Search This Blog

Sunday, 20 November 2022

NJIA NYEMBAMBA (2) - 4

 





    Simulizi : Njia Nyembamba (2)

    Sehemu Ya Nne (4)







    Ndio, kwa mujibu wa ratiba alikuwa yu sahihi. Saa yake ya mkononi ilimwambia ni saa tano asubuhi na sasa ilikuwa imebakia nusu saa tu ya yeye kuwa njiani kabla hajafika eneo analotakiwa kuwepo kwa ajili ya misheni.





    Akiwa ndani ya gari, alikuwa anatafakari. Ingawa mipango yake yote ilienda sawa, bado alikuwa na shauku la hofu. Hakutaka kufeli hata kidogo. Kwa namna yoyote ile aliadhimia kufanikisha aliyoyapanga, tena kwa muda.





    Ni siku moja tu nyuma, alimpata askari magereza, anayehusika na gereza linalomhifadhi Rose, na kumpatia pesa nyingi kwa ajili ya kumsaidia kwenye haja yake ya kumtorosha mwanamke huyo. Kwa donge hilo nono la pesa, askari alishindwa na tamaa, akaweka bayana taarifa nyeti.





    Hivyo basi Kone alikuwa anajua fika, wafungwa kadhaa watakuwa njiani wakipelekwa kufanya kazi za jamii mahala fulani. Na ndani ya gari hilo, atakuwapo Rose. Askari alimhakikishia hilo. Lazima atakuwepo, na kwa data zaidi atakuwepo kiti cha mwisho upande wa dirisha la mkono wa kulia.





    Kone akiwa ndani ya muda, alifika ndani ya msitu mwepesi barabara ikatizapo. Alifungua buti ya gari akatoa mtungi wa gesi alioulaza chini kana kwamba umetupwa. Alijiingiza kwenye gari lake na kujitokomeza mitini usijue kama yupo maeneo hayo.





    Iliwahi kusemwa; hakuna haraka Afrika: no hurry in Africa, msemo huu ulikuwa na kweli ndani yake. Kone alionekana kuusahau ama kutoujua kabisa. Alizingatia muda pasipo kujua kama anaowangoja watakuwa watiifu wa muda kama aenendavyo. Alingojea kwa masaa, kiasi kwamba akahisi ameachwa kwenye mataa. Ila moyo wake ulimpatia subira akaendelea kungoja.





    Ikiwa ni majira ya saa nane mchana, gari kubwa aina ya Fiat, kuukuu rangi ya bluu inayofanana na nyeusi, linachipuka na kushika barabara. Ubavuni lilikuwa kimeandikwa MAGEREZA kwa rangi nyeupe isiyo na nakshi. Madirisha yake yalikuwa ya wavu wa chuma. Vioo vyake vya mbele ya dereva vilikuwa vichafu huku kifuta maji na uchafu, ama waipa, kikiwa kimoja tu.





    Ndani ya gari hilo kulikuwa kuna wafungwa wanawake. Walionekana hovyo haswa. Walikuwa wamevalia nguo nyeusi zenye mistari meupe ambayo ilikuwa imefifia kwa uhaba wa matunzo.





    Askari walikuwa watatu ndani ya gari hilo mbali na dereva, wawili walikuwa na bunduki. Ajabu askari mwanamke alikuwa mmoja tu, tena mikono tupu. Alikuwa ameketi karibu na dereva akitazama mbele kana kwamba anasafiri kwenda kumsalimu mjomba kijijini.





    Gari lilisonga. Lilipokatiza mtungi wa gesi, askari mmoja alipaza sauti kuamuru lisimame. Askari huyu alikuwa amevalia sare chakavu, suruali yake ilikuwa ina kiraka pajani. Viatu vyake vilijaa kama mtumbwi. Alishuka akaufuata mtungi ule wa gesi na kuupakiza ndani.





    "Mali hii!" Alisema askari huyo akitabasamu. Wenzake hawakuhangaika naye, wakaendelea na kazi na safari yao.





    Walitembea kwa muda mfupi, mara gari likapoteza mwelekeo. Lilivamia miti ya kando na kukomea hapo. Uso wote wa gari wa mbele uliharibika vibaya, dereva akiwa mahututi. Paji lake la uso lilichanika na kuchuruza damu pomoni.





    Hakuna mtu yeyote aliyekuwa anajielewa ndani ya gari. Ni punde, Kone anaingia ndani ya chombo hicho na kuangaza. Alikuwa amevalia kinyago cheusi usoni. Mkono wake wa kuume ulikuwa umebebelea bunduki ndogo.





    Alimuona Rose kule kule alipopewa maelekezo, haraka akamfuata na kumbeba. Alimhamishia kwenye gari lake kisha akatimka toka eneo hilo upesi. Kasi yake ilikuwa inatisha.









    Bado siku haikuwa imeisha. Jua lilikuwa linaelekea kuzama anga likiwa jekundu kwa kufifia. Ndege walikuwa wanajirudisha viotani, na baadhi ya watu pia wakijirudisha kwenye maskani zao.





    Kulikuwa ni tulivu sana juu ya uso wa Liberia. Tulivu haswa isiyo na shari. Na pengine kuna waliodhani tulivu hiyo ingeendelea kudumu. Bahati mbaya walikosea. Tulivu hii ilikuwa inawindwa, na muda mchache mbeleni ilikuwa inaelekea kuvunjwa.





    Wanaume wawili waliokuwa wamevalia vinyago vyeusi, waliwasili karibu na nyumba ndogo kimipango iliyokuwa imezibwa kwa uzio wa bati. Nyumba hiyo ilikuwa ni ya rangi ya bluu iliyofifia. Ilikuwa na kibaraza kidogo chakavu kinachomkaribisha mgeni mlangoni.





    Wanaume hao waliovalia vinyago, walitazamana, wakatikisa vichwa. Migongoni mwao walikuwa wamebebelea vibegi vidogo tusivyojua vina nini. Walisukumiza mlango mdogo wa geti ukafunguka, wakazama ndani.





    Hawakufika mbali, mara wanashtuliwa na sauti kali ya mlio wa mbwa. Alikuwa ni mbwa mkubwa mweusi upande wao wa kushoto. Masikio yake yalikuwa yamesimama kama kidaka mawimbi. Sauti yake kubwa na nzito ilifoka kwa wingi. Alibweka akiwa amesimama, na akitazama mlangoni.





    Wanaume hawa hawakumuona mbwa huyu kabla ingali walipembua mazingira. Labda kwasababu ya uweusi wa mnyama huyo na uhaba wa mwanga hapo nje. Kulikuwa kuna taa moja tu. Mwanga wake ulikuwa mkali ila haukutosha kumulika eneo lote vema.





    Ilibidi haraka maamuzi yafanywe. Mwanaume mmoja alipeleka mkono wake pajani, mara akachomoa kisu alichokitupa kwa ustadi kumfuata mbwa, kisu kikazama kifuani mwa mnyama huyo na kumwangusha chini. Kukawa kimya.





    Haraka mbwa alihamishwa toka eneo la wazi, halafu wanaume hao wakajongea kuufuata mlango. Wakiwa wanajisogeza, walisikia sauti ya vishindo vya miguu inakuja mlangoni. Haraka wakabana ukutani.





    "Nimemsikia bobby anabweka!" Sauti ya mtoto wa kiume ilivuma.





    Mlango ulifunguliwa, kikachomoza kichwa cha mvulana. Kwa makidirio alikuwa na miaka saba. Macho yake yalikuwa makubwa, alivalia jezi nyekundu ya mpira. Aliangaza macho yake kumtafuta mbwa, mara akadakwa na kuzibwa mdomo kwanguvu.





    "Shhhh! ... tulia!" Aliamriwa kwa kunong'onezwa. Wanaume walizama ndani, mmoja akiwa amembana mtoto huyo. Sasa mikononi mwao walikuwa wamebebelea bunduki ndogo; aliyembana mtoto akiielekezea kwenye kichwa cha mateka wake huku mwenzake akiielekezea wanapoelekea.





    "Chini! Chini! Lala chini!" Amri ilitolewa. Kulikuwa kuna watu watatu sebuleni: mama mmoja mtu mzima, takribani miaka sitini na kitu, akiwa na watoto wawili mapacha wa kike mwenye makadirio ya miaka kumi na mitatu.





    Wote walilala chini upesi. Walishajawa na hofu juu ya uhai wao. Mikono vichwani. Mioyo ilikuwa inakimbia marathon. Mtoto yule wa kiume naye aliamriwa alale chini, haraka akatii.





    "Mwenye nyumba yupo wapi?"

    "Yupo kazini baba!" Aliwahi kujibu mama.

    "Anarudi saa ngapi?"





    Kulikuwa kimya kidogo. Jibu lilibanwa na kigugumizi. Kabla halijalazimishwa kutoka, sauti ya geti ilisikika. Wavamizi wakatazamana. Si bure akili yao iliwaambia mtu wanayemhitaji ndiye anakuja sasa, hivyo basi ilibidi wafanye kitu.





    Mwanaume mrefu mweusi aliyevalia sare za jeshi la Liberia, alikuwa ameingia ndani ya eneo hilo la nyumba. Mkono wake wa kushoto ulikuwa umebebelea mfuko mweusi wa nailoni. Mwendo wake ulikuwa mkakamavu, akisafisha koo mara kwa mara kutoa ishara ya mwenye nyumba kuwasili.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Mwanaume huyu alikuwa miongoni mwa wale waliofanya oparesheni kabambe ya kutokomeza kijiji cha wanamgambo wa AMAA. Alikuwa ni msaidizi wa oparesheni hiyo ya siri iliyoleta mafanikio makubwa. Damu aliyokuwa ameimwaga kwa ajili ya nchi na kiongozi wake, sasa ilikuwa inataka kumtokea puani.





    Mazingira ya nyumba yalikuwa kimya mno, kiasi akashangazwa. Ila hakutaka kujisumbua sana na hilo. Alitafakari kwa sauti;

    "Wamelala au?"





    Alikaribia mlangoni, kabla hajafungua mlango, akastaajabu kwa kutikisa kichwa;

    "Yani hata mbwa hawajamfungulia!"





    Bwana huyu hakuwaza mara mbili juu ya usalama wake na wa familia; sababu kubwa ilikuwa ni kutodhani kama ana sababu ya kufanya hivyo. Hakufikiri kama bado yupo vitani, alidhani vita imeshakwisha. Walishammaliza adui kwa milipuko ya mabomu na ncha za risasi, waliamini.





    Alitengua komeo la mlango akazama ndani. Kutazama, uso kwa uso na mdomo wa bunduki.





    "Karibu kaburini!" Alipokelewa kwa maneno ya shombo. Aliamriwa anyooshe mikono juu, akatii. Aliomba familia yake iachwe salama maana haina makosa, lakini hakuna aliyesumbuka kumsikiliza.





    Mwanamke yule wa makamo pamoja na watoto walifungwa kamba na kuzibwa midomo. Nyenzo zilitolewa toka kwenye mabegi. Walipofungwa walifungiwa vyumbani, wanaume wale wakibakia na mwanaume waliyemfuata.







    "Ukidhani umemaliza kazi, mzee?" Alisema mwanaume mmoja akichomoa pande la kisu toka begini.





    Walimfunga mikono mateka wao na kumpigisha magoti. Walimbandikia pia plasta kubwa mdomoni rangi ya silva.





    "Sasa mtakufa mmoja mmoja kama kuku!"

    Walimkata shingo mwanaume huyo wakimchukua filamu. Baada ya hapo waliutoa mwili wake na kuutupia chumbani. Kisha wakaondoka zao.





    Ni kwamba wakati tukio hilo likiwa linafanyika upande huu wa dunia, na mengine pia ya aina hiyo hiyo yalikuwa yanaendelea ndani ya muda huo huo upande mwingine wa shilingi. Wanaume hawa waliovalia vinyago vyeusi walikuwa kumi kwa idadi, na kwa mujibu wa orodha yao, watu waliotakiwa kumalizwa usiku huo ni wanajeshi watano, hivyo basi walijigawa wawili wawili kwa kila tageti.





    Harakati hizo za mauaji zilifanikiwa kwa kuwamaliza wanajeshi wanne, mwanajeshi mmoja akiponea chupuchupu. Kuna aliyeuawa karibu na maeneo ya bar, mwingine akiuliwa na kutupwa misituni, na mwenginewe akimalizwa kandokando ya barabara kwa njia ya risasi. Ilitegemea na wapi mlengwa alikutwa na kikosi cha umauti.





    Kwa namna moja sasa Mr. X akawa amerejesha tabasamu lake usoni, ingawa kumkosa huyo mmoja ilimuuma mno. Laiti isingelikuwa mwanajeshi huyo alipata udhuru wa ghafla wa safari, basi kwa sasa ingelikuwa simulizi tofauti. Simulizi ya ushindi mnono kwa Mr. X.





    "Si mbaya, maana hata sisi hawakutumaliza wote," alisema Mr. X. Mwanaume ambaye kwa sasa alikuwa na kikosi cha watu kumi na tano pekee, wanaume alionusurika nao kwa kujilaza ndani ya mahandaki siku ya mashambulizi.





    Wanaume hawa walikuwa kumi na tano, ila shughuli yao ni pevu. Walikuwa wamefundwa katika ujuzi wa kijasusi maridhawa. Walikuwa ndio wanaume pekee wanaokuwa karibu na Mr. X kwasababu ya kuaminika kwao kiimani, kiakili na kinguvu.





    Japokuwa walikuwa wachache lakini walimfanya Mr. X awe na kibri. Awe na imani maradufu kwamba anaweza kuiteka Liberia na kuiweka kiganjani.





    "Kesho tutashambulia sehemu nne za makutano kwa kutumia vilipuzi. Nahitaji watu si chini ya mia mbili wawe wameuawa ama kujeruhiwa. Vita yetu ndio imenza rasmi. Na hatutakoma mpaka pale tutakapokuwa tumeitwaa dola ya Liberia," alisema Mr. X.





    Walianisha na kuweka bayana mipango yao ya namna ya kushambulia. Kwa siku hiyo hiyo moja ya kesho, ndani ya muda mmoja, inabidi vilipuzi vyote viwe vimeshafyatuka. Kazi hiyo ilikuwa ni lazima ifanyike, lazima ifanikiwe.







    ***



    Kikao kilihudhuriwa na takribani watu kumi na mbili. Watu hawa walikuwa wamevalia suti nyeusi pasipo tai. Vichwa vyao vilikuwa vimefunikwa na kofia aina ya 'cow boy', wengi wakionekana wameambatana na mikongojo kama miti ya miamvuli.





    Walikuwa wamechukua uwanja wa mkutano unaopatikana juu kabisa ya hoteli ndogo ya kitalii. Eneo hilo lilikuwa ni tulivu na lenye wingi wa upepo. Watu hawa, ambao kwa wingi walikuwa ni watu wazima, walikuwa na nyuso ngumu zinazotisha.





    Wanaume watatu walikuwa wameketi mbele ya wenzao. Walitenganishwa na meza kubwa ndefu ya chuma. Bila shaka wanaume hawa walikuwa ni viongozi. Juu ya meza yao kulikuwa kuna vinywaji kadhaa, vyote vilikuwa vilevi. Ila hawakuwa wamekifungua chochote kile, vyote vilikuwa na mifuniko yake.





    Mwanaume mmoja miongoni mwa hao watatu, alisimama na kusafisha koo lake. Watu wote walimtazama kwa umakini. Aliangaza kila pande kabla hajafungua mdomo wake na kusalimu.





    "Leo tumekutana hapa kwa ajili ya kikao chetu cha pili, kama watu wa Malinke: watawala wakubwa waliowahi kutokea Afrika na duniani kwa ujumla chini ya empaya ya Mali. Lengo letu kubwa ni kutazamia wapi tulipofikia baada ya kikao cha kwanza, na pia wapi tunapotaka kuelekea. Kikao kimefunguliwa."





    Baada ya maneno hayo, muongeaji aliketi, na mara anasimama mwingine wa kando. Anasalimu na kufungua kijidaftari kidogo.





    "Mahudhurio yetu ya kikao kilichopita ilikuwa ni watu saba. Tulipata wasaa wa kujadili mambo kadhaa, hususan, kurudisha nguvu yetu inayoyumbayumba katika dola ya Guinea. Miongoni mwa tuliyokubaliana ikawa ni kuhakikisha kila wizara ya serikali hii mpya, itakuwa na mtu wetu. Lakini kubwa ni kwamba kumteua nani ambaye ataenda kuwa raisi wa nchi hii ya Guinea, yaani atakayesimama kugombea uraisi miezi miwili hapo mbele."





    Kukawa kimya kidogo. Muongeaji alisafisha koo kana kwamba alikuwa amebanwa, kisha akaendeleza soga;

    "Sasa basi kulikuwa kuna watu watatu walipendekezwa na wajumbe. Nao ni Aba, Jatoo na Sisawo. Bila shaka leo tutampata tunayemtaka ili tuanze kuainisha na kutekeleza mipango yetu ya kuhakikisha tunashika dola. Na hilo zoezi ndilo tutakaloanza nalo kwa sasa. Tutapitisha makaratasi na kila mjumbe atatia alama ya tiki kwa mteuliwa anayemuunga mkono."





    Zoezi hili lilidumu kwa takribani dakika tano tu. Kura zilihesabiwa na mshindi akawekwa bayana. Alikuwa ni bwana Sisawo, pande la mtu mweusi mwenye utajiri wa ndevu kipilipili. Bwana huyu ndiye alikuwa mmiliki wa eneo hilo la hoteli ambamo mkutano ulikuwa unafanyika.





    Kufuatia uchaguzi huo, wakateua pia na mawaziri kwa kila nyanja. Watu hawa walikuwa wanafanya haya katika namna ya kujiamini sana. Ni kana kwamba walikuwa tayari wameshashinda uchaguzi.



    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Walimaliza kila teuzi, kabla hawajaendelea zaidi, hoja ilichipuka ndani ya kikao. Mjumbe mmoja alipendekeza kufahamishwa. Aliuliza;

    "Vipi kama tukishindwa uchaguzi huu, kama vile tulivyofanyiwa pambe ya ndere kwenye uchaguzi uliopita?"





    Hoja hii ilizua gumzo. Msimamiaji wa kikao, alisimama na kuwaondoa shaka wajumbe juu ya jambo hilo.





    "Hilo jambo halitatokea. Hilo jambo, kamwe, halitawezekana! Uchaguzi huu lazima tushinde, iwe kwa njia halali ama ya panya. Na tayari tumejizatiti kuhakikisha hilo linatokea. Hapa tunavyoongea, kuna kikundi cha vijana mia moja na hamsini wapo mafunzoni wakijiandaa. Wana mafunzo ya kutumia silaha na mapambano ya vita. Mbali na hapo, tumeshawasiliana na wenzetu waliopo Guinea Bissau, Liberia, Ivory Coast, Mali, Gambia, Burkina Faso, Sierra Leone na Senegali. Wote wapo tayari kutuunga mkono. Lakini sisi pia kama wajumbe, tuna haja ya kutumia nafasi zetu kuhakikisha hilo linawezekana."





    Jibu hilo lilituliza munkari, kikao kikaendelea. Kilidumu kwa muda mfupi mbeleni kabla hakijafungwa na wajumbe kusambaa wakikubaliana kukutana baada ya majuma mawili.





    Wajumbe hao walijitoa jengoni, isipokuwa Sisawo, wakajipakia kwenye magari yao ya kifahari na kupotea eneo hilo.





    Ila kandokando mwa barabara kulikuwa na gari moja dogo, Suzuki Vitara. Vioo vyake vilikuwa vyeusi ti isipokuwa cha mbele atumiacho dereva kuangazia barabara. Gari hilo lilikuwa na rangi ya kijani kilichotota uweusi. Vioo vyote vilikuwa vimepandishwa juu kutokujua aliyemo ndani.





    Punde gari hilo linawashwa na kushika barabara. Linatokomea. Baada ya muda mfupi, simu ya Kone inaingia ujumbe. Kone aliiwahi simu hiyo na kutazama. Namba ilikuwa mpya.





    "Naomba tuonane. Ni jambo la haraka."

    "Wewe nani?" Kone aliuliza kwa ujumbe.

    "Mimi Amadu," akajibiwa baada ya muda mfupi. Alistaajabu. Alijaribu kupiga namba hiyo, haikupatikana. Alituma ujumbe;

    "Upo wapi?"

    Punde akajibiwa; "nipo kila sehemu."









    ****





    Kone akajikuta anatabasamu.





    "Sasa tunakutana wapi?" Alituma ujumbe. Baada ya muda fupi akajibiwa:

    "Nitakuambia karibuni. Ila itakuwa huko huko Sierra ulipo."





    Akatahamaki.





    "Umejuaje kama nipo Sierra?"

    "Nimekwambia nipo kila sehemu, Kone," ujumbe ulimjibu punde, akabakiwa mtupu asiye na maneno. Aliaga ila hakujibiwa tena, maongezi yakawa yamekomea hapo.

    "Amadu," Kone alijikuta akinong'oneza mwenyewe. Alitabasamu kabla hajaiweka simu mezani na kujinyoosha viungo. Ilikuwa ni usiku sasa wa saa moja. Alikuwa ameketi nje ya jengo pembezoni mwa bwawa kubwa la kuogelea.





    Alikuwa amevalia kaptula ya bluu inayokomea magotini. Kifua chake kilikuwa wazi. Alikuwa amejilaza kwenye kajitanda kadogo chembamba chenye michoro ya mistari mistari. Alikuwa hapo kajitandani peke yake.





    Eneo lilikuwa tulivu. Mbali na Kone, ni watu wawili tu ndio walikuwepo hapo, ila wakiwa mbali; walikuwa ndani ya maji wakiogelea. Hawakuonekana hata kama wanajua kama kuna mtu aitwaye Kone amejilaza.





    Hata naya Kone hakuwa anawatambua uwepo wa watu hao. Japokuwa macho yake yalikuwa pale, akili yake ilikuwa ikiwandawanda huku na kule. Alikuwa anatatua baadhi ya mambo kichwani. Na mambo haya yaliongezeka maradufu alipopokea ujumbe toka kwa Amadu.





    "Atakuwa yupo wapi? Anataka kuniambia nini? Mbona kanitafuta? Lazima kutakuwa kuna jambo. Tena hili jambo si haba," alitesa kichwa. Alibadili milalo mara mbili. Alikuja kung'amuliwa mawazoni na sauti ya mkewe, bi Fatma.

    "Mbona umekaa hapa mwenyewe?"

    "Kubadili tu mazingira mpenzi," alijibu kone akijisogeza kumpatia Fursa mkewe aketi.

    "Nimekutafuta ndani. Hukuniambia kama utakuwepo huku," alilalama Fatma.

    "Samahani, mpenzi," Kone akajitutumua kuomba msamaha. Alimshika mkewe mkono akimtazama usoni. Ila Fatma hakuwa anamtazama mwanaume huyo. Macho yake yalikuwa yanaangaza kuwatazama wale waliokuaa wanaogelea.





    Mwanamke huyo alikuwa amevalia gauni refu jekundu. Miguuni alivalia viatu vyeusi vyepesi vya kuchomeka.





    Macho ya Kone yalimjuza mkewe hayupo sawia. Alijua sababu itakuwa ni Rose tu, lakini hakutaka kuliweka hilo bayana. Aliuliza:

    "Mpenzi, nini kinakutatiza?"

    "Hamna kitu, nipo sawa tu," alijibu Fatma.

    Kauli hii aitamkapo mwanamke, inabidi uhofie. Mwanamke akikuambia vivyo basi ujue shida ipo. Na basi kama usipoliendelea kuuliza napo pia atakuchukulia haujali, na hata mwishowe humpendi.





    Kone akiwa tayari ameling'amua hilo, aliketi kitako akasogeza mdomo wake karibu na uso wa mkewe.





    "Nini shida mpenzi. Naomba unishirikishe."

    Kulikuwa kimya kidogo. Fatma alikuwa anatazama maji kana kwamba hajasikia kitu. Alikunjia mikono yake kifuani. Hata na mdomo alikuwa ameuvuta kidogo.





    Alishusha pumzi ndefu kwa pua, kisha akaguna kidogo.





    "Huyo Rose uliyesemea unaenda kumtoa, yupo wapi?" Aliuliza. Bado alikuwa anatazama kwenye maji. Kone alitabasamu kidogo alafu akamkumbatia mkewe kwa nyuma.

    "Nimeshamtoa mpenzi. Sikuona hekima kumleta hapa hivyo ameweka makazi yake sehemu nyingine mbali na hapa."

    "Utaenda kumuona lini?" Fatma aliwahi kuuliza haraka.

    "Nadhani kesho ndio nitaenda kumuona. Nilimuacha apate kupumzika kwanza."

    "Kone," Fatma aliita. Mara hii alimtazama Kone. "Hivi ni lini utaacha huu ukaribu wako na Rose?"

    "Fatma mpenzi," Kone alitikisa kichwa. "Mimi na Rose tunaunganishwa na kazi tu, hamna kingine chochote. Kama ingelikuwa ni kukusaliti, ningelifanya hilo kitambo sana, tena kipindi kile tulipokuwa na mgogoro ndoani. Tafadhali naomba uniamini kwenye hili."

    "Nakuamini sana, Kone,"alisema Bi Fatma. "Usidhani sikuamini, ila naogopa sana kukupoteza. Sitaweza kuishi utakaponiacha, Kone. Rose ni mwanamke mrembo sana, mjuvi na mcheshi. Ni mwanamke pekee aliye karibu na wewe."

    "Mbele ya macho yangu hamna mzuri kuzidi wewe, hakuna. Nilikuona na ndio maana nikapata haja ya kukuweka ndani. Kwangu maana ya mwanamke mzuri ni wewe. Kwangu mfano halisi wa mwanamke mzuri ni wewe, Fatma wangu."





    Fatma alishindwa kuzuia tabasamu usoni mwake aliposikia maneno hayo. Alimtazama mumewe kisha akamzawadia busu juu ya lips.





    "Nakupenda, Kone."

    "Nakupenda pia, Fatma."





    Punde ...





    "Ila mpenzi, fanya tuwe na makazi yetu. Nimechoka kuishi hapa hotelini. Natamani niwe napika na kuandalia familia yangu chakula," alisema Fatma kwa madeko. Alikuwa amejilaza juu ya kifua cha Kone.

    "Hata mimi hilo jambo lilikuwa kichwani. Kuna nyumba moja nimeiona karibu kabisa na maeneo haya, inauzwa. Kesho tutafute muda wa kwenda kuitazama. Ukiridhia, basi tuichukue."





    Fatma alijibu kwa tabasamu pana. Alimbusu mumewe shingoni mara mbili kabla hajajituliza kifuani mwa mwanaume huyo kama mtoto aliyeshiba na kubadilishwa nguo.







    ***



    "Tayari mkuu," alisema mwanajeshi mmoja aliyekuwa amesimama kwa ukakamavu. Macho yake makubwa yalikuwa yanamtazama Al Saed aliyekuwa ameketi ndani ya ofisi yake akitafakari.





    "Sawa, nakuja," alisema Al Saed, mwanajeshi akaondoka. Baada ya muda mfupi Al Saed alinyanyuka kisha akaenda chumba kingine ambapo huko alikutana na watu watatu wakiwa wamejiweka wakimngojea. Mmoja wa watu hao alikuwa ni mwanajeshi yule aliyesalimika kumalizwa na watumishi wa Mr. X.





    Eneo lilikuwa limejengwa katika namna ya mkutano. Meza kubwa ndefu inayong'aa ilikuwa imetapakaa pamoja na viti vikubwa vyeusi vya kurelaksi. Viti vilikuwa takribani kumi na tano kwahiyo basi vingine vilibakiwa tupu kutokana na idadi chache ya watu.





    Al Saed alijiweka kwenye kiti kikubwa kilichokuwa kinatazamwa na vingine vyote. Uso wake ulikuwa umepooza. Alitazama kwanza nyuso za watu waliokuwa wameketi kabla hajasafisha koo lake na kuongea kwa sauti ya kukoroma kana kwamba ametoka usingizini.





    "Nimewaita hapa kufuatia mauaji yaliyotokea jana. Sina haja ya kuelezea zaidi kuhusu hilo tukio, hatuna muda na kila mtu analifahamu. Ningeenda moja kwa moja kwenye hoja. Nimewaita hapa kuniletea mrejesho wa nani anayehusika na haya matukio. Najua mmefanya kazi kwa muda mchache mno ila nategemea mtakuwa mmepata angalau kitu."





    Al Saed aliposema maneno hayo aliweka kituo kirefu, akawatazama wanaume wawili wageni machoni.





    "Johnson, Rambo nipeni majibu. Nataka kumjua ni msaliti gani anayehusika haya mauaji!" Al Saed alibamiza meza kwanguvu.





    Wanaume hao wageni walitazamana, kisha mmoja, aliyekuwa amevalia miwani ya macho akawa wa kwanza kufungua mdomo. Jina lake Johnson.





    "Mkuu, tangu ulipotupatia kazi ya kuwafuatilia wale watu watatu juzi siku ya tafrija, kuna baadhi ya mambo machache tuliyagundua ingawa hatukuwa tumemaliza upelelezi wetu huu. Aidha twaweza kuunganisha taarifa hizi na tukio hilo la mauaji."





    Johnson alifungua faili lake rangi ya kijani iliyofifia. Macho yote yalikuwa yanamtazama akingojewa kwa hamu.





    "Kwa huo muda, yaani tokea juzi usiku mpaka leo hii usiku tukija hapa kikaoni, naweza kusema kwamba naibu wa kamati ya ulinzi wa taifa, ndiye mtuhumiwa wa kwanza na mkubwa kwenye hili. Yeye akisaidiana na mjumbe wa kamati ya ulinzi. Labda kwa kupitia wao wanaweza wakatusaidia kuwajua wengineo."

    "Mmejuaje kuhusu uhusika wao?" Al Saed aliuliza. Macho yake yalikuwa yamejifinyanga yakizama ndani.

    "Huko ndiyo naelekea mkuu," Johnson akadokeza na kisha akaendelea; "Ile siku ya tafrija, naibu wa kamati ya ulinzi alipotoka hapa alilekea kwenye glosari kubwa hapa mjini. Hapo alikaa kwa takribani lisaa limoja. Alikuwa anakunywa mvinyo mmoja mkubwa kwa taratibu mno, na macho yake yakiwa yanasumbuka kutazama mazingira mara kwa mara kama atafutaye jambo. Kila aliyeingia eneo hilo alimtazama na kumpekua."





    Johnson aliposema hayo alionyeshea picha za naibu huyo akiwa hapo glosari. Chini ya picha hizo kulikuwa kuna tarehe ya siku ambazo hizo picha zilichukuliwa.





    "Naibu huyu alikuwa hapa glosari kwa ajili ya kupoteza muda tu. Hakukuwa na la msingi alilokuwa anafanya. Aidha lengo lake lilikuwa ni kupoteza watu wanaomfuatilia, kama watakuwepo. Alikuwa anataka kujihakikishia usalama wake kwanza kabla hajaendelea na oparesheni zingine."





    Johnson akatoa picha zingine na kuzionyeshea. Picha hizi zilikuwa zinamuonyesha Naibu akiwa akiwa anatembea sasa kutoka glosari.





    "Baada ya Naibu kumaliza mvinyo wake, alitoka glosari hapo akitumia njia ya uchochoro. Alilaghai kama anaenda chooni, lakini akakatiza kando na kuiruka fensi ndogo ya maua ya glosari. Alielekea mpaka kwenye kibanda cha simu za jumuiya kinachopatikana karibu na glosari hiyo. Aliacha gari lake kwenye parking. Na hii ndiyo inayotoa picha halisi kwamba alikuwa amefuata simu pale, na si kinywaji.





    Sema maswali yanakuja, kwanini aliacha gari lake parking na kwanini alilifanya tendo hili kwa usiri hivi? Kwanini pia alikuwa anaenda kutumia simu ya jumuiya na si ya mkononi?





    Yote haya ni kuhakikisha usiri. Usiri ambao ndio unazua maswali na kuzaa mashaka.





    Aliongea kwenye simu kwa dakika kadhaa. Bado alikuwa anatazama tazama kuhakikisha usalama."





    Johnson alitoa tena picha akaonyeshea. Zilikuwa mbili kwa idadi. Zilikuwa zinamuonyesha Naibu huyo akiwa kwenye kibanda cha simu akitazama nyuma.





    Kwa namna picha hizo zilivyokuwa zimepigwa, zinaweza kukuachia maswali juu ya uweledi wa mpigaji wake. Zilipigwa katika namna ambayo ilimtoa vizuri mhusika, tena kwa usiri mkubwa mno!





    "Alimaliza kuongea na simu akarejea glosari. Alikaa hapo na punde akaondoka zake kurudi nyumbani," Johnson alimalizia taarifa yake hiyo akafunga faili.

    "Kama unavyojua mkuu, ni ngumu kupata taarifa za mteja anayetumia simu za vibandani. Na hili ndilo haswa lengo la Naibu kutekelezea mawasiliano yake kibandani hapo."

    "Sawa sawa," Al Saed alisema akitikisa kichwa. Alishusha pumzi ndefu kabla hajauliza:

    "Na vipi kuhusu huyo mjumbe?"





    Hapo Rambo, mwanaume aliyeketi karibu na Johnson, akateka zamu. Alifungua faili lake rangi ya chungwa akisema:

    "Mjumbe nitakayemuongelea hapa ni huyu." Rambo alionyeshea picha. Al Saed aliitazama akiendelea kuskiza.

    "Mjumbe huyu kuhusika kwake kunarandana na na yule wa kwanza ambaye ni Naibu wa kamati ya ulinzi. Huyu mjumbe ndiye alikuwa mtu wa kwanza kabisa kukutana na Naibu wa kamati ya ulinzi. Alikutana naye asubuhi na mapema jana. Lakini pia baada ya matukio, yani jioni wakakutana tena. Na mpaka tunakuja kwenye kikao, wamekutana tena majira ya mchana."





    Rambo alitoa picha tano akazionyeshea.





    "Mara ya kwanza walikutania nyumbani kwa Naibu, kama unavyoweza kuona hapo picha ya gari la mjumbe likiingia ndani ya jengo la Naibu. Ila mara zilizofuata wamekuwa wakibadili maeneo. Wamekuwa wakikutana kwa siri, na mara ya tatu walipokutana kuna mwanaume mmoja mgeni walikuwa naye. Alikaa kwa muda mchache akaondoka,"





    Rambo akaonyeshea picha.





    "Huu ukaribu wa hawa watu, na vikao vyao kwa muda mchache hivi, vinasababisha mashaka na hata kutufanya tuwatuhumu kwa pamoja."





    Al Saed alichukua mafaili yote, la Rambo na Johnson, akayaweka karibu naye. Alivunja kikao kwa kutoa agizo la watuhumiwa wote kutiwa nguvuni mara moja. Lakini pia akamteua mwanajeshi yule mnusurika, James Peace, kuwa msimamizi wa usalama tangu muda huo.





    "James, bila shaka umehama makazi na umedumishiwa usalama maradufu. Nataka hawa washenzi waliobakia wamalizwe upesi! Chagua wanaume kumi unaowaamini, kwenye kikosi chochote kile. Hakikisha mnapanga mipango yenu na kuja kuniona. Mtashirikiana pamoja na Rambo na Johnson."





    Al Saed akasimama.





    "Haya, twende msibani sasa."





    Wakiwa wanatoka, wanakutana na askari mwanajeshi mmoja aliyewahi kupiga saluti na kusimama kwa ukakamavu. Askari huyo mwanaume alikuwa mweusi. Uso wake ulikuwa umejaa umakini jasho likimchuruza.





    "Vipi?" Al Saed alitahamaki.

    "Mkuu!" Askari alipaza sauti. "Tumeshambuliwa mara nne kwa mabomu. Mji unateketea!"







    ****





    Kwa kutazama tu uso wa Al Saed ungelifahamu ni kwa namna gani habari hizo zilimgusa. Macho yalimtoka na uso ukawa mweusi kwa haraka mno. Kwa muda alichanganyikiwa akiwa hajui la kufanya. Alisaga meno akikunja ngumi.





    "Sawa, tutacheza kwa mujibu wa ngoma!" Alijikuta akisema.





    Mara aliamuru naibu mwenyekiti wa kamati ya ulinzi pamoja na mjumbe mtuhumiwa wauawe, tena kwa kunyongwa, punde tu baada ya kuwafanyia mahojiano. Hakutaka hata kuwatia machoni.





    "James!" Aliita. "Hamna muda wa kujiandaa tena. Kakusanye watu wako na muanze oparasheni mara moja!"





    Aliwatazama Rambo na Johnson, nao akawaambia:





    "Unganeni na James. Malizeni wale wasaliti kisha mkakate vichwa vya hao magaidi na kuniletea hapa!"





    Haraka James na wenzake wakatoka kwenda kutekeleza amri. Al Saed alirudi ndani akajiandaa na kutoka kwenda kufanya ziara maeneo yaliyorudhika na milipuko.





    Loh! Ilikuwa inatisha kuona. Jiji la Monrovia lilikuwa linateketea kama moto wa kifuu. Moto mkali mkubwa ulikuwa umetawala mitaani ukitafuna majengo. Zimamoto wachache waliokuwepo hawakuweza kabisa kuumudu.





    Al Saed alistaajabu sana kuona moto huo. Alihisi mwili unaishiwa nguvu. Jasho jepesi lilimteremka. Macho yake yaliweka ukungu wa machozi. Moyo ulimuenda mbio sana akipaliwa na ghadhabu kuu.





    Kila eneo lilikuwa limeshikwa na vilio. Kama siyo rafiki, basi ni ndugu ama jamaa alikuwa amekwapuliwa uhai na milipuko hiyo. Wengine walilia kwa hofu juu ya kesho yao iliyoonekena ni ya kubahatisha, wakati wengine wakizirai kwa kushindwa kuhimili.





    Ilikuwa ni ndani ya muda mfupi tu maisha yalikuwa yamegeuzwa juu chini, chini juu, mikono ikashika vichwa. Simanzi ilizizima.





    "Ni maeneo gani haswa yalilengwa?" Aliuliza Al Saed. Alikuwa amesimama kando na afisa wa kikosi cha zimamoto na uokoaji: mwanaume mnene mweusi aliyevalia nguo za kazi.

    "Jengo kuu la makutano ya biashara," alijibu afisa zimamoto. "Soko kuu na makutano ya maduka, mkuu."





    Al Saed akasonya kwa masikitiko. Maeneo hayo tajwa yalikuwa ni maeneo yanayokuwa na idadi kubwa ya watu kutokana na mizunguko yake ya kibiashara. Ni maeneo ambayo ni vitega uchumi vizuri vya taifa.





    Alishusha pumzi ndefu, akakamata kiuno chake akitazama anga la Liberia. Alijaribu, akilini, kukokotoa idadi ya watu watakaokuwa wamekufa na kujeruhiwa. Hakutaka hata kuuliza maana alihisi angeutoboa moyo wake.





    Alishuhudia namna watu wanavyowahishwa hospitalini wakiangua kilio, ama wengine wakiwa hawajiwezi abadani.





    Akiwa anaongozana na walinzi wake watatu, alitembea akikatiza mitaa. Akifariji na kutia watu matumaini. Matumaini ambayo yalikuwa kama vumbi jepesi kwenye pepo ya bahari. Macho ya wahanga yalikuwa yamebeba maumivu, na hasira.





    "Sitaki kuongea chochote!" Alisema Al Saed akiwatazama waandishi wa habari waliokuwa na kiu ya kusikia neno toka kwake. Waandishi hao walijazana punde tu walipojua uwepo wa kiongozi huyo mkuu maeneo hayo.





    "Kiongozi, naomba utuambie msimamo wa serikali yako kuhusiana na hili?" Ilisikika sauti moja ya mwandishi wa habari.





    Al Saed alishindwa kupuuzia swali hili. Aligeuza shingo yake akamtazama mwandishi aliyeuliza.





    "Msimamo wangu ni kuwaua wote waliohusika na haya mauaji," alijibu na kuongezea, "hakuna yeyote atakayetoka salama. Na wote nitawanyonga chaneli ya taifa ikionyesha mubashara."





    Baada ya kusema hivyo basi kazi ikawa kwa walinzi kuwazuia waandishi kwa kuwasukumizia kando wasimbughudhi mkuu kwani hawakukaukiwa maswali, bado waliendelea kuyatiririsha.





    Al Saed akipuuzia maswali hayo, alitoa simu yake mfukoni akapiga. Alikuwa anataka kuulizia oparesheni aliyoiagiza. Upande wa pili, bwana James alipokea simu hiyo mara moja!





    "Tayari tumewashawatia wote nguvuni, mkuu. Tupo nao tunawahoji muda huu!" James alinguruma hewani.

    "Safi sana," akasema Al Saed akitikisa kichwa. "Wabane wawatajie hao wauaji wenzao. Baada ya hapo malizeni kabisa!"

    "Sawa, mkuu!"

    "James, nataka mrejesho wa maana."

    "Bila shaka, kiongozi. Tutafanya kila liwezekanalo."





    Simu ilipokatwa, James aliwatazama walengwa wake waliokuwa wamefungwa kwenye viti: naibu mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na mjumbe wake. Watu hawa walikuwa wamelowana damu, sura zao zikitepeta kichapo.





    Mkononi mwa James kulikuwa kuna spana kubwa ya chuma. Spana hiyo ilikuwa imechafuka damu. Hata mikono ya James pia ilikuwa mekundu kuashiria imeshika majeraha.





    "Sasa tunaingia kwenye awamu ya pili," alisema James. Uso wake haukuwa na masikhara. Mdomo wake aliubinua katika namna ya kuonyesha kebehi.

    "Unataka nini tena na nimeshakuambia?" Alilalama mjumbe kwa tabu. Macho yake yalikuwa yamevimba. Mdomo wake ulikuwa unachuruza damu, huku ngao za mashavu yake zikiwa zimejazwa majeraha.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    "Hujaniambia ni wapi naweza nikawapata hawa walipuaji!" Alisema James akitikisa kichwa.

    "Kwasababu sijui wapi utawapata," akajibu mjumbe. "Hawana makazi ya kudumu kwa sasa tangu makazi yao ya kule kijijini yalivyoharibiwa. Wanakaa popote pale!"





    James alikuna kidevu chake. Alimtazama Naibu mwenyekiti wa kamati ya ulinzi, akamuuliza;





    "Nani anafadhili hicho kikundi?"

    "Sijawahi kuambiwa. Si kila kitu nafahamu kuwahusu," alisema Naibu. Uso wake ulikuwa umevujishwa damu za kutosha kukufanya upate shida kumtambua.

    "Kama nilivyokuambia hapo awali, walikuwa wananitumia kwasababu ya kuhofia usalama wangu. Kama ningeliwageuka basi wangelinimaliza."

    "Muongo!" Sauti ya Mjumbe ilidakia. James aliyarusha macho yake upesi kwa Mjumbe huyo.

    "Wote tulifanya hii kazi kwasababu ya ahadi!"

    "Ahadi gani?" Aliuliza James upesi.

    "Tuliahidiwa maisha mazuri, na vyeo vinono serikalini," alijibu Mjumbe. Alikuwa anapata wasaa mgumu sana kuongea.





    James alitikisa kichwa chake akisema:

    "Sawa, sasa tunakaribia kumaliza zoezi letu." Alimgeukia Naibu akamwambia:

    Ningependa kukupa nafasi yako ya mwisho ya uhai kwa kusema ukweli. Ni maeneo gani ninapoweza kwenda kuwatafuta hawa watu mbali na kule kijijini?"





    Naibu alimtazama James kwanza. Aliona namna gani uso wa James ulivyokuwa mkavu. Alishusha macho yake chini akiyaambatanisha na pumzi ndefu. Akataja maeneo matatu anayohisi yanaweza yakawa yanakaliwa na wanamgambo wa AMAA.





    Alipotoa taarifa hizo, James aligeuka malaika Israel akanyofoa roho zao akiwanyonga kwa mikono yake mwenyewe. Kisha akapiga simu kuwataarifu wenzake.



    ***



    Ndani ya sebule ndogo yenye samani zilizopangiliwa vema. Picha kubwa ya farasi wawili; mweusi na wa kahawia ilikuwa inaning'inia ukutani. Mezani kulikuwa kuna bakuli kubwa la kioo likibebelea matunda mbalimbali.





    Pembeni ya meza hiyo kulikuwa kuna makochi mawili tu ya ngozi rangi kahawia. Kila kochi likiwa limeegemea dirisha kubwa la chuma.





    Sebule hiyo ilikuwa pweke, na kulikuwa kimya. Ila baada ya muda mfupi, sauti zilisikika nje ya sebule. Ilikuwa ni ya mwanaume na mwanamke. Sauti hizo zilisogea karibu na sebule na mara mlango ukafunguliwa.





    Alikuwa ni Kone na Rose. Kone alikuwa amevalia kaunda suti rangi ya udongo, Rose alikuwa amejisitiri kwa kuvalia bukta ya kitenge na tisheti jeupe.





    "Karibu!" Alisema Rose akitabasamu.

    "Ahsante sana, Rose. Nimeshaingia sasa."





    Kone aliketi, Rose akamletea kinywaji; juisi ya embe ndani ya glasi kubwa. Kone hakutaka chakula.





    "Kazana kula, Rose. Umekonda sana," Kone aliteta. Rose akatabasamu.

    "Kwani nimekuwa mbaya?" Aliuliza.

    "Hapana, sema sijazoea kukuona hivyo. Naona kama unaumwa."





    Kwa mtu ambaye hakuwa anamfahamu Rose hapo kabla, asingegundua tofauti yoyote ile kwa mwanamke huyo. Bado alikuwa mzuri na mwenye kuvutia. Hakuwa ametia kikorombwezo chochote usoni mwake, lakini aliita.





    "Itabidi uzoee, Kone. Nataka kubakia hivi hivi niweze kufanya kazi yangu vizuri."

    "Kazi ipi?"

    "Ya kummaliza Talib! Siwezi nikamuacha hata kidogo kwa namna alivyon'tendea. Lazima nimmalize kwa mikono yangu mwenyewe!"

    "Si rahisi kihivyo, Rose."

    "Najua. Nitaenda na ugumu wake hivyo hivyo. Lazima nimuue, mara hii niende jela kwa kustahili!" Rose alipiga ngumi paja lake kwa msisitizo.

    "Nisingependa kukupoteza, Rose," Kone alisema akimtazama mwanamke huyo machoni. "Kuna mambo makubwa na muhimu sana tunapaswa kuyatekeleza. Na mambo haya si tu kwa faida yetu bali kwa taifa zima."





    Rose alimtazama Kone kwa umakini. Alikitikilia maanani kila litokalo kinywani mwa mwanaume huyo.





    "Hapa tunavyoongea, Guinea ipo kwenye hali mbaya. Vita yaweza kutukia siku yoyote. Natilia mashaka sana juu ya uchaguzi huu unaokaribia, hauwezi kuisha kwa amani ... sasa nataka tukaokoe jahazi nyumbani, Rose."



    "Umejuaje kuhusu haya, Kone?" Rose aliuliza, na kuongezea: "Ni kwa muda mrefu sina habari juu ya kinachoendelea huko."

    "Ni habari ndefu kidogo nitakayojaribu kuifupisha ..."





    Maongezi hayo hayakudumu, mara yakakatishwa na mlio wa ujumbe kwenye simu ya Kone. Mwanaume huyo alitoa simu yake mfukoni akaitazama. Alikuwa Amadu.





    "Kama una muda, naomba tuonane nje ya makazi yako sasa hivi." Ujumbe ulisomeka hivyo.

    "Sawa, nakuja." Kone akajibu upesi.





    Rose aligundua mabadiliko kwenye uso wa mwanaume huyo. Alipata hamu ya kujua, akauliza:

    "Vipi Kone kuna nini?"





    Kone akamueleza juu ya Amadu.





    "Tunaweza kwenda wote?" Rose aliuliza. Macho yake yalijawa na ashki. Alikuwa tayari ameshasimama.

    "Ngoja kwanza," Kone akamtuliza, kisha akamtumia ujumbe Amadu juu ya ujio wake na Rose.

    "Unamuamini?" Ujumbe wa Amadu uliuliza.

    "Ndio, namuamini sana," Kone akajibu.

    "Sawa, unaweza kuja naye." Akapewa ithibati.





    Rose alijiandaa upesi kwa kuoga na kujivika suruali, kisha wakatimka na Kone kwenda mahali walipoelekezwa na Amadu wakutane. Walifika eneoni wakakuta patupu.





    Amadu alikuwa ameketi kando akiwatazama. Zilipopita dakika tatu akihisi shwari, ndipo akajongea kuwafuata. Alikuwa amebebelea begi kubwa jeusi mgongoni. Alivalia tisheti jekundu, suruali nyeusi ya jeans na viatu vya wazi.





    Alisalimu kisha akapendekeza wakafanyie maongezi yao ndani ya gari alilokuja nalo; Suzuki Vitara. Pendekezo hilo likaungwa mkono na wote.





    "Kuna jambo nimeona ni vema nikakushirikisha Kone," alisema Amadu. Alikuwa amekaa viti vya mbele yeye na Kone wakati Rose akiketi nyuma. "Si tu kwamba kwasababu linakuhusu, bali unaweza ukatoa mchango wako mkubwa sana.





    Kwa muda mrefu sasa, mimi na wenzangu tulikuwa tumetenga muda wa kuchambua mambo kwa kina kuhusu siasa za huu ukanda wetu. Na yote hiyo ni kwasababu tuliona hatuwezi tukatibu nchi moja wakati zingine zikiendelea kuumwa, kwa maana nchi hizi huambukizana, huathiriana kwa namna kubwa mno. Kwa Liberia kuwa na amani, basi Sierra na Guinea zinapaswa kuwa tulivu. Vilevile kwa Sierra na Guinea. Hakuna anayebaki salama wakati mwenzake akiwa vitani.





    Tulikuja kugundua kwamba, unaweza ukawa unaipigania nchi yako ndani ya nchi jirani. Ukahangaika kusuluhisha na kumaliza migogoro yao kwa ajili ya kwako kuwe hai, kwasababu mbegu ya chuki, uhasama na ukabila huzaa mti mpana wenye matawi marefu yanayoziba mwanga wa jua. Siyo tu kwa aliyepanda, hata pia kwa majirani. Nyoka watakaokaa hapo, hawatamng'ata tu mwenye nyumba, bali pia na jirani.





    Hivyo basi kuukata mti huo si kazi ya mwenyenyumba pekee, yumo pia na jirani.





    Kulitambua hilo kukatupa nguvu na haja ya kusambaza watu wetu kila kona ya nchi hizi. Watu hawa kazi yao ilikuwa kuwa macho na masikio. Waone kila liendalo, wasikie kila lisemwalo. Kazi yao ilikuwa kukusanya taarifa za kutosha, za kina, ili tujue nani chanzo, nani mtekelezaji, nani funiko.





    Katika hilo tukafanikiwa, kilichobakia sasa ni utekelezaji. Hapa tuongeavyo, kikundi cha THE GHOST kipo tayari muda wowote kuanza kuisaka shwari. Katika hili, ningependa tuwe pamoja.





    Ila pia ningependa kukupa wasaa wa kufikiria."





    Amadu alifungua begi akatoa mafaili matatu na kumkabidhi Kone. Kila faili lilikuwa lina rangi yake, na juu ya kila faili kulikuwa kuna jina la nchi moja miongoni mwa Sierra Leone, Liberia na Guinea.





    "Kwenye kila faili, kuna picha na maelezo ya kila mmoja tunayetakiwa kummaliza, pia sababu na njia za kufanya hivyo. Chukua muda wako kapitie, alafu utanipa mrejesho karibuni.





    Muda si mpenzi wa kweli," Amadu alihitimisha.







    ****





    Kone hakuwa na la kusema, akabeba mafaili, yeye pamoja na Rose wakatoka kwenye gari la Amadu na kwenda kwenye usafiri waliokuwa nao. Wakajiweka ndani na kuwa na maongezi mafupi kabla hawajatia moto chombo.





    "Kone, hawa watu wanatisha," alisema Rose. "Kwa muda gani na kivipi wameweza kufanya haya?"

    "Sina jibu, Rose, ila ninawaamini," alijibu Kone. "Wana utashi mkubwa wa kazi. Wana ujuzi wa kufanya kazi zao vizuri sana. Bila shaka wakidhamiria hili litafanikiwa."

    "Utaungana nao?"

    "Sijajua bado. Ila pia sina sababu ya kunifanya nisijiunge nao. Nafikiri nitapata jibu mujarab nikipitia haya mafaili."

    "Natamani uyapitie pamoja nami, kama hautojali lakini."

    "Hamna shida, mimi mwenyewe ningependekeza iwe hivyo."

    "Tutafanya hilo zoezi lini?"

    "Tufanye kesho mapema. Leo hii acha nirudi kwa mke wangu, atakuwa ananingoja."

    "Naomba basi unipitishe nyumbani."

    "Bila shaka."





    Kone akampitisha Rose kwenye makazi yake kisha akaelekea nyumbani. Akamkuta mkewe na watoto wameketi mahala pa kulia chakula. Mwanamke alikuwa amevalia gauni jepesi rangi ya bluu, nywele zake zilikuwa zimefumwa vema kuthibitisha ametoka saluni.





    Kone akaketi na kuungana na familia. Muda mfupi watoto wakaondoka kwenda kupumzika na kuwaacha wazazi peke yao mezani.





    "Haki umependeza," Kone aliwasilisha pongezi zake kwa mkewe. Mke, bi Fatma, akatabasamu kifupi.

    "Ahsante mpenzi," akajibu na kuendelea kula. Punde akamtazama mumewe kama mtu aliyekumbuka jambo.

    "Umesikia kilichotokea Guinea?" Akauliza. Kone akatikisa kichwa akiubinua mdomo.

    "Hapana, kuna nini?" Akauliza upesi. Macho ya bi Fatma yalikuwa yanaonyesha habarize si njema, na hilo likapelekesha puta moyo wa Kone kwa muda.

    "Nimeona kwenye taarifa ya habari muda si mrefu, mke wa marehemu Raisi ameuawa."





    Kone akakunja usowe.





    "Mama Angela?"

    "Ndio. Ameuawa kwa kupigwa risasi ya kichwa na watu wasiojulikana."

    "Kuna madai yotote wameyaeleza juu yake?"

    "Hapana." Bi Fatma akatikisa kichwa. "Nilichosikia cha ziada ni kwamba alikuwa amepanga kugombea kiti alichokiacha mumewe."

    "Kupitia chama gani?"

    "Hicho hicho cha mumewe. Alishaanza kampeni na mipango ya chini kwa chini kusaka kiti hicho. Inasemekana ni chama ndicho kilimshawishi agombee."





    Kone akatekwa na mawazo. Kwanini mauaji hayo yatokee? Kuna nini nyuma ya pazia? Hili jambo linaweza likasisimua kulipuka kwa vita. Hakupata hamu ya kula tena.





    Akachoropoa simu yake afanye mawasiliano, akakuta ujumbe. Alishangaa umeingia muda gani kwani hakupata kuusikia wala kuuhisi. Alitazama kiooni akaona namba ngeni aliyoing'amua ni ya Amadu. Haraka akafungua ujumbe huo.





    "Kadiri tutakavyokawia, ndivyo mauaji yatakavyotokea," ujumbe ulisomeka hivyo. Haraka, Kone akauitikia ujumbe huo kwa kuuliza:

    "Unawajua waliohusika na tukio hilo?"





    Punde akajibiwa: "Pitia mafaili niliyokupa."





    "Vipi mpenzi, kuna tatizo?" Bi Fatma aliuliza. Kone akapachika tabasamu usoni mwake upesi.

    "Hamna tatizo, mpenzi."

    "Unandanganya."

    "Kweli hamna tatizo."

    "Tafadhali, usianze kuwaza na kuwazua ya Guinea."

    "Usijali, mpenzi. Sitafanya hivyo."





    Bi Fatma akanyanyuka na kumpoka mumewe simu. Akaiweka mezani na kisha akamkalia mapajani kama vile mwanaume apandavyo bodaboda.





    "Leo zamu yangu," akasema bi Fatma. "Leo zamu yangu na mimi unifikirie, na utibu matatizo yangu."





    Kone akatabasamu. Akamnyanyua mkewe na kumpeleka kitandani. Akamvua nguo na kumpeleka bafuni. Walipotoka wakarejea tena kitandani.





    Mwanaume akajitutumua kumfurahisha mkewe. Alimshika na kumgusa kila kona tata ya mwili. Alisimamia huduma yake kadiri ya uwezowe, ila bado maji yakazidi unga. Hakuweza.





    Akili yake haikuwa kitandani, bali Guinea. Kila alipojitahidi kuihamisha ilishindikana. Alikuwa anawaza mambo lukuki, muhimu na nyeti.





    Akajilaza pembeni akitazama dari.

    "Nini shida, Kone?" Bi Fatma aliuliza. Aliweka mkono wake juu ya kifua cha mumewe.

    "Siko sawa, kuna mambo yananitatiza," Kone akajibu. Akashusha pumzi mdefu kisha akailaza mikono yake na kuilalia kama mto.

    "Niambie basi nini kinakusumbua."





    Kone akaona huo ni wasaa wa yeye kueleza kinaganaga. Endapo angesema ni kuhusu Guinea, kifupi hivyo, basi Fatma angekasirika kwani aliomba siku hiyo apewe zamu.





    "Unamkumbuka Amadu - yule jamaa niliyekuwa nakuambia kuhusu Sierra Leone?"

    "Yule aliyewahi kuwa kwenye kundi la waasi?"

    "Ndio. Leo nilikutana naye baada ya muda mrefu sana. Kuna baadhi ya vitu aliniambia, na vina mahusiano na kifo hiki cha mke marehemu Raisi."





    Kone akamwambia mkewe kuhusu mafaili, ila hakuthubutu kumueleza kwamba naye alikuwa anahitajika kwenye vita hiyo, aliona kitasababisha mkewe akose amani na furaha.





    "Kesho nitayapitia vizuri hayo mafaili. Kuna mambo kedekede yatakuwa yameainishwa, nyeti na yenye tija. Haya mambo ni makubwa."

    "Kone, lakini haya mambo yasitufanye tukasahau ndoa yetu," akashauri bi Fatma.

    "Nitajitahidi mpenzi." Kone akajibu na kisha akazima taa.



    ***



    "Ndio hapa," sauti ikasema ndani ya gari kubwa, Land Cruiser, lenye vioo vyeusi. Mara wakashuka wanaume wawili ambao hawakuwa wanaonekana vema kutokana na giza.

    "Kwa sasa bado atakuwa hajawasili," Mmoja akasema akitazama saa yake ya mkononi.

    "Kwahiyo sasa?" Mwingine akauliza.

    "Twende tukaketi pale," mwenzake akajibu na kuongezea; "Nadhani hatutokaa muda mrefu."





    Wakajongea mahali fulani palipokuwa pametulia. Palikuwa na viti na meza kadhaa. Muziki laini ulikuwa unapigwa. Hapakuonekana mtu yeyote akiwa hapo japokuwa ni usiku, pengine ni kwasababu ilikuwa ni siku ya kazi ama usalama haukuwa unaridhisha.





    Wakaketi na mara mhudumu akaja. Wanaume hawa walikuwa wapya usoni. Walikuwa wamejazwa na ndevu wakivalia shati na suruali za kitambaa. Nyuso zao zilikuwa pole, makini.





    Mhudumu alikuwa mwanaume mrefu aliyekuwa hajavalia vema. Shati lake jeupe lilikuwa limejikunja, na suruali yake nyeusi ya kitambaa ilikuwa ina vumbi vumbi.





    "Naweza nikawasaidia?" Akauliza mhudumu.

    "Tuletee maji makubwa," mwanaume mmoja akaagiza. Uso wake ulikuwa na vidotidoti na macho yake yalikuwa makubwa.





    Mhudumu aliondoka kwenda kufuata alichoagizwa. Akawaacha wanaume wale peke yao.





    "Endapo kama leo hatutampata, hatutaeleweka," akasema mwa aume mmoja.

    "Ni kweli unachosema lakini tutafanyaje sasa. Ni kama vile jamaa huyu amejua janja yetu."

    "Kabisa. Amekuwa sio wa kutulia eneo moja. Hili litakuwa eneo la tatu sasa, tunamuenendea na hatumpati. Tukimkosa hapa, sijajua tutampatia wapi tena."





    Kukawa kimya kidogo. Wote macho yao yalikuwa yanatazama jengo fulani walilotegemea kumuonea mlengwa wao hapo.





    Mlengwa huyu hakuwa mwingine bali bwana Richard. Mwanaume aliyeagizwa kuuawa na Talib baada ya kupewa maneno chokonozi na Rauli kuhusishwa na kifo cha Freeman.





    Lakini jambo hili linageuka na kuwa mtihani mgumu. Mwanaume huyu amekuwa adimu mno kupatikana tofauti na ilivyodhaniwa kabisa. Amekuwa akihamahama makazi. Amekuwa si mtu wa kuonekanaonekana, na haya yalianza punde tu baada ya kifo cha Freeman, mwanzilishi wa oparesheni mwanzo, kati na mwisho ambayo haikufanikiwa kupiga hata hatua moja.





    Kifo hicho kilimfamya Richard ahisi usalama wake utakuwa hatiani. Na kweli hisia hizi zikamlipa fadhila.



    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Wanaume hawa wawili walikuwa wamezunguka na sasa walikomea kwenye eneo la tatu kwa idadi. Kote huko walipeleleza na kuweka kajikambi ka' masaa lakini hawakuvuna kitu. Kwenye nyonga zao walikuwa wamebebelea bunduki ndogo, agizo walilopewa ni kuua tu!





    Mhudumu alirejea akiwa amebebelea maji makubwa. Aliwagawia wateja wake kisha akachukua pesa na kuondoka. Wamaume wale wakajihudumia wakiendelea kungoja.





    Wakiwa katika hilo zoezi, mhudumu aliwatazama, na katika hali ya umakini, akaingia ndani ya chumba kidogo kinachotunza vinywaji. Akatoa simu ndogo mfukoni mwake kisha akapiga.





    "Halo! ... wengine wapo hapa, njoeni upesi!" Alinong'oneza. Alipomaliza, akarudisha simu mfukoni mwake kisha akatafuta mahali alipokuwa na fursa ya kuwaona wateja wake.





    Haikupita muda mrefu wanaume wale wawili wakamuona mtu akijongea karibu na jengo walilokuwa wanalitazama. Haraka wakamalizia vinywaji vyao na kunyanyuka upesi. Wakaelekea kule walipoona jambo.





    Wakachomoa bunduki zao na kuzikabia mikononi. Wakatembea haraka mno wakihakikisha macho yao hayabanduki kutazama mlango wa jengo wanaloliendea.





    Huku nyuma mhudumu alitoka, akawa anatazama wanaume hao wakienenda. Wakati huo akiwa ameshikilia simu mkononi anaongea na watu kuwaelekeza.





    Wanaume wale wakafika karibu na eneo husika. Wakajibanza mahali wasionekane. Walitazamana kupeana ishara, mmoja akaenda nyuma mwingine akabakia mbele.





    Walifanya mambo hayo katika ukimya mno. Miguu yao haikuwa inatoa sauti na ilhali walitembea na kukimbia. Hii ilikuwa nafasi yao ya kumaliza kazi iliyowasumbua kwa muda, na hawakutaka kuichezea, maana walijua gharama yake.





    Wakatulia kwa dakika kama mbili, kimya. Mara mlio wa risasi unavuma. Mlio huu ulitokea nyuma ya jengo. Mwanaume yule aliyekuwa mbele ya jengo akashtuka, hakujua hiyo risasi aliifyatua nani. Akapata hofu.





    Alijaribu kusogea, mara akapunyuliwa na risasi ya sikio. Akashika sikio lake kwa maumivu. Hakukaa vema, risasi zikarushwa kumfuata kama mvua. Hakujua zinatokea wapi. Akajikuta anakimbia kuokoa uhai wake.





    Akakimbia kufuata gari walilokuja nalo. Akafungua mlango na kuzama ndani. Kabla hajatia moto chombo, chuma cha risasi kikapasua dirisha la gari na kutoboa kichwa chake. Akafa papo hapo!





    Dakika nne mbele, wakajongea wanaume kumi wakiwa wamebebelea bunduki. Miongoni mwa hawa wanaume kuna nyuso mbili tunazozifahamu. Nyuso hizi tulishawahi ziona kwenye mauaji ya Freeman.





    Lakini zaidi yumo na yule mhudumu. Kumbe naye alikuwa ni miongoni mwa hawa watu na ndio aliokuwa anawasiliana nao. Kundi la waandamanaji waasi!





    "Tutawaangamiza wote hawa!" Alisema mmoja. "Wanadhani wakiwaingiza watu wao mtaani hatutuwafahamu!"





    Loh! Mpango wa Rauli ulianza kufeli.





    Kuangamiza kikundi cha waandamanaji wa kiasi kwa kutumia wapelelezi mitaani, ilishaanza kubumburukiwa. Bahati haikuwa kwa wanaume hawa wawili wapelelezi, wakiwa wanamfuatilia Richard wakajikuta wanazama mikononi ya wauaji wengine.





    Waandamanaji walikuwa wauaji. Wauaji wenye juzi na mtandao mpana. Hapakuwa salama kabisa.





    Richard, akiwa hajui kama mapambano yaliyotukia yalikuwa yanamhusu yeye, akatoka ndani ya jengo lake. Akachungulia kama kuna watu. Alipoona ni shwari, akatoka upesi na kukimbia!









    ***





    Majira ya saa nne asubuhi:





    Pembezoni mwa barabara kuu ya lami, Kone na Rose wanakutana. Walikuwa na miadi hapo.





    Kone alikuwa amebebelea begi kubwa la mkono mmoja. Rangi ya begi hili ilikuwa nyekundu. Alikuwa amevalia shati la mikono mirefu alilolikunja mikono pamoja na suruali nyeusi ya kadeti na raba nyeusi.





    Rose alikuwa amejivesha suruali ya kubana, tisheti ya njano na viatu vyeusi vya kuchomeka. Nywele zake alikuwa amezibana vema, usoni akipaka wanja pekee.





    Walibadilishana matabasamu, kisha pasipo kuongea wakaanza kujongea wakielekea kaskazini mwa barabara. Walitembea kidogo kabla hawajafika kwenye makazi ya Rose.





    "Ungefika usingenikuta," Rose akasema akitabasamu.

    "Ndio maana nikaamua kujiongeza, nikaona nikupigie simu kwanza."

    "Umefanya jambo jema sana."

    "Ila Rose hauogopi kutembea huko nje, tena ukiwa wazi hivyo?"

    "Sina sababu ya kuogopa, Kone. Serikali kwa sasa ipo bize ikihaha kupambana na waandamanaji. Hawana muda nami."





    Kone akatabasamu. Aliketi, Rose akaingia ndani kumletea sharubati baridi ya machungwa.





    "Usiku huu ulikuwa mgumu sana kwangu," Kone alisema akiweka glasi mezani. "Sikulala kabisa, si umesikia juu ya kifo cha mke wa Raisi?"

    "Ndio, nimesikia!" Rose alijibu akitoa macho ya staajabu. "Nani kamuua?"

    "Majibu yapo humu." Kone akaonyeshea begi alilokuja nalo. "Tukipitia hizi faili, tutapata kujua ama kupata mwanga."





    Wakiwa wanakunywa sharubati, wakaanza kukagua mafaili kwa kina, wakianza na la nyumbani: Guinea. Mcheza kwao hutunzwa, walisema waswahili. Macho yao yalizama ndani ya karatasi wakisoma maelezo.





    Kitu cha kwanza kukiona kilikuwa ni picha ya marehemu Raisi. Picha hiyo ilikuwa pana, ilimuonyesha Raisi akiwa anatabasamu akikunjia mikono yake kifuani. Chini ya picha hiyo yaliandikwa maneno machache:





    'Mtuhumiwa namba moja wa chuki za kikabila.'





    Tuhuma hizi zilikuwa mpya mbele ya Kone na hata Rose. Siku zote hawakuwahi kumtuhumu Raisi wao kuwa daraja la chuki hatari za kimakabila. Walitazamana kwa macho ya pazo, kisha kwa sauti, Kone akasoma:

    "Kwa takribani miaka miwili sasa tangu Raisi wa Guinea, akiwa kiongozi wa kundi la POWER lenye fanisi ya kuhakikisha kabila la Fula ama Fulani wanakuwa na kubakia madarakani.





    Ndani ya mwaka wake wa kwanza kama Raisi, na pia kama kiongozi wa POWER, alisababisha mauaji ya wanaume wawili kwa majina Robert Diallo na Bala Musa. Robert alikuwa anafanya kazi huko Addis Ababa, Ethiopia Umoja wa mataifa Afrika, na Bala Mussa alikuwa akifanya kazi serikalini kama katibu mkuu wa wizara ya usalama na ulinzi.





    Robert Diallo aliuawa kwa kupigwa risasi ya kifua na watu waliotuhumiwa kuwa majambazi. Lakini mazingira ya tukio hilo yanaonyesha watu hawa hawakuwa majambazi bali walitumwa kummaliza mtu huyu.





    Ndani ya siku hiyo, tarehe 12 January mwaka juzi, majira ya saa nne usiku, Robert Diallo akiwa nyumbani, wanaume watatu walimvamia. Walikatisha uhai wake pasipo kuchukua chochote kile. Walipotea na hakukuwa na uchunguzi wala ufuatiliaji wowote uliofanyika ukizingatia nafasi kubwa aliyokuwa nayo huyo mhanga.





    Mhanga wa pili, Bala Mussa, huyu aliuawa kwa kisingizio cha ajali. Akiwa ndani ya gari lake kurudi nyumbani, aligongwa na gari kubwa semi trella lililoacha njia yake na kumparamia. Inasemekana ni ajali ila kiuhalisia haikuwa hivyo.





    Dereva alilaghai kwamba tairi lilipasuka hivyo akashindwa kumudu chombo, ila halikuwa kweli. Dereva huyu hakudhurika hata kiungo kimoja ukilinganisha na uharibifu wa gari lake ulivyotokea. Lakini zaidi hakuchukuliwa hatua zozote, ikiwemo kushtakiwa.





    Dereva huyu ndiye tumembana, akatupa maelezo ya kweli. Tulimmaliza maana kama angeliendelea kuwa hai, basi angeliweza kusambaza habari juu yetu.





    Tulifanya ukaguzi ndani ya nyumba yake, tukakuta kinyago cheusi chenye umbo la simba na bunduki aina ya SMG. Vitu hivi ndivyo vilisadikika kutumiwa na majambazi waliomuua Robert Diallo.





    Mbali na hapo, Raisi wa Guinea akiongoza kundi lake la POWER, walikuwa wanakutana mara mbili ndani ya miezi sita. Wakijadili namna ya kuimarisha kabila lao na nguvu yao. Lakini pia wakifanya mambo katika namna ya kuficha kucha. Raisi hakuacha kuteua watu wa kabila zingine, lakini akifanya hivyo alihakikisha kwanza mtu huyo hatokuwa na madhara. Ama basi ni mtu wa karibu anayemjua nyendo.





    Hili linajionyesha kwa rafiki yake mkubwa aitwaye Suma Yakuba, afisa wa ikulu, ambaye amefanikiwa kupumbaza umma juu ya ukabila wa serikali.





    Uteuzi huu wa Yakuba haukuwa wa kukurupuka, la hasha, bali uliopangwa. Raisi alisoma na Yakuba shule moja tokea hatua ya awali mpaka walipokuja kutengana elimu ya juu. Huko kote walikuwa ni marafiki wa kutupwa.





    Kwa lengo la kulaghai macho ya wananchi, Raisi akaufanya uteuzi wa Yakuba kuwa wa kwanza kabisa kabla ya yote. Tukio hilo likavuta hisia za watu kwa mtu wa kabila 'A' kumteua wa kabila 'Be' kwa kipaumbele namna hiyo.





    Baada ya hapo kombe lilifunikwa, mwanakharamu akapita.





    Endapo Raisi huyu angeendelea kuvuta hewa ya dunia, kusingewahi kuwa salama ndani ya Guinea. Watu wa Malinke wasingewahi kuwa salama salmini.





    Sasa ameenda, ila POWER imebaki. Kundi hili kwa sasa limekaliwa na kiongozi mpya kwa jina Saikou Boubacar. Mtu huyu ni hatari sana kuliko aliyepita kwani hamini kwenye kula na kipofu.





    Dalili ya hatari ilionekana kwenye msiba wa Raisi. Saikou Boubacar akiongozana na wenzake watatu hawakumpa mkono wa pole bwana Yakuba. Walimruka na kwenda kusalimu wengine. Pia wakajitenga wakiketi eneo lao la peke yao.





    Bila shaka kwa minajili hii, tutaweza kushuhudia mauaji na uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu siku za usoni. Endapo bwana huyu na kundile hawataangamizwa."





    Kone aliweka kitu hapo kwa kushusha pumzi ndefu na kutazamana na Rose. Walilowanisha koo zao kwa sharubati kabla hajaendelea na kurasa ya pili ambapo kulikuwa kuna picha kadhaa za Saikou Boubacar, Yakuba na wahusika wengine wa kundi la POWER.





    Zaidi ya hizo picha kukiwa na vipande vya magazeti vikonyesha picha ya Saikou Boubacar akikataa mkono wa Yakuba. Picha zingine zikimuonyesha Yakuba akiwa na marehemu Raisi maeneo kadha wa kadha matabasamu yakipendezesha nyuso zao.





    Picha zingine za magazeti zikionyesha mabaki ya matukio ya ajali ya Bala Musa na mauaji ya bwana Diallo. Pia maelezo kadhaa ya mashahidi wa matukio.





    "Ngoma hii ngumu," Rose akasema akitikisa kichwa.

    "Ni kweli," Kone akaunga mkono hoja. "Ni kubwa kuliko ionekanavyo mbele ya macho ya kawaida. Kuna mizizi ya kukatwa, mti huu umekomaa."

    "Nikuongezee kinywaji?" Rose alimhamishia Kone kwenye ulimwengu mwingine. Mwanaume huyo hakujua hata kama sharubati imeisha kwenye glasi. Alitazama glasi akaiona tupu, akatikisa kichwa akitabasamu.



    "Nitashukuru."





    Rose akanyanyuka na kwenda kwenye jokofu. Akafungua na kumimina sharubati baridi aliyomletea Kone mara moja.





    "Karibu."

    "Ahsante, Rose."





    Kone akanywa fundo moja la nguvu.





    "Unatengeneza mwenyewe hizi?" Akauliza punde aliposhushia glasi mezani.

    "Ndio, natengeneza mwenyewe," Rose akajibu na kisha akauliza: "Vipi, umeipenda?"

    "Sana, una mkono wa jikoni kweli."

    "Ahsante, Kone."

    "Na pia una mkono wa kutoa, maana yale matunda uliyojaza kwenye jokofu si mchezo."





    Rose akaangua kicheko.





    "Umejuaje kama kuna matunda mule?"

    "Umesahau kitu cha kwanza kuniomba wakati tukiwa tunakuja eneo hili?"





    Rose akajaribu kukumbuka. Mara akaangua kicheko.





    "Nakumbuka. Nilikuomba unipe pesa ninunulie matunda."

    "Na leo tumekutana ukielekea wapi?"

    "Kuchukua matunda." Rose akaangua kicheko tena. "Acha bana mambo yako!"

    "Walaa! Mie nimesema tu."

    "Unadhani basi nayanunua hayo matunda?" Rose aliuliza. Kabla hajajibiwa, akaongezea: "Unamkumbuka yule mzee tuliyemuona siku ile gengeni?"

    "Yap!"

    "Hunipa matunda bure."

    "Bure?" Kone alitoa macho.

    "Ndio, bure." Rose akajibu akirembua macho. "Nadhani Kone umesahau ni namna gani nilivyo mzuri."





    Wakacheka kwa pamoja.





    "Na kweli nimesahau. Ila umuonee huruma mzee wa watu."

    "Nani kasema? Mpaka nihakikishe amemaliza mtaji wote. Ujinga kaupalilia mwenyewe na maji ya tamaa."

    "Ila usijali, hii kazi itatuondoa hili eneo muda si mrefu. Bila shaka babu wa watu atadumisha genge angalau."





    Wakacheka. Waliacha maongezi hayo wakarejea kwenye zoezi lao la kusoma faili waliloliacha kiporo kwa vidakika kadhaa. Walijivesha nyuso za kazi na macho ya umakini.





    Sasa ndani ya faili hili walikuwa wanamtazama pande lingine la jibaba, kwa jina Sisawo. Picha ya mwanaume huyo ilikuwa kubwa ikiwa imepigwa nyakati za jioni. Mandhari ya picha hiyo yalikuwa ya siri.





    Chini ya picha hiyo kulikuwa kuna maandishi machache yakisomeka: "Sisawo, nguzo ya damu ya Mandinka."





    Baada ya maneno hayo yalifuatia maneno yaliyokolezwa uweusi: *Tageti ya kwanza kabisa ya kuangamizwa ndani ya Guinea.*





    Picha ilikuwa moja tu ya mwanaume huyo. Japokuwa ilikuwa kubwa lakini bado haikuwa anaonekana vizuri, ila angalau ingeweza kumkumbusha mtu endapo angemuona mhusika huko njiani, kama angemtazama vema.





    Kwenye picha hiyo Sisawo alikuwa amevalia kofia kubwa 'cowboy' nyeusi. Alikula suti ya rangi ya kahawia na alikuwa anaingia mlangoni mwa mahala fulani palipokuwa panapendeza machoni.





    Mahala hapo palikuwa mithili ya hoteli ama mgahawa mkubwa.





    "Yani hadi Sisawo?" Alistaajabu Kone. "Huwezi mdhania kabisa!"

    "Huyu si ndiye yule anayesaidia watoto yatima na wazee?" Aliuliza Rose.

    "Ndiyo yeye!" Kone akajibu.

    "Ina maana naye anahusika na joto la Guinea?"

    "Bila shaka ndiyo maana yupo humu."





    Kone akaanza kusoma maelezo ya mwanaume huyo;

    "Mwanaume huyu mfanyabiashara mkubwa ndani na nje ya Guinea, ndiye tageti ya kwanza kwenye mauaji. Anafadhili jeshi la kikabila ambalo linapewa mafunzo ya kijeshi na kumiliki silaha za kisasa kabisa.





    Jeshi hili lina watu toka nchi mbalimbali, ila kigezo kikiwa kikuu kikiwa kimoja; lazima mtu huyo awe ni wa kabila lao. Huko mazoezini atafundwa ukakamavu, kuua na uvumilivu. Wanatolewa utu na kupandikizwa chuki dhidi ya wengine, lakini pia kiu ya kuua.





    Tulifanikiwa kumpandikiza mtu wetu kwenye jeshi hilo akakusanya taarifa kadhaa muhimu. Kiongozi na ratiba zao za mashambulizi. Lakini pia sauti ya Sisawo ikiwahamasisha wanaume hao wajitoe sadaka kwa ajili ya kabila lao.





    Endapo mauaji yoyote ya watu wa jamii ya Fulani yakijiri, basi ni hawa watu ndiyo wanahusika. Watawamaliza wale wote wanaoonekana wana ushawishi mbele za watu, na tishio kwa kabila lao."





    Kone aliweka nukta hapo akamtazama Rose.





    "Ina maana hawa ndiyo wamemuua mke wa Raisi?"

    "Inawezekana," Rose akajibu na kisha kuuliza: "ila kwanini wamuue mama wa watu?"

    "Inasemekana ndiye alikuwa mgombea mteule wa kuwania nafasi ya uraisi kwa kupitia chama cha mumewe."

    "Ndiyo wamuue?"

    "Inawezekana kuna kitu walikiona kwake, hawawezi wakamuua tu. Aidha waliona kuna hatari ambayo mwanamke huyu anaweza kuwasababishia."





    Kone aliacha kupekuwa faili akaingia mtandaoni kupitia simu yake. Aliandika jina la mwanamama huyo na kusachi. Taarifa lukuki zikaja. Alipembua taarifa hizo kwa dakika kama kumi, kisha akasema:

    "Sasa nimepata mwanga."

    "Niambie," Rose akadakia.

    "Katibu mkuu wa chama ndiye alimshawishi mama huyu kugombea. Waliamini ana mvuto kwa jamii, lakini haswa kwa wanawake wenzake ambao walimuona shujaa kwa kusimama mbele ya hadhira na kutema maovu aliyokuwa anafanya mumewe.





    Waliamini ni mwanamke shupavu ambaye anaweza kuvunja mfumo dume. Hivyo kupata ushawishi wake ni kuwapata wanawake, kupata wanawake ni kupata kura. Siku zote wanawake ndiyo wapigaji kura, wanaume waongeaji tu."











    ****







    Iliwachukua lisaa kumaliza kusoma faili la Guinea, ikawachukua tena lisaa limoja kulipitia la Sierra Leone, wakapumzika. Mambo yalikuwa mengi na hatari zaidi. Kila karatasi waliyoifungua ilikuwa na mambo mazito kuliko ya awali. Mambo yaliyowaacha mdomo wazi.





    Kama kuna somo kuu walilolipata kwa kupitia nyaraka hizo, basi ni kutoamini yale tu macho yako yanachoona. Ulimwengu ni zaidi ya hapo. Kuna mambo mengi yapo ardhini, kama usiposhika jembe ukalima basi maisha yako yote utaishia kusema dunia ni milima na mabonde.





    Walikunywa kahawa nyepesi wakati wakingojea maakuli jikoni yaliyokuwa yanaandaliwa na mkono wa Rose. Walisindikiza subira yao kwa soga za hapa na pale, walipomaliza kula wakaendelea na zoezi.





    Simu ya Kone iliita, ila hakuna aliyetambua kwani ilikuwa imewekwa mfumo wa kimya. Si chini ya mara tano simu hiyo iliita. Kone alikuja kulitambua hilo baadae baada ya kumaliza kupitia kila jambo mafailini. Alikuwa ni mkewe amuita.





    Alijaribu kumtafuta, salio likawa halijitoshelezi. Njia pekee aliyoiona sahihi ikawa ni kuondoka kwenda nyumbani.





    "Inanipasa niende," alimwambia Rose.

    "Kwahiyo vipi sasa?" Rose akauliza. "Tunaamua nini juu ya haya?" Alinyooshea mkono wake kwenye mafaili.

    "Tutakuja kuongea baadae, Rose."

    "Una uhakika tunaweza tukaongea baadae? Muda si rafiki, na sidhani kama Amadu atakuwa na uvumilivu wa kiasi hicho," alisisitizia Rose. Kone akashusha pumzi ndefu.





    Pengine angemwambia mwanamke huyo juu ya mkewe, angemuelewa. Ila hakutaka kufanya hivyo, aliweka siri. Alipima hoja ya Rose akaona ina mashiko. Hakukuwa na muda wa kusubiri tena, basi akajikuta anaamua kuketi. Kama moto basi ni moto na si vuguvugu.





    "Unaamua hili?" Aliuliza Kone akimtazama Rose machoni.

    "Ndiyo, naamua. Kwa akili zangu zote tena nikiwa timamu," Rose akajibu kwa kujiamini.

    "Kila mtu anajua kazi hii ni ngumu na hatari, ila hakuna wa kuifanya zaidi yetu," Kone alisema na kuongezea: "Ni sisi tu ndio tunangojewa ili mapambano yaanze. Kwahiyo kama nikimtaarifu Amadu, basi anaweza kutuambia tuanze mapambano mara moja. Hatujajua angelipendekeza iwe nchi gani ila inaweza ikawa yeyote ile, kwahiyo tunahitaji kujiandaa."

    "Ni kweli. Ila huoni kama ingekuwa vizuri kumwambia kwanza Amadu ili basi kama kujiandaa tujiandae kwa mujibu wa mpango? Bila shaka mipango haiwezi kufanana, na hata maandalizi yake pia."

    "Umeongea la maana," Amadu akaunga mkono hoja. Alifanya mpango akaongeza salio simuni kisha akamtumia ujumbe Amadu;

    "Tumeridhia kufanya kazi."

    "Kwanini usimpigie?" Rose akauliza.

    "Namba yake haipatikani," Kone akamjibu. "Nimejaribu mara kadhaa nikashindwa kumpata. Ni ujumbe tu ndiyo unaenda. Uzuri anajibu haraka."





    Kweli, ndani ya muda mfupi ujumbe unaingia kwenye simu ya Kone. Kone anaufungua na kuusoma kwanguvu Rose asikie.





    "Leo, majira ya saa tano usiku, kuna kazi ya kufanya ndani ya Sierra Leone. Ni kazi ya mauaji, takribani kilomita sitini na tano toka yalipo makazi yenu. Mtuhumiwa namba tano."





    Walirejelea kwenye mafaili yao kumtazama mtuhumiwa namba tano. Alikuwa ni mwanaume mrefu mpana. Mpenzi wa vileo na kuhudhuria kumbi za starehe.





    "Nitakuja kukupitia baadae," akasema Kone. Rose akatikisa kichwa.

    "Bila shaka ntakukuta umeshajiandaa," Kone akaongezea. Rose akatikisa tena kichwa. Kone akaaga aende sasa.







    ***

    ***

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/





    "Hatujampata, mkuu," Alisema Rauli ndani ya kijikao kidogo cha dharura alichoketi na Talib. Walikuwa ikulu ndani ya kajichumba kadogo ka mkutano.

    "Rauli," Talib aliita. "Hauna ambacho umefanikiwa kufanya?" Akauliza.





    Rauli alipepesa macho mdomo ukibanwa na kigugumizi. "Ki ... kip - o, mkuu."

    "Kipi?"

    "Nimeweka maajenti wangu mtaani, wanafanya skauti ya kuwatafuta waandamanaji."

    "Mpaka sasa wamekamata wangapi?"

    "Bado, mkuu. Wana ..."

    "Wao wameua maajenti wako wangapi?"

    "Watano."





    Talib akatabasamu.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog