Search This Blog

Sunday 20 November 2022

TAXI - 3

 





    Simulizi : Taxi

    Sehemu Ya Tatu (3)





    Michirizi ya machozi ilionekana kwenye mashavu yake na muda huo alianza kulia kwa uchungu kilio cha kwikwi. Alijiegemeza kwenye kiti chake huku akikumbatia zile picha kifuani kwake, akatoa leso na kupenga kamasi.



    Sasa mawazo yalimjaa kichwani, alikumbuka juu ya taabu zote alizokumbana nazo maishani mwake mpaka kufikia pale. Jina lake halisi aliitwa Nuru Mhina.



    Alikuwa na shahada zote za mwanamke mrembo, ingawa aliachishwa shule akiwa kidato cha nne, wakati huo alikuwa na umri wa miaka kumi na nane, baada ya kugundulika alikuwa na ujauzito wa miezi sita. Alikabidhiwa barua aliyotakiwa kuipeleka kwa mzazi wake nyumbani, lakini asifike baada ya kukumbuka maneno ya mama yake:



    “Unakwenda sekondari na umeshakuwa mwali sasa, kasome na uchunge sana kukaribiana na wanaume. Elimu ndiyo urithi wako pekee na siku ikitokea umefanya ujinga ukapata ujauzito basi utafute kabisa pa kwenda, usirudi hapa nyumbani…”



    Mama yake alikuwa amemtolea uvivu wakati akijiandaa kwenda kuanza kidato cha kwanza jijini Tanga. Wakati huo alikwishatimu miaka kumi na tano na chuchu za usichana zilikuwa zimechomoza kifuani kwake kama embe dodo changa na kutishia kutoboa kila blauzi aliyovaa. Alikuwa na uzuri wa asili na ulimbwende wake uliwaka kama karabai gizani.



    Lakini huko shule maisha yalikuwa magumu sana, alianza kuwa na kesi za shule kila iitwapo leo; hakuwa mtoro wala mjinga bali alikuwa na kesi za kukosa fedha ya michango ya hiki na kile. Hata fedha ya ada ilikuwa inalipwa kwa mbinde sana, kuna wakati alirudishwa nyumbani, wanakijiji wakachangishana ili kusaidia ndipo fedha ikapatikana. Kiujumla maisha yalimpigisha kwata na shule aliiona chungu.



    Maisha ya shida yalimfanya ajiulize kwa nini hakuzaliwa kwenye familia zenye ahueni kama wanafunzi wenzake? Mama na wadogo zake walilazimika kula mlo mmoja tu, tena kwa shida ili yeye aweze kusoma.







    Alijitahidi kuivumilia ile dhiki lakini mambo yalianza kufikia ukomo wa uvumilivu. Alipoingia kidato cha nne alikuwa anaelekea kutimiza mwaka wa kumi na nane tangu kuzaliwa, lakini kwa sababu maisha yalimpigisha kwata ungeweza kudhani alikuwa anaikimbilia miaka therathini tangu alione jua. Usichana wake ulishambuliwa na utu uzima uliomjia ukiwa umevikwa koti la umasikini.



    Lakini hadi wakati huo hakuwa amemfahamu mwanamume, alikuwa bado bikira! Ni katika kipindi hicho vishawishi vilizidi na yeye alitamani sana apendeze kama wasichana wenzake, hasa rafiki zake Mainda Shelukindo na Johari Mcharo. Nguo zake zilikuwa zimechakaa na hakuwa na viatu vya maana.



    Ilifikia kipindi alitamani atafute fedha. Angezipataje sasa? Hakukuwa na njia nyingine ya kuzipata isipokuwa kufanya kama rafiki zake, hasa Mainda aliyekuwa akimsaidia mara kwa mara kalamu na madaftari, na wakati mwingine alimpa hata nguo zake na viatu alivyovichoka. Lakini hakumpa hivi hivi bali alimsema kwanza kwa kutochangamka. Walikuwa wakimshangaa, walidhani labda alitaka kuwa Mtawa!



    Taabu ilikuwa kwamba hakuwa ameyazoea mambo ya umalaya. Haikuwa haiba yake kuukabidhi mwili wake kwa mwanamume kabla ya ndoa ili apewe fedha za kutatua matatizo yake. Hata hivyo, vishawishi kutoka kwa Mainda na Johari vilimpa kisebusebu. Roho ilimchonyota na fedha aliitaka.



    Tena aliitaka sana tu na ushawishi wa rafiki zake ulivyomvika nguvu, Nuru akayavua mashaka na kuamua kujitosa. Ni wakati huo ndipo alipokutana na kijana wa aina na kariba yake. Kijana huyo aliitwa Rafael Jengo na alikuwa mtanashati kweli kweli.



    Rafael ndiye aliyemwondolea ‘utoto’ wake na kumwingiza katika dunia ya watu wazima. Ndiye yeye aliyejitokeza kuwa faraja na furaha yake katika maisha yale ya shule, tangu alipoufahamu ulimwengu huu.



    Walianza taratibu, siku za mwanzo zilikuwa za maumivu makubwa, hata hivyo, hakuwa na namna. Kwani ukitaka kula sharti uliwe! Alijikaza kwa kuwa alifahamu anapaswa kuvumilia ili afanikiwe kama rafiki zake, hasa Mainda. Akakomaa kweli kweli na baadaye akazowea.



    Sasa alipopewa barua ya kumkabidhi mzazi wake hakuona sababu ya kurudi nyumbani, aliamua kwenda moja kwa moja eneo la Ngamiani alikokuwa akiishi Rafael, mwanamume aliyemkatizia ndoto yake ya kusoma ili aje kuwa mwanasheria.



    Alimkuta Rafael akiwa na msichana mwingine nyumbani, walikuwa kitandani watupu kama walivyozaliwa. Nuru alishindwa kuvumilia. Msirimbi wa kipaji cha uso wake uliumuka, milizamu ikatutusika chini ya masikio yake kama iliyopulizwa, na mara kikamtoka kikohozi kikubwa na michirizi ya machozi ikapasuka machoni mwake.



    Alilia kwa uchungu mkubwa mbele ya Rafael lakini mwenzake akakana kumfahamu yeye wala ujauzito wake. Kuona hivyo, Nuru hakutaka makuu, aligeuka akaondoka zake huku akilia kwa uchungu. Jambo moja lilimjia kichwani, atafute vidonge anywe ili afe yeye na mtoto wake tumboni.



    Sauti nyingine ilimwambia mtoto tumboni hakuwa na kosa na yeye hakutakiwa kukata tama, kwani hakuwa wa kwanza kupata ujauzito akiwa shuleni. Sasa hakuwa na namna nyingine ya kufanya isipokuwa kwenda kuomba hifadhi kwa rafiki yake Mary Mgaya aliyekuwa anaishi eneo la Kiriwani, barabara ya Pangani, nje kidogo ya jiji la Tanga.



    Nuru alikuwa amefahamiana na Mary aliyewahi kuishi kijijini Mkuzi kwa mama’ake mdogo, wakati huo Nuru akisoma shule ya msingi. Hivyo Nuru alimwomba Mary asimwambie yeyote kama yeye aliishi kwake. Alijifungua mtoto mzuri wa kike, kisha alirudi tena Ngamiani nyumbani kwa Rafael na kumbwagia yule mtoto, yeye huyo akatorokea jijini Dar es Salaam.



    Huko jijini Dar es Salaam alitafuta kazi kila sehemu, mwishowe aliajiriwa kazi ya kutunza nyumba na mama mmoja, mke wa meneja rasilimali-watu wa kiwanda cha Bora. Alilipwa mshahara kidogo wa kujikumu kwa mwezi, chakula bure, malazi bure, nguo alizozichoka mama mwajiri bure. Akatae? Ili iweje?



    Maisha mapya yakaanza. Kutokana na uzuri wake wa asili haikuchukua hata mwezi akamfadhaisha baba mwenye nyumba na kumtisha mama mwajiri. Matokeo yake alitupiwa virango, akalipwa mshahara wake na nauli juu, kisha akatakiwa kuondoka mara moja na kurudi kwao Tanga.



    Hakurudi. Afuate nini? Kwanza maisha ya nyumbani kwao yalikuwa magumu sana, maisha ya kuishi na mzazi mmoja tu wa kike, tena ya jembe na mpini wake! Halafu angemwambia nini mama yake? Aliamua kubaki Dar es Salaam. Kwa nini? Aliyekuwa baba mwenye nyumba alikuwa amenogewa na sasa alipanga kumlipia kodi kwa siri ili waendelee kubanjuka.



    Alipewa fedha nyingi kisha akatafuta chumba eneo la Magomeni Makuti. Chumba chake hakikuwa kikubwa, kilikuwa cha kawaida ila hakikutofautiana na stoo, kilibeba kitanda kidogo cha futi tatu na nusu kwa sita pamoja na majukumu yote ya sebule, jiko, stoo na mengineyo.



    Nyumba aliyopanga ilikuwa ya vyumba kumi, sita kwenye nyumba kubwa na vingine vinne vya mabanda ya uani. Alikuta wapangaji wengine, wengi wakiwa wasichana kama yeye, hivyo akawa amepata marafiki. Wakati huo ahueni ndogo ya maisha ilishamtembelea, alikuwa amepata wa kumpa vya kumuwezesha hata kupanga chumba kama kile.



    Miezi miwili tu tangu ahamie hapo akapata kazi katika kampuni moja ya samani za ofisini na majumbani kama mkaribisha wateja, baada ya kumfurahisha mfadhili wake.http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Nuru alianza kubadilika, alinawiri na kuwa mrembo kweli kweli, hata shoga zake walianza kumuonea donge. Chuki ikaanza kumea baina yao. Hakujali, kwani alikuwa na marafiki wengi wa kiume kuliko wa kike. Na ni hao ambao aliwahitaji zaidi. Mtaa ule akauhama na kwenda kuishi Kijitonyama, na hata jina alibadilisha, hakuitwa tena Nuru bali Madame Norah.



    Katika kipindi hicho alifanya makosa mara tatu, mara ya kwanza aliruhusu ujauzito bila taarifa wala hiyari, hakumjua aliyempa ujauzito huo wala hakuhitaji mtoto. Suluhu ikawa kuutoa. Haikuchukua muda mrefu mimba nyingine ikanasa. Nayo akaitoa.



    Mwaka mmoja baadaye akanasa ya tatu iliyomhenyesha kweli kweli! Hata hivyo, fedha kidogo alikuwa nayo, akampata daktari mmoja asiye na huruma aliyefanya kazi yake barabara, lakini yeye aliponea chupuchupu.







    Baada ya mwaka mmoja na nusu wa kufanya kazi katika kampuni ya samani za ofisini na majumbani aliachishwa kazi na kuanzia hapo hakutaka tena kuajiriwa, badala yake, alizidi kujitafutia riziki kutoka kwa wanaume mbalimbali, hakujali yupi ajaye, yeyote alikuwa sawa tu kwake ili mradi tu amkatie fedha za kutosha.



    Siku moja jioni akiwa katika mawindo eneo la Hoteli ya Mawenzi, alikutana na kijana mmoja wa kizungu kutoka Sweden, Karl Johan. Madame Norah akamfurahisha kweli kweli Karl, kiasi cha kukiri kuwa ingawa alishatoka na wasichana wengi lakini kwa Madame Norah alipiga saluti, sasa aliamua kuchonga mzinga.



    Karl akampeleka Madame Norah nchini Sweden, lakini mambo hayakwenda kama alivyopanga. Waliachana huku akimpa fedha nyingi za kujikimu pindi akirudi Tanzania. Lakini Madame Norah hakurudi Tanzania. Afuate nini?



    Aliamua kubaki huko huko Sweden akihangaika na haikuchukua muda akaangukia katika penzi la mzungu mwingine aliyeitwa Andreas Gunnar. Andreas aliwahi kuwa balozi wa Norway nchini Tanzania na walikutana katika klabu ya usiku ya Tradgarden iliyopo barabara ya Harmmaby Slussvarg, jijini Stockholm.



    Hapo ndipo bahati ya Madame Norah ilikuwa ikimsubiri, Andreas alikolea kweli kweli, kwanza akaamua kumpeleka shuleni akiwa na miaka 24 kumalizia masomo yake. Alimaliza na kupata ‘Daraja B+’, kisha alisoma katika Chuo cha Ubunifu cha Beckmans jijini Stockholm.



    Kisha Andreas alimnunulia lile jumba la kifahari la ghorofa tatu eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam na jumba jingine la vyumba vinne katika mji wa Göteborg, mji wa pili kwa ukubwa nchini Sweden. Hakuishia hapo, alimsaidia kuanzisha duka kubwa la vipodozi na nguo za kike jijini Dar es Salaam.



    Baada ya uhusiano wao uliodumu miaka kadhaa waliachana, Madame Norah akajiongeza na kuanzisha kampuni aliyoiita Nuru Group iliyokuwa mkusanyiko wa kampuni za vipodozi ya Madame Norah Cosmetics & Fashion; pamoja na kampuni ya Nuru Media iliyomiliki vituo vya Nuru FM na Nuru TV.



    Miaka michache baadaye alifungua kampuni ya samani za nyumbani na ofisini aliyoiita Madame Norah Furniture Centre na mgahawa wa kisasa wa Nuru Foods Café (NFC) katikati ya jiji la Dar es Salaam…



    Pamoja na mafanikio hayo bado hakuishi maisha ya furaha, alikuwa mtu mwenye maisha ya huzuni muda mwingi japo alijitahidi kuonekana mwenye furaha mbele ya watu. Tatizo nini? Kwanza suala la mtoto wake aliyembwaga kwa Rafael kule Ngamiani Tanga lilimsumbua sana.



    Kwa umri wake asingeweza kupata mtoto mwingine kwani alikwisha toa mimba takriban nne na daktari wa mwisho alimtoa kizazi chake. Hakuwa akijua kama mtoto aliyembwaga nyumbani kwa Rafael kule Ngamiani alikuwa mzima au hata yeye alikufa kwa moto.



    Alikuwa amekwenda Tanga kumtafuta Rafael baada ya kutoka Ulaya lakini taarifa alizozipata kule zilimchanganya sana, ile nyumba aliyoishi Rafael katika makutano ya barabara ya 10 na Mnyanjiani haikuwepo tena na badala yake ilijengwa nyumba nyingine mpya.



    Alipouliza aliambiwa iliteketea kwa moto baada ya kutokea hitilafu ya umeme na kuua watu wanne waliokuwa wamelala ndani akiwemo mtoto mdogo. Hakuna aliyekuwa na kumbukumbu ya majina ya waliokufa! Bahati mbaya Madame Norah hakuwahi kumuuliza Rafael alitokea wapi, huenda angelikwenda kwao kupata uhakika…



    Mara mlango wa ofisi yake ukagongwa na kumzundua Madame Norah kutoka kwenye lindi la mawazo. Alifungua mikono yake iliyokumbatia picha zake za usichana kifuani na kufuta haraka machozi yaliyomchuruzika kwenye mashavu yake, kisha alitoa leso na kupenga kamasi huku akizificha zile picha kwenye droo na kujiweka sawa.



    Muda ule aliisikia vyema sauti ya mtoto ikilia kwa uchungu masikioni mwake na kuacha mwangwi moyoni na kwenye ubongo wake. Mlango ukagongwa kwa mara ya pili.



    “Pita!” Madame Norah alisema kwa sauti tulivu huku akijiweka sawa kwenye kiti chake.



    Mlango ulifunguliwa na msaidizi wake Jessica alichungulia na kumwona kisha akaingia ndani. Kwanza alisita, akasimama akimwangalia Madame Norah kwa udadisi na kushusha pumzi za ndani kwa ndani. Lakini hakuuliza.



    “Unasemaje Jessica?” Madame Norah aliuliza huku akijaribu kuifanya sauti yake isikike ya kawaida.



    “Madame, yule dada wa ile demo ya kipindi cha fashion amekuja,” Jessica alisema huku akiwa bado anamtazama Madame Norah kwa udadisi.



    “Okay, mpeleke ukumbini anisubiri nakuja.”



    Jessica alitoka, akaufunga mlango nyuma yake na kumwacha Madame Norah peke yake akiendelea kutafakari.



    Jessica alikwenda moja kwa moja kwenye ukumbi kulikokuwa na wabunifu wa mavazi, alimkuta Joyce akiwa amesimama akiwatazama kwa makini wabunifu wa mavazi wakati wakikamilisha kazi zao za siku ile.



    Alimchukua hadi kwenye makochi ya sofa na kumwonesha sehemu ya kuketi ili amsubiri Madame Norah. Wakati akiketi mara akamuona Madame Norah akija kwa mwendo wa madaha, akasimama na kumlaki, wakasalimiana na kuketi kwa mazungumzo.



    Muda wote Joyce alikuwa anazungusha macho yake kustaajabu mandhari ya kupendeza ya eneo la ukumbi wa kisasa wa lile jumba la kifahari la Madame Norah.



    Madame Norah alimtazama kwa tabasamu, hata hivyo, bado alihisi huzuni ndani ya moyo wake ikishindwa kwenda likizo japo kwa muda. Alishusha pumzi za ndani kwa ndani na wakati huo huo Joyce aligeuza shingo yake kumtazama. Wakatazamana na kujikuta wakitabasamu.



    Kwa mara ya kwanza, Madame Norah alihisi faraja kwa mbali moyoni mwake na huzuni ikipotea taratibu baada ya kuliona tabasamu la Joyce. Muda huo huo Florian alitokea na kumsalimia Joyce kisha aliketi ubavuni kwa Madame Norah, akaupitisha mkono wake nyuma juu ya bega la Madame Norah na kujiegemeza kwenye kochi.



    Madame Norah alimtazama Florian kwa tabasamu na kunong’ona jambo kwenye sikio lake, Florian alimtupia jicho Joyce na kuinuka, akaondoka akiwaacha. Madame Norah alimtazama Joyce na kuachia tabasamu. Kisha kilifuata kitambo fulani cha ukimya.



    “Unajua kwa nini nimekuita? Nilipoiona demo ya kipindi chako ilinishtua sana… Ilinikumbusha kitu fulani cha miaka mingi iliyopita!” Madame Norah alianza kusema na kuvunja ukimya.



    “Baada ya hapo nikaanza kutafuta taarifa zako ili nikufahamu vizuri, niseme tu nimeipenda sana creativity yako na juhudi unazozionesha katika kutimiza ndoto zako. Keep it up, my dear.”







    “Thank you, Madame,” Joyce alisema huku akiachia tabasamu, alihisi fahari kubwa kupewa sifa na mtu kama Madame Norah.



    “Creative thinking kama yako ni muhimu sana katika kutimiza ndoto ya mtu, na tofauti kubwa kati ya mtu aliyefanikiwa na wengine ni moja tu, kuthubutu…” Madame Norah alisema na kunyamaza kidogo, alimtazama Joyce kwa kitambo kirefu kisha akaangalia kando. Huzuni ilianza kujionesha tena usoni kwake.



    Joyce hakuelewa kilichokuwa kikiendelea akilini kwa Madame Norah, alibaki kimya akisubiri kusikia zaidi kutoka kwa mtu aliyemhusudu na kutamani kufuata nyayo zake.



    “Kuthubutu…” Madame Norah alirudia tena neno lile la mwisho, kisha akaongeza, “Lakini huwezi kupata uthubutu kama bado unategemea kupangiwa kila kitu na mwanamume. Mimi nimefika hapa baada ya kutambua kuwa ili niendelee ninapaswa kuwa bosi wa maisha yangu mwenyewe.”



    Joyce alishtuka sana, akainamisha kichwa chake. Aliona kuwa Madame Norah alikuwa anampa mtihani mkubwa sana. Hata hivyo, Madame Norah alikuwa ameyasoma mawazo yake, akaachia tabasamu.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Samahani kwa kukwambia haya, wewe ni sawa na binti yangu… ni kwamba huko nyuma nimewahi kutendwa na mwanamume niliyempenda kuliko chochote, aliniharibia maisha yangu na baadaye akanifukuza kama mbwa nyumbani kwake, wakati huo nilikuwa binti mdogo tu, na kilichofuata baada ya hapo sipendi hata kukikumbuka…” Madame Norah alisita kidogo na kufuta machozi yaliyoanza kumtoka.



    Joyce alihisi kuingiwa huzuni lakini hakuweza kusema lolote, alibaki kimya akimtumbulia macho.



    “Kisha nikawa na uhusiano na wanaume kadhaa lakini wao pia walitaka kunitumia tu. Ninashukuru mmoja wao ndiye alinisaidia kufika hapa nilipo, lakini kwa sasa sitaki mume, sitaki kuwa chini ya mwanaume. Huyu kijana niliyenaye sasa ni kwa ajili ya kujifurahisha tu na siyo kwa ajili ya mapenzi. Ninao uwezo kama wanaume, ninatoa amri na wao wanatekeleza, hivyo sina haja ya mwanamume atakayeniweka chini ya amri zake. Ninaamini katika falsafa ya kuwa: utafanikiwa tu endapo wewe ndiye bosi wa maisha yako!” Madame Norah alisistiza na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Ila kwa wewe uliyeolewa sikushauri umwache mumeo kama hakuzuii kutimiza ndoto yako na usianze kujiona uko juu yake… I know you have an amazing husband and a very strong marriage,” (Najua una mume makini na ndoa imara) Madame Norah alisema na kuachia kicheko hafifu.



    Joyce aliachia tabasamu na kuangalia kando akiyakwepa macho ya Madame Norah.



    “Unachotakiwa ni kumfanya akuamini na kukusaidia kufikia ndoto yako, kama kweli anakupenda,” Madame Norah alisema na mara akaonekana kukumbuka jambo. Alimwita Jessica.



    “Nisamehe sana, binti yangu, nimesahau hata kukuuliza utatumia kinywaji gani?” Madame Norah alimuuliza Joyce kwa upole baada ya Jessica kufika.



    Joyce alimtazama Jessica kwa makini huku akizungusha macho yake kujaribu kufikiria, alivuta pumzi za ndani kwa ndani na kuminya midomo yake. “Mm… nitakunywa chochote,” hatimaye aliongea baada ya kufikiria kidogo.



    “Tuna chai, kahawa, soda, juisi za boksi, bia za kopo, mvinyo mweupe na mwekundu… sijui ungependa nini?” Madame Norah aliuliza tena kwa sauti tulivu huku macho yake yakiweka kituo kwenye uso wa Joyce.



    “Naomba juisi ya boksi… kama ipo tropical nitafurahi zaidi,” Joyce hakutaka kujivunga, alisema bila wasiwasi wowote.



    “Okay, chukua funguo uende ofisi kwangu, chukua tropical juice kwenye jokofu langu, na mimi niletee chupa yangu ya mvinyo wa Navette de Marseille, ipo juu ya meza yangu,” Madame Norah alimwambia Jessica huku akimkabidhi funguo za ofisi yake.



    Jessica alipokea kisha aligeuka na kuondoka haraka kutoka eneo lile, akaelekea kwenye ngazi za kuelekea juu. Madame Norah alishusha pumzi huku akimtupia jicho Joyce na kuachia tabasamu.



    “Kwa kweli sijui kwa nini ninasukumwa sana kutaka kukusaidia ili uweze kutimiza ndoto yako, nimefikiria hata kukutafutia personal assistant ambaye nitamlipa…”



    “Asante sana, mama… sijui nikushukuru vipi!” Joyce alisema huku akiinamisha kichwa chake mbele kwa heshima zote na kuikunjia mikono yake kifuani kuonesha shukrani za kipekee.



    “Usijali… usijali, hata hivyo nina ushauri mdogo kwako, kama kweli unataka kufanikiwa basi simamia ndoto yako bila kujali nani atasema nini juu yako, na usikubali kukatishwa tamaa! Hii imekuwa siri kubwa ya mafanikio yangu,” Madame Norah alisema kwa sauti tulivu ya upole.



    Muda ule ule Jessica alifika akiwa amebeba chano chenye vinywaji na bilauri, akakiweka juu ya meza ndogo iliyokuwa mbele yao kisha aliwakaribisha. Joyce aliitazama saa yake ya mkononi na kushtuka sana, ilikuwa imeshatimu saa mbili za usiku.



    Mara simu yake ikaanza kuita, aliitazama kwa makini na kushusha pumzi za ndani kwa ndani. Uso wake ulikuwa umesawajika kidogo kwani ilikuwa ni simu kutoka kwa mumewe Sammy na hakujua angemjibu nini.



    Madame Norah alimtazama kwa makini, alijua kwa vyovyote vile, kuna jambo lilimsumbua.



    “Ni mumeo huyo, bila shaka!” Madame Norah aliongea kwa sauti tulivu huku macho yake yakiweka kituo kwenye uso wa Joyce. Joyce alibetua kichwa chake kukubali na hapo Madame Norah alimuashiria apokee simu.



    “Ooh… mjibu kuwa upo njiani ili usije ukamkwaza, ngoja nikuwahishe mara moja na gari yangu,” Madame Norah alimwambia Joyce huku akiinuka.



    Joyce alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kubofya kitufe cha kupokelea, akaiweka simu kwenye sikio.







    “Nipo njiani nakuja!” Joyce alisema na kusikiliza kidogo huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani, “Haya!” alisema na kukata simu kisha aliinuka na kuchukua boksi lake la juisi. Wakatoka kuelekea kwenye gari la kifahari la Madame Norah.



    * * * * *



    Zilikuwa zimekwisha pita wiki mbili tangu Sammy aliposimamishwa kazi katika hoteli ya kitalii ya Udzungwa Beach Resort, kipindi chote hicho hakuwa amemweleza mkewe, kila siku alidamka alfajiri na kufanya mazoezi kama ilivyokuwa kawaida yake, kisha akajitayarisha na kuondoka kwenda Ilala Sharif Shamba kwa rafiki yake Elli.



    Hata hivyo, katika kipindi kile cha wiki mbili alikwisha fika Udzungwa Beach Resort mara tatu kwa ajili ya kufuatilia stahiki zake.



    Siku ya kwanza alimkuta Dk. Masanja aliyemtaka arudi kazini mara moja lakini alikataa akibainisha kuwa hakutaka tena kuajiriwa bali alitaka alipwe stahiki zake ili afanye shughuli zake. Dk. Masanja hakuwa na namna nyingine ila kutoa maagizo kwa mhasibu kuandaa hesabu na kumtaka Sammy arejee siku iliyofuata saa nne asubuhi.



    Siku iliyofuata Sammy alifika ofisini kwa Dk. Masanja saa nne asubuhi kama walivyokubaliana lakini alisita baada ya kumkuta Mr. Oduya ndani ya ile ofisi akimsubiri. Dk. Masanja alimtoa wasiwasi Sammy kuwa Mr. Oduya hakuja kwa ubaya na kumtaka aketi kwenye moja ya viti vilivyokuwa ofisini.



    Sammy aliketi lakini akiwa bado ana mashaka. Muda wote tangu alipoingia mle ofisini Mr. Oduya alikuwa yupo makini akimtumbulia macho kupitia juu ya miwani yake aliyoivaa kwa kuilegeza.



    Pamoja na kuwa na wasiwasi lakini bado Sammy aliwasalimia kwa adabu kisha Dk. Masanja alimweleza kuwa ameshawasiliana na mhasibu na kila kitu kilikuwa kinakwenda vizuri, pia alimweleza kuwa Mr. Oduya alifika pale akitaka wazungumze.



    “Kabla hatujaendelea mbele, vipi maisha yanakwendaje?” Mr. Oduya alimuuliza Sammy huku akitabasamu, macho yake yalikuwa yameweka kituo usoni kwa Sammy.



    “Maisha yanakwenda vizuri sana,” Sammy alijibu kwa kujiamini huku akimtazama Mr. Oduya kwa makini.



    “Vizuri… nimesikia kuwa hutaki tena kurudi kazini, kwa nini hutaki kazi?” Mr. Oduya aliuliza tena huku akiendelea kumkazia macho Sammy.



    “Kwa sababu sitaki kuendelea kuwatumikia watu wasio na shukurani, ninaowaingizia fedha nyingi ili wanilipe mshahara, sasa ninataka kuwa bosi wa maisha yangu mwenyewe…” Sammy alisema kwa sauti tulivu huku akijitahidi kuizuia hasira iliyoanza kuchipua ndani yake.



    “Mr. Kambona, naomba nisikilize kijana wangu, najua wewe bado kijana na una ndoto nyingi, ungependa kuwa na maisha mazuri zaidi, umiliki kampuni yako mwenyewe, watoto wako wasome kwenye shule bora zaidi na pengine nje ya nchi, utembelee magari ya kifahari na mambo mengine kadha wa kadha… nimekuja hapa lengo langu ni kutaka kukusaidia kutimiza ndoto zako…” Mr. Oduya alisema na kunyamaza kidogo, akameza mate kutowesha koo lake.



    “Kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikipata sifa zako kuwa wewe ni mwanamkakati mzuri sana wa kiufundi na matukio ndiyo maana umeipaisha sana hoteli hii na kupata tuzo nyingi… lazima niwe mkweli, unastahili makubwa zaidi, ndiyo maana niliposikia hutaki tena kazi nikataka uwe mshirika wangu kwenye masuala yangu ya…”



    “Hilo haliwezekani, Mr. Oduya. Siwezi kuwa na ushirika na wewe,” Sammy alimkatiza Mr. Oduya huku akitingisha kichwa chake taratibu.



    “Kama hilo haliwezekani then you’ll never make it,” Mr. Oduya alimwambia Sammy huku akitabasamu kwa dharau.



    “Now you’re threatening me, Mr. Oduya,” (Kwa hiyo sasa unanitishia, Mr. Oduya) Sammy alimwuliza Mr. Oduya huku akihisi damu mwilini mwake ikichemka na kwenda kasi kwenye mishipa yake ya damu.



    “This is not a threat, young man, this is a warning…” (Hiki siyo kitisho, kijana, hili ni onyo) Mr. Oduya alisema kwa sauti tulivu huku akiendelea kutabasamu kwa dharau.



    “Kama hutataka kushirikiana nami basi hutaweza kufanikiwa kwenye mambo yako, ninaweza kuyafanya maisha yako kuwa magumu zaidi,” Mr. Oduya aliongeza.



    “Tafadhali, mzee, usijaribu tena kunitisha…” Sammy alisema kwa hasira na kusimama, sura yake ilikwisha badilika na sasa alikuwa ameikunja na kutengeneza matuta madogo madogo usoni.



    “Calm down, Mr. Kambona. Lengo la Mr. Oduya ni zuri sana ni kwa vile hujamwelewa tu,” Dk. Masanja aliingilia kati kumtuliza Sammy.



    Sammy hakutaka kuketi, huku akionesha kujiamini aligeuka na kuanza kupiga hatua kutoka nje. Mr. Oduya alibaki akimtumbulia macho, wakati Sammy akijongea mlangoni na kutoka.



    Sammy alipotoka alipita kwa katibu muhtasi wa Dk. Masanja, mwanadada Salha Hamisi. Alimuaga kwa upendo pasipo kuonesha kama alikuwa amekerwa kule ndani, kisha akatoka na kuanza kuelekea nje ya jengo lile. Alipokuwa akipita eneo la mapokezi kuelekea kwenye lango kubwa ili atoke nje akamuona Salha akimjia mbio mbio huku akimwita.



    “Unasemaje Salha?” Sammy alimuuliza Salha huku akigeuka kumsubiri.



    “Bosi Masanja anakuita,” Salha alisema huku akihema kwa nguvu kutokana na kukimbia.



    “Bosi wako anataka nini tena kwangu?” Sammy aliuliza huku akikunja sura yake.



    “Sijui, wewe nenda kamsikilize, amesisitiza sana uende,” Salha alisema huku akimtazama Sammy kwa makini.



    Sammy alifikiri kidogo, akawa kama anajishauri kisha akakata shauri kutorudi tena kwenye ofisi ya Dk. Masanja siku ile.



    “Mwambie nitarudi siku nyingine, kwa sasa kuna sehemu natakiwa nifike kabla ya saa sita mchana,” Sammy alimwambia Salha na kuanza kupiga hatua za haraka kuondoka eneo lile huku akimwacha Salha anashangaa.







    Sammy alipotoka pale alielekea moja kwa moja kwenye mgahawa wa Elli’s, Ilala Sharif Shamba. Lakini hakumsimulia Elli wala yeyote kuhusu kilichokuwa kinaendelea kati yake na Mr. Oduya.



    Baada ya siku mbili alirudi tena Udzungwa Beach Resort na kwenda ofisini kwa mhasibu wa kampuni kufuatilia suala la kulipwa stahiki zake. Haikuchukua siku nyingi akawa amepewa hundi, sasa akawa anatarajiwa kupata fedha ambazo zingemwezesha kukamilisha ndoto yake…



    Siku ya Jumamosi na Sammy alikuwa nyumbani, hakujisikia kwenda popote, alihitaji kutulia na kupanga mambo yake vizuri kuhusu hatua ambayo ingefuata baada ya kukabidhiwa hundi yake siku mbili zilizokuwa zimeitangulia siku ile.



    Pia siku ile alihitaji nafasi ya kumweleza mkewe kwa utulivu kuhusu matatizo yaliyojitokeza kazini kwake na mipango yake ya baadaye kisha angempa nafasi aongee ili asikie mawazo yake, huu ulikuwa ushauri alioutoa kwa Elli aliyemweleza kuwa, ‘kuambiana ukweli ni muhimu katika kuijenga familia’.



    Siku ile alikuwa ameamka alfajiri kama ilivyokuwa kawaida yake akafanya mazoezi, kisha aliingia maliwatoni na kujiweka sawa, akarudi kitandani kulala. Alihisi uchovu hivyo uamuzi wake ulikuwa ni kulala tu hadi pale ambapo angehisi kuchangamka.



    Ilipotimu saa tatu na nusu, akiwa bado yupo kitandani alishtuliwa na mlio wa ujumbe mfupi kwenye simu yake ya mkononi. Alinyoosha mkono wake kuichukua na kufungua sehemu ya ujumbe mfupi. Ulikuwa unatoka kwa Elli: “Njoo hapa Ilala twende Kinondoni, kuna gari zuri sana limepatikana…”



    Sammy aliachia tabasamu pana huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani. Aliinuka na kuingia maliwato, akashevu ndevu zake vizuri kwa mashine maalumu ya kunyolea ndevu huku akikinga mkono wake kwenye bomba la maji na kunawa uso wake huku akijifuta kidevu chake vizuri kwa maji, alipomaliza alijitazama kwenye kioo.



    Alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kupapasa kindevu chake akionekana kuridhika, akabetua kichwa chake na kutoka chumbani, alielekea sebuleni alipomkuta mkewe ameketi, akamuaga kuwa alikuwa amepata ujumbe mfupi uliomtaka afike kazini mara moja, kwani kulikuwa na kazi ya dharura. Akatoka na kuelekea kituo cha daladala.



    * * * * *



    Saa nne ya asubuhi ilimkuta Zainab akiwa amejiegemeza ukutani chumbani kwake, alikuwa kitandani karibu kabisa na dirisha akiangalia nje kupitia ukuta msafi wa kioo cha dirisha, alikuwa akitazama mandhari nzuri ya kupendeza ya Paradise Club.



    Alikuwa akiangalia kwenye lile eneo la maegesho ya magari akitaraji kumuona Mr. Oduya wakati akiingia. Hakuwa na raha kiasi fulani ingawa alionekana kujilazimisha. Kitu alichokuwa amekishuhudia asubuhi ile kilikuwa kimekataa kabisa kumtoka akilini mwake.



    Hii ilikuwa ni baada ya kustafustahi na kuwasha runinga kisha aliweka chaneli ya taifa na kutazama taarifa ya habari, nia yake ilikuwa kujua kilichojiri duniani, hasa kwa kuwa tangu afike nchini alikuwa akishinda ndani na hakuruhusiwa kabisa kutoka nje.



    Hakuwa na shida ya kutoka nje kwani kila alichokitaka basi Lilian alikuwepo kumhudumia. Alikuwa kama malkia aliyekuwa akipewa huduma zote za kimalkia ndani ya jumba la kifalme. Akikohoa tu Lilian huyu hapa kumsikiliza!



    Taarifa ya habari ya asubuhi ile ilipofikia ukomo wake alitazama kipindi cha mapitio ya magazeti, kisha aliamua kubadilisha chaneli na kuweka ya burudani iliyorushwa na Nuru TV. Hapo ndipo alipokutana na kitu kilichoufanya moyo wake kumpasuka paa!



    Akili yake ilianza kupoteza utulivu huku mitupo ya mapigo ya moyo wake ikiongezeka kasi! Alitaka kupuuza kile alichokuwa akikiona akidhani labda alikuwa ndotoni, hata hivyo, milango yake ya fahamu ilikuwa makini zaidi, na aliishirikisha akili yake kikamilifu katika kumletea taarifa za kuaminika.



    Akajiambia kuwa wala haikuwa ndoto bali ni kitu halisi. Hali ile ikasababisha jasho jepesi lianze kumtoka mwilini huku mwili wake ukipigwa ganzi.



    “Oh my God!” Zainab alimaka kwa mshtuko huku akiikodolea ile runinga, hakuamini kabisa alichokiona. Alivuta pumzi ndefu ndani kisha alizishusha taratibu huku akiulegeza mwili wake na kujiegemeza pale kwenye sofa. Hata hivyo, alihisi kulikuwa na mtu aliyekuwa akimwangalia, akageuza shingo yake na kumuona Lilian aliyekuwa anapita kuelekea jikoni na kugundua kuwa alikuwa akimtazama kwa jicho la wizi.



    “Vipi dada, kuna shida yoyote?” Lilian alimuuliza Zainab baada ya macho yao kugongana.



    “Hapana, nimevutiwa sana na huyo mama anayeongea kwenye hiyo chaneli ya burudani,” Zainab alijibu huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Aah, huyo ni mwanamama anayejituma kweli kweli! Wengi wanamsifia kwani amekuwa mfano bora kwa wanawake wengi… ana mafanikio makubwa sana. Hiyo Nuru TV ni ya kwake, pia anamiliki kituo cha redio cha Nuru FM, mgahawa wa kisasa wa Nuru Foods Café na kampuni kubwa la vipodozi na nguo za Kike la Madame Norah Cosmetics & Fashion na mali zingine kibao,” Lilian alisema na kumfanya Zainab asisimkwe zaidi.



    “Kwani ni Mtanzania na anaishi hapa hapa Tanzania?” Zainab aliuliza huku akishindwa kuficha mshtuko wake, alionekana kushangaa sana na muda wote macho yake yalikuwa yameweka kituo kwenye ile runinga.



    “Ndiyo, ni Mtanzania ‘piwa’ na anaishi hapa hapa jijini Dar es Salaam, asili yake ni kutoka Mkoa wa Tanga…”



    “Anaitwa nani?” Zainab alimtupia Lilian swali jingine huku akionekana kuwa na shauku.



    “Anajulikana zaidi kwa jina la Madame Norah…”



    “Madame Norah!” Zainab alidakia akiwa haamini alichokisikia.



    “Ndiyo, Madame Norah. Ni mwanamke aliyejitosheleza hasa, anamiliki pia majumba ya kifahari eneo la Mikocheni alikoweka makao makuu ya ofisi za Nuru Group na eneo la Makumbusho kwenye vituo vyake vya redio na televisheni. Wanasema kuwa pia ana majumba Ulaya…” Lilian alisema maneno yaliyozidi kumchanganya Zainab na kujikuta akiishiwa nguvu.







    “Anaitwa Madame Norah!” Zainab aliwaza na kumeza funda kubwa la mate kutowesha koo lake lililokauka ghafla, aliyakaza macho yake kutazama kwenye runinga. Alijiuliza: Je, ndiye yeye yule aliyekuwa akimtafuta miaka yote hii au alikuwa amemfananisha? Na kwa nini atumie jina la Nuru kila mahali? Hapana huyo ndiye yeye!



    Aliwaza, asingeweza kukosea na wala macho yake yasingeweza kumdanganya. Ila lile jina la Madame Norah ndilo lililomchanganya kidogo, ni tafauti na lile alilokuwa akilifahamu. Hata hivyo, watu hubadili majina yako, huenda hata yeye alilazimika kubadilisha jina!



    “Mbona hata mimi nimebadili jina langu, badala ya Zainab Semaya sasa naitwa Suzanne Ross!” Zainab aliwaza na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Nimewahi kusikia habari za Madame Norah mara kadhaa kila nilipofuatilia habari za Tanzania wakati nikiwa Canada, ila sikujua kama mwenye jina hilo ndiye huyu ninayemshuhudia muda huu kwenye runinga!” Zainab alizidi kuwaza, uso wake ulizidi kupambwa na mshangao mkubwa.



    Kwa kweli ile habari aliyokuwa ameisikia kutoka kwa Lilian ilikuwa imemsisimua sana, hata hivyo, akili yake ilikuwa bado ikisumbuka katika namna ya kutaka kufahamu mengi yaliyomhusu Madame Norah.



    Alimtazama kwa makini Madame Norah pale kwenye runinga, alikuwa mrefu na mweupe mwenye umbo la kupendeza, alikuwa amevaa blauzi ya bluu ya mikono mirefu, suruali ya Jamsuit ya rangi nyekundu iliyolichora vyema umbo lake refu maridadi lenye kiuno chembamba lakini imara kikiwa kimebeba minofu ya mapaja iliyokaza.



    Madame Norah alikuwa akiongea na waandishi wa habari kutambulisha shughuli zake. Zainab alichukua rimoti ya runinga iliyokuwa juu ya mkono wa lile sofa alilokalia na kuongeza sauti.



    “…mwaka huu tutayatumia maonesho haya kuandaa pia chakula cha hisani na kuwakaribisha watu mbalimbali mashuhuri, taasisi za serikali, mashirika na watu binafsi ambao watachangia fedha. Na hata tusipofikia lengo la kiasi kilichokusudiwa hatutaacha kujenga… kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Simamia ndoto yako usijali wengine wanasema nini’.”



    Zainab alishusha pumzi huku akiwa ameyatuliza macho yake kwenye uso wa Madame Norah wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari huku tabasamu bashasha likiwa halimtoki usoni kwake. Zainab alikuwa na uhakika kuwa huyo ndiye na wala hakuwa amemfananisha.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Sasa alifikiria kuahirisha safari yake ya kurudi nchini Canada ili kuweka kwanza mambo sawa, aliamua kumsubiri Mr. Oduya ambaye alikuwa amemtuma mtu kwenda ofisi za shirika la ndege la Uholanzi la KLM kufanya mpango wa safari.



    Ndipo Zainab alipoinuka na kuelekea chumbani kwake, akaketi kitandani. Akili yake ilizidi kusumbuka: huyu Madame Norah alikuwa wapi miaka yote hiyo na aliwezaje kufikia mafanikio makubwa kiasi kile, kama alivyosikia kutoka kwa Lilian?



    Sasa kichwa chake kilianza kulemewa na mawazo, alikuwa akijiuliza maswali yaliyokosa majibu, kwani mwenye majibu alikuwa ni Madame Norah mwenyewe. Muda huo Zainab alikuwa ameketi jirani na dirisha akiyatazama magari yote yaliyoingia na kutoka katika eneo lile la Paradise Club akitaraji kumwona Mr. Oduya ili amsaidie kumpata Madame Norah.



    “Enhee! Afadhali amefika,” Zainab alijiambia huku akiliangalia gari la Mr. Oduya aina ya Range Rover Velar la rangi nyeupe lilipokuwa likiegeshwa eneo maalumu la maegesho la Paradise Club, kisha akamwona Mr. Oduya akishuka na kushika mkoba wake wa kiofisi, akaanza kutembea kwa haraka kuelekea kule ndani huku akimwacha dereva wake ndani ya gari akisubiri.



    Zainab alijiandaa kumkabili, baada ya dakika chache mlango wa chumbani kwake uligongwa, akakimbilia kuufungua.



    “Waoo! Pole sana mpenzi wangu, pole na kazi,” Zainab alimwambia Mr. Oduya huku akimpokea ule mkoba na kuupeleka moja kwa moja mezani.



    “Asante sana, mpenzi, mbona unashinda chumbani muda wote?” Mr. Oduya aliuliza huku akishusha pumzi. Alikaa kitandani.



    “Nimeingia muda si mrefu,” Zainab alisema, na kama kawaida yake, alimvua koti Mr. Oduya na kufungua tai yake na kumfungua shati lake vifungo kisha akamvua viatu na soksi.



    “Nimefanikiwa kila kitu nilichokuwa nakifuatilia…” Mr. Oduya alisema baada ya Zainab kumaliza kazi yake na kuketi kando yake huku akimtazama kwa makini.



    Zainab alishusha pumzi za ndani kwa ndani kisha akaitupia jicho saa yake ya mkononi. Saa nne na dakika arobaini. Alimtazama Mr. Oduya kwa kitambo kirefu, uso wake haukuonesha tashwishwi yoyote.



    “Vipi mpenzi, kuna tatizo lolote, naona kama hufurahii hiki kinachokueleza!” Mr. Oduya alimuuliza Zainab baada ya kuuona uso wake ukiwa hauna tashwishwi na yeye yupo kimya bila kuchangamka kama ilivyokuwa kawaida yake pindi walipokuwa pamoja.



    “Nimeamua kuahirisha safari yangu…” Zainab alisema kwa sauti ya chini iliyobeba huzuni.



    “What?” Mr. Oduya alimaka kwa mshangao mkubwa huku akimtazama Zainab kwa makini.



    “Siwezi kuondoka tena hadi nionane na mtu mmoja muhimu sana,” Zainab alisema huku akiyatuliza macho yake kwenye uso wa Mr. Oduya. Alionekana kumaanisha kile alichokuwa akikisema.



    “Ni mtu gani muhimu kuliko mimi? Mbona sielewi umepatwa na nini, mpenzi wangu?” Mr. Oduya aliuliza, uso wake ulikuwa bado una mshangao.



    “Nimemuona dada yangu mkubwa, unakumbuka niliwahi kukueleza kuhusu familia yangu na jinsi dada yetu mkubwa alivyotoroka baada ya kupata ujauzito wakati nikiwa nina miaka sita…”



    “Ndiyo nakumbuka.”



    “Leo nimemuona… I need to see her,” Zainab alisisitiza.



    “Umemuona wapi? Naona sasa unatafuta matatizo na ikigundulika kuwa upo nchini huoni kama itatuletea sote matatizo!” Mr. Oduya aliongea huku uso wake ukionesha mashaka.



    “Wala hakutakuwa na tatizo lolote. Nimemuona kwenye televisheni, ninachokuomba mume wangu, fanya vyovyote uwezavyo unikutanishe naye, hata kwa kumleta hapa, nahitaji sana kuongea naye.”



    “Sasa nitampata wapi, na anaitwa nani?”



    “Madame Norah…”



    “What?” Mr. Oduya alishtuka sana, akamkazia macho Zainab kwa mshangao. “Is Madame Norah your elder sister?” (Madame Norah ni dada yako mkubwa?)



    “Yes, she’s my sister, blood sister,” (Ndiyo, ni dada’angu wa damu) Zainab alisema huku akilengwa na machozi.







    “Oh my God!” (Mungu wangu!) Mr. Oduya alisema huku akiwa haamini alichokisikia. Alimtumbulia macho Zainab kwa muda, akajikuta akiachia mdomo wake wazi kwa mshangao zaidi. “Ni kweli mnafanana, tena mnafanana sana!” alisema huku akiachia mluzi mdogo wa mshangao.



    Kisha kilipita kitambo kirefu cha ukimya, walibaki wakitazamana kila mmoja akimezwa na ulimwengu wa tafakuri kabla Mr. Oduya hajachukua simu yake ya mkononi na kutafuta namba za Adam Mafuru. Alipozipata alipiga na kusikiliza.



    “Mr. Mafuru,” Mr. Oduya aliita mara tu alipogundua kuwa Mafuru alikuwa amepokea simu. Uso wake ulikuwa na mikunjo.



    “Yes, Boss,” sauti ya Mafuru ilijibu kwa adabu.



    “Naomba ufike hapa Paradise Club mara moja, kuna jambo muhimu sana unatakiwa kulifuatilia, it’s urgent please,” Mr. Oduya alisema huku uso wake uliondoa mikunjo, kisha ukaunda tabasamu pana.



    “Okay, Boss,” Mafuru alijibu. Mr. Oduya akakata simu na kushusha pumzi za ndani kwa ndani, aligeuka kumtazama Zainab huku akiendelea kutabasamu.



    “Don’t worry, my darling, kila kitu kitakwenda sawa,” Mr. Oduya alisema na kumfanya Zainab aruke kwa furaha na kumkumbatia.



    “Thank you, darling, thank you very much,” (Ahsante mpenzi, ahsante sana) Zainab alisema huku akimporomoshea Mr. Oduya mabusu mfululizo.



    * * * * *



    Saa nne na dakika arobaini asubuhi, Elli na Sammy walikuwa wanatoka ndani ya mgahawa wa kisasa wa Elli’s uliopo Ilala Sharif Shamba na kuingia ndani ya gari la kifahari aina ya BMW X6 xDrive 50i la rangi nyeupe mali ya Elli, lililokuwa kwenye maegesho ya magari ya mgahawa ule.



    Elli aliwasha gari na kuliondoa taratibu kutoka kwenye yale maegesho ya magari ya mgahawa wa Elli’s akazunguka na kuelekea kwenye geti kubwa la kutokea la jengo lile, akaliingiza barabarani huku akiendesha kwa umakini mkubwa. Ilikuwa safari ya kuelekea Kinondoni B.



    Kutoka pale mgahawa wa Elli’s gari lilikata kona na kuingia upande wa kushoto likaifuata barabara ya Uhuru iliyokuwa na msongamano wa magari muda ule, hivyo Elli alilazimika kuendesha kwa mwendo mdogo.



    Safari yao iliendelea huku wakiwa kimya, kila mmoja alikuwa akitafakari, walivuka eneo la Bungoni kisha wakayavuka majengo ya Kituo cha Amana Vijana, na mbele yake wakavuka vibanda vya wasusi wa Kimasai vilivyokuwa upande wao wa kushoto na kuingia upande huo huo wa kushoto wakiifuata barabara ya mtaa wa Mafao.



    Kwa kuwa barabara ile haikuwa na msongamano Elli aliongeza mwendo akiyapita majengo ya ghorofa ya Shirika la Nyumba la Taifa eneo la Ilala na baada ya safari fupi hatimaye wakaja kukutana na barabara ya Kawawa.



    Barabara ya Kawawa ilikuwa moja ya barabara kubwa na maarufu sana jijini Dar es Salaam iliyoanzia eneo la Veta Chang’ombe katika makutano ya barabara za Nyerere, Chang’ombe na Kawawa na kuishia katika eneo la Kinondoni Morocco kwenye makutano ya barabara za Ali Hassan Mwinyi, Mwai Kibaki, Bagamoyo na Kawawa.



    Elli aliingia kushoto akaifuata barabara ile ya Kawawa kuelekea Magomeni. Muda wote Sammy alikuwa yupo kimya akiwaza mbali sana, muda wote macho yake yaliangalia nje wakati gari likipita eneo la Msimbazi Centre kisha likavuka eneo la Kigogo Sambusa na baadaye Kigogo Mbuyuni, kwenye mzunguko wa barabara za Kawawa na ile ya Kigogo.



    Pilika pilika za wakazi wa jiji la Dar es Salaam zilikuwa zimeshamiri muda ule kwani eneo lile lilionekana kuwa na watu wengi, pikipiki na magari yaliyopishana kwenda sehemu mbalimbali zaa mji.



    Walipovuka eneo la Kigogo Mbuyuni walianza kuteremsha bonde la Msimbazi kisha mbele kidogo Elli aliongeza mwendo ili kulipita lori la wazoa taka lililokuwa mbele yao. Kisha waliivuka barabara ya Mikumi upande wao wa kushoto huku wakipishana na magari mengi yaliyoingia katika barabara ile.



    Baada ya safari fupi wakaanza kukivuka kituo cha daladala cha Magomeni Mikumi, Sammy akayatupa macho yake kutazama upande wake wa kulia, ng’ambo ya ile barabara ya Kawawa na kuiona yadi moja ya magari yaliyotumika, iliyokuwa na magari yasiyozidi ishirini yakiwa yameegeshwa kwenye uzio yakisubiri wanunuzi.



    Sammy aliyatazama kwa makini yale magari na kuliona gari moja lenye muundo wa kizamani aina ya Cadillac DeVille jeupe. Moyo wake ukapiga paa! Aliendelea kulikodolea macho lile gari wakati Elli akivuka eneo lile kuelekea kwenye taa za kuongozea barabarani za Magomeni, kwenye makutano ya barabara za Kawawa na ile ya Morogoro.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Stop the car,” Sammy alisema ghafla huku akilikodolea macho lile gari na kumshtua Elli aliyegeuza shingo yake kumtazama kwa mshangao.



    “Nimesema simamisha gari!” Sammy alisema tena, safari hii kwa sauti ya juu kidogo.



    “Nini!” Elli aliuliza huku akikanyaga breki kwa nguvu pasipo kufikiri, gari likajivuta na kusota kwenye ile barabara pana huku likiyumba, bahati nzuri gari halikutoka nje ya barabara.



    Muda huo huo walisikia sauti ya breki kali kutoka nyuma yao, dereva wa daladala linalofanya safari zake kati ya Gongolamboto na Masaki lililokuwa nyuma yao alikuwa akihangaika kukanyaga breki ya ghafla na kufanya gari lile liserereke na kusimama kando ya barabara.



    Kwa sekunde chache ilitokea taharuki ndani ya lile daladala, abiria walitaharuki sana. Daladala liliposimama walianza kutoa lugha kali ya matusi kwa Elli, wengine waliishia kusonya tu na mmoja wao aliinua juu kidole chake cha kati kuonesha hasira zake.







    Elli hakuwajali, alilipeleka gari lake kando kabisa ya barabara kwenye barabara ndogo ya waenda kwa miguu na kuliegesha huku akimuomba msamaha dereva wa daladala aliyeonekana kuchukizwa na tukio lile. Eneo lile lilikuwa jirani kabisa na kituo cha mafuta cha Gapco.



    Sammy aliteremka haraka na kuelekeza macho yake kuangalia kule kwenye yadi ya magari kulikokuwa na lile gari aina ya Cadillac DeVille, kisha alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kushika kiuno chake.



    “Nimeiona gari ninayoitaka,” Sammy alimwambia Elli, bila kusubiri alianza kupiga hatua zake haraka kuelekea kule kwenye yadi ya magari, akavuka barabara ya Kawawa na kutokea upande wa pili wa barabara. Hapo hakuwaza kitu kingine chochote bali alichowaza ni jinsi ambavyo angemiliki lile gari. Elli alibaki kimya akimtazama Sammy kwa mashangao.



    Elli aliwasha gari lake akaingia upande wa kile kituo cha mafuta na kulizungusha kisha akarudi tena barabara ya Kawawa na kukunja kuelekea upande wa kulia akimfuata Sammy. Alimkuta Sammy akiwa anaongea na kijana mmoja, mfanyakazi wa yadi ile ya magari.



    Kabla hajajua wanaongea nini akamwona yule kijana akichukua funguo kisha akaanza kuondoka kumfuata Sammy ambaye tayari alikuwa amesimama akilitazama gari moja jeupe lenye muundo wa kizamani aina ya Cadillac DeVille. Elli alimfuata Sammy lakini kabla hajauliza chochote Sammy alimweleza kuwa alitaka kununua lile gari, Elli akashangaa sana!



    Elli hakuwa na uhakika kama Sammy alikuwa ameushirikisha ubongo wake kabla hajafikia uamuzi wa kutaka kununua lile gari lenye muundo wa kizamani. Lakini Sammy alisisitiza kuwa alikuwa akilihitaji lile gari kwa sababu ya upekee wake.



    “Kwanza ni gari lenye upekee, pili lina muundo wa kizamani na tatu ni zuri sana,” Sammy alisema na kuingia ndani ya lile gari.



    “Na vipi kuhusu ubora wake? Usije ukanunua gari ukaliendesha mwezi mmoja tu kisha lianze kukuendesha wewe!” Elli aliuliza akiwa bado ana mashaka.



    “Hili ni gari zima kabisa, ni kama jipya licha ya uzamani wake, kwa kuonesha hivyo tunampa garantii ya miezi sita, kama ataona lina matatizo ruksa kulirudisha,” alisema yule Mwarabu kwa kujiamini.



    Sammy alitia ufunguo na kuwasha injini ya lile gari, gari likaunguruma bila shida yoyote. Sammy akapiga lesi huku akinesa nesa kwa mbwembwe na kuonekana kuridhika. Akaachia tabasamu.



    * * * * *



    Saa sita mchana Joyce alikuwa anawasili katika jumba la kifahari la Madame Norah lililozungukwa na ukuta mrefu wenye mfumo wa uhakika wa ulinzi na geti kubwa jeusi mbele yake. Jumba lile lilikuwa limejengwa ufukweni mwa Bahari ya Hindi eneo la Mikocheni.



    Toka kwa mbali uzuri wa jumba lile la ghorofa tatu ulionekana wazi, mandhari yake ilizungukwa na miti mirefu na mikubwa ya kivuli aina ya ‘Quercus virginiana’, kulikuwa na barabara ya lami yenye usafi wa hali ya juu iliyokuwa ikieleka katika jumba hilo na kupandwa miti ya kivuli iliyovutia na maua aina ya ‘lotus’.



    Kulikuwa na ukimya mkubwa eneo hilo. Joyce alisimama nje ya lile geti kubwa jeusi kisha akabonyeza kitufe cha kengele na mara geti dogo kando ya lile geti kubwa jeusi likafunguliwa, mlinzi mmoja aliyekuwa wamevaa sare maalumu za kampuni binafsi ya ulinzi akachungulia na kumuona Joyce kisha akaachia tabasamu.



    Alimsalimia kwa bashasha zote huku akimpisha aingie ndani. Hakumuuliza maswali yoyote kwa kuwa alimfahamu, kwani alikwishafika hapo mara mbili kabla ya siku ile na tayari walikuwa na taarifa kuwa angefika siku hiyo.



    Joyce alipoingia ndani ya ule uzio walinzi wawili waliokuwa katika kibanda cha walinzi upande wa kulia wa lile geti walimsimamisha, mmoja wao alichukua kifaa maalumu cha kukagulia akamkagua kuona kama alikuwa na silaha yoyote na alipohakikisha kwamba hakuwa na silaha yoyote wakamruhusu aendelee na safari yake.



    Joyce alipiga hatua zake taratibu kuelekea kwenye baraza kubwa ya mbele iliyokuwa na mlango mkubwa wa kuingilia ndani ya lile jumba, alikuwa akikatiza katikati ya bustani nzuri ya maua ya kupendeza aina ya ‘lotus’ na katikati ya bustani ile kulitengenezwa njia nzuri ya kutembea kwa miguu kwa vitofali vidogo vinavyovutia.



    Kabla hajafika kwenye ile baraza kubwa ya mbele iliyokuwa imepangwa seti moja ya makochi meusi ya sofa alimuona Madame Norah akitoka ndani ya lile jumba akiwa ameongozana na msichana mmoja aliyekadiriwa kuwa na miaka kati ya ishirini na sita na ishirini na nane.



    Alikuwa msichana mrefu na mrembo hasa, alikuwa na nywele nyingi nyeusi za kibantu zisizotiwa dawa, begani alitundika mkoba mzuri wa kike wa rangi ya pundamilia uliogharimu fedha nyingi.



    Alikuwa amevaa suruali ya jeans ya rangi ya bluu, blauzi nyekundu ya mikono mirefu na viatu vyekundu vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio. Mkononi alikuwa amevaa bangili nyingi za pembe.



    Madame Norah alikuwa amemuona Joyce wakati akiingia, hivyo aliachia tabasamu na kumpokea kwa bashasha zote.



    “Hello Joy, karibu sana, binti’angu. Habari za huko utokako?” Madame Norah alimsalimia Joyce kwa bashasha huku akimkumbatia na kumbusu kwenye shavu.



    “Nzuri tu, mama. Shikamoo!” Joyce alisema huku akiachia tabasamu.



    “Marhaba, pole na majukumu,” Madame Norah aliitikia huku akimwachia Joyce na kusimama akimtazama kwa makini. Macho yake yaliweka kituo usoni kwake.



    “Ahsante sana mama, vipi na wewe unaendeleaje?”



    “Sijambo kabisa, mumeo na wajukuu hawajambo?” Madame Norah aliendelea kumuuliza Joyce huku akijihisi faraja kubwa sana kila alipokutana naye. Alimchukulia kama binti yake wa kumzaa.



    “Wote hawajambo, mama…” Joyce alijibu huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani, kisha kikatokea kitambo kifupi cha ukimya kila mmoja akimwangalia mwenziwe kwa namna iliyokosa tafsiri, ilikuwa kama mzazi na bintiye waliopotezana muda mrefu na sasa walikuwa wanaonana kwa mara ya kwanza.



    Muda wote yule msichana aliyeambatana na Madame Norah alikuwa amesimama kimya akiwatazama kwa zamu. Uso wake ulikuwa umepambwa na tabasamu pana.



    “Nimefurahi sana kukuona tena, naomba mnifuate,” Madame Norah alivunja ukimya huku akiwaashiria Joyce na yule msichana wamfuate.



    Wote watatu walielekea upande wa kulia wa lile jumba kulikokuwa na bustani nzuri ya kupumzika na bwawa kubwa la kuogelea lililokuwa limezungukwa na viti vizuri vya kujipumzisha chini ya miamvuli mikubwa ya kivuli.



    “Joyce, kwanza kabisa ninakushukuru sana kwa kuacha shughuli zako na kuitika wito wangu, umekuwa unanipa heshima kubwa sana…” Madame Norah alisema baada ya wote kuketi kwenye viti, alikuwa anaonekana mtu mwenye furaha kubwa tofauti na siku nyingine.



    “Nisingeweza kukosa kuja kuonana nawe, mama yangu, wewe umekuwa mtu muhimu sana kwangu katika kutimiza ndoto zangu,” Joyce alisema huku akishusha pumzi.







    “Sasa nimekuita ili nikukutanishe na mtu atakayekusaidia kwenye majukumu yako kama nilivyokuahidi…” Madame Norah alisita kidogo na kugeuza shingo yake kumtazama yule msichana mrembo aliyeambatana naye.



    “Ni huyu hapa… anaitwa Nyaso Gilbert, ni binti mwanamkakati mzuri hasa, msomi wa Shahada ya Kwanza ya Sanaa katika Uchumi na Takwimu, naamini ataweza kusimamia vizuri program zako,” Madame Norah alimwambia Joyce.



    “Ooh, thank you, mam,” Joyce alisema huku akimkumbatia Madame Norah kwa upendo, kisha alimgeukia yule msichana. “Habari yako? Naona hata hatujasalimiana!” Joyce alisema kwa furaha huku akinyoosha mkono wake kumpa Nyaso.



    “Nzuri tu dada’angu, nimefurahi sana kukutana na wewe maana Madame alikuwa anakusifia sana,” Nyaso alisema huku akinyoosha mkono wake na kukutanisha kiganja chake na kile cha Joyce. Wakasalimiana kwa bashasha zote huku wakifurahi.



    Muda ule ule simu ya Madame Norah ilianza kuita, Madame Norah aliiangalia kwa makini na kuminya midomo yake huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani, kisha akaipokea.



    “Hello, Mr. Mafuru,” Madame Norah alitamka mara baada ya kuiweka simu sikioni.



    “Nipo hapa getini kwako,” sauti ya Mafuru ikasikika kutoka upande wa pili wa simu.



    “Ooh umeshafika, waambie wakuruhusu, nipo huku bustanini,” Madame Norah alisema huku akijiinua kutoka kwenye kiti.



    “Sasa Joyce, ngoja niwaache mpange mambo yenu, nimepata mgeni. Ila ukitaka kuondoka niambie ili nikupe dereva akuwahishe,” Madame Norah alisema huku akijiandaa kuondoka eneo lile.



    “Sawa, mama,” Joyce alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.



    Muda ule ule Mafuru alitokea na kusimama akiwaangalia kwa makini. Alikuwa amevaa suti ya kijivu na miwani myeusi na mkononi alibeba mkoba mdogo mweusi wa kiofisi.



    “Habari zenu warembo?” Mafuru aliwasalimia huku akiachia tabasamu.



    “Salama,” Joyce na Nyaso waliitikia kwa pamoja. Mafuru aliwatazama kwa makini, macho yake yakavutwa zaidi kumtazama Joyce. Alimtazama kwa kitambo hadi aliposhtuliwa na Madame Norah.



    “Twende basi, unatazama watu hadi wanaona aibu!” Madame Norah alimwambia Mafuru kwa utani.



    “Huyo ni binti yako, naona mnafanana sana!” Mafuru alimuuliza Madame Norah huku akielekeza kidole chake kwa Joyce.



    “Kwani umekuja hapa kuzungumza na mimi au kupeleleza maisha ya watu wanaonihusu?” Madame Norah alimuuliza Mafuru akionekana kukerwa kidogo.



    “Samahani! Sikukusudia kukuudhi,” Mafuru alisema kisha akaanza kumfuata Madame Norah aliyemuongoza kuelekea ofisini kwake ndani ya lile jengo huku wakiwaacha Joyce na Nyaso wameketi kwenye bustani wakipanga program zao.



    “Hongera sana Madame, wewe ni mwanamke jasiri sana ambaye juhudi zako zinastahili kuungwa mkono, umeonesha ujasiri mkubwa kwa hiki ulichoamua kukifanya. Kwa hilo lazima nikupongeze,” Mafuru alimwambia Madame Norah wakati wakiingia kwenye ofisi binafsi ya Madame Norah.



    “Ni wajibu wetu kurudisha sehemu fulani kwa jamii,” Madame Norah alisema huku akifungua mlango wa ofisini kwake na kumkaribisha Mafuru. Wakaingia na kuketi kwenye viti kwa mazungumzo.



    “Uliponipigia simu kuomba kuniona nilishtuka sana, hadi sasa bado nina mshtuko na sijui unahitaji kuongea na mimi kuhusu nini!” Madame Norah alimwambia Mafuru maara baada ya kuketi.



    “Kwanza kabisa naomba nikufikishie ujumbe wa Mr. Oduya kwako…” Mafuru alianza kuongea lakini akakatizwa.



    “Mr. Oduya! Anataka nini kwangu huyo mzee?” Madame Norah alionekana kushtuka sana.



    “Mbona umestuka sana, Madame, kwani Mr. Oduya hapaswi kukusalimia?” Mafuru aliuliza kwa sauti tulivu ya kusihi.



    “That old man is a monster… hata wewe sikuamini sana, nimekubali kuonana na wewe kwa vile tu pacha wako, Balozi Mafuru kamuoa mdogo wangu, vinginevyo sina ushirika na ninyi kabisa…” Madame Norah alisema na kushusha pumzi.



    “Halafu umenishangaza sana kuniambia una ujumbe wangu kutoka kwa huyo mzee wako wakati mimi na yeye hatuna mazoea, nadhani lazima kuna jambo analitafuta kwangu, siyo bure,” Madame Norah alisema huku akikunja uso wake na kutengeneza matuta madogo.



    “Watu hubadilika, Madame, hivyo usimhukumu mtu kwa aliyoyafanya jana wakati leo kabadilika… Mr. Oduya si mtu mbaya kama unavyomfikiria. Amenituma nikwambie kuwa anakupongeza sana kwa juhudi ulizozianzisha na anahitaji kuonana na wewe leo saa kumi na mbili jioni pale Paradise Club mjadili kuhusiana na hii project yako mpya. Ameguswa sana na anahitaji kuchangia…” Mafuru alisema na kumfanya Madame Norah amkate kauli.



    “Kwa hiyo anataka kunitumia kama mtaji wake wa kisiasa baada ya kuona mambo yamekwama, siyo? Mimi na yeye wapi na wapi! Toka lini tukachangiana fedha kwenye masuala ya kijamii!” Madame Norah alizidi kushangaa.



    “Mr. Oduya ni mtu wa kusaidia sana taasisi mbalimbali zinazofanya mambo makubwa kwa jamii, amekwisha saidia taasisi nyingi tu hadi sasa! Alipata taarifa zako kupitia runinga kuhusu lengo lako la kukusanya fedha kwa ajili ya kujenga kituo na shule ya watoto wenye mahitaji maalumu, pamoja na makazi bora ya wazee… hujui tu hiki ni kitu alikuwa nacho siku nyingi na ameguswa kuona wewe pia una wazo kama lake, hivyo anataka kutoa mchango wake. Hakutaka kuja mwenyewe lakini amenituma nikwambie kwamba anahitaji kuonana nawe jioni ya leo,” Mafuru alisema huku akimkazia macho Madame Norah.



    Kilipita kitambo kirefu cha ukimya, Madame Norah alionekana kuwaza sana, alikuwa njia panda ya ama akubali mwaliko au akatae.



    “Sijajua hasa kwa nini atake kufanya hivyo sasa na si wakati mwingine wowote, kwani siku zote alikuwa hajui kuwa huwa ninasaidia makundi yenye mahitaji maalumu?” Madame Norah aliuliza huku akiyatuliza macho yake kwenye uso wa Mafuru.



    “Hupaswi kuhofia, Madame, hakuna jambo lolote baya ingawa ni kweli kama ulivyosema kwamba wewe na yeye hamna mazoea ya karibu lakini naamini kuanzia sasa mtakuwa karibu zaidi, I’m here because I know something you don’t know,” (Nipo hapa kwa kuwa najua jambo usilolijua) Mafuru alimalizia kwa Kiingereza kuonesha msisitizo wake na kumfanya Madame Norah amtazame kwa mshangao Zaidi.http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Madame Norah alitulia kwa sekunde chache akijaribu kuyatafakari maneno ya Mafuru pasipo kupata majibu.







    “Mpe nafasi naamini kukutana kwenu kutakuwa na faida kwenu wote na hili suala linahitaji utayari wako tu, hayo mengine yote yatakushangaza na kukusisimua zaidi! Kama uko tayari niambie nimpigie simu hapa hapa mbele yako, la kama unadhani hauko tayari pia niambie nimweleze sasa hivi,” Mafuru aliongeza huku macho yake yakiwa yameweka kituo kwenye uso wa Madame Norah.



    Madame Norah alishusha pumzi za ndani kwa ndani, alikaa kimya kwa takriban dakika mbili akifikiria sana bila kupata majibu.



    “Unaweza kunidokeza, ni mambo gani hayo ambayo unayajua lakini mimi siyajui?” hatimaye Madame Norah alivunja tena ukimya, alikuwa bado ana wasiwasi.



    “Ni mambo mazito ambayo hayahitaji kuzungumzwa hapa na wala nisingeweza kukueleza kwenye simu. Ni wewe, yeye na mimi tu tunaopaswa kuendelea kuyajua kwa sasa, labda hadi hapo baadaye kama itahitajika,” Mafuru alisisitiza.



    “Okay, nipo tayari kuonana naye Paradise Club saa kumi na mbili jioni,” Madame Norah alisema na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.



    * * * * *



    Saa kumi jioni, Winifrida Kolimba alikuwa anatembea kwa maringo yaliyoonekana wazi. Hayakuwa maringo ya kutafuta kiki bali alijua wazi alivyokuwa mrembo na wengi walimchukulia kama malaika aliyekuwa ameshushwa duniani kimakosa, hivyo kuonesha maringo ilikuwa ni kichagizo tu cha jinsi alivyo.



    Alikuwa na umbile dogo lililovutia mno na kuonekana wazi hata kama angevaa sare za shule, umbile lake lilimshawishi kila mwanamume aliyekamilika kumwangalia kwa uchu wa mahaba mazito. Ilikuwa vigumu sana kwa Winifrida kupita mbele ya mwanamume bila kukata shingo kumwangalia. Kiukweli alikuwa amezawadiwa urembo wa kutosha!



    Kwa umbile lake na ile miondoko ya maringo alizidi kutoa tafsiri ya kuwa na ule uzuri usiomithilika, hasa kwa sababu ya weupe wake wa asili usiochanganywa na vipodozi vya aina yoyote na hivyo kuwafanya wanaume wakware wachanganyikiwe, pasipo kujali kama alikuwa mwanafunzi.



    Jioni hiyo Winifrida alikuwa anatoka twisheni akiwa amevaa sketi ya rangi ya samawati, blauzi ya rangi ya pundamilia ya mikono mirefu na begi kubwa la madaftari alilokuwa amelibeba mgongoni, na alikuwa anatembea taratibu kando kando ya barabara iliyoelekea mtaani kwao eneo la Tabata Chang’ombe, jijini Dar es Salaam.



    Wanafunzi wengine waliokuwa wameongozana naye walikuwa wakimkodolea macho wakati akitembea taratibu huku akionekana kutokuwa na haraka. Ni kweli hakuwa na haraka maana safari yake ilikuwa inaishia mtaa ule ule.



    Mbele yake kulikuwa na wanafunzi wengine watatu wa kike walioonekana wakitembea kwa kujikongoja kutokana na uchovu. Wote walikuwa wamebeba mabegi makubwa yaliyowaelemea kwa uzito.



    Winifrida alikuwa akiwacheka na kuwafanyia mzaha. Mara kwa mara walikuwa wakigeuka kumtazama kwa hasira lakini yeye aliendelea kuwafanyia mzaha.



    Walionekana kumsubiri ili wampe ‘displini’ lakini yeye aling’amua na kusimama kupisha kwanza gari lipite kisha alivuka barabara kuwakwepa na kuelekea upande wa pili wa ile barabara, kwani alikuwa amefika usawa wa nyumbani kwao.



    Wale wanafunzi walikonyezana kisha wakavuka barabara kuelekea upande wa pili wakiwa na lengo la kutaka kumkamata lakini Winifrida aligundua hila yao na kukimbilia ndani huku akiendelea kuwafanyia mzaha.



    Alipoingia sebuleni, alijitupa kwenye sofa na kulibwaga begi lake juu ya sofa, kisha akajiegemeza kwa mgongo na kupeleka macho yake kuangalia juu ya dari huku akionekana kuwaza.



    Mara simu yake iliyokuwa kwenye begi la madaftari ilianza kutoa mtetemo uliomshtua sana, aliangalia huku na kule kuhakikisha hakukuwa na mtu yeyote aliyeshtukia kisha aliinuka haraka, akachukua begi lake na kukimbilia chumbani kwake.



    “Jacky, nilishakwambia usinipigie simu hadi nikubip… sasa hivi nipo nyumbani, tutaongea usiku,” Winifrida alisema kwa sauti ya kunong’ona mara tu alipoingia chumbani kwake, kisha aliikata ile simu na kuizima kabisa.



    Alizungusha macho yake kukitazama kile chumba chake kwa makini, kilikuwa kikubwa kikiwa na kitanda kikubwa cha samadari cha futi sita kwa sita, cha mbao ngumu za mninga kikiwa na droo mbili kila upande na juu ya droo hizo kulikuwa na taa mbili zilizotoa mwanga hafifu.



    Kilikuwa na kabati la nguo la ukutani na pembeni ya lile kabati kulikuwa na meza ya vipodozi yenye kioo kirefu cha kujitazama. Chumba pia kilikuwa na madirisha mawili mapana yaliyofunikwa kwa mapazia marefu yenye nakshi za michoro ya maua yaliyodariziwa vizuri na kuyafanya yapendeze.



    Winifrida alijibwaga juu ya kitanda kilichokuwa kimetandikwa vizuri kwa shuka la rangi ya waridi lililofumwa maua katikati akionekana kuchoka, kisha akajilaza chali, miguu kaining’iniza sakafuni na kushusha pumzi. Sasa alionekana kujiwa na mawazo, aligaragara juu ya kitanda kile, kisha aliuchukua mmoja wa mito miwili iliyovikwa foronya rangi moja na ya lile shuka na kuukumbatia halafu akajilaza kifudifudi.



    Hapo tena fikra zilianza kutembea kichwani mwake na kuaza kujiuliza vipi angeweza kuendelea kuvikabili vishawishi kutoka kwa wanaume wakware waliokuwa wakimwita kila alikopita? Na vipi angeweza kuyakabili mapenzi ya kijana Jackson yaliyoanza kumwingia moyoni na kuitawala akili yake ilhali yu bado mwanafunzi?



    Alifikiria kwa kitambo kidogo huku fikra zikizidi kuranda na kupigana vikumbo ndani ya kichwa chake, mara aligutuka na kunyanyuka kutoka pale kitandani. Sasa mawazo yote aliyokuwa nayo yalipeperuka kwa muda na kuanza kuvua zile nguo alizovaa.



    Alipogeuka alikikabili kile kioo kirefu cha kujitazama kilichopachikwa kwenye meza ya vipodozi, na kama kioo kile kilikuwa kikimtua, aliinuka na kukisogelea. Alianza kujianglia kwenye kioo namna alivyoumbika. Alijitazama na kujitazama tena, halafu akageuka na kujitazama huku na huku na alipohisi hajajifaidi bado, alikwenda kufunga mlango.



    Alisimama mbele ya kioo akaendelea kuvua nguo zake na kubakiwa na chupi tu. Alijishika kiunoni kwa mikono yake na kujitazama tena huku na huku. Alijigeuza nyuma na kujiangalia matiti yake na kuyatomasatomasa huku akiyachezea.





    Alijigeuza tena mbele na nyuma na mara kwa ghafla, kama mtu aliyeshtuliwa, aliondoka mbele ya kioo na kufungua kabati la nguo, alitoa sketi fupi ya pundamilia na blauzi nyepesi nyeusi, akavaa haraka na kutoka.



    * * * * *



    Kwenye ukumbi wa kisasa wa chakula katika mgahawa wa Elli’s, Sammy na Elli walikuwa wameketi kwenye kona moja ukumbini wakinywa sharubati na kuongea. Sammy alikuwa na wasiwasi kuhusu namna ambavyo angemkabili mkewe kumweleza suala la kununua gari, kwa kuwa hakuwa amemshirikisha tangu mwanzo.



    “Ukweli hata mimi najiuliza, utamwelezaje mkeo, kwamba hili gari umelipataje?” Elli alimuuliza Sammy huku akimtazama kwa makini.



    “Hata sijui, maana ataniuliza kwa nini hatukushauriana kwanza kabla sijalinunua!” Sammy alisema huku akishusha pumzi.



    “Kwa hiyo bado utaendelea kumficha kuhusu matatizo ya kazini kwako?” Elli alimuuliza Sammy huku akimkazia macho.



    Sammy aliachia tabasamu, akashusha pumzi za ndani kwa ndani na kuzungusha macho yake mle ukumbini, aliwaangalia kwa muda wateja wachache waliokuwemo mle ndani muda huo, kisha akatoa leso mfukoni na kufuta paji la uso wake.



    “Sidhani kama bado nahitaji kumficha ukweli, nimefikia uamuzi wa kumweleza kila kitu leo, natumai atanielewa,” Sammy alisema na kumeza mate kutowesha koo lake.



    “Ni bora ufanya hivyo, maana hizi ni changamoto tu katika maisha na kila mtu humtokea, isitoshe mkeo ni mwelewa sana,” Elli alisema huku akibetua kichwa chake akionesha kukubaliana na Sammy.



    “Kumficha mkeo ni kuruhusu matatizo zaidi yaibuke ndani ya ndoa yenu, hasa pale atakapokuja kujua kuwa ulimficha. Si hivyo tu, anaweza kunichukia hata mimi kwa kudhani nilikupotosha. Kwa hiyo jaribu kuweka mambo wazi ili mjadili na msonge mbele,” Elli alisisitiza na kumfanya Sammy ashushe pumzi.



    “Sasa vipi kuhusu suala la vibali? Nataka gari lianze biashara mara moja.”



    “Suala la vibali niachie mimi, hilo limo ndani ya uwezo wangu. Ninaye mtu kwenye mamlaka husika, ni ndani ya siku tatu tu kila kitu kitakuwa kimekamilika,” Elli alisema akimhakikishia Sammy. Na hapo tabasamu pana likachanua kwenye uso wa Sammy.



    * * * * *



    Saa kumi na mbili kamili Madame Norah aliwasili katika viunga vya Paradise Club akiwa ndani ya gari lake aina ya Mercedes Benz E-Class la rangi nyeusi. Aliingia baada ya kuvuka vizuizi vitatu vyenye ulinzi wa uhakika.



    Alikuwa amevaa suti nadhifu ya kike ya rangi ya kijivu iliyokuwa imemkaa vyema na kumpendeza, begani alitundika mkoba mzuri wa nguo ya pundamilia uliomgharimu fedha nyingi na viatu vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio.



    Mkono wa kushoto alikuwa amevaa bangili nyingi za pembe na mkono wake wa kulia alivaa saa ghali ya kike aina ya Cartier La Dona iliyotengenezwa kwa dhahabu nyeupe ya karati 18, ikiwa na gerentii ya miaka hamsini.



    Aliambatana na wanaume wawili wenye miraba minne, walinzi wake waliokuwa wamevaa suti maridadi nyeusi, miwani mikubwa myeusi iliyofunika macho yao na miguuni walikuwa wamevaa buti ngumu nyeusi za ngozi imara ya mamba.



    Madame Norah na walinzi wake waliwasili na kupokewa na Mafuru aliyekuwa akiwasubiri muda wote katika viunga vya maegesho ya Paradise Club, kisha aliwaongoza kuelekea ghorofani kwa Mr. Oduya.



    Kama kawaida, wale walinzi hawakuwaruhusu wapite hivi hivi bila kukaguliwa, japo walikuwa na taarifa zao, waliwakagua na kuhakikisha hawakuwa na silaha au kitu chochote hatarishi walichobeba, kisha waliwaruhusu wapite.



    Mafuru aliwaongoza kuingia katika sebule kubwa walikomkuta Mr. Oduya akiongea na simu lakini mara tu alipowaona alisitisha mara moja maongezi na mtu aliyekuwa akiongea naye kwenye simu na kusimama kwa heshima kumlaki Madame Norah, huku uso wake ukipambwa na tabasamu la bashasha.



    “Madame, karibu sana Paradise Club,” Mr. Oduya alisema huku akimpa mkono Madame Norah.



    “Ahsante sana mheshimiwa Rais mtarajiwa,” Madame Norah alisema kwa utani na kuwafanya wote waangue kicheko.



    “Mdomo wako uwe wa heri, na iwe kama usemavyo,” Mr. Oduya alisema huku akiendelea kucheka kwa furaha kisha aliwaelekeza wageni wake sehemu ya kuketi.



    “Madame ni furaha yangu kukutana nawe siku ya leo na kabla ya yote

    ninapenda kwanza kusema ahsante sana kwa kukubali mwaliko wangu wa kutaka kuonana nawe jioni hii,” Mr. Oduya aliongeza baada ya wote kuketi kitako.



    “Kiukweli mwaliko wako umenishtua sana,” Madame Norah alisema huku akimtazama Mr. Oduya kwa makini.



    “Najua, hata hivyo mimi ni nduguyo kabisa, tena ndugu wa damu…”



    “Undugu huo veepe, mbona sikuelewi! Wewe Jaluo na mimi Mbondei wapi na wapi!” Madame Norah alisema huku akiendelea kumtazama Mr. Oduya kwa makini zaidi.



    “Ni ndugu kwa kuwa wote ni Watanzania, hata hivyo kabla ya yote sijui mtatumia vinywaji gani?” Mr. Oduya aliuliza huku akiwatazama kwa zamu.



    “Nadhani ungeeleza kwanza ulichoniitia, suala la vinywaji siyo lililonileta hapa,” Madame Norah alisema huku akionekana kuwa makini zaidi, hakuwa na muda wa kupoteza.



    “Okay, sitaki nichukue muda mrefu sana wa kuongea nawe… kwa kifupi nimefuatilia baadhi ya shughuli unazozifanya na nimejikuta nikiguswa sana. Hongera sana kwa kujitoa kusaidia jamii, ni wengi tunajaribu kufanya kama unavyofanya lakini wengi hatufanyi kwa kujitolea kama unavyofanya. Nimeguswa zaidi na hiki ulichoamua kukianzisha sasa…” Mr. Oduya alisema na kunyamaza kidogo. Madame Norah alibaki kimya akimsikiliza lakini akiwa makini kuliko simba jike.







    “Najua huamini hiki ninachosema, lakini sote lengo letu ni moja tu, kuisaidia jamii yetu ingawa ni kwa njia tofauti kidogo. Kwa hiyo ninataka tushirikiane katika suala hili ili wewe upate fedha za kusaidia wahitaji na mimi inisaidie katika kampeni yangu ya kuwania urais,” Mr. Oduya alisema kwa sauti tulivu.



    “Hilo haliwezekani Mr. Oduya. Siwezi kuwa na ushirika na wewe,” Madame Norah alisema huku akitingisha kichwa chake taratibu.



    “Kama unadhani hilo haliwezekani then you’re very wrong, my dear,” Mr. Oduya alisema huku akitabasamu.



    “I’m not wrong, Siku zote niko sahihi kwenye masuala yanayohusu mustakabari wangu,” Madame Norah alisema kwa kujiamini huku akiwa amekunja sura yake.



    “Lakini hilo ni jambo la kwanza kuna jambo la pili litakalokusisimua zaidi, ninakwenda kukuonesha kitu ambacho you’ve been dying to see,” Mr. Oduya alisema na kuinuka huku akimtaka Madame Norah naye ainuke. Muda huo huo walinzi wa Madame Norah nao wakainuka wakiwa tayari kwa lolote. Mr. Oduya aliwageukia huku akiachia tabasamu.



    “Mnaweza tu kusubiri hapa, she’ll be fine,” Mr. Oduya alisema lakini wale walinzi walionesha kutokukubaliana naye.



    “Msijali, hawezi kunifanya kitu chochote kibaya,” Madame Norah aliwaambia walinzi wake, wakaonekana kumtii kisha alimfuata Mr. Oduya kuelekea chumbani huku wakiwaacha walinzi wake na Mafuru pale sebuleni. Mlango wa chumbani ulifunguliwa, wakaingia.



    Madame Norah alisimama ghafla akiwa anashangaa, alikuwa anatazamana na mwanadada mrembo aliyekuwa ameketi kitandani huku machozi yakimbubujika machoni kwake utadhani mirija ya machozi ilikuwa imepasuka.



    Madame Norah alimtazama kwa makini Zainab, alihisi kumfahamu ingawa hakujua walikutana wapi, aligeuka kumtazama Mr. Oduya huku akiendelea kujiuliza ni wapi alikutana na mrembo yule kwani sura yake haikuwa ngeni kabisa machoni kwake.



    “What is the meaning of this, Mr. Oduya?” (Hii maana yake nini, Oduya?) Madame Norah alimuuliza Mr. Oduya kwa mshangao akiwa haelewi kilichokuwa kikiendelea.



    “Mi’ nilidhani ungefurahi baada ya kukutana na huyu mtu, kwani ulikuwa unaomba usiku na mchana ukutane naye, au siyo!” Mr. Oduya alimwambia Madame Norah huku akitabasamu.



    “Ni nani, mbona kama…!” Madame Norah alitaka kusema huku akimwangalia Zainab kwa makini lakini hakumalizia sentensi yake kwani Zainab alishindwa kujizuia, alimrukia Madame Norah na kumkumbatia kwa nguvu huku akizidi kububujikwa na machozi.



    “Dada Nuru!” Zainab alisema huku akilia kwa furaha na kuzidi kumng’ang’ania Madame Norah aliyekuwa bado amepigwa na butwaa.



    “Kwa-ni wewe n-ni nani?” Madame Norah aliuliza huku akijaribu kujinasua kutoka kwenye mikono ya Zainab aliyeendelea kulia kwa uchungu huku akiwa hataki kumwachia.



    “Mimi Zainab Semaya, mdogo wako!” Zainab alisema huku akilia.



    “Zainab who! Oh my God!” Madame Norah alimaka kwa mshangao mkubwa sana. Hakuwa ametegemea kabisa kuonana na Zainab baada ya miaka mingi kupita.



    Madame Norah hakuweza kujizuia, donge la fadhaa lilimkaba kooni, alijikuta akisononeka sana rohoni, mara kikohozi kidogo kilimtoka na nyuma yake wimbi la machozi lilikuja mbio, alijikuta akilia sana huku akimkumbatia Zainab.



    Kwa muda wa dakika kadhaa hali ndani ya chumba kile iligeuka kuwa sehemu ya vilio, wote walijikuta wakilia pasipo kupenda. Baada ya kitambo fulani Madame Norah alimwachia Zainab na kufuta machozi yake, kisha alimwangalia kwa makini.



    “Kweli wewe ni Zainab, sura yako haijabadilika kabisa!” Madame Norah alisema huku akishusha pumzi ndefu. Zainab alibaki kimya, alikuwa anafuta machozi.



    “Nadhani sasa niwaache, kwa vyovyote mtakuwa na mengi ya kuzungumza,” Mr. Oduya alisema huku akiachia tabasamu, kisha akaanza kupiga hatua kutoka, alipoufikia mlango aligeuka kumtazama Madame Norah.



    “Nadhani sasa huna sababu ya kukataa kushirikiana na mimi,” alisema na kufungua mlango, akatoka na kuurudisha nyuma yake.



    * * * * *



    Winifrida alikuwa amesimama kwenye karo la kuoshea vyombo, alikuwa akisuuza vyombo viwili vitatu alivyolia chakula na kuweka mabaki ya vyakula kwenye chombo maalumu cha kuhifadhia uchafu. Alionekana kuwaza mbali sana.



    Pendo alikuwa ananyata nyuma yake kwa tahadhari kubwa akitaka kumshtua lakini Winifrida alihisi uwepo wa mtu nyuma yake, aligeuka haraka lakini Pendo aliwahi kujificha huku akitabasamu.



    Winifrida alipuuza na kuendelea kusuuza vyombo. Pendo alijitokeza tena na kuanza kunyata taratibu kumsogelea, Winifrida aligeuka haraka huku akikodoa macho yake kwa hofu na kumuona Pendo akiwa takriban hatua tatu nyuma yake.



    “Mtu mwenyewe hujui hata kunyatia,” Winifrida alisema huku akiachia kicheko hafifu.



    “Eeh umeogopa! Umeogopa!” Pendo alisema kwa sauti ya juu huku akicheka kisha aliondoka na kuelekea ndani akimwacha Winifrida anamalizia kusuuza vyombo huku akionekana kuwaza mbali.



    Joyce alitokea na kusimama mlangoni, akamtazama Winifrida kwa makini. Macho yake yalikuwa yakikitazama zaidi kifua cha Winifrida aliyekuwa amevaa blauzi nyepesi nyeusi na sketi fupi ya pundamilia.



    Blauzi ya Winifrida ilikuwa imeloa maji kidogo eneo la kifuani na kuzifanya chuchu zake zilizochomoza juu ya matiti yake magumu ya mviringo ndani ya blauzi nyepesi aliyovaa kiasi cha kuvuta hisia za watu zionekane waziwazi.



    “Wee Winnie,” Joyce alimwita Winifrida na kumshtua sana.



    Winifrida aliiachia bilauri aliyokuwa akiizuuza kwa mshtuko, ikaanguka sakafuni na kupasuka. Aligeuza shingo yake kutazama kule mlangoni ambako sauti ya Joyce ilitokea na macho yake yaligongana na macho ya Joyce aliyekuwa amesimama akimtazama kwa makini.



    “Umenishtua sana, wifi. Nilisikia moyo umefanya, pah!” Winifrida alilalamika huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani. Aliyaondosha macho yake kwa aibu huku akiachia tabasamu la aibu.



    “Kwa nini umeshtuka sana! Kwani ulikuwa unawaza nini?” Joyce alimuuliza Winifrida huku akimkazia macho.



    “Aka! Nilikuwa siwazi chochote!” Winifrida alijitetea huku akionekana kutaharuki kidogo. Alimtazama wifi yake kwa jicho la wizi na kugundua kuwa alikuwa bado akimtazama kwa makini.







    “Kwani kuna nini, wifi?” Winifrida aliuliza huku uso wake ukionesha wasiwasi.



    “Usihofu, wifi yangu, kama umemaliza kuosha vyombo njoo sebuleni, nataka tuongee mambo ya kawaida tu yanayokuhusu. Hatujawahi kukaa tukazungumza vizuri,” Joyce alisema kwa sauti tulivu ya upole huku akiachia tabasamu.



    “Sawa, wifi,” Winifrida alisema huku akiendelea kuwa na wasiwasi, hakujua wifi yake alitaka kumwambia nini. Alikusanya vyombo vyake na kuelekea ndani.



    Baada ya dakika chache, Winifrida na Joyce walikuwa wameketi sebuleni, peke yao tayari kwa mazungumzo. Joyce alikuwa amemuondoa Pendo na kumtaka akacheze nje.



    “Sasa, Winnie, unafahamu kwamba hivi sasa wewe ni binti uliyepevuka,” Joyce alisema huku akimtazama kwa makini.



    Uchangamfu aliokuwa nao Winifrida ulitoweka ghafla na akawa makini akionesha woga kiasi. Alikaa kimya, Joyce alimkazia macho kwa makini.



    “Nadhani unaelewa?” Joyce alimuuliza huku akizidi kumkazia macho.



    Winifrida alibaki kimya akiangalia viganja vyake alivyoviweka juu ya mapaja yake. Joyce aliiona hali ya Winifrida kwa jinsi alivyoingiwa na hofu, alitabasamu na kutafuta namna ya kuyaelekeza mazungumzo.



    “Nimekwambia usihofu, wifi yangu, nataka nikwambie hivi, mwili wako sasa una mabadiliko makubwa sana. Umekua,” Joyce alisema na kunyamaza kidogo akiendelea kumtazama Winifrida kwa makini.



    Winifrida alivuta pumzi ndefu na kifua chake kikapanda na kushuka. Alitabasamu kidogo kwa ahueni huku akimtupia jicho la wizi wifi yake.



    “Najua umeshawahi kuona tofauti mwilini mwako, au siyo?” Joyce alimuuliza Winifrida kwa namna ya kubembeleza alipoona yupo kimya.



    “Naziona, wifi,” Winifrida alijibu kwa sauti ya chini.



    “Kama zipi?” Joyce aliuliza huku macho yake yakiweka kituo kwenye uso wa Winifrida.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Wifi bwana!” Winifrida alisema kwa aibu huku akitazama sakafuni.



    “Usiniogope, hapa tupo wawili tu, mimi na wewe, na wote ni wanawake. Huna sababu ya kunionea aibu, wifi yangu,” Joyce alisema kwa sauti tulivu ya upole.



    “Sawa, wifi,” Winifrida alijibu na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Sawa, tufanye kwamba umeziona hizo tofauti, je, unachukua hatua gani kuzikabili?” Joyce aliuliza tena kwa upole.



    “Hatua?” Winifrida aliuliza kwa mshangao huku akimtazama Joyce kutaka ufafanuzi wa neno hilo.



    “Labda niulize hivi, ni mambo gani unakumbana nayo kila siku unapokuwa shuleni au ukiwa njiani?” Joyce alijaribu kufafanua.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog