Search This Blog

Sunday 20 November 2022

NYUMA YAKO (3) - 1

 







    IMEANDIKWA NA : STEVE MOLLEL



    *********************************************************************************



    Simulizi : Nyuma Yako (3)

    Sehemu Ya Kwanza (1)





    ILIIPOISHIA



    “Basi tufanye vivyo,” Marshall akaafiki. Danielle akatabasamu na kumwambia, “hutokuja kujutia hili.” kisha akaongezea, “lakini bado tunamhitaji mtu mmoja.”



    “Nani huyo?” Marshall akauliza



    “Jack Pyong!” Danielle akajibu kwa tabasamu alafu akauliza, “Hauoni akikaa kwenye tarakilishi tutamaliza mambo mapema?”



    Marshall akajikuta akitabasamu kwa mara ya kwanza tangu alipoonana na Danielle.



    ENDELEA



    Zilipita siku nne kukiwa kimya kusiwe na habari yoyote ya kukamata vyombo vya habari. Kulikuwa shwari na amani japo bado watu walikuwa wakizungumza na kujadili matukio yaliyopita.



    Jua lilikuwa likizama na kutuama kwa utulivu. Lakini katika hayo si kwamba watu walikuwa wamelala ama tuseme si wote walikuwa wanalala.



    Watu hawa watatu: Marshall, Jack Pyong na Miss Danielle walikuwa macho karibia kila usiku. Walikuwa wakipanga na kupangua. Walikuwa wakiumba na kuvunja. Walikuwa wakiwaza na kuwazua, kuhesabu na kuhesabua.



    Wote hawa walikuwa wanafanana kitu kimoja; ni watu wenye ujuzi wa kufundishwa darasani na vipaji binafsi. Wote wakiwa watu waliolitumikia taifa kwa njia kubwa na pana, tena kwenye vitengo nyeti kabisa vya usalama vya nchi.



    Walipoona kila walilolipanga limekaa sawa, basi wakapumzika katika siku hii ya nne wakiwa wanangoja sasa utekelezaji.



    Mipango yao hii haikuwa statiki, lah! Walikubaliana itakuwa inabadilika kutokana na matukio yanavyokwenda, kutokana na mambo yatakavyoenenda. Lengo kuu likiwa ni kuisaka haki popote pale lakini pia na kuufunua ukweli kwa hadhira.



    Kulitimiza hilo kwa ufanisi, jamaa hawa wakawa wamekodisha eneo katikati ya jiji la New York maalumu kwa ajili ya kufanyia kazi zao ‘formal’ na zile ambazo ni za siri zaidi basi zitakuwa zikifanyiwa ndani ya nyumba maalum ambayo hii hawakuwa wameinunua katikati ya jiji bali mbali kabisa kwasababu za kiusalama.



    Wakiwa huko itakuwa rahisi kumtambua adui awajiayeh tofauti na wakiwa mjini. Na kwa usalama zaidi, nyumba hiyo ilikuwamo na handaki lakini pia njia za kutokea ambazo hazikuwa nyepesi kuonekana.



    Nyumba hii ambayo ipo mbali na jiji, itakuwa ikitumika kama ‘engine’. kama kitovu cha mambo yote yanayoendelea kwenye yale makazi ya kule jijini.



    Humo kutakuwa kukikaliwa na tarakilishi kubwa zenye uwezo lakini pia vifaa kadha wa kadha vya kisayansi kusaidia upelelezi. Humo sasa watakaa wanaume wawili ambao wanatafutwa, yaani Marshall na Jack Pyong.



    Watafanya kazi zao huko na pale itakapohitajika basi watatuma taarifa kwenye ofisi iliyokuwapo jijini, ambayo inakaliwa na Miss Danielle.



    Kwahiyo kwa mpango huu basi, Miss Danielle atakuwa anatumika kama ‘cover up’ ya mambo yote hayo. Kwa kupitia ofisi yake atakuwa anafuatilia na kufunua mambo ambayo aidha anafikishiwa na wakina Marshall ama anayafunua mwenyewe kwa upelelezi.



    Yale yote ambayo Marshall na Jack Pyong watakuwa wakiyapata, basi watakuwa wakimfikishia Miss Danielle kuyafikisha.



    “Wamesema itachukua mwezi kukamilika,” alisema Danielle akiwaambia Marshall na Jack. Mwanamke huyo alikuwa ametoka kufuatilia tena usajili wa kituo chake cha upelelezi binafsi. Mambo hayakuwa yanaenda vibaya, lah! Ila ni jambo linalochukua muda kuhitimu.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Lakini ni uhakika?” akauliza Jack.



    “Hamna shida,” Danielle akamtoa hofu akinyoosha miguu yake kwa kiti. “Kila kitu kitakuwa sawa lakini si kwamba tungoje. Inabidi tuanze kutekeleza mipango mara moja!”



    Basi ulipowadia wakati wa jioni wakakutana wote kwenye lile jengo ambalo lipo mbali na jiji. Huko wakakagua mdoli ambao ulikuwa umetengezwa maalum kwa ajili ya kujiveka bwana Marshall akienda kukutana na bibie Marietta.



    Kila kitu kilikuwa sawa.



    “Unaweza ukaujaribu,” akasema Miss Danielle. Mdoli huo ulikuwa unatengenezwa na mtu wao maalumu kwa hizo kazi, kwa jina Royal, mwanaume huyo alikuwa anahusika na kuwatengenezea midoli hiyo hata kwa shirika la CIA.



    Na kama haitoshi, msanii huyo alikuwa ni mtaalamu haswa wa kufanya ‘makeup’, si tu kipaji bali pia na taaluma. Angeweza kubadilisha kabisa uso wako ukaonekana mtu mwingine tofauti.



    Marshall akauvaa mdoli huo aliotengenezewa, na kila kitu kikawa sawa kabisa. Usingeweza kudhani kabisa kama ni Marshall bali ni mtu yule ambaye alikutana na Marietta na kukubaliana kupeana pesa kwa ajili ya taasisi yake ya watoto.



    “Aiseee!” Jack alishangaa alipotazama kazi hiyo. Alimkagua Marshall na akajikuta akishindwa kabisa kupata walakini. Marshall alikuwa amebadilika kabisa usimtambua kwa namna yoyote ile.



    “Ipo vipi?” Marshall akauliza akiwa amebadili sauti.



    “Iko bomba,” Jack akajibu akionyesha ishara ya dole gumba. Alikuwa amefurahishwa na mabadiliko yale.



    “Lakini kuna kitu cha ziada,” Marshall akawajuza wenzake. Wakaongozana mpaka chumbani ambapo aliwaonyesha chupa moja kubwa ya kioo, ndani yake kulikuwa na kimiminika chenye rangi ya maji.



    “Ni nini hicho?” akauliza Danielle akisogea karibu kutazama.



    “Ni Sodium Thiopental!” akajibu Marshall akiwa anatabasamu, Danielle akaachama kinywa, “Kweli?”



    “Yah! Ndiyo yenyewe.”



    “Umetoa wapi?” Jack akauliza akiwa anakodolea chupa hiyo.



    “Ni story ndefu. Siku nikiwa na muda na nipo kwenye mood, nitawaeleza,” akasema Marshall akiwa anatabasamu kwa mbali, basi Daniell akampongeza kwa kufikiria hilo kwani litawasaidia sana kwenye kazi zao.



    Lakini Sodium thiopental ni nini?



    Hii ni ‘chemical composition drug’ yenye fomula C11H17Na02S ambayo ni mashuhuri kwa kusababisha ‘Anesthesia’. Anesthesia ni ile hali ya mtu kupoteza ufahamu ama kujitambua kwa muda (temporary loss of sensation).



    Kemikali hii hutumika maalumu kwasababu ya kulazimisha kupata taarifa toka kwa mhanga. Kwa jina maarufu hujulikana kama ‘truth serum’ ambapo hufanya kazi kama kileo kwenye ubongo wa mhanga na hatimaye kumfanya aropoke kwa wepesi kile atakachokuwa anaulizwa.



    Ila kisheria kitendo hiki ni kinyume na katiba ya Marekani ingawa kimekuwa kikitumika mara kadhaa kwenye maeneo kadhaa haswa taasisi za upelelezi, kwa siri.



    “Itatusaidia kwa kuanza na Marietta,” alisema Marshall akifunga chumba. “Nitahakikishha napata kila taarifa aliyonayo kichwani.”



    “Lakini vipi akaja kutambua?” akauliza Jack Pyong. Marshall akatabasamu na kumtoa shaka, “Jack, najua namna ya kuenenda naye. Hilo lisikupe tabu kabisa!”



    Basi wakaketi sebuleni na hapo wakaendelea kuteta mambo kadhaa ikiwamo pia namna ambayo itakuwa inawaingizia pesa kwani watahitaji sana kwenye misheni zao.



    Wakiwa wanajadili hilo wakakubaliana kufungua baadhi ya miradi, lakini katika namna kidogo ya ajabu Marshall akawaambia kuna mahali pengine pa kupatia pesa.



    “Si kwa uhalifu, Marshall!” Danielle akaonya.



    “Si kwa uhalifu,” Marshall akasema akimtazama mwanamke huyo kwa tabasamu alafu akahamishia macho yake kwa Jack Pyong. “Na nadhani njia hiyo itamfurahisha sana mmoja wetu hapa.”



    “Njia gani hiyo?” Jack akapaliwa na swali.



    “Msijali. Harakaharaka haina baraka. Tuanze kwanza na la huyu mwanamke, Marietta. Ama mwasemaje?” alisema Marshall kisha akajaribu kuvua mdoli wake aliokuwa ameuvaa.



    Wenzake walikuwa wamejawa na shauku. Ungeona hilo kwenye nyuso zao.



    **





    Basi ikapita siku moja tu na ndipo mwanaume mmoja akaonana na Marietta kwenye hoteli ya nyota tano ndani ya jiji la New York.



    Marietta alikuwa amevalia suti nyeusi na skafu nyekundu shingoni ambayo aliifananisha rangi na mkoba wake. Kwa upande wa mwanaume yule mgeni, yeye alikuwa amevalia suti nyeusi kabambe na nywele zake amezilaza vema.



    Mwanaume huyo alikuwa akifanania ipasavyo na ule mdoli ambao uliandaliwa na msanii Royal kwa ajili ya kazi ya Marshall. Mwanaume huyo alikuwa ni Marshall mwenyewe!



    Lakini kwa jina la miungu nakwambia, usingeweza kumtambua mwanaume huyo kama ni Marshall hata tu kwa kuhisi. Si tu kwamba alikuwa hafananii, bali alikuwa haonekanii wala kusikika kama ni Marshall.



    Sauti yake, umbo na mavazi yake yalimfanya aonekane ni mtu wa tofauti kabisa na ambavyo ungewaza kichwani. Hata Marshall mwenyewe alipojitazama kwenye kioo alikiri kujisahau kwa muda!



    “Umewahi sana!” alisema Marietta akitazama saa yake ya mkononi. Uso wake ulikuwa umepambwa na tabasamu.



    “Hamna, si sana, hata wewe upo ndani ya muda,” akasema Marshall, naye asinyime tabasamu la mbali.



    Alimtazama Marietta ndani ya macho na kwa kiasi fulani mwanamke huyo akawa anaparanganyika. Umbo la Marshall si tu kwamba lilikuwa la kiume, bali pia matendo yake yalikuwa ya ki ‘gentleman’.



    Alimsogezea kiti Marietta aketi. Alikuwa anatabasamu kwa kiasi. Alimpatia Marietta glasi ya kinywaji baada ya kummiminia, na muda wote wakati Marietta alikuwa anangea, mwanaume huyo akawa anamtazama ndani ya macho, kwa utulivu na uskivu mkubwa.



    Kwa kiasi fulani, Marietta alijihisi mwanamke anayethaminiwa. Si kwamba wafanyakazi wake hawamtii na kumskiza, la hasha! Ile ilikuwa ni tofauti na muktadha wa aina hiyo.



    Alicheka kidogo akamwambia Marshall,

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Hatukuwa tumemaliza maongezi siku zile, ulikuwa na kipi cha kunambia?” wakati anauliza alikuwa amesimamisha wima mikono yake na kuipinda apate kuweka ncha ya kidevu chake papo. Tayari alikuwa anamtazama Marshall kwa namna ya kipekee, naye Marshall alikwishalibaini hilo.



    Akatafuna chakula chake kisha akajifuta na kitambaa na kusema kwa sauti ya chini, “Bibie Marietta, kwani una upesi sana?”



    Kabla Marietta hajajibu, Marshall akaendeleza maneno, “Japo ni kwa muda mfupi, nimefurahi sana kukaa nawe hapa. Mimi ni mtu wa kutunza sana muda lakini nimejikuta nikipuuzia. Samahani kama nakukwaza.”



    Marietta akatabasamu. “Hamna shida kabisa, hata nami nimefurahia sana. Sikuwa najua kama wewe ni mcheshi kiasi hiki!”



    Wote wakatabasamu.



    “Unajua muda mwingine kuna kitu huja pengine sababu ya nani uliyekaa naye karibu!” Marshall akadokeza.



    “Ni kweli!” Marietta akaunga mkono. “Mimi sikuwa najua kama nitafurahia nitakapokuwapo hapa. Unajua siku zangu zimekuwa za kawaida sana, muda mwingine kutingwa na kazi kunasaidia kusogeza muda zaidi siku iishe.”



    Basi mlango huu wa maongezi ukawafanya watu hawa waanze kuongelea mambo yao binafsi. Japo kwa uangalifu mkubwa kila mmoja akadokeza kile ambacho alikuwa anakiona kitampa ahueni dhidi ya mwenzake.



    Muda ukiwa unaenda katika maongezi hayo Marshall akapata kujifunza kuwa Marietta amekuwa akiishi maisha ya upweke sana, na kwa kiasi fulani amekuwa ni mtu asiye na furaha kwa mawazo ama majuto.



    Ndani ya lisaa limoja, Marshall akawa amefanikisha kabisa kumpeleka Marietta mpaka chumbani, mwanamke huyo akiwa hoi kwa pombe. Haikuwa kawaida yake kuwa hivi, yaani kulewa upesi, lakini hamadi alijikuta akiwa hajiwezi, kichwa kizito na anaropoka hovyo.



    Marshall alikuwa amemtilia madawa - Sodium Thiopental - kwenye kinywaji chake.



    Madawa hayo yalikuwa yakifanya kazi kama pombe kichwani mwa Marietta, hivyo kujumuisha na pombe ile ambayo alikuwa anakunywa, basi akajikuta hoi maradufu, taabani, dhoofu l’hali!



    Marshall alimkokota na kumbwagia kitandani kisha akavuta kiti na kukaa pembezoni mwa mwanamke huyo akilenga kumchokonoa zaidi ajue kuhusu Raisi.



    Lakini akiwa hapo kama dakika nane tu, mlango ukagongwa kwanguvu! Alishtuka kabla hajauliza ni nani yu mlangoni. Punde, sauti ya kiume ikamjuza, ni walinzi!



    “Walinzi gani?” akapaza sauti kujongea mlango, kidogo, mwanaume kwa nje akamjibu kwa uwazi kuwa ni walinzi wa Miss Marietta Abbay! Alipochungua nje kweli akawaona wanaume wawili papo.



    Akafungua mlango.



    Wanaume hao wakaingia ndani upesi na waliporusha macho yao kitandani wakamwona ‘boss’ wao akiwa amejilaza hoi.



    “Sidhani kama alikuwa anawahitaji,” alisema Marshall na kuongeza, “amepumzika!”



    Lakini wanaume wale hawakumsikiza, wakawa wanajaribu kumnyanyua Marietta waende naye.



    “Kwani kuna tatizo, maafisa?” Marshall akauliza akiwajongea. “Nadhani ni swala la kumuuliza mkuu wenu kama anahitaji kupumzika ama lah!”



    Wakiwa wanajitahidi kumnyanyua Marietta, ndipo mwanamke huyo akapaza sauti iliyoelemewa na ulevi. Alikuwa anataka aachwe upesi!



    Walinzi walijitahidi kumwelewesha lakini hakutaka kuwasikia abadani. Aliwafokea kama watoto akiwataka wamwache apumzike kwani hajawaita.



    Basi walinzi wakajikuta hawana chaguzi bali kutii maagizo ya mkuu. Kishingo upande, wakaenda wakiwa wanamtazama Marshall kwa macho ya ndita. Mwanaume huyo akatabasamu akiwapungia mkono wa kwaheri.



    Walipotoka, akaufunga mlango kwa komeo.



    Walinzi wakashuka mpaka kwenye magari yao, wakajipaki na kungoja. Walikuwa na mashaka kabisa juu ya mwanaume yule, yaani Marshall, lakini hawakuwa na budi.



    Waliona ni vema kungoja, na basi zitakapopita dakika kadhaa, mmoja wao ataenda tena kutazama usalama.



    Basi zikapita dakika kumi, kumi na tano, ishirini, ishirini na tano. Zilipofika dakika thelathini, wanaume wale wakaona ni stara sasa kwenda tena kwenye chumba kutazamia usalama wa mkuu wao.



    Hapa basi kugawanga majukumu, mmoja akaona aende na huku mwingine abaki kwenye gari pamoja na dereva.



    Jamaa huyo mmoja akapandisha ngazi upesi na kwa ukakamavu. Hakukuwa na shida sana kwenye upande wa ulinzi maana ilikuwa inatambulika wako pale kwa ajili ya nani.



    Alipofika kwenye chumba chenyewe, akabisha hodi.



    Kimya.



    Akabisha tena na tena. Kimya. Akaongeza nguvu kwenye mkono wake kwa kubisha zaidi na zaidi lakini bado matokeo yakawa yaleyale.



    Kimya!



    Kabla hajaamua kuchukua hatua yoyote, mara akasikia taarifa sikioni mwake kutoka kwa mwenzake. Taarifa ikimwambia,



    “Yule mwanaume huyu huku chini!”



    Upesi akamwambia mwenzake akimbize mwanaume huyo ilhali yeye anafanya namna akamwone mkuu anaendeleaje huko ndani. Baada ya muda mfupi, akawa ameshampata msimamiza na wakazama ndani.



    Humo wakakumta Marietta amelala.



    Yu salama salmini.



    Lakini bado vifua vikiwa na hofu.



    Nini kitakuwa kimetokea?







    Yule jamaa aliyemkimbiza bwana Marshall alikuwa anatota jasho na hakuwa amempata bwana huyo. Akiwa anajifuta na lesso aliteta akiwa anapambana kuhema.



    Alitafuta kila kona, kila barabara akakimbilia lakini hakupata kitu. Kote kulikuwa kukavu. Moyo ulikuwa unamwenda mbio ingali hajamwona mlengwa wake.



    Basi walichofanya ni kumbeba Marietta na kumweka kwenye gari kisha wakampeleka moja kwa moja hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Huko baada ya vipimo ikabainika mwanamke huyo alikuwa amekunywa pombe nyingi tu, hakuna cha zaidi.



    Hakuwa ameingiliwa wala kujeruhiwa kwa namna yoyote ile.



    Lakini hayo kama hayatoshi, walinzi wale wakafanya jitihada kutambua ni nini kilimtokea Marietta kwani bado walikuwa na mashaka na mwanaume yule waliyemwona naye.



    Basi kwa kupitia kamera za hotelini, wakanyaka uso wa mwanaume huyo na kuanza kusaka taarifa zake. Kwakuwa mwanaume huyo alikuwa amejitambulisha na kubebelea kitambulisho cha Umoja wa Mataifa, basi wakaanzia huko kumtafuta.



    Wakasaka sana pasipo majibu. Taarifa za Marietta zikamfikia bwana Ian na basi akafanya jitihada za makusudi kwenda kuonana na mwanamke huyo.



    Bwana Ian alikuwa amejawa na hofu. Akiwa njiani alipata kujiuliza sana ni nini ambacho kitakuwa kimemtokea mwanamke huyo kwani usalama wake upo mikononi mwake.



    “Nilikuambia uwe makini, Mareietta!” alifoka Ian ambaye kwa Marietta alikuwa anatambulika kwa jina la Dick. “Umefanya nini sasa? Unaendaje kuonana na watu usiowajua na unafahamu fika, unafahamu wazi namna tulivyo, mazingira tuliyomo!”



    Bwana Ian alikuwa amefura. Marietta alikuwa ameketi kwenye kochi akiwa ameegamia tama macho yanatazama chini. Alikuwa amenywea. Kichwa kilikuwa cha moto.



    Bwana Ian akashika kiuno kisha akakiachia, akakishika tena akitembea kwenda mbele na kisha kukata kona kurudi nyuma, alafu tena anaenda mbele.



    Uso wake ulikuwa umejawa na ndita. Hawezi hata kuhema vizuri, ni kana kwamba kiroba cha ndizi kimetuama juu ya kifua chake.



    Akajaribu kuketi. Akanyoosha miguu kisha akaikunja tena. Akakunja mikono na kulaza mgongo wake kwenye kiti, mara akanyanyuka na kumtazama Marietta, “Unakumbuka mambo uliyoyasema?” akauliza.



    Marietta akatikisa kichwa, “Sikumbuki nililofanya hata moja!”



    “Na vipi kuhusu maelezo yake ya awali?”



    “Alisema anafanya kazi Umoja wa Mataifa.”



    “Kitengo gani?”



    “Sikumbuki vema lakini ni kuhusu mambo haya ya watoto kama sikosei.”



    “Huna uhakika!”



    “Dick, tafadhali. Siko vizuri kwa sasa. Najua nimefanya nisivyotakiwa ila ndo’ kishatokea. Kama kuna cha kujadili hapa basi ni cha kufanya sio yaliyopita!”



    Japo Marietta alieleza vema, bado bwana Ian hakuwa anaelewa. Aliendelea kuporomosha lawama kwa Marietta kwa uzembe wake na ukaidi, ikafikia kipindi sasa Marietta akashindwa kuvumilia, naye akaja juu wakiwakiana.



    “Yote haya umesababisha wewe!” alifoka Marietta. “Wewe ni mwanaume gani, au kwasababu waona nimenyamaza basi wadhani ni mjinga, sio?



    Dick, tangu mume wangu apotee, umeonana na mimi mara ngapi? Tumekuwa pamoja mara ngapi? Kila siku umekuwa mtu wa kusingizia umebanwa na kazi. Unakimbia huku na kule. Haujali kabisa kuhusu mimi!”



    Alipofoka vivyo, akajikuta akiangua kilio. Alijifunika uso wake kwa viganja akamwaga machozi. Bwana Ian akamtazama lakini asimguse wala kuhangaika naye.



    Marietta akaketi kwenye kiti na kuendelea kulia. Baada ya kama dakika nane, akatulia kimya. Alikuwa anavuta makamasi mepesi na kupiga kwikwi za kilio.



    Kukawa kimya kwa kama dakika mbili. Bado bwana Ian alikuwa anamtazama Marietta pasipo kusema kitu, ila ndani yake alikuwa ni kama mtu anayejutia, pengine anakosa tu namna ya kuanza maongezi.



    “Nimekuwa nikiishi maissha ya ajabu sana,” akasema Marietta. “Nimekuwa mwenyewe sasa, mpweke niliyetelekezwa. Si wewe Dick ambaye ulikuwa hapo awali. Umebadilika kabisa na ninajua kwanini, umeshapata ulichokuwa unakitaka.



    Mimi sio mke wa Raisi tena. Sina thamani tena kwako, sio?”



    “Marietta,” akaita Ian akimsogelea mwanamke huyo karibu. “Sikulenga kukuumiza, na si kama unavyoniwazia. Mambo hubadilika.”



    Aliposema hayo Marietta akamtazama mwanaume huyo kwa macho yake mekundu yaliyolowana. Macho yake yalikuwa yamefichwa na ndita za mashaka na maulizo.



    “Mambo hubadilika, sivyo?”



    “Sijamaanisha hivyo unavyowaza!”



    “Usijali, Dick. Nimekuelewa vema. Nadhani sasa ni muda wa kila mtu kutenda na kuenda na njia yake.”



    “Marietta, umoja wetu ndiyo nguvu yetu.”



    “Umoja upi huo? Mbona sikuwa nauona siku zote hizo?”



    “Marietta, mimi na wewe tun--”



    “Sitaki kusikia kitu! Nakuomba nyanyuka uondoke kwangu.”



    “Tumefikaje huko?”



    “Sijui ila ndiyo tumeshafika. Toka kwangu!”



    Baada ya kuona Ian haelewi, Marietta akapiga kelele kuita walinzi na ndani ya muda mfupi walinzi wakafika na kumtaka bwana Ian aondoke kama alivyoelekezwa.



    Kidogo bwana huyo akawa mkaidi kusikia. Walinzi walimshika na kumvuta, akawasukuma na kuwafokea ataenda mwenyewe pasipo bughudhi.



    “Mkithubutu kunishika ..!” alifoka Ian akiwaonyeshea kidole walinzi, kisha akatengenezea koti lake la suti na kumtazama Marietta.



    “Unajua wapi pa kunipata,” akasema kwa ngita kisha akaenda zake.





    **



    Marshall alizima kifaa cha kurekodia sauti, alafu akawatazama wenzake, Danielle na Jack Pyong, kwa tabasamu.



    “Umesikia?” akauliza. Wenzake wakashusha kwanza pumzi ndefu kabla hawajatia neno. Mambo yalikuwa mazito haswa.http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Kumbe mke wa Raisi, bibie Marietta Abbay, alikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na bwana Ian Livermore, mahusiano hayo yakiwa yameanza kwa muda kipindi hicho bwana huyo akiwa anafanya kazi kama mlinzi wa Raisi!



    “Lakini kwanini aliamua kufanya hivyo?” Danielle akauliza. Basi kwa kuepusha kupoteza muda, Marshall hakucheza tena sauti bali akawahadithia wenzake mkanda mzima.



    Mkanda huo ni kama ifuatavyo.



    Hapo kabla ya mumewe kuwa Raisi, Marietta alikuwa akiishi na familia yake vema. Mapenzi yalikuwa mengi sana na wakiwa wenye ndoto kubwa kwa hapo mbeleni.



    Mume alikuwa ni seneta wa Florida kwa kupitia chama cha Democratic. Alikuwa ni mtu anayekubalika sana na watu na mwenye ushawishi mkubwa kwa wananchi wa ndani ya Florida na hata chamani.



    Kwa muda wote huo bibie Marietta Abbay alikuwa pembeni ya mume wake akimuunga mkono, lakini pasi na kujua kumbe mwanaume huyo alikuwa na mahusiano ya siri na mwanamke mwingine.



    Tena mcheza filamu za ngono!



    Swala hilo likamuumiza sana Marietta. Akawa akilia akijifungia ndani na tangu hapo akawa haonekani akizunguka na mumewe kama ilivyokuwa hapo nyuma. Alijihisi mpweke na aliyesalitiwa.



    Anaamini ni kwasababu hakuwa na uwezo wa kubeba mimba labda ndiyo maana mumewe akatafuta njia ya pembeni, lakini ni wapi wataweka nyuso zao ikibainika mtu mkubwa kama huyo amechepuka na mcheza filamu za ngono? Na kama haitoshi akambebesha na mimba?



    Hasira zake zikamtuma kumchukia mumewe lakini pia mwanamke aliyezaa naye. Basi kwa kuapa akasema kwamba kwa mkono wake atamwangusha mwanaume huyo kama vile alivyofanya jitihada za kumnyanyua.



    Pia atamsaka kwa namna yoyote mwanamke aliyezaa na mumewe na kumteketezea mbali.





    ****



    *SEHEMU YA 04*



    Baada ya mume kutambua dhamira ya mkewe, akafanya namna kumsafirisha ‘bibi wake mdogo’ pamoja na mwanaye kwenda Ulaya kwa usalama. Huko kwa siri akawalipia makazi na akawa anawatumia pesa za kujikimu.



    Hivyo tokea alipokuwa Raisi akawa anatunza siri hiyo na akihangaika kwa gharama yoyote ile, isije ikavuja kuchafua jina lake na hata jina la taifa kubwa la Marekani!



    Wakati huo mkewe akiwa anaishi kwa uchungu na sonona, ndipo akaanza kuingia kwenye mikono ya bwana Ian. Kwa mwanzoni si kwamba alikuwa anampenda bwana huyo bali kwasababu mbili kubwa: mosi, kulipiza kisasi kwa mumewe, pili, kukaa karibu na bwana huyo kutamfanya afahamu mambo ambayo mumewe anamficha.



    Taratibu wakaanzisha mahusiano yao kwa siri, na ndani ya muda mfupi Marietta akapata kujua wapi alipo bibi mdogo wa Raisi pamoja na mwanaye. Ni huko jijini Brussels, Ubelgiji.



    Baada ya kusema hayo, Marshall akaweka kituo. Wenzake wote walikuwa wanamtazama kwa hamu kweli, habari hiyo ilikuwa imewashika masikio na kupanua vinywa vyao.



    Ilikuwa ni habari nyeti. Habari adimu.



    “Kwahiyo alipojua, ikawaje?” akauliza Danielle. Alikuwa amepaliwa na hamu ya kujua.



    Basi Marshall akaendelea kuwa baada ya Marietta kutambua habari hizo akaanza kupanga mkakati wa kummaliza Britney, mwanamke aliyezaa na mumewe, pamoja pia na mtoto wake!



    Afanye vivyo sababu ya kupoza kifua chake dhidi ya chuki na uchungu alokuwanao lakini kabla hajaanza utekelezaji, bwana Ian akamtaka awe mtulivu kwani ana mpango kabambe kabisa.



    Wakati huo mapenzi baina yao yalikuwa yamekolea haswa. Marietta alishakuwa kipofu kwa Ian kwani mwanaume huyo aliziba kabisa pengo la mumewe na kumpa faraja hivyo hakuona kama kuna haja ya kumpinga mpenzi wake.



    Basi siku zilivyosonga ndipo bwana Ian akaja kumpa mpango mkubwa kwamba wasifanye vitu kwa hasira bali kwa faida. Japo mpango huo hakuwa anauelewa vema ila ulikuwa umejikita kwenye kutumia familia ya siri ya Raisi kumtumikisha mwanaume huyo kufanya jambo kubwa litakalowapa pesa kubwa sana.



    Wakishapata pesa hiyo wataondoka na kwenda kuishi maisha kwenye ulimwengu mwingine wakila raha mpaka kufa kwao.



    Marshall akakomea hapo.



    “Sasa ni mpango gani huo?” Jack akauliza.



    “Sijaujua bado. Taarifa zaidi atakuwa nazo bwana Ian, yeye ndo alikuwa anausuka mpango huo. Kwa nilivyoona, Marietta hakuwa anaelewa kwa undani kuuhusu ingawa alikuwa ameketi kungoja faida ya mpango huo.”



    Kukawa kimya kidogo wakitafakari, kidogo Danielle akauliza, “Familia ya Raisi ilikuwa Ujerumani si ndio?”



    “Ndio,” akajibu Marshall.



    “Kwahiyo kama ni hivyo, itakuwa walikamatwa huko Ubelgiji, walipokuwapo mwanzoni, na kupelekwa Ujerumani!”



    “Inawezekana,” Marshall akaunga mkono hoja.



    “Kwanini walipelekwa Ujerumani?” Danielle akauliza lakini kabla ya yeyote kutoa hoja, akaendeleza soga,



    “Unajua Raisi alipotea muda mfupi kabla ya kikao kikubwa cha kiuchumi duniani kufanyika Ujerumani. Pasipo shaka, kupotea kwa Raisi, kupelekwa kwa familia yake ya siri Ujerumani, na kile kikao kikubwa cha kiuchumi, vitakuwa na mahusiano!”



    Danielle akawa ameng’amua fumbo moja kubwa sana. Marshall akamuunga mkono na kuwataka wafanyie utafiti zaidi kuhusu mkutano ule. Wakina nani walikuwa wahusika na ulikuwa unahusu nini.



    Kuhusu mambo hayo ya kupembua rekodi, bwana Jack Pyong akaingia kazini kufukua kadiri anavyoweza ingali Marshall na Miss Danielle wakiwa wanapangilia zile taarifa ambazo bwana Marshall alikuwa amezipata toka kwa Marietta Abbay.



    Walizitunza taarifa hizo kwenye maandishi na pia wakiambatanisha sauti na baadhi ya picha. Kazi hizo zikadumu kwa masaa, mpaka inawasili saa nane usiku ndipo kila kitu kikawa sawia, wakapumzika.



    Kwakuwa muda ulikuwa umeenda sana, Danielle akaona ni vema akalala kwenye ile nyumba mbali na jiji. Alilala kwenye chumba chake binafsi ingali Jack Pyong na Marshall wakishea chumba kimoja.



    Wakiwa wamelala, kuna muda Jack Pyong akajikuta akiamka. Alipofumbua macho yake kuangaza akaona mwanga ni mkali chumbani, hawakuwa wamezima taa.



    Alipotazama kando, akamwona Marshall aliyekuwa amejilaza akiwa anatazama picha ya mwanamke. Alitahamaki mwanaume huyo kutokuwa amelala mpaka muda huo. Yalikuwa ni majira ya saa kumi na moja sasa!



    Akarusha jicho lake kutazama ile picha aliyokuwa anaitazama Marshall, kisha asijali sana akajilalia.



    Alipokuja kuamka jua likiwa limechomoza, akajikuta yu kitandani peke yake. Marshall hakuwepo chumbani wala ndani ya nyumba. Vilevile Danielle!



    Alikuwa yu peke yake, mpweke.



    “Hawa ni binadamu kweli!” akastaajabu akipiga mihayo. Asijali sana, akajiendea kukoga kisha kupata kifungua kinywa na kurejea mbele ya tarakilishi!





    **





    Baada ya hodi ya muda mfupi, bwana James Peak aliruhusu mtu anayegonga aingie ndani ya ofisi yake.



    Alipotazama mlangoni, akamwona mwanamke Marietta Abbay. Mwanamke huyo alikuwa amevalia suti kama kawaida yake, na shingoni alikuwa amevalia skafu rangi ya manjano ambayo amaefananishia rangi na mkoba na viatu vyake.



    Mwanamke huyo alikuwa ana macho mekundu na uso wake ulikuwa wa kichovu, ni kama vile mtu ambaye hajalala usiku wa kuamkia siku hiyo. Ungemtazama kwa umakini ungebaini macho yake yalikuwa yamevimba.



    “Karibu sana, madam!” bwana James alimpatia mkono Marietta, mwanamke huyo akajibu kwa tabasamu la uongo kisha akaketi kitini.



    Akasema amekuja papo kwa ajili ya kesi ya Marshall.



    “Nadhani nimekutana na Marshall jana,” alisema mwanamke huyo akitazama chini. Alikuwa amekabwa kwa mawazo kichwani.



    “Ulikutana naye wapi?” Bwana James akauliza. Kidogo Marietta akanyamaza kabla ya kuminya lips zake na kusema kwa sauti ya chini,



    “Hotelini. Lakini akiwa na mwonekano tofauti!”



    Baada ya hapo Marietta akafunguka ni namna gani alivyokutana na mwanaume huyo na kumwambia wanataka wafanye jambo kwa pamoja kuhusu watoto kabla hajamlewesha na kumpeleka chumbani.



    “Sijui alinifanya nini, lakini nahisi sipo salama,” alihitimisha mwanamke huyo kisha akameza mate.



    Bwana James akamtazama na kumuuliza, “Kwanini unajihisi haupo salama? Kwanini Marshall alikutafuta? Mlishawahi kuwa na mahusiano naye yoyote hapo kabla?”



    Kabla ya kujibu, Marietta akamtazama bwana James machoni kwa kama sekunde tatu, kisha akaangusha macho yake chini na kusema kwa sauti ya kunyong’onyea,



    “Sijawahi kumjua hapo kabla.”



    “Sasa ulijuaje kama ni Marshall?” bwana James akauliza. Kidogo Marietta akabanwa na kigugumizi.





    **





    Baada ya kujiumauma, Marietta akaeleza kwamba amedhania vivyo maana hana adui, mtu pekee ambaye angelenga kumtafuta na labda kummaliza ni bwana Marshall, kwani ndiye ambaye alikuwa anahusika na kumtafuta mumewe.



    Basi bwana James akaandika maelezo hayo pembeni akiwa anamsikiza vema mwanamke huyo. Alipomaliza kufanya naye mahojiano akampatia namba ya simu mwanamke huyo kwa ajili ya maongezi zaidi hapo mbeleni.



    Bibie Marietta akajikusanya na kwenda zake.



    Alijiweka kwenye gari na kutimka, kama kawaida alikuwa akiongozana na walinzi wake wawili watiifu. Lakini pasi na kujua, kulikuwa na mwanaume mmoja aliyekuwa ndani ya gari akimtazama mwanamke huyo akiyoyoma.



    Mwanaume huyo alikuwapo hapo tangu Marietta alipoingia ndani mpaka kutoka kwake.



    Alipoona Marietta ameenda zake, naye basi akahepa akielekea uelekeo mwingine.



    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    **



    “Una uhakika?” aliuliza Ian. Mwanaume huyo alikuwa ameketi kwenye ‘kiti chake cha enzi’, ndani ya suti rangi nyeupe, shati jeusi na tai nyekundu. Mkononi alikuwa amebebelea sigara kubwa inayomwaga moshi, mdomo wake ulikuwa mkavu na vuguvugu kwa moto wa sigara.



    Mbele yake alikuwa amesimama mwanaume yule ambaye alikuwa anamfuatilia bibie Marietta. Mwanaume huyo alikuwa amevalia koti la ngozi rangi nyeusi, mkononi alikuwa amebebelea funguo wa gari.



    “Ndiyo nina uhakika, mkuu, nimemwona kwa macho yangu kabisa!” alisema huyo mwanaume kisha akaenda zake akimwacha bwana Ian anafikiri.



    Kwanini Marietta ameenda kwa inspekta? Anataka kumwaga mchele ama? Anafahamu fika kuwa jambo hili la Marshall alitakiwi kufika polisi. Amefuata nini huko?



    Alijiuliza maswali yasiyo na ukomo.



    Alijiona yu hatarini na huenda Marietta akamgeuka hapa, basi kwanza akaamua kumpigia simu bwana Willy na kumtaka mwanaume huyo afike ofisini mara moja!



    “Nipo mbali, mkuu,” akasema bwana Willy simuni.



    “Willy!” bwana Ian akaita kwa kufoka kisha akabamiza meza. “Uwe mbali ama karibu, nakuhitaji hapa ofisini mara moja!” aliposema hivyo akakata simu yake na kuibamizia mezani.



    Kisha akavuta pafu kama nane za sigara. Alikuwa yu moto haswa.



    Kichwa kilikuwa kinamgonga, mkono aliobebelea sigara ukiwa unatetemeka.



    Alinyanyua simu kumpigia Marietta lakini mwanamke huyo hakupokea. Alijaribu tena na tena lakini bado. Akaamua kumwandikia ujumbe.



    Lakini kila alipouandika ujumbe, akaufuta kwa kuuona haufai. Alifanya hivyo takribani mara tatu mwishowe akaamua kuachana na zoezi hilo.



    Akabaki kuvuta sigara tu kama mwehu.





    **



    “Kwahiyo nifanye nini, mkuu?” lilikuwa swali la kwanza baada ya bwana Ian kumweleza bwana Willy kilichotokea. Bwana huyo alitumia masaa matano mpaka kuja kukutana na Ian.



    Wakati huo Ian alikuwa amekwishamaliza kama pakti tatu za sigara!



    “Unaniuliza ufanye nini?” Ian akafoka. “Ina maana hujui cha kufanya?”



    “Hapana mkuu!” bwana Willy akatanabaisha, “ni kwamba nilitarajia huenda ukawa na mawazo. Ila usijali, nitajua cha kufanya,” bwana Willy alivyosema vivyo akanyanyuka kumuaga bwana Ian.



    “Willy!” Bwana Ian akaita na kusema, “Naomba kazi hiyo iwe nadhifu!”



    Kazi nadhifu ni ile inayofanyika pasipo kuacha alama yoyote nyuma ya kutilia mashaka.



    Bwana Willy akaitikia na kisha akaenda zake.



    Alijipakia kwenye gari lake matata alafu akatimka upesi akielekea kwake. Alikuwa anafikiria kichwani juu ya mwenendo wake ujao na baada ya muda akaafiki kuwa anahitaji kwenda kuonana na bwana James.



    Si kazini, hapana, bali kwake kwa wakati huo wa usiku.



    Kwa mara ya kwanza alidhani itakuwa vema kama akienda kuonana na Marietta lakini baada ya kufikiria akakubaliana na kichwa chake kwamba mwanamke huyo hatoridhia kile ambacho ameenda kukisema, hivyo acha aanzie kwa bwana James.



    Huyo akikubali ama akikataa, ni lazima afe! Ni wazi amekuwa mkaidi asiyesikia la wakuu.



    Basi akafika nyumbani na kuoga vema kisha akaandaa nguo zake na vifaa vyake vya kazi. Nguo nyeusi, buti na barakoa. Bunduki na visu viwili vikubwa kwenye nyonga na nyuma ya mguu unaofunikwa na suruali.



    Pia akabebelea na ‘spray’ ya kemikali kwenye begi lake dogo aliloliweka mgongoni.



    Alipoona kila kitu kipo sawa, akajipaki kwenye gari lake na kuanza safari ya kuelekea kwenye makazi ya bwana James. Safari yake ikamchukua kama masaa mawili hivi.



    Alipofika, asiwe na haraka, akajiweka kando akisoma kwanza mazingira. Alizima taa za gari na hata gari lenyewe kisha akakaa hapo kwa kama nusu saa hivi kabla hajawasha tena gari na kuliacha ‘stand by’.



    Taratibu akasonga kuelekea nyuma ya nyumba ya bwana James, kwenye mlango wa nyuma akakomea hapo na kuzamisha mkono wake ndani ya begi.



    Humo akatoa pini ndogo yenye kung’aa kama dhahabu, akaikunja pini hiyo kwa mikono yake iliyofunikwa na glovu alafu akaizamisha kwenye kitasa na kukorokochoa, punde mlango ukafunguka!



    Kwa taratibu akausukuma na wenyewe haukutoa kelele hata kidogo. Alipoona kila kitu ni shwari, akazama ndani akitanguliza mguu wake wa kuume.



    **



    “Amekwishaingia!” sauti ilinong’ona.



    Alikuwa ni Harold akiwa amesimama mbali kidogo na nyumba ya bwana James. Mwanaume huyo akiwa amesimama hapo alikuwa amebebelea hadubini ambayo aliitumia kumtazamia bwana Willy akizama ndani.



    Pembeni ya Harold alikuwa amesimama bwana Gerrard, yeye mkononi alikuwa amebebelea bunduki ndogo na pia macho yake yakiwa yanatazama makazi ya bwana James Peak, mkuu wao.



    Mabwana hawa wawili, katika namna ya kutoonekana, walimfuatilia bwana Willy tangu akitoka kwenye nyumba yake.



    William hakuwa anafahamu hilo. Hakuwa anafahamu kama mabwana hawa walikuwa wameweka kambi kwenye makazi yake wala kama tayari ameshaundiwa kamati maalumu kwa ajili ya kumfuatilia kwa ukaribu.



    Wakati wa majira ya mchana, baada ya bwana James Peak kuongea na Marietta, aliweka madhanio kuwa huenda bwana yule anayewafuatilia atafuata kujua taarifa hiyo kutoka kwa yeyote kati yao.



    Hivyo wakachukua hatua.



    Wakati Willy anazima gari kukagua eneo, wakina Harold nao wakawa wanazima gari wakiwa umbali wa kutosha dhidi yake katika eneo la maficho.



    Wakati bwana Willy akishuka kwenda ndani ya jengo, Harold na Gerrard nao wakashuka kumtazama mwanaume huyo anafanya nini.



    Na kwa wakati wote huo wakiwa wanawasiliana na James.



    James ambaye yeye ndiyo yupo ndani ya jengo.



    “Kuweni tayari muda wowote!” sauti ya James ilisikika kwenye kifaa cha sauti kisha kukawa kimya.



    Harold na Gerrard wakawa wamesimama tenge kungoja agizo.





    **



    Basi bwana Willy, akiwa hana hili wala lile, akazidi kusonga ndani ya nyumba ya bwana James. Mkono wake wa kuume ulikuwa umebebelea bunduki, macho yamemtoka kukodoa na masikio yake yamesimama kuskiza.



    Alikuwa jikoni. Jiko lilikuwa kubwa na la kuvutia lakini lisilo na matumizi kwa mwenyeji tangu atengane na familia yake. Alipomaliza kukatiza jikoni, akashika korido inayoelekea sebuleni na chumbani.



    Hapo akasita kwanza kusikiza kama yu salama. Alipoona kimya, akapiga moyo konde na kusonga zaidi.





    *SEHEMU YA 06*

    Alisonga kushika korido ya kuelekea chumbani baada ya kuona sebule ni tupu. Alipopiga hatua kadhaa akawa amefikia chumba cha kwanza kati ya vinne.



    Akajaribu kufungua chumba hicho kikafunguka. Kwa taratibu akausogeza mlango na kutazama ndani, kulikuwa kutupu, basi kaachana na chumba hicho na kusonga mbele zaidi.



    Akakifikia chumba cha pili, lakini kabla hajakifungua, akasikia mlio wa mlango nyuma yake, akash’tuka! Upesi akatazama huko na kuona mlango wa chumba alichokipita ukiwa unachezacheza.



    Akaurudia mlango huo na kuufunga taratibu kisha akaendelea na mlango wa mbele. Akaufungua taratibu na kutazama, hamna kitu! Chumba kilikuwa kitupu.



    Mpaka hapo akawa ameshamaliza nusu ya vyumba, kumalizia vyote akageukia upande mwingine uliokuwa na milango miwili.



    Akaufungua mlango wa kwanza na kutupa macho yake. Hakuona kitu. Lakini kabla hajatoa kichwa humo, akabaini juu ya kitanda kulikuwa na nguo, hiyo ilikuwa ni ishara ya mtu kuwapo humo!



    Japo chumba hicho hakuwa anakitambua kama ni cha James, kumbuka alishawahi kuja hapo awali, lakini akavutiwa kuingia atazame zaidi.



    Bwana huyu atakuwa wapi? Alijiuliza akisonga. Mbona kwenye chumba chake hayupo? Ina maana hajalala leo kwake? Aliendelea kujiuliza akiwa anasonga zaidi na zaidi.



    Alipofikia kitanda akachukua nguo moja hapo na kuipeleka puani kunusa. Ilikuwa ni nguo iliyotoka kutumika muda si mrefu, pua yake ilitambua. Lakini kabla hajafanya kitu, akahisi kishindo cha mtu nyuma yake.http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Alipogeuka akamwona mtu akimjia! Upesi akanyoosha mkono wake wenye bunduki lakini usimsaidie kitu, mkono ukapigwa akadondosha silaha chini na kubaki mikono mitupu!



    “Nilikuwa natarajia ujio wako, Willy,” akasema mwanaume ambaye aliposonga kidogo mbele ukaonekana vema uso wa bwana James. Alikuwa amevalia sweta jeusi linalobana mwili pamoja na suruali nyepesi mithili ya ‘traki’, rangi nyeusi pia.



    Basi Willy pasipo kutia neno, akajiweka sawa kwa jili ya pambano, naye bwana James akatanua miguu na kukunja ngumi, tayari kwa ajili ya kumpokea mgeni wake katika namna ya pili.



    Pambano likazuka!



    Bwana Willy alirusha ngumi nyepesi na za haraka. Alikuwa mwepesi sana lakini mashambulizi yake hayakuwa na madhara. Mara kwa mara bwana James alitabiri mwenendo wake na hivyo basi ikawa rahisi kumkabili adui yake.



    Jambo ambalo bwana James hakuwa analifahamu ni kwamba, William alikuwa ana silaha zingine kwenye mwili wake, nazo ni visu. Na mwanaume huyo alikuwa mzuri zaidi kwenye matumizi ya silaha kuliko kombati ya kawaida.



    Basi wakiwa wanaendelea kupimana ubavu, bwana Willy akanyumbulika kurusha teke sanifu. Ni kwa haraka sana, alimgeuzia mgongo bwana James na kisha akapaa kidogo kwa kama urefu wa futi tano toka ardhini alafu akajigeuza akiwa ametanua miguu yake.



    Aliutanguliza ule wa kulia kwanguvu ukifuatiwa na wa kushoto!



    James akafanya jitihada za kujikinga na shambulizi hilo, lakini pasipo kujua kuwa ingali Willy akiwa hewani alichomoa kisu toka kwenye mguu wake na sasa amekiweka mkononi.



    Basi akiwa anajikinga na shambulio jingine, akatahamaki mkono wake umechanwa na unavuja damu.



    “Ni bora ukatulia ukafa kifo cha taratibu, James,” akasema Willy na kuongezea, “Leo ni siku yako ya kufa!”



    Kurupu akamfuata James, akarusha kisu, James akakwepa, alipotaka kurudisha mkono wake nyuma, usifike popote, James akauvutia na kuubana kwapani kwanguvu, alafu akauminya kuutengua.



    Willy akapaza sauti kuu ya maumivu!



    Akajaribu kuuokoa mkono wake kwa kuutuma mwingine lakini James akawa upesi zaidi kwa kuukita mkono huo ngumi nzito alafu akamshindilia Willy ngumi tatu za maana mbavuni na kumwachia huru.



    Willy akashika mbavu zake akiugulia. Alikuwa anahisi maumivu makali sana. Alihisi pengine moja ama zaidi ya mbavu zake zitakuwa zimevunjwa. Alitema damu ikaishia kwenye barakoa.



    Basi baada ya hapo akawa mdhaifu sana kupambana na James tena. Hata alipochomoa kisu kingine hakufua dafu kwani alikuwa anahisi maumivu makali mbavuni, hakuwa anaweza kutuma ngumi kwa ufasaha wala teke.



    Kitu pekee anachokumbuka kabla ya kupoteza fahamu ilikuwa ni kumwona James akiwa hewani baada ya kumsulubu kwa teke la kianzio. Hilo teke lingine lililokuja baada ya hapo, hata hakujua maumivu yake kwani lilimziraisha mara moja!



    **



    “Sogeeni!” sauti ilisema kwenye chombo cha mawasiliano, bwana Harold akamtazama mwenziwe, Gerrard, na kumpatia ishara ya kichwa, wakajongea ndani ya nyumba ya James.



    Walimkuta bwana huyo akiwa ameketi sebuleni anafunga jeraha lake kwa bandeji.



    Harold akauliza,



    “Yupo wapi?”



    “Chumbani,” bwana James akajibu akiendelea na zoezi lake, Harold na Gerrard wakaenda chumbani kumwona bwana Willy ambaye alikuwa hajitambui.



    Baada ya muda mfupi polisi wakafika eneo la tukio na bwana Willy akabebwa.



    **



    Asubuhi palipokucha tu, bwana Ian alipata taaria juu ya Willy. Aliyemfikishia taarifa hizo alikuwa ni moja ya mashushu wake waliokuwapo ndani ya polisi.



    Habari hizo zikamvuruga sana bwana Ian na kumkosesha raha. Alivuta sigara kama hana akili nzuri lakini hakupata ahueni. Alihofia huenda Willy anaweza akamwaga mchele panapo banda la kuku!



    Habari hazikuwa kificho tena. Kwenye majira ya mchana zilizidi kupamba moto na kushika karibia kila chombo cha habari Marekani, Ajenti wa FBI avamia nyumba ya inspekta na kutiwa nguvuni!



    Ulikuwa mjadala mkubwa na mzito.



    Mkuu wa FBI alijitokeza hadharani na kukana madai ya shirika lao kuhusishwa na tukio hilo akisema kuwa ameshangazwa na wao pia watalichukulia hatua.



    Zaidi ya hapo kila mtu akawa anaumba tukio lake kichwani na kujipatia sababu. Nyingi zikiwa ni sababu zisizo na mantiki ama zikiwa zimeenda kombo!



    “Unafikiria nini kuhusu hili?” Marshall alimuuliza Miss Danielle. Watu hawa wawili walikuwa kwenye gari wenyewe, Marshall akiendesha.



    “Walitaka kumuua James,” Danielle akajibu akitazama nje ya dirisha. Kiuhalisia mwanamke huyu alikuwa ana uwezo mkubwa sana wa kuchanganua mambo. Kasi ya akili yake ilikuwa inatisha.



    Jambo gumu angeweza kulifanya likawa jepesi kabisa kwa kulivunjavunja vipandevipande.



    “Kwanini unadhani hivyo?”



    “Ian hawezi akawa mwenyewe, ana timu yake udhalimu, bila shaka katika timu hiyo kuna huyo aliyekamatwa.”



    “Sawa, kwanini unadhani wanataka kumuua James?”



    “Wao na James wanashea kitu kimoja, wote wanakutafuta wewe. Ni swala la conflict of interest. Pengine James amepata kitu kuhusu wewe hivyo wanakitaka, ama wanataka swala hili la kukutafuta liwe binafsi kwenye mhimili mmoja ulio karibu nao, na si mwingine bali FBI.”



    “Kwahiyo vipi kuhusu Marietta? Unadhani atakuwa kwenye hatari pia?”



    “Bila shaka, kama tu watakuwa wamejua kuwa ulikutana naye.”



    “Ni lazima watakuwa wanajua hilo!”



    Basi Danielle akamtazama Marshall na kumwambia, “Kama ni hivyo, tutarajie Marietta kuuawa ama kupotea muda si mrefu.”







    Wakafika kwenye makazi yao mbali na jiji, huko wakapumzika wakiwa wamkutana na Jack alafu baada ya muda kidogo wakajumuika kwa pamoja kupata chakula cha usiku.



    Wakiwa hapo wakawa wanajadili mambo kadhaa. Mambo ambayo yametokea na ambayo yanafuatia.



    Lakini katika hayo swala la bwana Willy lilishika sana hatamu.



    “Unadhani bwana James atakuwa anafahamu kuwa jamaa huyo aliyekamatwa anahusika na bwana Ian?” akauliza Jack Pyong akitafuna.



    “Hataweza kujua,” akajibu Marshall baada ya kumeza. “Pengine kama atatumia njia mbadala ya kumlazimisha mwanaume huyo aongee kila kitu. Kitu ambacho ni ngumu sana kutokea!”



    Kukawa kimya kidogo wakitafuna. Baada ya vijiko viwili vitatu, Jack akasema,



    “Napata mawazo sana juu ya hili. Leo nimepekuwa magazeti kila moja na habari yake. Nimejiuliza, kama huyu bwana amekamatwa akiwa amejikamilisha kisilaha, yupo kwenye nyumba ya inspekta, vipi kuhusu maajenti wengine? Hamna ambao wapo pamoja naye pale shirikani?”



    Akiwa anasema hayo alimtazama Danielle. Mwanamke huyo akangoja kwanza ameze nipi ajibu. Ni Jack Pyong peke yake ndiyo alikuwa anaweza kuongea na chakula mdomoni.



    “Jack,” Danielle akaita na kugusia, “shirika ni kitu kikubwa chenye watu wengi. Ndani yake haiwezekani wote wakawa wema, kuna ambao ni mahasidi na kuna ambao wanalipigania taifa lao.”



    Basi baada ya hapo kukawa kimya zaidi watu wakila na kunywa. Baada ya kumaliza wakaendelea na mjadala wao.



    “Natazamia kama nitapata nafasi ya kuonana na rafiki yangu,” alisema Danielle na kuongeza, “pengine yeye atakuwa ananieleza ni nini kinaendelea kule shirikani.”



    “Itakuwa vema,”Marshall akaunga mkono, “Nadhani kutakuwa na mtandao fulani kwenye shirika na FBI unaoongozwa na wadhalimu. Endapo tukibahatika kumpata mtu hata mmoja, basi atatusaidia sana kwenye upelelezi wetu.”



    “Kabisa,” Danielle akaafiki. “Lakini pia wakati Jack anaongea kuhusu magazeti, nimejikuta napata wazo.”



    “Lipi hilo?” Jack akawahi kuuliza.



    “Mnaonaje kama tukaanzisha chombo cha habari?” Danielle akapendekeza.



    “Danielle, huoni ni gharama sana? Tutawezaje kuendesha chombo hicho ikiwa kinahitaji pesa sana kwenye uwekezaji?” Jack akawahi kupinga hoja.



    Lakini Marshall yeye alitulia. Alijua kuna kitu kichwani mwa Danielle hivyo akampa muda zaidi mwanamke huyo aongee.



    “Si kama unavyowaza, Jack,” akasema Danielle. “Ni gazeti tu! Na gazeti hilo litakuwa limesajiliwa na ‘farm’ yetu ya upelelezi. Litakuwa linatoa habari kwa kina na matazamio ya mambo mbalimbali kisiasa, kijamii na hata kiuchumi.



    Mitazamio ambayo itakuwa yakinifu na ya kiundani sana. Napata kuamini gazeti hilo litakuwa kubwa sana kutokana na habari zake, na hivyo basi litakuwa na wateja wengi, haswa kwenye kipindi kilichogubikwa na matukio kama hiki.



    Au mnasemaje?”



    Danielle akauliza akimtazama Marshall.



    “Ni wazo jema!” Jack akapaza sauti. “Naunga mkono hoja!”



    “Na vipi kuhusu wewe Marshall?” Danielle akauliza. “Wewe unalionaje hili?”



    Marshall akakuna kidevu akifikiri, kidogo naye akaunga mkono hoja na kuongezea habari, “itapendeza kama mhariri na waandishi wa hilo gazeti wakawa watu wasiofahamika kwa ajili ya ishu za usalama.



    Waandishi hao hawatakiwi kujulikana na jamii wala na vyombo vya usalama. Hilo pia litawafanya wafanye kazi kwa uhuru pasipo kuhofia.”



    “Ni wazo jema!” Danielle akasema akiliza vidole vyake. “Kama ni hivyo basi, hamna haja ya kusema gazeti hilo linamilikiwa na ‘farm’ yetu ya upelelezi. Mnaonaje?”



    “Ni wazo jema,” Marshall na Jack wakaunga mkono, lakini wakakubaliana kwamba jambo hilo litafuata baada ya kumaliza kwanza kusajili taasisi yao ya kipelelezi.



    Muda ulikuwa umebakia mchache kukamilisha hilo na kila jambo lilikuwa limeshawasilishwa kwenye mamlaka husika.



    Basi mjadala huo ukafungwa na sasa wajamaa hawa wakawa wamemwazima masikio bwana Jack ambaye alikuwa anaeleza yale ambayo ameyang’amua toka kwenye msako wake mitandaoni.



    Haswa kwenye lile swala la mkutano wa kimataifa uliokuwa unafanyika kule Ujerumani. Mkutano ambao ulifanyika muda mfupi baada ya Raisi wa Marekani kupotea.



    Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, bwana Jack alipata kubaini kuwa jambo kubwa lililokuwa linangojewa kwenye mkutano huo kama ajenda kuu ni swala la mabadiliko tabia nchi na kivipi nchi zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo zitachukua hatua kuhusu swala hilo.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Marekani ilikuwa radhi kuunga mkono jitihada za kupunguza idadi ya viwanda na haswa vinu vya nyuklia duniani, lakini si kila taifa lilikuwa linaunga mkono jambo hilo.



    Na zaidi, kulikuwa na mjadala mkubwa juu ya soko la mafuta na ushawishi wa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani.



    Kwenye sakata hilo, Marekani alikuwa amesimama kidete kupinga mfumuko wa bei ya mafuta duniani na haswa vikwazo ambavyo amewekewa dhidi ya mataifa ambayo yanaongoza kuzalisha mafuta duniani.



    Baada ya Jack kueleza hayo, Marshall na Danielle wakaanza kuchanganua taarifa hizo vichwani mwao kubaini wapi ulipotoka mkono uliompoteza Raisi.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog