Simulizi : Fumbo La Utambuzi
Sehemu Ya Pili (2)
Asubuhi ilimkuta Tom akiwa bado yupo kwenye kochi, aliinuka na hakutaka kwenda kuoga, alichofanya alibadilisha tu nguo na kuelekea kazini kwake. Njia nzima alikuwa anayafikiria matukio ya siku iliyopita na tukio alilokuwa analisubiri ni tukio la kutangaza kupinduliwa nchi.
Tom aliingia ofisini kwao na kila mfanyakazi alikuwa anamuangalia kanakwamba kuna kitu kilimtokea, wengine wenye mepesi walidiriki hadi kumpa pole, Tom aliitikia huku akiendelea kuishangaa hii miujiza inayomtokea na wala hakujua hizo pole anazopewa ni za nini.
Tom alielekea moja kwa moja mpaka kwenye ofisi ya bosi wake Othman Tafu na kuingia bila hodi, Othman Tafu alipoinua macho akashtuka,
"Aisee upo salama kweli?" Othman Tafu alimuuliza Tom huku akimkagua kwa macho,
"Niko salama mkuu, ila salama kiasi" Tom alijibu huku akikaa katika kochi,
"Kwanza pole" Othman Tafu aliongea na kufanya Tom ashangae,
"Pole ya nini?" Tom aliuliza,
"Usijifanye hujui, sisi tumeletewa habari zako zote" Othman Tafu aliongea na moyo wa Tom ukapiga kwa wasiwasi kwa maana alijua tayari ile video yake ya kule msituni imevuja,
"Habari gani?" Tom alijikaza na kuuliza,
"Kuna Dada alikuja hapa jana na kusema kuwa wewe unashikiriwa na usalama wa Taifa kwa kosa la uchochezi, ni kutokana na tangazo lako tulilolirusha jana kutwa nzima na ametuonya hilo tangazo lisitishwe kurushwa na sisi tumepewa muda wa wiki nzima wa kuomba msamaha na kukanusha kuhusu hiyo habari, na wewe usimamishwe kazi" Othman Tafu alimwambia Tom,
"Huyo Dada aliyekuja yupoje?" Tom aliuliza,
"Mweusi alafu mrefu, nywele zake ni fupi na akiongea mashavu yake yanabonyea" Othman Tafu alitoa maelezo ambayo hayakumuumiza kichwa Tom kujua kuwa huyo dada ni BQ,
"Ndio yeye" Tom aliongea peke yake bila kujua hiyo sauti yake imesikiwa na Othman Tafu,
"Ndio yeye nani?" Othman Tafu aliuliza,
"Usalama, Dada wa usalama wa Taifa" Tom aliamua kudanganya kwa maana aliona akisema ukweli inaweza kumuingiza matatani na washenzi kwa maana wana mtandao mkubwa,
"Sasa Tom itabidi usimamishwe kazi, ila mshahara wako nitakuwa nakupa ila hutakiwi kufika eneo hili la ofisi" Othman Tafu alimwambia Tom, na kumfanya Tom ainame akiwaza,
"Sawa, nimekuelewa" Tom alijibu kwa unyonge,
"Mimi najua lengo lako lilikuwa zuri, ulikuwa unapigania radio yetu ipate jina, ulikuwa pia unapigania nchi yako, ni jitahada nzuri, jitihada binafsi, na nimetambua kile ulichokuwa unakifanya na ndio maana nakusimamisha kazi huku ukiendelea kupokea mshahara" Othman Tafu aliongea huku akimpiga piga begani Tom ambaye kipindi hicho mawazo yake haya kuwa hapo, alichokuwa anakifikiria ni hatma ya ile video,
"Nashukuru kwa kutambua jitihada zangu" Tom alijibu kwa unyonge,
"Sasa Fanya kama serikali inavyotaka, achana kabisa na hizo habari za kufuatilia mambo yao, kipindi hiki ambacho nitakusimamisha kazi, kitumie ukiwa Morogoro kwa wazazi wako" Othman Tafu alimshahuri Tom,
"Nimekuelewa mkuu" Tom alijibu,
"Kamata hii bahasha ina barua yako ya kusimamishwa kazi na pia kuna pesa kidogo za nauli na za kujikimu siku mbili tatu" Othman Tafu aliongea huku akimpa Tom bahasha nyeupe yenye ukubwa wa wastani,
"Sawa nashukuru" Tom aliongea huku akiipokea ile bahasha,
"Sasa nenda ukapumzike, chochote kitakachokutokea nijulishe, na ukiwa na shida nijulishe pia" Othman Tafu alimwambia Tom,
"Sawa, nashukuru kwa kunijali" Tom aliongea kisha akasimama na kutoka nje kwa lengo la kurudi geto kwake.
Njiani alikuwa anashangaa ni kwanini mpaka muda huo hakuna habari yoyote iliyotangazwa kuhusu Rais? akawa anajipa moyo kuwa bora chochote kisitangazwe kwa maana itakuwa nafuu kwake.
Tom alifika kwake na kutoa ufunguo mfukoni kisha akaufungua mlango wake na kuingia ndani, akakutana na ajabu jingine, yule mtu asiye na nguo aliyekuwa anamfuatilia usiku uliopita alimkuta akiwa chumbani kwake, safari hii alikuwa amevaa nguo na amekaa kitandani kwa Tom, tena eneo lile lile alilokuwa amekaa usiku uliopita,,,,,,,,,,,,,.........
Safari hii Tom alisimama pale pale mlangoni, hakutaka kukimbia, akaganda mlangoni na huku macho yake akiwa amemkazia yule mtu,
"Wewe ni nani?" Tom alimuuliza kwa sauti kali na ya juu, lakini yule mtu hakumjibu,
"Si nakuuliza wewe ni nani?" Tom aliuliza tena huku akiwa amesimama pale pale mlangoni na kipindi hiki yule mtu hakujibu na badala yake akawa anamuangalia tu Tom na hapo ndipo Tom akagundua kitu kipya kwenye macho ya yule bwana, mboni zake za macho zilikuwa za bluu kama miale ya moto mkali, blue ile iliyopauka.
"Wewe vipi, mbona unaongea kwa sauti kubwa hivyo?" Sauti toka nje iliuliza na kumfanya Tom ageuke,
"Si yule mtu niliyekwambia amenitokea jana usiku, nimemkuta ndani kwangu sasa hivi na mlango nilikuwa nimeufunga" Tom alimjibu jirani yake huku akigeuka kumtazama,
"Ebu sogea nimuone" Jamaa aliongea huku akiingia ndani kwa Tom lakini hakumkuta mtu, hata Tom mwenyewe alishangaa baada ya kutomuona tena yule mtu,
"Yuko wapi sasa?" Jamaa aliuliza huku akimuangalia Tom,
"Alikuwa hapo" Tom akajibu huku akinyooshea kidole eneo ambayo yule kiumbe alikuwa amekaa,
"Hizi bangi za kuvuta ukiwa umejificha, ndiyo madhara yake hayo" Jamaa aliongea huku akitoka nje, alihisi Tom amechanganyikiwa kwa maana hata usiku uliopita alimsumbua hivyo hivyo.
Tom alisimama kwa muda pale mlangoni, na mwisho akaamua aingie ndani ila mlango aliamua auache wazi ili kujihami endapo kuna chochote kibaya kitamtokea, kwa maana yule mtu alishaanza kumtisha.
Sasa Tom aliamua atulize mawazo ili ajue cha kufanya katika muda wote ambao atakuwa hana kazi, akaikumbuka ile bahasha aliyotupiwa na Tammy Semmy, akaifuata na kuifungua, akaikuta ina pesa nyingi tu za kutosha, sasa wazo lililomjia ni kutoka nje ya nchi, alipanga kwenda Kenya kupumzika, aliona bora akakae Kenya ili awe jirani na aweze kuzipata kiurahisi habari zote zitakazojiri nchini kwake, rasmi sasa Tom alipanga kuondoka na muda huo alinyanyuka na kuelekea uwanja wa ndege kwa ajili ya kukata tiketi, na bahati ilikuwa kwake, alipata tiketi ya ndege ya mchana wa siku inayofuata, akarudi nyumbani na kutayarisha nguo za safari.
***************************
Huku upande wa serikali napo mambo yalikuwa sio mambo tena, habari mbaya ilikuwa inasambaa kwa kasi sana, habari ambayo ilisemekana Rais hajulikani alipo, hata familia yake nayo ilidai haijui alipo baba yao. Fumbo kubwa likawa ni kujiuliza ni wapi alipo Rais?
Serikali nzima ilikutana kwenye kikao cha dharula ambao kilimjumuisha makamo wa Rais, Waziri mkuu, mkuu wa majeshi na spika wa bunge na ajenda iliyowekwa mezani ilikuwa ni lile lile swali, wapi Rais alipo?
Kipindi chote cha mjadala huo uliohusisha watu hao wazito ndani ya nchi, hakuna aliyekuwa anajua ni kipi kilichomkuta Rais, isipokuwa Tammy Semmy ambae alikuwa ni makamo wa rais ambae naye alijifanya hajui lolote na muda wote alikuwa ana sura ya huzuni na kufanya watu waliopo kwenye kikao hicho wampoze kila dakika.
Kikao hicho kilidumu kwa muda wa saa nzima na nusu na uamuzi uliofikiwa ni kuwa nchi ishikiliwe na makamo wa Rais bwana Tammy Semmy kwa muda wote ambayo Rais atukuwa bado hajapatikana, hiyo ilikuwa ni faraja kwa Tammy Semmy kwa maana ndio ilikuwa lengo lake na baada ya hapo alikuwa ameshajipanga kuchukua madaraka ya moja kwa moja, alishawaandaa watu katika chama ili wampigie kura ya kuwa na imani naye ili apewe kibali cha kugombea urais, na alijipanga kupita katika kila hatua ya uchaguzi kuanzia chama mpaka uchaguzi wa nchi na hii ni kutokana na fedha alizokuwa nazo.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Pia kikao kile kiliamua kuwa jukumu la kutafuta wapi Rais alipo ni lazima libebwe na usalama wa Taifa na liwe siri, hakuna kutangaza kama rais amepotea na wala hakuna kutangaza kuwa Rais anatafutwa. Baada ya hapo kikao kikafungwa na wote wakatawanyika, sasa nchi rasmi ilikuwa kwa bwana Tammy Semmy, mtu aliyeitafuta hiyo nafasi kwa muda mrefu na sasa aliipata.
Tammy Semmy alipotoka kwenye kikao aliondoka kwa majonzi na kuelekea moja kwa moja kwenye ofisi ya rais, aliingia ndani na kujifungia ndani kisha akaanza kucheza kwa furaha kwa maana kwa asilimia kubwa alifanikisha hadhma yake. Alipomaliza kucheza alichukua makabrasha ya siri ya Rais na kuanza kuyasoma, makabrasha aliyoyachukua ni yale yaliyohusu mustakabali wa nchi na kuyapitia ambapo hakuona baya lolote, kisha akachukua linalohusu biashara na uchumi wa nchi, hapo ndipo alipoona mabaya mengi, lakini yalikuwa mabaya kwa upande wake, kwa mustakabali wa nchi yalikuwa ni mazuri tu. Alichotaka yeye Tammy Semmy ni biashara zote zitawaliwe na rafiki zake na zile za serikali azichukue yeye ili ziwe zake, hakutaka nchi iwe na uwezo wa kujiendesha yenyewe ila alitaka iwe tegemezi kwa baadhi ya watu wenye uwezo ambao kati yao walikuwa marafiki zake.
Alizipitia zile kabrasha kwa umakini na mwisho alizifunga, akanyanyuka na kuelekea yalipo makao makuu ya usalama wa Taifa na alipofika alipokelewa kwa heshima zote, akaambatana na mkuu wa usalama wa Taifa mpaka katika ofisi hii ya mkuu wa kitengo hiki, huyu alikuwa ni kibaraka wake. Walipoingia ndani ya ofisi walikumbatiana,
"Umefanya kazi nzuri mkuu, hongera sana" Mkuu wa usalama alimpongeza Tammy Semmy,
"Na wewe nakushukuru sana kwa kila hata uliyokuwa unapiga katika kuwafuatilia waliokuwa wakinifuatilia mimi" Tammy Semmy aliongea huku akitabasamu,
"Na nilifanya hivi kwa ajili ya wanangu na ndugu zangu, nataka waishi maisha mazuri ya kuogelea kwenye bahari ya hela" Mkuu wa usalama aliongea na kisha wakacheka sana,
"Ahadi yangu ni ile ile, nitakupa uwaziri wa mambo ya nje, cha muhimu utachoangalia ni jinsi ya kujinufaisha wewe, wananchi utakuwa unawadanganya kwa mambo madogo madogo tu" Tammy Semmy alimwambia mkuu wa usalama,
"Sasa si itabidi nigombee ubunge, nikishindwa itakuwaje?" Mkuu wa usalama aliuliza huku akicheka,
"Kushindwa hauwezi kwa maana mtandao wetu ni mkubwa na una nguvu, na kama ikitokea umeshindwa, nitakupa ubunge wa kukuteua, kwa hiyo utakuwa mbunge wa kuteuliwa" Tammy Semmy aliongea na wote wakacheka,
"Haya niambie mheshimiwa rais, ni kipi kinaendelea uko juu?" Mkuu wa usalama alimuuliza Tammy Semmy,
"Aisee nimekuja kukupa habari ya kikao tulichofanya leo na Waziri mkuu, mkuu wa majeshi na spika wa bunge, tulichodhamiria ni kuwapa nyie mfuatilie ili kujua ni wapi Rais alipo" Tammy Semmy alimwambia mkuu wa usalama,
"Wangejua kuwa hata wewe unajua ni wapi rais alipo, wala wasingesumbuka kumtafuta" Mkuu wa usalama aliongea na kisha wakacheka,
"Vipi na yule dogo Muandishi aliyekuwa anafuatilia mambo yetu, mipango yake ikoje?" Tammy Semmy alimuuliza Mkuu wa usalama,
"Dogo yupo, naona hali imekuwa ngumu kwake na hapa alipo amekata tiketi ya ndege na anaondoka kesho mchana" Mkuu wa usalama aliongea,
"Hakikisheni haondoki na kitu chochote kile ambacho kinaweza kuja kutuletea utata mbele ya safari" Tammy Semmy alimwambia mkuu wa usalama,
"Mimi nadhani bora asiondoke, tumzuie tu kwa maana anapokuwa ndani ya mipaka ya nchi hii ndio inakuwa rahisi kumfuatilia" Mkuu wa usalama alimwambia Tammy Semmy,
"Hiyo ni wewe utakavyoamua, maana mambo ya kuwafuatilia hao wanaonusa mambo yetu, yako juu yako" Tammy Semmy alimwambia mkuu wa usalama,
"Basi usijali mkuu, hapa ni mwisho wake, nitahakikisha nakula nae sahani moja" Mkuu wa usalama aliongea na wakacheka kwa furaha,
..
"Sasa acha nikuache, niende nikaongee na vijana wangu" Tammy Semmy aliaga,
"Sawa bwana, mimi nakutakie tu mafanikio katika hilo jukumu lako jipya" Mkuu wa usalama aliongea na kisha Tammy Semmy akaondoka zake kuelekea kwenye nyumba anayokutana na vijana wake, kina BQ.
Alifika na kuingia ndani, aliwakuta Waziri wa ulinzi, wale mabaunsa wawili na BQ wakicheza mziki huku wakinywa pombe, walikuwa wanafurahia kutekeleza kazi ngumu ya kupindua nchi, Tammy Semmy nae aliwasalimu na akajumuika kucheza nao mziki, sasa wakati wakicheza mziki walisikia mtu akigonga mlango na haikuwa kawaida kwa maana hakuna mtu mwingine anaelijua eneo hilo hata Tom aliingizwa akiwa amefungwa usoni kwa hiyo halijui eneo hilo. Ile hodi iliyogongwa kwa nguvu ilifanya wapate uoga, mziki ukasimama,
"Kafungue" Tammy Semmy alimwambia BQ ambaye alienda kwa tahadhari huku bastola ikiwa mkononi, alipofika hakukuta mtu isipokuwa flash tu, akawaita wenzake na kushauriana waichukue ili wajue kuna nini ndani, wakaichukua na kuipachika katika flat screen kubwa iliyopo hapo ndani, ndipo waliposhuhudia lile tukio la kumuua rais, na zaidi katika hiyo video hakuwa Tom pekee yake, na wao walionekana vizuri........
.hapo wote wakashtuka
Hapo wote kihoro kikawaingia, kwa Mara ya kwanza ile video ikawatetemesha na kila mmoja akabaki kumuangalia mwenzake, kitumbua kiliingia mchanga. Tammy Semmy ndio homa ilimpanda zaidi kwa maana yeye ndio mfanyakazi pekee wa serikali aliyeonekana kwenye video hiyo,
"Kuna msaliti kati yetu?" Waziri wa ulinzi aliuliza huku akimuangalia Tammy Semmy,
"Sidhani kama hilo linawezekana, ila nahisi kuna mtu alitega kamera zake eneo lile" Tammy Semmy aliongea,
"Ilo nakataa, kwa maana niliweka ulinzi mimi mwenyewe hakukuwa na kitu chochote cha kutia shaka, maana nilikagua kila eneo na kila mti uliozunguka eneo lile na hakukuwa na camera wala kiashiria chochote cha utata" BQ aliongea na kufanya wote wakae kimya, walimuamini sana huyo dada kuliko walivyojiamini wenyewe,
"Au yule dogo alifanya ujanja ujanja wa kutega camera bila sisi kujua?" Tammy Semmy aliuliza,
"Hata mimi nahisi hivyo" Jimmy aliongea, huyu jimmy ni baunsa mmojawapo kati ya wale wawili waliokuwepo hapo,
"Sasa tufanyaje ili tuhakikishe hili?" Waziri wa ulinzi aliuliza,
"Dogo anatakiwa akamatwe na aletwe hapa" Tammy Semmy aliongea,
"Tena akamatwe usiku huu kwa maana kesho anasafiri mchana, anaenda Kenya" BQ aliongea na kumuangalia Tammy Semmy,
"Nenda kamlete" Tammy Semmy alitoa tamko BQ hakutaka kungoja neno, alitoka na kwenda zake kwa Tom, huyu binti alijiamini sana.
"Mbona mambo yanaanza kuharibika mapema hivi?" Tammy Semmy aliongea huku akiwa amejishika kiuno,
"Huyu Tom anatakiwa auawe kabisa, maana amepewa nafasi ya kuishi alafu anatutishia maisha" Waziri wa ulinzi aliongea kwa sauti iliyojaa hasira,
"Hata akiletwa hapa, hatakiwi kuuawa" Jimmy aliongea,
"Kwanini hasife?" Waziri wa ulinzi aliuliza,
"Inawezekana hii video ameshaisambaza, itabidi tumbane kwanza mpaka tujue ukweli ndio baadae auwawe" Jimmy alijibu,
"Ni wazo zuri" Waziri wa ulinzi aliongea,
"Ila mimi bado akili yangu haiamini kama huyu dogo ndio amefanya hivyo, nahisi kama kuna watu wa usalama ambao sio wa mtandao wetu wamefanya hii kitu" Tammy Semmy aliongea,
"Sidhani kama inawezekana, kama BQ alisimamia suala la ulinzi eneo lile, basi hakuna shaka kuwa kote kulikuwa salama" Waziri wa ulinzi aliongea,
"Sawa, sawa, sawa" Tammy Semmy aliongea huku akijitupa kwenye kochi, mambo yalishawaharibikia kwa upande wao na hawakuwa na chakufanya, malaika aliingia kwenye kambi ya shetani.
************************
Katika makao makuu ya polisi nako hali ilikuwa tete, polisi walipata habari ya kuwepo kwa eneo nje ya mji ambapo inasemekana kuna kitu kilikuwa kimefukiwa kwenye shimo hilo na hakuna ambae alijua ni kipi kimefukiwa.
Polisi waliondoka na gari lao huku wakiwa wamebeba vifaa vya kuchimbia, walifika mapema katika hilo eneo ambalo watu walitilia shaka na kisha wakaanza kuchimba, ilikuwa kazi ngumu kuchimba kutokana na eneo lile kuwa na tope za kutosha, walichimba kwa kujituma na kwa bahati nzuri waliweza kuona dalili za mafanikio baada ya kuuona mfuko mkubwa wa plastiki ukichungulia kwa juu.
Wakakaza mikono na kuendelea kuchimba mpaka ule mfuko ukafanikiwa kuonekana wote, wakautoa nje na kwa kuangalia tu kwa juu waliweza kujua kuwa ndani ya ule mfuko kuna mwili wa mtu, pia harufu kali ya uozo ilitoka ndani ya ule mfuko.
Askari mmoja kiongozi aliyeitwa Said Mbegu, ndio alipewa jukumu la kuongoza kikosi iko, huyu bwana ana cheo kidogo tu cha ukoplo, wenzie walipenda kumuita Koplo Mbegu.
"Ebu fungua huo mfuko" Koplo Mbegu alitoa amri na kisha askari wakaufungua huo mfuko na kukuta ni mtu ndiye aliyekuwepo ndani ya mfuko huo,
"Mh mbona kama...." Koplo mbegu aliongea huku akiutazama kwa makini uso wa ule mwili,
"Ni mheshimiwa huyu" Askari mmoja aliongea baada ya kumuona Koplo Mbegu amesita,
"Dah hii imekuwa hatari, hakikisheni mtu yoyote haongei suala hilo mpaka habari za daktari zithibitishe suala hili" Koplo mbegu aliongea kwa sauti ya chini kuwaonya askari wengine waliokuwepo hapo, alitumia Sauti ya chini kwa maana kuna watu wengine wa kijiji hicho walikuwepo wakishuhudia uchimbuaji huo wa lile shimo.
Askari wote walikuwa wamepoa kama wamemwagiwa maji baada ya wao wenyewe kuamini huo mwili ni wa mkuu wao wa nchi na hawakuona heshima kuubeba ule mwili kwenye gari lao la polisi, Koplo Mbegu alipiga simu hospitali na ikaja gari la wagonjwa maalum na kuubeba ule mwili wa Rais.
Huku hakuna askari aliyeongea, wakati wote walikuwa wakikagua lile eneo kila mahali na mwisho waliweka miti na kufunga kamba za njano kulizunguka lile eneo la shimo, ikiwa na maana kuwa lile eneo lipo chini ya uangalizi maalum wa vyombo vya usalama.
Baada ya hapo Koplo Mbegu aliondoka na jopo lake la Askari na kuwaacha wengine kadhaa wakiwa eneo hilo kwa ajili ya ulinzi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Koplo Mbegu safari yake ilifikia katika kituo cha polisi na hapo ndipo alipotakiwa kufika moja kwa moja ofisini kwa mkuu wake.
Koplo Mbegu alienda na kumkuta mkuu wake akiwa na mtu ambaye alikuwa mgeni machoni pake, Koplo Mbegu akapiga saluti,
"Kaa hapo" Mkuu wa polisi alimwambia Koplo Mbegu na akatii,
"Taarifa ulizoenda kukutana nazo uko tumezipata, ni taharifa mbaya kwa Taifa na inafanya mustakali wa nchi kuyumba. Huyu unaemuona hapo ni mkuu msaidizi wa idara ya usalama wa Taifa na amekuja kuomba askari mmoja wa kupewa jukumu hili la kufuatilia hii kesi na mimi nimekuchagua wewe" Mkuu wa polisi aliongea na kumfanya Koplo Mbegu ashtuke kidogo,
"Na hiki ninakuambia ni siri, hili tukio limegubikwa na sintofahamu nyingi sana kwa vigogo, maana inaonekana kuna mtandao mkubwa sana ambao bado kiongozi wake hajajulikana ndio umehusika au umepanga mauaji haya, cha msingi ni kwamba hili tukio unatakiwa kulifuatilia kwa siri, mtu au chombo chochote kile cha usalama hakitakiwi kujua kuhusu upelelezi wako. Una swali?" Mkuu wa polisi alimaliza na kisha akauliza,
"Kwanini umenichagua mimi na wakati sina uwezo na wala sijawahi kupewa tukio la kupeleleza?" Koplo Mbegu aliuliza kwa adabu,
"Kama nilivyokueleza hawali, kuwa kuna mtandao inawezekana umehusika na tukio hili, kwa hiyo inawezekana wanamtandao wapo miongoni mwetu sisi polisi, kwa hiyo mimi nimekuchagua wewe kwa sababu nakujua vizuri" Mkuu wa polisi alimaliza,
"Lakini mkuu..."Koplo Mbegu alitaka kuongea,
.
"Sihitaji neno kutoka kwako, Fanya kama nilivyosema, ni amri" Mkuu wa polisi aliongea kwa amri,
"Sawa mkuu" Koplo Mbegu alijibu kikakamavu huku moyoni akiamini ameonewa kupewa lile jukumu,
"Hakikisha kuwa kila hatua muhimu utakayoifanya, basi unanitafuta mimi au huyu bwana, atakupa namba zake" Mkuu wa polisi aliongea huku akimpiga piga begani mkuu msaidizi wa usalama wa Taifa,
"Sawa mkuu" Koplo Mbegu alijibu,
"Haya nenda" Mkuu wa polisi alimuamuru Koplo Mbegu na Koplo akaanza kuondoka,
"Mbegu" Mkuu wa polisi akamuita kabla Koplo Mbegu hajatoka,
"Naam mkuu" Koplo Mbegu aliitika kikakamavu,
"Hiyo kazi unatakiwa uanze muda huu, tumia akili zako zote ili mtu yoyote asigundue unachofanya" Mkuu wa polisi alimwambia Koplo Mbegu,
"Sawa mkuu" Koplo Mbegu alijibu na kutoka zake nje huku mawazo yakianza kuutafuna ubongo wake, mawazo ya kupewa jukumu zito wakati yeye aliamini uwezo wake ni mwepesi, mbaya zaidi hakujua wapi aanzie Koplo huyu mwenye cheo kidogo na asiye na uzoefu na matukio ya kipelelezi....
Koplo Mbegu uwa hapendagi kabisa kazi wala michezo ya kuumiza kichwa, alishazoea kutelekeza tu maagizo ya wakubwa zake.
Sasa hadi kufikia muda huu tayari ile kesi ilishakuwa ya pande tatu, upande wa kwanza ni upande wa Tom, upande wa pili ni Tammy Semmy na kundi lake, na upande wa tatu ni wa polisi ambao jukumu lao lilibebwa na Koplo Mbegu.
Koplo Mbegu alirudi nyumbani kwake, huyu Jamaa ni msela tu, amepanga nyumba za uswahilini na uwa anaishi peke yake, hana mke ila ana mtoto mmoja wa kike ambae anaishi kwa wazazi wa Koplo Mbegu.
Koplo Mbegu alipofika kwake alijihisi mchovu sana, uchovu uliotokana na mawazo ya kupewa jukumu zito la kupeleleza juu ya kifo cha Rais, na kikubwa kilichomuumiza ni lile katazo la kumshirikisha mtu juu ya jukumu alilopewa kwa maana aliamini yeye ni mchanga kwenye masuala hayo ya upelelezi, kwa hiyo ingemuwia vigumu kufanya kazi bila kumshirikisha mtu.
Wakati akiwa bado amekaa ndani kwake, wazo likamjia kuwa ni lazima arudi eneo la tukio kwa maana anaweza kupata kitu chochote cha kuanzia juu ya upelelezi wake. Akavua gwanda za polisi na kuvaa nguo za nyumbani kisha akatoka zake kwake kwa ajili ya kwenda katika eneo ambalo waliikuta maiti ya Rais, eneo hilo walilibatiza jina na kuliita eneo la tukio.
**************
Tom alikuwa chumbani kwake akipanga vizuri baadhi ya vitu vyake ili akiondoka aviache katika usalama, wakati akiendelea kupanga ndipo aliposikia mtu akigonga mlango wake, akasita kufungua akawa anauangalia tu, aliogopa kufungua kutokana na muda huu kutojiona hayupo salama kabisa,
"Nani?" Tom aliuliza lakini hakukuwa na jibu badala yake alisikia akipenyeza funguo katika tundu la mlango wake, akishangaa kuona mlango unafunguliwa ingali ufunguo upo ndani, akabaki ametoa macho huku akisubiri kuona kitakachotokea,
"Usiwe muoga kiasi hicho, unatakiwa ujiamini" BQ aliongea baada ya kusukuma mlango na kumfanya Tom ashtuke,
"Hamna, kujihami ni lazima" Tom aliongea huku akiwa anaougopa ujio huo wa usiku wa mwanadada huyo katili,
"Mbona unapanga panga vitu, una safari ya wapi?" BQ aliuliza huku akijitupa kwenye kochi,
"Nipo tu, narekebisha tu mazingira" Tom aliongea huku akijilazimisha kutabasamu,
"Tunaweza kutoka kidogo?" BQ alimuuliza Tom,
"Twende wapi tena usiku huu?" Tom aliuliza huku akimuangalia,
"Twende kambini Mara moja, kuna tatizo limejitokeza" BQ aliongea huku akiwa anamsoma machoni Tom,
"Tatizo gani na mimi nahusikaje kwenye tatizo lenu?" Tom aliuliza huku akionekana kupingana na BQ,
"Sinaga muda wa kubembelezana, natumia busara tu kuongea na wewe kirafiki, naomba ufanye ninachotaka vinginevyo utafanya nitakacho huku ukiwa na maumivu" BQ aliongea huku akiwasha sigara yake,
"Niambie basi ni kipi kimetokea?" Tom aliuliza lakini kwa upole tofauti na mwanzo,
"Twende tu, utajua uko uko" BQ aliongea huku akihuruhusu moshi wa sigara kupita katika matundu ya pua yake.
Tom akakubali ili mambo yaishe, wakatoka kimya kimya na kwenda katika gari la kisasa lililokuwa limeegeshwa nje ya geti na wakapanda, BQ ndio alikuwa dereva na kwenye gari hakukuwa na mtu mwingine isipokuwa wao tu.
Bila Tom kujua anapopelekwa alikuwa ametulia tu kwa kuwa alikuwa hana la kufanya na isitoshe huyo binti alimzidi kila kitu Tom, kuanzia mapigano, akili, ukatili na hata kipato.
Gari ilitembea mwendo wa nusu saa na kuingia ndani ya nyumba moja nzuri ambayo Tom hakuitambua,
"Shuka, tumefika" BQ alimwambia Tom na Tom akatelemka kisha akawa anayaangalia mazingira ya mule ndani,
"Acha kushangaa shangaa, twende ndani" BQ aliongea huku akielekea ndani na Tom akamfuata na kuingia ndani, Tom akashangaa kuikuta timu ile ile iliyokuwepo kule porini siku ambayo Rais anauawa,
"Mbona umekuja nae kirafiki hivi, mi nilijua mpaka afike hapa atakuwa hana meno hata mawili" Jimmy aliuliza na kufanya Tom ahisi kuna kitu kibaya anatakiwa afanyiwe,
"Hakuwa mjeuri, ni mtiifu sana" BQ alijibu huku akimuonesha Tom sehemu ya kukaa,
"Sasa tusipoteze muda, muwekeeni hiyo video aione" Waziri wa ulinzi aliongea na ile video ikawekwa na Tom akapata fursa ya kuiangalia, hata yeye alishangaa kuiona video ile,
"Tuambie hii video umeshaisambaza kwa watu wangapi?" Tammy Semmy aliuliza baada ya ile video kuisha, hilo swali lilimshangaza Tom kwa kuwa ndio alikuwa anaiona kwa Mara ya kwanza hiyo video,
"Nimeisambaza?!!!!!!!!! mbona ndo naiona sasa hivi hiyo video" Tom alijibu huku akishangaa,
"Narudia tena kuuliza, hii video umeshaisambaza kwa watu wangapi?" Tammy Semmy aliuliza tena,
"Mimi siijui video hii, ndio kwanza naiona sasa hivi" Tom alijitetea,
"Jimmy mbebeni na mumpeleke kule torture chamber" Tammy Semmy aliongea na wale mabaunsa wawili wakambeba Tom juu juu na kumuingiza katika chumba kipana kidogo na kumshusha Tom juu ya kiti cha chuma kilichokuwepo humo ndani,
"Jamani nimewaambia mimi sijui kitu chochote kuhusu hiyo video, nieleweni jamani" Tom aliongea huku akilalamika,
"Utasema tu ukweli" Waziri wa ulinzi aliongea huku akiingia ndani ya kile chumba na nyuma yake alikuwepo Tammy Semmy na BQ,
"Ukweli gani?, mimi sijui kitu" Tom aliongea,
"Jimmy na Gabby hii kazi nawaachieni nyie, kabla hakujakucha nataka awe ameshatoa jibu linaloeleweka" Waziri wa ulinzi aliongea,
"Gabby hii ndo sekta yake, uwa hakoseagi" BQ aliongea huku akimtazama yule baunsa mwingine ambaye uwa haongei Mara kwa Mara,
"Sisi tunaenda, pombe mtachukua kule kwenye friji ya stoo, maana mateso bila pombe uwa hayaendi kabisa" Tammy Semmy aliongea huku akiwatazama wale mabaunsa wawili,
"Sawa mkuu" Gabby aliongea huku akitabasamu,
"Sisi tunaenda, hii kazi muimalize usiku huu" Tammy Semmy aliongea huku akianza kuondoka na Waziri wa ulinzi akamfuata,
"Nitakuja kukuona kesho Mme wangu mpya" BQ aliongea huku akimtazama Tom na kisha akatoa kicheko kikali cha kebehi na kumminyia jicho Tom kisha akaondoka zake na kuwaacha mabaunsa nao wakitabasamu huku Tom akiwa na mashaka makubwa juu ya usalama wake.
"Kalete vitendea kazi" Gabby alimwambia Jimmy na Jimmy akaenda kwenye kona moja ya kile chumba na kurudi na sahani kubwa ya chuma iliyokuwa na nyundo, bisibisi, misumari, viwembe, kisu na sindano za kushonea nguo. Tom alivyoona hivyo akajihisi kutaka kulia.
***********************
Koplo Mbegu alipotoka kwake alichukua bajaji na kwenda moja kwa moja katika eneo la tukio, eneo ambalo waliufukua mwili wa Rais.
Koplo Mbegu alifika eneo hilo na kukuta watu wameshatawanyika ila alikuta maofisa kadhaa wa usalama wakiendelea na mambo yao, hakutaka kuwasogelea wala kuongea nao kwa maana alishaonywa juu ya kumshirikisha mtu yoyote katika jambo hilo.
Koplo Mbegu alichofanya ni kujiingiza ndani ndani katika kijiji hicho kwa ajili ya kusikia habari zozote juu ya kifo cha Rais, kwa bahati nzuri aliweza kuona sehemu kuna mkusanyiko wa watu, akaona ni bora ajichanganye hapo. Akajipachika katika kundi, akagundua kuwa huo mkusanyiko wa watu ni kwa ajili ya msiba wa kijana mkata mkaa, msiba uliotokana na huyo kijana kupigwa na radi siku moja nyuma, siku ambayo Rais aliuawa.
"Unaambiwa siku ile Sudi amepigwa na Radi, kuna mtu alitokea, tena hakuwa na nguo" Kijana mmoja alikuwa anawaadithia wenzake na kufanya Koplo Mbegu asogee zaidi mahali alipo yule kijana,
"Kwanza huyo mtu hakuwa anaeleweka, Mara aonekane mara apotee, na zaidi alikuwa uchi kabisa, sasa huyo mtu ni nani?" Yule kijana alizidi kutoa ubuyu huku Koplo akisikia vizuri,
"Huyo mtu ni nani?" Koplo Mbegu alijikuta anauliza bila kutarajia na kufanya watu wote wamuangalie.........
"Hakuna anaemjua" Yule mtu alimjibu Koplo Mbegu na kuendelea kutoa hadithi hiyo, Koplo Mbegu alimsoma kijana huyo kwa muda mfupi na kugundua kuwa huyo kijana ni muongeaji sana, akapanga kumtafuta baada ya kumaliza kusimulia hiyo hadithi yake anayopigia watu.
Kwa bahati nzuri muda wa kupeleka mwili wa marehemu msikitini ulikuwa umefika, wanaume wakaubeba na kuanza kuupeleka msikitini, Koplo Mbegu akaona hiyo ndiyo nafasi ya kuongea na huyo kijana, lakini hakupata nafasi hiyo mpaka mwili ulipofikishwa msikitini.
Yule kijana hakuingia ndani ya msikiti, aliishia nje pamoja na watu wengine kadhaa ambao walikuwa na imani tofauti, hapo ndipo Koplo Mbegu alipopata nafasi ya kumsogelea yule kijana na kukaa jirani nae,
" aisee uchawi upo ndugu yangu, yaani nasikia huyu Jamaa amekufa kifo cha utata sana" Koplo Mbegu alianzisha maongezi mbele ya yule kijana kwa lengo la kumpeleleza tu ili apate chochote,
"We acha rafiki yangu, Sudi amekufa kifo cha ajabu sana, unaambiwa walikuwa wanne ila radi ikampiga peke yake" Yule kijana aliongea kwa masikitiko,
"Nasikia kuna mtu alitokea kipindi Sudi ameshakufa, na huyo mtu hakuwa na nguo" Koplo Mbegu aliuliza,
"Unaambiwa huyo mtu alikuwa hajulikani alivyo, kati ya wale washkaji watatu waliemuona hakuna hata mmoja anaeikumbuka sura yake, wanachodai ni kuwa alikuwa hana nywele kichwani, yaani alikuwa na upara" Yule Jamaa alizidi kutoa habari anazozijua yeye,
"Aisee huu ushirikina huu, ndio maana waafrika hatuendelei" Koplo Mbegu aliongea hili huyo Jamaa azidi kuongea,
"Kwanza inawezekana kabisa hata yule mtu aliyefukuliwa leo katika lile shimo kule shambani nae ameuliwa na huyo mtu" Yule Jamaa alizidi kuongea,
"Ni nani aliyefukuliwa leo?" Koplo Mbegu aliuliza kama hajui vile, alitaka kupima kama watu wa kijiji hicho wamegundua kuwa ule mwili uliofukuliwa hapo ulikuwa wa Rais,
"Hata hatujamjua yule mtu, ni mgeni machoni kwetu" Yule Jamaa muongeaji alijibu na kufanya Koplo Mbegu aone wanakijiji hawajagundua lolote kuhusu ule mwili uliofukuliwa,
"Mimi nadhani kuna haja ya sisi wanakijiji kumtafuta huyo mtu wa ajabu" Koplo Mbegu aliongea,
"Unachekesha rafiki yangu, unaambiwa huyo mtu haeleweki, labda twende na waganga wa kienyeji" Yule kijana aliongea huku akitabasamu,
"Itawezekana tu, hakuna kisichowezekana chini ya jua" Koplo Mbegu nae aliongea huku akitabasamu,
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Dah, mshkaji usinichekeshe, ebu twende tukasaidie kuubeba mwili wa marehemu, naona wameshamaliza kusali" Yule kijana aliongea huku akielekea kwenye mlango wa msikiti na wakati huo yule kijana hakumtilia mashaka yoyote Koplo Mbegu, aliamini ni mwanakijiji mwenzake.
Koplo Mbegu akajifanya kama anaambatana nae kisha akageuza na kuondoka zake huku kichwani akijiuliza huyo mtu ni nani?
**********************
Tom baada ya kuiona ile sahani iliyojaa kila kitu cha kutisha alianza kutetemeka kwa uoga, na pia aliendelea kuiwazia ile video aliyoiona muda mfupi uliopita huku akiamini ndio imemletea matatizo yote hayo na pia akijipa moyo kuwa uenda hiyo video ndio inayoweza pia kumuokoa endapo ile video anayeonekana yeye peke yake itavuja.
"Tumfunge kamba kwanza" Gabby aliongea huku akielekea mahali kudu zilipo,
"Kamba ya nini?, mtu mwenyewe unamuona alivyo lazy lazy" Jimmy aliongea na kumfanya Gabby asite kuendelea kuifuata kamba,
"Basi kalete pombe Ili tuanze kazi" Gabby aliongea na Jimmy akaenda kufuata pombe, baada ya dakika kumi alirudi na chupa mbili kubwa zenye pombe iliyokuwa na rangi ya maji na kuweka chini.
"Vipi dogo, unatumia hii" Jimmy alimuuliza Tom,
"Hapana" Tom alijibu,
"Kamletee soda huyu, sio vizuri sisi tunywe alafu yeye atuangalie tu" Gabby alimwambia Jimmy na kisha Jimmy akafuata soda baada ya muda kidogo akarejea,
"Utachagua mwenyewe unayoitaka" Jimmy aliongea huku akiweka chini ya miguu ya Tom soda za aina tatu, Tom akaichukua moja akaifungua na kujilazimisha kunywa ingawa hakusikia ladha kabisa kutokana na kichwa chake kufikiria mateso anayoenda kuyapata muda mchache ujao,
"Dogo kwanini usiwe muwazi tu, sema ukweli tu kabla hatujaanza kukuharibu mdogo wangu" Gabby aliongea kwa upole huku akimuangalia Tom,
"Na alivyo mrembo hivyo" Jimmy aliongea na kucheka mwenyewe,
"Ukweli gani mnaoutaka, au uongo wangu ndio ukweli wenu?" Tom aliuliza kwa huruma,
"Sawa endelea na ubishi wako, sisi sote wanaume humu, na ukisema ukweli hautodhurika kwa lolote" Jimmy alimwambia Tom,
"Ukweli ndio huu ninaouongea na naona madhara yake ndio hayo ya kutaka kuniumiza" Tom aliongea kwa upole,
"Dogo utakufa ujue, alafu kifo chako kitakuwa cha kujitakia mwenyewe" Gabby aliongea huku akimtazama Tom,
"Kama nitakufa itakuwa sawa tu, itakuwa mmetaka nyinyi kuniua na wala sio Mungu" Tom alijibu na kufanya wale vijana watabasamu,
"Gabby kazi ianze, huyu dogo hawezi kusema kitu mpaka apewe dawa" Jimmy aliongea huku akinyanyuka kumsogelea Tom na kufanya Tom aanze kutetemeka,
"Msinipige jamani" Tom aliongea huku akianza kulia, ila wakati anamaliza kuongea akashtukia chupa yenye soda ikimuijia usawa wa kichwa, akainama na ile chupa ikatua mgongoni na ikapasuka, chupa hiyo ilirushwa na Gabby,
"Huyu hatakiwi kuharibiwa sura, tucheze na mwili tu kwa maana sura yake ni nzuri, tukiiharibu atakosa wachumba" Jimmy aliongea huku akiirarua fulana aliyovaa Tom na kumuacha kifua wazi, kisha akachukua sindano mbili kubwa za kushonea nguo na kuzipachika kwenye mgongo wa Tom, Tom akatoa ukelele mkali ulioambatana na kilio,
"Hizo kelele hazitutishi, unaimaliza tu sauti yako bure" Gabby aliongea kisha akachukua msumari mrefu na kuanza kuugongelea kwenye paja la Tom, Tom akawa analia huku akiwa anajaribu kuzuia jambo hilo, lakini jitihada zake zilizimwa na ngumi kali ya uso aliyopigwa na Jimmy, Tom akaanza kuona Giza taratibu na mwisho akadondoka chini kama mzigo, akapoteza fahamu.
"Anatuletea maigizo huyu, hajazimia wala nini" Jimmy aliongea huku akimuinua Tom na kumuweka katika kiti,
"Ngoja nione kama kweli kazimia" Gabby aliongea na kuuchukua msumali mwingine mkubwa na kuuweka kwenye usawa wa mbele wa kichwa cha Tom, kisha akachukua nyundo kubwa, alikuwa anataka kuugongelea ule msumali kwenye utosi wa Tom.
*************************
Koplo Mbegu alivyotoka nje ya mji alirudi mjini na cha kwanza alichoamua alimtafuta rafiki yake aitwae Ghislain ambaye ni afisa usalama lakini yeye amebobea kwenye masuala ya michoro, akamuita nyumbani kwake,
"We Jamaa yangu siku hizi upo bize sana" Ghislain alimwambia Koplo Mbegu,
"Ubize wapi, sema nyakati hizi pesa hakuna kabisa, na wewe navyokufahamu kila tunapokutana unataka unywe tu" Koplo Mbegu alimwambia Ghislain,
"Kunywa ni lazima, na siku hizi ndo nimezidisha yaani" Ghislain alijisifia,
"Sasa ndugu ebu nisaidie kitu kimoja" Koplo Mbegu alimwambia Ghislain
"Kitu gani ndugu yangu?" Ghislain aliuliza,
"Kuna picha nataka unichoree" Koplo Mbegu aliongea,
"Picha ya Maelezo au kopi?" Ghislain aliuliza,
"Ni maelezo tu" Koplo Mbegu alijibu,
"Kuna kesi nini umepewa uifuatilie?" Ghislain aliuliza,
"Kesi wapi? Kuna mtu namsaidia ishu fulani hivi" Koplo Mbegu alimdanganya mwenzie,
"Ingekuwa umepewa kesi ningeshangaa, kwa maana wewe bado hujakomaa kwenye masuala hayo" Ghislain aliongea na kumfanya Koplo Mbegu acheke kimya kimya,
"Sasa nadhani nikupe vifaa tuanze kazi" Koplo Mbegu alimwambia Ghislain,
"Karatasi lazima iwe nyeupe A4 na penseli ya HB" Ghislain aliongea,
"Vyote vipo, niliviandaa kwa ajili ya kazi hii" Koplo Mbegu alijibu huku akiweka karatasi nyeupe na penseli juu ya meza,
"Haya anza kueleza jinsi huyo mtu alivyo" Ghislain aliongea huku akiwa tayari ameshajiandaa kuchora, Koplo Mbegu akaeleza kitu kulingana na maelezo ya yule mtu wa kule kijijini aliyekua anaongea sana msibani.
Ghislain alichora kulingana na maelezo hayo na hakukosea kitu hata kimoja, kisha akawa anaushangaa ule mchoro baada ya kumaliza kuuchora,
"Mbona unaushangaa hivyo?" Koplo Mbegu aliuliza baada kuona mwenzake akiendelea kuushangaa ule mchoro,
"Ebu uangalie na wewe" Ghislain aliongea huku akimrushia Koplo Mbegu ile karatasi iliyo na mchoro.
Koplo Mbegu Mbegu alipoiangalia aliguna kwa mshangao...........
"Kweli nimeamini huyu mtu sio wa kawaida" Koplo Mbegu aliongea baada ya kuushangaa kwa ule mchoro,
"Ni mtu au nini? Mtu gani wa ajabu hivyo au umekosea kunielezea?" Ghislain aliuliza huku akimcheka mwenzake aliyekuwa amezama kwenye huo mchoro,
"Kwa maelezo niliyochukua hakuna hata mahali nilipokosea" Koplo Mbegu aliongea huku akiendelea kuiangalia ile picha,
"Nahisi huyo mtu aliyekupa hayo maelezo ni mganga, itakuwa anamtafuta mchawi" Ghislain aliongea kwa utani huku akicheka peke yake,
"Ebu kausha, we kazi yako ilikuwa kuchora tu na si kufanya vitu vingine visivyokuhusu" Koplo Mbegu alimwambia Ghislain,
"Sasa kwani mimi nimefanyaje?" Ghislain aliuliza huku akicheka,
"Kwanini unacheka mchoro wangu sasa?" Koplo Mbegu aliuliza huku akijifanya amekasirika,
"Basi nisamehe, ebu nifanyie dawa kidogo maana nina kiu kinyama" Ghislain aliongea huku akimtazama Koplo Mbegu,http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Mimi nilijua tu lazima utake pombe, ila nilishajiandaa kwa hilo" Koplo Mbegu aliongea huku akielekea mahali friji lilipo,
"Acha maneno lete bia" Ghislain aliongea wakati Koplo Mbegu alipokuwa anafuata kinywaji hicho.
Koplo Mbegu aliporejea mezani, alirudi na bia, kisha akaweka juu ya meza,
"Hivi unajua habari yoyote kuhusu kinachoendelea ndani ya nchi?" Ghislain alimuuliza Koplo Mbegu wakati akimimina bia kwenye glass,
"Hapana, kuna nini kwani?" Koplo Mbegu aliuliza huku akihisi hiyo habari anayotaka kupewa itakuwa ni juu ya kifo cha rais,
"Tatizo lenu vyeo vyenu ni vidogo sana na ndio maana hamuambiwi matukio makubwa" Ghislain aliongea kisha akaigida ile pombe iliyokuwepo katika glass,
"Sasa hizo dharau, wewe si useme hiyo habari acha kuninyanyasa kwa ajili ya cheo changu" Koplo Mbegu alimwambia Ghislain,
" kwenye ukweli lazima tuseme, kihalisia unatakiwa kunipigia saluti, wewe bado dogo sana kwa cheo" Ghislain aliongea na kumalizia kwa cheko,
"Sawa mkuu, aya niambie kuna habari gani imetokea?" Koplo Mbegu aliuliza,
"Rais hatunae tena, asubuhi ya leo maafande wameukuta mwili wake umefukiwa katika shimo uko nje ya mji" Ghislain aliongea na kumimina bia kwenye glass,
"Acha story zako za uongo, kama Rais amekufa si wangetangaza kwenye vyombo vya habari?" Koplo Mbegu alijifanya kuuliza wakati anajua kila kitu na isitoshe yeye ndiye aliyekuwa kiongozi wa wale polisi walioufukua ule mwili wa Rais,
"Sio kila kitu kinatangazwa kwenye vyombo vya habari, vingine vinahitajika muda ili nchi ijipange vizuri kwa lolote litakaloweza kutokea, kwanza kifo chenyewe kina utata" Ghislain aliongea huku akiwa anamuangalia Koplo Mbegu,
"Mimi siamini bwana mpaka watangaze" Koplo Mbegu aliongea ili alete ubishi tu wa kumshawishi mwenzake aongee kila kitu anachokijua,
"Sisi ndio tunajua kila kitu kinachoendelea kwenye Taifa hili, kesho asubuhi ndio hiyo habari itatangazwa" Ghislain aliongea kwa kujiamini,
"Sasa ni nani amemuua Rais?" Koplo Mbegu aliuliza,
"Hakuna anaejua, unaambiwa wataletwa wapelelezi wa kimataifa kufanya upelelezi wa kumjua muuaji wa Rais" Ghislain aliendelea kuongea,
"Sasa nchi ipo chini ya nani?, au jeshi?" Koplo Mbegu alihoji,
"Acha ujinga wewe, kwani hii nchi imepinduliwa mpaka iwe chini ya jeshi? Nchi hii kwa sasa inaongozwa na makamo wa Rais bwana Tammy Semmy" Ghislain aliongea,
"Kwanza ilikuaje mpaka rais akafa?" Koplo Mbegu alimuuliza Ghislain,
"Sasa mimi nitajuaje, kwani wakati anakufa mi nilikuwepo?" Ghislain alijibu,
"Sema nyie usalama wa Taifa ni wapumbavu sana, yaani mmeshindwa kumkamata hata bodyguard wa Rais mumuhoji?" Koplo Mbegu aliuliza makusudi ili ajue kama bodyguard wa Rais ameshahojiwa,
"Unaambiwa siku hiyo alishinda nyumbani kwake tu na bodyguard yeye alipewa ruhusa ya kutoenda kazini siku hiyo, ila jioni ndo Rais alitoka na gari na alikuwa anaendesha mwenyewe" Ghislain alijibu na kisha akamimina bia nyingine kwenye glass,
"Mi naamini usalama uwa mnafanya upelelezi wa haraka sana kwenye mambo nyeti kama haya, ila kwa maelezo yako juu ya hiki kifo cha Rais naona kama mmelala hivi, au nyie ndio mmefanya mipango ili Rais auawe?" Koplo Mbegu aliuliza na kujifanya anatabasamu ili aonekane ameuliza kiutani,
"Ndani ya usalama wenyewe kuna makundi mawili, yaani kundi la watu tunaofanya kazi kwa haki na kundi jingine lipo kwa ajili ya vigogo, na kuna tetesi kuwa eti uenda sisi usalama tulikuwa tunajua juu ya mpango wa kifo chake" Ghislain aliendelea kuongea vitu ambavyo Koplo Mbegu hakuvijua,
"Kwa hiyo nyie ndio mmemuua?" Koplo Mbegu aliuliza,
"Hatujamuua na wala hatujui lolote kuhusu kifo chake, ila kuna tetesi kutoka kwa wafanyakazi wa serikalini wanadai sisi tulikuwa tunaujua mpango juu ya kifo cha Rais" Ghislain alimuelewesha Koplo Mbegu,
"Lakini binadamu wabaya sana, sasa Rais wetu alikuwa kipenzi cha wananchi alafu wamemuua, au mtu aliyefanya hivyo alikuwa na kisasi nae?" Koplo Mbegu aliuliza,
"Sidhani kama ni visasi, mimi nafikiri hayo yamefanyika kisiasa tu na ukizingatia uchaguzi mkuu ni mwaka ujao, wameona bora wammalize ili na wao wachukue nchi" Ghislain aliongea kitu bila kuwa na uhakika, lakini kiukweli huo ndio ulikuwa ukweli wenyewe,
"Unataka kuniambia kuwa vyama vya upinzani ndio vimefanya hivyo?" Koplo Mbegu aliendelea kuuliza,
"Dogo ebu tulia, mimi sijakwambia ameuwawa kwa siasa, hivyo vitu nilivyoongea ni kwa kutumia hisia zangu tu, na kama ningepewa jukumu la kuifuatilia hii kesi, basi ningeanza kuipeleleza kwa kuanzia upande wa siasa" Ghislain aliongea maneno yaliyompa mwanga kidogo Koplo Mbegu,
"Kweli aisee, ukiwa umelewa unaongeaga vitu vya maana sana" Koplo Mbegu alimtania mwenzake na kisha akacheka,
"Chupa zimekauka hizi, ebu niongezee nyingine" Ghislain aliongea huku akitikisa chupa tupu za bia zilizokuwepo hapo mezani,
"Sina hela bwana, kwanza ukilewaga sana unakuwa mzigo na unaweza ukatapika humu ukanipa kazi ya kudeki bure" Koplo Mbegu alimwambia Ghislain,
"Mpuuzi wewe, nimeshamaliza kazi yako ya kuchora ndio unaleta maneno yako ya kijinga" Ghislain aliongea na kumalizia na sonyo,
"Kama unataka soda sema nikuletee, hata kreti nakununulia" Koplo Mbegu alimtamnia Ghislain,
"Acha niondoke mie kwa maana umeanza dharau, mimi wa kunywa soda? au unataka nifuatwe na nyuki njia nzima?" Ghislain aliongea huku akinyanyuka kwenye kochi,
"Bora uende, maana Nina usingizi alafu nilikuwa naogopa kukwambia uondoke" Koplo Mbegu aliongea na kumcheka mwenzake,
"Sawa wewe lala, utapata shida siku nyingine, na siji ng'o" Ghislain aliongea wakati akitoka nje,
"Nikikwambia kuna bia utakuja tu" Koplo Mbegu alimtania mwenzake,
"Sawa, umekariri mimi mlevi? pombe zenyewe naacha muda si mrefu" Ghislain aliongea,
"Uache usiache mimi hainihusu, ila nakushukuru sana kwa mchoro Jamaa yangu" Koplo Mbegu aliongea,
"Sina haja ya shukrani yako" Ghislain alijibu na kubamiza mlango, akaondoka zake na kumuacha Koplo Mbegu akimcheka.
"Njoo uchukue nauli, au unayo?" Koplo Mbegu aliongea huku akifungua mlango,
"Sina shida vijisenti vyako" Ghislain alijibu huku akisimamisha bodaboda na kupanda kisha akaondoka zake na kumuacha Koplo Mbegu akicheka tu, kisha akarudi ndani na kufunga mlango wake.
Awa Jamaa wawili ni marafiki tokea shule ya secondary, walitokea kupendana sana kwa maana walikuwa na ndoto moja, walitaka kuwa wanajeshi ila Koplo Mbegu aliishia kuwa askari polisi baada ya kufeli kidato cha nne na Mjomba wake aliyekuwa askari alimsaidia kupata nafasi ya kuingia kwenye mafunzo ya uaskari mpaka alipoitimu na kupangiwa kazi. na kwa upande wa Ghislain yeye alipata bahati ya kumaliza kidato cha sita na kujiunga na jeshi, ila baada ya kuhitimu alichaguliwa kujiunga na usalama wa Taifa.
*******"********†******
Huku napo kwenye mateso ya Tom kulipamba moto, Gabby amechukua msumali ili amgongelee Tom utosini,
"Acha ujinga wewe, sasa si utamuua bure alafu tutakuwa hatujafanya kitu" Jimmy aliongea huku akimpora msumali Gabby,
"Kwani sina akili mpaka nimuue? Nilikuwa nataka kumpima tu kama kazimia kweli au lah!" Gabby alijitetea,
"Ukishakunywaga pombe unakuwa mnyama kabisa, ebu kalete maji kwenye friji tummwagie kichwani" Jimmy alimwambia Gabby na Gabby akaenda kuyaleta maji na kumwagia Tom kichwani, akazinduka,
"Dogo ujue utakufa, sema ukweli" Gabby alimwambia Tom,
"Kweli dogo, kuwa muwazi tu" Jimmy nae alimsihi Tom,
"Ukweli gani mnaoutaka?" Tom aliongea huku akivuja damu puani kutokana na ile ngumi ya kichwa aliyopigwa mpaka akapoteza fahamu,
"Ni nani aliyeichukua ile video kule msituni?" Gabby aliuliza huku amekunja sura,
"Ni mimi hapa" Sauti ya mtu ilisikika ikijibu na kuwafanya wote waangalie mlangoni, hapo ndipo Jimmy na Gabby wakakutana na sura wasiyoifahamu akiwa amesimama mlangoni huku miguuni akiwa amevaa buti kubwa wanazovaa wanajeshi au migambo, pia alitinga suruali ya jinsi ya bluu iliyombana mwili kutokana na ile suruali kuwa ndogo na juu alivaa koti kubwa jeusi lenye kofia yake, na ile kofia ya koti alikuwa ameivaa kichwani mwake na kuyaziba macho yake kidogo upande wa juu. Wakati wale mabwana wanamtazama, Tom nae alikuwa amemkazia macho akimtazama mtu yule,
"Mtu asiyekuwa na nguo" Tom aliongea baada ya kumtazama mtu yule na akajikuta anatabasamu, tabasamu ambalo hata yeye hakulijua lina maana gani.......
"Mimi ndiye niliyeichukua ile video" Yule kiumbe aliongea huku akiwa amesimama pale mlangoni na kuwafanya wale mabaunsa wapigwe na butwaa kwa maana mlango ulikuwa umefungwa sasa huyu mtu ameingiaje? ndio swali walilokuwa wanajiuliza huku wakiwa wamemtolea macho yule mtu.
"Umejileta mwenyewe kwenye mdomo wa mamba hata huogopi?" Gabby aliuliza huku akimsogelea mtu yule kwa tahadhari kwa maana alishamtia hofu kwa namna alivyoingia mule,
"Hakuna kiumbe aliyenizidi uwezo kwenye dunia hii" Yule mtu alijibu kwa kujiamini huku akiwa amesimama vile vile,
"Huyo Mbwa anatupotezea muda, ebu mshughulikie fasta nae tumuunganishe na huyu dogo" Jimmy aliongea baada ya kumuona Gabby anasita,
"Ngoja nimpe kubwa" Gabby aliongea kisha akaruka juu na kutua mbele ya yule mtu, Gabby akapiga ngumi mfululizo kama kumi hivi, cha ajabu yule mtu alizikwepa akiwa amesimama vile vile, Gabby akapiga hatua moja nyuma na kurusha teke kali ambalo liliilenga shingo ya yule mtu, yule mtu akayumba dizaini kama kamba iliyopulizwa na upepo, lile teke likapita mbele ya uso wa yule mtu, Gabby akahisi inawezekana huyu mtu ana mafunzo ya kutosha ya mapigano. Gabby akaamua abadilishe mtindo wa kupigana, akapiga hatua za haraka haraka kumfuata yule mtu mpaka ukabaki umbali wa inchi thelathini ili wagusane, hapo Gabby akavuta ngumi yake ya mkono wa kulia kwa nguvu zote ili ampige yule mtu, ila kabla hajairuhusu ngumi yake, alishtukia anapigwa ngumi nzito ya kifuani na kurushwa juu kama ametupwa na winchi, akaenda kudondokea kwenye miguu ya Jimmy.
"Kumbe unaweza eee, ngoja tuje wawili sasa" Jimmy aliongea huku akimsaidia Gabby kuinuka,
"Inahitajika akili sana kupambana nae" Gabby aliongea huku akisimama,
"Twende kwa pamoja, tushambulie kwa pamoja bila kumpa nafasi" Jimmy alimwambia Gabby, ila aliongea kwa sauti ya chini sana,
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Poa, twende" Gabby alijibu kisha wakatoka mbio kumuelekea yule mtu, walipomfikia Gabby aliseleleka chini ili amkwatue miguu yule mtu na Jimmy aliruka juu ili ampige usawa wa shingo, yule mtu alichuchumaa kisha akaruka kama kichura chura hivi bila kusogea mbele wala nyuma, Jimmy aliyeruka juu akapitiliza na kwenda kuupiga teke mlango, Gabby yeye miguu yake ilipita chini ya miguu ya yule mtu ila shingo yake ikajikuta imebanwa na mapaja ya yule mtu,
"Kiumbe hujaumbwa kunishinda mimi" Yule mtu aliongea kisha kwa kasi sana alinyanyuka na kumsukuma Gabby ambae aliseleleka na kwenda kugonga meza iliyokuwa na chupa za pombe na zile chupa zikadondoka na kuvunjika, harufu ya pombe ikaenea chumba kizima,
"Nitakuja kuwaona baadae" yule mtu aliongea kisha akatoka mbio kuelekea nje, Jimmy nae akanyanyuka kwa lengo la kumfukuza yule mtu, lakini jimmy alipofika sebuleni kwenye mlango wa kutokea nje, alikuta mlango umefungwa kwa ndani kama mwanzo alivyoufunga yeye na wala hakukuwa na dalili zozote zilizoonesha ule mlango umefunguliwa. Jimmy akaishia kukagua mule sebuleni na katika baadhi ya vyumba hili kuona kama yule mtu atakuwa mule ndani lakini hakumkuta na wala hakukuwa na dalili za mtu mwingine zaidi yao kuwepo mule ndani.
Jimmy akarudi katika torture chamber na kumkuta Gabby akijifuta vumbi na Tom alikuwa anamcheka utasema hayupo kwenye mateso.
"Vipi umeumia?" Jimmy alimuuliza Gabby,
"Hujamkamata?" Gabby aliuliza bila kujibu swali la mwenzake,
"Haonekani, huyu Jamaa ni professional" Jimmy alimjibu mwenzake,
"Haonekani vipi, amekimbia au?" Gabby aliuliza,
"Sidhani, kwa maana mlango umefungwa vile vile kwa ndani, ila nilipomtafuta sikumuona" Jimmy alitoa maelezo ambayo Gabby aliona kama hadithi tu za watoto,
"Hiyo kitu haiwezekani, ebu twende nikahakikishe" Gabby aliongea huku akielekea sebuleni na Jimmy nae akamfuata nyuma. Kweli Gabby alikuta kila kitu kipo kama alivyoambiwa na Jimmy, na hata walipomtafuta huyo mtu hawakumpata, wakachoka wenyewe kwa hilo tukio, wakarudi torture chamber na kumkuta Tom akiwaangalia,
"Dogo unamjua yule mtu?" Gabby alimuuliza Tom,
"Hapana simjui" Tom alijibu,
"Sasa mbona alivyoingia ulisema mtu asiye na nguo huyo, ulikuwa una maana gani?" Gabby aliuliza kwa hasira,
"Ngojeni niwaambieni, huyu mtu nilianza kumuona siku ile mmeniacha kule msituni naufukia mwili wa Rais, mvua ilikuwa inanyesha na kuna Radi kubwa sana ilipiga, baada ya ile kupiga kuna kichaka kilishika moto kutokana na Radi hiyo, na kupitia mwanga wa ule moto ndipo nilimuona mtu akiwa amesimama katika kile kichaka" Tom aliwaeleza ukweli anaoujua,
"Kwa hiyo na wewe humjui huyu mtu?" Jimmy aliuliza,
"Simjui, na huyo mtu haeleweki, nimeshawahi kumkuta Mara mbili ndani ya chumba changu na mlango nilikuwa nimefunga" Tom aliendelea kuongea,
"Atakuwa mchawi huyu" Jimmy aliongea,
"Sidhani, mimi nahisi huyu Jamaa atakuwa na mafunzo ya hali juu katika uchunguzi wa mambo" Gabby alizungumza,
"Sasa mimi si mniachie tu, kwa maana mtu mwenye hiyo video si mmemuona na yeye amekiri kuwa hiyo video ni yeye ndio aliyeichukua" Tom aliwaambia wale mabaunsa,
"Subiri hapo hapo mpaka wakubwa zetu waseme uachiwe ndio tunakuacha" Jimmy alimwambia Tom,
"Aisee tukalale, hii shughuli imekuwa nzito sana" Gabby aliongea huku akiinuka,
"Tuwapigie siku kwanza ili tuwajulishe kilichotokea" Jimmy alimwambia mwenzake,
"Achana nayo bwana, ukiwapigia simu muda huu wanaweza kutupa kazi nyingine na tukashindwa kulala usiku huu" Gabby alijibu huku akitoka katika kile chumba cha mateso,
"Dogo wewe utalala humu, nitakachokusaidia ni kukufungua kamba tu" Jimmy aliongea huku akimfungua Tom kamba alizofungwa katika kile kiti cha chuma,
"Naomba unisaidie na kuondoka hapa, kesho saa sita nina safari ndugu yangu" Tom aliongea kwa kumsihi Jimmy,
"Hilo lipo nje ya uwezo wangu, subiri wakubwa waje utaongea nao wewe mwenyewe" Jimmy aliongea huku akiondoka na kumuacha Tom akiwa anaranda randa tu katika kile chumba.
***************
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
SIKU MPYA..
_____________
Koplo Mbegu aliamka asubuhi na alichopanga siku ile ni kwenda kule nje ya mji akiwa na ule mchoro wa mtu ambaye alihisi inawezekana ndiye aliyemuua Rais.
Alichukua begi lake dogo la mgongoni na akavaa nguo zake za kiraia, kisha akatafuta usafiri ambao utamfikisha anapopataka.
Alichukua bodaboda na ikampeleka mpaka sehemu anayotaka kwenda, alifika vizuri kisha cha kwanza alichoamua ni kwenda pale palipokuwa na msiba kwa maana aliona ndipo patamsaidia kutimiza adhma yake.
Alifika katika eneo la msiba na kukuta kuna baadhi ya watu wachache na kwa bahati nzuri zaidi aliweza kumkuta na yule kijana mwenye maneno mengi, akamfuata na kumsalimia,
"Unaweza kunisaidia kitu?" Koplo Mbegu alimuuliza yule kijana,
"Unatakiwa uniambie kitu chenyewe alafu ndio nijue kama naweza kukusaidia au lah!" Kijana yule aliongea huku akicheka, alikuwa ni mcheshi kwa kweli,
"Jambo dogo tu, unaweza kunionesha watu waliokuwa na marehemu siku ambayo anakufa?" Koplo Mbegu aliuliza kwa sauti ya chini ili watu wa jirani nae wasisikie,
"Kwani wewe huwajui?" Kijana yule aliuliza,
"Sio kwamba siwajui, nimeangaza hapa hata siwaoni" Koplo Mbegu aliongea kana kwamba anawajua,
"Mbise alikuwepo hapa, aaah yule pale kwenye mkeka anacheza karata" Kijana yule aliongea na kumuoneshea kidole mtu mmoja aliyekuwa anacheza karata,
"Afadhali, maana nilikuwa nina shida nae. asante kwa msaada" Koplo Mbegu aliongea huku akielekea sehemu alipo yule mtu,
"Mbise samahani nakuomba pembeni Mara moja" Koplo Mbegu aliongea alipomfikia mbise,
"Kuna kheri lakini?" Mbise aliuliza huku akiinuka,
"Kheri tu" Koplo Mbegu alijibu huku akielekea nyuma ya zile nyumba kwa kuamini ndio litakuwa eneo salama,
"Mbona unanileta uchororoni, kuna nini ndugu yangu? unanitisha" Mbise aliuliza huku akiwa na hofu,
"Kuna kitu nataka unisaidie, wewe si ulikuwa ni mmoja kati ya watu walioshuhudia kifo cha mwenzako, bwana Sudi?" Koplo Mbegu alimuuliza Mbise,
"Ndio, ila mbona unazidi kunitisha kwa swali lako?" Mbise aliuliza kwa shaka,
"Usiogope, siku ile ya kifo cha Sudi si kuna mtu wa ajabu mlimuona?" Koplo Mbegu alimuuliza,
"Ndio, vyote unavyoongea ni sawa" Mbise alijibu,
"Ebu iangalie hii picha, alafu uniambie kama unamjua huyu mtu" Koplo Mbegu aliongea na kumpa Mbise ile karatasi yenye mchoro, Mbise akaifungua na kuiangalia, akajikuta anapiga kelele na kuitupa ile karatasi akawa anakimbia, Koplo Mbegu akashangaa kisha akainama chini ili aiokote ile karatasi yake yenye mchoro, akaikunja na kuitia mfukoni, alipoinua macho yake ndipo alipoona kundi la wanakijiji wakija mbio mbele yake na walikuwa wamebeba mapanga na mawe makubwa makubwa...........
Koplo Mbegu akahisi kuna hatari inamnyemelea, hata alipotaka kukimbia alikuwa ameshachelewa, watu walishamzunguka na wengi wao walionekana kuwa na hasira za wazi juu yake,
"Tumpige, tumpige, tumpige" Wanakijiji walipaza sauti zao na kufanya Koplo Mbegu ajiulize kwanini apigwe, akiwa bado anajiuliza alishangaa kuliona tofali kubwa likiwa juu linamfuata yeye, akasogea pembeni likapita,
"Jamani mnanipigia nini?" Koplo Mbegu alipaza sauti lakini hakuna aliyesikia wala aliyeelewa ile sauti, ndio mvua ya mawe ikazidi. akiwa hajui cha kufanya wala kujitetea, ndipo yule kijana mwenye maneno mengi alichomoza mbele ya kundi la wale watu huku akiwazuia kuacha kurusha mawe,
"Nyie hamumjui huyu?, mbona tupo nae muda mrefu hapa, mbona mazishi ya Sudi alishiriki mwanzo mpaka mwisho?" Yule kijana mwenye maneno mengi aliongea na kipindi hicho wanakijiji walisitisha kurusha mawe,
"We kihelehele toka hapo, tutakutoa macho" Wanakijiji walipaza sauti zao kumuelekea yule kijana mwenye maneno mengi,
"Ebu nisaidie ndugu yangu, mimi ni polisi" Koplo Mbegu aliongea na kumfanya yule kijana ageuke na kumuangalia, kwa maana kwa muda wote aliomjua Koplo Mbegu hakuwahi kudhani ni polisi,
"Lete kitambulisho chako niwaoneshe labda wanaweza kunielewa" Yule kijana mwenye maneno mengi aliongea na Koplo Mbegu akampa kitambulisho.
"Jamani mtu huyu ni polisi msimpige, msikilizeni atawaeleza ni kipi kilichotokea mpaka Mbise akakimbia" Kijana yule mwenye maneno mengi aliongea huku akikipunga juu kitambulisho cha Koplo Mbegu, kwa kufanya vile ilisaidia kwa maana wale watu walitulia baada ya kusikia kuwa mtu yule ni polisi.
"Sasa mimi nitaongea au kuwaeleza nini?" Koplo Mbegu alimuuliza yule kijana kwa sauti ndogo sana,
"Wewe ongea chochote ambacho unahisi kitawafanya awa watu wakuamini" Yule kijana mwenye maneno mengi alijibu huku akirudi nyuma na kumuacha Koplo Mbegu akiwa amesimama.
"Jamani wananchi, mimi sio mtu mbaya, mimi ni askari na hapa nipo kwa ajili ya kufanya uchunguzi juu ya kifo cha sudi na kifo cha mtu yule aliyekutwa amefukiwa katika shimo. Sasa mimi nashindwa kuelewa kwanini mnanivamia na kunirushia mawe, nimewakosea nini?" Koplo Mbegu alihoji kwa upole,
"Umemfanya nini Mbise, mbona ametoka anakimbia huku akipiga kelele?" Mwanakijiji mmoja alihoji huku akiwa ameshika fimbo ndefu na kavu kama za wachunga ng'ombe,
"Kama yupo hapa aje aeleze kama kuna kitu kibaya nimemfanya" Koplo Mbegu alizungumza na kufanya baadhi ya wanakijiji waanze kuangaliana na kuulizana kama Mbise yupo eneo hilo, ila alikosekana na ikabidi vijana wachache watumwe wamfuate nyumbani kwake ili wamuangalie kama yupo na wageuze nae.
Baada ya dakika zisizopungua kumi, wale vijana walirudi wakiwa na Mbise huku akionekana ni mwenye wasiwasi mkubwa sana kila amuangaliapo Koplo Mbegu,
"Amekufanya nini huyu?" Yule kijana mwenye maneno mengi alimuuliza Mbise kwa sauti kubwa iliyosikiwa na kila mtu,
"Picha, amenionesha picha" Mbise alijibu huku sura yake ikiwa na uoga na kufanya wanakijiji wajiulize hiyo picha ni picha gani?
"Picha? picha gani?" Kijana yule mwenye maneno mengi aliuliza,
"Picha ya mtu aliyetutokea msituni siku ile Sudi anakufa" Mbise alijibu na kufanya wanakijiji wapate shahuku ya kumjua huyo mtu aliyepo katika hiyo picha na hiyo pia ilimfurahisha Koplo Mbegu kwa maana aliamini ule mchoro uliochorwa na Ghislain ndio wa mtu halisi aliyekuwa anamtaka,
"Ebu hiyo picha" Kijana mwenye maneno mengi aliongea huku akimgeukia Koplo Mbegu, kisha Koplo Mbegu akaitoa na kumpatia yule kijana,
"Huyu mtu unamjua?" Kijana mwenye maneno mengi alimuuliza Koplo Mbegu baada ya kuiangalia ile picha kwa muda mrefu na kushindwa kukielewa ni kiumbe gani kilichokuwepo pale,
"Simjui" Koplo Mbegu alijibu,
"Kama humjui Sasa hii picha yake umeitoa wapi?" Mbise alimuuliza Koplo Mbegu,
"Mimi nimeshakwambia ni askari, tuna mbinu za kutafuta waarifu" Koplo Mbegu alijibu,
"Dah, sasa Mara ya kwanza ulivyonionyesha hiyo picha nikajua huyo mtu ni mwenzako na amekutuma kunidhuru" Mbise aliongea huku akimuangalia Koplo Mbegu,
"Hapana, mimi ni polisi na nipo hapa kuwasaidia ninyi dhidi ya huyo mtu" Koplo Mbegu alijibu na kisha ile picha ikawa inatembezwa kwa kila mwanakijiji hilo aione.
"Kumbe jamaa yangu ni polisi? siku zote nakaa na wewe hata huniambii?" Kijana mwenye maneno mengi alimuuliza Koplo Mbegu,
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Wakati wake ulikuwa bado haujafika" Koplo Mbegu alijibu huku akitabasamu.
Wanakijiji waliangalia ile picha na wengi wao walionekana kukishangaa kiumbe kile na wengine waliamua kukiwekea mjadala kabisa wakikihusisha na imani za kishirikina.
Baada ya pilika pilika zote kuisha, Koplo Mbegu aliwaachia na namba zake za siku kwa ajili ya mawasiliano pindi kile kiumbe kitakapoonekana tena kwenye kijiji kile.
Mwisho Koplo Mbegu aliondoka zake kwa makubaliano ya kurejea tena siku yoyote.
********************
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment