Search This Blog

Sunday 20 November 2022

NJIA NYEMBAMBA - 4

 





    Simulizi : Njia Nyembamba

    Sehemu Ya Nne (4)





    “Wauaji wakubwa! Nani kasema nyie ni wanamapinduzi? Mnaua watu wasio na hatia kwanini? … Hata Mungu hatosimama upande wenu. Nyie ni wadhalimu tu kama wafuasi wa Diarra!” Amadu alikuwa anafoka. Wanaume wale wanne walimpeleka mpaka ilipo chimbo wakamtupia humo. Chui alinyanyua miguu yake akasogelea chimbo kumtizama Amadu. Humo chimboni alikuwamo Amadu na mkuu wa mkoa wakati upande wa pili ukiwa umetenganishwa na miti alikuwepo Ulsher.

    “Nini umefanya, Amadu?” Chui aliuliza kwa sauti ya chini. Amadu akamtizama kwa macho yanayomimina machozi.

    “Ni bora nikakaa humu, Chui, kuliko kuwa sehemu ya wauaji wa watu wasio na makosa, kuliko kumwaga damu ya watu wanaoumia na kuteseka kama sisi. Sikujiunga MDR kuua watu masikini wasio na msaada bali kuwasaidia kwa kuwakomboa na kuwaweka katika mikono tunayodhani ni salama. Ya nini tumwage damu ya wanawake na watoto ingali si wao walioiingiza nchi machafukoni? Ni bora nikakaa humu nijue moja ya kwamba wakati wanafanya maovu yao, nilikuwa kifungoni.”

    Chui hakusema tena kitu. Alitoka akaelekea zake hemani akajilaza kitandani.

    Katikati ya usiku wa manane, Amadu alikuwa macho. Alikuwa kaegemea ukuta wa chimbo huku amekunja magoti ambayo juu yake alilaza kichwa chake. Mkuu wa mkoa alikuwa amelala na kukoroma kabisa: kitambi chake kilikuwa kinapanda na kushuka. Ghafla Amadu akiwa hapo alisikia sauti ya kike ikimuita. Aligundua ni sauti ya Ulsher. Aliamsha kichwa chake akaitika.

    “Wewe ni nani, Amadu? … Umetokea wapi?” Sauti ya Ulsher iliuliza.

    “Naitwa Amadu Laurent, nimetokea Freetown. Mtoto wa masikini aliyejitolea kulipiza kisasi kwa wote waliowaumiza na kuwaliza wana Sierra Leone: wakiwafanya vilema, wapoteze ndugu na wazazi, na hata uhuru wao.”

    “Pole sana, Amadu. Meli uliyoipanda kukufikisha huko si yenyewe.”

    “Naam. Sasa natambua, najionea huruma nafsi yangu na hata wananchi wenzangu.”

    Baada ya hiyo kauli kaukimya kalipasua anga kwa sekunde nne kisha Ulsher akatia neno:

    “Jana jioni alikuja yule mwanaume aliyenitoa kifungoni na kwenda kujaribu kunibaka. Alikuja kunidhihaki na kunitania, alikuja akiwa amelewa akaniambia wamemuua baba yangu huko Kenema: sasa nimekuwa yatima kamili.”

    “Anaitwa Talib. Kama sijakosea.”

    “Simjui jina lake, ila kamwe sitosahau matendo yake, yeye ndiye alipelekea kifo cha mama yangu, na akaenda kumuua na baba yangu. Hawezi akatoka kichwani mwangu.”

    “Pole. Ila baba yako amemwaga sana damu za watu wasio na hatia.”

    “Najua, Amadu. Ila bado haibadilishi ya kwamba ni baba yangu aliyenizaa.”

    Amadu hakusema kitu. Alitizama tu chini.

    “Amadu, je harakati zako zimeishia hapa?”

    “Kamwe, labda tu nife ila kama nipo hai sitoacha kuwateteta wana Sierra Leone wala kuwakomboa.”

    “Nakuomba, utakapopata nafasi unipe nami fursa ya kufuta makosa ya baba yangu. Unipe nami mwanya wa kuandikwa katika vitabu vya historia vya nchi hii kwa kutetea wasio na nguvu.”

    Amadu hakujibu kitu. Alitulia akisikilizia kama vile ambaye hakutegemea kauli hiyo toka kwa Ulsher. Alichokifanya ni kutabasamu kwa mbali na kukaa kimya. Punde wakaja wafuasi wawili wa MDR chimboni. Walifungua mlango wa chumba anachokaa Ulsher wakamtoa binti kwanguvu. Ulsher alilalama hataki kwenda na wamuache lakini wanaume wale wawili hawakumsikiliza wala kumjali, waliendelea kumsomba.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “We Mudy! Mudy! Mnampeleka wapi?”

    Amadu alipaza sauti yake kuuliza ila hakuna aliyehangaika naye. Ulsher alibebwa akatokomea. Amadu alibakia akiduwaa na kujiuliza. Baada ya lisaa Ulsher alirudishwa chimboni akiwa hoi asiye na nguvu.

    “Wamekufanya nini? ... Enh?” Amadu aliuliza. Ulsher alikuwa tu analia. Baada ya muda aliponyamaza ndipo akasema:

    “Ananibaka.”

    “Nani?” Amadu aliuliza kwa haraka.

    “Mkuu wenu.” Ulsher akajibu, “Si mara ya kwanza wala ya pili. Usiku wa wa manane huwa ananitoa mara kwa mara na kwenda kunibaka ofisini kwake. Tokea tupo Guinea.”

    Amadu alitikisa kichwa chake kwa masikitiko. Alisonya akatizama ukuta umtenganishao na Ulsher akasema kwa sauti ya taratibu:

    “Pole kwa unayoyapitia, mwanamke.”

    Ulsher aliitikia kwa kilio. Alilia na kulia mwishowe usingizi ulimpitia akalala. Siku inayofuata mida ya jioni, Chui na Mou walikuja chimboni kuleta chakula na kumpasha habari Amadu. Wakamuambia yaliyojiri kwenye mkutano ulioitishwa asubuhi na General Kessy.

    “Wanajeshi wa Guinea wanakuja kesho kuja kusaidia MDR. Wanakuja kwa lengo la kuhakikisha MDR inakamata dola ndani ya juma hili. Watakuja wanajeshi si chini ya elfu mbili pamoja na vifaa vizito.” Mou alieleza taarifa. Chui akaongezea:

    “Vita itakuwa very serious. Ndani ya jeshi la Sierra Leone kuna vibaraka wa MDR, wanaleta kila kinachoamuliwa huko makao yao.”

    Baada ya hyo taarifa, Amadu aliwashukuru wenzake ila naye akapata kuwaeleza jambo:

    “Mimi si mfuasi tena wa MDR. Sitotumia tena nguvu wala akili yangu kusaidia wauaji. Ila lengo langu la kuwakomboa wana Sierra Leone lipo pale pale. Naamini naweza kutimiza malengo yangu nje ya MDR bila kuwatesa wakina mama na watoto wasio na hatia. Kwa yeyote anayeona anakubaliana na ninachokisema naomba aniunge mkono.”

    Mou na Chui walitizamana kama watu wanaojiuliza, waliaga wakataka waende kufikiria walichoambiwa.

    Baadae ndani ya usiku mzito, wanaume wanne wa MDR wakiwa wamebebelea bunduki walikuja wakamtoa Amadu chimboni na kumpeleka msituni. Walimpigisha magoti na kumtaka asali sala zake za mwisho kwani sekunde chache mbele anaenda kuuwawa. Amadu akauliza:

    “Nani amewatuma?”

    Wanaume wale ambao walikuwa wamefunikwa na giza wakamdhihaki:

    “Ya nini ujue na unaenda kufa?” Kisha wakacheka na kukoki bunduki zao, wakamnyooshea Amadu. Amadu alitizama juu machozi yakamtoka. Ghafla milio ya risasi ikanguruma. Amadu alijitizama ajabu hakuona jeraha lolote. Alipowatizama wale waliomleta kule msituni akawaona wanadondoka chini na punde wakatokea wanaume wengine wanne: Chui, Farah, Ussein na Mou. Walimnyanyua Amadu wakamkumbatia.

    “Tupo pamoja. Eidha tufe ama tufanikiwe tukipambana.”

    Amadu alitabasamu. Macho yake yalilenga chozi. Aliwakumbata wenzake kwanguvu huku akiwashukuru. Baada ya kupongezana na kupeana shukurani, walianza kuteta:

    “MDR sio ulimwengu wetu tena, hatuna budi kupotea eneo hili. Ila wapi tunakwenda?” Mou aliuliza.

    “Hatujui wapi pa kwenda, ila tuondoke hapa. Tutajua huko mbele kwa mbele.” Farah alijibu.

    “Ila tunafanya nini kwa sasa na tumeachana na MDR?” Mou aliuliza.

    “Kwani kati yetu kuna ambaye dhamira yake imekufa na MDR?” Amadu aliuliza, wenzake wakawa kimya, akaendelea kunena:

    “Kabla ya kufanya lolote yatupasa tusemezane dhamira yetu ni ipi. Hatuna familia, hatuna lolote zaidi ya sisi wenyewe. Je tutakufa tukipigania nini?”

    “Mimi nitakufa nikipigania mapinduzi ya kweli.” Farah alijibu.

    “Na mimi pia, nitakufa nikipigania mapinduzi.” Ussein akasema.

    “Nitakufa kwenye mapinduzi ya kweli.” Mou naye alichangia, akabakia Chui. Wote wakamtizama.

    “Hii ndio njia niliyoichagua. Nitakufa nikiipigania.” Chui naye akatia neno. Wenzake wakatabasamu.

    “Basi kama tumeamua, tuwe na dhamira ya kweli. Hii ndio sehemu kundi letu lilipozaliwa. Tutapigania mapinduzi na hiyo ndiyo dhamira yetu na sababu yetu ya kifo.” Amadu alisema. Wote wakajibu:

    “Ndio!”

    “Kuanzia leo tutafuata njia yetu. Hatutajali uchache wetu kwani tunajiamini na kujitosheleza. Hatutamuacha mwenzetu yeyote nyuma hata pale risasi zitakapokuwa zinapita pembeni ya masikio yetu.”

    “Ndio!” Wote wakajibu.

    “Kuanzia leo tumezaliwa upya. Tunavua gamba la MDR na kujivika utawala mpya, tutajiita GHOST, kwa kuwa hatutaonekana wala kuzuilika.”

    “Ndio!” Wote wakajibu.

    “Kama tumekubaliana, tutakula kiapo huko tutakapokwenda. Ila kwa sasa turudi kambini.”

    “Kufanya nini, Amadu?” Farah aliuliza.

    “Kumkomboa Ulsher, binti waziri. Naye pia anataka hii nafasi.”

    “Huoni kama atakuwa mzigo?” Ussein aliuliza.

    “Hapana. Kumbuka wazazi wake wote wamekufa. Mama yake pia baba yake huko mjini Kenema kutokana na mauaji ya MDR. Kila siku anabakwa na Kessy, hatuwezi kumuacha. Tumpe nafasi, tukimuacha hapa si punde atauwawa.”

    Wakakubaliana.

    “Na vipi kuhusu wale watoto?” Farah aliuliza. “Je tunawaacha?”

    “Kwa sasa hatuwezi kuwapeleka popote: wapo wengi. Itakuwa ngumu kutoroka.” Amadu alijibu.

    “Kweli.” Mou akadakia. “Labda kwa huko mbeleni.”

    “Sawa, twendeni!” Farah alisema kwa sauti. Amadu alichukua bunduki moja ya wale wafu wakaanza kuenenda kufuata ilipo kambi. Ndani ya muda mchache wakawa wameshafika nyuma ya chimbo, walimuona mfuasi mmoja wa MDR akiwa lindo. Amadu alimnyatia mwana MDR huyo akamkaba na kumziba mdomo, akamvunja shingo kisha akafuata mlango wa Ulsher na kuufungua, akamtoa Ulsher wakapotea eneoni.











    http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    ******



    Magari makubwa ya kivita yakiwa yameongozana na yamebebelea wanajeshi yaliingia kwenye kambi ya MDR. Yalikuwa magari kumi kila mojawalo likiwa na wanaume wasiopungua thelathini wenye mabegi migongoni. General Kessy alipokea wageni hao, mmoja wa wageni akaongozana naye mpaka makaoni, wakakaa na kuteta:

    “Tumekuja hapa kwa oda ya mkuu wetu wa majeshi. Tupo hapa kwa ajili ya kuwasaidia kukamata dola ya Sierra Leone. Haitozidi wiki tatu tutatakiwa kurudi Guinea.”

    “Vipi kuhusu vifaa?”

    “Navyo vi njiani vyaja. Ndani ya muda mfupi vitakuwapo hapa. Bunduki, silaha nzito, mabomu na kadhalika. Hatutakuwa na muda wa kupoteza, kila siku tutafanya tukio kutimiza dhamira.”

    “Sawa. Lakini jua kwamba jeshi lako litakuwa chini yangu. Oda na amri zote zitatoka kwangu, sawa?”

    “Sawa. Hii ni nchi yako.”

    General Kessy alichukua ramani akaitandaza juu ya meza, akaanza kuelekezana na mwenzake.

    “Kesho utaenda Freetown wewe pamoja na wanajeshi wako kadhaa na wa MDR.”

    “Sawa. Nini misheni yetu?”

    “Kuvamia na kuharibu wizara ya ulinzi. Hakikisheni mnaharibu kila kitu, mnachakaza kila mtu. Kuna taarifa wana kikao kesho huko wizarani kujadili usalama wa nchi ya Sierra Leone, waziri na makatibu wote watakuwepo huko. Kikao kitafanyika saa nne ya asubuhi.”

    “Sawa.”

    “Wanajeshi wako wengine wataenda na wanajeshi wa MDR kuziba barabara kuu toka mji wa Kenema hata kushambulia, inasemekana kuna kundi la wanajeshi watatoka kuja maeneo ya karibu na Kabala kuzuia nguvu yetu ya mashambulizi.”

    “Sawa.”

    “Nadhani yote hayo yataenda vyema endapo tutapata pia hivyo vifaa. Kwa sasa unaweza kwenda na kuwapasha habari wenzako.”

    “Sawa.”

    Mwanajeshi wa Guinea alinyanyuka akatoka nje ya makao. General Kessy alitabasamu akalamba lips zake. Alifunga mlango wake kwa funguo akatoa simu yake kumpigia mtu aliyetunzwa kwa jina la Bakary. Simu iliita mara mbili ikapokelewa.

    “Tayari wameshafika, kuanzia kesho misheni zinaanza kutekelezwa … Usihofu kabisa kuhusu hilo … Nchi itakuwa chini yangu muda si mrefu … Vipi huko Liberia? …”

    Mara ngo! ngo! ngo! Maongezi yakakatishwa na hodi mlangoni, general ikabidi aage:

    “Tutaongea baadae.”

    Aliuendea mlango akaufungua akakutana na Talib.

    “Nini Talib?”

    “General, Amadu pamoja na wenzake hawaonekani.”

    General aliufungua mlango kwa upana zaidi Talib akaingia ndani na kuketi.

    “Ina mana Amadu hajauwawa?”

    “Hapana! Tumekuta wakina Agu wamekufa, na Amadu pamoja na wenzake: Mou, Farah, Ussein na Chui hawapo!”

    “Shiiit!” General alibamiza meza. Alitikisa kichwa chake kwa masikitiko akauliza:

    “Mbona mnakuwa wazembe kiasi hiki?”

    Talib kimya.

    “Mmeruhusu vipi hao watu wakaondoka?”

    “General, mimi mwenyewe nimeshangazwa na hizo habari. Isitoshe wametoroka na mateka, binti waziri.”

    “Pumbavu kabisa! … Mpaka wanafungua chimbo nyie mlikuwapo wapi?”

    “Alikuwepo mtu mmoja lindo, ila kauwawa!”

    “Talib, unaweza kazi huwezi?”

    “Naweza, mkuu!”

    “Nenda katafute hao watu sasa hivi! Sasa hivi! Potea!”

    Talib alitoka nje akawaita wafuasi kumi akapanda nao gari na kutoka eneo la kambini kwenda kuwatafuta wakina Amadu. General Kessy alifunga mlango wake akarudia kupiga simu yake ya hapo awali.

    “Ndio … Hakikisha ndani ya wiki hii mnafanikiwa kila kitu, kama mkikwama mtanitaarifu … Bakari, inabidi sasa muache habari za kupigana misituni kama masokwe ni wakati wa kuingia ndani ya mji, Liberia hawana usaidizi wowote kwa sasa si unajua utawala wake uliingia kwa mabavu … Nasubiria kusikia toka kwenu Bakari, kama sio sasa, basi ni kamwe.”



















    ****









    http://pseudepigraphas.blogspot.com/











    Ndani ya ofisi moja kubwa iliyonakshiwa na meza ya kioo, viti vyenye viuno vyembamba na picha kubwa za watu maarufu weusi kama Nelson Mandela, Steve Biko na Nkurumah Kwame, alikuwa ameketi bwana Assessoko akiwa amevalia kaunda suti nyeusi, pembeni yake alikuwa ameketi mwanaume mmoja mnene mweusi mwenye kiwaraza kikali, mwili wake ulikuwa umevikwa suti nyeupe kama yangeyange. Juu ya meza kulikuwepo na glasi zenye maji pamoja na chupa zake. Bwana Assessoko alikunya fundo moja la maji, akamtizama mwenzake.

    “Nimefurahi sana kusikia hivyo, hakika sasa njia ni nyeupe.”

    Mwanaume yule mweusi alitabasamu na kusema:

    “Sasa ni muda wa kusaini mkataba bwana Assessoko.”

    Alitoa faili toka kwenye mkoba wake akaliweka juu ya meza na kulifungua.

    “Inabidi sasa usaini mkataba ili tupate kuishi kwa amani.”

    “Kwani hamuniamini bwana Kolo?”

    “Hamna, Assessoko. Mambo siku hizi hayaendi hivyo. Inabidi utie sahihi yale tuliyokubaliana ili kila mmoja wetu awe ana sauti kwa mwenzie.”

    Assessoko alivuta faili karibu naye akapitisha macho kurasa baada ya kurasa, alipomaliza aliweka faili juu ya meza akashusha pumzi ndefu.

    “Kuna shida yeyote, bwana?” Mwenzake aliuliza. Assessoko akatikisa kichwa. Mwanaume yule mweusi akatoa peni yake mfukoni na kumkabidhi Assessoko. Assessoko akapokea peni na kumwaga wino juu ya karatasi mojawapo ya faili, kisha akalirudisha faili kwa mwanaume yule mweusi aliyelitizama na kutabasamu.

    “Sasa kazi imekwisha, mheshimiwa. Nashukuru sana kwa maridhiano.”

    Mwanaume yule mweusi alirudisha faili lake kwenye mkoba kisha akaaga na kuondoka.

    “**** Guinea!” Assessoko aliropoka. Aling’ata meno yake kwanguvu huku akigosha vidole vyake.

    “Wanadhani wao ni wajanja sio? … Nitawaonyesha!” Assessoko aliendelea kuongea mwenyewe. “Mimi ndo’ Assy. Hakuna anayeweza kushindana na mimi. Tutaona mwisho wa siku nani atakayekuwa mwanaume pekee anayesimamia miguu yake.”

    Alinyanyua glasi yake ya maji akabugia. Punde sauti ya mwanamke atangazaye habari ikamfikia masikioni, alirusha macho yake juu ukutani kwenye runinga akamuona mwanamke mmoja mzungu mtangazaji wa shirika kubwa la habari la uingereza akiwa anatangaza habari ya machafuko ya Sierra Leone. Assessoko alitabasamu kwa kebehi, akageuzia kiti chake vizuri kutizama habari.

    “Kwa sasa tunaongea moja kwa moja na katibu mkuu wa wizara ya ulinzi ya Sierra Leone apate kutuambia wamejipangaje kuhakikisha machafuko yanakoma nchini mwao na je watadhibiti vipi kundi la waasi la MDR … mheshimiwa karibu.”

    Mara runinga ikagawanyika mara mbili, sehemu moja akawa anaonekana mtangazaji wakati sehemu ya pili akiwa katibu wa wizara ya ulinzi ya Sierra Leone.

    “Ndugu muandishi hatuwezi tukaweka wazi ni nini tumepanga kufanya, ila tungependa kuchukua wasaa huu kuwatoa hofu wana Sierra Leone kuwa serikali yao haijalala na inalifanyia kazi lile linalotukia ili tuwahakikishie usalama”

    “Lakini muheshimiwa, watu wanazidi kufa. Mpaka hapo mtakapochukua hatua hamuoni kwamba mtakuwa mmechelewa?”

    “Ndugu muandishi, huwezi kukurupuka na kufanya maamuzi. Hili swala wote tunafahamu madhara yake. Sisi kama serikali tunaguswa sana na mauaji hayo, lakini hatujakaa kimya, la hasha! Tunajiapanga kufanya jambo la uhakika.”

    “Mheshimiwa, unaonaje sasa serikali yako ikakaa meza moja na kundi hili la waasi mkafanya majadiliano na hata mwishowe mkaelewana?”

    “Kwa sasa hatuwezi tukafanya hilo jambo, ndugu muandishi. Kufanya hivyo ni kudhihirisha udhaifu na kuwatangazia ushindi MDR. Tutapambana na tunaamini tutashinda.”

    “Mheshimiwa, je mnaongeleaje ukimya wa AU (African Union) katika hili swala lenu? Hamuoni kama wamewatekeleza?”

    “Ndugu muandishi ni mapema sana kusema hilo. Ila tunafahamu ya kwamba katika mkutano wa AU mwezi ujao mojawapo ya agenda kuu ni usalama wa Sierra Leone.”

    “Na je vipi kuhusu umoja wa mataifa?”

    “Nadhani halina haja ya kwenda huko, tutalimaliza sisi wenyewe.”

    “Mheshimiwa, unaongeleaje kauli ya raisi wa Marekani kwamba endapo vita ikiendelea na suluhisho halitopatikana, basi wataleta majeshi yao Sierra Leone?”

    “Ningependa kumwambia raisi wa Marekani ahangaike na mambo yake, hatuhitaji msaada wake wowote maana hatukuuona tokea serikali imeingia madarakani.”

    “Huoni sababu ni kuingia kwenu kwa mabavu serikalini, mheshimiwa? Na hali hii imepeleka kutoungwa mkono na baadhi ya washirika?”

    “Sidhani.”

    “Na je, unasemaje kuhusu ushiriki wa Guinea katika hali mliyopo kwa sasa?”

    “Tunatambua ya kwamba nchi ya Guinea inawasaidia MDR kimali na hali japokuwa wamekuwa wakikanusha hili kwanguvu zao zote. Tuna ushahidi wa kutosha wa picha na hili swala litapewa kipaumbele pia kwenye mkutano wa African Union.”

    “Nashukuru mheshiwa kwa taarifa. Tunakutakia siku njema.”

    “Nawe pia.”

    Assessoko alizima runinga akacheka kwanguvu. Alicheka mpaka akatoa machozi, alijifuta na leso akasema huku akitikisa kichwa:

    “Usilolijua ni usiku wa giza. Kikulacho ki nguoni mwako, katibu.” Baada ya kusema hayo maneno akaendelea kucheka zaidi.





















    ****



















    Ngo! Ngo! Ngo! Ngo!

    Mlango wa makao ya General Kessy uligongwa. General alishusha glasi yake ya kilevi juu ya meza akapaza sauti:

    “Ingia!”

    Mlango ukafunguliwa Talib akaingia. Alipiga saluti kisha akaketi kitini baada ya kuruhusiwa na mkuu wake.

    “Mkuu, hatujafanikiwa kuwapata. Tumewatafuta lakini …” Kabla kauli haijakwisha, Talib alizabwa kofi na General.

    “Mshenzi wewe! Hamjafanikiwa nini? Mnajua hao watu watatugharimu kiasi gani endapo wakiwa huko mitaani? Wanatujua ndani na nje, ni hatari kwa usalama wetu!”

    “Mkuu, sidhani kama kuna haja ya kuwahofia. Hawawezi kutufanya lolote, tupo na tutafanya kazi!”

    General Kessy alimzaba kofi lingine Talib, akafoka:http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Mpumbavu wewe nyamaza! Unaujua uwezo walio nao hao watu? Amadu kuwa hai na akiwa hayupo upande wetu ni hatari. Unajua uwezo wake? Nimekuwa na hili kundi tokea limeanza, hakuna mwanajeshi mwenye uwezo wa Amadu. Kitendo cha kuachwa hai tena akiwa na wenzake ni jinamizi na halitoacha kututafuna, Talib.”

    Talib alikunja sura, alinyanyuka akaondoka, General Kessy alimuita lakini hakugeuka, alitoka nje ya makao akabamiza mlango. General aliketi akamimina kileo pomoni kwenye glasi kisha akamwagia mdomoni mwake. Aliwasha msokoto wake wa bangi akawa anauvuta.

    Siku ikaenda.

    Jua lilipochomoza likachomoza na mipango ya MDR kama ilivyoanishwa. Wanajeshi walijigawa wengine wakaelekea Freetown wengine Kenema, miongoni mwa wanajeshi wa MDR walikuwapo pia watoto nane: walikuwa wamevalia nguo za kijeshi wakiwa wamebebelea bunduki kubwa, wengine walikuwa wamebebelea misokoto ya bangi midomoni mwao wakishea na wenzao, wakati wengine wakiwa wanashiriki kuvuta madawa na wanajeshi wa MDR.

    Baada ya masaa kadhaa magari ya MDR yalikuwa tayari yameshafika ndani ya mji wa Freetown. Mbele ya wizara ya ulinzi magari ya MDR yalijikita na kutema wanajeshi ambao walianza mapambano papo hapo. Risasi zikarindima na kuvuma. Mtaa ukageuka kuwa uwanja wa vita. Kundi la MDR lilishambuliana na wanajeshi wa serikali ambao kiidadi hawakuwa wengi. Wafuasi wa MDR walilipua jengo la wizara kwa makombora mazito. Wanajeshi wa serikali walipoona wanazidiwa walitoa taarifa kwa wenzao wakiomba msaada haraka iwezekanavyo, bahati haikuwa kwao, wenzao wakiwa njiani kuja kuwasaidia walivamiwa na kundi la MDR lililotumwa kwenda Kenema baada ya taarifa ya ujio wao kudakwa. Sasa kukawa hakuna msada kwa wanajeshi wa serikali, wanajeshi wa MDR wakateketeza kila kitu, pale walipojiaminisha hakijasalia kitu, walijitwika kwenye magari yao na mengineyo waliyoyateka wakatokomea.

    Halikuwa jambo dogo, vyombo vya habari vilitekwa na mkangamano wa habari ya uvamizi wa wizara ya ulinzi. Redio na runinga mbalimbali zilizowapa wananchi wa Sierra Leone fursa ya kuongelea hilo tukio, zilionyesha na kusimulia jinsi wananchi walivyokamatwa na hofu. Kama wizara ya ulinzi inaweza kufanywa tukio hilo, wananchi je wasio na ulinzi wowote? Lilikuwa swali kubwa. Mbali na hapo, baadhi ya wakuu wa nchi mbalimbali za Afrika na hata mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Afrika ya kusini, Senegal, Ghana na Tanzania nao walipewa uwanja wa kutema misimamo yao juu ya tukio hilo, wote wakikemea na kulaani vikali kile kinachoendelea kwa minajili ya usalama wa wana Sierra Leone. Lakini hakuna kiongozi hata mmoja aliyesema hadharani nchi yake itachukua hatua gani kurudufu hali ya Sierra Leone.

    Nyuma ya kioo cha runinga, alikaa katibu mkuu wa serikali ya Sierra Leone, bwana Momka Tejan. Uso wake ulikuwa mtulivu na juu ya meza yake palikuwepo na glasi ndogo ya maji ya kunywa. Baada ya kusafisha koo, katibu mkuu alianza kusema dhamira yake, ama tuseme dhamira ya serikali:

    “Tumesikitishwa sana na hali ya taharuki na sintofahamu kubwa ambayo imeivika nchi yetu pendwa kwa sasa. Sisi kama serikali tumeguswa kama wahanga wa kwanza na tumeteka fursa hii ya wazi kuwasiliana na wananchi wetu ili wapate kujua ni hatua gani stahiki ambayo tumeichukua. Tumekaa na kukubaliana kwamba, huu ndio muda, eidha tumechelewa au tumewahi, wa kukaa meza moja na kundi hili la MDR ili tuepuke kuwaumiza wananchi ambao ni ndugu, familia na jamaa zetu. Tunaomba sasa, sauti hii iwe kama sauti nyikani, na iwe mwanzo wa kutatua mgogoro huu unaofurukuta. Kiongozi wa MDR, atapata fursa ya kujadili na mkuu wa nchi mambo kadhaa ambayo yataepusha na hata pia kutupumzisha na vita hii. Tunatumai kwamba wito huu utakubaliwa na kuzingatiwa, na tutayamaliza haya yanayotukia. Nashukuru kwa kunisikiliza.”

    Kwa General Kessy, alitabasamu baada ya kupata huo ujumbe. Kwake ilikuwa ni kama alama ya ushindi. Hakuna maagano yatakayokubaliwa kati ya wao na serikali. Ndani ya usiku huo, mpango wa kuvamia ikulu na eneo analoishi Mkuu wa jeshi la ulinzi ulisukwa. Talib alipewa jukumu la kuvamia ikulu na kumteka raisi, ambatano naye alipewa wanajeshi mia mbili, makombora na maguruneti. Kiongozi wa wanajeshi wa Guinea, akapewa kazi ya kuvamia na kumleta Mkuu wa jeshi la ulinzi akiwa hai au amekufa, naye akaambatanishwa na wasaidizi na vifaa. Tukio likapangwa kufanyika siku inayofuata wakati wa usiku.

    Kutokana na matisho ya vita, hata barabara zilikuwa nyeupe. Magari yalikuwa machache au kutokuwepo kabisa si wakati wa usiku ama mchana. Hali hii general aliichukulia kama chochezi na kisaidizi cha kukamilisha mazoezi yao ya kuteka nchi.

    Katika usiku huo huo ndani ya kambi ya kijeshi ya Sierra Leone amri ilitolewa toka kwa Mkuu wa jeshi la ulinzi kujiandaa kwa ajili ya kushambulia mji wa Kabala. Mashambulizi yatatumia njia ya anga kutokana na majiribio ya ardhini kushindwa kufua dafu. Japokuwa njia ya mashambulizi ya anga ni hatia kwa usalama wa wananchi, hakukuwa na jinsi kwa mujibu wa Mkuu wa jeshi la ulinzi. Ndege nne aina ya chopa zilishtushwa injini kuwekwa sawa kwa mashambulizi yaliyopangwa kutukia pale jua litakapochomoza. Lakini kabla ya usiku huo kukoma, taarifa hiyo ikafika mikononi mwa General Kessy. Simu ya mkononi iliita na sauti moja kavu mithili ya majani ya uwanda wa savana ikamtaarifu General mpango wa jeshi la Sierra Leone. Silaha za makombora ya kudungua ndege zikaandaliwa kwa ustadi na kuwekwa kwenye maeneo yazungukayo kambi na kati kati ya kambi pia.

    Jua la siku iliyofuata lilikimbia na kufika utosini. Chopa nne ziliacha kambi ya jeshi zikifyatuka kwa kasi kubwa mno kuelekea upande wa mji wa Kabala huku marubani wake wakiwa wamejivika kofia ngumu zilizoshikilia miwani kubwa nyeusi zikiwa zimefunika vyema macho yao. Kutokana na kasi kubwa ya ndege hizo, haikuchukua zaidi ya dakika kumi kufika Kabala. Zikiwa zimerandana, marubani walitizamana na kupeana ishara ya kutikisa kichwa, ila kabla hawajabonyeza vitufe vya kuachia makombora, ghafla kombora moja likiwa linakimbia kwa kasi lilivamia chopa moja na kuibabua kwa mlipuko mkubwa. Kufumba na kufumbua, yalikuja makombora mengine matatu kwa kasi, chopa moja ikayeya na kukwepa huku zingine zikiishia kusombwa na mafuriko ya malipuko. Chopa iliyobakia ikageuza kama inarudi ilipotokea, kabla haijapotea, makombora manne yalitumwa kwa pupa, na huo ukawa mwisho wa rubani pekee aliyebakia, ndege ilisambaratishwa na kuwa vyuma chakavu vilivyodondokea chini.

    General Kessy aliitisha umati wa wafuasi wake. Aliamuru uvamizi wa ikulu na nyumba ya mkuu wa jeshi la ulinzi ufanyike mara moja, ilikuwa ni fursa adhimu kufanya hilo tukio kwa muda huo. Kama walivyopangiwa majukumu siku iliyopita, Talib na kiongozi wa jeshi la Guinea wakatoka na vikosi vyao na kwenda maeneo yao ya matukio.

    Masaa sita mbele, kila chombo cha habari kikatangaza kifo cha raisi na familia yake, pamoja na mkuu wa jeshi la ulinzi. Maiti zao zilionyeshwa zikiwa zinaburuzwa katika mitaa ya Freetown huku zikiwa uchi wa mnyama. Wafuasi wa MDR walitawala mitaa yote ya Freetown wakiwa wanashangilia ushindi kwa kuimba nyimbo zao za ukombozi huku wakiweka silaha zao angani. Miongoni mwao wakiwa watoto wadogo lakini wenye sura zilizokomaa na macho ya kuogofya. Watu walijifungia ndani ya nyumba zao, maduka na ofisi zilifungwa, hali hii ilipelekea jiji kuwa jeupe isipokuwa tu uwepo wa wafuasi wa MDR waliokuwa wakijimwaya na kujimwaga wanavyotaka. Wakivamia popote na kuchukua chochote, wakiiba vyombo vya usafiri na kuvitumia pasi na ustaarabu.

















    ****

















    Mazingira yalikuwa tulivu. Wanaume waliovalia nguo za jeshi zenye bendera ya Guinea mabegani walikuwa wanazunguka huko na huko wakiwa wamebebelea bunduki aina ya SMG. Nyumba iliyokuwa inalindwa ilikuwa kubwa mno yenye rangi nyeupe. Majani ya kijani kibichi yalikuwa yametapakaa yakizunguka nyumba hiyo kubwa, pia maua. Sehemu ya kuhifadhia magari ilikuwa ni kubwa na magari yaliyokaa hapo yalikuwa ni aina ya Rolls Royce, Mercedes benz, range rover, Ferrari na Lamorghini, zote zikiwa nyeusi kwa rangi.

    Ndani ya nyumba hiyo kubwa, sehemu moja iliyokaa kama kichumba kidogo cha kikao, walikuwa wamekaa wanaume wawili: Assessoko na raisi wa Guinea kwenye viti viwili vikubwa vyekundu vyenye miguu ya dhahabu. Mbele yao walikuwepo wadada warembo wawili wakiwa uchi wa mnyama, walikuwa wanacheza mitindo mbalimbali huku wakiwatizama wateja wao. Raisi wa Guinea alinyanyua mkono akawaonyesha wadada ishara ya kuondoka, wadada wakatoka. Raisi wa Guinea akamtizama Assessoko na uso wa tabasamu, akasema:http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Hongera sana. Hakika unastahili pongezi kwa dhamira yako uliyoisimamia mpaka dakika ya mwisho.”

    Walinyanyua glasi zao za vinywaji wakazigongesha klang! Kisha wakanywa fundo moja. Assessoko akasema:

    “Siwezi kukushukuru vya kutosha kwa msaada wako. Ila nipo kuonyesha kwamba nathamini kila tone la juhudi yako uliyoitoa. Pasipo mkono wako, ni wazi kurudisha heshima yangu inagalikuwa vigumu mno.”

    Raisi wa Guinea alitabasamu, akatikisa kichwa chake.

    “Usihofu, Assessoko. Sisi ni wamoja, leo wewe kesho huenda ikawa mimi. Ila … Nadhani huu ni wasaa wa kutupia macho yetu kwenye utekelezaji wa mkataba tuliojiwekea kati yangu na wewe.”

    “Aaahm … kuhusu hilo jambo la mkataba, siwezi kukupa jibu kamili kwa sasa mpaka pale nitakapojadiliana na mshirika mwenzangu, Kessy.”

    “Hapana! Hapana! Hapana! … hayo hayakuwa makubaliano yetu. Nilifunga mkataba na wewe na si mtu mwingine. Naomba makubaliano yaheshimiwe.”

    Assessoko aliria fundo moja la kinywaji. Alitulia kwa sekunde chache, akavuta pumzi kwa nguvu na kulonga:

    “Sawa, mheshimiwa. Kila kitu kitaenda sawa tu, hakuna haja ya kuhofia. Ila naomba basi muda kidogo maana nchi yenyewe ndiyo kwanza nimeikwapua, bado sijatulizana na kutizama rasilimali katika jicho yakinifu.”

    “Sawa.” Raisi wa Guinea alisema, “Unachokiongea ni hoja, nami niko radhi kukupatia muda.”

    Waligongesha tena glasi zao, wakapeleka vinywaji mdomoni.

    Wakati jua laelekea kuzama, Assessoko alikuwa karibu na General Kessy ndani ya nchi ya Sierra Leone. Walikuwa kwenye chumba fulani kikubwa wakiwa wamekaa kwenye viti vilivyotenganishwa na meza ya kioo ambayo juu yake kulikuwa na faili la mkataba. General alikuwa amevaa nguo zake za kazi: magwanda yasiyobeba bendera yoyote, wakati Assessoko alikuwa amevalia shati jeupe na tai nyembamba nyeusi iliyorandana rangi na suruali yake ya kitambaa.

    “Unaonaje kuhusu hili swala la mkataba. Kessy?”

    “Mkuu, kusema ukweli kutimiza yaliyoko humo ndani ni ngumu mno. Nimejaribu kuyarejelea, nimeona ni hasara kubwa tutakayobakiza endapo kama tukitoa maeneo hayo muhimu.”

    “Ni kweli. Ila sasa tutafanyeje na alitusaidia?”

    “Hatuwezi kukubali kutekeleza chochote kilichokuwemo ndani ya mkataba huo. Hata kama tukikataa, hawezi kuupeleka mkataba huu popote pale kwakuwa ni kithibitisho cha kwanza kwamba alitusaidia, kitu ambacho amekuwa akipinga kwanguvu zote mbele ya umma. Huu mkataba ni kama ghelesha tu, hautakuwa na madhara yoyote utakapokiukwa.”

    “Vipi endapo ataamua kuanzisha vita baina yetu na yeye?”

    “Hawezi. Anajua kwamba sisi pekee ndio washirika wake kwenye utunzaji wa siri yake ya kidhalimu. Ila hata kama atataka vita, tutapambana naye.”

    “Nani atakuwa upande wetu?”

    “Liberia.”

    “Umejuaje?”

    “Le tueurs wapo kwenye nafasi nzuri ya kushika dola sasa. Guinea hatokuwa na upande wa kumsaidia kutokana na shutuma zake za kuwasaidia waasi.”

    Assessoko alitabasamu huku akitikisa kichwa. Alinyanyuka, General Kessy naye akanyanyuka wakakumbatiana.

    “Mwishowe tumefanikisha, Kessy.” Assessoko alisema kwa furaha, akaongezea, “Sasa nenda kawaambie hao watu wa vyombo vya habari niko tayari kuhutubia wananchi.”

    General Kessy alitoka akaufuata mlango ulioukuwa upande wao wa kulia. Alirudi mkono wake wa kulia ukiwa nyuma. Alipomkaribia Assessoko alimkumbatia akautoa mkono wake nyuma ukiwa na kisu, akamchoma Assessoko tumboni mara tatu chup! Chup! Chup! Assessoko alilalama kwa maumivu. Alikodoa macho yake yaliyogeuka kuwa mekundu haraka na kuvujisha machozi. Huku mdomo wake ukitetemeka, Assessoko alimuuliza General Kessy:

    “Nini nimekukosea?”

    General alibinua mdomo wake akajibu:

    “Kosa ulilofanya ni kudhani nakufanyia kazi wewe muda wote huo. Samahani sana, mkuu. Na ahsante kwa mchango wako.”

    Baada ya kusema hayo, General Kessy alimuachia Assessoko akadondoka chini kama mzigo wa kuni. Shati lake jeupe lilikuwa limetapakaa damu. Macho na mdomo vilikuwa wazi.

    General Kessy alienda mbele ya kamera akahutubia umma. Alijitangaza yeye ndiye mkuu wa nchi kuanzia muda huo. Nchi itaongozwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu atakazoziweka kwani yeye ndiye katiba halisi.

    Si wafuasi wote wa MDR waliomuunga mkono General Kessy kuwa kiongozi wa nchi. Wafuasi kumi walijitenga na kusimamia msimamo wao wa kumtaka Assessoko ndiye akaimu madaraka. Taarifa zilipofikishwa kwa General Kessy, wafuasi hao walikamatwa na kupelekwa kwenye uwanja wa taifa, wakanyongwa papo. Kisha General akatoa tishio kuwa hilo ndilo litakalowakuta wale wote watakaokaidi na kupinga maamuzi yake.

    Wakati General Kessy akiwa ofisini kwa mkuu wa nchi. Simu yake ya mezani iliita. Alipokea akakuta ni raisi wa Guinea anamtafuta. Huku akiwa anatabasamu kwa kebehi, General Kessy aliongea:

    “… Halo! … General anaongea hapa … Assessoko? Ameshakufa, yupo kuzimu kwa sasa … mkataba gani? Mkataba uliweka na nani? … Ah! Ah! Siwezi nikafuata makubaliano ambayo sijayaweka ndugu yangu … Nikupe pole tu na nikutakie kazi njema.”

    General Kessy alirudisha simu mezani akacheka. Upande wa pili wa Guinea ilikuwa ni manung’uniko na hasira. Raisi wa Guinea alikuwa amekunja sura. Alirusha chupa ya mvinyo kabatini huku akitusi. Alibamiza meza akasema huku akiwa ameng’ata meno:

    “Naapa nitakufundisha somo, mshenzi wewe! Naapa kwa Mungu wangu!”















    ******



















    Baada ya mwezi mmoja tangu General Kessy aingie madarakani, nchi za Uingereza, Ufaransa na Marekani zilikata mahusiano na nchi ya Sierra Leone. Balozi za nchi hizo zilifungwa huku mawaziri wao wa mambo ya nje wakitupia maneno makali kwa utawala wa General Kessy kuingia na kutawala kwa mabavu, kunyima haki wananchi kueleza mawazo yao, kuvifungia vyombo vya habari, kukataza vyama na shughuli zozote za kisiasa. Akijibu hoja hizo, General alitumia runinga ya serikali akajibu kwa ufupi:

    “Nchi yangu inaweza kujiongoza bila ya msaada wowote wa mtu mwenye ngozi nyeupe. Wanaingilia mambo ya nchi yangu, mimi nimegusa yao?”

    Siku iliyofuata, Sierra Leone ikajitoa kwenye umoja wa nchi zilizowahi kutawaliwa na mwingereza, commonwealth. Katika siku hiyo hiyo, vipeperushi na matangazo yakabandikwa na kusambazwa mitaani yakiwa yamebebelea picha ya Amadu, Chui, Farah, Mou na Ussein. Zawadi nono kutolewa kwa yeyote atakeyetoa taarifa ya upatikanaji wao.







    Ndani ya nyumba kubwa ya saruji yenye ukubwa wa kati, bati chakavu lenye kutu na madirisha yasiyo na pazia, walikuwemo wamekaa Amadu, Chui, Ussein, Farah, Mou na Ulsher juu ya mkeka wenye michoro hafifu na majeraha kadhaa. Walikuwa wamekaa wakitengeneza mtindo wa duara, na katikati yao ilikuwa imeketi sinia kubwa la bati limejaa wali pomoni. Kila mtu alikuwa anajishughulisha na kula akitumia mkono wake kama kijiko. Baada ya maudhui ya sinia kupungua kwa kiasi cha nusu, Chui alifungua jamvi la maongezi akiuliza;

    “Mnakumbuka siku ile MDR walivyotapakaa mitaa ya Freetown baada ya kuvamia ikulu?”

    Kabla hajajibu mtu yeyote, Chui aliendelea kumwaga maneno kama vile kajibiwa na kuruhusiwa aendelee;

    “Kuna mzee jirani yetu kila siku analalamika, duka lake lilivamiwa na kukombwa karibia duka zima, si pesa, si bidhaa. Yani amekuwa ombaomba ghafula!”

    Amadu alitikisa kichwa chake huku akitafuna. Mou kabla hajameza alichokuwa anatafuna alidaka mada;

    “Washenzi sana wale. Sasa walikuwa wanaonyesha picha gani kwa wananchi wanaoenda kuwatawala?”

    Ulsher akajiweka madani kwa kuuliza,

    “Nani kasema MDR ni kundi la ukombozi?” Kabla wengine hawajafungua midomo, aliendelea kulonga, “Ni genge tu la wahuni waliojivika ngozi ya kudai ukombozi lakini nyuma ya mapazia wanaendeshwa na uroho wa madaraka. Makundi mengi ya waasi Afrika yanatumia mifadhaiko ya wananchi na ukosefu wao wa matumaini kwa serikali yao kama ngazi ya kutimiza adhma yao. Wanabaka wanawake, wanaua watoto, wengine wanawaingiza watoto kwenye uwanja wa vita huku wakiwapumbaza na madawa ya kulevya, vile vile wanaua watu wasio na hatia, unategemea mtu au kikundi cha namna hiyo kibadilike kitakaposhika madaraka?”

    “Sawa mwanafalsafa.” Chui alidakia, wote wakacheka, “Sasa nini kifanyike? Je tuuache utawala wa General Kessy?”http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Hapana.” Ulsher alijibu, “Kuuacha utawala wa kidhalimu na kimabavu wa General Kessy ni jambo lisilofichika kwamba litawagharimu sana wana Sierra Leone, hatuna budi kuuondoa kwa gharama yoyote ile.”

    “Lakini unapinga kundi la waasi, sasa tunafanyeje?” Chui aliuliza.

    “Kweli napinga makundi ya waasi,” Ulsher alijibu, “lakini hili la kwetu si la waasi. Hatutaasi misingi ya haki za binadamu wala amani ya wananchi. Hatutajificha kwenye kibanzi cha ukombozi wa uongo, bali ukweli.”

    “Upo sahihi.” Amadu naye akatia neno, “Kumuacha mtu msaliti kama General Kessy ni dhambi tutakayoshindwa kuitolea ufafanuzi mbele ya Mungu. Kama aliweza kumsaliti mtu aliyemfikisha pale kwa gharama kubwa mwishowe akamtoa sadaka ili apate uongozi, huyo ni mtu hatari. Hawezi kushindwa kuwasaliti wana Sierra kwa mlengo wake binafsi. Ila kuna jambo sasa naanza kulipatia mashaka. Mnakumbuka siku ile tulienda kuchukua silaha Liberia?”

    “Ndio.”



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog