Search This Blog

Sunday 20 November 2022

NYUMA YAKO - 4

 





    Simulizi : Nyuma Yako

    Sehemu Ya Nne (4)





    Henessy akamjibu lakini bado akiwa anamtazama kwa macho yaliyokaza. Nikamuuliza mwanamke huyo, “Tafadhali unaweza kujitambulisha?”

    “Oow!” akasema akivua miwani yake. Macho yake yalikuwa ya paka yakiwa na uchangamfu ndani yake. Akatabasamu na kunipatia mkono, “Naitwa Jolene! Ni rafiki yake na Britney.”

    “Oooh! Nimefurahi kukujua,” nikamjibu nisiongezee mengi. Akaniuliza, “na wewe? Wewe ni nani?”

    “Naitwa Rodney. Ni rafiki pia wa Britney!”

    Akaangaza kushoto na kulia. “Britney yupo wapi?”

    “Hayupo. Hatujaja naye hapa!”

    “Ooh! Yupo wapi kwa sasa. Ni muda sijawasiliana naye. Hata sasa imenichukua muda sana kumtambua Henessy!”

    “Ni simulizi ndefu kidogo,” nikamjibu na kumwomba, “tunaweza tukapata dakika kadhaa za kuongea?”

    Akaridhia baada ya kutazama saa yake ya mkononi. Tukasonga kwenda mahali fulani tulivu kwenye eneo hilohilo la ufukweni, hapo tukapata vinywaji laini na kupiga soga nikitaka kufahamu machache juu ya Britney lakini nikiwa nimemlaghai kuwa mimi na Britney ni mtu na mchumba wake. Tumekutana na akanieleza mambo kadhaa, ikiwamo kujihusisha na kucheza sinema za ngono.

    Kwa kufanya hivyo nilitarajia kumpa mwanya mwanamke huyo wa kutonificha kitu. Kumtengenezea mazingira ya yeye kuwa huru kunielekza lolote maana hata lile ambalo lingeweza kuwa siri, mimi tayari nalifahamu.

    “Umemjua Britney kwa muda gani?”

    “Miaka mingi tu. Alikuwa ni rafiki yangu toka High school!”

    “Kwahiyo ulikuwa unafahamu juu ya yeye kujihusisha na ile kazi?”

    “Yah! Ni rafiki yangu, nitashindwaje kujua hilo?”

    “Mlikuja kupotezana naye muda gani?”

    “Aaahmm kama mwaka mmoja na nusu hivi uliopita.”

    “Kwanini mkapotezana? Hakukuaga kama anakuja Ujerumani?”

    “Hakunambia! Nilistaajabu amepotea. Simu yake nayo haikuwa inapatikana.”

    “Lakini ulikuwa unajua kuwa ameenda Ujerumani?”

    Akabinua mdomo. “Napo nilikuwa sijui.”

    “Kwahiyo huku Ujerumani umekuja kufanya nini, Jolene?”

    “Kwenye matembezi yangu tu. In fact, kuna ndugu yangu anaishi huku. Nimekuja kumsalimu.”

    Akanywa juisi na kisha akaniuliza, “Vipi na wewe? Ni Mmarekani, sio?”

    “Ndio.”http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Kwahiyo ndiyo uko na Britney huku?”

    “Ndio. Nipo naye.”

    “Unatokea wapi Marekani na unajihusisha na nini?”

    “Mimi ni mwalimu High school! Natokea California.”

    “Ulikutanaje na Britney? Hakuwahi kunambia kuhusu wewe.”

    Nikatabasamu. “Nadhani kwasababu ulipotezana naye.”

    Akapandisha mabega. “Labda!” kisha akaniuliza, “So mtakuwa huku kwa muda gani?”

    “Si muda mrefu sana, tutarudi Marekani.”

    “Ooh! Basi si mbaya kesho mkaja nyumbani kwetu. Kuna tafrija ya siku yangu ya kuzaliwa. Nadhani Britney atakuwa anakumbuka hilo.”

    “Samahani, hatutaweza kuja.”

    “Kwanini?”

    “Kuna mahali tutaenda. Sidhani kama tutapata muda.”

    Akamtazama Henessy kisha akarudisha uso wake kwangu. “Mnaenda Marekani, sio?”

    “Hapana, si Marekani,” nikamjibu. “Ni hapahapa ndani ya Ujerumani.”

    “Ndiyo mkose muda wa kuja kuniona? Kweli? Sidhani kama Britney atakuwa amenisahau na kutonijali kiasi hiko!”

    Nikanyamaza nikikosa cha kumjibu. Nikanyanyua glasi ya juisi na kunywa fundo moja. Nikamwona yule mwanamke akifungua mkoba wake na kutoa simu. Akabonyeza kidogo na kuweka sikioni, “Njoo unichukue!” kisha akarejesha simu mkobani na kutoa bunduki! Akaninyooshea na kuniambia, “Ukifanya lolote la kipumbavu ntakugeuza mzoga!”



    **





    “Nyoosha mikono juu!” akaniamuru. Nami nikatii ikiwemo pia na Henessy naye akanyoosha mikono yake juu. Na mwanamke huyo akiwa ameiminyia silaha mbavuni mwangu katika namna ambayo haionekani na mtu mwingine, akaniamuru nielekee nje ya eneo hilo kuelekea moja kwa moja kule lami.

    Nikatii, tukatoka tukitembea kwa ukakamavu kuelekea huko. Tukiwa njiani mwanamke yule akawa anaangazaangaza huku na kule kuhakikisha usalama wake, nami kichwani mwangu nikifikiria namna gani ya kujichoropoa.

    Tukasonga mpaka mahali ambapo kwa mahesabu tulikuwa tumebakiza umbali mfupi kufikia ule usafiri ambao mwanamke yule anatupelekea. Ghafla, nikiwa hata sijui kinachoelekea kutokea, Henessy akachoropoka toka kwenye mikono ya mwanamke yule mtekaji na kukimbilia miongoni mwa watu waliokuwa wamejaa huko ufukweni!!

    Mwanamke yule, akiwa amechanganyikiwa, akamnyooshea bunduki Henessy, mara akapata fahamu kuwa hawezi kumfyatulia risasi hapo, basi akataka kurejesha bunduki kwangu, hapo nikakataa kwa kuudaka mkono wake kisha kuutegua kistadi, akaachia bunduki!

    Nikamnyooshea na kumwamuru atulie kama maji mtungini. Nikamtaka anyooshe mikono yake juu na kisha twende kule alipokuwa anataka kunipeleka. Akatii.

    Nikamwita Henessy na kumtaka akae mahali kuningojea, naja muda si mrefu. Naye akatii. Nikaongozana na mwanamke yule mpaka garini, Van nyeupe yenye vioo vyeusi. Hapo nikagonga mlango, punde ukafunguliwa na mwanaume mwenye kuvalia kapelo.

    Nikamkaba vema mwanamke yule niliyekuja naye kisha bunduki nikamwelekezea yule jamaa mwenye kapelo. Tukazama ndani ya gari.

    Swali la kwanza nikawauliza wametumwa na nani. Hapo nikiwa nimehakikisha kuwa uso wangu unaogofya.

    “Hamna mtu aliyetutuma,” akasema yule jamaa. “Ni sisi wenyewe ndiyo tumekuja hapa.”

    “Kufuata nini?”

    Kabla jamaa hajanijibu akamtazama kwanza mwenzake. Hapo nikaongezea nguvu kwenye kumkaba mwanamke huyo mpaka kusikia akikoroma.

    “Tulikuwa tumemfuata Henessy!” akaropoka jamaa. Nikamuuliza, “Mnamtakia nini na mumpeleke wapi?

    Jamaa yule akanyamaza akiwa anantazama. Nikarudia kumuuliza swali langu, hakunijibu, badala yake akaniuliza, “Wewe ni ajenti wa CIA, sio?”

    “Jibu nilichokuuliza!” nikamwamuru. Lakini hakuonyesha sura ya hofu, hata akatabasamu na kuendelea na maneno yake, “Hautafanikiwa kwenye hili,” akasema. “Una kazi ngumu sana, ajenti.”

    “Nami ndizo hizo ngumu napenda!” nikamjibu kisha nikamfyatulia risasi kuparaza sikio lake la kushoto. Haraka akalidaka sikio lake hilo akilalama kwa maumivu makali! Yule mwanamke nikamgonga na kitako cha bunduki chini ya kisogo chake, akazirai!

    Nikamfuata yule mwanaume na kumkwida shati, bado akiwa analalama kwa maumivu makali sikioni, nikamwamuru anijibu maswali yangu!

    “Ajenti!” akaniita. “hata kama nikijibu maswali yako haitasaidia kitu.”

    “Mambo ya kunisaidia au kutonisaidia nayajua mwenyewe. Nijibu kabla sijazibua sikio lako jingine!”http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Bado akawa mgumu. Nikageuza kitako cha bunduki na kumtwanga nacho kwanguvu kwenye shina la pua. Akapiga kelele za maumivu akidaka pua yake ambayo ilikuwa inachuruza damu.

    “Mmetumwa na nani?” nikafoka kumuuliza. Alikuwa analalama kwa maumivu mikono yake iliyoziba pua ikijawa na damu lakini bado akawa mbishi! Hakutaka kusema.

    Nikabana mikono yake na kumkandika tena kitajo cha bunduki kwenye pua yake yenye maumivu. Damu zikamruka akilalamika kwa maumivu makali. Akalia sasa kama mtoto uso wake ukiwa umefunikwa na damu nyingi.

    Nikarudia kumuuliza, “Mmetumwa na nani!”

    Bado akawa hasemi. Akalia na kulia tu kwa maumivu anayoyapata. Basi nikamkamata tena mikono yake ili nikamndike tena pua. Hapa akapiga kelele kali, “nasema! Nasema!”

    “Sema!” nikamkaripia.

    “Tumetumwa na Adolfo!”

    Hapa nikamkumbuka yule jamaa niliyemkamata na kumtesea kule hotelini. Kabla hajazirai alisema jina la Rodolfo. Ina maana ndiye huyu Adolfo? Nilipomuuliza huyu jamaa zaidi akasema ni Adolfo. Basi nilikuwa nimesikia vibaya toka kwa jamaa yule siku ile.

    Ila Adolfo ni nani haswa? Na kwanini anatufuatilia? Nilipomuuliza hilo, akashindwa kujibu. Nadhani nilikuwa nimemkandika sana. Nilimwona amelegea. Na hatimaye akazirai macho yakiwa hayajafumba vema.

    “Shit!” nikapiga dashboard. “Sasa nitapata wapi taarifa za Alfonso?”

    Kwa muda kidogo nikapata kufikiri. Nilihitaji sana kumjua huyu Alfonso.



    **



    Nadhani ilikuwa imepita lisaa tangu tutoke ufukweni mimi na Henessy kwa kutumia van ya wale wavamizi waliokuja kututeka.

    Tulipoenda ilikuwa mbali na mji, mbali na purukushani za watu, na huko nyuma ya gari tulikuwa tumewabebelea wale watu wawili, mwanamke na yule mwanaume ambao bado hawakuwa wamepata fahamu.

    Basi tukiwa hapo, nikawa nateta na Henessy nikimdadisi kwa maswali kadhaa kadhaa juu yake na mama yake. Hapo ndiyo nikapata kujua kuwa hata alipokuwa kwenye mikono ya watekaji, yeye pamoja na mama yake, alikuwa akipewa simu acheze ‘game’ lakini kwa uangalizi maalumu.

    Game alipendalo, Subway Surfers. Hata hapo aliniuliza kama simu yangu ina credit apate kulipakua toka mtandaoni.

    Laiti kama wale watekaji wale wangelijua kuwa game hilo ndilo lilikuwa njia ya kuwapata, wasimgeruhusu Henessy ashike simu yao.

    “Kuna muda nilikuwa naboreka sana,” alisema Henessy. “Ningekaa kwenye kona nikiwa sina raha, basi angekuja mmoja wao na kuniambia shika ucheze!”

    Nikatabasamu nikimwangalia. Alikuwa mtoto mchangamfu na mwenye akili. Hakustahili kupitia yote haya. Kweli dunia haina usawa. Nilimfinya shavu lake nikimchekea kisha nikampatia simu yangu acheze game lake.

    “Baba yako yuko wapi, Henessy?”

    “Hayupo!” akanijibu akibofyabofya simu.

    “Yuko wapi?”

    Akapandisha mabega pasipo kunena jambo.

    “Henessy, unamjua baba yako?”

    “Ndio. Mama aliwahi kunionyesha picha zake.”

    “Hujawahi kumwona kwa macho?”

    “Aaahm!” akatulia kidogo. Kuna kitu kilikamata macho yake kwenye simu. Alipotulia akaendelea kunena, “Baba yangu ni mtu wa kusafiri sana. Anashinda muda mrefu akiwa kwenye ndege na kwenye mabasi, hivyo amekuwa akija nyakati za usiku nikiwa nimelala tayari. Mama huwa ananiambia.”

    “Mara yako ya mwisho kumwona ilikuwa lini?” Akatulia kama hajanisikia. Alikuwa akitazama simu kwa umakini. Punde akanionyeshea kioo cha simu akiniambia, “ona alama zangu!” kisha akacheka. Nikamtazama nikitabasamu. Alikuwa anafurahia sana kile anachokitazama na kukicheza simuni, nikaona maongezi yetu hayatafika popote pale. Acha nimwache acheze baadae tutaongea.

    Kidogo, nikasikia mtu akijigeuza garini. Kutazama nikamwona yule mwanamke akirejea fahamuni. Alipotazama vema akanikuta ni mbele yake nikimnyooshea mdomo wa bunduki. Sura nimekunja kibabe, na nikasema maneno machache kwa kumaanisha,

    “Umeona kilichomtokea mwenzako?” akageuza shingo kutazama mwili wa mwenzake kando. “kitakutokea na wewe endapo utaleta ujuaji.”

    Akakunja uso wake kwa hofu akisema, “mimi sijui kitu!”

    Nikatabasamu kikebehi, “acha kunifanya mjinga. Kwahiyo ulitufuata kwa bahati?”

    Nikamdaka mkono na kumvuta kumketisha kitako. Nikamwambia, “Mwanamke, sina mzaha na wewe. Ni aidha unambie ama nikulaze hoi. Chaguo ni lako!”

    Macho yake yakajawa na machozi. “Nini unataka kufahamu toka kwangu?” akaniuliza.

    “Kila kitu unachodhani nastahili kujua!”

    “Mimi si rafiki yake Britney. Nilikuongopea tu.”

    “Kwanini uliniongopea? Nani alikutuma?”

    Akanionyeshea yule mwanaume aliyelala hajitambui pale kando.

    “Kwanini alikutuma?”

    “Sijui! Alinambie nimteke huyo mtoto.”

    “Alafu?”

    “Nimpatie!”

    “Mlijuaje kama tupo pale ufukweni?”

    “Tulikuona ukitokea ubalozini. Walikuwepo hapo wakijua utafika tu.”

    “Wakina nani hao?”

    “Huyu jamaa na wenzake! … mimi sihusiki. Kweli nakwambia!”

    Nikamtazama kwa macho makali kwa sekunde tatu alafu nikamuuliza, “Alfonso ni nani?”

    Alipotaka kusema hajui, kabla hajamalizia kauli yake, nikamkita na kitako cha bunduki pembeni ya jicho lake la kushoto, “Shenzi!”

    Akalia kwa maumivu. Alivuja damu. Nikamdaka nywele zake kwanguvu na kumuuliza tena, “Alfonso ni nani?”



    ***





    Jicho lake la kushoto lilivilia damu. Kweli aliumia. Ila sikumwonyesha uso wa huruma bali ule uonyeshao kuwa mengi yanafuata hapo mbele endapo akiwa mkaidi.

    Akalia kwa muda kidogo. Na mafua akapata. Akan’tazama na kunambia kwa uso mtakatifu, “Simjui Alfonso mimi!”

    Nikamdaka nywele zake kwanguvu sana kisha nikamuuliza amemjuaje Britney? Na zile soga alizokuwa ananipa je? Akasema alidanganya! Yeye si rafiki wa Britney kama alivyosema. Yote aliyosema alidanganya.

    Na vipi kuhusu Henessy? Alimjuaje? Nikapata swali. Nacho akaniambia hakuwa anafahamu lolote lile kumhusu. Yote hayo alipandikiziwa mdomoni akayaseme.

    “Nani alikupandikizia hayo?” nikamuuliza.

    “Huyu!” akaninyooshea kidole yule jamaa aliyelala kando. “Ni huyu hapaa!”

    Lakini hapana! Mimi haikuniingia akilini kuwa mwanamke huyu hajui lolote kumhusu Alfonso. Ni kwamba tu nguvu yangu haikutosha kuondoa gamba lake alimojifichia.

    Hivyo nikaona kuna haja ya mimi kuongeza ‘pressure’ kidogo niuone uhalisia. Endapo akifaulu jaribio hilo basi ningemwacha huru.

    Nikadaka mkono wake wa kulia na kuvunja kidole chake cha mwisho! Kat! Akapiga yowe kwa maumivu makali. Sikumwonea huruma, nikadaka tena kidole kinachofuata akiwa anajitetea kujikomboa, nacho nikakiminya kukivunja, akapiga kelele, “Najua!”

    “Unajua nini?” nikamuuliza nikiendelea kubinya kidole hicho karibu na kukivunja.

    “Namjua Alfonso! Tafadhali niachie!” nikamwachia na kumwambia, “Enhe, ni nani na wapi alipo?”

    Akatetema kwanza kwa kilio akitazama kidole chake kilichokuwa kimepinda. Akajaribu kukishika, akaishia kulalama kwa maumivu. Akavuta makamasi na kun’tazama kwa hasira na ghadhabu yenye maumivu ndani yake, “wewe ni mnyama!” akasema.

    “Mwanamke, sina muda wa kupoteza na wewe,” nikamwonya. “naweza kuwa mnyama wa kupeti ama wa kukutafuna kutokana na mienendo yako. Sasa utasema ama tuendelee kumalizia vidole?”

    Akajifuta makamasi na mkono wake wa kushoto kabla hajaanza kusema,

    “Alfonso ni bosi wetu, anaishi huku Berlin, Ujerumani. Anatulipa vizuri sana, na ametuahidi kutulipa zaidi tutakapomaliza kazi yetu.”

    “Kazi gani hiyo?”

    “Sikia, ajenti. Mimi sijui mengi sana, na ukinilazimisha niseme hivyo hivyo nitaishia kukudanganya. Ninachojua ni kwamba, Alfonso anamhitaji huyo mtoto, Henessy. Ndiye pekee aliyebakia baada ya mama yake kufariki.”

    “Kwanini anawahitaji hao watu? Wa kitu gani?”

    “Kwasababu ya Raisi! Raisi wa Marekani. Hii ni familia yake Raisi. Henessy ni …” nikamsihi apunguze sauti yule mtoto asisikie. “Henessy ni mtoto wa Raisi!”

    “Unatania, sio?”

    “Unauona huu ni muda wa matani, ajenti? Nikiwa nimevunjwa kidole na kubabuliwa kichwa?”

    “Umejuaje kama hii ni familia ya Raisi? Hamna mtu anayelijua hilo!”

    “Ndio ujue sasa kuwa ajenti hakumaanishi kujua kila kitu kuhusu Marekani. Hata Secret Service hawaitambui siri hii. Hii ni familia ya siri!”

    “Lakini …”

    “Sikia, unafahamu kuwa Britney alikuwa ni pornstar, mcheza picha za ngono maarufu, unadhani Raisi gani angebeba sifa hiyo? Tena amezaa naye! Angemwambia nani juu ya hilo? Huoni ni kujichafua, kuchafua chama, kuchafua taifa? … ndiyo maana ni familia ya siri! … Raisi alikuwa ana mahusiano na Britney! Mcheza sinema za ngono!”

    Habari hii haikuwa ya kawaida. Lilikuwa ni jambo kubwa tena likisemwa ndani ya van ya kawaida, nchi ngeni! Likikuwa ni jambo nyeti la kuteka vichwa vya habari ulimwengu mzima!

    “Una uhakika na unachoongea?”

    “Ajenti, kwa akili yako unadhani kuna haja gani ya kusumbuka na mcheza ngono? Sisi si ISIS au Boko Haram useme tunateka raia yeyote wa Marekani!”

    “Sasa kwanini Alfonso anataka hii familia? Na Raisi yupo wapi?”

    Nilikuambia awali, mimi sijui mengi. Na hata huyu uliyemziraisha hapa, hatokueleza kipya. Wote tunachojua na tulichopewa kufanya ni kutafuta familia hii na kuiweka mikononi mwetu. Hayo mengine, anayajua Alfonso tu!”

    “Niambie wapi anapatikana.”

    Kabla hajasema akasita kidogo.



    ***



    Basi safari yangu ya kurudi Marekani jioni ya hii siku ilibidi niifute ili nipate kufuatilia haya yaliyojiri.

    Nikiwa nimevalia nguo nyeusi ambazo nilizikwapua toka kwa yule jamaa wa kwenye van, nikashuka toka garini na kusonga kuifuata nyumba fulani kubwa inayopatikana upande wa magharibi wa jiji la Berlin.

    Nyumba hii ndiyo ambayo nimeelezwa kuwa ya Alfonso kwa mujibu wa mateka wangu. Kwahiyo nilikuwapo hapa nikiwa natarajia kupata majibu ya maswali yangu mawili, mosi, kwanini Alfonso anawinda familia hii ambayo nimeambiwa ni ya Raisi, na pili, Raisi yupo wapi? Niliamini atakuwa ana fahamu!

    Nikaudaka ukuta huu mrefu na kuukwea, kisha nikatumbukia ndani. Kwa ufupi, labda tuepushe kupoteza muda, nilitumia kama dakika nane kufika nilipokuwa natakiwa kuwapo. Na huku safari yangu hiyo ikiwa imegharimu maisha ya watu watano.

    Ilikuwa ni usiku wa saa tano, na tofauti na nilivyokuwa nawaza, nikamkuta huyu jamaa ambaye niliamini kuwa ni Alfonso, amelala akikoroma!

    Nikamuwekea silaha kichwani na kumnong’oneza aamke kwani nina maongezi naye machache. Alipoamka akashtuka kuonana na sura ngeni. Japo sikuwasha taa, tulikuwa tunaonana vizuri kwasababu ya mwanga wa taa za nje.

    Mwanaume huyu alikuwa wa makamo ya hamsini kwa umri japo nywele zake hazikuwa na tembe ya mvi. Mnene kwa umbo lakini anayejiweza. Alikuwa anazungumza kiingereza vizuri kwa lafudhi ya kimarekani hivyo nikajua moja kwa moja ni wa nyumbani..

    Akajivuta akiketi kitako kisha akan’tazama, pasi na woga, akaniuliza, “Unataka nini kwangu muda huu?”

    Kabla sijamjibu, yeye akaendelea kunena, “Sikia, ajenti.” Sijui alijuaje kama mimi ni ajenti. Pengine kwa namna nilivyozama ndani. Akiwa ananinyooshea kidole, akawa anasema, “kama umekuja hapa kwa kudhani nina majibu ya maswali yako na ya nchi yako …” akabinua mdomo, “hesabu umefeli!”

    “Maswali gani unayoyaongelea wewe?” nikamuliza. Akagunia kifuani. “Sijui Raisi wa Marekani alipo, sawa?’ akanambia akin’kodolea macho. “Kama wewe tu, sijui Raisi wenu alipo! Kama umekuja hapa kuniuliza hilo, basi umefeli.”

    Nikaketi kitandani. Sikuamini anachokisema, najua hata mwizi ni ngumu kukiri alhali umemkamata na ngozi.

    “Alfonso, haujui Raisi alipo ila unafahamu familia yake. Sio?”

    “Ajenti, nimefanya kazi na namiliki klabu nyingi za usiku jijini Los Angeles na Miami. Huko wanawake wanacheza uchi na wengine kujiuza. Britney alikuwa ni mfanyakazi wangu kwa miaka mitano. Unadhani kipi ambacho nisingekijua?”

    “Kwanini ukamteka? Yeye pamoja na mwanae!”

    Akatikisa kichwa na kusema, “Ungeniuliza kwanza kwanini nipo Ujerumani?”

    Kabla sijamuuliza hicho alichosema nimuulize, akakijibu yeye, “Nipo huku toka Marekani, ajenti. Kwasababu ya sera za mbovu za Raisi wako juu ya wawekezaji. Amenifilisi sana. Ameniangusha kiuchumi na sikudhani kama ningekuja kusimama tena. Kwa miaka yake miwili tu, ilitosha kunidhoofisha haswa. …

    Ajenti, unadhani nilikuwa tayari kurudi nilipotokea baada ya miaka mingi ya kujenga mfuko wangu?” akatikisa kichwa. “Hapana, siko tayari kupoteza yote ndani ya mfumbo mmoja wa macho. Kumteka kwangu Britney na mwanaye, ni kutaka pesa yangu irudi! Arudishe yale yote ambayo amenipotezea.”http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Kwahiyo umeshapata baada ya hapo?” nikamuuliza.

    “Aaaahmm .. kidogoo!” akanijibu akifumba jicho lake moja. “Ila si kama nilivyokuwa nikitarajia. Kama unavyojua, Raisi amepotea. Wapi nitapata pesa?”

    Sikumwamini maelezo yake. Niliona kuna haja ya kumsafirisha nimpeleke Marekani akatoe maelezo zaidi. Lakini akanitahadharisha, “Nikirudi Marekani, kila mtu atajua Raisi alitembea na kuzaa na mcheza sinema za ngono maarufu. Nadhani unajua itakuwa ni aibu kiasi gani!”

    Nikamtazama mwanaume huyo kisha nikamuuliza, “Alfonso, Raisi yuko wapi?”

    Akanipandishia mabega, “sijui! Ajenti, sifahamu hilo!” akasema akin’tolea macho. “mimi mwenyewe natamani apatikane nipate pesa yangu!”

    Hapa nikajikuta nanyong’onya. Nilidhani hatua hii itakuwa ya karibu kufikia lengo, kumbe nalijidanganya. Bado nipo mbali!

    Sasa na wale waliokuwa wanawashambulia wakina ajenti Daniele kule Marekani, kumuua pia O’Neil, ni watu wengine? Watu wasiohusiana na Alfonso?

    Kwa muda nikajikuta nikisahau kama nipo kwenye nyumba ya maadui.



    **



    Nilipomulikwa usoni ndipo nikagutuka na kurudisha akili tukioni. Nikakuna kichwa. Hapa nikambana Alfonso na kumtumikisha twende naye nje kwa usalama wangu. Lakini bwana huyu hakutaka katu hata kunitaka nimuue lakini hatatii agizo langu!

    Akacheka.

    “Bwana mdogo, hutoweza kutoka hai hapa. Ni bora uka surrender!” akanambia kwa kebehi. Nami nisitake maneno mengi, nikafyatua risasi mbili za upesi pembeni na kichwa chake. Nikamtengenezea maumivu makali sikioni, na kama haitoshi nikamtwanga risasi ya mguuni kisha nikaketi kando yake.

    “Haya sasa tukae, utakufa taratibu kwa kupungukiwa na damu!”

    Bwana huyo akawa analalama sana kwa maumivu. Huku masikioni na kule miguuni. Alivumilia sana na hakukuwa na wa kumsaidia kwani walinzi wake wasingeweza kuzama ndani kwa kuhofia nitammaliza kabisa mkuu wao.

    Nami nisiwe na habari yoyote, nikatoa risasi zangu toka kwenye bunduki, nikibakisha tatu, kisha nikizirudisha tena ndani ya bunduki. Nilipofanya mchezo huo kwa dakika kama tano, nikasimama na kuanza kupekua chumba cha Alfonso.

    Alfonso akaniita na kuniambia, “Ewe ajenti, nipeleke hospitali kabla sijafia hapa. Huoni kitanda changu kimefurika damu?”

    Nikamtazama na kisha nikaendelea na msako wa mule chumbani. Nikamjibu pasipo kumtazama, “Ulijifanya mkaidi, endelea kukaa hapo mpaka utakapoona kuna haja hiyo!”

    Akanisihi, “sikia, mruhusu mmoja wa vijakazi wangu twende nikuonyeshe njia ya kupita chini kwa chini tuondoke hapa. Nakuhakikishia utakuwa salama. Ila uniahidi kunipeleka hospitali!”

    Nikamtikisia kichwa, “Hapana, siwezi fanya hivyo. Hamna mtu mwingine yoyote atakayeongozana na sisi. Ni sisi peke yetu tu!”

    Akaleta ubishi kidogo hapa ila alipoona hali inazidi kuwa mbaya, akakubali. Nikamnyanyua na kutoka naye ndani ya chumba kuelekea chumba kinachofuata ndani ya nyumba hiyo, humo tukazama na kuuelekea mlango mdogo wa sakafuni, nikaufungua na kuzama humo.

    Ilikuwa ni njia ya kutokea nje kisiri. Na mlango huu unawekwa maalumu kwa ajili ya kipindi cha mashambulizi. Hivyo mkiwa mnashambuliwa inakuwa rahisi kwa mkazi kutoroka.

    Tukatembea humo na ndani ya kama dakika nane, tukawa tumefika mahali ambapo niliona kuna mwanga wa kutokea nje. Tukakazana, hapo nikiwa namburuta bwana huyu ambaye hakuwa anajiweza. Alikuwa mdhaifu sana na anayehisi maumivu.

    Lakini kwa namna alivyokuwa amechoka, hakuwa analalamika tena. Alikuwa ameachama kinywa wazi, anatokwa na jasho jingi. Kwa namna nilivyomwona hakuwa anaweza kudumu baada ya lisaa. Ilinipasa nikazane zaidi kama ningelitaka awe hai.



    **



    Nilishamkabidhi mtoto ubalozini na safari yangu nikiwa nimeisogeza mbele kwa siku mbili.

    Alfonso alikuwa hospitalini akipata matibabu, lakini chini ya uangalizi wa kiusalama. Na mimi … nilikuwa hapa mgahawani nikipata chakula cha mchana. Niliagiza kuku wa kuchoma na vegies.

    Si kwamba napendelea sana aina hiyo ya chakula, hapana, ila ndo’ chakula ambacho niliona naweza nikala hapa na kujihesabia nimekula.

    Nilipomaliza, nikaagiza sharubati na kunywa taratibu nikiwa natafakari baadhi ya mambo huku nikitazama picha kadhaa kwenye simu yangu, picha ambazo nilizipiga kwenye baadhi ya vitu vya Alfonso kule kwenye nyumba yake.

    Nikiwa nakaguakagua, simu yangu ikapigwa tokea ubalozini. Nilipopokea ilikuwa ni sauti ya kike ambayo iliteta maneno machache, “Fika ubalozini.”

    Nikalipia bili yangu ya chakula kisha nikaelekea huko upesi. Nikakutana na ‘director’, bwana Phillip, akaniambia baadhi ya mambo ambayo wameyapata toka kwa Alfonso.

    Watu hawa niliwaachia kazi kidogo ya kuulizia na kufuatilia nyaraka halali za bwana Alfonso hapa Ujerumani, ikiwemo pia na akaunti zake ili tuone uingizaji na utokaji wa pesa zake tangu Raisi alipopotea.

    Basi bwana huyu, Phillip kwa jina, akanambia kuwa wamefanikiwa kupata taarifa nilizoagiza. Jambo hili lilikuwa jepesi kwakuwa niliwapatia baadhi ya picha za kadi zake za benki ambazo mimi nilizitolea kule kwenye chumba cha Alfonso.

    Na kwa mujibu wa maelezo ya bwana Phillip, Alfonso alianza kupokea dola laki nane za kimarekani kila mwezi baada ya Raisi kupotea. Hivyo swala hili likanipa tena nguvu kuwa Alfonso atakuwa anajua wapi Raisi alipo. Au basi kama hajui, atakuwa anamjua mtu ambaye anajua.

    Kidogo akili yangu ikaanza kuwandawanda kabla sijaituliza kuskiza maneno ninayopewa.

    “Ni nani ambaye anamwingizia pesa hizo Alfonso?’ nikauliza.

    Bwana Phillip akakuna kidevu alafu akapekua karatasi zake na kunambia, “Anaitwa Payne! Payne Cluster.”

    “Umepata taarifa zake?”

    “Hapana! Tumejitahidi lakini swala hilo limekuwa gumu. Bado tunalifanyia kazi.”

    “imekuaje limekuwa gumu na jina la mwenye akaunti mnalo?”

    “Tatizo hatumii akaunti moja,” akasema Bwana Phillip. “Jina ni moja lakini amekuwa akitumia akaunti tofauti tofauti. Na kunaa …” akachomoa tena karatasi na kuitazama, kisha akanambia, “Ila mara ya mwisho, pesa zilitoka kwenye akaunti yenye jina la Katie Rodwell.”

    “Huyo mmepata taarifa zake?” nikawahi kuuliza. Akabinua mdomo na kutikisa kichwa. “Hapana. Tangu alipotuma pesa hiyo akaunti yake ikafa. Haipo tena!”

    Basi nikaona nisipoteze muda sana, nikachukua taarifa hizi na za maeneo ya uwekwaji wa hizo pesa kisha nikaondoka zangu.

    Kilinichomishangaza ni kwamba, maeneo matatu ya mwisho kwa Alfonso kuwekewa pesa ilikuwa ni Ujerumani! Yaani watu waliomwekea hiyo pesa walitumia benki za hapahapa Ujerumani. Inamaanisha watu hawa wapo hapahapa nchini!

    Sasa nitawapatia wapi? Nikajiuliza. Njia nyepesi ilikuwa ni kwa kupitia Alfonso mwenyewe. Hivyo nikapanga kwenda kumwona.

    Baadae majira ya jioni nikawa hospitalini pembeni ya kitanda cha Alfonso. Baada ya kumjulia hali, nikamuuliza maswali yangu, ni nani Payne na yule Katie ambaye walikuwa wanamwekea pesa kwenye akaunti yake?

    Akakohoa kwanza kisha akaniambia, “ajenti, nikikuambia siwafahamu utaamini?”

    Kabla sijasema jambo, akasema, “Siwafahamu hao watu. Na kama nilivyokueleza hapo kabla, nilikuwa napokea pesa kwa kuwa na familia ya Raisi. Mtu anayeniwekea pesa, mimi sijali. Najali pesa kuingia kwenye akaunti tu!”

    “Alfonso,” nikaita na kuuliza, “mara mbili za mwisho kuwekewa pesa zilitokea Ujerumani. Unanambiaje huwafahamu? Ina maana haukukutana nao?”

    “Sikukutana nao,” akanijibu kwa sauti ya chini. “Siwafahamu kabisa, ajenti. Mimi nalikuwa napokea pesa tu na si kingine.”

    Nikanyamaza nikimtazama. Naye akan’tazama kwa sekunde kadhaa kabla hajaniomba simu yangu aongee na mtu aliyemtambulisha kama binti yake wa pekee. Anahitaji kumwambia juu ya hali yake. Anadhani atakuwa amefanya jema kumjuza.

    “Yuko wapi huyo binti?” nikamuuliza.

    “Marekani,” akanijibu na kuongezea, “Anasoma huko. Yeye hana makosa na sitaki ahusishwe na mambo yangu. Nataka asome na aendelee na maisha yake kwa amani.”

    Mimi, pasipo ajizi, nikampatia simu yangu akapiga. Nikiwa nimesimamishaa masikio, nikasikia, “Halo, Perry. Unaendeleaje? … vipi shule? … Kuna shida yoyote? … nimekumiss sana mwanangu, natazamia kukuona karibuni, naona kuna haja hiyo … hamna shida, kuwa salama mpenzi wangu … niko sawa … kweli … nimepata majeraha kidogo, nikaja hospitali, Berlin … nitakuwa sawa, si kitu kikubwa. Kwaheri … nakupenda.”

    Akanikabidhi simu yangu akitabasamu kwa mbali. Nami nikamuaga na kwenda zangu nikiwa nimeshapanga kufuatilia namba ile alozungumza nayo kwa kumtumia ajenti Daniele.

    Nikiwa njiani, ili nisisahau hilo jambo, nikamtafuta ajenti Daniele na kumjuza juu ya Perry na namba yake. Nikamwamchia kazi hiyo anipatie majibu baadae. Nikaelekea kwenye makazi yangu, kisha nikaanza kujiandaa kwenda kule nyumbani kwa Alfonso. Nilihisi kule kutakuwa na kitu ambacho kitanisaidia kujua wapi pakuanzia kutafuta wale watu ambao walikuwa wanamtumia pesa.

    Mule chumbani, hamtakosekana nyaraka elekezi.

    Basi nikafika huko baada ya nusu saa tu, na kwasababu nilikuwa najua mlango ule wa siri, nikauzamia na kuibukia ndani kisha moja kwa moja chumbani mwa Alfonso.

    Nilifanya kila jambo kwa utulivu na ukimya kweli. Sikutoa hata punje ya sauti. Nikiwa nasakasaka, nikapata baadhi ya makabrasha ambayo niliyapiga picha kwa simu, ila kidogo nikasikia sauti ya gari ikiingia eneoni.

    Nikasonga dirishani na kuchungulia nje. Huko nikaoma BMW x6 nyeusi. Toka kwenye gari hiyo, wakashuka wanaume watatu waliovalia suti. Mmoja wao, hakuwa mgeni machoni pangu.

    Nilihisi nimeona vibaya, ila nilipozidi kuangaza nikagundua nilikuwa sahihi. Bwana huyo hakuwa mgeni machoni pangu! Bwana huyo alikuwa ni yule ajenti ambaye alikuwa anahusika na kumlinda Raisi kisha akapotea kwa kusemekana amefia ndani ya nyumba yake iliyoungua moto!

    Kumbe yu hai!

    Kumbe wanajuana na Alfonso!



    **



    Nikapata hamu ya kujua zaidi. Nikiwa nimejibana humo ndani watu wale wakaingia ndani ya jengo, na moja kwa moja wakaketi sebuleni huko wakiongea na kupanga mipango yao.

    Chumba nilichomo hakikuwa mbali sana na sebule hivyo nikawa nasikia baadhi ya mambo. Na watu hawa walikuwa wakizungumza kwa lugha ya kiingereza, tena kile cha Marekani.

    Wakaongea kwa muda mchache sana, kama dakika tano tu, kisha kikao kikakata, nilichokiambulia kikiwa ni haya machache: mosi, kumhusu Alfonso. Hapa waliteta kwa maneno mawili tu, kuwa wamkute, na baada ya hapo wakagusia swala la malipo, pesa itakuja, na mwisho nikiwa nimegundua kuwa bwana yule ambaye ni ajenti wa Secret Service akiitwa jina la PKP.

    Kidogo, gari lile BMW x6 likawashwa na watu wale watatu wakajikwea kwenye gari lao ma kuondoka. Hapo ndipo baada ya kama dakika mbili tu, simu yangu ikaita. Sauti ilikuwa kubwa kidogo ukizingatia na ule ukimya uliokuwepo. Nikapokea na kunena kwa kunong’ona. Alikuwa ni bwana wa ubalozini.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Akasema, “Ajenti, Alfonso ametoroshwa hospitalini!”

    Sikutaka maelezo zaidi maana sikuwa eneo zuri kuwasiliana hivyo nikapokea habari hiyo na kurudisha simu mfukoni. Kidogo tu, nikasikia mtu akija. Nikahisi mtu huyo atakuwa amesikia ule mlio wa simu yangu. Haraka nikajificha nyuma ya mlango, na punde tu, mlango ukafunguliwa!

    Kutazama, bwana huyo hakuingia ndani, aliangaza kwanza kwa kama sekunde nne, na nadhani alipoona cha kutilia shaka, ndipo akazama ndani. Nilipomtazama nikamwona akitazama kule kwenye droo, mojawapo ilikuwa wazi. Akasonga akitupa mlango kwanguvu ujifunge.

    Bahati hakutazama nyuma, akasonga kwenda mbele. Hapo ndipo mimi nikatumia hiyo nafasi kumfuata bwana huyo kwa ukimya wa hali ya juu. Nilipomkaribia, akageuka, ila akawa amekawia kwani nilimdaka shingo yake na kumtuliza pia nikambana kinywa.

    Alafu kwa usalama wangu zaidi, nikaufunga mlango kwa funguo.

    “Nijibu maswali yangu nami nitakubakizia uhai wako,” nikamwambia bwana yule niliyemuweka kwenye himaya yangu. Naye kwasababu alikuwa amebanwa hakuwa na uwezo wa kunena, ikabidi nimwache kidogo.

    Akahema kwanguvu sana akitoa macho. Nikampatia kama sekunde nne tu, kisha nikamuuliza, “Yule PKP ni nani yenu?”

    Bwana yule akaleta ukaidi. Nami nisifanye ajizi, nikamkaba tena kwanguvu mpaka nilipohisi amepata adabu ndipo nikamwacha na kumuuliza tena, akanijibu ni mshirika mwenzao! Kabla sijapata muda wa kuminya zaidi majibu toka mwilini mwake, huko nje ya chumba nikasikia wakimuulizia bwana huyu. Naye akanambia, “Watakuwapo hapa muda si mrefu na utakuwa mwisho wako!”

    Basi nikawa sina muda wa kupoteza tena hapa, nikamziraisha bwana huyu na kutoka humo ndani upesi. Nikaelekea kile chumba kinachofuata ambacho ndipo penye tundu la kuzamia chini kwa chini kutokea nje. Lakini kufika mlangoni hapo, nikaukuta umefungwa! Nilijaribu kuufungua pasipo mafanikio. Sikuelewa nani ameufunga na kwa muda gani! Na wakati huohuo, nikiwa nasikia sauti ya watu wakija huu uelekeo wangu!

    Hapa nikaona nichukue maamuzi ya upesi. Nikauvunja mlango huu kwa teke la nguvu kisha nikazama ndani na kuukimbilia mlango ule wa dharura. Nikaufungua na kudumbukia humo alafu upesi nikaanza kukimbia.

    Kidogo huko nyuma nikasikia sauti ya watu wakiteta na kufoka, na masikio yangu yakiwa sahihi, watu hao wakazama ndani ya ile chemba ya chini itokayo nje, humo ambapo mimi nilikuwamo!

    Nikakimbia sana. Punde sauti za risasi zikaanza kuvuma kuniwinda. Hata niliposhika ngazi kupanda juu, zingine zikagonga ngazi ile ya chuma na kusababisha kelele kali!

    Nilipotoka nikaendelea kukimbia, kidogo nikawa nimewahepuka maadui zangu nao hawakunikamata tena!



    **



    “Hamna mtu huyo!” sauti ya Daniele ilinguruma kwenye simu.

    “Una uhakika?” nikamuuliza kwa mashaka. “Jina lake ni Perry!”

    “Hayupo huyo mtu!” Daniele akasisitiza. “Tumefuatilia hiyo namba na kubaini haipo huku Marekani ingawa ina ‘code number’ za huku.”

    Hapa ndipo nikajiona mjinga. Alfonso alinizidi maarifa. Yule mtu aliyeongea naye hakuwa mwanaye kama alivyosema, bali mtu wake wa kazi. Na kwa kuongea naye akabaini wapi mwanaume huyo alipo na wakaja kumkomboa!

    Nikawaza sana. Na hapa ndipo nikajenga hoja kuwa Bwana yule ambaye alikuwa ni ajenti wa Secret Service, ndiye ambaye atakuwa anamtumia pesa huyu Alfonso. Asili ya jina lake hilo, yaani PKP, ni Payne, Katie na Perry! Hayo ni majina yake ya kujificha nyakati za haja.

    Hivyo basi, PKP ndiye ‘mastermind’ wa yote haya. Na kwakuwa alikuwaa ajenti anayehusika na kumlinda Raisi basi ni wazi atakuwa anafahamu wapi Raisi alipo!

    Ni lazima PKP atafutwe na kukamatwa popote pale kwa gharama yoyote ile. Pengine akiwa mikononi mwangu nitaelewa mtiririko wa yote haya.

    Nikafika hospitali na kisha ubalozini, nikapata maelezo juu ya namna ambavyo Alfonso alivyotoroshwa. Watu hao wavamizi walifika hapo hospitali kama majambazi kisha wakawaweka watu chini ya ulinzi na kumkwapua mtu wao!

    Hakukuwa na mtu aliyetambulika maana waliziba nyuso zao kwa barakoa. Na tukio hilo lilidumu kwa takribani dakika sita tu, wakawa wameshapotea!

    “Sasa tunafanyaje, ajenti?” akaniuliza director. Nikamwomba simu yake na kufanya mawasiliano na Daniele. Nikamjuza mwanamke huyo atafute kila taarifa anayoijua kumhusu ajenti yule wa Secret Service ambaye alipotea kwenye mazingira ya kutatanisha!

    Aliponiuliza sababu, nikamwambia kwa ufupi tu, bwana huyo yu hai na yupo Ujerumani.

    “Kweli?”

    “Ndio, na anashirikiana na Alfonso.”

    “Sawa. Nitalifanyia kazi!” akamalizia Daniele kisha akakata simu.



    **



    Nikiwa nimeamka na kuoga, Daniele akanipigia simu na kunipatia taarifa zote ambazo amezipata toka kwa yule ajenti. Kumbe jina lake ni Ian Livermore. Amefanyia kazi USSS kwa takribani miaka sita.

    Kuhusu familia yake, haikuwa inajulikana. Hakuwa na mke wala mtoto, wazazi wake inasemekana walishafariki miaka kadhaa huko nyuma.

    Na kuhusu akaunti zake nazo zilishafungwa. Hakuna rekodi yoyote ya kuingia wala kutoka kwa pesa tangu iliposemekana kuwa amekufa!

    Mambo hayo kidogo yakanivunja moyo. Sikuona mwanya wa kupata chochote kitu hapo, ila kwa mwishowe Daniele akanipa tumaini. Anamfuatilia rafiki yake na bwana huyo Ian akitarajia kupata kitu toka kwake.

    “Mpaka jioni ntakuwa na la kukwambia!” akamalizia vivyo kabla ya kukata simu.

    Nami kuendeleza upelelezi wa hilo jambo, nikaanza kutulia kuangaza yale makabrasha ambayo niliyapiga picha kule kwenye nyumba ya Alfonso. Nikitazama na kukagua vema, kuvuta picha kwa ukubwa na kwa udogo.

    Mojawapo ya nyaraka hizo nikagundua ni mkataba. Mkataba huu aliusaini ndugu mmoja anayeitwa Bevin Casen na Alfonso Lundergan. Ulikuwa ni mkataba wa mashirikiano kwa makubaliano ya kulipwa ujira wa takribani dola za kimarekani milioni moja kila mwezi!

    Huyu Bevin Casen ni nani? Nikapata maswali. Nikaendelea kupekuapekua na kuja kubaini kuwa pia kulikuwa na mawasiliano ya bwana Ian. Hapa nikajikuta natabasamu. Angalau nilipata pa kuanzia kumtafuta mtu yule.



    **



    “Ndipo hapa!” akasema dereva uber. Nami kabla sijafanya lolote nikatazama eneo hilo kwa wepesi alafu nikalipia na kutoka ndani ya gari.

    Nikatembea kuvuka barabara. Ila hamaki, gari likaja kwa upesi mno likilenga kunizoa! Nikalikwepa upesi ila likanisukumia kando kwanguvu mno! Sijajikusanya, risasi zikatupwa kwa fujo kunifuata! Moja ikajeruhi paja langu la kushoto!

    Nikajitahidi kunyanyuka, nikipuuzia maumivu, nikakimbia kidogo, ila napo kabla sijafika popote, nikadungwa risasi ya mgongo. Nikapoteza nguvu na kuanguka.





    Sikufahamu nini kiliendelea baada ya hapo, wala sikujua nilikuwa siko fahamuni kwa muda gani, nilikuja kuamka nikiwa eneo la giza! Sikuwa naona mbele wala nyuma yangu, kushoto wala kulia!

    Nikiwa nahema kwanguvu, nikakodoa lakini haikusaidia. Nilikuwa nimefungiwa kitini nisiweze kunyanyuka wala kujitetea. Na kiti chenyewe kilikuwa kimesimikwa chini kiasi cha kutoweza kukinyanyua!

    Nikajaribu kukumbuka nini kilitokea mara ya mwisho, sikuambulia kitu bali maumivu ya kichwa. Sikuwa nakumbuka jambo lolote. Kitu pekee nilichoambulia ni kuhisi maumivu kwenye paja langu la kushoto. Nilikuwa na jeraha hapo, nilihisi hilo, lakini sikuweza kugusa sababu ya mikono yangu kufungwa. Na pia, nilikuwa nahisi maumivu mgongoni.

    Mengine hayo sikuwa naweza ku … mara mlango ukafunguliwa na kusababisha mwanga mkali kuzama ndani na kunichapa usoni. Haraka nikafunga macho yangu na kuyaminya kwanguvu kujitetea na mwanga ule mkali hivyo sikupata kumwona aliyeingia. Lakini nikajua muda ule ulikuwa ni mchana.

    Mlango ulipofungwa, taa zikawashwa kufukuza kiza kile ndani. Hapo ndipo nikamwona mtu yule aliyekuja kunisabahi. Alikuwa mwanaume mrefu mwenye mwili mpana. Alivalia suruali ya jeans, koti la ngozi jeusi, na tisheti ya bluu kwa ndani ikiwa imeandikwa maneno ya njano – “GO **** YOURSELF!”

    Mwanaume huyo akasonga karibu yangu akivuta kiti alichokitwaa konani. Akakigeuza kiti hicho na kuketi akin’tazama. Alikuwa ni mwanaume mwenye miba ya ndevu mashavuni na kidevuni. Nyusi zake pana na lips zake nyembamba, kidogo zikiwa zimemezwa na hii miba ya ndevu.

    Hapa kabla mwanaume huyo hajasema jambo, nikafahamu kinachoenda kutokea. Mazingira haya hayakuwa mageni kwangu. Nimeshapitia mazingira kama haya maishani mwangu, kama si mara nne basi tano. Angalau nikaanza kuvuta kumbukumbu. Na kumbukumbu zangu hizo zikanambia kuwa mazingira hayo huwa hatarishi.

    Huwa yanaambatana na maumivu ya mateso kumlazimisha mtu kuongea kitu ambacho aidha anakijua ama hakijui. Anachohusika nacho ama lah! Lakini sasa mimi nitaeleza nini na kumbukumbu zangu bado hazikuwa zimenijia kichwani?

    Si hicho kilichokuwa kinanipa hofu, bali pia hali ile nlokuwamo ilikuwa ni tishio kwa usalama wangu kwani naweza jikuta nikitoa taarifa ambazo hazitakiwi kutolewa kwa adui!

    Unajua kabla ya kutumia ujuzi wa kudanganya na kulaghai lazima kwanza uwe unaujua ukweli ili ufahamu namna gani ya kuumba katika njia nyingine ya tofauti ambayo inafanana nayo. Sasa mimi sikuwa naujua huo ukweli. Nilitaraji bwana huyu angenitesa sana kuutoa mwilini mwangu, lakini angeambulia damu tu.

    Ila … mawazo haya yalikuwa kinyume. Bwana yule baada ya kunitazama, akaniuliza, “Unanikumbuka?”

    Nikatikisa kichwa, “Hapana.” Akatabasamu kisha akapitisha ulimi wake kusafisha meno. Ungepata kuuona ulimi huo kwenye lips zake ukiwa unatembea.

    Akaniuliza tena, “Unakumbuka mara yako ya mwisho ulikuwa wapi?”

    “Hapana,” nikamjibu.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Nini unakumbuka?” akaniuliza.

    “Mazingira haya,” nikamjibu. “Nadhani sio mageni.”

    “Yapi?”

    “Haya ya kufungwa kamba kitini, na mtu kukaa mbele yangu.”

    Akan’tazama kidogo alafu akanyanyuka aende zake. Nikamwita, “Tafadhali niambie hapa nipo wapi na nafanya nini?”

    Akan’tazama asiseme kitu alafu akaenda zake. Akaufungua ule mlango na kupotea ila saa hii akiwa ameacha taa zinawaka. Nikaangaza huku na huko ndani ya mahali nilipo. Hakukuwa na kitu isipokuwa meza na kiti upande wangu wa kulia, tena kwa mbali.

    Chumba kilikuwa cheusi na kisicho na dirisha. Ila kulikuwa na na viyoyozi ambavyo vilikuwa vinamwaga kipupwe cha baridi. Nikajiuliza hapa ni wapi? Kabla sijapata majibu, tena hata sijachukua sekunde tano, mlango ukafunguliwa akaingia mwanaume mwenye kimo cha kati akiwa anaongozana na mijibaba miwili kwa nyuma.

    Mwanaume huyo alikuwa na mustachi mweupe kama nywele zake za kichwani. Amevalia miwani ya jua na mkononi mwake ameshikilia sigara kubwa. Suruali nyeusi na buti kubwa huko chini.

    Akasimama karibu yangu, kiti na ile meza vikasogezwa karibu naye. Hapa ndiyo nikajua kumbe vitu vile vilikuwa vimetengwa kwa ajili yake. Lakini mbona hakuja yeye mwanzoni na badala yake akaja yule mwanaume mwingine?

    Akili yangu ikaniaminisha kuwa bwana yule alikuwa ametumwa aje kun’tazama kwanza kama najua jambo lolote, kama nakumbuka kitu, na alipoona hilo limefaulu ndipo akaja huyu.

    Kwahiyo hawa ndiyo watakuwa wanahusika na kupotea kwangu kwa kumbukunbu, nikaamini hilo. Nikamtazama bwana yule, naye akintazama akaketi. Akanyonya sigara yake kubwa alafu akantemea moshi pasipo adabu!

    Akaita, “Kijana!” nami nikamtazama pasipo kumsemesha.

    “Najua haukumbuki jambo, nami nipo hapa kukupatia machaguzi mawili ambayo ni juu yako kuchagua.” Aliposema hayo akavuta tena sigara, na tena pasipo adabu, akanipulizia usoni mwangu. Nilimtazama kwa hasira sana na kama ningekuwa na uwezo ningemdaka na kumfunda nidhamu!

    “Moja, ufanye kazi na sisi ukapate nyumba ya kukaa, ama mbili, tukuache ukarande mtaani ukiwindwa kama swala!”

    Nikashangazwa na hiyo kauli. Kwani wanadhani sina pa kwenda? Nikajiuliza. Wanadhani mimi ni mzururaji au? Wanadhani sina makazi wala kazi ya kufanya?

    Nikawauliza, “ninyi ni wakina nani na kwanini mmenikamata?”

    Bwana yule akaniambia, “Sipo hapa kwa ajili ya kuulizwa maswali na wewe. Nipo hapa kukupatia nafasi ya pili, kama uko tayari, sema, na pia kama haupo tayari.”

    “Nitakubalije kitu nisichokifahamu?” nikawauliza. Yule bwana hakujali swali langu, akanyanyuka na kwenda zake kuufuata mlango. Nikapaza sauti, “Ngoja!” akasimama pasipo kunitazama akiendelea kuvuta sigara yake.

    “Nimekubali,” nikamjibu. “Nimekubali kufanya kazi nanyi!” basi bwana huyo akarejea pale kitini kisha akazamisha mkono wake ndani ya mfuko wa koti na kutoa kikopo kidogo chenye tembe nyeupe, akasema, “Unaona hiki?” akitikisa hiko kikopo. “Ni dawa ya kurejesha kumbukumbu zako, na ukifanya kazi yetu kwa takribani juma moja tu, kazi moja tu, utapewa tembe hizi ukaendelee na maisha yako na pesa nyingi mkononi.”

    Aliposema hayo akavua miwani yake, hapo ndipo N jicho moja lililobovu, la kulia, na pia tattoo ya chozi jicho la kushoto.

    “Deal?” akaniuliza.

    Mimi nikamjibu kwa kumtikisia kichwa.



    **



    Leo nilikuwa najua ni siku gani na muda gani tofauti na ile jana yake. Nilipewa chai nzuri na muda wa kupumzika kwenye chumba ambacho ni ‘luxury’ chenye kila kitu akitakacho binadamu. Na pia jeraha langu lilipewa dawa na kufungwa bandeji.

    Sasa ningeweza kutembea, na nadhani hata kukimbia, kwani nilihisi maumivu kwa mbali, na nilitambua kuwa jeraha hilo halikuwa lililonichimba sana. Kama ndani ya majuma mawili ama matatu laweza likawa limepona kabisa.

    Nikiwa hapa sebuleni, baada ya kunywa chai, nikaendelea kuwazia kitu ambacho bado sikuwa nakipatia majibu. Hapa nipo wapi? Hawa watu ni wakina nani? Wanataka nini kwangu?

    Na kubwa zaidi MIMI NI NANI?

    Nikaja tu kuamini kuwa kujiuliza maswali hayo ni kupoteza muda tu maana nisingepata majibu abadani. Inabidi nipate zile tembe. Tembe za kumbukumbu. Lakini sasa nita ….

    Ngo! Ngo! Ngo! Sijajibu, mlango ukafunguliwa, akaingia yule mwanaume aliyekuja kunipa chaguzi jana yake kwenye kile chumba. Kama kawaida alikuwa anaongozana na wanaume wawili waliojaza misuli, akaketi kwenye kochi litazamanalo na langu kisha akaniuliza, “Unaendeleaje?”

    “Naendelea vizuri,” nikamjibu pasipo kutia neno lingine.

    “Sasa upo tayari kwa kazi yetu?” akaniuliza.

    “Kazi gani hiyo?” nami nikamuuliza. Akan’tazama kwanza kabla hajavua miwani yake.



    ***





    “Kumuua balozi!” akaniambia kwa sauti kavu. Nikatoa macho, “balozi gani?”

    “Balozi wa Marekani!” akanijibu kana kwamba ni kazi ya kumuua kuku kisha akanipatia na muda, “ndani ya siku tatu kazi hiyo inabidi iwe imeshakwisha kufanyika.”

    Mimi nikatikisa kichwa. “sitaweza.”

    “Unasema?”

    “Sitaweza!” nikarudia kauli yangu. Basi bwana yule akazamisha mkono wake ndani ya koti na kutoa kile kijichupa cha tembe na kunambia, “Ni uchaguzi wako, kufanya kazi yetu ama kwenda ukawe mbwa huko mtaani!”

    “Ni sawa!” nikawajibu kwa kiburi. “Niachieni huru ila siwezi kwenda kumuua mtu ambaye sijui sababu yake ya kifo!”

    Basi bwana yule akan’tazama kwa kukunja ndita alafu akawatazama wale wenzake wawili. Akanyanyuka akitaka kwenda zake.

    “Niambie mimi ni nani!” nikamwomba.

    Akanitazama pasipo kunisemesha kitu, akaondoka akiniacha na wale wanaume wawili waliojaza miili. Wanaume hao wakanisomba na kwenda kunitupia nje ya nyumba, huko barabarani, alafu kabla hawajaondoka mmoja wao akanambia, “akili itakapokukaa kichwani, unajua pa kurudi!”

    Sikumjali nikaenda zangu.

    Nikatembea ndani ya jiji la Berlin likiwa jipya kabisa machoni mwangu, sijui wapi pa kwenda wala pa kuelekea. Nikazunguka kwa kama masaa matatu kabla sijajikuta ufukweni nikiwa nimechoka.

    Sikuwa nakumbuka kitu! Nilidhani nitakumbuka lolote kwa kutazama watu na majengo lakini haikuwa kama nilivyowaza. Sikukumbuka hata tone ya jambo. Nikawaza niende hospitali na kuwaelezea shida yangu pengine watanisaidia lakini mfukoni sikuwa na pesa. Ni vipi watanielewa?

    Hapo ndipo nikakumbuka hata pesa ya chakula sikuwa nayo. Na nilipokumbuka hayo tu, nalo tumbo likanguruma! Nikaona nifanye stara kutafuta kazi yoyote ile ambayo itanipatia hata vijisenti kabla jua halijazama na kiza kutawala.

    Nikatafuta kwa kupita huku na huko, ila sikufanikiwa kupata kitu, kila nilipoenda hata kuomba kusafisha vyombo, waliniambia hawahitaji watu. Mpaka giza linaingia, sijapata kitu. Tumbo likawa linadai haswa.

    Sikuwa na namna bali kulala vivyo hivyo huko ufukweni. Nilitafuta mahali ambapo pangenikinga kidogo na upepo mkali wa bahari, kakibanda, nikajiegesha hapo nikijikunyata.

    Nikawaza sana sana pasipo mafanikio. Mwishowe usingizi ukanibeba, ila ukiwa ni wa kukatakata. Nadhani sababu ya njaa na kuhisi sipo eneo salama.

    Ukiwa ni usiku mzito, kama majira ya saa saba hivi, nikiwa nimefumba macho yangu, nikasikia sauti ya mwanamke ikipiga kelele. Nikashtuka na kuketi kitako upesi. Nikatazama kushoto na kulia, sikuona kitu!

    Sauti hiyo ikaendelea kulia na kunifanya ninyanyuke kuangaza maana ilikuwa inaomba msaada. Niliposkiza vizuri nikatambua inatokea upande wangu wa mashariki, upesi nikakimbilia huko, kidogo nikawaona wanaume wawili, mmoja alibebelea rungu la baseball na mwingine ana kisu wakiwa wanamkimbiza mwanamke fulani mnene.

    Kidogo wakamkamata mwanamke huyo na kumtupia chini! Mmoja akampokonya mkoba wake kwanguvu na kumwamuru anyamaze kimya.

    Hapo ndipo nikaona kuna haja ya kwenda kumsaidia mwanamke yule. Nikasonga pasipo kujiuliza mara mbilimbili mpaka karibia na eneo ambalo wapo. Nikapaza sauti, “Hey! Mwachieni mwanamke huyo huru!” nilikuwa natumia lugha ya kijerumani. Hicho sikuwa nimekisahau. Basi wanaume wale wakanitazama na kushtuana kwa mmoja kumgusa mwengine bega kisha wakajiandaa kwa kukamatia silaha zao.

    Mmoja, yule mwenye kisu, akanifuata kwa pupa. Akatupa mkono wake wenye kisu, nikaukamata na kuuvunja alafu nikamviringita na kumpatia teke kali la tumbo, akarukia huko!

    Mweziwe kuona hivyo basi naye kurupu akanifuata na rungu lake, naye nikamkabili kwa wepesi kabla sijampokonya rungu lake na kumwadhibu nalo kwanguvu mara tatu, akabaki hapo chini akilalamia maumivu. Kwanguvu nikampokonya mkoba wa yule mwanamke na kumfuata mhanga kumjulia hali.

    Mwanamke huyo kanambia yupo sawa, ni maumivu kidogo ya mgongo ndiyo alikuwa nayo. Nikampatia mkoba wake na kumtakia usiku mwema lakini kabla sijaenda akanishukuru sana na akaniuliza,

    “Mtu mwema kama wewe wafanya nini usiku huu hapa?”

    Nikatabasamu kidogo kabla sijamwambia jibu ambalo kwa namna moja lilimshangaza, “Sina makazi.”

    Akan’tazama kwa huruma.

    “Kweli?”

    “Ndio, nalikuwa nimelala kule ufukweni kabla ya kusikia sauti yako ikiomba msaada.”

    Akan’kagua upesi kabla hajatabasamu usoni mwangu.



    **



    “Hapa ni kwangu!” alisema akinifungulia mlango. Ilikuwa ni nyumba ya ukubwa wa wastani ikiwa imefumbwa na uzio mwepesi wa nondo zilizojenga mistari. Tokea eneo lile ambapo tukio la kukabwa lilitokea mpaka hapa ni kama umbali wa nusu maili.

    “Karibu sana, jisikie huru!” akanambia akionyesha meno yake madogo.

    “Ahsante!”

    Nikaketi kochini na kuangaza kidogo sebule yake ndogo iliyopambwa vema. Nikamuuliza, “Waishi mwenyewe hapa?”

    “Hapana, nipo na wanangu. Watakuwa wameshalala.”

    Akaketi na kuvua viatu vyake. Akanishukuru tena na kisha akanambia, “kama isingalikuwa gari langu kuharibikia huko mbali nisingekuwepo pale kwa miguu. Lakini Mungu wa ajabu, alimtuma malaika wake kuniokoa.”

    Nikatabasamu nisiseme kitu. Akan’tazama na kuniuliza, “Imekuaje hauna makazi?”

    “Hata nikikueleza sijui kama utaamini,” nikasema kabla sijatazama chini. Akan’toa hofu,

    “Usijali, ntakusikiliza.”

    “Sijui kwanini sina makazi,” nikamjibu. “Sijui kwanini nipo kwenye hali hii. Sikumbuki kitu chochote!” nikamweleza kisha kukawa kimya kidogo.

    “Nashukuru maana unenisaidia,” nikamweleza nikimtazama. “Sikuwa na pa kulala. Naomba unisaidie kwa kipindi kifupi, natumai kumbukumbu zangu zitarejea na kila kitu kitakuwa sawa.”

    “Usijali,” akaniambia akinitikisia kichwa. “Utapumzika hapa na tutaangalia cha kufanya.”

    Basi hatukukaa hapo sana maana ulikuwa ni usiku mkubwa na alitaka kupumzika. Akaniacha mimi pale sebuleni yeye akienda chumbani. Nikalala hapo mpaka asubuhi ambapo niliamshwa na makelele ya watoto.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Nilipofumbua macho nikamwona mtoto wa kiume na wa kike. Walikuwa wa makamo sawa, kama miaka mitano hivi. Walinitazama kwa mashaka kabla hawajaendelea na mbio zao kuelekea nje.

    Kidogo akaja msichana wa miaka kumi na, akanisalimu na kisha akaenda zake. Alikuwa amevalia begi mgongoni. Nadhani alikuwa anaenda shule ama chuo. Naye alinitazama kwa maulizo kabla hajapotelea zake.

    Nilipokaa hapo kwa muda kidogo, ikiwa ni majira ya saa tatu asubuhi kwa mujibu wa saa ya ukutani, mwanamke yule mwenye nyumba akanijia. Alikuwa ana tabasamu usoni mwake japo machoni bado usingizi ulikuwa umemjalia.

    “Umemkaje?”



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog