Search This Blog

Sunday 20 November 2022

NJIA NYEMBAMBA - 1





    IMEANDIKWA NA : STEVE MOLLEL



    *********************************************************************************



    Simulizi : Njia Nyembamba

    Sehemu Ya Kwanza (1)







    Mawimbi ya bahari yalipiga kwa pole katika bahari ipakanayo na Sulima, mji wa kusini mashariki mwa Sierra Leone. Ilikuwa ni mwisho wa wiki, watu walikuwa wamejazana kando kando mwa bahari wakila upepo na kusindikizia na muonekano mzuri wa bahari ishibishwayo vilivyo na mto mkubwa wa Moa.

    Nyuso za watu zilijawa na tabasamu na cheko. Ilikuwa ni raha sasa kwao kuonja matunda ya amani tangu vuguvugu la vita za wenyewe kwa wenyewe lipate kupita. Ni miaka takribani mitano tu hapo nyuma, watu wengi waliuwawa na wengine kuachwa na ulemavu wa kudumu pale vita ya mapinduzi ilipotokea, waziri wa ulinzi, Louis Diarra, akiongoza jeshi na kumng’oa madarakani raisi Mousa Assessoko. Si tu watoto walikuwa yatima kwa kupoteana ama kuuwawa kwa wazazi wao, bali damu ya watu wengi wasio na hatia ilimwagika. Hata wale waliosalimika dhidi ya midomo ya risasi, waliwindwa vikali na baa la njaa; harufu za maiti zikatapakaa kila kona.

    Watumishi wa raisi aliyepinduliwa, bwana Mousa Assessoko, walitiwa jela. Walipata mateso makali na kuuwawa kikatili. Wengine walifungwa kamba wakaburuzwa na gari barabarani. Wengine walinyongwa mbele ya kadamnasi ya watu wakati wengine wakitumika kujifunzia shabaha za risasi kwa kulengwa wakiwa wametundikwa mitini.

    Bahati mbaya ama nzuri, Mousa Assessoko alitoroka kabla hajajaa kwenye mikono ya mwindaji wake. Assessoko alikimbilia nchini Guinea. Kwa msaada wa siri wa rais wa Guinea, Assessoko alipatiwa makazi. Akiwa huko, Assessoko alianzisha kundi lake la wapiganaji pamoja na baadhi ya wafuasi wake aliotoroka nao likienda kwa jila la MDR (Mouvement de libération). Lengo lake kuu likiwa ni kurudi madarakani, kutafuta heshima yake iliyopotea na kuonyesha umwamba.

    Ni wananchi wachache mno wa Sierra Leone waliokuwa wanafahamu mahali alipo Moussa Assessoko, wala hasa anachokifanya. Hata wananchi wa Guinea na viongozi wengine hawakufahamu na wala hawakutakiwa kulifahamu hilo jambo kama njia mojawapo ya kuhakikisha usalama wa nchi na ufanisi wa kazi inayotendeka na MDR katika misitu mikubwa ipakanayo na nchi ya Sierra Leone.

    Chini ya uongozi wa General Kessy, kundi la MDR lilifanya mazoezi ya kutosha kila siku likiongeza idadi maradufu ya wafuasi waliokuwa wanawapata toka Guinea na Sierra Leone wakihadiwa nafasi, pesa na maisha mazuri baada ya mapinduzi. Kwa mkono wa raisi wa Guinea, MDR walipata silaha za kutosha na bora, vile vile malazi mazuri. Kila mwisho wa wiki, Moussa Assessoko alikuwa anatembelea kambi kuwapa motisha wapambanaji wake dhidi ya kazi kubwa iliyo mbele yao. Kila alipowatembelea, ilifanyika tafrija wanajeshi wakala na kunywa.

    Ndani ya siku moja ya ijumaa katika mji wa Kabala upakanao na nchi ya Guinea, watu wengi wakiwa wanaswali misikitini, adhana zikilia huku na huko, gari aina ya jeep ndogo ya kijani iliyobebelea wanaume watano ilivuka mpaka ikitokea Guinea ikaingia katika ardhi ya Sierra Leone. Mwendokasi ukiwa ni wa kawaida, gari lilisonga mpaka eneo la soko kuu la mji wa Sulima. Liltulia hapo. Wanaume watatu walishuka wakaegemea gari, wawili walibakia ndani ya usafiri, wote wakawa wanarusha macho yao huku na huko kama watafutao kitu.

    Labda kutokana na wanaume hao watano kuvaa gwanda za jeshi la Sierra Leone hakuna aliyewatilia shaka juu yao. Wananchi waliendelea na shughuli zao, wengine wakiuza na wengine wakinunua lakini idadi yao ikiwa si kubwa sana kama siku zingine mbali na ijumaa, pengine watu walikuwa ndani ya misikiti kwa wakati huo.

    Miongoni mwa wanaume wale wawili waliokuwa wamebaki garini, mmoja alishuka akaungana na wale watatu waliokuwa wameegemea chombo. Alikuwa ni mwanaume mrefu na mwenye mwili mpana. Usoni alivalia miwani meusi, kichwani kwake akiwa amenyoa mtindo wa panki kama vijana weusi wa miaka ya tisini nchini Marekani. Nyuma ya suruali yake ya kombati kiunoni alikuwa amechomeka bunduki ndogo. Mwanaume huyo alitizama kushoto na kulia kisha akajisogeza mbele zaidi kuelekea ndani ya soko. Baada ya muda kidogo aliwageukia wenzake na kuwapa ishara ya macho akivua miwani na kukonyeza. Papo hapo bunduki zilizokuwa zimelazwa kwenye sakafu ya gari ziliokotwa. Risasi zilipigwa kwa fujo kuelekea angani. Watu wakaamriwa wote walale chini.

    “Tulia hivyo hivyo kwa usalama wako!” Alifoka mwanaume yule mwenye panki akiwa amevalia miwani. Huku taharuki likiwa limetawala, watu wengine walishindwa kutii amri. Walikunjua miguu yao kukimbia. Hawakufika mbali, risasi zilifyatuliwa kuwakimbiza. Kama viroba walianguka chini wakilia maumivu ya vyuma vya risasi wakati wengine wakiwa tayari wameshadhulumiwa haki yao ya uhai.

    “Nimesema tulia mnajifanya werevu, sio!” Mwanaume mwanajeshi alifoka huku akiwa amekunja sura yake. Hofu ya kifo iliwameza watu; wengine walilia huku makamasi yakwatiririka. Zaidi wengine walishindwa hata kubana haja zao ndogo.

    Punde, jeep tatu za kijani zilizofanana na ile iliyotangulia ziliwasili katika eneo la soko vumbi kali likiwasindikiza. Kutoka kwenye magari hayo walishuka wanaume nane wakaungana na wale watano kutimiza idadi ya wavamizi kumi na tatu. Mmoja wao alimfuata mwanaume yule mwenye panki, akampigia saluti na kumpa taarifa;

    “Tayari mkuu. Tumeshaviweka vituo vyote vya polisi chini yetu.”

    “Vyema. Kaa simamia hapa!” Mwanaume mwenye panki alitoa amri kisha akaondoka na kulirudia gari alilokuja nalo yeye pamoja na wenzake aliokuja nao wakajipaki ndani ya gari na kuhepa toka eneo hilo kwa kasi kubwa nyuma wakiacha vumbi zito. Walielekea upande wa magharibi wa mji. Wakiwa wametimiza umbali wa kilomita moja na kidogo kwa mbele yao waliona wanajeshi watano wamekaa barabarani pembeni ya geti la kufunga na kufungua. Mwanaume yule mwenye panki alimtizama mwanaume aliyekaa naye kando na kumtikisia kichwa. Mwanaume aliyepewa ishara akapenyeza mkono wake chini ya kiti na kutoka na kombora akaliweka begani.

    “Fyuuuuuuum!” Kombora lilifyatuliwa kuelekea kwa wanajeshi wale watano waliokuwa getini. Kwa haraka kombora lilkimbia, ingawa wanajeshi waliokuwa getini walikimbia, hawakupata nafasi ya kutokomea, kombora liliwatawanya wakawa matambara. Geti nalo lilifumukia huko likawa vyuma vyakavu.

    Wanaume wale ndani ya gari wakaendelea kupeta na barabara, kwa mbele kidogo whttp://pseudepigraphas.blogspot.com/alikata kona nyumba moja kubwa ikaonekana. Ghafla walitokea wanajeshi wengine wakaanza kulishambulia gari kwa risasi. Hawakufua dafu, wanaume wale waliokuwa kwenye gari walitembeza vizuri silaha zao kwa kulenga sawia wakapukutisha wanajeshi wote na kutua kwenye kiwanja cha nyumba waliyoiendea.

    Haraka wanaume walishuka toka kwenye gari na kuingia ndani ya jengo kwa kujiamini huku wakiwa wameshikilia bunduki zao mikononi. Waligawana majukumu wawili wakaenda kushoto wawili kulia, mmoja mwenye panki akawa anaranda peke yake. Baada ya muda waliwatia nguvuni watu watatu waliokuwa wamejificha chumbani. Mmoja alikuwa ni mwanamke mtu mzima mwingine akiwa msichana mwenye makadirio ya umri kati ya 23 mpaka 25, wakati wa mwisho akiwa ni mtoto mwenye umri usiozidi kumi na tano wala kupungua kumi na tatu.

    “Mume wako yupo wapi?”

    Mwanaume mwenye panki aliuliza kwa ukali huku akimtizama mmama mateka.

    “Sijui jamani! Aliniaga anaenda kikaoni basi.”

    “Mmesachi vizuri huko mavyumbani?”

    “Ndio mkuu!”

    “Wapakizeni twende. Haraka!”

    Amri ilitolewa. Upesi, wanaume wakawapakia mateka na kuanza nao safari. Mwanaume yule mwenye panki alibandua radio call toka kwenye dashboard akaweka sikioni.

    “Nimempata mke wa waziri tu, mwenyewe hayupo, over! … Ndio tupo njiani, over! … Msituni? … sawa mkuu tunakuja huko, over!”

    Alipomaliza kulonga alibadilisha muelekeo wa gari.

    “Tumeambiwa tuwapeleke msituni.” Mwanaume mwenye panki aliwaambia wenzake kisha mwendo kasi wa gari ukaongezwa kuelekea huko.

    Baada ya muda kidogo kwa kupita vioo vya pembeni vya gari, magari mawili yalionekana yanakuja kwa kasi. Kabla wanaume wale watano hawajaamua cha kufanya, risasi nne zilipiga gari lao kwa mkupuo … Pah! Pah! Pah! Pah! Moja ilimpata mwenzao maeneo ya shingoni. Nyingine ilimtwanga mtoto kichwani akafa papo hapo.

    “Chukua kombora, fasta! Mnasubiria nini? Shambulia!”

    Mwanaume mwenye panki alifoka, wakati huo mateka wao wakiwa wameficha vichwa vyao katikati ya mapaja huku wakipiga makelele ya woga. Ni eidha walihofia mwendokasi wa gari ama risasi zilizorushwa, au vyote kwa pamoja.

    Milio ya risasi ilirindima kwa fujo kila pande ikishambulia. Mmojawapo wa wanaume aliyekuwa kwenye gari alinyanyua kombora akalielekezea kwenye magari yanayowakimbiza na kufyatua. Gari moja likalipuliwa. Lilipaishwa juu na kupasuliwa pasuliwa likawa gofu. Hakuna aliyepona humo. Lilibakia gari moja tu sasa lililokuwa linawakimbiza. Mwanaume mwenye kombora alifyatua tena, lakini akakosea target, kombora lilikwenda pembeni na kulipua mojawapo ya nyumba pembezoni mwa barabara. Alipojaribu kufyatua tena, hakukuwa na kitu; makombora yalikwisha. Alitizama wenzake akapayuka;

    “Makombora yamekwisha!”

    Mwanaume mwenye panki akafoka; “Pumbavu! … Mliweka mangapi?”

    “Matatu tu.”

    “Matatu? … Wapuuzi kweli!”

    Ghafla, risasi zilirushwa zikitokea kwenye gari lililobakia. Mwanaume aliyekuwa na kombora akalengwa mgongoni na kifuani. Kama fuko la taka, akaangukia wenzake. Idadi sasa ya walio hai ikabakia wanajeshi watatu wa MDR pamoja na mateka wao wawili. Mwanaume mwenye panki alimkabidhi mwenzake usukani kisha akachukua bunduki na kuanza kuzirusha risasi kama matone ya mvua kuelekea kule kwenye gari linalowakimbiza. Alivunja kioo na kumuua dereva, gari likaenda mrama na hatimaye likapinduka.

    “Kitu kidogo tu mpaka mhangaike hivyo!” Aling’aka mwanaume mwenye panki. Alirudisha bunduki kwa mwenye nayo akakamatia usukani. Mwendokasi uliongezwa maradufu. Punde tu wafuasi wale wa MDR wakawa tayari wameshaiacha ardhi ya Sierra Leone na kuingia nchini Guinea. Waliingia misituni mpaka ilipo kambi yao, huko barabarani wakipishana na wafuasi wenzao, wengine wakiwa mazoezini, wengine wakifanya kazi za mikono kama kupasua kuni na kubeba majabali.

    Ndani ya muda mfupi, walitua makao makuu. Ilikuwa ni hema kubwa mno lenye madirisha mapana. Hema hilo lilikuwa limezingirwa na mahema mengine madogo yatumikayo kama stoo za kuhifadhia chakula na vinywaji, mengine yakiwa ni makazi ya wafuasi.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Wanaume watatu walishuka pamoja na mateka wakasimama nje ya hema kubwa. Mwanaume mwenye panki akaita.

    “General, tumefika!”

    Sekunde mbili kupita, akatoka mwanaume mfupi mwenye mwili mpana kwa misuli akiwa kavalia kashati kakum’bana na kofia ya kijeshi, kwa jina, General Kessy. Wafuasi wale watatu walimpigia saluti na kusimama kiukakamavu.

    “Amadu. Ripoti?” General Kessy aliuliza.

    “Hatujafanikiwa kumpata waziri, hakuwepo nyumbani kwake. Tumempata huyu mke na mtoto wake.”

    “Enhe … “

    “Tumepoteza wapambanaji wawili na mtoto mmoja mdogo wa waziri njiani.”

    General Kessy alitikisa kichwa chake kwa masikitiko. “Natumai mmeleta miili yao, sivyo?”

    Mwanaume mwenye panki, ama Amadu kwa jina, alitikisa kichwa chake na kujibu.

    “Ndio, mkuu. Ipo kwenye gari.”

    General Kessy alilifuata gari na kutizama miili ya wapambanaji wake pamoja na wa mtoto wa waziri aliyekufa. Alimtizama Amadu akampandishia kichwa;

    “Fanya utaratibu wazikwe. Na hao mateka wapelekeni chimbo.” Alisema General Kessy kisha akarudi ndani ya hema lake. Wanaume wawili waliokuja na Amadu wakawapeleka mateka kwenye nyumba moja ndogo ya mitimiti wakawafunga mikono na miguu na kuwaswaga ndani. Amadu alifuata kengele kubwa iliyoning’inizwa hatua chache toka makaoni, akapiga mara tatu kwanguvu. Wafuasi wa MDR wakaja upesi na kujikusanya eneo la wazi. Kwa mahesabu ya haraka walikuwa kama wanaume mia nane. Walijpanga kwenye mistari ishirini kila mstari ukiwa na watu arobaini kwa makadirio. Amadu akiwa mbele yao amesimama kwenye eneo la juu anapoonekana na kila mmoja, alifungua mdomo kwa ukakamavu;

    “Mapinduziii!” Amadu alipiga kelele huku akipandisha ngumi juu.

    “Mapinduzi daima! Mapinduzi mbele! Mapinduzi nayaletaa!” Uliitikia umati wa wafuasi.

    “Tanzia! … Wenzetu wawili wametutoka kazini. Mpambanaji Mustapha na ViPetit. Kama utaratbu wetu usemavyo, hauruhusiwi kumuacha mwenzako nyuma, pambana na umlete apumzike sehemu anayostahili. Tuungane katika kumpuzisha mpambanaji mwenzetu, lakini tukae tukijua mwili wake tu ndio uliokufa, mawazo yake ya kimapinduzi bado yako nasi.”

    Baada ya hayo maneno, miili miwili ya wafuasi waliokufa iltolewa garini na kupelekwa bondeni. Mashimo yalichimbwa na miili ikapata kuzikwa. Wakati matendo hayo yakifanyika, nyimbo za mapinduzi zilikuwa zikiimbwa zikiongozwa na mwanaume mwembamba mrefu almaarufu kwa jina la Hando.

    Mbali kabisa na umati wa wafuasi wazikao, aliketi Amadu peke yake juu ya jiwe kubwa akiwa amekunja mguu wake mmoja na mkononi amebebelea chupa ya kilevi. Macho yake yalikuwa mekundu na yalionyesha yu kilomita kadhaa kwenye dimbwi la mawazo. Picha ya mama yake ilimjia akilini. Alimuona mama yake aliyepigwa risasi mgongoni akilia huku akiwa kamshikilia mkono. Alijiona akikimbia na dada yake huku wanajeshi wa Sierra Leone wakiwakimbiza. Picha ya dada yake akibakwa na wanajeshi mbele ya macho yake huku akiwa kashikiliwa hana cha kufanya ilimjia kichwani na kumtafuna. Taswira ya baba yake akinyongwa mbele ya umati ilimjia na kumfanyia apaliwe na hasira, alipasulia chupa ya pombe juu ya jiwe alilokalia akainamisha kichwa chake na kuanza kulia. Alikaa hapo kwa muda usiopungua wala kuzidi dakika ukumi na tano, akanyanyuka na kwenda kwenye hema lake akalala.

    Ukiwa ni usiku wa saa mbili, ndani ya makao makuu, hemani, General Kessy alikuwa ameketi na Assessoko kwenye meza moja wakijadili. Juu ya meza kulikuwa na ramani kubwa ya Sierra Leone na Guinea.

    “Hatuna tena muda. Inabidi tuhamie na kuweka kambi Kabala.” Alisema Assessoko huku akionyeshea mji wa Kabala juu ya ramani.

    “Sawa, mkuu. Kwa sasa wapo wapambanaji kadhaa huko, wameshaweka vituo vyote vya polisi chini ya ulinzi na kukomba silaha. Ila tutahitaji vifaa zaidi. Kuingia Sierra Leone ni kutangaza vita rasmi.” Alieleza Kessy.

    “Najua kuhusu hilo, Kessy. Vifaa vinakuja zaidi, jeshi la Guinea wameshanihakikishia hilo. Kesho vinakuja vifaru vinne hapa pamoja na silaha zingine nzito.”

    “Sawa, mkuu. Ila bado tutahitaji msaada toka Guinea, hatutoweza kuhamisha kila kitu kwa kesho tu, ni hatari kwa usalama wetu pia.”

    “Sawa, Kessy. Ila ndani ya wiki hii, tujitahidi, inabidi tuwe tayari tumeshaweka kambi Kalima. Ni lazima tufanye hivyo kwa usalama wa Guinea juu ya uso wa dunia.”

    “Haina shida mkuu. Litatimia.”

    “Taarifa zaidi?”

    “Tumemkamata mke wa waziri Mamadou, pamoja na mwanae.”

    “Najua hilo. Nimeliona kwenye taarifa ya habari. Poleni kwa msiba pia. Muongeze umakini hatuwezi tukapoteza wapambanaji zaidi na vita havijaanza.”

    “Tutajitahidi, mkuu.”

    “Zaidi ni kwamba. Nimewasiliana na kundi la ukombozi la Liberia, Le tueurs, wapo tayari kutusaidia silaha zaidi. Inabidi utume watu kesho waende kuzichukua mpakani mwa Sulima na Liberia. Wakifika hapo watawasiliana na hao watu. Hakikisha hizo silaha zinafika hapa, Kessy.”

    “Sawa, mkuu.”

    Jamvi la maongezi likafungwa. Assessoko alipanda gari lake Toyota Land Cruiser J200 akapotea toka eneo lile la kambi. Kazi ikabakia kwa General Kessy kuchagua wanaume wa kazi wakafuate silaha Sierra Leone.

    ******

    Usiku haukua mzuri kabisa kwa Amadu. Mawazo yaliyokuwa yamemtinga yaligeuka na kuwa majinamizi ya ndoto yaliyozidi kumuandama kichwani na kumkosesha raha. Kila alipolala aliishia kushtuka. Alitizama saa ya mkononi akakuta ni saa sita na madakika usiku. Aliamua kutoka nje ya hema lake na kuanza kurandaranda nje kupunga upepo. Alizunguka huku na kule mithili ya mlinzi aliye doria kichwani akijawa na mawazo. Alipofika maeneo ya chimbo alisikia sauti ya mtu akilia, akashtuka kidogo. Aiiifuatilia sauti inatokea wapi akagundua ni ndani ya chumba cha mateka. Alisogea hilo eneo akachungulia kwa ndani. Akamuona binti amekaa chini akiwa anahangaika na mamaye anayetapa tapa.

    Mwanga hafifu wa mwezi uliokuwepo ulimsaidia Amadu kuona japo kwa mang’amu ng’amu. Kwa muda kidogo alitekwa na tukio alilokuwa analifanya yule binti la kujaribu kumuamsha mamaye. Alipotaka kuondoka, roho ilisita akaamua kubaki na kuendelea kutizama. Imani ilipomshika, alifungua mlango na kuingia ndani.

    “Vipi, mbona makelele?”

    “Mama anaumwa. Vidonda vya tumbo huwa vinamsumbua.”

    Amadu alimtizama mama akamuona anaendelea kuhangaika hangaika akirusha rusha mikono na miguu yake iliyofungwa. Alimtizama yule msichana akamwambia;

    “Ngoja nakuja.” Kisha akatoka akafunga mlango na kuelekea hemani kwake. Baada ya muda, alirudi akiwa na chupa ya maziwa.

    “Mpe. Fanya haraka, itamsaidia.”

    Amadu alimuelekeza msichana huku akimpatia chupa.

    “Naomba unifungue. Siwezi kumpatia hivi.”

    Amadu alifikiria kidogo kisha akamfungulia binti mikono. Binti alimnyanyua mama yake na kumnywesha maziwa huku Amadu akiwa anawatizama. Baada ya kupata maziwa, mama alipata kidogo unafuu, akajilaza kando. Amadu aliwatizama kwa macho ya huruma. Ni kama vile aikuwa anajilaumu kuwa sehemu ya waliofanya wale watu wawe eneo lile kwawakati ule, ila hakuwa na la kufanya.

    Aliwatakia usiku mwema mateka, akageuka na kuwapa mgongo aondoke. Ghafla, miguu yake ilivutwa akadondoka chini. Upesi, msichana alitoka ndani ya chumba cha mateka na kukimbilia msituni.

    Macho yalimtoka Amadu. Alinyanyuka akaanza kumkimbiza mwanadada. Alikumbuka ameacha mlango wa wazi, akarudi haraka na kufunga kisha akakimbilia huko msituni kumtafuta mateka. Huku macho yakiwa yamemtoka, Amadu alipepesa huku na kule asimuone mateka. Aliamua kuacha kukimbia akawa anatembea taratibu taratibu huku akiacha masikio yake yafanye kazi kwa weledi mkubwa. Moyoni alijinong’oneza;http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Naomba nimpate kabla wengine hawajamuona … Naomba nimpate kabla wengine hawajamuona.”

    Baada tu ya dakika chache, alisikia sauti ya kakara kakara upande wake wa kushoto. Amadu alirusha macho yake upande huo na kuanza kuusogelea kwa tahadhari akiifuata miti iliyofungamana. Ghafla … nyuma ya miti alitokezea mtu akaanza kukimbia! Alikuwa ni mateka. Amadu alifungua miguu yake kumkimbiza mlengwa wake. Hawakufika mbali, Amadu akawa tayari amemuweka nguvuni.

    “Tulia na ufunge mdomo wako! … Hivi unajua kama ungekamatwa na watu wengine ungekuwa ndio mwisho wako? Wanajeshi wametapakaa huku misituni!”

    Amadu alifoka kwa sauti ya kunong’oneza. Mateka alimtizama Amadu kwa macho ya hasira akafungua mdomo wake apige kelele, upesi Amadu aliwahi kumziba mdomo kisha akampiga na upanga wa kiganja chake chini ya kisogo, mateka akazirai, Amadu akamnyanyua na kumuweka begani wakaanza safari ya kurudi kambini.

    Kwa mwendo wa dakika moja na nusu, walifika karibu na kambi. Amadu aliona wanaume wawili wakifanya doria mikononi wakiwa wamebebelea kurunzi na silaha, haraka akajificha nyuma ya mti macho yake akiwa kayakodoa.

    Wanaume wale wawili, wafuasi wa MDR, waliokuwepo doriani walisonga wakafika eneo alilopo Amadu lakini wakapitiliza na kuendelea zao na safari. Amadu akanyanyuka haraka akaelekea mpaka chimbo, alifungua mlango akamuingiza mateka ndani.

    “Umemfanya nini, mwanangu?” Amadu alipokelewa na swali toka kwa mke wa waziri. Hakujibu, alifunga mlango akaondoka kurudi hemani. Alipofika tu na kujilaza, usingizi ulimbeba. Zoezi alilolifanya lilitosha kumsahaulisha kama si kumpa ahuweni na mawazo aliyokuwa nayo.

    Ilipohitimu saa kumi na moja asubuhi, kengele iligongwa wanajeshi wa MDR wakakusanyika wote eneo moja la makutano. General Kessy akiwa yupo kifua wazi, kifua chake kipana kikiwa kimetuna, alisimama mbele ya umati wa wafuasi akapaza sauti;

    “Mapinduzi!”

    Umati ukaitikia; “Mapinduzi daima! Mapinduzi mbele! Mapinduzi nayaletaa!”

    General Kessy alitizama umati kwa muda kidogo kisha akashuka jukwaani na kuanza kupita pita miongoni mwa wanajeshi kama mtu anayekagua gwaride.

    “Siku ya leo ni siku maalum na muhimu kwenye harakati zetu za mapinduzi. Baada ya masaa kadhaa tutapokea ugeni toka jeshi la Guinea. Vitaletwa vyombo zaidi hapa vya kivita kutuongezea nguvu. Na leo hii, kikosi M na N vitaelekea Kabala kuongeza nguvu ya wenzetu waliokuwepo huko kuhakikisha mji unakuwa chini ya ngome yetu. Vilevile, wafuasi wafuatao, wataenda mji wa Sulima, mpakani mwa Sierra Leone na Liberia kuchukua silaha toka kwenye kundi la Le tueurs. Nikitoka hapa wanifuate makaoni; Amadu, Mou, Talib, Ussein na Farah. Tumeelewana?”

    “Yes, sir!”

    “Tumeelewana!”

    “Yes, sir!”

    “Mbali na hayo, nataka niwataarifu kwamba. Muda si mrefu, tutahamishia makazi na kambi yetu katika mji wa Kabala. Hatutaenda kwa mkupuo, bali kimakundi mpaka wote tutakapomalizika. Jiweke tayari muda wowote. Kwenda Sierra Leone ni kutangaza vita rasmi. Mapinduzii!”

    “Mapinduzi daima! Mapinduzi mbele! Mapinduzi nayaletaa!”

    General Kessy akaruhusu wanajeshi watawanyike. Walibakia wale tu aliowataja majina wakamfuata General mpaka makaoni. General aliweka ramani mezani akaanza kuwapa maelekezo;

    “Hapa ndipo mnaenda, mtawakuta wanawasubiri nyie. Mtakapofika tu hapa, dhahiri watawaona na kuwapokea. Inabidi muwe waangalifu sana tena sana ndani ya Sierra Leone. Tokea tukio la kuvamia nyumba ya waziri na vituo vya polisi litokee, ulinzi umeimarishwa haswa mabarabarani. Wanajeshi wanaranda randa kila mahali. Amadu!”

    “Mkuu!”

    “Wewe ndiye utawaongoza wenzako. Sawa?”

    “Ndio, Mkuu!”

    “Hakikisha silaha hizo zinafika hapa baada ya siku nne tu. Utakapohitaji msaada unajua jinsi ya kutupata.”

    “Ndio, mkuu.”

    “Jua mnaenda kwenye mdomo wa simba. Werevu unahitajika kujilinda. Sawa?”

    “Sawa, mkuu!”

    “Haya kajiandaeni!”

    Amadu na wenzake walitoka hemani wakaenda kujiandaa kwa kuvaa nguo za kiraia na kupaki vyakula vya makopo garini. Baada ya muda mfupi wakawa tayari wamejipaki kwenye gari lao aina ya jeep, safari ikaanza.

    Kasi kubwa ya gari iliwaingiza nchi ya Sierra Leone ndani ya muda mfupi. Walitumia njia za panya wakikwepa njia kuu na za lami mara kwa mara. Baada ya muda waliufikia mto Rokel, wakasimamisha gari kwenda kupata maji.

    “Fanyeni haraka, hatuna muda wa kupoteza!” Amadu alisihi wenzake waliokuwa wamesogelea mto, Mou alikuwa anakinga maji na kunywa, Talib na Ussein walikuwa wanavua nguo wapate kuoga. Farah alishuka na kusimama kando ya gari akiliegemea.

    “Maji ya baridiiiii!” Talib alipiga kelele baada ya kujitumbukiza majini. Yeye na Ussein walionekana kufurahia kile walichokuwa wanakifanya. Amadu alitikisa kichwa chake akawanyooshea kidole;

    “Nimesema hatuna muda wa kupoteza!” Alifoka. “We Mou, si umemaliza kunywa maji, unasubiri nini hapo, tuondoke!”

    Upesi Mou alinawa uso wake akarudi garini. Ussein alitoka kwenye maji akavaa nguo, wakati Talib anatoka, sauti ya Amadu ilisikika;

    “Fanya haraka kuna watu wanakuja!”

    Talib alivaa upesi, yeye na Mou wakakimbilia garini na chombo kikaondoka. Hawakufika mbali, wakasimamishwa na wanaume watatu waliokuwa wamevalia sare za jeshi la Sierra Leone.

    “Mmmetoka wapi, mnaenda wapi?”

    “Tumetoka Kabala, tunaenda Magburaka.” Alijibu Amadu. Wakati huo wanajeshi wawili wa Sierra Leone walikuwa wakilizunguka-zunguka gari waliloliweka chini ya ulinzi.

    “Mnaenda kufanya nini?”

    “Kufanya biashara.”

    “Ipi?”

    “Ya kununua vitu na kuvipeleka Kabala.”

    “Vitu gani?”

    “Bidhaa mbalimbali tu tunazozikuta bei rahisi zaidi ya huko tutokako.”

    “Shukeni chini tukague gari. Msishuke na chochote kile.”

    Amri ilitolewa. Amadu na wenzake walitizamana. Kwenye sakafu ya gari kulikuwa na bunduki wasingeweza kukubali kukaguliwa. Amadu alikonyeza kisha akafungua mlango kwanguvu na kumbonda mwanajeshi aliyekuwa amesimama kando ya gari. Kwa haraka, Ussein na Talib walikamatia silaha zao wakazifyatua kuwalenga wanajeshi wawili na kuwaua papo hapo. Alibakia mmoja tu aliyebamizwa na mlango wa gari, alikuwa chini Amadu akimnyooshea bunduki,

    “Tafadhali, usiniue! Nakuomba … nina familia!”

    Alilalama mwanajeshi aliyewekwa kwenye himaya ya MDR.

    “Mmalize bwana tuondoke zetu!” Farah alimwambia Amadu.

    “Hapana, atatusaidia huko mbele.” Alisema Amadu kisha akamuamuru mwanajeshi aliyemueka chini ya ulinzi aingie ndani ya gari. Alipoingia, aliwasha gari wakaondoka. Hawakusimama njiani mpaka wanafika mji wa Magburaka. Jua lilikuwa tayari lishazama na giza lilikuwa limetawala. Haikuwa ni saa moja, mbili wala tatu, ilikuwa ni saa nane ya usiku inayoelekea saa tisa, dereva akiwa ni Mou, Amadu amepumzikia Kando akiwa anamtizama vyema mateka wao.

    “Tupumzike hapo kwa sasa.”

    Amadu alisema wakapaki pembeni. Wengine walikuwa tayari wameshakula, Amadu alichukua chakula akampatia na mateka wake wakawa wanakula. Ussein, Talib, Farah na Mou wakapitiwa na usingizi, walimuacha pekee Amadu akiwa sambamba na mateka.

    “Unaonekana ni kijana mdogo sana, una miaka mingapi?” Amadu alimuongelesha mwanajeshi waliyemteka.

    “Nina miaka ishirini na tatu.”

    “Kwenu ni wapi?”

    “Nyumbani kwa wazazi wangu ni Freetown, ila mimi naishi Rokel barracks.”

    “Nani alikushawishi kuwa mwanajeshi wa Sierra?”

    “Wazazi wangu.”

    “Wewe hukupenda kuwa mwanajeshi?”http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Hapana, nilitaka kuwa mchezaji mpira.”

    “Uliwaambia wazazi wako?”

    “Hapana, mana nilijua isingewezekana.”

    “Kipindi cha miaka mitano nyuma, ulivyokuwa na mika kumi nane. Ulipata kushuhudia machafuko nchini mwako, si ndio?”

    “Ndio!”

    “Ulikuwa wapi kipindi hiko?”

    “Nilikuwa nasoma shule ya upili, nakumbuka shule zilifungwa tukaambiwa tubaki nyumbani. Maduka yetu pamoja na nyumba ziliharibiwa sana, hata mashamba yetu pia. Mama yangu alipata ukilema, baba alipotea hatukujua kaelekea wapi, baada ya miaka miwili ndipo alirejea, ila maisha hayakuwa kama ya zamani. Tuliishi maisha ya shida, hakukuwa na jinsi ikalazimika niende jeshini kwa kuwa kipindi hiko kulikuwa kuna mahitaji makubwa sana huko.”

    Amadu alimtizama mwanajeshi yule mateka akatikisa kichwa chake kwa masikitiko. Aliuliza;

    “Kama unajua serikali iliyopo madarakani ndio chanzo cha kufa kwa ndoto zako, kwanini unaitumikia?”

    Mwanajeshi mateka alitulia kwanza akala tonge moja ndio akajibu;

    “Kama sitofanya hii kazi, nyumbani kwetu watakufa njaa. Mshahara wangu zaidi ya nusu nautuma nyumbani wapate kula.”

    “Wewe ni sehemu ya matatizo”

    “Kivipi?”

    “Badala ya kuuondoa utawala uliokusababishia makovu yanayokutafuna mpaka sasa, wewe unausaidia kisa pesa?”

    Mwanajeshi alinyamaza, aliendelea tu kula.

    “Nakukaribisha kuwa mfuasi wetu wa MDR. Nakukaribisha kuwa mwanamapinduzi.” Amadu alimwambia Mwanajeshi mateka. Mwanajeshi akashtuka kusikia hivyo;

    “MDR?”

    “Ndio!”

    “MDR kundi la waasi?”

    “Sisi si kundi la waasi, ni kundi la ukombozi. Ni kundi la wale walioachwa na vidonda na makovu na Louis Diarra. Tumeungana kwa ajili ya kumtoa madarakani na kulipiza kisasi kwa kuua wazazi wetu pamoja na ndoto zetu. Jiunge nasi. Utapata hiyo pesa unayotaka ya kuwatumia wazazi wako. Kaa ukijua Sierra Leone inakuhitaji.”

    Mwanajeshi yule mateka hakusema jambo. Aliendelea kula, alipomaliza alijilaza usingizi ukampitia. Amadu alibakia macho mpaka mida ya saa kumi na moja alipowasha gari na kuendelea na safari. Wenzake walipoamka, aliwakabidhi usukani na yeye akapumzika. Kila kituo cha ukaguzi walipopita mateka wao aliwaokoa kwa uwepo wake ndani ya gari. Baada ya siku moja ikiwa mchana wakawa wamefika mpakani mwa Sierra Leone na Liberia, pembezoni kidogo tu ya mji wa Sulima.

    “Mbona hawaji?” Talib aliuliza huku akirusha macho yake huku na kule.

    “We tulia. Walisema tukishafika hapa watakuwa tayari wametuona.” Amadu aliwaondoa hofu. Kweli, baada ya muda kidogo yalikuja magari mawili aina ya Nissan Patrol, yakapaki pembeni ya gari la wakina Amadu. Amadu akashuka na kukutana na wanaume wawili walioshuka toka kwenye magari yale. Waliposalimiana na kutambulishana, Silaha zilitolewa toka kwenye magari mawili yaliyokuja zikahamishiwa kwenye gari la wakina Amadu. Zilikuwa ni bunduki aina ya SMG zikiwa na risasi za kumwaga pamoja na vipande vya mabomu, kazi ya kuhamishwa ikifanywa vilivyo na vijana watano wa Le tueurs wakati wakina Mou, Farah, Talib na Ussein wakiwa ndani ya gari lao.

    Zoezi la kupaki lilipokwisha, mwanaume aliyeonekana ni kiongozi wa kundi la Le tueurs alimpa Amadu mkono wa pongezi kisha akamkabidhi barua.

    “Hakikisha barua hii inafika mkononi mwa General Kessy. Usijaribu kumpa mtu yeyote, wala kuifungua huko barabarani.”

    General Kessy aliitizama ile barua kama mtu anayetamani kujua yaliyomo, mwishowe alipuuzia akaingia zake kwenye gari na safari ya kurudi kambini ikaanza. Moja kwa moja tairi za gari zilitembea mpaka mji wa Bo baada ya kuvuka mto Sewa. Wakiwa wapo njiani sasa kuutafuta mji wa Magburaka mida ya jioni ikimbiayo usiku, tairi mbili za gari za nyuma zilipasuka. Gari liliyumba na nusura lianguke kutokana na kuwa kwenye mwendo mkali, Amadu alijitahidi kulimudu alipoweka chombo sawia alizima gari, wote wakashuka kwenda kutizama matairi.

    “Duh! … Hapa kazi ipo!” Ussein alisema huku akishikilia kiuno.

    “Tubadlishe haraka, tutapoteza muda hapa.” Amadu alitoa maelezo, pembeni yake alikuwa amesimama mwanajeshi wa Sierra Leone.

    Talib na Mou walitoa matairi mawili nyuma ya gari pamoja na vifaa, shuguli ya kurepea ikaanza, Mou na Talib wakisimamia zoezi vyema, Ussein, Farah na Amadu wakiwa pembeni wanatizama lakini mara zingine wakiwa wananyoosha nyoosha miguu kwa kutembea tembea huku na huko.

    “Fanyeni haraka, hili eneo si salama.” Mwanajeshi wa Sierra Leone alitoa angalizo. “Kilomita tatu tu toka hapa kuna kituo kikubwa cha jeshi na huwa wanafanya doria mara kwa mara.”

    Likiwa tairi moja tayari na lingine lakaribia kukamilika, milio ya risasi ilisikika. Amadu na wenzake wakatahamaki.

    “Inatokea wapi hiyo?” Amadu alirudha swali huku akipepesa pepesa macho yake.

    “Inatokea huko huko nilipowaambia. Wanafanya mazoezi ya kijeshi kujiweka tayari na vita. Hapa si salama na natumai mbele tu kidogo tutakutana na kizuizi.”

    Zoezi la kuweka tairi lilipokwisha, walijipakia kwenye gari safari ikaendelea. Hawakuchukua hata muda, mbele yao waliona kikosi cha wanajeshi kikiwa kinafanya mazoezi ya kukimbia.

    “Geuza gari!” Mwanajeshi wa Sierra Leone alipaza sauti huku akimtizama dereva Amadu.

    “Kwanini?”

    “Hawatowaruhusu mpite. Watawakagua gari lote!”

    “Si upo na sisi?”

    “Si kila mara hilo litasaidia. Ni hatari kwa sasa. Wakiwa mazoezini huwa wana tabia ya kusimamisha magari na kuanza kuyapekua pekua, wakikuta vitu wanachukua.”

    Amadu aligeuza gari haraka kuanza kurudi walipotokea. Kitendo hiko kiliwapa shaka wanajeshi waliokuwa mazoezini mkubwa wao akatoa taarifa kituoni kwa radio call yake.

    Baada ya kurudi nyuma kwa mita kadhaa, wakina Amadu waliacha njia ya lami na kuchukua ya mavumbini wakaendelea na safari yao ya kurudi kambini. Hawakufika mbali na hiyo njia, mbele wakaona magari matatu defender za jeshi zikiwa zimeziba njia. Amadu alisimamisha gari akawatizama wenzake.

    “Hapa hakuna jinsi, lazima tupambane.”

    “Hapana! … Ngoja.” Mwanajeshi wa Sierra Leone aliyekuwepo ndani ya gari aliingilia kati. “Acha nikaongee nao.”

    “Ukaongee nao? … Sisi tutakuamini vipi?” Talib aliuliza.

    “Hapana! … Ataenda kutuuza, kaa humu humu!” Farah alieleza mashaka yake.

    “Hata mimi siliafiki hilo.” Mou naye aliunga mkono wenzake. Amadu alimtizama yule mwanajeshi machoni kwa muda kidogo akamuambia;

    “Nakuamini, nenda. Shika hii.”

    Alimpatia bunduki ndogo. Mwanajeshi yule akaweka silaha yake kiunoni akashuka garini na kusogelea magari yale matatu yaliyoziba njia, pembezoni mwake wakiwepo wanajeshi wanne wenye kubebelea bunduki kubwa.

    “Umefanya makosa Amadu!” Talib alilaumu.

    “Utatugharimu maisha huo ubishi wako.” Talib alisema kwa jazba. Amadu hakusema lolote, macho yake yalikuwa bize kumtazama mtu aliyemruhusu akaongee na wanajeshi walioziba njia. Alimuona mtu wake akitoa maelezo na wanajeshi wenzake wakimsikiliza, ila baada ya muda kidogo wanajeshi wawili waliongozana na yule mwanajeshi aliyetumwa na Amadu kufuata gari walilokuwepo wafuasi wa MDR.

    “Unaona sasa ametuchoma!” Talib aliweweseka.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Kila mtu ashike silaha yake!” Amadu alitoa amri. Kila mmoja akaweka bunduki yake tenge kwa shambulizi. Wanajeshi walipofika, waliwatizama wakina Amadu usoni wakawaamuru washuke chini. Kabla ya kutekeleza hiyo amri, mwanajeshi aliyetumwa na Amadu alionyeshea ishara ya kidole gumba kikikata koo akizuga kama mtu anayejikuna. Papo hapo, Amadu akasema; “Fire!” Ussein, Talib, Mou na Farah wakashambulia wale wanajeshi wawili kisha wakaanza kulenga yale magari matatu yaliyo njiani. Mwanajeshi aliyetumwa na Amadu alipanda kwenye gari haraka lakini kabla hajaingia mzima, alipigwa risasi ya mgongoni. Mashambulizi yalikuwa makali kila pande ikimwaga risasi. Vioo vya magari vilipasuka na vingine kuwa nyang’anyang’a. Amadu alivuta boksi la mabomu akatoa mabomu mawili aliyoyachomoa vipini na kuyarushia kwenye magari matatu yaliyo njiani. Magari yale pamoja na watu wake wakalipuka na kusambaratika. Gari la wakina Amadu likiwa sasa halina kioo cha mbele, likaanza kuchanja mbuga kwa mwendo kasi mkali japokuwa upepo wa nguvu ulikuwa unaingia kupitia uwazi ulioachwa na kioo. Kukabiliana na upepo, Amadu alitoa miwani yake kwenye dashboard akaivaa, huku akitizama mbele alizidi kuchochea gari. Alibadilisha njia akaacha ya kuelekea mji wa Magburaka na kuanza kusonga kuutafuta mji wa Koidu. Walipofika katika huo mji, walisimamisha gari kwa kulificha machakani. Amadu alishuka na kuamuru mwanajeshi wa Sierra Leone ashushwe, mwanajeshi akashushwa na kulazwa chini huku Ussein akiwa anatia mgandamizo kwenye jeraha la risasi kuzuia damu zisimwagike zaidi.

    Amadu alitizama jeraha la mwanajeshi yule kisha akatoa kisu chake kikubwa kwenye mfuko wa kiunoni.

    “Jikaze mwanaume, nataka nitoe hiki chuma ndani ya mwili wako.” Amadu alimwambia yule mwanajeshi ambaye alikuwa akihema na kukunja sura kwa maumivu makali aliyokuwa anayapata kisha akaokota kijiti na kumuwekea mdomoni;

    Ng’ata hii, usikiteme.”

    Mwanajeshi yule akaking’ata kijiti kwanguvu huku akifunga macho yake. Amadu alikata sehemu yenye jeraha, huku damu zikitiririka, alipanua jeraha akaingiza vidole viwili na kutoa risasi, wakati huo anayefanyiwa upasuaji huo mbadala akipiga kelele huku aking’ata kwanguvu kijiti mdomoni.

    “Lete sindano na uzi kwenye dash, fasta!” Amadu alimuamuru Farah. Haraka uzi na sindano ukaletwa, Amadu akaanza kushona jeraha. Mgonjwa alipiga makelele zaidi. Alng’ata kijiti mpaka kikavunjika. Mwishowe alizirai kwa kushindwa kuhimili maumivu. Amadu alipomaliza kufanya upasuaji, alimbeba mgonjwa akamuweka ndani ya gari.

    “Sasa huyu tunampeleka wapi? … Si tumuache tu ajifie huku?” Talib alimshauri Amadu.

    “Tunaenda naye kambini.” Amadu alijibu na kuongezea, “Haachwi popote.”

    “Tunaenda naye kambini kivipi na hatukuja naye?” Talib aliuliza.

    “Nimeshasema tunaenda naye, full stop!”

    “Kaa ukijua huna mamlaka yoyote juu yetu. Umechaguliwa tu uongoze na si kwamba unajua sana. Unavyojiamulia mambo yako mwenyewe maana yake nini?” Talib alisema kwa jazba.

    “Hatuendi na mtu yeyote yule kambini, unajuaje kama tunampeleka mamluki? … Wewe mbona akili yako imeganda?” Talib alendelea kuwaka. Amadu alimtizama kisha akaachana naye kwa kumpuuzia.

    “Si naongea na wewe, hunisikii au?”

    Amadu kimya.

    “Nimesema hatuendi na mtu yeyote, unataka kutuchoma nini wewe?” Talib aliendelea kumwaga sera. Ghafla, Amadu aligeuka akampa Talib ngumi nzito usoni Talib akadondoka chini.

    “Pumbavu wewe!” Amadu alitema cheche. “Unadhani mimi ni mjinga kama wewe! … Najua ninachokifanya!”

    Talib alinyanyuka kwa jazba akitaka kurudishia mashambulizi ila wenzake wakamuwahi na kumshika.

    “Niachie nimuonyeshe huyu mpumbavu!” Talib alifoka. Amadu alitabasamu akatikisa kichwa;

    “Embu muachieni nione anchotaka kufanya.” Amadu aliwaambia Mou na Farah waliokuwa wameshikilia Talib. Mou na Farah wakatekeleza agizo. Talib alikuja kwa kasi kumfuata Amadu, Amadu aliruka juu akajigeuza na teke kali lililobamiza kichwa cha Talib kwanguvu na kumrusha mwaume huyo mbali kama kikaratasi. Hakunyanyuka tena, badala yake akawa analalamika maumivu mikono ikiwa kichwani na miguu ikitapatapa.

    “Kuna mwingine anayebisha?” Amadu aliuliza. Hakuna aliyejibu, wote walikaa kimya.

    “Ahsanteni.” Amadu alisema kisha akaenda kujilaza kwenye kiti cha dereva. Giza la usiku lilipoingia, walikula lakini chakula hakikutosha. Amadu aliamuru wakatafute chakula kwenye vijiji vya pembezoni, wote wakaafiki isipokuwa Talib.

    “Siendi popote! Nitakaa hapa hapa. Chakula kilikuwa kinatutosha kabisa, nyie si mmebeba watu wasio na maana yoyote, katafuteni huko!”

    Amadu pamoja na wenzake, akiwamo mwanajeshi wa Sierra Leone, waliongozana kwenda vijiji vya pembezoni. Walivamia nyumba wakakwapua vyakula. Wakati wanarudi, Amadu aliona basi moja kubwa likiwa lmepakiwa kwa mbali kidogo, aliwakabidhi wenzake mzigo wake na kuwaambia watangulie yeye akaenendea lile gari. Alipasua mlango akaingia ndani mwa basi, chini ya usukani alikata nyaya fulani na kuziunganisha, basi likawaka, akaliondoa na kulipeleka walipo wenzake.

    “Hamisheni kila kitu tuweke huku!” Amadu alisema huku akielekezea kidole kwenye basi.

    “Amadu, huoni kama ni hatari kutembea na basi? … Ni rahisi kuonekana na halina mwendokasi mkubwa.” Ussein alitoa mawazo.

    “Hapana!” Amadu alijibu kisha akafafanua, “Gari letu halina tena kioo kwahiyo inakuwa ngumu kutembea kwa kasi yake, lakini pia hili basi litatusaidia kukwepa vizuizi vya mara kwa mara kwa kudhaniwa ni la abiria vile vile lina nafasi kubwa ya kuficha silaha zetu tutaziweka kwenye buti.”

    Mou, Farah Ussein na hata yule mwanajeshi wakaliafiki hilo jambo. Talib yeye alikuwa ametulia asishiriki kwenye lolote. Silaha zilianza kuhamishwa toka kwenye gari dogo kwenda kwenye basi. Zilipomalizika walipumzika wakalala humo humo basini.

    Katikati ya usingizi mzito, Talib alifungua macho akatizama pande zote. Alitoka kwenye gari ndogo akanyata kwenda kwenye basi akachungulia ndani na kuwaona wenzake wakiwa wamelala. Taratibu akalifuata buti na kulifungua akaanza kupakua silaha na kuzirudisha kwenye gari ndogo. Alipomaliza, alisukuma gari ndogo kutoka lile eneo alipofika mbali akapanda akawasha gari na kuyoyoma.

    Bado giza likiwa halijaacha uso wa ulimwengu lakini ni tayari asubuhi, Amadu alikuwa wa kwanza kufungua macho yake. Alitoka nje ya basi akaenda kukojoa, alipotizama kando hakuona gari ndogo. Alisogea eneo la tukio akarusha macho yake kutafuta gari asione kitu. Alipotizama basi aliona buti li wazi. Haraka akakimbilia hapo na kutizama. La haula! Hakukuta kitu. Alinyanyua mikono yake akaiweka kichwani.

    “Talib, unacheza na moto wa bluu.” Alisema huku akikunja ndita kwa hasira. Alifunga buti na kurudi ndani ya basi akawasha gari; wenzake wakashtuka na kuamka.

    “Talib ameondoka na silaha!” Amadu alifoka.

    “Ameenda wapi?” Farah aliuliza.

    “Sijui kaelekea wapi, anataka kuniletea majanga mshenzi huyu!” Amadu aliroroja kwa hasira.

    “Hakuna njia yoyote inayotoka hapa zaidi ya moja tu.” Mwanajeshi wa Sierra Leone alichangia, “Ukiachana na hii njia tuliyokuja nayo, endelea mbele kilomita tatu toka hapa ndio kuna njia panda.”

    Baada ya maelezo hayo, Amadu aliongoza gari kuelekea mbele kwa mbele kwa kasi kubwa mno. Jua lilichomoza wakiwa barabarani na bado hawajampata Talib. Walipofika njia panda walisimama wakashuka. Amadu alichuchumaa akatizama barabara ile ya vumbi kwa umakini.

    “Ameelekea huku!” Alisema Amadu huku akionyeshea kidole barabara ya kushoto.

    “Mmmh ila barabara hiyo inaelekea Kissidougou, Guinea.” Mwanajeshi wa Sierra Leone alitia shaka.

    “Guinea?”

    “Ndio!”

    “Ila matairi yanaonyesha kaenda huko! … Hiyo njia ni ndefu sana mpaka kufika kambini kwanini atumie hiyo njia?” Amadu alijiuliza. Mwishowe waliamua tu kufuatilia hizo nyayo za tairi ambazo mbele kidogo zilikata kona na kwenda njia ya kulia.

    “Nilijua hawezi akaenda hiyo njia.” Alisema mwanajeshi wa Sierra Leone. “Sasa hapa itakuwa rahisi kumpata, hii njia ipo moja tu na inaelekea mpaka Kabala baada ya siku moja. Ila kuna wanajeshi wengi, sijui kama huyo Talib ataweza kumudu.”

    Amadu alisonya bila ya kusema kitu. Alizidi ongezea nguvu kwenye pedeli ya mwendokasi, basi likazidi kupepea. Baada ya muda, basi lilifika kwenye kizuizi ila hakukuwa na mwanajeshi yoyote pande hizo. Kabla ya kupita na kuendelea na safari, Amadu alisimamisha basi akashuka na kuanza kupepesa macho yake. Kwa mbali kidogo na kizuizi akawaona wanajeshi wawili wamekufa, haraka akawasogelea na kupima miili yao kwa mgongo wa kiganja chake, alipomaliza akarudi kwenye gari upesi;

    “Talib amepita hapa muda si mrefu. Miili ya wale wanajeshi bado ya moto.”

    Amadu alisema kisha akaanza kuondoa gari lake upesi kumtafuta Talib. Mungu si athumani, akamuona kwa mbali. Amadu alitabasamu akamuonyeshe kidole Talib.

    “Yule kulee! … Aandike maumivu!” Amadu aliwaambia wenzake huku akikoleza mwendo.

    “Huyu jamaa ujue ni mshenzi sana.” Farah alisema macho yake yakiwa yanatizama gari alilomo Talib.

    “Sijui anafikiria nini?” Mou naye alichangia.

    “Talib hapendi kuongozwa. Ni mtu wa aina hiyo.” Ussein alitia neno, “ni mtu anayetaka kuongoza na si kuongozwa. Yani pale atakuwa tu anataka yeye ndio afikishe ule mzigo.”

    “Sidhani!” Farah alidakia na kuongezea,.”Mzigo tumetumwa wote, si yeye pekee. Lengo lake ni kumkomoa tu Amadu. Talib ni mtu wa visasi.”

    Baada tu ya hiyo kauli risasi sita zikapiga kioo cha basi zikitokea kwenye gari la Talib. Basi liliyumba lakini Amadu alilituliza na kulipunguza kasi, Talib akapata tena upenyo wa kupotea machoni mwa wenzake waliobaki na bumbuwazi. Baada ya hapo, Talib hakupata kuonekana tena hata kwa bahati mbaya, zilipotimia siku tano tangu watumwe, Amadu na wenzake ndio wakafika kambini asubuhi na kukuta gari lililokuwa linaendeshwa na Talib likiwa limesimama mbele ya makao makuu. Amadu na wenzake walitizamana wakaenda ndani ya makao wakamkuta General Kessy pembeni yake akiwa na maboksi ya silaha. Walitoa saluti, General Kessy akasimama.

    “Niliwategemea sana, hasa wewe Amadu. Nilitegemea mtatii amri milyopewa na kufuata kile mlichoambiwa mkakifuate, badala yake mmeenda na kujiamulia cha kufanya, sio?”

    “Hapana, mkuu!” Amadu alisema kwa ukakamavu.

    “Hapana nini? … Niliwaambia muwe hapa baada ya siku ngapi?”

    “Nne, mkuu!”

    “Leo ni siku ya ngapi?”

    “Ya tano, mkuu.”

    “Badala ya kuja na silaha jana, nyie mmekuja na mwanajeshi wa Sierra Leone na basi? … Akili hiyo?”

    “Hapana mkuu, kuna matatizo yaltokea njiani …” Amadu alijitetea, General Kessy akaingilia;

    “Usiniambie chochote. Talib amekwisha nieleza kila kitu.”

    “Hapana, mkuu. Talib ame…” Farah alitaka kutoa elezo, Kessy akamnyooshea kidole;

    “Wewe, nyamaza! … Sitaki kusikia ujinga wenu. Nilituma silaha ndani ya siku nne si kingine. Talib peke yake ndiye aliyetimiza hilo agizo baada ya kuona uzembe wenu. Sasa ni hivi, lazima muwajibike na kosa lenu. Amadu peleka huyo mtu wako chimbo alafu uje hapa.”

    Kabla Amadu hajatoka, alimkabidhi General Kessy barua yake aliyopewa na kiongozi wa Le tueurs. General Kessy alipoifungua barua alitaka watu wote watoke na kumsubiria nje. Wote wakatoka, Amadu akampeleka mwanajeshi wa Sierra Leone chimbo.

    “Usihofu utatoka tu, amini hivyo.” Amadu alimwambia mwanajeshi wa Sierra Leone wakiwa njiani kuelekea chimbo. “Utatoka na utatumikia mapinduzi. Ila kabla sijakuingiza ndani ningependa kujua jina lako, unaitwa nani?”http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    ”Naitwa Amir.”

    “Mi ningependa kukuita Chui.’

    “Kwanini?”

    “Kwasababu una kitu ndani yako kama chui. Bahati mbaya ni mimi pekee ndiye niliyekionai.”

    “Ahsante sana. Nakuamini.”

    Hayo yalikuwa maneno ya mwisho ya Amir ama Chui kama alivyobatizwa na Amadu kabla hajaingia ndani ya chemba yake binafsi na kufungiwa humo. Amadu alirudi makao makuu na kukuta wenzake wakiwa wanamngoja General Kessy, baada ya muda kidogo general alitoka akaangaza;

    “Amadu, ulifungua huu ujumbe uliopewa?” General Kessy aliuliza huku akionyeshea barua.

    “Hapana! Sijasoma mkuu.” Amadu alijibu.

    “Ni bora hiko ukisemacho kiwe kweli, maana nikigundua kinyume na hilo, utakuwa katika wakati mgumu.” General alitoa tisho kisha akaendelea, “Kachukueni vifaa vyenu mkakate magogo. Nahitaji magogo thelathini hapa kabla ya jua kutua. Potea!” Amadu, Farah, Mou na Ussein wakaenda mahemani mwao wakatoka na mashoka wakaelekea magharibi mwa kambi yao umbali wa nusu kilomita wakaanza kukata miti.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog