IMEANDIKWA NA : HASSAN O MAMBOSASA
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sauti ya kulalamika ilisikika ikitoka ndani ya chumba kimojawapo cha nyumba ya kifahari iliyopo katikati jiji la Tanga, ni ndani ya mtaa ambao una makazi ya watu wenye nazo katika jiji hili katika maeneo ya Raskazone. Kijana mmoja mwenye asili ya kisomali aitwae Hassan alikuwa akilalamika mbele ya pacha wake anayeitwa Hussein, machozi yenye kutiririka mithili ya chemchem ya maji ndiyo yalikuwa yamefunika mboni za macho yake hadi akawa anaona ukungu katika macho yake. Hussein alikuwa ana kazi ya kumbembeleza pacha yake huyo aliyelia akilitaja jina la msichana, kilio chake kilikuwa ni uchungu tosha kwa pacha wake aliyekuwa anambembeleza. Neno mapenzi ndiyo lilitawala kinywa cha Hassan muda wote aliokuwa analia, kupende ndiyo kulimliza kijana huyo. Muda wote mapacha hawa ambao wanapendana kwa dhati wakiwa wanabembelezana, hawakutambua kama waliacha wazi mlango wa chumba chao wanacholala zaidi ya mmoja kulia tu na mwingine akiweka mawazo yake katika kumbembeleza mwenzake.
"Hassan hebu nyamaza basi wanawake wapo wengi utapata mwingine tu" Hussein alimwambia pacha wake.
"Hussein unajua inauma sana yaani Jabir kaamua kumroga Mariam ili apendwe yeye inauma, inauma kuona mtu ninayempenda kwa dhati anachukuliwa na mtu mwingine ambaye ni rafiki wangu wa karibu" Hassan aliongea kwa masikitiko huku machozi yakimbubujika machoni mwake.
"hebu wacha fikra zako potofu, una uhakika gani kama kamloga Mariam. Kaka Mariam ndiyo kapenda pale, nakushauri tu uachane na fikra za huyo mwanamke. Tafuta anayekupenda" Hussein aliongea huku akiwa amemshika pacha wake bega.
"Mariam na urembo wake wote ule atampendaje masikini kama yule mwenye kusomeshwa na mfadhili tu halafu aniache mimi niliyekuwa nina uwezo wa kumlisha na kumvalisha" Hassan aliongea.
"kaka mapenzi si pesa wala mali ndiyo utayapata, mapenzi ni kuweza kuuteka moyo wa mtu ndiyo utayapata na moyo wa mtu hautekwi kwa pesa" Hussein aliongea.
"Hussein na wewe usinichanganye kabisa, nimekuambia namtaka Mariam na nitampata kwa gharama yoyote ile na hata ikiwezekana kuondoka na maisha ya mtu. Yaani kuogopa kwangu kumuambia kama nampenda ndiyo njia aliyoitumia Jabir kumpata yeye, nasema sikubali hata kidogo na Jabir nitamshikisha adabu kwa pesa tu. Mbele ya hela hakuna kinachoshindikana na hata mapenzi yanawezekana" Hassan aliongea kwa hasira kupingana na ushauri wa pacha wake.
"PWAA! PWAA! PWAA! PWAAA! PWAAA!" sauti ya mtu akipiga makofi ilisikika ikitokea mlangoni mwa chumba chao wanacholala. Wote kwa pamoja walishtuka kisha wakageuka upande ambao sauti hiyo imetokea, walishtuka zaidi baada ya kumuona baba yao akiwa amesimama katikati mlango akiwa anawatazama.
"sijaona mtoto wangu mwenye akili na mwenye kutoa ushauri mzuri na wenye manufaa kama wewe Hussein na sijaona mtoto asiye na akili na mwenye kudanganywa na pesa za baba yake kama wewe Hassan" Baba yao aliongea huku akitembea kusogea mahali walipo Hassan na Hussein hadi alipowafikia kisha akaendela kuongea, "pesa si chochote si lolote ndani ya dunia hii wanangu hasa kwenye mapenzi, yaani we Hassan nilidhani kukaa chuo miaka miwili utakuwa umekua kiakili kumbe bado huna akili hata za kufikiria. Kakuambia mwanamke analogwa ili kumpenda mtu ndani ya dunia hii, mwenzako kauteka moyo na usitake utende kosa kama nililotenda mimi baba yako ambalo ninalijutia hadi leo".
"kosa!, kosa gani hilo baba?" Hussein aliuliza huku uso wake ukionesha kutomuelewa baba yake, Hassan alibaki akimtazama baba yake anavyoongea.
"wanangu sikuwahi kuwasimulia kuhusu kilichowahi kunipata kipindi cha nyuma nilipokuwa kijana kama nyinyi kwasababu ya ujinga ambao hata Hassan anataka kuufanya, Hassan mwanangu pamoja na wewe Hussein tambueni tu kuwa na pesa si kupata kila kitu ndani ya dunia hii" Baba yao aliongea huku macho yake yakiwa yana dalili za kutoka machozi, hal hiyo ilisababisha hata Hussein na Hassan wamuonee huruma baba yao.
"baba tueleze" Wote waliongea kwa pamoja walipomsogelea baba yao wakiwa wamekaa pembeni yake, Hassan alikaa upande wa kulia na Hussein alikaa upande wa kushoto. Mapacha hawa walimpenda sana baba yao na kitendo cha baba yao kuonekana ana dalili za kutokwa na machozi, kwao ilikuwa ni huzuni tosha.
"nisubirini hapahapa narudi sasa hivi" Baba yao aliinuka akaelekea nje ya chumba hicho kisha akarejea akiwa ameshika shajara(diary) kubwa mkononi, aliwapatia shajara hiyo kisha akasema "someni hii nadhani itawapa fundisho na pia mtatambua kosa nililolifanya". Hassan na Hussein waliipokea shajara hiyo kwa haraka, waliifungua ukurasa wakawa wanaanza kusoma huku baba yao akiwa anatoka nje ya chumba chao.
"tukianza asubuhi hii hadi jioni tutakuwa tumemaliza yote kwani kuna maelezo marefu" Hussein aliongea.
"tulia basi tusome maneno ya nini?" Hassan aliongea kutokana na kukereka na maneno ya Hussein.
****
"Pesa unaweza ukawa nazo lakini usiwe na kitu ukopendacho ndani ya dunia hii, unaweza ukafanya chochote unachotaka bila kujali kama unakosea au unapatia. Hii ni pesa ilinifanya mimi Abdulhafidh nifanye vitu pasipo kufikiria, utajiri wa baba yangu ambaye ni raia wa Somalia ndiyo ulinipa kichwa mpaka nikajiona nina uwezo wa kufanya chochote. Mpaka sasa najuta kwa hili jambo nililolifanya bila ya kuelewa uzito wake na matokeo yake, yote haya yalianzia baada ya kufanya jambo lililonifanya nijutie nafsi yangu. Ilipita miaka kadhaa nikiwa nimelisahau jambo hilo nililolifanya na nikaamua kuwa mlevi ili kutuliza mawazo ya kumkosa yule ninayempenda ambaye amenikataa hata nilipotumia ushawishi wangu wote, nakumbuka vizuri ilikuwa ni jumapili tulivu nikiwa natoka klabu ya ya usiku ya bilicanas nikirejea nyumbani kwangu Masaki, nilikuwa nipo ndani ya gari yangu ya kifahari na pembeni yangu yupo changudoa niliyemuokota kwenye klabu hiyo kama ilivyo kawaida yangu kila mwisho wa wiki. Niliamua kununua machangudoa na kustarehe nao kwani sikutaka kuwa na mwanamke yoyote baada ya kukataliwa na Huwaida msichana mwenye asili ya kisomali kama mimi. Nilifanikiwa kufika nyumbani nikiwa salama pamoja na changudoa niiliyemchukua usiku huo kwa ajili ya kustarehe ili kutuliza mihemko ya mwili wangu kutokana na kuathirika kitendo cha kukataliwa na Huwaida tangu naanza chuo kikuu hadi muda namaliza na hadi naanza kuendesha makampuni ya marehemu baba yangu, usiku hu kabla sijaanza kustarehe na binti huyo nilianza tabia yangu kupenda kunyonya matiti ya wanawake. Kitendo cha mimi kulinyonya titi la changudoa niliyemchukua nilihisi kichwa kizito na hatimaye nikaanza kupoteza nuru katika macho yangu, hali hiyo nilijitahidi kuizuia nikajua ni dalili ya kuumwa lakini nilishindwa na hatimaye fahamu zikanitoka. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilikuja kugutuka baada ya kuhisi upepo mwanana ukiupiga uso wangu, nilipofumbua macho nilikumbana na anga murua lenye wingu pamoja na dalili ya kunyesha mvua. Sauti za ndege ndizo zilizo nikurupusha na nikaona hali tofauti na eneo nililolala usiku uliopita. Niljaribu kuvuta kumbukumbu ili kubaini kama nililala eneo hili lenye mchanga mwingi karibu na ufukwe wa bahari. Kumbukumhu zangu za mwisho zinaonesha sikuwa eneo hilo na nilikuwa nipo kitandani pamoja na changudoa niliyemchukua klabu ya Bilicanas. Nilibaki nimechanganyikiwa nisijue nimefikaje eneo lisilo na nyumba wakati usiku nilikuwa kitandani kwangu katika nyumba yangu, mwisho wake niliamua kuinuka na nikaanza kuzunguka maeneo ya eneo ambalo ni ngeni ili niweze kulitambua. Nilikuja kujua nipo kwenye kisiwa kidogo chenye kukaribiana na ukubwa wa nyumba yangu ya kisasa, hali ya kuchanganyikiwa ilinipata kuanzia muda huo na nikawa ninatembea kuzunguka kisiwa nyasi pamoja na miti kadhaa. Mwisho nilichoka na nikaamua kupumzika kwenye gogo nililoliona lipo katikati ya nyasi zilizopo kisiwani hapo, njaa na kiu nilianza kuhisi zikitafuna tumbo langu. Nilikuwa nahema kwa nguvu kutokana kuchoka nilipokuwa natembea kukizunguka kisiwa bila muelekeo, gogo nililokalia nilihisi likianza kusogea kwa taratibu. Nilipotazama upande wa kulia kwangu niliona nililodhani ni gogo likijikunjakunja huku likisogea mbele hadi nikawa naogopa, sikutambua kama nimekaa mgongoni mwa nyoka mkubwa ambaye hivi sasa kichwa chake kimeshaingia baharini.
"Mamaaaaa!" Nilijikuta nikitoa ukelele wa uoga kisha nikaanza kukimbia kuelekea upande wa pili wa bahari kwenye kisiwa hicho kisha nikajitupa kwenye maji, nilianza kuogelea kuelekea nisipopajua hadi nikawa nimepotea katikati ya maji na nguvu zikawa zimeniisha. Uzoefu nilionao katika kuogelea ndiyo ulinisaidia ndani ya siku hiyo, ndiyo maana hata nilipojitupa ndani ya maji sikuwa na hodu ya kufa maji na nilijua nitaweza kuogelea hadi niitafute nchi kavu. Sikuweza kutambua kutoka hapo nilipo hadi nchi kavu kuna umbali gani na pia sikutaka nikate tamaa na nife kirahisi wakati maisha bado nayapenda. Niliendelea kuogelea kwa taratibu nikiwa sina nguvu hivyohivyo hadi nilipouona mtumbwi kwa mbali ukiwa katikati ya bahari, kitendo cha kuuona mtumbwi huo kwangu ilikuwa ni tumaini jipya na nguvu mpya. Niliongeza nguvu katika kupiga mbizi hadi nikaufikia mtumbwi huo, niliupanda nikidhani nitapata mwiko wa kupigia kasia ili nisogee lakini sikuukuta zaidi ya kukuta karatasi yenye maandishi haya, 'MTUMBWI HUU NDIYO SALAMA YAKO, UKITAKA KUISHI BASI INABIDI UUPANDE NA UTULIE'. Hadi nilipomaliza kuisoma karatasi hiyo tayari nilikuwa nipo ndani ya mtumbwi huo nikiwa nimekaa tu nikihema kutokana na kuchoka, sikuweza kuongoza mtumbwi huo na ikanibidi nitulie hivyohivyo nikiwa nimejilaza ndani yake. Baada ya muda mfupi mtumbwu huo ulianza kutetemeka chini kuashiria kuna mashine, ulianza kuondoka kwa mwendo wa kasi kuelekea upande nisioujua kwa mwendo wa masaa kadhaa. Nilianza kuuona ufukwe wa bahari kwa mbali wenye mitumbwi mingi ya wavuvi ikiwa mitupu kwa muda huo wa mchana niliofika mahali hapo, mtumbwi niliopanda uliacha kusogea baada ya kukaribia ufukweni hapo kisha ukazama ndani ya maji kwa ghafla na kunifanya ninywe maji ya bahari bila kupenda hadi nilipoanza kuogelea kuelekea ufukweni. Kule ufukweni baadhi ya wavuvi waliona mtumbwi ukizama na walifika hadi kwenye maji kisha wakanitoa nje baada ya kuishiwa nguvu nilipofika kwenye maji yenye kina kifupi.
"is jy okay?(upo sawa)" Mmoja wa watu walionitoa kwenye maji aliniuliza kwa lugha ambayo nilikuwa siijui.
"is jy pyn(umeumia)?" Mwingine alishambulia kwa swali jingine ambalo nilikuwa silijui pia, nilibaki nikiwatizama kisha nikaanza kutazama mazingira ya eneo hilo nililolijua kwa umakini. Macho yangu yalitua kwenye kibao kilichopo kwenye barabara inayoingia eneo hilo, kibao hicho kiliandikwa maneno ya lugha ya kingereza niliyoyasoma 'WALVIS BAY'. Nilizidi kuchanganyikiwa zaidi na sikutambua nipo ndani ya nchi gani kwani Tanzania nilipozaliwa na kukulia hapakuwa na sehemu inayoitwa hivyo wala ufukwe wa namna.
"where am I?(nipo wapi)" Nilijikuta nikiwauliza wale watu walionitoa nje ambao kimuonekano walionekana ni wavuvi, watu hawa walitazamana kisha mmoja akaniuliza kwa tabu, "can you speak Afrikaas(unaweza kuongea kiafrikaas)?". Hapo ndipo nilipotambua nilipotambua kuwa watu hawa wanaongea lugha ya afrikaas inayoongelewa na watu wa kusini mwa Afrika, hivyo niliamua kutikisa kichwa kuonesha sikuwa na uwezo wa kuzungumza lugha hiyo.
"who are you and where are you from(we ni nani unatokea wapi?)" Yule mmoja wao aliniuliza tena huku akinitazama kwa huruma. Swali hilo nilishindwa kulijibu kutokana na kuhofia usalama wangu, neno pekee nililolitamka ni, "help me(nisaidie)" kisha nikapoteza fahamu baada ya kuhisi kichwa kimekuwa kizito.
Nilipokuja kuzinduka nilijikuta nipo kwenye kitanda kikukuu katika chumba chenye mwanga hafifu sana, dari la nyumba hiyo lilikuwa ni chakavu kuliko kawaida. Nilipoangaza pembeni yangu upande wa kulia nilikuta bakuli kubwa lenye uji likiwa lipo kwenye stuli iliyochakaa sana, nilipoangaza pembeni yangu upande wa kulia niliona mlango wa kuingilia katika hicho. Mazingira ya chumba hicho yalionesha wazi kuwa ni katika kijiji ambacho sikuweza kukitambua hadi muda huo, yalikuwa ni mazingira ambayo sikutegemea kama nitakuja kukaa walau hata kwa saa moja kutokana na maisha niliyokulia toka utotoni. Sikutegemea hata kama nitakuja kulala kwenye kitanda kichakavu ambacho kinaumiza mbavu na mgongo kama hicho, mtoto wa kitajiri niliyekulia kwenye utajiri na ninaishi kitajiri nije kulala mahali kama hapo nilipojikuta nimelala baada ya kurudiwa na fahamu. Ni ndani ya chumba ambacho nilikuwa nikiviona kwenye televisheni vikilaliwa na watu wenye hadhi ya chini ambacho kwangu nilikuwa nakiona kama choo, ewe mtoto wa kitajiri kama mimi usiombe ukalala kwenye chumba kama hicho kwani utajuta. Baada ya muda mfupi mlango wa chumba hicho uliojengwa na mabati ulifunguliwa kwa taratibu huku wakiingia watu watatu ambao wawili ni wanaume na mmoja ni mwanamke, watu hao walisogea hadi kitandani nilipolala huku wakingea lugha ya kiafrikaas. Sikuwaelewa kutokana na kutokuwa mzungumzaji wa lugha hiyo, watu hawa walizungumza kwa muda mfupi kisha wakanigeukia wote kwa pamoja wakawa wananitazama kwa tabasamu la matumaini baada ya kuniona nikiwa nimerejewa na fahamu. Kunitazama kwao huko kulisababisha niulize swali kwa lugha ya kiswahili pasipo kutambua nipo eneo lisilo na waswahili, "hapa nipo wapi?". Wote waliposikia lugha niliyozungumza walishtuka sana kisha mmoja wao akatoka nje kwa haraka sana akiwaacha wenzake ndani wakiwa wananitazama tu pasipo kuongea chochote. Baada ya dakika kadhaa ule mlango chumba nilichokuwemo ulifunguliwa tena, yule mtu aliyetoka aliingia na mwanaume mwingine ambaye baadaye nilikuja kumtambua ni mmoja kati ya wale watu waliokuwa kule ufukweni. Mtu huyu ndiye aliyekuwa ananiuliza maswali kwa lugha ya kingereza huku wenzake wakinilulza kwa lugha ya kiafrikaas, mtu huyu aliwaambia wale wenzake "ekskuuz(samahani)" huku akiwaonesha ishara ya wao kutoka nje ya chumba hicho. Wote walitoka nje ya chumba akabaki yeye pamoja na mimi, aliamua kuja kuketi kitandani nilipolala huku akinipa mkono wake.
"habari yako" Alinisalimia kwa kiswahili fasaha kabisa hadi nikamshangaa kutokana na lugha waliyokuwa na wanaongea wenzake, salamu yake hiyo nilishindwa kuijibu kutokana na mshangao niliokuwa nao muda huo.
"usishangae sana kuniona naongea kuswahili, mimi ni mtanzania niliyekimbia maisha ya Tanzania, Jonas naitwa nani mwenzangu" Aliniambia ili kuniondoa hofu niliyokuwa nayo moyoni mwangu kisha akajitambulisha jina lake.
"hapa ni wapi kwanza na nimefika vipi?" Nilijikuta nikiuliza swali badala ya kutoa utambulisho wangu kama alivyotoa wa kwake.
"hapa ni eneo la ghuba ya Walvis kijijini katika mkoa wa Erongo" Jonas alijibu swali huku akizidi kuniacha njia panda kutokana na kutoijua sehemu anayonitajia. Nilizidi kumuuliza zaidi, "Erongo?! Nchi gani?". Jonas baadaya kusikia swali langu hilo alinitazama kwa umakini kisha akasema,"Namibia". Nilijikuta nikishtuka sana baada ya kutajiwa nchi hii iliyopo Kusini mwa bara la Afrika ambayo niliwahi kufika maeneo ya Windhoek kibiashara na nilikaa katika hoteli ya nyota tano iliyopo katikati ya jiji la Windhoek.
"kwanza hujaniambia hata jina lako ndugu, pia hujaniambia ulifika pale kwenye ufukwe wa ghuba ya Walvis" Jonas alinisemesha kwa upole sana.
"naitwa Abdul" Nilijitambulisha kwa kutaja jina langu kwa ufupi kutokana na mazoea niliyokuwa katika kulitumia jina langu kwa namna hiyo kisha nikamueleza kutoka mwanzo hadi nilipojikuta kwenye kisiwa asubuhi. Maelezo yangu yalimfanya Jonas anitazame kama mtu niliyechanganyikiwa hasa nilioomuambia kwamba nililala kwenye kitanda changu cha kifahari nikaja kuamka nikajikuta nipo katika mchanga wa ufukwe wa kisiwa nisichokijua, Jonas alitikisa kichwa kwa masikitiko kisha akainuka huku akitoa bahadha ya kaki mfukoni mwake halafu akanipatia.
"hiyo bahasha imeletwa na mtoto mdogo aliyetuambia amepewa na mtu ailete, tumeitambua kuwa inakuhusu wewe kutokana picha yako kuwa juu ya bahasha. Kunywa uji huo upate nguvu mi nakuacha upumzike na uangalie kilichomo ndani ya bahasha hiyo" Jonas aliongea huku akielekea mlangoni akiniacha mimi nikiwa njia panda zaidi kutokana na mambo yaliyonikuta ndani ya maisha yangu kwa muda mfupi toka nilale na changudoa ndani ya nyumba yangu, muda mwingine nilidhani kuwa utajiri niliokuwa nao ilikuwa ni ndoto na sasa nimeamka usingizini kwenye mazingira yangu halisi ya maisha yangu ya kila siku. Nilikuwa nimechanganyikiwa kabisa na nilihisi naelekea kuwa kichaa kwa hayo yaliyonikuta ndani ya maisha yangu ndani ya muda huo, tajiri mkubwa kama mimi ambaye anamiliki kampuni kadhaa nchini Tanzania nipo kwenye nyumba mbavu za mbwa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
****
"Mmmh hivi ni kweli" Hassan alijikuta akimuuliza Hussein baada kuumaliza ukurasa wa kwanza wa shajara waliyopewa na baba yake.
"ebwanaeh utaniulizaje mimi tena, wa kuulizwa ni mshua" Hussein alimwambia Hassan huku akinyanyuka kitandani walipokuwa wamekaa halafu akasema, "muda wa msosi huu twende tukale". Wote kwa pamoja walitoka chumbani kuelekea kwenye ukumbi wa kulia chakula, walimkuta baba yao yupo mezani tayari akiwa anakula. Walijumuika naye mezani hapo huku wakimtazama sana usoni.
"hivi baba yale ni matukio ya kweli?!" Hussein aliuliza.
"kwa sasa siwezi kuwajibu mpaka mmalize kusoma yote" Baba yao aliwajibu.
"ni kisa chenye kuvutia sana" Hassan aliongea akiwa na tabasamu usoni hata kile kilio chake kilichokuwa kinamsumbua sana alikisahau kutokana na kuvutiwa na ukurasa wa kwanza wa maelezo yaliyomo ndani ya Shajara ya baba yake.
"malizeni kula kwanza ndiyo mengine yatafuata, kama kuongea basi ongeeni mkimaliza kula" Baba yao aliwaambia.
Hassan na Hussein walikula kwa haraka ili wawahi kuisoma ile shajara ya baba yao ambayo imetokea kuwa kivutio kwao, kisa walichokisoma kwa ukurasa mmoja tu kiliwavuta wakasome zaidi. Walipomaliza kula wakirudi hadi chumbani kwao walipoiacha shajara hiyo, jambo la kuisoma shajata kwa muda huo ndiyo lilikuwa katika akili zao. Vijana hawa ambao wapo likizo kubwa ya chuoni kwao, waliamua kuutumia muda wao huo wa mapumziko kwa ajili ya kuisoma shajara hiyo. Wote kwa pamoja walipanda kitandani kwao huku kila mmoja akitaka awahi kuishika shajara hiyo na kupelekea waanze kugombania kuishika shahara hiyo, walikuwa kama watoto wa shule ya msingi ya kata wakigombea kitabu darasani ili wasome darasani. Vijana hawa walianza kuivuta shajara hiyo kila mtu upande wake na hawakutaka waisome kama walivyosoma awali, yote haya ilikuwa ni papara za kutaka kuisoma shajara hiyo kutokana na kuvutiwa nayo.
"Hussein utaichana" Hassan alimwambia mwenzake kwa kulalamika.
"tulia basi na mimi nisome" Hussein aliongea akizidi kuivuta shajara hiyo.
"kwani mimi ndio sitaki kusoma" Hassan aliongea.
"basi tusome wote" Hussein aliongea huku akiiweka shajara katikati yao.
"mambo si hayo sasa, tuendelee kusoma" Hassan aliongea baada ya kuridhishwa na uamuzi wa Hussein.
****
Uji uliokuwa upo mezani niliunywa kwa pupa ingawa ulikuwa na ladha nyingine yenye kuvutia ambayo sikuwahi kuionja, ulikuwa ni uji ambao hata nyumbani Tanzania huwa hatuunywi kabisa na sikuweza kuutambua umetengenezwaje hadi kuwa hivyo ingawa ulikuwa ni wenye ladha nzuri sana. Nguvu za mwilini mwangu zilianza kunirudia kwa taratibu na nikajihisi mwepesi kutokana na uji huo ulionipa nguvu kidogo, jambo la kwanza kulifanya baada ya kumaliza kunywa uji huo ni kujinyoosha viungo vyangu ambavyo vilikuwa vikiniuma sana. Baadaye niliikumbuka bahasha niliyokabidhiwa na Jonas ambayo ina picha yangu ndogo, nilipoiona bahasha hiyo tu maswali mfululizo yasiyo na majibu yalianza kupita kwenye halmashauri ya ubongo wangu. Bahasha hiyo nilipoifungua nilokutana na karatasi yenye maneno machache sana ambayo niliyasoma kwa pupa, nilipomaliza kusoma karatasi hiyo nilizidi kushangaa sasa nikatambua kuna mchezo ambao siujui nachezewa na mtu anayenijua lakini mimi simjui. Karatasi hiyo iliandikwa hivi, 'ABDULHAFIDH KARIBU SANA NAMIBIA ILI UPATE SOMO JINGINE LA KUYAONGOZA MAISHA YAKO YALIYOPOFULIWA NA PESA ULIZONAZO, SASA UNACHEZA NA MTU MWENYE PESA KAMA WEWE NA MWENYE UWEZO WA KUFANYA LOLOTE KATIKA DUNIA HII NA HATA KUKUFILISI WEWE UKABAKI MASIKINI KATIKA MAISHA YAKO YOTE INGAWA SITAKI KUFANYA HIVYO. HUU NI MCHEZO KATI YANGU MIMI NA WEWE SASA JIANDAE KUCHEZA MCHEZO HUO NA MTU MWENYE PESA KAMA WEWE ASIYE NA MZIZI NDANI YA DUNIA HII, NAJUA UTAJIULIZA MIMI NI NANI NA NINAFANYA HAYA KWA LENGO GANI. UKITAKA MAJIBU YA HAYA MASWALI NA UKITAKA URUDI KWAKO SALAMA BASI USIJIFANYE MJUAJI KWANI NAKUONA ULIPO NA NAITAMBUA KILA HATUA YAKO, KILA LA HERI'. Karatasi hiyo ilizidi kunichanganya na nikajikuta sina la kufanya zaidi ya kuduwaa tu nikiwaza na kuwazua lakini sikupata jibu kabisa, mtu mwenye pesa kama mimi asiye na mzizi ndani ya dunia hii sikuweza kumtambua hata nilipoushughulisha ubongo wangu kwa kwa namna yoyote. Kichwa changu nilihisi kikishindwa kuhimilo haya matatizo ambayo yananikuta katika kipindi hichi cha maisha yangu kwa muda huu, nilizidi kuchoka bila hata kufanya kazi hasa kila nikiyafikiria mambo yanayonikuta katika maisha yangu. Tayari nilikata tamaa ingawa dini yangu ya kiislamu inaniambia anayekata tamaa ni yule asiye na imani na asiye miongoni mwa waumini, ndugu msomaji usiombe matatizo kama haya yakufike halafu dini una imani hafifu au umeiweka kando kama mimi. Utaomba dua zote unazozijua kwa Mwenyezimungu na utakumbuka uwepo wake katika matatizo kama haya kama ulikuwa dini umeiweka kando, pia unaweza kukanusha Mungu hayupo pamoja nawe ikiwa una imani ndogo katika dini yako. Haya mambo yanamkuta mtu yoyote na muda mwingine matatizo katika maisha ni sehemu ya kipimo cha imani yako , kwangu mimi mtoto wa tajiri aliyekuwa mwenye imani sana nilijikuta nikimkumbuka Mungu baada ya kuiweka dini kando kwa muda mrefu. Hakika matatizo yaliyoniweka njia panda yalinizidi uwezo na hata kuyamudu niliona sitoweza ingawa sikukubali ninyooshe mikono juu kuonesha nimeshindwa.
"Eeeeh! Mungu wee nimekosa nini mja wako mimi" Nililalamika peke yangu nikiwa namtamguliza Mwenyezimungu baada ya kumuasi kwa muda mrefu kwa mambo niliyokuwa nayafanya ambayo kwake yalikuwa hayampendezi hata kidogo, nafsi yangu iliniambia mimi ni mpotevu na sina kimbilio zaidi ya ninayemuabudu huku nikisahau kuwa nilikuwa nimefanya mambo yasiyompendeza kwa muda mrefu sana. Kumbukumbuza maneno ya marehemu baba yangu katika kuniusia kuhusu kuswali na kufanya mema ndiyo zilikuwa zinatafuna sehemu kubwa ya ubongo wangu, laiti kama nisingejiingiza kwenye mchezo wa kununua makahaba yote haya yasingenikuta na nisingekuwa hapa nilipo kwa muda huu. Usemi wa waswahili usemae 'majuto ni mjukuu' ndiyo sasa ulianza kuonekana katika haya mambo yaliyonitokea na nilitamani hata siku zirudi nyuma ili niweze kusahihisha mambo niliyoyafanya na hata kufuata ushauri wa marehemu baba, jambo hilo halikuwezekana kwani siku haziwezi kurudi nyuma haijawahi kutokea suala kama hilo. Msemo wa mwanafalsafa wa mwandishi wa kitabu kiitwacho STUDENT'S COMPANION chenye kusheheni misemo,nahau na methali mbalimbali za lugha kingereza, ndiyo niliweza kuuona ukiwa na ukweli ndani yake. Msemo huo 'what done can not be undone' uliotafsiriwa kwa kiswahili 'kilichofanyika hakiwezi kuwa hakijafanyika', ndiyo hasa ukweli wake umedhirika kwa kutoweza kuyafanya yaliyofanyika yawe hayajafanyika. Hakika mwandishi WILFRED D BEST wa hicho kitabu nilichopenda kukisoma kipindi nikiwa shuleni alikuwa na maana pana katika maneno yake ambayo nimekuja kuitambua nikiwa ugenini tena mbali na nyumbani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya saa moja kupita tangu nilipoisoma ile karatasi yenye bahasha ya rangi ya kaki, Jonas aliingia ndani ya chumba nilicholala ambacho kwangu kilikuwa kama kaburi kutokana na kuzoea maisha ya raha na kusahau kama kuna shida na dhiki katika dunia hii. Alikuwa amevaa mavazi mengine tofauti na nilyomuona nayo wakati anaingia kwa mara ya kwanza humu ndani na hata wakati ananiokoa kule ufukweni.
"Abdi nadhani upo sawa na unaweza kunieleza juu ya masaibu yaliyokupata" Jonas aliongea kwa upole huku akinitazama usoni, maneno yake yalinifanya nishushe pumzi kisha nikaanza kwa kumsahihisha kwa kulitamka jina langu tofauti na nilivyomwambia. Niliongea, "ni Abdul sio Abdi" kisha nikampatia karatasi niliyoikuta ndani ya bahasha halafu nikamwambia, "hebu soma hii kwanza halafu ulinganishe na maelezo yangu niliyokuambia hapo awali". Jonas aliipokea ile karatasi kisha akaanza kuisoma kwa umakini na aliirudia mara mbili ili ahakikishe kuwa kama alichokisoma ndicho au alisoma vibaya maelezo hayo, alipomaliza aliikunja ile karatasi halafu akanipatia.
"hiyo karatasi imetoka kwenye hiyo bahasha uliyonipatia" Nilimuambia huku nikiipokea hiyo karatasi niliyompatia.
"Abdul unajua mwanzo nilijua umechanganyikiwa kutokana na maelezo uliyoyatoa lakini sasa nimeanza kukuamini. Kwanza mra ya mwisho ni lini ulikuwa kwako?" Jonas aliongea.
"mara ya mwisho nakumbuka ni jana jumapili ndiyo nilikuwa kwangu na usiku niliingia na mwanamke na asubuhi nilikuja kuamka nikajikuta nipo kwenye kisiwa chenye nyoka mkubwa" Nilimwambia nikiwa nimeweka mikono kichwani kwangu kwa kukata tamaa na matatizo haya.
"unajua leo sio jumatatu mpaka useme jana ilikuwa ni jumapili, leo ijumaa ndugu na inawezekana umewekewa madawa ya kukulevya yaliyokulaza siku tano hadi leo" Jonas aliongea kunisahihisha kuwa nilikuwa nimekosea siku, hapo ndipo nilizidi kuchanyikiwa na nikawa naona watu walionifanyia hivi sio watu wa kawaida kabisa bali watakuwa ni wenye kujua kitu gani wanachokifanya.
"inamaana nimekuwa sijitambui kwa muda wa siku tano?!" Nilijikuta nikimuuliza Jonas kwa mshangao mkubwa sana.
"ndio maana yake, pole sana ndugu yangu kutoka katika nchi yangu" Jonas aliongea.
"Jonas umesema wewe ni mtanzania umefikaje huku" Nilimuuliza Jonas nikiwa nimeweka kando matatizo yanayonihusu na nikiwa nina shauku kubwa ya kutaka kujua zaidi kuhusu yeye.
"ni maisha tu ndugu yangu ndiyo yamenifikisha hapa nilipo, mimi nimezaliwa katika familia ya hadhi ya chini na nimekulia kimasikini. Nimesoma hadi kidato cha nne nikawa nimefanya vibaya na nikaamua kuzamia nikiwa na Afrika ya kusini kwa kutumia lori nikiwa na kaka yangu lori hilo lililotupeleka hadi Congo kisha tukaingia kwenye meli sehemu ya injini iliyokuwa inaelekea Afrila ya kusini kwa kupitia bahari hii ya Antlantiki, ilikuwa ni safari yenye misukosuko na hadi tunakaribia bandari ya Cape town Afrika ya kusini tuliamua kujitosa kwenye maji kisha tukaogelea hadi nchi kavu. Maskani yetu katika jiji hilo yalikuwa ya kuhamahama na kipato kilikuwa si cha kuridhisha kutokana kazi ndogo tunazozifanya, mwisho wake tukaamua kujiingiza katika ujambazi na uuzaji wa madawa ili tupate pesa kwa haraka tuwe na mafanikio tuliyokuja kuyatafuta. Kazi hii haramu hatukudumu nayo kwani kaka yangu aliuawa na wenzetu kwenye biashara hii na kigogo mmoja wa nchini humo ambaye ndiye mkuu wetu akanipa kesi hiyo mimi ili aweze kuniharibia maisha yangu. Hapo ndipo nikakimbila huku na nikaanza kutumia jina langu halisi na nikaacha jina bandia la Mike nililokuwa nalitumia" Jonas alielezea kwa kifupi historia ya maisha yako hadi akafikia hapo alipo katika nchi hii.
"pole sana ndugu" Nilimuambia kutokana na kusikitishwa na historia yake na magumu aliyopitia mpaka kuingia Afrika ya kusini kwa njia za panya, Jonas nilimuona ni mtu jasiri kwa matatizo hayo aliyoyapitia. Nathubutu kusema ingekuwa mimi mtoto niliyelelewa kwenye raha nisingeweza kufanya hivyo ila kwa huyu kijana shupavu na mjasiri imewezekana.
"Abdul unajua watanzania katika sehemu za ugenini kama huku huwa ndugu, hivyo ukae utambue kuwa sisi ni kitu kimoja na usiongee kiswahili tena maeneo haya ya Walvia" Jonas alinisisitiza.
"sawa nimekuelewa ingawa mimi hiyo lugha mnayotumia siijui nitatumia kingereza" Nilikubali maneno yake kwasababu yeye ndiye alikuwa mwenyeji wangu katika nchi hii ambayo ni ngeni kwangu na sikuwa naweza kumpinga mtu kama yeye aliyeniokoa na kunipa hifadhi.
"Kiafrikaas nitakufundisha ili uongee kama wengine katika kijiji hiki, sasa ngoja mimi jioni hii nielekee baharini maana uvuvi ndiyo kila kitu" Jonas aliniambia huku akielekea mlango.
"Jonas twende wote hapa kumeshanichosha kukaa ndani peke yangu muda wote huo najihisi mpweke" Nilimuambia Jonas huku nikisimama.
"kama upo sawa twende ili ujifunze na wewe kuvua" Jonas aliniambia huku akifungua mlango kwa ajil ya kutoka nje, nami nilimfuata nyuma kwani yeye kiongozi wa njia kwangu. Nilitoka nje ya kibanda hicho kwa mara ya kwanza tangu nilipoletwa nikiwa sijitambui, niliweza kuona mandhari ya eneo hilo vizuri ingawa tayari giza lilishaanza kuingia na taa mbalimbali zenye kutumia moto zikiwa zimesheheni katika vijumba vidogo vilivyojengwa kwa mabati katika kijiji hiki. Kilikuwa ni kijiji kilichochangamka sana kutokana uwepo wa watoto wenye uchangamfu kwa watu wazima na waliojaa adabu pia waliokuwa wakicheza michezo mbalimbali ya kitoto. Hakika walikuwa ni watoto wenye adabu na heshima tofauti na hawa wa nchini kwetu, kwani kila nilipopita walinisalimia kwa lugha ya kwao ingawa sikuwa naielewa.
" goeienaand(habari ya jioni)" nilipokea salamu hiyo ambayo sikuwa naielewa na niliishia kutabasamu tu huku nikiwapungia mkono. Jonas alikuwa akiwajibu,"goeienaand" kama walivyomsalimia. Watu wa kijiji hichi kidogo walionekana ni watu wastarabu sana kwani kila tulipopita tulikuwa tukipokea salamu mbalimbali za lugha ya Kiafrikaas ambazo nyingine niliishia kuzibahatisha kwa sababu zimeingiliana na lugha ya kingereza kimatamshi. kijiji hichi cha watu wa hali ya chini kilionekana kunivutia sana hasa muundo wa nyumba zao ndogo. Hadi tunafika baharini nilikuwa nimeburudika vya kutosha kwa kuangalia mazingira ya ugenini nilipo kwa muda huo kwa muda huo. Mtumbwi wenye shuka kubwa ndiyo uliokuwa upo kwenye maji ukiwa una vifaa vyote kwa kuvulia, naweza kusema hiyo ilikuwa ni siku nyingine katika maisha yangu kwani nilipata ujuzi mpya wa kimaisha wa kuweza kuvua samaki katika bahari. Tulifanya shughuli za kuvua wote kwa pamoja baada ya kuelekezwa vitu vidogovidogo katika uvuaji wa samaki, hadi inaingia usiku wa manane tayari mtumbwi wetu ulikuwa umejaa samaki na safari ya kurudi ufukweni ilianza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tulifanikiwa kufika ufukweni salama na tukashusha samaki wote kwa ajili ya kwenda kuuza. Muda wote huo nilikuwa bado sijasahau matatizo yaliyonikumba ingawa nilionekana kuwa na furaha iliyotokana na kupendezwa na mazingira mapya ninayoyakabili, kutabasamu au kufurahi katika kipindi cha matatizo kutokana na jambo lolote la kumfanya mtu atabasamu ni kawaida kwa binadamu yoyote hata awe na matatizo kiasi gani. Hata mimi nilifurahi sana kutokana na kuona ni jambo lenye kufurahisha moyo wangu uliojaa matatizo nisiyoyajua ni nini chanzo chake kwa muda huo. Hayo ndiyo maisha yangu mapya niliyoyaanza katika kijiji hicho kilichopo karibu na ghuba ya Walvis, nilikaa wiki moja katika ghuba hiyo pasipo kugunduliwa kama ni mzungumzaji wa kiswahili. Wiki ya pili ya kukaa katika ghuba hiyo ndiyo ilikuwa janga jingine kwangu, wiki hiyo nilipokea bahasha nyingine yenye rangi ya kaki ikiwa na ujumbe mzito uliobeba wajibu ambao nilitakiwa kuufanya kwa kuhofia kupoteza ninavyohusudu ndani ya dunia hii. Ujumbe huu ulizidi kunichanganya kwani kazi niliyotakiwa kuifanya ni kazi inayohitaji moyo la si hivyo huwezi kuifanya, matatizo ambayo yangetokea ndiyo yalipelekea niifanye kazi hii rahisi kwa kuitazama ilavni ngumu sana. Karatasi iliyokuwa ndani ya bahasha hii ambayo sikuitambua inatumwa na nani na anayenijua nipo ndani ya nchi hii, mtu anayenitumia karatasi hii alikuwa ananifahamu fika ingawa mimi sikuwa namfahamu. Kuchanganyikiwa ndiyo kulichukua nafasi yake katika kichwa changu, hata nilipomweleza rafiki yangu kipenzi Jonas naye hakuwa na njia ya kunisaidia. Karatasi yenyewe iliandikwa....
****
Walipofika mwisho wa ukurasa wa pili ili waendelee na ukurasa wa tatu, Hussein aliutoa uzi wa kuzuia kupotea kwa ukurasa ikiwa itaifunga shajara kisha akauweka katika ukurasa huo. Aliifunga shajara kwa nguvu huku akimtazama Hassan.
"Huasein mbona unaifunga diary wakati tumeishia katikati?" Hassan alimuuliza pacha akionesha kutofurahishwa na kitendo hicho.
"muda wa mazoezi huu wewe hujui kama tuna ligi ya chuo tukifungua tu" Hussein alimwambia Hassam huku akichukua shajara.
"dah! Halafu kweli, kwani saa ngapi?" Hassan aliuliza.
"saa kumi kasoro hii tuwahi graundi kama vipi?" Hussein aliongea huku akiiweka shajara kwenye meza, wote kwa pamoja walichukua vifaa vya mazoezi kisha wakaondoka kuelekea uwanjani. Vijana hawa mpira wa miguu ndiyo ilikuwa burudani yao kuu na waliupenda sana, mapenzi yao kwenye mpira wa miguu yalijulikana hata kwa baba yao na ndiye aliyewapa moyo wa kuendelea kuonesha kipaji chao kandanda. Mpira wa miguu kwao ilikuwa kama ni mchezo uliwapa umaarufu chuoni kwao na hata mtaa wanapoishi..
Hawakutumia muda mrefu sana kutoka nyumbani kwao hadi ulipo uwanja wa mpira, ni mwendo wa dakika tano tu ndiyo waliotumia kufika uwanjani hapo kwa ajili ya kucheza mpira. Walipofika walianza mara moja kukimbia kuuzunguka uwanja huo wa mpira kwa mizunguko ishirini ili kujenga pumzi yao ya uwanjani, walipomaliza walianza kufanya mazoezi madogo ya viungo kisha wakaanza mazoezi kwa kucheza 'opening space' wakiwa na wenzao kama ilivyo kawaida yao. Opening space ni mtindo wa uchezaji ambao hutumika mazoezini kwa kuweka timu mbili uwanjani kucheza bila kuwepo kwa magoli, ni mazoezi yanayohusisha pasi tupu baina ya vikosi vya timu moja mazoezini pasipo kuhusisha magoli wala uwepo wa golikipa. Hassan na Hussein pamoja na wengineo katika mazoezi hayo walicheza mchezo huo kwa muda wa nusu saa kisha wakapanga vikosi viwili tofauti kwa ajili ya kuanza mpira mara moja, siku hii mapacha hawa ambao ni viraka katika mpira walicheza vikosi tofauti na ikawabidi wakabiliane kutetea vikosi vyao. Kiraka ni mchezaji mpira mwenye uwezo wa kucheza namba yoyote uwanjani, Hassan na Hussein ni wachezaji wenye uwezo.wa kucheza namba yoyote uwanjani ndiyo maana wanaitwa viraka. Saa kumi na mbili jioni mazoezi yaliisha na mapacha hawa wakarudi nyumbani kwao, walipofika walisafisha miili yao kwanza kisha wakaifuata shajara ilipo. Waliichukua kisha wakajilaza kitandani kifudifudi ili waisome kwa pamoja, Hassan aliifungua shajara kwa papara hadi walipoishia kisha wakaanza kuisoma.
****
Karatasi yenyewe iliandikwa , 'ABDULHAFIDH NADHANI MUDA WA KUANZA KUJIFUNZA SOMO JIPYA LITAKALOKUFANYA UACHE JEURI YA PESA LIMEWADIA, SASA KAMA UNAHITAJI MALI ZAKO NA KILA KITU CHAKO UKIKUTE KAMA ULIVYOKIACHA INABIDI UFANYE NITAKAVYOKUAMRISHA VINGINEVYO NITAZICHUKUA MALI ZAKO ZOTE KWA KUGHUSHI SAHIHI YAKO. UBISHI WAKO UTAJUTA MAISHANI MWAKO NA UTIIFU WAKO UTAKUOKOA, NSHITAJI DOLA MILIONI MOJA ZA KIMAREKANI NDANI YA SIKU KUMI NA INABIDI UZIWEKE KWENYE SANDUKU LA POSTA AMBALO FUNGUO ZAKE NIMEZIBANDIKA NYUMA YA KARATASI HII. UTAKAPOZITOA HIZO PESA SIJUI ILA NA UKIWA HUNA MBINU ZA KUZIPATA HIZO BASI FUNGUO ZA SANDUKU HILO LA POSTA ZITAKUSAIDIA MBINU ZA KUZIPATA HIZO PESA IKIWA UTALIFUNGUA LEO HII. KILA LA HERI'. Hiyo ndiyo karatasi ya pili niliyotumiwa na mtu nisiyemjua ambayo imebeba wajibu ambao uliokuwa mrahisi kwa kuufikiria kwa kichwa na mgumu kama ukiamua kuufanya, nyuma ya karatasi hiyo kweli kulikuwa kumebandika funguo ndogo zenye namba ya sanduku la posta yenye kibango kidogo maandishi yaliyosomeka 'Sam Nujoma drive, Skeleton coast' mwisho wa maandishi haya kwenye kibango hicho kulikuwa kuna namba ya sanduku la posta. Nilikitoa kibango hicho kisha nikamuonedha Jonas ili nipate msaada wake muda huo huo wa asubuhi, Jonas aliweza kunisaidia kwa kunitajia eneo kuwa maandishi hayo yalikuwa yanaelekeza eneo la ofisi za posta zinapopatikana.
"ndugu unaweza kunipeleka zilipo ofisi hizo?" Nilimuuliza baada ya yeye kunifafanulia juu ya maandishi yao ambayo yalitaja barabara ya Sam Nujoma ambayo sikuwa naitambua ya nchini humo zaidi ya kuitambua barabara ya Sam Nujoma iliyopo jijini Dar es salaam katika wilaya ya Kinondoni, kumbe Namibia nayo ilikuwa na barabara yenye jina la baba wa taifa lao ambaye ni rais wa kwanza wa nchi hiyo ambaye anaitwa Samuel Daniel Shafiishuna Nujoma kwa kifupi Sam Nujoma. Hapo ndipo nilipotambua kuwa Tanzania imeamua kuipa jina barabara yake moja kwa kuenzi mchango wa huyu kiongozi hodari katika Afrika kwa kutambua mchango wake katika nchi ya Namibia kama ambavyo Afrika ya Kusini na Kenya zilivyoipa barabara zao jina la rais wetu wa kwanza na baba wa taifa la Tanzania mwalimu Nyerere. Jonas alitoka nje baada ya kumuambia suala la kunipeleka zilipo ofisi za posta nilizoelekezwa kutokana na ugeni wangu ndani ya nchi hii, aliniambia nimsubiri kwa muda wa dakika tano atarejea. Niliitikia nitamsubiri kwa dakika hizo kwakuwa sikuwa na njia nyingine ya mbadala, pia niliitikia tu ingawa sikuwa na saa ambayo ingeniwezesha kuhesabu dakika hizo zaidi ya kuzoea ahadi zetu za kiswahili tunazowekeana huko Tanzania. Yaani mtanzania mwenzangu anaweza akakuambia nipe dakika mbili narudi sasa hivi wakati anatambua kuwa huna hata hiyo saa hata simu ya kuhesabu dakika hizo mbili alizokuambia, ukweli wa ahadi hizi ni haziendi na muda uliotajwa bali hutumika kumpa mtu moyo wa kuendelea kusubiri na asikate tamaa na jambo analoahidiwa. Ndiyo maana Jonas aliniambia hivyo si kweli kwamba angeweza kurejea baada ya dakika tano, hiyo ni kutokana na kunipa moyo mimi nisichoke kumsubiri. Jonas alirejea baada ya dakika ambazo ungezikadiria basi zingekuwa ni dakika kumi na tano, alirejea akiwa tabasamu lililoashiria kuna jambo la faraja amekuja nalo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Abdul tumshukuru Mungu nimepata pikipiki ambayo itatusaidia kwenda eneo ofisi za posta, tuondoke haraka tuwahi kurudi" Jonas aliniambia akiwa amepambwa na tabasamu usoni mwake.
"Alhamdulillahi rabbil a'alamiiin(shukrani zote anastahiki Mwenyezimungu)" Nilijikuta nikimshukuru Mungu kwa faraja hii ndogo niliyoisikia kutoka kwa Jonas wakati mwanzo nilikuwa mchoyo wa kumpa shukrani kwa mambo makubwa aliyonifanyia na hata anayoendelea kunifanyia hadi leo hii, ewe mwanadamu mwenzangu unayepumua kama mimi usiombe ufikwe na tabu yaani hata kama Mungu ulimsahau katika maisha yako utamkumbuka tu. Hata mimi nilikuwa nimemsahau kwa neema alizonipatia kama vile kurithi mali nyingi na pesa nyingi pia alinijalia pumzi ambayo ninayo mpaka naandika mkasa huu ulionikumba, sikuwahi kumshukuru hata pale nilipoamka nilipoiona siku mpya lakini huku kwenye majanga ndiyo nilimkumbuka.
Siku hiyo nilivaa nguo mbili ambazo alinikabidhi Jonas pamoja na viatu vya ngozi vilivyochoka, kwa mtu tajiri kama mimi nilikuwa najiona kituko ila kwa walio katika hali ya chini walikuwa wananiona nimependeza. Ule usemi wa lulu kwako kwa mwenzio ni changarawe ndiyo nilianza kuuamini, yaani unaweza ukavaa ukaonekana umependeza kwa watu walio chini yako na ukaonekana umevaa kawaida kwa watu na kwa waliokuzidi ukaonekana hujavaa chochote. Tulitoka hadi nje ya kibanda tunachoishi nikiwa na muonekano ambao hata Jonas alinisifia nimependeza, nje ya kibanda tunachoishi kulikuwa kuna pikipiki ya kichina ambayo sikujua hata imefika muda kwani hata mlio sikuusikia. Nilijikuta nikimuuliza Jonas, "hii ndiyo pikipiki yenyewe tunayoenda nayo?"
"Ndiyo hiyo unaionaje?" Jonas aliniuliza akidhani labda nimeudharau muonekano wa pikipiki hiyo kumbe nilishanganzwa na jinsi ilivyofika pale kwani sikusikia mlio wowote wa pikipiki.
"iko vizuri, hivi Jonas hii pikipiki imefika vipi kwani sijasikia mlio wowote wa pikipiki?" Nilimuuliza Jonas.
"Nimeileta hapa kwa kuikokota" Jonas alinijibu huku akitoa kisimamio cha pikipiki kisha akaiwasha kwa kutumia kiwashio cha pikipiki ambacho wengi wetu tunapenda kukiita 'kick'. Pikipiki ilitii amri ya kuwaka ingawa ilikuwa ina makelele sana, Jonas aliniashiria nipande nami nikatii nikakaa nyuma safari ikaanza kuelekea katika ofisi ya posta. Siku hiyo nilipata bahati ya kulishuhudia jiji la Walvis upande wa mjini lililoonekana limechangamka kutokana na shughuli mbalimbali za watu wa nchi hiyo katika kujipatia maendeleo, baada ya dakika takribani thelathini tulikuwa tumefika katika ofisi ya posta kutokana na mwendo wa kifo aliokuwa anautumia Jonas tulipokuwa tunatoka kijijini. Mwendo huo niliuita wa kifo kwasababu ni mwendo mkali ambao ulisababisha hadi macho yangu yatoke machozi kutokana na upepo mkali, tulishuka nje ya ofisi hizo kisha pikipiki ikaegeshwa getini halafu tukaingia ndani hadi sehemu yenye visanduku vingi vyenye namba tofauti. Zoezi la kutafuta sanduku la posta lenye namba niliyoikuta kwenye barua ikaanza, tulitafuta namba hiyo kwa muda mrefu kutokana na wingi wa masanduku hayo. Tulipokuja kuipata namba tunayoutafuta niliingiza funguo katika sehemu ya kufungua kwa pupa kisha nikafungua, nilikuta bahasha mbili za kaki zenye picha yangu. Nilizitoa hizo bahasha kisha nikazifungua papo hapo kwa pupa, bahasha ya kwanza ilikuwa ina noti za dola za kimarekani na ya pili ilikuwa ina barua ambayo ndiyo ilielezea wajibu niliotakiwa kuufanya kwa upana. Barua hiyo ilikuwa imeandikwa hivi, 'UKITAKA KUZIPATA DOLA MILIONI MOJA ILI KUTIMIZA WAJIBU WAKO NI LAZIMA UFANYE KAZI HII AU TAFUTA KAZI ITAKAYOKUINGIZIA HELA HIZO KWA SIKU KUMI. KUNA WANAWAKE KUMI AMBAO WAMECHOSHWA NA KUTODHIRISHWA NA WANAUME WA NA NCHI HII HIVYO WANAHITAJI PENZI LA MWANAUME WA KUTANZANIA ALIYEZALIWA KATIKA JIJI LA MAPENZI(TANGA), WANAWAKE HAWA NI WANAKAA MTAA WA WATU WENYE HELA ZAO KATIKA MJI MKUU WA NCHI HII NA ORODHA YAO IPO NYUMA YA KARATASI HII SASA FANYA UFANYAVYO NDANI YA SIKU KUMI UWE UMETIMIZA WAJIBU HUU NA PESA ULETE KATIKA SANDUKU HILIHILI LA POSTA. UKAIDI WAKO UTASABABISHA KAMPUNI YAKO KOJA IUNZWE , KILA LA HERI'. Nilipomaliza kuisoma karatasi hiyo tayari nilijua natakiwaa nifanye kazi ya kutembea na wanawake kumi ili niweze kuzipata fedha ninazozihitaji, hii ndiyo kazi ambayo ni rahisi kuifanya kama utaifikiria kwa kichwa na ngumu sana kama utaikabili, hata nilipomwomba ushauri Jonas naye hakuwa na la kunisaidia. Pia hakuna njia nyingine ya kuzipata fedha nyingi namna hiyo ambazo zingebadilishwa kuwa za kitanzania basi utajihesabu ni milionea, sikuwa na jinsi zaidi ya kukubaliana na hali halisi. Pia kuikabili kazi hiyo katika mji wa Windhoek sikuwa na jinsi kwani sikuwa na kazi ya kawaida itakayoniwezesha kupata pesa hizo kwa siku kumi, nilipozihesabu zile dola za kimarekani zilizokuwa kwenye bahashe zilikuwa ni doka elfu kumi za kimarekani. Muda huo bado tulikuwa tumesimama kwenye eneo lenye masunduku ambako lilikuwa tupu halina watu kabisa zaidi yetu sisi wawili.
"Dah! Huyu mtu hata sijui nimemkosea nini?" Nilinung'unika nikijiona sina kosa kwa mtu anayenipa kazi nisizozitaka.
"Ndugu inakubidi utekeleze tu maana ukipinga utajipa hasara mwenyewe" Jonas alinishauri.
"Sina jinsi inabidi tu nifanye hivyo" Niliongea kwa kuonesha nimekubali kufanya jambo hilo.
"Inabidi uwahi leo leo ndugu ili uweze kuikamilisha si una majina na anuani zao?" Jonas aliniambia.
"ndiyo ninazo" Nilimjibu Jonas.
"funga sanduku tuondoke zetu" Jonas aliniambia huku akitoka kuelekea nje ya ofisi tulipoiacha pikipiki yetu, nilifunga masunduku hayo kisha nikamfuata kwa haraka. Tulipanda pikipiki tukitoka ofisi hizo za posta kuifuata barabara ambayo nilikuja kuitambua kama barabara ya Sam Nujoma, tulifika sehemu yenye barabara kubwa ambayo sikuitambua jina lake. Barabara hii inakutana na barabara ya Sam Nujoma eneo hilo, Jonas alikata kona kuingia upande wa kushoto kisha akatembea hadi mahali kwenye kituo kama cha daladala halafu akasimama.
"ndugu inabidi nikuache hapa kituoni upande mabasi madogo yatakayo kupeleka Widhoek likipitia Swakopmund hadi huko, kila la heri" Jonas aliniaga kisha akasema,"wewe ni ndugu yangu na ninahitaji kuwa pamoja nawe lakini kwa hili inabidi uende mwenyewe, tutaonana ukirudi". Jonas alinipatia dola kadhaa za kinamibia kisha akanipa mkono wa kuniaga, muda huo gari ndogo aina ya toyota hiace ilifika na ikasimama kwenye kituo hicho. Jonas akiniashiria niingie kwenye gari hiyo, nilimpungia mkono wa kumuaga huyu mwenyeji wangu katika eneo la ghuba ya Walvis na sasa nilikuwa najiandaa kwenda kwenye mji mwingine nikiwa sina hata mwenyeji ingawa katika mji huo niliwahi kufika nikiwa katika shughuli zangu za kibiashara. Nilipanda hiace hiyo kwa unyonge huku nikimpungia mkono wa kumuaga, nilikaa kwenye kiti cha gari hiyo kwa utulivu nikiwa mpweke kutokana na kutoweza kuongea kiafrikaas ambacho ndiyo kilikuwa kimetawala ndani ya gari hiyo Salamu za abiria wenzangu niliziitikia kama vile bubu kwani lugha yenyewe nilikuwa naibahatisha kuongea hata kule kijijini nilipofikia. Pembeni yangu upande wa kulia katika kiti kilichopo karibu na dirisha alikaa msichana mmoja ambaye ni shombeshombe na mwenye sura ya mvuto, msichana huyo ndiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kumuona na nikakiri kuwa hata Huwaida aliyenikataa tangu nipo chuo alikuwa haingii hata sumni. Ukweli binti huyo alinivutia na nilimtamani ingawa nilihofu nitaanza kuongea naye vipi kwani hiyo lugha hata aliyonisabahi nayo siijui zaidi ya kuambulia maneno machache, msichana huyu alionekana ni muongeaji kwani haikupita muda mrefu akaanza kuongea na mimi kwa lugha ya kiafrikaas akiujua mimi ni mwenyeji katika lugha hiyo kumbe ni mgeni tena asiyefikisha hata mwezi mmoja. Kunyamaza nisijibu lolote nikawa nashindwa kwa kuhofia nitaonekana nina dharau na itakuwa ndiyo chanzo cha kumkosa mrembo huyu, yaani kukijua kingereza kulisaidia sana kumudu kuongea naye kwasababu lugha imefanana na kingereza kwa maneno mengi. Uzuri wake na muonekano ulinifanya nisichoke maneno yake mengi anayoongea, uchangamfu wake ulinifanya nizidi kumfikiria sana moyoni mwangu. Nilijaribu kumlinganisha na Huwaida aliyenichanganya kiasi cha kuamua kumfanyia kitu kibaya Faiz ambaye ndiye aliyekuwa anapendwa na Huwaida, ukweli ni kwamba kama Huwaida na huyu binti wangekuwa ni mabehewa ya matreni basi huwaida angekuwa behewa la walalahoi na huyu binti angekuwa behewa la wenye nazo. Yaani uzuri wake kwangu ulikuwa ni kama sumaku iliyoyavuta macho yangu yasichoke
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
kumtazama, binti huyu hadi muda huo sikuelewa ni mchanganyiko wa wazazi wa asili kwani alikuwa ni chotara kimuoneksno aliyewashinda hata machotara wenzangu wa kisomali. Hapo ndipo nilipobaini kwamba ulevusemi usemao ukikaa pwani peke yake utasema mti mrefu kuliko yote ni mnazi, ukikaa bara utataja miti mingine unayoijua huku mnazi ukikataa sio mti mrefu na ukitembea kote ndiyo utajua kuna miti mirefu zaidi unayoiona huko unapoishi. Yaani namanisha hivi ukawa unakaa mji fulani na ukiulizwa yupi mrembo utasema ni msichana fulani. Ila ukizunguka pote ndiyo utajua kuna warembo zaidi ya unaowatambua, binafsi nilikiri Huwaida ni msichana mrembo jiji zima la Dar es salaam na kwingineko kutokana sijajionea mrembo zaidi yake. Huku Namibia nimemuona mrembo zaidi yake na nikakiri kamzidi kila kitu. Msichana huyu ndiye aliyenitoa kimawazo ndani ya gari hiyo nikajihisi nikiwa nipo naye katika dunia ya peke yangu, maongezi yake sikuwa nayasikia kutokana na ubongo wangu kuwa mbali kimawazo juu ya kumuwaza. Sikuwahi kumuwazia msichana yoyote namna hii hadi mawazo yangu yakahama kabisa, lakini hapa mawazo yalihama bila hata usafiro wowote. Msichana huyu muongeaji alizidi kuongea akijua nipo naye kutokana na mboni za macho yangu kumtazama yeye, kumbe nipo sehemu nyingine kimawazo.
****
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment