Search This Blog

Sunday 20 November 2022

ROMAN ABRAMOVICH: UTAJIRI WA DAMU, RISASI NA UMAFIA - 4

 





    Simulizi : Roman Abramovich: Utajiri Wa Damu, Risasi Na Umafia

    Sehemu Ya Nne (4)











    Kwa hiyo wapinzania wa Yeltsin au tuseme wapinzani wa ‘The Family’ wakaanza kujipanga kuzuia hicho ambacho kilikuwa kinataka kutokea. Iikuwa wazi kwamba Yeltsin amebakiza muda mchache madarakani, kwa wapinzani wa ma-oligarch hii ilikuwa habari njema kwao kwamba walau sasa na wao watapata zamu yao kufaidi mema ya nchi. Lakini baada ya kauli ya Yeltsin kwamba anatamani kurithiwa kiti cha Urais na Putin walielewa kwamba huu ulikuwa ni mkakati wa kuanza kumnadi Putin kwa wananchi. Kwahiyo nao wakaanza mipango ya kukwamisha suala hilo lisifanikiwe.







    Sasa,



    nimeeelza kwenye sehemu zilizopita kwamba Yeltsin alikuwa na upinzani mkubwa sana kwa wanasiasa wengine. Upinzani huu ulikuwa na historia ndefu hata kabla hajaanza kuwalimbikizia mali ma-oligarch.



    http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Tutazame kidogo kwa ufupi sana… Shirikisho la Russia lilivunjika December, 1991. Kama mwezi mmoja hivi baadae, yaani January, 1992 Rais Yeltsin alianzisha program mpya kukabiliana na hali ya mbaya ya kiuchumi ambayo ilisababishwa na kuvunjika kwa Shirikisho la Russia. Badala ya program ile kusaidia badala yake ilifanya hali ya kiuchumi kuwa mbaya zaidi. Yeltsin alipingwa vikali mno kwa sera hizo mpya ambazo alizianzisha kiasi kwamba mpaka makamu wake wa Rais alikuwa anazikosoa hadharani kabisa. Likatokea wimbi la wanasiasa wengi hata wa chama chake kujiweka mbali na Yeltsin na kujipambanua kupinga sera hizo mpya za kiuchumi za Yeltsin. Matokeo yake ni kwamba Yeltsin alikuwa akipeleka miswada au mapendekezo Bungeni ili yapitishwe yalikuwa yanakwamishwa makusudi ili kumkata makali ya kutekeleza sera zake za kiuchumi. Kipindi hicho Bunge la Russia lilikuwa linaitwa “Supreme Soviet”. Baada ya mvutano wa muda mrefu kati ya Yeltsin na Bunge hatimaye Yeltsin akatangaza kulivunja Bunge. Sasa katiba ya Russia kipindi hicho ilikuwa haimpi mamlaka Rais kulivunja Bunge, kwa hiyo wabunge wakagoma na wakawa wanaendelea na shughuli za kibunge. Yeltsin akaingiza vifaru vya kijeshi kwenye viwanja vya bungeni kutaka kuwatoa wabunge kwa lazima. Wabunge wakagoma… wafuasi wao wakaandamana mitaani pale Moscow… kukatokea mapigano makali kati ya wananchi waliokuwa wanaunga mkono bunge dhidi ya wafuasi wa Yeltsin na jeshi. Inakadiriwa karibia watu 1,500 walipoteza maisha kwenye yale mapigano na kuyafanya kuwa moja ya tukio baya zaidi kwenye historia ya Russia.







    Loh.! Nanogewa nichambue zaidi historia hii ya Russia… but let’s cut a long story short. Mapigano yale yalidumu kwa muda wa kama wiki mbili hivi kabla ya Rais Yeltsin na Bunge kufikia muafaka. Bunge walimpa masharti kadhaa ili waendelee kufanya naye kazi ‘smoothly’ na yeye Rais Yeltsin akatoa matakwa yake.



    Moja ya makubaliano makuu ilikuwa ni kuunda upya mfumo wa Bunge la ‘Supreme Soviet’. Yeltsin alihisi kwamba Bunge lilikuwa limepewa mamlaka makubwa mno kutokana na mfumo wa kijamaa ambao ulikuwa unatumika kuendesha nchi huko nyuma. Chini ya mfumo huu mpya, kwanza ‘supreme soviet’ litavunjwa na kuundwa ‘Federal assembly’ ambayo itakuwa na ‘chamber’ mbili. Kutakuwa na ‘Lower House’ kwa jina State Duma (au GosDumas kama warusi wenyewe wanavyooita), na pia kutakuwa na ‘Upper House’ kwa jina la Council of the Federation. (Mfumo huu bado ungali unatumika mpaka sasa).







    Kwanini nimegusia historia hii? Kuna vitu viwili ambavyo nataka uvione… kwanza ni uhasama wa Bunge na rais Yeltsin kwani hata baada ya mfumo mpya kuwekwa Bunge bado lilikuwa na kinyongo naye kutokana na kile ambacho kilitokea.



    Na jambo la pili nataka tufahamu kwamba ile lower house ya Bunge (State Duma) ndiyo ambayo ilikuwa na malamlaka ya kumthibitisha Waziri Mkuu mara baada ya kuteuliwa na Rais.





    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Sasa,







    Bada ya kauli ya Yeltsin kwamba anatamani Putin awe mrithi wake wa kiti cha Urais, wapinzani wa ‘The Family’ wakaanza kampeni ya chini kwa chini kushawishi wabunge wa GosDumas kumpiga chini Putin.







    Putin alikuwa anahitaji kura 226 ili kuthibitishwa kuwa Waziri Mkuu.







    Kambi ya Yeltsin ikagundua njama hii na mara moja wakaanza kuifanyia kazi. Wanasema pesa sabuni ya roho… haijalishi ni kabila gani au nchi gani… pesa inaweza kubadili moyo wa binadamu. Ma-oligarch wakaingia kazini kumwaga fedha kwa wabunge wa GosDuma.



    Siku ya August 16 kura zilipopigwa Putin aliponea chupu chupu kwa kupata kura 233. Kura saba tu zaidi.







    Kwa hiyo rasmi sasa Putin alikuwa ni waziri Mkuu wa Russia.







    Hatua ambayo ilikuwa inafuata ilikuwa ni kumjenga Putin kwenye mioyo ya wananchi. Kama ambavyo nimeeleza… vyombo vya habari vyote vilikuwa vinamilikiwa na ma-oligarch. Kwa hiyo kila siku vilikuwa vinaandaliwa vipindi malumu vya redio na televisheni… makala kwenye magazeti na makongamano na mikutano ya hadhara… vyote kumuhusu Vladimir Putin.



    Lakini moja ya matukio ambayo yalisaidia kumuweka Putin kwenye mioyo ya warusi ilikuwa ni namna ambavyo alishughulikia tafrani ambayo ilitokana na kulipuka kwa mabomu kwenye nyumba za kupanga kwenye miji mitatu nchini urusi… tukio ambalo linajulikana kwa jina maarufu la ‘Russia Appartment Bombings’. Tukio ambalo lilizua hofu kubwa ndani ya Urusi. Putin alionyesha ukakamavu wa hali ya juu na umahiri kulishughulikia suala hilo mpaka mwisho. Lakini pia Putin aliwakosha warusi kwa msimamo wake thabiti juu ya vita waliyokuwa wanaipigana Chechenya.







    Miezi mitatu baadae, yaani mwezi December 1999 Rais Boris Yeltsin alijiuzulu ghafla na kwa mujibu wa katiba ya Rusia Waziri Mkuu ndiye anachukua nafasi yake na kuikaimu mpaka uchaguzi mkuu uitishwe.







    Yeltisn alijiuzulu tarehe 31 December 1999… siku hiyo hiyo Putin akatangazwa kuwa Kaimu Rais wa Russia. Na siku hiyo hiyo akasaini ‘decree’ ya kwanza na muhimu sana kwenye historia ya Urusi. Decree hii ilikuwa na kichwa kinachosema, “On Guarantees of former President of the Russian federation and members of his family”. Decree hii iikuwa inatoa kinga kwa Rais Yeltsin na wanafamilia wake wote kwamba hawatashtakiwa kwa makosa yoyote yale kama ikionekana labda kulikuwa na makosa yoyote ambayo yalitendeka kipindi cha Urais wa Yeltsin.



    Na hii ilikuwa ni moja ya makubaliano kati ya Yeltsin na Abramovich kwa niaba ya ma-oligarch wenzake walipomtaka aachie ngazi… alitaka ahakikishiwe kwamba mali zake hatopokonywa na kamwe asishtakiwe.







    Miezi mitatu baadae, Putin aliitisha uchaguzi mkuu ambao alishinda kiulaini kabisa. Tarehe 7 May 2000, Vladimir Vladimirovich Putin alikula kiapo kuwa Rais wa Russia.







    Kazi ilikuwa imekamilika…. Abramovich… abracadabra.!!







    Swahiba wake ambaye ‘amemfinyanga’ kwa mikono yake na kumtengenezea njia sasa alikuwa amekalia kiti cha urais wa nchi.







    Kuna kitabu kitakatifu kinasema “tunakua kutoka utukufu mpaka utukufu”. Na haswaaa, hii ndio hulka yetu binadamu… haijalishi tuko kileleni kiasi gani… siku zote tunataka kuipanda ngazi inayofuata. Hata uwe na kikubwa kiasi gani, nafsini tunaona tulichanacho bado hakitoshi… haijalishi tunacho kingi kiasi gani. Tunatamani, tunatafuta, tunakipata alafu tunataka zaidi… wanadamu tumeumbwa na kiu ya “kukua kutoka utukufu mpaka utukufu”.







    Huu sasa ulikuwa ni wakati wa Abramovich kuhamia katika hatua ya pili ya ndoto zake… ndoto kubwa zaidi. Unaweza kudhani kumiliki Sibneft kampuni kubwa zaidi ya kuzalisha mafuta nchini Russia ilikuwa inatosha.. la hasha… Roman Abramovich alikuwa anataka zaidi, na alichikuwa anakitaka safari hii kilikuwa kimono zaidi pale Russia.. Abrfamovich alikuwa anataka kujimilikisha sekta ya Aluminum ndani ya nchi ya Russia. Sekta yenye utajiri mkubwa zaidi nchini Russia lakini pia ikiwa ni sekta hatari zaidi.



    Kuingia kwa Abramovich kwenye sekta hii kutakuja kuibua moja ya nyakati za hatari zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Russia na Ulaya mashsriki yote kiasi kwamba mpaka leo hii kipindi hicho kinajulikana kama nyakati za ‘Vita za Aluminum’.









    MUHIMU: Kabla sijaenda kwenye mada nijibu swali ambalo naulizwa kila mara kwenye comments na PM ili iwe clear. Utaratibu wa kujiunga na 'familia' yangu kule whatsapp ni malipo ya shilingi elfu tano kwa mwezi. That's it.

    And nimeweka namba yangu, kwa hiyo ni vyema unitumie meseji direct badala ya PM. Nafungua PM mara chache sana kwa hiyo unaweza kuona sijajibu meseji yako ukajiuliza huyu somo vipi tena. PM nyingi mno, zinanielemea kwa hiyo najikuta sifungui zote.

    And hili ni suala la hiyari, kwa wenye kupenda wamekuja wale ambao wanahisi hawawezi basi tutakuwa tunaonana hapa jukwaani. Nadhali hii imekaa sawa, hakuna haja ya kufanya kuhusu hili. Limeisha…







    Twende kwa Oligarch Abramovich….

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Nimewahi kuonana na wasomaji wangu wachache sana wa makala na vitabu vyangu. Sababu kubwa ya kutoonana sana na watu ni kwa vile katika maisha ya kawaida huwa siongei kabisa japo ni msikilizaji mzuri sana. Tunaweza kukaa nikakusikiliza kwa masaa manne straight bila kuchoka wala wala ‘kuboreka’. Ubaya ni kwamba watu wengi wanategemea uwaeleze mengi na ubaya ni kwamba kwa asili huwa siongei ndio maana nachagua kuandika sana labda ‘ku-compasate’ energy ninayo-reserve kwa kutokuongea. Hii ni moja ya sababu kwa nini mara nyingi huwa sionani na watu… I’m not a good company kama unahitaji mtu wa ‘kupiga story’. Lakini sababu ya pili ni umri… wengi wana picha fulani kichwani ya muonekano au umri wa huyu muandishi ‘The Bold’. Wachache ambao nimekutana nao wote kitu kimoja huwa wanakisema ni kwamba kwa umri huu nilionao nawezaje kuandika vitu ambavyo naandika? Inawezekana wanasema hivyo as a compliment but it makes me feel very uncomfortable. Kwa hiyo napendelea kuendelea kujificha kwenye kichaka cha ‘The Bold.’



    Kwa nini nasema haya… unapomsoma mtu kwa muda mrefu sana na mambo makubwa ambayo ameyafanya kuna wakati fulani unaanza kujenga picha ya nje ya uhalisia.

    Kwa mfano, kwa vitu vyote hivi ambavyo Roman Abramovich amevifanya… kufikia hatua ya hadhi ya Oligarch, kulichachafya Bunge la Russia, kumuondoa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, kujimilikisha kampuni kubwa zaidi ya mafuta ya serikali, kumshawishi Rais Boris Yeltsin kuondoka madarakani na kumtengeneza Rais mpya Vladimir Putin… unaweza kudhani kwamba Abramovich ni lizee fulani hivi lililo zaliwa na kukulia kwenye ‘system’… lakini nikukummbushe kwamba mpaka siku ile mwaka 2000 mwezi May kipindi Putin anaapishwa kuwa rais mpya wa Russia… Roman Abramovich alikuwa ni kijana wa miaka thelathini na tatu tu. Niweke mkazo kwa namba… miaka 33.



    Kwenye sehemu iliyopita nilieleza kwamba baada ya Abramovich kujihakikishia umilki wa Sibneft na kisha kumshawishi Rais Yeltsin kuachia ngazi na baadae kumfinyanga Putin na kumweka madarakani sasa uliwadia wakati wa kuingia katika ‘utukufu mpya’.

    Nchi ya Urusi kwa miongo mingi sana imekuwa ndio nchi inayoongoza duniani kwa uzalishaji wa aluminium na hata matajiri wa kubwa wa Russia utajiri wao unatokana na aluminium, mafuta na gesi. Kwa hiyo sekta hii ya aluminium ni moja ya uti wa mgongo wa uchumi wa Russia.

    Kwenye miaka ya tisini na mwanzoni mwa 2000 baada ya serikali kuanza ubinafsishaji holela wa mali za umma ushindani ulikuwa mkubwa haswa na Russia haijawahi kushuhudia vifo vingi vya watu mashuhuri kama kipindi hiki. Katika kipindi hiki zaidi ya matajiri mashuhuri 100 waliuwawa kinyama na miili yao kuokotwa barabarani.



    Kipindi hiki kichungu kinakumbukwa kama wimbi la ‘Aluminium wars’. Nitaomba kuchambua kwa kuingia miguu miwili yote nukta kwa nukta ili kukielewa nini kilitokea kwa sababu tukiweza kuelewa vyema nini kilitokea ni rahisi zaidi kuielewa hata hii Russia ya sasa na mwelekeo wake wa kisiasa.



    Ilikuwaje… tuanze kwenye mzizi.





    Ukuaji wa sekta ya aluminium nchini Russia ni matokeo ya miaka mingi sana ya serikali ya nchi hiyo kuwekeza nguvu kubwa sana kwenye kuendeleza sekta hii. Kama haujafahamu, aluminium inachimbwa kutoka kwenye migodi ya boksiti (bauxite) na kisha kuchakatwa kuwa alumina (aluminium oxide). Alumina iko kama unga unga fulani hivi mwepe au mfano mzuri kama ‘snow’ hivi. Hii ndio hutumika kuzalisha aluminium. Sasa Russia ni moja kati ya nchi za kwanza kabisa kufanya bunifu za kuchakata boksiti mpaka kupata alumina. Gunduzi za mwanasayansi kama Beyer ambaye alikuwa raia wa Austria miaka ya 1889 akiwa anafanyakazi St. Petersburg’s katika kiwanda cha kemikali cha Tenteleev ambapo aligundua mbinu ya kuchakata alumina kutoka kwenye boksiti kwa kutumia alkali za kaustiki. Baadae gunduzi za watu kama Muller na Packard ambao waligundua uvunaji wa alumina kwa kuifanyia decomposition ya aluminium hydroxide na kisha kufanyia electrolysis. Katika lugha nyingine twaweza kusema kwamba warusi ndio ‘pioneers’ wa namna za uvunaji alumina kutoka kwenye migodi ya boksiti. Hata mapinduzi makubwa ya upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini Russia ambayo yalitokea kwenye karne ya 20 kwa kiasi kikubwa kulitokana na uhitaji mkubwa wa viwanda vya kuzalisha aluminium na malengo ya nchi hiyo kutaka kuongeza uzalishaji kila mwaka.



    Kwa hiyo sekta hii ya aluminium kwa miongo mingi nchini Russia imekuwa haraka na kuwa sehemu ya uti wa mgongo wa nchi.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Sasa kwenye miaka ya tisini kipindi ambapo serikali ilikuwa inahama kutoka kwenye ujamaa na kuingia kwenye ubepari na kubinafsisha mali za umma kuna jambo la kiuhini likafanyika. Wafanyabiashara ambao walikuwa wananunua viwanda vya aluminium wakatengeneza mgogoro wa kubuni kwamba kuna upungufu mkubwa wa malighafi ya alumina ndani ya Russia ambayo ndiyo inatumika kuzalisha aluminium. Kwa kuwa serikali ilikuwa mkononi mwa ma-oligarch wakashawishi kwamba serikali iondoe kodi kwenye uingizaji alumina kutoka nje ya Russia ili ‘kuboost’ tena uzalishaji wa aluminium. Serikali ikaondoa kodi kwenye malighafi za utengenezaji wa aluminium na pia kubadilisha mfumo wa kodi kwenye bidhaa za aluminum. Kwa hiyo biashara ya aluminium ambayo tayari ilikuwa na fursa ya kujenga utajiri, utamu wake ukaongezeka zaidi.

    Ikafika kipindi kila oligarch alikuwa anataka kumiliki kiasi fulani cha sekta hii ya aluminium.



    Ubaya ni kwamba mifumo ya umilikiwa viwanda hii ambayo ilikuwa inatumika ni kama ule ambao Abramovich aliuanzisha Russia namna ambavyo alikuwa anaimiliki Sibneft kupitia msululu wa ‘private trusts’ na makampuni yaliyosajiliwa kwenye sehemu zinazojulika kwa ukwepaji kodi kama vile Cyprus, Jersey, Canyon Islands na kadhalika. Yaani makampuni yalikuwa yanamilikiwa kwa mifumo complex kiasi kwamba huwezi kujua ni nani hasa ni mmiliki wa kampuni. Hii ikatoa mwanya wa watu kufanya ‘hostile takeovers’ za kihuni. Nilieleza hii uko mwanzoni. Tajiri anawalipa hela genge fulani la mafia. Wanakuja wanakuteka… unasainishwa nyaraka kwa nguvu, unauwawa kesho mwili wako unaokotwa vichakani uking’ong’wa na nzi.

    Au mshindani wako unamtumia genge linampiga risasi mchana kweupe katikati ya mji.



    Kilikuwa ni kipindi cha hatari kiasi hicho. Matajiri wakubwa zaidi ya mia moja waliuwawa kinyama na miili kutupwa mitaani.



    Kipindi Putin anaingia madarakani May mwaka 2000 alikuta hizi ‘aluminium wars’ ziko kwenye kilele chake kabisa. Watu wanauwana kugombea rasilimali za nchi.

    Kuna mambo mengi unaweza usikubaliane na Putin lakini suala moja lazima umpe heshima yake ni jinsi ambavyo anaipenda nchi yake. Putin alipoingia madarakani alikuwa na falsafa kwamba ndani ya Urusi ni ruksa kutumia fursa ya ubepari kutengeneza utajiri lakini malengo yako hayo ya kujitajirisha hakikisha hayaathiri nchi. Kwa hiyo hizi vita za kugombea viwanda vya aluminium na namna ambavyo kwa miaka mingi matajiri hawa walikuwa wameachwa kukwepa kodi ilikuwa inamkera haswa. Alikuwa anahitaji suluhisho….



    Uzuri alikuwa na Roman Abramovich upande wake.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Nakumbuka siku ambayo Rais Donald Trump alipomteua mkwewe Jared Kushner kuwa mjumbe maalumu wa kusuluhisha mgogoro wa Palestine na Israel alisema kwamba, kama Kushner akishindwa kusuluhisha mgogoro huo hakuna ambaye atakuja kuweza. Unaweza kuhisi kwamba kauli hii ni ya kumkweza sana Kushner… lakini kwa watu ambao wanamfahamu Kushner watakueleza kwamba kauli ile ya Rais Trump ilikuwa na ukweli kwa silimia zote. Kushner ni moja ya wanamkakati bora zaidi dunia kuwahi kushuhudia.

    Ndicho hiki ambacho pia Putin alikuwa anakiona kwa Abramovich… hakuna mzigo mzito unaoweza kumshinda ‘myamwezi’ huyu.



    Baada ya Abramovich kupewa baraka na Putin kuingia kwenye sekta ya Aluminium kwanza kabisa akaanza kutengeneza mazingira mazuri kwa yeye kufanya kile ambacho alikuwaa anakikusudia. Masuala kadhaa…

    Kwanza kabisa akafungua kampuni ya ku-trade commodities. Kampuni hii iliitwa Millhouse Capital na aliisajili London Uingereza. Kupitia kampuni hii alikuwa ana-trade commodities kama vile mafuta, Gold, Silver n.k. Lakini kampuni hii ilikuwa na malengo makubwa zaidi.



    Abramovich alipoanza kujiingiza kwenye sekta ya aluminium kwanza kabisa alimuomba mentor wake bwana Berezovsky kumsaidia kwa ‘connection’ alizonazo kwenye ulimwengu huo wa hatari wa biashara ya aluminium. Kipindi hiki Berezovsky alikuwa amejiingiza kwenye siasa na alikuwa ni mwakilishi kwenye Bunge la GosDumas. Na kwa kipindi hicho ili ushinde kiti cha kisiasa nchini Russia lazima uwe na connections na makundi ya mafia kwa ajili ya protection na kuwafanyizia wapizani wako. Kwa hiyo Abramovich alikuwa anataka kutumia connection hizi za mentor wake.



    Berezovsky alimsaidia kwa kumtambulisha kwa watu wawili ambao walikuja kugeuka kuwa muhimu sana kwenye maisha ya Abramovich mpaka leo hii…



    Kwanza, tunakumbuka kwamba nilieleza kuwa wakati serikali ya Yeltsin inabinafsisha mali za umma hata televisheni ya taifa iliyoitwa Perviy Kanal (First Channel) nayo ilibinafsishwa na ambaye aliichukua alikuwa ni huyu Oligarch Boris Berezovsky. Sasa, baadae Berezovky allimuingiza Russia mtu anaitwa Badri Patarkatsishvili. Huyu alikuwa ni mfanyabiashra kutoka Georgia lakini ni myahudi wa Israel. Badri aliingizwa Russia na Berezovsky na kumpa jukumu la kuendesha kituo cha televisheni ambacho alikuwa amebinafsishiwa na serikali. Lakini uhalisia kamili ni kwamba Badri alikuwa anajua haswa namna ya 'kudili' na mafia na masuala ya 'underworld'. Kwa hiyo Badri alikuwa anahakikisha usalama wa Berezosky na pia kuhakikisha wapinzani wa Berezovky wanashughulikiwa ipasavyo.

    Huyu ni mtu wa kwanza ambaye Abramovich alitambulishwa na mentor wake Berezovky. Kupitia mtu Abramovich alilipa zaidi ya Dola milioni 500 kwenda kwa mafia kupitia kwenye mikono ya Badri Patarkatsishvili. Kwa ajili ya nini? Nitaeleza…



    Sasa ili kuelewa ni kwa namna gani Abramovich aliingia kwa kishindo kwenye sekta ya aluminium na ku-takeover tunapaswa kumchambua mtu wa pili ambaye Abramovich alitambulishwa na Berezovky.



    Pale Russia kuna bwana mmoja anaitwa Oleg Deripaska. Katika enzi za utoto wake bwana huyu alikuwa ni wale aina za watoto ambao wazungu wanawaita 'prodigy'. Watoto wenye vipaji vya kupindukia kwenye suala fulani. Deripaska alikuwa ni prodigy wa hesabu na sayansi. Kabla sijaenda mbali kuna ‘pettern’ hapa nataka uione nitakuja kueleza huko mbele… Pattern ya kwanza ni Berezovsky mentor wa Abramovich nilieleza pale mwanzoni alikuwa ni Profesa wa Hisabati kabla ya kujiingiza kwenye biashara, lakini pia huyu Oleg Deripaska ambaye Abramovich alitambukishwa kwake naye alikuwa ni nguli wa Hisabati tangu utoto. Pattern ya pili ambayo nataka uione ni hawa watu watatu… Abramovich, Berezovsky na Badri Patarkatsishvili wote hawa wana asili ya Israel. Utanilewa hapo mbele kwa nini nime-highlight hayo mambo mawili.



    Sasa ni namna gani huyu deripaska alimsaidia Abramovich kuingia kwenye biashara ya hatari ya Aluminium kwa kishindo… nitarudi kueleza.





    http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    (Wale wote waliojipa mission ya kunitukana na kunikashifu kwenye comments nina neno moja kwenu… nyinyi ni wana wa Mungu na kwa sababu hiyo nawapenda sana)





    Nilisema nitaeleza kidogo kuhusu Deripaska ambaye Abramovich alitambulishwa kwake na Berezovsky. Deripaska ni aina ya wasomi ambao wametumia taaluma yao vyema kujichumia utajiri. Tangu akiwa bado kijana mdogo tu Deripaska alikuwa na shauku kubwa mno ya kujisomea na kitu angalinacho hata sasa. Huyu bwana hata sasa ukifika ofisni kwake makau makuu ya Basic Elements jijini Moscow kwenye jengo hilo kuna kuta nyingi ambazo zina shelves za vitabu kuanzia chini mpaka juu. Deripaska alikuwa na kipawa kikubwa cha hisabati tangia utoto. Mwaka 1993 alihitimu chuo kikuu ‘with honors’ shahada ya fizikia kutoka Moscow State University. Miaka miwili baadae alihitimu shahada ya uzamili katika uchumi kutoka Plekhanov University of Economics.



    Ndoto ya awali Deripaska ilikuwa ni kuwa msomi mbobezi kama ‘Theoretical physicist’. Lakini utakumbuka kwamba kipindi hiki ndicho ambacho Soviet Union ilidondoka. Hapo awali wanafunzi wote walikuwa wanasoma kwa udhamini wa serikali lakini baada ya Soviet Union kudondoka elimu ikawa ghali na serikali kuacha kugharamia masomo ya wanafunzi. Kwa hiyo kwa kijana kama Deripaska ambaye mwenyewe anasema kwamba hata hela ya kula ilikuwa ni tatizo kwake kipindi hicho hakukuwa na uhalisia wa yeye kuweza kugharamia masomo yake mwenyewe.



    Lakini pia kipindi hiki kama tulivyoona awali kilikuwa ni kipindi chenye fursa nzuri kwa mtu kujilimbikizia utajiri. Kwa hiyo Deripaska akiwa na miaka 25 tu alishawishi wanasayasi wengine kadhaa manguli wa hesabu, fizikia na hata rocket science kuungana naye kuanzisha kampuni ya ‘ku-trade’ metals. Kampuni hii waliita VTK, na Deripaska ndiye alikuwa mwanahisa mkubwa kuzidi wenzake. Deripaska alikuwa ni moja ya watu wa mwanzo kabisa nchini Russia kutumia mifumo ya kisayansi na ‘systematics’ katika kutrade commodities. Unaweza kujiuliza namna gani anatumia sayansi kutrade commodities… binafsi huwa natrade currencies na huwa nawaambia watu ‘trading’ ni science and mathematics na ndio maana watu wengi hawako successful wakitaka kuwa traders… kwa nini? Kwa sababu sayanasi na hisabati sio kitu chepesi.

    Uzuri ni kwamba Deripaska alikuwa ni nguli wa hisabati kwa hiyo VTK ilikuwa kwa haraka sana. Deripaska alikuwa ananunua commodities kwa bei ya chini ndani ya Urusi na kwenda kuziuza kwa bei ya juu kwenye soko la dunia.



    Kwenye sehemu za mwanzo kabisa za makala hii nilieleza kwamba kipindi serikali ya Russia inabinafsisha viwanda na makampuni ya umma waligawa voucher kwa wananchi ili watumie voucher hizo kununua hisa kwenye makampuni ambayo yalikuwa yanabinafsishwa. Nilieleza kwamba kila mwananchi alipewa voucher ya Rubble 10,000 za Urusi. Kama ambavyo ilitokea hapa kwetu Tanzania wakulima walivyouza vocha za pembejeo za kilimo ndivyo ambavyo pia Warusi walivyouza voucher zao kwa matajiri. Deripaska ni moja ya matajiri hawa ambao waliwekeza hela ya kutosha kununua voucher kwa wananchi.



    Kama mwaka mmoja tu baadae Deripaska alitumia voucher zote na faida yote aliyoipata kwenye kutrade commodities kununua hisa kwenye kiwanda cha Sayanogorsk Aluminium Smelter. Hiki ndicho kilikuwa kiwanda kikubwa zaidi cha uzalishanji aluminium nchini Rusia. Uwekezaji wake huu mkubwa ulimpatia hisa 20% za kiwanda hiki. Kwa wingi huu wa hisa ulimfanya Deripaska kuwa mwanahisa mkubwa zaidi nyuma ya serikali kwenye kiwanda hiki. Yaani mwenye hisa nyingi zaidi alikuwa serikali na yeye alikuwa namba mbili.



    Kutokana na ushawishi huo mkubwa aliokuwa nao kwenye kiwanda cha Sayanogorsk Aluminium Smelter kwa sababu ya kuwa na hisa nyingi kuzidi mtu yeyote binafsi, mwaka 1994 Deripaska alifanya ushawishi kwa wanahisa wengine na kupewa Ukurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo. Nikukumbushe tu kwamba mwaka huo 1994 wakati anapewa ukurugenzi mkuu wa smelter kubwa zaidi nchini Russia alikuwa ana miaka 26 tu.



    Miaka mitatu baadae yani mwaka 1997 Deripaska alianzisha Sibirsky Aluminium Group ambayo aliitumia kama kampuni mama ‘kuhold’ kampuni zake zote nyingine na shares zake zote kwenye makampuni mengine.



    Kwa hiyo huyu ndiye mtu wa pili ambaye Berozovsky alimtambulisha Abramovich kwake.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Naweza kusema kwamba huyu pengine ndio alikuwa mtu muhimu zaidi kwa Abramovich kumfahamu labda nyuma ya Berozosky tu pekee. Licha ya umuhimu wake mkubwa ambao tutauona hivi punde lakini pia bwana huyu walikuwa na mengi ya kufanana. Ukipiga hesabu yako sawasawa utaona kwamba Abramovich alikuwa anamzidi mwaka mmoja tu Deripaska. Yaani kipindi kile Abrampvich anapewa Baraka na Putin kuingia kwenye biashara ya Aluminium akiwa na miaka 33, Deripaska alikuwa na miaka 32.



    Wote wawili walikuwa ni vijana wadogo sana. Wote wawili wametokea kwenye maisha ya hali ya chini sana. Wote wawili wanajua namna ya kuishi kimkakati. Wote wawili walikuwa na ushawishi mkubwa sana. Abramovich kwenye system ya serikali na Deripaska kwenye ulimwengu hatari wa biashara ya Aluminium.

    Wenye unyoya wa kufanana… huruka pamoja.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog