Simulizi : Mifupa 206
Sehemu Ya Tatu (3)
Pweza hakupoteza muda haraka bastola yake akailekezea kifuani kwa Zera kisha
akazisukuma risasi mbili ambazo ziliacha matundu mawili makubwa yakivuja damu
kifuani kwa Zera. Zera akapiga yowe kidogo na kulala pale chini huku roho yake ikiwa
mbali na mwili.
Shimo la kuuzikia mwili wake lilikuwa tayari limeshachimbwa kiasi cha umbali wa
hatua ishirini kutoka eneo lile. Shimo lile lilikuwa limechimbwa na Fulgency Kassy
na Kombe wakati ule Pweza alipokuwa ameenda kumchukua Zera kule nyumbani
kwake. Hivyo bila kupoteza muda Kombe akaibeba maiti ya Zera begani halafu wote
wakaanza kutembea wakielekea kwenye lile shimo.
Lilikuwa shimo refu kiasi lililochimbwa kando ya ule ufukwe hivyo walipofika
Kombe akainama na kuitupia maiti ya Zera kwenye lile shimo kisha kwa kutumia lile
chepe ambalo walikuwa wamekuja nalo hapo awali wakaanza kulifukia lile shimo.
Baada ya muda mfupi wakawa wamemaliza zoezi lile hivyo wakachukua lile chepe na
kuelekea kwenye lile gari huku wakiamini kuwa pindi maji ya bahari yatakapojaa jioni
ile yangelifunika kaburi lile vizuri na hivyo kuondoa ushahindi wowote wa kuzikwa
mtu eneo lile.
Muda mfupi uliyofuata walikuwa njiani wakirudi mjini na mkakati mpya wa
kumtafuta Stephen Masika.
_____
SIGARA NYINGI NILIZOZITEKETEZA WAKATI nikiisubiri simu ya Zera
nje ya mgahawa ule zilikuwa zimeyapasha moto mapafu yangu kiasi cha kutosha na
kwa kweli sikuzitamani tena kwa wakati huu. Ingawa ilikuwa ni starehe nzuri kwangu
lakini kila nilipokumbuka athari za uvutaji wa sigara nilijikuta nikiyaonea huruma
mapafu yangu.
Mara kwa mara nilikuwa nimepanga kuonana na kiongozi yeyote wa kiroho ili
anipatie mwarobaini wa kukata kiu ya starehe ile yenye madhara ya aina yake. Lakini
huwenda nikasema kuwa shetani alikuwa ameishtukia mapema dhamira yangu ya
kutaka kuikimbia bidhaa yake na hivyo kuninyima muda huo.
Niliitupia tena macho saa yangu ya mkononi na hapo nikayalaani masaa
yalivyokuwa yakitokomea. Ilikuwa ikielekea kutimia saa kumi na moja kasoro jioni
na matumaini ya kupokea simu ya Zera nayo yalikuwa yakiendelea kufifia. Mara kwa
maara nilijikuta nikishawishika kutaka kumpigia simu lakini nikajikuta nikiachana na
mpango huo pale nilipokumbuka kuwa sikuwa na namba ya Zera kwenye simu yangu.
Mvua kubwa ilikuwa ikiendelea kunyesha na kwa kweli mvua ile ilikuwa ikiendelea
kuleta madhara katika baadhi ya sehemu za jiji la Dar es Salaam. Lakini kwa wakulima
wa mashambani mvua ile ilikuwa ni neema ya aina yake.
Nilikuwa nimeamua kusogea karibu na makazi ya Zera ili pindi atakaponipigia
simu niweze kumfikia kwa haraka. Hivyo katika kufanya utafiti nikajikuta nimevutiwa
na mgahawa huu wa kisasa uliyopo Biafra eneo la Kinondoni B. Sikuwa nikihisi njaa
hivyo nikaagiza kikombe kimoja cha maziwa fresh na kuketi nje ya magahawa ule
sehemu yenye viti na meza inayotazamana na barabara kubwa ya lami.
Niliendelea kukaa eneo lile kwa muda mrefu huku nikisubiri simu ya Zera inifikie.
Mara kwa mara niliichukua simu yangu na kuitazama katika namna ya kutarajia
kuiona namba mpya ikianza kuita lakini hilo halikutokea. Mvua ilinyesha ikaacha
kisha ikanyesha na kuacha tena katika vipindi tofauti lakini simu ya Zera haikunifikia.
Kikombe cha maziwa kilipoisha nikaagiza kingine huku nikiendelea kuununua muda.
Watu walikuja na kuondoka wakiniacha bado nikiwa nimeketi eneo lile hata hivyo
simu ya Zera bado haiukunifikia. Mwishowe nikakata tamaa kabisa na kuamua
kufanya maamuzi ya kuondoka eneo lile.
Maelekezo juu ya wapi yalipokuwa makazi ya Zera nilikuwa bado nikiyakumbuka
vizuri hivyo nilipofika kwenye kituo cha daladala cha Kanisani katika barabara ya
Morocco nikaingia upande wa kulia nikikatisha katika barabara za mitaa. Haikuwa kazi
ngumu kuufikia ule mtaa wa Ukutavuka na baada ya kuchunguza na kuuliza hatimaye
nikaifikia nyumba aliyokuwa akiishi Zera. Nyumba hiyo ilikuwa ikitazamana na duka
kubwa la madawa liitwalo MM Pharmacy kama alivyokuwa ameniambia Zera mara ya
mwisho tulipokutana.
Niliegesha gari langu hatua chache kabla ya kulifikia geti la nyumba ile kisha
nikashuka na kuzitupa hatua zangu kwa utulivu kuiendea nyumba ile. Kulikuwa na
watu wachache waliokuwa wameketi nje ya baraza za nyumba za jirani zilizokuwa
zikitazamana na ile nyumba aliyokuwa akiishi Zera. Watu hao waligeuka wakinitazama
wakati nilipokuwa nikilikaribia geti la ile nyumba hata hivyo sikuwatilia maanani.
Nilipolifikia lile geti nikagundua kuwa mlango mdogo wa lile geti ulikuwa
umefungwa nje kwa komea hivyo nikalifyatua lile komea kisha nikausukuma ule
mlango na kuzama ndani. Kitendo cha kuuona ule mlango wa geti ukiwa umefungwa
kwa nje sikuwa nimetarajia kumuona mtu yeyote akija na kunikaribisha kwenye
nyumba ile kama siyo kuchungulia dirishani na hilo halikutokea. Ile nyumba ilikuwa
kimya bila dalili za uwepo wa mtu yeyote eneo lile.
Ilikuwa nyumba ndogo ambayo ujenzi wake ulikuwa ni wa namna ya kizamani
na usiyo wa gharama kubwa. Nje ya nyumba ile kulikuwa na bustani ndogo ya maua
yaliyopandwa bila kufuata mpangilio mzuri lakini bado yalipendeza. Nilimaliza
kuzipanda ngazi za baraza ya nyuma ile na hapo nikajikuta nikitazama na mlango wa
mbele wa ile nyumba.
Nilisimama kidogo nikiupima utulivu wa eneo lile kisha nikaanza kubisha hodi.
Hata hivyo nilibisha hodi mara kadhaa lakini hakuna mtu aliyeniitikia na hapo nikahisi
kuwa mle ndani ya ile nyumba hapakuwa na mtu. Hivyo nikapachika funguo zangu
malaya kwenye kufuli la mlango wa grill na baada ya muda mfupi kufuli lile likafunguka
hivyo nikaufungua ule mlango wa grill na kujikuta nikitazama na mlango mwingine
wa mbao ambao pia kwa msaada wa zile funguo mlango ule ulifunguka na hapo
nikausukuma na kuingia ndani.
Niliingia ndani ya nyumba ile na kusimama huku nikiyatembeza macho yangu.
Mandhari ya sebule ya nyumba ile yakanitanabaisha kuwa Zera alikuwa ni msichana
aliyekuwa akijipenda.
Kulikuwa na seti moja ya makochi ya sofa za kisasa,jokofu kubwa lililokuwa
kwenye kona ya sebule ile,sistimu nzuri ya muziki,meza fupi ya mbao iliyokuwa
katikati ya makochi yale na ukutani kulikuwa kumetundikwa picha ya Zera. Zaidi ya
pale sikuona kitu chochote cha kunivutia hivyo nikaelekea vyumbani.
Baada ya muda mfupi nikawa nimemaliza uchunguzi wangu mle ndani pasipo
kupata kitu chochote cha maana. Zera pia hakuwepo mle ndani na hapo nikaanza
kuhisi kuwa uchunguzi wangu mle ndani haukuwa na maana yoyote. Nilirudi tena
kule sebuleni huku nikiwa nimekata tamaa juu ya kile nilichokuwa nikikichunguza.
Nilitulia nikifikiri na hapo nikaanza kuhisi kuwa Zera alikuwa msichana tapeli
aliyekuwa akitaka kucheza na akili yangu. Hatimaye nikaketi kwenye kochi moja la
pale sebuleni huku nikitafakari namna ya kufanya. Nilipoitupia macho saa yangu ya
mkononi fikra mpya zikachipuka akilini wangu.
Ulikuwa umesalia muda mfupi kabla ya kutimia saa kumi na mbili jioni na kwa
mujibu wa kumbukumbu zangu ni kuwa ratiba ya Zera kuingia kule Vampire Casino
ilikuwa saa mbili usiku. Kwa dhana ile ni kuwa kulikuwa na muda wa masaa mawili na
ushei kabla ya kutumia saa mbili usiku. Hivyo muda huo wa masaa mawili ungeweza
kumtosha Zera kurudi kutoka huko alikokuwa na kujiandaa tayari kwenye kazini.
Fikra zile zikanirejeshea matumaini moyoni mwangu huku nikiuachia mwili wangu
ustarehe vizuri kwenye lile kochi nililoketi pale sebuleni. Subira ilikuwa silaha kubwa
katika harakati zangu hivyo niliendelea kuketi pale kwenye kochi sebuleni nikisubiri
huku nikiyatembeza macho yangu huku na kule.
Hatimaye macho yangu yakatua juu ya karatasi ndogo iliyokunjwa iliyokuwa chini ya
ile meza ndogo ya mbao pale sebuleni. Nikaichukua karatasi ile na kuanza kuichunguza
na wakati nikifanya hivyo kalamu ndogo ya wino ikaanguka chini. Nikaiokota kalamu
ile na kuanza kuichunguza na kwa kufanya hivyo mikono yangu ikapata muambukizi
wa harufu nzuri ya manukato ya kike. Hali ile ikanitanabaisha kuwa ile kalamu ilikuwa
imetoka kutumika muda mfupi uliyopita. Hatimaye nikaichukua ile karatasi na kuanza
kuipekua katika namna ya kutafuta wino wa kalamu ile ulipotumika.
Ilikuwa karatasi ndogo iliyochanwa kutoka sehemu fulani na mara tu nilipoifunua
karatasi ile nilichokiona lilikuwa ni jina la hoteli moja maarufu iliyopo kwenye ufukwe
wa Coco Beach jijini Dar es Salaam. Nilikuwa nikiifahamu vizuri hoteli ile kwani mara
kwa mara niliwahi kufika kwenye hoteli ile wakati nilipokuwa kwenye harakati zangu
huko nyuma.
Nililitazama jina la hoteli ile kwa uyakinifu huku nikishindwa kuunda hoja yoyote
kichwani mwangu. Hati iliyotumika kuandika jina la hoteli kwenye ile karatasi ilikuwa
mbaya sana kwani huwenda mwandishi alikuwa na haraka sana wakati alipokuwa
akiandika. Nikayapeleka macho yangu nikitazama pale juu ya ile meza na hapo
nikauona waya wa chaja ya simu ukiwa umetelekezwa.
Akili yangu ikaanza kufanya kazi haraka na kuniletea majibu kuwa kulikuwa na
simu iliyokuwa ikichajiwa pale mezani na simu hiyo ilipoanza kuita huwenda mpokeaji
alikuja na kuipokea kisha akatumia kalamu ile kuandika jina la hoteli ile kwenye
ile karatasi akiwa na nia ya kuweka kumbukumbu ya jina la hoteli aliloambiwa na
mpigaji wa simu hiyo. Hisia zangu zikaniambia kuwa sikupaswa kuendelea kukaa pale
sebuleni na kumsubiria Zera arudi mle ndani na badala yake nilipaswa kumfuta huko
alipokuwa.
Nilitoka nje ya nyumba ile na kufunga milango. Nilipotoka nje ya geti la ile nyumba
nikaharakisha kuliendea gari langu na muda mfupi baadaye nilikuwa mbali na mtaa
ule.
Nilikuwa na hisia kuwa endapo ningepita barabara kubwa ningeweza kuchelewa
kule niendako kutokana na foleni kubwa ya magari wakati ule wa jioni. Hivyo mara
baada ya kuingia barabara ya Morocco mbele kidogo upande wa kulia nikaingia barabara
ya mtaa wa Magangamwanza. Barabara ile ikanisafirisha hadi pale nilipokuja kukutana na
barabara ya mtaa wa Ruhinde halafu mbele kidogo nikaingia upande wa kulia nikiifuata
barabara ya Madai crescent. Mara tu nilipoingia kwenye bararabara ile nikapishana na
daladala chache zilizokatisha safari hata hivyo hakukuwa na foleni kubwa hivyo muda
mfupi baadaye nikaja kutokezea kwenye barabara kubwa ya magari ya Ali Hassan
Mwinyi.
Nilipoingia kwenye barabara ya Ali Hassan Mwinyi nikasafiri kidogo kama
ninayeshika uelekeo wa eneo la posta kuu lakini sikwenda mbali hivyo mbele
kidogo nikaingia upande wa kushoto nikiifuata barabara ya Bongo clos. Barabara ile
ikanikutanisha na barabara ya Kenyatta drive ambayo kwa mbele ilikuja kunikutanisha
na ile barabara ya Toure drive. Hivyo bahari ya Hindi nikawa nikiiona kwa upande wa
kulia kwangu.
Kulikuwa na foleni kubwa kiasi katika barabara ya Toure drive wakati huu wa jioni
hata hivyo ilinilazimu kwa mara kadhaa kuvunja sheria za barabarani na hatimaye
nikapata upenyo mzuri na kukanyaga mafuta na kuendelea na safari yangu. Niliendelea
kuendesha gari langu na baada safari fupi nikawa nauona ufukwe wa Coco beach kwa
upande wa kulia.
Usiku ulikuwa umeanza kuingia hivyo wakati huu mandhari ya bahari ya Hindi
yalikuwa ya kupendeza sana. Katika sehemu fulani niliziona taa kubwa za meli
zilizokuwa zikisogea taratibu kutia nanga katika bandari salama jijini Dar es Salaam.
Fikra zangu zilipotulia taswira ya Zera ikaumbika tena kichwani mwangu huku
nikianza kujiuliza maswali chungu mzima kichwani. Barabara ya Toure drive ilikuwa
tulivu kiasi na katika maeneo fulani barabara hiyo ilikatisha katikati ya vichaka vidogo
vya miti ya mikoko huku ikipakana na majumba makubwa na hoteli za kifahari
zilizokuwa zikitazamana na bahari.
Hatimaye nikakiona kibao kikubwa cha barabarani kinachoelekeza mahali
ilipokuwa ile hoteli ambayo jina lake nilikuwa nimeliona kwenye ile karatasi iliyokuwa
juu ya meza sebuleni kwa Zera. Kukiona kibao kile cha barabarani nikapunguza
mwendo na kukata kona nikiufuata uelekeo wa kile kibao upande wa kulia. Baada ya
umbali mfupi mara nikaiona ile hoteli.
Ilikuwa ni hoteli kubwa yenye hadhi ya nyota nne. Hoteli hiyo ilikuwa ikitazamana
na ufukwe wa bahari ya Hindi. Kulikuwa na magari machache yaliyokuwa yameegeshwa
nje ya hoteli ile hivyo nikatafuta sehemu nzuri ya maegesho na kuegesha gari langu.
Kabla ya kushuka nilitulia kidogo ndani ya gari huku nikiyachunguza mandhari
yale na wakati nikifanya hivyo nikaanza kuhisi ni kama niliyekuwa nikiendeshwa zaidi
na hisia zangu kuliko uhalisia wa mambo ulivyokuwa. Nilimkumbuka Zera na hapo
nikaanza kuhisi ugumu wa kumtafuta msichana yule niliyekuwa nikimfahamu kwa
jina moja tu katika hoteli kubwa kama ile kwani sikuwa na namba yake ya simu wala
anwani yake yoyote ambayo ingeniwezesha kumfikia. Kwa kweli nilikuwa nimefanya
makosa makubwa sana kwa kutokuchukua namba yake ya simu mara ya mwisho
tulipokutana kule kwenye kile chumba cha Vampire Casino.
Hatimaye niliyapeleka macho kuitazama saa ya kwenye dashibodi ya gari kisha
nikafungua mlango wa gari na kushuka nikielekea sehemu ya mapokezi ya ile hoteli.
Msichana mzuri mhudumu wa mapokezi yale akanikaribisha kwa bashasha zote
wakati nilipokuwa nikifika eneo lile.
“Karibu kaka”
“Ahsante!” nilimwambia msichana yule mrembo huku usoni nikitengeneza
tabasamu la kirafiki.
“Namuulizia rafiki yangu” nilimwambia msichana yule aliyekuwa ameketi nyuma
ya meza yenye umbo la nusu duara na kompyuta moja ya mezani mbele yake.
“Yupo hapa hotelini?”
“Bila shaka!” nilimwambia kwa kujiamini.
“Nitajie jina lake” yule msichana akaniambia na kwa kuwa sikuwa nikiyafahamu
majina yote ya Zera nikapata kigugumizi kidogo.
“Anaitwa Zera” nilimwambia yule mhudumu wa mapokezi na hapo nikamuona
akianza kushughulika na kompyuta yake pale mezani. Nilitulia huku nikiyatembeza
macho yangu mle ndani ukumbini na wakati huo pia nikiomba uchunguzi wangu
ufanikiwe.
“Alikuambia kuwa angefika hapa saa ngapi?” yule msichana akaniuliza huku
akiendelea kushughulika na kompyuta ya pale mapokezi.
“Kati ya saa nane na saa tisa mchana wa leo” nilimwambia yule msichana huku
nikifikiria na hapo nikamuona yule dada akiyapeleka macho yake tena kwenye kioo
cha ile kompyuta na hapo ukimya ukafuatia. Yule msichana akaendelea kushughulika
na ile kompyuta na baada ya muda akainua macho yake akinitazama.
“Katika orodha ya majina ya watu walioingia leo hotelini hapa hakuna jina hilo”
yule msichana akaniambia na nilipomchunguza nikaona hakika katika maneno
yake na hapo nikajisikia kukata tamaa.
“Anaitwa Zera” nilirudia kumwambia yule dada kwa msisitizo.
“Hatuna mteja mwenye hilo jina na kila mteja anayeingia ndani ya hii hoteli taarifa
zake ni lazima tuwenazo hapa mapokezi. Huna namba yake ya simu?” yule msichana
akaniuliza.
“Hapatikani kwenye simu” nilimwambia yule msichana huku nikifikiria nini cha
kufanya. Mashaka juu ya Zera yalikuwa yameanza kuniingia taratibu na kwa kweli
sikufahamu nilipaswa kufanya nini. Kulikuwa na hoteli nyingine za jirani na eneo lile
hata hivyo wazo la kwenda kwenye hoteli zile na kumuulizia Zera nikaliweka kando
pale nilipohisi kuwa huwenda mambo yangekuwa yaleyale.
“Nashukuru sana dada wacha niende kwani huwenda yeye ndiye aliyekosea
kunipa maelekezo”
“Karibu tena!”
Niliagana na yule msichana wa mapokezi na hapo nikaanza kuondoka eneo lile
nikielekea kwenye yale maegesho sehemu nilipokuwa nimeegesha gari langu. Wazo
la kuelekea Vampire Casino lilikuwa limenijia haraka akilini na sikutaka kujiuliza mara
mbili.
Niliingia kwenye gari langu na hapo nikaanza safari ya kuelekea Vampire Casino
huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu juu ya Zera. Niliendesha gari langu
taratibu huku akili yangu ikisumbuka kufikiria. Muda mfupi uliyofuata nikawa
nimetokezea kwenye barabara kuu ya lami iliyokuwa ikikatisha mbele kidogo ya
hoteli ile. Niliendelea kuendesha gari langu taratibu huku nikiyatembeza macho yangu
huku na kule katika namna ya kutafuta majibu ya maswali mengi yaliyokuwa yakipita
kichwani mwangu.
Niliendelea kuendesha gari langu huku mjadala mzito ukiendelea kupita kichwani
mwangu. Usiku ulikuwa umeingia na mvua kubwa ilikuwa imeanza kunyesha. Nikiwa
naendelea na safari yangu kwenye barabara ile kuu ya lami mara macho yangu
yakajikuta yakivutika na barabara nyingine ya lami ya zamani iliyokuwa ikichepuka
kuingia upande wa kushoto.
Kuiona barabara ile kukanipelekea nipunguze mwendo wa gari na kugeuka
nikiitazama vizuri ile barabara na hatimaye nikajikuta nikishawishika kuifuata barabara
ile. Hivyo nikaingiza gia na kukanyaga mafuta nikikunja kona kuufuata uelekeo wa
barabara ile hafifu ya lami ya zamani.
Ilikuwa ni barabara nyembamba ya lami iliyokuwa ikishuka kuelekea kwenye
fukwe ya bahari. Barabara ile yenye mashimo madogo madogo ilikuwa ikikatisha
katikati ya vichaka vya miti ya mikoko huku ikiwa imesongwa na nyasi ndefu zilizoota
kando yake.
Niliendesha gari langu taratibu huku nikiendelea kuichunguza barabara ile na kwa
kufanya vile haraka nikajua kuwa ilikuwa ni barabara isiyotumika mara kwa mara.
Niliendelea kuifuata barabara ile na mwisho nikakutana na magofu chakavu sana
yaliyotelekezwa miaka mingi.
Nilishuka kwenye gari na bastola yangu mkononi huku nikielekea kwenye yale
magofu. Nilipofika nikaanza kuyachunguza magofu yale chakavu na kwa wakati ule
yalikuwa yakionekana kama kuta mbovu za jengo la kale zilizosimama. Paa la gofu lile
lilikuwa limeezuliwa na milango na madirisha yake yalikuwa yameondolewa na kuacha
matundu makubwa yanayotisha kuyatazama gizani.
Niliingia ndani ya gofu lile na katika sehemu zake za ndani kulikuwa na nyasi
nyingi zilizoota na kutengeneza vichaka vidogovidogo.
Nilimaliza kuyazunguka magofu yale yaliyotelekezwa miaka mingi na matokeo ya
uchunguzi wangu yakanitanabaisha kuwa magofu yale yalikuwa ya Beach resort moja
maarufu iliyotelekezwa miaka mingi iliyopita. Magofu yale yakitazamana na fukwe
kubwa ya bahari ya Hindi yenye upepo mwanana.
Nilisimama mbele ya magofu yake huku nikiutazama ufukwe wa bahari ya Hindi
na kwa kweli hata ufukwe ule ulikuwa umetelekezwa kwani vichaka vya nyasi ndefu
vilikuwa vimeota kila mahali. Nilitazama upande wa kushoto na hapakuwa na njia ya
kuelekea mbele zaidi kwani sehemu ya ufukwe kwa upande ule ilikuwa imemezwa na
mwamba mkubwa wa matumbawe ya baharini hivyo hapakuwa na uelekeo wowote
kwa upande ule.
Upande wa kulia wa fukwe ile kulikuwa na mchanga mwingi hata hivyo baada
ya kuwasha kurunzi yangu na kumulika upande ule nikagundua kuwa hapakuwa na
dalili zozote za uwepo wa kiumbe hai eneo lile. Upepo mkali wa baharini ulikuwa
ukivuma na kwa mbali niliweza kuiona mandhari ya kupendeza ya jiji la Dar es Salaam
iliyotawaliwa na majengo marefu ya ghorofa yaliyokuwa yakiwaka taa usiku ule.
Kwa kweli sikuwa nimeongeza kitu chochote katika uchunguzi wangu eneo lile
na badala yake ni kama niliyekuwa nimeongeza idadi ya vificho vipya vya jiji la Dar
es Salaam nilivyowahi kuvifika. Hivyo hatimaye niliondoka sehemu ile na kurudi kule
nilipokuwa nimeegesha gari langu. Nilipofika nikafungua mlango na kuingia ndani
nikianza safari ya kurudi kule nilipotoka.
Usiku ulikuwa ukiendelea kunawiri na saa ya kwenye dashibodi ya gari mle ndani
ilionesha kuwa dakika chache zilikuwa zimesalia kabla ya kutimia saa mbili usiku.
Muda wa Zera kuingia kule Vampire Casino kama alivyokuwa amenieleza wakati
tulipoonana kwa mara ya mwisho.
Niliendelea kuwaza lakini kamwe sikuiruhusu papara katika harakati zangu. Hivyo
niliendesha gari langu taratibu na wakati nikifanya vile mawazo mengi yalikuwa
yakipita kichwani mwangu na kunifanya nihisi kuwa harakati zangu zilikuwa zikienda
taratibu sana tofauti na nilivyokuwa nikidhani hapo awali.
Niliendelea kuendesha gari langu taratibu na baada ya muda nikawa nimefika
sehemu fulani ambayo nilisimama baada ya kuona kuwa kando yangu upande wa
kushoto wa eneo lile kulikwa na barabara hafifu ya nyasi iliyokuwa ikishuka katikati
ya miti ya mikoko kuelekea chini kwenye ufukwe wa bahari. Nikashusha kioo cha
gari cha ubavuni na kuitazama vizuri barabara ile. Kwa kufanya vile nikagundua kuwa
barabara ile hafifu ya nyasi ilikuwa imepitiwa na gari muda mfupi kama siyo masaaa
machache yaliyopita.
Unapokuwa huna chanzo muhimu cha upelelezi kila kitu mbele yako unaweza
kukishuku hivyo nikaegesha gari langu kando ya barabara ile. Mvua kubwa ilikuwa
ikiendelea kunyesha hivyo nikalichukua koti langu refu na jeusi la mvua nililokuwa
nimeliweka kwenye siti ya nyuma na kulivaa kisha nikavuta droo ya kwenye dashibodi
ya gari na kuchukua bastola yangu mkononi. Hatimaye nikafungua mlango wa gari na
kushuka huku kwa msaada wa ile kurunzi yangu ndogo yenye mwanga mkali nikaanza
kumulika nikishuka kule chini kuifuata ile barabara hafifu ya nyasi ielekeayo ufukweni.
Hisia mbaya zikawa zikiongezeka taratibu kichwani mwangu kwa kadiri niliyokuwa
nikizitupa hatua zangu zilizopwaya kushuka kule chini. Wakati nikiendelea kutembea
nikaanza kuhisi kuwa hata mapigo ya moyo wangu nayo yalikuwa yameanza kwenda
mbio sambamba na baridi nyepesi iliyoanza taratibu kuutafuna mtima wangu. Hali ile
ikanipelekea niikamate vema bastola yangu mkononi.
Niliendelea kushuka kule chini huku nikiwa nimechukua tahadhari zote na baada
ya muda nikawa nimefika sehemu ambayo alama za magurudumu ya lile gari lililoingia
kwenye ile barabara hafifu ya nyasi zilikuwa zimekomea pale kabla ya gari hilo baadaye
kugeuza na kurudi lilipotoka.
Nilisimama eneo lile nikalichunguza kwa hadhari na kwa kweli sikuona viashiria
vyovyote vya sababu ya mtu kuingia na gari eneo lile na kusimama. Au labda ufanyaji
wa ngono ya wizi kwa watu maarufu waliokuwa wakiyakimbia macho ya watu.
Nilijikuta nikiwaza baada ya kukumbuka kuwa mchezo huo wa kishetani ulikuwa
umekithiri sana katika baadhi ya maeneo ya vificho vya jijini Dar es Salaam hususan
sehemu za fukwe ya bahari ya Hindi.
Nilimulika vizuri kwa kurunzi yangu eneo lile na hapo nikaziona alama za
magudurumu ya gari namna yalivyogeuza eneo lile na kurudi yalipotoka. Nikaendelea
kutazama alama ya magurudumu yale huku nikijiuliza kama dereva wa gari lile alikuwa
amekosea njia au lah!. Hata hivyo wazo langu liliyeyuka ghafla baada ya kuona alama za
viatu vya watu zilizoshuka kuelekea chini kwenye ile fukwe ya bahari. Nilipozimulika
alama zile za viatu nikagundua kuwa zilikuwa ni za viatu vya watu tofauti vikiwemo
viatu vya kike kwa namna visigino vyake vilivyochimba mchanga. Alama zile za viatu
ziliendelea kushuka kule chini zikikatisha katika vichaka vya miti ya mikoko.
Tukio lile likanistajaabisha sana na mara ile nikazidi kuwa makini nikizifuatilia
alama za viatu vile vya watu kwa nyuma. Niliendelea kuzifuatilia alama zile nikikatisha
katikati ya vichaka hafifu vya miti na hatimaye nikawa nimetokezea kwenye ufukwe
wa bahari. Kulikuwa na upepo mkali uliokuwa ukivuma eneo lile na matundu ya pua
yangu yalikaribishwa na harufu kali ya chumvi ya maji ya bahari.
Nilisimama kwa utulivu nikiutazama ufukwe ule ingawaje giza zito la eneo lile
halikunipa nafasi nzuri ya kufanya vizuri uchunguzi wangu. Nadharia ya wanajiografia
juu ya kupwa na kujaa kwa maji baharini ilikuwa ikifanya kazi eneo lile kwani wakati
ule wa usiku maji ya bahari yalikuwa yamejaa na kufunika sehemu kubwa ya fukwe ile.
Zile alama za viatu sasa zilionekana zimesimama eneo lile kwa namna mchanga
wake ulivyokuwa ardhini. Nilimulika eneo lile kwa kurunzi yangu mkononi huku
nikiendelea kuchunguza na badala ya kuona viashiria vyovyote vya matendo ya ngono
kama;nguo ya ndani ya kike au boksa ya kiume iliyosahaulika au mipira ya kondomu
iliyotumika nikashangaa kuona kikuku kilichotelekezwa kama siyo kusahaulika eneo
lile.
Niliinama na kukiokota kikuku kile mchangani na mara nilipokichunguza vizuri
koo langu likanikauka kwa mshtuko. Kile kikuku kilifanana na kikuku kilichokuwa
kimevaliwa na Zera mguuni wakati ule nilipoonana naye kule kwenye kile chumba
cha Vampire Casino. Kile kikuku kilikuwa ni kikuku cha aina yake kilichopambwa kwa
madini tofauti yanayometameta na kupendeza sana. Niliendelea kuchunguza eneo
lile na sikuona kitu kingine cha kuyavuta macho yangu hivyo kile kikuku nikakitia
mfukoni na kuendelea kuzifuatilia zile alama za viatu. Katika kuendelea kuzichunguza
alama zile nikashangazwa na kutoweka kwa zile alama za viatu vya kike hata hivyo
tukio lile halikunifanya nisitishe kuendelea na uchunguzi wangu.
Niliendelea kumulika eneo lile huku nikizifuata zile alama za viatu ambazo kwa
wakati huu zilikuwa ni alama tofauti za viatu vya wanaume watatu kwani zile alama za
vile viatu vya kike hazikuonekana tena na katika maeneo fulani niliziona alama zile za
viatu vya kiume zikiwa zinarudi kule zilipotoka.
Hatimaye nikawa nimefika eneo fulani lenye kichaka kikubwa zaidi cha miti ya
mikoko na hapo nikasimama baada ya kuvutiwa na vitu fulani. Mandhari ya eneo lile
yalikuwa yamekosa utulivu kwani nyasi zake hafifu zilikuwa zimekanyagwa ovyo na
zile alama za viatu zilikuwa zimeutibua mchanga wa eneo lile kila mahali.
Niliendelea kuchunguza zaidi eneo lile na mara nikashangazwa kuziona tena zile
alama za viatu vya kike vyenye visigino virefu zikionekana tena eneo lile.
Nilitulia kidogo nikifikiri katika namna ya kuunganisha mlolongo wa matukio
kichwani mwangu na majibu niliyoyapata yakanipelekea nizipanguse taratibu kingo za
mdomo wangu kwa ulimi.
Sasa nilifahamu kuwa yule mwanamke ambaye alama za viatu vyake nilikuwa
nimeziona kule mwanzo kuwa alikuwa amebebwa kutoka kule nilipoziona alama za
viatu vyake hadi sehemu ile niliposimama. Nilipoendelea kuchunguza zaidi nikaona
kuwa kulikuwa na damu katika maeneo fulani ya mchanga wa eneo lile na hali ile
ikazidi kunishangaza.
Hatimaye nikachuchumaa eneo lile na kuanza kuichunguza vizuri ile damu
ambayo sasa nilikuwa na hakika kuwa ilikuwa imetokana na majereha makubwa
mwilini yaliyotokana na shambulizi la risasi au kitu kingine chenye ncha kali kama
kisu. Nilipoendelea kuchunguza vizuri eneo lile mara nikaziona alama za viatu vya
kiume miongoni mwa zile alama tatu za vile viatu vya kiume zikitoka kwenye kile
kichaka na kuelekea mbele ya ule ufukwe.
Nilipozifuatilia kwa karibu alama zile za viatu mara nikaziona kuwa zilikuwa
zimepotelea kwenye yale maji ya bahari huku zikiwa zimechimba zaidi kwenye
mchanga na hapo hisia kamili zikajengeka kichwani mwangu. Hisia zikaniambia kuwa
sehemu fulani katika yale maji ya bahari yaliyojaa na kufunika ile fukwe kulikuwa na
kaburi la kificho. Moyo wangu ukapiga kite kwa nguvu pale nilipojikuta nikimfikiria Zera
Niliyatazama maji yale ya bahari na hapo nikayaona ni kama yaliyokuwa yameficha
siri kubwa sana za tukio lililotokea eneo lile masaa machache yaliyopita.
Usiku huu maji ya bahari yalikuwa yamejaa na hivyo kuimeza sehemu kubwa
ya fukwe ile hata hivyo nilikuwa makini sana kwenye hesabu za makadirio. Kwani
niliwaza kuwa kwa vyovyote vile endapo kungekuwa na kaburi eneo lile basi kaburi
hilo lisingekuwa mbali sana kutoka katika ufukwe ule wa bahari. Nilitaka kulithibitisha
hilo mapema kwani kusubiri hadi kesho kupambazuke huwenda kusingenipa nafasi
nzuri ya kufanya uchunguzi wangu.
Hivyo nikavua nguo zangu na kuziweka kando ya fukwe ile kisha nikaanza kuingia
kwenye yale maji ya bahari nikiufuata uelekeo wa zile alama za viatu. Niliingia kwenye
maji yale taratibu huku nikijaribu kuvuta hisia juu ya kile nilichokuwa nikikikanyaga
chini. Maji yalikuwa mengi na uzito wa mawimbi ya bahari mara kwa mara uliiyumbisha
miguu yangu pale nilipokuwa nikijaribu kukanyaga chini.
Baada ya hangaika ya hapa na pale hisia kutoka kwenye nyayo za miguu yangu
zikanitanabaisha kuwa nilikuwa nimekanyaga tuta dogo la mchanga sehemu ambayo
yale maji ya bahari yalikuwa yamenifikia kiunoni. Nilisimama eneo lile huku nikijaribu
kuvuta hisia juu ya kile nilichokuwa nimekikanyaga.
Hatimaye niliinama eneo lile na kuanza uchunguzi wangu. Sikuwa na nyenzo
yoyote ya kufukulia tuta lile la mchanga hivyo ilikuwa kazi ngumu. Mara kwa mara
maji yale ya bahari yalinisukasuka hata hivyo niliongeza jitihada zangu katika kulifukua
tuta lile la mchanga kwa mikono yangu na hatimaye nikafanikiwa.
Baada ya kufukua kwa muda mrefu tuta lile la mchanga hatimaye nikawa
nimefanikiwa kuushika mkono wa mtu. Kwa kweli roho iliniuma sana kila nilipojikuta
nikimfikiria Zera. Hata hivyo nikaendelea kufukua lile tuta la mchanga huku nikiuvuta
ule mkono. Baada ya kitambo kirefu cha lile zoezi likawa limekamilika.
Ulikuwa mwili wa mtu kwa namna mikono yangu ilivyohisi. Nikauvuta ule mwili
taratibu hadi kando ya ile fukwe ya bahari. Ilikuwa kazi ngumu kwa vile mwili ule
ulikuwa umeanza kuwa mzito kutokana na kukaa kwenye maji kwa muda mrefu.
Nilivyomaliza zoezi lile nikazichukua zile nguo zangu na kuzivaa kisha nikarudi pale
nilipouweka ule mwili wa yule mtu huku nikiwa na kurunzi yangu mkononi.
Nilifika pale nilipouweka ule mwili na kuanza kumulika kwa ile kurunzi yangu.
Nilichokiona pale chini kikapeleka simanzi kubwa moyoni mwangu. Mwili wa Zera
ulikuwa mbele yangu ukinitazama huku mdomo wake ukiwa wazi. Mikono na miguu
yake ilikuwa imekakamaa na nilipouchunguza uso wake nikaona kuwa ulikuwa na
majereha katika baadhi ya maeneo. Mdomo wake ulikuwa umechanika na damu
nyingi ilikuwa imevilia jichoni. Zera alikuwa amevaa mavazi yake vizuri mwilini na
hivyo nilipomchunguza nadharia ya kubakwa iliyoanza kujengeka kichwani mwangu
ikatoweka.
Niliendelea kuuchunguza vizuri ule mwili wa Zera na wakati nikifanya hivyo
nikagundua kuwa kulikuwa na matundu mawili ya risasi kifuani mwake na sumu ya
risasi hizo ilikuwa imeupelekea mwili wake kuanza kuvimba eneo lile. Kwa kweli
nilisikitika sana huku roho ikiniuma kwa kumpoteza rafiki yangu Zera. Kilichoniumiza
zaidi ni pale nilipohisi kuwa kifo chake kwa namna moja au nyingine kilikuwa
kimesababishwa na kule kuonana kwetu.
Swali likabaki kuwa ni kwa nini Zera aliuwawa kikatili namna ile?. Kipi kibaya
alichokuwa amekifanya hadi kosa lake lithaminishwe na kifo cha kikatili namna ile?.
Niliendelea kujiuliza pasipo kupata majibu na tukio lile lilikuwa limenisikitisha sana.
Sasa nilifahamu kuwa nilikuwa nikishughulika na mkasa hatari nisioufahamu
mwanzo wala mwisho wake. Sikuwa na shaka kuwa uwepo wangu sasa ulikuwa
ukifahamika na watu hao hatari na kwa maana nyingine ni kuwa watu hao walikuwa
tayari kuinunua roho yangu kwa gharama yoyote.
“Yeyote aliyehusika na kifo cha Zera alipaswa kujiandaa kulipa fidia” nilijiapia
huku nikiusogeza vizuri ule mwili wa Zera na kuulaza kwenye nyasi laini za eneo lile.
Sikutaka kuendelea kupoteza muda eneo lile hivyo niliusogeza mwili wa Zera na
kuuweka katika eneo lisiloweza kufikika na maji yale ya bahari yaliyokuwa yakiendelea
kuongezeka ili uweze kuonekana kwa urahisi. Nilipomaliza nikaanza kuondoa
viashiria vyote vya uwepo wangu eneo lile ili uchunguzi wowote ambao ungefanywa
na polisi usiweze kunihusisha. Kupitia kamera yangu ndogo ya digital iliyokuwa
mfukoni nikachukua picha chache za ile maiti ya Zera kama kielelezo makini cha
uchunguzi wangu.
Nilipomaliza nikaondoka eneo lile nikielekea kule barabarani nilipokuwa
nimeegesha gari langu. Zera alikuwa ameuwawa pamoja na taarifa muhimu ambazo
huwenda zingeweza kunisaidia katika upelelezi wangu. Sikuwa na namna ya kufanya
badala yake nilihitaji utulivu mkubwa katika kupanga juu ya hatua inayofuata.
Nilibonyeza kitufe cha mwanga na kutazama majira kwenye saa yangu ya mkononi
na hapo nikagundua kuwa dakika chache zilikuwa zimesalia kabla ya kutimia saa nne
usiku. Nilikatisha kwenye kichaka kile hafifu cha miti ya mikoko na baada ya muda
mfupi nikawa nimelifikia gari langu kando ya barabara ile ya lami pale nilipokuwa
nimeliegesha kisha nikafungua mlango na kuingia ndani. Sikuona kama lingekuwa
ni jambo la busara kuitelekeza ile maiti ya Zera katika ufukwe ule hivyo kupitia simu
yangu nikawapigia polisi na kuwafahamisha uwepo wa maiti ya Zera eneo lile huku
nikikwepa maswali mengine yasiyokuwa na msingi. Usiku bado ulikuwa na mengi ya
kusimulia.
KIJIOGRAFIA JENGO LA Vampire Casino lilikuwa kivutio kwa wateja
wastaarabu wasiopenda rabsha kwa namna lilivyokuwa kwenye mandhari
tulivu katikati ya majengo marefu ya ghorofa na majumba makubwa ya
kifahari ya watu waliowekeza vizuri duniani.
Kwa upande wa kushoto jengo laVampire Casino lilipakana na jengo refu la ghorofa
la kampuni moja maarufu ya mawasiliano. Kulia kwake jengo hilo lilipakana na hekalu
kubwa la mabaniani na baadhi ya maghorofa ya shirika la nyumba la taifa.
Nyuma yake jengo lile lilikuwa likitazamana na uwanja mkubwa wa golf,mabwawa
makubwa matatu ya kuogelea na viwanja vingine vya mazoezi ambavyo vilikiwa ndani
ya uzio mkubwa wa ukuta mrefu.
Ili kupata taswira nzuri ya kitu kilichokuwa kikiendelea upande wa mbele wa
Vampire Casino ingemlazimu mtu asimame mbele au kupanda juu ya jengo refu la
biashara la Rupture & Capture lililokuwa mbele kiasi cha umbali usiyopungua mita mia
mbili likitazamana na Vampire Casino kando ya barabara ndogo ya lami.
Uwepo wa ofisi nyingi tofauti katika jengo refu la ghorofa la biashara la Rupture
& Capture kulikuwa kumetengeneza mwanya mzuri kwa mtu yeyote kuweza kuingia
kwenye jengo lile la ghorofa la biashara bila kuulizwa wala kutiliwa mashaka na mtu
yeyote na kwa wakati wowote.
Muda wote wa mchana Koplo Tsega alikuwa ameutumia katika kufanya
uchunguzi kwenye lile jengo la Rupture & Capture akitathmini hali ya ulinzi na usalama
na miundombinu ya jengo lile kama mfumo wa lifti na ngazi zilizokuwa zikitumika
kutoka kwenye ghorofa moja kwenda kwenye ghorofa jingine. Mfumo wa nishati ya
umeme,vipenyo visivyo ramsi kama nafasi ndogo zilizokuwa baina ya bomba la maji
na kuta za jengo. Milango na madarisha ya dharura,sehemu za maliwato na eneo la
maegesho ya magari.
Ilipofika muda wa alasiri Koplo Tsega akawa amehitimisha uchunguzi wake hivyo
akashuka chini ya jengo lile la Rupture & Capture na kuliendea gari lake lililokuwa
sehemu ya maegesho ya magari ya jengo lile. Muda mfupi baadaye akaondoka eneo lile
huku kichwani akiwa na picha kamili ya mandhari yale ili wakati wa usiku atakaporudi
tena kwenye jengo lile aifanye kazi yake kwa hakika.
Kwa upande mwingine Koplo Tsega alikuwa akijivunia matunda ya utafiti wake.
Kabla ya kufika kwenye jengo lile la biashara la Rupture & Capture alikuwa amepeleleza
taarifa zote muhimu za mienendo ya mtu aliyefahamika kwa P.J.Toddo. Afisa
usalama,mwana itifaki na mkuu wa intelijensia ya tume ya upambanaji na udhibiti wa
biashara haramu ya dawa za kulevya nchini.
Miongoni mwa taarifa alizokuwa amezipata Koplo Tsega kutoka kwenye vyanzo
mbalimbali vya kuaminika ni kuwa mojawapo ya ratiba za P.J.Toddo ni kupenda
kuhudhuria Vampire Casino kila siku usiku baada ya masaa ya kazi. P.J.Toddo alikuwa
akiishi eneo la Mbezi beach na alikuwa ametengana na mkewe. Watoto wake watatu
wote walikuwa masomoni nchi za nje.
_____
SAA KUMI NA MBILI NA NUSU JIONI ILIPOTIMIA Koplo Tiglis aliegesha
gari lake kwenye viunga vya maegesho ya magari vya jengo la biashara la Rupture &
Capture. Wakati huu wa jioni magari yaliyoegeshwa kwenye yale maegesho ya magari
ya jengo lile yalikuwa yamepungua kidogo ukifananisha na ule wakati wa asubuhi na
mchana.
Baadhi ya wafanyabiashara wa jengo lile tayari walikuwa wamefunga biashara zao
na kuondoka hivyo Koplo Tsega hakusumbuka sana katika kupata sehemu nzuri ya
kuegesha gari lake. Muda mfupi uliyofuata Koplo Tsega akashuka kwenye gari lile
huku akiwa amebeba begi jeusi,refu na jembamba mgongoni mwake mithili ya begi la
kuhifadhia gitaa la mwanamuziki.
Jioni hii mwonekano wake ulikuwa tofauti na ule wa siku za nyuma tangu alipoingia
jijini Dar es Salaam. Alikuwa amevaa kofia pana na nyeusi aina ya Sombrero ivaliwayo
aghalabu na watu wa Hispania na Meksiko.
Zile Nywele zake ndefu na laini alikuwa amezinyoa katika mtindo wa kupendeza
uitwao Lowcut. Usoni alikuwa ameyaficha macho yake nyuma ya miwani myeusi
iliyoipendezesha vizuri sura yake. Mdomo wake wenye kingo nyeusi pana na laini
zilizokuwa zimekolea vizuri rangi nyekundu ya Lipstick ulikuwa umeongeza ziada
nyingine katika uzuri wake.
Koplo Tsega alikuwa amevaa Pullneck nyeusi iliyokishika vizuri kiwiliwili chake
huku chini akiwa amevaa suruali nyeusi ya jeans iliyoing’ang’ania vizuri misuli ya nyama
zake mapajani. Buti zake ngumu za ngozi miguuni aina ya Travolta zilimfanya atembee
vizuri kwa kujiamini huku akizitupa hatua zake ndefu kuelekea ndani ya lile jengo refu
la ghorofa la biashara la Rupture & Capture.
Koplo Tsega hakutaka kuyavuta macho ya watu eneo lile hivyo alizitupa hatua
zake kwa haraka akipotelea kwenye lifti ya jengo lile. Alipoingia kwenye chumba kile
cha lifti akabonyeza kitufe cha Top floor na kuiamuru lifti ile imfikishe kwenye ghorofa
ya juu kabisa ya lile jengo. Ile lifti haikuwa busy hivyo ndani ya muda mfupi akajikuta
amefika kwenye ile ghorofa ya juu ya lile jengo.
Kile chumba cha lifti kilipofika ghorofa ya juu na ule mlango wake kufunguka
Koplo Tsega akatoka na kujikuta katikati ya korido pana iliyokuwa ikitazamana na
milango ya ofisi za shirika la bima la Mwananchi Insuarance.
Kupitia milango ya vioo vya ofisi ile baadhi ya wafanyakazi walionekana wakiwa
wameinamia kompyuta zao mezani na wengine wakifanya shughuli nyingine tofauti
za kiofisi. Wafanyakazi wale wakionekana kuzama katika shughuli zao hakuna
aliyejisumbua kuinua kichwa chake na kutazama kwenye ile korido wakati Koplo
Tsega alipokuwa akipita. Milango ya ofisi zile ilikuwa imefungwa na hewa safi ya
kiyoyozi ilikuwa ikikazana kupeleka burudani ya aina yake kwa wafanyakazi wale.
Koplo Tsega aliendelea kutembea kwa haraka akiyakwepa macho ya wafanyakazi
wa ofisi zile na alipofika mwisho wa korido ile upande wa kushoto akajikuta
akitazamana na mlango mfupi mweusi ulioandikwa kwa maandishi meupe FOR
ADMINISTRATIVE USE ONLY.
Akiwa na hakika ya kule alipokuwa akielekea Koplo Tsega akafanya jitihada kidogo
za kufyatua kufuli la mlango ule mdogo. Kufuli lilipofyatuka haraka akaufungua ule
mlango na kuingia mle ndani kisha akaufunga ule mlango nyuma yake bila ya mtu
yeyote kumuona.
Kulikuwa na giza zito ndani ya chumba kile kidogo alichoingia Koplo Tsega hata
hivyo kwa msaada wa penlight ama kurunzi yake ndogo ya kijasusi na nyembamba
mithili ya kalamu ya wino aliweza kuona vizuri mbele ya chumba kile.
Upande wa kushoto wa chumba kile kidogo kulikuwa na Mainswitch iliyokuwa
ikisambaza umeme katika sehemu zote za lile jengo. Mainswitch ile ilikuwa na fyuzi
nyingi zilizopangwa kwa kufuatana na mpangilio wa ghorofa ya kwanza hadi ya
mwisho.
Mbele ya chumba kile kidogo kulikuwa na ngazi nyembamba. Ngazi hizo zilikuwa
zikielekea sehemu ya juu kabisa ya lile jengo la ghorofa la biashara la Rupture & Capture.
Koplo Tsega akazitazama kwa makini ngazi zile huku akiwa na picha kamili ya ile
sehemu ngazi zile zilipokuwa zikielekea. Aliporidhika na kumbukumbu zake akaanza
kuzikwea ngazi zile taratibu.
Alipofika mwisho wa ngazi zile akajikuta akitazamana na mfuniko mdogo wa
mlango wa chuma uliyobanwa vizuri kwa kufuli. Koplo Tsega akaifyatua kufuli ya
mfuniko ule kisha akausukuma ule mfuniko kwa juu na hapo akamalizia kuzikwea
zile ngazi. Muda mfupi baadaye akawa ametokezea sehemu ya juu kabisa ya lile jengo
la biashara la Rupture & Capture.
Mvua ilikuwa imeacha kunyesha hata hivyo manyunyu hafifu hayakukoma
kuanguka kutoka angani ingawa manyunyu hayo bado yasingeweza kumzuia mtembea
kwa miguu. Koplo Tsega mara alipofika kule juu akaurudishia vizuri ule mfuniko
mahala pake na hapo akajikuta akitazamana na mandhari ya sehemu ile ya juu kabisa
ya lile jengo la ghorofa yenye matenki makubwa ya maji. Mfumo wa mabomba mengi
ya maji yaliyotandazwa na kupishana kwenye sakafu ya juu ya jengo lile. Nyungo
nyingi za kunasa matangazo ya runinga pamoja na minara mitatu ya mawasiliano ya
kampuni za mawasiliano zilizokuwa na ofisi zao kwenye jengo lile.
Mandhari ya eneo lile yakampelekea Koplo Tsega atabasamu na kujipongeza
moyoni kwa kufanya uchaguzi makini wa jengo lile kwa kigezo kuwa lilikuwa ni
jengo refu zaidi kupita majengo mengine ya ghorofa yaliyokuwa eneo lile na hivyo
asingeweza kuonekana kirahisi na mtu yoyote wakati akiifanya kazi yake.
Akiwa sehemu ya juu kabisa ya jengo lile la ghorofa la Rupture & Capture. Koplo
Tsega akajikuta akivutiwa na muonekano mzuri wa mandhari ya jiji la Dar es Salaam
kwa baadhi ya sehemu. Mandhari hiyo ikiundwa na barabara nzuri za lami,mpangilio
mzuri wa makazi ya watu katika baadhi ya sehemu,bandari salama na majengo marefu
ya ghorofa yaliyokuwa yakiendelea kupandwa katika baadhi ya maeneo.
Koplo Tsega akayatembeza macho yake akiyatazama mandhari yale kwa utulivu
na hatimaye kuweka kituo akitazama kwenye uwazi mdogo uliofanywa baina ya tenki
moja la maji na ungo mdogo wa Dstv uliokuwa karibu na ukingo wa jengo lile na
hapo tabasamu hafifu likajivinjari usoni mwake. Muda mfupi uliofuata tayari akawa
amelifikia eneo lile na kuanza kazi yake.
Koplo Tsega akalivua begi lake kutoka mgongoni na kuliweka chini kisha
akasogea kwa tahadhari na kuchungulia chini ya jengo lile. Mahesabu yake yalikuwa ya
hakika kwani sehemu ya mbele ya lile jengo la Vampire Casino kutoka pale juu ilikuwa
ikionekana vizuri kuanzia kwenye mlango wa mbele hadi lile eneo la maegesho ya
magari.
Koplo Tsega aliyatuliza macho yake akitazama kule chini ya lile jengo huku
tabasamu jepesi likichomoza usoni mwake kisha akarudi kule alipoliacha begi lake
na kulifungua. Ndani ya begi lile kulikuwa na vifaa vingi tofauti vilivyotenganishwa ili
kurahisisha ubebaji wake. Koplo Tsega akavichukua vifaa vile na kuanza kuunganisha
kifaa kimoja akikipachika juu ya kifaa kingine kwa mikono yake imara iliyokuwa ndani
ya glovu nyeusi.
Muda mfupi uliofuata taswira kamili ya kazi ya mikono yake ikaanza kuumbika
machoni mwake. Mashine ya kutolea uhai wa binadamu kwa wepesi wa aina
yake. Bunduki ya kudungulia. Sniper rifle aina ya 338 Lapua Magnum ilikuwa mbioni
kukamilika. Koplo Tsega alipomaliza zoezi lile akaanza kuzipanga vizuri risasi kwenye
magazine ya bunduki ile na kisha kuipachika mahala pake. Mvua ilikuwa imeanza
kunyesha tena lakini hali hiyo haikuleta kikwazo chochote kwa Koplo Tsega.
Alipomaliza kuzipanga zile risasi akaingiza mkono kwenye lile begi na kuchukua
kifaa cha optic ama darubini kali ya kunasia taswira ya windo kwa wepesi wa aina yake
ambacho alikipachika juu ya ile bunduki na kulifinya jicho lake moja akirekebisha lenzi
hadi pale taswira nzuri ilipoweza kuonekana.
Muda mfupi uliyofuata kazi yote ikawa imekamilika hivyo Koplo Tsega akaichukua
ile bunduki ya kudungulia na kuisogeza kwenye upenyo mzuri uliokuwa ukitazamana
na ile sehemu ya mbele ya Vampire Casino. Alipopata pembe nzuri ya shabaha
akaifyatua Adjustable bi-pod stand ya 338 Lapua Magnum na kuitega vyema. Kilichofuata
baada ya pale ilikuwa ni kusubiri ule muda wa kufanya tukio ufike na tukio lifanyike
kama lilivyopangwa.
Koplo Tsega akajilaza kifudifudi huku kitako cha bunduki ile kikiwa kimetulia
vyema kwenye titi lake la kushoto. Mkono wake wa kushoto kwenye kilimi cha
bunduki na jicho lake moja kwenye Eyepiece lens ya darubini ya bunduki ile.
Mvua kubwa ilikuwa ikinyesha na hali ile haikumfurahisha hata kidogo Koplo
Tsega kwani mbele ya Vampire Casino kila mtu aliyefika na kushuka kwenye gari
alikimbia kwa haraka ndani ya casino ile kwa lengo la kujiepusha na mvua ile kubwa
iliyokuwa ikiendelea kunyesha na hivyo kutengeneza mazingira magumu ya kupata
shabaha nzuri kwa windo lake.
Kupitia ile darubini kali iliyokuwa juu ya bunduki yake Koplo Tsega aliweza
kuyachunguza kwa wepesi magari yote yaliyokuwa yameegeshwa kwenye eneo la
maegesho la Vampire Casino. Hakuliona gari la mtu aliyekuwa akimtafuta na hali ile
ikamtia mashaka huku akiwaza kuwa huwenda mtu huyo alikuwa amepata dharura
ambayo ilishindwa kumfikisha eneo lile kwa wakati kama siyo kutokufika kabisa. Hata
hivyo bado hakukata tamaa zaidi ya kuendelea kusubiri.
Mvua kubwa iliendelea kunyesha kisha ikaacha kabla ya kunyesha tena na hatimaye
kuacha katika vipindi tofauti.
Koplo Tsega aliendelea kujipa uvumilivu akisubiri huku mara kwa mara akiitazama
saa yake ya mkononi. Alipoitupia macho saa yake mara ya mwisho akagundua kuwa
muda wa masaa matatu tayari ulikuwa umetoweka tangu alipojibanza kwenye maficho
yale bila ya mtu aliyekuwa akimsubiri kujitokeza. Hatimaye akaanza kukata tamaa.
Koplo Tsega alipokuwa katika harakati za kutafuta mbinu nyingine mbadala ya
kutimiza lengo lake baada ya kuona masaa yanaenda bila ya mtu aliyekuwa akimsubiri
kujitokeza eneo lile mara darubini ya bunduki yake ikanasa taswira ya gari jeusi aina ya
Vw Amarok tdi likiingia na kutafuta maegesho kwenye lile eneo la maegesho ya magari
la Vampire Casino.
Tukio lile likampelekea Koplo Tsega aishike vizuri lenzi ya darubini ya bunduki
yake na kuirekebisha. Taswira nzuri ya sahani ya namba za gari lile ilipoenea vizuri
kwenye lenzi ya bunduki yake tabasamu maridhawa likajipenyeza usoni mwake na
hapo akapiga mruzi mwepesi wa kujipongeza kwa matokeo mazuri ya uvumilivu
wake.
Lile gari jeusi aina ya Vw Amarok tdi liliingia kwenye maegesho ya Vampire Casino
na kwenda kusimama umbali wa hatua chache kutoka kwenye ule mlango wa casino
kisha kikapita kitambo kifupi bila ya mtu yeyote kushuka kwenye gari lile.
Koplo Tsega alipokuwa mbioni kukata tamaa mara akauona mlango wa dereva
wa lile gari ukifunguliwa. Mwanaume mrefu mnene na mweusi mwenye kitambi
cha ukwasi aliyevaa suti nadhifu ya kodrai ya rangi ya ugoro akashuka kwenye gari
lile na kufunga mlango. Kisha akaanza kutembea taratibu kwa kujiamini akielekea
kwenye ule mlango wa mbele wa Vampire Casino. Umri wake alikuwa miaka hamsini
na ushei na alikuwa ameshika simu kubwa ya kifahari ama smart phone na funguo za
gari amening’iniza mkononi mwake.
Koplo Tsega akajisogeza vizuri kwenye ile bunduki yake huku akilifinya jicho lake
moja ili kuliruhusu jicho lake jingine kuona vizuri taswira ya kiumbe kile kilichokuwa
mbele yake kupitia ile darubini kali iliyokuwa juu ya bunduki yake ya kudungulia.
Alichokiona mbele yake kupitia darubini ile akapata hakika kuwa yule mtu
aliyekuwa akimsubiri kwa muda wa masaa matatu yaliyopita juu ya jengo lile la ghorofa
la biashara la Rupture & Capture alikuwa ndiye yule aliyekuwa akimuona mbele yake.
Mtu yule alikuwa ni P.J.Toddo.
Koplo Tsega aliendelea kumtazama P.J.Toddo kwa makini huku akiirekebisha
vizuri darubini ya bunduki yake. Taswira ya mgongo wa P.J.Toddo ilipoenea vizuri
kwenye msalaba wa shabaha Koplo Tsega akavuta pumzi nyingi na kuibana kifuani
kisha kwa utulivu wa hali ya juu akavuta kilimi cha 338 Lapua Magnum.
P.J.Toddo hakumaliza kupanda ngazi ya mwisho ya baraza ya Vampire Casino. Ile
risasi moja ya Sniper rifle yenye ukubwa sawa na ule wa kidole gumba cha mtu mzima
ikapenya mgongoni kwenye koti lake la suti upande wa kushoto na kumtupa hewani
huku ikiacha tundu kubwa kwenye moyo wake. Risasi ile ikatokezea mbele yake na
kusafiri ikienda kukichangua vibaya kioo cha mlango wa mbele wa ile casino na hapo
sauti mbaya ya mpasuko wa kioo kile ikasikika.
P.J.Toddo alipokuwa akitua chini risasi nyingine ikaichangua vibaya shingo yake
na kumtupa mbele huku funguo ya gari na ile simu yake mkononi vikimponyoka.
P.J.Toddo hakupata nafasi ya kuomba maji kwani alipotua chini ya sakafu ya
baraza ile kiwiliwili chake kilitikisika kidogo na kutulia huku majeraha yake yakivuja
damu nyingi.
Koplo Tsega akiwa ameridhika na kazi yake akachukua kitabu kidogo na kalamu
kutoka mfukoni mwake. Kitabu hicho kilikuwa na orodha ya majina ya watu aliokuwa
akiwatafuta. Akaanza kuyapitia majina yale hadi pale alipolifika jina la P.J.Toddo
ambapo aliweka kituo na kuchora alama ya X juu ya jina lile huku tabasamu jepesi
likijivinjari usoni mwake. Alipokirudisha kitabu kile mfukoni akachukua pipi ya kijiti
na kuimenya taratibu kisha akaitia mdomoni.
“Rest in fire P.J.Toddo,rafiki zako watakufuata hivi karibuni” Koplo Tsega akajikuta
akinong’ona huku akiifyatua na kuikunja vyema stendi ya Sniper rifle 338 Lapua Magnum
na kuelekea sehemu alipoliacha begi lake.
_____
NILIKUWA MIONGONI MWA WATU WACHACHE walioshuhudia kwa
ukaribu tukio lile la kupopolewa vibaya na risasi la mwanaume mmoja kwenye baraza
ya Vampire Casino. Muda mfupi uliyopita nilikuwa nimeingia na kuegesha gari langu
kwenye eneo la maegesho ya magari la Vampire Casino nikitokea kule kwenye ile fukwe
ya bahari ya Hindi alipouwawa Zera.
Akili yangu bado ilikuwa ikitafunwa na jinamizi la hisia mbaya za kifo cha Zera
hata hivyo kifo kile kilikuwa kimenijengea dhana timilifu katika fikra zangu. Dhana ya
kuwa wale watu waliomuua Zera walikuwa wakiutambua vizuri uwepo wangu. Hivyo
nilipaswa kuwa makini katika harakati zangu.
Wauaji walikuwa wakiniwinda na hali ile niliipenda sana kwani tafsiri yake ni kuwa
kadiri wauaji hao walivyokuwa wakinikaribia walikuwa wakiniweka karibu na majibu
ya maswali yangu. Niliwaona adui zangu kama watu waoga mno wasiokuwa na ujasiri
wa kunifikia na badala yake walikuwa wakijaribu kuniogopesha kwa kumuua Zera.
Mara baada ya kuegesha gari langu kwenye lile eneo la maegesho ya magari la
Vampire Casino nilikuwa nimeamua kutoshuka kwenye gari langu hasa baada ya
kukumbuka vizuri ule mtafutano niliyousababisha mara ya mwisho wakati nilipoingia
ndani ya casino ile na kuonana na Zera.
Hadi wakati huu nilikuwa na hakika kuwa taarifa zangu zilikuwa tayari zimeufikia
uongozi wa ile casino na polisi huku nikihusishwa moja kwa moja na lile tukio la kifo
cha yule mtu kwenye kile choo cha casino siku ya jana. Zera alikuwa amekufa katika
harakati za kunisaidia nionane na Milla Cash,msichana kahaba professional wa jiji la Dar
es Salaam. Lakini lengo lake lilikuwa halijatimia na hivyo nilikuwa nimeamua kuanza
kazi hii upya kabisa.
Ingawa nilikuwa sina ratiba kamili ya Milla Cash juu ya kuingia na kutoka kwake
kwenye casino ile hata hivyo nilikuwa nimeazimia kusubiri nikiwa ndani ya gari langu
hadi hapo nitakapoliona lile gari jeusi aina ya Texas Longhorn Tailgate Van linalomleta
na kumchukua Milla Cash ili nianze kazi yangu.
Nikiwa ndani ya gari langu niliendelea kuyatembeza macho yangu nikichunguza
vizuri kila mtu aliyekuwa akiingia na kutoka kwenye ule mlango wa casino. Huku
nikiamini kuwa huwenda kwa kufanya vile majibu ya maswali yangu mengi kichwani
yangeweza kupatikana kwa urahisi.
Nikiwa naendelea kusubiri ndani ya gari langu nje ya eneo lile la maegesho ya casino
mara macho yangu yakajikuta yakivutiwa na gari jeusi la kifahari aina ya Vw Amarok
tdi lililokuwa likiingia kwenye viunga vya maegesho ya magari ya casino ile na kutafuta
sehemu nzuri ya maegesho. Gari lile liliposimama mara nikauona mlango wa dereva
ukifunguliwa kisha mwanaume fulani akashuka huku mkononi akiwa ameshika simu
na amening’iniza funguo za gari.
Mwanaume yule mnene na mweusi mwenye kitambi cha ukwasi alikuwa amevaa
suti nadhifu ya kodrai ya rangi ya ugoro. Mara aliposhuka kwenye lile gari mwanaume
yule akaanza kutembea akielekea kwenye ule mlango wa casino.
Ilikuwa ni wakati mtu yule alipokuwa akimaliza kupanda ngazi ya mwisho ya baraza
ya casino pale kilipotokea kitu kilichonishtua sana. Ghafla nilimuona mwanaume yule
mrefu akisombwa hewani na kutupwa mbele ya baraza ya casino ile kama kishada.
Halafu muda uleule nikasikia sauti kali ya mpasuko wa kioo cha mlango wa ile casino
huku ile simu ya yule mtu ikiangukia kwenye sakafu ya baraza ile na kuchanguka ovyo
Watu wachache walioliona tukio lile wakashikwa na taharuki hata hivyo mimi
sikuwa miongoni mwao na badala yake fikra zangu zilijikita katika kutaka kujua nini
kilichokuwa kimemsibu mtu yule.
Nilifungua mlango wa gari langu haraka na kushuka huku uzoefu wangu ukinieleza
kuwa ile ilikuwa ni kazi ya kitaalam sana na ya aina yake kuwahi kutokea jijini Dar es
salaam. Wakati nikimkaribia yule mtu aliyeangushwa kwa risasi ambaye wakati huu
alikuwa amelala chali kwenye ile baraza ya casino huku akiwa hajitambui,fikra zangu
zikahamia kwa mdunguaji.
Yoyote aliyefanya tukio lile alipaswa kuitwa mdunguaji hatari wa daraja la kwanza
kabisa kwa ubora wa kazi yake na asiyekubali risasi yake ipotee bila majibu. Wazo hilo
likanifanya nigeuke haraka na kuanza kuyachunguza majengo ya ghorofa yaliyokuwa
jirani na eneo lile.
Nilikuwa sahihi kabisa na kama ningechelewa huwenda nisingefahamu haraka
kilichokuwa kikiendelea eneo lile. Juu ya jengo lile la ghorofa la biashara la Rupture &
Capture lililokuwa likitazamana na ile casino nilimuona mtu fulani aliyevaa kofia nyeusi
ya Sombrero na mavazi meusi akitokomea kwenye ukingo wa jengo lile. Hisia zangu
zikaniamba kuwa mtu yule alikuwa mwanamke kutokana na mwonekano wa umbo
lake na hapo maswali mengi yakaanza kupita kichwani mwangu huku nikishindwa
kuelewa kilichokuwa kikiendelea eneo lile. Hata hivyo wazo fulani likanijia kichwani
kuwa endapo ningeweza kucheza vizuri na muda ningeweza kulifikia lile jengo la
Rupture & Capture na kumtia mikononi yule muuaji ambaye nilikuwa na kila hakika
kuwa wakati ule bado alikuwa katika harakati za kulitoroka jengo lile.
Sikutaka kupoteza muda hivyo nilimsogelea yule mtu aliyedunguliwa vibaya kwa
risasi ambaye wakati huu alikuwa amelala chali kwenye ile balaza ya casino huku damu
nyingi kutoka kwenye majeraha yake ikiendelea kusambaa pale chini sakafuni.
Nilitaka kufahamu kuwa mtu yule alikuwa nani kabla ya mashuhuda wengine
hawajafika eneo lile. Hivyo haraka niliinama na kumchunguza vizuri yule mtu kwa
makini. Hata hivyo sikufanikiwa chochote kwani sura ya yule mtu ilikuwa ngeni kabisa
machoni mwangu. Bila kupoteza muda mikono yangu ikaanza kufanya ziara fupi
kwenye mifuko ya suti ya mtu yule.
Nilipomaliza upekuzi wangu nikawa nimefanikiwa kupata kadi ndogo ya
kitambulisho cha kazi cha yule mtu,leseni yake ya udereva na kadi ndogo ya mwanachama
wa Vampire Casino. Niliposoma maelezo yaliyokuwa kwenye kitambulisho cha kazi
cha yule mtu nikagundua kuwa yule mtu alikuwa ni mwanausalama mwenye cheo cha
juu sana na jina lake aliitwa P.J.Toddo.
Nilivirudisha vitambulisho vile mfukoni mwake na hapo nikaendelea kufanya
upekuzi kwenye sehemu nyingine za mwili wake. Bastola yake 38 Police automatic ilikuwa
kwenye mfuko wa koti lake la suti. Niliichukua haraka bastola ile na kuichunguza
na hapo nikagundua kuwa ilikuwa imejaa risasi. Hata hivyo sikuichukua badala yake
nikairudisha kwenye ule mfuko huku nikimwacha yule mtu na kusogea jirani kidogo
na eneo lile sehemu ilipoangukia ile simu yake ya mkononi.
Ile simu ilikuwa imechanguka na kila kitu kilikuwa kimesambaratikia sehemu yake.
Niliyatembeza macho yangu haraka eneo lile na hapo nikaiona Simcard ya ile simu ya
yule mtu iliyochanguka pale chini sakafuni. Nikaichukua ile Simcard haraka na kuitia
mfukoni.
Watu wachache waliokuwa wameanza kusogea eneo lile sikuwapa nafasi ya
kunishangaa na badala yake haraka nikajichanganya kati yao na kuwatoroka. Nilipofika
nje ya lile eneo la Vampire Casino nikaanza kutimua mbio nikielekea kwenye lile jengo
la ghorofa la biashara la Rupture & Capture lililokuwa likitazamana na lile jengo la
Vampire Casino.
Nilifika kwenye lile jengo la ghorofa la biashara la Rupture & Capture ndani ya muda
mfupi sana huku mawazo yangu yakanituma nielekee sehemu ilipokuwa lifti ya jengo
lile. Lakini kitendo cha kuiona lifti ile ikifika chini kwenye Ground floor kikanipelekea
nisite kukikaribia kile chumba cha lifti na hivyo kujibanza pembeni nyuma ya nguzo
moja ya jengo lile.
Mlango wa kile chumba cha lifti ulipofunguka mtoto mdogo wa kike aliyevaa sare
ya shule ya msingi akatoka huku akionekana kufurahia safari yake kwenye ile lifti na
mbali na pale hakukuwa na mtu mwengine yeyote ndani ya chumba kile. Kwa kweli
nilishangazwa sana na tukio lile.
Machale yakanicheza pale nilipowaza kuwa yule mdunguaji bado alikuwa ndani ya
lile jengo na huwenda alikuwa ameachana na wazo la kushuka chini ya lile jengo kwa
kutumia lifti baada ya kuhisi hatari ya kushindwa kulitoroka jengo lile.
Hisia zile zikanipelekea niharakishe haraka kuelekea upande wa kushoto mwisho
wa lile jengo sehemu kulipokuwa na ngazi za kuelekea ghorofa za juu za lile jengo.
Nilipozifikia zile ngazi nikaanza kuziparamia haraka nikizikwea huku nikiwa
nimechukua tahadhari za aina zote. Nilipofika ghorofa ya pili ya lile jengo sikumwona
yule mtu hivyo nikaendelea kuzikwea tena zile ngazi nikielekea ghorofa ya tatu.
Katika korido ya ghorofa ya tatu nilipofika nikakutana na kijana mmoja wa kiume
mfanyakazi wa ofisi za mawasiliano zilizokuwa eneo lile. Nikamuuliza kijana yule
kama alikuwa amemuona mtu aliyekuwa akifanana na maelezo yangu. Yule kijana
hakuonekana kuelewa chochote kilichokuwa kinaendelea kwenye jengo lile hivyo
nikaachana naye na kuzidi kukwea ngazi za kueleka ghorofa ya nne ya lile jengo.
Mara tu nilipoingia kwenye korido ya ghorofa ya nne ya lile jengo ghafla nikakutana
na yule mtu ambaye nilikuwa nimemuona kule sehemu ya juu ya lile jengo muda
mfupi baada ya yule mtu kupopolewa vibaya na risasi kwenye ile baraza ya Vampire
Casino. Nilikutana na mtu yule katikati ya korido pana ya ile ghorofa.
Alikuwa msichana wa makamo aliyevaa mavazi meusi na kofia ya Sombrero
kichwani. Mgongoni alikuwa amebeba begi jeusi,jembamba na refu la ngozi huku
macho yake akiwa ameyafunika kwa vioo vyeusi vya miwani yake. Sikupata nafasi ya
kumtathmini vizuri msichana yule usoni ingawa niliweza kuukadiria umri wake kuwa
ulikuwa ni kati ya miaka ishirini na tano hadi ishirini na saba.
Ingawa msichana yule alikuwa amevaa viatu virefu vya ngozi aina ya Travolta lakini
alikuwa akitembea haraka na kwa kujiamini huku mjongeo wake ukitengeneza starehe
ya kipekee iliyotokana na mtikisiko wa umbo lake la kike lakini kakamavu.
Mara tu nilipoingia kwenye korido ile yule msichana alikuwa akija mbele yangu
hivyo tulipishana huku akili yangu ikianza kufanya kazi haraka katika kutaka kuamua
nifanye nini. Hata hivyo sikuendelea mbele na safari yangu hivyo mara tu tulipopishana
na msichana yule nikageuka haraka na kumtazama. Bahati mbaya au nzuri ni kuwa
na yeye alikuwa na lengo kama langu la kugeuka na kunitazama. Hivyo macho yetu
yakakutana.
Nilichoweza kukiona katika uso wa msichana yule ni hasira na chuki mbaya
iliyoshindwa kujificha. Hisia zilikuwa ni jambo muhimu sana katika kazi yangu na
kamwe sikutaka kuzipuuza. Macho ya dada yule yaliyojificha nyuma ya miwani myeusi
yalipokutana na macho yangu yule dada aligeuka na kuendelea tena na safari yake
mara hii kwa haraka zaidi.
“Hey…!” nilimuita yule dada.
“Haloo...!” nilimwita tena yule dada lakini ilikuwa kazi bure kwani yule dada
hakuniitikia wala kusimama badala yake aliendelea kuharakisha akielekea mwisho wa
ile korido na hapo fikra fulani zikanijia akilini kuwa alikuwa akiiwahi lifti ya lile jengo.
Sikutaka kuendelea kumsubiri yule dada ageuke tena na kuniitikia hivyo nikageuka
na kuanza kutimua mbio nikimfukuza. Hata hivyo nilikuwa nimechelewa kwani
kile chumba cha lifti tayari kilikuwa kimefika kwenye ile ghorofa na mlango wake
ulipofunguka mwanaume mmoja alitoka. Tukio lile likampa fursa nzuri yule dada
niliyekuwa nikimfukuza aingie ndani ya chumba kile cha lifti huku akigeuka na
kunitazama kwa uso wa tabasamu jepesi lenye kunicheka.
Nilikuwa nimechelewa kwani wakati nilipokuwa nikikikaribia kile chumba cha lifti
mlango wake ukawahi kujifunga nikiwa nimesaliwa na hatua chache tu kukifikia kile
chumba.
Nikasimama ghafla huku nikiilaumu akili yangu kwa kuchelewa kung’amua
haraka hila ile. Hata hivyo sikukubali kushindwa hivyo haraka nikaanza kutimua mbio
kuzirudia tena zile ngazi za kushukia ghorofa ya chini ya jengo lile zilizokuwa mwisho
wa ile korido. Nilipofika nikaanza kushuka chini haraka.
Nilipofika chini kwenye ghorofa ya tatu ya jengo lile nikakiona kile chumba cha
lifti kikiendelea kushuka ghorofa ya chini bila kusimama. Hivyo nikaendelea kushuka
zile ngazi nikielekea ghorofa ya pili huku hasira ikizidi kuchemka mwilini mwangu
kwa kile kitendo cha kupigwa chenga kama mtoto.
Kile chumba cha lifti kilipofika ghorofa ya pili kikasimama na mlango wake
ukafunguka. Nikiwa katika hali ya kusubiri mara nikamuona yule dada akitoka kwenye
kile chumba cha lifti lakini kutokana na msongamano mkubwa uliyosababishwa na
wafanyakazi wengi waliokuwa wakitoka kwenye ofisini za jengo lile sikupata nafasi ya
kumfikia yule dada kwa urahisi.
Hivyo nikaanza kulipangua lile kundi la wafanyakazi waliokuwa wakitoka kwenye
zile ofisi nikimfuata tena yule dada. Kitendo kile kikawa kimemshtua yule dada
niliyekuwa nikimfukuza. Yule dada alikuwa tayari ameshajichanganya kwenye lile
kundi la wafanyakazi waliokuwa wakitoka maofisini na aliponiona nikilipangua lile
kundi la wafanyakazi kumfuata akawahi kuichomoa bastola yake mafichoni.
Muda uleule nikasikia milio mitatu ya risasi kwenye ile korido na ghafla kukawa
na giza zito mle ndani. Kilichofuata baada ya pale zilikuwa ni sauti za vilio na mayowe
zikihanikiza kila pembe kwenye korido ile. Moyo wangu ukapiga kite kwa nguvu
baada ya kuhisi kuwa kwa mara nyingine nilikuwa nimezidiwa ujanja na na yule dada.
Kuzidiwa ujanja kwa mara ya pili,hali ile iliusononesha sana moyo wangu. Hata
hivyo sikuwa na namna ya kuusuluhisha mgogoro ule mkubwa uliokuwa ukiendelea
kwenye nafsi yangu. Hivyo nikapiga moyo konde na kuitupa karata yangu ya mwisho
iliyosalia mkononi.http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Ramani ya jengo lile hadi kwenye ghorofa ya nne sasa nilikuwa nikiifahamu vizuri
kwa muda mfupi niliyofanikiwa kuwa mwenyeji wa jengo lile. Kutoka pale nilipokuwa
nilikuwa nimebakisha ngazi chache tu kufika ghorofa ya chini kabisa ya lile jengo.
Kutoka pale nilipokuwa sikuwa mbali sana na zile ngazi za kushukia ghorofa
ya chini kabisa ya lile jengo. Hivyo nilianza kutimua mbio nikilipangua lile kundi la
wafanyakazi waliokuwa wakihaha huku na kule baada ya ile milio ya risasi kusikika.
Nilizifikia zile ngazi na kuanza kushuka chini haraka huku nikiwapita wale
wafanyakazi ambao nao walikuwa wakitimua mbio kushuka kwenye ile ghorofa
ya chini. Nilipofika kwenye ghorofa ya chini ya lile jengo nikashika uelekeo wa
kilipokuwa kile chumba cha lifti lakini safari hii nikiwa nimeikamata vyema bastola
yangu mkononi tayari kujibu shambulizi lolote ambalo lingejitokeza mbele yangu.
Wakati nikikifikia kile chumba cha lifti mara nikauona mlango wake ukianza
kujifunga na nilipochungulia mle ndani hapakuwa na mtu yoyote. Nikasimama huku
nimeshikwa na mshangao usioelezeka.
“Yule dada alikuwa ameshatoka kwenye kile chumba cha lifti na kutokomea?”
nilijiuliza pasipo kupata majibu na nikiwa katika hali ile mara wazo fulani likanijia
akilini. Nikageuka haraka kutazama eneo la maegesho ya magari ya lile jengo na hapo
nikaliona gari dogo jeupe,teksi ya abiria aina ya Corolla limited likiacha maegesho ya
jengo lile na kuingia barabarani. Machale yakanicheza tena hivyo nikaanza kutimua
mbio nikiifukuza ile teksi. Sikufanikiwa kwani huwenda kila kitu kilikuwa kimepangwa.
Gari lile Corolla limited nyeupe yenye kibandiko cha teksi juu yake na ufito wa njano
ubavuni likaondoka kwa kasi eneo lile na kuingia barabarani huku mimi nikiwa umbali
usiopungua mita hamsini kutoka pale nilipokuwa.
Nikaendelea kutimua mbio nikilifukuza lile gari lakini nilikuwa ni kama mtu
niliyekuwa nikiendeshwa na nguvu za mwili na siyo utashi wangu kwani hapakuwa na
uwiano wowote kati ya mbio zangu za miguuni na magurudumu ya gari lile yaliyokuwa
yakizunguka kwa kasi ya ajabu. Hatimaye mdunguaji akawa ameniacha huku nikiwa
siamini macho yangu.
Nilisimama nikilitazama gari lile namna lilivyokuwa likitokomea mbele yangu
huku donge la hasira likiwa limenikaba kooni. Kwani kwa maana nyingine ni kama
niliyekuwa nimepoteza pointi zote muhimu za ushindi katika pambano langu.
Mwishowe nilikata tamaa kabisa na kuanza kutembea kivivuvivu nikirudi kule kwenye
eneo la maegesho ya magari la Vempire casino huku mawazo mengi yakipita kichwani
mwangu.
Kitu kingine cha kushangaza ni kuwa wakati nikilifikia lile eneo la maegesho la
Vampire Casino ule mwili wa yule mtu aliyedunguliwa vibaya kwa risasi kwenye baraza
ya casino ile muda mfupi uliyopita ulikuwa tayari umeondolewa na ile sehemu ya
baraza ilikuwa imesafishwa vizuri kiasi kwamba mtu yeyote ambaye angefika eneo lile
asingeweza kufahamu kitu kilichokuwa kimetokea muda mfupi uliopita.
Hali ile ikanishangaza sana huku nikijiuliza kama kulikuwa na ulazima wowote wa
polisi kufanya uchunguzi wao na kuuondoa haraka mwili wa yule mtu. Niliendelea
kulichunguza eneo lile na hapo nikagundua kuwa hata kile kioo cha mlangoni
kilichokuwa kimechanguliwa kwa risasi za mdunguaji nacho kilikuwa kimerudishiwa
kipya. Yaani mambo yalikuwa yameenda haraka mno kiasi cha kuzishangaza sana
fikra zangu huku nikishindwa kuelewa kilichokuwa kikiendelea kwenye casino ile.
Wakati huu yalikuwa yamesalia magari machache kwenye lile eneo la maegesho
la Vampire Casino. Hisia za kutopiga hatua yoyote katika harakati zangu bado zilikuwa
zikiisimanga nafsi yangu na kwa kweli hali ile iliidhoofisha sana akili yangu.
Nilimfikiria Milla Cash na kuanza kuhisi kuwa huwenda angekuwa chanzo
muhimu cha kusonga katika harakati zangu. Hata hivyo nilitambua kuwa suala lile
kwa sasa lisingewezekana kwa urahisi. Hivyo nikaingia kwenye gari langu na kuyaacha
maegesho yale.
_____
“NYINYI MNADHANI NI KITU GANI KINACHOENDELEA?” Fulgency
Kassy akawauliza wenzake ikiwa ni muda mfupi mara baada ya mwili wa P.J.Toddo
kuondolewa na kupelekwa kwenye chumba cha kuhifidhia maiti katika hospitali ya
taifa ya Muhimbili.
“Mimi ninahisi kuwa huwenda kuna mtu au watu fulani waliopo nyuma ya mpango
huu” Pweza akaongea kwa tafakuri na hapo Fulgency Kassy akageuka na kumtazama.
“Sitaki kukubali akilini mwangu kuwa vifo vya Guzbert Kojo na huyu P.J.Toddo ni
vya bahati mbaya kwani mkitafakari vizuri mtagundua kuwa watu hawa wameuwawa
nyuma ya mipango timamu” Pweza akaongea kwa msititizo.
”Taratibu hata mimi naanza kukubaliana na hoja yako lakini swali la msingi
linaendelea kubaki palepale kuwa ni nani aliyeko nyuma ya mpango huu?” Fulgency
Kassy akaongea huku akiendelea kufikiri.
“Hilo ndiyo suala tunalotakiwa kushughulikanalo kuanzia sasa vinginevyo kama
wangekuwa hai tungeweza kusema moja kwa moja kuwa ni wale Tumbili” Pweza
akaongea kwa utulivu
“Tumbili gani?” Kombe akauliza
“Koplo Tsega na Sajenti Chacha Marwa” Pweza akafafanua
“Mimi nina wazo moja” Kombe akaingilia kati na kuwapeleka wenzake wageuke
na kumtazama kwa shauku.
Wote walikuwa wamesimama nje ya jengo la Vampire Casino. Taarifa za kuuwawa
kwa P.J.Toddo zilikuwa zimewafikia muda mfupi uliyopita wakati walipokuwa
wakitoka kwenye ule ufukwe wa bahari walipomzika Zera. Walichokifanya mara
baada ya kufika pale casino ilikuwa ni kufanya taratibu za haraka za kuuondoa mwili
wa P.J.Toddo pasipo kuwashirikisha polisi kwa sababu walizokuwa wakizijua wao.
“Wazo gani?” Pweza akamuuliza Kombe kwa shauku. Kombe alikuwa
amechuchumaa nje ya baraza ya casino huku macho yake yakiendelea na uchunguzi.
“Risasi zilizomzimisha P.J.Toddo huwenda zikawa zimetokea pale juu” Kombe
akaongea kwa utulivu.
“Wapi?” wote wakauliza kwa shauku.
“Juu kabisa ya lile jengo la biashara la Rupture & Capture” Kombe akaongea na
hapo wote wakageuka na kutazama sehemu aliyokuwa akitazama.
“Kwanini unadhani hivyo?” Fulgency Kassy akauliza huku akiendelea kutazama
kule juu ya lile jengo.
“Ukitazama vizuri kule juu utagundua kuwa kuna pembe nzuri sana ya shabaha
inayoweza kutumiwa na mdunguaji” Kombe akaendelea kufafanua.
“Mdunguaji katika jiji la Dar es Salaam?” Pweza akauliza kwa mshangao
“Dar es Salaam bado haijafikia kuwa na matukio ya uhalifu wa namna hiyo”
Fulgency Kassy akaongea akionekana kupingana na wazo la Kombe.
“Nimelitumikia jeshi kwa zaidi ya miaka nane kwa hivyo ninauzoefu mzuri na
hiki ninachokizungumza. Mtu wa kawaida hawezi kuwa na ufundi wa kumdungua
mtu katika umbali huu tena bila kupoteza risasi hata moja” Kombe akaongea kwa
msisitizo huku akiendelea kutazama kule juu.
“Kwa hiyo unataka kutuambia kuwa P.J.Toddo ameuwawa kwa risasi za
mdunguaji?” Fulgency Kassy akauliza tena huku akimtazama Kombe kwa uyakinifu.
“Sina hakika lakini hilo linawezekana kufanyika” Kombe akaongea huku
akiendelea kufikiri.
Maelezo ya Kombe yakawapelekea Fulgency Kassy na Pweza wageuke na
kutazamana kisha ukimya ukafuatia baina yao huku kila mmoja akizishirikisha vizuri
hisia zake.
“Yeyote aliyemdungua P.J.Toddo anapaswa kuwa askari mzoefu na mdunguaji
makini” Kombe akaendelea kufafanua.
“Askari jeshi au polisi?” Fulgency Kassy akauliza kwa makini.
“Anaweza kuwa ni yeyote kati yao” Kombe akafafanua.
“Kwanini unadhani hivyo?” Pweza akauliza.
“Mara nyingi protokali za kijeshi hufuatwa pale siasa inapoonekena kushindwa
kufanya kazi” maneno ya Kombe yakawapelekea wenzake wageuke kumtazama kwa
shauku.
“Una maana gani kusema hivyo?” Fulgency Kassy akauliza kwa shauku.
“Huelewi nini hapo mbona kila kitu kipo wazi na kinajieleza. Nyinyi wote si
mnajua kuwa kazi tunayoifanya hapa kwa kiasi kikubwa ni kwa minajili ya kulinda
maslahi ya wanasiasa. Kumbukeni kuwa katika hii tume kulikuwa na wanajeshi ambao
kwa sasa tumewazika. Lakini hatuwezi kujua kuwa hao wanajeshi waliokuwa kwenye
hii tume kama walikuwa wao peke yao au lah!”
Maelezo ya Kombe yakawapelekea Fulgency Kassy na Pweza waupishe utulivu
vichwani mwao huku kila mmoja akionekana kuzama kwenye tafakuri nzito. Kitambo
cha Ukimya kikapita kabla ya Pweza kukohoa kidogo na kuvunja ukimya.
“Jambo la kwanza muhimu ni kuhakikisha kuwa polisi hawajitumbukizi katika
suala hili” Fulgency Kassy akaongea kwa utulivu.
“Mimi naona sasa ipo haja ya kumshirikisha mkuu” Pweza akaongea huku akifikiri
“Hilo ni wazo zuri lakini kwa sasa nafikiri bado tunayo nafasi ya kulimaliza suala
hili sisi wenyewe” Fulgency Kassy akadakia.
“Mimi nadhani suala hapa siyo nafasi ila ni kukaa chini mapema na kulipima
jambo lenyewe kama litaweza kutatulika kwa kigezo cha muda. Wakati fulani
unaweza kupewa muda mrefu wa kufanya mtihani uleule na kujikuta ukifeli. Hivyo
mimi nadhani tulitafakari hili suala kwa mapana yake kwani sote tuliamini kuwa
kwa kuwafumba mdomo Koplo Tsega na Sajenti Chacha Marwa ndiyo lingekuwa
suluhisho. Lakini sasa nafikiri kuwa huwenda hatukuwa sahihi. Guzbert Kojo na
P.J.Toddo wameuwawa na huwezi kujua nani atakayefuatia baada ya hapa. Hivyo
tusipokuwa makini kadhia hii itahamia kwetu” Kombe alimaliza kuongea huku
akisimama pale chini.
“Huwenda ukawa upo sahihi ingawa mimi nayaona mawazo yako ni kama
yanayoegemea upande mmoja. Sote tunajua kuwa P.J.Toddo alikuwa ni mkuu wa
kurugenzi ya mawasiliano ya rais Ikulu. Kama ni hivyo kwanini tusilichukulie hili suala
katika mtazamo wa kisiasa?. Mfano labda kifo chake kimetokana na yeye kuvujisha
siri za serikali kwa vyama vya upinzani baada ya kupewa pesa nzuri na vyama hivyo
vyenye nia ya kushika dola” Fulgency Kassy akaunda hoja nzuri iliyompelekea Pweza
atabasamu lakini uso wa Kombe haukuonesha tashwishwi yoyote.
“Huwenda ukawa upo sahihi” hatimaye Kombe akaongea kwa utulivu.
“Hatuna haja ya kuwa na wasiwasi. Mimi nafikiri ngoja kwanza tuone mambo
yatakavyokuwa halafu tutajua cha kufanya” Fulgency Kassy akahitimisha kwa
kuyaweka kando mawazo ya Kombe.
“Twendeni kule juu ghorofani tukachunguze huwenda tukapata chochote”
Kombe akavunja ukimya na wote wakakubaliana na wazo lake.
Muda mfupi baadaye walikuwa juu ya lile jengo la biashara la Rupture & Capture
na baada ya uchunguzi wa hapa na pale wakajikuta wakikubaliana na hisia za Kombe.
Pweza,yeye aliokota maganda mawili ya risasi za mdunguaji zilizotumika katika
kuupokonya uhai wa P.J.Toddo kwenye ile baraza ya casino. Huku Fulgency Kassy
akiokota ganda la pipi ya kijiti sawa na lile aliloliokota kule nyumbani kwa Guzbertkojo usiku ule alipouwawa
“Maganda haya ni ya risasi za bunduki nzito ya kivita na hakuna raia anayeruhusiwa
kumiliki silaha ya namna hii” Kombe akaongea kwa hakika huku akiendelea
kuyachanguza kwa ukaribu yale maganda ya risasi baada ya kuyachukua kutoka
mkononi mwa Pweza.
“Sasa naanza kupata picha kamili kuwa mtu aliyehusika na kifo cha Guzbert Kojo
ndiyo huyu pia aliyehusika na kifo cha P.J.Toddo” Fulgency Kassy akaongea kwa
utulivu huku akilifikicha lile ganda la pipi ya kijiti mkononi.
“Kwa vipi?” Kombe akauliza.
“Angalieni hili ganda la pipi” Fulgency Kassy akawaambia wenzake na kuwapelekea
wote wasogee karibu na kulitazama ganda lile la pipi mkononi mwake.
“Ganda la pipi lina shida gani?” Pweza akauliza huku akishindwa kuelewa.
“Niliokota ganda la pipi kama hili nyumbani kwa Guzbert Kojo usiku ule
alipouwawa na sasa nimeokota ganda la pipi kama lile hapa” Fulgency Kassy akaongea
huku akionesha mshango.
“Kwa hiyo unataka kusema kuwa muuaji ni mtu anayemumunya pipi ya kijiti
kila anapokamilisha dhamira yake?. Mh! hii ni ajabu sana na hainiingii kabisa akilini”
Pweza aliongea kwa mshangao huku akiendelea kulitazama lile ganda la pipi.
“Mauaji haya yanafanywa na mtu mmoja” Fulgency Kassy hatimaye akavunja
ukimya na kuongea kama mtu aliyezama kwenye tafakuri nzito.
“Unadhani mtu huyo anaweza kuwa ni yule Stephen Masika?” Kombe akauliza.
“Hakuna mwenye hakika ingawa miongoni mwetu tunaweza kuwaza hivyo.
Tunachotakiwa kufanya sasa ni kutafuta ukweli wa hisia zetu kwani hiyo ndiyo kazi
iliyoko mbele yetu kwa sasa. Tumtafute huyu muuaji na kumalizana naye mapema
kabla hajaendelea kutabaruku na roho zetu” Fulgency Kassy akaongea kwa hakika.
“Sasa tunaanzia wapi?” Pweza akauliza.
“Tunaanzia kwenye hili jengo kutafuta taarifa zitakazoweza kutusaidia kumnasa
huyu Tumbili mwingine”
“
HUYU MTU ANAYEFAHAMIKA KWA JINA LA STEPHEN MASIKA
amekuwa kama saratani mbaya inayohatarisha biashara yetu” Fred Bagunda
akaongea kwa utulivu huku mwili wake ukiwa umestarehe vizuri kwenye kiti
chake cha ofisini chenye foronya laini. Njama alikuwa mbele yake akimtazama kwa
makini.
“Umejuaje kuwa huyo mtu anaitwa Stephen Masika?” Njama akauliza kwa
mshango huku akiyatathmini kwa ukaribu maneno ya Fred Bagunda.
“Nilipigiwa simu na kuelezwa juu hali ya mambo ilivyo. Inavyoonekana sasa ni
kuwa huyu mtu anayefahamika kwa jina la Stephen Masika huwenda ndiye aliyehusika
na vifo vya Alba Gamo,Guzbert Kojo na P.J.Toddo. Nafikiri sasa unaweza kuvuta
picha kuwa huyu Stephen Masika ni mtu wa namna gani”
“Sasa unadhani jambo la busara litakuwa ni kuendelea kumuogopa na kumuacha
akiendelea kutamba mitaani?” Njama akauliza kwa utulivu.
“Nataka kwanza upate picha kuwa tunashughulika na mtu wa aina gani. Taarifa
nilizozipata ni kuwa kuna vijana watatu waliokabidhiwa kazi ya kumtafuta huyu
Tumbili” Fred Bagunda akafafanua.
“Unadhani huyu mtu ambaye sasa tunamfahamu kwa jina la Stephen Masika
anapata wapi nguvu za kupambana na huu mtandao?” Njama akauliza.
“Swali hilo ndiyo lililotufanya tukatoka kwenye kikao saa kumi usiku pasipo kupata
majibu ya kuridhisha. Hisia zetu zilikuwa zimejikita zaidi kwenye vyama pinzani
ambavyo hutafuta taarifa za udhaifu wa serikali kwa gharama zozote ili waweze
kuzitumia kama mtaji wa kisiasa kuombea kura kwa wananchi. Baadhi yetu walienda
mbele zaidi wakidai kuwa huwenda kuna watu fulani waliokuwa wakipanga kuipindua
serikali iliyoko madarakani”
“Kwanini mkafikiria hivyo?” Njama akauliza.
“Ni kutokana na tukio la kuuwawa kwa mkuu wa kurugenzi ya mawasiliano ya
rais Ikulu. P.J.Toddo ni mtu muhimu sana kiutawala na anayefahamu karibu kila kitu
kinachoendelea katika hii serikali”
“P.J.Toddo anaingiaje katika huu mkasa?” Njama akauliza.
“Hii kazi tunayoifanya ni kwa ajili ya maslahi ya baadhi ya wanasiasa na wanasiasa
hao ndiyo serikali yenyewe. Huwenda P.J.Toddo alikuwa akivujisha siri za mambo
yetu na hapo protokali ndiyo zikafuatwa”
“Kwa maana nyingine unataka kuniambia kuwa kifo cha P.J.Toddo kinatokana na
kuvujisha siri?” Njama akauliza.
“Huo ni mtazamo tu wa baadhi ya watu wakati tulipokuwa tukijadiliana”
“Mwisho wa mkutano wenu mkaazimia nini?”
“Ulinzi na umakini uongezwe na tahadhari zichukuliwe. Stephen Masika atafutwe
popote alipo na atakapopatikana azungumze yeye ni nani na anafanya kazi kwa
maslahi ya nani”
“Baada ya hapo?”
“Baada ya hapo protokari zitafuatwa”
“Vipi kuhusu mzigo wa yule mama?” Njama akauliza akihamisha mada.
“Nimeshafanya mawasiliano na White Sugar na hivi tunavyozungumza ameniambia
kuwa mzigo upo njiani” Fred Bagunda akaongea kwa hakika.
“Sasa yule mama amefikia wapi hapa jijini Dar es Salaam?”
“Yupo kwenye chumba kimoja cha Hotel Agent 11 hapa jijini Dar es Salaam
anaendelea kusubiri”
Maongezi baina ya Fred Bagunda na Njama yalikuwa yakiendelea katika chumba
kile cha ofisi za kampuni usafirishaji wa vifurishi vya kimataifa ya Intercontinental &
Overseas Parcels (I.O.P) iliyokuwa ikisemekana kumilikwa na wawekezaji wawili wa
ndani ya nchi.
___________
ILIKUWA IKIELEKEA KUTIMIA SAA MBILI ASUBUHI wakati
nilipoegesha gari langu kando ya kituo cha kujazia mafuta kinachotazamana na
barabara kuu ya Bagamoyo eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam.
Usiku mzima uliopita nilikuwa nimelala usingizi wa mang’amung’amu huku akili
yangu akisumbuka kwa kila namna katika kutengeneza mtiririko mzuri wa matukio
yote ili yaweze kuleta maana. Lakini suala hilo lilikuwa limeshindikana kwani matukio
mawili au matatu niliyoyachukua na kuyaunganisha yalikataa kuunganika na hivyo
nikaendelea kuteseka kitandani.
Hata hivyo baada ya kuwaza sana hisia fulani zilikuwa zimeanza kujengeka
kichwani mwangu kuwa yule mndunguaji aliyenitoroka usiku wa jana alielekea
kufanana na yule msichana niliyemfuatilia kutoka kule Vampire Casino hadi mtaa wa
Nkuruham siku chache zilizopita.
Foleni za magari zikiwa zimeanza kushamiri katika baadhi ya barabara za jiji
la Dar es Salaam hivyo mara tu nilipofika kwenye kituo kile cha kujazia mafuta
nikashuka kwenye gari langu kisha nikavuka barabara nikielekea kwenye kituo cha
teksi kilichokuwa karibu na eneo lile.
Kumbukumbu nzuri juu ya lile gari lililotumika jana na mdunguaji ilikuwa bado
timilifu kichwani mwangu. Nililikumbuka vizuri gari lile aina ya Corolla limited yenye
kibandiko cha teksi juu yake na ufito wa njano ubavuni kuwa lilikuwa likisaka mkate
wake wa kila siku katika kituo cha teksi cha pale Mwenge kutokano na utambulisho
wake ubavuni.
Madereva wa teksi wa kituoni pale walinikaribisha kwa bahasha zote huku
wakiniweka kwenye kundi la mteja lakini waliposikiliza shida yangu baadhi yao
wakanipa mgongo na kuendelea na hamsini zao. Mzee mmoja mkongwe dereva
wa teksi mwenye busara akabaki akinikata jicho la kunisahili. Hali ile ikanipa ujasili
wa kutumbukiza mkono wangu mfukoni na kuchukua karatasi ndogo niliyokuwa
nimeiandika namba za ile teksi ya mdunguaji kisha nikampa yule mzee.
“Nimesahau mzingo wangu kwenye teksi yenye hizi namba” nilimwambia yule
mzee huku nikiupima uzito wa maneno yangu.
“Mzingo gani?” yule mzee akaniuliza huku akiitazama ile namba ya teksi kwenye
ile karatasi bila kuishika.
“Begi langu dogo jeusi lenye vitu vyangu muhimu vya kusafiria ikiwemo pasipoti”
“Wewe ni mgeni hapa jijini Dar es Salaam?” mzee yule akaniuliza na kupitia
matamshi yake nikafahamu kuwa alikuwa Mngoni wa Ruvuma.
“Mimi ni mkazi wa Songea mkoani Ruvuma” nikamwambia yule mzee huku
nikinuia kununua urafiki.
“Oh! kumbe wewe ni mkazi wa Songea hata mimi natokea Songea. Mke wangu na
watoto wanakaa eneo la Mfaranyaki. Mimi nimewatoroka kidogo na kuja hapa Dar es
Salaam kuangalia upepo wa maisha” mzee yule mwanalizombe akaongea kwa furaha
sana huku akijihisi kuwa amekutana na ndugu yake wa karibu.
“Sasa nyinyi wazee mkikimbia miji yenu na sisi vijana wenu tufanyeje?”
nikachombeza utani kidogo.
“Hapana! mimi sijakimbia nyumbani. Unajua hii nchi yetu ni huru na kuna amani
ya kutosha. Ukikaa sehemu moja na kuona mambo yako hayakuendei vizuri upo
huru kujaribu kwingine kwani hakuna mtu aliyekushika miguu,alimradi tu usisahau
nyumbani” mzee yule akaweka kituo na kunitazama kabla ya kuniuliza
“Songea unaishi sehemu gani?” mzee yule akaendelea kurefusha maongezi huku
akionekana kufurahi na kwa kweli sikutaka kupoteza muda hivyo nilichukua noti
moja ya shilingi elfu kumi kutoka mfukoni mwangu na kumshikisha mkononi.
“Tafadhali! naomba unisaidie” nilimwambia yule mzee na nilichokiona usoni
mwake ni furaha ya kushtukiza iliyochanganyika na mipango ya kifungua kinywa
kizito katika fikra zake.
“Namba hii ni ya teksi ya Momba hata hivyo sijamuona kwa hizi siku mbili tatu”
“Anaishi wapi?” nilimuuliza yule mzee.
“Nyumbani kwake siyo sehemu ya kupotea. Shukia kituo cha ITV halafu
mkono wako wa kushoto utaona barabara. Shuka na barabara hiyo na mwisho wake
utakutana na barabara nyingine inayokatisha kwa mbele. Sasa wewe ukifika hapo
ingia upande wa kulia halafu hesabu hadi nyumba ya nne upande wa kushoto kwako
utaona nyumba yenye uzio wa michongoma. Hapo ndiyo nyumbani kwa Momba.
Ukimkosa rudi hapa ndugu yangu nitakusaidia” mzee yule akanielekeza kwa furaha
huku akiushikashika mfuko wa shati lake alipoitumbukiza ile noti ya shilingi elfu kumi
niliyompa.
“Ahsante!” nikamwambia mzee yule na kumuaga nikirudi kule nilipoegesha gari
langu.
Muda mfupi baadaye nilikuwa nimefika kwenye kituo cha daladala cha ITV.
Maelezo ya yule mzee yalikuwa sahihi kwani nilipofika tu kwenye kituo kile upande
wa kushoto kwangu nikaiona barabara ya gari inayokatisha mitaani. Nikakunja
kona kuifuata barabara ile na baada ya muda mfupi nikawa nimeifikia ile barabara
inayokatisha kwa mbele. Hivyo nilipofika pale nikaingia upande wa kulia na kwenda
kuegesha gari langu nje ya nyumba ya nne iliyozungushiwa uzio wa michongoma
upande wa kushoto wa barabara ile.
Kama zilivyokuwa nyumba nyingi za jijini Dar es Salaam nyumba ya Momba
ilikuwa imekula chumvi nyingi kwa mwonekano. Mabati ya paa lake yalikuwa
yameshika kutu kila mahali na hata aina ya ujenzi wa nyumba ile ulikuwa ni wa mtindo
wa zamani wa Mgongo wa Tembo.
Nilishuka kwenye gari langu na kuelekea kwenye ile nyumba huku nikitarajia
kuiona ile teksi Corolla limited nyeupe ikiwa imeegeshwa pale nje. Sikuiona na hapo
hisia za wasiwasi kuwa huwenda Momba alikuwa ametoka zikanijia huku nikijiuliza
kuwa Momba alikuwa na uhusiano gani na yule mdunguaji hatari. Niliufikia mlango
wa mbele wa ile nyumba na kuanza kugonga hodi. Hakuna mtu aliyeniitikia na ule
mlango ukanitazama kama uliokufa.
Baada ya kugonga sana bila kujibiwa nikaamua kuzunguka na kuchungulia
kwenye dirisha moja la ile nyumba. Hata hivyo ilikuwa kazi bure kwani mle ndani
hapakuonesha dalili za uwepo wowote wa kiumbe hai.
Muda mfupi uliofuata nilikuwa ndani ya ile nyumba kwa msaada wa funguo zangu
malaya. Sebule ya nyumba ile ilikuwa na samani chakavu zisizokuwa na mpangilio
unaoeleweka na hali ile ikanitanabaisha kuwa huwenda Momba alikuwa akiishi maisha
ya ukapera.
Upande wa kushoto na sebule ile kwenye kona kulikuwa na chupa nyingi za
bia zilizotumika. Nilipotazama juu ya meza ndogo chakavu iliyokuwa pale sebuleni
nikaiona simu ndogo ya mkononi. Moyo wangu ukapiga kite kwa nguvu. Fikra zangu
zikanieleza kuwa simu ile haikuwa imesahaulika kwa namna ilivyokuwa imetelekezwa
pale juu ya meza.
”Kitu gani kinachoendelea?” nilijiuliza huku akili yangu ikishikwa na mduwao.
Wakati nikiendelea kuwaza mara ile simu pale juu ya meza ikaanza kuita. Nilisimama
nikiitazama ile simu kwa mshangao huku shughuli za mwili wangu zikiwa zimesimama
kwa sekunde kadhaa. Hisia zangu zikaniambia kuwa lile lilikuwa ni tukio la hila hata
hivyo sikuweza kufahamu kuwa ile ilikuwa ni hila ya namna gani.
Namba iliyokuwa ikiita kwenye simu ile ilikuwa ngeni na yenye tarakimu tano tu
na haikuelekea kufanana na namba za simu zitumikazo nchini Tanzania. Niliendelea
kuipuuza ile simu na kuiacha iendelee kuita huku nikiyatembeza macho yangu mle
ndani kuchunguza.
Kwa kuwa nilikuwa nguli wa shughuli za kijasusi ndani ya muda mfupi chini ya ule
mlango wa sebuleni kwenye kitasa nikaona kidude kidogo mfano wa kifungo cheusi
cha nguo kilichokuwa kimebandikwa. Niliukaribia vizuri ule mlango na kuinama
nikikichunguza kwa ukaribu kidude kile na hapo nikajikuta nikitabasamu.
Kile kidude kidogo mfano wa kifungo cheusi cha nguo kilikuwa ni kifaa kidogo
chenye nguvu kubwa ya kunasa mawimbi ya sauti na kuyasafirisha maelfu ya maili.
Kifaa kile kilikuwa kimepandikizwa pale mlangoni ili mtu yoyote akiingia mle ndani
kifaa kile cha mawasiliano kiweze kunasa mawimbi ya sauti na kuyapeleka kwa
mhusika aliyekiweka pale kifaa kile kwa hila.
”Blood fool!” nilijisemea na mara hii ile simu pale juu ya meza ilikata na kuanza
kuita tena. Safari hii nilisogea pale mezani nikaichukua ile simu na kubofya kitufe cha
kupokelea pasipo kuongea neno lolote.
“Rafiki yako yupo nyuma ya jengo la BML Contractors,Tabata relini” sauti tulivu ya
kiume ikaongea kutoka upande wa pili wa ile simu.
“Wewe mwoga ni nani?” nilimuuliza yule mtu kwa shauku huku nikiinakili vizuri
sauti yake kichwani. Hata hivyo yule mtu hakunijibu na badala yake ile simu ikakatwa.
Nikiwa bado nimeishikilia ile simu sikioni nikajikuta nimeshikwa na mduwao
huku fikra zangu zikienda mbali zaidi kutafuta majibu ya maswali chungu mzima
yaliyokuwa yakipita kichwani mwangu. Nilihisi kuwa kwa vyovyote mtu yule aliyepiga
ile simu alikuwa akitaka kucheza na akili yangu na kunitia woga usiokuwa na maana.
Lakini hadi kufikia pale nilikuwa nimechoshwa na michezo ya namna ile.
Nilimkumbuka yule mdunguaji na kumeza funda kubwa la mate. Ghadhabu
zilinipanda hivyo nikaichomoa bastola yangu kutoka mafichoni na kuitazama kwa
makini kisha nikairudisha mahala pake.
Ile simu ya mkononi nikaipigiza ukutani huku roho ya utulivu ikiwa imenitoweka
kabisa. Niliufikia ule mlango na kukinyofoa kile kifaa cha kunasia mawimbi ya sauti
kisha nikakitupa chini sakafuni na kukisaga kwa soli ngumu ya kiatu changu.
Mche wa sigara ukiwa unateketea taratibu kwenye pembe ya mdomo wangu
nilitoka nje ya nyumba ile na kuelekea sehemu nilipokuwa nimeegesha gari langu.
Muda mfupi uliyofuata nilikuwa njiani nikielekea eneo la Tabata relini.
_____
BAADA YA FOLENI KUBWA YA MAGARI kupungua kwenye barabara ya
Sam Nujoma na ile barabara ya Nelson Mandela hatimaye nikafika eneo la Tabata relini.
Sikuwa mwenyeji sana wa eneo lile hivyo ikabidi niulize kwa watu mahali lilipokuwa
jengo la BML Contractors.
Watanzania ni watu wakarimu sana. Maelekezo ya wapita njia yakiniridhisha kuwa
jengo lile lilikuwa umbali mfupi baada ya kuupita uzio wa ukuta wa ofisi za Mwananchi
Communication. Hivyo niliingia upande wa kulia nikiambaa na barabara ya vumbi
iliyokuwa ikipakana na ukuta wa ofisi za Mwananchi Communication huku macho yangu
mara kwa mara yakitazama vioo vya gari vya ubavuni katika kutaka kujiridhisha kuwa
hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa amenifungia mkia.
Nyuma ya lile jengo la Mwananchi Communication umbali mfupi kutoka pale kulikuwa
na gereji bubu na katika gereji ile kulikuwa na magari mengi yaliyoegeshwa. Magari
yale mengi yalikuwa ni malori makubwa ya kubebea mizigo ya kwenda mikoani na
nchi za jirani yenye matela makubwa.
Niliingia kwenye gereji ile na kuegesha gari langu. Kijana mmoja fundi wa gereji ile
aliyevaa mavazi ya kazi yenye madoa makubwa ya mafuta machafu ya gari akanikaribia
huku akionekana kuchangamkia fursa.
“Ongeza upepo wa kutosha kwenye magurudumu yote” nilimwambia yule kijana.
“Ondoa shaka!” kijana yule akaongea kwa furaha na wakati alipokuwa akitathmini
ujazo wa upepo kwenye yale magurudumu ya gari langu nikamtumbukizia swali.
“Jengo la BML Contractors liko wapi?”
“Endelea mbele na hii barabara uliyokujanayo na ukifika mbele kidogo utaona
mteremko na upande wa kushoto kuna godauni la wachina. Mwisho wa godauni hilo
kuna kichochoro upande wa kushoto. Fuata kichochoro hicho mwisho utatokezea
kwenye reli. Ukivuka hiyo reli mbele yako utaliona hilo jengo la BML Contractors”
“Ahsante! sana fanya kazi yako. Wacha mimi ninyooshe miguu kidogo nitarudi
muda siyo mrefu” nilimwambia yule kijana.
“Usihofu tajiri wangu” yule kijana akaitika huku akielekea kuchukua pampu ya
upepo.
Nililiacha gari langu kwenye gereji ile kisha nikashika uelekeo wa ile barabara ya
vumbi inayoelekea kule mbele kama alivyonielekeza yule kijana wa gereji. Niliendelea
kutembea na baada ya safari fupi nikaanza kushuka mteremko hafifu. Nilipokuwa
nikishuka mteremko ule upande wa kushoto nikaliona jengo refu la godauni ya
wachina. Mwisho wa goduani ile nikakiona kichochoro upande wa kushoto.
Bila kupoteza muda nikaingia kwenye kichochoro kile kilichofanywa baina ya
kuta mbili ndefu. Mwisho wa kichochoro kile kirefu chenye giza hafifu nikaiona reli
ikikatisha mbele yangu. Maelekezo ya yule kijana yalikuwa sahihi hivyo nikakatisha
kwenye reli ile na nilipokuwa nikikatisha kwenye ile reli mbele yangu nikaliona jengo
kubwa la BML Contractors.
Kuliona jengo lile kukanipelekea niipapase vyema bastola yangu mafichoni.
Niliifuata ile reli huku hatua zangu zikipungua na nilipofika mbele nikachepuka upande
wa kushoto na hapo nikawa nimetokezea nyuma ya lile jengo la BML Contractors.
Kama yalivyokuwa maeneo mengi ya kampuni za ujenzi jengo lile la BML
Contractors lilikuwa limezungushiwa uzio wa mabati yaliyoandikwa jina la kampuni
ile ya ujenzi. Uzio ule hafifu kwenye baadhi ya vipenyo vyake viliniwezesha kuona
ndani. Baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ile walikuwa wakiendelea na shughuli zao.
Malori makubwa ya kokoto yalikuwa yameegeshwa huku winchi ndefu na mashine za
kuchanganyia zege zikiwa zinaendelea na kazi. Hali ile ikanitanabaisha kuwa nilikuwa
kwenye eneo sahihi.
Sasa fikra zangu zikaanza kufanya kazi huku nikiyatembeza macho yangu
kupeleleza eneo lile. Lilikuwa ni eneo lenye magari mabovu na mabaki ya mashine
mbovu za ujenzi. Nikasimama nikiendelea kulipeleleza eneo lile huku macho
yangu yakitarajia kumuona yule mtu niliyezungumza naye kwenye simu. Lakini hilo
halikutokea badala yake moshi wa takataka chache ulikuwa ukifukiza eneo lile.
Kabla ya kuendelea mbele zaidi nililichunguza jengo la ghorofa lililokuwa
limepakana na eneo lile. Lilikuwa jengo fupi chakavu la ghorofa sita na hapo wazo
fulani likachipuka akilini. Jengo lile lingeweza kumhifadhi mtu yeyote ambaye kwa
wakatu huu huwenda angeitumia nafasi ile kuzichunguza nyendo zangu. Hisia
zile zikaniongezea umakini zaidi na hapo nikaanza kuzitupa hatua zangu taratibu
nikilikagua eneo lile.
Nilizipita mashine mbovu za ujenzi zilizotelekezwa eneo lile nikiruka baadhi ya
vifusi vya mabaki ya ujenzi huku nikiyatembeza macho yangu huku na kule. Sikutaka
kuishika bastola yangu mkononi kwani kwa kufanya vile ningeweza kumjengea hoja
mtu yoyote ambaye angekuwa eneo lile akinitazama. Niliyapita magari mabovu mawili
yaliyokuwa eneo lile na wakati nikilikaribia gari jingine bovu nikasikia kelele hafifu za
mnyama akichakura nyuma ya gari lile bovu. Nikapiga moyo konde na kulisogelea lile
gari kwa nyuma.
Nilichokiona nyuma ya gari lile kikapelekea kwa sekunde kadhaa shughuli za mwili
wangu zisimame. Mwili wa mwanaume mmoja ulikuwa umekaa chini huku mgongo
wake ukiwa umeegemea lile gari bovu kwa nyuma. Ingawa sura ya yule mtu ilikuwa na
majeraha mengi usoni na damu nyingi iliyoganda katika majeraha yake lakini niliweza
kuukadiria umri wake kuwa ulikuwa ni kati ya miaka thelathini na nane na arobaini
na mbili.
Mwanaume yule mwenye afya njema alikuwa amenyongwa kwani nilipomchunguza
vizuri nikagundua kuwa mikono na miguu yake ilikuwa imefungwa na kukazwa kwa
waya mwembamba lakini imara kiasi cha kuzipelekea sehemu zile kwenye mwili
wake zivimbe na kuwamba. Mdomo na macho yake vilikuwa wazi na inzi wakubwa
walikuwa wakitabaruku.
Nikaokota jiwe na kuwafurusha mbwa koko wawili waliokuwa wakiitafuna miguu
yake iliyokuwa wazi. Yule mtu kifuani alikuwa wazi huku chini akiwa amevaa suruali
nyeusi.
Alikuwa mwanaume mwenye afya na nilipoichunguza shingo yake iliyovimba
nikauona waya mwembamba kama ule uliokuwa umefungwa kwenye miguu na
mikono yake ukiwa umeizingira shingo yake. Hali ile ikanifanya nihitimishe kuwa mtu
yule alikuwa amenyongwa hadi kufa.
Ingawa nilikuwa simfahamu yule mtu lakini hisia zangu zikanitanabaisha kuwa
macho yangu yalikuwa yakimtazama Momba. Hasira zikanipanda hata hivyo sikuwa
na namna ya kufanya huku roho ikiniuma sana.
Pembeni ya mwili ule niliiona simu ya mkononi kama ile niliyoiona juu ya meza
kule sebuleni kwa Momba na sasa simu ile ilikuwa imeanza kuita tena. Niliitazama
simu ile kwa hasira nikishawishika kutaka kuichukua lakini roho yangu ilinikataza
huku hisia zangu zikiniambia kuwa nigeuke nyuma na kutazama kule juu ya lile jengo
la ghorofa lililokuwa jirani na eneo lile.
Nilikuwa sahihi kwani ilianza risasi moja iliyoniparaza bega langu la kushoto huku
nikiitumia bahati ile kujitupa chini kisha nikajiviringisha na kujibanza kwenye kona ya
lile gari bovu nikiwa nimeshikwa na taharuki ya aina yake.
Mvua ya risasi ikaanza kurindima upande ule huku risasi hizo zikitoba bodi la lile
gari bovu nililokuwa nimejibanza. Nikajitahidi kuzikwepa risasi zile kwa kuhama hapa
na pale nikienda upande wenye afadhali.
Kutoka pale nilipokuwa hadi lilipokuwa gari bovu jingine hapakuwa na umbali
mrefu hata hivyo nilijionya kuwa endapo ningeendelea kujibanza eneo lile hatimaye
zile risasi zingenifikia. Zile risasi ziliendelea kurindima na wakati huo niliendelea
kujibanza huku nikitafuta upenyo mzuri wa kumchunguza adui yangu.
Mara nikawa nimepata uwazi mdogo ulioniwezesha kuona kule juu ya lile jengo
la ghorofa. Wanaume watatu walikuwa wemejibanza kwenye ukingo wa ghorofa
lile wakiendelea kufyatua risasi pale nilipokuwa. Angalau nikaridhika kuwa yule
mdunguaji hakuwa miongoni mwao. Nikaendelea kuwatazama wale watu huku akili
yangu ikisumbuka katika kutafuta namna ya kujinasua.
Umbali uliokuwa baina yangu na wale watu ulikuwa mrefu hivyo sikupata nafasi
nzuri ya kuziona sura zao. Kwa kweli sikupenda kuendelea kuwepo eneo lile kwani
zile risasi zingeweza kuwavuta watu na dhana ya kuwa mimi nilikuwa jambazi
ingeweza kuibuliwa hasa baada ya kukutwa pale na ule mwili wa Momba. Baada ya
hapo nilifahamu kuwa raia wasingekubali kuniachia hivyo sikutaka kusubiri.
Haraka nikajilaza pale chini kisha nikaanza kutambaa nikilitoroka eneo lile
kuelekea kwenye kifusi cha mabaki ya ujenzi kilichokuwa jirani na eneo lile. Kwa
kuwa nilikuwa nikitambaa kwa kuufuata ule usawa wa lile gari bovu wale watu juu ya
lile jengo la ghorofa walikuwa hawajaniona hivyo wakawa wakiendelea kufyatua risasi
zao ovyo bila malengo.
Nilikifikia kile kifusi na kujibanza nyuma yake huku nikipata nafasi nzuri ya
kulichunguza tena eneo lile. Kutoka pale kwenye kile kifusi na lilipokuwa gari jingine
bovu kulikuwa na umbali mfupi hivyo nikapiga tena mahesabu ya kulifikia lile gari.
Nikakusanya nguvu kisha kwa kasi ya ajabu nikakimbia na kwenda kujibanza nyuma
ya lile gari bovu.
Nikiwa nyuma ya lile gari bovu nikahisi kuwa angalau nilikuwa sehemu salama
kidogo kwani kutoka kwenye lile gari bovu nililojibanza eneo lililofuatia lilikuwa na
vichaka hafifu cha miti midogo na baada ya kulivuka eneo lile ningekuja kutokezea
kwenye ile reli.
Mahesabu yangu yalipokamilika nikaliacha lile gari bovu na kuanza kukimbia
nikitokomea kwenye kile kichaka na nilipokuja kuibuka upande wa pili nikawa
nimetokezea kwenye ile reli.
Baadhi ya wapita njia kwenye ile reli walinishangaa wakati nikijitokeza kutoka
kwenye kile kichaka hata hivyo sikuwatilia maanani badala yake nikawa natembea
kuelekea mbele nikiifuata ile reli. Wakati nikiendelea kutembea kwa mbali niliendelea
kuisikia ile milio ya risasi kule nyuma yangu. Mara nikajikuta nimechanganya miguu
na kuanza kukimbia nikielekea kwenye lile jengo la ghorofa walipokuwa wale watu
wakinifyatulia risasi.
Niliendelea kukimbia na ndani ya muda mfupi tu nikawa nimelifika lile jengo la
ghorofa na nilipolichunguza vizuri nikagundua kuwa jengo lile lilikuwa halitumiki
kutokana na taratibu ujenzi wake kuwa zimekiukwa. Sasa nilikuwa na hakika kuwa
tukio lile lote lilikuwa limepangwa.
Nilichokuwa nimepanga sasa ilikuwa ni kuingia ndani ya lile jengo la ghorofa na
kupanda kule juu walipokuwa wamejibanza wale watu ili nikawafanyie shambulizi
la kushtukiza. Lakini nilipokuwa katika harakati za kufanya vile mara nikajikuta
nikishtushwa na muungurumo wa gari lililokuwa likija kwa kasi kwenye lile jengo.
Tukio lile likanipelekea haraka niirudishe mafichoni bastola yangu niliyokuwa
nimeishika mkononi nikilikaribia lile jengo. Muungurumo ule wa gari ulizidi kusikika
ukija upande ule wa ghorofa na tukio lile likanipelekea nijibanze kwenye ukuta wa
jengo lile.
Nikiwa naendelea kuchungulia kule mbele mara nikaliona gari la polisi aina ya
Landcruiser likichomoza kwa kasi na kushika breki kali mbele ya lile jengo la ghorofa.
Askari wanne wenye bunduki mikononi mwao wakawahi kuruka chini katika mtindo
wa aina yake hata kabla ya gari lile halijasimama vizuri.
Haikunichukua muda mrefu kufahamu kuwa mara ile tena nilikuwa nimezidiwa
ujanja kwani uwezekano wa kutekeleza adhama yangu usingewezekana tena baada ya
wale polisi kufika eneo lile. Niliendelea kuwatazama wale polisi ambao sasa nilihisi
kuwa huwenda walikuwa wamepigiwa simu na msamaria mwema baada ya kusikika
kwa ile milio ya zile risasi zilizokuwa zikifyatuliwa na wale watu waliokuwa kule juu ya
lile jengo ghorofa.
Kitendo cha kumuona polisi mmoja akija kwenye ule ukuta niliojibanza
kikanipelekea niyaache taratibu maficho yale na kupotelea vichakani nikilikimbia
eneo lile huku jinamizi la kuzidiwa ujanja kwa mara nyingine likiendelea kuniandama.
Nilipenda nibaki eneo lile ile niweze kuona mwisho wa tukio lile lakini fikra zangu
zikanionya kuwa ile haikuwa sehemu salama tena kwangu.
Nilirudi kwenye ile gereji huku nikiwa nimekata tamaa sana na mwenendo
wa harakati zangu kwani tangu nianze kazi yangu sikuwahi kukutana na vizingiti
vya sampuli ile vinavyonifanya nikose hata sehemu ya kuanzia yenye chanzo cha
kuaminika.
Wakati nikimpa yule kijana malipo yake aliduwaa akishangazwa na kuchafuka
kwangu kuliko sababishwa na zile rabsha za kule nilipotoka. Hata hivyo sikushtushwa
na hali ile badala yake nilimuacha yule kijana akiendelea kunishangaa huku nikifungua
mlango wa gari langu na kuingia ndani. Muda mfupi uliyofuata nikageuza gari langu
na kushika uelekeo wa barabara ya Mandela.
MVUA KUBWA ILIYOKUWA IMEANZA KUNYESHA tena ilikuwa
imefanikiwa kuwafukuza watu katika barabara za mitaa ya jiji la Dar es
Salaam na hivyo kupelekea idadi ya magari barabarani iongezeke maradufu
kiasi cha kusababisha kero kubwa ya foleni.
Taarifa kupitia vituo mbalimbali vya redio zilikuwa zimejikita zaidi katika maafa
ya mvua ile kama;mafuriko katika baadhi ya maeneo,uharibifu wa miundombinu ya
barabara,mali na vifo vya watu. Wananchi waliojenga mabondeni waliendelea kuitupia
lawama serikali huku wajibu wao wa kuhama mabondeni wakiufumbia macho.
Labda serikali ilikuwa na sehemu yake ya kulaumiwa kwa uwepo wa miundombinu
mibovu ya maji taka na barabara kama siyo kuufumbia macho ujenzi wa makazi holela
ya watu katika baadhi ya maeneo. Kila mmoja alistahili lawama kwa upande wake.
Taarifa juu ya athari za mvua ile ziliendelea kumfikia Koplo Tsega kupitia redio ya
gari. Alikuwa ameegesha gari lake mkabala na ofisi za wizara ya ulinzi na mambo ya
ndani nyuma kidogo ya makutano ya barabara za mtaa wa Ghana na ule mtaa wa Ohio
eneo la posta jijini Dar es Salaam.
Mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha ilikuwa imepelekea maji mengi kutuama
barabarani. Maji ambayo kwa hakika hayakustahili kutuama endapo miundombinu
mizuri ya majitaka ingekuwepo kuyatapisha maji yale kwenye bahari ya Hindi ilikuwa
umbali mfupi kutoka pale.
Kitendo cha Koplo Tsega kuegesha gari lake Corolla limited nyeupe yenye kibandiko
cha teksi juu yake na ufito wa njano ubavuni sambamba na mvua kubwa iliyokuwa
ikiendelea kunyesha kilikuwa kimepelekea usumbufu mkubwa wa mara kwa mara
kugongewa vioo madirishani na watu waliokuwa wakihitaji huduma ya usafiri. Kazi
yake ikawa ni kuwajibu watu wale kuwa kuna mtu aliyekuwa akimsubiri.
Kero hiyo ilipozidi Koplo Tsega hakujishughulisha kuwajibu watu hao badala yake
akapandisha na kufunga vioo vya gari. Hivyo mtu yeyote aliyegonga alimpuuza huku
macho yake yakiendelea kutazama kwenye mlango wa mbele wa kutokea kwenye lile
jengo la wizara ya ulinzi na mambo ya ndani.
Tangu ilipotimia saa tisa alasiri Koplo Tsega alikuwa ameegesha gari lake eneo lile
huku macho yake yakiendelea kutazama mbele ya ule mlango wa lile jengo. Tangu
saa tisa alasiri na sasa ilikuwa imetimia saa tatu usiku akiendelea kusubiri ndani ya gari
lile lakini bado alikuwa hajakata tamaa. Alikuwa akimsubiri mtu mmoja aliyefahamika
kwa jina la Pierre Kwizera.
Kama Koplo Tsega asingekuwa ameliona gari la Pierre Kwizera Landcruiser V8
likiwa limeegeshwa kwenye eneo la maegesho la ofisi zile basi huwenda angekuwa
tayari amekata tamaa na kuondoka zake. Lakini kwa sasa uwepo wa gari lile ulikuwa
umemfanya aendelee kuwa mvumilivu akisubiri. Mara kwa mara akajikuta akitazama
kwenye mlango ule kila alipomuona mtu fulani akitoka kwenye lile jengo. Pierre
Kwizera bado hakuonekana.
Usiku huu wa saa tatmwinginea magari yalikuwa yamepungua sana kwenye
maegesho ya ofisi zile. Masaa ya kazi yalikuwa yamefika ukomo kwa siku ile hivyo
kila mfanyakazi aliyetoka kwenye lile jengo alielekea sehemu alipoegesha gari lake na
kuondoka. Pierre Kwizera hakuwa miongoni mwao.
Katika magari machache yaliyokuwa yameegeshwa kwenye eneo la maegesho
ya magari la ofisi zile gari la Pierre Kwizera lilikuwepo. Hivyo uwepo wa gari lile
ukampelekea Koplo Tsega aamini kuwa kulikuwa na wafanyakazi wengine wachache
waliokuwa wamesalia ndani ya lile jengo huku Pierre Kwizera akiwa miongoni mwao.
Koplo Tsega akaendelea kujipa moyo wa uvumilivu na wenye subira.
Haikuwa mpaka ilipofika saa nne usiku pale mwanaume mrefu na mwenye mwili
mpana alipojitokeza kwenye mlango ule wa kutokea nje ya ofisi za wizara ya ulinzi
na mambo ya ndani huku akiwa amevaa suti nadhifu nyeusi na begi dogo la ngozi
mkononi.
Macho ya Koplo Tsega yakarejewa na uhai wakati yalipomtazama mtu yule
akitoka kwenye ule mlango. Mara yule mtu alipotoka akasimama kidogo kwenye
baraza ya jengo lile huku akiitazama saa yake ya mkononi. Kisha akaanza kutembea
akishuka ngazi kueleka kwenye sehemu ya maegesho ya magari ya jengo lile huku
akiwa ameufyatua mwamvuli kujikinga na mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha.
Koplo Tsega alipomchunguza vizuri yule mtu haraka akagundua kuwa alikuwa ni
Pierre Kwizera na hapo tabasamu jepesi likajipenyeza usoni mwake. Pierre Kwizera
alitembea kwa kujiamini akielekea sehemu alipokuwa ameegesha gari lake.
Koplo Tsega hakutaka kuendelea kusubiri hivyo akashusha kioo cha mlango
wa gari hadi pale alipopata upenyo mzuri wa kuupitisha mdomo wa sniper rifle-338
Lapua Magnum. Kisha haraka akairekebisha lensi ya darubini ya bunduki yake huku
akiwa amelifinya jicho lake moja. Taswira ya kichwa cha Pierre Kwizera ilipoenea
vizuri kwenye msalaba wa shabaha wa darubini yake akavuta pumzi nyingi na kuibana
kifuani.
Koplo Tsega alipokuwa akijiandaa kuvuta kilimi cha bunduki ili ahitimishe safari
ya Pierre Kwizera akajikuta akisita kufanya hivyo baada ya mtu fulani kuanza kugonga
kioo cha dirishani cha gari lake. Tukio lile likamshtua na kumpelekea amlaani sana
mtu yule. Hivyo akaiondoa haraka bunduki yake na kuificha nyuma ya kiti chake cha
dereva.
Mwanaume mmoja aliyekuwa akigonga upande wa pili kwenye kioo cha gari lile
alikuwa akiulizia usafiri wa teksi kuelekea eneo la Magomeni Mikumi. Koplo Tsega
akashusha kioo cha gari akimtazama mwanaume yule na bila kuzungumza neno
akapandisha kioo kile cha gari na kukomelea kabari ya mlango.
Wakati Koplo Tsega akiyapeleka tena macho yake kumtazama Pierre Kwizera
kwenye yale maegesho ya magari hakumuona na badala yake akaliona lile gari la Pierre
Kwizera likaacha maegesho ya magari ya eneo lile na kuingia barabarani.
Koplo Tsega hakuwa na namna ya kufanya kwani alikuwa na kila hakika kuwa
jaribio lake la kwanza lilikuwa limeshindikana hivyo akajipa subira kidogo huku
akiliacha gari lile Landcruiser V8 liache maegesho yale na kuingia barabarani. Muda
mfupi uliyofuata Koplo Tsega akawasha gari lake na kuingia barabarani akilifungia
mkia lile gari kwa nyuma.
Uelekeo wa ile Landcruiser V8 ukamtanabaisha Koplo Tsega kuwa Pierre Kwizera
alikuwa akielekea nyumbani kwake eneo la Upanga. Foleni ya magari ilikuwa imepungua
kwenye barabara nyingi za jiji la Dar es Salaam hivyo lile gari Landcruiser V8 lilikuwa
likikata upepo barabarani pasipo pingamizi lolote. Koplo Tsega akajitahidi kwa kila
hali akihakikisha gari lile halimpotei.
Koplo Tsega akaendelea kulifuatilia gari lile kwa nyuma wakati lilipokuwa likiingia
barabara ya mtaa mmoja na kutokezea kwenye barabara ya mtaa mwingine huku
safari ikiendelea.
Mvua kubwa ilikuwa ikiendelea kunyesha sambamba na giza zito lililokuwa
limetanda angani hata hivyo macho ya Koplo Tsega hayakuacha kulitazama lile gari
la Pierre Kwizera mbele yake wakati lilipokuwa likiacha barabara ya mtaa mmoja na
kuingia barabara ya mtaa mwingine. Baada ya safari ndefu hatimaye wakafika eneo la
Upanga.
Baada ya kuzipita nyumba kadhaa za ghorofa za shirika la nyumba la taifa mara lile
gari Landcruiser V8 likabadili uelekeo na kuingia wa upande wa kulia lilikatisha katika
barabara pana ya lami. Barabara ile ilikuwa ikikatisha katikati ya majumba makubwa ya
kifahari yenye kuta ndefu zenye sistimu maalum ya umeme wa kuzuia wezi. Ndani ya
uzio wa nyumba zile sauti ya mbwa wakali wakibweka zilikuwa zikisika.
Mara kwa mara Koplo Tsega alilazimika kupunguza mwendo baada ya kuliona
gari lile Landcruiser V8 likipunguza mwendo katika nyakati tofauti. Hatimaye lile gari
likakata kona na kuelekea upande wa kushoto likikatisha katika mtaa tulivu wenye
barabara pana ya lami inayotazamana na mageti makubwa ya majumba ya kifahari.
Lile gari Landcruiser V8 hatimaye likaenda kusimamia mbele ya geti la nyumba ya
tano ya mtaa ule. Huwenda mwanga wa taa za gari lile ulikuwa umemshutua mlinzi
wa ile nyumba hata kabla honi ya gari haijapigwa. Kwani haukupita muda mrefu
lile geti likafunguliwa na mlinzi na lile gari taratibu likaingia mle ndani. Koplo Tsega
akapunguza mwendo wa gari lake huku akilitazama lile gari Landcruiser V8 wakati
likiingia kwenye ile nyumba. Wakati akipita mbele ya lile geti mlinzi wa ile nyumba
ndiyo alikuwa anamalizia kufunga lile geti hivyo Koplo Tsega akafanikiwa kuona
kwa sehemu tu ya mandhari ya mle ndani. Mara lile geti lilipofungwa Koplo Tsega
akakanyaga mafuta na kuendelea na safari na kwenda kuegesha gari lake mwisho wa
barabara ile sehemu yenye kona ya kuingia barabara ya mtaa unaofuata.http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Mlinzi akakisogeza kifuniko kidogo cha getini na kuchungulia nje kupitia tundu
dogo huku akishangazwa kidogo na utaratibu uliotumika na mgeni yule wa kugonga
geti badala ya kubofya kitufe cha kengele kilichokuwa pembeni ya geti lile ukutani.
Kitendo cha kumuona msichana mrembo akiwa amesimama nje ya geti lile
kikamtoa wasiwasi hivyo akaufunga ule mfuniko wa lile tundu kisha akasogea pembeni
na kufyatua komeo la mlango mdogo wa geti lile kumruhusu mgeni yule kuingia.
Mara tu mlango ule mdogo wa geti ulipofunguliwa Koplo Tsega akaitumia nafasi ile
kujikaribisha mle ndani. Mlinzi wa nyumba ile hakupata muda wa kufanya mahojiano
na Koplo Tsega kwani kufumba na kufumbua akapigwa mapigo matatu Smart ya
chapuchapu ya Karate. Mapigo mawili kifuani na pigo moja funga kazi la shingoni na
hapo shughuli za mwili za mlinzi yule zikasimama huku uzito ukimuelemea. Mlinzi
yule akafumba macho yake taratibu na kuanguka chini mzima mzima hata hivyo
Koplo Tsega akawahi kumdaka kabla hajafika chini kisha akamburuta hadi nyumba
ya kibanda chake cha kazi kilichokuwa kando ya lile geti.
Sauti za mbwa waliokuwa wakibweka zilisikika mle ndani hata hivyo Koplo Tsega
alipochunguza vizuri akagundua kuwa mbwa wale walikuwa ndani ya banda lililokuwa
nyuma ya kile kibanda cha mlinzi.
Jumba kubwa la kifahari lilikuwa limepandwa katikati ya uzio ule huku likiwa
limezungukwa na bustani ya maua mazuri na miti ya kuvutia. Lile gari Landcruiser V8
halikuonekana nje ya lile jumba lakini uwepo wa banda la kuegeshea gari lililokuwa
kando ya lile jumba ukaashiria kuwa lile gari lilikuwa limeingizwa ndani ya lile banda
muda mfupi uliyopita.
Taa ya sebuleni kwenye lile jumba ilikuwa ikiwaka ingawa mapazia mazito
yaliyokuwa madirishani hayakuruhusu mtu yoyote kuona kwa urahisi mle ndani.
Koplo Tsega akapanda ngazi za barazani na kuusogelea mlango wa mbele wa lile
jumba huku akizitupa hatua zake kwa utulivu. Hali ilikuwa shwari na dalili zikaonesha
kuwa ndani ya ile sebule hakukuwa na mtu yoyote hivyo Koplo Tsega akakishika
kitasa cha mlango ule wa mbele na kuusukuma ndani taratibu. Ule mlango ulikuwa
wazi hivyo hapakuwa na upinzani wowote.
Koplo Tsega alipoingia ndani akajikuta akitazamana na sebule kubwa yenye
samani za kisasa kama seti mbili za makochi makubwa ya sofa juu ya zulia la manyoya
laini la rangi ya kijivu. Katikati ya sebule ile kulikuwa na meza fupi lakini pana ya mti
wa mpingo. Upande wa kushoto kulikuwa na rafu kubwa ukutani iliyopangwa aina
tofauti za vitabu. Ukutani kulitundikwa picha nzuri za kuchorwa zinazovutia. Upande
wa mbele wa ile sebule kulikuwa na runinga pana juu ya meza fupi ya kioo iliyopakana
na kabati dogo lenye droo nne.
Pierre Kwizera hakuwepo pale sebuleni wala lile begi lake alilotokanalo ofisini na
badala yake jumba yote lilikuwa kimya hali ile ikiashiria kuwa Pierre Kwizera alikuwa
akiishi peke yake mle ndani.
Akiwa amejiridhisha kuwa Pierre Kwizera hakuwepo pale sebuleni Koplo Tsega
akaurudishia mlango wa pale sebuleni nyuma yake kisha akaichomoa bastola yake
kutoka mafichoni na kuikamata vyema mkononi. Ukimya wa mle ndani ukampelekea
ayasikilizie mapigo hafifu ya moyo wake yalivyokuwa yakihangaika ovyo kifuani
mwake.
Sehemu fulani ndani ya nyumba ile mlango ukasikika ukifunguliwa na kisha
kufungwa halafu baada ya hapo zikasikika hatua tulivu za mtu akitembea kuja pale
sebuleni. Mtu yule alikuwa ni Pierre Kwizera na wakati huu alikuwa amebadili mavazi
yake. Pierre Kwizera alikuwa amevaa suruali ya pajama na fulana ya mchinjo na
miguuni alikuwa amevaa viatu laini vya manyoya.
Pierre Kwizera akaendelea kutembea kwa kujiamini na alipofika pale sebuleni
akaelekea mlangoni ambapo aliufunga mlango ule kwa funguo. Alipomaliza akaelekea
kwenye madirisha ya pale sebuleni na kusogeza vizuri mapazia katika namna ya
kufunika sehemu zote zilizokuwa wazi. Hatimaye akaelekea kwenye makochi
yaliyokuwa pale sebuleni na kuwasha runinga huku akiketi kwenye kochi moja kati ya
makochi mengi yaliyokuwa eneo lile. Pierre Kwizera akiwa ameketi kwenye kochi lile
ghafla akahisi kuwa chuma cha baridi kilikuwa kikikigusa kisogo chake kwa nyuma.
Hali ile ikampelekea Pierre Kwizera ageuke kwa ghafla na kutazama nyuma yake.
Koplo Tsega ambaye alikuwa amejibanza nyuma ya ile rafu ya vitabu pale sebuleni
alikuwa amejitokeza tayari kumkabili Pierre Kwizera pale kwenye kochi. Pierre
Kwizera akageuka kwa ghafla kutazama nyuma yake na mshtuko alioupata baada ya
kumuona Koplo Tsega ukampelekea aduwae kwa muda na kuganda kama sanamu.
Alichokihisi baada ya pale ni kuwa sehemu fulani mwilini mwake jasho jepesi
lilikuwa likianza kutoka. Mapigo ya moyo wake yakasimama kwa sekunde kadhaa
kabla ya kuanza kwenda mbio kama mtu aliyekuwa akifukuzwa na mnyama mkali.
Macho ya mshangao yakamtoka huku koo lake likikauka taratibu na kwa mbali nyuma
ya masikio yake mishipa yake ya damu ilianza kutuna na kusukuma damu kwa kasi hali
iliyompelekea jasho jepesi lianze kushuka kwenye paji lake.
Pierre Kwizera hisia zake zikamueleza kuwa alichokuwa akikiona mbele yake
ulikuwa ni mzimu wa Koplo Tsega na hapo akili yake ikaanza kufanya kazi haraka.
Bastola yake ilikuwa kwenye droo ya tatu ya kabati dogo lililokuwa pembeni ya
runinga pale sebuleni. Kufumba na kufumbua Pierre Kwizera akafanya hila kwa
kulisukuma lile kochi kwa nyuma na hapo bastola ya Koplo Tsega ikamponyoka huku
yeye akijitupa upande ule uliokuwa na lile kabati dogo pale sebuleni kisha akavuta
droo ya tatu na kuichukua bastola yake
Makadirio ya Pierre Kwizera yalikuwa sawia kwani ndani ya muda mfupi akawa
amefanikiwa kulifungua lile kabati na kuichuka ile bastola yake. Lakini Koplo Tsega
hakumpa nafasi Pierre Kwizera ya kutimiza adhma yake kwani bastola ile aliipangusa
na kuitupilia mbali kwa teke lake. Hata hivyo Pierre Kwizera hakuwa mtu rahisi kwani
pigo la pili la teke la Koplo Tsega lilipokuja akawahi kuinama chini akilikwepa kisha
akamchota Koplo Tsega kwa mtama wa aina yake uliomrusha hewani na alipokuwa
mbioni kutua chini akamuwahi na kumtandika pigo la teke la tumbo lililomtupa
ukutani. Kisha Pierre Kwizera akajibetua na kusimama huku amepandwa na ghadhabu.
Koplo Tsega akaugulia maumivu makali ya kipigo kile huku akijilaumu kwa kufanya
makadirio ya chini dhidi ya adui yake. Pierre Kwizera hakumpa nafasi Koplo Tsega
hivyo kabla Koplo Tsega hajasimama pale chini akatupa pigo jingine la teke usawa wa
kichwa chake. Mara hii Koplo Tsega alikuwa mwepesi kujihami akijiviringisha haraka
mara mbili pale sakafuni kulikwepa pigo lile huku damu nyepesi ikimtoka puani.
Pigo jingine la teke la Pierre Kwizera lilipokuja Koplo Tsega akaliona na kulidaka
kwa nguvu zake zote kisha akauzungusha ule mguu na hapo Pierre Kwizera akarushwa
hewani. Lakini Pierre Kwizera hakwenda mbali kwani Koplo Tsega aliwahi kuivuta
fulana yake mchinjo kwa nyuma na kumshindilia mgumi mbili kavu za mgongoni
zilizompelekea abweke kama mbwa huku maumivu makali yakisambaa mwilini
mwake. Pierre Kwizera akayumbayumba akitafuta mhimili hata hivyo alichelewa
kwani teke jingine la Koplo Tsega likamtandika shingoni na kumtupia ukutani.
Pigo jingine la ngumi ya uso lilipomfikia Pierre Kwizera ambaye alishaanza kuona
dalili za kuzidiwa maarifa akawahi kulipangua kisha kwa nguvu zake zote akamsukuma
Koplo Tsega kwenye ile rafu ya vitabu iliyokuwa pale sebuleni. Ile rafu ikaanguka chini
huku vioo vyake vikipasuka na vile vitabu vikitawanyika ovyo pale chini sakafuni.
Koplo Tsega akapiga yowe la hofu kwani vile vioo vilikuwa vimemchana
mikononi. Pierre Kwizera aliwahi kumfikia Koplo Tsega pale chini akamvuta na
kumkaba kabari matata shingoni. Koplo Tsega akajaribu kufurukuta bila mafanikio
kwani Pierre Kwizera alikuwa mtu mwenye nguvu sana. Hata hivyo Koplo Tsega
hakukata tamaa badala yake aliendelea kurusha miguu yake huku na kule akitafuta
namna ya kujinasua. Pierre Kwizera akiwa amelitambua hilo hakumpa nafasi Koplo
Tsega ya kujinasua badala yake akaendelea kuikaza ile kabari na kumbeba juu juu.
“Si unajidai mzimu basi tulia nikuoneshe,ngedere mkubwa we!” Pierre Kwizera
akafoka huku akiendelea kumkaba Koplo Tsega shingoni kiasi cha kumnyima nafasi
nzuri ya kuhema. Koplo Tsega akaanza kupoteza matumaini huku akihema kwa taabu.
Huku akiwa ametoa macho Koplo Tsega akaanza kuhisi wingu jepesi la giza
likitanda mbele yake hata hivyo hakukata tamaa badala yake akaendelea kurusha
miguu yake huku na kule katika namna ya kutaka kujinasua.
Shughuli ilikuwa pevu hata hivyo mikikimikiki ile ikawapelekea taratibu wasogee
karibu na ukuta wa pale sebuleni. Walipoufikia ule ukuta Koplo Tsega akaitumia fursa
ile kuikita miguu yake ukutani kisha akakusanya nguvu za kutosha na kuusukuma
ule ukuta kwa miguu yake. Tukio lile likawarusha wote na kuwabwaga pale sakafuni
kwa kishindo. Pierre Kwizera akapiga yowe kali na hapo akaifungua ile kabari bila
kupenda. Alipotaka kusimama Koplo Tsega akamuwahi kwa kumtandika kiwiko
cha nguvu kilichoupasua mwamba wa pua yake na kumpelekea apige yowe kali la
maumivu kama aliyekalia msumari. Pigo la pili la ngumi lilipomfikia akawahi kuliona
hivyo akalikwepa kwa kujirusha pembeni hivyo pigo la Koplo Tsega likakata hewa
bila majibu.
Pierre Kwizera akiwa bado anaugulia maumivu ya pua huku kamasi za damu
zikimtoka akakusanya nguvu na kusimama hata hivyo akashangaa kujikuta akirudi
tena pale chini bila kupenda.
Koplo Tsega alikuwa ameishtukia haraka dhamira ya Pierre Kwizera hivyo akawa
amemuwahi kwa kumchota mtama wa chini uliompaisha hewani mzobemzobe.
Pierre Kwizera alipokuwa akitua chini akatua juu ya ile meza fupi ya mbao ya mpingo
iliyokuwa pale sebuleni huku mkono wake ukivunjika na hapo akapiga yowe kali la
maumivu.
Koplo Tsega hakumpa Pierre Kwizera nafsi ya kutafakari pale chini kwani
akamuwahi haraka kwa pigo moja madhubuti la judo kichwani. Pierre Kwizera
akatulia kimya akining’inia juu ya meza ile kama mbuzi kwenye kiti cha baiskeli huku
fahamu zikiwa mbali naye.
_____
FAHAMU ZILIPOMRUDIA Pierre Kwizera akajikuta amefungwa kwenye
kiti kikamilifu huku kamba iliyotumika kumfunga ikiwa ni pazia mojawapo la pale
sebuleni. Jicho lake moja lilikuwa limevimba na kuvilia damu. Sehemu ya juu upande
wa kushoto usoni alikuwa amechanika na damu ilikuwa ikiendelea kutoka kwenye
jeraha. Mdomo wake ulikuwa umechanika na jino lake moja lilikuwa limevunjika. Ile
fulana yake mchinjo ilikuwa imeraruka vibaya na kuning’inia kama mikia ya Pweza.
Maumivu ya ule mkono wake uliovunjika yakampelekea ayafumbe macho yake
taratibu huku akizipa uhai fikra zake. Koplo Tsega alikuwa ameketi kwenye kiti mbele
yake akimtazama.
“Unajisikiaje?” Koplo Tsega akamuuliza Pierre Kwizera kwa utulivu huku
akimtazama
“Wewe ni nani?” Pierre Kwizera akauliza kivivuvivu huku bado akiona
maruweruwe.
“Koplo Tsega mdunguaji na askari komandoo wa jeshi la wananchi Tanzania.
Usiniambie kuwa mara hii umenisahau” Koplo Tsega akacheka kwa kicheko hafifu
lakini kilichohifadhi chuki ndani yake.
“Koplo Tsega au mzimu wa Koplo Tsega?” Pierre Kwizera akauliza kwa taabu
huku akipambana na maumivu makali mwilini mwake.
“Koplo Tsega na siyo mzimu wa Koplo Tsega” maelezo ya Koplo Tsega
yakampelekea Pierre Kwizera afungue macho yake vizuri na kumtazama Koplo Tsega
mbele yake. Taswira ya Koplo Tsega ilipojengeka vizuri machoni mwake akashikwa
na mshangao.
“Koplo!...ni wewe?” Pierre Kwizera akauliza kwa mshangao.
“Ndiyo mimi hebu nitazame vizuri” Koplo Tsega akaongea huku akitabasamu
na hapo macho ya Pierre Kwizera yakaweka kituo yakimtazama Koplo Tsega mbele
yake.
“Sasa yule aliyezikwa ni nani?” Pierre Kwizera akauliza kwa mshangao.
“Rafiki yangu”
“Mbona sikuelewi?”
“Ni hadithi ndefu na hicho siyo kilichonileta hapa” maelezo ya Koplo Tsega
yakampelekea Pierre Kwizera azidi kushikwa na mshangao. Kitambo kifupi cha
ukimya kikapita kisha Pierre Kwizera akavunja tena ukimya.
“Sasa una shida gani na mimi hadi univamie usiku huu?” swali la Pierre Kwizera
likampelekea Koplo Tsega atabasamu tena kisha akaingiza mkono mfukoni kuichukua
ile bahasha yenye zile hundi. Koplo Tsega alipoifungua bahasha ile akapekuwa hadi
pale alipoifikia hundi yenye jina la Pierre Kwizera na kuichomoa.
“Nani anayewapa hizi fedha?” Koplo Tsega akavunja ukimya akimuuliza Pierre
Kwizera huku akimuonesha ile hundi yenye jina lake. Pierre Kwizera akaitazama ile
hundi kwa makini na hapo mshangao ukazidi kumshika.
“Nani aliyekupa hundi yangu?” Pierre Kwizera akauliza kwa hamaki.
“Bado hujanijibu swali langu komredi!” Koplo Tsega akaongea kwa msisitizo.
Pierre Kwizera akashikwa na kugugumizi huku akiendelea kuitazama ile hundi kwa
mshangao.
“Sifahamu chochote!” hatimaye akaongea kwa utulivu baada ya kukohoa kidogo.
“Ulikuwa ukitarajia hundi ya namna hii kukufikia?” Koplo Tsega akauliza huku
akiipigapiga ile hundi kwa kidole chake na wakati huo akimtazama Pierre Kwizera
mbele yake. Pierre Kwizera akaitazama tena ile hundi kwa utulivu huku akioneka
kama aliyekuwa njia panda katika kutoa jibu dhidi ya lile swali.
“Ndiyo!..ha..hapana!”
“Mbona hueleweki?”
“Jibu ni ndiyo” hatimaye Pierre Kwizera akaongea kwa kujiamini.
“Okay! tia sahihi yako hapa” Koplo Tsega akamwambia Pierre Kwizera huku
akimpa ile hundi na kalamu ya wino. Pierre Kwizera akaipokea ile hundi kwa taabu
kwani sehemu za mikono yake zilikuwa zimefungwa huku akiwa ameshikwa na
mshangao. Akamtazama Koplo Tsega kwa mashaka kisha akatia sahihi kwenye ile
hundi. Alipomaliza Koplo Tsega akaichukua ile hundi na kuitia kwenye bahasha
kisha ile bahasha akaitika mfukoni huku akimuacha Pierre Kwizera katika mshangao
usioelezeka. Hata hivyo hakuzungumza neno.
“Unaweza kuniambia ulikuwa ukitarajia kupokea hundi hii kutoka kwa nani?”
Koplo Tsega akauliza kwa utulivu baada ya kuiweka ila bahasha mfukoni. Pierre
Kwizera akamtazama Koplo Tsega kwa makini kama ambaye anajutia jibu lake
lililotangulia. Kisha kwa sauti ya uchovu akajitahidi kuzungumza
“Sifahamu chochote kuhusu hiyo hundi!”
“Nilitarajia jibu la namna hiyo kwako hata hivyo natambua kuwa unanidanganya.
Wewe na wenzako mmepewa pesa kwa ajili ya kuniua mimi na Sajenti Chacha Marwa.
Nafahamu kuwa yupo mtu anayewapa hizi fedha na ni afadhali ukamtaja kwani jaribio
lenu limeshindikana” Koplo Tsega akaongea huku uso wake ukiwa mbali na mzaha.
“Mbona sielewi unachosema?” Pierre Kwizera akaongea kwa utulivu huku
mshangao ukishindwa kujificha machoni mwake.
“Utaendelea kujidanganya kuwa huelewi hadi lini komredi wakati ukweli
unaufahamu vizuri?” Koplo Tsega akamuuliza Pierre Kwizera kwa utulivu.
“Koplo mbona unanichanganya kwa habari ambazo sizielewi?” Pierre Kwizera
akauliza huku akionesha kukata tamaa.
“Mtu wenu mliyemtuma hakuwa makini sana” Koplo Tsega akaendelea kuongea
kwa utulivu.
“Mtu gani unayemzungumzia?” Pierre Kwizera akauliza kwa shauku
“Meja Khalid Makame!”
“Nani aliyekwambia?” Pierre Kwizera akauliza kwa mshangao hali iliyompelekea
Koplo Tsega atabasamu kidogo.
“Hakuna mtu aliyeniambia komredi nimejionea mwenyewe kwa macho yangu.
Mtu wenu Meja Khalid Makame hakuwa makini katika kukamilisha mpango wenu na
mimi sikufanya makosa kumchakaza vibaya kwa risasi”
“Mungu wangu! kwa hiyo wewe ndiye uliyemuua Meja Khalid Makame?” Pierre
Kwizera akauliza kwa mshangao.
“Ndiyo! tena nimemuua kwa risasi zangu mwenyewe” Koplo Tsega akajigamba
kwa ghadhabu. Pierre Kwizera akamtazama Koplo Tsega kama ambaye hakumsikia
vizuri lakini ukweli ni kuwa alikuwa amemsikia vizuri Koplo Tsega na jasho jepesi
lilikuwa likianza kumtoka mwilini.
“Oh! my God umefanya nini Koplo?. Kwanini umuue Meja Khalid Makame?”
Pierre Kwizera akauliza kwa hamaki.
“Acha kuigiza komredi. Unadhani mazingira ya kifo cha Meja Khalid Makame
yametawaliwa na hisia?. Sijamuua kwa bahati mbaya na wala sijuti kwa nilichokifanya
kwani ningezembea kidogo angenimaliza na mipango yenu ingeenda sawa. Huwenda
muda huu mngekuwa mkifanya tafrija ya kujipongeza kwenye hoteli moja kubwa ya
kifahari hapa jijini Dar es Salaam” Koplo Tsega akaongea huku akiangua kicheko
hafifu cha dhihaka kisha akaendelea
“Sasa tafrija yenu imeanza kugeuka msiba mzito sana kwani nitawawinda mmoja
baada ya mwingine ili mfidie hasara ya maisha ya watu mliyowaua bila hatia. Kweli
hamna haya na ufedhuli wenu yaani kumbe shughuli zote zile tulizokuwa tukizifanya
kwenye hii tume ni kiini macho tu!. Kama hamkutuhitaji kwanini mlituita?” Koplo
Tsega akacheka tena kwa dhihaka kabla ya kuendelea
“Sasa kaeni chonjo kwani yule msiyemtaka amekuja” Koplo Tsega akaendelea
kuongea huku akicheka kwa dhihaka na hasira.
“Kuwa makini Koplo kwani sasa naanza kuhisi kuwa mapigano ya msituni
yamekuchanganya akili yako vibaya” Pierre Kwizera akaongea kwa hasira huku
akijitahidi kujinanusua kwenye kile kifungo bila mafanikio. Koplo Tsega akaendelea
kucheka na kicheko chake kilipofika ukomo akamkata jicho la hasira Pierre Kwizera
mbele yake.
“Kama isingekuwa bahati mbaya basi muda huu ungekuwa unatafutiwa sanduku
zuri la mzishi yako huku wataalam wakikuandalia wasifu mzuri wenye mbwembe na
heshima nyingi kwa wale wasiokujua”
“Una maanisha nini?” Pierre Kwizera akuliza kwa hasira.
“Risasi zangu mbili makini zingekuwa zimekufumania vizuri na kukifumua vibaya
kichwa chako wakati ulipokuwa ukitoka nje ya lile jengo la ofisi za wizara ya ulinzi na
mambo ya ndani muda mfupi uliyopita” Koplo Tsega akaongea huku akitabasamu.
Pierre Kwizera akashikwa na mshangao wa aina yake huku akilikumbuka gari dogo
jeupe aina ya Corolla limited aliloliona mara mbili na zaidi nyuma yake na kulipuuza
wakati alipokuwa akitoka ofisini kwenye lile jengo la wizara ya ulinzi na mambo ya
ndani.
“Koplo!...so you wanted to kill me?” Pierre Kwizera akauliza kwa mshangao.
“Definitely!...” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu huku uso wake ukishindwa
kuonesha tashwishwi yote.
“Why…?” Pierre Kwizera akauliza hata hivyo Koplo Tsega akalipuuza swali lile na
badala yake akatumbukiza swali lake.
“Nani anayewapa hizi fedha?”
“Sifahamu chochote Koplo” Pierre Kwizera akajitetea
“Huwezi kufa na siri hiyo moyoni komredi kwani haupo peke yako. Ukifa wewe
wenzako wataniambia tu!” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu
“Hufahamu unachokizungumza Koplo!” Pierre Kwizera akaongea kwa kulalama
huku akionekana kuzama kwenye tafakuri.
“Nafahamu kuwa kuna maslahi makubwa mliyoyapata au mliyoahidiwa kuyapata
mara baada ya vifo vyetu. Hizi hundi nimezikuta nyumbani kwa Meja Khalid Makame
mtu mliyemtuma D.R Congo kuja kutimiza mpango wenu mchafu. Bahati mbaya
sana mpango wenu umeharibika hivyo hamuwezi kupiga hatua nyingine mbele zaidi
bila ya kuniua mimi. Lakini mimi nimekufa na kila mtu ana amini hivyo na hali hiyo
ndiyo inayonipa nafasi nzuri ya kupambana na nyinyi huku nikiwa sipo katika fikra
zenu kabisa just because i am dead,burried and forgotten” Koplo Tsega akaongea huku
akiangua kicheko hafifu cha hasira na dhihaka.
“Nakushauri urudi nyumbani ukapumzike kwanza kwani akili yako inaonekana
imeathirika vibaya na milio ya mabomu na risasi msituni” Pierre Kwizera akaongea
kwa dharau huku tabasamu hafifu likipita usoni mwake. Koplo Tsega akamtazama
Pierre Kwizera kwa hasira bila kusema neno lolote badala yake akasimama na kuelekea
kwenye kochi lililokuwa jirani na eneo lile.
Aliporudi alikuwa ameshika kompyuta mpakato aliyoichukua kwenye begi la
ofisini la Pierre Kwizera kule chumbani kwake muda ule Pierre Kwizera alipokuwa
amepoteza fahamu baada yay ale mapambano makali.
Baada ya kuketi Koplo Tsega akaifungua ile kompyuta mpakato na alipoiwasha
akamtazama Pierre Kwizera kwa uyakinifu kabla ya kuvunja ukimya.
“Nahitaji password yako” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu huku akimsogezea
karibu Pierre Kwizera ile kompyuta. Pierre Kwizera akaitazama kompyuta yake kwa
makini hata hivyo hakuingiza password yake kama alivyoambiwa na badala yake akainua
macho yake akimtazama Koplo Tsega huku akitabasamu.
“Unadhani mimi ni mjinga kiasi hicho?” Pierre Kwizera akaongea huku akiendelea
kutabasamu. Koplo Tsega akamtazama Pierre Kwizera kwa kitambo huku akiyapima
maneno yake na hapo akagundua kuwa Pierre Kwizera alikuwa akimaanisha kile
alichokuwa akikisema. Hasira zikampanda Koplo Tsega huku akianza kupoteza moyo
wa uvumilivu.
“Nimewaua Meja Khalid Makame,Guzbert Kojo na P.J.Toddo hivyo kama
utaendelea kushikilia msimamo wako sioni sababu ya kukuvumilia komrade” Koplo
Tsega akaongea huku akimtazama Pierre Kwizera mbele yake. Pierre Kwizera
akashikwa na taharuki baada ya kuyasikia maelezo yale.
“My God! kumbe ni wewe…?”
“Don’t west my time comrade,I need your password please…!” Koplo Tsega akasisitiza
“Kwa hiyo umekuja kuniua na mimi?. Utaua watu wangapi Koplo?. Kwanini
ufanye makosa yasiyo na ulazima?. Serikali hii ina mtandao mkubwa itakufikia popote
utakapojificha. Utakamatwa na kufunguliwa mashtaka ya mauaji ya kukusudia na
mwisho wako ni kunyongwa tu”
”Unanitisha?. Unadhani utafanikiwa kunitisha?. Mimi siyo mwoga kama nyinyi.
hebu niambie komredi feki ni pesa kiasi gani mliyolipwa kuuondoa uhai wetu?.
Kwa miaka mingi mmekuwa mkifanya kiini macho kama Paka mwenye njaa kali
anayesalisha kundi kubwa la Panya huku akiwa amevaa rozari ya dagaa.
Nguvu kazi kubwa ya taifa hili imeharibika kwa ajili yenu. Pesa nyingi ya wazalendo
walipakodi wa taifa hili mnazitafuna na kujineemesha na familia zenu. Watoto wenu
wanasoma kwenye shule na vyuo vikubwa vikubwa nje ya nchi ili baadaye waje
kushika madaraka hata kama ni bongo lala. Wakati watoto wa masikini wanataabika
mitaani na ndiyo mnazidi kuwamaliza kwa biashara zenu chafu.
Kila kunapokucha tume zisizo na vichwa wala mikia zinaundwa kutatua
matatizo yasiyo ya lazima na matokeo yake ni utafunwaji wa mabilioni ye fedha kwa
wapumbavu wachache wanaojiita wajanja waliobarikiwa. Hii nchi mnataka kuipeleka
wapi nyinyi wapumbavu?” Koplo Tsega akaweka kituo akimtazama Pierre Kwizera
huku amepandwa na hasira.
“Huelewi unachokizungumza Koplo. Mimi nakuona kama unayepiga kampeni za
kisiasa” Pierre Kwizera akaongea huku usoni akiumba tabasamu la dharau.
“Mlidhani kuwa mambo yangekuwa rahisi komredi lakini mlikosea sana kwani
nimerudi nikiwa na nguvu za kutosha za kuwashughulikia mmoja baada ya mwingine.
Tafadhali! ingiza password yako kwenye hii kompyuta kwani muda wa nasaha
umekwisha” Koplo Tsega akaongea huku uso wake umejawa na chuki.
“Kwanini uning’ang’anize kuweka password kwenye kompyuta yangu?”
“Nahitaji faili langu” Koplo Tsega akaongea huku uso wake umetulia kama jiwe.
“Faili lipi?” Pierre Kwizera akauliza huku akimtazama Koplo Tsega kwa makini.
“Faili lenye taarifa zangu zote nilizozifanyia kazi wakati nikiwa kwenye hii tume”
Koplo Tsega akaongea kwa utulivu huku uvumilivu ukipungua. Pierre Kwizera
akamtazama kabla ya kuangua kicheko cha dhihaka.
“Hii ni serikali Koplo siyo Project ya mtu binafsi au Ngo’s. Unapoteuliwa kwenye
tume yoyote huwa kuna taratibu zake za kufuata na unapotolewa huwa ni vilevile. Hii
siyo miradi kama Mkukuta au Mkulabita. Unapoondolewa kwenye tume taarifa zako
huwa ni confidencial hivyo huna haki ya kuzidai tena.
Wewe,Sajenti Chacha Marwa na Meja Khalid Makame mlishaondolewa kwenye
hii tume hivyo huwezi kurudi kienyeji na istoshe kazi zenu walishateuliwa watu
wengine kuzifanya” Pierre Kwizera wakati akimaliza kuongea akajikuta akiambulia
kichapo cha nguvu kutoka kwa Koplo Tsega kilichomsababishia maumivu makali
mwilini.
“Ingiza password yako komredi ukaidi hautokusaidia kitu” Koplo Tsega akaongea
kwa hasira.
“Go on you bastad kwani najua kuwa huwezi kuniua” Pierre Kwizera akaongea huku
tabasamu lake likiwa limechanganyika na maumivu makali. Koplo Tsega kuona vile
akabadili mtindo wa mateso akimtimba Pierre Kwizera miguuni kwa kisigino cha
viatu vyake. Pierre Kwizera akaendelea kulalama pasipo kuweka password kwenye ile
kompyuta yake.
“Utaniua lakini hautafanikiwa kufika mbali Koplo”
“Subiri uone” Koplo Tsega akaongea huku akiikamata vyema bastola yake kisha
akaielekeza bastola ile kwenye paja la Pierre Kwizera na kuisukuma risasi moja. Pierre
Kwizera akapiga yowe kali huku akiwa haamini macho yake. Maumivu aliyoyapata
kutokana na lile jeraha la ile risasi yakamchanganya kabisa. Jasho likaanza kumtoka
huku akihema ovyo wakati alipoitazama damu yake kwenye lile jeraha.
“Nilikwambia kuwa ukaidi hautakusaidia kitu komredi. Tafadhali! ingiza password
yako kwenye hii kompyuta” Koplo Tsega akaongea kwa ghadhabu huku akiilekeza
bastola yake tena kwenye paja jingine la Pierre Kwizera. Pierre Kwizera kuona vile
akahamaki na kushikwa na hofu huku mdomo ukimchezacheza na mikono yake
ikitetemeka ovyo. Mara hii akaupeleka mkono wake taratibu na kuanza kubofya vitufe
vya keyboard ya kompyuta yake akiingiza password. Muda mfupi uliyofuata ile kompyuta
ikafunguka.
“Good boy!” Koplo Tsega akaongea huku akitabasamu kisha tabasamu lake
lilipofifia na kukoma sura yake ikavaa uso wa kazi na hapo akaikamata vizuri bastola
yake mkononi. Tukio lile likampelekea Pierre Kwizera aingiwe na hofu.
“Ukifika mwambie P.J.Toddo kuwa mimi ndiye niliyemuua”
“Nikifika wapi?’’ Pierre Kwizera akauliza kwa shauku lakini hakujibiwa na badala
yake risasi mbili za bastola ya Fort 12 iliyofungwa kiwambo maalum cha kuzuia
sauti zikapenya kwenye pafu lake la kulia na kutengeneza matundu mawili madogo
yanayovuja damu. Pierre Kwizera akapiga yowe kidogo na kutulia huku umauti ukiwa
tayari umemchukua.
Koplo Tsega akamtazama Pierre Kwizera kwa utulivu huku akitabasamu kisha
akachukua kitabu chake kidogo na kalamu kutoka mfukoni. Kupitia kitabu kile
akafunua kurasa hadi pale alipolifikia jina la Pierre Kwizera ambapo aliweka kituo na
kuweka alama ya X kisha akakirudisha kile kitabu mfukoni. Koplo Tsega hatimaye
akachukua pipi ya kijiti kutoka mfukoni kisha akaimenya taratibu na kuitia mdomoni.
Muda mfupi baadaye msako aliomaliza kuupitisha ndani ya nyumba ya Pierre
Kwizera ukawa umempatia vitu fulani muhimu alivyovihitaji. Koplo Tsega hakuwa
na muda wa kupoteza hivyo akafungua mlango wa ile nyumba na kutoka nje.
Mvua kubwa iliyokuwa ikiendelea kunyesha haikumzuia kuendelea na safari yake
wakati alipoitoroka nyumba ile na kupotelea mitaani.
KIKAO KILICHOFANYIKA MAPEMA SANA alfajiri juu ya jengo moja
la ghorofa lililokuwa kando ya jiji la Dar es Salaam kikiwashirikisha watu
wachache waliopigiwa simu usiku wa manane kilikuwa kimehitimika kwa
kufanyika maazimio kadhaa makubwa na muhimu katika namna ya kukabiliana na
mauaji ya maafisa wa vitengo nyeti vya usalama yaliyokuwa yakiendelea kutokea jijini
Dar es Salaam.
“Hatuwezi kusema nchi yetu ni kisiwa cha amani wakati mauaji ya viongozi
wa vitengo nyeti vya usalama vya nchi hii yanaendelea kutokea“ M.D.Kunzugala
mwanaume mrefu na mweusi mwenye mwili imara uliyojengeka vizuri kwa shibe isiyo
ya wasiwasi na mazoezi ya kutosha akaongea kwa hasira huku akiyatembeza macho
yake taratibu kuzitazama kwa makini sura za wajumbe waliofika kwenye mkutano ule.
Tangu pale alipogiwa simu kujulishwa juu ya taarifa za kifo cha Pierre Kwizera
usiku wa manane M.D.Kunzugala alikuwa hajatulia hata kidogo. Usingizi alioanza
kuutongoa kitandani ukawa umeyeyuka na baada ya hapo akawa akipokea na kupiga
simu kwa viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa nchi. Maswali yalipokuwa mengi
M.D.Kunzugala akatoka nje ya nyumba na kuwasha gari lake akielekea eneo la tukio.
Kwa mara ya kwanza akajikuta akianza kuichukia kazi yake na kuzitamani kazi
nyingine tofauti zisizokuwa na majukumu kama yake. Kwa muda wa miaka sita tangu
alipoteuliwa kushika kitengo hiki alikuwa hajakutana na misukosuko na changamoto
ambazo kwa sasa alianza kuzihisi kuwa zilikuwa mbioni kukitilia mchanga kitumbua
chake.
“Mauaji yameanza kwa Guzbert Kojo yakahamia kwa P.J.Toddo na sasa ni kwa
Pierre Kwizera. Hivi bado mnataka niamini kuwa mauaji haya yanatekelezwa na
wahalifu wa kawaida kama panya road?. Hilo mimi siliamini na sitaki katu kuliamini.
Binafsi nahisi kuna kitu fulani kinachoendelea na kilichojificha nyuma ya mauaji
haya. Hata hivyo sitaki tuamini sana katika hisia zangu ndiyo maana nikawaita hapa
ili tujadiliane nini cha kufanya kuikomesha hali hii” M.D.Kunzugala akaweka kituo
akikohoa kidogo kusafisha koo lake huku akionekana kufikiria jambo. Wakati akifanya
vile macho yake yakawa yakiendelea kufanya ziara kuzitazama sura za wajumbe
waliohudhuria mkutano ule mfupi wa dharura.
“Mimi naungana na wewe mkuu kwani tangu mauaji haya yameanza kutokea
mimi nimekuwa karibu sana na vyombo vya habari katika kutaka kujua vyombo vya
habari vinaongeleaje matukio haya.
Nataka nikwambie kuwa mtazamo uliopo kwa jamii kubwa ni kuwa serikali hii
ni dhaifu na imeshindwa kusimamia vizuri suala la usalama wa watu wake. Hivyo
nionavyo mimi ili kupambana na matukio haya ni lazima kufanyike mabadiliko
makubwa ya mfumo wa utendaji katika idara husika” Ghalib Chakwe,mwanaume
mfupi mnene mwenye macho makali na pia mkuu wa kurugenzi ya usalama ikulu
alimaliza kuongea huku akijiegemeza vizuri kwenye kiti na hivyo kuufanya mgongo
wake ustarehe lakini macho yake yakitulia kutazama juu ya meza kama anayefikiri
jambo.
“Yeyote anayefanya hivi ana malengo ya kuitia dosari serikali,kufanya hujuma
kama siyo njama za kudhoofisha utendaji wa serikali na hatimaye kuipindua. Mifano ya
namna hiyo tumeiona Bamako nchini Mali wakati Kepteni Amadou Sanogo alipoipindua
serikali ya rais Amadou Touman Touré tarehe 22 mwezi Machi mwaka 2012. Hujuma
za namna hiyo pia zimefanyika mjini Bangui kwenye nchi ya jamhuri ya Afrika ya
kati wakati waasi walipoipindua serikali ya rais Francois Bozize tarehe 24 mwezi Machi
mwaka 2013. Hivyo suala hili ni lazima lipewe uzito wa aina yake mkuu” Tiblus
Lapogo,mwanaume mrefu na mwanausalama mahiri kutoka kitengo maalum cha
upelelezi cha ofisi ya mashtaka ya DPP akaongea kwa msisitizo huku hoja yake ikielea
hewani.
“Mimi nafikiri hili suala ni muhimu tukavishirikisha na vyombo vingine vya
usalama likiwemo jeshi la polisi. Upelelezi wa kina ufanyike wahusika wakamatwe
na kuhojiwa ili tujue mauaji haya yanafanywa na nani na kwa sababu gani” Siraju
Chenga,afisa usalama na mwanakamati ya kudumu ya ulinzi na usalama wa jiji la Dar
es salaam alimaliza kuongea huku akiwatazama wenzake.
“Mimi naona tutoe matangazo kwenye vyombo vya habari kuwatahadharisha
wananchi juu ya matukio haya” Manyama Sululu akatumbukiza hoja yake baada ya
kuhisi kuwa huwenda wazo lake pia lingekuwa na msaada.
“Nionavyo mimi tusitoe matangazo hayo mapema kwani tutasababisha hofu
kwa wananchi na vilevile tutaonekana tumeshindwa kazi. Matangazo pia yatawafanya
wanaofanya mauaji haya wapate nafasi nzuri ya kujificha huko waliko. Katika mazingira
kama haya biashara ya kimyakimya ndiyo inayolipa. Tuvishirikisheni vyombo vyetu
vya usalama ambavyo vina weledi wa hali ya juu na uzoefu wa kutosha” Luteni Kanali
Davis Mwamba mkuu wa kamati ya dharura ya usalama wa nchi na itifaki za jeshi la
wananchi akapendekeza huku akiyatembeza macho yake kuzitazama sura za wajumbe
waliokuwa mle ndani.
“Mimi naona kabla ya kwenda mbele zaidi upelelezi ungefanyika kwanza katika
kuzifahamu nyendo za maafisa wote waliouwawa. Kuanzia hapo huwenda tukapata
sababu za vifo vyao na hiyo itatusaidia kwa hatua inayofuata” James Risasi akaongea
kwa utulivu huku akiupima uzito wa hoja yake.
Baada ya pale kikafuatiwa na wachangiaji wengine kutoka idara tofauti za usalama
wa taifa huku M.D.Kunzugala mkurugenzi mkuu wa usalama wa taifa akiwa ndiye
msemaji mkuu wa mkutano ule.
Hatimaye mkutano ule ukafika tamati huku maazimio yakiwa ni kuongeza ufanisi
katika utendaji na kumvua madaraka Abdulkadir Badru. Mkuu wa intelijensia ya
usalama wa taifa kwa kile kinachosemekana kuwa eti ofisi yake ilikuwa imeshindwa
kutoa taarifa za kueleweka juu ya matukio ya mauaji ya wanausalama yaliyokuwa
yakiendelea jijini Dar es Salaam.
Nafasi ya Abdulkadir Badru akawa amepewa Sulle Kiganja. Mtu mkorofi na mtata
katika kushughulika na wahalifu. Ile nafasi ya marehemu P.J.Toddo akawa amepewa
ndugu Miraji Kasena na zile nafasi zilizoachwa wazi za Guzbert Kojo na Pierre
Kwizera zikaazimiwa kuwa zingetolewa hoja na rais na ndiye ambaye angeamua nani
wa kumteua kwani tofauti na hapo ilikuwa ni sawa na kuingilia madaraka ya rais.
Hatimaye mkutano ule ukafika tamati na wajumbe wakaagana na kuondoka huku kila
mmoja akiwa amechiwa majukumu yake ya kufanya.
Kitendo cha Abdulkadir Badru ama Badru kama wengi walivyozoea kumuita
kuvuliwa madaraka pasipo kupewa ofisi nyingine kilikuwa kimemuacha njia panda
huku akijihisi kuwa ni kama waziri asiyekuwa na wizara maalum.
Mara baada ya wajumbe wale kuondoka Badru akabaki mle ukumbini huku
aliendelea kuwaza namna maisha yatakavyomwia vugumu baada ya kuvuliwa wadhifa
wake. Ikulu alikuwa akiingia na kutoka kama nyumbani kwake mara kwa mara kuonana
na viongozi wakubwa wa serikali. Safari zake nje ya nchi zilikuwa zikigharimiwa na
serikali huku akiendeshwa kwenye gari la kifahari na kupewa ulinzi wa kutosha.
Badru akaendelea kukumbuka hoteli za kifahari alizokuwa akifikia mara apatapo
safari za kikazi nje ya nchi huku akisindikizwa na posho za kila namna. Mawazo ya
kupoteza vitu hivyo vyote kwa wakati mmoja yakampelekea ajihisi mnyonge sana.
Siyo kweli kwamba Badru alikuwa hajafanya kitu chochote tangu mauaji ya
Guzbert Kojo yalipotokea. La hasha! hali haikuwa hivyo kwani tangu mauaji yale
yalipotokea Badru alikuwa hajalala usiku na mchana akiipanga vizuri safu yake
ya kiutendaji katika kuhakikisha kuwa muuaji anakamatwa. Safu yake ikiundwa na
Fulgency Kassy,Pweza,Kombe na watu wengine kutoka katika idara tofauti.
Hata hivyo kwa upande mwingine Badru alikuwa akiufahamu ukweli wa mambo
ingawa alikuwa ameshindwa kuushughulikia kikamilifu kutokana na hofu ya kugusa
maslahi ya wakubwa.
“Potelea mbali watajua wenyewe!” hatimaye Badru akajiambia huku akisogeza kiti
chake nyuma na kusimama baada ya wajumbe wote kutoka mle ukumbini. Mawazo
ya hisia za unyonge yakiendelea kumkabili Badru akapiga hatua zake hafifu akielekea
kwenye dirisha moja kubwa la kioo la mle ukumbini ili kujifariji na mandhari ya nje
ya lile jengo la ghorofa. Mara wakati Badru akilikaribia lile dirisha akasikia mkono
ukimshika begani na alipogeuka nyuma akajikuta akitazamana na Sulle Kiganja,mtu
aliyekabidhiwa kitengo chake.
“Pole sana Badru ila tambua kuwa cheo ni dhamana” Sulle Kiganja akaongea huku
akilazimisha tabasamu ingawa ile haikuwa hulka yake. Kwa muda mrefu Abdulkadir
Badru na Sulle Kiganja walikuwa kama Paka na Panya huku wakitiliana fitina za hapa
na pale kila nafasi ya kufanya hivyo ilipokuwa ikipatikana.
“Nishapoa!” Badru akaongea kinyonge huku akigeuka na kutazama dirishani.
“Hupaswi kumlaumu M.D.Kunzugala kwani hata yeye amepewa shinikizo kutoka
juu” Sulle Kiganja akaendelea kuongea huku akitabasamu.
“Simlaumu mtu yoyote kwani nadhani mchango wa kazi yangu haujaonekana
hivyo ofisi ipo huru kufanya vile inavyoona kuwa ni sawa” Badru akaongea bila
kumtazama Sulle Kiganja huku mikono yake akiwa ameiegemeza dirishani na macho
yake yakitazama nje kupitia kwenye kile kioo.
“M.D.Kunzugala anasema eti inawezekana kuwa mauaji haya yapo nyuma ya
mpango fulani hatari. Vipi wewe ulimuelewa wakati alivyosema vile?” Sulle Kiganja
akauliza baada ya kusimama pembeni ya Badru huku akitazama nje kupitia kile kioo
cha dirishani.
“Mimi sitafahamu kitu chochote ndiyo maana nimeondolewa kitengoni. Kwanini
hukumuuliza mwenyewe wakati alipoongea?” Badru akajibu kwa hasira huku
akimuona Sulle Kiganja kama aliyekuwa akichokonoa vitu ambavyo havikuwa na
maana tena kwake.
“Hapaswi kukasirika Badru kwani bado mchango wako unahitajika. Haya yote
yanafanyika ili kuimarisha usalama wa nchi. Hata rais hulazimika kubadili baraza lake
la mawaziri kila anapohisi kuwa ipo haja ya kufanya hivyo” Sulle Kiganja akaongea
huku akiendelea kutabasamu
“Naomba uniache kwanza kwani nahitaji faragha!” Badru akaongea kwa utulivu.
“Utakuwa na muda mrefu wa faragha baada ya kunikabidhi ofisi”
“Nitakukabidhi ofisi kesho asubuhi!”
“Kwanini isiwe leo Badru?. Huoni kuwa muuaji anaendelea kutabaruku?”
Maelezo ya Sulle Kiganja yakampelekea Badru ageuke kumtazama huku donge la
hasira limemkaba kooni.
“Tafadhali! naomba uniache nahitaji faragha” Badru akaongea kwa hasira.
“Okay! na vipi kuhusu wale vijana wako?” Sulle Kiganja akauliza kwa tahadhari
“Vijana gani?” Badru akauliza huku akigeuka na kumkata jicho la hasira Sulle
Kiganja pembeni yake.
“Fugnecy Kassy,Pweza na Kombe!”
“Wamefanya nini?”
“Kesho utakaponikabidhi ofisi utawaambia waripoti kwangu kwani nahitaji
kufahamu wamefikia wapi kabla sijaanza kazi yangu” Sulle Kiganja akaongea huku
akitabasamu hata hivyo Badru hakumjibu kitu badala yake akageuka na kutazama nje
ya lile jengo kupitia kwenye kile kioo cha dirishani huku mawazo yake yakiwa mbali
na eneo lile.
#111
SAA YA GARI LANGU KWENYE DASHIBODI ilionesha kuwa ilikwisha
timia saa tatu na robo asubuhi wakati nilipoegesha gari langu kando ya kituo cha
kujazia mafuta eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam. Asubuhi hii mvua ilikuwa
imeacha kunyesha na anga lote la jiji la Dar es Salaam lilikuwa tulivu.
Fikra zangu bado zilikuwa zimetawaliwa na lile tukio la jana la kule Tabata relini.
Kifo cha Momba kilikuwa kimeniweka katika wakati mgumu sana na sikutaka
kujilaumu kuwa mimi ndiye niliyesababisha kifo kile kwani nilikuwa na hakika kuwa
kifo chake kilikuwa kimetokana na kitendo cha kutumika kwa gari lake na yule
mdunguaji hatari.Hivyo hisia zangu zikanieleza kuwa watu wale waliomuua Momba
huwenda walimpata kwa urahisi baada ya kupeleleza gari lake katika vijiwe vya teksi
vya jijini Dar es Salaam.
Nikiwa naendelea kufikiri mara hoja nyingine ikachipuka taratibu kichwani
mwangu pale nilipowaza kuwa kitendo cha mdunguaji kutafutwa na wale watu kwa
maana nyingine ni kuwa watu wale hawakuwa na unasaba wowote na yule mdunguaji.
Hivyo baada ya mimi mdunguaji alikuwa ni adui namba mbili. Swali likabaki kuwa
yule mdunguaji alikuwa nani na kwanini alimdungua yule mwanaume nje ya Vampire
Casino usiku ule?. Majibu sikuyapata hivyo asubuhi hii nilikuwa nimeamua kurudi tena
kwenye kituo kile cha teksi ambacho Momba alikuwa akiegesha teksi yake ili nidadisi
kama ningeweza kupata chochote cha kunisaidia katika upelelezi wangu.
Nilisubiri magari yasimame kwenye foleni kisha nikatumia mwanya ule kuvuka
barabara nikikatisha kwenye uwazi mdogo uliofanywa baina ya gari moja na lingine.
Muda mfupi baadaye nikawa nimetokezea upande wa pili wa ile barabara.
Kituo cha teksi cha eneo la Mwenge hakikuwa mbali na pale hivyo nikakatisha
katikati ya vibanda vya wamachinga na ndani ya muda mfupi nikawa nimefika kwenye
kituo kile.
Wakati nikifika nikaanza kuyatembeza macho yangu nikiwatazama madereva
wa teski waliokuwa eneo lile huku moyoni nikiomba nimkute tena yule mzee wa
kingoni niliyeonana naye siku ya jana. Hata hivyo madereva wale hawakuonesha
kunichangamkia kama ilivyokuwa siku ya jana na sikutaka kukata tamaa.
Kijana mmoja dereva wa teksi mwenye umri unaolekeana na wangu alinikaribisha
kwa bashasha zote akidhani kuwa nilikuwa mteja na nilipomchunguza haraka
nikatambua kuwa hakuwepo jana wakati nilipofika.
“Karibu bosi wangu usafiri wa kuaminika huu hapa” kijana yule akanikaribisha
huku akitaka kufungua mlango wa teksi yake lakini nikamuwahi kwa kumshika begani
huku nikimpa ishara kuwa nilikuwa sihitaji huduma ya usafiri. Yule kijana kuona vile
akasimama na kunikodolea macho ya mshangao.
“Unashida gani?”
“Namuulizia dereva mmoja wa teksi mzee wa kingoni” nilimwambia yule kijana
na hapo akageuka na kunitazama kwa udadisi kisha akaniuliza kwa sauti tulivu ya
kukata tamaa.
“Mzee Ngonyani?”
“Ndiyo!” nilimjibu huku nikijiuliza kama mzee yule niliyeonana naye jana alikuwa
akiitwa Ngonyani au lah!
“Yuko upande ule pembeni ya fundi viatu” yule kijana akanielekeza upande
mwingine wa kile kituo cha teksi.
“Ahsante!” nikamshukuru yule kijana kisha nikaanza kukatisha katikati ya teksi
zilizokuwa eneo lile nikielekea kule nilipoelekezwa.
Mzee Ngonyani alikuwa amefungua mlango wa mbele wa teksi huku akiwa
amelala kwenye kiti cha dereva kifua wazi baada ya kufungua vifungo vya shati lake.
Mguu wake mmoja ulikuwa chini huku ule mwingine akiwa ameutundika mlangoni.
Bila shaka hakutarajia kuniona pale kwani niliubaini haraka mshtuko wake wakati
alipogeuka kunitazama. Hakunichangamkia kama jana na badala yake taratibu
akauondoa mguu wake pale juu ya mlango kisha akakaa vizuri akinitazama pasipo
kusema neno huku uso wake ukionekana kulemewa na lindi la mawazo.
“Shikamoo mzee!”
“Marahaba” yule mzee akanijibu kwa mkato huku akinitazama kwa utulivu.
“Unanikumbuka?” nikamuuliza yule mzee na huwenda swali langu lilimtatiza
kidogo kwani alikawia kunijibu huku akinitazama.
“Nakukumbuka vizuri. Wewe si yule kijana aliyefika hapa siku ya jana kumuulizia
Momba?”
“Ndiyo mimi” nikamwambia yule mzee na hapo akageuka na kunitazama kwa
utulivu bila kusema neno lolote.
“Nimekuja kukupa taarifa mbaya” nikavunja ukimya
“Nafahamu!” yule mzee akaniambia kwa mkato.
“Unafahamu kuwa Momba ameuwawa!”
“Ndiyo”
“Nani aliyekwambia?” nikamuuliza yule mzee kwa udadisi huku nikimtazama
usoni.
“Kila mtu anafahamu hivyo na habari za kifo chake zipo magazetini” mzee yule
akaniambia kwa huzuni na hapo nikakumbuka kuwa nilikuwa sijapitia vichwa vya
magazeti asubuhi ya leo.
“Hicho ndiyo kilichonileta hapa. Nilitaka nikupashe habari kwani hata mimi
nimeshtushwa sana na habari za kifo chake” niliongea kwa utulivu lakini mzee yule
hakuchangia mada na badala yake aliendelea kunitazama.
“Taarifa zinasema kifo chake kimetokana na nini?” nilimuuliza yule mzee kwa
utulivu.
“Amenyongwa na mwili wake umeokotwa nyuma ya jengo la BML eneo la Tabata
relini”
“Kuna mtu yeyote anayetuhumiwa kuhusika na kifo chake?”
“Hapana! hakuna mtu yeyote aliyekamatwa na polisi bado wanaendelea
na uchunguzi” yule mzee akanijibu huku akipunguza sauti ya redio ya gari na
nilipomtazama nikatambua kuwa bado alikuwa kwenye simanzi kubwa ya kifo cha
Momba. Kitambo kifupi cha ukimya kikapita huku nikifikiria juu ya hali ile kisha
nikavunja ukimya.
“Nani aliyekueleza kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi wa kifo chake?”
nikamuuliza yule mzee na swali langu bila shaka lilimshangaza sana kwani nilimuona
akigeuka na kunitazama vizuri usoni.
“Uhalifu wowote unapotokea ni lazima polisi wafanye uchunguzi kutaka kujua
nani aliyehusika ili sheria ichukue mkondo wake”
“Yaani ninachotaka kufahamu ni kuwa taarifa hizo za polisi kuendelea na
uchunguzi wa kifo cha Momba ni za kutoka magazetini au unauthibitisho nazo!”
nilimuuliza yule mzee huku nikitaka ufafanuzi wa maelezo yake.
“Ndiyo!” yule mzee akasisitiza.
“Unathibitishaje?” nilimuuliza yule mzee kwa upole na nilichokiona usoni mwake
ni kuwa maswali yangu yalikuwa mbioni kumchosha. Hata hivyo sikuwa na namna
ya kufanya.http://pseudepigraphas.blogspot.com/
“Hivi ninavyokueleza madereva wote wa teksi wa kijiwe hiki muda mfupi
uliyopita tumetoka mochwari ya hospitali ya Amana kuutambua mwili wa Momba”
yule mzee akanieleza na kabla hajamaliza kunieleza nikamuona kijana mmoja akija
pale tulipokuwa kisha akapenyeza noti ya shilingi elfu tano dirishani ambapo yule
mzee aliipokea.
“Niandike jina langu kabisa mzee Ngonyani” yule kijana akaongea huku akiondoka
na hapo nikajua kuwa alikua ameleta rambirambi na mzee Ngonyani ndiye aliyekuwa
mkusanyaji wa rambirambi kwa ajili ya msiba wa Momba kutoka kwa madereva
wenzake wa teksi wa kituo kile.
“Usijali Mashaka nakuandika sasa hivi kijana wangu” mzee Ngonyani akaongea
huku akifunua daftari lililokuwa kando yake na kuanza kuandika jina la Mashaka na
kiasi cha pesa alichotoa. Alipomaliza akaichomeka ile noti ya shilingi elfu tano katikati
ya lile daftari na kugeuka akinitazama.
“Mimi ni mwenyekiti wa madereva wa teksi wa kituo hiki hivyo nakusanya
mchango wa rambirambi kwa ajili ya marehemu Momba” mzee Ngonyani akaongea
katika namna ya kutaka nikitambue vizuri cheo chake. Nilimtazama mzee yule kwa
makini kisha nikatia hisani kwa kutumbukiza mkono wangu mfukoni na kutoa noti ya
shilingi elfu kumi ambapo nilimpa.
“Ongezea na hii” nilimwambia yule mzee na wakati akiipokea ile pesa uso wake
ukaonesha matumaini.
“Ahsante! sana kijana. Waswahili wanasema shida haina mwenyewe” mzee
Ngonyani akaongea wakati akifunua lile daftari la mchango wa rambirambi.
“Jina lako nani?” akaniuliza huku akigeuka na kunitazama
“Oh! haina haja ya kuniandika jina” nikamwambia na kwa kutaka kuondoa ubishi
nikamtumbukizia swali jingine.
“Mazishi ya Momba yatafanyikia wapi?”
“Tutamsafirisha baada ya uchunguzi wa polisi kukamilika kwenda huko kijijini
kwao Tanangozi mkoani Iringa”
“Loh! ni safari ndefu sana hiyo” niliongea huku nikifikiri kisha nikayarudisha
maongezi yetu kwenye mstari.
“Kuna askari yeyote aliyefika hapa kuwahoji?” nilimuuliza mzee Ngonyani huku
nikimtazama usoni.
“Hapana! ila kule hospitali tulipofika tulikutana na polisi watatu waliovaa kiraia
na ndiyo wao waliotueleza kuwa tusiwe na wasiwasi kwani wao walikuwa wameanza
kufanya uchunguzi juu ya kifo cha Momba”
Maelezo ya mzee Ngonyani yakaupelekea moyo wangu upige kite kwa nguvu na
hapo nikaanza kuhisi baridi nyepesi ikisafiri mgongoni mwangu. Fikra zangu zikawa
zimewakumbuka wale watu watatu walionishambulia kutoka juu ya ghorofa kule
Tabata relini.
“Wapoje hao askari?” hatimaye nikamuuliza mzee Ngonyani kwa utulivu.
Mzee Ngonyani akaanza kunipa maelezo juu ya mwonekano wa hao askari kanzu
aliyeonananao hospitali ya Amana wakati walipoenda kuutambua mwili wa Momba.
Mzee Ngonyani alipomaliza kunielezea nikawa nimepata picha kamili juu ya nini
kilichokuwa kikiendelea. Maelezo yake juu ya mwonekano wa hao askari yalikuwa
yamefanana kwa asilimia kubwa na wale watu walionishambulia kule Tabata relini
ingawa sikuwa nimewaona kwa ukaribu siku ile ambao sasa nilifahamu kuwa ndiyo
waliyomuua Momba.
“Waliwaonesha vitambulisho vyao?” nikamuuliza mzee Ngonyani
“Ndiyo!” jibu lile likanipelekea nimtazame mzee Ngonyani kwa tafakuri
“Hao polisi waliwahoji kitu chochote baada ya hapo?”
“Ndiyo”
“Waliwahoji nini?”
“Kama ni kweli tulikuwa tukimfahamu Momba,mwenendo wa maisha yake na
marafiki zake”
“Ulizungumza chochote kuhusu mimi?” nikamuuliza yule mzee na hapo
akashikwa na kigugumizi. Hata hivyo sikutaka kuendeleza mjadala ule kwani ukweli
nilishaufahamu na kwa kutaka kuyaweka sawa maongezi yetu nikaingiza mkono
mfukoni na kuchukua kitambulisho changu bandia kisha nikampa mzee Ngonyani.
Mzee Ngonyani akakipokea kile kitambulisho na kuanza kupitia maelezo yake.
“Wewe ni askari?” wakati mzee Ngonyani akiniuliza kwa mshangao mimi
nilikuwa tayari nimeshazunguka upande wa pili na kuingia ndani ya teksi. Mzee
Ngonyani akaendelea kunitazama kwa mshangao kama kipofu aliyeona mwezi. Pasipo
kumtazama mzee Ngonyani nikachukua sigara moja kutoka mfukoni na kuibana kwa
kingo za mdomo wangu kisha kwa msaada wa kiberiti changu cha gesi nikajiwashia
sigara ile na kuvuta mapafu kadhaa.
Nilipoupuliza moshi wa sigara yangu nje nikageuka na kumtazama mzee Ngonyani
pembeni yangu. Mzee Ngonyani hakuzungumza kitu chochote kwani bado alikuwa
kwenye mduwao nami nikaitumia nafasi ile kujieleza kuwa mimi ni nani. Maelezo
yangu yakianzia tangu siku ile ya jana nilipo onana naye.
“Nilikuwa kwenye harakati za kuyaokoa maisha ya Momba lakini sasa nakiri kuwa
nimechelewa” hatimaye nikahitimisha maelezo yangu.
“Ulijuaje kuwa Momba yuko hatarini?” mzee Ngonyani akaniuliza.
“Ni mkasa mrefu nadhani nitakusimulia pale utakapokuwa umekamilika”
“Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa wale watu waliojitambulisha kwetu kuwa ni
askari polisi ndiyo waliyomuua Momba?”
“Ukirejea maelezo yangu ya awali utagundua kuwa swali lako limekwishajibiwa”
nilimwamba mzee Ngonyani huku bado akiendelea kunishangaa.
“Duh! kweli nyinyi wapelelezi ni watu wa ajabu sana” mzee Ngonyani
akazungumza na mimi sikumfuatiliza maneno yake badala yake fikra zangu zilikuwa
zimezama katika tafakari nyingine.
“Nahitaji maelezo machache kutoka kwako kabla sijaondoka kwenda kuwatafuta
wauaji wa Momba”
“Maelezo gani?” mzee Ngonyani akashtuka na kuniuliza huku akinitazama.
“Nataka kufahamu Momba alikutana na nani kabla yangu” swali langu
likampelekea mzee Ngonyani azidi kunitazama kwa mshangao kisha akayahamisha
macho yake kutazama mbele. Nilipomchunguza vizuri nikagundua kuwa alikuwa
akijaribu kukusanya kumbukumbu za matukio ya nyuma katika fikra zake.
“Ni watu wengi ambao bila shaka ni abiria wake” hatimaye mzee Ngonyani
akaongea kwa utulivu.
“Siku za mwisho kabla ya kifo chake!” nikafafanua na hapo nikamuona mzee
Ngonyani akiupisha utulivu kichwani kwa kitambo kabla ya kuvunja ukimya
“Kulikuwa na mwanamke aliyekuwa akimzungumzia kuwa angelikodi gari lake
kwa siku kadhaa” maelezo ya mzee Ngonyani yakanipelekea nigeuke vizuri na
kumtazama kwa shauku.
“Mwanamke gani?”
“Hawakuwahi kuniambia kinagaubaga kuwa huyo mwanamke ni nani nami
sikutaka kumdadisi zaidi kwani huwenda hakupenda nifahamu. Si unajua hapa mjini
kila mtu na pilika zake” mzee Ngonyani akaongea kwa utulivu huku akionekana
kufikiri.
“Maelezo yake yalisemaje?” nikauliza kwa udadisi
“Kama nilivyokueleza kuwa kulikuwa na mwanamke fulani aliyedai kuwa
angelikodi gari lake kwa siku kadhaa. Hivyo alikuwa akinitahadharisha kuwa nisiwe na
wasiwasi pale ambapo ningekuwa simuoni hapa kijiweni”
“Hakukueleza kuwa huyo mwanamke ni nani na anaishi wapi?”
“Hapana!,hakuniambia jina lake ila alinigusia tu juu ya hoteli fulani ya hapa jijini
Dar es salaam” mzee Ngonyani aliongea huku akionekana kuzidi kufikiria.
“Alisemaje kuhusu hiyo hoteli?” nilimuuliza mzee Ngonyani huku nikimtazama
kwa makini.
“Aliniambia kuwa kuna mtu fulani alimpigia simu akimtaka aende kwenye hiyo
hoteli asubuhi ile na ninavyodhani huwenda mtu huyo ndiye alikuwa huyo mwanamke
aliyetaka kukodi gari lake”
“Kwanini unadhani hivyo?”
“Momba ni rafiki yangu hivyo namfahamu vizuri pale linapokuja suala la
wanawake” nilimtazama mzee Ngonyani kwa utulivu na hapo nikagundua kuwa
kulikuwa na hikika katika maneno yake.
“Hiyo hoteli inaitwaje?” nilimuuliza mzee Ngonyani hata hivyo hakunijibu kwa
haraka badala yake akaendelea kutazama mbele ya gari kama anayefikiri jambo kisha
akavunja ukimya
“Hotel 92 Dar es Salaam ipo nyuma ya stendi ya mabasi yaendayo kasi eneo la
Ubungo kama sijakosea” mzee Ngonyani akaongea kwa utulivu huku akiendelea
kutazama mbele ya ile teksi yake.
Maelezo yale yakanipeleka nimtazame mzee Ngonyani kwa utulivu moyoni
nikimsifu kwa kuweka kumbukumbu zile vyema kichwani mwake.
“Hotel 92 Dar es Salaam…” mara nikajikuta nikiongea kwa utulivu jina lile la hoteli
huku nikijaribu kuvuta picha kichwani mwangu.
“Baada ya hapo nini kilifuatia?”
“Hakuna kwani asubuhi ile ndiyo ilikuwa mara yangu ya mwisho kuonana na
Momba” mzee Ngonyani akaongea huku akitikisa kichwa chake kwa masikitiko.
Hatimaye nikavuta sigara yangu kwa utulivu huku nikiyahurumia mapafu yangu
kisha nikautoa mkono wangu dirishani na kukung’uta majivu ya sigara.
Mpaka kufikia pale akili yangu ilikuwa imeanza kupata afya njema katika ufikirivu.
Kwa tafsiri yangu ya wali kichwani ni kuwa mwanamke aliyampigia Momba simu
na kutaka waonane Hotel 92 Dar es Salaam alikuwa ndiye yule mdunguaji hatari
niliyemuona juu ya lile jengo la biashara la Rupture & Capture wakati nilipokuwa
nimeegesha gari langu nje ya Vampire Casino.
Nikaendelea kukumbuka namna mdunguaji yule alivyonitoroka kwenye yale
maegesho ya magari ya jengo la biashara la Rupture & Capture na ile teksi ya Momba
usiku ule. Bila shaka Momba alikuwa akifahamiana vizuri na mdunguaji yule hatari.
Nikahitimisha huku nikimalizia kuvuta sigara yangu kisha nikakitupa kipisi cha
sigara ile dirishani huku nikiupuliza moshi wake nje taratibu. Hatimaye nikageuka na
kumtazama mzee Ngonyani huku uso wangu ukiwa na matumaini.
“Nashukuru sana kwa maelezo yako kwani huwenda yakanisaidia katika kuwanasa
wauaji wa Momba” nikamwambia mzee Ngonyani kisha nikampa namba zangu za
simu.
“Naomba unipigie simu pale utakapowaona tena wale watu waliojitambulisha
kwenu kuwa ni askari”
“Bila shaka!” mzee Ngonyani akaongea kwa utulivu.
“Nakutakia kazi njema”
“Kazi njema na wewe pia” mzee Ngonyani akaniaga wakati nilipokuwa nikifungua
mlango wa teksi yake na kutoka nje huku macho yake yakinisindikiza kwa nyuma.
_____
WAKATI NILIPOKUWA NIKIENDESHA gari langu kuelekea Hotel 92
Dar es Salaam fikra zangu zilikuwa zimejikita kwenye mjadala mwingine. Mawazo
yangu yalikuwa yamehamia kwa yule mdunguaji huku nikiisumbua akili yangu katika
kutaka kufahamu mdunguaji yule hatari alikuwa nani na aliingiaje katika mkasa huu.
Halafu nikakumbuka siku ile mdunguaji yule hatari namna alivyompopoa vibaya yule
mwanaume kwenye ile baraza Vampire Casino.
Nikiwa naendelea kuvuta kumbukumbu zangu vizuri taswira ya mdunguaji yule
hatari ikaanza kujengeka vizuri kichwani mwangu huku nikikumbuka siku ile ya
kwanza nilipomuona na kuanza kumfuatilia kutoka kwenye maegesho ya magari ya
Vampire Casino hadi kule mtaa wa Nkurumah. Halafu nikaendelea kukumbuka namna
mdunguaji yule alivyonizidi kete na kunitoroka usiku ule kwenye lile jengo la biashara
la Rupture & Capture.
Nikaendelea kuwaza kuwa mtu yoyote ambaye angeweza kumdungua yule mtu
kwenye ile baraza ya Vampire Casino kutoka kule juu ya lile jengo la biashara la Rupture
& Capture alifaa kuitwa mdunguaji makini wa daraja la kwanza mwenye uzoefu
mkubwa wa kazi yake.
Swali likabaki kuwa ni idara gani ambayo ingeweza kumpata mtu wa taaluma ya
udunguaji makini namna ile kama siyo kwenye jeshi la polisi au jeshi la wananchi?. Na
kama mdunguaji yule alikuwa mwanajeshi sasa alikuwa amejiingiza vipi katika mkasa
huu?. Na kwanini wale watu walionishambulia kule Tabata relini walikuwa wakimtafuta
yule mdunguaji?. Maswali bado yalikuwa mengi na sikupata majibu. Kwa vile akili
yangu ilikuwa ikitaabika sana kutafuta majibu nikajitia utulivu wa fikra zangu kwa
mche mwingine wa sigara
Dondoo za mzee Ngonyani zilikuwa zimenipa wepesi kidogo katika harakati
zangu. Hata hivyo nilishindwa kuelewa kama nilikuwa nimepiga hatua yoyote katika
kile nilichokuwa nikikipeleleza ingawa sikutaka kukata tamaa.
_____
HOTEL 92 DAR ES SALAAM ilikuwa miongoni mwa hoteli nyingi za daraja
la kati zilizopandwa kwa fujo karibu kila kona ya jiji la Dar es Salaam. Hoteli hiyo
yenye ghorofa nane ilikuwa imepandwa nyuma ya stendi ya mabasi yaendeyo kasi
eneo la Ubongo huku ikizungukwa na makazi ya watu na majengo mengine marefu
ya ghorofa ambayo sikuweza kuyatambua kwa haraka kuwa yalikuwa yakitumika kwa
shughuli gani. Hoteli hiyo ilikuwa imezungukwa na ukuta mzuri na miti mirefu ya
miashoki iliyopandwa katika namna ya kuvutia.
Baada ya safari ya kitambo nikawa nimeifikia hoteli ile. Ile Hoteli ilikuwa kwenye
mtaa tulivu usiyokuwa na pilika nyingi za kibinadamu. Nilipofika nikapita getini kisha
nikasumbuka kidogo kutafuta maegesho ya gari langu kwani kulikuwa na magari mengi
yaliyokuwa yameegeshwa kwenye eneo la maegesho la hoteli ile. Hata hivyo nikajikuta
nikikata tamaa kidogo kwa kutoiona ile teksi ya Momba iliyokuwa ikitumiwa na yule
mdunguaji katika maegesho yale.
Niliegesha gari langu kisha nikafungua mlango na kushuka nikitembea taratibu
kuelekea kwenye mlango wa mbele wa hoteli ile na wakati nikifanya vile nikawa
nikiyatembeza macho yangu kutazama huku na kule katika namna ya kuyachunguza
magari mengine yaliyokuwa yameegeshwa eneo lile. Ile teksi ya
Momba bado sikuiona. Nilimaliza kupanda ngazi kisha nikapotelea kwenye
mlango wa mbele wa Hotel 92 Dar es Salaam.
Katika seti tatu za makochi ya sofa yaliyokuwa kwenye ukumbi wa chini wa
hoteli ile seti moja ilikuwa imekaliwa na wanaume wanne huku meza fupi ya vioo
iliyokuwa katikati yao ikiwa imebeba aina tofauti za vinywaji. Seti nyingine ya pili
ilikuwa imekaliwa na mwanamke na mwanaume ambao walionekana kwa kila hali
kuwa ni wapenzi. Seti ya mwisho ya makochi ilikuwa tupu. Runinga mbili kubwa
zilizokuwa zimetundikwa kwenye kuta za ukumbi ule zilikuwa zikionesha muziki hata
hivyo hakuna mtu aliyeonekana kuzitazama.
Kipande mstatili cha sakafu nzuri ya tarazo kikanichukia hadi eneo la mapokezi
la hoteli ile ambapo niliwakuta wasichana wawili wahudumu waliovaa sare za kazi.
Nyuso zao zenye furaha zikanieleza kuwa walikuwa wakiyazingatia vizuri maadili ya
kazi yao. Sikujishughulisha na macho ya watu wachache waliokuwa upande wa kulia
kwenye ukumbi ule wakijipatia mlo.
“Hamjambo warembo?” niliwasalimia wale wasichana wa mapokezi huku
nikiigemeza mikono yangu kwenye ukuta mfupi wa mbao uliyopakana na nondo za
eneo lile.
“Hatujambo!”
“Karibu kaka” msichana mmoja wa pale mapokezi akanikaribisha huku akijisogeza
karibu yangu.
“Ahsante!” nikamuitikia yule msichana huku nikayatembeza macho yangu
kuwatazama watu waliokuwa mle ndani. Sura zote mle ndani zilikuwa za kawaida
hivyo nikayarudisha macho yangu kuwatazama wale wasichana.
“Naomba maji baridi” nikamwambia yule dada aliyesogea karibu yangu huku
nikimroga kwa tabasamu langu maridhawa.
“Maji makubwa au madogo?” yule msichana akaniuliza.
“Makubwa tafadhali! niupoze mtima wangu kabla ya hili joto la jiji la Dar es
Salaam halijanitoa roho” nilimwambia yule mhudumu na maji yale yalipoletwa
nikafungua kizibo na kugida mafunda kadhaa kisha nikaitua ile chupa juu ya kaunta
na kuwatazama wale wasichana huku nikipumbazwa kidogo na uzuri wao.
“Mbona asubuhi yote hii inakunywa maji kaka?” yule msichana akaniuliza huku
akielekea kununua maongezi yangu.
“Afya yangu si mnaiona wenyewe kuwa siyo ya kubabaisha” nikawaambia wale
wasichana wa mapokezi huku nikiangua kicheko hafifu na kicheko hicho kilipokuwa
ukingoni nikavunja ukimya.
“Nimemfuata mgeni wangu ila huwenda msinielewe!” nikaongea kwa utulivu na
nilichokiona kwenye nyuso zao ni mshangao usioleweka.
“Kwanini tusikuelewe?” wote wakaniuliza kwa shauku.
“Jina lake silijui” nikawaambia wale wahudumu huku nikitengeneza tabasamu la
kirafiki usoni mwangu.
“Mh! sasa tutakusaidiaje kaka wakati wewe mwenyewe jina la mgeni wako hulijui”
“Mwanamke au mwanaume?” mwenzake akaniuliza.
“Mwanamke na pengine niseme kuwa ni wifi yenu ila msimuonee wivu”
nikawahadaa wale wasichana na hapo wakaangua kicheko cha kimbea.
“Mh! kaka yangu huo siyo mchepuko kweli?”
“Au umempata mitandaoni maana mapenzi ya siku hizi mh!” mwenzake akadakia
“Si bora ingekuwa mitandaoni jina lake ningelijua. Mimi nimeungwa nami
nikaunganika”
“Mh! wanaume nyinyi kwa michepuko” yule msichana aliyeniletea maji akaongea
huku akianguka kicheko hafifu na hapo mwenzake akaungana naye huku wote
wakionekana kufurahishwa na mkasa wangu na kutunga.
“Mh! mnatuonea tu wanaume kwani sisi tunachepuka na nani kama siyo nyinyi”
niliwaambia wale wasichana huku nikitoa noti ya shilingi elfu moja kuyalipia yale maji.
“Sasa huyo wifi yetu ina maana hata namba yake ya simu huna?”
“Ningekuwa na namba yake na jina lake pia ningelijua. Hilo ndiyo kosa nililofanya
tatizo ni kuwa mawasiliano yetu tumeyafanya kwenye simu ya rafiki yake na huyo
rafiki yake sasa hivi hapatikani kwenye simu ingawa alinihakikishia kuwa nikifika hapa
na kumuulizia nitampata”
Wale wahudumu wa mapokezi wakaniangalia kwa utulivu na nilichoweza
kukisoma katika macho yao ni kuwa walikuwa wamenijumuisha kwenye kundi la
wanaume mabingwa wa michepuka jijini Dar es Salaam.
“Sasa tutakusaidiaje kaka?” hatimaye wakaniuliza na swali lao likanipelekea nianze
kuelezea sifa za nje za mwanamke yule mdunguaji hatari. Nilipomaliza kutoa maelezo
yangu nikawaona wale wahudumu wakitazamana kisha mmoja akachukua kitabu
chenye orodha ya majina ya wageni waliofika pale hotelini na kupewa huduma ya
malazi kwa nyakati tofauti.
Halafu nikamuona yule mhudumu akipekua karatasi za kile kitabu kwa haraka
hadi pale alipokaribia ukurasa fulani na hapo akapunguza kasi na kuanza kupekua
kurasa taratibu. Yule mhudumu alipofika kwenye ukurasa fulani akaweka kituo na
kuanza kusoma maelezo yaliyokuwa kwenye ile kurasa halafu akayahamisha macho
yake kunitazama kisha akauliza.
“Mgeni wako ameingia hapa hotelini ndani ya wiki hii?”
“Ndiyo!” nikamwitikia kwa utulivu.
“Wateja wote walioingia hapa hotelini wiki hii wamelala siku moja na wote
wanaonekana kuwa walikuwa wakitoka mikoani” yule mhudumu akaniambia na
hapo nikamuona akinitazama tena. Tukio lile likanipelekea nitambue kuwa fikra zake
zilikuwa zimesimamishwa na jambo fulani.
“Vipi?” nikamuuliza kwa shauku.
“Wifi yetu bila shaka anaitwa Mona kwani hapa anaonekana kuwa ndiye mteja
wetu pekee aliyekaa kwa muda mrefu. Yupo chumba namba 33” yule mhudumu
akaniambia huku akianguka kicheko cha kimbea hata hivyo mimi nilifurahi tu kwani
nilikuwa nimerejewa na matumaini.
“Chumba namba 33 ghorofa ya ngapi?”
“Kipo ghorofa ya nne na ukimpata wifi yetu tupigie simu kaunta tuwaletee
maji baridi makubwa” yule mhudumu akaniambia huku akiangua kicheko hafifu.
Nikaungana naye nikicheka kidogo na kumkonyeza huku nikitabasamu kisha
nikashika uelekeo wa upande wa kulia na nilipozifikia ngazi nikaanza kuzipanda
nikielekea ghorofa za juu za ile hoteli huku ile taswira ya mdunguaji ikianza kujengeka
upya katika fikra zangu. Sikutaka kupanda juu ya lile jengo kwa kutumia lifti kwani
kwa kufanya hivyo ningejinyima fursa nzuri ya kuweza kuitalii Hotel 92 Dar es Salaam.
Nilipomaliza kuzipanda zile ngazi nikawa nimetokezea kwenye korido ya ghorofa
ya pili. Mwisho wa ngazi zile upande wa kulia kulikuwa na dirisha la kioo. Kupitia
dirisha lile niliweza kuliona jengo la stendi ya mabasi yaendayo kasi Ubongo jijini
Dar es Salaam lakini kwa sehemu tu ambayo ilitawaliwa na mapaa ya mabasi na kituo
cha kujazia mafuta. Pilikapilika za kibinadamu zilikuwa zikiendelea kama kawaida.
Nilisimama kidogo nikiitazama korido ile tulivu iliyokuwa ikitazamana na milango ya
vyumba kwa upande wa kushoto na kulia.
Mwisho wa korido ile kulikuwa na dirisha lingine lililofunikwa na pazia refu jeupe.
Nilitulia nikilitazama pazia lile namna lilivyokuwa likipepea taratibu na kwa mbali
niliweza kusikia sauti kutoka kwenye runinga zilizokuwa kwenye vile vyumba. Utafiti
wangu ukanitanabaisha kuwa muonekano wa korido ile usingetofautiana na korido
nyingine zilizokuwa kwenye jengo lile.
Nilikuwa sahihi kwani nilipofika kwenye ghorofa ya nne ya lile jengo la hoteli
nikatambua kuwa mandhari yale hayakutofautiana na yale mandhari ya ghorofa ya pili.
Kitu pekee nilichogundua kuwa kilikuwa kimeongezeka kwenye korido ya ghorofa
ile ilikuwa ni kengele ya tahadhari kwa ajili ya matukio ya moto na hatari nyinginezo.
Nilisimama kwenye korido ile nikiupisha utulivu kichwani mwangu na mara hii
nilijiona kuwa ni mpelelezi mwenye mafanikio niliyekuwa mbioni kuhitimisha mkasa
huu wenye mzongezonge ya aina yake. Taswira ya mdunguaji ikiwa imetafsirika
vizuri kichwani mwangu nikaanza kuvuta picha namna ambavyo fumanizi langu
litakavyomuacha mdomo wazi kama mnzinzi aliyedondosha pakiti ya kondomu
karibu na kapu la sadaka kanisani.
Tofauti na zile korido za chini za lile jengo la hoteli korido ile ilikuwa tulivu sana
na kama ningekuwa sikuhakikishwa uwepo wa mwenyeji wangu ndani ya chumba
33 kwenye korido ile basi huwenda ningeridhisha kuwa katika vyumba vya korido ile
hapakuwa na watu.
Hatimaye nikaupeleka mkono wangu mafichoni kuikagua bastola yangu na
uwepo wake ukaniongezea imani ya kumkabili adui wangu bila wasiwasi wowote.
Bila kupoteza muda nikaanza kuzitupa hatua zangu kwa utulivu kwenye korido ile
huku macho yangu yakitazama upande wa kushoto na kulia nikiikagua milango ya
mle ndani.
Baada ya hatua kadhaa hatimaye nikauona ule mlango wa chumba namba 33
huku namba zake zikiwa zimechongwa vizuri kwenye vibao vyeupe. Mlango wa kile
chumba namba 33 ulikuwa ni wa tano kutoka mwisho wa ile korido na juu ya mlango
ule kulikuwa na kioo kipana chenye mawimbi ya kumzuia mtu kuona ndani ya kile
chumba. Hata hivyo kupitia kioo kile nikagundua kuwa taa ya ndani ya chumba kile
ilikuwa ikiwaka na tofauti na pale chumba kile kilikuwa tulivu na chenye ukimya wa
aina yake.
Nikausogelea ule mlango huku nikitengeneza picha fulani kichwani ya mdunguaji
yule hatari labda akiwa maliwatoni,ameketi kwenye kochi au amelala kitandani
akiendelea kuuchapa usingizi.
Nikaupeleka mkono wangu kwenye mlango ule kisha nikaanza kugonga kwa
utulivu huku mkono wangu mwingine ukiwa tayari umezama mafichoni kuikamata
bastola yangu. Nikaendelea kugonga ule mlango hata hivyo sikupata mwitikio
wowote wala kufunguliwa mlango. Labda huwenda mdunguaji alikuwa akitafakari
kuwa mngongaji wa mlango ule angekuwa nani kama siyo kujadiliana na fikra zake
zilizompelekea ajihisi kuwa alikuwa ndotoni au pengine kilichokuwa kikifanyika
kilikuwa kweli.
Nilirudia kugonga mlango ule tena kwa kishindo zaidi cha kuweza kumwamsha
mwenyeji wa chumba kile kutoka katika usingizini mzito lakini ule mlango
haukufunguliwa wala sauti ya mtu yeyote kusikika.
Hatimaye nikakisogelea kitasa cha ule mlango na kutega vizuri sikio langu nikisikiliza
utulivu wa chumba kile. Mle ndani ya kile chumba kulikuwa kimya na hakuna sauti
yoyote iliyosikika. Nikageuka tena kutazama kwenye ile korido nikichunguza kama
kungekuwa na kamera za usalama. Sikuziona na huwenda hazikuwekwa kwa makusudi
katika namna ya kutunza siri za wateja waliokuwa wakiingia na kutoka kwenye vile
vyumba. Hali ile ikanifurahisha hivyo nikaichomoa bastalo yangu kutoka mafichoni
na kuikamata vema mkononi.
Kisha nikajipapasa mifukoni kuzichukua funguo zangu malaya hata hivyo
nilisitisha zoezi lile pale nilipokumbuka kuwa nilikuwa sijajaribu kufungua kitasa cha ule
mlango. Hivyo katika hali ya kutaka kutafuta hakika nikakishika kitasa cha ule mlango
na kukizungusha taratibu huku bastola yangu ikiwa mkononi. Kile kitasa kikafunguka
na hapo nikafanya jitihada kidogo za kuusukuma ule mlango. Kitu kilichonishangaza
ni kuwa mlango ule ulikuwa wazi na hapo mshangao ukazichukua fikra zangu huku
maswali mengi yakianza kupita kichwani mwangu. Niliusukuma mlango ule taratibu
huku nikiwa nimejidhatiti kikamilifu kukabiliana na masaibu ya namna yoyote mle
ndani. Muda mfupi uliofuata nikawa nimeingia ndani ya chumba kile.
Mara tu nilipoingia ndani ya kile chumba nikayatembeza haraka macho yangu
kukagua mandhari ya mle ndani. Upande wa kushoto wa kile chumba kulikuwa na
kabati la mbao lililojengewa ukutani. Kabati lile sasa lilikuwa wazi bila ya kitu chochote
ndani yake. Pembeni ya lile kabati niliuona mlango lakini mlango ule ulikuwa wazi.
Nikazitupa hatua zangu taratibu nikisogea na kutazama ndani ya ule mlango. Mandhari
ya mle ndani yakanijulisha kuwa kile kilikuwa chumba cha maliwato lakini mle ndani
hapokuwa na kitu chochote hivyo nikarudi kule chumbani.
Kilikuwa chumba kikubwa chenye dirisha pana lililofunikwa kwa pazia refu
jeupe lenye maua mekundu yaliyodariziwa vizuri. Katikati ya chumba kile kulikuwa
kitanda kikubwa kilichokuwa kimefunikwa kwa shuka safi za rangi ya kijivu huku
zikiwa zimeandikwa kwa maandishi makubwa Hotel 92 Dar es Salaam. Tafsiri ya haraka
niliyoipata ni kuwa hakukuwa na mtu mle ndani kwani kiyoyozi na runinga pana
vilivyokuwa ukutani mle chumbani vilikuwa vimezimwa.
Hatimaye nikasimama nikiyatembeza macho yangu mle ndani kwa utulivu na kabla
sijafanya uchunguzi wangu taswira niliyoiona kwenye kochi moja la sofa lililokuwa
kwenye pembe ya chumba kile ikaamsha hisia zangu upya. Kijana mzuri wa kiume
mwenye umri wa kati ya miaka ishirini na nne na ishirini na saba alikuwa ameketi
kwenye kochi lile huku akiwa kifua wazi baada ya shati lake kuraruliwa vifungo.
Ingawa macho ya kijana yule yalikuwa yamesimama yakinitazama lakini haraka
nilipoyachunguza nikagundua kuwa hayakuwa na uhai. Nikapiga hatua zangu taratibu
nikimsogolea pale alipoketi na hapo nikagundua kuwa uso wake ulikuwa umetaabika
kwa kuvumilia mateso makali kabla ya kifo chake. Mdomo wake ulikuwa wazi huku
damu nzito ikiwa imeganda na kuacha michirizi puani mwake. Nikasimama kwa
utulivu nikimtazama kijana yule na kwa kweli nilishikwa na hasira.
Risasi za muuaji zilikuwa zimeacha matundu mawili makubwa kwenye mbavu za
kijana yule na damu iliyotoka kwenye matundu yale ya risasi ilikuwa imetengeneza
michirizi mizito juu ya marumaru nyeupe zilizokuwa chini sakafuni kwenye
chumba kile. Alikuwa kijana mzuri na mtanashati ambaye uwepo wake tu ungeweza
kuwababaisha wasichana warembo wasiokuwa na uvumilivu. Pembeni ya kochi la
sofa aliloketi yule kijana kulikuwa na stuli ndogo yenye miguu mitatu na juu ya stuli ile
kulikuwa na chupa ya pombe kali aina Screw driver yenye kinywaji nusu huku pembeni
yake kukiwa na bilauri ya kioo.
Kwa kweli akili yangu ilikataa kabisa kufanya kazi kwani tangu kuanza kwa mkasa
huu mkusanyiko wa matukio ya namna ile ulikuwa bado haujanifungulia njia ya
kunifikisha kule ninapotaka.
Nilikumbuka kifo cha Zera kisha nikamkumbuka yule mtu aliyedunguliwa nje ya
Vampire Casino usiku ule halafu fikra zangu zikahamia kwa kifo cha Momba kabla ya
kumtazama kijana yule mzuri ambaye mwonekano wake ulitosha kunithibitishia kuwa
starehe zilikuwa kipaumbele namba moja cha maisha yake hapa duniani.
Kwa kweli nilisikitika sana nikijiegemea ukutani huku hisia zangu zikitafunwa na
jinamizi baya la muendelezo wa matukio ya mauaji yasiyokuwa na sababu za msingi.
Nilipokuwa katika hali ile fikra zangu zikahamia tena kwa mdunguaji na kabla sijaanza
kutengeneza hoja mara nikasikia mtu akigonga ule mlango wa kile chumba. Tukio
lile likapelekea moyo wangu upige kite kwa nguvu na hapo kijasho chepesi kikaanza
kupenya mgongoni.
Sikutaka kusubiri nini ambacho kingetokea mle ndani hivyo kufumba na kufumbua
nilikuwa chini ya kitanda cha mle ndani huku uwazi mdogo ulioachwa baina ya shuka
la kitanda kile lililokuwa likining’inia na ile sakafu ya marumaru ukiniwezesha kuiona
miguu ya mtu aliyeingia mle ndani baada ya kuchoka kugonga mlango bila kujibiwa.
Hatimaye mtima wangu ukatulia tuli baada ya kumuona mhudumu wa hoteli ile
akiingia mle ndani ambaye nilimtambua haraka kutokana na sare zake. Mwanamke
yule mnene mwenye umri sawa na wa mama yangu mzazi mkononi alikuwa amebeba
ndoo ndogo maalum kwa ajili ya kupigia deki na beseni lenye mashuka masafi ya
hoteli ile.
Mara baada ya kuingia mle ndani yule mama akasimama kidogo akionekana
kustaajabishwa kwa kuukuta mlango wa chumba kile ukiwa haujafungwa au pengine
kwa kukiona kitanda cha mle ndani kikiwa kimetandikwa vizuri.
Yule mwanamke alipogeuka akaiona maiti ya yule kijana kwenye lile kochi
lililokuwa kwenye kona ya kile chumba. Taharuki aliyomfika mama yule ikampelekea
atupe vifaa vyake vya kazi na kuanza kutimua mbio akitoka nje huku akipiga mayowe
ya hofu.
Nilifahamu kipi ambacho kingefuatia baada ya pale hivyo nikajiviringisha na
kutoka chini ya uvungu wa kile kitanda kisha nikaelekea kwenye ule mlango wa kile
chumba. Muda mfupi uliofuata nilikuwa nje ya kile chumba nikilitoroka eneo lile.
Wakati nikishuka ngazi kuelekea chini ya lile jengo nikakutana na mashuhuda
wengine waliokuwa wakizipanda zile ngazi kwa pupa kuelekea kwenye kile chumba
nilichotoka. Nilichokihitaji ilikuwa ni kuondoka haraka eneo lile kabla polisi
hawajaanza kunusa pua zao kwani hadi wakati ule nilikuwa nikiamini kuwa taarifa
zangu zilikuwa tayari zimewafikia polisi na kwa maana nyingine polisi hao walikuwa
mitaani wakinisaka.
Nilifika sehemu ya mapokezi chini ya ile hoteli na hapo nikagundua taarifa za kifo
cha yule kijana kule chumbani zilikuwa zimesambaa kwenye ile hoteli na kusababisha
taharuki ya aina yake. Hivyo wakati nikikatisha kwenye ukumbi ule kuelekea nje
hakuna mtu yoyote aliyeonekana kunitilia mashaka na hali ile ikanifurahisha.
Bastola yangu nikiwa tayari nimeichimbia mafichoni nikamaliza kushuka ngazi zile
za ukumbini nikiharakisha kuelekea nje ya ile hoteli sehemu nilipokuwa nimeegesha
gari langu. Nilipolifikia gari langu nikafungua mlango na kuingia ndani huku akili
yangu ikiwa hoi kwa kulemewa na mtiririko wa matukio yasiyoeleweka huku hisia
mbaya za kushindwa zikiendelea kuutafuna mtima wangu. Hata hivyo sikutaka kukata
tamaa.
Sikutaka kuendelea kuzubaa eneo lile hivyo nikawasha gari langu na kulitoa kwenye
maegesho yale na wakati nikifanya vile nikagundua kuwa kulikuwa na gari jingine
lililokuwa limeongezeka kwenye maegesho yale. Gari hilo jeusi aina ya Landcruiser
lilikuwa limeegeshwa baada ya kuyapita magari mawili upande ule nilioegesha gari
langu.
Kitendo cha kuliona lile gari kikanipelekea nipunguze mwendo na kugeuka
nikilitazama vizuri gari lile. Hata hivyo tinted nyeusi iliyokuwa kwenye vioo vya lile gari
haikuniwezesha kuona mle ndani ya gari ingawa hisia zangu zilinitanabaisha kuwa mle
ndani ya lile gari kulikuwa na watu waliokuwa wakinitazama.
Hisia hizo zikanishawishi nitake kulirudisha gari langu tena kwenye yale maegesho
ili nipate nafasi nzuri ya kuendelea kulichunguza vizuri lile gari. Lakini baada ya
tafakari fupi nikawa nimesita kufanya vile pale nilipohisi kuwa kitendo cha kulirudisha
gari langu kwenye yale maegesho kingepelekea mtu yeyote ambaye angekuwa ndani ya
lile gari Landcruiser ashikwe na mashaka na hivyo kujijengea hadhari.
Hivyo sikusimama badala yake nikaingiza gia na kukanyaga mafuta na kuendelea
mbele nikielekea kwenye geti la ile hoteli. Hata hivyo macho yangu yalijikuta yakivutwa
na namba za lile gari.
Namba za lile gari zilikuwa ngeni machoni mwangu na zisizofanana kabisa na
namba za magari yaliyosajiliwa nchini Tanzania. Kumbukumbu ya kifo cha yule kijana
niliyemuona kule chumbani muda mfupi uliyopita ikaninyima uhuru wa kuendelea
kufanya utafiti wangu hasa pale nilipohisi kuwa polisi wangekuwa mbioni kufika pale
hotelini.
Hivyo nikakanyaga mafuta na kutoka nje ya geti la hoteli ile na kuingia barabara
inayokatisha mbele ya ile hoteli nikishika uelekeo wa upande wa kulia. Kwa kweli
sikufahamu wapi nilipaswa kuelekea kwa wakati ule hata hivyo nilijitahidi kwa kila hali
kuupisha utulivu akilini mwangu.
Nikaendesha gari langu nikiifuata barabara ile na nilipofika mbele kulikuwa na
barabara nyingine iliyokatisha. Hivyo nilipofika kwenye barabara ile nikakunja kona
na kushika uelekeo wa upande wa kushoto nikitokomea katika vitongoji vya eneo la
Sinza.
Wakati nikiendelea na safari yangu kupitia vioo vya ubavuni vya gari langu mara
nikaliona lile gari jeusi Landcruiser lililokuwa limeegesha nje ya Hotel 92 Dar es Salaam
likiwa nyuma yangu. Tukio lile likanishtua hivyo nikapunguza mwendo kidogo ili
niweze kuliona vizuri lile gari nyuma yangu na mara hii nikapata hakika kuwa gari lile
lililokuwa nyuma yangu lilikuwa ndiyo lile lililokuwa kwenye maegesho ya Hotel 92 Dar
es Salaam muda mfupi uliyopita.
Kwa kweli nilishangazwa sana na tukio lile huku nikijiuliza maswali mengi
kichwani. Niliendelea kulitazama lile gari kupitia vioo vya ubavuni vya gari langu huku
nikiupisha utulivu kichwani mwangu. Kabla ya kufanya maamuzi yoyote nilitaka
kwanza kupata hakika kama nilikuwa nikifuatiliwa au lile gari lilikuwa kwenye ratiba
ya safari zake.
Hivyo nikaongeza mwendo na kwa kuwa nilikuwa fundi mzuri wa vichochoro vya
jiji la Dar es Salaam nikapanga kujizungusha zungusha kwenye mitaa kadhaa ya eneo
lile huku macho yangu yakiendelea kulitazama lile gari nyuma yangu kupitia vioo vya
ubavuni vya gari langu. Kwa kufanya vile ningegundua kuwa nilikuwa nikifuatiliwa na
lile gari au lah! na baada ya hapo ningejua nini cha kufanya.
Niliendelea kuendesha gari langu na nilipofika mbele kwenye makutano mengine
ya barabara nikapunguza mwendo na kuingia upande wa kushoto nikiifuata barabara
nyingine ya lami inayokatisha mitaani. Nikiwa kwenye barabara ile nikaongeza
mwendo kidogo huku macho yangu yakiendelea kutazama kwenye vioo vya ubavuni
vya gari langu. Sikuliona lile gari na hali ile ikanipa matumaini kuwa mambo yalikuwa
shwari na hapo nikaanza kuhisi kuwa nilikuwa nikipoteza muda wangu kwa kufanya
uchunguzi usio na tija.
Hata hivyo muda mfupi baadaye niligundua kuwa sikuwa sahihi kwani sikufika
mbali sana katika safari yangu pale nilipoliona tena lile gari Landcruiser jeusi likiingia
kwenye ile barabara na kunifuata kwa nyuma.
Kwa kutaka kujiridhisha zaidi nilipofika mbele kidogo nikaingia barabara nyingine
inayochepuka kuingia upande wa kulia huku nikiendesha gari langu kwa mwendo
wa wastani. Mara tu nilipoingia kwenye barabara ile haukupita muda mrefu mara
nikaliona tena ile gari Landcruiser nyuma yangu likikunja kona na kuanza kunifuata
tena. Tukio lile likanipelekea nishikwe na hasira hivyo nikaichomoa bastola yangu
kutoka mafichoni na kuiweka kando yangu tayari kukabiliana na rabsha za namna
yoyote.http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Kilichofuata baada ya pale ikawa ni kuingia barabara ya mtaa mmoja na kutokezea
kwenye barabara ya mtaa mwingine huku macho yangu yakiendelea kutazama kwenye
vioo vya ubavuni vya gari langu. Yeyote ambaye alikuwa akinifuatilia kwenye lile gari
nyuma yangu nilitaka nimfanye ajutie kwa kitendo kile na hatimaye nimtie hasira ili
aweze kuonesha vizuri hisia zake nami niitumie fursa hiyo vizuri kumshikisha adabu.
Baadaya kulichezesha shere za kutosha lile gari nyuma yangu sasa nilikuwa
nimeamua kugeuza gari langu na kuanza kurudi kule nilipotoka huku nikipunguza na
kuongeza mwendo hapo na pale katika nyakati tofuati. Lengo langu likiwa ni kutaka
kuliweka karibu zaidi lile gari nyuma yangu kwani kufikia pale nilikuwa na hakika
kuwa nilikuwa nimefungiwa mkia. Jambo lililonifurahisha ni kuwa lile gari Landcruiser
nyuma yangu halikutaka kuniacha hivyo nikawa nacheza na uwanja mpana nitakavyo.
Nikaendelea kuendesha gari langu kwenye barabara ile na nilipofika mbele
nikaingia kwenye kituo kimoja cha kujazia mafuta huku nikiwa tayari nimeshaiona
orodha ya mafuta yaliyokuwa yakiuzwa katika kituo kile kupitia bango kubwa
lililokuwa barabarani.
Mara tu nilipoingia kwenye kituo kile cha kujazia mafuta nikasimama na kuulizia
mafuta ambayo hayakuwepo kwenye ile orodha iliyokuwa kwenye lile bango la
barabarani. Lengo langu likiwa siyo kutaka kuongeza mafuta bali kuitumia nafasi ile
kuchunguza mtu au watu waliokuwa ndani ya lile gari nyuma yangu.
Nikiwa bado nimesimama kwenye kile kituo cha kujazia mafuta haukupita muda
mrefu mara nikaliona lile gari jeusi Landcruiser nalo likipunguza mwendo na kuingia
kwenye kile kituo cha kujazia mafuta. Nikiwa natarajia tukio lile macho yangu yalikuwa
makini kutazama mbele ya lile gari na hapo nikawaona wanaume wawili yaani dereva
wa lile gari na mtu mwingine aliyekuwa kando kwenye kiti cha abiria. Wale watu
walikuwa makini wakilitazama gari langu.
Nikiwa nimejiandaa vizuri kwa tukio lile mara tu lile gari jeusi Landcruiser
liliposimama mimi nikakanyaga mafuta na kuondoka eneo lile. Kwa kufanya vile mara
nikaliona tena lile gari jeusi Landcruiser nalo likiacha kile kituo cha mafuta na kuanza
kunifuata. Kwa kweli sikutaka kuendelea kufuatiliwa kama mtoto mdogo hivyo
nikaanza kufikiria namna ya kukabiliana na hali ile.
Nilitaka nipate hakika ya mambo machache kuhusiana na wale watu kwenye
lile gari nyuma yangu kabla ya kupiga hatua nyingine zaidi hivyo nikakanyaga vizuri
pedeli ya mafuta ya gari langu na hapo injini ya gari ikaniletea mrejesho maridhawa.
Sauti ya muungurumo wa injini ikabadilika kadiri nilivyokanyaga klachi na kutupia gia
nyingine. Mwishowe gari langu likawa jepesi huku usukani ukiwa laini hivyo nikawa
nauzungusha kwa mkono wangu imara nikishika uelekeo ninaoutaka. Watembea kwa
miguu kando ya barabara ile wakawa wamestaajabishwa sana na mwendo wangu wa
kasi hata hivyo dereva wa ile Landcruiser nyuma yangu alikuwa mwerevu kuishtukia
dhamira yangu hivyo naye akaongeza mwendo akinifuata.
Muda mfupi uliyofuata lile gari jeusi Landcruiser likawa limenifikia na hapo nikasikia
sauti kali ya dafrao nyuma yangu. Lile gari lilikuwa limenigonga kwa nyuma kiasi cha
kufanikiwa kuyumbisha kidogo uelekeo wangu. Nikayumba kidogo kwenye barabara
ile kabla ya kukaa sawa huku watembea kwa miguu kando ya barabara ile wakiogopa
na kurukia kwenye mitaro iliyokuwa kando ya barabara ile.
Gari langu lilipokaa sawa nikakanyaga klachi na kutupia gia nyingine huku
nikikanyaga vizuri pedeli ya mafuta. Injini ya gari ikalalamika kidogo na ilipotulia gari
likawa jepesi na hapo nikaushika vizuri usukani wa gari kwa mkono mmoja huku
mkono mwingine ukiichukua ile bastola yangu pembeni.
Hatimaye nikayapeleka macho yangu kwenye kioo cha ubavu cha gari langu
kulitazama lile gari jeusi Landcruiser lililokuwa nyuma yangu. Hata hivyo sikufanikiwa
kwani kile kioo cha ubavuni cha gari langu kiliondoshwa haraka kwa kuchanguliwa
vibaya na risasi iliyotoka nyuma yangu. Baada ya pale mirindimo ya risasi ikafuatia
huku baadhi ya risasi hizo zikitoboa vibaya bodi la gari langu. Nikiwa nimeanza
kuhisi hatari nikaongeza mwendo huku nikiliyumbisha gari langu upande huu na ule
ili kuzikwepa zile risasi lakini bado zile risasi ziliendelea kuniandama huku zikitoboa
vibaya kioo cha nyuma cha gari langu na kunikosakosa.
Hali ile ya hatari ilipozidi kuongezeka nikaikamata vyema bastola yangu mkononi
kisha nikashusha kioo cha dirishani. Hata hivyo nilipokuwa mbioni kufanya shambulizi
mara ile Landcruiser ikawa tayari imenifikia tena na kunigonga kwa nyuma. Tukio lile
likanipotezea umakini hivyo nikavuta kilimi cha bastola yangu pasipo kutaka na hapo
risasi moja ikachomoka kwa kasi na kuchana anga huku mlio mkali wa risasi ukisikika.
Sikutaka kuendelea kuiruhusu hali ile hivyo nikaukamata vizuri usukani wangu
kisha nikakunja kona ya ghafla mbele yangu nikiufuata uelekeo wa upande wa kulia.
Hata hivyo lile gari Landcruiser halikuniacha kwani muda mfupi uliyofuata likanifikia
na kuanza kunigongagonga ubavuni na kwa kuwa gari langu lilikuwa dogo kwa kweli
lilizidiwa nguvu na kupondekapondeka ubavuni huku likiminywa kwenye ukuta
wa pembeni wa kiwanda cha maji kilichopakana na barabara ile. Zile risasi zikawa
zikiendelea kuniandama na muda mfupi uliyofuata kile kioo cha nyuma cha gari langu
kikachanguka vibaya na kutawanyika. Hali ilikuwa mbaya na endapo ningeendelea
kuiruhusu hali ile wale watu wangeyakatisha maisha yangu kiulaini.
Gari langu lilikuwa limebanwa mno na kwa upande wa kushoto wa barabara ile
kulikuwa na mtaro mkubwa wa majitaka hivyo endapo ningeendelea kuiruhusu hali
ile basi huwenda ningesukumiwa mtaroni na hapo gari langu lingepinduka. Hivyo
nikaanza kufikiria njia mbadala ya kujinasua.
Nikapangua gia zote hadi kufikia gia namba moja kisha nikakaza mguu wangu na
kukanyaga pedeli ya mafuta. Kwa kufanya vile gari langu likapaa hewani na lilipotua
chini magurudumu yake ya upande wa kushoto yakahamia upande wa pili wa ule
mtaro. Hivyo ule mtaro wa majitaka ukawa katikati ya difu.
Lilikuwa tukio la hatari lakini salama. Lile gari Landcruiser kwa kuwa lilikuwa
limezoea kuniegemea hapo awali likapoteza mhimili na kuanza kuserereka likiyumba
ovyo barabarani. Hata hivyo yule dereva alikuwa mtundu wa kucheza na gari hivyo
hatimaye akafanikiwa kulituliza vizuri gari lake barabarani kisha akaanza kunifuata na
safari hii lile gari lilikuja kwa kasi zaidi.
Niliweza kuinusa hatari iliyokuwa mbioni kunikabili na sikutaka kuisubiri hivyo
nikaikamata vizuri bastola yangu na kuvuta kilimi chake nikiiruhusu risasi moja
kusafiri. Risasi ile ikasafiri na kuchana kioo cha mlango wa mbele wa ile Landcruiser
ikitokezea upande wa pili wa dereva. Wale watu ni kama walikuwa wameishtukia
mapema dhamira yangu hivyo wakawahi kulala chini na kuiacha risasi ile ikiparaza juu
ya vichwa vyao na hivyo kupunguza kasi ya lile gari kunifikia. Sikupunguza mwendo
hivyo baada ya muda mfupi nikawa nimeliacha lile gari nyuma yangu. Hatimaye
nikalirudisha tena gari langu barabarani huku kioo cha nyuma kikiwa kimeondoshwa
kwa risasi. Baadhi ya taa za nyuma za gari langu zilikuwa zimepasuka na matundu ya
risasi za wale watu yalikuwa yamelipelekea gari langu kwa baadhi ya maeneo lifanane
na chujio.
Zile risasi ziliendelea kuniandama na kweli nilijitahidi kuzikwepa kwa kila hali
nikiliyumbisha gari langu upande huu na ule barabarani. Watu waliokuwa wakitembea
kando ya barabara ile walipoona vile wakaruka kando huku wakipiga mayowe ya hofu.
Wakati nikifikiria namna ya kujinasua mara nikapata wazo na bila kupoteza muda
nikaubana usukani wa gari langu vizuri kwa mkono mmoja kisha nikakusanya nguvu
za kutosha. Nilipochungulia dirishani kutazama kule nyuma nikajua nini cha kufanya.
Risasi tatu makini nilizozifyatua moja ikachana kioo cha mbele na kutengeneza tundu
dogo lenye nyufa za mipasuko. Sikujua kama risasi ile ilikuwa imempata mtu au lah!
lakini risasi zile mbili zilizosalia angalau zilifanya kazi niliyoitaka. Risasi zile zikaiharibu
na kuitawanya vibaya kabari ya boneti ya ile Landcruiser kwa mbele na kwa kuwa lile
gari lilikuwa kwenye kasi sana hivyo upepo mwingi ukaingia kwenye lile boneti na
hapo lile boneti likafunguka vibaya kama soli ya kiatu iliyotatuka.
Lilikuwa pigo safi la kiufundi lenye matokeo mazuri ya kuridhisha kwani boneti
lile lilifumuka vibaya na kufunika kile kioo cha mbele cha ile Landcruiser. Tukio lile
likampelekea yule dereva wa ile Landcruiser apoteze ueleko kama kipofu. Lile gari
Landcruiser likaanza kuyumba ovyo likipoteza uelekeo. Watu waliokuwa eneo lile
kuona vile wakaanza kupiga mayowe ya hofu.
Dereva wa lile gari akajitahidi kwa kila hali kuuthibiti usukani wake hata hivyo
hakufanikiwa kwani hatimaye lile gari Landcruiser likagonga ukingo wa daraja dogo
la mfereji wa majitaka uliokuwa kando ya barabara ile. Tukio lile likayapelekea
magurudumu ya mbele ya lile gari yapande juu ya ukingo wa daraja lile dogo na hapo
nikaona tukio la kushangaza.
Katika hali ya kushangaza mara nikaliona lile gari Landcruiser likipaa hewani kama
mwanasesere na lilipotua chini likapinduka mara mbili kisha likaserereka na kwenda
kujikita mtaroni kando ya barabara ile na hivyo kulipelekea eneo lile lote ligubikwe na
wingu zito la vumbi na mnuko wa mafuta ya gari yaliyokuwa yakivuja kutoka kwenye
tenki.
Kwa kweli lilikuwa ni tukio la aina yake na muda mfupi uliyofuata mashuhuda
wakaanza kukusanyika eneo lile wakitaka kufahamu vizuri nini kilichokuwa kimetokea.
Niliegesha gari langu kando ya barabara kisha nikafungua mlango na kushuka
nikielekea kule lile gari Landcruiser lilipopinduka huku nikiwa nimeikamata vyema
bastola yangu mkononi pasipo kuitilia maanani halaiki ya watu iliyokuwa ikizidi
kuongezeka eneo lile.
Bastola yangu ikiwa mkononi muda mfupi tu mara nikawa nimelifikia lile gari
Landcruiser pale mtaroni. Lile gari Lilikuwa limepinduka vibaya na magurudumu yake
ambayo sasa yalikuwa yakitazama juu yalikuwa yakiendelea kuzunguka kwa kasi.
Kifuniko cha tenki la mafuta la lile gari kilikuwa kimezibuka na hivyo kupelekea
mafuta mengi kuvuja na kusambaa eneo lile. Kitu pekee kilichonishangaza ni kuwa
pamoja na hali ile lakini injini ya lile gari bado ilikuwa ikiendelea kuunguruma.
Nikasogea karibu na nilipochungulia ndani ya lile gari nikawaona wanaume wanne.
Watatu miongoni mwao walikuwa hawajitambui kutokana na mshtuko mkubwa wa
ajali ile kama siyo majeraha makubwa katika baadhi ya sehemu za miili yao. Mwenzao
mmoja alikuwa na nafuu kidogo kwani aligeuka taratibu kunitazama hata hivyo
hakuweza kufanya chochote kwani mguu wake ulikuwa umeminywa vibaya na kunasa
kwenye chesesi ya lile gari.
Nikafungua mlango wa dereva na kuwatazama wale watu kwa makini huku
nikijaribu kuzinakili vizuri sura zao akilini mwangu. Hata hivyo sura za watu wale
zilikuwa ngeni kabisa machoni mwangu. Nikamtazama yule mtu mwenye fahamu
mara mbilimbili kwa udadisi zaidi na hapo nikamuona namna alivyojawa na hofu.
Hofu iliyomfanya ayakwepeshe macho yake na kutazama pembeni.
“Mna shida gani na mimi?” nikamuuliza yule mtu ambaye ndiye pekee aliyekuwa
na fahamu mle ndani. Yule mtu hakunijibu badala yake aliendelea kunitazama huku
akilalamika maumivu ya mguu wake.
“Nakuuliza wewe mna shida gani na mimi?”
“Hakuna mwenye shida na wewe” yule mtu akanijibu huku akiuma meno yake
na kukunja sura katika namna ya kukabiliana na maumivu makali ya majeraha yake.
“Sasa kwa nini mnanifuatafuata kila mahali ninapokwenda?” nikamuuliza yule
mtu na nilipomuona akiendelea kunitazama bila kuongea chochote nikamzaba
makofi mawili ya nguvu kumuweka sawa. Wenzake bado walikuwa wakining’inia
kwenye mikanda ya viti za gari huku fahamu zao zikiwa zimewatoka.
“Nyinyi ni akina nani?” nikamuuliza yule mtu huku nikianza kuwapekua mifukoni.
Vitambulisho vyao vikanitanabaisha kuwa wale watu walikuwa ni askari wa vitengo
nyeti vya usalama wa taifa ingawa sura zao bado zilikuwa ngeni kabisa machoni
mwangu.
“Askari” yule mtu akaongea kwa taabu hata hivyo sikushtushwa na hali ya afya
yake badala yake nikamchapa tena makofi matatu mazito usoni mwake na hapo
kamasi nyepesi za damu zikaanza kumtoka puani.
“Nani aliyewatuma mnifuatilie?” nikamuuliza yule mtu huku akigugumia
maumivu.
“Hatujatumwa na mtu” yule mtu akaongea huku akilalama.
“Kama nyinyi ni wanausalama kweli kwanini msishughulike na mafisadi
wanaofahamika hadi magazetini kwa kuzitafuna pesa za walipakodi kama mchwa na
badala yake mnatumika kuwaonea wanyonge?” nikamuuliza tena yule mtu na mara
hii nikajihisi kama niliyekuwa nikijiongelesha mwenyewe kwani yule mtu hakunijibu
na nilipomchunguza vizuri nikagundua kuwa alikwisha poteza fahamu huku akiwa
ananing’inia kwenye mkanda wa kiti cha gari. Huwenda hali ile ilitokana na maumivu
makali ya majeraha aliyokuwanayo mwilini mtu yule.
Nikatulia kidogo nikiyatembeza macho yangu kuwatazama wale watu mle ndani
na hapo nikagundua kuwa wote walikuwa na bastola mikononi. Nilitaka kuendelea na
uchunguzi wangu lakini mazingira ya eneo lile hayakuniruhusu kufanya hivyo kwani
mashuhuda walikuwa wengi sana.
Sikutaka kupoteza muda hivyo nikaanza kupitisha msako makini mle ndani.
Kitu cha ajabu ni kuwa wale watu mle ndani ya lile gari hawakuwa na simu kama
nilivyodhani badala yake simu pekee iliyokuwa mle ndani ilikuwa ni simu ya
upepo kama zile zinazotumiwa na askari wa usalama barabarani ambayo ilikuwa
imechomekwa sehemu fulani kwenye dashibodi ya lile gari.
Mwishowe nikapata kadi ndogo ya biashara ama business card yenye anwani fulani.
Nikaichukua kadi ile na kuitia mfukoni na wakati nikijishauri nini cha kufanya mara
nikaliona lile kundi la mashuhuda likisogea kando taratibu na kutengeneza nafasi nzuri
ya kupita na hapo nikajua kuwa polisi wa usalama barabara walikuwa wamefika eneo
lile.
Sikutaka polisi wale wanikute hivyo nikatoka kwenye lile gari haraka na
kujichanganya kwenye kundi la wale mashuhuda huku bastola yangu nikiwa tayari
nimeichimbia mafichoni. Baadhi ya mashuhuda walinishangaa hata hivyo sikuwatilia
maanani.
Askari watembeao kwa pikipiki maarufu kwa jina la Vodafaster tayari walikuwa
wamefika eneo lile na kuanza kuwasogeza watu pembeni ili wapate nafasi nzuri ya
kufanya kazi yao.
Muda mfupi uliofuata nikawa nimelifikia gari langu kule nilipokuwa nimeliegesha
ambapo nilifungua mlango na kuingia ndani. Sikutaka kuendelea kuwepo eneo lile
hivyo nikawasha gari langu nikiliacha eneo lile.
_____
DAMU ILIKUWA IKINICHEMKA vibaya mwilini na mzuka wa kazi ulikuwa
umenipanda kichwani na moyo wangu nao haukupingana katu na hisia zangu. Wakati
nikiendelea na safari mawazo mengi yalikuwa yakipita kichwani mwangu. Nilikuwa
nikimtafuta mdunguaji kwa udi na uvumba lakini hadi wakati huu nilikuwa sijamtia
machoni.
Yule kijana aliyeuwawa kwenye kile chumba cha mdunguaji cha Hotel 92 Dar es
Salaam nao ulikuwa ni mkasa unaojitegemea. Niliwakumbuka wale askari wa usalama
wa taifa waliopata ajali wakinifukuza na hapo maswali mengi yakaibuka kwenye fikra
zangu. Askari wale wenye vitengo nyeti vya usalama wa taifa walikuwa wameingiaje
kwenye mkasa huu?. Nikajiuliza bila kupata majibu hata hivyo hisia zangu zikanieleza
kuwa huwenda kulikuwa na jambo kubwa lililokuwa limefichika katika mkasa huu na
huwenda jambo hilo lilikuwa na mtazamo wa kimaslahi kwa baadhi ya viongozi wa
serikali kama siyo serikali yenyewe.
Nilikuwa na hakika kuwa watu wale ndiyo waliohusika na kifo cha Zera na
Momba kwa nyakati tofauti na hapo nikajiuliza kuwa watu wale walikuwa wakitaka
kuzuia kitu gani hadi nguvu yao igharimu uhai wa watu. Jibu sikulipata hivyo fikra
zangu zikahamia kwa mdunguaji. Kwa namna nyingine sikuona sababu kubwa ya
kumchukia mdunguaji kwani mdunguaji yule alikuwa akisakwa kama mimi na hapo
ule msemo wa “Adui wa adui yako ni rafiki yako” ukajengeka kichwani mwangu.
Sikufahamu mdunguaji yule hatari alikuwa ameingiaje kwenye mkasa huu hata hivyo
moyoni niliomba nikutane naye kwa mara nyingine.
Saa saba kasoro mchana ilipotimia niliegesha gari langu lililopata misukosuko ya
kutosha nje ya jengo moja refu la ghorofa eneo la posta jijini Dar es Salaam. Bila
shaka gari langu lilikuwa kivutio kwa watu waliokuwa eneo lile kutokana na yale
matundu ya risasi,michubuko ya rangi ubavuni,kupasuka kwa taa za nyuma pamoja
na kutokuwepo kwa kioo cha nyuma cha gari langu.
Sikujali kitu badala yake mara tu niliposhuka kwenye gari langu nikaharakisha
nikielekea sehemu ilipokuwa lifti ya ghorofa lile na kwa bahati wakati nikifika eneo lile
na kile chumba cha lifti nacho ndiyo kilikuwa kinafika nchini ya lile jengo.
Mara tu kile chumba cha lifti kilipofika chini na mlango wake kufunguka msichana
mmoja mrembo akatoka na kupishana na mimi wakati nikipotelea ndani ya chumba
kile cha lifti. Nilipoingia kwenye kile chumba cha lifti nikabonyeza kitufe cha ghorofa
namba sita ya lile jengo. Muda mfupi baadaye kile chumba cha lifti kikatia nanga
kwenye ghorofa ya sita ya lile jengo na mlango ulipofunguka nikatoka na kujikuta
kwenye korido pana iliyokuwa ikitazamana na milango upande wa kushoto na kulia.
Kabla ya kuendelea mbele na harakati zangu nikaichukua ile business card
niliyoichukua kutoka kwa mmoja wa wale majeruhi kwenye ile Landcruiser na kuyapitia
maelezo yake. Kwa mujibu wa maelezo yaliyokuwa kwenye ile business card bado
nilikuwa sehemu hii. Hivyo nikaanza kutembea taratibu huku nikiitafuta namba ya
mlango iliyokuwa kwenye ile business card.
Kulikuwa na utulivu mkubwa katika eneo lile la ghorofa na kitu pekee nilichoweza
kukisikia eneo lile ni mashine za viyoyozi zilizokuwa zikiunguruma mle ndani. Sakafu
ya korido ile ilitengenezwa kwa marumaru safi zinazovutia na kulifanya eneo lile
lipendeze sana.
Niliitazama milango iliyokuwa kwenye korido ile huku nikijaribu kutengeneza picha
fulani akilini mwangu juu ya kitu ambacho kingekuwa kikiendelea mle ndani na kwa
kweli sikuwa na hisia ya kitu chochote. Hivyo hatimaye nikaanza kutembea taratibu
kwenye korido ile huku nikiyatembeza macho yangu huku na kule nikiichunguza
milango iliyokuwa ikitazamana na ile korido.
Maelezo yaliyokuwa kwenye ile kadi bado nilikuwa nikiyakumbuka vizuri hivyo
macho yangu yakaendelea kusumbuka huku nikiutafuta mlango niliokuwa nikiuhitaji.
Nikiwa mbioni kukata tamaa hatimaye nikauona ule mlango. Mlango huo ulikuwa
katikati ya milango miwili iliyoachana kwa umbali mrefu upande wa kushoto wa korido
ile. Niliyatembeza macho yangu upande wa kulia na nilipoihesabu milango iliyokuwa
upande ule nikagundua kuwa jumla yake ilikuwa ni milango kumi na mbili. Aina ile
ya ujenzi ilinishangaza sana kwani sikuwahi kuiona katika mejengo yote niliyobahatika
kuyafikia katika jiji la Dar es Salaam.
Kilichonishangaza zaidi ni kuwa milango yote iliyokuwa ikitazamana na ile korido
ilikuwa imetengenezwa kwa fomeka isipokuwa mlango mmoja mweusi uliokuwa
katikati ya ile korido upande wa kushoto ambao hata hivyo ulikuwa mkubwa zaidi ya
ile mingine.
Nikausogelea ule mlango na kusimama mbele yake huku maswali mengi yakipita
kichwani mwangu. Niliutazama ule mlango kwa makini huku nikijiuliza kwanini
mlango ule ulikuwa ukitofautiana na milango mingine ya mle ndani. Juu ya ule mlango
kulikuwa na namba na mara hii nilishtushwa sana na namba iliyokuwa juu ya mlango
ule.
Ilikuwa ni namba 666 iliyochongwa kwa ustadi kwa madini ya shaba. Chini ya
namba ile kulikuwa na maneno mengine yaliyoandikwa kwa hati nzuri ya kupendeza
kwa madini yaleyale ya shaba. Maneno hayo yakisomeka Restricted Members Only na
chini ya maandishi yale kulikuwa na mstari mnyoofu uliyoyakinga yale maneno kwa
chini na kufuatiwa na alama sita za nyota za shaba.
Niliutazama mlango ule kwa makini huku nikiupisha utulivu kichwani mwangu
kisha nikaanza kugonga na wakati nikifanya vile nafsi yangu ikaanza kusumbuka katika
kuwaza juu ya kitu gani ambacho kingetokea mbele ya safari. Baada ya kugonga kwa
muda mrefu hatimaye nikapumzika kidogo na wakati nilipokuwa nikijiandaa kugonga
kwa mara ya pili ghafla nikasita baada ya kuuona ule mlango ukifunguliwa.
Ule mlango ulipofunguka mbele yangu nikajikuta nikitazamana na msichana mzuri
sana ambaye kwa kumbukumbu zangu za haraka sikuwahi kumuona msichana mzuri
kiasi kile tangu nizaliwe. Yule msichana alikuwa mrefu zaidi yangu na mwembamba
kiasi. Manukato yake ya gharama yakaziroga pua zangu wakati nilipoyatembeza
macho yangu taratibu kumtazama. Msichana yule mrembo alikuwa amevaa gauni
jepesi la hariri ya rangi nyekundu lakini hata hivyo gauni lile halikuwa na maana
yoyote machoni mwangu kwani wepesi wake ulilichora bila kificho umbo lake refu
la ulimbwende na kuziacha chuchu zake zilizotuna na kusimama wima kuzivuruga
kabisa hisia zangu.
Uso wangu ukiwa tayari umetengeneza tabasamu la kirafiki taratibu nikaanza
kuyatembeza macho yangu nikimtazama mrembo yule kuanzia juu mpaka chini na
mara hii nikagundua kuwa mrembo yule hakuwa amevaa nguo ya ndani. Nikalitazama
gauni lake na hapo nikagundua kuwa lilikuwa limeishia kwenye mapaja yake marefu
yaliyohifadhi misuli laini.
Mikono yake ilikuwa mirefu na inayopendeza yenye kucha ndefu sana zilizopakwa
rangi nzuri inayoendana na vazi lake. Nikayahamisha macho yangu tena kumtazama
kichwani. Nywele zake ndefu,nyeusi na laini zilining’inia hadi mabegani mwake na
kuifanya sura yake nyembamba kiasi ipendeze. Pua yake nyembamba ya kisomali
ilitengeneza kionjo kingine cha uzuri juu ya mdomo wake wa kike wenye kingo pana
na laini zilizokolezwa lipstick nyekundu. Shingoni alining’iniza mkufu mwembama
sana unaometameta wa madini ya almasi nyeupe. Nilipomchunguza masikioni
nikagundua kuwa sikio lake la upande wa kulia halikuwa na kitu lakini lile la kushoto
lilikuwa limetogwa herini nne tofauti ambazo zilikuwa zikimetameta ingawa sikuweza
kufahamu kuwa herini zile nzuri zilitokana na madini gani.
Hata hivyo pamoja na uzuri wa kustaajabisha wa yule msichana lakini bado moyo
wangu ulishtuka sana na kuingiwa na hofu pale nilipoyatazama macho yake. Niseme
kuwa sikuwahi kumuona shetani kwa haya macho yangu ya nyama zaidi ya kuona
matokeo ya kazi zake hapa duniani. Lakini kwa muonekano wa macho ya msichana
yule sikuwa na shaka kusema kuwa huwenda yule alikuwa ndiye shetani mwenyewe
aliyekuwa akizungumziwa na waumini wa dini mbalimbali kama siyo dada yake,wifi
au ndugu yake wa karibu sana. Kwani macho yake yalikuwa yakimetameta sana katika
namna ya kuniogopesha mno. Yale macho yake yaliyokuwa yakimetameta yalifunikwa
kwa kope zake nyeusi na ndefu sana na kumfanya azidi kuonekana msichana wa ajabu.
Nilikuwa mbioni kujishauri kuwa nimtake radhi msichana yule kwa usumbufu
uliojitokeza huku nikidanganya kuwa nilikuwa nimekosea mlango kisha niondoke
eneo lile. Hata hivyo sikufanikiwa kwani yule msichana akawahi kuvunja ukimya huku
akitabasamu.
“Karibu ndani” akaongea kwa sauti ya kubembeleza iliyotuama vyema kwenye
sakafu ya mtima wangu. Moyo wangu ukapiga kite kwa nguvu na kusababisha
usumbufu mdogo wa nafsi na hapo ujasili wangu wote ukatokomea kusikojulikana.
Hivyo nikabaki nikitabasamu tu mbele yake.
“Pita ndani kaka” yule mrembo akanikaribisha na sikutaka kujiuliza mara mbili
badala yake nikapiga hatua zangu taratibu kuingia mle ndani na wakati nikimaliza
kuingia nyuma yangu nikausikia ule mlango ukifungwa. Mara tu nilipoingia mle ndani
haikunichukua muda mrefu kutambua kuwa nilikuwa nimeingia kwenye mazingira
tofauti yenye hisia za hofu.
Harufu ya mle ndani ilikuwa tofauti kabisa na sehemu nyingine zote nilizowahi
kufika hapa duniani. Kwa kweli sikuipenda kabisa harufu ile na hewa ya mle ndani
haikuwa nyepesi wala nzito.
Mara tu tulipoingia mle ndani yule dada akageuka kidogo kunitazama huku
akitabasamu na wakati akifanya hivyo nikaiona tatoo iliyokuwa shingoni mwake.
Ilikuwa ni tatoo ya namba 666 iliyochorwa kwa ustadi sana na ufundi wa hali ya juu
na chini yake kulikuwa na tatoo nyingine ya nyoka aliyeachama mdomo na kutoa nje
pacha ya ulimi wake. Nikaitazama tatoo ile na kweli hofu ikazidi kuniingia hata hivyo
sikusema neno.
Mwanga hafifu wa mle ndani ukaniwezesha kuona mle ndani kwa sehemu
tu. Tulikuwa kwenye chumba kipana lakini kisichokuwa na kitu chochote.
Nilipoyatembeza macho yangu haraka mle ndani mara ukutani nikaiona michoro
mbalimbali ambayo katu haikunivutia kabisa kuitazama ingawa nilihisi kuwa huwenda
ilikuwa imechorwa kwa sanaa ya hali ya juu.
Mchoro mmoja ulionesha kichwa cha mwanamke mzuri lakini mwenye kiwiliwili
cha nyoka. Mchoro mwingine uliwaonesha wanaume wakilawitiana. Mchoro
mwingine uliyofuata ulikuwa na umbo la dunia lililozungukwa na moto mkali. Kisha
kukafuatiwa na michoro mingine kama ya;pete,mnyama fulani asiyeeleweka mwenye
miguu ya binadamu. Mchoro mwingine ulikuwa ni wa mwanamke aliyekuwa uchi wa
mnyama huku amempanda farasi mwenye kichwa cha binadamu. Kwa kweli michoro
ile sikuipenda.
Hatimaye nikayapeleka macho yangu kutazama kwenye sakafu ya kile chumba.
Kwa kufanya vile nikauona mchoro mkubwa wa popo aliyetanua mbwawa zake.
Miguu ya popo yule ilikuwa na misuli imara kama ya simba na mwili wa yule popo
ulikuwa wa binadamu mwanamke mwenye matiti. Nilikuwa nimesimama juu ya
mchoro ule bila kujua na yule msichana akanisukuma kando kwa nguvu za ajabu
zilizonishangaza huku macho yake makali yakinionya kuwa nisilete upinzani wa
namna yoyote.
“Usirudie tena kukanyaga hapa!” yule msichana akanifokea kwa hasira na wakati
nikitafakari yale maneno yake mara nikamuona akitabasamu tena na kwa kweli kitendo
kile kilinichanganya sana na kuniongezea mshaka.
“Wewe ni mwanachama wa humu ndani?” yule msichana mrembo akaniuliza kwa
utulivu huku akiwa amesimama kando yangu.
“Hapana!” nikamjibu huku nikitafakari matokeo ya jibu langu
“Hukusoma maelekezo yaliyokuwa mlangoni kabla kuingia humu ndani?”
“Kuhusu nini?” nikamuuliza kwa shauku
“Aina ya watu wanaotakiwa kuingia humu ndani” yule msichana akaniambia na
hapo nikakumbuka yale maelezo yaliyokuwa juu ya ule mlango wa kuingia mle ndani
yakisomeka Restricted Members Only na hapo jasho jepesi likaanza kunitoka. Hata hivyo
nilipomtazama yule msichana nikamuoana akizidi kutabasamu.
“Basi naomba uniruhusu nitoke nje” nikamwambia yule msichana huku nikianza
kupiga hatua zangu kuuendea ule mlango wa kuingilia mle ndani. Hata hivyo yule
msichana aliwahi kunizuia huku akiniambia
“Usijali kaka,nifuate!” yule msichana akaniambia na hapo tukuanza safari huku
yeye akiwa ametangulia mbele. Sehemu fulani katika ukuta wa kile chumba upande wa
kushoto nikamuona yule msichana akibonyeza tarakimu fulani katika vutufe vyenye
namba vilivyokuwa ukutani katika mlango uliokuwa eneo lile. Kwa kufanya vile mara
nikauona ule mlango ukifunguka. Mlango ule ulipofunguka tukaingia mle ndani kisha
ukajifunga nyuma yetu.
Mara baada ya mlango ule kujifunga tukawa tumetokezea kwenye eneo jembamba
lenye ngazi za kushuka chini. Tukasimama kidogo tukilitazama eneo lile na hapo yule
msichana akageuka na kunitazama huku akitabasamu. Kisha tukaanza kwenda chini
kwa kushuka zile ngazi taratibu na wakati tukishuka yule mrembo akawa akigeuka tena
mara kwa mara kunitazama huku akitabasamu nami nikafanya hisani kwa kutabasamu
kidogo ingawa kwa wakati ule tabasamu halikuwa nafsini mwangu. Hivyo nikapiga
moyo konde na kuendelea na ile safari.
Mwanga hafifu wa taa zilizokuwa ukutani kwenye zile ngazi ukaniwezesha kuona
maandishi yaliyokuwa ukutani eneo lile yakisomeka Vampire Casino-Our place in Dar
es Salaam. Nikayatazama maandishi yale huku nikishtuka sana hata hivyo sikutaka
mshtuko wangu uonekane kwa yule msichana wakati alipogeuka na kunitazama.
“Tunaelekea wapi?” hatimaye nikamuuliza yule msichana.
“Hutaki kuwaona wenzangu?” yule msichana akanijibu huku akitabasamu.
“Ni wazuri na warembo kama wewe?” nikatumbukiza utani kuzipeleleza hisia
zake.
“Nilipokutazama tu nikajua haraka kuwa unapenda wasichana wazuri ndiyo
maana nikakukaribisha humu ndani” yule msichana akaongea huku akiangua kicheko
hafifu. Nilicheka kidogo nikikubaliana naye ingawa ile haikuwa dhamira yangu.
Hatimaye tukawa tumefika kule chini mwisho wa zile ngazi na hapo tukawa
tumetokezea kwenye ukumbi mdogo wenye watu wasiopungua hamsini. Mara hii
nikashtuka sana nilipowatazama wale watu. Ulikuwa mchanganyiko wa wanaume kwa
wanawake vijana kwa wazee. Kitu kilichonishtua zaidi ni kuwa baadhi ya watu wale
nilikuwa nikiwafahamu. Kulikuwa na wanasiasa maarufu,wanamuziki,wanamichezo
na hata viongozi wa dini wakubwa niliokuwa nikiwafahamu.
Watu wale walikuwa wameketi wakimsikiliza kwa makini mtoa mada aliyekuwa
ameketi mbele yao kwenye kiti kama mfalme huku amevaa majoho mekundu. Kitu
kilichonishangaza ni kuwa wakati tukipita eneo lile wale watu hawakujishughulisha
kututazama badala yake waliendelea kumsikiliza mtoa mada mbele yao.
“Wale watu wanafanya nini?” nilimuuliza yule msichana huku nikishangazwa sana
na hali ile.
“Siwezi kukuleza mpaka uwe miongoni mwetu” yule msichana akaniambia huku
tukiendelea na safari.
“Kwani nyinyi ni akina nani?” nikamuuliza yule msichana na wakati huo tulikuwa
tumefika kwenye korido nyingine nyembamba tofauti na ile ya awali. Wakati
tukiendelea na safari nikayatega masikio yangu vizuri mle ndani na kwa mbali niliweza
kuzisikia kelele za vitoto vichanga vikilia kwa sauti kubwa mle ndani. Hali ile ikazidi
kunichanganya kwani mandhari ya mle ndani hayakufaa kufananishwa na wodi ya
wazazi. Kitu kilichonishangaza zaidi ni kuwa kelele zile zilikuwa zimeambatana na
sauti ya vicheko vya wanawake.
Nikiwa nyuma ya yule msichana nikachungulia kwa jicho la pembe ndani ya
vyumba tulivyopishanavyo. Kwa kufanya vile mle ndani nikawaona wanaume kwa
wanawake wakiwa wamevaa makoti marefu kama yale yanayovaliwa na madaktari
na glovu nyeupe mikononi. Wale watu walikuwa wakiweka vitu fulani vyeupe
kwenye mifuko ya nailoni ingawa sikuweza kuona vizuri. Mara hii tena nafsi yangu
ikanitahadharisha kuwa nilikuwa nimejitumbukiza kwenye hatari nisiyoifahamu.
Tulimaliza kuivuka korido ile kisha tukaingia upande wa kulia na hapo nikasikia ile
sauti ya vicheko ikiongezeka. Sikutaka kumuuliza yule msichana kwani niliamini kuwa
majibu ya maswali yangu yalikuwa mbioni kupatikana
#121
Katika upande ule wa kulia tulioingia kulikuwa na milango mingine. Tulipoifikia
ile milango yule msichana mbele yangu akasimama kisha akageuka na kunitazama.
Nikatabasamu kidogo katika hali ya kuonesha kuwa sikuwa na wasiwasi wowote
ingawa hali iliyokuwa ikiendelea moyoni mwangu nilikuwa nikiifahamu mwenyewe.
Yule msichana alipoacha kunitazama akageuka na kufungua ule mlango kisha
akaniashiria nisogee karibu na kuchungulia mle ndani. Nikasogea na kuchungulia mle
ndani na kwa kufanya vile nikawaona wasichana wadogo vigoli. Uzuri wa wasichana
wale kwa kweli ulinibabaisha na kuziamsha hisia zangu.
Wale wasichana wakageuka mara tu mlango ule ulipofunguliwa wakitutazama
ingawaje nilikuwa na kila hakika kuwa walikuwa wakinitazama mimi zaidi kuliko yule
mwenyeji wangu. Labda kwa sababu nilikuwa mwanaume peke yangu eneo lile. Mara
wale wasichana vigoli wakaacha walichokuwa wakikifanya na kuanza kunifuata pale
mlangoni lakini yule mwenyeji wangu aliwahi kuwakemea hivyo wakarudi.
Yule dada akanisukuma pembeni na kufunga ule mlango na hapo safari yetu
ikaendelea huku yule mwenyeji wangu akiendelea kufungua milango ya vyumba
vingine vilivyokuwa vikifuatia ambapo mle ndani kulikuwa na wasichana wengine
wazuri sana wa rika tofauti. Niliwatazama wasichana wale na kwa kweli niseme kuwa
mwanaume yeyote mkware asingekubali hazina ile impite hivihivi.
Hatimaye safari yetu ikaishia ndani ya chumba kipana chenye kitanda kikubwa
cha futi sita kwa sita kilichofunikwa kwa shuka safi zenye rangi ya kupendeza na mito
miwili ya kuegemea. Pembeni ya kitanda kile kulikuwa makochi mawili makubwa ya
sofa na meza fupi ya kioo katikati yenye kibeseni kidogo cha majivu ya sigara mfano
wa fuvu la mtu.
Nikayatembeza macho yangu na kwenye pembe ya chumba kile kulikuwa na
jokofu dogo la vinywaji lililopakana na kabati lililofungwa ambalo sikuweza kufahamu
haraka kuwa mle ndani yake kulikuwa na nini. Kiyoyozi murua kilichokuwa mle ndani
kililifukuza joto kali la jiji la Dar es Salam na kunipelekea niyafurahie sana mandhari
yale tulivu.
“Karibu uketi” yule msichana akanikaribisha na nilipomchunguza niliweza
kuukadiria umri wake kuwa ulikuwa ni kati ya miaka ishirini na mbili na ishirini nne
huku akionekana kujiamini sana. Hatimaye nikaenda na kuketi kwenye kochi moja
miongoni mwa yale makochi mawili yaliyokuwa mle ndani. Mara tu nilipoketi mbele
yangu nikajikuta nikitazamana na runinga pana iliyokuwa kwenye kona ya kile chumba.
“Ahsante!” nikaongea na kuketi.
“Utatumia kinywaji gani?” yule mrembo akaniuliza na hadi kufikia pale niliweza
kuhisi kuwa alikuwa na wadhifa wa juu mle ndani.
“Maji baridi tu tafadhali!” nikamwambia yule mrembo na hapo nikamuona
akienda kufungua lile jokofu la mle ndani kisha akachukua chupa kubwa ya maji baridi
na bilauri ya kioo halafu na yeye akajichukulia kinywaji baridi cha Malta na kuja na
kuketi mbele yangu kwenye lile kochi jingine ambalo lilitupelekea tuketi katika mtindo wa kutizamana
Kwa vile nilikuwa nikihisi kiu nikaichukua ile chupa ya maji na kuifungua kisha
nikaanza kugida mafunda kadhaa ya maji pasipo kuitumia ile bilauri. Nilipoiweka ile
chupa juu ya meza ilikuwa imebaki nusu hivyo nikachukua pakiti ya sigara kutoka
mfukoni na kutoa sigara mbili ambapo moja nilimpa yule mrembo na nyingine
nikaitia mdomoni na kuilipua kwa kiberiti changu cha gesi. Ile sigara ilipowaka na
kukolea vizuri nikamrushia kile kiberiti yule mrembo ambapo alikidaka kwa ustadi na
kujiwashia sigara yake.
“Jina lako unaitwa nani?” nikamuuliza yule mrembo baada ya kuitoa sigara yangu
mdomoni na kuupuliza moshi pembeni
“Oga” yule mrembo akanijibu kwa utulivu huku akiendelea kuvuta sigara yake
“Jina zuri”
“Na wewe je?”
“Remy” nikamdanganya
“Siyo Stephen Masika tena?” yule mrembo akaniuliza na hapo moyo wangu
ukalipuka kwani Stephen Masika lilikuwa jina langu la bandia ambalo nilikuwa
nimelitumia kujiandikisha uanachama kule Vampire Casino. Nikaumeza mshtuko
wangu kwa kuivuta sigara yangu taratibu na nilipoitoa nikamuuliza yule mrembo kwa
shauku
“Umenijuaje?”
“Ulinidanyanga ikidhani sikufahamu?” yule mrembo akaniuliza huku akivuta pafu
jingine la sigara na alipoitoa ile sigara mdomoni akaendelea huku akiupandisha mguu
wake mmoja juu ya mwingine na hivyo kulipelekea gauni lake fupi lipande juu na
hapo nikayaona mapaja yake yaliyonona. Ili kuurudisha vizuri mhimili wa nafsi yangu
nikaanza kumkemea pepo mchafu ingawa sidhani kama maombi yangu yalikubalika
kwani nafsi yangu bado iliendelea kusukwasukwa ovyo na jinamizi la ngono.
“Huwenda ukawa unajua kila kitu kuhusu mimi Oga hebu niambie” nikamwambia
yule mrembo huku nikitengeneza uso wa tabasamu.
“Kwa sehemu tu ndiyo maana nikakuleta humu ndani” Oga akaniambia kwa
utulivu kisha akaivuta sigara yake na alipoitoa na kupuliza moshi pembeni akaniuliza
“Tafadhali! niambie wewe ni nani hasa na umefika hapa kufanya nini?”
“Nahitaji kufahamu nyinyi ni akina nani na mnashughulika na mambo gani humu
ndani” nikamuuliza yule mrembo huku nikimtazama kwa makini.
“Nani aliyekuelekeza humu ndani?” yule mrembo akaniuliza na kabla sijamjibu
nikamuona akisimama na kuanza kunifuata pale nilipoketi. Kufumba na kufumbua
akaitoa bastola yangu kutoka nyuma kiunoni nilipokuwa nimeibana kwa mkanda
kisha akaifyatua magazine yake na kuitupia pale kitandani. Tukio lile likanipelekea jasho
jepesi lianze kufanya ziara kwenye sehemu mbalimbali za mwili wangu. Kitendo kile
kikanifanya nijihisi kuwa nilikuwa nimemkadiria vibaya yule mrembo. Hata hivyo
sikutia shaka yoyote.
“Nimeokota business card yenu hivyo nikaona si vibaya kuja kuwatembelea”
nikamwambia yule mrembo huku nikiendelea kuivuta sigara yangu taratibu.
“Na hiyo bastola ni ya nini humu ndani?” yule mrembo akaniuliza huku
akinitazama kwa makini.
“Kujilinda pale inapobidi”
“Nani aliyekwambia kuwa humu ndani kuna hatari?” swali la Oga likanipelekea
nimtazame mrembo yule kwa makini. Nilikuwa na uzoefu mkubwa kwa wasichana
wenye tabia kama za Oga. Hivyo nilifahamu kuwa ili kupata matokeo mazuri ya kazi
yangu nilihitajika kuwa mtulivu na mwenye moyo wa subira. Hatimaye nikaitia sigara
yangu mdomoni na kuivuta taratibu. Nilipoitoa sigara yangu mdomoni nikayakung’uta
majibu kwenye kile kibeseni cha majivu pale mezani kisha nikavunja ukimya
“Jina langu naitwa Chaz Siga” nikamwambia yule mrembo huku nikiiacha sigara
yangu ikiteketea katika pacha ya vidole vyangu.
“Vizuri!,endelea nakusikiliza” Oga akaongea huku akitabasamu.
“Mimi ni mpelelezi wa kujitegemea” nilikatisha maongezi kisha nikaipeleka sigara
yangu mdomoni na kuivuta taratibu. Nilipoitoa sigara mdomoni nikaupuliza moshi
pembeni na kuendelea
“Sikuwahi kufika humu ndani pamoja na kuzaliwa na kukulia hapa jijini Dar es
Salaam kwa muda mrefu. Lakini sasa nafurahi kupafahamu mahali hapa na huwenda
majibu ya maswali yangu yakaanza kujibiwa”
Oga alikuwa ameketi kwenye kochi mbele yangu huku mguu wake mmoja
ameupandisha juu ya mwingine na sigara yake ikiendelea kuteketea taratibu mkononi.
Ingawa Oga alikuwa akitazama dirishani lakini nilikuwa na kila hakika kuwa masikio
yake alikuwa ameyatega vizuri kunasa kile nilichokuwa nikikizungumza.
“Unapeleleza nini?” Oga akaniuliza
“Kifo cha rafiki yangu” nikaongea kwa utulivu
“Jina lake?”
“Gabbi Masebo” nilimwambia Oga na hapo nikamuona akitabasamu kidogo
kisha tabasamu lake lilipokoma akaniambia
“Okay! endelea”
“Rafiki yangu ametoweka miaka kumi iliyopita katika mazingira ambayo siyaelewi”
“Nini kinachokusukuma uje kufanya upelelezi wako humu ndani?” Oga akaniuliza
huku akiyakung’uta majivu ya sigara yake kwenye kile kibeseni pale mezani.
“Mpaka sasa bado sijafahamu kama nimefika hapa kupeleleza ua lah!” niliongea
huku nikimtazama Oga na safari hii uzuri wake ulizidi kunichanganya. Umbo lake
maridhwawa lilikuwa limechoreka vyema ndani ya gauni lake jepesi na laini alilolivaa.
Mikono yake mirefu na imara pamoja na vishimo vyake vidogo mashavuni vikaongeza
ziada nyingine katika uzuri wake.
“Hicho ndiyo kilichokupelekea kumuua mlinzi wetu?” swali la Oga likanipelekea
nigeuke na kumtazama kwa shauku.
“Wapi?”
“Vampire Casino”
“Umejuaje?” nikamuuliza Oga huku nikimkazia macho.
“Walinzi wawili uliopambana nao wakati ukijaribu kutoroka walitueleza habari
zako na kamera za usalama za casino zikatuhakikishia” Oga akaongea kwa utulivu.
“Hao walinzi wamewaeleza wewe na nani?” nikamuuliza Oga huku nikitabasamu
“That’s non of your business!” Oga akafoka kwa hasira huku akinitazama kwa makini.
“So what kind of business is yours?” nikamuuliza Oga kwa utulivu huku nikiyakung’uta
majivu ya sigara yangu kwenye kile kibeseni cha majibu pale mezani kisha nikaendelea
“Unaweza kuniambia kuwa mnawapata wapi wale mabinti wadogo kule
vyumbani?” nikamuuliza Oga na hapo akaangua kicheko kilichonishangaza.
“Nilidhani umesahau. Vipi unataka mmoja?” Oga akaniuliza huku ekiendelea
kucheka lakini ghafla kicheko chake kikakoma huku sura yake ikiwa mbali na mzaha
na tabia yake ile ya kubadilikabadilika ikazidi kunichanganya.
“Bado hujanijibu swali langu mrembo” Oga akanitazama kwa utulivu na uso wake
haukuonesha tashwishwi yoyote’’
“Tayari umechelewa kwani hata nikikupa hizo taarifa hutofanikiwa kufikanazo
kokote”http://pseudepigraphas.blogspot.com/
“Una maanisha nini?” nikamuuliza Oga kwa utulivu.
“Umefanya makosa sana kuingia humu ndani”
“Mbona unanitisha mrembo”
“Unadhani kuwa nakutisha basi umekosea sana kwani huu ndiyo mwisho wako
na habari zako zitaishia humu ndani’’
“Una maanisha nini?’’
“Subiri na utanielewa muda siyo mrefu. Najua umekuja humu ndani kupeleleza
kinachoendelea lakini nataka nikufahamishe kuwa hilo ni kosa kubwa sana ulilowahi
kulifanya siku za uhai wako hapa duniani. Baada ya kumtafuta Milla Cash kwa muda
mrefu na kumkosa naona sasa umeamua kufanya uamuzi wa busara kwa kujileta
mwenyewe’’
Nikamtazama Oga kwa shauku kwani kitendo cha kumtaja Milla Cash bila
shaka kilikuwa kimeanza kutanzua wingu zito lililotanda kichwani mwangu. Kwa
kweli nilianza kuhisi wepesi fulani katika fikra zangu na hapo nikaupachika mche wa
sigara yangu mdomoni na kuvuta mapafu kadhaa huku nikiupisha utulivu kichwani.
Nilipoitoa sigara mdomoni nikaupuliza moshi pembeni huku nikimtazama Oga kwa
utulivu.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment