Search This Blog

Friday 18 November 2022

BARADHULI MWENYE MIKONO YA CHUMA (1) - 2

 






Simulizi : Baradhuli Mwenye Mikono Ya Chuma (1)

Sehemu Ya Pili (2)





Inspekta Vitalis alipekua ofisi na macho yake yaliyotembea kila eneo. Aligundua dirisha la ofisi ilikuwa wazi, alilisogelea akatizama mazingira ya hapo kabla hajatoa shingo yake nje na kutizama kama kuna kiashiria chochote cha mvamizi.



Hakuona kitu.

Aliendelea kupekua asipate kitu cha kumsaidia kwenye upelelezi. Mwishowe akamtaka mkuu wake ajaribu kuwaita na kuwauliza watu waliokuwepo doria ya ulinzi siku hiyo, ama watumie mrejesho wa kamera za cctv kama watapata jambo.



Kabla halijaamuliwa la kufanywa, simu ya Mtemvu iliita. Alikuwa ni bwana Pius akimtaarifu mwenzake yaliyojiri usiku wa kuamkia hiyo siku. Mtemvu alipopata hizo taarifa za Pius alishangazwa mno na kuzidi kuogopa. Hakukaa tena ofisini, aliongozana na inspekta Vitalis waende nyumbani kwa rafiki yake: Pius upesi.



Walijiweka kwenye gari chombo kikaondoka kwa mwendo wa wastani. Wasichukue hata muda mrefu barabarani, vioo vya kando vya gari vikamuonyesha inspekta Vitalis kwamba kuna gari linawafuata. Tena gari lile lile lililokuwa linawafuatilia mwanzoni!



Inspekta Vitalis alilitizama gari hilo kwa makini taratibu akikanyagia mafuta. Baada ya muda gari hilo lilipotea. Halikuonekana wapi limeelekea. Inspekta Vitalis aliwaza na kuwazua ila mwishowe akajaribu kupuuzia na kuendelea na safari. Usipite muda mwingi, inspekta Vitalis aliliona lile gari lililopotea kwa mbele.



Hapo moyo ukampasuka kwa hayo mazingaombwe. Aliongeza mwendokasi wa gari kulikaribia lile gari alilolitilia mashaka ili apate kumuona dereva. Lakini walipokata tu kona, lile gari halikuonekana tena. Lilitokomea kwa mara nyingine mbele ya macho ya inspekta Vitalis!

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Inspekta alishusha pumzi ndefu akikaza macho ya mashaka. Kama alihesabu muda basi ilichukua dakika mbili tu, gari lililotokomea likaonekana tena mbele ya macho yake. Sasa lilikuwa nyuma yao kwa mujibu wa vioo vya pembeni. Na tena likiwa linakuja kwa kasi kuwafuata kama vile linadhamiria kuwagonga!



“Mkuu funga mkanda!” Inspekta Vitalis alipayuka akiliondoa gari kwa kasi kubwa. Alikwepa magari yaliyo mbele yao kwa pupa na kusababisha tafrani barabarani. Honi nyingi ziliita. Na magari mengine yaligongana yakijitahidi kumkwepa. Muda mchache baadae, inspekta Vitalis akiwa katika kasi yake kubwa, alitizama kwenye vioo asione tena lile gari.



Bwana Mtemvu aliyekuwa anahema kwa nguvu uso wake ukivuja jasho, alitizama nyuma kama ataona kitu. Akauliza:

“Inspekta kuna nini?”



Inspekta Vitalis akashusha pumzi.

“Mkuu, kuna mtu alikuwa anatufuatilia.” Mtemvu akageuka tena na kutizama nyuma.

“Nani?”

“Sijui! Kuna gari lilikuwa linatufuatilia tokea tumetoka nyumbani.”

“Umefanikiwa kumuona dereva?”

“Hapana! Nimejitahidi kutizama lakini sijaona mtu.”

“Na plate number?”

“Haikuwa na plate number, mkuu.”



Mtemvu alitikisa kichwa chake akakiegemeza kwenye kioo cha dirisha la gari. Uso wake ulizama kwenye dimbwi la mawazo. Nani anamfuatilia na anataka nini kwake? Hakupata jibu kabisa. Kuna muda alifikiri yupo kwenye ndoto ya kutisha na anatamani aamke lakini haikuwa hivyo.



Kunyamaza kwake kulisababisha ukimya ushike gari na hakuna mtu aliyefungua kinywa mpaka wanaingia kwenye kiwanja cha bwana Pius walipokuta watu kadhaa tayari wameshawasili wameketi chini ya maturubai.





Mtemvu alishuka, nyuma akiwa anaongozana na Inspekta, moja kwa moja alielekea kumfuata bwana Pius aliyekuwa ameketi pembezoni kidogo mwa umati. Pius alipomuona Mtemvu, alinyanyuka akamfuata na kumkumbatia. Akaanza kulia.



“Nyamaza, ndugu yangu.” Mtemvu alimbembeleza. “Ndio uanaume huo. Embu niambie kipi kilitokea.” Mtemvu alivuta kiti akakaa kando yake. Nyuma yao aliketi Inspekta macho yake yakiwa yanaranda randa kama taa.



“Ni kama maigizo.” Pius alianza kusimulia. “Nilisikia sauti ya mtu anagonga dirishani nikatoka nje. Nikamkuta mlinzi na mbwa wamekufa, wanamwaga damu. Mara nikaanza kusikia sauti za ajabu ajabu na mtu akipita pita kwa haraka vuup! Vuup!



Nilifyatua risasi zikaisha! Nilikimbilia mlango nirudi ndani, he! Mlango ukajifunga. Nilipokimbilia dirisha la chumba changu, nikamuona mtu fulani hivi anatoka kabatini …”



“Mweusi?” Mtemvu alidakia.

“Ndio! Yani kama moshi mweusi yaani, mweusi ti!” Pius alijibu, Mtemvu akashadadia, “Ndio huyo huyo! Huyo ndiye nilikuwa nakuambia! ... Enhe, endelea.”



“Basi bwana, yule mtu akagawanyika mbele ya macho yangu alafu akamuingia mke wangu! Damu zikaanza kumtoka masikioni, mdomoni na masikioni kwa fujo mpaka akafa! Baada ya hapo, akapotea na kunitokea mimi ndugu yangu, akaniambia yeye ni mgeni wangu na ametumwa roho yangu!”



“Aisee!” Mtemvu aliduwaa. “Kwanini anatufuatilia hivi? Tumemkosea nini?” Aliuliza akitikisa kichwa chake kwa masikitiko. Pius alitizama huku na huko. Alitaka kusema jambo ila alikwazwa na uwepo wa Inspekta nyuma yake.



Alitoa ishara ya macho kumuonyeshea Mtemvu juu ya Inspekta, Mtemvu akamuomba Inspekta faragha naye akasogea kando kidogo. Bwana Pius akafungua kinywa.



“Kuna jambo kabisa linanijia kichwani, Mtemvu! Ni kuhusu haya mauza uza tunayoyaona.”

“Jambo gani hilo?”

“Hisia zangu zinanituma huyu muuaji ana mahusiano kabisa na marehemu Malale. HakyaMungu nakuambia! Roho ya Malale bado ina tanga tanga, na hii ndio inatuwinda!”



Mtemvu akaguna kama asiyeamini. Bwana Pius akaendea:

“Nakuambia ukweli, Mtemvu. Ni lazima tu kuna mahusiano. Mbona hayakutokea kabla ya kifo cha Malale? Mbona yametokea punde tu baada ya kifo cha Malale?”



Kidogo hilo likajenga hoja kichwani kwa Mtemvu. Alielekea kuamini kabisa.

“Vipi, umewataarifu na wengineo?” Mtemvu aliuliza.

“Hapana! Nilikutaarifu wewe tu.”



Bwana Pius alimjibu akimnyooshea kidole. Mtemvu alichomoa simu yake mfukoni akawataarifu wenzake wote walioshiriki kwenye magendo juu ya yale yaliyomsibu Pius. Baada ya muda mfupi wote waliwasili eneo la tukio. Walijitenga kidogo mbali na umati wa watu wakawa wanateta.



“Jamani, hili swala ni kubwa na ni hatari kuliko hata tulivyokuwa tunafikiri hapo awali. Tushauriane nini cha kufanya. Bila hivyo sote tutakwisha! Hakuna atakayebaki hata mmoja!” Mtemvu alihutubia wenzake wakimsikiliza.



“Ndugu yetu hapa kwa macho yake ameshuhudia kifo cha mkewe. Na kwa masikio yake amesikia akiambiwa roho yake inatafutwa kama vile nami nilivyoambiwa. Nyie mwaonaje hili jambo? Hamuoni kama lina mahusiano yoyote na kifo cha Malale?”



Filbert akaguna akisema kwa woga: “Si mnaona jamani! Mie niliwaambia. Niliwashauri kuhusu Malale lakini hamkutaka kunisikia kabisa. Oneni sasa!”



K square akasonya. “Unaongea nini, wewe?”

“Naongelea mlichokifanya!” Filbert akajibu na kuongezea:

“Kwani tulikuwa tuna ulazima gani wa kumuua Malale? Kulikuwa kuna sababu gani ya kumwaga damu yake?”



Aliuliza akizungusha uso wake kutizama wajumbe. Raheem akambeza:

“Wewe unaongea nini?” Aliuliza kwa sauti yenye jazba ndani yake. “Unadhani kama tusingefanya hivyo ingekuwaje?”

“Ingekuwaje!” Filbert akatahamaki, “Hakukuwa na haja yoyote ya kumuua Malale. Huo ndio ukweli, ni unyama wenu tu na ukatili. Haya sasa mnafanyaje sasa hivi?”

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Raheem akamtolea macho makali akiinuka. “Wewe ni mwanamke – tena kahaba! Na mimi ndio mana nilipinga sana wewe kuingizwa kwenye hili dili. Najua wewe ni mama – mwanaume mwenye roho ya kike!”



Filbert aliinuka kwa hasira arushe ngumi, Mtemvu na K square walimuwahi na kumtuliza jazba.

“Hebu kuweni na aibu!” K square alifoka kwa kunong’ona akitizama umati.

“Tupo msibani alafu mnataka mpigane? Badala ya kujadili tufanye jambo gani, nyie mnataka kupigana. Ni akili hiyo?”



Filbert alinyanyuka tena akiwa amefura, akasema akinyooshea kidole njiani: “Mimi naomba niondoke. Mtajua wenyewe na damu mliyoimwaga!”

Aliondoka akawaacha wenzake katika butwaa. Raheem alitikisa kichwa chake akishika kiuno.



“Si unaona!” Aling’aka. “Unadhani sasa anaenda kufanya nini? Si mnaona niliyowaambia? Huyu ni mwanamke kabisa!”

“Tulia, Raheem.” Mtemvu alihasa. “Hakuna haja ya kuzozana. Tutizame nini cha kufanya kwa sasa.”



“Kabisa!” K square akaunga mkono. “Tutizame mbele na si nyuma.” Naye alishauri. Wakati huo wote Pius alikuwa kimya tu. Alikuwa anawatizama wenzie wakiteta na kuzoza. Utulivu ulirudi kwenye kikao, majadiliano yakaendelea.



“Ok. Mimi nina wazo juu ya nini tufanye.” K square alinadi, wenzake wote wakamtizama.

“Kwa mujibu wa maelezo ya Pius na bwana Mtemvu hapa, ni wazi kwamba roho ya tuliyemuangamiza inatapatapa. Inabidi tuitulize haraka iwezekanavyo.



Twendeni kwa mtaalamu tu – mganga!” Raheem akaguna. “Hapana!” Alisema kwa msisitizo. “Mie siendi kwa mganga kabisaa! Siamini hayo mambo yenu ya kishirikina! Mnitoe.”



Mtemvu na K square wakatizamana. Walimtizama na Pius pia kisha wakarudisha nyuso zao kwa Raheem.

“Unasemaje?” K square aliuliza. Raheem alibinua mdomo wake akajibu: “Kama mlivyonisikia. Siendi kwa mganga. Na sioni kama kuna haja hiyo. Unajua tatizo lenu nyie ni moja.



Mmeruhusu taswira ya Malale iwatawale. Imekaa kwenye subconscious yenu na ndiyo hiyo inawatesa sasa. You are in psychological torture, aren’t you aware of that simple phenomena? Tangu lini marehemu akarudi? Tuacheni kujiongopea – Hakuna kitu kama hicho!”



Raheem alisema kwa kujiamini. Pius akafungua mdomo wake kwa mara ya kwanza tangu kikao kianze.

“Usiwe mjinga, Raheem. Huu si muda wa kuleta ujuaji. Unadhani kuna mambo ya saikolojia kwenye kuonekana na kupotea kwa mtu mbele ya macho yako? Tena mpaka anaua ukishuhudia?”



“I am telling you, Pius. Hakuna kitu kama hiko!” Raheem alishikilia msimamo wake. “Hamuwezi kuniita hapa kujadili mambo ya kufikirika na mambo ya kishirikina. Kwa jinsi akili yako ilivyoathirika, unaweza ukaona kikombe kimedondoshwa na upepo kikavunjika ukadhania ni Malale.



Msimamo wangu mimi ni kama vile tulivyokubaliana kwenye kikao cha awali, tuongeze tu ulinzi miongoni mwetu. Hiyo pesa mnayotaka kwenda kumpa mganga, wasomi kama nyie, mkampe mtu wa counselling awasaidie. Otherwise, I am out!”



Raheem alisema kisha akanyanyuka na kuondoka.

“Achaneni naye, bado hayajamkumba. Anaona ni hadithi tu za kufikirika. ” Mtemvu alisema akaongezea: “Mimi nipo radhi twende kwa mganga.”

“Hata mimi!” Pius akadakia.



“Na mimi pia!” K square akamalizia. Walipanga siku ya kwenda kwa mganga kwa makubaliano thabiti. Walipomaliza hicho kikao chao cha siri, walijirudisha kuchangamana na watu wengine waliodhuria msibani.



Inspekta aliketi nyuma ya bwana Mtemvu akitizama usalama. Macho yake yalikuwa hayapumziki yakienda magharibi na mashariki, yakipanda kaskazini na kushuka kusini.



Ratiba ya msiba iliendelea kama ada. Ulifikia muda watu wakawa wanajipatia chakula. Ni wakati huo ndio inspekta Vitalis akaona mtu mwenye rangi ya kivuli akikatiza kwa haraka kwenye dirisha la sebule ya Bwana Pius. Hilo lisimchukue muda mrefu akalitambua kama doa kwenye usalama.



Kimyakimya, alijitoa nyuma ya bwana Mtemvu afuate sebule. Alifungua mlango na kuingia ndani, akakuta watu kadhaa wameketi kwenye viti. Aliwauliza kama kuna mtu yeyote aliyekuwa anakimbia wakakanusha. Alishika korido akaelekea mpaka chumbani. Alikagua chumba baada ya chumba. Alipotoka kwenye chumba cha mwisho, simu yake iliita. Ilikuwa ni namba ya ajabu isiyoeleweka ni ya nchi gani. Inspekta alipokea akaiweka simu sikioni.



“Halo! … Wewe nani? ... Unasema?”

Simu ikakata. Haraka inspekta Vitalis alikimbilia sebuleni. Alichungulia nje lakini hakumuona bwana Mtemvu kwenye kiti alichomuacha. Haraka alitoka akakimbilia nje. Alipepesa macho yake huku na kule asimuone Bwana Mtemvu. Aliuliza majirani, wakamuambia mkuu wake alielekea maliwatoni.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Haraka Vitalis alikimbilia huko. Njiani alikutana na Bwana Mtemvu akiwa anafunga zipu ametokea mlango wa maliwato. Alishusha pumzi ya afadhali, ila papo hapo ujumbe mfupi ukaingia kwenye simu yake:

‘Ndani ya robo saa ijayo, atakufa.’



Ujumbe huo haukuambatana na namba yoyote. Inspekta alipousoma hakumuonyesha mkuu wake, alimuongoza tu kumrudisha alipoketi awali kisha akaanza kurusha macho yake pande zote za ulimwengu kumtafuta anayemchezea.



Kila mara alitizama saa yake ya mkononi na mkono wake wa kulia ukiwa karibu na bunduki aliyoichomeka nyuma ya suruali. Mapigo yake ya moyo yaliongezeka kila dakika ziliposonga.



Ilihitimu dakika ya kumi na tano kusiwe na chochote kilichotukia, inspekta alitizama saa yake kana kwamba haamini. Akiwa bado katika hilo ombwe, akasikia simu ya mkuu wake inaita. Aliikwapua simu hiyo akisema:

“Naomba nipokee mimi, Mkuu.” Mtemvu akaridhia.



“Haloo!” Inspekta Vitalis aliipachika simu sikioni.

“Wewe nani? … Enhe …” Akasita. “Maeneo gani? ... Sawa, ahsante sana kwa taarifa.”

Inspekta Vitalis alikata simu Mtemvu akimtizama kwa shauku.

“Nani huyo?”

“Msamaria mwema.”

“Anasemaje?”

“Kuna ajali imetokea.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Ajali!”

“Ndio. Bwana Filbert amegongwa na lori la mchanga maeneo ya Mbweni.”

“Wasema?”

“Ndio hivyo mkuu!”

“Embu twende, twende haraka!” Mtemvu alinyanyuka kama mtu aliyechanganyikiwa akapiga hatua tatu mbele kisha akasimama:

“Ngoja kwanza niwape taarifa wakina Pius.”



Upesi alikimbilia kuwatafuta Pius na K square nyuma yake akiwa anafuatwa na Inspekta. Hakukuwa na muda wa kujiuliza kwa undani yule aliyepiga simu alikuwa ni nani na alitoa wapi namba ya Mtemvu. Nani alikuwa anajua aidha ni mtego?



Swali hilo lilikuja kichwani mwa Inspekta lakini hakukuwa na chumba kikubwa kuruhusu kulitafutia jibu. Pius na K square walipopatikana, Mtemvu aliwapasha habari, na wakati huo simu ya Inspekta ikatetemeshwa mfukoni kwa ujumbe mfupi.







‘NA HUKO SAFARINI NDIPO MKUU WAKO ATAKAPOKUFA’

Ujumbe kwenye simu ya Inspekta ulisomeka hivyo. Kabla Inspekta hajafanya lolote juu ya ujumbe huo, alisikia sauti ya Mtemvu ikisema:



“Tupande gari langu.” Kisha Mtemvu na wenzake: K square na Pius, wakaamka na kulifuata gari. Walifungua milango wakajiingiza ndani wakimsubiria inspekta Vitalis ambaye naye hakujivuta, alijipaki na kuwasha gari kichwani akibanwa na mawazo kede.



“Ndugu yangu mbona tutakwisha sasa!” Bwana Pius alibwabwaja na sauti iliyokaribu na kilio. Gari lilitoka eneo la msibani likakamata barabara.



“Hapana, usihofu!” Mtemvu alimtia moyo mwenzake. “Tatizo Filbert alipaniki sana! Nadhani hiko ndio kimemsababishia ajali.”

“Ni kweli!” K square aliunga mkono. “Wakati anaondoka alikuwa amekanganyikiwa – uso wake ulionyesha.



Tungejua tusingemruhusu aondoke kabisa.”

“Ila we unadhani aliyoyaongea ni sahihi?” Pius aliuliza.

“Kuhusu ya bwana Malale?”

“Ndio! Unahisi aliyosema yana ukweli wowote ndaniye?”



Kabla swali halijajibiwa Mtemvu aliwataka wenzake wanyamaze maana waongeayo yanazidi kumchanganya. Alishusha pumzi ndefu akitizama mbele waelekeapo.



“Tuhamishie hizo nguvu zetu kwenye kumuombea tu awe salama. Tutapata kujua kilichojiri kwa kupitia yeye tujue kwamba ni alichanganyikiwa ama kuna mauzauza mengine.”



Waliridhia wakafunga vinywa wakaacha safari iendelee kwa ukimya kidogo. Ukimya huo ulimfanya inspekta Vitalis awe makini zaidi kurusharusha macho yake huku na huko kuwajulia hali wakuu wake walio nyuma.



Huku mkono wake wa kulia ukiwa juu ya usukani, wa kushoto ulikuwa umekaa karibu kabisa na bunduki. Usipite hata muda mrefu wakakutana na foleni nyepesi. Gari mojawapo mbele yao lilikuwa limezima hivyo ikawalazimu nao kusimama kwa muda.



Wakiwa hapo, macho ya Inspekta yalimuona mtu mwenye shati la njano kwenye vioo vya kando akiwa amesimama nyuma ya gari pasipo kufanya jambo. Alikuwa ni mwanaume mrefu mwenye nywele nyingi nyeusi. Haikuhitaji hata sekunde kadhaa kwa Inspekta kutambua na kutia walakini.



Alipiga honi kumshitua mtu huyo lakini hakushituka wala kutikisika kana kwamba hajasikia lolote. Inspekta alifungua mlango akatoka nje kumfuata, ajabu hakumkuta mtu yeyote nyuma. Aliinamisha mgongo wake kutizama uvunguni mwa gari pia asione yeyote.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Akisimama apate kutafakari, alishituka kuona magari yote ikiwemo na alilokuwa anaendesha yanaenda baada ya lile gari bovu kupona. Alibutwaa kwa muda kabla hajaanza kulikimbiza kwa kasi gari walilomo wakuu wake akilibamiza na kuliamuru lisimame.



Kwenye kioo cha gari hilo aliwaona Mtemvu pamoja na wenzake wakiomba msaada kwa sura za woga, alipotizama sehemu ya dereva alimuona mwanaume mwenye shati la njano!



Hakuweza kukimbizana na kasi ya gari japokuwa alikimbia kama mwehu. Alidanda nyuma ya gari akakwea mpaka kwenye paa akitawanya mikono na miguu yake apate balansi. Gari lilienda pupa kushoto na kulia lakini Inspekta hakuacha kung’ang’ania paa abadani mpaka pale alipoacha mkono mmoja umbebe kisha akajirusha na kupasua kioo cha pembeni ya dereva kwa miguu yake yote miwili ajikute yu ndani kwenye kiti. Alikamatia usukani akiuliza kwa kuhema:



“Mpo sawa?” Pasipo kuangalia nyuma. Mtemvu na wenzake kwa haraka yenye hofu wakajibu wapo sawa. Walikuwa wanahema mno na tayari walilowanisha nguo zao kwa jasho.



“Nani alikuwa anaendesha? Alitokea wapi?”

“Hatujui ni nani na wala alipotokea!” Alijibu Pius macho yake yakiwa mekundu. “Tumeshangaa tu ametokea mtu ghafula gari likaanza kwenda!”

“Hata sura yake hatujaitambua!” Mtemvu naye alidaka, “Uso ulikuwa mweusi … Ana afro!”



“Na wapi amepotelea?” Inspekta Vitalis aliuliza.

“Hatujui! Amepotea kama upepo!” K square alijibu upesi kisha ukimya ukashika gari kwa dakika chache.

“Dawa yake ipo jikoni.” Mtemvu alivunja ukimya kwa majigambo. “Muda wake wa kutuchezea ni mfupi sana. Lazima nimuoneshe, hawezi kuninyima raha hivi!”



“Ni nani huyo?” Inspekta Vitalis aliuliza. Mtemvu na wenzake wakatizamana.

“Sijamjua bado.” Mtemvu alijibu. Hakuthubutu kusema wanachowaza, ya kwamba ni Malale.







Walifika eneo la ajali wakashuhudia gari la Filbert likiwa nyang'anyang'a damu zimetapakaa. Lori la mchanga halikujeruhiwa sana zaidi ya kubondeka kidogo kwa mbele. Watu kadhaa walikuwa wamezingira magari hayo wakiwa na nyuso za huruma mchanganyiko na mshangao.







"Samahani, wahanga wa ajali wapo wapi?" K square alimuuliza mmojawapo wa watu waliojikusanya pale wakati Mtemvu na Inspekta wakiwa wanarusharusha macho yao kana kwamba wanatafuta kitu.







"Wameshachukuliwa. Ambulance imewabeba muda si mrefu yani!"

"Wamewapeleka wapi?" K square akaongezea swali. Kabla hajajibiwa, sauti ya king'ora ilivuma. Gari la kubebelea magari yaliyoharibika liliingia eneo la ajali likakusanya gari la Filbert. Haikujulikana nani aliyetaarifu watoaji hao wa huduma, labda walipata taarifa juu ya aliyepata ajali ni mtu mzito na huenda ikawa ni fursa.







“Twendeni hospitali." Inspekta Vitalis aliwaambia Mtemvu na K square. "Kwa taarifa nilizopata ambulance iliyokuja kuwachukua wahanga ilikuwa imeandikwa MASSANA HOSPITAL ubavuni. Hivyo tuelekee huko."

"Sawa!"







Walipoingia kwenye gari ndipo wakagundua Pius hakuwepo pamoja nao. Walitizamana kabla hawajaulizana na kushuka kwenye gari wamtafute mwenzao. Kila mmoja alichukua njia yake kusaka akiita.







Kwa mbali ndani msitu, Inspekta aliona kitu chenye rangi ya njano kikiishilia. Hakujiuliza mara mbili akafungua miguu yake kukimbilia kule alipoona alichotilia shaka. Alitoa bunduki yake akaishikilia mkononi akiendelea kuzama msituni.







Macho yake yaliyokuwa yanapepesa huku na kule yalimuona mtu aliyevalia nguo ya njano akikimbia, mkononi kambebelea mtu kwa mbele. Alimtizama vizuri mtu aliyebebwa kwa haraka akagundua ni bwana Pius kwa mujibu wa nguoze. Alifyatua risasi kumlenga mwanaume mwenye shati la njano lakini mwanaume huyo hakukoma kukimbia haraka kana kwamba hajaguswa na risasi! Mwishowe risasi za inspekta Vitalis ziliisha mwanaume yule hata asisimame.







Inspekta aliongeza kasi zaidi ya kukimbia hatimaye akamshika bega mwanaume mwenye shati la njano na kumvuta kwanguvu. Ghafula mwanaume huyo akapotea! Yeye pamoja na Pius!







Inspekta alisimama ameshika kiuno akitizama kila upande kama mtu anayefikiria jambo. Ghafula alisikia mtu amekatiza nyuma yake upesi, alipogeuka hakuona mtu yeyote isipokuwa miti tu.







Alihisi kabisa kuna mtu karibu yake japokuwa hamuoni. Aliinama akachota mchanga na mkono wake wa kuume kisha akatumikisha milango yake ya fahamu kutambua alipo mtu anayemtafuta, akagundua yupo nyuma yake. Kugundua yu upande gani sasa huko nyuma aliumwaga mchanga kwa kuzungusha mkono, mahali mchanga ulipogota akaagiza teke kali lililomsulubu vema aliyekuwa haonekani na kumtupia chini. Alionekana kwa punde alafu akapotea tena.







Inspekta Vitalis alitumbua macho kutafuta. Hakuona wala kuhisi kitu kwa dakika tatu. Simu yake ilitetemeka mfukoni akaitoa na kuitizama – Mtemvu. Aliipokea haraka akaiweka sikioni.







“Ndio mkuu … Nipo msituni namtafuta bwana Pius … Upo nae? … Sawa, sawa basi ntakuwepo hapo muda si mrefu!”







Alikata simu na bumbuwazi la kupata taarifa Pius amepatikana ilhali anaenyeka kumtafuta. Ila zaidi ya hapo alipata hofu – huyo kweli waliye naye ni Pius, ama ni mtu mwenye shati la njano? Kama ndiye, je mtu mwenye shati la njano yu pande zipi huku hajamuona wala kumuhisi kwa dakika kadhaa? Atakuwa ameelekea huko? Inspekta alichanganyikiwa na maswali. Hakuwa na la kufanya zaidi ya kuanza kukimbia kwenda alipoitwa akifuatisha nyayo za viatu vyake asipotee msituni.







Alifika akamkuta Mtemvu na wenzake wawili ndani ya gari wakionekana wamechoka kwa kungoja.







“Pole sana inspekta kumbe alikuwa ametoka kwenda kukojoa. Tuondoke sasa, tunazidi chelewa.” Alisema Mtemvu.

“Sawa.” Inspekta Vitalis akaitikia kwa kumezea. Alimtizama Pius kwa macho ya mashaka. Na alifanya hivyo safari yote akitumia kioo cha gari kilichoketi juu ya kichwa chake lakini hakupata lililothibitisha walakini wake.





Muziki ulisikika kwenye simu kubwa nyeupe iliyokuwa imelala juu ya meza ya plastiki ya kampuni ya Serengeti. Bwana Raheem aliyekuwa amekaa peke yake kwenye kona ya bar maarufu jijini Dar aliitizama simu hiyo kiooni akaona jina la Mtemvu. Alisonya kisha akaendelea kunywa kinywaji chake kilichokuwa ndani ya glasi ndefu yenye kiuno chembamba.







Simu ilipiga muziki mwishowe ikakata. Ila baada ya muda kidogo, ikapiga tena muziki. Raheem aliitizama kwa jicho la hasira kabla hajaamua kuipokea ili kumuepushia usumbufu zaidi.







Alifoka:







“Nini!” Akiwa amekunja sura. Ila baada ya muda alinywea na kuwa mtulivu zaidi akiubinua mdomo wake.

“Muda gani? ... Kwahiyo mpo wapi kwa sasa? ... Ok, nitakuwa hapo muda si mrefu!”

Aliirudisha simu juu ya meza akakuna ndevu zake.

“Hiki kijamaa kina matatizo sana!” Aliongea mwenyewe. Alikunywa kinywaji chake mafundo kadhaa kisha akaendelea kuteta kama vile kuna mtu anamsikiliza.

“Kwanza kioga kama mwanamke! ... Sijui kilienda wapi huko kikabinuliwa na lori!”







Akanywa tena mafundo mengine na kumaliza kabisa knywaji chake.







“Najuta sana kufanya kazi na hawa watu waoga hivi. Kama ningelijua mapema lile dili nisingeliwashirikisha kabisa. Hivi inakuaje kumuua mtu mmoja tu inakuwa ishu kubwa hivi? Suush! Huu ni wakati wangu muafaka wa kujutia kumtupilia mbali na kumlaghai bwana Kim. Najua asingenisumbua katu! Uoga wangu waniponza vibaya sana.”







Alipiga kichwa chake kofi akiing’ata lips.





http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Ni miezi kadhaa tu huko nyuma alikuwa mtu wa kwanza kushirikishwa wazo adhimu la kuua tembo na kuwapokonya pembe ili wapate zisafirisha kwenda Asia kwa kupitia madalali wa ulaya. Wazo hilo lilikuja mezani kwake pale alipokuwa anaperuzi barua pepe akakuta ametumiwa kipande kidogo cha habari kutoka kwa bwana Kim, kikieleza faida kinaganaga za pembe za tembo huko mashariki ya mbali. Kwa mara ya kwanza alipuuzia ujumbe huo ambao haukuambatana na maneno mengine yeyote, ila baada ya bwana Kim kumshawishi zaidi kwa kumtumia namba za madalali hao wa ulaya akiweka wazi pesa nono za biashara hiyo, Raheem akadakwa uchu.







Kwa siri, tena kubwa sana alisuka mpango huo na bwana Kim ya kwamba atumie dhamana ya cheo chake kizito bandarini kufanikisha hilo. Ila alikuja kugundua asingeweza kufanikisha kazi hiyo mwenyewe. Angekwapuaje pembe hizo za tembo huko mbugani kwa wepesi? Ilimlazimu amtafute na amshirikishe bwana Pius wa TANAPA. Kuhusu usalama wake na wa bidhaa alimtafuta Mtemvu wa jeshi la polisi huku usafirishaji wa bidhaa hiyo mpaka ulaya akimshirikisha Filbert na K square kwa kutumia kampuni zao kubwa za usafirishaji wa bidhaa baharini.







Tamaa hulevya. Raheem aliona mgao wa bwana Kim wa asilimia sitini na tano ni mkubwa mno, angepata pesa ndogo. Alihamishia biashara yote kwa wenzake kwa makubaliano kwamba atachukua asilimia arobaini na tano na itakayobaki atawapa wagawane, makubaliano yakapita. Bado pesa ilikuwa ni nyingi mno.







Raheem alitikisa kichwa chake akijitahidi kufuta kumbukumbu hiyo akilini. Aliiona ni kama jinamizi linalomuandama na sasa lataka kumtoa roho. Alilipia kinywaji akanyanyuka kufuata gari lale la kisasa aina ya Jaguar. Alitokomea eneo hilo kwa mwendokasi mkubwa akifurahia mlio wa nguvu unaotoka kwenye gari lake uliofanya wapita njia na madereva wengine wamtizame.







Furaha hiyo ya majigambo ilikuja kukoma pale kwa kutumia kioo cha dereva alipomuona mtu kwenye viti vya nyuma. Haraka aligeuza shingo kutizama asione chochote, aliporudisha uso mbele akamkuta mtu yule kwenye kiti cha mbele alafu kufumba na kufumbua akapotea!







“Shit! What the ****!”







Raheem alitoa macho. Alipoteza umakini, gari likayumbayumba. Alijitahidi kulimudu na kulirudisha mstarini akafuta uso na kiganja chake kama mtu ambaye haamini alichokiona. Alishusha pumzi ndefu akakung’uta kichwa chake kofi.







“Na mimi naanza kuwa kama wale wapumbavu!”







Akasonya. Mapigo yake ya moyo na pumzi vilirejea katika hali ya kawaida lakini macho yake bado yalikuwa yanarandaranda yakitizama kila upande. Ndani ya dakika zisizopungua tatu, simu yake ikaita. Ilikuwa imejilaza kwenye kiti jirani. Alishituka. Kutizama ni nani akaona namba mpya. Alinyakua simu na mkono wake wa kushoto akaibandika sikioni.







“Haloo! … Ndio mimi, nani mwenzangu? ... Mgeni yupi? … Shenzi!” Alikata simu akasonya kwa hasira.

“Pumbavu kweli! Unadhani mimi wa kuchezewa chezewa enh? Kawatishe haohao!”







Alipomaliza tu, ujumbe ukaingia kunako simu. Mlio ulimjulisha hilo, akaiteka simu na kiganja cha mkono wake wa kushoto akaibia kuusoma ujumbe.







‘Tizama kushoto.’ Ujumbe uliagiza. Raheem pasipo kujiuliza mara mbili akageuza uso kutizama alipoelekezwa. Aliona Lori lililobeba mawe makubwa laja kwa kasi likitokea barabara ya kuchepukia iliyokuwepo hatua kadhaa kwa mbele. Haraka alisinya breki kwanguvu zote bila ya mafanikio – gari lilizidi kwenda. Nalo lori lilipiga honi kali likiendelea kutiririka kana kwamba breki zimefeli.







Gari la Raheem ghafula lilizima hatua kadhaa tu mbali na lori linalokuja kama faru aliyejeruhiwa. Moyo wa mwanaume huyo ulidunda kama ngoma ya mtaa. Milango haikufunguka wala gari halikusonga. Hakuwa na la kufanya zaidi ya kufunga macho yake angojee kifo.







Muda ulipita asihisi chochote. Alifungua jicho moja kwa uwoga akatizama, hakukuwa na lolote lile lililotukia. Sauti za honi na za watu zilisikika tokea nyuma ya gari lake.







"Wewee sogea bwana unatuchelewesha!"







Pipiiiii! Pipiiiiiii!







Foleni ya dharura ilikuwa tayari ishajiri. Raheem akiwa hajielewi, alikanyaga mafuta akaduwaa gari lasonga mbele. Kwa muda kidogo akili yake iliganda akabaki ameachama. Alikuja kushtushwa na muziki wa simu lakini hakuthubutu kupokea wala kuitizama mpaka pale aliposikia mlio wa ujumbe, akainyakua simu asome.







'Pole muheshimiwa, mengi yaja. Hautofaidi hizo pesa kamwe!'



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Raheem akang'ata meno na kupiga ngumi usukani. Kwa pupa aliajiri vidole vyake juu ya vibonyezeo akaandika akibonyeza kwanguvu.







"Wewe ni nani?"





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog