Search This Blog

Sunday 20 November 2022

MSAKO WA HAYAWANI - 3

 





    Simulizi : Msako Wa Hayawani

    Sehemu Ya Tatu (3)







    Kembo akamtazama Kassim na kumwambia, "Bwana Kessy, kajaze magazeti ya zamani kwenye mkoba."





    *****************************





    "Huyu nguruwe ni Hoza Kamkimbile, kama kitambulisho chake ni cha kweli." Alisema Dennis akikitumbukiza mfukoni kitambulisho hicho.

    Bessy akamkuta, "Denny! Unafanya nini?"

    "Enh?"

    "Huruhusiwa kuchukua chochote."

    "Ooh, ninakiazima kwa muda mfupi tu. Nitawarudishia kesho. Pamoja na huu ufunguo. Ni ufunguo wa chumba Namba 408 cha Tupetupe Hotel."

    Bessy akatikisa kichwa kwa masikitiko. "Denny, ikigundulika......."

    "Nitabeba lawama zote."



    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Dennis akaanza kuivika maiti. "Ana makovu kadhaa ya visu. Mawili mabaya. Moja ni la zamani sana, zaidi ya miaka kumi iliyopita. Ndiyo kusema ukora aliuanza utotoni."

    "Ni hilo ulilogundua?"

    "Nimegundua pia alikuwa mtu wa madawa ya kulevya. Aliyauza na kuyatumia. Mtu wa aina yake hawezi kuwa mgeni kwenu. Lazima mtakuwa na faili lake. Pengine amewai hata kufungwa."





    "Sawa nitakwenda kupekua." Alisema Bessy na kuongeza, "Ni wazi ametumwa na huyo Kassim Hashir."

    "Ni wazi." Alijibu Denny. "Ni madawa ya kulevya yanayowafanya wawe na shida kali ya pesa. Ni ghali mno na wanapoyatumia huwapa ujasiri wa bandia, huwafanya watende lolote lile bila woga."

    Bessy akakubali kwa kichwa. "Ndiyo maaana katika nchi zingine kama Arabuni na Indonesi, adhabu yake ni kifo."





    Baada ya kimya kifupi, Dennis akasema, "Unaweza kwenda kuwapigia simu wenzako. Mimi hawatanikuta. Nakwenda nyumbani. Na wewe pia nenda nyumbani ukapumzike. Weka mtu mwingine wa kulinda, ingawa sidhani kama patatoke lolote jingine usiku huu."

    "Denny utakwenda Tupetupe?" Denny akasita kabla ya kujibu. "Labda usiku wa manane, baada ya usingi wa masaa mawili au matatu."

    "Lazima twende sote."

    "Hapana Hoteli hiyo hawaendi wanawake wenye heshima zao."





    ***************************************





    Naam, palikuwa mahali pazuri kwa mahepe, ngoma ya wanga. Palikuwa kimya na patupu. Hapakuwa na wapita njia, na magari yalipita kwa nadra sana.

    Taa za barabarani zilikuwa pande zote mbili za daraja. Lilikuwa daraja refu lakini haukuwa mto mkubwa. Na kwa vile ilikuwa kiangazi, ulijaa zaidi mchanga kuliko maji.





    Wakiwa wamevaa nguo nyeusi, chini ya daraja, Chiko na Fensy walikuwa kama vivuli. Walijibnza sehemu nzuri, wakikiona wazi wazi kibanda cha simu. Fensy akasema, "Nina kiu ya sigara."

    "No." Akamaka Chiko. "Hakuna kuvuta. Hakuana kubananga."

    "God! Sikujua kama patakuwa na baridi kiasi hiki! Kwa ninitukaja mapema kiasi hiki.... kabla hata ya saa tano!"





    "Ulitaka tuje saa sita kamili?" Aliuliza Chiko. Unajua vizuri sana ilibidi tuje mapema. Huyo mwanaharamu anaweza kuwa hapahapa anatuangalia."

    "Kama atakuwa eneo hili ana digrii ya kazi hii. Nimelikagua eneo lote na sikuona hata mzoga wa panya."





    "Kama hayupo basi ni chizi, amevamia kazi asiyo na ujuzi nayo. Laiti ningekuwa mimi ningeitumia simu ile pale, na kisha nisingeondoka mahali hapa mpaka hizo pesa zimeletwa. Na nisingezichukua mpaka nimehakikisha hakuna unyayo wowote. Nisingeacha nitumbukie katika mtego wa kipumbavu hivi!"





    "Wewe ungechukua tahadhari hizo kwa sababu kwanza, hii ni kazi yako, na pili unafahamu kuwa Bwana Kessy ana watu kama Kembo na sisi. Nina hakika huyo Bob hafahamu hivyo. Anadhani kuwa Bwana Kessy yuko peke yake. Ndiyo maana Kembo alitutaka tuwe kimya kabisa wakati anazungumza naye simuni. Hakutaka kumgutusha. Alitaka abaki na uzumbukuku wake."





    "Na kweli ni zumbukuku kweli kweli. Bila ya kuchukua tahadhari yoyote mbele ya milioni saba, kama vile zinatingishwa mtini

    "Ooh, karibu watu wote wanaodaipesa za kifumba mdomo ni wapumbavu." Alisema Fensy. "Hugundua siri ya mtu kwa bahati tu, kisha huingiwa na tamaa na kuanza kudai, bila kufikiri wala kupanga. Wakati mwingine matokeo yake huwa ndio haya - kumdai kifumba mdomo mtu kama Kessy."





    Wakasikia mvumo wa gari, wakaona VW [kobe] kuukuu likivuka daraja na kuegsha pembeni, mkono wa kulia, kama hatua thelathini kutoka kwenye kibanda cha simu.

    "Wako wawili." Alisema Chiko akiitazama saa yake. "Saa sita kasoro tano. Ni wehu. Siyo wapumbavu."

    "Utakuwaje na hakika kuwa ndio wao?" Fensy aliuliza.

    "Unataka tuwekeane dau? Hamsini kwa laki."

    "Sina pesa ya kuchezea."





    "Sikiza." Chiko akasema kikazi. "Ni mmoja tu atakayeshuka kuufuata mkoba wa fedha. Huyo atakuwa ndiye wako. Atakaye baki garini ndiye wangu. Wako usimcheleweshe. Tutamhoji atakayebaki garini."

    "Sawa."

    "Sasa tumsubiri Kembo alete hiyo fedha." Alisema Chiko na kuitizama saa yake tena. "Bado dakika mbili."









    Luteni Dennis Raymond Makete aliwasili Tupetupe Hoteli dakika chache kabla ya saa sita kamili, akiwa amepumzika masaa mawili, ameoga, amekula na amebadili nguo na kuvaa kiraia suruali ya jinsi na T- shirt. Huo ndio ulikuwa wakati wa hoteli kupamba moto kwa pirikapirika za kila aina. Huko ndani magoma ya disko yakihanikza, hapo nje biashara za ufuska na ufisadi ziliendelea mtindo mmoja. Magari, hasa teksi, yaliwasili na kuondoka kila dakika.





    Palikuwa mahali pa aina ya pekee katikati ya jiji hilo, palipopendwa na vijana wa kazi,wakora, mapusha, washarati na kadhalika.

    Akiteremka garini Dennis akamuona fuska mmoja akimjia. Alikuwa mwana mama wa makamo aliyejiremba kwa wanja na rangi na nywele za bandia ili aonekane mwana mwali.





    "Daling, come wiz me," Alisema, kidogo akiyumba. Alikuwa amelewa, pengine ulevi na mchanganyiko wa kila kitu.

    "Come wizi me. Very flesh. Milk standing. Five dolaz only."

    Denny, huku akiufunga mlango wa gari, akamtazama kama anavyotazama kinyesi alichokikanyaga uchochoroni. Akamwambia, "Go screw yourself!"

    "Shit! You no man! Anaza shoga!" Lililalama guberi hilo na kukimbilia gari jingine lililokuwa likiwasili.





    Kabla ya kuufikia mlango wa hoteli Denny akaguswa bega na kijana mmoja. Alikuwa amevaa kidani na hereni moja.

    "Hapa, mista," alisema. "Kila kitu poa. Poda, stiki, pilis. Kila kitu. Mali safi kabisa. Na bei poa kabisa."

    Denny akamwangalia kwa makini na kumwambia, "Hoza ndio pusha wangu."

    "Hayupo leo." Pusha huyo akajibu haraka. "Amesema ana kazi mhimu. Wateja wake wote nawahudumia mimi. Usiwe na wasi wasi."

    "Mbona wewe sikufahamu?"

    "Naitwa Dikwe. Kila mtu ananifahamu. Siuzi mali feki mimi muulize yeyote yule. Muulize hata Hoza."

    "Ni rafiki yako?"

    "Sana."

    "Umesema kenda wapi?"

    "Hakuniambia alikokwenda. Kasema yupo bize, ana kazi mhimu sana. Ya milioni mbili, kanambia niwahudumie wateja wake bila mshikeli. kwa hiyo usiwe na wasi wasi."

    "Sawa." Dennis akasema pasipo na jazba.

    "Nisubiri hapahapa. Acha nikamcheki chumbani kwake. Pengine anaweza kuwa amerudi lakini hukumwona."

    Psha Dikwe akainua mabega, ishara ya kusema, 'shauri yako, poteza muda wako kama hauna thamani'.





    Denny akalisukuma guberi jingine lililotaka kumshika mkono. Akaingia ndani ya lifti na kupaa hadi ghorofa ya nne.

    Korido ilikuwa tupu yenye harufu nzito. Magoma yalisikika kwa mbali. Vicheko vya kiguberi vilisikika hapa na pale,nyuma ya milango iliyofungwa.

    Denny akatembea kwa hatua madhubuti hadi kwenye chumba Namba 408, akisikiliza kwa makini. Akautoa ufunguo alioutoa kwenye mfuko wa Hoza, akataka kutumbukiza kwenye tundu la kitasa, akasita. Alihisi uepo wa mtu au watu humo ndani. Akaugonga mlango kwa mgongo wa kidole cha shada.





    Mlango ukafunguliwa na kachero Inspekta Bessy, aliyesimama akitabasabu, bastola mkononi.

    "Wewe!" Denny akashangaa.

    "Si yeyote mwingine," Alijibu msichana huyo, akirudusha bastola yake kwenye mkoba wake wa begani.

    "Nilidhani unakoroma saa hizi," Aliroroma Denny.

    "Nilale wakati nina kazi ya kufanya? Na kwa taarifa yako, sina tabia ya kukoroma."

    "Iko siku nitahakikisha. Tena naamini siku hiyo haiko mbali sana."

    "Tutaona. Karibu ndani."



    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Denny akaingia ndani. Akaona makachero wawili wako kazini, mmoja alipekuwa chumba. Mwingine akitafuta alama za vidole.

    Bessy akamuuliza Denny, "Hivi kweli ulidhani nitakusikiliza, niache kufanya kazi niende kulala? Nikuache uje hapa na uvuruge kila kitu badala ya kuleta wataalamu? Hakika hujui kumthamini mtu...."

    Denny akainua mikono. "Ok! Nilifanya kosa." Akauliza, "Hebu niambie, mmeingiaje humu ndani?"

    "Tumefunguliwa na meneja wa hoteli. Ulidhani tumeingia kinyemela kama ulivyotaka kuingia wewe?"

    "Sasa mnaendeleaje?"





    Bessy akatikisa kichwa. "Tunakaribia kumaliza." Alisema, "Kama ulivyoshuku, Hoza alikuwa pusha. Vielelezo vipo tele, lakini hatukuweza kupata chochote cha kumhusisha yeye na Kassim Hashir."

    "Haishangazi." Alisema Denny.

    "Kwa hiyo sina chochote cha kufanya hapa. Nakwenda zangu nyumbani kulala. Na wewe nakushauri ufanye hivyo hovyo. Umekuwa wima tangu asubuhi. Kesho inaweza kuwa siku ngumu zaidi."

    "Oh, nimeshazoea kufanya kazi masaa arobaini na nane."

    "Si mazoea mazuri. Utazeeka haraka." Alisema Denny na kutoka.





    *****************************************************************





    Chiko na Fensy, wakiwa wamelala kifudifudi kama wanajeshi wa msituni, wakaisikia saa ya mnara wa saa ikianza kugonga. 'Ngooo..! Ngooo...! Ngooo...! Bila kutarajia, Chiko na Fensy wakajikuta wakizihesabu 'ngoo' kimoyomoyo. Ilipofika 'ngoo' ya saba wakausikia mvumo wa gari juu ya daraja. Benzi jeupe likalivuka daraja polepole.

    Lilipofika usawa wa kibanda cha simu likapunguza mwendo zaidi. Mlikuwa na mtu mmoja tu humo garini.





    Mkoba wa 'fedha' ukarushwa. Gari likachochewa moto na kuyoyoma.

    Ndani ya VW, Kikoti akaugusa mkono wa Bob. "Lile ndio gari la Bwana Kessy, lakini anayeliendesha siye yeye. Ni rafiki yake Bwana Kembo."

    "Akh, unajali nini?" Bob akauliza.

    "Tunachokitaka ni fedha, siyo mletaji. Awe jini, awe shetani, kwangu ni mamoja."





    Akateremka na kuufuata ule mkoba kwa hatua za hima lakini kwa tahadhari, akitupa macho huku na kule.

    "Sasa!" Chiko akaamuru kwa mnong'ono mkali. Kila mmoja bastola mkononi, wakauanza mwendo wa kinyoka, wakitumia magoti na vifundo vya mikono na ncha za viatu. Hata hivyo walikwenda kwa kasi na kimya.





    Bob alikwisha fika, alikwishainama, amebakiza sentimita tu aguse mkoba, alipohisi hatari. Akageuza kichwa atazame nyuma.

    Akajikuta anatazamana na mdomo wa mtutu. Macho yakamtoka pima. Akafumbua mdomo. Aseme neno au apige yowe? Hakuna ajuae.

    Bastola ya Fensy ikabweka mara mbili kwa mishindo mikubwa na cheche za moto. Risasi zote zilipenya ubavuni. Bob akapepesuka kama mlevi na kuanguka chini.





    Fensy akaanza kupekuwa mifuko yake. Mishindo ya bastola ya Fensy ilimgutusha Kikoti vibaya sana. Akitetemeka kama ukuti akaanza kuhangaika na mlango wa gari. Alipofanikiwa kuufungua akasukumwa kwa nguvu na kurudi garini.

    "Ni nani wewe?" Chiko akafoka kwa sauti ya Kisajinimeja.

    "Kikoti. Naitwa Kikoti. Tafadhali bwana mkubwa."

    "Na mwenzako? Ni nani mwenzako?"

    "Bob. Anaitwa Bob. Trafiki. Askari wa barabarani. Bwana mkubwa.....ndugu yangu...."

    "Mliijuaje siri ya Bwana Kessy?"

    "Miye nafanya kazi kwake. Shambaboi....Mtunza Bustani."

    "Ni nani mwingine anaijua siri hii?"





    "Hakuna. Hakuna, bwana mkubwa. Butu kakataa kushiriki."

    "Ndiye nani huyo Butu?"

    "Mwenzake na Bob, askari pia. Trafiki. Kakataa kushiriki, katukataza lakini hatukumsikiliza. Loh,tumefanya makosa makubwa sana, bwana mkubwa. Nakuomba."





    ****************************************





    Denny alitoka nje ya hoteli akaangaza kulia na kushoto. Kijana mmoja akamfuata. "You wanna shot,mister?" Denny akamtazama. Hakuwa Dikwe. "**** - off." Akamwona Dikwe. Akamwendea. "Twende garini." Alimwambia na kuelekea alikoegesha gari la babake.





    Dikwe akamfuata bila swali lolote kama vile hilo lilikuwa jambo la kawaida kabisa kwake. Denny akaufungua mlango wa gari, akaingia garini na kuufungua mlango wa upande wa kushoto.

    "Ingia garini."

    Dikwe akaingia. Hilo pia lilikuwa jambo la kawaida kabisa kwake. Akauliza nikupatie nini?"

    "Siyo hapa." Denny akalitia gari moto, akaligeuza na kuliingiza barabara kuu.



    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    "Tuna kwenda wapi?" Huyo pusha aliuliza.

    "Uwanja wa gofu."

    "Mbona ni mbali mno?"

    "Ndiko ninakofanyia vitu vyangu."

    "Akh, kuna sehemu nyingi nzuri hapa karibu tu."

    "Sikiza, mteja ndiye kingi. Nimesema Uwanja wa Gofu, hivyo ni Uwanja wa Gofu.Si kokote kwingine."

    "Itakugharimu pesa zaidi, kwa maana muda wangu."

    "Usijali pesa, jali kuridhika kwangu."

    "Oh, utaridhika tu. Sijawai kumwangusha mteja."

    "Nami natazamia hivyo."





    Baada ya dakika kama kumi za mwendo mkali wakafika Uwanja wa Gofu.Denny akalipeleka gari katikati ya uwanja, mbali sana na barabara kuu.

    Akalizima moto bila kuzizima taa za mbele. Akateremka, akazunguka na kuufungua mlango wa mkono wa kushoto. Akasema. "Nje."

    Dikwe akateremka akisita. Bila shaka kwa sababu ya kubadilika kwa sauti ya mteja wake. Akauliza kizembezembe, "Unatumia nini?"

    "Situmii hata sigara ya kawaida." Denny akamjibu. "Achilia hayo madude yenu yaliyolaaniwa."

    "Ebo! Sasa hapa umenileta kufanya nini?"

    "Maswali."





    Denny akamkuda huyo pusha na kumsukumia mbele ya gari ambako mwanga wa taa ulishamiri kikamilifu na kumpofua kwa muda.

    "Ni nani wewe?"

    "Kashkash." Denny alimjibu kwa sauti tulivu kabisa.

    "Kashkash?"

    "Ndyo. Jini mbaya kuliko majini yote."

    "Wewe ni askari?"

    "Sasa hivi utaomba uwe katika mikono ya Polisi. Ungekuwa katika mikono salama kabisa."





    Kufumba na kufumbua, kisu cha springi kikawa kwenye mkono wa Dikwe, kimeshafyatuliwa. Kilikuwa cha nchi sita,kipya, kinachometa, kinachotisha, chenye ncha ya sindano na makali huku na huku.

    Denny akakitazama kama unavyoutazama mswaki uliovunjika. Usio na kazi tena.

    Dikwe akakurupuka mzimamzima. Siyo tu kisu kikakata hewa, bali pia, katika nukta hiyo hiyo mkono wa Dikwe ukadakwa akarushwa msobemsobe.





    Akiwa hewani mfupa wa mkono ukalia 'ko'! Akadondoka chini kwa kishindo, akiguta. "Mamaa! Mkono wangu!"

    Mbudu zilishaota umande wa usiku wa manane, na harufu ya janikiwitii ilizagaa kote. Dikwe, pua chini, aliipata harufu hiyo kikamilifu.

    "Bado unayo mifupa mingine." Denny alimwambia. "Kama unaithamini utanieleza kila kitu kuhusu Hoza."

    "Nikueleze nini?" Dikwe alilalama. "Kwa nini usimuulize Hoza mwenyewe? Unamwogopa kwa vile ana bastola. Unanionea mimi mnyonge!"





    "Siwezi kumuuliza kitu Hoza."

    "Ndiyo. Unamwogopa. Ana bastola!"

    "Hoza ameshakufa mpumbavu mkubwa we. Na kwa taarifa yako kauliwa na kigori tu."

    Dikwe akaanza kutambaa kwa magoti na mkono mmoja. Akainuka na kuanza kukimbia kilevilevi.

    Denny akamtazama anavyoyumba huku mkono mmoja kaukumbatia. Kwa hatua chache tu ndefu akamfikia. Akampiga ngwara. Akaanguka tena kifudifudi. Denny akaiteremsha soli ya kiatu chake kwa nguvu kwenye mguu wa huo pusha. Mfupa mwingine ukalia 'ka'.





    "Mamaa! Mguu wangu!" Dikwe akaanza kupiga mayowe. "Nakufa! Mama nakufa! Jamani nauwawa!"

    Lakini hata yeye mwenyewe alitambua kuwa anafanya kazi bure. Mhali hapo palikuwa kama kisiwa kisicho na watu. Hata mivumo ya magari yanayopita kule barabarani haikusikika.





    "Sikiza!" Denny alifoka kuyakatiza mayowe yake. "Endelea kuleta ufal@ na hutabakiwa hata na mfupa mmoja mwilini mwako."

    "Unanionea bure. Mimi sijui chochote." Alilalama tena Dikwe. "Sijui chochote."

    "Umesema Hoza ni rafiki yako sana." Denny alimkumbusha. "Umesema leo anakazi ya maana, kazi ya milioni mbili. Ni kazi gani hiyo?"





    "Ya kumlipua mtu."

    "Ni nani mtu huyo?"

    "Simjui. Hakuniambia."

    "Ni babangu. Unaona? Mtu aliyetumwa akamwue ni babangu mzazi. Kwa hiyo lazima uniambie ni nani aliyemtuma Hoza akamwue babangu, na utaniambia tu utake usitake. Ikibidi tutakesha hapahapa nikikuvunja mfupa mmoja mmoja. Chaguo ni lako. Sasa, ni nani aliyemtuma Hoza akamwue babangu?"

    "Simju. Naapa simjui. Hoza hakuniambia." Dikwe alisema kwa sauti ya kilio.





    Denny akatikisa kichwa. "Haitasaidia kitu. Ni lazima nimjue tu mtu huyo. Na kama nilivyokwambia Hoza ameshakufa. Hivyo hawezi kunisaidia."

    "Sasa mimi nifanyeje?"

    "Lazima kuna mtu anayemfahamu mtu aliyemtuma Hoza. Watu wa aina ya Hoza huishi katika vikundi. Lazima atakuwa na marafiki. Nawe lazima utakuwa unawajua. Nataka majina yao na jinsi ya kuwapata."





    "Siwezi kukutajia."

    "Kwa nini?"

    "Ni watu wabaya sana. Wataniua."

    "Unadhani mimi ni mtu mzuri?" Denny alimuuliza kibezo. "Unadhani baada ya kuimaliza mifupa yako yote utakuwa ungali hai? Uti wa mgongo na mfupa wa shingo ndivyo nitakavyokumalizia. Watu wa aina yako hamna thamani hata ya panya. Hamstahili kuishi."





    Dikwe akabaki akitweta na kuugulia. Kaloa jasho mwili mzima ingawa kibaridi cha usiku wa manane kilishakolea.

    "Ni nani mwenzake Hoza?" Dennya akamuuliza.

    "Chiko na Fansy." Dikwe akajibu kifisifisi.

    "Ni watu wabaya sana, wote wana bastola, wote ni wauaji."

    "Nitawapateje?"

    "Sijui. Hawakai mahali pamoja muda mrefu. Huhama hama."

    "Wamewai kukaa Tupetupe Hoteli?"

    "Ndiyo."

    "Kwa heri." Denny akaanza kuondoka na kueleke alikoliacha gari.

    "Huwezi kuniacha hapa!" Dikwe alipiga kelele, "Nitaliwa na mbweha!"

    "Nawatakia karamu njema."









    Pamoja na hekaheka zote za usiku, Denny aliamka mapema, akaoga, akavaa na kumuaga mamake. "Nakwenda hospitalini. Hapana haja ya kwenda sote asubuhi hii, wewe utakwenda baadaye."

    "Sawa." Alijibu mamake kwa sauti yake ndogo. "Naandaa kifungua kinywa."

    "Vizuri kabisa. Nitakaporuridi nitakuwa nimebanwa na ubao." Denny alijibu kumchangamsha mamake ambaye aliguna tu na kwenda jikoni.





    Denny akatoka na kuingia garini. Dakika chache baadaye akaliegesha gari nje ya hosptali ya kuu ya taifa. Akaukuta mlango wa chumba cha babake ukiwa wazi, Dk. Beka akimkagua mgonjwa, akamuamkia "Shikamoo mjomba."

    "Marahaba Denny," alijibu Dk. Beka, "Karibu"

    "Asante." Denny akasimama akimwangalia babake aliyelala ametulia tuli akipumua taratibu.

    "Ganzi imeshamtoka." Alielekeza daktari huyo.

    "Nimemdunga sindano ya usingizi. Alipozinduka tulizungumza maneno machache." (Kama vile alikuwa anahitaji ushauri wangu)!





    "Lakini ukweli ni kwamba anahitaji mapumziko kadri iwezekanavyo. Ukumbuke hilo. Akiamuka usizungumze naye sana."

    Denny akakubali kwa kichwa. Akauliza. "Nini hali yake kiujumla?"

    "Ni ya kuridhisha kabisa. Hayuko katika hali mbaya. Naamini baada ya wiki mbili au tatu, sanasana wiki nne atarudi nyumbani."

    "Akitembea mwenyewe?"

    "Denny usitazamie babako kutembea mwenyewe hivi karibuni. Kwa vyovyote sio chini ya mwaka mmoja." Dk.Beka akainuka. Akauliza , "Mamako ana hali gani?"

    "Hajambo. Ni mnyonge tu."

    "Ni jambo linaloeleweka alisema." Alisema Dk. Beka.

    "Tutaonana baadae. Nakwenda kuhudumia wagonjwa wengine."





    Mara tu baada ya Dk. Beka kutoka, Bessy akaingia

    "Denny!" Denny aliekuwa ameketi akainua uso. "Bessy alfajiri yote hii!"

    "Denny kuna mambo yasiyo ya kawaida yametokea jana usiku." Alisema msichana huyo. Kisha akakumbuka ustaarabu. "Lakini kwanza, vipi hali ya mzee?"

    "Hajambo. Dk.Beka amemaliza kumkagua sasa hivi. Ni mambo gani yaliyotokea jana?"





    "Mengi yametokea jana usiku, kama kawaida ya jiji hili. Lakini mawili si ya kawaida. Askari mmoja, Sajini Bob, amekutwa ameuwawa nje ya gari lake karibu na daraja la Singisa. Ndani ya gari mlikuwa na maiti nyingine. Wote wamepigwa risasi."

    "Na tukio jingine?"

    "Pusha mmoja aliyetambulika kwa jina la Dikwe amekutwa kaliwa na fisi kwenye Uwanja wa Gofu. Mawindo ya kawaida ya pusha huyo ni nje ya Tupetupe Hoteli."

    "Sikioni cha ajabu."

    "Denny! Jana usiku ulifika Tupetupe."

    "Kwa hiyo?"

    "Denny kama ni wewe ulimpeleka Dikwe Uwanja wa Gofu, unacheza mchezo mchafu."

    "Kumgonga babangu kwa gari ni mchezo safi? Kutaka kumwua akiwa mahututi kitandani ni mchezo safi?"

    "Unakili kuwa ni wewe uliyempeleka Dikwe Uwanja wa Gofu?"

    "Sikili chochote. Akh, Bessy, kumetukuchia vibaya. Twende zetu nyumbani tukafungue kinywa. Hukuja na mtu yoyote wa kumlinda wa kumlinda babaangu?"

    "Askari mmoja yuko nje. Twende zetu."





    **************************************



    Mara tu Denny alipoufungua mlango wa mbele, pua zao zikadaka harufu tamu ya staftahi. Akaita. "Mama, nimekuja na Bessy."

    "Karibuni huku jikoni." Mama Denny alijibu. "Kila kitu kiko tayari." Wakaingia jikoni. Bessy akasema. "Shikamoo mama."

    "Marahaba Bessy, karibu. Utapenda mayai ya kukaanga au macho ya ng'ombe?"

    "Macho ya ng'ombe. Lakini si ungeniachia niyatengeneze mwenyewe?"

    "Hapana. Labda iko siku jiko hili litakuwa lako. Lakini kwa leo acha nikuandalie. Ketini."





    Denny Bessy wakatazamana wakiketi. Bi mkubwa akauliza. "Kaamukaje mzee wenu?"

    "Kaamuka vizuri kabisa." Alijibu Denny. "Ganzi imemtoka, lakini mjomba amekataza kuzungumza naye kabisa. Amemdunga sindano ya usingizi. Ukumbuke utakapokwenda usizungumze naye sana. Anahitaji mapumziko. Mjomba amesema anaweza kurudi nyumbani baada wiki mbili au tatu tu."

    "Lakini hatakuwa yeye yule tene." Alisema Bi mkubwa kwa sauti nzito.

    "Ndiyo, utapita muda ndiyo aweze kutembea mwenyewe. Pengine mwaka mzima."

    "Siyo kutembea tu."



    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Denny akainua uso na kumtazama mama yake. Macho yake yakimsaili. Yakionyeshwa kutatanishwa. Baada ya kimya cha muda, Bi mkubwa akasema. "Nimemwota yule msichana." Alisema hayo kwa sauti nzito zaidi. Iliyojaa majonzi. Sura yake ilikuwa kama hakuwa hapo, yaani mbali sana.

    "Msichana gani?" Denny akauliza alipomwona mamake haendelei.

    "Aliyeuliwa na Kassim Hashir." Alijibu Bi mkubwa. "Ameniomba...hapana. Ameniamuru nikueleze kisa chote, bila ya kukuficha lolote."

    "Kisa cha huo uhasama kati ya baba na huyo Kassim Hashir?"

    "Ndiyo."





    Denny akasuburi, nusu akiwa na shauku ya kukisikia kisa hicho,nusu akimhofia mama yake. Akimhurumia kusimulia kisa ambacho dhahiri ni kichungu. Akasema. "Mama ,hatuwezi kusubiri mpaka baada ya kula?"

    "Unadhani nitatokwa na machozi tena?" Bi mkubwa akatikisa kichwa. "Kipindi cha majonzi kimepita. Nimelia kiasi cha kutosha jana usiku. Usingizini, wakati nikiota ndoto hiyo. Nahisi kuishiwa kabisa na machozi."





    Baada ya kimya kifupi Bi mkubwa akaendelea.

    "Ilikuwa ni miezi michache tu baada ya mimi na Ray kufunga ndoa. Siku moja msichana huyo akaja hospitalini. Akatukuta mimi nikiwa nesi wa zamu na Ray daktari wa zamu."

    "Alikuwa msichana wa kati ya miaka kumi na sita na nane aliyevaa sare za sekondari. Akampa Ray karatasi..."

    "Dk.Raymond Makete, wakati huo akiwa kijana kabis, akakipokea kikaratasi hicho. Akakisoma, kiliandikwa, 'Daktari wa zamu, mshughulikie msichana huyo. Kassim Hashir.'





    Hakuna hata tafadhali. Wakati huo Kassim Hashir alikuwa kigogo serikalini, mtu wa kuogopwa. Ukimuudhi yeye, umemwudhi fasishti Ibrahim Mbelwa. Ungeweza kuhatarisha maisha yako,au ukatupwa kizuizini na kuteswa kikatili. Dk. Makete akamuuliza msichana huyo, 'Kwani una matatizo gani?'

    "Msichana akanong'ona maneno ambayo Makete hakuyaelewa. Akamwuliza, 'Kitu gani?' 'Nna mimba.' alisema msichana huyo kwa sauti ndogo sana.





    'Hilo si tatizo, Makete akamwambia. Ni kawaida kwa mwanamke kupata mimba. Au inakusumbua?'

    'Hapana'

    'Kumbe?'

    'Ni ya Kassim.'

    'Kwa hiyo.'

    'Haitaki. Kanambia niitoe.'

    'Hiyo ni bahati mbaya sana. Hapa hatufanyi kazi ya kuua, tunafanya kazi ya kuokoa maisha.'

    "Msichana akaumauma mdomo wake wa chini machozi yakimlengalenga.

    Dk. Makete akamwuliza, 'Ni ya miezi mingapi?'

    'Mnne.'





    'Nakushauri usiende ukajaribu kuitoa wewe mwenyewe huko nyumbani.'

    'Lakini ningali nasoma'

    'Itakubidi uache shule.'

    'Babangu...babangu!'

    "Dk. Makete akatisa kichwa...'Nashindwa kuelewa kwa nini mnafanya mambo haya na hali mkijua kuwa matokeo yake ni matatizo matupu!'

    "Msichana akageuka aondoke."

    'Sikiliza!'

    "Akageuka tena."

    "Pia nakushauri usirudi kwa Kassim Hashir." Dk. Makete alimwambia msichana huyo. "Kassim Hasshir si binadamu. Ni mnyama. Ameshaua watu kadhaa, mmojawapo akiwa babake mzazi."





    "Miezi mitatu au mine ikapita." Mama Denny aliendelea kusimulia kisa hicho kwa sauti yake ndogo, ya chini, iliyojaa majonzi. Alizungumza kama anayeota, au mtu anaye zungumza peke yake, kichwa kakiinamisha kama mtu anayesali.

    Denny na Bessy wakaendelea kuganda. Hawali,hawaongei,hawakohoi. Hata kupumua hawakupumua kikawaida. Zilikuwa pumzi ndefu, waliziachia pale tu ilipolazimu, haiwezekani tena kuibana. Walikuwa kama watu wanaoangalia sinema ya kusikitisha sana.





    Lakini hawakuwa wanasikitishwa na kisa chenyewe. Kwanza. kilikuwa hakijafika mbali. Hadi hapo hapakuwa na chochote cha kuwasikitisha. Miaka nenda, miaka rudi, daima wasichana wasomao walilifanya kosa hilo alilolifanya msichana huyo anayesimuliwa. Kwa sababu moja au nyingine, wanafunzi hufanya mapenzi , hushika mimba, na kuzitoa. Lilikuwa jambo la kawaida kabisa. Na pengine litakuwa hivyo mpaka mwisho wa dunia.

    Pili kisa chenyewe kilitoke zamani sana, pengine kabla ya wao kuzaliwa. Na tatu, na hili lilikuwa mhimu zaidi kwao, kisa hicho, kadri walivyokitambua wao, hakikuwahusu sikio wala ndewe.





    Kilichowasikitisha wao ni jinsi Bi mkubwa huyo mwenye mvi za kurashia, sura karimu na sauti adhimu ilivyosikitisha. Ni dhahiri alikuwa katika wakati mchungu mno sasa na hapo kale. Kidhati walitamani asiendelee na simulizi ile, lakini midomo yao ilikuwa mizito kama iliyoshonwa.

    "Mama.." Denny akajikuta akiupanua mdomo wake, kwa juhudi kubwa "Mama..."

    Bi mkubwa akatikisa kichwa, bila ya kukiinua.

    "Nakwambia kaniamuru." Akasema kwa sauti ndogo, na ya chini.





    "Mama, hakuna mtu yeyote duniani wa kukuamuru kufanya jambo usilotaka kulifanya." Denny akiwa wima, ganzi ya uzezeta ikiwa imemtoka. "Hakuna, si mimi, si baba, si yeyote."

    "Denny, aliyeniamuru hayuko duniani."

    "Ooh, ndoto! Mama!" Denny akaliza ulimi. Si songo, si bezo. Ni masikitiko tu. "Mama, kwa kweli unanishangaza. Sikutazamia kama ungeweza kuwa mtu wa kuweza kusumbuliwa na ndoto."

    "Denny, haikuwa ndoto ya kawaida."

    "Kuna ndoto za kawaida na zisizo za kawaida?"





    "Ndiyo, Denny. Hata mimi nilikuwa silijui hilo. Hata mimi ningebisha, lakini hii haikuwa ndoto ya kawaida. Sijapata kuota ndoto kama hii. Nyinyi pia hamjapata. Si kila mtu humjia. Hii si ndoto,ni kama ... kama maono."

    "Vizuri, utatusimulia siku nyingine. Sasa acha tuendelee na kula."

    "Na hali jana mlinibembeleza niwasimulie!" Akakumbusha Bi mkubwa.

    "Ooh, sasa si mhimu tena.Dakika yoyote ile sasa tutamshika huyo firauni. Isitoshe, baba ameshazinduka. Atatusimulia yeye kisa hicho."

    "Baada ya wiki mbili au tatu?"

    "Nakuambia sasa si muhim tena."

    "Hapana, Denny huyo msichana kaniamuru na nimemwaidi. Anajua mimi sivunji ahadi. Kwa hiyo keti usikilize."





    "Mama, unataka kunilazimisha kusikiliza kisa cha kipumbavu na kisichonihusu?"

    "Laiti ungejua!" Uso ukambadilika Denny.

    "Naam?"

    "Laiti ungejua." Bi mkubwa alirudia kwa sauti yake ndogo.

    "Laiti ungejua. Na hilo tatizo lenyewe."

    Denny akapumua na kurudi kitini.









    Kembo alikuwa anatoka bafuni kuoga, kengele ya simu ilipolia sebuleni. Akajifunga taulo vizuri na kuokota mkono wa simu. Akasema, "Yees?"

    "Mzee, mimi ni chiko."

    "Kitu gani asubuhi yote hii?" Kembo aliuliza kwa ikirahi, akijua ni masula ya pesa tu.

    "Mzee, lazima nikuone. Mambo si mazuri." Alijibu chiko.

    "Unamaana gani?"

    "Hoza amekufa. Na Dikwe ameliwa na fisi baada ya kutekelezwa Uwanja wa Gofu. Bila ya shaka alihojiwa."

    "Ndiye nani huyo Dikwe?"





    "Rafiki yake Hoza." Alijibu Chiko, akipumua kwa nguvu. "Jana usiku polisi walikwenda Tupetupe Hotel. Wakakipekua chumba cha Hoza na kuwahoji mapusha na maguberi kadhaa. Sisi hatukulala tupetupe, kwa kuhofia wanaweza kurudi."

    "Uko wapi sasa hivi?"

    "Karibu na soko kuu."

    "Umeshafungua kinywa?"

    "Bado."

    "Nenda Pundamilia Inn, kijichumba namba nane, agiza utakacho. Muhudum akikwambia hicho ni kijichumba maalumu, nitaje mimi."

    "Sawa mzee."

    "Nitakuwa nawe baada ya dakika kumi au kumi na tano." Alisema Kembo na kuikata simu.





    Akabonyeza namba aliyoizoea. Sauti nzito ya Kassim Hashir ikasema, "Yees?"

    "Bwana Kessy, ni Kembo hapa."

    "Unasemaje?"

    "Unatazamia kutoka asubuhi hii?"

    "Siyo kabla ya saa nne. Kwani vipi?"

    "Kijana wangu mmoja amenipigia simu sasa hivi. Anashuku mambo si mazuri."

    "Mabaya kiasi gani?"

    "Siwezi kusema mpaka nikutane na kuzungumza naye. Nitamwona baada ya robo saa hivi."

    "Unanishauri vipi? Niyeyuka?"





    "Hapana , ni mapema mno kwa hatua kama hiyo. Haitatokea haja ya kuchukua hatua kama hiyo. Sioni kwa nini nishindwe kuyadhibiti mambo. Pengine Chiko anataka kutaharuki bure. Pengine anataka kunifanya fal@ anipune kuliko tulivyopatana."

    "Sasa unanishauri nini?"

    "Tulia. Nitakuja mara tu baada ya kuzungumza na huyu kijana."

    "Vizuri"





    *************************************





    Miezi mitatu au minne ikapita. Kisa cha roba karne kikaendelea. Ndipo Bwana na Bibi Makete walipomona tena yule msichana. Na ndipo walipolijua jina lake Asha Rajabu.

    Safari hii hakwenda hapo hospitalini kwa miguu yake, bali kwa ambulance, na kukimbizwa thieta kwa machela, akiwa na majeraha mawili mabaya kwenye tumbo lake lililo fura.





    Siku hiyo Dr. Makete na mkewe walipangiwa shughuli za thieta. Wao na msichana huyo walikuwa kama waliopangiwa na Mungu mara hizo mbili.

    Mambo yakawa haraka haraka. Wataalamu wa vyombo vya upasuaji, Dk.Makete, mkewe... kila mmoja alikuwa kama cherehani cha umeme.





    Ni wakati akimwandaa kwenye meza ya upasuaji ndipo Bi. Makete akamtambua yule msichana. Akaguta, "Ray! Ray! Ni yule msichana wa Kassim Hashir!"

    "Ndyo." Akakubali yule msichana kwa sauti dhaifu.

    "Ndiye mimi Asha Rajabu."





    Kila jozi ya macho ikaenda mezani. Dk. Makete akajongea kando ya meza, huku akiendelea kuvaa glovu za kupasulia. Akasema, "Gosh! Ni yeye!" Kisha akameuliza , "Imekuwaje tena mama?"

    "Kassim kanipiga kisu." Alijibu Asha.

    "My God! Nilikwambia usirudi kwake!"

    "Baba kanifukuza nyumbani. Nilihitaji nauli niende kwa mjomba." Alisita akikusanya pumzi, kisha akaendelea. "Mimi sijali kufa. Lakini mwanangu... angali hai. Tafadhali..."

    "Nitahitaji kuwaokoa nyote."





    Bi mkumbwa akashusha pumzi na kuendelea. "Operation ikaanza. Ilikuwa ngumu kuliko tulivyotazamia. Ray akapambana nayo kwa karibu masaa mawili mazima."

    Akatikisa kichwa. "ilikuwa kazi bure. Wote tuliokuwa humo ndani tulijua kazi bure. Kisu kilikata sehemu mbili nyeti sana. Afadhali ingekuwa sehemu moja. Lakini sehemu mbili , ilikuwa ni operesheni tata ajabu. Lakini Ray hakukubali kushindwa. Wote alitushangaza. Alifanya kazi isivyo kawaida, huku akivujwa jasho usoni. Mungu peke yake ndiye anyefahamu idadi ya vitambaa nilivyovitumia kumfutia jasho."





    Bi mkubwa akatikisa tena kichwa. "Ilikuwa kazi bure. Mtu wa kwenye mashine ya mapigo ya moyo aliita mara tatu. 'Dokta... Dokta ... Dokta ...lakini aliendelea tu kushughulika. Kakata hiki, kaunga hiki, katoa hiki, kasafisha hiki... Ikanibidi nimshike bega na kumwambia, 'Ray, it's all over. She is gone! She is dead.'

    'God! Ooh Lord! It is horrible!' Ray aliduwaa kama asiyeyaamini macho yake. Msichana yule alikuwa kama ... kama mtu anayemhusu - anaetuhusu kwa karibu sana.





    Kwa mara ya kwanza na ya pekee - nikamwona Ray akitokwa machozi, tena hadharani. Sikuweza kujizuia. Hakuna alieweza kujizuia humo chumbani."

    Bi mkubwa akatoa leso na kupenga .

    Denny akauliza kwa sauti kavu, "Huyo mnyama hakufanywa chochote?"

    "Jesus, Denny!" Bessy akaguta. "Badala ya kuuliza habari za yule mtoto!"

    "Habari za yule mtoto nazifahamu."

    "Are you joking?"

    "No, I am bloody not."





    Bi mkubwa, kama vile vijana hao hawakusema lolote, akasema, "Kassim Hashir afanywe nini? Nani kati yetu athubutu kushitaki? Na hata kama tungeshitaki, asingefanywa lolote, alikuwa kama nusu - Mungu. Tungejitafutia matatizo ya bure tu."

    "Mama," Bessy akauliza kwa sauti ndogo, "Nini matokeo ya mtoto wa Asha, alinusurika au nae alikufa pia?"





    "Hapana, yeye alinusurika, mtoto wa kiume mwenye afya nzuri. Kisu kilimkata begani na takoni. Tukamshona na kumfunga. Hadi leo anayo makovu hayo. Atakufa nayo."

    Mabega ya Bi mkubwa yakaanza kucheza kabla ya sauti kusikika. "Atakufa nayo." Alirudia. "Atakufa nayo."

    Denny akaenda kumshika bega.

    "Mama umesema mwenyewe kipindi cha machozi kimepita."









    Zebra Inn ilikuwa uchochoroni, nyuma ya majengo mawili ya kale, ya kutunzia nyaraka za serikali. Pamoja na kuwepo bango getini lenye picha ya pundamilia, ungeweza kuupita mgahawa huo kama si harufu ya kukata pua ya vyakula mbalimbali.

    Na ulikuwa mgahawa wa aina yake. Ulikuwa kama uwanja wa tenesi. Katikati palikuwa na meza chini ya miavuli, na pande tatu zilikuwa na vyumba vidogo vya mbao na milango ya pazia za shanga. Upande wa nne kulikuwa na kaunta kwa wapendao kuketi juu ya stuli. Na nyuma ya kaunta kulikuwa na jiko.





    Mgahawa huo ulikuwa na sifa kubwa ya upishi wa kimataifa. Lakini bei za vyakula zilikuwa za kuchinja koo. Chiko aliingia humo akaenda moja kwa moja kijichumba Namba 8. Mlikuwa na meza ya wastani iliyozungukwa pande tatu na kitu kama siti ya nyuma ya gari la kifahari. Mara tu Chiko alipoketi, mhudumu aliyevaa suti nyeupe yenye picha ya pundamilia kwenye mfuko wa kifuani akaingia.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    "Mheshimiwa." Alisema mhudumu huyo kwa adabu, "Hukioni hicho kibao kisemacho 'private' hapo mezani? Twende nikupeleke chumba kingine."

    "Hapana. Ni Bwana Kembo aliyeniambia nije hapa. Yeye atafika sasa hivi."

    "Ooh! Samahani sana."

    "Hapana shaka." Alijibu Chiko kimkogo.

    "Nipatie kifungua kinywa."

    "Nikupatie menu?"

    "Hapana, nipatie kifungua kinywa kamili." Mhudumu akasita. Akasema, Naamini unaijua bei yake."





    Chiko akabetua midomo na kuuliza. "Unamashaka kuwa Bwana Kembo atashindwa kulipa?"

    "Ooh, hapana. Hapana, bwana mkubwa. Samahani sana."

    "Hapana shaka, usijali." Chiko akavua miwani yake ya jua na kuiweka mezani.

    "My God!" Akawaza. "Kuitwa 'bwana mkubwa' na mhudumu wa Pundamilia! Pesa! Laiti angejua!"





    Kembo akafika akaketi. "Tatizo gani linakusumbua? Simuni ulisikika kama kigoli aliyedondokewa na nyoka kitandani!"

    "Nilikuwa sijapata shoti yangu ya asubuhi." Alikiri Chiko. "Vitu vyangu vipo Tupetupe ambako naogopa kwenda, polisi wazaweza kuwa wananiwinda."

    Akiwasha sigara, Kembo akasema, "Chiko, huo wasi wasi wako ni wa kweli au...au."

    "Au kitu gani Bwana Kembo?"

    "Isiwe unataka kunitoa pesa za ziada. Kama ni pesa sema wazi tu."

    "Bwana Kembo, ingawa watu hustihizai, lakini umeshawai kumwona mtu aliyekata tawi alilolikalia?"

    "Sijawai. Na sitazamii kumwona."





    "Isitoshe, kama ningekuwa mtu wa tamaa, ningemdai rafiki yako kifumba mdomo. Na usitazamie nitakuwa mpumbavu kama Kikoti."

    "Alichokifanya rafiki yangu unakijua?"

    "Sikijui kwa hakika, lakini nashuku anatafutwa na polisi kutokana na swala la yule Daktari aliyegogwa na gari jana asubuhi."

    Kembo akainua mikono, ishara ya kumnyamazisha, kwani mhudumu aliingia.

    "Shikamoo Bwana Kembo."

    "Marahaba. Za asubuhi?"

    "Shwari." Alijibu mhudumu, akiandaa vitu mezani. "Nikupate nini?"

    "Kahawa tu kama kawaida. Bila ya sukari, bila ya maziwa."





    Mhudumu alipoondoka Kembo akayarudisha macho yake kwa Chiko. "Naamini hutafanya kitu kama hicho."

    "Kitu gani?" Chiko aliuliza akijikorogea chai.

    "Kumdai rafiki yangu kifumba mdomo."

    "Alaa, ningekuwa na hata chembe cha wazo hilo, ningekwambia niliyokueleza?"





    Kembo akaafiki kwa kichwa. Akasema, "Subiri kahawa yangu iletwe kisha nieleze kila kitu."





    *****************************************





    "Twende Kituo Kikuu." Alisema Bessy akiingia garini, Denny akaliwasha. "Kuna nini Kituo Kikuu? Nilikuwa na mipango mingine."

    "Kama ipi?"

    "Kama kumtafuta mkora mmoja anaitwa Chiko." Denny aliligeuza gari na kulielekeza mjini.

    "Chiko? Jina hilo si geni kwangu, lakini sura imenitoka. Kwani wa nini?"

    "Ni rafiki yake Hoza."

    "Unataka kumtafutia wapi?" Bessy aliuliza.

    "Katika sehemu za kijinga kama vile Tupetupe."

    "Unamjua alivyo?" Denny akatikisa kichwa. "Simjui."





    "Basi twende Kituo Kikuu kwanza. Pengine tuna picha yake. Isitoshe," Bessy akaendelea, "Nataka kumhoji Butu."

    "Ndiye nani huyo Butu?"

    "Ni mwenzake Bob, askari wa barabarani aliyeuwawa jana usiku. Kifo chake kinanitatanisha na kunikereketa. Yeye na Butu walikuwa pamoja jana asubuhi, kwenye ajali ya babako walikuwa biti moja. Mara kwa mara walipangwa pamoja. Nadhani walikuwa marafiki. Nataka kufuatilia nyendo za Bob kwa jana. Pengine Butu anaweza kuwa anajua kitu kuhusu kifo cha rafiki yake. Nilipokwenda asubuhi, alikuwa hajawasili. Nikaacha maagizo afikapo anisubiri, asipewe biti."





    "Inaelekea unashuka kifo cha huyo Bob kinahusia na mkasa wa babangu."

    "Kuna kitu kinaniambia hivyo ubongoni mwangu." Alikri Bessy.

    "Hisia ya sita?"

    "Kitu kama hicho. Hebu niambie jambo moja. Mama alishawahi kukusimulia kisa kile,siyo?"

    "Hata mara moja."

    "Kumbe, kwa nini ukasema unazifahamu habari za mtoto wa Asha kabla ya mama kutusimulia?"





    "My God! Bessy! Sikujua kama unaweza kuwa zumbukuku kiasi hicho!" Alisema Denny kwa ikirahi. Akalisimamisha gari pembeni ya na kuanza kufungua vifungo vya shati.

    "Denny unataka kufanya nini?" Denny hakujibu. Akalifungua bega lake la kushoto. Bessy akatoa macho na kupiga yowe. "Nooooo!"

    "Hilo jingine," Akasema Denny akivifunga vifungo, "Utaliona siku nyingine."

    "Ooh! My God Denny, I'm sorry. Terribly! sorry!"





    "Wanajeshi wenzangu hulitazama kovu hili kwa heshima kubwa, wakidhani nimelipata kishujaa."

    "Lakini Denny, umelipata zaidi ya kishujaa. Mungu wangu,Denny umeanza kukwepa visu tangu ukiwa tumboni! Ndiyo maana huviogopi."

    "Nani kakwambia uongo huo?" Denny aliuliza akiling'oa gari.





    "Palikuwa na kimoja - tena cha kijahili, karibu na maiti ya Dikwe, huyo pusha aliyetafunwa na fisi. Kilikuwa na alama za vidole vyake."

    "Kwa hiyo?"

    Msichana Bessy akainua mabega. "Ni dhahiri kuwa yeyote yule aliyempeleka Uwanja wa Gofu , akamnyuka na kumtelekeza haogopi visu."





    **********************************





    "Sijui niazie wapi." Alisema Chiko. "Mambo yenyewe yananitatanisha hata mimi."

    "Anza tangu mwanzo." Alishauri Kembo.

    "Mwanzo wake unaujua. Ulimtuma Hoza akamlipue yule bwana aliyegogwa na gari, mgonjwa wa jengo D, chumba namba 13. Hakufanikiwa. Badala yake kalipuliwa yeye. Tena na msichana tu - Kachero Isnpekta Bessy. Kumbe yule mgonjwa analindwa na polisi masaa ishirini na nne."





    Kembo akameza funda la kahawa yake chungu. Akasema, "Mpaka hapo sikioni cha kukipigia mayowe."

    "Sio hilo tu. Pana mengine. Wakati sisi tuko kule darajani, polisi walikwenda Tupetupe. Bila sha Hoza alitembea na ufunguo wa chumba chake. Hata hivyo hawakuutumia, walimwamuru meneja afungue mlango. Kwanza walikuwa watatu, Bessy na makachero wawili wa kiume. Kisha akafika wa nne,kijana mdogo tu."

    "Sasa wewe umeyajuaje yote hayo?"

    "Bwana Kembo unadhani mimi naishi kijinga? Sehemu kubwa ya mapato yangu inaishia kwa washikaji zangu. Hapo Tupetupe watu kibao hufaidi fadhila zangu.





    "Watumishi wa hoteli hiyo, mapusha, mashangingi na hata mashoga. Hata meneja wa hoteli hiyo hupokea fadhila zangu."

    "I see!"

    "Mimi na Fensy tuliporejea hapo hatelini jana usiku tulidakwa na washikaji kabla ya kuingia ndani. Walishanong'onezwa na meneja na watumishi wengine nini kinachoendelea. Mmojawapo akiwa Dikwe, jambo ambalo linanishangaza."

    "Kwa nini?"

    "Yeye alikubali kuchukuliwa na huyo askari wa nne na kupelekwa Uwanja wa Gofu."

    "Labda hakujua kuwa askari."

    "Inawezekana. Hata Chox ana mashaka kama jamaa ni askari. Aliwasili hapo Tupetupe na gari la aina ya kipekee. Linaitwa Bentley.





    Lilly akataka kumdaka akaambiwa, 'Go screw yourself!' Dikwe akamtachi. Kijana huyo akasema anamtafuta Hoza,ambaye alidai ndie pusha wake wa kawaida. Kisha akaingia ndani na kwenda ghorofa ya nne, kwenye chumba cha Hoza. Chox akamfuta Dikwe akamuuliza, 'Vipi, yule kijana ni kastama wako?' Dikwe akajibu ni wa Hoza. "Sijapata kumwona ." Alisema Chox.

    "Hakumwambia Hoza hayupo?"

    Dikwe akasema alimwambia, lakini hata hivyo alikwenda juu kuhakikisha.





    "Hukumwambia chumbani mwake kuna unaa?" Chox akamwuliza Dikwe.

    "Dikwe akasemaje?"

    "Akasema hafanyi kazi ya kanisa."

    "Enhe, kisha?"

    "Kijana huyo akaingia chumbani mwa Hoza, lakini hakukaa sana. Lakini habari zilishazagaa aliposhuka chini , Chox, ambaye hakuwa na chochote maungoni ili amcheki vizuri. Akamuuliza kama alihitaji huduma."

    "Akamjibuje?"

    "**** off."

    "Kuna chochote katika jibu hilo?"

    "Ni vigumu teja kumjibu hivyo pusha. Wao ni watumwa wetu, kwa kawaida hutunyeyekea."

    "Kisha ikawaje?"

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    "Kijana huyo akamwendea Dikwe. Wakaingia ndani ya gari lake. Chox akataka kwenda kumshitua Dikwe lakini hakuwahi. Udhaifu wa Dikwe ni kwamba alikuwa na tamaa sana. Na alikiamini sana kisu chake."

    "Unasema alimpeleka wapi?"

    "Uwanja wa Gofu."

    "Kijana huyo ni kachero," Kembo aliuliza, "Kwa nini ampeleke Uwanja wa Gofu badala ya kumpeleka kituoni?"

    "Ni wazi ili akamhoji. Na alitaka majibu ya haraka. Huwezi kupata majibu ya haraka kituoni."







    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog