Search This Blog

Sunday, 20 November 2022

MSAKO WA HAYAWANI - 5

 





    Simulizi : Msako Wa Hayawani

    Sehemu Ya Tano (5)





    Dennis na Bessy, baada kuelekezwa vizuri na Butu, hawakupa shida kupapata kwa shangazi Suzy. Bessy alilitengua wazo lake la awali la kumvamia na kumpekua kwa kuhofia kukosa ushirikiano na msaada wake. Hivyo wakamwendea kirafiki.

    Wakamkuta chumbani mwake, ndiyo kwanza amalize mlo ambao kwake ulikuwa mchanganyiko wa staftahi na chakula cha mchana. Kipolo cha wali na mchuzi wa samaki, vitumbua, chapati, mayai ya kukaanga na chai.





    Wakabisha hodi, na walipokaribishwa wakaingia. Alikuwa peke yake humo ndani, "Shikamoo, Shangazi,"

    "Marahaba." Sauti yake haikulingana na umbo lake kubwa. "Karibuni." Aliwakaribisha, bila ya shaka akiwadhania ni wateja.

    "Asante." Alisema Bessy, akiufungua mkoba wake na kutoa kitambulisho chake. "Mimi ni Kachero Inspekta Bessy na mwenzangu ni Luteni Dennis Makete."





    Shangazi akataka kuinuka kama vile mto wa sofa ulishika moto ghafla. Bessy akamzuia kwa kumshika bega kirafiki.

    "Hapana Shangazi, keti tu. Tumekuja kuhusu kifo cha Bob." Alisema, naye aliketi akimfanyia Denny ishara Denny afanye hivyohivyo.http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Denny akaketi

    Bessy akauliza, "Unayo habari kuwa Bob na Kikoti wameuawa?"

    "Ndiyo." Alijibu shangazi. "Butu alipitia hapa alipotoka hospitalini kuziona maiti."

    Denny akauliza, "Alitaka nini?"

    "Sijui. Kunitaarifu, bila shaka. Lakini alikuwa na wasiwasi na akibabaika kama-kama..."

    "Kama aliyeona jini?" Bessy alimsaidia.

    "Naam, kama aliyeona jini." Shangazi alikubali.





    "Hakuuliza chochote?" Denny aliuliza.

    "Alitaka kujua ilikuwakuwaje kama vile mimi nilikuwa pamoja nao katika matembezi yao. Alikuwa akibabaika, akilalamika na akilaani. Hata sikuwa namwelewa. Bila shaka lilikuwa pigo kubwa sana kwake."

    "Hilo limeshatokea. Kilichotuleta ni kutaka msaada wako."

    "Abee?" Shangazi hakumwelewa.





    "Ni kisa kirefu, lakini kwa kuwa tunahitaji msaada wako, ni bora ukifahamu angalau kifupi. Ni hivi. Kuna mtu mmoja tajiri sana na wa hatari sana ambaye anatafutwa na polisi. Yeyete atakaewezesha mtu huyo akamatwe atapata zawadi ya milioni moja. Kikoti akagundua kuwa mtu huyo si mwingine bali ndiye mwajiri wake. Kwa vile yeye ni mbumbumbu akawataka Bob na Butu wamsaidie kuipata zawadi hiyo. Sijui unanielewa?"

    "Nakuelewa vizuri sana."



    "Bob," Bessy akaendelea, "Akaiona milioni moja ni ndogo. Akawashauri wenzake wamdai huyo tajiri kifumba mdomo. Kikoti akaafiki, lakini Butu akakataa. Akajaribu kuwakataza wenzake lakini walimpuuza. Akakasirika na kuondoka."

    "Hivyo ndiyo maana jana aliondoka mapema?" Shangazi aliuliza.

    "Ndyo." Bessy akakubali. "Kudai kifumba mdomo ni kosa la jinai, hata kama huyo anayedaiwa ni mhalifu. Na adhabu yake ni kali. Hivyo Butu hakutaka kushiriki. Lakini ni kosa la jinai pia kuficha siri ya uhalifu. Ukiwa askari kosa hilo huwa kubwa zaidi. Ndiyo maana ukamwona Butu akihaha."

    "Maskini! Sasa yuko wapi?"

    "Yuko ndani. Nimemfungulia shitaka la kuficha siri ya uhalifu. Ilimpasa awaripoti Bob na Kikoti mara moja."

    "Maskini, asingeweza. Bob ni - maskini! - Alikuwa rafiki yake mkubwa."





    "Nafahamu, lakini amekula kiapo cha kipolisi kabla ya kukabidhiwa madaraka, tunaapa kuwa tutatekeleza wajibu wetu ipasavyo hata kama mhalifu ni baba au mama mzazi. Yeye hakutekeleza wajibu wake. Na sasa ona matokeo yake - kapoteza maisha ya Bob na huyo Kikoti."

    Shangazi akatisa kichwa na kuliza ulimi kwa majonzi.

    Denny akamuuliza, "Ni wateja wako wakubwa?"

    "Sana."

    "Hata kikoti?"

    "Hapana. Yeye anamiezi michache tu hapa."

    "Ni lazima tumpate huyo mwajiri wake, ndiye aliyewatuma wakora wawauwe Bob na Kikoti. Humjui ni nani na anaishi wapi?"

    "Mwenyewe husema - hasa anapolewa na kutaka mkopo - anafanya kazi sehemu za Buffalo Hill, kwa Bwana Kessy."





    "Hayo tunayafahamu, katueleza Butu, lakini ni msaada mdogo sana. Buffalo Hill ni eneo kubwa sana. Lina maelfu, kama si malaki ya wakazi. Na jina la Kessy ni la kawaida kabisa. Linatumiwa na watu mbali mbali, waislamu, wakristo na hata wapagani. Bessy akadakia, "Kikoti hakuwai kusema huyo Kessy yukoje. Anakaa mtaa gani, nyumba yake ikoje - chochote kile cha kutusaidia kumpata?"





    Shangazi aliwaza kidogo kisha akasema, "Alewapo aliropoka mengi lakini hakuna aliyemtia maanani. Wakati mwingine mazungumzo yake yaliwakera Bob na But."

    "Jaribu kukumbuka chochote alichoropoka kuhusu huyo mwajiri wake."

    "Mengi ya kipuuzi. Kama vile huyo Bwana Kessy kakaa kizungu zungu, tajiri sana, hubadili magari kama mashati, jumba ni la kifahari lenye bwawa la kuogelea."

    "Hakuwahi kusema lipo mtaa gani?"

    "Nadhani aliwahi kusema lakini sikutia maanani. Ilikuwa ni lugha ya kukopea, kama vile huyo tajiri yake ndiye mdhamini wake."





    "Kama utakumbuka mtaa huo , piga simu Kituo Kikuu uniarifu. Kama sipo acha ujumbe. Jina langu, kama nilivyokwambia, ni Bessy."

    Denny akasema, "Je, kazi ya huyo Kessy, Kikoti hakuwai kuitaja?"

    "Alikuwa akijigamba kuwa bosi wake ni mfanyabiashara wa kimataifa, anasafiri mara kwa mara, hasa nchi za Ulaya. Na wageni wake ni watu wakubwa wakubwa, ikiwa ni pamoja na vigogo wa vyama vya siasa na serikali."

    "Sasa." Alisema Bessy. "Hebu tueleze yote yaliyotokea hapa kwako jana jioni, yaani kati ya Bob na Kikoti."





    "Bob na Butu walitangulia kufika. Bob akaketi hapa na Butu akaketi hapo. Wakaagiza bia. Punde Kikoti naye akaingia. Alikuja na chupa ya wiski. Wakaniomba glasi tupu, nikawapatia. Wakaendelea kunywa. Walinikaribisha nikakataa. Mimi na wiski tuko mbalimbali. Nikaenda uani kuwahudumia wateja wengine. Niliporudi Butu hakuwepo, na Bob alikuwa akiandika namba alizokuwa akipewa na Kikoti."

    "Bila shaka zitakuwa namba za simu ya Kessy." Alisema Denny, "Huwezi kuzikumbuka?"

    "Siwezi. Yalikuwa ni maongezi ya wawili na sikutilia maanani hata chembe."





    "Hukuwauliza Butu kaenda wapi?"

    "Sikuwauliza. Nilijua katoka kidogo. Kaenda kujisaidia au kununua sigara."

    "Enhe, kisha ikawaje?"

    "Bob naye akatoka, akisema atarudi punde tu. Na kweli baada ya muda mfupi akarudi."

    "Alikwenda kumpigia simu Kessy." Alisema Bessy. "Sasa jaribu kuwa makini na mazungumzo yako."

    "Lakini sikuyatilia maanani sana. Na nilikuwa situlii, mara niko ndani, mara niko nje."

    "Haidhuru, jaribu kadri ya uwezo wako."





    "Bob aliporudi akasema, 'Tayari, keshanasa mshenzi. Milioni saba! Hayo nayakumbuka vizuri, kwani ndio maneno aliyoingia nayo. Na uso wake ulijaa furaha."

    "Hakuna kingine chochote unachokumbuka?"

    Shangazi alitikisa kichwa alisema, akitafakari. "Bob alisema kitu kama wameukata."

    "Kisha ikawaje?"

    "Wakaendelea kunywa. Kwa mara ya kwanza nikamuona Bob akimnunulia bia Kikoti, huku akimwambia wasilewe sana,kuna kazi muhimu inayowasuburi. Bob alimshauri Kikoti asiendelee kunywa wiski."

    "Kisha?"

    "Kwenye saa nne hivi Bob akatoka tena. Vile vile hakuchelewa kurudi."

    "Safari hii akasemaje?"

    "Alisema tutakabidhiwa mzigo wetu saa sita kamili karibu na daraja la Singisa. Akampa mkono Kikoti. Nilidhani wamelewa, kumbe wanapeana mkono wa buriani!"











    Katika chumba kimoja cha ghorofa ya pili katika jengo linalotizamana na Tupetupe Hotel vijana watatu waliketi wakimung'unya kuku wa kuoka na chipsi na kuteremshia kwa vinywaji.

    Chox aliketi kando ya dirisha, mara kwa mara akichungulia nje, hasa kwenye uwanja wa kuegesha magari na mlango wa mbele wa Tupetupe Hotel. Fensy aliketi mezani kando ya chupa za vinywaji na vifurushi vya kuku na chipsi. Chiko yeye aliketi kitandani, kando yake pakiwa na darubini.





    Chiko akasema, "Kwa hiyo tumeelewana, Chox?"

    "Manta hofu." Alijibu Chox, akivunja mifupa. Mbele yake palikuwa na kichuguu cha mifupa cha kudhibitisha aliwaacha mbali wenzie. Na alikuwa na mwili kuliko wenzake. Akasema, "Hata ukitaka niwe Profesa nitakuwa Profesa. Na utashangaa."

    "Hapana, nataka uwe daktari wa kawaida tu."

    "No sweat." Akatema mifupa na kuzidi kukikuza kichuguu chake. Akachungulia nje, akisema, "Lakini una hakika yule kijana atarudi tena hapa Tupetupe?"





    "Sina hakika, nnasikia tu." Alijibu Chiko. Hatufahamu ni nini Dikwe ameloloma. Alikuwa anafahamu kuwa mimi na Fensy tuna vyumba Tupetupe."

    "Kama atarudi kwa nia hiyo, atataka kuvipekua vyumba vyenu."

    "Hataambulia kitu. Nimempigia simu Osiga na kumwambia avisafishe. Amenihakikishia vitapakwa na rangi upya."

    Chox akatoa guno la kuridhika na kuchukua paja jingine. Chiko akamuuliza, "Lakini ukimwona utamtambua?"

    "Hapana shaka." Chox alijibu, Akachungulia nje na kustuka. "Yulee! Gari lake lilee!"

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Chiko na Fensy wakakurupuka na kukimbilia dirishani. Wakaliona Bentley likiegeshwa. Chiko akaipeleka darubini usoni. Akawaona waziwazi Denny na Bessy wakitoka garini. Akauliza, "Ndiye?"

    "Ndiye." Alijibu Chox baada ya kuwatazama kwa darubini. "Yuko na yule msichana nuksi, Kachero Inspekta Bessy."

    Chiko akaichukua tena darubini. Akasema, "Ni mtoto mdogo kabisa. Wote wawili ni watoto wadogo kabisa. Natamani hata niwadungue hapo hapo walipo." Alisema Fensy.

    "Acha uchizi, hapa noma." Chiko akadakia.

    "Nafahamu hapa hapafai. Naifurahisha nafsi yangu tu. Lakini ingekuwa rahisi kabisa,"

    "Umbali huu ungehitaji kitu kikubwa zaidi kuliko .36 yako."

    "Nafahamu, Chi, nafahamu." Alisema Fensy, akiirudisha bastola yake kwenye soksi. "Nilikuwa naifurahisha nafsi yangu tu."

    "Naam," Alisema Chox, akiwaangalia Denny na Bessy wakiingia Tupetupe. "Dikwe ameimba kama chiriku."





    *************************************





    Mchana Tupetupe Hotel ilikuwa na sura tofauti kabisa na ile ya usiku. Palikuwa kimya na pamepooza. Bessy akiongoza, yeye na Denny walienda moja kwa moja kwenye mlago ulioandikwa MENEJA. Bila ya kubisha, Bessy akaufungua wakaingia ndani. Ilikuwa ofisi finyu yenye meza ndogo na viti viwili mbele yake. Mezani palikuwa na simu na kibao chenye jina la mwenye ofisi hiyo - Konga Osiga.

