Simulizi : Oktoba 15 Rais Anaenda Kufa
Sehemu Ya Tatu (3)
Baadaye waliletewa gari, kwa ajili ya kuelekea walikohisi wamtafutaye kakimbilia. Mjini Lumesule. Mji mkubwa kidogo, kulinganisha na Lukwika. Mwendo haukuwa wa kawaida. Ulikuwa mwendo mkali, lengo walikute gari ielekeayo huko kwa muda huo njiani, kama bado haijafika. Waliomba njia,
“Abiria wote warudi kwenye siti zao,” alisema kiongozi wa oparesheni, akiwa kasimama mlangoni mwa gari. Ambayo ni kosta.
Abiria walitii, huku wakiwa na wingi wa hofu kulikoni. Kikubwa kilichowatisha ni sare. Na namna sura za askari zilivyotishatisha. Wengi wao walikuwa wamekunja ndita. Waliingia ndani ya gari, kila abiria akiwa ameketi kwenye siti yake kusubiri kifuatacho. Nini wataambiwa, ndicho kikubwa walichokisubiri. Askari mmoja wao, alipita siti moja baada ya nyingine kuwachunguza watu waliopo, ila yule wamtakaye hakuwepo. Walivyochunguza kiundani, wakabaini matone ya damu, yaliyoishia kwenye siti mbili zilizokuwa tupu. Watu walioketi, walishawahi kuteremka. Ni miongoni mwa wale watatu.
“Hapa walikaa kina nani?” aliuliza kiongozi wa oparesheni.
“Alikuwa mama mmoja hivi, na mgonjwa wake, ambaye hatukumbaini ni wa jinsia gani, maana alikuwa kafunikwa nguo karibu mwili nzima,” abiria jirani na siti hizo walijibu.
“Mumewaona walivyoteremka wameelekea wapi?”
“Ndiyo. Walielekea huko chini na usafiri wa bajaji,” alisema mmoja wa abiria, huku akiwa amenyosha kidole kuonyesha uelekeo wa bajaji ilikoelekea.
“Ya rangi gani?”
“Kijani!”
“Ahsanteni, munaweza kuendelea kushuka,” alisema yule kiongozi, kisha waliteremka na kufuata uelekeo wa kule walikoelezwa.
Hawakuhitaji kutumia gari. Walitoka mbio, taratibu, huku wakiangaza angaza pembezoni wakiamini lazima wafanikiwe kuiona. Kalumbwe na Aisha nao walikuwa nyuma yao, kila hatua waliyobandua wao walikanyaga. Hivyo walishuhudia kila kitu, japo kwa umbali, kilichokuwa kinafanywa na wale wa oparesheni. Hata walivyokuwa wametoka mbio, kufukuzia bajaji, waliona, nao kuunga kinyumenyume. Kwa ustadi wa hali ya juu, wasibainike kama wanawalea rada. Umbali mita kadhaa. Takribani mia moja hamsni, waliiona bajaji ya kijani imepeki uchochoroni. Katika mazingira korofi yaliyowapa ishara moja kwa moja, kuwa hiyo ndiyo bajaji waifuatiliayo. Pasi na chelea, waliifuata. Walivyoifikia walimkuta dereva pekee, huku kwenye siti kukiwa na matone ya damu yaliyowaaminisha moja kwa moja wale wanaowafuatilia walikuwemo humo. Walimtaka hali, na kwenda moja kwa moja kwenye mada.
“Kuna watu wawili tunawatafuta. Mmoja ni mwanamke, mwingine ni mgonjwa, kafunikwa shuka. Tumefanya uchunguzi na kubainika bajaji yako imetumika kuwasafirisha hao watu toka pale kituo cha mabasi.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Yeah! Kuna watu wa aina hiyo niliwapakiza. Lakini sikuwafikisha mbali, mita chache tu toka pale kituoni waliomba niwateremshe nami kufanya hivyo.”
“Halafu ikawaje?”
“Baadaye nilimuona yule mama akiita bajaji nyingine na kurudi tena kituoni. Si kuna bajaji ya bluu mumepishana pindi munakuja huku?”
Walikaa kimya, kama sekunde saba hivi. Baadaye walipatwa na mshituko uliowatambulisha kuna kitu wamekumbuka.
“Mmmmh!...sahihi. Kwa hiyo itakuwa wamerudi tena stendi?” walijiuliza kwa pamoja.
“Yawezekana!”
Hatimaye walirudi tena kituo cha mabasi, walifanya uulizaji wa hapa na pale, lakini majibu waliyopatiwa hayakuendana na hisia zao. Wahusika hawakuonekana. Ina maana hawakurudi kituoni walielekea sehemu nyingine. Hivyo hawakuwa na budi, kuridhia matokeo. Walizidiwa ujanja, mbinu na mambo mengineyo. Hatimaye waliianza mipango ya kurudi watokako ili wafikishe ujumbe kwa wakuu wao. Pindi wao wanajiandaa kurejea mjini Lukwika, Kalumbwe na Aisha, wanafanikiwa kumbananisha vilivyo yule dereva bajaji awaeleze alichowaeleza waliopita. Mbano huo uliambatana na vitisho lukuki vya sirisiri wengine wasione. Alinyooshewa kisu, sindano na bastola tumboni zana ambazo zilizuiwa na vitambaa fulani walivyovifunga mkononi. Hofu ikamvaa dereva. Al-manusra haja ndogo imporomoke, kutokana na zana alizonyooshewa. Kitendo ambacho, katu hajawahi kukutana katika maisha yake.
“Fanya chap utuambie nini ulichozungumza na wale watu kabla hatujamwaga damu,” alisema Aisha. Kauli iliyoambatana na kitendo cha kushindilia kisu na sindano mwilini mwake, alizokamatia katika mikono yake yote mawili. Mmoja kisu, mwingine sindano.
“Aaah!...Hatuj…hatujazungumza kitu chochote kibaya. Walikuwa wananiulizia kuhusu wateja ambao niliowabeba,” alinena kijana huyo. Ki-jasho chembamba kikimtiririka, ijapokuwa ka-upepo kadogo kadogo kilikesha kupuliza.
“Ukawajibu vipi?”
“Niliwaeleza kuhusu habari za hao abiria wakaondoka zao.”
“Wako wapi hao abiria?”
“Waliteremkia njiani.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Jinsia zao ni zipi?”
“Ni mama mmoja, bonge bonge hivi. Halafu huyo mwingine sifahamu ni jinsia ipi. Ila nahisi ni wa kiume japo sijaiona sura yake, maana kafunikwa shuka mwili mzima,” aliteta dereva. Wajihi umejaa hofu ya waziwazi.
Kwa hayo machache, yaliyokosa mwanga, wakayaamini yanaweza kuwa msaada kwao. Walikonyezana, na kumuamuru dereva aondoke mazingira hayo haraka iwezekanavyo. Huku wakimmiminia vitisho vya kumtaka afanye siri kilichojiri. Wakibainika, watakula naye sahani moja, pale watapobahitika kunusurika. Dereva alivyoondoka, nao huku nyuma walifuatia kupiga hatua kuelekea sehemu wasiyoifahamu. Walijiingiza kwenye doria pasipo matarajio. Doria iliyowalazimisha kukatiza mitaa mingi na sehemu mbalimbali za vichaka vilivyopo karibu na mji. Mizunguko waliyokesha nayo haikuwa ya muda mfupi. Ilikuwa ya muda mrefu, kiasi kwamba jasho jingi liliwatiririka mithili ya wanariadha. Lililolowanisha sehemu kubwa ya nguo walizovaa. Leso walizonazo hazikusaidia. Kwani, mfuto mmoja tu, zililowana chapachapa, kama zimetumbukizwa ndani ya ndoo iliyojaa maji. Baadaye walitafuta eneo zuri wakaketi. Kupumzisha miili na akili pia, iliyokuwa inaelekea kuchoka kutokana na ufikiriaji wa muda mrefu.
Walitumia dakika kumi na mbili kupumzika. Baada ya hapo walinyanyuka kisha wakaendelea na safari, huku jasho likiwa lishakauka na kuacha harufu iliyomtambulisha kila waliyepishana naye, hali gani wanayo. Taratibu kiza kilianza wapokea. Hata kabla halijaitimisha vyema kuuzuia mwanga uzalishwao na jua. Wakati huo, walikuwa katikati ya kichaka. Ikiwa njia moja wapo ya kuuacha mji huo waendelee na miji mingine, sikio likiwa tegoni kusikilizia alipoonekana yule wamtafutaye. James! Hatua chache kabla hawajaifikia barabara kuu, ielekeayo mjini Lukwika, Kalumbwe alishuhudia lundo la nguo kadhaa zilizolowana damu. Haraka! Wakachomoa bastola kujikinga na lolote, kwa kujua wameingia sehemu mbaya, ambayo hutumiwa na asilimia kubwa ya wanaume wa mjini waliojihalalishia uhalifu. Kadri walivyopiga hatua kusogelea eneo zilizopo, fikra mpya nazo zikazidi chipua kuhusu hicho wakionacho mbele yao.
“Mbona kama ni mtu?” aliuliza Aisha. Wakizidi vuka nyasi zilizojenga kichaka.
“Nahisi eeh!” Kalumbwe alichangia. Kauli iliyofuatia na tukio la kukoki bastola zao. Mwendo ukiwa ni wa mnyato. Ulioambatana na utoaji wa ishara fulani za kiusalama zifahamikazo CRE (close range engagement) ambazo mara nyingi hutumika kwa lengo la kumhadaa adui. Wasipate tambua maana ya kile kizungumziwacho.
Walivyozifikia, mmoja wao, ambaye ni Kalumbwe, aliisundika bastola kiunoni, Aisha akabaki kufanya ulinzi wa kuangaza huku na kule kwa pande zote za ulimwengu. Pale chini, Kalumbwe alianza fanya uchambuaji. Kwa kuondoa nguo moja moja hadi alivyokifikia kitu husika kilichofunikwa.
“Tumechezewa,” alisema Kalumbwe. Macho pima kwenye hicho kitu. Kilichomshinikiza Aisha naye, aache ulinzi aliokuwa anaendelea nao akapiga goti chini ajionee kwa uzuri.
“Ni nini hii? Ina maana unataka kuniambia kuwa kinahusiana na yule tumtafutaye?” aliuliza Aisha.
“Inaweza ikawa.”
“Haaa! Huyu kiboko. Sasa kaweza vipi kupita sehemu hizo zote?”
“Nami nashangaa. Kwa hiki, basi huyo ampatiaye msaada ni fundi wa michezo michafu.”
Vifaa vingi vihusiavyo tiba vya hospitalini ndivyo vilivyojibainisha kwenye mboni zao, na mdoli wenye muonekano wa binadamu uliofungwa dripu zilizoruhusu kuvujisha damu.
“Tumtafutaye kabaki kulekule tutokako,” alisema Kalumbwe.
“Tena inavyoonekana, huyo aliye nyuma yake ni fundi na bingwa wa michezo michafu,” aliendelea kunena.
“Sahihi. Kwa hiyo tunaamuaje?” aliuliza Aisha.
“Haina haja ya kupoteza muda. Turudi.”
Hawakuwa na budi. Walifunga safari kurejea mjini Lukwika. Vichwa vikitawaliwa na mawazo lukuki, watafanikisha vipi kazi iliyopo mbele yao. Ya kumuondoa James ulimwenguni, ili waendelee kutunza sifa ya idara yao.
****
Taarifa za tukio alilohusishwa James, lilimfikia mama Tausi (Dkt. Tausi Cheyaya). Alihuzunika, huzuni iliyojidhihirisha usoni kwake na baadaye kumsukuma atoe machozi tele, yaliyotengeneza madoa kwenye shati jeupe alilovaa. Kilichomhuzunisha, ni utambuzi wa sheria za idara waliyoopo. Inakuaje mtumishi akihusishwa kwenye matendo ovu. Ilimuumiza sana. Kiasi kwamba hata hamu ya kuendelea nacho kile alichokuwa anafanya ilimtoka. Muda huo alikuwa anajiandaa kwa safari ya kurejea mjini Lidede kuendelea na majukumu yake mengine ya kiofisi. Baadaye huzuni ilizalisha huruma ndani yake. Na moyo wa msaada japo ni tendo lililo kinyume na sheria. Aliingiwa na moyo wa kumsaidia, ili aweze kumuokoa kwenye lindi kubwa la matatizo lililomzonga. Hivyo, alifanya tafakuri ya kina maamuzi gani achukue, takribani dakika kumi, lakini hakupata muafaka. Hali iliyochangiwa na halmashauri ya kichwa chake kuruhusu mafikirio mengine. Mafikirio ya uwepo wake ndani ya mji wa Lukwika, ulishamalizika, alilazimika kuwepo ndani ya mji wa Lidede kwa siku hiyo, kuendelea na majukumu yake ya ulinzi wa mheshimiwa Waziri Mkuu, Prof. Moteja Mwome.
“Dah!... James. Sijui nikusaidie vipi uepukane na hilo tatizo,” alijisemeza kimyakimya. Mkono mmoja tamani, machozi yakiendelea mbubujika.
“Pole sana. Ila ndiyo kawaida ya idara yetu…” alisema. Ila hakumalizia kauli yake. Alisitishwa na muito wa simu yake ya mkononi.
Aligeuza shingo kuiangalia, baada ya kumtambua mpigaji aliyejibainisha kwa jina kwenye skrini ya simu. Mheshimiwa Rais, Ndg. Mohammed Mlunji. Chap, alifuta chozi na kubonyeza kitufe cha kupokelea.
“Hallo! Mheshimiwa,” alisema mama Tausi. Mara baada ya kuweka usawa wa sikio.
“Mmmh! Guardner, nahitaji msaada wako.”
“Nipo tayari kukusaidia kiongozi wangu. Msaada upi unaouhitaji?”
“Nahitaji James anusurike Kwenye ajali iliyopo usoni kwake.”
“Ondoa shaka. Nitatekeleza hilo. Na naamini, atakuwa salama hadi mwisho wa majukumu yaliyopo mkononi mwake.”
“Dokta, nakutegemea,” alisema Rais Mlunji kisha akakata simu.
Rasmi. Mafikirio yake yalisitishwa. Sasa akawa na jukumu moja tu, la kumsaidia mheshimiwa Rais, kumfanikishia kile anachohitaji. Halali ya kutekeleza ilikuwa mikononi mwake, baada ya mheshimiwa Rais kumhalalishia. Siku hiyohiyo aliingia kazini. Tena pasi na kuchelea, ikiwa ni lengo la kumsaidia James na Rais pia, aliyehifadhi siri nzito kifuani kwake. Siri ambayo ili apate itoa, jamii washawishike kukubaliana nayo na kumrejeshea mapendo, ilimlazimu apate maelezo toka kwa watu hao watatu aliomtuma James akaonane nao. Ndipo aiweke hadharani. La sivyo, hata akiiweka pasipo kupata maelezo toka kwa watu hao, jamii haitomuelewa, na wanaweza mgeuzia kibao. Kwa kumuona ndiyo mhusika mkuu tofauti na watu ataowataja.
Pindi kundi kubwa la watu wenye hasira kali iliyozalishwa na tukio la mauaji ya Mashaka, likimfuata James nyumbani kwake, kule alikopanga, mama Tausi aliwahi nyumbani kwa Mashaka (Joram Isaac). Akiwa na moja ya gari alizokuwa anatumia awali. Alivyowasili, alipaki gari yake sehemu fulani. Jirani tu na nyumba ya Joram. Aliangaza huku na kule, alivyoona hamna mtu anayemshuhudia aliingia ndani ya nyumba kwa uharaka. Baada ya kuusukumiza mlango ulioegeshwa na komeo iliyoharibika. Ndani mlitawaliwa na kiza. Ila mwanga wa tochi iliyopo kwenye simu yake ndogo, ulimpatia mwangaza wa kushuhudia mazingira ya ndani yalivyo. Yalikuwa shaghala baghala, ila hakujalisha. Alichojali yeye ni kufuata kitu alichodhamiria. Ambacho si kingine, bali ni mwili wa Joram. Alizidi kupiga hatua kusonga mbele, huku akiruka dimbwi za damu zilizoanza kunyonywa zikielekea kukauka.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hatua kadhaa mbele, alikutana na mwili wa Joram. Sehemu ndogo ikiwa imefunuliwa, na kuonyesha majeraha yaliyokuwa yanatoa damu kipindi cha nyuma kabla haijakata. Hakuamini, moyo ukajaa unyonge na simanzi tele iliyomshinikiza kutoa kilio cha chinichini. Ila baadaye alijikaza. Alilazimika kufanya hivyo, hata kama alikuwa na machungu kiasi gani, dhidi ya watu waliofanya unyama huo. Kwani, alienda hapo kwa lengo la kumsaidia James, na sio kitu kingine. Alipaswa kutoa msaada aliodhamiria kutoa kwa haraka asije kutwa.
“Mwenyezi Mungu akupumzishe mahali pema peponi. Amin!” alijisemeza. Huku akitoa glavus katika moja ya mfuko wake wa suruali aliyovaa.
Alivyozitoa, alizinyoosha zikae sawa, kisha moja baada ya nyingine aliiva katika mkono husika. Simu akaibana mdomoni, akafuatia kupiga goti chini na kuufunika vizuri mwili wa Joram. Alivyoridhishwa na ufunikaji alioufanya, alijitutumua, kuvuta nguvu na kuubeba juujuu mwili wa Joram akatokanao nje. Kila kitu alifanya kwa wepesi, asifumaniwe na kuambatanishwa kwenye tukio hilo. Hakukawiza, aliungiza ndani ya gari, siti za nyuma. Akauweka vyema kisha akazungukia upande wake, akapanda na kuondoa gari kwa kasi ya ajabu. Safari yake haikuwa ya mbali sana. Kwani hata dakika saba hazikufika, akaegesha gari yake maegesho ya chini ya jengo moja chakavu lililotawaliwa na utambulisho wa kujengwa enzi za mkoloni, likipambwa kwa michoro ya bawa na vidani vya rangi mbalimbali ukutani Pasi na sahau paani. Mazingira yaliyowatetemesha raia wengi, na kuwapa fikra, kuwa jengo hilo ni moja ya majengo yamilikiwayo na watu wanao abudu mashetani. Kabla hata hajateremka, walinzi wawili walimpokea. Kwa kuizingira gari yake na kuifanyia ukaguzi kwa kutumia vifaa maalumu vyenye hisio kali la kutambua vitu ovu. Alivyoteremka walisitisha. Wakamtupia jicho lililompatia utambuzi kuwa anahitaji kujitambulisha.
“One six-four-five (16-4-5)” alisema mama Tausi. Kauli iliyoeleweka vyema kwa walinzi wale. Na kwa uthibitisho zaidi, walionyeshwa namba aliyoitamka kwenye kidani chenye nembo ya bawa alichovaa kifuani mara baada ya kukigeuza kwa nyuma.
“Heshima yako mkuu,” walisema wale walinzi, pindi wakibana mikono na kukakamaa ishara ya kutoa heshima kwa mama Tausi, ambaye alikuwa mkubwa kwao. Mlinzi na mshauri wa karibu (Guardner) wa nne, miongoni mwa washauri watano waliopo nchini kwao. Ndiyo maana ya ile namba aliyoitamka (16-4-5).
Baadaye alizungukia upande ule aliouweka mwili wa Joram, akiambatana na wale walinzi. Walisaidizana kuushusha, walivyofanikiwa waliupakiza juu ya kitanda chenye magurudumu manne, wakaingia nao kwenye lifti wakapandanao juu. Kwani jengo hilo lilikuwa la ghorofa. Ghorofa tatu. Safari yao iliishia ghorofa ya pili. Lifti ilifunguka wakatoka, na kuongoza moja ya chumba kilichoandikwa DUMU mlangoni. Mlango ulifunguliwa, masanduku mengi yakajibainisha mbonini, yaliyotundikwa picha ya mtu juu yake. Kuashiria mtu aliyelala ndani ya sanduku hilo ndiye aonekanaye pichani. Walilitafuta moja lililo wazi, wakauhifadhi vizuri mwili wa Joram kisha wakaondoka.
Jitihada hizo zilikuwa sehemu ya msaada mkubwa na wa kutosha kwa James. Aliamini, alichofanya. Kuwa ndiyo ukombozi pekee. Kwani wale wanaomtuhumu watakosa uthibitisho wa kuthibitisha James kahusika kwenye mauaji. Huo haukuwa msaada pekee. Alikuwa na muendelezo, wa kumuweka mbali James na hatua kali za kisheria za idarani. Ambazo daima haziyumbishwi mtumishi yeyote akienda kinyume nazo. Kwa kudhamiria ama pasipo madhamirio. Lazima adhabu zichukuliwe, na adhabu pekee itolewayo ni mauaji.
Haraka sana aliifikirisha akili yake. Namna ya kumtoa James katika uso wa kifo ambao ulianza mnyemelea toka kwa wananchi wenye hasira kali na watu wa idarani kwao.
“James! Lazima nikuokoe,” alisema. Akiwa kaukamatia usukuni vyema katikati ya barabara akielekea kule yalipo makazi yake.
Alivyowasili, aliteremka garini akaelekea chumbani kwake. Ambako alibadili mavazi, na kuchukua zana fulani zilizoonekana kufunguliwa akaziweka kwenye begi dogo la mgongoni. Alipoona ashakamilisha kila kitu hitajika aliondoka. Hatua kadhaa toka nyumbani kwake akaita bajaji. Akamuamuru dereva ampeleke hospitalini. Ilikuwa safari fupi, walivyowasili alimlipa dereva nauli kisha akaongoza kuelekea mazingira ya ndani ya hospitalini. Ambako alikesha kuzunguka ndani ya majengo katika wodi mbalimbali sambamba na ofisi za ki-utawala. Lengo kusoma mazingira yaliyotawaliwa hapo ni mazingira ya aina gani. Hasahasa yamhusuyo James. Alivyohitimisha kwenye majengo alihamia katika makundi ya watu, lengo apate dondoo za hapa na pale. Alichangamana nao, tena sio kundi moja, mengi na muda mwingine alimfuata mtu mmoja mmoja. Ambapo alimchombeza kwa kina awe na ufahamu wa kutosha katika jambo atalothubutu kulitenda. Taarifa asikiazo hakupuuzia. Alizihifadhi katika mfumo wake wa akili wa kumbukumbu, ili baadaye aanze kuzitekeleza. Hata kama iliongelewa na mtu asiye na utimamu wa akili, hakuiacha, kwani aliamini zote zina msaada mkubwa kwake.
Utambuzi wa mazingira aliyozungukwa nayo James aliyafahamu baada ya kuzipambanua zile taarifa alizozisikia, sambamba na ile doria aliyoifanya ya kuzungukia majengo. Akafahamu, hali ya ulinzi uliopo na matibabu apatiwayo yanaenda kwa namna ipi.
“Inavyosadikika. Wanaweza mwamisha kumpeleka hospitali ya taifa hali ikizidi kuwa mbaya,” alikumbuka mama Tausi. Kauli aliyoisikia toka kwa mmoja wa wauguzi aliopishana nao pindi akiranda randa mazingira ya karibu na chumba alicholazwa James.
“Sasa kabla wao hawajaamua. Acha mimi niwaamulie cha kufanya,” alijisemeza. Pindi akivuka lango la kuingilia kisha kutokomea kabisa mazingira hayo ya hospitalini.
Mbeleni aliita bodaboda.
“Nipeleke uwanja wa ndege,” alimuamuru. Akiwa tayari kashapanda na kuvaa kofia ngumu.
“Ni elfu tatu,” alisema dereva.
“Hamna shida,” mama Tausi alimjibu. Huku akitoa hela kwenye moja ya mfuko wa suruali akamkabidhi.
Dereva akapiga gia kufuata uelekeo alioambiwa. Mwendo wa dakika kumi na tano, pikipiki ikaegeshwa eneo la maegesho la uwanja mdogo wa ndege. Aliteremka, kisha kuongoza sehemu fulani ambayo hata hakukawia sana, akarejea kwenye ile barabara waliyokuja nayo na bodaboda kwa mguu. Alitembea kwa haraka sana. Mtembeo uliobeba uashirio kuwa kuna kitu anakiwahi. Aliambaa ambaa na msitu mdogo, ulioambatana na kichaka kilichosheni nyasi fupi zilizokauka. Mita mia nne toka uwanjani akachukua maficho. Kwa kuingia kichakani na kwenda kuweka makazi kwenye mti mkubwa wa ukwaju uliosimamia juu ya kichuguu. Kutaka asionyooshewe vidole na watembezi wapitao barabarani, aidha, kwa miguu au vyombo vyovyote vya usafiri aliteremsha begi na kutoa vile vifaa pamoja na koti kubwa lenye rangi ya zile nyasi zilizomzunguka. Akalivaa.
“Sasa kwisha habari yenu. James atakuwa mikononi mwangu kuanzia hivi punde,” alisema. Huku akitoa Ipad kwenye lile begi.
Haikumchukua muda, kuielekeza akili yake kwenye hicho kifaa. Akakesha nacho, kwa kubuni vitu mbalimbali na kuandika kisha akatuma sehemu fulani. Yote ni katika harakati za kumsaidia James. Alibuni anuani ya barua pepe ionekanayo ya wizara ya afya, kisha akaandika barua iliyoamrisha James afanyiwe uhamisho kutoka hospitalini hapo apelekwe hospitali ya taifa kwa matibabu zaidi akaituma kwenye barua pepe ya hospitali ya Lukwika. Pia aliandika barua nyingine, ya kuwaamuru wale madaktari waliohitajika kuwasili mjini Lukwika kwa ajili ya matibabu ya James, wasitishe safari zao za kwenda huko badala yake waelekee hospitali ya taifa mjini Lidede.
“Kazi ishakamilika. Acha nisubiri jibu,” alijisemeza. Kauli iliyofuatia na kikohozi huku akiizima ile Ipad na kuirejesha begini.
Barua zote zilikuwa makini, zenye kukosa chembe ya shaka kwa mfikiwa aionapo. Kote alikotuma waliiamini. Hivyo wakaanza fanya maandalizi ya utekelezaji wa kile walichoambiwa baruani. Haraka, pasipo ruhusu sekunde ipite pasipo utendaji, maandalizi ya kusafirishwa kwa James yalifanyika na kuchukua muda mfupi kuhitimishwa. Kutokana na umbali uliopo toka mjini Lukwika na Lidede, usafiri wa haraka ukapendekezwa. Ili awahishwe kufika aendelee na matibabu. Usafiri wa anga ndiyo ulipendekezwa. Kila kilichofanywa, kilifanywa kwa uharaka. Hivyo maafikiano yalivyofikiwa, tayari walishaweka oda moja ya ndege za kukodi zipatikanazo ndani ya mji huo.
“Waambie vijana wako wafanye maandalizi ya kutosha kwa ajili ya upokeaji, maana gari ndiyo inatoka muda huu,” alisikika Mganga Mkuu, pindi akiwasiliana na mtu wa upande wa pili wa simu.
James alipakizwa ndani ya gari ya wagonjwa. Ikiwa chini ya usindikizaji wa askari polisi walio na bunduki zenye risasi za moto, wakijihami kwa lolote baya liwezalo tokea. Pamoja na daktari mmoja na wauguzi wawili waliokesha kumwangalia na vifaa tiba vilivyopo mwilini mwake visitoke kutokana na kutingishika tingishika kwa gari ipitapo sehemu yenye mashimo na matuta. Wakati huo, mama Tausi alikuwa anakamilisha kufunga vile vifaa na kupatikana umbo la bunduki aina ya DP-12 double barrel pump action. Akiambatanisha na kiwambo mbele yake, ili afanyapo mashambulizi kusisikike sauti yoyote ya utokaji wa risasi.
“Naamini, litakuwa shambulizi la nguvu litalotimiza takwa langu,” alijisemaza. Huku akifunga darubini juu ya bunduki na nyingine akaivaa shingoni.
Kila kitu kilivyotayarika alipanda juu ya ule mti. Wa ukwaju. Akatafuta maficho mazuri yaliyomzuia zaidi asionekane, na matawi ya mti huo. Akakoki kabisa, kisha kuketi mkao mzuri wa kuikita vyema bunduki yake katika nyama ya bega. Ili apigapo asiyumbishwe sana na ile nguvu ya utokaji wa risasi. Punde! Umbali mrefu kidogo, alianza sikia mlio wa king’ora kilichompa ishara ya uwazi kuwa gari hiyo ni gari ya wagonjwa. Tena ndiyo ile aliyopakizwa James akipelekwa uwanja wa ndege kwa ajili ya kumsafirisha kumpeleka mjini Lidede kwa matibabu. Gari aliyoisubiri kwa hamu kubwa, na udi na uvumba. Alivyohisi ishakaribia eneo alilopo, alikita begani bunduki yake. Jicho moja kafumba, lingine likiwa makini kuoanisha vilengeo huku pumzi akiiachia taratibu tayari kwa kuibana kabisa wakati wa kupiga. Asipoteze shabaha.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Lengo lilivyosoma kwenye vilengeo vyake hakukawiza. Alibana pumzi na kugusa trigger (kifyatua risasi) kuruhusu utokaji wa risasi zilizopo kwenye kisanduku cha risasi kungoza lengo lilipo. Mwendo wa risasi, hautofautiani na mwendo wa mwanga, hivyo haraka sana zilitua eneo hitajika na kuruhusu kwa mara nyingine risasi kadhaa nazo zitoke kuelekea zilipolengeshwa. Ndani ya sekunde tatu, aliruhusu risasi tano, zilizokita sehemu tofauti tofauti ya gari. Hasahasa kwenye tairi na sehemu ndogo ya bodi. Kitendo kilichopelekea gari kugonga mti, kukita chini na kuwahimiza waliomo ndani kutoka kwa pupa wajinusuru.
Kuona hivyo, mama Tausi aliliendeleza tena. Ili wasibaini ukweli wa kile kilichotokea. Alipiga risasi kadhaa za mpira, zilizowaketisha chini na kuwapatia maumivu yaliyowafanya washindwe kuinuka. Wale askari walishindwa kujibu mashambulizi, kwani walipigwa risasi mikononi na miguuni pia zilizochangia kwa asilimia kubwa kuwadondoshea bunduki zao umbali mfupi toka wao walipo. Dereva, daktari na manesi nao, hawakuwa na la kufanya, zaidi ya kutafuta sehemu wajifiche ili waombe msaada. Lakini hawakuwahi, mama Tausi aliteremka chap mle mtini, kisha kuambaa ambaa na kichaka hadi alivyowakaribia akawapulizia spray yenye sumu iliyowafanya kuwa legevu na hatimaye kupitiwa na usingizi. Hata askari nao aliwapulizia, na alivyojihakikishia washalala kabisa pasipo kujitambua, aliwafunga kudu, akakusanya bunduki akaficha sehemu. Umbali mdogo toka eneo la tukio.
Baadaye alitumia mwanya huo kumteremsha James na kuondoka naye. Hadi kwenye korongo moja, upande mwingine wa barabara tofauti na kule alikoweka makazi yake mwanzo.
“James, lazima umuokoe Rais wetu na hii aibu imkumbayo. Iliyotengenezwa na iendeleayo kutengenezwa na watangulizi wake,” alijisemeza mama Tausi. Huku akimweka vyema James begani alipombeba.
Alitafuta eneo zuri, alivyolipata, alimteremsha na kuhifadhi vile vitu vyake vingine pia. Baada ya hapo alielekea eneo fulani. Mazingira hayohayo ya korongo. Alivyofikia eneo husika, ambalo lilionekana kufunikwa na turubai nyeusi, alilifunua hilo turubai, mdoli wenye muonekano wa binadamu uliovalishwa mavazi mazito, kufungwa vifaa tiba vivujishavyo damu taratibu na kuzungushiwa shuka kubwa mwili mzima, likiacha sehemu ya uso lilijibainisha. Alimchukua, na kuondoka nao. Hadi barabarani. Barabara nyingine, tofauti na ile iendayo uwanja wa ndege. Taratibu, akawa anatembea nao. Mithili ya mgonjwa mahututi, huku wakiacha alama ya matone ya damu yaliyokuwa yanadondoka kuonyesha waendako. Alivyokutana na watu alimfunika, ili wasimuharibie dili lake. Lengo kupoteza maboya, watao thubutu kumfuatilia James. Pale alipoona vyombo vya usafiri wa moto. Pikipiki, bajaji ama gari, vikielekea kule aelekeako, alijaribu kupiga mkono kuvisimamisha ili apatiwe lifti ila hakufanikiwa. Baadaye sana. Akiwa katembea umbali wa kilomita takribani mbili na mita mia tatu, ndipo alifanikiwa kupata kosta moja ya abiria ikitokea Lukwika kwenda Lumesule.
Abiria hawakuacha mshangaa. Lakini aliwapotezea. Na wale waliodiriki kumhoji kulikoni, hakuacha waongopea kwa maneno yaliyowapa ono la huruma.
“Tulikuwa hospitalini hapo mjini Lukwika, ila tumeshindwa kuzimudu gharama uongozi ukaamua kutufukuza,” lilikuwa jibu pekee alilowapatia, kwa kila aliyediriki muuliza.
Habari za kufuatiliwa na kikosi kidogo cha oparesheni hakutambua. Japo akili haikuacha kuwa na hisia, kuhisi kwa namna yoyote watajitokeza watu wa kufanya shughuli hiyo. Hivyo akawa ameketi kwa machale, macho yote nje kuangaza mazingira wapitayo yana nini. Walivyofika sehemu zenye vituo vya askari wa usalama barabarani, ndiyo alizidi. Kiasi kwamba mwili hukuisha kutetema, mtetemo uliomshtua abiria mwingine aliyeketi siti jirani.
“Aaah…samahani, nina homa, hivyo naomba univumilie,” alisema pale aliposhtukia anapigwa jicho kali lililojaa shaka.
“Hamna shida, kuwa na amani,” alijibu yule abiria aliyeketi naye jirani. Kwani siti za gari hiyo zilikuwa katika mfumo wa moja kwa tatu.
Kilichomfanya awe hivyo ni kukosa sehemu ya kujitetea endapo atafumaniwa. Kutokana na ule usawa alioketi hakukuwa na kioo dirishani, zaidi ya bati lililopigiwa misumari. Wafanikiwapo kupita salama alimshukuru Mungu, na kuongeza sala afanikiwe kufika salama sehemu aendayo. Kweli! Baada ya mwendo wa dakika kadhaa gari ilipaki sehemu ya maegesho ndani ya kituo cha mabasi mjini Lumesule. Japo alikuwa ameketi siti za kati, ila yeye ndiye wa mwanzo kutoka wakafuatia abiria wengine. Hiyo yote ilichangiwa na huruma iliyowajaa sababu ana mgonjwa. Ila laiti wangelifahamu wachezewacho, hakika, mama Tausi asingelibaki salama. Angelikuwa mikononi mwa vyombo vya dola muda huo.
“Duh! Pole sana mama yetu, hayo ni mapito tu yataisha.”
“Mungu awe pamoja nanyi mama yetu.”
Walisikika abiria, pindi avukapo siti moja baada ya nyingine. Waliojitia kimbelembele kwa kutaka kumsaidia kumbeba yule mdoli aliyewaongopea kuwa ni mtu auguaye, haraka sana aliwakata kauli hata kabla hajagusa sehemu ya nguo alizomvisha.
“Hapana!...hapana, usihangaike, nammudu,…nammudu,” alisema mama Tausi.
Alivyofanikiwa kuteremka, chap aliingia kwenye bajaji kisha kumuamuru dereva ampeleke nyumbani kwake, ilhali hana makazi yoyote ndani ya mji huo. Dereva alitii. Tena pasi na ubishi, wala kuhoji hoji kuhusu yule aliyeambatana naye. Alijali hela, na sio umbeya ambao haukuwa na msaada wowote kwake.
“Ni mtaa upi mama yangu?” aliuliza yule dereva bajaji, akiwa kashaliacha umbali mdogo eneo la stendi.
“Mtaa wa sita, nyumba namba arobaini na tano.”
“Huko ni elfu nne.”
“Hamna shida, nitalipa.”
Neno la uhakikisho wa kulipwa nauli aliyoitamka, iliongeza morali kwa dereva ya kuzidisha kasi ya mwendo wapate kuwahi kufika. Maana kulikuwa na umbali mrefu toka kituoni hapo. Ila hawakufika mbali, mita mia tatu toka stendi, mama Tausi akamuamuru dereva awateremshe. Dereva alivyojaribu kuhoji kulikoni, aliongopewa. Jibu lililomkatisha hamu ya kuendelea kuuliza.
“Nahisi kutapika, hivyo acha tu ndugu yangu tutembee kwa mguu,” alisema mama Tausi, pindi akimlipa dereva kiasi cha nauli kile alichotajiwa mara baada ya kuteremka.
Dereva akabaki kuduwaa. Jicho kali kuwatathmini, ila cha kushangaza, hatua chache tu, toka alivyoiacha ile bajaji, mama Tausi aliita bajaji nyingine. Yenye rangi tofauti na ile aliyoipanda mwanzo. Akaanza safari upya. Ila si kwa kuelekea kule alikokuwa anaelekea na bajaji ya awali, hapana. Alirudi atokako. Lakini sio stendi, alielekea sehemu nyingine ambayo hata hakufahamu atakutana na mazingira ya aina gani aendako. Hiyo yote, ni kuwapoteza kabisa wote wamfuatiliao, ambao aliwashuhudia baadaye wakiingia pale stendi pindi aondokapo. Awamu hii alisafiri umbali mrefu na ile bajaji. Tena waliishia kukata vichaka vilivyowatanabaisha kwamba wanaelekea mji mwingine. Mama Tausi akawa na kazi ya kuvisaili, kwa kuangaza pande zote, huku na kule, akiwa na tafakuri nzito akilini.
“Hapa panafaa,” aliwaza. Pindi wakilivuka bonde la mto, ufahamikao mto Mara.
“Dereva naomba ututeremshe hapa,” alisema baadaye, alipoona ka-barabara kyembamba kilichoelekea kichakani.
“Mama vipi? Mbona unashukia sehemu hatarishi hivi, na ukiangalia kiza kinaanza ingia, huogopi?”
“Niogepe nini baba yangu. Tunaenda kwenye tiba, kwa mganga hapo juu.”
“Kwanini nisiwapeleke mpaka huko? Sitowatoza pesa nyingi.”
“Hapana. Tutatembea.”
Dereva bajaji hakuendelea kung’ang’ana. Alivyolipwa nauli akageuza kurudi mjini akamuacha mama Tausi anajikokota kuingia zake kichakani kufuata ki—barabara alichokiona. Kiza, kilichoanza poteza mwanga na nguvu ya jua, kikamsaidia, kumficha katika tendo alilokuwa anaenda kulifanya wakati huo. Alivyofika umbali fulani, aliouamini hawezi onekana barabarani, aliutupa ule mdoli kisha akarejea stendi, ambako alipanda gari kurudi mjini Lukwika. Usiku wa saa 2:48 ndiyo aliwasili kituo cha mabasi Lukwika. Kwani hakutaka kuteremkia pale msituni usawa aliomuacha James angelitoa sintofahamu na maulizo kwa abiria wengine. Hivyo alilazimika kusafiri hadi Lukwika mjini alivyoteremka, akarejea kule alikomuacha James kwa mguu.
Mwendo wa dakika kadhaa alilifikia eneo husika. Hakuchelea, alimtwaa juujuu, pamoja na zile zana zake zingine kisha akaondoka. Alitembea umbali mrefu kuitafuta barabara aitakayo. Alivyoifikia alimtua akaanza punga mkono kusimamisha bodaboda zipitazo. Gari hakuwa na habari nazo. Alipunga mbili—tatu, zikawa zimempita pasipo kusikiliza haja yake. Hadi akakata tamaa, kwamba yawezekana asipate usafiri wa kumtoa hapo kumfikisha atokako. Ila alivyoipungia ya nne, ikasimama.
“Nahitaji nifike Namalembo,” alisema mama Tausi.
“Una pesa ya kutosha?”
“Ondoa shaka. Fanya nitakacho utafurahia malipo nitayokupatia.”
“Okay! Panda tuondoke.”
Maongezi yalivyohitimishwa, tayari mama Tausi na James walishakuwa juu ya bodaboda. Walivyoketi sawa, dereva alipiga gia kukitafuta hicho kijiji, ambacho kipo umbali wa kilomita tisa toka mjini Lukwika.
Naam! Giza liliwasaidia kutooneka na kutambuliwa kirahisi. Hadi wamulikwe na mwanga ndipo sura zao ziweze kujibainisha ni kina nani. Hivyo hata dereva hakuweza watambua. Kingine kilichosaidia, James alivikwa kapelo iliyomzuia uso na bwelasuti iliyoficha sehemu kubwa ya maungo ya mwili wake yaliyoharibika. Ambayo yamejaa viashiria vya ugonjwa. Walivyowasili eneo husika, waliteremka, mama Tausi alilipa nauli kisha wakaongoza kwenye nyumba moja chakavu iliyojipambanua kwa kujengwa muda mrefu. Miaka mingi iliyopita. Alibisha hodi. Iliyopokelewa na bibi mmoja, mwenye nyumba, aliyetawaliwa mikanda mingi ya shanga pamoja na hirizi mwilini mwake. Ni mganga wa jadi. Furaha ikajivika usoni, punde walivyoonana baina ya wawili hawa, mama Tausi na bibi aliyejitokeza ndani ya nyumba, walionekana kufahamiana.
“Karibuni,” alisema yule bibi, huku akimpisha mama Tausi apite kwa kusogea pembezoni mwa mlango kuacha uwazi wa kumwezesha mtu kupita.
“Ahsante. Tushakaribia,” akasema mama Tausi, pindi akimweka James mkekani.
“Haina haja ya kupoteza muda, mpeleke chumbani kwetu.”
Mama Tausi alitii agizo. Alimbeba kwa mara nyingine hadi kwenye chumba fulani kilichosheni usasa tofauti na mazingira ya nje ya nyumba. Akamlaza kikitandani, mara baada ya muda mfupi akaingia yule bibi akiwa na muonekano tofauti na alivyompokea mama Tausi. Yale mahirizi na mashanga yaliyozunguka mwili wake aliyavua, akavaa bwelasuti nyeupe lililo na nembo ya bawa akiwa kakamatia vifaa tiba mbalimbali kwenye sahani. Punde, akaanza mhudumia James, mama Tausi akiwa kaketi pembeni akitazamia namna bibi huyo anavyoshughulika.
Shughuli ilikuwa pevu, na ngumu. Kwani ilimchukua takribani saa tatu kukamilisha, baada ya hapo waliondoka mule chumbani wakabaki kuwa na moyo wa matazamio wa matokeo gani yatayotokea kwa kazi waliyofanya.
Bibi huyo, afahamikaye kwa jina la Bi. Matata. Jina maarufu ndani ya mji huo, hakuwa mganga wa jadi kama anavyojipambanua kwa kuvaa mahirizi na mashanga mengi mwilini. Alitumia muonekano huo kuficha uhalisia wake. Kwani, ni afisa wa usalama wa taifa. Mkongwe na mmoja miongoni mwa waasisi wa idara hiyo, aliye na taaluma ya udaktari. Walifikia kwenye mkeka, wakaanza habarishana kuhusu tukio lililojiri na mpango mahususi wa yote yatendekayo ni upi.
Saa thelathini na sita baadaye, James akarejewa na fahamu. Toka alivyopatiwa yale matibabu. Aliweweseka, kwa kushangaa mazingira aliyopo, alivyokuja kaa sawa, akakumbuka kelele za wananchi waliojaa hitajio la kumuondoa duniani. Purkushani za hapa na pale ziliwainua mama Tausi na Bi. Matata pale sebuleni, wakakimbilia chumbani aliko wakajionee kilichomsibu. Walivyofika walimtuliza. Akatulia tuli, kisha yalifuatia maongezi mafupi ambayo yaliombwa na James afahamishwe kilichotokea. Mama Tausi akakamatia usukani, wa kumfahamisha kila kitu afahamucho kuhusu tukio lililojiri. Simulizi ilikuwa ya takribani dakika tano, alivyoweka tuo kuhitimisha, James akatoka na kauli.
“Vifaa vyangu vya kazi viko wapi?”
“Vifaa vipi tena?”
“Mimi nimekuokoa wewe, habari za vifaa sifahamu, yamkini vilichukuliwa na askari ama wananchi waliozingira nyumba awali.”
“Hapana! Lazima nikavifuatilie,” alisema James. Huku akijaribu kuinuka pale kitandani, ila maumivu aliyoyasikia yalimsitisha na kumrudisha tena kitandani.
Baadaye ilibidi amfahamishe mama Tausi kuhusu hivyo vifaa aliviacha katika mazingira gani ili aweze kuvifuatilia. Kweli! Siku iliyofuata mama Tausi akafunga safari hadi mjini Lukwika, alivyoteremka stendi akaongoza hadi sehemu aliyoelezwa. Kule alikokuwa anaishi James. Ila cha ajabu alikuta mazingira yamebadilika, tofauti na vile alivyoambiwa. Nyumba ilibomolewa, na kuna shughuli za ujenzi zilizokuwa zinaendelea. Hivyo alikuta watu wengi mno waliokuwa wanashughulika huku na kule. Wapo waliokuwa wanachimba msingi, kusomba mawe, kuteka maji na wengine kumuongoza dereva wa katapila kusawazisha baadhi ya sehemu. Matumaini ya kupata alichoambiwa yakapotea. Shughuli zote hizo ziendeleazo watashindwa vipi kuona? Hali iliyomsukuma kujifikiria sana, ila baadaye alikata shauri, akatafuta eneo akaketi kushuhudia kifanywacho, ili punde waondokapo, ajaribu bahati yake ya kutafuta vifaa husika ambavyo vilihifadhiwa sandukuni vikachimbiwa ardhini.
Akili ikaanza pambanua, namna atayotumia, maana mazingira yaliharibiwa kiasi kwamba uhalisia wa eneo ambalo aliambiwa hakulitambua. Alipaswa kufanya ubashiri katika utafutaji ataouanza, kwa kupita kila eneo akikosa, atafute mbinu nyingine. Hatimaye alijikuta kwenye tafakuri iliyomchukua muda mwingi, iliyochangia kwa kiasi kikubwa kudhorotesha akili na mwili pia. Kwani kile alichokuwa anafikiria hakikuwa na manufaa katika kujenga mwili. Alitoka kwenye tafakuri hiyo, aliposhtushwa na sauti ya nguvu ya mmoja wa wafanyakazi waliokuwa wanachimba msingi.
“Eeh! Bwana ee…ardhi ishakuwa machimbo sasa. Fuko la dhahabu hili hapa,” alisikika mfanyakazi mmoja wapo. Kauli iliyomwinua mama Tausi pale alipoketi kisha kumuangalia mtu aliyetamka kauli hiyo.
“Dogo acha kuzingua, piga kazi za watu tuondoke zetu,” alisikika mfanyakazi mwingine. Akimsihi mwenziye aache mapuuza.
Mama Tausi, akapiga jicho la umakini. Kuangalia kilichokutwa na namna aserebukavyo kijana huyo aliyeokota.
“Ni sanduku,” alijisemeza baadaye. Pindi kijana huyo akitoka shimoni kwenda kuhifadhi.
Kweli! Lilikuwa sanduku. La chuma, lililojitambulisha kwa kutu iliyong’ang’ania sehemu ya nje. Ikabidi amfuatilie, wapi aendako kuhifadhi. Alipopashuhudia, alihama eneo na kwenda kuketi usawa uleule lilikohifadhiwa. Ambapo aliamini kutakuwa na ukaribu atapojawa na moyo wa kufanya kitu kibaya kitachomwezesha kuondoka nalo. Baadaye aliingia kwenye mkesha wa maombi. Kuomba dua asifukuzwe, na ikiwezekana wale wafanyakazi walisahau.
“Ewe Mwenyezi Mungu. Tia baraka katika hili zoezi. Litalomwondoa Rais wetu katika kashfa nzito isiyomhusu,” alisema mama Tausi kimoyomoyo. Wakati huo kajikunyata mithili ya kidume aliyeshikwa na ngiri. Huku akiiba jicho kuwaangalia wafanyakazi waendeleavyo kushughulika.
Dakika kumi baadaye alishtushwa na kelele za wafanyakazi wengi kwa mara nyingine. Waliokesha kutoa sauti zilizokithiri huruma. Kumhurumia mfanyakazi mwenzao aliyekuwa anagaa gaa chini, damu nyingi zikimtoka kichwani sanjari na povu mdomoni. Punde akashuhudia wengi wao wakikimbilia huko, tukio lilikotokea. Hali iliyomfanya aingiwe na fikra ya kutenda kilichompeleka.
“Huu ndiyo wasaa, wa kukamilisha takwa langu,” alisema. Taratibu akianza nyanyuka na kutembea kwa kunyata kulifuata sanduku lilikohifadhiwa.
Hali inakuja tulia, tayari, mama Tausi alishafikisha Namalembo na kumkabidhi James.
“Ni lenyewe?” aliuliza mama Tausi, James akiwa analikagua kagua kuhakikisha.
“Mmmh!...yeah!...ndilo lenyewe, naomba mnihifadhie,” alisema James. Huku akimrejeshea mama Tausi akalihifadhi.
****
Wakuu wa majeshi na idara zote za ulinzi na usalama hawakukaliana, punde zilivyowafikia taarifa ya kutoroka kwa James. Taarifa iliyowashinikiza wakutane usiku usiku, kujadili mustakabali wa tukio, na ripoti waliyopatiwa na kundi la doria (oparesheni) iliyofanyika. Amani ilitoweka. Katika kichwa cha kila mmoja wao aliyopo ndani ya kumbi ya mkutano huo, kufikiria ataonekana vipi mbele ya jamii na wanaijenga vipi taswira ya Rais kwa wananchi. Picha ya moja kwa moja ikawakumba, kuwa wanaenda mharibia zaidi mheshimiwa Rais kwa kuonekana ndiye mtendaji wa matukio yote yanayojiri.
“Nani alitoa ruhusa ya kuhamishwa?” aliuliza Mkuu wa jeshi la ukombozi wa wananchi. Jenerali Timtim Anyilwisye.
“Yafaa kufahamu hilo,” Mkurugenzi wa idara ya usalama wa taifa, Kanali mstaafu Faidha Mwembere alichangia hoja.
“IGP, sakata linaangukia kwako. Tunahitaji tufahamu undani wa tukio kabla mambo hayajaharibika zaidi,” aliendelea kunena Jenerali Anyilwisye.
“Undani upi? Sisi hatufahamu lolote.”
“Kama hamfahamu askari wako wangelisindikiza? Tuletee wale askari waliosindikiza na kamanda wao wa mkoa watueleze vizuri hii habari,” alisema Jenerali Anyilwisye. Kwa sauti iliyojaa ngurumo iwezayo mtisha mtoto mdogo.
“…pasipo kusahau uongozi wa hospitali na ule wa wizarani nao,” aliendelea kusema. Kwa sauti ileile iliyomtengenezea uchafuko wa nafsi.
Kikao kikahairishwa kwa muda. Hadi hao waliohitajika walivyowasili ndipo kiliendelea. Hakika, kilikuwa kikao kikubwa na nyeti. Kwani, kilitawala umakini na utulivu uliokosa kuonyesha hata chembe ya mzaha. Uongozi wa hospitali, askari wasindikizaji na kamanda wa polisi mkoa wa Michiga, walijieleza kwa namna yao. Kulingana na ufahamu na hali ilivyokuwa. Na wale toka wizarani pia, ambao ni Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu.
“Hizo barua ziko wapi?” aliuliza Jenerali Anyilwisye, mara baada ya mganga mkuu wa hospitali ya Lukwika kuhitimisha maelezo yake.
“Ninazo hapa,” alisema. Huku akichambua kwenye bahasha alikozihifadhi. Alizitoa akamkabidhi.
Zilichambuliwa. Na kila mmoja, ili mwishoni atoe mawazo yake nini kakigundua. Hawakuishia kwa walewale waliomo ukumbini pekee, baadaye waliitwa wataalamu wa teknolojia wazichambue kwa kina. Wapate kufahamu nani mtumaji na mmiliki wa ile anuani ya barua pepe iliyotumika. Zoezi hilo lilichukua saa tatu ndipo wakaja baini uhalisia wa yote.
“Hii anuani imefungwa. Jambo lililopelekea tushindwe kufahamu ukweli,” alisikika mtaalamu mmoja wapo, pindi akifuta jasho jembamba lililokuwa linamtiririka kwa kutumia leso laini.
“Ina maana kwamba?”
“Hizi barua ni feki. Zimegushiwa.”
“Mmmh!...mmh!...nani huyo anayecheza na serikali?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hili ni balaa afande.”
“Kabla balaa halijazidi, hili lililopo lizuiliwe. Hivyo tujitahidi kuifanya iwe siri na yeyote atayediriki kunyanyua mdomo kuzungumzia kwa lengo la kumchafua mheshimiwa Rais nahitaji afungwe mdomo wake. IGP, Kamishna wa uhamiaji na Mkurugenzi wa usalama wa taifa nawaachia kazi.”
“Tupo tayari kutekeleza afande.”
“Juu ya hilo, nahitaji timu itayoweza kumfuatilia na kumtia nguvuni huyu mgonjwa aliyetoroka.”
“Lishatekelezwa,” wanasema kwa pamoja wale wakuu wa idara zingine za ulinzi.
Mwisho, wakahitimisha kwa kuunda kikosi kazi (Task Force) toka ndani ya jeshi la polisi, ambapo walichukua kundi lilelile liongozwalo na Asp Nendakulola, kwa sababu walishakuwa na ufahamu kidogo kuhusu kilichotendeka. Kikapewa majukumu ya kufahamu undani wa mwili uliopotea, mgonjwa aliyetoroka, maana hadi muda huo walishakuwa njia panda, japo kuna muda waliamini kauli ya Mkurugenzi wa usalama wa taifa, Kanali mstaafu Faidha Mwembere kuwa aliyehudhurika sio James. Muda mwingine, waliamini ndiye James ila walikuwa wanaongopewa. Hivyo ili kupata na kutatua fumbo hilo, iliwalazimu mgonjwa apatikane wathibitishe mbivu na mbichi ni zipi. Mwisho, wahakikishe wanampata aliye nyuma ya mgonjwa huyo.
Kufanya kazi na mnafiki, ni mwiko uharibuo mipango. Daima hamna chenye manufaa kitachozaliwa, zaidi ya kuyumba na anguko la hicho kiafikiwacho. Kanali mstaafu Faidha Mwembere, ni mnafiki katika mipango hii. Mtu wa ngozi mbili. Mwenye rangi nyeupe nje, ndani akigubikwa na muivo wa rangi nyekundu. Hakuwa mtu mwema. Tena hata kidogo. Katika mipango yote ya kuhakikisha wanamtoa Rais kwenye kashfa zimkabilizo. Sambamba na James. Ambaye ndiye alikuwa msaada nambari moja katika mipango ya kumsaidia Mheshimiwa Rais. Ndg. Mohammed Mlunji. Maana habari ya ujio wake nchini alikuwa nayo. Na kazi ipi aendayo kuifanya, alifahamu pia, lakini hakutaka kuwa muwazi kwa wakuu wenzake. Kwanini anaamua kufanya haya? Ni fumbo, tena fumbo ngumu linalohitaji akili ya ziada kulitatua.
Maana juu ya kuwa ni takwa la kisheria, mtumishi wa idara ya usalama wa taifa anapoharibu adhabu yake ni kuuwawa, lakini upande wa pili, Kanali mstaafu Faidha Mwembere, alikuwa na shinikizo la kufanya mauaji kwa James toka kwa watu fulani. Kina nani? Ni siri yake. Na vipi kuhusu watu wanaohitajika kuonana na James? Nani anayekatisha uhai wao? Ni mtihani.
Na ilikuwa vipi hadi mheshimiwa Rais ashinikizwe na lundo la wananchi wengi wa daraja la chini ajiuzulu?
Wataalamu hunena, siasa ni sayansi. Itumiayo akili ndogo sana katika kutafuta utatuzi wa jambo. Asiye mwerevu pasipo pambanua hoja aambiwazo, hukesha na imani ongofu ziletazo matokeo haribifu baadaye.
Punde, kikao kilivyohairishwa, Kanali mstaafu Faidha Mwembere, aliingia ndani ya gari yake. Aina ya Nissan V8 yenye rangi nyeusi iliyopambwa na tinted nyeusi. Mara baada ya kuketi alichukua simu yake, akapangusa kutafuta namba fulani, alivyoifikia, alipiga kisha kuweka simu sikioni. Haikuchukua muda mrefu kupokelewa. Na kuwa kwenye maongezi na mtu wa upande wa pili.
“Fanyeni kama nilivyowaagiza mwanzo. Maana bado wapo na James,” anasema, Kanali mstaafu Faidha Mwembere.
“Vipi kuhusu msaada wake?”
“Sababu hatuna uhakika kama yupo amsaidiaye, tupeleke nguvu zetu kwa huyuhuyu aonekanaye.”
“Sawa kiongozi.”
“Nawaamini, hamtoniangusha.”
“Ondoa shaka,” alisema yule wa upande wa pili wa simu kisha akakata.
Hatimaye kazi ilianza. Kwa kikosi kazi kukabidhiwa faili maalumu lihusulo sakata hilo lililotishia amani ya nchi endapo watu wa ulinzi na usalama wakifanya vibaya. Kazi ikaanza upya. Kwa kikosi kazi kukutana kujadili taarifa iliyopo kwenye faili, pamoja na uhakiki wa vielelezo vilivyopatikana. Zoezi lililowachukua zaidi ya saa saba kufikia tamati. Kila walilofanya walifikisha ripoti kwa viongozi wa juu. Lakini haikuacha kuvuja, kupitia Kanali mstaafu Faidha, aliyekuwa anawaambia kina Kalumbwe. Taarifa zilizowataarifu waanzie wapi na wafanye nini ili kuwawahi kikosi kazi.
Kikosi kazi kilianza doria ya ufuatiliaji wa nyendo walizozihisi James kapita siku moja mbele, toka ile waliyokabidhiwa jukumu. Ilikuwa ya mtaa kwa mtaa, ndani ya Lukwika na miji mingine. Kwani walipewa kibali cha kufanya kazi nchi nzima. Ili wasipate sumbuka mambo ya ombaomba wakihitaji kuingia mji mwingine ulioko nje ya wilaya wafanyayo kazi. Kalumbwe na Aisha nao wakawa wanafuatilia nyayo zao, wakati mwingine wakawa wanawatangulia wakishahisi kiendwacho kufanywa ni nini. Mambo yalienda hivyo. Tena kimyakimya, raia wasitambue, kwani utambuzi wao ni mwanzo wa mpango kuharibika. Muda mwingine ilibidi watumie hisia. Na ndiyo silaha kubwa na ya kipekee waliyotumia kudhania yale maeneo korofi wahalifu wengi hupendelea kukimbilia.
Waliorodhesha miji kadhaa, na barabara zitumiwazo sana na watu wafanyao matendo ovu wakimbiapo. Katika zoezi hilo, wakapata miji minne korofi, ambayo waliamini kwa namna yoyote, wamtafutaye atapatikana. Na barabara sita zitumikazo na waovu. Sababu walikuwa watu wachache, waliomba ongezewa nguvu, ya askari wengine watao-kava kwenye hizo barabara, kisha wenyewe wakajipa majukumu ya kuzungukia miji waliyoichagua kuwa ni korofi. Ombi lao halikukataliwa, tena walitekelezewa kwa haraka sana. Dakika nne tu, toka walivyotoa ombi askari ishirini wakaongezwa. Wafanye doria katika barabara zilizochaguliwa, wengine wakapewa jukumu la kuweka pointi sehemu moja ifahamikayo Darajani. Ambapo kulikuwa na daraja liunganishalo mji wa Lukwika na Naipingo.
Hapo darajani waliwekwa askari kadhaa. Wapatao sita, waliofanya kazi ya kukagua watu wapitao na mizigo wabebayo. Iwe kwenye magari ama sehemu yoyote. Na kigezo cha kuweka pointi ya ukaguzi sehemu hiyo, ni sehemu pekee itumikayo sana kwa kivuko kuelekea miji mingine ndani ya Mangaka toka Lukwika. Kwani zaidi ya hapo hakukuwa na sehemu nyingine iwezeshayo kuvuka kuelekea miji ya ndani ya Mangaka. Hata zile barabara walizowekea doria zilikuwa zinatokezea nchi jirani zilizopakana na Mangaka. Hivyo darajani ilikuwa sehemu ya kutorokea kwa watu wanaohitaji wabaki nchini na wale wanaohitaji watoke ndani ya nchi hutumia hizo barabara.
Wale askari wa darajani walifanya kazi yao vyema, na inavyopaswa. Hawakuacha kukagua kitu chochote kipitacho, ili wasije fanya uzembe wa kupitisha mhalifu mwingine ama yule wamtakaye. Kawaida yao, wakawa wanawekeana zamu. Wanafanya kazi kwa awamu, kila baada ya saa saba linaingia kundi lingine, lengo wasichoke wote kwa pamoja. Namna walivyojenga umakini kwenye hiyo shughuli ilipelekea hata raia kuwachukia. Laiti kungelikuwa na sehemu nyingine ya kupita, wangelitumia hiyo lakini haikuwepo. Wakawa wanalazimika kupita hapohapo. Mioyo ipende isipende.
Walifanya hivyo, ila siku kadhaa mbeleni, umakini ulianza potea. Kama ilivyo itikadi. Ya majeshi mengi ndani ya Mangaka, hutawaliwa na umakini wa kufuatilia jambo siku za mwanzoni baada ya kutokea tukio hatarishi. Baadaye hali hubadilika, mazoea na mzaha hurejea. Kurejea tena kwa umakini labda hadi wasikiapo taarifa za kukaguliwa na afande wao, ukaguzi ukishapita, umakini nao unatokomea. Ndivyo ilivyokuwa kwa hawa siku za mbeleni. Askari wa nyongeza. Umakini ulipungua, wakaingiza mazoea na mizaha mingi. Hasahasa walivyozoeana na watu waliokuwa na kawaida ya kupita kila baada ya muda fulani na kila siku. Walifanya ukaguzi wajisikiapo. Kuna muda waliacha tu watu wapite, tena wahisivyo unyong’onyo na wakati mwingine ndipo walikagua. Ila si kwa umakini na utaratibu unaohitajika, walikagua basi tu, kutimiza wajibu. Hakika walianza kuzembea.
Siku ambazo uzembe uliongezeka zaidi, ni siku walizojawa na matarajio ya kupata pesa. Aidha posho au mshahara halafu usitoke, ilhali wamezungukwa na shida lukuki za kuzitatua na walishaweka ahadi kufikia siku hiyo atatatua. Hapo ndipo mambo huaribika. Kiasi kwamba hata raia wapitao hubaini kiwatatizacho kutokana na malalamiko wakeshayo kutamka.
“Dogo twende tukapige mzigo, wenda serikali itatufikiria leo?” alisikika askari mmoja akimwambia wenziye aliyelala ndani ya hema lililotengenezwa kando kidogo ya daraja maalumu kwa kupumzika.
“Naitolea wapi morali ya kufanya kazi wakati hawajatupatia mshahara?”
“Na wametunyoosha mbaya. Maana zimepita takribani siku nne toka tutarajie kupokea halafu hawajafanya kitu.”
“Sasa unaenda kufanya kazi ya nini? Njoo lale hapa acha ujinga. Kwani huyo wamtafutaye akipita utaathirika nini?”
“Kweli mwanangu. Lala basi vizuri tulale wote,” alisema yule askari ambaye alikuwa na morali ya kufanya kazi huku akielekea pale alipo mwenziye.
Mambo yaliendelea hivyo, siku hadi siku. Wapokeapo mishahara yao hupiga kazi kwa uzuri. Huku wakijawa bashasha tele.
Jitihada za Bi. Matata, akisaidizana na mama Tausi zilichukua wiki saba na kutoa mafanikio yaliyorejesha ubora wa afya ya James. Sasa akapata wasaa wa kuhakiki utimilifu wa vitu vyake, alipoona viko timamu, akapanga mwendelezo wa safari kukamilisha mpango alioagizwa. Hivyo aliwaaga wenyeji wake, nao kumpatia baraka zote katika hilo. Lakini kabla hajaianza walifanya rada ya kutafuta sehemu ipi imfaayo kutumia kumfikisha kule anakohitaji. Kila uchao wakawa wanashinda maeneo ya karibu na darajani kuangalia kiendeleacho huku wakitathmini cha kufanya kitachomwezesha kusonga mbele.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Utendaji wa kazi wa askari ukawapa matumaini ya kupita. James naye akawathibitishia na akawa tayari kwa kuondoka kupitia hapohapo darajani safari ya Nanderu, kumtafuta Kasanjara Chomeko. Rada yao waliifanya kwa muda wa wiki mbili, mwanzo wa siku ya wiki ya tatu maandalizi ya safari yalianza na kuiva. Yalikuja kamilika siku ya nne ya wiki ya tatu. Siku ya tano, safari ikaanza rasmi, mnamo majira ya saa kumi na moja jioni. Walikodi taksi, ikaendeshwa na Bi. Matata kuanzia Namalembo hadi darajani tayari kwa kulivuka kuuacha mji wa Lukwika. Mwendo haukuwa wa kasi sana. Kiwango cha kati, kilichowawezesha kupiga stori kwa wingi. Walivyowasili walipaki gari kwenye foleni kubwa waliyoikuta. Iliyosababishwa na mabadiliko ya zamu ya askari, hivyo walilazimika wasubiri askari wakabiziane ndipo ukaguzi uendelee.
“Si wangetuachia tupite, halafu hao wafuatao ndiyo wangeendelea nao na ukaguzi,” alisema James. Jicho kalitoa pima kule waliko askari, waliokesha kuandika andika vitabuni.
“Yumkini wameambatana na afande wao ndiyo maana wamefanya hivi. Si unakumbuka juzi pindi wanabadilisha waliwaachia watu wapite?”
“Eeh!...nakumbuka, tena sio juzi tu. Hata siku zingine pia tulizokuja pindi wanabadilisha walikuwa wanafanya hivyo.”
“Basi tambua hilo, wacha tusubiri tuone matokeo,” alisema Bi. Matata na kutulia tuli. Huku akimuunga mkono James kutumbua macho kule alikokuwa anashangaa.
Wakati huo James alikuwa kajikoki vyema. Kavaa mavazi makubwa yapotezayo uhalisia wa mtu, sambamba na miwani, imzuiayo miale ya mwanga pasi na sahau kapelo kubwa aliyoishusha karibu na usawa wa macho. Iliyomsukuma, akihitaji kumwangalia mtu ainue uso wake juu kidogo apate mwanya wa kuona. Makabidhiano yalivyotamatishwa, wale askari walioingia zamu muda huo wakaanza kukagua. Wapitao kwa miguu waliangaliwa vyema, na wale waliopo kwenye magari waliamrishwa kuteremka, na kukaguliwa wakiwa chini baada ya hapo wanaruhusiwa kuingia kwenye gari waendelee na safari yao. Ni kitendo kilicholeta kero kwa wenye magari na abiria wanaosafiri kwa magari makubwa, lakini walilazimika kutii takwa hilo.
Taratibu foleni ilisogea. Kisha wale wa nyuma ku-kava nafasi ya mbele iliyo wazi. Baada ya ukaguzi wa gari kumi, ikafikiwa ile waliyopo kina James. Askari wakisimama huku na kule. Mmoja mlango wa mbele upande wa kuume mwingine mlango wa mbele pia, upande wa kushoto. Mmoja wao akagonga kwenye kioo, huku akitoa malalamiko yaliyoonekana kuwahusu moja kwa moja wale waliopo ndani ya gari hiyo. Kina James.
“Ukiona zamu yako ishakufikia unateremka mwenyewe garini, sio hadi ugongewe, unatusumbua na kutuumiza viganja vya vidole vyetu,” alisikika yule askari.
“Samahani kaka yangu. Nilikuwa sifahamu utaratibu,” alisema Bi. Matata, wakati huo James anafungua mlango tayari kwa kutoka.
“Haya jitayarishe kwa ukaguzi,” walisikika wale askari kwa pamoja.
“…ondoa hayo mavitu yako yaliyozuia sura nikuone vizuri,” aliendelea kusema yule askari aliyoko na James.
James alitii takwa. Huku mapigo ya moyo yakichipua kwenda kasi, kwamba anaenda kukamatwa kirahisi kabisa tofauti na wao walivyotaraji. Kwamba watafanikiwa kupita pasipo bughuza yoyote, ndiyo maana wakachagua kupita muda huo, utumikao mara nyingi sana askari kubadilishana zamu. Sababu huwaga wanakosa umakini. Kwa watokao na wale waingiao, kutokana na kuwa na hali ya ufikiriaji. Watokao hufikiria safari ya kuelekea nyumbani, na wanaoingia, namna ya kulimudu lindo kwa masaa waliyopangiana. Kitu cha kwanza, aliondoa kapelo. Kisha akapeleka mkono kwa mara nyingine aondoe miwani, jicho la askari likiwa linamwangalia pasipo upepesi. Ila hakufanikiwa, kwani kitendo cha kugusa vidole kwenye kishikio tayari kwa kuivua, radio call za askari kwa pamoja zilisikika zikiongea. Jambo lililomsitisha asitoe kumpa nafasi askari aliyonayo ambaye alianza muona akihangaika kutoa redio sehemu aliyoihifadhi. Mfuko wa suruali.
“Mwewe kumi! Mwewe kumi, kwa Anga…,” ilisikika redio kwa mara nyingine. Maneno ya siri yatambuliwayo na askari pekee. Wakati huo tayari ashafanikiwa kuitoa. Alibonyeza kitufe kimoja wapo, akasogeza karibu na mdomo akazungumza.
“Anga nakupata. Ujumbe kwangu,” alisema yule askari.
“Vyema. Ungana na afande kunguru moja ana lolote kwako,” ilisikika sauti ya mtu aliyopo chumba cha kuongoza mawasiliano ya redio hizo kwa askari.
“Afande kunguru moja, afande maelekezo.”
“Punde kuanzia sasa, msafara wa mheshimiwa AA uelekeo kwako, nyuma yake, kuna msafara wa benki kuu unaosafirisha njuruku, hivyo weupe! Weupe, unahitajika hapo kwako,” alisikika yule aliyeunganishwa naye. Kauli iliyomtaka daraja liwe wazi, pasiwepo na raia yoyote ama gari ya raia yoyote ili msafara alioambiwa, msafara wa Waziri Mkuu uweze pita pasipo usumbufu.
“Nguvu ya kiganja. Tunatekeleza hilo afande,” alisema na kuirejesha redio mfukoni.
Wakaambizana askari wote. Kisha kwa pamoja wakawa himahima kuwataka wale raia waondoke haraka sana mahali hapo. Raia walitii agizo, tena wakiwa wanguwangu kupishana, kitendo kilichotumia dakika saba tu, na kufanya daraja lote lisalie askari pekee. Muda mchache baadaye, kama walivyoambiwa, walishuhudia msafara wa mheshimiwa Waziri Mkuu ukipita hapo kwa kasi ya ajabu. Hazikupita dakika kumi, msafara wa gari za Benki Kuu (Bank of Mangaka) zipatazo mbili, zikisindikizwa na gari ya askari walio na silaha kubwa kubwa za mashambulizi. Misafara husika ilivyomalizika, zoezi la ukaguzi likaendelea, kwa gari na watu walioanza kupita.
Kitendo cha kuondolewa kwa uharaka, ndiyo ikawa nafasi pekee ya James kuokoa. Mapigo ya moyo yalirejea mahali pake na akili pia ilitulia. Safari ikawiva, tena bwerere kabisa, pasi na chembe ya shaka.
“Nakushukuru ewe baba wa mbinguni uliye hai, kwa kuniweka mahali salama, na kuniondolea mabalaa mpaka sasa,” alijisemeza James kimoyomoyo, huku Bi. Matata akizidi kanyaga mafuta kutafuta uelekeo wa safari yao.
Ukaguzi wa kamera za CCTV zilizofungwa hapo darajani, ufanywao kila siku asubuhi katika chumba maalumu kilichofungwa mitambo ya kuongozea kamera hizo zinakuja mbainisha James, kupitia sehemu ndogo ya uso wake baada ya kuvua kofia, alivyokuwa anaanza ivua ile miwani.
“Ni mwenyewe. Ndiyo, ni yeye, hebu angalia, ona…ona…,” alisikika askari mmoja aliyekuwa anafanya kazi ya kuonyesha matukio yote yaliyojiri jana yake.
“Rudia, tuangalie kwa makini,” walisema wale wengine kwa pamoja. Huku wakiinamisha chini vichwa vyao kidogo kuelekezea skrini ioneshayo waweze jionea kwa uzuri zaidi.
Naam! Tukio hilo lilirudiwa. Wote macho yakiwa hapo, ilivyomalizika, ilirudiwa kwa mara nyingine hadi walivyoridhika nayo.
“Sahihi! Ni mwenyewe,” walithibitisha kwa pamoja.
Baadaye aliitwa ASP Nendakulola na timu yake waje waiangalie. Walivyowasili walionyeshwa, karibu mara tatu, nao wakaafiki. Kuwa aonekanaye kwenye picha hiyo ya video ndiye mtafutwa. Taarifa hiyo haikuishia hapo, ilipanda ngazi za juu na kutumiwa picha ya video waiangalie. Kila aliyetumiwa alirudi na mrejesho kuwa huyo ndiyo wanayomtafuta, ambao wao walimfahamu kwa jina la Sadiki. Hivyo wakaanza upya kumfuatilia. Kuanzia gari aliyopanda. Namba za usajili, rangi na aina ya gari. Baada ya hapo wakahamia kutazama ushukaji ulikuwaje. Walivyoona kuna uchelewaji fulani umejitokeza baina ya mtu wa kwanza alivyoteremka naye, basi moja kwa moja wakajua hawajakosea. Ikabidi wanakili vile vitu vya muhimu kwenye daftari zao za kumbukumbu na vitabu vya kipolisi wakiamini vitakuwa msaada tosha kwao. Mwisho wa tukio hilo, ulikuwa mwanzo wa safari. Kikosi kazi, kilifunga safari, kuelekea kule ambako gari aliyopanda James imeelekea. Japo hawakufahamu ni wapi, ila walijawa na imani, uelekeo waendao hawajakosea. Hapa walitumia hisia, kama walivyoanza tumia mwanzo, zenye kiwango kikubwa cha uaminisho katika watendayo.
“Safari yetu iishie Nanderu, hapo tufanye uchunguzi kwa siku kadhaa, tusipopata dondoo za hapa na pale turudi kujipanga upya,” alisema ASP Nendakulola, wakati huo gari waliyopanda LX V8 Toyota Land Cruiser ikizidi chanja mbuga.
“Hamna shida afande. Naamini hapo akili zitapumzika na kupata mbinu mpya zenye kuleta mafanikio kwa urahisi,” alichangia hoja askari mwingine. Sajini Zena.
Hatimaye wakajikuta kwenye lindi la maongezi, walilokesha kujadiliana namna wanayopaswa kufanya, wafanikiwe kumtia James mikononi mwao. Maongezi yaliyowashinikiza muda mwingine waangue kicheko kilichozalisha machozi. Walikuja sitisha, punde ilivyofungwa breki ya ghafla na kuzalisha ukimya mithili ya maji yawapo ndani ya rumbi.
“Nini tena?” walitokwa na swali kwa pamoja kumwendea dereva.
“Kuna kibati fulani nimekiona hapo nyuma kifananacho bati la namba ya usajili wa gari,” alisema dereva.
“Sasa wewe cha nini?”
“Huwezi jua. Yumkini ndiyo namba ya gari iliyokuwa inatumika kwenye taksi tuifuatiliayo.”
“Aaaah…hamnaga kitu kama hicho. Kama vipi nenda kahakikishe, ila tambua kwamba tunachelewa.”
Dereva aliteremka. Kisha akafanya mabio ya hapa na pale hadi alipoliona hilo bati. Akaliokota na kurejea garini.
“Angalieni hiyo,” alisema, huku akiwakabidhi na kuanza kukanyaga mafuta kuendelea na safari.
Chap! Walifungua shajara zao. Hadi kurasa walizoandika kumbukumbu zihusianazo na tukio waliloliona kwenye kamera za CCTV. Wakaanza fanya ufananishaji. Kati ya ile waliyoandika wao na iliyopo kwenye lile bati. Ilifanana!
“Afande ndiyo yenyewe,”
“Ina maana wamebadili ama itakuwa gari yao inatembea na chassis namba?”
“Mmmmmh!...shughuli ni pevu.”
“Tena sio kidogo. Ila tusikate tamaa, tutafanikiwa kumkamata.”
Hadi kufikia eneo walilookota kibati hicho, walikuwa washazikata kilomita nne, huku wakivipita vijiji mbalimbali na miji midogo. Ambayo waliamini haiwezi muhifadhi mhalifu. Miongoni mwa vijiji walivyopita, ni kijiji cha Fidla. Kijiji maarufu kwa utoaji wa burudani ya chombo hicho, fidla al-maarufu vayolini. Jina la kijiji hicho kilitokana na burudani hiyo ilivyoanza miaka ya nyuma. Burudani iliyogeuza miaka ya nyuma kijiji hicho kuwa kijiji cha kitalii. Kwani watu wengi walitoka kwenye miji yao kutembelea hapo kujionea namna chombo hicho kipigwavyo na uchezaji wake pia.
“Kunguru moja! Kunguru moja, kwa Anga…” ilisikika redio iliyotegwa garini. Kauli iliyomsukuma ASP Nendakulola kuinua mkono wake na kuchukua kipokeleo.
“Anga, ujumbe kwangu.”
“Haya,…afande Mlima moja, afande Mlima moja ana lolote kwako…”
“Afande Mlima moja na Kunguru moja.”
“Eeh!... Kunguru moja, usisahau kupita hapo Fidla, maana kuna nyakati hukusanya watu wengi sana. Wakiwemo wahalifu,” alisikika afande Mlima moja. Ambaye ni RPC wa mkoa wa Michiga. Jina hilo hutumika kuficha uwazi wananchi wasielewe.
“Utekelezaji afande,” alisema ASP Nendakulola. Muda huohuo gari ikageuzwa kurudi Fidla walikoambiwa.
Walirudi kwa kasi. Mwendo wa dakika saba tu ziliwawezesha kuwasili kijiji husika na kuzuru kambi mbalimbali za starehe. Walienda kila kumbi ya starehe. Iwe kubwa ama ndogo, ili-mradi imeitwa kumbi. Walivyoingia hakuisha kumtazama mtu mmoja baada ya mwingine, kwa wale ambao nyuso zao zilikuwa hazionekani vizuri, kutokana na kuvaa vitu vilivyowazuia, aidha miwani au kapelo, waliamriwa kuvua.
“Bado kumbi moja,” alisikika Sajini Zena Chaula, wakati huo wakikazana kuiendea hiyo kumbi iliyofahamika kwa jina la KUMEKUCHA.
Saa za simu zao zilisomeka 7:55 usiku, ndipo kikosi kazi kiliwasili ndani ya kumbi ya Kumekucha, nje watokako kukitawaliwa na kiza cha kutosha kilichopoteza nuru ya uonaji wa mbali katika mboni za binadamu. Ila mwanga wa balbu chache za rangirangi zilizofungwa pembe zote za ukuta wa kumbi hiyo uliwezesha uonaji kwa kiasi kidogo. Kama ilivyo ada, kwa lengo la kutoharibu burudani ya waburudikaji, walianza zunguka huku na kule. Mtu na mtu, ila ghafla, walishtushwa na kauli ya mshehereshaji aliyekuwa ndani ya banda dogo lilipo mbele ya kumbi hiyo.
“Haya ndugu zanguni, kila lenye mwanzo halikosi mwisho. Zimesalia dakika tano tuhitimishe burudani yetu. Twende…tusisimke na midundo ya mwisho hiyo mithili ya riwaya zipatikanazo ndani ya kurasa ya Tanuru la simulizi,” alisema mshereheshaji. Huku wapiga fidla wapatao tano wakiwa wameketi kwenye chumba chao maalumu walichojengewa ili wasibughuziwe.
“Naam!...naam!...lete mambo ya mwisho mwisho hayo,” walisikika waburudikaji, huku wengine wakianza jiondoa.
Tamko hilo likawafanya waone zoezi lao kutofanikiwa. Ikabidi wakutane chap na kujadiliana kwa sekunde chache kisha kutawanyika kila mmoja kona yake, mwingine, ambaye ni ASP Nendakulola akaelekea chumba cha mshereheshaji akamuamuru atengue kauli. Kwa kumtaka burudani izimwe kabisa halafu watu waliomo wasiondoke. Yule mshereheshaji hakupinga. Akafanya kama alivyoambiwa. Burudani ilizimwa, watu wakaanza kusanyana makundi makundi kujihoji kulikoni. Wale walioleta ubishi wa kulazimisha kutoka, wakakutana na kiunzi mlangoni. Kwani askari wengine, wawili, waliketi hapo kuzuia watu wasitoke.
“Ku-nani?”
“Ku-nani?”
Walijiuliza pasipo pata ufumbuzi wa maswali yao. Hali iliyohimiza mioyo yao ihangaike kutafuta habari nini kilichojiri. Wale vimbelembele wakaanza walisha wenzao matango pori, kwa kuwaeleza habari zisizokuwa na uhakika, sababu tu, halmashauri ya vichwa vyao vimehisi. Dakika mbili baadaye ufumbuzi ukapatikana. Watu walivyoanza kutoka, mmoja mmoja, tena akifanyiwa uchunguzi wa kina.
“Ni askari bhana!”
“Hee! Ndiyo. Halafu naona wanakagua watu watokao, sijui kitu gani kimetokea.”
Walisikika waburudikaji. Walio na roho nyepesi wakaanza ingiwa woga. Huku wale wajihusishao na matendo haramu wakachanganyikiwa, na kuzifanya akili zao ziwe na fikra za kutafuta mbinu ya kuwakwepa. Haikuchukua muda mrefu, vikaanza sikika vishindo kwa nje. Vilivyoashiria kuna watu wanaruka sehemu. Kweli! Walivyopiga tochi kumulika, walishuhudia namna watu walivyokuwa wanaparamia ukuta na kurukia upande mwingine. Kitendo hicho ikawabidi wale askari wajigawe tena. Wengine nje, kule warukiako watu. Ikiwezekana wawakamate baada ya kuhisi kwa namna moja ama nyingine kuwa ni wahalifu. Waliosalia ndani wakaendelea na zoezi. Lakini hawakufanikiwa hata kuwasaili watu wanne, wakaanza sikia purkushani za watu wakipigana.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ikawabidi wale walio ndani nao wote waelekee nje kujionea kiendeleacho. Walivyofika, walikuta askari akipigana na mwanaume mmoja aliyeonekana kuwa mwingi wa kilevi.
“Nyie mnatuonea onea pasipo sababu, shenzi… acha niwaoneshe kazi,” alisema yule mwanaume mlevi, huku akitupa makonde mfululizo usoni kwa askari aliokuwa anapigana nao.
Wakaingilia!
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment