Simulizi : Nyuma Yako
Sehemu Ya Tano (5)
“Salama. Vipi wewe?”
“Salama tu. Ule pale ni mlango wa bafuni na choo. Waweza kwenda kuoga kisha upate kifungua kinywa.”
“Ahsante.”
Nikafuata maelekezo yake kwenda huko. Nikiwa bafuni nakoga, kama baada ya dakika tano tu, nikasikia mlango wa bafu ukigongwa kwa nguvu. Sijaitikia, yule mwanamke akafungua na kunisihi kwa sauti ya woga. “Usitoke humu ndani ya bafu. Tafadhali!”
Hakuwa ananitazama, bali akirushia macho yake pembeni asinione uchi. Kabla sijamuuliza chochote, akawa ameshatoka na kuufunga mlango akiniacha na maswali.
Sikuendelea kuoga tena.
Nilitega masikio yangu nipate kusikia kinachojiri. Nilisonga karibu na mlango nikiwa nimejiveka taulo kwa dharura ya lolote litakalotokea basi lisinikute uchi. Niliposkiza kwa ufupi nikajua kuna magombano, watu wawili walikuwa wanazoza kwa kutumia lugha ya kijerumani, mmoja mwanaume ambaye sikumtambua kwa sauti yake na mwingine mwanamke ambaye ni wazi alikuwa ni yule mwanamke mwenyeji wangu.
Kama haitoshi magombezano hayo yaliambatana na kuvunjwa kwa vitu kadhaa.
“Yuko wapi?” Mwanaume alifoka. “Nasema yuko wapi? Sema kabla sijakuua!” Baada ya hapo nikasikia sauti ya kofi na yowe toka kwa mwanamke. Kidogo nikasikia sauti ya kishindo cha mtu na mara mlango wa bafuni nilimo ukafunguliwa kwanguvu! Uso kwa uso nikakutana na mwanaume mpana mrefu aliyekuwa amefura haswa.
Alinikodolea na kusema akininyooshea kidole, “Umekwisha!” Akazama ndani ya bafu na kujaribu kunishambulia. Nilimsihi aniskize lakini hakuwa tayari, alidhamiria kuniumiza ama tuseme kuniua kabisa, hivyo ikanipasa nitetee uhai wangu.
Sikuhangaika naye sana, alikuwa ni mtu mwenye ‘maguvu’ mengi na mzito. Nilifanikiwa kumkabili kwa mapigo matatu akawa yu chini hoi. Nikatoka bafuni na kwenda kukutana na yule mwanamke mwenyeji wangu, yeye alikuwa amelala chini akiwa analia.
Nikamnyanyua na kumtazama, uso wake ulikuwa unavuja damu, alikuwa amjeruhiwa vibaya. Nikamsihi nimpeleke hospitali lakini hakuwa tayari kabisa badala yake akawa ananishauri niondoke upesi kwa usalama wangu.http://pseudepigraphas.blogspot.com/
“Nenda, nitakuwa salama usijali!” Aliniambia akinisukuma, lakini ningemwachaje vile? Nilimwomba aende hospitali basi hata pale nitakapoondoka, bado akaendelea kunisisitiza niende na saa hii akinipa vitisho, “atakumaliza yule! Si mtu mzuri kabisa!”
Akiwa analia akanambia kuwa watoto wake walikutana na baba yao huyo na kumwambia kuwa yupo na mwanaume nyumbani. Alikiri mume wake ni mhalifu na mkatili, ni mtu ambaye hafikirii mara mbilimbili kummaliza mtu.
“Nisingependa nikuweke matatizoni, tafadhali nenda.” kauli yake hiyo ilinisababishia maumivu makali kwani niliona mimi ndiye nilimsababishia matatizo. Nilitamani sana kumsaidia, roho yangu haikuwa radhi kabisa kumwacha hapo. Lakini kwasababu ya shinikizo lake nikaona nitimize agizo lake. Nikanyanyuka na kujongea mlango, nikajiendea.
Nilipiga hatua kumi na mbili, kama nipo sahihi, mbali na eneo lile. Ghafla nikasikia makelele ya mwanamke toka kwenye nyumba ile, hapo nikasita nikisimama na kuwekeza jitihada kwenye masikio yangu. Alikuwa ni yule mwanamke anapigwa, halikuhitaji elimu kulibaini hilo. Sikuweza kuvumilia, basi nikarejea kumsaidia.
Nilifungua mlango kwa pupa na kuangaza. Nilichokiona ni yule mwanaume akiwa amemshika mwanamke yule nywele zake, mkono wake ukiwa unachuruza damu. Nikamwamuru, “Mwachie huyo mwanamke upesi!” nikamwamuru nikiwa namkodolea haswa. Mapigo yangu ya moyo yalikuwa yanaenda mbio kwa hasira. Nilimwona mwanaume huyu ni mnyama kabisa.
Kwa kiburi, akaniambia, “Utanifanya nini nisipomwacha?” kabla sijajibu nilimwona mwanamke yule akipambana kunusuru nywele zake. Alikuwa anahisi maumivu, ungeliona hilo kwa namna alivyokuwa amekunja sura yake akiugulia na kugugumia.
“Usipomwacha nitakuadhibu kwa kipigo ambacho hujawahi pewa tangu uzaliwe!” nikamwambia nikimnyooshea kidole. Basi akamtupia kando yule mwanamke na kunifuata. Laiti angelijua niliyokuwa nimempangia kichwani mwangu basi asingediriki kupiga hata hatua moja karibu yangu. Niling’ata meno na kukunja ngumi, nikamwona akichomoa kisu nyuma ya mgongo wake.
“Nitakuua na kukufukia nyuma ya bustani. Na hamna mtu atakayekuja kuniuliza chochote!” alibwatuka, nami nisiseme kitu bali nikimngoja nimfundishe adabu.
Alipokaribia, naam, nikampa kitu roho inapenda. Nilimsubiri arushe kisu chake, nikaudaka huo mkono na kuutegua uache silaha kisha nikamvuta na kumwadhibu kwa kumtwanga ngumi nzito chini ya kidevu chake. Akiwa anapepesuka, nikamzika na teke zito lililonyanyua mwili wake mzito kwa kiasi chake na kisha kumbwagia chini. Alikuwa hoi asiyejiweza.
“Twende!” nikamwambia mwanamke yule nikimsogelea. Nikamnyanyua na kutoka naye ndani kwenda nje. Moja kwa moja nikamwongoza mpaka hospitali ambapo aliingia ndani kupata huduma mara moja. Uzuri alikuwa na kadi yake ya afya akiambatana nayo. Kumbe wakati mwanaume huyo anamdaka alikuwa yu njiani kujiondokea zake.
“Sasa kwanini haukutaka kwenda na mimi?” nikamuuliza. Alikuwa tayari amehudumiwa, kwa kiasi uso wake umefunikwa na bandeji.
“Nimeshakuambia, sitaki kukuingiza kwenye matatizo,” akaniambia akiwa ananitia huruma haswa. Nilikuwa naona hastahili yale anayopitia. Kila alipokuwa anateta neno moyo wangu ukawa unapiga kwa kunigusa.
“Matatizo yapi?” nikamuuliza. “Mume wako naweza kummudu, hawezi kunipa shida kabisa.”
Akan’tazama. Jicho lake la kushoto lilikuwa limefunikwa kiasi na bandeji.
“Unaweza kupambana naye lakini vipi kuhusu kundi lake? Hayupo mwenyewe!” aliposema hayo akapangusa pua yake kwa mgongo wa kiganja kisha akasema kwa sauti inayotikiswa na kilio.
“Watakusaka na kukuua kisha wakakutupie baharini. Nami sitaishi kwa amani tangu leo.”
Nikampa moyo, hatokumbwa na lolote mimi nikiwa hai. Ila kitu kilichokuwa kinanifikirisha ni namna gani atarudi kule kwake kwa yule mwanaume katili.
“Inabidi utafute mahali pengine pa kukaa, sawa?” nikamshauri. “Kuhusu watoto wako nadhani wataelewa maamuzi yako.” alipofuta makamasi mepesi yalokuwa yanamchuruza, akasema akiwa anatazama chini, “Wale si watoto wangu bali wa mume wangu.”
Hapa nikaona basi ni rahisi kwake yeye kuwa salama, lakini pia nikapata picha kwanini watoto wale waliweza kwenda kumpandikiza maneno baba yao huko walipokutana naye.
“Kwanini usiwe mwenyewe? Kwanini unaishi na mwanaume katili kama yule?”
Hapo ndipo nikajifunza kuwa mwanamke huyo hayupo kimapenzi na yule jamaa, bali kwa hofu. Yapata miaka mitatu iliyopita ndipo mahusiano yao yalianzia baada ya mwanaume huyo kumpoteza mke wake kwenye mazingira ya kutatanisha. Kwa muda wote huo alikuwa akiishi akijua mke wa mwanaume huyo alipata ajali, lakini siku moja alikuja kuubaini ukweli baada ya mwanaume huyo kumwadhibu na kumtamkia kuwa akiendelea kuwa mkaidi basi atammaliza kama alivyofanya kwa mkewe na kisha akamtupia baharini!
“Nisingeweza kumtoroka, mtandao wake ni mkubwa hapa Berlin. Ningejifichia wapi?” alimalizia kwa kauli hiyo akiwa anadondosha machozi.
Tuliondoka hapo hospitali tukaenda mahali pa kupumzikia alipopalipia kwa kutumia pesa yake mwenyewe. Huko tukakaa kwa siku mbili kwa amani kabisa, yeye akiwa kwenye chumba chake na mimi changu. Nilijitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu kumjali lakini bado nikajiona napwaya. Nilihisi nahitaji kufanya kazi niingize kipato. Nisingeweza kumtegemea mwanamke huyo siku zote hizo.
Usiku wa siku ya tatu, pasipo kuaga, nikatoka na kwenda kwenye moja ya klabu ya usiku. Huko nikajitahidi kukutana na wafanyakazi wa klabu hiyo na kujinasibu nahitaji kazi ya kulinda eneo hilo.
“Wewe?” aliuliza mmojawao, jamaa mwenye mwili mpana na uso mwekundu. Sikio lake la kulia alikuwa amelitoboatoboa na hereni kadhaa. Mdomo wake mdogo ulikuwa umefichwa na ndevu nyingi mithili ya beberu asiye na matunzo.
“Ndio, mimi!” nikamjibu nikimtazama usoni pasi na kupepesa mboni. Basi akanitazama kwa sekunde kadhaa kisha akanipa ishara ya kichwa kuelekea upande wake wa kulia. Nikaongozana naye na punde nikajikuta ndani ya ofisi ndogo alimokuwa amekaa jamaa mwembamba ndani ya suti. Jamaa huyo hakuwa anaonekana vema kutokana na kuchezacheza kwa mwanga. Alikuwa anavuta sigara kubwa na amezungukwa na wanawake takribani saba ambao vifua vyao vilikuwa wazi.
“Vipi?” akamuuliza yule mwanaume aliyenileta, yule jamaa akajieleza kunihusu na kisha akakaa kando akiwa amefumbata mikono yake.
“Sogea karibu kijana!” yule jamaa akaniamuru. Niliposonga karibu zaidi ndipo nikamgundua bwana huyo, si kwa jina, lah! Bali umri wake. Alikuwa makamo sawa na mimi. Haikunishangaza kwa namna anavyoheshimika, alikuwa ni ‘mkuu’. Nadhani ndivyo ilivyo popote pale.
“Kipi kinachokufanya udhani unaweza kazi hii?” akaniuliza akinitazama. Niliona macho yake mara kadhaa mwanga ulipopita na kujiendea.
“Kwasababu naweza kupambana,” nikamjibu. Hiko ndicho kitu pekee ambacho nalikuwa na uhakika nacho kuwa naweza. Uzuri nilijithibitishia hilo mara mbili ama tatu hapo nyuma baada ya kupoteza kumbukumbu zangu zote.
Lakini bwana yule alionyesha wazi hakuniamini. Alimtazama jamaa yule aliyenileta na kisha akampa ishara ya kichwa, nikashangaa bwana huyo ananifuata.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Kabla sijauliza bwana huyo akanikamata na kuninyanyua juu kisha akanikung’uta kichwa cha kifua na kunibwaga chini. Nilibanwa sana na kifua. Nilikohoa mara kadhaa nikijaribu kuvuta hewa kwa wakati huohuo. Sijakaa vema, bwana huyo kama mtu ambaye hakuridhika, akanifuata kwa upesi. Hapa ikanilazimu namna kujikomboa la sivyo nitapewa kadhia nisiyotarajia.
Upesi nikafyatua miguu yangu kufyagia miguu ya mwanaume huyo lakini sikufanikiwa, bwana huyo aliyumba kana kwamba meli dhorubani akitazamia kutafuta balansi. Nami nisimruhusu asifanye hivyo, nikajiamsha upesi na kumkandika teke! Bado hakudondoka. Aliyumbayumba sana. Nami saa hii sikumfanya jambo nikamwacha ajitulize.
Akanguruma kama simba akinitazama. Akakunja ngumi zake na kunifuata akipiga hatua kubwa. Aliponikaribia akatupa ngumi kama tano, zote nikazikwepa na kisha nikamtafutia nafasi ya kumkandika ngumi moja ya pua, akachuruza damu! Kuanzia hapo akawa haoni vema. Sasa nikafanya vile nilivyokuwa nataka mimi.
Nikapata fursa ya kumpa mapigo matatu na bwana huyo akalala usingizi mzito chini akiwa hajiwezi. Nikamtazama kwa uhakika, na mara nikasikia mtu akipiga makofi. Nilipotazama nikamwona yule jamaa aliyekuwa ameketi kochini akinyanyuka. Bado sigara yake ilikuwapo mdomoni.
“Safi sana! Safi sana!” akapayuka baada ya kutoa sigara kinywani. “Umepata kazi moja kwa moja.”
“Nashukuru sana!” nikamtazama na kuinamisha kichwa kidogo.
“Unaitwa nani? Sogea … sogea karibu!”
Nikasonga na kumtazama usoni. “Naitwa Tarrus,” nikajisemea jina la kwanza kuja kichwani mwangu.
“Tarrus!” akastaajabu. “Jina zuri kabisa! Kuanzia sasa utakuwa mlinzi wa chumba cha watu wa hadhi ya juu, sawa?”
“Sawa.”
“Sasa nenda nyumbani kesho uwapo hapa majira ya saa tatu usiku. Umenielewa?” aliuliza akiwa ameweka mkono wake begani mwangu.
“Ndio, nimeelewa,” nikamjibu na kwenda zangu. Nilifika kwenye makazi yangu majira ya saa nane kasoro usiku. Njiani kwenye basi watu walikuwa wakinitazama sana kwa kunihofu. Nalikuwa nimetapakawa na damu. Sikuwa naonekana sawa. Lakini sikujali, na kifuani mwangu kilichokuwa kinanifurahisha ni kwamba nimepata kazi, basi.
Nilimkuta mwenzangu akiwa amelala, na wala nisimsumbue nikajiendea kuoga na kisha nikapumzika. Kesho yake kwenye majira ya saa tatu asubuhi ndipo tukaonana na nikatambua kuwa mwanamke huyo alifahamu kuwa jana niliondoka.
Alinitazama kwa jicho fulani kisha akanywa fundo moja la hai na kuuliza, “Mbona hukuniaga?” nikamtazama kana kwamba sijui anachokiongelea.
“Ulitoka jana. Ulidhani sitajua?”
Nikatabasamu kisha nikanywa mafundo mawili ya chai iliyokuwa inaelekea kuwa vuguvugu, “Yah! Nilitoka mara moja. Nilitumai kurudi mapema.”
“Ulienda wapi?” akaniuliza akinitazama. Nilijihisi nafanyiwa usahili. Sikujua nini alikuwa ananiwazia kichwani ila ni bayana hakikuwa chema.
“Nilienda kutembea tu, kwani kuna shida?” nikatania, lakini bado sikuweza kuuvunja uso wake uliokuwa ‘serious’. Akiwa ananitazama, akasema, “Tafadhali usijiingize kwenye uhalifu.” hapa sasa nikajua nini alikuwa anawaza.
“Mji huu si rafiki wakati wa usiku! Tafadhali usije ukaingia kwenye hayo mambo!” aliendelea kusisitiza. Niliona namna macho yake yalivyokuwa yamebeba dhamira kubwa. Hakuwa anatania. Kwa muda kidogo nikapata kuwaza namna ambavyo mwanamke huyo anavyowaza kichwani mwake. Kwanini alikuwa anaongelea vile? Kwa namna moja ama nyingine nikakubaliana na nafsi yangu kuwa mwanamke huyo alikuwa ana kovu la uhalifu.
“Najua ninachofanya. Siwezi nikajihusisha na mambo kama unayoyawazia,” nikamtoa hofu.
“Unajua,” akadokeza na kusema, “Sikufahamu hata jina lako ni nani? Sijui hata wapi unatokea, ukipata matatizo utaniweka shidani … na ..” akaweka kituo kwanza. Niliona macho yake yakidondokea mezani akisema “… nitakuwa mpweke nisiye na amani.”
Nikamtazama na kutabasamu kwa mbali. Nikamshika bega lake na kumwahidi nitakuwa naye na nitamlinda kwa kadiri niwezavyo. Lakini kumtoa hofu zaidi nikamwambia kuwa nilienda kutafuta kazi na nimepata. Kuanzia siku hiyo majira ya saa tatu usiku nitakuwa natoka kwenda kazini.
“Nimelazimika kufanya hivyo, hali yetu haiwezi kuwa hivi milele,” nilimwambia nikiwa natazama macho yake. Alinishangaa kwa muda kidogo alafu akatabasamu kiuwongo.
“Unadhani hiyo ni kazi sahihi kwako?” akaniuliza.
“Sipo kwenye nafasi ya kuchagua kazi saa hii!” nikamwambia nikimshika mkono wake wa kushoto. “Tunachohitaji hivi sasa ni pesa. Tutaishije katika jiji hili pasipo fedha?”
“Najua …” akasema akiwa anatazama chini. Mara akanitazama na kuniuliza, “Utakuwa salama kweli?”
“Ndio, kwanini nisiwe?” nikamwambia kwa kujiamini. “Nitakuwa salama na wewe pia utakuwa salama, nimekwishakuahidi hilo. Umesahau?”
Hapa nikamwona akitabasamu kweli. Hakutia tena neo bali akaendelea kunywa zake chai. Yalipofika majira ya mimi kwenda kzi nikajiandaa na kumuaga. Akanisisitiza tena niwe salama. Nikamkubatia na kwenda zangu.
Nilipofika maeneo ya kazi nikaonana na yule jamaa aliyenipokea jana, yaani yule mwanaume mpana mwenye mwili niliyepambana naye. Uso wake ulikuwa mwekundu, pua yake ameifunika na bandeji. Akanitazama kwa macho ya paka na mbwa alafu akanionyeshea ishara ya kichwa. Nikaongozana naye mpaka kule kwenye ofisi ya yule mwanaume meneja. Tulimkuta akiwa ameketi kwenye kochi lake kama ada ila akiwa mwenyewe. Nadhani muda wa wale wasichana kuja haukuwa umefika au siku hiyo hakuwa na ratiba nao.
Mezani alikuwa na vileo kadhaa kana kwamba kuna tafrija ilhali yupo mwenyewe.
Huko nikapewa nguo ya kazi, tisheti nyeusi yenye maandishi meupe mgongoni, ‘SECURITY’, na pia vifaa kadhaa vya vya kufanyia kazi mathalani vifaa vya ukaguzi na pingu.
“Kuwa makini,” akaniambia yule bwana meneja. “Walinde wateja na sio uwaangamize,” akanipa angalizo kabla hajatoa ishara ya sisi kutoka humo chumbani. Tulipotoka tukaenda ndani ambapo watu walikuwa wakifurahia kwa kucheza muziki na kunywa. Huko tukasimama kana kwamba masanamu tukitazama watu wakiwa wanaburudika.
Hakika hii kazi inachosha, yaani wenzako wakiwa wanakula raha wewe umekaa kuwakodolea. Sikuwa na budi bali hivyo. Niliwakodolea kila pande mpaka mpaka pale yalipofika majira yangu ya kuondoka, saa kumi na moja asubuhi.
Nikiwa nimechoka kwa kusimama na kutembeatembea, nilipoketi kwenye basi nikajiona kama nipo peponi. Nilijihisi amani mpaka moyoni mwangu. Mwili ulipoa kabisa mifupa ya jointi ikihema.
Nilipofika nikamkuta mwanamke Katie, yule mwanamke ninayekaa naye, akiwa amekwisha amka. Alikuwa ameketi sebuleni akiwa anakunywa chai. Jina hili la Katie si jina lake halisia, nilimpachika tu kama vile ambavyo mimi nilijipachika jina la Tarrus. Niliona akitumia jina bandia litamsaidia kiusalama.
“Karibu!”
“Ahsante, mbona mapema sana?” nilimuuliza nikiketi kochini.
“Nilikuwa macho tangu saa kumi, nilidhani utakuja muda huo,” alinijibu akinitazama kana kwamba mama amtazamavyo mwanaye mpendwa.
“Uwe unalala tu!” nikamshauri. “Mimi nitarejea tu, hakuna tabu!”
Hakunijibu kitu, akatabasamu kisha akaendelea kunywa chai. Nilipotoka kuoga na kuketi naye ndipo akaniuliza ya kazini. Hali ilikuwa shwari kabisa, na kwa namna moja ama nyingine kila mmoja wetu alikuwa na matumaini juu ya siku za usoni.
Lakini siku moja …
… Nilijawa na hofu sana. Ikiwa ni siku ya tano tangu nimeanza kazi, nilikawia sana kurudi nyumbani. Ikiwa ni majira ya saa kumi na moja kabla sijatoka, meneja akaniita akitaka kuonana na mimi. Siku hiyo kulitokea na vurugu kubwa toka kwa wanaume wanne walevi lakini nikajitahidi kwa uwezo wangu kuwamudu na kuwafanya wateja wawe salama. Meneja alinipongeza kwa kazi niliyofanya na kwa kiasi fulani akajawa na mashaka juu ya uwezo wangu huo.
Kwa muda kidogo akanifanyia ‘interview’ ambayo hapo awali hakunifanyia. Nilistaajabu kidogo. Alitaka kujua wapi nimetokea na nilikuwa najishughulisha na nini. Sikutaka kumwongopea, ila ni hakika ningemwambia kuwa sina kumbukumbu yoyote, asingeniamini. Hivyo basi kwa kubuni tu taarifa nikamwambia kuwa nilikuwa mwalimu wa mojawapo ya ‘gym’ hapo jijini. Na kwakuwa tulishindwana mahesabu ndipo nikaacha na kutafuta kazi nyingine.
Basi baada ya interview hiyo nikawa nimekawia kwa kama lisaa ama masaa mawili. Nilipofika nyumbani, tofauti na vile nilivyokuwa nimezoea, sikumkuta Katie. Mahali anaponywea chai palikuwa patupu na hata mazingira ya makazi yalikuwa pweke.
Nikaita pasipo na majibu. Nikagonga mlango wa chumbani mwake pasipo mafanikio. Nilipoufungua na kuangaza, sikumwona mtu. Nikajiuliza ni wapi atakapokuwa amekwenda. Kwa usalama wake nafahamu asingeliweza kutoka na kwenda kuzurura!
Nikapekua shuka lake na kubaini kulikuwa na damu. Nilipoenda bafuni na kutazama vema, nikabaini pia kuna matone ya damu karibia na mlango huo kwa ndani! Hapa nikajawa na mashaka sana. Nikatoka na kwenda kumuuliza mhudumu kumhusu Katie lakini naye akasema hakumwona.
“Uliona mtu yeyote akiingia ndani mbali na yeye?” nikauliza.
“Hapana, sijamwona yoyote,” akanijibu na kuongezea, “Labda kama yule mwenzangu atakuwa ameona vivyo. Yeye ameondoka hapa asubuhi ya mapema.”
Mbaya mimi na Katie hatukuwa na mawasiliano, nilishindwa hata kusema nimpigie simu na kumuuliza. Nikiwa hapo ‘counter’ kidogo nikakumbuka namna ambayo inawez kutusaidia. Nikimtazama mhudumu nikamuuliza, “Tunaweza tukaangalia kwenye cctv?” nikiwa nanyooshea kidole cctv kamera ambayo imetundikwa juu ya kuta konani. Yule mhudumu akatanua lips zake na kutikisa kichwa, “Hazifanyi kazi hizo!”
Nilipotaka kulaumu nikajikuta nikikumbuka gharama ya eneo hilo. Si bure ni bei nafuu! Nikadaka kiuno changu nikiwa nawaza kweli. Je nirudi kule nyumbani kwa Katie nikamtazame? … ama niripoti polisi?
Mmmh polisi? Hapa nikajiuliza mara mbilimbili. Vipi kama rekodi yangu ya nyuma si nzuri, si nitakuwa nimejipeleka mdomoni mwa mamba?
Nikangoja kama nusu saa, nilipoona bado kimya, nikajikusanya toka kwenye kiti cha maulizo na kuusongea mlango wa hoteli niende zangu nyumbani kwa Katie. Nikiwa nimeacha mlango wa hoteli kwa kama hatua tano, nikastaajabu kumwona Katie! Kwa upande wa mashariki ya hoteli alikuwa anasonga karibu akitembea upesi.
Nilimjongea na kuzama naye mpaka ndani. Nilimweleza shaka langu naye akanijibu alikuwa ametokea hospitali baada ya kuumwa ghafla.
“... hazikuwa siku zangu lakini nilimiminikwa na damu nyingi. Nilikuja kubaini hilo wakati naamka majira ya saa kumi. Nilidhani nitarejea kwenye hali yangu ya kawaida lakini haikuwa vivyo. Niliendelea kutokwa na damu tu. Nilikungoja lakini ulikawia, hivyo nikaona niende hospitali mwenyewe.” alipomaliza kusema hayo akanitazama na kisha akasema kwa sauti ya chini, “Samahani kama nilikusababishia hofu.” sauti yake hiyo ilinifanya niwe ‘mlaini’ katika namna ya ajabu. Niliishia kutabasamu na kusema, “Usijali.” alafu baada ya kumtazama kidogo nikamuuliza,
“Sasa upo sawa?”
Akanitikisia kichwa. “Nipo sawa, nashukuru.”
Siku ikawa imeenda vivyo. Lakini, katika namna ya ajabu, kuna muda fulani nikawa nawazia safari ya mwanamke huyo kwenda hospitali. Si kwamba nilikuwa siamini kama ameenda huko, lah! Bali nilikuwa natilia shaka usalama wake.
Vipi kama huko njiani akawa ameonekana? Au kuna mtu alikuwa anamfuatilia kubaini wapi anaishi? Basi nilijikuta nawaza na kupuuzia mawazo hayo …
Nawaza na kuyapuuzia.
**
Majira ya saa tatu usiku, klabuni …
Nikiwa kwenye majukumu yangu ya kila siku, si muda mrefu tangu nimewasili, mara mwanamke fulani mrefu akanijongea na kusimama karibu kabisa na mimi. Mwanamke huyu nikamtambua kama Jolene, mwanamke anayehudumu ndani ya klabu kwa kucheza mbele za wageni na hata siku zingine kuhudumu vinywaji kwa wale wageni wenye hadhi ya juu.
Mwanamke huyu alikuwa ni mrembo haswa, mwongeaji na pia mcheshi. Sikuwa nimezoeana naye, kiuhalisia sikuwa nimezoeana na mtu yeyote hapo, aidha walinzi wenzangu ama wanawake wa ndani. Mimi nilikuwa ni mtu wa kufanya kazi na kurudi nyumbani tu, hivyo kwa kiasi fulani nilishangaa kumwona mwanamke huyo akinijongea.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Akanitazama kwa kunirembulia alafu akasema, “Hellow handsome guy!” kisha akalamba lips.
“Una shida gani, Jolene?” nikamuuliza nikimkazia macho lakini hakuonyesha woga. Akanitazama kana kwamba pipi ya kijiti alafu akauliza kwa kuninong’oneza, “nikikwambia nina shida gani utanisaidia?” nikashusha pumzi ndefu kwa pua na kusema, “Jolene, nipo kazini. Waweza kuniacha tafadhali?” akanikonyeza. Akaweka kidole chake kwenye lips zangu na kisha akakipeleka kwenye lips zake alafu akajiondokea akinong’ona, “Tuonane baadae!”
Nikabaki namtazama mpaka anaishia. Sikuwa naelewa nini mwanamke huyo alikuwa ananiwazia kichwani. Nikiwa kwenye lindi hilo, mara nikasikia sauti ya kiume ikisema kando yangu, “Kuwa makini.” nilipotazama upande wangu wa kushoto nikakutana na mlinzi mwenzangu.
“Ni demu wake Mike. Nadhani unafahamu mahusiano yako na Mike yapoje,” aliposema vivyo hakungoja hata nimuulize, akaendelea zake na doria. Mike ni yule jamaa ambaye alinipokea na kunipeleka kwa meneja, kisha niapewa usahili wa kupambana naye. Sikutaka kuwazia sana hayo mambo nikaendelea na kazi yangu.
Kwenye majira ya saa kumi na moja alfajiri, nikarejesha vifaa vyangu vya kazi na kwenda kupata maji alafu nikabadili nguo niondoke. Lakini nikiwa naondoka, nikasikia sauti ya kike ikiniita. Nilipotazama nikamwona Jolene.
“Ningoje twende wote!” alipaza sauti. Sikumngoja nikaendelea na safari yangu. Huko nyuma yangu nikamsikia akikimbia. Aliponikaribia akaniuliza, “Una shida gani, Tarrus?” alikuwa amevalia suruali ya mpira inayombana, rangi ya kijivu, na topu rangi ya pinki aliyomechisha na raba zake mguuni.
“Mbona upo hivyo?” akaniuliza akinikunjia sura.
“Kwani unataka nini Jolene?” nikamuuliza. Akashika kiuno chake na kusema, “Nataka tu nikupongeze kwa kile ulichofanya jana. Kama isingekuwa wewe wale watu wangenijeruhi!”
“Usijali, ni kazi yangu,” nikamjibu vivyo na kwenda zangu, nyuma akanifuata. Nilipofika karibia na lango ndipo nikagundua Mike, akiwa amesimama na wenzake wawili kwenye sakafu ya juu, alikuwa ananitazama kwa umakini.
***
“Jolene!” mara Mike akaita. Jolene alipogeuka na kutazama, akamwonyeshea Mike kidole cha kati kisha akaendelea zake na safari ya kunifuata. Tulikuja kuachana kwenye vituo vya basi mimi nikielekea upande tofauti na yeye. Njiani alikuwa akiniuliza maswali mbalimbali juu ya maisha yangu binafsi, wapi nakaa, nini napenda kunywa na kadhalika. Nilimjibu maswali yake hayo kwa neno moja moja tu.
Nilipofika nyumbani nikamkuta Katie akiwa ameketi kunisubiri. Siku hiyo nikajadiliana naye kuondoka mahali pale tulipokuwa tunaishi. Tunatumia pesa nyingi sana kukaa hapo tofauti na kama tungetafuta sehemu, hata kama ni ndogo, tukakaa vema.
“Ni wazo zuri, Tarrus!” akasema kwa tabasamu kisha akaniuliza ni wapi ningependelea kuishi.
“Katie, unajua fika mimi sina kumbukumbu hizo. Hata kama ningekuwa nazo bado nisingefaa kuchagua hilo. Unaonaje ukapendekeza wewe?” baada ya kufikiri kidogo akasema, “Vipi kama leo tukatembea mji huu na kuamua hilo kwa pamoja?” nikaona wazo lake ni jema. Basi nikapumzika na kwenye majira ya saa kumi kasoro jioni tukatoka kwenda kuutembelea mji tuone wapi patatufaa.
Tulifanya zoezi letu kwa kama masaa matatu, tukapata eneo moja zuri, nafuu na karibu zaidi kwa kazi yangu. Tukakubaliana na mwenye makazi kuwa malipo nitayafanya mwishi wa juma hilo, naye pasipo ajizi akanikubalia.
“Karibu sana,” akasema na kuongezea, “kama kutakuwa na mabadiliko yoyote basi mtanijuza.” tukamshukuru na kwenda zetu. Tukapitia mgahawani kupata chakula na kusogeza muda. Nilikuwa nimeazimia kupitia kazini moja kwa moja nikiachana na Katie.
Hapo tukala na kuongea kwa kama masaa mawili tena. Tulicheka na kupiga soga. Tuliteta na kunanga. Ilipowadia saa tatu ya usiku, nikaona nimuage Katie niende kazini naye aende nyumbani.
Lakini kabla sijafanya vivyo, nilihisi kuna mtu anatutazama. Mwanaume huyo mnene aliyekuwa amelaza nywele zake kwa ustadi alikuwa akitutazama kwa jicho la kando tokea upande wetu wa mashariki kusini. Sahani yake ndogo ilikuwa tupu kwa muda akijisomea gazeti.
“Unamjua mwanaume yule?” nikamnong’oneza Katie nikionyeshea ishara kwa mboni zangu za macho. Katie alimpotazama mwanaume huyo akanirejeshea uso na kutikisa kichwa. Niliona chembe za hofu usoni mwake. Sikutaka ahofie hivyo nikafanya namna ya yeye kupuuzia hayo, “Nimependa suti yake. Unadhani nitapendeza nikivaa vivyo?”
Akatabasamu na kuzungusha macho yake kutazama dari. “Kwanini umefikiria hivyo?”
Nikatabasamu.
“Kuna ubaya?”
“Hamna. Nadhani utapendeza, Tarrus. Inabidi uvae hivyo siku tukitoka tena.”
Nikatabasamu pasipo kumwonyesha meno alafu nikamtaka anyanyuke sasa twende. “Nitakusindikiza kwenda nyumbani.”
“Hautaenda kazini tena?” akawahi kuniuliza akinitolea macho yake kwa mbali.
“Nitaenda,” nikamjibu na kuongeza, “lakini nitajihisi mwenye amani nikikufikisha nyumbani.”
Basi tukajiendea zetu nikiwa makini kutazama kama jamaa yule atakuwa anatufuata. Sikumwona kabisa mpaka nafika nyumbani kumwacha Katie.
Nilipohakiki kuwa mazingira ni salama, nikajiondokea kwa kujiweka kwenye basi kwenda kazini moja kwa moja. Baada ya kuvuka vituo viwili ndipo nikamwona mwanaume yule niliyemtilia mashaka mgahawani akipanda basi hilo, mkononi akiwa ameshika gazeti lake.
Nilimtazama lakini yeye hakufanya vivyo. Aliketi kabisa mbele yangu na muda wote akawa anatazama mbele, kwa kadiri nilivyomtazama hakukuwa na muda ambapo alikunja shingo yake kun’tazama.
Basi kwasababu za kiusalama, nikaona itakuwa vema kama nikashuka kituo tofauti na kile cha kazini, endapo mwanaume huyo atakuwa ananifuata basi itakuwa rahisi kumpoteza.
Lakini je atakuwa ametufuatilia mpaka kule kwenye makazi yetu? Nilijiuliza.
Nikajongea mlangoni nikimtazama mwanaume yule. Bado hakunitazama. Nikashuka na kuanza kurusha miguu nikistaajabu kuona basi haliendi. Sikutazama nyuma. Kidogo nikahisi mtu anatembea.
Nikaongeza mwendo wangu maradufu, na baada ya kutembea kwa kama hatua thelathini nikatazama nyuma. Hapo ndipo nikakutana na yule mwanaume macho kwa macho! Alikuwa kama umbali wa hatua kumi na mbili tokea nilipo. Macho yake makubwa na mustachi mwembamba juu ya mdomo. Mkono wake wa kuume umebebelea gazeti.
Pasipo kuongea tukatazama kwa kama sekunde nne na mara mwanaume yule akapiga hatua moja kurudi nyuma na kisha akaanza kukimbia!
“Wewe ngoja!” nikabweka nikimkimbiza. Mwanaume huyo alikuwa ni mnene kwa umbo ila mwepesi haswa. Koti lake la suti pamoja na tai vilipepea akiyoyoma. Nilijitahidi kumkimbiza lakini bado akiwa ameniacha kwa umbali kiasi. Nilitumai atachoka karibuni hivyo sikukata tamaa.
Nilimkimbiza mpaka mahali ambapo niliona akizamisha mkono ndani ya koti lake la suti na punde akachomoa bunduki ndogo. Hapo upesi nikajibana kwenye ukuta, akageuka na kutupa risasi mbili kisha akaendelea kukimbia. Mulikuwa ni vichochoroni. Nilipokuja kutoka na kumfuatilia, nikawa nimempoteza! Sikumwona tena.
**
“Unakuja kazini saa hii?” ilikuwa ndiyo salamu niliyopewa na Mike. Alikuwa amesimama langoni yeye pamoja na wenzake wawili. Yalikuwa ni majira ya saa tano ya usiku.
“Kulikuwa na dharura,” nikamjibu nikitaka kuingia ndani. Akaniwekea mkono wake mpana kifuani mwangu akisema, “Si haraka hivyo!” nikamtazama kumsikiza.
“Sikia we boya, sawa? … kaa mbali na Jolene kabla sijatenganisha kiungo kimoja kimoja cha mwili wako na kumpa mbwa wangu. Tumeelewana?”
Nikamtazama kwa kama sekunde tano kisha nikasema, “Sina muda na wewe, wala huyo mwanamke wako, sawa? … alafu siku nyingine ukinifanyia huu ujinga, nitapoteza meno yako yote ya mbele. Tishia hao mbwa wako nyuma!”
Akataka kuanzisha mapambano lakini upesi wenzake wakawahi kumtuliza. “Hey Mike, huu si muda wa kufanya haya mambo! Chill!” akanitazama na uso wake mwekundu, mimi nikazama zangu ndani ya klabu pasipo kumjali. Nikabadili nguo zangu na kuchukua vifaa vya kazi, nikaanza kutazama usalama.
Nilipofanya kazi yangu kwa muda kidogo nikagundua kuna kitu hakipo sawa. Sikumwona Jolene mahali anapokuwa kila muda wa kazi. Sikujali sana lakini kadiri muda ulivyoenda nikiwa simwoni nikapata haja ya kutaka kujua.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Nikamfuata mmoja wa washirika wa Jolene na kumuuliza kumhusu mwenzake. Mwanamke huyo alikuwa ametingwa sana na kazi. Alinitazama kwa ufupi na kuniambia, “Kamtazame chumba chekundu.” kisha akaendelea na kazi zake.
Chumba chekundu ama ‘red room’ ni chumba ambacho wanawake hao wahudumu huwa wanakitumia kwa ajili ya maandalizi kabla ya kuanza kazi. Humo kuna nguo zao za kazi lakini pia na vifaa vya kujifanyia urembo.
Basi nikasonga huko, nilipofika karibu na mlango wa chumba hicho nikasikia sauti ya mwanamke ikiwa inagugumia kwa kilio. Nikagonga mara tatu kisha nikafungua mlango huo na kutazama ndani. Kwenye kona, godoroni, nikamwona mwanamke akiwa amejikunyata analia. Kwikwi zimemkaba akipambana kuvuta makamasi.
Mwanamke huyo nilimtambua kama Jolene.
Nikamjongea nikimuulizia hali yake. Hakuwa anajibu. Nilipomvuta kichwa na kumtazama, alah! Nikamwona akiwa ana majeruhi makubwa usoni na anatiririsha damu pomoni.
Nikahamaki sana na kumwonea huruma. Lakini zaidi nikapatwa na hasira. Sikumuuliza nini kilitokea kwani nilishafahamu. Nikanyanyuka na kuuendea mlango upesi! Damu yangu ilikuwa inachemka.
Kama mbogo aliyejeruhiwa nikamwendea Mike aliyekuwa amesimama nje, nikakomea mbele ya uso wake nikimtazama kwa hasira. “Nisikie wewe mpumbavu!” nikapaza sauti yangu na kufanya watu kadhaa waliokuwepo hapo nje kunitazama. “Hili ni onyo langu la mwisho kwako. Onyo langu la mwisho, sawa? … ukimgusa yule mwanamke tena, kwa namna yoyote ile, nitakuvunjavunja usiamini macho yako. Nitakufanya hata mama yako mzazi asitambue maiti yako!”
Mike akaangua kicheko mpaka kuinama akiwa ameshika tumbo lake. Anacheka sana na hata wale wenzake waliokuwa nyuma wakamuunga mkono kwa kukenua. Walipomaliza, Mike akiwa bado ana makandokando ya kicheko, akanitazama na kusema, “we fala umesemaje?” kabla sijajibu akasema haya, “Nitamfanya chochote nitakacho na hakuna yeyote atakayeingilia. Si wewe wala mdudu yeyote!”
Alipomalizia kusema hayo alikuwa amesogea zaidi karibu yangu. Kwakuwa alikuwa amenizidi urefu basi akawa anan’tazama kwa chini akiwa amefuma ndita zake. Sikuwa namwogopa abadani, zaidi alikuwa ananipandisha hasira zaidi.
Nilijitahidi kwanguvu zangu zote nisifanye jambo la kipumbavu lakini niliona stara yangu ikiniponyoka. Nashukuru kabla ya kufanya jambo, kuna mtu akaja na kutuambia tunaitwa na meneja.
Kumbe meneja alikuwa anatutazama kwa kupitia kamera wakati tukiyafanya yote hayo.
Tukatoka na kuongozana mpaka ofisini kwa meneja, huko tukamkuta mwanaume huyo akiwa anatazama video zake kadhaa ambazo zinaletewa taarifa na kamera ambazo zimesambaa maeneo mbalimbali klabuni. Pamoja naye walikuwapo wanawake watano waliokuwa wamevalia chupi pekee, vifua wazi.
Hapo tukasimama kwa kama dakika moja pasipo meneja kutuongelesha. Alikuwa anavuta sigara yake kubwa akiwa anaendelea kutazama video zake.
Mike akanitazama kwa jicho baya na kunisemea jambo kwa kunong’ona. Nami nikamtazama pasipo kusema jambo. Kwa ufupi nikatoa macho yangu kwake maana niliona ningeweza kufanya jambo ambalo ningelijutia.
Ikiwa inaelekea dakika ya pili, meneja akageuza kiti chake na kutuuliza kama tumechoshwa na kazi. Alimpa kila mtu wasaa wa kujieleza. Mike akatumia muda wake kunikanda na kugusia namna ninavyomfuatilia na kumsababishia matatizo.
Ulipofika wasaa wangu, nikaeleza kwanini nalikuwa kwenye mgogoro na Mike. Mimi kama muajiriwa wa eneo hilo nalikuwa na jukumu la kuhakikisha usalama wa watu wote, ikiwamo na wafanyakazi wenzangu, hivyo nimezama kwenye mgogoro na Mike kwasababu tu ya kutimiza jukumu langu hilo.
“... Amemsababishia Jolene majeraha makubwa. Badala ya kufanya kazi yake, sasa amejifungia akilia na kugugumia chumbani!”
Niliposema hayo nikaona uso wa meneja ukibadilika. Alimtazama Mike na kumuuliza kama niyaongeayo ni kweli, Mike akakanusha. Basi upesi meneja akaagiza Jolene afike ofisini. Alipofika akamtazama na kuthibitisha kuwa mwanamke huyo alikuwa ameadhibika. Tena si kidogo.
“Nini kimekutokea Jolly?” Meneja akauliza akimtazama Jolene kwa macho ya kuguswa. Jolene alikuwa anatazama chini, bado akiwa amebanwa na kwikwi.
“Ni Mike,” Jolene akajibu kwa ufupi. Meneja akaagiza Jolene apatiwe huduma ya kwanza upesi, na akiwa amefura akamzaba Mike kofi kali na kumwonya, “Ukirudia tena kufanya huo upuuzi wako, nitakupoteza! Nadhani unanifahamu vizuri, Mike!”
Mike hakusema jambo. Alikuwa anatazama chini mikono akiwa ameifumbata nyuma.
“Na kuanzia leo, utakuwa chini ya Tarrus, sawa?” meneja akafoka. Akamfukuza Mike atoke ofisini, nikabaki mimi na yeye pekee.
“Sikia Tarrus,” Meneja akasema akiwa anaketi. Akaweka sigara yake mdomoni na kunyonya mapafu mawili kabla hajaendelea kuongea, “Nimekukabidhi majukumu makubwa, nadhani na wewe unalitambua hilo, si ndio? …” akavuta tena sigara. Hakuwa ameniuliza ili nijibu bali ahakikishe kwamba nipo naye pamoja.
“Kama kutakuwa na tatizo basi utaniambia, sawa? Mambo mengine tutayajadili kadiri siku zinavyoenda. Ila kuanzia sasa ukae ukijua kwamba siku yoyote, muda wowote naweza kukuita kwa ajili ya ulinzi, sawa?”
Nikatikisa kichwa kumkubalia.
“Usijali,” akasema uso wake ukiwa umefunikwa na moshi wa sigara. “Hata malipo yako nitayaongeza kuwa mara mbili na sasa.” aliposema hayo akaniruhusu nikaenda zangu. Sikuona kama kazi hiyo aliyonikabidhi ni kubwa sana, lah! Niliona ni yaleyale tu ya kila uchwao mpaka pale kesho yake nilipobaini majukumu zaidi.
Mwanamke mmoja afanyaye kazi ndani ya eneo hilo, alinijia nikiwa katika majukumu yangu akaniambia naitwa na meneja ofisini. Nilipofika huko nikamkuta meneja akiwa ameketi mwenyewe, ‘amekunja nne’.
Akaniambia kuna watu watafika hapo muda si mrefu na alikuwa anataka niwe naye karibu.
“Kuwa macho, Tarrus,” aliniambia sentensi fupi yenye uzito. Nilibaini alikuwa anamaanisha anachokisema kwa namna alivyon’tazama. Nami kumwonyesha tupo pamoja, nikamtikisia kichwa na kukaa bayana.
Muda si mrefu, kama baada ya dakika sita tu tangu tuongee, meneja akasema, “wameshafika,” akiwa anatazama moja ya runinga zake. Niliporusha macho yangu kuangaza, nikawaona watu wanne wakiwa langoni. Watatu walikuwa wamevalia suti nyeusi na mmoja akiwa amevalia shati la ‘beach boy’ pamoja na bukta. Haikuwia ugumu kufahamu wale watatu walikuwa ni walinzi wakimlinda yule bwana aliyevalia bukta.
Punde meneja akaniagiza nishuke chini na kuwaongoza wale mabwana mpaka ofisini. Nikafanya vivyo, muda si mrefu tukawa wote ofisini. Bwana yule aliyevalia bukta alikaa akitazamana na meneja, walinzi wake wakiwa nyuma yake. Mimi nilikuwa nyuma ya meneja. Mtu mmoja pekee.
Wakaongea kwa muda kidogo na mara meneja akafungua mojawapo ya droo yake na kutoa mifuko miwili yenye unga mweupe ndaniye. Akaweka mifuko hiyo mezani na kumtazama yule bwana. Hakumesemesha jambo lakini walielewana. Bwana yule akavuta mfuko mmoja na kuutoboa kwa kidole chake cha mwisho kisha akatia kidole mdomoni kuonja.
Baada ya muda kidogo akamwambia meneja kuwa pesa yake itatumwa punde atakapouza kitu hicho. Akiwa anasema vivyo akawa ananyoosha mkono wake achukue mfuko wa pili wa unga, mara meneja akamdaka mkono wake na kusema, “Hapana! Sitakubali iwe vivyo saa hii!” kisha akavuta mifuko yake karibu.
“Una shida gani, G?” akauliza yule bwana akiwa ameduwaa. Akawatazama watu wake kwa mshangao na kisha akarudisha macho yake kwa meneja. “Tangu lini hauniamini?”
“Tangu ulipokaa pasipo kunilipa kwa miezi sita sasa!” akafoka meneja na kuongezea, “sasa hivi sitafanya biashara kichaa na wewe tena.”
Yule jamaa akashusha pumzi ndefu kisha akafikiri kwa muda kabla hajasema, “Sawa, nitakupa pesa ya mzigo wako uliopita, alafu huu tutaongea zaidi mbele.”
Meneja akatikisa kichwa. “Utanipa pesa yangu, na huu hautaondoka nao mpaka uulipie!”
Kidogo kukawa kimya. Walitazamana kwa kama sekunde tano alafu yule jamaa akamgusa mlinzi wake mmoja kwa kiwiko, hapa nikawa ‘attention’ zaidi, mlinzi huyo akatoa mkebe na kuuweka mezani, ulikuwa umejawa na pesa.
Yule bwana akamwambia meneja atazame hizo pesa na yeye yupo radhi kumwachia kama watakubaliana. Bado meneja akashikilia msimamo wake. Mara hii akabamiza meza kwanguvu akiwa anafoka.
“Sirudii nilichosema, Lorenzo!”
Hapa nikaona mlinzi mmoja aliyekuwa ameambatana na yule jamaa akichomoa kitu nyuma ya kiuno chake.
Nikawa ‘attention’ zaidi. Nadhani mlinzi yule hakuwa anadhani kama anaonekana. Mwangu ulikuwa ni hafifu, taa za klabu zikikatiza na kujiendea lakini kwangu bado hazikunifanya nisione kinachoendelea.
Nilimwona vema bwana yule na kwasababu za kiusalama, lile lilikuwa tishio la uhai. Haikuhitaji ujuzi mkubwa sana kubaini kwamba maongezi kati ya meneja na yule bwana, yani Lorenzo yalikuwa yanaenda kukomea kwenye kushurutishana ama kumwaga damu.
Basi kwa upesi, nikatengua kiti cha meneja na kukibeuzia kwnagu, alafu kwa wepesi wa ajabu nikamvuta meneja na kumweka nyuma yangu kisha nikakita teke kile kiti alichokuwa amekalia meneja, kiti kikaserereka kidogo tu kabla hakijanyanyuka kabisa na kuwavamia wale wajamaa wote kwa mkupuo!
Kwa haraka kabisa nikamtemngua miguu meneja kumlaza chini. Nilifanya hivyo kwasababu ya usalama wake ‘in case’ wale jamaa wakianza kufyatua risasi.
Baada ya kufanya vivyo, nikarusha macho yangu kuwatazama maadui, wanaume wawili walikuwa wamechomoa na kushikilia bunduki. Kama nisingelifanya maamuzi ya haraka basi ilikuwa bayana ningepoteza maisha yangu na ya meneja pia.
Ni upesi, ninaposema upesi namaanisha upesi haswa. Sikuwa nafahamu ni kwanini akili yangu ilikuwa inafanya kazi haraka ndani ya sekunde. Na kama haitoshi mwili wangu ukipokea maelekezo ya akili yangu na kuyafanyia kazi. Yote haya ni kwakuwa nilipoteza kumbukumbu zangu.
Laiti ningelikuwa najua kuwa mimi ni afisa wa CIA, nisingalishangazwa na uwezo wangu huo.
Nilibinua meza iliyokuwa hapo uwanjani, meza iliyokuwa inatumikia kwa ajili ya maongezi, kwa kuisigina tu na uzito wa guu langu alafu nikaidaka meza hiyo na kujikinga nayo. Risasi kama nne zikatupwa. Ni kheri meza ile ilikuwa ngumu sana, haikupenyeza ncha yoyote ya risasi.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Haraka nikawasogelea wale maadui nikiwa na nilipowakaribia nikawatupia meza ile kwanguvu. Upumbavu wakaidaka. Nisijiulize mara mbili nikajitupa juu na kuachanisha mapaja yangu nikituma teke la haja, likakita meza na kuwatupia kando! Bunduki pembeni.
Wanakuja kuamka, tayari nimewaweka chini ya ulinzi. Punde wakafika na walinzi wengine wa klabu kuja kuhakikisha usalama. Wakakuta mambo yote yapo ndani ya kiganja.
Wakawatia kambani maadui wale na kwa maelekezo ya meneja wakawamaliza kwa kuwamiminia risasi isipokuwa bwana Lorenzo peke yake.
“Namhitaji akiwa hai,” alisema meneja akijifuta jasho kwa leso yake ya pamba. Wale waliouawa ikatoka agizo wakatupiwe baharini.
“Well well well, bwana Lorenzo, ni nini ulikuwa unataka kufanya?” akauliza meneja akiwa anamtazama Lorenzo aliyekuwa amejawa na shaka kiasi. Macho yake alikuwa ameyakaza lakini ukiyatazama vema kwa ndani alikuwa na hofu.
“G, tufanye yameisha sawa?” akasema Lorenzo. “Umeshapata pesa zako, nadhani tumemalizana.”
“Tumemalizana?” akastaajabu meneja. “Tunamalizanaje na ulikuwa umekuja hapa kunipora? Deni langu halikukutosha Lorenzo, sio?”
Nikamtazama Lorenzo. Hakusema jambo. Meneja akasimama na kumshika nywele zake kwanguvu, “sikia! Utalipa kwa haya uliyoyafanya. Utalipa mara tatu zaidi, Lorenzo. Umenisikia? Sidhani kama ungetaka habari hizi zimifikie Don Cartel.”
Nikamtazama zaidi bwana Lorenzo, kwa namna fulani alikuwa kama mtu aliyekosa cha kusema kwa kuchanganyikiwa. Hakuwa sawa.
Baada ya kama nusu saa meneja akaachana naye akimuhifadhi kwenye chumba cha chini kisha akaniita na kuwa na maongezi machache pamoja naye.
“Tarrus, leo umefanya kazi nzuri sana. Umenifurahisha hakika. Sasa niambie ni kiasi unataka nawe ukafurahie leo.”
“Usijali, mkuu,” nikamtoa hofu. “Nilikuwa natimiza kazi yangu tu.”
“Najua hilo, kwani kuna ubaya endapo nikakupatia zawadi?” akaniuliza akiwa anafungua ule mkebe wa Lorenzo. Mkebe uliokuwa umejawa na pesa.
“Chochote utakachonipatia nitashukuru,” nikamwambia na kuongezea, “maana ni nje ya ujira wangu.”
Sikufahamu ni kiasi gani alikitoa kwa ule muda. Alinipatia vufurushi viwili vya pesa na kuniambia nikatumie nitakavyo, na kama haitoshi akaniambia nimchukue mwanamke moja wa kwenda kulala naye siku hiyo.
“Hapana, inatosha hiki ulichonipa,” nikashukuru nikitabasamu kwa mbali.
“Kweli?”
“Yah! Inanitosha sana tu.”
Akan’tazama kwa sekunde tatu kisha akatikisa kichwa chake na kuniruhusu niende zangu. Nikahifadhi pesa nilizopewa na kisha nikaendelea na majukumu yangu ya kila siku.
Nilipofika ukumbini wenzangu walinipongeza sana kwa kazi niliyofanya. Niliona kila mtu akinitazama kwa tabasamu na kunipatia ishara ya pongezi. Nilikuwa maarufu ghafla hata kwa baadhi ya wateja.
Lakini nilifahamu wazi swala lile halikumpendeza Mike na wenzake wawili. Walin’tazama kwa macho makavu yaliyojawa na husda.
Sikuwajali.
Asubuhi na mapema nikarudi nyumbani na siku hiyohiyo ndipo tukahama na Katie kwenda kwenye makazi mapya yaliyokuwa bora zaidi. Kila mtu alikuwa na furaha sana. Samani zilikuwa za kupendeza na hata mandhari.
“Sikutaraji kabisa!” alisema Katie akiwa amewekea viganja vyake mashavuni kwa mshangao. Alinikumbatia mara kadha wa kadha. Sikuwahi kumwona akiwa na furaha kiasi kile.
Baada ya kula na kuongea kidogo, nikapumzisha mwili kwajili ya kupata nguvu ya kutenda kazi baadae, lakini nikiwa katikati ya mapumziko yangu hayo, nikahisi mtu akinijongea karibu. Kidogo nikahisi kiganja cha mtu kikinipapasa mgongoni.
Kikipanda juu mpaka kushuka chini karibia na kiuno. Nilipofungua macho yangu kuangaza, nikamwona Katie. Alikuwa amevalia ‘top’ nyepesi ya kulalia ambayo ilisadifu kifua chake ambacho hakikuwa haba.
Macho yake yalikuwa yamelegea na mdomo wake ameuweka wazi kana kwamba amebanwa na mafua.
Hakusema jambo. Nami sikusema jambo. Tulitazamana macho yetu yakisema kila kitu. Sikujua nini kilitokea, nilijikuta nipo mdomoni mwa Katie huku nikiwa nimeuficha mwili wake kwenye mikono yangu mipana.
Alinibusu kwa ustadi na kunishika kiutaalamu. Huwezi amini hatukuongea mpaka lilipotimia lisaa limoja na nusu tena mimi na yeye tukiwa tunatazama kwa macho yaliyo hoi.
“Ilikuwa ni ndoto yangu, Tarrus,” alisema kwa sauti ya puani.
“Kwanini haukuwahi kusema?” nikamuuliza.
“Hauoni kama matendo yanaongea mengi?” akasema kisha akatabasamu na kunibusu, baada ya hapo tukapumzika kwa pamoja mpaka pale nilipokuja kuamka saa mbili usiku. Ulikuwa ni muda sahihi wa mimi kujiandaa kwenda kazini.
Nikamuaga Katie lakini kabla sijaondoka akanitaka nimbusu na kumkumbatia. Nikafanya vivyo na kisha nikaenda zangu. Sikujua kwanini ila siku hiyo nilijihisi mwenye furaha sana.
Nilipofika kazini nikaendelea na majukumu yangu kidogo nikaitwa na meneja ofisini kwake. Alikuwako na wanaume wawili. Aliniambia nimngoje kwa muda kidogo nje ya mlango, na kweli kama baada ya dakika sita, akatoka na kuniambia niongozane naye kwenda kwenye gari. Alikuwa pamoja na wanaume wale wawili.
Tukafika kwenye gari, mimi nikaketi nyuma pamoja na mwanaume mmoja, na kule mbele akaketi meneja na jamaa mwingine. Tukatembea kwenye gari kwa kama lisaa hivi tukikomea kwenye jengo la ghorofa chache. Hapo tukashuka na kuzama ndani.
Humo palikuwa patulivu sana. Sakafu ya chini haikuwa na watu, nadhani japo sikuwa na uhakika. Mwanga wake ulikuwa ni hafifu rangi ya bluu. Sakafu ya pili ilikuwa na watu kadhaa waliokuwa wamesimama kiulinzi.
Sakafu ya tatu kulikuwa kumechangamka. Muziki ulikuwa unapigwa na watu kadhaa, kama vile ishirini na tano, wanaume wachache na wanawake wengi, wakicheza hapo taratibu.
Nilijaribu kwa kadiri ya uwezo wangu kukagua mazingira yale kila nilipopata nafasi. Tukaendelea kusonga na kuja kukomea kwenye sakafu ya nne na ya mwisho. Hapo kulikuwapo na uwanja wenye ukubwa wa wastani, meza kubwa pamoja na wanaume wanne waliokuwa wameketi.
Mwanga wake haukuwa mkali sana wala uliopooza. Ungeweza kumwona kama ungemtilia maanani.
Meneja akasalimiana na wale wenyeji kisha akaketi. Punde kidogo wakawa wanaongelea kuhusu biashara yao ya madawa. Sikuwa napenda kazi hii lakini sikuwa na budi. Nikiwa hapa nikawa nawaza zangu kichwani nifanye namna ya kujipatia pesa za kutosha na kisha nikaendelee na maisha yangu mengine.
Nikiwa hapo nawaza vivyo, nikabaini kuna mmoja wa wale wenyeji alikuwa akin’tazama sana. Nilipomtazama mtu huyo akaondoa uso wake kwa haraka toka kwangu ila tangia hapo nikawa nimemweka kwenye mazingatio.
Nilimtazama na kujiuliza pasipo majibu mpaka pale tulipomaliza kilichotuleta na kurudi kwenye gari. Tuliwaacha watu wale wawili njiani alafu mimi na meneja tukaongozana mpaka kule klabuni.
Nikamfikisha meneja kwenye ofisi yake lakini nilipotaka kuondoka, akaniita kwa sauti ya wastani na kuniagiza nivue shati langu. Sikuelewa ni nini anamaanisha japo sikumuuliza. Nikavua shati na kumtazama.
“Vua na suruali,” akaniagiza tena akipandisha kichwa chake. Hapo nikasita kidogo. Nikamtazama meneja kwa macho ya maulizo pasipo kusema jambo. Akarudia agizo lake. “Vua suruali, Tarrus. Unadhani mimi shoga?”
Basi nikavua suruali na yeye akasimama kunijongea. Akanitazama mguu wangu mpaka mapajani na kukomea kiunoni, kisha akan’taka nijiveshe nguo zangu na nisimame kumtazama. Nikafanya vivyo.
“Tarrus,” akaniita na kuniuliza, “Una hakika wewe ni mwaminifu kwangu?”
Kabla sijafikiria vizuri, nikamjibu, “Ndio, nina uhakika.”
Akawasha sigara yake na kuvuta pafu moja tu, alafu akasema kuhusu kile alichotoka kunifanyia ya kwamba alikuwa anataka kuhakiki kama kile alichokisikia kuhusu mimi ni kweli ama lah.
“Kitu gani hicho?” nikamuuliza kwa hamu.
“Usijali, kaendelee na kazi yako,” alisema akin’tupia mkono kwenye mwelekeo wa mlango. Punde kidogo simu ya mezani ikaita. Nikamtazama kwa muda mfupi na kisha nikajiondokea nikisonga taratibu.
Nikaurudishia mlango wa ofisi lakini kabla sijauacha kwa mbali, nikapata wazo la kuskiza kile ambacho meneja atakuwa anaongea simuni.
Nikasonga mlangoni na kuweka sikio.
“ … Najua cha kufanya … hapana! Sikia, sikia … sikia, najua nini nifanye na kwa muda gani, sawa? …” aliposema hayo akaibamiza simu mezani. Mimi sikukaa tena nikaondoka zangu kushuka chini.
Nikiwa naendelea na kufanya kazi yangu, nikawa nawaza sana juu ya ile safari ya meneja na ukaguzi wake. Nilihisi kuna kitu hakipo sawa. Niliwaza sana na mwishowe nikaamua kupuuzia nisije kujiumiza kichwa.
Kwenye majira ya saa tisa nikaonana na Jolene na kumuulizia hali yake. Alikuwa anendelea vema japo bado hakuwa amerudi kwenye majukumu yake. Alinishukuru tena kwa kunikumbatia na kunibusu.
“Nina zawadi yako, Tarrus,” alisema akin’tazama kwa macho ya furaha.
“Zawadi gani hiyo? Mbona haukun’letea mpaka nije?”
“Nilipanga kukupatia lakini kwasababu umekuja mwenyewe, sina budi kukupa,” alisema akitabasamu. Nami nikanyamaza nikingoja zawadi hiyo.
Punde nikamwona akirejea na chupa kubwa nyeupe yenye kileo cha vodka, akasema, “Ona nimekuletea mpenzi mkubwa kabisa. Natumai utakuwa na wakati mzuri sana pamoja naye!”
Nikatabasamu na kumweleza kuwa mimi si mnywaji. Akastaajabu, “Alah! Bwana Tarrus wewe ni mtu wa aina gani? Haunywi wala haupendi wanawake?”
Nikatabasamu na kumuuliza, “Nani kakuambia sipendi wanawake?”
Akaguna. “Kwani hilo ni mpaka useme, si laonekana tu? … sikia,” akasonga karibu na mimi na kusema, “tangu nifanye kazi hapa hakuna mwanaume ambaye hajawahi kunitaka, isipokuwa wewe. Najisogeza na kujipendekeza lakini haushtuki! Ajabu.”
Nikatabasamu nisiseme jambo. Akan’tazama kwa jicho la pembeni na kuniuliza taratibu, “Tarrus, wewe ni shoga? Siulizi kwa ubaya wala kukuvunjia heshima. Nataka tu kujua.”
Kabla sijajibu nikafikiria hilo neno alilosema nalikuwa nakutana nalo kwa mara ya pili sasa katika siku moja ndani ya masaa machache. Sikuonyesha kukasirika nikamjibu kuwa mimi si shoga na wala sina hisia hizo.
Basi akanilazimu sana nipokee zawadi yake kwani hakuwa na kitu kingine zaidi ya kile. Alin’tazama kwa macho ya huruma kana kwamba mtoto anaomba peremende. Nami nilipomtazama kwa muda kidogo nikaguswa naye, sikuona haja ya kumvunja moyo.
“Sawa, nitaichukua.”
Akafurahi sana. Saa kumi na moja ilipowasili nikaibeba chupa hiyo na kurudi nayo nyumbani.
“Katie, ona nilichokuja nacho!” nilipaza baada ya salamu. Nikatoa chupa ile kubwa ya vodka na kumwonyeshea nikiwa natabasamu.
“Wow!” akakodoa macho akisonga upesi. “Leo tutakuwa na tafrija eenh?”
“Nadhani,” nikamjibu na kumuuliza, “Utakunywa?”
“Kwanini nisinywe!” akajibu upesi. Sidhani kama alilifikiria swali langu, ila baada ya muda kidogo akan’tazama kama mtu aliyejishtukia na jibu lake, akaniuliza kwa sauti ya chini, “Wewe je? Utakunywa?”
“Nitakunywa nawe,” nikamjibu akafurahi. Basi nikala na kupumzika kidogo alafu baadae Katie akanipatia kile kinywaji akiwa amechanganya na juisi ya matunda aliyotengeneza kwa mkono wake.
Tukanywa sana na mwishowe tukaishia kujitupia kitandani na kufanya mapenzi yasiyokuwa na mwisho.
Kwa ulevi wangu nikapitiliza mpaka muda wa kazi. Nilikuja kuamka majira ya saa sita usiku, napo kichwa kikiwa kinanigonga sana. Nikajitahisi kunywa maji mengi na kisha nikarudi tena kitandani. Nilikuwa sijiwezi.
Asubuhi tulipoamka nikamweleza Katie yale yote yaliyon’tokea. Akacheka sana na kuniambia namna ya kufanya endapo siku nyingine ikinitokea hali kama hiyo.
“Hakutakuwa na siku nyingine, Katie!” nikamwambia nikitikisa kichwa. “Sitakunywa tena mimi. Si kwa mateso yale.”
Basi nikatumia siku nzima kuwa naye mpaka usiku muda wa kwenda kazini. Nilipofika na kusalimu wenzangu ndipo nikapashwa habari kuwa usiku wa jana yake walikuja wanaume wawili kuniulizia.
Kwa mujibu wa taarifa, wanaume hao hawakuketi baada ya kuambiwa sipo, na wala hawakuaga.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
“Walikuwa wanaonekanaje?” nikauliza. Wakanielezea lakini nisiambulie kitu. Hakuna niliyekuwa namfahamu.
Nikiwa najiuliza, nikaletewa ujumbe kwamba nahitajika ofisini kwa meneja.
***
*NYUMA YAKO --- MWISHO WA MSIMU WA KWANZA
ENDELEA KUFUATILIA MSIMU WA PILI
0 comments:
Post a Comment