Simulizi : Baradhuli Mwenye Mikono Ya Chuma (1)
Sehemu Ya Tano (5)
Moyo wa Miraji ulikimbia kwa kasi mno. Jasho lilimvuja. Alimtizama Jombi akamuuliza:
“Tutafanikiwa kweli?”
“Hilo sio ombi.” Jombi akajibu kwa kujiamini. “Ni lazima!”
Miraji alihisi Jombi anatania kusema maneno hayo katika hali waliyopo. Alitikisa kichwa chake akitizama vioo vya pembeni vya gari akashuhudia polisi wanakuja kwa kasi. Moja kwa moja akaona picha moja akiwa jela, nyingine akiwa amefariki kabisa, hayo ndiyo machaguzi mawili aliyoyapata kichwani.
“Hamia siti za mbele!” Sauti ya Jombi ilimshitua Miraji toka fikirani.
“Nageuza gari muda si mrefu kurudi tulipotoka. Nikigeuza, fungua mlango wako, tutawamwagia risasi za kushtukiza hao mbwa kufumba na kufumbua.” Jombi alitoa maelezo, Miraji pasipo kuuliza akayafuatisha.
Gari lilipiga breki kali likageuka pasipo polisi kutegemea. Kabla polisi hawajajipanga, Miraji alishafungua mlango, Jombi akishusha kioo. Risasi zilimiminwa kuelekea kwenye gari la polisi ambao hawakuwa na la kufanya kwa muda huo zaidi ya wengine kujificha wengine wakisulubishwa na risasi.
Vioo vya gari la polisi vilivunjika matairi yakipasuliwa. Jombi na Miraji walitokomea kwa kasi wakiwaacha polisi wasijue la kufanya.
Walipita nyumba fulani isiyokaliwa na mtu, Jombi akapaki gari hapo. Walivua vinyago wakatumia daladala kama usafiri kurudi majumbani mwao.
Miraji aliamini ni Mungu tu ndiye aliyewaokoa, tena kwasababu ana dhamira safi ya kulipa damu ya baba yake iliyomwagwa pasi na hatia.
Asubuhi ilikucha kwa Ali wa Fatuma. Kibanda chake kidogo mbavu za mbwa kilikuwa kinamimina moshi mzito ukitokea kwenye madirisha yake madogo.
Sauti ya kukohoa ilisikika ndani ya kibanda hicho, baada ya muda kidogo mlango ukafunguliwa akitoka mzee Ali wa Fatuma. Alikuwa kavalia kaniki nyeusi kiunoni. Mdomoni mwake alikuwa ana kijiti kirefu alichotumia kusafishia meno. Mkononi alishika kopo kubwa lililobebelea maji.
Alinawa uso. Asimalize, akatoka mwanamke mweupe mchanga, Chausiku, akaungana naye kufanya shughuli sawa.
“Chai tayari, mume wangu.”
“Ahsante. Yani leo nina kazi kubwa sana. Umentilia maziwa?”
“Ndio, kila kitu kama ulivyotaka. Hiyo kazi unayoniambia tangu jana, ni kazi gani?”
“We acha tu. Kwanza wateja wenyewe ni watu wakubwa, si unawajua wale mabosile wangu? ... Pili wanakabiliwa na janga kubwa. Kubwa, mke wangu!”
“Mbona unantisha sasa?”
“Wala! Ila ndio uhalisia huo. Nataka nipate chai nzito ya kun’toa jasho. Alafu nipakie kwenye mkoba vile vitu vyangu nilivyovitenga jana pembeni.”
“Sawa.”
Ali wa Fatuma alimaliza kunawa uso akaelekea bafuni na ndoo yenye maji. Chausiku, mwanamke mbichi ambaye unaweza dhani ni mwanae, alijirudisha ndani ya kibanda akatazama sufuria yenye chai ndani yake.
Miaka mitatu nyuma Chausiku alilazimishwa na wazazi wake kuolewa na Ali wa Fatuma kama malipo ya fadhila kwa mganga huyo ambaye aliwasaidia kumpa ahueni mama yake aliyekuwa mahututi. Ilimchukua muda mrefu mwanamke huyo kukubali hiyo hali ya kuwa mke wa mtu mwenye umri unaorandana na baba yake, ila mwishowe alizoea, maisha yakasonga.
Kiredio cha mbao kiliruruma kwa mbali kikiwa kimebandikwa dirishani. Taarifa ya habari ilisikika mtangazaji akiongea kwa sauti nzito na ya kushiba. Chausiku hakuvutiwa na taarifa hiyo ya habari, ilikuwa inaboa, mara zote kwake huwa hivyo.
Aliendelea kufanya shughuli zake kana kwamba hasikii chochote. Laiti kama isingelikuwa mume wake asingelikuwa anasikiliza taarifa ya habari hata kidogo. Kusikia taarifa ya habari hapo nyumbani ilikuwa ni alama tosha Ali wa Fatuma yupo nyumbani.
Ila siku hiyo ilikuwa tofauti. Ndani ya muda mfupi, kuna sauti ilitoka redioni ikateka hisia zake:
TAARIFA ZILIZOTUFIKIA HIVI PUNDE.
Chausiku aliacha shughuli zake akatega sikio.
“Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya usafirishaji majini, AFRI CARGO, bwana Katende Katende amekutwa amefariki nyumbani kwake usiku wa kuamkia leo mwili wake ukiwa na idadi ya risasi tano. Wanaume wawili wasiojulikana wanatuhumiwa kuhusika na tukio. Kwa taarifa zaidi endelea kusikiliza redio wani … ”
Chausiku akaachama mdomo kwa kubung’aa.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Katende?” Alijiuliza.
“Katende wa usafirishaji? ... Mmmh … Si ndo’ huyu wa mume wangu? Au nafananisha?” Chausiku alisimama kwa muda akitafakari. Alipuuzia akaendelea na shughuli yake. Ali wa Fatuma alipotoka bafuni, akampokea na swali:
“Mume wangu, hivi yule bosi wako wa mambo ya usafirishaji anaitwa nani?”
“Ushamsahau?” Ali wa Fatuma aliuliza akitabasamu. Ni kama vile alijivunia kuwa na mteja wa aina hiyo
“Anaitwa Katende Katende au K square.”
“Basi kafariki usiku wa kuamkia leo. Ameuwawa na majambazi.”
“Unasema?”
“Amefariki! Sasa hivi wametoka kutangaza brekingi nyuzi redio wani.”
“Embu nipatie simu yangu mara moja, haraka!”
Chausiku alikimbilia simu chumbani akamletea mumewe.
“Haloo, bwana Mtemvu. Nimesikia taarifa ya habari kuhusu Katende, vipi? ... Sawa, nakuja sasa hivi!”
Ali wa Fatuma alikata simu akamuhakikishia mkewe juu ya zile habari. Ilikuwa ni kweli. Alikunywa chai upesi akavaa na kujipakiza kwenye gari lake Vitz nyekundu tayari kwa ajili ya safari.
Alitoka kwa kasi. Alisahau kubeba mizigo yake aliyomwambia mkewe amwekee mkobani. Alifika barabarani ya lami akakumbuka. Aligeuza gari haraka akarudi nyumbani upesi.
Alipofika alipiga kelele kumuita mkewe amletee mkoba ila mke hakuitika wala kuonekana. Alishuka akaenenda ndani. Huko alimkuta mkewe amelala chini akimiminika damu toka shingoni kama mtu aliyechinjwa.
Alipigwa na butwaa. Alitizama huku na kule asione mtu. Alichuchumaa akamshika Chausiku. Alimuita machozi yakimlenga lenga lakini Chausiku hakuamka.
Ghafula upepo ulimpita mgongoni, akashituka. Alitizama asione kitu. Alishika mkoba wake pembeni akauvuta. Aliufungua ndani asikute kitu.
“Silaha zangu zimeenda wapi?” Aliduwaa.
Upepo ulimpitia tena nyuma yake, akashituka. Alinyanyuka akielekea mlangoni, mlango ukajifunga.
Ndani kulikuwa giza totoro. Sauti ya Ali wa Fatuma akihema kwanguvu ilisikika. Ghafula ikanyamaza. Sauti kali ya kelele ikapasuka:
Aaaaaaaaahh!
Mlango ulipojifungua, Ali wa Fatuma alionekana amelala chini, shingo yake imekatwa. Macho yalikuwa yamemtoka nje. Mdomo ulikuwa wazi. Muda mfupi nzi walimzonga kutafuta chakula.
Simu yake aliyoiacha kwenye gari iliita mpaka basi. Jina la Mtemvu lilishika kioo kumtafuta mganga pasipo matunda. Mganga alishageuka marehemu aliyemuua asijulikane.
Hakuna chombo cha habari kilichokuwa nyuma kurusha tukio la msiba wa bwana Katende. Kila chaneli na stesheni ilijitawaza kurusha matangazo moja kwa moja toka eneo husika.
Wananchi pia wasibaki nyuma, wengi wao walikodolea vioo vya televisheni ama kukinga masikio redioni wapate kupashwa habari juu ya kifo cha ghafula cha mtumishi huyo mkubwa na muhimu nchini, hamu yao kubwa ikiwa ni kufahamu nani alikuwa nyuma ya kifo hiko ukizingatia kwa muda wa karibuni kumekuwa na mfululizo wa vifo vya watu wazito.
Kila mtu alisema yake. Wengine waliamini watakuwa wamedhulumiana hivyo wanauwana wenyewe. Wengine walienda mbali wakidhani wanagombea hawara, lakini hakuna hata mmoja aliyediriki kubashiri kwa kutaja jina la Miraji, mtoto wa marehemu Malale.
Mambo yaligeuka pale ilipofikia mida ya saa saba kamili ya mchana. Picha ya muuaji ikiwa imechorwa ikaoneshwa kwenye televisheni. Jeniffer, mtoto wa K square, alitumia kipaji chake cha uchoraji akachora picha nzuri sana ya Miraji kwa mujibu wa kumbukumbu zake pale alipomuona muuaji huo akijimulika usoni.
“Ni nani huyo muuaji?”
Swali hilo lililoshika vinywa vya watazamaji lilijibiwa pale Mtemvu alipohojiwa.
“Ni mtoto wa kwanza wa aliyekuwa afisa wa serikali, bwana Malale Kombo.”
“Kwanini anafanya mauaji hayo ya watu ambao walikuwa karibu sana na baba yake kipindi chake cha uhai?”
“Ni kitu cha kushangaza kwanini anafanya haya mauaji. Sijui hasa lengo lake ni nini!” Mtemvu alijibu akipandisha mabega yake juu.
Japokuwa aliulaghai umma kwamba hana wazo lolote juu ya sababu za Miraji kuua, kichwani kwake alishapata jibu ni kwasababu ya kisasi cha marehemu baba yake. Mama yake atakuwa kampandikiza chuki, aliwaza. Alipata hofu endapo Miraji akikamatwa na kuhojiwa anaweza akamwaga mchele wote, aliendelea kuwaza.
Alitoa amri kwa mapolisi kumtafuta Miraji na kuhakikisha anataarifiwa punde tu atakapotiwa nguvuni. Na kuhusu mama wa mtuhumiwa, Bernadetha, naye akamatwe, asihojiwe na mtu mwingine yeyote isipokuwa yeye.
Wakati chaneli za televisheni zikiendelea kurusha matangazo hayo ya mauaji ya K square moja kwa moja, Bernadetha alikuwa analia tangu alipoona picha ya mwanae. Pembeni yake aliketi mtoto wake mdogo, Marietta, naye akilia kwa kumuona mama yake anafanya hivyo.
“Kwanini umefanya hivi, Miraji?” Bernadetha alilia sana akiuliza.
“Nitabaki na nani mimi? Kwanini hukutaka kunisikiliza? Unamuacha mama yako na nani sasa?”
Sauti hiyo ya kilio ilitosha kabisa kumsumbua jirani. Lakini haikudumu kwa muda mrefu ikamezwa na sauti kali ya king’ora cha polisi.
Magari mawili aina ya defender yalisimama mbele ya nyumba ya marehemu mzee Malale wakashuka askari sita waliovalia kofia na mavazi magumu wakibebelea bunduki mikononi mwao.
Haraka na kwa tahadhari waliingia ndani. Walimuweka chini ya ulinzi Bernadetha. Walivamia vyumbani kumtafuta Miraji lakini hawakupata kitu.
Bernadetha pamoja na mwanaye walichukuliwa kwa lengo la kusaidia polisi kwenye upelelezi. Nyumba ilibaki tupu. Televisheni peke yake ilibakia ikinena asiwepo mtu wa kuitizama.
Jua likazama.
Katikati ya usiku wa siku hiyo, ndani ya nyumba ndogo ikivutia kwa mapambo na mpangilio wake, sebuleni aliketi Jombi pamoja na Miraji. Mezani kulikuwa na chupa kubwa ya kilevi Johnny Walker na glasi ndogo mbili.
Vidoleni mwa watu hao wawili kulikuwa na misokoto ya bangi ikienda midomoni mwao zamu kwa zamu.
Baada ya kupiga pafu kadhaa za bangi, Jombi alikunywa fundo moja la kinywaji chake, akasema:
“Kwahiyo tunafanyaje sasa man?”
Miraji akanyonya kwanza msokoto wake wa bangi.
“Mpango wetu upo palepale.” Alisema kisha akaongezea. “Ila kwa sasa kuna wazo ninalo. Tutakapomvamia Mtemvu itabidi nichukue pesa za kutosha niende zangu nje, hapa si salama tena kwangu.”
Jombi hakuzingatia Miraji alichosema. Alifikiria kwa muda akaendelea na mazungumzo ya uvamizi kana kwamba hoja ya Miraji haina mashiko.
“Kazi iliyopo mbele yetu kwa sasa si ndogo kabisa. Ni vita kubwa sana. Inabidi tujipange haswa jombaa.”
“Niambie, nakusikiliza.” Miraji alisema kwa hamu.
“Tunahitaji silaha kubwa. Tunahitaji sniper gun ya kulenga masafa marefu.”
“Tutaipatia wapi hiyo, Jombi? Si pesa ndefu sana?”
“Tutaipata tu. Nipe leo na kesho itakuwa mikononi mwangu.”
“Kwahiyo tunahitaji hicho tu?”
“Hapana. Tunahitaji pia sumu.”
“Sumu?”
“Ndiyo. Tutahitaji sindano za sumu kama tatu hivi. Pia na mabomu ya moshi.”
“Tutayapata wapi yote hayo?”
“We tulia. Niachie mimi hiyo kazi.”
“Sawa, nakuaminia bro!”
Baada ya hivyo vitumaongezi, Jombi alinyanyua simu yake akampigia mtu aliyemtunza kwa jina la ‘Mkuu’. Simu ilipopokelewa akasogea pembeni kidogo.
“Samahani mkuu kwa kukupigia muda huu, nina shida … Kuna silaha nahitaji, bunduki ya kudungulia, mabomu ya moshi na sindano za sumu … Kesho? ... Sawa Mkuu … Kazi inaenda vizuri, wamebakia wawili tu … Hakuna mtu yeyote anayejua uwepo wetu, wote wanamjua ni Miraji tu analipa kisasi … Usihofu Mkuu, haitozidi majuma mawili waliobaki watakuwa jehanamu.”
Jombi alikata simu akamrudia Miraji. Waliendelea kuvuta na kunywa mpaka kila mtu alipozima ndani ya usingizi.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jua liliamka likamkuta Miraji akiwa juu ya kitanda, Jombi asionekane alipo. Miraji alitazama huku na kule. Alijinyanyua akaandaa chai na kupata kifungua kinywa hiko akiwa anatazama uchambuzi wa magazeti kwenye televisheni.
Taarifa ya mauaji ya Katende pamoja na picha yake zilitawala vichwa vya kila magazeti ila hazikuonekana kumshitua sana Miraji. Macho yalimtoka pale habari juu kukamatwa kwa mama yake iliposomwa.
“Mama wa mtuhumiwa akamatwa, asema hajui sababu inayomfanya mwanae afanye mauaji.”
Chai ilikuwa chungu. Machozi yalibubujika juu ya uso wa Miraji. Alipiga ngumi juu ya meza kwanguvu akisaga meno. Alitafuta simu yake akampigia Jombi.
“Upo wapi? Wamemkata bim’kubwa … Sasa? ... Njoo basi, fanya haraka!”
Hazikupita dakika tano Jombi aliwasili. Alikuwa kabebelea mifuko miwili ya nailoni akaiweka mezani na kuketi kumsikiliza Miraji.
Akiwa na pupa ya jazba pamoja na macho yanayovuja machozi, Miraji alieleza kile alichokiona na kukisikia kwenye televisheni.
“Hakuna haja ya kuhofia, Miraji. Mama yako hatosema lolote. Mwishowe watamuachia tu.” Jombi alimpa moyo.
“Lakini huko polisi ndipo alipo Mtemvu!” Miraji alisema kiwoga.
“Na hiyo ndio sababu mama yako hatosema kitu chochote. Niamini. Tumalize kwanza kazi yetu, na tena sasa tuanze na huyo Mtemvu. Unaonaje?”
Miraji alifikiria kidogo kisha akasema:
“Sawa. Tufanye hivyo.”
Jombi akatabasamu na kumkumbatia.
Zilipita siku nne tangu msiba wa K square uvume. Siku hiyo Mtemvu alikuwa na miadi ya kuonana na mheshimiwa Waziri Mkuu katika hoteli kubwa ya PWEZA LA VIDA maeneo ya posta kandokando na bahari ya hindi.
Akiwa katika maandalizi nyumbani kwake, Mtemvu alitazama kioo chake kikubwa akatabasamu mwenyewe. Suti ilikuwa imemkaa vema. Mama Beatrice naye alisogea kiooni akajitizama. Gauni lake lilimpendeza. Walikumbatiana wakapeana busu kisha wakaongozana kutoka nje walipomkuta inspekta Vitalis yu tayari anawasubiri.
Walipanda garini, safari ikaanza.
Hatua kama kumi na tano nyuma yao pikipiki kubwa iliwafuata. Iliwabebelea wanaume wawili wote wakiwa wamevalia kofia ngumu, makoti meusi yaliyobana miili yao na miwani ya jua. Mwanaume wa nyuma alibebelea begi kubwa jeusi mgongoni mwake.
Inspekta Vitalis aliona pikipiki hiyo ikiwafuata. Aliongeza kidogo mwendo kasi wa gari akiwakumbusha mkuu wake na mkewe wafunge mikanda kwa usalama.
Walikata kona ya pili, pikipiki ile kubwa ikapotea. Inspekta Vitalis alizururisha macho lakini hakuona kitu. Mpaka wanafika hotelini taswira ya pikipiki haikujiri machoni mwake.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mtemvu na Mama Beatrice walishuka kwenye gari wakachukua hatua kwenda ndani. Kabla inspekta Vitalis hajawafuata alitizama kioo cha kando ya gari akamuona mwanaume akiwa amevalia koti jeusi, miwani na begi mgongoni anaingia kwenye jengo lililo karibu na hoteli. Uso wake ulikuwa umeelekea chini akitembea kwa haraka.
Inspekta Vitalis alishuka garini akamfuatilia mwanaume yule aliyemtilia shaka. Alitembea kwa haraka macho yake yakiwa makini kumtizama mhusika wake.
Japokuwa watu walikuwa wengi barabarani, aliwakwepa bila ya kutikisa macho na hata pale alipokumbana nao vikumbo hakusema jambo, aliwaacha wahanga waropoke yeye akiendelea kufanya kazi yake.
Huku hotelini, PWEZA LA VIDA, mwanaume wa pili akiwa kavalia koti jeusi na miwani aliingia ndani. Alitembea kwa haraka uso wake ukitizama huku na kule kana kwamba anamtafuta mtu. Alichukua lifti akaiamuru kwa kubonyeza vitufe impeleke sakafu za juu.
Juu, sakafu ya sita ndani ya hoteli, mambo yalishakwiva. Mtemvu, Waziri Mkuu pamoja na wake zao waliketi kwenye meza iliyopambwa sahani zenye vyakula na vinywaji vya gharama. Nyuma yao walisimama wahudumu wawili na walinzi, wanaume wawili warefu mwenye mwili mpana ndani ya suti nyeusi.
Waziri alitoa ishara kwa wahudumu na walinzi hao anahitaji faragha. Wakapishwa na kubakia watu wanne tu ambao walimimina vinywaji vyao kwenye glasi wakavigongesha na kuvimiminia mdomoni.
“Ni muda mrefu tangu tuonane, bwana Mtemvu. Mbona kimya hivyo?”
“Majukumu, mheshimiwa. Si unajua tena hizi kazi zetu za usalama.”
“Aaah bwana ndio uwe kimya kiasi hiko? Eti shemeji?”
Mama Beatrice alitabasamu asitie neno.
“Kazi tu mheshimiwa. Hakuna kingine.” Mtemvu alisema akitabasamu.
“Nafurahi sana kusikia hivyo.” Waziri Mkuu alisema na kuongezea, “Najua utakuwa umeshangazwa na taarifa ya ghafula juu ya kikao hiki. Ila nimekuita hapa kwa mambo makuu matatu. Mosi, ni kujuliana hali kama familia. Pili, ni kuhusu hali ya usalama kwa sasa. Mwisho, ni kuhusu uhakiki wa taarifa fulani ambayo nimeipata hivi majuzi juu yako.”
“Ndio, mheshimiwa.” Mtemvu aliitikia akiacha kula.
Waziri Mkuu alikata nyama iliyokuwepo kwenye sahani akaitia mdomoni. Aliwatizama wanawake kisha akanywa kinywaji kidogo.
“Mwaka jana, mwezi wa saba, kama nakumbuka vema, ndio ilikuwa mara yangu ya mwisho kukutia machoni wewe na shemeji. Ilikuwa ni Arusha, si ndio shemeji?”
“Ndio.”
“Mlikuwa mmeongozana na watoto, mbona leo hamjaja naoh?”
“Wapo shule.” Mtemvu alijibu mkewe akiongezea: “Wanasoma Afrika ya kusini huwa wanakuja huku likizo tu.”
“Ooh! Hongereni sana!”
“Vipi wakina Berham, wapo?” Mtemvu naye aliuliza. Mke wa waziri akawahi kujibu.
“Wapo! Sasa hivi wanamalizia mwaka wao wa mwisho chuoni Uingereza.”
Walijichekesha wakiendelea kula.
Kabla halijatiwa tena neno lingine, ilisikika sauti ya ndogo ya kioo ikipasuka Waziri Mkuu akipokea risasi mbili kifuani. Alitoa kelele za maumivu akidondoka chini kama mzigo.
Mtemvu aliamrisha wanawake walale chini haraka. Walinzi wa waziri walifungua mlango wakaingia ndani kwa pupa. Walipokelewa na risasi wakadondoka chini na kufa.
Risasi zote zilipitia kwenye kuta ya kioo zikiacha matundu na nyufa. Ziliendelea kufululiza zikishambulia hatimaye vioo vya hoteli vikapasuka pasuka katika vipande milioni.
Risasi zote hizo zilitokea sehemu moja, kwenye dirisha la jengo refu lililopakana na hoteli. Jengo kubwa ambalo lilikuwa bado halijamaliziwa. Humo alikuwa amelala mwanaume mwenye sura nyeusi akiwa na bunduki ndefu iliyosimamia miguu miwili. Mwili wake ulikuwa umeveshwa koti na miwani meusi.
Alimaliza kufyatua akaanza kuitengua bunduki yake aiweke kwenye begi. Kabla hajafunga begi na kuhepa, inspekta Vitalis aliingia eneoni akihema kwanguvu kwa kutoka mbioni. Mkononi alishikilia bunduki ambayo haraka aliinyooshea kwa mwanaume yule muuaji.
"Mikono juu!" Inspekta aliamuru. Mwanaume akatii haraka.
"Piga teke begi lije huku!" Inspekta aliamuru tena.
Mwanaume yule akatabasamu kwa mbali. Alivuta na kulinyanyua begi kama mpira akalirushia kando ya inspekta Vitalis.
Inspekta Vitalis alihamisha atensheni yake kwa kujaribu kudaka hilo begi. Mwanaume yule akajiangusha chini akitoa kifaa cheusi cha mviringo mfukoni akakibamiza chini, moshi ukafuka kwa haraka.
Inspekta alifyatua risasi mbili asimpate mlengwa wake aliyekuwa anajiviringita. Baada ya muda mfupi, moshi ulitapakaa kuonana ikawa shida.
Inspekta Vitalis akibung’aa kutafuta, alijikuta akipigwa teke tumboni akainama kwa kusikilizia maumivu. Kabla hajakaa vema, teke lingine lilimsomba kichwa na kumpeleka chini kama kiroba cha viazi.
Alifyatua risasi kadhaa akibashiri alipo mlengwa wake. Moshi ulipopungua makali, hakuona mtu. Aliachwa mwenyewe mwanaume muuaji akikaribia kumaliza jengo.
Alinyanyuka upesi akatazama upande wa jengo la hoteli. Aliona watu wamejazana ndani ya eneo walilokuwa wameketi Waziri Mkuu na Mtemvu. Alitizama chini barabarani akawaona wanaume wale wawili wakijichanganya kati kati ya umati wa watu wanayoyoma.
Haraka alishuka. Alitazama kushoto na kulia lakini hakuwaona walengwa wake. Aliendea gari akaliwasha, ila kabla hajatoka kwenda popote, ving’ora viliita. Magari mawili ya polisi yalifika eneo la tukio, wakashuka polisi wanne wakibebelea bunduki.
Baada tu ya muda mfupi, walisogea polisi wengine ndani ya defender. Walivalia makofia na miwani wakibebelea pia bunduki. Inspekta alitoka ndani ya gari akawafuata. Aliwaoneshea kitambulisho chake akiwauliza;
“Wakati mnakuja mlipishana na watu wawili juu ya pikipiki kubwa?”
“Ndio. Kona ya pili tu hapo.” Alisema dereva akielekezea kidole barabarani.
Haraka inspekta Vitalis alipanda gari la polisi akalitimua kwa kasi akielekea alipoelekezwa. Kwa kuwa aliwasha king’ora, magari na watu walimpisha barabarani, ndani ya dakika chache akawatia machoni wanaume wawili juu ya baja.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Aliongeza kasi zaidi na zaidi, sasa ikabakia umbali mdogo kuwakarabia walengwa wake.
“Man, ni muda wa plan B sasa.” Mwanaume aliyekuwa anaendesha alimshitua mwenzake aliyeketi nyuma.
Mwanaume wa nyuma alijigeuzia upande wanaotokea akatoa bunduki begini na kuelekezea kwenye gari la inspekta Vitalis linalokuja kwa kasi.
Risasi zilifyatuliwa kwa pupa kushambulia gari, pikipiki ikipenya penya ubavuni na kati ya magari mengine. Inspekta alijitahidi kukwepesha gari kwa kulipeleka kushoto na kulia. Ila mwishowe risasi zilipiga kioo cha gari kikawa nyang’anyang’a.
Kumaliza kabisa kazi, mwanaume muuaji alilenga matairi ya gari alilomo inspekta Vitalis, matairi yakapasuka, safari ya Inspekta ikakomea hapo hapo.
Inspekta alisaga meno kwa hasira. Kwake ilikuwa ni nafasi nzuri sana ya kumaliza kazi, na ameipoteza kizembe, aliwaza. Alilaza kichwa chake kwenye usukani akashusha pumzi ndefu.
Kupita dakika ishirini, ndani ya jumba kubwa lililoachwa solemba na mji, pikipiki ilipakiwa humo wakishuka wanaume waliotoka kufanya tukio.
Walivua sura bandia walizovaa, hapo ikajionyesha kumbe alikuwa Jombi na Miraji. Miraji akiwa mwanaume aliyebebelea begi lenye bunduki.
Walibadili pia na mavazi kisha wakatoka ndani ya jengo wakitumia gari dogo, Toyota Passo, ambayo vioo vyake vilikuwa vyeusi ti.
Muziki uliita kwa mbali ndani ya gari kwa muda watu wakiwa kimya. Baadae Jombi alisafisha koo akasema:
“Kazi inakuwa ngumu zaidi.”
Miraji akamtizama asitie neno.
“Kosa ulilolifanya la kulenga litatugharimu sana. Ilikuwa ni nafasi yetu nzuri mno.”
“Najua hilo.” Miraji alisema akitizama chini. “Ila nilikuambia, Jombi, mie sina utaalamu wa kulenga vizuri umbali huo.” Miraji alijitetea.
“Umbali haukuwa mkubwa ilibidi tu utulize mchecheto. Sikuwa na budi kukuachia wewe ufanye lile jambo, si ulisema unataka uwaue kwa mkono wako mwenyewe?”
Miraji kimya.
“Ulinipa kazi nikatafute wapi walipoketi, nikafanya na nikakujulisha. Lakini ukafanya uzembe!”
“I am sorry, Jombi. Mi mwenyewe imeniuma sana.”
Walinyamaza kidogo, Miraji akasema:
“Vipi sasa kuhusu hivyo vifaa vingine vya kumalizia kazi. Tutavipatia wapi?”
“Usiogope kuhusu hayo maswala, bro. Kila kitu niachie mimi.” Jombi alijigamba.
“Naogopa sitakuwa na pesa ya kukulipa vyote hivyo.” Miraji alisema kinyonge. Jombi akamshika bega.
“Umesahau wewe ni rafiki yangu? Usijali sana kuhusu pesa. Tufanye kazi kwanza.” Jombi alisema akitizama mbele.
“Ahsante sana, Jombi. Wewe ni rafiki wa kweli. Hakika Mungu atakulipa.”
Miraji alisema machozi yakimlenga.
Saa ya ukutani ilisema ni saa moja na nusu asubuhi, Mtemvu na inspekta Vitalis wakiketi sebuleni. Mezani kulikuwa na vikombe viwili vikubwa vilivyobebelea kahawa nyeusi ikifuka moshi. Pembeni kidogo ya vikombe hivyo kulikuwa na magazeti mawili yamejiweka hapo kana kwamba nayo yanafanya kikao.
Mtemvu alishika tama asionekane na dalili za kunywa wala kutaka kahawa. Inspekta alikuwa amekunja nne, mguu wake ulio juu akiutikisa tikisa kwa mbali. Taratibu yeye alikuwa anapeleka kahawa mdomoni akiinywa kwa tahadhari asiunguze mdomo.
“Yani sina amani kabisa. Nashindwa kufanya kazi zangu kwasababu ya kuwindwa mithili ya swala. Sijui nifanye nini?” Mtemvu alilalama akitikisa kichwa.
Inspekta alipeleka kwanza kahawa mdomoni ndipo akafungua kinywa;
“Usihofu, mkuu. Mimi nipo na nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu kukuhakikishia usalama. Muda si mrefu nitawatia nguvuni kuna mipango nimekwishaipanga na nina uhakika lazima watanasa. Ninachokuomba tu ubaki nyumbani kwa majuma mawili. Yanatosha sana kumaliza kazi yangu.”
“Nitajitahidi kwa hilo, Inspekta. Sina mahala pa kwenda sasa tangu rafiki yangu pekee aliyekuwa amebakia, Pius, naye kuvamiwa na kuwawa.” Mtemvu alisema akiongezea:
“Ila nashukuru sana, Inspekta, hata hivyo unajitahidi sana. Naomba uwatie nguvuni hao watu haraka iwezekanavyo. Kuendelea kwao kuwa huru ni hatari kwa usalama wangu na wa watu wengine pia.”
“Ondoa shaka.” Inspekta Vitalis alisema kisha akanywa fundo moja la kahawa.
“Ila mkuu, nadhani huu ni wakati muafaka wa kunijuza kinaga ubaga kwanini mtoto wa rafiki yenu ahangaike kutaka kuwaua. Kuna nini kati yenu?” Inspekta Vitalis alidadisi.
Mtemvu alimtizama Inspekta alafu akajilazimisha kutabasamu. Kwa mara ya kwanza alinyanyua kikombe cha kahawa akanywa fundo moja.
“Sijajua kwanini. Mimi na baba yake tulikuwa marafiki mno tuliosaidiana kwa kila njia. Mpaka baba yake anakufa mie nilikuwa pembeni ya kitanda chake.”
Inspekta alitulia kwanza. Alikunywa mafundo matatu ya kahawa kisha akauliza:
“Unamkumbuka Jeniffer?”
Mtemvu akatikisa kichwa.
“Yes. Si yule mtoto wa K square aliyechora picha ya muhalifu?”
“Ndiye huyo.”
“Enhe …”
“Nilipata wasaa kidogo wa kuongea naye. Aliniambia muuaji kabla hajafanya mauaji, alidai amekuja kuchukua roho ya K square kama wao walivyoichukua roho ya baba yake, Malale. Unasemaje kuhusu hilo?”
Mtemvu alipaliwa na kahawa. Alikohoa kwa muda kidogo kusafisha koo lake kabla hajatia neno:
“Unajua vijana wa siku hizi sijui wamerukwa na akili. Sijui wanakula nini kinatibua bongo zao – nadhani ni bange tu. Miraji hajui aongeacho. Puuzia hayo maneno, fanya kazi yako. Umesikia Inspekta? Masikio hayalali njaa. Utasikia ya kila aina.”
Mtemvu alisema kwa mkazo kisha akanywa fundo la mwisho na kuaga anaelekea chumbani atarudi punde.
Inspekta alikunywa fundo moja akabinua mdomo wake akitikisa kichwa.
“Kuna kitu hakipo sawa.” Alisema na kuongezea:
“Ni lazima nijue.”
Muda mfupi mbele, Mtemvu alikuja akiwa amevalia suti wakaondoka na inspekta Vitalis kuelekea kituo cha polisi. Huko Mtemvu alikutana na Bernadetha aliyekuwa rumande, akaomba faragha apate kuongea naye.
“Unataka nini kwangu? Bado hujatosheka, sio?” Bernadetha aliongea kwa jazba.
Mtemvu alitabasamu akamwambia:
“Sijaja hapa kuzozana na wewe, Bernadetha. Ila nimekuja kukusaidia,”
“Wewe mwanahayawani unisaidie mimi?” Bernadetha alijikuta akitabasamu.
“Unataka kuonana na wanao, ama hutaki?” Mtemvu aliuliza. Bernadetha akamtizama kwa macho ya husda.
“Kama ukitaka kunijua mimi ni nani, gusa watoto wangu. Nitahakikisha nakuanika uchi hadharani!”
Mtemvu alitabasamu akitikisa kichwa.
“Nimekuambia sijaja kuzozana. Nataka nikuache uende ukakutane na familia yako. Hujammisi mwanao, Marietta? Je Miraji?”
Bernadetha alinyamaza kimya. Mara akaanza kulia.
“Shhh! Usilie. Nipo tayari kukupa nafasi nyingine ya kuonana nao.”
“Unataka nini, kwangu?” Bernadetha aliuliza. “Najua kuna kitu unataka, nini hiko?”
“Sasa hapo umeongea.” Mtemvu alisema akitikisa kichwa.
“Let us make a deal. Nakuachia huru ukaonane na wanao, ila kwa masharti mawili.”
Mtemvu aliweka kituo ameze mate, alafu akaendelea:
“Kwanza, ufunge mdomo wako kabisa. Sitaki kusikia unasema chochote kuhusu mimi na mumeo kwa yeyote yule. Pili, umwambie mwanao, Miraji, aache kunifuatilia, nami nitajitahidi kufanya sakata lake lipotee pasipo watu kugundua. La sivyo nitampotezea mbali kimya kimya. Tumekubaliana?”
Bernadetha hakujibu. Alimtizama Mtemvu na macho mekundu ya hasira.
“Tumekubaliana ama niondoke usiione familia yako milele?”
Bernadetha kimya. Mtemvu aligeuka akatishia anaondoka, mara Bernadetha akamuita.
“Sawa, nimekubali.”
Mtemvu akatabasamu na kuonya:
“Endapo utakiuka tulichokubaliana, nitakufanya kitu mbaya hutonisahau maishani mwako. Umesikia?”
Bernadetha hakujibu. Aliishia tu kumtizama Mtemvu kana kwamba anataka kummeza. Mtemvu alitabasamu akamuaga akimuahidi kutimiza walichoadhimia.
Ilikuwa inakaribia kumalizika majuma mawili tangu tukio la PWEZA LA VIDA lijiri na juma moja tokea Pius amekatwa pumzi. Vyombo vya habari viilivyokuwa havina habari mpya ya kuuza, viliendelea kujadili na kudadavua matukio hayo makubwa nchini kuwahi kutokea. Mbali na hapo kulikuwa tu tulivu, jiji la Dar es Salaam likielekea kutimiza majuma hayo bila mtu mwingine mzito kuaga dunia.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ikiwa ni usiku wa saa nne, Mtemvu na mkewe: Mama Beatrice, walikuwa wanatizama marudio ya taarifa ya habari kwenye televisheni yao kubwa. Mama Beatrice alilala kwenye mapaja ya mumewe akijikunyata, Mtemvu akitizama simu yake mara kwa mara kana kwamba kuna kitu anategemea. Palikuwa tulivu usibashiri kama kuna jambo lolote linaweza kutokea kuharibu amani hiyo.
Dakika tatu mbele, nje ya nyumba ya Mtemvu kwa mbali kidogo, lilisogea gari wakashuka wanaume wawili wenye sura za kizungu wakibebelea mabegi migongoni. Walifuata uzio wa nyumba kwa tahadhari. Upesi walirusha kamba zao kutani wakapanda na kukata nyaya za umeme. Walidumbukia ndani ya uzio wakifikia kuchuchuma.
Simu ya Mtemvu iliita kamlio kadogo cha kushitua. Inspekta aliwabipu. Upesi Mtemvu na mkewe walitoka sebuleni wakakimbilia chumbani kujifungia. Ni kama vile ule mlio wa simu uliwaagiza wafanye hivyo.
Inspekta Vitalis alishuka kwenye mti mkubwa uliopakana na nyumba ya Mtemvu. Akatoa redio call akiongea;
“Kaa atensheni huko barabarani endapo watakimbia. Ova!”
Wakaonekana wanaume waliobebelea bunduki wakitapakaa barabarani umbali kidogo na nyumba ya Mtemvu.
“Sogea eneo la karibu, weka gari lao chini ya ulinzi. Ova!” Inspekta alitoa tena amri. Wanaume wengine watano wakatokea vichakani wakibebelea bunduki wakalizingira gari lililowaleta wavamizi.
Inspekta aliingia ndani ya uzio akisogea kuelekea ndani. Nyuma yake waliongezeka wanaume wawili wakimfuata lakini walijigawa, mmoja akaenda kushoto mwa nyumba mwingine akielekea kulia.
Wanaume wale wawili wenye sura za kizungu wakiwa koridoni wanajongea vyumbani, ghafula, walisikia vishindo nje nyumba. Walitizamana kitahadhari, mmoja wao akasema:
“Kuna watu nje. Tumeingia kwenye mtego, Miraji. Haukuwaua walinzi?”
“Hakukuwepo na mlinzi yeyote. Kibanda kilikuwa cheupe nikahisi labda watakuwa wametoka na tutamaliza kazi yetu haraka.”
“Umefanya uzembe, haiwezekani kukawa patupu. Watakuwa walijificha.”
“Sasa tunafanyaje. Hatuwezi tukapoteza nafasi hii tena.”
“Yes. Muda wa plan B.”
Haraka walichomoa mabomu mawili mabegini wakayapachika kutani wakiyaruhusu yasome tarakimu.
Mlango wa sebuleni ulifunguliwa akaingia inspekta Vitalis. Wanaume wale wawili wakasikia hilo. Wakati Inspekta anasogea kuja walipo, mmoja alilenga swichi kubwa ya umeme kwa risasi, umeme ukakata ndani ya nyumba kukawa giza totoro.
Vishindo vya miguu vilisikika vikitafutana milio ya risasi ikivuma. Sauti ya alarm ya bomu ililia kwanguvu, haraka inspekta Vitalis akarukia nje akipitia dirishani. Mabomu yalilipuka yakafanya nyumba iwe ghofu kufumba na kufumbua. Hakuna kilichobakia ndani.
Wanaume wale wawili wenye sura za kizungu walishatoka nje ya nyumba na tayari waliwamaliza wanaume wawili walioongozana na inspekta Vitalis. Walifuata ukuta haraka wapande, wasifanikiwe kumaliza, risasi ziliwalenga na kuwadondosha chini.
Mmoja alitulia kama aliyefariki tayari, mwingine akiugulia maumivu – alikuwa amejeruhiwa vibaya bega lake la kulia. Ila alinyanyua bunduki na mkono wa kushoto apambane. Kabla hajafyatua risasi, alijeruhiwa tena bega la kushoto akabaki analia kwa maumivu.
Inspekta alimsogelea karibu akamnyooshea mdomo wa bunduki, nyuma yake akiwa na wanaume wawili. Alivua sura bandia za mateka wao, akapata kuona sura ya Jombi na Miraji, Miraji akiwa yule mwanaume aliyetulia – mapigo yake ya moyo yalikuwa yanapiga kwa mbali akihema kwa kusita sita.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sali sala zako za mwisho.” Inspekta Vitalis alifoka akielekezea mdomo wa bunduki kwa Jombi.
“Usiniue, tafadhali. Usiniue!” Jombi alilia.
“Unaweza ukanipa sababu ya kuubakiza uhai wako?”
“Ndio!” Alisema Miraji na kuongezea; “Nitakuambia ukweli usiojua. Nitakuambia yule aliye nyuma ya mchezo huu.”
*** MWISHO WA MSIMU WA KWANZA ***
FUATILIA MSIMU WA PILI
0 comments:
Post a Comment