Search This Blog

Sunday, 20 November 2022

TAXI (2) - 3

 







    Simulizi : Taxi (2)

    Sehemu Ya Tatu (3)







    Saa sita mchana, Pendo na Winifrida walikuwa wamekaa juu ya sofa kwenye sebule ya nyumba moja kubwa ya kisasa ya ghorofa moja katika eneo la Kurasini. Sebule hiyo ilikuwa na samani mbalimbali za gharama kama seti mbili za makochi ya sofa ya kifahari yaliyopangwa kwa ustadi wa hali ya juu katika mtindo wa kuizunguka ile sebule na katikati ya sebule kukiwa na meza fupi ya kioo yenye umbo la yai.



    Pendo alikuwa kifua wazi na alikuwa anagombana na Winifrida aliyekuwa anamlazimisha kuvaa shati. Muda huo huo mwanamke mmoja mwenye umbo kubwa kiasi lililokuwa linavutia mno aliingia pale sebuleni baada ya kusikia kelele za Pendo. Alikuwa mrefu wa wastani, mweupe kiasi mwenye mashavu mfano wa chungwa na nywele zake zilikuwa nyingi na nyeusi fii.



    Mwanamke yule alikuwa amevaa gauni jepesi na pana kiasi lililoishia magotini na kuifichua miguu yake mizuri huku ikilichora vyema umbo lake maridhawa. Gauni lile lilikuwa linalichora vyema tumbo lake lenye ujauzito wa miezi saba na kiuno chake chembamba lakini imara kilichoshikilia minofu ya mapaja yake iliyokaza kutoka na ratiba nzuri ya mazoezi. Aliitwa Victoria, alikuwa mke wa Elli Kiango.



    “Pendo, unagombana nini na anti Winnie?” Victoria alimuuliza Pendo kwa upole huku akiketi karibu yake na kumshika kichwani.



    “Eti anti Winnie ananilazimisha kuvaa shati.”



    “Sasa kwa nini hutaki kuvaa?”



    “Kuna joto, anti.”



    “Unasikia joto? Kama unasikia joto sawa,” Victoria alisema kwa upole huku akishusha pumzi. “Lakini...” alitaka kuongeza lakini akakatishwa na sauti ya kengele ya getini iliyoashiria kuwa kulikuwa na mtu nje ya geti.



    “Dada!” Victoria alipaza sauti kumwita msichana wa kazi aliyekuwa sehemu fulani mle ndani.



    “Abee!” yule mfanyakazi alipaza sauti yake kuitika na baada ya sekunde chache akatokea, alikuwa mdada ambaye kiumri alikuwa na miaka isiyopungua ishirini na tano na hakuzidi miaka therathini. Alikuwa na mwili mpana ila mkakamavu na alivalia gauni refu na kujifunga apron, akionekana alikuwa jikoni akiandaa chakula.



    “Hebu kaangalie getini kuna nani!” Victoria alimwambia yule mdada wa kazi.



    Yule mdada ambaye aliitwa Lucy alielekea getini, akafungua geti dogo lililokuwa kando ya lile geti kubwa na kuchungulia nje, akamwona mwanadada mmoja mrefu na maji ya kunde mwenye nywele fupi na laini alizozitia rangi. Wakatazamana kwa sekunde kadhaa halafu yule mwanadada akaachia tabasamu lililovifanya vishimo vidogo kwenye mashavu yake vichomoze. Yule mwanadada alikuwa Tunu.



    Tabasamu lile likamfanya Lucy naye aachie tabasamu huku akiyatupa macho yake kulitazama gari alilokuja nalo aina ya Toyota Prado.



    “Karibu, sijui naweza kukusaidia?” Lucy alimuuliza Tunu akiwa amelifungua lile geti dogo nusu, kichwa kipo nje na kiwiliwili chake chote kikiwa ndani, mkono wake ulikuwa karibu kabisa na mlango kwa lolote ambalo lingetokea.



    Tunu alimwangalia kwa makini huku akiendelea kutabasamu na kusema, “Ndiyo, tafadhali unaweza kuniruhusu kuingia ndani?” Tunu alisema kwa sauti tulivu.



    Kidogo Lucy akaonekana kusita, hakumwamini mgeni wake. “Unaweza kuniambia hitaji lako?”



    “Naomba uniruhusu niinge ndani, ninahitaji kuonana na Winifrida, nimeelekezwa hapa na kaka’ake anayeitwa Sammy,” Tunu alisema na kugeuza shingo yake, akatazama kushoto na kulia kwake kuhakikisha kuna hali ya usalama kisha halafu akamtazama tena Lucy.



    Lucy akashusha pumzi. Kimya kifupi kikapita huku Lucy akionekana kutafakari kisha akauma magego na kufanya mataya yake kuchezacheza kama aliyekuwa anatafuna kitu kigumu. Mara ikasikika sauti ya Victoria, “Dada, kwani unaongea na nani?”



    Lucy aligeuza shingo yake na kumwona Victoria akiwa amesimama kwenye baraza kubwa ya ile nyumba. “Anasema amekuja kumwona Winifrida, ameelekezwa hapa na Sammy,” Lucy alisema.







    Victoria alielekea kule getini na alipofika alichungulia nje, akamwona Tunu akiwa bado amesimama pale pale huku tabasamu usoni kwake likiwa halijaenda likizo. Victoria alimtazama kwa makini. “Habari yako, dada?” Victoria alimsalimia.



    “Nzuri, anti... naitwa Tunu na...” Tunu aliitikia na kuanza kujitambulisha.



    “Ooh, Tunu! Karibu ndani,” Victoria alisema na kuachia tabasamu pana kisha akamgeukia Lucy. “Mfungulie geti aingize gari lake.”



    Lucy alishusha pumzi na kulifungua lile geti kubwa akimruhusu Tunu kuingia. Tunu aliingiza gari lake ndani ya uzio wa ile nyumba, akaliegesha kwenye eneo la wazi jirani na banda maalumu la wazi la maegesho ya magari. Ndani ya banda lile kulikuwa na magari mawili, moja lilikuwa Toyota Hilux double cabin la rangi nyeupe na jingine ni aina ya Landcruiser GX V8 rangi nyeusi.



    Alitulia kidogo ndani ya gari akiliacha liungurume kwa dakika chache kisha akazima injini na kushuka. Victoria alimwongoza kuelekea ndani ambako walimkuta Pendo akiwa ameketi juu ya sofa, peke yake, akionekana mwenye huzuni. Winifrida hakuwepo.



    Wakati Tunu anaingia Pendo alimwangalia pasipo kuonesha tashwishwi yoyote usoni kwake, akili yake ya kitoto ilikuwa inawaza mbali sana. Alikuwa akimwaza mama yake.



    “Shemeji Sammy alinipigia simu kunijulisha kuhusu ujio wako, nilipoona muda unazidi kwenda nikajua labda umeahirisha. Karibu sana, Tunu,” Victoria alisema wakati wanaketi juu ya masofa pale sebuleni.



    “Ahsante. Kuna mambo fulani yaliingiliana, ikanibidi kwanza niyaweke sawa ndipo nije huku,” Tunu alisema huku akishusha pumzi kisha akaendelea. “Na kwa kuwa nimechelewa kidogo ningeomba twende moja kwa moja kwenye suala lililonileta hapa... shida yangu ni kuongea na Winifrida, sijui yupo?”



    “Alikuwapo hapa sasa hivi, nadhani kaingia chumbani maana tangu tukio la jana hawajihisi tena kama wapo salama,” Victoria alisema na kugeuza shingo yake kumwangalia Pendo. “Huyu ni mtoto wa Sammy.”



    “Okay!” Tunu alisema huku akimtupia jicho Pendo, “Hujambo, mtoto mzuri?”



    “Sijambo, shikamoo anti!” Pendo alisalimia, hakuonesha ule uchangamfu ambao amekuwa nao siku zote.



    “Marhaba!” Tunu alisema huku akiachia tabasamu pana.



    “Pendo nenda kamwite anti Winnie,” Victoria alimwambia Pendo. Pendo akatoka na kuelekea chumbani huku akiita kwa sauti. “Anti Winnie!”



    “Nawahurumia sana hawa watoto, hawako sawa kisaikolojia,” Victoria alisema kwa huzuni.



    “Mnapaswa kuhakikisha wanaonana na mwanasaikolojia wa watoto ili ajaribu kuwaweka sawa,” Tunu alishauri.



    “Ndiyo maana wapo hapa kwani hiyo ndiyo taaluma yangu. Nimeomba ruhusa ya siku saba kazini ili kushughulikia suala hili,” Victoria alisema na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Umefanya vyema. Hili ni suala tata zito sana na watoto hawa hawawezi kulibeba,” Tunu alisema huku akishusha pumzi. “Pia, awali ya kila jambo tunatakiwa kumshukuru Mungu.”



    “Kabisa!” Victoria aliafiki na wakati huo huo Winifrida na Pendo wakaingia sebuleni. Winifrida alimtazama Tunu kwa wasiwasi mkubwa, akashusha pumzi na kumsalimia kisha akaketi juu ya sofa.



    Victoria na Tunu wakaangaliana kwa muda kisha Victoria akakohoa kidogo ili kusafisha sauti yake. “Winnie, huyu dada anaitwa Tunu, ameelekezwa hapa na kaka’ako, anataka kuongea na wewe,” Victoria alisema na kuinuka, akamshika mkono Pendo.



    “Sasa, da’ Tunu, ngoja tuwaache wenyewe muongee kwa uhuru zaidi,” Victoria alisema huku akianza kuondoka.



    “Haina shida, dada. Tukimalizana nitakwambia,” Tunu alisema huku akijiweka sawa pale kwenye sofa. Kikatokea kitambo kifupi cha ukimya, kila mmoja alionekana kutafakari. Winifrida alikuwa anamwangalia Tunu kwa jicho la kuibia, uso wake ulionesha wasiwasi fulani.



    “Winnie, kwanza nikupe pole kwa yote yaliyotokea jana usiku... Najua hivi sasa unapitia mengi tu na huoni mtu wa kumweleza. Labda si kosa lako. Na sijui ni kwa nini umeshindwa kumweleza hata kaka’ako, au unaogopa?” Tunu alimuuliza Winifrida huku akiwa ameyatuliza macho yake kwenye uso wake.



    Winifrida hakujibu, alibaki kimya akiangalia viganja vyake alivyoviweka juu ya mapaja yake. Tunu aliiona hali ya Winifrida kwa jinsi alivyokuwa na hofu, akatabasamu na kutafuta namna ya kuyaelekeza mazungumzo.



    “Niko hapa mimi na wewe, wawili tu...” Tunu alisema na kusita, akashusha pumzi za ndani kwa ndani huku akionekana kama aliyekuwa akitafakari nini cha kusema. “Labda nikutoe wasiwasi, mimi nafanya kazi usalama wa taifa na chochote utakachoniambia, kama hupendi kaka’ako ajue kitabaki kuwa siri kati yetu. Nikutoe hofu kuwa wote waliofanya tukio hilo la kinyama watapatikana tu kama utakuwa muwazi...” Tunu alinyamaza kidogo ili maneno yale yamwingie Winifrida.



    “Kwa sasa polisi wapo kazini wanawatafuta, mimi pia nimejitolea kusaidia ili kuhakikisha wote wanakamatwa... labda tu nikudokeze kuwa wapo watu ninaowahisi kufanya tukio hilo na ninazo picha zao, kwa hiyo huna sababu ya kunificha chochote unachokijua.” Tunu aliweka kituo, akaminya midomo yake yenye maki na kuficha vishimo vidogo vijitokeze kwenye mashavu yake.



    “Sijui umenielewa?” Tunu alimuuliza Winifrida huku akimwangalia kwa makini.



    “Nimekuelewa, dada,” Winifrida alisema, akavuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu huku akifanya kifua chake kipande na kushuka. Matiti yake madogo yaliyochongoka yalimiliki vyema eneo la kifua.



    Tunu alitoa simu yake ya mkononi, ilikuwa simu nzuri na mpya kabisa aina ya iPhone 11 Pro Max, akaanza kupekuapekua kwenye ile simu kisha akamwonesha Winifrida picha ya Spoiler. “Ulimwona mtu mwenye sura kama hii?” alimuuliza huku akimtazama katika hali ya kumkagua.







    Winifrida aliiangalia ile picha kwa makini, akaonekana kutafakari kwa sekunde chache kisha akatingisha kichwa chake kushoto na kulia taratibu akionekana kutokuwa na uhakika. Tunu akashusha pumzi na kupekua tena, akapata picha ya Uledi na kumwonesha Winifrida.



    Winifrida aliitazama ile picha na kuonekana kukumbuka jambo fulani, akakunja uso wake huku akishindwa kuficha hofu aliyokuwa nao. Tunu aliiona hali ya Winifrida kwa jinsi alivyoingiwa na hofu, akatabasamu na kutafuta picha nyingine. Ilikuwa ni picha ya Dulla Mcomoro, akamwonesha tena Winifrida.



    Winifrida aliitazama ile picha mara moja tu na kuonesha mshituko mkubwa huku akionekana kuumia sana moyoni. Machozi yalianza kumlenga lenga machoni kwa namna alivyoumia. Tunu alimsogelea, akamkumbatia katika hali ya kumfariji huku akimpigapiga mgongoni.



    * * * * *



    Ndani ya ofisi za Mr. Oduya zilizo kwenye ghorofa ya sita ya jengo la ghorofa kumi na mbili katika barabara ya Bagamoyo, jijini Dar es Salaam, Mr. Oduya alikuwa amesimama karibu ya dirisha akiangalia nje. Macho yake yaliangalia barabarani kulikokuwa kunapita magari. Kisha yakahama na kuangalia chini ya lile jengo la ofisi zake kwenye viunga vya maegesho ya magari, kulikuwa na machache yaliyoegeshwa katika sehemu hiyo.



    Kwa dakika kadhaa Mr. Oduya alitulia pale dirishani akitazama barabara ya Bagamoyo kana kwamba alikuwa anaiona kwa mara ya kwanza katika maisha yake. Aliendelea kutazama eneo lile kwa makini na asijue alikuwa akiangalia nini. Uso wake haukuweza kuficha hali ya wasiwasi aliyokuwa nayo moyoni kwa wakati huo.



    Macho yake yalikuwa mekundu na uso wake ulikuwa umesawajika mno akionekana kuwa hoi na mchovu, ni kama vile mtu ambaye hakuwa amepata usingizi kwa juma zima.



    Alichukua pakti ya sigara aina ya Parliament toka katika mfuko wa koti lake na kutoa sigara mbili, moja akaipachika kwenye pembe ya mdomo wake na kuchukua kiberiti cha gesi, akaiwasha ile sigara na kuvuta mkupuo mmoja mkubwa wa pafu la moshi kisha akatoa moshi mwingi nje kupitia mdomo na tundu za pua. Muda wote alionekana kutatizwa sana na jambo.



    Ndani ya ile ofisi walikuwa wawili tu, yeye na Mr. Mafuru aliyekuwa ameketi kwa utulivu kwenye kiti kimojawapo ya viti vilivyopo mle ndani. Muda wote Mr. Mafuru alikuwa akimtazama Mr. Oduya kwa wasiwasi. Uso wake pia ulikuwa umesawajika mno na moyo wake haukuwa kwenye mapigo ya kawaida.



    Baada ya kupiga mikupuo mitatu mikubwa na kisha kuutoa moshi wa sigara, Mr. Oduya aligeuza shingo yake kumtazama Mr. Mafuru. Wakaangaliana kwa kitambo kirefu pasipo kusema chochote, kila mmoja aliendelea kuwa kimya. Mr. Oduya alikohoa kidogo kusafisha koo lake.



    “Mafuru, usimchukulie kirahisi kabisa Madame Norah, muone hivyo hivyo tu, ni mtu wa hatari sana pale unapogusa maslahi yake au mtu anayemhusu...” Mr. Mafuru alisema kisha akavuta tena pafu kubwa la moshi wa sigara na kuutoa ule moshi taratibu huku akiutazama kwa makini.



    “Hapaswi kabisa, kwa namna yoyote ile, kufahamu kuwa ni watu wetu ndio waliofanya kitendo hicho kwa mwanawe, na endapo akifahamu basi tutakuwa tumeharibu kila kitu,” Mr. Oduya alisema na kuanza kupiga hatua taratibu kurudi kwenye kiti chake.



    “Na vipi kuhusu Tunu, is there any information about her?” Mr. Mafuru aliuliza baada ya kutafakari kidogo kisha akashusha pumzi ndefu.



    “Huyo ndiyo hapaswi kabisa kuwa hai. Ni bora hata Madame Norah ambaye unaweza kumweleza akakuelewa kuliko Tunu,” Mr. Oduya alisema na kuketi kwenye kiti chake kikubwa cha magurudumu yanayokiwezesha kutembea, kisha akapiga mkupuo mwingine mkubwa wa moshi wa sigara na kukiminya kipande cha sigara ndani ya kisahani kidogo cha kuwekea majivu.



    “Mwenyewe unakumbuka kuwa Tunu alikuwa mtu wetu, anayajua mengi n ahata tulipomshtukia tukajaribu kumtia mikononi mwetu mara tatu lakini mara zote ameweza kutoweka. Tukishindwa kumpata safari hii itakuwa ngumu sana kumpata tena… na kama tukifanikiwa kutakuwa na gharama yake! Tena gharama kubwa sana!” Mr. Oduya alisema na kuwasha ile sigara nyingine, akaendelea kuvuta taratibu.



    “Lakini naamini safari hii hana ujanja ni heri kama angeendelea kujificha, maana kazi haitakuwa ngumu sana kama ilivyokuwa hapo mwanzoni,” Mr. Mafuru alijaribu kumtoa hofu Mr. Oduya.



    Mr. Oduya alitingisha kichwa chake taratibu na kucheka, “Mafuru, you are serious at all, sijui kama unajua unachoongea. Kutakuwa na gharama, tena kubwa sana kumtia Tunu mkononi!”



    Mr. Mafuru alitaka kusema lakini Mr. Oduya akamtatisha. “Muda mfupi tu uliopita Silas na Job walikuwa wanamfuatilia, tena kwa tahadhari kubwa bila yeye kujua lakini unajua kilichotokea?” Mr. Oduya alimuuliza Mafuru kisha akajijibu mwenye. “Kawapiga chenga ya akili na mwili wasijue alikoelekea. Na taarifa nilizozipata alitua Dar es Salaam jana asubuhi, anaonekana anazo taarifa nyeti kutuhusu ambazo zinaweza kutuharibia kila kitu,” Mr. Oduya alisema kwa wasiwasi.



    “Nadhani sasa unaweza kuelewa nini naongelea,” Mr. Oduya alimwambia Mafuru kisha akavuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu huku akiegemeza mkono mmoja kwenye kiti na kuvuta sigara yake kwa pupa kama hana akili nzuri.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Sasa tunafanyeje, boss, ili tuwe salama? Ina maana hauna mpango kabisa?” Mr. Mafuru aliuliza huku hofu ikijionesha waziwazi usoni kwake.







    “Siwezi kukosa mpango... ninao watu wengi kwenye vyombo vya dola wenye kila aina ya mbinu walio kwenye payroll yangu,” Mr. Oduya alisema huku akiutazama kwa makini ule moshi wa sigara wakati akiutoa. “Nimeshampa kazi Victor, yule shushushu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, anamfahamu vyema Tunu kwa kuwa ni rafiki’ake mkubwa, yeye ndiye aliyempokea jana wakati anatua kiwanja cha ndege. Kwa kumtumia yeye itakuwa ni kete yetu muhimu ya kumpata. Tukishindwa kuitumia nafasi hii then we are fucked up!”



    * * * * *



    Baada ya maongezi yake kwenye simu na Mr. Mafuru, Madame Norah aliwageukia watu wengine na kuwatazama kwa muda kama aliyekuwa anatafuta namna ya kuanza kujieleza. Aliwatazama kwa zamu akianza na Sammy, kisha akamtazama Jengo na baadaye macho yake yakaishia kwa Bi. Pamela.



    Wakati akiwatazama kwa zamu Madame Norah alikuwa ameuona mshangao kwenye macho ya Sammy, hali ya kusawajika kwenye macho ya Jengo na chuki ya waziwazi kwenye macho ya Bi. Pamela. Alidhani kuwa pengine Bi. Pamela hakuwa amefurahishwa kabisa na ujio wake katika maisha yao.



    Ni kweli. Bi. Pamela alihisi donge la wivu likimkaba kooni, ulikuwa ni wivu wa hofu ya kunyang’anywa vyote; mumewe Jengo na Joyce aliyekuwa amuaminisha kuwa yeye ndiye mama yake.



    Hata hivyo, Madame Norah alikuwa na ya kwake moyoni, yeye hakumfikiria kabisa Jengo bali mwanawe Joyce. Hadi muda ule hakuyaamini macho yake wala masikio yake. Alijitahidi kuishirikisha akili yake kikamilifu katika kumletea taarifa za kuaminika. Ni kweli alikuwa amempata mwanawe aliyempoteza miaka therathini na mbili iliyopita!



    Mwanawe alikuwa hai ingawa muda huo alikuwa akiyapigania maisha yake kitandani, jambo hilo lilimhuzunisha sana Madame Norah, lakini ingalau alijua kuwa Joyce ndiye mwanawe! Kuna muda alihisi labda yupo ndotoni. Hata hivyo, hakutaka kabisa ile iwe ndoto. Kila alipomtazama Jengo na mkewe aliwaona wakiyaepuka macho yake. Ni Sammy peke yake ambaye, mbali na kuwa na majonzi, alikuwa katika hali ya kawaida japo mshangao ulikuwa haujamtoka.



    Eneo lile lilianza kutawaliwa na hali ya ukimya ulioanza kumtisha kila mtu. Madame Norah hakuwa ametegemea kama ingemtokea katika Maisha yake, siku kama hiyo, siku ambayo ilimtaka kusimama kidete ili kuhakikisha anairudisha tena furaha iliyomponyoka kwa miaka zaidi ya therathini. Kuna wakati alitamani mambo hayo yaoze na kuteketea kabisa katika roho yake, bahati mbaya hakuwa na namna ya kuyasahau.



    “Yaelekea leo ni siku ya ajabu,” Madame Norah aliwaza. “Hakika leo Mungu kaamua kutenda jambo,” alijikuta akisema kwa sauti na kuwafanya watu wote wamtazame kwa mshangao.



    Alipogundua kuwa watu wote walikuwa wanamtazama kwa mshangao, Madame Norah alishauri jambo, “Nadhani ninyi wanaume mnaweza kwenda kupumzika mkatuachia kazi hii sisi wanawake, mimi na bibie,” Madame Norah alisema huku akimwangalia Bi. Pamela. “Mwanamke mwenzangu, naomba tuwe na mazungumzo kidogo, kama wanawake.”



    Jengo alimtazama Madame Norah kwa mshangao, alionesha kusita sana. Hata Bi. Pamela pia alionesha kusita. Alijiuliza mwanamke yule alitaka kuzungumza naye kuhusu nini lakini hakuweza kubaini. Iliwachukua takriban dakika kumi na tano kufikia mwafaka wa kuzika tofauti zao ili kuangalia namna ya kumsaidia Joyce aweze kupona na kurudi katika Maisha yake ya kawaida.



    Kisha Sammy na Jengo wakaondoka wakiwaacha wanawake wawili ambao waliamua kwenda kuketi katika mgahawa uliomo ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Amana kwa maongezi kama wazazi wa Joyce, mmoja akiwa mama mzazi na mwingine mama mlezi.



    * * * * *



    Saa saba kasorobo mchana ilimkuta Tunu akiwa katika eneo la Magomeni Mikumi, alikuwa ametulia ndani ya gari aina ya Toyota Prado alilolichukua kutoka kwa Victor, alikuwa akimsubiri Victor waliyekubaliana kukutana hapo.



    Kwa kiasi fulani alikuwa amefarijika moyoni mwake baada ya kuanza kupata mwanga wa kile kilichomsumbua kushindwa kukikamilisha kwa miaka mitatu. Katika mazungumzo yake na Winifrida aliweza kupata picha kamili ya nani waliomshambulia Joyce. Jambo lililomtatiza kwa nini walikuwa wanatumia nguvu kubwa kupambana na Sammy?



    Jambo moja alilolijua ni kwamba gari la Sammy aina ya Cadillac DeVille lilikuwa likimilikiwa na Omari Oduya, mtoto wa kwanza wa Mr. Oduya ambaye alikimbilia nchini Marekani baada ya kufanya mauaji akimuua aliyekuwa mpenzi wake, Layla Adil.



    Wakati huo Tunu alikuwa amerudi toka Israel na alipopata taarifa za mauaji ya Layla, aliumia sana kwa kuwa alimfahamu vyema Layla kwani walisoma darasa moja katika Shule ya Jangwani. Layla alikuwa chotara wa Kiarabu na mwonekano wake mzuri uliwafanya watu wengi kudhani alikusudiwa kuumbwa malaika badala ya binadamu!



    Tunu aliamua kufuatilia sakata hilo ili haki itendeke baada ya kuhisi polisi hawakujishughulisha na kesi hiyo kwa kuwa aliyefanya hivyo alikuwa mtoto wa mtu mzito. Kwa kuwa alikuwa na taaluma iliyohitajika sana ya Computer System Analysis alifanikiwa kujipenyeza na kupata kazi kwenye kampuni ya Mr. Oduya ya The Splendid Ltd.



    Alipofuatilia aligundua kuwa mapenzi kati ya Omari na Layla yalijaa ukatili na unyanyasaji ambao Layla alishindwa kuvumilia na kuamua kuachana na Omari. Chanzo cha haya yote ni Omari kutokukubali kuachwa.



    Omari alikuwa akimnyanyasa sana Layla kingono n ahata kwa vipigo na vitisho vya bastola kuwa angemuua. Miezi miwili kabla ya kifo chake Omari alimchukua kinguvu Layla na kumfungia ndani ya nyumba akimpa vipigo na akiwa hawezi kutoka nje. Tukio hilo liliwafanya ndugu wa Layla kuomba msaada kwa jeshi la polisi ili kumtoa ndugu yao ndani ya nyumba hiyo.



    Baada ya kufanikiwa kumtoa walipanga kumwondoa nchini na kumpeleka Kenya ili kusitisha uhusiano huo. Ni katika kipindi hicho Omari alimbembeleza sana Layla amrudie lakini Layla alimshauri atafute kwanza msaada wa kisaikolojia kama alitaka warudiane, kwa kuwa alimwona ni mtu wa hasira kila wakati, vipigo visivyoisha na mbaya zaidi akimtishia kumuua mara kwa mara, kitu ambacho siyo cha kawaida.



    Aliendelea kumtaka kuwa akishapata msaada wa kisaikolojia ndiyo angekuwa tayari kuwa naye tena ila kwa muda huo alitaka aachwe kwanza. Omari hakukubali, aliamua kuwatumia watu wa baba’ake; Dulla na Uledi kumteka Layla na hatimaye akatekeleza mauaji hayo. Kisha kwa msaada wa baba yake alitorokea nje ya nchi bila kutiwa nguvuni...







    Akiwa anaendelea kufanya kazi katika kampuni ya The Splendid Ltd aliweza kugundua mambo mengine zaidi ya kutisha kuhusu biashara za bilionea huyo, washirika wake na mikakati yake ya kutaka kuingia ikulu kwa gharama yoyote ile. Aliweza pia kubaini suala la mateso n ahata mauaji ya wote waliojitokeza kuwa tishio kwa maslahi ya bilionea huyo kama ilivyokuwa kwa Jaji Lutego.



    Mawazo yalizidi kupita kichwani kwa Tunu yakimkumbusha moja ya kumbukumbu mbaya sana iliyomfanya aape kuwa lazima siku moja Omari na baba yake Mr. Oduya walipe gharama za uhalifu wao na haki itendeke. Katika uchunguzi wake ndipo likaja sakata la memory card ambayo aliipoteza siku hiyo hiyo, ikaangukia mikononi mwa watu wa Mr. Oduya lakini sasa ilikuwa mikononi mwa Winifrida. Ni kitu kilichomsisimua zaidi. Memory card!



    Alishaanza kukata tamaa ya kuipata tena na wakati mwingine alidhani angetumia nguvu kubwa zaidi kuipata, lakini sasa alikuwa ameaminishwa na Winifrida kuwa ndiye aliyekuwa akiishikilia kwa wakati huo na kwamba alikuwa ameiacha kule nyumbani kwa Sammy, akiogopa kutembea nayo kwani ni kitu hatari kuliko hata hatari yenyewe.



    Jambo lililomuumiza zaidi kichwa Tunu kwa wakati huo ni jinsi ya kuipata tena hiyo memory card toka nyumbani kwa Sammy kabla haijaangukia tena kwenye mikono ya watu wengine. Alipaswa kuipata haraka iwezekanavyo kabla mtu mwingine hajaipata ila asingeweza kwenda nyumbani kwa Sammy na kuingia ndani pasipo msaada na uwepo wa Winifrida, ambaye kwa wakati huo alikuwa nyumbani kwa Elli na hakutakiwa kutoka nje.



    Pia Tunu asingeweza kumwambia Sammy kuhusu kadi hiyo kwa kuwa Winifrida alimsihi sana asimwambie Sammy juu ya uwepo wa kadi hiyo wala suala la yeye kumiliki simu ya mkononi.



    Tunu alijikuta akisisimkwa mwili kila alipoifikiria ile memory card akiamini kuwa endapo angeitia mkononi basi angekuwa na ushahidi mzito wa kumfanya Mr. Oduya na genge lake wasalimu amri kwani wasingekuwa na mahali pa kutokea.



    Muda wote wa mawazo yale Tunu alikuwa amejiegemeza kwenye siti ndani ya gari lakini macho yake yakiwa yanatazama nje ya gari. Alizungusha macho yake huku na kule kana kwamba alikuwa anatafuta kitu fulani. Alipokosa anachokitafuta, akafumba macho yake na kurejesha mawazo yake kwenye jukumu lililokuwa mbele yake.



    Alishtuka akaitazama saa yake ya mkononi, ilimwonesha kuwa dakika therathini na tano zilikuwa zimeshakatika tangu afike mahali hapo walipokuwa wamekubaliana kukutana. Dakika therathini na tano! Tunu alishtuka sana, muda huo kwake ulikuwa ni kama amesubiri kwa siku nzima. Hakuwa na muda wa kupoteza kwa sababu kwake muda ni mali ati!



    Aliendelea kuikodolea macho saa yake na kutingisha kichwa chake taratibu kushoto na kulia huku akisonya kwa masikitiko. Laiti ingekuwa ni saa ya kawaida angesema labda ina kasoro. Lakini saa yake, kama ilivyo kwa vitu vyake vingi, haikuwa ya mchezomchezo. Ilikuwa ni saa ghali aliyoinunua nchini Switzerland ikiwa na gerentii ya miaka hamsini.



    Hata hivyo, hakuwa na namna nyingine ya kufanya isipokuwa kuendelea kusubiri, akashusha pumzi za ndani kwa ndani na kutoa simu yake, akajaribu kumpigia Victor lakini mlio aliousikia toka upande wa pili wa simu ulimwonesha kuwa simu ile ilikuwa ‘busy’ muda wote. Tunu akashusha pumzi na kuanza kuperuzi kwenye mtandao wa intaneti akisoma habari maana tangu afike jijini Dar es Salaam hakuwa na mud ahata wa kusoma magazeti. Ingalau sasa alikuwa na kitu kilichokuwa kinamsogezea muda.



    Baada ya kama dakika kumi, akaliona gari aina ya BMW X6 xDrive 50i lililokuwa likija mbele yake katika barabara ile ya Mikumi likitokea upande wa Mwembechai, aliweza kulitambua vyema kuwa ndilo gari alilokuwa amemwachia Victor. Akamwashia taa mara mbili kama ishara ya kumjulisha kuwa amemuona. Victor naye aliwasha taa mara mbili kisha alimpita kidogo na kuliegesha nyuma ya gari alilokuwemo Tunu, takriban mita ishirini kutoka alipokuwa Tunu. Akashuka haraka na kumfuata Tunu.



    “Mbona umechelewa sana?” Tunu alimdaka Victor juu kwa juu baada ya kumfikia, alimuuliza huku akimtazama kwa makini pasipo hata kupepesa macho yake.



    “Nisamehe, nilikuwa na ishu fulani nyeti ya kumalizia. Pole sana kwa kusubiri,” Victor alijitetea huku akiachia tabasamu, akatazama kando kuyakwepa macho makali ya Tunu yaliyokuwa yanamtazama kwa makini pasipo kupepesa.



    “Dah, n’tafanyaje! Hata nikisema nikulaumu bado haitasaidia. Unajua nina mambo kibao ambayo natakiwa niyakamilishe leoleo, sijui kama nitaweza ku-meet deadline,” Tunu alisema huku akifungua mlango wa gari alilokuwemo na kushuka.



    “Kwani una mishemishe gani mjini, naona tangu umekuja uko mbiombio tu na wala hatuelezani!” Victor alimuuliza Tunu huku akimtazama kwa makini katika namna ya kumkagua.



    “Nitakueleza, ngoja kwanza niweke mambo fulani sawa kabla hayajaharibika,” Tunu alisema na kupokea ufunguo wa gari lake toka kwa Victor kisha akataka kupiga hatua kuelekea kwenye gari lake lakini akaonekana kukumbuka jambo na kugeuka, akamtazama Victor kwa makini.



    “Gari langu halijakuletea usumbufu wowote?” Tunu aliuliza huku akimkazia macho Victor.



    “Usumbufu wa vipi labda?” ilikuwa ni zamu ya Victor kuuliza, uso wake ulionesha mshangao.



    “Hakuna watu wowote waliokuwa wanakufuatilia?” Tunu aliuliza tena huku akiendelea kumkazia macho Victor.



    “Kunifuatilia kuhusu nini? Kwani kuna nini kinaendelea?” Victor naye aliuliza tena swali badala ya kujibu, akaongeza, “Inaonesha una vitu unavijua lakini hutaki kunishirikisha!”



    “Nitakwambia siku nyingine, ngoja niwahi sehemu,” Tunu alisema na kuanza kuondoka lakini Victor akamzuia. Wakatazamana moja kwa moja machoni kama vile walikuwa wanasomana mawazo yao.







    “Dah! Naona sasa hivi hatuaminiani tena, mshikaji wangu! You don’t trust me any more,” Victor alilalamika huku akiendelea kumkazia macho Tunu.



    “Don’t be silly... you know the rule of the game. Muda mwafaka ukifika utayajua yote unayotaka kuyajua,” Tunu alisema huku akitaka kuondoka lakini Victor aliushika mkono wake, safari hii aliung’ang’ania.



    Wakatazamana tena kwa kitambo fulani kisha Victor akashusha pumzi na kuachia tabasamu. Halikuwa tabasamu la furaha bali lilikuwa limeficha kitu fulani kisichoeleweka ndani yake.



    “Okay! Nakutakia mafanikio mema, ukihisi unanihitaji unajua wapi pa kunipata,” Victor alisema huku akiendelea kutabasamu.



    Tunu alimtazama Victor kwa umakini zaidi, alihisi kugundua kitu kama kebehi katika sauti yake. Naam, aliweza hata kuiona waziwazi katika macho yake ambayo yalikuwa yakimdhihaki waziwazi ingawa mdomo wake ulikuwa hauna dhihaka yoyote.



    “Haina shida, nitakutafuta,” Tunu alimjibu kwa sauti tulivu kisha akauondoa mkono wake toka kwenye mikono yenye nguvu ya Victor na kuanza kupiga hatua kuelekea kwenye gari lake. Akasita tena baada ya kuhisi kulikuwa na mtu mwingine wa tatu aliyekuwa anawatazama kwa makini.



    Tunu aligeuza shingo yake kuangalia upande wake wa kushoto alikokuwepo yule mwanamume, akamwona mwanamume mmoja mwenye mwili alioshiba akiwa ameketi kwenye kiti cha plastiki katika kibanda cha muuza chipsi. Alikuwa amevaa suti maridadi nyeusi, miwani mikubwa myeusi ya jua iliyoyafunika macho yake na kofia kubwa ya pama. Tunu alimtazama kwa makini lakini hakuweza kumtambua.



    Mwanamume yule alikuwa ametulia tuli kwenye kiti chake akiwa ameshika gazeti la Kiingereza la Daily News akionekana kujisomea gazeti lakini Tunu aliweza kugundua kuwa hakuwa akilisoma lile gazeti bali macho yake yalikuwa yakiwatazama kwa kuwachunguza. Mbele ya yule mtu kulikuwa meza ndogo ya plastiki ikiwa na sahani yenye mabaki ya chipsi iliyokuwa tupu na chupa ya soda. Tunu akashangaa sana, kwani kwa muda wote aliokuwa akisubiri eneo lile hakuwa amemwona yule mtu.http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    “Unamjua?” Tunu alimuuliza Victor kwa sauti ya kunong’oneza huku akimwoneshea kwa ishara mahali alipoketi yule mtu. Victor aligeuza shingo yake na kumtazama yule mwanamume mara moja tu na kisha kuurejesha uso wake kwa Tunu, akatingisha kichwa chake taratibu kukataa.



    “Sidhani kama ana lolote la maana la kutufanya tumzingatie, au wewe umeona nini cha ajabu kwake?”” Victor alisema huku akishusha pumzi. Hata hivyo, Tunu aliweza kugundua kitu fulani kisicho cha kawaida kwenye sauti na macho ya Victor. Fadhaa.



    Tunu akajifanya kutabasamu na kuzungusha macho yake kutazama sehemu nyingine ingawa akili yake ilikuwa kwa yule mwanamume. “Kuna ubaya wowote mtu kuchukua tahadhari?” akamuuliza Victor huku akishusha pumzi.



    “Hakuna ubaya. Nadhani inapendeza zaidi kuwa na tahadhari kwa kila jambo,” Victor alisema na kuachia tabasamu pasipo kuonesha meno yake kisha akaingia ndani ya gari lake na kuwasha injini. “Okay, basi tutawasiliana,” alisema na kuondoa gari pasipo kusubiri jibu la Tunu.



    Tunu alizidi kushangaa, alishusha pumzi na wakati huo akili yake ilikuwa inafanya kazi haraka haraka. Alijiuliza yule mwanamume ni nani na kwa nini alionekana kuwachunguza? Kwa nini Victor anaonekana kubadilika na kwa mara ya kwanza kuzipuuza hisia zake? Tunu alihisi kuwepo kwa kitu kisicho cha kawaida kwa Victor. Alihisi kuona kitu kisicho cha kawaida, ila hakujua aliona nini.



    Akaelekea kwenye gari lake na kuingia kisha akatulia kwenye usukani wake kwa dakika kadhaa akimchunguza yule mwanamume. Mara akamuona akiitazama kwa makini simu yake ya mkononi iliyokuwa inaita kisha akaipokea na kuipeleka sikioni. Aliongea kwa sekunde kadhaa na kuonesha mshtuko, akageuza shingo yake na kutazama kwa wizi kule lilikokuwa gari la Tunu, kisha akabetua kichwa chake na kuinuka.



    Tunu aliendelea kutulia kwenye siti yake akimfuatilia yule mwanamume kwa kila hatua aliyokuwa akiifanya, akamwona akijinyoosha kisha akawa anazungumza na kijana muuza chipsi huku macho yake yakiwa makini kumtazama Tunu. Tunu alichukua simu yake lakini kabla hajafanya chochote akamtupia tena jicho yule mwanamume, hakumwona! Tayari alikuwa ametoweka, na wala Tunu hakujua amelekea wapi.



    Aliminya midomo yake, akawasha gari na kuondoka. Alikuwa anaelekea hospitali ya Amana kuonana na Sammy ili ampe tahadhari kutokana na mambo fulani aliyoyagundua. Aliingia barabara ya Kawawa na mwendo wake ulikuwa wa wastani huku akiwa makini kuangalia nyuma kama kulikuwa na gari lolote alilolitilia shaka likimfuatilia lakini hakuona. Akashangaa.



    Aliendesha akilivuka bonde la Kigogo, bado mwendo wake ulikuwa ni wa wastani hadi alipofika kwenye mzunguko wa barabara za Kawawa na Kigogo akaamua kuiacha barabara ya Kawawa na kungia kushoto akiifuata barabara ya Kigogo iliyokuwa inapita jirani na Shule ya Msingi Gilman Rutihinda, akachunguza nyuma yake. Hakuona gari lolote lililokuwa linamfuatilia. Akashtuka.



    Akahisi kuwa jambo hilo halikuwa la kawaida. Hakujua ni nini kilikuwa kinaendelea lakini hisia zake zilimtanabahisha kuwa hali haikuwa shwari kama alivyotaka kujiaminisha. Siku zote hakupenda kuzipuuza hisia zake, alichukua simu yake na kumpigia Tom, akamweleza kuhusu alichokuwa akihisi na kumpa taarifa za mambo mengine yote kuwa yalikuwa yameenda kama yalivyopangwa.







    Waliongea kwa dakika kadhaa kisha wakakubaliana, alipokata simu akabadili uelekeo, badala ya kuelekea hospitali ya Amana akaelekeza gari lake eneo la Shaurimoyo, Ilala.



    * * * * *



    Sammy na Jengo walipoondoka pale hospitali ya Amana na kuwaacha Madame Norah na Bi. Pamela, walielekea moja kwa moja katika mgahawa wa kisasa wa Elli’s ili kupata chakula. Wakati wakienda huko hawakujua kuwa walikuwa wanafuatwa. Kulikuwa na gari jingine aina ya Toyota Vanguard jeusi lenye vioo vya tinted visivyomruhusu mtu kuona ndani lilikuwa linawafuatilia.



    Walipofika hapo Elli’s Sammy aliegesha gari lake kwenye maegesho, wakaingia ndani ya mgahawa na iliwachukua dakika arobaini na tano kupata chakula na kutoka nje tayari kwa safari ya kuelekea kwenye makazi ya Sammy. Waliagana na Elli kwa ahadi ya kumpitia pale kwenye mgahawa muda wa jioni wakati wanaelekea hospitali ya Amana.



    Wakajipaki kwenye gari lao walilokuja nalo na kutimka eneo hilo. Dakika takriban mbili tu tangu waondoke, lile Toyota Vanguard likawashwa na kuanza kuwafuatilia, lakini wakiwa na tahadhari zote, hadi walipofika nyumbani kwa Sammy eneo la Tabata Chang’ombe.



    “Karibu sana, baba,” Sammy alimkaribisha baba mkwe wake, Jengo mara tu walipoingia ndani.



    “Ahsante sana, mwanangu,” Jengo alijibu huku akijipweteka juu ya sofa. Alionekana kuchoka sana na macho yake yalikuwa yamelewa kutokana na kukosa usingizi.



    Sammy aliyabeba mabegi waliyokuja nayo na kuelekea vyumbani akiyapeleka kwenye chumba maalumu cha wageni akimwacha Jengo mpweke. Baada ya kama dakika tano hivi alirejea na kumkuta Jengo akinyemelewa na usingizi pale pale sebuleni kwenye sofa. Miguu yake alikuwa kainyoosha. Alikuwa mchovu aliyechoshwa na mambo mengi, usingizi, safari na mawazo juu ya hali ya binti’ake Joyce.



    Sammy alimwangalia kwa makini akamhurumia kisha alimwamsha na kumwelekeza chumba ili akajipumzishe kisha yeye alielekea chumbani kwake na kuingia moja kwa moja bafuni ili kupooza mwili wake. Alijimwagia maji harakaharaka kisha akajirejesha pale sebuleni ambapo alishangaa kumkuta mkwe wake akiwa bado ameketi palepale, sasa usingizi ulikuwa umemchukua kabisa.



    Sammy hakutaka kumwamsha, akaketi na kuwasha runinga huku akiweka sauti ndogo akichelea kumwamsha mkwewe. Si kwamba alikuwa anatazana runinga hiyo bali ilikuwa inampa tu ‘kampani’ na kujaribu kumsahaulisha huzuni ya mkasa uliomkuta mkewe. Alijaribu kuwaza mambo kadhaa kuhusu mkasa ule, mara akahisi sauti hafifu ya kishindo ndani ya uwa wa nyumba yake.



    Alinyanyuka haraka akatazama dirishani na kisha mlangoni, hakuona mtu. Akaelekea upande wa mlango wa jikoni, patupu! Akatoka nje na kuzunguka kuelekea upande wa mbele alipoegesha gari lake, akabaini kulikuwa na sauti ndogo ya kubipu. Alipata shaka, akatazama huku na kule akisaka na baada ya sekunde kama tano hivi akabaini kulikuwa na kitu fulani kimepachikwa kwenye gari! Akahisi kuwa eneo lile halikuwa salama.



    “Bomu!” Sammy akawaza, na hapo akili yake ikafanya kazi haraka sana. Alirudi ndani haraka, akamshtua Jengo kuhusu uwepo wa bomu, wakatoka na kukimbilia upande wa nyuma wa ile nyumba kulikokuwa na geti dogo la dharura. Muda huo bomu lilikuwa limebakia kama sekunde tano tu kulipuka. Hata hivyo alibaini kuwa wasingeweza kufanikiwa kufungua lile geti na kutoka ndani ya muda.



    “Baba, lala chini!” Sammy alimwamuru baba mkwe wake huku yeye mwenyewe akijitupa chini na kulala kifudifudi. Sekunde mbili baadaye ukasikika mlipuko mkubwa na kuisambaratisha kabisa nyumba ya Sammy. Sammy na Jengo wakaangukiwa na mabaki ya ile nyumba. Fahamu zikawapotea.



    * * * * *



    Gari la kifahari aina ya Range Rover Velar la rangi nyeupe liliingia kwenye geti la kuingilia la hospitali ya Amana na kuelekezwa moja kwa moja kwenye viunga vya maegesho, likaegeshwa. Mr. Oduya na Mr. Mafuru wakashuka toka ndani ya gari na kuanza kukatiza eneo lile la maegesho. Mr. Mafuru alitoa simu yake na kumpigia Madame Norah.



    “Madame, tayari tumeshafika hapa hospitali ya Amana, uko sehemu gani?” Mr. Mafuru aliongea baada ya simu kupokelewa.



    “Njooni hapa kwenye mgahawa, mtatukuta tumeketi hapa,” Madame Norah alisema na mara simu ikakatwa.



    Wakati wakielekea pale kwenye mgahawa kama walivyoelekezwa na Madame Norah, simu ya Mr. Oduya ikaanza kuita. Aliitoa na kuiangalia, akashusha pumzi na kuminya midomi yake, kisha akaipokea na kuiweka moja kwa moja sikioni. “Hallo!”



    “Mzee, tayari kazi imeisha. Nimeshatekeleza ule mpango mzima na hakuna kilichotoka ndani,” sauti toka upande wa pili wa simu ikasikika.



    “Umehakikisha haujaacha kielelezo chochote?” Mr. Oduya akauliza kwa sauti iliyoonesha wasiwasi ili kupata uhakika.



    “Usiwe na wasiwasi, mkuu, kila kitu kimekwenda kama kilivyopangwa. Bado yule malaya tu,” mtu upande wa pili wa simu alijibu kwa kujiamini.



    “Vizuri, lakini kumbuka yule ni mtu hatari mno na wewe kazi hii ni mpango wa kando, kosa lolote hata dogo linaweza kukugharimu na kitakachofuata kinaweza kuwa kibaya siyo kwako tu, bali kwetu sote, sijui umenielewa?” Mr. Oduya alisema huku akipiga hatua taratibu.



    “Kwa hilo wala usijali, mkuu. Niko makini sana,” alisema yule mtu na simu ikakatwa. Mr. Oduya akaachia tabasamu na kutembea haraka kwa kujiamini akimfuata Mr. Mafuru aliyekuwa ametangulia mbele.



    Walipotokea jirani na mgahawa wakamwona Madame Norah aliyekuwa anapunga mkono wake kuwaonesha mahali alipoketi akiwa ameketi na mwanamke mwingine ambaye hawakuweza kumtambua. Mr. Oduya na Mafuru wakamfuata, wakawasalimia wote huku wakiwapa pole kwa mkasa ule uliotokea.





    “Pole sana, Madame... poleni kwa mkasa huu wa kusikitisha!” Mr. Oduya alisema huku akimkumbatia Madame Norah katika hali ya kumfariji kisha akaanza kumpetipeti mgongoni.



    “Nashukuru sana, Mr. Oduya. Nawashukuruni nyote kwa kuja kunifariji katika kipindi hiki kigumu sana. Kwa kweli tukio hili limeniumiza mno kuliko maelezo!” Madame Norah alisema huku machozi yakimlengalenga machoni.



    Mr. Oduya na Madame Norah wakaachiana na wote wakaketi kwenye viti. Madame Norah akamtambulisha Bi. Pamela kwa Mr. Oduya na Mafuru, kuwa ni mdogo wake na ndiye mama aliyemlea Joyce tangu utoto wake.



    “Okay! Nice to meet you, poleni sana kwa mkasa huu, naamini Mungu atamsaidia mgonjwa aweze kupata nafuu” Mr. Oduya alisema huku akimpa mkono Bi. Pamela.



    “Amen, baba!” Bi. Pamela aliitikia huku akimpa mkono Mr. Oduya. Wakasalimiana.



    “Vipi kuhusu hali ya mgonjwa? Inaendeleaje?” Mr. Oduya alimuuliza Madame Norah huku sura yake ikionesha simanzi ingawa moyoni mwake hali ilikuwa tofauti.



    “Hadi sasa hali yake siyo nzuri, bado hajaweza kuamka,” Madame Norah alisema kwa huzuni huku akilengwa na machozi.



    “Nimekufahamu kwa miaka mingi lakini sikujua kama una mtoto!” Mr. Oduya alimwambia Madame Norah huku akimtazama kwa makini. “Kwani alikuwa anaishi hapa hapa Dar es Salaam?”



    “Hapa hapa Dar es Salaam, kwa sasa ndiye ninayemwandaa kwenye shughuli zangu zote, na hata lile tamasha letu ni yeye anapaswa alisimamie. Kwa sasa nimechanganyikiwa wala sijui itakuwaje!” Madame Norah alisema kwa huzuni huku akifuta machozi yaliyoanza kumtoka kisha akashusha pumzi.



    “Oh! Pole sana...” Mr. Oduya akasema kisha akaendelea. “Ni nani hasa waliofanya unyama huu?”



    “Hadi sasa bado haijajulikana, lakini naamini siku zao zinahesabika,” Madame Norah alisema kwa uchungu mkubwa huku akionekana kutoneshwa kidonda cha majonzi.



    “Kwa vyovyote hawa waliofanya hivi hawana roho ya ubinadamu hata chembe. Hivi umejaribu kutafakari lengo lao hasa lilikuwa nini?” Mr. Oduya aliuliza ili kutaka kujua huku akiyatuliza macho yake kwenye uso wa Madame Norah.



    “Kwa inavyoonekana mlengwa wa tukio lile alikuwa ni mumewe Joyce, Sammy, bahati yake hakuwepo nyumbani muda huo,” Madame Norah alisema kisha akayapandisha juu mabega yake na kuyashusha papo hapo.



    “Kwani huyo Sammy kawakosea nini hao watu! Jeje hajakwambia kama ana fununu zozote kuhusiana na jambo hili?”



    “Anasubiri ripoti ya polisi. Hata hivyo kama kuna watu kawakosea au hajawakosea siyo ishu maana katika hii dunia tunayoishi mtu huwezi kukosa adui hata kama hujamkosea mtu yeyote. Mwingine anaweza kukuchukia tu bila sababu,” Madame Norah alisema na kuinamisha kichwa chake chini.



    “Inasikitisha sana kwa ukatili huu kufanyiwa mtu asiye na hatia kama Joyce...” Mr. Mafuru alisema kwa huzuni huku akimtupia jicho la chati Mr. Oduya.



    “Kwa kweli hawa watu wanatakiwa wasakwe hadi wapatikane na wafundishwe adabu. That’s why I’m here to help you,” Mr. Oduya akadakia kumwambia Madame Norah kwa sauti tulivu.



    “Msijali, shemeji zangu... nawahakikishia hawa watu watapatikana tu wherever they are. Kama walizoea kuwafanyia wengine mambo haya basi hapa wamekanyaga waya wa umeme wakiwa pekupeku, hawatachukua hata round,” Madame Norah alisema kwa hasira huku akipigapiga ngumi juu ya paja lake na kuwafanya Mr. Oduya na Mafuru waangaliane. Macho yao yaliweza kuongea mengi zaidi ya ambavyo angeongea kwa mdomo.



    “They will all pay! They must pay for what they did to my daughter!” Madame Norah aliongeza huku akiyasaga magego yake kwa hasira.



    “Brave woman, you and me we’ll meet later and have a nice talk,” Mr. Oduya aliwaza huku akimtazama Madame Norah kwa hisia kisha akalazimisha tabasamu.



    “Unajua wewe kwa sasa ni mshirika wangu, yeyote anayekufanyia ubaya basi kanifanyia mimi pia. Kuanzia sasa tuko vitani kuhakikisha hawa watu wanapatikana. Kwa hiyo naomba ukipata taarifa zozote nyeti nijulishe, nitatumia hata rasilimali zangu kuhakikisha wanatiwa nguvuni na kuozea jela,” Mr. Oduya alisema kwa uchungu.



    Muda huo huo simu yake ya mkononi ikaanza kuita. Aliitazama kwa makini na kukunja sura yake kisha akamtupia jicho Mafuru na kushusha pumzi huku akisimama na kujitenga kidogo na wengine ili aweze kuongea kwa uhuru na simu ile aliyodai ni ya muhimu sana.



    Baada ya dakika mbili za kuongea na simu sura yake ilibadilika sana, alionekana ni mtu mwenye wasiwasi mkubwa tofauti na alivyokuwa mwanzo. Alirudi pale kwenye meza na kuwaaga Madame Norah na Bi. Pamela akiwaeleza kuwa kulikuwa na jambo la dharura lililojitokeza na alitakiwa kwenda kulishughulikia haraka.



    Wakaaga na kuondoka wakimwahidi Madame Norah kuendelea kuwasiliana ili kujua maendeleo ya mgonjwa.



    * * * * *



    Honi ya gari aina ya BMW X6 xDrive 50i ililia mara mbili mbele ya geti la nyumba moja iliyopo katika mtaa wa Sonega eneo la Shaurimoyo, Ilala. Kijana mmoja mtanashati mwenye mwili wa kimazoezi akachungulia nje na kuliona lile gari kisha akaachia tabasamu na kufungua geti haraka, lile gari likazama ndani. Yule kijana ni Tom.



    Muda huohuo wanaume wengine wawili wakatokea wakiwa tayari wameshika vifaa maalumu kwa ajili ya kuanza kazi ya uchunguzi, wakamtazama Tunu kwa macho ya kuuliza.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Ninahisi gari hili limewekwa GPS device ili kuni-track waweze kujua kila ninapokwenda,” Tunu alisema.



    Wale wanaume wakaanza kulikagua gari wakianzia kwenye sehemu za ndani ambazo magurudumu hufungwa kuona kama vifaa vya GPS vilikuwa vimepachikwa lakini hawakuona kitu, inaaminika kuwa kwa vyovyote mtu mtaalamu wa mambo hayo asingeweza kufunga kifaa kama hicho sehemu hiyo.



    Wakafungua boneti la gari na kuchunguza kila sehemu kwa uangalifu sana, walikagua injini nzima kwa kutumia kioo maalumu na tochi lakini hawakuona chochote. Wakachunguza chini ya gari wakiiangalia injini kutokea chini hadi juu lakini hakukuwa na kifaa chochote cha GPS. Wakafungua siti za gari na kuangalia chini, pia hakukuwa na chochote.



    Walipokosa maeneo yote hayo wakaondoa redio kwenye dashbodi na kuchunguza kwa ndani na kila sehemu, hakukuwa na kitu. Kisha wakaondoa paneli za milango na kava za spika na kuchunguza. Walipokosa wakaangalia kwenye mikono ya milango (handles) na kwenye vifungo vyake, wakakiona kifaa kimoja cha GPS kilichokuwa kimewekwa kitaalamu sana kwenye kifungo cha mkono wa mlango wa kushoto, kiasi cha kumfanya mtu asiye mjuzi wa mambo hayo asiweze kugundua.







    Tunu na Tom wakaangaliana, macho yao yaliweza kuongea mengi kuliko ambavyo wangeweza kuongea kwa midomo yao kisha Tunu akashusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “You were right! Ulikuwa umechezewa mchezo ili waweze kujua kila unapokwenda,” Tom akasema huku akiweka mikono yote miwili kwenye kiuno chake. Alikuwa anatweta.



    “I dont believe this, Victor ndiyo kaamua kunichezea mchezo, siyo? I knew it!” Tunu alisema kwa sauti tulivu lakini iliyobeba hasira ndani yake huku akimtazama Tom. Aliuma midomo yake na kushusha pumzi kisha akabetua kichwa chake huku akijitahidi kudhibiti hasira zake.



    “Hivi huyu ni Victor yupi?” Tom akauliza huku akimtazama Tunu kwa makini.



    “Nitakuelezea baadaye, I truted the guy lakini kumbe ni nyoka! Hata sijui kwa nini roho yangu ilikuwa nzito sana kumweleza chochote kuhusiana na mambo haya japo alikuwa ananiuliza maswali mengi sana yaliyonifanya kuanza kuwa na shaka kidogo!” Tunu akasema na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.



    Wale wanaume wa kazi walimaliza kazi yao kulikagua lile gari kwa makini katika kila sehemu waliyodhani kungeweza kufichwa kifaa cha GPS na hakuona kifaa kingine. Wakampatia Tunu kile kifaa walichoking’amua, Tunu akakitazama kwa makini na kuachia tabasamu la uchungu, kisha akabana taya zake na kuanza kukereza meno yake huku akizuia hasira zilizoanza kumpanda.



    “Sasa nitawafanyia uhuni ambao hawajawahi kufanyiwa, ninakwenda kukitelekeza hiki kifaa Central Police, hapo ndipo watakapofurahi na roho yao!” Tunu alisema kisha wote wakaangua kicheko. Alitoka nje na kuwaacha wanaendelea kurudishia vitu vyote kwenye gari kwa usimamizi wa Tom, yeye akakodi pikipiki na kuelekea moja kwa moja Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam.



    * * * * *



    Magari mawili ya zimamoto na ving’ora vya magari ya polisi yalionekana yakielekea katika mtaa ilipokuwa nyumba ya Sammy, eneo la Tabata Chang’ombe yakiwa katika mwendo wa kasi. Yalipofika kazi ya kuuzima moto ilianza harakaharaka ili kuzuia moto ule usiweze kusambaa katika nyumba za jirani na kusababisha maafa zaidi na baada ya muda mfupi juhudi zao kuuzima moto huo zikaonekana kufanikiwa.



    Nyumba ya Sammy ilikuwa imebomoka na kubaki kama gofu huku gari lake aina ya Cadillac DeVille likiwa limeteketea kabisa na kubakichuma chakavu.



    Ndani ya muda mfupi barabara zote za kuingia na kutoka katika mtaa ule zilikuwa zimewekwa kizuizi cha askari na eneo la nyumba ya Sammy likazungushiwa utepe maalumu wa njano maarufu kama Barricade tape wenye maandishi ya “Police Line Do Not Cross”. Kila mtu aliyetaka kupita eneo lile alisimamishwa, akahojiwa na kama alionekana hahusiki basi alizuiwa kupita.



    Dakika zilizofuata eneo lote lilijaa magari, yakiwemo ya polisi, mawili ya jeshi la wananchi na magari mawili ya wagonjwa yaliyokuwa yameegeshwa kandokando ya barabara kulizunguka eneo lile huku askari wenye silaha wakishika doria kulinda iwapo kungetokea vibaka waliotaka kupora. Askari wale walikuwa makini sana wakizungusha macgo yao pembe zote. Pia walikuwepo wataalamu wa mabomu toka jeshini waliokuwa wakikagua eneo lote kuona kama kulikuwa na mabomu mengine ambayo hayajalipuka.



    Makundi mbalimbali ya watu yalikuwa yamekusanyika katika eneo lile, watu hao, wakubwa kwa wadogo, walikuwa wanashangaa na wengine wakisimuliana jinsi walivyoshuhudia mlipuko mkubwa ulioliteketeza kabisa gari la Sammy na kubomoa ile nyumba. Hakuna kati yao aliyekuwa anaruhusiwa kusogea karibu na eneo ambalo mlipuko huo au kuvuka uzio uliokuwa umewekwa kwa hofu kuwa huenda kulikuwa bado na masalia ya mabomu mengine.



    Kati ya watu waliokuwepo eneo lile wakionekana kushangaa ni mwanamume mmoja mrefu mwenye ndevu nyingi aliyekuwa amevaa suti nzuri ya rangi ya hudhurungi na viatu vyenye rangi hiyo hiyo. Alitembea kwa hatua za wastani, macho yake yakilenga zaidi kuangalia kwenye kifusi cha nyumba kuona kama kulikuwa na majeruhi yeyote wa lile tukio. Alipobakiza kama hatua mbili kuufikia ule uzio wa njano wenye maandishi ya “Police Line Do Not Cross” alijitoa katika kundi la watu wengine, akajiegemeza ukutani mwa duka moja la Mangi.



    Alisimama pale akawa anashangaa huku akijaribu kuuliza kama kuna mtu yeyote aliyeokolewa kwenye lile tukio akiwa hai. Hakuna aliyejishughulisha naye kwani wote aliokuwa akiwauliza na wao walikuwa wamefika hapo muda mfupi tu kabla yake, akatoa sigara yake na kuwasha kisha akawa anavuta taratibu huku akiangaza macho yake pembe zote, kisha akayatuliza kwa wanajeshi wa kutegua mabomu na askari wa uokoaji ambao walikuwa wanafukua kifusi kuona kama kulikuwa na mtu yeyote aliye hai.



    Muda huohuo gari la Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam likaingia. Naibu Kamishna Ramon Mamboleo akashuka haraka toka kwenye gari lake na kuanza kutembea kwa ukakamavu huku akiangaza macho yake pembe zote kama aliyekuwa anachunguza kitu. Alikuwa askari makini sana na mkakamavu asiyeruhusu makosa ya kipumbavu yaliyoashiria uzembe yatokee awapo kazini.



    Kabla ya kupandishwa kuwa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna Mamboleo alikuwa Mkuu wa Upepelezi. Hakuwa na mzaha kabisa awapo kazi, angeweza kumfuatilia hata shetani katika harakati zake za kuharibu Amani au maadili mema ya wana wa Mungu na akamtia mbaroni kisha akamburuza mahakamani, tena peke yake.







    Waandishi wa habari waliokuwepo eneo lile walianza kumzonga wakitaka kupatiwa maelezo ya tukio zima: ni nani washukiwa wa uhalifu huo kwani mlolongo wa matukio hayo ulionekana kuikumba familia ile katika kipindi kisichozidi saa kumi nan ne. Usiku watu wasiojulikana walivamia nyumba na kumpiga risasi mke wa Sammy, na sasa wamerudi tena na kutega bomu, nadhani wakikusudia kumuua Sammy mwenyewe ambaye hadi wakati huo haikujulikana kama yupo hai au amekufa.



    Kamishna Mamboleo, kutokana na kuchanganyikiwa hakupenda kuongea hata na mmoja wao. Aliwaomba wawe wavumilivu, wasubiri kwanza ripoti ya wataalamu wa upelelezi, aidha, hakuwaruhusu hata askari wake mmoja aongee na mwandishi wa habari yeyote juu ya matukio hayo.



    Wakati huo askari wengine wa upelelezi walikuwa wakiwahoji majirani na baadhi ya wapita njia waliodai kushuhudia tukio hilo. Watu saba, wakiwamo Godlove Nyari maarufu kama Mangi aliyekuwa na duka katika mtaa huo na mwanafunzi mmoja wa shule ya sekondari aliyekuwepo dukani kwa Mangi wakati mlipuko huo unatokea walihojiwa na polisi.



    Katika watu hao saba, wanaume watano, mwanamke mmoja na yule mwanafunzi walipohojiwa na askari wa upelelezi, watatu akiwemo yule mwanafunzi walikiri kuliona gari moja aina ya Toyota Vanguard jeusi lenye vioo vya tinted visivyomruhusu mtu kuona ndani likifika eneo lile dakika tano tu baada ya gari la Sammy kuingia, na mtu mmoja mwanamume aliyekuwa amevaa kofia pana ya pama iliyoficha sura yake na miwani mikubwa ya jua alishuka toka ndani ya gari lile, kisha lile gari likaondoka.



    Baada ya hapo, yule mwanamume alionekana akiangalia huku na kule kama aliyekuwa akitafuta kitu kabla hajaondoka na kuambaa ambaa na ukuta wa nyumba ya Sammy, akaelekea upande wa nyuma wa nyumba. Hata hivyo, watu wote waliomwona yule mtu hakuna aliyemfuatilia kujua alikuwa anakwenda wapi kwa kuwa hawakujua kama alikuwa na lengo baya.



    Baada ya maelezo, wale askari wa upelelezi waligundua jambo ambalo lingeweza kuwaongoza katika upelelezi wao kwenye maelezo watu wawili tu, Mangi na yule mwanafunzi wa sekondari na waliwataka kwenda nao kituoni kwa mahojiano zaidi. Mkuu wa kitengo cha upelelezi wa Ilala, Inspekta Abel aliondoka nao, wakaelekea kituoni.



    Wakati huo huo wale askari wa uokoaji waliweza kugundua uwepo wa mtu katika kifusi baada ya kuona akihangaika kuinuka, lakini kwa kuwa alikuwa amekandamizwa hakuweza kuinuka. Kwa kushirikiana na wanajeshi wa kutegua mabomu walifanikiwa kumtoa yule mtu ambaye alikuwa na michubuko midogo midogo na hakuonekana kuwa na majeraha makubwa sana. Hata hivyo alikuwa analalamika maumivu mwilini.



    Kisha wakamwona mtu mwingine mwanamume akiwa pia amenasa kwenye kifusi. Huyu alikuwa amejeruhiwa eneo la kichwani na alionekana ama amekufa au amepoteza fahamu, lakini walipomchunguza kwa makini waligundua kuwa yeye pia alikuwa bado yupo hai. Haraka sana walileta machela wakambeba na kumkimbiza kwenye gari la wagonjwa, huku yule mwanamume mwingine akisaidiwa kutembea na kuingizwa kwenye gari lile lile la wagonjwa, kisha wakakimbizwa hospitali.



    Yule mwanamume mrefu mwenye ndevu nyingi aliyevaa suti ya hudhurungi aliwashuhudia wale watu wawili waliojeruhiwa, na aliamini kuwa mmoja wa watu hao ni Sammy, wakiondolewa pale na kuingizwa ndani ya gari la wagonjwa, kisha lile gari likaondoka toka eneo lile likisindikizwa na magari mawili ya polisi wenye silaha.



    Moyo wake ukapiga mshindo mkubwa! Sigara aliyokuwa anavuta ikadondoka. Alilitazama lile gari kama vile chui aliyejeruhiwa amtazamavyo mwindaji aliyemjeruhi. Akavuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu kisha alitoa simu yake ya mkononi na kuanza kuondoka eneo lile.



    Haukupita muda mrefu tangu tukio la kulipuliwa kwa nyumba ya Sammy litokee, habari zilizagaa karibu kila mahali jijini Dar es Salaam na hata nje ya jiji na nchi. Taarifa zilienea haraka kama moto wa kifuu kupitia mitandao ya intaneti, hasa mitandao ya WhatsApp na YouTube. Watu walitumiana picha na vipande vifupi vya video za tukio. Elli akiwa ofisini kwake aliziona taarifa zile za kushtusha baada ya kutumiwa picha na mmoja wa rafiki zake.



    “Oh my God!” Elli aling’aka kwa mshtuko mkubwa. Alijikuta akichanganyikiwa, akajaribu kumpigia simu Sammy lakini simu yake ilikuwa haipatikani. Akaingiwa na hofu kubwa huku hisia mbaya zikianza kumtawala juu ya usalama wa Sammy na familia yake. Hakutaka kusubiri, aliingia kwenye gari lake aina ya BMW X6 na kuondoka haraka, akaelekea eneo la Tabata Chang’ombe, nyumbani kwa Sammy.



    Akiwa katika eneo la Malapa Hostel aliona msafara wa magari matatu ukielekea upande wake kwa mwendo wa kasi huku magari mengine yakiwekwa pembeni, yeye pia alikaa pembeni na kuliona gari la wagonjwa lililokuwa katika mwendo wa kasi huku likisindikizwa na magari mawili ya polisi yakipita kuelekea hospitali ya Amana. Hata hivyo, Elli hakujishughulisha nao, yeye mawazo yake yalikuwa ni kufika nyumbani kwa Sammy tu, hivyo alikanyaga pedeli ya mafuta kuelekea Tabata Chang’ombe.



    Alipokaribia eneo hilo alishtuka baada ya kuona kulikuwa na ulinzi mkubwa askari wenye silaha waliokuwa wametanda eneo lile. Elli alihisi mwili wake ukiishiwa nguvu. Hata hivyo, hakutaka kuegesha gari lake pembeni, akazidi kusonga mbele huku moyo wake nao ukizidi kupiga mshindo mkubwa. Katika eneo lile kulikuwa na magari ya polisi na mengine yaliyokuwa yameegeshwa pembeni mwa barabara. Askari mmoja mwenye silaha akamsimamisha.



    “Unaelekea wapi, si unaona barabara imefungwa na hakuna mtu anayeruhusiwa kupita mtaa huu!” yule askari akamuuliza Elli kwa ukali huku akimkazia macho yake kwa makini.





    “Afande, mwenye nyumba iliyopata tatizo ni ndugu yangu, nataka kujua kama kuna mtu yeyote ameokolewa hai kutoka katika nyumba hiyo,” Elli alisema huku akishuka na kumkabili yule askari. Mwili wake ulikuwa unatetemeka kwa hofu na alikuwa akiomba Mungu jambo lile liwe ni ndoto tu.



    “Sijui kama atakuwa ni mmoja wa waliookolewa, hadi sasa tumepata watu wawili waliojeruhiwa, wote wanaume na tayari wamekimbizwa hospitali ya Amana, unaweza kwenda huko kuangalia kama yumo huyo ndugu yako. Mambo mengine ni kama unavyoyaona. Bado tunaendelea na zoezi la uokoaji kuona kama kuna chochote tunaweza kuokoa,” yule askari mwenye silaha alimwambia Elli kisha akaondoka eneo lile kwenda kuwazuia vibaka waliotaka kujipenyeza kwenda kuiba.



    Ilimchukua Elli takriban dakika kumi na tano akiwa bado amepigwa na butwaa, alikuwa amesimama pale pembeni ya barabara akiiangalia nyumba ya Sammy ilivyobomoka na kubaki kama gofu, gari lake lilikuwa halitamaniki kwani kilichoonekana pale ni chuma chakavu tu. Michirizi ya machozi ilionekana kwenye macho ya Elli na mikono yake ilikuwa kichwani.



    Baada ya dakika kumi na tano Elli alionekana kuzinduka, akatoa mikono yake kichwani na kufuta michirizi ya machozi, kisha akaliendea gari lake na kuingia, akatia moto na kuondoka eneo lile kwa mwendo wa kasi kama aliyepandwa na wazimu.



    * * * * *



    “Unawaza nini, Tunu?” Tom alimuuliza Tunu baada ya kumwona akiwa kimya kabisa amejiegemeza kwenye gari lake aina ya BMW X6 xDrive 50i huku akionekana kuzama kwenye lindi la mawazo.



    Tunu alionekana kuzinduka na kushusha pumzi ndefu, akamtazama Tom na kuachia tabasamu, hata hivyo tabasamu lake halikuwa la furaha kwani macho yake yalionesha wasiwasi fulani. “Kuna kitu bado kinanitatiza kidogo hapa,” Tunu alisema akiwa anatazama kifikra.



    “Najua, Tunu...” Tom alisema huku akiachia tabasamu kisha akaongeza. “Ni kuhusu hawa jamaa zetu, siyo?” alisema kwa sauti ya kunong’ona huku akigeuza shingo yake kutazama kule walikoingia wale wanaume waliokuwa wakikagua gari la Tunu.



    Tunu alibetua kichwa chake kukubali. “Kwa vyovyote watu wa Mr. Oduya watafuatilia hapa kujua kilichotokea, naogopa hawa jamaa wasije wakabanwa halafu wakaropoka kila kitu,” Tunu alisema huku usoni kwake akionesha shaka fulani.



    “Wala huna haja ya kuhofu kuhusu hawa jamaa. Ni watu wetu, tena watu wa kazi kwelikweli! Huwa tunawatumia pale idarani kama informers wetu katika oparesheni za hatari zinazohusisha uhalifu mkubwa,” Tom alisema.



    “Vipi kuhusu wenye jengo hili, hawawezi kubanwa wakasema?” Tunu aliuliza tena huku akiyatuliza macho yake kwenye uso wa Tom.



    “Hata wakija hapa hawawezi kukuta mtu, hili jengo halikaliwi na mtu. Ni mali ya Idara ya Usalama wa Taifa na ni maalumu kwa kazi maalumu...” Tom alisema na kushusha pumzi, kisha akaendelea, “Uliponipigia simu kunieleza kuhusu wasiwasi wako nami nikawapigia hawa jamaa na ndani ya dakika kumi tu wakafika hapa. Hivi sasa kwa kuwa wamemaliza kazi yao, wanasepa wala huwezi kujua wamepitia wapi.”



    Baada ya hapo walipanga ratiba ya shughuli zao, wakakubaliana kuongeza nguvu kwa kuwajumuisha wale jamaa waliokagua gari la Tunu, pamoja na kina Bob ili kupambana na watu wa Mr. Oduya. Kisha Tunu akaaga kuwa alikuwa anaelekea Hospitali ya Amana kuonana na Sammy.



    Tunu alijipakia kwenye gari lake, akawasha injini ya kulitoa nje, kisha akaliegesha kando ya barabara ya mtaa na kuonekana akiangaza macho yake kila pembe kuhakikisha usalama wake. Alitazama vioo vya pembeni vya kuangalia vitu vilivyo nyuma yake ili kuhakikisha usalama, punde akaliona gari moja aina ya Toyota Cresta gx100 jeupe likijiegesha nyuma kwa mbali kidogo.



    Alilitazama kwa makini lakini hakuona kama alipaswa kuwa na shaka, kwani mtaa ule wa Sonega na eneo lote la Shaurimoyo, Ilala lilikuwa ni eneo la pilika pilika na magari mengi yalifika hapo kutokana na uwepo wa maduka mengi ya kuuza vipuri vya magari. Tunu alishusha pumzi za ndani kwa ndani, akaendelea kuangazaangaza macho yake na kuridhika na hali ya pale nje.



    Akaandika ujumbe kwenye simu yake na kumtumia Tom, “Baadaye, hapa nje hali ni shwari!” alipomaliza akaondoa gari lake na kuingia barabara ya Shaurimoyo, akakunja kushoto na kujichanganya na msururu wa magari mengine.



    “Tumfuate!” mwanamume mmoja aliyekuwa ndani ya lile gari aina ya Toyota Cresta gx100 jeupe alisema baada ya Tunu kuondoka. Ndani ya lile gari kulikuwa na watu wawili, kumbe walikuwa wanamfuatilia Tunu.



    “Hakuna haja ya kumfuata, ngoja tuone nani mwingine atatoka humo ndani,” mwanamume mwingine aliyekuwa kwenye usukani alisema. “Tunachotakiwa kujua ni nani anashirikiana naye, basi!”



    Yule aliyekuwa ameketi kwenye usukani alikuwa ni Victor na alikuwa ameshika kamera ndogo akipiga picha eneo lile kwa tahadhari. Mara wakamwona Tom akitoka ndani ya lile jengo na kupiga hatua zake haraka haraka huku akitazama chini, kisha akazama kwenye gari moja na kuondoka zake.



    Wale watu waliokuwemo kwenye gari walimtazama kwa makini wakaonekana kumtambua, wakajikuta wakitabasamu.



    “Dah! Nilihisi kitu kama hiki kutokea, hatimaye tumepata jibu. Sasa ni Tom na Tunu!” Victor alisema kisha akaangua kicheko hafifu kilichokuwa kimebeba uchungu na hasira huku akimtazama mwenzake aliyekuwa amekaa kando. “Nadhani sasa umenielewa, siyo?”



    “Ulikuwa sahihi, Victor!” yule mwingine alisema huku akishusha pumzi ndefu.



    “Nilikwambia tuliza kimuhemuhe kila kitu kitajulikana...” Victor alisema na kuwasha gari lake, wakaondoka.



    * * * * *



    Jitihada za madaktari na wauguzi hatimaye zilikuwa zimezaa matunda, Joyce alikuwa amezinduka na alishangaa sana kuona akiwa katika chumba chenye mitambo mingi pamoja na computer, yeye akiwa amelala kitandani amevishwa mitambo maalumu ya kumsaidia kupumua. Alizungusha macho yake huku na kule na kuwaona wauguzi wawili wakiwa bize kuchunguza hiki na kile ndani ya chumba kile.







    Aliutazama mkono wake wa kulia uliokuwa umechomekwa sindano yenye mrija ambao ulipeleka damu kwenye mishipa yake ya damu, akashusha pumzi za ndani kwa ndani na kufumba macho yake kwa kitambo kifupi. Alipoyafumbua tena yalitua moja kwa moja kwenye uso wa muuguzi mmoja ambaye alikuwa amesimama jirani yake akirekebisha mwendo wa matone ya damu yaliyokuwa yakidondokea kwenye mrija uliopeleka damu kwenye mshipa wake wa damu.



    Joyce alishusha pumzi za ndani kwa ndani huku akiminya midomo yake. Alikuwa akiuhisi mwili kama si wake. Yule mhudumu aliyekuwa akimhudumia alipogundua kuwa Joyce alikuwa amezinduka aliachia tabasamu. Joyce alitaka kutabasamu lakini hakuweza, akayahamisha macho yake kumtazama muuguzi mwingine ambaye alikuwa amekaa mbele ya kioo kikubwa cha computer iliyokuwa ikionesha mwenendo wa mapigo ya moyo.



    Alimtazama yule muuguzi kwa makini kwa kitambo kifupi kisha aliyaondosha macho yake na kuyarudisha tena kwa yule muuguzi wa kwanza ambaye sasa alikuwa amesimama akimwangalia kwa upole, machozi ya huruma na furaha yalikuwa yakimlengalenga machoni.



    “Pole sana, Mungu atakusaidia dada’angu, utapona tu. Kwa kuwa umeamka ngoja niwaite ndugu zako!” yule muuguzi alisema akimwambia Joyce kwa sauti ya upole kisha akatoka kuelekea nje huku macho ya Joyce yakimsindikiza nyuma yake.



    Kule nje ya kile chumba yule muuguzi aliwakuta Madame Norah na Bi. Pamela wakiwa wameketi kwenye benchi, walionekana wenye sura za uchovu na simanzi na hawakujua hatma ya hali ya Joyce. Walishtuka kumwona yule muuguzi akiwajia huku amepambwa na uso wa tabasamu, kasha akawapa taarifa kuwa Joyce alikuwa ameamka.



    Wote waliinuka, wakakimbilia ndani. Madame Norah alikuwa wa kwanza kuingia mle wodini, akafuatiwa na Bi. Pamela aliyekuwa nyuma yake, wote walikuwa wana shauku ya kumwona Joyce na kuisikia sauti yake. Joyce alimwona Madame Norah, kabla hajajua afanye nini akamwona Bi. Pamela akiwa nyuma yake, akapatwa na mshangao mkubwa. Aliwatazama wote wawili kwa zamu huku akionekana kuwa na maswali mengi kichwani kwake.



    Alitamani sana kujua ni kwa nini alikuwa amelazwa ndani ya chumba kile chenye mitambo maalumu? Kwani ni nini hasa kilikuwa kimemtokea? Alijaribu kufikiria lakini akawa hakumbuki chochote. Madame Norah na Bi. Pamela walikuwa wamesimama hukuwakimwangalia kwa macho yenye upole yaliyojaa machozi ya furaha.



    Waliendelea kumtazama kwa makini kisha wakaangaliana na kushusha pumzi za ndani kwa ndani na kuinua mikono yao juu kumshukuru Mungu.



    Joyce alikuwa bado ana maswali lukuki kichwani, hakujua Sammy alikuwa wapi muda huo! Hakuwa amemtia machoni kabisa! Alijikuta akiingiwa na wasiwasi mkubwa. Alitaka kuinuka lakini akahisi maumivu makali sana eneo la kifuani na sehemu ya mgongoni. Madame Norah, kwa kushirikiana na yule muuguzi walimuwahi, wakamshika na kumzuia asiinuke.



    Joyce alitii na kutulia huku akiendelea kuwaangalia Madame Norah na Bi. Pamela kwa zamu. Akalazimisha tabasamu na kufumba macho yake.



    Wakiwa bado wamesimama pale wakamwona Daktari Mshana akiingia haraka, sura yake ilikuwa imesawajika kidogo na alikuwa anahema kwa nguvu. Alisimama, akawaangalia watu wote waliokuwemo mle ndani kisha macho yake yakatua kwa Joyce. Akaonekana kusita sana.



    “Madame!” Daktari Mshana alimwita Madame Norah, uso wake ulikuwa na wasiwasi.



    “Vipi dokta, kuna tatizo lolote?” Madame Norah aliuliza huku akiyatuliza macho yake kwenye uso wa Daktari Mshana.



    “Samahani kwa usumbufu, naomba tuongee kidogo hapo nje,” yule daktari alisema kwa wasiwasi kisha akatoka nje bila kusubiri jibu la Madame Norah.



    Madame Norah na Bi. Pamela wakaangaliana kwa mshangao na Madame Norah akanyanyua mabega yake juu na kuyashusha papo hapo, kisha akashusha pumzi na kutoka nje kumfuata yule daktari.



    “Sijui umepata taarifa kuhusiana na shambulio lililotokea mchana huu?” yule daktari alimuuliza Madame Norah huku akimtulizia macho yake.



    “Shambulio?” Madame Norah aliuliza kwa mshangao. “Shambulio gani, dokta?”



    “Ina maana hamjapata taarifa zozote za kuhusiana na shambulio lililotokea muda mfupi uliopita?” yule daktari akauliza tena huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Hapana hatuna taarifa zozote. Ni shambulio gani tena hilo?” Madame Norah alizidi kushangaa. Sasa alihisi jasho jepesi likianza kumtoka sehemu mbalimbali za mwili wake na mapigo ya moyo wake yakibadili mwendo wake na kwenda mbio isivyo kawaida!



    “Nyumba ya mume wa huyo mgonjwa wenu imeshambuliwa kwa bomu na watu wasiojulikana muda mfupi uliopita...” yule daktari alisema huku akifuta jasho usoni kwake kwa kitambaa.



    “Oh my God!” Madame Norah aling’aka kwa mshtuko mkubwa, “Ilikuwaje? Vipi watu wamesalimika kweli?” aliuliza huku akihisi ubaridi mkali wa woga ukimtambaa mwilini. Midomo yake ilikuwa inamchezacheza.



    “Mmoja hali yake ni mahututi, kiukweli kama ataweza kufika kesho asubuhi basi atapona, na hivi nilivyokuja kwako kuna utaratibu unafanywa apelekwe Muhimbili haraka...” yule daktari alisema, “Ila mwingine hali yake siyo mbaya, ana maumivu ya hapa na pale tu lakini hajaumia sana. Ndiye aliyenituma nije kukupa hizi habari.”







    Madame Norah alishindwa aseme nini tena, aliweka mikono yake kichwani huku michirizi ya machozi ikianza kuonekana kwenye macho yake. Alibaki kimya kwa kitambo kifupi akionekana kuwa mbali sana kifikra kisha akamwashiria yule daktari amsubiri palepale. Akafuta machozi na kuingia ndani huku akijitahidi kutokuonesha hisia zozote za majonzi ingawa uso wake ulisindwa kuficha ile hali ya kunyong’onyea. Mikono alikuwa ameikunjia kifuani.



    “Vipi, dada, kuna nini kimetokea?” Bi. Pamela alimuuliza Madame Norah huku akimtazama kwa makini.



    Madame Norah alimtupia jicho Joyce ambaye pia alikuwa anamtazama usoni, akashusha pumzi na kulazimisha tabasamu ingawa bado tabasamu lake halikuweza kuiondoa hisia ya majonzi usoni kwake. Alibaki amesimama akiwa kimya huku akionekana kutafuta neno la kumwambia Bi. Pamela kwani hakutaka kuongea mbele ya Joyce kwa kuhofia kumsababishia matatizo mengine.



    “Kuna nini?” Bi. Pamela aliuliza tena.



    “Kuna matatizo fulani yametokea ofisini kwangu, nahitajika kwenda mara moja kuyashughulikia. Sasa njoo tuongee mara moja,” Madame Norah alimwambia Bi. Pamela aliinuka na kumfuata, wakatoka nje ambako walimkuta Daktari Mshana akisubiri.



    “Sasa sikiliza, naomba uwe jasiri kwa hiki ninachokwenda kukwambia, sawa...” Madame Norah alianza kusema, “Nyumba ya mkweo Sammy imeshambuliwa na watu wasiojulikana wakati wao wakiwamo ndani...” Madame Norah alisema kwa sauti ya kumtetemeka.



    “Mungu wangu! Wamesalimika kweli?” Bi. Pamela aliuliza kwa huku akihisi mwili wake ukiishiwa nguvu.



    “Nimeambiwa mmoja wao yupo mahututi na mwingine kaumia kidogo tu, sasa sijajua ni nani aliye mahututi na nani hajaumia sana...” Madame Norah alisema huku akishindwa kuzuia machozi. Bi. Pamela naye hakuvumilia, akaanza kulia.



    Daktari Mshari aliwataka wamfuate, wakaondoka hadi kwenye chumba kimoja ambako walimkuta Jengo akiwa amepumzishwa, mwili wake ulikuwa umelowa damu na alikuwa amefungwa bandeji kichwani na kwenye jeraha katika mkono wake wa kulia lililokuwa linatoa damu. Mwili wake wote ulikuwa unamteteteka kwa hofu ya kile alichokuwa amekishuhudia siku hiyo.



    Madame Norah na Bi. Pamela walimtazama kwa mshangao mkubwa, kisha wakaangalia kwa kitambo pasipo kuongea chochote. Sammy hakuwemo katika chumba hicho. Kisha Madame Norah aliyarudisha macho yake kumwangalia Jengo huku mwili wake ukitetemeka. Machozi yalianza kububujika machoni na midomo yake ilishindwa kutulia, alikuwa anatetemeka japo alijitahidi kubana meno yake lakini bado haikusaidia.



    Moyo wake ulikuwa umevunjika, hakutegemea kabisa kama siku ile ingegeuka kuwa ya huzuni kiasi kile badala ya kuwa siku ya furaha, furaha ya kumpata binti yake waliyepotezana kwa miaka therathini na mbili. Moyo wake sasa ulikuwa kama unaovuja damu ndani kwa ndani. Japo amewahi kupita katika mapito magumu sana lakini hakuwahi kuhisi hisia kama hizo hapo nyuma. Hakuwahi kuhisi namna ile tangu kuzaliwa kwake, hisia mchanganyiko wa hasira, uchungu na mfadhaiko kwa pamoja! Alitamani kupiga yowe kali kwa ghadhabu lakini hakuweza.



    “Mkwe wangu yuko wapi, mbona simuoni hapa?” Bi. Pamela alimudu kuuliza baada ya kimya kirefu kutamalaki mle ndani.



    “Hali yake ni mbaya sana, tulichohitaji ni kuwapa taarifa kuwa anapelekwa moja kwa moja Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, tayari taratibu zingine zote zimeshafanyika,” Daktari Mshana alisema huku akiangalia saa yake ya mkononi.



    “Kwa hiyo dokta, huyu mwingine hajaumia mahala kokote?” Bi. Pamela alimuuliza Daktari Mshana huku akimtazama Jengo kwa namna ya kumkagua.



    “Hata sijielewi elewi. Najihisi kama mtu niliyekufa,” Jengo alijibu huku akijitazama kwa namna ya kujikagua.



    “Usiseme hivyo, hujafa. Bado unaishi...” Bi. Pamela alisema huku machozi yakimlengalenga machoni, kisha akaongeza, “Kwani hakuna sehemu yoyote inauma?”



    “Ninasikia maumivu makali hapa katika mkono wa kulia labda kidogo kichwani na chini ya mguu wa kushoto,” Jengo alisema huku akionesha maeneo yenye maumivu.



    “Pole sana,” Bi. Pamela alisema kwa upole huku akijifuta machozi.



    Wakati hayo yanaendelea Madame Norah alikuwa bado amezama kwenye dunia yake, dunia ya kisasi. Sasa alikuwa anahisi kifua chake kikiwaka moto utadhani alikuwa anataka kulipuka! Aliapa kushughulika na yeyote aliyefanya hivyo. Donge la hasira lilikuwa limemkaba kooni na alikuwa anapumua kwa shida kama mgonjwa anayepigania pumzi ya mwisho.



    Alichokumbuka kuongea muda huo ilikuwa kuomba ruhusa ya kumwona Sammy kabla hajapelekwa Muhimbili. Wote waliongozana hadi nje walikolikuta gari la wagonjwa likiwa tayari kuondoka. Sammy alikuwa kalala kwenye kitanda maalumu hajitambui, alikuwa kama mfu akiwa anapumua kwa msaada wa mashine maalumu ya kumsaidia kupumua na alitundikiwa chupa maalumu ya maji aina ya Normal Saline yaliyowekwa dawa maalumu ndani yake ili kusaidia kuyafanya mapigo ya moyo yasishuke.



    Wote walishindwa kuyazuia machozi, walijikuta wakilia kwa uchungu huku wakimwangalia Sammy ambaye alikuwa ametulia, hatingishiki. Madame Norah alimwita Sammy huku akibubujikwa na machozi kana kwamba ni mama aliyempoteza mwanawe wa pekee kwenye shimo refu sana, alimwita huku akilia kilio cha uchungu.







    Muda huo Madame Norah alikuwa anatiririkwa na jasho jingi hali iliyoanza kuwapa wasiwasi mkubwa walinzi wake na watu wengine waliokuwepo mahali hapo.



    * * * * *



    Tunu aliufungua mkoba wake, akatoa noti moja ya shilingi elfu kumi na kumpatia mlinzi mmoja kijana aliyekuwa akilinda katika eneo la viunga vya maegesho ya magari la mgahawa maarufu wa Elli’s. alimpa ile fedha kama ‘tip’ akimwomba kumwangalizia gari lake makini ili mtu yeyote asilifikie na kupachika kifaa. Tunu alikuwa ameamua kwenda kuliacha lile gari pale Elli’s kutokana na kuhisi usalama wake ungekuwa shakani endapo angeendelea kulitumia.



    Alikuwa amepata wazo la kwenda kuliacha lile gari pale kwenye mgahawa wa Elli’s wakati alipokuwa akitoka Shaurimoyo, japo alikuwa amefanikiwa kung’amua mtego wa adui zake kumwekea kifaa cha GPS lakini aliamini kuwa wangeendelea kumwandama, hasa baada ya kugundua kuwa alikwisha ng’amua mtego huo.



    Sasa alikuwa akimtilia shaka kila mtu, hakutaka kumwamini mtu kirahisi hasa kila alipokumbuka kuwa hata Victor, mtu aliyemwamini sana aliweza kumsaliti, hivyo alijiambia kuwa alipaswa kuwa makini zaidi. Ndipo alipofikia hatua ya kupeleka gari lake pale Elli’s akiamini kuwa hiyo ndiyo ilikuwa sehemu pekee kwa wakati huo ingeweza kuwa salama kwa gari lake.



    Eneo la viunga vya maegesho ya magari la Elli’s lilikuwa na ulinzi madhubuti likiwa limezungushiwa kamera za ulinzi kila sehemu. Hata hivyo, hakutaka kuzitegemea kamera peke yake, ndipo alipoamua kumtafuta yule kijana mlinzi ambaye kwa macho tu aliweza kutambua kuwa alikuwa mwaminifu. Akamwachia jukumu hilo na kumtaka ampigie simu endapo angehisi jambo lolote lisilo la kawaida kwenye gari lake. Muda huo eneo lile lilikuwa na magari yasiyopungua therathini, mengi yakiwa ya watu wenye vipato vya juu.



    Baada ya kuachana na yule mlinzi, Tunu alitoka na kuelekea sehemu zilipokuwa zimeegeshwa taxi, upande wa pili wa barabara. Alitazama pande zote mbili kabla hajavuka barabara na kwenda kuingia kwenye taxi moja, ambayo dereva wake alikuwa mtu mzima, mrefu na mwembamba mwenye sura ya ucheshi muda wote akiwa amevaa kofia aina ya baragashia, shati la mistari ya pundamilia, suruali ya kijivu na makubazi meusi ya ngozi miguuni.



    Kwa mtazamo wa haraka haraka Tunu aliona ile taxi ingemfaa sana, alipoifikia alifungua mlango wa nyuma na kuingia haraka, akaketi huku akimtaka dereva ampeleke hospitali ya Amana. Yule dereva aliwasha injini, akaliondoa gari taratibu na kuifuata barabara ya lami iliyokuwa inakwenda kutokea hospitali ya Amana. Zikapita kama sekunde tano tu tangu waondoke eneo la maegesho ya taxi, gari jingine aina ya Toyota Wish la rangi nyeusi ambalo lilikuwepo karibu na maegesho yale ya taxi, nalo likaondoka kuwafuata.



    Ile taxi haikwenda mbali kabla Tunu hajakumbuka wajibu wake. Toka katika siti ile ya nyuma aliyoketi alikizungusha kichwa chake taratibu kutazama nyuma bila kumshtua dereva na hapo mwili wake ukajikuta ukiingiwa na ubaridi wa ghafla. Aliliona lile gari aina ya Toyota Wish lenye watu wawili mbele likiwa nyuma yao.



    Alikumbuka kuliona lile gari likiwa limeegeshwa karibu na maegesho ya taxi pale nje ya mgahawa wa Elli’s wakati alipofika kutoka Shaurimoyo na kuingiza gari lake ndani ya viunga vya magari vya mgahawa wa Elli’s, hata alipotoka na kuvuka barabara kisha akaingia ndani ya ile taxi alikuwa ameliona tena lile gari likiwa palepale, na sasa lilikuwa nyuma yao. Aligeuka na kumtazama dereva wake kwa udadisi na kugundua kuwa alikuwa hafahamu chochote kilichokuwa kikiendelea. Tunu akageuka tena kutazama kule nyuma.



    Lile gari aina ya Toyota Wish lilikuwa nyuma yao kiasi cha umbali wa mita therathini hivi na lilikuwa linakuja kwa mwendo wa kasi likionekana kutaka kuwapita. Kilichozidi kumtia hofu Tunu ni kuwa wale watu sasa walionekana wazi kuwa walikuwa wamedhamiria kumfuatilia pasipo uficho wowote. Akapanga kubadilisha mwelekeo ili kuwapoteza.



    “Dereva, ongeza mwendo na uhakikishe gari lolote toka nyuma yetu lisitupite,” Tunu alimwambia yule dereva, na pasipo kuhoji chochote yule dereva aliongeza mwendo.



    Kwa kitendo kile cha lile taxi kuongeza mwendo Tunu alikuwa na uhakika kuwa kingetosha kabisa kuwafahamisha wale watu kwenye lile gari lililokuwa nyuma yao kuwa tayari alikuwa ameshawashtukia hila yao, hata hivyo, hilo halikumpa shida. Akili yake sasa ilikuwa makini mno kupanga mikakati ya namna ya kuwapoteza wale watu.



    Hakutaka wajue kama alikuwa anakwenda Amana, kwani alihitaji sana kuongea na Sammy ili amweleze ukweli kuwa yeye ni ofisa wa usalama na kwamba alikwisha gundua kuwa adui yake ni Mr. Oduya, hivyo alipaswa achukue tahadhari.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Dereva, naomba ukifika mwisho wa hii barabara ingia kulia,” Tunu alimwambia yule dereva na kumfanya ashangae kidogo.



    “Kwani tunaelekea wapi, bosi wangu? Mimi nilidhani tunaelekea hospitali ya Amana!” yule dereva alihoji kwa mshangao huku akimtupia jicho Tunu kupitia kwenye kioo cha kati cha gari kinachotumika kutazama vitu vilivyoko nyuma.



    “Hatuelekei tena Amana kuna mtu nahitaji kuonana naye kwanza kabla ya kuelekea huko,” Tunu alimdanganya yule dereva huku akiwa anafikiria cha kufanya endapo lile gari lililokuwa nyuma yao lingefanikiwa kuwafikia au kuwapita. Alipeleka mkono wake kiunoni, akaigusa bastola yake ndogo aina ya Glock 19M ambayo hutumiwa na wapelelezi wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), mwili ukamsisimka.





    “Oh! kumbe umebadili mawazo, ungeniambia ni wapi tunapoelekea sasa badala ya kusema tu ingia kulia!” yule dereva alisema kwa jazba kidogo. Wakati huo ile taxi ilikuwa inafika mwisho wa ile barabara, dereva akaingia kulia.



    “Wewe fuata maelekezo yangu, suala la fedha siyo tatizo,” Tunu alimjibu kwa sauti tulivu lakini akionekana kukerwa kidogo.

    “Sawa basi usijali bosi wangu, wewe kwangu siyo mfalme tu, hata ukitaka urais nakupa. Wewe sema popote nitakupeleka,” yule dereva alisema huku uso wake ukitengeneza tabasamu la kirafiki.



    “Ingia upande wa kulia hapo kama unaifuata barabara ya Uhuru kisha uingie kushoto kuufuata mtaa wa Tukuyu,” Tunu alimwambia yule dereva wakati wakiifikia ile barabara ya Uhuru iliyokuwa na msongamano wa magari muda huo.



    Dereva akafanya kama alivyoagizwa. Aliliingiza gari lake katika barabara ya Uhuru kama aliyekuwa anaeleka Buguruni kisha akachepuka na kuufuata ule mtaa wa Tukuyu huku gari likikosakosa kugongana na daladala linalofanya safari zake kati ya Mnazi Mmoja na Banana. Pasipo kujali matusi ya dereva na abiria wa lile daladala, yule dereva aliongeza mwendo wakapita mtaa ule uliokatiza katikati ya makazi ya watu hadi walipoufikia mtaa wa Kasulu.



    Walipokuwa mwishoni mwa mtaa ule wa Tukuyu kabla hawajaufikia mtaa wa Kasulu Tunu akageuka tena nyuma kulitazama lile gari lililokuwa limewafungia mkia kwa nyuma. Bado lilikuwa likiwafuatilia na sasa lilikuwa likiufuata mtaa ule wa Tukuyu likiwa katika mwendo wa kasi. Ilionekana wazi kabisa kuwa watu waty hawakuonekana kuwapa mwanya wa kuwatoroka.



    Kengele ya hatari ikalia kichwani kwa Tunu, sasa alihisi kuwa wale watu walikuwa wamedhamiria kufanya jambo baya zaidi, pengine walidhamiria kuua. Hakuona tena sababu ya kuendelea kumficha dereva wake, kwani kumficha kungemfanya kuwa na wakati mgumu sana wa kuwapoteza wale watu.



    “Naomba nisikilie, sina sababu ya kukuficha kwa sababu nakuamini. Kuna gari nyuma yetu linatufuata tangu tulipotoka kule Elli’s, fanya namna yoyote ya kuhakikisha unawapoteza kwani sitaki kabisa wajue naenda wapi, sawa?” Tunu alimwambia yule dereva kwa sauti ya kuamuru.



    Yule dereva akaangalia nyuma na kuliona lile gari aina ya Toyota Wish likizidi kuwasogelea, akaonekana kushtuka sana na kumtupia Tunu jicho huku wasiwasi ukijengeka usoni kwake. “Kwa nini wakufuatilie, kwani umewafanya nini, dada?” yule dereva aliuliza huku akihisi jasho likimtoka mwilini.



    “Yule ni mume wangu, nimemtoroka nyumbani. Naomba fanya nilivyokwambia mambo mengine nitakueleza tukishawapoteza,” Tunu alisema huku akigeuza shingo yake kutazama nyuma. Dereva akamwelewa na kuchepuka kuufuata mtaa wa Kasulu upande wa kushoto. Muda huo Tunu aligeuka tena kutazama nyuma akaliona lile gari likizidi kuwasogelea, akatabasamu huku akijisemea moyoni, “Nyie subirini tu, dawa yenu ipo jikoni.”



    Sasa dereva wa taxi alianza kuendesha gari kama aliyepandwa na kichaa, alipoufikia mtaa wa Arusha akakunja kushoto akiufuata ule mtaa kisha akakunja kuingia kulia na kuufuata mtaa wa Pangani kisha akakunja tena kuingia kulia akiufuata mtaa wa Mwanza. Mtaa ule ulikuwa mfupi, akakunja kuingia kulia kwake akiufuata mtaa wa Tanga, akawa anarudi nyuma kwenda kutokea tena mtaa wa Arusha.



    Walipoingia tena kwenye barabara ya mtaa wa Arusha Tunu akageuka tena kulitazama lile gari kwa nyuma, akafarijika kutoliona likiwa nyuma yao na hapo akageuka tena mbele kumtazama dereva ambaye alikuwa anatabasamu. Katika mtaa ule wa Arusha dereva aliingia kushoto na walipofika Pangan Water, Ilala Depot akaingia kulia kuufuata mtaa mmoja wa barabara ya vumbi hadi alipoufikia tena mtaa Tukuyu.



    Walipokuwa wanaingia katika mtaa ule wa Tukuyu Tunu alipogeuka tena kutazama nyuma, na hapo moyo wake ukapiga kite kwa nguvu kama aliyepigwa konde zito la kushtukiza kichwani. Lile gari aina ya Toyota Wish lilikuwepo nyuma yao. Akashtuka sana. Hata yule dereva pia alishtuka sana. Tunu alimwona yule dereva akibabaika kidogo.



    “Usijali, wewe nyoosha moja kwa moja, nitakwambia cha kufanya,” Tunu alimwambia yule dereva huku akipeleka mkono wake kiunoni, akaishika bastola yake akiwa tayari kwa lolote. Dereva wa taxi aliongeza mwendo. Wakati huo akili ya Tunu ilikuwa inafanya kazi haraka sana ili aweze kujinasua kutoka kwenye mawindo ya wale watu walioonekana kuwa na uchu wa kuutoa uhai wake.



    Wakati wakikaribia kwenye fremu za maduka yanayozunguka Kanisa la Anglikana, Tunu alitoa noti tatu za shilingi elfu kumi kumi na kuzirushia mbele kwa dereva, “Ukifika mtaa wa Moshi kunja kulia na kuufuata mtaa huo, kisha punguza kidogo mwendo, nishuke halafu wewe ongeza mwendo ili kuwapoteza, sawa?”



    Yule dereva aliitikia kwa kichwa huku akilitupia jicho lile gari lililokuwa nyuma yao. Akakunja kuingia kulia akiufuata mtaa wa Moshi huku akimkwepa mtoto mmoja aliyekuwa anakatiza barabara. Muda ule ule Tunu aliufungua mlango akashuka haraka na kuusukuma ule mlango, ukajibamiza. Akachepuka na kujibanza nyuma ya mti mmoja mkubwa wa kivuli jirani ya nyumba moja ya wageni.



    Lile gari lililokuwa nyuma yao pia liliingia barabara ile lakini kwa kuchelewa kidogo likaongeza mwendo kuifuata ile taxi. Dereva wa taxi aliufikia mtaa wa Arusha na kuuvuka, akaendelea mbele akiifuata barabara ile ya vumbi. Sasa alikusudia kuwafanya wale watu waamini kuwa yule dada alikuwa bado yumo ndani ya ile taxi.



    * * * * *



    Kwa mara ya kwanza tangu alipoanza harakati zake za kutaka kuingia ikulu, Mr. Oduya alijikuta katika hali ya wasiwasi na mashaka makubwa. Kwa mbali hofu ilikuwa ikitishia kuutawala moyo wake, hasa kwa hisia zilizokuwa zikimnong’oneza kuwa mambo yameanza kumwendea mrama. Alikuwa amekanganyikiwa akiwa ameketi kwenye kiti chake cha kuzunguka ofisini kwake.









    Mambo hayo hayakuwa yakimwingia kichwani kwake kabisa, alikuwa anajiuliza ni vipi Tunu akafanikiwa kuwatoroka watu wote waliowekwa kumfuatilia? Tena watu wenye ufanisi mkubwa katika kazi hiyo na wenye silaha? Kidogo akawa amejifunza ni mtu wa aina gani alikuwa anasumbuka naye ndiyo maana baadaye aliamua kuwatuma watu maalumu kwa kazi moja tu, kuua. Watu hao walitakiwa kumuua Tunu popote ambapo wangemwona.



    Mr. Oduya aliamini kuwa Tunu hakuwa mtu wa kawaida kama alivyokuwa anamchukulia mwanzo, mbaya zaidi, hata yule dereva teksi Tom ambaye walimtegemea kwa shughuli za kuchukua watu wake na kuwakimbiza huku na kule pia alikuwa amejiunga na Tunu!



    Sasa Mr. Oduya alianza kujiuliza iwapo aachane na ndoto ile ya urais kisha atoroke nchi na kukimbilia nchini Canada ambako alikuwa amewekeza kwa kiasi kikubwa, akaishi kwa raha mustarehe na mpenzi wake Zainabu, akitumia utajiri wake mkubwa. Hata hivyo, wazo hilo alilipinga kwa kuona kuwa hiyo ilikuwa dalili ya mtu mwoga. Yeye hakuwa mwoga, hivyo alipaswa kupambana hadi dakika ya mwisho.



    Kichwa chake kilikuwa kimechemka utadhani ubongo wake uligeuka kuwa volcano iliyotishia kulipuka wakati wowote, aliuhisi ubongo wake ukiwaka moto na muda wowote kichwa kingelipuka na kusambaratika. Hadi muda huo hakuwa ameambua japo lepe la usingizi, kwa siku mbili mfululizo tangu alipogundua kuwa lile gari aina ya Cadillac DeVille lenye muundo wa kizamani lilionekana Mzizima TV na sasa lilikuwa linamilikiwa na mtu mwingine.



    Kwa kuiamini timu yake iliyoongozwa na Spoiler, Mr. Oduya alitegemea suala la kumpata mmiliki mpya wa lile gari na kuliteketeza lile gari lingekuwa rahisi na kuchukua muda mfupi, lakini tangu kuibuka kwa yule binti, Tunu, ambaye alionekana waziwazi kuanzisha vita ili kumkwamisha, mambo yakaanza kwenda mrama.



    Timu yote aliyoitegemea kuifanya kazi hiyo ilionekana kuzidiwa akili na yule binti. Mr. Oduya hakujua Tunu alikuwa ana nini hasa? Ni mara ngapi amejaribu kwa uwezo wake wote kutaka kumtia mkononi lakini binti huyo amekuwa akiikwepa mitego yote na kuwapotea katika mazingira ya utata?



    Alikuwa ameketi pale kwenye kiti chake kwa takriban dakika arobaini na tano akiwa hajui afanye nini, hiyo ilikuwa ni baada ya kuongea na vijana wake aliowafokea sana kuhusiana na kitendo cha wao kuendelea kuzidiwa akili na Tunu.



    “Ninaomba maelezo mafupi sasa hivi, kwa nini mmeshindwa kumnasa huyo binti?” Mr. Oduya aliwauliza Spoiler, Victor na Job waliokuwa wameketi mbele yake huku wamejiinamia.



    Spoiler, Victor na Job waliinua nyuso zao, wakatazamana na Spoiler akawa wa kwanza kusema. “Nadhani, bosi hatutakuwa na maelezo ya kukuridhisha kwa nini hatujafanikiwa kumtia mbaroni hadi sasa, kwa sababu…”



    “Ni wazembe tu!” Mr. Oduya alimkatiza Spoiler kwa kufoka, uso kaukunja na kutengeneza ndita usoni. “Au mna sababu nyingine?”



    Spoiler aliwatupia jicho Victor na Job mara moja kisha akaketi vema kitini. Alishaanza kuingiwa na hofu iliyochanganyika na woga. Alikuwa na kila sababu ya kujisikia vile. Mr. Oduya alikuwa mtu katili sana asiyeruhusu makosa ya kipumbavu yaliyoashiria uzembe yatokee kwenye kazi zake, ingawa machoni kwa watu alionekana mnyenyekevu na mwenye kusaidia jamii lakini ukweli ni kwamba alikuwa hana tofauti na mnyama yeyote wa porini.



    “Siyo wazembe bosi,” Spoiler alisema kwa sauti ya chini.



    “Kumbe nini?” Mr. Oduya aliuliza huku akimtolea macho. “Mlishajua kuwa Tunu tayari amekutana na Sammy na kisha akagundua kuwa gari lake limewekwa GPS device. Hakukuwa tena na sababu ya kuendelea kumwacha akiwa hai, mlikuwa mnasubiri nini, pingu? Sasa amefanikiwa kuwatoroka, mnataka kusema nini? Ni uzembe tu!” Mr. Oduya alifoka.



    Victor alishusha pumzi, akawageukia akina Spoiler na Job waliokuwa wanamtumbulia macho Mr. Oduya kwa wasiwasi.



    “Inawezekana kweli kuwa ni uzembe wetu, mzee,” Victor alijikakamua na kusema, “lakini hapa tunamzungumzia Tunu Michael, shushushu mbobezi aliyepata mafunzo maalumu ya kijeshi na mwenye shahada ya umahiri ya ujasusi wa mambo ya usalama na mapambano dhidi ya ugaidi, isitoshe ni ninja na kama ilivyo kwa maninja wote ni kama wanatumia nguvu za mizimu…”



    “Upumbavu!” Mr. Oduya alisema huku akishusha ngumi nzito mezani iliyowashtua watu wote. “Hatuzungumzii nguvu ya mizimu katika kazi kama hizi, Victor… wewe na Job pia ni mashushushu. Wewe umekaa miaka mitatu nchini Cuba ukijifunza upelelezi wa kisasa na bado unazungumzia nguvu ya mizimu…” Mr. Oduya alikuwa amefura kwelikweli, sasa alikuwa anaongea kama anayetaka kupiga kelele. “Au mlitakaje? Tuwachanje kwanza chale mwilini ndipo mumkamate Tunu?”



    Victor alimlaani sana Mr. Oduya kimoyomoyo, alitamani kumtukana kisha ainuke na kuondoka zake lakini akaogopa, kwani yule mzee hakuwa tajiri tu wa kawaida, alikuwa na nguvu kubwa sana serikalini na ndani ya vyombo vya usalama akiaminiwa na watu wengi kama bilionea anayesaidia jamii.



    “Hatuhitaji kuchanjwa chale, mzee, hilo tunalijua. Lakini Tunu, si kama unavyomjua… huyu ni shushushu hatari sana aliyepata mafunzo ambayo katika nchi hii wapo wawili tu, mafunzo hayo ndiyo humsaidia kung’amua jambo lolote hatari kabla halijatokea. Sisi si wazembe, kama unavyotutuhumu. Tumefanya kazi ngapi kubwa na za hatari, mzee?” Victor alisema kwa sauti kakamavu iliyoficha hasira ndani yake.









    Mr. Oduya alishusha pumzi, akajiegemeza kitini. Ni kweli kabisa Victor na Job walikuwa mashushushu shupavu ambao serikali ilikuwa ikijivunia kuwa nao. Walikubali kukiuka misingi ya kazi yao ya usalama wa taifa ili kumtumikia katika uhalifu wake, wakifanya kazi kwa kujituma bila ya kuhitaji kusimamiwa au kuhimizwa. Mr. Oduya mwenyewe aliwategemea katika kazi zake na aliwaahidi kuwapa nafasi nyeti ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa pindi akishika madaraka ya nchi.



    Sasa walikuwa wameondoka kwenda kusaidiana kumtafuta Tunu, alikuwa amewataka wasirudi hapo bila taarifa ya kifo au kichwa cha Tunu, haijalishi kama Tunu ni ninja au anatumia nguvu ya mizimu. Ni kweli Tunu alikuwa shushushu hatari, mbobezi, ninja au vyovyote ambavyo angeitwa, lakini Mr. Oduya alikuwa na uhakika kuwa pamoja na sifa zote hizo bado alikuwa na mwili wa nyama, na risasi haichagui raia, shushushu au ninja.



    Jambo lililompa ahueni kidogo Mr. Oduya ni kwamba, aliamini kuwa Tunu bado alikuwa hayajui mambo mengi yaliyokuwa yanaendelea kwenye harakati zake ingawa kitendo chake cha kufanikiwa kukwepa mitego yote aliyowekewa kilitosha kumpa salamu Mr. Oduya kuwa alikuwa anadili na mtu wa aina gani. Shushushu hatari, mbobezi na ninja, kama alivyosema Victor.



    Hilo lilizidi kumtisha Mr. Oduya kwani pamoja na kuweka watu wake karibu maeneo yote ya mji na yale aliyodhani Tunu angeweza kufika ikiwemo hospitali ya Amana na Muhimbili, bado hawakufua dafu. Aliona kuwa anatakiwa kutafuta njia mbadala za kumpata Tunu, lakini sasa angempataje? Aliona kichwa chake kinakaribia kupasuka kwani bila kumpata Tunu mambo yake yote yangeharibika. Njia mbadala ya kumpata ilikuwa ni kwa kupitia Victor, lakini sasa wameshaitifua.



    Akiwa bado amezama kwenye lindi la fikra alishtuliwa na mtu aliyegonga mlango wa ofisi yake mara moja kisha mlango huo ukafunguliwa. Aliingia mtu aliyevaa suti maridadi ya kijivu mmoja na Mr. Oduya alipomtazama akamtambua mara moja na kushusha pumzi. Alikuwa Dk. Masanja.



    Mr. Oduya alishangaa maana hakuwa na miadi yoyote na Dk. Masanja siku hiyo, tangu kikao chao cha kupanga mikakati kilipovunjika usiku ule baada ya taarifa za kuonekana kwa lile gari aina ya Cadillac DeVille lenye muundo wa kizamani, hawakuweza kuongea tena. Dk. Masanja hakuwa na kawaida ya kumtembelea ofisini kwake na hata kama angefika pale ilikuwa ni mpaka wakubaliane. Dk. Masanja alijikaribisha mwenyewe kwenye kiti kisha wakasalimiana.



    “Kwani ni kipi kilichotokea, naona hadi leo bado haupo katika hali yako ya kawaida!” Dk. Masanja alimuuliza Mr. Oduya huku akimtazama usoni kwa makini.



    “Ni mambo ya kifamilia tu, nisingependa kuyaongelea,” Mr. Oduya alisema huku sura yake ikishindwa kuficha wasiwasi aliokuwa nao, “ni kwamba ninahitaji siku mbili zaidi ili kuyaweka sawa kabla hatujaendelea na mipango yetu.”



    “Okay!” Dk. Masanja alisema kisha akajiweka sawa kwenye kiti, “Maana hatujawasiliana wala hujatokea pale Paradise Club jambo ambalo si kawaida yako, imenipa wasiwasi kidogo.”



    “Uihofu juu yangu, hata hivyo nimeshangaa kidogo kwa ujio wako maana ungeweza kunipigia simu tu badala ya kusumbuka kuja huku.”



    “Ni kweli, ila sikutaka kufanya hivyo maana mambo mengine hayafai kuzungumzwa kwenye simu, si unajua tena tupo kwenye ulimwengu wa teknolojia, watu wanaweza kudukua mawasiliano…” Dk. Masanja alisema na kuendelea, “Nilihitaji kujua kuhusu suala la huyu bwana mdogo Sammy!” Dk. Masanja aliuliza huku akimkazia macho Mr. oduya.



    “Kuhusu nini?” Mr. Oduya aliuliza huku akionesha mshtuko usoni kwake.



    “Naamini unafahamu kilichompata. Nilitaka kujua kama unahusika!” Dk. Masanja aliongea huku kamkazia macho Mr. Oduya.



    “Nimesikia yaliyompata lakini si mimi niliyehusika,” Mr. Oduya alisema huku akitingisha kichwa chake kushoto na kulia kukataa.



    Dk. Masanja akamtazama kwa sekunde kadhaa kabla hajashusha pumzi na kutia neno, “Mr. Oduya, mimi sipo hapa kukuhukumu ama kukutuhumu. Nipo hapa kuona namna gani tunaweza kufanya ili polisi wasiweze kugundua lolote. Labda nikwambie, nimefuatwa ofisini na maofisa wa polisi wakitaka maelezo yangu kama bosi wa Sammy.”



    Mr. Oduya akashtuka kidogo, “Kwani hujawaambia kama alikwisha acha kazi katika hoteli yenu?”



    “Sijawaambia lakini wanajua kuwa aliacha kazi, walitaka kujua aliacha lini na kwa nini! Hapa nipo njia panda kwa kuwa inaonekana wanazo taarifa nyingi kuliko tunavyodhani, ndiyo maana nimekuja kwako,” Dk. Masanja alisema na kumeza funda la mate kutowesha koo lake lililokauka.



    Mr. Oduya alibaki kimya, alikuwa ametahayari sana. Uso wake haukuweza kuficha hofu aliyokuwa nayo.



    * * * * *



    Tangu aliposhuka toka ndani ya ile taxi iliyomchukua toka katika mgahawa wa Elli’s, Tunu alitembea kwa tahadhari kubwa huku akiwa na wasiwasi mkubwa. Kubwa lililomsumbua ni jinsi watu wa Mr. Oduya walivyoonekana kupania kumpata kwa gharama yoyote. Alijiuliza, ilikuwaje huko nyuma baada ya kuachana na yule dereva wa teksi? Je, walifanikiwa kumpata? Na kama walimpata walimuhoji? Aliwajibu nini?



    Tunu alikuwa na wasiwasi na yule dereva kwani alishaanza kuonesha dalili za hofu na wasiwasi. Kama alihojiwa, akaudhihirisha wasiwasi wake, yawezekana waliamua kumtumia kama chambo ili kuja kumnasa Tunu, au pengine walimpeleka nyumba ya mateso. Yawezekana muda huo alikuwa anapokea mateso wakiamini kuwa alikuwa anayajua mengi.



    Mawazo yalikuwa yakipita kichwani kwa Tunu wakati akiambaa na ukuta kuelekea kwenye jengo la wadi ya wagonjwa mahututi wenye kuhitaji uangalizi maalumu katika hospitali ya Amana. Muda wote alikuwa makini sana akizungusha macho yake kila pembe ili kubaini mtego wowote uliokuwa umewekwa dhidi yake. Mawazo hayo yaliufanya moyo wake uongeze kasi ya mapigo yake. Alivuta pumzi ndefu kisha akazishusha taratibu.







    Alikuwa ameingia ndani ya eneo la hospitali ya Amana baada ya kuruka ukuta, pasipo kuambiwa alitambua kuwa watu wa Mr. Oduya wangekuwepo pale hospitali kumsubiri, hivyo ilimbidi kuwakwepa na kuzunguka nyuma ya hospitali ambako alifanikiwa kuingia ndani.



    Haikuwa rahisi kuingia ndani ya uzio wa hospitali ile, kwani alipotoka mtaa wa Moshi, alitembea haraka huku akiwa makini kuangalia pande zote na kuvuka barabara ya Uhuru, akaelekea kwenye vibanda vya wasusi wa Kimasai ambapo alipita, akashika njia kama anakwenda kwenye maghorofa ya Ilala. Alipofika eneo lile aliyazungusha macho yake pande zote kutazama kama kulikuwa na mtu yeyote aliyekuwa akimfuatilia, hata hivyo hakumwona mtu yeyote hivyo aliendelea na safari yake akiyapita maghorofa ya Ilala na kuambaa ambaa na ukuta wa hospitali.



    Aliporidhika kuwa hakuna aliyekuwa akimtazama alichepuka chini ya miti mikubwa iliyokuwa imepandwa kandokando ya ukuta wa Hospitali ya Amana na kwenda kwenye ule ukuta wa hospitali. Akafanikiwa kuufikia ukuta ule ambapo kwa mbinu zake za kijasusi alifanikiwa kuupanda kama anayeruka mtaro mdogo wa maji machafu. Muda mfupi baadaye akatua upande wa pili ndani ya ukuta.



    Mara tu alipotua mle ndani alisimama akachunguza vizuri mazingira ya eneo lile. Kulikuwa na miti miwili mikubwa eneo lile na hakukuwapo mtu karibu, na hapo akaanza kutembea kwa tahadhari akiambaa na ukuta huo kuelekea ilipo wadi maalumu ya wagonjwa mahututi wenye kuhitaji uangalizi maalumu.



    Alisimama ghafla baada ya kuona eneo lile la nje ya wadi ya wagonjwa mahututi likiwa linalindwa na askari watatu wenye silaha. Askari wale walikuwa makini sana wakizungusha macho yao pembe zote kuhakikisha usalama unakuwepo. Tunu alipochunguza kwa makini akagundua kuwa kila aliyepita eneo lile alisimamishwa na kuhojiwa, na pengine alikamatwa au alizuiwa na kutakiwa kurudi alikotoka.



    Alitweta, akajiuliza iwapo alitakiwa aendelee na safari yake au arudi. Katikati ya mawazo hayo, mlio hafifu wa simu yake ya mkononi ukamshtua! Tunu aliiangalia ile simu kwa makini, akaliona jina la Tom. Alijibanza sehemu akaipokea na kuongea, “Hallo!”



    “Uko wapi?” Tom aliongea kwa sauti iliyoonesha wasiwasi kidogo.



    “Nipo sehemu fulani kuna kitu nafuatilia. Wewe upo wapi?” Tunu alisema huku akizungusha macho yake pembe zote kuhakikisha usalama wake.



    “Pia nipo sehemu fulani nimetulia, nilitaka kukwambia kwamba, kuwa makini sana na kila mtu unayepishana naye wakiwemo baadhi ya askari polisi, kuna wauaji wawili wa kukodiwa wamepewa kazi ya kukufuatilia kokote uliko na kukuua, hawatakiwi kufanya kitu kingine isipokuwa kukuua tu,” Tom alisema kwa wasiwasi.



    “Usijali kuhusu mimi, watakufa wao kabla hawajafanikiwa kuniua,” Tunu alijibu kwa sauti tulivu ingawa mapigo ya moyo wake yalikuwa yanakwenda mbio isivyo kawaida.



    “Vipi umesikia kuhusu kilichompata Sammy?” Tom aliuliza kwa wasiwasi.



    “Hapana, amepatwa na nini?” Tunu aliuliza huku akihisi ubaridi mwepesi ukimtambaa mwilini mwake na kuzifanya nywele zake kusisimka.



    “Walimtegesha bomu kwenye gari lake, likalipuka wakati ameliegesha na kuingia ndani. Hivi sasa yupo hospitali akiwa mahututi…”



    “What?” Tunu aling’aka kwa mshtuko mkubwa. Alihisi kama vile moyo wake uliyasahau mapigo yake kwa muda, na yaliporejea yalianza kwenda mbio isivyo kawaida. “Dah! Yupo hospitali gani?” Tunu aliuliza baada ya kitambo.



    “Walimpeleka Amana, hali ikaonekana ni mbaya zaidi, wakamhamishia Muhimbili.”



    “Okay! Vipi kuhusu wewe, bado hawajakushtukia?”

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Dah, sijui nikwambie nini! Ninasakwa kwa udi na uvumba. Nimekutana na rafiki yangu mmoja huwa tunapaki wote pale Elli’s, akanitonya kuwa natafutwa kama gaidi na watu fulani ambao wamemwaga fedha kwa siri pale kijiweni ili nikionekana tu wapewe taarifa. Ila usijali niko poa,” Tom alisema na kushusha pumzi.



    “Basi nitakupigia baadaye ili tujue cha kufanya,” Tunu alisema na kukata simu baada ya kuhisi kulikuwa na watu waliokuwa wanaelekea kule alikokuwa. Hakuona sababu ya kuendelea kuwepo pale, akaondoka haraka na kurudi alikotoka akitumia mbinu ile ile ya kijasusi kuupanda ukuta na kurukia nje. Sasa alihisi kuwa eneo lile lilikuwa halifai tena, alipaswa aende sehemu akajipange kwanza kabla ya kuendelea na harakati zake.



    * * * * *



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog