Search This Blog

Sunday 20 November 2022

NYUMA YAKO (4) - 2

 





    Simulizi : Nyuma Yako (4)

    Sehemu Ya Pili (2)







    “Nawe umeanza kutapika?” Marshall akauliza. “Nilidhani ni mzoefu!”



    Kelly akauweka mfuko kando kisha akajifuta mdomo wake kwa mgongo wa kiganja. Akamtazama Marshall kisha akatazama chini na kuvuta hewa ndefu kwa pua yake nyembamba.



    “Ni nini unataka Marshall?”



    “Sikaribishwi?”



    Marshall akasonga karibu na mwanamke huyo. Akamtazama kidogo na kumuuliza, “Kwanini Abdulaziz alitoa amri uuawe?”



    Kelly akabinua mdomo wake. Akajifuta tena na mgongo wa kiganja chake na kutulia.



    “Kuna tatizo lolote? Tujuze. Unajua tupo pamoja kwenye hili.”



    Mara boti ikayumba kwanguvu! Ni kheri walikuwa wamejishikiza. Angalu boti ilivyotuliatulia, Kelly akamtazama Marshall na kumwambia kwa sauti ya chini,



    “Sijui ni nini kinatokea. Huenda Abdulaziz akawa ameshamshtukia Marietta.”



    “Kivipi? - ulisema yeye hajui kama unamtumikia?”



    “Sijui, Marshall! Nami nipo njia panda kama wewe. Tutakapofika nchi kavu nitawasiliana na Marietta nipate kujua.”



    Kukawa kimya.



    “ … Pengine Captain alimwambia tupo zaidi ya idadi,” Kelly akaongezea maneno. Mara hii Marshall akawa kimya kumtazama Kelly kwa umakini. Mwanamke huyo alikuwa anaonekana hayuko sawa. Uso wake ulikuwa kielelezo.



    “Kelly, kuna shida yoyote?”



    Kimya.



    “Kelly, unaweza uka-share nasi. Tupo kwenye boti moja.”



    Kelly akamtazama Marshall usoni. Macho yake yalikuwa yamelegea kiasi. Mdomo wake ulikuwa wazi akihema.



    “Nataka tu kuwa mwenyewe, Marshall. Hilo tu.”



    Marshall akanyanyuka.



    “Tutaonana baadae!”





    **http://pseudepigraphas.blogspot.com/





    Saa kumi na moja asubuhi …





    “Nasemaje! --” Abdulaziz akafoka. “Sitaki kusikia mtu yeyote amegusa nchi kavutokea huko baharini isipokuwa kwa bandari pekee!” mate yalikuwa yanamruka toka kinywani. Macho yalikuwa yamemtoka.



    “Ongezeni walinz bandarini na pwani yote!” aliposema hayo akapachika simu mezani. Akang’ata meno yake na kunyanyua tena simu kumpigia Jamal.



    “Bado!!” alifoka haswa. “Jamal, Jamal, kama hao watu hawatapatikana kwa siku ya leo. Utafute mahali pa kujifichia. La sivyo ni----” simu ikakata -- tiii-tiiii!



    “Pumbavu!” akatusi. Akaweka namba tena na kupiga. Namna alivyokuwa anabonyeza namba hizo ni kana kwamba anataka kutoboa simu.



    Simu ikaita pasipo kupokelewa. Akatusi na kutusi kupita kiasi.



    **



    “Jamal, anachosema Mahmoud kina ukwel wowote?”



    Kwenye sebule hii ya kifahari walikuwapo watu wanne: wa kwanza alikuwa ni Aziz, crown prince, pili bwana Mahmoud, tatu Jamal na nne mpambe wa Aziz, bwana Ramadan.



    Aziz, mwana wa mfalme anayeandaliwa kupokea madaraka, alikuwa amevalia kanzu yenye darizi za dhahabu. Mkono wake wa kushoto ulikuwa na saa aghali mno. Miguuni alikuwa amevaa sendozi zilizosanifiwa kwa ngozi ya simba.http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Kitendo cha bwana Mahmoud kuwapo hapa, kulikuwa ni kumaanisha kuwa mpango wa ule wa bwana Aziz waliokuwa wameuadhimia ulikuwa umetimia.



    Mahmoud alifanikiwa kuonana na bwana Ramadan na kumpa kila ‘sumu’. naye bwana Ramadan, akitaka kuonekana mtu mtenda kazi, akafikisha habari upesi kwa ulimi wake. Sasa alikuwa hapa akitazama kwa macho yake makubwa namna mambo yanavyoenda.



    “Ni kweli kabisa,” akasema Jamal. “Abdulaziz anataka madaraka yako kwa njia yoyote ile. Na hapa tuongeapo, anamshikilia bwana yule wa Marekani akilenga kumtumia kama ushawishi kwenye kikao cha hadhara.”



    Basi bwana Aziz kusikia hayo, akaamuru Abdulaziz akamatwe mara moja na aletwe mbele yake upesi!



    **





    Baada ya lisaa limoja tangu kikao kihairishwe …



    “Kama haya yote yakija kuwa kweli, basi utakuwa na nafasi kubwa sana,” alisema bwana Ramadan. Kinywa chake kilikuwa wazi kwa furaha. Macho yake yalikuwa yamebebelea ahadi.



    Ingawa akiwa anaongea, alikuwa ameweka mkono wake kwenye bega la Mahmoud. Walikuwa wapo koridoni wakitembea pasi na haraka.



    “Unasema kweli?” Mahmoud akauliza. Uso wake ulikuwa unaonyesha anajua jibu. Alikuwa anasanifu.



    “Kweli kabisa!” Ramadan akaapa kwa kuchinja shingo yake na kidole. “Nasema kweli tupu, kweli kabisa, Mahmoud! Umekuwa rafiki yangu sasa, tutasaidiana sana mbeleni. Vivyo ndo’ maisha yalivyo!”



    Wakapeana mikono.



    “Tutaonana muda si mrefu, Ramadan,” Mahmoud akasema akitikisa kichwa.



    “Insha-allah. Hakikisha unakuwa karibu na mawasiliano.”



    “Bila shaka.”



    Basi Mahmoud akaenda zake. Kwa usalama wake akawa amekabidhiwa wanaume wawili wa kumlinda. Walikuwa wamebebelea bunduki wakivalia sare za jeshi. Wanaume hao akaongozana nao kwa kama nusu njia kabla hajawataka waende zao kumwacha peke yake.



    “Una uhakika?”



    “Yah. Nitakuwa salama, nashukuru.”



    Mahmoud akaendelea na safari yake akitumia usafiri wa umma. Alipokuwa chomboni, akapigiwa na Marietta. Punde akapokea na kuweka simu sikioni.



    “Wamefika,” sauti ya Marietta iliteta kwenye simu.



    “Umeshaonana nao?”



    “Hapana. Ndo nafanya namna hivi sasa.”



    “Sawa. Utanambia kitakachotokea.”



    “Wewe upo wapi?”



    “Njiani. Nadhani kila kitu kimeenda sawa.”



    Simu ikakata.



    Mahmoud akaendelea na safari yake. baada ya mwendo wa kama lisaa hivi, mara gari likasimama. Kulikuwa na foleni hapo ndefu kidogo.



    Kwa mbele kidogo barabarani kulikuwa na kizingiti. Magari yalikuwa hayapiti hapo pasipo ukaguzi. Hapo kwenye kizingiti walikuwapo wanajeshi kama nane kwa idadi. Walikuwa wamebebelea bunduki na nyuso zao zikiwa ni za kazi.



    Haikuwa inafahamika nini wanachokisaka.



    Basi muda kidogo tu ukapita hapo, kwa kupitia maneno ya watu ndani ya basi bwana Mahmoud akatambua kuwa msako huo ulikuwa umeanza jana yake na hakuna mtu anayetambua haswa ni nini mabwana hao wanachokitafuta.



    Wanachokifanya ni kukagua ndani ya gari na pia sehemu ya mizigo. Huwataka watu wanyooshe nyuso zao juu na hata kutoa vitambulisho vyao vya uraia mara moja.



    Endapo kama mtu ni mgeni basi atahojiwa kwa muda mchache kabla ya kuachiwa huru.



    Basi likasonga kidogo mbele. Bwana Mahmoud akawa anajiuliza kichwani mwake juu ya msako ule. Kwakuwa alikuwa ameketi dirishani, basi akachomoza kichwa chake na kuangaza.



    Akaona namna ambavyo wanajeshi wanavyowashusha watu kwenye baadhi ya magari na pia wanavyopekenyua kila kona ya usafiri. Kidogo akapata shaka.



    Kichwani mwake akaanza kuunda mawazo ambayo yalimtaarifu kuwa hayuko salama. Hivyo kidogo akanyanyuka na kuanza kusonga kuelekea mlangoni. Akashuka toka kwenye gari na kutazama kule mbele kwenye kizingiti.http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Pasipo kurejesha tena uso huko, akayeya zake!



    Lakini mmoja wa mabwana wale waliokuwa wanahusika na kulinda pale kwenye kizingiti, alimwona bwana Mahmoud akiwa anatembea kwa kasi kwenda mbali zaidi na walipo.



    Basi akamshtua na kumjuza mwenzake. Upesi mwanajeshi aliyekuwa amebebelea kipaza sauti akatupa sauti yake kumtaka huyo mwanaume asimame mara moja hapohapo alipo!



    Mahmoud asijali, akaongeza mwendo maardufu! Na isipite muda akaanza kukimbia kwa kadiri ya miguu yake. Alishikilia kanzu yake akikata mitaa haswa.



    Baada ya kama dakika moja tu, magari mawili ya jeshi yakaanza kumfukuza. Ilikuwa ni jijini. Haikuwa rahisi sana kwa magari kupenya baadhi ya maeneo ambayo Mahmoud aliyakatiza.



    Na kwa kutumia nafasi hiyo Mahmoud akajibana kwenye uchochoro na kutulia hapo tuli. Punde gari lililobeba wanajeshi likakatiza kwenye barabara ya mbele likiwa linaenda kwa mwendo wa wastani.



    Wanaume wawili walikuwa wanarusha macho yao kumtafuta mlengwa lakini hawakufanikiwa. Mahmoud alikuwa amejibana kana kwamba mtoto mdogo nyuma kidogo ya ndoo ya kuhifadhia takataka!



    Gari lilipopita, akatoka papo na kuchungulia. Alipoona hewara, akachoropoka kukimbilia mbali zaidi.





    **



    Zii-ziii-ziiii! Zii-ziii-ziiii! Simu ilinguruma kwenye mfuko wa Marietta. Mwanamke huyo alikuwa amevalia nikabu nyeusi akiacha macho peke yake kuonekana.



    Alisimama akachomoa simu yake mfukoni na kutazama. Alikuwa ni Mahmoud.



    “Kuwa makini, wanajeshi wametapakaa ndani ya jiji,” Mahmoud alitahadharisha.



    “Wa upande gani?” Marietta akauliza. Macho yake yalikuwa yanatazama kukagua usalama.



    “Sijajua wa upande gani lakini si salama kukutwa na wa upande wowote ule kwa sasa.”



    “Nilidhani umeyaweka sawa na Aziz!” Marietta alinong’ona akikazana.



    “Shanny, hamna mtu anayejua kuhusu wageni wako. Ulitaka nisemeje kuwahusu?”



    “Sawa. Nikukute wapi?”



    “Ngome ya zamani,” Mahmoud akajibu na simu ikakatwa. Marietta akaendelea na safari. Muda kidogo akakutana na wageni wake ndani ya boti, Marshall na wengineo. Wakaungana kwa pamoja kuchukua taksi kuwapeleka kule kwenye ‘Ngome ya zamani’ kama ambavyo Mahmoud alivyoagiza.



    “Poleni, ilikuwa bahari rafu sana. Natumai mpo salama. Karibuni Morocco,” alisema Marietta kwa sauti. Taksi ikaenda kidogo kwenye lami kabla ya Marshall kuulizia usalama wao ndani ya jiji.



    “Ilikuwa almanusura huko baharini. Hawakutaka kuelewa wala kuskiza. Laiti tusingekuwa na plan ya pili basi kazi nzima ingeishia huko,” alisema Kelly.



    Marietta akatabasamu kidogo, ungeweza kuhisi tabasamu lake hilo kwa kutazama macho yake. Alitazama nyuma kwa kupitia ‘sight mirror’ - kioo kinachoning’inia kwenye paa la gari kisha akasema,



    “Najua mngedumu. Msingeweza kufa upesi hivyo!”



    “Ni nini kinatokea?” Kelly akadadisi. “Mbona walikuwa wakaidi?”



    “Ni bayana kuna mpasuko hivi sasa. Unajua ni ngumu kuelewa kila kitu kinavyoendelea ndani ya nchi kwa sasa. Jambo hili linaweza likawa jema kwetu kama tukilifanya likatunufaisha!”



    “Kivipi?” Marshall akauliza.



    “Ngoja tuone,” akajibu Marietta. “Hapa si sehemu sahihi kuzungumza.” akisema vivyo akamtupia jicho dereva.



    Basi taksi ikaendelea kusonga.



    Wakatembea kwa kama dakika nane kabla ya taksi kujikuta lipo kwenye foleni. Ilikuwa ni foleni ndefu kiasi. Ilikuwa pia ni ya ukaguzi!



    Marietta akatazama kwa mbele na kubaini uwepo wa wanajeshi wawili wenye silaha. Wanajeshi hao walikuwa wanapita kutazama gari moja baada ya jingine. Kwa magari makubwa walikuwa wanazama ndani na kwa yale madogo basi wakiinamisha kichwa kuangaza.



    Alipotazama nyuma, hakukuwa tena na nafasi ya kutoka. Tayari magari matano yalishaweka uzio nyuma ya taksi!



    “Dereva, hatuwezi tukachoropokea njia ya kurudi?” Marietta akauliza. Macho yake yalikuwa hayatulii. Alishahisi ukosefu wa amani ndani ya nafsi yake!



    Dereva akamtazama kwa mshangao kidogo,



    “Tutarudije?” akauliza na kuongeza, “Unaona njia ya kurudi ilivyojaa alafu mbele kuna ukaguzi!”



    “Tafuta namna!” Marietta akabweka. Macho yake yalitoka kumtazama dereva kwa kitisho.



    Lakini kiuhalisia hakukuwa na namna hapa. Upande wao wa kushoto ulikuwa unapitiwa na watu wengi wanaotumia miguu. Upande wao wa kulia kwenye njia ya kurufi pia kulikuwa kumetingwa na magari mengi.



    Dereva angelifanyaje?



    “Namna gani madam? Nitapita wapi hapa? Nitapaa?”



    Marshall akatazamana na Danielle kisha na Jack. Vifua vyao vilikuwa an fukuto kiasi.



    Mara Marietta akatoa bunduki na kumwonyeshea dereva, kisha akafoka,



    “Utafanya nitakachokuambia, sawa!?”



    Dereva akahofu sana. Pumzi yake ilibadili kasi na mikono yake ikatetemeka. Hakuwa anajua cha kufanya. Lakini pengine hakuwa na haja ya kujua cha kufanya kwani angelipewa maelekezo na ‘mtekaji’ wake.



    “Sawa!” akasema akitikisa kichwa. “Sawa, sawa, nitafanya!”



    “Haya geuza gari upesi turudi tulipotoka!” Marietta akaamuru.



    “Hapana!” Marshall akapaza sauti. “Hamna haja ya kufanya vivyo.”



    “Tufanyeje?” Marietta akamtazama mwanaume huyo kwa maulizo.



    “Hataweza kugeuza gari kabla hatujakamatwa,” akasema Marshall. “Nyuma kuna gari ipo karibu mno, na mbele pia. Akiwa anahangaika kutoka tutakamatwa kwa upesi zaidi!”



    “Sasa tufanyeje?” Marietta akapaza. “Tukae hapa kungoja kukamatwa?”



    “Ni salama zaidi wakija kuliko tukitoroka hapa,” Marshall akapendekeza, “Wapo wawili, tunaweza kuwamudu kama kukiwa na ulazima huo!”



    Kabla Marietta hajafanya jambo, akamtazama Danielle, Jack na kisha Kelly. Akatazama na mbele yao. Wanajeshi walikuwa magari matatu tu mbali na wao.http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Akashusha pumzi na kutulia. Damu ilikuwa inazunguka kwa wepesi mwilini.



    Baada ya kama dakika sita, mwanajeshi mmoja akawa ameshafika kwenye dirisha la gari yao. Bwana huyo akainama na kutazama waliomo ndani.



    Dereva alikuwa anachuruza jasho haswa. Macho yake alikuwa ameyakodoa na pumzi yake iko ‘marathon’. Ukimtazaa vidole vyake vya mkononi, vilikuwa vinatetemeka!



    “Hey, uko sawa?” afisa akamuuliza dereva. Dereva akatikisa kichwa pasipo kusema jambo.



    “Afisa, mimi ni mwongoza watalii,” akasema Marietta, “Hawa ni wageni wetu tokea Uingereza nikiwaonyesha mandhari ya jiji letu.”



    Afisa akawatazama tena Marshall na wenzake kisha akarejesha macho yake kwa Marietta.



    “Fungua nikuone uso wako!” akaamuru.



    “Hapana, afisa. Siwezi nikafanya vivyo,” alisema Marietta. Alijua fika angeacha uso wake bayana basi angetiliwa shaka. Hakuna mtu asiyejua uso wa mke wa Raisi, ama tuseme wa aliyewahi kuwa Raisi wa Marekani.



    “Nimesema fungua nikuone. Sitarudia mara mbili!” afisa akafoka. Basi taratibu Marietta akaupeleka mkono wake kwenye bunduki.





    **





    Kabla hajafanya jambo basi bwana yule mwanajeshi akajikuta akipokea muito toka kwenye ‘radio call’. ilikuwa ni sauti nzito kidogo na ilikuwa inasikika vema toka kwenye chombo.



    “Sitisha mara moja zoezi hilo!” sauti ilisema toka kwenye radio call. “Narudia, sitisha mara moja zoezi hilo!”



    Ilikuwa ni agizo toka kwa mkuu! Nani atabisha? Basi upesi bwana huyo mwanajeshi akasitisha zoezi lake na kwenda kukutana na mwenzake kumpasha habari.



    Tunatakiwa kusitisha zoezi letu mara moja!



    Hiyo ikawa salama ya Marietta na watu wake. Na basi watu hao wakaelekea moja kwa moja kule kwenye ‘Ngome’ ambapo ndipo Mahmoud alipomwelekeza mwanamke huyo.



    Huko kulikuwa ni jumba fulani lililotekelezwa. Jumba hili lilikuwa ni kuukuu haswa.



    “Kama nilivyokueleza, Aziz ameshatoa amri ya kukamatwa kwa Abdulaziz hivyo tungoje tuone itakavyokuwa,” akasema Mhmoud.



    “Hapana!” Marietta akatikisa kichwa. “Huu ndo muda wa kufanya kazi yetu inavyotakiwa Mahmoud. Wakati hawa ndugu wakiwa wamekorofishana. Haufikirii vivyo?”



    Mawazo hayo ya Marietta yakaungwa mkono na wote. Sasa ni wafanye namna kumkomboa mume wa Marietta katika muda huo.



    “Sasa tutampatia wapi?” akauliza Marshall. Hapo hata Marietta akamtazama Mahmoud. Ni yeye ndo’ alikuwa na taarifa zaidi kuhusiana na hilo.



    “Kuna sehemu mbili nipadhaniapo. Moja kwenye makazi yake ya zamani, pili kwenye makazi yake mapya. Hamna sehemu nyingine anaweza mficha mtu zaidi ya hapo.”



    “Una uhakika?” Danielle akauliza. “Kama ni moja ya kiongozi mkubwa si kwamba atakuwa ana maeneo kadha wa kadha?”



    “Ni kweli lakini Abdulaziz si mtu wa kujiamini sana na watu wanaomzunguka. Huamini mikono yake kuliko ya mtu mwingine. Huko nilipotaja ni sehemu bora zaidi kuanzia.”



    Wakakubaliana kufanya kazi hiyo kesho punde pale jua litakapozama. Ni misheni kubwa inayofanyika mahali penye ulinzi mkali hivyo yawapasa kujipanga haswa.



    “Nna hoja,” akasema Danielle. “Kama Abdulaziz akikamatwa na Aziz kama ambavyo imedhamiriwa, si kwamba itakuwa hatari zaidi kwetu kumpata mlengwa wetu? Hamwoni kama Aziz anaweza kutumia nafasi hiyo kujinufaisha?”



    Hoja hiyo ikazua maneno miongoni mwao. Ilikuwa na kweli ndani yake. Habari inaweza ikabadilika kabisa punde Aziz atakapomweka Abdulaziz mikononi. Hakuna aliyekuwa na uhakika na masaa machache mbele yao.



    Vipi Aziz akitumia mwamvuli huo kwenye mvua hii?



    Sasa?



    “Tutafanya leo usiku,” akasema Marietta. Akamtazama Mahmoud na kumuuliza, “Sawa?”



    Mahmoud akashusha pumzi ndefu asiseme jambo.





    **



    Ndani ya usiku huu mambo hayakuwa madogo. Bwana Marshall pamoja na wenzake walikuwa tayari wameshasonga kwenye eneo la tukio, makazi ya bwana Abdulaziz, kwa ajili ya kutekeleza kazi yao.



    Kwa ujumla alikuwapo Kelly, Danielle, Marietta, Mahmoud na Marshall mwenyewe. Watu hawa walikuwa kwenye gari umbali mfupi tu toka kwenye kasri ya mlengwa wao.



    Walishavalia nguo za kazi na vifaa pia wanavyo. Walibebelea bunduki na kwa mkono wake bwana Mahmoud alikuwa ameshatengeneza gesi ya sumu kwa ajili ya kazi.



    Gesi hiyo alikuwa ameihifadhi kwenye mtungi mkubwa mweusi. Mtungi huo haukua wenyewe, lah! Kulikuwa pia na mitungi mingine minne, yani kwa kila mmoja.



    Basi punde wakavaa vinyago vya kujikinga na madhara ya sumu kisha wakashuka wote isipokuwa Mahmoud. Yeye aliacha kwenye usukani. Watu hao kwa utulivu wakajongea zaidi na zaidi kufuata eneo walilolenga.



    Ndani ya kasri …



    Bwana mmoja mlinzi aliyekuwa amevalia nguo za jeshi alikuwa yu kwenye zamu. Bwana huyo alikuwa na mustachi mpana na mrefu. Macho yake yalikuwa ya kufumba na mwendo wake ulikuwa mpana ndani ya buti.



    Alisonga akitazamatazama usalama. Uso wake ulikuwa wa kazi haswa. Nyuma yake kwa kama hatua kumi na tano alikuwa amesimama mwenzake pia kuhakikisha usalama.



    Basi bwana huyu mwenye mustachi akaendea kona na kuikata. Ilikuwa ni ubavuni wa mashariki wa kasri Alipotembea kidogo akahisi harufu fulani asiyojua inatokea wapi.



    Akavutavuta harufu hiyo akijitahidi kuitambua ni ya nini, mara kidogo akadondoka chini kama mzigo, akaachama kinywa na macho akayarembua.



    Yule mwenzake aliyekuwa nyuma yake kwa hatua kadhaa naye akasonga mbele zaidi akielekea upande alodondokea mwenzake. Hakuwa na hili wala lile.



    Alipiga hatua kujongea konani lakini kabla hajafika akahisi harufu pia. Hakuwa anajua harufu hiyo ni ya nini. Alipomaliza kona akamwona mwenzake akiwa yu chini!



    Upesi akachomoa ‘radio call’ yake atoe taarifa lakini kabla hajafanya hilo akajikuta akiihttp://pseudepigraphas.blogspot.com/shiwa nguvu! Macho nayo yanapoteza uwezo wa kuona. Kidogo akadondoka chini kama mwenzake na akawa kimya tuli!



    Basi zikapita dakika kadhaa. Harufu ile ikazidi kusambaa ndani ya makazi. Taratibu lakini kwa uhakika. Watu waliokuwa wamejifunika vinyago vya kujizuiza walikuwa wana ‘pump’ gesi toka kwenye mitungi yao mgongoni!



    Ndani ya kasri, kwa juu kabisa, kulikuwa na wanaume walinzi wawili ambao nao walikuwa wanafanya doria ya kuhakikisha usalama. Mabwana hao walipotazama chini wakabaini kuna wenzao walikuwa wamejilaza chini.



    Walijaribu kuwasiliana nao kuona nini tatizo lakini hakukuwa na mrejesho. Ingali bado hawajatambua vema ni nini kinachoendelea, ukizingatia mabwana hao hawakuwa wanaathirika na gesi ya sumu huko juu, wakadhamiria kutoa taarifa mbali zaidi kuhusu tukio hilo.



    Lahaula! Kabla nao hawajafanya jambo wakatunguliwa na risasi. Risasi ya masafa ya mbali.



    Risasi hiyo ilitumwa na mwanaume Mahmoud aliyekuwa ameketi ndani ya gari kwa kutumia bunduki ya mdunguaji. Bunduki yenye kioo cha hadubini kali inayoweza kuvuta vitu vya mbali kwa ukaribu bora kabisa.



    Basi ndani ya dakika kumi na tano tu, kasri nzima ikawa ndani ya himaya ya wavamizi. Walikuwa wameshika kila pembe walinzi wakiwa hoi chini.



    Marshall pamoja na wenzake wakakagua chumba kimoja baada ya kingine kumtafuta ‘mtu wao’. Kwenye moja ya chumba kilichopo chini kabisa. Chini. Huko wakakuta mabaki tu ya nguo lakini kusiwe na mtu,



    “Hayupo hapa!” akasema Marietta. Kwakuwa alikuwa amejivika kinyago, sauti yake ilikuwa ya kunguruma. “Upesi tutoke na kwenda mahali pengine!”



    Sasa wakatoka humo ndani upesi. Wakatembea makoridoni na kupita milangoni wakiwaruka wajakazi waliokuwa chini na pia walinzi waliokuwa hoi.



    Walipofika kwenye gari wakajipaki na Marietta akamtaka Mahmoud awapeleke kwenye eneo la pili. Huko wakaendeleze msako.



    “Hata Abdulaziz hayupo?” akauliza Mahmoud.



    “Hayupo,” Marietta akajibu. “Nyumba nzima imekaliwa na walinzi na pia vijakazi!”



    Mahmoud akatia neno, “Hata wale walinzi si wa Abdulaziz. Watakuwa wametumwa hapo na Aziz kutazama usalama!”



    Basi wakatimka.





    **







    “Naomba uniletee kahawa hivi sasa!” alisema Azizi akimwagiza kijakazi. Bwana huyo alikuwa amekunja nne akiwa ameketi kwenye kiti chake cha thamani. Alikuwa amevalia suruali nyeusi maridadi na shati jeupe la dizaini ya kupendeza.



    Begani upande wa kulia kulikuwa na michirizi mekundu mitatu iliyoshuka mpaka kifuani mwake, na kwenye kola ya shati kulikuwa kumedariziwa na rangi ya kijani.



    Rangi hizo zilikuwa zinawakilisha bendera ya Morocco.



    Mbele yake alikuwa ameketi mpambe wake, bwana Ramadan. Bwana huyo alikuwa amevalia kanzu ya njano iliyofifia na kizibao cheusi pamoja na kofia yake.



    Meza ndogo ya kioo iliyokuwa mbele yao ilikuwa tupu.



    “Nashindwa kuelewa shida ni nini?” akasema bwana Aziz. “Mpaka sasa hivi Abdulaziz hajapatikana. Hii si ishara nzuri kabisa.”



    “Usijali, mwana mfalme. Abdulaziz atatapatapa tu lakini mwisho wake ni uleule. Kama si hivyo basi ataishi maisha yake kama digidigi. Hamna haja ya kuhofia kabisa!”



    “We unadhani atakuwa wapi kwa sasa? - kwenye makazi yake yote hakuwapo!”



    “Atakuwa anarandaranda huko kwengine. Lakini yatupasa tuwe makini sana. Kuna namna Abdulaziz akawa anapata maneo haya. Najua jeshini kuna watu ambao ni watiifu kwake, watu wa kutoka upande wa kabila la mama yake.”



    “Unataka kusema Jamal?”



    “Hapana. Jamal yu tayari upande wetu lakini kuna watu wengine mbali na yeye.”

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Aziz akaguna. Akakuna kidevu chake na kuwaza kidogo.



    “Unajua sitaweza kukaa kwa amani mpaka bwana huyo atakapokuwa mikononi mwangu. Kila muda unavyosonga nahisi kuna jambo.”



    Ramadan akatabasamu.



    “Jambo gani mwana wa mfalme? Hakuna kitakachotokea kipya. Abdulaziz hana nguvu kama yako kwa watu na wala serikalini.”



    “Unadhani vivyo?”



    “Ndio. Hata wewe unalijua hilo.”



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog