Simulizi : Nyuma Yako (2)
Sehemu Ya Pili (2)
Nilitazama kando na kando, nilikuwa mwenyewe. Sauti za mashine zilikuwa zinalia kwa mbali.
Nikachomoa sindano ya dripu mkononi na kuishikilia vema mkononi. Ilikuwa ndiyo silaha ambayo ningeweza kuitumia kwa muda huo. Punde mlango ukafunguliwa, akaingia daktari.
Alirusha macho yake kwenye mashine alafu akanijongea kunitazama. Hapo kifuani mwangu nikasema, “hii ndiyo nafasi,” haraka macho yangu yakatazama shingo yake kubaini ‘point’ dhaifu.
***
Upesi nikanyanyua mkono wangu na kutoboa upande wa kushoto wa shingo yake, karibia kabisa na shina, kisha nikamdaka akiwa amedhoofu na hajiwezi. Nikamlaza chini kwa utulivu na kisha nikamjulia hali kama hatokuwa na madhara kwangu ndani ya muda mfupi ujao.
Alikuwa amepooza. Macho yake yalikuwa yanafanya kazi lakini mwili wake ukiwa kama wa mtu mfu, hakuwa anajiweza. Ni vema. Nikafunga mlango na kumvua nguo zake nizichukue. Baada ya hapo nikatoka nikiwa nimevalia kinyago cha kufunika pua na mdomo wangu - kinyago ambacho nilikiopoa ndani ya chumba kile cha watu mahututi.
Nikiwa natembea kwa kujikaza nisionyeshe dosari, nikakatiza mbele kabisa ya wodi mbele ya askari kisha nikadaka korido. Nilikuwa natazamatazama kila kona kuhakikisha usalama wangu, lengo langu lilikuwa ni kuhakikisha nakuwa wa kwanza kuiona hatari kabla ya hatari kuniona mimi.
Lakini bado sikuwa vema kiafya. Nilihisi mwangu ukiwa dhaifu usiojiweza katika namna ya uhai. Kuna muda nilikuwa nahisi kupoteza uwezo wangu wa kuona ama viungo vikiwa dhaifu lakini bado sikusimama, nilikazana, huo ulikuwa ni muda wangu na ilinipasa nivune kila jema niwezalo.
Nilipoacha korido kwa kuikata kona, nikasikia sauti nyuma yangu inapaza, hey ngoja! Heey! Nilibaini alikuwa ni askari alikuwa akiniita. Nilihofia sana kwani bado ungali mapema, sikutaka niharibu kazi yangu.
Basi nikakazana kutembea na huku nikifikiria nini nifanye. Ubaya sikuwa naijua hospitali ipasavyo, sikupata fursa hiyo, ni kitu kigumu sana kwa mfungwa kutembelea hospitali kwa kuikagua, hilo lilikuwa bayana.
Nilichokuwa nakifanya ni kutembea kwa makisio tu na kusema vibango vya juu ya milango. Nilikuwa naomba nipate stoo ama chumba chochote ambamo humo nitapata kujificha kwa muda nikijua kinachoendelea lakini pia na kusoma ramani.
Nyuma nikasikia vishindo vya mtu akikimbia. Vilikuwa vinakuja kwa kasi, lakini kabla havijanifikia, vikasimama na nikasikia sauti ya watu wakiteta, hapo nikapata kujua kuwa askari alikuwa amesimama kuongea na mtu ambaye nilipishana naye muda si mrefu.
Nikaongeza kasi zaidi na punde nikazama ndani ya chumba cha maabara. Humo kulikuwa na wanaume wawili waliokuwa wakiendelea na kazi zao. Walinitazama na wakiwa hawana mashaka nami, wakaendelea na majukumu yao. Nalijua hawakuwa wakinifahamu.
Basi nikasonga kando na kuwaita, walipokuja nikawashughulikia, kwa kama sekunde kadhaa tu, wakawa chini. Kitendo tu cha kumaliza, nikasikia mlango wa maabara unagongwa mara mbili na kisha mlango ukafunguliwa. Alikuwa ni askari!
Alirusha macho huku na kule asione jambo. Nilikuwa nimejibana kwenye moja ya meza kuu zilizokuwa zinapatikana kwenye maabara. Mkono wake wa kuume alikuwa ameuweka kiunoni akiwa ameshikilia kitako cha bunduki.
Nilimwona uso wake ukiwa umejawa na shaka. Bila maulizo, alikuwa akinitafuta. Alikuwa amenigundua ama? Sikuwa najua japo niliamini vivyo, lakini nilikuwa nina uhakika kuwa hajatoa taarifa kwa wenzie. Kama angelikuwa amelifanya hivyo, king’ora kingaliwaka hospitali na humo wangetiririka askari kadhaa.
Akiwa ameuacha mlango wazi akajongea kuzama ndani, bado mkono wake ulikuwa kwenye kitako cha bunduki. Alipopoa macho kukodoa akizidi kupiga hatua kuzama.
“Hellow! Kuna mtu yeyote ndani?” akapaza kuuliza. “Kuna yeote humu!” akapaza zaidi. Alikuwa anzidi kusonga na kusonga.
Kumpoteza uelekeo, nikatupia kifaa cha maabara upande wake wa kushoto, upesi akatazama, aliporejesha uso wake alipokuwa ameuweka awali, akawa amekawia, nilisharuka kumdandia!
Nilidondoka naye chini na kumbamizia kichwa sakafuni, papo hapo akazirai! Nikasimama nikijiuliza nifanyeje.
Upesi nikampekua mfukoni mwake na kumkuta akiwa na kitambulisho, nikakitazama na kuona kuna namna naweza kukilaghai. Nikatazama kwenye meza ya maabara na kubandua ‘bubble gum’ iliyokuwa imebandikwa mbali kidogo na mimi.
Nikasoma baadhi ya kemikali kwenye vyupa alafu nikachagua moja, kwa kutumia usanifu wangu, humo nikaloweka bubble gum niliyoinyofoa mezani na kisha nikachukua kipande cha chupa ya kifaa kile nilichokitupa kumpoteza mwelekeo askari.
Kwa kutumia kipande hicho, nikamnyoa askari yule ndevu zake, mustachi, alafu nikajibandikia mimi kwa kutumia bubble gum ile niliyoiloweka kwenye kemikali, mustachi ukakaa vema.
Nikamvua sare zake na kuzivaa alafu upesi nikamuhifadhi kule ambapo nimewahifadhi wale wataalamu wa maabara. Sasa nikatoka nikiwa ‘askari’ si ‘daktari’ tena. Kofia nilizibia macho na kufanya mustachi tu ndiyo uwe unang’aa kulaghai mwonekano wangu.
Nikiwa nimeweka mkono wa kushoto ndani ya mfuko, nikatembea kwa kujiamini. Ndani ya muda mfupi nikafanya namna ya kupapata mahali pa kuhifadhia miili ya watu waliokufa, hapo nikamkuta askari mmoja na mtaalamu aliyekuwa anafanya kazi ya uhakiki na kurekodi miili.
Lakini kabla sijafanya jambo, king’ora sasa kikaanza kulia kuashiria kuna hatari. Sasa wakawa wameshajua kuna mchezo umefanyika, mfungwa ametoroka!
Wale askari niliowakuta pale, upesi wakatoka katika lile eneo wakimwacha mtaalamu, wao wakakimbilia huko kwenye tukio. Nikasonga kumfuata yule mtaalamu na kumtaka aendelee na kazi yake kwani miili yapaswa kupakiwa na kutoka upesi kwa ajili ya maziko.
“Lakini king’ora kimelia!” akaniambia kwa tahadhari.
“Unadhani sijasikia kama kimelia?” nikamuuliza nikimkazia macho, wakati huo nikaanza kuhisi mwili wangu ukiwa dhaifu zaidi. Nilihisi miguu inataka kunidondosha na macho yanapoteza uono.
Basi yule mtaalamu akaguna kwa kushusha pumzi puani alafu akafanya utaratibu wa kupakia miili ile kwenye gari maalumu kwa ajili ya kupeleka miili nje ya gereza, na mimi nikapanda humo ndani.
Gari likatembea kidogo na kukomea mahali ambapo uhakiki ulikuwa unafanyika tena. Hapo kulikuwa ni kituo chenye askari kama nane, walipanda wawili na kutazama ile miili yote, ilikuwa minne, kisha gari likakaguliwa na mimi, kama askari sasa, nikiulizwa kuhusu mrejesho.
Baada ya kila kitu kuwa sawa, akapanda askari mwingine ndani, sasa tukawa watu wanne mule, mimi, dereva, na wahusika wawili wa uzikaji, kisha gari likaruhusiwa tukaendelea na safari, ila bado atujalifikia lango kuu. Gari lilikuwa linasonga kwa taratibu kabisa, nikitamani hata nilisukume.
Yule askari aliyepanda akanisogelea karibu na kunisalimu, kisha akaketi kando kando na mimi.
Tukasonga. Tulipofika kwenye lango kuu, hatukukaa sana, likafunguliwa tukapita, hapo angalau nikapata ‘pumzi’. Nilianza kuona mpango wangu unakamilika.
Gari likaongeza mwendo na baada ya kama nusu kilometa, nikamwona askari yule aliyekuwa amekaa kando kidogo na mimi akiwa anasinzia. Kichwa chake kilikuwa kinaenda mbele na nyuma, muda mwingine akijitahidi kukaza macho pasipo mafanikio.
Baada ya mwendo mchache zaidi, nikasikia sauti ikitoka kwenye ‘radio call’ ya askari huyo. Sauti hiyo ilivuma kwa muda kidogo lakini askari yule akiwa hana habari, alikuwa anapambana na usingizi. Nilitamani sana niisikie sauti hiyo lakini ilikuwa mbali na mimi. Nilitaka nijue ilikuwa inahusu nini.
Mara punde nikamwona askari huyo akikodoa! Sikujua nini kilimstusha. Upesi akadaka radio call yake na kuwasiliana, alafu punde kidogo akaamuru gari lisimame! Akasimama akiendelea kuwasiliana na radio call yake hiyo.
Kama sekunde nne tu, nikamsikia akipaza sauti,
“Rudisha gari gerezani!”
ENDELEA
Nikapatwa na mshtuko haswa kusikia kauli hiyo, yani turudi tena kule! Haiwezekani.
Katika namna ya upesi kabisa, nikafanya jitihada za kumkwatua askari huyo miguu, puh! Akadondoka chini na kujigonga kwenye kingo ya kiti, papo hapo alikuwa amepoteza fahamu. Alikuwa anavuja damu akiwa ameachama mdomo wake kama shimo.
Basi upesi nikadaka silaha yake na kuwaweka wote waliokuwemo mule ndani chini ya ulinzi. Wakanyoosha mikono kutii. Nikiwa nimeweka sura ya kazi, nikawaamuru wote washuke chini, wakatii.
Waliposhuka nikadaka usukani na kuendesha gari hilo kwa takribani kilomita moja kabla sijashuka na kudaka gari jingine kwa ajili ya usalama. Wakati huo nilikuwa tayari nimebadili nguo zangu kwa kuvaa nguo fulani ambazo zilikuwamo ndani ya gari.
Baada ya hapo nikapotelea kabisa ndani ndani mpaka pale nilipojihisi kuwa nipo salama. Kwa macho yangu nikashuhudia habari zikitangazwa kwenye runinga na hata kuzisikia redioni juu ya utorokaji wangu gerezani huku donge nono la zawadi likiwa nimetangazwa kwa mtu yeyote yule atakayetoa taarifa juu ya upatikanaji wangu.
Nikahakikisha naficha uso wangu ipasavyo kwa kutumia sweta lenye kofia na kisha nikashika barabara kwenda kwenye anwani ya makazi ya Jack Pyong, huko kulikuwa karibu kupafikia. Ilikuwa ni safari ya masaa yasiyozidi matatu tokea nilipokimbilia.
Nikiwa kwenye gari sasa, nimeegemeza kichwa changu kwenye kioo, nikawa natazama mikono tangu nikijaribu kuwaza kichwani. Nilikuwa nimetingwa haswa, lakini pia hali yangu ya kiafya haikuwa njema. Sikuwa poa kama ninavyojifahamu.
Nilitamani kwenda hospitali lakini sikuwa naweza. Kwenda huko kungekuwa ndiyo njia ya kwanza kabisa kukamatwa, ilinibidi tu nijikaze nikitumaini nitakapofika nyumbani kwa Jack Pyong basi matatizo yangu yatatafutiwa ufumbuzi kwa namna moja.
Sikuwa najua nitakachokikuta huko wala ya mbeleni.
**
“Kila kitu kipo tayari?” aliuliza Jack Pyong akimtazama Violette. Mwanamke huyo aliyekuwa amevalia gauni fupi linalokomea kwenye magoti yake, alikuwa akijikwatua uso wake mbele ya kioo.
“Bado kidogo, mpenzi. Ningoje!” alisema akijipakaa poda.
“Muda wote huo!” Jack akalalama na kisha akatazama saa yake ya mkononi. “Tumeshachelewa, ujue!”
“Namalizia, mpenzi!” akasema Vio na kisha akafumba mdomo wake akiupakaa lipstick. Basi Jack kujiepusha na kukwazika akatoka hapo chumbani na kwenda kuketi sebuleni, alikuwa yu tayari kabisa kwa ajili ya safari, amevalia suti nyeusi na kiatu chake cha ngozi kinang’aa.
Nywele zake zameta na ananukia marashi mazuri. Amekuwa akimngojea Vio kwa takribani lisaa sasa.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Akasonya na kutazama saa yake kwa mara nyingine. Akiwa anaelekea kuboreka kwa kukaa kwenye kiti kwa muda, akanyanyuka na kuendea jokofu apate kutoa kinywaji.
Akatoa chupa ya juisi na kunywa mafundo mawili akiegemea jokofu. Lakini akiwa hapo ndipo akasikia sauti ya kitu ambacho kilimfanya ajongee dirisha kutazama. Ni kama vile kishindo cha mtu. Hakuwa na uhakika.
Alitazama nje pasipo kuona jambo, lakini punde akasikia tena kishindo cha mtu, mara hii alikuwa na uhakika zaidi. Ni kidogo tu ndipo akaona mtu akizama ndani ya eneo lake kwa kuruka ukuta!
Alikuwa ni mtu aliyevalia ngo nyeusi na kuficha uso wake kwa barakoa rangi ya pinki. Mkononi mwake alikuwa amebebelea bunduki!
Jack akamezwa na hofu! Upesi akakimbia kumfuata Vio apate kumtaarifu kuhusu uvamizi. Alipofika, akiwa ametumbua macho na kukunja ndita, akapaza sauti: “Vio jifiche upesi!”
Vio akamtazama kwa mshangao, hakuwa amemaliza.
“Jifiche!” Jack akaropoka. “Kuna majambazi!”
Pupa zikamjaa Violette. Hakuna alilofanya likaeleweka. Alisimama akiwa ametumbua macho na kukung’uta viganja vyake, aliachama mdomo kwa hofu na akatumbua macho kwa woga.
“Jack, kweli? Jack!”
Upesi Jack akamdaka na kumkimbizia kabatini, hakuwa anatosha, upesi tena akamlaza na kumtaka aingie chini ya kitanda.
“Kakaa humo na unyamaze!” Jack akamsihi alafu akatoka kwenda kuifuata silaha yake kabatini. Alitazama kuitafuta lakini hakuiona.
“Shit!” akalaani. “Imeenda wapi?” akajiuliza akiwa anatota jasho. Akainamisha mgongo kutazama chini ya kabati lakini napo hola, hakukuwa na kitu.
“Mungu wangu!”
Mara akasikia mlango ukibamizwa na watu wakizama ndani.
“Nimekwisha leo!” akajikuta akisema ingali akitetemeka vibaya mno, hakujua cha kufanya, alijikuta akisimama na kungoja. Punde majambazi wakawa wamezama ndani na kumfikia, wakamwamuru apige magoti na aseme kile wanachokitaka kama anataka abakiwe na uhai wake.
Mmoja alikuwa amevalia barakoa nyeusi na mwingine akiwa amevalia barakoa nyeusi.
“Hatupo hapa kupoteza muda na wewe!” alisema yule mwenye barakoa ya pinki. Alikuwa ni mwanamke kwa sauti yake. “Tupo hapa utueleza Marshall yupo wapi?”
Swali hilo likamshangaza Jack. Kwa mara ya kwanza alidhani amesikia vibaya ikampasa aulize.
“Umetusikia vema,” akasema yule jambazi wa kike, “Tunataka kujua Marshall yupo wapi? Sema haraka kabla hatujakumiminia risasi kutoboa kichwa chako!”
Basi Jack akasema hafahamu lolote kuhusiana na Marshall. Kitu pekee anachojua ni kwamba mwanaume huyo amekamatwa na anatumikia kifungo chake jela.
“Unatutania, sio?” akafoka jambazi mwenye barakoa nyeusi, yeye alikuwa ni mwanaume. “Unatufanya sisi ni wehu. Marshall ametoroka gerezani, tuambie ameenda wapi? - nakuhesabia mpaka tano!”
Jack akawatazama wale majambazi akiwa ametabasamu,
“Ametoroka kweli? - ametoroka?”
Na nusu akaangua kicheko. “Nilijua tu Marshall hatokufa kizembe namna hiyo!”
Alikuwa kama mtu aliyerukwa na akili. Majambazi walitazamana kwa mshangao kisha yule wa kike akamkita na kitako cha bunduki kichwani, akalalama kwa maumivu!
“We mpumbavu hatupo hapa kwa ajili ya matani! Moja, tueleze alipo, mbili, tatu! Nne…”
“Sijui jamani!” Jack akapaza sauti akijicha kichwa chake kwa mikono. “Nawaapia sijui alipo. Kama ningekuwa najua, ningekuwa wa kwanza kwenda kuonana naye… nisingalikuwapo hapa!”
“Tano!” akasema yule jambazi mwanaume, akataka kubonyeza kitufe cha kutolea risasi lakini ghafla akajizuiza baada ya kusikia sauti ya kike ikisema, “Ngoja! Usimfyatulie risasi tafadhali!”
Vio akatoka uvunguni na kunyoosha mikono yake juu. Macho yake yalikuwa yanatiririsha machozi, akitazama chini.
“Hatujui Marshall alipo. Kama tungelikuwa tunajua tungewaambia.”
Jambazi yule wa kike akamdaka Vio na kumburuza chini, akamnyooshea tundu la bunduki akimtazama Jack. “Kama usiposema, nitamuua huyu malaya itakapofika tatu. Moja! …”
“Sijui!” Jack akalia. “Tafadhali, usimuue!”
“Mbili …” jambazi akaendelea kuhesabu. “Tatu!”
Mara sauti ya bunduki ikavuma, paaah! Naye Jack akapasa sauti kulalama, lakini ajabu akamwona yule jambazi wa kike akidondoka. Hajakaa vema, sauti nyingine ya bunduki ikatwaa hewa na mara yule jambazi wa kiume akadondoka pia.
Wote walikuwa wamelala chini wakiwa wanavuja damu.
Jack alipotazama risasi zimetokea wapi, akamwona Marshall akiwa amesimama mbele kidogo ya mlango. Mlango wa chumba chake ulikuwa unatazama na wa ule sebuleni.
“Marshall!” Jack akajikuta akipaza, ila punde akamwona Marshall akidondoka chini kama mzigo tih!
Haraka akamkimbilia na kumtazama. Alikuwa amefumba macho yake lakini bado akiwa na ufahamu. Alikuwa akihema lakini amechoka mno.
Jack akamlaza kitandani na kumpatia huduma ya kwanza. Marshall aliporudi kwenye hali yake, yaani angalau kwa unafuu, Jack akamuuliza nini anajisikia, Marshall akasema ya kwamba kichwa kinamuuma na mwili hauna nguvu.
“Inabidi upumzike, Tony!” akasema Jack. Kwa mara ya kwanza Marshall akasikia akiitwa jina lake tangu muda mrefu. Tony. Ni Jack ndiye mtu pekee ambaye amezoea kumuita vivyo.
Akatabasamu akimtazama Jack, rafiki yake wa kale. Hakutarajia kama atamwona. Ilikuwa ni kama miujiza. Japo hakuwa anajisikia vema, ndani ya moyo wake yalikuwa vema.
“Nimefurahi sana kukuona, Jack,” akasema kwa sauti ya chini. “Nilipokuwa ndani nilikuwa nahofu sana nani ataweza kukaa na wewe. Uchizi wako hauna mithili.”
Jack akatabasamu, “Kwahiyo unataka kusema Vio hatoweza kukaa nami ama?” akauliza akimtazama mpenzi wake aliyetabasamu kwa upana. Naye Marshall akatabasamu, “Anakuvumilia sana. Kwakweli ukimpata mtu anayeweza kukuvumilia mshike sana Jack!”
Baada ya matani hayo yaliyochukua muda kidogo, Marshall akamtaka Jack ahame eneo hilo analoishi kwani si salama tena kwake na kwa mpenzi wake. Tayari maadui wanaomfuatilia wanajua makazi yake.
Wasipoteze muda, Jack akamkokota Marshall mpaka kwenye gari akiwa ameongozana na mpenzi wake Vio. Wakajikwea na kwenda mbali, mbali kwenye makazi mengine ambapo watakuwa salama.
“Kuna mtu aliyekutafuta Jack? - mwanamke yoyote?” Marshall akapaza sauti kuuliza. Alikuwa amejilaza kwenye viti vya nyuma ingali Jack na Vio wakiwa wamekaa viti vya mbele. Ingali anauliza macho yake alikuwa ameyafumba na mikono yake ameilaza kifuani.
“Mwanamke?” Jack akauliza, kabla hajapokea majibu, akaema, “Marshall ni leo tu umetoka jela na unataka kuniharibia mahusiano yangu. Nitafutane na mwanamke gani mwingine zaidi ya mwenza wangu Vio?”
“Jack nipo serious unajua!” Marshall akajikakamua kuuliza. Japo alijitutumua, sauti haukutoka kabisa, ni kama vile alinong’oneza.
“Hamna mwanamke aliyenitafuta Tony,” akasema Jack. “Labda kama unaongelea Jolene, yule mwanamke mwenye miwani mikubwa kule ofisini. Miwani kama kiota!”
Kidogo Marshall akazama kwenye dimbwi la mawazo. Ina maana Katie hakumtafuta Jack kama vile alivyomwambia? Kwanini hakufanya vivyo? Je atakuwa salama tena wakati huu akiwa ametoroka gerezani?
Alitolewa kwenye dimbwi la mawazo punde Jack alipokanyaga breki kwa upesi. Alitazama na kuuliza nini tatizo. Aliporusha macho akamwona bibi moja akiwa anavuka barabara taratibu.
“Hawa wazee wana matatizo!” Jack akalaani. “Hata hatazami kama gari linakuja ama lah, anakatiza tu!” baada ya bibi huyo kuvuka na kwenda zake, Jack akakanyaga mafuta na safari ikaendelea kama ada.
Baada ya lisaa limoja wakafika kwenye makazi pweke, hapo Jack akazama ndani na kurejeshea geti alafu akamwingiza ndani mgeni wake.
“Nadhani hapa tutakuwa salama,” alisema Jack akiwa anarusha macho yake kukagua sebule, kisha akatabasamu.
“Jack, hii nyumba umeipata lini?” Marshall akauliza naye akiwa anajitahidi kuangaza. Hakuwa anaona vema ila angalau, hakuwa sawa na chongo.
“Kwenye mambo yangu ya hapa na pale,” Jack akajibu na kucheka. Akamweleza rafiki yake kuwa ni muda mrefu sana umepita akiwa mbali kabisa na Marekani hivyo asingeweza kufahamu yale yaliyokuwa yanatukia.
“Usijali, Tony. Tutaongea zaidi,” akahitimisha Jack. “Tuna mengi sana ya kujadili. Pumzika kwanza.”
**
Yalikuwa ni majira ya saa tatu na nusu usiku. Nyuma ya nyumba ya Jack kulikuwa na bwawa la kuogelea na kando yake kukiwa na vitanda viwili vya kujilazia kulowana. Kwenye kivutanda hivyo ndipo Jack alikuwa amejilaza yeye pamoja na rafiki yake, Marshall.
Hali ya hewa ilikuwa tulivu kabisa, na inaunga mkono zoezi la kuogelea.
Hapo wakiwa wametulia kwa ukimya, wakapata kuteta mambo mengi sana. Mambo ambayo Marshall hakuwa anayafahamu.
“Tony, nimepitia matatizo sana hapa karibuni. Hali haikuwa nzuri kabisa kazini. Huwezi amini niliwekwa chini ya uchunguzi mkali kwasababu ya ukaribu wangu nawe. Kama haitoshi niliwajibishwa kwa njia kadhaa wakiwa wanaamini nitakuwa najua yale uliyoyafanya.
Ilikuwa ni matatizo juu ya matatizo. Hata hapa ninapooongea nawe, nimesimamishwa kazi. Nitapumzika kwa muda usiojulikana ingali nikiwa nachunguzwa pia ni kwa namna gani nitakuwa nahusika na yale ambayo umetuhumiwa kuyatenda.”
Jack aliposema hayo, akaweka kwanza kituo. Uso wake ulikuwa ‘serious’ tofauti kabisa na awavyo kila uchwao. Alikuwa anamtazama Vio akiwa anaogelea lakini akiwa mbali kimawazo.
Akaendelea kumweleza Marshall kuwa ilimpasa asimamishe mipango yake yote ya kufunga ndoa na Vio, moja kwasababu rafiki yake kipenzi alikuwa mbali lakini pia alikuwa akiandamwa na matatizo.
Akaenda mbele zaidi kwa kumweleza Marshall ni namna gani kila mtu aliaminishwa kuwa yeye ni gaidi, yupo kwenye upande wa maadui wa Marekani.
“Marshall, simu yako ambayo uliipoteza Hong Kong bado ipo hewani. Na ndiyo hiyo ambayo ilifuatiliwa na kupatikana na sauti lakini pia jumbe mbalimbali za wewe ukiwa unaongelea swala la kupotea kwa Raisi.”
Kama haitoshi Jack akamwambia Marshall ni namna gani picha zake akiwa Ujerumani zilivyodakwa na CIA na kutumiwa kama kielelezo cha kumfanya awe na shutuma ya kujibu.
Kwa ushahidi Jack Pyong akatoa simu yake na kumwonyesha picha hizo Marshall.
Marshall alipozitazama akaduwaa kujiona, lakini akaduwaa zaidi kuona zilikuwa ni picha za yeye akiwa anapambana na maadui, wa kwanza ni wale maadui ambao alikutana nao mwanzoni kabisa baada ya yeye kufika Berlin, Ujerumani, pili, ni wanaume aliokuwa anapambana nao ingali anafanya jitihada za kumwokoa Britney na Henessy toka kwenye mikono ya watekaji!
Na tatu, akiwa na bosi wake wa klabu ya usiku.
Kilichomshangaza si picha bali namna gani alipigwa? Ina maana akiwa anafanya yote hayo kuna mtu alikuwa akimpiga picha? Iliwezekanaje? Ina maana alikuwa anafuatiliwa tokea alipokanyaga Ujerumani? Na dhumuni kubwa likiwa ni kum - ‘frame’, sio?
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
“Wote hawa uliokuwa unapambana nao ni maajenti wa CIA,” alisema Jack.
Hapo ndipo Marshall akaeleza kuwa yale yote aliyoenda kuyafanya huko Ujerumani yalikuwa yameratibiwa. Yale yote aliyokuwa anayafanya huko yalipangwa ayafanye kutimiza haja za watu waliokuwa nyuma ya mgongo wake kwa muda wote huo.
Akashusha pumzi ndefu.
Kwanini imetumika njia kubwa hivyo kumfanya awe mbuzi wa kafara?
Ilikuwa wazi kuna watu wamempoteza Raisi. Wamefanya hivyo kwasababu zao binafsi na kisha kulifutilia mbali wakamtumia Marshall.
Ni wakina nani hao? Na wamefanya hivyo kwasababu gani?
Raisi amepotea kweli? Ameuawa ama amefichwa?
Kichwa cha Marshall kiliuma kwa mawazo. Alimweleza Jack yale yote aliyoyapitia huko Ujerumani na Jack pasipo kusita akasadiki kila alichosikia. Ni yeye ndiye alikuwa anaamini, ndani yake kabisa, kuwa Marshall hajafanya kile alichokuwa anashutumiwa.
Basi baadada ya majadiliano hayo, Marshall akamweleza Jack juu ya haja yake, kwa mkono wake anataka kuwasaka watu wanaohusika, mmoja baada ya mwingine, na kuwatia adabu.
Hatajali itachukua muda gani, ila atawakamata asibaki hata mmoja.
“Kesho tutaenda kuonana na Miss Danielle,” akasema akiwa anakotoa vidole vyake. Alikuwa amejawa na fikira lakini pia hasira.
****
Basi usiku huu ukaenda kwa mang’amung’amu sana. Kila alipokuwa akijilaza kuutafuta usingizi, haukuja, mwishowe akaamua kutoka kitandani na kujongea dirisha, akakamata nondo na kutazama nje akiwaza.
Alikuwa amebebelea uchungu usiomithilika ndani yake. Alikuwa anahisi kifua chake kizito, kizito kwa kinyongo, alikuwa anahisi kichwa chake kizito, kizito kwa mawazo. Kwa mara hiyo alitamani angepata kidongea ama dawa yoyote ya kumfanya alale.
Mwili ulikuwa mchovu lakini kila akifumba macho usingizi hauji! Ni kama alikuwa amepewa laana.
Akiwa hapo dirishani anaendelea kuwaza na kuwazua, akasikia sauti ya kike. Hakujua sauti hiyo imetokea wapi lakini alikuwa ana uhakika inatoka nje.
Alikuwa anaota ama? Ni maruweruwe ya kukosa usingizi ama? Alijikuta akijiuliza, lakini alipotega sikio zaidi, akabaini si kwamba alikuwa amekosea, ni kweli kuna sauti ilikuwa inasikika kwa nje.
Basi akarusha macho yake kuangaza huku na kule, ni nani huyo alikuwa akiongea muda huo? Saa ya ukutani ilikuwa inasema saa nane na robo!
Alipoangaza zaidi, kwa mbali, kama macho yake hayakuwa yanamdanganya, akamwona mtu. Alikuwa amewekelea simu yake sikioni akiongea, alikuwa kwenye giza hivyo ngumu kutambulika.
Punde mtu huyo akamaliza kuongea na simu yake na kisha akapiga hatua kurudi ndani, hapo ndipo Marshall akapata uhakika kuwa kulikuwa na mtu, na mtu huyo alikuwa ni Vio, mpenzi wake Jack!
Mwanamke huyo alikuwa amevalia gauni jeupe la kulalia, na akiwa anajirejesha ndani alikuwa akiminya simu yake kubwa. Marshall akamtazama mpaka alipoishilia.
Akabakiwa na maswali, kwanini mwanamke yule alikuwa ameenda kuongelea simu yake kando? Anamficha nini Jack?
Badala ya kupunuguza mawazo, akajikuta akiyaongea maradufu. Sasa hakuwa na uhakika atalala muda gani.
**
Alipoufikia mlango, Vio akapunguza ukali wa vishindo vyake vya miguu, akanyata taratibu na kutengua kitasa cha mlango.
Kabla hajazama akarrusha macho yake kutazama hali ya Jack, alah mwanaume huyo alikuwa anakoroma, basi akazama ndani na kuurejeshea mlango taratibu. Sasa akajihisi yu salama, akashusha pumzi ndefu na kwenda zake bafuni.
Punde akatoka huko na kujirejesha kitandani, akajilaza kandokando ya Jack, lakini asichukuliwe na usingizi upesi, akatazama dari kwa mawazo.
Muda si mrefu simu yake ikamulika, haraka akaitazama na kuikwapua, na kabla hajafanya kitu, akamtazama kwanza Jack, bado mwanaume huyo alikuwa amelowea usingizini.
Basi akafungua simu yake kwa kutumia alama ya kidole, akatazama na kukuta ujumbe, mtu aliyemtumia ujumbe huo hakuwa ametunzwa kwa jina bali namba tu.
Ujumbe ulisomeka, ‘Usiku mwema, kipenzi. Natazamia mengi.’
Vio akaufuta ujumbe huo upesi alafu akazima simu na kufumba macho yake.
**
EDGAR HOOVER, Makao makuu ya FBI.
“Umeshafanya ile kazi?” mwanamke mrefu mwembamba aliinama kidogo apate kuongea na Miss Danielle. Mwaname huyo alikuwa ameseti vyema nywele zake na mwili wake ukiwa umekaa vema ndani ya suti yake nyeusi.
Macho yake makali yalimkodolea Danielle, punde Danielle akanyoosha mkono wake kwenye meza yake na kumpatia mwanamke huyo faili fulani.
“Calm down, miss Danielle,” akasema mwanamke yule mwembamba, acha tumwite Beatha. Kwa sas alipoozesha macho yake akiwa anamtazama Danielle kwa namna ya kuguswa.
“Beatha, nilishakwambia nipo sawa,” akasema Danielle, “Waweza kunielewa hata mara moja?”
“Lakini hauonekani kama upo sawa!” Beatha akasisitiza akiwa amekunja ndita.
“Nipo sawa,” Danielle akasema akimtazama Beatha usoni. “Nipo sawa sawia.”
Basi Beatha akamtazama Danielle kwa muda kidogo kisha akasema, “Najua hili swala ni kubwa sana kwako. Pengine mabega yako yameelemewa, lakini litapita tu. Usijali.” aliposema hivyo akaweka mkono wake begani mwa Danielle na kumpatipati,
“Si kila mara aliye mwema hushinda, na si kila mara nyota hung’aa angani,” Beatha akasema na kisha kwenda zake. Danielle akabaki akiwa mpweke ametingwa na kazi.
Mwanamke huyu mrembo alikuwa ameketi nyuma ya meza iliyokaliwa na tarakilishi lakini pia faili kadhaa. Pembeni yake kulikuwa na kuta zenye kubebelea vipande vingi vya magazeti na ramani. Nyuma yake kulikuwa na picha kubwa ya Raisi wa nchi.
Ofisi yake ilikuwa imetulia lakini kichwani mwake kukiwa na fujo. Tangu kesi ya kupotea kwa Raisi imalizike hakuwa na furaha kabisa. Alijiona amefeli, alijiona amepwaya.
Ingawa kesi ilikua imefutwa, bado kichwani mwake ilikuwa inaendelea na kumtafuna vilevile.
Alivuta kikombe chake cha kahawa akakiweka kinywani, akanywa mafundo mawili alafu akakirejesha kikombe hicho mezani na kutazama tarakilishi yake. Kidogo simu yake ikaita, alipotazama akaona jina ‘Adv. Marble’.
Akapokea simu na kuiweka sikioni.
“Tunaifuta kesi, sio?” aliuliza mtu kwenye simu, yaani Adv. Marble.
“Ndio, futa na ikiwezekana uache kun’tafuta kabisa, sawa?” alisema Miss Danielle kisha akakata simu, kidogo tena, simu ikaita. Miss Danielle alipotazama akaliona jina lilelile lililotoka kumpigia hapo punde, akasonya, akapokea na kuweka sikioni, “unasemaje?http://pseudepigraphas.blogspot.com/
“Vipi kuhusu malipo yangu?” aliuliza Marble.
“Malipo gani?” Danielle akauliza akikunja uso. “Si nimeshakupa pesa yako yote, ama?”
“Hapana,” Marble akajibu na kuongezea, “Bado ya usiri. Unakumbuka tulivyokubaliana?”
Basi Miss Danielle kuondoa zogo, maana hakuwa kwenye ‘mood’ hiyo, akamwambia bwana Marble kwamba atamtumia pesa yake hiyo jioni. Baada ya maongezi hayo, akakata simu na kuizima kabisa.
Bwana Marble ni nani? - ndugu huyu, mwanaume mrefu mwenye nywele ‘blonde’ na macho yanayofunikwa na vioo, ni wakili ambaye alikuwa akiisimamia kesi ya Marshall ingali yu gerezani baada ya kuhukumiwa kifo.
Bwana huyu alikutana na Miss Danielle siku ambayo mwanamke huyo alienda kukutana na Marshall gerezani, na kwa makubaliano, bwana huyu alipeleka kesi mahakamani kupinga hukumu ya Marshall kwa lengo moja tu, la kusogeza muda wa Marshall kuwapo gerezani.
Kwasababu basi kesi ilikuwa inanguruma mahakamani, ndiyo maana siku ya kunyongwa kwa Marshall ikawa inasogezwa mbele na mbele kuitikia rufaa.
Lakini kwenye zoezi hilo, bwana Marble alikubaliana na Miss Danielle kwamba mlolongo wote huo wa kesi utakuwa wa siri, Miss Danielle hakuwa anataka kujulikana kama ni yeye ndiye anamlipa wakili huyo kwasababu za kiusalama. Endapo ingebainika basi ingemletea matatizo.
Basi kwasababu hiyo, Marshall akapata kutekeleza haja yake ya kutoroka, na sasa, Marble akiwa anatumia fursa, anataka pesa zaidi.
Miss Danielle akashusha pumzi ndefu akikuna kichwa chake kilichojaa nywele. Hakuwa na cha kufanya isipokuwa kuitikia hitaji la bwana Marble. Na hivi ambavyo Marshall ametoroka gerezani, akibainika itakuwa shida sana.
**
Saa mbili usiku …
Chumba kilikuwa kina giza nene, lakini kiza hakikudumu, mlango ukafunguliwa na mara taa ikawashwa tap! Mwanga ukatamalaki, alikuwa ni Miss Danielle. Mkononi alikuwa amebebelea koti lake la suti akiburuza miguu.
Akarusha macho yake vitini, akamwona Marshall na Jack. Walikuwa wameketi hapo isijulikane ni muda gani waliingia.
“Marshall!” Danielle akatokwa na maneno.
Aliketi pamoja na wanaume hao na kuanza kuteta juu ya hatma yao, kwanza Marshall alimshukuru Danielle kwa mchango wake na kisha akamweleza yale yote aliyoyapitia mpaka muda ule, Danielle akaachama mdomo kwa mshangao.
Akampa pole sana Marshall lakini pia hongera kwani amefanya kazi kubwa kutetea haki yake.
“Nilijua haukuwa na hatia Marshall,” alisema akitikisa kichwa. “Kesi yetu ilikuwa ni kubwa mno na kwa namna fulani haikuwa ipo tayari kumalizika. Ilikuwa ni fumbo, tena fumbo gumu ambalo jibu limefichwa kwa makusudi.”
Marshall akashusha pumzi ndefu kisha akatazama vidole vyake, hakujua ni kwasababu gani, ila vilikuwa vikitetemeka. Alikunja ngumi akamtazama Danielle, “Inabidi nipiganie haki yangu, hata kama ni kwa kumwaga damu.” kisha akaita, “Danielle,” na kuongezea, “Najua utanisaidia kwenye hili, sio?”
Danielle akatikisa kichwa. “Pasipo shaka, Marshall, tutakuwa bega kwa bega.” lakini akamwonya Marshall kuwa yampasa kuwa makini kwani watu ambao wanahangaiki kumwangusha yawezekana wapo karibu na wana hamu kubwa ya kuona anguko lake.
“Si wewe tu, kwakuwa tupo pamoja kwenye hili, yatupasa wote tuwe makini.”
“Bila shaka,” Marshall akaitikia ujumbe huo kisha akauliza, “Hauna lolote la kuniambia Danielle? - hususani kwenye hii kesi kikanisaidia wapi pa kuanzia?”
“Yapo mengi sana,” akasema Danielle akimtazama Marshall kwa uhakika, “Kuna mambo mengi sana lakini sitakuwa na uwezo wa kuyakumbuka yote isipokuwa yale muhimu. Punde tu kesi ilipofutwa, faili langu lilichukuliwa hivyo kuna baadhi ya taarifa nitazikosa.
Lakini si zote.”
Kauli hiyo ya mwisho ikampa faraja sana Marshall ambaye alijitengenezea vema apate kusikia.
Mosi, Danielle akasema alipata wasaa wa kuonana na mke wa Raisi lakini kwa mara moja tu, na anakumbuka mara ya kwanza kabisa alipopata fursa ya kufanya naye maongezi, hali haikuwa nzuri.
Hakuwa anataka kujibu maswali kama alivyokuwa anatakiwa, ila zaidi alisema hakuwa anayejua mengi sana kumhusu Raisi kwani kwa muda kiasi kabla ya kupotea kwake hawakuwa na mahusiano mazuri, kulikuwa na msuguano kati yao.
Akiwa anaongea, kuna muda angeng’ata meno yake na kukunja ngumi, lakini pia akitusi na kulaani. Hakukaa naye muda mrefu, mwanamke huyo akaondoka zake akiwa anamwaga machozi.
“Sijajua ana nini,” alisema Miss Danielle na kuongeza, “lakini ana kitu kifuani mwake. Kwa nilivyomtazama machoni, kuna kitu kinamkaba.”
Marshall aliyekuwa anarekodi yote hayo kwa kichwa chake, akauliza, “Unajua alipo mwanamke huyo kwa sasa?”
Danielle akabinua mdomo, “Sijui, sijamfuatilia sana hapa karibuni baada ya kesi kufutwa lakini mara ya mwisho kabisa kuwa naye kwenye mahusiano ikiwa ni muda mfupi tangu nifanye naye yale mahojiano mafupi, alikuwa ameenda nchini Morocco. Sijajua tena baada ya hapo.”
Marshall akafikiria kidogo na kusema, “Ana taasisi yake ya kusaidia watoto wasiojiweza, nadhani bado inajiendesha nchini, sio?”
“Bila shaka,” Danielle akasema akitikisa kichwa. “Ni juzi tu taasisi hiyo ilikuwa inafanya kongamano la kuhamasisha wananchi wajitolee kwenye kuwasaidia watoto yatima na wa mitaani.”
“Vema,” akasema Marshall na kuongezea, “Sasa tumepata pa kuanzia.”
“Lakini Marshall,” Danielle akatia walakini, Marshall akamtazama kwa hamu ya kuskiza.
“Kuna kitu nataka nikuambie,” alidokeza Danielle, “Ni kuhusu ile kesi yako ingali upo gerezani.”
Basi Marshall akampatia masikio yote akimtazama kwa umakini.
“Kuna shida kidogo ilitokea.”
“Shida gani hiyo?”
**
“Kwahiyo? - utaanza na lipi sasa mtaalamu?” aliuliza Jack Pyong punde baada ya kuingia na Marshall kwenye makazi yao. Makazi yalikuwa tulivu kabisa, haswa baada ya Jack kuzima gari. Kidogo Marshall akafikiria kisha akasema, “Nitajua jua litakapopambazuka.”
Akafungua mlango wa gari na kwenda zake ndani akimwacha Jack garini. Jack akakaa humo kwa kama dakika tano akitazama simu yake kabla hajaizima na kuiweka mfukoni.
“Ulikuwa unachat na nani?” mara akasikia sauti, alipotazama kando ya mlango wa gari, akamwona Vio akiwa amesimama ameshikilia kiuno. Kumbe alikuwapo hapo kwa muda na yeye hakulitambua.
“Sikuwa nachat na mtu,” akajitetea akipandisha mabega, “nilikuwa natazama tu mambo yanayoendelea mtandaoni na si vinginevyo!”
Vio akanyoosha kiganja chake kumfuata Jack, “Naomba hiyo simu nione.”
Jack akakunja uso, “Uone nini? - huniamini ama?”
“Nipe simu nione!” Vio akakazana. Uso wake ulikuwa upo ‘serious’ pasipo lepe la utani. Jack kwa kuhofia maneno mengi ambayo yatamnyima hata usingizi, akaamua kumkabidhi Vio simu hiyo na kisha akatoka kwenye gari kwenda zake ndani. Alimwacha Vio peke yake nje.
Lakini kabla hajampatia Vio simu hiyo, kwa siri, alibonyeza mara mbili kitufe fulani kilichopo kushoto mwa simu yake, na alafu kwa kukusudia ama kwa kutokukusudia akabinya na ‘button’ kubwa mbele ya simu.
Basi Vio alitia ‘password’ na kuzama ndani. Akatazama ghala la picha na kisha jumbe, lakini ndani ya muda mfupi tu, simu ikaanza kuchemka kupita kiasi. Vio alihisi kiganja chake kinaungua kana kwamba amekiweka juu ya jiko la umeme.
Kwa kupapatika, akaachia simu hiyo ikadondoka chini!
“Jaaaack!” akapaza sauti kuita akishika kiuno. “Jaaack!” akazidi kuita akielekea ndani.
Baada ya hapo makazi yakarudi kwenye ukimya wake.
**
Saa tatu asubuhi … (Tall building Law firm)
Bwana Marble alipokunywa fundo moja la kahawa, alifungua tena tarakilishi yake apate kutazama barua pepe, hakukuwa na kitu, ujumbe pekee ambao ulikuwepo juu kabisa ulikuwa ukitoka kwa mtu ambaye hakuwa anajulikana, anonymous, ukisema maneno machache, “Fanya namna tuonane.”
Ujumbe huo haukuwa umejibiwa, na bwana Marble aliutazama na kwa kuupuzia akatoka kwenye uwanja wa barua bebe mpaka kwenye mafaili yake mengine.
Macho yake yaliyokuwa yamezibwa na vioo yaliperuzi mafaili hayo kwa muda kidogo kabla hajanyanyua simu yake ya mezani na kupiga simu kadhaa.
Alipomaliza, akatazama tena na simu yake, hakukuwa na kitu. Kote kulikuwa kukavu.
Basi akakata shauri na kumpigia Miss Danielle, simu ikaita mara ya kwanza pasipo majibu. Ikaita tena kwa mara ya pili na tatu, bwana Marble akalaani akiweka simu yake mezani.
“Unajifanya mjanja sio?” akajikuta akiongea mwenyewe, akanywa fundo la kahawa kisha akasema, “Nitakuonyesha.”
Akafungua tena uwanja wake wa barua pepe na kwenda moja kwa moja kwenye ule ujumbe wa kwanza wa mtu asiyejulikana, akaufungua na kuuanza kuchapa kuujibu, ‘Tukutane wapi na ---” kabla hajaumalizia, simu yake ikaita, alikuwa ni Miss Danielle.
Akapokea na kuweka sikioni.
“Nitamtuma mtu akuletee pesa majira ya saa mbili usiku. Utanitumia ujumbe utakuwa wapi, na naomba uwapo mwenyewe,” alisema Danielle kisha akakata simu.
Bwana Marble akatabasamu kwa mbali, akafuta ujumbe aliokuwa anauandika alafu akaendelea na kazi zingine, sasa akiwa na amani kuwa pesa inaingia.
Lakini baada ya muda, tamaa ikamvaa zaidi, akiwa amekaa kwenye kiti chake anawaza, akapata wazo. Kwanini asile pesa kotekote?http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Alijikuta akitabasamu hovyo. Alijikuna kidevu chake akiendelea kuwazua. Mwishowe kweli akaingia mkenge, akarudi kwenye uwanja wake wa barua pepe na kumtumia ujumbe yule mtu asiyejulikana,
“Tukutane wapi na saa ngapi?”
**
Basi punde akapokea majibu kuwa wakutane wapi na muda gani, roho yake ikasuuzika kabisa akitabasamu kwa upana. Akatoka kwenye uwanja wa barua pepe na kuendelea na kazi yake sasa.
Ilipofika saa mbili usiku, akatafuta mahali binafsi na akaketi hapo kumngoja wakala wake aliyekuwa anamletea pesa. Alikuwa ameketi pembezoni ya ufukwe ndani ya gari yake. Kwa mbali muziki ulikuwa ukipiga kumpunguzia makali ya kungoja.
Basi baada ya muda kidogo, hakungoja sana, akaja bwana mmoja aliyegonga kioo cha mlango. Bwana huyo alikuwa amevalia jaketi la saizi ya kati, rangi nyeusi, na mkononi amebebelea mkoba, mkoba ambao una pesa.
Alipogonga mara tatu, bwana Marble akashusha kioo chake akiwa na matumaini anakutana na mgeni wake, lakini akashtuka kumwona mtu aliyevalia barako nyeusi. Mtu huyo alikuwa na mwili na anatisha.
“wewe ndiye wakala?” akauliza kwa hofu, basi mtu yuke akatikisa kichwa na kisha akaminya mlango akitaka kuzama ndani, mlango ulikuwa umefungwa, ikambidi bwana Marble atoe ‘lock’ kumruhusu bwana huyo azame ndani. Alipoingia, bwana Marble akazima taa ndani ya gari kukawa kiza.
Hakuwa anaweza kuona kitu isipokuwa macho ya bwana yule aliyesema ni wakala. Punde bwana huyo akafungua briefcase yake na kumwonyesha bwana Marble, hakuwa anaongea kitu bali akitoa tu ishara.
Bwana Marble alipoona pesa akafurahi sana. Zilikuwa zimejaa mkoba. Mate yalimtoka alipochukua bunda moja la pesa na kulitazama, loh! Ilikuwa ni pesa ya kweli, ilikuwa ni ‘madola’, basi akiwa ametabasamu kwa upana akamwambia wakala amfikishie salamu Miss Danielle kwamba mzigo wake umefika na amefurahi sana.
Pasipo kuongea jambo, wakala huyo akashuka toka kwenye gari na kuyoyomea kizani. Bwana Marble alirusha macho yake kumwangazia lakini haikupita muda akapotea kabisa.
Asijali, akawasha gari lake na kujiondokea. Alipofika nyumbani akapakua pesa hizo na kuziweka mahali salama alafu akaendelea na maisha yake ya kawaida.
Kabla hajalala, akafungua tarakilishi yake kutazama kinachoendelea. Alikuta jumbe mbili toka kwa mtu yule asiyejulikana akimpasha habari kuwa kesho yake atakuwa amebanwa majira ya mchana kwahiyo basi waonane majira ya jioni kwenye chumba namba 348, La chica Hotel.
Pasipo kufikiri mara mbili bwana Marble, akaitikia wito huo, na basi pasipo kusahau akamwambia mtu huyo, anonymous, kwamba afike na pesa kabisa kukamilisha kila kitu.
Mtu huyo, yaani anonymous, alikuwa akitaka taarifa tu toka kwa bwana Marble kwamba ni nani aliyekuwa yupo nyuma ya kesi ile ya Marshall ingali akiwa gerezani. Nani alikuwa anamlipa na yupo wapi kwa muda huo.
Pesa zilimuuza bwana, pesa zina laana, pesa hutoka kwenye kiganja cha shetani. Bwana huyo alikuwa ameahidi kutoa mara tatu ya kile kiasi cha pesa ambacho Miss Danielle alikitoa, atawezaje kukataa dili nono kama hilo?
Akiwa amejilaza kitandani, alijiweka mbali na mkewe kabisa akiwa ametekwa na mawazo matamu matamu kichwani. Alijikuta anatabasamu mwenyewe kila baada ya muda fulani. Kichwani mwake alikuwa anajenga ghorofa, alikuwa anajenga kasri na kulibomoa, alikuwa akijenga bwawa na kuogelea, alikuwa akisafiri kwenda miji mbalimbali ya kitalii.
Alisahau msemo huu, kamwe usihesabu vifaranga kabla havijatotolewa.
Muda haungoji, kama kawaida ulivyo na manwa ukapaa mpaka kufikia kesho yake ambapo jua lilichomoza na kuangaza ulimwengu. Siku hiyo Marble, kama kawaida yake, akawahi fika ofisini kwenye majira ya saa kumi na mbili.
Alikuwa amevalia suti yake nyoofu, mkononi amebebelea mkoba, mkoba wenye pesa, pesa zile alizopewa na mwanaume mwenye kuvalia barakoa nyeusi. Nani angelitambua? Alikuwa na mpango wa kupeleka pesa hizo benki pindi tu atakapopata muda wa kupumzika.
Basi akaweka mkoba wake chini ya meza na kufanya kazi yake kama kawaida, kila muda akitazama mkoba wake kama upo. Yalipofika majira ya saa sita mchana, akatoka na mkoba wake huo, mpaka benki ambapo aliweka pesa zake na kujihisi salama zaidi sasa.
Alipata chakula cha mchana na kisha akarudi kazini mpaka muda ule wa jioni kabisa alipotoka. Moja kwa moja akaenda La Chica hotel, akaketi eneo la mgahawani akingoja muda wake wa miadi uwasili.
Aliagiza chupa moja ya vodka pamoja na kilainishi chake na basi taratibu akawa anakunywa, na kwa kutokupoteza muda zaidi, akaunganisha tarakilishi yake na ‘wifi’ aendelee kufanya kazi zake.
Ulipowasili muda wa miadi, saa mbili kamili, ujumbe ukaingia kwenye simu yake, ‘Njoo chumbani.’ basi pasipo kupoteza muda akanyanyuka na kwenda huko.
Hakutoka tena akiwa hai.
**
Saa tatu usiku …
Gari jeusi liliingia kwenye eneo la maegesho ya Hoteli ya La Chica, akashuka bwana mmoja aliyevalia suti na shati nyeusi pia. Bwana huyo alikuwa ni Mmarekani mweusi mwenye makamo ya miaka arobaini na jambo, shingoni mwake alikuwa ananing’iniza ‘badge’ ya polisi, jina lake aitwa James Peak.
Alisonga kuzama ndani ya hoteli na punde akakutana na askari ambaye alimpatia mkono kisha akajitambulisha,
“Inspekta James Peak!”
Alikuwa ndiye mpelelezi aliyepewa kazi ya kufuatilia kesi hiyo. Basi akiwa anaongozana na askari akaelekea moja kwa moja mpaka kwenye chumba ambacho mauaji yalitokea, chumba namba 348, ama kwa jina jingine chumba ‘Mount Everest’.
Hapo inspekta akapata kuuona mwili wa bwana Marble ukiwa umelala kitandani umevujilia damu, shingo yake ilikuwa imekatwa, macho yake ameyakodoa.
Inspekta akautazama mwili huo na pia akakagua eneo zima ambapo tukio lilitokea kisha akauliza maswali kadhaa wale askari aliowakuta na pia wahudumu wa hoteli.
Baada ya mahojiano ya kutosha kwa takribani lisaa limoja na nusu, inspekta akawa amebaini mambo kadhaa, haswa muuaji alikuwa ni mtu mwenye barakoa nyeusi.
Ilikuwa ni ajabu kwa namna yake kwani aliyeenda mapokezi na kulipia chumba alikuwa ni mwanamke mzee mwenye miaka themanini kamili ambaye jina lake alikuwa anaitwa Laurene. Kwa mujibu wa maelezo ya wahudumu, bibi huyo aliwasili hapo hotelini kwenye majira ya asubuhi akiwa anasema amekuja hapo kama moja ya kituo chake akiwa anaelekea Texas.
Alikuwa ni mwanamke mzee lakini mwenye nguvu zake hivyo hawakuhofia sana juu ya makazi yake ya upweke hapo hotelini, lakini baada ya hapo hawakumwona tena huyo bibi na hamna ambaye alijisumbua kufuatilia.
Basi kwasababu eneo la mapokezi kulikuwapo na kamera, picha ya bibi huyo ikapatikana na akaanza kusakwa, ajabu aikuchukua muda mrefu akapatikana. Alikuwa anapatikana mtaa wa tatu tu toka pale hoteli ilipo, na bibi huyo hakuwa mtu mwenye makazi bali ombaomba tu.
Alipohojiwa na mpelelezi akabainisha kuwa alilipwa kiasi fulani cha pesa kwasababu tu ya kwenda ku ‘book’ chumba hicho, na alipofanya vivyo, akampatia funguo mtu ambaye alilimpa na akajiendea zake.
“Kama nisingefanya vivyo, si tu kwamba ningekosa pesa bali pia angeniua,” alimalizia bibi huyo akiwa ameukumbatia mkoba wake. Basi inspekta James akashusha pumzi ndefu akijilaza kwenye kiti.
“Unaweza kuniambia mwanaume huyo alikuwa anaonekanaje?” akauliza.
Bibi akaeleza kila anachokijua na inspekta akaondoka zake, alipofika ofisini akajitahisi sana kughani mhusima wa tukio hilo akijitahidi kuunganisha na matukio ya nyuma, akapata pia na wasaa wa kuongea na mke wa Bwana Marble, huko akapata machache ambayo nayo hayakumtosheleza.
Kesi ilikuwa ngumu.
Basi ilimpasa atumie muda mrefu kung’amua kwa taratibu na kwa umakini.
**
Saa nne asubuhi …
Marshall alikuwa anachezea tarakilishi akiwa eneo la kulia chakula, alikuwa ameketi mwenyewe hapo na kando yake kukiwa na kikombe chenye chai ya moto. Mwili wake alikuwa ameuvisha kaushi nyeupe na bukta tu.
Akiwa anaendelea na kazi yake, Vio akajitokeza koridoni na kumchungulia, mwanamke huyo alikuwa amevalia gauni jepesi lakini ndani akiwa amesitiri sehemu zake za siri. Alimtazama Marshall kwa muda kidogo kabla hajamjongea na kumsalimu, alikuwa anatabasamu kwa upana , macho yake yalikuwa yamechoka kiasi, alitoka kitandani muda si mrefu.
Baada ya kujuliana hali, Vio akamwomba Marshall radhi kama atamsumbua lakini alikuwa na maongezi naye machache, Marshall pasipo kusita, akamkaribisha, aliwea tarakilishi yake pembeni akimwazima Vio masikio na macho.
“Tony, najua wewe ni rafiki wa muda mrefu wa Jack, tafadhali waweza niambia mpango wake ni nini kwangu?”
Jack Pyong hakuwapo katika hayo mazingira, alitoka kidogo kwenda kufuata baadhi ya mahitaji kwa ajili ya matumizi ya ndani. Tangu aondoke ilikuwa imeshapita lisaa limoja.
“Unamaanisha nini, Vio?” Marshall akauliza.
“Ni kuhusu ndoa yetu,” akasema Vio. “Simwoni kama ana dalili yoyote! Tokea aliponiveka pete, sijajua lengo lake ni lipi?”
Marshall akatikisa kichwa chake akitabasamu kwa mbali, akamtoa hofu Vio kuwa Jack ni mwanaume wake na hana haja ya kuhofia kabisa kwani anampenda kuliko yeye adhaniavyo.
“Lakini muda unaenda sana, Tony. Ni mpaka nizeeke ama? Kuna muda ---” akashika nywele zake akiinamisha uso chini “… nawaza labda ana mipango mengine.”
Marshall akamwekea kiganja begani na kumsihi hana haja yakuhofia, kuna mambo kadhaa hayajakaa sawa kwa muda huo na basi ampatie muda.
“Mimi ni balozi wako, Vio, nitahakikisha ahadi yenu inatimia,” Marshall akamtia moyo na hatimaye mwanamke huyo akatabasamu. Punde wakasikia honi getini, Vio alipoenda kutazama akakuta ni Jack.
Mwanaume huyo akazama ndani na baada ya kusalimiana na Marshall akaelekea ndani moja kwa moja akiongozana na Vio, kwa muda Marshall akaendelea na kazi yake.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Alifanya vivyo kwa siku nzima mpaka usiku wa saa mbili ambapo alipata wasaa wa kuketi na Jack, hakuwa anapenda kumsumbua mwanaume huyo maana alikuwa akimpatia muda zaidi wa kukaa na mpenzi wake, Vio.
Walipopata wasaa huu, Marshall akapendekeza wakaketi nje pembezoni mwa bwawa la kuogelea.
“Nadhani kila kitu kipo tayari,” akasema Marshall akimtazama Jack.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment