Simulizi : Nyuma Yako (2)
Sehemu Ya Tatu (3)
“Sasa hivi hakutakuwa na haja ya kuua yeyote?” Jack akauliza akikodoa. Miguuni mwake alikuwa amevalia ‘sandles’ za Vio, na Marshall alipomtazama vema akabaini hata mwanaume huyo alikuwa amevalia chupi ya mkewe, kwa juu ya kuno chake ungepata kuona.
“Jack,” Marshall akaita na kuuliza, “Hiyo ni chupi ya Vio?” akauliza akinyooshea kidole kiunoni mwa Jack, upesi Jack akapandisha bukta yake alafu akamtazama Marshall, “Macho yako yalikuwa yanafanya nini kiunoni mwangu?” akauliza akijihami.
Marshall akatikisa kichwa, kabla hajasema jambo, Jack akamwambia, “Tony, umeanza tabia za ushoga?”http://pseudepigraphas.blogspot.com/
“Aliyeanza tabia za ushoga ni nani? Mimi au wewe unayevaa chupi ya kike?” Marshall akauliza.
“Sio ya kike!” Jack akajitetea, “ni rangi ya waridi tu lakini si ya kike!”
Marshall akaangua kicheko, “Vipi, ni bikini ama?”
Jack akatoa macho, “Tony, sitaki matani na wewe!”
Marshall akacheka mpaka macho yakawa mekundu, Jack akanyanyuka akitishia kwenda, basi akamtuliza na wakaendelea na maongezi yao.
“Hakutakuwa na haja ya kumuua yeyote Jack, labda kama kutakuwa na ulazima huo!” akasema Marshall.
“Ulazima gani?” Jack akauliza akitoa macho. “Umeona namna yale mauaji ya mwanasheria yalivyopamba moto nchi nzima?”
Marshall akaminya lips zake na kusema, “Jack, kuna sadaka inabidi itolewe. Ni kawaida. Siko tayari kurudi nilipotokea, na basi ikitokea basi niwe nimeshamaliza kabisa kazi yangu.”
Akakunja ngumi na kuendeleza maneno, “Sitakubali yoyote yule asimame mbele ya njia yangu, Jack.”
Kumbe mwanaume yule mwenye barakoa nyeusi alikuwa ni Marshall! Ni yeye ndiye aliyemmaliza bwana Marble baada ya kubaini ni msaliti na mtu asiyeaminika tena tangu amnase kwenye mtego wa kufanya vivyo.
Bwana yule hakuwa wa kuaminika tena, kadiri avutavyo pumzi ndivyo mkakati wa Marshall ulivyohatarini.
Kwa kufanya utaalamu wa udukuzi, Jack Pyong alizama ndani ya uwanja wa barua pepe wa bwana Marble kwa kutumia kirusi. Alipokuwa huko akafanya namna na kupata mawasiliano yote ambayo Bwana Marble alikuwa akiyafanya, na siku ya miadi yake akaenda kukutana na mwanaume mwenye barakoa.
Kabla ya bwana Marble kuuawa, Marshall akapata ‘access’ ya pesa zake kwa kupitia ‘check’ na sasa walikuwa na pesa za kutosha kwani bwana Marble alikuwa tayari ameshaingiziwa pesa ya makubaliano yake ya pili.
Sasa vipi kuhusu yule bwana anonymous? Yule ambaye alikuwa akiwasiliana na bwana Marble apate kujua nani aliyemuagiza kukabiliana na kesi ya Marshall?
“Leo nitenda kukutana naye?” akasema Marshall.
“Lakini inabidi uwe makini sana Tony,” akashauri Jack. “Bila shaka yeye atakuwa tofauti na bwana Marble.”
“Najua hilo,” akasema Marshall kisha akakuna kidevu chake. “Hakuna mwanaume yeyote atakayekaa mbele yangu, labda awe amevaa chupi ya kike.”
Jack akamtazama kwa kukunja sura.
**
Saa tano asubuhi - Makao makuu ya FBI (J. Edgar Hoover)
Alikuwa ameshamalizana na kazi yake ya kwanza na pili, sasa alikuwa anamalizia kiporo chake cha kazi yake ya tatu.
Miss Danielle alikuwa ametulia sana mbele ya tarakilishi yake.macho yake ya kazi yalikuwa matulivu lakini vidole vyake vikiwa vinachapa kazi, alikuwa aki - ‘scan’, akitoa ‘copy’ na pia akiandika maelezo kuhusu kesi mbalimbali.
Akiwa anaendelea na kazi yake, mara simu yake ya mezani ikaita, alipopokea alikuwa ni mwana wa mapokezi, akaambiwa kuna mgeni anamhitaji.
“Mruhusu,” akatoa maagizo na kisha akaweka simu yake pembeni akiendelea na kazi. Kidogo ofisini mwake akaingia mwanaume mwenye mwili mpana ndani ya nguo nadhifu, koti amelining’iniza mabegani, mkononi mwake amebeba mkoba.
Alikuwa ni mpepelezi, bwana James Peak. Alimpatia Miss Danielle mkono wa salamu kisha akajitambulisha.
“Naweza kukusaidia?” akauliza Miss Danielle.
“Swadakta,” akaitikia bwana James akitua koti lake.
**
Alikuwa amekuja hapo kwa ajili ya kesi ya Mwanaume mwenye barakoa. Kwa mujibu wa tafiti zake aliona kuna haja ya kuonana na mwanamke huyu ili apate kujua tokea kwenye mzizi, kesi ya mwisho kabisa ya bwana Marble ilikuwa ni ile ya Marshall akiwa gerezani, na Marshall alikuwa mwenza na Miss Danielle kwenye kesi ya kupotea kwa Raisi, kwahiyo aliamini Miss Danielle angekuwa na kitu cha kumweleza.
Alimuuliza kama anamjua bwana Marble, alishawahi kufanya naye mawasiliano yoyote, kwa hilo Miss Danielle akalipinga kuwa hamfahamu bwana Marble kwa namna yoyote ile.
“Afisa, kama umekuja hapa kwasababu ya hilo basi jua sina chochote cha kukusaidia,” alisema Miss Danielle akimtazama Bwana James Peak.
“Na vipi waweza kuniambia kidogo kumhusu bwana Marshall?” Bwana James akauliza. Miss Danielle akamtazama kwa kitambo kidogo kisha akatikisa kichwa chake, “Siwezi kukwambia kitu, ni mambo confidential, samahani kwa hilo.”
Bwana James akatabasamu kinafki kisha akafungua faili lake na kuperuzi kwa muda kidogo kabla hajauliza, “Miss, kuna picha zako hapa …” akasema akiziweka picha tatu mezani, “zinakuonyesha ukiingia ndani ya jengo alimokuwa anafanyia kazi wakili Marble,” akaweka kituo akimtazama Miss Danielle alafu akamuuliza, “Vipi waweza sema kitu hapo?”
Miss Danielle akashusha pumzi. “Bwana mpelelezi, hatuwezi kwenda maeneo kutembea hivi sasa? Mfano, leo nikatoka na kwenda dukani kununua bidhaa, kesho yake muuza duka akafa, mimi nitakuwa ni mmoja wa watuhumiwa? Sababu tu nilienda hapo?”
“Inategemea uliendaje?” akasema bwana James na kuongezea, “Hata muuaji anaweza akawa ameenda hapo kama mteja.” baada ya hiyo kauli kukawa na ukimya kidogo kabla ya Bwana James Peak kuuvunja kwa kusema, “Mauaji yametokea mara mbili yakiwa yamefanywa na mtu mmoja, mmoja aliyeuawa ni wakili Marble na mwingine ni mtu ambaye alikuwa anawasiliana naye kwa njia ya barua pepe. Kama unaweza kutupatia jambo, basi utanitafuta.”
Bwana James aliposema vivyo akanyanyuka na kujiveka koti lake mabegani kisha akasema, “Natumai msaada toka kwako, miss.”
Danielle hakusema jambo, akamtazama bwana huyo akitoka nje ya ofisi yake alafu akajilaza kwenye kiti akishusha pumzi ndefu. Aliona mambo yanamfikia kooni.
Zile picha za cctv ingali akiwa kwenye ofisi ya bwana Marble ni hakika zitamuweka matatani. Aliwaza akihisi mwili unapata joto zaidi.
Akanyanyua simu yake ya mezani na kuiweka sikioni, akakumbuka ni simu ya ofisi, upesi akairejesha simu kwenye kitako chake alafu akatafuta simu yake binafsi na kupiga.
Simu ikaita na punde ikapokelewa.
“Inabidi tukutane … leo usiku, sawa?” alisema vivyo kisha asiongeze kitu akakata. Kabla hajaiweka simu yake mezani, aliing’ata kwanza akiwaza alafu punde akasimama na kwenda nje ya ofisi.
Alikuwa amefuata maji ya baridi.
**
Saa nane mchana …
Bwana James Peak alikuwa kwenye kiti chake ndani ya ofisi akiwa anayasoma kwa umakini yale maelezo aliyopewa na yule mwanamke mzee kule mtaani, Bibi Laurene, juu ya mwonekano wa mwanaume aliyempa agizo la kuwekea oda chumba ndani ya hoteli ya La Chica, chumba namba 348.
Aliyasoma maelezo hayo na kisha akahamishia macho yake kwenye video zilizokamatwa na kamera zilizotundikwa maeneo ya mapokezi ya hoteli. Alichambua kila mtu na kwa mujibu wa macho yake akawatambua wanaume kama wanne ambao walikuwa wanafanania kabisa na maelezo ambayo yalitolewa na bibi Laurene.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Basi akamwita mmoja wa wasaidizi wake na kumwagiza atoe picha za watu wale wanne kisha ampatie, ndani ya muda mfupi picha zikawa tayari akakabidhiwa.
Alizitazama picha hizo lakini hazikuwa zinaonekana vema, haswa za watu wawili ambao nyuso zao zilikuwa kinyume na jicho la kamera, katika hao wanaume wawili, mmoja alikuwa akitazama chini kabisa. Kwa namna moja, bwana James akahisi anaweza akwa mtu anayemtafuta.
Akashusha pumzi ndefu.
Akaziweka picha zile kando alafu akaita wasaidizi wake wawili na kuwapa maagizo juu ya Miss Danielle.
**
Saa tatu usiku …
“Unahisi anaweza akapata ushahidi kamili?” akauliza Marshall akimtazama Miss Danielle. Walikuwa wameketi ndani ya gari, kimya, limezimwa. Danielle alikuwa ameketi kwa kukunja mguu wake wa kushoto akitazama mbele, alikuwa amemezwa na fikira.
“Sijajua atapata nini,” akasema mwanamke huyo. “Ila ni wazi atakuwa ni mtu wa kumtazama kwa ukaribu sana, anaweza akawa hatari sana Marshall.”
Marshall akatulia akiwazua, “Kwa sasa atakuwa anakushuku lakini hana kithibitisho cha kukutia hatiani,” akasema na kuongeza, “Kinachotupasa kufanya ni kuhakikisha hapati anachokitafuta.”
“Na tutalifanyaje hilo?” akauliza Miss Danielle, sasa akimtazama Marshall.
“Itabidi tupunguze mawasiliano,” akasema Marshall, “najua kwasasa atakuwa anatafuta link kati yako na mimi. Kwa namna yoyote, tuliepushe hilo mpaka pale mambo yatakapotulia.”
Miss Danielle akatulia akiwazua.
“Na tutakapoona anakuwa hatari zaidi, basi naye nitammaliza,” akapendekeza Marshall, hapo Miss Danielle akamtazama kwa mshangao, “Marshall, you are not serious! Tutaua wangapi?”
“Yoyote atakayekaa mbele yetu!” akasema Marshall akikaza macho.
“Hapana, kumuua kutafanya jambo hili lizidi kuwa zito haswa kwangu!”
“Sasa tutafanyaje tutakapoona maji yanazidi unga?”
Miss Danielle akawaza kidogo kisha akasema, “Inabidi tumpumbaze!”
Marshall akatoa macho. Danielle akatikisa kichwa chake kukazia, “Ndio, inabidi tumpumbaze!”
**
Usiku wa saa tano …
“Hamna haja ya kutumia tena njia hiyo!” alisema Jack. “Tumeshawamaliza sasa wawili, nini umepata?”
“Tumekuwa salama zaidi,” akajibu Marshall. “Sikia, Jack, kama bwana Marble angeendelea kuwa hai, hamna ambaye angekuwa salama baina yetu.”
“Na vipi kumhusu anonymous?” Jack akauliza akikodoa.
“Yeye alikuwa anataka kuniua,” Marshall akajitetea, “Nilifanya vivyo kwajili ya usalama wangu na si vinginevyo!”
Jack akashika tama, mara akalitoa na kutikisa kichwa, “Inabidi utafute njia mbadala, Marshall.” kisha akasimama na kumuaga Marshall yeye anaenda kulala, basi Marshall akabaki mwenyewe.
Akakaa hapo kwa kama masaa matatu kabla hajaenda chumbani kwake ambapo alikaa tena kwa masaa kadhaa kabla hajaanza kutekwa na usingizi.
Akiwa anafumbafumba macho, akasikia sauti ya mlango ukifunguliwa taratibu, upesi akaamka na kuangaza. Alisimamisha masikio yake kama mbweha akijitahidi kusikia kila kitu.
Akaendelea kusikia sauti ya mlango ikizidi kulia na mara ikakoma, alipokaa kidogo akasikia vishindo vya mtu dirishani, upesi akafanya kujihami kwa kujitupia chini.
Alirusha macho yake dirishani lakini hakuona kivuli cha mtu, na vishindo taratibu vikapotelea mbali.
Basi taratibu akanyanyuka na kujongea dirisha, alafu akashika ncha ya pazia na kulifungua taratibu atazame nje kunani.
Aliporusha macho yake akabaini kile kitu alichokiona siku zile, alikuwa ni Vio pembezoni mwa bwawa la kuogelea akiongea na simu!
Kwa umakini akamtazama mwanamke huyo na huku akijaribu kuskiza kama ataambulia kitu. Kwanini huwa anaenda kuongelea kando huko na tena kwenye majira kama yale ya usiku? Alishindwa kupata majibu.
Alijaribu kuwaza akiwa anamtazama mwanamke huyo na huku akiwa anaangalia muda ambao anatumia, ilikuwa yaelekea nusu saa sasa tangu amwone akiwa anateta!
Vio alitabasamu na kusema kwa sauti ndogo, “Nitatazama lakini si upesi hivyo, D.” ingali akiwa anaongea alikuwa akijibaraguza kwa kusimamisha mabega na kuzungusha zungusha mwili wake. “Wajua mambo yalivyo, sio? … “ aliendelea kuteta, akaskiza kidogo alafu akatabasamu na kusema, “Sawa!”
Lakini alihisi kuna kitu dirishani mwa chumba cha Marshall, alihisi pazia halipo sawa, alipotuma macho yake kutazama, haraka pazia likajirudi asione jambo.
“Kwaheri, D, yanipasa nirudi ndani,” akaaga na kisha akakata simu yake. Kabla ya kurudi ndani akatazama tena dirisha la chumba cha Marshall, hakuona jambo lakini moyo wake haukuwa shwari. Upesi akarudi na kujilaza.
**
Majira ya asubuhi, South Carolina …
Ngo! Ngo! Ngo! Ngo!
“Nakuja!” alipaza sauti mwanamke mwenye nywele nyekundu, makamo ya miaka thelathini na tano. Akiwa amevalia sweta lake kubwa, alikuwa jikoni akitengeneza chai, kwa mwili alikuwa mpana ila mkakamavu.
Punde tu baada ya kuepua chai yake, akasonga mlangoni kuitikia wito. Alipofungua akakutana na mwanaume mpana aliyevalia koti lenye kofia kuficha uso wake, kidogo akahofu.
“Naweza kukusaidia?” akauliza akiwa ameweka mkono wake karibu kabisa na mlango kwa lolote litakalotokea. Mwanaume yule akaonyesha sura yake na kusema, “Ndio, tafadhali tunaweza kwenda kuongelea ndani?” alikuwa ni Marshall.
Kidogo mwanamke yule akasita, hakumwamini mgeni wake basi akauliza, “Waweza kusema hitaji lako hapa?”
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Marshall akatazama kushoto na kulia kwake alafu akasema kwamba amekuja hapo kwasababu ya Katie, mwanamke huyo alimweleza kuwa yupo hapo kwa shangazi yake. Kidogo mwanamke huyo akamtazama Marshall na kisha akaufungua mlango waingie ndani.
Akampatia Marshall kikombe cha chai na wakaketi sebuleni kwa ajili ya maongezi. Mwanamke huyo akajitambulisha kwa jina la Sarah, dada wa mbali wa mama yake Katie.
“Alikuwapo hapa kwa muda kidgo lakini kwa sasa ameondoka. Hakuwa anajihisi kama yupo salama,” alisema Sarah baada ya kunywa fundo moja la chai kuondoa baridi mwilini.
“Vipi hamna namna naweza kumpata?” akauliza Marshall, “Ni muda mrefu sasa sijaonana naye.”
Sarah akabinua mdomo, “Sidhani kama itakuwa rahisi hivyo maana amerudi Ujerumani na ni mara chache sana amekuwa akinitafuta. Anadai hayupo salama, sijajua kama unafahamu kuhusu hilo.”
Marshall akatikisa kichwa kuitikia, akatazama chini akijiuliza kwa ufupi alafu akauliza kwa sauti ya upole, “Anaendeleaje na hali? Yuko salama?”
Sarah akanywa kwanza fundo moja la chai kisha akasema, “Yu salama salmini. Alikuwa na matatizo kadhaa mwanzoni lakini mpaka anaondoka, alikuwa ameshajijenga kiafya.”
Basi Marshall akawa ameshindwa kutimiza hitaji lake la kumwona Katie. Alisononeka moyoni. Alikuwa amefunga safari yake ndefu isiyokuwa na mafanikio. Akampatia Sarah namba zake za simu kwa mawasiliano endapo kama Katie atahitaji kumtafuta kisha akashukuru na kwenda zake.
Sarah akamsindikiza mwanaume huyo mpaka nje kisha wakaagana. Alipohakikisha mwanaume huyo amepotelea ndipo akazama ndani na kuketi. Punde, Katie akaungana naye akitokea chumbani.
“Ndiye yeye?” Sarah akauliza akimtazama Katie, mwanamke huyo bado alikuwa amejiveka nguo za kulalia, uso wake ukiwa mchovu, akaketi kwenye kiti akitikisa kichwa kuafiki pasipo kusema jambo.
“Sitaki awe anafika hapa, Katie!” akapaza Sarah, “Unajua ni hatari kiasi gani kuonana na mtu kama yule, Katie?”
Katie hakujibu kitu, alikuwa anajikuna mkono wake wa kuume akitazama chini na macho yake yalojawa na ulevi wa usingizi, bila shaka alikawia kulala.
“Anatafutwa nchi zima. Endapo ikibainika alikuja hapa, nitakamatwa na hutaniona tena. Ndiyo furaha yako?”
Shangazi akaongea sana lakini Katie asirudishe neno. Alikuwa ameghafirika hata kwanini Katie alimpa anwani ya makazi yake. Akamsihi sana, kwa usalama wake, na wa mtoto wake tumboni, akae mbali na Marshall.
“Kama usipofanya hivyo, basi nitatoa taarifa polisi Katie!” Shangazi akahitimisha kisha akamezea na chai yake. Katie akasimama na kwenda zake chumbani.
“Umenisikia, Katie!” shangazi akapaza sauti Katie akifunga mlango, bado Katie hakujibu.
Alijitupia kwenye kitanda chake akitiririsha machozi. Hakutaka kabisa kuishi maisha kama yale. Alishika tumbo lake akazidi kububujikwa.
**
Baada ya juma moja …
“Jack,” Vio aliita baada ya kutoka bafuni, alikuwa akijifuta maji kwa taulo huku akiwa anamtazama Jack ambaye alikuwa amejilaza kitandani, Jack akamuitikia kwa kumtazama.
“Vipi kuhusu kile kitu nilichokuambia?” Vio akauliza.
“Kitu gani hiko?”
“Kumhusu Tony!” Vio akasema kwa mkazo.
“Tony? Amefanyaje?” Jack akauliza kana kwamba ni mada mpya masikioni, Vio akasonga karibu yake na kuketi kitandani. Akamwambia hataki kumwona Tony pale nyumbani kwani ameshakaa kwa muda wa kutosha, si salama kwake kuendelea kukaa pale.
“Hauoni ni stara sasa akatafuta makazi mengine mbali na hapa?”
“Kwanini afanye hivyo na mimi nipo?” Jack akauliza na kisha akasisitiza kwamba hawezi kumfukuza Marshall kwa namna yoyote ile, labda tu kama atahitaji kwenda mwenyewe. Swala hilo likamkasirisha Vio.
“Ina maana Tony ni wa muhimu sana kwako, sio?”
Jack akamtazama mwanamke huyo kwa mazingatia alafu akamuuliza, “Kwanini unataka aondoke?”
“Si nimeshakuambia? Hatupo salama hapa akiwapo!”
“Tangu lini?”
“Tangu alipokuja.”
“Kwanini hukuniambia muda wote huo?”
“Kwasababu sikujua kama atakaa kwa muda mrefu.”
“Sikukuambia hilo?”
Baada ya kuzozana kwa muda mfupi, Jack akatoka chumbani na kwenda kuketi sebuleni, muda mfupi Marshall akaungana naye papo, wakajuliana hali na baada ya hapo, Jack akamuuliza Marshall juu ya mpango wake ujao.
Ni jana yake tu walikuwa tayari wameshatoka kubaini kwamba namba ya simu ya Marshall ilikuwa hewani, lakini pia walishawasiliana na taasisi ya kusaidia watoto wasiojiweza ambayo ipo chini ya mke wa Raisi, wakiwa wanataka kuonana na uongozi kwani wanataka kutoa msaada mkubwa.
Kati ya pande hizo mbili Marshall hakuwa anajua aanze na kipi, hata kichwa chake hakikuwa vema tangu alipofanya jitihada za kumtafuta Katie.
Aliomba muda apumzike na kuwaza, katikati ya siku hiyo, akastaajabu akipigiwa simu na alipotazama ilikuwa ni namba mpya, akawaza kidogo kabla ya kupokea na kusikia sauti ya kike.
“Ni Katie,” sauti ikasema na kuuliza, “Naongea na Marshall?”
“Ndio!” Marshall akapokea kwa tabasamu, “Upo wapi Katie?”
“Nipo mahali fulani, twaweza kuonana?” Katie akauliza.
**
Haikuwa na chaguzi kwa Marshall bali kwenda huko upesi, alikuwa anataka kuonana na Katie kwa hamu zote, kwake ilikuwa ni nafasi adhimu kabisa.
Basi upesi akajiandaa na kutoka akitumia usafiri wa Jack, baada ya masaa mawili akawa yu pamoja na Katie eneo fulani tulivu, hapo wakateta mambo mengi ikiwamo mahusiano yao lakini pia na yanayoendelea.
Katie alimwambia Marshall kuwa alishakata tamaa ya kuonana naye lakini bado hakuwa ametoka kichwani mwake, zaidi akamweleza Marshall juu ya shangazi yake, bibie Sarah, kuwa sio mtu anayeyafurahia mahusiano yao kabisa! Hata pale ametoroka nyumbani pasipo kumuaga.
“Najua asingeniruhusu ama angelinitilia mashaka, sikutaka iwe vivyo.” aliposema hayo akamtazama Marshall na kutabasamu, kisha akamkumbatia kwanguvu. “Nakupenda sana, Marshall.”
Naye Marshall akamkumbatia kwanguvu na kumweleza hisia zake. Hakuna mtu aliyekuwa anataka kumwacha mwenzake aende, walitamani maisha yao yangekomea pale lakini haikuwa inawezekana. Muda mwingine ni bora ukaishi ndotoni kwani maisha halisi yanakuwa katili mno.
Wakatumia masaa mengi pamoja, jua lilipoanza kuzama ndipo ikampasa Katie amuage Marshall kwa busu na kisha akampatia picha yake, “Utaitunza hii, na utaitazama punde utakaponikumbuka.”
Basi Marshall akaiweka picha hiyo sehemu ya faragha, alafu naye akatia mkono wake mfukoni na kutoa mkufu ambao alimveka Katie na kupendezwa nao sana.
“Nimeununua mkufu huu nikiwa njiani. Niliona utakupendeza sana,” alisema Marshall kwa tabasamu alafu akambusu Katie na kukumbatiana kabla hawajaachana kila mtu aende na zake.
Akiwa njiani Marshall akajawa na furaha sana, alihisi moyo wake umekuwa mwepesi kwa kumwona Katie - mpenzi wa moyo wake. Alitamani afike upesi nyumbani ili apate kumhadithia Jack.
Lakini akiwa anaendesha akakumbuka jambo, alipaswa kumsihi Katie awe makini zaidi kwa usalama wake, akajaribu kuvuta simu yake apige lakini akabaini haikuwa na salio, basi akaona awe mvumilivu afike dukani na kuongeza ili apate kuwasiliana na mwanamke huyo.
**
“Umetoka wapi?” aliuliza Sarah akimtazama Katie, mwanake huyo alikuwa ameketi kwenye kiti chake akishona kitambaa. Macho yake yalikuwa yanamtazama Katie nje ya miwani.
Katie akatabasamu kinafki na kujibu, “Nimetoka kutembea,” kisha akashika mwendo kuelekea chumbani. Sarah akamwita na kumtaka asogee karibu, aliongea kwa ukali na kwa msisitizo, basi Katie akatii, akasonga na kuketi karibu.
“Nasikia marashi yake,” akasema Sarah akiwa anamtazama Katie kwa ukali.
“Marashi ya nani?” Katie akauliza akitoa macho. Sarah akafuma kitambaa chake mara mbili alafu akauliza, “Ulienda kukutana naye, sio?”
“Sijui unaongelea nini shangazi!” Katie akajitetea akipandisha mabega. Sarah akamwambia asimfanye mtoto kwani anajua ametoka kuonana na mwanaume wake ingali alimkataza. Marashi anayoyasikia, alipata kuyasikia Marshall alipokuja kipindi kile kumtembelea, juma moja lililopita.
Pasipo kujali Sarah aliteta nini, Katie akaendelea kukana na kukana mpaka pale simu yake ilipoita, alipotazama akaona namba mpya lakini akiwa ameibaini ni ya Marshall. Alihofia kuipokea, alimtazama shangazi yake na shangazi yake akamtazama, kulikuwa na ukimya kidogo simu ndiyo ikinguruma tu.
“Mbona hupokei?” Sarah akauliza, badala ya kujibu Katie akasimama aende zake.
“Katie!” shangazi akaita, sasa alikuwa akimtazama Katie kishetani. “Nimesema rudi hapa!” akafoka akionyeshea kidole chake kitini, Katie akapuuza na kwenda zake chumbani, akajifungia na kupokea simu.
Sarah akatabasamu akiwa anasaga meno yake. Kwa hasira akachana kitambaa alichokuwa anakifuma na kisha akakitupia mbali.
Si kwamba alikuwa anafuma kitambaa hicho kwa matumizi, lah! Sarah huwa na desturi ya kufuma pale anapokuwa na hasira, ni moja ya njia zake za kujipooza kurudi kwenye hali ya kawaida kama iwavyo kwa watu wengine ambao hunywa maji wakiwa wamepandwa na munkari.
Kabla ya Sarah kubaini njia hii ya kutuliza hasira zake, alikuwa akifanya mambo ya ajabu apandwapo na hasira, mambo ambayo hayasimuliki, au hata kama tukiyasimulia hayatapendeza masikioni.
Kwasababu ya hasira aliharibu maisha yake kwa kumpoteza mumewe kwa talaka na hata wanawe wawili kuamriwa na mahaka wakae mbali na yeye.
**
Baada ya siku mbili …
“Unadhani itachukua muda gani mpaka kukamilika?” aliuliza mwanaume mpana aliyevalia suti moja nadhifu sana, mwanaume huyo alikuwa amevalia miwani ya kuzuia miale ya jua na mdomo wake mdogo ulikuwa umefunikwa na masharubu.
Mbele yake alikuwa ameketi mwanamke nadhifu pia, suti rangi ya waridi na skafu shingoni, mwanamke huyo alikuwa maarufu nchi nzima kwa jina akiitwa Marietta Abbey, mke wa Raisi aliyepotea ama twaweza sema mstaafu maana kwa sasa kuna Raisi mwingine madarakani.
Mwanamke huyo hakuwa mnyimi wa tabasamu na kwa muda wote huo ambao alikuwa akiongea na mgeni wake alikuwa akitabasamu na kuskiza kwa umakini. Maongezi yao yalichukua kama lisaa limoja kabla ya kupeana mkono na kisha mgeni wake akaondoka.
Mgeni huyo alipofika kwenye gari lake, limousine nyeusi, akafunguliwa mlango na kijakazi wake na yeye akaza ndani viti vya nyuma gari likaondoka.
Punde gari lilipong’oa nanga, mgeni huyo akavua miwani yake na masharubu aliyoyabanika, kumbe alikuwa ni Jack Pyong! Alimpigia simu Marshall na kumwambia kila kitu kimeenda kama kilivyopangwa, muda si mrefu watakuwa pamoja kuteta.
Basi Jack akarudisha gari lile alilokodi mahali pake kisha akajipakia kwenye gari lake apate kuondoka, lakini kabla hajafanya vivyo akastaajabu vioo vya gari lake vyagongwa, alipotazama akawaona wanaume wawili waliosimama wakiwa wamevalia suti, akahofu.
Kwa usiri akazamisha mkono wake pembezoni mwa kiti chake na kushika bunduki kisha akashusha kioo na kuuliza ni nini anaweza wasaidia wanaume wale. Pasipo kunena, wanaume wale wawili wakatoa vitambulisho vyao na kumwonyesha, walikuwa ni maajenti wa FBI, na walikuwa wanamhitaji Jack kwa ajili ya maongezi.
“Haitachukua muda,” alisema mmoja, mwingine akaongezea, “Kama hautakuwa mjinga.”
Jack akafikiri kidogo kisha akauliza, “tunaenda kufanyia maongezi hayo wapi? Kwanini si hapa?”
“Ndani ya usafiri wetu itapendeza zaidi,” akasema mmoja wa wale wageni lakini Jack akasita kuafiki hilo, “Kwanini tukafanyie huko? Kwani kuna kitu chochote mnaficha?”
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Wanaume wale wakatazamana na kuafiki kuongelea pale. Wakamuuliza Jack kumhusu Marshall maana ilikuwa inafahamika alikuwa ni mmoja wa watu wa karibu hivyo walikuwa wanaamini Jack atakuwa anafahamu mahali Marshall alipo.
Jack akakana kufahamu, akaapa mara yake ya mwisho kuonana na Marshall ilikuwa ni pale alipomtembelea gerezani na si vinginevyo.
Wanaume wale wakatazama kwa amcho ya taarifa, alafu mmoja wao akauliza, “Na vipi kumhusu Miss Danielle? Mara yako ya mwisho kuwasiliana naye ni lini?”
Jack akaguna, “Ni muda mrefu kidogo, sikumbuki haswa ni lini!”
Mara akaona mwanaume akizamisha mkono wake ndani ya koti, haraka akatoa bunduki yake apate kujihami lakini kabla hajafanya kitu, mwanaume mwingine akawa ameshamdaka mkowe na kumpoka silaha hiyo.
“Tulia vivyo hivyo ndugu, kwa faida ya pumzi yako!”
**
Jack akaogopa sana, hata akadhani huenda huo ukawa mwisho wa maisha yake. Wanaume wale wakamtwaa na kumweka kwenye gari lao kisha safari ikaanza kuelekea asipopajua. Mwanaume mmoja alikuwa dereva ingali mwingine akiwa ameketi na Jack huko nyuma.
Wakiwa wameendesha kwa muda wa kama robo saa, Jack akahisi kitu. Aligeuza shingo yake kutazama nyuma na kwa mbali akaona gari fulani alilolitambua, hapo akatabasamu, alibaini Marshall yupo nyuma yao.
Basi akasafisha koo lake na kuanza kuwaambia wale wanaume wawili juu ya hatari wanayoweza kukumbana nayo kwa kumkamata na kumpeleka mahali pasipo ridhaa yake. Kwa sauti kubwa kabisa akaeleza namna gani ambavyo hajapenhda lile tukio na atachukua hatua kuwaadhibu.
“Kama mnajali uhai wa maisha yenu basi mniachie sasa!” alimalizia kwa kusema hayo akiwa ametumbua macho, basi wale wanaume wawili waliomteka wakaangua kicheko haswa, walimwona Jack ni mtu wa masikhara haswa, mtu ambaye hajagundua yupo kwenye janga gani mpaka muda ule.
Lakini kwa kutokutambua, ni wao ndio walikuwa kwenyge janga, tena janga kubwa haswa. Punde gari lao likabamizwa kwa nyuma! Tih! Hawajakaa sawa, gari likabamizwa pembeni na kuanza kupoteza mhimili wake!
Kutazama wakaona gari aina ya Nissan Patrol rangi nyekundu pembeni yao. Vioo vikashushwa alafu silaha zikaanza kumwagwa kama njugu kumfuata dereva, hakika hakusalimika, ndani ya punde kioo chake kilipasuka na akala risasi kama tatu hivi kwa uchache! Gari likaanza kuyumba kwa kukosa nahodha.
Huko nyuma Jack naye akatumia nafasi hiyo hiyo kujinasua, ingali mwanaume aliyemuweka chini ya ulinzi akiwa anapambana kutupa risasi kwenye gari Nissan, akatumia fursa hiyo kumbamiza kichwa kwanguvu na kumziraisha, hata yeye hakuamini kama hilo limetokea!
Gari liliendelea kuyumbayumb kana kwamba boti ndogo inayokubwa na dhoruba. Ilibamiza pembeni na pembeni, ilijikwatua na kujichetua kihatari! Ikakwangua magari mengine barabarani na ata kuyasukuma, magari mengine yalipisha njia huku madereva wakirusha maneno makali.
Basi upesi Jack akajikongoja na kushika usukani, alafu akalituliza gari hilo na kupotelea huko.
**
Jioni ya saa kumi na moja, (CHARITY HOME)
“Madam, kuna mgeni anataka kuonana na wewe!” ilikuwa ni sauti ya secretary akiongea na Marietta Abby kwa kupitia simu ya mezani.
“Mgeni muda huu?” Marietta akastaajabu. “Ni nani huyo?”
“Bwana Dickson,” secretary akajibu upesi na punde Marietta aliposikia jina hilo akashtuka kidogo kabla hajamruhusu mgeni wake azame ndani. Kidogo mlango wake ukafunguliwa na akaingia mwanaume aliyekuwa amevalia shati nyeupe na tai nyeusi iliyokomea juu ya kichwa cha mkanda, mwanaume huyo alikuwa amelaza nywele zake vema na mkono wake wa kuume alikuwa ameuzamisha mfukoni.
Alikuwa ni bwana Ian Livermore, afisa wa zamani wa shirika linalohusika na kulinda viongozi wa juu na familia zao, yaani USSS (Secret Service). bwana huyu ndiye ambaye inasemekana na kuaminika alifia kwenye ajali ya moto iliyoteketeza nyumba yake mpaka kuwa majivu.
Alikuwa na majina mengi, alipokuwapo Ujerumani alikuwa akijulikana kwa jina la PKP, na sasa yupo nchini Marekani akitajwa kama Dickson! Ila jina lake lililopo kwenye vyeti ni bwana Ian Livermore.
Kuna umuhimu wa kushika jina hili vema.
Marietta akasimama na kusalimiana na bwana huyo kwa kumpatia mkono kisha wakaketi.
“Ni muda mrefu sasa!” akasema Marietta. Bwana Ian akatikisa kichwa chake na kusema, “Ni muda mrefu kweli. Natumai unaendelea vizuri.”
“Bila shaka,” Marietta akajikomba na kuongezea, “naona ulinitupa kabisa Ian. Kuna kitu nilikukosea?”
Wakateta kwa muda mchache kabla ya Ian kusema jambo lililomleta hapo. Mbali na kwamba alimkumbuka sana Marietta, kuna jambo lingine kubwa.
“Nadhani umesikia kuhusu Marshall,” alisema Ian, Marietta akatikisa kichwa kuafiki. “Nimelisikia, Ian na limenishangaza haswa kwani nilijua mmeshamalizana naye!”
Ian akatikisa kichwa, akamwambia Marietta kwamba alitaka kufanya mikono yake iwe safi kwa kuiachiha serikali immalize kwa kauli yake lakini mambo yamekuwa tofauti, anajutia sana kutoitumia fursa.
“Hapana, Ian, ilibidi iwe vile!” Marietta akampa neno, “Kama tusingefangya vile, tungelimalizaje hili swala la kupotea kwa Raisi, huoni bado ingekuwa ni mjadala wa moto?”
Ian akatulia kidogo, akashusha pumzi yake na kumwomba Marietta kipande cha sigara, alikuwa anafahamu mwanamke huyo ni mvutaji hivyo hawezi kukosa burudani hiyho karibu na mazingira yake.
Marietta akavuta droo na kutoa pakti la Chesterfield, akamrushia Ian.
“Nashukuru!”
Ian akatoa kiwashia moto mfukoni alafu akaziwasha sigara mbili kwa mkupuo na kuziweka mdomoni, akavuta na kuvuta pafu moja zito kabla hajatemea moshi nje. Alikuwa anafikiria jambo, vidoleni, mkono wake wa kuume, akiwa amekamatia sigara mbili.
“Marietta, Marshall ni mtu wa hatari sana. Ni kheri swala hili la Raisi lingeendelea kuwa la moto lakini mwanaume yule akiwa mfu.” akavuta tena pafu zito na kulitemea mbele ya uso wake, akawa haonekani bali sauti yasikika, “alikuwa mikononi mwetu kwa bahati, sasa ametoka, itakuwa ngumu sana kumrejesha … kutakuwa na gharama yake!”
Marietta akamtoa hofu Ian kwamba mbali na wao kumtafuta pia vyombo vyote vya serikali vinamtafuta, hivyo kazi haitakuwa ngumu sana kama ilivyokuwa hapo mwanzoni, lakini pia katika hilo Ian akamweleza na wao kazi yao itakuwa ngumu maradufu maana inabidi pia wajifiche toka kwenye mikono ya vyombo vya usalama.
Mwanaume huyo alitikisa kichwa na kidogo akacheka, “Marietta, haupo serious hata kidogo, sijui kama unajua unachoongea. Kutakuwa na gharama, tena kubwa, kumtia tena Marshall mkononi!”
Baada ya kusema hayo, Ian akaeleza ni namna gani vijana wake wawili walivyokumbwa na kadhia wakiwa wenye mchakato wa kumfuatilia rafiki yake na Marshll, bwana Jack Pyong.
Kati ya hao, mmoja amekutwa darajani akiwa ameandikwa mwili mwake kwa kutumia ncha ya kisu na mwingine hajulikani alipo mpaka muda huo!
“Nadhani sasa unaweza kuelewa nini naongelea, Marietta,” alisema bwana Ian kisha akalaza mgongo wake kitini na kunyonya sigara kama ana akili nzuri.
“Sasa tunafanyaje Ian? Ina maana hauna mpango kabisa?”
“Siwezi nikakosa mpango,” akasema Ian uso wake ndani ya moshi. “Nina mpango mmoja kabambe, nadhani huo utakuwa ndio tegemea kubwa la sisi kummaliza Marshall … ni sehemu ya udhaifu wake. Tukishindwa kutumia nafasi hiyo basi we are fucked up!”
Kukawa kimya kidogo.
“Nakushauri urudi kwanza Uarabuni,” akasema Ian.
“Hapana,” Marietta akatikisa kichwa, “Si kwa muda huu, kuna kazi kwanza namalizia.”
“Kazi gani?” Ian akadadisi.
“Kuna pesa inatarajia kuingia muda si mrefu toka kwa ‘donor’, hivyo naingojea.”
“Donor?”
“Ndio, kuna mtu anataka kujitolea kusaidia watoto. Ni pesa kubwa kama tukimalizana.”
“Una uhakika?”
“Bila shaka, leo nilionana na mtumishi wake tukateta,” Marietta akadadavua na kuongeza, “muda si mrefu nitaonana na mhusika na kujadili zaidi. Nitakapokamilisha hilo, nitasafiri tena.”
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
***
Basi baada ya kuteta hayo, watu hawa wakaagana wakipeana miadi ya kuonana muda si mrefu. Marietta akafanya kazi zake kwa muda kidogo kabla hajatoka kazini kwenda kupumzika.
Pamoja na kwamba alikuwa ni mke wa Raisi aliyepita, bado ulinzi wake ulikuwapo kama kawaida. Wanaume wawili walikuwa wanamlinda kumhakikishia usalama. Wanaume hao walikuwa wamevalia suti na masikio yake yakiwa yamezibwa na namna za mawasiliano.
**
Saa tatu usiku …
Jack alifunga mlango na kumsukumia Marshall kando, Marshall alikuwa yu kifua wazi akitweta jasho, Jack yeye alikuwa na mavazi yake kama kawaida lakini mikononi akiwa amevalia glovu nyeupe. Glovu zake hizo zilikuwa na mabaki ya damu.
Hawakuwa wametoka ndani ya nyumba bali kwenye chumba cha nje ambacho kinatumika kama sehemu ya kuhifadhia vifaa kadhaa. Ndani ya chumba hicho ungeweza kuona mwanga hafifu kwa ndani.
Jack akarudishia mlango na kumwambia Marshall huku akiwa anamtazama kwa kumkodolea, “bwana, ukiendelea kufanya vivyo, utamuua!” sauti yake ilikuwa ya chini lakini yenye uzito.
“Jack,” Marshall akaita na kunena, “Unadhani hawa huwa ni wepesi kusema nani aliyewatuma? Wamefunza kuvumilia mateso!”
Jack akatikisa kichwa, “Sawa, lakini siyo hayo unayotoa wewe. Mara ya pili hii …” Jack akaonyeshea vidole vyake, “.. mara ya pili hii sasa anazirai, matokeo yake nini? Si kufa kabisa!”
“Kama akifa basi!” Marshall akatanua mikono yake mipana. “Sikia, Jack, kama yeye amedhamiria kufa, basi atakufa pasipo kusema hata tumfanyeje, cha kufanya ni kutumia tu yale yote tunayoyajua. Kama haitaleta bahati basi!”
Jack akaguna, “hamna namna nyingine? Yani njia mbadala wa hii?”
“Hamna!” Marshall akajibu akimtazama Jack kwa macho makavu. “Akizima ataamka tena na tena mpaka atakapotia adabu!” kisha aliposema hayo akamsogeza Jack kwa mkono wake wa kuume kisha akazama tena ndani.
Jack akabaki na maswali, alishika mlango aingie ndani lakini ah-ah! Akaona hataweza kuvumilia zaidi, yeye akaenda zake ndani, alipofika huko hakumkuta Vio chumbani. Hakujali sana akanyookea bafuni kukoga na punde akatoka akiwa anajifuta, alipotazama, bado Vio hakuwa ndani!
Akajifunga taulo kiunoni na kuanza kumsaka mwanamke huyo ndani ya jengo, alitazama jikoni, eneo la kulia chakula na mwishowe sebuleni, kote hakuona kitu! Akastaajabu mwanamke huyo atakuwa ameenda wapi?
Akajaribu kumpigia simu ikaita pasipo kupokelewa, basi akakata shauri kwa kungoja pale sebuleni mpaka atakaporejea. Kila alipoketi kwa muda fulani akawa ananyanyua simu yake na kupiga, bado haikuwa inapokelewa. Akaghafirika zaidi.
**
Ndani ya gari ..
Mulikuwa na giza. Ni mara moja moja mwanga ulikuwa ukiibuka pale ambapo simu ilikuwa inaita. Vio alitazama simu kisha akaipuuzia na kuendelea na mambo yake, alikuwa ameketi viti vya mbele kabisa na mwanaume kipara mwenye kujaliwa ndevu.
Mwanaume huyo alikuwa amevalia shati la kijivu ambalo limekatwa mikono, mwili wake ulikuwa mpana, mkono wake wa kuume umechorwa fuvu la binadamu likiwa lavuta sigara kisha maneno chini yake yakisomeka, ‘F*CK YOU!’.
Jina la mwanaume huyu ni Gotham.
Sauti yake ilikuwa nzito na ya chini, ingali wanaongea Vio alikuwa ameweka mkono kwenye paja nene la mwanaume huyo.
“Kwanini haukuacha simu hiyo ndani?” akauliza Gotham.
“Kama ningeacha basi angeifungua na kutazama,” akajibu Vio.
“Basi izime,” akashauri Gotham.
“Hapana, ataona nimemfanyia kusudi, acha iite nitajua cha kumwambia.”
“Sure?”
“Yah! Usijali, hana shida.”
Alichokifanya Vio ni kugeuzia kioo cha simu chini ili isiwasumbue kwa mwanga na kisha wakaendelea na maongezi yao, sasa kukiwa ni kiza totoro muda wote, ungeweza kutofautisha sauti tu kujua nani kaongea nini.
Wakateta kwa kama nusu saa zaidi alafu Vio akamuaga Gotham kwa busu.
“Kukiwa na tatizo, utanitaarifu!” Gotham akatupa kauli akimtazama mrembo akienda zake.
Kisha akameza mate.
**
Marshall akiwa amekaa sehemu ya kulia chakula, alipata kumwona Vio akiingia ndani. Bado Jack alikuwa ameketi pale sebuleni akiwa amefunga taulo lake, alikuwa amechoka, kabla ya Vio kuja alikuwa akisinziasinzia na kutazamatazama muda.
Kwa jicho la mbali Marshall akawa anatazama kinachoendelea, matundu ya masikio yake yalikuwa yamefunikwa na ‘earphone’ hivyo hakuwa anasikia lakini akibashiri nini kinachoendelea.
Jack alisimama akimfokea Vio huku akionyeshea simu, naye Vio akawa amekuja juu wakijibizana, hatimaye Vio akaachana na Jack baada ya kupungia mkono wake hewani, huyo akaelekea zake chumbani!
Marshall akaendelea kutazama, alikuwa akinywa maji kwenye glasi taratibu huku akiacha macho yafanye kazi yake. Akamwona Jack akiwa ameinamisha kichwa chake, mara anaegemea kiti akitazama dari.
Hakutaka kumsumbua, akaendelea kumtazama mpaka pale Jack aliponyanyuka na kwenda zake chumbani pasipo kuaga. Marshall akamalizia maji yake kwenye glasi kisha akayaweka mengine akitulia papo.
Alikuwa anawaza mambo kadhaa kichwani mwake.
Alikunywa maji taratibu kana kwamba juisi, alipomaliza akaenda zake bwawani kuogelea, huwa anafanya hivyo kama njia ya kujipa mazoezi kabla hajaenda kupumzika.
Alipojiweka kitandani akampigia simu Kate na wakaongea kwa muda fulani kabla hajakata na kubaki mpweke.
Alimuwazia rafiki yake Jack.
Alifikiria ni njia gani ya kumsaidia.
Lakini akiwa anafanya vivyo Marshall alijikuta akibaini kwamba kadiri siku zinavyoenda ndivyo utu humtoka. Amekuwa si mtu wa kujiuliza mara mbili kumuumiza ama kumuua mtu. Anaweza fanya vivyo na kisha asiwaze kabisa.
Hakujua roho hiyo ameitolea wapi.
**http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Sarah alisikia gari likikoma na baada ya muda mchache mlango wake ukagongwa mara mbili. Kabla hajasimama kwenda kuitikia wito huo akatabasamu kwanza na kisha akaweka uzi wake na sindano pembeni.
Akafungua mlango na kukutana na wanaume wawili waliovalia suti, wanaume hao walijitambulisha kama maafisa wa usalama kabla hawajazama ndani.
“Tumeitikia wito wako, bila shaka tupo mahali sahihi!”
“Kabisa, karibuni sana,” Sarah akawakarimu wageni wake na kuwauliza wangependelea kifungua kinywa kipi, chai ama kahawa.
“Hapana, tunashukuru,” akasema mmoja wa wale wanaume wawili kisha wakaenda moja kwa moja kwenye kilichowaleta, “Huyo mtu yuko wapi?”
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment