Search This Blog

Friday 18 November 2022

FUMBO LA UTAMBUZI - 1

 







IMEANDIKWA NA : ALEX KILEO



*********************************************************************************



Simulizi : Fumbo La Utambuzi

Sehemu Ya Kwanza (1)





Ni jumatatu tulivu ndani ya kituo cha kituo mmoja cha radio cha mtu binafsi ambacho hakikuwa na umaarufu sana nchini, na siku hiyo ndani ya kituo hicho cha radio kulikuwepo na mkutano baina ya wafanyakazi na viongozi.



Wafanyakazi wenyewe hawakufika hata kumi hii kwa jumla ya idadi ya ofisi nzima na hao waliopo hapo wengiwao walikuwa hawana sifa ya utangazaji wala uhandishi wa habari na hao wengine wenye sifa hizo zinazotakiwa walikuwa hapo kwa ajili ya kutafuta uzoefu tu, huku wakiwa bado wanaangaika kutafuta kazi katika media nyingine zenye umaarufu zaidi.



Miongoni mwa watu waliokuwa na sifa za uhandishi katika ofisi hiyo, alikuwepo bwana mmoja aliyetambulika kama Thomas Anthony.



Huyu Thomas Anthony ni muhitimu wa stashahada ya uhandishi wa habari aliyoipata Pale Mwanza katika chuo cha St Augustine University of Tanzania (SAUT) na alihitimu miaka miwili iliyopita, katika pilika pilika zake za kutafuta hajira kwa miaka yote miwili hakubahatika kupata kitu, ndipo mjomba ake mmoja alipomtaftia mahali pa kujishikiza wakati akitafuta hajira itakayomnufaisha, maana hata hapo mshahara hawakuwa wakipewa, labda waokoteze vijisenti vidogo vidogo kutoka kwa mmiliki wa radio siku akijiingizia pesa za kutosha.



Kwa kweli Thomas alionekana kutofurahia maisha yake, kwa maana alikuwa hapati pesa kwa muda na hata akiipata haimtoshelezi mahitaji yake, kwa kuwa hakuwa akikaa kwao ila alipanga chumba kimoja katika sehemu yenye utulivu kidogo ingawa hata kodi yenyewe alikuwa akiilipa kwa mbinde kweli.



Wazazi wake wote wawili wapo hai ila wanaishi uko morogoro na wala hawamtegemei Thomas kwa kila kitu, Baba yake mzee Anthony ni mfanyakazi mstaafu wa serikali na amestahafu miaka mitatu iliyopita kwa hiyo bado alikuwa na fedha zake za kutosha za kifuta jasho.



Muda wa kikao ulikuwa umefika na kila mtu alikuwa hajui ni kitu gani kitakachoenda kujadiliwa, mtu pekee aliyekuwa anajua kinachoendelea ni Mkurugenzi tu wa hiyo radio aliyokuwa anaitwa Othman Tafu, na ndio maana radio yake ikaitwa Tafu Radio.



Wafanyakazi wote walikuwa wamekaa katika chumba cha mkutano na walikuwa wanamsuburi mkurugenzi wao bwana Othman Tafu ili aje na wajue ni ajenda gani itakayojadiliwa.



Baada ya dakika kumi aliingia bwana Othman Tafu huku akiwa amevaa kanzu yake nadhifu na chini alitililia makobazi ya yaliyokuwa yameusitiri miguu wake uliofunikwa na soksi nzito nyeupe.



Huyu Bwana Othman Tafu alikuwa ni mtu mwenye asili ya kiafrika ya kaskazini, alikuwa muarabu ambayo alikuwa anakijua vizuri kiswahili, inawezekana babu zake ndio walikuwa wanatoka katika nchi hizo, yeye mwenyewe alizaliwa na kukulia hapa hapa nchini.



Othman Tafu baada ya kuingia katika chumba cha mkutano, alikaa kisha akawasalimia wafanyakazi wake,



"Kikao cha leo najua kimewashangaza kwa maana ajenda sijaiweka wazi kama vikao vingine, naona tokea nimefika wote mnanitumbulia mimacho kama mjusi kabanwa na mlango" Othman Tafu aliongea na kufanya wafanyakazi wake wacheke, kwa maana huyu bwana alikuwa na maneno mengi alafu alikuwa ni mswahili sana,



"Sasa bwana wadogo zangu bila hata ya kupoteza muda, Mimi naona nielekee moja kwa moja katika ajenda yetu iliyowafanya niwaite hapa. Ajenda yenyewe ni kuwa nataka niifanye hii radio kuwa kubwa, yaani kuwa na wasikilizaji wengi, lakini ni nini kifanyike ili tuwe wakubwa?" Othman Tafu aliuliza na kukaa kimya kidogo ili kuona kama kuna mtu atamjibu, lakini hakuna aliyejitokeza kujibu, wafanyakazi wote walikuwa kimya.



"Naimani hata radio yetu ikiwa kubwa ni lazima nasisi maisha yetu yatabadilika, na sisi tutakuwa na uwezo wa kununua hata usafiri, au mnadhani Tom anapenda kutembea kwa miguu kila Siku kuja kazini? Masikini kijana wa watu anatembea mpaka unyayo unachakaa, juzi nimemkuta mitumbani anaulizia nyayo za mtumba" Tafu aliongea kwa kuongezea utani kidogo na kufanya wafanyakazi wacheke, kwa maana huyu bwana ilikuwa ni nadra sana kuongea bila kuweka utani katika maneno yake.



"Achaneni na mzaa wangu, shikeni vya maana tu ninavyoongea. Sasa basi ni lazima tufanye kazi, kazi kweli kweli tena kazi za uhakika ili tuweze kuwavutia watu wa matangazo. Sasa narudia swali langu, ni nini tufanye ili tuwe wakubwa?" Othman Tafu aliuliza na kuwaangalia vijana wake kama kutakuwa na mwenye wazo, lakini hali ilikuwa kama mwanzo, hakuna aliyejibu,



"Eti tufanyaje jamani, Juddy wewe una wazo gani?" Othman Tafu aliamua kumtaja mtu kabisa ili ajibu swali lake,



"Mimi nadhani ni vyema tukaomba ushirika na radio maarufu ilo linaweza kutusogeza" Juddy alijibu na kutulia kimya huku akisubiri neno kutoka kwa othman Tafu,



"Ni wazo vzuri Juddy, ila ushirika unaweza ukafanya tukanyonywa zaidi, maana radio maarufu ni radio kubwa sasa tukiamua kushirikiana nao ni lazima tupoteze brand yetu" Othman Tafu alijibu na kutulia kidogo,



"Kwanini tusijitanue na kufanya tusikike zaidi ya hapa, maana tunasikika mikoa miwili minne tu, kwanini tusiongeze hata mingine miwili iliyo na watu wengi, ili litatusaidia nadhani" Mfanyakazi mwingine alitoa mchango wake,



"Sasa hapo katika kuongeza mikoa ya kusikika ni kuzungumzia matumizi ya pesa, yaani inabidi utoe pesa ili kujenga minara katika mikoa husika, na lengo langu mimi si kutoa pesa, nimeileta ajenda ili tuingize pesa" Othman Tafu alijibu na kunywa maji yaliyokuwepo katika glass yake mbele ya meza aliyokuwa amewekea lap top yake,



"Nafikiri ni vyema tulete wafanyakazi wenye elimu ya hii kazi, hilo litakuwa jambo bora nadhani" Mfanyakazi mwingine alichangia na kufanya wale wafanyakazi wasio na vigezo kumtupia hicho lenye hasira kwa maana alikipendekeza kitu kilichoonekana kitawaharibia kazi,



"Hilo sidhani kama ni sababu ya sisi kutoendelea, maana ukizungumzia wafanyakazi wenye elimu ya uhandishi wa habari ndio unawazungumzia wakina Tom ambao wapo hapa, sasa umeshawahi kujiuliza mchango wa Tom ni nini? yeye ana elimu ya hii kazi lakini utendaji wake wa kazi ni mbovu kuliko mtu yoyote, yeye ndio anaofanya mimi nisiwe na hamu hata kuleta wasomi wengine hapa kwa maana nahisi wasomi wa habari ni lazy lazy kama mwenzao Tom" Othman Tafu aliongea na kufanya wafanyakazi wengine wacheke huku wakimuangalia Tom ambaye yeye alitulia tu huku Yale maneno yakimchoma sana, tena yalimuingia haswa kwa kuwa aliona kama anadhalilishwa mbele ya wenzake,



"Au nasema uongo Tom?" Othman Tafu alimuuliza Tom baada ya kumuona kama amekosa raha baada ya kauli zake,

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Unaongea kweli, ila sisi watangazaji tunatakiwa kutangaza tu habari zinazoletwa na waandishi" Tom alijitetea huku akimtazama Othman Tafu,



"Hiyo haiko sawa, wote mnatakiwa mtafute habari, tena habari ambazo ni mpya, achana na zile habari zako unazozitoaga mitandaoni alafu unazitangaza, hizo uwa zimeshaenea na kutangazwa sana, sasa unapozitangaza tena wewe unakuwa unafanya marudio tu, habari mnatakiwa mkazitafute wenyewe na kuzitangaza kwa Mara ya kwanza nyie wenyewe, hapo inaweza kutusaidia" Othman Tafu aliongea huku akimtazama Tom,



"Tunazipataje sasa wakati hatuna vitendea kazi?" Tom alimtupia swali jingine Othman Tafu,



"Unapozungumzia vitendea kazi unazungumzia nini?" Othman Tafu akamchapa swali Tom,



"Recorder, hapa nazungumzia voice and video na pia usafiri wa kutufikisha eneo ambalo kutakuwa na tukio au chanzo cha habari" Tom alijibu kitaalam,



"Kila mtu ana smart phone hapa, hizo zote zina uwezo wa kurekodi video na audio, kuhusu usafiri sidhani kama ni kweli unapata shida Tom, gari ipo ya ofisi" Othman Tafu allimjibu Tom,



"Gari bovu kabisa, muda wote inashinda garage" Tom aliongea,



"Tembea na miguu, mbona uwa unatoka kwako kwa miguu?, acha kuwa mvivu Tom, we ni lazy lazy sana my friend" Othman Tafu alitoa tena kauli iliyomfanya Tom apate hasira kwa maana hakupenda kuonekana lazy kazini, na pia alidharauliwa kutokana na kuonekana yeye ni moja ya chanzo cha radio yao kutojitanua kwa watu kwa kuwa ana elimu ya kazi hiyo ila anashindwa kufanya kile kinachohitajika,



"Nafikiri mfanyie kazi jambo hilo la habari, kikao nakifunga maana nimeitwa Mara moja nyumbani" Othman Tafu aliongea na kunyanyuka kisha akatoka nje na kuwaacha wafanyakazi nao wakiinuka katika buti vyao na wengine wakiwa wanajadiliana mawili matatu kuhusu kikao hicho na wengine wakimtania Tom kwa kumuita neno lile lile "lazy" na kumfanya kijana wa watu akose raha mpaka ikampelekea kukasirika na kutoka nje ya ukumbi wa mikutano.



Jioni ilipofika alirudi kwake na kuingia ndani huku lile neno " lazy" likijirudia kichwani make kwa kila anachokifanya, akajiona mkosaji sana kwa maana bosi wake amemchukulia ni mtu mvivu kazini wakati uwezo wake unatosha kuikuza radio yake,



"Tatizo mi lazy lazy sana" Tom akajikuta analitamka neno hilo, baada ya kutaka kuwasha runinga ila remote ilikuwa mbali na kujikuta akiona uvivu kwenda kuichukua, baada ya kujiita lazy mwenyewe akajikuta anajichukia huku nafsi yake ikikubali ukweli kuwa lile jina "lazy" linamfaa kwa ajili ya matendo yake,



"Usikute ningekuwa hata Muandishi wa kimataifa, kazi natafuta kivivu, dah kweli lazy" Tom aliongea peke yake huku akijisikia uvivu hata wa kwenda kuoga muda huo na hivi hali ilikuwa ya baridi baridi ndiyo ilimchochea kabisa asiende bafuni,



"Ila ipo siku sitaitwa lazy" Tom aliongea na kutabasamu mwenyewe, ila hakujua neno "lazy" litakuja kuzaa matukio mabaya sana kwake, matukio yatayogharimu watu wengi sana katika ofisi yao....





Tom alijikuta akitafakati kwa muda mrefu huku akiwa bado hajavua hata nguo zake alizotoka nazo kazini,



"Njaa imeshaanza kuuma, sijui kwanini sijapitia hapo nje kununua chipsi?" Tom aliongea mwenyewe huku akijalaumu kwa uzembe wa kutokukumbuka kununua chakula ambacho kilikuwa kinauzwa nje tu ya nyumba yao, alijisikia uvivu tayari, akaitoa simu yake mfukoni na kuanza kuperuzi peruzi habari ili aipate ya kuitangaza kesho au awajulishe wenzake waliopo kazini muda huo.



Katika pita pita zake mtandaoni ndipo alipokutana na habari iliyotikisa nchi mwaka mmoja uliopita, habari iliyopewa jina la MEMORY CARD, habari iliyomuhusu waziri wa ulinzi na watu wake kutaka kuipindua nchi, ni habari iliyowapa ushujaa askari mpelelezi aliyetambulika Kama Sajenti Minja na mwanadada komando aliyekuwa akihishi ughaibuni na bila kumsahau mwandishi wa habari ambayo kwa sasa alikuwa ndio mkurugenzi wa shirika la habari nchini, bwana Edward Sambo na kijana mchezo filamu maarufu aliyeitwa Jackson Mtei.



Ila hiyo habari tayari watanzania wengi walikuwa wameshaisahau kutokana na tabia zao za mambo ya maana kuyasahau haraka kuliko yale ya kijinga ambayo ukaa nayo muda mrefu ubongoni mwao.



Tom alijikuta akivutiwa na ile habari kutokana na mtiririko wake wa uhandishi na wala sio kitu kingine, akajikuta anamsifia sana yule Muandishi ambaye aliandika habari ile ambaye hakuwa mwingine isipokuwa ni Edward Sambo,



"Amefuata kanuni zote za uhandishi, ndio maana amepewa cheo cha ukurugenzi Mkuu wa shirika la utangazaji, huyu mzee kiboko, anajua sana" Tom aliongea huku akiendelea kuangalia ile habari ambapo baadae katika kuisoma soma akagundua kuwa Edward Sambo mwenyewe alikuwa ni mmoja kati ya watu waliojitoa katika kufuatilia mpaka lile tukio likakamilika na wahusika wakakamatwa,



"Kumbe alijitoa mhanga huyu mzee!?, je na hao wenzake alioshirikiana nao Wapi wapi?, huyu sijui Sajenti Minja na huyu Sarah, huyu Jackson ni msanii najua pa kumpata, ila atakubali kweli kuhojiwa na Mimi muandishi nisiyejulikana? Lazy lazy" Tom alijiuliza na kujikuta anajicheka mwenyewe.



Kitu ambacho Tom hakukijua ni kuwa anapovutiwa kuisoma hiyo habari ndivyo alivyokuwa anajiongezea mambo ya kudadisi katika hiyo habari.



Mwisho usingizi ulimpitia huku simu yake ikiwa mkononi na nguo zake alizotoka nazo kazini bado zilikuwa mwilini.



Huyu Jamaa alikuwa lazy sana, ukiacha kushindwa kwake kwenda kuoga, hata chakula alishindwa kwenda kununua kutokana na kuona uvivu kwenda nje.



**************



Ilikuwa yapata saa moja asubuhi ndipo Tom alibahatika kufungua macho yake na kupokelewa na mwanga wa jua ulioingia kupitia dirisha lake alilosahau kulifunga usiku uliopita, akakurupuka kutokana na kuona dirisha lake limelala wazi, akahisi uenda vibaka walitumia fursa hiyo wakamkwapua, cha kwanza alichokimbilia kuangalia ni simu yake, akajikuta yupo nayo kitandani, kisha akatupia macho runinga yake ndogo iliyokuwa na jina la Phillips hotel yenye ukubwa wa inch 18 na kuikuta ikiwa wazi inaonesha taharifa ya habari kupitia katika kituo maarufu cha habari cha marekani kijulikanacho kwa jina la CNN.



Akajiinua kitandani na kwenda kuizima taa iliyolala inawaka pia, kisha akavua nguo alizolala nazo na kujifunga taulo na kuelekea bafuni kuoga.



Baada ya dakika kumi na tano alikuwa tayari ameshamaliza kuoga, akarudi chumbani kwake na kuangalia ukutani ambapo kulikuwa na nguo zake zilizotundikwa katika misumari, akaindea na kuichukua shati moja la mikono mirefu lililokuwa na rangi ya damu ya mzee, akalivaa kisha akatungua suruali nyeusi nayo akaivaa, akawa anazitafuta soksi zake bila mafanikio, hakukumbuka hata alipoziweka.



Mwisho aliinua godoro na kuzitoa soksi kuu kuu ambazo inaonekana alizitelekeza huko muda mrefu, akazivaa na kisha akavaa viatu vyake vyeusi aina ya moka. Alikuwa nadhifu sana. Alipomaliza kuvaa akaendea dressing table yake na kuchukua body spray na kujipulizia, kisha akajiangalia kwenye kioo na kutabasamu.



Baada ya hapo akachukua simu yake na wallet na kutoka zake nje, safari ya kwenda ofisini ilianza na hapo ilikuwa yapata saa tatu na dakika zake.



Akaamua kupitia mgahawani kwa maana njaa ilimshika kweli, akatafuta meza isiyokuwa na mtu na kwenda kukaa, ndipo alipoikumbuka simu yake na kuitoa mfukoni, kwa maana tokea alipoingia kwenye mtandao siku iliyopita hakutoka tena mpaka alipopitiwa na usingizi.



Alipoibonyeza simu yake ikampeleka pale pale kwenye ile ile habari ya Memory card, safari hii akaamua aisome ili aielewe vyema kwa maana ilianza kumvutia kuanzia upelelezi wake mpaka mwisho wake pia. Akaanza kuisoma tena upya huku akiweka umakini zaidi kwenye matukio kuliko kwenye upangaji wa matukio kama hawali, mwisho akajikuta amezama kabisa kwenye ile habari na taratibu akaanza kuyajenga maswali lukuki kuhusu ile habari.



"Kaka nikuhudumie nini?" Muhudumu wa mgahawa alimuuliza na kumtoa katika bahari ya udadisi iliyomzamisha kwa muda,



"Kuna kongoro?" Tom akauliza huku akimtupia macho yule binti,



"Ipo" Muhudumu alijibu,



"Nipatie kongoro na chapati nne. Inakuwa shilingi ngapi hapo?" Tom aliuliza,



"Kongoro elfu moja, chapati nne nazo ni buku, jumla elfu mbili" Muhudumu alijibu,



"Mh...punguza chapati, nipe chapati mbili" Tom aliongea baada ya kugundua mfukoni ana elfu mbili hiyo hiyo, kwa hiyo akiimaliza yote itakuwaje?



Muhudumu akaondoka na kuekekea sehemu yalipo majiko na kumuacha kijana Tom akiendelea kusoma habari.



Baada ya dakika tano muhudumu alirejea na kuviweka mezani vitu alivyoagizwa. Tom akaachana na simu na kuanza kula, alipomaliza aliondoka haraka haraka kwa maana muda ulikuwa umeenda sana kwa hiyo aliohofia anaweza kuchelewa kazini.



Aliingia ofisini na kukutana na utani ule ule anaotaniwaga wakuitwa lazy, hakuupenda ila yeye mwenyewe alikubali Ilo jina linamfaa kutokana na tabia yake,



"Leo lazy umechelewa sana" Muddy alimtania wakati wakipishana na kumfanya Tom amkate jicho Kali,



"Lazy, bosi alikuwa anakutafuta" Mtu mwingine alimwambia wakiwa wanapishana, hakutaka hata kuuliza zaidi, alielekea moja kwa moja kwenye ofisi ya bosi wake, bwana Othman Tafu, alikuta mlango upo wazi na kuingia moja kwa moja bila hodi, ndivyo alivyozoea hivyo,



"Saa tatu kasoro hii, unalala sana siku hizi" Othman Tafu alimwambia Tom,



"Hata hivyo hakukuwa na haja ya kuwahi, mi kipindi changu kinaanza saa saba mchana" Tom alimjibu bosi wake,



"Ila si lazima ufanye maandalizi mapema?" Othman Tafu alimuuliza,



"Ndio maana nimekuja saa tatu" Tom alijibu kifupi,



"Sasa leo itabidi kipindi chako kifanywe na mtu mwingine" Othman Tafu aliongea huku akiendelea kuandika andika,



"Kwanini bosi, au kwa kuchelewa huku?" Tom aliuliza baada ya kuhisi inawezekana kuchelewa kwake kumemuhudhi bosi wake,



"Hapana, unatakiwa kwenda shirika la habari la utangazaji, kuna semina pale nilitakiwa nifike Mimi, ila kwa kweli kazi zimenibana sana" Othman Tafu aliongea,



"Saa ngapi?" Tom aliuliza huku akifurahia fursa hiyo kwa kuwa ni moja ya ndoto zake kuwa mtangazaji hapo, akaona hiyo nafasi inaweza kumsaidia kupata kitu ndani shirika hilo,



"Saa nne, yaani muda mfupi kutoka sasa" Othman Kazi alijibu,



"Ninaenda peke yangu au kuna mwingine?" Tom aliuliza,



"Utaenda peke yako, maana wewe kidogo una elimu hii. Sasa usiwe mzembe kwenye kuandika au kurekodi kila mtakachoongea uko" Othman Kazi aliongea,



"Sasa pale naenda kuchukua habari au naenda kwenye semina?" Tom alimuuliza bosi wake huku akimshangaa,



"Kachukue vyote" Othman Tafu alijibu,



"Sawa, sasa vipi kuhusu usafiri maana mfukoni nina jero tu" Tom aliongea huku akiwa amepunguza sauti kidogo,



"Ila uko mkimaliza Semina mtapewa posho zenu, na chakula kitakuwa cha bure" Othman Tafu alimwambia Tom,



"Hujanielewa, namaanisha sina nauli ya kunifikisha pale, au nipeleke na gari lako basi" Tom alimwambia Othman Tafu,



"Gari ya ofisi si ipo?" Othman Tafu aliuliza,



"Asalaleh! gari ipo garage karibia wiki hii yote" Tom alijibu,



"Mbona sikupewa taharifa?" Othman Tafu aliuliza,



"Kamuulize dereva, maana hicho sio kitengo changu" Tom alijibu,



"Haya wahi basi, ukitoka uko upitie hapa" Othman Tafu aliongea huku akimrushia Tom noti ya shilingi elfu kumi. Tom akaidaka na kutoka zake nje, alikuwa anaelekea shirika la utangazaji la Taifa sasa, ambapo uko ndipo atakapoanzia upelelezi wake ambao utamsababishia matatizo ya kutisha sana, ila yeye hakulijua hilo, yeye alikuwa na furaha ya kwenda eneo hilo, na pili aliona furaha kwa kuwa alikuwa anaenda kumuona Edward Sambo, mwandishi ambae amemvutia kwa muda mfupi tu baada ya kuisoma habari yake aliyoipa jina la memory card....







Alifika maeneo ya shirika la utangazaji la Taifa yapatapo saa nne kasoro dakika chache sana, alielekea mpaka lilipo geti la kuingilia ila alikutana na upinzani mkali sana kutoka kwa Askari aliyekuwepo getini hapo,



"Unaenda wapi?" Askari alimuuliza Tom aliyeonekana ana haraka sana,



"Mimi ni mmoja wa wanahabari, tuna semina ndani" Tom alijibu huku akitabasamu,



"Kitambulisho kiko wapi?" Askari alimuuliza Tom na kumfanya ajisachi bila mafanikio na kukumbuka kuwa hajabeba kitambulisho,



"Nimesahau bro, ila naomba uniamini" Tom aliongea kwa upole,



"Nenda kalete kitambulisho chako, waandishi wote waliokuja kwenye semina wamekuja na vitambulisho vyao, sasa wewe hujabeba kitambulisho nitakuaminije?" Askari aliuliza,



"Dah, nimekisahau ndugu yangu, naomba uniamini tu" Tom alisisitiza kwa upole,



"We nenda kakifuate tu" Askari aliongea huku akimsukuma Tom aliyekuwa mguu mmoja ameuingiza ndani ya geti, na kumfanya Tom arudi nyuma huku akiendelea kumsisitiza Askari ampe nafasi ya kuingia ndani, lakini Askari huyo aliendelea kumuwekea ngumu.



"Vipi hapo?" Edward Sambo aliuliza baada ya kufuatilia kwa muda kilichokuwa kinaendelea getini, aliuliza huku akielekea pale pale getini,



"Ni huyu kijana anataka kuingia ndani, anadai yeye ni muandishi wa habari" Askari alimjibu Edward Sambo,



"Sasa si umruhusu, unavyomchelewesha hivyo ujue anachelewa semina ndani, alafu imeshaanza" Edward Sambo aliongea huku akimtazama askari,



"Tatizo hana kitambulisho" Askari alimjibu Edward Sambo,



"Ebu kijana sogea hapa" Edward Sambo alimuita Tom aliyekuwa amesimama nje ya geti akifuatilia maongezi ya Askari na Edward Sambo.



Tom akaingia ndani ya geti na kumsalimia Edward Sambo, tena alimsalimia kwa heshima zote kwa maana ilikuwa ni kama ndoto yeye kumuona mtu aliyeifuatilia kazi yake kwa siku moja iliyopita na kumfanya aupende mfumo aliotumia katika kuandika habari iliyotikisa nchi.



"Unatokea chombo gani cha habari?" Edward Sambo alimuuliza Tom,



"Natokea Tafu Radio" Tom alimjibu,



"Bosi wako anaitwa nani?" Edward Sambo alimuuliza,



"Anaitwa Othman, Othman Tafu" Tom alijibu,



"Pita ndani uwahi semina, ila acha uzembe wa kusahau kitambulisho, maana kwa hizi kazi zetu bila kitambulisho ni ngumu sana kuaminika" Edward Sambo alimwambia Tom aliyekuwa na tabasamu baada ya kuruhusiwa kuingia,



"Nimekisahau bahati mbaya tu, kwa kuwa nilikuwa na haraka" Tom alijibu huku akiwa bado na tabasamu,



"Aya kimbia ndani uwahi semina, wenzako wameshaanza" Edward Sambo alimwambia Tom huku akimsukuma sukuma,



"Baada ya semina nitahitaji kuongea na wewe" Tom aliongea huku akimgeukia Edward Sambo,



"Kimbia ndani bwana, acha uzembe kijana" Edward Sambo aliongea kwa ukali huku akimsukuma Tom na kufanya Tom aondoke huku akiwa mnyonge kwa maana alihisi ombi lake limegonga mwamba.



"Chumba cha semina kipo wapi?" Tom aliuliza baada ya kutembea mwendo kidogo,



"Hapo kwenye mlango unaokuangalia, ukiingia ndani, mlango wa pili kushoto" Edward Sambo alijibu na Tom akafanya kama alivyoelekezwa.



Aliingia akiwa amechelewa, alitafuta kiti kisicho na mtu na kukaa, kisha akatoa simu yake na kuiwasha sehemu ya kurekodi sauti na pia alichukua kidaftari chake kidogo akawa anaandika.



Baada ya Massa manne semina ilikuwa imekwisha na kila muandishi aliyefika pale alipewa kifuta jasho chake cha kuhudhuria semina ile.



Tom alitoka nje na kuangaza angaza, alikuwa anamtafuta Edward Sambo lakini hakumuona, akaamua aende getini kumuulizia,

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Bro samahani, hivi yule mzee aliyekuja kuniruhusu niingie ndani, ofisi yake ipo wapi?" Tom alimuuliza yule yule Askari aliyemzuia Mara ya kwanza,



"Ofisi yake wewe unaitaka ya nini? Ondoka bwana, nenda kaandike barua ya kuonana nae" Askari aliongea kwa mamlaka na kumfanya Tom awe mpole,



"Bro naomba unisaidie, nina shida nae muhimu" Tom aliongea kwa kusisitiza,



"Unapenda sana kusaidiwa, maana tokea nimekuona kauli yako ni hiyo hiyo ya kuomba kusaidiwa. Wewe ondoka tu, kafuate utaratibu niliokuambia hapo hawali" Askari aliongea huku akiacha njia wazi ili Tom apite. Tom akaona bahati haikuwa yake siku hiyo, akatoka nje ya geti na kuanza kuondoka huku ndani ya moyo wake akimlaani sana yule Askari aliyekuwepo pale getini kwa maana alimuona ni mtu aliyekuwa na chuki naye.



"Wewe kijana" Mtu alimuita Tom kwa sauti na kumfanya ageuke nyuma, ndipo alipomuona Edward Sambo akiwa getini. Tom akageuka kwa furaha na kwenda mpaka alipo Edward Sambo,



"Ulisema unataka kuongea na mimi, sasa mbona unaondoka?" Edward Sambo alimuuliza Tom,



"Nilikuwa naenda kununua chakula, alafu ningerudi" Tom aliongea huku akimuangalia Askari wa getini aliyekuwa anasikiliza maongezi yao,



"Kwani hayo maongezi yanahusu nini mpaka unataka tuongee ukiwa umeshiba?" Edward Sambo aliuliza huku akicheka,



"Ya kawaida tu mzee wangu" Tom nae alijibu huku akiwa anatabasamu,



"Tunaweza kuongelea hapa?" Edward Sambo aliuliza,



"Kwa hapa inawezekana" Tom alijibu huku akiwa anaangalia angalia mazingira,



"Ila twende ofisini, hapa njiani bwana" Edward Sambo aliongea huku akiwa amekwishaanza kutembea na kufanya Tom aanze kumfuata.



Walitembea mpaka sehemu kulikopokuwa na mlango wa kibuluu, Edward Sambo akausukuma na kuingia ndani na Tom nae kukaribishwa ndani ambapo tena walikuta kuna mlango wa vioo na Edward Sambo akaufungua tena na wote wakaingia ndani na Tom akakaribishwa katika kiti kilichopo pale.



"Kuwa huru kijana, hapa ni ofisini kwangu" Edward Sambo akaongea huku nae akikalia kiti chake,



"Asante, asante sana mkuu" Tom alijibu huku akiikagua ile ofisi kwa macho kuyapeleka kila upande wa ofisi ile,



"Kwanza chukua hii ndio tuelewane" Edward Sambo aliongea huku akimpa chakula Tom kilichokuwa kimefungwa kwenye karatasi ngumu za nailon,



"Asante, ila ungekula wewe mzee wangu, Mimi nikitoka hapa naenda kula hapo ng'ambo ya barabara" Tom aliongea huku akiwa anagoma kukipokea kile chakula,



"Chukua wewe, Mimi ninacho cha kwangu" Edward Sambo aliongea huku akitoa chakula kingine,



"Kwa hiyo hiki kilikuwa ni kwa ajili yangu?" Tom aliongea huku akikipokea kike chakula,



"Hutakiwi kujua hilo, wewe unachotakiwa ni kula tu" Edward Sambo aliongea huku akikifungua kile chakula ambacho kilikuwa ni chipsi zilizoambatanishwa na finyango chache za kuku,



"Nashukuru kwa chakula, lakini sioni vinywaji" Tom aliongea huku akicheka, alishaanza kumzoea Edward Sambo,



"Vinywaji nunua wewe sasa, maana Mimi nimenunua chakula" Edward Sambo aliongea na wote wakacheka,



"Kwanza nishukuru kwa ukarimu wako, pili nishukuru kwa kunikaribisha hapa" Tom aliongea huku akiwa anamtazama Edward Sambo,



"Usijali kijana, naona uelekee moja kwa moja kwenye point iliyokufanya utake kuzungumza na Mimi" Edward Sambo aliongea,



"Kwanza napenda ujue kuwa Mimi ni mmoja wa watu waliotokea kupenda uandishi wako wa makala mbalimbali na habari, yaani umenifanya niipende kazi hii kwa muda wa Siku moja tu, yaani jana nimesoma kazi yako na nikajifunza vitu vingi sana" Tom aliongea kisha akachukua paja la kuku na kulipachika mdomoni,



"Sawa nimekuelewa na nashukuru kwa kusema Mimi ni mmoja kati ya watu wanakuvutia katika uandishi wa habari" Edward Sambo aliongea,



"Sasa kati ya habari ulizoandika, kuna moja nataka niiendeleze kwa kuifuatilia zaidi, nimeona pale ulipoishia wewe sio mwisho, nadhani natakiwa kujua maendeleo ya watu waliohusika na lile tukio wapo wapi na wanaendeleaje kwa sasa",Tom aliongea na kujiachia nafasi ya kumeza mate,



"Ni habari nyingi nimeandika, wewe unataka kuifuatilia habari ipi?" Edward Sambo aliuliza huku akiwa na shahuku ya kuijua hiyo habari,



"Ni ile habari ya MEMORY CARD" Tom aliongea na kumfanya Edward Sambo aangushe chakula ambacho kilikuwa mkononi mwake, na hata sura yake ilibadilika ghafla....







Ile hali ilimfanya Tom ashtuke kidogo na kumkazia macho Edward Sambo,



"Vipi mzee mbona hivyo?" Tom aliuliza huku akiwa bado anamuangalia,



"Ni bahati mbaya tu imetokea" Edward Sambo alijibu huku akinyanyuka na kusogeza kiti chake, akachukua kitambaa kidogo na kuanza kufuta chini katika eneo ambalo chakula kilidondokea, zoezi hilo alilifanya kwa dakika mbili kisha akachukua ule mfuko na kwenda kuuweka ndani ya kindoo cha plastiki kilichokuwa ndani ya ofisi yake, kisha akarudi kukaa kwenye kiti chake.



"Kwanini umeamua kuifuatilia hii habari?" Edward Sambo aliuliza, tena safari hivi hata sura yake ulikuwa tofafauti na mwanzo, muda huu alikuwa ni mtu makini kabisa,



"Nadhani mlolongo mzima ulivyokuwa umeuandika, nimependa niufuatulie ili na mimi niandike kitu hapo" Tom alijibu huku akioyaona mabadiliko yaliyokuwa dhahiri usoni mpwa Edward Sambo,



"Sasa ni sababu gani iliyokufanya uje kwangu, kwanini usingeanza tu kuifuatilia?" Edward Sambo aliendelea na maswali,



"Nimekuja kuomba kuiendeleza kwanza hii habari, na pili nimekuja kukuomba ushahuri ili nipate pa kuanzia" Tom aliongea huku akijitahidi kumuangalia Edward Sambo,



"Nafikiri wewe kama Muandishi hukupaswa kufanya hivyo vyote, ulichotakiwa kufanya ni kuanza tu kufanya uchunguzi wako taratibu juu ya unachokitaka, alafu ungeibuka na habari yako" Edward Sambo alimwambia Tom,



"Ni sawa mzee, ila hapa kama utanisaidia namba za watu mliokuwa mmeshirikiana kutekeleza ule mpango, nikawatembelea kidogo ili nao nisikie mawili matatu kutoka kwao, itanisaidia kidogo" Tom alijitahidi kuongea ili kumuelewesha Edward Sambo,



"Fanya nilichokwambia, hizo namba unazozitaka itakuwa ni hatua ya mwisho kabisa ya kazi yako" Edward Sambo aliongea,



"Alafu naomba nikuulize kitu kingine" Tom aliongea,



"Uliza tu" Edward Sambo alimruhusu,



"Kwanini ulishtuka nilivyosema habari ninayotaka kuifuatilia ni hivi ya memory card?" Tom aliuliza kwa kujiamini,



"Wewe si umesema unataka kuifuatilia? Ifuatilie tu alafu utayapata tu unayoyataka" Edward Sambo aliongea na kumtia hofu kidogo Tom,



"Unamaanisha nini kusema hivyo?" Tom aliuliza,



"Kama umedhamiria kufanya hivyo, pambana sana, ni vita ya wakubwa hiyo" Edward Sambo aliongea na kuzidi kumchanganya Tom,



"Ila kauli zako zinanitisha mzee" Tom aliamua kuongea ukweli uliokuwa moyoni mwake,



"Hapana sikutishi, kama unaona unachokifanya kitakusaidia, basi usirudi nyuma, shikilia maamuzi yako, epuka kuwa lazy" Edward Sambo aliongea kwa hisia,



"Ila Mimi sio lazy mzee" Tom aliongea huku akionekana kukereka na lile neno,



"Sijakuita lazy, nimekwambia epuka kuwa lazy" Edward Sambo aliongea,



"Sasa kwa ukongwe wako katika tasnia hii, ungenishauri nianzie wapi nikitoka hapa?" Tom aliuliza,



"Mimi sina cha kukusaidia, ila cha kukushauri ni kwamba unatakiwa kwenda sehemu ya mwisho iliyotoa hukumu kwa wahusika" Edward Sambo aliongea,



"Unamaanisha mahakamani?" Tom aliuliza,



"Hapo ndipo unatakiwa kuanza napo" Edward Sambo aliongea,



"Basi nashukuru, naomba uniruhusu niondoke" Tom aliongea huku akijenga tabasamu usoni,



"Sawa nenda, karibu sana ofisini kwangu" Edward Sambo aliongea huku akisimama na kumsindikiza Tom ambaye alikuwa anajiandaa kuondoka.



Wakatoka mpaka lilipo geti la kutokea na kurudia tena kuagana kwa kushikana mikono na Tom akawa anaondoka zake huku Edward Sambo akiwa amesimama pale pale walipoachana akimuangalia Tom.



"Dogo" Edward Sambo alimuita Tom aliyekuwa tayari amemuacha umbali kidogo,



"Naam" Tom aliitika na kusimama kisha akageuka kumtazama Edward Sambo,



"Kuwa makini sana, jiandae kwa kila kitu" Edward Sambo aliongea kisha akageuka na kuondoka zake, hakutaka kusubiri neno lolote kutoka kwa Tom.



Tom alizidi kuogopeshwa na maneno ya Edward Sambo, mpaka akawa anajiuliza ni kwanini Edward Sambo anamsisitiza kiasi kile. Ila wakati ule msisitizo wa Edward Sambo ukimpa mashaka, ndio wakati huo huo ule msisitizo ulimuongezea shauku ya kutaka kujua zaidi ni kipi kinafanya mpaka Edward Sambo amsisitize namna ile.



Tom alifika ofisini kwao ikiwa imeshaingia mida ya jioni, alipitiliza moja kwa moja kwenye ofisi ya Othman Tafu na kumkuta akiwa amejiweka kwenye kiti chake cha kuzunguka. Othman Tafu alipomuona Tom tu, alianza kutabasamu,



"Tugawane bwana pesa ya semina" Othman Tafu aliongea huku akitabasamu,



"Ni ndogo tu, wewe na mapesa yako yote uliyonayo bado unataka tu kuninyonya mimi masikini?" Tom nae aliuliza huku akicheka.



"Naimani semina ilikuwa nzuri, haya niambie ni nini kilichoongelewa uko?" Othman Tafu alimuuliza Tom.



Tom hakujibu na badala yake alitoa simu yake na kumsikilizisha Othman Tafu kila kitu kilichoongelewa uko,



"Naona muda unaenda tu alafu hiyo audio ni ndefu sana, kwanini nisikurushie tu kwenye simu yako ukasikilizie kwako?" Tom alimuuliza Othman Tafu,



"Kwani unawahi wapi?" Othman Tafu alimuuliza Tom,



"Nimechoka sana, nahitaji nikapumzike mzee" Tom alijibu huku akiweka sura ya unyong'onyevu,



"Basi nirushie, nitaisikiliza nyumbani nikiwa nimetulia" Othman Tafu alimwambia Tom ambaye alianza kufanya kazi ya kumrushia ile audio muda huo huo,



"Alafu bosi Nina ombi" Tom aliongea wakati akirusha ile audio,



"Ombi gani hilo, isiwe unataka kuniomba ruhusu ya kutokuja kazini, maana ulivyo lazy hivyo unaweza kusingizia hata hii semina imekuchosha" Othman Tafu aliongea huku akimuangalia Tom,



"Kweli, nilikuwa nataka ruhusa ya kutokuja kazini kesho" Tom aliongea huku akimtazama bosi wake,



"Si unaona?! nilisema mimi. Nipe sababu itakayokufanya usije kazini kesho" Othman Tafu aliuliza,



"Kuna habari naifuatilia" Tom alijibu.



"Habari gani hiyo?" Othman Tafu aliuliza kwa shauku, na Tom akamueleza kila kitu kilivyokuwa,



"Kwa hiyo cha muhimu ni kumuangalia mtu mwingine wa kumpachika katika kipindi changu kwa muda wote ambao sitokuwepo kazini,



"Ni wazo zuri, sasa umejiandaaje kwa upande wa masuala ya pesa, maana kwa uzoefu wangu, kuifuatilia habari inahitajika fedha ya kutosha" Othman Tafu aliongea huku akiwa anaing'ata kalamu yake,



"Tukubaliane kitu, hivi habari nikiifuatilia kwa gharama zangu alafu nikafanikisha, nitawauzia nyie kwa pesa ninayotaka Mimi, ila kama mtanigharamia kila kitu, basi habari itakuwa ya ofisi hii" Tom aliongea huku akimuangalia Othman Tafu aliyekuwa anaitafakari ile kauli,



"Wewe ni mfanyakazi wa hapa, kwa hiyo kila ambacho unakihitaji katika ufuatiliaji wa habari yako, ni lazima tugharamie sie" Othman Tafu aliongea baada ya tafakari ya muda,



"Basi kesho naanza kazi, gharama za safari yangu kesho itabidi mnipe leo" Tom aliongea huku akimuangalia Othman Tafu,



"Kwa kesho katumie gharama zako, alafu jioni utanitumia jumla ya pesa uliyotumia alafu nitakutumia katika simu, angalia sana usitumie pesa hovyo" Othman Tafu alimuonya Tom.



Wakafanya na makubaliano mengine na kisha Tom akaondoka zake kwenda kwake kwa ajili ya kupumzika ili kesho aianze kazi yake.



******"*************



Asubuhi kulipambazuka na Tom alijitahidi kupambana na usingizi na akaushinda, akaamka na kwenda kujifanyia usafi wa mwili, alipomaliza alitoka mpaka mgahawani kupata kifungua kinywa na alipomaliza aliamua kuelekea mahakamani ambapo alishauriwa na Edward Sambo kuwa aanzie hapo.



Alipofika mahakamani alielekea moja kwa moja kwa karani wa mahakama na kumueleza shida yake, karani akamuelekeza mtu wa kuongea nae ambae alikuwa ni mtu wa makamo kidogo,



"Mimi naitwa Thomas Anton, ni Muandishi wa habari wa Tafu Radio" Tom aliongea huku akimtazama yule mzee,



"Haya sema kijana, una shida gani?" Mzee alimuuliza Tom,



"Nahitaji kupata file la maamuzi ya kesi ya memory card iliyofanyiwa maamuzi ndani ya mahakama hii" Tom aliongea huku akimtazama yule mzee aliyepata mshtuko wa ghafla,



"Kijana ondoka, mimi bado naupenda uhai wangu" Mzee aliongea huku akitetemeka na pia akimuangalia Tom kwa uoga...







Kauli ya yule mzee iliendelea kuongeza hisia za vitisho kwa Tom na iliongeza hamu ya kujua ni kipi kilichomtia hofu Edward Sambo na mzee huyo wa mahakama.



"Kwanini unasema hivyo mzee wangu?" Tom alimuuliza yule mzee aliyekuwa na kila dalili za hofu usoni mwake,



"Usiulize hivyo wakati wewe mwenyewe unajua" Mzee alitoa kauli nyingine tata,



"Najua nini sasa mzee wangu?, Mimi nimekuja kufanya kazi na wala sijui chochote" Tom alijibu huku akimshangaa yule mzee,



"Isije ikawa mnanitegea mtego, kwa maana mnajua niliyebaki najua siri hiyo ni mimi peke yangu tu" Mzee alihoji huku akiwa na hofu,



"Mzee wangu ujue unaongea mambo ambayo siyajui kabisa" Tom aliongea huku akiwa amemkazia macho yule mzee,



"Naweza kukuamini au kutokukuamini unachosema, lakini nataka unihakikishie usalama wangu kwanza" Mzee aliongea huku macho yakiwa makavu kabisa. Watu waliokuwa pembeni hawakujua kinachoongelewa kati ya awa mabwana wawili.



"Usalama upo mzee wangu" Tom aliongea huku akiwa hajui ni usalama gani mzee anaoulizia,



"Upo? upo kiaje sasa?" Mzee alihoji huku akimuangalia Tom,



"Usijali mzee wangu, Mimi ni usalama wa Taifa, kwa hiyo kila ninachokifanya kipo chini ya usalama mkubwa sana" Tom aliamua kudanganya kwa maana aliona bila kufanya hivyo hawezi kupata habari yoyote kutoka kwa huyo mzee,



"Mimi nilivyokuona nilikujua tu, maana muandishi wa habari hawezi kuwa hivyo" Mzee aliongea huku akimkagua Tom kwa macho,



"Si unajua ni lazima tuwe na njia nyingi za kuwaingilia nyie wananchi wa kawaida" Tom aliongea huku akitabasamu,



"Lakini bado sikuamini, maana miongoni mwenu maafisa usalama wapo wale watu" Mzee aliongea na kumfanya Tom azidi kujiuliza ni kitu gani kilichokuwepo katika ile kesi ya memory card kiasi kwamba Mzee yule alishindwa kujiamini kabisa?



"Mzee mimi nipo hapa kwa ajili ya nchi yangu, na ukweli wako ndio utaisaidia hii nchi, kwa hivyo kuwa huru na niambie kila kitu unachojua kuhusu ile kesi ya Memory Card" Tom aliongea huku akiwa amemkazia macho yule mzee,



"Nadhani uje kesho kijana, leo nitakuwa nakudanganya kwa maana ni mlolongo mrefu sana" Mzee alimwambia Tom,



"Basi niambie hata kwa ufupi tu mzee wangu" Tom aliongea huku akimtazama yule mzee,



"Hapana, nadhani kesho ndio itakuwa siku nzuri kwa maana itakuwa jumamosi, kwa hiyo nitakuelekeza uje nyumbani kwangu kutokana na hili eneo kutokuwa salama kutokana na miongoni mwao wale watu wabaya kupachikwa kati yetu" Mzee aliendelea kuongea,



"Sawa basi nielekeze kwako ili kesho nije" Tom aliamua kukubali ingawa alijua kuwa kesho ni mbali. Mzee akamuelekeza nyumbani kwake.



"Nije muda gani ndio utakuwa umeshaamka?" Tom alimuuliza mzee,



"Mimi kila siku naamka saa kumi na moja alfajiri na kufanya usafi wa nyumba na mazoezi, kwa hiyo njoo hata saa moja asubuhi" Mzee alimjibu Tom,



"Kwanini ufanye wewe usafi, si wafanye wanao au mkeo?" Tom aliuliza kwa utani huku akitabasamu,



"Naishi peke yangu, sina make wala watoto" Mzee alijibu kwa unyonge,



"Wpo wapi sasa?" Tom aliuliza huku akimuangalia yule Mzee,



"Yote utayajua kesho mwanangu, tuombe uzima tu" Mzee aliongea kwa masikitiko na kumfanya Tom azidi kuhisi kuna mengi sana hayajulikani kuhusu hii kesi ya memory card.



"Sawa mzee wangu, je naweza kuwapata mahakimu waliokuwa wanaiendesha hii kesi?" Tom aliuliza na kumfanya mzee awe mnyonge zaidi,



"Wote wamekufa" Mzee alijibu na kumzidishia maswali Tom,



"Kwanini sasa?" Tom aliuliza,



"Shika hizi, alafu naomba uniache tutaongea kesho" Mzee aliongea huku akimpa karatasi iliyokuwa na ramani iliyoonesha mitaa ya eneo Fulani,



"Hii ya nini sasa?" Tom aliuliza,



"Hizi ni ramani za kukufikisha walipokuwa wanaishi hao mahakimu, nenda na ukazihoji familia zao, zinaweza kukusaidia kidogo" Mzee aliongea kwa sauti ya chini kidogo,



"Kwanini usinipe habari zao kidogo?" Tom alimuuliza mzee,



"Kijana nenda tu, nimeshakwambia hapa sio mahala salama pa kuzungumzia hayo" Mzee alijibu baada ya kumuona yule Dada karani akiwatazama sana kwa jicho la chini chini,



"Saw a basi acha Mimi niende, kesho nitaamkia kwako mzee" Tom aliongea huku akinyanyuka katika kiti,



"Sawa we nenda, Mimi hata sikutoi" Mzee alijibu huku akimpa mkono Tom kama ishara ya kuagana salama, kisha Tom akawa anaondoka kuelekea zake nje.



"Kaka huagi?" Dada karani ambaye ndiye aliongea mwanzoni na Tom aliongea huku akitabasamu,



"Samahani Dada, Nina mambo mengi" Tom alijijitea huku nae akitasamu,



"Mmeshaongea nae mzee?" Dada karani aliuliza huku tabasamu lake likiwa bado halijamuacha,



"Tumeongea kidogo, kasema mengine tutayaongea kesho nyumbani kwake" Tom alijibu kwa uchangamfu,



"Sawa, yule mzee ni mjomba wangu" Dada karani aliongea,



"Kumbe mjomba wako?, safi sana. Mjomba wako ni mtu poa sana" Tom aliongea huku akimtupia hicho yule mzee ambaye walikuwa nae umbali mrefu kidogo lakini yule mzee alikuwa akiwaangalia huku sura yake ikiwa imenesha imenyong'onyea kabisa kutokana na kile kitendo cha Tom kuongea na dada ambae ni karani,



"Sawa bwana, acha sisi tuendelee na kazi" Dada karani alimwambia Tom,



"Sawa bwana, kazi njema" Tom aliongea huku akiwa anaondoka pia akiishangaa hali ya yule mzee aliyekuwa na sura ya kukata tamaa, alitamani kurudi kumuuliza ila alijipa moyo kuwa kesho ikifika atamuuliza yote hayo.



Tom alitoka nje na kutafuta usafiri uliomfikisha mpaka anapokaa na siku hiyo hakutaka kununua chakula, aliamua apike mwenyewe geto kwake pale, kwa kuwa alikuwa na jiko la gesi na vyombo vichache anavyotumiaga, aliamua apike ugali na mboga alipika mayai aliyoyakaanga kwa kuchanganya nyanya na kitunguu na huo ndio ukawa mlo wake wa mchana kwa siku hiyo.



Alipomaliza kula alitoa karatasi na kuandika kila kitu alikifanya siku hiyo kuhusu habari ya memory card, na hakuficha chochote mpaka wasiwasi aliokuwa nao yule mzee aliuandika na mwisho Tom akajikuta anacheka peke yake, cheko la furaha baada ya kuona kazi yake ameianza vizuri bila kikwazo chochote.



Mwisho wa maandishi yake alimaliza kwa kuandika " MWISHO WA SIKU YA KWANZA".



Baada ya hapo alichukua karatasi nyingine na kuandika kupiga hesabu ya gharama alizotumia siku hiyo na kupata kuwa ni shilingi elfu saba tu,



"Sasa hapa itabidi niweke elfu ishirini, watajua wenyewe" Tom aliongea huku akiziweka zile karatasi pembeni na kisha alitumia muda huo wa mchana kulala kwa ajili ya uchovu alioupata kutokana na mzunguko alioufanya siku hiyo.



***************"******



Siku iliyofuata asubuhi na mapema, Tom aliamka na kujiandaa kwa ajili ya safari ya kwenda kwa mzee, aliona bora akatafute kabisa kifungua kinywa kwa maana alishajua kuwa mzee anaishi peke yake kwa hiyo hakuwa na uhakika wa kuweka kupata mlo wowote kwa huyo mzee.



Alipomaliza kunywa chai aliondoka na kuelekea kituo cha daladala na kujipakia, safari ya kwenda kwa mzee ikaanza. Muda wote ndani ya daladala Tom alikuwa ana furaha, furaha ya kwenda kujua kitu kilichokuwa kinawapa hofu Edward Sambo na Mzee.



Baada ya kushuka katika gari, alianza kupatafuta kwa mzee kwa kutumia ramani aliyopewa na mzee siku iliyopita, alifanikiwa kufika mpaka kwenye nyumba ya mzee, ila kuna kitu kilimshangaza, alikuta nyumba imezungukwa na watu wengi sana wakiwemo polisi, Tom akapata wasiwasi kuwa uenda mzee alimdanganya kuwa anaishi pale kumbe haishi pale.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Tom akapiga moyo konde na kuanza kujisogeza eneo hilo ili hata kama sio kwa yule mzee, basi apate kujua kilichotokea hapo kwa kuwa na yeye ni mwandishi wa habari aliamua kufuatilia kilichotokea hapo,



"Aisee kuna nini hapa?" Tom alimuuliza mwanadada aliyekuwa anajichomoa kujiondoa katika lile kundi la watu,



"Mzee anayeishi humu amekutwa amechinjwa" Mwanadada alimueleza Tom,



"Yupi, ni yule wa mahakamani?" Tom aliuliza huku akiwa ametoa macho,



"Ndiyo huyo huyo, maskini mzee wa watu alikuwa mpole sana" Mwanadada alimalizia kwa masikitiko huku akiondoka.



"Sasa kwanini ameuawa?" Tom alijiuliza mwenyewe huku akishangaa namna mambo yanavyoharibika.



Tom alishtuliwa na mlio wa simu yake iliyokuwa inaita mfukoni, akaitoa na kukuta ni namba ngeni inampigia, akaiangalia sekunde chache huku akijaribu kuikumbuka bila mafanikio,



"Hallow" Tom aliongea baada ya kuipokea,



"Unaona sasa balaa ulilolianzisha?, Mzee Bonny ameuawa kwa sababu yako kijana" Mpiga simu aliongea na kumfanya Tom apate mshtuko kwa maana aliyempia simu hamjui na amejuaje habari zake na mzee bonny aliyechinjwa?



"Kwani naongea na nani?" Tom aliuliza huku akiwa bado anashangaa,



"Mimi ni Edward, Edward Sambo" Mpigaji alijibu na kukata simu na kumuacha Tom akiendelea kuongeza idadi ya viulizo na mishangao ndani ya kchwa chake......









Tom akabaki ameduwaa huku akiwa anashangaa mambo yanavyomuendea,



"Huyu Edward Sambo amejuaje kuwa Mimi niliongea na mzee Bonny, na kwanini aseme kuwa Mimi ndiye nilimponza mzee Bonny mpaka akachinjwa? mh...hapa sio bure, ni lazima Edward Sambo atakuwa anajua kitu hapa" Tom alijiuliza huku akiwa amesimama peke yake.



Wakati akiwa bado amesimama huku mwili wake ukiwa umepigwa na ganzi, ndipo aliposhuhudia mwili wa Mzee Bonny ukipakiwa katika gari ya polisi huku ukiwa umefunikwa na shuka mwili mzima, Tom akaamua asogee karibu ili ahakikishe kama ni kweli yule mzee waliyeongea nae siku iliyopita ndio amekufa au? Tom akasogea mpaka lilipo gari la polisi lililokuwa na mwili wa mzee Bonny ila alishindwa kuufunua kwa kuwahofia maaskari,



"Vipi wewe, mbona unautazama mwili wa marehemu kwa wasiwasi namna hiyo?" Askari aliyekuwa ndani ya gari alimuuliza Tom,



"Mimi ni Muandishi wa habari kaka, nilikuwa nataka kupata picha ya huu mwili ukiwa bila shuka, sasa nikawa nafikiria namna ya kukuomba hiyo nafasi" Tom aliongea huku akitabasamu,



"Kwani ndani humkupata nafasi ya kupiga picha?" Askari alimuuliza Tom,



"Yaani mimi ndio nafika eneo la tukio" Tom alimjibu askari,



"Ebu leta kitambulisho chako" Askari alimwambia Tom ambaye alikitoa kitambulisho bila kusita na kumpa Askari ambaye alikipokea na kukitazama kwa muda,



"Nitakufunulia eneo la juu tu, yaani kifuani mpaka kichwani" Askari aliongea huku akimuangalia Tom,



"Sawa, nitakushuru sana" Tom alijibu huku akikirudisha kitambulisho chake mfukoni,



"panda juu ya gari" Askari aliongea na Tom akapanda katika gari kisha mwili wa Mzee Bonny ukafunuliwa na Tom akaupiga picha mbili za haraka haraka. Ulikuwa ni mwili wa mzee yule yule waliyeongea nae siku iliyopita, hakika mwili ule ulitisha kwa maana ulikuwa mwili usiokuwa na kichwa, kichwa kilichokatwa kiliwekwa juu ya kifua chake.



"Nashukuru sana kwa msaada wako, hapa habari yangu itakuwa imekamilika" Tom aliongea huku akiwa anajiandaa kushuka,



"Ebu niachie hela ya chai" Askari aliongea huku akiivuta shati ya Tom kwa nyuma, Tom akajisachi na kutoa elfu tano na kumpatia,



"Hapo poa eeeh?" Tom alimuuliza baada ya kumpa hela,



"Hapa sawa" Askari alijibu wakati Tom akitelemka katika gari.



Tom alivyoshuka katika gari alikuwa amechanganyikiwa kabisa, yaani kifo cha Mzee Bonny kilimvuruga kabisa, alishindwa kuelewa kabisa kinachoendelea, alisimama eneo la tukio kwa muda huku akitafakari kuwa aanzie wapi baada ya Mzee Bonny kuuawa?



"Jana kule mahakamani kulikuwa na binti aliniambia huyu mzee ni mjomba wake, ngoja nianzie uko, najua ni ngumu kumkuta ila naweza kupata mawasiliano yake" Tom aliwaza na kuwazua na mwisho aliamua kwenda mahakamani.



Alienda mpaka barabarani kwa ajili ya kusubiri daladala, hakukaa sana kabla ya daladala kufika, akajipakia na safari ya mahakamani ikaanza.



Njia nzima bado alikuwa anafikiria tu lile tukio la Mzee Bonny, pia alianza kuamini inawezekana yeye ndio chanzo cha kifo cha mzee yule.



Daladala ilisimama katika kituo anachoshukia Tom, akatelemka na kuongoza moja kwa moja katika ofisi aliyoenda siku iliyopita, ofisi aliyokuwa anakaa Mzee Bonny, ila pale hakwenda kwa ajili ya Mzee bonny, alikwenda kwa ajili ya yule Dada aliyejitambulisha kuwa ni mjomba wa mzee Bonny.



Aliingia katika ofisi ile na kuwakuta wakinamama watu wazima wawili na wote walikuwa na sura za majonzi, Tom aliwasalimia kwa heshima na kisha akajitambulisha,



"Sasa kilichonileta hapa sio marehemu Mzee Bonny, ni yule mjomba wa kike wa mzee Bonny ambae ni karani wa mahakama hii" Tom aliongea na kufanya wale wanawake waangaliane kwa muda,



"Mzee Bonny hakuwa na ndugu ofisi hii" Mama mmoja akajibu huku akimshangaa Tom,



"Jamani jana nilimkuta Dada kasimama pale na yeye ndiye alinielekeza niende kwa Mzee Bonny ndio mwenye uwezo wa kusikiliza matatizo yangu, na wakati wa kuondoka aliniita na kuniambia yeye anamuita Mzee Bonny Mjomba" Tom aliwaelewesha wale wakinamama,



"Mimi nilikuona wakati unaondoka, na yule Dada uliyekuwa unaongea nae wala sio mfanyakazi wa hapa na wala hana undugu na mzee Bonny, anakujaga tu mara kwa mara hapa ofisini kwetu, labda ana kesi zake anafuatilia" Mwanamama akampa Maelezo Tom, Maelezo yaliyokuwa na muendelezo wa kumvuruga Tom,



"Kwa hiyo sio ndugu wa Mzee Bonny na wala sio mfanyakazi wa hapa?" Tom aliuliza kanakwamba hakuyasikia Maelezo ya yule mwanamama,



"Nilichokueleza ndio hicho, yule Dada hatumjui ingawa kila siku anakuja hapa muda mchache baada ya marehemu Mzee Bonny kuingia" Mwanamama aliendelea kumueleza Tom,



"Leo hajaja?" Tom aliuliza kwa pupa,



"Hajafika, na uwa anakujaga mapema tu, nashangaa leo hajafika mpaka muda huu" Mwanamama aliendelea kusema anachokijua,



"Kwani wafanyakazi wengine wote mnaofanya nao kazi katika ofisi hii wamefika leo?" Tom aliuliza,



"Wote wamefika na wamesaini, ila tulipopata taharifa ya msiba, ndio wameelekea huko msibani" Mwanamama aliongea,



"Msiba si utakuwa pale pale nyumbani kwake?" Tom aliuliza swali la kimitego ili ajue kama mzee Bonny ana ndugu katika maji huu,



"Ndio, ila Kule kwake kwa zamani ambapo anaishi mkewe na watoto" Mwanamama alitoa jibu lilimuongezea swali Tom,



"Aisee mimi hata sipajui, unaweza kunielekeza?" Tom aliuliza na kuelekezwa na kisha akaondoka huku akijiuliza kuwa yule Dada aliyejitambulisha kuwa Mjomba ake ni Mzee Bonny, ni nani yule Dada?, aliwaza sana lakini hakupata jibu lililokuwa Kamili, akaamua asiumize kchwa huku akiamini ukifika muda sahihi atajua ukweli wa Mambo.



Alipotoka eneo la mahakamani aliamua aelekee shirika la habari kwa maana aliona kule atapata mwanga kutokana na Edward Sambo kujua anajua vitu fulani kuhusu mauaji ya Mzee Bonny.



Safari hii alitafuta boda boda kwa maana aliona daladala zitamchelewesha tu. Alipata usafiri wa kumpeleka shirika la utangazaji, alishuka na kumpa haki dereva wa bodaboda na akawa anaelekea katika geti la shirika la utangazaji, alipofika getini hata hakusumbuliwa sana kama kipindi cha kwanza, aliambiwa aoneshe tu kitambulisho kisha akaruhusiwa kuingia ndani ya geti.



Alinyoosha moja kwa moja mpaka katika ofisi ya Edward Sambo, kwa kuwa hakuwa mgeni sana kipindi hiki, aliweza kufika ofisini kwa Edward Sambo na bahati nzuri hakukuta mgeni mwingine, akapitiliza moja kwa moja mpaka ndani ya ofisi na kumkuta Edward Sambo akiwa anaandika andika mambo yake,



"Kijana ujio wako hapa unaweza kunisababishia matatizo, maana umeshakuwa kama kirusi" Edward Sambo aliongea huku akiwa hamuangalii kabisa Tom na badala yake aliendelea kuandika mambo yake,



"Samahani, Mimi nimekuja kwa swali moja tu, ni nani amemuua mzee Bonny na kwanini?" Tom aliuliza huku akimuangalia Edward Sambo,



"Sasa mbona hayo ni maswali mawili, nani na kwanini" Edward Sambo alijibu huku akifunika makaratasi yake mezani,



"Sawa ni maswali mawili, naomba unisaidie kuyajibu yote" Tom aliongea huku akiona kweli Edward Sambo ni mtu makini,



"Mimi nitajibu swali moja hapo, sasa wewe chagua nikujibu lipi?" Edward Sambo aliuliza,



"Ni kwanini Mzee Bonny ameuawa?" Tom aliamua kuchagua hilo swali kwa sababu aliona jibu la hilo swali linaweza kumfanya amjue na muuaji,



"Ameuawa kwa sababu alitakiwa asiitoe siri ambayo aliitaka kuitoa kwako" Edward Sambo alijibu Tom,



"Siri gani hiyo?" Tom aliuliza,



"Nilitakiwa nijibu swali moja tu, na nimeshalijibu" Edward Sambo aliongea na kufunua karatasi zake na kuendelea kuandika,



"Dah mbona mambo yanazidi kuwa mazito hivi?" Tom aliuliza huku akiwa hategemei jibu lolote kutoka kwa Edward Sambo,



"Samahani, naomba uniache nifanye shughuli zangu, maana hii ni ofisi yangu na nahitaji kuwa peke yangu" Edward Sambo aliongea huku akimaanisha baada ya kuna Tom anampigia kelele tu,



"Lakini mzee ninahitaji msaada wako kwa maana inaonekana wewe unajua kitu" Tom aliongea huku akimuangalia Edward Sambo,



"Unapenda kuna kilichotokea kwa mzee Bonny kinatokea na kwangu?" Edward Sambo alimuuliza Tom,



"Hapana, sitaki kuona" Tom alijibu,



"Basi naomba uniache na hizo habari, wewe nenda zako na utafute njia nyingine za kupata habari unayoitaka" Edward Sambo alimjibu Tom,



"Mzee lakini kuficha uharifu ni uharifu pia, unakubali kuwa muharifu?" Tom alimuuliza Edward Sambo,



'Nilishakwambia siwezi kujibu swali lolote kutoka kwako, nakuomba uondoke kabla sijaita askari wa ulinzi hapa" Edward Sambo aliongea huku akionekana kutopenda uwepo wa Tom mule ndani ya ofisi.



Tom aliamua kuondoka zake kwa maana aliona Edward Sambo hatanii. Tom alitoka kinyonge na kuelekea nyumbani kwake.



Alipofika nyumbani kwake, Jamaa ambae wamepakana nae chumba alimpatia bahasha ya kaki,



"Hii imetoka wapi?" Tom aliuliza huku akiipokea,



"Imeletwa na Dada mmoja asubuhi ulivyotoka, amesema ni mzigo wako" Jamaa alijibu huku akiondoka zake, hakutaka maswali zaidi.



Tom akaiangalia ile bahasha kwa muda, akaipuuza na kuingia nayo ndani. Akavua nguo na kwenda kuoga, alipotoka bafuni akaenda kununua chakula na kurudi nacho ndani kisha akala.



Alipomaliza kula ndipo alipoikumbuka ile bahasha, akaichukua na kuifungua, ndipo alipokutana na karatasi kubwa nyeupe iliyokuwa na maandishi yaliyosomeka "SIO KILA NGOMA INACHEZEKA, NYINGINE NI ZA KUSIKILIZA TU NA KUZIACHA KAMA ZILIVYO"



NIMELETA HILO ONYO, NA USISUMBUKE KUNIJUA, NIMEKUWEKEA NA PICHA YANGU KABISA"



ndio ujumbe ulisomeka hivyo. Tom akaamua kuifungua tena ile bahasha baada ya kuona ule ujumbe umesema kuna picha imewekwa ndani, kweli akaiona picha ndogo yenye ukubwa wa passport, akaichukua na kuiangalia, aliyemuona kwenye picha ndiyo alifanya akachoka zaidi.........





Ilikuwa ni picha ya yule Dada aliyejitambulisha kuwa ni mjomba wa mzee katika siku iliyopita. Tom akajikuta anacheka bila kutegemea maana mambo yalizidi kumtatiza kabisa.



"Mbona naanza kujuta kuifuatilia hii habari, inaelekea kuna kitu kikubwa sana kinafichwa" Tom aliongea huku ile picha ya yule Dada ikiwa bado mkononi mwake.



"Sasa itabidi nitumie akili ya ziada ili nichimbe yote yaliyojificha na wote wanaohusika" Tom aliendelea kuwaza huku akiwa bado yupo kitandani.



Akiwa bado anawaza, simu yake ilianza kuita tena, alipoitazama alikuta namba ngeni, hakutaka kuipuuza, aliipokea moja kwa moja,



"Hallow" Tom aliongea huku akiwa na wasiwasi,



"Thomas Anthony, wewe ni kijana mdogo sana, angalia umaarufu na sifa unayoitaka vinaweza kukupeleka kaburini" Sauti laini ya mwanamke iliongea na kumfanya Tom atetemeke,



"Sijui naongea na nani?" Tom alijikaza na kuuliza,



"Mimi yule Dada wa mahakamani, mzee bonny ni mjomba wangu" Sauti laini alijibu kwa madaha na kumfanya Tom akae sawa kwa maana alikuwa anashida sana na huyo Dada,



"Tunaweza kuonana?" Tom aliuliza,



"Zingatia onyo nililokupa katika bahasha, vinginevyo ukionana na mimi mara ya pili, ujue ndiyo itakuwa siku ya kifo chako" Ile sauti ilijibu na simu ikakatika,



Tom akaiangalia ile namba na kuipiga tena, lakini jibu lililokuja ni kuwa simu haipatikani, akajaribu tena na tena lakini jibu likawa ni lile lile. Tom akaitupa simu pembeni na kupembua mawazo yake vizuri mpaka usingizi ulipompitia.



Kesho yake asubuhi na mapema alidamka na hakuwa na ratiba nyingi, ratiba aliyoipanga siku hiyo ni kwenda tu nyumbani kwa mahakimu waliouwa, ila kabla hajafanya hayo kuna akili ilimjia, akili ambayo aliiona inaweza kufanya wahusika wa kesi ile wamfuate wenyewe kwa njia za vitisho.



Tom alidhamiria kuifuata hiyo akili, aliamua aende kwanza ofisini kwao, alichukua bajaji na kuelekea ofisini kwao ambapo hakutaka kuonana na bosi wake, bwana Othman Tafu.



Tom aliingia ofisini kwao na kuonana na mkurugenzi wa vipindi radio hapo,



"Nasikia unataka kuja kipindi bab kubwa" Mkurugenzi wa vipindi alimuuliza Tom baada ya kusalimiana,



"Cha kawaida tu, sasa nimekuja moja kuna shida naomba unisaidie" Tom alimwambia Mkurugenzi wa vipindi,



"Shida ipi tena hiyo?" Mkurugenzi wa vipindi aliuliza kwa shahuku,



"Nataka nitengeneze tangazo la kipindi changu kipya, ila nahitaji ilo tangazo lipigwe kwenye kila kipindi na lipigwe zaidi ya Mara tatu" Tom aliongea huku akimtazama yule Mkurugenzi wa vipindi,



"Sasa itakuwaje uchukue nafasi kubwa hivyo? au una wadhamini wataokuwa wanalipia baadhi ya matangazo yako?" Mkurugenzi wa vipindi aliuliza,



"Sina mdhamini, ila nakuomba ufanye hivyo, kama hujaridhika na ninachokwambia, basi kamueleze bosi alafu msikilize atasemaje?" Tom alimwambia Mkurugenzi wa vipindi,



"Sasa si bora ukamuombe yeye alafu ndiyo uje uniambie" Mkurugenzi wa vipindi aliongea,



"Mimi sihitaji kufanya hivyo, mimi naingia studio kutayarisha tangazo alafu utajua mwenyewe ulipige kama nilivyosema, au uliache" Tom aliongea huku akiondoka kwa maana alishajiamini kuwa anachofanya ni kitu muhimu kwa radio yake na taifa lake.



Aliingia studio na kuandaa tangazo ambalo lilikuwa linawaambia wasikilizaji wakae tayari kwa ajili ya habari ya memory card, ile habari iliyofunua mambo yaliyo nyuma ya pazia, mambo yaliyomuhusu waziri wa ulinzi, sasa ile habari ipo, na inaendelea kuwamaliza watu mtaani, je unataka kumjua aliye nyuma ya hili? Basi tayarisha masikio yako kwa ajili ya kipindi kipya kitakachoitwa lipua Bomu"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Hayo ni maneno yaliyokuwepo katika tangazo hilo, maneno ambayo Tom aliyapanga kwa ajili ya kufanya wote waliohusika na habari ile washtuke na wamtafute.



Tom alitoka chumba cha studio na kumkabidhi mkurugenzi wa vipindi lile tangazo,



"Kuanzia kesho, hilo Tangazo lipigwe kuanzia kipindi cha asubuhi mpaka usiku, na si chini ya Mara tatu kwa kila kipindi" Tom aliongea na kuondoka zake akimuacha Mkurugenzi wa vipindi akimuangalia bila kutia neno.



Tom aliondoka huku akipanga kwenda nyumbani kwa hakimu wote walioshiriki kesi ya Memory card.



Alikuwa na ramani mbili alizopewa na Mzee Bonny, ramani ambazo alizitumia kumfikisha mpaka eneo la ambalo alikuwa anahishi hakimu mmoja wapo kati ya wawili walioshiriki katika kesi ile.



Alifika katika nyumba ile ambayo ilionekana ya kisasa kwa maana ya ujenzi wake. Tom aliweza kugonga hodi katika geti na kusubiri kwa muda, ambapo mlango ulikuja kufunguliwa na mama mmoja wa makamo kidogo,



"Nafikiri hapa ni kwa Salmon Denyo?" Tom aliuliza baada ya kumsalimia yule mama,



"Ndio hapa, karibu ndani" Mama yule mstaharabu aliongea huku akilifungua zaidi geti, Tom akapita ndani na mwenyeji wake akamuongoza mpaka katika sebule iliyokuwa na kila kitu cha kuitwa sebule ya hadhi ya juu,



"Karibu ukae baba, sijui unatumia kinywaji gani? lakini kisiwe kilevi kwa maana sisi watu wa imani sana" Mama yule mstaharabu aliongea huku akitoa tabasamu mororo,



"Maji tu yatanitosha mama, maji ya baridi, kwa maana hili joto si mchezo" Tom alijibu huku nae pia akitabasamu,



"Ndio mji wetu huo, hilo joto lipo tu si masika si kiangazi" Mama yule aliongea huku akielekea mahali friji ilipo.



Baada ya muda yule mama alirejea huku mkononi akiwa na jagi la maji na glass, akaenda kuviweka juu ya meza iliyokuwa mbele ya Tom.



"Haya baba jitambulishe, maana nimekukaribisha tu bila kukujua" Mama yule mstaharabu aliongea kwa lafudhi yake ya watu wa pwani,



"Sawa mama, naitwa Thomas Anthony, ni mwandishi wa habari" Tom aliongea na kumuachia nafasi ya kuongea yule mama,



"Mwandishi wa habari!?, ni kipi kimekuleta, maana ni Mara ya kwanza kutembelewa na mwandishi wa habari hapa nyumbani kwangu" Mama yule mstaharabu aliuliza kwa shahuku,



"Kuna habari nazihitaji kutoka kwako, nahitaji sana ushirikiano wako kwa vyote unavyovijua kuhusu kifo cha mume wako" Tom aliongea na kumuangalia yule mama,



"Sasa ni kipi unachotaka kujua mwanangu?" Mama alimuuliza Tom,



"Cha muhimu ni mazingira ya kifo chake" Tom alijibu na kumfanya yule mama akae kimya kidogo huku akitafakari,



"Aisee mwanangu ninachojua ni kuwa mume wangu aliuawa, ila sijui aliyemuua isipokuwa ninachokijua ni kuwa aliyetumwa kumuua alitumwa na mtu mkubwa serikalini" Mama yule mstaharabu alijibu,



"Sababu ya kuuawa kwake unaweza kuijua?" Tom aliuliza,



"Ndio, nikutokana na ile kesi ya memory card, alitakiwa atoe hukumu batili, yaani watuhumiwa washinde kesi, alipewa mpaka hongo ila alikataa, akauawa hata kabla hajatoa hukumu na kesi ikahamishiwa kwa hakimu mwingine ambaye nae nilisikia aliuawa pia" Mama yule mstaharabu alijibu,



"Hajawahi kukugusia kuwa ni nani aliyekuwa nyuma ya ile kesi?" Tom aliuliza,



"Hapana, alikataa kabisa, alidai kuwa endapo nitamjua basi maisha yangu yatakuwa hatarini, alichoniambia kuwa ni kigogo wa serikali" Mama yule mstaharabu alijibu,



"Na baada ya kifo chake hakuna mtu aliyekuwa akikusumbua sumbua kwa kukupeleza kama unajua kitu chochote kuhusu kifo cha mmeo?" Tom aliuliza,



"Kuna binti mmoja mweusi mfupi kiasi, alinisumbua sana, ila alikuja akapotea tu mwenyewe, nadhani alikuja kuujua ukweli kuwa Mimi sijui kitu" Mama yule mstaharabu alijibu na kumfanya Tom ahisi kuwa huyo binti ni lazima atakuwa ni yule aliyemkuta mahakamani na pia ndiyo huyo huyo aliyemtumia ujumbe kwenye bahasha,



"Binti mwenyewe ndiyo huyu?" Tom aliuliza huku akimpatia picha aliyotumiwa na yule binti siku iliyopita,



"Ndio yeye kabisa, yaani ni huyu huyu" Mama mstaharabu alijibu baada ya kuiangalia ile picha kwa muda mfupi,



"Sawa mama, nashukuru kwa msaada wako, nitarejea tena pindi nitapohitaji msaada mwingine" Tom aliongea huku akinyanyuka,



"Sawa baba yangu, karibu tena" Mama Mstaharabu aliongea huku nae akisimama na kisha akamsindikiza Tom mpaka nje ya geti wakaagana na Tom akaenda zake.



Alipotoka hapo aliamua aelekee kwenye msiba wa mzee Bonny, siku hiyo alikuwa anaagwa ili maiti isafirishwe iende kwao Mwanzo.



Msiba ulikuwa kwa mke wa Mzee Bonny, Tom alishapewa ramani ya kufika katika hiyo nyumba.



Tom aliingia msibani kukuta umati mkubwa wa watu hapo msibani, wengi wao walikuwa na majonzi, Tom kilichompeleka kilikuwa ni kutaka kumjua mke wa Mzee Bonny na familia yake kwa ujumla, hakupanga kuwahoji kwa maana alijua uchungu walionao.



Wakati pilika pilika za kuendelea kuaga zikiendelea, Tom alijichanganya na kundi jingine la waandishi waliokuwa wanapiga picha eneo lile.



Baada ya kupiga picha kadhaa, haja ndogo ilimshika Tom, akaamua kuingia chooni mara moja, sasa wakati anaingia chooni akashikwa begani upande wa nyuma, alipogeuka ndipo macho yake yalikutana na yule Dada akiwa na miwani nyeusi, tena akiwa na tabasamu pana sana usoni mwake.......





Tom alipata mshtuko, ila alijatahidi kuuficha na kuutoa ule mkono wa yule Dada ambao ulikuwa begani kwake,



"Bado unaendelea kufuatilia vitu visivyokuhusu?" Dada alimuuliza Tom huku akitoa tabasamu la dharau,



"Hivi wewe ni nani? mbona utambulisho wako una utata hivyo?" Tom aliuliza huku akimuangalia kwa makini,



"Siko hapa kujitambulisha, nipo hapa kukuonya kwa Mara ya pili, limebaki honyo moja tu la mwisho" Dada aliongea kisha akaondoka zake na Tom akabaki anamuangalia mpaka yule dada alipotokomea katika kundi la wakinamama waliokuwepo hapo msibani.



Tom akasonya zake na kurudi chooni.



Alipotoka tena chooni akawa anaendelea kumtafuta yule Dada kwa kuangaza kila upande ila hakufanikiwa, kwa bahati nzuri tu alifanikisha kilichompeleka pale msibani, aliweza kumtambua mke wa marehemu Mzee Bonny na baadhi ya ndugu wa mzee Bonny.



Ilipotimia muda wa kuanza kuundoa mwili wa mzee Bonny kwa ajili ya kuupeleka uwanja wa ndege kwa ajili ya safari, Tom nae alianza kuondoka huku akiwa bado anamuwazia yule Dada.



Tom alijirudisha nyumbani na kuandika kila kitu kilivyoenda katika siku hiyo, baada ya hapo aliamua aende mtaani kutembea kwa kuwa hakuwa na cha kufanya muda huo na isitoshe aliwahi sana kurudi. Aliamua aimalizie siku yake kwa kuzunguka tu mtaani.



****************



Siku iliyofuatia, asubuhi na mapema aliamka ila hakuwa na sehemu ya kwenda muda huo, akawa amekaa tu kitandani akisikiliza radio, hapo ndipo alipolisikia lile tangazo lake likipigwa katika radio yao, akajikuta anatabasamu peke yake,



"Sasa wahusika wasiponitafuta kwa nguvu safari hii, naamini basi hakutakuwa na kilichofichwa nyuma ya kesi hii ya memory card" Tom aliongea huku akiwa bado yupo kitandani.



Saa mbili na nusu asubuhi ilimkuta Tom akiwa barabarani kuelekea katika nyumba ya hakimu wa pili ambayo nae inasadikika aliuawa.



Alifika katika nyumba hiyo ambayo hii nayo ilikuwa ya kifahari ila ilikuwa na eneo kubwa sana kuliko ile nyumba ya mwanzo, na katika eneo hilo ambalo lilikuwa ndani ya uzio wa matofali, lilikuwa limepandwa miti mbalimbali ikiwemo miti ya matunda na mwenyeji aliyempokea alikuwa ni kijana wa kiume ambae umri wake ulirandana na Tom, kijana yule hakumuingiza Tom ndani ila alimkaribisha chini ya mti ambapo kulikuwa na viti,



"Kama nilivyojitambulisha hapo hawali, naitwa Tom, ni askari wa kitengo cha usalama" Tom aliongea, aliamua kumdanganya yule kijana,



"Karibu sana" Kijana aliongea huku akimuangalia Tom,http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



"Marehemu Zuwena Kota alikuwa nani yako?" Tom alimuuliza yule kijana,



"Ni Dada yangu" Kijana alijibu,



"Mume wake au watoto wake naweza kuwaona?" Tom aliuliza,



"Hakuwahi kuwa na mtoto, ila mume wake walishaachana miaka iliyopita na huyo mwanaume alioa mwanamke mwingine kipindi marehemu yupo hai" Kijana alijibu,



"Huyo mume wake bado mna mawasiliano nae?" Tom aliuliza,



"Mawasiliano ya kawaida yalikuwepo, ila nae amefariki juzi, alikutwa nyumbani kwake amechinjwa" Kijana aliongea na moyo wa Tom ukapata mshtuko kwa maana alihisi huyo anayezungumziwa atakuwa ni mzee Bonny,



"Mume wake alikuwa anaitwa nani?" Tom aliuliza,



"Boniface Masanja, ila watu walizoea kumuita Mzee Bonny" Kijana alijibu na kumfanya Tom afute jasho, alishaona ile kesi inazunguka tu eneo lile, yaani kama wahusika wote ni watu wanaojuana,



"Okey, na kifo cha Zuwena kilikuwaje?" Tom aliuliza,



"Alikufa tu usingizini, ila baadae madaktari walipomfanyia vipimo ikagundulika kuwa alipuliziwa hewa ya sumu" Kijana alijibu,



"Polisi walipofuatilia waligundua nini?" Tom alimuuliza yule kijana,



"Sisi hawajatuambia kuwa ni nini kiligundulika baada uchunguzi wao, maana hata tulipofuatilia zaidi tuliambiwa kuwa yule polisi aliyepewa jukumu hilo, alihamishwa mkoa pia" Kijana alijibu na kumfanya Tom ajikune kchwa huku akitafakari,



"Huyo askari alikuwa ni wa kituo gani?" Tom aliuliza,



"Alikuwa ni askari wa kituo kikuu cha mkoa" Kijana alijibu.



"Sawa nashukuru, nitarudi tena siku nyingine" Tom aliongea huku akiinuka na yule kijana akawa anamsindikiza ili kumtoa nje, walipofika waliagana na Tom akapanda bajaji.



Tom sasa aliamua kwenda gerezani ili kuonana na walinzi wa ulinzi aliyefungwa kwa lile tukio la memory card.



Tom alifika katika gereza ambalo alifungwa waziri wa ulinzi na moja kwa moja akataka amuone waziri wa ulinzi,



"Wewe ni nani yake?" Askari magereza alimuuliza Tom,



"Mimi ni ndugu yake?" Tom alijibu kwa kujiamini,



"Ok , nifuate" Askari magereza aliongea huku akielekea sehemu zilipokuwepo ofisi.



Walipofika katika ofisi moja, Askari magereza alibisha hodi na mtu wa ndani akaitikia na kisha yule Askari magereza na Tom wakaingia ndani ambapo walimkuta mtu mmoja mwanaume wa makamo amekaa katika kiti kizuri na mbele yake kulikuwa na kibao ambacho kilimtambulisha kuwa ni mkuu wa gereza.



Askari magereza alisimama kikakamavu na kumpigia saluti yule mkuu wa magereza,



"Shida?" Mkuu wa gereza aliuliza baada ya kupigiwa saluti,



"Nimekuletea huyu mtu umsikilize" Askari magereza aliongea,



"Sawa, wewe nenda" Mkuu wa gereza alijibu na kumruhusu yule askari magereza aondoke,



"Sema Thomas, una shida gani?" Mkuu wa gereza alimuuliza na Tom akapata mshangao kwa kutajwa jina lake na yule mkuu wa gereza,



"Nina shida, nahitaji kumuona aliyekuwa waziri wa ulinzi" Tom alijibu huku akijifanya hajashtuka kwa kuitwa jina lake,



"Wewe ni nani yako?" Mkuu wa gereza alimuuliza huku akiwasha sigara yake iliyotoa moshi mwingi uliomkera Tom,



"Mimi ni Muandishi wa habari, kuna mambo nataka kuyajua kutoka kwake" Tom aliamua kusema ukweli,



"Sasa kwanini ulidanganya kuwa wewe ni ndugu yake?" Mkuu wa gereza aliuliza na kumfanya Tom ashangae huyu amejuaje kuwa alidanganya wakati anaingia getini,



"Nadhani ningejitambulisha kuwa mimi ni Muandishi wa habari, hakuna askari ambaye angeniruhusu kuingia ndani" Tom alijitetea,



"Nani yupo nyuma yako ambaye anakupa nguvu ya kufuatilia hii habari?" Mkuu wa gereza alihoji huku akiipuliza sigara yake,



"Ni mimi mwenyewe tu niliamua kuifuatilia hii habari" Tom alijibu huku akikereka na maswali ya mkuu wa gereza,



"Sema ukweli, hakuna kiongozi yoyote aliyekutuma?" Mkuu wa gereza alimuuliza tena,



"Hapana, ni utashi wangu tu umenituma kufanya hivyo" Tom alijibu huku akiweka tabasamu feki usoni mwake,



"Mzee Bonny amekufa kwa ajili yako, lakini wewe bado hukomi kufuatilia hii habari" Mkuu wa gereza aliongea maneno yaliyozidi kumchanganya Tom,



"Wewe habari za mzee bonny umezijuaje na umejuaje Mimi ndio nilisababisha kifo chake?" Tom alihoji huku jazba zikianza kumpanda,



"Sikiliza kijana, bahati uliyonayo ni kwamba ulionywa na mwanadada ambaye uwa haonyi ila anaua, sasa wewe amekuonya Mara mbili na hukusikia" Mkuu wa gereza aliongea na kufanya Tom apate wasiwasi kuwa uenda na huyo Mkuu wa gereza ni miongoni mwao,



"Mbona unaonekana unajua mambo mengi kuhusu mimi?" Tom alimtupia swali mkuu wa gereza,



"Sijui chochote kuhusu wewe, ila ila najua vyote unavyovifuatilia wewe" Mkuu wa gereza alijibu na kukitupa kishungi cha sigara katika kisosi kidogo cha cha udongo kilichopo chini ya meza,



"Nimefurahi kusikia hivyo, unaweza niambie kwa uchache vyote unavyovijua?" Tom alimuuliza mkuu wa gereza,



"Ndio, ila kwa sharti" Mkuu wa gereza aliongea huku akimtupia jicho Tom,



"Sharti lipi?" Tom aliuliza, ila mkuu wa polisi hakujibu na badala yake alipiga simu na kuongea na mtu na kisha akakata simu.



"Ngoja mashahidi waje ndio tufanye makubaliano" Mkuu wa gereza aliongea na kuwasha tena sigara nyingine.



Baada ya dakika moja waliingia askari magereza wanne, na wote walikuwa wana miili mikubwa kama wanyanyua vyuma.



"Sharti lenyewe ni lazima uuawe baada ya kuambiwa hiyo siri, upo tayari?" Mkuu wa gereza aliuliza na kumuangalia Tom,



"Ngoja nikafikirie, nitarudi siku nyingine" Tom aliongea huku akiinuka kwa lengo la kuondoka, lakini hata kabla hajapiga hatua alishtukia anapigwa kichwani na kitu kizito na hakuwa na uwezo wa kuona tena, macho yake yaligubikwa na giza zito, Tom akadondoka chini kama mzigo na kupoteza fahamu......







Wale Askari magereza walioingia, walimbeba Tom na kumuweka katika mfuko mkubwa wa salfeti na kumbeba juu juu mpaka nje, hakuna aliyeweza kujua kilichobebwa.



Ile salfeti ambayo aliwekwa Tom iliwekwa katika buti ya gari na wale askari wanne wakajipakia katika gari na kuondoka na mwili wa Tom kuelekea wanapojua wao.



Walitumia muda mfupi tu mpaka kufika wanapoenda, waliingia katika nyumba kubwa nyeupe iliyoonekana anakaa mtu mkubwa serikalini au tajiri mkubwa.



Tom akiwa katika ule mfuko aliingizwa ndani ya geti la ile nyumba na ndani ya geti kulikuwa na nyumba mbili kubwa, wakampeleka katika nyumba iliyokuwa inaangalia geti na kuingia nae ndani na kukuta sebule kubwa ambayo ukutani kulibandikwa picha ya rais lakini iliwekwa alama ya X, wakamtupa Tom juu ya kochi la sofa na kuiwasha feni kisha wakaigeuzia upande alipokuwepo Tom, muda huu walikuwa wameshamtoa katika salfeti, baada ya kufanya hayo, wakaondoka zao wakimuacha Tom akiwa amelala pale pale bila fahamu.



Tom alizinduka muda mfupi baada ya askari magereza wale kuondoka, fahamu zilipomrejea Tom, alijikuta akiwa amelala juu ya kochi kubwa na juu ya meza alikuta kuna jagi la kioo lina juisi.



Tom akajiinua katika kochi na kuanza kuangaza kila upande wa ile sebule na mwisho akaenda kujaribu kufungua mlango na haukufunguka kutokana na kufungwa kwa nje.



"Hapa sijui ni wapi?" Tom alijiuliza huku akiendelea kuutikisa mlango kwa nguvu bila mafanikio.



Baada ya jitihada zake za kufungua mlango kushindikana, aliamua kutoa simu mfukoni mwake ili apige picha ile mandhari ya pale, lakini alipojipekua hakujikuta na simu wala karatasi zake anazotumiaga kuandikia kila tukio analokumbana nalo, ila pesa yake mfukoni aliikuta ipo vile vile haijapunguzwa hata kidogo.



"Wajinga sana awa, sijui wanataka kunifanyaje huku, wataniacha mzima kweli?" Tom aliwaza huku hofu ikianza kumuingia.



Akiwa bado anawaza alishtukia mlango ukifunguliwa na wakaingia watu watatu wote wanaume. Mmoja alikuwa ana ndevu nyingi na kitambi na wawili waliobaki walikuwa ni vijana mabaunsa ambao ilionekana ni kama walinzi wa yule mwenye ndevu nyingi.



"Pole kwa uchovu kijana" Bwana yule mwenye ndevu nyingi alimwambia Tom huku nae akijiweka Kitano katika kochi,



"Asante" Tom alijibu huku akiwa na hofu,



"Karibu juisi, jisikie upo nyumbani" Bwana yule mwenye ndevu aliongea na kumimina juisi katika glasi nne zilizokuwepo juu ya meza,



"Asante" Tom alijibu huku akipata mashaka ya kunywa kwa kuhisi uenda kuna sumu katika zile juisi.



"Nasikia ulitaka kuonana na mimi?" Bwana ndevu aliuliza na kugida fundo la juisi kinywani mwake na kumfanya Tom nae anywe ile juisi baada ya kujiaminisha haina sumu,



"Mimi?, hapana bwana mimi sikutaka kuonana na wewe" Tom alijibu huku akishangaa,



"Sasa ulivyoenda gerezani ulitaka kuonana na nani?" Bwana ndevu aliuliza huku akimuangalia Tom,



"Nilienda kuonana na aliyekuwa Waziri wa ulinzi" Tom alijibu,



"Basi ndiye mimi hapa, hizi ndevu zinafanya niwe tofauti" Bwana ndevu aliongea na kufanya Tom amkazie macho zaidi na kweli alikuwa yeye, waziri wa ulinzi wa zamani, Tom akapigwa na butwaa la mshangao,



"Ni kweli, nilikuwa nataka kuzungumza na wewe" Tom aliongea huku akikaa vizuri juu ya kochi,



"Ulikuwa na shida gani kijana?" Waziri wa ulinzi aliuliza kirafiki,



"Shida yangu ni kutaka kujua ni kwanini hakimu wote waliokuwa katika kesi yako, yaani ile kesi ya memory card waliuawa?" Tom aliuliza bila uoga,



"Waliipenda sana haki ndio maana waliuawa" Waziri wa ulinzi alijibu huku macho yakiwa makavu,



"Kivipi?, kwani we hupendi haki?" Tom aliuliza huku akimshangaa,



"Duniani hakuna haki mdogo wangu, haki ipo mbinguni na ndio maana nimewapeleka kwenye haki hao mahakimu" Waziri wa ulinzi alijibu,



"Na umewezaje kuwa huru wakati ulihukumiwa kifungo cha maisha?" Tom aliuliza,



"Ujue mimi nilifungwa lakini Mimi nilikuwa kibaraka tu, muhusika mkuu alikuwa uraiani na yeye ndiye aliyenitoa" Waziri wa ulinzi aliongea, na alikuwa wazi hakutaka kuficha kitu kwa maana aliona Tom hana nguvu yoyote katika jamii na isitoshe hata radio anayotoka ni ndogo na haisikilizwi na watu wengi.



"Ni nani mtu huyo unaemzungumzia?" Tom alihoji,



"Utamuona tu, kama sio leo hata kesho" Waziri wa ulinzi alijibu,



"Na kwanini mzee Bonny mlimuua?" Tom aliuliza,



"Hii habari ni U.U.L.U" Waziri wa ulinzi alitoa jibu fupi lakini ambalo Tom hakujua maana yake isipokuwa alilikuta tu kwenye ile habari ya Edward Sambo,



"U.U.L.U maana yake nini?" Tom aliamua kuuliza,



"Maana yake ni UJUE, USIJUE, LAZIMA UFE, mzee Bonny alishajua na hakuwa na faida kwetu na tulimpa Uhuru wa kuishi kwa sharti la kuitunza hii siri na alikuwa chini ya uangalizi wa BQ, ila mzee Bonny alitaka kukupa hii siri bila kukwambia sharti" Waziri wa ulinzi aliongea,



"BQ ndio nani?" Tom aliuliza,



"Black Queen, yule Dada anayekufuatilia na wewe" Waziri wa ulinzi aliongea na kumfanya Tom amkumbuke yule mwanadada,



"Ndiyo yeye aliyemuua Mzee Bonny kifo cha kinyama namna ile?" Tom aliuliza,



"Ndiyo ni yeye, ila kile sio kifo cha kinyama, mbona kamuua kawaida tu" Waziri wa ulinzi alijibu huku akiupandisha mguu wake juu ya mguu mwingine na kufanya itengeneze umbo la nne,



"Kwa hiyo kile ni kifo cha kawaida, kifo cha kuchinjwa?" Tom aliuliza huku akimuangalia Waziri wa ulinzi,



"Ndio dawa ya usaliti, msaliti anatakiwa afe kinyama" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Tuachane na hayo, ulisema mtu akitaka kujua siri yenu ni lazima akubali sharti?" Tom aliuliza,



"Bila shaka" Waziri wa ulinzi alijibu,



"Sharti gani hilo?" Tom aliuliza,



"U.U.L.U" Waziri wa ulinzi alijibu,



"Sawa, unaweza kuniambia sasa ni nini lengo lenu kwa sasa?" Tom aliuliza,



"Kwanza kubaliana na Sharti letu" Waziri wa ulinzi aliongea huku akimuangalia Tom aliyekuwa anatafakari kwanza,



"Sawa, ila umesema cha muhimu siri nisiitoe kwa mtu mwingine, si ndio?" Tom aliuliza baada ya kutafakari kwa muda,



" kwa hiyo umekubaliana na sharti letu?" Waziri wa ulinzi aliuliza,



"Ndio" Tom alijibu lakini lengo lake lilikuwa ni kupata habari na kuitangaza,



"Leteni documents" Waziri wa ulinzi aliongea na baunsa mmojawapo kati ya wale alioingia nao alifungua begi dogo alilokuwa amelivaa shingoni na kutoa karatasi ambazo alitakiwa azitoe na kuziweka mezani,



"Chukua zipitie alafu ukishakubali hayo masharti ya kupewa hii siri, utaonyeshwa sehemu ya kusaini" Waziri wa ulinzi aliongea na Tom akazichukua zile karatasi na kuanza kuzipitia,



"Tayari mkuu" Tom alijibu baada ya kuzipitia kwa dakika kumi na tano,



"Weka sahihi yako hapo chini kushoto" Waziri wa ulinzi aliongea huku akimuonesha Tom sehemu ya kuweka saini, Tom akaweka,



"Kijana umehidhinisha kifo chako" Waziri wa ulinzi aliongea baada ya Tom kumaliza kuweka saini, tena aliongea huku akiichomoa bastola yake kutoka kiunoni na kuwafanya wale mabaunsa watoe tabasamu kwa pamoja.....



"Kivipi?" Tom aliuliza kwa uoga,



"Si umesaini mwenyewe, kwani kuna mtu alikulazimisha au alikushika mkono usaini?" Waziri wa ulinzi aliongea huku mdomo wa bastola yake akiulekeza kwa Tom aliyekuwa ametoa macho na haamini kinachomtokea.....







"Mbona una hofu kijana?" Waziri wa ulinzi alimuuliza Tom huku bastola bado ikiwa inamuangalia Tom,



"Nashindwa kuelewa unataka kufanya nini" Tom alijibu huku bado wasiwasi ukiwa umemtawala,



"Aah ni hii inakunyima amani?" Waziri wa ulinzi aliongea na kumpa baunsa mmoja ile bastola na kufanya Tom ashushe pumzi,



"Mzee tayari nimeshasaini, sasa sijui unaweza kunipa habari Kamili kuhusu ile kesi ya memory card na jinsi waliokuwa wanajua mambo yenu namna mlivyowaua?" Tom aliuliza huku akimuangalia Waziri wa ulinzi,



"Ulisoma vizuri habari ya memory card, ile iliyoandikwa na Edward Sambo?" Waziri wa ulinzi aliuliza na kumkata jicho Kali Tom,



"Nimeisoma, vizuri sana" Tom alijibu,



"Unaweza kuniambia lengo la kuficha ile siri iliyokuwepo kwenye Memory card, ilikuwa ni nini hasa lengo?" Waziri wa ulinzi aliuliza,



"Nafikiri lilikuwa ni kupindua nchi" Tom alijibu,



"Sio unafikiri, lengo letu ni kupindua nchi na bado tunaendelea na lengo letu na litatimia saa chache zijazo" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Unaposema saa chache zijazo unamaanisha nini?" Tom aliuliza swali la kipuuzi,



"Acha ujinga kijana, saa chache zijazo hujui maana yake?, hujui kusoma saa? " Waziri wa ulinzi aliuliza na kufanya Tom aone nchi itaingia machafukoni muda si mrefu,



"Huoni kufanya hivyo inaweza kuleta mtikisiko kwa Taifa?" Tom aliuliza,



"Kila kitu kinahitaji maandalizi mdogo wangu, hatukurupuki kufanya hivi, ni mipango iliyosukwa kwa muda wa kutosha" Waziri alijibu kwa utulivu,



"Nakumbuka ulisema wewe ni kibaraka, je unaweza kuniambia ni nani yupo nyuma yako?" Tom alimuuliza Waziri,



"Nisingetaka umjue, ila kwa kuwa unataka kumjua basi nitakuambia, aliyeko nyuma yangu ni mheshimiwa, mheshimiwa Tammy Semmy" Waziri wa ulinzi aliongea na kumfanya Tom ashtuke, kwa maana huyo aliyetajwa ni makamo wa rais na isitoshe ni swahiba mkubwa sana wa rais,



"Lakini hilo litawezekanaje wakati Tammy Semmy ni rafiki wa raia?" Tom aliuliza kwa mshangao,



"Kwani mwaka wa ngapi huu rais ameshikilia madaraka?" Waziri aliuliza,



"Kumi na moja, lakini sioni tatizo kwa kuwa demokrasia ipo na katiba yetu inaruhusu kugombea urais bila kikomo" Tom aliongea,



"Ngoja nikwambie mdogo wangu, yule rais hawezi kutoka madarakani kwa kuwa ndani ya chama chetu yeye anakubalika na kwa wananchi anakubalika, Sasa Tammy Semmy nae anahitaji madaraka na isitoshe kuna biashara nyingi tu anataka kuzifanya Ikulu" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Kweli kikulacho ki nguoni mwako" Tom aliongea kwa huzuni,



"Saa ngapi sasa hivi?" Waziri aliuliza huku akiwaangalia mabaunsa,



"Saa moja na robo" Baunsa mmoja alijibu,



"Mfungeni huyu usoni ili asiweze kuona kitu na twendeni nae akafanye ile kazi" Waziri wa ulinzi alitoa amri ambayo ilimfanya Tom ahisi hatari mbele yake, kengele ya hadhari iligonga kichwani mwake na hakuwa na cha kufanya,



" ni wapi mnanipeleka jamani, tafadhali msiniue" Tom aliongea wakati akifungwa kitambaa cheusi machoni na kumfanya Waziri amcheke kutokana na uoga aliouonesha,



"Kwanini ufe? twende ukafanye kazi na uachiwe huru" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Kazi gani?" Tom aliuliza,



"Utaijua uko uko" Waziri alijibu na kisha akainuka na kuelekea nje huku wale mabaunsa wakimfuata pamoja na Tom ambaye alikuwa hawezi kuona kutokana na kitambaa alichofungwa machoni.



************************



Tom alifunguliwa kitambaa alichofungwa usoni na kuanza kufikicha macho kwa kuwa alikuwa haoni, na isitoshe Giza lililokuwepo usiku huo lilimchanganya,



"Songa mbele" Baunsa mmoja aliongea huku akimsukuma Tom,



"Jamani sioni" Tom alilalamika baada ya kujikwaa kwenye jiwe,



"Ebu washeni tochi" Waziri wa ulinzi aliongea na baunsa akawasha Tochi, hapo kidogo Tom aliweza kuona na safari ikawa inaendelea huku ukimya ukiwa umetawala.



Ni safari ya mwendo wa miguu baada ya kushuka katika gari waliloliegesha barabarani.



Wakiwa wanatembea katika msitu ule, kwa mbali Tom aliweza kuona miale ya mwanga wa Tochi na pia kuona watu kwa mbali.



Walijitahidi kutembea mpaka wakafika kwenye lile kundi na kwa Mara ya kwanza Tom aliweza kumuona Tammy Semmy kwa macho yake na mbele ya Tammy Semmy kulikuwa na kiti ambacho aliwekwa mtu ambayo alifungwa kamba na pia alivalishwa kitambaa usoni, Tom hakuweza kumtambua.



"Mmechelewa sana" Tammy Semmy aliongea huku akimuangalia Waziri wa ulinzi,



"Kweli, nilikuwa namwambia lengo letu huyu kijana" Waziri wa ulinzi aliongea huku akimpiga piga begani Tom,



"Huyu ndiye yule kijana anayetaka kujua mambo yetu? , na leo ameuteka kweli mji kwa tangazo lake katika radio, naona umeipa umaarufu radio yako" Tammy Semmy aliongea huku akitabasamu mbele ya Tom,



"Yupo vizuri, anautendea haki uhandishi wake" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Nadhani tusipoteze muda, kazi ianze tu" Tammy Semmy aliongea na kisha vijana wengine wawili ambao wakina Tom waliwakuta walimfunua yule mtu aliyefunikwa usoni, alikuwa ni rais wa nchi, Tom roho yake ikapasuka kwa mshtuko.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



"Vipi, amekufa nini?" Waziri wa ulinzi aliuliza baada ya kumuona Rais akiwa amefumba macho na amelegea tu.



"Hapana hajafa, huyu ilibidi tumpige sindano ya usingizi, maana wakati nataka kumteka alianza kushtukia mchezo, ndipo nikamuwahi na sindano" Tammy Semmy aliongea kwa kujiamini,



"Sawa, ni nani aliyekuwepo kule kwenye shabaha?" Waziri wa ulinzi aliuliza huku kidole chake akinyooshea upande wenye muinoko uliopo mashariki mwao,



"Kule yupo BQ" Tammy Semmy alijibu,



"Safi, mtengenezeni vizuri rais wenu ili asionekane amekufa" Waziri wa ulinzi aliongea na mabaunsa wakamuweka sawa Rais, wakamuegemeza katika kiti Ili aonekane amekaa tu,



"Wewe kijana shika hii, kisha sogea pale mbele ya Rais" Tammy Semmy aliongea na kumpa bastola Tom ambaye alikuwa anatetemeka tu kwa maana aliona yeye ndiye atakayeambiwa amuue Rais,



"Isije ikawa umempa yenye risasi?" Waziri wa ulinzi aliuliza,



"Haina kitu hiyo" Tammy Semmy aliongea na kufanya Tom ajiulize kama amepewa bastola isiyo na kitu, amepewa kwa lengo gani?,



"We mfukunyuzi mambo ebu sogea mbele ya hicho kiti alichokalia mtukufu rais wako" Waziri wa ulinzi alimwambia Tom na Tom akatii kisha Tammy Semmy na Waziri wa ulinzi wakawa kama wanajadiliana jambo na Tom yeye alikuwa amemkazia macho Rais aliyekuwa juu ya kiti na hakuwa na fahamu,



"Dogo piga hatua nne kurudi nyuma" Waziri wa ulinzi alimwambia Tom na Tom akatii,



"Sasa hiyo bastola ielekezee kwa Rais fanya kama unampiga hivi, usiogope, hiyo bastola haina kitu. Fanya kama unampiga na usishushe bastola mpaka tukwambia ufanye hivyo" Waziri wa ulinzi alitoa maelekezo na Tom akatii, masikini ya Mungu Tom hakujua kitu chochote kinachoendelea.



Baada ya Tom kufanya alivyoelekezwa, Waziri wa ulinzi na wenzake wakasogea hatua kumi kutoka alipokuwa Tom na Rais, na kisha lile eneo alilopo Tom kuliwashwa taa na Tom na Rais wakawa wanaonekana vizuri na hapo hapo vijana watatu waliokuwepo hapo walikaa pande tatu kumzunguka Tom na wote walikuwa na camera za kisasa, wote walikuwa wanachukua tukio analolifanya Tom.



Baada ya watu wote kukaa sawa, Tammy Semmy alitoa ishara fulani kwa kumulika kwa tochi upande ambao inasemekana alikuwepo BQ na hapo hapo ulisikika mlio wa bunduki na risasi mbili zikapenya sawia kwenye kichwa cha Rais na Rais akafa pale pale, Tom sasa alielewa maana ya kufanya vile, maana baada ya tukio lile wale vijana watatu walipongezwa kwa kuchukua vizuri tukio lile na zile camera wakamkabidhi Tammy Semmy.



"Safi sana vijana wangu, simameni hapo kwenye mwanga niwapige picha ya ukumbusho kwa tukio hili la kihistoria" Tammy Semmy aliongea huku akifurahia lile tukio na wale vijana kwa furaha wakasogea katika eneo waliloambiwa, Tom akaambiwa asogee pembeni.



Wale vijana wakiwa wamesimama pale na sura zikiwa za furaha, walishangaa wakipigwa risasi mmoja mmoja, tena risasi zilitoka pasipokujulikana eneo zitopokapo, Waziri wa ulinzi akachanganyikiwa, akahisi tayari wamevamiwa....







"Tumevamiwa, tukimbie" Waziri wa ulinzi aliongea huku akimuangalia Tammy Semmy, lakini Tammy Semmy hakuonesha uoga wowote na badala yake alikuwa anacheka tu,



"Hawa ni virusi, nao walitakiwa wafe, samahani sikukwambia kuhusu hilo" Tammy Semmy aliongea huku akiwaangalia wale vijana watatu waliokuwa wamelala chini, tayari kifo kiliwachukua,



"Dah, Mimi nilijua mambo yameharibika" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Hakuna, ni mipango tu niliipanga iwe hivyo" Tammy Semmy aliongea na wakati huo huo yule Dada anayetambulika kwa jina BQ alikuwa anaingia, usoni alijifunga kitambaa cheusi kilichoziba pua na mdomo na mgongoni alibeba begi kubwa lililokuwa na bunduki kubwa iliyotoka kufanya maangamizi muda mfupi uliopita.



BQ alipofika pale alifungua kitambaa alichojifunga puani na kukivuta chini kikawa kinaning'inia shingoni, kisha akamtupia jicho Tom na kisha kutoa tabasamu la kiaina utasema hajatoka kuua vile, Tom akawa anamuangalia tu huku akilinganisha uzuri wa sura yake na roho yake.



"Ni vitu viwili tofauti" Tom alijisemea kwa sauti ya chini na kipindi hicho BQ alikuwa anapongezwa na mabosi wake kwa tukio alilolifanya.



"Kesho asubuhi taifa litaamka na habari mbaya, habari za kifo cha rais na muuaji atayeshikwa atakuwa ni wewe" Waziri wa ulinzi aliongea na kumnyooshea kidole Tom na kisha Tammy Semmy na BQ wakacheka,



"Lakini Mimi sijaua" Tom aliongea huku akiwaangalia,



"Njoo, njoo kijana, njoo uone" Waziri wa ulinzi alimuita Tom na Tom akamsogelea,



"Ebu angalia hii video" Waziri wa ulinzi aliongea huku akimuonesha video ambayo alionekana Tom akiwa amekaa mbele ya Rais aliyekuwa amefungwa kamba katika kiti, Tom akiwa ameshika bastola na muda huo huo ukasikika mlio wa bunduki na ikaonekana kichwa cha rais kikifumuka, alipigwa risasi za kichwa na hapo ndipo Tom akaelewa kuwa anaingizwa hatarini,



"Ni nani huyo aliyeshika bastola mbele ya Rais?" Waziri wa ulinzi alimuuliza Tom,



"Ni Mimi lakini sijampiga risasi" Tom alijitetea,.



"Katika hiyo video uliyoiona nioneshe mtu mwingine aliyeonekana humo kwenye video" Waziri wa ulinzi aliongea kwa dharau na kumfanya Tom aone mambo yamemuwia vigumu,



"Kwanini umenifanyia hivyo, nimewakosea nini mimi?" Tom aliuliza huku akilalamika,



"Hujui kosa lako?" Waziri wa ulinzi aliuliza,



"Sina kosa, kosa langu mimi ni nini?" Tom aliuliza kwa sauti iliyosikika kama inataka kutoa kilio,



"Kuingilia ligi za wakubwa, yaani kufuatilia mambo ya wakubwa ndio kosa lako" Waziri wa ulinzi alijibu na kufanya wenzake wacheke,



" nini kinafuata sasa?" Tammy Semmy alimuuliza Waziri wa ulinzi,



"Huyu dogo inatakiwa auchukue huu mwili wa Rais na kuutia kwenye mfuko wa plastiki" Waziri wa ulinzi alijibu,



"Hapana, mimi siwezi kufanya hivyo" Tom aliongea,



"Hatutaki kukupiga, ila unachotakiwa ni kufuata maagizo yetu, kumbuka upo chini ya himaya yetu, na ukishindwa kutekeleza hilo agizo, tunakukamata na kukupeleka polisi, utafungwa dogo, ushahidi tunao" Waziri wa ulinzi alimwambia Tom,



"Fanya ulichoambiwa mpenzi wangu mpya, fanya ili hiyo video isionyeshwe hadharani, tutaificha hii video" BQ aliongea na kumalizia kwa cheko kubwa la kebehi lililopokelewa na tabasamu kutoka kwa washenzi wenzake,



"Sawa, naomba hiyo video msimuoneshe mtu, nitauweka huu mwili kwenye mfuko" Tom aliongea na kuruhusu wale mabwana wamcheke, tena kwa cheko kubwa sana,



"Unaleta ubishi wakati sisi tumeshika mpini, utaumia mdogo wangu" Waziri wa ulinzi aliongea na kumrushia mfuko mkubwa wa plastiki na Tom akaupokea na kuufungua kamba mwili wa Rais na kisha akajitahidi kuubeba na kuuingiza ndani ya ule mfuko, kipindi hiki BQ alikuwa ndio ameshika camera analichukua hilo tukio, Tom alipomaliza, alipigiwa makofi na Tammy Semmy na kisha Waziri wa ulinzi akamuita,



"Angalia na hii video" Waziri wa ulinzi aliongea huku akimuonesha Tom ile video yenye tukio la Tom kuweka mwili kwenye mfuko na kisha Waziri akacheka,



"Baada ya lile tukio la kumuua, hapa inaonekana unamtia kwenye mfuko sasa" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Alafu bado moja la kumzika" Tammy Semmy aliongea na wenzake wakacheka, Tom sasa uvumilivu ulimshinda lakini hakuwa na cha kufanya, hasira zake zilitoka kupitia macho, Tom alikuwa analia tu, kihele hele chake kilimponza.



"Sasa tuondokeni, kazi imeshaisha, hii nchi tumeshaichukua, jiandaeni kula pesa" Tammy Semmy aliongea huku akitoa tabasamu la ushindi,



"Sasa huu mwili tunauacha hapa hapa kwenye mfuko?" BQ aliuliza,



"Muachieni huyo mwanahabari, atajua mwenyewe cha kuufanya" Waziri wa ulinzi aliongea huku akimuangalia Tom,



"Huyu si tunaondoka nae?" Tammy Semmy aliuliza,



"Huyu muacheni auzike huu mwili, na hakuna haja ya kumuua kwa kuwa tulichomfanya hapa hatokaa afungue mdomo wake" Waziri wa ulinzi aliongea,



"Haya kijana, sisi tunaenda, usijali kuhusu usalama wako" Tammy Semmy alizungumza,



"Huo mwili unatakiwa uuzike ili watu wasumbuke kidogo kuupata, na hiyo kazi utaifanya peke yako, shimo lipo hapo mbele" Waziri wa ulinzi alimuambia Tom huku akimuelekeza mahali shimo lilipo,



"Fanya kwa ufanisi kijana, chukua na hii pesa kwa kazi nzuri uliyoifanya" Tammy Semmy aliongea na kumtupia bahasha ya kaki Tom,



"Simu yangu ipo wapi?" Tom aliuliza huku akimuangalia Waziri wa Ulinzi,



"Usijali, utaipata tu na sitaki kuulizwa swali jingine" Waziri wa ulinzi aliongea kwa nyodo na kuanza kuondoka, na wenzake wa wakamfuata na nyuma alikuwa Black Queen (BQ) na begi lake lenye bunduki na hali ya hewa ya usiku huo ilikuwa ni ya mawingu na muunguromo wa radi wa kila mara.



"Mvua hiyo baba, jikaze umalize kazi fasta" BQ aliongea na kumalizia kwa kucheka cheko lake la kebehi na kumfanya Tom awaangalie tu kwa huruma wakati watu wale wakiondoka zao kwa madaha.



Tom alikaa dakika nzima akitafakari na hali ya kuchanganyikiwa ikionekana kumtawala, mwisho akakata shauri, akauchukua mfuko uliokuwa na mwili wa Rais na kuuvuta mpaka sehemu lilipo shimo, kisha akausukimia ule mfuko na kuanza kufukia shimo, na mvua ilishaanza kunyesha ikiambatana radi Kali.



Wakati akiendelea kufukia lile shimo, Mara ghafla ikapiga radi Kali eneo zima likawa jeupe kama kumewashwa taa na ghafla kukarudi kama mwanzo, ila radi ilisababisha kichaka kilichopo mita chache kutoka Tom alipokuwepo kuwaka moto kutokana na ile miale ya Radi, Tom uoga ukamuingia ila akajitahidi kuendelea kufukia lile shimo, alitumia saa zima kufukia shimo.



Alipomaliza alianza kuondoka na njia aliyokuwa anapita ni hapo hapo kwenye kile kichaka, ila kabla hajakifikia aliweza kumuona mtu akiwa amesimama na hana nguo, aliweza kumuona vizuri kutokana na msaada wa mwanga wa ule moto.



Tom akasita kusonga mbele, ila ghafla yule mtu akapotea, Tom ikabidi aende katika ile njia kwa kuwa hakukuwa na njia nyingine, alipita kwa mwendo wa kasi katika eneo lile na alipofika mbele aligeuka nyuma kuangalia kama yule mtu yupo na hakumuona, akaendelea kukimbia mpaka mbele kidogo alipoweza kuwaona watu wapatao wanne wakiwa na tochi, walikuwa wamemzunguka mwenzao mmoja aliyeonekana amepoteza maisha kwa kupigwa na radi ile Kali, aliligundua hilo baada ya kusikia majadiliano ya watu hao.



Tom hakutaka kujiweka hadharani kutokana usiku huo kutokuwa mzuri kwake na isitoshe hakuwajua watu hao ingawa walionekana ni wachoma mkaa kutokana na tanuri la mkaa lililokuwepo umbali mdogo kutoka walipo.



Tom alijibana katika kichaka na kunyata kwa hadhari ili watu hao wasigundue uwepo wake katika eneo lile, Tom akafanikiwa kuwapita watu wale bila kumgundua.



Baada ya dakika ishirini za kukimbia, hatimaye Tom aliweza kufika barabarani na kuanza kutembea huku akigeuka nyuma kila dakika, alitembea dakika tano akahisi kama kuna mtu anamfuatilia, akageuka nyuma na kumuona mtu yule yule asiye na nguo akimfuata, Tom akaanza kukimbia tena mpaka alipofika eneo lenye makazi ya watu, alipogeuka nyuma akamuona yule mtu bado yupo, Tom akaendelea kukimbia mpaka alipokutana na bajaji, akaisimamisha na kupanda, akamuelekeza dereva eneo analokwenda, safari hii alipogeuka kuangalia alipotoka, hakumuona tena yule mtu asiye na nguo ambaye alikuwa akimfuata kwa nyuma.



Bajaji ilienda mpaka nje ya geti la nyumba anayokaa Tom na kumshusha, kisha Tom akamlipa Dereva wa bajaji na bajaji ikaondoka. Tom akausukuma mlango na kuingia ndani, lakini akasikia vishindo vya mtu akitembea nje ya geti, alipochungulia alimuona mtu yule yule asie na nguo akielekea pale pale alipoingia yeye Tom, akatoka mbio na kwenda mlangoni kwake, akafungua haraka na kuingia ndani, hakutaka hata kuwasha taa, baada ya kuingia ndani akachungulia dirishani na hakumuona tena yule mtu, ila sasa ndani akahisi kuna mtu mwingine maana alisikia kama mtu anahema kwa kasi sana, akajaribu kuzuia pumzi yake lakini bado sauti ya mihemo iliendelea, na tena mihemo iliyosikika ni kama ya mbwa aliyetoka kukimbia, Tom akawasha taa ghafla na ndipo alipokutanisha macho yake na yule mtu asie na nguo, na alikuwa amekaa kitandani akimuangalia Tom, Tom akapigwa na butwaa huku asijue mtu yule ameingiaje ndani angali mlango umefungwa.........







Tom akahamaki, akataka apige kelele, ila ghafla yule mtu akapotea, Tom akaamua atoke nje kwa maana aliona ndani sio sehemu salama kwake, akaenda mpaka katika mlango wa jirani yake na kugonga,



"Vipi Tom mbona usiku huu tunaamshana?" Jamaa aliyefungua mlango aliuliza kwa sauti ya usingizi,



"Samahani kwa kukuamsha ndugu yangu, namuomba mdogo wako mmoja nilale naye kwangu" Tom aliongea kwa sauti ya upole,



"Kwanini, na hiyo tabia ya kutaka watu walale kwako umeianza lini? wewe si hutakagi watu waingie chumbani kwako?" Jamaa aliuliza huku akimtazama Tom,



"Ebu nisaidie ndugu yangu, au kama kuna nafasi uko kwenu naomba nije nilale" Tom aliongea kwa huruma,



"Huku nafasi hakuna, alafu mbona leo hueleweki, matope yamekujaa mwili mzima na isitoshe sio kawaida yako kuomba mtu wa kulala nae, una nini leo?" Jamaa alimuuliza huku akiwa anaishangaa hali aliyokuwa nayo Tom,



"Hata nikikuhadithia huwezi kuniamini, ila elewa kuwa ndani kwangu kuna mtu wa ajabu hata simuelewi, alafu hana nguo" Tom aliongea,



"Sasa si ungesema hivyo?, ebu twende tukamuone huenda ni mchawi" Jamaa aliongea huku akitoka chumbani kwake na kuongozana na Tom mpaka chumbani kwake, wakaingia ndani,



"Yuko wapi mtu mwenyewe?" Jamaa aliuliza,



"Alikuwa amekaa hapo kitandani" Tom alijibu huku akimuangalia yule Jamaa,



"Leo jirani naona haupo sawa, ebu lala kesho tutaongea vizuri" Jamaa aliongea huku akielekea nje, kwa maana alimuona Tom kama mwendawazimu,



"Usiondoke jirani, usiniache peke yangu" Tom aliongea huku akimvuta mkono yule Jamaa,



"We ebu niache, nitakupiga, nitakuvuruga vibaya, huu ni usumbufu unaonifanyia, umeniasha na hamna cha maana kilichoendelea" Jamaa aliongea kwa hasira huku akimsukuma Tom aliyekuwa amemshika mkono, Tom akaangukia ndani kwake na kuamua kutulia, aliona kama yule mtu ni mbaya basi acha amdhuru, kwa maana hakuwa na simu na wala hakuwa na sehemu ya kwenda usiku ule.



Akajinyanyua pale sakafuni na kukaa katika kochi, aliogopa kabisa kukaa kitandani kutokana na yule mtu aliyemuona,



"Kama kunidhuru si angenidhuru kule porini?" Tom alijiuliza mwenyewe huku kila dakika macho yake yakidhuru katika chumba chake, akatupa macho juu ya meza yake ndipo alipokutana na simu yake ambayo alipokonywa kipindi alipopoteza fahamu kule ofisini kwa mkuu wa gereza, Tom akatoa macho huku akiendelea kuyashangaa yale maajabu, Simu ilikuwa juu ya kijidaftari kidogo ambacho Tom alikuwa akitembea nacho kwa ajili ya kuandikia mambo yake anayokutana nayo kwa siku nzima.



Tom akasimama huku akiitumbulia macho simu yake, akakata shauri na kuichukua, akakuta ina missed call zaidi ya kumi, na zote zilitoka kwa bosi wake bwana Othman Tafu, alipoangalia upande wa ujumbe mfupi wa maneno alikuta message mbili tu, ya kwanza ilikuwa ya Othman Tafu ikitaka kujua kwanini Tom hapokei simu? na ya pili ilikuwa imetoka katika namba isiyojulikana, ilisomeka,



"Vifaa vyako hivyo hapo tumekurudishia kipindi upo msituni, mimi mpenzi wako mpya BQ" ndivyo ujumbe ulisomeka hivyo na kumfanya Tom ashushe pumzi kidogo na kufikiria kumpigia simu bosi wake, ila aliona kwa usiku haitokuwa ustaharabu kumpigia Othman Tafu, Tom akaitupa simu juu ya meza na kisha akaanza kutafakari jinsi kesho kutakavyopambazuka na habari za mshtuko kwa nchi, pia akafikiri zile picha zinazoenekana yupo mbele ya Rais na akiwa ameshika bastola endapo zitavuja, atakimbilia wapi?, si atakuwa adui wa Taifa?, ni nani ataamini utetezi wake wakati picha na video zinaonesha kuwa muuaji ni yeye, ni nani atakuwa upande wake?, maana hata wale washenzi waliomtendea unyama huo hakutaka kuwaamini tena.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Machozi yakaanza kumtoka bila kutarajia huku sasa majuto yakichukua nafasi yake ndani ya moyo, alijuta kuifukunyua habari ile na alijuta kusomea uandishi wa habari, alihisi kama alikosea kusomea fani ile, akajuta kupata kazi katika radio ile, akaona ni bora angekuwa kijana tu wa mtaani asiye na kazi, akaona ni bora angekuwa tu morogoro kwa wazazi wake, angewasaidia hata kusimamia mashamba ya kwao. Majuto yote hayo yalitoka katika kichwa, yakaenda machoni na kutoka nje kwa njia ya machozi. Usiku huo hakulala kabisa, usiku wote ulimpita akiwa amekaa tu katika kochi.



************************



ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog