Search This Blog

Sunday, 20 November 2022

URITHI WENYE UMAUTI - 1

 





    IMEANDIKWA NA : POWEL CHEMOS



    *********************************************************************************



    Simulizi : Urithi Wenye Umauti

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali iliendelea kunyesha hivyo kusababisha ardhi iwe yenye matope mazito.Niliendelea kukimbia huku nikichukua muda mfupi sana kupumzika bila ya kusahau kuangalia usalama wa eneo hilo.Giza nalo lilikuwa limetanda eneo lote mpaka nikashindwa kuisoma ramani niliyokuwa nimepewa na baba yangu,Yohana Sikazwe.Angalau kungekuweko na mwanga ningejua nilipokuwa naelekea.Nilijivuta kwa nguvu mpaka kwenye mti niliokisia kuwa wa mbuyu kutokana na umbo wa matawi yake.Kwa kweli nilikuwa nimeloa chapachapa,kaptura na shati zikawa zimenikwamilia mwilini.Niliuegemea mti huo huku nikitazama upande niliotoka.



    Nusu saa hivi,niliona mwanga kutoka chini ya kilima nilichokuwa nimeukwea muda mfupi tu nyuma.Dakika chache baadaye nikawaona watu wawili wakiungana na yule wa kwanza kutokea pande tofauti tofauti za msitu huo.Niliendelea kuwatazama,nikagundua kuwa walikuwa wakinifuata kutumia uelekeo wa alama za miguu yangu,nikang'amua kuwa uwepo wangu pale ungeniletea umauti.Niliikunja ramani yangu, niliyokuwa nimepata ugumu wa kuisoma,na kuiweka kwenye mkoba kisha kwa tahadhari ya hali ya juu,nikapenyeza kati ya msitu na kupotea.Nilipopotea kwenye upeo wa wakimbizaji wangu,nilitimua mbio za kikweli huku kila baada ya muda mfupi nikiangalia nyuma.Sikuwa najua ninakokwenda,mwisho wa mbio zangu sikung'amua ungekuwa wapi.Nilikuwa nimegeuka kuwa mkimbizi asiyekuwa na mbele Wala nyuma.Nilikuwa nikitembea kwa shida kutokana na kutokuwepo na mwanga wa aina yoyote,hata mbalamwezi au nyota angani.Hali hii ikafanya nikwaruzwe na vijiti na pia kugongana na mashina ya miti



    Anga lilikuwa limegubikwa na mawingu mazito yaliyosababisha mvua kubwa ikiambatana na radi.Mara anuwai niliweza kutazama kutumia mwanga uliosababishwa na radi ila nikapata ugumu wa kutumia kuisoma ramani niliyopewa na baba kwani mwanga ule ulidumu kwa sekunde chache tu.Mwendo wangu ulikuwa wa wastani hii ni baada ya kuwapoteza wale watu waliokuwa wakinifuata kutokea nyumbani kijijini Kiwanika tulikokuwa tunaishi.Taswira niliyoipata nyumbani kwetu jioni ile iliendelea kujirudia akilini.Kitendo cha baba na mama kuchinjwa Kama kuku kilinighadhabisha sana.Sikuwa mjuzi wa masuala ya kijasusi lakini kwa mtazamo wa jumba letu,niligundua kuwa lilikuwa limepekuliwa kwa ustadi na uangalifu wa hali ya juu.Niliingia kwenye chumba cha wazazi wangu kwa tahadhari nikitafuta chochote ambacho kingenipa mwanga wa unyama ule.Wakati wote huo,mtima ulikuwa ukinidunda mpaka nikawa nausikia kwa mbali bila ya kusahau mitiririko ya jasho usoni na mgongoni.Chumba hakikuwa kimeguswa,vitu vyote vilikuwa vimepangwa vizuri.Macho yangu yakang'amua uwepo wa karatasi ya kitabu iliyokuwa na maandishi ya kalamu dirishani.Nilisogea polepole Kisha nikaichukua na kuanza kuisoma.Ilikuwa barua fupi iliyosomeka hivi:"Mwanangu Roy,mimi na mamako hatuna muda mrefu wa kuishi ila twakutakia maisha mazuri hapo baadaye.Nataka kukupa urithi wa Mali yangu yote ila utabidi ujikaze kiume kwani tunaandamwa nawe utaandamwa.Usimwamini mtu yeyote.Chukua ufunguo kwenye kabati nimeificha Kisha uondoke.Baaada ya yote kupita,mtafute Padre Hiza Sibomane Marcus atakusaidia.



    **Wako akupendaye Yohana.Ilisomeka barua ile.Bila kupoteza muda,nilikimbilia jikoni nikafungua kabati ya vyombo na kweli baada ya upekuza,nikafaulu kupata ufunguo uliokuwa na umbo la kipekee,ukiwa umefichwa chini ya kikombe cha udongo.Ghafla,nikasikia sauti ya mkwaruzano wa ardhi na gurudumu la gari.Moyo ukaanza kunidunda,sikujua ni hatari ipi nilikuwa nikabiliane nalo.Nilichungulia dirishani na kwa usaidizi wa taa za nje,nikaiona gari aina ya Harrier yenye rangi nyeusi.Dakika chache baadaye milango ikafunguka kila upande kuwaruhusu wanaume wanne wenye miili iliyojengeka kimazoezi kushuka.Mwendo wao na jinsi walivyokuwa wakitazama ikanipa wasiwasi mkubwa.Mara moja wote wakachomoa bastola kutoka kwenye makoti yao na kuzikoki nami nikajua kuwa kazi imeanza.Niliondoka pale dirishani baada ya kugundua mmoja wa watu wale alikuwa ametazama pale kwa muda napo pakawa pamemvutia kwani alipakodolea macho sana.Singeweza kuwatambua moja kwa moja kwani walikuwa wamejivika miwani myeusi usoni.Nilitembea haraka haraka nikielekea pande za vyoo.



    Dhamira yangu ilikuwa kutorokea kule lakini kumbe mpango wangu ulikuwa umegonga mwamba.Kabla niufikie mlango huo,nikasikia mlio wa mtu akizungusha kitasa hivyo nikalazimika kujificha kwenye kona ya mlango.Polepole mlango ukafunguliwa kisha kiwiliwili cha mtu kikafuata.Alikuwa amekamata bastola mkononi huku domo lake likiwa limeelekezwa mbele."Ninaingilia upande wa vyoo,hakikisheni mnamtafuta na kuchukua ufunguo kwani bosi anahitaji.Harakisheni"mtu yule alisema akiwa ameegemeza kichwa upande wa kulia.Hapo nikajua kuwa walikuwa wanatumia redio za wanapolisi.Uwezekano wangu wa kutoka pale ulikuwa mdogo sana,nilihitaji kujitetea,lakini sikuwa na silaha yoyote ambayo ningetumia ila funguo na mkoba wangu.Kwa nyota ya jaha,nililiona spana alilokuwa akitumia baba kutengenezea gari lake wakati gurudumu lingekuwa na hitilafu.Nililiokota polepole bila kumshtua mtu yule kisha kwa nguvu zangu zote,nililinua juu na kumteremshia pigo lenye uhakika.Dhoruba lile likaipasua kichwa cha mtu yule nao mguno wake ukawa hafifu sana,akaanguka chini na kutulia kimya huku damu ikianza kuchuruzika kama bomba bovu la maji inayovuja.



    Nilichukua bastola yake na kijiredio cha kipolisi alichokuwa nacho.Niliisunda mfukoni na kuelekeza bastola ile mbele kama njia ya kujihakikishia usalama tosha.Hiyo ndiyo ikawa mara yangu ya kwanza kushika bastola.Nilinyata mpaka chooni nikachunguza nitakapotorokea,mara moja nikakumbuka mfuniko wa choo uliokuwa na mfereji kuelekea kwenye bwawa la kukusanya uchafu wa choo na maji machafu kutokea maliwato.Nje nilisikia sauti ya watu wale wakitembea kuja uelekeo wa vyoo.Haraka haraka niliinua kifuniko Kisha nikatanguliza mkoba wangu nami nikafuata.Harufu ya mle ndani ilikuwa ya kutapisha ila nilijikaza kiume,bastola nikiwa nimeikamata sawasawa mkononi.Mwendo wangu mle ndani ulikuwa wa haraka kwani kinyesi na mkojo vilisababisha utelezi mkubwa.Mavazi yangu yote yakawa yameloa kwa uchafu ule.Sikuwahi kufikiri ikiwa mimi,mwana wa bilionea mashuhuri,ningejipata katika hali hiyo.



    Safari ile ya dhiki ikaishia kwenye bwawa la kinyesi iliyonifikia kiunoni.Nilijikakamua nikaruka na kukipiga kifuniko cha kufunika bwawa lile kwa teke yenye nguvu,nikapata uwazi wa kutokea.Sikutaka kupoteza muda mwingi hivyo nilijivuta mpaka nje,nikapata kuvuta hewa safi iliyonirudishia uhai na uchangamfu.Nilichukua mkoba wangu na kuondoka pahali pale haraka.Baada ya kupiga hatua kadhaa tu mbele,nilisikia michakato ya miguu ikija upande ule.Haraka nikajibanza kwenye maua yaliyokuwa yameota pale bastola ikiwa tayari kutema cheche za moto.Muda mfupi tu baadaye,watu watatu wakatokezea wakiongea kwa sauti ya juu,dalili tosha kuwa nilikuwa natafutwa mzima au mfu.Mmoja wao aliusogea mfuniko wa bwawa lile na baada ya kuchunguza kwa umakini,akawaita wale wenzake.



    Niliwaona wakielekeza vidole vyao pale kisha mmoja akatoa kurunzi ndogo iliyofanana na kalamu kwa muonekano lakini yenye mwanga mkali sana.Alianza kuja uelekeo niliokuwa kwa kufuata matone ya kinyesi yaliyokuwa yakianguka toka mwilini mwangu,hapo nikajua kitumbua kimeingia mchanga.Nilijipa ujasiri na kujichomoza toka nyuma ya mti ule na kuiruhusu bastola kuachilia risasi ambazo sikujua idadi yazo kuwaelekea wale watu.Kitendo kilichotokea pale kiliniwacha mdomo wazi ,wanaume wale walijiviringisha hewani kwa sarakasi ya hali ya juu na kujitupa kwenye maua.Hakukutokea ukelele wowote kwani bastola ile ilikuwa imefungwa kiwambo cha kuzuia sauti,hivyo kukasikika sauti mfano wa kikohozi cha mzee mkongwe.Mvua ilikuwa imeanza kunyesha lakini kidogo sana.Mara moja moja kulisikika mlio wa radi na mwangaza uliofanya giza lipotee kwa muda mfupi.



    Watu wale hawakuwa wakionekana licha yangu kuchunguza kwa uangalifu eneo walikoangukia.Sikutaka kutumia risasi zingine maana ingekuwa kazi bure.Sauti fulani ndani yangu ilinitahadharisha-usalama wangu eneo lile ulikuwa wa kutilia shaka.Nilichukua begi langu mgongoni kisha bastola mkononi,nikatundika guu begani nikifuata uelekeo wa msitu Nyangumi.Punde tu niliporuka uzio wa nyumbani uliokuwa umetengenezwa kwa saruji na matofali,nikasikia sauti ikiniamrisha tokea nyuma."Simama pale au nikugeuze marehemu wewe kijana".Nikajua pale maji yalikuwa yanataka kunifika shingoni.Sikutaka kujipeleka mikononi mwa wale watu kikondoo kwani nilikuwa nimemwua mmoja wao.Nilijirusha chini na kuanza kutambaa kuelekea kwenye kichaka kilichokuwa hapo karibu haraka sana.Nyuma nikasikia usalama wa bastola ukiondolewa,sauti mfano wa nyuki wakinipita,karibu na sikio la kulia nikausikia.Risasi aliyokuwa amefyatua,mmoja wao,ilinipita sentimita chache na kuichimba ardhi.Mwili wote ukashtuka,mikono ikawa inanitetemeka kama matawi msimu wa vuli.Muda mfupi baadaye utulivu ukarudi eneo lile kando na sauti ya wadudu waliokuwa katika harakati zao ambazo Muumba aliwapa.



    Bila ya kupiga kelele,niliendelea kutambaa huku nikiwa siamini ikiwa nilikuwa hai mpaka muda ule.Nilipofaulu kufika kwenye msitu ule,nilikimbia sana mpaka kwenye barabara kuu.Ilikuwa imefika saa tatu usiku kwenye saa yangu ya mkononi,saa za Afrika mashariki.Nilitembea kando kando ya barabara ile huku mara kadhaa wa kadha nikiangalia nyuma.Sikumtilia shaka yeyote maana niliweza kukutana na watu wachache sana.Magari yote yaliyokuwa yakipita yalikuwa ya kibinafsi na chache sana zikiwa Lori ya kubeba mchanga,kokoto na mawe nami sikutaka kuanguka mtegoni kwani wale watu niliowakimbia nyumbani walikuwa wakitumia gari la kibinafsi.Hili lilinilazimisha kujificha kila niliposikia mngurumo wa gari lolote.Matone ya mvua yalikuwa yakiongezeka muda ulivyokuwa ukisonga.Hali hii ikawa afueni kwangu kwani maji hayo yalikuwa yakisafisha mwili wangu kutokana na uchafu nilipopitia kwenye bomba la choo.



    Nilitembea kwa masaa mawili Kisha nikatafuta pahali chini ya mti,kando ya barabara ile kupumzika kwani nilikuwa nahema kwa nguvu nayo mbavu zilikuwa zikiniuma sana.Mawazo yangu yote yalirudi kwa wazazi wangu waliokuwa,ikiwa ni sahihi kusema marehemu nyumbani kwetu.Machozi yalinitiririka njia nne nne,nikafikiri nipo ndotoni lakini hali ilikuwa halisi.Nikiwa katika fikira nzito,nikakumbuka ufunguo alionipa baba kwa maelezo kwenye barua yake fupi hivyo nikafungua mkoba na kuichukua.Nikaitazama kwa umakini,umbo lake lilikuwa la kawaida ila katikati kulikuwa na mchoro wa mnyama ambaye sikuweza kumjua kutokana na Mimi kutumia hisia za mguso.Giza lilikuwa limeigubika nchi nzima.



    Sikutaka kuchukua muda mrefu pale hivyo niliirudisha funguo ile pahali pake mkobani kisha nikainuka kuendelea na safari yangu ambayo sikujua mwisho wake ungekuwa wapi.Kwa mbali niliona taa za barabarani na za kwenye duka zikiwaka,nikajua karibu nakaribia Mji mkuu wa Sogomo.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog