya nini?”
Mke wa Dokta Masawe alitaka kujua, kwani mumewe haijawahi kutokea hata mara moja akafatwa na polisi namna vile, kwake kilikuwa ni kitu cha ajabu sana.
Lakini hakuna askari yeyote kati ya wale sita waliokuwa mle ndani, nadhani hata askari wa saba aliebaki kwenye gari ambae ni Dereva kama angeweza kumueleza yule mama, mumewe alichofanya!
Hata Mjumbe Bwana Mohamed Mwinyi Kheri alipoamua kubaki na wale askari nyumbani kwa jirani yake, hakuwa Dokta Masawe wala simu yake aliepatikana mpaka jua likawapambazukia.
Wana Usalama wale wakaondoka na mjumbe wa shina huku wakiwa patupu!
Siku ya jumanne saa mbili asubuhi Inspekta Jamila alikuwa yupo Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili kwa mambo mawili.
Kwanza kuchukua maelezo ya wagonjwa wake!
Pili kumkamata Dokta Masawe kwa mikono yake, baada ya Afande Kubuta kumpa taarifa kwa ufupi kupitia njia ya simu kuwa hawakufanikiwa kumtia mbaloni, kwani hakulala nyumbani kwake!
Dokta Masawe huwa ana Clinic siku ya jumanne pale muhimbili, kitengo cha MOI.
Hivyo kwa vyovyote vile angekwenda kazini tu, na yeye angemtia mikononi kiulaini!
Akaamua aanzie katika wodi ya Kibasila walipokuwa wale majeruhi wake waliolala na pingu mikononi mwao.
Jibu alilolipata huko lilimrudisha nyuma hatua hamsini kikazi!
“Ninasikitika Afande tumejaribu kuokoa maisha ya hawa wagojwa bila mafanikio, kwani huyu mmoja moyo wake ulikuwa umepasuka na kumwaga damu nyingi ndani kwa ndani. Lakini hata katika kichwa chake amepata athali kubwa, kwani ubongo wake wa nyuma katika kisogo MEDULA OBLANGATA ulivurugika na damu, hivyo katika hali kama hiyo mtu hawezi kuishi; huyu alifariki dakika ishirini toka kufikishwa hapa!”
Daktari aliekuwa anawatibia wale jamaa wawili alikuwa anamfahamisha Inspekta Jamila namna ya yule jamaa aliepambana nae namna alivyokuwa ameumia na kupelekea kifo chake, akalikumbuka teke lake aina ya MAIGERI, lilivyotua usawa wa kifua na jinsi yule jamaa alivyoangukia kisogo.
Mara moja akatambua Medula Oblangata pale ndipo ilipochokozwa!
“Dah nimekuelewa Daktari je na yule mwenzake nae vipi?”
Inspekta Jamila alitaka kujua kuhusu yule jambazi aliyepinduka na gari baada ya yeye kupiga mipira yote miwili ya nyuma ya gari ile kwa risasi na kupelekea kupinduka kwa gari ile.
“Yule nae alifariki saa mbili baadae tangu alipofikishwa hapa. Yule alikuwa na tatizo la kukosa hewa kwani mbavu zake sita zilivunjika, tatu kila upande na hata kama angepona asingefanya kazi yoyote yule!”
Hiyo ilikuwa ni ripoti ya Daktari aliekuwa akiwahudumia wagonjwa wale toka walipofikishwa Hospitalini pale jana yake.
Inspekta Jamila alipelekwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti pale Muhimbili na kuonyeshwa maiti zile, na akawatambua na akawapiga picha katika nyuso zao!
Kiasi Roho ya Inspekta Jamila iliingia simanzi kidogo alipoiona ile maiti ya yule jamaa aliemwambia “UHAI WAKO NIMEUSHIKA UPO MKONONI MWANGU”
Inspekta Jamila alitoka katika wodi ya Kibasila na kuelekea Moi, ofisini kwa Dokta Masawe, alisubiri sana, sasa akiwa yupo katika benchi walilokalia wagonjwa waliokuwa wanasubiri huduma ya Dokta Masawe, lakini hadi inatimu saa nne kulikuwa hakuna dalili za Dokta Masawe bali daktari mwingine aliingia kwa dharula na kuwahudumia wagonjwa!
-
Inspekta Jamila akakata shauri kuwa, kwa kuwa waliahidiana wakutane pale Amana Ilala, basi akaandae mtego wake. Alitoka nakuiendea gari yake akiwa yupo katika mawazo tele na mwendo wa haraka mara, simu yake ya mkononi ilikuwa inaita. Ilikuwa ni namba iliyopigwa katika mfumo wa Private namba!
Inspekta Jamila akasita pale alipo, kisha kabla hajapokea simu ile aligeuka na kuangalia sehemu yote ile ili kuangalia kama kuna mtu yoyote anaepiga simu, akaona patupu!
Akaendelea kuifata gari yake huku simu ile ikiendelea kuita, akafungua mlango wa gari na kuingia ndani!
Na ile simu ikakatika wala na yeye asihangaike tena na simu ile,kwani alikumbuka yeye alivyomcheza shere Dokta Masawe, akachelea na yeye asije fanywa hivyo!
Inspekta Jamila alikuwa akiendesha gari yake kuelekea ofisini kwake walipokubaliana na Afande Kubuta wakutane ili ikiwezekana leo wafunge kazi, kwa kuwakamata wahalifu wale wanaotoa roho za watu kwa sababu ya mali ambayo hawakuitolea hata jasho katika kuichuma. Kwani mwenye mali masikini ya mungu huangaika kwa miaka na miaka, kisha hawa madhalimu wanakuja kuchukua kwa siku moja, lakini pia wanakutoa na roho yako au wakuache majeruhi! Udhalimu wa hali ya juu kabisa huu.
Inspekta Jamila aliendesha gari yake akitokea Muhimbili, akaingia Mtaa wa Malik, alipofika Makutano ya Malik na Umoja wa Mataifa, aliacha barabara ya Mtaa wa Malik na kupinda kushoto kuchukua barabara ya Umoja wa Mataifa. Asubuhi ile kulikuwa na foleni kidogo hivyo alitembea na gari taratibu kiasi, hadi akafika Makutano ya Barabara ya Ally Hassan Mwinyi na Umoja wa Mataifa, akakata kulia kushika njia ya Ally Hassan Mwinyi akaendesha gari yake kwa kasi kidogo kwa kuwa askari aliyesimama pale kwenye taa za Makutano ya barabara inayokwenda AGA KHAN HOSPITAL na ALLY KHAN ROAD, alikuwa anazivuta sana, gari zinazotoka daraja la Salender katika barabara ile ya Ally Hassani Mwinyi.
Katika makutano ya barabara ya Ohio na Ally Hassan Mwinyi , alichepuka kushoto kuelekea Mtaa wa Ohio na kabla hajafika Jengo la PPF akakata kulia kuingia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, akapitiliza hadi nyuma katika ofisi za mbao ambapo ndipo ofisi yake ilipo, akaiegesha gari yake katika maegesho, na kushuka kuelekea ofisini kwake ambapo baada ya kuingia tu alimkuta Afande Kubuta ameshajaa tele kama pishi ya mchele akimsubiri!
Baada ya salaam za utii za itifaki walikaa kujadili namna ya kuendelea na upelelezi kutoka pale walipofikia.
Afande Kubuta alitoa taarifa kwa kirefu namna walivyokwenda kwa Dokta Masawe kwani alishampa ripoti ya jambo hili, ila alimpa kwa muhtasari tu, sasa akamweleza A – Z.
“Hadi ninakuja hapa askari tuliembakiza kuangalia kila anayeingia na kutoka kwa Dokta Masawe bila yeye kujulikana amenipigia simu muda si mrefu kuwa Dokta Masawe hajarudi nyumbani kwake!”
Afande Kubuta alikuwa anampa ripoti yake Inspekta Jamila.
“Sawa Afande kazi nzuri, sasa mimi nina simu ambayo jana niliongea na Dokta Masawe baada ile ya Voda kumkosa, hivyo nataka tumpigie kutumia simu namba ile.”
Inspekta Jamila alimwambia Afande Kubuta, na Afande Kubuta akashangaa aliposikia neno hilo, akashindwa kujizuia na akasema.
“Afande tunachelewa tumpigie sasa hivi.” Alisema Afande Kubuta!
“Hapana Afande Kubuta, huyu tunatakiwa tumpigie simu tukiwa Computer Room, na kama atapokea simu wakati huo, basi atakuwa anatusogeza hatua thelathini mbele.”
Inspekta Jamila alimwambia Afande Kubuta, na hata alipokwisha kusema maneno yale, Afande Kubuta alikuwa anatabasamu huku akimpa tano Inspekta Jamila.
Wote kwa pamoja Inspekta Jamila na Afande Kubuta walinyanyuka vitini wakaelekea katika chumba cha mawasiliano kilichosheheni Computer, wakaeleza shida yao kwa mtu wa mawasiliano anaeitwa Dihenga ambaye pia ni askari.
baada ya kuweka mambo sawa Inspekta Jamila akampigia simu Dokta Masawe huku akiomba mungu simu ile isiwe imezimwa.
Na baada ya sekunde kadhaa simu ya Dokta Masawe ikawa inaita.
“Hollow nani mwenzangu?!”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Dokta Masawe alipokea simu huku akiwa anahema ile mbaya.
Wakati huohuo Dihenga bila kufanya ajizi akafanya vitu vyake!
“Jenifa hapa Dokta nilikuwa nakukumbusha kuhusu ahadi yetu.”
Inspekta Jamila alianzisha mazungumzo mara moja.
“Dah! Afadhali nimekuona, Aha Samahani afadhali nimekusikia, kwani nilikuwa natafuta namna ya kukupata nikawa nashindwa kwani namba yako ya simu hukunipa. Nimepatwa na dharura nimesafiri toka jana usiku hapa nipo Moshi. Sasa ile kazi yako sitoweza kuifanya kwa kweli. Kwani sitarajii kurudi siku za hivi karibuni. Hivyo tafuta Daktari mwingine.”
Dokta Masawe huku akibabaika kweli kweli, alisema kisha akakata simu, kabla Inspekta Jamila hajaongeza neno lolote, kwani alishambaini kuwa yule ni askari kanzu na wala hana mgonjwa!
Inspekta Jamila ilipokatwa ile simu, akamgeukia afande Dihenga, kama mtu aliekuwa anataka kuelezwa kitu!
Afande Dihenga, akiwa anavua vifaa vya mawasiliano masikioni mwake, alimnyooshea alama ya kidole gumba Inspekta Jamila.
Inspekta Jamila, kwa wahka mkubwa akamwambia afande Dihenga.
“Nipe uelekeo tafadhali.”
“Tabata Segerea, Bs motel”
Afande Dihenga alijibu huku akitazama compyuta ilyokuwa mbele ya macho yake.
Bila ya kupoteza muda, Inspekta Jamila alimpa tano afande Dihenga, akatoka na afande Kubuta, wakiwa tayari kuelekea Tabata Segerea.
Askari wale wakiwa katika gari lenye namba za kiraia, mali ya Jeshi la Polisi gari aina ya Toyota Soluna walikuwa wanaitafuta Tabata Segerea.
Dakika arobaini baadae gari ile waliiegesha nje ya jengo la Hotel ya BS, pale eneo la Segerea.
Afande Kubuta na Inspekta Jamila wakateremka ndani ya gari ile wakionekana kama Bibi na Bwana wakajichoma ndani ya Hoteli ile.
Walipoingia tu pale ndani katika sehemu ya kupatia vinywaji, walikutana uso kwa uso na Dokta Masawe akiwa anapata kilevi.
Hali aliyokuwa nayo Dokta Masawe baada ya kumuona Inspekta Jamila, pombe yote ilimtumbukia nyongo!
Kwani alitahayari kama mtu aliyefumaniwa akiwa katika ugoni.
Inspekta Jamila na Afande Kubuta wakakaa katika viti vitupu vilivyokuwa katika meza ya Dokta Masawe na Inspekta Jamila akamsalimia Dokta Masawe.
“Habari ya safari ya Moshi Dokta vipi umerudi kwa concord?!”
Ilikuwa ni salamu ya uzushi na dharau kutoka kwa Inspekta Jamila.
Dokta Masawe hakuweza kusema chochote bali alikuwa amejiinania huku akiwa na wasiwasi na hofu.
Kitendo bila ya kuchelewa Afande Kubuta alitoa pingu akamfunga nazo mikononi Dokta Masawe.
“Kwa nini mnanifunga pingu hali sijakataa kwenda huko mnapotaka kunipeleka. Hii siyo sheria bwana, nitawashitaki kwa kitendo hiki cha kunidhalilisha!”
Dokta Masawe alikuwa anatatalika kama bisi kikaangoni.
Lakini wapi bwana alichukuliwa kituuteni hadi ndani ya gari na safari ya mjini ikaanza.
Dokta Masawe hakika alikuwa amepatikana kweli kweli, ikawa hana jinsi ila kuyakubali matokeo, akawa muumini mtiifu wa ule msemo usemao, kubali yaishe!
Wakati Afande Kubuta alikuwa anaendesha gari, Inpekta Jamila alikuwa anamchunga Dokta Masawe aliyekaa naye katika kiti cha nyuma ya gari ile, huku akiiperuzi simu ya Dokta Masawe.
Katika kupekua pekua kwake, akakutana na ujumbe uliomsisimua.
Ujumbe huo ulikuwa unasomeka hivi;
“Dokta kuwa makini na yule dada uliyekuwa unaongea naye pale friends corner Hotel, kaa naye mbali kwani yule dada ni shushushu. Hivyo kwa taarifa kamili tutaongea hiyo kesho saa tisa kama tulivyopanga tukikutana pale Baracuda, nikuandikiapo ujumbe huu tayari ameshawamaliza Juja na mwenzake Mwaky, hivyo kuwa makini sana hakikisha leo hulali nyumbani kwako”!
Inspekta Jamila alipoangalia namba iliyotuma ujumbe ule na muda, aliona jina lililotuma ujumbe ule limeandikwa MWAIPOPO.
Na ametuma ujumbe ule jana saa moja usiku.
Inspekta Jamila akamuuliza, Dokta Masawe, wakati huo gari yao ikiwa katika eneo la Sanene kule Tabata Segera wakirudi mjini.
“Huyu Mwaipopo ni yule Geradi Mwaipopo uliyekuwa naye jana mchana pale Friends Corner Hotel?”
Dokta Masawe hakujibu kitu alikaa kimya. Inspekta Jamila akamwambia.
“Bado muda wako Dokta Masawe, bali muda ukifika utatueleza kila kitu na wewe mwenyewe utatupeleka kwa hao jamaa zako.”
Inspekta Jamila alizungumza kwa hasira, huku aiuma meno yake, na uendelea kumsimanga Dokta Masawe.
“Daktari kama wewe serikali inakuamini, lakini wewe umeshindwa kuibeba amana, yani wala huelekei kwani unalipwa pesa nyingi sana kwa kwenda kwako kazini siku ya Jumanne na Alhamisi, Yaani siku saba za wiki wewe unakwenda kazini siku mbili na bado una Zahanati yako bila shaka hata wale wagonjwa unawahamisha kutoka katika hospitali ya serikali na kuwapeleka katika Zahanati yako, kwa tamaa iliyokujaa ya pesa. Ukisikia Wachaga kwa kutafuta pesa wanaongoza, basi ndio utafute hata pesa za roho za watu?!”
Afande Kubuta aliendesha gari,na sasa alikuwa yupo katika maeneo ya Tabata Sigara wakienda ofisini kwao. Nusu saa baadae wakawa wanaingia katika jengo la Wizara ya mambo ya ndani ya nchi.
Dokta Masawe akatelemshwa ndani ya gari ile, wakaingia nae ofisini wao.
Walipofika ndani ya ofisi, Inspekta Jamila aliangalia saa ya ukutani iliyokuwa ofisini mle, nakuona ilishatimu saa saba na nusu za mchana, alitoa simu yake katika mfuko wa suruali aliyovaa ya kitambaa cha suti iliyomkaa vyema, ikimbana sehemu ya mapajani na kuonyesha hipsi zilivyotokeza, na makalio yalivyotuna kwa nyuma, na chini suruali ile ilimwaga katika mtindo wa Bwanga huku miguuni akiwa amevaa viatu vya ngozi vya kutumbukiza.
Alibonyeza namba kadhaa na baada ya muda simu ya upande wa pili ikawa hewani,na Inspekta Jamila akatoa maelekezo.
“Nendeni mkatege katika eneo la Baracuda Baa, pale katika kona yakwendea Tabata Chang’ombe na Vingunguti machinjion. Kwani mnamo majira ya saa tisa, yule mualifu tunaemtafuta, Jeradi Mwaipopo atakuwa maeneo yale.”
Baada yakuongea maneno yale akakata simu.
“Hivi mnanikamata kwa kosa gani, mpaka mnanidhalilisha kiasi hiki?!”
“Dokta Masawe unajuwa tulilokukamatia, na kitu tunachotaka kutoka kwako”
Inspekta Jamila alimjibu Dokta Masawe alieanza kupata sauti baada ya kusikia na mwenzake akiwindwa!
“Sawa lakini huna ushahidi wowote kama mimi na wewe tuliwahi kupanga mpango wowote, lakini pia sijashiriki jambo lolote baya na wewe ukalishuhudia, basi kama hivyo ndivyo kosa langu lipo wapi?”
Dokta Masawe alijaribu kujitetea, na Inspekta Jamila hakumjibu kwa mdomo, alichofanya aliivua Flash Disc yake kutoka shingoni alipokuwa ameivaa, nakuipachika katika sehemu yake katika Computer iliyokuwa mle ndani ya ofisi,na kuifungua.
Baada ya sekunde zisizozidi ishirini, Computer ile ikaifungua ile Flash Disc na kuisoma.
picha za Video zenye sauti zikawa zinaonekana!
Dokta Masawe akajishuhudia toka alipokuwa anainuka katika meza aliyokuwa amekaa na wenzake hadi alipofika katika meza ya Inspekta Jamila.
Ngoma haikuishia hapo! Alionekana mzee wa kithethe alipoyaingilia maongezi yao, picha zikamalizia kwa wale jamaa zake waliokuwa wamekaa nae awali akiwemo Geradi Mwaipopo!
Ama kwa picha zile Dokta Masawe alifadhaika sana, kiasi alipoteza matumaini kabisa yakunusurika na kifungo pindi ushahidi ule ukifikishwa mahakamani, kwani atakuwa hana la maana atakalojitetea kwalo!
“Ndugu zangu naomba tuyamalize maswala haya hapahapa yasifike mbele!”
Dokta Masawe alianzisha mazungumzo yakupelekea kutoa hongo.
Afande Kubuta alitaka kusema neno, Inspekta Jamila alimzuia kwa ishara ya mkono kisha akamuuliza Dokta Masawe.
“Unataka tuyamalizeje sema tunakusikiliza”
“Mimi nipo tayari kutoa kiasi chochote cha pesa ili mambo haya yaishie hapahapa”
Dokta Masawe alikuwa anatafuta MLISI! Inspekta Jamila akamwambia.
“Sisi tupo tayari kukuachia bila ya kuchukua hata senti tano yako, lakini tunataka utupe ushirikiano ututajie wale wahusika wenzio majina yao na wanapokaa, lakini pia unafahamu nini kuhusu kifo cha Marehemu Bartazal na mkewe Hamida.ukitwambia hayo kwa ufasaha tutakuachia, kinyume na hivyo wewe utaozea jela uwaache wenzio walioshirikiana na wewe wawe wanapeta mitaani kwa kunywa Lager!”
Maneno yale yalimchoma sana Dokta Masawe na kwa kweli hakuwa tayari kwenda jela, hivyo akajikuta katika wakati mgumu, hatimae akaanza kutapika mambo ambayo Inspekta Jamila na Afande Kubuta yaliwaacha midomo wazi!
Dokta Masawe alianza kwa kusema.
“Mimi na Bwana Bartazal tulifahamiana kiasi miaka mitatu iliyopita, mara ya kwanza kuonana na Bwana Bartazal, ilikuwa pale kazini kwangu Muhimbili alipokuja kutibiwa mguu baada ya kuvunjika katika ajali ya gari. Nilipomfanyia upasuaji na kumuunga mguu wake alianza kuwa Karibu na mimi, kiasi yeye na mkewe walikuwa wakija katika Zahanati yangu mara kwa mara, Bwana Bartazal akiwa na hamu sana ya mtoto na mkewe alikuwa haonyeshi dalili ya ujauzito!
Bwana Bartazal siku moja akasema nikiwa mimi na yeye na mkewe. Dokta Masawe kama mke wangu akijaaliwa kupata ujauzito, mali zangu zote nitamuandikisha yeye! Kwani yeye ndiyo mimi na mimi ndiyo yeye pamoja na mtoto wetu mtarajiwa, kwani mimi binaadamu sina uhakika na mwisho wa maisha yangu, hivyo nachelea nisije kufa kisha mtoto na mke wangu wakaja kunyang’anywa mali na ndugu zangu, kama baadhi ya Jamii nyingine za Watanzania zinavyofanya!”
Dokta Masawe alisimama kidogo, kisha akaendelea.
“Baada ya kuniambia maneno yale, miezi miwili baadae Hamida alinijia peke yake akaniambia kwamba, nina mpango wangu nakuomba sana utilie baraka zako, kwani mume wangu wewe anakuamini sana, hivyo chochote utakacho mwambia wewe atakikubali! Mimi kuanzia sasa naweza kuachika katika ndoa, kwa sababu mume wangu anataka mtoto, na mimi sina uwezo wa kuzaa’ kwani nilipokuwa shuleni nilipewa mimba na mwalimu wangu wa darasa, kisha akanipeleka kwa Daktari mmoja rafiki yake akanitoa mimba ile! Kumbe alinitoa vibaya akasababisha mfuko wa uzazi kuuharibu! Hivyo hata ningekutana na wanaume wa dunia nzima, Hamida mimi siwezi kupata ujauzito! Chondechonde nakuomba nistili na ndoa yangu.”
Kama kulikuwa kuna mtu katika wakati ule alikuwa na huzuni na uchungu, basi alikuwa ni Inspekta Jamila.
Kwani alikamatika kusikiliza mkasa ule kwa shauku kubwa. Na Dokta Masawe akaendelea kusimulia mkasa ule mzito.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mimi nikamuuliza nawezaje kukusaia na kuiokoa ndoa yako?! Yeye akanambia, mimi nataka kujidanganya kuwa ninahisi mimba, hivyo kwa vyovyote vile mume wangu atanileta kwako ili uje kunithibitisha kama kweli nimenasa! Sasa ikitokezea tukaja kwako, usifanye makosa, nithibitishe kuwa ninayo mimba tena ya mtoto wa kiume!
Aliponiambia maneno hayo, nikamwambia itakuwa ngumu sana kufanya hivyo, kwanza itaniharibia CV yangu, lakini pia mumeo akishajua kwamba huna mimba bali ulikuwa ukimuongopea si ndipo utakapoachika? Akasema laa, yeye hatofika huko mpaka kujua kuwa anamuongopea, kwani atakapo mwambia kuwa ana mimba na mimi nikaithibitisha, Mumewe atamuandikisha mali zake zote!
Nae baada yakuandikishwa mali hizo, haitochukua muda mrefu atamuua mumewe, ili Dili lake lisibumbuluke!”
Alipofika hapa Inspekta Jamila alianza kumchukia Marehemu Hamida, nakumuona kuwa yeye ndiyo chanzo cha mambo yote haya kwa tamaa zake!
“Ehee baada ya hapo nini kikaendelea?”
Inspekta Jamila akamuimiza Dokta Masawe ili aendelee kwani alitaka kujua hatima ya jambo lile lilivyokuwa.
“Mimi nilikataa katakata, kwani sikuiona faida nitakayoipata katika jambo lile zaidi ya dhambi. Lakini Hamida alinihakikishia kuwa, kama nitakubali kushirikiana nae katika mpango wake huo, atanigawia Robo ya mali yake yote atakayoandikishiwa na mumewe! Nami Shetani akanitawala, nikashawishika nikajikuta nashiriki katika mpango huo!”
Dokta Masawe alizungumza huku machozi yakimtoka, akionyesha kujutia kitendo kile, lakini wapi Maji yakisha mwagika hayazoleki.
Dokta Masawe alifuta machozi kisha akaendelea.
“Nilipomkubalia alinipiga busu zito, akaniachia na pesa shilingi Elfu hamsini tasilimu, akaniaga nakutoka. Baada ya kama wiki tatu baadae Hamida alikuja na mumewe ili kuja kupima ujauzito, nami nikajua mchezo umeshaanza! Nilimchukua vipimo vya damu ya mshipa pamoja na mkojo wake nikajifungia navyo maabara, nilipotoka nilimpa Hongera Bwana Bartazal na atarajie mtoto wa kiume!
Kwa kweli Bwana Bartazal alionyesha furaha isiyo kifani, kwani alimkumbatia mkewe na kumbusu mbele yangu, huku akiniambia, Dokta niliwahi kuahidi mbele yako kuwa mke wangu akipata ujauzito, nitamuandikisha mali zangu zote, kwa kuwa hili limetimia, basi na mimi sina budi ila kutimiza ahadi yangu kwani Ahadi ni deni!”
“Bwana Bartazal alimuandikisha mali zake zote mkewe.
Ilipofika miezi mitatu Hamida akanijia nakuniambia, sasa umefika wakati wakupata Robo ya mali yangu, kama tulivyokubaliana, na ili jambo hilo litimie, bado juhudi zangu zinahitajika!
Nazo nikumpa mbinu ya kumuuwa mume wake mpendwa Bwana Bartazal Halim.
Nikifanikisha hilo, muda si mrefu nitafungua Hospitali kabisa, badala ya Zahanati! Nami kwa kuwa Shetani alikuwa anatawala mbele yangu, nikampa vidonge vya SALBUTAMOL kumi ili amtilie kwenye Juice. Nakweli Hamida alivichukua vidonge vile nakumtilia mumewe vyote kwenye Juice kama nilivyomuagiza, na mara yule bwana alipokunywa Juice ile, saa moja baadae akawa marehemu Baltazar!”
Inspekta Jamila na Afande Kubuta walikuwa wanatingisha vichwa kwa huzuni ,wakimsikitikia marehemu Bartazal kwani niya yake njema, imemtoa roho yake
Dokta Masawe alifuta machozi kisha akaendelea.
*Nilipomkubalia alinipiga busu zito, akaniachia na pesa shilingi Elfu hamsini tasilimu, akaniaga nakutoka. Baada ya kama wiki tatu baadae Hamida alikuja na mumewe ili kuja kupima ujauzito, nami nikajua mchezo umeshaanza! Nilimchukua vipimo vya damu ya mshipa pamoja na mkojo wake nikajifungia navyo maabara, nilipotoka nilimpa Hongera Bwana Bartazal na atarajie mtoto wa kiume!
Kwa kweli Bwana Bartazal alionyesha furaha isiyo kifani, kwani alimkumbatia mkewe na kumbusu mbele yangu, huku akiniambia, Dokta niliwahi kuahidi mbele yako kuwa mke wangu akipata ujauzito, nitamuandikisha mali zangu zote, kwa kuwa hili limetimia, basi na mimi sina budi ila kutimiza ahadi yangu kwani Ahadi ni deni!*
*Bwana Bartazal alimuandikisha mali zake zote mkewe.
Ilipofika miezi mitatu Hamida akanijia nakuniambia, sasa umefika wakati wakupata Robo ya mali yangu, kama tulivyokubaliana, na ili jambo hilo litimie, bado juhudi zangu zinahitajika!
Nazo nikumpa mbinu ya kumuuwa mume wake mpendwa Bwana Bartazal Halim.
Nikifanikisha hilo, muda si mrefu nitafungua Hospitali kabisa, badala ya Zahanati! Nami kwa kuwa Shetani alikuwa anatawala mbele yangu, nikampa vidonge vya SALBUTAMOL kumi ili amtilie kwenye Juice. Nakweli Hamida alivichukua vidonge vile nakumtilia mumewe vyote kwenye Juice kama nilivyomuagiza, na mara yule bwana alipokunywa Juice ile, saa moja baadae akawa marehemu Baltazar!*
Inspekta Jamila na Afande Kubuta walikuwa wanatingisha vichwa kwa huzuni ,wakimsikitikia marehemu Bartazal kwani niya yake njema, imemtoa roho yake.
Ama kwa hakika Mbega hufa kwa uzuri wake!
Dokta Masawe alikuwa anafuta machozi pamoja na uharamia wake alioufanya lakini alikuwa anaijutia nafsi yake, ama kweli Damu nzito kuliko maji.
*Okey nini kikaendelea?*
Afande Kubuta akamuuliza Dokta Masawe.
*Kilichoendelea Hamida saa moja baadae alipohakikisha kuwa mumewe amekwisha fariki, alikwenda kuimwaga ile juisi iliyobaki, na akatungua kilio kikubwa ili kujaza watu, na kweli majirani zake wakajaa nyumba tele nakuuliza kulikoni, akawaambia kilichojiri ni kwamba, yeye Hamida alikuwa amelala akamuacha mumewe anaangalia Tv, sasa baada yakugeuka nakuona mumewe hajarudi kitandani, akatoka sebuleni ndipo alipomkuta mumewe yupo katika hali hiyo wanayomuona nayo, huku akisisitiza kuwa ameshamuamsha sana bila mafanikio!
Na hapo wale majirani wakatoa wazo la mwili ule kupelekwa Hospitali ili ukachunguzwe kilichomsibu bwana Bartazal, lakini pia Daktari ndiyo akathibitishe kama Bartaza amekufa!
Hapo Hamida akashauri mwili ule uletwe kwangu kwakuwa mimi ndiyo Daktari wao, na hata waliponipigia simu kunifahamisha kilichojiri, mimi niliwaambia nitakwenda mwenyewe pale kwake ili nikamchunguze na kumchukua vipimo!
Hata nilipofika pale na kumchunguza yule Bwana ukweli ulibaki palepale kuwa yule bwana alikwisha fariki!
Niliwathibitishia kwamba mwili ule ni wa marehemu, na amekufa kiasi cha saa moja nyuma, na kilichosababisha kifo chake ni Presha! Iliyosababishwa na mshtuko wa kuona au kusikia jambo lililompa mshtuko nakupelekea kifo chake!*
*Sawa Dokta Masawe hadi sasa tumeelewa Makoko na Matandu ya kifo cha Bwana Bartazal Halim, je na kifo cha Hamida nini kilikuwa chanzo kwa jinsi unavyoelewa, kumbuka kutuambia ukweli kwako kunaweza kusababisha tusichukue hata senti tano yako, na wewe tukakuachia huru!*
Inspekta Jamila alikuwa anatumia DIPLOMASIA zaidi ili kumlegeza Dokta Masawe, kuliko kutumia nguvu isiyokuwa na lazima.
Kama wafanyavyo baadhi ya askari wenzake, wanapotaka kujua jambo Fulani kwa mtuhumiwa!
*Kifo cha Hamida kwa kweli kilitokana na yeye kunizima mafao yangu. Baada yakumkamilishia kazi yake, kwani alikuwa ananikimbia akabadilisha mpaka namba ya simu, kwa kuwa Mshahara wa dhambi ni mauti, nami sikukubali kupata Dhambi za kuua bure bileshi, hivyo nikawatuma majambazi wakenda kummaliza Hamida ili tukose sote. Nalitote tugawane mbao!*
Dokta Masawe kwakadiri alivyokuwa akisema ukweli, alijuwa baadae atakuwa huru hivyo hakuona sababu ya kupindisha maelezo!
Afande Kubuta akamuuliza Dokta Masawe. *Hao Majambazi uliowatuma uliwapataje?*
*Majambazi walio wengi ninawafahamu. Kwani wanapopambana na polisi,na kujeruhiwa na risasi huja katika Zahanati yangu nami huwatibia kwa siri, kisha hunipa pesa nyingi sana, ambapo mgonjwa wa kawaida hawezi kutoa pesa hiyo hata kwa nini, na kwa kiasi kikubwa ukiwa na watu wale kazi ya Udaktari utaiona inalipa sana, ingawa kuanzia sasa sitaki tena kufanya biashara ile!*
Inspekta Jamila akamuangalia Dokta Masawe kutoka chini hadi juu, kisha akatingisha kichwa na akasema.
*Unazo taarifa kama Dereva wa Taxi anaeitwa Mwaduga Dingo, yupo ndani mahabusu kwa kosa la mauaji ya Hamida? Na Je! Unamfahamu kijana huyo, na anahusika na chochote katika mauwaji yale, kwani wewe ndiyo ulieyapanga mauaji ya Hamida na unawajuwa watu waliofanya mauwaji yale!*
*Hapana yule Chalii hausiki hata kidogo, kwani yule aliwapakia kina Baajuni siku ile wakitokea Zahanati kwangu kuchukua malipo ya kazi yao, na walikuwa wanakwenda Baa ya Macheni ili kukutana na Kiongozi wao, ambae mimi sijawahi kukutana nae hata siku moja.
Sasa walipofika pale wakawaona askari wa Doria, na wao kwa mapepe yao wakakimbia bila sababu, wakidhani kuwa bosi wao ameshakamatwa, na pale walikuwa wanasubiriwa wao, kumbe sivyo!*
Dokta Masawe alikuwa akimkataa Mwaduga Dingo kwamba hamfahamu ila bahati mbaya tu imemkumba kwani LILILOKUWA LA KUKUPATA, HALIKUWA LA KUKUKOSA NA LAKUVUNDA HALINA UBANI!
Na mara simu ya Inspekta Jamila ikaita. Alipoangalia saa yake ilikuwa inaonyesha ni saa tisa na robo!
*Duh kumbe muda umekwenda hivi!* aliwaza kisha akaipokea simu, mambo aliyoelezwa kwenye simu kamwe hakuyaamini masikio yake, lakini ndivyo ukweli ulivyotokea.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wale askari walioagizwa na Inspekta Jamila kwenda kule Baracuda, wamempigia simu wakimueleza kuwa; Jambazi Geradi Mwaipopo limevunja mtego wa polisi, nakufanikiwa kutoroka, lakini pia amejeruhi askari wawili kwa risasi!
Taarifa hiyo ilimpa wakati mgumu sana Inspekta Jamila na hakutaka kusema taarifa ile kumwambia Afande Kubuta mbele ya Dokta Masawe, hivyo wakaendelea kunyonya taarifa kutoka kwa Dokta Masawe mpaka waliporizika kwa yale waliyoyapata!
Ila kitu ambacho sio Dokta Masawe, wala Afande kubuta alichokuwa anajuwa kuwa mazungumzo yale Inspekta Jamila alikuwa Anaya record kupitia Simu yake kwa njia ya Video na Audio!
*Haya sasa jamani yote mliokuwa mnayataka kutoka kwangu, nimewaeleza,na hata aliyonihadithia Marehemu Hamida nimewaambia, basi tumalizane ndugu zangu na nawaahidi sitofanya tena jambo kama lile Yesu na Maria!*
Dokta Masawe alikuwa anataka msamaha kwa gharama yoyote ile!
*Sawa Dokta Masawe tumekuelewa, lakini bado hujatupeleka au kutuelekeza wanapo patikana wale watu tunaowatafuta, hivyo kuwa kwako nje kutatufanya tuharibu upelelezi, au kwa njia rahisi tu niseme, sisi askari polisi, hatuna mamlaka ya kumaliza kesi kienyeji, hivyo fanya subira ili sheria ichukue mkondo wake, kwani hadi hapa tulipo una mashitaka mawili yakujibu tena yote ya mauaji, yaliyotokea katika nyumba moja na yanawahusu Mke na mume!*
Inspekta Jamila aliposema maneno haya, Dokta Masawe alikuwa analia kama mtoto mdogo aliekimbiwa na mzazi wake!
****
Siku ya jumatano katika jiji la Dar es salaam, upepo ulikuwa unavuma kutoka mashariki kwenda magharibi, hivyo kufanya eneo lile la Mwambao wa pwani, kuwa na hewa safi.
Watu walikuwa wengi katika eneo la Mahakama ya Mkoa wa Dar es salaam, Maarufu kwa jina la Mahakama ya Kisutu.
Mahabusu walikuwa wameshaletwa kutoka magerezani na vituo vya Polisi, miongoni mwao alikuwepo mtuhumiwa wa kesi ya Mauaji, dereva wa Taxi, Mwaduga Dingo aliekuwa ameshika tama muda wote toka waliposhushwa kutoka katika basi la magereza wakitokea Gereza la Keko, wakikutana na watuhumiwa kutoka katika gereza la mahabusu la Segerea.
Nje ya mahakama walikuwepo watu wengi waliokuwa wakiwafuatilia ndugu zao, walikuwepo waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali, na katika pembe moja ya eneo lile alikuwepo Eshe Muhidini mke wa Mwaduga Dingo, na jirani yao Bwana Masudi pamoja na mkewe.
mtoto wa Mwaduga anaeitwa Marijani, anaepata miaka mitatu na nusu au mine akiwa amekaa chini katika kivuli cha mti, jirani na mama yake akichezea kokoto wala hana habari na dunia inavyokwenda. Mara ikasikika sauti ikisema
*Mahakama karibu inaanza, hivyo wale wote waliokuja katika mashauri ya kesi, waingie mahakamani na muhakikishe mnazima simu zenu*
Lilipokwisha tangazo lile, Eshe alimbeba mtoto wake na akajongea Karibu huku akiwa ana kiherehere cha hali ya juu sana.
*COOOOOOOOOOOORT*
Sauti ya askari mkakamavu ilikuwa inaashiria kuwa Muheshimiwa Hakimu alikuwa akiingia mahakamani hivyo pia kuashiria watu wote wasimame ili kumpa heshima muheshimiwa.
Muheshimiwa Hakimu mkazi alikaa katika sehemu yake, na mara moja taratibu za kimahakama zikaanza.
Kesi ya tatu kutajwa ilikuwa inamuhusu Mwaduga Dingo,na ilipotajwa namba ya kesi yake na karani wa Mahakama, Mwendesha mashtaka wa serikali akasimama baada ya karani kukaa katika kiti chake, akiwa na faili la kesi ile akasema.
*Niipendeze Mahakama yako Muheshimiwa, naitwa Mabewa wakili wa Serikali naiwakilisha Jamhuri, Shauri hili lilikuja kwa kutajwa upelelezi wake bado unaendelea, ila kutoka kwa mkurugenzi wa mashitaka kanda ya Dar es salaam nina NOLLE PROSEQUI UNDER SECTION 91(1) OF CRIMINAL PROCEDURE ACT, 1985 (CAP 20 R.E 2002)*
Ilikuwa ni kauli ya muendesha mashtaka Wakili wa Serikali akiifahamisha Mahakama hatua ya kesi ya Mwaduga ilipofikia wakati huo huo alifungua Jalada la Kesi ile na kutoa Ganda gumu la njano na kumkabizi Karani wa Mahakama ili ampe Muheshimiwa Hakimu kwa uthibitisho, na hatimae kutoa maamuzi.
*Mshitakiwa Mwaduga Dingo kuanzia sasa Mahakama yangu imekuachia huru unaweza kwenda.*
Muheshimiwa hakimu baada ya kuipitia ile karatasi ya njano, alitoa maamuzi.
Ama kwa hakika Mwaduga Dingo aliiona nyota ya Jaha!
Furaha iliyochanganyika na huzuni ilitawala katika kichwa chake, akashindwa kuamini ukweli kwamba yupo huru,alihisi yupo ndotoni.
machozi yakambubujika mfululizo, huku akiwa anateremka kutoka kizimbani, akawa anajisemea ndani ya moyo wake.
*Yote yalionifika, namuachia manani
Ni yeye alietaka, mimi kuwa gerezani
Tabu dhiki na mashaka, nivijuwe kwa undani
Katu sidai fidia, mola atanilipia!*
*Mke wangu mtukuka, na mwanangu Marijani
Sameheni bila shaka, mtaingia peponi
Kila linalokufika, mja kwako mtihani
Katu sidai fidia, mola atanilipia!*
*Kusamehe kwa hakika, ndiyo bora duniani
Kwa dhati ninatamka, sina kinyongo moyoni
Ila hayatafutika, hadi niwe kaburini
Katu sidai fidia, mola atanilipia!*
Eshe akiwa na mtoto mgongoni, alishindwa kujizuia alipomuona mumewe anatoka nje ya Mahakama ile akiwa huru, alilia kilio cha furaha huku mke wa Masudi akimbembeleza.
Mwaduga alipotoka tu pale nje ya mahakama waandishi wa habari walimzonga, huku Camera zao zikichukua picha kwa ajili ya magazeti na picha za Televisheni.
Wakiwa katika mahojiano. Mara walitokea polisi na kutimua watu kisha wakamkamata Mwaduga na kumtia ndani ya gari ya polisi aina ya Land Rover Difender 110 na kuondoka nae kituuteni, hadi kituo cha kati cha polisi mkabala na Relwe Stesheni.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
-
Huku nyuma yakaachwa maswali kadhaa, huku wale waandishi wakifanikiwa kupiga picha za video tukio lile!
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment