Search This Blog

Sunday, 20 November 2022

URITHI WENYE UMAUTI - 2

 





    Simulizi : Urithi Wenye Umauti

    Sehemu Ya Pili (2)



    Mji uliokuwa umewameza vijana na wazee waliokuwa wapenda raha,si disko,si baa za kunywa pombe,si madanguro ambako mapenzi ya kiholela yalikuwa yakifanyikia.Almuradi chochote ambacho kilikuwa ni cha kuwafurahisha wapenzi wa anasa kilipatikana mjini Sogomo.Ari ya kutembea niufikie mji huo ikawa imeniingia,nikapata nguvu ya kutembea kufika kule.Mvua sasa ilikuwa imeongezeka, mitaro kando kando ya barabara ikaanza kupwa.Dakika hamsini baadaye nikawa niko hoi bin tiki kwani sikuwa mzoefu wa kutembea masafa yale marefu bila ya gari ya baba niliyokuwa nimezoea kuiendesha.



    Nikajibwaga chini kama mfuko wa viazi kwenye nyasi ndefu kando ya barabara.Nikiwa naendelea kupumzika pale,ghafla nikasikia gari likifungia breki mita takribani kumi toka nilipokuwa nimelala.Taa zote zilikuwa zimezimwa.Niliinuka polepole na nilipochungulia nikawaona watu wale wale niliokuwa nimewaacha nyumbani kwetu huku wakiwa na bunduki kubwa kubwa.Kufikia hapo sikutaka kupoteza muda nikingoja niuawe.Nilichomoka toka pale chini na kutokomea kwenye shamba la miwa lililokuwa karibu na barabara ile."Simama Roy!Hatuna nia ya kukudhuru"sauti ya kiume ilisikika tokea nyuma.Nilishangaa watu wale kuniita kwa jina.Maswali ambayo sikuwa na majibu yakanipitia akilini.Kwa nini wanifuate na silaha za Moto ikiwa hawana nia mbaya?Mbona baba na mama wageuzwe wafu bila sababu?Uzumbukuku haungeniingia niwaamini wale watu na kurudi au kusimama.Niliendelea kukimbia huku nikiziwacha shina kadhaa za miwa zimevunjika.Kelele ya matone ya mvua juu ya matawi ya miwa ikasababisha mimi kutojua walipokuwa watu wale.



    Nilipiga magoti mchangani na kuangalia nyuma nilikotoka vyema;hakukuwa na dalili ya mtu yeyote ila hili halikunifanya kupuuza hisia zangu kuwa eneo lile lilikuwa hatari kwangu.Muda mfupi nikasikia matawi ya miwa yakitoa sauti karibu tu na pahali nilipokuwa nimejificha.Kiwiliwili cha mtu kikajitokeza huku mtu yule akitazama kwa umakini,mkononi alikuwa amebeba sigara aliyokuwa akivuta kwa mikupuo,ila ikambidi kuiwasha mara kwa mara kwani maji ya mvua yaliizima.Sikuona silaha aliyokuwa amebeba mwanzo,ila mara moja moja nikaona chuma iking'aa sigara yake ilipokuwa ikitoa mwanga mdogo, uthibitisho kuwa alikuwa na silaha.Alinitafuta kwa kupigapiga matawi ya miwa kutumia bunduki ile ila akawa amenikosa.



    Muda mchache mtu yule akatokomea kwenye majani akifuata uelekeo wa tulipotokea baada tu ya maji kuizima sigara yake tena.Sikujua wale wengine walikuwa wametokomea wapi licha ya kuisikiliza redio niliyokuwa nimempokonya mmoja wao kule nyumbani.Akilini nikajua mchezo wangu umeshtukiwa.Kimya kimya nikaanza kutambaa ardhini nikielekea mbele na baada ya muda mfupi nikasikia sauti ya maji mengi Kama ya mto uliofurika mpaka kuvunja kingo zake.Nilijivuta matopeni nikielekea kulikokuwa kuna yale maji.Umbali wa takribani mita ishirini,nikayaona maji ya mto ule yaliyokuwa yakienda kwa kasi huku matawi ya miti yakiwamo.Nililisaili eneo lile na baada ya kuhakikisha usalama nikaketi kando ya mto ule ambao sikuwa najua jina lake kwa sababu yangu kuishi Uingereza na hata kusomea kule kabla ya kuitwa nyumbani na baba wiki chache tu zilizokuwa zimepita.Mara kadhaa nililetwa na baba nchini kuwatembelea nyanya na babu nyakati za likizo licha yangu kuzozana naye mara nyingi."Sasa ni kwa nini usije ujuane na wenzio?



    "Baba alipenda kuniuliza kila nilipoleta upinzani wa kurudi nchini"Mbona Mimi sioni shida kuishi huku baba?Nitawajua baadaye"nilikuwa nikimjibuu baba."Lazima uje Roy,hivi ukijipata umempachika mimba msichana wa ukoo wenu bila kujua kutokana na mahusiano yenu Yale ya kiholela utaficha wapi uso wako?"Baba angesema nami kwa kukosa be wala te ningekubali lakini shingo upande kurudi nchini Umalia.Nilikuwa najaribu kupata hewa safi na kupumzika.Sauti ya bastola ikiondolewa usalama ndiyo ilikanigutua kutoka kwa tafakuri yangu nzito,ikawa kupoteza muda pale kulimaanisha kupoteza uhai kiuzembe.Nilijitupa kwenye mto ule huku sauti hafifu ya risasi ikiibusu maji sentimita chache toka mguu wangu ulipokuwa kisha baadaye nikasikia sauti ya watu wakilumbana kwa muda mfupi tu maana maji yale yalikuwa na nguvu na yenye kelele nyingi.Yalinisukuma na kuniteremsha ila ujuzi wangu wa kupiga mbizi ukawa umeniokoa,nikaendelea kuelea huku nikijitahidi kuangalia ule upande niliotokea.Kwa taabu nikaweza kuwaona wanaume wale wakimulikamulika majini na kurunzi kubwa kubwa kwa jitihada za kunisaka kwani lazima walikuwa wakijipa moyo kuwa nilikuwa palepale



    Baadaye nikawapoteza kwenye macho yangu kutokana na kusukumwa na maji yale umbali mrefu sana.Nikamshukuru Mungu kwa kuniokoa toka domoni mwa simba.Maji Yale yalinipeleka mpaka pahali fulani nilipoanza kusikia sauti kubwa ya maji iliyotokana na muanguko wake kwenye mawe nami nikajua nimefikia (waterfall).Nilijua iwapo ningeendelea kubebwa na Yale maji,ningepasuliwa juu ya mawe chini ya waterfall ile.Kwa kutumia nguvu zangu za mwisho,nikapiga mbizi na kujivuta kutumia mizizi ya miti iliyokuwa imejitokeza kwenye kingo ya mto huo mpaka nikafaulu kutoka,licha ya kuwa nilikuwa nahema sana.Kufikia pale nilikuwa nimeloa chepechepe,yale mavi ambayo yalikuwa mwilini yakawa yameoshwa mbali nami nikawa nimeyabugia maji ya kutosha.Nilipofika ukingoni nilitulia kuvuta hewa baada ya patashika ya muda huo mrefu iliyokuwa imeniwacha hoi kwelikweli.



    Usaili wangu wa mazingira niliyokuwa ulinidhibitishia kuwa upande niliokuwa kulikuwa na msitu ambao sikujua ukubwa wake,ila nikakumbuka baba akiniambia uliitwa Msitu Nyangumi.Alinisimulia jinsi yeye na ndungu zake Mapipa na Sebastian walikuwa wakiwawinda ndege na wanyama wengine wadogo mle msituni.Kweli niliwaonea fahari maana baba alikuwa akinisimulia kwa namna ya kuvutia sana.Pale kijijini Kiwanika,baba alikuwa akiheshimika sana kutokana na utajiri wake bila kusahau misaada tofauti tofauti alizokuwa akiwapa wanakijiji bila kusahau genge la vibarua ambao walikuwa wameajiriwa kuchapa kazi shambani.Ndugu wa baba hawakuwa wakiishi Kijiji kile Bali walikaa mbali,kijijini Mapweke.



    Ami Sebastian hakuwa na mazoea ya kufika pale nyumbani ikilinganishwa naye ami Mapipa.Kando na hayo kulikuwa na mapenzi makubwa kati ya baba na ndugu zake.Upande mwingine wa mto ule kulikuwa na muendelezo wa shamba lile la miwa.Nilitoa mkoba wangu mgongoni nikafungua ndani na kuchomoa simu yangu ya mkononi iliyokuwa imetengenezwa mpaka haingeweza kuharibiwa na maji,kwa kimombo ikiitwa "waterproof".Niliifungua na kupunguza mwanga wake Kisha nikagundua ami Mapipa Yohana alikuwa amenipigia mara tano.



    Sikujua ikiwa alikuwa akinitafuta kuhusiana na kifo cha baba na mama au alitaka kuhakikisha usalama wangu.Kuachana na pale,niliingia kwenye mtandao wa WhatsApp,nikapata missed call nne za mpenzi wangu Sofia huku ikiambatana na jumbe chungu nzima alizokuwa amenitumia akinitafuta,jumbe ambazo sikuweza kuzisoma kutokana na mazingira na hali niliyokuwamo.Kengele ya tahadhari ikagonga kichwani mwangu baada ya kukumbuka missed call za ami ila sikujua ni kwa nini nilihisi vile kumhusu lakini singeweza kupuuza hisia zangu.Mbona mjomba na mpenzi wangu wananisaka namna hii?Niliirudisha simu ile mfukoni kisha nikaipachika mgongoni na kusimama.



    Mwendo wangu ulielekea upande wa msitu ule ambao sikuwa naujua kwa vyovyote.Ilikuwa ni afueni kuwakuta wanyama wakali kuwaliko wale watu waliokuwa wakinifuata,dhamira yao ikiwa ni kuniangamiza.Mvua iliendelea kunyesha hivyo kusababisha matope kuwa mengi ardhini, mwendo ukawa wa konokono.Baada ya kusonga umbali wa takribani mita hamsini hivi,nikageuka na kuona mwanga wa kurunzi uliokuwa na nguvu,mhusika akiwa anamulika pale nilipokuwa nimeketi hapo awali.Hisia zangu zikanitahadharisha kuwa eneo lile pia kulikuwa kumetangazwa vita kirasmi.Bastola ya wale watu niliyokuwa nayo sikujua ilikuwa imebaki na risasi ngapi nami sikutaka kubahatisha hivyo nikajaribu kuvuta chini kunakowekwa risasi.Juhudi zangu ziligonga mwamba kwani sikuwa na ujuzi wa kutumia silaha.Niligeuka na kuingia msituni nikiwa nakimbia.



    Mwili ulikuwa umekufa ganzi lakini singeiruhusu hali hii kunisimamisha.Niliendelea kuingia ndani kabisa huku nyuma nikiwa nafuatwa na wale watu unyo unyo.Giza totoro lilikuwa limetanda kotekote mpaka uwezekano wa kutazama sentimita chache tokea usoni ulikuwa mchache ila sikutaka kutumia mwanga wa rununu yangu maana ungekuwa chambo cha kuwavutia wale watu.Masaa mawili niliyatumia kuwahepa wale watu tu ila wahenga waliamba,mbio za sakafu huishia ukingoni,kwa mbali nikaona maji yaking'aa ardhini nikajua nimefikia barabara ya lami.Punde nikasikia sauti ya mngurumo wa Lori likija upande niliokuwa.Mwingereza alisema "opportunity avails only once' yaani bahati huja mara moja.Ilinipasa niitumie Lori lile kama njia ya kusafiri toka eneo lile.





    Mvua ilikuwa inanyesha kwa matone hafifu tulipokaribia mji wa Sogomo.Biashara kadha wa kadha zilikuwa zikifanyika huku wachuuzi wa vyakula aina tofauti tofauti wakiwauzia watu.Kelele zilikuwa nyingi pahali pale,nayo ikawa ni bahati upande wangu kwani licha ya kutua chini kwa kishindo,hamna aliyenitilia shaka au kuvutiwa nami.Labda walidhani nilikuwa omba omba wa mitaani.Niliyapita majumba ya disco yaliyokuwa yakipiga mziki kwa sauti ya juu.Wasichana waliovaa nusu uchi huku wakijiviringishia kwenye nguzo zilizokuwa zimetengenezwa katikati ya meza walikuwa kiburudisho kwa wahusika mle ndani.Kulikuweko na akina baba waliokula chumvi,rika la kuitwa babu na akina mama ambao waliteremsha vyupa zaidi ya viwili vya pombe kwenye matumbo yao.Almuradi burudani yoyote ilikuwa inapatikana humo.





    Mguso wa mtu kwenye bega la kulia ndiyo iliyonigutua toka kwenye mawazo yangu.Kugeuka nikakutana na tabasamu nyororo ya changundoa wakijulikana sana kwa jina la malaya kule Sogomo.Alikuwa amevalia sketi fupi na iliyokuwa imembana sana mpaka mchoro wa nguo yake ya ndani ikawa ikionekana."Naitwa Emma,Emma Mwagasaya.Ungependa tupitishe usiku huu nawe?"Aliniuliza "Sidhani"nilimjibu kwa mkato kwani sikutaka kuendelea na mazungumzo yale maana sikuwa na uhakika wa usalama eneo lile.Kwisha kumjibu,nikageuza na kujipenyeza katikati ya majumba mawili yaliyokuwa yamepakana.



    Uchochoro ule ukanifikisha mbele ya gereji la magari iliyokuwa na magari mabovu takribani ishirini kwa hesabu ya haraka.Wahandisi wanne walikuwa wakiikarabati shangingi moja aina ya Vitz nyeusi yenye nembo ya kikundi cha YDI ubavuni.YDI kilikuwa kikundi cha kuwainua vijana kiuchumi kwa kuwapa mikopo ya kuanzisha biashara ndogo ndogo humo nchini,kwa kirefu ikijulikana kama Youths Development Initiative.Mwili wangu ulikuwa umegubikwa na uchovu,nikaamua kuwaulizia wale wahandisi kulikokuwa na majumba ya kukodi ya kulala.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog