IMEANDIKWA NA : STEVE MOLLEL
*********************************************************************************
Simulizi : Nyuma Yako
Sehemu Ya Kwanza (1)
Hongkong, China. 2018.
.
.
Jana nilikuwa ufukweni mpaka majira ya saa tisa za usiku. Nilikunywa pombe nyingi na kula pia, vyakula vya kichina nadhani wavijua, vingi vya ajabu, kama isingelikuwa ni kwa ushawishi wa rafiki yangu, Jack Pyong, haki nisingetia mdomoni chochote kile kati ya nilivyokula.
.
.
Jack Pyong, jamaa mfupi wa kichina, ni rafiki yangu kwa muda mrefu sasa, takribani miaka nane. Amekuwa ni kiongozi wangu kila nijapo China, na zaidi mshawishi wangu mkubwa wa kuja huku China kila tupatapo likizo.
.
.
Ni mwanaume mcheshi sana. Ana asili ya China ila kiuraia yeye ni Mmarekani. Na kwasababu anapenda sana kushinda akitazama tarakilishi, macho yake yamekuwa mabovu, haoni vizuri pasipo msaada wa miwani, hivyo muda mwingine huwa namuita macho manne.
.
.
Jana hiyo usiku, kama nakumbuka vema na si akili ya pombe, Jack Pyong alinitambulisha pia kwa mwanamke fulani wa kizungu mkazi wa New Zealand. Mwanamke huyo alikuwa na macho yaliyojawa na haya, nywele nyeusi ndefu na gauni lake lilikuwa jekundu lenye dotidoti zinazong'aa.
.
.http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Hivyo tu! ... ni hivyo tu ndivyo ninavyovikumbuka toka usiku wa jana, hamna kingine. Ni Jack, huyo mwanamke na kula na kunywa, basi! Mengine kichwa changu kimegoma kabisa kuyakumbuka.
.
.
Hapa niwapo kitandani, hata macho sijayafumbua, najaribu sana kukumbuka ila wapi! Nadhani sasa napaswa kuamka. Niamke na kumtafuta Jack, nadhani yeye atakuwa ana kumbukumbu nzuri kuliko mimi.
.
.
Lakini hayo ya jana ya nini? Sidhani kama yana umuhimu wowote. Nilisonya na kuminya lips, nikajigeuza upande mwingine wa kitanda na kuendelea kulala. Sikujali mwanga wa jua ulikuwa umeshaingia vya kutosha ndani ya chumba changu. Nilijisemea nipo likizo basi acha nilale mpaka usingizi ukate kabisa.
.
.
Sikujua hata nini kilikatisha usingizi wangu mpaka kuwaza yale ya jana. Nilipuuzia nikarudi kwenye jitihada zangu za kuutafuta usingizi ila punde zikakatishwa kiukatili na hodi mlangoni. Kabla huyo aliyegonga sijamsikia sauti yake, nikawa nimeshajua atakuwa ni Jack Pyong! Hakuna mtu ambaye angegonga mlango wangu kwanguvu zaidi ya mpuuzi huyu!
.
.
"Amka we zoba!" Alifoka Jack Pyong akibamiza mlango. Haki nilimchukia kwa dakika hizi. Nilijibandua kitandani, kiuzembe nikaujongea mlango na kuufungua nikiwa nimekunja ndita.
.
.
"Jack unaweza niacha nikakaa kwa amani, tafadhali?"
.
.
Alikuwa ameshika simu yake mkononi, amevalia pajama ya pinki! Hivi mwanaume unavaaje pajama ya pinki? Nikiwa namshangaa, kabla sijasema kitu, akan'tolea macho yake akinionyeshea kioo cha simu, "hivi we lofa, hujaona calls za general?"
.
.
"General? ... unamanisha inspector general?" Nikababaika. Hapa kidogo mawazo yangu yakatoka kwenye pajama ya Jack Pyong na macho yakakauka usingizi.
.
.
"Ndio, general!" Jack Pyong akanijibu akizama ndani. Akashusha pumzi ndefu akiketi kitandani, "Amenipigia mara nane! Mara nane, Tony," alisema huku mimi nikifunguafungua mashuka kutafuta simu yangu. "Nilivyopokea tu, kitu cha kwanza kuniuliza yu kwapi Marshall?"
.
.
"Ukamjibuje?" Hapa nikauliza huku nikiendelea na msako wangu. Kusema ukweli sikuwa najua wapi niliweka simu yangu. Nilikuwa natafuta hapa kitandani ila sina uhakika. Pombe ya jana ilikuwa imenivuruga akili. Nilikuwa natafuta huku kichwa kikiniwaka, nitakuwa nimeitupia wapi?
.
.
"Nikamjibu haupo karibu na mimi," akanguruma Jack Pyong, "akaniambia nikutafute haraka iwezekanavyo!"
Kumbe ndo' maana ulikuwa umevaa pajama ya kike? Nikajisemea mwenyewe kifuani huku nikiendelea kutafuta. Nikamaliza msako pasipo kuona.
.
.
"Jack, haukuona simu yangu?" Nikamuuliza nikiwa nimeshika kiuno, macho yanatazama huku na kule kusaka.
.
.
Akan'tazama,
.http://pseudepigraphas.blogspot.com/
.
"Simu yako mimi natolea wapi? ... Tony, au ulimhonga yule mwanamke?"
.
.
"Mwanamke yupi?"
.
.
"Si yule ... yulee ..."
.
.
"Unamaanisha yule m-new Zealand?"
.
.
"Hahah nilitaka nikuone tu, kumbe unamkumbuka enh?"
.
.
"Jack, huu si muda wa masikhara. Mbona mimi sikuhangaika na hiyo pajama yako ya kike?" Hapa Jack Pyong akajitazama kisha akaniangalia kwa hasira.
.
.
"Sioni simu yangu, Jack. Nisaidie kutafuta."
.
.
"Mie najua ilipo? ... sikia, Tony, chukua simu yangu uongee naye, acha kun'potezea muda."
.
.
Nikachukua simu hiyo na kuweka namba za simu, nilikuwa nimezihifadhi kichwani namba za General, nikapiga na kuweka simu sikioni.
"Tony, umefunguaje simu yangu?" Jack Pyong akaniuliza akininyooshea kidole. "Umejuaje password yangu? We mjinga, umejuaje password yangu?"
.
.
Sikumjibu, punde General akapokea.
.
.
"Mkuu, unaongea na Anthony Marshall hapa."
.
.
"Marshall," General akaita na kusema, "nataka ufike ofisini haraka iwezekanavyo!"
.
.
"Sawa."
.
.
Akarudia tena, "namaanisha haraka iwezekanavyo!" Kisha akakata simu. Nikamtazama Jack Pyong na kumuuliza, "Umesikia General alichosema?"
.
.
"Nitasikiaje na wewe ndo' ulikuwa unaongea naye?" Jack akateta akinipokonya simu yake.
.
.
**
.
.
Kabla sijaendelea nadhani kuna haja ya kujitambulisha. Kwa jina, nadhani hilo tayari ushalijua, acha niachane nalo. 'Anyway', naitwa Anthony Marshall, ndilo jina langu rasmi. Jack hufupisha kuniita Tony, ila kazini najulikana zaidi kwa jina la Marshall. Mimi ni mkazi wa New York, Marekani. Ni ajenti wa shirika la upelelezi la Marekani, CIA (Central Intelligence Agency).
.
.
Sina mke wala mtoto, wala mchumba. Ndio. Na si kwamba umri haujafikia, hapana. Nina miaka thelathini na tano hivi sasa. Pengine sijapata mwanamke sahihi, au ni kazi zinanibana sana. Ila hiyo sababu ya kwanza ndiyo yenye mantiki zaidi.
.
.
Kwa upande wa kazi, sasa ni takribani miaka nane tangu niwe katika shirika la CIA, nikihusika zaidi na kategoria jenzi ya watu waliopotea na kutekwa.
.
.
Mpaka sasa, kwa mkono wangu, nimeshasaidia uokozi wa wamarekani kumi na moja waliopotea na watano waliotekwa nchi mbalimbali haswa Somalia na uarabuni. Nimekwepa risasi zisizohesabika na kupata jeraha karibia kwenye kila sehemu ya mwili wangu.
.
.
Sina haja ya kukwambia nimepitia magumu kiasi gani. Hatari kiasi gani. Bila shaka mwajua ajenti wa taasisi ya siri ya upelelezi anayoweza kukumbana nayo anapokuwa kazini. Lakini ajabu ni kwamba nimekuwa nikiyafurahia hayo. Napenda kazi yangu. Napenda ninachokifanya.
.
.
Tatizo ni kwamba, nakaa muda mwingi sana mbali na nyumbani. Kuna muda mpaka naweza jisahau kama kwangu ni New York! Kukaa miaka mitano, mitatu, miwili au hata kumi ukiwa nchi ya ugenini ni jambo la kawaida kwa ajenti wa CIA. Kukutana na watu wageni machoni, kuzungumza lugha za kigeni kama mzawa, kubanwa kiuno na bunduki, ni mambo ya kila siku hayo, si ya kushangaza tena.
.
.
Kazi yangu kama ajenti, pasipo kujali ni wapi natumwa, ni kukusanya taarifa nyeti na muhimu kisha kuzituma nyumbani kwa ajili ya hatua zaidi. Na pale panapohitajika, kujiingiza kwenye kombati kwa ajili ya jambo fulani, haswa kujiokoa pumzi yako na wale ambao unawalinda.
.
.
Sababu hiyo basi, natakiwa kuwa mkufunzi wa mapambano pasi na silaha na nikiwa na silaha pia. Lakini zaidi, kuwa mwepesi mno kwenye kuchambua hali na kufanya maamuzi yenye tija. Ninaposema mwepesi mno, namaanisha kweli hivyo. Mimi na Jack Pyong, huwa tunasema kabla risasi haijakufikia, inabidi uwe umeshaamua cha kufanya.
.
.
Hivi hilo litawezekanaje? Kuna muda tunajazana ujinga sana na Jack! Ila tu ni kuonyesha namna gani ambavyo mtu inabidi uwe mwerevu na mwenye akili nyepesi sana. Na hivyo basi ndo' maana CIA huwa inaweka madaraja na kuwa wachaguzi sana kwa watu wanaowaajiri.
.
.
Wakikagua kuanzia GPA ya mtu awapo kozi, lakini pia namna anavyojieleza, kuchambua na kuhitimisha mijadala yenye mikanganyiko ndani ya muda mfupi. Mtu mwenye 'sense' zaidi ya tano za binadamu. Zaidi ya hapo, akiwa tena mwenye ujuzi wa lugha nyingi, haswa Kiarabu, Dari, kikorea, kituruki, kichina, kisomali, kiindonesia na kadhalika.
.
.
Kwa upande wa Jack Pyong, aaaahmmm, sijui kwanini walimchukua kwakweli. Hajui kupambana, hajui lugha yoyote zaidi ya kiingereza na kichina. Utumizi wake wa silaha ni hafifu haswa na ninapomsihi ajifunze zaidi huniambia hana muda huo kwani CIA hawakumchukua kwa ajili ya kupambana.
.
.
Labda anachojivunia ni utaalamu wake nyuma ya 'keyboard' na ujuzi wake kwenye mambo ya sayansi. Ni mwerevu sana kwenye hayo, na basi hataki mengine kabisa.
.
.
Lakini mbali na ubishi huo, ni rafiki mmoja mzuri sana, japo kuna muda huwa ananipotosha. Ni mtu wangu wa karibu sana na mara nyingi nakuwa naye kazini na mbali ya kazini.
.
.
Yeye pia hana mke wala mtoto, bali mchumba tu ambaye huitwa Violette. Mwanamke huyo ni Mmarekani na amekuja naye hapa Hong Kong kwaajili ya likizo hii.
.
.
Nadhani utambulisho huo unatosha. Mengine utayajulia kadiri nikusimuliapo yanayotukia kwenye kisa hiki cha kukuacha mdomo wazi. Kisa ambacho nimekipa jina la NYUMA YAKO kwa maana kwamba, si kwasababu unatazama mbele, ukadhani nyuma ya mgongo wako mambo yamesimama. Lah! Ukiwa unatazama mbele, nyuma pia kuna mambo yanaendelea, na mambo hayo yanaweza yakawa ya hatari kuliko uwazavyo.
.
.
Na kwasababu haujayapa kipaumbele kama yale ya mbele, mambo haya ya nyuma huwa ya ghafla na hatarishi zaidi, yakikuacha ukiwa umelala chini hujiwezi, damu zakububujika.
.
.
Tazama nyuma yako. Huenda kuna mchezo unaendelea ambao hauuoni.
.
.
.
***
Ni kwa muda mfupi kwa kadiri tulivyoweza tukawa tumefika Marekani, New York. Safari hiyo ni ya umbali wa masaa kumi na tano na dakika thelathini na tatu. Lakini kwasababu ya mambo ya masaa, kijografia Hong Kong ipo mbele kimajira kuliko Marekani hivyo tukafika siku hiyo hiyo tuliyotokea Hongkong, Jumatano, huku Marekani yakiwa ni majira ya mchana.
Ni ajabu enh? Basi ili tusipotazane hapa, maana kuna mikanganyiko zaidi huko mbele, acha tueleweshane kwa ufupi. Dunia huzunguka toka Magharibi kuelekea Mashariki, kwahiyo basi upande wa Mashariki huwai kuliona Jua kuliko ule wa Magharibi. Tupo pamoja?
Kwahivyo basi, ukiwa Hong Kong unatangulia kuliona na kulichoka jua kabla hata Marekani hawajaliona. Na wakuta Hong Kong ikiwa ni Jumatano, bado Marekani ni Jumanne au Jumatatu usiku baadhi ya maeneo machache ya Magharibi ya mbali. Kwahiyo kusafiri kutoka Hongkong kwenda Marekani, ni safari unayopoteza muda, yaani badala ya muda kuongezeka, unakuwa unapungua maana umetoka Mashariki kurudi Magharibi ambapo kupo nyuma kimasaa.
Natumai umenielewa.
Lakini hapa New York si ambapo tulikuwa tunaelekea. Makao makuu ya CIA yapo Virginia, umbali wa maili mia nne na nane toka jiji la New York. Kwa mwendo wa basi ingetugharimu masaa saba kasoro, hatukuwa na muda huo wa kupoteza kwahiyo ikatulazimu kuchukua ndege ili angalau tutumie lisaa limoja na robo hivi kufika Virginia.
Tukafanya hivyo, pasipo kupumzika, tukafika Virginia majira ya saa tisa alasiri. Nikamwacha Jack Pyong na mpenzi wake mie nikienda mpaka makao makuu kukutana na Inspector General, bwana Ethan Benjamin, mwanaume wa makadirio ya miaka hamsini kasoro haba.
“Karibu, Marshall,” akanikaribisha akinionyeshea kiti. Nikaketi na kumtazama. Alikuwa tayari ananitazama kwa umakini kana kwamba mwalimu wa usafi akitafuta kasoro kwenye sare ya mwanafunzi.
Bwana Ethan ni mtu mmoja mpole sana. Ni mara chache sana utamsikia akipaza sauti yake. Hupenda kutumia macho na maneno machache tu haswa akikukumbusha juu ya uwepo wako kwenye taasisi nyeti kama hiyo, CIA.
Mara kadhaa amekuwa akisema kabla ya kuwaruhusu maajenti wakafanye kazi zao, CIA ni moyo wa Marekani, hivyo msifanye taifa kuwa mfu.
Ni ngumu sana kumjua kama yupo kwenye msongo wa mawazo ama furaha. Uso wake ni mfichavi mzuri sana wa hisia. Najaribu sana kuwa kama yeye, lakini naishia kushindwa. Haswa nikiwa na mpumbavu Jack Pyong.
Akasafisha koo lake na kuniambia, “Marshall, nina kazi kubwa sana ya kukupatia. Najua hautaniangusha.” Akili yangu ikaanza kuwaza itakuwa kazi gani hiyo ya kunitoa kwenye likizo yangu na kuitwa moja kwa moja na Inspector General? Ndivyo tulivyofundishwa. Yakupasa kuwaza ya mbele, hata kubashiri kwa mantiki pale unapoona kuna haja ya kufanya hivyo. Halikuwa kosa.
Ila sikuweza kuwaza sana kwa maana nilipaswa pia kuweka akili na masikio yangu kwenye kinywa cha mkuu wangu wa kazi.
“Hapa tuongeapo, Raisi amepotea,” akasema kisha akanyamaza akin’tazama kwa kunisoma. “Alikuwa njiani akielekea Berlin, Ujerumani, kwenye mkutano wa mataifa makubwa kiuchumi, lakini mpaka sasa tuongeapo hajulikani alipo, na inasemekana ndege yake imeanguka huko mbali ya bahari ya Pasifiki.”
Kauli hiyo ikatosha kunitoa macho kwa mshangao. Nikajitengenezea vema kitini na kumtazama Mkuu akinena.
“Taarifa haijatangazwa rasmi, lakini haiwezi kukaa kabatini kwa muda. Hili laweza kuwa shambulizi la kigaidi, nina mashaka nalo. Na mpaka kukuita hapa maana yake ni kwamba nina mashaka nalo.”
Akanyamaza na kunitazama kwa sekunde mbili, alafu akaniita, “Marshall.”
“Ndio, Mkuu.”
Akasema, “Nishatoa maelezo haya kwa mkuu wako wa kitengo. Unachotakiwa kukifanya ni kwenda kumtafuta Raisi popote alipo. Kama amekufa, tuletee mwili wake hapa niamini. Na pia … vichwa vya hao waliohusika!” akiwa anasema hayo maneno ya mwishoni alikuwa anaminyia kidole chake juu ya meza, macho akiyakaza.
Kwa kuongezea zaidi akaniambia nitashirikiana na inspekta wa FBI (Federal Bureau of Investigation) Miss Danielle James kuhusiana na chochote kile cha upelelezi ntakachokihitaji ndani ya nchi. Hii ni kwasababu CIA huwa wanahusika zaidi na mambo ya nje, nchi za kigeni, wakati FBI wao wakihusika na intelijensia ya ndani ya nchi, kukusanya taarifa, ushahidi, na kushurutisha sheria.
Hivyo kuna nyakati huwa tunategemeana kutekeleza majukumu yetu.
“Utamkuta hapo nje,” akasema mkuu na kumalizia tena, “Usiniangushe, Marshall. CIA ni --”
“Moyo wa Marekani,” nikamsaidia kumalizia kisha nikatikisa kichwa na kutoka nje ya ofisi. Nikakutana na Danielle, mwanamke mkakamavu mwenye nywele nyekundu akiwa amevalia suti rangi ya kahawia. Akanisalimu nami pia nikamsalimu kisha nikaenda kukaa naye kwa ofisi yangu kwa muda mchache mno, nikionelea ni kheri kwanza niende kwenye eneo la tukio kumtafuta Raisi, alafu nitakuja kurejea kuongea naye zaidi.
“Kwahiyo unaonaje?” akaniuliza. Kwakweli sikuwa najua nini ametoka kuongelea, kwani mawazo yangu yalikuwa mbali kidogo. Nilikuwa najaribu kuwaza ni wakina nani watakuwa na ‘guts’ za kufanya tukio kubwa kama hilo? Na amewezaje kufanya vivyo ingali ulinzi wa Raisi huwa ni wa hali ya juu?
“Daniella, tutaonana. Sawa?” nikamuaga nikinyanyuka kuuendea mlango, nikaufungua na kumtazama. Mwanamke huyo akatikisa kichwa kabla hajanyanyuka na kujiendea zake. Mimi nikarejea pale kitini na kuwaza kwa muda kidogo juu ya namna ya kuenenda. Punde nikatungua koti langu jeusi lililopo ndani ya ofisi, nikaliweka begani na kutoka.
**
Ni hivi, katika oparesheni kama hii, siwezi kwenda mwenyewe. Nahitaji msaada toka kwa watu wengine ambao tutaunda timu ya kufanya kazi. Ndani ya CIA kuna kitengo cha shughuli maalum, kwa jina ‘The Special Activities Centre’, kifupi SAC. Kitengo hichi kimegawanyika kwenye makundi mawili; PAG na SOG.
Oparesheni za kisiasa na kiuchumi huendeshwa na ‘The Political Action Group’, kifupi PAG. Hawa wanahusika na ushawishi wa kisiasa na wa kichumi wa Marekani dunia nzima. Na oparesheni zenye hatari ya juu kijeshi hufanywa na ‘The Special Operation Group’ kifupi SOG.
Wahusika wa SOG huwa hawabebelei nguo au kitu chochote cha kuwaonyesha kuwa wao wametokea Marekani. Na hii ni kwasababu muda wowote ule ambapo mambo yakienda kombo, basi Marekani wanaweza kukana kuhusika nao.
Ndani yake kunakuwa na watu wenye ujuzi wa hali ya juu, ambao wengi wao hutolewa kwenye kitengo cha special force au tuite komando toka jeshini. Na kwakufanya mambo kuwa mepesi na ‘manageable’ huwa wachache tu kwa kila oparesheni.
Hivyo basi kwakuwa kila kitu kilishakuwa bayana, nilipoonana na mhusika wa kitengo cha SAC (The Special Activities Centre), akanikabidhi vijana wanne kwa ajili ya kazi akiwa amefuata maelekezo ya Inspector General. Kwahiyo kutokana na kazi tuliyokuwa tunaelekea kufanya, sisi tukawa ni SOG (The Special Operation Group).
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
**
Ulikuwa ni usiku sasa wa saa mbili tukiwa angani ndani ya ndege ya mapambano. Tukiwa tumekaa kwa kutazamana, tukamsika rubani akitangaza kusema tunaingia eneo la tukio hivyo basi tuanze kujiandaa kwa ajili ya kuchumpa.
Tukaweka kila kitu sawa; begi la parachuti na miwani ya kutusaidia kuona usiku. Tulikuwa tumevalia nguo nyeusi za kombati zisizo na bendera, pia tumebebelea vifaa kadhaa vya kutusaidia kimapambano na kuzamia. Punde rubani aliposema tumefika, mkia wa ndege ukafunguka nasi tukarukia nje pasipo kujiuliza.
Tukachukua kama dakika sita tukiwa hewani tukibebwa na maparachuti tunasukumwa na upepo. Tulipotua, ilikuwa ni kisiwani, tukiwa tunafuata ramani, tukatembea upesi mpaka kufika eneo la ufukweni. Palikuwa kimya haswa. Nikatazama tena kwenye ramani yangu kuhakikisha. Ni kweli nilikuwa mahali ninapostahili.
Hapakuwa na alama ya kitu chochote hapo. Maji yalikuwa yanasukumwa na upepo kutengeneza mawimbi, na miti inatikisika kutengeneza muziki.
Hapa ndiyo nikajua ya kuwa sisi ni watu wa kwanza kufika hapo. Ina maana tangu Raisi aangukie maeneo hayo, hakuna mtu aliyewahi kukanyaga hapo.
Kidogo nikapata maswali juu ya namna gani jambo hili lilivyokuwa la siri. Siri mpaka pale aidha mwili wa Raisi utakapopatikana au mpaka pale wahusika watakapojulikana. Lakini itachukua muda gani? Hapa nikakumbuka kauli ya Inspector General, kuwa jambo hili haliwezi kukaa kabatini kwa muda mrefu.
Na kwa kuwaza tu, tayari mashaka yatakuwa yameshaambaa miongoni mwa watu. Raisi wa Marekani kutoonekana kwenye mkutano mkubwa kama huo na ingali huku nchini ameshaaga, ni wazi kabisa, ni kitu cha kuzalisha mashaka na maswali.
“Tazama kule!” alisema kamanda mmoja niliyeambatana naye. Tulisonga huko alipokuwa ameelekezea, tukakuta mojawapo ya mabaki ya ndege, kidogo tena tukaona zaidi na zaidi, hapa tukapata maswali, ni kwamba ndege ililipuka kabla ya kuzamia ndani ya maji ama?
Ila hapana. Mabaki haya hayakuonyesha dalili ya kuungua. Huenda wakati ndege inapoteza mwelekeo na kwenda kombo, baadhi ya viungio vyake vilishindwa kukinzana na upepo mkali basi vikabanduka na kunyofoka.
Japo tuliweza kung’amua jambo hilo na kujiaminisha kuwa kweli ndege ilikatiza eneo tulilopo, tukajikuta tukiwa na matumaini mfu sasa juu ya uhai wa Raisi. Ni wazi ndege itakuwa imezama majini, na kwa mahesabu ya kawaida mpaka muda huo tangu tukio litokee, ni ngumu kwa mtu kuwa hai ndani ya maji.
“Sasa tunafanyaje?” akaniuliza mmoja wa kamanda niliyekuwa naye kikosini.
“Tunazama ndani ya maji,” nikamjibu nikimtazama. “Ni lazima tupate mwili wa Raisi, hai au mfu!” nikaongezea taarifa kisha nikatazama huku na kule ndani ya msitu wa kisiwa.
Kulikuwa ni giza na kimya.
Giza na kimya.
**
Sauti ya ndege wa kwanza iliniamsha toka usingizini. Nilijua ni asubuhi sasa japo hakukuwa kumekuchwa na jua. Niliamka na kuangaza, wenzangu walikuwa wamelala. Nikanyanyuka na kuifuata bahari kwa ukaribu. Hapo nikiwa nimeweka mikono yangu mfukoni, nikangaza mandhari, pia nikajiuliza maswali kadhaa ya kipuuzi.
Muda kidogo wenzangu nao wakaamka, basi bila kupoteza muda tukaanza kufanya mpango wa kuzamia ndani ya maji. Wawili miongoni mwetu walikuwa ni watu wenye ujuzi huo, walivalia mitungi ya gesi na vinyago vya majini kisha wakazama.
Tukawangoja kwa takribani lisaa limoja, wakaibuka wakiwa na watu wawili ambao tuliwatambua kama marubani kutokana na sare zao. Kwa kusaidizana, tukapeleka miili hiyo ufukweni.
“Ndege ipo kwenye kina kirefu sana,” alisema mmoja wao aliyezamia. “Yachukua muda kufika na kurudi toka huko, takribani zoezi la dakika ishirini.”
“Hamjauona mwili wa Raisi?” nikawauliza.
“Hapana, hatujauona. Ila hatujamaliza kukagua ndege nzima.”
Wakazama tena, na ikatuchukua kama lisaa lingine kwa wao kuibuka tena juu. Mara hii walikuwa wamewabebelea watu wengine wawili ambao walikuwa wafanyakazi wa ndani ya ndege. Nikawauliza tena kuhusu Raisi, wakanijibu hamna. Hawajamwona.
Nikamwambia mmoja wao, “Nikabidhi nami vifaa nizamie.”
Tukazama humo na mie nikatafuta sana ndani ya mabaki yale ya ndege. Sikuona mwili wa Raisi, zaidi ya kukutana na miili ya watu wengine, wafanyakazi na maajenti wa secret service ambao wanahusika na ulinzi wa Raisi. Nilikaa humo sana nikikagua kila eneo pasipo mafanikio. Mwishowe mpaka mtungi wa gesi ukaanza kuishiwa. Sikuwa na budi kupanda juu kabla mtungi huo haujawa mzigo.
“Vipi, umeona kitu?” akaniuliza mmoja wa wenzangu.
“Hapana,” nikamjibu nikitikisa kichwa. “Nimeambulia hiki tu.” nikawaonyesha tai mkononi mwangu. Wakaichukua na kuitazama. Wote tukakubaliana kuwa tai ile ilikuwa ni ya Raisi. Nyuma yake ilikuwa na bendera na nembo ya Marekani.
“Sasa itakuaje?” akauliza mmoja wao. “Ina maana atakuwa ameangukia kwengine?”
“Inawezekanaje?” nikawahi kutia shaka. “Inawezekanaje aangukie kwengine alafu tai ikabakia ndani ya ndege.”
“Sasa atakuwa wapi?”
“Sijajua,” nikajibu nikiangaza msitu. “Ni ajabu kwake kutoonekana na huku tai kubakia ndani ya ndege! Hii inamaanisha alikuwapo ndani. sasaa …” kwa muda kidogo nikawaza. “Pengine yatupasa kuanza msako wa kisiwa hiki kizima na maeneo yake ya karibu.”
Basi tusipoteze muda tukaanza kufanya hivyo. Tukazunguka kisiwa kizima kwa masaa kadhaa tusione lolote. Hakukuwa na alama yoyote ya binadamu humo. Zaidi tukiwa tunakaribia kufanya kazi yetu hiyo, nikaona mojawapo ya nyayo za binadamu ufukweni. Nikaita na kuwataarifu wenzangu.
“Unadhani itakuwa ni ya nani?”
“Pengine wavuvi. Au wewe unadhaniaje?”
“Wavuvi?” nikapata swali. “Wavuvi tokea wapi?”
Tulipotazama kwa mbali upande wetu wa kaskazini, tukagundua kuwapo kwa kisiwa kingine. Kisiwa hicho kilikuwa kikubwa kuliko hiki cha sasa, nacho kikiwa kimezibwa na misitu ya kijani.
“Twende huko tukatazame,” mmoja akashauri, lakini mimi nikasita, “Sidhani kama Raisi atakuwapo huko.”
“Sasa unadhani atakuwapo wapi?”
“Sijui, ila nahisi ni maeneo ya hapahapa karibu.” nikashauri, “turudi kule kwenye ndege.”
“Kufanya nini huko na tumeshatoka?”
Hapa nilipata shaka na nikajilaumu kwanini mawazo niliyokuwa nayawaza muda huo sikuwa nayo hapo kabla. Nilihisi kuna haja ya kuhesabu wale watu waliokuwemo ndani ya ndege. Juhudi kubwa ni kung’amua kuna maajenti wangapi waliobakia humo ili tutambue kama Raisi alitokomea mwenyewe au alitokomea na baadhi ya maajenti wa secret service.
Tukipata jibu la swali hili basi kwa namna moja ama nyingine tutajua nini cha kufanya. Kufanya hilo vema, tukawasiliana kwanza na kitengo cha Secret service watujuze idadi kamili ya maajenti walioongozana na Raisi, pia wafanyakazi waliokuwamo ndani ya ndege.
Baada ya kujua hilo, tukarejea kule kwenye ndege na kuzamia tena, mara hii nikizama peke yangu kutokana na uhaba wa mtungi wa gesi. Ulikuwa umebakia mmoja ambao ndiyo upo kamili. Nikiwa nafanya hili kwa ustadi, nikagundua kulikuwa na upungufu wa maajenti wawili wa secret service.
Hapa sasa nikapata mashaka. Nao watakuwa wapi? Wameenda na Raisi ama walipotelea maeneo tofauti? Lakini kwanini wao na si wengine?
Maswali haya yalinifanya kichwa changu kiwake moto na hata hatimaye kuishia kuona kuna haja ya sisi kuondoka huko kisiwani ili twende tukatafute majibu nchini kisha tujue namna ya kuenenda.
Lakini kabla ya kwenda huko, nikaona pia ni stara tukaenda kupekua na kisiwa kile ambacho ni kikubwa kipakanacho na hichi tulichopo kwa upande wa kaskazini. Lengo ni kuhakikisha hakuna makandokando yoyote tuliyoyabakiza kwenye eneo la tukio. Tukiondoka basi tumeondoka ‘for good’.
Tukaogelea kwa dakika kadhaa. Tulipofika huko, tukashikilia silaha zetu vema na kuanza kuzama ndani ya kisiwa. Kadiri tulivyokuwa tunazama humo na giza likawa linakua. Miti ilikuwa mingi sana na tena yenye matawi na majani mapana.
Tukatembea kwa muda wa kama dakika nane, mmoja wetu akaona damu ardhini.
“Unadhani kutakuwa na watu hapa?” akauliza. Kabla hatujajibu tukastaajabu nyavu imetusoma na kutukusanya, alafu ikatupeleka juu kabisa ya mti! Nyavu hiyo ilikuwa ngumu haswa na ilitubana mno kiasi cha kuhema kwa tabu.
Tulizama mtegoni! Na hatukuwa na ujanja wowote ule wa kufanya kwani viungo vyote vilikuwa vimebaniwa mwilini. Kurusha macho huku na huku, kidogo tukasikia sauti ya filimbi, na kitu cha mwisho kabisa kukikumbuka ikawa ni maumivu ya kitu kama mwiba mgongoni mwangu. Nikapoteza fahamu.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Nilikuja kugundua baadae ya kwamba tulichomwa sindano za sumu.
**
Nilikuwa kizani sifahamu kinachoendelea, ila kadiri muda ulivyokuwa unaenda, nikaanza kujihisi mwili wangu. Nilijihisi nipo chini tena sina nguo. Mwili unapigwa na baridi kali.
Kichwa nacho kilikuwa kinanigonga, na kwa mbaali nasikia sauti za ngoma. Nikajaribu kufungua macho nitazame. Sikuwa naona vema, nadhani ni kwasababu ya madhara ya ile sumu tuliyochomwa nayo. Nilikuwa naona maruweruwe, watu kama mawingu!
Watu hawa walikuwa wanacheza kwa kuzunguka. Walikuwa wengi na katikati yao kulikuwa na kitu. Ni nini hiki? … nilijaribu kutazama lakini sikuwa naona vema. Mwili ulikuwa mdhaifu na uliochoka sana.
Niliwaza, je watu hawa ndiyo watakuwa na mwili wa Raisi na wale maajenti wa secret service? Nikajikakamua nisimame lakini sikuweza abadani! Sikujua walikuwa wametutilia nini. Nilijihisi mzembe kwa kiwango cha lami! Maungio ya mwili yalikuwa hayajiwezi, mdomo umekauka na masikio nayahisi yamoto!
Kuna muda ulimi nao nilikuwa nauhisi mchungu sana. Nikimeza mate ni kana kwamba yananikaba ama kuniunguza koo! Nilijichukia sana. Kama ningeweza kujitoa kwenye mwili huo, ningefanya vivyo niwe huru. Niliuhisi mzigo.
Kidogo nikawakumbuka wenzangu. Nikajikunja mwili na kuangaza ndani ya eneo tulilopo. Sikuwa naona kitu. Kulikuwa ni kiza tu. Hata nilipokaza macho yangu ya kilemavu kutazama, sikuambulia!
Kwa mbali nilisikia sauti ya mtu akikoroma, ila sikuwa namwona. Nikatamani kumwita mtu huyo, koo likagoma kabisa. Sauti haikuwa inatoka. Nilijitahidi hata nipaze sauti ya kuhema kwanguvu kama ishara lakini ikashindikana, ni kama vile koo lilijawa na vidonda, na mapafu nayo yamesinyaa!
Kusema ukweli sijui ni nini ambacho tulitiliwa. Sijui ni sumu ya namna gani yenye kumtenda mtu vibaya kiasi kile mpaka utamani kufa.
Kwa ustadi wangu wote, sikuwahi kukutana na sumu ile. Nilijiuliza wametumia kitu gani hicho, mti gani? Ua gani? Mmea gani huo? Kweli sikuwa na majibu.
Nilijikuta nikirejea sakafuni na kulala maana hakuna cha maana nilichokuwa nafanya. Kama niko sahihi, baada ya dakika kama tano hivi, nikasikia sauti ya mlango ukifunguliwa. Sikujua kilichoendelea, ila kidogo mkono wangu ukadakwa, nikanyanyuliwa vuup! Nikaburuzwa kupelekwa nje ya jengo tulokuwapo huku watu wawili waliokuwa wananibebelea wakiwa wanaongea lugha nisiyoelewa.
Kama baada ya dakika moja, wakanibwagia chini, pale eneo ambao niliwaona watu wakiwa wanacheza ngoma, kisha sauti nzito ikasema maneno ya ajabu kwanguvu, mara ngoma ikakoma.
Kidogo nikawasikia na wenzangu wakiwa wanatupiwa hapo chini. Bado kulikuwa kimya. Na nadhani tulivyomalizika kutupiwa hapo chini ndipo nikasikia kishindo cha mtu.
Kishindo kilikuwa kikubwa kiasi cha kunifanya niwaze atakuwa ni nani huyo? Mtu mwenye mwili mpana na uzito wa mtoto wa tembo?
Nikadakwa kama kikaratasi na kisha kunyanyuliwa niketi kitako. Nikapanuliwa mdomo na kumiminiwa kimiminika kichungu haswa. Nilipomeza, japo kwa tabu mno, nikaanza kupata ahueni. Kimiminika kile kilinikata sumu kabisa na kunifanya nianze kujihisi ahueni ya binadamu. Macho yalipata uwezo, mwili ukawa na nishati.
Nilistaajabu ni dawa gani ile ambayo iliweza kunipa ahueni haraka vile. Japo nimetumia dawa nyingi za hospitali, sikuwahi kuona ahueni ya upesi kiasi kile. Nilitazama, mbele yangu, nikamwona mtu mmoja mpana kana kwamba mbuyu. Nywele zake zilikuwa nyeusi na ndefu.
Mwili wake umejawa na michoro mbalimbali, shingoni amevalia mkufu wa mifupa ya wanyama na amejisitiri sehemu zake za siri kwa majani yaliyofumwa vema.
Hakuwa na sura ya urafiki. Macho yake yalikuwa makubwa na mekundu yakitingwa na ndita pana kama matuta. Alinitisha. Na namna alivyokuwa ananitazama, nilihisi anataka kunimeza.
Mbali na yeye, watu wengine wote ambao walikuwa wamesimama wakitutazama, nao walikuwa wametukodolea macho. Nao nyuso zao zatisha. Sijui walikuwa wamepakaa nini usoni. Mikononi wamebebelea mikuki mirefu yenye kupambwa na manyoya ya tai. Wanawake kwa wanaume, watoto kwa watu wazima.
Sasa yule mwanaume ambaye amenipatia dawa, mwanaume mpana mwenye uso wa kutisha, akaniuliza, "Sheeta ghasi cha?" Akinikazia macho.
Watu wote walikuwa kimya kana kwamba hamna mtu. Nikatambua kuwa mtu huyu atakuwa ni mwenye nafasi ya juu katika jamii hii. Mtu mwenye kuogopwa na kuheshimiwa. Aidha ni kiongozi au tabibu mkuu.
Lakini lugha aliyoizungumza kwangu ilikuwa mpya. Sikumwelewa. Nilitikisa kichwa na kumwambia kwa lugha yangu kuwa sijamwelewa. Sijawahi kusikia lugha yake hata mafunzoni japo tumesoma lugha kadhaa huko.
Basi mtu huyo akawatazama wenzake na pasipo kusema kitu, mmoja wao akasonga mbele. Huyu alikuwa ni kijana fulani mrefu mwembamba. Nywele zake zilikuwa fupi nyeusi, macho yake makubwa na makali.
Akanitazama, kisha akanisogelea karibu na kuniuliza, "mmetokea wapi? Na hapa mmekuja kufanya nini?"
Nikatambua kuwa kijana huyo alikuwa anazungumza lugha yetu. Nilistaajabu kidogo. Huenda ni mtu ambaye alishawahi kutoka na kwenda kuyajua ya nje ya jamii yao. Kumbe hata yule bwana alipoangaza kando, alikuwa amempa ishara ya yeye kuongea nasi.
Kidogo nikapata tumaini. Kama watatuelewa basi wangeweza kutusaidia na hata kutuachia huru maana hatukuja kuwadhuru bali kutimiza kazi yetu ya msako.
"Tupo hapa kutafuta miili iliyo--"
"Anguka toka kwenye nyota juu?" Akanikatisha kwa swali. Nikamtikisia kichwa, "ndio. Miili iliyoanguka toka kwenye nyota. Nyota ya juu!"
Akamtazama yule bwana mkubwa na kumwambia kwa ile lugha yake. Yule bwana mkubwa akanitazama alafu akaukita mshale wake chini kwa mkono wake wa kushoto.
Akataka kusema nami jambo, akakumbuka hatuelewani, akamtazama yule bwana mdogo na kumwambia nini aniulize.
"Je, mmeshapata mlichokuwa mnakitafuta?"
"Hapana!" Nikawahi kujibu na kisha kuwauliza, "mmeona chochote kile?" Hakunijibu, badala yake akafikisha taarifa kwa yule bwana mkubwa.
Sikujua walikuwa wanawaza nini vichwani mwao, ila walionekana kujawa na mashaka fulani baada ya kuwajibu maswali yao machache. Walijadili kidogo, kama wakielekezana kitu, na mara wakalipuka kwa hasira.
Nikiwa namwona yule bwana mkubwa akiwa amefura, akamimina maneno yake kwa yule bwana mdogo ambaye punde akanieleza kilichosibu.
"Hata kama tungeona kitu, tusingewaeleza. Hatutaki kuhangaika nanyi wauaji na waharibifu wa amani. Tutawaua hivi punde mkawe chakula cha samaki!"
Nikashangazwa, "ni nini kosa letu?" Yule bwana mdogo akafoka akieleza kuwa sisi ni maadui kwao. Tulishawahi kuvamia kijiji chao na kuwamaliza wenzao, ikiwemo kiongozi wao na hata wazazi wa huyo bwana mdogo aliyekuwa mkalimani!
Habari hizi zikanishtua. Na hata kama wale wenzangu wangelikuwa wazima kama mimi, yaani wamepewa dawa ile ya unafuu, wangelishtuka pia. Sikujua ni nini watu wale walikuwa wanazungumzia.
"Hii ni mara yetu ya kwanza kuj--"
"Mwongo!" Nikakatishwa na yule bwana mdogo. Uso wake ulikuwa umebadilika, anang'ata meno na kunitazama kiuchungu.
"Ninyi ni wauaji! Mlidhani tutawasahau? Mlinifanya kuwa yatima, na sasa mmerudi kutuangamiza sote?"
"Sijui nini wazungumza," nikajitetea. "Sijui lolote kati ya hayo mnayotuhusisha nayo. Hatujawahi kuja hapa isipokuwa mara hii..." nikiwa naongea kujieleza, mara watu hao wakaanza kugongesha vitako vya mikuki yao chini na kuimba kwa pamoja "hal! Hal! Hal! Hal!" Sauti yao ilikuwa kubwa kiasi nikaamua kunyamaza maana sikuwa nasikika.
Lakini zaidi nikaogopa maana sikuona kama ni ishara njema. Japo sikuelewa kilichokuwa kinazungumzwa, ila matendo yalinipasha maana. Anamaanisha nini mtu aimbaye hivyo na huku akikata shingo yake kwa kiganja cha mkono?
Tukanyanyuliwa na kutiwa nyavuni,nyavu ngumu iliyotuteka mtegoni, alafu tukaanza kuburuzwa kupelekwa eneo ambalo hatukuwa tunalijua, huko kwenda kuadhibiwa pia kwa kosa tusilolijua.
Tulizama zaidi misituni, mbali na kijiji. Safari nzima wakiwa wanaendelea kuimba "hal! Hal! Hal!" Wakigongesha mikuki ardhini!
Kwa takribani kama dakika nane tukitembea, ndipo wakasimama na kukoma kuimba. Nilipolikagua eneo hilo, nikaona miti mikubwa ikiwa imetengeneza umbo la pembe tatu. Miti hiyo mipana kana kwamba mibuyu, ilikuwa imechorwachorwa sura za ajabu na imefungwafungwa kamba.
Sikufahamu kwanini miti hiyo ilikuwa mikubwa kuliko mingine iliyokuwa imezunguka hapo. Na pia kwa muda huo sikuwa najua kwanini wametuleta kwenye miti hiyo na si mingine. Ila niliwaza pengine ilikuwa ni miti ya madhabahu. Sehemu ambapo wanafanyia shughuli zao za kidini kama vile matambiko na ibada.
Sasa hapo walituleta kutufanyia nini?
Yule bwana mkubwa, kiongozi, akawatazama vijana wanne wa kiume, wakasonga mbele na kutunyaka alafu wakatutia kambani na kutufungia mitini. Wakatukaza haswa kisha wakaimba hapo kwa muda kidogo yule bwana mkubwa akitunyunyizia maji yake ya dawa. Walipomaliza wakaanza kujiondokea.
"Tafadhali msituache hapa!" Nikawaita na kuwasihi. "Hatuhusiki na mlichokisema, tunaomba mtuache huru!"
Hakuna aliyejali, ila yule bwana mdogo alibaki nyuma ya wenzake waondokao. Naye alikuwa wa mwisho akitutazama. Na kabla hajatokomea, akanisogelea karibu na kuniambia,
"Unaona hizo sura mitini, ni za wale tuliowafungia hapa na kuwaacha. Unajua kwanini miti hii ni minene? ... Ni kwasababu inakula watu!" Alafu akatabasamu.
Nikamuuliza, "lakini mbona wewe ni wa tofauti na wenzako? Umejuaje lugha yetu?"
Akaniuliza, "hayo ndiyo maneno yako ya mwisho ukielekea kufa?" Kisha akatikisa kichwa. "Nilidhani wewe ni mwerevu."
**
Na asiendelee kuongea nami, akashika njia aende zake. Nikamwita asijali. Akaendelea kuondoka akipiga mluzi. Lakini nilipomwambia maneno haya, akasimama.
"Nina kitu kwa ajili yako!"
Akanitazama na kisha akakunja sura kama atiaye shaka alafu akanijongea na kuniambia, "sina muda wa kupoteza nawe ewe bwana wa manjano. Ni nini hiko wataka kuniambia?"
"Kama unataka nikuambie niweke huru toka kwenye nyara hizi!" Nikamsihi. Akatabasamu na kisha kucheka kidogo kana kwamba mtu mwenye utumbo mtupu. "Unadhani mimi ni mjinga kama wewe?" Akaniuliza.
"Ujinga wangu uko wap?"
Akatahamaki, "hujioni ulivyo mjinga? Uliwaua watu wa kijiji hiki alafu ukaja tena ukiwa hujiwezi. Unadhani wewe ni mwerevu?"
"Sikuwahi kuj--"
"Ishia hapo! Siko kuskiza ngonjera zako. Kama huna cha kuniambia, acha niende kwa amani nawe ubaki hapa kutafunwa na mti!"
"Ninacho ... ninacho cha kukuambia. Na najua utafurahi ukikisikia."
Akabaki akin'tazama kwa macho ya mchoko. Hakutaka tena kusema kitu bali asikie hicho ambacho nataka kumwambia.
"Umeona ewe bwana mdogo, nina namna ya kukufanya uishi chini ya maji!"
Nikamwaona akikunja ndita za umakini kwa mbali. Hapa nikajua mada yangu imemgusa.
"Kama afanyavyo samaki, nawe utaishi, kuona na kuzamia. Je, hiko si kitu cha maana kukwambia?"
Nilitazamia jambo hilo litakuwa geni kwake. Niliomba iwe hivyo, kwani kama ingelikuwa tofauti, basi ningeambulia kuachwa nijifie. Hapana. Nilikuja hapa kumsaka Raisi na si kifo.
Akanicheka. "Unamaanisha mtungi wa hewa na mawani ya kuziba macho?" Akaniuliza akibinua mdomo. Akacheka tena mpaka akidaka magoti yake na kushikilia tumbo lake.
"Skiza ewe mtu wa manjano. Mimi si mjinga kama unavyofikiri kichwani mwako. Unadhani sijui unavyovizungumza?"
Akanipa maswali juu yake, mbona ni mwerevu kiasi hiki? Kumbe mtu huyu si tu kwamba anajua lugha yetu, bali pia na teknolojia! Hapa ilinibidi nifanye kazi ya ziada.
"Sawa, basi nitakupa cha kukufanya uone nyakati za usiku!" Nikasema kwa kujivuna. "Utatembea kama mchana usijikwae kisiki au kudumbukia shimoni!"
Hapa akanyamaza kwa muda, macho yakiwaza, alafu akaniuliza, "sasa umeona unidanganye?"
Nikajua hili kwake ni geni.
"Nidanganye ya nini na wakati naomba kubakiziwa uhai tena nikiwa nimezingirwa na maji pande zote?"
Akabinua mdomo na asiseme chochote, akaenda zake. Nikamwita asigeuke nyuma abadani mpaka anatokomea. Nikalaani sana. Nikajiuliza ni nini nitafanya na wakati mikono na miguu yangu imefungwa kwa kamba kiasi kile?
Tukio hilo likanikumbusha mbali sana. Mbali ya mwaka juzi ambapo niliagizwa kwenda kuwakomboa baadhi ya mateka wa kimarekani waliokuwa wanashikiliwa na wanamgambo wa Boko Haram huko nchini Nigeria.
Nakumbuka, nikiwa nimeambatana na wanaume wanne , wamarekani weusi, wa kikosi maalum (special forces), tukiwa mgahawani, tulizingirwa na kuwekwa chini ya ulinzi na watu sita ambao walikuwa wameficha nyuso zao na kubebelea bunduki aina ya ak 47.
Watu hawa kwa namna tulivyowatazama walikuwa ni wanamgambo wa Boko Haram, haswa kutokana na mitandio waliyokuwa wamejivika nayo usoni mbali na kombati walizovaa.
Walituamrisha tunyooshe mikono juu na kututaka tuendee gari walizokuja nazo. Tukafanya hivyo pasipo ubishi. Wakatusweka na kutimka tukielekea mahali tusipopajua kwa maana walitia vichwa vyetu ndani ya mifuko meusi.
Wakiwa wanatupeleka huko, wakawa wanateta kwa lugha ya kiarabu ambayo tulikuwa tunaisikia, wakifurahia kukamatwa kwetu na namna ambavyo wao watanufaika kwa kuongeza mateka wa kimarekani kwenye ghala.
Lakini walijuaje kama sisi ni wamarekani? Ilikuwa ni rahisi sana, na 'in fact' ni sisi ndiyo tulifanya wakatujua hivyo. Hapo mgahawani tulikuja na gari, Nissan double cabin nyeupe, yenye chapa ya USAID ubavuni. USAID ni shirika la Marekani.
Tukiwa mgahawani, tukawa tukizungumza kiingereza chetu, kiingereza cha lafudhi ya Marekani. Na zaidi mgahawa huo ulikuwa ukipatikana katika moja ya kanda ambazo ni mhanga wa mashambulizi ya mara kwa mara ya Boko Haram, kaskazini mashariki wa Nigeria, hivyo kutokea kwa wale wajamaa kilikuwa ni kitu cha kutegemewa. Kitu ambacho unaweza kukibashiri!
Wakiwa wanazungumza hayo yao, tena sisi tukiwa tunawaelewa, nasi tukawa tunazungumza kwa ishara, 'sign language' pasipo wao kuhisi wala kuelewa.
'Sign language' ama 'paralinguistic language' ni lugha isiyo na maandishi ama sauti. Ni utaalamu wa kufikisha ujumbe kwa namna ya kupeana ishara 'signals' na mwenzako akakuelewa na kujibu.
Hiki ni miongoni mwa vitu tujifunzavyo tuwapo mafunzoni kwaajili ya kujiandaa na mazingira mbalimbali ukiwa mhitaji wa kuwasiliana.http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Kwa kutumia miguu yetu, tukaminyana, na pia kwa kutumia mikono yetu ambayo ilikuwa imefungwa, tukagusana kwa vidole tukifikishiana ujumbe.
Baada ya hapo, tukangoja. Mwendo wa kama nusu saa tukiwa kimya, ila sio tukiwa malofa. Mmoja wetu tulimpatia kazi ya kuhesabu majira na zoezi la kutushtua pale atakapokuwa ameona mahesabu tuliyoyapanga yametimia.
Kwa muda wa kawaida, kama tulivyokuwa tukiwaza kuwa watu hawa watakuwa wanatupeleka msitu wa Sambisa ambao ni moja ya ngome ya Boko Haram, ilikuwa yachukua kama lisaa limoja na dakika kumi na mbili endapo gari ikienda kwa mwendo wa kilomita themanini kwa lisaa.
Na kama halitoenda kwa mwendo huo, basi tena linakuwa jukumu na mpanga mahesabu kupiga mahesabu hayo kutokana na mwendo ulivyo. Kwa nilivyokuwa nahisi, gari lilikuwa linaenda kilomita mia na ishirini kwa lisaa. Sikuwa mbali na ukweli. Kidogo mahesabu yangu yalikaribiana na mkokotoaji yakiachana kwa kama sekunde kumi na sita tu!
Nikabinywa pajani. Hiyo ilikuwa ni ishara kuwa muda uliokuwa umetengwa sasa umekaribia, zimebaki sekunde nne tu. Nikabinywa na vidole vinne, vitatu, viwili, mwishowe kimoja! Kidogo gari likazama kwa korongo barabarani, hapo hapo, ndani ya dakika chache, tukanyanyuka na kutupa miili yetu mahali tulipokuwa tukisikia sauti za watu na kuhisi uwepo wao!
Ilikuwa ni kitu cha upesi na kushtukiza!
Kule kwenye bodi mulikuwa na wanamgambo sita, watatu wakikalia kushoto na watatu kulia, na basi kwasababu sisi tulikuwa watano kwa idadi, ilikuwa rahisi kuleta shambulizi lenye tija kwa kufuata mipango tuliyopanga kuwa wawili wataenda huku na watano wataenda upande mwingineo.
Ilikuwa pia rahisi kwasababu wanamgambo wale hawakuwa kwenye balansi muda mfupi baada ya gari kupitia mtikisiko. Hivyo, baada ya kufanya hivyo, nikawahisha kichwa changu kwenye mikono ya mwenzangu, akanivua mfuko kichwani.
Kutazama, nikawaona wanamgambo wawili wakiwa wanajiweka tenge kushambulia kwa risasi. Wawili walidondoka chini barabarani, wawili wengine wakiwa wameshikilia bomba la gari kutafuta balansi!
Haraka nikajitupa samasoti kwa chini kuwafuata. Nikamtengua mmoja miguu, na yule mwingine alipotaka kunishambulia, nikajikinga na mwili wa mwenzake, alafu nikampokonya bunduki yule niliyemtumia kama ngao na kisha mwili wake nikamtupia mwenziwe, wote wakadondoka chini!
Nikasikia ti-ti-ti-ti! Haraka nikajilaza chini. Kutazama nikaona mwenzetu mmoja akiwa amedondoka kwa kushindiliwa risasi! Tulikuwa tukishambuliwa na dereva.
Nikatulia na kufyatya risasi moja, ikamdungua kichwa na kummaliza papo hapo, gari likaanza kwenda mrama, lakini kabla halijaleta madhara, mmoja wetu akaliwahi na kuliweka kimyani, kisha tukaendeleza na safari kwenda huko msituni.
Basi kwakuwa wale wenzangu walikuwa na ngozi nyeusi wakajivika nguo za wale wanamgambo na kisha kuigiza kuwa wameniteka kwa lengo la kuzama ndani ya ngome.
Kwa kufupisha habari hiyo, ambayo pengine nitakuja kuisimulia vema siku nyingine, kilichonifanya niikumbuke ni namna tulivyokuta mateka wakiwa wamefungwa kamba mitini, wamarekani na wengine toka nchi za Ulaya. Na kwasababu za kioparesheni, nami nikatiwa kambani kama wale mateka wengine, lakini kamba yangu ilikuwa legevu kwa maana kwamba punde mambo yatakapoharibiwa nitoke hapo.
Ilikuwa ni tofauti na oparesheni ya Raisi kule kisiwani kwani kamba ya kisiwani ilikuwa imekazwa haswa na hakukuwa na namna ya mimi kuchoropoka isipokuwa kwa msaada. Na tofauti kabisa na Nigeria, siku hiyo wenzangu wote walikuwa hawajiwezi. Hawakupewa tiba kama ilivyokuwa kwangu, hivyo siku hiyo mimi ndo' nilikuwa na jukumu la kuwaokoa.
Muda ukaenda na giza la usiku likafika. Punde kidogo, baada ya giza hilo kuingia, nikaanza kutambua kwanini tulifungiwa kwenye miti ile mipana. Nilianza kuhisi mgongo wangu unafinywa kuzamia ndani, na kadiri muda ulivyokuwa unaenda, nikawa nahisi maumivu makali ya mgongo.
Nikajitahidi kujichoropoa, wapi! Zaidi nikajiongezea maumivu zaidi. Niliporusha macho kuwatazama wenzangu, nikawaona wakiwa wametulia tuli. Hawakuwa na fahamu!
Nikahisi usiku huu ndiyo mwisho wetu.
Hata nikainamisha kichwa changu kama kristo msalabani, sasa nimekwisha. Mwanaume miliyeshiriki kwenye misheni kadhaa za hatari, nakuja kuuawa na hawa washamba wa msituni. Aibu iliyoje?
Ila, nikajadili na nafsi yangu, haikuwa kama nilivyokuwa nawaza. Hamna mtu aliyedhani hapa kuna watu, na zaidi ya yote, kwenye shambulio la kushtukizwa, hamna mjanja. Atakayemuwahi mwenziwe basi ndo anakuwa mshindi. Hata simba akiwa mbugani, anawezwa wahiwa na nyoka, akamalizwa!
Hapa tulikuwa tumewahiwa, na japo lilikuwa jambo chungu kwangu, ila ndiyo ulikuwa uhalisia. Sikuwa na ujanja wa ziada.
Nikiwa nimejikatia tamaa, nangoja sasa 'nimezwe' na ule mti kama tulivyonenewa, nikahisi kitu huko msituni! Masikio yangu yakasimama na macho yangu yakang'aza. Ilikuwa ni kama kishindo cha mtu au mnyama ila sikuona kitu!
Kishindo hicho hakikukoma, kikaendelea tena na tena na kunijaza hofu huenda akawa mnyama wa mwituni. Endapo akitokea hapo tutajiteteaje? Nikapata mawazo yaliyonipa tena nguvu ya ajabu kupambana na kamba nilizofungiwa.
Nikapambana kujisukuma na kusukuma, waapi! Zaidi nikajitia alama nyekundu mwilini, pia majeraha na maumivu tu! Sikufanikiwa wala kwa dalili!
Kishindo kikaendelea kusikika huko gizani msituni na mara sauti ikasema, "ewe mtu wa manjano, bado upo?"
Nikaitambua sauti hiyo kuwa ya bwana yule mdogo. Bwana azungumzaye lugha yetu. Yeye alitokea upande wangu wa kushoto baada ya punde na kisha kunisogelea kwa karibu.
Akanitazama machoni. "Naona bado upo. Vipi, unaendeleaje?"
"Hali inazidi kuwa mbaya," nikamjibu na kumsihi, "naomba uniweke huru!"
"Si kwa haraka hivyo," akasema akitikisa kichwa chake, kisha akahema akinitazama kama mtu anayefurahia mateso yangu. Akaniuliza, "kwanini mlivamia kijiji chetu? Ni nini tuliwakosea?"
Nikamtazama kwa macho yangu malegevu. Uso wake ulikuwa unang'azwa na mwanga wa mbalamwezi. Nikafungua kinywa changu kikavu na kumwambia, "sijawahi kuja hapa, hii ni mara yangu ya kwanza. Nikuambieje unielewe?"
Mara akatoa kijiwe fulani nyuma ya mgongo wake. Kilikua ni kijiwe kidogo kimachong'aa. Kwa mwanga ule uliokuwepo nilikiona ni kijiwe chenye rangi nyekundu, sikujua mwangani mwa jua kingeonekanaje.
Akaniuliza akinionyeshea kijiwe hicho, "ni hichi ndicho mnatafuta?"
"Hapana!" Nikajikakamua kukanusha. "Sina shida na chochote toka kwenu. Nimefika hapa kumtafuta mtu aliyepotea, na si vijiwe!"
"Mtu gani huyo? Yule aliyedondoka toka kwenye nyota?" Akaniuliza akishika kidevu chake.
Nikamkazia, "Ndio huyohuyo! Je, umemwona?"
"Ndio. Nimemwona."
Hapa nikatoa macho. "Yupo wapi? ... tafadhali nipatie mtu huyo nasi tutaondoka msituone tena!"
Akatulia kidogo. Akanitazama kwa mafikirio alafu akaniuliza, "nikikuonyesha utanipatia nini?"
"Chochote kati ya tulivyokuja navyo!"
"Mi' nataka kile cha kuonea usiku. Mimi ni mwindaji. Nahisi kitanisaidia sa--"
"Nitakupatia, usijali!" Nikamkatiza. "We twende nionyeshe wapi alipo mtu huyo!"
Basi akanifungua kamba na tukaanza safari. Lakini hakuwa mjinga, aliniweka mbele yeye akiwa nyuma yangu. Mkononi alibebelea mkuki na kinywani alikuwa ameshikilia filimbi kwa lips zake. Filimbi hii, kwa alivyoniambia, ingemwamsha kila mtu kijijini aje kunitafuta endapo ningejitia ukaidi.
Sikupanga kuwa mkaidi. Lah! Hamu yangu ya kuuona mwili wa mtu ambaye nilihisi ndiye namtafuta ilikuwa kubwa kuliko kufanya njama za kutoroka.
Tukasonga, akiwa ananielekeza, mpaka eneo fulani ambapo alinitaka nisimame na kutulia. Nikafanya hivyo. Hapo toka kwenye kibanda kimoja kidogo kilichotengenezwa kwa matawi ya miti, akapenyeza mkono wake na kutoa mti mmoja mrefu, sikujua wa nini, akatoa pia na dude fulani kama rungu kisha akaniambia tuendelee na safari.
Tulipotembea kwa muda kidogo akaniamuru nisimame na kisha akaniambia, "mwili huo upo humo shimoni, utazama humo uangaze, nami nitakuvuta kwa mti utoke nje!"
Alipoyasema hayo akaniwashia lile dude nililodhani ni rungu, tena kwa haraka akitumia mawe, alafu akanishikisha ule mti mrefu nami nikazama na ginga la moto ndani ya shimo.
Lilikuwa ni shimo refu, na kadiri nilivyokuwa nazama nikawa nahisi harufu ya mzoga puani mwangu. Zaidi na zaidi. Na nikiwa sasa nimefikia nchani mwa fimbo ile ambayo nimeishikilia, nikawa nimefika chini kabisa! Kumbe ile fimbo ilikuwa na vipimo sawia kulingana na shimo.
Nikaangaza kutazama na ginga langu la moto, humo nikaona miili kadhaa, na mmoja kati yao, ambao ulikuwa mpyampya tuseme, ukawa umekamata macho yangu. Mwili huo ulikuwa mpana na wenye kuvalia suti nyeusi. Ulikuwa umelala kifudifudi.
Nikachuchumaa na kuugeuza niutazame. Haukuwa wa Raisi! Nikawaza utakuwa ni miongoni mwa wale maajenti wasiokuwepo kule ndani ya ndege. Sasa mwili wa Raisi utakuwa wapi? Nikajiuliza nikiendelea kuangazaangaza. Sikuuona!
Nilishika kiuno changu na kushusha pumzi ndefu.
"Vipi? Si huo?" Akaniuliza yule bwana mdogo juu ya shimo.
"Hapana, si wenyewe!"
Nikamwomba mti, anivute juu. Nilipopanda nikakung'uta mwili wangu na kumuuliza, "hakuna mwingine ninaoweza kutazama?"
Nikamwona akibinua mdomo wake. "Hapana, hili ndilo shimo pekee lililopo hapa."
Nikanyamaza nikiwaza. Akan'tazama na kunitahadharisha, "lakini makubaliano yetu si yapo palepale?"
Sikumjibu. Mimi nilikuwa na mawazo yangu kichwani. Akili yangu yote ilikuwa inawaza namna gani ambavyo naweza kuupata ama kuuona mwili wa Raisi. Hali hiyo ikampatia hofu yule bwana mdogo, nadhani akahisi nitamgeuka. Akanionyeshea mkuki wake na kuniambia tena, "makubaliano yetu si yapo palepale?"
"Ndio," nikamjibu kumtoa hofu. "Makubaliano yetu yapo palepale!"
Kidogo akatulia. Kwa muda huu nikawa nimemtengeneza rafiki. Nikapata mwanya wa kumuuliza kwanini aliniamini akanifungulia pale mtini ilhali mwanzoni walin'tilia shaka.
Akanitazama kwanza. Akatabasamu kwa mbali na kuniambia, "wewe sio kama wale! ... wale waliokuja kutuvamia na kuwaua wenzetu!"
"Umejuaje kuwa sisi sio wale?"http://pseudepigraphas.blogspot.com/
"Kwasababu ya kile kijiwe!" Akanijibu aking'aza macho. "Watu wale waliokuja na kuwaua wenzetu hawakuwa wanataka kingine zaidi ya mawe! ... wewe nilikuona upo tofauti. Sikuona tamaa ndani ya macho yako punde nilipokuonyesha kile kijiwe."
"Lakini tuliwaambia mwanzoni kuwa sisi tunamtafuta mwenzetu!"
"Ndio, ila si rahisi kuamini ... poleni."
"Basi naomba ukawasaidie wale wenzangu kama ulivyofanya kwangu."
"Siwezi!"
"Kwanini?"
"Mimi sina ile dawa waliyokupa wewe."
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment