Search This Blog

Friday 18 November 2022

BARADHULI MWENYE MIKONO YA CHUMA (2) - 3

 






Simulizi : Baradhuli Mwenye Mikono Ya Chuma (2)

Sehemu Ya Tatu (3)







Kaguta akatabasamu. “Hayo ndio mambo sasa! … Kwanza, yule mzee uliyekuwa naye ni nani?”

“Anaitwa Isaac Makongo. Ni mkuu wetu.”

“Mkuu wenu kivipi?”

“Yeye ndiye coordinator. Kila kitu kutoka kwa mkuu hupitia kwake. Kuanzia pesa mpaka vifaa.”

“Kwahiyo ndio upo naye kimahusiano?”







Hapo Sandra alitulia kwanza na kupunguza kasi yake ya kujibu. Alitizama chini, Kaguta akarudia kuuliza swali.







“Si kwamba nipo naye kimahusiano.”

“Bali?”

“Ananitaka na sijui njia ya kumkatalia.”

“Hujui? Kwani wengine unawakataliaje?”

“Kumbuka nimekuambia yule ni mtu mkubwa. Kumkatalia maana yake ni kujiweka kwenye mazingira magumu mno hata kufa pia!”

“Kwahiyo kila mwanamke akitaka kuwa naye anampata, sio?”

“Nadhani.”

“Na vipi kumhusu Roby?”

“Kaguta, hakuna yeyote ninayempenda kati ya hao. Ni mazingira tu yananibana na kuniacha bila ya jinsi.”

“Na utakuwa mtumwa hivyo mpaka lini, Sandra?”







Sandra alidondosha chozi kusikia hilo swali. Alijifuta na vidole vyake vitatu lakini bado hakujibu, alikuwa anatizama tu chini mithili ya mtu anayejutia.









“Nani alikuingiza katika huu mtandao, Sandra?”









Kaguta aliuliza kwa sura ya huruma. Sandra hakujibu, bado alikuwa ameinamisha uso wake akitiririsha machozi. Baada ya dakika kama tano, Sandra ndipo akatia neno kwa sauti ya kukoroma tena huku akivuta makamasi ya kilio.









“Tokea nikiwa na miaka mitano, nilikuwa tayari nina chapa mwilini mwangu. Baba yangu alikuwa mtumishi mkubwa wa bwana Kim kiasi kwamba aliahidi familia yake yote kumtumikia mungu mtu huyo, Kim. Hata mama yangu pia akapigwa chapa na kuwa mfuasi, bahati mbaya yeye na mumewe hawakudumu. Waliuwawa wakiwa kazini na kuniacha yatima asiye na baba wala mama isipokuwa tu chapa niliyo nayo ya bwana Kim.”











Machozi yakawa kama mto kwenye mashavu ya Sandra. Alishindwa tena kuongea, akawa analia tu. Kaguta alimvuta na kumkumbata.









“Usilie, Sandra. Yatakwisha.”

“Hayawezi kwisha Kaguta, kamwe.” Sandra alisema kama mtu mwenye uhakika haswa na jambo analolitema. Kaguta alimbembeleza kama mwanaye, Sandra alipopoa ndio maelezo yakaendelea;

“Tokea hapo, nilichokuwa nakula, nakunywa na navaa ilikuwa ni juu ya taasisi ya bwana Kim. Nilikulia katika mikono hiyo mpaka leo hii najitambua japo siwezi kufanya lolote lile.”

“Hakuna jaribu lisilo na njia ya kutokea.”

“Hapana, Kaguta. Lipo na hili ni mojawapo. Ni ngumu mno kumshikia bwana Kim chini, nchi nzima ipo mikononi mwake. Serikali na mitaa yote ni ya kwake. Unaanzia wapi?”

“Amini mlango upo. Ila tu umepakwa rangi inayofanana na ukuta. Hatuna budi kuutafuta, kwa pamoja tutaweza.”

“Kwa pamoja?”

“Ndio, wewe na sisi.”









Sandra akatabasamu kidogo kisha akatikisa kichwa chake kwa mbali.









“Huwezi ukafanya lolote kwa sasa. Wewe ni mfuasi wa bwana Kim, hiyo chapa uliyo nayo haitokuruhusu ufanye jambo.”

“Hapana. Chapa hii itanizuia tu kutoa siri na si kufanya mengine.”

“Nani kakudanganya? … Ukishawekwa hiyo chapa, huyo aliyechorwa hapo mkononi mwako anaona kila unachokifanya. Kila hatua unayochukua. Kila utakachokuwa unakifanya atakutangulia kwa hatua tatu mbele. Weka hilo akilini mwako. Na hakuna lolote utakalofanya dhidi ya Mr Kim ukafanikiwa.”











Kaguta alitizama tattoo yake mkononi kwa uso wenye ndita. Aling’ta lips akashusha pumzi ndefu. Kwa muda kama wa kasoro dakika kukawa kimya. Kaguta alikumbuka yake yaliyokuwa yanatukia kule kisiwani akijaribu kulinganisha na kile akisemacho Sandra. Ni kweli walikuwa wanatanguliwa hatua tatu mbele? Alijiuliza hilo swali, sidhani kama alipata majibu, akamgeukia Sandra.







“Wapi naweza kumpata Isaac?”

“Wa nini, Kaguta? … Nimeshakuambia haiwezekani.”

“Nijibu maswali yangu.”

“Anaishi kurasini, nyumba namba 898.”

“Unaweza nambia anapendelea kitu gani, ama kutembelea maeneo gani … au ni mtu wa aina gani?”

“Anapenda sana mpira. Huwa hakosi kwenda kutizama mpira hasa Samaki Samaki ya maeneo ya Mbezi beach.”

“Ok.”











Kaguta akachukua simu toka mfukoni mwake akapakua application ya mpira na kuangalia ratiba ya mechi kubwa iliyo karibu, akaona mojawapo iliyopo kesho tena ikiwa ya ubingwa wa ulaya. Alitabasamu, akaenda kwenye reminder ya simu na kuweka tarehe ya mechi hiyo. Alipomaliza, alinyanyuka akamtizama Sandra na macho ya ahadi.











“Naomba niende nikuache upumzike. Tutaonana karibuni.”

“Okay. Take care.”

“You too!”









Kaguta akauendea mlango na kutoka nje. Sandra alivaa nguoze akajilaza kitandani. Hakuoneana yupo sawa. Si kingine itakuwa ni mawazo yalikuwa yanambana. Ila baada ya muda mafuriko ya usingizi yalimsomba na kumpeleka ng’ambo.







Ndani ya asubuhi ya saa mbili na nusu, Kaguta akawasili kwenye nyumba ya inspekta Vitalis Byabata. Alipiga honi akatoka mama Miraji, ama Bernadetha kwa jina alilopewa na wazazi wake. Wakasalimiana kwa bashasha la furaha kisha Kaguta akamuulizia inspekta.







“Hayupo, ametoka muda si mrefu. Nilidhani mmewasiliana.”

“Hapana. Atakuwa kaenda wapi?”

“Ameniaga anaenda hospitali kwenda kumuona dokta Rajesh Deepti wa Royal Hospital.”

“Kuna tatizo lolote?”

“Hapana. Ni ameenda kufanya tu upelelezi wake. Dokta Rajesh ndiye alikuwa daktari wa mume wangu, na yeye ndiye alikuwa anaujua ukweli wote kuhusu kifo cha mume wangu kabla ya kuupotosha umma kwa sababu zisizojulikana.”

“Sawa. Vipi mtoto ameenda shule? Yani leo nilipitiwa na usingizi kama mzoga.”







Bernadetha alicheka kidogo kisha akajibu;







“Usihofu. Vitalis ameenda naye alipoamka tu asubuhi.”

“Afadhali. Sasa acha mie niende huko hospitali nikaonane naye.”

“Safari njema.”

Kaguta aliwasha gari, ila kabla hajasogea, Jombi alitokezea tokea ndani.

“Aaaah bwana Kaguta, kweli unataka uondoke hata hatujasalimiana?”







Kaguta alicheka kwanza ndio akajibu.







“Aisee. Samahani sana ndugu yangu. Si unajua tena, haraka haraka! Vipi lakini?”

“Safi tu. Wewe je?”

“Aaah … Nipo njema tu!”

“Nadhani sasa ni bora ukashuka unywe chai kabisa.” Bernadetha alishauri.

“Najua hujatia chochote mdomoni, Kaguta. Wala usifikirie kunipiga sound zozote.” Bernadetha alisisitizia. Kaguta akabakia bila ya maneno, alishuka akaungana na Jombi na Bernadetha wakaenda ndani.







Huko ndani ya Royal hospital kwenye sakafu ya tano, Vitalis alikuwa mbele ya mlango mpana ulioandikwa jina la Doctor Rajesh Deepti. Chini ya jina hilo kulikuwa na ratiba ya maonano, Vitalis aliitizama kisha akagonga mlango.









“Who is it?”







Sauti iliuliza ikitokea ndani. Vitalis hakujibu. Alitulia kama vile hakusikia hilo swali.







“Ingia.”









Vitalis akafungua mlango na kuingia ndani.









“Nani wewe? Taka nini hapa jaona ratiba ka mlango?” Mtabibu aling’aka.





Vitalis aliketi taratibu kisha akamtizama daktari aliyekuwa na uso na nywele za kihindi usoni akiwa na miwani ya macho.









“Naitwa Inspekta Vitalis Byabata.” Inspekta akaonyeshea kitambulisho chake. “Nina maongezi na wewe.”

“Maogezi bhanaa … Taka nini kwangu?”

“Unamjua huyu?” Vitalis alitoa picha ya Malale akamuonyeshea mtabibu. Mtabibu akashtuka.

“Sijui mimi!”







Vitalis akatabasamu kwa dharau.









“Mbio zako hazitokupeleka popote, dokta. Ni bora ukaeleza ukweli bila shuruti.”

“Kweli gani nataka phephe? … Sijui kitu. Toka kwa ofisi yangu bhana niko bhize. ”









Vitalis alinyanyuka akaufuata mlango akaufunga na komeo. Mtabibu Rajesh akawahi kuchukua simu yake ya mezani, kabla hata hajasema lolote, Vitalis akawa tayari ameshamfikia na kumpokonya simu kisha akatoa bunduki yake na kumuonyeshea.









“Kwanini uliongopa juu ya kifo cha Malale?”







Uso wa Vitalis ulibadilika na kuwa mchungu ghafula, hakuonyesha masikhara hata punje. Rajesh alikuwa mpole ghafla, macho yalimtoka na pumzi yake ilikuwa inapanda na kushuka kwa haraka.









“Usiniue, takwambia … takwambia kila kitu!”

“Sema kabla sijakupa tiketi chap ya kwenda jehanam!”

“Nilitumwa! Kama singalifanya. Ingeniua!”

“Nani?”

“Temvu … Temvu na wenzhake.”

Vitalis alishusha mkono wake wenye bunduki akaketi.

“Si nimeshaambia wewe. Nenda bhasi.”

“Inabidi twende wote kituoni. Una mashtaka ya kujibu.”

“Hapana! Hapana kwenda kituoni mimi.”

“Embu tusipotezeana muda bwana mzee. Simama twende kituoni, si mpaka tulazimishane.”









Japokuwa Vitalis alitia msisitizo, Rajesh hakuwa tayari kwenda popote. Ilibidi nguvu itumike. Vitalis alimnyanyua mtabibu kwa nguvu kwa mtindo wa kukwida akamburuzia mpaka mlangoni.









Akiwa katika purukushani ya kutaka kuufungua mlango, Vitalis akaona kitu kiunoni mwa mtabibu baada ya shati la mtuhumiwa wake kupanda. Aliona tattoo! Tattoo ile ile ambayo yeye anayo ikiwa imefunikwa na shati lake la kitenge.











“Umenidanganya, sio? Wewe ni nani?”









Vitalis aliuliza kwa sauti ya kufoka. Huku akimuonyeshea bunduki mtabibu Rajesh.







“Si ameshaambia wewe. nini taka kwangu?”

“Wewe ni mfuasi wa Mr Kim. Si ndio? … Hiyo tattoo umetoa wapi?”









Rajesh akashikwa na kigugumizi. Alichomekea shati lake akatengenezea miwai yake iliyokaa upande.









“Taka nini kwangu phephe?”

“Jibu swali langu, upesi!” Vitalis aliamuru. Kufumba na kufumbua, Rajesh alinyanyua mguu wake wa kuume akatandika mkono wa Vitalis uliobebelea bunduki. Bunduki ikarukia kando. Haraka kama upepo, Rajesh akaruka teke na kumsigina Vitalis kifuani, Vitalis akadondokea chini kama fuko la marando. Rajesh akavua koti lake la utabibu akaliweka juu ya meza.







“Si unataka vita, acha uipate sasa.”



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/





Alisema Rajesh tena kwa lafudhi nzuri tu tofauti kabisa na ile ya mwanzoni aliyokuwa anaigiza.







Vitalis alichumpa kwa kutumia mikono yake akanyanyuka na kumtizama Rajesh. Wote wakakunja ngumi kwa mtanange.









Rajesh alirusha teke akiwa hewani, Vitalis akakwepa, lle kujiweka tu sawa, zikarushwa ngumi zingine mbili za haraka, Vitalis akaipangua moja na kuikwepa nyingine ambayo ilienda na kurudi kama kiwiko haraka kikambatua inspekta kichwani. Rajesh akatabasamu. Vitalis akaguna.









“Umemaliza?” Vitalis aliuliza. Vuup! Likaja teke lingine likifuata tumbo la Vitalis, Vitalis akajiweka ubapa haraka, teke likapita kama gari moshi. Rajesh alipolirejesha teke lake kwa mfumo wa goti, Vitalis akadaka goti lile na kulisukumia kando. Rajesh akaja tena kwa pupa, mara hii akitishia kurusha teke la mguu wa kulia ingali anataka kuleta la kushoto.









Vitalis akamtangulia Rajesh hatua mbele, akauwahi mguu ule wa kushoto kwa kuukanyaga kama mtu anayepiga breki ya gari na ule wa kulia uliokuwa unatishia akaudaka na kuurejesha chini.









“Kuna jipya? Au nianze na mimi kushambulia?”









Vitalis aliuliza. Upesi, Rajesh akachukua waya wake wa vipimo uliokuwa mezani akautuma umchape Vitalis usoni. Bahati haikuwa yak wake kwani Vitalis aliinama, waya ukapita kisha akapiga ngumi mkono wa Rajesh mbele kidogo ya kwapa, Rajesh akapigwa na ganzi paaap! Waya ukadondoka chini.











“Mi naona twende tu kituoni. Tunachoshana hapa!”









Vitalis alisema huku akitengenezea shati lake na kuigiza kama mtu afutaye vumbi. Rajesh alimtizama kwa hasira, akajaribu tena kushambulia kwa kupiga sarakasi atue na miguu kichwani mwa Vitalis, ila haraka mikono yake ikatenguliwa na miguu ya Vitalis akadondoka chini!









Vitalis akasonya kisha akaanza kuifuata bunduki yake. Alipoikota na kuiweka kiganjani akasikia mlio mkali wa kioo. Alipotizama, hakumuona tena Rajesh! Haraka akakimbilia dirishani kuchungulia, akamuona Rajesh kwa chini akiyoyoma.











“Shit!”









Vitalis alifoka. Alipepesa pepesa macho yake huku na huko ndani ya ofisi, akaona simu kubwa LG nyeusi akaitwaa na kuiwasha. Ubaya akashindwa kutambua pattern iliyowekwa, ila hakuiacha, aliiweka mfukoni akaondoka zake. Baada ya dakika ishirini akawa yupo nyumbani. Alikutana na Bernadetha ama mama Miraji akamueleza kila jambo alilokumbana nalo huko.









“Kama ilivyokuwa msaada wa Jombi kwa Miraji. Daktari naye aliwasaidia wakina Mtemvu ili wamalizane wenyewe kwa wenyewe bila wao kujua. Nimeona ile tattoo kiunoni mwake, ina maana ni mfuasi wa bwana Kim.”







Alisema Vitalis kwa kujiamini.









“Mmmh … huyu bwana Kim ananitisha kusema ukweli. Inspekta, najua kwako ni vigumu, ila kama waweza naomba uachane naye tupate kuishi maisha yetu tu ya kawaida. Ni kama vile tunapambana na bahari, ni mkubwa mno.”

“Hapana, mama. Siwezi kumuacha. Embu fikiria ni wangapi amewaumiza kwa biashara zake haramu? … Vijana wengi huko mitaani wanakufa kwasababu yake. Nchi yetu i mashakani na dhambini kwa ajili yake. Najua yeye ni goliath ila nasi tutajitahidi tuwe Daudi.”

“Sawa. Nakuombea kila siku Mungu akupe salama. Sitaki kukupoteza, kila unapotoka na kurudi nyumbani salama ni ahueni kwangu.”

“Nashukuru sana kwa kujali. Umekuwa mama yangu wa pili sasa.”









Bernadetha alicheka kidogo akamtizama Vitalis.







“Kujali ni jukumu mojawapo la mwanamke.”









Vitalis akatabasamu na kutizama chini. Kwa muda usiopungua wala kuzidi dakika mbili kukawa kimya. Vitalis alimtizama Bernadetha machoni, naye Berna akafanya vivyo hivyo. Ni kama vile kuna kitu walikuwa wanakiona sisi tusikione. Vitalis alinyanyua mkono wa kuume wa Bernadetha akaushika kama vile anataka uvalisha pete. Aliupeleka mkono huo kinywani akaubusu. Bernadetha akatabasamu.











“Nashukuru kwa yote unayonifanyia.” Vitalis alisema kwa sauti ya chini. Bernadetha hakusema jambo, aliacha macho yake makubwa yaseme kila kitu kwamba anafurahi kusikia vile. Labda ndio kilikuwa kipindi muafaka naye akajihisi mwanamke tangu mumewe afariki.









Kwa muda wakaendelea kutizamana wasione lolote linaloendelea ulimwengu mwingine. Huko nje ya nyumba, Kaguta aliwasili. Alikuwa amewekelea earphone masikioni kichwa chake kikidunda kama kitenesi. Alipopanda kibarazani kabla hajagonga mlango macho yake yaliruka ndani, na humo akamuona Vitalis akiwa na Bernadetha katika mkao ule wa mtizamano. Kaguta akatabasamu, na bila ya kusema lolote akageuza na kunyata taratibu akaondoka eneo lile.













Vitalis aliuteka mkono mwingine wa Bernadetha akaushikilia, sasa mikono yote akawa nayo. Taratibu akapeleka mdomo wake kinywani mwa Bernadetha akambusu mwanamke pap na kuacha kama vile alikuwa anataka kusikilizia mtendwa atasemaje.











Bernadetha akawa kimya zaidi alitabasamu. Vitalis akapeleka tena mdomo wake kwa Bernadetha, Bernadetha akaupokea mdomo wa Vitalis kwa kuufunda. Ila mara wakasikia mlango wa chumbani unafunguliwa, zoezi lao likakomea hapo. Punde Jombi akawa amefika sebuleni na kusalimia.











“Hivi mnajua leo ni siku ya ripoti ya Miraji?”







Jombi aliuliza. Vitalis na Bernadetha wakatizamana. Bernadetha akatabasamu.









“Najua. Naenda huko jioni hii. Acha nikajiandae.” Bernadetha alisema kisha akatoka na kuelekea jikoni akawaacha wanaume wale wawili watete mawili matatu. Vitalis akamueleza Jombi yale yaliyotukia hospitali. Jombi akaonekana kushtushwa na taarifa hizo.

“Bwana Rajesh ni coordinator wa bwana Kim kwa wahindi wote walipo hapa nchini. Kumpata kwake ni mojawapo ya hatua japo ya mbali ya kumpata bwana Kim.”

“Una maanisha nini kusema coordinator wa wahindi.”

“Ni hivi, kila race iliyopo nchini ina coordinator wake, ama tuseme muwakilishi kwa mr Kim. kwa watu weusi, coordinator ni bwana Isaac Makongo. Kwa wahindi ni huyo, Rajesh Deepti. Na kwa wazungu ni bwana Wayne Ford. Si rahisi kuwapata hao watu. Wana viapo vya binafsi.”

“Unaweza ukaniambia nitawapata wapi?”

“Kusema ukweli, sijui. Hawana makazi ya kudumu yanayojulikana. Ni watu wa kuhama hama pia kusafiri huku na kule.”









Inspekta alishusha pumzi ndefu akashika tama. Ni wazi aliona kuna mlima mkubwa mbele yake anaotakiwa kuusogeza. Kazi haikuwa nyepesi hata punje. Alinyanyuka akaaga, akaenda kuoga kisha akashika tanakilishi yake na kuitia modem, akaanza kuperuzi mtandaoni.









Aliandika jina kamili la bwana Kim na kubonyeza kitufe cha kutafuta, paap majibu kadhaa yakaja. Bwana Kim akatambulishwa kama mfanyabiashara mkubwa wa mambo ya mawasiliano kwa kupitia kampuni yake ya Bartel yenye makao yake Barmuda.







Zaidi ya hapo, picha mbalimbali za bwana Kim zikarushwa na hata makampuni ambayo ana ubia nayo, hadi ambazo ameweka hisa zake kwa wingi; makampuni ya vinywaji laini, makampuni ya bidhaa za wanawake, makampuni ya kilimo na kadhalika. Mitandao ikaendelea kumwaga maneno juu ya bwana Kim kuwa ni mfanyabiashara mkubwa na mwenye nguvu katika bara la Afrika na Amerika ya kaskazini.











Inspekta aliporidhika na taarifa alizozipata, akafunga tanakilishi yake na kujilaza kitandani. Alikuja kuamshwa baadae na sauti ya Kaguta. Ilikuwa ni jioni, jua limeanza kupoteza nguvu zake. Inspekta alinyanyuka akaenda sebuleni kukutana na Kaguta ambaye alikuwa amekaa na Jombi kwenye kochi. Wakasalimiana na kujuliana hali, Kaguta akaanza kueleza alichokipata toka kwa Sandra, mpaka kumtambulishwa kwake kwa bwana Isaac Makongo.











Inspekta na Jombi wakashtushwa na taarifa za bwana Makongo, nao huo ukawa mwanya mzuri kwao kuanza kumtafuta mtuhumiwa wao huyo baada ya inspekta naye kueleza ni wapi alipogumana nalo hilo jina.









“Kwa mujibu wa maelezo ya Sandra, Isaac Makongoanaishi kurasini, nyumba namba 898. Picha zake hizi hapa. Anapendelea sana kutizama mpira, na maeneo yake ni Samaki Samaki mbezi beach.” Kaguta alimwaga maelezo huku akiwa kazitandaza picha juu ya meza.

“Basi hatuna tena muda wa kupoteza, nadhani ni muda wa kuanza kufanya kazi. Tupange ni jinsi gani tunaweza kumpata huyu wakala haraka iwezekanavyo.” Inspekta alisihi.

“Kweli, ila inabidi tuwe waangalifu mno. Huyu mtu si wa kawaida.” Jombi naye akasisitiza.

“Kabisa!” Kaguta akadakia na kuendeleza maneno, “Inabidi tuanze pole pole. Kesho kutakuwa na mechi kubwa ya UEFA, najua hatokosa maeneo yake hayo. Alimradi najua sura yake, nitamfuatilia. Niacheni hiyo kazi.”

“Hakuna shida. Ila hakikisha unatupasha kila kinachotukia huko.” Inspekta alisema.

“Nitafanya hivyo.” Kaguta akamtoa hofu.

“Mbali na hayo, kuna baadhi ya taarifa nimezipata toka mtandaoni; makazi ya bwana Kim.” Inspekta alieleza. Jombi akatikisa kichwa chake huku akipunga mkono kama vile mtu anayeaga,

“Hakuna kitu cha ukweli huko. Hakuna mtu anayejua makazi ya bwana Kim hata wafanyakazi wake. Mitandao yenyewe haina data halisi juu ya huyo bwana.”

“Sasa ni wapi tutapata taarifa zake?” Inspekta akauliza.

“Ni kuzitafuta tu. Otherwise hakuna lolote.” Jombi alishauri. Inspekta na Kaguta wakawa kama wamekamatwa na kabutwaa.

“Kwanza, hakuna aneyejua sura halisi ya bwana Kim. Sura ambazo zimewekwa mitandaoni si za kwake, ni bandia na za kutengenezwa. Ni watu wachache mno wanaomjua the real Kim, watu wake wa karibu mno, kama vile familia yake.”

“Sasa hata hiyo familia yake tutaikotea wapi?” Kaguta aliuliza.

“Hapo ndipo kwenye shida. Kama nilivyosema mwanzo. Hakuna mtu anayejua haswa maelezo ya karibu ya bwana Kim. Ni kazi ya kutafuta hayo.”

“Hakuna linaloshindikana. We shall do it.” Inspekta Vitalis alisema kwa kujiamini. Kaguta akatikisa kichwa kumuunga mkono.

Baada ya muda mfupi, simu ya inspekta ikaita. Alipigiwa na Bernadetha, alipokea akaweka simu sikioni;

“Hallo … Hospital? … Haya sawa, nitakuwa hapo muda si mrefu.”







Simu ilipokata akawatonya wenzake;









“Miraji ameruhusiwa kutoka. Inabidi niende nikamtoe, si unajua tena mambo ya utaratibu.”

“Twende!” Kaguta akatamka.

“Na mimi naomba niende.” Jombi naye akatia neno. Wakajiandaa na kujipakia kwenye gari, wakaelekea hospitali na kurudi na Bernadetha pamoja na Miraji. Miraji alionekana kuchoka. Macho yake yalikuwa yanafunguka na kufunga. Ni kama vile alikuwa amelemewa na usingizi mzito.

“Daktari amesema anahitaji mapumziko. Asifanye kazi yoyote ngumu kwa sasa zaidi ya mazoezi madogo madogo.” Bernadetha alilonga.









Jombi akishirikiana na inspekta Vitalis wakamshusha Miraji na kumpeleka moja kwa moja kitandani kwenye chumba alalacho Jombi.









“Mungu mkubwa. Sikujua kama kuna siku mwanangu atatoka hospitali.” Bernadetha alisema kwa tabasamu.

“Atapona tu, na atarudi katika hali yake.” Inspekta akamtia moyo mwanamama.



*****





Wakati saa ya ukutani inatamka ni saa moja kasoro tano tu, Inspekta Vitalis alikuwa tayari yupo sebuleni akiwa kavaa shati la kitenge na suruali nyeusi ya kitambaa.









Ilipohitimu tu saa moja kamili, Marietta akatoka chumbani akiwa kavalia sare za shule akaenda kukutana na inspekta sebuleni. Punde, mama mtu, Bernadeta, naye akatoka akiwa kajitanda khanga. Walisalimiana na inspekta kisha wakaagana.









“Leo una ratiba gani, baba?” Bernadetha aliuliza na uso mkarimu.

“Nampeleka mwanangu shule.” Inspekta akajibu na tabasamu kisha akamtizama Marietta.

“Baada ya hapo?”

“Baada ya hapo, narudi nyumbani.”

“Mmmh … Unaniongopea.”







Inspekta alitabasamu kisha akambeba Marietta.









“Kuna sehemu hivi nitapita. Kuna kakazi kadogo nataka kukamalizia.”

“Utarudi saa ngapi?”

“Mapema tu. Nitampitia na mtoto.”

“Haya sawa. Kazi njema.”

“Ahsante. Kwaheri!”









Inspekta alifungua mlango akatoka nje na Marietta aliyemshusha chini wakawa wanatembea. Mpaka wanapotelea, Bernadetha alikuwa ameshika mlango akiwatazama kwa macho yaliyojaa tenzi ya furaha. Taratibu chozi likamshuka. Akalifuta huku akitabasamu. Alifunga mlango akarudi ndani na kuanza kufanya kazi za hapa na pale; kuosha vyombo, kufagia, kudeki na kuandaa chai.











Wakati saa ya ukutani ikitamka ni saa tano kamili, inspekta alikuwa yupo kituo kikubwa cha polisi ofisini kwake, akiwa anaandika maelezo kwenye faili moja lililobebelea maandishi makubwa yasomekayo; MTEMVU’S CASE kwa rangi nyekundu. Pembeni ya meza yake, kulikuwa na kikombe cheupe kilichobebelea kahawa nyeusi ifukayo moshi. Mara kwa mara wakati anaandika, akawa anapeleka kikombe kile cha kahawa mkononi na kuria mafundo kadha wa kadha.











Alipomaliza kuandika. Alivuta tanakilishi iliyokuwepo mezani kwake akaandika jina la Isaac Makongo na kuanza kuperuzi. Majibu yakaja na picha pia kwamba ni mfanya biashara mkubwa asafirishaye nyama za kusindika nchi za nje, lakini pia ni mchezaji mpira mkongwe aliyewahi kuiwakilisha nchi vizuri kimataifa kwa kuchezea klabu kubwa duniani ya Ajax ya uholanzi na Marseille ya ufaransa.









Wakati inspekta Vitalis akiendelea kuperuzi, kwa kupitia dirisha la ofisi yake tunamuona mwanaume mmoja mwenye mwili mnene akitoka kwenye ofisi ilyopachikwa kibandiko kilichosomeka; OCD. Mwanaume huyo alipoufunga mlango sauti ikazalishwa na kufika masikioni mwa inspekta Vitalis ambaye aliacha kidogo kutazama skrini ya tanakilishi yake na kurusha macho huko.











La haula! Akamuona mtu anayemperuzi; bwana Isaac Makongo. Inspekta hakuamini, alitizama picha za kwenye mtandao kisha akarudisha tena uso wake kwa mtuhumiwa wake, bahati mbaya hakumuona tena, alikuwa ashapotea eneo la mlangoni mwa OCD. Inspekta akanyanyuka haraka akatoka ofisini kwake na kuelekea nje, huko akakuta gari moja aina ya Suzuki vitara nyeusi yaondoka.









Inspekta alipepesa macho yake huku na huko akaona pikipiki ya polisi. Alirudi ofisini haraka akakwapua ufunguo kwa mwenzake akapanda pikipiki na kuanza kufuatilia gari lile Suzuki Vitara kwa nyuma taratibu.









Baada ya mwendo wa dakika kumi, Suzuki ikapaki hoteli moja kubwa. Isaac akashuka na kuingia ndani. Inspekta naye akafanya hivyo, akapaki pikipiki yake na kuingia ndani. Bahati mbaya hakumuona tena bwana Isaac. Alitumia kitambulisho chake cha polisi kupita kila eneo lakini hakufanikiwa. Isaac hakuwepo kabisa kila eneo.













Inspekta alitoka ndani ya hoteli na kwenda nje kwa mlengo wa kumngoja mlengwa wake atoke. Ajabu, hata gari la mtuhumiwa wake hakulikuta. Alimwendea mlinzi akamuuliza. Mlinzi akamuambia hilo gari limetoka muda mrefu tu. Inspekta akashika kiuno huku akitoa macho yake kama ndubwi. Alimezwa na butwaa. Hakuelewa kilichojiri. Alipanda pikipiki akarudi kituoni akaenda kuonana na OCD.











“Samahani, mkuu. Kuna mwanaume ametoka ndani ya ofisi yako muda si mrefu, amevalia suti na miwani ya macho. Naweza nikamjua ni nani?”

OCD alishusha miwani yake akamtizama inspekta.

“Kwani kuna tatizo, inspekta?”

“Hamna, nahisi nimemfananisha hivi …”

“Na nani? Ulimuonea wapi?”

“Aaahm … Ni kwanba kuna kesi fulani hivi naifuatilia. Na kuna mtu mithili yake ndio mana nikauliza.”







OCD alikunja sura yake kidogo akalaza mgongo wake kwenye kiti chake kirefu na kumtizama Vitalis kwa sekunde kadhaa kisha akafungua mdomo;

“Anaitwa Isaac Makongo, ni mfanyabiashara.”

“Hakuna kingine unakijua zaidi ya hapo?”

“Hapana. Wewe je?”

“Hamna.” Inspekta alijibu kisha akanyanyuka. “Nashukuru, mkuu. Naomba niende.” Inspekta alisema kisha akajigeuza kuufuata mlango. Aliposhika kitasa, OCD akamuita. Inspekta akageuka.

“Naomba ulete hapa hilo faili la kesi ya Isaac.”

“Unasema?”

“Hiyo ni amri. Lete hapa hilo faili la kesi ya Isaac, upesi!” Uso wa OCD uligeuka na kuwa wa mbogo. Inspekta akashangazwa na hiyo hali.

“Unasubiri nini? Kalete!”





http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Inspekta aliendea ofisi yake akapekua na kumletea OCD faili jingine. OCD akalipokea na kuliweka juu ya meza yake.









“Kesi hii imeshafungwa. Rasmi.” OCD alisema huku akimtizama inspekta Vitalis. Inspekta hakusema jambo, alitoka akarudi ofisini kwake akiwa na sura ya mawazo. Alishika tama akiwa amewekea ndita. Kwa muda kama wa dakika kumi na tano akawa anaatafakari. Mwishowe alizima kila kitu akatoka ofisini.







Ndani ya usiku wa saa nne maeneo ya Samaki Samaki Mbezi beach makonde, Kaguta alikuwa yumo hapo akiwa amekaa kwenye kiti kirefu mbali kidogo na runinga kubwa. Watu walikuwa pomoni wakiwa wameshikilia vinywaji vyao walivyokuwa wanavipeleka vinywani huku macho yao yakipewa ajira ya kutizama kioo kikubwa kilichokuwa kinaonyesha mechi ya nusu fainali ya kombe la UEFA kati ya Juventus na Altetico Madrid.











Macho ya Kaguta yalikuwa yanatizama huku na kule kumtafuta bwana Isaac Makongo. Hakuwepo katika lile eneo, ila baada ya dakika kadhaa akafika akiwa katika mwendo mkali. Tukio lake la kwanza kulifanya ilikuwa ni kutizama dakika ngapi za mpira zimempita kisha akaagizia kinywaji na kuketi vizuri aufaidi mchezo.











Kwa dakika kama tano, Kaguta akamsoma bwana Isaac Makongo anashaingilia timu gani. Alipogundua hilo, taratibu akajisogeza karibu na mlengwa wake akaanza na yeye kushangilia kwa pupa timu ile ile anayoishangilia bwana Isaac.









“Funga haoo mbwa! Leo Juventus wataisoma nambaa!” Yalikuwa maneno ya Kaguta. Aliendelea kushangilia na kushangilia. Taratibu Isaac akaanza kumuongelesha.

“Umeona pale … Daah yani asingemkata angefunga! Alafu refa kanyamaza. Fala kweli!” Isaac alitupa lawama.

“Kweli. Hawa wanabebwa!” Kaguta akaunga mkono hoja.











Mchezo ukaendelea. Bwana Isaac akijua kapata mshabiki mwenzake aliyekuwa anamshirikisha mara kwa mara kwenye kila tukio linalotokea uwanjani. Ulipofika muda wa mapumziko, Isaac alitoka akafuata gari lake. Kaguta akamuita mhudumu;









“Mambo?”

“Poa!”

“Naweza nikapata grants ndogo?”

“Ndio!”

“Naomba basi.”







Mhudumu alienda akarudi na alichotumwa.









“Ahsante. Mbona unaonekana umechoka mpendwa?”









Mhudumu alitabasamu pasipo kutia neno.









“Naitwa Erick, mwenzangu unaitwa nani?”

“Naitwa Salome.”

“Wow! Una jina la mama yangu!”

“Kweli?”

“Ndio. Pole mama kwa kazi.”

“Ahsante.”

“Sasa unaonaje ukapata na wewe moja mbili tatu? … Siwezi nikakaa hapa nakunywa wakati mama yangu amejikunyata tu.”

“Ahsante. Nashukuru.” Salome alisema kwa tabasamu nene.

“Naomba basi uniletee na maji ya kunywa.” Kaguta aliagiza tena. Mhudumu akashika njia kwenda kufuata maji, Kaguta akamsindikiza kwa macho yaliyokita maeneo ya kiunoni na makalioni.

“Mungu wetu mkubwa jamani, khaa! Wote huo wa kwake?” Kaguta alijisemesha na kutabasamu mwenyewe kisha akajilamba kama vile mtu aliyetoka kula chakula kitamu. Muhudumu aliporudi, akamtaka wakae pamoja.

“Niko bored hapa kwa kweli. Naomba basi kampani, mama yangu.”

‘Tatizo boss. Akiniona nimekaa atakasirika.”

“Usijali, nitaongea naye.”









Salome akaketi pembeni ya Kaguta na kuagiza kinywaji aina ya savanna. Wakawa wanapiga soga za hapa na pale na Kaguta ambaye kwa muda alisahau kama mechi inaendelea na mlengwa wake amesharudi.











“Yani wewe bwana unan’chekesha kweli!” Salome alisema huku akicheka kwanguvu.

“Kweli nakuambia. Mie dada yangu alikuja kuomba kazi hapa wakamkatalia katakata kwa kuwa si mzuri. Miguu imeelekea kusi-kaskazi!”

“Mmmh labda kama kuna vigezo vingine, si hiko. Mbona tuliokuwepo hapa ni kawaida tu.”

“Wa kawaida? … Nani kasema? Yani hapa natamani nikuagiza tena nikuone tu unavyotembea.”









Salome akaangua kicheko.









“Wapi bwana. Kawaida tu!”

“Agiza! … Agiza! Mbona umemaliza alafu upo kimya, mama?”









Salome akaagiza tena Savanna nyingine. Taratibu zikaanza kumuingia kichwani. Kaguta naye akazidisha maneno kumsifia mwanamke kama vile anaoga na mafuta ya nazi ananawia uso maziwa fresh. Mwanamke akaanza kurembua na kurembua. Cheko mia nane.









Kaguta alipokuja kushtuka, bwana Isaac Makongo hakuwepo. Watu ndio walikuwa wanatawanyika mechi imekwisha. Kaguta akanyanyuka na kwenda kutizama parking, loh! Hata gari la Isaac halikuwepo. Alijilaumu kwa kutukana matusi mbalimbali. Aliamua kurudi ndani na kuendelea na Salome ambaye alimng’ang’ania mpaka wakaondoka wote kama fidio la siku yake aliyoipoteza kizembe.











Siku iliyofuata akakutana na wenzake; Vitalis na Jombi akawaeleza kilichotokea. Naye Inspekta Vitalis akaeleza ilivyotokea baada ya kumuona bwana Isaac Makongo kituoni, wakashangazwa na mfanano wa matukio hayo.











Hapo ndipo Kaguta akakumbuka kauli ya Sandra … “Hakuna chochote mtakachofanikiwa mkiwa na hizo chapa. Kila mnalopanga mtatanguliwa hatua tatu mbele.” Kabla Kaguta hajawaambia wenzake chochote, simu ya inspekta Vitalis ikatetema. Ujumbe uliingia ukitokea namba mpya. Vitalis aliufungua akausoma;









“Acheni kupoteza muda wenu, ndugu zangu. Nadhani sasa ni wasaa wa kujenga taifa letu.”







Aliwaonyeshea wenzake huo ujumbe, wote wakawa wanajiuliza swali la nani kautuma ujumbe ule na ulikuwa una maana gani. Punde, sauti ya Miraji ikasikika toka chumbani;

“Sitaki! Sitaki nasema!”









Ghafla Miraji akaja sebuleni akiwa anapepesuka na mama yake anajitahidi kumsimamisha. Aliwatizama inspekta na Kaguta kwa ghadhabu akaropoka;









“Siwezi nikaishi na hawa mbwa! Nataka kwenda kwetu, sasa hivi!” Macho yake yalikuwa yanavuja machozi na uso wake ulikuwa umefungamana na hasira. Hakusubiri hata jibu, akaanza kuufuata mlango na mwendo wake wa kusuasua. Mama alimshika mkono, Miraji akautoa na kumsukuma mama mbali kisha akaendelea kuufuata mlango. Aliposhika tu kitasa, akadondoka chini kama mzigo puuh!









“Mungu wangu mtoto wangu!” Bernadetha alilalama huku akiweka mikono yake kichwani. Vitalis alimbeba Miraji akamuweka kwenye gari wamuwaishe hospitali. Kaguta akashika usukani, Jombi akaachwa atizame nyumba.









Hazikupita dakika kumi, Kaguta akaingiza gari hospitalini. Vitalis alimbeba Miraji wakamuingiza mpaka ndani wakapokelewa na kitoroli cha wagonjwa kikambeba Miraji mpaka chumba ambacho Miraji aliingia, wengine wakazuiwa.









“Ngojeni hapa.” Dokta alisema kisha akaenda ndani kumuhudumia mgonjwa. Inspekta, Kaguta na Bernadetha wakaketi kwenye benchi kungoja majibu. Uso wa Bernadetha ulieleza hofu, machozi yalikuwa yanamtiririka, alilaza kichwa chake kwenye mkono wa inspekta, inspekta akamfuta machozi na kiganja chake akimtaka aache kulia.

“Nilijua amepona sasa. Sikutegemea kama atarudi tena hospitali mapema hivi.” Bernadetha alisema kwa sauti nyong’onyevu.

“Usihofu. Atapona na tutaondoka naye.” Inspekta Vitalis alisema kwa kujiamini. Kaguta naye alimwaga tabasamu kuonyesha matumaini.









Baada ya muda wa dakika ishirini, daktari akaja kutoa majibu.









“Uti wake wa mgongo bado haujatengemaa, kusimama na kutembea kunakuwa shida, lakini pia hata fahamu zake zinakuwa na kasoro ndogo ndogo mara zingine. Ila yupo sawa, na mnaweza mkaondoka naye. Hakikisheni apate mapumziko zaidi na mazoezi ili kurudufu afya yake kwa haraka.”









Baada ya hapo, Miraji akachukuliwa na kurudishwa kwenye gari. Gari lilipowashwa Miraji akamwambia mamaye;







“Nipeleke nyumbani. Sitaki kwenda na hawa watu.”











Mama hakuzozana, akamtaka tu waende kwa inspekta ili wamchukue Marietta alafu waende nyumbani.Miraji akakubali. Marietta alienda kuchukuliwa kisha gari likaelekea nyumbani kwa wakina Miraji. Walipofika, inspekta alitaka kumsaidia Miraji kutembea, Miraji akakataa. Hakutaka ashikwe na yeyote isipokuwa mama yake.









“Nitakuona lini tena, anko?” Marietta alimuuliza inspekta. Inspekta akatabasamu na kuchuchumaa wakawa sawa kimo.

“Utaniona mara nyingi tu, umesikia?”

“Ndio.”

“Haya, usiku mwema eenh …”









Maerietta alitabasamu akaenda ndani, akamuacha mama yake na inspekta Vitalis wamesimama karibia na mlango.









“Samahani kwa yote yaliyotokea, Vitalis.” Bernadetha alisema huku akimtizama inspekta Vitalis machoni. Inspekta alitabasamu kama vile hakuna lolote liendealo, akamkumbatia Bernadetha na kumnong’oneza;

“Usijali, nipo sawa. Naelewa.”

Bernadetha alimkumbatia inspekta Vitalis kwanguvu akamwambia;

“Nitakumiss sana. Naomba uwe unakuja kun’tembelea.”

“Nitakuja. Kamwe usitie shaka juu ya hilo.”









Baada ya hayo maongezi, inspekta Vitalis na Kaguta wakaaga. Walimuacha Bernadetha pale pale mlangoni machozi yakimtoka. Baada ya gari kutokomea, ndipo Bernadetha akaingia ndani.











“Sasa itakuaje, Vitalis?” Kaguta aliuliza.

“Kuhusu nini?”

“Mama Miraji.”

“Sijui. Nilikuwa tayari nimeshamzoea.”

“Usihofu. Yule mtoto ana kimuhe muhe. Akitulia atajua jinsi maisha yanavyokwenda.”

“Natumai itakuwa hivyo.”









Inspekta hakusema tena neno lingine mpaka anafika nyumbani kwake. Yeye na Kaguta walishuka wakaingia ndani, wakaendeleza kikao chao pamoja na Jombi.











“Kuna jambo moja alipata kunambia Sandra juu ya hizi chapa. Alinambia hakuna kitu tutakachofanya kikafanikiwa tukiwa nazo. Kila tutakachopanga tutanguliwa hatua tatu mbele.” Kaguta alimwaga maneno.

“Tutatanguliwa na nani?” Inspekta Vitalis aliuliza.

“Hakuna mwingine, ni jitu la kuangamiza.”







Inspekta alitulia macho yake yakionyesha anatafakari, baada ya sekunde nne akalipuka na hoja;

“Kumbee! Ina mana hata kule kisiwani ilikuwa ni vivyo hivyo, sio?”

“Ndio!” Kaguta akajibu.

“Sasa tunafanyeje?” Inspekta aliuliza. Wote wakamtizama Jombi kama vile ndiye aliyekuwa na majibu.

“Sijui cha kufanya!” Jombi alijipambanua. “Ni vyema sasa tumegundua kumbe twakimbiza kivuli.”

“Kuna haja ya kuondoa haya matattoo!” Inspekta alisema kwa uso mkakamavu.

“Tutaondoaje sasa?” Kaguta na Jombi wakauliza.

“I must figure the way out of this! … Lazima nitapata njia.”

“Haya. Utakapopata, usisite kutujulisha na sisi.” Kaguta alisihi, kikao kikafungwa wakaenda kulala.







Asubuhi na mapema, inspekta Vitalis aliamka na kwenda kazini. Alipofika alifungua droo yake akatoa faili lililoandikwa MTEMVU’S CASE kwa wino mwekundu, akalifungua na kulitizama kwa dakika kadhaa akitizama picha za matukio mbali mbali.











Aliliweka faili juu ya meza, akawasha tanakilishi yake na kwenda moja kwa moja kwenye faili ya kesi ya Mtemvu, akafungua na kuanza kuongezea baadhi ya taarifa mpya. Wakati anafanya hivyo, dirisha lake linalotizamana na la OCD likamteka akili.











Alimuona OCD anaongea na simu huku akiwa ameshikilia mkononi lile faili alilompatia kwa kulaghai ndimo lina kesi ya bwana Isaac Makongo. Baada ya OCD kumaliza kuongea na simu, aliliweka lile faili kwenye mkoba wake na kuanza kupanga panga makabrasha mezani. Wakati wote huo, inspekta akawa anatizama kwa umakini.









Masaa yalipita, inspekta akaendelea na kazi zake na mara moja moja kwa kuibia ibia akawa anatizama dirisha la mkuu wake. Alimaliza kazi yake ila hakutaka kuondoka. Alitulia kwenye kiti chake akawa anamtizama OCD kila anachokifanya. Ilipofikia mida ya saa nane za mchana, OCD akafungua ofisi yake na kutoka mkononi akiwa kabebelea ule mkoba aliloweka faili. Inspekta Vitalis naye alitoka ofisini kwake, taratibu akawa anamfuatilia OCD kwa nyuma.











OCD alipanda gari lake, akaondoka kituoni. Inspekta Vitalis alichukua pikipiki ndogo ya polisi akawa anamfuatilia OCD kwa mbali. Gari la OCD lilisimama eneo moja la kiwanja, baada ya muda mfupi likaja gari lingine, Suzuki Vitara nyeusi, na kupaki karibu na gari la OCD, OCD akafungua mlango wa gari lake akatoka na ule mkoba akaingia ndani ya gari lililokuja. Ilichukua dakika kumi OCD kurudi kwenye gari lake na kuondoka, nalo Suzuki Vitara liliwashwa na kuondoka. Inspekta Vitalis akaanza kulifuatilia Suzuki Vitara kwa mbali.





Kilomita nne zilitafunwa barabarani mpaka kufikia eneo ambalo Suzuki Vitara iliingia. Ilikuwa ni nyumba kubwa mno yenye geti pana la mbao. Inspekta Vitalis alisogea hilo eneo akasoma namba ya nyumba … 898. Akakumbuka maneno ya Kaguta ya kwamba bwana Isaac Makongo anaishi kurasini nyumba namba 898. Inspekta Vitalis alishuka kwenye pikipiki, akasogelea geti na kugonga. Mlinzi akafungua kitundu kilichokuwepo kwenye geti na kuuliza;

“Wewe ni nani?”







Inspekta Vitalis akaonyesha kitambulisho chake cha kazi. Mlinzi hakuuliza tena, akafungua geti na kumruhusu inspekta aingie. Ajabu inspekta alipoingia alimkuta mlinzi mwenye mapembe. Inspekta alistaajabu mno, mlinzi alitabasamu na kumwambia;

“Karibu. Wakati mkuu anapita alinambia kuna mgeni atakuja muda si mrefu. Kumbe ni wewe. Umekuja muda muafaka.”









Inspekta hakusema jambo, bado alikuwa kwenye butwaa kwani kadiri mlinzi yule alivyokuwa anaongea alikuwa anaongezeka kimo na kuwa mrefu, mrefu na mrefu zaidi.







“Leo ni mwisho wako, Vitalis Byabata.”









Mlinzi alisema kwa sauti nzito, haikuwa tena kama ya mwanzoni. Macho yake yalibadilika na kuwa ya simba. Mkia ulichomoza na makucha yakaamka, mwili wake ukawa mkubwa mithili ya mbuyu wa kale. Inspekta Vitalis alitumbua macho kuona yasiyoaminika. Alifungua miguu yake kufuata geti ila alishikwa na kubamizwa kwa nguvu ukutani. Alikabwa koo akatoa macho kama ngumi. Jasho lilimtiririka, alijitahidi kuvuta pumzi ila hakuipata. Alijitahidi kufurukuta ila hakuweza.









Mishipa ya kichwa ilimsimama. Alirusha miguu kwa kutapatapa. Macho yalianza kupanda juu ishara ya mwili kuwa tayari kupokea kifo kwa sasa. Zikiwa zimebakia sekunde kadhaa tu inspekta aende na maji, jitu lilimwachia kwa kumtupa chini. Inspekta akadaka hewa na kuivuta kama vile yupo mashindanoni.











Alishika shingo yake huku akikohoa. Mapafu yalipanda na kushuka kama vile puto. Taratibu mlinzi alirudi kwenye hali yake kama mwanzoni, japokuwa mapembe yalibakia palepale. Alifungua geti, akanyooshea mkono wake nje;

“Toka upesi!”









Alifoka. Inspekta alijikusanya taratibu akatoka nje. Mlinzi akafungua kisehemu cha wazi cha geti na kusema kwa tabasamu;

“Karibu tena.”









Inspekta alijikokota akaendea pikipiki yake akapanda. Kabla hajaondoka alitumia dakika mbili kutizama lile eneo kama vile haamini kilichotokea mule ndani. Alikohoa akajiuliza;

“Kwanini ameniacha hai?”











Aliwasha pikipiki akarudi ofisini. Nguo zake zilikuwa zimechafuka. Alipaki pikipiki akaelekea nyumbani moja kwa moja. Aliketi kwenye kochi sebuleni akawa anafikiria. Kwa muda wa dakika kumi na tano alikaa pale na kutafakuri. Mwishowe alinyanyuka na kuchomeka pasi kwenye umeme, pasi ilipopata moto wa kutosha alikunja mkono wa shati lake akabandika pasi eneo lenye tattoo. Alipiga kelele kali mno.











Alibandua pasi ikatoka na ngozi, ikabakia jeraha kubwa hapo. Jombi alikuja sebuleni akamkuta inspekta ana alama kubwa nyekundu ya kuiva mkono wake wa kushoto huku akiwa amekunja sura kwa ukali wa maumivu anayoyahisi.









“Inspekta, umefanya nini?” Jombi aliuliza. Inspekta hakujibu, alikuwa tu anaugulia. Jombi alihisi harufu, alipepesa macho yake kutizama akaona pasi ipo kwenye moto, na tena ina mabaki ya damu. Jombi alichomoa waya wa pasi toka kwenye umeme kisha akamgeukia inspekta Vitalis.









“Inspekta inabidi twende hospitali!”

“Hapana! .. Mpigie Bernadetha, mwambie aje upesi.” Inspekta aliingiza mkono wake mfukoni akatoa simu. Jombi akaipokea na kumpigia mama Miraji. Ndani ya muda mfupi mama Miraji akawasili maeneo

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/









. Bila kupoteza muda alianza kumuhudumia inspekta Vitalis kwa kumpakaa mafuta ya bunduki na asali kwa mbali kwenye jeraha. Zaidi ya hapo akampatia dawa ya kukabili maumivu na kumjuza utaratibu wa kupaka mafuta ya bunduki na asali kama tiba.









Inspekta alimtizama Bernadeta akatabasamu. Bernadetha naye akatabasamu na kuuliza;

“Mbona wafurahi?”

“Kwasababu mbili.” Vitalis alijibu.

“Zipi?”

“Moja, nimekuwa huru kuanzia sasa, sina tena chapa ya wadhalimu. Pili, nimekuona.”









Bernadetha alimwaga tabasamu pana, akasema;

“Nashukuru. Nimefurahi kukuona pia. Leo Marietta hajaenda shule kwa ajili yako.”

“Kwa ajili yangu?”

“Ndio. Anakungoja umpeleke shule.”

Inspekta alicheka kidogo akatia neno;

“Mwambie nakuja kumpeleka kesho. Naahidi.”

“Sawa.”

“Vipi Miraji anaendeleaje?”

“Anaendelea vyema tu. Yupo. Miraji ana hasira na ninyi, anaamini mpo upande ule ule na wale waliomuua baba yake.”

“Umemuambia chochote kuhusu mimi na Kaguta?”

“Hataki kusikia kitu kuhusu nyie. Ilibidi niongope ndio nipate kuja huku.”

“Pole sana. Atakuja kuelewa tu.”









Baada ya maongezi, mama Miraji aliingia jikoni akapika chakula kwa ajili ya majeruhi, Vitalis, kisha akaaga. Jombi akataka kwenda na Bernadetha akamjulie hali Miraji.









“Sasa mgonjwa unamuacha na nani?” Bernadetha aliuliza.

“Hapana. Mwache aende tu, mimi nipo sawa tu.” Inspekta Vitalis aliruhusu. Jombi na Bernadetha wakaondoka.







Jua likazama na kuchomoza.









Ingawa mkono wake ulikuwa unamuuma, inspekta Vitalis hakutaka kubakia nyumbani mwenyewe. Angeboreka. Alijinyanyua akajiandaa na kwenda kazini kama kawaida huku mkono wake akiwa kaufichama kwenye mkono mrefu wa shati lake jeusi. Ilikuwa ngumu kujua kama ana jeraha mpaka umtizame kwa makini jinsi anavyoulinda mkono wake huo na kutoupa kashkash za hapa na pale.











Kwa kuwa alingoja mpaka apate daladala lenye siti tena isiyo na bugdha, alichelewa kufika ofisini. Ilikuwa ni mida ya saa tatu tofauti na mida yake aingiayo ofisini ya saa moja. Alinyookea mlango wa ofisi yake, ajabu alipoushika ukafunguka bila ya kwazo.









“Alaah! Ina mana sikuufunga huu mlango?” Alijiuliza. Aliingia ndani akaanza kupekua mafaili yake, akakuta faili la MTEMVU’S CASE halipo. Haraka aliwasha tanakilishi yake akatizama faili la MTEMVU’S CASE lililopo humo, nalo halikuwepo.











Macho yalimtoka inspekta Vitalis. Alitoka kwa jazba akafuata ofisi ya OCD, aliposhika kitasa akasita. Alirudi ofisini kwake akafunga na kuamua arudi nyumbani. Aliketi sebuleni akawa anawaza. Alitikisa kichwa chake mara kwa mara huku akisonya. Mwishowe mawazo yake hayo yalimbeba kwa njia ya usingizi. Ni Kaguta ndiye alikuja kumuamsha na kumtoa akarefresh akili bar. Huko wakapiga soga, inspekta akamueleza Kaguta yote yaliyojiri.









Inspekta alikuwa anakunywa Heineken, Kaguta alikuwa anasukuma chupa kubwa ya Jack Daniels.







“Pole aisee. Inabidi uwe makini sana na OCD huyo.”

“Mshenzi sana huyo! Yani amenivunja moyo kabisa. Faili la ile kesi ina taarifa nyingi mno na za maana, kupotea kwake kumenirudisha nyuma mnooo.”

“Kabisaa.” Kaguta aliitikia kisha akapeleka fundo mbili za kinywaji chake. “Sasa kaka, kazi iliyokuwepo mbele yetu ni …” Kabla Kaguta hajamalizia, inspekta Vitalis alimzuia na kumuonyeshea alama ya tattoo mkononi mwake.

“Unakumbuka? … Hakuna litakalofanikiwa. Hatuwezi kupanga lolote ukiwa nayo.”









Kaguta aliitikia lakini macho yake yalionekana kutekwa na kitu nyuma ya inspekta Vitalis. Kaguta alifikicha macho yake kama mtu ambaye haamini anachokiona kisha akapiga fundo moja na kusema;











“Vitalis, yule ni Bakari au pombe zangu?” huku akionyeshea ishara kwa kichwa. Inspekta akajigeuza na kutizama.

“Eh! … Ndio yeye. Yupo na nani pale?”

“Sio Roby yule?”

“Ndio! Yule ni Roby!”

“Ina maana Bakari, hakufa?”

“Ndio mana tunamuona pale. Ila anaongea nini na Roby? Wanaongea kama watu wanaojuana kabisa. Ina maana Bakari …”









Kaguta alinyanyuka akataka kwenda, Vitalis akamshika mkono.









“Tuliza mihemko. Ngoja.”









Kaguta akakaa wakawa wanatizama huku wakishushia na vinywaji vyao. Roby na Kaguta waliongea kwa dakika kumi na tano tokea wakina Vitalis walipowaona, walipomaliza walilipa wakanyanyuka na kutoka nje ya bar, inspekta na Kaguta wakawafuata. Huko nje Roby na Bakari waliingia kwenye gari moja wakaondoka.











Vitalis na Kaguta wakazama kwenye gari lao na kuanza kuwafuata. Baada ya muda wa dakika tano za matembezi, gari la wakina Roby lilisimama, Bakari akashuka na kuaga. Vitalis na Kaguta nao wakashuka na kuanza kumfuatilia Bakari kwa nyuma mpaka sehemu fulani ambapo Bakari alikutana na wenzake ambao Kaguta na inspekta walivyotizama vizuri wakagundua hao watu ni wale wavuvi waliowakuta siku zile walipokwenda kisiwani.











Kwa umakini, inspekta na Kaguta wakawa wanawatizama wale wavuvi. Wavuvi waliongea kwa muda kidogo kisha Bakari akaingiza mkono wake mfukoni akatoa mifuko ya kaki aliyomkabidhi kila mmoja wao pale kisha kila mmoja akaenenda na njia yake.









Kaguta na inspekta walimfuata Bakari kwa kumnyatia mpaka alipofikia kwenye nyumba fulani ya saizi ya kati, hapo Bakari akagonga na kuingia ndani. Kaguta na inspekta Vitalis wakasogea mpaka dirishani wakachungulia ndani, wakamuona Bakari akiwa anaongea na simu ya mkononi. Mara ghafla Bakari alikunja sura akiwa anaongea, alirusha macho yake dirishani Kaguta na inspekta wakawahi kujificha.











Haraka Bakari akakimbia kuufuata mlango wa nyuma, inspekta Vitalis na Kaguta wakashtuka, haraka waliupiga teke mlango wakaingia ndani, haraka walikimbia kumfuata Bakari, Bakari akaufungua mlango akatoka nje na kuanza kukimbia. Inspekta na Kaguta walimkimbiza kwa kasi, Bakari akajikwaa akadondoka chini. Inspekta na Vitalis wakamkamata na kumuweka chini ya ulinzi.











“Shenzi sana wewe!” Inspekta alifoka. “Kumbe ulikuwa unatu-enjoy sio? … Sasa mwisho wako umefika!”











Inspekta na Kaguta walimbebelea Bakari msobe msobe mpaka kwenye ile nyumba Bakari alipotorokea. Walimkalisha chini wakaketi kitako na kumtazama kwa nyuso kavu.









“Anza kueleza mwenyewe nini ulitufanyia siku zile ... Na usitupotezee muda.” Inspekta Vitalis alieleleza. Bakari akajifanya hatambui muamala anaoulizwa. Alisema hajui lolote kuhusu wao: Vitalis wala Kaguta. Ilibidi inspekta Vitalis atumie nguvu ya ziada kupata majibu wanayoyataka toka kwa mtuhumiwa wao: ngumi kadhaa ziliajiriwa na baada ya muda Bakari akakiri kusema:

“Tulitumwa kufanya ile kazi. Tuliahidiwa pesa nzuri endapo kama tutafanikisha hiyo kazi.”

“Kazi ipi?” Kaguta aliuliza.

“Kazi ya kuwapoteza muelekeo, kazi ya kuwafanya mpotee na hata kwenda kufa huko!”

“Kwahiyo unataka kunambia kwamba yale yote mliyokuwa mnafanya kabla ya kutupeleka huko ilikuwa ni maigizo?” Inspekta Vitalis aliuliza.

“Ndio. Si kingine. Ni maigizo tu kuwaleta kwenye uhalisia.”

“Na nyie mlijuaje kama tunakuja?” Inspekta Vitalis aliuliza.

“Tulipewa taarifa juu ya ujio wenu.”

“Na nani?” Inspekta Vitalis aliuliza.

“Na bwana Roby. Alituambia mu njiani mwaja.”







Inspekta Vitalis alimtizama Kaguta, Kaguta akamuonyeshea tattoo aliyonayo mkononi.









“Kwahiyo ukweli ni upi? Wapi tulipokuwa tunatakiwa kwenda kukutana na yule tuliyemuhitaji?” Inspekta aliuliza. Ila kabla ya Bakari kujibu, Kaguta alionyeshea ishara ya kukaa kimya kwa kuweka kidole chake kwenye lips kisha akamtizama inspekta na kumuonyeshea tattoo aliyo nayo mkononi.









Inspekta alitikisa kichwa chake kisha wakamnyanyua Bakari na kumpeleka garini, wakaenda kwenye jumba lao bovu na kumfungia Bakari huko. Walimrudia siku inayofuata Kaguta akiwa hana tattoo mkononi mwake bali alama ya kuungua kwa pasi.











“Wapi tunaweza kumpata tunayemuhitaji?” Inspekta alirudia swali.

“Kule baharini kuna visiwa viwili: kimoja wapo ndicho anachokalia Alwatan Kombo.”

“Unaweza ukatupeleka?” Kaguta aliuliza. Bakari akasita kwa muda kidogo kutoa majibu ila kwanguvu ya msisitizo, akatoa majibu:

“Ndio naweza kuwapeleka.”









Inspekta Vitalis na Kaguta wakatizamana na kutabasamu. Kesho yake walijiweka kwenye gari pamoja na Bakari wakaenda bagamoyo. Walipanda mtumbwi wakafika kisiwani.









Huku Bakari akiwa mbele, safari ilielekea mpaka kwenye nyumba fulani kubwa na ya kisasa. Walibisha hodi wakafunguliwa na mmama mmoja mnene mwenye mvi. Aliwakaribu ndani, wakaingia na kuketi kwenye makochi yaliyojaa sebuleni.











“Tumemkuta bwana Alwatan Kombo?” Inspekta Vitalis aliuliza.

“Ndio. Ametoka tu kidogo, anakuja. Mna shida gani?”

“Tunataka tu kuonana naye kuna mambo tunataka atunyooshee.”











Punde mlango ulifunguliwa akaingia mzee mfupi mweusi akajitambulisha kwa jina la Alwatan Kombo.Aliwachukua wakina inspekta akaongozana nao kwenda nje ya nyumba mpaka kwenye kijumba kidogo walichoingia kwa kuinama. Humo ndani Alwatan Kombo akaketi kwenye kiti chake na kuuliza:









“Naweza nikawasaidia?”









Bakari aliwatizama inspekta Vitalis na Kaguta akawaona wanatizama ukutani mwa kile kijumba. Kwenye ukuta kulikuwa na mchoro kadhaa, mojawapo ulikuwa ni wa jitu, pembeni ya jitu kulikuwa na vitu vinne: mti wa mchungwa, mtu wa mbao, ndege wa ajabu na saa.











Pembeni ya hiyo michoro kulikuwa na michoro mingine: Nyoka mkubwa mwenye vichwa vitatu, Simba, alama za maji na namba 898. Wakati wakina inspekta wakibung’aa, Alwatan Kombo aliwashtua kwa kuwamwagia matone ya maji toka kwenye kikombe chake kilichokuwa kimekaa kando.











“Elezeni shida zenu vijana.”

“Mzee, sisi tumekuja hapa kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa baadhi ya mambo tu toka kwako.” Inspekta Vitalis alisema kisha akatoa kitambulisho chake na kumuonyeshea mzee Alwatan Kombo.

“Tuna maswali machache tu toka kwako,tunaomba utupatie majibu. Mosi, bwana Kim Salvatore ni nani kwako?”

Alwatan Kombo alitabasamu kwa kejeli akatizama chini kwa muda kisha akaurudisha uso wake kwa inspekta.

“Hiko ndicho kimewaleta?”

“Ndio!” Inspekta Vitalis alijibu kwa kujiamini. Alwatan Kombo aligeuza uso wake akatizama ukuta wake. Alichovya kiganja chake kwenye maji kisha akapiga ukuta wake mara tatu … pah pah pah.









Mara kukaanza kutokea mtikisiko. Mchoro wa jitu ulianza kutokota na kukua. Inspekta Vitalis na Kaguta walitizamana kwa macho ya mshangao. Mchoro ulikua na hatimaye ukawazidi hata kimo. Alwatan Kombo alisimama akaamuru;

“Ondokeni kwa usalama wenu!”









Uso wa Bakari ulikuwa umelowana hofu, aliwataka wenzake aliokuja nao waondoke upesi. Kaguta alimtizama inspekta Vitalis na kumpa ishara ya kuafiki walichoamriwa. Walitoka ndani ya kijumba cha Alwatan Kombo wakasimama umbali wa hatua thelathini.











“Sasa tunafanyaje?” Kaguta aliuliza.

“Tuondokeni hapa jamani! … Tuondokeni tutakufa!” Bakari aliropoka. Inspekta Vitalis alikuwa kama mtu anayewaza jambo: hakusema kitu kwa muda kama wa sekunde tano. Alishusha pumzi ndefu akasema:

“Tuondoke!”









Hatua tatu mbele magari mawili aina ya defender yalitokeza yakiwa yamebebelea waliobebelea bunduki. Haraka inspekta Vitalis na Kaguta wakahisi kuna hatari.











Inspekta alimshika mkono Bakari wakaacha njia kuu na kukimbilia kando kujibanza kwenye jengo, wakiwa wanakimbia risasi ziliporomoshwa kuwafuata kwa fujo. Wanaume saba walishuka toka kwenye defender wakiwa wamebebelea SMG, mmoja wao akawaambia;

“Hatuna muda hapa. Dakika mbili tu!”









Haraka wanaume wale wakagawanyika wakielekea eneo walilokimbilia wakina inspekta. Walitafuta maeneo hayo wakapekua kwa macho yao makali lakini hawakuona kitu. Mpaka dakika mbili zatimba hakuna kitu walichopata. Walirudi kwenye magari yao wakarudisha ripoti:











“Hatujaona kitu, mkuu!”

“Hamjaona kitu?” Robson aliuliza: alikuwa ameketi kwenye kiti cha mbele kabisa cha dereva.

“Ndio! Hatujaona kitu.”

“Tuondoke. Pandeni haraka! Watu watajazana muda si mrefu.”









Wanaume wale saba haraka walipanda kwenye magari yao wakaondoka eneo lile ambalo watu walianza kujazana ndani ya muda mfupi tu wakiwa wanazoza juu ya lile tukio. Ndani ya watu hao waliosogea eneoni walikuwepo wakina inspekta.











Walikuwa wamechafuka mno kwa udongo, walinyooka na barabara mpaka eneo la mitumbwi wakapanda mtumbwi kwenda ng’ambo. Walijiweka kwenye gari lao wakaanza safari ya kurudi Dar es salaam. Mara hii alikuwa anaendesha inspekta Vitalis na kasi yake ilikuwa kubwa mno.











“Wanaweza wakaenda kumjeruhi Bernadetha. Inabidi tuwahi!” Inspekta Vitalis alisema kwa mjazo.

“Sidhani kama wana haja ya kufanya hivyo.” Kaguta alisema.

“Vita haina macho, Kaguta. Huwezi jua.”

“Kweli, tahadhari inabidi ichukuliwe. Ila Vitalis, kuna jambo lolote umeligundua pale kwa Alwatan Kombo?”

“Kuna mambo nimeyaona yananitatiza akilini.”

“Kama yapi?”

“Ile michoro.”

“Exactly. Ila ina maana gani? … Pembeni ya mchoro wa yule jitu kuna mchoro nimeuona wa mti wa mchungwa.”

“Una nini?”

“Huo mti ndio ambao nilipambana nao kule kisiwani?”

“Really?”

“Ndio!”

“Alafu hata mimi nimeona mtu wa mbao pembezoni ya mchoro huo huo wa jitu. Na huyo mtu ndiye niliyepambana naye pia kule kisiwani!”

“Je yule ndege, ulimuona?”

“Nilimuona!”

“Ndiye yule aliyekuwa kambeba Jombi kule kisiwani!”

“Sasa naanza kupata picha kamili. Hata ile saa tuliyoiona pembeni ya yule jitu maana yake ndio ule muda tuliokuwa tunapewa kule kisiwani na kila baada ya huo muda kukawa kunatokea majanga!”

“Haswaa!”

“Kwahiyo … Kwahiyo sasa … ina mana ile michoro kwanini ilikuwa pembezoni mwa yule jitu?”

“Hapo ndipo kuna la kupambazua.”

“Nadhani hivyo ndivyo vitu vinavyomtimiza huyo jitu. Ama ndivyo vitakavyokuwa power yake.”

“Labda. Kwahiyo ina maanisha tukitaka kumkabili yule jitu ni lazima tupitie hayo majaribu?”

“Bila kipingamizi, hivyo ndivyo. Lakini kuna jambo lanipa mashaka.”

“Lipi?”

“Kwanini huyo jitu haruhusiwi kutumaliza badala ya kuhangaika nasi kwa bunduki?”









“Sijajua mpaka sasa. Kuna jambo lipo nyuma ya pazia.”

“Na inatulazimu kuling’amua. Pia umeona namba 898?”

“Nimeiona.”

“Itakuwa ina maanisha nini?”

“Sijajua. Ila si unajua nyumba ya bwana Isaac Makongo ina namba 898?”

“Ndio. Kuna kitu pia katika hiyo namba.”









Baada ya dakika ishirini na tano wakawa tayari wameshawasili jiji la Dar es salaam. Bakari alishushwa wakina inspekta wakaelekea mpaka nyumbani kwa Bernadetha.









“Karibuni!” Bernadetha aliwakaribisha kwa tabasamu pana.

“Ahsante!”









Waliketi kwenye viti inspekta Vitalis akamueleza Bernadetha yaliyotokea. Zaidi inspekta Vitalis akamtaka Bernadetha ahamie kwake kwa usalama. Jambo hilo likawa gumu.









“Mwanangu Miraji hataki kabisa hata uongelewe humu ndani. Inakuwa ugomvi kabisa, sembuse kuja kukaa kwako.”

“Mueleze hali halisi. Muambie mpo hatarini.”

“Sidhani kama itaweka mabadiliko yoyote. Anawahesabu nyie kama wauaji wa baba yake, hapo ndipo ugumu unakuja. Ila nitajitahidi sana kumueleza.”

“Sawa. Itakuwa vyema.”

“Vipi Kaguta, mbona mkono wako una bandeji?”



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/





Kaguta akaeleza yaliyotukia. Bernadetha akachukua wasaa wake kumpa huduma ya kwanza kama ile aliyompa inspekta Vitalis kisha akamtaka Kaguta asifunge hilo jeraha. Baada ya hapo, wakina inspekta waliaga. Bernadetha aliwatoa mpaka nje, akamkumbatia inspekta Vitalis na kumbusu shavuni.









“Utakapohisi tatizo, nipigie immediately. Na usisahau kumsalimia Marietta akirudi.” Inspekta Vitalis alimwambia Bernadetha. Bernadetha akatikisa kichwa kukubali alichoambiwa. Mpaka wanaume wanatokomea na gari lao, Bernadetha akawa yu kibarazani anawatizama. Chozi lilimshuka akalipangusa na kiganja chake.









Alitizama chini akajigeuza na kurudi ndani. Kumbe wakati yupo hapo kibarazani Miraji alikuwa anamchungulia dirishani. Baada ya mama kuingia ndani, Miraji alifunga dirisha lake akajilaza kitandani akarusha macho yake darini kama mtu anayewaza jambo.











Katikati ya mida ya saa mbili za usiku, Bernadetha alikuwa na wanawe: Marietta na Miraji wakiwa wanapata chakula kwa pamoja. Kulikuwa ni kimya kati yao kwa muda wa dakika kadhaa, vijiko tu na sahani ndivyo vilikuwa vinapiga makelele. Miraji alimtizama mama yake, akamtizama na mdogo wake, Marietta, kisha akaamua kuufungua mdomo kwa kuuliza:









“Mama, mbona siku hizi hauna raha?”









Bernadetha alimtizama Miraji akatabasamu kiuongo.









“Kwanini unasema hivyo mwanangu? … Nipo sawa tu.”

“Hapana. Mara kwa mara nimekuwa nikikuona unaketi nje peke yako, unadondosha chozi. Umekuwa ni mtu wa kuketi kiupweke. Umekuwa ukichelewa kulala na hata mara nyingine kulala sebuleni. Nini tatizo, mama?”











Bernadetha aliyafichama yote yaliyosemwa na Miraji kwa tabasamu pana lililojaza uso wake. Akasema:

“Mwanangu, hakuna lolote. Labda kwa kuwa hujaniona kwa muda.”

“Mama, kwani uncle Vitalis amesema anakuja lini?” Marietta aliingilia kwa kuuliza.

“Atakuja tu.”

“Lini? Mi nimemkumbuka. Basi twende kwake.”









Marietta alizidi kusisitiza. Bernadetha akamtizama Miraji kwa jicho la tahadhari, Miraji hakusema jambo, aliendelea tu kula kama mtu ambaye hajasikia lolote.









‘Tutaenda tu, usihofu mwanangu.” Bernadetha alimwambia Marietta, Marietta akatabasamu na kuendelea kula. Miraji alipomaliza alinyanyuka akaondoka zake kwenda chumbani.











Baada ya muda mfupi, Marietta naye alinyanyuka akaenda kuoga na kulala, alibakia Bernadetha peke yake sebuleni akiwa anatizama runinga. Mara simu yake ya mkononi iliita na kutetemeka, akainyakua toka mezani na kuitizama, akaona ujumbe toka kwa inspekta.









“Helo … Umelala?”

Bernadetha akatabasamu na kubonyeza vitufe vya simu kujibu.

“Hapana, nipo tu natizama televisheni.”

“Upo salama?”

“Am ok. Wewe?”

“Nipo salama. Jus missin yu.”

Bernadetha alitabasamu tena, kisha akajibu:

“Me too.”

“Unakuja lini kuniona?”

“Nadhani wknd hii. Marietta pia anataka kukuona.”

“Nimemmis sana. Karibuni.”

“Ahsante. Mkono wako unaendeleaje?”

“Naendelea vyema tu. Upo na nani hapo?”

“Mwenyewe. Wewe je?”

“Nipo mwenyewe pia.”

“Wapi?”

“Chumbani. Naona nyumba imekuwa kubwa mno. Nakumiss kweli.”

“Sana?”









Marietta alituma ujumbe huku aking’ata lips zake. Bahati mbaya hakujibiwa. Alikaa dakika kama tano bila ya majibu. Simu ilikuwa imekata mtandao. Alitoka nje akanyanyua mkono wake kutafuta mtandao bila ya mafanikio.











Hata pale mtandao uliporudi hakuona ujumbe mwingine, alienda chumbani kwake akalala ila kila muda akawa anahisi sauti ya ujumbe kuingia ila alipotizama hakuona kitu, mwishowe usingizi ulimpitia akajikuta asubuhi simu yake ikiwa imejaa jumbe nyingi toka kwa inspekta Vitalis. Akatabasamu na kuanza kuzijibu kabla ya kufanya kitu kingine chochote.







Ndani ya mida ya jioni jua likiwa tayari limezama na kilichobakia ni miale yake ya njano tu, inspekta Vitalis alijirudisha nyumbani kwake akiwa kabebelea mkoba wa ngozi. Alipoingia sebuleni aliutupia mkoba juu ya meza akaketi kwenye sofa.







“Jombii!”

“Yeeeah!”









Sauti ya mwanaume iliitikia kwa ndani, punde Jombi akaja sebuleni wakasalimiana.









“Afadhali umekuja. Simu yako imenisumbua siku nzima ya leo.” Jombi alianzisha mada.

“Simu yangu ipi?” Inspekta Vitalis aliuliza kwa mshangao.

“Hii hapa!” Jombi akatoa simu kubwa nyeusi aina ya LG. Inspekta akaachama mdomo kwa bumbuwazi. Aliikwapua simu toka mkononi mwa Jombi akaitizama.

“Hii ni simu ya dokta Rajesh! … Gosh! … Umeionea wapi?”

“Chumbani kwangu, chini ya uvungu. Imeita sana.”

“Aisee, nilikuwa nimeisahau kabisa!”











Inspekta alinyanyuka akaubeba mkoba wake na kwenda chumbani. Aliwasha taa kisha akailaza simu ya dokta Rajesh kuhakisi mwanga wa taa kwenye kioo cha simu, akaona alama za michoro. Akaweka kidole chake kwenye kioo na kuchora, simu ikafunguka.











Alifungua mkoba wake akatoa note book na kalamu akaanza kupitia missed calls. Miongoni mwazo akaona ina jina la Wayne Ford, nyingine I. Makongo. Akaziandika hizo namba kwenye note book yake. Baada ya hapo akaanza kupitia jumbe zilizokuwemo ndani ya simu. Moja ya jumbe ikakamata hisia zake.









“Kumbuka unadaiwa damu ya watu kumi na mbili. Hakikisha leo unauwa watu hao na kuleta damu hiyo. Its urgent.”













Inspekta aliandika kwenye note book namba iliyotuma huo ujumbe kwa dokta na kwenye simu ya dokta ilikuwa imeseviwa ‘Sahayoogee’. Inspekta akaanza kufuatilia conversation kati ya Sahayoogee na dokta Rajesh Deepti.













Alipomaliza, akaendelea kutizama jumbe zingine, akakutana na jumbe moja kati ya dokta Rajesh Deepti na mtu aliyeseviwa Svaamee Math. Kabla hajaendelea, inspekta alichukua simu yake akatafuta maana ya neno ‘Svaamee’ akagundua ni neno la kihindi lenya maana ya mkuu. Sasa likabakia neno ‘Math’ maana yake nini? Wakati inspekta anafikiria alikumbuka maneno mawili yanayoishia na hilo neno, akayatamka:









“Rosemath stationary chini ya Mikmath company”











Akafikiria tena kwa muda, taratibu akaanza kulinyambua neno ‘Mikmath’, hapo akapata kutambua neno Mik maana yake ni Kim likiwa limegeuzwa kwa kinyume. Sasa akarudi tena kwenye jumbe kati ya Svaamee Math na dokta Rajesh. Akakuta jumbe nane tu:











“Let us meet in Delhi.”

“Let us meet in Barmuda … urgent.”

“Let us meet in Dar es salaam, at Serena Hotel after 30 minutes.”

“If there’s any problem, consult me.”









Hizo zote zikiwa zimetumwa na Svaamee Math, na jumbe nne zilizobakia zikiwa ni za kujibu hizo jumbe nne kwa neno moja tu lililojirudia.









“Yes, master.”









Mara simu ya dokta ikaita, bwana Isaac Makongo akiwa ndiye mpigaji. Inspekta alitizama kioo cha simu kwa dakika moja akaamua kupokea.









“Mbona ulikuwa hupokei simu, Rajesh?”

“Ilikuwa mbali. Lete habari.” Inspekta aliongea huku akijitahidi kuiga sauti ya Rajesh.

“We have to meet kesho asubuhi saa tatu maeneo ya masaki, Mr Wayne Ford atakuwepo pia. Ni kuhusu our spreading propaganda.”











Baada ya hayo maneno, simu ikakata. Inspekta Vitalis akabakizwa na maswali: Masaki sehemu gani wanapoenda kukutana? Baada ya muda kuna kitu kikamjia kichwani … namba 898. Inspekta akatabasamu na kutikisa kichwa chake. Alinyanyua simu yake na kumtaarifu Kaguta habari nzima. Wakapanga kesho waende huko Masaki.









Masaa yakaenda na asubuhi ikawasili. Inspekta na Kaguta walikutana na kujiweka kwenye gari mpaka masaki, taratibu na kwa tahadhari wakakaa umbali wa mita kadhaa mbali na jumba kubwa lililobebelea namba 898. Wakiwa hapo wakarusha macho yao eneo la tukio, punde wakaonamagari matatu meusi aina ya benzi yanaingia ndani ya lile jengo kisha geti likafungwa.













Inspekta Vitalis na Kaguta wakashuka garini na kuanza kusonga kufuata nyumba ile kubwa. Hatua kama saba, ghafla likatokea gari aina ya van nyeusi, mlango ulifunguliwa akatokeza mwanaume mmoja aliyebebelea bunduki kubwa SMG, kabla wakina inspekta hawajafanya lolote, mwanaume yule aliyebebelea bunduki alimimina risasi kadhaa zikamlenga Kaguta kifuani na inspekta Vitalis miguuni. Wote wakadondoka chini. Van ikaondoka kwa kasi na kupotea.











Inspekta alimtizama Kaguta akamuona yu kimya. Alimtikisa huku akimuita jina lakini Kaguta hakusema neno lolote. Alikuwa kimya tuli kama maji mtungini. Mara machozi yakaanza kujaa kwenye macho ya Vitalis. Alikuwa amekodoa kama vile haamini kinachotokea. Aliita kwa sauti kubwa lakini haikuleta tofauti yoyote, Kaguta alikuwa kimya.











Inspekta alinyanyuka, huku miguu yake ikivuja damu, alimbeba mwenzake akampeleka mpaka kwenye gari walilokuja nalo kisha akawasha gari na kuondoka eneo hilo mpaka maeneo ya ufukwe mwa bahari. Alizima gari na kumtazama Kaguta aliyekuwa amekaa nyuma ya kiti akiwa amelala kama mfu kisha akaegemea usukani mwa gari akaanza kuangua kilio kama mtoto. Ni kama vile ndoto, tena ya jinamizi mbele ya macho ya inspekta. Hakutaka kuamini, kila mara aligeuka na kumtizama Kaguta labda atakuwa amefungua macho lakini wapi.















Mwishowe alitoka ndani ya gari akasogelea maji ya bahari akayachota na kiganja chake akanawa uso. Akiwa hapo alitizama maji ya bahari yakicheza kwa kwenda mbele na kurudi nyuma. Alitizama meli na boti kwa mbali zikipita. Alitizama watu aliowaona kwa mbali wakiwa ufukweni wakifurahia mandhari hayo, wakati huo yeye alikuwa anamimina machozi ambayo hayakuonyesha yatakatika muda gani na huku suruali yake ikiwa imelowa damu maeneo ya mapajani.











Anayelala na mgonjwa ndiye anayejua miugulio. Haikuhitaji shahada kujua Vitalis amekwazika hisia, amebeba gululi la majonzi ndani yake. Neno ulikataalo, ndilo Mungu apendalo jama, inspekta alisema na nafsiye. Baada ya kutizama bahari kwa muda na uso wake pozo, alisema kama vile anamwongelesha mtu anayemuona:











“I am sorry my friend: nimekuleta kifoni.”













Maneno hayo yalisindikizwa na machozi yenye kina kirefu. Ijapokuwa aliyafuta kwa kutumia vidole vyake bado yaliendelea kutiririka kiasi kwamba akawa haoni tena mbele.











Alikamua macho yake kwa kuyabinya kwanguvu kisha akageuka na kulifuata gari, muda huu alitembea akiwa anachechemea na uso wake ukipokea hilo jambo kwa kukunjamana. Aliwasha gari akaanza safari, alichojoa simu yake mfukoni akampigia Bernadetha.













“Naomba uje nyumbani muda si mrefu. Nakuhitaji.”











Aliongea maneno hayo tu kabla ya kurejesha simu yake mfukoni na kuendelea na safari. Mara ghafla akasikia mtu akikohoa nyuma ya gari. Alirusha macho yake mekundu kwenye kioo cha gari kilichoketi juu ya kichwa chake akamuona Kaguta akijinyanyua.











Inspekta Vitalis akatoa macho ya tahamaki. Haraka alipeleka gari kando kulipaki kisha akageuza uso wake na kutizama nyuma. Alaa! Akamuona Kaguta akiwa kakaa sasa amekunja uso wake na kiganja chake chaperemba kichwa kama mtu anayehisi maumivu.









“Kaguta!” Inspekta Vitalis aliita, uso wake ukiwa umechangamana hisia za mshangao na furaha.

“Nini kimetokea, Vitalis?” Kaguta aliuliza, “mbona kichwa chaniuma hivi?”

“Ulipigwa risasi kifuani ukadondoka! … How come upo mzima?” Vitalis aliuliza huku akitizama maeneo ya kifuani mwa Kaguta. Kaguta alitabasamu kidogo akauliza:

“Mbona macho yako mekundu, umelia?”











Inspekta Vitalis alitabasamu kama mtu ambaye hakuwa na mpango wa kufanya hivyo. Alitikisa kichwa chake akauliza:











“Kaguta, tell me imekuaje?”

“It’s proof. Nilivaa bullet proof, Vitalis.” Kaguta alijibu huku akibinya kifua chake na kidole.

“Usiniambie hukugundua hilo, Vitalis.”

“Sikugundua, labda kwakuwa umevaa koti jepesi.”

“Hapana. Ni kwakuwa ulimezwa na hofu yako.”

Inspekta Vitalis alitabasamu akashika usukani gari likaondoshwa.



“Nadhani ni kwasababu alidondoka akajigonga kichwa.” Bernadetha alisema huku akimtizama inspekta Vitalis aliyekuwa amejilaza kwenye kochi.

“Nilidhani amekufa. Really!”





http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Kaguta na Bernadetha walicheka baada ya hiyo kauli, Bernadetha akatia neno:

“Hakuwa mbali sana na kufa. Ni uzi mwembamba sana unaotenganisha uhai na kifo pindi unapokuwa hauna fahamu.”

“Usihofu, Vitalis. Mi bado nipo sana tu.” Kaguta alisema kwa sauti yenye kubeba utani ndaniye. Wote wakacheka.

“Una bahati sana we kima. Sijui nani alikuambia uvae bullet proof leo!” Inspekta Vitalis alinena kisha akauliza huku akimtizama Bernadetha:

“Na vipi kuhusu mimi, nesi?”









Bernadetha akapasua mdomo wake kwa tabasamu kabla hajajibu.











“Inabidi uende hospitalini. Kutoa risasi mwilini bado hakutoshi, huenda ukawa umevunjika ama jeraha likawa na madhara zaidi.”

“Aaah! … Kwenda hospitali? Nachukia sana kwenda hospitali.”

“Itabidi uende tu. Hivyo vidonda ni vikubwa.”

“Nitaangalia.”

“Tafadhali usizembee katika hilo.”

“Sawa, nesi.”

“Naweza nikaenda? Nimemuacha Jombi peke yake na Miraji.”

“Mbona unawahi? … Ngoja basi tule.”

“Kweli!” Kaguta alidakia, “Itakuwa si vizuri endapo ukiondoka bila kula. Jombi yupo na mgonjwa, usihofu. They are bestfriends.”









Bernadetha akaridhia. Alienenda jikoni akapika chakula: Wali nyama na mboga za majani, akapakua na kuweka chakula mezani, akawakaribu Kaguta na Jombi. Wakati wanakula wakaendeleza soga:











“Kwahiyo, vipi kazini?” Bernadetha alimuuliza Vitalis.

“Nitawapa taarifa kesho.” Vitalis alijibu.

“Hakutakuwa na shida yoyote?”

“Sidhani. Nimepata ajali kazini.”

“Sasa utaendaje kuwapa taarifa?” Kaguta aliuliza.

“Nitawapigia simu. Au utan’saidia kwenda kutoa taarifa?”

“Sio mbaya. Kama ukin’taka nifanye hivyo, nitafanya.”

“Nitashukuru sana.”











Baada ya maongezi hayo madogo na kula, Bernadetha aliaga. Alimbusu Vitalis shavuni akaenda zake. Kaguta akabaki na inspekta.











“Ujue wewe Vitalis ni mjinga?”

“Kivipi?”

“Unajua kabisa wewe sasa hivi ni kilema alafu unamwachia Bernadetha anaondoka bila ya kumsisitizia aje hapa awe anakuhudumia. Unadhani mie nitaweza kukaa hapa muda wote? Nitaenda saa ngapi kunywa kidogo na watoto?”

“Nani kakuambia siwezi kujihudumia?”

“Maiti haiulizi sanda, ndugu.”

“Naweza kujihudumia mwenyewe. Wewe nenda unapotaka kwenda wala usijibane.”

“Hapana! Siwezi kukuacha mwenyewe hapa. Ila zingatia ushauri wangu, brother.”









Inspekta Vitalis hakusema tena kitu. Alijinyamazia kama mjinga.







Mlango wa nyumba ulipofunguliwa, Miraji na Jombi walirusha macho yao wote kuona nani anaingia. Hakuwa mwingine bali Bernadetha, mama Miraji, aliingia ndani akatengeneza tabasamu usoni.









“Mnaendeleaje?”

“Safi tu. Vipi huko utokako?” Miraji aliuliza.

“Kwema tu.”

“Kweli?”

“Ndio. Kwema.”

“Sidhani kama ni kwema. Gauni lako lina damu.”









Bernadetha akashtuka kusikia hivyo, alitizama gauni lake kwa chini kweli akaona alama za damu. Macho yakamtoka.











“Mama, hakuna haja ya kunidanganya. Najua umetoka kwa inspekta. Vipi ana jeraha?”









Bernadetha alishusha pumzi ndefu akatikisa kichwa chake kama mtu akubaliye jambo. Akasema:









“Ndio, ana jeraha. Umefurahi?”









Hakusubiria jibu. Alienenda zake kwa mwendo wa haraka kuelekea chumbani. Miraji na Jombi wakamsindikiza kwa macho mpaka anazama.











“Naomba niondoke, Miraji. Inaelekea kuna tatizo huko nyumbani.”

Jombi aliaga. Miraji akanyanyuka na kumtoa mpaka nje.

“Kwaheri, Jombi.”

“Kwaheri. Hakikisha unazingatia na kuyatafakari yale niliyokuambia.”

“Sawa.”









Jombi alishika njia akaondoka. Miraji alirudi sebuleni akajilaza kwenye kochi. Baada ya muda mama yake akaja na simu na daftari akaketi papo, akawa anapiga mahesabu ya biashara zake. Kwa muda kama dakika kumi, hakuna aliyeongea na mwenzake mpaka pale mama alipofunga daftari lake la mahesabu.











“Mama, mbona umetoa picha ya baba sebuleni?” Miraji aliuliza. Mama akamtizama bila ya kumjibu, akaendelea kubofya simu yake.

“Mama, nimeuliza. Mbona umetoa picha ya baba sebuleni?”

“Kwani umeona leo?”

“Ndio, nimeona leo haipo.”

“Embu wacha nikuulize. Hii nyumba ya nani?”

“Ya kwetu.”

“Ulitoa hata sumni kuijenga?”

“Si alijenga baba yangu.”

“Mpumbavu wewe! Funga bakuli lako. Kwa kazi gani ya maana aliyokuwa nayo baba yako ajenge nyumba kama hii peke yake? Hii nyumba tumejenga mimi na baba yako, tukijibana na kujinyima kadiri tulivyoweza. Baba yako amefariki, hii nyumba ni ya kwangu, usinipangie nini cha kufanya. Umesikia?”

“Mama, jua mimi ni mwanao …”

“Kama ungekuwa unalijua hilo, ungekuwa na adabu na mimi. Umekuwa mtoto wa ajabu sana. Adabu huna, unanipandishia sauti kama vile unaongea na housegirl. Umekuwa wa kunchagulia wapi pa kwenda, kipi cha kuongea. Nikitoka uniulize nikirudi uniulize, naishi mahakamani?”

“Mama nafanya yote hayo kwa ajili yako.”

“Nimekuomba? Wakati unaumwa umelala kitandani hujielewi kwa lolote, nani alikuwa ananilinda? Mimi sio dada yako, mama yako!”

“Mama yote hayo ni kwa ajili ya …”

“Funga mdomo wako! Ishia hapo hapo.”











Macho ya Bernadetha yalikuwa mekundu. Alifura kama simba aliyejeruhiwa. Alikuwa anahema juu juu. Alikwapua daftari lake kama kibaka akarudi chumbani.











Zilipita siku tatu mwisho wa wiki ukabisha hodi. Bernadetha akatimiza ahadi yake kwa mwanae, Marietta, aliongozana naye kwenda kumtembelea inspekta Vitalis. Huko wakamkuta inspekta akiwa amekaa kwenye kiti cha matairi, Jombi akiwa ndiye dereva wake akimpeleka huku na huko.













“Hukuenda hospitali, Vitalis.” Bernadetha alitamka akiwa na uso usio na utani.

“Ndio, sikwenda.”

“Kwanini?”

“Nimeshindwa kwenda.”

“Umeshindwa? … Kivipi?”









Inspekta Vitalis hakupewa muda wa kujibu, Marietta alikuja haraka akitokea nje akamrukia Vitalis.











“Mariettaaa, si nimekuambia uncle anaumwa? Nenda nje kacheze.” Bernadetha alifoka. Marietta akasimama na kunywea ghafla.

“Muache bana. Njoo Marietta.” Vitalis alimvuta Marietta akamshika mkono. Marietta akamuangalia Vitalis kwa tabasamu.

“Utapona lini uncle uje kwetu?” Marietta aliuliza.

“Muda si mrefu napona. Ila ukitaka nipone haraka uwe unakuja kun’tembelea.”

“N’takuja kila siku.”

“Nitafurahi kweli. Haya shika hii kanunue chocolate. Si unapenda chocolate?”

“Ndio.”

“Haya kanunue.”













Inspekta Vitalis alitoa elfu moja mfukoni akampatia Marietta. Marietta alishukuru kisha akatoka ndani akawaacha Bernadetha na inspekta Vitalis. Wakaendelea kuteta:













“Tokea nimetoa taarifa kazini hakuna lolote ambalo nimefanyiwa. Hakuna hatua yoyote ambayo wameichukua. Sina pesa, Bernadetha.”

“Una uhakika taarifa imewafikia?”

“Exactly. Nimepiga mpaka na simu, wameishia kunipatia kiti tu cha matairi.”

“Labda wapo kwenye process. Nina uhakika watafanya jambo, Vitalis.”

“Lini? Hali yangu haisubiri.”

“Naamini hawatokuacha. We usichoke kuwasumbua kuwapa taarifa.”

Kinyume kabisa na alivyosema Bernadetha, majuma yakazidi kukata bila ya inspekta Vitalis kupokea mkono wowote wa msaada toka kazini kwake.













Mara kwa mara Bernadetha alikuwa anakuja kumuona na kumjulia hali, vile vile Kaguta. Hata inspekta alipokwenda kazini akiwa kwenye kiti cha matairi, hakuna alichoambulia zaidi ya ahadi tu. Mwishowe alikata tamaa. Kama haitoshi, akatumiwa barua ya kufukuzwa kazi.











“Siwezi amini kama haya ndio malipo ya kazi yote ile niliyofanya.” Vitalis alimwambia Kaguta kwa sura ya uchungu.

“Nilijitolea kwa hali na mali kupambana na kutimiza majukumu yangu, leo hii naishia kuwa fukara kilema?” Vitalis alitabasamu huku akitizama chini. Kaguta akamshika bega na kumpa moyo:

“Yote ni maisha, Vitalis, usinononeke sana. Mimi nipo, hakuna litakalo kwenda kombo.”











Vitalis akageuka mlevi. Kila siku alitaka aletewe pombe na Kaguta, na hata pale ilipokosekana kabisa alidiriki kumtuma Jombi kiroba hata cha mia tano apate kunywa.











Hakuweza kulala akiwa na akili timamu bali pombe. Hakuwa na hamu ya kula, Bernadetha alijitahidi kumpikia ila akiondoka tu, anaacha papo hapo. Hata afya yake ikaanza kuzorota. Miguu yake ikalemaa kabisa kutokana na kutokula wala kutotaka kufanya mazoezi. Hakuwa tena Vitalis yule, bali Vitalis aliyekuwa hajipendi wala kujijali tena.











“Naomba ukakae nae, hakuna tena jinsi. Yupo stressed sana, hali yake inaweza ikawa mbaya zaidi.” Kaguta alimwambia Bernadetha. Bernadetha alitizama chini kama mtu anayefikiria, uso wake ulikuwa umenyong’onyea mno. Alinyamaza kwa muda kidogo machozi yakambubujika.

“Nitajitahidi kulifanyia kazi, Kaguta.”

“Please. Vitalis anakuhitaji sana kwa sasa.”

“Nitajitahidi Kaguta.” Bernadetha alisisitizia. Kaguta alinyanyuka akaaga. Bernadetha akabaki mwenyewe sebuleni na uso wake uliopoa. Kwa muda wote waliokuwa wanaongea na Kaguta Miraji alikuwa ametega sikio mlangoni akisikiliza.











Kaguta alipoondoka, Miraji akafungua mlango na kwenda kumkuta mama yake sebuleni. Aliketi kando akamtazama mama yake aliyekuwa anabubujikwa na machozi, akamshika mkono.









“Mama.” Miraji aliita. Mama akageuza uso na kumtizama.

“Mara yangu ya mwisho kukuona katika hali uliyopo ni kipindi kile baba alipokufa. Haukuwa na raha. Ulikonda kwa mawazo. Hukutaka kuongea na mtu yeyote zaidi ya kulia kila uchwao. Na yote hayo ni kwakuwa ulimpoteza mtu uliyempenda. Siwezi kukuona ukipitia katika hali ile kwa mara ya pili kwa mana najua jinsi ninavyojisikia nikikuona hivyo. Nakuomba futa machozi mama. Nenda kapiganie maisha ya unayempenda.”











Miraji alisema kwa sauti ya chini na punde machozi yalimtoka. Mama yake alimtizama huku naye machozi yakimbubujika. Alimvuta mwanaye akamkumbatia kwanguvu na kumwambia:











“Ahsante. Wewe ndiye Miraji niliyekumis kwa muda wote huo tangu ulipodondoka.”

Miraji alitabasamu, akasema:

“Nisamehe mama kwa kukatili moyo wako kwa muda wote huo. Sasa naelewa ni jinsi gani Vitalis anamaanisha kwako.”







Alimfuta machozi mama yake kwa kutumia vidole vyake, akamwambia:

“Nenda mama.”

Mama akamjibu:

“Nataka twende wote.”

Miraji akatikisa kichwa.





Bernadetha pamoja na familia yake walihamia kwa Vitalis. Kwa sababu ya kipato, Bernadetha alilazimika kutumia vyeti vyake vya taaluma kutafuta kazi ya unesi hospitalini. Alipata kazi, sasa ikamlazimu biashara yake ya kuuza vitenge amkambidhi mwanae,







Miraji, aendeleze nayo, wakiwa pamoja na Jombi wakajitolea kufanya biashara hiyo, yote hayo yakiwa yamelenga kukuza kipato kwa ajili ya kumsaidia Vitalis. Baada ya muda wa wiki mbili Vitalis alipelekwa hospitalini, Bernadetha akawa anamuhudumia huko. Mara kwa mara Kaguta alikuwa anakuja kumjulia hali rafikiye hospitalini, pamoja na Jombi na Miraji.







Siku moja wakati Bernadetha akiwa anaongea na Vitalis kwenye kitanda cha hospitali, alikuja mwanaume mmoja mnene aliyevaa shati jeusi na suruali ya bluu ya jeans akamuita Bernadetha nje. Bernadetha akabadilika sura kwa kunyong’onyea, alimuaga Vitalis na kwenda nje.







“Sasa inakuaje lile ombi langu. Tangu umepata kazi umen’sahau kabisa na unajua usingeipata bila yangu.” Sauti ya kiume ilisikika.

“Najua. Ila tafadhali naomba muda.” Sauti ya Bernadetha ilivuma.

“Mpaka lini sasa?”

“Muda si mrefu. We nivumilie tu.”

“Nataka kesho unipe jibu langu.” Sauti ya kiume ilisema kisha punde Bernadetha akarudi ndani ya chumba alicholazwa Vitalis. Hakujua kama Vitalis kasikia kila kitu.

“Nani huyo?”

“Aah jamaa fulani hivi … mkurugenzi wa hospitali.”

“Anasemaje?”

“Alikuwa ananikumbushia tu baadhi ya majukumu.”







Vitalis hakuuliza tena. Waliendelea na habari zingine. Siku iliyofuata Kaguta alikuja kumjulia hali Vitalis, Vitalis akamueleza juu ya saga la mkurugenzi wa hospitali na Bernadetha.







“Nataka umfanyie kazi huyo mbwa. Haraka iwezekanavyo.” Vitalis alimwambia Kaguta. Kaguta akatabasamu na kuuliza:

“Lishakwisha hilo, kuna lingine?”

Vitalis alitabasamu akasema: “Hakuna mkuu.”







Kaguta akatabasamu.







Kesho yake asubuhi Kaguta akiwa kavalia miwani ya macho, suti nyeusi matata na tai, mkononi akiwa kashikilia briefcase alienenda mpaka mapokezi akapokelewa na mwanadada mwembamba mweupe.









“Naweza nikakusaidia?”

Kaguta alimtizama yule mdada na macho nje ya miwani, akasema:

“Sorry, My name is Peltridge Allan from Detroit, USA. I want to see your manager.”









Kaguta alinena kwa lafudhi ya muamerika mweusi. Macho yake yalikuwa yanaonyesha kujiamini na akiamini kile anachokinena. Mdada wa mapokezi alimtizama mwenzake aliyekuwa naye kwenye chumba, akamwambia:







“Leo tumepata muamerika, mweh!”







Kaguta alitabasamu kidogo kisha akaurudisha uso wake katika hali ya u-serious. Mdada wa mapokezi alimtizama kisha akamuelekeza:







http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Just take this corridor till you see a door with a badge written ‘manager’. There you are.”







Kaguta alitabasamu, akatikisa kichwa chake kimaridhiano.









“Thanks madam.”









ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog