Search This Blog

Sunday 20 November 2022

NYUMA YAKO - 2

 





    Simulizi : Nyuma Yako

    Sehemu Ya Pili (2)





    "Nani anayo?"

    "Yule aliyekupa wewe. Anaitwa Toliso."

    "Hauwezi kwenda mwomba? ... hauwezi ukamwambia kuwa sisi si kama wale waliokuwa wanawadhania?"

    Bwana yule akanyamaza. Akausimika mkuki wake ardhini na kisha kidevu chake akakiweka juu ya kitako cha mkuki. "Si rahisi kama unavyodhani," akanijibu akiwa ameng'ata meno yake.

    "Bwana yule, Toliso, ni mkatili na mkali. Hawezi kunielewa."

    Nikamsogelea karibu na kumshika bega. "Tafadhali, sisi hatuna hatia. Hakukuwa na haja ya kutuadhibu namna ile. Kama kuna namna yoyote ambayo naweza kukusaidia kupata hiyo dawa, nambie nami nitafanya kwa moyo wote!"

    Akatikisa kichwa kisha akafungua kiganja chake. "Kabla hatujaendelea na majadiliano yoyote, nipe kwanza kile ulichoniahidi."

    "Nitakupatia il--"

    "Nipe!" Akasisitiza akinikazia macho , basi nikaona si tabu, nikaongozana naye mpaka kule upande tulioingilia kisiwani. Huko tukute vile vitu tulivyoviacha, mitungi ya hewa na hata hiyo miwani ya kutazamia usiku.

    Bahati tukavikuta, nikamkabidhi. Akajaribisha na kuona ni vema, imempendeza. Akafurahi sana. "Hii nitaitumia kuwindia nyakati kama hizi!" Akasema akitabasamu. Hata meno yake yaling'aa kinyume na kiza.

    Nikamkumbusha, "fanya basi tukapate ile dawa!"

    Akaiweka ile miwani kibindoni alafu akanitazama, "ewe bwana wa manjano, mbona wewe mbishi sana! Huoni kheri nimekusaidia ukaenda zako?"

    "Nitaendaje pasipo wenzangu? Moyo wangu utakuwa mzito!"

    "Sikia ... si kwamba sitaki kukusaidia. Namwogopa sana Toliso. Mkono wake ni mwepesi sana kutoa adhabu. Si mtu anayejishauri mara mbilimbili kummaliza mtu!"

    "Nitakusaidia dhidi yake."

    Akatabasamu, "wewe? ... unadhani unaweza kupambana na Toliso?"

    "Kwanini nisiweze?"

    Akashindwa kujibana na kicheko. Alipomaliza kucheka akaniambia, "mwili wako unaingia mara mbili na nusu ya Toliso. Akikudaka na mikono yake kama mibuyu, atakukamua mpaka hayo macho yatoke nje. Hujionei huruma?"

    "Bwana mdogo," nikamwita nikimtazama. "Nitafanya lolote lile, nitapita kwenye hatari yoyote ile kuwasaidia wenzangu. Naomba tusipoteze muda, tuelekee huko haraka!"

    Akanitazama katika namna ya kunionea huruma. Kwa namna hiyo nikajua ni kwanini anamzungumzia Toliso katika namna ya hofu. Ila nadhani bado nami hakuwa ananijua vema. Hakuwa anajua mimi ni mtu wa namna gani. Tangu tuingie kwenye mikono yao, hajaona vumbi langu. Sikushangaa kwanini alikuwa ananitilia shaka.

    Hakuwa anajua japo mimi si nyani mzee, nimekwepa ncha nyingi za mishale!

    Basi kwakuwa nimemlazimisha na kumsihi sana, tukaenda huko.





    Ilikuwa ni safari iliyotuchukua muda wa dakika kama kumi na tano hivi, tukawasili mbele ya kijumba kidogo, mbavu za mbwa. Nyumba iliyotindwa na majani na kusimikwa na miti minene. Haikuwa na madirisha, mlango ulikuwa wazi.

    Kutoka humo, mtu alikuwa akikoroma sana kana kwamba simba au mtu aliyekabwa. Bwana mdogo yule, ambaye sasa njiani aliniambia jina lake, aitwa Buyu, akaniambia huyo akoromaye ni Toliso. Kijiji kizima wamfahamu kwa tabia yake hiyo, lakini kisitupumbaze kwani amekuwa akisemwa kuwa hulala macho!

    Yaani japo anakoroma hivyo, huwa macho, na kitu kidogo tu chaweza kumwamsha na kumdaka mvamizi wake. Nilijifunza kuwa Toliso ni mtu mwenye kupewa mawazo mengi ya kutisha. Mtu anayeogopwa na kudhaniwa si wa kawaida. Niliendelea kulithibitisha hilo kadiri tulivyozidi kusonga, ila kwangu mimi halikunijengea woga hata kidogo.

    Sikuona kama mtu wa kunifanya nihofie. Nimepita sehemu nyingi nikakutana na wengi wa kunihofisha na wote nikawalaza chini. Atanishindaje huyu wa kwenye ulimwengu wa nyuma?

    Bwana mdogo akanitazama na kuniambia, "sasa nazama ndani, niombee nitoke salama. Na kama si hivyo, usidiriki kujitokeza ukapambana, we nenda zako!"

    Sikutaka kubishana naye hapa, nikamkubalia kazi iende kwa wepesi. Akazama ndani na kwa uangalifu, nikiwa namchungulia mlango akasonga akinyata.

    Alipozidi kuzama ndani nikawa simwoni sasa kutokana na giza, na ndani hakukuwa na mwanga hata kidogo kutokana na ukosefu wa madirisha. Sasa nikawa nategemea masikio yangu kusikia kinachoendelea japo nayo muda fulani yalikosa taarifa kutokana na ukimya wa hatua za bwana mdogo yule, Buyu.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Zikapita sekunde kama kumi hivi, nadhani alikuwa akiangaza kutafuta ile dawa. Kwenye sekunde ya kumi na moja, kwa mujibu wa makadirio yangu, nikahisi sauti ya kitu kikidondoka! Moyo wangu ukafanya pah! Nilihofu huenda Toliso akaamka na kumsababishia matatizo Buyu, ila haikuwa hivyo, nikaendea kusikia sauti ya mtu akikoroma. Angalau nikapata afueni.

    Nikaendelea kutulia nikiskiza. Zikapita tena sekunde tano, hapo ndiyo nikapata jaka la moyo! Sauti ya mtu akikoroma ilikata ghafla na mara sauti nzito ikavuma kusema, "Taris khanje?"

    Na kabla sijasikia chochote, nikaona mwanga umewaka ghafla mule ndani. Hapo nikamwona Toliso akiwa chini ameshikilia taa mkono wake wa kushoto! Taa hiyo haikuwa kama ambayo waijua wewe. Lah! Ilikuwa ni kama buyu lililozungushiwa utepe unaopitisha mwanga, ndani yake kulikuwa na wadudu wadogowadogo wengii ambao mikiani mwao walikuwa wakitoa mwanga.

    Nilishangazwa na sayansi hii! Baadae nilikuja kujifunza kuwa, kuwasha taa hiyo, ni kwa kutikisa hao wadudu waliomo ndani, wakiamka hujiwasha kama ni kiza. Ukiweka buyu chini, basi nao hulala na kujizima!

    Basi kuamka kwa Toliso hakukuwa jambo la kawaida kwa Buyu, hata kwangu pia. Bwana huyo, mzito mrefu na mpana, alisimama akimtazama Buyu ambaye alikuwa amesimama pembeni ya shelfu yake nyeusi. Buyu akahofu sana, nilimwona akitetemeka. Aliwahi kuomba msamaha na kuomba abakiziwe uhai wake. Japo sikuwa najua lugha anayoizungumza, matendo yake yalionyesha hayo niyasemayo.

    Nikamwona Toliso akiweka taa yake chini, kisha akabinjua vidole vyake na kuviliza mifupa. Akanguruma akisema lugha yao ya ajabu kisha akamnyaka Buyu na kumnyanyua juu kwa mkono mmoja!

    Hapo nikamwona Buyu akibadili sura. Hakuwa mwenye huruma tena bali aliyefura hasira. Na akiwa amekabiwa juu, akawa anarusharusha mateke na ngumi ambazo hazikusaidia chochote kwa Toliso! Zaidi mwanaume huyo akacheka na kukodoa macho yake ya kutisha! Akamminya zaidi Buyu.

    Hapo ndiyo nikaona ni muda wangu muafaka wa kujongea kumwokoa Buyu. Nikazama kwa fujo!

    "Mwache!" Nikaropoka. Bwana yule akanitazama na kisha akasema kwa lugha yake nisiyoielewa, akamtupia Buyu chini na kunisogelea. Akanitazama na kutabasamu.

    "Usidhani kama mimi nakuogopa," nikamwambia nikimnyooshea kidole na kumtazama machoni. Alikuwa ni mrefu kuliko mimi. Alinitazama kana kwamba mtoto mdogo!

    Ghafla akanisukumia nje ya jengo lake, nikipaa nikatua chini na kujibamiza mgongo! Mgongo uleule ambao ulikuwa na maumivu ya pale mtini!

    Akanisongea kwa hatua zake nzito, kisha akasimama karibu na mimi. Hapo akajivuna kwa lugha na sauti yake ya kukoroma. Kidogo nikasikia sauti kali ya filimbi! Aliipuliza Buyu. Sikujua ni kwasababu gani. Basi bwana yule, Toliso, akaninyanyua juu na kunisogeza usoni mwake, akanitazama kwa sura ya kebehi.

    Hakuwa anajua 'anadeal' na mtu wa aina gani. Bila shaka alidhani mimi na wale watu anaowatawala tuko sawa. Nikaona sasa ni muda wa kumwonyesha utofauti.

    Hataka nikamkita kwenye 'angle' dhaifu ya shingo, akaniachia na kudaka shingo yake. Hajakaa sawa, nikazunguka na kumzaba teke kali la uso, akadondoka chini kama mzigo!

    Kutazama nikaona watu wakiwa wamejongea hapo. Walikuwa wamebebelea mikuki mikononi mwao, ila hawakunidhuru. Wakawa wamesimama wakinitazama mimi na Toliso. Hapo ndiyo nikajua maana ya ile filimbi ya Buyu!

    Kidogo Toliso akajikusanya na kuamka. Akanyoosha shingo yake kah-kah! Alafu akanguruma na kunifuata kwa hatua pana. Hatua moja tu akawa amenifikia, akarusha ngumi yake, nikaikwepa kisha haraka nikakwea kifua chake na kumtifua na goti la kidevu! Akazubaa kwa maumivu. Nikapaa juu na kumzika na teke la kisogo, akadondoka chini asiamke tena!

    Hapo Buyu akanisogelea na kunitazama kwa mshangao. "Umemmaliza!" Akatahamaki. Akanikumbatia kwanguvu na kunishukuru sana kisha akawageukia watu wake na kuwaongelesha maneno nisiyoyelewa. Baadae ndipo nikaja kujua kuwa Toliso alimwambia Buyu kuwa yeye ndiye aloyewamaliza wazazi wake kwakuwa walikuwa wakaidi.

    Na baada ya kufanya hivyo, akasingizia mateka wa kizungu waliokuja kuvamia kijiji hicho. Basi, katika namna hiyo, nikawa mkombozi! Wanakijiji wakaninyanyua juu kwa shangwe wakiimba nyimbo zao, lakini mimi nikawasihi kwanza wakawasaidie wale wenzangu kule msituni mitini!

    Upesi wakachukua dawa na taa ya Toliso, tukaelekea huko msituni na kuwapatia dawa wale wenzangu. Angalau wakapata ahueni, wakapatiwa pumziko maana walikuwa wamechoka mno! Tuliwakuta wakiwa wamebabuka migongoni. Migongo imekuwa mekundu kama bendera.

    Hivyo usiku huo ukawa umepita hivyo. Nililala kwa uzito sana maana nilikuwa nimechoka sana kwa purukushani, lakini hata hivyo, kama ilivyo kawaida, nikajitahidi kuamka mapema, japo si mapema yangu iliyozoeleka. Niliamka jua likiwa limeshang'aza.

    Kutazama nikaona wanakijiji wakiwa wanaendelea na shughuli zao. Wengine walikuwa wanatwanga, wengine wanakata nyama, wengine wanakata matawi na magome ya miti, wengine wakiwasha moto na kadhalika.

    Mimi nilikuwa ndani ya chumba kidogo, sikujua ni cha nani, tangu nilipoingia usiku mpaka muda huo wa asubuhi sikuona mtu humo, nadhani walinipatia kwa heshima. Nilitoka humo na kuangaza angaza pia kujinyoosha mwili wangu alafu nikamtafuta bwana yule mdogo na kumweleza haja yangu, "naombeni mnisaidie kumsaka Raisi wangu. Naamini atakuwapo maeneo haya."

    Basi kwa kushirikiana na watu wao, tukaanza kusaka kila eneo. Wale wenzangu walikuwa bado wapo mapumzikoni, bado hawakuwa wanajiweza kuzungumka. Tukazunguka kisiwa kizima na baada ya hapo tukazunguka na baharini kwa kutumia mitumbwi yao. Hatukuona kitu kabisa!

    Sasa imani yangu ikaanza kunitoka. Raisi hakudondokea huku. Au Raisi hakuwa kwenye ndege! Sikudhani kama kazi hii ingeanza kwa ugumu mapema hivi ...





    Saa nne asubuhi, jengo la J. Edgar Hoover, makao makuu ya FBI.



    Nilikuwa hapa nikiwa na shida ya kumwona Miss Daniele James, mpelelezi wa ndani wa swala hili la kupotea kwa Raisi. Alikuwa mtu aliyetingwa sana, alikuwa akitoka hapa na kuingia kule, kule na hapa, alipokuja kutulia ilikuwa ni kama baada ya dakika kumi tangu niingie hapo.

    Akanitazama kwanza alafu akachukua faili toka kwenye shelfu, akalipekua upesi na kisha kama mtu anayenidhihaki kwa mbali, akaniuliza, "umepata nini huko, Anthony?"

    Nikashusha kwanza pumzi ndefu, nikatikisa kichwa changu na kubinua lips pasipo kusema kitu. Akatabasamu kwa mbali. Akatazama tena faili lake kwa ukimya kidogo, nikamuuliza,

    "Ni nini wewe umepata?"

    Akanitazama kwanza, akafunga faili lake na kunitazama kwa macho ya kichovu ila yaliyo imara. Akaniuliza, "nikikuambia Raisi ametekwa, utasemaje?"

    "Kwanini unasema hivyo?" Nikamuuliza. Sentensi yake hii ilinivuta na kunifanya niwe makini zaidi. Akakuna kwanza kichwa chake.

    "Anthony, kwa namna nilivyofuatilia na kutazama baadhi ya matukio, natokea kuamini kuwa huenda Raisi akawa ametekwa, tena kabla ya ndege kupaa!"

    "Lakini imewezekanaje hilo?"

    "Sijajua, badi sijalikamilisha jambo hilo. Lakini kwa ushahidi nilioupata, naona niko sahihi kusema ninayoyasema."

    "Naomba basi unijuze," nikamsihi.

    "Usijali, wewe ni mshirika wangu kwenye hili, ila ..." akanitazama akinikodolea. "Unajua hivi sasa upo kwenye ardhi ya Marekani, I am the boss here, sawa? Utafuata yale nitakayokuwa nakuambia na kukuelekeza."

    Kabla sijajibu, akaendelea kumwaga maneno. "Kutokana na utafiti mdogo nilioufanya, nikisaidiwa na Secret services, nimebaini kuwa Raisi alikuwa anaumwa hapa karibuni. Hali yake kiafya haikuwa nzuri sana, tuseme hivyo. Na kama utakuwa ulifuatilia vema utakuwa umegundua hakuwa akihudhuria baadhi ya office matters kwa sometimes."

    "Sikuwa nafuatilia," nikawahi kumhabarisha. "Nilikuwa zangu likizo, na kidogo nikajitenga na mambo haya ya kuumizana vichwa."

    Lengo langu la kumweka bayana ni kumtengenezea mazingira ya yeye kunihabarisha juu ya kila kitu anachokijua. Nilitaka adhanie kuwa mimi ni pipa tupu na hivyo basi anijaze na kila taka anayoijua yeye.

    "Basi kama haukuwa unajua, ndo' nakujuza. Swala hili lilinifanya nifuatilie kidogo hili jambo na kuona ni kwa namna gani linaweza likawa na mahusiano na kupotea kwa Raisi, ila bado sikuona mahusiano ya moja kwa moja."

    "Sasa mbona ukasema Raisi huenda akawa ametekwa?" Nikamuuliza. Akafungua droo yake na kutoa chupa fulani aitumiayo kuhifadhia vikorokoro, humo akatoa mashine ya kumsaidia mtu mwenye pumu kuhema.

    Mashine hiyo ilikuwa imehifadhiwa ndani ya kifuko kidogo kilaini. Akanionyeshea, "unaona hii? Ni ya Raisi!"

    Nikakidaka na kukitazama vema. "Umekipata wapi?"

    "Uwanja wa ndege!" akanijibu akifunga droo yake. "Kilikutwa kikiwa chini. Haingii akilini kuwa kitu hicho kitakuwa kimedondoka kwa bahati tu. Raisi huwa nacho muda wote, aidha mkononi au mfukoni. Na hatua nne toka kilipookotwa, kuna alama mbili za tairi ya gari!"

    Akanitolea picha na kunionyesha. Kwa namna alama hizo zilivyo, ilionyesha wazi kuwa usafiri ulotumika hapo ulikuwa ni mdogo. Kwa mahesabu ya upesi, ni vile vigari vidogo viwavyowandawanda uwanja wa ndege.

    Ina maana kimojawapo kitakuwa kilihusika na kumsafirisha Raisi? Lilikuwa fumbo. Nikiwa natazama picha hiyo, simu yangu ikaita mfukoni. Nikaitoa na kutazama. Ni Jack Pyong! Nikapokea na kumuuliza, "nini shida?'

    "Njoo ofisini mara moja. Una mgeni!" Aliniambia hivyo kisha akakata simu. Nikafiriki kidogo juu ya alichoniambia kabla sijarudisha kichwa changu kwenye ile picha na kisha usoni mwa Daniele.

    "Kuna kingine ulikipata?"

    "Hapana, si rahisi kama unavyowaza, Anthony."

    "Najua. Vipi umefanya mawasiliano na watu wake wa karibu?"

    "Mkewe hayupo kwenye mood ya kuongea. Tangu mumewe aliporipotiwa kupotea, amekuwa wa kulia na kujitenga. Sijajua kwa sasa kama atakuwa radhi."

    "Ni muhimu kuongea naye."

    "Najua, Anthony. Nataka sana kufanya hilo ila siwezi kumlazimisha. Yuko depressed hivi sasa, nadhani muda unaweza kumtuliza."

    "Vipi kuhusu makamu wa Raisi?"

    "Nimeongea naye mara moja. Unajua hivi sasa amekuwa busy sana maana ni yeye ndiye aliyekaimu kiti cha Uraisi. Natazamia kuonana naye hapa karibuni kwa mazungumzo zaidi."

    "Basi utakapoenda huko, usisite kunihabarisha twende wote. Sawa?"

    Akanitazama kwanza kisha ndiyo akasema, "sawa, usijali." Kidogo nikahisi sauti ya mngurumo mfukoni. Ilikuwa ni simu. Nikaitoa na kuitazana, nikaona ishara ya ujumbe toka kwa Jack Pyong. Sikuusoma, nikanyanyuka na kumuaga Daniele.

    "Tutaonana muda wowote!"



    **http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    "Kama utakuwa hujaniitia la maana wewe macho manne, nitakumaliza!" Niliropoka nikiingia ofisi ya Jack Pyong. Ofisi yake na yangu hutenganishwa kwa umbali wa hatua thelathini za mtu mzima. Kwenye upande wa kuingilia ndani ya jengo, ofisi yake i karibu na mlango, ila kwa upande wa kutokea, yangu i karibu. Kama hujalelewa, achana nayo isikuumize kichwa.

    Nilimkuta Jack Pyong akiwa amerelaksi kwenye kiti chake, miguu ameweka juu ya meza na mikono yake ameifanya mto kulazia kichwa. Ana 'swing' kutoka kushoto kwenda kulia, kulia kwenda kushoto. Mezani hapo kuna kopo kubwa la kahawa nyeusi.

    Akanitazama na kutabasamu.

    "Nawe ukaja upesi, sio?" Kisha akacheka na kugonga vivanja vyake. "Mjinga kweli wewe. Mgeni gani huyo wa kuja kukufuata huku?" Hapo nikachomoa simu yangu na kuutazama ule ujumbe alionitumia nikiwa na Daniele,

    'Yule dada wa Hong Kong yupo hapa!'

    Laiti ningeusoma ujumbe huu nikiwa kule kwa Daniele, nisingesumbuka kuja kwa huyu lofa. Ningejua ananidanganya wazi kwani mwanamke yule hakuwa anatambua kama mimi nafanya kazi CIA. Sikumwambia hilo.

    Nikamzaba Jack Pyong kofi la kichwa na kumwambia, "hivi unajua nilikuwa kwenye mambo ya maana?"

    "Yapi?" Akaniuliza kwa masikhara. "Hata hili nililokuitia ni la maana!"

    "Lipi hilo?"

    "Si la huyo mgeni! Huyo mwanamke! ... kuwa mkweli, Anthony. Bado unamkumbuka, sio?"

    Nikavuta kiti na kuketi. Nikamtazama Jack Pyong na kumwambia, "kama kuna kitu nitakuwa nakumbuka kuhusu huyo mwanamke, ni simu yangu tu. Si vinginevyo. Nahisi yeye ndo' alichukua simu yangu."

    "Hapana, Tony," Jack akatikisa kichwa. "Ni moyo wako ndio aliuchukua, si simu!"

    "Jack, hivi kuna muda unaacha masikhara na kuwa serious?"

    Akanyamaza. Akanitolea simu yake mfukoni na kisha kuifungua. Akanipatia. "Ebu tazama!"

    Nilipoangaza nikaona 'chatting' zake na mtu fulani kwenye mtandao wa whatsapp. Nilipotazama picha ya mtu huyo anayechat naye, nikagundua ni yule mwanamke mzungu wa kule Hong Kong! Nikamtazama Jack nikimtumbulia,

    "We macho manne, kumbe ulikuwa na namba yake!"

    "Sikuwa nayo. We huoni mwanzo wa text? ... ni yeye kanitafuta. Hata jina bado sijamtunzia."

    "Amekupataje?"

    Akapandisha mabega juu, "sijui!"

    Nikatazama tena zile jumbe. Walikuwa tu wamejuliana hali na kukumbushiana ile siku. Nikamuuliza, "Kwanini hukumuuliza juu ya simu yangu?"

    "Simu ipi, Tony? ... unadhani ana simu yako?" Jack akaniuliza akinitazama. Akanipokonya simu yake na kuendelea kutext.

    "Anaweza akawa anajua. Jaribu kumuuliza."

    Hakunijibu, kidogo akatulia kisha akasema, "Usijali, anakuja Marekani. Utamuuliza hayo yote."

    "Are you serious?"

    Akanionyeshea simu yake. "Yes, I am."

    Niliposoma hizo texts nikaona ahadi ya mwanamke huyo kuja Marekani mwisho mwa juma. Kidogo nikatahamaki.

    "Sasa ushindwe mwenyewe!" Jack Pyong akasema na kunikonyeza. Pasipo kumuaga, nikanyanyuka na kutoka ndani ya ofisi yake. Huko nyuma akapayuka, "baadae saa tatu tukutane dinner!"

    Sikumjibu, nikaenda zangu. Nilipofika ofisini nikaketi na kuwaza juu ya mambo yale ambayo Daniele alinieleza. Mosi, Raisi kuumwa. Pili, kifaa chake cha kupumulia kuokotwa uwanja wa ndege. Kidogo nikawa nimepotezwa fikirani mpaka pale ambapo mlango wangu uligongwa.

    "Nani?"

    Sikujibiwa, mlango ukafunguliwa. Alikuwa ni mwanamke mrefu mwembamba mwenye miwani mikubwa ya kumsaidia kuona. Mwanamke huyu aitwa Jolene, ni mfanyakazi mwenzangu, yeye akijihusisha kama secretary.

    "Nina ujumbe wako," alisema akinijongea.

    "Sasa Jolene si uwe unabisha hodi?"

    Hakunijibu. Akanitazama na macho yake kama ya paka kisha akaweka kikaratasi mezani na kwenda zake. "Yani mwanamke huyu ana matatizo kweli!" Nikalalama nikiokota kile kikaratasi.

    Niliposoma nikakutana na ujumbe, "NITAFUTE" kisha chini yake kuna namba za simu na anwani ya eneo.



    **



    Nilitaka kumwita Jolene nimuulize kuhusu huo ujumbe ila nikaona si staha. Kwanza kwa namna nilivyomuona ni kama vile amechoshwa, lakini zaidi ya hapo, anaweza akawa hana majibu ninayotaka. Nikafikiri kidogo kisha nikanyanyua simu yangu na kupiga simu ile iliyoandikwa karatasini.

    Ikaita mara mbili na kupokelewa. Kabla sijanena, nikaulizwa, "Marshall?" Sauti ilikuwa 'moderate', si nzito wa nyepesi. Ila ndani yake ilikuwa na mkazo.

    "Ndio, ni mimi. Wewe ni--"

    "Fanya tuonane," sauti ikanikatisha. "Fuata anwani iliyoandika hapo, fika." Kabla sijanema tena, simu ikakatwa. Hapo nikabakia na maswali. Ni nani huyu mwenye kuniamuru kiasi hiki?

    Niliweka simu yangu mezani nikiwaza. Sikutaka kwenda huko. Lakini pia kwanini nisiende? Huwezi jua ... ila nitabainishaje kuwa si mtu mbaya? ... kapata wapi namba yangu ya simu?

    Niliona sasa nina haja ya kwenda kuonana na Jolene kwa maswali haya, lakini sikunyanyuka ujumbe ukaingia kwenye simu yangu, "nina jambo la kukuambia kuhusu Raisi!" Nilipotazama namba, ilikuwa ni ileile niliyotoka kuwasiliana nayo hapo awali.

    Nikanyanyuka na kuweka koti begani, nikatoka ofisini. Kurusha macho kumtafuta Jolene, sikumwona. Sikujibughudhi, nikaelekea nje na kujipaki kwenye gari langu kisha nikatimka kwenda huko kulikoelekezwa kwenye anwani. Kimahesabu haikuwa mbali sana na mahali pangu pa kazi, kama vile kilomita kumi tu.

    Nikiwa barabarani, nikapata wazo la kumshirikisha Daniele kuhusu hili. Kiutaratibu hii ilikuwa ni kazi ya FBI agent, yaani Daniele, ila kwasababu nalipokea wito, sikuona haja ya kuuvuka.

    Nikanyanyua simu na kumpigia. Kwa umbali, toka kule Washington DC mpaka hapa Langley, Virginia, ni maili mia moja sabini na tisa. Kwa mujibu wa taarifa za GPS waweza kutumia masaa matatu kasoro kufika hapa endapo ukitumia usafiri wa gari, kama ndege ni dakika arobaini tu, ndiyo maana haiwii ugumu sana kuonana na Daniele, huko Washington DC.

    Simu iliita kidogo akapokea. Nikamsihi aje huku mikimwelekeza eneo na sababu. Nikahisi kabisa amejawa na hamu. Habari hiyo ilimpa msukumo uliomfanya upesi aniambie, "nakuja!" Kisha akakata simu.

    Nilifanya hivyo si tu kwasababu ya utaratibu, la hasha, bali pia usalama wangu na kesi ile mezani. Endapo basi litakapotokea lolote lile, kuwapo na mtu atakayeweza kutoa taarifa nyuma yangu.

    Basi nikaendesha baada ya hapo, kwa kama dakika kadhaa tu, nikawa nimefika kwenye nyumba elekezi. Ilikuwa ni nyumba ya ukubwa wa wastani, mbele yake kukiwa na bustani ndogo ya majani na maua.

    Kabla sijashuka na kwenda, nikaikagua kwa macho ya wepesi. Nilipojiridhisha, nikatoka garini na kugonga mlango mara mbili. Kidogo ukafunguliwa na mtoto mdogo wa kike, makadirio ya kama miaka nane, tisa ama kumi hivi. Akanitazama kwa kunikagua.

    "Hey, upo na yeyote ndani?" Nikamuuliza. Hakunijibu. Akaendelea kunitazama na kisha akaufungua mlango kwa upana. Nikazama ndani. Hapo nikiwa nimejikamilisha kwa kubebelea bunduki yangu ndogo ndani ya koti kwa dharura ya ulinzi.

    Nikaketi sebuleni. Yule mtoto akaenda chumbani, pasipo kuniongelesha, na punde akarejea akiwa na mwanaume mwenye makamo ya umri wa miaka hamsini hivi kama sijakosea.

    Mrefu na mwenye mwili mpana. Uso wake kama mstatili na kidevu chake ni pacha. Akanitazama kwanza kisha akajongea na kuketi.

    "Anthony Marshall?"

    "Ndio, ni mimi."

    "Karibu. Naitwa O'neil," akanipatia mkono.

    "Nashukuru kukufahamu bwana O'neil. Nimeitikia wito wako."

    Kabla hajaendelea akarusha macho yake dirishani na kisha akaniuliza, "una uhakika umekuja peke yako?"

    "Nadhani ..."

    "Inabidi uwe na uhakika."

    "Sijaangaza kama kuna mtu ananifuata. Hukuniambia hilo hapo awali."

    "Yah! Nilifanya makosa. Hapa unatakiwa kuja mwenyewe, Marshall." Alisema hayo akiwa ananitazama kwa umakini sana kana kwamba mtu anayecheza mchezo wa 'chess'. "Sitaki mtu yeyote aanze kunifuatafuata. Nina mjukuu wa kumtazama. Na maisha yangu napenda yakiwa yangu binafsi."

    Nikatulia na kumuuliza, "Ulitoa wapi mawasiliano yangu?"

    "Kutoka kwa mkuu wako," akanijibu kwa kujiamini kisha akasema, "sikia Marshall, unaweza ukawa haunijui, ila mimi ni mtu ambaye nimetumikia taifa kwa miongo mingi. Inaweza ikawa haina haja sana ya kusema hivyo, ila lililo kuu ni kwamba mimi ni rafiki wa mtu huyo aliyepotea. Huyo ambaye unamtafuta kama nipo sahihi."

    Nikanyamaza kimya nimsikize.

    "Pengine naweza nikawa nahusika na upoteaji wa Raisi. Sasa nalijua na kujilaumu sana kwa hilo. Kama ningelichukua hatua mapema, huenda hivi sasa ningekuwa naye hapa badala yako. Najuta sana..."

    Akanyamaza kidogo. Bado sikuongea. Nilimpa nafasi aendelee kujieleza pasipo kuhukumu kwa wepesi ama kuingilia alimradi alikuwa ameniita kunieleza jambo.

    "Siku mbili kabla ya Raisi hajasafiri, nilionana naye. Hakuwa na muda wa kukaa na mimi sana kwani alikuwa ametingwa na kuna mahali anaenda. Ilikuwa ni upesi tu, na hata alipokuja hapa, hakuwa akiongozana na watu wengi kama mjuavyo, bali na watu wanne tu ambao walikuwa wamevalia suti nyeusi.

    Alifika na ndani ya dakika akawa ameondoka! Mkononi mwangu aliniachia ujumbe huu," akaingiza mkono mfukoni na kutoa kipande kidogo cha karatasi ngumu nyeupe, akanikabidhi.

    Nilipokisoma kilikuwa na ujumbe ulioandikwa kwa kalamu nyeusi ukisema, "NIPO SHIDANI." Nikamtazama yule mwanaume mwenyeji wangu, yeye akaendelea kunena.

    "Sikupata muda wa kumuuliza ni shida gani hiyo ... kama unavyojua, si rahisi kuwasiliana na Raisi. Huwa ni mpaka yeye anitafute. Mara ya mwisho alipon'tafuta, ikawa ni siku yake ya kusafiri. Alimtuma mtu mmoja ambaye hakunieleza jina, na mtu huyo akaja kunifikishia ujumbe mwingine."

    Akaweka kituo alafu akatoa tena karatasi toka kwenye mfuko wa pili. Mara hii huu ujumbe alikuwa ameuandika mwenyewe kwa mwandiko wake akiwa amenakili ujumbe aliopewa na mtu huyo.

    "MUNICH, 2345," ujumbe ulisomeka hivyo. Nilipomuuliza maana yake, akaniambia hajui. Na hata huyo mtu aliyemletea, hakumwona tena tangu hapo.

    "Unaweza ukamtambua mtu huyo ukimwona?"

    Akanitikisia kichwa. "Hata picha zake ninazo."

    "Naomba nizione."

    Akageuza uso wake na kumtazama yule binti aliyenifungulia mlango. Akamtikisia kichwa kwa ishara na binti huyo akaenda chumbani. Kidogo, akarejea na picha mkononi, akanikabidhi.

    Nikazitazama picha hizo. Nikagundua zilikuwa zimetolewa kwenye CCTV camera. Hazikuwa na ubora mkubwa ila angalau ziliweza kutambulika.

    "Ni ajenti wa Secret service," akaniambia bwana yule. Nikazihifadhi picha hizo na kumuuliza, "sasa kwanini wahofia na kuishi hivi kama swala?"

    "Nishakuambia mwanzoni," akanijibu. "Sitaki kuharibu maisha yangu. Hata wewe nimekutafuta kwasababu nahisi rafiki yangu atakuwa anahitaji msaada huko aliko!"

    "Wapi?"

    "Sijui! Na ndiyo maana nikafanya utaratibu wa kukutafuta. Huenda taarifa zangu zikakusaidia! ... na kwa usalama wangu, sitaonana na wewe tena baada ya hapa."

    "Vipi kama nikihitaji taarifa nyingine toka kwako?"

    "Sina taarifa ya zaidi na hiyo, Marshall. Kama nikiipata, basi nitakutafuta kama nilivyofanya leo. Kwani ulijua kama kuna mtu kama mimi?"

    Basi nikamuaga na kwenda zangu, kichwani nikiwa nimepanga kumtafuta ajenti yule wa Secret Service na kisha, kama itawezekana, maana ya ujumbe ule wa MUNICH.

    Nilipozama ndani ya gari na kuendesha kidogo, Daniele akanipigia. Nikapokea na kumwelekeza wapi tukutane. Ndani ya muda mfupi tukawa ndani ya gari langu. Nikamweleza yale niliyoyapata kwa mwanaume yule.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Maelezo hayo yakamfanya atamani sana kumwona yule bwana O'neil. Akanisihi huenda akawa anamfahamu mtu huyo na hivyo basi nimpeleke akahakikishe. Japo nilimwambia bwana huyo hatapendezwa na hilo, hakunisikia. Sikuwa na namna bali kumpeleka.

    Tukachukua kama robo saa kufika. Nikagonga mlango na kuita. Kimya. Nikagonga tena na kuita kwanguvu, bado kimya! Kidogo mbeleni tukagundua kuwa bwana huyo hakuwapo tena hapo.

    Tulivunja mlango na kusaka. Hakukuwa na kitu.







    “Atakuwa ametoroka,” akasema Daniele.



    “hapana,” nikakataa. “sidhani kama huku ni kutoroka bali kujiepusha. Kama nilivyokuambia hapo awali, hakutaka haya mambo?”



    “Kwani ni nini anachoficha?” Daniele akauliza akinishikia kiuno.



    “Anaficha uhai na usalama wake,” nikamjibu na kisha nikatembea kuelekea gari. Naye Daniele akanifuata. Alipoingia tukajadili maswala kadhaa na kunifunza kuwa “Secret Service” hawakuwa wakihusika na upelelezi wa swala hili la upotevu wa Raisi.



    “Kwa sababu za kiuwajibikaji, hawakuhusishwa ili kutoa mwanya wa mkono wa ziada kuwapeleleza hata wao endapo kutakuwa na mahusiano yoyote yale,” Daniele alisema akiwa anatazama mbele kana kwamba gari lipo kwenye mwendo.



    Kisha akanitazama na kuniambia kiudadisi, “tunaweza kwenda Washington?” Sikujibu akaongezea, “inabidi tukatafute taarifa za huyo ajenti wa Secret Service ambaye akimletea ujumbe huyo mzee!”



    Secret Service ni taasisi ya kiintelijensia inayohusika na ulinzi wa Raisi, Makamu wa Raisi na familia zao kwa ujumla. Wao ni chombo shurutishi cha kisheria kama ilivyo kwa FBI japo majukumu hutofautiana. Kwa ufupi taasisi hiyo huitwa USSS.



    “Ni sawa,” nikamjibu Daniele. Niliona wazo lake linapendeza. Inawezekana kumpata ajenti huyo wa Secret Service ikawa ni hatua ya muhimu kwenye zoezi letu. Basi tukaenda huko kwa kutumia ndege. Tulipowasili, tukanyookea moja kwa moja kwenye makao makuu ya United States Secret Service (USSS). Huko tukakutana na Director, bwana Owen Allen, mwanaume mwembamba mwenye masikio mapana, macho madogo na lips nyembamba. Tukamweleza shida yetu.



    Akiwa ameshikilia picha ya mtu tumtakaye, akasema, “huyu alikuwa ni miongoni mwa waliokuwa zamu ya kumlinda Raisi.” Kisha akaminya lips na kufinya macho. “ila siku ambayo Raisi alipotea, hakuwa zamu. Hakuambatana naye.”



    “Sasa yupo wapi?” akauliza Daniele akimtazama Director kwa umakini.



    “Amefariki,” Director akajibu kisha akatupatia picha tatu toka kwenye droo yake. Zilikuwa ni picha za jengo linaloungua kuelekea majivuni.



    “Tunaamini alifia humo. Mwili wake ulipatikana ukiwa umejeruhiwa sana, ngumu kutambulika. Hatukuwa na namnna zaidi ya kuufanyia taratibu za kuuzika.”



    “Na vipi kuhusu familia yake?” nikamuuliza. “hana mke wala watoto?”



    “Hakuwa na mtoto. Alikuwa anaishi na mwanamke ambaye aliachana naye muda mrefu kidogo kabla ya ajali hiyo kutokea.”



    “Una picha ya mwanamke huyo?”



    “Hapana.”



    “Kuna habari yoyote ambayo aliwahi kufikisha kuu ya usalama wa Raisi?”



    “Hamna habari ya kushtua. Zilikuwa ni habari za kawaida kutokana tu na majukumu yake.”



    “Nino chanzo cha ajali yake hiyo? Mmechunguza mkajua?”



    “Kwa mujibu wa wataalamu, ni ajali ya gesi. Bwana huyo alikuwa akitumia gesi kupikia.”



    “Kabla ya ajali hiyo, hakuna dalili au mabadiliko yoyote ambayo bwana huyo aliyaonyesha?”



    Director akabinua mdomo na kutikisa kichwa. Akaongezea, “alikuwa ni mfanyakazi mzuri sana. Sidhani kama anastahili kutiliwa shaka.”



    “Vipi kuhusu bwana ---” nikasita. Niliona si stara kuntambulisha bwana O’neil. Kwa namna hiyo niliona ni kheri nikanyamaza kama ambavyo yeye alivyokuwa anahitaji. Faragha ya maisha yake.



    Basi tukaaga na kwenda zetu.







    ***







    Saa tatu usiku, Mgahawa wa Lemaire, Virginia.







    Mezani nilikuwa na Jack Pyong na mchumba wake, Violette. Tulifika hapo muda si mrefu na hata bado hatukuwa tumeagiza chochote toka kwa mhudumu. Wakati Jack anaangaza macho yake, nikamuuliza, “kwanini mgahawa huu, Jack?”



    “mzuri!” akanijibu kifupi na kisha akaniuliza, “kwani kuna tatizo bwana Tony?”



    “Hapana, ila ni kama vile hamna mgahawa mwingine ndani ya jiji hili.”



    “Tony, hapa kakuita nani?”



    “Wewe!”



    “Na mimi ndiye ntalipia bills, shida yako nini?”



    “Kwani nilikuomba uniite?”



    “Sasa mbona ukaja?”



    Kabla sijajibu, jibu ambalo natumai lingemkera, mhudumu akawa amefika hapo. Mdada mrembo mwenye tabasamu usoni.



    “Naweza kuwasaidia?”



    Tukamuagiza chakula, nami angalau kinyongo changu kifuani dhidi ya Jack kikawa kimekauka.



    “Nadhani sasa hivi ungekuwa kwenye kitanda chako cha baridi umejikunyata. Si ndiyo Tony?” Jack akan’chokoza. Sikutaka kumjibu. Chakula kilikuwa kitamu kuliko maneno yake ya kijinga. Huenda hii ndo’ ikawa sababu yake kupendelea mgahawa huu, chakula cha moto na kitamu.



    “Maisha ya upweke mabaya sana Jack,” akaendelea kuhororoja. “inabidi ufanye namna uwe na pa kupumzikia!” hapa Violette akamwonya juu ya mdomo wake lakini nikijua ni kazi bure maana Jack hatosikia.



    Uzuri sikujali, na kulikuwa na sababu nyingine ya kunifanya nimpuuzie. Chakula. Niliujaza mdomo wangu chakula, nikatafuna nikitazama wateja wengine waliofika hapo.



    Sikukaa muda mrefu, nikasikia sauti ya mtu akikokota viatu vyake. Kabla sijageuka, sauti hiyo ikakoma na mara kutazama, mtu akaniangukia, nikawahi kumdaka! Naye Jack Pyong akainama kama aliyetaka kumdaka. Kumtazama mtu huyo, nikamkumbuka! Alikuwa ni yule mwanamke niliyekutana naye kule Hong Kong!



    Nikiwa katika mshangao huo, mara nikashuhudia Jack Pyong akipiga magoti na kufunua kidude kidogo cha rangi ya zambarau. Akiwa amemtazama Violette, akamwambia, “Utakubali kuwa mke wangu?”



    Violette alikuwa amepigwa na duwaa. Hakutegemea kile kitu. Hata mimi sikutaraji kabisa. Na hapa ndipo nilipofahamu ya kuwa mwanamke yule ambaye tulikutana naye Hong Kong, ndiye aliyeleta pete ile. Kwahiyo, Jack alikuwa ametufanyia surprise watu wawili kwa mpigo!



    Akakumbatiana na Violette na sisi, mimi na yule mwanamke mgeni, tukaishia kupiga makofi na kuwapongeza.



    “Jack, uliwezaje kuliweka siri hili hata kwangu?”



    Akatabasamu. “Nilipanga kukwambia, ila niliona nawe uwe ni miongoni mwa watakaoshangazwa. Vipi? Nadhani umependa wazo langu sio?”



    Nikamtazama yule mwanamke kando yangu. Alikuwa ndiye yuleyule. Macho makubwa, nywele nyeusi. Hakika alikuwa anavutia. Na kwa namna alivyokuwa ananitazama alinifanya nihisi maungio yangu ya mwili hayafanyi kazi.



    “Umekuja kufanya nini Marekani?” nikamuuliza. Akan’tazama na kutabasamu.



    “Kutalii.”



    “Kweli?”



    “Ndio! Kwani haiwezekani? Au Marekani si sehemu ya kutalii kama Hong Kong?”



    “Ni majuzi tu umetoka Hong Kong, itawezekanaje uwe huku kutalii?”



    Akamtazama mhudumu aliyekuwa amefika hapo, akamwagiza kinywaji na kisha akan’tazama kuendeleza soga.



    “Nimekuja kusoma, Tony.”



    “Na unajua jina langu!”



    Akacheka kidogo akifunika kinywa chake. “kwanini nisijue. Uliniambia mwenyewe? .. aah sasa naamini siku ile ilikuwa ni pombe ipo kichwani sio?”



    “Siku gani?”



    “Kule Hong Kong kwenye party!”



    “Tulitambushana mimi na wewe?”



    “Maskini Tony. Ilikuwa ni mara yako ya kwanza kunywa?”



    “Yah! Kama si huyu fala, nisingegusa kilevi!” nikasema nikimtazama Jack Pyong.



    “Kwahiyo haukumbuki hata kama ulinibusu na kunikumbatia?”



    “Nilifanya hivyo?” Nikauliza nikikodoa. Akacheka tena akifumba mdomo wake kwa kiganja. “Kipi sasa wakumbuka Tony?”



    “Nadhani ni sura yako tu. Hiko kitu hakikutoka kichwani.”



    “Kweli, naona.” Alisema hivyo kisha akanitazama akiwa kimya. Kwa muda nikahangaika kutafuta kauli yangu mdomoni. Na kama vile mtu aliyefahamu ‘struggle’ ninayopitia akatabasamu kwambali kisha akaniuliza, “vipi Tony, kuna kitu unataka sema?”



    Kabla sijasema jambo, mhudumu akampatia juisi na mrija. Ilikuwa ni juisi baridi ya tufaha. Hapo akanywa mafundo kadhaa kabla hatujaendelea na maongezi yetu machache. Alijitambulisha kwa jina la Kelly na kama alivyoniambia hapo awali, yeye alikuwapo hapo kwa ajili ya kusoma, chuo kikuu cha Harvard kitivo cha sheria.



    Nilipotaka kufahamu juu ya wapi alipotokea, akanisihi nisiwe na haraka. Kila kitu kitajulikana taratibu.



    “Maisha yangu yapo ‘simple’ and ‘straight’, Tony. Utajua kila kitu ndani ya muda mfupi. Lakini ukiwa ‘interested’.”



    Baada ya hapo, Jack Pyong na Violette hawakukaa sana, wakatuaga wanaenda zao. Jack akanikonyeza akiwa anaenda zake.



    “Sasa,” Kelly akachokoza mada. “Wewe hauondoki? Unalala hapa nini?”



    Nikatabasamu kisha nikatazama saa yangu. Yalikuwa ni majira ya saa tano sasa usiku. Kweli muda ulikuwa umeenda. Nilimtazama Kelly na kumuuliza juu ya makazi yake, akaniambia kuwa amefikia kwenye apartment moja ndani ya Virginia.



    “Kwanini Virginia na si Massachusetts huko karibu na chuo cha Harvard?”



    Akatabasamu pasipo kuonyesha meno. Mashavu yake yalituna na macho yake kujifinya.



    “Kwasababu ndo’ sehemu ambapo nina mwenyeji!”



    “Mwenyeji? Hapa Virginia?”



    “Ndio.”



    “Wapi huko?”



    Kabla hajajibu akaingiza mrija mdomoni mwake na kufyonza juisi.







    .

    .

    Alifyonza akiwa ananitazama, na alipohakikisha hakuna alichobakiza ndani ya glasi, akajisafisha lips zake kwa ulimi kisha akasema, “Nadhani unamjua mtu huyo. Hivyo ni bora kukwambia ni nani kuliko mahali.”

    “Ni nani huyo?”

    “Jack. Jack Pyong.”

    “Serious?”

    “Yah! Yeye ndo’ mwenyeji wangu hapa.”

    “Kelly, umekuwa ukijuana na Jack kwa muda gani?”

    “Kwa muda kidogo …” akatazama saa yake ya mkononi. “Tony, nimekawia. Sipendi kutembea nyakati za usiku. Naomba niende sasa.”

    “Usijali, nitakusogeza na gari yangu.”

    Hatukukaa tena hapo, tukanyanyuka na kuendea usafiri nilokuja nao, tukajipaki na tukaanza safari ya kumpeleka kwake, huko ambapo amefikia. Tukiwa safarini nikaendeleaa kumdadisi juu yake na Jack Pyong.

    “Nilijuana naye kwa muda kidogo. Ni mtu mwenye maneno mengi na mcheshi pia hivyo haikuchukua muda kuunda naye urafiki!”

    Kwahiyo basi kwa mujibu wa Kelly, walikutana na Jack Pyong huko kwenye mtandao wa Facebook na kuwa marafiki. Na kwakuwa walikuwa wote ndani ya Hong Kong basi ikawa rahisi kukutana na kutambulishana. Hapa sasa nikafahamu kuwa Jack alikuwa na mengi ya kunifahamisha kuhusu Kelly. Sikutaka kumchosha mwanamke huyu kwa maswali yangu yasiyokuwa na mwisho.

    Basi baada ya habari hiyo, sasa ikawa ni kama zamu ya Kelly kuniuliza mimi. Aliniuliza maswali lukuki juu ya kile kinachoendelea ndani ya Marekani, haswa kupotea kwa Raisi. Kabla sijaendelea, acha nikuweke wazi kuwa ingawa Raisi alikuwa kweli amepotea, bado serikali ya Marekani haikuwa imekiri hilo wazi.

    Hii ilikuwa ni aibu kubwa kwa taifa kama la Marekani linalosifika kwa intelijensia ya hali ya juu. Ilikuwa ni dhihaka na matusi makubwa kwa taasisi zote za kiintelijensia, ni kivipi Raisi apotee? Hata mtu ukimweleza kuwa Raisi wa Marekani amepotea ni wazi atakuna kichwa chake akijiuliza inawezekanaje?

    Hivyo basi, taarifa zisizo rasmi zilikuwa zikisimamia kuwa Raisi anaumwa na yupo chini ya uangalizi. Kitu ambacho kilikuwa kinyume kabisa na ukweli. Ingawa tulifanya hivyo, lakini bado minong’ono ikazagaa na watu wakiwa wananena hata huko mtaani kuwa huenda wanadanganywa. Mbona huyo Raisi anayesemekana kuumwa, haijulikani yupo hospitali gani na nini haswa kinachomsumbua?

    Hivyo kwa namna moja ama nyingine sikushtushwa sana na maswali ya Kelly. Nilijitahidi kutoonyesha hisia zozote usoni, nikazidi kumpumbaza kuwa Raisi anaumwa na yupo chini ya uangalizi na uchunguzi, na si zaidi ya hapo. Niliendelea kusimamia kile ambacho tulitaka jamii iamini wakati tukihaha kuutafuta ukweli.

    “Ni kweli, Tony?”http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Yah! Ni kweli. Kwanini unnauliza hivyo? Vipi, kuna lolote ulilosikia?”

    “Vipi kama Raisi atakuwa amepotea?” akauliza akiwa anatazama kana kwamba mtu anayetoa masimulizi. “Hivi Marekani itafanyaje? Patakalika kweli?”

    Nikatabasamu pasipo kumjibu. Punde akanisihi nisimamishe gari. “Nimeshafika!” akanishukuru na kisha akafungua mlango wa gari akiniaga. Nikamtazama aelekeapo. Alipotelea njiani nisijue ameenda wapi. Sikujali sana, nikatimka zangu.



    **



    ‘Kuna kitu umepata?’

    ‘Hapana. Marshall, nadhani kuna haja ya kwenda Munich!’

    Usiku huu wa saa sita nilikuwa nachat na ajenti Daniele. Nikiwa nimejilaza kitandani, yeye pamoja na timu yake walikuwa wakihaha kukusanya kila taarifa wanayoweza kupata juu ya swala hili la upotevu wa Raisi kutokana na data tulizopata toka kwa bwana O’Neil.

    Hawakuwa wakilala wala kupumzika, kazi ilikuwa pevui haswa tofauti na kwa upande wangu.

    ‘Kuna haja ya kwenda Munich. Nadhani tunaweza kupata kitu huko Marshall!’ Daniele aliendelea kupendekeza. Na kwakweli niliona kuna haja hiyo japo bado kile kitendawili cha Munich 2345 hakikuwa kimeteguliwa.

    Kidogo nikapata mawazo hapa. Ile namba 2345 ilikuwa inamaanisha nini haswa? Ni mwaka? Masaa? Ama anwani ya nyumba? Njia pekee ya kupata majibu hayo ilikuwa ni kwenda Munich, Ujerumani.

    Na basi Daniele akaniambia kuwa, wakati yeye akiwa huku nchini, atahakikisha anaonana na mke wa Raisi na pia Makamu wa Raisi kwa taarifa na mahojiano zaidi. Ilikuwa ni kama vile tumegawiana majukumu. Kuchati kukaishia hapo.

    Kabla sijalala nikamtafuta Jack Pyong kwa njia ya ujumbe nikimtaka afanye anachokijua kuhusu MUNICH 2345. Nikakaa kusubiri majibu, kama lisaa hivi, kimya. Nadhani alikuwa amelala au yupo busy na mchumba wake. Mwishowe nami nikalala.

    Asubuhi kuamka, majira ya saa kumi na moja, nikakuta ujumbe kwenye simu yangu toka Jack Pyong.

    ‘Ndo nini hiyo?’ sikumjibu. Nikaona kuna haja ya kuonana naye uso kwa uso nipate kumweleza, pia kumjuza juu ya safari yangu kwenda Munich. Basi nikajiandaa na katika majira ya saa mbili asubuhi nikakutana na Jack faragha. Nikamweleza kile ninachotaka kukijua, akaniahidi atalifanyia kazi. Kwa mara ya kwanza alikuwa ameongea la maana.

    Nilipomwambia kuhusu safari ya Munich, nikimshawishi twende wote, hapa akasita. “Nitamwachaje Violette? Unajua ni jana tu nimetoka kumvesha pete!”

    “Jack, kumbuka hii kazi ni kubwa. Tunapigania taifa. Tafadhali fikiria mara mbili.” Kisha nikaondoka nikaenda kukutana na Mkuu wa kazi na kumweleza juu ya mipango yangu, kwenda huko Munich. Jioni ya siku hiyo akanihakikishia kwenda huko kila kitu kikiwa tayari.

    Ilipofika majira ya saa moja jioni, nikawa nipo ndani ya ndege, United Airlines, nikielekea Munich, Ujerumani. Safari itakayonigharimu takribani masaa kama kumi na dakika thelathini. Nikafika Franz Josef Strauss Airport majira ya asubuhi ya saa mbili, nikajipatia chumba ndani ya MOXY Munich hotel nilipopumzikia kabla ya kuanza harakati zangu.

    Nilipitiwa na usingizi nikiwa nangojea ujumbe toka kwa Jack Pyong. Nilikuja kuamka baada ya kusikia hodi mlangoni mwangu ambapo baada ya kusonya, nikajongea mlango na kuufungua. Alikuwa ni mhudumu wa kike akinijia kunieleza juu ya malazi na chakula kisha akaenda zake.

    Baada ya hapo nikaoga na kutoka kwenda kutalii mji wa Munich. Kulikuwa na haja ya mimi kulijua jiji hilo kwa namna fulani kwakuwa nilitarajia kulifanyia kazi. Nikatembea mitaa kadhaa, hata kula nikala huko , chakula cha mchana na jioni. Kwenye majira ya saa mbili usiku, nikapanda usafiri wa uma nirudi hotelini.

    Sikuona haja ya kupanda taksi kwasababu nilikuwa nataka kujua zaidi kuhusu jiji hilo.

    Nikiwa ndani ya usafiri, nikaketi nyuma kabisa nikiwa nimepakana na mwanaume mmoja atafunaye bubblegum. Alivalia koti jeusi la ngozi na uso wake ulikuwa serious akitazama mbele. Kitu ambacho kingenifanya nimkumbuke mwanaume huyo ni namna ambavyo mustachi wake ulikuwa mpana na mrefu, na pengine macho yake ya kusinzia.

    Mbali na hivyo sikumjali sana. Nilipowasili nimapotakiwa kushuka, nikanyanyuka, na yeye huku nyuma yangu akasimama, sikujali sana, nikashuka na punde naye akafanya hivyo.

    Hapa niliposhukia palikuwa na umbali kidogo na hotelini. Tuseme ni kama mwendo wa dakila kumi. Na nilishukia hapa, kwa makusudi ya kuendeleea kuusoma mji kwani niliona ni vema pia endapo nikafahamu eneo linalozunguka mahali nilipofikia.

    Nikatembea nikiwa nimedumbukiza mikono yangu mfukoni. Hatua zangu zikiwa pana ila za taratibu nikirusha macho kushoto na kulia.

    Nikiwa katika zoezi langu hilo, kama baada ya dakika mbili, nikagundua kuna watu wawili wananifuata kwa nyuma. Wote walikuwa wanaume na sikuwaona vema kutokana ma uelekeo wa mwanga. Ila kidogo baada ya kusonga, nikamtambua mmoja wao kuwa ndiye yule niliyekaa naye kwenye usafiri wa basi. Mwanaume mwenye mustachi na koti la ngozi.

    Sikujua wanataka nini kwangu, ila ni wazi niliamini dhamira yao si safi, basi nikaongeza ukubwa wa hatua zangu na mikono nikaitoa mfukoni iwe huru kwa kufanya lolote lile.

    Nilipofanya hivyo nao wakajiongeza. Nikahisi hatua zao zimeongezeka na sasa wanakaribia kukimbia. Hapa nikawaza upesi, je swala langu la kukimbilia hotelini litakuwa na maana? Vipi kama hawajui ninapokaa, si n’takuwa nimewapeleka? Lakini pia nikawaza, je watakuwa ni watu wenye taarifa za ujio wangu wa kigeni katika jiji hili, nchi hii?

    Watakuwa ni watu wanaohusika na kupotea kwa Raisi?

    Maswali haya yakanifanya nisione stara kuwakimbia. Pengine naweza kupata kitu kitakachonisaidia na upelelezi wangu. Basi nikafanya hiyana na kujifichia ndani ya kichochoro fulani. Hapo punde nikawaona wakija, wakaduwaa kutafuta na kutazama.

    Mimi nilikuwa nimejibana nyuma ya ndoo kubwa ya malighafi ya chuma nyepesi, ndoo ya kuhifadhia uchafu. Kwakuwa kichochoro hiki hakikuwa na taa, haikuwa rahisi kwao kuniona. Lakini … walianza kuhisi nitakuwa nimejifichia hapo. Nikawaona wakitazamana na mmoja akamtikisia kichwa mwenzake kisha taratibu wakaanza kusonga wakifuata ndoo niliyokuwa nyuma yake!

    Mikono yao ya kulia niliiona ikiwa imezama kotini. Bila shaka kushikilia bunduki.

    Hapa ikanilazimu nifanye maamuzi ya upesi kuokoa roho yangu.



    **



    Ni upesi nikanyanyuka nikiwa nimebebelea ile ndoo ya taka, nikawatupia! Wakiwa wamedaka na kudondoka nayo chini, nikawawahi nisiwape muda wa kujiandaa. Mmoja nikampoka bunduki na kisha nikamdaka na kumwekea tundu la bunduki kichwani nikimwamuru mwingine aweke silaha yake chini.

    “Fanya upesi kabla sijammwaga mwenzio ubongo!”

    Huyu niliyekuwa nimemdaka alikuwa ni yule mwanaume niliyekuwa naye kwenye basi. Mwenzake, mwanaume mrefu mwenye mwili mpana, akan’tazama kwa mashaka kama mtu ajiulizaye nini cha kufanya.

    “Nimesema weka silaha chini!” Nikamwamuru. “sitasema tena sasa hivi, utaokota maiti ya mwenzako!”

    Basi akainama na kuweka silaha yake chini akiwa anan’tazama kwa kukodoa.

    “Ninyi ni wakina nani?” nikauliza. “Kwanini mnanifuata?”

    Kimya. Hamna aliyenijibu. Nikarudia tena kuwauliza mara hii nikikaza sauti zaidi, lakini haikuleta tofauti! Hakuna aliyenijibu.

    “Sina muda wa kupoteza na ninyi! Kama hamtanipa majibu ya maswali yangu basi nitawamaliza maana haitakuwa hasara kwangu.”

    Nilipomaliza tu hiyo kauli, bwana yule niliyekuwa nimemkaba, akawahi kuudaka mkono wangu wenye silaha, akajigeuza upesi akitaka kufanya shambulio kwa ngumi ila kwa upesi nikamkwepa, na nilipoona yule mwenzake ametwaa bunduki aliyoiweka chini, nikafanya jitihada za haraka za kumdaka mwanaume yule mwenye mustachi na kisha nikajikinga naye.

    Hapo mwenzake akapata kigugumizi cha kufyatua bunduki, nikamtupia risasi mbili na kumlaza chini hajiwezi. Kisha mwanaume yule niliyemkaba nikamziraisha na kumweka begani. Ikanipasa niondoke mapema eneo hilo kwani milio ya bunduki ingewafanya vyombo vya usalama kujongea hapo muda si mrefu.



    **



    Saa moja usiku …



    Baada ya kutoka kuoga, nilijifuta maji na kisha kumjongea mateka wangu ambaye nilikuwa nimemfungia kitini. Alikuwa bado hajarudi fahamuni hivyo nikamwagia maji na kumtaka ajibu maswali yangu kama salama ya roho yake.

    Lakini mwanaume huyo hakuogopa kabisa. Akiwa anan’tazama usoni, akaniambia hatajibu swali langu hata moja. Na nikitaka nimuue pasipo kujichosha. Hapo ikabidi nitafute namna ya kumfanya aongee.

    Nikamnyanyua na kumpeleka bafuni. Nikamvika mfuko wa kitambaa kichwa kizima na kuanza kumwagia maji usoni mwake kumnyima pumzi. Akahangaika sana. Lakini kila nilipouvua mfuko huo na kumuuliza, bado hakuwa tayari!

    Nikamtesa sana mpaka mwishowe akawa amepoteza nguvu kabisa. Macho yalilegea na mdomo akaacha wazi akitapika maji, ila bado hakuwa amenipa majibu ya maswali yangu. Bado alikuwa na roho ngumu!

    Basi nikaona nimpe mapumziko alafu tutaendelea tena muda utakaporuhusu, kwa muda huo nikawasiliana na Daniele na kumwambia yaliyotukia. Naye akaniambia hatua aliyofikia pamoja na timu yake. Siku hiyo alikuwa ameonana na Makamu wa Raisi na pia mke wa Raisi. Wote alifanikiwa kuwafanyia mahojiano lakini hakuna kikubwa alichoking’amua, zaidi mke wa Raisi alikuwa anaumwa na anatazamia kwenda kwao, Australia, kwa ajili ya mapumziko.

    Na zaidi ya yote, alipata taarifa kuwa O’Neil, yule bwana aliyetupatia kiasi kidogo cha taarifa, amekutwa akiwa amekufa huko Massachusetts! Mwili wake umekutwa ukiwa mtupu na ishara ya kupitia mateso.

    Habari hiyo ikanishtua kwa namna yake. Nani atakuwa amemuua O’Neil? Na je kifo chake kitakuwa na mahusiano na taarifa zile alizotupatia?

    Nikamtaka Daniele afuatilie kwa undani juu ya kifo hicho kwani kitakuwa nacho kina mlango wa kutupeleka tunapopahitaji. Basi hata nilipokata simu, nikaendelea kuwaza juu ya kifo cha O’neil. Si bure mzee yule hakuwa anataka kujihusisha na haya mambo!

    Lakini kifo hiko kikanipa maswali sana juu ya wauaji. Je pia watakuwa wanajua kuhusu mimi na taarifa zile za bwana O’neil?

    Mara mlango ukagongwa na kuniamsha toka kwenye lindi la mawazo. Nikanyanyuka toka kitandani na kwenda mlangoni kumkuta mhudumu. Mwanamke mrembo mwenye mashavu mekundu. Aliniambia kuhusu chakula, kipo tayari kwenye hall, lakini kabla hajaenda, bwana yule niliyekuwa nimemfungia bafuni, akaanza kupiga kelele akigugumia!

    Mhudumu akan’tazama kwa hofu, nami kumpoza nikamwambia huyo ni mwenzangu yu hoi anaumwa. Lakini ni wazi maneno hayo hayakumkosha mhudumu, akaenda zake akiwa na sura ya mashaka, na hata mwendo wake ukiwa wa kasi!

    Muda kidogo, kama dakika mbili, mlango ukagongwa kwanguvu. Kabla sijauendea nikauliza, “Nani?” sauti ya kiume ikanijibu, “Staff!”

    Taratibu nikasonga na kuchungulia nje kwa kupitia tundu mlangoni. Huko nikaona majibaba mawili wakiwa wamevalia sare za hoteli. Walikuwa ni walinzi. Hapa nikapata kujua kuwa mhudumu yule alienda kutoa taarifa juu ya sauti ile alosikia chumbani mwangu.

    Nikaufungua mlango, na pasipo kuonyesha lolote usoni mwangu, nikawauliza, “naweza kuwasaidia?”

    “Tumekuja kufanya ukaguzi chumbani mwako!” mmoja akajibu akinitazama machoni.

    “Mtakaguaje chumba cha mteja?” nikawauliza nikiwakunjia ndita.

    “Ndugu, ni jukumu letu kuhakikisha kuna usalama ndani ya hoteli. Kama unaona ni shida, basi tuwaite polisi watekeleze hilo!” akasema yule bwana aliyejielezea hapo awali. Kidogo nikafikiria na kuona ni kheri nikawaruhusu watu hao waingie ndani na kufanya ukaguzi kuliko ujio wa polisi hapo.

    Basi, kama watu wanaofahamu kinachoendelea, wakanyookea bafuni, huko wakamkuta bwana yule niliyemfungia. Wakamfungua kamba toka kwenye kiti na kumweka huru. Kisha mimi wakaniweka chini ya ulinzi wakinituhumu kama mtekaji!

    “Upo sawa?” Mmoja akamuuliza yule bwana waliyemwacha huru. Naye kwa uchovu akawajibu, “nipo sawa, nashukuru.”

    Wakamuuliza kwanini mimi nilimfungia kule bafuni, naye akatoa maelezo ya wongo kuwa nilitaka kumuua kisa nikitaka pesa toka kwake, basi walinzi wakapiga simu polisi kutoa taarifa juu yangu.

    “Huyo anawaongopea,” nikapaza sauti. “ni yeye ndiye anataka kuniua. Yeye pamoja na mwenziwe!”

    Lakini nani aniamini? Mazingira yalikuwa yananisaliti na kuninyooshea kidole kuwa mimi ni muuaji. Basi tukiwa hapo, ndani ya muda mfupi tu, yule jamaa, jambazi, kwa upesi akawadhibiti walinzi wa hoteli na kuwaweka chini ya ulinzi. Alitumia bunduki niliyompokonya. Bunduki hiyo nilikuwa nimeiweka kwenye droo ya kitanda.

    Alipofanikisha hilo, akaninyooshea tundu la risasi na kuniamuru niseme kile kilichonileta Ujerumani. Tena niseme upesi kabla hajanimaliza aende zake.

    Nikamwambia huku nikinyoosha mkono juu, “mimi ni mtalii tu! Sitambui kwanini wanifuatilia namna hii!”

    “Usinifanye mimi ni mjinga! Natambua kinachoendelea na kama uki—” hakumalizia, nikawa nimemtupia stuli iliyokuwa imesimama kando yangu. Stuli hiyo kwakuwa niliitupa kwanguvu, ikafyeka miguu yake na kumwangusha chini! Kabla hajaamka, walinzi wakamuwahi kumpokonya silaha, ila ajabu akafurukuta kwanguvu na kumtupa mlinzi mmoja kando kwa kumkandika teke zito. Na huyo mwingine akamchapa kiwiko na kisha ngumi nzito, akalala kando amezirai.

    Kabla hajateka tena bunduki, nikajitupa na kuunyoosha mguu wangu kuisogezea mbali kwa teke, alafu nikaunyanyua kutaka kumkandika kifuani. Akakwepa. Akajirushia mgongo kunifuata. Akatupa ngumi yake, nikaiyeya, ya pili nikaidaka na kuiviringita! Akajizungusha na kutupa kiwiko, nacho nikakisogezea pembeni na alafu kumdaka shingo yake na kumkaba kwanguvu zangu zote.

    Akatapatapa akituma viwiko vyake. Havikunipata. Ila kimoja kilitifua mbavu yangu na kunipa maumivu makali. Nikavumilia na kuendelea kumkaba. Akatupa tena kingine, hakikunipata, cha tatu kikanitifua tena. Hapo nikashindwa kuvumilia!

    Bwana huyu akajichomoa toka kwenye mikono yangu na kisha akaniadhibu kwa ngumi ya shavu la kulia. Mdomo ukalowana damu. Lakini sikumruhusu achukue bunduki. Alipotaka kufanya hivyo, nikamuwahi kumvuta. Akatupa teke, nalo nikamdaka na kumvuta kwanguvu, alafu nikamrukia mgongoni na kumkaba tena. Mara hii mikono yake niliikandamizia na magoti yangu, hakuweza kufurukuta!

    Akapoteza kabisa nguvu. Macho yakaanza kuelekea juu. Nikalegeza mikono yangu na kumuuliza ametumwa na nani. Kwa mbali nikamsikia akisema, “Rodolfo!” kisha akazirai!



    ***



    Basi nami sikukaa tena hapo kwakuwa polisi walikuwa njiani na mimi sikutaka kusumbuana nao. Nikawaaga wale walinzi, na kwasababu walishaona ya kuwa sina tatizo, wakaniacha nikaenda zangu. Kutoka tu ndani ya hoteli, nao polisi wakafika hapo wakitumia gari dogo. Upesi wakazama ndani.

    Nikasimama hapo kutazama, punde nikaona wakitoka wakiwa wamemshikilia yula jamaa. Wakamzamisha ndani ya gari lao na kutimka. Nikashusha pumzi ndefu na kuendelea na safari yangu.

    Nikajongea kwa umbali mdogo kabla sijasimamisha taksi inipeleke hoteli nyingine. Huko nikachukua chumba namba 289, na kujipumzikia kitandani nikitafakari yale yaliyotoka kujiri.

    Rodolfo ni nani? Nilijiuliza hilo swali. Atakuwa ni mtu wa aina gani huyo na kwanini ametuma watu kunifuata? Hapa nikajikuta nikiamini kuwa Rodolfo atakuwa anahusika na MUNICH 2345. Hata hivyo anaweza akawa anahusika na kupotea kwa Raisi!

    Nikajigeuzia upande wa kushoto nikiendelea kutafakari namna ambavyo matukio haya yalivyosukwa. Huku O’neil anauwawa kwa kuteswa huko Marekani, nami navamiwa na kutishiwa uhai! Hakika hapa palikuwa pana fumbo.

    Mara simu ikaita, nikainyakua na kuiweka sikioni. Alikuwa ni Jack Pyong!

    “Hey Jack, vipi?”

    “Hali si nzuri, Tony!” sauti ya Jack ikaongea kwa kutetemea. Tangu nimjue Jack sikuwahi kumsikia akiongea katika namna ile. Nilihisi sauti yake imetepeta woga ndani yake.

    “Kuna nini, Jack?” nikauliza nikiwa najitengeneza kitandani. Niliketi kitako na kukunja sura kulazimisha umakini.

    “Sijui nini kinaendelea, Tony. Leo nimenusurika kupigwa risasi na mtu nisiyemfahamu!”

    “Serious?”

    “Ndio. Hapa nahofia hata kwenda nje!”

    “Umetoa taarifa kazini?”

    “Hapana, sijatoa. Nahofia, Tony. Nahofia kumhusu Violette!”

    “Sikia, basi fanya hivi, toa taarifa makao, alafu utanambia nini watafanya!”

    Simu ikakata. Hapana, nikaipiga upesi na kuibandika sikioni.

    “Tony, umenielewa?”http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Akacheka. “We fala umeamini nilichokuambia?” Nikanyamaza kwa hasira. Nikang’ata meno yangu nikinguruma. “Jack, unajua mambo mengine usiyaletee masikhara!”

    “Wewe ukiyafanya sio masikhara sio?” akajibu kwa kebehi. Nikasonya na kumuuliza,

    “Sema umenipigia nini?”

    “Nataka nikupe marejesho ya kazi yako! Ile ya MUNICH 2345.”

    “Enhe ni nini umepata?”

    “Vitu vingi tu. Nashindwa kujua nishike lipi niache lipi!”

    “We niambie vyote, nami nitajua cha kufanya…”

    Basi akapendekeza kunambia kimtiririko maana moja laweza pelekea jingine, nami nikatumia akili yangu kukitunza alichoniambia na hata nikapanga kesho yake asubuhi na mapema, kwenda kuitafuta nyumba nambari 2345 ndani ya jiji hili la Munich.

    Mengine utayafahamu baadae… huna haja ya kupapatika, mambo bado ni mengi mbeleni.



    **





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog