Search This Blog

Sunday 20 November 2022

MSAKO WA HAYAWANI - 4

 





    Simulizi : Msako Wa Hayawani

    Sehemu Ya Nne (4)





    Kembo akatikisa kichwa. "Sidhani kama polisi wanaweza kuchukua hatua kama hiyo. Hasa kwa kesi ya kugongwa na gari, na aliyegongwa hajafa."

    "Kumbuka kuna kitendo cha Hoza kwenda hospitalini kummaliza."

    "Nakumbuka. Lakini je, haupo uwezekano wa Dikwe kupelekwa huko Uwanja wa Gofu na mtu mwingine baada ya kuachana na huyo kijana?"

    "Chox anasema haupo. Anasema kijana huyo ingawa ni mdogo kuliko mimi, si wa kawaida. Hasa macho yake."

    "Yana nini?"

    Chiko akabetua mabega. "Sijui."





    Kembo alikiondoa kikombe mdomoni akailiza, "Sasa wasiwasi wako ni wa nini?"

    "Dikwe anaweza kuwa kaimba."

    "Kuna lolote la maana alilolijua?"

    "Machache. Kama vile mimi na Hoza tulikuwa marafiki, na sote tuna vibweka. Alijua kwa sasa niko Tupetupe. Ndiyo maana nasita kwenda huko."

    "Sikiza." Alisema Kembo. "Cha kufanya ni kupata uhakika kijana huyo ni nani. Kama ananunulika, anunuliwe. Kama hanunuliki,alipuliwe. Mimi na wewe hatujashindwa jambo hata siku moja.





    *************************************





    "Butu ameshafika?" Bessy alimuuliza sajini wa kwenye kaunta. "Ndiyo afande." Akajibu sajini huyo. "Yuko nyuma."

    "Mwambie aje ofisini mwangu." Bessy akataka kuondoka, akakumbuka. "Na sajini, waulize watu wa kompyuta kama kuna faili la mkora aitwaye Chiko. Kama lipo waniletee."

    "Sawa afande."





    Bessy na Denny wakazipanda ngazi, huko juu wakaingia katika chumba cha wastani chenye meza mbili ndogo,viti vitatu na benchi moja. Ukutani palibandikwa ramani ya jiji na matangazo kadhaa.

    Denny akaenda kuketi nyuma ya meza ya pili, ambayo haikuwa na chochote. Haikuwa hata na simu wala trei la majalada.

    "Nikilazimishwa nishinde mchana kutwa katika chumba hiki," Akasema Denny, "Naweza nikajirusha dirishani."

    Besy akatoa kicheko kidogo. "Unadhani mimi hujifungia mchana kutwa?"

    Mezani pake palikuwa na simu na mafaili mawili matatu. Akalifungua la juu. Akasema. "Ooh, Ni ripoti za matukio ya jana usiku. Bob na huyo mwenzake waliouwawa kwenye saa sita za usiku. Walilipuliwa na bastola tofauti. Kwa hiyo wauaji walikuwa wawili. Kwa vyovyote si chini ya watu wawili."





    "Ina maanisha chochote?"

    "Sijui. Isipokuwa mauaji haya yanazidi kutatanisha." Bessy akasoma ukurasa mwingine. Akasema. "Na Dikwe alikufa karibu na alfajiri. Alivunjwa mfupa wa mkono wa kulia na wa mguu wa kushoto kabla ya kufa. Madaktari wanasema mifupa hiyo haikuvunjwa kwa meno ya fisi."

    Dennya akataka kusema neno lakini mlango ukagongwa, na Kostebo mwenye jalada mkononi akaingia. Akasema. "Faili la Chiko afande."





    Bessy akalipokea na kulifungua. Baada ya kulipitia haraka haraka, akamwambia Denny, "Ameshawahi kufungwa, lakini karibu miaka miwili iliyopita. Kifungo cha miezi sita, kwa kukutwa na bangi. Baada ya hapo amekuwa akikamata mara kwa mara na kuachiwa kwa ukosefu wa ushahidi wa kutosha."

    "Picha je?"

    "Ipo moja nzuri."



    Denny aliinuka na kulichukua faili na kurudi mezani. Akajikuta anamtazama kijana mwenye sura ya kawaida kabisa. Akatikisa kichwa. "Nani angeweza kuamini anaweza kufanya kitendo kama kile?"

    "Kitendo gani?"

    "Cha kule Uwanja wa Gofu."

    "Dennya sijaanza jana wala juzi kazi ya upolisi. Mtu aliyemvunjavunja Dikwe na kumtelekeza Uwanja wa Gofu si Chiko wala mtu mwingine yeyote zaidi yako."

    "Bessy!"

    Bessy akainua viganja. "Usiwe na wasi wasi! Sina hata chembe ya ushahidi."

    "Ungekuwa nao?"

    "Ooh! Usiniulize maswali yasiyojibika."





    Wakakodolena macho kwa nukta mbili au tatu. Kisha Denny akasema, "Bessy, hatujaoana hali hii, ugomvi kila wakati, tutakapooana itakuwaje?"

    "Yaelekea una uhakika kabisa na jambo hilo."

    "Kabisa."

    "Unataka tupinge?"

    "Sawa, konzi kwa konzi."

    "La wapi?"

    "Mshindi ndiye mchaguzi."











    Baada ya kupiga honi na kufunguliwa geti la jumba Na.21, Mtaa wa kitosi, Buffalo Hill, Sam Kembo aliliendesha gari lake ndani. Hakuweza kujizuia kuangalia bustani, nusu akitazamia kumwona Kikoti akimwagia miwaridi.

    Mtumishi mmoja alimlaki Kembo na kumwelekeza aliko tajiri yake. Kassim Hashir alikuwa nyuma, akiogelea bwawani.





    "Good morning Mr. Kessy." Kembo akamsalim.

    "Oh, morning Sam." Alijibu Kassim, "I hope it's good morning." Akayakata maji kwa michapo miwili mitatu ya nguvu na kutoka majini. Akaliokota taulo lililokuwa kwenye kiti na kuanza kujifuta, "Well, is everything ok?"

    "Usiwe na wasiwasi, ni asubuhi njema."

    "Keti." Wote wakaketi. "Kwa hiyo," Kassim akaendelea, "Si chochote?"

    "Ammm, kwa upande tunaweza kusema hivyo."





    Mtumishi akamletea Kassim glasi ya maziwa, bila ya sukari. Mtumishi alipoondoka, Kassim akauliza, "Una maana gani, Sam...kwa upande!"

    "Nna maana Chiko hakuwa akilaghai. Tuna tatizo dogo. Lakini si la kutubabaisha."

    "Tatizo gani?"

    "Mawili, kwa kweli, si moja. Yule kijana tuliyemtuma akaifanye ile kazi ya hospitalini kaboronga, pengine halikuwa kosa lake. Dk.Makete analindwa masaa ishirini na nne, naye alikuwa halijui hilo. Akauwawa na askari mmoja wa kike maarufu sana hapa jijini, Kachero Inspekta Bessy."



    Kahawa yake ikaletwa, akanyamaza akijijazia kikombe.

    "Enhe?" Kassim akauliza akiuangalia mgongo wa mtumishi wake aliyekuwa akiondoka.

    "Kwa njia moja ama nyingine,Bessy akagundua kijana huyo, Hoza, aliishi Tupetupe Hoteli. Mambo yakaharibika zaidi."

    "Kivipi?"

    "Hoza alikuwa pusha, na alikuwa rafiki wa Chiko. Kisha kijan mmoja ambaye tunamwita X kwa sababu mpaka sasa hatuna uhakika kama ni askari au ni nani, alimnasa pusha mmoja hapo Tupetupe na kumpeleka Uwanja wa Gofu. Tunashukuru alumhoji kifasishiti."





    "Huyo pusha anaweza kuwa alilijua hilo?"

    "No way. Hata Hoza hakuwa akilijua."

    "Sasa pana nini tena zaidi?" Kassim aliuliza na kupeleka kuipeleka glasi ya maziwa kinywani.

    "Tatizo ni kwamba Dikwe, huyo fal@ aliyepelekwa Uwanja wa Gofu, alifahamu kuwa Chiko na Fansy ni marafiki wa Hoza. Na Chiko na Fensy wanakufahamu. Jana usiku niliwaleta hapa."

    "Ulifanya kosa kubwa kuwaleta."

    "Hapana. Ilibidi wawe karibu, wewe mwenyewe unafahamu hivyo. Hatukujua nini Bob atasema. Hatukujua atasema pesa zikadondoshwe saa sita. Je,angesema zikadondoshwe dakika ile ile - ndipo tungeanza kuwatafuta Chiko na Fensy?"





    "Oh! Hell!" Kassim aliyamalizia maziwa , akaiweka glasi tupu mezani na kuwasha moja ya sigara zake nene zenye harufu nzito. Akauliza, "Kama watabambwa, na kutikiswa kidogo, wanaweza wakaghani?"

    "Chiko sina wasi wasi naye," Alijibu Kembo. "Alishatishwa mara kadhaa. Akiamua kuwa bubu, huwa bubu kweli kwel. Lakini Fensy," Kembo akatikisa kichwa, "Sina imani naye."





    Kassim aliliondoa sigara lake mdomoni, akageuza kichwa na kumtazama Kembo usoni. Macho yakagongana na kung'ang'aniana.

    Kembo akajikuta akiyaangalia macho yasiyo ya kawaida. Akasisimuka mwili mzima. Akayakumbuka maneno ya Chiko. 'Chox anasema huyo kijana siyo wa kawaida hasa macho yake.'





    Kembo alidhani Chox alipayuka, lakini sasa aliamini kuna macho yasiyo ya kawaida. Tena macho ya bepari huyu yalizungumza kama yenye sauti.

    "Kessy!" Ilikuwa ni mara ya kwanza Kembo kumwita hivyo tajiri huyo, "Kessy, hunitumi nikamtume Chiko kumuua rafiki yake!"

    Kassim akalirudisha sigara lake mdomoni na kuyaangalia maji ya bwawa. "Huoni kuwa hiyo ndiyo njia fupi ya kulimaliza tatizo hili?"





    ***********************************





    Kwa dakika mbili au tatu ofisi ilikuwa kimya kabisa, mrembo Kachero Inspekta Bessy akipekua mafaili. Kisha akainuka, akaenda dirishani na kuangalia nje. Bila kugeuka akaita kwa sauti ndogo, "Denny."

    "Yes?"

    "Denny - huoni kuwa ingekuwa busara zaidi kama ...kama ungetuachia sisi tuendelee na kazi hii?"

    "Kwa nini?"

    "Kwa sababu Kassim Hashir ni...ni..."

    "Ni bull shit!" Denny alibweka. "Kassim Hashir ni bull shit. Hanihusu chochote mimi. Baba yangu ni Dk.Raymond Makete."

    "Oh, niwie radhi." Kabla ya Denny kujibu,mlango ukagongwa. Bessy akageuka na kusema "Ingia."





    Koplo Butu akaingia ndani kinyonge na kupiga saluti. Alikuwa katika sale yake ya usalama barabarani, ambayo siku hiyo ilionekane kumpwaya. Hata hivyo, V zake mbili za shaba zilimeta kwenye mkono wa shati lake.

    "Karibu Butu," Bessy alimwambia. Akautazama uso wake uliopooza. Akasema, "Yaelekea umeshasikia."

    "Ndiyo, afande. Nilikwenda hospitalini kuiangalia maiti." Alijibu Butu. Akamtazama Dennis. Macho yao yalipokutana wakakumbukana.

    "Wewe siye..." Akaanza Denny, lakini Butu akamkatiza.

    "Ndiyo,Luteni." Alisema Butu.

    Bessy akauliza, "Vipi mnafahamiana?"





    "Tulikutana jana katika mazingira ya ajabu ajabu." Alijibu Denny. Nilipokuwa nikiingia jijini kutoka Ndala, yeye na mwenzake wakiwa katika kigofu wakaniandama. Bila shaka ili wanikamate kwa kwenda kasi."

    "Oh!" Bessy alishangaa. Akasema, "Huyo mwenzake bila shaka atakuwa ni Bob, sivyo Butu?"

    "Ndiyo, afande."

    "Keti."

    Butu akaketi kwenye benchi, macho chini.

    "Enhe," Bessy akamuuliza Denny,huku akirudi kuketi mezani pake, "Kisha ikawaje?"

    "Waliniandama hadi hospitalini." Denny akaendelea.





    "Bob akamsakizia Butu, yeye akabaki garini. Huyu bwana akanifuata.Lakini baada ya kunisimamisha, akabadili mawazo ghafla. Akaamua kudharau kila kitu. Alifanya jambo la busara sana. Sijui alikwenda kumwambia nini Sajini wake."

    "Eti," Bessy akauliza, "Ulikwenda kumwambia nini Bob?" Butu akabaki kimya, akiendelea kutazama chini.

    "Oh, niwie radhi." Bessy akasema haraka, "Sikunuia kustihizai. Alikuwa ni rafiki yako siyo?"

    "Sana." Alijibu Butu, akikubali pia kwa kichwa.

    "Inasikitisha sana kifo chake. Lakini ilikuwaje auwawe vile, mbona inatatanisha!"

    Butu hakujibu.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    "Ni dhahiri kauliwa na wakora," Bessy akaendelea. "Tena wakora hatari. Lakini kwa nini? Na kwa nini mahali pale? Au alikuwa na uhusiano na wakora - wamedhulumiana?"

    Butu akatikisa kichwa akisema, "Hakuwa na uhusiano na mkora yeyote ."

    "Kama angekuwa na uhusiano nao ungefahamu?"

    "Naamini hivyo."

    "Mlikuwa marafikia kiasi hicho?"

    "Ndiyo. Alikuwa hanifichi jambo."

    "Jana mliachana wakati gani?"

    "Jioni," Alijibu Butu.





    Denny akamuuliza, "Matembezi yalikuwa pamoja kila siku baada ya kazi?"

    Butu akasita.

    "Oh, nilisahau kukufahamisha," Alisema Bessy. "Huyu ndiye mwanae Dk.Makete. Yeye ni komandoo Luteni Dennis Makete. Tafadhali mjibu maswali anayokuuliza. Je, ulikuwa ukitembea na Bob kila siku jioni?"

    "Ndiyo, afande."

    "Wapi?"

    "Kwanza kwa Shangazi Suzy,kisha Lulu Night Club."

    "Kwa shangazi Suzy ndiyo wapi?" Denny aliuliza. "Ni baa au stoo au kilabu?"

    "Hapana, ni nyumba ya kawaida, Mtaa wa Mshoneni. Huyo 'Shangazi' anauza bia na mapuya."





    "Kwa hiyo mlitoka kwa shangazi Suzy mlikwenda Lulu."

    "Ndiyo."

    "Kisha?"

    "Mara kwa mara tulirudi Polisi Laini kulala. Siku moja moja, hasa siku za Jumamosi, tulikwenda disko au dansini."

    "Sasa tueleze mzunguko wenu wa jana," Alisema Denny, akaongeza, "Kikamilifu."

    "Tulipomaliza zamu tulirudi Laini kuoga na kubadili nguo,kisha tukaenda kwa shangazi."

    "Hukutaja kula.Au mlikuwa mkila kwa huyo shangazi?"





    "Hapana, tulikwisha kula kantini. Sisi hula kantini. Mimi sijaoa, Bob kakimbiwa na msichana aliyekuwa akiishi nae. Tulijipikia kwa nadra sana."

    "Sawa. Mkaenda kwa huyo shangazi?"

    "Ndyo."

    "Kwa gari la Bob?"

    "Ndiyo."

    "Ilikuwa saa ngapi?"

    "Kwenye saa tisa. Saa tisa na robo au na dakika ishirini."





    Denny akamtazama Bessy. Msichana huyo alikuwa akiandika kwa spidi ya ajabu. Denny akakisia alikuwa akiandika katika hati mkato. Akaridhia kimoyomoyo na kumuuliza Butu, "Hapo kwa shangazi Suzy palikuwa na watu wengi?"

    "Uani walikuepo watu wakinywa mapuya, lakini sisi hukaa ndani, chumbani mwake shangazi."

    "Hamkuwa na watu humo chumbani?"

    "Hamkuwa na mtu mwingine zaidi ya Shangazi."

    "Enhe, ikawaje?"

    "Tukaagiza bia na kuanza kunywa."

    "Kisha?"

    "Muda mfupi baada ya saa kumi nikajisikia ovyo; nikaamua kuondoka."

    "Una maana gani - 'ukajisikia ovyo?' Ulijisikia vibaya? Ulihisi kuumwa?" Denny akamuuliza.





    "Si kuumwa hasa,"Akajibu Butu. "Nilihisi kupachoka mahali hapo, kama vile palinikifu."

    "Ukaondoka peke yako?"

    "Ndiyo. Bob alikuwa na makubaliano fulani na huyo shangazi, mara kadhaa nimeshawai kumwacha hapo. Hivyo halikuwa jambo la ajabu. Niliondoka na kumwacha hapo akiendelea kunywa."

    "Wewe ukaenda wapi?"

    "Mimi nikaenda Lulu, nikitazamia pengine Bob angekuja baadae kujiunga nami."

    "Akaja?"

    "Hapana, hakuja. Nilipomuaga hapo kwa shangazi Suzy ilikuwa ndiyo mara yangu ya mwisho kumuona akiwa hai."





    "Wewe ulirudi Laini saa ngapi?"

    "Kwenye saa tano."

    "Ukaenda kwenye kota ya Bob?"

    "Ndiyo."

    "Alikuwepo?"

    "Hapana, hakuwepo."

    Ukafanya nini?"

    "Nikaenda kulala."

    "Hukuingiwa na wasiwasi?"

    "La, sikuwa na wasi wasi. Kwanza ilikuwa bado mapema. Siku zingine tulirudi saa sita au saba. Hata saa nane za usiku. Na pilihalikuwa jambo geni kwa Bob kulala nje, wakati mwingine palepale kwa shangazi.





    "Asubuhi je, ulikwenda kumtazama?"

    "Ndiyo,"

    "Ulipoona hayupo, bado tu hukuwa na wasiwasi?"

    "Niliingiwa na wasiwasi kidogo, kuona angechelewa kuripoti kazini."

    "Hukuwa na wasiwasi kwamba pengine kafikwa na jambo?"

    "Hapana, wasi wasi huo sikuwa nao."

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Bessy akaacha kuandika. Akashusha pumzi na kuuliza, "Huyo shangazi Suzy anakuhusu?"

    Akajibu Butu haraka,"Hapana, kila mtu anamwita hivyo. Na nyumbani pake panaitwa kwa Shangazi Suzy."

    "Yukoje?"

    "Ni mama wa makamo, wa miaka kati ya thelathini na tano na arobain, na ana mwili."

    "Umesema anauza nini na nini?"

    "Ni bia na mapuya. Ni pombe ya kienyeji inayotengenezwa kwa ulezi na mahindi au mtama."

    "Una hakika anauza vitu hivyo tu?"

    "Sijakuelewa afande."

    "Una hakika hauzi vitu vingine kama vile gongo,bangi, madawa ya kulevya?"

    "Hapana afande, hauzi."

    "Una hakika?" Bessy alisisitiza. "Ujue tutakwenda kuvamia na kumpekua, na baadaye kumhoji."

    "Ah,nasikia anauza gongo siku moja moja."

    "Na hivyo vingine? Unga? Bangi? Madawa ya kulevya?"





    "Kama hivyo navyo anaviuza, basi anafanya hivyo kwa siri sana. Sina habari navyo."

    Bessy akaandika haraka kisha akasema, "Sasa nataka ulijibu swali hili kwa makini sana. Kumbuka vizuri sana, kisha ndipo ujibu. Je, ulipomwaga Bob ulimwacha humo ndani akiwa peke yake au akiwa na watu wengine?"

    Butu akataka kujibu,akasita.





    "Kumbuka vizuri," Bessy alirudia. "Ni lazima utoe jibu sahihi. Jibu lako likitofautiana na huyo shangazi, na ikija kugundulika kuwa jibu lake ndilo sahihi, ndugu yangu hizo V zitakuwa si zako tena, kwani hutastahili kuitwa Koplo."

    Butu akaanza kupumua kwa taabu, na vitone viwili au vitatu vya jasho vikimuota usoni. Hatimaye akasema kwa sauti ya kulazimisha, "Alikuwapo mtu mwingine,"

    Ghafla Bessy akaketi mkunjuko,kama aliyeguswa sehemu nyeti.

    "Ni nani mtu huyo?"

    "Kikoti."Alinong'ona Butu.













    "You are nuts. Plain nuts." Sam Kembo alibweka.

    "Ndiyo! Wewe ni chizi kabisa."

    "How dare!" Kassim akafoka, macho yakiwaka moto. "Unathubutuje kuniambia hivyo, we tumbili mweusi?"

    "Nathubutuje?" Kembo aliuliza kwa mshangao. Kisha akakiangua kicheko.Alianza kidogo kidogo kama mzaha. Kisha akakiachia. Akacheka, akacheka, akacheka.





    "Good - Kembo ! Umeehuka nini?" Kassim aliuliza .

    Kembo akatikisa kichwa, akajitaidi kujizuia. Hatimaye akasema. "Mwenye kasoro ni wewe rafiki yangu, tena kasoro kubwa. Siyo mimi."

    "Mimi? Nina kasoro gani?"

    "Tena kubwa." Kembo alirudia.

    "Hivi bado tu hujatambua kuwa enzi za ufarao wako imekwisha?"

    "Una maana gani?"

    Kembo akatikisa tena kichwa.





    "Lazima ukubaliane na ukweli, Kessy kitendo ulichokitenda jana ni cha kipumbavu kweli kweli. Hata taahira asingeweza kukifanya. Sasa hapo ulipo upo katika lindi la tope hadi shingoni. Na hakuna wa kukusaidia isipokuwa mimi. Hivyo, rafiki yangu, wewe kwangu mimi si chochote isipokuwa ni toto la bandia katika mikono yangu."

    "Umemaliza?" Kassim akauliza.

    "Una maana gani, 'nimemaliza' - unadhani ninadhihaki?"

    "Tatizo lako rafiki yangu, ni kwamba elimu yako ni duni sana, hivyo fikra zako ni finyu. Hivi hufahamu kuwa wewe uko katika hali mbaya zaidi kuliko mimi?"

    "Mimi? Niko katika hali mbaya zaidi?"

    "Mtu niliyemgonga mimi," Kassim alifafanua. "Hajafa... na inaelekea hatakufa kutokana na ajali ile. Lakini wewe umemuua yule askari na Kikoti."





    "Ni mimi niliyewaua?" Kembo aliuliza.

    "Unadhani Chiko na Fensy watakubali kunyongwa peke yao?"

    "Ni kauli yao dhidi yangu."

    "Wawili kwa mmoja? Na hawa hawawezi kukosa marafiki wa kuwaunga mkono na kuongeza na kuongeza uzito kwenye mizani." Kembo akabaki mdomo wazi.





    "Unaona, rafiki yangu." Kassim akaendelea, "Kama mimi nipo ndani ya lindi la tope hadi shingoni, wewe upo katika lindi la mimavi hadi kidevuni. Mwenzako nina pesa, na simaanishi pesa za madafu. Nna pesa za kimataifa. Dola za Kimarekani, pauni za Kiingereza, Yuro, Yen za Kijapani, zote hizo zimetulia kwangu. Popote ukinigusa unatekenya pesa mtakato. Kokote kule naweza kwenda kujisweka na kuishi maisha yangu yote. Wewe je? Nina mashaka hata kama una milioni kumi za madafu."





    Kassim akaliweka sigara lake mdomoni, akalivuta na kuupuliza moshi taratibu. Akatikisa kichwa na kusema, "Hapana, rafiki yangu, wewe umo ndani ya lindi la haja kubwa."





    **************************************





    Bessy hakumsikia Butu. Akamuuliza, "Ni nani?"

    "Kikoti." Akarudia Butu. Safari hii kwa sauti ya kusikika, na akipumua vizuri tena. "Anaitwa Kikoti."

    "Ni nani yeye? Ni mteja wa kila siku hapo kwa shangazi?"

    "Ndiyo, afande."

    "Ni rafiki yenu?"

    "Si rafiki hasa. Alipenda tu kukaa na sisi. Ni ile aina ya watu duni wanaopenda kujipenyeza kwenye vikundi vya watu wasio daraja lao. Hata mazungumzo yao huwa duni. Sijui kama umenielewa."





    "Nadhani nimekupata." Alisema Bessy. Akaongeza, "Bob aliuwawa pamoja na mtu mwingine. Mtu huyo ni mwembamba, mfupi na alivaa koti dogo lililochakaa. Je, anaweza kuwa ndie Kikoti?"

    "Ndiye." Alikubali Butu akisisitiza kwa kichwa.

    "Una uhakika?"

    "Ndiyo. Nilipokwenda hospitali kumtazama Bob nikataka kujua ni nani huyo aliyekufa naye. Nikakuta ni Kikoti."

    "Sawa. Sasa tueleze kila kitu ukijuacho kuhusu huyo Kikoti."

    "Sijui chochote." Alisema Butu.

    "Yeye ni mgeni hapo kwa shangazi? Jaribu kukumbuka vizuri, tuko giza kuhusu mtu huyo. Mfukoni mwake hamkuwa na kitambulisho wala kitu chochote cha kutufahamisha yeye ni nani. Hujui alikuwa anafanya kazi gani na wapi?"





    "Sijui." Alijibu Butu. "Sidhani kama alikuwa na kazi maalimu. Nadhani alikuwa akidaka kibarua hapa na pale."

    "Mahali alipokuwa akiishi je?"

    "Sikujui."

    "Bob alikuwa na desturi ya kumpakia katika gari lake?"

    "Hapana."

    "Sasa jana kwa nini akampakia."

    "Sijui."

    "Unayo habari kuwa maiti yake ilikutwa katika gari la Bob?"

    "Ndiyo nimeambiwa hivyo."

    "Dennis akadakia, "Sikiliza Koplo, hebu twende hatua kwa hatua. Ni nani aliyetangulia kufika hapo kwa shangazi Suzy, ni wewe na Bob au yeye Kikoti?"

    "Sisi."

    "Kikoti akawasili wakati gani?"

    "Muda mfupi tu baadaye."

    "Akafanya nini, au akasema nini?"

    "Akaagiza bia?" Butu akasita

    "Akaagiza mapuya?" Dennis akauliza.

    "Hapana..."

    "Kumbe akafanya nini?" Sauti ya Denny ilipanda kidogo kwenye neno la mwisho. Akaongeza "Alikaa tu kama sanamu?"

    "Hapana."





    "Butu," Bessy akaita kwa sauti ndogo, "Hii ni kesi ya mauaji . Hupaswi kuficha kitu. Sema waziwazi. Kikoti aliagiza nini?"

    "Hapana."

    Huku akiinuka Denny akasema, "Unahitaji makofi mawili matatu ndipo uchangamke?"

    Bessy akamzuia Denny kwa ishara ya mkono, na wakati huohuo akimfokea Butu, "Koplo! Kikoti! alimuagiza nini huyo shangazi aliyelaaniwa? Gongo? Unga? Kitu gani?"





    "Hakumuagiza kitu." Butu akajibu, "Alikuja na chupa yake."

    "Chupa ya nini?" Bessy akauliza.

    "Ya wisk."

    "Sasa ulikuwa unasita nini?"

    Butu akasita tena kabla ya kusema, "Chupa hiyo ... chupa hiyo ilikuwa ya wizi."

    "Koplo." Bessy akamwambia, "Katika kesi ya mauaji hapana kuficha kitu. Nikigundua kuwa kuna kitu kingine unajaribu kuficha, utatoka humu bila V zako na pingu mikononi. Sasa tueleze kila kitu kuhusu hiyo chupa.





    "Kikoti alikuja nayo katika mfuko wa karatasi. Akaitoa, akaiweka mezani na kutukaribisha. Tukamwomba shangazi glasi tupu."

    "Kisha?"

    "Baada ya muda mfupi nikaondoka."

    "Kabla au baada ya kuimaliza chupa hiyo?"

    "Kabla."

    "Kwa nini, wewe hutumii wisk?"

    "Natumia.

    "Sasa kwa nini ukaondoka na kuwaacha wenzako wakiendelea?"

    "Nilijisikia ovyo."

    "Kama ulijisikia ovyo, ungeenda nyumbani au ungeenda maktaba au mpirani au kokote kule. Usingeenda Lulu na kuendelea kunywa, tena peke yako." Butu hakijibu.









    "Koplo," Denny akamwita, "Hebu niangallie," Butu akainua uso na kumwangalia.

    "Je," Denny akamuuliza, "Nna sura ya zumbukuku?"

    "Sijakuelewa."

    "Nafanana na pimbi?"

    "Hapana."

    "Je, Inspekta Bessy anafanana na pimbi?"

    "Hapana."

    "Basi tafuta hadithi nyingine tupigie. Hiyo katafute pimbi uwapigie."



    http://pseudepigraphas.blogspot.com/







    "Akh, huoni kuwa tunazungumza kama machizi wawili?" Sam Kembo aliuliza kwa karaha. Kassim Hashir akainua mabega. "Ni wewe uliyeleta kauli ya kutishana. Sijui jeuri hiyo umeitoa wapi?"

    Akaliweka sigara lake mdomoni na kulivuta kidogo. Akaendelea, "Ukitaka tukubaliane na ukweli, ukweli ni kwamba mimi na wewe tunahitajiana. Mimi nakuhitaji wewe, na wewe unanihitaji mimi zaidi kuliko mimi ninavyokuhitaji wewe."





    Kembo akajiwashia sigara nyingine. Akasema, "Ukweli ni kwamba sote tumo ndani ya lindi la choo, na ni wewe uliyenitumbukiza humo."

    "Kwa ujira na ridhaa yako mwenyewe." Kembo akatahayari na kuyatazama maji ya bwawa yaliyong'arishwa na jua la asubuhi. "Jambo la busara kufanya sasa ni kujitoa katika lindi hili." Aliendelea Kassim. "Naamini tunaweza kufanya hivyo iwapo tutavitumia vizuri vichwa vyetu. Hebu tuangalie tatizo moja moja. La kwanza ni huyo Daktari mstaafu ambaye angali hai na analindwa masaa ishirini na nne."





    "Ndiyo,lakini yuko taabani. Sidhani kama anaweza kusema lolote la maana leo au kesho. Na akisema amegongwa na Kassim Hashir sidhani kama watamsadiki. Kassim Hashir alifia huko Kenya miaka kadhaa iliyopita. Ulimgonga bure kabisa yule mzee."





    "Nakwambia nakubali nilifanya kosa. Nakwambia nilitaharuki. Wewe hujawai kutaharuki? Na mahali penyewe palikuwa pazuri. Uchochoro ulikuwa mtupu kabisa. Na sikutazamia kama angepona. Laiti angekufa palepale mambo yengeishia pale pale. Hata wewe yasingekuhusu."





    Kembo akatikisa kichwa. "Hapana, rafiki yangu, siyo kutaharuki kulikokufanya umpamie yule mzee. Wewe una asili ya ujahili. Wewe husikia raha kujerui, kuumiza, kutoa roho. Wapo watu wa aina hiyo. Wawili wengine niliotokea kuwafahamu walikuwa Hitler na Iddi Amin."





    "Ah, ya Hitler na Idd Amin tuwaachie Hitler na Iddi Amin. Tuangalie yetu. Ya kwetu yanatutosha bila kujitwisha ya wengine."

    "Enhe,tatizo la pili?"

    "Tatizo letu la pili liko kwa huyo Fensy. Si umesema akibanwa na kutikiswa kidogo anaweza akayaleta mambwa hadi hapa?"

    "Kwa nini usihame hapa?"Kembo aliuliza. "Kwa nini usiliuze jumba hili na kununua au kupanga mahali pengine?"

    "Sam, wakati mwingine huwa unazungumza kama mtoto mdogo."

    "Kwa nini?"

    "Tatizo langu sio dogo kiasi hicho. Tatizo langu sio kujificha tu. Tatizo langu ni kungundulika mimi ni nani."

    "Yaani kujulikana kuwa wewe ndiye Kassim Hashir?"

    "Hapana, kujulika Habib Kessy ndiye nani."

    "Mbona sikuelewe!"

    "Unaijua kampuni iitwayo H.K. International?"





    "Nani asiyeijua? Ni kampuni kubwa ya kimataifa inayouza magari ya Kijapani na bidhaa toka Ulaya." Akapiga pafu jingine refu la sigara kisha akaupuliza hewani moshi huku akiutazama unavyoyeyuka hewani, macho kayaminya. Kisha akaendelea, "Na inapeleka bidhaa Ulaya toka Afrika, kama vile pamba,buni, tumbaku na hata dhahabu na madini mbali mbali." Kembo alisema.





    "Swadaktaa!" Kassim aliitikia na kuuliza, "Je, unamjua mwenye kampuni hiyo?"

    "Hapana, simjui."

    "Mwenyewe ni H.K." Kembo akabaki na sura ya kifal@fal@.

    "Sam," Kessy akamwita, "Bado tu hujazibuka masikio?"





    Ghafla Kembo akakunja uso. Akasema, "Kess - Habib, unataka kunambia, kunambia..." Kassim akakubali kwa kichwa.

    "Mungu wangu - Ka!"

    "Sawa kabisa. Hicho ndicho kizingiti chenyewe. Hata mwenyewe wakati mwingine hunitoka." Kembo akatikisa kichwa akisema, "Nilijua kuwa wewe una pesa, lakini kha! H.K. Habib Kessy! H.K.Internatioal! Nani angetegemea? Kha!





    "Ibrahim Mbelwa alikuwa rafiki yangu mkubwa, pamoja na kunizidi umri kwa miaka kumi." Kassim alisimulia, "Ajabu yenyewe ni kwamba tulikutana dansini, wakati huo nikiwa ningali nasoma Chuo Kikuu,na yeye akiwa Sajini meja Jeshini. Alipenda sana wasichana warembo 'dogodogo' kama mimi, lakini yeye alikuwa hajui kutongoza, ambapo mimi nilikuwa kama sumaku kwa wasichana. Hivyo tukawa marafiki wakubwa.





    "Mbelwa alipopora madaraka na kujitangaza Rais, hapakuwa na mtu mwingine aliyemwamini kuliko mimi. Akanifanya waziri nisiye na wizara maalumu. Kazi yangu kuu ilikuwa kutafuta fedha za kigeni kwa njia yoyote ile na kuzipeleka Ulaya. Kazi hiyo aliyonipa niliifanya vizuri sana." Kassim aliendelea "Katika miaka michachealiyotawala kimabavu nilitorosha mamilioni ya Dola, Pauni na kila pesa ya kigeni yenye kuthaminiwa kimataifa.

    Na wala sikuziacha zitulie benki. Nikaanzisha H.K.International. Sikuwa na nia mbaya. Siku yoyote Ibrahim ingehitaji pesa ningempatia, na faida juu. Hata kwa kuiuza au kuiua hiyo kampuni, kama unavyojua, aliuwawa alipopinduliwa. Na kibunda chote kikawa changu peke yangu. Naam. Peke yangu kabisa."





    Kembo akapumua kama aliyetua mzigo na kusema, "Una mwiko wa kutokunywa asubuhi? Kisa chako kimenikausha koo. Kha! Kuna mijitu yenye bahati duniani!"

    Kassim akatabasamu. "Na wala si asubuhi tena." Akasema, akiitazama saa yake, Rolex ya dhahabu. "Inakaribia saa tano. Kinywaji changu cha saa hizi ni Gin na Tonic. Je, na wewe utatumia kinywaji gani?"

    "Hiyohiyo Gin na Tonic itatosha."

    Kassim akaita, "Kijana!" Mara mtumishi akatokea. "Jin na Tonik tafadhali." Kassim akamwambia.





    Baada ya huyo mtumishi kuleta chupa ya Jin na chupa mbili za soda chungu na kuondoka, Kembo akauliza, "Sasa tatizo lako liko wapi?"

    "Nyumba hii niliinunua kabla ya kurudi hapa nchini." Alijibu Kassim. "Aliinunua wakili wangu kwa niaba ya H.K.International. Hivyo, hata kama sipo, polisi wakiivamia watagundua kuwa nyumba hii ni mali ya kampuni hii."

    "Kwa hiyo?"

    "Sisemi kwamba polisi wetu wana mbongo zinazovuja masikioni. Lakini anaweza katokea chakaramu mmoja akaweka mbili na mbili na kupata jibu sahihi, yaani nyumba hii ni ya H.K.International. Na anayeishi hapa ni Habib Kessy."

    "Kwani pana ubaya gani ikigunduluka Habib Kessy ndiye mmiliki wa H.K.International?"

    "Lahaula! Sam, mpaka nikuchoree picha? Iwapo yule Daktari atasema kagongwa na Kassim Hashir, na kama polisi watagundua kuwa Kassim Hashir anaishi hapa, watagundua kuwa Habib Kessy ndiye Kassim Hashir. Na wakigundua kuwa Habib Kessy ndiye Kassim Hashir nimekwisha."

    "Kivipi?"





    "Kila kitu. Vile Kassim Hashir alikuwa akitafutwa na serikali ya nchi hii kwa kuhujumu uchumi na kutorosha fedha za kigeni na kuwa ndiye aliyesababisha vifo vya watu wawili watatu enzi zile - na sasa kuna shitaka jingine la kujaribu kuua kwa gari. Si tu kuwa nitakuwa na kesi mbaya ya kujibu hapa bali hata Interpol itaingilia kati jambo ambalo litasababisha kuchunguzwa kila tawi la kampuni yangu Afrika na kote duniani. Matokeo yake akaunta zangu zote popote ziliko zitapigwa tanchi. Hakuna cha kutoka, ila kuingia tu. Na mimi mwenyewe nitasakwa kila pembe ya dunia na hali nikiwa hohe hahe. Kwani kifedha, rafiki yangu mpendwa Sam, mimi na wewe tutakuwa hatuchekani."





    "Gosh, Kessy, sikujua kuwa mambo yanaweza kuwa mabaya kiasi hicho."

    "Sasa unaona kwa nini jana nikataharuki na kumgonga yule mzee? Picha ya kupatikana kwangu ilinijia mbele ya macho yangu. Ni miaka mitano sasa tangu nirejee nyumbani, baada ya kuhakikishiwa na watu kadhaa, mmojawapo akiwa bosi wako, kwamba nimeshasahauliwa kikamilifu. Kuwa asingetokea mtu mwenye shida na mimi. Sasa katokea mtu huyo.Basi ni dhahiri wapo wengine, isipokuwa wanaamini nimeshakufa. Wakizibuliwa masikio watajitokeza. Watataka wanikodolee macho na kunitoboa kwa madole yao ya shahada."





    Baada ya kugida, Kassim akaendelea. "Nimekueleza yote hayo ili ujue hali halisi na msimamo ulivyo. Mimi ni mtu mhimu sana katika chama chenu na mstakabali wa taifa hili. Huwezi kuniongopea kuwa kuna mfadhili mwingine anayewasaidia au atakaeweza kuwasaidia kama ninavyowasaidia mimi. Hivyo nikiyoyoma ujue nchi imekwisha. Mmekwisha kabisa.Nyote kaputi."





    *************************************





    Baada ya kimya kifupi, kachero Inspekta Bessy akasema, "Tatizo lako Butu ni kuwa hujui kuongopa. Ni dhahiri kabisa kuwa wewe hukuondoka hapo kwa shangazi Suzy kwa sababu ya kujisikia ovyo. Inaelekea palitokea kutoelewana kati yako na Bob au na Kikoti. Au na huyo shangazi."

    "Hataa..." Butu alijaribu kukanusha,akiangalia chini, lakini sauti yake ilikuwa ndogo na isiyo na nguvu.

    "Je, Bessy akauliza, "Ni kuhusu hiyo chupa ya wisk ya wizi?"

    Butu akakawia kujibu, Denny akasema, "Wewe ulijuaje kuwa chupa hiyo ni ya wizi, au Kikoti mwenyewe aliwaeleza hivyo, na hali mkiwa askari? Au hakujua kuwa ninyi ni askari?"

    "Nadhani alijua."

    "Hata hivyo bado akajigamba kuwa chupa hiyo kaiiba?"

    "Yeye hakusema kaiiba, ila mimi nilishuku tu."

    "Kwa nini?"

    Butu hakujibu.

    "Yeye alisema kaipata wapi?"

    "Alisema kapewa."

    "Na nani?"

    "Na... na tajiri yake."

    "Lakini wewe hukuamini?"

    "Sikuamini."

    "Kwa nini?"

    Butu hakujibu.

    "Kwani wisk ilikuwa ya aina gani?"

    "Sijui, sikumbuki. Ni ya kutoka ng'ambo."

    "Ghali?"

    "Bob alisema ilikuwa ghali sana."

    "Ilikuwa chupa ya ukubwa gani?"

    "Ya wastani."

    "Ilikuwa nzima, au ilikuwa imeshafunguliwa?"

    "Ilikuwa imeshafunguliwa. Ilikuwa nusu chupa."

    "Na wewe ukashuku kuwa kaiiba?"

    "Ndiyo."

    "Hicho ndicho kilichokuondoa hapo?" Denny aliuliza.





    Butu akasita kisha akakubali kwa kichwa.

    Bessy akatikisa kichwa. "Bado tuko mbali kabisa," Alisema akaita, "Butu, acha nikukumbushe tena Hii ni kesi ya mauaji. Sijui kama sababu iliyokuondoa hapo kwa shangazi Suzy ina uhusiano au haihusiani na kuuawa kwa Bob na Kikoti, lakini ni kazima nijue. Hivyo hutoki humu ndani mpaka umenieleza."





    Ikapita dakika nzima ndipo tone la kwanza likamdondoka Butu, huku akisema, "Niliwakataza ! Naapa niliwakataza! Lakini hawakunisikia!"

    Deny na Bessy wakatazamana na kuafikiana kwa macho. Wakampa Butu dakika tatu za kutanua mbavu, kupenga na kujifuta uso. Kisha Bessy akamwamuru, "Anza tangu mwanzo."





    Lakini zikapita dakika tatu nyingine, ndipo Butu alipoweza kujizatiti kikamilifu. Akainuka, akasimama mbele ya meza ya Bessy na kupiga saluti ndefu. Kisha akaivua kofia na kuiweka mezani. Akauvua mkanda na kuuweka mezani. Akazivua V na kuziweka mezani, kisha akarudi kuketi na kuanza kuzungumza.











    "Ninachohitaji ni muda." Kassim Hashir aliendelea. Muda wa kubadili kila kitu. Kumuua Habib Kessy na kampuni yake na kuibuka mtu mpya na kampuni mpya yenye shughuli tofauti kabisa na shughuli za H.K.International."

    "Utaweza kufanya hivyo?" Kembo akauliza.

    "Kwa nini nisiweze. Iwapo kwanza nilikumuua Kassim Hashir? Ninachohitaji ni muda tu."

    "Muda gani?"

    "Mimi kugeuka mtu mwigine si tatizo. Nina paspoti nyingine maalum kwa dharura kama hii. Lakini kuuza na kufungua kampuni nyingine kubwa kama H.K.International na akaunta zake kutachukua muda."

    "Ndiyo. Muda gani?"

    "Kwa vyovyote vile siyo chini ya mwezi mmoja, pengine miwili."





    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    "Jesus!"

    "Jambo hili limetokea wakati mbaya sana. Tatizo ni kwamba kwa sasa ninabidhaa nyingi kuliko fedha taslimu. Na bidhaa nyingine ziko njiani. Kuna meli nzima ya makontena toka Ulaya bado haijawasili. Kuna meli nyingine ina magari zaidi ya miambili kutoka Japani iko njiani. Meli nyingine mbili zina malighafi toka Afrika bado hazijatia nanga Ulaya. Vitu vyote hivyo vina thamani ya mamilioni kwa mamilioni kama si mabilioni ya pesa za kigeni. Na sina ujanja hadi vifike vinakokwenda. Kama ni Mungu amepanga jambo hili litokee wakati huu ni yeye pekee anayejua. Nahitaji muda vibaya sana."





    "Mambo yakituchachia," Kembo akasema. "Hapatakuwa na muda wowote."

    "Hayawezi kutuchachia iwapo tutavitumia vichwa vyetu wenyewe vizuri. Wa kuwashughulikia ni wawili tu. Fensy na huyo Daktari mstaafu."

    "Umemsahau mtu wa tatu."

    "Mtu wa tatu?" Kassim aliuliza.

    "Ndiyo. Huyo kijana X aliyempeleka Dikwe Uwanja wa Gofu."

    "Oh!"

    "Lakini yeye si tishio. Kamuonea Dikwe kwa sababu Dikwe alikuwa pusha wa kawaida tu, tena mwanafunzi aliyetegemea kisu. Hakuwa katika daraja la Chiko na Fensy."

    "Kwa hiyo?"

    "Ni moja kati ya mawili kwa kijana huyo. Anunuliwe au alipuliwe chaguo ni lake."

    "Kwa hiyo tatizo liko kwa Dokta Makete ?" Kassim aliuliza.

    "Hapana. Tatizo lipo kwa Fensy. Ni kweli akishikwa mambo yanaweza kuwa mabaya."

    "Kwa nini asifikwe na 'ajali'?"

    "Nitafikiria. Kwa sasa atapiga mbizi. Sitaki kupoteza wangu ovyo. Nilipo nina pengo la mmoja."

    "Hoza."

    "Ndiyo."





    Baada ya kupuliza moshi angani, Kassim akasema, "Umesema huyo Dk .Mstaafu si tatizo?"

    "Si tatizo. Nilifanya kosa pale mwanzo kumtuma Hoza aende hospitalini na kibweka. Nilipaswa kumpeleka Daktari wa bandia."

    "Na sindano ya sumu?"

    "Yes."

    "Good. I'll fix you up with BMV - Black Mamba Venom. Hutumiwa na Vets [Madaktari wa wanyama] kuwaulia mbwa,farasi n.k. wenye maumivu makali ambao hawana matumaini ya kupona. Ni safi sana. Sekunde thelathini, garantii."





    *****************************





    Kwa sauti madhubuti kabisa Butu akasema, "Humo chumbani mwa shangazi mna radio. Katika taarifa ya habari ya saa kumi ilitangazwa ajali ya Dk.Makete. Ikatangazwa ile zawadi ya milioni moja kwa yeyote atakayemtaja mtu aliyemgonga Dokta huyo. Kikoti akapandwa na jazba, akidai anamfahamu mtu huyo. Na kuwa ndiye mwajiri wake. Akatuomba tumsaidie kuipata hiyo zawadi."





    Bessy na Dennis wakatazamana, macho ya msichana huyo yakiwaka moto kwa ghadhabu. Dennis akarudisha macho kwa Butu na kumwambia, "Endelea."

    "Bob akaingiwa na tamaa. Akataka kujua kama huyo mwajiri wake alikuwa tajiri wa kuweza kutoa milioni mbili au tatu za kufumba mdomo. Kikoti akamhakikishia kuwa ni tajiri sana, na kwamba angeweza kutoa hata zaidi. Bob akasema basi ya nini kudai milioni ikiwa wanaweza kupata milioni mbili au tatu.

    "Nikajaribu kuwakataza." Butu akaendelea, "Naapa niliwakataza, lakini hawakukubali. Bob akanambia niachane nao na nisimwambie mtu yeyote. Nikaondoka na kuwaacha."





    Bessy akatikisa kichwa. "Butu, Butu, Butu! Na ukabaki kimya kweli!"

    "Ningefanyeje, afande? Bob alikuwa rafiki yangu mkubwa. Nisingeweza kumsaliti. Lakini baada ya kuwaza usiku kucha nilipania kumlazimisha aje kukuona asubuhi. Angekataa, mimi ningekuja kuripoti. Lakini asubuhi hakuwepo nyumbani kwake. Na nilipofika hapa kituoni nikapata habari kuwa kauwawa. Nikapapatika, nisijue la kufanya."

    "Unajua ni lazima nikuweke ndani na kukufungulia shitaka la kuficha siri za uhalifu?" Butu hakujibu. "Kwa vyovyote vile" Bessy akaendelea, "Umeshakwishapoteza kazi yako. Hustahili kuwa askari."





    Denny akauliza, "Ni nani huyo mwajiri wa Kikoti?"

    "Simjui." Butu akajibu kinyonge. "Kikoti alimwita Bwana Kessy. Jina hilo moja tu."

    "Kwa hiyo uliongopa uliposema hakuwa na kazi maalumu?" Bessy akauliza.

    "Hapana hata kwa huyo Bwana Kessy nadhani alikuwa kibarua tu. Hakuwa na muda mrefu hapa jijini."

    "Alikuwa anafanya kazi gani kwa huyo Kessy?"

    "Nadhani alikuwa mtumishi wa nyumbani."

    "Sehemu gani hiyo?"

    "Nadhani itakuwa Buffalo Hill."

    "Nadhani. Nadhani. Nadhani. Ni msaada mkubwa kweli kweli !" Bessy alifoka. Akaongeza, "Na alipokuwa akiishi Kikoti hukujui?"

    Butu akatikisa kichwa.

    "Ona sasa! Katika kuogopa kumsaliti ndugu yako, umeyaponza maisha yake!"

    "Najuta sana, afande, najuta sana."

    "Majuto ni mkuu." Bessy alisema kwa ghadhabu.

    "Hayasaidii chochote. Angalia ulivyoboronga! Tulikuwa na nafasi ya kuwabamba wote. Huyo aliyemgonga Dk.Makete, hao wauaji, huyo Bob pamoja na Kikoti wake. Na sasa tuko wapi? Pale pale tulipoanzia!"





    "Butu," Denny aliita kwa sauti tulivu kabisa. "Unadhani kitu gani kilitokea pale kwa shangazi Suzy baada ya wewe kuondoka?"

    "Sijui,Luteni."

    "Hukuisikia mipango ya Bob na Kikoti?"

    "Hata kidogo. Sikutaka kujihusisha na mipango ya kifumba mdomo."

    "Afadhali ungesuburi uisikie mipango yao pengine tungejua anapoishi huyo mlaaniwa!" Bessy alilalama.





    Kama vile msichana hakuwa amesemalolote, Denny akaendelea kwa sauti yake tulivu. "Tunafahamu kuwa mtu aliyemgonga ni Kassim Hashir, lakini anatumia jina jingine. Jina Kassim Hashir lilishakufa siku nyingi. Umenielewa Butu?"

    "Ndiyo, Luteni."

    "Sasa, kama mwajiri wa Kikoti ndiye aliyemgonga babangu na naamini ndiye, ama sivyo Bob na Kikoti wasingeuwawa. Na kama mwajiri wa Kikoti anaitwa Kessy,basi ndiye Kassim Hashir. Sawa Butu?"

    "Sawa, Luteni."

    "Ni jambo linalofahamika dhahiri kuwa Kassim Hashir, kwa jina jingine Kessy ni mtu mbaya kweli kweli. Ni mnyama. Na anawakora wauaji. Watatu tunawafahamu. Chiko,Fensy na Hoza. Huyo wa tatu sasa ni marehemu. Inspekta Bessy akamuwahi. Je, haikujii akilini mwako kuwa waliowaua Bob na Kikoti ni Chiko na Fensy?"

    "Inawezekana kabisa." Alikubali Butu.





    Denny akamtazama Bessy na kumwambia, "Tafadhali uliza chumba cha kumbukumbu kama wana faili la Fensy" Bessy akainua simu na kuzungumza na masijala. Kisha akaurudisha chini mkono wa simu,akitikisa kichwa. "Hawana."

    "Si kitu." Alisema Denny. "Waambie makachero wako waanze kuwasaka Chiko na Fensy."

    Bessy akainua tena mkono wa simu.









    Walikuwemo watu watatu katika gari la Kembo. Yeye Kembo mwenyewe, akiendesha na Chiko aliyeketi kando yake, na Fensy aliyeketi kiti cha nyuma.

    "Tumejadili kwa kirefu swala hili na Bwana Kessy." Alisema Kembo, "Na kufikia maamuzi kadhaa. Jambo mhimu ni kwamba ni lazima mjihadhari. Kama Dikwe amewataja, mnaweza kuwa mnatafutwa na polisi."



    "No sweat." Alisema Chiko. "Haitakuwa mara yao ya kwanza kunitafuta. Na kunikosa."

    "Hata hivyo ni lazima mjihadhari." Alisisitiza Kembo. "Msizurure ovyo. Chiko, bila shaka picha yako wanayo. Fensy je?" Fensy akatikisa kichwa, akasema, "Hawana."

    "Good. Jambo la pili ni kuhusu yule kijana aliyempeleka Dikwe kule Uwanja wa Gofu. Angali ananitia wasiwasi."

    Chiko akasema, "Vile n'na imani kuwa atarejea pale Tupetupe, kuna wazo lililonijia."

    "Wazo gani?"

    "Unajua, lile jengo linalotazamana na Tupetupe Hotel, lina vyumba vya kukodi ghorofani. Panaitwa Flamingo. Nataka nichukue chumba kimoja cha mbele. Kisha nitamchukua Chox akae dirishani na kusubiri. Kijana huyo akitokea nataka anionyeshe. Kumjua adui ni nusu ya kushinda vita."



    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    "Sawa. Lakini akikubali kununuliwa ni bora tumnunue."

    "Ok."

    "Sasa kuhusu yule Daktari mstaafu," alisema Kembo. "Bwana Kessy amenipatia sindano na kichupa cha black mamba venom. Kifo katika nukta thelethini tu. Haiogopi wala haikopeshi. Tunachokihitaji ni Daktari wa bandia tu."

    "Chox anatosha. Hakuna wa kumpata kwa kugeresha. Kuna wakati hujifanya askari na kuwashika askari wa kweli kweli."





    ************************************







    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog