Search This Blog

Sunday, 20 November 2022

NJIA NYEMBAMBA (2) - 3









    Simulizi : Njia Nyembamba (2)

    Sehemu Ya Tatu (3)





    Baada ya muda alimuona mfanyakazi, akamuita na kumuuliza wapi alipo Rose. Kwa hofu, mfanyakazi alijibu hajui wapi alipo mtu huyo kwani hakumuona tangu alipoingia chumbani kwake.



    “Ebu niletee kinywaji haraka!” Talib akaagiza. Basi upesi mfanyakazi akapanda ngazi za juu kufuata jokofu kubwa la kuhifadhia vinywaji. Alifungua jokofu akatwaa kinywaji mmoja kilichofadhiwa kwenye chupa yenye chapa ya Jack Daniels. Alitwaa na glasi ndefu akaziweka kwenye sahani ndefu ya aluminiam tayari kwa ajili ya kumpelekea Talib.



    Ila kabla hajashika ngazi ya kushuka chini, alisikia akiitwa kwa sauti ya chini. Aligeuka akaangaza, hakumuona mtu! Aliogopa.



    “Tazama nyuma ya ua kubwa hapa,” sauti ilisema. Mfanyakazi akatazama. Loh! Akamuona Rose. Kwa namna alivyokuwa amejibana kwenye ua hilo kubwa, ni labda tu malaika akuambie kuna mtu hapo, la sivyo huwezi ukagundua.



    Mfanyakazi alisogea kwenye ua hilo, Rose akamnong’oneza.



    “Mtilie sumu!”

    Macho ya dada wa kazi yakatumbuka.

    “Siwezi!”



    Rose alichukua glasi akatia kitu kama mchanga wenye rangi nyeusi. Ni kama vile alijiandaa na lile tukio, haikujulikana wapi alitolea kile kitu alichokitia glasini. Alirejesha glasi kwenye sahani kisha akamtaka mfanyakazi aende kumpatia Talib kinywaji.



    “Hakikisha anakunywa,” alisisitizia. “Nenda!”



    Dada wa kazi aliondoka akiwa anatazama nyuma. Ni kama vile hakuamini macho yake. Alijawa na shaka, mikono yake ilikuwa inatetemeka.



    “Mbona umechukua muda hivyo?” Aliuliza Talib.

    “Nil – nilikuwa nakuchagulia …”

    “Nini?”

    “Kinywaji mhesh-imiwa.”

    “Ndio muda wote huo?”

    “Samahani mheshimiwa.”



    Dada wa kazi alifungua kinywaji, akamiminia kwenye glasi. Sasa alikuwa anatetemeka mno kiasi kwamba alishindwa kabisa kutulizia mdomo wa chupa glasini. Talib alimtazama, akamuuliza:



    “We mwanamke una shida gani?”









    “Ah – ah! Sina shida!” Alijibu mfanyakazi akitikisa kichwa. Macho yake hayakuwa yanamtazama Talib, aliogopa. Talib alimdaka mkono uliobebelea kinywaji, akamkazia macho yake makali.



    “Una nini?”



    Macho ya mwanamke yalikuwa mekundu, na ghafla yakaanza kujaza machozi.



    “Sina kitu mheshimiwa!”



    Talib alikwapua chupa ya kinywaji, akamwamuru mfanyakazi apotee mbele ya macho yake. Hakuona tena haja ya kutumia glasi iliyokuwa imetapakaa kinywaji, basi akapeleka mdomo wa chupa kinywani mwake na kunywa mafundo kadha wa kadha kana kwamba anakunywa juisi.



    Aliendelea kunywa na kunywa akiwaza na kuwazua, akingoja Rose aletwe mbele yake kwa ajili ya adhabu. Alimaliza chupa yote pasipo mrejesho wowote wa oparesheni, akampigia simu kiongozi kumuuliza kinachoendelea.



    “Bado hatujampata, mkuu. Tunaendelea kutafuta!”



    Talib alingoja akibinua mdomowe. Kinywaji kimoja alichokunywa kilimtosha asihitaji kuongeza cha ziada. Kichwa kilikuwa kinapiga marimba kwa mbali, Jack Daniel akizurura. Basi taratibu usingizi ukaanza kumkweza.



    Walinzi lukuki waliokuwa wamekaa nje, hawakuwa wanajua kinachoendelea huko ndani. Macho na midomo yao ya bunduki ilikuwa imeelekezea nje wakiwa wamejiweka tayari kabisa kwa ajili ya kupambana dhidi ya watu wa aina yeyote watakaotishia uwepo wa amani. Hawakujua adui mkubwa zaidi alikuwepo ndani na si nje.



    Baada ya muda kupita, Rose aling’amua ya kwamba Talib alikuwa amelala usingizi wa kilevi kochini. Taarifa hiyo alipewa na mfanyakazi wake baada ya kukiri kushindikana kwa zoezi la kwanza – kumpatia sumu ‘adui’. Alichungulia kuhakikisha. Akatazama pia na nje, mazingira yalikuwa sawia.



    Alienda jikoni kutwaa kisu. Mkono wake ulikuwa unatetemeka. Alisogeza hatua zake kufuata ngazi za kushuka chini sebuleni. Kichwa chake kilikuwa kinagonga kwa mawazo, vipi kama akishindwa? Lakini moyo wake ulimwambia vipi kama akifanikiwa? Na huo ndio uliofanikiwa kumshinda.



    Huu ulikuwa ni wasaa wake wa kumaliza mzizi wa fitna. Kwa namna moja ama nyingine alijehesabia kama akifanikiwa kufanya hilo tukio, basi ataonekana shujaa mbele ya wafanyakazi lakini pia wale wote wanaoteseka kwa njia moja kwasababu ya utawala wa Talib. Aliwaza pia huo ndio utakuwa mwanzo wa mapinduzi ya kweli nchini Sierra Leone.



    Mapigo yake ya moyo yalikimbia, jasho likamtiririka. Macho yake kama mbwa mwizi yalizunguka huku na kule akihema taratibu.



    Kweli alikuwa amelala. Rose alisimama mbele ya Talib pasipo mwanaume huyo kufanya chochote, isipokuwa kukoroma. Aliutoa mkono wake uliobebea kisu nyuma ya mgongo, akaukutanisha na mwingine kushikilia mpini.



    Lahaula! Kabla ya ncha ya kisu kutoboa kifua cha Talib, ghafla mkono mnene wa Taib ulidaka mikono yote miwili ya Rose. Macho mekundu ya mwanaume huyo yalitoka nje kwa namna ya kuogopesha. Mkono wake mwingine ulikwapua kisu toka kwenye mikono ya Rose, kisha ukamzaba kofi zito. Rose akarukia maili moja mbali!



    “Pumbavu uliyekithiri!” Talib alilaani akinyanyuka, mkono wake wa kulia ulikuwa umebebelea kisu.



    “Unadhani mimi nakufa kikondoo hivyo? Nimekwepa risasi nyingi mpaka kuwepo hapa. Mikono mingi ya wanaume ilishindwa, itaweza ya mwanamke malaya kama wewe!”



    Rose hakujibu kitu. Uso wake upande wa kushoto ulikuwa mwekundu kana kwamba bendera. Kiganja na vidole vya Talib vilikuwa vimemwachia chapa ya uhakika. Macho yake yalikuwa mekundu pia mdomo wake akiubenua.



    Mlinzi mmoja alifungua mlango kutazama usalama, Talib akamwagiza awahabarishe wenzake warejee kwani ameshampata mhusika. Mlinzi akafunga mlango na kutekeleza agizo.



    “Sasa leo itakuwa ni siku yako ya kujifunza,” alisema Talib. “Kama mama yako alishindwa kukufunda, acha nimsaidie.”



    Alivua mkanda wa sare yake ya jeshi, akaukamata mkononi. Alimtandika nao Rose kana kwamba anamchapa punda. Rose alipiga kelele kali za maumivu, ila hakuna aliyediriki kuja kumsaidia. Mfanyakazi wake aliyekuwa anatazama zoezi hilo kwa mbali aliishia kububujikwa tu na machozi. Alitamani kumkomboa lakini asingeweza kuthubutu abadani.



    Mwili wa Rose ulikuwa mwekundu. Ulivijilia damu na hata kutokwa na majeraha yaliyosababishwa na chuma cha mkanda wa Talib. Hakukoma kupokea kipigo mpaka pale alipozirai. Talib alikuwa anavuja jasho kwa kazi hiyo pevu, hata pumzi yake alikuwa anahangaika kuitafuta.



    “Beba katupieni jela akafie huko!” Aliagiza Talib juu ya Rose. Wanajeshi walimbeba Rose kama kiroba cha bidhaa, wakamtupia kwenye gari lao.









    ***







    Mwanaume aliyevalia kombati nyeusi alikuwa amesimama mbele ya kundi la watu mia tatu kwa idadi ya haraka. Kichwa chake kilikuwa kimefunikwa na kiremba cheupe, uso wake ulikuwa umejawa ndevu. Mwanaume huyu, mwenye ‘ka asili’ ka uchotara wa kiarabu na ngozi nyeusi, macho yake yalikuwa makubwa na ya kutisha. Uso wake ulikuwa mgumu na wenye dhamira.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Miaka ya nyuma alikuwa mshiriki mkubwa wa mapinduzi ya Liberia akiwa na nyadhifa kubwa tu ndani ya kundi la Les Tueurs lililofanikiwa kutwaa dola ya Liberia. Ilikuwa hivyo mpaka pale alipokuja kukosana na wenzake kwa kutaka kuingiza itikadi kali za dini, hali iliyoleta mpasuko kundini.



    Watu kadhaa waliomuamini na kumwona yupo sahihi walienenda naye, huku waliobakia, chini ya Al Saed, wakiendeleza harakati. Ila kabla ya kwenda, alimwachia Al Saed ujumbe mzito. Ujumbe ambao unamtesa mpaka leo hii.



    Ilikuwa ni siku moja tu baada ya yeye kujiengua toka kundini kwa misingi ya dini. Siku hiyo ilikuwa ndefu mno kwa kundi la Les Tueurs kwani kwanzia alfajiri walikuwa kwenye mpambano mazito na wanajeshi wa Liberia: pambano la pili toka mwisho kuelekea kutwaa dola. Ikiwa wamepumzika toka kwenye siku hiyo ambayo iliisha kwa kupata ushindi wa mbinde, mwanaume huyu alizama kambini.



    Ndani ya kambi iliyokuwa na wanaume lukuki, tena wakiwa na silaha, alipita kwa ustadi akilenga kwenda kuonana na Al Saed ndani ya hema lake lililopo katikati ya kambi. Mpaka anafika hapo hemani, alikuwa amefanikiwa kuwamaliza wanaume watano kwa kuwanyonga, hakuna aliyepiga kelele! Al Saed alijua ya kwamba amevamiwa baada tu ya zipu ya hema kufunguliwa.



    “Samahani kwa kuja pasipo mwaliko,” alisema mwanaume huyu akitabasamu. Alikuwa amevalia kombati za jeshi, kwenye paja lake la kuume alining’iniza bunduki ndogo, paja lake la kushoto likibebelea kisu kirefu.



    “Unataka nini kwangu?” Al Saed aliuliza. Mwanaume huyu akaketi pasipo ruhusa.



    “Huu ni ujio wangu wa mwisho kwako. Baada ya hapa, ni wewe ndiye utakayekuwa unanitafuta.”



    “Unataka nini kwangu?” Al Saed alirudia swali.



    “Nataka kukupa nafasi ya mwisho,” mwanaume huyu akajibu. “Badili mawazo yako kabla hujakawia.”



    “Ni wewe ndiye utabadili, si mimi!” alisema Al Saed kwa kujiamini kisha akaamuru;

    “Toka machoni mwangu kabla sijakuvunja vipande vipande!”



    Mwanaume huyu alisimama akachomoa kisu chake na kukichomeka mezani kwanguvu.



    “Hili litakuwa agano langu na wewe!”



    Wapambanaji wa Al Saed waligundua kwamba wamevamiwa. Walifurika mbele ya hema la kiongozi wao wakiwa wamebebelea silaha. Al Saed aliwakataza kuingia ndani. Hata pale alipomalizana kuongea na mgeni wake huyu, alitaka aachiwe aende kwa amani.



    Tangu hapo alipotea, na alipokuja tena kwenye macho na masikio ya Al Saed, jina lake halikuwa Odong tena kama alivyokuwa anajulikana huko nyuma, bali Mr. X. mwanaume mwenye jeshi sasa akidhamiria kumtoa Al Saed madarakani na kuanzisha utawala wa kidini.



    Mkononi mwake akiwa na silaha aina ya SMG, alitazama wapambanaji wake kama mtu achambuaye chuya toka kwenye mchele. Watu hao waliokuwa wamesimama kwa ukakamavu walivalia kombati za kijani, mkononi mwa kila mmoja kukiwa na bunduki kama ya kiongozi wao.



    Mazingira yaliyokuwa yamewazunguka yalikuwa ni tulivu mno wakizingirwa na milima na miti iliyojazana kedekede. Hakika ilikuwa ni sehemu salama kwa mafunzo na makutano yao. Lakini kama vile haitoshi bado kulikuwa kuna walinzi maili kadhaa toka eneo hilo la kazi wakihakikisha usalama zaidi.



    Mr. X alisafisha koo lake kisha akasema:



    “Pongezi sana kwa oparesheni ya mwisho, bila shaka itakuwa salamu nzuri sana kwa makafiri!”



    Wanamgambo wake wakanyoosha bunduki zao juu na kupiga kelele za kushangilia.



    “Hatutakoma mpaka pale tutakapohakikisha tunawamaliza wote, na kuliweka taifa kwenye mikono ya mwenyezi Mungu! Ukae ukijua kila siku, unapokuwa vitani kupambana, haupambani kwasababu yangu; haupambani kwasababu yako; haupambani kwasababu ya wa Liberia, bali unapambana kwa sababu ya mwenyezi Mungu pekee!”



    Wanamgambo wake wakanyoosha bunduki zao juu na kupiga kelele za kushangilia.



    “Zawadi na malipo yetu hayapo duniani bali akhera!”



    Wanamgambo wakanyoosha bunduki zao juu na kupiga kelele za kushangilia.



    Baada ya kusisimuana huko, Mr. X alichukua wasaa wake kuanza kueleza mipango ya mbele, hufanya hivi kila baada ya muda fulani kwa ajili ya kuondoa sintofahamu ndani ya kundi lakini pia kutengeneza njia ya kutimiza malengo yao. Aliteua wanaume watano kwa kuwaita majina, wanaume hao kwa utiifu mkubwa wakajongea mbele kiukakamavu. Walikuwa na miili ya mazoezi na sura za kazi. miongoni mwao, ni mmoja tu aliyekuwa mfupi na mweupe, wote walikuwa wanaikimbiza anga kwa urefu na ngozi zao zikiwa nyeusi barabara.



    “Siku ya keshokutwa, kuna ujio mkubwa nchini. Wanadiplomasia watano toka nchi kubwa ughaibuni watakuja kwa ajili ya kuketi meza moja na Al Saed kujadiliana kuhusu mustakabali wa nchi … nataka wanadiplomasia hao wakiwa wafu! Kwa njia na gharama yoyote ile.



    Kwenye majira ya saa tisa jioni, watatua kwenye uwanja wa ndege wa Monrovia wakitokea kwenye ndege ya shirika la ndege la Delta. Siku hiyo usalama utakuwa mkubwa uwanjani hapo, hivyo mnatakiwa kuwa makini sana. Muweke vichwani kwamba sehemu pekee ya kuwamaliza wanadiplomasia hao kiurahisi ni hapo uwanjani pekee. Hivyo ni lazima wauawe siku hiyo!”



    Baada ya maelezo hayo walitawanyika ila wanaume wale watano wateule waliongozana na Mr. X mpaka makaoni, chini ya msikiti. Mr. X alitoa ramani ya uwanja wa ndege toka kwenye nyaraka zake, akaitandaza mezani. Aliwaelekeza wapambanaji wake kitu cha kufanya, na namna ya kufanya kuhakikisha kila kitu kinaenda kama kilivyopangwa. Alipomaliza alimkabidhi mmojawapo ramani ile.



    “Sitegemei kushindwa. Bila shaka mnajua gharama ya kushindwa.”

    “Ndio, mkuu!”

    “Mnaweza mkaenda.”









    ***









    Giza liliingia kwa haraka siku hiyo, kwa sasa ilikuwa ni saa nne usiku. Ndani ya kituo walikuwepo polisi wachache sana, watatu tu kwa idadi. Polisi hao walikuwa wote wapo kaunta, wawili walikuwa wamelala mmoja akiwa anachezea simu yake kwa kuperuzi mitandaoni.



    Mazingira ya kituo yalikuwa hafifu, taa moja kubwa iliyokuwa mbele ndiyo pekee ilisimama huko nje, nyuma ya kituo kulikuwa ni giza totoro. Kwa upande wa ndani, ni kaunta tu ndipo kulipokuwa na mwanga, lakini huko kwengine kwa mahabusu kulikuwa ni giza totoro. Shukrani kwa wale ambao vyumba vyao vilikuwa vinaibiaibia mwanga wa ile taa moja ya nje.



    Polisi hao wakiwa hawana habari, na aidha wakiwa wanauvuta muda kutafuta siku mpya wapate kumaliza ‘shifti’ yao warudi nyumbani, mara mambo taratibu yanaanza kwenda kombo.



    Sauti kubwa ya mahabusu mmoja inaita kwanguvu.



    “Afandee, kuna mtu kazidiwa! Afandee!”



    Polisi aliyekuwa anaperuzi alisonya na kupuuzia, wenzake hata hawakushtuka. Sauti ya mahabusu haikukoma kuita, ikaendelea kuomba msaada. Mwishowe polisi mmoja aliyekuwa usingizini akaamka kwa kufungua jicho moja.http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    “Kuna nini?”

    “Si hao wajinga wameanza usumbufu!” Alijibu polisi anayechezea simu.

    “Kawasikilize basi.”

    “Siendi, sina muda huo.”

    “Nenda kawasikilize bana, si unajua wakifia humo ndani huwa bonge la ishu!” aliendelea kusisitizia polisi yule akiwa anatazama kwa jicho moja asiupoteze usingizi wake.

    “We nawe ni usingizi tu ndio unaokusumbua,” alilalama polisi aliyekuwa anachezea simu. “Unanisumbua tu ili ulale.”



    Aliamka akaenda huko sauti ya kuitwa inapotokea. Alisimama mlangoni mwa mahabusu akatazama ndani. Kulikuwa kuna mwanga hafifu, hususani kwake kulikuwa giza totoro kwakua alitoka kwenye mwanga – wa taa na wa simu. Hivyo ikawa inamchukua muda kuona ndani.



    Ghafla alijikuta amedakwa shingo, akavutwa kubamizwa kwenye nondo za mlango wa mahabusu, kang’! Akazirai. Haraka kabla hajadondoka chini, ufunguo wa mahabusu uliokuwa unaning’inia kiunoni mwake ukachomolewa, na mlango wa mahabusu ukafunguliwa upesi.



    Mwanaume wa kwanza kutoka ndani, alikuwa Kone. Mkononi mwake ndiye alikuwa amebebelea funguo!







    ****







    Baada ya muda mchache Kone alikuwa nyumbani kwake. Mikono na nguo yake vilikuwa vina mabaki ya damu. Alionana na kusalimia na mlinzi kisha akaingia ndani upesi. Ilimchukua dakika tano tu kumaliza kilichomuingiza ndani, akatoka. Alikuwa amevalia nguo safi, mkononi akibebelea funguo ya gari na bunduki ndogo.



    Aliwasha gari baada ya kumuachia mlinzi maagizo kadhaa, kwamba hataonekana kwa muda, ila lazima atarudi. Kwa muda wote huo ambao hatakuwapo, basi atazame nyumba maana anamwamini.



    Aliondoa gari lake mpaka sheli alipojaza mafuta kujaza kibubu cha gari. Alipotoka hapo akaenda kwenye kiotomotela, akatoa pesa za kumtosha. Sasa akawa tayari kufanya kazi yake mujarabu. Kazi aliyopata kuitandaza kichwani.



    Sasa huu ulikuwa ni muda wake kuonyesha na kuyatumia mafunzo yake ya jeshi, na hata karate aliyowahi kuyapata huko nyuma. Maisha yake yalichezewa vya kutosha na sasa moyo wake ulisema basi.



    Alijikuta anakunja lips zake. Macho yake yalikuwa njiani lakini akili haikuonekana pale. Macho yake yalikuwa mekundu na machungu. Mishipa ya damu ilijichora kwenye mikono yake kana kwamba barabara. Damu ilikuwa inazunguka mwilini kumpatia joto. Mwili wake ulipokea mapokeo toka ubongoni juu ya shughuli iliyo mbele yake.



    “Mungu atanisamehe,” alijikuta anasema mwenyewe. Alikuwa sasa anakaribia jengo mbadala la Raisi. Alipaki gari lake mbali kidogo na jengo hilo kabla hajakaa humo kusoma eneo lake la tukio. Alihitaji dakika tatu tu kutimiza kazi yake hiyo.



    Kulikuwa tulivu sana. Mbele ya geti kulikuwapo na wanaume wawili aliowaona wamebebelea bunduki. Walikuwa wamevalia sare za jeshi, warefu. Kwa ukimya uliokuwepo na umakini wake aliweza kusikia hatua zao wakiwa wanatembea kwenda huku na huko.



    Kone alivesha mdomo wa bunduki yake kiwamba cha kumezea sauti, kiwamba hiki alikitoa kwenye kadroo kadogo ndani ya gari, kisha akaichomeka bunduki yake nyuma ya kiuno na kushuka garini kujongea jengo lengwa. Alipopiga hatua kadhaa tu, tayari walinzi wale, wanajeshi, wakawa wameshamrushia macho. Kuwaondoa mashaka, alitengua mwendo wake kuigiza mlevi.



    Hapo akahitaji tena kama dakika moja na nusu kukaribia mahali alipoweza kufanya jambo. Kama angeendelea kusogea zaidi, ni wazi walinzi wale wangemfuata ama kumtia kwenye rada za ushambuliaji. Haraka mno alichomoa bunduki yake akawafyatua walinzi. Ajabu ni kwamba wote aliwalenga eneo moja, karibia na shina la shingo. Wakadondoka chini na kuwa kimya.



    Alisogea mpaka getini akajaribu kuufungua mlango mdogo, ulikuwa wazi. Aliingia ndani kwa haraka, akaufuata mlango wa kuingia ndani ya jengo. Huo ulikuwa umefungwa. Aliuvunja kwa kuupiga teke. Sauti hiyo ikamshtua Raisi aliyekuwa amelala kitandani, kandokando na Bi Fatma.



    Alijaribu kutumisha masikio yake kama atasikia jambo, hakuambulia kitu. Aliamka akavuta droo ya kitanda na kutoa silaha, bunduki ndogo, kisha akafuata mlango wa chumba na kuufungua. Alishika korido akienenda katika njia ya tahadhari. Alipaza sauti yake kuuliza:



    “Nani? – kuna mtu ndani?” Hakukuwa na majibu. Ghafla alisikia sauti ya kitu cha glasi kuvunjika, moyo ukapiga fundo. Alisimamisha bunduki yake akiangaza. Alisogeza miguu yake taratibu kwenda sebuleni. Alifika pasipo kuona kitu. Aliita walinzi wake, hakuna aliyeitika.



    Walinzi wote walikuwa wapo chini wakivuja damu – wa nje na ndani. Kama Raisi angetoka ndani ya sebule kwenda nje, mlangoni tu angekutana na mwili wa mlinzi wa ndani ambaye aliuawa punde tu baada ya Kone kuuvunja mlango. Na basi kama angelimalizia kutoka getini, angeliiona mingine.



    Haya yalikuwa makazi ya siri ya Raisi. Si bure ni kama sehemu yake ya kufanyia maovu. Hakutaka kabisa sehemu hii ijulikane na hivyo ndio maana sehemu hiyo ulinzi wake ulikuwa kawaida sana, pia Raisi kutumia kwake magari ya kawaida kuingilia na kutokea ndani ya jengo hili, yote haya yalikuwa jitihada tu za kufanya eneo hilo lisitiliwe shaka.



    Sasa leo mambo haya yalikuwa yanamgeukia.



    Akili yake pevu ilimfanya ajione yupo hatarini na hawezi tena kujificha humo ndani kama kweli anahitaji uhai. Macho yakiwa yamemtoka, moyo unakita, alikimbia kurudi chumbani mwake apate kupiga simu ya msaada haraka. Alifungua mlango akazama ndani, macho kwa macho akakutana na Kone!



    Mifupa yake ya magoti ililia kah-kah! Baridi kali lilimpitia kwanzia kichwani mpaka kwenye ncha ya vidole vya miguu upesi.



    Mdomo wa bunduki ya Kone ulikuwa unamtazama. Sura ya Kone haikuwa na masikhara hata kidogo. Pembeni ya mwanaume huyo alikuwa amesimama Bi Fatma ambaye uso wake ulikuwa umejeruhiwa. Ni wazi alikuwa amepata majeraha hayo toka kwenye mikono ya Raisi baada ya ukaidi.



    “Kone!” Raisi aliita. Kone hakuitika, zaidi alimtaka aweke silaha chini na kuisukumizia kwake kwa kutuma mguu.



    “Naomba tuyamalize, Kone,” Raisi alinguruma. “Hatuna haja ya kufikia hatua hii.”

    “Kama usingetaka yafikie hapa, basi usingenifanya uliyonifanya,” Kone akajibu kwa sauti ya msisitizo. Alisogelea bunduki ya Raisi akaiokota na kuiweka kibindoni.

    “Nilijituma sana kutimiza kazi zako. Sikujali uhai wangu kwa kuamini kufanikiwa kwako ndiyo kufanikiwa kwa nchi yangu. Kumbe nilikosea. Wakati nahangaika usiku na mchana, basi nawe ukawa unahangaika vivyo hivyo kuharibu furaha yangu.”

    “Sio hivyo unavyofikiri Kone,” Raisi alijitetea. Kabla hajaendelea, Kone akampa ishara ya kumtaka aufunge mdomowe, alafu akamwambia maneno machache:

    “Sali sala yako maana nakumaliza.”



    Raisi alijiona kama mtoto mbele ya simba mwenye njaa, hakuwa na wa kumuokoa. Mwili wake ulitetemeka kwa hofu ya kifo, ndani tu ya hiyo punde alikuwa amelowa jasho mgongoni. Pumzi yake ilikuwa inaenda upesi kadiri ya mapigo yake ya moyo.



    “Tafadhali usiniue, Kone. Nitakupa hata nusu ya mali zangu ila unibakizie tu uhai wangu.”

    “Nitaamini vipi?”

    Kone aliapa.

    “Hapahapa nitakupatia pesa, dola za kimarekani, za kutosha. Naomba tu unipatie simu yangu.”



    Kone alitabasamu tabasamu la kando.



    “Unaniona mjinga enh?”

    “Basi kama hauamini, ichukue wewe hiyo simu mimi nitakuelekeza,” Raisi alinena akitia huruma. Kone alimtazama Fatma, mwanamke huyo akampatia simu ya Raisi aliyoifungua baada ya Raisi kumpatia nywila, ilikuwa mwaka wake wa kuzaliwa.



    Kwa maelekeo ya Raisi, Kone alifanikiwa kuhamisha kiasi chote cha pesa kilichokuwemo kwenye mfuko benki wa Raisi, akaumwagia kwake. Baada ya hapo, Kone alimtaka Raisi aeleze miradi yake yote ya siri aliyonayo, Raisi akatii amri. Alimweleza mwanaume huyo ya kwamba ana nyumba nyingi alizozijenga huko nchi za magharibi ambazo yupo tayari kumpatia baadhi.



    Kone aliona hiyo ni fursa. Kwa namna moja aliona nyumba hizo zaweza kumsaidia kumpatia hifadhi pale atakapokuwa anatafutwa baada ya kummaliza huyu adui yake. Ndio. Hakuwa na malengo ya kumwacha hai. Alijua kabisa akifanya hivyo, atakuja kujutia sana huko mbeleni. Raisi hatokuwa radhi kumwachia aishi ingali anajua siri zake, ni lazima atataka kumnyamazisha. Lakini juu ya yote kuonyesha umwamba wake.



    Baada ya Kone kuyapata yale aliyokuwa anayahitaji, alifyatua risasi yake kulenga paji la uso la Raisi. Asiombe hata maji, Raisi akadondoka chini kama mzigo. Alikuwa maiti tayari.



    Haraka Kone na Bi Fatma walitoka ndani wakakwea kwenye gari na kutimkia kwa mama yake Fatma. Ulikuwa ni usiku mzito na hali ya hewa ilikuwa tulivu. Lami iliwachukulia kama dakika kumi na tano tu kufika walipokuwa wanaelekea. Kutokuwepo kwa foleni, na mwendo mkali wa Kone ulifanikisha hilo.



    Ngo! Ngo! Ngo! Ngo! Kone aligonga geti. Ni mwenyewe ndiye alishuka toka kwenye gari akimwacha Fatma ndani. Aliligonga geti kwanguvu kiasi kwamba hakuwa na haja ya kuligonga tena ili wenyeji wasikie.



    “Kone, vipi muda huu?” ilikuwa sauti ya mamaye Fatma. Ilikuwa imejaa usingizi ndaniye.

    “Naomba watoto. Upesi tafadhali,” Kone aliamuru. Sura yake ilikuwa imejikunja. Dhahiri hakutaka kurudia ujumbe wake mara mbili.

    “Kuna nini?” usingizi ulimuisha mama Fatma. Alipata wasiwasi. Kuna jambo halikuwa sawa.

    “Nawaomba watoto kwa sasa, tutaongea mengine baadae.”

    “Wamelala.”

    “Waamshe,” Kone aliagiza. “Mama naomba ufanye upesi!”



    Mama Fatma aliingia ndani akatoka na watoto wawili wa Kone baada ya dakika zisizozidi nane. Kone aliwaamuru watotowe wapande gari upesi wakati yeye akimuaga mama Fatma.



    “Kone, nini kinaendelea? – Fatma yupo wapi?” Mama Fatma alipaliwa na hofu. Kone hakumpatia majibu zaidi ya kumuaga na kumpa ahadi atamueleza yote siku za mbeleni. Alirudi kwenye gari akatimka.



    Kwa usiku mzima, gari lilitembea juu ya lami. Mpaka unafikia wakati ambao jua linakaribia kuchomoza, akawa amefika mpakani mwa Sierra Leone. Alizama nchini humo akaendelea na safari iliyoenda kukomea kwenye hoteli ya hadhi ya kati, akachukua vyumba viwili hapo kwa ajili ya mapumziko.



    Hapo alikuwa salama, moyo wake ulimwambia hivyo. Nchi ya Guinea na Sierra Leone ni wahasimu, tena wakubwa. Alijua fika akiwamo ndani ya nchi ya Sierra Leone, hakuna mtu yeyote atakayetishia uhai wake, wala kuhangaika kumtafuta. Akiwa juu ya kitanda aliwaza na kuwaza, mwishowe usingizi ukampitia. Fatma alikuwa tayari yu usingizini, pia na watoto.







    ***





    Habari kubwa ilishika anga, Raisi ameuawa. Habari hii ilikuwa ni zaidi ya kushtua kwa wananchi wa Guinea. Hata yule ambaye hana hulka ya kusikiliza redio, kutazama video, ama kusoma magazeti, hakuikosa.



    Lakini habari hii ilijawa na utata. Wapi Raisi alipouawa? Alikuwa anafanya nini huko? Alikuwa na nani? Maswali haya yaligonga vichwa vya watu. Walinzi waliokuwa wanamlinda Raisi ndio walikuwa watu pekee wenye majibu mazuri, ila kwa muda huo wote walikuwa hospitalini wakiuguza majeraha. Ni ajabu kabisa walikuwa wazima.



    Na hapa ndipo panapoweka wazi kwanini Kone alikuwa amewalenga walinzi hao kwenye eneo moja tu la mwili, kando ya shina la shingo. Ni ajabu kusema alifanya jambo hili kwa bahati mbaya, lah! Pengine hakutaka kuwamaliza watu wasio na hatia mbele ya macho yake.



    Wakati kila chombo cha habari kikisema jambo linalolijua, Kone akiwa mlengwa mkubwa wa mauaji hayo, mke wa Raisi anaibuka na kufanya mambo kuwa makubwa zaidi. Mwanamke huyo aliyekuwa kwao kwa muda wote huo, anavuta vyombo vya habari kwa maneno yake makali na mdomo uliokosa staha. Tuhuma zake kali juu ya marehemu zinawafanya watu kubaki midomo wazi.



    “Kone alikuwa ananisaliti kwa kutembea na mke wa Kone, mmoja wa watumishi wake wakubwa. Kwasababu ya mwanamke huyo, alisahau kabisa kukaa ikulu akahamia kwenye makazi yake ya siri nisiyoyajua. Hakuwa anaonana na mimi kwa njia yoyote ile zaidi ya kuwasiliana tu kwa njia ya simu. Alikuwa ananipiga mara kwa mara, nikachoshwa na kuondoka nyumbani.”



    Raisi aliuawa kwasababu ya hawara? Tena mke wa mtu? Mke wa mfanyakazi wake! Sasa vyombo vya habari vikachafuka mpaka huko mitandaoni, huku televisheni ya taifa ikiwa ndiyo chombo pekee kilichoifumbia macho habari hiyo kana kwamba hakijasikia wala kuona chochote.



    Kadiri muda ulivyokuwa unasonga, salamu za rambirambi zikawa zinatumwa toka nchi za nje, na mipango ya msiba ikaanza kuainishwa vilevile uratibu wa kiutawala.



    Ikiwa harakati hizo zinaendelea, Talib alikuja mbele ya hadhira akitumia chombo cha habari cha taifa, mada kuu mezani ikiwa ni salamu za rambirambi kwa kifo cha Raisi wa Guinea. Maelfu ya watu walitega masikio yao kusikiliza ni nini Talib ataongea juu ya kifo cha kushtukiza cha Raisi huyo aliyekuwa hawaivi naye chungu kimoja.



    Maji makubwa pamoja na glasi yake vilikuwa vimekaa juu ya meza. Kwenye kiti kikubwa cheusi, cha starehe, alijaa Talib aliyekuwa tayari ameshaveshwa kidaka sauti. Mwanaume huyo alikuwa amevalia sare ya jeshi iliyokuwa imebandikwa kila aina ya cheo ulimwenguni.



    Alikunywa kwanza mafundo mawili ya maji kisha akatabasamu akiweka chupa yake kando.



    “Ni siku njema tena nakuja mbele ya hadhira ya wananchi wangu, na hata dunia nzima. Siku hii imekuwa njema si tu kwasababu Mungu ametupa fursa ya kuamka salama, bali pia ametupa ahueni kwa kumuondoa mmojawapo wa watu ambao walikuwa mzigo hapa ulimwenguni.”



    Kuongea tu maneno hayo kukatoa taswira halisi kwa yale yote aliyoyadhamiria kuyatema siku hiyo – chuki, dhihaka na shutuma. Hotuba yake yote alikalia kumsema Raisi wa Guinea kwa kumuita jirani mnafiki, mhalifu na pia mwizi wa wake za watu, utadhani ya kwamba yeye alikuwa amedondoshwa toka mbinguni siku hiyo.



    Alipohakikisha hajabakiza lolote kifuani mwake, alihitimisha kwa kusema:



    “Mungu akulaze unapostahili. Na ashukuriwe kwa kutupunguzia tatizo mojawapo duniani.”



    Alikunywa tena fundo moja la maji kabla ya runinga kuzima.









    **







    Kutokana na msiba mkubwa wa Raisi wa Guinea, safari ya wanadiplomasia toka Ughaibuni kwenda Liberia, kukutana na Al Saed, ilisitishwa ghafla na kupangwa siku mbili baadae. Al Saed alipanga kwenda kuhudhuria msiba huo hivyo asingalikuwapo kuwapokea wageni.



    Pasipo kukawia, taarifa hiyo inamfikia Mr. X, na basi mipango ikabidi itenguliwe kuendana na mandhari husika. Mr. X aliwapigia simu watu wake aliowatuma kwa ajili ya kazi, akawaelekeza namna ya kufanya.



    “Mtumie siku hizo kusoma mazingira yenu ya kazi, kugawana majukumu na kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa.”



    Agizo hilo la Mr. X lilitiliwa maanani. Pasipo kupoteza muda kazi ya kupekua eneo la tukio inaanza. Miongoni mwa wanaume wale watano, anatoka majira ya jioni kwenda uwanja wa ndege. Alikuwa amevalia suruali ya kadeti rangi ya kaki na tisheti rangi ya maziwa. Uso wake ulikuwa mtulivu, ila macho yake yakiwa kazini kuyasoma mazingira vema.



    Alizunguka maeneo kadha wa kadha ya uwanja ndege. Alichukua muda wake kuketi kwenye moja ya benchi nje ya uwanja wa ndege, akaendelea na zoezi lake la kupekua mazingira. Baada ya kutosheka na alichokipata akatoka eneo hilo kufuata barabara ya lami, pale uwanjani alipoteza kama lisaa limoja.



    Alisimamisha taksi moja, akakwea na kuondoka. Ila nyuma yake kuna gari likawa linamfuatilia.





    Baada ya kama nusu saa, kutokana na foleni za hapa na pale, mwanaume huyo anashuka mbele ya jengo moja la ghorofa tatu lililokaliwa na maduka mengi kwenye sakafu yake ya chini. Anatazama kushoto na kulia kisha anapenya kwenye uchochoro mmoja unaomtokeza karibia na mapokezi, anapojitambulisha na kuingia zake ndani.



    Ni chumba kikubwa chenye kitanda kipana, juuye wakiwa wamelala wanaume wanne waliovalia nguo nyepesi nyepesi, mathalani bukta na kaushi, huku mmoja tu akiwa kifua wazi: kifua chake kilikuwa kama ubao kikiwa kimejazwa na nywele lukuki. Wote walitazama mlangoni wakati mwenzao akiingia na kuurudishia mlango upesi.



    “Kila kitu kipo kwenye mstari,” alisema mwanaume yule aliyetoka nje akiketi kitandani. Alieleza yote kinaganaga akiufafanua uwanja wa ndege kana kwamba upo kichwani mwake, ama kana kwamba alikuwa mhandisi aliyeujenga. Alitumia karatasi akichora kusadifu macho na akili yake. Alipoweka kituo, wenzake wakampongeza.



    “Kazi yako kabambe, sasa tumebakiza tonge moja tu kumaliza chakula chetu,” alisema mwanaume mmoja mwenye sauti nzito, kisha akaanza kuainisha ‘tonge’ hilo moja lililobaki.



    “Inabidi sasa tujue njia zote ziingiazo na zitokazo; fupi na ndefu; nyoofu na zilizopinda.”



    Karatasi nyingine ikachafuliwa kwa kujazwa mipango. Macho ya kila mmoja wao mule ndani yalitazama karatasi hiyo kwa umakini kana kwamba wanafunzi wafanyao mtihani uliovuja. Zoezi hilo lilipokoma akateuliwa mtu wa kuitenda, naye hakuwa mwingine bali yule aliyekuwa kifua wazi, twaweza kumuita kifua ubao.



    “Uwe macho muda wote,” alipewa angalizo. “Hakikisha unakuwa mwenyewe na hakuna mtu anayekufuatilia. Na pia kumbuka kutunza kumbukumbu vema.”



    Wanaume hawa hawana desturi ya kurekodi mambo yao vitabuni, hilo lingeweza kupelekea wakatiliwa shaka na watu na hatimaye kukamatwa. Macho yao na ubongo wao ndivyo vitu pekee wanavyovitumia. Wakiwa kwenye eneo la kazi basi macho yataachwa yafanye kazi na huku ubongo ukitunza kila jambo muhimu.



    Mpaka usiku unaenda hawakuwa wameteta kingine isipokuwa tu baadhi yao kuwasiliana na familia zao. Ila hakuna aliyesema ni kazi gani anafanya kwa muda huo, wala yupo eneo gani. Aidha walihofia kudukuliwa na kudakwa kwa taarifa zao.









    ***

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/





    Asubuhi na mapema ya saa kumi na moja, mlango unafunguliwa anatoka kifua ubao. Alikuwa amevalia suruali nyeusi inayombana, tisheti nyekundu na koti la ngozi rangi ya kaki, miguuni moka. Anatazama kando na kando akiurudishia mlango. Anatoka kwa mwendo wa haraka mpaka mapokezi anapoaga na kisha kuendea barabara.



    Macho ya mwanaume huyu yanarandaranda kwa kasi mno. Anatazama huku na kule. Akiwa kwenye gari kuelekea uwanja wa ndege, basi anatumia mwanya wa madirisha vilivyo kwa kuangaza njia ndogo zinazochipuka na pana zinazoingia. Anafanya zoezi hilo kwa ustadi sana kiasi kwamba hata jirani yake hakugundua hilo. Kuhangaika kwake kwa macho hakukuhusiana na shingo kabisa.



    Ila kuna jambo alitakiwa alifahamu. Mwanaume huyu alikuwa anafuatiliwa. Tangu pale alipotoka ndani ya jengo waliloweka makazi, kuna mwanaume, aliyekuwa amevalia kofia mithili ya turubai na jezi za michezo, alimuweka kwenye rada zake. Hali ya mwanaume huyu mfuatiliaji kuwapo eneo hilo kwa muda wa saa kumi na moja, kulitoa namna mbili: aidha alikuwepo hapo tangu jana usiku, yani amelala hapo, au amewahi sana kuja kukaa hapo.



    Aliipanda daladala tofauti na ya mlengwa wake. Alikaa eneo zuri garini la kumuwezesha kuona gari la mbele yake, na hata pale ikitokea mlengwa wake akishuka. Macho yake hayakubandika kwenye gari alitazamalo mpaka wanafika uwanja wa ndege ambapo mlengwa wake alishuka. Naye akashuka. Alivua kofia yake akaiacha garini.



    Kifua ubao alitazama kushoto na kulia. Alianza kutembea kuingia uwanja wa ndege, ila asiyeketi, akawa anazungukazunguka huku na kule. Alichambua barabara zote za karibu. Kama haitoshi, akafuatilia barabara moja baada ya nyingine, tena kwa kutumia miguu. Mpaka anamaliza zoezi lake hilo, alikuwa amezunguka kwa wastani wa kama kilomita tatu toka uwanjani kuelekea kila upande. Ilimtosha.



    Mwanaume aliyekuwa anamfuatilia naye hakuwa nyuma. Alimpa nafasi mlengwa wake kwa umbali mkubwa. Ila si tu hilo, kuna njia nyingine alikuwa anafanya. Mwanaume huyu alibadili nguo yake ya juu mara mbili, hatufahamu alitolea wapi ila kwa njia moja ama nyingine, tena kubwa ilimsaidia kumuepusha dhidi ya kugundulikana.



    Kifua ubao alipanda daladala akarudi kwenye makazi yake. Alikuwa mwangalifu kweli ila hakufua dafu. Alifika chumbani ikiwa ni majira ya mchana ya saa nane, wenzake wakafanya mpango wa chakula. Wakiwa wanakula, maongezi yakaendelea kuchukua nafasi. Maongezi ya mipango yao.



    Kifua ubao alieleza kila alichokinukuu. Alikuwa mwepesi sana kukumbuka mambo kedekede pasipo kukosea. Alizielezea barabara kana kwamba anaziona kwenye televisheni, lakini pia mwishoni akatoa ushauri ni barabara ipi itumike kuchoropokea toka uwanjani. Barabara fupi zaidi kutoka nje ya jiji, na yenye upungufu wa msongamano vikiwa vigezo vilivyotumika.



    Sasa mipango ilikuwa kamili, kilichokuwa kinangojewa ni utekelezaji tu. Kifua ubao alikabidhiwa zoezi la uendeshaji gari, wakati wengine wakibakia na jukumu la kurusha risasi kwa wanadiplomasia.



    “Asubuhi tutakodi taksi, tutamteka dereva na kulitumia. Tukipata taksi itakuwa rahisi sana kwenye parking lakini pia kupunguza mashaka juu yetu. Dereva atatushusha mbali kidogo na uwanja wa ndege kisha tutatembea mpaka huko uwanjani. Tukishafanya tukio, tutakutana na taksi, mahali tulipopanga, na kutimka.”



    Walielewana wakajipumzisha kukusanya nguvu za kesho.









    ***







    Usiku ukiwa unasogea sasa, wanaume sita waliovalia sare za jeshi wakiwa wamebebelea bunduki, wanajongea karibu na hoteli iliyowatunza wanamgambo watano wa AMAA. Wanajeshi hawa wanawasiliana kwa ishara. Wanafika uwanja wa mapokezi na kujitambulisha kisha wanajigawa, watatu wakienda kushoto na wengine kulia.



    Wanafanya matendo yao kwa ukimya na ustadi. Hakuna hata mtu yeyote ndani ya vyumba aliyefahamu juu ya ugeni huo. Wanatembea kwa kunyata mpaka mlangoni mwa chumba kinachowahifadhi watumishi wa mr. X, hapo wanatazamana na kupeana ishara ya kuhesabu vidole – moja, mbili, tatu! Mara mlango unavunjwa, wanazama ndani.



    Wanamgambo wa AMAA walishtuka mno. Hawakuwa na namna yoyote ya kupambana, walishachelewa. Walikuwa tayari wamezingirwa na midomo ya bunduki ikiwatazama. Walinyoosha mikono yao juu kusalimu amri. Waliamriwa wapige magoti chini, wakatii, wakafungwa pingu na kuamriwa walale chini.



    Baada ya muda mfupi, yalifika magari mawili ya jeshi. Mateka wakaswekwa ndani na kutimka, huo ukawa mwisho wa misheni ya kuua wanadiplomasia. Ila yanabakia maswali: kazi hii maridadi aliifanya nani? Mtu huyu hakuwa mwingine, bali Al Saed. Ila kwa muda gani? Aliwaza nini?

    Kichwa cha mwanaume huyo kilishachambua na kubainisha mambo kadhaa ndani ya mwamvuli wake wa utawala. Alijua kabisa kuna watu asiotakiwa kuwaamini, na hili halikuhitaji ufanisi wa hali juu kulitambua, bali jicho tu la karibu kwenye kazi zilizofanywa karibuni. Mazingira ya kazi hizo yalionyesha wazi kuna mtu kwenye meza yake anampatia chakula adui, mr.X, kiasi cha kumpa kiburi.



    Hilo lilikuwa mosi, pili: alishajua fika taarifa za ujio wa wanadiplomasia toka ughaibuni zitakuwa zimemfikia mr. X na kwa namna moja ama nyingine atataka ama kujaribu kufanya jambo. Alikuwa na uhakika na hili kwa asilimia zote maana aliitisha kikao cha usalama ikulu kwa ajili ya kujipanga. Na ndani ya kikao walikuwepo wale wote aliowashirikisha hata kwenye mipango ya awali.



    Ila ambacho hawakujua ni kwamba, Al Saed aliendesha kikao kingine binafsi baada ya kile. Hiki cha pili akiwa na watu wawili tu anaowaamini. Watu hao wakiwa ni wanajeshi wa kawaida, wasio na cheo chochote ndani ya jeshi. Walipanga namna ya kufanya, tena kwa usiri.



    “Wote wanajua wageni wanakuja mtondogoo, ila ukweli ni kwamba wanakuja kesho. Nimeshaongea nao, mtaenda kuwapokea kama watu wa kawaida na kuwapeleka mahali nilipowaelekeza. Kisha baada ya hapo kazi yenu itakuwa kutazama uwanja wa ndege kwa macho makubwa. Hakikisheni maeneo yote ya kungojea wageni, na pia rekodi za kamera zinatazamwa kuwapata wahalifu.”



    Ratiba hiyo ya wageni haikuingiliwa hata na msiba wa Raisi wa Guinea. Wakati Al Saed anaenda msibani, wageni walikuwa tayari wameshawasili na kuweka makazi yao kwenye hoteli moja kubwa ndani ya jiji. Walishawasiliana na Al Saed akawapa miadi ya kuteta baada ya kurejea toka msibani.



    Mr. X alizidiwa kete. Na sasa tayari watu wake walikuwa kwenye mikono ya Al Saed, mahali pasipo julikana.









    ***







    Kwenye chumba chenye giza totoro, mara taa inawashwa na watu watano waliokalia kwenye viti wakiwa wamefungwa mikono, miguu na kufunikwa vichwa, wanaonekana. Mara punde wanatokea wanaume watatu waliovalia sare za jeshi, wanawasogelea wanaume hao watano na kuwavua mifuko iliyowafunika vichwa.



    “Karibuni,” alisema mwanajeshi mmoja akitabasamu. Wenzake walikuwa wamenyamaza wakiwa nyuma yake.



    “Najua mnajua kwanini mpo hapa, kwahiyo tusipoteze muda. Hatuna haja ya kuumizana wala kutoana ngeu.”



    Mwanajeshi huyo aliuliza taarifa za kikundi cha AMAA, na pia juu ya kiongozi wao; wapi walipo, wapo wangapi, wana itikadi na malengo gani. Bahati mbaya, hakuna yeyote aliyekuwa tayari kujibu swali lolote. Walikula yamini kutosema, afadhali tu wakauawa.



    Ilibidi sasa mbinu ya kutafuta majibu ibadilishwe, wanajeshi wakatumia nguvu na njia ya maumivu. Waliwatesa mno mateka wao mpaka pale walipohakikisha watu hao wamelowana damu na kujazwa majeraha. Walikuwa hoi kwa kipigo kizito, lakini bado hamna aliyekuwa tayari kusema lolote.



    “Tuue, hatutasema kitu,” alisema kifua ubao akicheua damu.



    “Sawa, ngoja tuone,” akadakia mwanajeshi kiongozi akiwa na uso wa mauaji. Alimtazama mwenzake akampa ishara kwa kichwa, mwenzake akatoka ndani, baada ya muda akarejea akiwa amebebelea simu mkononi.



    “Sasa basi kama uhai wenu hamuuonei huruma, vipi wa familia zenu?”



    Hakuna aliyejibu.



    “Hatutahangika na nyie tena, bali wake na watoto zenu. Na kama mnadhani hatujui walipo basi mnakosea sana.”



    Mwasiliano ya wanamgambo hao wa AMAA yalikuwa yamedukuliwa, ikabainika kuna ambao waliwasiliana na watu wao wa karibu muda si mrefu. Namba hizo ziliangazwa na kutoholewa taarifa muhimu. Walijaribu pia na kutafuta taarifa za Mr. X, zoezi likashindikana. Laini yake ya simu haikuwa kwenye mfumo wa mawasiliano kabisa. Laiti kama wangelipata, wasingelikuwa na haja ya kusumbuana na mateka wale.



    “Sasa basi ni jukumu lako kuamua. Aidha unatupa tunachotaka, ama tukamalizane na familia na watu wenu?” Kauli hiyo ilikuja baada ya mwanajeshi huyo muongeaji kusema kwa uwazi ni wapi familia hizo aziongelezo zilipo. Na bahati njema au mbaya, yote aliyosema yalikuwa yana kweli ndani yake.



    Hakuna mfuasi yeyote wa AMAA aliyejibu, wala kusema jambo. Walitazamana kwa macho ya dosari kisha wakaendelea kufunga midomo yao wakiutunza ukweli vifuani.



    “Sawa kama mmeamua hivyo,” alisema mwanajeshi. “Tutawaletea vichwa vya wapenzi wenu hapa.”



    Baada ya kusema hivyo, alitazamana na wenzake wakapeana ishara ya kutoka. Ila kabla hawajafika mlangoni, mara wanaitwa.



    “Nitasema, tafadhali msiue familia yangu!” Alikuwa mwanaume mmoja kando na kifua ubao. Alijawa na shaka. Wenzake walimtazama kana kwamba wanataka kumtoa roho.



    “Abdul, unataka kufanya nini?” Aliropoka kifua ubao. “Unataka kufanya nini Abdul? Unakumbuka kiapo chako!” alifoka.



    “Hakuna kitu kikubwa kama familia yangu,” akajibu mwanaume huyo, Abdul. Mara akapunguza sauti, ananong’oneza:

    “Mke wangu ana mimba. Siwezi nikaruhusu yeye na mwanangu wapoteze uhai.”







    Taswira ya jiji la Freetown ilikuwa imefifia, halikuwa linatamanika tena. Magari yalikuwa machache na hata watu pia. Ungeweza kusema ni jangwa, ama mji wenye watu wachache kabisa juu ya uso wa dunia. Hii yote ilitokana na upungufu maradufu wa usalama nje ya milango. Bado maandamano, tena yanayoambatana na vurugu kali, yalikuwa yanaendelea kuzizima ndani ya jijii. Hakukuwa salama.



    Watu kadhaa waliripotiwa kuuawa wengine wakijeruhiwa vibaya. Makundi ya watu walioongozwa na hamu kali ya kuuondoa utawala wa Talib walirandaranda huku na kule kuutafuta ushawishi. Kila mwananchi alitakiwa kuwaunga mkono la sivyo angelionjeshwa joto. Haikuwa ombi sasa kumpinga Talib, bali ni amri! Kwa yule aliyekaidi angeachwa anatiririka mito ya damu.



    Ikiwa ni majira ya mchana sasa wa saa nane, ndani ya nyumba kubwa mno nyeupe inayovutia machoni, chumbani, anaonekana naibu kiongozi wa ulinzi wa taifa: Meja jenerali Edward Simon akiwa amevalia nguo za kutafutia joto. Ingawa kiyoyozi kilikuwa kinapuliza kwa wingi, bado alionekana kutotosheka.



    Chumba kilikuwa kikubwa kama uwanja wa mchezo wa tenesi. Kitanda kilitapakaa kikiwa kimefunikwa na sufi laini nzito. Madirisha, mawili, yalikuwa mapana mno kiasi cha kutengenezea milango. Viti na meza, pamoja na maua feki yaliyokuwa chumbani humo, kwa macho tu, yalieleza bei yake ya kikubwa. Palikuwa pazuri mno usitamani kutoka ukiingia.



    Ni siku ya tatu sasa meja jenerali huyu hajaenda ofisini kwa sababu ya usalama. Amekuwa akibakia ndani kwake tena akiwa amezungukwa na wanajeshi kadhaa waliobebelea silaha za kisasa. Mke na watoto wake wawili pia walibakia nyumbani, shule na shughuli zao zikisitishwa kwa muda usiojulikana.



    Mitaani hakukuwa shwari. Wanajeshi si wengi kama wananchi. Hata kwa wingi wao silaha bado hakufui dafu. Wananchi hawana sare hivyo basi haujui yupi aliye mawindoni na yupi aliye mafichoni, yupi anataka tabasamu lako ama damu yako!



    Mwanamke mnene aliyevalia taulo pekee kifuani anaingia chumbani akitokea kwenye bafu. Mwili wake umejazwa na matone matone ya maji. Kichwani amejifunika na taulo dogo jeupe kama pamba. Mwili wake rangi ya maji ya kunde wenye umbo zuri la chupa. Ila uso wake ulikuwa wa mwanamke mchanga. Alionekana mdogo asiye hata na miaka ishirini na tatu.



    “Mpenzi,” mwanamke huyo aliita akijifuta kichwa na taulo. Meja akamtazama mwanamke huyo pasipo kusema jambo.



    “Nahitaji kutoka mara moja leo.” Alisema mwanamke.



    “Kwenda wapi?” Akawahi kuuliza Meja.



    “Kwa rafiki yangu – Diana.”



    “Una matatizo gani Sarah? Utaacha utoto lini wewe? Hivi niwe nakuimbia kila siku kwamba huko nje si salama?”



    “Sasa mpenzi, tutakaa humu ndani mpaka lini? Si nitaongozana na walinzi? Shughuli zangu nyingi zinakwama.”



    “Shughuli zipi hizo?”



    Mwanamke akaguna, “basi yaishe.”



    “Au unataka kwenda kwa hivyo vijana – vijana vyako huko?”



    “Sasa hayo yanaingiaje hapa?”



    “Nakwambia hivi, nikija kugundua unaendelea na huo ujinga wako. Nitakuua!”



    Mwanamke akaguna kwa kubinua mdomowe.



    Si bure kwa Meja kuhofia. Umri wake ni kama mara tatu ya binti huyu mchanga mrembo, ni wazi mwanamke huyu anaweza akawa anatafuta injini zingine huko nje zenye moto zaidi, pengine.



    Mwaname alifuata kabati lake la nguo akalifungua. Lilikuwa limesheheni nguo. Akiwa anatazama ni nguo ipi inayoweza kusitiri mwili wake, mara sauti kali ya mlio wa risasi inasikika. Anashtuka! Anageuka upesi kumtazama mumewe akitumbua macho.



    Meja alikuwa tayari ameshasogea dirishani kuchungulia.



    “Kuna nini?” Sauti ya hofu ya mwanamke iliuliza.



    Meja hakujibu, aliendelea kukazana kutazama. Ila baada ya sekunde chache aligeuka akamtazama mkewe kwa sura yenye mushkeli wa mashaka.



    “Watoto wapo wapi?” Aliuliza.



    “Kuna nini?” Mwanamke akajibu kwa swali. Alikuwa ameshapata woga, mikono yake ikitetemeka.



    Milio ya risasi iliita tena, mara hii mara tatu kwa fujo kuu! Mwanamke alichanganyikiwa akakimbilia kufungua mlango.



    “Watoto wanguu!” alipiga yowe. Alitoka chumbani haraka akakimbilia sebuleni alipoangaza na kisha haraka akaenda vyumbani, akatoka na watoto wawili wa kike. Walishika korido, wakakutana na Meja, mkononi alikuwa amebebelea bunduki ndogo.



    “Nendeni chumbani mjifungie!” Aliagiza Meja, mwanamke akiongozana na watotowe wakazama chumbani na kuupiga mlango kufuli.



    Meja alisogelea sebuleni. Kulikuwa kuna kelele za watu huko nje. Aliangaza macho yake upesi akaona simu ya mezani, aliikimbilia apate kupiga. Aliinyakua simu hiyo haraka akaiweka sikioni na kubofya namba kadhaa. Simu ikaita.



    Makelele ya watu, yakiwa ni ya kufoka, yalizidi kuongezeka. Yalisikika yakikaribia mlango, na bado simu haikuwa imepokelewa.

    Macho ya Meja yalitazama mlangoni kwa mashaka. Mkono wake uliobebelea bunduki ulielekea pia huko. Alilaani kwanini simu haipokelewi, alichanganyikiwa. Punde mlango unagongwa na mara unavunjwa!



    Haikudumu muda mrefu, mwanamke aliyekuwepo chumbani, anasikia sauti ya risasi inayojibiwa na risasi nne huko sebuleni. Walikuwa ndani ya kabati yeye pamoja na wanawe wakiwa wamejikunyata kama wanaosikia baridi kali.



    Sauti za kufoka na kuropoka zinaendelea. Kwa mujibu wa sauti hizo waweza sema kulikuwa kuna idadi toshelezi ya watu. Sauti hizo zinaruruma, zinasogea karibu chumbani, baada ya muda mlango unavunjwa. Hapo kabla ilisikika milango miwili ikitendwa vivyo hivyo.



    “Wako wapi?” Sauti moja inauliza. Kwa kupitia ka-mwanya ka mlango wa kabati, wanaonekana wanaume kama nane hivi, watatu wakiwa wamebebelea bunduki kubwa ndefu na wengineo wakiwa wamebebelea mapanga.



    “Tafuteni! Tafuteni kila sehemu!” Inatoka amri kwa mmoja wao. Wanaume hao wanagawanyika kutazama huku na huko. Punde kabati linafunguliwa, mwanamke na watoto wake wanatolewa kwa nguvu. Wanarushiwa sakafuni kama mizigo.



    Taulo liliacha mwili wa mwanamke, akabakiwa mtupu: mbele ya watoto na wageni wake wa lazima.



    “Naam! Wewe si miongoni mwa wale wanaokula jasho letu, sasa leo utaliwa wewe!” alisema mwanaume mtoa amri. Macho yake yalikuwa yameshatepeta uchu.



    Pasipo kujali kama kuna watoto, alivua suruali. Mwanamke alilia, pamoja na watoto pia wakiomba mama yao aachwe, hawakusikilizwa. Mbele ya macho ya watoto, mama akabakwa kwa zamu mpaka alipopoteza fahamu.



    Wanaume walimaliza haja zao, wakammaliza mwanamke huyo na watoto wake kwa kuwakatakata mapanga. Palitapakaa damu kana kwamba machinjioni. Viungo vilitenganishwa mwili ukipasuliwa kama kuni.



    Watu hawa hawakuwa hata na lepe la huruma. Waliwakata binadamu wenzao kana kwamba wanamkata mnyama. Walipomaliza wakatokomea.





    ***





    NDANI YA KUNDI LA WHATSAPP …





    “Tukutane wote kwenye mazishi ya Bernard pasipo kukosa.”



    “Tutafika kumpumzisha mpambanaji mwenzetu.”



    “Nani anayefuata kwa sasa baada ya yule mbwa tuliyempeleka jehanamu?”



    “Tutalitazamia hilo siku za usoni.”



    “Unajua haya mambo yanahitaji utulivu na mipango.”



    “Ni kweli.”



    “Kweli, tusije tukaingia mkenge.”



    “Unachokisema ni sahihi.”



    “Ila tutampata mwingine mwenye mwanamke mtamu kama yule malaya?”



    Viwanasesere vya kufurahi vinatumwa kwa wingi kundini.



    “Aisee yule mwanamke ni mzuri bwana. Hata tukimkuta mwingine ni bibi, tuwafanye tu! tena sasa hivi wakiwa wanaona tunavyowashughulikia wake zao kama wao walivyotushughulikia kwa muda wote huo.”



    “Wazo zuri!”



    “Tunaweza tukanogewa tukakamatwa.”



    “Ni muda wa hawa watu kuumia. Hawastahili kufa hivihivi.”



    “Hey, tukutane kwenye mazishi ya Bernard. Tutaongea na kupanga mengi huko.”



    “Mustafa anasisitizia tusikose kufika.”



    Jumbe zinaendelea kutiririka na kutiririka, mamia.





    ***





    Mwanga wa simu ulifukuza kagiza kalichoanza kujirundika chumbani. Ilikuwa ni majira ya jioni sasa lakini chumba hakikuwa kimewashwa taa. Mwanga huu wa simu ndani ya kiza unadumu kwa sekunde kadhaa kabla ya mlio wa soketi kuita, na mara chumba kinakuwa cheupe.



    Anaonekana Kone akiwa amevalia bukta fupi nyeusi ya drafti drafti. Mkononi mwake alikuwa amebebelea simu, ile iliyokuwa inatoa mwanga. Anaitazama tena simu hiyo kabla hajayarusha macho yake kwa bi Fatma aliyekuwa amejilaza kitandani.



    Mwanamke huyo alikuwa amejifunika kwa nguo nyepesi iliyosadifu mwili wake vema. Alionekana amechoka, mdomo wake ulikuwa wazi akikoroma kwa mbali.



    Kone aliweka namba fulani kwenye simu yake alafu akapiga, namba haipatikani. Alijaribu tena, bado majibu yalikuwa hayo hayo. Alisonya akamuamsha mkewe kwa sauti chovu.



    “Bado hapatikani,” alisema. “Inabidi niende kwake sasa.” akaongezea.



    “Kuwa makini sana, Kone,” alisema Fatma mwenye mang’amung’amu ya usingizi. “Inawezekana kuna kitu kikawa kimemtokea kikakuweka nawe hatarini.”



    “Najua hilo, usijali. Lazima Rose atakuwa yupo shidani, hii si kawaida. Alikuwepo wakati nikimuhitaji, na sasa ni wakati wa mimi kuonyesha kujali kwangu.”



    “Lakini … huoni kama unaweza kuharibu kote kote, Kone. Tutakimbilia wapi?”



    Kone aliweka mkono wake begani mwa Fatma. Akamtazama katika namna ya kumuondoa hofu.



    “Niachie mimi, najua cha kufanya.”



    Alinyanyuka akatumia dakika kumi tu kujiandaa. Alivalia suruali nyeusi ya kadeti pamoja na tisheti nyeupe iliyofunikwa na koti kubwa refu rangi ya kaki lenye vifungo vinene. Aliaga akaondoka.



    Akiwa yu njiani, ndani ya gari lake, kuelekea kwa mwanamke Rose, mawazo yanakula kichwa chake. Mwanzoni alikuwa anafikiria usalama wa Rose kwenye mikono ya mshenzi Talib, ila baadae, katika kasi ya ajabu, mawazo juu ya mkewe yalimparamia.



    Usiku wa kuamkia siku hiyo haukuwa mwepesi kwake hata kidogo. Ulikuwa ni usiku wa mzozano na malumbano baina yake na mkewe. Ulikuwa ni usiku wa kukata mzizi wa fitna, kudadavuliana kwanini na sababu za mambo mbalimbali, haswa mahusiano ya Fatma na marehemu Raisi wa Guinea.http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Ukweli una gharama kubwa, waliwahi sema wahenga. Japokuwa Kone aliuhitaji ukweli, ulimuumiza. Alipata kujua mambo kadhaa ambayo yaliutoboa moyo wake na kuufanya chujio. Akili yake ilitibukwa na nyongo ikapasuka.



    Ni baada tu ya miaka miwili ya yeye kuwa kazini kama mhusika muhimu kwenye usalama wa taifa, alijikuta anateuliwa kuwa mtu muhimu kwa usalama wa Raisi. Maisha yalienda kasi sana. Aliaminiwa sana na Raisi akapewa kazi ambazo hakustahili, bali wale walio juuye.



    Kwa muda wote huo alikuwa akiamini kazi, vyeo na mshahara wake mnono ni majibu ya kazi yake aliyoifanya kwa utashi mkubwa. Kumbe lah! Jasho na damu aliyoimwaga kwenye uwanja wa vita, huku na kule, havikuwa vishawishi hata kidogo, bali mkewe, bi Fatma.



    Mkono wa Raisi uliokuwa unampapasa mkewe pindi anaposafiri, ndio huo huo uliokuwa unatia saini kwenye izimisho za mishahara na cheo chake. Hili lilikuwa chungu.



    Ilikuwa ngumu kwake kuamini. Hapana. Hapana. Hapana. Alisema na moyowe. Ila Bi Fatma hakutaka kumficha, alimweka wazi. Hakuna yeyote aliyekuwa anajua mchezo huo isipokuwa mke wa Raisi aliyewahi kuwafumania siku moja wakiwa Ikulu. Na hiyo ndiyo sababu mke huyo, wa Raisi, akajiondokea.



    Moyo wa Kone ukawa mgumu mno kama jiwe, aliuhisi kifuani ukiguruguta kama wataka kuchomoka. Alijizuia sana kutoa machozi siku hiyo. Alijikaza kisabuni mwanamke andelee kumwaga mboga.



    "Sio kwamba nilifanya hayo kwasababu ya kazi yako tu, bali pia na usalama. Kuna kipindi alinitishia endapo nisipofanya anayoyataka, basi atateketeza familia yangu. Nilishindwa kumkwepa kila ulipokuwa unaondoka kwani alikuwa anajua ratiba zako. Ndio maana nilikuwa nakusisitizia sana ubaki nyumbani japokuwa sikuweza kukwambia haswa kwanini."



    Maneno hayo yalitafuna mtima wa Kone. Aliambiwa usiku wa kuamkia siku hiyo lakini ni kana kwamba aliambiwa dakika moja tu nyuma. Aliyasikia yakiimba vizuri masikioni mwake. Yalimuumiza.



    Alijitahidi kujikomboa toka kwenye mawazo hayo, ikawa ngumu. Ni mpaka pale kafoleni kepesi kalichokuwa kamemzinga kalipoanza kutembea, basi ndipo akili yake ikahamia barabarani. Alitembea mpaka karibu na jengo la Rose, ilikuwa majira ya saa tatu usiku, akarusha macho yake getini. Aliwaona wanaume watatu ndani ya jezi za jeshi wakiwa wamebebelea bunduki.



    Alisogeza gari lake mbali alafu akalizima na kutoka ndani akiwa amebebelea bunduki ndogo.



    Tusijue kwa namna gani, Kone anaingia ndani ya jengo pasipo walinzi kushtuka hata kope. Anazama mpaka ndani, mfanyakazi, aliyekuwa jikoni, anashtuka akiitwa kwa kunong'oneza.



    "Ssshhhhh! ... ni mimi, Kone. Unanikumbuka?"



    Mfanyakazi anatikisa kichwa chake kwa uoga. Haraka mwili wake ulianza kutetemeka.



    "Mimi rafiki yake Rose. Hukumbuki nilishawahi kuja hapa?"



    Hofu iliziba kumbukumbu ya dada wa kazi. Alifanya jitihada za ziada kumkumbuka Kone. Bahati nzuri haikuchukua muda mrefu.



    "Ndio, nimekukumbuka!"



    "Rose yupo wapi?" Kone aliwahi kuuliza.



    Dada wa kazi alibanwa kigugumizi. Ilimbidi ashushe pumzi kwanza kabla hajateta:



    "Dada amechukuliwa na wanajeshi, walisema wanampeleka jela!"



    Alieleza tukio zima lilivyokuwa, Kone akaishiwa nguvu kwa upungufu wa matumaini. Ni jela gani atakayokuwa amepelekwa Rose? Hakuweza hata kubashiri. Kichwa chake kiliingia kazini upesi, punde akapata jibu, ila jibu hili lilikuwa na ukakasi: njia yake ya mafanikio ilikuwa nyembamba.



    Yuko radhi kuipita?



    Hakukuwa na namna sasa, ilimlazimu Kone awarudie wale walinzi getini. Kwa namna moja ama nyingine watakuwa na majibu ya maswali yake kadhaa. Alijaribu sana kulikwepa hili, ila halikuwezekana. Hiki kikombe kilikuwa chake.







    ***







    Alirudi huko kwa utulivu na ukimya. Alichungulia nje, akaona ni shwari. Alitoka ndani ya jengo asogelee geti, lakini upesi akamuona mlinzi mmoja aliyebebelea bunduki, haraka akajificha kwenye mgongo wa mti mmojawapo uliomo humo ndani.



    Alitulia hapo akimtazama mlinzi. Alingojea kidogo tu, mlinzi akasogea karibu kabisa na yeye. Upesi alimdaka akamvunja shingo pap - pap! mlinzi akadondoka chini kama zigo. Kone akalifuata geti na kuligonga mara mbili kwa konzi ya vidole vyake.



    Geti lilifunguliwa, haraka Kone akamkwapua mlinzi aliyelifungua. Alimpiga shingo, kwa kutumia mgongo wa kiganja chake, katika namna ambayo ilimpiga ganzi na kumlegeza mlengwa wake. Alitoka nje ya geti upesi akawamudu wengineo kwa kuwafyatulia risasi ambazo hazikutoa sauti.



    Wote aliwaingiza ndani ya geti akalifunga. Alimtwaa mlinzi wa kwanza kumkabili, alikuwa kama ametoka pigwa na shoti. Aliweka mdomo wa bunduki shingoni mwa mlinzi huyo akamuuliza:

    "Rose yupo wapi?"



    Mlinzi alimtazama kwa macho ya ghadhabu, akamjibu kwa pupa:

    "Unaongelea nini? - Sijui nini wasema!"

    "Sina muda wa kupoteza hapa na wewe, ndugu," Kone aliwaka. "Rose, mwanamke aliyekuwa anaishi humu ndani, mmempeleka wapi? Aidha unijibu au nifumue shingo yako ukawakute wenzako!"



    Kone alididimizia mdomo wa bunduki shingoni mwa mlinzi. Mlinzi akagugumia kwa maumivu.



    "Atakuwa alipelekwa jela!" Alinena akiukunja usowe kwa hisia za maumivu.

    "Jela ipi?"

    "Sijajua ni ipi - inaweza ikawa Pademba ama jela kuu ya Freetown. Huko ndio kuna wafungwa wanawake."



    Kone hakuwa na haja ya kuuliza kuhusu hukumu hiyo. Alijua fika mdomo wa Talib ndio mahakama, na neno lake ni sheria. Alimmaliza mlinzi huyo aliyekuwa anaongea naye kwa kumnyonga, akimviringita shingo kama udongo wa mfinyanzi, kisha akaondoka.



    Ilibidi afanye mauaji hayo kwasababu ya kulinda harakati zake. Endapo angemwacha hai mlinzi huyo basi taarifa zake juu ya msako wa Rose zingefika kwa Talib. Na basi kitumbua kingekuwa kimeingia mchanga.



    Kwakuwa alishampanga dada mfanyakazi, mauaji yale ya walinzi yangeonekana yalifanywa na waandamanaji tu wenye hasira kali. Hilo ni heko kwake.



    Aliondoka eneoni akiwa sasa anawaza ni namna gani atapata upenyo wa kumkomboa Rose toka kwenye mdomo wa jela. Jela ambayo hakuwa ameijua haswa ni ipi kati ya mbili zilizotajwa.





    ***

    ***



    Oparesheni ya chini kwa chini ya mtawala; Al Saed, haikukoma kuvuma na kuita.



    Kikosi kazi kilichokuwa kimeundwa na wanaume kumi, kikiwa tayari kimetandaza mipango yake kama vile walivyopewa maelezo na mateka, kilisogea karibu kabisa na maeneo nyeti ya kikundi cha AMAA.



    Walitumia miguu wakilenga kutoonekana ama kugundulikana mapema. Miguu yao pamoja na macho vilifanya kazi kwa ufanisi mkubwa sana. Walinyata wakiangaza.



    Wakiwa wanafahamu kabisa wanachokifanya, waliwaua wanaume watano waliokuwa kwenye lindo la ulinzi. Walijua fika wanaume hao walipokuwa wamejificha na hata silaha walizobebelea. Taarifa zote hizo juu yao walikuwa wamezikusanya toka kwa mateka. Ni mlinzi mmoja tu ndiye alikaribia kunusurika, ila naye domo la kifo likammeza.



    Alikuwa ametoka lindoni akifuata chupa ya maji kwenye makazi yake. Alitwaa chupa hiyo na upesi akarudi kazini. Akiwa yu njiani, fahamu zake zilimtonya kuna mushkeli. Ukimya ulikuwa mkubwa mno na hata pale alipojaribu kumuita mwenzake, hakukuwa na majibu.



    Kitendo chake cha kwenda kutazama usalama wa mwenzie ndiyo kikawa cha mwisho. Alivamiwa na pande la mwanaume lililompeleka chini na kumshindilia kisu cha kifua.

    Kikosi kazi cha Al Saed, kwa nidhamu ya hali ya juu, kilijigawa na kukizunguka kijiji cha wanamgambo wa AMAA pasipo mtu yeyote wa ndani ya kijiji kufahamu. Wengi wa wanamgambo hao walikuwa wamelala, wachache wakiwa macho wakiusogeza usiku huo kwa vijisimulizi vya hapa na pale.



    Kikosi hiki kilitega mabomu lukuki kila upande. Walijua fika kupambana na maadui zao mtu kwa mtu (man against man) wasingeliweza kufua dafu kutokana na idadi yao, na hata pia ugeni wa eneo ukizingatia ni usiku.



    Baada ya kupandikiza mabomu hayo, taratibu walijiondoa eneoni. Waliyarudia magari yao wakaketi humo wakingojea muda kidogo kuyaruhusu waliyoyapandikiza yafyatuke.



    Punde mwanaume mmoja anatazama saa yake ya mkononi na kutikisa kichwa.



    "Tayari!" Alimwambia mwenzie aliyekuwa amebebelea kifaa cheusi kizito chenye vitufe kadhaa. Tip! Tip! Vitufe vilibonywa, na mara sauti kubwa za milipuko zikaanza kujibu kwa kishindo.



    Milipuko hiyo inasababisha tetemo kubwa la ardhi. Mwanga mkali uliosababishwa na moto nao unaangaza kana kwamba umeme. Kabla vitu hivyo havijakoma, wanaume hawa wanapeana ishara na mara haraka wanatoka kwenye gari na kurudi kule kijijini mwa wanamgambo.



    Walijigawa kama hapo awali. Kazi yao sasa ilikuwa ni kuwatafuta masalia, walionusurika kifo, na kuwamaliza kwa kuwashindilia risasi. Walifunua vyote vilivyokuwa vimefichwa na kuviweka bayana. Walitazama kila chochoro na chaka, hakukuwa na cha kubakiza!



    Kazi hiyo ikadumu kwa dakika chache tu, kijiji kikawa kimya, mizoga ikitapakaa. Wanaume lukuki wa kikundi cha AMAA wanaachwa wakiwa maiti, wakimimina damu.

    Je kazi yaisha?



    Al Saed angalipumua sasa.



    ***

    ***



    "Hili jambo halivumiliki hata kidogo. Ni upumbavu wa hali ya juu!" Alifoka Talib. Mishipa ya shingo ilikuwa imemsimama. Kinywa chake kilifunguka mpaka kwenye komo.



    Ni punde tu toka atoke kwenye msiba wa Meja jenerali aliyeuawa na kikundi cha waandamanaji. Lakini pia tangu apewe taarifa ya mauaji ya walinzi kwenye nyumba ya Rose. Haya kwake hayakuwa mepesi kuvumilia.



    "Inatosha!" Aliwaka. "Sihitaji tena kikao chochote baada ya hapa, bali utekelezaji. Nataka hawa wauaji wote wanyongwe, tena mbele ya umati: uwanja wa taifa!"



    Kulikuwa kimya. Wanaume kumi na mbili waliokuwa wanamtazama, wakiwa wamevalia sare za jeshi zenye utitiri wa vyeo, walikuwa kimya na watulivu.



    "Jenerali Freeman!" Talib aliita.

    "Ndio mkuu!" Freeman akaitikia kwa ukakamavu. Alikuwa ni mwanaume mnene mweusi. Sare ilikuwa imembana kana kwamba inachanika dakika moja mbele.



    "Nataka washenzi wote hawa ndani ya vitanzi! Umenielewa?"

    "Ndio, mkuu!"

    "Nakupa juma moja tu, moja! Silaha unazo, watu unao. Ukiwapata, unitaarifu. Nitakuja kuwafunga vitanzi kwa mikono yangu."

    "Sawa, mkuu!"

    "Kuna swali lolote?" Aliuliza Talib akiwatazama wajumbe wake kwa macho makali na ya udadisi.

    Kulikuwa kimya. Pengine uoga ulitawala. Nyuso za wajumbe zilikuwa zinatazamana kana kwamba wanataka kumshitaki yeyote atakayeongea.

    "Basi kama hamna maswali, tukatekeleze," alimalizia Talib kisha akaondoka zake. Mwendo wake ulikuwa wa kasi. Ilikuwa ni wazi hakuwa na hamu ya kuongea. Uso wake ulikuwa mweusi zaidi, na macho mekundu yaliyovimba.

    "Sasa tunafanyaje?" Aliuliza Freeman. Hakuwa anajua cha kufanya, kwa mujibu tu wa macho yake. Ni kana kwamba mtoto anayemtafuta mamaye akafika njia panda asijue pa kuelekea.



    Kwa muda kulikuwa kimya. Kila mtu alikuwa anatafakari namna ya kufanya. Baada ya kama dakika tatu za utulivu, mmoja, mwembamba maji ya kunde kwa rangi, anavunja ukimya akisema:

    “Nina wazo.”

    Wenzake wote wanamtazama.



    “Kwanini tusiitishe mkutano wa usalama tukajumuika na hawa waandamanaji?”



    Wazo hilo likawa kituko. Liliwasahaulisha watu matatizo kwa kuwaangulisha kicheko.

    “Richard, we mzima kweli?” aliuliza Freeman. “Umemsikia mkuu amesemaje hapa? Anawahitaji watu hawa vitanzini, tena alivyovifuma mwenyewe, wewe unakuja kutuambia tuitishe mkutano? Tujadiliane kitu gani na hao wauaji?”

    “Nadhani mngenisubiri nimalize ninachotaka kuongea,” alijitetea mtoa hoja, Richard kama alivyotambulishwa na wenzake.



    “Richard, huna haja ya kumalizia,” alisema Freeman. “Mkutano hauwezekani kabisa! Hilo futa kichwani mwako. Hatuwezi kukaa meza moja na mwivi.”



    Baada ya maneno hayo, Richard anafunga mdomo wake, haongei tena. Freeman akishirikiana na wenzake, ambao yeye ndiye alikuwa anawaongoza, wakapanga na kukubaliana juu ya mkakati wao. Waliupachika jina la oparesheni mwanzo, kati na mwisho.



    Kwenye mkakati wao huo hakukuwa na mambo ya kubembelezana. Maeneo yaliyoripotiwa kuwa na vurugu kwa kiasi kikubwa yalitengewa nguvu ya ziada, wakikubaliana kila kijana ndani ya maeneo hayo atakamatwa, maelezo atayatolea ndani.



    Wafungwa hao watawataja wenzao na mmoja baada ya mmoja atasakwa, atatiwa nguvuni na mwishowe kuuawa. Mwisho wa mpango.



    “Ndani ya siku tatu tu, tunamaliza huu mchezo!” alitamba Freeman.

    “Mkuu, atafurahi sana kumaliza jambo hili ndani ya muda mfupi.”

    “Bila shaka, tunaweza ongezwa hata marupurupu.”



    Kicheko kikajaza vifua vyao. Nyuso zilikuwa nyepesi sasa tofauti na mwanzo. Hii ndiyo nguvu ya tumaini. Japokuwa hawakuwa bado wamefanikisha, ila walitumai.



    “Haki huu mpango hautafanikiwa,” alisema Richard. Sauti yake ilikuwa kama hatua za mwalimu karibu na darasa la wanafunzi wapiga kelele. Wote walinyamaza wakimtazama, kwa mshangao.



    “Freeman, tuache kupeana matumaini mepesimepesi. Mnajua fika huo mpango wenu hautafanikiwa hata lepe,” alisema Richard kwa kujiamini. “Tumemfanya adui yetu aonekane mdogo sana kuliko uhalisia. Tunalifanya hili tatizo liwe dogo ili kujipa ahueni. Tunakosea.”

    “Richard!” Freeman akang’aka. “Wewe ni nani wa kuchambua na kupima oparesheni zangu?” aliuliza. “Ina maana mkuu hakukuona wewe mpaka akaniteua mimi? Naona umesahau mimi ni nani kwako, ukiendelea basi nitakukumbusha katika njia ngumu.”



    Kikao kilifungwa namna hiyo kila mtu akapata kuenenda katika njia yake. Makubaliano yakiwa kwamba utekelezaji wa oparesheni mwanzo, kati na mwisho utaanza moja kwa moja siku inayofuatia.



    Ila basi kama kuna mahali Mungu ametupatia sie binadamu, ni kutojua ya mbele yetu, hata kwa sekunde. Mawazo na utashi wetu havina uwezo wowote wa kubashiri, haijalishi ni namna gani tulivyo werevu.



    Freeman alirudi nyumbani kwake punde tu baada ya kutoka kupitia bidhaa kadhaa ndani ya duka kubwa lililopo ndani ya kambi ya jeshi. Akiwa na walinzi watatu ndani ya gari lake, anaongozana mpaka nyumbani kwake anapopokelewa na geti kubwa rangi nyekundu pamoja na walinzi watano waliovalia sare za jeshi wakibebelea mitutu.



    Geti linafunguliwa anazama ndani. Walinzi wanatangulia kushuka kabla yake kwa ajili ya kutazama usalama. Freeman anaingia ndani akiwaacha walinzi wakidumisha usalama maradufu.



    Hatukujua yaliyoendelea humo ndani, ila baada ya punde, kama robo saa, jambo fulani linatukia. Wanajeshi waliokuwa lindo wanabadili zamu. Gari la jeshi linalorandana muundo na fuso, lililokuwa limewabebelea wanaume sita wenye silaha, linasimama mbele ya uzio na kuwashusha wanaume watano isipokuwa dereva.



    Wanaume hao wanasalimiana na wenzao wanaowapokea lindo, kisha wanashika zamu wakiwashuhudia wenzao wakiyoyoma na gari lililowaleta.



    Baada ya gari kupotea kabisa lisionekane, wanaume, hao watano walioletwa na gari, wanatazamana na kupeana ishara ya macho. Geti linagongwa mara mbili, mara linafunguliwa.



    Wanaume hao watano wanazama ndani ya jengo kwa mkupuo. Wanafyatua risasi kuwalenga walinzi watatu waliokuwemo ndani. Tukio hilo linadumu kwa haraka mno. Walinzi wanalazwa chini wakivuja damu. Wavamizi wanaingia ndani kwa kuvunja milango.



    Punde…



    “Nisameehee!”



    Sauti kali ya kiume ilisikika. Bila shaka alikuwa Freeman. Mlango wa sebuleni unafunguliwa, Freeman, akiwa amevalia nguo ya ndani pekee, anarushwa nje kama zigo. Anatua kwenye sakafu kwa kukita. Anapata majeraha kadhaa ya kuchubuka mkono ukitenguka.



    “Nisameheni jamani. Nisamehe!” alilia. Alitia huruma: macho yalimtoka, mdomo ukiachama. Alivuja jasho jingi. Mstari wa jasho ulijichora kwenye nguo ya ndani.

    “Mtaenda mmoja baada ya mmoja!” alisema mwanaume mvamizi. Alikuwa ni yule aliyekuwa anatoa amri pia kwenye tukio la kuuawa kwa meja.

    “Taratibu taratibu, mpaka tutamfikia huyo mshenzi wenu. Hamna yeyote atakayepona. Mtajua kwamba nchi hii ni ya wafanyakazi, na si viongozi waliojawa na tamaa na mapuuzo.”

    “Jamani nina familia,” alijitetea Freeman. “Sihusiki na lolote kwenye mambo ya utawala. Sihusiki kabisa!”

    “Na vipi kwenye mauaji? Sio wanajeshi waliokuwa wanaua watu? Mlidhani nyie ndio watu pekee mlio salama nchini, si ndio?”

    “Hapana! Hapana!” Freeman alisema akikumbatisha mikono yake kama mtu anayesali. “Sijahusika na oparesheni yoyote ya kuua watu jamani. Naombeni mnisamehe.”



    Alipiga magoti. Punde alijikuta yupo chini baada ya kupigwa teke zito la kichwa. Pua yake ilichuruza damu, na mdomo pia. Macho yake hayakuwa yanaona vema, ni kama vile mtu aliyekuwa amedumu gizani kwa muda mrefu alafu ghafla akahamishiwa penye mwanga, tena mkali.



    Kwa mbali alikuwa anasikia namna akitukanwa matusi ya nguoni. Alivuliwa nguo yake ya ndani akabakizwa uchi. Alipigwa picha kedekede kisha akafumuliwa kichwa kwa risasi. Huo ukawa mwisho wake: muasisi wa OPARESHENI MWANZO, KATI NA MWISHO.





    *Oparesheni hiyo itakufa? Talib atafanyaje akipata hizo habari? Richard alitaka sema nini? Je Mr. X kaenda na maji? Wapi The GHOST?*







    Ni furaha kubwa kwa Al Saed. Fursa ya kuhema ilikuwa imepatikana sasa baada ya kunyanyaswa kwa muda. Alikutana na kikundi chake cha oparesheni huko ikulu kwa ajili ya kuwapongeza. Aliwaalika pia na viongozi wake wa usalama ambao kwa muda wote huo alikuwa amewaficha aliyokuwa anafanya.



    Kwa idadi walionekana watu ishirini na tano ndani ya uwanja wa tafrija wa ikulu. Mikononi walikuwa wamebebelea glasi za vinywaji vilivyokuwa vinapitishwa kila pale vilipokauka vyomboni. Hakukuwa na viti, watu wote walikuwa wamesimama. Taratibu muziki laini ukiwa unasindikiza shughuli.



    “Leo ni siku ya furaha sana kwangu, na kwa taifa kwa ujumla!” alipaza sauti Al Saed akinyanyua juu mkono wake uliobebelea glasi ya kinywaji. “Sina haja ya kusema sana, nimepaliwa na furaha. Kazi ambayo imewashinda simba, fisi wakaitekeleza.”



    Maneno hayo yaliwafanya viongozi wa usalama watazamane kwa macho ya tai. Midomo yao haikutema kitu ila kwa namna waliguswa. Walitabasamu kwa aibu.



    “Najua kuna wanafki miongoni mwetu,” aliendelea kumwaga Al Saed. “Hapa wamevaa ngozi ya kondoo ila ndani ni fisi. Ni kitendo tu cha muda, nitawagundua. Na punde nitakapowagundua, watafia mikononi mwangu.” Alisema Al Saed akionyeshea ngumi yake nzito.



    Kulikuwa tulivu muziki ukiwa unavuma kwa mbali. Sauti ya Al Saed ilikuwa inanguruma kama simba mwituni. Kila mtu alikuwa amenyamaza akimtazama kwa kuguswa. Sura yake ilikuwa imejifuma katika namna ya umakini akimaanisha ayasemayo.



    “Ni aibu sana!” alipaza. “Ni aibu kuona kazi zinaenda pale tunapoifanyia vichochoroni. Kisa tu watu wachache! Watu ambao hawataki kuiona Liberia inatamalaki kwa amani.”



    Alisafisha koo lake, akanywa fundo moja la kinywaji. Ni kana kwamba maigizo jukwaani namna watu walivyokuwa wanamtazama.



    “Hii ni nafasi yao ya pili; nafasi ya kujitazama, kujikosoa, kujitathmini. Na ni kwasababu naamini kwenye nafasi ya pili. Nafasi ya pili, nafasi ya mwisho. Tufurahi!”



    Alinyanyua tena mkono wake juu, watu wakagongesha glasi na kuendelea kunywa. Tafrija ilidumu kwa masaa mawili mbele kabla haijakoma na watu kundoka zao.





    Punde gizani …



    “Haikuwa rahisi, mzee. Kazi ilisukwa kwa usiri sana. Tusingewezeza kutambua hata punje,” sauti ilisema. Kulikuwa giza chumbani.



    "Unajua uzembe wako umenigharimu kiasi gani?" Sauti ilifoka. "Wapambanaji wangu lukuki wameuawa. Makazi yao yameharibiwa. Unataka nianzie A na nipo Che? Unajua itanihitaji rasilimali ngapi kujenga ngome hiyo tena?"

    "Nisamehe mkuu."

    "Samahani yako itarepea majeraha yangu?"





    Kulikuwa kimya kwa muda. Ni kana kwamba hakukuwa na mtu hapo. Ndani ya giza hili ungejiuliza wanaonanaje.



    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    "Najua wanadhani nimekufa," ilisema sauti. "Hii ndiyo nafasi yetu kubwa kupanga mashambulizi mazito; mashambulizi ya kushtukiza! Na tutakapoanza, haitakoma kamwe."

    "Ndio mkuu. Kipi naweza kufanya kusadia?"

    "Nataka uanze kufanya kwa kufanya kazi moja kwanza. Nataka hao watu wote waliohusika na mauaji na uvamizi, nipate kuwafahamu. Nahitaji picha na maelezo juu yao. Wapi wanaishi, kikosi gani wanafanya kazi. Nataka taarifa hizo kesho!"

    "Sawa mkuu."

    "Nitawachinja kama kuku. Na video zao zitasambaa dunia nzima!"





    Baada ya tisho hilo, simu ikakata na kukaendelea kuwa kimya.



    ***

    ***



    Talib alizima sigara yake kubwa kwenye uso wa kisosi kisha akaufunika mdomo wake kwa kiganja. Macho yake yalizama fikirani. Hakuonekana mwenye furaha. Alitikisa miguu yake juu ya meza akigonganisha visigino.





    Alikuwa mwenyewe kwenye chumba kikubwa cha makutano. Viti vilikuwa vitupu. Ndani kulikuwa kuna kajoto chepesi cha kiyoyozi kuzimwa karibuni.

    Runinga kubwa ukutani ilikuwa inaonyesha taarifa ya habari. Mtangazaji alikuwa amevaa suti nyeusi kama ngozi yake. Miwani yake ya macho ndiyo kidogo ilimfanya aonekane vema. Sauti yake kavu ilisikika vizuri ingawa msikilizaji hakuwepo.





    Kwa muda mchache mtangazaji aliongea. Kadiri alivyokuwa anatema habari, taratibu akaanza kukamata mishipa ya fahamu ya Talib. Hatimaye mwanaume huyo alitupia macho kideoni apate ona na kuskiza vema. Aidha angeweza kupata jambo.





    Baada ya muda mfupi tu aliona habari mbaya, mtangazaji akiwa ni yuleyule kiooni. Sauti kavu ya mtangazaji huyo ilimuumiza masikio ikifikisha ripoti juu ya namna kundi la waandamanaji nchini Sierra Leone lilivyogeuka kuwa kundi la waasi. Kundi tishio.





    Nani anayelifadhili kundi hili? Ndiyo hoja iliyokuwepo mezani. Swali hilo lilikuwa limeandikwa kwa rangi nyeupe juu ya ubao mwekundu chini ya runinga. Kwa namna chanya lilimfanya Talib alizingatie.





    "Kumekuwa kuna ushawishi na nguvu kubwa nyuma ya kundi hili la waandamaanaji. Wana silaha nzito na hata mfumo wao wa mawasiliano si haba. Wanapanga mikakati ya kuwaua viongozi na familia zao katika namna ya ustadi. Hapa lazima kutakuwa na namna,"alisema mchambuzi wa mambo ya siasa za Afrika magharibi, bwana Rigorbet Ayatoye.





    Kana kwamba anatazama tamthilia sisimuzi, Talib alitega sikio.





    "Pasipo shaka tukio hili sio la mwisho. Yataendelea zaidi na zaidi. Kwa serikali ya kidikteta kushindwa kuhimili kitu hiki, kinaashiria tatizo si dogo. Kinaashiria mizizi mikubwa ambayo imeijenga kikundi hiki, na hili linaweza likaleta athari kubwa kwa siasa za Afrika ya magharibi. Wengine wanaweza kuliiga." Alinguruma mchambuzi.

    "Sawa sawa," akadakia mtangazaji. "Na unaongeleaje juhudi za Al Saed, wa Liberia, kwenye kutokomeza uhasi. Kwa muda huu anaonekana kama mshindi. Ameibuka na kukamata anga la habari kwa sasa."

    "Alichofanya Al Saed ni jambo la kishujaa. Al Saed ni mhasi mstaafu, ametumia namna nzuri sana ya kupambana nao kwa kupanga mipango madhubuti. Ila mpaka sasa haijulikani kama kiongozi wa kundi la waasi ameuawa ama lah! Ndio, inasemekana amekufa ila hamna ushahidi wowote, na mimi nitakuwa mtu wa mwisho kuamini kama alikuwamo na kufia ndani ya kile kijiji."

    "Unadhani ni kwanini vita ya uasi inakuwa ngumu sana kukoma, haswa katika maeneo haya?"

    "Tatizo kubwa ni madaraka, ndugu mtangazaji. Kila mtu ana haja na madaraka. Uchu. Kila mmoja anataka kiti cha dhahabu. Na shida kubwa inakuja kwamba mataifa haya ni mahasimu. Hakuna anayemsaidia mwengine, na wengine wanashutumiwa kuhusika na kuwafadhili waasi wa nchi jirani."

    "Unadhani nini sasa kifanyike, mchambuzi, ili kurudisha shwari?" Aliuliza mtangazaji. Mchambuzi akasafisha koo lake kwanza kabla hajajibu;

    "Nadhani ni wakati sasa wa mataifa makubwa na mashirika ya kimataifa kurushia macho yao kwenye haya mambo kabla hayajawa mabaya zaidi. Hali ya Sierra Leone itasisimua uhasi Liberia, na hata Guinea vilevile. Tunaweza tukajikuta tunarudi kwenye jinamizi la mauaji makubwa kama miaka ya nyuma. Hakuna anayejua, ila yanaweza kutabirika."





    Baada ya maneno hayo kipengele cha mchambuzi kilikoma vikaendelea vingine ambavyo havikumgusa Talib. Mwanaume huyo alizama fikirani akipembua mambo kadhaa. Baada ya dakika kama mbili tatu hivi alinyanyua mkonge wa simu na kuita.



    "Njoo mara moja," aliagiza. Punde akaja mwanaume mmoja, mwanajeshi, aliyekuwapo kwenye kikao cha kuwatokomeza waandamanaji. Alikuwa ni miongoni mwa wale waliokuwa wanaunga mkono mikakati ya Freeman, marehemu: Oparesheni mwanzo, kati na mwisho. Kwa jina alifahamika kama Rauli, ama mbweha kwa jina la utani.





    "Freeman ameshaenda. Hali naona inakuwa mbaya zaidi," alinena Talib kwa utulivu. Hakuwa na hasira bali umakini, kama alikuwa nayo basi alifanikiwa kuifichama.

    "Tunahitaji mrithi wake, tena haraka, ambaye atafanikisha kazi hii pasipo na makosa kabisa. Na nimetazama upana wa jaruba hili, nikaona wewe unastahili kufanya hii kazi."

    "Mimi?" Rauli alijinyooshea kidole.

    "Ndio, wewe. Vipi, huwezi?"

    "Hapana, naweza mkuu!"

    "Nakupa siku moja tu, utanianishia mipango yako yote ya kumaliza hao wapumbavu. Kaa na wenzako muone mnafanyaje alafu mtanishirikisha."

    "Sawa."

    Ila kabla Rauli hajaondoka, anasema:

    "Mkuu, kuna jambo."

    Talib anampatia macho ya kuguswa.

    "Ni kuhusu kifo cha Freeman."





    Uso wa Talib unaungana mkono na macho yake. Alionekana ana hamu ya kujua zaidi kuhusu hiyo mada.

    "Kifo cha Freeman kilitupatia maswali mengi sana. Na kwa namna moja, tulijikuta tunaamini kwamba kina mkono wa mmoja wetu."

    "Unamaanisha nini?"

    "Namaanisha kwamba kuna mmoja wetu alimuua ama kupanga mauaji ya Freeman."

    "Nani huyo na mmemjuaje?"

    "Ni Richard. Tukiwa kwenye kikao alipinga kabisa mipango ya Freeman na aliapa kabisa mpango huo hautafanikiwa kwa vyovyote vile. Siku hiyo hiyo muda mchache mbele, Freeman anauawa. Inakuaje Richard alikuwa anajiamini kiasi kile? - Na alichobashiri kitimie?"





    Talib alivuta pumzi ndefu. Alilaza mgongo wake kwenye kiti akitafakari kwa dakika mbili kabla hajasema:

    "Unajua kweli inawezekana kukawa kuna mtu ndani ya mfumo wetu akawa anashirikiana na hawa wapuuzi!"

    "Ndio, mkuu. Inawezekana." Alisema Rauli kabla hata ya kufikiria.

    "Hao waandamanaji walijuaje kama Freeman alikuwa anaelekea kuwatokomeza? Itakuwa kuna mtu amewapasha habari!"

    "Ndio, mkuu. Na si mwingine bali Richard. Ni yeye tu!"

    Talib alivaa uso wa chui. Aling'ata meno yake kwanguvu. Akiwa ameyabana meno vivyo hivyo kana kwamba anataka kuyang'oa, alibamiza meza kwa ngumi yake nzito akisema ;

    "Nataka kichwa cha huyo hanisi hapa!"





    Hiyo ilikuwa amri. Rauli alisimama akatoa salamu na kuondoka kwenda kuitimiza.



    ***

    ***



    "Naona leo umetingwa," sauti ya Bi Fatma iliita nyuma ya mgongo wa Kone. Mwanaume aligeuka na kumtazama mkewe kwa macho ya karibu.

    "Kiasi tu mpenzi. Si nimekaa hapa muda si mrefu tu."

    "Muda si mrefu? Aah aah ... mi nakuhitaji kitandani bwanaa," alisema Bi Fatma kwa sauti ya puani. Alimsogelea Kone akampapasa mabega kwa viganja vyake vilaini.

    "Twende baaasi."

    "Embu kaa hapa." Kone alimvuta mkono mkewe na kumketisha kando.





    Bi Fatma alikuwa amevaa gauni jepesi pekee. Kone alikuwa amevalia bukta rangi ya bluu iliyokoza kifua chake kikiwa wazi. Mbele yao kulikuwa na tarakilishi mpakato Kone akihangaika nayo kwa muda wote ule.





    "Unajua kuna mambo hayajakaa vizuri huko nyumbani,"alisema Kone kwa uso tashtiti. "Hali ya kisiasa si shwari kabisa. Inasemekana kuna vuguvugu la mapinduzi ya jeshi. Ndani ya chama tawala mpaka sasa hakuna maridhiano juu ya nani atakayekaimu nafasi hiyo, ni hovyo. Watu wamegawika kimakabila; wa Fula na wa Malinke. Kila mmoja anataka kushika hatamu. Kuna uwezekano mkubwa viita ikajiri."





    Bi Fatma alimshika mumewe shavu akimtazama kana kwamba mtoto mdogo.





    "Mpenzi, unaweza ukasahau kuhusu Guinea hata mara moja?" Aliuliza kwa sauti karimu. "Lini utapata amani ya moyo wako? Jaribu kupumzika, na kufanya mengineyo. Siasa za Afrika ni mapacha wa mama mmoja."

    "Mama," Kone akaita. "Kumbuka Guinea ni kwetu, ni nyumbani. Wazazi, ndugu jamaa na marafiki zetu wote wapo huko. Nitaipuuziaje? Watoto wetu wataishi katika ardhi ngeni mpaka lini? Daima?"

    "Hapana mume wangu. Ila hauna chochote cha kufanya kubadili hali hiyo, sasa ya nini kukonda na mawazo?"

    Kone alitikisa kichwa.

    "Cha kufanywa hakikosekani mpenzi, ila tu namna ya kukifanya. Na namna itapatikana tu. Siwezi nikakaa nikishuhudia mambo yaenda kombo chomboni. Hata nafsi yangu itanisuta."





    Bi Fatma alibadilisha sura. Hakupendezwa na mwenendo wa mumewe. Alijinasua karibu akaenda zake.





    "Mpenzi!" Kone aliita. Alinyanyuka akamfuata mke wake. Alimdaka kiuno akamgeuza.

    "Nini mpenzi wangu?"

    "Unaniudhi sana!" Alijibaraguza Bi Fatma. Aliufuma uso wake kwa maudhi. Alideka.

    "Tuachane na hayo basi mke wangu," alisema Kone. Alimbeba mkewe akampeleka kitandani alipombwagia.

    "Niahidi kwanza, hautafikiria tena hayo mambo ya siasa," alisema Bi Fatma. Alimtazama Kone machoni kana kwamba kachero anambana jasusi wa kigeni.

    "Nakuahidi mpenzi, sitafikiria tena," alisema Kone. Ila sauti yake ilimsaliti.

    "Najua unanidanganya, Kone. Naju ..."

    "Sshhh ... yameshapita hayo mpenzi," alinong'oneza Kone akiweka kidole chake kwenye lips za mkewe. Alimbusu shingoni na kumkumbatia vizuri ...





    Masaa yalipoenda, jua liliamka kukawa na mwanga, ila dhoofu. Siku ilikuwa na kaubaridi cha upepo na anga lake liliahidi kuleta mvua muda si mrefu ujao.





    Fatma alikuwa amejikunja akijifunika shuka gubigubi. Kitandani alikuwa peke yake. Joto alilolipata toka shukani lilimpa hamasa zaidi ya kutaka kuendelea kuchapa usingizi. Ila alipokuja kugundua yu peke yake, baada ya kunyoosha mkono, alikurupuka akaangaza.





    Alitoka kitandani akatazama kila eneo isipokuwa tu vyumba vya watoto, hakumuona Kone. Alijaribu kupiga simu lakini nayo haikupatikana. Alifura.

    "Kone, unataka nini zaidi ya maisha yako?"

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Mara aliona kikaratasi kidogo mezani. Alikisogelea akakikwapua. Kilikuwa kimeandikwa ujumbe kwa maneno madogo ya mwandiko wa kiume:

    "Nimetoka kwenda kumtoa Rose. Niwie radhi sijakuaga."





    Fatma alichana hicho kikaratasi katika vipande milioni. Alirudi kitandani akaketi na kudaka kichwa chake kana kwamba kilikuwa kimemzidi uzito. Alitibua nywele akiukunja uso.





    Alighafirika. Alishiriki kwenye kidonda cha wivu na sasa alikuwa anaumia.





    **

    **





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog