Simulizi : Nyuma Yako (2)
Sehemu Ya Nne (4)
Basi Sarah akawaelekeza mabwana hao juu ya wapi watampata Katie akiwa pamoja na Marshall, mwanaume ambaye anatafutwa kwa udi na uvumba. Kwa mujibu wa Sarah, taarifa hizo alizipata toka kwenye maongezi kati ya Katie na Marshall nyakati za usiku.
“Una uhakika kabisa?”
“Ndio, nina uhakika maafisa.”
“Sawa, tunashukuru,” mabwana hao wakasema na kunyanyuka.
“Vipi sasa kuhusu pesa yangu?” Sarah akawahi kuuliza.
“Usijali,” wakamtoa shaka, “utapata pesa pale ambapo taarifa zako zitazaa matunda.”
Baada ya kusema hayo, wanaume hao wakarudi kwenye gari lao na kuanza safari. Wakiwa njiani wakawataarifu na wenzao wengine juu ya tukio wanaloenda kufanya.
Haikuchukua muda mrefu wakawasili na ndani ya muda mfupi wakawa wameshamwona Katie aliyekuwa ameketi kwenye mchanga akitazama maji ya bahari, Marshall haikuonekana yupo wapi.
Basi wakapashana habari, walikuwa ni watano kwa idadi, mawasiliano yao yalikuwa bora kabisa wakitumia vifaa binafsi.
“Kagua eneo zima,” agizo likatoka, “atakuwa ndani ya eneo hilihili!”
Ukaguzi ukafanyika kwa siri na kwa uadilifu kuangaza eneo zima la fukwe pamoja na viunga vyake vya karibu.
Wakiwa wanafanya msako huo, mmoja wao akamwona mtu ambaye alimtilia mashaka, mtu huyo alikuwa ni mwanaume aliyevalia bukta nyepesi na kofia ya kujikinga na jua, alikuwa anaingia kwenye kiunga kilichokuwa kinatumika kama sehemu ya kutolea haja.
Basi kufuatia shaka lake, mwanaume huyo akajongea, hakuona stara kuwataarifu wenzake maana bado hakuwa na uhakika. Akiwa ameshikilia silaha yake mfukoni akapiga hatua nzito kusonga.
Akazama kiungani, alipotazama akaona milango miwili, mmoja ukiwa umechorwa mtu wa jinsia ya kike na mwingine ukiwa kinyume. Hapo akangoja kumwona mwanaume yule aliyezama ndani.
Alipongoja kwa kama dakika mbili, akatoka huko mwanaume mzee mwenye mvi kichwani na miwani usoni. Mzee huyo alikuwa amevalia bukta tu na kandambili nyekundu, mahadhi ya fukweni, alikuwa ni tofauti kabisa na yule ambaye alionekana akizama ndani, hivyo bwana yule mpepelezi akastaajabu.
Kuhakiki akasonga na kuzama ndani choo, alipotazama hakuona mtu, lakini kabla hajajinasua kujitoa humo, akajikuta hawezi!
Hakukumbuka hata aliona nini, ni kufumba na kufumbua akawa yuko kizani. Kiza totoro.
**
“Hey Dennis! Upo sawa?” sauti ilitoka kwenye kifaa cha mawasiliano.
“Dennis! … Dennis!” sauti ikarudia tena kushika mawimbi, mara hii ikajibiwa, “Nipo sawa, nipo sawa mkuu!”
“Vipi haujafanikiwa kuona kitu?” sauti ikauliza tena.
“Hapana, sijafanikiwa, mkuu. Vipi wewe umeona jambo?”
“Hapana, bado tunatafuta. Hatujajua ameelekea wapi!”
“Vipi mwanamke?”http://pseudepigraphas.blogspot.com/
“Bado yuko mwenyewe. Sasa amesimama anachezeachezea maji!”
Baada ya mawasiliano hayo kukawa kimya, likapita kama lisaa limoja kabla ya mkuu wa oparasheni kurejea kwenye gari kwasababu ya kuteka hadubini, alikuwa anataka amwone Katie ameelekea wapi ndani ya maji, mwanamke huyo alikuwa amezamia asionakane kwa urahisi tena.
Akafungua mlango wa gari na kunyooshea mkono kwenye dashboard, akafungua na kutazama, akaiona hadubini, basi akaivuta kuijaza mkononi lakini kabla hajatoa kichwa chake garini akashtushwa kwa kuona miili kwenye viti vya nyuma! Ilikuwa miili miwili, tena ya wenzake aliokuja nao.
Basi akapandwa na hofu sana, akatazama kando na kando asione cha kutia shaka, akazama ndani ya gari kuwajulia hali wenzake na kheri akamkuta mmoja ambaye bado alikuwa anaweza kuzungumza, alikuwa hoi sana akipandisha macho juu na mdomo wake ameachama, anahema kama mtu aliyebanwa na mbavu!
“Vipi?” akauliza jamaa, “nini kimewatokea?”
Yule mmoja mwenye angalau akasema akiwa anajaribu kunyoosha kidole, ni kana kwamba mkono ulikuwa mzito sana kuunyanyua, akasema, “yupo … yupo ana ---” akakata pumzi!
Upesi bwana huyo akamtazama mwilini na kubaini alikuwa amevujia damu kooni na pia mbavu zake upande wa kushoto zilikuwa uji! Kidogo tu huyo mwanaume aliyekata pumzi akaanza kuchuruza damu mdomoni, damu ambazo zilikuwa zinaongezeka kwa wingi kadiri muda unavyoenda.
“Shit! Shit! Shit!” akalaani yule bwana akitoa kichwa chake garini, alikuwa amefura lakini pia amechanganyikiwa. Akawataarifu wenzake, wawili kwa idadi, juu ya yale yalitokea na kuwataka wamkamate Kate popote pale watakapomuona kwani mambo yalikuwa yanaelekea kuharibika.
Baada ya kusema hayo akaenda kusaka, alipofika majini akarusha macho yake kwa kupitia hadubi akikagua kila eneo la kwenye maji asimwone Kate kabisa. Ni kwamba amepotelea kwenye maji ama amepotelea nchi kavu?
Akakimbia fukweni akitupa macho yake lakini muda si mrefu akapata taarifa sikioni kuwa Kate ameonekana na tayari ameshakamatwa!
“Yuko wapi?” akauliza akiwa anahema kama mbwa, alipopewa maelekezo akaelekea huko upesi kutazama, ilikuwa ni garini. Alipofika akarusha macho yake na kuambulia kuona maiti nyingine ya tatu!
Mwenzake mwingine alikuwa ameuawa. Sasa walikuwa wamebaki wawili tu, wale wanaume pekee ambao walikuwa wameenda kuonana na Sarah kabla ya kuja huku fukweni.
“Tobias, mwingine ameuawa!” alisema kwenye kifaa cha mawasiliano. Uso wake sasa ulionyesha woga, macho yake yalibeba hofu.
“Serious?” sauti ikauliza kifaani.
“Ndio, serious! Sasa nimebaki na wewe tu.”
“Umemuona Katie?”
“Hapana, sijamwona. Vipi wewe?”
“Sijaona kitu! Sasa tunafanyaje?”
“Tuendelee kutafuta, yupo hapahapa anatutazama. Ukimpata Katie mshikilie, atatuletea Marshall mkononi!”
“Na vipi tusipompata?”
“Tumtafute Marshall.”
Kukawa kimya kidogo, kisha,
“Henry!”
“Toby!”
“Marshall huyu hapa.”
“Wapi?”
“Yupo hapa mbele yangu.”
“Toby kuwa serious!”
“I am serious! Marshall yupo hapa mbele yangu. Tumefeli.”
Baada ya hapo kukawa kimya. Bwana huyu akaitwa jina la mwenzake pasipo majibu. Akahofu sana na sasa akaafiki kwamba hana la kufanya. Ni kana kwamba Marshall amekaa pembeni akiwatazama wanahangaika, basi upesi akarudi kwenye gari na kuwasiliana na makao alipotoka kwamba misheni yao haijazaa matunda, mpaka muda huo ni mmoja tu ndiye amesalia kati ya watano.
Alikuwa anaongea kwa kuyumbisha sauti, macho yake yakiangazaangaza huku na kule huko nje, alikuwa anahofia usalama wake. Alipomaliza kutoa taarifa, akakata mawasiliano na kisha akawasha gari ili apate kuondoka.
Akatekenye funguo mara ya kwanza, hola! Akatekenya ufunguo mara ya pili, napo hola, gari haikuwaka. Akapiga usukani mara mbili akitusi, akachomoa ufunguo ili achomeke tena, ufunguo ukadondoka chini kwa papara! Mikono ilikuwa inamtetema.
Akainama kuuokota, na aliponyanyua kichwa , uso kwa uso akakutana na Marshall mbele ya gari! Akanyanyua kwapa ampate kumdungua na bunduki, hajafanya kitu, akasikia sauti ya kike ikimwamuru aweke silaha chini na kutulia kama maji mtungini!
Alipotazama kwenye kioo juu ya kichwa chake, akamwona Katie akiwa amemuelekea bunduki.
**http://pseudepigraphas.blogspot.com/
“Mkuu, inabidi uone hiki!” alisema kijakazi akiwa anamtazama bwana Ian Livermore. Bwana huyo alikuwa ameketi kwenye kiti kikubwa nyuma ya meza yake ya thamani. Juu ya meza hiyo kulikuwa na visosi vitatu vyenye kubebelea majivu ya sigara.
Basi akanyanyuka kuitikia wito wa kijakazi wake, akatoka nje ya jengo na kuona gari kwenye uwanja wa maegesho.
“Tumelikuta barabani hapo nje tukalisukuma kuingia ndani. Hamna aliyerudi salama,” akasema kijakazi akionyeshea mkono wake ndani ya gari, bwana Ian akatazama humo na kuona maiti za watu watano, wote wakiwa ni watumishi wake!
Basi akajikuta akicheka sana. Akashika kiuno chake na kutikisa kichwa.
“Nilijua … nilijua we fucked up!”
Akarudi ndani na kuwaza sana, alimaliza pakti mbili za sigaa akiwaza na kuwazua. Mwishowe akawaita watu wake, walikuwa takribani sitini na tano, akawaambia ni namnga gani anataka Marshall ashughulikiwe haraka na katika namna ipasayo.
Hakuwa na haja ya Marshall kukamatwa, alichokuwa anataka ni mwanaume huyo afe tu, afe tu basi!
“Nataka kichwa chake hapa!” alisema akibonyezea kidole chake mezani, “Nataka kusikia habari za kifo chake, mmenielewa!!” alipaza sauti kwa ukubwa kana kwamba anaongea na watu waliojiketia maili nane mbali na yeye, baada ya kusema hayo akatulia akiwa anafikiri, mdomo wake ulikuwa mkavu kwa kukaushwa na moshi wa sigara lakini pia ukiwa unanuka harudu ya pakti.
“Atakayefanya jitihada za kumuua Marshall, ama kuniletea hapa mwili wake nitamlipa dola milioni mia moja mkononi! Papo hapo!”
Alipotoa ahadi hiyo akawataka wote waondoke wamwache akiwa anawaza cha kufanya. Kuna muda akahisi kuna haja ya ‘wanaume’ wake wote wafike eneo lile kwa ajili ya kazi moja ya kumshughulikia Marshall.
Asingeweza kupumzika mpaka mwanaume huyo atakapofukiwa ardhini.
“Nataka wote mje Marekani!” aliteta na watu waliopo Ujerumani, kwa ufupi na wazi, kisha akaweka simu yake mezani na kudaka kichwa chake. Hakujua kama siku yake ingekuwa mbaya kiasi kile. Alipoambiwa kwamba taarifa ya kupatikana kwa Marshall imepatikana alikaa tenge kungoja mambo mazuri!
Baada ya kufikiri tena kwa muda kidogo akanyanyua simu yake na kumpigia kijakazi wake anayehusika na mawasiliano, huyo akamwambia achapishe matangazo mengine ya kuongeza donge nono kwa watakaotoa taarifa juu ya Marshall, pesa mara mbili ya awali!
Kijakazi huyo akapokea agizo na kuanza kulifanyia kazi. Alichokuwa anakifanya ni kuchapisha tena matangazo yaliyotolewa na polisi na kuyasambaza zaidi. Walikuwa wameshafanikiwa kudukua namba za kitengo hicho na basi kufanikiwa kupokea simu yoyote ile ya mwananchi atakayekuwa anatoa taarifa kuhusu upatikanaji wa Marshall.
Swala hilo halikuwa gumu sana kwa bwana Ian kwani vijakazi wake wengi walikuwa ni watu ambao wanafanya kazi kwenye taasisi za usalama, hususani FBI na CIA. Maajenti hao walikuwa wakimtumikia Bwana huyu kwasababu za kiusalama zaidi, kwani kwa mujibu wa bwana Ian alikuwa na taarifa na shahidi zao kedekede kuhusu uhalifu waliokuwa wakiufanya kwa kutumia migongo ya taaluma zao.
Kuepusha ubaya, watu hawa walikusudia kuungana na kufanya kazi yoyote alimradi itawapatia pesa ya maana, hata kama itakuwa ni kwa kuliumiza taifa lao!
**
“Hapa patakufaa!” alisema Marshall akitazama nyumba ndogo iliyokuwa imesimama mbele yao, yeye na Katie. Ilikuwa ni nyumba yenye ukubwa wa wastani ikiwa imefumwa vema na mbao.
“Yah! Patanifaa,” Katie akajibu na kisha akamgeukia Marshall, “Kwahiyo utakuja lini kuonana na mimi?” alimtazama Marshall kwa mapenzi huku akitabasamu.
“Usijali, nitakuja,” Marshall akamjibu akimwekea mkono begani. Wakazama ndani ya makazi hayo na Katie akapapekua na kuridhika napo, japo palikuwa padogo, vyumba viwilii tu, sebule na jiko, palikuwa pazuri panapovutia.
“Pazuri sana!” Katie alisema aking’aza macho.
“Nilipaona kupitia mtandaoni, nikaona patakufaa. Si nyumba ya kukufanya uhisi mpweke hata nisipokuwapo, ni padogo,” alisema Marshall akimtazama Katie anayekagua makazi yake mapya.
Katie akamtazama Marshal kisha akambusu na kumwambia kwa kumnong’oneza, “hata kama pangekuwa padogo kama stoo, bado nitahisi upweke usipokuwapo, Tarrus!”
“Ni Marshall.”
“Tarrus. Nakujua kwa jina la Tarrus na nitakuita vivyo peke yangu!”
Marshall akambusu Katie kisha akamwuaga aende zake. “Kwa leo acha niende, kuna baadhi ya kazi namalizia alafu tutakuwa pamoja, sawa?”
“Kazi gani hizo, Tarrus?” Katie akauliza kwa sauti ya puani. Alimtazama Marshall kwa macho ya huruma akiwa amemkumbatia kwanguvu asimwachie.
“Rafiki yangu yupo matatizoni, napaswa kumsaidia.”
“Nani? - yule Jack?”
“Yah! Kuna mambo hayapo sawa na maisha yake, siwezi kumwacha peke yake.”
Katie akamtazama Marshall kwa kitambo kidogo alafu akakubali japo kishingo upande. Marshall akambusu na kwenda zake.
**
Saa nne usiku …
“Ulitarajia nini, Tony?” aliuliza Jack akimtumbulia macho Marshall. “Amekwisha kufa!”
Marshall akanywa maji kwenye glasi yake na kuuliza, “Kwahiyo yupo wapi?”
“Yupo kule kule ulipomuweka!” akajibu Jack na kuweka kituo. Marshall akamalizia maji yake kwenye glasi kisha akajifuta mdomo kwa kutumia mgongo wa kiganja chake, akamtazama Jack kwa kitambo kidogo, hakuwa sawa, lakini hakutaka kuzua jambo muda huo, akanyanyuka akauone mwili wa yule mateka wake.
Ni kweli akaukuta ukiwa mfu, akauweka kwenye kiroba na kumtaka Jack wakautupie huko mbali. Wakaongozana naye kufanya vivyo.
“Tony, hii tabia ya kuua watu inabidi upunguze, imezidi sasa!” Jack alisema wakiwa njiani kurudi. Aliuwa anahofia mauaji, aliamini kama yamgeendelea basi mwisho wa siku yangewatia hatiani ingali mikono yao ni safi.
“Jack, huwezi kuelewa,” Marshall akadokeza, “Ulimwengu huu haupo sawa kama wewe udhaniavyo. Muda mwingine yakupasa kufanya vivyo kabla ya wewe kufanyiwa vivyo, lakini pia muda mwingine unafanya kwa ajili ya kutuma ujumbe. It is die-or-survive world!”
Wakafika nyumbani na kupumzika. Tangu Marshall alipoingia kwenye makazi hayo hakuona Vio akiongea na Jack. Walikuwa wakipishana kama magari moshi. Marshall aliona yote hayo lakini hakutia neno.
Usiku ukazidi kukua, na siku hiyo Marshall akiwa amelala akasikia tena mtu akifungua mlango na kutoka. Pasipo kujiuliza mara mbili alifahamu kuwa ni Vio.
Mwanamke huyo alitazama usalama na kujiona yu sawa, basi akanyata mpaka kuufuata mlango wa nyuma, akatoka na kisha akaurudishia mlango huo taratibu pasipo kelele. Alipofanikiwa akasonga mbali asisikike.
“Gotham, usinipigie kwa muda tafadhali, sipo kwenye hali nzuri na Jack,” alisema Vio kwa kunong’ona. “we ngoja mpaka pale nitakapokutaarifu, sawa?” akaendelea kuteta, “acha ubishi basi, ninavyokuambia hivyo nina maana yangu. Kuna mambo hayajakaa vizuri, ndio ni kuhusu ile ishu. Nakuomba uelewe hata mara moja, kwaheri!”
Akakata simu na kushusha pumzi kisha akatikisa kichwa chake kwa maulizo.
Alipogeuka, akashtuka kukutana uso kwa uso na Marshall!
“Mungu wangu!” moyo wake ulienda mbio na ghafla akahisi mwili unamtetemeka.
Marshall akamuuliza, “Ulikuwa unaongea na nani?”
Akabanwa na kigugumizi. Alitazama simu yake kisha akarudisha macho kwa Marshall, hakuwa na cha kusema. Marshall akarudia tena kuuliza, mara hii Vio akasema hakuwa anaongea na mtu, basi Marshall akamtaka ampatie simu aone.
“Siwezi kukupatia simu yangu, wewe kama nani?” Vio akamkazia macho Marshall. Marshall akamsogelea karibu zaidi na kumwambia, “Nadhani unajua mimi ni tofauti kabisa na Jack. Sina uvumilivu wala ujinga wake. Usinijaribu, sawa?”
Baada ya hapo Marshall akamwambia Vio kumhusu mwanaume wake, Gotham na amekuwa akimfuatilia kwa muda sasa.
“Huwezi kuniongopea kitu, Vio. Nataka tu nijue kwanini unamfanyia Jack hivi?”
Basi Vio kusikia hivyo, mara akadondoka na kuzirai! Marshall akambeba na kumpeleka ndani alipomuweka kwenye kiti na kwenda zake kulala, alipokuja kuamka akajikuta hapo na akajikongoja kwenda zake chumbani kumkuta Jack.
Hakulala usiku huo mpaka asubuhi.
**
“Tunaweza kuonana leo?” sauti ilisema kwenye simu ya Marietta Abbey. Mwanamke huyo alikuwa yupo ofisini kwake akiwa ameketi kwenye kiti chake kipana, hakuwa na kazi nyingi za kufanya muda huo bali akingoja miadi yake. Alikuwa amevalia suti rangi ya udongo na miguuni amevalia viatu vya visigino virefu ambavyo ungeviona kwa upesi kama ungeingia tu ndani ya ofisi, alikuwa ameweka miguu juu ya meza.
“Kuna nini, Dick,” akauliza Mariett akiwa anarembua kuangazia dirisha lake la kioo. Ofisi yake ilikuwa imechukua jengo zima, ghorofa kumi na mbili, ukuta wake ukiwa vioo vigumu vinavyopendezesha mandhari.
“Umesikia habari?” Ian akauliza kwenye simu.
“Habari zipi?”
“Za mauaji!” Ian akapaza sauti kujibu.
“Mauaji ya nani?” Marietta akauliza akikunja ndita. Aliondoa miguu yake juu ya meza na kutulia kwa umakini asikie, basi bwana Ian akamwambia kuhusu yale mauaji ya wanaume watano ambao walikuwa wametumwa kwenda kumkamata Marshall.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Habari hizo zikamshtua sana Marietta lakini pia zikampa hofu.
“Dick, mbona mambo yanazidi kwenda kombo?” akauliza na kuongeza, “Ina maana mmeshindwa kabisa kumshughulikia huyo mtu?”
Kidogo Ian akahema, mdomo ulikuwa mzito na kichwa kinamuuma. Akamwambia Marietta kwamba hofu yake si kufa, maana kila mtu hufa mwisho wa siku, lakini ni nini Marshall atafanya? Kwani kadiri alivyo hai ndivyo habari na mambo yao yalivyokwenye hatari ya kubainika.
“Sasa umechukua hatua gani, Dick?” akauliza Marietta, sasa alikuwa ‘serious’ tofauti na mwanzo wakati anaongea na simu, kwa mbali tumbo lake lilikuwa linamuuma.
“Nimeagiza vijana wote waje Marekani, nimetangaza pia donge nono zaidi, pengine inaweza ikasaidia?”
Marietta akauliza kama bwana Marshall ana watu wake wa karibu ambao wanaweza kutumika kumpata, wanaweza kuwashikilia watu hao na kutoa agizo mpaka Marshall apatikane.
“Tumeshafanya hilo, Marietta ” Ian akampasha, “lakini haikuzaa matunda, vijana wote waliuawa na ubaya ni kwamba rafiki yake aitwaye Jack alipumzishwa kazini na mpaka sasa tumeshindwa kujua makazi yake yapo wapi!”
Mazingira yalionekana magumu. Marietta alisonona na kupatwa na mawazo. Halikuwa jambo dogo kabisa hilo.
“Kuwa makini,” Ian akashauri, “Huwezi jua ni muda gani Marshall atakugongea mlango!” aliposema hayo akakata simu na punde kidogo simu yake ya mezani ikaita!
Akashtuka sana! Aliweka kiganja chake kifuani akashusha pumzi ndefu. Alikuwa ni secretary wake akimpigia, basi akapokea simu hiyo na kuiweka sikioni.
“Kuna mgeni anataka kukuona.”
“Nani?”
“Yule donor.”
“Sawa, mruhusu!”
Alipoweka simu chini zikapita sekunde chache, mwanaume mrefu mwenye nywele ndefu nyeusi akiwa amevalia suti mraba akawa ameingia ndani, Marietta akamkaribisha na kumkarimu sana.
Mwanaume huyo akajitambulisha kwa jina la Timothy Clean, mmoja wa mabalozi wa kusaidia watoto na wahanga toka Umoja wa mataifa, kwa kuthibitisha hilo akatoa nyaraka zake kadhaa ambazo alimpatia Marietta kwa ajili ya kujihakiki.
Zilikuwa ni nyaraka safi na zenye mihuri ya kutosha kuondoa shaka. Marietta alizipitia upesi nyaraka hizo na kuziweka pembeni. Hakujisumbua sana, kwani unahitaji uthibitisho gani kupata pesa?hakuna haja ya kujisumbua sana zimetoka wapi alimradi zimekwisha ingia!
“Nimefurahi sana kuona shirika langu limetambulika na kupewa uzito mbele ya macho yenu. Ni jambo la kunipa faraja kwakweli.”
Bwana Timothy akatabasamu, akarejesha nyaraka zake ndani ya mkoba na kisha akamweleza Marietta kuhusu mpango wake, kwamba pesa zitatolewa kwa awamu lakini kwenye ofisi ndogo za Umoja wa mataifa.
Lakini akaweka bayana kwamba pesa hizo zitakapoingia basi watakuwa na makubaliano binafsi. Yote hayo Marietta akayaafiki na kisha akamsindikiza bwana huyo kwenda zake nje ya ofisi kabla ya kuagana kwa kupeana mikono.
**
Saa kumi na moja jioni …
Jack aling’ata ‘sausage’ yake kisha akatazama tena nje ya gari. Mkononi alikuwa ameshikilia sausage nne nyingine ikiwa mdomoni. Alirusha macho yake huku na kule kana kwamba anamtafuta mtu. Alipokosa anachokitafuta, akarejesha kichwa chake kwenye kiti na kuendelea kutafuna.
Akatazama saa yake ya mkononi. Muda ulikuwa umeenda tangu afike hapo. Alitikisa kichwa chake akaendelea kungoja kwa kutafuna, angalau alikuwa na kitu kilichokuwa kinamsogezea muda.
Baada ya kama dakika tano, akamwona mtu, alikuwa ni mwanamke aliyevalia ‘jeans’ nyeusi na topu nyeupe akiwa amelaza nywele. Alimtambua mwanamke huyo kuwa ni Miss Danielle, basi akabonyeza honi ya gari mara mbili kumshtua mwanamke huyo, Danielle akasonga karibu naye.
“Mbona umekawia hivyo?”
“Kulikuwa na kazi namalizia, pole lakini.”
“Ahsante. Watumia?” Jack akamuuliza Danielle huku akimwonyeshea sausage zake.
“Hapana, nashukuru. Endelea tu.”
Basi Jack akamweleza Danielle sababu ya wito wake ya kuwa amemwita hapo kwa ajili ya kumwongelea Marshall. Amekuwa akihofia sana namna ambavyo mwanaume huyo anaenenda, na sasa anahofia sana kwani ameanza kuhusika na aliyekuwa mke wa Raisi, bibi Marietta, endapo naye akimuua kama alivyofanya kwa wengine itazua mzozo mkubwa nchini na watakuwa kwenye mazingira magumu.
“Nakuomba Danielle, kama unaweza ukae naye umweleze kuhusu haya, labda wewe atakuelewa,” Jack alishauri.
“Unadhani atanielewa?” Danielle akauliza.
“Pengine, lakini ni bora ukajaribu,” akasihi Jack, basi Danielle akafikiri kidogo kisha akamuahidi kujaribu hilo atakapopata muda.
“Naomba liwe haraka kabla mambo hayajaharibika,” Jack akasisitiza.
“Nitajitahidi,” Danielle akaahidi na kisha akaenda zake. Alipotokomea, Jack akamalizia sausage zake kisha akawasha gari na kuondoka.
Aliposhika barabara kubwa akaongeza kidogo mwendo, lakini nyuma yake umbali mfupi, kulikuwa na gari linamfuatilia. Gari hilo lilikuwa ni la chini lenye kuzibwa na vioo vyeusi, mwendo wake ulikuwa ni wa wastani hata pale Jack alipokuwa akiuongeza wake, pengine ni kwasababu ya kutoamsha mashaka mapema.
Basi Jack akaendelea na safari yake mpaka alipoenda kukomea kwake asijue kama anafuatwa. Alipozama ndani ya nyumba ndipo gari lile lililokuwa linamfuatilia likakoma, hapo vioo vikafunguliwa na wanaume wawili, washirika wadogo wa bwana James Peak, waliokuwa ndani yake wakatazama makazi yale na kuyapiga picha, kisha wasikae sana wakaenda zao.
**
Saa mbili asubuhi …
Mezani mwa inspekta James kulikuwa na picha nne na kandokando ya meza hiyo walikuwa wamesimama wanaume wawili, wale waliomfuatilia Jack mpaka kwenye makazi yake.
Inspekta alikuwa ameegemea kiti akiwa anawaza jambo. Alikuwa amevalia kizibao cheusi, shati jeupe na tai nyeusi. Sasa alikuwa amepata pa kuanzia lakini akiwa bado hajajua aanzaje.
Ilikuwa ni kheri kwake, vijana ambao aliwapa kazi ya kumfuatilia Miss Danielle kuambulia mlango wa ziada.
Lakini mlango huu waweza kuwa wa kuzimu ama wa mbinguni.
**
Siku inayofuata, inspekta James Peak akiwa ameongozana na maafisa kadhaa wa usalama, wakafika kwenye makazi ya Jack na kutaka kukagua nyumba nzima. Walikuwa wanahisi kwamba hapo patakuwa panatumika kumhifadhi bwana Marshall ambaye wanamtafuta kwa udi na uvumba kama mtuhumiwa namba moja wa mauaji kadhaa.
Kwenye makazi hayo alikuwawapo Jack pamoja na mpenzi wake Vio. Walishangazwa kuvamiwa katika namna ile lakini hawakuwa na cha kufanya zaidi ya kutoa kibali cha ukaguzi. Ilikuwa ni kama kheri watu hao hawakumkuta Marshall humo, alikuwa ametoka kwenda kuonana na Katie tangu majira ya asubuhi na mapema.http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Basi wana usalama wakakagua makazi yote na walipofika kule ‘store wakabaini vitu kadhaa ambavyo viliwapa mashaka, matone ya damu na kile kiti ambacho kilimtunza mateka ambaye aliletwa na Marshall. Hapo bwana James akapakagua na kuchukua baadhi ya mabaki kwa ajili ya upimaji wa vinasaba.
“Ni kweli afisa, hamna cha ziada,” alijitetea Jack, “Alikuwa ni mnyama ambaye nilimuhifadhi store kabla ya kumchinja na kumla.”
Bwana James hakupoteza muda kuzoza na Jack, wakaondoka akiwa amebebelea mabaki yale ambayo yalimfanya Jack apoteze kujiamini kabisa, alihofia sana. Vipi kama majibu ya vinasaba yakamhukumu, atakuwa na wapi pa kujifichia?
Alishika kichwa akiwaza asipate majibu, basi hapo ndipo Vio akatumia fursa kumkumbusha Jack kuhusu Marshall, si mtu wanayepaswa kukaa naye kwani ni hatari kwa usalama wao.
Jack hakusema jambo japo maneno hayo yalileta mantiki kichwani.
**
“Si sehemu salama tena!” alisema Jack akiwa anaongea na simu. Alikuwa akiongea na Marshall muda si mrefu baada ya wale wana usalama kufanya ukaguzi.
Alimwambia Marshall yale yote yaliyotokea na baada ya Marshall kupata kujua hayo basi akamsihi hata na Jack kuondoka upesi kwenye makazi hayo kwani si salama tena. Baada ya maongezi hayo mafupi, Jack akakata simu.
“Kwahiyo?” Vio akauliza akimtazama Jack, walikuwa wote wameketi kitandani, basi Jack akamweleza Vio juuu ya mpango wake kuwa ni kuhama hapo kwenye makazi yao kwa muda mpaka pale mambo yatakapotulia.
“Tutaenda wapi Jack?” akauliza Vio. Kwa namna moja alikuwa na mashaka. Jack akamtoa hofu akimwambia hawatakosa pa kwenda, cha kufanya ajiandae na achukue kila kilicho cha muhimu. Bas upesi Vio akatii, naye Jack akaanza kufanya maandalizi ya kuhama.
**
Usiku wa saa mbili …
Ndani ya gari alikuwapo Gotham na Vio. Gari lilikuwa limefurika kwa moshi wa sigara kuonana ikiwa tabu. Vio alikuwa anachezea simu yake ingali Gotham akiwa anavuta sigara na kunywa pombe ndani ya chupa.
Kwa mbali muziki ulikuwa unaita, muziki aina ya Rock.
“Vio,” Gotham akaita. “Ni muda sasa huu kabla na wewe haujaingia kwenye matatizo. Unaweza ukatumia hili jambo kama sababu. Amka!” Gotham alinguruma,Vio akaweka simu yake pembeni akiwaza kidogo. Hakuwa na la kusema.
“Kama ukiendelea kujivuta unaweza kujikuta upo hatiani, utajitetea na nini?” akauliza Gotham akimtazama Vio. “Kaa chini fikiria usalama wako. Fikiria namna tunavyoweza kufaidika na hili, sawa?”
Baada ya Vio kufikiri kwa muda kidogo akasema, “Nitalifanyia kazi.” kisha akadaka simu yale na kuendelea kuitazama na kuperuzi. Kidogo ujumbe ukaingia toka kwa Jack, Vio akaona ni muda sahihi kwa yeye kuaga aende zake.
“Tutaonana Gotham!”
Gotham akamtazama.
“Tutakapoonana hakikisha kichwa chako kiwe na akili.”
Basi Vio hakuongezea neno, akaenda zake. Gotham akamalizia sigara yake na pombe mkononi alafu akawasha gari na kwenda zake.
**
Pua yake haikumdanganya. Alihisi harufu ya sigara kwenye mavazi ya Vio na kinywa cha mwanamke huyo pia kilikuwa kinanukia pombe.
Jack alijiuliza na kujiumiza, hakujua Vio ametokea wapi na kufanya nini. Alingoja mwanamke huyo alipotoka bafuni ndipo kwa ustaarabu akamuuliza kuhusu kunuka kwake sigara na pombe.
“Mimi?” Vio akashtuka. Macho yake yalitazama kwa kubisha. Jack akamrushia nguo yake na kumwambia ainuse kisha amwambia ni nini anahisi.
“Jack kwani hauwezi kukutana na wavuta sigara huko nje?” Vio akauliza. Akajitetea kwamba harufu hiyo aliipata pale alipokwea gari la uma na si vinginevyo. Lakini ni basi gani hilo ambalo abiria akivuta sigara ndani yake?
Jack alibaini Vio anamdanganya lakini hakutaka kuzoza naye, alikuwa na mambo kadhaa kichwani mwake hivyo akamkubalia Vio kwa kile anachokisema.
Usiku huo Vio akawa sana alipokuwa kitandani. Ni wazi Jack ameanza kumhisi tofauti, macho ya mwanaume huyo yalikuwa yanasema tofauti na alichosema na kinywa chake, lakini pia kama haitoshi tayari Marshall ameshagundua hila zake, nini afanye?
Vipi kama akija kukamatwa pamoja na Jack? Na vipi kama akipata pesa nyingi alafu akatokomea na mpenzi wake Gotham kwenda kula raha?
Aliwaza sana.
**
Usiku wa manane …
“Tarrus!” Marshall alisikia sauti kwa mbali, alikuwa ni Katie ambaye amelala pembezoni mwake basi akafungua macho yake kiusingizi na kumtazama mwanamke huyo,
“vipi Katie?”
“Najihisi vibaya,” akasema Katie. “sijapata kulala kabisa!”
Marshall akanyanyuka kumtazama. Mwanamke huyo akamwambia kwamba anajihisi vibaya na mule ndani kunamfanya akose hewa. Basi Marshall akaamua atoke naye nje kwenda kuketi kibarazani. Huko kulikuwa na upepo, kukamfanya Katie ajihisi vema zaidi.
“Tarrus, sitaki utoke mikononi mwangu tena,” alisema Katie akiwa amelaza kichwa chake kwenye mapaja ya mwanaume huyo. Wote walikuwa wakitazama nje kwa kupitia matundu ya kuta, kwa mbali wangeweza kuona barabara ikiwa inakatizwa na gari moja moja.
“Umenisikia, Tarrus?”
“Nakusikia, Katie.”
“Niahidi kwamba hautaniacha.”
Kidogo Marshall akawa kimya, Katie akanyanyua shingo yake na kumtazama, “Tarrus?”
“Katie unajua mazingira yangu yalivyo, siwezi tabiri kesho yangu,” Marshall akaeleza akimtazama Katie, akamwona mwanamke huyo akivunjika kihisia.
“Si kwamba nitakuacha mwenyewe Katie, si kama hivyo unavyoweza kuwaza,” alisema Marshall, “Naweza kuondoka, ndio, lakini sitachukua kitambo kukurudia. Nakuahidi Katie.”
Katie akashika mkono wa Marshall kwanguvu, “Usiniache Marshall. Unapokuwa haupo ulimwengu unakuwa tofauti kabisa. Uulimwengu unakuwa mkatili kwangu kupita kiasi. Sitaweza kuvumilia kwa muda. Tafadhali, Tarrus.” Katie alisema hayo kwa machozi.
Marshall akamfuta na kumuahidi atakuwa naye mpaka mwisho. Anampenda sana, hapendi akimwona amegubikwa na huzuni. Atafanya kila jambo lilio ndani ya uwezo wake kuhakikisha mwanamke huyo anafurahi, na kwa nguvu zake zote atamuadabisha yeyote yule atakayemgusa.
“Nakuahidi hilo kwa moyo wangu wote, Katie.” akambusu mwanamke huyo na kumweka kwenye mapaja yake mpaka mwanamke huyo alipolala kabisa, akambeba na kumrejesha kitandani.
**
Zilipita siku tatu. Katika siku hizo maafisa wa usalama walifika katika makazi ya Jack kumtafuta mwanaume huyo pasipo mafanikio. Walikuwa wameshapata majibu yao ya vinasaba na vilionyesha kwamba mabaki yale ya damu yalikuwa ni ya binadamu na si mnyama kama ilivyoelezwa na bwana jack.
Walifanya jitihada za kutafuta rekodi za bwana huyo waliyepata majibu yake kwenye vinasaba lakini hawakufanikiwa kabisa. Bwana James Peak alihisi pengine mtu huyo alikuwa ameuawa na Marshall kwasababu zake binafsi, lakini kwanini? Hakuwa na majibu.
“Vipi, umepata kitu?” aliuliza bwana James Peak akiwa anamtazama mtu wake wa taarifa.
“Hapana,” mtaalamu akajibu, “bado hatujapata kitu!”
Alishamaliza kutazama rekodi mahali mbalimbali pasipo matunda, lakini ulipowadia muda wa mchana mtaalamu huyo wa kutafuta data akabaini kuwa bwana yule ambaye walikuta mabaki yake kule kwenye ‘store’ ya makazi ya Jack alikuwa ni afisa wa FBI!
“Kweli?” bwana James akauliza akiwa anatazama taaria hizo kwenye tarakilishi. Ni kweli kile kilichokuw kimesemwa! Mbona kulikuwa na ugumu kupata taarifa hizo? Kidogo ilimshangaza bwana huyu.http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Basi akawapasha washirika wake na kuwataka wajiandae kwani kuna kazi za kuzifanya na mahali pa kwenda.
**
“Hili hapa!” alisema Danielle akimkabidhi faili mmoja wa wafanyakazi wenzake ndani ya makao makuu. Mwanamke huyo akatabasamu na kumshukuru Danielle lakini kabla ya Danielle kuendelea na mambo yake, akajikuta akimwona bwana James Peak pamoja na wenzake wakinyookea kwenye ofisi ya mkuu wa kitengo.
Akapata shaka. Aliwatazama wanaume hao wakizama ndani wasitoke, kichwani akapata kujiuliza maswali kadhaa. Nini watu wale walikuwa wamefuata? Na mbona wamenyookea kule?
Upesi akarudi kwenye ofisi yake, alipoketi na kupita kama robo saa, akapigiwa simu anahitajika. Alipoenda akakutana na mkuu wa FBI pamoja na wale maafisa wa usalama.
Alishajua mambo yatakuwa yameharibika japo hajajua kwa namna gani na kiasi gani. Kidogo alipaliwa na hofu, vidole vyake vilikuwa vinatetemeka kwa mbali.
Alipoketi akaulizwa juu ya mahusiano yake na bwana Marshall kama yaliendelea baada ya mwanaume huyo kukamatwa, akakana, akaulizwa pia kuhusu mahusiano yake na bwana Jack Pyong, afisa wa CIA ambaye ni rafiki mkubwa wa Marshall, hapo kidogo akabanwa na kigugumizi.
“Sidhani kama ni vibaya kuwasiliana na mtu, nina uhuru kama raia wengine,” alijitetea.
Basi akapata kuhabarishwa juu ya majibu ya vinasaba vya afisa wa FBI kwenye ‘store’ ya bwana Jack Pyong, habari hizo zikamshtua, akatazama majibu hayo na kujitetea kwamba hajui lolote kuhusiana na hayo, kuonana kwake na Jack hakukuwa na mahusiano yoyote na habari za mauaji.
“Samahani kama nitakuwa nimeenda nje ya mada lakini ingetupasa tujue afisa huyo wa FBI alikuwa na mahusiano gani na bwana Jack au Marshall,” alishauri Danielle.
Lakini hakuna aliyejali sana maongezi ya mwanamke huyo, waliongea kwa upana sana hapo nyuma, basi mkuu akatoa amri mwanamke huyo asimamishwe mara moja kazi kwa ajili ya kuruhusu uchunguzi dhidi yake ufanyike.
Baada ya hapo, bwana James Peak na washirika wake wakaondoka na bibie Danielle wakiwa wamemfunga pingu.
**
“Danielle,” Bwana James Peak aliita punde baada ya kuweka kinywaji chake mezani, alikuwa amesimama mbele ya Miss Danielle ambaye alikuwa ameketi na kuweka mikono yake yenye pingu juu ya meza.
Walikuwa ndani ya chumba hiki wenyewe, lakini pia huko nje ya chumba kukiwa na watu watatu waliokuwa wanawatazama kupiti kioo kigumu, kioo ambacho wale waliomo ndani hawakuwa wanaweza kuwaona wale waliopo nje.
“Tafadhal naomba unisaidie kmpata Marshall, najua unafahamu alipo,” alisema Bwana James akiketi. Alimtazama Danielle, mwanamke huyo alikuwa amefumba mdomo asioenekane mwenye dalili ya kunena kitu.
“Unajua ni namna gani mtu huyo alivyo hatari, sio? Mchango wako hautakuwa na msaada kwangu tu bali kwa taifa zima!” Bwana James aliongea na kuongea Danielle akiwa anamtazama tu, mwisho wa siku akabamiza meza na kufoka,
“Utasema ama unanipotezea muda wangu?”
“Unajipotezea tu muda wako,” Danielle akamjibu James na kuongeza, “sitaongea kitu mpaka mwanasheria wangu atakapokuwapo hapa!”
Bwana james akamtazama Miss Danielle kisha akang’ata meno na kutikisa kichwa, akaondoka zake pasipo kuaga.
Alipofika mlangoni, akamtazama Miss na kumwambia, “Tutaona.”
**
Mlango wa gari ulifungwa kisha Jack akashusha pumzi ndefu.
“Vipi?” Vio akamuuliza, “Marshall anaendeleaje?”
“Yuko poa, twende,” Jack akasema akiwa anafunga mkanda wa kwenye kiti, basi Vio akawasha gari na kutoka kwenye makazi ya Marshall, alipoendesha baada ya muda kidogo akauliza,
“Vipi Marshall amekuambia nini?”
Jack akamtazama,
“Una maanisha nini?”
“Hajakuambia kitu?”
“Kitu? Kitu gani haswa unachomaanisha wewe?”
“Jack, kwani una shida gani? Mbona umekuwa mkali hivyo? - nataka tu kuju kuhusu maongezi yenu, kuna ubaya?”
Jack akawa kimya, ni kama vile alifunga kinywa kupumzisha akili yake. Vio akamtazama kisha akarejesha uso wake mbele,
“Jack, uko sawa?”
“Ndio. Labda ningeuliza kwanini haukutaka twende wote kumwona Marshall?”
“Kwani kulikuwa na haja hiyo?”
“Kwanini kusiwe na haja hiyo?”
“Jack, nimechoka tu, unajua hilo. Tumehamisha vitu kadhaa, nilikuwa nahisi uchovu.”
Jack akamtazama Vio pasipo kutia neno. Hakuwa anajua kwanini Marshall alimwambia awe makini na mwanamke huyo. Ni kama vile Marshall alikuwa na kitu cha kumwambia lakini akiona muda auruhusu.
Aliweza kuhifadhi kitu hicho kifuani mwake mpaka mwisho wa safari.
**
“Tumesahau kuchua cornflakes, Jack!” alibutwaa Vio muda mfupi tu baada ya kuwasili kwenye makazi yao mapya. Ndio kwanza alikuwa amechomoa ufunguo toka kwenye shingo ya usukani.
“Inabidi nikazifuate, siwezi kuamka asubuhi nisipopata kifungua kinywa hicho!” alisema Vio na punde akawasha gari akimuaga Jack, Jack akabaki amesimama akimtazama mwanamke huyo anaenda zake.
Vio alipotoka kwenye uzio akaongeza mwendokasi na muda si mrefu akawa pamoja na Gotham, mwanaume wa moyo wake. Akiwa hajazima gari, walikuwa wameketi kwenye viti vya mbele.
“Nadhani muda ndo’ sasa,” alisema Vio akimtazama Gotham kwa tabasamu, “Nimeshapajua aishipo Marshall!”
“Serious?” Gotham akabutwaa.
“Ndio, leo nimetoka na Jack huko!”
Basi wakakumbatiana kwa furaha na sasa Gotham akamtaka mwanamke huyo asikawize muda, watoe taarifa hiyo wavune pesa na kutokomea zao wakiwa salama salmini.
“Ungependa kwenda wapi?” akauliza Vio kwa tabasamu pana.
“Unapajua mpenzi,” akajibu Gotham, “Ibiza, Hispania!”
“Hata nami ningependa kwenda huko kabla ya kukoma kwa maisha yangu!” Vio akasema kwa furaha. Wakakumbatiana tena na tena. Walikuwa na furaha sana, waliona sasa wameshaukwaa.
Lakini pasipo kujua, Jack Pyong alikuwa amesimama mahali akiwatazama, moyo wake ukiwa unavuja damu.
“Vio,” Jack akaita kwa kunong’ona. “Nimekukosea nini?” akauliza kana kwamba Vio yu pembeni yake kisha akajikongoja taratibu kulifuata gari.
Alipolifikia hakufanya kitu bali akaendelea kutazama mpaka pale aliposhtukiwa. Vio alibumbuwaa kumwona Jack, na kwa kiasi fulani akahofu, lakini kwa upande wa Gotham kwake ilikuwa kinyume, ni kama vile alikuwa anatarajia ujio wa Jack kwani hakuwa anahofu wala kuhenya, alimtazama Jack kisha akampuuza.
“Vio,” Jack akaita na kuuliza, “nimekukosea nini wewe?”
Mashavu yake yakafunikwa na machozi, alikuwa anang’ata meno kwa uchungu. Kidogo Vio akabanwa na haya.
Lakini kadiri muda ulivyokuwa unaenda, Jack akawa anapatwa na hasira. Akajikuta akitaka kumdaka Vio na kumwadhibu kadiri awezavyo lakini Gotham akammudu mwanaume huyo na kumkandika makonde kadhaa kabla ya kumwacha hapo akiwa anavuja damu na hajielewi.
Uso wa Jack ulikuwa unavuja damu, jicho lake moja limevimba na tumbo lake linauma haswa kwa kukandikwa ngumi! Lakini Jack hakuwa anaumizwa sana na hayo majeraha bali kutendwa kwake na Vio.
Huko kulimuuma kusipokuwa na mithili. Alihisi moyo wake unasinyaa kwanguvu kumimina damu.
“Kwanini Vio?”
Alijikunyata akiwa gizani.
**
Saa mbili asubuhi …
“Nyanyuka twende!” alisema bwana Charles Smith akimtazama Miss Danielle, bwana huyo aliyekuwa amevalia suti nyeusi iliyobana mwili wake mwembamba.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Alikuwa ni mwanasheria wa Danielle. Punde alikuwa ametoka kuongea na inspekta James Peak na kaufikiana kulipeleka shauri hilo mahakamani, mahali ambapo mteja wake atapata haki yake.
Basi Danielle akanyanyuka na kuongozana na bwana Charles mpaka kwenye gari na kutimka toka kituoni. Mwanamke huyo alikuwa amejikunyata akiwa amemezwa na mawazo.
“Usijali, miss,” Charles akamtoa hofu. “Ni kesi ndogo sana isiyo na ushahidi. Tutakapoenda mahakamani haitachukua muda kuimaliza na kuifutilia mbali!”
Na zaidi bwana huyo akapendekeza waweke fidia ya juu kwa serikali kwa kumpotezea muda mteja wake na pia kumchafulia taswira yake mbele ya jamii.
“Unaonaje?” akauliza bwana Charles akitabasamu.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment