Simulizi : Baradhuli Mwenye Mikono Ya Chuma (2)
Sehemu Ya Pili (2)
Kaguta alimuita muhudumu akalipia chakula kisha wakanyanyuka yeye na Sandra wakiwa wameshikana mikono wakalifuata gari. Kaguta alimfungulia mwanamke mlango, ndipo na yeye akaingia na kuwasha chombo.
Tofauti kabisa na siku zingine, Kaguta aliendesha kwa mwendo wa kawaida usio na papara. Aliwasha radio yake ya gari na kuchomeka flash iliyokuwa imeketi juu ya dashboard, muziki ukaanza kufanya kazi yake ya kuwakonga nyoyo huku wakipashana habari za hapa na pale. Ni baada ya muda kidogo, Kaguta aligundua kuna pikipiki inawafuatilia nyuma. Aliongeza kidogo mwendokasi akamwambia Sandra;
“Itabidi ukalale kwangu leo.”
“Kwanini?”
“Kwa usalama wako.”
“Usalama wangu? … Kivipi?”
“Tizama hapo kwenye kioo.” Kaguta alionyeshea kioo cha gari kilichojishikiza darini. “Umeona hiyo pikipiki, inatufuatilia.”
Sandra alitzama kwa umakini kiooni. Uso wake ulianza kujenga hofu akawa anatizama tizama nyuma kila muda.
“Usihofu, funga mkanda.”
Upesi, Sandra alifunga mkanda akamtizama Kaguta; “Tayari!”
“Mbona una woga hivyo, unamjua huyo anayetufuata?”
“Ndio. Ni Roby … Robinson!”
“Unamuogopa enh?”
“Si mtu mzuri, Kareem. Kaa naye mbali sana.”
“Kwanini?”
“Huwa hajiulizi mara mbili kumuua mtu. Ni muuaji!”
“Kwanini atufuatilie? … Anataka nini kwetu?”
“Sijui!”
“Hapana, Sandra. Kuna kitu unanificha. Hawezi akatufuatilia hivi hivi. Au unataka kuniua, Sandra?”
“Hapana!”
“Bali?”
“Kusema ukweli nilikuongopea. Mimi na Robinson tuna mahusiano, ni mchumba wangu. Atakuwa amenifuatilia toka nyumbani. Ni mtu mwenye wivu sana, mkali na asiyeelewa.”
“Unakaa naye?”
“Hapana. Ila huwa anakuja kunitembelea mara kwa mara. Si mtu wa kukaa sana, huwa anabanwa sana na kazi.”
“Ulinambia ni mfanyakazi mwenzako, uongo kweli?”
“Kweli. Ni mfanyakazi mwenzangu.”
“Anafanya kazi wapi? … Stationary?”
“Hapana. Tuko kampuni moja tu, ila vitengo tofauti. Yeye husimamia usalama pamoja na usiri wa kampuni.”
“Kampuni yenu inaitwaje?”
“Mikmath Company Limited.”
“Makao yake makuu yapo wapi?”
“Barmuda. Ila kwa hapa Tanzania yapo Posta mpya.”
Kaguta hakuuliza tena swali jingine. Aliacha barabara kuu ya lami akashika ya vumbi.
“Acha nikuonyesha shoo.” Kaguta alimwambia Sandra kwa sura ya tabasamu. Alizima taa za gari na kuburuta matairi kwenye vumbi kwanguvu huku gari likiwa haendi popote. Vumbi lilitapakaa kama wingu kisionekane cha mbele. Robinson alipunguza mwendo akapita kwa uangalifu ndani ya vumbi lile nene.
Alipochomoza upande wa pili, hakuona kitu. Hakukuwa na ishara yoyote ya gari mbele yake wala mbali yake. Alisimama kwa muda kutazama apate jua cha kufanya. Ghafla … Taa za gari zilimmulika usoni! Gari lilichomoza toka kwenye eneo lenye mifungamano ya miti na kuifuata pikipiki kwa haraka na kuigonga tairi la mbele kabla Robinson hajachukua hatua yoyote.
Pikipiki ilirukia kando ya barabara dereva wake akirushwa mbali. Tairi lake la mbele lilipinda na kutengeneza umbo la zigzag. Kaguta alirudisha gari lake nyuma na kuliondoa kwa kasi kufuata barabara ya lami. Ndani ya muda mfupi akawa tayari ameshafika nyumbani kwake. Alishuka akamfungulia Sandra mlango na kuingia ndani.
“Umeinjoy show yangu?” Kaguta alimuuliza Sandra kwa sauti ya kebehi. Sandra alifungua mikono yake akamkumbatia Kaguta na kumbusu.
“Leo umekuwa shujaa wangu.”
Kaguta alipeleka mdomo wake kwenye mdomo wa Sandra wakaanza kunyonyana ndimi. Hawakukomea hapo, mikono yao ilifanya kazi ya kupapasana huku na kule kwa papara. Ni Sandra ndiye aliyekatisha hilo zoezi kwa kusema;
“Twende tukaoge kwanza.”
Hao walielekea chumbani. Kaguta alivua nguo zake kisha akahamia kwa mwanadada, Sandra. Kwa taratibu na kwa madaha, Kaguta alifungua zipu ya gauni la Sandra na kuishusha chini, Sandra akabakia na sidiria na tight nyeupe.
Kaguta aliondoa sidiria akahamia kwenye tight nayo akaishusha chini. Mwanamke akabakia na bikini nyeupe, sasa hapo Kaguta akapata kuona tattoo kubwa pajani mwa Sandra. Tattoo ya mtu kivuli. Tattoo ya mtu mteketezaji. Kaguta alipigwa na butwaa kutazama mchoro huo. Sandra akiwa na macho ya kilevi, aliuliza;
“Vipi, kuna lolote baya?”
“Hapana!” Kaguta aliwahi kusema. “Nilikuwa nashangaa tu hii tattoo.”
“Umeipenda?”
“Inatisha. Sema tu ipo kwenye paja lako, ingekuwa kwenye paja la mwingine ningezirai.” Alitania Kaguta huku akishusha nguo ya mwanadada iliyobakia. Walienda kukoga, walipojilaza kitandani waliacha tamaa za miili yao ziongee, wakatimiziana haja.
Jua lilichomoza upande wake ule ule wa mashariki, watu wakaamka na kujiandaa kwenda makazini.
Juu ya kitanda cha Kaguta bado walikuwepo watu wawili wakiwa wamejilaza hawala hili wala lile. Nguo zilikuwa chini wao wakiwa uchi wa mnyama wamekumbatiana. Baada ya muda, Kaguta aliamka na kutizama saa yake ya ukutani, ilikuwa ni saa tatu yaelekea na nusu asubuhi.
“He! … Wewe Sandra, amka!”
Sandra alijivuta vuta kiulevi akamtizama Kaguta.
“Enh? …”
“Saa tatu na nusu hii!”
Sandra alitoa macho kama samaki majini. “Unasema? … Mungu wangu! … Mbona hukunamsha?”
“Mimi mwenyewe ndio naamka saa hii!”
Sandra alijitazama akashusha pumzi ndefu. “Hivi ulitumia kinga kweli?” Aliuliza. Kaguta akatikisa kichwa chake; “Hapana! Hatujatumia!”
“Mungu wangu! … Kwanini?”
“Sijui hata! … Mbona hukunikumbusha?”
“Mimi hata sikujielewa yani.”
“Pombe. Ile pombe tuliyokunywa ndio tatizo. Sasa itakuwaje?”
“Embu nipeleke ofisini kwanza.”
Walioga wakavaa. Kaguta alimpeleka Sandra nyumbani kwake akavaa wakaelekea ofisini. Mpaka wanafika ofisini ilikuwa ni saa tano ya asubuhi. Kaguta hakushuka wala kwenda kuwasalimia wakina Winner, alimpa Sandra salamu zake azifikishe huko, yeye akatembea kwenda nyumbani kwa inspekta.
Alipofika hakumkuta inspekta. Alipiga simu kumtafuta, inspekta akamuelekeza yupo kwenye canteen ya hospitali. Kaguta akaelekea huko na kumkuta inspekta akiwa na mama Miraji wanakunywa chai. Juu ya meza kulikuwa na tanakilishi mpakato ya inspekta.
“Karibu.”
“Ahsante, habari zenu?”
“Njema.”
Kaguta alikaa akaagiza chai, wakati anakunywa maongezi yalichukua nafasi.
“Jana hatukupata nafasi ya kuongea. Kuna mambo niliyapatakuyaona kwenye ile flash uliyoniletea nikaona si mbaya kumshirikisha na mama Miraji maana kuna mambo yanamhusu.”
“Ndio.” Kaguta aliitikia na kunywa fundo moja la chai.
“Wakati natizama tizama jana, niligundua kuna baadhi ya nyaraka ambazo zilimshirikisha mume wake, Mr Kim Salvatore, Mtemvu na wenzake kwa madhumuni ya biashara za magendo; kuteka na kusafirisha wanyama pori kwenda Italia. Kwa bahati nzuri, mikataba hiyo haikupata kutokea yani haikupata kutiwa sahihi na kutendeka. Kwa mujibu wa mama Miraji, mume wake alifanya kazi moja tu na hiyo ndio mwishoni iligundulika akauwawa.”
“Enhe…?”
“Sasa hapa ndio naanza kuunganisha doti … Naanza kupata kidogo mwanga kwanini Mr Kim alikuwa yupo nyuma ya mauaji ya Mtemvu pamoja na wenzake, yote ni kwasababu ya biashara walizokuwa wanafanya. Eidha walisalitiana ama kugeukana. Na kutokana na maelezo ya mama Miraji, mume wake hakusaini mkataba na Mr Kim, kwahiyo walikuwa wamemgeuka huyu bwana na hapo ndio ukawa mwisho wa biashara yao.”
“Aisee. Sasa tunafanyaje? … Unadhani tunaweza tukatumia nyaraka hizo kumtia Mr Kim nguvuni?”
“Hapana! Hizi haziwezi kutosha, zinaweza kukanushwa kiurahisi kwa kusema ni za kughushi. Ukiachana na hivyo, Mr Kim ni mtu mkubwa mno. Hatuwezi kumtia nguvuni kiurahisi.”
“Sasa tunafanyaje, Vitalis?”
“Inabidi tuwe waangalifu wakubwa mno. Mr Kim ana mtandao mpana mno kila sehemu. Ila itabidi twende Italy.”
“Italy!”
“Ndio. Ili tupate baadhi ya taarifa na vielelezo ni lazima twende huko. Kuna baadhi ya nyaraka hapa zinatuelekeza vizuri tu wapi pa kuanzia.”
“Haya, tutaenda. Ila barua ya maelezo utatuma wewe huko makaoni.”
“Haina shida. Ila unakumbuka kuhusu ile mipango ya mauaji kwenye zile barua?”
“Ndio!”
“Mojawapo ni leo. Umejiandaa?”
“Kujiandaa kivipi? … Anytime mimi niko ready. Alafu ndugu yangu, jana kuna mtu alikuwa ananifuatilia wakati nikiwa na yule binti wa kule Stationary. Alikuwa na pikipiki na ndiye jamaa anayetuma hizo barua za kifo, anaitwa Robinson.”
“Really?”
“Yap. Huyo demu niliyekuwa naye ameniambia huyo Robinson huwa hafikirii mara mbili kuua mtu. Na ndiye anahusika na usalama na usiri wa kampuni yao inayoitwa Mikmath yenye makao makuu posta mpya.”
“Siku ambayo mke na mtoto wangu waliuwawa, nilikuta nyayo za tairi za pikipiki kwenye uwanja wa nyumba.
“Bila shaka atakuwa ni huyo huyo.”
“Siku nitakayomkamata huyo mtu ataimba haleluya, ukweli nakuambia.”
Mama Miraji alitabasamu kidogo aliposikia hiyo kauli.
“Unadhani mama, nitamnyoosha kweli” Inspekta Vitalis alimwambia mama Miraji kwa msisitizo.
“Ila Vitalis.” Kaguta alidakia. “Kama nilivyokuambia kilichonitokea jana. Hudhani ni hatari kwa mama Miraji kuwa mbali na sisi labda? … ni mawazo tu.”
“Hapana, mimi nipo sawa tu.” Mama Miraji alisema kwa tabasamu kubwa.
“Kwangu mimi sidhanikama ni swala la usalama ndilo hoja, kumbuka mke wangu na mwanangu waliuwawa wakiwa palepale nyumbani pamoja na kuwa na askari.”
“Ni wazo tu.” Kaguta alisema kisha akanywa chai yake kama vile hakusema jambo. Mama Miraji na inspekta walitizamana kisha wakatabasamu.
Baada tu ya muda kidogo, inspekta na Kaguta walimuaga mama Miraji wakaondoka zao. Walielekea nyumbani kwao wakaweka silaha kwenye mkebe na kuvaa nguo za kazi. Inspekta alivalia traki nyeusi na shatinyekundu inayobana mwili. Kaguta alivalia traki ya kijivuna body nyeusi. Walijipaki kwenye gari wakaelekea mpaka maeneo ya Kawe, kama anwani ya mtu anayetakiwa kuuwawa inavyosema.
Walifika eneo husika wakaketi pembezoni kidogo mwa nyumba kubwa yenye uzio mpana. Macho yao yakiwa tenge na yaliyojaa tahadhari, walipepesa huku na huko mikononi mwao wakiwa wameshikilia bunduki.
Ghafla … Risasi tatu zilipiga kioo cha gari! Kaguta na inspekta waliinamisha vichwa vyao. Macho ya inspekta yalitizama kwenye sight mirror yakaona pikipiki mbili zinakuja kwa kasi kuwafuata. Upesi alimtizama Kaguta na kumuamuru;
“Endesha, wanakuja!”
Kaguta aliwasha gari na kuliondoa kwa kasi. Nyuma yao pikipiki ziliendelea kuwafuata huku risasi zikirindima. Walipofika konani, Inspekta alifunga mlango wa gari akatokea kwa chini akiwa amebebelea bunduki akamimina za haswa akiwalenga watu wawakimbizao, ndani ya sekunde tu chache wakawa wamewamaliza wale watu juu ya pikipiki, wote walikuwa chini.
“Sasa?” Kaguta aliuliza.
“Twende kwenye lile jengo tukamuone huyo aliyekuwa kwenye orodha ya kuwawa. Anaweza akatupa kitu juu ya Mr Kim.”
“Na vipi kuhusu hawa?”
“Wapigie simu polisi, waje wawabebe.”
Kaguta alivuta dashboard akatoa simu yake. Kabla hajapiga, namba mpaya ilijitokeza kwenye simu yake ikimpigia. Akapokea.
“Haloo!”
“Eeh … Al kareem, njoo upesi huku stationary, Robinson anampiga Sandra vibaya mno!”
Ilikuwa ni sauti ya Winner, mfanyakazi wa Rosemath stationary. Kabla Kaguta hajasema jambo, simu ilikata.
“Vipi tena?”
Inspekta aliuliza.
“Sandra, yule manzi wa kule stationary, anapigwa na Robinson!”
“Robinson?”
“Ndio!”
“Kwani Robinson hayupo pale chini?”
“Sidhani!”
Kaguta alisogeza gari kwa wale wanaume waliokuwa wamelala chini kwa kupigwa risasi wakashuka na kuwatazama.
“Hayupo Robinson hapa!” Kaguta aliduwaa.
“Tunafanya nini sasa?”
“Acha nikimbie huko stationary kukabiliana naye, we maliza hapa!”
Kaguta alikimbilia ndani ya gari akawasha na kutokomea. Ndani ya muda mfupi, magari ya polisi yalifika eneo la tukio, inspekta alitoa maelezo kisha akaelekea kwenye nyumba iliyokuwa inataka kushambuliwa, aligonga geti akamuonyesha mlinzi kitambulisho akimtaka aonane na mkuu wake.
Geti lilifunguliwa, inspekta akaingia na kukutana na mwenye nyumba. Mmama mmoja mnene kiasi mwenye mvi za kuhesabika kichwani. Waliketi kwenye viti vilvyo na meza yake bustanini wakapeana mikono;
“Karibu!”
“Ahsante. Naitwa inspekta Vitalis Byabata.” Inspekta alionyesha kitambulisho chake. “Bila shaka wewe ni bi Edna?”
“Ndio. Naitwa Edna Mshoke.”
“Nashukuru bi Edna. Nina maswali machache nataka kukuuliza, natumai nitapata majibu kutoka kwako.”
“Bila shaka inspekta, karibu. Lakini ningependa kujua hayo maswali yanahusu nini? Kampuni yangu, ama?”
“Ni kuhusu mahusiano yako na Mr Kim.”
“Mr Kim?”
“Yes.”
“Mr Kim Salvatore?”
“Exactly.”
“Okay. Unataka kujua nini, inspekta?”
“Wewe na Kim, mna mahusiano gani?”
“Mr Kim alikuwa business partner wangu. Kampuni yangu na yake zilikuwa kwenye ubia wa biashara.”
“Jina la kampuni yako?”
“Wonders Limited Company.”
“Na kampuni ya Mr Kim?”
“Mikmath Company.”
“Ubia wenu wa biashara ulikuwa unahusu nini?”
“Kampuni yangu inahusika na urembo wa wanawake. Kutengeneza lipstick, wanja, lipbam. Wigs, weaving na vitu kama hivyo. Mr Kim aliingia ubia na mimi wa kununua na kusambaza hizo bidhaa nje ya nchi kwa jina lake.”
“Kwanini atake kukuua?”
“Nani?”
“Kwanini Mr Kim atake kukua?”
“Umejuaje kama anataka kuniua?”
“Hujasikia milio ya risasi nje ya uzio wako?”
“Nimesikia.”
“Walikuwa ni watu wanaokuja hapa. Ni vijana wa Mr Kim. Kwanini anataka kukua?”
Bi Edna alishika kichwa chake akashusha pumzi ndefu. Alimtizama inspekta na macho yake ndani ya miwani akamwambia;
“Miezi michache ilyopita mimi na Mr Kim tulivunja mkataba. Sikutaka tena anunue bidhaa zangu, wala kuzisambaza kokote. Nlikuja kujua anachafua brand yangu kwa kutumia vitu vyangu kufanyia biashara yake haramu.”
“Biashara ipi?”
Kabla Bi Edna hajajibu, Ghafla milio miwili ya risasi ilivuma! Bi Edna alipiga kelele za maumivu, haraka inspekta aliingia chini ya meza risasi zingne zilizofululiza zikamkosa. Aliporusha macho yake juu ya uzio kutafuta risasi zinapotokea, alimuona mwanaume mwenye bunduki akiwa anachungulia, alikuwa ni Robinson.
Kufumba na kufumbua, Robinson alipotea, aliachia ukuta akadondoke huko nje. Haraka inspekta aliufuata ukuta akaurukia na kujidondoshea upande wa nje, alitazama kushoto na kulia akamuona Robinson akiwa anakimbia, naye akaanza kumfukuza kwa mbio pana.
Kila kona, inspekta aliibuka na Robinson. Kila uchochoro inspekta alizama na kuchomoza na mtu wake, hakumuacha hata chembe. Robinson alipiga kona za hapa na pale huku akijificha ficha kwenye miili ya wapita njia hali iliyomfanya inspekta ashindwe kutumia bunduki yake kumaliza kazi. Mara kwa mara, Robinson aligeuka na kufyatua risasi kumlenga inspekta lakini hakufanikiwa, risasi zilienda kombo ama kulenga watu wengine wasio na hatia.
Walipofika kwenye barabara ya lami, Robinsonalidandia daladalaaina ya DCM akaweka watu chini ya ulinzi na kumtaka dereva afuate maelekezo yake. Inspekta alikaa katikati ya barabara akasimamisha Noah, alipanda akaanza kufukuzia DCM iliyotekwa.
“Fasta, kanyaga mafutaa!” Robinson alimuamuru dereva huku macho na mkono wake wenye bunduki akiuelekezea kwa abiria. Dereva alikanyaga mafuta gari likazidi kupepea na kupepea. Nyuma yao, Noah alilomo inspekta nalo lilichochea moto kufukuza DCM.
“Haloo!” Robinson aliweka simu sikioni. “… Yes, nimeshamaliza kazi … nipo kwenye DCM la Kawe mbezi nakaribia kwenye kona ya kuelekea Mwenge … fanya fasta mwela ananikimbiza … yupo kwenye Noah nyeupe nyuma yangu … ”
DCM ilipofika konani kuelekea mwenge, yaliyotokea magari mawili kwa kasi nyuma ya Noah. Moja lilienda kushoto na lingine kulia, Noah likaekwa katikati. Gari lililokuwa upande wa kushoto lilibamiza kwanguvu Noah kwa ubapa, wakati Noah laenda kwa kasi upande wa kulia liliposukumiwa, gari lililokuwa upande wa kulia lilipiga breki kali na kuligusa tairi la Noah kidogo tu, Noah likapinduka na kubiringita mara mbili. Magari yale mawili yakapotea kwa kasi mno.
Mlango wa gari la Noah ulisukumwa na teke, inspekta akatoka nje akiwa anavuja damu kichwani, mkononi alikuwa kabebelea bunduki yake ndogo. Alitizama barabarani asione magari yale mawili wala DCM. Punde alianza kuhisi kizunguzungu akadondoka chini na kuzirai.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Macho ya inspekta yalipokuja kufunguka, alikuwa juu ya kitanda cha hospitali kichwani akiwa na bandeji kubwa. Aligeuza shingo yake kutizamapembeni akamuona Kaguta akiwa amesimama na daktari wanaongea lakini hakusikia nini kinaongelewa. Alifunga macho yake na kujaribu kukumbuka nini kilitokea, ghafla mpasuo wa maumivu ulipita kichwani kwake, akatoa sauti ya kulalamika. Kaguta na daktari wakamsogelea.
“Pole, inspekta.” Dokta alimwambia Vitalis.
“Ahsante.”
“Usihofu, ni jeraha la kawaida tu. Utarudi katika hali yako muda si mrefu. Kichwa kiligongwa kwanguvu.”
“Ahsante, daktari.”
Daktari alimeukia Kaguta akampa maelekezo; “Usimchoshe. Inabidi apumzike sana.” Kaguta aliitikia, daktari akaondoka na kuwaacha wawili.
“Pole, Vitalis.”
“Ahsante, nimeshapoa. Vipi kule ulipoenda?”
Kaguta alitikisa kichwa chake akasonya. “Hakuna kitu ndugu yangu. Sikukuta chochote.”
“Hukukuta chochote kivipi, Sandra hakuwepo?”
“Alikuwepo, ila Robinson hakuwepo. Nilivyouliza wakaniambia eti walikuwa wananipima.”
Inspekta alitikisa kichwa akatabasamu.
“Vipi, mbona umefurahi?”
“Tumeingizwa mkenge. Tumedanganywa na tukaingia kichwa kichwa. Robinson hakuwepo huko, Robinson alikuwepo kule uliponiacha na akatekeleza adhma yake ya kuua.”
“Ah! … Kweli tumepatikana.” Kaguta aling’ata kidole kwa kujilaumu.“Ilikuwaje sasa ukapata ajali, maana dokta kanambia ulipata ajali ya gari.”
“Ni wakati namkimbiza Robinson. Kuna magari mawili sijui yalitokea wapi yalipush gari nililokuwepo likapinduka.”
“Aisee! … Sandra na wenzake wanajikuta ni wajanja, sio?” Kaguta alijiuliza huku akitizama dirishani.
“You have to be careful, Kaguta. Huwezi jua wana mipango gani. Kumbuka, they are in the same team.”
“I am very sorry, Vitalis. I let you down.”
“Usihofu, tushukuru Mungu tupo wazima. Bado kazi yaweza kufanyika.”
“Ni kweli. Kuna kazi yoyote ya kufanya tena kule stationary?”
“Hapana. Kwa sasa cha kufanya ni kuwafuatilia wale watu waliokuwepo kwenye zile barua. Bahati mbaya tuliyempata kauwawa, alikuwa na taarifa nzuri na za muhimu sana.”
“Umepata taarifa gani?”
“Kuna kampuni inaitwa Wonders ya Bi Edna Mshoke inahusiana na bidhaa za wanawake, ilikuwa na mahusiano na kampuni ya Mr Kim. Lakini baadae walikata mahusiano kutokana na Mr Kim kuharibu brand ya Wonders kwa kufanya biashara haramu. Ila sijapata kujua hiyo biashara haramu ni ipi na ilikuwa inaharibuje brand ya Wonders kwani mwanamama huyo alipigwa risasi za kifua na Robinson akafa.”
“Umesema hiyo kampuni inaitwa Wonders?”
“Ndio.”
“Inatengeneza mawig na maweaving?”
“Ndio!”
“Dada yangu anafanya kazi hapo.”
“Kweli?”
“Ndio. Si unamjua Sarah?”
“Ndio.”
“Ndio huyo huyo!”
“Basi, anaweza akatusaidia kupata baadhi ya taarifa.”
Jioni ilipotinga, inspekta akiwa na bandeji yake kichwani aliongozana na Kaguta wakaenda hospitali kumuona Jombi. Walibeba chakula na maji makubwa. Walimjulia hali Jombi, wakaketi pembeni.
“Tumekuletea chakula, amka ule, kijana wangu.” Inspekta alisema huku akifungua mfuko aliokuja nao na kutoa hotpot la chakula. Jombi aliinuka akaketi kitako.
“Sasa hiki chakula kimepikwa na wanaume wenzako, kwahiyo unavyokula usianze kujudge judge sijui chumvi sijui mafuta … aah … aah!” Inspekta alitania wakacheka.
“Leo mama Miraji haji?” Jombi aliuliza.
“Hatujui, kwani huwa anakuja kila siku?” Inspekta aliuliza.
“Ndio, kila siku huwa anakuja.”
Ispekta alimsogezea hotpot Jombi akaanza kula.
“Mmmh … umepika wewe, inspekta?”
“Ndio, vipi?”
“Kitamu sana.”
Kaguta alicheka akapiga makofi; “Huwa hakosei huyu jamaa. Sijui kwanini alioa?”
Wote walicheka huo utani. Jombi alipiga matonge matatu, inspekta akaanza kuongea kiofisi;
“Jombi, kuna kitu kinanitatiza juu yako. Kwanini ulikuwa unawindwa uuwawe?”
“Siwezi kusema chochote, inspekta. Mimi ni mtu niliyefanya makosa, na nastahili kufungwa. Nilikuwa mtu muovu na mwenye kundi baya, nashangaa kwanini mnanijali kiasi hiki?”
“Usijali, Jombi. Sisi tuna dhumuni safi la kukusaidia. Ila hatuwezi kama hautotupa nafasi ya kufanya hivyo.” Inspekta alieleza.
“Natamani sana kusema na kujibu mnayouliza. Ila siwezi.” Jombi alisema na uso wake uliopoa.
“Tunajua ni kwasababu ya kiapo chako, si ndio?” Kaguta alimuuliza Jombi. Jombi alishtuka kidogo kusikia habari za kiapo.
“Umejuaje kuhusu kiapo?”
“Wenzako wametuambia. Hawawezi kusema kitu kwasababu ya kiapo.”
“Ni kweli. Hatuwezi tukakiuka hilo. Tutakapofanya kinyume, ni kifo tu ndicho kitatuangamiza.”
Inspekta alimtizama Kaguta kisha akauliza;
“Ila Jombi, kwanini wenzako walikuwa wanakutafuta wakuue ingali wanajua ushakula kiapo na huwezi kufungua mdomo?”
“Hiyo ni kanuni. Mtu yeyote akikamatwa inabidi auwawe kabla hajasema chochote kwasababu …” Jombi alikatisha maneno. “Siwezi nikasema. Nitakufa.”
Inspekta alitikisa kichwa akamshika mkono Kaguta; “Tuondoke.”
Walinyanyuka Kaguta akainama na kumshika bega Jombi. “Ugua pole. Tutakuja kukuona siku nyingine.”
Waliondoka wakaelekea kwenye gari la Kaguta na kupanda.
“Tunaelekea wapi?”
“Kigamboni kwa Mr Bomba. Yule ambaye amepangiwa kuuwawa leo na Robinson. Leo ni kuchagua mawili, tumuokoe mtuhumiwa au tumkamate Robinson. Huyu ni mtu wa mwisho, Robinson akifanikiwa kumuua tutakuwa tumepoteza sana.”
“Usihofu, Vitalis. Tutamkamata.”
Kaguta aliondoa gari wakaanza safari ya kuelekea kigamboni. Walipofika kwenye nyumba husika, walishuka upesi na kuelekea ndani ya uzio wa nyumba. Walibisha hodi, lakini hakuna aliyeitikia. Kaguta alipiga mlango kwa teke kali, ukavunjika wakaingia ndani.
Walikuta mwili mwa mwanaume mnene mwenye kiwaraza ukiwa umejilaza chini panga pembeni, shingo imekatwa. Kabla hawajafanya chochote, ghafla, walisikia vishindo vya mtu nje ya nyumba. Haraka walitoka nje wakamuona mwanaume mmoja anakwea ukuta na kurukia nje ya uzio.
Kama upepo, inspekta na Kaguta walikimbilia ukuta na kuchumpia nje kama nyani. Kwa mbio zote walimfukuza yule mwanaume ambaye aligoma kabisa kugeuza shingo yake nyuma.
Inspekta alitoa bunduki yake akaifyatua kumlenga mwanaume yule mguuni mara mbili bila ya mafanikio. Kaguta alimpokonya inspekta bunduki akafyatua risasi kumlenga mguuni mwanaume wanayemkimbiza, akafanikiwa.
“Pumbavu!” Kaguta alipaza sauti. Huku akimnyooshea bunduki mwanaume aliyemlenga, walisonga karibu naye na kumuamuru aweke mikono juu. Walipomtizama waligundua ni Robinson.
“Oooh … Mr Robinson!” Kaguta alisema kama mtu atangazaye shughuli.
“Leo umeingia katika mikono yangu, mbwa wewe!” Inspekta alisema kwa hasira. Alimpiga teke kali Robinson tumboni. Kama hatoshi, alimpiga tena na tena. Kaguta alimtuliza inspekta akamsogeza kando.
“Utamuua sasa mapema yote hii!”
Walimnyanyua Robinson aliyekuwa anachechemea wakampeleka kwenye gari lao kisha wakaenda moja kwa moja kwenye jengo lao la mateso. Walimfungia Robinson mstimuni, miguu na mikono ikabanwa kwa kamba nene.
“Leo utaeleza kwanini popo hatagi?” Inspekta alitoa kitisho huku akivua shati lake na kubakia na kaushi, wakati huo Kaguta akiwa anatabasamu tu akimtizama inspekta.
Inspekta alimpiga ngumi Robinson mpaka akatoa damu mdomoni na puani. Inspekta akiwa anahema kwa kuchoka kurusha Makonde, simu yake iliita mfukoni. Ilkuwa ni namba private, alimuonyeshea Kaguta, Kaguta akapandisha mabega kuashiria hana la kusema. Inspekta alipokea akaweka simu sikioni.
“Haloo … eenh? … wewe! … “ Simu ilikata.
“Vipi?” Kaguta aliuliza.
“Wamemteka mama Mraji. Wapo nyumbani kwangu na wamesema niende na wewe pamoja na mtu wao.”
Inspekta na Kaguta wakiwa wanatizamana kwa mabumbuwazi, sauti ya kicheko ya Robinson iliwashtua.
“Mlidhani yanaisha, ndio kwanza yanaanza.” Robinson alisema kwa kebehi.
“Una uhakika wapo kweli na mama Miraji?” Kaguta alieleza shaka.
“Ndio! … Nimesikia sauti yake kabisa!”
Hakukuwa na jinsi, walimfungua Robinson wakampakiza garini na safari ikaanza ya kuelekea kwa inspekta.
“Sasa tunafanyaje, Vitalis?”
“Sijui hata. Kichwa kimegoma.”
Walifika nyumbani wakawakuta wanaume wanne mapande ya watu wakiwa wamemshikia bunduki mama Miraji. Robinson aliachiwa akaungana na wenzao, bunduki zikaelekezewa kwa inspekta na Kaguta.
“Tuna taarifa nzuri na mbaya kwenu. Taarifa nzuri kwenu ni kwamba, hatutowaua. Taarifa mbaya kwenu ni kwamba, kitu mlichokuwa mnakipinga na kukizuia, itabidi muungane nacho.” Alisema mwanaume mmoja mweusi kuliko wote.
“Sogea hapa, inspekta.” Mwanaume yule mweusi alimuamuru inspekta, inspekta akasogea kwa mwanaume mmoja aliyekuwa amekaa kwenye kochi. Mwanaume wa kochini akafunua mkono wa inspekta na kutoa mashine ya kuchora tattoo.
“Unataka kufanya nini?” Inspekta alipokonya mkono wake. Bunduki zikaelekezwa kwake.
“Toa mkono huo!” Amri ilitolewa. Inspekta hakutoa mkono wake. Bunduki ikaelekezwa kwa mama Miraji.
“Peleka huo mkono ama napasua kichwa cha huyu mama.”
Inspekta alirudisha mkono wake kwa mchoraji, mchoraji akaanza kazi yake. Alipomaliza, akafuatia Kaguta naye akachorwa tattoo. Tattoo zilipokamilika, upepo mkali ulipuliza watu wote wakadondoka chini.Ghafla giza lilitawala na Jitu likatokea! Mbele ya macho ya watu, jitu lilijigawa mara mbili na kuzama kwenye mikono ya Inspekta na Kaguta pale pale palipochorwa tattoo.
Zoezi hilo lilipokamilika, mwanga ulirudi ghafla. Inspekta na Kaguta walikuwa wamelala chini, hawakuwa na fahamu. Wale majambazi yalipeana ishara wakapotea lile eneo wakamuacha mama Miraji.
Mama Miraji aliisogelea mwili wa Kaguta na inspekta akilia. Aliita na kuita lakini wanaume hawakuamka. Walikuwa kimya, hata vifua vyao vilikuwa vinapanda na kushuka kwa mbali mno. Mama wa watu alikimbilia jikoni na kurudi na ndoo ya maji. Ajabu, hakuwakuta watu. Walikuwa wametokomea! Alitizama huku na kule asione chochote. Alifungua mlango akatoka nje ya nyumba akazunguka huku na huko asipate kuona kitu. Mwishowe alikaa chini akaanza kulia.
Katika ulimwengu mwingine mbali kabisa na ulimwengu wa nyama na damu, ndipo walipokuwepo inspekta na Kaguta. Kulikuwa ni kiza totoro. Inspekta na Kaguta walipeleka shingo zao kushoto na kulia lakini hawakuona chochote. Kwa mbali na ghafla, waliona mwanga wa moto. Bila ya kusemezana lolote na wakiwa kama watu wasiojitambua, walianza kusonga mbele kuufuata mwanga wa moto. Walipoufikia, walisimama na kusimamisha mikono yao ya kuume yenye tattoo wakasema kwa pamoja;
“Tumekuja hiji sisi tulio wapya. Tumekuja kula kiapo sisi tulio wapya. Tumekuja kujisalimisha sisi tulio wapya. Utuongoze na hekima yako. Utufunge mdomo na mioyo yetu tukapate kufanya kazi yetu vyema, kwa ufanisi na kwa siri.”
Baada ya kusema hayo, mwanga wa moto ulikuwa mkubwa ghafla na katikati yake akaonekana jitu la uteketezaji.Kufumba na kufumbua, jitu lilitoka kwenye moto na kuwazunguka haraka inspekta na Kaguta kisha likarudi motoni, mara mikono ya Kaguta na inspekta ikaanza kumwaga damu zikitoka eneo la tattoo. Wakati damu inamwagika wakawa wanaongea;
“Tunakula hiki kiapo kwa damu inayomwagika. Na tutakapokikiuka, tutaadhibiwa na damu inayomwagika mara nne zaidi!”
Maneno hayo yalipokoma, moto ulizima. Ghafla, inspekta na mwenzake walidondoka chini kama mizigo. Walipokuja kufungua macho walijikuta nje ya nyumba ya inspekta wakiwa uchi wa mnyama.
“Kaguta mbona upo uchi?” Inspekta alishangaa.
“He! Wewe je? … Hujioni?”
Walijitizama wakanyanyuka kukimbilia ndani, sebuleni walimkuta mama Miraji kalala kwenye kochi, haraka walifunga mlango wakatoka nje na kusogea mbali.
“Sasa tunafanyaje?” Kaguta aliuliza.
“Twende tupitie mlango wa nyuma!” Inspekta alishauri. Haraka walielekea nyuma ya nyumba wakafungua mlango na kuingia ndani.Walivaa nguo wakaketi juu ya kitanda.
“Tumekwisha, Vitalis. Hatuna ujanja tena!” Kaguta alilalamika huku akitikisa kichwa. Inspekta alishika tama, hakuwa na la kusema.
“Sasa tunafanyaje, Vitalis? … Tumeshawekwa chapa na kiapo tumekula. Sielewi hata ilikuwaje nikasema yale maneno.” Kaguta aliendelea kulalamika. Inspekta alikuwa kimya tu, kichwa chake kikibebwa na tama.
“Sasa mbona huongei, Vitalis?” Kaguta aling’aka.
“Sina hata cha kusema ndugu yangu. Sijui nitafanya nini sasa na tayari nieshaapa?
“Hapana! Inabidi tutafute cha kufanya, hatuwezi tukatulia tu hivi bila ya kuchukua hatua yoyote.”
“Kweli. Ila kwa sasa, nahisi kama kichwa changu kimepooza. Hakifikirii kabisa.”
“Najua. Lakini … ” Kaguta hakumalizia kauli yake mlango ukagongwa.
“Hodii! … Inspekta? Mpo ndani?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa sauti ya mama Miraji. Inspekta na Kaguta walitazamana, Inspekta alinyanyuka na kuufuata mlango akafungua.
“Kumbe mpo ndani? … Mie nimewatafuta mpaka basi!” Mama Miraji alitanabahi kwa mshangao.
“Nakuja huko sebuleni muda si mrefu, mama.” Inspekta aliongea kwa upole. Mama Miraji alishika njia akaelekea sebuleni. Baada ya muda mfupi, inspekta pamoja na Kaguta wakaja sebuleni.
“Hao majambazi walikukamatia wapi?” Inspekta alimuuliza mama Miraji.
“Wakati natoka nyumbani, nilipotoka tu mlangoni lilikuja gari moja kwa kasi likasimama mbele yangu, walishuka wanaume watatu wakanikamata na kuniingiza garini wakanileta kwako.”
“Pole sana.” Inspekta alimpoza mama Miraji.
“Nimeshapoa. Ila nimeshindwa kuelewa, kwanini wale watu wamewachora tattoo mikononi? … Ilikuwa ina maana gani wao kunikamata ili tu wawachore nyie?” Mama Miraji aliuliza.
“Kusema ukweli hizi tattoo walizotuchora ni agano la kuwa katika kundi lao. Hawa majambazi ukiachana na kwamba shughuli zao hutumia mwili wa nyama, kuna ulimwengu wa kiroho unaowaongoza na kuhakikisha hawatoi siri za kazi zao, wala mkubwa wao.
Hiyo roho ili ipate kuingia kwenye mwili wa binadamu, lazima achore tattoo na ale kiapo cha damu. Atakapogeuka kiapo hiko, damu yake lazima imwagike, na inamwagika zaidi.” Inspekta alielezea. Mama Miraji akaachama mdomo kwa kushangaa.
“Kwani mmekula kiapo? … Si mmechorwa tu?”
“Tumekula na kiapo!” Kaguta alijibu.
“Saa ngapi?”
“Hatujui ni saa ngapi. Ila ninachokumbuka, ghaflatulitokea kwenye ulimwengu tusioufahamu. Kulikuwa ni giza na huko ndipo tulipokula kiapo. Sijui hapa tumefikaje, tulijikuta nje ya nyumba tena tukiwa uchi wa mnyama.” Inspekta alifafanua. Mama Miraji akazidi kuachama mdomo mithili ya pango.
“Mweh! … Baba sasa itakuaje?” Mama Miraji aliuliza huku akitumbua macho yake kama vile mtu aliyekabwa na tonge.
“Ila mimi sina hofu.” Kaguta alisema, mama Miraji na inspekta wakamtizama. “Mimi naona hii tattoo inadhuru pale tu mtu anapojaribu kutoa siri na si vinginevyo. Hakuna haja ya kuhofia.” Kaguta alidadavua.
“Una uhakika gani kama haina madhara kwa upande mwingine?” Inspekta aliuliza.
“Sidhani. Si unakumbuka Jombi mwenyewe alikuwa anataka kuuwawa na wenzake? … Sasa kama ingekuwa ni ishu ya tattoo wangewezaje kumdhuru au kutaka kumuua mwenzao? … ” Kaguta alimwaga maneno. Inspekta alifikiria kisha akatabasamu.
“You are right! … Sidhani kama itatuzuia kufanya kazi yetu.” Inspekta alikenua wakagongeshana mikono na Kaguta. Baada ya muda mama Miraji akaaga anataka kwenda nyumbani. Kabla hajaondoka, Kaguta alimuita inspekta pembeni wakateta jambo;
“Vitalis, hivi mpaka huyu mama afe ndio uone anahitaji kuwa na wewe? … Watamuua huyu nakuambia. We kaa naye si atalala hata vyumba vingine. Atakapokuja kufa utalalamika? … Utajilaumu kwasababu kwa njia moja ama nyingine utakuwa responsible for her death. Take this key kama utataka kumsindikiza.” Kaguta alisema kwa mkazo.
“Lakini, Kaguta … ”
“Lakini nini? … Sitokuambia tena hili swala.” Kaguta alisema kisha akaondoka zake kurudi sebuleni. Baadae kidogo, inspekta naye akaja sebuleni na kumtaka mama Miraji aongozane nayekwenda nje. Mama Miraji alimuaga Kaguta akatoka nje kuungana na inspekta aliyekuwa ameingia ndani ya gari la Kaguta. Alipoingia tu garini, inspekta aliwasha gari wakatoka lile eneo.
“Nataka kukupeleka ukamchukue mwanao huko shuleni.”
“Hatuendi nyumbani?”
“Tunaenda, ila nataka leo uhamie kwangu, wewe pamoja na mwanao.”
“Unasema?”
“Nataka uhamie kwangu, wewe pamoja na mwanao.”
“Kwanini?”
“Kwasababu ya usalama wenu. Si salama kukaa peke yako kwako.”
“Ila inspekta huoni kama … ”
“Sioni chochote. Nataka uwe karibu na mimi hapo tu ndipo nitahisi upo salama. Ntajitahidi kwa nguvu na akili zangu zote kukuhakikishia usalama. Sitaruhusu nifanye kosa lingine kama lile nililolifanya kwa mke na mtoto wangu.”
“Jamani inspekta … ”
“Nakuomba. Nakuomba uhamie kwangu. Sitasamehe nafsi yangu endapo utapata tatizo na sikufanya juhudi yoyote kukusaidia.”
Mama Miraji hakutia tena neno. Alihamishia macho yake nje akawa anatizama tu miti inavyokimbia. Kwa muda kidogo palikuwa kimya asiwepo wa kuongea. Baada ya muda, inspekta aliomba maelekezo kuelekeaa shule kumchukua Marietta. Walielekea huko wakamtwaa mtoto kisha wakaenda nyumbani kwa mama Miraji walipochukua baadhi ya nguo na kurudi kwa inspekta.
Siku iliyofuata ikiwa ni asubuhi ya saa mbili, Kaguta na inspekta waliongozana wakaenda kwa Sarah. Bahati mbaya hawakumkuta mwenyeji wao. Waliita na kubisha hodi lakini hawakupata majibu yoyote. Kaguta alitoa simu yake mfukoni akapiga.
“Sister upo wapi? … Mie nipo nyumbani kwako hapa … Ok, nakungoja basi.”
Alikata simu akamtizama inspekta; “Tumngojee anakuja muda si mrefu. Ametoka kidogo.” Inspekta alitikisa kichwa chake kwa masikitiko; “Sasa wewe kwanini hukumpigia tokea tupo nyumbani?”
“Nilisahau. Alafu nilijua nitamkuta coz hatokagi tokagi.”
“We mume wake mpaka ujue ratiba yake? … Umefanya mistake, tungoje tu.”
Punde Sarah akaonekana kwa mbali. Kaguta alimshtua inspekta na kumuonyeshea kule atokako Sarah.
“Yule anakuja, si nilikuambia anakuja sasa hivi?”
“Ndio yule mwenye hips nene?”
“Acha mambo yako basi, we umeona hips tu?”
“Aisee! … Ana vipisto!”
“Acha basi!”
“Eeeh … Wewe inakuuma enh? Lakini dada za wenzako … aah! aah!”
Sarah alipofika alimkumbatia kaka yake akawakaribisha wageni ndani, aliwaletea vinywaji wanavyotaka wakaketi na kuanza kuongea.
“Huyu anaitwa Sarah, ni mdogo wangu. Sarah huyu anaitwa Vitalis ni mfanyakazi mwenzangu.” Kaguta alitambulisha, Sarah na Vitalis wakapeana mikono punde tu Kaguta akawaachanisha.
“Inatosha!”
Inspekta na Sarah wakacheka. “Hujaacha tu wivu kwa dada yako?” Sarah alisema huku akitabasamu.
“Sasa anakushika muda mrefu hivyo?”
“Jamani, muda mrefu wapi?” Sarah alisema inspekta akadakia, “Mie mwenyewe nashangaa!”
Baada ya kutaniana kwa muda kidogo, walianza kuongelea mambo yaliyowaleta.
“Sarah, bado unafanya kazi kule Wonders?” Kaguta aliuliza.
“Hapana. Niliacha kitambo tu.”
“Kwanini uliacha?”
“Walikuwa wanazingua. Kwa muda mrefu tu hatukulipwa pesa zetu, nikaamua kusepa mie.”
“Kwanini hamkuwa mnalipwa?” Inspekta aliuliza.
“Kusema ukweli sijui. Ila kuna watu walikuwa wanasema kwamba yule mmama wa kampuni alikuwa kaiuza kampuni kwa mdosho fulani hivi ambaye alishindwa kuiendesha.”
“Mmmh … Ujue nilikutana na huyo mama anayemiliki hiyo kampuni, bi Edna. Akaniambia kwamba kampuni yake ilikuwa imeingia mkataba na mfanyabiashara fulani hivi mkubwa. Lakini akaja kuvunja mkataba baada ya kuona huyo mfanyabiashara anaharibu brand yake kwa kufanya biashara haramu. Ni kweli hayo?"
“Mmmh ... labda inaweza ikawa kweli. Ujue kuna kipindi fulani hivi kuna watu walikuwa wanatuletea vtu fulani hivi kama unga unga tuviweke kwenye masidiria, mawigi na maweaving. Tukimaliza wanachukua na kuweka kwenye mikoba yao wanaondoka. Wengine walikuwa wanasema eti ni madawa ya kulevya, lakini mie sina uhakika na hilo. Na huyo mama huyo bi Edna, mbona na yeye ndio alikuwa anakuja kila siku na kutuambia kwamba tufunge midomo yetu tusiseme chochote popote pale.”
Kaguta na inspekta walitizamana, inspekta akaguna.
“Kwahiyo bi Edna alikuwa anaunga mkono hiko kilichokuwa kinafanyika, sio?”
“Eeeh … Ndio!”
“Mlikuwa mnalipwa kiasi gani? Na mliacha lini kuweka hayo mavitu kwenye masidiria na hayo manywele?”
“Wakati tunaweka hayo maunga tulikuwa tunalipwa vizuri kweli, na ndio hapo nikajenga na hii nyumba mnayoiona. Ila baada tu ya kuacha hiyo kazi, ndio tukaanza kutokulipwa mpaka nikaondoka.”
“Sasa wewe mbona hukunambia?” Kaguta aliuliza.
“Si nimesema kwamba hatukutakiwa kusema lolote.” Sarah alijibu.
“Inaelekea kuna kitu bi Edna na mfanyabiashara mwenzake walikwaruzana.” Inspekta aliongea kama vile mtu mwenye uhakika. Sarah akadakia; “Ni kweli, maana ni ghafla tu lile zoezi lilikatizwa na hatukuliona tena. Alafu, nasikia yule mama kauwawa, tena yeye pamoja na kaimu wake.”
“Kaimu wake? … Yupoje?”
“Mbaba fulani hivi mnene mnene ana bonge la kibaraza kichwani.”
Inspekta alikunja sura akamtizama Kaguta.
“Kuna haja ya kwenda kwa yule mbaba?”
“Yupi?”
“Yule tuliyemkuta kauwawa. Ndio huyu ambaye Sarah anamuongelea.”
“Okay. Mie nipo tayari.”
Walinyanyuka wakaaga. Sarah aliwasindikiza mpaka nje ya nyumba, wanaume wakapanda gari na kuondoka kuelekea kwa yule mzee kaimu wa Wonders Limited.
Ila wakiwa njiani, simu ya inspekta iliita. Alikuwa ni mama Miraji anampigia, inspekta alipokea akaiweka sikioni;
“Haloo … Enh? … Upo sehemu gani? …. Haya sawa nakuja sasa hivi … Hakikisha haukai sehemu yoyote peke yako …”
Simu ikakata.
“Vipi, kuna nini tena?”
“Mama Miraji! … Anasema kuna mtu anamfuatilia kwa nyuma tokea anampeleka mtoto shule! … Embu geuza haraka twende!”
“Wapi?”
“Mbele ya St Marry mbezi beach.”
Haraka gari liligeuzwa na kuanza kwenda Mbezi beach kwa mwendokasi mkali. Wakiwa wamekaribia kufika, inspekta alimpigia simu mama Miraji amuelekeze alipo, mama Miraji akafanya hvyo na ndani ya dakika Kaguta na inspekta wakawa wameshafika mbele ya mama Miraji.
“Yuko wapi?” Inspekta aliuliza kwa jazba.
“Yulee! … Yulee anakimbia! … Anakimbia!” Alikuwa ni mwanaume mwembamba aliyevalia suti. Aliwapa wakina inspekta mgongo huku akikimbia kwa kasi.
“Ingia kwenye gari, haraka!” Inspekta alimuamuru mama Miraji. Mama Miraji aliingia kwenye gari, gari likaondolewa kwa kasi kumfukuzia yule mwanaume akimbiaye. Yule mwanaume alipoona gari lamsogelea aliacha njia kuu akashika vichochoro.
Gari lilisimama kwa breki kali, inspekta akashuka na kuanza kumkimbiza mwanaume yule kwa kasi mno. Ndani ya sekunde chache, inspekta akawa tayari amemkaribia yule mwanaume, alimshika koti akamvuta akampa ngumi nzito ikampeleka mwanaume yule chini na kumvujisha damu puani.
“Wewe nani?” Inspekta aliwaka. Mwanaume yule hakujibu, badala yake alitabasamu na kumuonyesha inspekta ishara ya kidole cha kati. Inspekta alighafirika, alikunja mikono ya shati lake na kuacha tattoo yake wazi, mwanaume yule akaiona. Inspekta alimnyanyua mwanaume yule juu juu kwa staili ya kumkwida. Ajabu mwanaume yule hakuonyesha kupinga lolote, badala yake alipeleka mkono wake ndani ya suruali akawa anakunja na kunyoosha vidole kama mtu ajikunaye.
Ghafla, inspekta alimuacha mwanaume yule na kushika kichwa chake akilalamika maumivu. Mwanaume yule hakukoma, aliendeleza zoezi lake huku akionyeshwa kufurahishwa na ile hali aipitiayo inspekta ya kulalamika kichwa. Baada ya muda, inspekta alidondoka chini akapoteza fahamu. Mwanaume yule akapotea.
“Mbona harudi?” Mama Miraji aliingiliwa na hofu, Kaguta alishuka garini akaenda kumtafuta inspekta. Baada ya dakika kumi alimpata inspekta akiwa amelala hajielewi. Alimuita lakini hakuitika. Alimnyanyua akampeleka garini.
“Mungu wangu! Amefanya nini?” Mama Miraji aliuliza macho yakimtoka.
“Sijui! Tumuwahishe hospitali.”
Gari liliondoshwa kwa kasi na Kaguta kuelekea hospitalini. Inspekta akafanyiwa vipimo, daktari akawapasha majibu hakuna kitu chochote kikubwa alichopata kuona, labda tu mgonjwa alikuwa na uchovu wa jua kali. Kaguta na mama Miraji wakashangazwa na hayo majibu. Walingoja inspekta aamke warushe mashaka yao kwa njia ya maswali. Ikiwa lisaa limepita ndipo inspekta akaamka akirudi fahamuni.
“Vitalis, nini shida?” Kaguta alirusha swali, mama Miraji naye akaonyesha shauku kubwa la kutaka kufahamu.
Inspekta alishika kichwa chake akakunja sura. Macho yalikuwa yamemlegea akionekana kutawaliwa na uchovu. Alimtizama mama Miraji kisha akayarudisha macho yake kwa Kaguta.
“Kichwa kinaniuma.”
“Pole sana, inspekta.” Mama Miraji alisabahi.
“Vipi kwani ilikuaje?” Kaguta aliuliza.
“Sijui hata ilikuaje! … Wakati napambana na yule jamaa kichwa kilianza kuniuma ghafla kwa maumivu makali.” Inspekta alieleza, “Nilishangaa, badala ya yule adui kujilinda na kushambulia, alipeleka mkono wake ndani ya suruali hapo hapo kichwa kikaanza kunikata.”
Kaguta akaguna.
“Uliona alichokuwa anakifanya huko?”
“Hapana. Nashindwa kuelewa ni sayansi gani ilitumika. Tokea nianze mapambano na hawa watu sijawahi kukumbana na kitu kama hiki.”
Walitulia kwa muda kidogo wakifikiria Kaguta akalipuka na wazo; “Tattoo. Itakuwa ni tattoo.”
“Tattoo kivipi?” Inspekta aliuliza huku akirembua.
“Sijui kivipi, ila kwa njia moja ama nyingine itakuwa inahusiana na agano la mchoro.”
Baada ya masaa matatu ya kupumzika na kurudi kwenye hali yake ya kawaida, inspekta akiongozana na Miraji walielekea hospitalini kukutana na Jombi wakiwa wamebebelea chakula vya wagonjwa. Inspekta alimueleza Jombi kila kilichotokea, Jombi akaguna na kumtizama inspekta kwa jicho la mshangao.
“Inspekta, umechorwa tattoo?”
Inspekta na Kaguta wakatazamana.
“Ndio, tumechorwa wote wawili.” Inspekta alijibu na kuuliza, “Umejuaje?”
Jombi akatikisa kichwa chake kusikitika, “hilo huwa linatokea kwa wale tu wanaokuwa na tattoo hiyo. Unapokula kiapo maana yake unaridhia kufanya kazi ya mkuu kwa pamoja. Yeyote anayekuwa na hiyo tattoo hana uwezo wa kumshambulia mwenzake.
Endapo yule anayeshambuliwa atakapokuna au kukwangua sehemu ya tattoo na kufanya ichuruze damu, mshambuliaji atapata matatizo kama hayo yaliyokukuta wewe ukafikia hiyo hali.”
Inspekta aliweka mikono kichwani, “Mungu wangu. Sasa tunafanyaje?”
“Hapo kusema ukweli sijajua.” Jombi alijibu kwa sauti yenye lafudhi ya kukata tamaa, akauliza. “Wamewachora eneo gani?”
“Mkononi.” Kaguta aliwahi kujibu.
“Mkononi? … Kwanini?”
“Hatujui, kwani kuna utofauti wowote?” Kaguta aliuliza kwa pupa.
“Ndio. Kuna utofauti. Kuna wengine huchorwa kiunoni kama sisi, it means tupo grade ya pili. Walio juu yetu wao huchorwa mgongoni. Na wa juu zaidi, wanakuwa na tattoo shingoni.”
“Kwahiyo wewe ungepanda grade inayofuata wangekufuta hiyo ya kiunoni? Au?” Inspekta alipeleleza.
“Hapana, siwezi kufutwa. Hizi tattoo milele hazitoki. Na milele mimi nitabakia grade ya pili. Ni hivi, mtu wa grade ya kwanza ambao ni nyie wanaochorwa mkononi, wao huwa wamelazimishwa, si kwa matakwa yao. Grade ya pili, wanakuwa wameridhia kufanya kazi wakijua matokea yake. Grade ya tatu, ni wale wanaowafunda wote wa chini. Grade ya nne na ya mwisho, ni waanzilishi ama waasisi, mfano Mr Kim.”
“Umewezaje kusema hayo yote na ni ya siri?” Inspekta alidadisi.
“Si siri tena kwenu. Nyie mmekuwa wenzetu, kuwataarifu nyie si kuvujisha siri kwa kuwa nyie wenye agano ndio vinywa vyenu vimeuliza.”
“Naomba nirudie swali, Jombi. Kwanini wewe walitaka kukuua na ingali una tattoo huwezi kutoa siri?”
Jombi alitabasamu kwanza ndio akajibu, “Hiyo ni kawaida. Mtu anapokamatwa na kuwa chini ya adui, sharti auwawe, kwani akishatoa siri haijalishi tu ataangamizwa, bali siri inakuwa si siri tena.”
“Unatushauri tufanye nini sasa, Jombi?” Kaguta akauliza.
“Kama habari yenu ya kuwa na tattoo itakuwa imesambaa kote, hamtokuwa na la kufanya. Lakini kama sio, mnaweza mkaendelea na shughuli zenu. Ila ninachowashauri, kwa sasa inabidi msipige matawi ya miti, anzeni mizizi.”
“Kumaanisha?” Inspekta alidakia.
“Kumaanisha kwamba, nyie mnapambana na matawi ya miti lakini hamtafuti mizizi. Hamuwezi mkawamaliza wafuasi wa Mr Kim nchi hii, kila siku wanazalishwa wapya huko sehemu wanapopewa training. Inabidi muangamize kwanza hivyo viwanda, mengine ndio yafuate.”
“Unaweza ukatutajia hizo sehemu?” Inspekta aliuliza.
“Ndio, naweza nikawatajia. Ila sizifahamu zote, nitakutajia baadhi lakini mkae mkijua zipo kila mkoa wa Tanzania zikiendeshwa kwa siri mno. Kumbukeni hamuwezi mkaripoti hiki kitu popote pale, mkifanya hivyo utakuwa ni mwisho wenu.”
“Sawa. Nina swali la mwisho kwako.” Inspekta alisema.
“Uliza tu.”
“Ni kumhusu yule jitu. Mbona kwa sasa hapatikani? … Yani sioni wala sisikii akifanya mambo yake kama alivyokuwa akiwaendesha wakina Mtemvu. Kwanini watu wa Mr Kim wahangaike ingali jitu yupo?”
Jombi alishusha pumzi ndefu akajitengenezea kitako. Akamtizama inspekta.
“Kwanza awali ya yote, hakuna mtu awezaye kupambana na yule jinni. Ana nguvu mno na akidhamiriacho hakuna budi kutokea. Ila anaendeshwa, na anayemuendesha hupokea amri kutoka kwa mkuu juu ya nini cha kufanya. Mtu anayemuendesha huyo jinni anaishi Bagamoyo, anaitwa Alwatan Kombo, ni mzee maarufu sana ukimuulizia humkosi. Hayo mengine sifahamu.” Jombi alifunguka. Inspekta akaguna,
“Kazi ipo. Sijui hata tunaanzia wapi?”
“Popote pale.” Kaguta alitoa jibu jepesi.
“Ila kama mtahitaji, mnaweza mkaningoja. Tabibu amesema kesho nitaruhusiwa. Naomba niwarudishie fadhila kwa kuwasaidia.”
Inspekta alimtizama Kaguta, Kaguta akawahi kujibu; “Sawa, tutakungoja.”
Maongezi hayo yalipokoma, Kaguta aliwataka inspekta na mama Miraji waende kupumzisha akili zao ufukweni mwa bahari kwa kuwa ni mwisho wa wiki. Mama Miraji akapinga;
“Mimi siwezi, namsubiria mwanangu atoke shule.”
“Oooh! … Haina shida. Mpaka Jombi amalize kula muda muda utakuwa umeshawasili, tutamchukua mwanao alafu twende wote tukasahau ya ulimwengu kidogo.”
Mama Miraji akatabasamu, “Sawa, haina shida.”
Jombi alikula akamaliza, walimpitia pia Miraji kumjulia hali baada ya hapo wakaenda kumchukua Marietta shuleni akabadili nguo wakaelekea ufukweni mwa bahari ya indi. Ndani ya hoteli ya White sand ndimo walipokuwepo. Walipata chakula, kisha wakaenda jilaza kwenye vitanda vyembamba virefu vya ufukweni upepo ukiwa unawapuliza na simuliza za hapa na pale zikipigwa.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Twendeni tukaogelee!” Inspekta alipendekeza.
“Tutaendaje sasa na hatujaja hata na nguo ya kuogelea?” Mama Miraji alisema, alikuwa amevalia suruali pana na top miguuni akiwa kavalia viatu vya wazi. Inspekta alikuwa amevaa pensi na tisheti jepesi wakati Kaguta akiwa kavalia bukta fupi juu ya magoti. Marietta alikuwa kavalia katop keupe na taiti nyeusi.
“Twende basi hata tukachezee maji tutoe kanuksi.” Inspekta alizidi kushawishi.
“Nyie tangulieni, nakuja.”
“Aaah jamani twendeni bana.” Kaguta alichochea.
“Kweli, nyie tangulieni naja.” Mama Miraji alisisitizia. Inspekta alinyanyuka pamoja na Kaguta, Inspekta akamnyooshea mkono Marietta, mtoto wa mwisho wa mama Miraji.
“Twendee!”
Marietta alimtizama mama yake kama mtu aombaye ruksa, mama akamruhusu aende. Inspekta alimnyanyua mtoto akamuweka mabegani wakayafuata maji. Wakiwa pamoja na Kaguta walichezea chezea maji kwa kurushiana rushiana.
Marietta alikimbia huku na huko wakifukuzana na inspekta. Walirushiana maji, wakalala kwenye michanga na kwenda tena kuoga. Mama Miraji alikuwa amekaa tu akiwatizama tabasamu likitambalia uso wake.
“Twende kwenye maji marefu!” Inspekta alimwambia Marietta huku akitabasamu.
“Akaa naogopa!”
“Kwanini?”
“Si n’tazama!”
“We ulishawahi kumuona mtu anazama?”
“Ndio! Tena kuleee!” Marietta alionyeshea kidole upande wake wa mashariki.
“Leo unaendaaa…!” Inspekta alisema kwa utani, Marietta akaanza kukimbia. Hao wakaanza kufukuzana huku na kule, “Njooo!”
“Sitakiii!”
Inspekta alimkamata Marietta akaanza kumrusha rusha juu juu. Wakiwa katika hilo zoezi, haraka Kaguta alikuja akitokea kwenye maji ya marefu alipokuwa anaoga.
“Vitalis, umeona kule?” Kaguta alielekezea uso wake kule alipokuwa amekaa mama Miraji. Inspekta alitizama akamuona mwanaume amejilaza juu ya kitanda alichokuwa amelala yeye.
“Nani yule?”
“Sijui! Nenda katizame.”
Inspekta alianza kusogea eneo la tukio mtoto akiwa kambebelea mgongoni. Macho yake alikuwa kayarusha kule aendapo akijitahidi kung’amua akionacho.
“Unaenda kumchukua mama?”
“Eeeh na yeye aje kucheza na sisi. Au hutaki?”
“Nataka. Alafu tukimchukua tunaenda kenye maji makubwa?”
“Ndio. Tunaenda kuleee kwa bluu.”
“Kule kwenye maboti?”
“Enhee huko huko!”
“Wewe huogopi?”
“Siogopi mimi.”
“Unajua kuogelea?”
Inspekta alikaa kimya, akili yake ilitekwa kidogo na kumtizama mwanaume aliyekuwa ameketi na mama Miraji kwani alikuwa tayari amekaribia na bado hajamng’amua ni nani hasa.
“Unajua kuogelea? Mbona hunijibu!” Marietta alipaza sauti yakekumuuliza inspekta.
“Eeeh najua kuogelea.” Inspekta alijibu huku akimtua Marietta ambaye moja kwa moja alimfuata mamaye.
“Habari yako?” Inspekta alimsalimu mwanaume yule aliyejilaza; alikuwa na kifua kilichotuna kwa kiasi chake wakati tumbo lake likiwa limepambwa na matuta. Nywele zake ndefu alizitia dawa zikawa zinameta meta.
“Njema tu, vipi?”
“Shwari. Unaweza ukanambia wewe ni nani?”
Mwanaume yule alitabasamu kidogo akalamba lips zake.
“Naitwa Hervey. Au unaweza ukaniita the handsome African. Vipi kwani?”
“Hapo unafanya nini?”
“Nimechil tu na mrembo hapa, kuna ubaya?”
“Wewe kuwa na adabu …” Mama Miraji aliingilia kati, inspekta akamtuliza na kuendelea kuongea na yule jamaa.
“Umechil ukiwa unataka kufanya nini?”
“Aaah bro, maswali gani hayo? Unauliza nini sasa?”
“Jibu swali langu.”
“Kwani vipi kaka?” Mwanaume yule alisimama. “Wewe ni bahasha wake nini huyu manzi. Mbona maswali ya kijinga jinga, si unasema tu unaeleweka.”
Inspekta alimtandika kofi la nguvu mwanaume yule akadondoka chini.
“Potea hapa!”
Mwanaume yule alinyanyuka kwa hasira akamtizama inspekta.
“Hivi wewe unanijua mi nani?” Alifoka huku akimfuata inspekta. Alirusha ngumi, inspekta akaidaka na kuiviringita kisha akamsukuma, mwanaume yule akadondoka chini.
“Ngoja sasa nikuonyeshe. Nisubirie hapo kama wewe mwanaume kweli.” Alisema mwanaume yule huku akitokomea. Inspekta alitikisa kichwa chake akamgeukia mama Miraji,
“Vipi upo sawa?”
“Nipo fresh tu. Alikuwa ananisumbua sumbua tu huyo mtu.”
“Pole sana. Twende basi tukatembee tembee hapa naona tumeshageuka kideo.”
Mama Miraji alinyanyuka na mwanae wakaongozana kuelekea kule alipo Kaguta. Inspekta alimbeba Marietta mabegani, mkono wake wa kulia akiwa amemshikilia mama Miraji. Kaguta alitoka kwenye maji akaungana nao, ila aliona jambo;
“Vitalis, kuna watu kama vile wanakufuata.”
Inspekta aligeuza shingo akaona wanaume wanne, mmoja wapo akiwa yule mwanaume aliyemzaba kofi. Inspekta alimshusha mtoto chini, akamtaka mama Miraji akae nyuma yake.
“Wakina nani hao?”
“Yule fala aliyekuwa amekaa na mama Miraji, kaenda kuita wenzake.”
“Wanataka nini?”
“Wanataka kuvunjwa vunjwa.”
Kaguta alitabasamu akaweka mkono wake kifuani mwa inspekta, “Niachie mimi. Sijanyoosha viungo muda kidogo.” Alisema kisha akasogea mbele kukutana na wanaume wale wanne.
“Tunaweza tukawasaidia?”
“Wewe nani wa kutuuliza hivyo? … Tunamtaka huyo mbwa mwenzako. Au amekutuma wewe umsaidie?” Mwanaume yula aliyezabwa kofi alitema cheche.
“Kwa ushauri tu wa bure. Kimbieni angali mnaweza.” Kaguta alisema huku akikuna kichwa chake. Wanaume wale walitizamana, mmoja akarusha teke, Kaguta alidaka kisha akammanua mwanaume yule na kupiga sehemu zake za siri kwanguvu, kamlio ka mbwa koko kakasikika … “Uuuuuu!” Wakati mwanaume yule akidondokea chini huku akiugulia. Mwaume mwingine alirusha ngumi, Kaguta naye akarusha ngumi zikakutana kwanguvu. Jamaa aliyerusha ngumi naye akatoa sauti yake kilio huku akiugulia kwa kuuning’iniza mkono wake mpaka chini alipodondokea.
Mwingine alinyanyua mguu akilenga kurusha teke lakini kabla halijafika popote, Kaguta alirudisha teke hilo kwa teke lake kama mtu anayesinya taka kisha akatoa teke lake sasa matata ambalo lilimkumba mwanaume yule kifuani akarukia kwenye maji. Sasa akabakia yule aliyeenda kuita wenzake.
“Njoo basi fasta, sina muda wa kupoteza.” Kaguta alimwambia yule mwanaume. Yule mwanaume akataka kukimbia, Kaguta alimshika akamvuta.
“Niliwaambia mkimbie wakati mnaweza.”
Mwanaume alirusha ngumi, Kaguta akarudisha uso wake nyuma ngumi ikavuka alafu akafunguka na ngumi yake kali iliyotua kwenye uso wa mwanaume yule na kumdondosha chini. Mwanaume aliyevunjwa mkono alinyanyuka, Kaguta akamrudisha chini na teke la kichwa lililomziraisha mlengwa.
“Vitalis, mbona umenipa visharobaro hivi havina hata changamoto!”
Inspekta alitabasamu; “Si uliwataka mwenyewe.” Muda huo watu walikuwa wamejazana wakitizama. Waliamua waondoke zao kufuata gari wakaondoka hilo eneo na kuelekea nyumbani.
Siku iliyofuata, ilikuwa tulivu na labda ilikuwa inatofautiana na jana yake kwa tarehe tu. Ila inspekta na Kaguta waliamka wakiwa tayari wamedhamiria kuifanya iwe ya pekee. Walimbeba Marietta wakampeleka shule, baada ya hapo wakaelekea hospitali na kumtwaa Jombi safari ikaanza kuelekea bagamoyo kwa Alwatan Kombo.
Baada ya lisaa na madakika kadhaa wakawa tayari wameshatia miguu yao ndani yabagamoyo. Walishuka garini wakaanza kumuulizia mzee Alwatan Kombo.
“Mmmh yule mzee amekwisha hama pale. Saa hii anakaa kuleeee … unapaona kulee!” Muelekezaji alionyesha kidole chake kisiwani. “Kule ndipo anakaa.”
“Kisiwani?” Inspekta alishangaa.
“Ndio, kisiwani. Nyie nendeni pale kwa wale wavuvi wanaweza wakawapeleka huko.”
Kaguta, Jombi na inspekta walishika njia wakaelekea huko walipoelekezwa. Walipowafikia wavuvi, inspekta akaelezea haja. Wavuvi walikuwa watano, wote waliacha kazi zao wakawatizama wageni.
“Hatuwezi kuwapeleka huko!”
“Kwanini?” Kaguta aliuliza.
“We jua hivyo, hatuendi.” Alijibu mvuvi mmoja kwa niaba kisha wakaendelea na kazi zao. Wengine wakipara samaki zao walizovua usiku, wengine wakitengenezea nyavu wapate kuanza safari.
Wakina inspekta walitizamana wakajadili cha kufanya, Kaguta akapata wazo;
“Tuwatajie pesa ya maana, watakubali tu.”
Wakakubaliana.
“Mnataka shilingi ngapi kutupeleka?” Kaguta alichombeza.
“Tumesema hatutaki. Hatuendi sisi huko! … Kha!” Aling’aka mvuvi mmoja kisha zogo likazuka miongoni mwao,
“Hawa jamaa vipi, wanataka wakatutoe kafara nini? … Nani aende kufa huko?”
“Nashangaa. Japo maisha magumu, hatutaki kufa.”
Wakina inspekta walitizamana kwa nyuso za maswali.
“Jamani kwani kuna nini huko?” Kaguta aliuliza. Inspekta akapandisha mabega yake juu. Jombi akabinua mdomo wake. Kaguta aliwageukia wavuvi akawashawishi tena;
“Kuna elfu hamsini hapa kwa atakayetupeleka.”
Wavuvi wanne wakaendelea kung’aka kwamba hawataki hata kwa pesa gani. Mmoja akasema;
“Twendeni. Ila tunawashusha na kugeuza papo hapo!” Wenzao wakamshangaa;
“We Bakari wewe wataka makubwa?”
Mvuvi yule hakujali, aliwapandisha wakina inspekta na safari ya kuelekea kisiwani ikaanza. Baada ya dakika ishirini, walifika. Mvuvi aliwashusha akadai pesa yake, Kaguta akampatia. Mvuvi alipogeuka apande mtumbwi wake alishangaa kuuona umesogea kwenda mbali kama vile kuna mtu ameusogeza.
“Mungu wangu Bakari mimi!”
Mvuvi aliweka mikono kichwani. Puh! Akajirushia kwenye maji na kuanza kupiga mbizi kuufuata mtumbwi wake. Ajabu, mtumbwi ukazidi kusogea kila ulipokaribiwa. Mwishowe Bakari akachoka, alitizama kisiwa akaona ndio sehemu pekee karibu kwake, akarudi haraka kwa mbizi na kuwakuta wakina inspekta bado wamesimama wakimsubiri.
“Bakari kwani kuna nini?” Inspekta alitaka kujua. Bakari hakujibu kitu, aliketi kitako machozi yakibisha hodi. Inspekta, Kaguta na Jombi wakamsogelea.
“Bakari, mbona unatuweka njia panda? … Unaweza ukatuambia nini kinaendelea?” Inspekta aliuliza huku akimshika bega Bakari.
“Najuta kuja hapa! Najuta! Najua nitakufa tu!”
“Kwanini ufe?”
“Hiki kisiwa kina majini! Unadhani kwanini wenzangu walikuwa hawataki kuja huku? … Masikini mie!”
Inspekta akatizamana na wenzake kwa macho dunguri.
“Mmesikia? Sasa tunafanyaje?” Inspekta aliuliza.
“Tuondokeni tu!” Jombi alijibu bila ya kufikiria kwamba hakuna usafiri.
“Tunaondokea na nini?” Kaguta aliuliza. “Kama tumeamua kuja hapa, tufanye kilichotuleta.”
“Wewe huogopi?” Jombi aliuliza.
“Hata kama naogopa itasaidia nini tena na tushafika hapa na mtumbwi umekwisha kwenda?”
“Si tunaomba msaada wa kuokolewa?”
“Hatokuja mtu yeyote hapa!” Bakari akadakia, “hakuna mvuvi anayesogelea hiki kisiwa.”
“Kwahiyo? … Tutakaa hapa hapa ama tutajaribu kufanya jambo?” Kaguta alishawishi. Kwa muda wa dakika moja watu wakawa kimya, inspekta ndiye akalonga kwa kujiamini;
“Twendeni. Tusiruhusu Imani zitukate maini.”
Jombi, Kaguta na inspekta wakashika njia kuelekea ndani wakifuata kabarabara kadogo. Bakari yeye akakataa kwenda.
“Nyie nendeni, mie nitabaki mwenyewe hapa!”
Alipoona wenzake wanaishia alinyanyuka akawakimbilia.
“Yani ndo’ mnaniacha kweli nibaki mwenyewe!”
“Si umetaka?” Kaguta alimjibu.
“Sasa nikiwaelekeza mtaniongezea pesa?”
“Unapajua?” Inspekta aliuliza.
“Ndio, napajua. Mtaniongezea pesa?”
“Ndio. Tupeleke huko.”
Bakari akachukua nafasi na kujiweka mbele ya wote. Aliongoza njia wakipanda na kushuka. Baada ya dakika kumi na mbili, upepo ulipuliza kwa ukali wakadondoshwa chini na kuanza kubiringishwa. Wakajitahidi kujishkiza kwenye miti na kung’ang’ania vichaka lakini upepo ukaonekana na nguvu mno kwani ulizidi kuwaburuza ukiwapeleka upande wa magharibi. Kwa muda wa dakika mbili upepo ukavuma. Ulipokoma, kila mtu alikuwa mwenyewe asimuone mwenzake. Kila mtu alikuwa amepeperushwa pande yake.
Inspekta alipepesa macho yake kushoto na kulia, juu na chini hola! Hakujua hata aelekee wapi. Alikuwa katikati ya msitu wenye nyasi na miti mirefu.Alivuta na kushusha pumzi ndefu, akaita;
“Kagutaaaaa!” mara mbili lakini hakukuwa na majibu. Ghafla, akasikia vishindo vya miguu nyuma yake, kugeuka akakutana na jitu nene mwenye mwili wa mti! Macho yake yalikuwa makubwa kama ngumi ya mtu mzima. Mikono ilikuwa minene yenye kiganja kikubwa. Miguu ilikuwa mifupi minene yenye nyayo pana. Mdomo wake ulikuwa mkubwa kama beseni.
Inspekata akatoa macho kwa mshangao. Taratibu akaanza kurudi nyuma huku akimtizama jitu mti.
“Unadhani unaenda wapi?”
“Wewe ni nani?”
“Huna haja ya kunijua maana muda si mwiingi utakuwa mfu!”
“Nimekuja kuonana na Alwatan!”
“Una mualiko?”
“Hapana!”
“Wewe ni mvamizi!”
Baada tu ya hiyo kauli, jitu mti lilianza kumkimbiza inspekta kwa kasi. Inspekta alikimbia kuokoa maisha yake. Alikunja kunja kona huku akaenda kule, kule akaenda huku. Ila baada ya muda, alikamatwa akaning’inizwa juu chini.
“Nadhani leo utakuwa kifungua kinywa changu!”
Alisema jitu mti kisha akaanza kumpeleka inspekta mdomoni. Upesi inspekta akatoa bunduki yake kiunoni akafyatua macho yote mawili ya jitu mti. Jitu likamuachia inspekta huku likilalamika kwa maumivu. Inspekta akaanza kukimbia. Hamaki, jitu mti nalo likaendelea kumkimbiza inspekta likifuatisha sauti ya vishindo. Kila inspekta alipokata kona, jitu hili hapa. Kila inspekta alipokanyaga, jitu likapita.
Baada ya kukimbia kwa dakika saba, inspekta akaona mto mkubwa mbele. Ulikuwa unapitisha maji kwa kasi mno. Aliinama akaokota mawe matatu makubwa akaendelea kukimbia. Alipofika kwenye kingo ya mto alisimama na kusonga kando akarusha mawe yale matatu majini. Jitu likapitiliza kufuata vishindo vya mawe. Kama unyoya maji yakambeba na kumpoteza. Inspekta akashusha pumzi. Akarusha macho yake kuangaza mandhari ya kisiwa kwa uso wa kuduwaa. Akaona miti ya kijani isiyoonyesha dalili za ukomo. Alitikisa kichwa akatizama alipotokea. Aliita tena;
“Kagutaaa!” kwa sauti ya juu lakini hakusikia kitu. Alichuchumaa akakinga maji na kiganja chake akanawa uso. Akakinga tena na kunywa, ptuuuh! Akatema.
“Chumvi. Shit!” Alilaani.
“Ila huu mto unatoka wapi?” Alijiuliza huku akijitahidi kuangaza maji yanapotokea.
“Mbona hiki kisiwa kinaonekana kikubwa mno na nilikiona kidogo?” Aliendelea kujiuliza maswali ambayo hakuyapatia majibu.
“Wakina Kaguta watakuwa wapi? Na sasa naelekea wapi?”
Haikusaidia jambo, alibakia amesimama kama mnara. Mbali yake kabisa ndipo alipokuwepo Kaguta naye akibung’aa bung’aa na akihangaika kuita jina la mwenzake bila ya majibu. Hata pale alipobadili na kuita jina la Jombi ama Bakari majibu yalikuwa yale yale, kimya. Wakati anatembea kwa mbali kidogo upande wa kushoto, Kaguta aliona mti wa machenza. Aliusogelea akachuma moja na kuanza kulimenya apate kula.
Ghafla sauti inasikika;
“Nani kakuruhusu?” Kaguta akashtuka. Akatizama nyuma asione kitu. Akatizama pembeni asione kitu.
“Nani kakuruhusu uchume?” Sauti ya kuuliza ikajirudia.
Kaguta akadondosha chenza na kuanza kusogea taratibu kurudi nyuma huku akiutizama mti wa mchenza kama vile amesikia sauti ikitokea hapo. Hatua ya kwanza nyuma, ya pili, tatu, nne, mti wa mchenza ukaanza kunyanyuka! Mizizi yake ikachipuka kwa kasi!
Kaguta aligeuka akaanza kukimbia. Hakufika mbali, mzizi ulikamata kiatu chake na kumburuza kuelekea kweye mti. Kaguta akanyanyua jiwe, akapiga mzizi uliomkamata bila ya mafanikio. Akazidi tu kusogezwa kuufuata mti.
Haraka, akili ikamjia. Alifungua kamba za kiatu, mzizi ukaenda na kiatu. Alinyanyuka akakimbia kwa kasi, nyuma yake mizizi ikimkimbiza. Alipoona inamkaribia, alikunja kona akauzunguka mti mmoja mkubwa mara nne mizizi ikajiviringitia hapo na kukoma. Kaguta akatabasamu.
“Shenzi!”
Mara ghafla, mzizi mmoja ukamfuata kwa kasi toka kwenye mti wa mchenza na kumchapa kwanguvu mgongoni. Ile anaugulia maumivu, mzizi ule ukamdaka mguu wake maeneo ya gotini na kuanza kumvuta kwa kasi kuufuata mti wa mchenza. Wakati Kaguta anaburuzwa kuufuata mti wa mchenza, alidaka shina la mti mmoja akaung’ang’ania. Huku mzizi ukivuta mguu kwanguvu, naye aling’ang’ania shina kwanguvu asitake kuachia hata kidogo.
Kadiri muda ulivyokuwa unaenda, Kaguta alianza kupoteza uvumilivu. Mzizi ulimvuta kwanguvu dhidi ya mikono yake. Aling’ata meno kwa uchungu. Alirusha macho yake pembezoni kutafuta pembejeo ya kujiokolea akaishia tu kuona mawe ya mduara yasiyo hata na ncha. Akili yake ikakokotoa. Aliacha kushika shina la mti akakwapua mawe yale mawili. Huku akivutwa kuelekea kwenye mti, aligongesha yale mawe kwanguvu yakapasuana na kutengeneza ncha. Akanyanyua mkono wake kwanguvu na kuukata mzizi.
Alipofanikiwa alijinyanyua akakimbia toka eneo lile. Alifika mbali akautizama ule mchenza kwa macho ya kuduwaa. Akastaajabu mizizi ikiwa inajirudisha chini ya ardhi na mazingira yakarudi vile vile kama yalivyokuwa hapo mwanzoni. Chenza alilolidondosha akiwa kalimenya kidogo, lilirudisha ganda lake na kurudi mtini! Mdomo wa Kaguta ukaachama. Haraka akakimbia toka eneo lile akielekea mbele kwa mbele.
Nyuma ya Kaguta kilomita kede, alikuwapo Jombi macho yake yakiangaza kutafuta njia, miguu yake ikipambana na nyasi ndefu na vichaka ambavyo vilikuwa vinamzonga mara kwa mara. Masikio yake hayakuwa yanasikia kitu chochote isipokuwa milio ya ndege tena kwa mbali ikitokea kwenye viota vilivyoketi kwenye matawi ya miti mirefu. Kwa taratibu, alitembea. Muda mwingine alisimama na kutambaza macho yake kila pande. Mkononi mwake alikuwa kashikilia gongo kubwa alilokuwa analitumia kutawanyia majani na vichaka apate kupita kwa ahueni.
“Watakuwa wapo pande gani hawa?” Jombi alisimama akashika kiuno. Ni kama vile alichoka kutembea.
Alifuta jasho kwenye uso wake na kuvuta pumzi kadhaa. Alipotizama pembeni mita kadhaa akaona jambo. Alisogea vizuri kushuhudia akaona nyayo kubwa juu ya udongo. Alichuchumaa akaitizama vizuri ile nyayo. Aliingiza mguu wake kwenye ile nyayo ukazama wote. Akajiuliza;
“Huu mguu wa nani?” Huku akitizama alama za madole yale manene. Alinyanyuka akarusha macho yake kufuatilia nyayo zile akaona zaelekea mbali upande wake wa magharibi. Akataka kuzifuatilia ila akasita. Akabakia akitizama kwa uso wenye maswali mchanganyiko wa mashaka na hofu.
Akiwa hapo bado hajaelewa cha kufanya, ghafla vuuup! Akanyanyuliwa na ndege mkubwa mithili ya popo! Alikuwa ni mweusi ti mwenye mdomo mrefu kama chuchunge. Mabawa yake yalikuwa mapana na yenye nguvu ingali macho yake yakiwa mekundu yenye mfumo wa paka.
Jombi alifurukuta lakini hakufua dafu kwenye kucha za miguu ya yule ndege wa ajabu. Kucha mbili zilikuwa zimekamata bega lake kwa kupenya. Kucha zingine zilikuwa zimekamata shati kwa nguvu. Sasa alikuwa juu ya msitu, hata ile miti aliyokuwa anaiona ni mirefu akaiona mifupi kutokana na kimo alichopelekwa na yule ndege. Kila alipotizama chini aliishia kufunga macho kwa woga, hata mapigo yake ya moyo yalilipuka. Akaogopa hata kufurukuta kwa kuhofia akidondoshwa itakuwaje.
Vuup! Vuup! Vuuup! Vuup! Mabawa ya yule ndege yalitoa mlio huku yakizalisha pepo kali. Uso wa Jombi ulijawa na hofu, hata hema yake ilikuwa ni dhahiri ya woga. Alitizama kila pande lakini hakuona mwisho wala mwanzo wa kisiwa. Alitizama chini, napo hakuona hata wenzake. Ila kwa chini, juu ya ardhi, Kaguta alimuona ndege huyo kwa mbali angani akiwa amebebelea mtu. Bila kupoteza wasaa akaanza kukimbia akimfuatisha ndege yule aelekeapo.
Huko juu kwa mbali, Jombi akaona mto mkubwa. Aliutizama ule mto uso wake ukionyesha kama mtu awazaye jambo. Na kweli, ndege alipokaribia mto, Jombi aliushika miguu ya yule ndege kwanguvu akaanza kuhangaika kwa nguvu zake zote akienda huku na huko. Ndege akayumba yumba mwishowe ashati la Jombi likachanika na kumuacha ndege yule wa ajabu akiwa amembebelea Jombi kwa mguu mmoja tu, wa kulia. Hapo Jombi akageuza shingo akiyavumilia maumivu, akang’ata mguu wa yule ndege kwanguvu, ndege akamuachia. Huyooo Jombi akaanza kushuka chini akielekea kwenye mto.
Puuuv!
Sauti ya maji ikasikika wakati Jombi akitua. Alipopanda tu juu ya maji, kwa fujo maji yakaanza kumburuta kumpeleka asipokujua. Wakati anahangaikia uhai wake kwa kupiga mbizi akamuona Kaguta kwenye kingo ya mto akikimbia naye sambamba.
“Jisukumie huku! Jisukumie hukuu!”
Kaguta alielekeza huku akionyeshea nchi kavu. Jombi akaanza kujisukuma taratibu huku akikinzana na maji yaendayo kwa kasi. Kaguta akarukia tawi refu la mti akalivunja, akawa anakimbia nalo. Jombi aliposogea karibu naye alielekezea ule mti mtoni ili Jombi audake. Mara puuh! Akajikwaa na kudondoka chini. Bahati jema mti hakuuachia, ila sasa Jombi akawa amemuacha kwa umbali mrefu hatua kama ishirini za mtu mzima. Alinyanyuka akaendelea kukimbia akiongeza kasi zaidi na mti wake ulio mkononi.
Baada ya muda alimfikia tena Jombi. Alisogeza mti wake kwa muhusika, Jombi akaukamata. Lakini sasa Kaguta hakuwa na nguvu za kutosha, labda alikuwa amechoshwa na purukushani alizozipitia. Alimvuta Jombi lakini nguvu ya maji ikamshinda.
Mungu si athumani! Mbele yao wakamuona inspekta. Kaguta alipaza sauti kumjulisha inspekta ujio na uhitaji wao wa kusaidiwa. Inspekta akajiweka tayari. Alimkata kwa nguvu Kaguta wakamvutia Jombi nje.
Wakiwa wanahema hata hawajaulizana nini cha kujifanya na wapi walipotokea, walisikia vishindo vikuu nyuma yao. Walipogeuza shingo wakastaajabu. Waliona mbwa mwitu wanne wenye rangi ya fedha, mgongoni wakiwa na rangi nyeusi. Miili yao ilikuwa mikubwa kuliko mbwa mwitu wa kawaida. Ndimi zao zilikuwa zimetoka nje zikichuruza mate. Jombi akasema huku akitetemeka;
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Jamani … Jamani twafa!”
Wakatizamana kwa hofu. Inspekta akapayuka; “Turukie majini!” Kabla wenzake hawajajibu, alikuwa tayari asharukia majini. Jombi na Kaguta nao wakafuatia. Mbwa mwitu wakapiga kelele kali za malalamiko kwa kukosa kitoweo. Lakini kama vile haitoshi, walianza kuwafukuza wakina inspekta pembezoni mwa mto wakienda nao sambamba kwa kasi kubwa.
Baada ya muda wa dakika ishirini, mbwa mwitu wakachoka. Wakasimama na kuwatazama wakina inspekta wakizidi kupelekwa na maji yasiyoonekana kikomo kwa macho. Dakika kumi tokea hapo, mto ulifikia kwenye maporomoko yake makuu, inspekta na wenzake wakamiminwa kwa nguvu. Na kutokana na maji kupunguza kasi, wakaogelea kwenda nchi kavu na kujipumzisha wakiwa wamechoka mno, wanahema kwanguvu kama wametoka mbioni.
Pumzi kadhaa zilipovutwa, wakaanza kuteta;
“Bakari yupo wapi?” Kaguta aliuliza.
“Sijui yupo upande upi wa kisiwa, na sijui kama atakuwa mzima huko.” Inspekta alieleza.
“Tangu upepo ule ulivyopuliza na kunipeleka nisipopajua, sijamuona tena Bakari.” Jombi naye akapata kusema.
“Sasa, tunaelekea wapi? Maana sijui hata hapa tulipo.”Kaguta aliuliza huku akiangaza angaza macho.
“Tuifuate ile njia!” Inspekta akaonyeshea njia fulani nyembamba aliyoiona kwa juu kidogo. “Hamna anayejua tulipo, tuifuate ile njia tuone itatupeleka wapi!”
Walikubaliana wakanyanyuka na kuifuata njia elekezi. Taratibu wakaanza kuifuatisha ikiingia ndani ya msitu.Sauti za ndege zilikuwa zinapaza huku na kule, milio mingine ikiwa ya ajabu na migeni. Zilipotimia dakika nane wanaume hao watatu wakiwa wanatembea kwenye ile njia nyembamba, ghafla mawingu yakaanza kufunga anga na punde tu giza likawa limetawala. Wakina inspekta wakapigwa na duwaa. Giza limeingiaje ghafla vile?Wakiwa katika hilo duwazo, ghafla mwanga mkali kama wa gari ukawamulika usoni na kuwafanya vipofu kwa muda wasione chochote. Hapo sauti nzito ambayo haikujulikana wapi inatokea ikawauliza;
“Mnafanya nini katika hiki kisiwa?”
Inspekta, huku akiwa amekinga uso wake dhidi ya mwanga mkali ummulikao, akajibu;
“Tumekuja kuonana na Mzee Kombo!”
“Mna miadi naye?”
“Hapana!”
“Basi nyie ni wavamizi. Je, hamkupata kusikia yale yaongelewayo kuhusu hii mahali?”
“Tumesikia ila tuna shida?”
“Shida isiyo ambatana na miadi kwetu ni ukaidi. Poteeni kwenye hiki kisiwa. Tafuteni njia mtokomee la sivyo kila baada ya dakika kumi na tatu, mtapata jaribu mpaka pale mtakapokwisha kabisa!”
“Basi tunaomba utuonyeshe njia!” Jombi akasema huku akitizama chini, uso wake ameukunja na kauziba na kiganja.
“Kama mlivyokuja, ndivyo mtakavyotoka. Hamkupewa mualiko kuingia na hamtosindikizwa mkitoka. Kumbuka, ni kila baada ya dakika kumi na tatu, hesabu tokea sasa!”
Paap! Mwanga ukapotea. Taratibu mawingu yakaanza kufunguka na kukawa mchana kama awali. Inspekta akanyanyua mkono wake wa kushoto kutizama saa, akaona ni saa nane na nusu. Akawaambia wenzake hayo majira.
“Sasa tunafanyaje? Tunatokea wapi?” Jombi aliuliza.
“Mi nadhani tutumie akili zetu tu.” Inspekta alipendekeza, “mi ninavyojua, mto huwa unamwagia maji baharini. Tuufuatishe mto huu mpaka pale unapomwagia maji yake.”
Kaguta na Jombi wakaafiki. Hao wakaungana na inspekta kuanza kufuatilia maji ya mto yaendako. Huku wakiruka viunzi kama mawe na mabanzi ya miti wakasonga. Baada ya dakika kadhaa, saa ya mkononi ya inspekta ikapiga alarm … ti! ti! Inspekta akaitizama. Akaona sasa ni saa nane na dakika arobaini na tatu. Kabla hajafungua mdomo kulonga lolote, Jombi alipaza sauti huku akionyeshea upande wa pili wa mto;
“Bakari! Bakari yulee!”
Inspekta na Kaguta wakatizama upesi. Wakaona mwili wa mtu ukiwa umejilaza pembezoni mwa mto, nguo na hata umbo likiwa la Bakari.
“Atakuwa amekufa nini?” Kaguta aliuliza.
“Labda. Twendeni tukamtizame, hatuwezi tukamtelekeza.” Jombi alitoa wazo. Haoo, yeye na Kaguta wakaanza kuongozana wakiruka juu ya mawe waende upande wa pili. Inspekta yeye akasita. Jombi na Kaguta walipovuka mto, wakamtizama.
“Njoo bana! Kumbuka huyu jamaa alijitolea kutuleta hapa!” Kaguta alieleza. Inspekta akaamua avuke na kuungana nao wakausogelea mwili wa Bakari uliokuwa umelala kifudifudi.
“Kuna kitu kitakuwa kimemkuta.” Jombi alisema kwa uhakika. Alichuchumaa akataka kumgeuza Bakari alale chali. Upesi, inspekta akamkataza kufanya hilo baada ya kuona kucha ndefu kwenye vidole wa Bakari. Kufumba na kufumbua, Bakari akaamka na kumkwaruza Jombi kifuani! Macho yake yalikuwa mekundu mno kama bendera, meno yake yalikuwa kama ya popo na kuchaze zikiwa ndefu mno. Jombi akasogea haraka huku akimtizama Bakari wa ajabu.
“Bakari, vipi?” Jombi alitahamaki. Kifua chake kilikuwa kinachuruza damu toka kwenye mikwaruzo.
“Huyo si Bakari!” Inspekta aling’aka. “Hilo ni jaribu, dakika ya kumi na tatu imeshatimia.”
Kauli hiyo ilipokoma, Bakari wa ajabu akamrukia inspekta na kwenda naye chini. Bakari yule wa ajabu akanyanyua mkono wake wa kuume amrarue inspekta, Inspekta akauzuia mkono huo na kumtupa Bakari mbali kwa teke. Bakari akanyanyuka haraka, ila kabla hajamrukia tena inspekta, Kaguta akakabiliana naye kwa kwa kumrushia teke, Bakari akalidaka na kumtupia Kaguta pembeni kama karatasi. Jombi akasogea na kurusha ngumi, Bakari akadaka mkono na kuuviringita kisha akampa teke matata Jombi, Jombi akarukia kando.
Inspekta aliokota gongo akalirusha kwa Bakari wa ajabu, Bakari akalidaka. Inspekta akarusha teke, nalo likadakwa kisha Bakari akafunguka kumpa teke la kifua inspekta,inspekta akarushwa kando! Haraka Kaguta alinyanyuka akamsogelea Bakari wa ajabu, Jombi naye akajongea, wakamuweka Bakari kati. Kaguta alirusha ngumi, Bakari akakwepa. Jombi alirusha teke, Bakari akainama kisha ghafla akaruka na kujizungusha hewani akifungua miguu yake ambayo iliwanasiibu vizuri Kaguta na Jombi kwenye mapaji yao ya uso, wakadondokea kando!
Upesi inspekta akanyanyuka na kumrudia Bakari. Alirusha ngumi yake ya kulia, Bakari akaipangua. Alirusha ngumi yake ya kushoto, Bakari akaitoa. Alirusha tena ya kulia, Bakari akaidaka na kumzungusha inspekta kama mtu achezaye blues kisha akamtupia huko kwa teke kali. Sasa wanaume wote watatu; Kaguta, inspekta na Jombi wakawa wapo chini wakigugumia maumivu.
Bakari wa ajabu akacheka sana. Kisha akauliza kwa kebehi;
“Hiko ndicho mlicho nacho?”
Kaguta akakunja sura kwa hasira. Akataka kunyanyuka ila inspekta akamshika mkono na kumuambia;
“Hiyo si suluhishi. Kwa mmoja mmoja hatutoweza, twende kwa pamoja ila kwa akili nguvu na zaidi.”
Kaguta akatikisa kichwa kukubali. Wakanyanyuka na kumfuata Bakari wa ajabu, inspekta akakaa kwa mbele, Kaguta akakaa nyuma yake. Inspekta akatishia kurusha ngumi, Bakari akasogea kidogo. Inspekta akanyanyua mguu wake wa kushoto akitishia kurusha teke, Bakari akajiandaa kulipokea, haraka inspekta akabadili maamuzi, aliruka juu akiwa amekunja goti lake kumshambulia Bakari, Bakari akawahi kujikinga kichwa, na hapo ndipo Kaguta akatelezesha mguu wake kumkata mtama Bakari. Wakati Bakari anaanguka alifungua mikono yake iliyokuwa imemkinga kichwa, huo ukawa upenyo kwa inspekta akampatia goti la meno na kumvujisha damu.
“Pumbavu!” Bakari aling’aka baada ya kutema damu pembeni. Aliwatizama wakina inspekta akawaona wamejipanga vile vile, inspekta mbele Kaguta nyuma. Alipotizama kando, akamuona Jombi, alikuwa ameketi kitako kama mtu atizamaye sinema.
Bakari akaguna huku akibinua mdomowe. Haraka akatumia mikono yake kujifyatua na kusimama. Akakunja ngumi na kuwapa ishara wakina inspekta washambulie. Inspekta bila kulaza damu akakunja goti na kurusha teke, Baraka akalidaka, ila kabla hajafanya lolote na mguu alioudaka, Inspekta akautumia huo mguu kujinyanyulia juu na kurusha teke lingine lililombamiza Bakari usoni na kumpeleka chini. Baraka akanyanyuka tena kwa hasira, alirusha ngumi inspekta akaikwepa Kaguta akaidaka.
Alipotaka kunyanyua mguu arushe teke, inspekta akazuia mguu kisha akampiga Bakari ngumi ya tumbo, wakati Bakari wa ajabu akiguguma na maumivu ya tumbo, mkono wake uliorusha ngumi ulivutwa na Kaguta kisha akapewa ngumi kubwa ya uso akadondokea mti, ukampenya kifuani na kutokea mbele, huo ukawa mwisho wa Bakari wa ajabu.
Inspekta, Kaguta na Jombi wakapongezana. Inspekta akatizama saa yake ya mkononi akaona ni saa nane na dakika hamsini na tatu. Zilisalia dakika tatu tu kutimia dakika kumi na tatu ya pili. Inspekta akawashika wenzake mkono na kuwavuta.
“Tuna dakika tatu tu kabla ya jaribu lingine kuja!”
Kama upepo wakaanza kukimbia kwa haraka mno kuufuata mto. Baada ya muda kidogo, mto ulikata kona wakina inspekta wakashangaa kuona shimo kubwa mno mbele yao. Ndani ya shimo hilo kubwa, ndipo maji yote ya mto yakawa yanamiminikia humo.
“Duh! Sasa tunafanyaje?” Inspekta akauliza huku akihema. Kaguta akainama akashika magoti yake. Jombi akashika kiuno huku akitota jasho. Hawakusema kitu chochote zaidi ya kujitahidi kuvuta pumzi walizoziteketeza mbioni. Ila zoezi lao hilo kabla halijakamilika, lilikatishwa na mlio wa saa ya inspekta. Ilikuwa ni saa nane na dakika hamsini na sita! Inspekta aliwaambia wenzake wakaanza kupepesa macho yao pande zote nane za dunia.
Ajabu hawakuona kitu. Ila baada ya sekunde kadhaa, kwa mbali upande wa kusini wakaanza kushuhudia tukio la ajabu. Miti ilikuwa inadondoka kwa kasi. Ndege walikuwa wanaruka na kukimbia ila hakikuonekana ni kitu gani chafanya hayo!Hapo, inspekta akashauri warukie shimoni mule maji ya mto yaendako. Kaguta na Jombi wakachungulia shimo wasipate kuona kikomo chake. Kidogo wakatia ashki.
“Hakuna njia nyingine, guys. Mmekiona hiko kinachokuja?” Inspekta alionyeshea kidole anapopaongelea.
“Ila unajuaje kama humo shimoni ni salama kuliko hiko kijacho?” Jombi aliuliza.
“Ukiona maji yanaingia mahali, ujue kuna sehemu yanatokea. Simple geography.” Inspekta alisema lakini muda huu hakungoja tena maswali, alishika mikono ya Kaguta na Jombi akajirushia shimoni. Walikuwa hewani kwa takribani dakika tano kabla hawajafika chini walipozama na kuibukia baharini. Walipotizama nyuma yao, wakakiona kisiwa kwa mbaali, kikiwa na udogo wake ule ule.
Walivuka mtihani. Ila sasa tabu ikawa je, watafikaje nchi kavu na hawana chombo chochote? Waliulizana pasipo kupata majibu. Bahati jema, kwa mbali kidogo inspekta akaona mtumbwi wa Bakari. Wakaufuata na kupanda. Huku wakitumia mikono yao kama mapakuo ya maji, wakasogea taratibu taratibu mpaka wakafika nchi kavu.Waliposhuka tu, wavuvi wakawazingira.
“Mwenzetu yupo wapi?”
Inspekta akatizamana na wenzie. Hakuna aliyejibu, wote walitoa tu macho. Wavuvi wakarudia swali;
“Bakari yupo wapi, au mmeshamtoa kafara?”
“Hapana. Kusema ukweli hatujui alipo.” Inspekta alijbu.
“Hamjui alipo? Si mmeondoka naye hapa!” Mvuvi mmoja aliuliza kwa jazba.
“Ndio, tumeondoka naye. Lakini tulipofika kule kisiwani akatupotea. Hatujajua atakuwa wapi.” Kaguta alieleleza. Wavuvi wakatizamana, mvuvi mmoja akawaonyeshea ishara wenzie kwa kupandisha nyusi moja, ghafla wavuvi wakawavamia wakina inspekta na kuanza kuparangana.
Bahati mbaya hawakufua dafu, wakagaragazwa na kufanywa mahututi kwa mateke na ngumi za haja. Inspekta akawaomba radhi kwa usumbufu kisha akashika njia yeye na wenzake waondoke zao. Walipopiga hatua sita mbele, sauti ikawafikia;
“Majambaaaziii!”
Mvuvi mmoja alipaza sauti, mara wenzake nao wakamuunga mkono kwa kuita. Punde, watu waliokuwa maeneo yale wakarusha macho yao kule sauti ilipotokea. Jombi kwa woga akaanza kukimbia. Amah! Watu wakaanza kutiririka kuwafuata wakina inspekta wakiwa wamebebelea silaha. Hakukuwa na jinsi, inspekta na Kaguta wakaanza kukimbia kwa kasi, nyuma yao rundo la wananchi likiwafukuza.
Mawe yalirushwa kama risasi, moja likambonda inspekta mgongoni kwanguvu na lingine likamtwanga Kaguta maeneo ya shingoni, ila hawakukoma kukimbia. Waliziba vichwa vyao na mikono, miguu ikafanya kazi yake ya kuwatoa hatarini.
Baada ya dakika tatu wakalifikia gari, walifungua milango na kuingia kwa pupa gari likahepa milango ikiwa wazi. Kabla gari halijatokomea wananchi walirusha mawe, kioo cha nyuma cha gari na shepu ya gari vikawa nyang’a. Milango ya gari ikafungwa huko mbele ya safari, wakina inspekta wakawa wameokoka.
“Aisee! Ilikuwa bado kidogo tu.” Kaguta alisema huku akitikisa kichwa chake.
“Tatizo Jombi ulikimbia.” Inspekta alisema na kuongezea, “Ungetulia tu, ulipokimbia ndio ukawa umewasha moto sasa.”
“Mimi niliogopa ndugu yangu” Jombi alijinasibu, “kusikia tunaitiwa majambazi utulivu ukanitoka kabisa.”
“Unapokimbia ndio unakuwa umethibitisha kwamba wewe ni jambazi. Ila tushukuru maana ni Mungu tu,kama tungetiwa mikononi sijui ingekuwaje?” Inspekta alieleza.
“Yani sipati picha. Yani leo lazima niende kupiga kinywaji kwanza kujipongeza, maana si kwa ile shughuli.” Kaguta naye akaeleza.
“Ila jamani, Bakari atakuwepo wapi?” Jombi alirush swali.
“Hakuna anayejua, ila nadhani atakuwa kauwawa kwenye kile kisiwa. Kuna majaribu mengi sana mule.” Inspekta alitoa maoni yake, Kaguta akamuunga mkono;
“Hauko mbali na mimi kabisa. Huo ndio ukweli.”
Walipofika Dar, wakaenda kumpitia Marietta shuleni na kwenda nae nyumbani. Walimkuta mama Miraji akiwa amejaa tele sebuleni macho yake yakiwa yapo bize kuangalia runinga.
“Karibuni jamani.” Mama Miraji alisema kwa tabasamu pana. Wakina inspekta wakaingia pamoja na mtoto wakaketi na kupeana salamu.
“Inaelekea huko mlipotoka ilikuwa purukushani eenh, naona mmebadili rangi za mavazi kabisa.” Mama Miraji alitumbuiza.
“Yani we acha tu. Kutuona hapa hai ni kama miujiza!”Inspekta alisema huku aktikisa kichwa chake. Mama Miraji akaona jeraha la Kaguta shingoni.
“Mmmh … Kaguta, upo sawa?”
“Nipo sawa tu!”
“Mbona una jeraha shingoni latoa damu?”
Kaguta akajishika kwenye jeraha na kutizama vidole vyake, akaona damu. Akatabasamu kiuongo.
“Kidogo tu si saana. Ni pakuosha tu na kutia spirit.”
“Pole sana.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hapana shida hapa dada.”
Inspekta alinyanyuka na kuwatakawenzake waende chumbani wakajiweke safi, wote wakanyanyuka na kwenda, mama Miraji akaona alama ya damu mgongoni mwa inspekta, akaishia kutikisa kichwa na kusema;
“Kuna kitu.”
Alimvua mwanae nguo za shule akampa chakula. Baada ya hapo, akapakua chakula na kukiweka mezani kwenye hotpot tayari kwa ajili ya wanaume watatu waliojileta nyumbani. Baada ya kula, Kaguta akaaga na kuahidi kurudi baadae. Nyumbani akabaki Jombi, mama Miraji na Marieta.
Baada ya muda kidogo, Jombi akaenda kupumzika kwenye chumba cha wageni, naye Marieta akaenda kujipumzisha kwenye chumba cha pili cha wageni alalamo yeye na mamaye, sasa akabaki inspekta na mama Miraji sebuleni, peke yao. Walipiga soga ila baada ya muda zikakata. Inspekta naye alijinyanyua akajinasibu anaenda pumzika, ila kabla hajaondoka mama Miraji akamuuliza;
“Inspekta, naweza nikakuhudumia?”
Inspekta akawa mkanganyikoni. “Kunihudumia kivipi yani?”
“Mgongoni kwako bado unavuja damu. Naomba nikuhudumie.”
Inspekta kwa sura ya haya akatabasamu. Hakuwa ametegemea kama mama Miraji aliona jeraha lake. Na labda kwa haya yake hiyo akawa hana budi kuvua shati lake na kujilaza kwenye kochi apate huduma.
Mama Miraji akaelekea ndani na kutoka na kiboksi kidogo chenye msalaba mwekundu, akakifungua na kutoa pamba na dawa fulani ya buluu kwenye kachupa kadogo kisha akajivika glovu na kuanza kutizama jeraha la inspekta.
“Mmmh umechimbika. Ulipigwa na nini hapa?”
“Jiwe.”
“Ilikuaje mpaka ukapigwa hivi?”
“Kuna wapumbavu walituitia mwizi.”
“Aisee! … Poleni. Vipi mmempata huyo mzee?”
“Hapana. Huwezi amini tumemtafuta bila ya mafanikio, zaidi kuona mauza uza tu.”
“Poleni. Si kazi ndogo kabisa.”
Wakati hayo maongezi yanachukua nafasi, mama Miraji taratibu alikuwa akisafisha jeraha kwa dawa. Inspekta alikuwa amefumba macho akisikilizia kila hatua.
“Ulishawahi kuwa nesi nini?” Inpekta aliuliza huku akitabasamu kwa mbali.
“Hapana, ila nina diploma ya nursing. Kabla sijaenda kazini niliolewa na mume wangu hakutaka niendelee na hiyo taaluma tena.”
“Pole.”
“Nishapoa kitambo mpaka naona n’shasahau kabisa hayo mambo.”
“Hujasahau bana, mbona bado una hiko kitu kabisa mikononi?”
“Kweli?”
“Kweli.”
“Ahsante. Ni kitu ambacho nilikuwa nakipenda tangu utotoni.”
Baada ya hayo maneno, kaukimya kakatawala anga. Ni sauti tu ya mikono ya mama Miraji ndiyo ikawa inasikika ikichua eneo la maumivu. Baada ya dakika moja, mama Miraji akasema;
“Inatakiwa ushonwe hapa. Pamechimbika.”
“Si unishone wewe nesi?”
“Mimi?”
“Ndio!”
“Ila sijawahi.”
“Si ulisomea?”
“Ndio.”
“Fanya basi.”
Mama Miraji alivuta na kushusha pumzi ndefu, akatoa uzi ndani ya kiboksi chake pamoja na kakipini akaanza kushona jeraha la inspekta kwa taratibu na kwa uangalifu mkubwa. Bila ya ganzi tendo likafanyika, inspekta aking’ata tu meno kwa maumivu.
Tendo lilipokamilika, mama Miraji akashusha pumzi tena kama mtu aliyetoka kufanya shughuli pevu mno. Akampongeza inspekta na kumuambia amemaliza.
“Hongera.” Inspekta alitoa pongezi huku akijigeuza na kuulalia mgongo.
“Ahsante. Natumai sijakuumiza sana.”
“Hujaniumiza, nashukuru sana kwa huduma yako.”
“Karibu muda wowote.”
Inspekta alinyanyuka akaketi kitako wakawa wanatizamana na mama Miraji bila ya kuongea kitu. Kwa muda wa dakika moja waliacha macho yao yatizamane, kisha taratibu wakaanza kusogezeana usokama watu wanaotaka kubadilishana mabusu. Kabla hawajafikiana, sauti ya Marieta ikasikika;
“Mama!”
Haraka inspekta na mama Miraji wakatengua pozi lao na kukaa kama vile hawakuwa pamoja.
“Nini mwanangu?”
“Nasikia kiu.”
Marieta alisema huku akifikicha fikicha macho yake kwa usingizi. Mama Miraji akanyanyuka na kwenda kumchotea mwana maji. Inspekta akaegeshea shati lake mwilini naye akaaga anaenda chumbani.
Akiwa ameketi juu ya kiti kirefu mikono yake kaigemeza kwenye meza ya glocery, Kaguta alikuwa akipata kinywaji kigumu aina ya spirit tena kwa tarumbeta huku taratibu akitingiha tingisha kichwa chake kuonyesha kuvutiwa na muziki upigwao.
Baada ya kumaliza kinywaji chake akaagiza tena kingine kama kile kile akaendelea na starehe zake. Ila baada ya muda kama dakika tano tangu aagize kinywaji kipya, akamuita muhudumu na kumuuliza;
“Bhoke yupo wapi?”
Muhudumu akabinua mdomo na kurembua macho.
“Bhoke hayupo zamu leo, ila mimi nipo sema tu shida yako.”
Kaguta akatabasamu.
“Wewe utaniweza?”
“Kwanini nisikuweze? … Ngoma kubwa hii!”
Hapo Kaguta akacheka na kutikisa kichwa chake.
“Hapana! Hapana kwa kweli. Am sorry. Mi namtaka Bhoke, mtoto mashaalah sana yule, mie ndio type zangu zile!”
“Haya, ndio hayupo sasa!”
“Niitie basi, n’takutoa kidogo.”
“Shing’api?”
“Aaaah we niitie bwana hatuwezi shindwana.”
Mhudumu akampigia simu Bhoke. Baada ya dakika zisizozidi dakika kumi na tano Bhoke akaingizana eneoni na bodaboda. Alikuwa amevalia kimini kuntu chekundu akiacha mapaja yake makubwa rangi ya chocolate yabarizi. Kwa furaha walikumbatiana na Kaguta wakajuliana hali.
“Mbona umen’tupa hivyo, Benson?”
Bhoke alisema kwa tabasamu pana.
“Kazi zinanibana, Bhoke.”
“Kazi wapi wewe sema kama umepata uchi mwingine.”
“Aaaah Bhoke, nani kasema tena hayo?”
“Tatizo lako hata namba zako hukunipa nashindwa hata kukutafuta kwa njia yoyote ile.”
“Hata kama nikikupa namba yatakuwa yaleyale maana nabadili mara kwa mara. We tulia tu n’takuwa nakutafuta kama hivi.”
“Haya bana. Mie sina neno.”
“Nichum basi mtoto.”
Bhoke akambusu Kaguta shavuni.
“Utanibusuje shavuni bana kama mama yako?” Kaguta alilalamika. Bhoke akampa ulimi kabisa.
“Sasa je, mambo si ndio hayo. Kaa hapo unywe mrembo.”
Bhoke akaketi kwenye kiti cha pembezoni na Kaguta akaagiza safari, taratibu akaanza kuisuuza nafsi kwa kinywaji hiko huku wakipiga soga.
“Sasa mtoto, leo si unaenda kulala kwangu?”
“Unavyotaka wewe, mi sawa tu. Ila utanileta kazini kesho maana zamu yangu mchana.”
“Hilo tu, kuna kingine?”
“Walaah sema tu nimemis shoo zako za kibabe.”
Wakacheka na kugongeshana viganja. Kaguta akanyanyuka akalipia vinywaji na kumtoa muhudumu ngalawa kadhaa kisha wakaaga wakaondoka wakiwa wameshikana viuno. Wakati wanatoka kwenye geti la baa, wakapishana na Sandra. Kaguta hakuamini macho yake alidhani labda ni ulevi, alitikisa kichwa akatizama vizuri, akamuona kweli Sandra.
“Si unajua gari langu? Shika funguo, tangulia naja.” Kaguta alimpa maelekezo Bhoke.
“Unaenda wapi tena?”
“We tangulia, naja.”
Kaguta alisema kisha akashika njia kurudi ndani ya bar. Alimtizama Sandra anaelekea wapi, akamuona amemfuata mwanaume mmoja hivi mzee, yule aliyemtoa Robson polisi kipindi kile alivyokamatwa barabarani. Sandra akakumbatiana na huyo mzee na kupeana mabusu kisha wakaketi. Kaguta alitoa simu yake ya mkononi akaanza kuwarekodi kwa tahadhari asionekane.
Ali zoom na kuhakikisha amewajaza wahusika wake kwenye kioo barabara. Hapo akapoteza dakika kama tatu kabla ya honi ya gari haijamshtua na kukumbuka kuna mtu anamsubiria.
“Muda wote huo? Au ulikuwa na kademu kengine huko?”
“Wala! Kuna mtu nilipotezana naye muda sasa nikamuona leo, si unajua tena.”
Kaguta alijitetea, akawasha gari wakaondoka eneo lile.
Asubuhi palipokucha, Kaguta aliamka mapema akamuacha Bhoke kitandani amelala, akavaa nguoze za mazoezi na kutoka nje akaanza kupasha viungo vyake kwenye uwanja wa nyumba yake. Alipiga push up kadhaa, akaruka kamba. Alijog na kukimbia. Alipomaliza akarudi ndani na kumuamsha Bhoke waende kuoga.
Wakaenda kukoga na wakapata kifungua kinywa. Baadae Kaguta akampeleka Bhoke kazini kwake kisha yeye akaelekea Rosemath stationary. Alipaki gari lake upande wa pili wa barabara akawa anatizama eneo la stationary kwa mbali.
Muda ukayoyoma kama masaa mawili hivi likaja gari jeusi Suzuki Escudo likapaki nje ya stationary. Honi ilipigwa akatoka Sandra huku akiwapungia wenzake mkono wa kwaheri, akaingia ndani ya Escudo na gari likaondoka. Taratibu Kaguta akaanza kulifuatilia lile gari kwa nyuma.
Baada ya dakika kadhaa Escudo likapaki mbele ya duka kubwa la nguo maeneo ya Sinza, mzee akashuka na Sandra wakaingia ndani ya duka. Kaguta akawachukua video bila ya wao kujua. Baada ya kama lisaa yule mzee na Sandra wakatoka dukani na kurudi garini kisha Sandra akarejeshwa stationary na gari likaondoka.
Kaguta alipaki palepale alipokuwa amepaki awali. Alifungua video zake akawa anazitizama kwa makini. Alipomaliza aliweka simu yake kando, akalaza kiti na kutulia. Jioni iliposonga, stationary ikafungwa. Wadada wakatoka ofisini mwao na kutawanyika kwenda majumbani. Sandra akaja kuchukuliwa tena na gari lile lile, Escudo nyeusi, akapelekwa mpaka nyumbani kwake kisha gari likaondoka. Lilipotokomea, Kaguta akashuka na kuanza kuisogelea nyumba ya Sandra.
Akiwa ndani ya chumba chake, Sandra alivua nguo akavaa taulo jepesi kisha akaelekea bafuni kukoga. Alipotoka bafuni akamkuta Kaguta kajilaza kitandani. Akapigwa na butwaa.
“Wewe unafanya nini hapa?”
Kaguta akatabasamu.
“Vipi, kwani Roby anakuja?”
“Umeingiaje humu?”
“Kupitia mlangoni.”
“Mlango mbona nimefunga?”
“Haukufunga vya kutosha kunizuia nisiingie. Ila tuachane na hayo, njoo basi.”
“Wapi?”
“Aaah aah! Kwani kuna shida gani, Sandra?”
“Hujui? Mimi sina urafiki na maaskari.”
“Ndio mana ukanchoma siku zile ili bwana’ako afanye tukio?”
Kimya. Kaguta akasimama na kumsogelea Sandra akamshika kalio. Sandra akausukumizia pembeni mkono wa Kaguta.
“Usinishike!”
Kaguta akacheka kisha akawa serious ghafla.
“Kwanza mimi si askari. Si umeona hii?” Kaguta alionyeshea tattoo yake mkononi baada ya kukunja shati lake.
“Pili, siku zile ulinichomea na kunifanya nionekane mpumbavu, bwana’ako akafanya uhalifu. Leo ni zamu yako. Umeona hii?”
Kaguta akaanza kuonyeshea video za Sandra alizorekodi.
“Lazima zimfikie Roby. Kwahiyo jiandae.”
Kaguta alisema kisha akageuka na kuufuata mlango atoke. Ghafla Sandra akamshika mkono. Kaguta alipogeuka akamuona mwanamke kama alivyozaliwa.
“Tafadhali Kaguta, usifanye hivyo. Hujui ni kwa kiasi gani utafanya mambo yawe magumu kwangu na kwa Roby pia. Utasababisha vita kubwa. Please.”
Kaguta akatabasamu na kusema;
“Nitafanya utakavyo, endapo tu utanipa maelezo yote ninayoyahitaji. Upo tayari?”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sandra alitizama chini na macho yaonyeshayo njia panda. Ni kama vile alikuwa ng’ombe mwembamba aliyelazimishwa ale majani ya shamba nzima ili kesho awe mnene mnadani. Mwishowe aliamua aketi kitandani na kumtizama Kaguta, akafungua mdomo kwa sauti iliyo karibu na mashaka;
“Unataka kujua nini toka kwangu?”
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment