Search This Blog

Sunday 20 November 2022

TAXI - 4

 





    Simulizi : Taxi

    Sehemu Ya Nne





    Winifrida alishusha tena pumzi ndefu za ndani kwa ndani, na taratibu kujiamini kukaanza kumrudia.



    “Kama kufuatwa na wavulana, wananiita na kuniambia wananitaka.”



    “Sasa hao wavulana unawachukuliaje, maana inaonekana ni wengi wanaokuita na kukutaka!” Joyce aliuliza huku akiachia tabasamu.



    “Mimi wananikera tu, huwa siwajibu kitu,” Winifrida alisema huku akiukunja uso wake.



    “Unayosema ni ya kweli, wifi?” Joyce alimuuliza akiwa kamkazia macho usoni.



    “Kweli, wifi,” Winifrida alisema huku akipitisha kidole chake cha shahada shingoni na kukikung’uta hewani.



    “Mbona hujawahi kuniambia?” Joyce alimuuliza tena huku akimkazia macho.



    “Nilikuwa naogopa.”



    “Uliogopa kunieleza? Kwa nini uniogope?” Joyce aliuliza na kumfanya Winifrida abaki kimya asijue la kusema. Alikuwa akinyonganyonga vidole vyake.



    “Hakuna mvulana yeyote uliyewahi kumkubalia au hata aliyewahi kukushika shika kifuani na kukwambia una matiti mazuri?”



    Winifrida alitingisha kichwa chake kukataa. Joyce alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu.



    “Hebu angalia kifua chako, jinsi matiti yako yanavyochomoza juu ya blauzi na nguo nyingine unazovaa! Usipende kuvaa nguo nyepesi kama hivyo, mtoto wa kike unatakiwa kuusitiri mwili wako ili kuwapunguzia wavulana shauku,” Joyce alisema kwa sauti ya upole.



    “Kama ulikuwa umeanza mchezo mbaya au ulifikiria kuuanza naomba uache kabisa, kazania masomo, wanaume ni walaghai tu, watakudanganya wanakupenda kumbe wanataka kukuchezea tu, na pengine wakuambukize magonjwa ya zinaa au ukimwi, nadhani unafahamu hilo. Pia kuna mimba, nadhani umenielewa vizuri wifi yangu,” Joyce alitoa nasaha zake.



    Winifrida alibetua kichwa chake kukubali.



    “Sawa, kuanzia leo anza kuusitiri mwili wako vizuri, usivae nguo kama hizi mbele ya kaka yako, si heshima. Inabidi sasa uwe unavaa sidiria nilizokununulia ili kusitiri matiti yako, na hivi vinguo vyako vya ajabu ajabu usivivae tena. Ni hayo tu wifi yangu,” Joyce alisema na kuinuka, akaelekea jikoni.



    Winifrida alishusha pumzi ndefu za ahueni.



    * * * * *



    Saa kumi na mbili na nusu jioni, Sammy alikuwa akiendesha gari lake aina ya Cadillac DeVille akipita barabara iliyotoka Tabata Barakuda kuelekea nyumbani kwake Tabata Chang’ombe.



    Aliiacha ile barabara kubwa ya lami na kuchepuka kuingia kushoto akiifuata barabara iliyoelekea nyumbani kwake, alizipita nyumba kadhaa za jirani na kufika mbele ya nyumba yake. Alikunja na kuingiza gari lake kwenye uwanja mpana wa mbele ya nyumba, akasimamisha gari mbele ya geti kubwa jeusi lililokuwa mbele ya ile nyumba yake na kupiga honi.



    Baada ya kitambo kifupi geti dogo lililokuwa kwenye lile geti kubwa likafunguliwa nusu na muda huo huo Winifrida akiwa ameongozana na Pendo walichungulia nje na kuliona lile gari lakini hawakujua ni la nani.



    Walibaki wakilitazama kwa makini kwa kitambo huku wakionekana kujiuliza maswali yaliyokosa majibu. Sammy aliendelea kutulia ndani ya gari lake akiwatazama kwa tabasamu pasipo kuwashtua. Pendo alilisogelea karibu lile gari na mara akamuona Sammy na kuruka kwa furaha.



    “Baba! Baba!” Pendo aliita kwa nguvu na kumfanya Winifrida asogee karibu zaidi, akamtambua Sammy na kuachia yowe dogo la mshangao huku akibaki mdomo wazi.



    “Ha! Kaka Sammy!” Winifrida alisema huku akifungua geti kubwa haraka kuruhusu lile gari liingie ndani ya uzio wa ile nyumba.







    Sammy alimfungulia mlango wa abiria Pendo ili apande, kisha aliliingiza lile gari ndani ya uzio na kutulia ndani ya gari akiliacha liungurume taratibu. Baada ya dakika kama mbili alizima injini.



    Alichomoa ufunguo na kuushika mkononi kisha aliteremka kutoka ndani ya lile gari akiwa kashika ufunguo wake na mkono mwingine alimshika mkono Pendo huku akitabasamu.



    Winifrida aliendelea kumtazama Sammy kwa mshangao kisha akaligusa lile gari katika namna ya kulishangaa kabla hajageuka kumtazama Sammy.



    “Kaka, hili gari la nani?” Winifrida alimuuliza Sammy kwa shauku.



    “Kwani unalionaje! Zuri au baya?” Sammy alimtupia swali badala ya kumjibu.



    Winifrida alikunja sura yake huku akilitazama lile gari kwa makini kwa namna ya kulikagua zaidi na kushusha pumzi za ndani kwa ndani kama aliyekuwa akitafuta jibu, kisha alifungua mlango wa mbele upande wa abiria na kuingia, akaketi kwenye siti ya abiria huku akiendelea kulitazama kwa mshangao.



    “Unalionaje, zuri au baya?” Sammy aliuliza tena swali lile lile huku akiachia tabasamu.



    Winifrida alimtazama na kunyanyua juu mabega yake huku akibetua midomo. “Sijui!”



    “Basi na mimi sikwambii ni la nani,” Sammy alisema huku akiendelea kutabasamu.



    “Ayi jamani, kaka!” Winifrida alilalama huku akimtazama Sammy kwa shauku ya kutaka kusikia kuwa ni gari lake. Sammy na Pendo wakaanza kucheka.



    Joyce alikuwa amesikia muungurumo wa gari lakini aliamua kusubiri kwanza huku akitaraji kuona wageni wakiingia ndani lakini hakuwaona bali alikuwa akisikia wanaongea na kucheka. Aliamua kuchungulia nje kupitia mlango wa barazani uliokuwa umefunguliwa nusu, akamuona Sammy akiwa amemshika Pendo na wakati huo Winifrida alikuwa ameketi kwenye siti ndani ya gari.



    Joyce aliwatazama kwa mshangao mkubwa asijue kilichokuwa kikiendelea pale nje ya nyumba. Hata hivyo, hakutoka nje bali alirudi ndani na kuendelea na shughuli yake.



    Sammy alimshika Pendo akamwongoza kuelekea ndani huku wakimwacha Winifrida anaendelea kulikagua lile gari kama aliyekuwa akilifanyia matengenezo. Kwanza alivuta droo iliyokuwa kwenye dashibodi na kuanza kuchakurachakura akitafuta kilichomfaa. Kisha alianza kuchunguza hapa na pale, na baadaye aliinama kuchungulia chini ya dashibodi.



    Hakuridhika, aliinama zaidi na kusukuma siti ya abiria huku akitazama chini kabisa ya siti, akaona kadi ndogo itumikayo kuhifadhi kumbukumbu kwenye simu maarufu kama memory card (Micro SD) iliyokuwa imepachikwa kwa ustadi mkubwa chini ya ile siti ya abiria.



    Winifrida aliitoa ile kadi huku akiitazama kwa udadisi zaidi, alikunja sura yake akijaribu kufikiria. Alidhani labda Sammy au mtu mwingine yeyote alikuwa ameidondosha, lakini akajiuliza mbona kama ilioneka kama imefichwa!



    Muda huo huo Sammy alitoka nje huku akimwangalia kwa makini. Winifrida alimuona na kuificha ile kadi. Alifungua mlango wa gari na kushuka huku akicheka, kisha akaelekea ndani na kumwacha Sammy akimsindikiza kwa macho hadi alipoingia ndani.



    Sammy aliachia tabasamu na kubetua mabega yake juu huku akitingisha kichwa chake taratibu. Hakujua nini kilichokuwa kinaendelea kwenye akili ya Winifrida. Alifunga milango ya gari vizuri na kurejea ndani.



    * * * * *



    Ilikuwa saa moja jioni, Mr. Oduya alikuwa amewaacha ndugu wawili; Madame Norah na Zainab wameketi kitandani wakiongea kwa furaha na kusimuliana masaibu waliyopitia kwa kila mmoja wao hadi kufika hapo. Kwa kweli ilikuwa ni jioni ya kusisimua sana kwa ndugu wale wawili.



    Aliyeanza ni Zainab aliyemsimulia kila kitu Madame Norah pasipo kuacha kitu, alisimulia tangu makuzi yake baada ya Madame Norah kupata ujauzito na kutorokea kusikojulikana, masomo yake hadi kuajiriwa Kilimanjaro Hotel alikokutana na Hemed Kimaro.



    Hakuacha kitu jinsi mgogoro katika ndoa yao ulivyoanza na hatimaye kuingia katika mtego wa Mr. Oduya na mauaji ya Hemed, kisha alilazimika kwenda uhamishoni Canada, alikoanza maisha mapya akiitwa Suzanne Ross.



    Muda wote Madame Norah alikuwa akimsikiliza kwa makini, kuna wakati alisisimkwa mwili na kuna wakati alihuzunika, hata hivyo kubwa zaidi ilikuwa kumpata mdogo wake akiwa mzima wa afya.



    Madame Norah naye alimsimulia Zainab maisha aliyopitia, tangu alipomtelekeza mtoto wake nyumbani kwa Rafael Jengo kule Ngamiani Tanga na kutorokea jijini Dar es Salaam, maisha aliyoyaishi jijini Dar es Salaam na jinsi jina la Madame Norah lilivyopatikana kabla hajakutana na Karl Johan aliyempeleka nchini Sweden alikokutana na Andreas Gunnar.



    Masimulizi kuhusu maisha ya ndugu wale wawili yalikuwa mfano wa filamu mbili za kusisimua sana, kila mmoja alikuwa akisisimkwa kusikia mapito ya mwingine.



    “Sikutegemea kabisa kukutana na wewe tena, nilijua umeshakufa dada’angu,” Zainab alimwambia Madame Norah huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Hapana mdogo wangu, Mungu ni mwema japo maisha yangu yamekuwa ya huzuni sana, hasa kwa kuwa mama alikufa kabla hajanisamehe na mtoto pia nimemkosa. Bora hata ya kwako,” Madame Norah alijibu huku akishusha pumzi ndefu.



    “Hata hivyo, suala la wewe kuhusishwa na kifo cha mumeo kabla haijaripotiwa kuwa umetoweka ni moja ya mambo yaliyoniumiza kichwa na kunifanya niishi maisha ya huzuni miaka yote hii nikiwa sijui kama uko hai au umekufa, nilihuzunika kuwapoteza wote, wewe na mama,” Madame Norah aliongeza huku akimtazama Zainab kwa huzuni.



    “Kwa kweli mdogo wangu umepitia mambo makubwa sana,” Madame Norah aliongeza akisema kwa sauti tulivu huku akiwa ameyatuliza macho yake kwenye uso wa Zainab.



    “Sikufikii wewe, dada!” Zainab alisema huku akibetua mabega yake juu, na kuongeza, “Hivi una taarifa zozote za dada Zuena?”



    “Zuena yupo Ghana, mambo yake si mabaya. Ameolewa na Dk. Aden Mafuru, Balozi wa Tanzania nchini Ghana,” Madame Norah alisema na kumfanya Zainab ashtuke.



    “Huyo balozi ana uhusiano gani na huyu Mafuru, mwanasheria wa Mr. Oduya?” Zainab aliuliza kwa mshangao.



    “Ni mapacha. Yule balozi ni mkubwa huyu mwanasheria ni mdogo,” Madame Norah alisema huku akijiweka sawa pale kitandani kisha akainua mkono wake kutazama saa yake ya mkononi.



    “Kwa hiyo dada Zuena anaishi Ghana?” Zainab aliuliza tena kwa mshangao uliochanganyika na furaha.







    “Ndiyo maana yake, ila yeye hakupata changamoto nyingi kama sisi. Baadaye nitampigia simu nimtaarifu jambo hili…” Madame Norah alikatishwa na simu yake ya mkononi iliyoanza kuita, aliitazama vizuri na kuguna, kisha alipokea na kuongea kwa kitambo kifupi.



    “Nilisahau, nina kikao muhimu sana na wadau wangu wa mitindo, nitakutafuta kesho tuongee vizuri, mdogo wangu,” Madame alisema huku akiinuka, waliagana na Madame Norah akatoka.



    * * * * *



    Saa tatu na nusu usiku iliwakuta Sammy na Joyce wakiwa chumbani kwao, Sammy alikuwa amevaa bukta na singlet na kuketi kwenye pembe ya kitanda na Joyce alikuwa amevaa nguo ya kulalia na alijilaza chali huku akiegemeza kichwa chake kwenye mto laini.



    Usiku ule Sammy alikuwa amedhamiria kumweleza ukweli Joyce, kama alivyokuwa ameshauriwa na Elli. Alikohoa kusafisha koo lake akijiandaa kusema jambo lakini alionekana kusita sana.



    Joyce alimtupia jicho Sammy kwa makini na kuminya midomo yake. alijua kuwa lipo jambo lililomtatiza Sammy, hata hivyo, aliendelea kubaki kimya akisubiri kuona mwisho wake.



    Sammy alikuwa anaangalia chini akionekana kuwaza kwa kitambo kirefu kisha aliinua uso wake kumtazama Joyce na kushusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani.



    “Mbona sasa hutaki kusema ulichotaka kuniambia!” Joyce alimuuliza Sammy baada ya kumwona muda mrefu akiwa kimya.



    Sammy alishusha tena pumzi za ndani kwa ndani na kujisogeza karibu ya Joyce, alijiegemeza kwenye mto huku akimwangalia Joyce kwa makini zaidi. Alikohoa tena kusafisha koo lake.



    “Amm…” Sammy alitaka kusema neno lakini alisita kidogo, alijikuta akipata wakati mgumu, mawazo yalianza kumjia, akajiuliza vipi kama Joyce angepokea taarifa tofauti na matarajio yake?



    Alianza kupata wakati mgumu sana. Picha ya mtafaruku kati yake na Joyce ilianza kujengeka kichwani kwake, alihisi huenda mambo yangekuwa kama hivi:



    “Unajua… nilikuwa nimekuficha ila ukweli ni kwamba nimefukuzwa kazi,” Sammy alimwambia Joyce kwa sauti tulivu.



    Joyce alishtuka sana na kumkodolea macho Sammy.



    “Sijakuelewa, hebu fafanua,” Joyce alisema huku akijiinua kutoka pale alipokuwa amelala na kuegemea ukuta huku akimtumbulia macho Sammy.



    “Nimefukuzwa kazi takriban mwezi sasa, siku ile niliporudi nimelewa chakari ndiyo siku niliyokuwa nimepewa barua ya kuachishwa kazi, tangu wakati huo nipo tu kijiweni… na hili gari nimelinunua kwa fedha ya…” Sammy alijaribu kujieleza.



    “Stop!” Joyce alimkata kauli huku akiyatuliza macho yake usoni kwa Sammy, “Umefukuzwa kazi takriban mwezi sasa halafu unakuja kuniambia leo! Hivi wewe ni mume wa aina gani!” alisema kwa hasira na kunyanyuka, akasimama mbele ya Sammy huku akiwa kashika kiuno chake. Alimtazama Sammy kwa kitambo huku akiwa kachukia sana.



    Sammy naye alisimama, akataka kusema neno lakini Joyce alimfanyia ishara ya kuwa hakutaka kabisa kumsikiliza.



    “Uliamua kunificha, sasa kilichokutuma leo kunieleza ni nini?” Joyce alimuuliza Sammy huku akiendelea kumkazia macho kwa hasira.



    “Lakini…” Sammy alitaka kujitetea lakini Joyce alimkata tena kauli.



    “Sihitaji kusikia chochote kwa sasa, kama umeweza kuniaminisha siku zote kuwa unakwenda kazini na kumbe kazini ulikuwa huendi, unadhani nitaweza tena kukuamini!” Joyce alibwata kwa hasira. Sasa alikuwa anatokwa na machozi. Sammy alibaki kimya akimkodolea macho.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Au unaye mtu unayemweleza matatizo yako? Ndiyo maana unaniona mimi mpumbavu, siyo?” Joyce aliuliza huku akilia kwa uchungu.



    “Sioni kwa nini unapaniki kiasi hiki, hili ni suala la kukaa na kuongea, mke wangu. Sioni kama…” Sammy aliongea lakini Joyce alimkatisha.



    “How could you do this to me, Sammy, uh? Umekuwa ukiniaminisha kuwa unakwenda kazini kumbe huendi, nitakuamini vipi huko ulikokuwa unashinda?” Joyce aliuliza kwa hasira, alikuwa anapumua kwa nguvu.



    “Kwa vyovyote ningekwambia, wewe ni mke wangu na ndiye mtu muhimu kwangu…”



    “Liar! Mimi nina umuhimu gani kwako?” Joyce aliuliza huku akimkazia macho Sammy.



    “Swali gani hilo unauliza Joyce? You are my wife and you are important to me,” Sammy alijaribu kujitetea.



    “Save your breath, Sammy. I mean nothing to you.”



    “Una hakika na hayo unayoyasema?” Sammy alimuuliza Joyce huku akimkazia macho.



    “Ningekuwa na thamani kwako basi ungenithamini na kunieleza ukweli siku ile ile na usingefanya uamuzi wa kipumbavu kama ulivyofanya. Sikutegema kama…” Joyce alisema kwa hasira lakini sammy alimkatisha.



    “Mama Pendo, naomba iwe mwanzo na mwisho kunitusi, sawa!” Sammy aliongea kwa hasira huku akinyoosha kidole chake kumwelekea Joyce.



    “Huwezi kunizuia kuongea, Sammy, nitaongea chochote na hutanifanya kitu,” Joyce alifoka huku akimtazama Sammy kwa hasira. Hakuwa akimwita tena Baba Pendo bali Sammy.



    Maneno yale ya Joyce yalionekana kumuumiza sana Sammy, alimsogelea Joyce na kumshika kwa nguvu, akamtingisha kwa hasira.



    “Mama Pendo, nakupa onyo la mwisho, naomba tafadhali usithubutu kunijibu namna hiyo…”



    “Usinitishe, kama umenichoka ni bora uniache kwa amani…” Joyce aliongea kwa sauti ya juu na kwa kujiamini.



    Sammy alimshika shingoni kwa hasira, akamminya. “Nilikuoa kwa sababu nakupenda, kwa hiyo usijaribu kutaka kunitingisha, ukiendelea kutoniheshimu nitakuvunja shingo yako,” Sammy alisema kwa hasira na kutoka mle chumbani. Akaubamiza mlango.



    Joyce alionekana kuogopa, ujasiri wote aliokuwa nao ulianza kutoweka, alijikuta akiogopa ghafla kwani hakuwahi kumwona Sammy akiwa amekasirika namna ile.



    “What a stupid husband,” Joyce alisema kwa sauti ndogo huku akijibwaga juu ya kitanda.







    Sammy alikwenda kuketi kwenye sofa sebuleni, mara akawaona Pendo na Winifrida wakimfuata pale kwenye sofa huku wakionesha wasiwasi mkubwa. Sammy alimkumbatia Pendo na wakati huo Winifrida aliketi kimya kwenye sofa huku akimtazama Sammy kwa makini.



    “Joyce hajawahi kunidharau kama alivyofanya leo. Nlijua tu mambo kama haya lazima yatatokea ndiyo maana nilikuwa nasita kumweleza ukweli. Cha msingi hapa ni kukabiliana na chochote kitakachojitokeza,” Sammy aliwaza huku akiwa amefura kwa hasira.



    Aliendelea kuketi pale akiwa amemkumbatia Pendo aliyekuwa akimtazama kwa makini pasipo kusema chochote. Sammy alikuwa bado ameduwaa, hakujua afanye nini.



    Mara walimuona Joyce akitoka chumbani akiwa amevaa gauni na mkononi alikuwa anaburuza begi kubwa la magurudumu. Wote walimtazama kwa mshangao.



    “Nashukuru kwa kunionesha kuwa mimi ni mtu nisiye na maana, narudi kwa wazazi wangu Tanga,” Joyce alisema na kuanza kupiga hatua zake taratibu kuelekea kwenye mlango mkubwa ili aondoke.



    Sammy alionekana kuchanganyikiwa, aliinuka haraka na kujaribu kumshika Joyce katika hali ya kutaka kumzuia lakini Joyce alimsukuma kisha akamzaba kibao kikali cha shavuni. Alikuwa amekasirika sana na macho yake yalikuwa yanawaka kwa hasira.



    “Niache niondoke. Siwezi kukuamini tena!” Joyce alisema kwa hasira.



    “Ungenisikiliza kwanza basi…” Sammy alisema huku akimkodolea macho yaliyokuwa yakibembeleza.



    “Muda huo sina, wapo watu wa muhimu kwako watakaokusikiliza siyo mimi!”



    Pendo alianza kulia kwa uchungu huku akimshika mama yake miguuni kumzuia asiondoke. Winifrida alikuwa amesimama akiwaangalia wote kwa zamu, hakujua afanye nini. Alimshika Pendo aliyekuwa analia kwa uchungu na kumtoa eneo lile akitaka kumpeleka chumbani, japo Pendo alikuwa akirusharusha miguu akitaka aachwe.



    “Mwache!” Joyce alisema kwa hasira na kumshika Pendo mkono huku akiwatazama Sammy na Winifrida kwa uchungu.



    “Naondoka na mwanangu, siwezi kumwacha kwa mwanaume mwongo na laghai kama wewe,” Joyce alisema na kuanza kupiga hatua huku kamshika Pendo aliyekuwa bado analia. Walitoka nje wakimwacha Sammy amepigwa butwaa.



    Sammy alitaka kusema neno lakini sauti haikutoka. Winifrida alisimama akimtazama Sammy kwa huzuni na kushusha pumzi, kisha alitingisha kichwa chake kwa huzuni na kuelekea chumbani kwake…



    “Baba Pendo, mbona umenikodolea macho tu na husemi ulichotaka kunimbia, kwani kuna nini!” sauti ya Joyce ilimgutusha Sammy kutoka kwenye mawazo yake.



    Sammy alimtazama Joyce na kushusha pumzi za ndani kwa ndani, alishukuru Mungu kuwa yalikuwa ni mawazo tu yaliyompeleka mbali sana kiasi cha kumwogopesha hata kumweleza Joyce alichokusudia kusema. Uso wake ulikuwa umefifia na alionekana kusita sana.



    Joyce alimtazama kwa udadisi zaidi, akajiinua kutoka pale kitandani na kujiegemeza kwenye ukuta huku akiendelea kuyatuliza macho yake kwenye uso wa Sammy.



    “Una nini, Baba Pendo, mbona unanitisha!” Joyce alisema huku akimeza mate kutowesha koo lake lililoanza kukauka.



    Sammy alimtazama Joyce kwa makini na kushusha pumzi huku akilazimisha tabasamu, alionekana kusita sana. Picha aliyoiona mawazoni kwake iliendelea kumtisha, alihisi kuwa endapo angemweleza ukweli Joyce basi hali ingekuwa kama ambavyo picha ile ilionekana mawazoni mwake.



    “Amm… amm… hakuna kitu!” Sammy alimudu kusema na kumfanya Joyce ashangae zaidi. Alimkodolea macho Sammy kama vile alikuwa ameona kiumbe cha ajabu kutoka sayari ya mbali.



    “Hakuna kitu! Mbona sikuelewi? Ni nini kinachoendelea ambacho hutaki nikijue?” Joyce aliuliza huku akimtazama Sammy kwa udadisi.



    Sammy alionekana kupata kigugumizi, aliangalia chini kwa kitambo kifupi akiwa hana cha kusema, aliogopa kumpoteza Joyce. Wakati huo Joyce aliendelea kumkazia macho Sammy kwa udadisi.



    “Mimi ni mkeo, kama unanificha jambo unadhani ni nani wa muhimu kwako wa kumweleza? Halafu hadi sasa hujanieleza kuhusu hili gari ulilokuja nalo!” Joyce aliuliza na kumfanya Sammy ahisi kijasho chembamba kikimtoka, hata hivyo aliamua kuuvaa ujasiri. Aliachia tabasamu, akakohoa kusafisha koo lake.



    “Nimeamini kweli unanijali mumeo, nilitaka kukupima nione… ukweli ni kwamba niliamua kukufanyia sapraizi…” Sammy alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Sapraizi ya nini?” Joyce aliuliza huku akiendelea kuyatuliza macho yake kwenye uso wa Sammy akijaribu kuyapima yale maneno.



    “Nimepandishwa cheo kuwa Naibu Meneja Mkuu, na hilo gari nimepewa, ni la kwangu. Ni la kwetu, Mama Pendo!” Sammy alisema huku akiachia tabasamu pana na kumfanya Joyce amtazame kwa kitambo bila kusema neno akiwa haamini alichokisikia.



    Sammy alimtazama Joyce kwa wasiwasi hadi pale alipoliona tabasamu pana likichanua usoni kwake.



    “Ooh… hongera sana mume wangu!” Joyce alisema kwa furaha huku akimkumbatia Sammy kwa nguvu



    “Ni wewe unayestahili pongezi, mafanikio yangu yote yamechangiwa na wewe,” Sammy alisema huku akishusha pumzi za ahueni, hata hivyo, dhamiri yake ilikuwa inamsuta.



    * * * * *



    Saa tatu na nusu za usiku Mr. Oduya alitoka kwenye jengo lake la ghorofa kumi na mbili katika barabara ya Bagamoyo, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, baada ya kuwa na kikao kifupi na Balozi Aldolf Mageuzi.



    Balozi Mageuzi alikuwa amefika ofisini kwa Mr. Oduya kwa mazungumzo mafupi ili kumpa mrejesho wa kile walichokubaliana walipokutana mara ya kwanza. Hakutaka kumweleza kwenye simu kwa kuogopa mawasiliano yao yangeweza kudukuliwa.



    “Enhe, nipe mrejesho mheshimiwa Balozi,” Mr. Oduya alisema kwa shauku baada ya Balozi Mageuzi kuketi.



    “Mambo siyo mabaya, mzee Fabian Magulu ameonesha kukuunga mkono katika harakati zako kutokana na jinsi unavyojitoa kukisaidia chama na jamii, hii ni habari njema na kama ujuavyo, huyu mzee ni mtu mwenye ushawishi mkubwa ndani ya chama na serikalini…” Balozi Mageuzi alisema na kumfanya Mr. Oduya aachie tabasamu pana.





    “Pia amesikitiswa sana na kitendo cha mheshimiwa Tumbo kuanza kampeni mapema huku akitumia siasa za majitaka kuchafua wengine. Kwa kutumia umaarufu na nguvu alizo nazo ndani ya chama amekwishaanza kukigawa chama, tumenasa mawasiliano ya simu akipanga mambo machafu dhidi ya wanasiasa anaodhani ni tishio kwake, jambo hili limemkasirisha sana mzee Magulu na anatarajia kupeleka maoni yake kwa Rais ili Tumbo aitwe Kamati Kuu na kujadiliwa. Hili peke yake linaweza kumpotezea sifa…”



    “Wow! Hahahaaaa… that’s good news! Hahahaaaaa,” Mr. Oduya alisema na kucheka kicheko kikubwa sana kwa furaha baada ya kusikia taarifa ile.



    “Ila kuna jambo sijakueleza bado,” Balozi Mageuzi alisema baada ya kicheko kile kwisha, huku akimtazama Mr. Oduya kwa makini.



    “Jambo gani tena Balozi?” Mr. Oduya aliuliza kwa pupa huku akionekana kushtuka kidogo, lile tabasamu pana usoni kwake liliyeyuka ghafla na badala yake alimkazia macho Balozi Mageuzi.



    “Katika uchunguzi wangu nimegundua kwamba mzee Magulu ana imani kubwa na Dk. Hussein Abbas, na anampa nafasi ya kwanza wakati wewe amekuweka ya pili…” Balozi Mageuzi alisema kwa sauti tulivu.



    Maneno yale yalikuwa kama msumali wa moto uliochoma moyo wa Mr. Oduya, alijikuta akiwa hana la kusema na kubaki kimya akimkodolea macho Balozi Mageuzi.



    “Najua wewe ni mpambanaji… hili ni jambo dogo sana, kama mheshimiwa Tumbo mwenye mtandao mkubwa na tishio ndani ya chama anamalizwa kirahisi, kwa vyovyote vile Dk. Hussein Abbas ni kazi ndogo zaidi,” Balozi Mageuzi alisema huku akiachia tabasamu.



    “Una uhakika, Balozi?” Mr. Oduya aliuliza huku sura yake ikionesha shaka kidogo.



    “Naomba uniamini, ninao watu wa kusaidia kwenye hili, ni suala la muda tu na kila kitu kitakaa sawa.”



    “Oh, thank you, Mr. Ambassador, sijajua hadi sasa nikutunuku zawadi gani…” Mr. Oduya alisema huku matumaini yakirejea.http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    “Usijali, suala la kuvuka daraja tutalijadili tukishaufikia mto,” Balozi Mageuzi alisema huku akiinuka kutaka kuondoka, kisha kama aliyekumbuka jambo alimkabili tena Mr. Oduya.



    “Jambo lingine, tafuta mtu ambaye ni mwanamkakati mzuri wa kiufundi na matukio, mkutanishe na mimi ili nimpe mbinu za kukuandalia mikakati na utekelezaji wa jinsi gani utafanikisha mambo yako,” Balozi Mageuzi alisema huku akimpa mikono wake Mr. Oduya, wakaagana wakiahidiana kupeana taarifa kila kunapotokea jambo jipya.



    Kwa kweli ilikuwa ni habari njema kwa Mr. Oduya iliyomuongezea matumaini fulani. Mr. Oduya aliingia kwenye gari lake la kifahari aina ya Range Rover Velar la rangi nyeupe, Madjid Chege akaliondoa gari na safari ya kuelekea nyumbani kwake ikaanza.



    Kauli ya kwamba atafute mwanamkakati mzuri wa kiufundi na matukio ilimfanya amfikirie Sammy, hakuona mtu mwingine mzuri zaidi ya Sammy.



    Sasa alipanga kwenda ofisini kwa Dk. Masanja kesho yake asubuhi ili kumtaka amshawishi Sammy akubali kujiunga na timu yake, na kama angeendelea kukataa basi angetafuta njia nyingine ya kumlazimisha.



    Kutoka pale ofisini kwake Kijitonyama waliifuata barabara ya Bagamoyo iliyokuwa na msongamano mkubwa wa magari, hivyo safari yao ilikuwa ya taratibu na muda huo ilikuwa inakaribia kabisa saa nne ya usiku.



    Moyoni Mr. Oduya alikuwa ana amani ya kutosha sana kwani Balozi Mageuzi alikuwa ameusuuza sana moyo wake kwa habari mpya alizompa kuhusu uamuzi wa Fabian Magulu kumuunga mkono.



    Hata hivyo, alijua kuwa akifika nyumbani tu ni lazima kungekuwa na kitimtim kwani alikuwa na takriban wiki nzima hajalala nyumbani kwake. Alimfahamu sana mke wake Dk. Oduya. Alikuwa mwanamke mwenye hasira za karibu sana na alikuwa radhi kufanya uamuzi wowote ule. Ilikuwa yataka moyo sana kuishi na mwanamke yule.



    Madjid alipofika katika eneo la Tume ya Sayansi na Teknolojia aliingia kulia akaifuata barabara ya Rose Garden iliyokwenda kutokea eneo la Mikocheni kwa Mwalimu Nyerere. Barabara ile ilifunikwa na vivuli vya matawi makubwa ya miti kando yake.



    Muda wote Mr. Oduya alikuwa amezama kwenye kutazama nje kupitia ukuta msafi wa kioo cha dirisha akiangalia mandhari ya ile barabara. Kupitia pale dirishani aliweza kuona mawingu mepesi yaliyokuwa yakijikusanya angani kana kwamba mvua ya rasharasha ilitaka kunyesha.



    Walipofika mwisho wa barabara ile ya Rose Garden katika eneo la Mwalimu Nyerere, Madjid alikunja kona kuingia kushoto akaifuata barabara ya Mwai Kibaki akiwa katika mwendo wa wastani.



    Waliyavuka majengo mazuri ya makazi ya viongozi wastaafu, maduka, supermarket, vituo vya kujazia mafuta, ofisi za binafsi na migahawa ya kisasa iliyopakana na barabara.



    Baada ya safari fupi hatimaye wakaja kukutana na barabara ya CocaCola kwa upande wa kushoto. Barabara ya CocaCola ilikuwa ni barabara maarufu eneo lile na yenye msongamano mkubwa wa magari yaliyotoka na kwenda eneo la Mwenge yakipitia eneo la kiwanda cha soda za CocaCola.



    Baada ya umbali mfupi walifika kwenye daraja, wakalivuka na mbele kidogo wakayavuka majengo ya Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT Mlalakua) upande wao wa kushoto, hapo dereva akaongeza mwendo na kulipita lori la mafuta lililokuwa mbele yao.



    Baada ya mwendo wa dakika kadhaa mbele yao wakalivuka jengo la kampuni ya teknolojia ya Infortech upande wao wa kulia halafu wakaufikia mzunguko wa barabara ulioziunganisha barabara za Mwai Kibaki na Old Bagamoyo.



    Dereva akauvuka ule mzunguko na kuifuata barabara ya Mwai Kibaki iliyoelekea eneo la Mbezi Beach huku wakipishana na magari mengi ya kifahari katika barabara ile.



    Baada ya safari ndefu katika barabara ile ya Mwai Kibaki wakayafikia makutano ya barabara ile za Mwai Kibaki na Ally Sykes, wakavuka na baadaye wakaikuta barabara ya Bahari kwa upande wao wa kulia. Dereva akaingia upande ule akiufuata ile barabara iliyopita katikati ya majumba ya kifahari yaliyozungukwa na kuta zenye ulinzi hadi alipokutana na barabara nyingine ya Ufukweni iliyoelekea kushoto, akakunja kuelekea kushoto akiifuata ile barabara.







    Baada ya mwendo wa dakika mbili wakaikuta barabara nyingine ya Hassan Oduya, iliyopewa jina kwa heshima ya bilionea Hassan Oduya iliyoingia upande wa kulia ikielekea ufukweni mwa Bahari ya Hindi kwenye majumba ya kifahari.



    Ilikuwa barabara ya kisasa yenye lami na isiyokuwa na msongamano ikikatisha katikati ya yale majumba makubwa ya kisasa yenye ulinzi madhubuti. Kulikuwa na utulivu wa hali ya juu katika barabara ya Hassan Oduya na hata msongamano wa watu na magari haukuwepo.



    Baada ya kitambo kifupi cha safari dereva alipunguza mwendo na hatimaye akasimama nje ya geti kubwa jeusi kwenye kasri la kifahari la Mr. Oduya, kisha akapiga honi mara mbili. Haukupita muda mrefu geti dogo lililokuwa kando ya lile geti kubwa likafunguliwa na askari mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi akachungulia.



    Alipoliona gari la Mr. Oduya hakuuliza chochote, alifungua lile geti kubwa la mbele na Madjid akaingiza gari ndani ya uzio wa lile jumba na geti likafungwa nyuma yao, na hapo akajitokeza askari mwingine aliyeshika bunduki yake mikononi na kusimama kando akilitazama lile gari kwa makini.



    Gari lilianza kupita katika barabara ya vitofali iliyopakana na bustani nzuri ya maua, miti ya kivuli na nyasi laini na kwenda kusimama mbele ya baraza pana ya jumba lile. Na hapo wale askari wa ulinzi wakarejea kwenye kibanda chao cha ulinzi mle ndani kando ya lile geti.



    Madjid aliposimamisha gari, alifungua mlango na kushuka kutoka garini pasipo kuzima injini na kuzunguka upande alikokuwa amekaa Mr. Oduya. Alimfungulia mlango, na muda huo huo kijana wa kazi alitoka haraka ndani ya nyumba baada ya kusikia gari limesimama mbele ya nyumba na kumpokea Mr. Oduya kwa adabu zote.



    Wakati huo ilikuwa kama majira ya saa tano kasoro dakika tano hivi. Hali ya jumba lile ilikuwa ya ukimya sana na ilitisha kweli kweli. Mr. Oduya aliingia na kupanda ngazi haraka haraka hadi ghorofa ya kwanza.



    Alipoingia tu chumbani alimkuta mkewe Dk. Oduya akiwa amefura kwelikweli, alikuwa amesimama mlangoni huku akimsubiri kwa hamu.



    “Haya niambie mwanaume wewe, wiki nzima ulikuwa unalala wapi na nani hadi leo ndiyo unarudi usiku wote huu?” Dk. Oduya aliuliza kwa sauti iliyoonesha wazi kuwa alikuwa amechukia kwelikweli.



    “Sasa ndiyo maswali gani hayo, mke wangu? Inamaana hujui kuwa niko bize na mchakato wa kukutana na watu muhimu wa kunisapoti kuwania nafasi ya urais wa nchi hii?” Mr. Oduya alimjibu kwa swali.



    “Mimi ni mke wako hivyo ninapaswa kujua ulikuwa unashinda na kulala wapi na ulikuwa na nani!”



    “Hivi humu ndani nani ni mwanamume hasa? Mbona unazidi kunipanda kichwani wewe mwanamke?” Mr. Oduya alimjibu mkewe kwa fedhuli.



    “Okay! Kwa kuwa wewe ni mwanamume na mimi mwanamke ndiyo unaniletea dharau siyo?” Dk. Oduya aliongea kwa hasira, na kuongeza, “Kumbuka mimi si mtoto mdogo na wala si mpumbavu kama unavyofikiria, naelewa kila kitu kinachoendelea kwako.”



    “Humu ndani mimi ndiye kichwa cha familia na ndiye ninayevaa suruali, kwa hiyo naomba unipe heshima yang...”



    Mr. Oduya alikatishwa na kibao kikali cha ghafla ambacho hakukitegemea kabisa kilichotua kwenye shavu lake na kumpeleka sakafuni. Alishangaa sana, akajishika shavu lake akiwa haamini macho yake huku akimkodolea macho Dk. Oduya.



    Hakupewa hata nafasi ya kutafakari, Dk. Oduya akaanza kumshushia makofi mfululizo yaliyopigwa pasipo mpangilio mwilini mwa Mr. Oduya huku akilia kwa uchungu. Aliporidhika alifungua mlango na kutoka nje ya kile chumba huku akimwacha Mr. Oduya akiugulia maumivu makali.



    Hakurudi, alikwenda kulala kwenye chumba cha wageni katika ghorofa ya tatu na kujifungia humo hadi asubuhi.



    * * * * *



    Wiki mbili baadaye, majira ya saa tano asubuhi, katika eneo la Ilala Sharif Shamba, bibi mmoja mwenye umri wa miaka sitini na ushee alikuwa anatembea kwa kujikongoja akielekea katika uelekeo wa mgahawa wa kisasa wa Elli’s.



    Yule bibi alikuwa nadhifu na mfupi mwenye ngozi ya rangi ya maji ya kunde na alikuwa amevaa vazi la kitenge lililoshonwa na kudariziwa vizuri na kilemba kikubwa kichwani. Mkononi alikuwa amebeba begi lake dogo na mfuko mdogo wa plastiki uliopigwa marufuku na serikali.



    Alikuwa akiyakaza macho yake kutazama eneo la nje la maegesho ya magari mbele ya mgahawa wa Elli’s, eneo ambalo gari la Sammy aina ya Cadillac DeVille la rangi nyeupe lenye muundo wa kizamani lililokuwa na kibao chenye maandishi ya “Taxi” juu yake lilikuwa limeegeshwa.



    Sammy alikuwa amesajili kampuni ya magari ya kukodisha (car rental), lakini kwa kuwa alikuwa na gari moja aliamua kulitumia kama teksi. Alikuwa amejiegemeza kwenye gari lake na alionekana mtanashati kwelikweli. Alivaa suti nzuri ya rangi ya kijivu, shati la rangi ya samawati na tai ya rangi ya bluu.



    Yule bibi alizidi kusogea karibu huku akimkazia macho Sammy aliyekuwa kashika simu yake ya mkononi akionekana kuperuzi. “Hiyo ni teksi?” yule bibi aliuliza kwa shauku alipokuwa takriban mita ishirini kutoka lilipokuwa lile gari la Sammy.



    “Ndiyo bibi, ni teksi,” Sammy alisema baada ya kugeuka na kumwona yule bibi akimtazama kwa makini.



    “Niwekee kwenye gari,” yule bibi alisema huku akimwashiria Sammy amsaidie mzigo wake kuuweka kwenye gari.



    Sammy alimfuata yule bibi akionekana kuchangamka, akapokea lile begi dogo na ule mfuko wa plastiki, akafungua mlango wa nyuma wa gari lake na kuviweka kwenye siti. Kisha alimshika mkono yule bibi kwa upole na kumsaidia kuingia ndani ya lile gari, akaketi kwenye siti ya nyuma. Yule bibi alimtazama Sammy kwa jicho la shukrani.



    “Asante sana mjukuu wangu,” yule bibi alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Usijali bibi… natakiwa kuwatendea wateja wangu kwa namna ambayo ningependa mama yangu atendewe,” Sammy alisema huku akifungua mlango wa dereva, akaingia na kuketi.







    “Wewe ni kijana mwema… sasa unaweza kunipeleka Karakata,” yule bibi alisema huku akiachia tabasamu.



    “Hakuna tatizo bibi, shilingi elfu tano tu,” Sammy alimwambia yule bibi huku akigeuza shingo yake kumtazama.



    “Sawa, lakini tupitie barabara inayoelekea Mnazi Mmoja,” yule bibi alisema huku akijiegemeza kwenye siti.



    “Huko tutakuwa tunazunguka sana, bibi… ipo barabara rahisi ya kupitia Mnyamani halafu Vingunguti kisha tunakwenda kutokea Karakata…”



    “Sijali kama tutakuwa tunazunguka, sina haraka,” yule bibi alisema huku akiachia tabasamu.



    “Lakini gharama inaweza kuwa kubwa zaidi.”



    “Usijali kuhusu gharama, wewe fuata maelekezo yangu.”



    Sammy alimtazama yule bibi kwa makini kupitia kioo cha katikati cha gari kinachotumika kuangalia nyuma na kushusha pumzi za ndani kwa ndani. Yule bibi alitulia tuli huku akiwa amejiegemeza kwenye siti, alionekana kuchoka sana.



    “Daktari wangu ameniambia kuwa ninahitaji kufurahi zaidi ili niweze kuishi muda mrefu kidogo, vinginevyo sina muda mrefu wa kuishi,” yule bibi alimwambia Sammy huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.



    Sammy hakusema neno, alibaki kimya huku akimtupia jicho yule bibi kupitia kile kioo cha katikati cha gari kinachotumika kuangalia nyuma, alibana taya zake na kuwasha injini ya gari, akaliondoa gari lake taratibu akiingia katika barabara ya lami iliyokuwa ikienda kutokea hospitali ya Amana.



    Walipita kwenye ile barabara iliyokatisha katikati ya majumba mazuri na makazi ya kisasa ya watu wenye ukwasi yaliyozungukwa na kuta zenye usalama wa uhakika. Na baada ya mwendo mfupi wa safari yao waliyafikia makutano ya barabara ile na barabara iliyoelekea Hospitali ya Amana.



    Sammy alikata kona na kuingia upande wa kulia akaenda kuungana na barabara ya Uhuru katika eneo la Amana Vijana, kisha akakunja tena kuingia upande wa kushoto akiifuata barabara ya Uhuru.



    Katika barabara ile ya Uhuru kulikuwa na msongamano mkubwa wa magari, hivyo safari yao ilikuwa ya taratibu. Yule bibi alikuwa hasemi kitu badala yake alikuwa amezama kwenye kutazama mandhari ya ile barabara ya Uhuru.



    Ule mwendo wa wastani ulimruhusu yule bibi kuona vizuri mandhari ya nje. Alikuwa anaona vitu vikiwa vinapita mbele ya macho yake na kurudi nyuma taratibu wakati lile gari likiwa linakwenda, mara wakayapita mabanda yaliyotumika kama vyumba vya wasusi wa Kimasai.



    Akiwa bado anayatazama yale mabanda ya wasusi wa Kimasai kwa makini wakaikuta barabara ya Mafao iliyokuwa ikiingia kushoto, wakaivuka na kulipita jengo refu zaidi maarufu kama Mafao House. Yule bibi alilitazama lile jengo kwa makini na kuminya midomo yake.



    Baada ya safari fupi hatimaye wakalifikia jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, eneo la Ilala Boma. Yule bibi aliliangalia kwa makini lile jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kukohoa ili kusafisha koo lake, kisha akamuonesha Sammy jengo hilo.



    “Enzi za ujana wangu nilifanya kazi hapo kama Katibu Muhtasi,” yule bibi alisema. Sammy alilitupia jicho lile jengo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kubaki kimya.



    Muda huo walikuwa wamefika katika makutano ya barabara ya Kawawa na Uhuru kwenye taa za kuongozea magari barabarani. Bahati nzuri walimkuta askari wa usalama barabarani aliyekuwa akiruhusu magari na kuwaruhusu wapite.



    Gari la Sammy likapita huku watu wakilisindikiza kwa macho yaliyoonesha kulishangaa na baadaye wakazipita daladala zilizokuwa zimesimama katika kituo cha daladala cha Karume. Kisha wakaikuta barabara ya Shaurimoyo upande wao wa kulia na kuipita, na hapo Sammy aliongeza mwendo na kuyapita majengo ya kiwanda cha bia (TBL).



    Lile gari lilizidi kwenda mbele na kuvuka taa za kuongozea magari barabarani katika makutano ya barabara za Msimbazi na Uhuru, eneo la Kariakoo. Sammy aliendelea kuendesha gari kimya kimya akiifuata barabara ile ya Uhuru hadi walipozifikia taa za kuongozea magari barabarani katika makutano ya barabara za Uhuru na Lumumba.



    “Endelea mbele hadi utakapofika Mtaa wa Indira Gandhi, kisha uingie kushoto kuufata mtaa huo,” yule bibi alimwambia Sammy huku akitupa macho yake nje na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.



    Sammy alitii na kuendesha akizivuka taa za kuongozea magari barabarani za makutano ya barabara za Uhuru na Lumumba, akakivuka kituo cha daladala cha Mnazi Mmoja, kisha akazivuka taa nyingine za kuongozea magari barabarani katika makutano ya barabara za Uhuru na Bibi Titi Mohammed.



    Baada ya mwendo mfupi hatimaye wakaufikia Mtaa wa Indira Gandhi, Sammy akakata kuingia kushoto akiufuata ule mtaa hadi mbele kidogo walipoukuta Mtaa wa Aggrey uliokatiza mbele yao.



    “Umeiona hiyo hoteli hapo mbele, ni hoteli ambayo mimi na marehemu mume wangu tulikuja kwa ajili ya fungate mara tu tulipotoka kufunga ndoa,” yule bibi alimwambia Sammy huku akimwonesha kwa kidole. Sammy aliiangalia ile hoteli akiwa hajui aseme nini.



    “Unaweza kusimama hapo kando?” yule bibi alimuuliza Sammy, na bila kuchelewa alisimamisha gari lake kando ya barabara ya mtaa ule. Yule bibi alibaki kimya kabisa akilitazama lile jengo la hoteli kwa kitambo kirefu.



    Sammy alionekana kukerwa kidogo lakini hakuwa na namna ya kufanya. Aliwaza: kama kazi ya kuendesha teksi ilikuwa na usumbufu kiasi kile ni heri angetafuta kazi nyingine ya kufanya. Alikuwa amepatikana! Kutoka Meneja Matukio katika hoteli kubwa yenye hadhi ya nyota tano hadi kazi ya kuendesha teksi! Haiaminiki kabisa!



    Alitaka amweleze ukweli yule bibi kuwa hakupendezwa na kile kilichokuwa kikiendelea na ikibidi amtake atafute gari nyingine lakini alipokumbuka maneno ya yule bibi kuwa, “daktari wake alimtaka kufurahi zaidi ili aweze kuishi muda mrefu kidogo…” alishindwa kusema chochote.





    Alimtupia jicho yule bibi kupitia kile kioo cha katikati cha gari kinachotumika kuangalia nyuma huku akijilaumu kukubali kumchukua, aliamua kuwa mvumilivu na hakutaka kumkera bibi wa watu. Yule bibi aliendelea kuliangalia lile jengo la hoteli kwa kitambo kirefu kisha alionekana kuridhika, akashusha pumzi ndefu.



    “Ahsante sana mjukuu wangu, kwa kunikumbusha enzi za ujana wangu, nimeridhika. Sasa tunaweza kwenda Karakata,” yule bibi alisema huku akijiegemeza kwenye siti yake, akafumba macho.



    Sammy alimtupia jicho yule bibi na kushusha pumzi kisha akaondoa gari lake taratibu akiendesha kimya kimya kuelekea Karakata. Aliufuata Mtaa wa Aggrey hadi alipoikuta barabara ya Bibi Titi Mohammed, akakata kuingia kushoto akiifuata ile barabara.



    Safari yao iliendelea kimya kimya, muda ule yule bibi alikuwa amepitiwa na usingizi. Sammy alikwenda hadi alipoikuta barabara ya Nkrumah, akaifuata barabara ile hadi kwenye makutano ya barabara za Nkrumah, Msimbazi, Nyerere na Gerezani.



    Sammy aliitazama saa yake ya mkononi na kugundua kuwa ilikuwa imekwishatimu saa sita mchana, akashusha pumzi akiifuata barabara ya Nyerere iliyokuwa na magari machache muda ule, akaongeza mwendo.



    Baada ya safari ya takriban dakika arobaini walifika eneo la Jet Club, Sammy akaamua kumwamsha yule bibi na kumuuliza uelekeo wake. Yule bibi alimweleza aingie kulia na kuifuata barabara nyembamba ya vumbi iliyopita katikati ya viwanda na kwenda kutokea reli ya kati kisha akakunja kushoto akiifuata ile barabara nyembamba.



    Walipovuka reli waliikuta barabara nyingine ya vumbi iliyopita mbele ya shule za Majani ya Chai na Ilala, yule bibi akamwelekeza kuwa aelekee upande wa kushoto akiifuata ile barabara na baadaye aingie upande wa kulia kabla hajayavuka majengo ya Veta Kipawa.



    Aliingia akiifuata barabara nyingine nyembamba ya vumbi akayavuka majengo ya Veta kipawa yaliyokuwa upande wake wa kushoto, na baada ya safari ya takriban dakika tano yule bibi alimwonesha Sammy nyumba moja iliyokuwa mbele yao.



    Ilikuwa nyumba ndogo lakini ya kisasa ikiwa imezungushiwa ukuta mfupi na ilikuwa na geti kubwa la rangi ya damu ya mzee mbele yake. Sammy alisimama mbele ya ile nyumba, kisha alifungua mlango na kushuka, akazunguka kumfungulia mlango yule bibi.



    Wakati yule bibi akishuka, Sammy alishusha begi lake dogo na ule mfuko wa plastiki. Muda ule ule alijitokeza binti mmoja aliyekuwa na umri wa miaka isiyozidi ishirini, akapokea lile begi huku akimsalimia Sammy kwa adabu.



    “Ubarikiwe sana kijana wangu, leo umempa bibi yako furaha isiyo na kifani, furaha itakayoniongezea siku za kuishi. Ahsante sana,” yule bibi alisema huku akifungua pochi yake, akatoa noti tatu za shilingi elfu kumi kumi na kumpa Sammy. Kisha akaanza kupiga hatua kuelekea ndani kabla Sammy hajasema chochote.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    * * * * *



    Saa sita mchana kwenye ukumbi mkubwa wa kisasa wa burudani wenye jukwaa la kisasa lililotazamana na viti vingi kwenye ghorofa ya saba ya jengo la kituo cha runinga, Nuru TV, kulikuwa na warembo kadhaa waonesha mitindo ya mavazi waliokuwa wakifanya mazoezi jukwaani.



    Jengo lile la ghorofa saba la kituo cha Nuru TV lilimilikiwa na Madame Norah, lilikuwa katika Barabara ya Bagamoyo eneo la Makumbusho.



    Ndani ya ule ukumbi Joyce alikuwa amesimama akiwatazama wale warembo jinsi walivyokuwa wakipita jukwaani kwa miondoko ya aina yake wakionesha ubunifu wake. Walikuwa katika hatua za mwisho za kufanya, mazoezi yaliyochukua takriban wiki mbili, kabla ya tukio rasmi lililopangwa kufanywa na Joyce.



    Joyce alikuwa amevaa gauni refu la kitenge cha wax la mikono mirefu lililoshonwa kwa ubunifu wa hali ya juu, mtindo wa pencil dress, likiwa limedariziwa kwa nyuzi za dhahabu na kuushika mwili wake huku likilichora vyema umbo lake maridhawa.



    Mkononi Joyce alikuwa ameshika picha za warembo wakiwa katika mitindo tofauti na michoro mingine mbalimbali ya mitindo ya mavazi. Joyce alikuwa makini zaidi akifuatilia mazoezi ya wale warembo pale jukwaani



    Kando yake alisimama msaidizi wake, Nyaso Gilbert Nyaso aliyevalia blauzi nyepesi ya pinki na suruali ya jeans ya rangi ya bluu mpauko yenye matobo maeneo ya mapajani na iliyombana na kulichora vyema umbo lake refu maridhawa lenye tumbo dogo.



    Mkononi alikuwa amevaa bangili nyingi za pembe, miwani myeusi ya jua usoni, viatu vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio miguuni na wigi la nywele ndefu kichwani lililomfanya aonekane mrembo hasa. Pia kulikuwa na mpiga picha mmoja aliyekuwa akipiga picha za video za mazoezi hayo kwa maelekezo ya Nyaso.



    Madame Norah akiwa ameongozana na msaidizi wake, Jessica waliingia mle ukumbini na kusimama wakiwaangalia kwa makini wale warembo walivyokuwa wakifanya mazoezi. Joyce alimuona Madame Norah na kuachia tabasamu pana kisha akamfuata pale alipokuwa amesimama, walisalimiana kwa bashasha zote.



    Madame Norah alifika hapo kutaka kujua maendeleo ya Joyce na ule mradi wake mkubwa na wa kwanza kufanywa na Joyce tangu aingie kwenye tasnia ya mitindo.



    Madame Norah hakuwa akijua kilichokuwa kinaendelea kwenye ule mradi, hasa tangu alipomkabidhi Nyaso kuwa msaidizi wa Joyce na yeye akasafiri kwenda nchini Ghana kumuona mdogo wake Zuena, mke wa Balozi wa Tanzania nchini Ghana, Balozi Mafuru.



    Ilikuwa ni safari ya ghafla iliyoibuka baada ya kukutana na Zainab, waliyepotezana miaka mingi na wasijue alikokuwa amekimbilia baada ya kutuhumiwa kwenye mauaji ya mumewe Hemed Kimaro, miaka kumi na mbili iliyokuwa imepita.



    Ni baada ya safari ile ya Ghana walikokutana ndugu watatu, wakaongea na kupeana ahadi ya kuendelea kuwasiliana na kushirikiana kwa kila kitu, ndipo Madame Norah alipoanza kuhisi ile furaha iliyokuwa imetoweka miaka mingi maishani kwake ikianza kurejea.



    Alikuwa mtu mwenye furaha kiasi na Joyce aliweza kubaini mara moja ingawa hakumuuliza. Madame Norah na Joyce waliongea kwa kitambo kirefu wakipeana mikakati ya namna ya kufanikisha mradi ule mkubwa wa Joyce.



    Jambo ambalo Madame Norah hakulijua na aliendelea kujiuliza bila majibu ni kwamba: kwa nini aliamua kumsaidia Joyce aliyemhesabu kama mmoja wa washindani wake kwenye tasnia ya mitindo? Tena hakumsaidia tu kwa kumtafutia msaidizi, ukumbi au kulipia gharama za maandalizi, bali alifikia hadi kumpa mikakati na mbinu mbalimbali za kufanikisha mradi ambao ungekuja kuwa tishio kwake!







    Huyu Joyce alikuwa na nini hasa kilichomfanya Madame Norah afanye yale asiyokusudia kuyafanya? Hata hivyo, kitu kimoja alichokuwa na uhakika nacho ni kwamba alijisikia furaha sana moyoni kila alipoamua kumsaidia Joyce, basi!



    Baada ya kitambo kirefu cha majadiliano kati yao, Madame Norah aliaga na kuondoka akiwaacha Joyce na Nyaso wanakamilisha maandalizi ya mradi ule.



    * * * * *



    Baada ya kutoka eneo la Karakata, Sammy alimchukua mtu mmoja aliyemkuta Jet Club na kumpeleka katika ofisi za Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) zilizopo barabara ya Mandela, katika eneo la Tazara.



    Alimwacha yule abiria pale TSN kisha akageuza gari lake na kutaka kuingia katika barabara ya Mandela akitaka kwenda Ilala Sharif Shamba, mara akamuona mwanamume mmoja raia wa kigeni aliyekuwa anatokea ndani ya majengo ya kituo cha Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) aliyemjia mbio huku akimpungia mkono.



    Alikuwa mwanamume wa makamo, mrefu na kipande cha mtu aliyejazia vyema. Mwili wake ulichorwa michoro mbalimbali na alikuwa amevaa fulana nyeusi ya mikono mifupi, kaptura ya rangi ya khaki yenye mifuko mikubwa pembeni na miguuni alivaa raba. Mgongoni alikuwa amebeba begi kubwa la safari.



    Sammy aliamua kumsubiri. Hata hivyo, alikuwa amesimama katikati ya barabara ya mchepuko iliyotokea katika jengo la TSN na hivyo kuzuia magari mengine. Gari moja aina ya Toyota RAV4 jeusi lililokuwa nyuma yake likitaka kuingia katika barabara ya Mandela lilianza kupiga honi, dereva wa gari lile alionekana kutokuwa na uvumilivu.



    Sammy aliendelea kusubiri pasipo kumjali yule dereva wa RAV4 aliyeendelea kupiga honi kwa fujo. Hakutaka kumkosa yule abiria Mzungu aliyekuwa akivuka barabara ya Mandela akionekana kuwa na safari muhimu.



    Baada ya dakika takriban mbili yule mwanamume alifanikiwa kuvuka ile barabara na kufungua mlango wa nyuma wa gari la Sammy kisha aliliweka begi lake na kuingia, akakaa katika siti ya nyuma.



    “Airport please… and thanks for waiting,” (Kiwanja cha Ndege tafadhali… na ahsante kwa kusubiri) alisema yule mwanamume wa kizungu huku akijiegemeza kwenye siti.



    Sammy aliliondoa gari lake na kungia katika barabara ya Mandela bila kumjibu chochote yule mwanamume wa kizungu kisha akakata kushoto akiifuata barabara ya Nyerere iliyoelekea Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere.



    Muda ule wa mchana barabara ya Nyerere haikuwa na msongamano mkubwa wa magari, hivyo Sammy alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi. Walikuwa kimya kabisa.



    Kufumba na kufumbua gari lilikuwa likiivuka yadi ya kuhifadhi makontena ya African Inland Container Depot (AFICD) katika eneo maarufu la Mchicha na sasa walikuwa wakilisogelea eneo la Karakana ya Tazara, hapo yule mzungu akakohoa kidogo kusafisha koo lake kisha akaanzisha mazungumzo.



    “Do you know English?” (Unajua Kiingereza?) yule mzungu alimuuliza Sammy huku akiachia tabasamu pana la kirafiki.



    “Yes,” Sammy alijibu kwa ufupi bila kumtazama yule mwanamume.



    “How did you get this car? I real like it, it’s a unique type of taxi that everyone should want to use it,” (Umeipataje hii gari? Nimeipenda sana, ni aina ya teksi yenye upekee ambayo kila mtu angependa kupanda) yule mzungu alimuuliza Sammy huku akimtazama kwa makini.



    Sammy aliachia tabasamu huku akimtupia jicho yule abiria wake kupitia kioo cha katikati cha gari kinachotumika kuangalia nyuma.



    “You know…” (Unajua…) Sammy alianza kujieleza lakini akasita baada ya kumuona Winifrida akiwa hajavaa sare za shule na badala yake alivaa suruali ya kubana ya jeans rangi ya samawati yenye matobo mapajani na kitopu cheupe na mgongoni alikuwa amebeba begi lake la madaftari.



    Winifrida alikuwa ameongozana na kijana mmoja wa kiume aliyekadiriwa kuwa na miaka ishirini na ishirini na mbili, akiwa amevaa suruali nyeupe ya jeans na fulana nyeusi, kichwani alivaa kofia nyeusi ya kapelo. Alikuwa mrefu maji ya kunde na mtanashati sana.



    Walikuwa wanatembea taratibu huku wameshikana mikono wakiifuata barabara ya vumbi iliyokatisha katikati ya majengo ya kampuni za Spedag Interfreight na Bureau Veritas Tanzania kuelekea eneo la Kiwalani.



    “Shit!” Sammy aling’aka kwa hasira huku akipiga ngumi juu ya usukani na kukanyaga breki ya ghafla, gari lake likaserereka huku likiyumba barabarani na kusimama kando ya barabara ya Nyerere, usawa wa jengo la kampuni ya Bureau Veritas Tanzania.



    Alishuka haraka akimwacha abiria wake na kukimbilia kule walikokuwa Winifrida na yule kijana huku akiwa amekasirika sana. Yule kijana alishtuka na kutazama nyuma, alipomuona akija mbio alikimbia akimwacha Winifrida ambaye hakuwa na ujanja. Sammy alimfikia Winifrida na kumkamata mkono kwa nguvu huku akifoka.



    Winifrida aliishiwa nguvu, Sammy alimkokota kumpeleka kwenye gari lake lililokuwa limesimama kando ya ile barabara ya Nyerere. Muda wote yule abiria mzungu aliyekuwa ndani ya lile gari la Sammy alikuwa amepigwa na butwaa.



    Kama mtu aliyeshtuka aliiangalia saa yake ya mkononi na kusonya huku akionekana kukata tamaa. Kwa vidole vyake viwili vya shahada na dole gumba vya mkono wa kulia aliminya pua yake kama anayevuta kamasi huku akiwatazama kwa makini Sammy na Winifrida wakivutana. Akaangalia tena saa yake ya mkononi.



    “What’s wrong with you?” (Una shida gani?) yule mzungu alimuuliza Sammy kwa mshangao huku akishuka kutoka ndani ya lile gari la Sammy, mara akaiona teksi ikija upande ule, akaipungia mkono, “Taxi! Taxi!”



    Ile teksi ilipunguza mwendo na kusimama mbele ya gari la Sammy, yule mzungu alifungua mlango wa nyuma wa gari la Sammy na kuchukua begi lake, akamtazama Sammy kwa mara ya mwisho huku akitoa kadi yake.



    “You’ve been a prank but I want to give you a second chance, not for you but for the car. I may need it for one of my representative’s meetings,” (Umenifanyia mzaha lakini nataka nikupe nafasi nyingine, siyo yako bali kwa sababu ya gari lako. Huenda nikalihitaji kwenye moja ya mikutano yangu) yule mzungu alisema huku akimpa Sammy ile kadi yake.







    Sammy aliipokea ile kadi huku akiitazama kwa makini na kubetua kichwa chake. Yule mzungu aliingia kwenye ile teksi aliyoisimamisha, kisha ikaondoka kwa mwendo wa kasi na kuyafanya magurudumu yake yachimbe ardhi.



    Winifrida aliingalia kwa makini ile teksi iliyombeba yule mzungu wakati ikiondoka kisha akageuza shingo yake kulitazama gari la Sammy kwa udadisi, akakiona kibao kidogo chenye maandishi ya ‘Taxi’ juu ya gari. Akashangaa sana.



    “Kumbe wewe ni dereva wa teksi! Mi’ nilidhani meneja!” Winifrida alisema kwa mshangao huku akimkazia macho Sammy.



    “Achana na habari za teksi, niambie kwa nini hujaenda shule na badala yake unazurura na wanaume?” Sammy alimuuliza Winifrida huku akionekana kukasirika sana.



    “Nakubali nimekosa, na wewe kwa nini unaendesha teksi badala ya kuwa ofisini?” Winifrida naye alimuuliza Sammy huku akimtazama kwa makini.



    Sammy alitaka kusema neno lakini akasita, aligeuza shingo yake kulitazama gari lake, akakiona kile kibao chenye maandishi ya ‘Taxi’ na kushusha pumzi za ndani kwa ndani huku akijiegemeza kwenye gari. Sasa siri yake ilikuwa imefichuka! Winifrida alilitambua hilo na kuachia kicheko hafifu.



    “Naamini hutapenda wifi ajue kuhusu jambo hili!” Winifrida alisema huku akiendelea kumwangalia Sammy kwa makini.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Tafadhali usitake kuingiza mambo yasiyohusiana, suala hapa ni kwa nini huendi shule na badala yake unakuja huku ukiwa umevaa nguo za ajabu ajabu?” Sammy alimuuliza Winifrida huku akijaribu kumtisha.



    “Sawa nimekosa, lakini na wewe kwa nini umdanganye wifi kuwa umepandishwa cheo kumbe siku hizi unaendesha teksi? Unataka nimwambie ukweli?” Winifrida aliongea kwa msisitizo bila kuteteleka.



    “Naomba usithubutu kumweleza chochote wifi yako, haya mambo hayakuhusu! Ninachotaka uniahidi kuwa utaacha huu ujinga na kwenda shule,” Sammy alisema kwa sauti ya kusihi.



    “Ukinisamehe sitasema chochote kwa wifi,” Winifrida alisema huku akifungua mlango wa nyuma wa gari la Sammy na kuingia.



    Sammy alimtazama kwa makini na kushusha pumzi za ndani kwa ndani kisha akaingia ndani ya gari, akaliondoa na kuelekea eneo la Vingunguti, alipofika usawa wa jengo la kampuni ya East African Cables (Tz) Ltd aliliingiza gari kwenye barabara mchepuko na kugeuza kurudi alikotoka.



    Gari liliongeza mwendo likiyapita majengo ya East African Cables (Tz) Ltd, Hoteli ya Blue Supphire, Azania, Spedag Interfreight, Bureau Veritas Tanzania, Karakana ya Tazara na African Inland Container Depot, katika eneo maarufu la Mchicha, wakachepuka na kuingia barabara ya Nyerere, kisha safari ikaendelea.



    * * * * *



    Saa nane mchana, gari dogo la kifahari aina ya Range Rover Sport L494 la rangi ya bluu lilikuwa linaegeshwa kwenye viunga vya maegesho vya jengo la ghorofa saba la Nuru TV, eneo la Makumbusho jijini Dar es Salaam.



    Ndani ya lile gari kulikuwa na watu watatu. Dereva wa gari na mwanamume mmoja mrefu mwenye umbo kubwa kakamavu kutokana na mazoezi makali. Kwenye siti ya nyuma aliketi kijana mtanashati aliyeonekana kujiamini sana. Hakuwa mwingine bali mwanamuziki maarufu wa Bongo Fleva, Dynamo Plus, aliyekadiriwa kuwa na umri wa miaka thetathini.



    Alikuwa mrefu kiasi mwenye mwili mdogo lakini uliojengeka kwa mazoezi, akiwa amevaa suruali nyeupe ya jeans iliyokuwa imechanwa chanwa sehemu ya mapajani hadi uswa wa magoti na fulani nyeusi yenye picha yake kifuani.



    Kichwani alikuwa amezisuka nywele zake katika mtindo wa rasta na alivaa kofia nyeupe ya kapelo na miwani mikubwa ya jua usoni.



    Kwa kiasi fulani Dynamo Plus alikuwa amejitosheleza, kwani mbali na muziki alikuwa anamiliki miradi kadhaa ikiwemo studio ya kurekodi muziki, na alikuwa mbioni kuanzisha vituo vya redio na televisheni, kwa msaada wa Madame Norah.



    Kwa kifupi Madame Norah alimshawishi Dynamo Plus na wakakubaliana kuingia ubia ili waanzishe vituo hivyo vya runinga na redio kwa kuwa Dynamo Plus alijionesha kuwa kijana mbunifu na mwenye kujituma sana, kiasi cha kuwa mfano kwa wasanii wengi.



    Dynamo Plus alishuka kutoka kwenye gari lake na kuongozana na mlinzi wake huku wakimwacha dereva ndani ya gari. Aalipiga hatua akitembea kwa mwendo wa kunesa kuelekea ndani ya jengo akifuatisha midundo ya muziki aliousikiliza kupitia spika (headphone) alizovaa masikioni.



    Alielekea kwenye lango la kuingia la jengo lile la Nuru TV huku ile suruali yake ikiwa imevaliwa chini kidogo ya kiuno chake. Alipokuwa akikaribia lile lango la kuingilia alimwona mwanadada mmoja mrembo aliyevaa gauni refu la kitenge cha wax lenye mikono mirefu la mtindo wa pencil dress, akitokea ndani ya lile jengo akionekana kuwa na haraka kidogo.



    Dynamo Plus alimtupia jicho mara moja tu na kuendelea na safari yake kuelekea ndani lakini alisita baada ya kusikia sauti laini ikimsemesha.



    “Kaka Nasri, hata salamu?” yule mwanadada alimwambia Dynamo Plus na kumfanya ageuza shingo yake kumtazama kwa makini na hapo akakutana na macho legevu ya Joyce yaliyong’ara.



    Dynamo Plus alimwangalia Joyce kwa wasiwasi kidogo huku akijiuliza ni wapi alikutana na mwanadada yule, kwani hata jina alilomwita ni jina lake halisi lililojulikana na watu wachache wa karibu. Jina lake halisi aliitwa Nasri Abood.



    Dynamo Plus alikunja mkono wake wa kulia na kuupeleka kifuani kwake huku akiinama kidogo mbele katika hali ya kuomba radhi kwa kutosalimia.



    “Wakati mwingine unaweza kupoteza video vixen hivi hivi... huyu mdada anafaa sana kupamba video yangu mpya,” Dynamo Plus aliwaza na kuachia tabasamu.



    Walitazamana, Joyce naye aliachia tabasamu kabambe huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.



    “Habari yako dada yangu?” Dynamo Plus alisalimia huku akinyoosha mkono wake kumpa Joyce.



    “Salama, sasa mambo si hayo? Kwani ulivyonisalimia umekufa?” Joyce alisema na kumfanya Dynamo Plus acheke kidogo.



    “Nimefurahi sana leo nimekutana na wewe, mimi ni shabiki wako. You are my favorite musician,” Joyce alisema huku tabasamu pana likishindwa kwenda likizo usoni kwake.



    Dynamo Plus alijisikia fahari sana kusifiwa na Joyce, aliendelea kuung’ang’ania mkono wa Joyce huku akimtazama kwa makini usoni.



    “Nafurahi kusikia kwamba hata watu kama ninyi mnazikubali kazi zangu,” Dynamo Plus alisema huku akishusha pumzi.









    “Kwani mimi nina tofauti gani na watu wengine?” Joyce aliuliza huku akimkazia macho Dynamo Plus.



    “Wewe ni mtu mkubwa, watu kama ninyi muda mwingi mko bize, sina hakika hata kama mnapata muda wa kusikiliza nyimbo zetu,” Dynamo Plus alisema huku akipitisha ulimi kuilamba midomo yake mikubwa.



    “Nina ukubwa gani mimi!” Joyce alisema na kuangua kicheko hafifu, akaendelea, “Tuyaache hayo, Aisha yuko wapi siku hizi? Nimemmisi sana,” Joyce aliuliza huku macho yake yakiwa yameweka kituo usoni kwa Dynamo Plus.



    “Aisha dada’angu! Kwani mnafahamiana?” Dynamo Plus aliuliza kwa mshangao baada ya kufikiria kidogo.



    “Ni best wangu sana, nilisoma naye kidato kimoja Sekondari ya Wasichana ya Tabora.”



    “Anaishi Sweden siku hizi. Nimefurahi sana kukufahamu dada…” Dynamo Plus alisema na kuonekana kusita kidogo na kuachia kicheko hafifu huku akishika kichwa chake kuonesha kuwa amelisahau jina la Joyce.



    “Joyce… Mrs. Joyce Kambona,” Joyce alisema huku akiachia tabasamu.



    “Oh yes, dada Joyce… you are a fashion designer, right?” Dynamo Plus alisema huku akimtazama Joyce kwa makini. Joyce aliachia tabasamu pana zaidi la bashasha.



    “Yeah! How do you know?” Joyce aliuliza huku akihisi furaha moyoni kwa kuwa Dynamo Plus alionesha kumfahamu.



    “Nadhani tumewahi kukutana, pia nimekuwa nikisikia habari zako. Hasa Madame Norah amekuwa anakuongelea sana. She real admires you!” Dynamo Plus alisema na kumfanya Joyce azidi kujisikia fahari baada ya kugundua kuwa kumbe watu walikuwa wanaongelea habari zake.



    * * * * *



    Saa kumi alasiri, kwenye viunga vya maegesho ya magari vya mgahawa wa kisasa wa Elli’s, mtangazaji na mtayarishaji wa kipindi maarufu cha ‘Mbunifu Wetu’ katika kituo cha runinga cha Mzizima, Maximilian Njamba alikuwa amesimama kwa mbali akionesha kidole chake lilipokuwa limeegeshwa gari aina ya Cadillac DeVille lenye muundo wa kizamani likiwa na kibao cha “Taxi” juu yake.



    Maximilian Njamba alikuwa mwanamume wa makamo mwenye umri wa kati ya miaka arobaini na tano na hamsini, si mrefu wala mfupi kwa kimo, pia hakuwa mwembamba wala mnene na alikuwa na sura ya ucheshi muda wote.



    Alasiri ile Maximilian alikuwa amevaa kofia nyeusi ya pama, shati la mikono mirefu la pundamilia, suruali pana ya kijivu na viatu vyeusi ya ngozi miguuni.



    Alikuwa amefika katika mgahawa wa kisasa wa Elli’s baada ya kuambiwa na rafiki yake kuhusu uwepo wa gari aina ya Cadillac DeVille lililosajiliwa kuwa teksi, alipoliona alijikuta akiupenda sana ubunifu uliotumika kulifanya lile gari kuwa la kibiashara.



    Muda ule alikuwa ameshika kipaza sauti chenye nembo ya Mzizima TV akiwa mbele ya mpiga picha wake. Alikuwa akielezea jinsi alivyovutiwa sana na ubunifu uliotumika kwenye lile gari aina ya Cadillac DeVille.



    Hii ilikuwa baada ya kumtafuta mmiliki wa gari lile, Sammy Kambona na kutaka kufanya naye mahojiano lakini Sammy alikataa katakata na kumuonya Maximilian asijaribu kulipiga picha gari lake bila idhini yake.



    Kwa kuwa Maximilian aliiona ile teksi kama njia nzuri ya kuhamasisha ubunifu aliamua kuitumia ile fursa adimu ili kuwavutia watazamaji wa kipindi chake waweze kuhamasika kufikiria ‘nje ya boksi’ kwa kufanya vitu ambavyo watu wengine wangedhani haviwezekani.



    Lakini tatizo lilikuwa ni Sammy, alikuwa amekataa kuhojiwa wala kupigwa picha, hivyo Maximilian aliamua kuvizia, pindi Sammy alipoingia ndani ya ule mgahawa wa Elli’s, akasimama kwa mbali lakini akihakikisha lile gari linaonekana kwenye kamera na kumtaka mpiga picha wake kulivuta gari karibu ili liweze kuonekana vyema.



    Baada ya mpiga picha kuweka sawa mitambo yake na kumpa ishara kuwa alikuwa tayari, Maximilian alianza kazi iliyompeleka pale huku akiwa makini.



    “Huu ni ubunifu wa hali ya juu sana, ila tunasikitika mmiliki wake amekataa kufanya mahojiano nasi, tungefahamu alifikiria nini kulifanya gari hili aina ya Cadillac DeVille lililotengenezwa zaidi ya miaka hamsini iliyopita kuwa teksi! Kwa kweli hii ni teksi inayovutia hasa, na kila mtu angependa kuwa abiria wake…” alisema yule mtangazaji wa kipindi maarufu cha ‘Mbunifu Wetu’ kilichorushwa na Mzizima TV.



    “Na cha ajabu zaidi, licha ya kuwa ni gari la kizamani lakini ni kama mpya, haina matatizo yoyote na inaweza kukufikisha kokote uendako pasipo hofu ya kuharibika njiani… sasa ngoja nisikie maoni ya wakazi wa jijini Dar es Salaam kuhusu gari hili,” alisema Maximilian na kuelekea mtaani akijaribu kupata maoni ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam.



    Aliwauliza hasa wakazi walioishi jirani na eleo la mgahawa wa Elli’s kama wameshawahi kuliona gari aina ya Cadillac DeVille la muundo wa kizamani lililokuwa likitumika kama teksi na nini maoni yao kuhusu gari lile.



    Wapo wakazi waliosema kuwa hawajawahi kuliona na wale walioliona walionekana kusifia sana akili ya kibunifu iliotumika kulifanya lile gari aina ya Cadillac DeVille la muundo wa kipekee kuwa teksi, wakidai kuwa lilikuwa ile hali ya upekee ingeweza kuwavutia watu wengi kutaka kuwa abiria wake na hivyo kulifanya gari liwe bidhaa adimu.



    Wapo waliodai kuwa japo walikuwa wameliona ndani ya siku chache tu lakini tayari lilikwisha fahamika sana utadhani lilikuwa lina zaidi ya mwaka mmoja, wote walikiri kuwa wangependa kuwa abiria siku moja kutokana na upekee wake.



    * * * * *



    Saa moja jioni Sammy alikuwa anatoka ndani ya mgahawa wa kisasa wa Elli’s uliopo Ilala Sharif Shamba na kutembea haraka akikatiza kwenye viunga vya maegesho ya magari vya mgahawa ule, akalifikia gari lake aina ya Cadillac DeVille na kufungua buti la gari.







    Alitoa supana, akaanza kukifungua kibao chenye maandishi ya “Taxi” kilichokuwa kimepachikwa juu ya gari na kukitoa, kisha akakificha ndani ya buti la gari. Alipomaliza akafunga buti na kuingia kwenye gari.



    Jioni ile aliokuwa na mawazo na alichoka sana, nadhani ilitokana na pilika pilika za kutwa nzima za kupeleka abiria huku na kule ambazo hakuwa amezizoea. Alifunga mkanda wa siti yake na kuliondoa gari taratibu kutoka kwenye maegesho ya magari ya ule mgahawa wa Elli’s na kuingia barabarani.



    Muda huo gari lilionekana likiwa halina kibao cha kulitambulisha kuwa ni teksi, aliamua kufanya vile kila siku alipotaka kurudi nyumbani hadi siku ambayo angemweleza ukweli mkewe.



    Saa moja jioni jiji la Dar es Salaam lilikuwa limemezwa na pilika pilika za aina yake za watu zilizoshamiri katikati na kwenye viunga vya jiji hilo kubwa zaidi Tanzania na hali ya hewa ilikuwa ya joto sana kama kawaida ya jiji hilo.



    Uso wa Sammy ulikuwa umesawajika, alikuwa na mawazo mengi kwani hakutegemea kama Winifrida angeweza kugundua siri yake mapema vile kuwa lile gari lilitumika kama teksi. Aliendesha gari lake kwa utulivu hadi alipofika nyumbani kwake eneo la Tabata Chang’ombe.



    Akionekana kuchoka sana, alifika mbele ya nyumba yake kwenye geti kubwa la mbele akapiga honi mara moja tu na kuinamisha kichwa chake kwenye usukani akisubiri kufunguliwa geti, mara usingizi mwepesi ukamchukua.



    Alikuja kushtuliwa na Winifrida aliyekuwa anagonga kwenye kioo cha dirisha lake, Sammy aliinua kichwa chake kumtazama Winifrida, akaachia tabasamu na kuliingiza gari lake ndani kisha akalizima na kushuka akibeba mkoba wake wa kiofisi.



    Alitembea taratibu kuelekea ndani na mlangoni akapishana na Joyce aliyekuwa akielekea dukani. Walisalimiana na Sammy akaingia ndani na kuelekea moja kwa moja chumbani kwake alikokwenda kuuweka mkoba wake wa kiofisi na kuanza kuvua nguo zake.



    Alianza kwa kuvua koti lake na kulitupa kitandani, akalegeza tai yake na kuivua ikifuatiwa na shati, vyote akavitupia kitandani kisha akavua viatu na kuviweka kwenye stendi maalumu ya viatu, halafu akavua soksi na kuzitupia kitandani na mwisho akavua suruali na kutoa mkanda kisha akaitupia kitandani. Alipomaliza alivaa bukta na fulana nyepesi.



    Akachukua shati lake alilovua na kuanza kusachi kwenye mifuko ya shati, akatoa vijiti vitatu na nusu vya kuchokonolea meno na kuvitupa ndani ya kapu dogo la taka lililokuwa limewekwa kwenye kona moja mle chumbani.



    Kisha alichukua koti lake na kupekua kwenye mifuko akianza na mifuko ya nje kabla hajahamia mifuko ya ndani, akatoa kadi fulani mbili tatu, mojawapo ikiwa ile kadi aliyopewa na abiria wake mzungu na karatasi fulani, akaviweka kando na kuchukua suruali yake.



    Alianza kukagua mifuko ya mbele kwanza kwa kutoa nje vitambaa vyake, akatoa simu yake ya mkononi na kuiweka kitandani, kisha alitomasa mfuko wa nyuma lakini hakuhisi kitu. Aliamua kuingiza mkono uliotoka patupu! Hakukuwa na kitu.



    Akaiachia suruali ile ikaanguka chini kisha akashika kiuno akionekana kufikiria kidogo. Alionekana kung'aa macho akionekana kujiuliza maswali kisha akatazama kitandani. Alionekana kushtuka na kutoka chumbani haraka, akamkuta Winifrida akiwa ameketi sebuleni.



    “Hebu niangalizie pochi yangu, nadhani nimeiacha ndani ya gari,” Sammy alimwambia Winifrida na kujibwaga juu ya sofa, mara akagutuka na kuinuka haraka, akaingia chumbani kwake kwa kujikongoja.



    Aliuchukua mkoba wake wa kiofisi na kuufungua, akaangalia ndani na kuiona pochi yake. Akaifungua na kuziona fedha, alizihesabu kwa macho. Zilizokuwa kama noti kumi na mbili za shilingi elfu kumi kumi na noti nyingine kadhaa za elfu tano tano na elfu mbili mbili. Sammy aliachia tabasamu na kuiweka vizuri pochi yake ndani ya droo iliyokuwa kando ya kitanda.



    Kisha alizichukua nguo zake pamoja na soksi na kuzitumbukiza kwenye tenga la nguo chafu lililokuwa limewekwa sehemu fulani ndani ya kile chumba. Kama aliyekumbuka kitu, aligeuza shingo yake na kujiangalia kwenye kioo kirefu cha meza ya vipodozi. Kisha alitoka kuelekea sebuleni na hapo akawaona Winifrida na Joyce wakiingia huku wameongozana.



    “Sijaiona,” Winifrida alimwambia Sammy.



    “Usijali nimekwisha iona, ilikuwa kwenye mkoba wangu!” Sammy alisema na kujibwaga tyena kwenye sofa, akavuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu huku akifumba macho yake. Alionekana kuzama kwenye mawazo.



    Winifrida aliketi kwenye sofa huku akimtazama Sammy kwa kuvizia vizia. Joyce alielekea moja kwa moja jikoni na baada ya muda mfupi aliandaa meza kwa ajili ya chakula cha jioni na kusogea mbele ya Sammy, akasimama kwa heshima.



    “Karibu chakula, Baba Pendo,” Joyce alisema huku akimwangalia Sammy kwa makini usoni.



    Sammy alishtuka na kufumbua macho yake, akamtazama Joyce kwa kitambo kidogo bila kusema neno, kisha aliachia tabasamu kwa mbali na kujizoazoa taratibu kutoka pale kwenye sofa na kuelekea kwenye meza ya chakula.



    “Naona leo hauko sawa, kuna tatizo?” Joyce alimuuliza Sammy huku akiwa bado anamwangalia kwa udadisi.



    “Nimechoka tu,” Sammy alisema huku akiketi kwenye kiti chake.



    Meza ya chakula ilikuwa imejaa mapochopocho: kulikuwa na wali mweupe, mchuzi mzito wa kuku, bakuli lenye nyama za kuku, bakuli la maharage yaliyoungwa kwa nazi, bakuli la mboga za majani, bakuli la saladi, matunda mchanganyiko kwenye sinia pamoja na jagi la maji ya kunywa na bilauri nne.



    Ilikuwa imekwishatimu saa mbili na nusu usiku wakati Sammy na familia yake wakikaa mezani kwa ajili ya chakula cha jioni. Joyce alimnawisha Sammy mikono, kisha akamnawisha Pendo na kuwakaribisha.







    Winifrida alinawa mikono huku akiendelea kumtazama Sammy kwa kuvizia vizia, kila mmoja alijipakulia chakula kwa kadiri ya tumbo lake, Winifrida alikuwa akimtazama Sammy kwa jicho la wizi wakati akijipakulia chakula.



    Sammy alijipakulia wali wa kumtosha kwenye sahani, akawekea mchuzi wa kuku na kumwagia maharage kwa wingi, kisha aliweka mboga za majani nyingi na kujisogezea huku akiketi kitako. Alionekana kupoa sana jambo lililomshangaza kila mtu isipokuwa Winifrida, kwani yeye alifahamu ukweli kwa nini Sammy alikuwa amepoa sana siku ile.



    Joyce alikuwa akimtupia Sammy jicho la wizi wakati akisogeza poti la chakula, akampakulia Pendo kidogo na kumwekea mchuzi mzito wa kuku na maharage kisha akampa na kuanza kujipakulia chakula chake mwenyewe, alipomaliza alianza kula taratibu.



    Winifrida naye alijipakulia chakula huku Sammy akimtazama kwa makini, hakusema kitu lakini alionekana kuwa na donge moyoni. Alitamani kumwambia Joyce ni wapi alimkuta Winifrida akiwa na mwanamume lakini alihofu siri yake ingefichuka.



    Pendo alimtazama baba yake kwa udadisi, Sammy naye alishusha macho yake kumtazama Pendo akiwa mtulivu sana. Akachota chakula na kuanza kula.



    Siku hiyo meza ya chakula ilitanda ukimya mzito wakati wote wa chakula, hakuna aliyeongea na kilichokuwa kikisikika muda ule kilikuwa ni mgongano wa vijiko na vyombo vingine vya mezani, wakati wakila.



    * * * * *



    Saa sita na nusu usiku Winifrida, mtoto wa kike mchache wa miaka lakini mwingi wa maneno, alikuwa ameketi kitandani chumbani kwake, akiwa amejiegemeza kwenye ukuta akiwaza. Usiku huo ulikuwa mrefu kwake kuliko kawaida na usingizi ulikuwa adimu.



    Rohoni mwake mlikuwa na shauku kubwa. Alipomaliza kula usiku ule aliingia chumbani kwake akapanda juu ya kitanda chake, si kulala bali kuendelea na fikra zake zisizokuwa na mwisho kuhusu Jackson. Kijana mtanashati na mcheshi sana.



    Alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kugeuza shingo yake kumtazama Pendo aliyekuwa katika sayari ya mbali muda ule akikoroma, alikuwa akivuta pumzi taratibu na kuzishusha.



    “Hmm, utoto raha sana! Unakuwa huru na huna stress, hufikirii maisha wala mapenzi kama ilivyo kwa wakubwa,” Winifrida aliwaza.



    Alizungusha macho yake kukitazama kile chumba chao kwa makini kana kwamba alikuwa akikiona kwa mara ya kwanza, akafumba macho yake, mawazo yalizidi kumsonga usiku huo, aliwaza vitu vingi: alifikiria masomo, maisha, mapenzi. Alimwaza Jackson, kijana aliyetokea kumpenda sana. Alitamani usiku ule angekuwa na Jackson mle chumbani, wakiwa wao wawili tu. Lakini hakukuwako!



    Kilichokuwa pamoja naye usiku ule, ukimwacha Pendo aliyelala fofofo kitandani, ni mito miwili mikubwa, alifumbua macho yake na kuutazama mto mmoja, akauvuta kisha aliubana kifuani kwake na kuubusu.



    “Jackson,” Winifrida aliuita ule mto huku akiyafumba macho yake, “Nakupenda sana mpenzi wangu. Tafadhali niambie kama nawe wanipenda kwa dhati.”



    Kisha alitegesha sikio lake kwenye ule mto akifanya kama anayesikiliza, kwa mbali katika sikio lake la mawazo alimsikia Jackson wa ndotoni akimjibu, “Winnie, mpenzi wangu, ni wewe peke yako ninayekupenda hapa duniani. Nakupenda na nitaendelea kukupenda hadi mwisho wa maisha yangu…”

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Winifrida alihisi mapigo ya moyo wake yakiongezeka maradufu na joto lake likizidi kupanda. Akaubusu tena ule mto kama aliyepatwa na wazimu. Hakuamini kama yote yale alikuwa anafanya na ule mto, wala Jackson hakuwako.



    Aliendelea kuubusu ule mto mpaka aliporudiwa na fahamu. Akaona haya, japo Pendo alikuwa amelala na hapakuwa na mtu mwingine aliyeuona upumbavu wake. Aliusukuma ule mto pembeni, akaridhika kuwa alikuwa na Jackson muda ule.



    “Lo, Jackson! Laiti ningekuwa na uwezo ningehama naye hapa duniani, nikajifiche naye pahala pa peke yetu, sina hofu ya pute wala vijicho, ni mimi na yeye tu, kutwa kucha,” Winifrida aliwaza na kushusha pumzi.



    Akakumbuka alivyokutana na Jackson mara ya kwanza, ilikuwa mwaka uliokuwa umetangulia, miezi sita tu iliyokuwa imepita, wakati huo Winifrida akiwa kidato cha tatu na Jackson akiwa kidato cha nne. Ilikuwa ni katika mashindano ya ujirani mwema yaliyofanyikia Shule ya Sekondari ya Azania na kuzikutanisha shule kongwe za jijini Dar es Salaam.



    Siku ile wanafunzi wa Zanaki walipanda jukwaani kuonesha mchezo wa kuigiza ulioitwa ‘Hadi Lini!’ na yeye Winifrida alicheza nafasi ya mhusika mkuu. Ulikuwa mchezo uliomwelezea mwanamke jasiri aliyepambana kunusuru ndoa yake pale mumewe aliyempenda alipoamua kumsahau na kumpenda mwanamke mwingine, baada ya kufanikiwa.



    Winifrida alicheza nafasi ya mke mtii kwa ndoa yake ambaye mume wake alipata penzi jipya. Alicheza nafasi hiyo kwa uthabiti na kuuvaa uhalisia wa kweli, hasa pale aliposimamia kile alichokiamini na kuwafanya nusu ya watazamaji wasisimkwe na kupiga kelele za shangwe.



    Walipomaliza tu onesho lao Jackson alimfuata alipokuwa amesimama na wenzake na kumpongeza. Winifrida alibinya mikono yake kwa shauku, raha iliyoje kupongezwa na kijana kama Jackson. Ni yeye Winifrida aliyetamani kumpongeza kwanza Jackson kwa onesho lake lililomsisimua kila mtu ukumbini. Ni Jackson aliyepanda jukwaani kabla yao.



    Jackson alikuwa amejaaliwa sauti tamu na kipaji cha kuimba na alipokuwa jukwaani kila mtu alipagawa! Winifrida alihisi damu ikimchemka, roho ikamlipuka, miguu ikamcheza na moyo kumpapatika.



    Kwa kweli Jackson alijaaliwa sauti nzuri na alijua hasa kuburudisha mashabiki awapo jukwaani, ndiyo maana haikuwashangaza wengi kuona wimbo wake wa ‘Nadhiri Yangu’ aliokuwa ameuachia kipindi hicho ukifanya vizuri sana kwenye vituo mbalimbali vya redio na runinga kuliko hata nyimbo za wakongwe.







    Sasa Jackson na Winifrida walikuwa wamesimama wakitazamana kwa makini, kila mmoja alikiona kitu fulani kwenye macho ya mwenzake. Penzi changa! Kwa muda mfupi tu waliosimama na kupongezana ulitosha kuwajulisha kuwa kila mmoja alikuwa amevutiwa na mwingine. Na kuanzia siku hiyo ukawa mwanzo wa kuchipua kwa penzi lao, ingawa hadi wakati huo hawakuwa wamekutana kimwili.



    Kabla ya hapo, Winifrida hakuwa akijihusisha kabisa na uhusiano wowote wa kimapenzi japo hakuacha kubughudhiwa kila alipopita mtaani, kama alivyojiwekea nadhiri kutojiingiza katika uhusiano wa kimapenzi hadi amalize shule, ni hivyo hivyo alivyoishi. Hakuringia uzuri wake lakini hakutaka pia usumbufu unaopitiliza kutoka kwa wavulana.



    Kuanzia kidato cha kwanza hadi hapo alipofikia alikuwa na msimamo thabiti sana, hata hivyo, maringo yake yalifichwa na werevu wake darasani. Ilikuwa ni warembo wachache sana wa aina yake waliofanya vizuri kimasomo, jambo hilo liliwavutia walimu na wanafunzi waliopenda maendeleo kimasomo.



    Lakini sasa Jackson alikaribia kumfanya aivunje nadhiri yake aliyojiwekea. Japo alikuwa amemwambia Jackson asubiri kwanza amalize kidato cha nne lakini Jackson alikuwa na maneno matamu sana yaliyokaribia kumtia wazimu.



    Winifrida alianza kuwa mzembe darasani, badala ya kumsikiliza mwalimu, mawazo yake yote yalikuwa kwa Jackson.



    Ndiyo maana haikushangaza siku ile mchana aliamua kutoroka shule na kuandamana na Jackson kwenda nyumbani kwao Kiwalani, alikuwa tayari kwenda kumpa penzi, lakini kaka yake Sammy… ah, sijui alitoka wapi na kutibua mipango yao!



    Winifrida alijiona kuwa hakuwa huru kama wasichana wenzake. Alidhani kuwa hapa duniani hakuna kitu kizuri kuliko uhuru; uhuru wa kufanya apendacho duniani.



    Kwa mara ile ile aliutamani ukubwa ikiwa udogo maana yake ni kudhibitiwa, lakini pia aliuchukia ukubwa ikiwa maana yake kudhibiti wadogo. Sasa alikwisha ingia katika mtihani mgumu wa mapenzi. Alimfikiri Jackson kila wakati, akimwona kila pahala, tangu katika sahani ya chakula hadi kitandani.



    Alichukua begi lake la madaftari na kupekenyua sehemu fulani kwenye mifuko ya lile begi na kutoa simu yake ya mkononi aliyokuwa akiificha ili isionwe na kaka yake au wifi yake. Ilikuwa ni simu aina ya Huawei aliyonunuliwa na Jackson ili kuwarahisishia mawasiliano.



    Alifungua sehemu ya kuhifadhi majina na kulitafuta jina la Jackson, alipoliona alilitazama kwa makini akitamani kumpigia simu, lakini akasita.



    Mara akakumbuka jambo na kuinuka haraka, akalifuata kabati la nguo na kulifungua, akapekua pekua kwenye nguo zake na kutoa kadi ndogo ya kuhifadhi kumbukumbu kwenye simu (Micro SD). Ni kadi aliyoipata kwenye gari la Sammy siku ya kwanza tu Sammy alipokuja na gari nyumbani.



    Winifrida aliketi juu ya kitanda, akatabasamu huku akiiangalia kwa makini ile kadi ndogo ya kuhifadhi kumbukumbu kwenye simu kisha akageuka kumwangalia Pendo aliyekuwa anakoroma. Aliifungua ile simu na kuiweka ile kadi ndani yake.



    Ile kadi ilionekana kujaa picha, sauti na video. Winifrida alipotaka kuingiza picha zake yakatokea maandishi kwenye kioo cha simu yake: “Micro SD is Full do you want to format it?” Winifrida alishusha pumzi huku akiangalia juu, aliwaza kidogo na kuuma midomo yake.



    Alitaka kufuta vitu vilivyokuwemo lakini akasita na kuamua kuifungua ile kadi kuona kilichokuwemo. Alikuta picha kadhaa za jengo la kisasa lenye chumba chenye vifaa ambavyo hakuvielewa, video moja na sauti ya kurekodiwa. Aliamua kuisikiliza ile sauti na alichokisia kilimtisha sana.



    Ilikuwa ni rekodi ya maongezi ya simu kati ya mtu mmoja aliyeonekana kuwa ni mwanasiasa au mtu mwenye mamlaka makubwa serikalini na muuaji wa kukodiwa. Katika maongezi yao walikuwa wanapanga mikakati ya mauaji ya mtu waliyekuwa wakimtaja kwa jina la JM.



    Winifrida aliyasikiliza kwa makini maongezi yao huku akihisi kuogopa mno. Ubaridi wa woga wa aina yake ulimtambaa mwilini na mapigo ya moyo wake yalibadili mwendo wake na kwenda mbio isivyo kawaida! Nywele kichwani kwake zilisimama na mwili kusisimka. Hakumaliza kusikiliza maongezi, akayaondoa na kuamua kutazama ile video.



    Lahaula! Alijilaumu kwa nini aliitazama ile video. Ilikuwa video ya mauaji ya kutisha, hakuamini alichokiona, alidhani labda ni sinema ya kutengenezwa. Lakini alipoitazama vizuri alihisi ilikuwa na uhusiano na yale maongezi aliyoyasikia awali. Hata hivyo, kuna jambo lilimshtua zaidi, gari la Sammy lilionekana kwa mbali!



    “Lilifuata nini gari la Sammy kwenye ile video ya mauaji?” Winifrida alijiuliza swali lile na maswali mengine kibao: Je, mauaji yale yalikuwa yanahusiana vipi na Sammy? Ile kadi ya kumbukumbu kwenye simu aliyoikuta kwenye gari la Sammy ilifikaje? Je, Sammy alikuwa anaelewa chochote kuhusiana na yale mauaji?



    Winifrida alijawa na hofu kubwa. Kichwa chake kilikuwa kimejawa na mawazo na kuchanganyikiwa kwa wakati mmoja. Alijihisi moyo wake ukilemewa na msukumo mkubwa wa damu na asijue la kusema. Hakuwa na majibu ya yale maswali.



    Aliogopa sana na kuitoa ile kadi haraka, akaificha kabatini huku akihisi kama Sammy alikuwa akimchungulia dirishani, kwa mara ya kwanza alianza kumwogopa kaka yake. Alipanda kitandani, akajilaza na kujifunika shuka gubigubi huku akijikunyata kwa woga.







    * * * * *



    Saa tatu na nusu asubuhi, katika Shule ya Sekondari ya Zanaki, Winifrida alikuwa ameketi darasani akiwa mkimya mno jambo lililowashangaza wanafunzi wenzake, kwani haikuwa kawaida yake kutulia vile. Kwa tabia yake ya uchokozi kwa wengine na sauti yake kali ilikuwa rahisi kuhisi uwepo wake, na siku ambayo hakufika shule kila mtu angejua kuwa hayupo.



    Hata hivyo, kimya cha siku ile kilikuwa cha sauti tu, kwani kichwani mwake mlikuwa mmejaa mawazo yaliyokuwa yakisokotana na kumfanyia kelele ambazo mtu yeyote hakuweza kuzisikia ila yeye mwenyewe.



    Hakuwa na furaha kabisa moyoni mwake kutokana na kumbukumbu mbaya ya picha alizozishuhudia usiku uliokuwa umetangulia kwenye kadi ya simu aliyoiokota kwenye gari la kaka yake.



    Ndani ya darasa lile la kidato cha nne kulikuwa na utulivu mkubwa, wanafunzi walikuwa wakimsikiliza mwalimu wao wa sayansi, Mwalimu Josephat Igembe. Hata hivyo, Winifrida aliyeonekana kama alikuwa akimsikiliza Mwalimu Igembe kwa makini, aliishia kumwangalia tu pasipo kusikia chochote alichoongea, mawazo yake yote yalikuwa mbali kabisa, nje ya zile kuta nne za darasa.



    Kila mara alijitahidi kuyarudisha mawazo yake yawemo darasani, na hata alipopata nafasi ya kumsikiliza mwalimu, Kiingereza chake kilikuwa rahisi sana, lakini ule ujumbe uliokuwemo katika maana ndiyo uliokuwa mgumu. Winifrida aliviajiri viungo vyote vya mwili wake vimfikishie ujumbe, lakini wapi!



    Maneno yaliteleza kinywani mwa Mwalimu Igembe utadhani maji yakiteremka mlima, kwa hali hiyo aliacha wazi masikio yake na kuyasabiria maneno ya mwalimu yule ili kuelewa maana ya neno moja moja.



    Mara alishangaa kuona wanafunzi wenzake wote wakigeuka kumtazama kwa mshangao, na yeye akawatazama kwa mshangao. Kabla hajujua kulikoni, akashtuliwa na sauti ya Mwalimu Igembe, “Winifrida, mbona ni swali rahisi kabisa, sijui kwa nini unafikiria kiasi hicho!”



    Winifrida alimkodolea macho Mwalimu Igembe, hakujua ajibu nini kwani hata swali lenyewe hakuwa amelisikia. Alishusha pumzi ndefu huku akiiminya midomo yake.



    “Okay, mwingine anayejua jibu lake atusaidie, naona Winifrida leo hayuko sawa, pengine akili kazisahau nyumbani!” Mwalimu Igembe alisema na kuwafanya wanafunzi wote, isipokuwa Winifrida, wacheke. Hata hivyo, hali hiyo ilimfanya Winifrida ashushe pumzi za ahueni japo alikuwa anatweta kama aliyekuwa amekoswa na risasi.



    “Sijui nifanye nini sasa? Naona hali hii inaanza kuathiri hata masomo yangu! Naogopa nikimuuliza kaka naweza kusababisha matatizo makubwa na nikimwambia wifi sijui kama atanielewa! Na hata akinielewa itakuwaje endapo ni kaka Sammy ndiye mhusika wa tukio lile? Halafu watakapojua kuwa nina simu watataka kujua nimeipata wapi? Ah… Mungu niepushe na balaa hili…” Winifrida aliwaza, mara mawazo yake yote yalivutwa na picha za tukio la mauaji, sasa alikuwa kama anaona tukio lile likifanyika mbashara mbele ya macho yake



    Aliwaona wanaume wawili ambao walizishika bastola zao sawasawa kwenye mikono yao, wakazielekeza kwa mwanamume mmoja na kummiminia risasi kama mvua, kisha wakamweka kwenye kiroba na kukiburuta kuelekea nje…



    Winifrida alijikuta akipiga kelele kwa nguvu bila kujitambua, darasa zima wakageuka kumtazama kwa mshangao. Mwalimu pia aliacha kufundisha na kugeuka kumtazama kwa mshangao, hakuelewa nini kilikuwa kimemsibu Winifrida siku hiyo.



    "Is she dreaming?” (Anaota?) Mwalimu Igembe aliwauliza wanafunzi wengine huku akishangaa sana.



    Darasa lote wakacheka kwa nguvu, lakini kicheko chao kilikatika ghafla baada ya kumwona Winifrida akilia kwa hofu huku akitetemeka sana, na kabla hawajajua kilichokuwa kinaendelea walimwona akisimama na kutoka nje mbio huku akilia.



    “Zaituni, mfuate ujue ana tataizo gani?” Mwalimu Igembe alimtaka mwanafunzi mmoja wa kike aliyekuwa rafiki mkubwa wa Winifrida kumfuata.



    Zaituni aliinuka na kutoka nje haraka kumfuata Winifrida huku wanafunzi wengine wakibaki wamepigwa na butwaa. Darasa lote lilikuwa na utulivu mkubwa sana.



    * * * * *



    Saa nne kasorobo asubuhi, Sammy na Elli walikuwa wanaingia katika ofisi za West Car Rentals zilizopo kwenye ghorofa ya kwanza ya jengo la ghorofa mbili lililoko katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi eneo la Upanga Mashariki, jijini Dar es Salaam.



    Baada ya kujadiliana kuhusu mwenendo wa biashara ya Sammy hatimaye walikubaliana kwenda kumwona rafiki wa Elli aliyemiliki kampuni ya ukodishaji magari kwa ushauri zaidi, wakiamini kuwa Sammy angejifunza mengi na pengine kubadili mtazamo wake kuhusu biashara ya teksi.



    Walipoingia ndani waliurudishia mlango taratibu na kusimama wakiwatazama watu sita waliowakuta mle ndani wakiwa wamekaa kwenye makochi, katika eneo la mapokezi ya ofisi ile, kati yao Waafrika walikuwa wawili vijana na wazungu wanne, wanawake wawili na wanaume wawili.



    Wale watu waliokuwa mle ndani waligeuza shingo zao kuwatazama Sammy na Elli, kasoro mwanadada mmoja aliyeonekana kutingwa mno na shughuli kwenye kompyuta yake.







    Mwanadada yule aliitwa Cynthia West, alikuwa na umri wa miaka 25, sura yake ilikuwa ndefu kiasi na pua ndogo ndefu. Alivaa sketi fupi iliyoishia sentimita chache juu ya magoti yake, ilikuwa nyeusi yenye miraba myeupe, blauzi nyeupe ya mikono mirefu na viatu vyeusi vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio



    Alikuwa chotara wa kizungu mwenye shingo ndefu kiasi iliyobeba mabega ya kike na shingoni alivaa kidani cha dhahabu kilichoning’inia kifuani kwake na kuzama katikati ya uchochoro wa matiti yake ya ukubwa wa wastani.



    Elli na Sammy waliwasalimia kwa Kiswahili wale watu waliowakuta mle ndani. Ni wale Waafrika pekee walioitikia ile salamu kwa pamoja, kasoro wale wazungu na yule mwanadada aliyeko kwenye kompyuta.



    Kisha Sammy na Elli waliwasalimia wale wazungu kwa Kiingereza huku wakipunga mikono yao ya kulia na kuwafanya wale wazungu waitikie kwa bashasha zote.



    Muda huo yule mwanadada aliyeko kwenye kompyuta aliinua uso wake mara moja na kuwaangalia Sammy na Elli. Macho yake yakagongana na yale ya Elli na Sammy. Yule mwanadada akaachia tabasamu pana na kurudisha macho yake kwenye kompyuta.



    “Cynthia, hujambo dada’angu?” Elli alimsalimia yule binti kwa bashasha.



    “Sijambo, kaka Elli, shikamoo,” Cynthia alisema huku akiacha kuchapa huku akiendelea kutabasamu.



    “Marahaba. Pole na kazi,” Elli aliitikia huku akimsogelea.



    “Asante, karibuni sana,” Cynthia aliitikia kisha akageuza shingo yake kumtazama Sammy huku akiendelea kutabasamu.



    “Shikamoo,” alimsalimia Sammy kwa hesima zate.



    “Marhaba, za kazi?” Sammy aliitikia huku naye akitabasamu.



    “Nzuri,” Cynthia alisema huku akiyarudisha macho yake kwenye kompyuta mara moja na kuyarudisha tena macho yake kuwaangalia wageni wake huku akionekana ni mtu mwenye furaha muda wote.



    Kabla Elli hajamuuliza Cynthia chochote mlango wa ofisi ile ulifunguliwa na mwanamume mmoja mnene na mrefu aliyefuga rasta aliingia. Alikuwa pia chotara wa kizungu na aliitwa McDonald West. Alipowaona Elli na Sammy aliwasogelea haraka huku akimtazama Elli kwa mshangao kama vile hakuwa ametegemea kumwona pale muda ule.



    “Umepaa?” McDonald alimdaka Elli juu kwa juu bila hata ya salamu.



    “Wala sijapaa, barabara tuliyojia haikuwa na foleni kabisa, askari wa usalama barabarani walikuwa wakiziita gari, nadhani kuna mkubwa fulani alikuwa anaandaliwa kupita,” Elli alisema huku akinyoosha mkono wake kumsalimia McDonald. Wakasalimiana kwa furaha kisha McDonald aliwakaribisha ofisini kwake.



    Kilikuwa ni chumba cha ofisi cha ukubwa wa kawaida chenye samani chache muhimu za kiofisi. Kulikuwa na zulia lenye rangi za bendera ya taifa la Tanzania sakafuni, meza kubwa ya kiofisi ambayo juu yake kulikuwa na kompyuta aina ya Acer i5 na kioo cha flat, kiti kirefu cha ngozi halisi cha kiofisi chenye magurudumu madogo yaliyokiwezesha kusogea, na kilikuwa kinazunguka.



    Mbele ya ile meza kulikuwa na viti viwili pamoja na kochi moja la sofa kwa ajili ya wageni, meza ya kioo ya pembe nne na chini ya meza ile kulikuwa na magazeti na majarida kadhaa yaliyoandikwa “Dar Guides”. Juu ya meza ile kulikuwa na vitabu, nakala chache za magazeti ya siku ile na nakala kadhaa za ramani kubwa ya Tanzania ikionesha maeneo ya vivutio vya utalii.



    Kwa pembeni kulikuwa na rafu iliyopangwa vitabu na majarida chungu nzima ya utalii na ukutani kulikuwa na ramani kubwa ya Tanzania, yenye kuonesha maeneo mbalimbali yenye vivutio. Elli na Sammy waliketi kwenye viti vilivyokuwa mbele ya meza ya McDonald.



    “Uliponipigia simu nilikuwa maeneo ya Muhimbili nikadhani huenda ningekuwahi, enhe nipe habari?” McDonald alisema baada ya Elli na Sammy kuketi kitako.



    “Ni kama nilivyokueleza, huyu ni ndugu yangu, anaitwa Sammy…” Elli alianza kuelezea huku akimwoneshea Sammy kwa McDonald.



    “Sasa, ngoja kwanza niwatoe hawa jamaa hapo mapokezi, wametokea Uswisi jana na walipaswa kuwa safarini kuelekea Iringa leo hii…” McDonald alisema na kuinuka, akatoka nje ya ofisi yake akiwaacha Sammy na Elli.



    Muda huo huo simu ya Sammy ilianza kuita, alipoiangalia kwa makini akagundua kuwa ilikuwa simu kutoka kwa Dk. Masanja. Sammy alisita kidogo kisha akaamua kuipokea.



    “Hello!” alisema mara tu alipoiweka kwenye sikio. Akasikia mwangwi wa sauti yake ukimrudia, akashtuka. Hii ilimaanisha kuwa simu ilikuwa imewekwa sauti ya juu ‘Loud speaker’ ili kumwezesha mtu au watu wa upande wa pili kusikia yanayoongelewa upande wa pili wa simu pasipo kuiweka sikioni.



    “Hujambo, kijana wangu?” ilikuwa sauti ya Dk. Masanja aliyeongea kwa sauti tulivu.



    “Sijambo, shikamoo.”



    “Marhaba, vipi unaweza kuwa na nafasi ufike hapa ofisini kwangu leo?” Dk. Masanja alisema kwa sauti tulivu.



    “Leo! Sidhani kama nitaweza kufika, nipo mbali kidogo, labda kesho kama itawezekana,” Sammy alisema huku akionesha kusita. Akasikia sauti ya Mr. Oduya ikiongea upande wa pili wa simu kumtaka Dk. Masanja amuulize alipo ili wamfuate. Sammy alishtuka kidogo, hata hivyo hakutaka kumwonesha Elli kuwa alishtuka.



    “Kwani upo wapi, naweza hata kukufuata huko huko uliko!” Dk. Masanja alimuuliza Sammy.



    Sammy alibaki kimya kwa muda akifikiria nini aongee, kwani alianza kuhisi kuwa kulikuwa na jambo lisilo la kawaida likiendelea. Alikumbuka jinsi alivyogombana na Mr. Oduya walipokutana ofisini kwa Dk. Masanja pale alipomtaka awe mshirika wake. Akajiuliza, huyo mzee alikuwa anamtakia nini!



    “Sammy, are you there?” Dk. Masanja aliuliza kwa wasiwasi baada ya kuona kimya.



    “Mmh… kwani ulikuwa unasemaje mzee, wangu? Labda naweza kukujibu hata humu kwenye simu.”



    “Ah, kuna mambo haipendezi kuyaongea kwenye simu, ndiyo maana nilitaka kujua upo wapi!”



    “Kuna tatizo lolote?” Sammy aliuliza huku akikunja sura yake na kuminya midomo.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Hakuna, kuna mambo fulani nataka nikushirikishe,” Dk. Masanja alisema na kushusha pumzi.



    “Unishirikishe?” Sammy aliuliza huku akiwa bado amekuja sura yake.



    “Ndiyo, kwani kuna ubaya kukushirikisha? Au mimi na wewe tumeshakuwa na uadui siku hizi?”



    “Hakuna ubaya, lakini kwa leo haitawezekana. Nipo nje ya mji na ninatarajia kurudi kesho.”



    “Kesho saa ngapi nikutegemee?”



    “Ngoja nione halafu nitakujulisha,” Sammy alisema na kukata simu, akashusha pumzi za ndani kwa ndani. Elli alimtazama kwa makini.









    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog