Simulizi : Nyuma Yako (4)
Sehemu Ya Tano (5)
Alihangaika sana lakini hakuna mtu aliyehangaika naye mpaka walipofika mahali walipokuwa wanaelekea, ngome. Humo gari likasimama na Abdulaziz akashushwa na kuzamishwa ndani. Akawekwa kitini na kisha akafunguliwa kinywa sasa.
“Mtajuta kwa hiki mnachofanya!” akafoka. “Nitawakatakata na kuwatupia simba wangu wa uani!”
Aliendelea kuropoka na kutoa vitisho. Akijitangazia cheo chake na madara yake lakini hakuna mtu aliyekuwa anahangaika naye zaidi aliambulia kofi alilokandikwa na kitako cha bunduki, akatema damu!
“Funga bakuli!” Marshall akamwamuru kisha akavuta kiti karibu na mateka wake.
“Sikia, sina muda wa kupoteza hapa, sawa? Kwahiyo jiepushie maumivu zaidi kwa kunipa ninachokitaka. Sioni shida kukukandika ngumi mpaka uso wake ubadilishe rangi, kwahiyo kuwa na hekima.”
Abdulaziz akacheka. Kinywa chake kilichokuwa kinatiririsha damu kikamwaga mchuzi zaidi.
“Wamarekani wote watabusu matako yangu!” akacheka tena kati ya maumivu na kisha akaendelea kutusi basi Marshall akaghafirika na kujikuta akimkanda Abdulaziz ngumi kubwakubwa nzito mpaka mwanaume huyo akapoteza ‘mtandao wa kichwa; kwa muda kidogo.
“Inatosha Marshall!” Marietta akaingilia. Aliudaka mkono wa Marshall uliokuwa unaendelea kumwadhibu Abdulaziz. “Kwanini tusitumie tu njia nyepesi ya kumnyesha dawa?”
“Hastahili njia nyepesi huyu mshenzi!” akasema Marshall. Akavuta pumzi ndefu kujipoza kabla hajasonga nyuma.
Abdul alikuwa anavuja damu nyingi sana usoni. Kwa hali hiyo asingeweza kuongea hivyo basi wakampatia mapumziko kabla ya baadae kumrejea tena.
Huko ndani na nje ya jiji wanajeshi wakawa wanakatiza huku na kule wakifanya doria. Mara kadha walisimamisha magari na kuwauliza watu maswali kadhaa,hata pia walikuwa wanaingia kwenye baadhi ya makazi ya watu kufanya ukaguzi.
Lakini hawakuwa wanasema ni nini wanatafuta. Ilikuwa ni siri.
“Muda umeshafika,” alisema Marshall. “Hatuna muda zaidi wa kungoja, nadhani mnalijua hilo. Hatupo salama hapa.”
Alikwishakwapua dawa yake mkononi. Basi akamjongea Abdulaziz na kumnywesha kisha akamwamsha. Baada ya kama dakika tano, akaanza kumuuliza bwana huyo maswali. Pasipo kudhamiria, Abdulaziz akajikuta akiweka kila kitu bayana.
Alieleza wapi ambapo mlengwa wao yupo na yu katika hali gani. Basi baada ya hapo, Marshall pamoja na wenzake wakawa wameshapata wanachotaka lakini bado hawakumwachia Abdul. Wakamweka kwenye gari na kwenda moja kwa moja kule ambapo pameelekezwa.
Lakini haikuwa rahisi. Mji mzima ulikuwa umetwaliwa na wanajeshi. Walifanya namna ya kukwepa njia kuu lakini bado kazi ilikuwa mbombo ngafu, na ukizingatia wana mwili wa Abdul basi ndo ikawa tabu mara tatu yake.
Walipotembea kwa kama robo saa wakasimamishwa na wanajeshi kumi waliokuwapo barabarani. Gari likaamriwa liegeshwe kando upesi.
Mahmoud, ambaye alikuwa ni dereva, akatii amri na kuegesha. Kwenye viti hivyo vya mbele alikuwapo yeye na Kelly tu na huko nyuma hakukuonekana watu. Mahmoud akajitambulisha na pia akamtambulisha Kelly kama mkewe.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Kelly alikuwa amejilaza akionekana hoi. Macho yake yalikuwa yanarembua na kinywa chake kilikuwa wazi. Alikuwa anaonekana amechoka sana, hajiwezi.
Wanajeshi wakataka kukagua gari.
“Tafadhali maafisa,” akasema Mahmoud. “mke wangu yu hoi anaumwa. Naombeni nimwahishe hospitali asije akatufia hapa.”
Alipomaliza kauli yake tu, Kelly akashindwa kujizuia kutapika. Alirushia matapishi kioo cha mbele kana kwamba bomba, hali hiyo ikawashtua wanajeshi ambao walitazamana kwa mshangao. Upesi wakawaruhusu watu hao waende kupata matibabu.
“Kelly, upo sawa kweli?” aliuliza Mahmoud akiwa amekanyaga pedeli ya mafuta. Gari lilikuwa linanuka sasa.
**
Walienda kwa mwendo kidogo kabla ya kusimama kumpa nafasi Kelly. Alikuwa anaumwa. Hakuwa anajisikia vema kabisa. Macho yake yalikuwa yaamelegea na mwili wake umepungukiwa na nguvu.
“Utaweza kweli kwenda kufanya misheni?” akauliza Marietta akiwa ameuweka mkono wake kwenye bega la Kelly. Mwanamke huyo pamoja na Marshall na Danielle walikuwa wamejificha nyuma ya gari na kufunikwa na shuka jeusi wakati wa ukaguzi.
Basi baada ya Kelly kujisikia vema wakatoka naye na kwendelea na safari. Mwanamke huyo alisema atajikaza na atakuwa sawa tu. Wakatembea barabarani kwa kama nusu saa kabla ya kufika eneo walilokuwa wamekusudia. Hapo walipoambiwa ndipo kuna mwili wa mlengwa wao.
Marietta akashusha pumzi akitazama jengo hilo. Aliamini litakuwa ndilo la mwisho kabla ya kumtia machoni mpenziwe. Baada ya kulikagua kwa sekunde kadhaa wakashuka, isipokuwa Mahmoud, sasa wakiwa wamejiandaa kimapambano ya vita. Kila mmoja wao alikuwa amebebelea bunduki.
Jengo lilikuwa lipo kwenye ulinzi mkali wa wanajeshi kadhaa. Haikuwa inajulikana kwa watu nini wanajeshi hao wanalinda hapo. Ilikuwa ni ‘verified restricted area’. Marshall pamoja na wenzake wakajigawa upanda na kuweka ‘target’ yao katikati, mashambulizi yakaanza.
Walikuwa vema. Na kwasababu walikuwa ndo wavamizi basi maadui zao hawakuwa wamejiandaa vema kuwapokea. Waliwatupia risasi na kuzama ndani ya eneo baada ya kukata nyaya na sinyenge zilizokuwa zimepachikwa juu ya kuta.
Wakawatekeza walinzi na kwenda taratibu kwa tahadhari, hatimaye wakazama kabisa ndani, kulikuwa kukubwa, wakagawana mwelekeo kila mtu akienda na njia yake. Ndani ya muda mfupi wakawa wamewateketeza walinzi karibia wote ingali wao wakiwa salama salmini.
“Ni lile lango!” akasema Marietta akinyooshea kidole upande wao wa mashariki. Wakasonga huko kwenda kukutana na chumba kilichozibwa na mlango mkubwa wa chuma. Hapo ikawapasa wapate namna ya kuzama humo. Mlango ulikuwa unafunguliwa na alama ya kidole.
“Tumtumie huyo mlinzi!” bwana Marshall akapendekeza akiwa anamtazama mlinzi aliyekuwa amelala mfu kwa pembeni yao.
**
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
“Mkuu, unadhani watakuwa wapi?” aliuliza mwanajeshi akimtazama bwana Masoud. “Tumetafuta kwa masaa sasa lakini hamna mrejesho.”
Masoud alikuwa ametulia kwa mawazo. Alikuwa anatafakari mambo kichwani. Kidogo wazo kubwa likamjia na kuwaamuru wanajeshi wake wote waongozane naye. Bwana huyo aliwaza kama wamarekani watakuwa wamemteka bwana Abdul basi watakuwa wamempeka wapi?
Moja kwa moja mawazo yake yakaelekea kule kulipokuwa na mateka wao - mateka wa Abdulaziz. Wamarekani hao watakuwa wanataka kumkomboa mtu wao kisha watoroke.
Basi magari pamoja na pia helikopta za kijeshi yakaelekea huko kwa wingi. Vyote vilikuwa kwenye mwendokasi mkubwa.
**
“Upesi! Upesi!” Marshall alisihi. Mwanume huyo alikuwa amemweka mtu mongoni akiwa ana ‘trot’, nyuma yake alikuwapo Marietta, Danielle na Kelly.
Watu hao walikimbia mpaka kufikia mahali Mahmoud alipoegesha gari. Mahmoud alipoona wenzake naye upesi akashuka kusaidizana na Marshall. Wakauweka mwili aliokuwa ameubeba Marshall mgongoni alafu wakajipaki garini.
“Yu mzima?” Mahmoud akauliza.
“Ndio, ila yupo hoi sana!” akajibu Marshall. Gari likatimka na wasifike mbali mara taa kubwa ikawamulika tokea juu. Tayari helikopta za kijeshi zilikuwa zimewasili. Isichukue muda, risasi zikaanza kutupwa kufuata gari hilo. Kwakuwa risasi zilikuwa zinatoka juu basi zilikuwa kana kwamba mvua.
“Usifyatue risasi hovyo!” Masoud akapaza kwenye ‘radio call’. Yeye alikuwa kwenye gari linaloenda kwa kasi. “Labda Abdulaziz yupo humo, usifyatue risasi kwa fujoo!”
Basi baada ya amri hiyo risasi zikaacha kutupwa na helikopta mbili sasa kwa idadi zikawa zinawafukuzia wakina Marshall kimyakimya. Magari nayo yalikuwawa yanasogea kwa ukaribu zaidi.
“Sasa tunafanyaje?” akauliza Kelly. Mambo hayakuwa mambo kabisa. Usalama wao ulikuwa hatarini. Ni kama vile kila mtu alikuwa ameshikwa na kigugumizi.
“Yatupasa tuwashambulie,” akasema Marshall. Kwake hakuona kama kuna njia mbadala kwani maadui walikuwa wanawasogelea zaidi.”Bwana Mahmoud mpatie Danielle usukunai tafadhali, sisi wengine yatupasa tupambane sasa.”
“Lakini tutawezaje kupambana na watu wengi vivyo?” Marietta akauliza. Uso wake ulikuwa umejawa na shaka. Danielle akamtazama na kumwambia itakuwa rahisi kufanya vivyo tofauti kabisa na mawazo yao kwani wale wanajeshi watakuwa wanahofia kuwashambulia.
“Kwanini?” Marietta akauliza.
“Kwasababu Abdulaziz yupo humu. Kama hawajui basi tuwajuze hilo,” Danielle akatoa maelezo. Punde akakabia usukani na Marshall akapasua kioo cha nyuma na kuonyeshea mwili wa Abdulaziz. Sababu mwanga wa helikopta ulikuwa mkubwa hivyo mwili ulionekana vema.
“Mkuu, mwili wa Abdulaziz upo ndani ya gari! Upo ndani ya gari, over!” alisema bwana aliyekuwapo kwenye helikopta, basi bwana Masoud akata agizo gari hillo lisishambuliwe ili kuulinda usalama wa kiongozi wao.
Lakini kinyume na matarajio yao, wakaanza kushambuliwa na wakina Marshall. Kwa ustadi kabisa bwana Marshall akazidungua helikopta zote mbili kwa risasi nne tu! Helikopta ziliyumbayumba na kugongana na kisha kuangukia magari yaliyokuwa yanaongozana nayo. Magari matatu yakalipuka papo apo, na matatu yakavamiana na kugongana vibaya.
“Tazama! Tazama!” Masoud alibwatuka kumwonyesha dereva wake kigingi cha gari mbele yao. Dereva alikikwepa wakaendelea kusonga mbele. Ni magari nane tu ndo yalifanikiwa kutoka salama na kuendelea kuwafukuza wakina Marshall.
Nayo magari hayo yakakumbana na shurba za risasi haswa. Marshall, Kelly na Mahmoud walikuwa wanatumia risasi zao vema kufyatua na kubangua. Walichokuwa wanakifanya ni wengine wakiwa wanelenga vioo vya magari, Marshall yeye alikuwa analenga sehemu za kuhifadhia mafuta.
Kila alipotupa risasi mbili alikuwa anaangusha gari. Muda si mfupi, yakabakia magari mawili tu yakiwa yanazungusha matairi.
Bwana Marshall akatoa kurunzi kubwa iliyokuwapo nyuma ya gari, akawamulika wale waliokuwa wanawafuata na kuwafanya wapoteze mwelekeo kabisa. Madereva hawakuweza kumudu mwanga mkali wa kurunzi, basi wengine wakagongana na kuumizana.
Dereva aliyekuwa anamwendesha bwana Masoud yeye akasimamisha gari kwa usalama. Zaidi Risasi zikatupwa kutoboa kioo cha gari hilo na kummaliza dereva mara moja. Ni kheri bwana Masoud yeye aliwahi kuinama na kujiweka salama zaidi.
Baadae Masoud alipokuja kuamka, hakuweza tena kuendelea. Alikuwa ameshindwa. Hakuamini macho yake alipotazama kando na nyuma yake, watu walikuwa wamejeruhiwa vibaya hata kufa. Alikuwa amepoteza wapambanaji wengi sana.
Kwa hasira akapaza sauti kuu atoe mzigo wa ghafira kifuani mwake.
**
Bada ya masaa manne…
“Ngoja tuone,” alisema Danielle. “Nadhani ataamka.”
Mwanamke huyo alikuwa ametoka kumtazama mlengwa wao waliyetoka kumwokoa. Kwasababu alikuwa ana taaluma hafifu ya mambo ya uuguzi, alitumia karama hiyo. Mlengwa wao alikuwa amekonda sana, afya yake ilikuwa imedorora kweli. Ni wazi alikuwa hapewi chakula ama basi hakuwa anakula kwa kusudi.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Kumtazama ilikuwa yataka moyo.
“Itachukua muda gani kuamka?” Mariett akauliza.
“Sijajua. Tumpe muda kidogo. Mwili wake ulikuwa na upungufu wa maji sana,” Danielle akaeleza. Basi baada ya muda kidogo, kweli, mgonjwa akaamka. Basi kwanza Marietta akapewa nafasi ya kwenda kuonana na kuongea na mumewe kabla ya yeyote.
Ikapita kama dakika kumi, mara Marietta akatoka ndani ya chumba na kuja kukutana na wenziwe. Uso wake ulikuwa na tembe za shaka.
“Hakumbuki kitu,” akasema mwanamke huyo. “hakumbuki chochote. Si mimi wala si Marekani. Hamna kitu anajua!” Marietta akaanza kulia.
Ilikuwa ni ajabu kidogo, kwa uhakiki Marshall na pia Danielle wakaenda kumwona mlengwa wao. Na kweli wakagundua hakuwa na kumbukumbu yoyote ile! Kila mtu kwake alikuwa mgeni asiyemtambua!
"Huenda wakawa wamempatia madawa?" Marietta akauliza. Alikuwa na hofu. Vipi kama mumewe hatokumbuka tena kitu milele yake? Atakuwa vivyo mpaka lini?
Walifikiri na hakukuwa na namna ya kufanya isipokuwa tu sasa wafikirie kumsafirisha bwana huyo kwenda Marekani. Huko kwa ubora wa tiba lakini pia kwa nafasi yake atapata huduma upesi na kurejea kwenye hali yake.
Lakini ni wazi hilo halikuwa jambo jepesi hata kidogo. Ni katika siku hiyohiyo nyakati za usiku, wakasikia geti likigongwa kwanguvu. Walikuwa ni wanajeshi wa doria!
Upesi walitoka ndani ya eneo kwa kuuruka ukuta. Marshall alikuwa amemweka mume wa Marietta mgongoni mwake, ingali Mahmoud yeye alikuwa amebebelea mwili wa Abdulazizi. Hawakuwa wanauacha maana ulikuwa muhimu sana kwenye swala la usalama.
Walipotua upande wa pili, wakakimbia lakini wasifike mbali milio mingi ya risasi ikaanza kuwafuata. Ni Mahmoud ndiye alikuwa amekaa kwa nyuma akiwa amembeba Abdulaziz.
Mwanaume huyo alitifuliwa risasi ya mguu akapiga yowe kali la maumivu. Kabla hajasaidiwa, zikatupwa tena risasi mbili lakini kheri hazikumpata na badala yake zikazama kwenye mwili wa Abdulaziz!
Upesi Danielle akasimamisha gari kwa kutumia tundu la bunduki kisha wakakwea humo watimke. Mahmoud alijikongoja kufuata gari walilozama wenziwe, lakini asitimize adhma, akatunguliwa risasi ya kichwa!
Mahmoud alikuwa amefia papo hapo asiombe hata maji. Kwakuwa alishafika karibu na gari, Marshall akafanya jitihada kuvuta mwili wa Mahmoud pamoja pia na wa Abdulaziz huku gari likienda zake.
Gari likashambuliwa sana na risasi. Nalo lilipoenda kwa kama umbali wa wa robo kilometa tu, ajabu likatokea gari kubwa upande wao wa kushoto na kuwabamiza kwa mbele. PUUH!!
Gari lilikuwa limechakaa. Mbele kwenye boneti palikuwa panafuka moshi mzito na panakoroma! Pamefunuka na kupindapinda.
Waliokuwemo ndani; Marshall, Marietta, Kelly, Jack na Danielle, walikuwa hoi kwa maumivu lakini wakiwa wazima. Danielle aliyekuwa ndiye mshika usukani yeye alikuwa anavuja damu kichwani, si kwa wingi sana.
Ni kheri gali hilo halikuwa limebamiza walipokuwa wameketi bali tu sehemu ile ya mbele.
Basi Danielle akarudisha gari nyuma na kulitengenezea kisha akalikimbiza kwa fujo kana kwamba ni jipya toka kiwandani. Tairi la kushoto la mbele lilikuwa linaonekana lote mpaka na shina zake zilizoshikilia.
Hapa ndo' Danielle akaonyesha umwamba wake kwenye usukani. Akaonyesha dhahiri kwanini bwana Marshall anapendelea kumpatia nafasi ya kushika usukani.
Alitimua haswa kuelekea baharini. Wale waliokuwa wanamfukuza wakapata changamoto haswa kumtia nguvuni. Mwanamke huyo alikuwa anacheza na magari mengine barabarani akiyasukuma ama kuyachokoza kama anayagonga ili apate kuwaziba wanaomfuata.
Kwenye kona alikuwa mahiri kwa kwenda mzima pasipo kukanyaga pedeli ya breki, na pia alikuwa mashuhuri kwenye kuyakwepa magari barabarani kwa ustadi.
Ndani ya nusu saa, akawa ameshawaacha kabisa walokuwa wanamkimbiza. Akatimba baharini na huko wakateka boti kubwa ya kutorokea.
"Hii itatuondoa hapa upesi!" Akasema Marshall.
Basi akaiwasha lakini kabla hajaondoka akastaajabu kumwona Marietta na Kelly wakiwa wamesimama upande mmoja wakiwatazama. Kufumba na kufumbua Marietta akawanyooshea bunduki na kuwaambia,
"Safari imeishia hapa! Nashukuruni kwa kila kitu."
Marshall akamtazama Danielle na kisha Jack. Wote walikuwa wamepigwa na bumbuwazi. Hawakuwa wanaamini kile kilichokuwa kinatukia mbele ya macho yao.
Basi kwakuwa walikuwa wameonyeshewa silaha, hawakuwa na ujanja. Wote wakanyoosha mikono juu na kutii. Marietta akawataka waende nje na kujitupia majini.
Taratibu wakasonga, kabla hawajafikia mlango, sauti ya koki ya bunduki ikaita. Kutazama alikuwa ni Kelly. Mwanamke huyo alikuwa amemnyooshea Marietta bunduki kichwani.
"Weka silaha chini!" Akafoka.
"Kelly!" Marietta akastaajabu. Alitoa macho ya woga na mashaka.
"Weka silaha chini sasa hivi!"
"Kwanini unafanya hivi?" Marietta akauliza.
"Nina mimba ya Jack. Mtoto wangu hawezi kuwa yatima. Ni hivyo."
Marietta akang'ata meno yake kwanguvu. Akajilaumu kwanini hakufikiria kuhusu hilo swala mara zote vile alipokuwa anamwona Kelly akihangaika.
Akajiona mjinga.
Lakini hakutaka kutii amri. Hakutaka kushindwa. Aliamishis mkono wake wenye silaha kwa Kelly lakini asiwe mwepesi vya kutosha , Kelly akamuwahi na kumshindilia risasi ya bega!
Asiridhike, akataka kufurukuta tena, sasa ikamlazimu Kelly atumie risasi nyingine kumkalisha. Risasi hiyo ilitoboa shingo ya Marietta na kumlaza mwanamke huyo akiwa hoi bin' taaban chini.
Anavuja damu kupita kiasi. Mkono wake wa kuume ulokuwa umebebelea bunduki sasa umeshikilia jeraha lake.http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Japo alikuwa ni mdhalimu, alitia huruma. Kinywa chake kilikuwa kinatema damu nyingi kwa mtindo wa kwikwi! Kidogo akakata pumzi.
Watu wote walikuwa wanamtazama wakijawa na maswali. Hawakuwa na cha kufanya kumsaidia.
"Mmezungukwa na wanausalama!" Mara wakasikia sauti toka kwenye kipaza. "Wasilisheni silaha zenu na mtoke mikono ikiwa hewani!" Sauti ilinguruma. Kweli walipotazama wakapata kuona wakiwa wamezingirwa na boti tatu na ufukweni kuna watu kadhaa wakiwa wamenyooshea bunduki zao kwao.
Tangazo likarudiwa tena. Mara hii msemaji akasema kwamba hatorudia tena maneno yake kabla hajaruhusu risasi zimwagike hewani!
"Sasa tunafanyaje?" Kelly akauliza. Jack akamtazama mwanamke huyo na kusema, "ni kweli una mimba yangu?"
"Ndio!" Kelly akajibu.
Jack akamsogelea karibu Kelly na kumkumbatia. Alifurahi kusikia habari hiyo japo muda haukuwa sahihi. Angetamani aonane zaidi na Kelly lakini pia na mtoto wao lakini ni wazi muda haukuwa upande wao.
Kitendo hicho kikamgusa Marshall katika namna ya kipekee. Alikuwa amechoka kumwona Jack akiwa hana furaha mbele ya macho yake. Hakuwa radhi hali hiyo iendelee.
Kichwani mwake aliamini, nafasi ya kuchoropoka hapo ilikuwapo. Ndio ni ngumu lakini ipo.
"Moja!" Sauti ikavuma toka kwenye kipaza. Wanajeshi wote walikuwa wamejiandaa kushambulia.
Marshall alitazama pande zote nane za dunia. Akapiga mahesabu yake kichwani juu ya namna watakavyopata salama. Ilikuwa ni ndani ya sekunde tatu tu.
Mara akaropoka, "laleni chini!" Kisha akalitimua boti kwa fujo kufuata boti moja ya wanajeshi. Alipoikaribia akakata kona kali kuibamiza kwa ubavu, alafu akatokome alipopata njia. Huko nyuma risasi zikiwafuata kana kwamba mvua.
**
Baada ya lisaa limoja ...
"Tumeipata. Over! Tumeipata boti, over!" Alisema mwanaume mmoja ndani ya boti ya kijeshi. Mbele ya macho yake kulikuwa na boti kubwa. Boti ambayo ilitumiwa na wakina Marshall kumtimikia.
Basi wakaijongea boti hiyo na kuikagua. Muda si mrefu zikafika hapo boti zingine nne zenye kubebelea wanajeshi. Walipotazama ndani wakapata kukuta mwili wa Abdulaziz. Tayari ulikuwa mfu.
Mbali na hapo hakukuwa na mwili mwingine isipokuwa kutapakaa kwa damu. Walitafuta boti nzima wasione jambo. Sasa Marshall na wenzake walikuwa wapi?
"Hamjawaona?" Sauti ikauliza kwenye radio call.
"Hapana mkuu. Kuna maiti ya Abdul pekee, over!"
Wakati huo kwenye masafa ya maji umbali kabisa na nchi ya Morocco, Marshall alikuwa ameketi kwenye kiti cha mbele cha boti. Mkono wake ulikuwa umebebelea kinywaji kwenye glasi na pembeni yake alikuwa ameketi bwana James Peak.
Bwana huyo alikuwa amevalia suti yake maridadi kabisa, naye mkononi alikuwa amebebelea glasi yenye kinywaji. Huko nje kulikuwa na makomando waliokuwa wamebebelea bunduki wakitazama usalama.
Boti hiyo ilikuwa na chapa ya bendera ya Marekani ubavuni mwake.
"Ulijuaje yote haya?" Akauliza Marshall akimtazama James. Kwanza James akatabasamu,
"Kila mtu anajua ulimwenguni kinachoendelea Morocco. Unadhani nisingefahamu na Marietta alikuwa ameelekea huku? Nalijua nanyi mtakuwapo. Ian amenieleza mengi sana."
"Na vipi ukapewa vyote hivi na serikali?"
"Sababu ya vielelezo vya Ian na vyangu pia. Anyways, mimi sikuwa polisi mpelelezi tu kama ulivyokuwa unajua wewe."
Marshall hakuuliza tena. Alitaka tu kupumzika hivi sasa. Alimuaga James na kwenda zake ndani kukutana na wenziwe. Haikuwa rahisi kabisa. Hata alipowaona wakiwa hai alipata kufurahi sana moyoni mwake.
Hakika ilikuwa ni misheni ya aina yake.
**
Baada ya mwezi mmoja ...
"Anaendeleaje kwa sasa?"
"Yu vema."
"Amerejesha kumbukumbuze?" Marshall akauliza tena.
"Kwa kiasi kikubwa. Kadiri anavyokaa na mwanaye maendeleo yake hushamiri. Muda si mrefu atakuwa na uwezo wa kueleza kila kitu."
"Nashukuru, James."
"Hillton. Ni bwana Hillton, Marshall."
"Hilo la James limekaa sana. Itachukua muda kidogo kulifuta. Anyways, nashukuru na uwe na siku njema."http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Marshall akakata simu na kwenda kujumuika na wenzake. Alimkumbatia Danielle akambusu kisha akamtaka Jack apandishe sauti ya muziki.
"Huoni itamwathiri mtoto wangu?" Jack akauliza akishika tumbo la Kelly. Wote wakajikuta wakicheka.
"Jack," Danielle akaita na kuuliza, "hautaki tumfuatilie tena yule mwingine na bwana wake?"
Jack akakunja sura. Wote wakacheka tena.
**
MWISHO
0 comments:
Post a Comment