    Mwenyewe alikuwa ameketi nyuma ya meza, akisoma gezeti. Alikuwa mtu mwembamba, mwenye sura ya kitumbili, aliyevaa suti iliyohitaji kupigwa pasi. Akainuka haraka, akisema, "Karibu Inspekta Bessy." Huku akichanua tabasamu la kizandiki.





    Bila kuketi wala kusalimu, Bessy akasema, "Tunawataka Chiko na Fensy. Wako vyumba gani?"

    "Bahati mbaya Inspekta, wameshahama." Alisema Osiga kama mwenye masikitiko ya kweli.

    "Tangu lini?" Denny aliuliza.

    "Jana afande. Jana mchana."

    "Wamehamia wapi?"

    "Ntajuaje, afande? Sikuwa na uhusiano wowote nao zaidi ya kuwa wapangaji wangu."

    Bessy akasema, "Unajua Osiga, utasababisha hoteli ifungwe."

    "Kwa nini Inspekta? Hatuna kosa lolote. Hatudaiwi chochote na serikali. Tunalipa kodi zetu kama kawaida."

    "Unadhani kuhifadhi wakora wauaji si makosa?"





    "Huo ni uonezi Inspekta. Tutamjuaje mtu kama ni mkora au padri? Hawana alama usoni."

    "Unataka kuniambia kuwa hukujua kuwa Chiko na Fensy ni wakora?"

    "Naapa Inspekta, sikujua. Nipe Biblia nishike kama huniamini."

    "Kama vile hukujua kuwa Hoza alikuwa mkora na pusha!"

    "Sikujua, Inspekta, naapa. Nipe msahafu..." Denny akamkatiza. "Nitapenda kuviona vyumba vyao."

    "Twende mkavione kama itasaidia. Vinapakwa rangi."

    "Kitu gani?" Bessy alimaka.

    "Vinapakwa rangi, Inspekta. Tunaikarabati hoteli yetu."

    "Kwa kuanzia kwenye vyumba vya hao wakora?"

    "Ndivyo vitupu, afande. Hatuwezi kupaka rangi vyumba vyenye watu, eti, tunaweza?"





    Kengele ya simu ikalia. Osiga akaomba radhi, Akasema, "Tupetupe Hotel hapa." Akasikiliza kidogo kisha akasema, "Ndiyo, Inspekta Bessy yupo hapa. Ndiyo, pamoja na mwenzake. Nasikitika jina lake silijui. Naam, unataka kuzungumza naye? Sawa."

    Osiga akamtazama Denny, akasema, "Ni yako afande." Denny akamtupia Bessy jicho la mshangao kisha akaupokea mkono wa simu. Akasema,"Hallo!" Sauti nzito tulivu ikamwambia, "Hujambo, School Boy?"

    "Ni nani wewe!" Denny akauliza.

    "Chiko." Denny akamtupia tena jicho Bessy ambaye alibetua kichwa, ishara iliashiria aliweza kusikia anazungumza na nani.





    Chiko akaendelea, "Nasikia unanitafuta. Ni nani wewe?"

    "Komandoo Luteni Dennis Raymond Makete."

    "Oh, ni komandoo!" Chiko alibeza. "Na inaelekea una uhusiano na yule mzee aliyegongwa na gari jana asubuhi."

    "Ni babangu mzazi mliyemgonga, na mnayetaka kumuua kule hospitalini."

    "Sikiza, babako amegongwa kwa bahati mbaya. Aliyemgonga anasikitika na yuko tayari kulipa fidia."

    "Kiasi gani?"

    "Tamka mwenyewe. Huyo bwana ni tajiri sana. Hana tatizo la pesa."

    "Nataka kichwa chake."

    "Kitu gani?"

    "Nataka kichwa chake. Hiyo ndiyo bei yangu.Nipatie kichwa cha Kassim Hashir na ugomvi unakuwa umekwisha."

    "Ndiye nani huyo Kassim Hashir?"

    "Ndiye aliyemgonga babangu."

    "Umekosea, School Boy. Huyo bwana haitwi hivyo."

    "Anaitwaje?"

    "Potelea mbali anaitwaje. Wewe sema bei yako."

    "Nimekutajia bei yangu. Ni kichwa chake."

    "Wewe mtoto chizi nini? Kichwa chake kwa sababu ya kumgonga babako kwa bahati mbaya? Tena hakuafa!"

    "Kwa manufaa yako, hakumgonga kwa bahati mbaya. Isitoshe, hilo ni dogo sana , silo hasa ninalomtakia."

    "Kumbe unamtakia nini?"

    "Analijua yeye."

    "Sikiza School Boy. Wewe ni mdoga sana kwa kufa. Mimi si Dikwe au Hoza."

    "Unadhani mimi ndiye Kikoti au Bob?"

    "Shauri yako, umeshaonywa."

    "Unataka tuteue kilingo?"

    "Ukiwa peke yako au na nusu ya jeshi la polisi likiwa nyuma yako."

    "Peke yangu. Wewe ukiwa na mwenzako Fensy."

    "Yaelekea fal@ Dikwe kakupakia upuuzi wa kutosha."

    "Wa kutosha, tena kilingo na muda mchague wenyewe."

    "Kiwanda cha zamani sukari, leo saa kumi na moja jioni."





    *******************************************





    Wakinywa chai ya saa kumi nyumbani kwa Bessy, msichana huyo akasema, "Hivi kweli Denny hutaki kuniambia Chiko amesema nini?"

    "Nakwambia hakusema lolote la maana." Alijibu Denny. "Kazungumza upuuzi mtupu."

    "Nataka kuusikia huo upuuzi."

    "Kwamba Kassim Hashir yuko tayari kunilipa fidia kubwa kwa kumgonga babangu."

    "Kiasi gani?"

    "Nitakacho."

    "Ukamwambiaje?"

    "Nataka kichwa chake."

    "Upuuzi mwingine?"

    "Akatishia kuwa ataniua, akajigamba kuwa yeye si Hoza au Dikwe."

    "Na kuhusu kilingo?"

    Dennis akasita kujibu. Bessy akakaza sauti. "Denny mmepatana kukabiliana!"

    "Ndiyo."

    "Wapi na saa ngapi?"

    "Mahali fulani muda fulani."

    "Denny lazima nifahamu."



    "Aakk. Siwezi kukwambia hilo. Si sasa hivi, anyway. Utavuruga kila kitu. Utataka kulipeleka jeshi zima mahali hapo."

    "Lakini Denny hatuwezi kwenda peke yetu. Wanaweza wakawa wengi."

    "Hatuendi sote. Nakwenda peke yangu."

    "Una wazimu wewe, Denny! Je, wakiwa watano? Je, wakiwa kumi?"

    "Shauri yao, watajijua."

    "Unadhani nitakuacha ukawe bango la shabaha? Una wazimu! Akina Chiko ni wehu, ni watu hatari. Na wewe huna silaha yoyote. Huna hata manati!" Denny hakujibu.





    Bessy akakiweka kikombe chake mezani akainuka. Akazunguka nyuma ya Denny na kumshika bega. Baada ya kumkanda kidogo, akainama na kumbusu shavuni. Akasema kwa sauti tulivu sana. "Denny tafadhali nisikilize."

    "Bessy, hakuna njia nyingine." Denny alisema kwa uchungu. "Nimemwaidi Chiko kwenda peke yangu." Msichana akazunguka na kumtizama Denny usoni kwa macho makali. "Ahadi kwa jambazi? Ina thamani gani? You can bet bloody ass yeye hatakuwa peke yake."

    "Hatakuwa peke yake. Nimemwambia awe pamoja na Fensy."

    "Na bado unataka kuhatarisha maisha yako? Na pengine wasiwe wawili tu. Pengine wawe kumi! Pengine wawe wakora wote wa jiji hili lote lililolaaniwa!"

    Dennis akabaki kimya.





    Bessy akapumua na kusema kwa sauti yake ya kawaida, "Kama ungekuwa na busara, Denny wala usiingeenda wewe mwenyewe. Wewe umeshamaliza kazi yako. Ungewaachia polisi wakapambane na hao wehu."

    "Lakini kwa nini hutaki niende?" Denny aliuliza kwa karaha, "Huna imani na mimi?"

    "Hapana."

    "Kumbe?"

    "Sitaki uumie."

    "Kwa nini? Mimi ni mwanajeshi."

    "Kwa sababu... kwa sababu... ooh, mpaka nigeuze wimbo niimbe?"

    "Ndiyo geuza wimbo uimbe."

    "Aah, haya! Kwa sababu umeshaanza kuniingia moyoni kharamu we!"





    Taratibu Denny akakiweka chini kikombe cha chai. Taratibu akainuka, akasimama wakatizamana, hakuna aliye pepesa jicho. Hatimaye Denny akauliza, "Bessy , unasema kweli au unanitania?"

    "You idiot! Jambo kama hilo ni la kudhihaki?"

    Kufumba na kufumbua wakajikuta wamevaana.











    Sam Kembo aliingia haraka katika jengo lililotazamana na Tupetupe Hotel. Akazikwea ngazi hadi ghorofa ya pili. Akaenda na kubisha hodi kwenye mlango wa chumba Na. 202. Chiko akaufungua, akisema, "Karibu Kembo."

    "Asante."

    Kembo akaingia akaona chumba kitupu. Akageuka na kuuliza. "Vipi, mbona uko peke yako? Na unaonekana huna furaha."

    "Aah. Yule mtoto amenichefua kwelikweli ." Alijibu Chiko akiurudisha mlango. Kembo akaketi mezani na kuwasha sigara. "Mtoto gani?"

    "Aliyempeleka Dikwe Uwanja wa Gofu."

    "Kwa hiyo kaja kama ulivyotazamia?"

    "Ndiyo. Alikuja na Inspekta Bessy. Kumbe ni mwanae Dk.Makete. Ni kitoto kidogo tu. Hata mambo yake ni ya kitoto. Eti kinajiita komandoo. Hizi sinema zinawaharibu sana. Bila shaka anajiona kama Rambo au Anorld Schwarzenegger."

    "Uliweza kuzungumza naye?"

    "Ndiyo. Kwa simu yangu ya mfukoni."

    "Kwa hiyo amekataa pesa?"

    "Kakataa. Kasema anakitaka kichwa cha aliyemgonga babake. Unaona? Ni mambo ya kitoto kabisa. Ni balehe inayomsumbua. Hata aliyemgonga babake hamfahamu. Anamwita - anamwita nani vile? Ooh ndiyo, anamwita Kassim Hashir."

    "Eti nani?" Kembo aliuliza, uso ghafla umejikunja.

    "Kassim Hashir."

    "Gosh, una hakika?"

    "Nweza kuwa nimekosea, lakini sidhani. Kwani vipi?"





    "Kama ni hivyo Dk.Makete ameshazungumza. Yuko wapi Chox?"

    "Amekwenda hospitali kumshughulikia huyo daktari. Kwani vipi?"

    "Ni kazi bure. Tunachotaka kumzuia mzee huyo asikiseme ameshakisema."

    "Yaani yule School Boy hakuwa akizungumza utumbo? Yaani Bwana Kessy ndiye Kassim Hashir?"

    "Achana na hayo." Kembo alisema kwa karaha. Akauliza, "Umezungumza nini na huyo kijana?"

    "Hatukuzungumza mengi. Eti anataka tukabiliane. My God, laiti angejua mimi ni nani!" Chiko akatikisa kichwa. "Acha tu, nitaikomesha balehe yake."

    "Wapi saa ngapi?"

    "Saa kumi na moja jioni. Kiwanda cha zamani cha sukari."

    "Chiko unaweza kuwa mtego!"

    "Mimi wa kunaswa katika mtego wa kijinga? Bos, unanionaje? Hivi sasa Fensy yuko huko anavinjari. Anapiga simu ya mfukoni kama hii niliyonayo. Akiona kitu chochote zaidi ya huyo School Boy ataniarifu na kuyeyuka. Tutampata huyo 'Rambo' wakati mwingine, mahala pengine."

    Kembo akakubali kwa kichwa, akasema, "Kuweni waangalifu."

    "Usiwe na wasiwasi bos. Mwingine huyo School Boy kwenye orodha ya marehemu. Ikiwezekana angeshauriwa apitie kwanza kanisani akajiombea kabisa misa ya wafu kabla hajaenda huko kiwanda cha sukari."





    **********************************





    Mama Denny aliufungua mlango Na. 13 akaingia ndani.Kachero Koplo Koba aliyekuwa ameketi akainuka. akasema, "Karibu, Bi mkubwa. Shikamoo."

    "Asante mwanangu," Aliitikia Mama Denny. "Anaendeleaje mgonjwa?"

    "Vizuri, ningekushauri usimchoshe sana kwa mazungumzo marefu."

    "Nafahamu."

    "Nanyosha miguu kwenye korido." Aliendelea Koplo Koba." Nauacha wazi mlango, ukiwa na shida yoyote niite. Kama jina umelisahau, ni Koplo Koba."

    "Vizuri mwanangu."

    Mama Denny akaenda kando ya kitanda na kukifumbata kiganja cha mumewe kwenye viganja vyake. Mzee Makete akafumbua macho. Akasema kwa sauti dhaifu, "Ooh, ni wewe mama Denny!"

    "Ndiyo mpenzi. Unajisikiaje?"

    "Uchovu tu."

    "Vumilia mpenzi, ndiyo hali ya dunia. Dk.Beka amesema atakuruhusu baada ya siku chache tu."





    Baada ya kimya kifupi Mzee Makete akasema, "Mpenzi, Kassim Hashir angali hai. Ndiye aliyenigonga."

    "Nafahamu. Polisi tiyari wanamtafuta."

    "Huoni kuwa ni wajibu wetu kumweleza Denny ukweli?"

    "Nimekwisha mueleza."

    "Asante sana. Umenipunguzia mzigo mkubwa sana."

    "Nimemweleza kila kitu, tangu mwanzo hadi mwisho. Hata jinsi alivyopata yale makovu."

    "Akasemaje?"

    "Unamjua jinsi Denny alivyo. Hakubadilika. Kama vile nimemsimulia kisa cha mtu mwingine kabisa."

    "Kuna wakati huyu mtoto hunishangaza na kunitia wasiwasi."

    "Si peke yako."

    "Kama vile ana kasoro." Aliendelea Mzee Makete. "Kama vile si mtu wa kawaida!"

    "Yaani taahira?"

    "Hapana. Hapana, Denny ni mzima kabisa. Ana akili kama mtu wa wastani. Isipokuwa ana tofauti kidogo na mtu wa kawaida. Hupenda kuishi porini, kufanya mazoezi magumu, kwake hakuna kinachomstua na haogopi kitu hata kama kwa wengine kitaonekana ni kigumu na cha hatari kiasi gani. Inatokana na viini chimbuko bila shaka. Yaani jenetiki."





    "Tulifanya makosa kumchukua hali tukijua anaweza kuwa na jenetiki za Kassim Hashir?"

    "No. Hapana. Hatukufanya kosa hata kidogo. Tusingemchukua sisi angechukuliwa na mtu mwingine. Au pengie angepelekwa kwenye makazi ya watoto yatima. Pengine asingepeta malezi kama tuliyompa. Hapana, hatukufanya kosa hata kidogo kumchukua."





    Bi mkubwa akashusha pumzi. Akasema, "Sijui ningejisikiaje ungesema tulifanya kosa. Unajua tumejizuia kuzaa kwa kuogopa kuja kugawa upendo. Hakuna wa kuthubutu kuninyang'anya Denny wangu. Hakuna."

    "Mpenzi,mpenzi,mpenzi - hakuna wa kukunyang'anya Denny wako. Awe taahira, zuzu, awe na bongo au la ni wako. Kihaki, kisheria na Kimungu."





    Kachero Koplo Koba alimuona daktari tangu alipozimaliza ngazi na kuingia kwenye korido. Alikuwa mgeni kabisa kwake, lakini tena, hakuwa akiwafahamu madaktari wote wa hospitali hii kubwa. Isitoshe, hakuwa na tofauti yoyote na madaktari wengine. Kama ilikuwepo, basi ni ya huyu kuonekana ni daktari aliyekamilika.

    Alivaa kidaktari, pamoja na pima moyo shingoni, Na hata tembea yake ilikuwa ni ya kidaktari.





    "Habari za hapa kijana?" Chox alitamka kwa sauti nzito, ya uhakika.

    "Salama tu Dokta."

    "Good. Very good." Chox alisema akiridhika kwa kichwa. "Dk.Makete yuko peke yake au kuna mtu mwingine ndani?"

    "Yuko na mkewe. Amewasili sasa hivi."http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    "Good. Good. Very good."

    Chox akapenya kwenye mlango uliokuwa wazi. Akasema, "Shikamoo Mama Makete."

    "Marahaba Dokta. Karibu."

    "Asante." Alijibu Chox. Akavichukua vyeti vya matibabu kitandani. Akauliza, "Anajisikiaje mgonjwa wetu?"

    "Hajambo. Yuko macho."

    "Good. Very good."





    Chox akavirudisha vyeti na kumkaribia mgonjwa. Akamuuliza, "How do you feel Doctor?"

    "Still very weak." Alijibu Mzee Makete.

    "Expected. Most expected. You'll be as good as a new born in no time. You'll see."

    Chox akakichukua kipimamoyo na kuanza kumpima mgonjwa. Akasema, "Good. Very good. Very normal. Utahitaji sindano hii moja kwa jioni ya leo." Akaingiza mkono mfukoni na kutoa sindano na kichupa cha dawa. Mzee Makete akasema, "Mpe mke wangu anidunge."

    Chox akasita.

    "Ooh, usiwe na wasiwasi Dokta." Alisema mama Denny akiinuka. "Mimi ni nesi kamili. Wajua, ni mimi ninayemdunga sindano nyumbani."

    "Good. Very good. Very good."

    "Chox akampa Mama Denny sindano na kichupa kile cha dawa. Akasema, "Just 2cc"





    Mama Denny akaijaza sindano dawa, akakiweka kichupa mezani. Akainua sindano na kupunguza dawa, akitafuta usawa wa 2cc.

    "Good. Very good. Exllent. Chox aliafiki akiiangalia sindano.











    Bessy akakijaza kikombe cha chai, akauliza, "Ilikuwaje usiwe na msichana hadi makamo hayo?" Dennis akakipokea kikombe akasema, "Huko ninakoishi wasichana ni bidhaa adimu sana. Mno ni manyani tu."

    Bessy, akakijaza kikombe chake. Akatabasamu na kuketi akauliza, "Ulitarajia kuishi porini huko hadi lini?"





    "Sijui." Denny alijibu. "Jana nilipoirudisha jeep na kuomba likizo ya dharura, Kanali aliniambia nakaribia kupewa Ukapteni na kuhamishiwa kitengo kingine."

    "Kitengo gani?"

    "Hakusema waziwazi ni kitengo gani. Lakini nashuku kitakuwa kitengo cha Busara - yaani Intelligence - Makao Makuu."

    "Itakuwa safi sana. Tutakuwa tukionana mara kwa mara."

    "Lakini patakuwa na mafunzo kwanza bila shaka. Pengine ng'ambo."

    Denny akanywa funda la chai. Akauliza, "Wewe je?"

    "Mimi kitu gani?"

    "Imekuwaje usiwe na mvulana?"

    "Ooh, nimeshafanya urafiki na wavulana wawili watatu. Mara mbili nilikaribia kufunga ndoa, lakini mara zote nikaghairi dakika za mwisho."

    "Kwa nini."

    "Kila mtu humwona ana walakini - maneno mengi, ahadi tele, mbwembwe, mikogo... aah, unafiki mtupu!"

    "Wasichana wengi huvutiwa na hayo." Alisema Denny.

    "Nao pia ni wanafiki." Alijibu Bessy

    "Au ni mazumbukuku."

    "Mimi je? Ni mnafiki pia?"





    "Ooh, wewe uko tofauti. Kwani mwenyewe hujioni ulivyo?"

    "Kuna mtu anajiona alivyo kikweli kweli?"

    "Wapo." Alijibu Bessy. Kisha akaminya uso. "Lakini hapana. Nadhani ni kweli. Hakuna mtu anayeweza kujiona alivyo. Hao wanaodhani wanajijua walivyo wanajihadaa. Kila mtu hujiona mwema, mzuri. Hata Hitler, Amin na Mobutu walijona kama malaika."

    Denny akakubali kwa kichwa akasema, "Hebu niambie. Umesema niko tofauti nikoje?"

    "Ooh, uko kama nyani."





    Wote kwa mara ya kwanza tangu wakutane wakacheka, kicheko cha dhati. Bessy akasema, "Hebu niambie, ni kitu gani kilichokuvutia kwangu?"

    "Sijui." Alijibu Denny. "Labda kwa vile wewe ndiye mrembo wa kwanza na wa pekee kukutana naye tangu niachane na manyani wenzangu. Lakini nadhani hasa ni kwa sababu ya jeuri yako. Msichana mrembo kama wewe hupaswi kuwa jeuri hivyo."

    "Mimi jeuri?"

    "Mwenyewe hujijui?" Wakacheka tena. Baada ya kimya kifupi Bessy akasema. "Kwa hiyo tumekubaliana?"

    "Ndiyo." Denny alijibu haraka.

    "Chagua siku uipendayo. Mimi niko tayari kabisa. Nna hakika."

    Bessy akaminya uso akauliza, "Unazungumzia nini wewe?"

    "Harusi yetu."

    "Idiot! Sijakwambia nakupenda. Sijakwambia niko tayari kuolewa na wewe?"

    Denny naye akakunja uso. "Kumbe unazungumzia nini? Tumekubalina kitu gani?"

    "Kwenda kupambana na Chiko>"

    "Aah! Hilo mbona tumeshalimaliza."

    "Denny, huwezi kwenda peke yako."



    "Sikiliza. Ngoja nikwambie mambo mawili. La kwanza, ninapotoa ahadi, iwe kwa Musa au kwa Firauni sirudi nyuma. Na pili Chiko akiona tupo wengi atakimbia. Tutakuwa hatukufanya lolote."

    "Sikiliza. Acha nichukue watu wawili au watatu tu. Watajibanza garini. Nitachagua watu wa uhakika."

    Denny akatikisa kichwa. "No way, baby."

    Bssy akakibamiza kikombe mezani na kufoka, "Laanakum wewe! Laanakum wewe! Mbishi kama - laanakum."





    ****************************************





    Chiko aliipunguza mwendo pikipiki, akaiacha barabara kuu na kupinda kulia. Akaongeza mwendo na kutimua vumbi, akiukumbatia mkoba wa ngozi uliokuwa mbele yake kwenye tanki la petroli.

    Kiwanda cha zamani cha sukari kilikuwa kilometa nne kutoka barabara kuu. Kikiwa kimekufa miaka kadhaa nyuma. Kilichobakia ni magofu tu yaliyotelekezwa na kushambuliwa na wezi wa mabati, mbao, milango, madirisha na chochote kile chenye manufaa.



    Sasa yalikuwa magofu uchi, yapigayo miayo, yaliyonyukwa na mvua kadhaa za masika na jua kali la viangazi na kuzungukwa mbudu na ukoka. Upande wa pili palikuwa na masalia ya majengo ya ofisi, na kushoto masalia ya korona na ghala, na katikati palikuwa na uwanja.

    Ilimchukua Chiko dakika chake tu kufika hapo, wakati jua likianza kuwa jekundu upande wa Magharibi. Akaiona pikipiki ya Fensy iliyoegeshwa mbele ya jengo la korona.





    Akaisimamisha pikipiki yake kando ya pikipiki ya Fensy. Akaizima na kuteremka, akiuchukua mkoba wake wa ngozi. Fensy akachomoza kwenye kona ya lango la korona. Chiko akamwuliza, "Mambo?"

    "Poa kama jahannam,"Alijibu Fensy.

    "Hakuna chochote kilichotokea?"

    "Si mtu, si jini. Upepo tu ukipiga miluzi kwenye haya magofu ya kichawi. Unaonaje, inawezekana asije?"





    Chiko akaitazama saa yake. Akasema, Tutaonana baada ya robo saa. Kama ana chembe ya busara hatakuja." Akaufungua mkoba na kutoa SMG iliyokatwa kitako. "Au atakuja na kikosi. Nyuma kuko wazi?"

    "Wazi kama jahannam - hakuna kikwazo ." Alijibu Fensy. Akaongeza, "Lakini nisingependa kuiacha pikipiki yangu, ingawa imechakaa."

    "Hata mimi . Naamini hatutaziacha."





    *************************************





    Dennis aliitizama saa yake, akasema, 'wakati' na kuinuka. Bessy akainuka pia, macho yamemuwiva. Akasema, "Denny, uwe mwangalifu tafadhali."

    "Ndiyo, nitakuwa mwangalifu." Alisema Dennis. "Sikiliza, usitoke hapa. Kuwa karibu na simu. Ukiona kimya hadi saa kumi na moja na nusu, chukua kikosi mje kiwanda cha zamani cha sukari. Niahidi utafanya hivyo, na si lolote jingingine."





    Dennis akawasili kwa kasi kiwanda cha zamani cha sukari, akitimua vumbi. Akaziona pikipiki zilizoegeshwa mkono wa kushoto, akalisereresha gari mkono wa kulia. Likaenda kutulia mbele ya gofu la mwisho, mabaki ya ofisi ya meneja wa kiwanda hapo zamani.

    Akaufungua mlango wa gari, akachupa na kujibiringisha, akifuatiwa na mvua ya risasi za SMG iliyokuwa ikichakarika kwenye lango la korona.





    Alipopenya tu ndani ya gofu hilo, Denny akainuka, akaichomoa bastola na kuangaza haraka humo ndani. Uwazi wa mahali lilipokuwa dirisha la nyuma ukamkenulia. Akaruka na kusimama nyuma ya gofu, akisikiliza kwa makini.

    Kwa nukta kadhaa kote kulikuwa kimya isipokuwa kuvuma kwa upepo. Kisha akaisikia sauti ya Chiko ikiita kwa mbali. "Hey! School Boy! Niko hapa." Dennya akatambaa kinyoka kwenye majani yaliyozunguka gofu hilo akachomoza kichwa na kuliona gofu la korona. Akamuona Chiko akizungumza na kumfanyia ishara mwenzake. Kisha akaachia risasi za mfululizo, akilishambulia gofu la ofisi.





    Wakati huohuo Fensy akatoka mbio, bastola mkononi akilifuta gari. Akachungulia ndani, akitazama kama mlikuwa na watu waliojifcha. Kisha akanyata, akajibanza na kuchungulia ndani ya gofu. Alipohakikisha liko tupu akapenya ndani kwa tahadhari, bastola ikilenga mbele.

    Denny akajikunja na kumfuata. Akamkuta akivhungulia kwenye uwazi wa dirisha. Ingekua rahisi sana kumrukia hata kama Denny asingekuwa na Bastola mkononi. Lakini badala yake, akamwamuru, "Ganda."





    Fensy hakuganda. Alishtuka, akageuka kwa kasi, akiachia risasi ovyo. Zote zilipita juu, Kwani Denny alikuwa amechutama. Akaachia risasi mbili. Zikamsomba Fensy mzimamzima na kumrusha nje ya uwazi wa dirisha na kudondoka chini kwa kishindo.

    Denny akageuka na kuchungulia nje, kwenye gofu la korona. Kote kulikuwa kimya, kumetulia tuli, isipokuwa upepo ukipeperusha vumbi. Akatambaa hadi nyuma ya gari na kujibanza. Akaukinza mdomo wake kwa viganja na kuita, "Chiko!"





    Chiko akachomoza uso kwenye lango la korona na kuita "Fensy? Vipi?" Denny akalitambua kosa la Chiko. Alimdhania mwenzake,Denny akaamua kubahatisha. Akaukinza tena mdomo wake na kusema, "Tayari mshenzi kaniumiza mguu."

    Chiko akasita kidogo, kisha, akachomoza, SMG madhubuti mkononi. Akaanza kutembea kwa tahadhari, macho yake na mdomo wa mtutu kwenye mlango wa mabaki ya ofis ya meneja wa kiwanda.





    Alipofika katikati ya uwanja, Denny akainuka ghafla nyuma gari, mdomo wa bastola ukikilenga kichwa cha mkora huyo. Akamwamuru, "Dondosha."

    Chiko akaganda, akageuza kichwa, akatoa kichwa kwa mshangao wa dhati. Akanong'ona kama anayeota, "School Boy!"

    "Ndiyo." Dennya alimjibu. "Ni School Boy yuko darasani. Dondosha hiyo Bunduki."





    ************************************





    Bessy aliposema angevuja jasho kila nukta ya dakika hizo zote hakuwa akidhihaki. Kwa sababu kama - kama hapakuwa na sababu yoyote nyingine ya maana - kwa sababu kama Dennis angefikwa na balaa lolote huko kiwanda cha zamani cha sukari, hata kujeruhiwa tu, yeye Bessy angewajibika.

    Akiwa afisa wa polisi hakupaswa kumwacha mtu ahatarishe maisha yake kwa kupambana na magaidi hatari. Hata kama mtu huyo alikuwa ni komandoo wa Jeshi la Ulinzi. Hii ilikuwa ni kazi ya polisi. Hivyo sasa Bessy alikuwa anajuta.





    Muda wote huo akitokwa jasho. Na hakuweza kutulia. Mara aketi, mara ainuke na kutembea tembea hapo sebuleni. Na wakati wote mara aiangalie saa yake, mara aiangalie simu, huku akihimiza, "Come on boy! Come on boy! Come on boy!"

    Hivyo, simu ilipolia, jinsi alivyoruka ni kama aliyegusa umeme. Haishangazi. Akaunyakua mkono wa simu na kusema, "Hallo Denny!"

    "Bessy?"

    Haikuwa sauti ya Denny bali ya Kamishna Msaidizi wa polisi. "Bessy . Mbona hujaripoti mpaka saa hizi?"

    Bessy akakumbwa na fazaa. Akababaika, "Mzee, Mzee, nna - nnamsubiri Denny."

    "Kwa nini?"

    "Amekwenda - amekwenda kiwanda cha zamani cha sukari."

    "Kufanya nini?"

    "Kukutana na Chiko."

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    "Mbona sikuelewewi, Bessy!" Alisema Kamishna Msaidizi. "Unazungumza kitu gani?"

    "Ooh, samahani sana kwa kukuficha Mzee. Ukweli ni kwamba Denny anakichwa kigumu sana. Amepatana na Chiko kukabiliana huko kiwanda cha sukari, na amekataa kufuatana na mtu yoyote."

    "Mungu wangu, Bessy! Umeruhusu kitu kama hicho?"

    "Ningefanya nini, Mzee? Amesema hakuna njia nyingine. Vinginevyo tutamkosa Chiko, na yeye ni Komandoo."

    "Hata angekuwa nani!" Kamishna Msaidizi alifoka. "Yeye si polisi. Ni afadhali kumkosa huyo mlaaniwa kuliko kuhatarisha maisha yake. Akiumia sisi wote tutaonekana wazembe wakubwa! Sasa sikiliza. Jitayarishe. Natuma watu watatu wakupitie."

    "Lakini Mzee, nimemwahidi sitafanya lolote hadi saa kumi na moja na nusu."

    "Sitaki kusikia upuuzi wowote. Gari litakuwa hapo baada ya dakika mbili au tatu."





    Simu ikakatwa. Bessy akapumua. Kwa upande alifurahi. Kwani alikuwa akitii amri ya mkuu wake, hakuwa akivunja ahadi kusudi.

    Alipomaliza kufunga milango tu akasikia king'ora cha gari la polisi likija kwa kasi















    Chiko akasita, macho yake yakizungumza waziwazi mawazo yake. Alikuwa akikadiria ingemchukua sehemu gani ya sekunde kuugeuza mdomo wa bunduki mzunguko wa nyuzi kama ishirini au thelathini,na ingemchukua Denny sehemu gani ya nukta kukivuta kilimi cha bastola yake iliyokuwa imemlenga.

    Kisha akaona macho ya Denny yanavyowaka. Akasisimka mwili mzima na kuibwaga SMG. Ulikuwa mtego. Denny naye akaidondoasha bastola na kuanza kumfuata kwa hatua za polepole, macho yao yameumana.





    Alipobakiza hatua tano, Chiko kwa kasi ya chui akaichupia SMG. Vidole vyake vilikwishagusa chuma alipofumuliwa teke la kifuani lililompindua chali.

    "Inuka." Denny alimwamuru.

    Chiko akakurupuka kama nyati aliyejeruhiwa. Akakutana na teke la mzunguko lililombwaga kifudifudi. Denny akamkwida ukosi na kumwinua. Akamzungusha na kumnyuka ngumi nne za mfululizo.





    Chiko akapepesuka. Akakung'uta kichwa kuondosha ulevi na nyota zilizomzonga. Akajizatiti na kukumbuka yeye ni nani. Akakurupuka tena! Akarusha ngumi, akarusha teke. Vyote viliambulia patupu. Akajirekebisha na kujaribu kujiweka sawa. Akarusha ngumi, akarusha teke. Akajikuta anakata tena hewa na kuzidi kujichosha. Denny akajizungusha na kumfumua teke la juu kwa juu. Chiko akapepesua. Akafumuliwa teke la usoni. Akadondoka 'puu' kama gunia la mchanga. Alipotaka kuinuka Denny akamkanyaga kwa nguvu kwenye uti wa mgongo. Mfupa ukalia 'ko', Chiko akapiga yowe na kurudi chini kifudifudi.





    "Huo," Denny akamwambia, "Ni mfupa wa kiuno. Ili kuhakikisha huinuki tena katika maisha yako yote. Wala huketi. Wala huchutami. Wala hutambai. Sasa wewe ni mtu wa kubebwa na kugeuzwa tu kama maiti. Na huo ni mwanzo tu." Denny alimfahamisha. Akamuuliza kwa ukali. " Wapi anaishi Kassim Hashir?"

    "Go to hell."

    "Hajahamia huko bado." Denny akamnyuka teke la mdomoni. Chiko akatema damu na meno mawili.

    "Wapi nitampata Kassim Hashir?"

    "Nakwambia simjui jamaa huyo." Chiko aliloloma.

    "Namtaka mtu aliyemgonga babangu. Na utaniambia tu alipo, pamoja na ubabe wako. Ikibidi nitakung'oa meno yote. Na kisha niivunjevunje mifupa yako yote."

    "Nakwambia aliyemgonga babako haitwi hivyo."

    "Potelea mbali anaitwaje. Nataka kujua anakoishi."





    "Sikujui anakoishi."

    "Sikuamini."

    "Shauri yako."

    Chiko akala teke jingine na kutema jino jingine. Akaloloma, "Nakwambia kweli. Sijui anakoishi. Nilikwenda kwake mara moja tu, tena usiku. Huko Buffalo Hill."

    "Ulifikaje?"

    "Nilipelekwa na...na..."

    "Na nani?"

    Chiko akabaki kimya. Denny akainua mguu, lakini Chiko akamzuia. "Subiri! Nilipelekwa na Kembo. Sam Kembo."

    "Ndiye nani huyo?"

    "Rafiki yake huyo aliyemgonga babako."

    "Yaani ndie mtu wa kati baini yenu na huyo Kassim Hashir?"

    "Ndiyo."

    "Nitampata wapi?"

    "Sijui"

    Denny akaanza kulitayarisha teke.



    "Subiri!" Chiko akasema kwa haraka. "Anatusuburi Flamingo Guest House, chumba Namba 202."

    "Kama unanidanganya, ole wako. Nitakurudia. Na ujue nitakukuta hapa hapa, hivyo hivyo ulivyo."

    "Kwa nini nidanganye? Mimi nimekwisha, kwa nini wao wapone?"

    Denny akaifuata bastola. Alipoinama aiokote akasikia king'ora cha polisi. Akaiokota, akageuka na kuitazama barabara.





    Golf ilikuwa ikija kasi, ikitimua vumbi. Ikaserereka na kusimama. Bessy akatoka mbio, akaita "Denny!" Akajitupa kwenye kifua cha Denny, huku akicheka na akilia wakati huo huo.

    Denny akampigapiga mgongoni, akimwambia, "It's okay baby. It's okay." Akawatazama askari watatu wakitoka garini, kila mmoja kakumbatia SMG. Akawaambia, "Naona mmechelewa kidogo mabwana. Mchezo umekwisha. Majeruhi huyo hapo, na mzoga uko nyuma ya gofu lile."





    "Ni wao wawili tu?" Askari mmoja aliuliza.

    "Ni wao tu."

    Askari mmoja akamwendea Chiko na kumtekenya kwa kiatu. Hey, wewe! Inuka twende."

    "Siwezi." Chiko alilalama. "Mwanakharamu kanivunja kiuno."

    Bessy akamtazama Denny, macho yake yakimshutumu.

    "Kaniita School Boy."

    "Hilo ni tusi kubwa?"

    "Akha, shika!" Akamkabidhi bastola yake. "Twende zetu. Kuna kazi ya kufanya."

    "Wapi?" Bessy aliuliza, wakielekea kwenye gari.





    "Flamingo Guest House. Kukanyaga ngazi ya mwisho. Mtu mmoja aitwaye Sam Kembo. " Denny akaliwasha gari na kuling'oa. Akasema, Kwa hiyo hukuweza kusubiri hadi saa kumi na moja na nusu?"

    Hapana, Nimelazimishwa na Kamishna Msaidizi nikufuate pamoja na wale askari watatu. Lakini nilifurahi. Jinsi nilivyokuwa nikitokwa na jasho ningerukwa akili."

    "Ndiyo maana unanukia vizuri zaidi. Nitakufanya utokwe jasho kila siku."

    "Shetani mkubwa we."





    Baada ya kimya kifupi Bessy akasema, "Nasikitika kufanya kile kitendo cha kipimbavu mbele ya wenzangu."

    "Kitendo gani?" Denny aliuliza.

    "Kule kukuvamia nilipoona uko salama."

    "Hakikuwa kitendo cha kipumbavu. Ulionyesha jinsi unavyonipenda. Ulinifurahisha sana."

    "Sikukuvamia kwa sababu nakupenda, you idiot. Nilifurahi kukuona uko salama. Ungeumia ningefukuzwa kazi."





    ********************************





    Punde akalisimamisha gari nje ya Flamingo, picha ya ndege huyo, korongo mweupe aliyesimama kwa mguu mmoja, akipatangaza mahali hapo.

    Wakazipanda ngazi hadi ghorofa ya pili. Mbele ya mlango wenye nambari 202 Denny akamfanyia ishara Bessy abishe. Akaugonga mlango.

    Sauti nzito ikauliza, "Nani?"

    "Ni mimi." Bessy alisema kwa sauti laini ajabu. "Nifungulie."





    Mlango ukafunguliwa kidogo. Denny akaupiga kikumbo na kuingia nao ndani. Huku akipepesuka kwa hicho kikumbo, Kembo akaupeleka mkono wake ndani ya koti.

    Denny akamkwida na kumbamiza ukutani. Akamnyang'anya bastola aliyokuwa ikiitoa. Akamzungusha na kumsukumia mlangoni. "Twende."

    "Wapi?" Kembo aliuliza, akijifuta damu mdomoni. "Nyie ni nani?"

    "Ni Inspekta Bessy na Dennis Makete. Tupeleke kwa rafiki yako, Kassim Hashir."

    "Simjui mtu huyo." Denny akamnyuka Kofi la kelbu. "Usimwige Petro."

    "Ndiye nani huyo Petro?"

    "Jesus Christ! Hata Petro humjui! Ni Mkristo kweli wewe?"





    "Sikiliza," Kembo alihema kwa nguvu. "Sikilizeni. Mimi si mtu wa ghasia."

    "Alaa! Ndio maana ukawatuma akina Chiko wakufanyie ghasia zako?"

    "Chiko!" Kembo aliguna kizembezembe. "Yuko wapi Chiko?"

    "Nilidhani utasema naye pia humfahamu!" Denny alisema, akiufungua mlango na kumsukumia Kembo nje. "Chiko na Fensy wa wanakostahili kuweko - Jehanamu."





    Wakaziteremka ngazi. Chini Denny akamrushia Bessy funguo za gari. "Endesha wewe." Alimwambia. "Sisi tutastarehe kwenye siti ya nyuma na huyu rafiki yangu."

    Wakaingia garini. Bessy akalitia moto. Akauliza, "Buffalo Hill?"

    "Buffalo Hill." Denny alimjibu. Akamtekenya Kembo kwa mdomo wa bastola yake mwenyewe. "Mtaa gani?"

    "Kitosi." Kembo alijibu bila ya kusita.

    "Namba?"

    "Ishirini na moja."http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    MWISHO WA MSIMU WA KWANZA



    ENDELEA KUFUATILIA MSIMU WA PILI



    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog