IMEANDIKWA NA : EDDIE GANZEL
*********************************************************************************
Simulizi : Msako Wa Hayawani
Sehemu Ya Kwanza (1)
KAMBI YA NDALA.
MWANGAZA hafifu wa mapambambazuko
uliwafanya Luten Dennis Raymond Makete na wenzeke waonekane kama vivuli.Walikuwa katikati ya msitu wa Ndala wakienda mbio za mchakamchaka.
Wote walikua katika vazi kamili la kombati,bunduki mkononi ,mkoba mgongoni.
Rekuruti au 'Kuruta' wanaochukua mafunzo ya Uwanajeshi wa kawaida huamushwa mapema kuanza mazoezi.Lakini wanajeshi wanaojitayarisha kuchukua kozi ya ukomandoo huamushwa mapema zaidi -aghalabu hukesha na kufanya mazoezi usiku na mchana.
Na mazoezi yao huwa magumu kupindukia .Kwani lengo kuu ni kumkomaza mwanajeshi afikie kiwango cha hali ya juu kabisa ya ukakamavu na ujasiri ili awe tayari wakati wowowte ule kuhimili mazingira ya aina yoyote,hata mateso.Kwani iwapo atakuja shikwa na adui hapaswi kutoa siri.Anachopaswa kufanya ni moja wapo tu kati ya mambo matatu:Kuhimili mateso,kutoroka au kujiua.
Sehemu kubwa ya mazoezi yenyewe kwa kweli ni mateso matupu,Kwanza kabisa,mwanajeshi hutakiwa aishi maisha magumu kadri iwezekanzvyo.Kula kwa taabu,kunywa kwa taabu,kulala kwa taabu .Jua liwe lake ,mvua yake,baridi yake.Hakuna cha kukwepa .
Na juu ya hayo,kuna amri za ajabu ajabu ambazo lazima zitiiwe bila ya kusita .Kama vile kutembea au kukimbia msituni usiku wa manane .Kuchimba handaki katika muda mfupi usio wa kawaida .Pengine kwa kutumia zanz zisizo za kawaida,bakuli la mesi au hata vidole vitupu.Kupanda mti ambao pengine hata Nyani asingeweza kupanda.Kuvuka mto ambao mtu wa kawaida asingeweza kuuvuka ,tena na mzigo mgongoni na bunduki mkononi. Na kadhalika.
Baada ya mazoezi hayo ambayo huchukua takribani miezi mitatu,na ambayo hudhihirisha ukakamavu na ujasiriwa mutukabla ya kuchaguliwa kuanza kozi yenyewe ya ukomandoo,mwanajeshi hutakiwa adhihirishe pia kiwango cha hali ya juu cha werevu,busara,maarifa,ujanja utundu.
Kwa hiyo si ajabu kuona idadi ya makomandoo ni ndogo sana katika jeshi lolote lile duniani.Kwani hatimaye,idadi ya wanaofaulu kuteuliwa kuchukua kozi yenyewe huwa aghalabu haifikii asilimia hamsini.Na kati yao, wanaohotimu na kuwa makomandoo kamili huwa wachache zaidi..Mmoja au wawili-wakati mwingine zaidi ,kufia mafunzoni ni jambo la kawaida kabisa.Kwani mtihani wa mwisho ni wa kupambana kwa kutumia silaha za kweli kweli.
katika hali kama hiyo ,si ajabu pia kuona kuwa mwanajeshi huwa kwa kawaida halazimishwi kuchukua mafunzo ya ukomandoo.kila mmoja hujitolea yeye mwenyewe.
Na kawaida ,hakuana anaelazimishwa kumaliza kozi yote.Ye yote ,wakati wowote,anapoona imetosha huinua mokono juu na kurudia uanajeshi wa kawaida.
Na hakuna anayemcheka .Huwa kinyume chake.Hupongezwa na kila mmoja .Kwani yeye angalau ameweza kujaribu kuishi jehannam kwa siku chache,wiki chache au miezi michache.
*************
Dakika chache kabla ya saa nne kamili Dr.Raymund Makete aliliegesha gari lake aina ya Bentley kwenye uwanja wa kuegeshea magari nyuma ya Benki ya wakulima .Akateremka na kuelekea barabara ya Nkurumah ,uliko mlango wa mbele wa benki hiyo.
Dr.Makete alkua mtu mzima wa zaidi ya miaka sitini.Nywele zake zilikua nusu nyeupe nusu nyeusi.Lakini hata hivyo,hakuwa mkongwe aliekongoka .Akiwa na mwili wa wastani na wajihi mtulivu wa kiungwana .Alikuwa angali imara,nadhifu,alietembea kwa hatua madhubuti za uhakika.Si za pupa wala si za kinyonga .Suti yake ya kiafrika-ya mikono mifupi na kola pana -ilimkubali kikamilifu.
Aliumaliza uchochoro wa benki akaingia mtaa wa Nkurumah na kupinda kushoto.Hatua chache zaidi zikamfikisha kwenye mlango wa mbele wa Benki ya Wakulima.
Alipousukuma mlango huo ukamgonga mtu aliekuwa anataka kutoka ambaye macho yake yalikuwa kwenye karatasi alizozishika mkononi.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Alkua mrefu ,aliyenawili vizuri,wa umri wa kati ya miaka hamsini na tano,mwenye haraza kubwa lililotenganisha nywele kama matuta .Suti yake ya kunguru ilionyesha wazi kuwa ni ya thamani,Na yeye mwenyewe alionyesha wazi hakuwa na tatizo la ukwasi.
"Kumradhi,"Mzee Makete alisema haraka kama vile kosa la kumgonga mtu huyo lilikuwa lake peke yake.Mtu huyo alipoinua uso,macho yake na ya Mzee Makete yakafungamana.Macho yake yalikua makubwa kuliko kawaida,tena makali,ya dharau na jeuri.Ya mtu ayenata.Mtu anaeaminianaweza kupata chochote akitakacho au kufanya lolote apendalo.
Mzee Makete akaganda,macho yake mapole ameyafinya ,mdomo nusu wazi kwa mshangao na msituko .Kumbukumbu ya mambo ya kutisha ikamjia akilini.Akauliza kwa sauti kama si yake,"Wewe siye Kassim?"
"Nani?" Ingawa mtu huyo aliuliza kijeuri lakini uso ulikwishambadilika ghafla .Ulimwiva,na alikua akipumua kwa nguvu .Macho yake makubwa yaliingiwa na kila dalili ya hofu.Mshituko wake ulikua mkubwa zaidi kuliko wa Dr Makete.
Ingawa walitazamana kwa nukta moja au mbili tu,lakini ilikuwa kama muda mrefu zaidi ulipita kabla ya Dr.Maketekusema "Kassim Ha....."
#12
"Siye mimi."Mtu huyo alimkatiza,akijaribu kutoka haraka .Akaongeza,"Umekosea."
Mzee Makete akabaki mlangoni ameduwaa,amechanganyikiwa,akimtazama mtu aliemdhania kuwa ni Kassim akiondoka kwa hatua ndefu na za hima.Hatimaye,mtu huyo alipopinda kulia na kuingia uchochoro wa banki,akielekea kwenye egesho la magari,Makete alivuta pumzi ndefu na kuingia ndani.
Huku akipambana na mawazo yaliyomchafuka,alikwenda kwenye meza iliyotupu.Akaketi na kutoa kitabu cha hundi na kalamu.Lakini alipotaka kuandika hundi aliona kalamu inacheza,mkono ulikua unamtetemeka!
Hapana,alijiambia. Hawezi kuwa amekosea.Yule ndie Kassim.Asingeweza kuwa mtu mwingine.kama hakuwa yeye, kwa nini alisituka vile?
Sasa nifanye nini? Makete alijiulza.Kalamu ikiendelea kucheza mkononi.Wajibu wangu,alijijibu,ni kwenda kuripoti Polis.Lakini mbona imeshapita miaka mingi?Mingapi vile?Ishini na mnne?Au na mitano?Au na sita? Watanitia maanani? Si wanaamini kuwa Kassim Hashir ameshakufa zamani!
Au niache mambo kama yalivyo-yaliyopita yamepita? Mzee Makete aliendelea kujadiliana na nafsi yake.Nitapata usingizi kweli? Kwa vyovyote itanibidi nimweleze mama Denny. Kwa vyovyote sitaweza kumficha mke wangu jambo kama hil. Akiniona tu atajua nina kero moyoni.
Mzee Makete akajaribu kifikiria hali ya mkewe itakavyo kuwa asikiapo Kassim angali hai. Akajiuliza kama wangeweza kuendelea kuishi kwa raha na furaha kama wanavyoishi sasa.Mkewe lazima angekereka zaidi. Angefadhaika na kuhuzunika na kusononeka.Waliposikia Kassim amekufa walisali sala maalumu-sala ya kuuzika mzoga wa hayawani.
Na sasa....!
Alijaribu tena kuiandika hundi,akashindwa tena.Akarudisha kalamu na kitabu cha hundi mfukoni na kuinuka. Lazima arudi nyumbani na kushauriana na mkewe.Hili halikua jambo la kuamua yeye peke yake.
Akatoka na kuelekea kwenye egesho la magari.Alipokaribia kuumaliza uchochoro akasikia mvumo wa gali lijalo kwa kasi nyuma yake.Akageuka na kulitizama kwa mshangao.Uchochoro huo haukua wa kupita magari.
Gali hilo lilikua hatua chache tu nyuma yake.Lilikuwa Benz jipya jeupe,likiendeshwa na mtu ambaye Makete aliamini kuwa ndiye Kassim. Uso wake sasa ukiwa wa ulikuwa wa kihayawani,na ulionyesha waziwazi dhamira yake.
Dr.Makete akapigwa na butwaa,mwili mzima ukamfa ganzi.Kufumba na kufumbua,kabla ya kuweza lolote,gali hilo likamparamia na kumrusha hatua kadhaa.
***************
Siku ilikuwa ingali changa lakini jua lilikwishwa pamba moto. Kila mmoja alikuwa akivujwa jasho. Denny. akiongoza,aliinua mkono kuashiria kusimama. Akasema,"Tutapumzika kwa nusu saa"
Wote wakapumua kwa sauti. Wamekuwa mbioni tangu saa kumi na moja alfajiri. Denny akajiuliza kama anawaendesha wenzake kupita kiasi au kama hawakustahili kuwa makomandoo.Yeye,alikuwa na hakika angeweza kuendelea kwa masaa manne zaidi bila ya takilifu.
Ingawa alikua anakaribia kutimiza miaka ishirini na sita,pamoja na urefu na ukakamavu wake, Denny bado alionekana kama mwanafunzi wa sekondari.
Alikuwa na uso mtulivu wenye macho maangaavu.Yeyote asiyemjua asingeamini kuwa kijana huyo ni komandoo kamili.
Lakini hakuwa komandoo tu. Alikua mkufunzi wa kozi ya ukomandoo.Alipewa kazi hiyo mara tu baada ya yeye kufuzu miaka miwili nyuma.Nidhahiri alifuzu vizuri.
Ilibidi afuzu vizuri. Tangu utotoni darasani alikuwa mwerevu na ulingoni alikuwa na kipaji.Alikuwa mwanariadha na mshiriki wa michezo kadhaa,hasa masumbwi na kandanda.
Denny alijiunga na jeshi miaka mitano nyuma,mara tu baada ya kumaliza kidato cha sita.Baba yake alipendelea aendelee na masomo hadi awe mhandisi au daktari kama yeye lakini haikuwezekana.
Gari la polisi na gari la wagonjwa yaliwasili nyuma ya Benk ya wakulima karibu wakati mmoja.
Kwenye gari la polisi waliteremka watu watatu. Wanaume wawili na mwanamke mmoja. Wanaume walikuwa Sajini Bob na Koplo Butu. Wote walikuwa katika sare zao za usalama barabarani.
Mwanamke alikuwa kachero Inspekta Bessy. Alikuwa katika milango ya miaka ishirini na saba,mrefu wa kuvutia. Alivaa sketi ya kijivu, shati jeupe na kikoti cha kijivu. Begani alibeba mkoba mweusi.
Kwenye gari la wagonjwa waliteremka watu watatu pia. Wawili walibeba machela na nesi mmoja ambaye baadaye alijitambulisha kwa jina Miriam.
Wote walikuwa katika sare zao nyeupe.
Nesi alipomuona tu majerui akaguta, "Mungu wangu! Ni Dk. Makete!"
"Unamfahamu? " Inspekta Bessy alimwuliza, akitoa kalamu na kijitabu kwenye mkoba wake.
"Ndiyo."Miriam alijibu kwa sauti ya mtetemo. "Ni Dk.Makete. Alikuwa Daktari wetu Mku, sasa amestaafu.
"Mtazame kama angali hai."
"Nesi akachutama na kuchunguza mapigo ya moyo.Akasema, Angali hai"!
"Mkimbizeni hospitali." Wakati Dk. Makete akiwekwa kweny machela,Bessy alimwuliza nesi, "Unalijua gari lake?"
"Ndiyo."
"Lipo hapa?"
Miriamu akageuza kichwa. Akaliona "Lile."
"Vizuri." Bessy akawatazama Bob na Butu. Akawaambia, "Anzeni kazi, mnajua nini cha kufanya."
**************************************
Kilometa kadhaa nje kidogo ya jiji, Benzi jeupe liliacha barabara kuu. Lilipinda kulia na kuingia eneo la Buffalo Hill. Barabara za eneo hilo zilikuwa nyembamba lakini nzuri, na nyumba zilikuwa mbalimbali. Karibu kila nyumba ilizungukwa na wigo wa aina moja au nyingine.
Katika mtaa wa kitosi Benzi lilipenye kwenye geti lenye namba ishinirini na moja.Likapita katikati ya bustani nzuri na kusimaa mbele ya jumba la kifahari la ghorofa moja. Mtu aliemgonga Dk. Makete akateremka na kulikagua gari upande wa mbele. Boneti na bampa lilikuwa limebonyea kidogo.
Kassim akajikuna utosi,macho yake yakionyesha alikuwa na mawazo mazito. Akatoa leso na kupangusa uso wake uliomeremeta kwenye mwangaza wa jua.
Wakati akirudisha leso mfukoni,alisikia hatua nyuma yake. Akageuka. Akamuona Isidori. Mtumishi mkuu wa jumba hilo,akitokea ndani. Akamuuliza, "Kuna habari yoyote?" Sauti yake ilikuwa ya kawaida kabisa -ya mtu mwenye uwezo mkubwa .
"Bwana Kembo alipiga simu." Alijibu mtumishi huyo. Alikuwa nadhifu kama mazingira ya hapo. Suruali nyeusi, shati jeupe na tai nyeusi. "Amesema umpigie."
"Sawa." Kassim akatoa kikebe cha dhahabu akakifungua na kutoa sigara nene ya kahawia,ya kutoka Havana -Cuba. Akaiweka mdomoni na kuiwasha kwa kiberiti cha gesi.
"Lipeleke hili gari gereji." Alisema baada ya sigara kukolea moto. "Waambie wanyoshe hapa.Kazi hiyo waifanye sasa hivi. Na waifanye vizuri, isijulikane kama limebonyea.Isipowezekana waweke boneti na bampa jipya.Wasijali gharama. Sawa?"
"Ndiyo Mzee."
"Na Isidori....."
"Ndiyo Mzee?"
"Koti hili linanibana. Alisema Kassim, akilivua koti lake la thamani.
"Hebu lijaribu."
Isidori alilipokea na kulivaa koti hilo akiwa na uso wa furaha na mshangao.Akasema, "Sawa kabisa." Ingawa lilimpyaya kidogo.
"Lako."
"Asante sana, Mzee."Akaanza kufungua vifungo .
"A-aah! Usilivue.Livae tu likuzoee.Ingawa halifanani na suruali yako lakini limekupendeza." Isidori akakifunga kifungo alichokifungua. Akaufungua mlango wa gari.
"Na Isidori...."
"Isidori akageuka. "Ndiyp mzee?
"Kuna jambo nataka ulifahamu."
"Ndiyo,Mzee.?
"Ennh....Kuna mtu nimemgonga mjini,nyuma ya Benki ya Wakulima.Ndiyo sababu ya boneti kubonyea." Isidoria akabaki kimya wakati sigara ikipelekwa mdomoni na kuondolewa.
"Ilikuwa bahati mbaya." Kassim akaendelea. "Lakini sikusimama. Unajua nini hutokea katika jiji hili....Yaani ukimgonga tu mtu na kusimama hata kama kosa ni lake,wahuni hukuvami na kukushambulia huku wakipora kila wawezacho kukitia mkononi.
"Naelewa, Mzee." Isidori alikubali huku akisisitiza kwa kichwa. "Kwa hiyo sikusimama." Kassim akaendelea.
"Kwa vile mwendo haukuwa mkubwa, sidhani kama mtu huyo ameumia sana. Na sidhani kama kuna mtu aliewahi kuchukua namba za gari. Hapakua na watu wengi."
Sigara ilibandikwa mdomoni ikabanduliwa.http://pseudepigraphas.blogspot.com/
" Lakini kama ikigundulika ....ikigundulika kama ni mimi ndie niliefanya ajali hiyo yatakua makubwa. Si tu faini na fidia itakua kubwa -hilo sijali bali heshima yangu katika jamii pia itaathirika."
Kassim aliivuta sigara akasema, "Iwapo itagundulika nataka useme ni wewe uliekuwa unaendesha. Hakuna usumbufu wowote utakaoupata. Ondoa shaka kabisa, wakili wangu Bw. Benson atasimamia mambo yote.Sana sana itakua faini na fidia ambayo nitalipa ndani ya nukta.Na nitakupa zawadi ya kukufaa katika maisha yote -kitu kama nyumba au gari. Chaguo lako"
Baada ya kuibandua sigara mdomoni,Kassim akauliza, "Sawa?" Kama mtu alielishwa limbwata,Isidori akajibu, " Sawa, Mzee."
Kassimu aliliangalia Benzi likitoka nje ya geti kisha akageuza kichwa na kumtazama mtunza bustani. Alikuwa kama hatua arobaini mbali naye,akimwagilia miwaridi. Akajiuliza kama ameweza kusikia kuyasikia mazungumzo yao. Alizungumza kwa sauti ndogo kwa ajili yake. Akaamua asingeweza kumsikia. Akageuka na kuingia ndani.
Vyumba vyote vya kulala vya jumba hilo vilikuwa ghorofani. Sehemu kubwa ya chini ilikuwa ukumbi mkubwa uliopambwa vilivyo. Sakafu yote ilifunikwa na zulia. Upande mmoja ulitawaliwa na meza iliyozungukwa na viti kumi na viwili. Upande mwingine ulikuwa na TV na rafu za vitabu,mapambo na vinywaji, hasa vikali na aina kadhaa za mvinyo aghali toka ng'ambo. Hapa na pale palikuwa na seti za sofa na vimeza vifupi. Ngazi za kwenda ghorofani zilikuwa mkabala na mlango wa mbele.
Kassim alikwenda moja kwa moja kwenye rafu ya vinyaji. Akatoa chupa ya kinywaji kikali na kjitilia robo glasi. Akaimeza kwa mkupuo.
Kisha akaenda kwenye simu iliyokuwa pembeni. Baada ya kubonyeza namba atakazo na kujibiwa, akasema "Nipatie Bwana Kembo." Punde sauti upande wa pili akasema, " Kembo hapa." Kassim akatamka neno moja tu, "Vipi?"
"Ohh, Bwana Kessy! Nahitaji kukuona. Tuna tatizo."
"Na mimi pia nina tatizo."
"Tatizo gani?" Kembo aliuliza kwa mashakamashaka.
"Tuna watu karibu sehemu zote mhimu."
"Vizuri. Kuna mtu alifikwa na ajali ya gari nyuma ya Benki ya Wakulima muda mfupi uliopita. Nataka kujua ni nani mtu huyo na hali yake ikoje. Unaweza kufanya hivyo?"
"Hakuna lisilowezekana, Bwana Kessy. Hakuna lisilowezekana."
"Fanya hivyo halafu njoo unione,"
***********************
Bessy hakua mgeni na Dk. Beka, Daktari Mkuu wa hospitali kuu ya serikali. Tangu avishwe uinspekta mwaka mmoja na nusu nyuma, alikwisha kutana nae mara kadhaa,kuhusiana na kesi mbalimbali.
Kwa hiyo alipofika hapo hospitalini alikwenda moja kwa moja ofisini kwake. Akabisha na alipoambiwa aingie, akaufungua mlango na kuingia.
"Ohh, ni wewe Inspekta." Alisema Dk. Beka kwa suti yake tulivu na ya chini. Leo Bessy aliona,ilikuwa ya chini zaidi - ya huzuni.
Akasema, "Ni kuhusu Dk. Makete." Naye pia alitumia sauti ndogo. Dk.Beka akaitikia kwa kichwa. akaivua miwani yake na kuyafikicha macho yake machovu.
"Ikoje hali yake?" Bessy aliuliza,akiketi na kukitoa kijitabu chake.
"Nasikitika kusema si nzuri. Bado yuko thieta anashughulikiwa na wataalamu wa hali ya juu."
"Uko uwezekano wake wa kuishi?"
"Kitu kama hamsini kwa hamsini,"
Bessy alikwishaizoea kauli hiyo. Dk. Beka hakupenda kumkatisha mtu tamaa,hata kama alijua kuwa mgonjwa huyo asingetoka thieta akiwa hai.
Akauliza, "Aliwai kurudiwa na fahamu?"
"Alizinduka thieta kwa nukta chache tu kabla ya ganzi kumkolea sawasawa."
"Aliwai kusema lolote lile katika nukta hizo chache?" Bessy aliuliza kwa matumaini kalamu ikisubiri mdomoni.
"Alisema maneno machache. Lakini hakusikika vizuri. Alikuwa kama anaeota - anaeweweseka. Sauti yake ilikuwa ya chini sana, na maneno hayakuwa ya kuleta maana. Nilichoweza kukidaka ni maneno mawili tu - kama tutayaita maneno - 'kassi hashi.' Aliyarudia maneno hayo mara mbili tatu."
Baada ya kuyaandika maneno hayo,Bessy akasema kwa sauti ya mkazo , "Dk. Beka, lazima nizungumze na Dk. Maketemapema iwezekanavyo - kabla....kabla mambo hayajawa mabaya zaidi. Dk. Makete aligongwa kusudi. Na kwa bahati mbaya hakuna aliewai kuzisoma namba za gari."
"Una maana haikuwa ajali ya kawaida?" Dk. Beka aliuliza kwa mshangao wa kutoamini.
"Hapana! Lilikuwa jaribio la kuua!" Sauti ya Bessy ilikuwa imepanda. Akavuta pumzi na kuendelea kwa sauti ya kawaida. "Nadhani Dk. Makete anamfahamu mtu aliemgonga. Na sababu yake. Huwezi kumgonga mtu kusudi bila sababu."
" Una uhakika haikuwa ajali? Madereva wengi wanapomgonga mtu...."
"Najua. Hukimbia. Hukimbilia polisi kujisalimisha. Lakini huyu hakufanya hivyo. Zaidi ya masaa mawili sasa yameshapita. Nina hakika hata jisalimisha. Isitoshe, uchochoro aliogongewa Dk. Makete hautumiwi na magari, na kama kuna gari litapita, basi si kwa kasi ya kuweza kusababisha ajali.
Dk. Beka akatikisa kichwa kwa majonzi.
Inspekta Bessy akaendelea, "Isitoshe tuna ushahidi. Ingawa kichochoro kile - kichochoro cha Benki ya Wakulima - hakina pilika za watu. Tumebahatika kupata watu wawili walioshuhudia tukio hilo. Wote wanaelekea kuwa watu wa kuaminika. Wote wapo tayari kuapa kuwa Dk.Makete aligongwa kusudi."
Dk. Beka alifumbua mdomo ili aseme neno lakini akabadili mawazo na kuufumba
Bessy akaendelea, "Mashahidi hao wanatoa sababu mbili. Kwanza. Dk Makete hakuwa katikati ya njia. Alikuwa pembeni. Alifuatwa. Pili, gari lililomgonga lilimnyemelea. Liliongezwa mwendo ghafla lilipomkaribia. Mmoja kati ya mashahidi hao aliwai hata kuguta. Hakumbuki alisema kitu gani. Bila ya shaka kitu kama 'Hey...! au 'Wewee...!' Hajui kama alikuwa anamkemea yule dereva au anamtahadharisha Dk. Makete. Anasema alikuwa katika mshituko wa kuruka akili. Ndiyo maana hakuweza kuzisoma namba za gari."
Dk.Beka akatikisa tena kichwa. Akasema, "Nashindwa kuamini."
"Amini usiamini, hivyo ndivyo mambo yalivyo. Dk. Makete amegongwa kusudi."
"Hukunielewa. Nina maana....." Beka alitafuta maneno ya kumalizia sentesi yake lakini hakuyapata. Akasema, "Namfahamu Dk. Makete vizuri sana. Nimefanya nae kazi kwa zaidi ya miaka ishirini. Miaka kumi nikiwa msaidizi wake mkuu. Ni rafiki yangu mkubwa. Tumekuwa kama ndugu. Siri yake ni yangu. Mkewe ananiita shemeji, na mwanae ananiita mjomba. Hata siku moja sijaona wala kusikia Raymond akikorofishana na mtu. Nakuhakikishia yeye si mtu wa kuweza kuwa na adui hata mmoja hapa duniani."
"Na mimi nakuhakikishia kuwa anao. Angalau mmoja. Na ni wajibu wangu kumtia mbaroni. Nina imani Dk. Makete anamfahamu mtu huyo. Kwa hiyo lazima nizungumze nae kabla hali yake haijawa mbaya zaidi."
Dk. Beka aliinua uso akauliza, "Unamaana iwapo hata .... hatarudiwa na kauli, mtu huyo hataweza kupatikana?"
Badala ya kujibu swali hilo Inspekta Bessy alisema kwa sauti kavu, "Dk. Beka tafadhali usinifiche niambie ukweli. Dk. Makete atatoka thieta akiwa hai au maiti?"
"Mimi siyo mtabiri! Wala siyo Mungu!" Ingawa maneno hayo yalitamukwa kwa sauti ndogo lakini ilikuwa sauti ya ukali. Iliyojaa uchungu na ghadhabu. Dk. Beka akapumua na kusema kwa sauti yake ya kawaida, "Bessy, hatuwezi kufanya miujiza, kufanya lisilowezekana. Hatuwezi kufufua maiti. Hakuna anaeweza kufanya hivyo zaidi ya Yesu."
"Ndiyo kusema Dk. Makete hana tumaini?"
"Sijasema hivyo. Raymond hajawa maiti. Hivi tunavyozungumza anashughulikiwana mabingwa. Wanaweza wakafaulu kuyaponya maisha yake, wanaweza wasifaulu. Ikishindikana, hakuna yeyote wa kuweza kufanya lolote."
Bessy alikunja uso na kusema. " Kuna sindano ya kuua ganzi na kumzindua mtu na kumfanya aweze kijibu swali moja au mawili kabla ya kukata roho.Kama Dk. Makete hana tumaini lazima sindano hiyo itumiwe ili atutajie mtu alie mgonga."
"Dk.Beka akamtazama Bessy kwa mshangao. Akamwuliza, "Umeisikia wapi hiyo sindano?"
"Katika kitabu."
"usiamini kila unachosoma kwenye vitabu vya hadithi."
"Hakikuwa kitabu cha hadithi."
Kimya kizito kikazagaa humo ndani kwa nukta kadhaa. Hatimaye Bessy akauliza "Sindano hiyo ipo au haipo?"
"Ndiyo - ipo."Dk. Beka alijibu kwa karaha. "Lakini haitumiwi ovyo. Kwa sababu humumaliza kabisa mgonjwa. Hata kama alikuwa asife atakufa."
"Kwa mtu asie na matumaini ....?"
"Ni nani wa kuamua kuwa hana matumaini? Si mimi. Ninavyoamini mimi, mtu anaepumua ni mzima, Hata kama tumaini la kupona ni moja katika milioni. Oh, tunapoteza bure wakati kuizungumzia sindano hiyo. Kwanza hatuwezi kuitumia bila amri toka juu. Ni nani wa kwenda ikulu? Wewe?
Na hata kama nitalazimishwa kuitumia sitaitumia. Nitajiuzulu. Kwa sababu moja tu. Siwezi kukubali kuua - kumwua mtu yeyote yule, achilia mbali mtu huyo kuwa rafiki yangu mkubwa."
Bessy alishusha pumzi ndefu akasema. "Nimekuelewa, Dk. Samahani."
Dk. Beka akapumua pia. Akasema, "Kuhusu swali langu?"
Enspekta Bessy aliinua mabega kidogo akasema. "Tunafanya - na tutaendelea kufanya kila tuwezalo ili tumpate mtu huyo. Kwa bahati mbaya kama nilivyokwambia, hakuna aliewahi kuzisoma namba za gari lililomgonga Dk. Makete. Mara tu lilipomgonga lilipinda na kutoweka. Tunachokifahamu ni kuwa gari hilo ni jeupe - pengine Benzi. Na aliekuwa akiendesha alivaa koti au jaketi la kunguru. Ni msaada mdogo sana."
Dk. Beka akatikisa kichwa.
"Tegemeo langu kubwa lipo katika kumhoji Dk.Makete." Bessy aliendelea.
"Nadhani sasa unauona umhimu wa kuzungumza naye mapema iwezekanavyo."
"Tutaangalia atakapo zinduka. Lakini usitegemee kuwa itakuwa leo au kesho. Upasuaji anaofanyiwa ni mkubwa na mgumu. Ameamua vibaya. Ni bahati kuwa hai hadi hivi sasa. Kinachomsaidia ni kuwa alikuwa na afya nzuri sana."
"Jambo moja jingine." Alisema Bessy akiifunga kalamu. "Atakapotoka thieta lazima apewe chumba cha peke yake."
"Hilo sio la kusema, Raymond atahudumiwa kama Rais."http://pseudepigraphas.blogspot.com/
"Ninazungumzia usalama wake."Besy alisema kwa sauti kavu huku akiendelea.
"Atakuwa na askari chumbani mwake masaa ishirini na nne. Aliejaribu kumwua, naamini ni mtu alietaharuki. Katika hali ya kawaida huwezi kufanya kitendo kama kile, kujaribu kuua kwa gari hadharani. Ni bahati yake namba za gari hazikupatikana, ama sivyo tayari angeshakua pabaya."
"Unawasiwasi anaweza kujaribu tena - hapa hospitalini?"
Bessy alikubali kwa kichwa, "Akisikia Dk. Makete angali hai atazidi kutaharuki. Acaha huo uhasama wao wa mwanzo.Makete akipona na kumtaja, atakamatwa na kufunguliwa shitaka la kujaribu kuua. Hilo si shitaka la mchezo.Lazima atakuwa anafahamu hivyo.
Dk.beka hakusema neno.
Bessy akaendelea, "Kwa hiyo lazima alindwe usiku na mchana. Na uhakikishe watu wanaoingia chumbani mwake kumhudumia - madkatari, wauguzi,wafagiaji na kadhalika ni watu waaminifu wa hali ya juu. Mmojawapo ni yule nesi aliekuwa kwenye gari la wagonjwa." Bessy alikifungua kijitabu chake akalitafuta jina la nes huyona kusema ,"Miriam"
"Hakuna wa kumdhuru hapa hospitalini."
Alisema Dk.Beka .
"Anapendwa na kila mmoja. Wengi wao walitokwa machozi kwenye karamu ya kumuuaga."
"Kama miaka minne hivi iliyopita. Minne na nusu."
"Na tangu wakati huo hakuna watumishi wowote walioajiriwa?"
"Oh,wapo. Kila mwaka tunapokea wawili watatu wapya. Hata hivyo sidhani kama kuna wa kumdhuru."
"Huwezi kujua. Kuna kitu kiitwacho pesa. Watu wanafanya mambo ya ajabu sababu ya pesa."
"Vizuri, nitakuwa macho." Alisema Dk. Beka. Akauliza, Kwa nini umempendekeza nes Miriamu?"
"Alipoona aliegongwa ni Dk. Makete alifadhaika mno.
Alijijasirisha kiume asitokwe machozi hadharani. Lakini alipoingia garini wakati akinipa jina lake, machozi yalikuwa yanamlengalenga."
Dk. Beka akakubali kwa kichwa . "Miriam alimhusudu Dk. Makete. Na Raymond alimpenda Miriam kama mwanae."
"Huyo ndio wa kumhudumia Dk. Makete."
"Lakini Miriam hakuwa mtu wa pekee kumhusudu Dk. Makete. Wengi walimhusudu. Karibu watumishi wote. Huwezi kufanya kazi na mtu kama Raymond bila ya kumhusudu. Alipokuwa kiongozi wa hosptitali hii hakuna shida hata ya mtu mmoja aliyoipuuza, iwe shida kubwa au ndogo. Mara kadhaa alitoa pesa mfukoni mwake kuwasaidia waliokwama.
"Katika miaka kumi ya uongozi wake," Dk. Beka aliendelea, "Hakuna mgogoro wowote mkubwa uliotokea isipokuwa mmoja tu. Wa wizi wa mhasibu wetu wa zamani. Hata hivyo Raymond alimpa nafasi ya kurudisha pesa alizoiba, ili mambo yaishe na yasifike kokote. Lakini Bosco - huyo mhasibu ambaye sikufichi alikuwa hapendwi na kila mtu alijiona majanja sana. Aliamini kuwa mahakamani angeshinda. Hakushinda. Alifungwa miaka saba. Na bado Raynmond alimsikitikia kama vile hakustahili adhabu ile,na hali alidokoa mali ya umma. Kusema kweli Bessy, mimi sina moyo huo.
"Yaelekea wewe na huyo Bsco mlikuwa mlikuwa mbalimbali."
"Si mimi tu. Bosco alikuwa na tabia mbaya. Licha ya kuwa na dharau na kiburi, alikuwa na tabia yakuchelewesha kusudi malipo ya watu mpaka apewe chochote. Na wakati mwingine alichukua Benki pesa za mishahara ya wafanyakazi na kuzizungusha kwanza kwenye biashara zake kisha baade ndio huja kulipa. Tulimwonya lakini wapi. Kama mimi ningekuwa ndio Raymond ningekwishamtimua mapema sana, hata huo wizi usingetokea."
Bessy akashusha pumzi. Baada ya kurudisha kalamu na kitabu mkobani.
Akasema, "Ninavitaji vitu vilivyokuwa katika mifuko ya Dk. Makete. Ni kutapatapa tu, lakini imewai kutokea kitu kimoja kutoa mwanga. Na gari lake lazima likaondolewe pale lilipo. Nitazihita pia funguo."
"Nitakupatia."
"Na familia yake je,imekwishaarifiwa?"
"Ndiyo. Hilo lilikuwa jambo la kwanza. Mkewe amekwisha fika. Ilibidi na yeye adungwe sindano ya kumtuliza. Tumempa kitanda apumzike. Mwanae ni mwanajeshi. Yuko Ndala nimekwisha yaarifu Makao Makuu ya Jeshi. Watamfahamisha."
******************************
Mafunzo ya ukomandoo hutolewa hatua kwa hatua, sehemu mbalimbali . Karibu kambi zote za mafunzo ya msingi huwa msituni, kwa nchi zenye misitu. Kwa baadhi ya nchi zisizo na misitu huwa hata mapangoni.
Katika kambi hizo wanajeshi hujifunza mambo mbalimbali, kama vile ukakamavu,ujasiri, uvumilivu, kutumia silaha mbalimbali, kupigana, kujificha na kufichua,kukimbia na kukimbia masafa marefu usiku na mchana kwa kutumia ramani, dira, jua, mwezi hata nyota. Na wakati wote hujifunza kuua bila kusita wala kuona kinyaa au kuchafukwa matumb. Kuua kwa kutumia chochote kile.
Kambi ya Mafunzo ya Msingi ya Ukomandoo (KMMU) ambako Luteni Dennis Makete alikuwa Mkufunzi mmoja wapo, ilikuwa katikati ya msitu wa Ndala,zaidi ya kilomita mia na hamsini kutoka jiji la mji mkuu.
Ilikuwa kambi ya siku nyingi lakini haikua na jengo la kudumu hata moja.Palikuwa na mahema tu.
Sajini Bob alikazana kujipepea kwa gazeti. Yeye na Koplo Butu walikuwa wameketi ndani ya gari lao la polisi waliloliegesha pembeni, karibu na makutano ya barabaraya Wazawa.
Palikuwa mahali pa pirikapirika za magari. Taa za barabarani, ambazo zilikuwa za kisasa, za kuning'inia juu,zilikazana kuamuru maderevakusimama na kuondoka. Bob na Butu walikuwa wakisubiri mtu avunje sheria wamtoe upepo au wamchukulie hatua, mno hilo la kwanza.
Bob ambaye alikuwa mnene, na hasa sehemu ya tumbo alikuwa akitokwa jasho, pamoja na kujipepea kwa nguvu na kuuacha wazi mlango wa upande wake. Butu, aliekuwa mwembamba, alikuwa mkavu kabisa. Alikuwa anavuta sigara na kuuangalia kwa jicho moja moshi aliokuwa akiupulizia pembeni. La pili likiyavinjari magari yaliyosongamana barabarani, akiomba kimoyomoyo mojawapo livunje sheria.
"Unaweza kuvuta katika fukuto kama hili?" Bob alimwuliza. Yeye hakuwa mvutaji. Alikuwa mtu wa lawalawa. Hata dakika hiyo alikuwa akimung'unya moja. Alitaka kumuuliza, Na wewe unaweza kufutuka mtumbo katika usawa mgumu kama huu.? Lakini akajikuta akisema , "Ni mazoea, Bob mazoea." Akaongeza, "Wanasema mazoea ni kitu kibaya sana. Nadhani ni kweli. Kusema kweli, mimi hukushangaa wewe kuweza kumung'unya pipi wakati wote.Mdomo haochoki?"
Bob akaguna. Akaitazama saa yake na kusema, "Nadhani tunapoteza bure wakati wetu hapa." Kisha akatega masikio.
Wote wakausikia mvumo wa injini inayolalamika kwa kulazimishwa. Wakageuza kichwa. Wakaliona gari lenyewe. Lilikuwa Jeep la kijeshi likitokea upande wa Ndala na kuelekea mjini. Taa zote za gari hilo zilikuwa zikiwaka, honi ikihanikiza, likichenga magari mengine kama mchezaji wa mpira aliepania kufunga goli.
Bob akatikisa kichwa. Akasema kwa karaha, "Hawa wanajeshi wakati mwingine hujisahau kabisa. Huyu lazima tumfunze adabu. Ndio wanaosababisha ajali za kipumbavu kama ile iliyotokea nyuma ya benki leo asubuhi."
"Ile haikuwa ajali ya kawaida, Bob." Butu alimkumbusha. "Ilikuwa kusudi."
"Hata huyu akigonga itakua kusudi." Ingawa taa za barabarani zilimuamuru derva wa Jeep asimame lakini hakusimama. Huku matairi yakiuma lami na kulalama, akapinda kushoto na kuendelea na safari yake kwenye barabara ya Wazawa."
Bob akaufunga mlango wa gari kwa nguvu kupita kiasi na kuamuru, "Mwandame!" Butu akasita. Akasema, "Bob unadhani hakutuona?'
"Una maana gani?"
"Katuona!"
"Kwa hiyo?"
"Ametudharau!"
"Nimesema mwandame!" Bob alifoka kwa sauti yake ya kisajini. "Tutaona mwisho wa dharau yake!"
Butu alitia moto gari. Huku king'ora kikibweka na kimwelumwelu kikimetemeta,wakaliandama Jeep.Lakini hakuweza kulikamata.
Hatimaye likapinda kushoto na kutulizwa kwenye uwanja wa kuegesha magari wa Hospitali Kuu ya Serikali. Mwanajeshi aliekuwa akiliendesha akateremka na kuelekea lango kuu.
"Kamkamate!" Bob alimwamuru Butu,baada ya mwenzake kulisimamisha gari kando ya Jeep lililotapakaa vumbi.
Butu akasita. Akasema, "Bob yule ni Luteni," "Kwa hiyo?" Huoni kama ni bora uende wewe?" "Hapana! Nenda wewe. Akileta ukorofi nitakuja kukusaidia."
Kwa shingo upande, Butu akateremka na kumfuata mwanajeshi yule, ambaye alikuwa akilikaribia lango. Akamwita, "Luteni!"
Mwanajeshi akasimama na kugeuka taratibu. Akauliza, "Kitu gani?" "Kuhusu uendeshaji wako .... Butu akauhisi mdomo wake ukiwa mzito.
Akajikuta anaangalia macho ambayo hajapata kuyaona maishani mwake .Yalikuwa kama ya Nyoka alieghadhabika. Kama yanatoa cheche . Kama yanayosema , "Ropoka neno moja tu la kipuuzi na utaingizwa humu ndani kwa machela."
Ghafla, Butu akaanza kutokwa jasho jembamba .Mwanajeshi aligeuka na kuingia hospitalini.Kwa hatua nzito za kupwaya Butu akaanza kurudi kwenye gari lao. Akilini akishindwa kuamini kijana kama yule kuweza kuwa na macho kama yale, pamoja na kuwa mwanajeshi.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
"Vipi?" Bob alimwuliza. Butu alijikuna kichwa na kusema, "Alikuwa na sababu ya kuendesha vile."
"Sababu?" Bob akauliza. "Sababu gani?"
"Eee. Ya usalama." Usalama? Usalama gani?"
"Usalama wa Taifa," Alijibu Butu huku akiingia garini. "Bob akauliza, "Usalama wa Taifa?"
"Bob, acha kuwa kama kasuku." Alisema Butu akilitia gari moto. "Kijana yule si wa kawaida. Achana naye. Twende zetu."
Dennis alitembea kwa hatua ndefu, sakafu ikivuma kila alipokutana na soli ya kiatu chake cha kijeshi.
Alikwenda moja kwa moja kwenye ofisi ya Daktari Mkuu, ambayo zamani ilikuwa ofisi ya babake. Alipotaka kubisha mlango ulifunguliwa na Dr. Beka akachomoza, akiwa anataka kutoka.
"Ooh, Denny!"
"Mjomba! Imekuwaje?"
"Mzee amegogwa na gari. Ametolewa thieta sasa hivi. Twende tukamwone."
Wakaanza kutembea kulekea kwenye majengo ya kulala wagonjwa. "Hali yake ikoje?" Dennis aliuliza.
"Ni mapema mno kusema lolote la uhakika. Jambo mhimu ni kwamba angali hai."
"Mama je?"
"Alishituka mno. Ikabidi adungwe sindano ya kumtuliza. Amepewa kitanda apumzike."
"Ajali hiyo imetokeaje?"
"Bora akueleze Inspekta Bessy, anaeifanyia uchunguzi. Yupo hapa hapa hospitalini, anamsubiri mama yako aamke."
Waliingia jengo D, wakapanda ngazi hadi ghorofa ya pili. Kila upande kulikuwa na vyumba. Wakasimama mbele ya mlango Namba 13. Dk.Beka akaufungua, wakaingia.
Kilikuwa chumba cha ukubwa wa wastani,chenye kitanda kimoja, viti viwili, sofa moja dogo, kimeza na kabati. Madirisha yote yalikuwa wazi, pazia zimekunjwa. Juu pangaboi lilizunguka kwa kasi ya wastani.
Kwenye kiti kimojawapo aliketi kijana ambaye alionekana wazi kuwa ni askari, ingawa alivaa kiraia. Kitandani alilala Mzee Raymond Makete, macho amefumba,akiongozewa damu iliyokuwa inaning'inia kando ya kitanda.
Dk. Beka akainama na kumchunguza mapigo ya moyo. "Ni dhaifu," Alisema, "Lakini si hali ya kutisha. Ni jambo la kawaida kwa mtu aliefanyiwa operesheni ngumu kama yake. Twende tukamuone mama yako."
Alipofika mlangoni, Dk.Beka akakumbuka jambo. Akageuka na kumwambia kijana alieketi kitini. "Huyu ndiye Luteni Dennis Makete." Kijana huyo alikubali kwa kichwa na kusema. "Ndiyo mzee."
***********************
"Butu, ulisema yule kijana sio wa kawaida. Ulikuwa na maana gani?" Bob alimuuliza mwenzake. Walikuwa wanakula chakula cha mchana katika kantini ya Kituo Kikuu cha Polisi.
Tonge mdomoni, Butu alitikisa kichwa. Akatafuna na kumeza. Akasema, "Kusema kweli, Bob, sijui." Akawaza kwa nukta mbili tatu, huku akifinyanga tonge jipya. Yeye hakuwa akitumia kijiko kama mwenzake. Hatimaye akasema. "Huoni kuwa si jambo la kawaida kijana kama yule kuwa Luteni?"
"Kwa nini?"
"Ni mdogo mno. Sana sana atakuwa na miaka ishirini na tatu au na nne tu. Mimi nakaribia kutimiza miaka thelathini, wewe umekwishavuka. Lakini tazama - wewe ungali Sajini na mimi Koplo."
"Hilo si ajabu. Mbona hushangai yule msichana, Bessy kuwa Inspekta, na hali ni mdogo kuliko sisi? Tena mwanamke. Si kwa sababu unafahamu amesoma kuliko sisi. Ana shahada ya Sheria. Pengine yule Luteni pia amesoma kuliko sisi. Au pengine katenda kitendo cha kishujaa. Wanajeshi wana nafasi nyingi za kupandia vyeo, sio kama sisi wachunga magari."
"Tonge mdomoni, Butu akasema kama anaewaza kwa sauti. "Lakini macho yake....."
"Macho yake? Bob aliuliza, akiwa ameachwa mbali. "Macho yake yana nini?"
"Si ya kawaida - kwa kijana mdogo kama yule." Alijibu Butu, uso ameukusanya, akiwaza kwa dhati. "Yanatisha. Ni ya mtu asieogopa chochote, anaeweza kufanya lolote. Sitashangaa kusikia amekwishaua. Yaani kikazi. Jinsi gari lake lilivyochafuka, bila shaka ametoka Ndala."
"Ndala?"
"Usianiambie kuwa hujui nini kinachoendelea katika msitu wa Ndala."
"Oh, kuna kambi ya wanajeshi."
"Si wanajeshi wa kawaida. Ni makomandoo. Makomandoo si watu wa kuchezea hata kidogo. Kozi wanayochukua ni ngumu mno. Huwezi kuichukua bila kutafuta uchizi kidogo. Kwao kuua na kuuawawa ni jambo la kawaida kabisa."
Bob alibaki kimya.
Butu akaujaza mdomo. Akasema huku akitafuna, "Unakumbuka mwaka jana - Kikosi 32x kilipoasi na baadhi yao wakakimbilia msituni? Walitumwa makomandoo wachache tu kwenda kuwashughulikia waliokataa kujisalimisha. Hawakuwa zaidi ya makomandoo ishirini, lakini waliwateka waasi zaidi ya miatatu na kuwaua zaidi ya mia."
"Na wao?" Bob aliuliza huku akitafuna.
"Hakuna hata mmoja aliyejeruhiwa! Inawezekana mmoja wapo alikuwa yule Luteni."
Uso wa Bob ukanywea. Akabaki akiuchezea wali wake kwa kijiko. Hatimaye akasema, "Na kuhusu usalama wa Taifa? Ulikuwa na maana gani?"
Butu akaanguka kicheko kirefu. Kiliwafanya wote waliokuwa humo ndani wageuke kumtazama. Alikuwa kama aliepagawa. Alipoweza kujizuia akamwuliza, "Bob, uliamini?"
Uso ukiwa bado umemnywea, Bob akatikisa kichwa.
"Kijana yule," Butu alinong'ona, "Hakusema lolote zaidi ya kuniuliza, "kitu gani?" basi."
Taratibu uso wa Bob ukaanza kuchanua . Akatabasamu. Ghafla na yeye akakiangua kicheko chake cha mwaka. Butu akamtazama kwa mshangao. Akashindwa kujizuia. Akajiunga naye.
Askari aliekuwa meza ya pili akawatazama kwa mshangao. Nae pia akashindwa kijizuia akajiunga nao. Akamwambukiza askari wa kike alieketi naye. Kufumba na kufumbua, ukumbi mzima ukalokezwa. Kila mmoja aliekuwemo humo akawa anacheka kama aliepagawa.
Mbele ya jumba namba 21 Mtaa wa kitosi,eneo la Buffalo Hill, palikuwa na bustani nzuri ya maua iliyokuwa ikitunzwa na kijana wa makamo aliejulikana kwa jina la Kikoti, kwa sababu kikoti shake kikuukuu kilikuwa hakimtoki mwilini, iwe siku ya joto au baridi, mvua au jua.
Nyuma ya jumba hilo palikuwa na bwawa kubwa la kuogelea. Kando yake, hapa na pale, palikuwa na miamvuli mikubwa ya rangi mchanganyiko.
Chini ya mwamvuli mmojawapo waliketi Kassim na Kembo kwenye viti vya kukunja vya kitambaa cha turubai. Kati yao palikuwa na kimeza kifupi chenye chano chenye chupa ya pombe kali, glasi mbili,kibakuli cha vidonge vya barafu na kibakuli cha bisi.
Kassim alikuwa amevaa kaptura nyeupe kama ya kuchezea tenesi, na shati jepesi ambalo halikufungwa vifungo. Alikuwa akivuta sigara yake ya kahawia ya kutoka Havana.
"Mtu wako ni daktari mstaafu Raymond Makete." Alisema Kembo akijichanganyia kinywaji, baada ya Isidori aliyewaandalia, kuondoka.
"Raymond Makete?" Kassim aliuliza akiwaza. Kembo alikubali kwa kichwa, akimeza funda. Alikuwa hajatimiza hata miaka arobaini, lakini alikuwa na mvi. Zilimfanya aonekane mkubwa zaidi kuliko alivyokuwa.
Akasema, "Alikuwa daktari mkuu. Alistaafu miaka mnne au mitano iliyopita." Kassim akatingisha kichwa. "Simfaham.Sijui alinijuaje! Ikoje hali yake?"
"Mbaya, mahututi. Amefanyiwa operesheni ngumu iliyochukua masaa. Ametolewa thieta muda mfupi tu uliopita. Yuko jengo D, ghorofa ya pili,chumba namba kumi na tatu - cha mwisho mkono wa kulia."
"Kwa ujumla ikoje hali yake?"
"Sijui. Mpaka anafikishwa hospitalini alikuwa hajitambui. Sijui huko thieta. Lakini jinsi hali yake inavyosemekana ilivyo, haiyumkini kusema lolote la maana."
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Kembo aligida funda akauliza, "unasema alikutambua - una maana gani?"
"Nilikuwa natoka benki. Tukagongana mlangoni. Akanitazama kwa macho makali na kuniuliza kama ndie Kassim. Alinishitua sana."
Kembo alisogea kwenye ncha ya kiti akamkazia macho mwenyeji wake na kumwuliza, "Bwana Kessy, wewe ndie uliemgonga?"
"Nilitaharuki!" Kassim alimaka. "Jinsi alivyonitazama ,nina hakika kuna kosa nililomtendea siku za nyuma. Sijui ni kosa gani, lakini inaelekea ni kubwa, lisiloweza kusameheka pamoja na miaka kupita. Kosa ambalo lingeweza kuniangamiza kama angeripoti."
Kembo alivuta pumzi akajiwashia sigara.
Kassim akaendelea, "Kwanza sikukusudia kumgonga. Nilisubiri mbele ya benki ili akitoka nimtazame vizuri, pengine ningemkumbuka na kukumbuka nilichomtendea. Hakukawia kutoka. Hilo liliniongezea hofu. Ilikuwa wazi hakufanya chochote humo ndani, kama vile aliairisha shughuli zake kwa sababu yangu."
Baada ya kuibandika sigara mdomoni na kuibandua, Kassim akaendelea, "Nikaamua kumfuata nione anaelekea wapi. Akaelekea nyuma ya benki. nikajua anaelekea polisi. Nikafikia upeo wa kutaharuki. Nilipoona sehemu yenyewe haina watu nikaona la kufanya ni moja tu - kummaliza hapohapo. Kwa vile bastola sikuwa nayo...."
"Hukummaliza sawasawa." Alisema Kembo. Akauliza, "Unauhakika hakuna mtu alieiona ajali hiyo? Hakuna aliechukua namba za gari?"
"Sijui. Eneo lote la karibu lilikuwa tupu kabisa. Isitoshe, niliwahi kukata kona na kutoweka. Kitendo chote kilitendeka katika nukta chache tu."
Kembo akatikisa kichwa. Akasema, "Mzee Mustafa atakaposikia hatafurahi. Tulipo tuna matatizo ya kutosha. Kuna watu wenye silaha - bunduki, bastola, nondo na mapanga waliofanya ghasia leo asubuhi katikati ya jiji. Kadhaa wamekamatwa, baadhi yamejeruhiwa, wawili wamekufa hapo hapo. Idadi ya wafu, bila shaka itaongezeka. Serikali na viongozi wa vyama vingine vya upinzani wanadai watu hao ni wetu."
Baada ya kuipeleka glasi mdomoni na kumeza, Kembo akaendelea, "Jambo hili la Dk. Makete si dogo. Linaweza kuharibu kila kitu. Watu kadhaa wanajua kuwa Mzee Mustafa ni rafiki yako, na unamsaidia katika kampeni yake. Baadhi yao ni maadui zetu. Lakini hakuna anaeijua historia yako ya kweli. Kila mtu anaamini kuwa Kassim Hashiri ameshakufa siku nyingi. Ikijulikana kuwa ndio wewe ..." Kembo akatikisa tena kichwa. "Hapana! Mzee Mustafa hatafurahi hata chembe."
"Mustafa ananihitaji mimi zaidi kuliko ninavyomhitaji yeye."Kwa hivi sasa ndiyo. Lakini atakapokuwa Rais ..."
"Hataweza kuwa Rais bila msaada wangu!"
"Bwana Kessy, usidhani uko peke yako unaemsaidia Mzee Mustafa ashinde katika uchaguzi ujao hata kama utajitoa ..."
"Ah! Sasa tunazungumza kama wapumbavu."
Alisema Kassim. "Ile ajali ilitokea saa nne asubuhi. Sasa ni saa tisa. Masaa matano yamekwishapita. Polisi wangezipata namba za gari yangu wangeshakuwa hapa zamani. Ingewachukua muda mfupi tu kujua anaemiliki na anapoishi."
"Dk.Makete angali hai." Kembo alimkumbushia.
"Dakika yoyote anaweza kuzinduka na ..."
"Ulisema una watu wako hospitalini?"
"Kwa hiyo?"
"Lazima nikuchoree picha?"
"Bwana Kessy, kutaka kuelezwa jina la mgonjwa na hali yake ilivyo ni jambo moja. Kutaka mgonjwa huyo amalizwe ni jambo jingine kabisa."
"Watu wako wameshafanya vitimbi vikubwa zaidi kuliko kumchinja lagalagamauti. Isitoshe, kila siku wewe hudai hakuna lisilowezekana."
"Hili litakugharimu pesa. Kitita cha kutakata."
"Usijali gharama. Niko tayari kutoa kiasi chochote kile. Milioni mbili, tatu..hata tano...hata kumi ikibidi! Mtu yule akipona na kunitaja maisha yangu yatakuwa hatarini. Kwa kosa la kujaribu kuua tu naweza kufungwa maisha, achilia mbali hayo makosa mengine."
Kembo akakubali kwa kichwa, macho yake yakimeta kwa matumaini. Akasema kwa sauti tulivu, ya kirafiki, iliyojaa huruma na upendo. "Niachie mimi."
Dk. Beka aliufungua mlango wa chumba cha mapumziko namba Namba 4 wakaingia wodini. Kilikuwa chumba kidogo chenye kitanda na kiti kimoja. Kwenye kiti aliketi Bessy, kalamu mkononi, kijitabu chake gotini. Kitandani alilala Mama Denny, Bi mkubwa wa makamo. Alikwishaamuka lakini macho yake yangali na machovu.
Kufunguliwa kwa mlango kulimfanya ayapeleke macho yake upande huo. Akamwona mwanae. Akasema, "Denny!"
"Mama!" Dennis akavuta hatua mbili ndefu na kukifikia kitanda. Akaketi nchani na kuufumbata mkono wa mamake. Akamuuliza
"Unajisikiaje sasa mama?"
"Sijambo."Sauti yake haikuwa madhubuti kama aliyoizoea Dennis. Alivikanda vidole vyake,alimwambia. "Punguza wasiwasi. Baba atapona tu."
"Oh! Denny! Nilishituka mno!"
"Hata mimi nilishtuka niliposikia. Baradhuli aliyeniarifu alisema hali ni mbaya sana."
Bi mkubwa akashusha pumzi. Dennis akaendelea. "Madamu ametoka thieta salama, atapona tu. Mjomba amemkagua sasa hivi. Amesema anaendelea vizuri, hana hali ya kutisha."
Kikapita kimya cha nukta mbili tatu. Dk.Beka akakivunja kwa kusema, "Denny, huyu ndiye Kachero Inspekta Bessy."
Dennis akageuzwa kichwa. Ajikuta anatazamana na msichana wa rika lake. Tena wa kuvutia. Na kwa mara ya kwanza tangu aingie humo humo ndani akaisikia harufu ya marashi anayoyapenda - ya Gucc. Akashangaa kimoyomoyo kwa nini vitu hivyo viwili, uzuri wa binti huyo na manukato yake, hakuvigundua mapema!
Ulipita muda ndipo Dennis akajitambua kuwa alikuwa anakodoleana macho na msichana huyo. Bila ya kujijua ikamtoka "Oh!" kwa sauti ndogo.
Bessy akanyoosha mkono. Dennis akaupokea. Akashangaa kuona haukuwa legelege kama alivyotazamia. Ulikuwa mkakamavu karibu sawa na mkono wa kiume.
Akasema, "Inasikitisha kukutana nawe mahali kama hapa. Ilifaa tukutane mahali pachangamfu zaidi."
"Kama vile kwenye karamu, au dansini?" Sauti yake haikuwa na stihizai hata chembe.Ilimfurahisha Dennis na kumpunguzia majonzi.
"Dr.Beka akauliza. "Umeambua lolote la kukusaidia kutoka kwa mama Denny, Inspekta?"
"Ameamuka punde tu." Alijibu Bessy. "Alichowai kunieleza ni kwamba Mzee Makete aliondoka asubuhi nyumbani kwenda benki kuchukua pesa."
"Hilo nilikuwa nikilifahamu. Katika vitu nyake vya mfukoni mlikuwa na kitabu cha hundi. Kinachoshangaza ni kwamba hakuandika hundi yoyote leo, na hali aligongwa wakati anatokea benki,na sio akienda benki."
"Ajali yenyewe ilitokeaje?" Dennis aliuliza.
"Nasikitika kusema hadi hivi sasa tunachokijua kwa hakika ni kidogo mno. Tunaamini baba yako amegogwa na Benzi jeupe nyuma ya Bnki ya Wakulima. Aliemgoga hakusimama, na hakuna aliewai kuchukua namba za gari. Tunashuku alimgonga kusudi.
Mdomo wazi kwa mshangao, Dennis akauliza. "Unamaana alitaka kumwua?"
"Nasikitika yaelekea hivyo." Alijibu Bessy.
Baada ya kushusha pumzi akaendelea, "Kwa hiyo inaelekea kuna mtu mwenye uhasama na baba yako. Uhasama mkubwa."
"Huo ni mzaha!" Dennis alimaka, akikiri kimoyomoyo alishindwa kutumia neno 'upuuzi' kwa sababu ya staha.
Bessy akainua mabega. Baada ya kupumua kwa nguvu, Dennis akauliza. "Ndiyo kusema huyo mwendawazimu amepuruchuka?"
"Ni mapema mno..."
Dennis akamkatiza. "Hamna fununu yoyote?" Akamtazama Dk. Beka . "Baba hakuwahi kusema lolote?"
Ni Bessy aliemjibu. "Katika maneno aliyoyatamka ni mawili tu yaliyosikika vizuri. 'kasi hashi.' Je yana maana yo...."http://pseudepigraphas.blogspot.com/
"Kassim Hashir!"
Wote wakageuza vichwa kumtazama mama Denny.
Kwa sauti yake dhaifu, akarudia,"Kassim Hashir!" Kisha akaongeza kwa uchungu "Oh,Mungu, hapana! Oh, Mungu wangu!"
*********************************
Kikoti alikuwa mdaku. Wakati akiusokota mpira wa maji, alipolipua, mawazo yake yalikuwa mbali. Hakuwa na furaha.Yeye alikuwa mtu asiyependwa kupitwa na jambo. Lakini leo, aliamini, palikuwa na jambo linalotaka kumpita. Na huo ni mwiko wa mdaku.
Mapema alichanganywa na vitendo vya mwajiri wake - kumwona akilikagua gari lake kwa uso mzito na kijasho usoni, kama vile lilikuwa na dosari kubwa; kumwona akimwonyesha Isidori sehemu ya mbele ya gari; kumwona akimpa koti lake jipya na la thamani.
Lakini juu ya yote, ilikuwa kumwona akimsimulia Isidori kisa kirefu. Haikuwa tabia yake. Tabia yake kwa watumishi wake ilikuwa ni kutoa amri. Neno moja au mawili tu. Basi kwisha. Siyo kutoa maelezo ya dakika kadhaa.
Hapana. Palikuwa na jambo linalotaka kumpita.
Kuhusu lile koti, moyo ulimwuma. Kwa nini asipewe yeye maskini wa Mungu? Isidori alishawahi kupewa nguo mara kadhaa. Si mpya na za zamani kama lile koti, lakini nguo ni nguo. Isitoshe, alikuwa akishonewa nguo za kazi.Juu ya hayo, ilikuwa dhahiri mshahara wake ulikuwa mkubwa kuliko wake. Mshahara na marupurupu. Na nafasi ya vitu vya... vya 'kuokota' katika jumba hilo.
Lakini, Kikoti aliiuliza nafsi yake, kama koti lie angepewa yeye angelifanyia nini? Asingeweza kulivaa. Yeye alikuwa mfupi na mwembamba. Na wala asingeweza kulipeleka kwa mshoni alipunguze. Ni dhahiri angeliuza.
Je, hilo ndilo lililomfanya Mzee asimpe yeye?
Alitaka kumpa mtu wa kuweza kulivaa na kumwona amelivaa muda wote? Kwa nini Isidori baada ya kulijaribu,alipotaka kulivua alikatazwa? Kikoti alikiona wazi wazi kitendo hicho. Hata kauli ya mzee aliisika - "A-a! Usilivue. Livae tu likuzoee....limekupendeza."
Kikoti hakudhani hivyo. Hakudhani lilimpendeza Isidori. Aliona limempwaya na halikuchukuana na weusi wake wa mpingo. Au ni maya? Kisa cha sungura na zabibu? Na lile gari je? Lilikuwa na dosari gani
Na ile risala je? Mbona ilikuwa ndefu vile? Na Mzee alizungumza kwa sauti ya chini, mara moja moja akimtupia jicho yeye, kama vile hakutaka amsikie, kama vile ilikuwa siri kubwa.
Hata hivyo alidaka maneno mawili matatu, kama vile 'ajali, heshima yangu, faini na fidia...'
Hapana. Lilikuwepo jambo linalotaka kumpita. Jambo kubwa. Asipokuwa makini, alijiambia, litampita kweli. Na huo ni mwiko kwa mdaku.
"Ni nani mtu huyo?" Bessy aliuliza kwa sauti kali. Lakini mama Denny alikwishageukia ukutani na kuanza kulia kimya kimya.
Bessy akainuka na kumfanyia Dennis ishara ya kichwa kutaka watoke nje. Wakati wakitoka nje. Dk. Beka alijongea kitandani kumfariji mke wa rafiki yake.
Mara tu baada ya kutoka na kufunga mlango, Bessy akauliza kwa matuamaini makubwa. "Ni nani huyo Kassim Hashir?"
"Sijawai hata kumsikia katika maisha yangu." Dennis alijibu uso ukiwa umemnywea. Bessy akakunja uso.
"Itakuwaje usimfahamu na hali wazazi wako wote wawili wanamfahamu?"
"Unategemea kuwa nawafahamu watu wote wanaofahamiana na wazazi wangu? Mimi ni mwanajeshi, wakati mwingi huwa sipo nyumbani."
"Inalekea babako na mamako wanamfahamu vizuri mtu huyo. Nadhani mama yako anaufahamu uhasama uliopo kati ya babako na mtu huyo. Lakini katika hali aliyonayo hawezi kutueleza lolote. Ni vyema tumwache atulie."
Dennis akakubali kwa kichwa.
Baada ya kuwaza kidogo, Bessy akasema. "Twende zetu Makao Makuu ukachukue gari la babako. Na tukapekue mafaili. Pengine huko Kassim Hashir si mgeni nasi."
"Itabidi nifike Makao Makuu yetu kwanza nikarudishe gari lao na kuomba likizo ya dharura. Ikiwa nimeweza kuchokoa vikaragosi vya vichakani hakitanishinda cha mjini."
*********************
Siku hiyo Kikoti 'aliokota' nusu chupa ya wiski iliyosahauliwa chini ya meza,kando ya bwawa la kuogelea. Aliiona chupa hiyo kwa macho yake makali mara tu alipotokeza nyuma ya jengo hilo, akitokea kwenye stoo ya kuhifadhia zana za kazi yake.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Alipoina na kuikota na kuifutika kotini, mwenyewe alidhani hakuna mtu aliemwona. Lakini Kassim Hashir alikuwa dirishani, ghorofani, akimtazama. Hakujali. Si kwa vile alikuwa na mambo makubwa zaidi akilini, bali nusu chupa ya wiski ilikuwa si chochote kwake. Aliona kama vile mtumishi wake amefanya jambo zuri kuondoa takataka. Kwa upande mwingine, kitendo hicho kilimwongezea fahari, furaha,na utamu wa ukwasi - kuona kuna watu dhalili wanaodiriki kuiba hata chupa karibu tupu.
Nje ya geti, Kikoti alielekea kwenye kituo cha basi akiwa ameridhika kabisa na vuno la siku hiyo. Alijua nini cha kufanya. Atakwenda moja kwa moja kwa Shangazi suzy anakokunywa mapuya kila siku. Hapo asingekosa mtu wa kuelewana naye kwa namna moja ama nyingine.
*******************************
Alasiri hiyo, ulifanyika mkutano mfupi katika ofisi ya Daktari Mkuu. Kama kawaida, mwenyekiti alikuwa Dr.Beka mwenyewe. Wengine walikuwa madaktari bingwa wanne waliomshughulikia Dk. Makete thieta.
Baada ya wote kuketi, Dk.Beka akasema, "Sawa. Nipeni mawazo yenu."
"Ana matumaini makubwa." Alisema bingwa wa kwanza. "Tumejitaidi kadri ya uwezo wetu. Sidhani kama kuna mtu angeweza kufanya zaidi ya tulichokifanya. Naweza kusema tumefanya kazi nzuri."
Dk,Beka kakubali kwa kichwa. Akamtazama bingwa mwingine.
"Jambo zuri ni kwamba alifikishwa hospitali haraka." Alisema bingwa huyo. "Hakuwai kuvuja damu ndani kwa undani. Na vitu viwili mhimu, moyo na ubongo, havikuathiriwa."
"Na alikuwa na bahati nzuri," Alisema bingwa wa tatu. "Sisi sote tulikuepo na hatukuwa na shughuli mhimu."
"Likini itamchukua muda kupona sawasawa."
Alisema bingwa wa mwisho. "Na hata hivyo hatakuwa kama alivyokuwa zamani. Ninashuku itabidi atembelee kiti cha magurudumu maisha yake yote yaliyosalia."
"Cha mhimu ni uhai," Alisema Dk.Beka. "Ninachoombea, apone." "Tuna imani atapona. Tumefanya kazi nzuri sana."
*********************
Masjala ya Makao Makuu ya Polisi ilikuwa kubwa. Ilijaa rafu na makabati ya mafaili. Pia mlikuwa na meza mbili tatu, lakini Bessy na Dennis walipoingia, meza moja tu - ile kubwa kuliko zote ndiyo ilikuwa na mtu. Alikuwa amevaa kiraia.
Alisema, "Karibu Inspekta." "Asante Robby."
Bessy akajibu, akivuta kiti. Akaketi na kumwashiria Dennis aketi kando yake.
"Mbona umeadimika, Bessy?" Robby aliuliza.
"Siku nyingi sijawa na kesi mhimu. Leo nimeamua kujipa moja. Wengine walikataa. Walidhani ni ajali ya kawaida."
"Sasa nikusaidie nini?"
"Tuna habari zo zote kuhusu mtu aitwaye Kassim Hashir?"
Robby akabonyeza vibatani, akaliandika jina 'Hashir' kwenye kompyuta iliyokuwa mezani pake. Mashine ile ikaanza kuchakarika,ilipotulia Robby akasema, akisoma kwenye kioo. "Tuna Hashir mmoja tu. Kassim Ismail Hashir. Namba ya faili yake ni 997/69...."
"Sitini na tisa!?" Bessy aliuliza kwa mshangao. "Una maana faili hilo lilifunguliwa miaka ishirini na nne iliyopita?"
"Ndiyo na likafungwa mwaka 1974"
"Baada ya miaka mitano? Ilichukua muda huo kuikamilisha kesi yake?"
"Hapana. Kesi yake haikuwai kukamilika. Kassim hakuwai kukamatwa. Afariki."
Bessy akamtazama Dennis,macho yake yakimsaili. Alipokosa jibu akayarudisha kwa Robby. Akamwuuliza, "Kesi yake ilihusiana na nini?"
"Kwa hilo, maka tulipekue faili lake."
"Unaweza kutupatia,tafadhali?"
"Bila ya tabu." Robby akainuka na kuelekea kwenye rafu za mwisho. "Inaweza kuwa mzee amekosea - si Kassim aliemgonga?"
"Sijui." Alijibu Dennis."Lakini kadri niwezavyo kukumbuka, sijawai kumwona akikosea."
"Kumbuka hakuwa katika hali ya kawaida."
Kabla ya Dennis hajajibu, Robby alirejea mezani akiwa na faili ambalo halikuonyesha dalili yoyote ya kuwa na umri wa miaka ishirini na nne. Bessy akalipokea na kulifungua. Lilikuwa na ukurasa mmoja tu na picha ya kijana wa kati ya mika ishirini na mitano na thelathini mwenye uso wa duara na macho makubwa. Baada ya Bessy na Dennis kuitazama kwa muda, wakausoma ukurasa huo.
Kifupi,ulieleza kwamba Kassim Hashir alituhumiwa kutorosha kiasi kikubwa cha fedha za kigeni, dhahabu, almasi, na madini mengine ya themani, na vipusa, pembe za tembo na ngozi za chui. Vyote hivyo alivitorosha wakati wa utawala wa fasishti Ibrahim Mbwelwa. Kassim aliyeyuka muda mfupi kabla ya Mbelwa kuangushwa.Ilihisiwa alikimbilia Ulaya alikolimbikizia utajiri mkubwa. Alifia Kenya, mwaka 1974 katika ajali ya gari.Chini ya maelezo hayo palikuwa na saini.
Bessy akauliza, "Hii siyo sahii ya Mzee Maliki?"
"Ndiyo, ni yake." Robby alijibu. Lakini wakati huo hakua Kamishna Msaidizi."
Bessy akaitazama saa yake. Akaunyakua mkono wa simu na kusema. "Nipatie Mzee Maliki, kama angalipo ofisini mwake."
"Tangu lini akaondoka kabla ya taa kuwashwa?"
Aliuliza opareta. Kisha akasema, "Zungumza nae."
"Mzee? Ni Bessy hapa.Nataka kukuona."
"Kuhusu?" Ilikuwa sauti nzito, tulivu."
"Kassim Hashir."
"Kassim Hashir? Sidhani kama namfahamu."
"Si ajabu. Ni miaka mingi imekwishapita. Ulimfungulia faili mwaka 1969. Nitakuja nalo faili hilo."
"Sawa."
Faili mkononi, Bessy akainuka na kumwambia Dennis, "Twende kileleni."
Kwa Shangazi Suzy palikuwa na mambo. Mojawapo lilikuwa ni lile la watu kutengwa kufuatana na daraja. Wateja wa daraja la kwanza - 'maofisa' waliwekwa chumbani, ambamo mlikuwa na kitanda maridadi, seti ya sofa, viti na meza. Labda waliwekwa humo kwa vile hawakuwa wengi. Na walikuwa wasafi. Na hawakupendelea sana mapuya. Zaidi walikunywa bia na konyagi.
Wateja wa daraja la pili - 'waungwana,' waliwekwa ukumbini kwenye mabenchi. Hakuna alieweza kukisia sababu ya wao kuwekwa hapo. Wengi wao walikuwa wa umri mkubwa. Mno walikunywa mapuya. Waliagiza konyagi kwa nadra. Bia - mwaka mara moja. Sikukuu hadi sikukuu.
Wateja wa daraja la tatu na la mwisho - vichwa vya panzi - waliwekwa uani, ambako walikalia chochote kile, kuanzia matofali hadi chini aridhini.
Sababu za wao kuwekwa huko zilikuwa wazi. Kwanza walikuwa wengi, na wengi wao walioga na kufua kauka nikuvae, Jumapili hadi jumapili. Pili walikuwa hususani watu wa mapuya. Tatu, walikuwa wadoezi na wagandaji - yaani nusu lita ilimfanya mtu agande hapo tangu asubuhi mpaka usiku wa manane. Na nne walilipata jina lao 'vichwa vya panzi' - kwa sababu walikuwa hawakawii kulewa . Na hapo huwa wenye kelele, wagomvi, waimbaji na wachezaji.
Lakini ajabu ni kwamba hakuna hata mmoja, hata siku moja, alielalamikia ubaguzi huo. Kila mmoja alipajua mahali pake na aliridhika napo.
Lakini kwa Kikoti alikuwa tofauti kidogo. Yeye alijipandisha ngazi moja moja. Alianzia kwa 'vichwa vya panzi' alipokuwa hana kazi maalum, ndiyo kwanza aingie jijini.
Akahamia kwa 'waungwana' alipopata kibarua katika kampuni moja ya ujenzi. Akahamia kwa 'maofisa' alipota kazi ya kuhudumu huko Buffalo Hill.
Hata huvyo, kwa kuwa hakuwa mgeni mahali popote, na alikuwa 'memba' kila siku,ilikuwa juu yake mwenyewe kuchagua pa kuketi - aghalabu kutokana na mfuko wake au mwaliko.
Siku hiyo, mfuko wa karatasi mkononi, alipitiliza moja kwa moja hadi chumbani akawakuta 'maofisa' wawili wa kudumu, Bob na Butu, wamekwisha fika,walikuwa wakinywa konyagi.Bob, kwa sababu ya kitambi chake, katika nguo za kawaida alionekana kama meneja wa benki.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Bila ya kusema neno, Kikoti aliitoa chupa ya wiski na kuikita mezani. Bob akaitazama kwa makini. Akainua uso na kuuliza. "Umeipata wapi wiski hii, Kikoti? Ni ya thamani sana!"
"Kanipa tajiri yangu." Kikoti aliongopa, macho makavu. "Huyo ndie tajiri wa kumtumikia. Nikichoka kufokeana na madereva wakorofi, nitakwambia unipeleke na mimi nikaombe kazi."
"Shangazi yupo wapi utupe glasi?" Kikoti akauliza. "Atakuwa wapi kama sio kwa vichwa vya panzi?" Butu alimwuliza.
**********************
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment