Search This Blog

Friday, 18 November 2022

BARADHULI MWENYE MIKONO YA CHUMA (1) - 1

 









IMEANDIKWA NA : STEVE MOLLEL



*********************************************************************************



Simulizi : Baradhuli Mwenye Mikono Ya Chuma (1)

Sehemu Ya Kwanza (1)







Dar es Salaam, miaka ya karibuni.

Jua lilikuwa njiani kukomaa. Sauti za magari zilinguruma zikijaza pande zote nane za jiji la Dar – jiji karimu kwa joto na karaha za usafiri.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Wakati ikiwa ni saa tano tu iliyo njiani kuitafuta saa sita iwe mchana, tayari maeneo ya Mbezi beach mpaka Mwenge palishatapakaa foleni ya kushiba ikisababishwa na ajali mbaya iliyotokea maeneo ya Kawe darajani kati ya magari manne binafsi na bodaboda.



Kutokana na ukubwa wa foleni hiyo isiyoleta matumaini ya kusonga, watu wengi wakashuka kwenye magari yao binafsi na kuketi nje ama basi watembee kupunguza uchovu. Abiria wengi wa madaladala nao wasiwe nyuma, wakaradhi washuke kutembea ama kunyoosha viungo vyao; hali hiyo ikapelekea barabara kufurika watu kana kwamba kuna maandamano ya kisiasa.



Katika msururu huo wa magari, binafsi na daladala, yakiwa yamejipanga kutengeneza umbo la nyoka mkubwa, miongoni mwa daladala mojawapo la Mwenge-Tegeta lililokuwepo maeneo ya Makonde, upande wa kushoto dirishani aliketi mwanadada mmoja mweupe.



Alikuwa mwembamba mno kwa umbo akibarikiwa uso mrefu wenye paji kubwa, macho rangi ya kahawia, mdomo mweusi na nywele ndefu nyeusi ti ila zilizonyimwa taratibu ya kuvutia.



Msichana huyo alikuwa anatizama nje kupitia dirishani macho yake yakionyesha ametekwa kitafakuri. Mara zingine alitikisa kichwa chake mdomo ukionekana unateta jambo ambalo halikupata kusikika na mtu mwingine yeyote ndani ama nje ya gari.



Zilipita dakika kadhaa mwanamke huyo akadondosha chozi asioneshe kujali. Chozi hilo likishuka, ghafula akapiga yowe kali na kuwashitua abiria waliosalia chomboni.

“Niache!” Alifoka. “Niache, si’ mimi!”





Alihangaika huku na huko kama aunguzwaye na moto, watu wote garini wakamtizama. Ana nini huyu?

Hakukoma, aliendelea kujirusharurusha huku na huko akijibamiza mpaka pale alipovunja kioo na kujijeruhi vibaya, damu zilimchuruza kichwani kama maji.



Wanaume wawili garini walijitolea kumtuliza lakini hawakufanikiwa, walizidiwa nguvu wakarushwa mbali mhanga akaendelea kujiadhibu kwa kujibamiza; damu zikimmwagika, mdomowe bado ukilalama sio yeye na anakufa!



Isichukue muda mrefu, mwanamke yule akalala chini na kutulia tuli. Abiria walimsogelea wakamtazama.

Amekufa? Damu bado ziliendelea kuchuruza kichwani kwake na kutapakaa garini. Dereva alitikisa kichwa chake akatoa mlio wa kuita paka.

“Mkosi gani huu!” Alilaumu.



“Huyu mwanamke kapatwa na nini?” Aliuliza kana kwamba kuna ajuaye kwa undani kilichojiri. Swali hilo likazua mzozo kila mtu akajaribu kueleza anavyofahamu yeye: wengine wakasema ana mapepo, wengine wakahukumu alikuwa na msongo wa mawazo kwa hoja kwamba tangu apande gari alionekana ana mawazo mengi.



Ila kwa muda huo kondakta alikuwa kimya akiutathmini mwili wa mwanamke huyo. Na baada ya sekunde chache alikumbuka jambo.

“Huyu mdada alipandia gari maeneno ya Mbuyuni. Nakumbuka wakati anasimamisha gari alikuwa anakimbia akitazama nyuma. Sijui kuna mtu alikuwa anamkimbiza, sifahamu!”



Kauli hiyo ya konda ikazidi kuleta mkanganyiko. Walimpekua yule dada mifukoni wakakuta kitambulisho kilichomtambulisha kama karani wa kampuni ya Kim na Kamugisha (K&K) inayopatikana maeneo ya Kunduchi Beach karibu na shule ya Bahari. Abiria mmojawapo alijaribu kupiga namba elekezi iliyoainishwa kitambulishoni, ikapokelewa.



Alifafanua juu ya dhamira ya simu yake, akapewa ahadi ya hilo jambo kufanyiwa kazi ndani ya muda mfupi. Baada ya muda kidogo gari la wagonjwa likiwa linapata taabu kukatiza pembezoni mwa barabara ya lami, likafika eneoni na kumchukua mlengwa kwa msaada wa maelekezo ya abiria.



Lilitokomea upesi likirudi Tegeta. Tungeweza kubashiri lilikuwa laenda hospitali ya IMTU. Lilikakata kona na kupenya penya mithili ya panya. Likiwa limekaribia kuwasili kwenye hospitali hiyo iliyopo karibu na hayo maeneo, ghafula likapoteza muelekeo baada ya kujaribu kujinusuru kukumbana uso kwa uso na bodaboda iliyokuwa inakuja kwa kasi.



Dereva alishindwa kumudu gari hilo hatimaye likavamia gari lingine.

Watu wote ndani ya gari la wagonjwa walifariki papo hapo!



NINI JAMBO NYUMA YA PAZIA?





http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

***

SURA YA PILI:

Dar es Salaam, miaka kadhaa nyuma:

Mida ya mchana ilipofika, Marietta, msichana mwenye miaka kumi, mrefu na mwenye uweusi wa kung’aa, alitoka eneo la shule akijirudisha nyumbani. Alikuwa amechoka kwa mujibu wa mwendo wake. Alitembea kigoigoi akiburuza miguu. Aliufungua mlango kivivu akaingia ndani.

Cha kwanza kufanya ikawa kuita:

“Mamaaa!”



Aliijitupia kochini. Alinyamaza kwa muda kidogo kusikilizia majibu lakini hakusikia kitu.



Alinyanyuka akaenda jikoni moja kwa moja mpaka kwenye masufuria aliyoyafungua na kutizama kama kuna chochote kitu. Hakukuwa na lolote, pakavu. Alisonya akaelekea chumbani, akajilaza kitandani na sare zake za shule tumbo likinguruma kwa njaa.



Wazo lilimjia, alinyanyuka akafuata jokofu kutizama kilichomo ndani, lakini bado majibu yakawa yaleyale, hakukuwa na kitu chochote cha kutia mdomoni. Alivuta mdomo akajipiga mapaja. “Jamani! Aaah! Tokea jana mi s’jala. N’taishije sasa? ... Nasikia njaa!” Alifoka.



Aliifuata simu ya mkononi maeneo ya kabatini akaweka namba na kuziita. Baada ya muda kidogo …“Mama! ... Mi nasikia njaa, mbona chakula hamna sasa? ... We unakuja saa ngapi? ... Upo ospitali? ... Sasa mimi je? ... Mi siwezi kuvumilia mama … Njaa inauma!”



Simu ikakata. Alijaribu kupiga tena, mara hii akaambiwa salio halitoshi. Aliitupa simu chini akarukia kochi na kuanza kulia. Hakunyamaza mpaka pale usingizi ulipomtwaa. Alilala kwa masaa mawili akaja kurupushwa na sauti za kilio tokea nje. Sauti mojawapo aliitambua ni ya mama yake, haraka akalifuata dirisha na kuchungulia.



Aliona gari moja kubwa: Toyota Prado nyeusi, pamoja na mzee mmoja mnene mwenye kiwaraza akiwa kamshikilia mama yake aliyekuwa analia. Alitoka nje upesi akitwaliwa na hofu. Alimuuliza mamaye kwanini analia lakini hakupewa jibu, wala yule mzee mwenye kiwaraza, kwa jina Mtemvu, hakumsemesha. Alikuwa bize akimbembeleza mama yake wakielekea ndani.



“Pole, shemeji. Yote ni mipango ya Mungu.” Mtemvu alifariji. Mama Marietta, ama Bernadetha kwa jina, akamjibu kwa kilio cha nguvu ambacho kilichukua muda kukoma. Marietta naye alilia asifahamu anacholilia ni nini.



Bernadetha aliingizwa ndani bado akiendelea kulia na Marietta naye akifichwa kilichojiri…Ndani ya muda mchache watu walijaa kwenye nyumba hiyo kila mmoja akimnyookea mama Marietta na kumpa mkono wa pole.



Hapo ndio Marietta akafahamu nini kilichojiri – Baba yake, bwana Malale, aliyekuwa amelazwa kwa miezi kadhaa, amefariki dunia. Alilisikia hilo kwenye kinywa cha mmoja wa waombolezaji waliofika nyumbani kwao. Basi huo kwake ukawa muendelezo wa yeye kulia, akijumuisha na njaa aliyokuwa anasikia hapo awali, ambayo kwa dakika kadhaa ilikoma.



Watu walizidi kufurika kwenye makazi hayo, wengi wakija na magari yenye plate number: STK ama DFP. Maturubai yaliletwa uwanjani yakafungwa na viti vya plastiki navyo waombolezaji wapate kukaa. Michango ya mamilioni ilitolewa.



Siku iliyofuata mtoto wa kwanza wa marehemu mwenye miaka ishirini na tatu, kwa jina Miraji, alirejea nchini akitokea India alipokuwa akisomea udaktari. Kwa mujibu wa Imani za wafiwa, marehemu akazikwa siku hiyohiyo.



Kijikao cha familia kiliitishwa kikiundwa na watu watano: mke wa marehemu: Bernadetha, mtoto mkubwa wa marehemu: Miraji, pamoja na kaka na dada wa marehemu.



Waliketi sebuleni nyuso zao zikitandazwa na huzuni.

Waliswali kikao kikafunguliwa na kaka wa marehemu, bwana Tahid. Mbaba mwenye mwili mpana na ngozi nyeupe pe!



“Natumai tu salama salmini baada ya kutoka katika shughuli pevu hapo jana na hata juzi. Ningependa kuchukua nafasi hii sisi kama familia kujulishana hasa ni nini kitakachofuata baada ya mwenzetu, mwanafamilia mwenzetu kutwaliwa na mwenyezi Mungu.



Kama tunavyofahamu, japokuwa kulikuwa na matatizo ya hapa na pale yaliyopelekea mwenzetu kutengwa na jamii, vilevile kusalitiwa na muajiri wake, serikali, sisi katika muda huu ndiyo yatupasa tuwe zaidi ya kitu kimoja.”



Akaweka kituo. Alisafisha koo akaendelea:

“Basi kutokana na hali iliyopo sasa, makubaliano na maagano yetu kama familia yatakuwa hivi: nyumba ya marehemu itakuwa chini ya mkewe na wanawe.



Mwanaye mkubwa atabaki nyumbani kwasababu hakuna pesa ya kusoma huko nje tena, wote tunafahamu kwamba bwana Malale alifilisiwa kila kitu pamoja na miradi yake yote na serikali. Kwahiyo sisi kama ndugu tutachukua jukumu la kuchangia familia kwa kile chochote kitakachopatikana pale patakapokuwa na muhitaji. Nadhani tumeelewana.”



Hoja zilizosemwa na bwana Tahid hazikupingwa na yeyote kikaoni. Wote waliafiki makubaliano hayo. Bernadetha alitizama chini machozi yakaanza kumbubujika tena upya. Miraji alimbembeleza akimtaka anyamaze asije mkufuru Mungu, mama akainua uso wake wenye uchovu akisema:



“Yupo wapi huyo Mungu, mwanangu? Baba yako alikuwa anafanya kazi kama punda, si Mungu wala serikali yake ilimuona. Pesa ilikuwa shida. Hamkusoma wala kula vizuri. Angefanyaje na yeye ni baba?



Alirubuniwa akajiingiza kwenye biashara za magendo - hakuwa na namna. Na hapo ndio maisha yalibadilika, mkasoma na kula vizuri. Lakini ndivyo havikudumu wakamuabisha, wakamdhalilisha na mwishowe kumuua kabisa!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Usikufuru, shemeji.” Bwana Tahid alimkatiza. “Yote hiyo ni kazi ya Mwenyezi Mungu. Wote tunajua ya kwamba mdogo wangu aliumwa.”

“Aliumwa?” Mama Marietta aliwaka. “Kuumwa gani kule? Ameumwa baada tu ya kuvamiwa hapa nyumbani na kupuliziwa madawa yaliyomfanya awe hoi kwa kuzidiwa.



Kama haitoshi hata huko hospitali wakaendelea kuisaka roho yake kwa udi na uvumba tukawa tunahama hospitali kila baada ya siku chache lakini bado haikusaidia. Majibu yake yalionyesha ameuwawa kwa sumu lakini hakuna aliyejali! Hakuna!”



Mama Marietta alikabwa na kilio, alishindwa kuendelea. Alinyanyuka akajiendea zake chumbani na kujifungia nyuma akiacha mzozo ukizizima.

“Alichokisema mama ni kweli bam’kubwa?” Miraji aliuliza.

Tahid alishusha pumzi yake ndefu mithili ya kuli aliyetua mzigo kisha akatizama chini. Shangazi, dada wa marehemeu, akateka zamu na kusema:



“Mwanangu, usijali ya Mungu mengi. Mama yako kwa sasa hayuko sawa. Ni vyema tukamuacha tu, mdomo wake unasukumwa na uchungu alio nao.”



Jibu hilo halikuonekana kumkosha Miraji – halikukunjua uso wake uliokunjamana. Aliminya lips akarusha macho yake kando. Kichwani sauti ya mama yake ilikuwa nzito kuliko zile hoja nyepesi alizopewa na ndugu.





Punde bwana Mtemvu aliposhuka kwenye gari, alitoa simu yake mfukoni akampigia mtu aliyemtunza kwa jina la Ninja. Aliongea naye kwa muda mfupi tu kisha akairudisha simu yake mfukoni akielekea kwenye kiti cha mgahawa mkubwa wenye jina la STEERS. Aliketi hapo akichezea simu yake kubwa nyeupe.



Ndani ya muda mfupi mhudumu alikuja na kumsikiliza, akahudumiwa. Ndani ya dakika zisizozidi kumi na tano magari mengine mawili yenye nembo za STK yakafika eneo la mgahawa. Watu wanne walishuka na kuelekea upande alipo mzee Mtemvu. Nao walisikilizwa na kuhudumiwa na wahudumu kisha maongezi yakachukua nafasi.





“Tujipongezeni jamani, hatimaye tumerudisha amani mioyoni mwetu … Cheers!” Mtemvu alibwabwaja wakagongesha glasi zao za mvinyo wakizisindikiza na matabasamu mapana usoni mwao. Waliongea maneno machache huku vicheko vikiwa vingi.



Baada ya muda waliagana na kutakiana kazi njema lakini mzee Mtemvu hakuondoka pale mgahawani. Baada ya dakika kadhaa alijumuika na kijana mmoja aliyekuwa anamuita kwa jina la Ninja. Alikuwa ni kijana mrefu mno mwenye misuli minene na kifua kikubwa kama makalio.



Alikuwa kavalia kombati la jeshi na macho akiyafunika kwa miwani kubwa ya jua. Alisalimia kisha akaketi wakaanza kuteta na mzee Mtemvu kwa sauti ya chini mno wakitazama usalama. Mzee Mtemvu aliingiza mkono mfukoni mwa koti akatoa shilingi milioni moja na kumkabidhi Ninja ambaye hakupoteza tena muda pale, akajiondoa.



Huko nyuma, mzee Mtemvu naye alitizama kushoto na kulia kisha akalifuata gari lake na kutokomea. Ila kulikuwa kuna mtu anamtizama muda wote akiwa pale mgahawani. Hakujua. Na si tu kumtizama, bali sasa alikuwa anamfuatilia hatua kwa hatua akiwa katika muonekano wa kivuli kilichoonekana pale tu mwanga wa jua ulipokiangazia.



Gari la Mtemvu, mtumishi mkubwa wa serikali, sasa liliacha lami likashika barabara ya vumbi iliyoelekea moja kwa moja na kukomea mbele ya geti kubwa jekundu lililojishikiza kwenye ukuta mrefu mnene wa rangi ya samawati. Hapo geti lilifunguka lenyewe gari likaingia na kisha geti likajifunga.



“Mpenzi, nimerudi nyumbani!” Mtemvu alipayuka baada tu ya kumaliza kuongea na dereva wake.



Nyumba ilikuwa kubwa na ya kuvutia; vigae vyekundu viliezekwa kwa juu, madirisha yake makubwa yalipachikwa vioo, chini kulitandikwa tiles, kuta zilipakwa rangi nyeupe, na bustani kubwa ya maua ya kupendeza ilitambaa mbele ya uso wa nyumba. Ilipendeza.



Mtemvu alifika mlangoni, mkewe: Mama Beatrice, akatoka na kumkumbatia.

“Karibu, mpenzi.” Alimbusu mumewe kwenye lips.

Japokuwa umri wao ulikuwa si haba, mapenzi yao hayakusita kujionyesha. Mtemvu alirudishia busu wakaingia ndani.



Walioga na kula wakajipumzisha sebuleni. Mtemvu alivalia bukta fupi rangi ya manjano na kaushi nyeupe huku mkewe, Mama Beatrice, akijisitiri kwa khanga pekee. Walikuwa wanapiga soga za hapa na pale haswa juu ya msiba wa karibuni. Watoto hawakuwepo hivyo walikuwa huru kushikana na hata kutomasana mara zingine.



Baada ya muda kidogo walinyanyuka kwa milengwa ya kueleka chumbani kujilaza. Ila kabla hajajitoa sebuleni, Mtemvu aliendea dirisha akafungua pazia na kuchungulia nje, akaliona gari lake. Alitahamaki.



“Mbona Mustafa hajaondoka?”

Alikunja sura.

“Si nimemwambia apeleke gari service?”



Mustafa, mwanaume wa makadirio ya miaka hamsini na mbili, ni miongoni mwa watu wapole wenye sauti ya chini. Ndiye mtu aliyekuwa anayempa kampani Mtemvu muda mwingi kwa kuwa naye garini.



Anamfahamu mkuu wake akiwa katika hali yoyote ile; anajua wakati ambao mkuu wake anamtaka aongee na wakati gani anaomtaka anyamaze. Zaidi ya yote anafahamu vyema siri za mkuu wake, pengine kuliko mkewe.



Mtemvu alipata shaka. Alitoka nje akalifuata gari, alipolifungua mlango akakuta Mustafa amelalia usukani. Alimuita lakini hakuitika. Alimshika begani akamvuta kumnyanyua.



La haula!



Mustafa alikuwa anamimina damu mdomoni na uso wake haukuonyesha kutojitambua. Moyo wa Mtemvu ulitetemeka na akajikuta anahisi hofu imemtambaza.



“Mustafa! Mustafa!” Aliita akimtikisa lakini Mustafa alikuwa kimya. Alimshusha kwenye gari akamlaza chini. “Mustafa! ... What is this? Mama Beatrice! Mama Beatrice!” Mtemvu aliita. Aliinamisha kichwa chake akakilaza kifuani mwa Mustafa: kifua kilikuwa kimya, tuli.



Aliponyanyua kichwa chake, mkewe – mama Beatrice – alikuwa tayari ameshafika, na msichana wa kazi – Habiba – alikuwa amesimama mlangoni. Mvulana wa kazi naye – Lupi – alikuwa amefika eneo la karibu.



“Nini baba?” Mama Beatrice alichuchumaa. “Nini kimetokea?”

“Sijui! Nimemkuta Mustafa hivi. Anatoka damu na mapigo yake ya moyo yamesimama!”

“Tumpeleke hospitali! … Au mpigie dokta wako!”

“Dada, embu niletee simu yangu hapo kwenye kochi.”



Dada, msichana mchanga mwenye umri kati ya 15 mpaka 18, aliyevalia gauni lake la pink iliyofifia na kiremba kichwani, mwembamba mrefu na mwenye uso wa upole, alielekea alipotumwa akarejea na simu ya bosi.



Mtemvu akampigia dokta.

Dokta aliwasili ndani ya dakika thelathini. Aliukagua mwili wa Mustafa kwa dakika kadhaa, akatikisa kichwa.



“Amefariki.”

“Nini kimemuua?” Mtemvu alidakia. Dokta akameza kwanza mate.

“Sijui, bado sijafahamu. Nahitaji kuufanyia uchunguzi zaidi.”

“Sawa. Acha basi nitoe taarifa polisi.”



Mtemvu alichukua simu yake akapigia polisi. Ndani ya muda mchache polisi walifika wakahoji na kufanya msako mwepesi bila ya matunda, mwili wa marehemu ulichukuliwa polisi wakaenda na daktari. Mtemvu pamoja na mkewe walirudi ndani tukio hilo bado likiwa kichwani na midomoni mwao. Walijilaza kitandani giza la usiku likazidi kudaka umri.



Ila Mtemvu hakupata usingizi.





Alikuwa akijigeuza huku na kule kichwani akimrejelea Mustafa. Hivi ni kweli amekufa ama naota? Ilikuwa ngumu kuamini. Nani aliyemuua ama kipi kilichomuua? Hilo ndilo lililomuumiza haswa kichwa na kumkosesha amani.



Kuna muda alihisi kulala ndani ilhali jambo kama hilo limetukia ndani ya uzio wake ni uzembe. Vipi kama muuaji bado yu ndani anatafuta roho yake? Aamke akamsake? Hapana! Roho ilikataa. Kwakuwa mkononi alikuwa amelala na bunduki yake ndogo hivyo hakuwa na haja ya kuogopa, alijifariji.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Baada ya masaa kadhaa macho yake yaliyokuwa yanapepesa huku na huko yalichoka, yalifumba pasipo kupenda. Alijitahidi kupambana nayo lakini mwishoni alikuwa mshindwa akatwaliwa na usingizi mzito uliokuja kukatishwa kikatili asubuhi na mapema na sauti ya mkewe.



“Amka uende kazini, muda umewadia!” Aliamrisha Mama Beatrice. Ilikuwa ni mara yake ya nne akijaribu kufanya hilo zoezi pasipo na mafanikio na sasa alifaulu baada ya kuropoka.



Mtemvu aliuvuta mwili wake kivivu akaketi. Alitazamatazama kushoto na kulia asione bunduki yake. Mkewe alitikisa kichwa akamwambia:

“Imedondokea huko chini! … Sijui ulikuwa unamlinda nani na hiyo bunduki usiyojua hata ilipo.”



Mtemvu aliichukua bunduki yake akaitizama, kumbe hata ndani haikuwa na risasi!l Aliitupia kando akapiga mhayo wa nguvu. Alitikisa kichwa chake akanyanyuka aende bafuni akijitahidi kukaza macho yake mekundu yaliyokuwa yanafumba mara kwa mara pasipo ruhusa.



Alifuata kioo cha bafu akajitizama, aliteka mswaki na kuudumbukiza mdomoni aswaki. Alipiga mswaki chapuo la kwanza, akainama na kutema povu. Kimbembe alipoamsha sura yake atizame tena kioo; ajabu alikutana na sura ya mtu mwingine kiooni! –Sura ya mwanaume mweusi mno mwenye macho makubwa meupe na lips zenye nyama nene.



Mtemvu aliduwaa akadondosha mswaki. Moyo wake ulisimama kisha ukaanza kukimbia mbio mno. Alihisi mwili umekuwa wa baridi ghafla. Kufumba na kufumbua taswira yake ilirejea kwenye kioo, maandishi yakajichora:



‘Nadai roho yako ila sina papara nayo’

Alifikicha macho yake na kutizama tena. Maneno hayakuonekana!

“Iishh! Hivi naota au?”

Alinawa uso wake na maji aondoe maulevi ya usingizi. Alitizama tena kioo asione kingine chochote isipokuwa taswira yake. Aliishia tu kutikisa kichwa akamalizia kujihudumia na kutoka nje ya bafu.





Mama Beatrice alikuwa ametoka ndani ya chumba lakini akiwa tayari ameshamuandalia mumewe nguo akiwa amezilaza kitandani. Kwa haraka Mtemvu alijiandaa akitizama saa yake ya mkononi mara kwa mara. Akiwa anavalia viatu vyake apate kuhitimisha zoezi hilo, mara alisikia sauti kali ya ukunga – sauti ambayo haikumchukua muda kuigundua kuwa ni ya mkewe, Mama Beatrice.



Kabla hajamaliza kuvuta pumzi, Mama Beatrice alikuwa tayari ameshafungua mlango kwanguvu. Alimtizama mumewe na sura iliyotepeta hofu. Aliongea kwa pupa la kigugumizi akionyeshea kidole alipotokea.



“Baba Bite! – mama yangu – kule! Twende ukaone! Twendee!”

“Kul – kule wapi? Kuna nini?” Mtemvu aliuliza kwa papara. Uso wake ulibadilika ukafanana na ule wa mkewe.



“Wamekufa!” Mama Beatrice aliropoka kisha akanyamaza ameze mate na kuvuta pumzi.

“Habiba – Lupi! Wameuwawa! Uwiiiiii! – Wote wamekufaa!”



Haraka Mtemvu alikwapua bunduki akaunyakua mkono wa mke wake wakaelekea huko tukioni. Hakukumbuka hata kama hiyo bunduki haikuwa na risasi japokuwa alishaitazama.



Walifika eneo la tukio, nje kibarazani, Mtemvu akatokwa na macho. Alishuhudia miili ya Habiba na Lupi ikiwa imelala kibarazani inaogelea kwenye dimbwi la damu nzito, damu zilitokea kwenye matundu mawili marefu yaliyotobolewa kwenye kila shingo ya marehemu. Kwa mujibu wa michoro ya damu ilikuwa ni wazi miili hiyo iliiburuzwa tokea vyumbani mpaka pale.



“Mtemvu, kuna nini kinaendelea?” Mama Beatrice alilia. “Kuna nini humu ndani? Kuna nani humu ndani?” Aliuliza Mama Beatrice akiwa karibu mno na mume wake. Mwili wake ulikuwa unatetemeka kwa baridi na akivuja jasho kwa muda huo huo. Moyo wake ulikuwa unaenda kasi na alihisi maumivu ya kichwa.



Mtemvu alijivika ujasiri akaanza kupekua nyumba nzima huku mkono wake uliobebelea bunduki ukiwa mbele kumlinda na kumuepushia shari, nyuma yake Mama Beatrice hakubanduka hata kidogo. Walimaliza nyumba nzima wasione kitu. Hakukuwa na mtu yeyote isipokuwa wao wenyewe!



“Wapigie simu polisi waje! … Mie siwezi kukaa hapa tena.” Mama Beatrice alisema kwa sauti ya chini akimtizama mumewe na macho yanayovuja machozi.



Baada ya nusu saa polisi walifika na kufanya upekuzi. Waliuchukua miili ya marehemu wakaongozana pamoja na Mtemvu na mkewe kwenda kutoa maelezo wakati huo miili ikitangulizwa hospitali. Baada tu ya dakika thelathini Mtemvu na mkewe wakatoka kituoni wakiwa wameongozana na polisi mmoja mrefu mwembamba ila mwenye mustachi mpana.



“Pole sana, Mkuu. Kama isingelikuwa wadhifa wako ungelikuwa matatani sana. Nakushauri umtafute inspekta Vitalis, huwezi jua maadui wako wamepanga nini mbele yako. Usalama wako u matatani sasa.” Polisi alishauri. Mtemvu akatikisa kichwa.



“Sahihi. Nadhani huo ni ushauri mzuri, nitaufanyia kazi lakini hakikisheni habari hizi hazienei popote pale. Hakuna sikio lolote litakalosikia hizi taarifa.”



“Halina shida hilo. Siku njema, mkuu.”

“Nanyi pia. Ila dokta anaweza akaja kuonana na nyie akitoka hospitali kuikagua ile miili. Endapo akija mumpe ushirikiano.”

“Sawa, Mkuu.”



Mtemvu alijiweka kwenye gari pamoja na mkewe wakahepa. Alimpitisha Mama Beatrice kwa dada yake Kigamboni, yeye akajipata pembezoni ya bahari, ndani ya hoteli moja kubwa ya kifahari akijaribu kufanya jitihada za kuburudisha akili yake dhidi ya tafrani lililotoka kumkabili.







Upepo mwanana wa bahari na kinywaji laini kilichokuwa kinakanda koo lake kavu, vilimbembeleza akasinzia kwenye kiti. Baada tu ya muda mfupi akili yake ilianza kumrejeshea yale yaliyopita.



Miezi kadhaa tu nyuma akiwa kwenye kikao cha siri pamoja na wenzake wanne: Bwana Pius Mbwambo, Raheem Victor, Filbert Waziri na Katende Katende, almaarufu kama K square.





“Mzigo umeshafika Rome, sasa tunafanyeje?” Sauti nyepesi ya bwana Katende iliuliza jopo. “Inabidi mmoja aende huko.” Mtemvu akashauri na kuongezea, “Mimi nimeshamaliza kazi yangu ya kuhakikisha usalama, tumteue mmoja akasimamie zoezi hilo.”



Bwana Pius akagonga meza.

“Nani akubali kwenda huko?” Aliuliza akitoa macho. “Kusema ukweli mimi sipo tayari! Hili jambo ni hatari sana!”



Raheem akatabasamu. “Sasa mnadhani ni nani atakayeamua kujitoa sadaka?” Alidhihaki. “K square upo tayari? ... Filbert upo tayari? ... Pius upo tayari? ... Mtemvu je? ... Si unaona? Hakuna anayekubali.



Tulifanya ujinga sana kuanza kufanya hii kazi kabla ya kupanga nani atakayesimamia hilo swala kwa uaminifu mkubwa. Unaona sasa inavyotugharimu? Tumepewa taarifa mzigo umewasili, then what is next? Tutawaachia wale wazungu?”



Kimya kikatwaa umati kwa dakika kadhaa kabla ya bwana Filbert Waziri kutia neno: “Kwani hatumuamini Amerigo? Tumuache asimamie tu!”



“Hapana!” Mtemvu akapayuka. “Unadhani hii ni biashara ya nyanya? ... What if akatudhulumu? Unaenda kushtakia wapi? Unampatia wapi? Hatujafikia kiasi cha kumuamini kina hiko.” Mtemvu alitema cheche, bwana Pius na wengineo wakamuunga mkono.



“Ni kweli!” Alisema K square. “Hatuwezi kumuamini kirahisi rahisi hivyo, haswa kwenye biashara kama hii. Tunamuhitaji mtu mwingine mbali na sisi kwasababu ya usalama. Mtu tutakayemuamini, mtu ambaye tunajua anatokea wapi na tutampatia wapi akileta ushenzi. Au nyie mnaonaje?”



“Ila tutampatia wapi huyo mtu wa kumuamini kiasi hiko?” Filbert Waziri aliuliza. Baada ya mafikirio kidogo, Mtemvu alipendekeza:

“Bwana Malale!”

Wenzake wakamtizama na macho yaliyotaka kufahamu zaidi.



Bwana Malale … Bwana Malale … Bwana Malale … Sauti ya kunong’oneza ilisikika ikififia masikioni mwa Mtemvu. Alikurupuka toka usingizini. Alitizama pande zake zote nne kisha kashusha pumzi ndefu akitikisa kichwa chake kwa masikitiko. Alichoropoa simu yake mfukoni akapiga.



“Haloo! Yes Pius, unaweza ukaja Palace hotel mara moja? Ni muhimu sana.” Alipokata simu akamuita pia Katende na Filbert pamoja na Raheem ambaye yeye alitoa udhuru. Baada ya dakika chache tu, wakawa tayari wamewasili kuitikia wito.



“Niambie Pius! Vipi huko mbugani wanyama wanasemaje?”

“Aaah safi tu!” Alijibu Pius kisha haraka akaeleza hofu yake: “Vipi, mbona ghafula? Kuna chochote au una dili jipya?”



Muhudumu alikuja akawahudumia. Mvinyo na nyama choma ziliteka meza na kufanya iwe ndogo kuliko uhalisia. Ilikuwa ni Pius, Filbert na K square tu ndio waliokuwa wanakula, Mtemvu alitumia maji pekee baada ya kumaliza glasi yake ya sharubati.



“Samahani sana kwa kuwaharakisha na wito wangu wa ghafula. Nina tatizo linanikabili. Can you imagine ndani ya usiku mmoja wamekufa watu watatu nyumbani kwangu katika mazingira ya kutatanisha?”



Swali hilo likateka nyuso za wenzake walioguswa kwa namna moja ama nyingine. Waliacha kula wakamtizama Mtemvu.

“Bro, are you serious?” Filbert aliuliza. Mtemvu aliminya mdomo wake alafu akanena kuonyesha ametingwa.



“Ndani ya usiku mmoja.” Mtemvu alianza kufafanua, “Dereva wangu amekufa na wafanyakazi wawili wa ndani. Vifo vyao mpaka sasa hivi sielewi nini kimesababisha. Nimewakuta wakiwa wanamwaga tu madamu huku anayetenda hayo asionekane kabisa! Sielewi kuna nini! Mbali na hapo nimekuwa nikiona mauzauza! Nahisi kuna mtu ananifuatilia! Si bure kanisa!”



Kabla ya kutia neno Filbert Waziri alitazamana na wenzake kwa bumbuwazi kisha akaguna akimtizama Mtemvu.

“Mtemvu, are you serious or unatutania? Mbona leo sio sikukuu ya wajinga brother?” Mtemvu akatizama chini akikuna kiwaraza chake. Alikunywa kwanza fundo moja la maji ndipo akaendeleza soga yake ya kutisha.



“Sio kwamba nawatania ndugu zangu. Nawaeleza ukweli, ukweli ulio uchi kabisa! Hamjapata kusikia lolote juu ya hayo kwasababu tu ya cheo changu huko usalama, la sivyo sijui!” Akaweka kituo anywe maji.



“Ila kama nilivyowaeleza, dereva wangu: Mustafa, pamoja na wafanyakazi wangu wa ndani wameuwawa. Simjui muuaji ni nani na sijui anataka nini. Sijui ametumwa na nani?”



Zaidi tu ya kushtukiza, kila mtu akatandwa na hofu. Chakula hakikulika tena wala vinywaji havikugusa koo. Nyuso zenye taharuki na ukakasi wa mawazo zilitungwa wakiwa wanajaribu kufumbua fumbo lililoonekana ni gumu sana kung’amuliwa. Kabla lisaa halijamegeka, daktari wa Mtemvu alifika hotelini.



“Bwana Mtemvu, wakati unanipigia ndio nilikuwa namalizia ile shughuli. Kusema ukweli nimeshangazwa na hivyo vifo vingine. Kwa mujibu wa chunguzi, Mustafa amekufa kutokana na kupasuka kwa mishipa ndani ya mwili wake hivyo kupelekea damu kuvujilia ndani kwa ndani mpaka kifo.



Na kuhusu wafanyakazi wako wa ndani, vifo vyao ni vya kufananana – kutobolewa na kitu kirefu chenye ncha kali shingoni mwao. Lakini ajabu sijaona michubuko wala chochote kuashiria kama walipitia purukushani zozote kabla ya vifo vyao. Inaonyesha muuaji ni mtu mwenye utaalamu wa hali ya juu. Bado sijajua alitumia mbinu gani!”



“Si unaona!” Mtemvu alishadadia. “Niliwaambia mimi, kuna tatizo jamani!”

“Sasa tunafanyaje?” Filbert akauliza kwa hofu. Macho yalikuwa yamemtoka ndita za woga zikijichora kwenye paji la uso. Hakuna kingine walichokiamua zaidi ya kuimarisha ulinzi maradufu, wawe macho zaidi na lolote litakalotokea wajulishane.



Kikao kilifungwa wakatawanyika. Mtemvu alielekea kuichukua miili ya marehemu na hatua za mazishi zikafanyika zikichukua siku mbili tu baada ya miili ya marehemu kurudishwa kwenye makazi yao huko vijijini. Habari hazikusambaa hata kidogo. Hakuna aliyejua nini kilijiri ndani ya uzio wa nyumba ya bwana Mtemvu isipokuwa daktari, marafikize na polisi.



Kwa siri alipeleka miili hiyo huko vijijini akitoa pesa taslimu kufanikisha na kumaliza zoezi. Siku ya tatu aligeuka kurudi nyumbani kwake. Kwakuwa Mama Beatrice alikuwa bado yupo nyumbani kwa dada yake ilimlazimu siku hiyo akae peke yake nyumba nzima, hakuwa na jinsi.



Alipiga moyo konde akijiaminisha ya kuwa yeye ni mwanaume na yupo radhi kupambana na adui yake. Mkononi akiwa ameshikilia bunduki yake ndogo alijipumzisha kwenye kochi atizame televisheni.



Kwakuwa alikuwa amechoka mno na purukushani za msiba na hakupata muda wa kupumzika huko vijijini, usingizi haukupata vizingiti kumtwaa haraka; macho yalifumba mdomo ukaachama akilegea na kuacha bunduki yake ikae mbali. Muda mfupi tu baada kuanza kukoroma, akapata mgeni.



Hakuwa mgeni wa kawaida! Kilikuwa ni kivuli kilichopita kwenye mwanya wa mlango kisha kikajisogeza mbele kabisa ya Mtemvu na kusimama papo. Baada ya muda si mwingi, Mtemvu alijikuta akiwa amelala bafuni. Hakuwa na nguo yoyote, na kwenye kioo cha bafu aliachiwa ujumbe uliosomeka:



‘Mpaka pale wasaa utakapowadia’http://deusdeditmahunda.blogspot.com/





*****





Usiku bado haukuisha. Ulizidi kuwa mweusi kadiri muda ulivyozidi kukua na kukua. Mwezi ulijifinya ukawa mdogo. Mawingu meusi yaliuficha mwezi huo na muda mwingine ukawa hauonekani kabisa.



Ni kama vile mvua ilitaka kunyesha kutokana na uweusi wa mawingu na upepo wa baridi uliokuwa unapuliza muda huo. Kulikuwa kimya. Vimilio vya mbwa kubweka ndivyo viliharibu sare hiyo baadhi ya maeneo.



Nyumba kubwa ya bwana Pius, afisa mkubwa wa serikali kwenye shirika la maliasili TANAPA, ilikuwa imetulia kando kando kidogo tu mwa barabara ya vumbi ielekeayo kanisa kubwa la katoliki.



Haikuwa imepakana na nyumba zingine kwa karibu sana isipokuwa umbali wa hatua kadhaa uliofanya nyumba hiyo kuwa pweke na ndogo haswa wakati huu wa usiku ambapo giza lilikuwa limemeza sehemu kubwa ya nyumba hiyo haswa upande wake wa nyuma.



Bwana Matata, mzee wa miaka hamsini aliyekuwa ndani ya sare za walinzi, mdomoni mwake alikuwa amepachika sigara akiivuta kwa madaha macho yake yakiranda randa huku na huko ndani ya jengo la bwana Pius. Hakuwa na kitu cha kuhofia.



Kwa miaka kadhaa sasa yupo hapo analinda na hakuna hata siku moja ambayo aliwahi kukumbana na purukushani zozote zile. Waya za umeme juu ya kuta ndefu za nyumba ya bwana Pius zilimfanya aheme na kuwa na amani nyeupe, zaidi ya yote, bobby, mbwa wake mweusi anayetisha kwa ukali na mwili wake mpana na mrefu alimpa faraja na kujiona ya kwamba kulinda eneo hilo ilikuwa ni kama kumsukuma mlevi.



Kuna ugumu gani ukizingatia mkuu wake alimpenda na alipata chakula safi kila siku?

Hakujua.



Bwana Matata hakujua ya kwamba usiku ule ulikuwa tofauti na alizowahi kuzipitia. Akiwa ameketi kwenye kiti chake ndani ya kijumba kidogo cha mlinzi, alisikia bobby akibweka kwanguvu akielekeza uso wake getini.



Bwana Matata alirusha macho yake kumtizama bobby alafu akampuuza, ni kama vile alijua mnyama huyo atanyamaza tu kwani huwa anabweka na kutulia. Ila haikuwa hivyo, bobby aliendelea kubweka kwanguvu na kwanguvu mwishowe bwana Matata alinyanyuka akaenda kutizama hicho anachobwekea mbwa wake.



Hakukuta kitu, alighafirika akambwekea bobby:

“Embu acha kunipigia kelele!”



Kisha akasonya na kurudi alipotokea. Bobby alinyamaza kwa muda kidogo kabla tena hajaanza kubweka kwanguvu. Mara hii aliusogelea mti wa mtiki uliokuwa umesimama bustanini. Hakudumu hapo, ghafula akanyamaza na kufyata mkia. Alikimbilia kwenye kijumba cha mlinzi akajificha nyuma ya mlango.



“Afadhali umeamua ulale. Kumbe usingizi ndio ulikuwa unakusumbua eenh?” Aliroroma Bwana Matata kwa kejeli. Sentensi yake hiyo ilipokoma, ghafula umeme ulikata kukawa giza totoro.



Bobby alibweka kwanguvu kwa mara ya mwisho. Hakusikika tena. Sekunde chache mbele umeme ulirudi ukawakuta Bobby na Bwana Matata wakiwa tayari maiti zilizoachwa zikivuja damu! Kivuli cha mtu asiyeonekana kilitoka nje ya jengo hilo kikaelekea upande wa nyuma ya nyumba.



Si tu kwamba Pius na mkewe hawakuwa wanafahamu kinachoendelea huko nje, bali hawakudhani wala kubashiri jambo kama hilo. Kila mtu alikuwa kwenye shughuli yake ndani ya nguo nyepesi walizokuwa wamevaa. Bwana Pius alikuwa akiandika barua pepe kwenye tarakilishi mpakato wakati mke wake akiperuzi riwaya ya Stephen King: ‘Under the dome’.



Ndani ya chumba kulikuwa tulivu kiyoyozi kikipuliza kwa mbali. Ilikuwa ni hivyo mpaka pale Bwana Pius aliposikia sauti ya kugonga dirishani akaacha shughuli yake na kusogelea dirisha afungue pazia kushuhudia. Hakuona kitu. Alisonya kana kwamba amejidharau, alirudi na kuendeleza shughuli yake, ila haikuchukua muda mrefu dirisha likagongwa tena … Kap! Kap! Kap! Bwana Pius akasonya akimtizama mkewe.



“Hivi huyu Matata, anan’tafuta nini?”

Mkewe akamtizama asijue kinachoendelea. Alirudisha macho yake kwenye karatasi za riwaya kana kwamba hajasikia lolote.

Kap! Kap! Kap! - Tena!



“Pumbavu!” Pius akafoka. Alinyanyuka kwa hasira akafuata dirisha na kutizama akitumbua macho. Hakuona kitu. Ila kabla hajafunga dirisha kwa pupa, kuna kitu aliona. Kulikuwa kuna maandishi kiooni yakiwa yameandikwa kwenye mvuke ulioshika kioo kutokana na ubaridi wa kiyoyozi. Bwana Pius alisogeza uso wake karibu akasoma maandishi hayo:



“Kuna mgeni aliyetumwa kuchukua roho yako.”

Alifunga dirisha haraka akamtizama mkewe na kumtaarifu. Mke akaja kutizama ila ajabu hakukuta chochote, maandishi hayakuwepo tena. Kioo kilikuwa kisafi kama vile kimepigwa maji na kufutwa na dekio.



“Kwani kuna nini, mbona mie sikuelewi?”

Mwanamke aliuliza huku kidole chake kikiwa ndani ya riwaya asije akapotea alipoishia.



“Kwani wewe ulikuwa husikii kuna mtu anagonga dirisha?”

“Sijasikia chochote mie. Nilikuwa nakuona tu unavyohangaika.”



Bwana Pius alidhani labda mkewe hakusikia sauti hiyo kwasababu ya utamu wa riwaya, ila ni kweli hakusikia kitu. Ni yeye peke yake ndiye aliyekuwa anasikia sauti hiyo ya kugongwa kwa dirisha, na ni yeye peke yake pia aliyeyaona maneno yale juu ya kioo. Wakati mke wake akijirudisha kitandani aendelee na riwaya yake, yeye alifungua kioo cha dirisha amuite mlinzi. Aliita pasipo mafanikio moja kwa moja akajua mlinzi amelala.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Hiyo si mara yake ya kwanza, alijisemea mwenyewe. Ila na mbwa je? Amelala? Mbona hajabweka? Pius alipata shaka kidogo. Alitwaa bunduki yake ndogo akatoka nje ya nyumba aelekee kwenye kibanda cha mlinzi. Kabla hajafika huko aliona damu zilizochuruzika tokea kwenye kibanda hicho.



Haraka bwana Pius alikumbuka kisa cha Mtemvu – macho yakamtoka. Aliona sasa leo ni zamu yake. Alihisi mwili wake umepitiwa na mtetemeko ghafula na ubaridi wa ajabu. Bunduki yake mkononi haikumpa ujasiri ijapokuwa alikuwa kaielekezea mbele mithili ya mwanajeshi aliyekuwa vitani.



Aliita kwa hofu:

“Bwana Matata!”

Huku akiwa amesimama na uso wake usitulie kwa kutizama huku na huko. Alishusha pumzi ndefu akajongea taratibu kwenda kibandani. Moyo wake ulikuwa unafukuta kwa mapigo.



Hatua zake za kutetemeka zilimfikisha ndani ya kibanda akaona jambo ambalo alizoea kuliona kwenye tamthilia. Bwana Matata pamoja na mbwa wake wote walikuwa wamelala chini damu zikitoka kwenye matundu ya puani, mdomoni na masikioni.



Pius akiwa hapo anashangaa, ghafula alisikia mtu amekatiza nje ya kibanda kwa kukimbia. Alitoka nje ya kibanda lakini hakukuta mtu huko nje. Alirusha macho yake huku yakienda huko. Akahisi kwenye mti wa mtiki ndipo alipo muuaji. Basi taratibu akaanza kuufuata mti huo akielekezea bunduki yake.



“Toka mwenyewe kabla sijakushushia mvua ya risasi!” Pius alitishia. Kijasho chembamba kilikuwa kinamchuruza. Mkono wake uliokuwa umebebelea bunduki ulikuwa unatetemeka. Kama kuna siku aliomba Mungu awe karibu na binadamu, basi ilikuwa ni hiyo. Roho ilikuwa mkononi!



Kinyume kabisa na mategemeo yake kwamba muuaji yupo mtini, alisikia vishindo vya miguu nyuma yake. Kwa pupa aligeuka na kufyatua risasi zilizoenda bure. Haikupita sekunde akasikia tena vishindo nyuma ya mgongo wake. Aligeuka akafyatua risasi hovyo mwishowe zikaisha. Sasa vishindo vya miguu vikakoma, sauti ya vicheko visivyojulikana ni wapi vinatokea vikaanza kumnyima raha masikioni.



Pius alichachawa, kwa muda akawa kama mtu asiyejua nini anataka kufanya mpaka pale alipoona mlango wa nyumba yake ukiwa wazi akaanza kuukimbilia. Mlango ulijifunga na komeo la ndani. Haukufunguka abadani pamoja na kwamba Pius alitumia nguvu zake zote akipiga makelele ya kilio na kuubonda mlango huo kana kwamba umemfanyia makusudi.



Alipoona hapo hakuna matumaini, upesi alikimbilia dirisha la chumba chake akapiga kioo akimuita mkewe aliyekuwa anamuona kwenye kauchochoro ka pazia akiwa anaendelea kusoma riwaya yake.



Hamaki mwanamke hakusikia kitu kabisa! Hakusikia dirisha likigongwa wala kumuona mtu dirishani. Alifungua tu karatasi za riwaya na macho yaliyozidiwa utamu.



Pius akiwa hapo dirishani asiwe na la kufanya, alishuhudia mlango wa kabati la chumbani mwake ukifunguka akatoka mwanaume wa ajabu. Mwanaume mrefu kwenye umbo la moshi mweusi ti. Mwanaume mwenye mwili mpana macho yake yakiwa mekundu kama moto.



Pius alipiga kelele kumshitua mkewe pasipo mafanikio. Mbele ya macho yake alishuhudia mwanaume huyo akijitapanya akawa moshi kisha akamuingilia mke wake kwa kupitia matundu ya pua, masikio na mdomo.



Mbele sekunde chache tu, mke alitapatapa damu zikimtoka mdomoni, puani na masikioni. Ndani ya muda mfupi mke akawa marehemu. Aligeuka historia tena mbele ya macho ya mume wake aliyekuwa hana msaada wowote zaidi ya kushuhudia.



Pius aliishiwa nguvu. Alibakia akiwa amesimama kama mnara wa babeli. Hakujua nini cha kufanya. Uso wake ulikuwa umeduwaa macho yakibubujika machozi. Alijikuta akiuliza kwa sauti ya chini kana kwamba kuna mtu anamsikia:

“Wewe ni nani?”



Majibu yake akayapata kwenye kioo cha dirisha yakijiandika na damu.

‘Mimi ni mgeni wako niliyetumwa roho yako. Tatizo sina haja ya kuwahi kukupeleka kuzimu.’

Pius akajikuta akidondoka chini na kupoteza fahamu.





Baada ya hodi fupi wakati huu ambao ulikuwa unaelekea mchana, Mama Beatrice alimuita mfanyakazi wake mpya wa ndani, Rema, na kumuamuru akafungue geti.



Mwanaume mrefu mwenye mwili uliojaza misuli barabara akiwa kavalia suti nadhifu na tai akaingia ndani ya uzio wa nyumba ya Mtemvu. Mwendo wake ulikuwa mkakamavu akijiamini. Uso wake ulikuwa mrefu na wenye ndevu zilizochongwa vyema.



Macho yake yalikuwa tulivu na taratibu yalikuwa yanapekuwa mazingira aliyokuwepo. Kwa jina afahamika kama Vitalis – Vitalis Byabata. Inspekta wa polisi aliyerudishwa nyumbani baada ya kutumika kama ajenti wa polisi wa kimataifa ‘interpol’ kwa takribani miaka kumi na tano akiwa mwanaume aliyechangia vyema harakati za kudidimiza na kutokomeza ugaidi duniani.



Mwanaume aliyetia mkono wake kwenye mauaji ya viongozi wa kigaidi wa Al-Qaeda: Anwar Al Awlaki, Saleh al-Somali na Abu Ayyub al-Masri pamoja na wale wa kundi la kigaidi la Taliban Abdul Ghani Beradar na Baitullah Mahsud.



Pamoja na mchango wake wote huo, si dunia wala watanzania waliokuwa wanamjua kwa mapana na marefu. Ukiachana na usalama wa taifa, jeshi la polisi na Interpol hakuna mtu mwingine yeyote aliyekuwa anafahamu nondo za ngumi zake, akili yake pevu kwenye ugunduzi wa hatari na wepesi wake kwenye kufanya maamuzi yaliyokuwa yanawaacha hoi maadui zake ndani ya muda mfupi. Wenzake huko Interpol walikuwa wamembatiza jina la ‘the black angel’.



“Karibu sana, inspekta Vitalis.” Mama Beatrice alisema kwa tabasamu akisimama.

“Ahsante sana, mama. Habari ya saa hizi?” Vitalis aliuliza wakibadilishana mikono.

“Njema. Ni kitambo sana sijakuona, wanasemaje huko ulaya?”



“Hawana usemi. Sijui nyie huku nyumbani?”

“Mmh, ni majaribu tu huku kwakweli. Nimefurahi sana kukuona. Nimeanza kupata ahueni mapema.”

“Mkuu, amenieleza yanayowakumba. Tutasaidiana kutatua tatizo, naamini.”



Inspekta Vitalis aliketi kwenye kochi lililokuwa limekaa hapo nje pamoja na Mama Beatrice, baada ya muda mfupi bwana Mtemvu akatoka ndani akiwa amevalia vema na briefcase mkononi. Inspekta Vitalis alisimama akampatia salamu ya kijeshi Mtemvu alafu wakaongozana mpaka kwenye gari na kuondoka, inspekta Vitalis akikamatia usukani.



“Hapa unavyoona, nikitoka tu mke wangu naye anapanda gari lake kwenda kwa dada yake, anaogopa sana kukaa nyumbani. Inabidi uwe makini sana, Vitalis. Huyo mtu mtu anayenifuatilia si wa kawaida. Ni hatari mno. Mauaji yake ni ya kutisha na hayabakizi dalili zozote za mapigano wala purukushani.”



Mtemvu alisema kisha akatengenezea miwani yake ya macho.

“Usihofu mkuu. Nitajitahidi kwa nguvu na akili yangu yote kukuhakikishia usalama.”



Wakati gari lajongea na mwendokasi wake wa kawaida, haikuchukua muda mrefu Vitalis kugundua kuna gari lawafuata kwa nyuma. Alitizama vioo vya ubavu wa gari akalisoma gari hilo kwa makini lakini jitihada zake za kung’amua sura ya dereva ziligonga mwamba.



Aliongeza mwendokasi akijaribu kuyavuka magari yaliyokuwa mbele yake, baada ya muda alilipoteza gari lililokuwa linamfuatilia. Hakuliona tena kwenye vioo mpaka wanafika ofisini.



Inspekta Vitalis hakumwambia mkuu wake alichokiona, alimfungulia mlango wa gari akaongozana naye mpaka mlangoni mwa ofisi. Waliingia ndani ya ofisi wakakuta vitu shaghalabaghala. Makaratasi yalikuwa yametupwa na kuchanwa chanwa. Hakuna kitu kilichokuwepo kwenye hali yake ya kawaida – ofisi ilikuwa mithili ya eneo lililopigwa bomu. Jambo hilo likamshangaza Mtemvu pamoja na inspekta Vitalis.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Mkuu, uliacha ofisi hivi?”

“Hapana! Nashangaa.”

“Ngoja basi kidogo papo hapo.”





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog