Search This Blog

Friday, 18 November 2022

BARADHULI MWENYE MIKONO YA CHUMA (2) - 1

 








IMEANDIKWA NA : STEVE MOLLEL



*********************************************************************************



Simulizi : Baradhuli Mwenye Mikono Ya Chuma (2)

Sehemu Ya Kwanza (1)



SURA YA KWANZA (MSIMU WA 02)





MAUAJI TENA!







Kichwa kimojawapo cha gazeti kilisomeka hivyo. Chini yake kulikuwa na picha tatu ambazo kama hutozitizama vema basi utaishia kusema ni maghofu ya miji ya kale. La hasha! Kumbe ni mabaki ya nyumba ya Mtemvu, ama tumuite marehemu Mtemvu kwa sasa – aliyekuwa afisa polisi kanda maalum Dar es Salaam.









Yeye pamoja na mkewe wote waliaga dunia ndani ya mlipuko mkubwa wa mabomu. Hakuna masalia yoyote ya miili yao









Mtemvu pamoja na mkewe walifariki ndani ya nyumba, pia nyumba yao kuteketea kwasababu ya kukawia kwa zimamoto. Zaidi ya hapo, watuhumiwa wa tukio walikuwa chini ya ulinzi hospitali wakipata matibabu. Kwa upande wa Miraji hali yake haikuwa tenge kabisa, ni kama vile alikuwa wa kwenda ndani ya muda mchache ujao; risasi ya mgongo iliyotuama kwenye uti wake wa mgongo ilimweka katika hatari ya kupooza mwili. Kichwa kingine cha habari ilikuwa ni juu ya kuachiwa huru kwa bibie Bernadetha Kombo, yeye pamoja na binti yake, Marietta, ambaye alikuwa chini ya uangalizi maalum wa watoto.







Hakukuwa na gazeti, chaneli wala stesheni iliyokwepa habari hizo. Lakini swali kubwa lililotawala ni kwanini Miraji auwa washirika wa karibu wa babaye? Kutafuta majibu ya swali hilo, waandishi wa habari wakawa wanazonga hospitalikwa ajili ya Miraji na nyumbani kwa marehemu mzee Malale wakiwahitaji wahusika wawapatie majibu. Bahati mbaya Mama Miraji, Bernadetha, hakuwa tayari kuongea na waandishi wa habari kuhusu chochote na kwa Miraji bado hakuwa na afya ya kutosha kumfanya afungue kinywa.









Siku moja inspekta Vitalis akiwa ameketi pembeni ya kitanda alicholazwa Jombi, alianza kudadisi kutaka kufahamu nini kinachoendelea nyuma ya pazia la mashambulizi. Aliamuru polisi na manesi wampe faragha, wakafanya hivyo na kumpa mwanya wa kuongea. Baada ya kujiridhisha yupo mwenyewe na mhusika wake, alianzisha soga;









“Uliniahidi kuniambia nini kipo nyuma ya yote haya. Sasa waweza kuniambia?” Alisema inspekta Vitalis katika sauti ya kuuliza. Jombi alishusha pumzi ndefu kisha akang’ata lips zake. Alinyanyua mkono wake usio na pingu akajikunia kichwa na kusema;









“Ndio, naweza.” Alijibu na kuongezea. “Mimi ni mtu tu niliyejitolea kumsaidia Miraji kutimiza adhma yake ya kulipiza kisasi, na si zaidi ya hapo hivyo sikuona kama nastahili adhabu ile ya kifo.”

“Kisasi?” Inspekta Vitalis alijita. “Kisasi kwa kina nani na kwanini?”

“Kisasi kwa wale wote ambao walishiriki kumuua baba yake.” Alijibu Jombi.

“Una uhakika kwamba baba yake aliuwawa?”

“Ndio. Miraji aliambiwa kila kitu na mama yake juu ya kifo cha baba yake.”

“Kwamba?”

“Baba yake aliuwawa na washirika wenzake baada ya dili ya magendo waliyoifanya kubumburuka. Hivyo wakamtoa sadaka kuficha identity na reputation zao mbele ya jamii.”

“Miraji alikuambia kuhusu hilo dili?”

“Kidogo. Aliniambia lilikuwa linahusu kusafirisha pembe za tembo kuelekea Italy, Rome. Na watu walioshiriki ni wale wote ambao tumewaua.”

“Una uhakika na unachokiongea?”

“Absolubtely. Nimekuambia kile chote nikijuacho.”









Inspekta alitulia kwanza kwa muda kama mtu anayefikiria jambo. Kisha akaendelea kuuliza;

“Wewe na Miraji mna mahusiano gani?”

“Ni rafiki yangu tokea zamani sana, tangu tupo kindergarten.” Jombi alijibu kwa kujiamini.

“Na kwa sasa wewe unafanya kazi gani?”

“Nafanya biashara tu.”

“Ipi?”

“Ya kuuza nguo. Nina duka langu la nguo maeneo ya Tandika.”

“Na kuhusu silaha na vifaa, mlikuwa mnavitolea wapi?”









Jombi alinyamaza kwa muda kidogo baada ya hilo swali. Ni kama vile alikuwa anafikiria cha kujibu. Inspekta alimtazama kwa kumkazia macho, akatazama chini.









“Tulikuwa tunanunua.”

“Pesa mlikuwa mnapata wapi?”

“Tulikuwa tunakwapua pesa toka nyumbani kwa wakina Miraji.”

“Yote hiyo ya kununulia vifaa kama vile?”









Baada ya hilo swali, ghafla Jombi alishika kichwa na kulalama kinamuuma. Hakuweza kuongea tena zaidi alikuwa akilalamika na kugugumia kwa maumivu ya kichwa. Inspekta akampa muda wa kupumzika, ila wakati inspekta ananyanyuka apate kwenda, Jombi alijikakamua kuongea akamuomba simu inspekta kwa madai ya kuwasiliana na kuwajuza nduguze, bila hiyana, inspekta akampatia kisha akasonga pembeni. Jombi aliweka namba akapiga. Sauti yake aliishusha ikawa ya kunong’ona.









“Haloo boss…Jombi hapa…ndio, Jombi kijana wako…nipo Regency hospital kwa sasa, ila nipo chini ya ulinzi…naomba uniokoe boss wangu…kazi nimeshamaliza…Miraji bado, ila atakufa muda si mrefu sana hivyo sio wa kumuhofia kabisa…sawa sawa…ni ghorofa namba mbili, wodi ya tatu…sawa boss wangu…”







Alikata simu haraka baada ya kuona inspekta anakuja akiongozana na polisi. Inspekta aliposogea alitwaa simu yake na kuaga akiahidi kurudi baadae. Huku nyuma, Jombi alibakia akitabasamu na uso wake ulionyesha matumaini.







Usiku ulipoingia, macho ya Jombi yalikuwa yakipepesa pepesa huku na kule huku akipumua kwanguvu. Ni kama vile mtu aliyekuwa anategemea kitu muda si mwingi. Kushoto kwake alikuwa ameketi polisi aliyevalia bunduki, kulia kwake kulikuwa na vitanda vingine kadhaa vikiwa vimebebelea wagonjwa, na kitanda cha tatu toka cha kwake alikuwa amelala Miraji akiwa hana fahamu.







…moja…mbili…tatu…nne…tano…







Miraji alikuwa anahesabu kwa kunong’ona huku akipangua vidole vyake. Ilipofika kumi, mwanaume mrefu mweusi aliyekuwa kavalia nguo za daktari aliingia wodini. Macho yake yalitizama huku na kule kama mtu atafutaye ufunguo kwenye mchanga. Pap! Alikutana macho kwa macho na Jombi. Taratibu akaanza kusogea akimfuata Jombi. Tap! Tap! Tap! Viatu vyake viligonga sakafuni. Alipofika aliwasha tabasamu lake akamsalimia polisi kisha akamsalimia na Jombi.









“Unaendeleaje?” Alimtanabahi mgonjwa.

“Naendelea vizuri tu, dokta.”

“Sawa sawa. Sasa…” Dokta alisema kisha akakatisha ghafla na kumtizama polisi.

“Naomba utupishe kidogo, tuna maongezi ya siri na mgonjwa wangu.”







Polisi bila ya kuuliza akasonga nje ya wodi akasubiria mlangoni. Mwanaume yule aliyevalia kama daktari akamuuliza Jombi,







“Umemwambia yeyote kuhusu boss?”

“Hapana. Hakuna anayejua.” Jombi alijibu.









Mwanaume yule aliyevalia koti la daktari, aliingiza mkono wake kwenye mfuko akatoa sindano iliyobebelea kimiminika cha rangi ya njano. Ghafla, akamziba Jombi mdomo na kumshindilia sindano kwenye mguu wa kulia. Jombii alitapatapa kwa muda kidogo tu kisha akalegea kama mtu asiye na nguvu. Haraka mwanaume yule akatoka wodini isijulikane wapi alielekea. Polisi aliporudi alimkuta Jombi anamimina povu,macho yamepanda juu huku akitikisa miguu kwa mbali kama mtu akataye roho.









Haraka polisi alitoka mbio akarudi na daktari.





Asubuhi iliwasili. Pamoja nayo, ilikuja na wingi wa shughuli kama kawaida katika mji wa Dar es Salaam. Magari na watu walikuwa wanapishana, hawa wakienda huku wengine walienda kule ilimradi tu pamekucha kila mtu aenda kutafuta ridhiki.







Baada ya mlango wa nyumba ya mama Miraji kufunguka, alitoka Marietta akiwa kavalia sare za shule na begi lake mgongoni. Hatua tatu tu mbele yake alikutana na inspekta Vitalis Byabata, akamsalimia.









“Mama yupo?”

“Ndio, yupo.” Alijibu Marietta kwa tabasamu pana.

“Haya, masomo mema mama eeh.”

“Ahsante.” AlisemaMarietta kisha akaendelea na safari yake. Inspekta alimtizama mpaka anaishia. Alitikisa kichwa chake na kutabasamu kama mtu akumbukaye jambo la kufurahisha. Akageuza na kuufuata mlango. Ngo! Ngo! Ngo!

“Hodiii!”

“Karibu!” Sauti iliitikia kwa ndani. Baada tu ya muda mchache, mama Miraji akawa tayari ameshafungua mlango.

“Karibu.”

“Ahsante. Naitwa inspekta Vitalis Byabata.” Inspekta alisema huku akionyeshea kitambulisho.

“Wewe ni mke wa marehemu Malale?”

“Ndio.”

“Nashukuru. Mimi ni supervisor wa kesi ya mwanao pamoja na mshirika wake. Naweza nikaingia ndani?”









Kabla ya kusema jambo, mama Miraji alimtizama inspekta na uso uliojikunja na macho ya mkazo.









“Karibu.”

Inspekta akaingia ndani na kuketi kwenye kiti.

“Nikusaidieje?”

“Nimekuja hapa kupata baadhi ya taarifa toka kwako…”

“Taarifa gani?”

“Kumhusu mwanao na kumhusu mumeo kidogo.”

“Unataka kujua nini? Si mumemkamata? Mnataka nini kingine, roho yangu?”

“Calm down, mama. Sipo hapa kwa ajili ya kugombana. Nina dhumuni la kuwasaidia.”

“Kutusaidia? Kamsaidie kwanza mwanangu uliyemlaza kitandani. Kawasaidia hao wezi na wauwaji unaowalinda, sio mimi!”

“Calm down, mama. Naomba utulize moyo wako. Naomba ushirikiano nipate kujua nini kinacoendelea.”

“Sitaki kuongea chochote. Naomba uende!” Mama Miraji alifoka huku akinyooshea kidole mlangoni. Haikujalisha inspekta aliongeaje, mama Miraji hakubadilisha msimamo wake. Alimtaka inspekta atoke nyumbani kwake. Inspekta hakuwa budi, aliaga na kuondoka zake.







Akiwa anatembea kuelekea barabarani, simu yake iliita akapokea akapewa taarifa juu ya kile kilichotukia hospitali usiku wa kuamkia siku hiyo.Upesi alidandia daladala akaelekea hospitalini. Alimkuta Jombi akiwa hana nguvu, mdomo wake umepauka, macho yake yakiwa mekundu mno na ngozi yake ikiwa imesinyaa. Maelezo ya daktari yakasema ameingiziwa sumu kali mno, kama wasingeliwahi kumuhudumia asingelikuwapo hai. Mtuhumiwa wa tendo hakujulikana. Kilichopatikana ni maelezo tu kuwa alivalia nguo za kitabibu.









Inspekta akapata maswali juu ya hilo jambo. Nani anataka kumuua Jombi, na kwanini? Alitamani kumuuliza Jombi lakini haikuwezekana, hali yake bado haikuruhusu. Ila tokea siku hiyo aliamua kuwalinda Miraji na Jombi yeye mwenyewe, hivyo akamtaka polisi apumzike kwa hilo.









Baada ya siku mbili kupita. Alikuja mwanamke mmoja mnene aliyevalia dera jekundu na njano. Alibebelea sahani, hotpot kubwa na chupa ya chai. Alijitambulisha anaitwa Miriam, ndugu yake Jombi, amekuja kumhudumia ndugu yake. Kabla ya kuruhusiwa kwenda ndani ya wodi, inspekta alimtaka afungue hotpot na aonje chakula alichokileta. Bila kusita, Miriam alionja chakula kumhakikishia inspekta kwamba kipo sawa. Kama hiyo haitoshi, inspekta alimsindikiza Miriam mpaka alipo Jombi ambaye walimkuta bado akiwa vilevile kama jana yake.













Japokuwa Miriam alimsalimia, Jombi hakusema kitu. Macho yake yalikuwa yamefumba, mdomo wake ukiwa wazi kama lango la mlanguzi. Hakuonyesha dalili yoyote ya kusikia aambiwacho. Miriam alimpa pole kisha akaanza kulia. Inspekta alimtaka anyamaze, naye akafanya hivyo. Alinyanyuka akaenendea hotpot alilokuja nalo akaanza kupakua. Ila kisiri na kwa utaratibu, aliupeleka mkono wake chini ya hotpot akaanza kufungua kitako. Wakati huo inspekta alikuwa ameketi juu ya kitanda na Jombi. Ghafla, Miriam aligeuka akiwa na kisu kidogo mkononi, alinyanyua mkono akitaka kumkita Jombi kifuani, haraka inspekta akauwahi mkono ule na kumtandika teke kali Miriam lililomrushia mbali.











Ajabu, mwanamke alisimama haraka. Alikunjia dera lake kiunoni akabakia na tight nyeusi. Akatoa mtandio wake shingoni na kuuhamishia mkononi. Upesi akarukia dirishani akipasua vioo, akiwa hewani alirushia mtandio wake dirishani ukanasa, akatua chini taratibu na kupotea eneo lile.









Inspekta akabaki na maswali. Nini wanamtafutia Jombi hivi? Alijiuliza asipate kabisa majibu. Baadae giza lilipoingia, alipokea ujumbe kwenye simu yake.











“Wakati unalinda mjinga wako, ulisahau familia yako. Sasa utamuacha mjinga wako kutafuta familia yako.”









Mdomo wa inspekta ukaachama.









“Oh my God!”







Haraka alitafuta namba ya mkewe kwenye simu akapiga. Simu iliita bila kupokelewa. Mwishowe inspekta alichoka akaamua aitupie simu mfukoni. Kwa dakika kama moja insekta akawa kama mtu aliyewehuka asijue cha kufanya. Alienda mbele na kurudi nyuma. Alitoka nje ya wodi kisha akarudi ndani. Alitoka akarudi tena, macho yakiwa yamemtoka kama tufe.









“Mungu wangu…what should I do now?” Alijisemesha mwenyewe. Ndani ya muda kidogo tena, alikurupuka na kutoa simu yake mfukoni. Alipiga simu polisi akawataka waje kuwalinda watuhumiwa yeye kapata dharura isiyokwepeka. Baada ya dakika tu chache, polisi walifika inspekta akang’oa nanga. Alikodisha pikipiki toka nje ya hospitali ikamuwahisha kwa kasi nyumbani kwake. Alipofika, kabla ya kuingia ndani, alianza kuita.









“Mama Joons!...Mama Jooons!...Jooons!”







Hakukuwa na majibu. Si mama wala mtoto aliyeitikia wito. Inspekta alifu gua mlango akaanza kupekua kila eneo la nyumba. Alipomaliza ndani alihamia nje ya nyumba lakini hakumuona mtu yeyote. Wakati anafanya hayo, macho yalianza kuwa mekundu kama mtu mwenye malengo ya kudondosha chozi.









“Mama Joons!...Mama Joons!”











Aliita kwa sauti hafifu isiyotosha hata kumshtua kuku anayedoea mchele. Baada ya kuzunguka bila ya mafanikio, aliamua kukaa chini akashika tama. Mara simu yake ikaita. Alishtuka akaitizama, ilikuwa ni namba ya mkewe. Haraka alipokea akaiweka sikioni.









http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Haloo mama Jons!” Inspekta aliwahi kuongea. Hamaki sauti ya kiume ndiyo ikasikika sikioni kwake.

“Wewe nani? Mke wangu yupo wapi? Mtoto wangu yupo wapi?” Inspekta alifululiza maswali.

“Mke wako na mtoto wako tunao. Kama unataka kuwapata, tukabidhi mtu wetu haraka iwezekanavyo la sivyo utakosa familia yako muda si mrefu ujao.” Sauti toka simuni ilitishia.

“Mpo wapi sasa? Nitawaleteaje mtu wenu na sijui mlipo?”

“Ukiwa na mtu wetu tutaarifu, tutakwambia tulipo tukutane utupe mtu wetu tukupe wako. Na kaa ukijua hatuna muda wa kupoteza. Keshokutwa tunamuhitaji mtu wetu, la sivyo mtoto au mke wako atatangulia kuzimu.”

“Sasa jamani si mnajua siwezi tu kumtoa mtu ambaye yupo chini ya ulinzi kwa haraka hivyo?”

“Hilo ni juu yako, utachagua mwenyewe. Mtuhumiwa wako au familia yako. Na nikukumbushe tu, mwisho keshokutwa.” Simu ikakata.







Mithili ya kifaranga aliyemwagiwa maji, inspekta alinywea. Kama kuna muda tokea aanze kazi aliwahi kuwa katika njia panda, huu ndio ulikuwa wenyewe. Uso wake ulionyesha utupu. Macho yake yalichora simanzi na uso wake ulitambulisha ukosefu wa amani ndani ya nafsi.









Alinyanyuka akatembea kuelekea chumbani. Akiwa na viatu na nguoze, alijirushia kitandani akatizama dari kama mtu anayepanga mchoro. Alijigeuza kila upande wa kitanda. Alijigaragaza huku na kule, mwishowe usingizi ulimkwapua toka kwenye fahamu zake.



Asubuhi ya mapema, muda ukiwa unaruhusu kwa wageni kutembelea wagonjwa, mama Miraji alikuwa tayari amekaa kandokando ya mwanaye asiye na ufahamu. Polisi pia alikuwa nao kwa kando zaidi. Macho ya mama Miraji yalikuwa mapole yakimtizama kinda lake. Mkono wake wa kuume alikuwa kauweka kichwani mwa mwanaye, kiganja chake alikuwa anakipeleka mbele na nyuma kama mfugaji ampetiye mbwa wake.









“Mwanangu, mama yako nipo hapa. Fungua basi macho baba upate kuniona.” Mama alinong’ona. Hakuweza kuvumilia, machozi yalianza kumchuruza. Alinyanyua khanga yake akajifuta. Lakini zaidi machozi yaliendelea kumtiririka na kumtiririka. Alishindwa kuyazuia. Alinyanyuka akashika korido akielekea nje ya wodi, mlangoni akapishana na inspekta akiingia ndani, ingawa inspekta alimsalimia, hakuitika.







Alielekea zake njeakaketi pembezoni mwa kuta ya sakafu akawa anatizama chini magari na watu wakiingia hospitalini. Aliacha macho yake mekundu yaangaze angaze huku na kule kutizama majengo. Angalau hapo macho yake yakakata machozi. Ingawa alikuwa anatembeza macho yake sehemu mbalimbali lakini hakuonekana kama mtu anayejali kile anachokitizama. Eidha mawazo yake hayakuwa pale ama hakuwa na muda wa kujadili kile anachokitazama. Akiwa hapo, inspekta aliungana naye akasimama pembeni yake wote wakawa wanatizama majengo na watu bila ya kusemeshana. Baada ya muda, inspekta alivunja ukimya akaongea kwa sauti ya chini.







“Wameteka familia yangu; mke na mtoto wangu. Wanataka niwakabidhi Jombi kwao ili waachie familia yangu huru. Wamenipa leo tu, kesho mwisho, bila ya hivyo watamuua mwanangu ama mke wangu.”

Mama Miraji taratibu aligeuza uso wake akamtazama inspekta.

“Wakina nani?” Aliuliza mama.

“Sijajua wakina nani.” Inspekta alijibu na kuongezea,“na sijui kwanini wanamtaka Jombi kwanguvu hivyo. Walijaribu kumuua mara mbili bila ya mafanikio, sasa wameona kuteka familia yangu ndio njia ya kutimiza malengo yao.”









Baada ya huo usemi, ukimya ulipuliza kati yao kwa muda kidogo wakaacha macho yao yaendelee kuzurura maeneo kadha wa kadha. Ukimya ulipovunjwa, alikuwa ni inspekta ndiye aliyekuwa na nyundo.









“Samahani sana, ndugu yangu. Najua mimi ndiye ninayehusika na kumlaza mwanao juu ya kitanda, ila tambua sikuwa na budi, nilikuwako kazini. Lakini kwa sasa nahisi kuna mambo mengi yaliyo nyuma ya pazia, na mengine nilikuwa nafichwa na mkuu wangu. Nimejaribu kupeleleza lakini sijafinikiwa, mtu pekee aliyetoa ushirikiano kwangu ni Jombi. Naye pia kuna ambayo amenificha. Kwa sasa yupo kitandani hajielewi, sina wa kumuuliza. Naomba unifungue macho, mama. Nataka kujua pumba kwenye mchele. Naomba unisaidie.” Inspekta aliongea kwa utaratibu huku akimtizama mama Miraji usoni kisha kimya kikatawala tena. Mama Miraji alisafisha koo lake kwanza akaongea,









“Mume wangu aliuwawa na wenzake kwa ajili ya kuficha siri. Miezi kadhaa iliyopita, walishiriki kufanya dili ya magendo. Japokuwa hakuwa na lengo, na mimi nilisimama kidete kupinga, umasikini na ufukara wetu ulimzidi nguvu. Nakumbuka aliniambia ‘mke wangu, nimefanya kazi kwa miaka yote hiyo lakini hali yetu haijabadilisha sare. Naomba nijaribu upande wa pili wa shilingi. Mara moja tu’. Masikini hakujua kama huo ndio utakuwa mwisho wake. Tokea apotee ulimwenguni, si rafiki yake wala nani niliyemuona tena. Maisha yamekuwa magumu zaidi.”









Mama Miraji alianza kumimina machozi upya. Inspekta alimtizama akatikisa kichwa kwa huzuni.









“Pole sana, mama. Hao washirika wake walikuwa ni wakina nani? Na je unaweza ukanambia walimuuaje mumeo?”









Mama Miraji alivuta kwanza vimakamasi vya kilio, akanena;









“Nakumbuka siku moja tukiwa nyumbani majambazi walituvamia wakiwa na bunduki. Hawakuchukua kitu hata kimoja. Walimpulizia mume wangu dawa kisha wakatokomea. Baada ya hapo tu mume wangu akaumwa hoi mno nusura kufa. Hata pale tulipompeleka hospitali, walimfuata tu na huko. Wakamuwekea sumu kwenye dripu yake na huo ndio ukawa mwisho wake.”







Inspekta alishusha pumzi ndefu akaguna.









“Vipi uliwahi sema hiki kitu popote pale labda?” Aliuliza.

“Hapana.” Mama Miraji alijibu. “Nilipanga kufanya hivyo lakini nguvu zilinisha pale dokta alipoamua kukengeuka na kusema uongo mbele ya wandishi wa habari. Alikana yale yote aliyoyasema akiwa na mimi. Badala yake alisema mume wangu kafa na ugonjwa tu, hakuna kiashiria chochote cha sumu ndani ya mwili wake, nani angeniamini mimi?”

“Pole sana mama. Huyo daktari anaitwa nani na anafanya kazi wapi?”

“Ni daktari fulani hivi mhindi, anaitwa Rajesh Deepti. Anafanya kazi Royal Hospital.”

“Sawa. Na vipi kuhusu Jombi, unamuelewaje wewe? Una kipi cha kumzungumzia?”

“Jombi ni rafiki wa mwanangu. Walianza urafiki kitambo lakini baadaye baba yake Miraji alikuja kugundua Jombi hakuwa mtu sahihi na mzuri. Aliwahi kushikiliwa na kesi ya madawa ya kulevya lakini baadae alikuja kutolewa, hatukujua kivipi. Basi kwakuwa urafiki wa Miraji na Jombi ulikuwa mgumu kukatika, baba yake Miraji aliamua kumsafirisha Miraji akasomee India. Bahati mbaya mume wangu alipofariki, ilibidi mtoto arudi nyumbani na hata shule hakuendelea tena na ndio hapo akakutana tena na Jombi.”

“Sawa sawa. Kwahiyo Jombi alikuwa anamsaidia rafikiye kulipiza kisasi? Sio?”

“Sijajua kwa kweli. Ila ndivyo inavyoonekana.”

“Na Jombi alinambia kwamba, pesa za vifaa na silaha walikuwa wanazikwapua toka nyumbani kwako, ni kweli?”

“Pesa za silaha?”

“Ndio. Kwa mujibu wa maelezo yake.”

“Hapana kwa kweli. Ndio pesa zilikuwa zinaibiwa lakini si za kutosha kununulia silaha. Kwa hilo si kweli.”

“Sawa, mama. Hapa kuna jambo linatia shaka. Kuna kundi au mtu yupo nyuma ya Jombi. Na ndiye atakuwa anahusika au wanahusika na kumpa silaha. Swali la kujiuliza ni kwamba, je watakuwa wanafaidika nini na mauaji hayo yaliyofanyika? Na je wanahusikaje na kutaka kumuua Jombi?”









Maswali hayo yaliwafanya inspekta na mama Miraji watulie kwa muda wakionyesha nyuso za mawazo. Hakuna yeyote aliyeonekana anaweza yajibu. Baada ya muda mchache, daktari alikuja.Inspekta na mama Miraji waliongozana naye kuwafuata wagonjwa wao. Daktari alianza na kitanda cha Jombi, mama Miraji na inspekta wakawa wapo pembeni kusikiliza. Baada ya daktari kumtizama na kumkagua Jombi kwa macho na kuperuzi taarifa zake alizokuja nazo alifungua mdomo kutema maneno;











“Mgonjwa anaendelea vizuri tu. Fahamu zake zitarejea taratibu taratibu natumai siku si nyingi atakuwa katika hali yake ya kawaida. Tuvute tu subira.” Daktari alitia nasibu, lakini pia hakusita kuongezea,

“Sumu aliyotiwa mwilini ni hatari mno. Imeathiri kwa kiasi kikubwa maini yake kwa kuayaunguza na figo yake pia ipo katika mushkeli, haifanyi kazi ipasavyo. Tumeona kuna uhitaji mkubwa wa kufanyiwa upasuaji hapo kesho.”

“Haina shida dokta.” Inspekta alimtoa daktari hofu. “Afanyiwe tu alimradi arudi katika hali yake ya kawaida.”

“Sawa.” Daktari aliitikia kisha akasonga kufuata kitanda alicholazwa Miraji, nyuma yake akifuatiwa na inspekta pamoja na mama mtoto. Daktari alifungua kadi yake akaitizama kwanza kisha akamtizama mgonjwa na kutikisa kichwa.

“Recovery yake ni ya taratibu mno. Kuna some nerves zimekuwa damaged na jeraha la risasi. Ingawa atapona, kuna hatari kubwa ya kupooza. Pia consciousness yake iko damaged, itahitaji muda pia kurecover. Kwa muda huu wote atakuwa anahitaji kula kwa mipira.”









Daktari alipomaliza tu kusema hayo maneno, machozi yalikuwa tayari yameshateremka kwenye uso wa mama Miraji. Kwikwi za hapa na pale nazo zilizuka zikiambatana na mafua.









“Pole sana, mama. Yatakwisha.” Daktari alihitimisha kisha akaondoka zake. Mama Miraji naye hakukaa sana, alimuaga inspekta anarudi nyumbani kumuandalia mwanaye, Marietta, chakula, atakuja baadae. Ila kabla ya kuondoka inspekta alimuomba namba ya simu, akampatia. Alipoondoka, Inspekta akabaki na polisi mwenzake sambamba na wagonjwa. Ingawa alikuwa na hiyo kampani, inspekta hakufungua tena mdomo wake kunena lolote. Alikuwa ameshika tama, uso wake ukitambuza fikira zinazomtambaa akilini.











Baada ya dakika kadhaa zisizopungua dakika thelathini wala kuzidi arobaini na tano, inspekta alikuwa tayari ametoka wodini. Alikuwa ameketi mgahawani akipata chakula cha mchana. Kwa taratibu mno, alikuwa anakula. Kijiko kilikuwa kinaenda mdomoni kila baada ya muda mrefu kidogo, na hata kutafuna kwake kulikuwa kumepooza. Alitoa simu yake mfukoni akawa anaitizama majina. Alipofika kwenye jina la mkewe, alijaribu kupiga lakini simu haikupatikana. Akaachana nayo na kuendelea kutazama majina mengine, alipofika kwenye namba aliyosevu ‘Mama Miraji’, alitulia akaitizama namba hiyo, kisha akapiga.











“Haloo…vipi umefika salama?...vipi nyumbani?...okay, samahani, naomba nikuulize kitu…unafahamu eneo alilokuwa anaishi Jombi?...enhe pembeni ya barabara…nyumba ya tatu…aaah sawa sawa nyumba nyeupe…kwa nje kuna uzio?...mweupe nao…sawa nimekuelewa…nashukuru sana, baadae!”











Alipomaliza kuongea na simu, aliongeza kasi ya kula akamaliza chakula na kupotea eneo lile. Moja kwa moja alielekea nyumbani kwa Jombi, alifungua mlango kwa waya maalum wa silva baada ya kudumbukiza kwenye kitundu kidogo kilichokuwepo kwenye kitasa. Aliingia na kutembea kwa tahadhari, mkono wake wa kuume haukuwa mbali na mfuko wa bunduki.











Alikagua sebule lakini hakuona kitu. Aligeuka kutaka kuelekea chumbani, hapo akatandikwa teke la nguvu mgongoni likitokea nyuma Kiiihh! Akarushiwa ukutani mithili ya karatasi puh! Alipogeuza shingo alikutana uso kwa uso na pande la mtu, mnene, mrefu akiwa kajazia misuli ya kutosha.











Inspekta alijaribu kuupeleka mkonowe kiunoni atekebunduki yake lakini upesi pande la mtu lilivuta stuli na mguu wake akamrushia inspekta. Kabla inspekta hajajipanga, jitu tayari lilikuwa lishamfikia likamkwida na kumnyanyua juu juu.









“Wewe nani?” Jitu liliuliza na sauti yake nzito ya kukwaruza. Inspekta hakujibu, badala yake alinyanyua mguu wake wa kulia kwanguvu akamtandika teke kali adui wake sehemu za siri. Jitu likapiga kelele kali za maumivu. Lilimwachia inspekta alafu likapiga magoti kusikilizia maumivu. Hapo inspekta akapata upenyo, alimtandika jitu teke kali kichwani, jitu likaangukia chini puh! Kama kiroba cha mchanga. Inspekta akatengenezea koti lake mwilini na kuelekea kwenye chumba cha kwanza, sasa mkononi akiwa kashikilia bunduki.











Alipiga teke mlango akaingia ndani. Alikuta silaha na vifaa kadhaa; kamba, mabomu, nguo, viatu, stendi za bunduki na bunduki zenyewe. Alipekuwa pekuwa kama kuna mtu anakitafuta, alipomaliza alienda chumba kingine mwendo ukawa ule ule wa kutafuta. Kwenye chumba cha mwisho, akaonekana kupata alichokuwa anataka. Alikuta karatasi kubwa ya nailoni imefunika kifaa kikubwa. Alipoivutia kando nailoni hiyo, alitabasamu na macho yake yakasema furaha.









“It is the time now bitches!”









Alisema inspekta huku akipiga ngumi hewani.







Pembezoni mwa bahari, upepo ukiwa unavuma kwa kasi, kulikuwa kumepakiwa magari mawili, prado nyeusi. Vioo vyake vilikuwa tinted, na wanaume watatu wenye miili mikubwa wakiwa wamevalia miwani meusi na nguo zinazobana misuli yao walikuwa wameegemea magari hayo, mikononi walikuwa na bunduki.









Baada ya muda kidogo, gari ndogo ya kijivu aina ya Toyota Altezza ilifika eneo hilo tulivu ambalo watu hawakuwapo zaidi tu ya wale wanaume watatu. Gari hilo liliposimama, kioo cha nyuma kilishuka akaonekana Jombi, alivalia miwani akiegemea kochi. Baada ya hapo, kioo kilipandishwa na kufunga. Sauti ya inspekta ikasikika tokea kwenye radio call waliyokuwa wamebebelea wanaume wale wa shoka.







“Nami naomba nione familia yangu.”









Mwanaume mmoja aliyekuwa na bunduki akaligonga gari kama ishara, kioo kikashushwa mke na mtoto wa inspekta wakaonekana. Walikuwa na sura zenye hofu. Sauti ya inspekta ikaendelea kusema;

“Nipo peke yangu, mpo watatu tena wenye silaha, mtanipaje uhakika na uhai wangu na wa familia yangu endapo nikiwapa mtu wenu?”









Mwanaume aliyeshikilia radio call akamjibu,









“Hatuna shida na wewe wala familia yako, tunamtaka mtu wetu tu.”

“Okay. Nitahesabu mpaka tatu, utaachia familia yangu, nami nitamuachia mtu wenu. Sawa?”

“Sawa!”

“Moja…mbili…tatu!”









Milango ya magari ikafunguka. Mke na mtoto wa inspekta wakatoka kuifuata Altezza, Jombi naye akatoka akawa anaifuata prado huku akitembea kwa shida kama vile mtu mwenye mpango wa kudondokea kwa mbele. Wakati wanapishana, Jombi alinong’ona akamuambia mke wa inspekta;

“Ukiingia tu ndani endesha, potea.”











Kwa kuwa mwendo wa Jombi ulikuwa ni wa kusua sua alikawia kidogo kuwasili. Alipowafikia tu wanaume wale mabaunsa, Altezza ikawashwa na kuanza kuondolewa. Hapo hapo Jombi akamkamata Baunsa aliyekuwa karibu naye akampiga na kiwiko usoni. Pale tu mabaunsa wengine waliponyanyua silaha zao, ghafla, milio ya bunduki ilisikika, kufumba na kufumbua wote wakawa chini! Punde mwanaume mmoja akiwa amebebelea bunduki, akatoka majini. Alipovua mask yake akaonekana ni inspekta akiwa anatabasamu huku akimtizama Jombi.











Loh! Mara naye yule mwanaume aliyekuwa na sura ya Jombi akajishika shingoni na kuvuta kwanguvu ngozi yake, sura ya Jombi ikabanduka kama nyoka ajivuae gamba. Kumbe alikuwa ni mwanaume mwingine, kwa jina alikuwa anaitwa Kaguta, almaarufu kama “The red bullet”.









“Kazi nzuri sana, broh!” Inspekta alimpongeza mwenzie kwa kumkumbatia. “Naona sasa umerudi rasmi kazini.”

“Ahsante, Vitalis. Nilimiss sana hizi mishe. Natumai utanipa sehemu mujarabu za kutumia ujuzi wangu niliojifunza.”

“Ha ha ha na huko Cuba wamekuharibu kweli. Usikonde kazi zipo nyingi sana. Kuna mlima mkubwa upo mbele yetu unasubiri kusogezwa.”

“Mlima tu. Hata kama ni kukausha bahari am jus ready! Sema nini, sasa ninachokimiss ni warembo wa Cuba. Nawakumbuka kweli!”

“Ha ha ha umeanza Kaguta! Utaacha lini mambo yako?”

“Bado kidogo tu. Wewe si umeoa bwana!”

“Wewe nani kakukataza kuoa? Si hutaki.”

“Najua siwezi kutulia na bucha moja japo nyama ile ile. Vipi, tusepe, au?”

“Ngoja kwanza kidogo.” Inspekta alisema kisha akafuata miili ya watu waliowashambulia na kuanza kuipekua mifukoni huku akikusanya silaha zao. Kwenye mwili wa mmoja akakuta kitambulisho cha mpiga kura, na kwenye miili ya wengine akatohoa simu za mkononi.

“Sasa tunaweza tukaondoka.” Inspekta alimwambia mwenzake wakapanda gari moja wapo la majambazi wakaondoka eneo lile. Wakiwa njiani wakatoa taarifa polisi, ndani ya muda finyu polisi wakiongozana na magari ya kubebea majeruhi walifika sehemu ilipofanyikia tukio.







Jua likazama.









Ndani ya bar pana iliyoezekwa na makuti makavu watu wakiwa wamefurika na meza zikiwa zimechafuka na vilevi, kwenye upande mmoja wa ndanikidogo, alikuwa ameketi Inspekta na Kaguta. Bia kadhaa zilikuwa zimejaa mezani kwao. Kaguta alikuwa akipiga tarumbeta kama wasemavyo wanywaji, akiweka mdomo wa chupa kinywani na kumiminia humo, kwa upande wa inspekta alikuwa anatumia glasi kubwa akiwa anaijazia bia humo pomoni.









“Kama nilivyokuambia ndugu yangu, stori nzimandio hiyo. Nategemea kesho ama kesho kutwa nianze kufuatilia kile kitambulisho labda kinaweza nisaidia kujua hiyo gang inapatikana wapi na ipo chini ya nani.”









“Nakutakia kazi njema. Utakapohitaji msaada wangu, usisite kun’taarifu.” Kaguta alitia neno likafuatiwa na mafundo kadhaa ya bia.“Ila mwanangu kwa jinsi ulivyonambia, inabidi uwe makini. Inaonyesha jamaa wako very well equipped.”

“Hilo kweli, wako vizuri. Wanazo hadi mashine za kutengenezea sura bandia, Fake the face make up!”

“Ila kama isingekuwa yule mama, tusingeweza kufanya ile make-up vizuri.”

“Mama Miraji?”

“Huyo huyo. Yuko vizuri sana.”

“Ni kweli. Msaada wake umetusaidia sana.”

“Namuonea huruma hana mwanaume wa kumliwaza, lazima atakuwa mpweke sana.”

“Nani kasema? Au mawazo yako tu?”

“Kwani hilo nalo mpaka lisemwe? Hujui wimbo wa Yvonne Chakachaka ‘Every woman needs a man?” Aliuliza Kaguta kisha akaanza kuimba wimbo huo kwa sauti akiigiza kama mtu anayetumbuiza jukwaani. Inspekta akamzuia.

“Acha bana, huoni watu wote wanatutizama?”

“Aaaah!...unaogopa watu?”

“Zishapanda kichwani eenh?”

“Waaapi…bado sana, yani hapa wala sisikii. Sijui ni juice hizi au bia? Pombe Cuba bwana.”

“Kila kitu Cuba. Khaa!”









Kaguta akacheka baada ya kusikia hiyo kauli. Waliendelea kupiga soga hapo bar, giza likizidi kuwa nene. Lakini kinyume na muda, kadiri ulivyokuwa unasonga watu wakawa bado wanafurika eneo hilo kustarehe. Pale saa ya inspekta iliposema ni saa nane ya usiku, ndipo mabwana hao wawili waliponyanyuka na kuacha bar nyuma ya migongo yao kwenda kupanda gari la Kaguta, Toyota Mark 2.









“Utaweza ku-drive kweli, Kaguta?”

“Kwanini nisiweze?”

“Ah-ah! Umekunywa sana bwana, lete ufunguo niendeshe.”

“Vitalis, nipo sawa. Mbona muoga sana wewe.”

“Nina familia ndugu yangu.”

“We twende, nimekuambia nakuua mie.”











Walipanda kwenye gari, Kaguta akawa dereva. Kabla ya kuondoka, inspekta alihakikisha kafunga mkanda kwa usalama wake. Gari liliondolewa kwa kasi likawekwa kwenye barabara ya lami, mwendo ukawa wa ku-overtake. Ndani mziki mkubwa ukitema sauti ya Samba Mapangala na kibao chake maridhawa ‘Dunia tunapita’.









.Wakiwa wapo barabarani tayari wameshaacha bar kwa maili zisizopungua tatu, kwa mbali kidogo mbele yao upande waliokuwemo walishuhudia lori lililobebelea mifuko ya saruji, lilikuwa linatembea kwa mwendo wa taratibu huku mara kwa mara taa zake nyekundu za nyuma zikiwa zinawaka. Inspekta alitizama lile lori kwa makini na kwa sura ya woga;









“Angalia usiparamie ilo lori ndugu yangu.” Alitoa nasaha. Kaguta huku akiwa ametabasamu, alipindisha tairi ghafula akahamia upande wake wa kushoto toka upande lilipo lori, kisha akaongeza kasi kwa malengo ya kuliweka nyuma lori lile ili arudi upande aliokuwemo, wa kulia.











Gari la Kaguta lilipofika katikati ya lori, ghafula lori lilianza kusogea upande wao kwa kasi. Kaguta alipiga honi kutahadharisha lakini ilikuwa kazi bure. Lori lilizidi kuja! Upesi Kaguta alipunguza mwendokasi, bahati mbaya ama nzuri akakwangua taa za nyuma za lori za upande wa kushoto.











“We mshenzi wewe! Pita basi mbwa wewe!” Kaguta aliwaka kama moto wa kifuu.











Lori lilizidi kuja upande wao, ila kabla halijakaa vizuri kwenye mstari wa barabara waliopo wakina inspekta, lilikunja kona kali kurudi lilipotokea. Hapo sasa shughuli ikawa kubwa. Wakati kichwa cha lori kikirudi upande wake, mkia wake ulifuata gari la wakina inspekta kwa kasi ukabamiza kwa ubapa … buuh! Gari likapoteza dira, kama tamthilia kwenye runinga, lilipinduka likabiringita mara tatu! Bumbum!…bumbum!..bumbum!









Lori lililofanya tendo likapunguza mwendo na kusimama. Walishuka wanaume watatu waliobebelea bunduki kubwa ‘SMG’ mikononi mwao, wakalifuata gari la wakina inspekta na kuanza kulimiminia risasi za haja.











Tu!-tu!-tu!-tu!-tu!-tu!-tu!-tu!-tu!-tu!-tu!-tu!-tu!









Gari likawa nyambu nyambu kwa matundu, baada tu ya dakika moja likalipuka boooom! Moto mkubwa ukalitekeza ndani ya muda mchache. Wanaume wale baada ya kushuhudia hayo, walipeana tano za kupongezana kisha wakalirejea lori lao. Walipolifikia, mmoja wao alidanda akitaka kufungua mlango. Mara puh! Mlango ulisukumwa kwanguvu na teke kali tokea ndani ukawasomba na kuwaangusha wanaume wawili waliotoka kushambulia. Papo kwa papo, mwanaume mmoja akatoka kwenye lori kwa kasi akiruka kama ngedere akamvamia mwanaume aliyebakia amesimama kwa teke kali la kifuana kwenda naye mpaka chini akampokonya bunduki.











Hamaki, yule mwanaume alikuwa ni Kaguta! Wanaume wale wawili waliodondoshwa na mlangowalijikusanya na kushikilia bunduki wakiwa huko huko chini wakamnyooshea Kaguta. Katika hali ya wepesi, Kaguta alimgeuza mwanaume aliyedondokea naye chini akajiziba naye. Risasi zikamkosa wakati zikimiminika kwa mtu aliyemfanya ngao yake.











Haikuchukua muda sana, risasi zikakata, ni wazi nyingi ziliishia kwenye kulipua gari. Hapo ndio Kaguta kwa nguvu zake zote akamrusha mwanaume aliyemtumia kama ngao ya risasi kwa wenzake. Wenzake wakafanya kosa kwa kumtizama na kufungua mikono yao kumdaka mwenzao aliyerushwa, Kaguta akatumia mwanya huo mujarabu, haraka aliubeba mwili wake na mikono akaruhusu miguu yake iambae na kuwabetua wanaume wale wawili waliokuwa wamempokea mwenzao, kisha akawaweka chini ya ulinzi.









“Tulia hapo hapo. Sogeza hata kope muone!” Kaguta alitoa tisho kwa macho makali mithili ya mbwa mkali aliye mawindoni. Alipiga mluzi, mlango wa lori ukafunguliwa akatoka inspekta.







“Umemaliza?”

“Yap! Kazi ndogo sana hii?”

“Sasa tutatumia gari gani na wameshalipua letu?”

“Tutatumia lori lao. Tutafanyaje sasa?”









Inspekta alisogea vizuri akaanza kuwapekuwa wale wanaume, ambao ni wawili kati yao ndio walikuwa wazima. Mmoja alikuwa kitambo ameshafariki.











“Kwahiyo mlikuwa mnatufatilia, sio?” Aliuliza Kaguta kwa sauti kali.

“Ndio.”









“Hongereni sana. Bahati mbaya hamtokuwa na second chanceningewaelekeza kazi kama zile mnafanyaje.” Kaguta alimwaga maneno.“Ila labda mnaweza pata nafasi nyingine, ya Mungu mengi. Siku nyingine mkiwa mnataka kupindua gari hakikisheni mnaotaka kuwapindua wapo ndani ya gari. Nilikwangua taa za nyuma za gari lenu, ila hamkujali. Giza lililokuwepo lilitufanya sisi kuhamia kwenye trela bila nyie kufahamu. Mkapindua gari na kwenda kuliteketeza bila kuhakikisha tena kama kuna watu, kosa la pili. Kosa la tatu, hamkumuacha mtu kwenye lori. Poleni.” Alihitimisha Kaguta.









Waliwachukua wale wanaume wakawafunga kwa kutumia mashati na kuwatupia ndani ya lori kwa nyuma wakapeleka maiti mochwari na wengineo wakapelekwa eneo lililopo nje kidogo ya mji kwenye jengo fulani kubwa lililokuwa limemaliziwa nusu. Hapo wakawafungia wanaume wale wawili kwenye nguzo na kuondoka, wakawarudia kesho asubuhi na kuwakurupua kwa ndoo za maji.









“Habari za asubuhi?” Aliuliza inspekta kwa sauti ya mzaha. Kaguta alikuwa amekaa kwa mbali kidogo akivuta sigara na kupulizia moshi juu.









“Sasa tusipotezeane muda. Kuna maswali mawili matatu tu nataka kuyapatia majibu kutoka kwenu. Na natumai mtaonyesha ushirikiano bila kushurutishwa.” Alisema inspekta kisha akaweka kituo kidogo apate kumeza mate.









“Nani aliyewatuma na kawatuma kwa malengo gani?” Swali lilirushwa kwa watuhumiwa. Wanaume wale wawili kabla ya kusema lolote walitizamana kisha wakatabasamu, mmoja akajibu;

“Usipoteze muda wako, inspekta Vitalis Byabata. Hatutosema lolote, tuue tu.”

Inspekta akatabasamu na kutikisa kichwa. “Siwezi kuwaua. Ila mtakachokipitia, ni kheri ya kifo.”







http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Baada ya kusema hayo, inspekta alimtizama Kaguta na kumuelekezea wale watu kwa kichwa. Kaguta akadondosha sigara yake na kuisinya, kisha akawasogelea wanaume wale wawili na kuanza kuwasambazia kipigo kikali.Watuhumiwa wakavujishwa na kumiminwa damu. Walikua nyang’anyang’a kwa kipigo lakini bado hawakutereresha msimamo wao ‘Hatutosema kitu’. Mwishowe Kaguta alichoka. Hata pale inspekta alipompokea, hakufanikiwa, mambo yalikuwa ni yale yale mpaka watuhumiwa wakapoteza fahamu.













“Tuondoke. Tutawarudia baadae hapa mikono yote inaniuma!” Inspekta alishauri.

“Duuh! Kweli. Tuondoke tu.” Kaguta akamuunga mkono.











Ila kabla hawajaondoka, inspekta aliona kitu kiunoni mwa mwanaume mmoja mtuhumiwa. Alisogea akatizama vizuri alichokiona kwa kushusha kidogo suruali ya mlengwa, akaona ‘tattoo’. Ilikuwa ni tattoo ya mtu kivuli. Mtu aliyewasumbua vibaya mno Mtemvu na wenzake. Mtu wa ajabu aliyemaliza familia ya Ali wa Fatuma. Inspekta akaguna. Aliamua kumsogelea mwanaume mwingine akamtizama pia. Akakuta tattoo hiyo hiyo eneo hilo hilo. Hapo inspekta akapata walakini. Haraka waliondoka na Kaguta wakaelekea hospitali mpya walipowaamishia Jombi na Miraji kwa sababu za kiusalama.











Akiwa ameketi kwenye kitanda, Inspekta alishusha kidogo suruali ya Jombi akamtizama kiunoni. La haula! Aliona tattoo ile ile aliyoiona kwa wale watuhumiwa waliowateka nyara. Tattoo ya mtu kivuli; mtu muuaji, mtu mteketezaji!











“Vipi Vitalis, kuna nini?”

Kaguta aliuliza. Alitafuta nafasi naye akakaa juu ya kitanda.

“Hawa watu wanasharetattoo sehemu ya kiunoni…”

“Enhe?”

“Nashindwa kuelewa ina maanisha nini? Ila ni kithibitisho kuwa wapo pamoja.”

Kaguta alisogea karibu akatizama tattoo aliyonayo Jombi kwa macho ya umakini.

“Ina maana gani hii?”

“Sijajua, ila ni lazima itakuwa na maana yake.”









Ukimya fulani ukapita katikati yao. Baada ya muda kidogo walinyanyuka wakaelekea mgahawani kupata chakula. Walijadiliana mambo kadhaa kuhusu kesi yao. Walipomaliza waliagana, Kaguta alishika yake, inspekta Vitalis akaelekea ofisi ya mtaa wa Kilongawima mkononi akiwa na kitambulisho cha kupiga kura cha mmoja wapo wa wale wanaume waliopata kuwaua ufukweni mwa bahari.









“Samahani, naitwa Inpekta Vitalis Byabata.” Inspekta alionyesha kitambulisho kwa mwanaume mzee aiekuwa ameketi kitini, meza ndogo ikiwa mbele yake.

“Karibu, inspekta.”

“Ahsante.”

“Naweza nikakusaidia?”

“Bila shaka. Nimemkuta mwenyekiti?”

“Ndio mimi.”

“Ahsante.”











Inspekta alikiweka kitambulisho cha mpigakura cha mtuhumiwa wake juu ya meza akamsogezea mwenyekiti.









“Kwa mujibu wa maelezo yaliyo kwenye hiko kitambulisho, huyo ni mkazi wako. Kitambulisho hiko kimepatikana kwenye eneo la tukio la uhalifu, ningependa kupata taarifa zaidi juu yake kutoka kwako.”









Mwenyekiti alikitizama kile kitambulisho kwa umakini hasa sehemu za usoni, akasema;

“Ila huyu kijana ni marehemu kwa sasa, inspekta.”

“Najua.” Inspekta alijibu. “Nataka kufahamu wapi anaishi, wazazi wake na shughuli alizokuwa anajihusisha nazo.”







Mwenyekiti alirudia tena kutizama kitambulisho. Alishusha pumzi akasonya kimasikitiko;

“Kuhusu wazazi wake, ni mzazi mmoja tu ndiye amebakia ambaye ni baba. Mama alifariki muda tu. Na huyu kijana alikuwa anafanya shughuli za gym; haya mambo yao ya kupandisha na kushusha mavyuma.”

“Unaweza ukanielekeza nyumbani kwao na wapi hiyo gym ilipo?”

“Halina shaka hilo, ngoja nikupe kijana akupeleke huko mara moja.”









Mwenyekiti alimuita mesenja akampatia melekezo. Inspekta aliongozana na mesenja mpaka mbele ya nyumba moja kubwa kuukuu, walibisha hodi pasiwe na majibu, waliachana napo wakaelekea gym. Huko wakakuta wanaume wanne wakiwa wanapasha misuli.









Ilikuwa ni ndani ya jengo kubwa ambalo halikuonekana kama li tayari kwa ajili ya matumizi. Madirisha yalikuwa amefunikwa na matambaa. Ukutani kulikuwa kumechorwa chorwa matusi na michoro mingine ya ajabu. Watu wawili walikuwa wamelala kwenye mabenchi wakipandisha na kushusha vyuma, mmoja alikuwa akipiga push-up na aliyebakia akiwa anapandisha chuma akipeleka juu na kushusha chini. Ukutani kulikuwa na kitambaa kikubwa kikisomeka…NGOME YA MHARAMIA.











“Habari zenu?” Inspekta alipaza sauti. Wanaume waliokuwa wanapasha misuli waliacha shughuli zao wakamtizama kwa macho makali.







“Naomba niende.” Mesenja alisema kwa sura ya hofu. Kabla hajajibiwa, alikuwa tayari ameshapotea eneo lile.

“Wewe ni nani?”

“Inspekta Vitalis Byabata.”







Wanaume wale walitizamana baada ya kusikia hilo jibu. Ni kama vile macho yao yalitangaza vita.









“Unataka nini?”

“Nina shida na maelezo kadhaa kutoka kwenu.”

“Maelezo gani?”

“Kuhusu huyu mtu.”Inspekta alionyesha kitambulisho cha mpiga kura. Wanaume wale wakatizamana kwa mara nyingine kwa macho yaliyobeba tahadhari.

“Hatumjui!” Alijbu mwanaume alikuwa anapiga push-up. Inspekta alitabasamu kidogo kisha akaketi kwenye moja ya mabenchi yaliyokuwepo. Aliingiza mkono wake mfukoni akatoa pipi na kuirushia mdomoni.

“Awadhi ni rafiki yenu. Alikuwa anafanya hapa mazoezi, mtaa mzima unafahamu. Sijui mnapolikataa hilo mnaamanisha nini na ni kwa malengo gani?” Alinena inspekta huku akimung’unya pipi.

“Awadhi ameshakufa. Unamtakia ya nini?” Aling’aka mwanaume aliyekuwa amejilaza kwenye benchi hapo awali.

“Alikuwa anafanya shughuli gani ya kumuingizia kipato?” Inspekta aliuliza.

“Alikuwa anafanya kazi hapa gym.”

“Basi?”

“Ndio.”

“Kitambulisho hiki kimepatikana eneo la tukio la uhalifu, mna taarifa yoyote juu ya hilo?”

Wanaume walitizamana, mmoja akaropoka; “Hatuna. Hatujui chochote.”

“Mlikuwa hamjui kama rafiki yenu ni mhalifu?”

“Hatujui lolote!”











Inspekta aliona picha za watu zimebandikwa ukutani kwa mbali kidogo tokea eneo alipo. Alinyanyuka akaziendea na kuzitizama kwa umakini. Zilikuwa ni picha mbili za wanaume zikiwa zimeandikwa R.I.P kwa juu yake. Inspekta alinyanyua kitambulisho chake akafananishia picha ya kitambulisho na mojawapo ya zile.









Aliona zaendana. Picha zile zilikuwa ni za mojawapo ya watu waliouwawa kwenye tukio la kukomboa familia ya inspekta. Inspekta akiwa hapo anabung’aa, alisikia mlango unafungwa. Aligeuka akakuta wanaume wale wanne wamesimama mlangoni kama watu waliojiandaa na mapambano.









Inspekta alitoa simu yake mfukoni akaweka pembeni. Alitoa pipi nyingine mfukoni akabugia.











“Miili yote hiyo ni waoga kiasi hiki?”

“Nani muoga? Umeingia kwenye ngome. Hauwezi ukatoka kama ulivyoingia.”

“Hakika siwezi kutoka kama nilivyoingia, nitatoka nikiwa nimewamaliza wote. Kama mnajiamini njoo mmoja mmoja.”











Wanaume walitizamana kama vile wanajiuliza nani apate kutangulia. Mmoja wao alisogea mbele kumfuata inspekta. Alirusha ngumi yake ya kulia kwanguvu zote. Inspekta aliinama ngumi ikavuka kama upepo. Kwanguvu, inspekta alimkandika mwanaume yule konde la kifua chembeni mlengwa akadondokea kando akilalamika kwa maumivu.











Kwa mkupuo wanaume wawili walimfuata inspekta. Haraka inspekta aliinama akanyoosha mguu wake wa kulia na kuupitisha haraka kama feni ikamzoa mwanaume mmoja mpaka chini. Aliyebakia akisimama alinyanyua mguu wake kama mchezaji anayetaka piga shuti mpira, inspekta akawahi kutengua mguu uliosimama kwa kuugonga kwanguvu kwenye ugoko akitumia kisigino kigumu cha kiatu chake.











Haraka mwanaume wa nne alisogea na ngumi nzito imlengayo inspekta. Inspekta kwa upesi zaidi akaipiga teke ngumi ile na mguu wake wa kulia kisha akageuka na kuutumia mguu wake wa kushoto kukabidhi teke matata mno la tumboni akitumia kisigino cha kiatu; mwanaume alilalamika kwa maumivu huku akiyumba.













Ghafla, teke kali lilimpiga inspekta mgongoni likamdondosha. Wanaume wawili walimsogelea haraka, mmoja alimshika nguo akitaka kumnyanyua. Inspekta alivuta chuma kidogo kilichokuwa pembeni akamzaba nacho kwanguvu aliyemshika nguo. Damu ziliruka kama maji wakati mwanaume aliyepigwa chuma akidondoka chini kama mzigo. Akiwa bado yupo chini, inspekta alitumia kilekile chuma, alipiga mguu wa mwanaume wa pili kwanguvu … koooh!











Mwanaume yule alilia kama mtoto mdogo huku akishikilia mguu wake uliopinda. Mwanaume pekee aliyebakia akiwa amesimama akawa mmoja tu. Yule aliyekung’utwa teke la tumbo. Alimsogelea inspekta kisha akarusha teke na mguu wake wa kulia. Inspekta alidaka mguu kisha akausukuma kwa pembeni na kumfanya mwanaume yule azunguke kama pia. Alipokaa usawa wa inspekta, inspekta alimkandika tena teke la tumbo kwa kutumia kisigino cha kiatu. Mwanaume yule akadondoka chini damu zikimtoka mdomoni.











Inspekta alipogeuka nyuma akamkuta mwanaume aliyemkata mtama anaamka. Alimtizama mwanaume yule kwa jicho kali. Alimtishia kama anamfuata, yule mwanaume akarukia nje kwa kupitia dirisha lililo wazi na kutokomea. Inspekta alitikisa kichwa akatabasamu. Aliwatizama wanaume watatu waliobakia akawaona wote wapo chini wakiugulia kasoro mmoja aliyepigwa ngumi ya chembe, yeye alikuwa kimya tuli macho yamefumba.













Inspekta alisogea akamtizama mwanaume yule aliyetulia. Alipandisha body yake aliyoivaa akamtizama kiunoni akaona ile tattoo. Alifuata simu yake akapiga polisi, ndani ya muda mchache polisi wakafika na defender mbili. Wanaume wale watatu wakatiwa ndani ya gari polisi wakatokomea.







Kagiza chepesi kalikamata anga. Mataa ya nyumba mbalimbali yaliwashwa na kumetameta. Ila pembezoni kidogo mwa mji kwenye jumba walilofungiwa watuhumiwa lilikuwa ni kiza. Hakukuwa na taa. Giza lilikuwa totoro kama vile ni saa nane ya usiku. Mara ghafla taa kubwa iliwaka na kuwamulika watuhumiwa.











Hapo ikaonekana hawakuwa wawili tena kama hapo mwanzo, waliongezeka wanaume watatu wale waliokamatwa kwenye gym. Wote walikuwa wamefungwa kamba zikiwashikiza kwenye mistimu. Walikuwa wameinamisha macho yao chini huku wakikunja sura kutokana na mwanga mkali kuwapiga nyusoni.











“Mtasema hamsemi?” Sauti ya inspekta ilisikika lakini haikujulikana wapi imetokea.

“Najua mnaomba niwaue ila kama nilivyowaahidi, hamtokufa. Ila mtakachopitia ni kheri ya kifo. Hamtokula kwa muda wote mtakaokuwepo hapa. Chakula chenu kitakuwa ni kilio na maumivu. Kushiba kwenu itakuwa kuzirai.”









Baada ya kauli hiyo, vishindo vya miguu vilisikika. Inspekta alitokea akiwa na plies mkononi, nyuma yake aliongozana na Kaguta ama ‘The red bullet’ yeye akiwa amebebelea gongo kubwa mkono wake wa kulia. Walimsogelea mtu wa kwanza ambaye alikuwa ni mpya huku wakiwa wameipa migongo mwanga mkali umulikao.











“Ni nani mnayemfanyia kazi?”









Inspekta alimuuliza mtu aliye mbele yake huku akimsaidia kwa kumkingia mwanga na mgongo wake.

“Simfanyii kazi mtu yeyote.”











Inspekta alitabasamu baada ya kusikia hiyo kauli. Aliupisha mwanga ukammulika mwanaume yule usoni.









“Nilitegemea jibu la aina hiyo.” Inspekta alisema. Baada ya hapo kilifuata kilio kikali cha uchungu. Kaguta alimpiga mwanaume yule na gongo sehemu ya goti. Kama vile haitoshi, alimpiga zaidi na zaidi. Mwanaume yule alipiga kelele mno. Ni pale tu inspekta aliposema basi, Kaguta akaacha kuadhibu.







“Vipi, upo tayari kusema au tuhamie upande wa pili?”











Inspekta aliuliza. Mwanaume yule alikuwa analia kama mtoto achomwaye sindano. Makamasi na machozi vyote vilimtiririka.









“Tuhamia upande mwingine?”

“Hapanaaa!” Mwanaume alilia.

“Basi nijibu swali langu.”

“Naogopaa…siwezi!”

“Kwanini huwezi?”









Mwanaume yule alikaa kimya kwanza akipiga kwikwi na kuvuta makamasi. Inspekta alirudia kuuliza swali. Mwanaume yule akamjibu;

“Naogope. Kama nikikuambia nitauwawa.”

“Nani atakuua na upo hapa na sisi?”

“Kuna mtu atakuja kuniua.”

“Nani?”









Mwanaume yule hakusema tena kitu baada ya hapo zaidi tu ya kulia. Inspekta alimruhusu Kaguta aendelee na kazi yake ya kutwanga goti la pili, Kaguta alipopiga goti mara moja kwanguvu, mwanaume yule alipiga kelele kali mno;

“Nasemaaa…uuuuwii…nasemaaa!”













Uso wake ulieleza ni maumivu ya aina gani anayopitia. Hata kama angeachwa aondoke zake, alikuwa tayari ameshapata ukilema.

“Naogopa, nikisema nitauwawa! Naogopa jamani! Naumiaaa!”

“Unamuogopa nanii?”

“Tulikula kiapo cha damu. Hakuna yeyote anayeweza sema chochote. kama ukikiuka, damu yako itafuatwa popote ilipo. Huwezi ukakimbia wala huwezi kujificha.”

“Oooh sawa. Basi tutaendelea kutwanga huo mguu mpaka utakapo kiri. Kaguta, fanya kazi yako.”











Kabla Kaguta hajafikisha gongo kwenye goti, mwanaume yule alipayuka;

“Nasema…nasemaaa! Tunamfanyia kazi Mr Kim. Yeye ndiye anatulisha kutuvisha na kutupa chochote tunachotaka.”

“Mr Kim? … Yupi?”

“Mr Kim Salvatore; mfanyabiashara.”

“Mr Kim from Bermuda?”

“Ndio!”











Mwanaume huyo aliposema tu hayo, wenzake walipaza sauti kumshtumu. Walimtukana na kumuita mwanamke; amekiuka masharti na punde roho zao zitafuatwa.







“Tusamehe sio sisi! Tusamehee!” wanaume wale walilia. Inspekta na Kaguta walishangazwa na hilo.













Haukupita muda, mwanaume yule aliyefungua mdomo kusema alianza kulalamika anaungua. Alihangaika kutaka kujinasua lakini hakuweza. Alilalamika anaungua kiunoni moto unapandisha kwa juu. Inspekta alimvua suruali akiwa anatafuta huo moto upo wapi. Hamaki! Aliona tattoo inavuja damu.





http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Kaguta, unaona?” Inspekta aliduwaa huku akionyeshea tattoo ile ivujayo damu. Kaguta alishangaa. Wakati huo bado yule mtu akilalamika anaungua mwili mzima sasa.











Ghafla, taa ilizima. Iliwaka ikazima tena. Iliwaka na kuzima, iliwaka na kuzima. Ilipowaka, mwanga haukuwa tena mweupe bali mwekundu kama damu. Kaguta alimtizama inspekta kwa macho ya mshangao. Wanaume wale kazi yao ilikuwa ni kulia tu huku wakiomba msamaha.











Punde katika mwanga ule mwekundu kilionekana kivuli cha mtu. Alikuwa na kichwa kikubwa kikiwa na vitu kama viluwiluwi vikichezacheza. Vidole vyake vilikuwa virefu na vyenye ncha kali. Na macho yalikuwa mekundu mno. Pap! Taa ilikata mwanga. Pap! Mwanga ukarudi, mwanaume yule aliyefungua mdomo wake alikuwa tayari ameshauwawa. Shingo yake ilikuwa inachuruza damu kama bomba la maji.











“Mungu wangu!”











Alitahamaki inspekta. Yeye na Kaguta walikuwa wametoa macho kama vile madunguri.











Pap! Taa ilikata tena. Mwanga uliporudi, mtu wa pili akawa tayari naye ameshaenda. Shingo yake ilikuwa inamwaga damu. Walibakia wanaume watatu wakiwa wamefungwa. Wote walikuwa wanalia kwa hofu ya kifo.











Tap! Taa ikazima na kuwaka, ikazima na kuwaka. Watu wawili wakaenda na kifo kilekile. Taa ilipozima tena, haraka inspekta aliwasha tochi na kummulikia mwanaume aliyebaki. Ajabu, hakukuwa na kitu kilichotokea.









“Tuondoke hapa! Tuondoke Vitalis!” Kaguta alinasihi.

“Ngoja kidogo.” Inspekta alijibu; macho yalikuwa yamewatoka huku wakihema pumzi yenye hofu.











Taratibu inspekta alianza kusogea akimfuata mwanaume aliyebaki huku akimmulika na mwanga wa tochi yake. Miguu ya inspekta ilikuwa inatetemeka lakini bado alisonga. Kaguta alibaki nyuma, hakutaka kusoea popote, alikuwa tayari ameshakaa kando na mlango.









Inspekta alimfikia yule mwanaume akamuona anavuja damu maeneo ya kiunoni. Lakini zaidi ya yote kulikuwa kama kuna kitu kinahangaika. Mwanaume yule alikuwa anapiga kelele za maumivu. Inspekta alishusha suruali ya mwanaume yule akaona kitu cha ajabu. Ilikuwa ni mtu si mtu, dubwana si dubwana likihangaika kutaka kutoka ndani ya tattoo. Inspekta alishtuka mno. Tochi ilimponyoka ikadondokea chini na kuzima papo hapo.











Inspekta alipapasa papasa kutafuta tochi. Alipoipata aliiwasha kummulika mwanaume yule mtuhumiwa. Akamkuta ameshauwawa. Shingo yake ilikuwa tayari imeshafyekwa. Na papo hapo taa kubwa iliwaka kama hapo mwanzoni. Inspekta alipepesa macho yake kumtafuta Kaguta, lakini hakuonekana.











“Kagutaa! Kagutaa!”













Inspekta aliita lakini hakukuwa na majibu zaidi tu ya mwangwi kumrudia. Pap! Taa kubwa ilizima. Ilipowaka, Inspekta hakuonekana. Chumba hakikuwa na mtu yeyote. Kilikuwa tupu na taa peke yake.











Ni huko nje ndipo inspekta alipoonekana akiwa anatizama tizama huku na huko kama mtu anayetafuta njia. Kwa mbali kidogo aliona taa za gari zimewaka, alikimbilia eneo hilo akiwa na uso wa hamu ya kufahamu. Aliposogea karibu zaidi, aligundua ni gari la Kaguta.











“Kaguta!”

Inspekta aliita.

“Ingia ndani tuondoke. Haraka!” Sauti ya Kaguta iliamuru. Inspekta aliingia ndani, gari likaondoshwa kwa kasi mno vumbi tu likitimka.

“Uliondoka saa ngapi mbona sikukuona?” Inspekta aliuliza.

“Niliona huna mpango wa kuondoka, mimi nikaondoka zangu. Taa ilikuwa imezima ndio mana hukuniona.”

“Ulintisha ujue. Mie nikajua umebebwa na lile jitu!”

“Wewe ndo’ ulikuwa unantisha. Nakuambia tuondoke hutaki, nikajua ushaingiliwa.”





“Hapana. Kuna kitu niligundua, yule mtu alikuwa anajitokeza pale tu taa ilipozima. Uliona nilivyowasha tochi hakuonekana!”

“Sikuona. Labda tayari nilikuwa nishaondoka.”

“Labda. Huwezi amini zile tattoo walizochora si tu ni tattoo, bali ndio jitu lenyewe. Na hata Jombi anayo, sidhani kama ataweza kusema yale nitakayomuuliza.”

“Mmmh ngoma nzito! … ila, mbona lile jitu halikutumaliza sisi? Au ni bahati tu?”

“Hapana. Hatukuwa tu kwenye ratiba yake. Si unakumbuka wale wengine walianza kulia baada ya mwenzao kuongea?”

“Yap!”

“Ni kiapo wamekula. Tena kiapo cha damu.”

“Sasa kweli tutaweza kupambana nao?”

“Naamini kila kitu kina njia. Ila kupambana na lile jitu inabidi utumie akili mara mbili zaidi ya kawaida. Na kuna kitu chanishangaza, nashindwa kuelewa”

“Na vipi kuhusu Mr Kim?”

“Mmmh hapo ndipo kazi ilipo. Mr Kim ni mfanyabiashara mkubwa mno na anayeheshimika mpaka na serikali, ila sikuwahi kufikiria kama anaweza kujihusisha na mambo ya kidhalimu kama haya. Ila ninachotaka kukifahamu hasa ni kwanini Mr Kim yupo nyuma ya hili kundi, na ana kipi cha kuhusika na vifo vya Mtemvu na wenzake kwani kijana wake ni mmoja wa watu waliokuwa wanashughulikia hilo na bila shaka alikuwa anapata silaha toka kwenye kundi lake hili.”

“Sasa tutampatia wapi Mr Kim?”

“Ni ngumu sana kumpata Mr Kim. Si mtu wa kuonana naye hivi hivi. Cha kufanya inabidi tutafute sababu ya kufanya akutane nasi. Na Kuanzia sasa tuwe karibu na ratiba yake.”

“Sawa. Sasa? Mimi napitia bar mara moja nikastue. Siwezi nikalala hivi hivi.”

“Umeanza!”

“Nini sasa? Kwani nimefanya dhambi gani? Siwezi kulala kusema ukweli kama sijastua maana kile nilichokiona si kheri kabisa.”











Gari lilipaki kwenye bar kubwa. Kaguta pamoja na Inspekta walishuka na kufuata viti virefu vilivyokuwa vimeketi pembezoni mwa kaunta iliyokuwa imejaa kila aina ya vinywaji kuanzia maji, bia mpaka mvinyo na whisky. Kaguta aliagiza chupa ndogo ya Jack Daniels wakati inspekta akiagiza maji makubwa ya Kilimanjaro. Kila mmoja alipiga pafu moja, soga zikatwaa nafasi;











“Kwahiyo mke na watoto wako wapo wapi kwa sasa?”

“Nyumbani. Sema ni nyumba nyingine, niliwahamisha kule kwa usalama.”

“Unalala nao?”

“Ndio. Siwezi nikalala mbali nao. Hapa tu yenyewe nahofia huko walipo.”

“Pole. Usihofu Mungu yu nao. Kwani vipi haukuomba wapewe ulinzi?”

“Niliomba. Wapo polisi wawili hapo nyumbani ila bado siwezi nikajiamini kihivyo.”

“Usiogope rafiki. Kila kitu kitakuwa sawa.”









Waliendelea kunywa taratibu vinywaji vyao huku macho yao yakitizama wahudumu warembo waliokuwa wanakatiza hapa na pale. Kwa mara kadhaa walikuwa wanatekwa na runinga kubwa iliyokuwa inaonyesha mpira lakini hawakuonekana kuvutiwa sana na hilo, ni pale tu makelele ya watu wanaoshangilia yalipowika ndipo Kaguta na inspekta wakarushia macho yao kideoni kutizama kinachojiri.











Baada ya nusu saa inspekta akiwa kabakisha kiasi kidogo cha maji kwenye chupa yake, alinyanyuka akatoa pesa mfukoni mwake na kumkabidhi mwanamke aliyekuwa amejaa tele kaunta akihudumia.











“Ahsante dada.” Inspekta alisema kisha akamtizama Kaguta aliyekuwa bado ameketi asionekanehata na dalili ya kuondoka.

“Tuondoke, baba.”

“Mapema hii, mie siendi popote.”









Kaguta alisema kisha akamtizama mdada wa kaunta na kumkonyeza. Mdada alitabasamu akasogeza glasi kubwa mezani na kuimiminia kinywaji cha Jack Daniels.











“Hiyo glasi ya nani?” Inspekta alitahamaki.

“Yangu!” Kaguta alijibu na kuongezea, “Ngoja basi nimalizie hii alafu tuondoke.”

“Dah! Aisee.” Inspekta aliduwaa. “Kama unataka nikae kukusubiria unywe na hiyo, tukubaliane gari naendesha mimi.”

“Sawa. Haina shida. Utaendesha tu.”









Kaguta alimgeukia mdada wa kaunta akalamba lips zake na kurembua kidogo macho yake mekundu yaliyolowea kileo.











“Njoo basi kwa hapa.” Alisema Kaguta huku akionyeshea kiti kirefu cha pembeni yake. Mdada alitabasamu akasogeza glasi kwa Kaguta akisema;

“Nakuja.”









Alimuita mwenzake akamuomba asimamie kuuza vinywaji. Alitoka akaungana na Kaguta kwenye kiti alichoelekezwa. Inspekta alitikisa kichwa chake akanong’ona;

“Unafanya nini sasa, Kaguta?”









Kaguta alitoa ishara ya kumtaka inspekta atulie. Inspekta bila kuleta zogo alitulia. Wakati anasubiria, aliamua aagize kinnywaji laini kuvutia subira.









“Niambie mrembo.”

“Safi tu nakus’kiliza wewe.”

“Unaitwa nani?”

“Naitwa Bhoke.”

“Unatumia kinywaji gani mtoto?”

“Safari lager.”

“Agiza basi.”











Bhoke alimtizama mwenzake na kumtikisia kichwa. Mwenzake aliyekuwa kaunta alipangua safari mbili baridi toka kwenye jokofu akazifungua na kumpatia Bhoke. Taratibu Bhoke alianza kupanda mlima huku akiwa anapiga simulizi na Kaguta. Kaguta alikuwa anaongea kwa taratibu na macho yake yalikuwa yanatizama kifua cha Bhoke kilichojaa pamoja na miguu yake meupe iliyochomoza toka kwenye sketi fupi nyeusi aliyovaa.













“Umependeza kweli.”

“Aaah wapi na uniform?”

“Ndio. Kwani haiwezekani?”

“Sidhani.”

“Basi wacha nirekebishe kauli. Wewe ni mzuri, Bhoke.”

“Ahsante sana.”









Bhoke alitabasamu na kupeleka bia yake mdomoni akagida mafundo kadhaa.











“Vipi tunaweza tukaenda wote home?”

“Home mapema yote hii? Mbona una haraka?”

“Usiku mrefu mama. Nipo mpweke kazi kujigeuzia huku na kule, kitanda kikubwa.”

Bhoke alitabasamu tena; “Wewe una vituko kweli.”

Kaguta alimiminia kinywaji chake mdomoni, alipokiweka chini alifungua kinywa;

“Ni kweli ninayokuambia. Sasa mrembo, utaenda nami angalau usiku wangu leo ukawe wa kumbukumbu?”

“Naweza nikaenda nawe ila nitaachaje ofisi sasa?”

“Si kuna mtu mwingine anakaimu nafasi yako.”

“Hapana, ni zamu yangu hii nastahili kuwa hapo. Na pia kuna bosi, naye akisikia sipo ataleta matatizo.”







Bhoke alimwaga maelezo. Kaguta alitikisa kichwa akanywa fundo moja la ukweli. Aliingiza mkono wake mfukoni akatoa elfu kumi kumi kadhaa nyingi na kuzitupia mezani.











“Mpe bosi wako hiyo, mwenzako wa kukushikia zamu na wewe.”







Bhoke aliwahi kuchukua pesa na kuziweka kwenye sidiria yake.









“Sasa tunaondoka wote?” Kaguta aliuliza.

“Ndio. Nisubirie basi nikawape pesa zao tuondoke.” Bhoke alisema kisha akanyanyuka na kwenda. Kaguta akamsindikiza mwanadada na macho yaliyonawiri tamaa. Aligeuka kutizama nyuma yake alipokuwa amekaa inspekta, hakuona kitu. Alirusha macho yake huku na huko ndani ya bar kumtafuta inspekta lakini hakukuwa na sehemu alipoonekana.



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Inspekta alikuwa yupo ndani ya gari kwenye kiti cha dereva akiwa amelala. Vioo vilikuwa vimepandishwa na ndani redio ilikuwa inapiga muziki kwa sauti ya chini.









Inspekta aligutuka toka usingizini aliposikia gari latikisika. Aliporusha macho yake nje alimuona Kaguta pamoja na Bhoke wakiwa wamesimama mlangoni mwa gari. Alifungua lock ya milango, Kaguta na Bhoke wakaingia kukaa viti vya nyuma. Inspekta aliwatizama kwa kupitia kioo kilichokaa juu yake akawaona wanatomasana na kupapasana. Alitikisa kichwa akaliondoa gari.









Ndani ya dakika ishirini, inspekta alishafika sehemu anaposhukia. Alizima gari akamkabidhi funguo Kaguta. Aliaga na kushika njia nyembamba isiyopitika na gari. Haikupita napo muda mrefu, Kaguta aliliondoa gari kuelekea kwake akiwa na mrembo wake aliyemnasibu toka bar.











Baada ya sekunde chache tangu Kaguta aondoke eneo aliposhukia inspekta, pikipiki kubwa ilisogea eneo hilo ikiwa imebebelea wanaume wawili waliovalia kofia ngumu nyeusi za pikipikina suti za jeans. Mwanaume aliyekuwa ameketi nyuma alitoa simu yake mfukoni akavua kofia yake na kupiga huku akishuka.







“Yes boss … ameshashuka … sawa … haina shida mkuu.”











Simu ilikata. Mwanaume yule alimtizama mwenzake na kutikisiana vichwa kisha akashika njia ile ile nyembamba aliyoenendea inspekta.



Inspekta alitembea kwa taratibu akielekea nyumbani kwake. Hatua zake zilikuwa ni ndogo ndogo na vishindo vyake vya miguu ndivyo pekee vilikuwa vinasikika. Ilibakia hatua chache kumaliza safari yake fupi. Alitoa simu yake mfukoni baada ya kusikia inatetemeka, alikuwa ni mke wake anapiga. Alipokea kisha akaiweka sikioni.







“Nakuja mama, ndio nipo hapa kwa nje.”











Alisema inspekta kisha akakata. Ila ghafla wakati anarudisha simu yake mfukoni, alisikia sauti kama ya majani makavu yakikanyagwa.Alisimama akatizama nyuma lakini hakuona kitu. Alirudi hatua kadhaa chache nyuma huku akitizama lakini hakuna kilichoonekana. Alisonya akaendelea na safari yake ya kuelekea nyumbani.











Kwa nyuma, kulikuwa na mtu anamfuatilia inspekta. Alikuwa ni yule yule mwanaume aliyekuja na pikipiki akaongea na simu.Mwendo wake ulikuwa ni wataratibu akikanyaga chini kwa ustaarabu wa hali ya juu huku macho yake yakiwa yanatizama mbele alipokuwa anamuona inspekta akitembea.









Baada ya inspekta kuingia ndani ya nyumba yake, mwanaume yule aliyekuwa anamfuatilia alirudi pale alipomuacha mwenzake na pikipiki. Walipeana ishara ya dole gumba kisha wakapotea lile eneo.









***







Ni ndani ya nyumba kubwa kuukuu ya wazazi wake bwana Awadhi, mwanaume aliyepatikana na kitambulisho cha mpiga kura eneo la tukio, ndipo alipokuwepo inspekta akiwa ameketi kando kando na baba yake marehemualiyekuwa amejilaza juu ya kitanda duni. Baba alikuwa amevaa shuka alilolivuta mpaka kifuani. Hali yake haikuonyesha kuridhisha; alikuwa mwembamba kupindukia, mdomo wake ulikuwa kama uliopakwa chaki na uso wake ulikuwa ni wa kukomaa huku mifupa ya mashavu ikiwa imemsimama. Alitema mate mazito pembeni akamtizama inspekta na macho yake yaliyo hoi.









“Sikuwa na jinsi. Japokuwa nilimkana sana Awadhi kujihusisha na hilo kundi, sikufanikiwa kabisa. Bado alikuwa mbishi mno na hiki kifo chake ni kitu nilichokitegemea, ila sikudhani kama ingekuwa mapema hivi. Nilidhani ningelitangulia mimi kwanza.” Baba alisema kwa sauti ya chini. Alikohoa mara tatu akatema tena mate pembeni.









“Umeiona hiyo nyumba ndogo hapo nje?” Baba aliuliza.

“Ndio. Nimeiona mzee.”

“Hiyo nyumba ndiyo tulikuwa tunaishi mimi na familia yangu. Hii unayoiona kwa sasa, aliijenga Awadhi kwa pesa za biashara zake ambazo sikupata kufahamu ni zipi. Aliisusa hii nyumba bila kuimalizia kwasababu ya kuona napinga mambo ayafanyanyo na ndio maana unaona ipo hivi.”

“Na vipi kuhusu afya yako mzee. Nini hasa kinakusumbua?”









Baba alitulia kwa muda kidogo kama mtu anayewaza jambo. Alinyanyua mkono wake mwembamba akajikuna kichwa na kifua chake kigumu.









“Sijui naumwa nini. Napukutika, sina nguvu, sina hamu ya kula wala kunywa. Hali yangu inakuwa mbaya kila uchwao muda si mwingi nitamfuata mke wangu huko aliko.”

“Umewahi kwenda hospitali kujua nini shida?”

“Hapana. Hamna haja ya kwenda huko.”

“Kwanini?”

“Mimi na mke wangu tulikuwa na afya njema kama watu wengine. Shughuli yangu ya kuniingizia kipato ilikuwa ni uvuvi, japokuwa haikuwa inakidhi kila haja yangu, lakini hatukukosa cha kula wa kunywa. Mambo yalikuja kubadilika pale tu siku moja tulipojaribu kumzuia Awadhi asiende kwenye shughuli zake kama wazazi wake. Tulifunga milango na kumkalisha kitako. Lakini ajabu, palitokea na jitu kubwa jeusi.









Lilimnyanyua mke wangu na kumtupia hukoo! Nilipojaribu kumsogelea alininyanyua bila kunishika akanibamizia ukutani. Kabla hatujanyanyuka, alituonyeshea mikono yake vumbi jeusi likatoka na kutuvamia. Tulikohoa mno kwa kupaliwa. Sikuona kingine zaidi tu ya kusikia sauti ya Awadhi ikimtaka jitu lile liache anachokifanya. Pale macho yangu yalipokuja kuona, hakukuwa na mwingine zaidi ya Awadhi. Nilijitahidi kunyanyuka lakini sikuweza. Miguu haikuwa na nguvu kabisa. Mpaka leo sijawahi pata ahueni.”









Wakati baba anamaliza kuongea hayo machozi yalimtiririka. Inspekta alitikisa kichwa chake kwa huzuni akampa pole.









“Lakini mzee, unamjua ni nani anayehusika na kufadhili hawa wakina Awadhi?”

“Mmmh hapana, sifahamu kabisa. Nimejaribu sana kumpeleleza Awadhi lakini hakuwahi kusema hata mara moja nani ndiye mkuu wao. Aliishia tu kusema hayanihusu.”

“Na je ulishawahi kusikia kwa mtu mwingine yoyote labda kuhusu mtu anayewafadhili?”

“Hapana. Imekuwa ni siri sana. Sijawahi kusikia hata tetesi.”









Kabla ya inspekta hajaongeza neno lingine, simu yake iliita. Aliitoa simu yake mfukoni akaitizama na kuona ni mkewe ndiye anapiga. Alibofya kitufe akaweka simu sikioni.











“Haloo … eeh … wageni? … wageni gani? … wanasemaje? … haya nakuja … sawa nitawahi.” Inspekta alirudisha simu yake mfukoni na kumtizama baba Awadhi.

“Mzee naomba niende. Nitakuja siku nyingine. Nashukuru sana kwa ushirikiano wako.”

“Karibu sana, inspekta. Naomba ukitoka, hapo nje uniitie Swaumu, yule binti uliyenikuta naye.”

“Sawa, mzee.”









Inspekta aliaga akaondoka zake baada ya kutimiza kile alichoelekezwa na baba Awadhi. Alipanda daladala na aliposhuka alichukua pikipiki apate kuwahi. Alipofika kwenye uwanja wa nyumba yake alishuhudiaalama za tairi ya pikipiki kwenye mchanga. Aichuchuma akatizama vizuri alama zile ambazo kwa mbele kidogo zilionekana kuserereka. Alizipuuzia alama hizo akanyanyuka na kuuelekea mlango wa sebule.











Hapo napo alitulia kidogo akatizama viatu. Kulikuwa na viatu pea mbili tu; vya kike na vya mtoto wa kiume. Inspekta alionekana kama mtu mwenye shaka. Alifungua mlango akaingia ndani lakini hakukuta mtu yeyote. Alitizama chini sakafuni akaona matone ya damu. Macho yakamtoka ilihali na mdomo ukaachama kwa bumbuwazi.







“Mama Joons!”















Inspekta aliita. Haraka alikimbilia chumbani huko akakuta mwili wa mkewe pamoja na wa mtoto wake ikiwa imelala chini palipotapakaa damu, vichwa vikiwa vimekatwa na kuwekwa pembeni. Inspekta alihamaki akashika mdomo wake kwa kuduwaa. Alipiga magoti pembeni ya miili ya familia yake. Aliita na kuita lakini ilikuwa bure kwani watu walikuwa wafu.











Baada ya muda akiwa analia, inspekta alitazama pembeni akaona bahasha ya barua. Aliivuta akaitizama kwa kuigeuza akaona maandishi yakisomeka; To you, Inspekta Vitalis Byabata. Alichana bahasha ndani akakuta ujumbe;









Kwako, mpuuzi inspekta.











Barua hii haina kichwa cha habari. Ila kuja kwake imegharimu vichwa viwilivya familia yako.











Tunataka kukupasha habari kwamba, mbio unazozianza kushindana nasi hujui wapi zitakupeleka. Refa ni wa kwetu na barabara pia.











Kichwa kimoja baada ya kingine kitapotea kwa yeyote yule atakayekuwa karibu nawe. Kama unapenda marafiki na majamaa zako, acha mara moja kutufuatilia.









Wako mchinjaji.











Barua ikakomea hapo. Inspekta aliichana chana kwa hasira akatupia vipande huko na kuendelea kulia.





Wiki moja ilipita.









Inspekta alikuwa ameketi kwenye kiti kirefu cha bar akinywa mvinyo kwa mtindo wa tarumbeta. Macho yake yalikuwa mekundu na ni kama vile alikuwa amezama kwenye lindi la fikra. Alimaliza chupa nzima, akaagiza chupa nyingine, nayo akamaliza yote. Akiwa anakunywa chupa ya tatu, Kaguta alitokea eneo hilo akaungana naye.













“Aisee, Vitalis, haya madude yatakugarimu. Acha kuyaendekeza sana, unadhani hii ni suluhisho?”









Kimya. Inspekta alipeleka mdomo wa chupa kinywani akapiga mafundo kadhaa. Kaguta alimpokonya inspekta chupa akaiweka kando.













“Hapana, inatosha.”











Kaguta alimgeukia dada muuzaji akamuuliza;

“Dada amekunywa ngapi huyu?”

“Mbili, hiyo ya tatu.”











Kaguta akatahamaki. Alinyanyuka akalipia kisha akamnyanyua inspekta na kumburuta kwenda ndani ya gari.Moja kwa moja walielekea nyumbani kwa inspekta, inspekta akajilaza kwenye kochi. Kaguta aliwasha runinga akawa anatizama.











“Ni wakati wa kutulia huu ndugu yangu. Najua una mawazo sana, ila yasiwe kigezo kwako kulowea kwenye ulevi.”













Kaguta alitema cheche. Inspekta hakusema jambo. Alikuwa ametulia kimya tu. Ghafla, aliamka akaketi kitako huku akitoa macho yake.













“Vipi!” Kaguta alishangaa.

“Barua!”

“Barua imefanya nini?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/













Inspekta hakujibu. Haraka aliinuka akaelekea kufuata dustbin yake na kuanza kuokoteza vipande vya barua alivyovichana chana. Alivikusanya vyote akarudi sebuleni na kuviweka juu ya meza. Akawa anavitizama kwa umakini zaidivile vipande vilivyounda bahasha kuliko vile vya barua.











Baada ya muda aligundua jambo.













“Kaguta. Embu sogea karibu.” Inspekta aliita. Kaguta alisonga karibu na kutizama vipande vya bahasha alivyovipanga inspekta. Akafungua kinywa;











“Haya si maandishi? Au macho yangu?”

“Ndio. Umeona yameandikwa nini? Mimi sikuyaona kabisa.”

“Rosemath Stationary.” Kaguta alisoma maneno yale huku akiyafuatisha na kidole kisha wakatizamana na inspekta kwa macho yaliyobebelea kiulizo.

“Ndio nini?” Kaguta aliuliza.

“Hii bahasha ilikuwa imebebelea ujumbe nilioachiwa na wauaji siku waliyomuua mke wangu na mwanangu. Hii stationary itatusaidia kuwapata.”

“Una uhakika gani tukiipata hiyo stationary tutawapata?”

“Kuipata hii stationary ni hatua ya kwanza kuwatia nguvuni. Amini hivyo.”

“Sawa. Kwahiyo tunaenda kuitafuta saa ngapi?”

“Saa hii.”

“Acha masihara wewe! Na ulivyo chakari hivyo, uende na nani?”

“Nani kakuambia nipo chakari?”

“Kwani mpaka niambiwe. Si naliona mwenyewe hapo. Pumzika tutafanya hiyo kazi kesho.”

“Hapana! Hapana Kaguta! Siwezi nikakaa hapa bila ya kufanya lolote. Roho ya mke wangu na mwanangu inanidai.”

“Basi fanya hivi. We pumzika, acha mimi niende.”

“Uende mwenyewe? Hapana!”

“Acha ubishi basi ndugu yangu. Huniamini?”

“Nakuamini.”

“Sasa shida nini? … Acha niende. Wewe pumzika, nitakuletea feedback.”









Inspekta hakutia neno lakini uso wake ulionyesha kama vile hakuridhika pamoja kwamba ulisadifu uchovu wa kilevi.













Kaguta alisimama na kuaga akaelekea kwenye gari lake. Aliwasha gari na redio juu. Huku mziki ukitwanga alipata kujongea kwenda aelekeapo. Ndani ya dakika chache, alikuwa tayari ameshafika eneo la Rosemath stationary; jengo kubwa jeupe lenye kuta na milango ya vioo. Kaguta alishuka akatengenezea vizuri koti lake na kuingia ndani baada ya kusukuma mlango wa kioo.













Ndani ya jengo la Rosemath stationary kulikuwa kumetapakaa hali ya hewa ya kiyoyozi. Wahudumu walikuwa watatu wote wakiwa wanawake warembo waliovalia sare za makoti meusi na suruali za vitambaa. Mashine za kuchapisha na kufyatulia kopi zilikuwa zimejaa zikirandana na tanakilishi mpakato na zile za mezani. Kwenye ukuta, kulikuwana runinga kubwa isiyo na kisogo ikionyesha video za miziki mbalimbali.











Kaguta alisogelea mezani akakaribishwa na tabasamu pana la mwanadada;

“Karibu.”

“Ahsante.”









Kaguta alirusha macho yake kutizama huku na kule juu ya mashelvu huku aking’ata lips yake. Aliporudisha macho yake kwa mhudumu alitabasamu akauliza;

“Kama vile nimewahi kukuona sehemu?”

Mwanadada alitabasamu na kubinua mdomo wake.

“Wapi?”

“Maeneo ya Mwenge.”

“Mwenge kwa nyuma hivi kwenye mwamvuli?”

“Ndio.”

“Labda, huwa napandia daladala hapo asubuhi.”

“Unapanda daladala? Aaah bwana ofisi yote hii?”

“Ha ha ha! Kwani ya kwangu? Si nimeajiriwa tu hapa.” Mhudumu alisema kwa sauti yake nyororo. Mteja mwingine aliingia na kuelekea mahali alipo Kaguta na mhudumu.











Mhudumu alisogea kidogo kumsikiliza. Kaguta alipepesa macho yake kwa chini akaona kibandiko kidogo chenye kipini kikiwa kimeandikwa Sandra. Kilikuwa ni kibandiko cha kuweka kifuani kwa ajili ya kujitambulisha kwa wahudumu. Kaguta alitabasamu akatoa ulimi wake nje na kujilamba kisha akakaa tenge kumngojea mhudumu amrudie baada ya kumaliza kumuhudumia mteja aliyeingia karibuni.











“Kwani huwa unakuja saa ngapi kazini niwe nakupitia?” Kaguta alimpokea mhudumu kwa swali. Mhudumu alitabasamu akatengenezea nywele zake ndefu zisimkere.

“Wala! Nashukuru sana.”

“Karibu, Sandra.”









Mhudumu alitoa macho kumtazama Kaguta; “Umejuaje jina langu?”









Kaguta alitabasamu akatikisa kichwa kama vile mtu anayesikitia jambo. Alilamba lips zake akamtizama mhudumu machoni.









“Si nilikuambia nakujua. Wewe ndio hunijui. Anyway, naomba unitolee kopi kitambulisho changu hiki nataka nikasajili line.”











Kaguta alitoa kitambulisho cha mpiga kura pamoja na elfu kumi akamkabidhi Sandra.

“Kutoa kopi shingapi?”

“Mia mbili tu.”

“Haya nitolee basi kopi mbili.”









Sandra alifuata mashine ya kutolea kopi akaweka kitambulisho cha Kaguta na kuamrisha mashine ifanye kazi. Kaguta alimtizama Sandra kwa macho ya matamanio. Sandra alikuwa na mvuto, si tu wa sura bali wa umbo pia. Nyonga zake zilikuwa nyembamba wakati mapaja yake yakiwa ya kujaa na mwenye kalio la wastani. Alipomaliza kutoa kopi, alimrudia Kaguta akiwa kashikilia chenji mkononi.













“Hii hapa.” Sandra alitoa kopi pamoja na kitambulisho. Baada ya hapo akatoa na chenji.











“Hapana! Utakunywa soda hiyo.” Kaguta alimwambia Sandra. Kabla Sandra hajatia neno, Kaguta alikuwa tayari ameshatoka ndani ya jengo. Alifuata gari lake akajiweka ndani akatizama jengo la Rosemath kwa muda kidogo kisha akapotea eneo lile.



Akiwa amejitanda khanga, mama Miraji alikuwa ameketi kwa utulivu juu ya kitanda pamoja na mwanae mkubwa wa kiume asiye na fahamu.







Umbali wa hatua chache tu alikuwa amejilaza Jombi. Hakuonekana tofauti na Miraji kwa kutulia kama maji ya mtungini. Kitu pekee kilichokuwa kinaonyesha kwamba wapo hai ilikuwa ni pumzi tu waliyokuwa wanatoa ikiashiriwa kwa kutanuka na kusinyaa kwa vifua vyao.







Kila baada ya muda kidogo, Mama Miraji alihamia kitanda kingine na kutazama mgonjwa. Alifanya hivyo kwa mara tatu, akanyanyua simu yake na kupiga.







“Haloo inspekta … Eeh baba, mbona kimya sana siku hizi sikuoni, kuna tatizo? … He! We! We! We! … Mbona hukunambia baba? … Mungu wangu! … sasa hivi upo wapi? … eeh we nielekeze tu … Haya, naja baba … muda si mrefu.”







Mama Miraji alisimama akiwa na uso wa papara. Alivaa viatu vyake vilivyokuwa vimeacha miguu kipindi amekaa kitandani akatoka nje ya wodi. Akiwa anatembea haraka, alikatiza mtaa mpaka kituoni alipopanda daladala na kuelekea kwa inspekta. Inspekta akiwa amejilaza kochini na sura iliyojaa uchovu, sauti ya mama Miraji iliita mlangoni.







“Hodiii!”







Inspekta alinyanyuka akaenda kumfungulia mlango. Waliketi sebuleni wakaanza kuteta juu ya vifo vya familia ya inspekta, habari hizo zikionekana kumshangaza na kumstaajabisha mama Miraji. Katika wasaa huo, Kaguta alitia miguu nyumbani hapo naye akaungana na maongezi. Baada ya muda usiozidi lisaa, mama Mriraji aliaga akaondoka, wanaume wakabaki wenyewe.







“Vipi, mbona hukunipa taarifa?” Inspekta aliuliza. Kaguta alitabasamu akasugua viganja vyake.

“Mwanangu, acha tu. Nimefika pale nikakuta wadada watatu visu.”

“Eeeh … mi ndo’ mana nilikuwa sitaki uende!”

“Aaah baba … Hakuna kilichoharibika mbona. Sema nimetumia teknik moja matata sana, itanufaisha pande zote mbili.”







Inspekta hakutia neno, aliacha macho yake ya mshangao pamoja na kebehi yamtizame Kaguta.







“Sasa nikawaza nitumie njia gani ya kumwingilia. Maana huwezi tu ukaanza eti wewe unamjua mwanaume mmoja alikuja hapa kununua barua sorry bahasha. So nikaanza kutumia njia laini, mtoto akatabasamu…”

“Sasa ni hivi, kesho naenda mwenyewe.” Inspekta alimkatisha Kaguta.

“Wapi?”

“Hapo stationary, naona unazingua tu, Kaguta.”

“We vipi Vitalis? … Nimekuambia hiyo kazi nitaifanya mie. Tatizo lako unataka kila mtu atumie njia zako. We acha nikuonyeshe sio tu njia yako ndio ielekeayo mbinguni.”







Inspekta alitikisa kichwa chake akanyanyuka na kuliendea jokofu akatoa chupa ya maji ya baridi na kuiweka mezani akiambatanisha na kikombe. Alipiga mafundo kadhaa akajilaza kochini. Kaguta alimtizama mwenzake akapiga mguno wa kicheko.







“Hivi umekula hata? … Alafu nikuambie kitu, ungemuambbia yule mama akupikie. We umemuacha kaenda hivi hivi.”







Inspekta kimya.







“Ila usikonde mwanangu mimi si nipo. Nitakupikia.”







Inspekta akashtuka. “Hapana! Leo napika mimi. Ule ugali wa jana hapana. Ugali una sura ya dodoki, uji mixer mabuje, mweh mtori si mtori. Ah ... ah!” Inspekta alinyanyuka akaelekea jikoni. Kaguta alibaki sebuleni akicheka mbavu hana.







Usiku wa siku hiyo uliishia nyumbani kwa inspekta. Asubuhi ya saa kumi na mbili ilipojiri, Kaguta alikuwa yupo kwenye gari lake tayari amevaa na kujiweka sawa. Aliondoa chombo mpaka maeneo ya mwenge akapaki sehemu ya wazi na kurusha macho yake chini ya mwamvuli wa kituo cha daladala. Kulikuwepo na watu kadhaa ambao Kaguta aliwatizama na kuachana nao.







Alikuwa kama kuna mtu anamtafuta ama kumngojea. Ilipofika mida ya saa moja Kaguta akiwa anapiga piga mihayo, alimshuhudia Sandra akiwa ndani ya sare anajongea kwenye kituo cha daladala akaketi pembezoni ya mwamvuli. Kaguta alitabasamu kisha taratibu akalisogeza gari lake eneo alilopo mwanamke Sandra. Alishusha kioo akamtizama Sandra na macho yaelezeayo utulivu na dhaka ya uanaume wa kistaarabu.







“Twende basi nikupeleke mama.”







Sandra alitabasamu akatikisa kichwa. Alinyanyua miguu yake minene na kufuata gari akienendea mlango wa nyuma. Kaguta alimshtua na kumtaka akae naye mbele. Sandra hakuleta ubishi, alihamia mbele akaketi na Kaguta.







“Umependeza.”

“Mmmh jamani, kweli?”

“Kweli.”

“Mbona nilikuwa hivi hivi hata jana?”

“Kila siku ni tofauti, unajua?”

“Ahsante sana.”

“You are welcome.”







Walinyamaza kwa muda. Baadae kidogo Kaguta alivunja ukimya.







“Hivi mfano nikitaka kuandika barua, mnaweza mkanisaidia pale ofisini kwenu?”

“Barua ya aina gani?”

“Ya kiofisi labda … ”

“Naweza nikakusaidia.”

“Wenzako je?”

“Hapana, haiwezekani. Labda kama ni ushauri ila si kumuandikia mtu barua. Kwanini umeniuliza?”

“Basi tu. Nilikuwa nina shida ya kuandikiwa barua.”

“Lini?”

“Hata leo.”

“Twende ofisini naweza nikakusaidia.”







Waliposhuka mbele ya ofisi, waliongozana mpaka ndani. Wahudumu wengine wawili walikuwa tayari wameshafika, walisalimiana, Kaguta akakabidhiwa kiti kilichokaa mbadala na meza iliyobebelea tanakilishi.







“Fungua Microsoft Word uendelee, nakuja. Au hujui?” Sandra alimuongelesha Kaguta.

“Najua. Ila usichelewe basi.”

“Usihofu, napanga panga hapa nakuja.” Sandra alisema kisha akafuata shelvu na kupukutisha faili kadhaa akaanza kuzipekua. Kaguta alivuta kipanya akabofya program ya Microsoft word. Ilipofunguka alifungua karatasi mpya na kuanza kuandika mithili ya barua hapo.







Huku macho yake yakiwa na tahadhari, muda mwingine Kaguta aliacha kuandika barua na kuanza kupekua nyaraka zingine zilizoandikwa karibuni. Alizifungua na kuzipekuwa kwa siri moja baada ya nyingine. Alizimaliza zote lakini haikuonekana hata moja iliyokamata hisia zake. Alinyanyua shingo akatizama tanakilishi za wahudumu wengine. Kwa siri alipenyeza mkono wake kwenye C.P.U akanyofoa nyaya fulani, tarakilishi ikazima.







“Sandra, imezima.”

“Hilo computer nalo!” Alilaumu Sandra huku akisogea karibu ya Kaguta. Aliitizama tanakilishi huku akijaribu kuiwasha bila ya mafanikio.

“Winner!” Sandra aliita.

“Abee!” Mwenzake aliitikia.

“Naomba huyu kaka aje hapo kwenye PC yako mara moja anahitaji kuandika barua, yangu imezima.”

“Mwambia aje tu. Ila kaka fanya haraka kuna kazi zinanisubiria.”

“Hana utaalamu sana na hayo mambo.” Sandra alimtetea Kaguta.

“Usiofu nitajitahidi tu. Si unajua tena ukiwa shidani.” Kaguta alijikomboleza huku akielekea kwenye tanakilishi elekezi. Alikaa na kufungua karatasi mpya akawa anaandika mithili ya barua. Ila kwa wakati huo huo akaanza kuufanya mchezo aliokuwa anaufanya hapo awali; wa kufungua na kusoma nyaraka zilizopata kuandikwa hapo mapema.







Wakati anafungua fungua, alikutana na nyaraka iliyobeba jina la Robson. Ndani ya hiyo nyaraka kulikuwa na nyaraka ndogo ndogo nane. Moja baada ya moja, Kaguta alianza kuzifungua kwa kuibia.







Nyaraka ya kwanza ilikuwa barua;







Kwako mshenzi mpuuzi.







Barua hii haina kichwa cha habari ila punde itadai kichwa chako na cha mshenzi mwenzako.







Hili ni onyo. Acha kutufuatilia. Endapo ukikaidi, utajuta wewe na kizazi chako.







By Mchinjaji Batili.









Kabla hajaendelea kusoma nyaraka nyingine, Kaguta aliingiza mkono mfukoni mwake akatoka na flash. Alikata sauti ya tanakilishi kwa kuhofia inaweza toa mlio wa tahadhari atakapoiunganisha na flash. Kwa haraka alinyonya nyaraka zile kisha akaendelea na igizo lake la kuandika barua.







Baada ya dakika chache Sandra alimjia Kaguta wakasaidiana kumaliza barua. Kaguta alitoa pesa barua ikaprintiwa akakabidhiwa kisha aliaga akaondoka zake.







“Mmmh Sandra, umemtoa wapi huyo kibopa?” Winner aliuliza kwa kipashkuna. Sandra alitoa cheko nene akalegeza na kurembua macho yake.

“Watu na bahati zao bibi eeh …”







Wote wakaangua kicheko na kugongeshana mikono. Hawakujua, Kaguta aliyekuwepo kwenye gari akielekea nyumbani kwa inspekta alikuwa amebebelea nyaraka muhimu, na si tu muhimu bali za siri.







Ndani ya dakika zisizozidi kumi na tano, Kaguta akawa tayari yupo nje ya nyumba ya inspekta. Upesi alishuka garini na kuingia ndani. Alimuita inspekta sebuleni akimuagiza aje na tanakilishi mpakato (laptop). Inspekta alikuja sebuleni akapokelewa na taarifa za Kaguta huko atokako. Waliketi na kuanza kuperuzi nyaraka zilizokombwa toka Rosemath Stationary.







“He! Kaguta. Hii ndio barua niliyotumiwa!” Inspekta alitahamaki kuona nyaraka yenye maandishi sawa sawa na yale aliyopata kuyasoma pindi mtoto na mke wake walipouwawa.

“Ina maana na hiz barua zingine ni mauaji tayari yameshafanyika?” Kaguta aliuliza.

“Bila shaka.” Inspekta alijibu. Waliendelea kufungua na kuzisoma barua. Walipofika kwenye nyaraka moja kabla ya kuifungua, walishangaza na maelezo ya juu yake.







Ilikuwa imebebelea tarehe ya kesho kutwa. Walipoifungua na kuisoma, walikuta maudhui yale yale ya mauaji. Mwisho wa barua anwani ya eneo inapotakiwa kutumwa ikiwa imewekwa. Inspekta na Kaguta walitizamana kwa mshangao. Hata pale waliposoma barua mbili zilizosalia, mtindo ulikuwa ni ule ule wa tarehe ya siku za mbele ikiwa imebeba miadi ya kuchinja na mchinjaji batili.







“Kwahiyo ina mana kuna mtu anapewa kuzipeleka hizi barua, ama? Anwani za nini?” Kaguta aliuliza.







“Ngoja kwanza. Tusachi hizi tarehe za barua zilizopita tuone kama kweli zote zina mauaji.” Inspekta alitoa wazo. Walifungua mtandao na kuweka tarehe zile husika, majibu yakaja yakionyesha mauaji sehemu mbali mbali jijini Dar es Salaam. Wahusika wakiwa wamechinjwa.







“Kazi ipo, Vitalis.” Kaguta alinena.

“Inabidi tuzuie mauaji haya ya mbele. Lazima tumtie huyu mshenzi nguvuni. Ila kuna haja ya kurudi Rosemath Stationary.”

“Kufanya nini?”

“Inaelekea kuna mambo mengi ya kuyafahamu huko.” Inspekta alisema, Kaguta akatabasamu.

“Si nilikuambia. Niamini. Ila mwanangu kuna mtoto kisu!”

Inspekta alitabasamu akamshika rafikiye bega; “Fanya kazi kaka.”

“Sijakataa. Ila siwezi nikamuacha.”

“Haya. Kumbuka upo kwenye mdomo wa simba.”

“Wala! Wao ndio wapo kwenye mdomo wa mamba.”







Inspekta alitabasamu baada ya kusikia hiyo kauli. Alinyanyuka akaelekea jikoni na kurudi na sahani iliyo na maandazi manne na mayai mawili ya kuchemsha pamoja na kikombe cha chai, akaweka mezani kisha akaleta na maji ya kunawa.







“Karibu.”

“Ahsante. Ulijuaje kama nina njaa?”

“Si ulitoka bila ya kunywa chai.”

“Nashukuru sana.”

Kaguta alinawa mikono akamega andazi.

“Mmmh … umenunua wapi haya?” Alitahamaki.

“Kwani vipi?”

“Matamu!”

“Nimepika mwenyewe.”

“Wapi wewe. Au yule madha kaja kukupikia?”

“Nimepika mwenyewe. Unadhani mimi kama wewe?”

“Aisee kama unajua kupika hivi, ulioa ya nini?”

“Umeanza mambo yako sasa.” Inspekta alisema kisha akanyanyuka. “Naelekea chumbani, ukimaliza utanikuta huko.” Aliongezea na kuanza kuondoka.

“Poa. Ila zingatia ushauri wangu.”

“Upi?” Inspekta alisimama akamtizama Kaguta aliyekuwa anakunywa chai.

“Yule mama yule.”

“Mama yupi?”

“Mama Miraji.”







Inspekta alisonya akitikisa kichwa chake na kujiondokea.









Masaa yalichukua nafasi na kuuleta usiku kwa kasi. Inspekta pamoja Kaguta hawakwenda popote katika wasaa huo, waliketi sebuleni na kuchosha macho yao kwa kuangalia movie za kizungu. Usingizi ulipowaahidi makao, walizima kila kitu wakaenda kulala. Ndani ya asubuhi ya mapema, Kaguta alidamka na kumwacha inspekta kitandani.









Alichukua shati la inspekta kabatini akalinyoosha na kuliweka mwilini. Alipanda gari akaelekea moja kwa moja kule alipokwenda jana yake; maeneo ya Mwenge.









Alikaa hapo kusubiria, ndani ya muda mfupi mno akatokea mwanadada Sandra. Ila hakuwa mwenyewe, alikuwa anaongozana na mwanaume mmoja mrefu wa wastani akiwa amevalia suti ya kijani. Walikuwa wanateta. Kabla ya Kaguta kusogeza gari lake aliwatizama kwa dakika zisizozidi mbili akapiga ngumi usukani.







“Mbona haondoki?” Aling’aka. Aliwasha gari akalisogeza mpaka mbele ya Sandra, akapiga honi na kushusha kioo.

“Mambo?” Kaguta alirusha salamu.

“Poa, vipi?” Sandra alijibu na kurudishia.

“Shwari tu.” Kaguta alijibu kisha akamtazama yule mwanaume aliyekuwa Sandra.

“Oya vipi?” Kaguta alisalimia. Mwanaume yule hakusema kitu. Alimtizama Kaguta kwa macho makali. Sandra alijitabasamisha akaaga;

“Mi naondoka Roby. Baadae.” Alimwambia mwanaume aliyekuja naye kisha akafuata gari la Kaguta na kuondoka.

“Jamaa yako nini yule?”

“Hamna ni mfanyakazi mwenzangu.”

“Mbona jina lake la kike, Roby?”

“Ha ha ha hapana. anaitwa Robson. Sema huwa nafupisha tu.”

“Anaitwa Robson?”

“Ndio.”





http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Uso wa Kaguta ukaonekana kumezwa na mawazo. Ni kama vile alisikia kitu cha kushangaza. Japokuwa macho yake yalikuwa yanatizama mbele, lakini alionekana hayupo pale kifikra. Nyuma yao, Robson bado hakuwa ameondoka pale kituoni. Alikuwa analitizama gari la Kaguta likiishia. Lilipopotea kabisa, alitoa simu yake mfukoni akapiga.







“Yeah … nimemuona yule jamaa wake inspekta … yupo na Sandra … Muda si mrefu … Fanya uje unichukue hapa kituoni …”









Alikata simu. Baada ya muda kidogo, pikipiki ilkuja kumchukua. Ilikuwa ni pikipiki ile ile iliyomfuatilia inspekta na Kaguta siku zile.







“Twende huku! Fasta!” Robson alimuelekeza mwenzake akinyooshea kidole kule gari la Kaguta lilipoelekea. Pikipiki ilendeshwa kwa kasi. Baada tu ya muda kidogo, waliliona gari la Kaguta.









“Walee! Wafuatilie taratibu tu tuone wapi wanaelekea.” Robson aliwika. Dereva wa pikipiki aliweka sawia pikipiki yake kwenye mstari lililopo gari la Kaguta kisha akapunguza mwendo.

“Inabidi huyu mpumbavu afe. Si chini ya leo na kesho. Huwezi jua amepata nini toka kwa Sandra.” Robson alimwaga maneno.

“Kweli. Ila inabidi tuwe makini, mkuu. Hawa jamaa wapo vizuri.”

“Hamna lolote!” Robson alipuuza, “wapo vizuri kwa watu wengine, si kwangu.”







Dereva hakutia tena neno. Wote walinyamaza wakawa wanatizama mbele waendako. Baada ya muda mfupi, polisi wa barabarani aliwapungia mkono na kuwataka wapaki chombo pembeni.









“Shit! Nini tena hiki?” Robson alilalama.

“Tusimame, mkuu? … au nipitilize?” Dereva aliuliza.

“Simama tuepushe matatizo mengine.” Robson alitoa maelezo. Pikipiki ilisimama ikapaki pembezoni mwa barabara, polisi akasonga.

“Habari zenu?”

“Safi tu afande, za kazi?”

“Njema. Kwenu helmet ni nini?”

“Helmet?”

“Ndio, hujanisikia? … kwenu nyie helmet ni nini?”

Dereva aligeuza shingo akamtizama Robson.

“Samahani Afande, tumesahau.” Robson alijitetea.

“Sawa mie naweza nikakusamehe lakini ajali je? Umeipa taarifa?” Afande aliongea kwa sura isiyo na utani. Robson alitazama barabara akaona gari la Kaguta linaishia. Haraka alishuka akangiza mkono wake mfukoni na kutoa shilingi elfu hamsini.

“Poza basi na hii, Afande. Tuache twende.”

“Kwahiyo unanihonga, sio?” Afande aliuliza kwa kebehi. Ghafla, bunduki ndogo ikadondokea kiatu cha Robson. Alikuwa kaiweka nyumaya suruali kiunoni. Afande alipoona bunduki, alitoa macho kwa kustaajabu. Upesi alinyofoa bunduki yake iliyokuwa imekaa kwenye kamfuko kadogo hips ya kulia akawanyooshea watuhumiwa.

“Mikono juu! … Sogeza hiyo bunduki huku!” Afande aliamuru. Robson alipiga teke bunduki kumfuata Afande.

“Shuka! … Upesi! … Nimesema mikono juu!” Afande alimwamuru dereva. Dereva alishuka akaungana na mwenzake aliyesimama mikono ikiwa hewani.









Afande alitoa radio call yake iliyokuwa imeshikishwa na kamba kifuani akaweka kinywani na kupasha taarifa wenzake. Ndani ya muda mfupi, defender ilikuja ikiwa na maaskari watatu, Robson na mwenzake wakaswekwa ndani ya gari pamoja na pikipiki yao.Upande wa pili wa shilingi, gari la Kaguta lilikuwa tayari lishatua mbele ya ofisi ya Rosemath Stationary.







Kaguta alishuka akamfungulia mlango bibie Sandra mithili ya malkia. Sandra alishuka kwa mbwembwe na madaha, wakaongozana na Kaguta kwenda ndani.









“Karibuni!” Winner aliwakaribisha kwa tabasamu pana.

“Ahsante, Winner. Tumekaribia.” Sandra aliitikia.

“Habari za asubuhi?” Kaguta aliwasalimu wadada wawili aliowakuta; Winner na Rahma.

“Njema tu. Za kwako?”

“Safi. Mmependeza mno kama vile mwaenda maonyesho.”







Winner na Rahma walicheka kusikia hilo.









“Ahsante. Hata wewe pia umependeza.”

“Mmmh … kweli?”

“Kweli.”

“Basi kheri. Mungu ashukuriwe.”

“Sio mke?” Winner aliuliza kichokozi. Sandra na Rahma wote wakamtizama Kaguta.

“Hapana jamani. Sijaoa mie, nipo nipo tu. Single but lazy to mingle.”







Wanawaka wakadondosha cheko tena.









“Vipi lakini, mlifanikiwa kutengeneza ile computer yenu?” Kaguta aliuliza kwa kumtazama Sandra.

“Hapana! … Yani hapa mpaka fundi aje.”

“Ohoo! … Huyo fundi anakuja lini sasa?”

“Anaweza akaja siku yoyote, tumeshawasiliana na bosi.” Rahma alieleza.

“Mpaka aje huyo fundi si mmepata tabu sana. Naweza nikajaribu kuitengeneza?” Kaguta alijinasibu.

“Unaweza tu. Huogopi kupigwa shoti?” Sandra aliuliza.

“Hapana. Kwani hutaki nife?”

“Ndio sitaki!”

“Kwanini? … unaogopa mzoga ofisini mwako?”

“Hapana. Sitaki tu ufe.”

“Ahsante. Nimefurahi kusikia hilo.” Alisema Kaguta na kusogelea tanakilishi ya Sandra. Huku kichwa chake kikienda huku na huko, alipepesa macho yake kuitizama tanakilishi kama mtu atafutaye kitu kibovu.









Baada ya kuzunguka zunguka na kutizama tizama aliketi kwenye kiti na kufungua CPU. Wakati huo Sandra na wenzake walikuwa wakiendelea na shughuli zao zingine.







Kaguta alishika waya aliouchomoa siku ya jana yake, akauchomeka na kuwasha tanakilishi, ikawaka. Kabla ya kuwaambia wakina Sandra alichomeka flash yake na kuanza kunyonya mafaili kadha wa kadha. Alipomaliza, alishusha pumzi ndefu akatabasamu.









“Tayari! … Njoeni muone.” Alitangaza ushindi. Haraka, Sandra, Winner na Rahma wakajongea kuja kuona ya Musa.

“Wow! … Kumbe we ni fundi?” Sandra alitahamaki.

“Tutakuwa tunakuita wewe uje kututengenezea.” Winner aliongezea.

“Nashukuruni sana. Sema nimegundua kuna kitu kina mushkeli kidogo kwenye PC zenu. Kama mnaweza kuniruhusu, ningependa kurekebisha kwenye mashine ya kila mtu ili isije kuwasumbua tena.”

“Anza na ya kwangu!” Winner aliwahi kunyoosha mkono.

“Mie wala sishindani. Ukimaliza tu baba hamia kwangu.” Rahma alisema kwa mng’ao wa tabasamu.

“Basi sawa.” Alisema Kaguta kisha akanyanyuka kuifuata tanakilishi ya Winner na kuanza kuipekua pekua kama vile anatafuta ufunguo uliopotea mchangani.









Alipopata wasaa aliketi na kunyonya mafaili ambayo hayakubeba jana. Kila kitu kilichokuwa kwenye faili alikibeba na kukitupia kwenye flash. Mchezo ukawa huo huo na kwenye tanakilishi ya Rahma. Alipomaliza aliweka flash yake mfukoni akasimama na kujinyoosha.









“Tayari jamani. Mie naomba niende tu.”

“Umemaliza?” Rahma aliuliza.

“Ndio. Nimekamilisha kila kitu.” Kaguta alisema kwa majivuno.

“Ahsante sana. Tukulipe sh’ngapi?” Winner aliuliza.

“Aaah jamani, mnilipe tena? …Wala! Mie nimewafanyia tu.”

“Ahsante sana. Alafu wenzako hatujui hata jina lako, yani tunashindwa hata tukuiteje.” Rahma alitanabahi.

“Naitwa Alkareem.”

“Unafanya kazi wapi?” Rahma aliongezea swali.

“Mmm … Nanyiee! Mbona maswali mengi!” Sandra aliingilia kati. Kaguta akamtuliza;

“Acha tu waulize.” Kisha akamgeukia Rahma,“Mimi ni mjasiriamali. Nachukua mizigo toka China kuileta hapa.” Kaguta alijibu kimujarab. Wanawake wakatabasamu na kushukuru wakaendelea na kazi zao. Kaguta alimsogelea Sandra akamnong’oneza.

“Please naomba nikutoa dinner leo?”









Sandra alitabasamu akamtizama Kaguta kwa macho fulani hivi yasemayo ahsante.









“Sawa. Haina shida., utancheki basi kwa namba yangu.” Mwanamke alisema kwa sauti yake nyororo. Kaguta alimtizama akalamba lips zake. Aliaga wakina Winner na kufuata gari lake akahepa.

“Mmmh … Sandra umeshanshinda tabia, mama.” Winner alisema huku akishikilia kiuno chake. “Naona unawaokoteza tu, utuachiage na sie mweh!”

Rahma na Sandra wakaangua kicheko.

“Nakuambia mahandsome wote yeye. Kuanzia Roby mpaka Alkareem.” Rahma alijazia maelezo.Sandra aliangua tu kicheko, alipomaliza akashika kiuno.

“Jamani sijawaambia kilichonitokea leo. Si nilikuwa na Roby wakati nakuja kupitiwa na gari!”

“Enhe?” Rahma alidakia. “Ikawaje na ninavyomjua Roby kwa wivu.”

“We acha tu. Niliaga nikaondoka ila ile hali niliyomuacha nayo. Sijui!” Sandra aliongea na kubinua mdomo wake.

“Kuwa mwangalifu, mama. Si unajua Roby si mtu mzuri?” Winner alishauri. Waliacha kupiga stori wakaendelea na kazi.









Upande wa kwanza shilingi, nje ya kituo kikubwa cha police Oysterbay, Robson alionekana akiwa na dereva pamoja na mwanaume mwingine mzee aliyevalia shati la kitenge na suruali nyeusi ya kitambaa. Walikuwa wanatembea wakitoka eneo la polisi, dereva akiwa anakokota pikipiki. Walipolifikia gari jeusi aina ya Suzuki Escudo, walisimama hapo.









“Kuweni makini bwana. Mim sitokuja kuwatoa tena kwa makosa ya kizembe kama haya. Umesikia Roby?”

“Ndio.”

“Umesikia Yobo?”

“Ndio.”









Mwanaume yule aliyevalia shati la kitenge alishika mlango wa gari, Roby akamuita.







“Ila bosi. Kuna jambo nataka nikueleze.”

“Nini tena, Roby?”

“Kuna mtu anatusumbua, tunataka tummalize.”

“Sasa? … Unataka nini? … Si ummalize?”

“Nahitaji pesa bosi.”

“Unataka kiasi gani Roby? … na huyo mtu ni nani kwani?”

“Ni jamaa fulani hivi, mjinga mjinga hivi, mmojawapo wa wale waliowauwa wenzetu.”







Mzee kusikia hivyo, alitahamaki.









“Ina mana mpaka leo hii wapo hai? … Roby unafanya kazi gani sasa?”

“Hapana bosi … tayari tumeua familia ya mmoja wao.”

“**** you! … Familia yao ndio umepunguza idadi yetu? …kwahiyo ina mana bado wote wawili wapo hai? … What the **** are you doing? Umeshindwa kazi?”

“Hapana bosi!”

“Hapana nini? … Baadae uje kuchukua pesa, na nakupa wiki moja tu sitaki kusikia ushuzi wa hao watu.” Mzee alifungua mlango wa gari akaingia na kuubamiza kwanguvu. Aliwasha gari akapotea.







“Tuondoke, Yobo.” Robson alimwamba dereva wakapanda pikipiki nao wakaondoka.





****

Pipiiii!







Kaguta alipiga honi nje ya nyumba ya inspekta. Alishuka akiwa na furaha mkononi kabebelea flash yake. Huku akipiga mluzi alitembea kwa kudunda mpaka mlangoni. alifungua mlango akamkuta inspekta pamoja na mama Miraji. Tabasamu la uongo likajaa usoni mwake.









“Habari zenu jamani?”

“Njema tu. Karibu.” Mama Miraji alisema kwa tabasamu wakati inspekta akiwa kimya anamtizama tu Kaguta.

“Ahsante … Ahsante sana, mama.” Alisema Kaguta bila hata ya kuingia ndani. Alimrushia inspekta flash kisha akamkonyeza.

“Mie wala siingii. Nilikuja tu kuleta mzigo huo, baadae!” Alisema Kaguta, kabla hata hajajibiwa alishafunga mlango na kushika njia.

“Mbona hujamkaribisha mwenzio?” Mama Miraji alimuuliza inspekta. Inspekta alitikisa kichwa akaguna.

“Ana yake huyo. Si mgeni wa kukaribishwa.”







Mama Miraji alitabasamu na kucheka kidogo; “Haya bana, waarabu wa pemba mwajuana kwa viremba.”









Walicheka kwa pamoja kisha wakatizamana kama watu wasio na maneno mapya ya kuongea.







“Sasa … acha basi nikuandalie chakula mgeni wangu upate kula.” Inspekta alinyanyuka.

“Hapana bana. Usijichoshe bure.”

“Bure? … si bure kukupikia. Nisingependa mgeni utoke hapa bila ya kutia chochote mdomoni maana hata kinywaji umekataa.”

“Hamna shida bwana, inspekta. Mie nipo sawa tu.”

“Tia hata sunna basi.”

“Mila zetu haziruhusu mwanamke kukaa alafu mwanaume aingie jikoni. Naomba basi nikusaidie kupika.”

“Jamani, mgeni tena?”

“Kwani kuna shida?”

“Hapana. Haya twende nikuelekeze. “







Mama Miraji alisimama na kuongozana na inspekta mpaka jikoni. Wakati akiwa anapika, inspekta alileta tanakilishi mpakato yake sebuleni akachomeka flash na kuanza kuperuzi kilichowekwa humo na Kaguta.

Baada ya muda si mrefu, chakula kilikuwa tayari juu ya meza.









Inspekta akishirikiana na mama Miraji waliweka sahani mezani, maji ya kunywa na kunawa pamoja na matunda kadhaa. Chakula kilikuwa wali njegere ukiwa na nyama ndani yake.









Inspekta alimnawisha mikono mama Miraji, mama Miraji naye akafanya vivo hivyo. Wakaanza kula.









“Kwahiyo kwa sasa unajishughulisha nini, mama?”

“Nabangaiza na vibiashara vyangu. Nauza vitenge na madela kwa kupitisha pitisha majumbani.”

“Hongera sana.”

“Kwa lipi?”

“Kutafuta pesa. Familia inakula hapo.”

“Nashukuru Mungu, anajaalia.”

“Mtoto wako anaendeleaje?”

“Marietta anaendelea vizuri. Muda si mrefu sana atarudi toka shule. Alafu nimekumbuka, nimepitia hospitali wakati nakuja huku. Jombi ameanza kuongea japokuwa kwa shida.”

“Kweli?”

“Ndio. Daktari amesema muda si mrefu atarudi katika hali yake ya kawaida. Ila kuna kitu nimegundua, hii hospitali waliyopo sasa wanahudumiwa vizuri kuliko kule.”

“Yap. Ile hospitali ni ghali kuliko ile ya mwanzo.”









Walimaliza kula wakakaa kwa muda kidogo Mama Miraji akaaga anaenda nyumbani kumuwahi mwana. Inspekta alimsindikiza mpaka barabarani akamkodishia mwanamama pikipiki. Walihaidiana kuonana tena kesho hospitalini.









Baada ya masaa kadhaa jua likiwa tayari limeshazama, Kaguta alirudi nyumbani kwa inspekta. Akiwa na tabasamu pana, alimkumbatia mwenzake kwanguvu;

“We jembe! … Jembe haswaa? … Vipi anasemaje?”

“Nani?”

“Aaah … Hujui namuongelea nani banaa? … Si mama Miraji!”

“Tumepiga naye tu story, ameshaondoka. Picha ya mke wangu bado imeng’ang’ania ubongo wangu, Kila nikikaa na mama Miraji namkumbuka mke wangu.” Inspekta alisema kwa sauti ya upole. Kaguta akamshika bega.

“Najua jinsi unavyojisikia. Lakini huwezi ukaishi hivi milele, Vitalis? Inabidi ufungue moyo wako upate angalau faraja.”

“Sijui. Labda huko mbele. Embu kaa kwanza tufanye kazi kuna vtu nimeviona kwenye ile flash.”

“Wee nani akae sasa hivi? … Tutafanya baadae bwana saa hizi nina miadi na mtoto mzuri tunaenda kupata dinner.”

“Duh! … nani tena?”

“Sandra. Anafanya kazi kule Rosemath stationary.”

“Haya dinner njema.”

“Baade kaka.”

“Poa, take care.”









Kaguta alitoka nje akakwea garini na kupotea eneo lile. Ni baada ya dakika kama thelathini tu alikuwa tayari ameshafika eneo la miadi. Haikuchukua muda, mrembo Sandra naye akatokea.









Alikuwa amenoga mno kwa gauni lake refu jeusi la kumeta-meta. Gauni lilimbana vizuri na kumchora umbo lake kuntu namba nane. Lips zake zilitiwa nakshi ya lipstick kwa mbali na sura yenye make-up kwa wastani.







Kaguta alinyanyuka akampa mwanamke kumbato. Alisogeza kiti akamkaribisha malkia. Mhudumu alisogea na menyu, wahusika wakaagiza chakula na vinywaji wavitakavyo.









Wakiwa wanapata chakula, kwa nje ya hoteli. Pikipiki ilijisogeza eneo la kupaki ikiwa na mtu mmoja tu aliyevua kofia yake ngumu nyeusi akaiweka juu ya usukani. Loh! Alikuwa ni Robson. Alinyofoa ufunguo wa pikipiki na kuingia ndani ya hoteli. Moja kwa moja alienda kukaa sehemu aliyokuwa anawachora Kaguta na Sandra kwa mbali.









“You really look very beautiful. Sitosheki kukutazama.” Kaguta alinong’oneza huku akitizama macho ya Sandra.

“Ahsante. Usin’sifie sana n’tashindwa kula mwenzio.” Sandra alisema kwa tabasamu jembamba macho yakielekea chini.

“Kizuri kipe sifa yake, mama. Mimi si wale wasemayo ya moyoni mtu angali maiti.”

“Nashukuru, Al Kareem. Kama jina lako lilivyo, wewe ni mkarimu sana.”

“Kweli?”

“Haswaa!”

“Nafurahi kusikia hayo toka katika kinywa chako kitamu. Natumai yametoka katika moyo wako uliolemewa na upendo.”







Sandra alitabasamu akachoma kipande cha chips na uma akapeleka mdomoni.









“Una maneno wewe, Kareem. Kama vile unanishushia mashairi.”

“Hamna bana, mie na ughani wa mashairi wapi na wapi. Sema tu nasema kile kilichopo moyoni. Heri kufa macho, Sandra, kuliko moyo.”

“Ni kweli.”









Kaguta alikunya fundo moja la mvinyo, akakata kipande cha kuku na kukiweka mdomoni. Alipotafuna na kukimeza, alilonga;

“Una muda gani pale kazini kwako?”

“Miaka miwili na nusu sasa.” Sandra alijibu.

“Upo tayari kuacha kazi yako?”

“Mmmh … Hapana. Hata kama nitakuwa tayari sitaweza.”

“Kwanini? … Wanakulazimisha?”

“Hapana. Ni mkataba wangu tu ndivyo usemavyo.”

“Kwamba hakuna kuacha kazi?”









Sandra alipeleka kwanza glasi yake ya mvinyo mdomoni akanywa mafundo mawili;

“Huwezi kuelewa, Kareem. Tuachane tu na hayo maongezi.”









Kaguta hakuongeza tena neno. Alimaliza mvivyo wake kwenye glasi akawa anamtazama tu Sandra.









“Umekasirika?”

“Hapana. Sidhani kama naweza kupata sababu ya kumkasirikia mrembo kama wewe.” Alisema Kaguta huku akilazimisha tabasamu. Sandra alitabasamu na kutikisa kichwa bila kusema kitu, aliacha mikono na mdomo wake vifanye kazi ya kujaza tumbo kwa chakula na kinywaji. Alipomaliza, alijifuta mdomo wake na tishu akamtazama Kaguta na jicho lililosikia mvinyo.



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/





“Ahsante sana. Umefanya siku yangu ya leo iwe very special.”

“Usihofu, malkia. Wastahili haya.” Alisema Kaguta kwa pambe. Alinyanyua tishu yake akaondoa kajipande ka chakula kalichobakia shavuni mwa Sandra.

“Ahsante.”

“Karibu sana.”









ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog