Simulizi : Nyuma Yako (3)
Sehemu Ya Nne (4)
Ikiwa ni usiku, mandhari haya yakawa yamenawiri kwa mwanga toka kwenye kwenye taa zilizonakshiwa kwa urembo. Taa hizo zilikuwa za rangi mbalimbali mathalani bluu, nyekundu na manjano.
Mahali palikuwa panavutia haswa. Viti na meza vilikuwa vichache vikipeana nafasi ya faragha. Kwa mbali wimbo ulikuwa unapiga, wimbo wa mahadhi ya 'country' akiwa anaimba mwanamke maarufu wa miondoko hiyo, kwa jina Dolly Parton.
Jack aling'aza macho yake, hakuwa amefika hapo muda, ndani ya muda mfupi mhudumu ambaye amevalia sare nadhifu alifika na kumwonyesha tabasamu pana.
"Naweza kukusaidia?"
"Oh! Ndio, tafadhali waweza niletea sharubati ya matufaha tafadhali?"
"Bila shaka!"
Mhudumu akaenda zake na baada ya punde akaleta glasi kubwa iliyojaa sharubati ya baridi. Jack akashukuru na kisha mhudumu akaenda zake baada ya kuonyesha tabasamu.
Jack akakaa hapo kwa kama robo saa mbele ndipo Kelly akaonekana. Alifurahi sana kumwona. Alimkarimu mwanamke huyo kwa furaha kisha mhudumu akaja na mwanamke huyo kuagiza kinywaji laini pia.
"Ni muda mrefu sasa!" Alisema Kelly. "Unaendeleaje lakini?"
"Niko poa," Jack akajibu akipandisha mabega. "Maisha yamekuwa yakitutenganisha, si unajua?"
"Ni kweli!"
Kukawa kimya kidogo. Kelly akanywa mafundo mawili kisha akamtazama Jack aliyekuwa anatazama glasi yake. "Jack, nimesikitishwa sana na kile ulichonambia. Pole, ndiyo maisha."
Jack akatabasamu kiuongo.
"Yah! Ni kweli. Lakini sijutii sana."
"Kweli? Ni kazi gani sasa unafanya kuingiza kipato?"
"Aahm, sifanyi kazi yoyote kwa sasa."
"Kabisa? Sasa unaishije?"
Jack akatabasamu. Sasa hivi tabasamu lake lilikuwa la kweli.
"Usijali, utajua kadiri muda unavyosonga."
"Ni vibaya kujua saaa hivi?"
"Hapana, ila si muda muafaka."
Kelly akanywa juisi yake na kunyamaza.
"Nadhani sijakukwaza," Jack akasema kwa tahadhari.
"Hapana! Haujanikwaza!" Kelly akajibu kisha akatabasamu kana kwamba ameshangazwa na swali hilo.
"Unajua mimi si mzoefu sana wa wanawake!"
"Kivipi? Umekuwa kwenye uchumba kwa muda mrefu, ama ulin'danganya?"
"Hapana. Ni kweli kabisa. Mimi na vio tulidumu kwa muda mahusianoni lakini namna ambavyo mahusiano yetu yalivyoishia inanifanya niamini hiko nilichokisema. Mimi si mzoefu wa wanawake."
"Kumaanisha nini Jack?" Akauliza Kelly. Sauti yake ilikuwa laini na nyororo. Alimtazama Jack machoni kwa sura iliyoguswa kihisia.
"Nilifanya kila jambo lililopo ndani ya uwezo wangu kumfurahisha Vio lakini vyote hivyo havikutosha. Bado alikuwa na mwanaume mwingine. Sijui ni namna gani alikuwa anataka. Sikujua anahitaji nini!"
"Usihuzunike Jack. Kila kitu hutokea kwa sababu, naamini hivyo."
Kukawa kimya kidogo. Ni Jack alikuwa amatafakari jambo kichwani. Kelly alimtazama mwanaume huyo na kumuuliza kwa sauti ya chini, "nini Jack?"
Kwa kumtazama tu ungebaini Jack alikuwa ameguswa kihisia. Uso wake ulibadilika, macho yake yakapooza.
"It's ok, Jack," Kelly akasema akimshika Jack bega. "Huna haja ya kunung'unika vivyo kila uchwao. Acha lililopita liende."http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Jack akanywa juisi mafundo manne makubwa kukausha glasi yake. Angalau moyo wake ukawa umetulia sasa. Akavuta hewa ndefu kwa pua yake na kuishusha.
"Samahani, Jack. Sikujua kama tutafikia huku!" Kelly akaomba radhi.
"Usijali," Jack akasema na punde akatazama kumtafuta mhudumu. "Unakula nini?" Akamuuliza Kelly. Muda si mrefu mhudumu akaja wakaagiza chakula na kula huku wakiendelea kupiga soga.
Walifurahi sana.
Lakini ghafla furaha yao ilifikia kikomo pale Kelly alipomuulizia bwana Marshall. Jack hakupenda hilo jambo. Aliona kama bado mwanamke huyo ametwaliwa na Marshall kichwani.
Kitu hicho kilijidhirihisha tangu Kelly alipoonana na Marshall huko Hongkong. Kipindi hiko halikuwa jambo kubwa kwa Jack Pyong lakini sasa hivi lilikuwa linamuumiza.
Kwa kiasi tayari alikuwa ameshamuingiza mwanamke huyo kwenye korido ya moyo wake.
"Sikudhamiria kukuudhi, Jack!" Alijitetea Kelly. "Sikutaraji kama ningekukwaza. Nisamehe."
"Usijali. Ni ujinga wangu, nilipaswa kujizuia."
"Nilitaka tu kufahamu hali yake. Naamini utakuwa unajua yupo wapi."
Jack akanyamaza kimya asitie neno. Badala yake akaendelea kutafuna. Basi Kelly kuona hivyo, akaona aachane na hiyo mada.
Wakala na kama baada ya nusu saa wakaongozana kutoka eneo hilo. Jack alilipia 'bill' na pia akamkarimu Kelly atumie usafiri wake kumpeleka huko anakokaa.
Pasi na tatizo, Kelly akajumuika na Jack kwenye safari iliyogharimu masaa mawili mpaka kufikia kikomo. Mbele ya nyumba kubwa ghorofa, Jack akasimamisha gari lake na kumtazama Kelly.
"Nadhani tumefika!"
"Yah! Nashukuru sana Jacky. Nashukuru sana Jack, umekuwa mkarimu sana kwangu."
"Usijali. Ni kawaida tu japo naumia sana kukuacha uende."
"Kweli?"
"Yah. Nilishajisahau kwa muda mchache niliokuwa na wewe. Nilidhani ni jambo la kudumu!"
Kidogo wakatazamana. Kelly akacheka kwa haya.
"Ulikuwa unasemaje, Jack?" Akauliza kwa sauti ya puani. Kope za macho yake zilikuwa zimelegea.
"Sina usemi. Inabidi niamini kila lenye mwanzo lina mwisho wake."
Kelly akatabasamu. Akamshika Jack mkono akiwa anamtazama mwanaume huyo. Kidogo Jack akapoteza akili.
"Nimefurahi sana kuwa na wewe. Umeniondoa upweke wangu wa siku nzima!"
"Kwani ulikuwa mpweke?"
"Ndio," Kelly akajibu akikuna kichwa chake kwa kucha ya kidole cha kati. "Nadhani nimezoea sasa japo kuna muda inazidi. Nimekuwa nikiishi peke yangu tangu nilipokanyaga Marekani!"
"Ndiyo maana hata lafudhi yako bado haijabadilika!" Jack akatania, wakacheka. "Sasa naweza kuja kukuondolea upweke kwa leo?" Jack akauliza. Alijitahidi macho yake yamtazame Kelly.
Kelly akatabasamu.
"Bwana, mbona itakuwa mapema sana Jack?" Akauliza kwa sauti ya puani. Uso wake ulisaliti maneno yake.
***
Mlango ulifunguka akaingia Kelly.
"Utaniwia radhi, sebule yangu ipo hovyo sana!"
Punde naye Jack akazama ndani. Macho yake yalipekua sebule kwa upesi. Ilikuwa ni sebule yenye samani za kawaida na kwa chini kulikuwa makaratasi kadhaa hususani ya biskuti na chokoleti.
Runinga ndogo ukutani. Picha kadhaa za Kelly ukutani na kati ya picha hizo kuna mojawapo ilikuwa ni ya bendera ya New Zealand. Sofa mbili za ngozi na zulia rangi ya kahawia.
Jack akatulia hapo sebuleni na Kelly akaingia ndani. Kelly aliporejea, wakakaa pamoja kwa kama lisaa hivi kabla watu hawa hawajajikuta wakianza kutomasana, kushikana na kujitupia kitandani.
Walifanya lile tendo na kuishia kulala fofofo. Katikati ya usingizi, simu ya Jack ikaita sana. Alikuwa ni Marshall anampigia.
Bwana huyo akiwa ameketi na Danielle alikuwa amejawa na mashaka juu ya Jack, rafiki yake. Hakuwa amesema kama atalala huko bali atarejea.
Simu iliita mara nne, mara Kelly akaamka na kuitazama. Akaona ni jina la Marshall! Ubaya simu hiyo ilikuwa inaonyesha pia na namba ya mpigaji.
Basi upesi Kelly akanakili namba ya Marshall kwenye simu yake kisha akaendelea kulala.
"Yani huyu fala hapokei!" Marshall akalalama. Alitupia simu yake chini akiwa na uso wa tafakuri.
"Pengine atakuwa amelala huko. Usihofu sana," Danielle akasema akimshika Marshall bega.
"Dani," Marshall akaita na kuuliza, "unajua password ya tarakilishi?"
"Ipi? Ile anayotumia Jack?"
"Yah! Nilijaribu kuifungua lakini sikufanikiwa."
"Naijua."
"Naomba unifungulie."
Danielle akamfungulia Marshall tarakilishi na upesi bwana huyo akazama kwenye jumbe kati ya Jack na Kelly.
Alipotazama jumbe hizo kadhaa akajikuta ana hamu ya kujua zaidi nini kitakuwa kimemtokea Jack na Kelly huko walipo.
Alichukua tena simu yake na kupiga lakini majibu yakawa ni yaleyale. Jack alikuwa hoi haswa. Alilala kana kwamba mfu. Kwenye majira ya saa tisa inayotafuta saa kumi ndipo Jack akashtuka na kukodoa.
Usingizi ulikuwa umekata. Akajitazama pale alipokuwa amelala kisha akaufyagia uso wake kwa kiganja. Punde akapiga mihayo.
Alipotazama kando akamwona mwanamke Kelly akiwa amejilaza anakoroma kwa mbali. Kidogo akatekwa na mawazo.
Kama vile mtu ambaye hajui hapo amefikaje, akajiulizauliza kabla hajavuta simu yake kutazama muda. Loh! Muda ulikuwa umeenda! Alijisemea mwenyewe kifuani.
Alibaini pia kuna 'missed calls' kadhaa, akafanya namna kuzitazama.
"Aagh! ... Marshall!" Akajikuta akinong'ona huku amefumba kinywa. Alijiona mkosefu. Hakumtaarifu bwana huyo kama atalala.
Basi upesi akaandika ujumbe kuomba radhi na kueleza ya kwamba yu salama.
Alipomaliza akaweka simu kando na kwenda bafuni kukojoa. Alipokuwapo huko akanawa pia na uso. Akajitazama kwenye kioo akiwa na akili chafu kichwani.
"Ni lazima nitakuwa handsome!" Alijisemesha akitabasamu mwenyewe kama mwehu. "Inanipasa niamini vivyo kwani kama nisingekuwa handsome basi Kelly asingenikubalia."
Hoja hiyo ikampa furaha sana moyoni mwake. Akakagua bafu kwa ujumla kisha akarudi zake chumbani. Kabla hajajilaza, akabaini kijitaa cha simu yake kilikuwa kinawakawaka kwa kukonyeza.
Kijitaa hiko kilikuwa ni kielelezo kwamba kuna 'notification' simuni.
Akafungua simu yake na kutazama. Akakuta ujumbe toka kwa Marshall. Hakuwa amelala? Akajiuliza akiufungua ujumbe huo.
"Kuwa makini," ujumbe ulisomeka vivyo. Jack akaguna kwa kutolea hewa puani kisha akaandika, "najua kujilinda Marshall. Haukumbuki nilikuja kuwakomboa kule mlipotekwa?"
Akatuma ujumbe huo kwa tabasamu. Punde ujumbe ukaingia kumjibu.
"I am serious."
Naye akabofya vitufe kujibu,
"Hata mimi nipo serious." Alipotuma ujumbe huo akaweka simu pembeni na kujilaza zake. Alimuwazia kidogo Marshall. Ina maana anamwonea wivu ama?
Akajikuta anatabasamu. Mbona mimi simwahangaikii? Akaendelea kuwaza. Kwanza nimemwacha na Danielle peke yake huko nyumbani, muda wa kunitafuta anatolea wapi?
Basi aliendelea kuwaza akijivutia usingizi lakini hakuupata abadani. Alijuta hata kwanini aliamka. Hakuwa na dalili kabisa.
Kukesha kwake usiku kulikuwa kumemuathiri.
Alipojilaza kwa muda mrefu pasipo usingizi, akanyanyuka na kuketi kitako. Kulikuwa ni kiza lakini macho yashazoeza hivyo aliona vema tu.
Akatazama juu na chini na basi punde akafuata kabati la Kelly na kulifungua. Kabati hilo lilikuwa limesimikwa ukutani. Ilikuwa ni samani nzuri inayovutia.
Alitazama kwa muda mfupi akabaini boksi fulani gumu lililokuwa limekaa kwenye kona ya kabati. Akagusa boksi hilo, lilikuwa ni la chuma na zito.
Akajiuliza kuhusu hilo lakini hakujisumbua sana, akatoka hapo aende zake sebuleni. Bila shaka Kelly angemkuta hapo kabatini asingependezwa nalo, alijiwazia mwenyewe.
Hapo sebuleni akawasha runinga na kutazama. Alikaa sana hapo mwishowe akapitiwa na usingizi ikiwa ni saa kumi na mbili kasoro asubuhi!
**
Kelly alifungua macho yake taratibu na kuangaza. Hakumwona Jack kitandani. Alikodoa kutazama chumba kizima lakini bado hakumwona mwanaume huyo.
Alinyanyuka na kutupia macho yake kwenye mlango wa bafu huku akisimamisha masikio kuskiza kama mwanaume huyo yupo huko, napo akatoka kapa.
Basi akalazimika kutoka chumbani aende sebuleni, huko akamkuta Jack akiwa amelala. Angalau akashusha pumzi.
"Jack ... Jack! ... wewe Jack!"
"Naam!" Jack akatikia akirembua. Alikuwa ameelemewa na usingizi.
"Mbona umelala hapa?"
Jack akatazama alipokuwapo. Ni kana kwamba alisahau kuwa amelala hapo. Alipiga mihayo na kujinyoosha. Jua lilikuwa limeshachomoza. Aliamka na kumsalimu Kelly asieleze hata sababu iliyomfanya akalala hapo.
"Nataka kwenda chuo sasa," alisema Kelly.
"Sawa, tujiandae. Hata mimi yanipasa kuondoka hivi sasa."
Basi wakarejea chumbani, Kelly akavua nguo na kujiveka taulo kisha akaenda zake bafuni. Kitendo cha mwanamke huyo kufungua kabati ili achukue taulo, kikamkumbusha Jack kuhusu ile boksi aliloliona kabatini hapo awali.
Kelly alipoanza kujimwagia maji, Jack akasogelea kabatini. Kabati halikuwa limefungwa tangu Kelly alipotoa taulo lake.
Jack akatazama boksi hilo. Nalo halikuwa limefungwa. Lilikuwa limechorwa alama ya kopa nyekundu juu ya kifunikio chake.
Akafungua boksi hilo na kutazama ndani, kulikuwa na nyaraka kadhaa kama vile passport kadhaa, makaratasi ya benki na pass. Lakini pia kulikuwa na bunduki ndogo!
Hakuwa na muda wa kutazama zaidi, alitoka papo na kurejea kitandani. Muda si mrefu Kelly akatoka bafuni akiwa anajifutafuta.
"Heater yangu imefeli. Itabidi uoge na maji ya baridi."
"Haina shida," Jack akasema akisimama. Naye akaelekea bafuni.
Akiwa anaoga, Kelly akaendelea kujifuta. Mwanamke huyo alipomaliza, akaendea kabati lake apate kutoa mafuta ya kujipaka mwili.
Kabla hajabeba mafuta hayo na kuondoka zake, akaona kuna kitu hakipo sawa. Ilikuwa ni boksi lake. Kishikio chake kilikuwa kwa juu kitu ambacho kidogo kilimpa shaka.
Hakukumbuka kama aliacha boksi hilo vivyo.
Basi akalifungua upesi na kutazama ndani. Kila kitu chake kilikuwa sawa. Akashusha pumzi akitafakari.
Ni mawazo yangu ama?
Alichukua mafuta na kujipaka. Akatengenezea nywele zake kwa kutumia kioo cha kabati kisha akavaa nguoze. Hakujiremba wala kupaka chochote usoni.
Bado alikuwa mrembo.
Kidogo naye Jack akatoka akajiandaa wakatoka na Kelly. Walijipaki kwenye gari Jack akiadhimia kumbeba Kelly mpaka chuoni kisha yeye aende zake na safari.
KWANINI KELLY ANA PASSPORT KADHAA? NA BUNDUKI PIA NI YA NINI?
**
"Ni siku ya pili sasa," alisema Marietta akimtazama mwanamke fulani aliyevalia baibui nyeusi. Mwanamke huyo alikuwa na pua nyembamba ndefu, macho makubwa na lips nyembamba. Mikono yake ilipambwa na hina.
Makamo ya umri wake ni arobaini.
Mwili wake ulikuwa ni mwembamba na sauti yake nyembamba ya chini. Kwa jina Zainab.
"Ngoja, Shanny," alisema Zainab. "Leo atakuja kuonana na wewe kama alivyoahidi."
"Lakini muda umeenda sana. Ni mchana hivi sasa, kuna mahali nataka kwenda!"
Kabla Zainabu hajatia neno, mara mlango ukagongwa akaingia mwanaume aliyevalia kanzu rangi ya samawati. Alikuwa ni jamaa mrefu mwenye ndevu nyingi nyeusi, kichwani amejifunika kiremba.
Nyusi zake zilikuwa nene na macho yake yalikuwa makubwa. Kwa makamo alikuwa anawiana na Zainab. Jina lake ni Mahmoud.
"Asalaam aleykum!" Akasalimu kisha akaketi kitini.
"Umeniweka sana. Kulikuwa na shida?" Akauliza Marietta.
"Ndio, kulikuwa na tabu kidogo, Shanny, lakini nadhani sasa kila kitu kitakuwa poa," alisema Mahmoud. Sauti yake ilikuwa inatetema.
Basi kidogo Marietta na Mahmoud wakaondoka hapo na kwenda kujipaki kwenye gari kuondoka zao. Zainab akawatazama wakiyoyoma kisha akanyanyua mikono yake na kusema,
"Alhamdulillah!"
Akarudi zake ndani.http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Ndani ya muda mfupi Marietta ambaye huku anatambulika kama Shanny akafika kwenye jumba moja kubwa sana la kifahari. Hapo gari likasimama na wakajitua.
Kwenye uwanja wa nyumba kulikuwa na magari takribani kumi na mbili na yote yakiwa yale ya kifahari, bei mbaya. Magari hayo yalikuwa yameandikwa namba kwenye ‘plate’ yani moja, mbili, tatu na kuendelea.
Walipokelewa na wahudumu wawili ambao wamevalia hijabu. Wanawake wembamba warefu wenye matabasamu mazuri kabisa kisha wakaelekezwa mpaka mahali pa kumsubiria mwenyeji.
Mahali hapo palikuwa na makochi yenye maumbo ya mitumbwi. Makochi hayo yalikuwa yamejaa minofu ya magodoro huku yakiwa yamefunikwa na kitambaa kigumu kilichodariziwa na uzi wa dhahabu.
Kwa chini kuliwa na zulia zito la manyoya, rangi nyeupe. Manyoya ya zulia hilo yalikuwa ni marefu kiasi kwamba miguu ya wageni ilikuwa imepotelea manyoyani!
Kwa juu kulikuwa na taa kubwa zenye nakshi zikininginia. Ukutani kulikuwa na urembo wa kila aina mathalani rangi mbalimbali, marumaru, mawe na pia picha kubwa kubwa.
Kwa hapa wanapopumzikia wageni, kulikuwa na picha nne kubwa za kijana wa kiarabu aliyevalia nguo za kisherehe. Sare nyeupe zenye mkanda wa dhahabu, kofia ameweka kwenye kwapa la mkono wake wa kushoto na jambia refu amelishika kwa mkono wake wa kuume.
Kijana huyo alionekana mkakamavu, lakini zaidi anayeahidi kwa yajayo. Mdomo wake uliozungukwa na ndevu ulikuwa unatabasamu na macho yake ya ukubwa wa wastani yalikuwa yanakodoa.
Kidogo, kama baada ya dakika tano tangu Marietta na Mahmoud wafike hapo, akaja mwanaume aliyevalia kanzu ya thamani. Kichwani alikuwa amevalia baraghasia yenye unyoya uliodondokea kushoto mwa uso wake.
Alitabasamu alipomwona Marietta na hapo ndipo picha yake kamili ikaja. Alikuwa ni yule mwanaume aliyebandikwa ukutani! Kwa jina ni Abdulaziz Mohammed.
“Nimefurahi kukuona Shanny,” alisema Abdulaziz tabasamu lake likiongezeka upana. Marietta akamjibu kwa tabasamu la uongo.
“Niambie, kuna tatizo? Mbona uso wako hauna furaha?” akauliza Abdulaziz.
“Unajua kwanini,” akasema Marietta. “Nadhani utakuwa umebadili mawazo yako kama vile tulivyoongea.”
Abdulaziz akatabasamu. Lilikuwa ni tabasamu la wongo. Aliweka mkono wake kwenye akasugua hapo akiwaza.
“Shanny, si rahisi kama unavyowaza,” akasema Abdulaziz. “Ninajitahidi kadiri niwezavyo lakini bado inakuwa ngumu. Nipatie muda zaidi.”
“Mpaka lini?” Shanny akapaza sauti. Mishipa ya shingo ilikuwa imemsimama akikodoa macho. Abdulaziz alimtazama pasipo kusema jambo, na punde Marietta akatambua alichokifanya si sahihi.
Akashusha pumzi ndefu na kuomba radhi. “Sikudhamiria kufanya vivyo. Samahani kwa kushindwa kujihimili.”
“Usijali, lakini nadhani tumeelewana,” akasema Abdulaziz kisha akanyanyuka.
“Mbona unaenda?” Marietta akatahamaki.
“Tumemalizana,” Abdulaziz akamjibu kisha akataka kwenda zake.
“Ngoja!” Marietta akasimama. “Naomba nisamehe upuuzi wangu, sikudhamiria.”
Abdulaziz akamtazama mwanamke huyo kisha akamsogelea karibu na kumtazama machoni. “Kama ningelikuwa sijakusamehe, basi ungelikuwa umeshakufa muda mrefu tu.”
Aliposema hayo akamgeuzia mgongo Marietta.
“Abdul! Tafadhali. Ulichokuwa unakitaka umeshakipata sasa. Kuna nini kingine?” Marietta alizungumza nusu ya kulia. Abdulaziz akamtazama kwa macho ya kebehi alafu akamuuliza, “Una uhakika nimekipata?”
“Kwani ni nini unataka?” Marietta akauliza.
“Utakijua muda si mrefu ni nini nataka. Upo Morocco, ardhi jua linapolalia. Hauna haja ya kuhofia. Kama unataka ulinzi, nitakupatia kama linavyolindwa hekalu!”
Abdulaziz alipomaliza kusema vivyo akaenda zake. Marietta akamtazama Mahmoud. Mwanaume huyo alikuwa anatazama akifinyafinya vidole vyake.
“Mahmoud, ulikuwa unayajua haya yote sio?”
Marietta alimsogelea Mahmoud na kurudia swali lake kwa ukali. “Kwanini haukuniambia Mahmoud?”
“Usingenielewa, Shanny” Mahmoud akasema kwa upole kisha akasimamisha uso wake kumtazama Marietta. “Niliona nikuache ujionee mwenyewe.”
“Siwezi nikakubali!” Marietta akafoka. “Siwezi nikakubali kabisa! Kabisa!” macho yake yalijawa na machozi upesi. Mdomo wake ulipinda kona taya zikitetemeka.
“Tafadhali, Shanny, naomba twende. Tutaongelea mengine huko. Hapa si mahala sahihi, labda tu kama unataka kufa,” Mahmoud akasihi. Basi wakaenda nje na kujipaki kwenye gari. Wakati huo Abdulaziz akiwa dirishani anawatazama.
**
Saa tisa jioni …
Zainab alijaza kahawa kikombeni kisha akakisogezea kwa Marietta. Alipofanya vivyo, akamiminia pia na kwenye vikombe viwili zaidi kisha akaketi. Kikombe kimoja akachukua Mahmoud na kilichobaki Zainab mwenyewe.
Marietta alikuwa amenywea. Ni kama vile hakuona kikombe alichopewa. Macho yake yalikuwa yanatazama meza lakini fikra zikiwa mbali.
“Ulisema unahitaji kahawa,” Zainab alisema kumshtua mwanamke huyo. Marietta alipozinduka akaangaza, akakidaka kikombe na kunywa fundo moja. Mahmoud na Zinab walikuwa wanamtazama.
“Pole sana, Shanny,” akasema Mahmoud. “Kama kuna kuna kitu ningekushauri hivi sasa basi ni kuondoka Morocco haraka iwezekanavyo. Si salama tena kwako.”
Marietta akanywa kahawa mafundo mawili. Hakusema jambo. Aliweka kikombe mezani akatulia.
“Abdulaziz anataka nafasi ya baba yake,” akasema Mahmoud. “Ni kijana wa mwisho hivyo ni wazi, ni ngumu kwake yeye kuwa mfalme mbele ya kaka zake wanne waliomtanngulia. Hivyo mateka wake watamfanya apate haki hiyo ya lazima anayoililia.”
Hapo Marietta akanyanyua uso wake na kumtazama Mahmoud kwa umakini.
“Lakini sivyo tulivyokuwa tumekubaliana!”
“Ni kweli. Alikulaghai. Mahmoud sio mtu wa kutumia akili lakini kwa hili alituzidi. Ametufanya tuonekane wapumbavu.”
“Na kisha akifanya vivyo?” Marietta akauliza.
“Akishakuwa mfalme, bila shaka ataanzisha vita ya kisasi dhidi ya Marekani,” akasema Mahmoud. “Kitu ambacho kitaweka taifa hatarini. Bado hatuna uwezo wa kupambana na Marekani!”
Marietta akashusha pumzi. Kidogo akatekwa na mawazo na kukumbuka mbali sana.
Kichwa chake kilimpeleka ndani kabisa ya ikulu mwaka mzima uliopita. Akiwa amesimama koridoni, alichungulia ndani ya chumba alimokuwa mumewe. Mwanaume huyo akiwa amekwisha vaa suti yake, alikuwa anaongea na mtu kwenye simu.
“Ndio, hakikisha familia yangu inakuwa salama tu. Niko tayari kuupoteza Uraisi ila si familia yangu … nitafanya chochote mnachotaka … I will take the consequences ...”
Hakuishia hapo, akakumbuka mpaka siku ambayo alikuwa amesimamisha gari lake nje kidogo ya uwanja wa ndege mpaka pale alipopokea taarifa kuwa zoezi la kumteka Raisi limekamilika!
Na zaidi, akakumbuka pia siku alipotoa maagizo kuwa nyumba ya bwana Ian ichomwe moto.
Kumbe si Ian aliyechoma nyumba yake na kupotea, bali ni Marietta! Baada ya Ian kumtaarifu mwanamke huyo, akamwambia atumie nafasi hiyo kupotea kwani ni wazi atakuwa anatafutwa na serikali kwa kutuhumiwa kumpoteza Raisi kwani siku hiyo alikuwa zamu.
Zamu ambayo Marietta alimfanya asiitekeleze kwa kuficha nguo zake punde walipotoka kufanya mapenzi.
Wakati Ian akipanga yake huko Ujerumani, Marietta aliyapanga yake Marekani. Ian alidhani anamtumia Marietta, ila yeye ndiye aliyetumika kwa kufanyiwa ‘framing’ ingali Marietta akiwa huru. Hakuna aliyemdhania.
Mwanamke huyo hakutaka kabisa mumewe kwenda Ujerumani baada ya kuona ataenda kupoteza kila kitu kwa mwanamke ambaye ni mcheza ngono sababu tu amemzalia mtoto.
Aliona ni kheri, akamtoa mumewe sadaka kwa familia aliyobebea ubini kuliko kumpoteza kwenye mikono ya ‘malaya’.
Shanny.
**
*SEHEMU YA 21*
Lakini aliwezaje kuyafanya yote hayo?
Ni kwa kipindi kifupi sana, ndani ya siku nne tu, Marietta aliweza kubadili mchezo wote ukawa juu chini. Baada ya kugundua kuwa ataenda kupoteza kila kitu, Marietta aliwasiliana na Mahmoud, binamu yake wa mbali, akamwambia hali ilivyo akiwa hatambui kabisa anachotaka kukifanya.
Kwakuwa Mahmoud anafanya kazi kwenye kasri ya mfalme na alikuwa ana mahusiano mazuri na bwana Abdulaziz, wakasuka mipango katika muda mfupi mno ambapo Abdulaziz alimtafuta shushushu ngangari na timu yake (mercenaries) akawakabidi kazi ya kumsaidia Marietta kufikisha lengo lake.
Mashushu hao wa viwango vya juu kabisa, wakiwa wanashirikiana na Marietta aliyekuwa anachota taarifa toka kwa Ian, wakafanikiwa kuwapata wanaume watatu wa USSS na kuwamaliza kabisa kisha wakachonga sura zao na kwenda kumteka Raisi uwanja wa ndege!
Walipomaliza zoezi lao wakasafisha pia na wale waliokuwa wanaonekana ni hatarishi kwa siri zao, akiwemo bwana O’neil, rafiki wa Raisi, na wanaume wengine watatu kisha wakaacha wenzao wawili kuendelea kutazama hali.
Lakini haya yote yalifanyika kwa Marietta na familia ya ubini wake kuahidiwa pesa kubwa sana huku Abdulaziz akisema anataka taarifa kadhaa tu toka kwa Raisi huyo kuhusu Marekani.
Lakini mpaka muda huo hakuna chochote ambacho kilikuwa kimetolewa na Abdulaziz zaidi tu ya ahadi. Hata sasa Marietta hakuwa anataka pesa tena, bali tu mumewe awe huru na yeye apotelee zake mbali.
Kitu ambacho Abdulaziz hakuwa radhi kukiafiki.
**
Usiku wa saa sita …
Marshall alikuwa ameketi kwenye kiti akitazama tarakilishi yake ndogo mezani. Alikuwa amezama haswa. Yu bize akichati mtandaoni.
Alikuwa akiandika na kusoma jumbe kadha wa kadha. Lakini akaunti aliyokuwa anatumia haikuwa yake bali ya Jack Pyong, na mtu aliyekuwa anachat naye hakuwa mwingine bali Kelly.
Wakati huo Marshall akifanya hayo, Jack alikuwa amelala fofofo kitandani. Kwa makusudi, Marshall alimtilia rafiki yake madawa kwenye soda ili apate kutimiza adhma yake.
“Marshall,” sauti ya kike ikamuita. Hakusikia. Alikuwa bize sana. Sauti ikarejea mara mbili na sasa akatazama. Alikuwa ni Danielle amesimama pembeni kidogo ya korido. Amevalia gauni la kulalia na mkononi amebebelea kikombe cha udongo.
“Haujamaliza tu?”
“Bado … bado kidogo.”
“Mpaka saa ngapi?”
“Musa di mrefu ntakuwa nimemaliza.”
Danielle akanywa kilichopo kikombeni huku akimtazama Marshall. Punde akamwona Marshall akimfanyia ishara ya kumwita, akasonga karibu.
“Tazama!” Marshall akamwonyeshea Danielle kiooni. Danielle akatazama asitambue jambo, akauliza, “Kuna nini?”
“Tazama location hizo,” Marshall akamsihi. “Hamna hata picha moja ambayo location yake ni New Zealand!”
Danielle akamtazama Marshall.
“Kwani kuna shida gani? Sijakuelewa.”
“Mara ya kwanza tulivyokutana na huyu mwanamke kule Hongkong alisema kwao ni New Zealand. Nimekagua profile yake na mara zote alipokuwa tagged, hamna New Zealand hata sehemu moja.”
Kabla Danielle hajatia neno, Marshall akamwonyesha tena picha nyingine. Ilikuwa ni ya mwanaume mfupi aliyevalia miwani akiwa amevalia kombati ya kaki na kaushi.
“Huyu ni Keen!”
“Ndo’ nani?”
“Sijajua ni nani, ila wakati niliposaka jina la Kelly niliona mwanaume huyu akiwa amemtag Kelly kwenye mojawapo ya picha zake za mwanzoni.”
“Sasa Marshall kumtag Kelly kuna shida gani?”
“Yeye ndo’ mtu pekee aliyemtag Kelly. Sijaona popote mtu mwingine pale. Atakuwa anajuana na Kelly bila shaka. Na zaidi mwanaume huyu yupo Marekani!”
“Marshall unataka kuniambia utamfuatilia huyo mwanaume?”
Kabla Marshall hajamjibu Danielle akamwonyesha mwanamke huyo picha moja ya Keen ambayo aliizoom na kutazama magharibi yake.
“Umepaona hapa?” Marshall akaonyeshea kidole kwenye sehemu ndogo ya jengo inayoonekana pichani. “Ni moja ya sehemu inazohifadhi kundi kubwa la kihuni nchini Mongolia.”
Aliposema hayo akamtazama Danielle na kusema, “Pengine Kelly hayupo Marekani kusoma.”
Mwanamke aliingia ndani ya ofisi yake akimletea gazeti. Lilikuwa ni MWAMBA. Mwanamke huyo aliweka gazeti mezani kisha akamtazama inspekta James na kumwambia,
“Gazeti lako hilo! Nimepata shida kweli kulipata. Linagombewa kupita kiasi.” kisha akaenda zake.
Bwana James alikuwa anatazama simu. Hata wakati mwanamke huyo anayemletea gazeti alipoingia ndani, hakuhamisha macho yake. Kuna kitu kilikuwa kimemtinga kidogo.
Punde akaachana na simu yake na kuvuta gazeti la MWAMBA kuliweka machoni. Kuna nini leo? Alijiuliza akiwa analifungua gazeti hilo na ile kulitia tu machoni, akaona picha ya bwana Ian.
Akajikuta anatabasamu.
“Nilijua tu. Hawa wapumbavu wapo mbele ya muda,” alisema akifunua na kupekua. Akasoma kwa utulivu kabisa akiwa anang’amua kila anachokiona na kukiweka mazingationi.
Zaidi ya ilivyokuwa kwenye simu yake, hapa alilowea zaidi.
Alipomaliza kusoma gazeti hilo, habari aliyokuwa anaitaka, akalitupia gazeti mezani alafu akampigia simu mwanaume anayeitwa Smith, afisa upelelezi anayefanya naye kazi ndani ya kituo kimoja.
Punde akaja mwanaume mnene aliyevalia suti, makamo ya umri wake yalikuwa ni arobaini na tano hivi. Mguu wake wa kushoto ulikuwa ni mfupi, alikuwa akitembea kwa kuchechemea.
“Umeona habari kwenye gazeti?” akauliza James akimtazama Smith. Kabla Smith hajajibu, James akamsogezea mwanaume huyo gazeti, naye Smith akalinyaka na kupitisha macho.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Bwana huyu alikuwa ni afisa mpelelezi aliyekuwa anahusika na mauaji yale yalotokea kwenye jengo la bwana Ian. Baada ya Marshall na wenzake kuhepa kwa kutoroka, maafisa polisi walifika hapo na kukuta miili tu iliyokosa uhai.
Bunduki, risasi na damu za kutosha. Kwa mujibu wa nyaraka za ofisi jengo hilo lilikuwa linamilikiwa na bwana Nathan Jensen, mwanaume aliyekufa miaka miwili huko nyuma.
Mbali na hapo serikali haikuwa inamtambua mmiliki rasmi wa hilo eneo wala shughuli inayoendelea hapo.
Bwana Smith alitazama kichwa cha habari akaona picha ya Ian. Hakuwa anaelewa kwani hakufahamu kama kesi yake inahusika na bwana huyo.
Akakunja uso wake na kumtazama James.
“Huyu bwana si yule ajenti wa USSS aliyefia kwenye ajali ya moto?”
“Ian Livermore.”
“Ndio, bwana Ian.”
“Yah.”
“Anahusikaje na kesi yangu?”
“Ndo’ maana nikakupa gazeti usome.”
Smith akachoma muda wake kusoma kile alichoelekezwa. Alitumia kama dakika nane kabla hajamtazama James na kumuuliza,
“Una uhakika gani kama hizi taarifa ni za kweli?”
Jame akafungua droo yake na kutoa magazeti matatu ya MWAMBA akamkabidhi bwana Smith.
Bwana huyo alipopitia magazeti hayo akabaini habari kadhaa ambazo ziliandikwa hapo nyuma na zikatokea kama zilivyosemwa. Akashangazwa. Akageuza gazeti apate kuona maelezo ya wafanyakazi, mahali panapochapishiwa na pia mhariri mkuu lakini hakukuta.
Akamtazama James kwa mashaka.
“Ni wakina nani hawa?”
“Nadhani cha umuhimu ni hiyo habari na sio hao watu. Hivyo wanavyovijua ndivyo hivyo umeviona hapo.”
“Sasa imekuwaje Ian yupo hai? Ina maana --”
“Anahusika na kupotea kwa Raisi,” James akamkatiza. “Simple. Na ndiye huyo aliyekuwa anawatuma watu wake kunizuia nisifanye ile kazi yangu ya kumtafuta Marshall.”
“Kwanini?”
“Sijajua. Alitaka pia kumuua na Marietta Abbay!”
“Kwanini?”
“Smith hatuna muda mrefu sana wa kujadili. Nyanyuka twende!”
“Wapi?”
“Kwani hujasoma gazeti?”
“Ina maana hujaelewa, sio?”
“Labda sijaelewa ambacho wewe umekielewa.”
James akasimama akitikisa kichwa. Akamtaka Smith anyanyuke pia waongozane.
**
Saa tano asubuhi …
“Ni maeneo haya,” alisema James akisimamisha gari. Ilikuwa ni maeneo ya ufukweni. Upepo ulikuwa unapuliza, hali ya hewa imetulia kabisa.
Ni watu wachache walikuwa ufukweni kwasababu haikuwa mwisho wa wiki. Ungeweza kuona watu wasizodi watano wakiwa wamejilaza michangani na kama wawili tu wakiwa wanaogelea majini.
Basi James na Smith wakashuka na kusonga kuelekea kaskazini mwa gari lao. Walipotembea kwa kama nusu kilometa wakawa wamefika mahali ambapo si watu wengi hujongea.
Hapo kulikuwa na miamba mingi sana iliyokuwa imetafunwatafunwa na kuliwa na chumvi. Sakafu ya miamba hiyo ilikuwa ni ngumu na inayoumiza.
Kwa ukaribu kabisa, miama hiyo ilikuwa imepakana na bahari. Na kwa hapo, hata kwa kutazama tu, ungegundua kuwa maji yalikuwa ni marefu.
“Ni hapa!” alisema James akiangaza.
“James, mbona mimi sikuona hii sehemu kwenye gazeti?”
James hakuangaika na Smith, aliendelea kuangaza. Na punde akagundua pango ambalo alimwonyeshea Smith na kumtaka walifuate.
Walipofika huko na kuzama ndani wakamkuta mtu akiwa amelazwa amefungwa kamba mikono na miguu na kinywa chake kimefunikwa na ‘solo tape’ kubwa.
Waligundua mtu huyo ni Ian.
Ian Livermore.
Bwana James akatabasamu akimtazama Smith.
“Sikuwa nimekosea.”
“Lakini ulijuaje?”
“Kwa kusoma nyuma ya mistari. Sijajua wapi itaishia lakini gazeti lile lililenga kutusaidia.”
Basi wakapiga simu kwa kitengo cha huduma na maafisa wengine wakafika eneo la tukio na Ian akafanyiwa uchunguzi wa kiafya.
Alikuwa yu sawa isipokuwa alinyeshwa kiasi kikubwa cha kilevi ambacho kilipumbaza akili yake na kumlaza akiwa hajitambui.
Baada ya hapo, habari ikasambaa kwenye vyombo vya habari vyote kuhusu upatikanaji wa Ian. Afisa wa usalama ambaye alishukiwa kufa kwenye ajali ya moto.
Zaidi akiwa zamu ya Raisi aliyepotea!
**
*SEHEMU YA 23*
Kumbe ilikuwa uongo? Ndilo ambalo lilisemwa mitandaoni na huko kwneye vyombo vingine vya habari. Ina maana muda wote huo bwana Ian alikuwa hai akidunda na maisha?
Ilikuwa ni mada ya moto. Na kwasababu hiyo basi vyombo vyote vya habari vikaanza kuongelea upya swala la kupotea kwa Raisi. Na kwa namna ya pekee basi bwana Ian akaanza kunyooshewa vidole kwamba huenda bwana huyo akawa anajua wapi ambapo Raisi yupo.
Kwanini aliudanganya umma? Je alitumika na mataifa maadui kutekeleza mpango wa kumpoteza Raisi?
Habari hiyo ilisambaa sana. Si tu Marekani bali dunia nzima.
“Ni habari njema kwako Shanny?” Zainab aliuliza akimtazama Marietta. Wanawake hawa walikuwa wameketi sebuleni wakitazama runinga.
Mazingira yalikuwa yametulia mbali na sauti ya runinga.
“Si habari njema kabisa, Zainab,” akasema Marietta akitikisa kichwa. Macho yake yalikuwa yanatazama runinga kwa umakini kana kwamba kaambiwa kna mtihani baada ya hapo.
“Bila shaka Ian atanitaja kuwa na mahusiano naye. Hilo halitaniweka salama.”
“Kwani si ulishaenda kuonana na inspekta ukamweleza hayo?” Zainab akauliza.
“Ndio,” akajibu Marietta na kuongeza “lakini si kama atakavyoeleza Ian. Lazima tu nitakutwa na hatia.”
“Lakini anaweza asiseme. Ni mtu ambaye ana mafunzo. Anaweza akakana na asikutwe na hatia.”
“Sidhani,” akasema Marietta. “Bwana huyo amekutwa akiwa amefungwa kamba mikono na miguu yake. Bila shaka ametoka kwenye mikono ya Marshall, yule ajenti niliyekuambia. Huko atakuwa amesema kila kitu anachokijua.”
“Umejuaje?”
“Nishawahi kuwa kwenye mikono ya Marshall.”
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
“Ukasema kila kitu?”
Marietta akamtazama Zainab.
“Si kila kitu bali kile ambacho nilikuwa nimejilazimisha kuamini muda wote huo.” aliposema vivyo akarudisha macho yake kwenye runinga.
“Marshall alinitilia dawa. Kama nisngekuwa na zile kinga mlizokuwa mnanipa sidhani kama ningeweza kubana siri zangu. Ian ameshakamuliwa kila kitu anachojua.”
“Sasa? Nini utafanya?” Zainab akauliza.
“Nawaza,” Marietta akasema akikuna kichwa chake. Baada ya muda kidogo akasema, “Marekani si sehemu salama kwangu kwa sasa.”
“Hata hapa pia si salama,” akasema Zainab. Macho yake yalikuwa yamejawa na maulizo.
“Ni kweli, lakini kuna utofauti,” akasema Marietta kisha akamtazama Zainab. “Hapa naweza kupafanya pakawa salama.”
Zainab akatumbua macho.
“Shanny, unajua unachokiongea? Abdulaziz ana nguvu sana. Ni mkatili pia na si mtu anayefikiria mara mbili. Ni hatari!”
“Ndio lakini kuna namna. Ni lazima nije na mpango wa kunitoa kwenye ginga hili.”
“Kuwa makini. Hatuna vitu vya kupoteza kwa sasa,” Zainab akatoa angalizo.
**
Saa kumi na moja jioni …
“Kwahiyo nitakuona tena lini?” Jack alituma ujumbe wake mtandaoni kumwendea Kelly. Alikuwa ameketi sebuleni nyumba nzima akiwa mwenyewe.
Akatazama Kelly akichapa ujumbe, na punde akajibiwa,
“Si nilishakuambia?”
Akachapa, “Lini ulinambia?” akatuma.
“Kwani mara ya mwisho kuchat na wewe ni lini?” ujumbe wa Kelly ukauliza. Kabla Jack hajajibu, Kelly akaongezea, “Ina maana umesahau?”
Jack akajaribu kuwaza. Hakukumbuka kama alichat na Kelly na kuambiana hayo. Lakini kwa kuepusha maneno, akaona akwepe swali hilo, kwani aliamini huenda jana yake kabla hajalala kama mfu alichat na Kelly.
Lakini ….
Akatazama jumbe za juu. Hakuna alipoona kitu kama hicho. Sasa ni nini? Jack akajiuliza asiwe na jibu.
“Nambie basi ratiba yako ya juma. Nadhani nitakuwa free kwa siku mbili tatu,” akaandika na kutuma ujumbe huo.
Punde Kelly akauona na kabla hajaujibu akatikisa kichwa.
“Huyu mwanaume ana nini?” akajiuliza. “Mbona anarudiarudia kuniuliza mambo tuliyokwishaongea?”
Alikuwa ameketi kwenye mgahawa akila chakula cha mchana. Amevalia sweta jepesi na suruali ya jeans. Nywele zake amezibana na macho ameyafunika kwa miwani.
Basi akaweka simu kando na kumalizia chakula chake kisha akalipa na kwenda zake.
Mgahawa huu ulikuwa karibu na barabara. Magari yalikuwa yanapita kwa wingi kwenda na kurudi. Kelly alitazama kushoto na kulia kwake alafu akavuka barabara akielekea upande wa magharibi wa mgahawa.
Alitembea kwa muda kidogo kabla hajazamisha mkono wake ndani ya mfuko na kutoa simu. Akampigia mtu mmoja na kumuuliza, “Umeshafika?”
Alipojibiwa akaweka simu mdukoni na kuendelea na safari yake.
Lakini kuna watu walikuwa wanamfuatilia.
Hakuwa anajua.
Alifika mahali, kwenye kijiduka fulani cha ice cream, hapo akazama ndani na kwenda kukaa mwishoni kabisa na kutoa simu yake akibofya. Punde kidogo kuna gari likaja hapo eneoni na kujiegesha kwa kujibana alafu akashuka mwanaume aliyevalia kaushi, suruali ya kombati na buti nyeusi.
Mwanaume huyo alikuwa na asili ya Asia maeneo ya thailand ama singapore na Indonesia. Mfupi kiumbo lakini mkakamavu.
Bwana huyo ndiye yule aliyeonekana kwenye picha ambayo Marshall alimwonyesha Danielle kwenye mtandao wa Facebook. Kwa jina bwana Keen.
Bwana huyo akatazama kushoto na kulia kabla hajazama humo ndani kwenda kumkuta Kelly.
Kabla ya kusalimiana, kila mtu akatazama tena kushoto na kulia yake kabla ya kuendelea na mengine.
“Umepigiwa simu?” Keen akauliza. Uso wake ulionyesha ametoka kufanya kazi kwani alikuwa amelowa japo hatujui kazi gani hiyo.
“Hapana, vipi wewe?” Kelly akauliza. Kabla Keen hajajibu, akatazama tena kushoto na kulia yake. Alikuwa hajiamini na pale alipo.
“Usihofu, Keen,” Kelly akasema kwa sauti ya chini. “Hapa hamna kamera wala walinzi. Tupo huru.”
Baada ya Kelly kusema vivyo ndipo angalau Keen akajipa ahueni.
“Jana usiku nimepigiwa simu na A (ei). amesema muda si mrefu atatuhitaji.”
“Wapi?” Kelly akauliza kwa kuguswa.
“Morocco!”
“Serious? Lakini hatuna makubaliano hayo. Kwani kuna jambo?”
“Sijajua, ila ni wazi kuna jambo. Na tena si dogo, kubwa.”
Kelly akashusha pumzi, kabla hajasema jambo mhudumu akafika, ikabidi abane pumzi yake.
“Habari zenu?” mhudumu akasalimu kwa tabasamu. “Samahani kwa kukawia, nilikuwa nimebanwa kidogo. Naweza kuwasaidia?”
Alikuwa ni mwanamke mnene ndani ya sare. Nywele zake nyeupe zilikuwa zimebanwa kufunikwa na kofia kiasi ili kuzuia kuharibu vinavyotiwa mdomoni.
“Usijali, naomba utuletee vanilla cups mbili,” Kelly akaagiza na punde mhudumu akaaenda zake. Wakaendelea kuteta.
“Vipi kuhusu Shanny? Umewasiliana naye?” Kelly akauliza.
“Hapana,” Keen akatikisa kichwa. “Vipi wewe?”
“Sijawasiliana naye. Nilidhani A alivyokutafuta, na yeye angekucheki maana yupo hukohuko.”
“Hapana, lakini sidhani kama kuna haja kubwa ya kusikia toka kwake. Yeye si mkuu wa kazi yetu kumbuka.”
Mhudumu akawa ameshafika. Akaweka alichoagizwa kwenye meza kisha akaenda zake. Watu hawa wakaendelea kuteta kwa muda kidogo huku sasa wakiwa wanalainisha makoo yao kwa vanilla.
Baada ya kama robo saa tangu vanilla ziletwe, Kelly akalipa na wakajiondokea. Walijipaki kwenye gari alilokuja nalo Keen wakatimka eneo hilo.
Lakini kama dakika tatu tu tangu gari hilo liondoke, gari jingine likawashwa na kuanza kuwafuatilia.
“Nikuache wapi?” Keen alimuuliza Kelly pasipo kumtazama. Macho yake yalikuwa bize yameganda barabarani.
“Leo nitaenda kwako tu,” akasema Kelly akimtazama Keen.
“Kwangu?”
“Ndio. Vipi mbona umeshtuka? Kuna ubaya kwani?”
“Hapana. Nimeshangazwa maana si kawaida yako.”
“Najua. Ni leo tu nimejikuta nikisongwa sana na upweke.”
“Unajua lakini ni hatari. Hatutakiwa kuwa pamoja.”
“Najua. Kwani ni mara ngapi tumekaa pamoja, si leo tu?”
Basi Keen hakuongea tena, wakaendelea na safari yao mpaka walipokomea kwenye nyumba fulani yenye uwanja mkubwa kwa mbele. Uwanja huo ulikuwa umejawa na bustani ya kijani kibichi.
Mbele ya nyumba hiyo kulikuwa na sanduku la kupokelea barua na bango kubwa lilioandikwa kwa herui kubwa - TO RENT.
Hapo wakazama ndani na gari likaegeshwa mahali pake kabla wahusika hawajashuka na kuzama ndani.
Ilikuwa ni sehemu tulivu sana lakini pia pa kifahari. Bila shaka malipo ya hawa watu yalikuwa makubwa sana isipokuwa tu kwa Kelly ambaye yeye alilazimika kupanga mahali pa kawaida ili alete mantiki kusema yeye mwanafunzi.
“Karibu sana.”
“Ahsante.
Kelly alitazama mazingira kwa kurusha macho. Akaketi na kukunja nne alafu mkoba wake mdogo akauweka pembeni yake. Bwana Keen yeye akaenda ndani akimwacha Kelly mpweke kwa kama dakika tano.
Ingali anarudi sebuleni, hakumkuta Kelly kitini alipomwacha. Kitu pekee alichokiona hapo kilikuwa ni mkoba tu.
Akarusha macho huku na kule lakini pia hakumwona Kelly. Alishangaa mwanamke huyo atakuwa kapotelea wapi ndani ya muda mfupi hivyo?
Kabla hajaita, akasikia sauti ya kugonga kitu kutokea chumba pweke. Akajongea kwenda chumba hicho. Alipofika akafungua mlango akiita. Kelly akaitika.
“Ingia.”
Alipoingia, akamwona Kelly akiwa amelala kitandani. Lakini mkono wake ulikuwa ndani ya mkoba.
**
Danielle alikuwa amejilaza lakini Marshall akiwa makini kutazama jengo lile, jengo la Keen. Alikuwa ametulia tuli na akiwa tenge kana kwamba ameambiwa kuna kitu kitatokea.
Ni kidogo tu wakasikia mlio wa kitu kikubwa, hawakuwa wanajua ni mlio wa nini haswa kwani walikuwa mbali sana. Walikuwa wanatazama jengo kwa kutumia hadubini kali. Hapo Danielle akanyanyuka na kumuuliza Marshall nini kimetokea.
Muda kidogo, Marshall akamwona Kelly akiwa anatoka kwenye jengo akiwa anatembea kwa upesi. Mwendo wake ulikuwa ni wa kutupa miguu, anatazama kushoto na kulia nywele zikipepea. Macho yake yalikuwa yamefunikwa na miwani tofauti na alivyoingia.http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Mkono wake ameuzamisha mkobani.
Basi upesi Marshall akavuta kamera iliyokuwepo pembeni yake, akampiga Kelly picha za kutosha mpaka pale mwanamke huyo alipozama kwenye gari la Keen na kuondoka zake.
Kamera aliyokuwa anatumia Marshall ilikuwa na lenzi kali sana. Japo Kelly alikuwa mbali, kamera hiyo iliweza kumnyakua vema kabisa.
Basi Kelly alivyotokomea, Marshall akasogeza gari mbele kidogo, alafu wakashuka na kuzama mule ndani. Walitaka kujua ni nini Kelly alichokifanya. Na baada ya muda mfupi wakahakikisha kile walichokuwa wanakiwaza.
Keen alikuwa amelala mfu. Kichwa chake kilikuwa kinamwaga damu toka kwenye tundu aliloachiwa kwenye paji lake la uso!
“Shit!” Marshall akalaani. Akachukua picha kadhaa za Keen na kisha wakaanza kufanya upekuzi.
**
*SEHEMU YA 25*
Kabla hawajafika mbali yoyote, Danielle akabaini kuna sauti ndogo ya kubipu. Alipata shaka. Alitazama huku na kule akisaka na baada ya muda akabaini kulikuwa na bomu limepachikwa ukutani!
Akamshtua Marshall upesi. Bomu lilikuwa limebakia kama sekunde sita tu kulipuka. Haraka wakakimbia kufuata mlango lakini ni bayana wasingeweza kutimiza ndani ya muda.
Ikabidi wafuate dirisha na kuchumpa walivunje kutokea nje!
Kitendo cha kuwa hewani kupasua vioo vya dirisha, bomu likajitusu kulipuka haswa. Walijikuta wanarushiwa mbali wakifuatwa na mabakimabaki ya dirisha.
Haraka wakajikusanya na kuondoka zao.
“Kwanini amelipua nyumba?” Marshall akauliza. Si kwamba alikuwa anataka jibu bali alikuwa anafikiri. Alishangazwa na lile tendo.
“Bila shaka kuna vitu alikuwa anataka viwe salama,” akasema Danielle.
“Salama kwa kuvichoma?”
“Ndio, kama vikichomwa vitapatikania wapi? Kuna kitu Kelly alikuwa anataka kuficha ama kuna vitu hakuwa anataka vijulikane kuhusu Keen na ndiyo maana akamuua na kupotea kila kitu kilichomo ndani.”
“Lakini kwanini amuue Keen? Mtu ambaye yu pamoja naye kwa muda?” Marshall akauliza. Hakuna mtu aliyekuwa na jibu na hilo lakini ni wazi lilikuwa ni jambo kubwa.
Si bure.
**
“Nimeshamaliza,” Kelly alisema akiongea na simu. Alikuwa kwenye taksi ambayo ameidaka baada ya kuliacha gari la Keen kwa mbali.
“Ndio,” akaendelea kuongea. Kisha “Sawa,” akamalizia na kuweka simu yake mkobani.
Taksi ikampeleka mpaka eneo lake la makazi, hapo akalipa na kuzama ndani.
**
“Amesemaje?” Zainab akamuuliza Marietta. Wanawake hao walikuwa ndani ya gari.
“Amefanikisha,” Marietta akasema akiweka simu yake kando kisha akamtazama Zainab. “Tayari Abdulaziz alishawasiliana nao waje huku Morocco.”
“Kufanya nini?” akauliza Zainab.
“Kufanya nini??” Marietta akastaajabu. “Hii maana yake Abdulaziz ana mpango wa kabambe wa kufanikisha kazi yake. Ndo’ maana alikuwa anawaita.”
“Sasa?” Zainab akauliza. “Tunafanyaje kuhusu hili?”
“Sijajua, Zainab. Na sijali,” alisema Marietta akiegemea kiti. Alikuwa ametingwa na mawazo. “Ninachotaka kukifanya hivi sasa ni kummaliza tu Abdulaziz.”
“Serious??” Zainab akatahamaki. Alimtazama Marietta akikodoa.
“Ndio, unadhani nitampata mume wangu pasipo kumuua Abdulaziz?”
“Lakini Shanny, kuna haja gani ya kumkomboa mumeo na ilhali ulimtenga na kumsababishia yote haya? Atakuelewa kweli? Huoni itakuwa hatari kwako?”
Marietta akatabasamu. Akatikisa kichwa na kumtazama Zainab.
“Nimekwishaharibu vya kutosha Zainab. Nataka kufanya jambo moja tu la kheri kabla ya kufa kwangu.”
Mwanamke huyo akatazama chini kisha akaendelea kunena, “nimefanya makosa sana. Jehanamu ni yangu tu. Nimemweka mume wangu kwenye fedheha na hatari. Sijui atakuwa ananionaje huko alipo. Nimemkosea sana na hata pia nimemkosea Mungu wangu kiasi kwamba naona hata aibu kuomba msamaha.”
Akamtazama Zainab.
“Sitaomba msamaha kwa Mungu. Bado sijamaliza kazi zangu. Bado sijajua nitaua wangapi hapo mbeleni. Nitakapomaliza kabisa nitamwomba Mungu wangu anirehemu. Aniandalie makao huko jehanamu.”
Alipomaliza kusema hayo macho yake yalikuwa yanavuja machozi.
“Kwahiyo unafanyaje Shanny?” akauliza Zainab. Alikuwa ameguswa na namna Marietta alivyokuwa amenyong’onyea.
“Namngoja mtu wangu. Akija tutafanya kazi.”
“Atakuja lini?” akauliza Zainab. “Atawahi kabla Abdulaziz hajakuwahi?”
Marietta akatabasamu. Tabasamu lake lilikuwa la shari.
“Abdulaziz,” akaita jina hilo kwa kebehi kisha akaguna kwa sauti yake ya puani. “Abdulaziz hawezi kunifanya lolote lile. Nakuapia.”
“Shanny, usisahau Abdulaziz ana watu wake kwenye jeshi. Ndege wafananao ndio wanaruka pamoja. Watu wenye uchu wa madaraka wapo pamoja naye karibia kila nyanja. Si salama kujiamini kiasi hicho.”
“Zainab,” Marietta akaitaza akigeuza shingo kumtazama mwenziwe. “Nadhani wewe ndo’ umesahau uwezo wangu. Unadhani mtu yeyote wa kawaida anaweza kumpoteza Raisi wa nchi kama Marekani?”
Zainab akafunga kinywa chake.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
“Niko radhi kufa Zainab hata sasa, lakini mpaka pale nitakapotimiza adhma yangu kwanza. Na naamini nitalitimiza hilo kabla Abdulaziz hajaweka mkono wake juu yangu. Kama ikishindikana, basi kuna moja. Lazima Abdulaziz afe. Siwezi nikakosa vyote.”
Kukawa kimya kidogo. Marietta alikuwa anafikiri jambo. Alitazama mbele kisha akabinua mdomo wake na kuafiki kwamba anahitaji kuonana na Mahmoud.
“Sijajua alipoenda lakini atarejea,” alisema Zainab.
“Una uhakika?”
“Shanny, ni mume wangu yule!”
Hapo Marietta akatabasamu. Hakusema kitu akawasha gari na kutimka.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment