Search This Blog

Friday 18 November 2022

BARADHULI MWENYE MIKONO YA CHUMA (1) - 4

 






Simulizi : Baradhuli Mwenye Mikono Ya Chuma (1)

Sehemu Ya Nne (4)







Marietta hakusema jambo. Akitizama chini, aliondoka bila kuaga akaelekea chumbani kwake na kufunga mlango na komeo. Bernadetha alishusha pumzi ndefu akazaba kofi paji lake la uso.







“Mungu baba!”

Alitikisa kichwa. Alishika kiuno akafuata jiko na kuanza kuandaa chakula.







Mshale wa saa ulizunguka duara toka kwenye 2 mpaka kwenye 8. Giza lilivamia nchi. Mataa yaliwashwa kupunguza ukali wa giza watu wapate kuona.







Gari la Jombi lilisogea likapaki karibu na maeneo ya nyumba ya marehemu Malale. Ndani ya chumba, Miraji alikuwa ndio anamalizia kujiandaa kwa kuvaa. Alifungua dirisha akatoka nje na kufuata gari, wakatokomea.







Wasifike mbali, Bernadetha alienda mlango wa chumba cha Miraji akagonga akiita jina. Aligonga na kugonga asipate majibu. Alifungua mlango akakuta kitanda kitupu.







“Jamani! Jamani! Jamani! Mirajii!” Bernadetha alilia. Kilio chake hakika hakikufika kwa Miraji aliyekuwa tayari kilomita moja na nusu mbali naye.

“Hakuna muda wa kufanya makosa, Miraji.” Jombi alikumbushia. Miraji akatikisa kichwa. Akatoa picha ya baba yake toka kwenye begi akaitizama.







Walipofika, aliirudisha picha kwenye begi akafunga macho yake asali. Baada ya hapo, alifungua mlango wa gari Jombi akimtakia bahati njema.







Alivalia kinyago akaweka begi mgongoni. Alisogelea jengo la Raheem kwa nyuma akilifuata bomba la kutolea maji machafu.









Miraji alivua begi lake mgongoni akatoa kamba yenye kishikizi na kuirushia ndani. Aliijaribu kwa kuivuta, akaona imekamata. Alihamishia begi kwa mbele, kifuani, akaanza kujivuta na kamba aingie ndani. Alipoingia alichuchumaa akaikusanya kamba yake na kuitia ndani ya begi, akafuata zizi na kujibanza hapo huku akitizama mazingira ya nyumba.







Kulikuwa kimya. Sauti za watu zilikuwa zinasikika toka ndani ya nyumba. Kwenye uwanja kulikuwa na gari aina ya Toyota carrier pekee. Gari atumialo Raheem halikuonekana, labda halikupatikana tokea lipotee siku ile hospitali.







Pembeni ya geti la nyumba kilijishikiza kibanda cha mlinzi. Na hapo ndipo Miraji alipoanza kuelekea kwa kunyata. Ila kabla hajafika, sauti ya mbwa ilibweka nyuma yake, aligeuka akaona mbwa mkubwa mweusi anamfuata.







Haraka alirudi zizini kwa kukimbia akifungua begi lake na kutoa mfuko wa nailoni. Alitoa kipande cha nyama akamrushia mbwa. Mbwa akadaka na kunyamaza kimya akitafuna.







Sekunde tatu mbele, mbwa alidondoka chini akafa. Kabla Miraji hajaenda popote, mwanga wa kurunzi ulimmulika mbwa. Alikuwa ni mlinzi. Haraka Miraji alitia kamba ndani ya begi akatoa kitambaa kidogo cheupe akakipulizia spray.







Mlinzi alimsogelea mbwa haraka akiita;

“Simba! Simba!”







Alitizama pembeni akaona kipande cha nyama. Alitoa bunduki yake mgongoni akaihamishia mikononi kurunzi yake akawa anaipepesa huku na kule akiisindikiza na kitundu cha bunduki yake kubwa na macho yake yaliyokuwa hayana chembe za utani. Wakati huo Miraji alikuwa ametulia akimchungulia mkono wake wa kulia ukibebelea kitambaa.







Taratibu mlinzi alilifuata zizi. Alisogea taratibu asijue anamsogelea Miraji ambaye alitokea ghafula nyuma yake akaipiga bunduki ikarukia mbali kisha akamkaba akimziba mdomo na pua kwa kitambaa.

Isichukue muda mrefu, mlinzi akapoteza fahamu.







Miraji alinyanyuka akafuata dirisha na kuchungulia ndani, akawaona watu wawili: mwanamke mtu mzima na mtoto wa kike wakiwa wanatizama televisheni. Alitoa bunduki yake toka nyuma ya kiuno akaiweka mkononi na kuufuata mlango.









Ngo! Ngo! Ngo!

“Naniii?” Sauti ya kike iliuliza tokea ndani. Miraji akanyamaza kimya.

“Huyo atakuwa li mlinzi?”

“Kama kawaida yake, atakuwa anataka maji. Mchukulie hapo juu ya friji mpelekee.”







Zikapita sekunde kadhaa mlango kufunguliwa, alikuwa ni binti mdogo akiwa amebebelea jagi la maji. Miraji alimdaka binti huyo kwa mkono wake wa kushoto akamkaba akimziba na kitambaa huku akiingia naye ndani ameelekezea bunduki kwa mwanamke aliyeketi sebuleni.









“Raheem yupo wapi?” Miraji alifoka akimuuliza mwanamke aliyeketi kochini.







Binti aliyekuwa amezibwa na kitambaa alidondoka chini akapoteza fahamu. Miraji aliachana naye akamsogelea sasa mwanamke yule kwenye kochi. Miraji alihisi ni mke wa Raheem. Alikuwa anatetemeka mno akijivuta nyuma ya kochi kana kwamba pana njia ya kwenda sehemu nyingine hapo.



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Raheem, yupo wapi?” Miraji alirudia kuuliza. “Sitouliza kwa mara nyingine, nitazamisha chuma cha risasi nikubadilishe jina sasa hivi!” Miraji alisema akitumbua macho.

“Yupo ndani! Amelala!”

“Ssssh! … Taratibu. Chumba gani?”

“Cha mwisho kabisa.”

Miraji alimziba mwanamke huyo na kitambaa, akazirai. Alisogelea chumba alichoelekezwa, akafungua mlango akioneshea bunduki kitandani.

“Hey Mr. your time to die!” Miraji alipayuka.







Raheem aliamka kwa pupa. Alitoa macho yake kwa woga. Alinyoosha mikono yake juu akiomba;







“Tafadhali usiniue! Chukua unachotaka!”

Miraji akatikisa kichwa.

“Baba yangu ulimuacha?”

Raheem akashituka akiachama.

“Baba yako? ... Baba yako yupi? … Wewe ni Miraji?”

“Ndio. Bahati mbaya umekuwa wa kwanza kwenye orodha. Rest in hell.”

“Tafadh …”







Kabla ya sauti haijamalizika, mlio wa risasi ulivuma tundu likijichora kwenye paji lake la uso. Alilala damu pomoni zikimchuruza.









“One down!”







Miraji alisonya akitoka chumbani. Alifuata gari la Jombi kwa njia ile ile aliyotumia kuingilia. Alipofika alivua kinyago chake wakatokomea haraka toka eneo lile.









“Vipi umefanikisha?” Jombi aliuliza.

“Yap! Tayari nimemaliza.”

“Vizuri sana!” Jombi alitabasamu. “Sasa tujipange kwa ajili ya kazi nyingine. Natumai waliobaki wataweka ulinzi imara wakipata hizi habari. Inabidi tutulie, tuchore mipango ndio tushambulie.”

“Sawa. Kwa sasa tageti yetu ya sasa ni Mr Filbert, yupo hospitali. Nadhani itakuwa rahisi kumuingilia endapo tukitumia fursa ya wageni wanaomtembelea, au unaonaje?”

“Hospitali anafanya nini?”

“Amelazwa. Alipata ajali. Nimezipata hizo taarifa kwa mama.”

“Ok. Inabidi tukamtembelee tujue na kuchambua mazingira yake.”

“Lini?”

“Nitakutaarifu, wacha msiba wa Raheem upite kwanza.”

“Je akiruhusiwa? Huoni tutakuwa tumepoteza njia rahisi?”

Jombi akafikiria kidogo na kusema:

“Basi ngoja nitakutaarifu. Kuwa tayari muda wowote.”







Baada ya maongezi hayo machache, injini tu ya gari ndiyo ilisikika mpaka wanafika mbele ya nyumba ya marehemu Malale, kwa wakina Miraji, waliagana Jombi akaondoka.







Miraji alisogea akachungulia dirishani. Alimuona mama yake amelala kwenye kochi. Alivua viatu vyake akavishika mkononi.







Alifungua mlango taratibu akanyata akielekea chumbani, kabla ya kutimiza adhma, sauti ya Bernadetha ikawika nyuma yake.







“Miraji, ulikuwa wapi?”

Miraji akashituka. Alisimama kama askari wa gwaride asijue la kufanya.

“Si nakuuliza wewe, unatoka wapi mwanangu saa hizi saa tano kasoro?” Bernadetha aliuliza kwa sauti yenye huruma na hasira ndani yake.

Miraji aligeuka akamtizama mama yake, alitabasamu kiuongo akimsogelea.

“Mama … Shikamoo.”

“Ulikuwa wapi?”

“Nilikuwa kwa rafiki yangu.”

“Nani?”

“Mshikaji wangu tu.”

“Nani? ... Jombi?”

“Aah-aah!”

“Mwanangu, unapotea. Hii tabia ya kutoka na kurudi usiku umeanza lini? Simu hupatikani, mama yako nakaa roho juu juu sina amani. Kwanini unafanya hivi lakini? Likikutokea la kukutokea huko utaniweka kwenye hali gani mimi? Baba yako amefariki, wewe ndio mtoto mkubwa ninayemtegemea nawe unaanza kuwa hivi? Unataka kuniua?”

“Hapana, mama.”

“Baba, mwenda tezi na omo marejeo ungamani. Usiku mwema.”







Bernadetha alinyanyuka akaelekea chumbani. Miraji alibaki akiwa ameduwaa. Aling’ata lips zake huku akitizama chini. Alifuata kiti akaketi, mkono akauweka shavuni. Ni miguu yake ndio ikawa inacheza cheza huku sura yake ikiwa imejaa ndita.







Baadae usingizi ulimpitia akalala papo.





Asubuhi iliwasili. Siku ilikuwa kavu isiyo na dalili zozote za kunesha. Anga lilikuwa na rangi ya bahari, mawingu yakijitengeneza umbo la mawimbi.







Mbele ya nyumba ya Mtemvu, ilisimama gari dogo nyekundu Toyota Vitz. Mlango ulifunguliwa akatoka mzee mrefu mweusi mwenye ndevu nyingi na kiwaraza kikali akiwa amevalia kaunda suti ya kijivu, mkononi akibebelea rambo kubwa nyeusi. Moja kwa moja mzee huyo alifuata geti akabonyeza kengele.







Mlinzi alifungua kidirisha kidogo kilichopo kwenye geti akamtazama.







“Nikusaidie nini?”

“Samahani. Naitwa Ali wa Fatuma. Nina shida ya kuonana na mwenye nyumba.”

“Shida gani?”

“Za kibiashara.”

“Zipi?”

“Ni mambo binafsi.”

“Yapi?”

“Ndugu, ambacho hatuelewani ni nini? Mwambie bosi wako kuna mgeni anaitwa Ali wa Fatuma, yupo nje anamsubiri.”

“Ametoka.”

“Ameenda wapi?”

“Kwenye biashara zake.”

“Zipi?”

“Ni mambo binafsi.”







Ali wa Fatuma alitikisa kichwa akitabasamu.







“Wewe ni mgeni hapa, enh?” Aliuliza na kuendelea: “Si bure ndio mana huna adabu. Mwambie mama Mtemvu, Ali wa Fatuma yupo nje. Tusigombane bure.”







Mlinzi alimtizama mgeni yule kuanzia juu mpaka chini akatikisa kichwa. Aliondoka akimuacha Ali wa Fatuma nje ya geti, baada ya muda akarudi na Mama Beatrice.







“Ndio huyu hapa!” Mlinzi alimnyooshea kidole Ali wa Fatuma kana kwamba anamshtakia.

“Ooh Mtaalamu!” Mama Beatrice alilipuka kwa furaha. “Karibu! karibu sana!”

“Ahsante, mama.”

“Wewe! Ebu fungua geti!” Mama Beatrice alimuamuru mlinzi, haraka geti likafunguliwa mgeni akaingia.

Ali wa Fatuma alimtizama mlinzi na jicho kali asiseme kitu. Mlinzi alinywea kana kwamba amemwagiwa maji ya baridi.

“Mtaalam, umeacha gari leo?”

“Kuna mtu analitumia, amenishusha hapa na kwenda zake.”

“Oooh! Karibu bwana.” Mama Beatrice alisema akifungua mlango. Waliingia wakaketi sebuleni.

“Unapendelea kinywaji gani, mtaalam?”

“Nashukuru, wala usijichoshe mama. Mzee nimemkuta?”

“Hapana. Vipi hujawasiliana naye?”

“Simu yangu imeharibika kioo jana baada ya kuikalia hivyo nilishindwa kabisa kumtaarifu. Lakini anafahamu kwamba ningekuja, niliwaambia wasinifuate, nitawafuata mwenyewe.”

“Basi wacha nimpigie.”

“Itakuwa vema.”







Mama Beatrice alienenda chumbani baada ya muda kidogo akatoka akishikilia simu mkononi.







“Anakuja.” Alimpa taarifa Ali wa Fatuma ambaye alitikisa kichwa kwa mapokeo.







Ndani ya muda usiozidi robo saa, Mtemvu alitia mguu ndani. Tabasamu lake lilikuwa pana alipomuona mgeni, walikumbatiana kwa furaha wakaketi kwa karibu. Mwanamke akawapa faragha.







“Kama nilivyokueleza juu ya tatizo letu. Tumekuwa watu wa mikasa mikasa na sisi, hatupati usingizi vizuri, hatuli kikashuka kabisa!”







Ali wa Fatuma alicheka akitingisha mabega yake. Aliponyamaza aliweka uso wa kutisha kama vile si yeye aliyetoka kukenua.







“Tatizo lako limeisha!” Alisema kwa kujiamini, “Alimradi Ali wa Fatuma ameshafika, tatizo lako limekwisha!” alisema huku akitikisa kichwa kwa uhakika.

“Nitashukuru sana, Mtaalam. We niambie tu nini vinahitajika, mimi nitakupatia.”

“Sawasawa.” Ali wa Fatuma aliitikia.







Alifunua rambo lake akatoa vibuyu viwili, moja kikubwa na kingine kidogo. Alitoa mkia wa ng’ombe akauweka pembeni kisha akatoa na kaniki nyekundu na nyeupe zikifuatiwa na kioo cha saizi ya kati.







Alisimama akajivesha kaniki yake. Aliendea kona ya nyumba akasimama hapo mkononi akishikilia mkia wa ng’ombe ambao aliupeleka kushoto na kulia, kulia na kushoto. Baada ya hapo alipangusia makalio yake hapo na kusimama akiwa anarusha rusha macho yake kama vile anatafuta kitu kinachotambaa kwenye dari.



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Alitikisa kichwa akisonya. Alifuata kioo chake akakipangusia na mkia wa ng’ombe, akawa anakitizama.







“Bwana Mtemvu, huyo mtu anayekusumbua ndie huyu?” Ali wa Fatuma aliuliza akimuoneshea Mtemvu kioo.

Mtemvu alitizama macho akajikuta akiropoka: “Ndiye yeye huyo huyo!”







Ali wa Fatuma akacheka.







“Matatizo yako yamekwisha. Nilikuambia.”

“Sasa mtaalam nilikuwa nataka kujua. Huyo mtu katumwa na nani?”

“Ili tupate kujua mengi inabidi tutoe kafara. Kuku mweupe anahitajika kwa ajili ya kujua nani kamtuma na mbuzi mweupe kwa ajili ya kumdhibiti.”

“Hilo halina shida. Lini sasa?”

“Hata leo kama inawezekana.”

“Sawa! Basi ningoje hapa mtaalam nika …”

Simu ya Mtemvu iliita. Aliitizama akapokea.

“Eeenh shem, habari yako? … Mmevamiwa? Usiku huu wa kuamkia leo? ... He! Wewe! … Nakuja nakuja! Sasa hivi!”

Alikata simu akamgeukia Ali wa Fatuma na uso wenye mashaka na woga akamtaarifu aliyopashwa kwenye simu.

“Naomba urudi kesho. Sina jinsi tena kwa sasa.”

Ali wa Fatuma aliridhia. Mtemvu alimkabidhi noti kadhaa nyekundu kisha akamuita mke wake na kumpa taarifa alizozipata. Akaaga na kwenda zake.

“Inspekta, upo wapi? ... Naelekea kwa Raheem, ameuwawa jana usiku na majambazi … Basi nakupitia hapo muda si mrefu … Sawa.”







Simu ikakatwa na kurushiwa kwenye kiti jirani.







Dakika chache kupita gari likazima katikati ya barabara. Mtemvu alishuka akafungua boneti asione tatizo. Alipiga tairi teke akilaani. Alifungua mlango wa gari akachukua simu yake. Alikuta ujumbe umetumwa na namba ngeni muda mfupi uliopita:







‘Sasa kuna mawakala wawili wa kifo. Jiandae vema kwa yeyote atakayekutangulia.’







Alimaliza kuusoma huo ujumbe, ghafula gari kubwa aina ya Scania likabamiza nyuma ya gari lake kwanguvu. Mtemvu alirushwa mbali vioo vikimfuata na kumchana chana.







Gari lake liliserereka kwa kusukumwa na Scania, likaenda kubamiza gari lingine kwa mbele.

Ni kama vile maigizo yakitukia mbele ya macho ya Mtemvu. Alijaribu kunyanyuka lakini ghafula mkono ulimzuia tokea nyuma.







“Tulia kwanza mzee.”

Alikuwa ni kijana mwembamba aliyevalia hovyo, mdomoni mwake akibebelea sigara.







Ndani ya muda mfupi, watu walisogea na kujaa eneo la tukio. Mtemvu aliwekwa katikati ya umati akidhaniwa amechachawa na ajali. Mashahidi walisogelea Scania kumtizama dereva ila hawakumkuta.







“Ameshakimbia!”

“Ametokea wapi?”

“Sijui! Labda dirishani!”

“Vipi mzee unajisikiaje?” Shahidi mmoja alimuuliza Mtemvu kama aliyeguswa.

“Ni mgongo tu unanivuta kwa maumivu.” Mtemvu alijibu akijikanda mgongo. Mara akajipapasa mifukoni.

“Simu yangu? ... Kuna yeyote amenionea simu yangu?”







Hakuna aliyejibu. Watu wengine walianza kuondoka eneo la tukio.







Mtemvu alinyanyuka akafuata gari lake akishikilia kiuno chake na kujikongoja. Kabla hajalifikia alirudishwa alipotoka na mlipuko mkali!







Gari lake liliwaka moto kama kifuu. Kwa haraka lilianza kuyaambukiza magari mengine yaliyo karibu – eneo likageuka tanuru. Makelele na mayowe yakarindima. Kila mtu alikimbilia alipopahisi yeye ni salama.







Hapo ghafula Mtemvu alikurupuka akihema kwa pupa. Kumbe alikuwa anaota. Bado alikuwa ndani ya gari lake lililozima.







Alitizama kwenye kochi la pembeni akaona simu yake, aliichukua akaitizama. Mara ikaita namba kwa namba ngeni. Mtemvu aliitizama bila ya kuipokea. Simu ikakata.







Iliita tena na tena, badala yake Mtemvu aliamua kuizima kabisa. Ajabu ikaita tena! Mtemvu alikodoa macho ya mshangao. Alitoa betri akaitenganisha na simu, ajabu simu ikaendelea kuita.







Aliinyanyua akairushia nje kisha akafunga kioo. Alihema juu juu macho akiyakodoa kwa kutoamini. Kama vile haitoshi, simu iliita tena! Mara hii sauti ikitokea viti vya nyuma.







Mtemvu aligeuza shingo kutizama akamkuta mtu mwesu ti akiwa amejivika joho. Mtu huyo alimdaka koo kwanguvu akamminya. Mtemvu akahangaika mno kutafuta hewa bila ya mafanikio. Macho yalimtoka na mishipa ikamsimama. Alijua sasa kifo chake kimewadia japokuwa bado alikuwa mgumu kukubali.







Ilikuwa ni kama bahati, Inspekta akawasili hilo eneo kana kwamba alitaarifiwa kinachoendelea. Alijaribu kufungua milango ya gari la Mtemvu kwa nguvu zake zote bila ya kufanikiwa. Alichungulia ndani akamuona Mtemvu anazidiwa na isingechukua muda zaidi ya dakika moja tu apoteze uhai.







Alipiga ngumi kioo cha mlango wa gari akakivunja kisha akafungua mlango kwa ndani. Mtu mweusi akapotea kufumba na kufumbua.







“Mkuu, upo sawa?”







Koh! Koh! Koh! Mtemvu alikohoa akijitahidi kutafuta hewa kwanguvu. Inspekta alitizama kushoto na kulia, nyuma na mbele. Honi za magari zilikuwa zinaita, magari mengine yaliwavuka yakipita pembeni.







Baada ya Mtemvu kuvuta hewa ya kutosha, Inspekta alimtazama akamuuliza:







“Nini kimetokea?”

Mtemvu alibung’aa kama mtu mtu aliyeshushwa katikati ya jiji asilolijua. Alifagia uso wake na kiganja mara mbili, akamtizama Inspekta.

“Tuondoke!” Aliropoka. “Tuondoke hapa, Inspekta!” Inspekta akamshika mkono.

“Naomba niendeshe, Mkuu. Tafadhali.” Inspekta alipendekeza. Alijiweka kwenye kiti cha dereva akakanyaga mafuta, gari likasonga mbele kinyume kabisa na hapo mwanzo lilipogoma.

“Tunaelekea kwa Raheem kama kawaida, Mkuu?”

“Ndio. Tuelekee huko.”







Kisha kimya kikatawala miongoni mwao.







Walifika kwenye nyumba ya Raheem wakakuta watu tayari wamejazana. Walishuka wakaungana na kadamnasi.







Mtemvu alimfuata mke wa Raheem kumuuliza kilichotukia. Muda mfupi, Pius na K square nao wakafika eneoni kuungana na jumuiya ya waombolezaji. Wakati huo Inspekta alikuwa ameketi, lakini macho yake yalikuwa yamesimama yanatembea huku na huko kutizama usalama.







Haukupita muda mrefu, Pius, K square na Mtemvu wakaitana kando kuteta. Ilikuwa siri, hata Inspekta hakuhusishwa. Macho yao yalikuwa yanazurura mara kwa mara kutizama na kuhakikisha kama kweli wapo wenyewe.







“Mke wake amesema walivamiwa na mtu wasiyemjua. Hajachukua chochote zaidi ya kumuulizia na kumuua Raheem.” Mtemvu aliwaambia wenzake.







“Mmmh.” K square akaguna. “Jamani, mbona tunaishi kwa hofu hivi? Huku mambo ya ajabu huku majambazi! Roho zipo mkononi! Tutapona kweli?”

“Vipi kumhusu mtaalamu?” Pius aliuliza. K square akatikisa kichwa kama mtu aliyependezwa na hilo swali.

“Mtaalamu yupo.” Mtemvu alijibu. “Nimemuambia aje kesho nyumbani. Alikuja leo lakini taarifa za msiba zikaingilia kati.”

“Hawezi akaja hata hiyo kesho!” K square alitamka. “Itabidi tuwe tunashughulikia mazishi ya Raheem. Labda umwambie aje keshokutwa.”







Baada ya mabishano kidogo, walikubaliana juu ya hilo.







“Ila mnahisi ni nani atakuwa kamuua Raheem? Kuna mtu yeyote aliyekosana naye?” K square aliuliza.

“Sijui!” Mtemvu akajibu. “Sina taarifa yoyote juu ya hilo. Una ufahamu wowote kuhusu hilo?” Mtemvu aliuliza huku akimtazama Pius.

“Hapana. Sina.” Pius alitikisa kichwa. “Unajua Raheem si mtu wa kuweka wazi sana mambo yake. Ni mtu wa kujivuna muda mwingine. Huwezi jua alikuwa na maadui gani.”

“Ila hao maadui hawana uhusiano wowote na sisi?” Mtemvu aliuliza. Walitizamana kwa macho ya viulizi. Hakuna mtu aliyejibu swali. Mwishowe walifikia makubaliano kama ya awali, kuongeza ulinzi miongoni mwao lakini mara hii wakingojea ya mtaalamu.







Tip! Tip! Tip! Tip! Simu iliita. Iliketi juu ya kitanda cha Miraji. Mkono uliivuta simu hiyo na kuipeleka usoni mwa mwenye nayo. Ulikuwa ni ujumbe mfupi ukisomeka: ‘nipo nje nakusubiri.’







Miraji alinyanyuka akanawa uso. Alitoa begi lake kabatini. Alivalia nguo nyeusi kisha akatoka nje kupitia dirishani.







Ilikuwa ni usiku. Taa za majumba zilikuwa zimewaka. Kwa mujibu wa saa ya mkononi ya Miraji, ilikuwa ni saa nne kasoro.



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Twende!” Sauti ya Miraji ilisikika. Gari likachoropoka kwa kasi. Dereva alikuwa Jombi mdomoni akitafuna mirungi.

Walielekea moja kwa moja mpaka hospitalini. Walipofika walizima gari na kutulia humo ndani kwa muda.

“Chukua mfuko mweusi hapo nyuma” Jombi alielekezea kidole chake viti vya nyuma. Miraji akavuta mfuko na kuufunua, ndaniye akatoa joho refu jeupe.

“Vaa hilo.” Jombi alioda. Miraji alivaa hilo joho akatengeneza mithili ya daktari.

“Sasa uwe makini sana. Hakikisha hufanyi makosa. Baada ya dakika kumi na tano kamba itakuwa dirishani tayari.”

“Usihofu.” Miraji alisema akichomeka kisu nyuma ya kiuno chake. Alitoka ndani ya gari, kwa kujiamini akatembea akielekea ndani ya hospitali. Hatua zake zilitengeneza sauti kutokana na ukimya ulioanza kujijenga kwa mujibu wa muda mbali na hapo alitembea kwa ukakamavu akijazwa na dhamira.







Kabla asiingie ndani ya jingo la hospitali, sauti ya kuamuru iliita nyuma yake.







“Wee simama hapo!”







Walikuwa ni walinzi. Wawili kwa idadi. Walishikilia virungu vikubwa mkononi mwao. Miraji alijigeuza akawatizama.







“Samahani. Tunaomba kitambulisho chako.” Mlinzi mmoja alisema huku akinyoosha mkono.







Miraji alikaa kimya. Ni kama vile alikuwa amepigwa bumbuwazi. Alitumikisha akili yake ajue cha kufanya haraka iwezekanavyo kabla mambo hayajaharibika.







“Tunaomba kitambulisho chako, hujasikia?” Mlinzi mwingine alirudia swali.







Watu walitekwa na hilo tukio, walisogea, wengine waliopo mbali wakafuatilia kwa makini.

Miraji aliwatizama hao watu kisha akakunja sura akiwatizama walinzi.







“I do not understand you. What do you want? You are wasting my time, I have patients to look after.”

Miraji alisema kiingereza hiko kwa kujiamini. Walinzi wakatizamana.

“Umemuelewa?”

“Hapana!”

“Atakuwa daktari, tumeingia choo cha kike.”

“Muombe msamaha sasa.”

“Kwa kiingereza? ... Mie sijui!”

“Sorry dokta! … Sorry.” Mlinzi alijikomba kwa Miraji akijilazimisha kutabasamu. Miraji alitikisa kichwa chake kisha akaondoka. Alishusha pumzi ndefu akauweka mkono wake palipo na moyo.







Nusura nikamatwe, alijisemea mwenyewe akitabasamu.







Alitizama saa akaongeza kasi ya kutembea. Alipofika mlangoni mwa chumba alichokuwepo Filbert alimkuta mwanaume ameketi kwenye viti vya nje akichezea simu. Alimsalimia akaingia ndani.







Alifunga mlango na komeo akamuamsha Filbert akimuita jina lake mithili ya mtoto anayemuamsha babaye mpenzi.







“Shikamoo, mzee.”

“Marhaba.” Filbert aliitikia akistaajabu. “Wewe ni dokta mpya?”

“Ndio.”

“Mbona sikuambiwa kama amebadilishwa?”

“Watakuwa wamesahau.”

“Vipi, mbona umekuja muda huu?”

“Kuna ujumbe nataka kuufikisha kwako.” Miraji alisema kisha akatizama saa yake.

“Ujumbe wa nani?”

“Wa bwana Malale.”

“Bwana Malale?” Filbert alikodoa macho. Alijitahidi kunyanyuka maumivu yakamshinda.

“Bwana Malale yupi?”

“Malale mliyemuua wewe na wenzako.” Miraji alisema akitabasamu.







Filbert alitaka kupayuka haraka Miraji akamziba mdomo na mkono wake wa kushoto, wa kulia akachomoa kisu.







Mlangoni hodi ilibishwa. Mwanaume aliyekutwa kwenye kiti akichezea simu alibamiza mlango akitaka kuingia, mlango haukufunguka.







Aliita daktari daktari lakini hakukuwa na majibu. Aliita Filbert Filbert asisikie kitu. Aliita walinzi wakaja, mlango ukavunjwa. Ndani wakamkuta Filbert ametapaliwa na damu kifuani. Hakukuwa na mtu mwingine ndani ya chumba. Ila dirisha lilikuwa wazi.







“Kuna mtu aliingia humu! Alikuwa amevalia kidaktari!” Mwanaume aliwaambia walinzi.

“Rambo, washtue getini fasta!” Mlinzi mmoja alimwambia mwenzake. Mwenzake akanyofoa redio call kifuani mwake akaiweka mdomoni na kuwataarifu walinzi wa getini wazuie watu wote watokao.







Hawakufua dafu. Mtu waliyekuwa wanamtafuta alikuwa tayari ameshapotea eneo hilo kwa kasi kubwa ya gari.







Jombi aliondoa chombo kama chizi. Hakusimama wala kupunguza mwendo mpaka walipopotea kabisa maeneo ya karibu na hospitali. Kituo cha kwanza kilikuwa mbele ya nyumba ya wakina Miraji. Miraji aliagana na Jombi akanyookea dirishani kwake.







Alijaribu kufungua dirisha lakini hakufanikiwa, dirisha lilikuwa limefungwa ndani na komeo.







“Oh no!” Miraji alilalamika. Hakuwa na chaguzi lingine zaidi ya kuufuata mlango. Alijua wazi mama yake atakuwepo sebuleni na ni ngumu kukatiza asigundue.







Alipiga moyo konde akisema:







“Leo nitakuwa mwangalifu zaidi.”







Alitembea pole pole akaufungua mlango na kuurudishia taratibu. Alivuta pumzi ndefu akaanza kunyata akihakikisha hakuna mlio wowote unaotokana naye, alifanikiwa katika hilo.







Ila mlio wa alarm toka kwenye simu ya mama yake ukatia mchanga kitumbua. Bernadetha aliamka kutizama simu yake akamuona mwanae.







“Miraji, umetoka wapi?”







Miraji kimya. Bernadetha aliamka akamsogelea mwanae. Alimtizama usoni, Miraji akatizama chini.







Bernadetha alimtizama vema mwanae akaona ana damu mkono wake wa kuume. Kama mtu ambaye hakuamini, aliuliza:

“Miraji, nini hiki?”







Alipeleka pua yake akanusa kabla Miraji hajaupokonya mkono wake kwanguvu.







“Miraji, hiyo si damu?” Bernadetha aliuliza.

“Ndio.” Miraji akajibu.

“Umeitoa wapi?”

“Niliumia.”

“Wapi? … Lete nione.”







Miraji hakutoa mkono wake. Bernadetha alijikuta akinyanyua mkono wake wa kuume akamzaba kofi.









“Umetoa wapi hiyo damu?” Bernadetha aliendelea kuuliza Miraji asijibu kitu.

“Lete begi hilo.” Bernadetha aliwaka akivuta begi la Miraji.







Miraji alitoa mikono ya mamaye kwanguvu kwenye begi lake kisha akaelekea chumbani na kujifungia.







Bernadetha akaangua kilio. Alimuita Miraji lakini hakutoka. Alikaa mlangoni mwa chumba cha Miraji akililia hapo.







Miraji alijilaza kitandani pembeni yake akiweka picha ya marehemu baba yake. Sauti ya kilio cha mama yake ilimfanya ashindwe kujizuia, naye akajikuta analia. Ila roho yake ilimwambia anachofanya ni sahihi na alitegemea mama yake angekuja kuelewa hapo baadae.



Siku tatu zilipita msiba wa Filbert ukivuma na kutika.







Haikuwa jambo jepesi kwa Mtemvu na wenzake ambao sasa walishapata jibu kamili kwamba huyo muuaji atafuata pia roho zao. Wazo lao kuongeza ulinzi likionekana kukosa mashiko, uhitaji wa mganga ukawa juu kuliko awali. Waliamini hata huyo jambazi anayeua atakuwa na mahusiano na mtu yule wa ajabu, mtu mweusi, hivyo kumzuia ingehitaji pia nguvu za giza.







Kwenye kikao cha dharura walichofanya baada ya mazishi ya Filbert, waliafiki mtaalamu, Ali wa Fatuma, afike siku inayofuata kwa gharama zozote, huku tayari wakijiandaa kwa mahitaji ya kuku na mbuzi weupe kungoja ibada.







Jambo ambalo hawakulijua ni kwamba usiku wa siku hiyo, mmojawao alikuwapo kwenye orodha ya mauaji ya Miraji, ilibidi afe asione jua lingine likichomoza. Hiyo siku ndio ilikuwa siku yake ya mwisho kuvuta pumzi ya ulimwengu.







Gari la Jombi lilisimama mbali kidogo na nyumba ya K square. Ndani yake walikuwapo Miraji na Jombi vidoleni mwao wakishikilia misokoto ya bangi wakijaza moshi mzito garini. Kwa mbali redioni muziki wa rege uliita, Bob Marley akitumbuiza na wimbo wake wa taratibu Redemption song.







Jombi alinyonya msokoto wake wa bangi akameza moshi akiutolea puani kisha akamtazama Miraji na macho yake mekundu kama nyanya.







“Upo mwake?” Aliuliza. Miraji akatikisa kichwa akinyonya msokoto. Alipopuliza moshi nje akajibu,

“Nipo fresh. Wewe tu.”



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Jombi alivuta pafu la mwisho kisha akazima msokoto na kuuweka ndani ya droo ya gari. Humo drooni alitoa bunduki ‘mguu wa kuku’ akamkabidhi Miraji. Akatoa tena bunduki nyingine akaikoki na kuishika. Aliibusu akitikisa kichwa.







“Leo ndio leo.” Alisema akitabasamu.

“Sasa ni hivi. Walinzi wapo watatu. Wewe utaingilia nyuma mimi nitaingilia mbele. Fanya kama tulivyokubaliana. Tumia bunduki kama tu ukiona hakuna namna nyingine, tusije tukajaza watu mapema bure.” Jombi alielekeza.







Walivaa vinyago na mabegi madogo migongoni. Walitoka garini wakagawana njia. Mwingine alienda nyuma ya nyumba mwingine akafuata geti na kutulia hapo kama anayesubiria jambo.







Miraji alikwea mti mkubwa ulio karibu na uzio wa nyumba. Alipofika juu alijirushia ndani ya jengo akafikia kwa mtindo wa kuchuchumaa bila ya kutoa kelele.







Haraka alikimbilia nyuma ya jiko la nje ya nyumba akajificha. Alivua begi lake akatoa mfuko wa mkubwa uliobebelea vyupa akaanza kuzitandaza kwa haraka eneo linalomzunguka. Alitoa mshipi akaufunga upande moja mlango wa jikoni pande nyingine akaishikilia yeye akiwa amejificha kisha akatoa chupa ya bia begini na kuibamizia ukutani kwanguvu.







Walinzi walishituka. Wawili haraka walikimbilia eneo la tukio na kumuacha mmoja getini. Hapo ndio Jombi akaweka kifaa kidogo getini kikatoa sauti ya gari lipigalo honi.







Kwakuwa hakukuwa na sehemu ya uwazi getini, mlinzi aliyebakia akawa hana namna, aliburuza geti kando ili apate kuchungulia. Hilo likawa kosa.







Kutoa uso wake kulimpa mwanya Jombi aliyekuwa amejibanza getini. Alishika kichwa cha mlinzi na kubamiza kwanguvu ukutani. Mlinzi akazirai.







Jombi aliingia ndani akafunga geti.







Huko nyumba upande wa jikoni, mlinzi mmoja tayari alikuwa amelala juu ya vyupa akimwaga damu. Mwenzake alikuwa kando damu zikimvujilia kichwani, pembeni kukiwa na jiwe ukubwa saizi ya kati. Miraji aliwatemea mate akiwatizama kwa kinyaa. Alishamaliza kazi ya kuwateketeza ndani ya muda mfupi tu.







Aliachana na hiyo miili akakimbilia mbele ya nyumba huko akaungana na Jombi wakaingia ndani ya nyumba kwa kuvunja mlango wasikute mtu sebuleni.







Walitazamana wakapeana ishara ya kusonga vyumbani, wakaanza kupita chumba baada ya chumba. Walivunja milango na kujitenga pembeni kusikilizia. Katika vyumba vinne walivovunja hawakukuta mtu yeyote. Na sasa kilibakia chumba kimoja tu wamalize vyote.







Kabla ya kuvunja mlango wa hicho chumba, Jombi alifuata swichi kubwa ya umeme akakata umeme. Alivunja mlango kisha akawasha kurunzi moja na kuirushia ndani.







Risasi zikashambulia hiyo kurunzi kana kwamba kuna mtu ameibebelea. Hiyo ikawa nafasi mujarabu kwa Jombi ambaye alibashiri vema risasi hizo zinapotokea akalenga risasi nne, sauti kali ya maumivu ikamjibu.







Miraji alipomulika kurunzi wakamuona K square amelala anaugulia maumivu akishikilia tumbo lake linalovuja damu. Miraji alimsogelea K square akavua kinyago chake na kumtizama mwanaume huyo aliyekuwa anagugumia akiomba abakiziwe roho yake.







“Nadhani unaijua hii sura.” Miraji alimulika uso wake. “Sina muda wa kupoteza. Nimekuja hapa kuchukua roho yako kama vile mlivyoichukua ya baba yangu, mzee Malale. Kawakute wenzako jehanamu.”







Miraji alitoa bunduki yake akampiga risasi kichwani K square kisha akamtemea mate kana kwamba ananuka.







Haraka walitoka ndani wakafuata gari lao na kutimka.







Ila hawakufahamu, ndani ya kabati la chumba hicho kilichoshuhudia mauaji kulikuwemo na watoto wawili mapacha wa K square: Jeniffer na Jenister. Makamo yao ya umri kumi na tano.







Watoto hao walishuhudia kila kitu kilichofanyika kwa baba yao kupitia upenyo wa kabati. Majambazi walipoondoka watoto hao walitoka kabatini wakaulilia mwili wa baba yao wakimimina machozi na makamasi.







Jombi na Miraji wasifike mbali na gari lao lililoendeshwa kasi kama upepo wakakutana na gari la polisi konani. Lilikuwa limeziba njia polisi watano wakitanda na bunduki barabarani wakiwaamuru washuke na kujisalimisha.





http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Shiit!” Jombi alipiga ngumi usukani. “Atakuwa alitoa taarifa polisi yule mshenzi!”

“Sasa tunafanyaje?” Miraji aliuliza akitizama kwa woga.

“Funga mkanda. Hatuwezi tukakamatwa kirahisi hivi!”







Jombi alisema kimajigambo. Aliweka gia na kukanyaga mafuta akavamia vichaka vya kando ya barabara akatokea upande mwingine kwa kasi kubwa mno. Polisi wakaanza kufukuzia kwa nyuma ving’ora vikiita.









ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog