Search This Blog

Friday, 18 November 2022

SALA YA SARAH - 2

 






Simulizi : Sala Ya Sarah

Sehemu Ya Pili (2)







Kipindi hicho chote Sarah alikuwa ameshafika mbali sana, kumbe hakuingia ndani ya gari la dalali, badala yake Sarah alimuuliza dalali kama kuna njia nyingine ya kuondoka eneo lile tofauti na hiyo inayotumiwa kila siku, ndipo dalali aliposema kuwa njia ipo ila ni ya watembea kwa miguu tu, vyombo vya moto haviwezi kupita kwa maana mbele kuna mto umekatiza na hakuna daraja kubwa, kuna kadaraja kadogo tu kwa ajili ya watu.



Sarah ndipo akachagua kupita njia hiyo, alifanya hivyo baada kuhisi huenda vijana wa Taita wanaweza kusambazwa njia kubwa na ikawa kazi kwake kutoka salama eneo hilo. Sarah akaamua kupita uko huku akimwambia dalali watawasiliana baada ya muda mchache.



Sarah alifanikiwa kutembea mpaka alipofika eneo lenye watu wengi, akachukua simu yake na kumpigia dalali ili amfuate, haikuchukua muda Mrefu sana dalali akafika eneo lile na kisha sarah akaingia ndani ya gari, tena siti za mbele,



"Kwanini ulipita ile njia?" Dalali alimuuliza Sarah,



"Kuna kitu nilienda kununua, maana nilielekezwa kinapatikana mitaa ile" Sarah alimdanganya dalali,



"Basi mwenzako mbele nilikutana na maaskari sijui wale, wakanisimamisha, inaelekea kuna mtu wanamtafuta" Dalali aliongea na kufanya Sarah ashtuke, ila hukuonesha mshtuko wake,



"Huenda kuna kibaka au jambazi wanamtafuta, huenda waliambiwa yupo mtaa ule" Sarah aliongea huku akiuficha mshtuko wake,



"Wasumbufu tu wale" Dalali aliongea,



"Waache wafanye kazi" Sarah aliongea na kisha yakafuata maongezi mengine ya kawaida mpaka walipofika kwenye hiyo nyumba ambayo Sarah ameenda kuiangalia.



Wakashuka na kisha Dalali akaenda kumchukua mwenye nyumba, hakuwa mbali na pale,



Kipindi dalali ameenda kumchukua mwenye nyumba, Sarah alitumia muda huo kuikagua ile nyumba kwa kuizunguka, baada ya dakika tano dalali alifika huku akiwa ameongozana na mwenye nyumba,



"Karibu binti" Mwenye nyumba aliongea huku akimpa mkono Sarah,



"Asante, shikamoo baba" Sarah alimsalimia huku akimpa mkono,



"Marahaba binti, nyumba umeiona?" Mwenye nyumba alimuuliza Sarah,



"Nimeiona kwa nje, nimeridhika ila bado sijajua kwa ndani ikoje?" Sarah alijibu,



"Twendeni ndani ili apaone" Mwenye nyumba alimwambia dalali kisha wakaanza kuelekea ndani ya nyumba, walifika mlangoni kisha mwenye nyumba akafungua mlango na wote wakaingia, Sarah akaanza kuikagua ile nyumba, alikagua kila chumba na kila kitu ndani ya ile nyumba, akaridhika nayo.



"Nimeridhika Mzee wangu, je naweza kuipata leo, yaani tukauziana na kumalizana leo leo?" Sarah alimuuliza mwenye nyumba,



"Mbona haraka hivyo?" Mwenye nyumba aliuliza kwa mshangao,



"Nahitaji leo Mzee, naomba tumalizane tu" Sarah aliongea kwa mkazo,



"Sawa, twende kwa mwenyekiti wa kijiji na pia unatakiwa na mashahidi wawili" Mwenye nyumba aliongea,



.



"Shahidi yupo mmoja, huyu dalali, sina ndugu Tanzania" Sarah aliongea na kufanya wenzie wamtolee macho,



"Wewe ni mgeni?" Mwenye nyumba aliuliza,



"Mgeni, sina ndugu wala sina rafiki" Sarah alijibu,



"Umetoka nchi gani?" Mwenye nyumba aliuliza,



"Uingereza" Sarah alijibu,



"Mbona unaongea kiswahili safi?" Dalali aliuliza,



"Nilijifunza na pia Nina kidogo hapa nchini kwenu" Sarah alijibu,



"Sawa mama nimekuelewa, sasa itabidi uwe na kila kitu ili tufanikishe kuuziana hii nyumba, hata ikishindikana kufikia makubaliano leo, basi kesho naamini tutamalizana" Mwenye nyumba aliongea,



"Itabidi iwezekane leo, maana sina pa kulala" Sarah aliongea na kufanya wenzake wacheke wakidhani utani wakati mwenzao alidhamiria.



Baada ya hapo wakatoka mpaka kwa mwenyekiti wa mtaa na kuanza hatua za kuuziana nyumba, ingawa kulikuwa na hatua nyingi na ngumu, ila baada ya masaa matatu kila kitu kilienda sawa, Sarah akachukua nyumba yake, kisha akaenda mjini na kununua samani za ndani na kuchukua vijana watano kwa ajili ya kumsaidia kufanya usafi.



Baada ya masaa mawili kila kitu kilikuwa safi, nyumba ilinoga, na ikawa ndio makazi rasmi ya Sarah.



Akawalipa vijana wale kisha wakaondoka zao, yeye akaelekea bafuni kuoga, alipomaliza akaingia chumbani kwake na kuvaa suruali nyeusi na fulana nyeusi, usoni alivaa miwani yenye kioo cheupe, hiyo ilikuwa yapata saa kumi na mbili jioni.



************************



Mishale ya saa moja jioni, Taita na jopo lake la watu muhimu walikuwa wanaingia vin hotel, moja kwa moja wakaelekea kwenye chumba kidogo cha mikutano kwa ajili ya kujadili shambulio la bomu lilimuua kijana wao mmoja.



Mwenyekiti wa kikao alikuwa Taita, ila kabla hawajafungua rasmi kikao, mlango wa kile chumba ulifunguliwa na mlangoni alisimama binti akiwa na nguo nyeusi, Taita na wenzake wakabaki wamemtolea macho............

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



????????Ila huyu aliyesimama mlangoni hakuvaa suruali na fulana, alivaa suti ya kike nyeusi, alikuwa ni muhudumu wa pale Vin hotel,



"Samahanini, hamuhitaji vinywaji?" Muhudumu aliwauliza huku akiwa amesimama pale pale mlangoni,



"Kwa sasa hatuhitaji, tutakuita tukihitaji" Taita aliongea na kumfanya yule dada ageuke na kuondoka.



Ndani ya chumba cha kikao walikuwepo watu sita tu, yaani Taita mwenyewe, Trigger, Harry, Dula ambaye hufahamika kama strategic na Toisa.



Niwakumbushe tu kuwa huyu Strategic ni mtaalam wa mipango na mbinu za kumuingilia adui, wakati Toisa ni mjanja mjanja wa kupenya penya na kumuadaa adui.



"Kilichopo mbele yetu mnakijua, ni kuhusu huyu adui ambaye hatujui lengo lake ni nini hasa, au kuna mtu ana uadui na mtu kati yetu?" Taita aliuliza huku akiwatazama wenzake ambao walikuwa kimya,



"Ukimya wenu una maanisha kuwa hakuna mtu mwenye adui, sasa huyu mtu atakuwa anataka nini kwetu?" Taita alitupa swali jingine,



"Labda tukuulize wewe, huna adui ambaye hatumjui?" Harry alimtupia swali Taita,



"Ujue ukiwa na maendeleo huwezi kukosa maadui, sasa inawezekana maadui wapo ila bado sijawatambua" Taita alijibu,



"Lakini huyo adui mnayemzungumzia ni tofauti sana, kama mmesema alishajionesha zaidi ya mara moja, basi huyo mtu sio wa masihara hata kidogo, anajiamini" Strategic aliongea na kutabasamu kidogo,



"Ukitoa kujiamini pia inaonekana anafanya haya matukio kwa akili na mipango ya kutosha, maana anajua kabisa kuwa baada ya kumfanyia kitu adui na matokeo ambayo yatachukuliwa na adui" Tekso aliongea,



"Sasa kilichotuleta hapa sio kumzungumzia, ila ni nini tufanye ili tumtie mikononi" Trigger aliongea baada ya kuhisi wenzake wanatoka nje ya mada,



"Ni lazima tujue tabia zake ili tupate mbinu za kumuingilia" Strategic alimjibu Trigger,



"Sasa kwa tabia zake hizo chache mlizozijua, umepata jibu gani la kumuingilia?" Trigger aliuliza huku akimtupia jicho Strategic,



"Kabla hatujapata mbinu za kumuingilia, ni lazima tumjue yeye kwanza, sio juu juu kama sasa hivi, ni lazima tumjue hata kwa kumuhisi alafu ndio tutafute mbinu za kumjua vizuri" Strategic alijibu na kumfanya Trigger acheke,



"Hiyo njia ni ngumu sana" Trigger aliongea huku akicheka,



"Kwa maelezo ya dada wa guest, anadai aliondoka na gari ndogo nyeusi, kwanini msingemuuliza huyo dada kama anaifahamu hiyo gari?" Strategic aliuliza huku akimgeukia Tekso,



"Isingesaidia" Tekso alijibu,



"Nadhani ingeweza kusaidia endapo kama huyo mfanyakazi wa guest anaifahamu hiyo gari, ni swali muhimu hilo alilouliza bwana strategic" Harry aliongea,



"Kweli, nadhani mlitakiwa mmuulize huyo dada wa guest" Taita nae aliunga mkono,



"Na kama halijui hilo gari?" Tekso aliuliza,



"Basi tutaangalia namna nyingine" Taita alijibu,



"Na pia Mzee unadai huyo binti ameshawahi kukuletea zawadi, ingekuwa vizuri kama tungepata alama za vidole vyake" Strategic aliongea huku akimtazama Taita,



"Kwenye lile box ni ngumu kupata alama zake, maana nimelishika shika sana, mtakuta alama za vidole vyangu tu" Taita alijibu,



"Basi kesho asubuhi shughuli ianzie pale guest, Tekso utaenda mapema" Trigger aliongea huku akimtazama Tekso,



"Sawa mkuu" Tekso alijibu ingawa hakuamini kama hiyo itamsaidia kwa maana katika lile gari hawakumkuta mtu mwingine zaidi ya dereva.



" kwa leo kikao kiishie hapa, kama Tekso atakosa jibu kesho, basi tutarudi tena hapa kesho, na hata akipata tutarudi tena kesho" Taita aliongea,



"Naamini majibu yatakuja mazuri" Strategic aliongea,



"Acha tuamini hivyo" Taita alijibu huku akiinuka katika kiti chake,



"Unaelekea wapi muda huu?" Harry alimuuliza Taita,



"Naenda kupata kinywaji kidogo na kuangalia wafanyakazi wa hapa wana mpya gani, alafu nitaondoka" Taita alijibu huku akielekea nje na kufanya wenzake nao waanze kuondoka mmoja mmoja.



Kila mtu alitoka na kuelekea katika gari lake na kuondoka.



Harry yeye alipotoka aliingia kwenye gari aliingia kwenye gari lake na kubonyeza simu yake kwa muda kisha akawasha gari na kuliondoa taratibu, ila nyuma yake kulikuwa na gari ndogo inamfuata, ilikuwa gari ya dalali.



Harry aliendesha kwa muda gari lake akahisi kuna gari inamfuata kwa nyuma, akapata wasiwasi na kukunja barabara iliyoingia mitaani na kuiacha barabara kuu, ile gari iliyokuwa inamfuata ikapita barabara kuu na wala haikumfuata tena.



Harry akarudi barabara kuu na kushika njia ya kwenda nyumbani kwake bila kuiona tena ile gari, harry alifika getini na kupiga honi, geti likafunguliwa na mlinzi, Harry akaingiza gari ndani na kushuka, akamuuliza mlinzi habari za pale na mlinzi akajibu ni nzuri.



Harry akaingia ndani kwake, alipofika sebuleni tu akashtuka, hakukuta hali si ya kawaida, alimkuta Sarah ndani, ya juu ya kochi akiwa amekunja nne, usoni alivaa kinyago kilichoanzia puani na kushuka chini mpaka kidevuni kama mkionacho kwenye jalada la riwaya yetu.



Hapo mke wa Harry alikuwa amelazwa sakafuni huku amefungwa kamba mikononi na mdomoni alibandikwa gundi ya karatasi iliyomzuia kupiga kelele.



Sarah alikuwa amekunja nne, mkono wa kulia alishika bastola ndogo ya rangi ya dhahabu na mkono wa kushoto alishika bilauri ya kioo iliyokuwa na maji,



"Karibu mwenyeji wangu, ila leo wewe utakuwa mgeni kwa muda" Sarah aliongea kisha akatabasamu, bahati mbaya Harry hakuweza kuliona hilo tabasamu kutokana na kinyago alichovaa Sarah, Harry alipigwa na mshangao tu huku hakiwa hajui afanye nini,



"Sema unataka nini, iache familia yangu nitakupa utakacho" Harry alijikaza na kuongea,



"Utanipa utakacho? una uhakika?" Sarah aliuliza huku akimkazia macho,



"Ndio, sema unataka nini?" Harry aliuliza kwa kujiamini ila akiwa na wasiwasi,



"Nataka roho yako" Sarah aliongea huku akiwa bado anamuangalia na kumfanya Harry akune kichwa, hakutegemea kusikia kitu kama hicho,



"Nipe sasa ili niiache familia yako" Sarah aliongea baada ya kumuona Harry amekosa cha kuongea,



"Taja kitu chochote cha thamani tofauti na roho yangu na familia yangu" Harry alipata cha kuongea,



"Ni kipi rahisi kwako, kuchukua roho ya mtu au kutafuta pesa?" Sarah alimtupia swali Harry,



"Kutafuta pesa" Harry alijibu huku akitetemeka,



"Umejibu vizuri, ila kuna kipindi hukuwahi kufikiria kitu kama hicho" Sarah aliongea huku akisimama,



"Unamaanisha nini kusema hivyo?" Harry aliuliza,



"Maana yangu utaijua, utaijua siku nitayoamua kuja rasmi kwa ajili yako, leo sikuja kwa ajili yako" Sarah aliongea huku akiwa anazunguka zunguka ndani ya sebule ya Harry,



"Naomba uiache familia yangu" Harry aliongea,



"Kaa kwenye kochi kwanza" Sarah alimwambia Harry aliyekuwa amesimama, Harry akaenda kukaa kwenye kochi,



"Una elimu gani?" Sarah alimuuliza Harry,



"Mimi ni mwanasheria" Harry alijibu na kufanya Sarah atoe kicheko kwa sauti ya wastani,



"Sijakuuliza wewe ni nani? haya tuachane na hayo, nataka kuondoka sasa" Sarah aliongea huku akimuangalia,



"Sawa Dada, naomba utuache Salama" Harry aliongea huku akipiga magoti,



"Nakuacha Salama, ila una vitu viwili vya kuchagua, upo tayari?" Sarah alimuuliza Harry,



"Nipo tayari ili mradi visiwe na athari kwenye familia yangu" Harry alijibu,



"Cha kwanza, nikupe nafasi ya kutoka dakika mbili uende nje, ila usimwambie mlinzi wako kama kuna mtu hatari ndani, au nikufunge kamba na kukuwekea makaratasi mdomoni Ili niondoke kwa amani?" Sarah aliuliza huku akimuangalia,



"Nitoke nje" Harry alijibu huku akiamini kufanya hivyo kutamsaidia kupata msaada kutoka kwa mlinzi na pia atafunga mlango kwa nje ili kumzuia Sarah asitoke,



"Nenda, ila kumbuka kutomwambia mtu yoyote kama kuna mtekaji ndani, ukijaribu utajuta" Sarah aliongea na kumruhusu Harry aende nje, Harry akatoka nje mbio, alipotoka tu, akaufunga mlango kwa nje, kisha akakimbilia kwa mlinzi,



"Tumevamiwa, unakaa getini kizembe hujui hata kama ndani kuna uvamizi" Harry aliongea kwa hasira na kumfanya mlinzi ashtuke, maana hakuamini maneno ya bosi wake,



"Ndani? mbona hakuna mtu aliyeingia?" Mlinzi aliuliza huku akishangaa,



"Beba silaha twende ndani tukamdhibiti" Harry aliongea kisha mlinzi akabeba bunduki yake, ingawa mlinzi alihisi bosi wake huenda amelewa au amechanganyikiwa tu.



Wakasogea mpaka mlangoni, mlinzi akaanza kufungua mlango haraka haraka,



"Fungua taratibu" Harry aliongea kwa kunong'ona na kisha mlinzi akafuata maelekezo ya Harry, baada ya sekunde mlinzi akafanikiwa kufungua mlango na kisha akaingia sebuleni kwa fujo, hakumkuta mtu zaidi ya mke wa bosi wake akiwa amefungwa kamba,



"Yupo wapi?" Mlinzi aliuliza huku akimtazama Harry, Harry mwenyewe hakujua ni wapi mvamizi alipo,



"Ngoja" Mlinzi aliongea huku akielekea sehemu za vyoo, alipofika uko pia hakukuta mtu, akarudi sebuleni na kumkuta Harry akimfungua kamba mke wake,



"Ameelekea chumbani kwa watoto" Mke wa Harry aliongea baada ya kufunguliwa, alitoa kauli iliyofanya utumbo wa Harry ujikunje kwa maana alihisi hakutakuwa na usalama tena chumbani uko,



"Nenda sasa wewe kafungue, unazubaa zubaa nini wewe?" Harry alimwambia mlinzi wake kwa ukali na kufanya mlinzi aanze kuusogelea mlango wa chumba cha watoto,



"Hapana, huyo mlinzi hatomuweza huyo msichana, ni bora tumfungie mlango kwa nje alafu tuite polisi" Mke wa Harry aliongea na kufanya mlinzi asimame na ahache kuusogelea mlango,



"Ufunge huo mlango kwa nje" Harry aliongea kwa ukali huku jasho likimtiririka na kufanya mlinzi ausogelee mlango na kuufunga kwa nje, wakamsikia Sarah akicheka kwa ndani na kisha kikafuatia kilio cha mtoto wa Harry alafu kukawa kimya ghafla, ukaanza kusikika mziki tu kutoka katika chumba kile cha watoto. Hapo akazidi kuchanganyikiwa zaidi hata simu hakuweza kupiga, ilimbidi mlinzi ndio awataharifu polisi juu ya uvamizi ule.



Iliwachukua dakika tano tu polisi kufika pale, wakaelezwa juu ya kile kinachoendelea pale, polisi wakauzunguka ule mlango, kisha mmoja akaufungua na mwingine akaingia kwa fujo, alivyoingia tu ikasikika sauti kama amegongwa na chuma kichwani, akatoa ukelele, ingawa haukuwa ukelele mkubwa ila watu wote waliokuwepo pale ndani waliusikia vizuri na kufanya wasiwasi uongozeke katika familia ya Harry.........





Askari wengine wakawa wanajipanga namna ya kuingia ndani baada ya kuhisi mwenzao ameshambuliwa ndani ya chumba kile,



"Ingieni nyie" Askari wa ndani alizungumza na kufanya wenzake wapate mshtuko, hawakuingia kwa maana walihisi adui anawafanyia mtego, wakaendelea kusimama pale mlangoni.



Baada ya sekunde mlango wa chumba kile ukafunguliwa na akatoka mwenzao akiwa amembeba mtoto wa kiume, Harry na mke wake wakamkimbilia yule askari,



"Vipi mzima?" Harry aliuliza kwa pupa huku akimtazama mwanae aliyekuwa amezama ndani ya usingizi mzito,



"Sijui" Askari alijibu huku akimlaza juu ya kochi kisha akarudi chumbani kule ambapo alikuta wenzake wameshaingia tayari na walikuwa wanafanya ukaguzi wa macho ndani ya kile chumba,



"Mbona ulivyoingia uliguna alafu tukasikia kama umegongwa na chuma?" Askari alimuuliza mwenzake,



"Kulikuwa na Giza, sasa nilivyoingia nikagonga chuma hiyo chini, nimeumia sana, maana bado nahisi maumivu" Askari yule alijibu,



"Huyo mvamizi hukumkuta?" Askari akauliza tena,



"Hapana, nahisi atakuwa ametokea dirishani, maana si mnaona chuma cha dirisha kimekatwa na pia kioo kimesukumwa upande mmoja" Mwenzake alijibu na wote wakakubaliana kuwa mvamizi ametokea dirishani.



"Mtoto ndio mmemkuta huyu tu?" Harry aliuliza huku akiingia ndani ya chumba kile walichopo askari,



"Tumemkuta huyo tu, kwani wanalalaga wangapi huku?" Askari alijibu kisha akauliza,



"Mwingine hamkumkuta?" Harry aliuliza huku akiwa ameonekana kuchanganyikiwa,



"Wanalalaga wangapi chumba hiki?"Askari aliuliza tena,



"Wanakuwaga wawili" Harry alijibu,



"Kwanza fanyeni mpango huyo mtoto aliyepo apate Huduma, piga simu hospitali" Askari alimwambia Harry baada ya kuona amechanganyikiwa. Harry akatoka mpaka sebuleni na kuichukua simu yake iliyopo juu ya meza na kupiga simu hospitali akihitaji gari ya wagonjwa, alipokata tu simu yake na kuirudisha mezani, simu yake ilianza kuita tena, alipoangalia katika kioo akakuta namba ngeni, akapuuza kuipokea na kuendelea kushughulika na mwanae ambae alionekana amepoteza fahamu.



Simu ya Harry ikaanza kuita tena na namba iliyoonekana kwenye kioo ni ile ile aliyoipuuza hawali,



"Pokea simu" Mke wake alimwambia,



"Namba ngeni" Harry alijibu,



"Pokea huenda inatoka hospital ulipoagiza gari la wagonjwa" Mke wake aliongea na hapo Harry akapokea simu,



"Hallow" Harry aliongea kwa sauti iliyopoa,



"Umevunja makubaliano, nilikupa chaguzi mbili, ukaichagua moja ya kutoka nje na kutotoa taharifa ya uvamizi, lakini ulipotoka ulitoa taharifa, sasa mwanao ninae, jiandae kwa habari mbaya" Sauti ya kike iliongea, ilikuwa sauti ya Sarah iliyozidi kumchosha kabisa Harry,



"Upo wapi na unataka nini?" Harry aliuliza kwa pupa,



"Nipo kwangu, ninachokitaka nimekipata, ni hii damu yako niliyonayo" Sarah alijibu kisha akacheka na kukata simu,



"Hallow, hallow" Harry aliongea lakini simu ilikuwa imeshakatwa muda mrefu tu, Harry akaangalia kioo cha simu yake na hakukuta kitu kipya,



"Ni nani?" Mke wake alimuuliza,



"Ni yule Dada aliyetuvamia" Harry alijibu kinyonge,



"Anasemaje?" Askari aliuliza,



"Anasema mtoto amemchukua, na anadai nijiandae kupokea habari mbaya" Harry alijibu na kumfanya mkewe aangue kilio, maana alijua mwanae atakufa muda sio mrefu,



"Tupe hiyo namba yake" Askari aliongea na kumfanya Harry achukue simu yake na kwenda eneo la simu zilizompigia, akashtuka,



"Namba haionekani" Harry alijibu na kufanya askari wamshangae,



"Si dakika hii hii amekupigia, au umefuta?" Askari aliuliza,



"Sijafuta, hata mimi nashangaa" Harry aliongea kwa mshangao huku akirudia tena kuangalia,



"Ebu simu" Askari aliongea huku akiichukua simu ya Harry, nae akaangalia lakini hakukuta namba,



"Huyo sio mtu wa kawaida, kwanza njia aliyotumia kuingia na kutoka sio mtu yoyote hapa anaweza kufikiria" Harry aliongea na kipindi hicho gari ya wagonjwa ilikuwa ikisimama nje ya geti, wahudumu wakashuka na kitanda cha matairi na kuingia ndani, kisha wakambeba mtoto wa Harry na wakatoka nae nje na kumpakia ndani ya gari upande wa nyuma na kumlaza kitandani, pembeni alikuwepo mama yake, gari lile la wagonjwa likaondoka kwa kasi kumuwahisha mtoto hospitali.



Ndani ya nyumba alibaki Harry na Askari na mlinzi,



"Ngojeni na mimi niwahi hospitali" Harry aliwaambia askari,



"Kwa hiyo suala la mtoto wako kutekwa unalifikiriaje?" Askari mmoja alimuuliza Harry,



"Mimi nitafanyaje sasa, nimewaachia nyie askari" Harry alijibu,



"Dah, mtihani huo, basi wewe nenda hospitali, alafu kesho uje mapema polisi" Askari aliongea na kisha wakakubaliana hivyo na Harry, askari wakaondoka zao na Harry akaelekea hospitali.



*******************



Sarah alipoingia chumba cha watoto, alitoa kichupa kidogo cha spry na kupuliza katika kile chumba, kisha alitumia Bomu dogo sana kulipua dirisha, na alipofanikisha alimbeba mtoto mmoja wa Harry wa kike na kuruka nae ukuta na kutokea upande wa pili kisha akaliendea gari dogo la dalali alilokuja nalo na kumuingiza mtoto, kisha nae akaingia na kuliondoa gari.



Alifika kwake na kuliingiza gari ndani ya geti kisha akamshusha mtoto na kumuingiza chumbani kwake na kumlaza kitandani, Sarah akaenda sebuleni na kutoa maji kisha akanywa,



"Muda wa kuwapa jamba jamba huu, mpaka wakonde" Sarah aliongea kisha akatabasamu, akavua nguo pale sebuleni na kuingia bafuni kuoga, alipotoka alielekea chumbani kwake kisha akazima taa na kupanda kitandani, akalala jirani na mtoto wa Harry,



"Unisamehe malaika, sina nia mbaya na wewe" Sarah aliongea kisha akambusu yule mtoto kwenye paji la uso, mtoto alikuwa hana fahamu.



Baada ya hapo Sarah akavuta shuka na kujifunika, kisha akalala.



******************



Asubuhi ilipambazuka kwa kikundi chote cha Taita kuwa na habari za kuvamiwa kwa harry na kutekwa kwa mtoto wake mmoja. Ilikuwa ni hali mbaya sana ndani ya kikundi hicho, isitoshe aliyekuwa anawasumbua ni binti mdogo tu.



Taita alichoamua ni kuwatuma vijana wake waende kwenye ile guest aliyokuwa akiishi Sarah ili wakafanye kile walijadili kwenye kikao cha siku iloyopita, na uzuri ni kwamba Harry alidai alikuwa anafuatiliwa na gari ile ile iliyoonekana ikiondoka na Sarah guest.



Kazi hiyo ya kwenda guest walipewa vijana wawili, Tekso na Toiso.



Waliondoka na gari mpaka kwenye ile guest na kumkuta Dada yule yule wa mapokezi aliyekuwepo siku iloyopita,



"Dada tumerudi tena" Tekso aliongea baada ya kumsalimia yule dada,



"Karibuni tena" Dada aliwakaribisha baada ya kumkumbuka Tekso,



"Leo tunaomba utusaidie kitu kimoja kidogo tu" Tekso aliongea huku akijikuna kidevu,



"Kipi hicho?" Dada wa mapokezi aliuliza kwa shahuku,



"Ile gari iloyombeba yule binti jana, unamjua yule dereva?" Tekso aliuliza,



"Ndio, yule kaka ni dalali" Dada wa mapokezi alitoa jibu lililowafanya vijana wale watabasamu,



"Tunaweza kumpata wapi?" Tekso aliuliza,



"Kijiwe chao kipo hapo mbele, njia mliyotokea mwisho kule kuna kijiwe cha kahawa" Dada wa mapokezi aliwaelekeza,



"Anaitwa nani?" Toiso aliuliza,



"Jina kwa kweli simjui, ila anapatikana pale" Dada wa mapokezi alijibu,



"Asante, shika hii utakunywa soda" Tekso aliongea huku akiweka noti ya shillingi elfu tano mezani kisha wakaondoka kuelekea hapo katika kijiwe cha madalali.



Walipofika walikuta watu wengi wa rika tofauti wakiwa kijiweni hapo, wakaenda moja kwa moja kwa muuza kahawa, wakamsalimia,



"Samahani, yule dalali mwenye gari ndogo nyeusi, umemuona maeneo haya?" Tekso alimuuliza muuza kahawa,



"Yule ametoka, mnataka chumba au nyumba?" Muuza kahawa aliuliza,



"Tunashida na yeye" Toisa alijibu kifupi,



" msubirini" Muuza kahawa nae akawapa ushauri kisha vijana wale wawili wakaelekea kwenye gari waliyokuja nayo,



"Wewe baki umsubiri hapa, ngoja nikaongeze mafuta" Tekso alimwambia Toisa,



"Sawa, akija kabla hujatokea mimi nitakupigia simu" Toisa alijibu kisha akatelemka kwenye gari na kujichanganya na watu wengine wanaokunywa kahawa, kwa kuwa huyu Jamaa sifa yake ni ujanja ujanja, haikumchukua muda mrefu kukizoea kijiwe.



Baada ya dakika mbili tu za Tekso kuondoka, Toisa alilishuhudia lile gari dogo likija maeneo yale, Toisa akatoa simu mfukoni na kumpigia Tekso, lakini hakufanikiwa, simu yake ilimuishia chaji, akaamua amsubiri tu.



Wakati akiendelea kusubiri ndipo alipoiona ile gari ndogo ya dalali ikianza kuondoka, Toisa akahisi akizubaa anaweza kupoteza nafasi, akanyanyuka na kuikimbilia ile gari,



"Vipi bro? Kwema?" Toisa alimsalimia dalali,



"kwema, nambie?" Dalali aliongea,



"Bro samahani, jana wakati unatoka pale guest, uliondoka na dada mmoja hivi, yule dada tulipakana vyumba ndani ya guest uliyomchukua jana, kuna kitu cha thamani alikiangusha, sasa naomba unipeleke alipo kama unapajua" Toisa aliongea huku akijifanya ana busara,



"Kitu gani?" Dalali aliuliza,



"Elewa ni kitu cha thamani, kama unanipeleka nipeleke, utakijua uko tukifika" Toisa aliongea na kumfanya dalali afikirie kwa muda, akaona bora ampeleke kwa kuwa kitu chenyewe kaambiwa ni cha thamani na isitoshe kwa sasa yeye dalali anamchukulia Sarah kama ndugu yake kwa namna walivyozoeana kwa muda mfupi tu.



Dalali akageuza gari na kumwambia Toisa aingie ndani, Toisa akaingia huku akijitahidi kuangaza kama atamuona Tekso lakini hakumuona, ubaya hata simu yake yeye Toisa iliisha chaji kwa hiyo ikawa ngumu hata kumtaharifu ni wapi anaelekea kwa sasa.



Dalali akaliondoa gari taratibu huku akijaribu kumshawishi Toisa amtajie ni kitu gani cha thamani alichokiokota, lakini Toisa alitia ngumu kutaja, kitu ambacho dalali hakujua ni kuwa Toisa alitumia ujanja tu ili kupelekwa alipokuwepo Sarah.



Gari ya dalali ilisimama nje ya geti la nyumba ya Sarah,



"Anakaa hapa, wewe shuka mimi naondoka kuna mtu namuwahi'" Dalali aliongea kisha Toisa akatelemka, dalali akaondoa gari na kumuacha Toisa akiwa amesimama getini.



Gari ilivyopotea machoni pa Toisa, Toisa hakutaka kuingia ndani ya geti, alichofanya alijifanya anatembea mpaka akafika upande wa nyuma wa nyumba, akaruka ukuta na kuingia ndani ya uzio, akawa anachungulia kila dirisha la chumba, hakuona mtu, ila alipofika kwenye dirisha la sebuleni, aliweza kumuona Sarah akiwa amelala kwenye sofa huku akitazama runinga, Toisa akaelekea kwenye mlango wa kuingilia na kuminya kitasa kwa taratibu, mlango ukafunguka na Toisa akatokea sebuleni,



"Leo umepatikana kirahisi" Toisa aliongea na kufanya Sarah ashtuke na kugeuka nyuma, hapo ndipo Sarah alipokutana na mdomo wa bastola ukimuangalia..........







"Sidhani kama upo sahihi kusema hivyo" Sarah aliongea huku akirudisha macho yake kwenye runinga na kumfanya Toisa ajiulize ni kipi kinachompa kiburi huyu binti?



"Mikono juu, au nakufyatua risasi" Toisa aliongea kwa sauti kubwa kidogo ila Sarah wala hakujali, badala yake Sarah alimgeukia Toisa na huku mkononi akiwa na remote,



"Unaona hii? hii ni remote ya Bomu, mtoto wa Harry yupo ndani nimemfunga bomu" Sarah aliongea kwa sauti tulivu ila iliyobeba maana ya kile alichokizungumza, Toisa kusikia hivyo kidogo akapoa, ila hakutaka kushusha bastola chini,



"Mtoto yupo wapi?" Toisa aliuliza,



"Yupo ndani kalala" Sarah alijibu,



"Sasa kalala na bomu? likimlipukia je?" Toisa aliuliza kwa mshangao,



"Haliwezi kulipuka mpaka liruhusiwe" Sarah alijibu huku akitabasamu, tabasamu alilitoa baada ya kuona tayari amemuweza Toisa,



"Kamlete, nimuone" Toisa aliongea,



"Kwanza weka bastola chini alafu uisukume kwangu kwa mguu" Sarah alimwambia Toisa ambaye alitii,



"Haya kamlete mtoto nimuone" Toisa aliongea huku akiwa amemkazia macho Sarah.



Sarah akaikota ile bastola na kuishika yeye, kisha akaangaza macho kushoto na kulia, akakiendea kiti cha mbao kilichopo pembezoni mwa ukuta na kukibeba kisha kumpa Toisa,



"Kaa hapo nikufunge kamba" Sarah aliongea kwa jeuri huku akimtazama,



"Wewe mpumbavu nini, makubaliano ni kumleta mtoto na wala sio kufungana kamba" Toisa aliongea kwa hasira, Sarah akakinyanyua kile kiti na kumpiga nacho Toisa begani, Toisa akataka apambambane,



"Ukithubutu hata kutingishika nakufumua mwili" Sarah aliongea huku akiwa ameishika ile bastola ya Toisa, ila Toisa hakutaka kuitii ile amri ya Sarah, Toisa akarusha teke Kali kumuelekea Sarah, Sarah akainama kisha akanyanyuka kwa kasi na kuushika mguu wa Toisa kabla haujafika chini, alafu akachukua bastola na kupiga risasi goti la Toisa, Toisa akatoa ukelele wa maumivu huku asiamini kile anachofanyiwa,



"Nilikwambia usithubutu kutingishika, ukapuuza" Sarah aliongea huku akimsukuma Toisa na kumuangushia kwenye kiti, na kipindi hicho mtoto wa Harry alikuwa anatoka ndani, nadhani sauti ya bastola ndio ilimshtua.



Mtoto wa Harry alipotoka ndani hakuonekana kuwa na dalili yoyote ya kufungwa bomu, Toisa akajiona mpumbavu kwa kitendo chake cha kuamini pasipo kuona,



"Aunty umemfanya nini Toi?" Mtoto wa Harry aliuliza baada ya kumuona Toisa akitoka damu gotini huku akiugulia maumivu,



"Princess kumbe unamjua huyu?" Sarah alimuuliza mtoto wa harry huku akimshika begani,



" Anko Toi, rafiki ake baba" Princess alijibu, princess ndio jina la mtoto wa Harry,



"Anko Toi ameumia, ameanguka" Sarah aliongea kirafiki na princes,



"Pole anko Toi, nenda hospital" Princess aliongea kwa huruma huku akimshika Toisa,



"Usijali princess, nitampekeka. Unataka juice au chocolate?" Sarah alimuuliza Princess,



"Oooh, chocolate" Princess alijibu kwa furaha,



"Nenda kachukua kwenye droo ya kitanda, usije huku mpaka nikuite ee?" Sarah alimwambia Princess,



"Sawa aunty" Princess alijibu huku akikimbilia chumbani na kuwaacha Toisa na Sarah.



"Sitokuumiza tena endapo utanijibu vizuri maswali nitayokuuliza" Sarah aliongea huku akimuangalia Toisa aliyekuwa ameshikilia goti lake,



"Kwenye kundi lenu mpo wangapi?" Sarah aliuliza huku akimtupia jicho Toisa, ila Toisa hakujibu,



"Unajifanya kiburi sio?" Sarah aliuliza huku akiitoa bastola yake chini ya kochi na ile bastola ya Toisa akaitupa pembeni,



"Nakuuliza kwa mara ya mwisho, mpo wangapi kundini?" Sarah aliuliza huku akifunga kiwambo cha sauti katika mdomo wa bastola ili akifyatua risasi sauti isitoke.



Toisa hakujibu tena swali hilo, Sarah akaelekeza mdomo wa bastola katika goti la pili la Toisa na kumfyatulia risasi nyingine iliyofanya Toisa apige kelele kubwa zaidi ya aliyopiga mwanzo,



"Nauliza kwa mara ya tatu, mpo wangapi?" Sarah aliuliza huku akiielekezea bastola kwenye kiwiko cha mkono wa Toisa,



"Niue tu, yanini unitese hivi" Toisa alijibu kijeuri,



"Kifo na mateso ni kipi bora?" Sarah aliuliza huku akitabasamu,



"Niue Malaya wewe, sitaki maswali" Toisa aliongea kwa ukali na kumtemea mate usoni Sarah,



"Naheshimu chaguzi yako" Sarah aliongea kisha akajifuta mate usoni kwa kiganja cha mkono, kisha akamfyatulia risasi kichwani Toisa, Toisa akafa pale pale.



Sarah akambeba Toisa mpaka katika chumba kimojawapo ndani ya nyumba yake. Chumba kilikuwa kimejaa visu, misumeno na vitu vingi vya kifundi selemala. Sarah akachukua kisu na kukikata kichwa cha Toisa, kisha akaenda kwenye kona moja iliyokuwa na friji, akakiingiza kile kichwa ndani ya friji.



Sarah akaurudia mwili wa Toisa na kuanza kuukata kata vipande vipande, kisha akaviingiza katika mifuko mikubwa mieusi miwili na kuiweka kwenye pembe ya kile chumba, baada ya hapo akarudi sebuleni na kusafisha damu iliyotapakaa pale sakafuni kisha akamuita Princess.



"Anko Toi ameenda hospitali?" Princess aliuliza baada ya kufika sebuleni,



"Ameondoka, unampenda ee?" Sarah alimuuliza huku akimuangalia,



"Ndio, ananipaga soda" Princess alijibu na kumfanya Sarah ahisi uchungu.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Atakuja baadae, atakuletea soda" Sarah aliongea kisha akambeba Princess na kumpakata.



"Atakuja na baba?" Princess aliuliza,



"Ndio, watakuja wote" Sarah alijibu,



"Alafu aunty, nataka chocolate tena" Princess aliongea,



"Kwa siku unatakiwa kule chocolate tatu tu, ukila nyingi meno yako yataoza, sawa?" Sarah alimuuliza Princess,



"Sawa aunty" Princess alijibu,



"Leo umekula ngapi?" Sarah alimuuliza Princess,



"Tatu" Princess alijibu,



"Kachukue maziwa kwenye friji, chocolate utakula kesho" Sarah alimwambia Princess kisha Princess akaelekea kwenye friji ya pale sebuleni na kutoa pakiti ya maziwa.



***************



Baada ya siku tatu ya Sarah kumteka Princess na siku mbili za kutoonekana kwa Toisa, kambi ya Taita iliingia na hofu juu ya mtu wanaetaka kupambana nae, kwa upande wa Harry alichofanya ni kutoa taharifa katika vyombo vya habari juu ya kupotea kwa binti yake, na akatangaza pesa kubwa kwa mtu yoyote atayefanikisha kupatikana kwa mtoto wake.



Siku hiyo kila gazeti lililotoka lilitoka na tangazo hilo linalohusiana na kupotea kwa mtoto wa Harry, muda huu gazeti lilishikwa na dalali wa Sarah, baada ya kuona picha ya Princess pale kwenye gazeti, dalali alishtuka kwa maana huyo mtoto anamuona kila siku yupo na Sarah kule nyumbani kwa Sarah, ila kilichomtatiza Dalali ni ile pesa iloyowekwa kwa mtu atakayefanikisha kupatikana kwa mtoto huyo, Dalali tamaa ikamuingia. Uzuri ni kwamba katika magazeti yote yaliyotolewa juu ya habari za kupotea Princess, ziliwekwa na namba za Harry.



"Kwani mama yangu yule, tumefahamiana kwa ajili ya kazi tu, acha niongee ninachokijua, pesa yote hiyo kweli niiache?" Dalali aliongea na moyo wake kisha akaachia tabasamu laini kutoka moyoni ila likapenya mpaka mdomoni na kufanya meno yake meupe yaonekane.



Dalali akajinyanyua kutoka kwenye kijiwe cha kahawa na kulifuata gari lake akaingia. Alikuwa anatafuta eneo lenye utulivu ili aweze kusikilizana na baba wa mtoto.



Dalali baada ya kuingia katika gari, alichukua simu yake na kuipiga ile namba ya Harry ila simu ya dalali ikaonesha haina salio la kutosha, akakopa mtandaoni na kupata kifurushi, kisha ukaingia ujumbe wa maneno kutoka kampuni ya simu uliomtahadharisha kukumbuka kulipa deni hilo.



Dalali akaenda kwenye kumbukumbu ya watu aliowapigia na kuikuta ile namba ya Baba wa mtoto, akapiga na simu ikaanza kuita, moyo wa dalali ukafurahi kwa hatua hiyo aliyofikia.



Simu ikapokelewa na Harry mwenyewe,



"Hallow" Harry aliongea kinyonge,



"Hallow, hali yako kaka?" Dalali alimsalimia Harry,



"Salama, naongea na nani?" Harry aliuliza,



"Mimi ni msamalia mwema, nimeona tangazo lako kwenye gazeti" Dalali aliongea,



"Eee, niambie" Harry aliongea huku akiwa na shahuku ya kutaka kujua ni kipi kitazungumzwa,



"Aisee kaka huyo mtoto nimemuona katika nyumba moja hivi anaishi na mdada" Dalali alitoa neno lililomfanya Harry ashushe pumzi, maana hakuamini kusikia kuwa mwanae bado anaishi,



"Maeneo gani?" Harry aliuliza,



"_mimi nitakupeleka, kwanza nataka unipe uhakika wa kupata pesa uliyoitangaza" Dalali aliongea na kunyamaza,



"Pesa ipo, pesa kwangu si kitu, ninachotaka ni mwanangu tu" Harry aliongea kwa jazba,



"Tufanye makubaliano kwanza, nikifika utanipa nusu, na ukimuona mwanao utamalizia iliyobaki" Dalali aliongea,



"Sawa, upo wapi nije?" Harry alimuuliza Dalali,



"Nielekeze ulipo nije kukuchukua, maana nina gari" Dalali aliongea,



"Nipo osterbay, nyumba namba 53" Harry alijibu,



"Nipe robo saa, nitakuwa hapo" Dalali alijibu kisha akakata simu, akatoa tabasamu jingine la pesa, maana aliamini muda mchache ujao atakuwa tajiri mkubwa katika ukoo wao.



Kwa upande wa Harry baada ya simu kukatwa, akamtupia jicho Taita, maana muda huo walikuwepo wote wakijadili jambo hilo na pia juu ya kupotea ghafla kwa Toisa. Simu ya dalali ilipokatwa, Taita na wenzake wakakusanya vijana wapatao kumi, ndio wakapanga wataongozana na huyo msamalia ataekuja kuwapeleka kwa huyo Dada anateishi na mtoto wa Harry.



Harry alikuwa na haraka na mchecheto wa kutaka kumuona mtoto wake, na muda huo alikuwa anahesabu kiasi cha pesa ili amkabidhi huyo msamalia mwema atakayekuja, kwake Harry pesa hakuona tamu muda huo, alimuhitaji binti yake tu.



Vijana wa Taita wakiwa getini pamoja na wakuu zao, ndipo walipoiona gari ndogo ikisimama mbele yako na dereva wa gari ile akashusha kioo, ila cha ajabu watu wote pale walikuwa wamepigwa na butwaa na kumfanya Dalali ashindwe kuelewa sababu ya watu wale kumtolea macho,



"Mkamateni mpumbavu huyu" Harry aliwaamrisha vijana wa Taita kwa hasira na kufanya Dalali achoke kabisa, akahisi amegeukwa...........



Bumbuwazi likaamia kwa dalali sasa, akawa anajiuliza kule ni kugeukwa ama ni kitu gani? Dalali akiwa bado katikati ya maswali, tayari vijana wa Taita walikuwa wameshamkamata na kumshusha kwenye gari kwa amri ya Harry.



Kipindi chote hicho Taita mwenyewe alikuwa akishangaa huku akiwa hajui ni kwanini msamalia mwema huyo anafanywa hivyo,



"Mpelekeni chumba cha mateso" Harry aliamrisha vijana,



"Mateso tena?" Dalali aliuliza huku akiwa ahamini kinachomtokea,



"Kaa kimya, hutakiwi kuongea" Harry alifoka kwa hasira,



"Lazima niongee kama naona jambo haliendi sawa" Dalali aliongea ila safari hii hakujibiwa kwa mdomo, alijibiwa na makofi kutoka kwa vijana wa Taita waliokuwa wamemshika na kumpeleka ndani, katika chumba cha mateso.



Huku nje alibaki Harry, Trigger, Taita na Tekso ambao walikuwa makini kufuatilia kile kinachofanywa na vijana wao,



"Harry sielewi ni kwanini unamfanya hivi huyu mtu ambaye ni msamalia mwema" Taita aliongea huku mshangao ukijionesha dhahiri machoni pake,



"Hii gari aliyokuja nayo ndio gari ambayo ilikuwa ikinifuatilia siku ile nilipovamiwa nyumbani kwangu" Harry aliongea na kumfanya Taita ashtuke sasa,



"Yeah, gari ndio hili hili tulilokuwa tunalifuatilia kutokana na maelekezo ya yule Dada wa guest kule" Tekso aliongea huku akitingisha kichwa chake,



"Sasa mtekaji si ni mwanamke? kwanini mnataka kumuadhibu huyo mwanaume?" Taita aliuliza swali la kipumbavu,



"Kama gari iliyotumika ni moja, basi inawezekana kabisa wanafahamiana" Tekso alitoa jibu,



"Twendeni ndani tukamuhoji" Harry aliongea huku akielekea ndani na wenzake wakamfuata, walielekea moja kwa moja mpaka ndani ya chumba cha mateso na kumkuta bwana dalali akiwa amewekwa juu ya kiti huku mikono yake ikifungwa kwa nyuma kwa kutumia kamba ngumu.



"Ndugu yangu, hatutaki kukutesa wala kukuumiza, tunachotaka ni ukweli wako tu" Harry aliongea huku akiwa amesimama mbele ya Harry,



"Ukweli upi? Kama ukweli niliouongea umenifikisha hapa na kufanywa mateka" Dalali aliongea huku akitabasamu, halikuwa tabasamu la furaha,



"Hiyo gari uliyokuja nayo ni ya nani?" Harry aliuliza,



"Ni gari yangu" Dalali alijibu,



"Unafanya kazi gani?" Tekso aliingilia kati na kuuliza,



"Mimi ni dalali, tena maarufu sana" Dalali alijibu,



"Ndiyo huyu huyu" Tekso aliongea huku akimgeukia Taita na kufanya Dalali ajiulize maswali kibao,



"Tofauti na wewe, ni nani anayeendeshaga gari yako?" Harry alimtupia swali Dalali,



"Ndio huyo Dada sasa ambaye ndio yupo na huyo mtoto wa kike mnayemtafuta" Dalali alijibu,



"Huyo Dada mna uhusihano naye gani?" Taita aliuliza,



"Mimi ndiye nilimsaidia kupata nyumba ambayo anaishi mpaka sasa, ndipo tukafahamiana mpaka leo" Dalali alitoa jibu na kufanya Harry na Trigger watazamane,



"Unaweza kutupeleka anapoishi?" Trigger aliuliza,



"Ndicho kilichonileta hapa, ila sio bure, maana tangazo lenu linasema msamalia mwema atalipwa" Dalali alijibu,



"Utalipwa" Harry alijibu,



"Sasa kulikuwa na sababu gani ya kunikamata na kunifunga?" Dalali aliuliza,



"Sababu umeshaijua, mfungueni" Trigger alijibu kisha akatoa amri iliyotekelezwa na vijana, Sasa Dalali alikuwa hana kamba tena mwilini, alikuwa huru,



"Tupeleke sasa" Harry aliongea,



"Ngojeni kwanza, ni nani nilikuwa naongea nae kwenye simu?" Dalali aliuliza huku akimtupia macho kila mmoja,



" ni mimi hapa" Harry alijibu,



"Nipe advansi kwanza kabla sijawapeleka uko, alafu mkishampata mtoto wenu mtanimalizia pesa iliyobaki" Dalali aliongea huku akimtazama Harry,



"Twende wewe, ujue tumekuheshimu sana ndio maana hatujakudhuru?" Tekso aliongea huku akimvuta Dalali kwa lengo la kumuinua kwenye kiti,



"Muache kwanza" Harry aliongea kisha akatoa pesa kwenye mifuko yake ya suruali na kumkabidhi Dalali, Dalali akaanza kuzihesabu,



"Hapo sawa, maana hii ni biashara" Dalali aliongea huku akitabasamu,



"Haya tupeleke sasa" Taita aliongea na kisha Dalali akasimama na kutangulia mbele huku wakina Taita wakimfuata kwa nyuma mpaka nje ambapo ndipo kulikuwepo na magari,



"Lete funguo ya gari lako, nitaendesha mimi na wewe utakaa pembeni utakuwa ukinielekeza" Harry aliongea huku akiwa amesimama kwenye mlango wa dereva wa gari la Dalali,



"Sawa, ni wewe tu bosi" Dalali aliongea huku akitabasamu na kumpa funguo Harry. Harry akaingia ndani ya gari na kuiwasha, ila kabla hajaondoka simu yake ilianza kuita, akaitoa mfukoni na kuangalia namba ya mpigaji, haikuwa ngeni, aliikumbuka kuwa ni ile aliyowahi kutumia mtekaji baada ya kumteka mwanae, Harry akapokea na kuweka simu sikioni huku akiwa na wasiwasi,



"Nakupa siri Harry, toka mwenyewe na uangalia kwenye injini,ya hilo gari ulilokuwepo alafu ukimaliza nitakupigia" Sauti ya kike iliongea na kukata simu, Harry akataka amshirikishe dalali ila akasita, akahisi lao moja, Harry akazima gari na kutoka na funguo, akaenda mpaka mbele ya gari na kufungua boneti, hapo ndipo alipoliona Bomu likiwa limepachikwa pembeni ya rejeta, Harry akapiga kelele huku akikimbia na kufanya wenzake wahisi kuna hatari. Dalali akabaki anashangaa huku akiwa ahisi kitu, ila alichofanya ni kufungua mlango ili atoke aulize, alipofungua tu mlango tena kabla hajashusha hata mguu, bomu likaitika, tena lililipuka kwa nguvu na kuirusha ile gari juu angani na kuitupa chini na kuiacha ikiwaka moto.



Muda huo Taita na wenzake walikuwa wamelala chini ya magari yao huku wakiushuhudia ule mchezo wa hatari uliokuwa ukifanyika mbele ya macho yao, na Harry alikuwa kwa mbali akilitazama lile tukio huku akiwa amepoteza matumaini ya kumpata binti yake.



Harry akaanza kuwasogelea wenzake huku akiliangalia lile gari likiteketea na chini alikuwepo yule bwana Dalali akiwa amelala huku akiwa hana miguu na mwili wake ulionekana hauna dalili tena za uhai.



Harry akiwa amewakaribia kabisa wakina Taita, simu yake iliita, alipoiangalia namba alikuta ni ile ya mtekaji, Harry akapokea haraka,



"Kwanini unataka kuniua?" Harry aliuliza kwa hasira baada ya kupokea simu,



"Ningetaka kukuua wala nisingekuambia uangalie kwenye injini, ningelipua tu bomu na ungekufa" Sarah aliongea kisha akacheka,



"Na kwanini hukutaka nife?" Harry aliuliza huku akishangaa jibu la huyo mwanadada,



"Najua hupendi kufa, ila sikutaka ufe kwa sababu nataka nikuumize kihisia, kisaikolojia na kimwili mpaka utakapoona ni bora ufe, hapo ndipo nitakuua" Sarah alijibu katika sauti tulivu na kumfanya Harry jasho limtoke,



"Hivi wewe ni nani na unatutaka nini sisi?" Harry aliuliza kwa upole,



"Mtanijua wakati ukifika, na siku ambayo mtanijua, ndiyo hiyo siku nitaanza kuwaua nyie viongozi wa kakikundi chenu cha kishenzi, acha nidili na vibaraka kwa sasa" Sarah alijibu,



"Nikupe nini ili umuache mwanangu?" Harry aliuliza,



"Sitaki chochote, mwanao nitamrudisha kesho, kesho jioni" Sarah alijibu,



"Nakuomba ufanye hivyo" Harry aliongea,



"Nipe niongee na Taita, namuona yupo upande wako wa kushoto" Sarah aliongea na kufanya Harry ageuke huku akiamini Sarah yupo eneo hilo, Harry akampa simu Taita kisha Harry akamfuata Tekso na kumnong'oneza afanye kitu katika mtandao ili wajue Sarah yupo upande gani? Tekso akatoa simu yake kisha akabonyeza bonyeza na hapo ile sauti ya Sarah ikawa inasikika ndani ya simu mbili, yaani simu ya Harry ambayo alikuwa anaongea nayo Taita, na simu ya pili ni simu ya Tekso.



"Taita, Taita, vijana wako waambie mimi sio mtu wa kawaida, wajiangalie namna ya kunifuata, vinginevyo nitawamaliza wote" Sarah aliongea kisha akaweka kituo,



"Mbona hakuna kijana wangu anaekufuatilia" Taita aliongea huku akiwa hajiamini,



"Toisa nipo nae hapa, au sio kijana wako huyu?" Sarah aliuliza,



"Sina mtu anaeitwa hilo jina" Taita alijifanya hamjui kijana wake,



"Sawa, nitamleta kesho pamoja na mtoto wa Harry, ili umkane akiwa anakusikia. Nawatakia majukumu mema, tchao" Sarah aliongea kisha akakata simu.



Kipindi hicho ambacho Sarah alikuwa akiongea na Taita, tayari Tekso akiwa na vijana wawili walikuwa wanafuatilia eneo ambao mpiga simu huyo alionekana kuwepo, kwa maelezo ya simu ya Tekso yalionesha mpigaji yupo mtaa huo huo, na hata Sarah alipokata simu bado simu ya Tekso iliendelea kusoma alipo mpigaji.



Tekso na wenzake walitembea mpaka katika nyumba moja iliyopo mtaa huo huo na kusimama getini, wakaanza kugonga, ila hawakujibiwa, wakaamua waruke ukuta na kuingia ndani. Bado simu ya Tekso ilikuwa ikaendelea kuonesha na muda huu iliekekeza mpigaji yupo kwenye kajumba cha pembeni yao, baada ya kukachunguza kale kajumba waligundua ni choo cha nje, wakajipanga mlangoni na kuvamia kwa fujo, hawajakuta mtu isipokuwa simu tu iliyokuwa juu ya sinki la choo,



"Aaaagh shit, ichukue hiyo line" Tekso aliongea kwa hasira na kutoka zake nje na kumuacha kijana wake mmoja akiokota mfuko wa nylon na kuuvaa ili aichukue ile simu.



***************



Kitu ambacho Sarah alikifanya ni kufunga vinasa sauti kila sehemu ya gari la Dalali, na pia hata lile bomu aliliweka siku nyingi huku akiamini ni lazima ipo siku lile gari linaweza kumuweka hatiani, ila hakujua kuwa yule Dalali pia anaweza kumuingiza matatizoni.



Na hata Dalali alipowasiliana na Harry, Sarah alisikia kila kitu, alichofanya ni kusogea tu eneo ambalo Harry alimuelekeza Dalali ajongee. Sarah alipofika aliingia kwenye nyumba ya tano kutoka nyumba ya Taita na kuanza kufuatilia namna Taita na wenzake wanavyojipanga kwa ajili ya kwenda kumvamia yeye Sarah.



Sarah alichofanya ni kuilipua ile gari ya Dalali huku Dalali akiwa ndani kwa maana aliamini mtu mwenye ramani ya kuwafikisha maadui kwake ni dalali peke yake, pia alifanya hivyo kwa maana aliona dalali hakuwa mtu mwema tena kwake, Sarah aliiamini sana ile misemo ya "dawa ya ubaya ni ubaya na dawa ya moto, ni moto".



Baada ya hiyo, Sarah akaiweka simu chooni na kuondoka zake baada ya kugundua kuna vijana wa Taita wanamfuata eneo lile.



************



Siku iliyofuata ambayo ndio Sarah aliahidi kumrudisha mtoto wa Harry.



Mida ya saa kumi jioni mlinzi wa Taita aliingia sebuleni huku akiwa amebeba mabox mawili, moja kubwa na jingine dogo, na yote yalikuwa yamefungwa na karatasi za kuwakawaka au karatasi za zawadi "gift paper". Sebuleni walikuwepo wote, walikuwa wanasubiri kupigiwa simu na Sarah, maana waliamini hivyo kwa kuwa Sarah aliwaahidi kuwapelekea mtoto wao.



"Zimetoka wapi?" Taita aliuliza kwa uoga huku akiwa hajiamini kabisa,



"Zimeletwa na gari za airport, zile zinazoletaga bahasha mizigo kutoka kwa Vin" Mlinzi alijibu,



"Aah sawa" Taita alijibu kisha akabeba box moja lile kubwa na kuiondoa ile karatasi ya Zawadi,



"Box zito hilo, sijui vin amenitumia nini?" Taita aliongea kisha akakichomoa kikaratasi kidogo kilicho na maneno kilichokuwa juu ya box, kilikuwa kimeandikwa. "Kubwa ni lako, na dogo ni la Harry"



Baada ya kusoma hivyo, Taita akatabasamu,



"Leo Vin amekukumbuka" Taita aliongea huku akimpa kile kikaratasi Harry aliyekuwa na mawazo, Harry akakisoma kisha lile box dogo akalivutia kwake,



"Fungua tuone zawadi" Trigger alimtania Harry huku akicheka ila Harry wala hakujisumbua kutaka kufungua lile box.



Mzee mzima Taita alikuwa akiendelea kupasua lile box, na sasa ilifika hatua moja tu ya kulifungua ili ajue zawadi iliyomo, macho ya watu wote yalikuwa ndani ya ilo box, Taita akalifungua, wote wakashtuka baada ya kukuta kichwa cha mtu, tena Taita aliruka kidogo adondoke,



"Kitoe" Taita alimwambia Trigger huku Taita akiwa amesimama mbali kabisa, Trigger akakitoa kile kichwa, hapo ndipo wate walipigwa na mshangao, kilikuwa kichwa cha Toisa, kilitisha kwa kweli na puani kiliwekewa karatasi iliyokuwa na maneno yaliyoandikwa "ndio haki ya mwenye dhambi, kila damu yenye dhambi itaigharimu familia yake. Mchuma janga hula na ndugu zake"



Hayo maneno na kilichomo ndani ya box lile kubwa kilimtisha sana Harry pamoja na wengine.



Harry akaamini sasa lile box dogo litakuwa na kichwa cha mwanae. Harry akalifungua kwa pupa na kukuta karatasi iliyoandikwa "leo ni siku ya kukumbukwa katika familia yako, hii Zawadi haijatoka kwa Vin, ni zangu mimi mtu mbaya kabisa"



Baada ya Harry kusoma maneno hayo, nguvu zikaanza kumuishia na kushindwa kufungua box, Trigger akaliendea box na kulifungua, Harry akashindwa hata kuangalia, machozi yalikuwa yakimtoka huku Trigger aliyekuwa jirani na box akibaki na mshangao.............





Mshangao aliokuwa nao Trigger ulikuwa mkubwa sana, akawageukia wenzake na kuwakuta nao wakimtazama yeye kwa maana wao walikuwa mbali huku wakitegemea kuwa na lile box dogo litakuwa na kichwa cha mtu, tena kichwa cha Princess ambaye ni mtoto wa Harry.



Trigger akarudisha macho kwenye box na kuingiza mkono kisha akalichana zaidi lile box na kilichopo ndani kikaonekana, ilikuwa ni keki iliyokuwa na neno "HAPPY BIRTHDAY PRINCESS HARRY", hapo Harry akasogea jirani na Trigger kisha akatabasamu peke yake, alikumbuka kuwa ni kweli hiyo tarehe ya leo ni siku ya kuzaliwa binti yake huyo.



Harry alitabasamu lakini hakuwa na furaha, kwa maana hakuwa na uhakika na uhai wa mwanae ingawa alipewa hiyo keki na mtekaji kama Zawadi ya mwanae, Harry akiwa amesimama tu huku akiwa hajui afanye nini, simu yake ilianza kuita, alipoitazama alikuta ni namba ya mtekaji, tena ile ile ya kila siku, Harry akaipokea simu kwa pupa,



"Pole kwa presha mwanasheria, chukua hiyo keki ipeleke nyumbani kwako, utamkuta mwanao" Sarah aliongea kisha akakata simu na kumuacha Harry akiitazama simu yake, Harry akaamua ampigie mke wake ili amuulize kama kweli Princess amerudishwa, lakini simu ya mke wake ikawa haipatikani,.



"Vipi kuna usalama?" Taita alimuuliza Harry,



"Sijajua bado, ila mtekaji amenipigia simu na kuniambia mtoto mmempeleka nyumbani" Harry alijibu Taita,



"Mpigie mkeo umuulize" Taita alimwambia Harry,



"Simu yake haipo hewani" Harry alijibu,



"Basi twende kwako" Taita alimshauri Harry,



"Sawa twende" Harry aliongea huku akitangulia kutoka nje na Taita akimfuata kwa nyuma, walipofika nje wakaingia ndani ya gari na kuliondoa.



*******************



Sarah alikuwa ndani ya bajaj huku akiwa amempakata Princess. Bajaj ilipofika katika mtaa anaoishi Harry, nyumba ya tano kutoka nyumba ya Harry, Sarah aliiamuru bajaj isimame, kisha Sarah akatelemka na kumlipa pesa yake dereva bajaj, kisha bajaj ikaondoka,



"Unapajua nyumbani?" Sarah alimuuliza Princess,



"Ndio, palee" Princess alijibu huku akionesha kwa kidole nyumba yao,



"Haya nenda" Sarah alimwambia Princess,



"Twende wote aunty, unataka kunitoroka" Princess aliongea huku akiwa amemshika mkono Sarah,



"Tangulia Princess, ngoja nikanunue chocolate" Sarah aliendelea kumbembeleza Princess,



"Sitaki aunty, unataka kuniacha" Princess aliendelea kumshika Sarah huku akilia,



"Shika hii, ipeleke ndani alafu urudi ili tuondoke wote tukanunue chocolate" Sarah aliongea huku akiivua saa yake na kumpa Princess,



"Sitaki aunty" Princess aligoma, tayari alimpenda Sarah kwa namna alivyoishi nae vizuri,



"Shhhhhh.....si unajua sipendi mtoto mkorofi? Nenda ndani kwanza" Sarah aliongea kwa ukali na kumfanya Princess akubali kuondoka ila kwa shingo upande, Sarah alisimama huku akimuangalia Princess aliyekuwa anatembea huku kila muda akigeuka nyuma kuangalia kama Sarah bado yupo. Princess alivyoingia tu ndani ya geti, Sarah akageuka na kuanza kuondoka taratibu na muda huo alikuwa anapishana na gari aliyokuwepo Harry na Taita, Sarah aliwaona akatabasamu peke yake ingawa wanaume hao hawakuweza kumgundua Sarah kutokana mavazi aliyovaa, alivaa dela pana na kichwani alijifunga ushungi huku macho yake yakiwa yamefunikwa na miwani pana za kisasa.



Harry alipofika getini alishuka taratibu huku akiwa hana uhakika kama kweli mtoto wake amerudishwa. Harry alipofika getini ili asukume mlango, alishangaa kuona mlango ukifunguka, ulifunguliwa na mke wake ambaye nae alikuwa anatoka mbio huku akiwa amemshika mkono Princess,



"Yupo wapi?" Mke wa Harry alimuuliza Princess,



"Aunty alikuwepo pale, atakuwa ameenda dukani kununua chocolate" Princess alijibu huku akionesha kwa kidole eneo ambalo alikuwa amesimama Sarah hapo hawali,



"Nani, eti Princess?" Harry aliuliza kwa wasiwasi huku akimbeba mwanae,



"Anadai amekuja na aunty yake, ndio nataka anioneshe yupo wapi huyo aunty yake?" Mke wa Harry alijibu,



"Twendeni ndani" Harry aliongea huku akisukumia mkewe ndani, nae akaingia huku Taita akija kwa nyuma.



Safari yao iliishia sebuleni kwa Harry,



"Princess amekuja muda gani?" Harry aliuliza,



"Sawa hivi yaani, hana hata dakika tatu" Mke wa Harry alijibu,



"Toto hujaumizwa?" Harry alimuuliza mtoto wake huku akimgeuza geuza,



"Sijaumia" Princess alijibu,



"Ulikuwa wapi?" Harry alimuuliza,



"Kwa aunty" Princess alijibu,



"Wapi?" Harry aliuliza tena,



"Kwenye nyumba yake, kuna chocolate na maziwa, anko Toisa anapajua" Princess alijibu na kufanya Taita amtazame Harry,



"Anko Toisa ulimuona kumbe?" Harry aliuliza,



"Alikuja alafu akaondoka kuniambia, alinitotoka" Princess alijibu,



"Acha maswali na wewe, twende tukatoe taharifa polisi" Mke wa Harry aliongea, kisha Harry akaondoka na mke wake na wakaelekea kituoni kutoa taharifa.



Taita alirudi moja kwa moja kwake na kukuta vijana wake wakiwa wamesimama tu wakikiangalia kichwa cha Toisa,



"Trigger na wewe umekuaje siku hizi, yaani umekosa maarifa ya kukifanya hiki kichwa?" Taita aliuliza kwa ukali,



"Tumeshakubaliana kuwa tutakizika na shimo tumeshachimba, ila sasa tulikuwa tunakusubiri ili tuone kama una wazo tofauti na letu" Trigger alijitetea,



"Kazikeni tu, tena kwa uangalifu sana" Taita aliongea huku akielekea chumbani kwake,



"Alafu kuna ujumbe mwingine chini ya box" Trigger aliongea na kumfanya Taita asimame,.



"Umeandikwaje?" Taita aliuliza,



"Mungu naomba nikiwa mkubwa niwe nawaka kama moto" Trigger alisoma ujumbe ulivyosomeka na kumfanya Taita afikirie kidogo kwa muda,



"Hayo maneno kama nayajua, sijui nimewahi kuyaona wapi?" Taita alijiuliza mwenyewe,



"Sio kwenye biblia?" Trigger aliuliza,



"huenda" Taita alijibu na kuupuuza na kuingia zake ndani na kuwaacha vijana wake wakikibeba kichwa cha Toisa na kuelekea nacho nyuma ya nyumba.



******************



Jumapili moja tulivu, Sarah alielekea makaburini kule walipozikwa baba na mama yake, akaenda moja kwa moja na kupiga magoti katikati ya makaburi, akafunga macho,



"Sidhani kama ninachokifanya kinaudhi, naimani mnakifurahia kwa maana sifanyi kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu. Kazi niliyoianza sio rahisi, ni ngumu sana na inahitaji utulivu wa mwili na akili. Nimeficha sana wajihi wangu kwa maadui, sasa nadhani nahitaji kujionesha, nahitaji wanijue ili wajue kwanini nafanya hivi" Sarah aliongea kwa mtindo wa sala kisha akafungua macho yake na kuvitoa vikaratasi viwili vyenye maneno na kuvibandika juu ya makaburi ya wazazi wake.



Sarah alipotoka hapo alielekea kanisani, lile kanisa ambalo alitoa Sarah ambayo ilifanya watu wote waangue kicheko. Sarah akaomba aonane na askofu mkuu wa kabisa, akaelekezwa ofisi ilipo na kuingia,



"Naitwa Sarah, mimi ndiye niliyeomba ile sala iliyobandikwa pale mbele katika kabisa, nilifanya hivyo miaka kumi na Tisa iliyopita" Sarah aliongea na kufanya askofu ashangae,



"Ulikuwa Wapi muda wote? tulikutafuta sana kwa maana walitokea watu waliovutiwa na kile ulichokiomba na wengi walikuwa wanataka kukudhamini, ni raia wa nje" Askofu alimuuliza Sarah,



"Nilikuwa uingereza, nimerudi kutimiza ile Sarah" Sarah aliongea na kumfanya Askofu amshangae,



"Kivipi? kwa hiyo sasa hivi unawaka kama moto?" Askofu aliuliza,



"Ndio, naweza kumuunguza yoyote" Sarah aliongea kisha akacheka ili kufanya maongezi yake yawe kama utani,



"Karibu Sarah, umetuletea kutoka uingereza?" Askofu aliuliza,



"Sijaleta kitu kwa kweli, ila nitawafanyia kitu kabla sijarudi uingereza" Sarah aliongea,



"Ooh kumbe sio mkaaji tena nchini, unasoma uko?" Askofu aliuliza,



"Hapana, ni mfanyakazi wa serikali ya uingereza" Sarah alijibu,



"Hongera sana Sarah, itabidi nikakutambulishe kwa maana sala yako bado maarufu mpaka leo" Askofu aliongea,



"Sawa" Sarah alijibu huku akitabasamu.



Askofu alimchukua Sarah na kuongozana nae mpaka ndani ya kanisa, uzuri walikuta misa ya kwanza ikielekea ukingoni na pale ulikuwa muda wa kusoma matangazo.



Askofu akaenda mpaka kwa padri aliyekuwa anaongoza misa na kuongea nae kidogo kisha wakakaa kimya wakimsubiri mtoa matangazo amalize.



Baada ya muda yule bwana aliyekuwa anatoa matangazo alikuwa amemaliza na sasa askofu akachukua kipaza sauti, kisha akawasalimu waumini waliohudhuria ibada, baada ya hapo akairudia ile sala iliyowahi kuombwa na Sarah miaka mingi iliyopita, wakati akiirudia ile sala, Taita alishtuka, tena uzuri alikuwa amekaa kiti cha mbele kabisa pamoja na Harry ambaye nae alipata mshtuko,



Masikio na mwili wa Taita vikapata ubaridi kwa pamoja wakati askofu akiirudia ile sala, Taita akakumbuka na ule ujumbe aliouona kwenye box upande wa chini, box ambalo kiliwekwa kichwa cha Toisa, ila bado Taita alisubiri kusikia ni kipi askofu ataongea baada ya kuirudia sala ile,



"Sasa baada ya kuirudia sala hii iliyowahi kuombwa na mtoto mdogo miaka kumi na Tisa iliyopita, leo hii huyu mtoto yupo hapa, namuomba asogee mbele" Askofu aliongea kisha Sarah akawa anajongea mbele huku waumini wakimpigia makofi. Sarah alipofika mbele akapewa kipaza sauti,



"Naitwa Sarah, Sarah Isack" Sarah aliongea kisha akatupia macho mahali walipokaa Taita na Harry na kuwaona namna walivyopata mshtuko, tena sio kidogo........





Sarah akatabasamu, halikuwa tabasamu alilolipanga, lilikuwa ni tabasamu lililokuja ghafla baada ya kuwaona maadui zake walivyopata mshtuko baada ya yeye Sarah kujitambulisha.



"Mimi ndiye yule mtoto niliyetoa sala miaka kumi na tisa iliyopita, na niliitoa nikiwa na maanisha kile nilichokiomba, sikuwa nasali tu ili mradi maneno yanitoke, nilitaka niwe mkubwa na niwe moto, tena moto kweli, nashukuru nimekuwa hivyo" Sarah aliongea na kufanya baadhi ya waamini wabaki na maswali, sio hao tu, mpaka askofu mwenyewe sura yake ilionesha ana swali,



"Umekuaje moto sasa?" Askofu alijikuta anauliza bila kutegemea,



"Na ninaposema nimekuwa moto simaanishi nawaka, hapana, maana yangu ni ule uwezo niliokuwa nao wa kushinda kila kikwazo kilichopo mbele yangu, na nadhani hiyo yote ni kutokana na Mungu kusimamia kila nifanyacho. Nawashukuru sana, maana mimi ni muongeaji sana, mnaweza shangaa naongea tu mpaka nachukua muda wa misa zote" Sarah alitania kisha waumini wakacheka, Sarah akarudisha kipaza sauti kwa askofu.



"Pia napenda kuwaambia habari njema kuhusu Sarah, Sarah ametoa ahadi ya kutoa mifuko mia moja ya cement kwa ajili ya kabisa" Askofu aliongea na waumini wakalipuka kwa furaha na huku wengine wakipiga makofi na vigele gele.



"Basi nadhani tutegemee kumuona hapa sarah mara kwa mara kwa maana amekuzwa na imani yetu" Askofu aliongea kisha akaweka kipaza sauti sehemu husika, kisha wakaongea kidogo na Sarah na baada ya hapo Sarah akawapa mikono mapadri na watumishi waliokuwepo mbele ya kanisa, kisha Sarah na askofu wakaanza kutoka kuelekea nje ya kanisa.



Walipokuwa wanatoka ndipo Sarah akayapeleka macho yake sehemu alipokuwa amekaa Taita, wakagongana macho, Sarah akatabasamu kisha akambinyia jicho Taita ambaye muda wote alikuwa amekamatwa na mshangao.



Sarah alitoka moja kwa moja mpaka ofisini kwa askofu,



"Sina muda tena was kukaa hapa, labda unisaidie tu namba ya account ya benk ambayo inatumiwa na kanisa" Sarah aliongea huku akimtupia jicho askofu ambaye alikuwa ameshika pen na akachukua karatasi akaandika namba ambayo Sarah anaihitaji,



"Mbona haraka hivyo" Askofu alimuuliza huku akimpatia ile karatasi,



"Kawaida, nitarudi siku chache zijazo baba askofu, ila pesa nitaiingiza kesho mapema kwenye account ya kanisa, kwa maana leo jumapili benki zimefungwa" Sarah aliongea huku akinyanyuka katika kiti,



"Sawa haina shida" askofu aliongea huku akipeana mkono na Sarah, kisha Sarah akaondoka zake.



Sarah alipotoka kwenye mlango was askofu, alipiga hatua za haraka haraka mpaka nje ya uzio wa kanisa na kwenda kuingia kwenye bajaj ambayo ndiyo ilimleta eneo lile la kanisa,



"Subiri kidogo, kuna mtu namsubiri" Sarah alimwambia dereva bajaj ambaye alitaka aiwashe bajaj yake,



"Sawa bosi" dereva bajaj alijibu na kutulia.



Baada ya dakika chache waumini walianza kutoka katika jengo la ibada kumaanisha kwamba misa imeisha, hapo ndipo Sarah aliweza kumuona Taita na Harry wakitoka, akashuhudia namna wanavyoangaza angaza macho wakiashiria kuwa kuna kitu wanatafuta.



Baada ya muda aliwashuhudia wakiongozana kuelekea ofisi ya askofu, Sarah akatabasamu peke yake,



"Haya washa bajaj tuondoke" Sarah alimwambia dereva Bajaj ambaye alitii na kuiwasha bajaj kisha wakaondoka taratibu na kupotea eneo lile la kanisa.



********************



Taita na Harry walielekea moja kwa moja mpaka mlangoni kwa askofu na kubisha hodi, askofu akaitikia na kisha wakaingia ndani, wakamsalimia askofu na kujikaribisha wenyewe kwenye viti,



"Samahani kwa kukuingilia" Taita aliongea huku akitabasamu,



"Bila samahani" Askofu alijibu,



"Nilikuwa nahitaji kuonana na yule binti, Sarah" Taita aliongea huku akimtazama askofu,



"Una maongezi nae labda, au kuna chochote?" Askofu alimuuliza Taita,



"Yule ni mtoto wa marehemu Dada yangu, baada ya Dada yangu kufariki miaka kumi na Tisa iliyopita, Sarah aliondoka na kwenda kusoma uingereza, sijawahi kubahatika kumuona tena mpaka leo" Taita aliongea,



"Kwa hiyo anakuita Mjomba?" Askofu alimuuliza,



"Ndio" Taita alijibu,



"Sawa, ila kwa bahati mbaya huyo Sarah ameshaondoka" Askofu alitoa jibu lililofanya Harry na Taita watazamane,



"Ameondoka muda mrefu?" Harry aliuliza,



"Sasa hivi tu" Askofu alijibu,

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"OK, basi nisaidie namba yake ya simu" Taita aliongea huku akiitoa simu yake mfukoni,



"Bahati mbaya ameniambia kuwa hana simu" Askofu alitoa jibu jingine lenye ukakasi,



"Dah, hajasema hata eneo analoishi?" Taita aliuliza tena,



"Hapana, ila kama shida yako ni kuonana nae tu, mtaonana, maana atakuwa anakuja hapa mara kwa mara" Askofu akajibu,



"Sawa askofu, akirudi basi naomba unifahamishe, maana ni mtu muhimu sana kwangu" Taita aliongea,



"Sawa"'Askofu alijibu kisha Taita na Harry wakaondoka zao na kumuacha Askofu akiendelea na mambo yake.



Taita na Harry walielekea moja kwa moja kwenye gari walilokuja nalo na kumkuta Trigger akiwa anawasubiri ndani ya gari,



"Mbona ibada imeisha muda tu, alafu ninyi mnatoka sasa hivi?" Trigger aliwauliza huku akiwasha gari,



"Trigger moto umewaka sasa, ni jinsi gani tutauzima?" Taita aliuliza huku akijifuta jasho. ila swali alilouliza ni kwamba Trigger hakulielewa,



"Moto umewaka wapi?" Trigger aliuliza huku akimtupia jicho bosi wake huyo,



"Kumbe matukio yote tunayofanyiwa na mtu asiyejulikana, kumbe mtu huyo ni Sarah" Taita aliongea huku macho yakiwa mbele,



"Sarah kale kabinti ka kipindi kile, Dada ake vin?" Trigger aliuliza kwa mshangao,



"Ndio huyo huyo" Taita alijibu kinyonge,



"Yaani kale katoto ndio kamekuwa hatari hivyo?" Trigger aliuliza huku akitoa tabasamu lililoambatana na mshangao,



"Nadhani amekuja kulipa kisasi, sasa basi umakini uongezeke, jambo zuri ni kwamba tumeshamjua adui yetu" Taita aliongea,



"Jioni itabidi tuitishe kikao, lazima tujadili hili jambo" Harry aliongea,



"Ni kweli" Taita alijibu wakati gari ikiingizwa ndani ya uzio wa nyumba yake.



**"****************



Sarah alielekea moja kwa moja mpaka katika sehemu ambapo yanauzwa magari, akaingia ndani na kuwasalimia wahusika,



"Nimekuja kuangalia magari" Sarah aliongea baada ya salamu,



"Karibu, twende upande ule" Kijana aliyekuwa muuzaji aliongea huku akinyooshea kidole upande ambao anatakiwa aende.



Wakaelekea mpaka katika huo upande ambao kulikuwa na gari ndogo nyingi, Sarah akaanza kutafuta gari ambayo alihisi itamfaa. Baada ya dakika ishirini alisimama mbele ya gari ambayo ilionekana ameipenda, ilikuwa ni range rover sports, nyeusi.



"Bei gani hii" Sarah aliuliza huku akiikagua tairi zake, muuzaji akamtajia bei,



"Mnapokea cash au cheque?" Sarah akauliza,



"Tunapokea vyote, ila cash nadhani ndio haina mlolongo mrefu, ukishakabidhi tu unapatiwa gari, ila cheque ukikabidhi hupatiwi gari mpaka benki itoe uhakiki kuwa ni kweli account yako ina fedha hizo" Kijana muuzaji alitoa ufafanuzi,



"Sawa, nitatoa cash" Sarah aliongea huku akitabasamu,



"Ikague kwanza vizuri gari yako, alafu twende ofisini tukakabidhiane pesa" Kijana muuza magari aliongea huku akifungua mlango was ile gari na kisha Sarah akaanza kuikagua upande wa ndani, alipojiridhisha, walienda ofisini na kukabidhiana pesa, kisha Sarah akatoka na gari yake.



*****************



Mida ya saa kumi jioni, Taita na vijana wake walikuwa Vin hotel wakiendelea na kikao kizito kumuhusu Sarah,



"sasa mnaona kipi kifanyike kumdhiti au kummaliza kabisa Sarah?"Taita aliuliza,



"yaani suala la kumdhiti au kummaliza yote hayawezekani, kwa maana yeye anatujua vizuri sisi kuliko sisi tunavyomjua yeye" Tekso alijibu katika sauti ya utulivu,



"nadhani kumdhibiti tunaweza" Trigger aliongea kisha akachukua glass ya maji na kuipeleka kinywani na wenzake wakawa wanangojea kumsikiliza,



"tunamdhibiti vipi sasa?"Harry aliuliza baada ya kumuona Trigger yupo kimya ingali amemaliza kunywa maji,



"babu yake Sarah si yupo? nadhani tunatakiwa tumteke, alafu Sarah ni lazima ajue tu, akishajua ni lazima atatutafuta" Trigger aliongea na wenzake wakampigia makofi,



"hiyo ifanyike lini? " Taita aliuliza huku akitabasamu,



" leo hii, maana tukichelewa yule demu anaweza kutuzidi akili " Trigger alijibu,



"safi, nadhani muda huu Trigger chukua vijana na muende mkafanye hichi tulichopanga" Taita aliongea huku akimtazama Trigger.



********************



Mishale ya saa mbili usiku Sarah alikuwa yupo juu ya sofa ndani ya sebule yake akicheza game, play station, alikuwa akicheza game ya kivita, kitu ambacho hakukijua ni kuwa muda huo Trigger na vijana wake walikuwa wameizunguka nyumba ya babu yake.



Trigger baada ya kuizunguka nyumba ile na kujiridhisha hakuna kitu chochote cha kuwazuia, aliwahamrisha vijana wake na kuusogelea mlango, walipoufikia waligonga hodi, mlango ukafunguliwa na babu yake Sarah, ila cha ajabu alikutana na mdomo wa bunduki,



"eh!!! Shusha bunduki wewe" Babu Sarah alijikuta akitamka hayo maneno Bila kutegemea,



"Trigger akikunyooshea bunduki uwa haishushi chini mpaka risasi itoke" Trigger aliongea huku akitabasamu kisha akafyatua risasi kumuelekea babu yake Sarah................



Risasi ilitoka moja kwa moja na kutua kwenye bega la kulia la babu yake Sarah, wenzake na Trigger wote wakapata mshtuko kwa maana hawakuambiwa wamdhuru yule mzee,



"umefanya kosa mkuu, hakutakiwa apigwe risasi huyu mzee" Strategic aliongea kwa upole,



"kosa sio langu, ni sheria tu nilizojiwekea ndio zimefanya nimpige huyu mzee" Trigger aliongea huku akimtazama babu yake Sarah aliyekuwa amelala sakafuni huku akiwa amepoteza fahamu,



"sheria gani hizo mkuu?" Strategic aliuliza huku akitabasamu,



"Trigger akikuelekezea bastola uwa haishushi mpaka itoe risasi" Trigger alijibu na kipindi hicho baba yake mdogo Sarah alikuwa akijongea sebuleni baada ya kusikia kelele za watu, alipotokezea tu sebuleni alikutana na mdomo wa bastola, ila hakunyooshewa na Trigger, alinyooshewa na Tekso,



"hatutaki kelele, Kaa chini" Tekso aliongea na kumfanya baba yake mdogo Sarah atii amri, ila alipotupa macho kwa mbele alimuona baba yake akiwa amelala sakafuni huku damu zikiwa zimetapakaa, Baba yake mdogo Sarah akanyanyuka na kukimbilia eneo alilokuwa amelala baba yake, alimpomfikia alimgeuza na kumuangalia kwa umakini huku akimuita baba yake,



"mmemfanyaje baba yangu" Baba yake mdogo Sarah aliuliza huku akinyanyuka kwa hasira, hakujali midomo ya bastola iliyokuwa inamuangalia,



"tulia hapo hapo, endapo utapiga hatua nyingine itakuwa umejitakia mwenyewe kifo" Trigger aliongea huku akiichomoa bastola yake iliyokuwa kiunoni, lakini baba yake mdogo Sarah hakuonekana kujali hilo onyo, alizidi kumsogelea Trigger, Tekso kuona hivyo, akapiga hatua moja ya haraka na kwa kutumia kitako cha bastola yake alimpiga kisogoni baba yake mdogo Sarah na kuanguka palepale, akapoteza fahamu.



Tekso alifanya hivyo kuhofia huenda Trigger anaweza kumnyooshea mdomo wa bastola baba yake mdogo Sarah na mwisho akamuua.



"mbebeni huyo mzee na mumpeleke nje kwenye gari" Tekso aliongea kwa ukali na kufanya vijana wamchukue babu yake Sarah na kumpeleka nje kwenye gari.



"na huyu tunamfanyaje" Strategic aliuliza huku akimuangalia baba yake mdogo Sarah aliyekuwa amelala chini,



"nae aingizwe ndani ya gari" Trigger alijibu huku akiipachika kiunoni bastola yake, vijana wakaubeba mwili wa baba yake mdogo Sarah na kuupeleka nje.



"tuikague nyumba kabla hatujaondoka" Strategic alitoa ushauri,



"hamna haja ya kukagua nyumba, wote tutoke nje" Trigger aliongea huku akielekea nje na kufanya wenzie wabaki wakitazamana na walionekana hawajamuelewa mkuu wao huyo,



"ebu tukague bwana, huenda huyo Sarah yupo humu" Tekso aliongea huku akianza kupiga hatua kuelekea vyumbani, ila ghafla alishuhudia moto mkubwa ukiwaka kupitia dirishani, akashtuka,



"tutokeni, kuna moto nje" Tekso aliongea huku akianza kupiga hatua kuelekea nje, wenzake wakamfuata na wote wakatoka nje na kumkuta Trigger akiwa ameshikilia kibiriti na pembeni yake kulikuwa na dumu la petrol,



"mnapoambiwa tokeni, muwe mnaelewa" Trigger aliongea kisha akawasha kibiriti na kukitupia mlangoni, moto ukashika zaidi na kuwaka kwa kasi na kufanya wenzake wazidi kushangaa,



"sasa mkuu ndani kama kuna watu wengine?" Strategic alimuuliza Trigger kinyonge,



"kawaokoe" Trigger alijibu huku akiingia ndani ya gari na kuliwasha,



"twendeni" Trigger aliongea huku akiwatizama wenzake hao, wakapanda kwenye gari na Trigger akaliondoa kwa kasi.



***************



Sarah wakati akiendelea kutazama runinga aliona kuna habari iliyokuwa ikirushwa muda huo, ni habari za papo kwa papo, ni habari iliyokuwa ikionesha nyumba ikiwaka moto na haikujulikana kama kuna watu ndani ya nyumba au lah, Sarah hakuitilia maanani sana ile habari, aliichukulia ni habari ya kawaida tu, akazima runinga na kuelekea chumbani kwake Kulala, ila alijihisi yupo tofauti sana usiku huo, alihisi kama ana hofu au wasiwasi fulani, akachukua simu yake na kuingia mtandaoni, akakuta habari inayozungumziwa ni ile ile ya nyumba kuungua, hakuona habari mpya, akaipuuza kisha akazima simu yake na Kulala.



*****************



Sarah aliamka asubuhi na kufanya mazoezi ya viungo, kisha akaelekea bafuni kujiswafi mwili, baada ya hapo akaenda jikoni na kutengeneza kifungua kinywa, alipomaliza alienda sebuleni na kuwasha runinga, akakuta habari ile ile ya nyumba kuungua, ikabidi ategee masikio ili kuisikiliza vyema ile habari, sasa hapo ndipo alichanganyikiwa, Sarah aligundua nyumba iliyoungua ni ya babu yake, ingawa habari ilieleza chanzo cha moto hakijajulikana, ila Sarah alihisi huenda ni kazi ya Taita, na alihisi Taita amefanya vile ili kumkomoa.



Sasa kwa mara ya Kwanza Sarah alihisi kuchanganyikiwa, aliona amefanya uzembe mkubwa sana kwa kujitambulisha kwa adui zake bila kuweka ulinzi kwa ndugu zake. Hata chai haikunyweka asubuhi hiyo, akataka aende eneo la tukio ila akaona itakuwa hatari zaidi, akahisi huenda vijana wa Taita watakuwa wapo maeneo hayo wanamwinda, akafikiri sana na mwisho akatabasamu, akaichukua chai yake na kuanza kuinywa, Sarah aliamua kupuuza hilo tukio, ndicho alichofundishwa jeshini, kuwa kama itatokea adui atataka kucheza na saikolojia yako, mpuuze, alafu athari kubwa itamrudia adui kama alitumia nguvu kubwa kukufanyia mchezo huo.



Sarah alipomaliza shughuli zake, alielekea mjini na gari lake, siku hiyo alipanga kuanza kufuatilia utaratibu wa kufungua kampuni yake ya kuingiza na kutoa mizigo nje ya nchi ili iwe kama kivuli cha kuficha matendo yake, hasionekana yupo mjini bure, siku hiyo alianzia TRA.



*******************



Ndani ya kituo cha polisi, mkuu wa polisi alikuwa juu ya kiti na mezani kulikuwa na makabrasha kadhaa ya kesi za zamani ambazo ziliachwa juu juu bila kufanyiwa kazi, kupitia hayo makabrasha sio aliamua tu, aliamua kutafuta kabrasha la nyumba iliyowahi kuchomwa moto huku ndani kukiwa na watu, alifanya hivyo baada ya tukio lililopita siku moja tu, la nyumba ya babu yake Sarah kuchomwa, akakuta hiyo nyumba iliyoungua siku iliyopita na ile nyumba iliyochomwa miaka 19 iliyopita, zote ni za mmiliki mmoja, ambaye ni Isack, Baba yake Sarah,



"inawezekana haya matukio yana uhusiano?" Mkuu wa polisi alijiuliza mwenyewe huku akijikuna kichwa, akaamua aangalie ni askari gani alipewa aifuatilie ile kesi ya nyumba iliyochomwa moto miaka 19 iliyopita, akakuta kuna jina Moses Mahenge, akaamua aendelee kusoma ni wapi askari huyo alipoishia katika upelelezi wake, akakuta upelelezi ulifungwa baada ya Moses Mahenge kupigwa risasi hospitali na watu wanaosemekana hawajulikani.



Akatabasamu baada ya kuona kesi iliamriwa kufungwa baada ya askari wa upelelezi kuogopa kuifuatilia ile kesi baada ya mwenzao kupigwa risasi,



"askari gani wa ajabu kiasi hiki?" Mkuu wa polisi alijiuliza mwenyewe kisha akachukua simu yake na kupiga namba anayoijua yeye, baada ya kuongea kwa sekunde tano, akakata simu.



Baada ya dakika moja aliingia kijana ndani ya ofisi ile ya mkuu wa polisi, alipoingia alionesha heshima kwa kupiga salute, kisha akaambiwa akae chini, akapatiwa makabrasha yote mawili yenye kesi za nyumba za mtu mmoja kuungua katika miaka tofauti, Yule kijana akapitia maelezo ya mule kwa muda wa dakika ishirini kisha akayarudisha mezani,



"umegundua nini hapo?" Mkuu wa polisi aliuliza,



"ni nyumba za mtu mmoja" Kijana alijibu,



"sasa nakupa hiyo kesi ya nyumba kuungua jana, uifuatilie kwa maana inasemekana kulikuwa na watu wanaishi mule ndani, ila hawajaonekana mpaka sasa hivi?" Mkuu wa polisi aliongea huku akimtazama yule kijana,



"sawa mkuu" kijana alijibu kikakamavu,



"unaanza kuifuatilia muda gani, leo au kesho?" Mkuu wa polisi alimuuliza,



"nitaenda kukagua usiku eneo la tukio labda naweza kupata chochote kitakachonipa mwanga" kijana alijibu kikakamavu,



"sawa, unaweza kuondoka" Mkuu wa polisi aliongea kisha kijana akapiga salute na kuchukua yale makabrasha mezani na kutoka nayo.



*****************



Usiku wa saa tano, Sarah alikuwa chumbani kwake akivaa, alivaa suruali nyeusi ya mpira iliyoushika mwili wake, na ilikuwa na mkanda mmoja kila paja, Sarah alipachika bastola mbili katika kila mkanda, juu alivaa blazia na koti kubwa jeusi, usoni alivaa half mask, yaani kinyago kilichoziba nusu ya uso wake, yaani kilianzia puani kushuka chini, macho yalikuwa wazi na nywele zake ndefu zilikuwa wazi, akaziachia zining'inie.



Sarah aliamua aende kwenye nyumba ya babu yake iliyochomwa moto, aliamua kufanya hivyo kama mtego huku akiamini anaweza kumkuta kijana yoyote wa Taita, na nia ya Sarah ilikuwa ni kumuua vibaya kijana yoyote wa Taita atakayemkuta eneo lile ili iwe fundisho na pia awatishe kambi ya Taita.



Mishale ya saa sita na nusu usiku, Sarah aliiegesha range Rover yake mtaa wa pili, kisha kwa umakini mkubwa akajongea mpaka kwenye nyumba ya babu yake, kwa jinsi alivyoiona alisikitika, aliikuta imeungua yote limebaki pagale, akaingia ndani ya lile pagale akaanza kuzunguka zunguka, kwa bahati nzuri akaona kuna kipande cha picha mbele yake chini, akainama na kukiokota, akakitia mfukoni, wakati anainuka alishangaa akishikwa mkono kwa nguvu,



"wewe ni nani" Sauti iliuliza kwa ukali huku akiwa bado ameushika mkono wa Sarah, alikuwa ni yule kijana polisi,



Sarah akutaka kujibu, aliamini huyo ni kijana wa Taita, Sarah aligeuka na kuuvuta mkono wake kwa nguvu kisha akaachia teke jepesi ila lina madhara makubwa, yule kijana akayumba lile teke likampiga shingoni, kijana akapepesuka kisha akakaa sawa. Yule kijana akaamini sasa huenda huyo binti anahusika na uchomaji wa hiyo nyumba, akaahidi moyoni mwake kuwa ni lazima amdhibiti.



Wakati kijana akiwaza hayo, huku Sarah alikuwa anatafakari namna pigo lake aliloliamini namna ambavyo halikumletea madhara yule kijana.



Sarah akakunja ngumi akairusha, kijana akainama kisha akamchota mtama mkali Sarah, wakati Sarah akiwa hewani, yule kijana alirusha buti kali lililomkuta Sarah mbavuni, Sarah akarushwa mbali na kujipigiza ukutani. Sarah akauma meno kwa maumivu, kisha taratibu akainuka huku akiwaza kuwa leo amekutana na fundi haswa, Sarah akakunja ngumi tena, akamuendea kwa mtindo ule ule alioutumia hawali, Sarah alimsogelea na kurusha ngumi, Kijana akainama tena, safari hii alivyoinama tu, alikutana na kifuti kizito kilichomkuta yule Kijana katika miwani yake, upande wa jicho la kushoto, kioo cha Miwani kikatia nyufa, kijana akahisi hilo pigo sio geni sana,



"Sarah?" kijana aliita huku akimtazama Sarah, Sarah kusikia huyo kijana anajua jina lake, akahisi kabisa ni Kijana wa Taita, Sarah hakuitika, akarudi nyuma na kuruka teke kali, kijana akamdaka mguu na kuachia ngumi kali iliyotua kwenye kifua cha Sarah, Sarah akadondoka chini na kukohoa, kijana kuona hivyo, akawa anamuendea kwa pupa Sarah, alipomfikia alimuinamia, kwa kasi ya ajabu sana, Sarah aliinua jiwe kubwa na kumtwanga nalo pale pale kwenye kioo cha miwani kilicho na nyufa upande wa kushoto wa miwani, kile kioo kikapasuka kabisa, yule Kijana akarudi nyuma na kuamua kuiondoa kabisa miwani machoni mwake, alipoitoa ile miwani ndipo alipoonekana vizuri, jicho lake la kushoto lilikuwa bovu, alikuwa na chongo..................



Naaam ndugu msomaji nadhani umeshamtambua huyo kijana askari.





Naam, huyu kijana askari alikuwa ni Sajenti Minja, yeye ndio alipewa hii kesi aifuatilie.



Sarah akabaki na kiulizo kuhusu huyu mtu, alishangaa uwezo wake wa kupambana ingali ana jicho moja. Sarah sasa kwa spidi ya mwanga, akachomoa bastola yake, Sajenti Minja kuona hivyo, akaruka hewani na kujipindua, kisha akaachia teke kali lililotua kwenye mkono wa Sarah, Sarah akaangusha bastola huku akirudishwa nyuma na lile teke na kumfanya apepesuke, Sajenti Minja akamuwahi na kumkamata shingo yake kwa kutumia mkono wa kushoto kisha akamnyang'anya na ile bastola aliyobaki nayo, Sarah ikambidi apoe, leo alikuwa amepatikana haswa.



Sajenti Minja akamuachia Sarah shingo, ila alimuelekezea bastola,



"wewe ni nani? Vua hicho kinyago" Sajenti Minja alimuuliza Sarah, sasa Sarah akapata mshangao, anajiuliza kwanini huyu mtu amuulize yeye ni nani wakati alimuita jina lake muda mchache uliopita,



"toa kinyago kwa hiyari yako au nikutoe mimi kwa maumivu?" Sajenti Minja alimuuliza tena baada ya kumuona yupo kimya, ila hata kipindi hiki Sarah hakujibu kitu,



"wewe si ni kiburi?" Sajenti Minja aliongea huku alimsogelea Sarah, Sarah akaona hiyo ni nafasi kwake ya kujitetea, Sarah akapiga hatua mbili za haraka kumsogelea Sajenti Minja, huku akijua kabisa ni lazima Sajenti Minja achanganyikiwe kwa ile kasi aliyomfuata nayo, na kweli, hicho ndicho kilichotokea, Sajenti Minja alishangazwa na wepesi wa yule binti, Sajenti Minja akakimbilia kubonyeza kifyatua risasi, alikuwa ameshachelewa muda tu, Sarah alishakishika kitako cha bastola na kukifungua, risasi zote zikamwagika chini, Sajenti Minja akiwa bado anashangaa, alipigwa ngumi ya mdomo, akarudi nyuma akatema mate, yalikuwa na damu, Sajenti Minja akatoa bastola nyingine aliyomnyang'anya Sarah,



"nakufumua ubongo, toa kinyago iko" Sajenti Minja aliongea kwa hasira,



"piga tu" Sarah aliongea kwa nyodo huku akiwa hajali, kuona hivyo Sajenti Minja akashusha bastola usawa wa miguu ya Sarah, akafyatua risasi, lakini haikutoka,



"unajua sana kufyatua risasi eeeh?" Sarah aliuliza kwa kejeli, Sajenti Minja akataka kuinama kuokota risasi zile zilizoanguka kwenye bastola ya hawali, Sarah hiyo ndio nafasi aliyokuwa anaitaka, aliupiga mkono wa Sajenti Minja, ile bastola ikaruka juu, Sarah akaidaka kisha akaachia teke kali lililomkuta, Sajenti Minja ubavuni, Sajenti Minja akarushwa kidogo, Sarah akainama na kuiokota ile bastola nyingine, kisha Akainama, akaruka dirishani na kuanza kukimbia, aliona mtu anayepambana nae hakuwa wa kawaida, aliona akiendelea kupambana nae anaweza kuotewa na akadhibitiwa,



Sajenti Minja kuona anakimbiwa, nae akanyanyuka na kuanza kumkimbiza, lakini Sarah alikuwa mwepesi zaidi, kila anapopiga hatua mbili, huku Sajenti Minja alipiga hatua moja, mwisho wa siku Sarah akalifikia gari lake na kupanda kisha akaliondoa kwa kasi, Sajenti Minja akakuta vumbi tu, ila aliambulia namba za gari, hiyo ilikuwa nzuri sana kwa upande wake.



Akatoa simu yake mfukoni na kuandika hizo namba, kisha akageuka nyuma na kurudi ndani ya lile pagale, alirudi na kuokota zile risasi zile zilizotoka kwenye bastola ya Sarah,



"huu nao ni ushahidi mzuri" Sajenti Minja aliongea huku akitoa mfukoni kimfuko kidogo cha nylon, kisha akaziweka zile risasi, akaiokota miwani yake na kuitia kwenye mfuko wake wa shati na kuondoka zake.



*************************



Sarah alipoingia ndani kwake, alijitupa juu ya kochi na kuingiza mkono katika koti lake na kuitoa ile pcha aliyoikota kule kwenye pagale, akaiangalia, ilikuwa ni picha ya familia yao, katika picha alikuwepo Sarah, sebastian na wazazi wao, Sarah akaitupa ile picha juu ya meza, akavua viatu vyake, kisha akashusha pumzi ndefu.



"yule bwege ni nani? naona Taita atakuwa amedhamilia kupambana na mimi. Pale kwa Taita hakuna kijana anaweza kupambana namna ile, itakuwa amemtoa nje ya nchi, ila mbona anaongea kiswahili kizuri? Nitamfuatilia vizuri" Sarah aliongea peke yake,



"na babu itabidi kesho nijue kama yupo salama au la" Sarah aliongea mwenyewe kisha akanyanyuka na kwenda kwenye droo ya kabati na kutoa dawa za kuchua, alifanya hivyo ili kujichua sehemu zenye maumivu aliyoyapata kutokana na mapigo ya Sajenti Minja.



"kesho nitaanzia polisi kwa ajili ya kufuatilia mambo yangu ya kampuni" Sarah aliongea huku akijipaka dawa.



******************



Hakuna kipindi Taita alichanganyikiwa kama hiki, maana alitegemea kupokea simu ya Sarah na Sarah hakupiga, sasa Taita usiku huu alikuwa amekaa amepoa, mawazo yalimtawala, aliwaza ni kipi Sarah awazacho, alihisi Sarah atakuwa anaandaa shambulizi baya sana.



"Trigger na wewe umekosea, kwanini uliichoma ile nyumba ya yule mzee?" Taita alimuuliza Trigger ambaye alikuwa amekaa mbele yake,



"hakukuwa na njia nyingine ya kufanya" Trigger alijibu kwa upole,



"kumbuka huyu tulimuhitaji kama chambo tu, lakini wewe hukuliona hilo, ukampiga risasi, ukachoma nyumba yake, wewe unadhani Sarah anaandaa kitu gani kwa ajili yetu" Taita alihoji huku akimuangalia Trigger, lakini Trigger hakuwa na jibu, akakaa kimya,



"mzee mmemuhoji nini?" Taita alimuuliza Trigger,



"tumemuuliza tu ni wapi Sarah alipo" Trigger alijibu,



"amejibu nini", Taita akauliza tena,



"amesema yupo uingereza" Trigger alijibu,





"hujamuuliza kama wameonana siku za karibuni?" Taita aliuliza,



"anadai mara ya mwisho kuonana na Sarah ni miaka kumi na tisa iliyopita, zaidi ya hapo uwa wanawasiliana kwa simu tu" Trigger alijibu,



"kazi ipo, basi huenda Sarah hajamwambia babu yake kama amerudi nchini" Taita aliongea na kumimina maji kwenye glass na kuyanywa,



"nadhani hatupaswi kufikiria sana, nadhani atatutafuta tu" Trigger Aliongea kwa kujiamini,



"mzee amejua ni mimi nimemteka?" Taita alimuuliza,



"si ulisema hatakiwi kujua, basi hatujamwambia" Trigger alijibu,



"na yule mtoto wake mmemuhoji?" Taita aliuliza,



"ndio, ila Majibu yake ni kama ya baba yake, labda inawezekana wanachoongea ni kweli" Trigger alijibu huku akijikuna kichwa,



"nasikia ulitafuta daktari na kumpeleka kule ndani kumtibu yule mzee?" Taita alimuuliza Trigger,



"ni kweli, maana hali ya mzee niliona ikibadilika ndio maana nikaamua kufanya hivyo" Trigger alielezea hali halisi,



"huoni hiyo ni hatari sana, au unafahamiana na huyo daktari?" Taita alimuuliza,



"hapana, nimemdanganya na pesa, na pia nimemtisha kuwa endapo atasema chochote, nitammaliza, ameogopa nadhani" Trigger alijibu,



"haya sawa, ngoja tusubiri mpaka kesho, kama Sarah asipotutafuta, nahisi tutakuwa na hali mbaya, itabidi niongezewe ulinzi" Taita aliongea huku akimaanisha anachosema,



"usiogope mkuu, akija atakuja kwa adabu tu" Trigger aliongea kwa kujiamini,



"we Kaa kimya, maana hujawahi kukutana nae, muulize Harry, maana anajua balaa la huyo mtoto" Taita aliongea huku akinyanyuka,



"siku nitakayokutana nae, ndio siku atakayokutana na Israeli mtoa roho" Trigger aliongea kwa kujiamini,



"ulishindwa kumuua akiwa mtoto, utamuweza muda huu akiwa tayari ni mkubwa, tena sio mkubwa tu, ni mkubwa anaewaka kama moto " Taita aliongea huku akiingia ndani kwake na kumuacha Trigger akitafakari maneno ya bosi wake,



"nitamuweza tu, nitamfanya kitu kibaya ili bosi arudishe imani kwangu" Trigger aliongea kisha akanyanyuka kutoka kwenye kochi na kuelekea nje.



***********************



Sajenti Minja asubuhi ya leo ilimkuta yupo ofisini kwake, alikuwa yupo makini na computer yake, alikuwa akizifuatilia zile risasi alizoziokota kule pagaleni, aliamua kuzifuatilia baada ya kukuta zimeandikwa kwa nyuma sehemu zilipotengenezewa.



Baada ya kuzifuatilia kwa muda, aligundua zile risasi zimetengenezwa na kampuni ya jeshi la kiingereza, na kwa maelezo aliyoyasoma pale, yalionesha kuwa risasi zile uwa zinatumika katika bastola zake ambazo ni maalum na zinatengenezwa na kampuni hiyo hiyo, na zaidi ni Kwamba hizo bastola hazitumiwi na watu tofauti zaidi ya wanajeshi wa uingereza. Kwa maelezo hayo tu, ilibidi Sajenti Minja agune,



"kwa hiyo yule mwanadada ni mwanajeshi wa uingereza, au ni Sarah amekuja kwa mission nyingine?" Sajenti Minja alijiuliza, ila Sarah aliyemdhania yeye sio huyu Sarah Isack, Sarah aliyemdhania yeye ni yule mwanadada komando aliyesumbuana nae kwenye riwaya ya MEMORY CARD.



"sasa yule ni mwanajeshi wa marekani, na huyu wa jana anaonekana ni muingereza, au ndio yeye ila ameamua kutumia vitu vya kiingereza?" Sajenti Minja aliendelea kujiuliza,



Wakati Sajenti Minja akiendelea kujipiga maswali, alishtuka baada ya kuiona Ranger Rover nyeusi ikipaki mbele ya kituo cha polisi, aliiona kupitia dirisha la kioo, akaikumbuka hiyo gari kuwa ndiye ile iliyomkimbia usiku uliopita.



Wakati akishangaa hiyo hali, alishuhudia mwanadada mrembo akishuka katika ile gari, alikuwa ni Sarah, alienda hapo kukamilisha mpango wake wa kufungua kampuni, alifika hapo kwa ajili ya kuongea na mkuu wa polisi ili apatiwe askari ambao watakuwa wakiboresha ulinzi nje ya geti la kampuni yake.



Sarah aliposhuka alienda moja kwa moja mpaka kaunta na kuomba kuonana na mkuu wa kituo, akaelekezwa ofisi ilipo na akaenda huko kuongea nae.



Baada ya nusu saa, Sarah alikuwa amemaliza kuongea na mkuu wa polisi, Sarah akaelekea nje huku akiwa ametinga baibui pana nyeusi.



Alipolifikia gari lake akafungua mlango, wakati anataka kuingia ndani ya gari, alishtuka akishikwa mkono kwa nyuma, Sarah akageuka na huku akijiuliza ni nani huyo aliyemshika,



"samahani" Sajenti Minja aliongea huku akiwa bado ameushika mkono wa Sarah kwa mkono wa kushoto na wakati huo mkono wake wa kulia aliutumia kuivua miwani yake, macho yakabaki wazi na kufanya jicho lake moja la kushoto lenye chongo lionekane vyema, hapo ndipo Sarah akachanganyikiwa kabisa, akaikumbuka ile methali isemayo "ndege mjanja hunasa kwenye tundu bovu"







"bila samahani" Sarah aliongea huku akijitahidi kuficha mshtuko wake,



"habari yako" Sajenti Minja alitoa salamu kwanza,



"nzuri" Sarah alijibu huku akili yake ikimwambia asifanye kitu chochote cha ajabu,



"hii gari ni yako?" Sajenti Minja alimuuliza Sarah,



"ndio ni yangu, vipi kwani?" Sarah alijibu huku akimuangalia Sajenti Minja,



"naweza kuikagua?" Sajenti Minja aliuliza na kumfanya Sarah azidi kuhisi hatari,



"ruksa, ikague" Sarah aliongea na kufanya Sajenti Minja azunguke nyuma ya ile gari ili asome namba, ila alikuta namba ni tofauti na zile alizozinakiri usiku uliopita.



Sajenti Minja alirudi upande aliposimama Sarah,



"nashukuru kwa ushirikiano wako, nadhani nimefananisha gari" Sajenti Minja aliongea huku akitaka kuondoka,



"samahani, mbona unakagua tu gari yangu alafu unaondoka, hunipi hata sababu ya kuikagua?" Sarah alimuuliza Sajenti Minja huku akionesha hajakifurahia kitendo kile,



"nimeshakuambia kuwa nimefananisha gari" Sajenti Minja aliongea,



"sawa, hilo gari lilifanya kosa gani? " Sarah aliuliza,



"mwanamke acha maswali, Wewe elewa hivyo" Sajenti Minja aliongea huku akiondoka na kumfanya Sarah abaki anamuangalia tu.



Sarah akarudi ndani ya gari na kuiwasha kisha akaondoka zake,



"kumbe huyu jamaa ni askari, anajiamini sana alafu ana dharau" Sarah aliwaza peke yake wakati akiendesha gari yake, baada ya mwendo wa dakika tano, aliegesha gari yake kwenye duka kubwa, akashuka na kuchukua mahitaji yake ya nyumbani, baada ya hapo akaenda kulipia bidhaa alizonunua, kisha akatoka nje huku akiwa ameongozana na muhudumu wa pale ambaye alikuwa akimsaidia kusukuma kikapu cha matairi ambacho Sarah aliweka vitu vyake.



Baada ya Sarah kumaliza kuingiza vitu vyake ndani ya gari, na yeye aliingia ndani ya gari na kuiwasha kisha akaondoka zake, wakati akitoka eneo la dukani na kuingia barabara kubwa, aliweza kushuhudia gari aina ya harrier ikikatiza mbele yake, na ndani alimuona Trigger ambaye ndiye alikuwa dereva na pembeni ya Trigger alikaa binti mmoja mwembamba mwenye mwili kama Sarah.



Sarah akaona kuliko kwenda nyumbani, ni bora awafuate tu ili aone wanapoelekea.



Trigger aliendelea kuendesha gari huku hajui kama anafuatwa na adui yake, ile safari ya Trigger iliishia ndani ya majengo makubwa ya ghorofa ambayo Sarah hakusumbuka kujua pale ni hospitali.



Baada ya Trigger kusimamisha gari, alitelemka yule mwanamke ambaye alikaa pembeni ya Trigger, kisha akaingia ndani ya lile jengo, baada ya kupotelea ndani ya jengo, Trigger akageuza gari na kuanza kutoka kwenye eneo lile la hospitali, getini alipishana na gari la Sarah ambaye yeye alikuwa akiingia ndani ya eneo lile la hospitali.



Sarah aliingiza gari eneo la hospital na Kuliegesha, Sarah aliamua kudili na huyo dada tu, aliamini huyo dada huenda ana uhusiano na Trigger, iwe wa kimapenzi au ni ndugu, pia akahisi kama sio vyote hivyo, huenda huyo dada ni mmoja kati ya vijana wa Taita.



Sarah alitelemka na kuingia haraka haraka ndani ya jengo lile lile alipoingia yule dada, kwa bahati nzuri alimkuta yule dada akiwa bado eneo la mapokezi na alionekana akiongea kwa uchangamfu na yule dada wa mapokezi. Sarah akakaa katika kochi hapo na kujifanya anabonyeza simu yake.



"dokta pendo wahi bwana kuna wagonjwa wanakusubiri, ukiwa unatoka utanisimulia vizuri" Dada wa mapokezi alimwambia yule mwanadada aliyeletwa na Trigger,



a



"unajua leo natoka saa ngapi?" Mwanadada aliyeletwa na Trigger alimuuliza yule dada wa mapokezi,



"saa kumi na mbili kama kawaida, au?" Dada wa mapokezi alijibu,



"leo natoka saa mbili, maana nitamsaidia na dokta swai, kaniomba nimshikie mpaka muda huo ambao ndio ataingia hospitali" Mwanadada aliyeletwa na Trigger aliongea,



"mi natoka saa kumi na mbili, tutaongea kesho basi" Dada wa mapokezi aliongea,



"usijali shoga yangu" Dada aliyeletwa na Trigger aliongea huku akiondoka eneo hilo, na muda huo sasa Sarah ndio akaelewa kuwa yule dada ni daktari wa ile hospitali, akajua na jina lake anaitwa pendo, ila hivyo havikuwa vitu muhimu sana kwake, kwake kitu muhimu ambacho aliona amekiona, ni kujua muda wa kutoka wa yule daktari, hilo ndilo lilikuwa jambo muhimu kwake, sasa swali alilojiuliza ni kuwa huo muda wa huyo binti kuondoka, atafuatwa na Trigger au lah?



Sarah aliamua kuondoka muda huo, ila muda wote alikuwa akichekecha ubongo wake namna atakavyofanikisha mpango wako dhidi ya daktari yule wa kike, ajulikanaye kama Pendo.



Sarah alirudi nyumbani kwake, na kufanya shughuli zake ndogo ndogo za nyumbani huku akiwa makini na muda wake.



Baada ya shughuli zake kukamilika, hakutaka kuingia kusafisha mwili, alichofanya alibadili nguo na kuondoka, hakutoka na gari yake, aliamua kukodi boda boda iliyomfikisha mpaka mjini, kisha akamlipa dereva wa boda, alafu akakodi taxi ambayo ndio alipanga imfikishe hospitali anayofanyia kazi yule daktari wa kike.



Sarah alifanikiwa kupata taxi,



"nipeleke amani hospital" Sarah alimwambia dereva taxi huku akiingia siti za nyuma za taxi ile.



Dereva taxi akawasha gari na kuiondoa, njia nzima hakuna aliyemuongelesha mwenzake, Sarah alikuwa kimya na dereva taxi pia alikuwa kimya.



Dereva taxi akiwa yupo makini na barabara, alihisi kitu cha baridi kikigusa kisogo chake, dereva taxi akapata hofu kuu, kidogo agonge Kingo za barabara,



"simamisha gari, iweke pembeni" Sarah aliongea katika sauti laini na dereva taxi akatii ile amri,



"shuka na usizime gari" Sarah aliongea huku bastola yake ikiwa mkononi, ila dereva taxi akataka kuleta shida, alitaka kuchomoa funguo na kukimbia, Sarah akamuwahi kwa kumpiga na kitako cha bastola yake, dereva taxi akapoteza fahamu, Sarah akataka siti za nyuma na kuelekea mbele, akamsukuma dereva na kuanguka pembezoni mwa barabara, Sarah akawasha gari na kuiondoa mpaka nje ya hospitali ile.



Sarah alipofika alitelemka na kuanza kuchungulia kupitia katika uzio wa hospitali, alifika pale saa moja na nusu usiku, ila mpaka saa mbili na dakika tano hakumuona dokta Pendo akitoka, akasubiri nusu nyingine ila pia hakumuona dokta Pendo akitoka, akataka aingie ndani ndipo kwa mbali aliweza kumuona dokta Pendo akitoka. Dokta Pendo alipotoka, alienda kupanda coaster ambayo ilikuwa ndani ya uzio wa hospitali, hakuwa peke yake, aliongozana na kundi lingine la wafanyakazi wenzake ambao ilionekana muda wao wa kutoka ulikuwa umehitimu.



Sarah aliendelea kusimama pale pale mpaka alishuhudia ile coaster ikianza kusogea getini, na yeye akaenda kuingia kwenye ile taxi aliyokuja nayo.



Coaster ilipotoka nje ya geti, ilikamata barabara na kuondoka kwa mwendo wa wastani, Sarah akawasha gari na kuanza kuifuatilia kwa mbali, ile basi ambayo ilikuwa inawarudisha nyumbani wafanyakazi wa hospitali, iliendelea kuzunguka kupita kila mtaa na kumshusha kila mfanyakazi, mpaka ilipomshusha Dokta Pendo.



Dokta Pendo alipotelemka aliagana na wenzake, kisha akapiga hatua kuelekea kwenye nyumba iliyokuwa ikimtazama, zilikuwa ni nyumba za kota, Dokta Pendo alipoufikia mlango, alitoa funguo na kufungua mlango, alipoingia ndani, aliwasha taa na kujitupa katika kochi na kuanza kuvua viatu, wakati akiendelea kuvua viatu alisikia mtu akigonga hodi mlangoni kwake,



"watu wengine bwana, hata mtu hajatulia kwake wanakuja kumsumbua" Dokta Pendo alinung'unika huku akielekea mlangoni, alipofika alifungua mlango na kukutana na ngumi kali ya pua iliyomfanya apepesuke na kurudi nyuma,



"pole mrembo, naimani wewe ni dokta mzuri, utajitibu nikiondoka" Sarah aliongea huku akiingia ndani na kuufunga mlango, wakati huo Dokta Pendo alikuwa yupo chini huku damu ikimvuja puani.



"sijaja kwa ubaya, wala sina ubaya na wewe, nimekuja nina shida ndogo na wewe" Sarah aliongea huku macho yake yakitalii ndani ya sebule ya Dokta Pendo.



Dokta Pendo akajaribu kupiga kelele, Sarah akaruka na kutua mbele yake, kisha akampiga kofi kali sana, Dokta Pendo akajikuta analia badala ya kupiga kelele,



"Niue Niue" Dokta Pendo aliongea huku akilia,



"kwanini nikuue, mimi sijaja kukuua hapa, we ni mwanamke mwenzangu, na mimi ni mwiko kumdhuru mwanamke mwenzangu" Sarah aliongea kwa sauti tulivu,



"sema unataka nini?" Dokta Pendo aliongea kwa hasira,



"nilikuona mchana ukiwa kwenye gari aina ya harrier, ulikuwa na mwanaume, ni nani yako?" Sarah aliuliza huku akitabasamu,



"we mpuuzi nini, kumbe unanipiga kwa ajili ya mwanaume?" Dokta Pendo aliuliza kwa jeuri,



"naona hutaki kujibu, ila unataka tuulizane tu, itabidi nitumie hasira" Sarah aliongea huku akiitoa bastola na kuiweka mezani, hapo Dokta Pendo akapata uoga,



"yule ni mume wangu, je mna uhusiano nae?" Sarah aliuliza tena huku akimtazama,



"hapana, sina uhusiano nae", Dokta Pendo alijibu,



"mbona alikubeba kwenye gari na akakupeleka kazini? Kuwa mkweli, vinginevyo nitakuumiza vibaya mno" Sarah aliongea,



"nimeshakuambia Sina uhusiano nae" Dokta Pendo aliongea, na kufanya Sarah aikoki bastola yake na kumuelekezea,



"ni nini kinaendela kati yenu? Sitoona tabu kukuua endapo utakuwa hujibu ninavyotaka" Sarah aliongea na kumsogelea jirani kabisa,



"sawa, nitakujibu. Yule uliyeniona nae ni mtu ambaye aliniteka na kunilazimisha nimtibu mzee mmoja ambaye pia wamemteka" Dokta Pendo alitoa jibu lililomsisimua Sarah na kuhisi huyo mzee huenda ni babu yake,



"huyo mzee anaumwa nini?" Sarah aliuliza,



"ana jeraha juu ya bega, alipigwa risasi" Dokta Pendo alijibu,



"uwa anakufuata au unaenda mwenyewe?" Sarah alimuuliza,



"uwa ananifuata kila siku saa mbili asubuhi" Dokta Pendo alijibu,



"sawa" aliongea kisha akampiga kichwani na kitako cha bastola, Dokta Pendo akazimia, akambeba na kutoka nae nje, akamuingiza katika gari na kuondoka nae.



Sarah alipofika kwake, alimuingiza ndani Dokta Pendo, kisha akamuingiza katika chumba chake cha siri, akamlaza kitandani na kumpaka dawa anayojua yeye, alimpaka usoni, baada ya dakika moja ile dawa iliganda usoni kwa Dokta Pendo, Sarah akaibandua kama mask, kisha akaimwagia kemikali anayoijua yeye, alafu akaiingiza kwenye jiko la kukaushia, baada ya dakika tano akaitoa, ilikuwa ni mask ya sura ya Dokta Pendo, Sarah akaivaa usoni mwake, naam hicho ndicho alichokuwa anakitaka, alifanana kabisa na Dokta Pendo, Sarah akatabasamu.



********************



Mishale ya saa mbili asubuhi, Trigger aliegesha gari yake nje ya nyumba ya Dokta Pendo, kisha akapiga honi, baada ya dakika chache akatoka Sarah, ila ilikuwa ngumu kumtambua kutokana na ile mask aliyoivaa yenye sura ya Dokta Pendo.



Sarah akaingia ndani ya gari, akakaa pembeni ya Trigger,



"leo naona kama hips zako zimeongezeka" Trigger alimtania huku akitabasamu,



"macho yako tu" Sarah alijibu huku nae akitabasamu, kisha ukimya ukatawala mpaka gari ilipoegeshwa nje ya nyumba moja nzuri nzuri, Trigger akashuka,



"telemka tumefika, au leo hutaki kushuka" Trigger aliuliza huku akitabasamu na kufanya Sarah akurupuke na kushuka,



"nilikuwa mbali kimawazo" Sarah aliongea huku wakielekea ndani.



Safari yao iliishia ndani ya chumba kimoja ambacho ndani yake alikuwepo babu yake Sarah, Sarah alishtuka ila alijikaza,



"kaendelee na kazi" Trigger alimwambia Sarah kisha Trigger akasimama pale mlangoni, Sarah akamsogelea babu yake,



"babu mimi ni Sarah" Sarah aliongea kwa sauti ndogo ila iliyosikika vyema kwa babu yake,



"Sarah??? Kumbe wewe ni Sarah mjukuu wangu?" Babu yake Sarah aliongea kwa sauti kubwa iliyosikiwa vyema na Trigger, Trigger akachomoa bastola na kumuelekezea Sarah......



"umeharibu babu" Sarah aliongea katika sauti iliyokata tamaa............







Sarah hakua na jinsi, alichomoa kisu kutoka katika koti lake la kidaktari na kukirusha kwa kasi kumuelekea Trigger, Trigger akaruka pembeni na kushuhudia mkasi ukija usawa wa kichwa chake, Trigger akainama, aliponyanyua uso hakukuta mtu mwingine zaidi ya babu yake Sarah ambaye alikuwa akimshuhudia mjukuu wake akipambana.



Trigger akatoka mbio kuelekea nje, koridoni aliweza kuwapita vijana wake wakiwa wamelala chini kutokana na kipigo walichokipata kutoka kwa Sarah.



Trigger alitoka mpaka nje na kukuta gari yake ikiondoka kwa kasi, ilikuwa ikiendeshwa na Sarah, Trigger baada ya kushuhudia ule mwendo, alijikuta akipata uvivu hata kuchukua gari nyingine ili akimbizane na Sarah, na wakati huo vijana wengine walikuwa wakitoka ndani kuungana nae,



"tuchukue gari tumfuate?" kijana mmoja aliuliza lakini Trigger hakujibu, badala yake aliingia ndani mpaka katika kile chumba ambacho alifungwa babu yake Sarah, na kumtazama mzee yule kwa muda, kisha akatoka zake nje na kuufunga ule mlango.



Trigger akaelekea mpaka nje na kuchukua gari nyingine, akaingia ndani ya lile gari na kuliwasha, kisha akamuita kijana mmoja,



"mtu asiingie, wala mtu asitoke ndani ya nyumba hii" Trigger aliongea huku uso wake ukionekana umejaa ghadhabu,



"sawa mkuu" kijana alijibu kisha Trigger akaondoka na ile gari.



Safari Trigger iliishia nyumbani kwa Taita, akaiingiza gari ndani ya geti kisha akatelemka na kuingia moja kwa moja ndani ya nyumba, safari yake iliishia sebuleni kwa Taita, bahati nzuri alimkuta Taita akiwa amekaa na Harry sebuleni, wote walipata mshangao baada ya kumuona Trigger muda huo.



"we vipi, mbona sa hivi upo hapa?" Taita aliuliza huku akiiangalia saa yake ya mkononi,



"huko sio kwema hata kidogo?" Trigger alijibu huku akikaa kwenye kochi na kufanya wenzie waogope,



"kuna nini?" Taita alimuuliza,



"Sarah ametuvamia" Trigger alitoa jibu lililomfanya Taita macho yamtoke,



"kwa hiyo umemkimbia?" Taita aliendelea kuuliza,



"yeye ndio amekimbia" Trigger alijibu,



"ebu tueleze vizuri, mbona kama unatuvuruga" Harry aliongea baada ya kuona hamuelewi Trigger, kisha Trigger akaelezea mwanzo mpaka mwisho,



"kwa hiyo unataka kuniambia kuwa yule Dokta ni Sarah" Taita aliuliza,



"inawezekana" Trigger alijibu,



"Sidhani, kama angekuwa ni Sarah angeshamsaidia babu yake tangu mwanzo" Harry alijibu,



"kwa hiyo wewe unahisi nini?" Taita alimuuliza Harry,



"Mimi nadhani inawezekana Sarah alimteka daktari na kumshurutisha aeleze ana uhusiano gani na sisi" Harry aliongea hisia zake,



"basi kwa namna yoyote ile hata huyo Dokta Pendo anahusika, kwa maana nilimwambia iwe siri, yeye ameshindwa kutunza" Trigger aliongea,



"unapafahamu anapoishi huyo Dokta?" Harry alimuuliza Trigger,



"ndio" Trigger alijibu,



"kwanini usiende nyumbani kwa huyo Dokta Pendo?" Harry aliuliza,



"nadhani hatuwezi kumkuta, atakuwa amekimbia" Trigger alijibu,



"Mimi nadhani yule mzee inahitajika ahamishwe, aondolewe pale" Taita alimwambia Trigger,



"tumpeleke wapi?" Trigger aliuliza,



"nadhani tumpeleke kwa Harry" Taita aliongea,



"kwangu!!!!!?? Hapana mkuu, naomba hayo mambo muyaweke mbali na familia yangu" Harry aliongea kwa jazba,



"nitawapeleka kwangu, ila yule mwanae itabidi tumuachie tu" Trigger aliongea,



"bora iwe hivyo, maana wakiendelea kukaa pale itakuwa hatari" Taita aliongea,



"dah, tujitahidi tumdhibiti sasa hivi, maana tukishindwa kumdhibiti muda huu, wote tutakufa" Harry aliongea kwa sauti tulivu.



"basi acheni mimi nikafanye utaratibu wa kumuamisha yule mzee, alafu nitarudi baadae" Trigger aliongea huku akinyanyuka kwenye kochi,



"hujaniambia hali ya mzee lakini, anaendeleaje?" Taita alimuuliza Trigger,



"mzee anaendelea vizuri" Trigger alijibu,



"anahitaji daktari tena?" Taita aliuliza,



"Sidhani, ngoja nikaangalie hali yake alafu nitakupa jibu" Trigger alijibu huku akiondoka,



"kuwa muangalifu" Taita aliongea wakati Trigger akipotelea mlangoni.



"hii ni hatari sana, yaani adui anaingia mpaka ndani na hawajamtambua? Kwa hiyo bila ya yule mzee kulopoka basi wote wangekufa" Harry aliongea huku hofu ya wazi ikijionesha machoni mwake.



"kweli ni hatari sana, ila Harry kumbuka hii ni vita, hatutakiwi kurudi nyuma wala kuogopa, uzuri ni kwamba adui yetu tumeshamjua" Taita aliongea kwa kujiamini huku akimtazama Harry,



"ubaya ni kuwa yeye anatufahamu vizuri, na ndio maana anaweza kwenda katika nyumba ya yoyote kati yetu, sisi hatujui anapokaa" Harry aliongea kwa sauti tulivu,



"kutudhuru hawezi na ndio maana mpaka sasa hajafanya hivyo" Taita aliendelea kujiamini,



"sawa bwana, ila nilichofanyiwa si unakikumbuka?" Harry aliuliza,



"naona uoga umeshakuingia, ila kumbuka, hakuna mtu yoyote atakayetoka nje ya hii vita, na yoyote atakayesaliti hii kitu ni lazima auawe" Taita aliongea na kusimama kisha akaelekea zake chumbani na kumuacha Harry akiwa katika fikra nzito.



**********************



Sarah alivyoondoka na gari ya Trigger, alienda nalo mpaka mjini na kulitelekeza, akachukua bajaj iliyompeleka mpaka nyumbani kwake, alipofungua mlango tu alishtuka kuona anakabwa shingo, sema kabali yenyewe haikuwa nzito ila ilionesha mkabaji alidhamilia kufanya kitu, Sarah alifanya kama anainamia mbele kisha akamtupa kwa mbele mkabaji, alikuwa ni Dokta Pendo.



Alivyotupwa kwa mbele akainuka na kukunja ngumi, Sarah akajikuta anatabasamu, kwa maana alishaona huyo mtu hawezi chochote,



"ebu Kaa kwenye kochi tuongee, sina ubaya na wewe" Sarah aliongea huku akimuangalia Dokta Pendo,



"sitaki kuongea na wewe, ninachotaka ni kurudi kwangu" Dokta Pendo aliongea kwa ukali,



"kwako utarudi, ila nisikilize kwanza nataka nikwambie nini, upo hatarini wewe" Sarah aliongea kwa upole,



"sema" Dokta Pendo aliongea huku akiwa amesimama,http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



"yule mzee unaepelekwa kumtibu, ni babu yangu na alitekwa na yule niliyekuona nae kwenye gari jana, na wala sio mume wangu kama nilivyosema hapo hawali" Sarah aliongea kisha akameza mate na kumfanya Dokta Pendo amtolee macho,



"samahani kwa yote niliyokufanyia jana, ila lengo langu halikuwa baya kwako, nilichotaka ni kukuteka na mimi nichukue nafasi yako ili yule bwana anaekufuataga akija anichukue mimi badala ya wewe" Sarah alizungumza na kisha Dokta Pendo akaamua akae kabisa,



"unasema yule aliyetekwa ni babu yako?" Dokta Pendo aliuliza,



"ndio, yule ni babu yangu, na wale wana lengo baya na mimi na wala sio yule babu, na hapa wanachofikiria ni kukudhuru na wewe, wanadhani kuwa umenisaidia kunionesha kambi yao ilipo" Sarah aliongea,



"na kwanini wakufanyie wewe, umewakosea nini?" Dokta Pendo aliuliza,



"nitakuadithia hapo mbele nikishaimaliza kazi yangu, Maana sio hadithi nzuri" Sarah Aliongea huku akiwa ameinamisha kichwa,



"pole sana, je unaweza ukaniruhusu niondoke?" Dokta Pendo aliuliza,



"kuondoka unaweza, ila uko unapotaka kwenda, usalama haupo, watakuwa tayari wameshakuweka kundi moja na mimi" Sarah aliongea,



"Mimi hawatanifanya kitu, nitawaambia uliniteka" Dokta Pendo aliongea,



"umesema makubaliano yako wewe na Trigger ilikuwa ni kutomwambia mtu kuwa mule ndani uwa unaenda kumtibu mtu, je huoni umeshakiuka makubaliano?" Sarah alimuuliza Dokta Pendo,



"Mimi naenda hivyo hivyo, hawawezi kunifanya kitu" Dokta Pendo aliongea kwa kujiamini,



"sawa, usijali shoga yangu, mimi naomba tushinde wote, tule tushibe, alafu nitakurudisha usiku" Sarah alimwambia Dokta Pendo,



"nataka niende muda huu" Dokta Pendo aliongea,



"sasa hivi haiwezekani, naomba uniamini tu, wale watu muda huu watakuwa maeneo yale yale wanakuwinda" Sarah alimuelewesha Dokta Pendo,



"sawa, acha nikuamini" Dokta Pendo aliongea na kuonesha amekubaliana na Sarah.



**************************



Mishale ya saa tatu usiku, Sarah alikuwa nyumbani kwake na dokta Pendo,



"twende mi nimeshajiandaa" Sarah alimwambia Dokta Pendo,



"Mimi mwenyewe nipo tayari, nirudishe kwangu shoga" Dokta Pendo alimjibu Sarah,



"samahani, naomba nikufunge kitambaa cheusi machoni, maana sihitaji mtu apajue ninapoishi" Sarah alimwambia Dokta Pendo,



"kwanini hutaki mtu apajue hapa?" Dokta Pendo alihoji,



"ni sababu tu za kiusalama" Sarah alijibu,



"si uniambie hizo sababu shoga yangu" Dokta Pendo alimsihii Sarah,



"nitakuambia siku nyingine shoga yangu" Sarah alimjibu hivyo huku akitabasamu,



.



"haya Bwana, nifunge" Dokta Pendo aliongea kwa upole na Sarah akachukua Kitambaa na kumfunga, kisha akamshika mkono na kutoka nae mpaka nje, Akamuingiza ndani ya gari na safari ikaanza.



Ndani ya gari walikuwa na maongezi ya hapa na pale, iliwachukua nusu saa kufika nyumbani kwa Dokta Pendo, walipofika Sarah aliegesha gari yake upande wa pili wa barabara.



Ila waliweza kukuta vijana kadhaa wenye silaha wakiwa wameizunguka nyumba ya Dokta Pendo, hapo Sarah alimtoa kile kitambaa cheusi machoni na dokta Pendo akaweza kuwashuhudia wale vijana,



"wale ni polisi?" Dokta Pendo aliuliza, na wakati huo ndani Alikuwa akitoka Taita na Trigger,



"sio polisi wale, ni watu wako hao wanakutafuta" Sarah alijibu,



"ebu ngoja nishuke nikaongee nao" Dokta Pendo aliongea huku akitaka kufungua mlango,



"subiri kwanza, usiwe na pupa" Sarah alimwambia Dokta Pendo na wakati huo Trigger na Taita waliweza kuiona ile gari ambayo alikuwepo Sarah na dokta Pendo, ila hawakuweza kujua mtu aliyekuwepo ndani ya ile gari, ila waliitilia mashaka, Taita akiwa na Trigger waliamua kuisogelea ile gari huku bunduki zikiwa mkononi, walihisi kabisa mule ndani ya gari hakukuwa na watu wazuri.



Sarah aliweza kuona namna Taita na Trigger wanavyokuja, akawasha gari, lakini gari haikuwaka, akajaribu tena na bado gari haikuwaka, na kipindi hicho Taita na Trigger walibakiza hatua mbili tu waifikie gari ya Sarah, hapo Sarah akapata kihoro, tumbo joto.



Akajaribu tena kuwasha ila gari ikagoma,



"Shuka kwenye gari malaya wewe" Taita aliongea huku mtutu ukiwa usawa wa kichwa cha Sarah, kwa maana hiyo walikuwa tayari wameshamfikia Sarah, Sarah akatabasamu, halikuwa tabasamu la furaha, ila ni tabasamu la kukata tamaa na muda huo Taita alitoa tabasamu la ushindi, Sarah akanyoosha Mikono juu ikiwa ni ishara ya kutii amri..................



Sarah akili ikachemka, na vile hujiamini kwa kasi aliyokuwa nayo, alichofanya ni kuushika mkono wa Taita wenye bastola na kuuvuta kwa nguvu mkono wa Taita wenye bastola na kuuvuta kwa nguvu kisha akaachia ngumi nyepesi iliyompiga Taita kooni, Taita akajikuta akiiangusha ile bastola yake mapajani mwa Sarah, kisha Sarah akaikota ile bastola na kumuwekea Taita usawa wa kichwa huku akiwa amemkaba Taita,



"waambie mbwa wako waweke silaha chini na wasogee nyuma" Sarah aliongea huku mdomo wake ukiwa jirani na sikio la Taita, Taita akaona bora atii amri, akajitahidi na kupaza sauti akiwaamuru vijana wake waweke silaha chini na kurudi nyuma, vijana wakatii amri ya mkuu wao, kisha Sarah akatoka ndani ya gari na kumuamuru Taita aingie katika siti za nyuma za gari, Taita akatii kisha nae akaingia na yeye siti za nyuma,



"Dokta Pendo endesha gari" Sarah alimwambia Dokta Pendo ambaye muda wote alikuwa akitetemeka,



"gari si imekataa kuwaka?" Dokta Pendo aliuliza huku akitetemeka,



"we washa bwana, jaribu huenda itakubali" Sarah aliongea na kufanya Dokta Pendo asogee upande wa dereva na kujaribu kuwasha gari, ikawaka,



"tunaelekea wapi?" Dokta Pendo aliuliza,



"nenda eneo lolote lile ambalo unajua kuna pori" Sarah aliongea na kisha Dokta Pendo akaondoa gari, kuna vijana kama wawili walitaka kuokota silaha ili waishambulie gari, Sarah akawawahi na kuwafyatulia risasi, wakafa palepale. Kipindi hicho chote Taita alikuwa tumbo joto, hakuamini kama ametekwa kizembe hivyo, ila hakuwa na cha kufanya.



********************



Sajenti Minja alikuwa bize na lap top yake, bado alikuwa akifuatilia kuhusu ile nyumba iliyoungua, bahati nzuri aligundua kuwa mwenye ile nyumba pia alimuoa mwanamke aliyeitwa margret ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa serikali, baada ya kumfuatilia margret kupitia mtandao akagundua kuwa ana undugu wa karibu na Taita, pia akagundua kuwa hata ile hotel iliyojengwa kwenye ile nyumba iliyoungua zamani, ni hotel ya Taita,



Sajenti Minja akakuna kidevu, akaamua amtafute Sarah yule rafiki yake wa kwenye memory card, alimtafuta kwa njia ya mtandao, aliutumia whatsap kwa kuwa alikuwa na namba yake ya simu,



"upo wapi mrembo?" Sajenti Minja aliuliza baada ya salamu,



"nipo marekani, vipi kwani?" Sarah alihoji,



"hakuna kitu, nimekukumbuka tu" Sajenti Minja aliongea,



"bado wewe ni polisi?" Sarah alimuuliza Sajenti Minja,



"bado ndugu yangu, hizi kazi zetu ngumu kuziacha"Sajenti Minja alijibu huku akitabasamu,



"komaa bwana, endeleza mapambano" Sarah aliongea,



"poa bwana, wacha nikuage" Sajenti Minja aliongea,



"poa afande, nashukuru kwa kunikumbuka" Sarah aliongea huku akitabasamu,



"usijali, nitaendelea kukumbuka" Sajenti Minja aliongea,



"poa" Sarah alijibu kisha akakata mawasiliano.



Sajenti Minja akabaki anawaza, swali alilojiuliza kuwa yule binti aliyepambana nae kule pagaleni ni nani?



Mwisho Sajenti Minja akaamua aende Vin hotel, aliamua akamtafute Taita ili aweze kumuuliza maswali machache kuhusu margret na familia yake, aliamini kufanya hivyo kunaweza kumpa mwanga kidogo juu ya kile anachokitafuta.



Akatoka nje ya jengo la polisi na kuelekea moja kwa moja kwenye gari lake, akaingia na kuliondoa.



*******************



Kwenye kambi ya Taita kulikuwa na majonzi makubwa, walikuwa hawajui kiongozi wao yupo kwenye hali gani?



Muda huo aliyekuwa akiumiza kichwa sana ni Trigger, kwa maana tukio zima lilitokea mbele yake, na muda huo bado alikuwa eneo lile lile la nyumbani kwa Dokta Pendo, alikuwa na vijana wake, akawaamuru vijana wakapumzike majumbani mwao, kisha yeye akaingia kwenye gari lake alilokuja nalo na kuamua kwenda moja kwa moja nyumbani kwa Taita.



Wakati akiwa ndani ya gari alijitahidi sana kuwapa taharifa watu muhimu katika kundi lao, hakutaka kuwaambia ukweli, alichowaambia ni kuwa wote wakutane muda huo nyumbani kwa Taita, kuna tukio lisilo la kawaida limetokea.



Baada ya muda Trigger aliwasili nyumbani kwa Taita, akaingiza gari ndani, akaelekea moja kwa moja sebuleni, akawakuta Tekso na Strategic wakiwa wanamsubiri,



"Harry yupo wapi?" Trigger aliuliza,



"bado hajatimba, ila nadhani tunaweza kuendelea na kikao" Tekso alijibu,



"na bosi naye yuko wapi?" Strategic aliuliza lakini Trigger hakuonekana kuwa tayari kujibu hilo swali, na muda huo Harry alikuwa anaingia huku akionekana hajafurahishwa na kikao hicho cha usiku. Harry akawasalimia wenzake na kisha akakaa kwenye kochi,



"nadhani tunaweza kuanza kikao" Trigger aliongea huku akiangalia chini,



"Taita yuko wapi, maana yeye ndio anatakiwa aongoze kikao na sio wewe" Harry aliongea huku akionekana kumshangaa Trigger,



"lengo la kikao ni hilo, kuwajulisha ni wapi alipo Taita" Trigger aliongea na kufanya wenzake watege vizuri masikio yao,



"ukiwa unaeleza kitu unatakiwa uende direct kwenye jambo husika, sio kukatisha katisha maneno" Harry aliongea kwa ukali baada ya kutofurahishwa na mtindo anaoutumia Trigger katika kuongea,



"ok, ni hivi, Taita ametekwa na Sarah muda mchache uliopita" Trigger aliongea na kufanya miili ya wenzake ipigwe na ganzi,



"bado sijakuelewa, unasema?" Harry aliuliza tena kanakwamba hajasikia kilichozungumzwa na mwenzie huyo,



"ilikuwaje kuwaje yaani?" Tekso nae akapandishia swali jingine.



Mpaka kufikia hapo wote walikuwa wamechanganyikiwa, maana walikuwa wanamjua vyema Sarah katika suala zima la kufanya unyama, na hakuna hata mmoja aliyekuwa na imani ya bosi wao huyo kurudi akiwa hai.



"tueleze basi kilichotokea" Harry aliongea baada ya kumuona Trigger akiwa kimya,



Trigger akaeleza kila kitu, hakuficha chochote.



"tunafanyaje sasa?" Tekso aliuliza ila hakuna aliyemjibu, hali ilikuwa mbaya sana kwenye hii kambi,



"sasa mbona hamjibu?" Tekso aliuliza tena, ila safari hii alitumia sauti kubwa kidogo Baada ya kuona wenzie hawakutilia mkazo swali Lake la hawali,



"taratibu basi, hilo swali ulilouliza halihitaji jibu la kukurupuka, linahitaji nafasi ya kufikiria" Strategic alijibu huku akiwa amefunga macho,



"kweli tunahitaji muda kiasi wa kupata cha kufanya kuhusu hili suala" Harry alionekana kumuunga mkono Strategic,



"ndio tufikirie hapa hapa na tupate jibu" Trigger aliongea,



"na hiyo pia haiwezekani, inaweza kutuchukua siku mbili au tatu kuweza kupata fikra sahihi" Strategic aliongea,



"siku mbili au tatu? Wewe una wazimu nini? Siku hizo zote utakuwa unafikiria nini?" Trigger aliongea kwa jazba huku akionekana amekereka kutokana na majibu ya Strategic,



"Trigger kwani wewe unapajua alipopelekwa Taita?" Harry aliuliza huku akimuangalia Trigger,



"sipajui, ningekuwa napajua si ningeshaenda?" Trigger alijibu,



"unajua ni wapi Sarah anapokaa?" Harry akamtupia swali jingine Trigger,



"hapana" Trigger akajibu,



"sasa kwanini Strategic anaposema hili suala itabidi lichukue siku mbili au tatu kuweza kupata fikra sahihi, Wewe unakuwa unapinga wakati unajua kabisa adui tunaepambana nae hatujui pa kumpata?" Harry aliongea huku akimtazama Trigger,



"Tekso si yupo, anaweza kucheza na technolojia tugundue chochote" Trigger aliongea,



"kwani uko alipo Taita ameenda na simu?" Tekso aliuliza,



"simu ameiacha ndani ya gari" Trigger alijibu,



"dah, basi ni ngumu sana kujua alipo" Tekso alijibu na kufanya Trigger achoke kabisa,



"mi nadhani tutawanyike tu, kesho asubuhi tukutane ili tujue cha kufanya, na kila mtu akalale huku akitafuta njia ya kuweza kumpigania Taita" Harry aliongea huku akiwatizama wenzake,



"nyie nendeni, mimi nitabaki hapa nikilinda nyumba, maana hakuna mtu zaidi ya mlinzi" Trigger aliongea,



"sawa, mimi naenda, ila kesho tukutane hapa asubuhi kama nilivyosema" Harry aliongea huku akiinuka kwenye kochi,



"sawa mkuu, naimani kesho tutakuwa na mbinu zozote" Tekso alijibu huku nae akiinuka katika kochi,



??



"na wewe uende, mimi nataka nifunge mlango" Trigger alimwambia Strategic aliyekuwa bado amekaa,



"taratibu mkuu, kila kitu kinahitaji mpangilio, nasubiri wenzangu wapite mlangoni na mimi ndio nifuate" Strategic alijibu katika sauti tulivu,



"nyanyuka bwana, unajifanya mtu wa mipango wakati umeshindwa kupanga namna ya kumkomboa Taita" Trigger aliongea huku akimvuta Strategic ainuke, strategic akainuka na kuondoka zake huku wakimuacha Trigger akiwa amesimama mlangoni akiwatazama.



*********************



Usiku huu Sajenti Minja aliingia Vin hotel na kuelekea moja kwa moja mapokezi,



"nahitaji Kuongea na meneja wa hapa" Sajenti Minja aliongea huku akionesha kitambulisho chake, dada wa mapokezi akamuelekeza ofisi ya meneja ilipo, akaenda na kumkuta msichana akiwa ndio meneja wa pale, akamsalimu,



"kama nilivyosema hawali, mimi ni askari na hapa nimekuja nikiwa nataka kuonana na mmiliki wa hii hotel" Sajenti Minja aliongea kwa utulivu,



"Mimi hapo sina cha kukusaidia, labda tu nikupe namba yake" meneja aliongea kinyenyekevu,



"pia huo ni msaada" Sajenti Minja aliongea huku akiitoa simu yake na kisha yule dada Meneja akamtajia namba ya Taita, Sajenti Minja akainakiri katika simu yake.



"usimpigie usiku, mtagombana" Meneja alimtahadharisha Sajenti Minja,



"usijali, nitampigia kesho asubuhi" Sajenti Minja alijibu huku akitabasamu na kutoka zake nje, akaelekea kwenye gari yake na kuingia ndani, alipoiwasha ili aondoke, ndipo alishuhudia gari aina ya range Rover likikatiza mbele yake huku likiwa katika mwendo mkali, akalikumbuka hilo gari kuwa ni la muharifu anayemtafuta.



Sajenti Minja nae akaitoa gari yake kwa kasi kuifuata ile Range Rover, alijitahidi kuifanyia ishara zote ili ile Range Rover isimame, badala yake iliongeza mwendo, alafu eneo ilipokuwa inaelekea ni eneo la porini.



Sajenti Minja akaamua atumie akili ili kuweza kuikamata ile gari, akaendelea kuikimbiza kwa nusu saa, akafanikiwa kuipita kisha akaisimamisha kwa ghafla gari yake katikati ya barabara, ile Range Rover nayo ikaminya breki, Sajenti Minja akawasha tochi yake na kummulika dereva wa ile gari, alikuwa ni Dokta Pendo, tena alikuwa na hofu tele.



Sajenti Minja akachomoa bastola yake na kushuka ndani ya gari,



"telemka chini, Mikono ikiwa juu" Sajenti Minja aliongea huku bastola yake akimuelekezea Dokta Pendo, hapo Dokta Pendo akazidi kuchanganyikiwa, akashuka kwenye gari.



"mpo wangapi kwenye gari na mmebeba nini?" Sajenti Minja aliuliza lakini Dokta Pendo hakujibu, ni machozi tu yalimtoka,



"wewe mwanamke si nakuuliza?" Sajenti Minja aliongea kwa ukali, lakini Dokta Pendo hakujibu, aliendelea kulia kimya kimya, sasa Sajenti Minja akahisi ndani ya gari kuna kitu na ndio maana yule dada analia, Sajenti Minja akalisogelea gari na kufungua mlango wa nyuma kwa nguvu.......





Sajenti Minja alikutana na teke kali lililotua kwenye mkono wake wenye bastola, bastola ikamdondoka, alichofanya Sajenti Minja ni kuushika mguu wa Sarah na kumvuta nje kwa nguvu, Sarah akatoka kama mzigo na kupigizwa chini, kwa kuwa hakuwa na mask, alichofanya alitoa kitambaa na kujifunika kuanzia puani na kushuka chini.



Sajenti Minja hakufanikiwa kumuona vizuri Sarah, ila Sajenti Minja aliruka juu kumuelekea Sarah, Sarah hakutaka kupoteza muda, alimsubiri Sajenti Minja atue chini, alipotua alikutana na mateke ya haraka haraka ya mbavuni na Sajenti Minja akajikuta ameinama baada ya kuhisi maumivu kwenye mbavu, Sajenti Minja alipoinama tu, akapigwa ngumi tatu za kisogoni na kuanguka chini, alipoteza fahamu pale pale, leo Sajenti Minja alipigwa kiurahisi sana, mpaka Sarah mwenyewe akashangaa, hakutegemea kushinda kiurahisi vile.



"iondoe hiyo gari yake hapo barabarani" Sarah alimwambia Dokta Pendo ambaye alielekea mpaka ilipokuwa gari ya Sajenti Minja na kuiondoa barabarani, kisha akarudi alipokuwa amesimama Sarah,



"itabidi niwe dereva muda huu" Sarah aliongea huku akiingia kwenye gari yake na Dokta Pendo akaingia kushoto mwa gari,



"mzee bado hajahamka" Dokta Pendo aliongea huku akimuangalia Taita aliyekuwa amelala nyuma ya gari,



"huyo kuamka ni mpaka kesho, hiyo sumu niliyomnusisha sio nzuri, inachukua masaa mengi kutoka mwilini" Sarah alijibu,



"sasa shoga yangu, mi nadhani unirudishe nyumbani tu" Dokta Pendo aliongea,



"wewe hata huogopi? Hujaona tulivyowakuta wakikuwinda pale kama mnyama?" Sarah aliuliza kwa mshangao,



"nirudishe nikachukue nguo zangu tu ili nihame pale, sina mpango wa kuishi pale" Dokta Pendo aliongea,



"hapo sawa" Sarah aliongea huku akiongeza mwendo wa gari yake,



"na yule uliyepambana nae kule ni mmoja wao?" Dokta Pendo alimuulizia Sajenti Minja,



"yule ni askari" Sarah alijibu katika sauti tulivu,



"askari???? Sasa mbona umempiga? " Dokta Pendo aliuliza kwa mshangao,



"pale sijampiga, nilichofanya ni kujilinda, kanuni za kijeshi zinasema ni bora ujilinde huku ukiwa unashambulia" Sarah alimjibu Dokta Pendo,



"kanuni za kijeshi? kwani wewe ni mwanajeshi?" Dokta Pendo alihoji,



"hapana, ila najua mambo mengi ya kijeshi" Sarah alijibu huku akiegesha gari yake mtaa ule ule anapokaa Dokta Pendo, ila alipaki mbali kidogo ingawa nyumba aliiona vizuri.



"subiri kwanza nikaikague nyumba yako" Sarah aliongea Kisha Sarah akatelemka na kuelekea kwenye nyumba ya Dokta Pendo kwenda kuikagua, alienda kiuangalifu mpaka alipofika mlangoni, akachomoa bastola yake na kisha akagonga hodi, lakini hakujibiwa, akarudia tena kugonga hodi na hali ikawa ile ile, akasukuma mlango na mlango ukafunguka, akaingia ndani na kukuta hakuna mtu, akaikagua nyumba yote mpaka chooni pia hakukuta mtu, akaridhika na ukaguzi wake, Sarah akatoka nje na kuelekea kwenye gari,



"unaweza kwenda, ila mimi naondoka, Wewe cha kufanya ni kukusanya vitu vyako haraka na kuondoka" Sarah aliongea,



"usijali shoga yangu, situmii hata muda mrefu" Dokta Pendo alijibu kisha wakaagana na Sarah, Sarah akawasha gari na kuondoka zake.



Safari ya Sarah iliishia nyumbani kwake, akaingiza gari ndani ya geti na kisha akafungua mlango wa nyuma wa gari, akamtoa Taita, hakuwa na uwezo wa kumbeba, alimburuta mpaka ndani, akamuingiza ndani ya chumba chake cha siri, kisha akamfunga mikono na miguu, na mdomoni alimziba na plasta nzito ambayo ilimzuia Taita kutoa sauti endapo atarejewa na fahamu zake.



Baada ya kujiridhisha na hayo, Sarah alielekea sebuleni, alifikia kujitupa kwenye kochi kisha akatabasamu,



"sasa wao wameshika makali, mimi nimeshika mpini" Sarah aliongea peke yake huku akitabasamu, aliamini kufanya kabisa kwa kitendo kile cha kumshika Taita, basi tayari ameshaiweza kambi yote ya Taita, aliamini kinachofuata ni kuwaendesha tu kimabavu.



Sarah akasaula nguo pale pale sebuleni, kisha akaingia bafuni kujiswafi mwili, alitumia nusu saa ndani ya bafu, kisha alitoka na kuingia chumbani kwake, akavaa nguo za kulalia, kisha akatoka na kuelekea sebuleni, akaelekea kwenye friji na kutoa pakiti ya maziwa, akapitia kwenye kabati na kuchukua glass, akaelekea kwenye kochi kisha akawasha runinga, Sarah aliimaliza siku yake vizuri.



*************************



Sajenti Minja alikuja kuzinduka huku akiwa na maumivu sehemu za mbavu na kisogoni, hizo ndizo sehemu alizoshambuliwa na Sarah.



Sajenti Minja alipozinduka akatupa macho kushoto na hakuona kitu isipokuwa alama za matairi ya gari, alipotupa macho kulia aliweza kuiona gari yake ikiwa imewekwa pembeni ya barabara, akaisogelea na kuikagua kama kuna chochote kibaya, hakuona kitu chochote kibaya, Sajenti Minja akaingia ndani ya gari yake na kukaa huku akijishika kichwa kutokana na maumivu pia mawazo.



"huyu binti ni nani? mara ya pili hii tunakutana kiutata utata tu" Sajenti Minja alijiuliza mwenyewe huku akiangalia kama funguo ya gari yake ipo,



"huenda kweli ni mwanajeshi" Sajenti Minja aliongea kisha akawasha gari yake na kuiondoa kwa kasi.



Safari ya Sajenti Minja iliishia nyumbani kwake, hakutaka hata kupoteza muda, alipofika nyumbani kwake aliingia chumbani na kuwasha laptop yake kisha akaandika mambo yote aliyoyajua kuhusu huyo binti aliyemshambulia dakika chache zilizopita, kwake yeye aliamini huyo binti ni mtu mbaya sana, aliamini huyo binti anastahili kufuatiliwa kwa jicho la karibu sana.



*********************



Dokta Pendo hakutaka kabisa kuhama nyumbani kwake, na pia aliamini kuwa kundi la Taita alitomfanya kitu, kwa hiyo baada ya kuachwa na Sarah, alichofanya yeye ni kwenda moja kwa moja kuoga, alipotoka kuoga alitoka nje na kwenda kununua chakula, alirudi ndani na kula kisha akalala zake huku akibaki na maswali mengi kumuhusu Sarah, hakujua ni mtu wa aina gani, ni mtu mbaya au mtu mwema? Hakupata jibu sahihi, alichoamua ni Kulala usiku huo.



********,********



Asubuhi palipokucha, Dokta Pendo alidamka mapema na kujitayarisha kwa ajili ya kuwahi kazini, maana alikuwa na wasiwasi wa kufukuzwa kazi baada ya kutokwenda kazini katika siku iliyopita na hakutoa taharifa.



Dokta Pendo alitoka na kuchukua bajaj iliyompeleka mpaka kazini kwake, alipofika alielekea moja kwa moja ofisini kwa bosi wake, alipoingia alimsabahi,



"jana mbona hukuja kazini?" boss wake alimuuliza kwa ukali,



"nilikuwa na matatizo" Dokta Pendo alijibu kwa unyekekevu,



"taharifa ulimpa nani?" Boss wake aliendelea kumbana kwa maswali,



"kwa aina ya matatizo niliyoyapata ilikuwa ngumu kupata muda wa kuja hapa kazini na kutoa taharifa" Dokta Pendo alijibu,



"ni matatizo gani hayo?" Boss wake alimuuliza,



"nilitekwa, kuna mtu alinivamia juzi usiku na kuniteka?" Dokta Pendo alitoa jibu lililomuogopesha boss wake,



"na nani?" Boss aliuliza kwa mshangao,



"hata sijamjua mpaka sasa, maana aliniteka akiwa amejifunga kitambaa usoni na alinipa dawa iliyonifanya nipoteze fahamu, nilizinduka jana usiku na nilikuwa nipo ufukweni" Dokta Pendo alidanganya,



"basi kama ni hivyo, nenda katoe maelezo polisi kwanza, alafu ndio sisi tukupokee" Boss wake alimwambia,



"sawa, nashukuru" Dokta Pendo aliongea huku akinyanyuka na kuelekea nje, akachukua usafiri uliomfikisha mpaka kituo cha polisi, alipofika alienda mpaka kaunta na kumkuta askari akiwa amekaa eneo, akamueleza shida yake, yule askari hakuwa na uwezo wa kuisikiliza ile kesi, akamuonesha ofisi ya kwenda.



Dokta Pendo akaenda mpaka kwenye mlango mmoja, akagonga hodi, akaitikiwa kisha akafungua mlango ili aingie, alipofungua mlango tu alishtuka, maana mwenye hiyo ofisi ni Sajenti Minja,



"karibu ukae" Sajenti Minja alimkaribisha, Dokta Pendo hakuongea kitu ila alienda kukaa alipotakiwa kukaa, aliamini Sajenti Minja amemsahau,



"za tangu jana usiku?" Sajenti Minja aliongea huku akitabasamu na kumfanya Dokta Pendo ashtuke,



"sio nzuri" Dokta Pendo alijikaza na kujibu kwa sauti ya upole,



"naona umekuja kujisalimisha" Sajenti Minja aliongea huku akiandika andika mambo yake,



"sijaja kujisalimisha, nimekuja kutoa taharifa" Dokta Pendo alijibu,



"taharifa zipi?" Sajenti Minja aliuliza huku akiacha kuandika na kumuangalia Dokta Pendo,



"kuhusu yule dada uliyenikuta nae jana, aliniteka na kuniamrisha niendeshe ile gari yake, kuna mwingine alikuwa amemteka na alikuwa amekaa nae siti ya nyuma" Dokta Pendo aliongea,



"baada ya hapo?" Sajenti Minja aliuliza huku akiwa hamuamini kabisa yule mwanamke,



"baada ya kukamilisha kazi yake aliniachia" Dokta Pendo alijibu,



"alikuacha bila ya kukudhuru?" Sajenti Minja aliuliza,



"aliniacha kirafiki tu na kaniomba nisije kutoa taharifa polisi, pia nikamkubalia kuwa rafiki yake" Dokta Pendo aliendelea kutoa maelezo ambayo Sajenti Minja aliyaona ya kitoto tu.



"una namba yake ya simu?" Sajenti Minja alimuuliza,



"hapana" Dokta Pendo alijibu na kisha Sajenti Minja akacheka,



"sasa ndio rafiki gani hata namba yake ya simu huna? Unafanya kazi?" Sajenti Minja alimuuliza,



"ndio, mimi ni daktari wa hospitali binafsi" Dokta Pendo alijibu,



"vitambulisho vyako viko wapi?" Sajenti Minja aliuliza huku akiwa amemkazia macho, Dokta Pendo akatoa vitambulisho vyake na kuviweka juu ya meza, Sajenti Minja akaviokota na kuanza kuviangalia,



"sasa tukubaliane jambo moja, nitakupa namba yangu ya simu, huyo rafiki yako ukimuona popote unipe taharifa" Sajenti Minja aliongea huku akimrudishia Dokta Pendo vitambulisho vyake,



"sawa haina shida" Dokta Pendo alijibu,



"sawa unaweza kwenda" Sajenti Minja aliongea,



"natakiwa nipewe karatasi ambayo itaonesha kama nimekuja polisi kutoa maelezo, bila hivyo itakuwa ngumu kukubaliwa kurudi kazini" Dokta Pendo aliongea, kisha Sajenti Minja akachukua karatasi na kuiandika na kisha akampatia Dokta Pendo.



"asante" Dokta Pendo aliongea huku akiipokea ile karatasi kisha akaondoka zake, akarudi hospitali na kumpelekea boss wake kile kikaratasi alichopewa polisi, boss wake akamruhusu akaendelee na kazi.



**************



Mishale ya saa mbili usiku, Sarah alikuwa eneo la hospital akikagua kama Dokta Pendo ameenda kazini, kwa bahati nzuri aliweza kumuona Dokta Pendo akitoka, akamkimbilia na kumsalimia,



"umehamia wapi shoga yangu?" Sarah alimuuliza,



"sijahama shoga, nipo pale pale" Dokta Pendo aliongea na kufanya Sarah ashtuke,



"huogopi hata hali ya usalama wako?" Sarah aliuliza,



"hawatanifanya kitu shoga, mimi mwanamke bwana, nina mbinu za kupambana nao" Dokta Pendo aliongea huku akitabasamu,



"ingia kwenye gari nikupeleke, ila huame pale shoga, sio pazuri pale" Sarah alimsisitiza Dokta Pendo huku wakiingia kwenye gari,



"usijali shoga yangu, kuwa na amani tu" Dokta Pendo aliongea wakati Sarah akiondoa gari eneo la hospital,.



Ndani ya gari waliendelea na maongezi yao, ila kitu ambacho Sarah hakukijua ni kuwa muda huo Dokta Pendo alikuwa akichat na Sajenti Minja, alikuwa akimtaharifu kuwa yupo na Sarah na alimtaharifu kuwa muda huo wanaelekea nyumbani kwake yeye Dokta Pendo, Sajenti Minja akahakikishia kuwa anakuja muda sio mrefu.



Sarah alipofika mtaa ule anaokaa Dokta Pendo, aliiegesha gari yake mbali sana na nyumba ya Dokta Pendo, alifanya vile kwa sababu za kiusalama.



Wakatelemka na kutembea mpaka mlangoni kwa Dokta Pendo,



"karibu shoga" Dokta Pendo alimkaribisha Sarah,



"Mimi mwenyeji hapa shoga yangu" Sarah alijibu huku akitabasamu na pia alikuwa akiingia ndani. Wakaelekea sebuleni na kuanza kuongea, ila muda wote Dokta Pendo alikuwa akichat,



"ngoja nikakuchukulie soda" Dokta Pendo aliongea huku akinyanyuka,



"acha tu, usijisumbue" Sarah aliongea,



"sio vizuri bwana" Dokta Pendo aliongea huku akitoka nje.



Baada ya dakika mbili aliingia Dokta Pendo na soda mkononi, akaenda kukaa pembeni ya Sarah, mara ghafla mlango ukafunguliwa, alikuwa ni Sajenti Minja, Dokta Pendo akanyanyuka haraka na kukimbilia nyuma ya Sajenti Minja.



Sarah akabaki ameganda vile vile, hakutaka kugeuza sura yake mbele ya adui,



"hahaha atimaye leo nimekupata ukiwa huna mask usoni, geuka basi niione sura yako mrembo" Sajenti Minja aliongea huku akicheka na muda huo bastola ilikuwa mkononi, Sarah hakuwa na ujanja, alibaki akisali moyoni mwake Mungu amuepushe na kikombe kile...................





Sarah aliendelea kuganda vile vile huku moyoni mwake akiamini amechezewa mchezo, na wala hakujisumbua kuwaza ni nani aliyemchezea huo mchezo, aliamini ni Dokta Pendo, taratibu aliamini ameshashikwa leo mtegoni ila akajiapiza endapo atapelekwa polisi, atatoroka ila akirudi uraiani, Dokta Pendo atakuwa mmoja kati ya watu wataopata patashika kutoka kwake.



"ina maana husikii nilichosema?" Sajenti Minja alihoji huku akiikoki bastola yake, Sarah akanyoosha Mikono juu, akasimama huku akijiandaa kugeuka, ila pasipo kutegemea kikasikika kishindo kizito Kama mtu amepigwa na kitu kizito, ndipo Sarah alipogeuka haraka, akamkuta Sajenti Minja akiwa yupo chini amepoteza fahamu na wakati huo Dokta Pendo akiwa amesimama huku ameshika kipande kikubwa cha jiwe,



"ondoka shoga yangu, kimbia shoga" Dokta Pendo aliongea huku akimtazama Sarah na kufanya Sarah abaki na mshangao huku akijiuliza kama Dokta Pendo ndio alimuitia askari, ni kwanini amsaidie?



"nikiondoka si utabaki hatiani?" Sarah alimuuliza Dokta Pendo,



"shoga wewe nenda tu, sitokosa cha kumdanganya" Dokta Pendo aliongea huku akiwa anamtazama Sarah,



"dah, nina maswali mengi kwa hiki ulichokifanya leo" Sarah alizungumza huku akiwa bado amesimama,



"utaniuliza siku nyingine, sasa hivi ondoka tu shoga yangu, huyu asije akaamka yakawa mengine tena" Dokta Pendo aliongea kwa hamaki,



"sawa, nashukuru kwa yote uliyonifanyia leo" Sarah aliongea kisha akatoka ndani ya nyumba ya Dokta Pendo na kumuacha akimpepea Sajenti Minja.



Baada ya dakika kumi za kuondoka kwa Sarah, Sajenti Minja alipata fahamu na kumkuta Dokta Pendo akiwa amevaa gloves huku pembeni kukiwa na chupa ndogo ndogo za dawa pamoja na pamba zilizokuwa na damu. Shati alikuwa ameondolewa na jirani yake kulikuwa na feni iliyokuwa ikimpuliza.



Sajenti Minja ndio akakumbuka tukio gani lililokuwa likiendelea hapo, akapeleka mkono wake kisogoni akasikia maumivu na pia akahisi amefungwa bandeji,



"ni nani alinipiga kisogoni?" Sajenti Minja alimuuliza Dokta Pendo,



"kwanza pole, wakati umemshikia bastola yule dada, kuna mwanaume ameingia na tofali na kukupiga nalo, alafu amemchukua yule dada ameondoka nae" Dokta Pendo aliongea kwa huruma, lakini maneno yote yalikuwa ya uongo,



"wewe hawajakudhuru?" Sajenti Minja aliuliza,



"kwa kweli hajanidhuru" Dokta Pendo aliongea,



"huyo mwanaume umeshawahi kumuona kabla?" Sajenti Minja aliuliza,



"ile sura ndiyo naiona leo, ila nikikutana nae mahala popote nitamkumbuka" Dokta Pendo aliongea na wakati Sajenti Minja alikuwa akiinuka,



"silaha yangu ipo wapi? au wameichukua?" Sajenti Minja alimuuliza Dokta Pendo,



"hiyo hapo chini ya meza" Dokta Pendo alijibu na kisha Sajenti Minja akainama na kuichukua, akaiweka kiunoni,



"kama nilivyokwambia kule ofisini, ukimuona tena huyu mwanamke au huyo mwenzake aliyekuja kumuokoa, nijulishe" Sajenti Minja alimkumbusha Dokta Pendo,



"usijali Kaka yangu, nitakutaharifu" Dokta Pendo alijibu, kisha Sajenti Minja akatoka zake nje huku akiwa amejishika kisogoni.



Sajenti Minja alivyotoka tu, Dokta Pendo akaenda kumchungulia kwa dirishani na kushuhudia Sajenti Minja akiingia kwenye gari yake na kuiondoa.



"mbona Sarah mtu mwema tu? Au hata kama ana ubaya wake hajawahi kunifanyia mimi, aliniteka na akanipa sababu za kuniteka, nikamuelewa na akanirudisha salama, sasa kwanini nimsababishie matatizo?" Dokta Pendo alijiuliza mwenyewe huku akiwa bado yupo pale dirishani.



Baada ya kukaa kwa muda pale dirishani, akaamua aende zake chumbani.



Akafika na kuvua zile nguo alizitoka nazo hospitali, kisha akaingia bafuni kuoga.



**********************



Usiku huu Sarah alirudi nyumbani kwake huku akiwa hamuamini kabisa Dokta Pendo, ingawa alimsaidia ila alipanga kujihadhari sana mbele ya Dokta Pendo ingawa alitaka kujenga urafiki ili amuamini ila aliamua kukaa nae mbali.



Mawazo hayo yote alikuwa anayawaza huku akiwa juu ya sofa ndani kwake. Ila kumbuka siku nzima ya leo hajaingia katika chumba chake cha siri kumuona Taita, aliyafanya yote kwa makusudi kwa ajili ya kumtesa Taita na njaa, aliamini kufanya hivyo kunaweza kumpa nafasi nzuri ya kumuuliza Taita na kujibu vizuri kutokana na njaa ambayo atakuwa nayo mjomba ake huyo.



Sarah akaitoa bastola yake na kuiweka juu ya meza, kisha akavua raba zake.



"hata leo sitoenda kumuona, acha akae na njaa ili aone watu masikini wanavyotesekaga na njaa" Sarah aliongea kisha akamalizia na sonyo kali, akanyanyuka kwenye kochi na kuingia chumbani kwake kwenda kupumzika.



********************



Asubuhi Sarah aliamka mapema na kufanya mazoezi kama kawaida yake, hutumia masaa mawili kufanya mazoezi mchanganyiko, baada ya hapo akaenda bafuni kujiswafi mwili wake, bafuni hutumia saa moja.



Akishatoka bafuni huenda sebuleni na kuwasha runinga, kisha huangalia taharifa ya habari na mambo mengine ya kisiasa, hapo pia hutumia saa moja na nusu, kisha huzima runinga na kuwasha radio kwa ajili ya kusikiliza mziki laini ambao hutumika kumuweka vizuri akili yake.



Ilipofika saa tatu na nusu, aliingia jikoni na kuandaa kifungua kinywa, baada ya dakika thelathini alimaliza na kwenda kwenye kabati na kutoa kikombe, akarudi jikoni na kumimina maziwa kwenye kikombe, akapakua na tambi na kuelekea moja kwa moja kwenye chumba chake cha siri, ambapo alimfungia Taita.



Alipofungua tu mlango wa kile chumba, akawasha taa na kumfanya Taita afunge macho kutokana na macho yake kukosa mwanga kwa muda mrefu.



Sarah akaingia na kuvuta kiti kisha akakunja nne na kuanza kula huku akimuangalia tad Taita,



"husikii njaa?" Sarah alimuuliza Taita ambaye alikuwa akimuangalia kwa tabu,



"wewe Sarah we ndio wa kunifanyia hivi?" Taita aliuliza huku akimtazama Sarah,



"leo ndio umejua mimi naitwa Sarah? Si uwa unaniitaga malaya? Uwa nafurahi zaidi ukiniita malaya" Sarah aliongea huku akitabasamu,



"wewe ni mwanangu, kipindi nakuita malaya nilikuwa bado sijakutambua" Taita alijijitea



"nina maswali mawili tu kwako, la kwanza, kwa nini umemteka babu yangu?" Sarah aliuliza,



"nilimteka kwa sababu nilitaka nionane na wewe" Taita alijibu,



"haya tumeshaonana, ulitaka kuniambia nini?" Sarah aliuliza swali Lake la pili,



"nilitaka nikuombe msamaha kwa kile kilichotokea miaka kumi na tisa iliyopita" Taita alijibu,



"kwanza kabla hatujaendelea zaidi, nahitaji nyumba ya babu yangu mliyoichoma moto ijengwe" Sarah aliongea kisha akanywa maziwa,



"hiyo nyumba ikijengwa ndio utaniachia?" Taita aliuliza,



"ndio, endapo nyumba itajengwa nitakuachia" Sarah alijibu na kumfanya Taita atamani hata nyumba ijengwe ndani ya siku moja,



"kwanini nisinunue nyingine kwa jina la babu yako?" Taita aliuliza



"ni wewe tu, ili mradi babu yangu akitoka apate pa kuishi" Sarah alijibu,



"nisaidie simu niongee na Trigger" Taita aliongea,



"unataka kuongea nae nini?" Sarah alimuuliza,



"nataka nimwambie afanye hiyo kazi ya kununua hiyo nyumba leo hii hii ili mimi niwe huru" Taita aliongea,



"ngoja nimpigie" Sarah aliongea huku akiitoa simu yake mfukoni na kupiga namba ya Trigger, Trigger alipopokea, Sarah akampa simu Taita, Taita akaanza kuongea kwa kujuliana hali na kijana wake huyo kisha akamsisitiza sana akachukue pesa bank,



"nikachukue shilingi ngapi?" Trigger alimuuliza Taita,



"akachukue shilingi ngapi?" Taita akamuuliza Sarah,



"million sitini, nadhani nyumba ya million sitini itakuwa bomba zaidi" Sarah alimjibu Taita,



"Trigger akatowe million sitini" Taita alimpa jibu Trigger,



"alafu nazipeleka wapi?" Trigger akauliza,



"kanunue nyumba popote" Taita alijibu,



"lete hiyo simu" Sarah aliongea huku akimpora Taita simu,



"wewe mtumwa wa Taita, hiyo pesa inabidi unikabidhi usiku wa leo" Sarah aliongea na Trigger baada ya kumpora simu,



"sawa, tukutane wapi?" Trigger alijibu kwa sauti tulivu,



"nitakuambia baadae, ila naomba msifanye ujanja ujanja wowote, vinginevyo nitammaliza bosi wenu" Sarah Alimwambia Trigger,



"amini hakuna ujanja wowote utakaofanyika, ukija unachukua pesa yako na kuondoka" Trigger alijibu kwa upole, kisha Sarah akampa simu Taita na kumwambia awatahadharishe vijana wake wasifanye kitu chochote cha tofauti pindi atakapoenda kuchukua hiyo pesa usiku.



"Trigger huyu Sarah atakapokuja kuchukua pesa naomba msimgeuke wala msimshike, maana huku roho yangu nimeiweka rehani" Taita alimsihi Trigger,



"hatutakuwa na shida, aje na achukue huo mzigo" Trigger alijibu kisha Sarah akampora Taita simu na kobonyeza kitufe cha kukatia mawasiliano.



"hilo la Kwanza likiisha bila shida, kuna la pili" Sarah aliongea huku akinyanyuka kwenye kiti,



"la pili lipi tena? Si baada ya kupata pesa utaniachia?" Taita aliuliza,



"sio baada ya kupokea pesa, baada ya kupata nyumba ndio nitakuachia" Sarah aliongea huku akiondoka, na kumuacha Taita asijue la kuongea, baada ya muda Sarah alirudi akiwa na chakula na kukiweka mbele ya Taita, kisha akamfungua kamba.



"kula mjomba, nitarudi baadae" Sarah aliongea kisha akazima taa na kutoka zake nje akimuacha Taita akiwa hana la kuongea.



******************



Muda wa saa tano usiku, Sarah akiwa amevaa kikazi aliegesha gari yake, kisha akashuka na kutembea mwendo wa dakika ishirini na kuingia kwenye jengo moja la ghorofa ambalo halijakamilika.



Alipanda mpaka juu ya ghorofa na kumkuta Trigger akiwa ameshika begi jeusi kubwa,



"naona umekuwa sasa" Trigger aliongea huku akimuangalia Sarah,



"nimefuata pesa, sihitaji habari nyingine" Sarah aliongea huku akiwa amesimama,



"chukua hizi hapa" Trigger aliongea na kumtupia Sarah lile begi, Sarah akalidaka na kuanza kuondoka. Wakati akiwa amepiga hatua tatu, mbele yake waliibuka vijana kama ishirini wote wakiwa na bastola, alipogeuka nyuma akakuta vijana wengine wengi wakiwa wamesimama na Trigger na wote wana bastola,



"wewe unadhani mjanja nani kati yetu na wewe?" Trigger aliuliza huku akiijaza bastola yake risasi.........





http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"unafikiri unaweza kunifanya chochote?, jitathimini mtumwa mkubwa wa fikra wewe" Sarah aliongea huku akimtazama Trigger,



"mwachieni njia aondoke" Trigger aliongea huku akitabasamu kwa dharau, vijana wakaacha njia Sarah akapiga hatua tano mbele, kisha akamgeukia Trigger na kuichomoa bastola yake,



"nasikia unaweza kuchezea sana silaha, ipo siku nitakufundisha namna nzuri ya kucheza nazo" Sarah aliongea huku akiirusha rusha bastola yake na kipindi hicho Trigger alikuwa anatabasamu tu.



Sarah akageuza shingo yake na kuondoka, akakatiza pale pale katikati ya vijana wa Taita na kutelemka mpaka chini ya ghorofa.



"tumfuatilie?" Tekso alimuuliza Trigger,



"hapana, kufanya hivyo ni sawa na kumuua Taita" Trigger alijibu,



"si tutamfuatilia bila yeye kujua" Tekso aliongea,



"sio mjinga huyo, atakuwa ameweka mitego yake ili kujua tutafanyaje baada ya yeye kuondoka? Huoni hata alivyokuwa akijiamini?" Trigger aliuliza na kufanya wenzake wakubaliane nae.



"kwa hiyo tutegemee boss ataachiwa lini?" Strategic aliuliza,



"nadhani ni leo au kesho, lakini bado sina uhakika sana kwa sababu mwenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Sarah mwenyewe" Trigger alizungumza,



"lakini hela si tumempa? Kwanini asimuachie sasa?" kijana mwingine aliuliza kwa jazba,



"hela ni nini kwani? Hapa tunazungumzia mamlaka na wala sio pesa" Trigger aliongea huku akimuangalia yule kijana,



"ila naamini hawezi kumdhuru" Tekso aliongea,



"kumdhuru kwa kweli hawezi, kwa sababu babu yake tunaye, ila bila hivyo huenda hata Taita angekuwa marehemu muda huu" Trigger alijibu huku akielekea kwenye ngazi za kushukia kwenye lile ghorofa ambalo halijakamilika na wenzake wakamfuata kwa nyuma.



"kwa hiyo sisi tunatakiwa tufanye nini kwa muda huu?" Tekso aliuliza,



"kukaa na kusubiri" Trigger alijibu huku akiwasha sigara yake.



****************



.

.



Sarah alipochukua pesa wala hakutaka kuhakikisha kama zipo sawa, alibeba begi akaondoka zake, hakwenda moja kwa moja kwenye gari lake, alichofanya aliingia katika kichochoro kimoja na kuangalia ni kipi vijana wa Taita watafanya?



Baada ya dakika kumi za Sarah kubana pale kichochoroni, aliweza kuwaona vijana wa Taita wakitoka ndani ya lile jengo bovu, akawashuhudia wakiingia kwenye gari na kuondoka, Sarah akaendelea kubana kwa dakika kumi nyingine huku akitazama usalama wake, alipojiridhisha yupo salama, alitoka kichochoroni huku akiwa na begi lake lililojaa pesa. Akatembea kwa mwendo wa nusu saa na kuikuta gari yake, akapanda na kutulia kwa dakika kumi nyingine kwa lengo lile lile la kuangalia usalama.



Alipoona pako sawa, akawasha gari yake na kuiondoa kwa mwendo wa taratibu, njiani alikuwa makini kuangalia vioo vya pembeni vya gari ili kuona kama kuna gari inamfuata, lakini hakufanikiwa kuona kitu.



Sarah aliingia kwake saa za usiku sana, alipofika aliingiza gari yake kwenye uzio wa nyumba yake, na kisha akaingia ndani, akapitiliza moja kwa moja chumbani na kutupia kitandani lile begi lililokuwa limejaa pesa, kisha akavua nguo zake za kazi na kujitupa kitandani, alipanga Kulala tu muda huo, mambo mengine alipanga kuyafanya siku inayofuata.



****************



Asubuhi ya leo Sajenti Minja aliamka na wazo la kwenda ofisini kwa Taita, maana yake siku iliyopita alimpigia sana simu Taita kwa namba aliyopewa kule Vin hotel, lakini simu ya Taita haikuwa ikipatikana.



Sajenti Minja aliamka na kujifanyia maandalizi ya mwili, kisha akaondoka zake mpaka kwenye jengo moja kubwa katikati ya mji lililokuwa na jina Dennis tower, kumbuka jina halisi la Taita ni Dennis, hilo Taita alipewa kutokana na pesa alizokuwa nazo.



Sajenti Minja aliegesha gari yake nje na kisha akaingia ndani ya lile jengo, akaelekea sehemu ya mapokezi na kueleza shida yake, akaambiwa apande mpaka ghorofa ya kumi na mbili ndipo zilipo ofisi za mkurugenzi wao, Sajenti Minja akapanda lift mpaka ghorofa ya kumi na mbili na kisha akaanza kusoma vibao vya juu vya kila ofisi, mpaka alipofika kwenye kibao kilichoandikwa "PRESIDENT" akatabasamu na kugonga mlango, mtu aliyekuwepo ndani akaitikia, Sajenti Minja akaingia ndani na kumkuta mtu wa makamo akiwa amekaa juu ya kiti ambacho mbele kulikuwa na meza, huyo mtu hakuwa Taita, maana Sajenti Minja anamfahamu vizuri Taita ingawa hawana na ukaribu. Sasa huyu aliyekuwepo mbele yake ni Harry, alikuwa yupo bize na computer,



"karibu ukae" Harry aliongea huku akiendelea kubofya,



"asante, nina shida na Taita, sasa sijui nimemkuta?" Sajenti Minja aliuliza,



"huo sio utaratibu kijana, utaratibu ni kujitambulisha kwanza, alafu ndio unasema shida yako" Harry aliongea huku akijitahidi kuonesha tabasamu,



"naitwa Joel Minja, ni askari kutoka kituo kikubwa cha polisi, nina shida na Taita" Sajenti Minja aliongea,



"shida ya kiofisi au binafsi? Kama shida ni ya kiofisi hata mimi naweza kukusaidia" Harry aliongea huku akapata uoga baada ya kujua huyo kijana anayeongea nae ni polisi,



"ni shida binafsi" Sajenti Minja aliongea na kufanya Harry wasiwasi umuongezeke zaidi,



"kama ni shida binafsi huyu bwana hayupo, amesafiri ameenda nje ya nchi" Harry alijibu kwa utulivu,



"atarudi lini?" Sajenti Minja aliuliza,



"kwa kweli hakuna anaejua, kwa sababu huyu bwana uwa hasemi siku atayorudi" Harry alijibu,

.



"sawa, nashukuru kiongozi, nadhani nitarudi tena siku nyingine" Sajenti Minja aliongea huku akinyanyuka kwenye kiti,



"sawa, karibu tena" Harry aliongea huku akimpa mkono Sajenti Minja, kisha Sajenti Minja akaondoka zake huku akiwa na imani kuwa ni kweli Taita amesafiri, kumbe yupo tu nchini ila ametekwa.



Hata baada ya Sajenti Minja kuondoka bado Harry hakuwa na amani kabisa, muda wote alikuwa anajutia maisha yake ambaye aliishi nyuma, alikuwa anaumiza kichwa sana ili aweze kujinasua kwenye kundi la Taita, lakini alishindwa kutokana vitisho alivyopewa na Taita, maana aliambiwa yoyote atakayeisaliti vita wanayoshindana na Sarah, ni lazima afe.



Baada ya muda mrefu wa kutafakari, Harry aliamua ni bora wote wafe, yaani Sarah na Taita, na aliona kwa kuwa Taita ametekwa muda huu na hajulikani alipo, ni bora aanze na Sarah.



Akaichukua simu yake na kupiga namba anayoijua,



"hey Aisha, habari yako?" Harry aliongea baada ya simu kupokelewa,



"poa, naongea na nani?" Aisha alijibu upande wa pili,



"ina maana namba yangu ulifuta?" Harry aliuliza,



"kuulizana ulizana ni kupoteza muda, sema wewe ni nani?" Aisha aliuliza huku akionekana hajapenda maswali,



"Mimi Harry, mwanasheria" Harry alijitambulisha,



"ooh kumbe wewe, leo umenikumbuka boss?" Aisha aliuliza huku akicheka,



"kuna mission nataka nikupe, upo wapi?" Harry aliuliza,



"nipo mjini, Wewe upo wapi?" Aisha aliuliza,



"nipo mjini, kama inawezekana tuonane muda huu?" Harry aliongea,



"njoo nipo hapa Rock restaurant, uje boss wangu" Aisha aliongea,



"poa, nakuja" Harry aliongea na kukata simu, kisha akainuka na kuelekea kwenye gari lake.



Aisha ni msichana ambaye historia yake hajulikani, ila walikutana na Harry katika mambo yao ya kazi haramu, huyu Aisha alikuwa ni mtu anaetumwa kufanya kazi za kuua, hukodiwa na watu tofauti wa mataifa mbalimbali kwa ajili ya kazi hiyo.



Harry alifika rock restaurant na kuangaza angaza akaweza kumuona Aisha Akiwa amekaa, akamfuata kisha wakakumbatiana kwa furaha,



"unakunywa nini?" Aisha aliuliza,



"maziwa fresh" Harry alijibu kisha Aisha akaenda kumuagizia na kurudi,



"najua umeniitia kazi, haya niambie" Aisha aliongea huku akitabasamu,



"Kuna mwanamke ananinyima raha, nataka ummalize" Harry aliongea,



"demu wako nini?" Aisha aliuliza huku akicheka,



"hapana, we fanya kazi tu, hupaswi kujua kingine" Harry alijibu,



"million hamsini ipo?" Aisha aliuliza,



"pesa sio kitu, mimi nataka furaha tu" Harry alijibu



"una picha yake?" Aisha aliuliza, Harry akatoa simu na kumuonesha picha ya Sarah,



"mrembo kabisa huyu, anapatikana wapi?" Aisha aliuliza,



"huo ndio mtihani, utatumia mbinu unazozijua wewe kumpata, kwa mimi sijui anapokaa" Harry alijibu,



"dah, poa, tanguliza malipo ya hawali, million thelathini, alafu nyingine utamalizia baada ya kazi " Aisha aliongea,



"Mimi nakupa pesa yote, sitaki kutoa nusu nusu" Harry aliongea,



"sawa boss, nitakutumia namba ya account yangu kwenye simu yako, Wewe unachotakiwa ufanye ni kunirushia hiyo picha ya huyo dada" Aisha aliongea,



"poa, tutawasiliana" Harry aliongea kisha akanyanyuka na kuondoka zake.



****************



Mishale ya mchana Aisha akiwa kwenye duka la silaha aliweza kumuona msichana akiingia hapo, alimpomtazama hakuwa mgeni kwake, ndipo alipotoa simu yake na kuiangalia, alikuwa ni Sarah, Aisha akatabasamu.



Sarah alielekea moja kwa moja kwa muuzaji na kumsabahi, kisha akaingiza mkono mfukoni na kutoka na risasi,



"risasi ya namna hii naweza kuipata hapa?" Sarah aliuliza,



"hiyo hamna dada yangu, hazipatikani kabisa" muuzaji alijibu kisha Sarah akaondoka zake, Aisha akaanza kumfuatilia kwa nyuma.



Sarah alipotoka hapo alielekea kwenye mgahawa wa jirani na hapo, akaagiza chakula na kula taratibu.



Muda huo Aisha nae aliingia ndani ya mgahawa huo na kuagiza juisi.



Sarah alipomaliza kula, akanyanyuka na kuelekea chooni, Aisha nae akamfuata.



Sarah akiwa chooni anajiangalia kwenye kioo, alishangaa mtu akisimama nyuma yake na kutabasamu, Sarah akageuka haraka na kumuangalia,



"hujambo mrembo?" Aisha aliongea huku akimsogelea Sarah, tena usogeleaji wa kishari. Sarah akaona bora aondoke, wakati akapiga hatua ili aondoke alikamatwa shingo na Aisha, Sarah akarusha ngumi ikadakwa kisha akapigwa pingu ya mkono mmoja, aliporusha ngumi ya pili ikadakwa na kuunganishwa katika pingu na mkono wa hawali, Sarah akakosa ujanja.



Alipojaribu kurusha teke, Aisha alimdhibiti kwa kumbana ukutani na kisha akatoa kisu chake mfukoni,



"wewe ndio unasumbua mabosi mjini?" Aisha aliuliza huku akitabasamu kisha kisu akakiweka shingoni kwa Sarah, akaanza kukikandamiza taratibu na damu ikaanza kumchuruzika Sarah, Sarah machozi yakaanza kumtoka na kuona ndoto yake ya kulipa kisasi ikimalizwa chooni, tena na mwanamke mwenzake ambaye hata hamjui.......





Ila kile kisu hakikuingia sana shingoni mwa Sarah, kiliingia kidogo na ndio maana kikasababisha ile damu shingoni mwa Sarah.



Aisha akakitoa kile kisu shingoni kwa Sarah na kisha akamuachia Sarah miguu yake, Aisha akaelekea moja kwa moja sehemu ambapo ziliwekwa toilet paper, akakata kipande kidogo na kisha akafutia damu iliyokuwepo kwenye kisu chake.



Muda wote Sarah alijitahidi kujishika shingoni na Mikono yake ingawa alifungwa pingu.



"bahati yako bado sijalipwa pesa yangu, maana siuagi mtu bila kukamilishiwa madai yangu ya hawali" Aisha aliongea huku akimfuata Sarah, alipomfikia alifungua pingu alizomfunga na kuziweka mahali pake, Aisha akawa anapiga hatua ili aondoke, Sarah akamuwahi na kumrushia teke, Aisha akamkwepa, Sarah akaona Kama amedharauliwa vile kwa kufanyiwa udhalilishaji ule na Aisha.



Sarah akarusha ngumi, Aisha akaikwepa tena na kufanya mkono wa Sarah uangukie mgongoni kwake, alichokifanya Aisha ni kukimata kichwa cha Sarah na kukibamiza kwenye kioo cha pale chooni, mpaka kile kioo kikapasuka,



"hao wapuuzi wanavyokusifia nilidhani labda unajua sana kupambana, kumbe fala tu" Aisha aliongea huku akijipangusa mikono yake kisha akawa anatoka zake kuelekea nje.



Sarah akajibandua pale kwenye kioo na kuona damu kidogo ikimchuruzika kwenye kichwa juu ya sikio, akatoa kitambaa chake na kujifuta, kisha nae akatoka nje, ndipo alipomshuhudia kwa mbali Aisha akiondoka kwa mwendo wa madaha huku baadhi ya wanaume wakwale wakimtupia jicho la matamanio kutokana na umbo lake la kike kumvaa vyema, Sarah akajikuta anawachukia wale wanaume bila ya sababu ya msingi,



"wangejua kuwa lile lijanamke ni likatili wala wasingethubu kuliangalia kwa matamanio hivyo" Sarah aliongea peke yake na kumalizia na sonyo la chini chini.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Sarah nae akaamua aelekee nje ili kumuwahi Aisha ili amfuatilie anapoelekea. Sarah akatembea kwa mwendo wa haraka mpaka nje ya mgahawa, akatupa jicho kushoto hakumuona Aisha, akatupa jicho kulia pia hakuona mtu, akasimama kwa muda huku akijilaumu kwa kuchelewa kutoka nje, mwisho nae akaamua aondoke zake, akaelekea sehemu alipoegesha gari lake, uwa anaegesha mbali sana na eneo ambalo huenda.



Sarah alivyopotea eneo lile ndio muda ambao aliibuka Aisha baada ya kujificha katika kichochoro kimoja eneo lile, Aisha uwa hatumiii gari pindi anapokuwa mjini, uwa anatumia njia za mkato sana, ni mwanamke ambaye amezoea sana maisha ya uswahilini na hata tabia zake ni za kiswahili tu.



Aisha alipotoka mafichoni, aliangalia uelekeo alioelekea Sarah kisha akatabasamu huku akitikisa kichwa, alafu mdogo mdogo akaingia zake kichochoni na safari ya kwenda anapopajua yeye ikaanza.



*****************



ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog